Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Deo Kasenyenda Sanga (28 total)

MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-
Serikali ilichukua eneo kubwa kwa ajili ya kujenga Soko la Kimataifa, Makambako na iliahidi kulipa fidia wananchi waliopisha ujenzi huo; na Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni aliahidi kuwalipa fidia hiyo:-
Je, ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi hao?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Makambako, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa mpango wa kujenga Soko la Kimataifa la Makambako ni wa muda mrefu na suala la wananchi kulipwa fidia limechukua muda mrefu pia. Sababu zilizosababisha kuchelewa ni ufinyu wa bajeti na hivyo kusababisha kurudia kufanya tathmini ya mali na mazao ya wananchi waliotoa maeneo ya kupisha mradi huu. Tathmini ya kwanza ilifanyika mwaka 2011 na kurudiwa mara ya pili mwaka 2015 baada ya muda wa kulipa fidia kisheria kupita.
Mheshimiwa Spika, tayari Mthamini Mkuu wa Serikali amepitisha tathmini hii mpya na hivyo, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji wa Makambako itatenga fedha kwa ajili ya malipo ya fidia katika mwaka wa fedha 2016/2017. Kwa hiyo, wananchi waliotoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa Soko la Kimataifa, Makambako watalipwa fidia katika mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-
Serikali imeshaweka Mkandarasi ambaye kwa sasa yuko site anaendelea na kazi ya Mradi wa umeme katika Vijiji vya Mawande-Utengule, Luhota, Ngamanga, Ikwata, Mlowa, Mkolanga, Ibumila, Mahongole, Manga Usetule, Kifumbe, Mtanga, Kitandililo, Ibatu, Nyamande, Mtulingala na Mbugani;
Je, ni lini mradi huo wa umeme katika vijiji hivyo utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyanda Sanga, Mbunge wa Makambako, kama ifuatavyo:-
Ni kweli kwamba Serikali imeweka Mkandarasi Lucky Exports ambaye kwa sasa anatekeleza mradi wa REA awamu ya pili Mkoani Njombe. Mkandarasi huyo amepewa Vijiji vya Ikwata, Kifumbe, Luhota, Manga, Mlowa, Mwande, Ngamanga, Usetule pamoja na Utengule, ambayo amepatiwa kama kazi ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kazi ya usanifu tayari imekamilika na kwa sasa Mkandarasi anasubiri kusaini Mkataba kati yake na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kabla ya mwezi Machi mwaka huu, ili aanze utekelezaji wa mradi. Kazi ya kupeleka umeme katika vijiji hivi unajumuisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomiti 38.8, lakini pia ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilomita 51, ufungaji wa Transfoma 19 ambapo transforma nne za ukubwa wa kVA 25 na transfoma 15 za ukubwa kwa kVA50. Hii ni pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 1,875. Kazi hii itachukua miezi sita kukamilika na itagharimu shilingi bilioni 3.3.
Mheshimiwa Spika, Vijiji vya Mahongole, Manga, Mbugani, Mtanga, Mtulingala, na Nyamande vimewekewa umeme kwenye Mradi wa awamu ya tatu, (REA phase III) inayoanza utekelezwa hivi karibuni. Kazi ya kupeleka umeme kwenye Vijiji hivi inajumuisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33, yenye urefu wa kilomita 73, ujenzi wa njia ya umeme wa msongo kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilomita 36, ufungaji wa transfoma 14 ambapo transfoma tano za ukubwa wa kVA 25 na transfoma tisa za ukubwa wa kVA 50. Hii ni pamoja na kuwaunganishia umeme wateja awali 1493. Kazi hii itaanza Julai mwaka huu na itagharimu shilingi bilioni 4.05.
Mheshimiwa Spika, Vijiji vya Ibatu, Ibumila na Kitandililo tayari vimefanyiwa tathmini ya gharama za kupeleka umeme na kazi inatakiwa kufanyika kwenye kazi za nyongeza lakini kutokana na gharama kuwa kubwa itajumuishwa kwenye mradi wa awamu ya tatu.
Mheshimiwa Spika, kazi ya kupeleka kwenye vijiji hivi inajumuisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu kilomita 11, ujenzi wa njia ya umeme wa msongo kilovoti o.4 yenye urefu wa kilomita 13 pamoja na ufungaji wa transfoma tano ambapo transfoma ambapo transfoma moja ina ukubwa wa kVA 50 na transfoma Nne za ukubwa kVA 100.
