Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Ridhiwani Jakaya Kikwete (10 total)

MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE (K.n.y MHE. KHATIB SAID HAJI) aliuliza:-
Kutokana na Sheria ya Makosa ya Kimtandao (Cyber Crime Act) kuanza kutumika hapa nchini:-
Je, ni mafanikio gani yamepatikana na kuanza kutumika kwa sheria hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khatibu Said Haji, Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 13 ya mwaka 2015 iliyoanza kutumika Septemba, 2015 ililenga kuainisha makosa yanayohusiana na matumizi ya mfumo wa kompyuta na teknolojia ya habari na mawasiliano, kuweka utaratibu wa upelelezi, ukusanyaji na matumizi ya ushahidi wa kielektroniki. Kupungua kwa makosa ya mtandao, kuchukua hatua stahiki pindi makosa yanapotendeka na kuimarika kwa matumizi salama ya mtandao katika shughuli mtambuka ikiwemo fedha, biashara, elimu na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuwepo kwa Sheria ya Mtandao kumesaidia kupungua kwa usambazaji wa ujumbe wa uchochezi ambazo zingepelekea uvunjifu wa amani, kupungua kwa uwekaji wa picha za ngono kwenye mitandao ya kijamii ambapo zingepelekea uporomokaji wa maadili, kupungua kwa makosa ya udhalilishwaji kwa njia ya mtandao na kupungua kwa usambazwaji wa nyaraka za siri za Serikali kwenye mitandao ya kijamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia Agosti 2014 hadi Septemba 2015, kabla ya Sheria kuanza kutumika uwekaji wa picha za ngono mtandaoni, matukio yalikuwa 459 yalitolewa taarifa Polisi, usambazaji wa ujumbe wa uchochezi matukio yalikuwa sita, matumizi mabaya ya mtandao matukio yalikuwa 117 na usambazaji wa nyaraka za siri za Serikali matukio yalikuwa tisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu zinaonesha kuwa kuanzia Oktoba, 2015 sheria hii ilipoanza kutumika hadi Mei 2016 tukio moja lilitolewa taarifa Polisi kuhusu uwekaji wa picha za ngono. Usambazaji wa ujumbe wa uchochezi hakukuwa na tukio lolote, matumizi mabaya ya mtandao hakukuwa na tukio lolote na usambazaji wa Nyaraka za siri za Serikali matukio mawili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutumika kwa sheria hii, baadhi ya makosa ya mtandao yameshafikishwa mahakamani ikiwa ni pamoja na kesi nne za uchochezi kwa kutumia mtandao, kesi moja ya kutoa taarifa ya Uchaguzi wa 2015 bila kibali cha Tume ya Uchaguzi, kesi moja ya kutengeneza na kusambaza Matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 yasiyo sahihi kwenye mtandao na kesi moja ya kutoa taarifa zisizo sahihi kwa njia ya mtandao.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE Aliuliza:-
Kwa kipindi kirefu wananchi wa Halmashauri ya Chalinze wamekuwa katika sintofahamu juu ya lini mradi wa maji wa Wami - Chalinze utakamilika ili wananchi hao waweze kunywa maji safi kama walivyoahidiwa.
(a) Je, Serikali inaweza kueleza ni lini mradi utakamilika?
(b) Kwa kuwa mradi huu umekuwa unakwenda taratibu sana; je, tatizo lake ni nini?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Kikwete, Mbunge wa Chalinze, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, Benki ya Maendeleo ya Waarabu yaani BADEA, Washirika wa Maendeleo (DPs) kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP) na Mkopo kutoka Serikali ya India kupitia Exim Bank kwa pamoja zimetoa jumla ya shilingi bilioni 164 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji Chalinze kwa Awamu ya I, II na III. Gharama
ya utekelezaji wa miradi hiyo ni shilingi bilioni 23.4 kwa Awamu ya I, Awamu ya II ni shilingi bilioni 53.7 na shilingi bilioni 86.9 kwa awamu ya III.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kukamilika kwa Awamu ya I na ya II ya mradi wa Chalinze jumla ya vijiji 88 vimenufaika na kupelekea hali ya upatikanaji wa maji Chalinze kufikia asilimia 88 ya wakazi wote waishio katika eneo lote linalopitiwa na mtandao wa maji. Vijiji 12 vya Mwidu, Visakazi, Lulenge, Tukamisasa, Kinonko, Bwawani, Sinyaulime, Gwata, Ngerengere, Kidugalo, Kambi ya Kinonko na Sangasanga ambavyo vipo katika Awamu ya II vitaanza kunufaika na huduma ya maji ifikapo mwishoni mwa mwezi Aprili, 2017 baada ya kukamilika majaribio ya bomba kuu. Vijiji vitatu vya Kwang’andu, Kifuleta na Kwaruhombo vitaanza kupata maji baada ya mkandarasi kufanya maboresho ya pampu
ambazo zimeonekana hazifanyi kazi ilivyotarajiwa. Mkandarasi ameagizwa kuhakikisha pampu hizo zinafanya kazi kabla Juni, 2017.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali inatekeleza mradi katika Awamu ya III ambapo kazi zitakazofanyika ni pamoja na upanuzi wa mtambo wa kuzalisha maji, ujenzi wa mabomba makuu ya kusafirisha maji (kilometa 115), ujenzi wa mfumo wa mabomba yakusambaza
maji (kilometa 1022), ujenzi wa matanki makubwa 19 na ujenzi wa vituo tisa vya kuchotea maji na ujenzi wa vioski vya kuchotea maji 351. Awamu hii kimkataba ilitakiwa iwe imekamilika tarehe 22 Februari, 2017, mpaka sasa ni asilimia 23 tu ya kazi ndiyo imefikiwa. Serikali imechukua hatua za kimkataba ikiwemo kutoa notice ya siku 100 ili aongeze kasi vinginevyo tutasitisha mkatabaifikapo tarehe 31 Mei, 2017.
MHE. ORAN M. NJEZA (K.n.y. MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE) aliuliza:-
Hivi karibuni kumetokea mapigano baina ya wakulima na wafugaji ambayo yamesababisha baadhi ya Watanzania kupoteza maisha na wengine kupata ulemavu wa maisha:-
Je, Serikali imejipangaje kupambana na janga hilo?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Kikwete, Mbunge wa Chalinze, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kumekuwa na migogoro kati ya wakulima na wafugaji katika maeneo kadhaa ndani ya nchi yetu ambayo yamesababisha Watanzania kupoteza maisha na wengine kupata ulemavu wa kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na hali hiyo Serikali kupitia Jeshi la Polisi inaendelea kushauriana na Mamlaka zinasosimamia matumizi bora ya ardhi, kutenga maeneo yatakayotumiwa na wakulima na wafugaji ili kuepusha migogoro na kutoa elimu kwa wakulima na wafugaji juu ya mazingira bora ya matumizi ya ardhi. Aidha, Jeshi la Polisi hufanya doria na misako na kukamata wale wanaovunja Sheria punde panapokuwepo na mwingiliano wa matumizi bora ya ardhi katika maeneo yanayosababisha migogoro.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA (K.n.y. MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE) aliuliza:-
Maeneo ya Munguatosha na Hondogo ni baadhi ya maeneo ambayo yanahitaji transfoma ili umeme uwake.
Je, Serikali ina mpango gani juu ya kupeleka transfoma katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Kikwete, Mbunge wa Chalinze kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Hondogo kimewekwa katika mradi wa REA Awamu ya III kupitia Mradi wa Densification Awamu ya Kwanza ulioanza mwezi Machi, 2017 unaotekelezwa na kampuni ya STEG. Mkandarasi tayari amesimamisha nguzo 111 na kuvuta waya wenye urefu wa kilometa 4.5. Hatua inayofuata ni ufungaji wa transfoma yenye uwezo wa kVA 50 itakayofanyika mwishoni mwaka mwezi Novemba, 2017. Wateja wapatao 65 wanatarajiwa kuunganishiwa umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kitongoji cha Munguatosha kilichopo katika Kijiji cha Makore kimejumuishwa na kitapatiwa umeme kupitia REA awamu ya III chini ya Grid extension utakaotekelezwa na kampuni ya Sengerema Engineering Group Limited.
Kazi ya kupeleka umeme katika Kitongoji cha Munguatosa inajumuisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa mbili, ufungaji wa transfoma yenye uwezo wa kVA 50 pamoja na kuunganisha wateja wapatao 46. Utekelezaji wa mradi huu ulianza mwezi Julai, 2017 na utakamilika mwezi Juni, 2019.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE aliuliza:-