Hii pia itaunganisha pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 589. Kazi hii itaanza Julai, 2016 na itagharimu takribani shilingi milioni 885.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-
Miradi ya Maji Manga pamoja na Kijiji cha Mutulingara inasuasua tu mpaka sasa.
Je, ni lini miradi hii itapatiwa fedha ili iweze kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Jimbo la Makambako, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Miradi ya Maji ya Manga na Mutulingara, ni miongoni mwa miradi ya Vijiji 10 inayotekelezwa katika Halmashauri ya Mji wa Makambako. Kazi ya ujenzi wa Mradi wa Maji katika Kijiji cha Manga inaendelea na hadi kufikia mwezi Machi, 2016, utekelezaji wake ulifikia asilimia 90. Serikali tayari imemlipa mkandarasi kiasi cha shilingi milioni 235.08 kati ya shilingi milioni 491.9 anazodai.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ujenzi wa Mradi wa Mutulingara, bado haujaanza kutokana na changamoto ya upatikanaji wa fedha. Serikali itaendelea na utekelezaji wa mradi huu katika awamu ya pili ya Program ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Aidha, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 992.8 kwa ajili ya miradi ya maji katika Halmashauri ya Mji wa Makambako.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-
Serikali ilipandisha hadhi Kituo cha Afya cha Makambako kuwa Hospitali lakini tatizo kubwa lililopo ni ukosefu wa vifaa tiba na kufanya watu wengi kwenda kutibiwa Kibena, Njombe au Ilembula.
Je, ni lini Serikali itapeleka vifaa hivyo ili watu wasipate taabu ya kwenda kutibiwa Kibena, Njombe au Ilembula?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Makambako, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kupandisha hadhi Kituo cha Afya Makambako kuwa Hospitali, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilitoa vifaa mbalimbali vikiwemo vifaa vya umeme chumba cha upasuaji, kitanda cha kufanyia upasuaji na seti tatu za vifaa vya upasuaji akina mama wajawazito na seti mbili za upasuaji mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizo, tukiri kwamba bado upo upungufu wa vifaa kama vile X-ray, Ultrasound, ECG machine na mashine ya dawa za usingizi, pulse oxymeters, monitors, seti ya mashine ya kufulia nguo na vifaa vya meno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 imetenga shilingi milioni 20.9 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kupitia vyanzo vya mapato ya ndani. Aidha, Halmashauri imepanga kukopa shilingi milioni 154.2 kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-
Kutoka Kijiji cha Mutelewele kwenda Makambako ni kilometa tano wakati kwenda Halmashauri ya Wanging‘ombe ni kilometa 65; kutoka Kata ya Soja kuja Makambako Mjini ni kilometa 25 na kwenda Halmashauri yao ya Wanging‘ombe ni kilometa 88 na kutoka Kijiji cha Nyigo kuja Makambako ni kilometa 8 wakati kwenda Halmashauri ya Mufindi ni kilometa 88 na huduma zote zikiwemo matibabu wanazipata Makambako; kutoka Kijiji cha Igongolo ni umbali wa kilometa 6 kwenda Makambako wakati kwenda Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ni kilometa 54.
(a) Je, Serikali itakuwa tayari kugawa mipaka upya ili wananchi wapate huduma karibu na Halmashauri yao ili iendane na kauli mbiu ya kusogeza huduma karibu na wananchi?
(b) Je, ni lini sasa Serikali itapima upya mipaka hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Makambako, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo, Vijiji vya Mutewele na Saja viko katika Halmashauri ya Wilaya ya Wanging‘ombe na Kijiji cha Nyigo kiko katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi. Aidha, ni ukweli usiopingika kuwa vijiji hivyo kijiografia viko karibu na Halmashauri ya Mji wa Makambako kwa maana ya huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na nia njema ya Mheshimiwa Mbunge ya kusogeza huduma za jamii karibu na wananchi vipo vigezo na taratibu zinazozingatiwa katika kusajili au kubadili mipaka ya vijiji. Mapendekezo haya yanapaswa kujadiliwa kwanza katika Mikutano Mikuu ya Vijiji, Kamati za Maendeleo ya Kata, Mabaraza ya Madiwani ya Halmashauri zote, Kamati za Ushauri za Wilaya (DCC) na Kamati za Ushauri za Mikoa. Hii ni kutokana na ukweli kuwa mabadiliko ya mipaka hiyo yataathiri mipaka ya utawala ya Mikoa ya Iringa na Njombe ambapo lazima wadau wa pande zote wakubaliane kuhusu maamuzi hayo.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika sehemu (a) ya jibu hili, napendekeza haya yapitishwe kwanza kwenye vikao vilivyotajwa na endapo vitaridhiwa, Ofisi ya Rais, TAMISEMI itayafanyia kazi mapendekezo hayo sambamba na maombi yaliyowasilishwa kutoka maeneo mengine.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-
Serikali iliahidi kujenga Vyuo vya VETA kwa kila Wilaya ili kuwasaidia vijana
kujifunza stadi za kazi mbalimbali:-
(a) Je, hadi sasa ni Vyuo vingapi vya VETA vimeshajengwa katika nchi
nzima?
(b) Je, ni lini Chuo cha VETA kitajengwa katika Wilaya ya Njombe?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,
napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa
Makambako, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa Serikali kupitia Mamlaka ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA imeshajenga na kumiliki vyuo 29 vya
ufundi stadi vya ngazi ya Mkoa, Wilaya na vyuo maalum vya ufundi. Vyuo hivyo
orodha yake ni Mikoa ni Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Lindi, Mtwara, Moshi,
Manyara, Dodoma, Kigoma, Mbeya, Iringa, Mwanza, Kihonda na Tabora. Vyuo
vya Wilaya ni Dakawa, Mikumi, Singida, Songea, Mpanda, Shinyanga, Kagera,
Mara, Makete, Ulyankulu na Arusha ambapo vyuo maalum vya ufundi ni pamoja
na Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro, Chuo cha Mafunzo ya TEHAMA
Kipawa na Chuo cha Mafunzo ya Hoteli na Utalii -Njiro.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa sasa haina mpango wa
kujenga chuo cha ufundi stadi katika Wilaya ya Njombe, badala yake
itaviboresha Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi - Njombe na Ulembwe na
kuvijengea uwezo ili viweze kutoa mafunzo ya ufundi stadi sanjari na mafunzo ya
maendeleo ya wananchi. Aidha, Mkandarasi wa ujenzi wa Chuo cha VETA cha
Mkoa wa Njombe ameshapatikana ambaye anaitwa Herkin Builders Limited na
yupo katika eneo la kazi, Kijiji cha Shaurimoyo Wilaya ya Ludewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo hicho kinajengwa katika eneo hilo
kimkakati kutokana na miradi ya chuma na makaa ya mawe ya Mchuchuma na
Liganga. Vilevile, Wizara kupitia bajeti ya mwaka 2016/2017 imetenga fedha kiasi
cha shilingi milioni 450 kwa ajili ya kujenga bweni katika chuo cha VETA Makete ili
kuongeza udahili kwa wanafunzi wanaotoka maeneo ya mbali.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-
Mwaka 2014 Rais wa Awamu ya Nne alipokuja Makambako aliahidi kutoa Sh.600,000,000/= ili zisaidie kuboresha au kuchimba bwawa la maji Makambako litakalotoa huduma ya maji kwa wananchi wa mji huo:- Je, ni lini fedha hizo zitatolewa ili zifanye kazi iliyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Jimbo la Makambako, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Awamu ya Kwanza ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji imekamilisha usanifu na uandaaji wa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya mradi wa maji Makambako. Mradi huu utahusisha ujenzi wa bwawa eneo la Tagamenda, chujio la kutibu maji, matanki ya kuhifadhi maji na ulazaji wa bomba kuu na mabomba ya kusambaza maji. Mradi huu unatarajiwa kugharimu dola za Marekani milioni 38. Serikali imepata mkopo wa gharama nafuu kutoka Serikali ya India kwa ajii ya utekelezaji wa mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali wakati inasubiri utekelezaji wa mradi huo mkubwa imechukua hatua za dharura za kuboresha hali ya huduma ya maji mjini Makambako kufuatia ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alipotembelea Mji wa Makambako. Mradi huu unakadiriwa kugharimu kiasi cha shilingi milioni 654. Kazi zitakazotekelezwa kwa mradi huu ni pamoja na ujenzi wa kitekeo, tanki, bomba kuu, pampu ya maji na nyumba ya pampu. Kiasi cha shilingi bilioni mbili kimetengwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha 2016/2017 na zabuni imetangazwa tarehe 4/1/2017 na ujenzi wa mradi unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-
Bomba la mafuta la kwenda Zambia limepita katikati ya Mji wa Makambako na barabara ambayo ipo juu ya bomba hilo hairuhusiwi kutengenezwa hivyo kuwa na mashimo mengi na kuhatarisha maisha ya watu wanaoitumia barabara hiyo.