Maeneo mengi ya Halmashauri ya Chalinze yamefaidika na Mradi wa REA Awamu ya Pili lakini katika utekelezaji wa mradi huo Miji ya Kiwangwa, Hondogo, Mkange na Kibindu bado haijafikiwa. Je, Serikali ina mpango gani wa kuifikia miji hiyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Kikwete, Mbunge wa Chalinze, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Kiwangwa katika Jimbo la Chalinze umepatiwa umeme kupitia mradi uliotekelezwa na TANESCO kwa ufadhili wa Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) awamu ya kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu ulishakamilika na wateja zaidi ya 600 wameunganishiwa umeme. Kijiji cha Hondogo kimepatiwa umeme kupitia mradi wa densification awamu ya kwanza uliokuwa unatekelezwa na Mkandarasi Kampuni ya STEG international Services kutoka Tunisia. Kazi za mradi huu zimegharimu shilingi bilioni 1.16 ambapo wateja zaidi ya 66 wameunganishiwa umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kijiji cha Mkange kitapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA Peri Urban utakaotekelezwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2018/2019. Mradi huu unahusisha ujenzi wa njia za umeme wa msongo wa kilovolt 33 wenye urefu wa kilometa 26 kutoka Miono hadi Saadani utakaonufaisha Vijiji vya Manda, Mazingara na Gongo. Gharama za kuvipatia umeme vijiji hivi ni shilingi bilioni tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kijiji cha Kibindu kitapatiwa umeme kupitia njia ya umeme ya msongo wakilovolt 33 yenye urefu wa kilometa 66 kutoka shule ya sekondari Changarikwa. Njia hii ya umeme itanufaisha pia vijiji vya Kwaruhombo, Kwamduma, Kwamsanja na Kwankonje. Gharama ya kufikisha umeme katika vijiji hivi ni shilingi bilioni tano. Kazi hizi zitatekelezwa kupitia mradi wa REA Awamu ya Tatu, mzunguko wa pili unaotarajiwa kuanza mwezi Julai, 2019 na kukamilika mwaka 2021. Ahsante. (Makofi)
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE aliuliza:-
Ni Sera ya Serikali kuhakikisha mawasiliano baina ya watu wake katika maeneo ya nchi yanawezeshwa na kujengwa kikamilifu:-
Je, Serikali imejipangaje kuhusu utekelezaji wa ahadi ya ujenzi wa Daraja la Wami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Kikwete, Mbunge wa Chalinze, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kuwa Daraja la sasa la Wami lenye urefu wa mita 88.75 lililopo Mkoa wa Pwani ambalo ni jembamba ni kiungo muhimu katika Barabara Kuu ya Chalinze – Segera. Kwa kutambua umuhimu huo, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imeanza maandalizi ya ujenzi wa daraja jipya litakalojulikana kwa jina la Daraja Jipya la Wami (New Wami Bridge) ambapo mnamo tarehe 28 Juni, 2018, ilisaini mkataba wa ujenzi na Kampuni ya Power Construction Corporation ya Nchini China kwa gharama ya Sh. 67,779,453,717 na muda wa ujenzi ni miezi 24. Daraja Jipya la Wami litakuwa na urefu wa mita 513.5 na upana wa mita 11.85 na litajengwa umbali wa mita 670 pembeni ya daraja la zamani kwa upande wa chini yaani Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu na wananchi kuwa ujenzi wa daraja hili jipya utagharamiwa na Serikali kwa asilimia 100 na utajumuisha ujenzi wa barabara unganishi za daraja kwa pande zote mbili zenye jumla ya kilometa 3.82 ili kuweza kuunganisha daraja jipya na Barabara Kuu ya Chalinze – Segera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa mkandarasi yuko kwenye hatua ya maandalizi ya ujenzi, yaani ujenzi wa ofisi na nyumba za wafanyakazi pamoja na kuleta vifaa, mitambo na wataalam ili kazi ya ujenzi wa daraja ianze.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE aliuliza:-

Katika kikao cha kazi, Mheshimiwa Rais akiwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Hamis Kigwangalla na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega alitoa maelekezo ya kutoondoa Vijiji vilivyomo katika maeneo ya Hifadhi:-

(a) Je, tangazo hilo linamaanisha kuwa wameruhusiwa kuendelea na shughuli za kiuchumi katika maeneo yao wanayoishi?

(b) Je, ni lini sasa Serikali itashughulikia migogoro ya mipaka baina ya Vijiji hivyo na Hifadhi au kwa tamko lile maana yake Wanavijiji waendelee kama vile hakukuwahi kuwa na migogoro?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tarehe 15 Januari, 2019, Mheshimiwa Rais Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa agizo la kutoviondoa vijiji 366 vilivyoainishwa kuwa na migogoro na maeneo ya hifadhi. Aidha, alisisitiza kwamba agizo hilo halina maana kwamba sasa wananchi wanaruhusiwa kuvamia maeneo ya hifadhi.

Mheshimiwa Spika, baada ya Mheshimiwa Rais kutoa maelekezo hayo, Kamati Maalum kwa lengo la kumshauri Mheshimiwa Rais namna bora ya kutekeleza agizo hilo iliundwa. Kamati hii inaongozwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi. Wizara nyingine zinazohusika ni Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Wizara ya Maliasili na Utalii, Mifugo, Uvuvi, TAMISEMI, Ulinzi, Kilimo na Maji. Jukumu la Kamati litakapokamilika, taarifa itawasilishwa kwa Mheshimiwa Rais na maelekezo yatatolewa kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, kufuatia Kamati kukamilisha kazi yake na taarifa kuwasilishwa kwa Mheshimiwa Rais, Wizara ya Maliasili na Utalii itapitia upya mipaka ya hifadhi mbalimbali kwa kuzingatia ushauri wa Kamati na maelekezo ya Mheshimiwa Rais. Kazi hii itahusisha uwekaji wa vigingi vipya (beacons) katika mipaka yote.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE aliuliza:-

Wakati wa ziara ya Makamu wa Rais Wananchi wa Halmashauri ya Chalinze walihakikishiwa kuwa maji yataanza kutoka kuanzia tarehe 31 Disemba, 2018 lakini hadi leo hali imekuwa mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa mwanzo?

(a) Je, Serikali inawaambia nini wananchi wa Chalinze juu ya hali mbaya ya upatikanaji wa maji?

(b) Je, Waziri yupo tayari twende pamoja Chalinze kufanya Mkutano kuwaambia wananchi juu ya hali ya maji katika Halmashauri yetu na lini sasa wananchi wa Chalinze watarajie maji kuanza kutoka kwenye mabomba?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Kikwete Mbunge wa Jimbo la Chalinze lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya upatikanaji wa hali ya maji katika Jimbo la Chalinze. Katika kuhakikisha changamoto hiyo inatatuliwa, Serikali imeshakamilisha mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji kwa awamu ya kwanza na Awamu ya II. Kwa sasa Serikali inatekeleza mradi wa maji Chalinze kwa Awamu ya III kwa upanuzi wa mtambo wa kuzalisha maji na mtandao wa usambazaji maji katika maeneo mbalimbali. Katika utekelezaji wa Awamu ya II tayari vituo vya kuchotea maji 96 vimeunganishwa na wananchi wanaendelea kupata maji.

Mheshimiwa Spika, ili kuongeza hali ya upatikanaji wa maji wa wananchi wa Chalinze, Serikali inatekeleza mradi mwingine mkubwa kutoka Mlandizi hadi Chalinze Mboga. Mradi huu utakapokamilika utamaliza kabisa tatizo la maji katika eneo la Chalinze.

Mheshimiwa Spika, nipo tayari kufanya ziara pamoja na Mheshimiwa Mbunge katika Jimbo la Chalinze na kuwaeleza wananchi mipango mbalimbali ya Serikali katika kutatua tatizo la maji.
MHE. BONNAH L. KAMOLI K.n.y. MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itawalipa fidia Wananchi wa Chalinze waliopisha ujenzi wa miundombinu ya miradi ya kusafirisha umeme kutoka Kinyerezi na Bwawa la Mwalimu Nyerere?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Kikwete, Mbunge wa Chalinze, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TANESCO inatekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 400 kutoka Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Mwalimu Julius Nyerere hadi Chalinze lakini pia ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme katika Kijiji cha Chaua - Chalinze.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TANESCO imekamilisha tathimini ya mali za wananchi na Taasisi zilizopisha utekelezaji wa mradi huu na fidia kuidhinishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali. Jumla ya shilingi bilioni 42.3 zimetengwa katika bajeti ya mwaka 2021/2022 kwa ajili ya malipo ya fidia kwa wananchi waliopisha mradi. Fidia ya wananchi hao itaanza kulipwa muda wowote kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 baada ya taratibu zote kukamilika.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Bonde la Ruvu linatumika kwa kilimo cha umwagiliaji ili kukabiliana na changamoto ya usalama wa chakula?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Kikwete Mbunge wa Jimbo la Chalinze kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Bonde la Ruvu ni moja kati ya mabonde yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji ambacho kinasaidia uhakika wa chakula na kukabiliana na changamoto ya usalama wa chakula. Serikali imeianisha takribani skimu 21 zenye eneo la ukubwa wa takribani hekta 85,075 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji katika Bonde la Ruvu katika Mikoa ya Morogoro na Pwani. Aidha, jumla ya hekta 1,284 zimeendelezwa kwa kuwekewa miundombinu ya umwagiliaji na wakulima wanatumia eneo hilo kwa ajili ya uzalishaji wa mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kuendeleza ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu zote zilizopo katika Bonde la Ruvu kama zilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Umwagiliaji wa mwaka 2018. Aidha, utekelezaji wa mpango huo umeshaanza katika skimu za Tulo (Morogoro DC), Msoga (Bagamoyo DC), Kwala (Kibaha DC) na Bagamoyo.