(i) Je, ni lini Serikali italihamisha bomba hilo?
(ii) Je, kwa nini barabara hiyo isitengenezwe, ili wananchi waendelee kupita kwa urahisi wakati Serikali inajipanga kulihamisha bomba la mafuta?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Makambako, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua usumbufu wanaopata wananchi wa Makambako kutokana na bomba la mafuta kwenda Zambia (TAZAMA) linalopita katika Mji wa Makambako. Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inawasiliana na Kampuni ya Tanzania na Zambia ya kusafirisha mafuta kutoka Tanzania kwenda Zambia (TAZAMA Pipeline Limited) kuainisha hatua stahiki zitakazochukuliwa kuondoa tatizo hilo. Wakati mawasiliano yanafanyika pamoja na kuainisha hatua za gharama zitakazotumika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania itatengeneza maeneo yaliyoharibika, ili wananchi waweze kutumia barabara hiyo bila matatizo.
MHE. MAHMOUD H. MGIMWA (K.n.y. MHE. DEO K. SANGA) aliuliza:-
Serikali iliahidi kufuta Ushuru mdogo mdogo unaokusanywa na Halmashauri ili wajasiriamali wadogo wakiwemo akina mama lishe waweze kuongeza kipato kupitia shughuli zao.
Je, ni lini Serikali itatoa tamko rasmi kwa Halmashauri zetu nchini ili wasikusanye tena ushuru huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyanda Sanga, Mbunge wa Makambako kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefuta ushuru na tozo ambazo zilikuwa zinatozwa kwa wafanyabiashara wadogo wadogo wasio rasmi na wanaofanyia biashara katika maeneo yasiyo rasmi mfano Mama Lishe, wauza mitumba wadogo wadogo, wauza mazao ya kilimo wadogo wadogo kama mboga mboga na ndizi na matunda isipokuwa biashara za migahawa na maduka na wale ambao wako kwenye maeneo rasmi. Vilevile wafanyabiashara wadogo walio nje ya maeneo maalum ya kibiashara wenye mitaji chini ya shilingi 100,000 hawatatozwa ada, kodi na tozo zozote. Kodi nyingine zilizofutwa ni ushuru wa huduma (service levy) kwenye nyumba za kulala wageni, ada za vibali vinavyotolewa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo zilikuwa zinatozwa na TFDA, OSHA, Fire na Bodi ya Nyama na ada ya makanyagio.
Serikali pia imepunguza ushuru wa mazao kutoka asilimia tano haid asilimia mbili kwa mazao ya chakula na asilimia tatu kwa mazao ya biashara. Aidha, mazao yanayosafirishwa kutoka wilaya moja hadi nyingine yasiyozidi tani moja hayatatozwa ushuru wa mazao.
MHE. EDWARD F. MWALONGO - (K.n.y. MHE. DEO K. SANGA) aliuliza:-
Mji wa Makambako unakabiliwa na tatizo kubwa la maji kutokana na ongezeko la watu na Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni aliahidi kuanza kwa ujenzi wa mradi wa maji na kazi ya usanifu wa mradi huo imeshafanyika:-
Je, ni lini sasa ujenzi wa mradi huo wa maji utaanza?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Jimbo la Mkambako, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia awamu ya kwanza ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP I) imekamisha upembuzi yakinifu na usanifu wa mradi wa kuboresha huduma ya maji katika Mji wa Makambako. Kazi zitakazotekelezwa katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa Bwawa Tagamenda, uchimbaji wa visima virefu vya Idofi na chemichemi ya Bwawani, ujenzi wa bomba kuu na mfumo wa usambazaji wa maji na matanki makubwa ya kuhifadhi maji. Mradi huo unatarajiwa kunufaisha wananchi wapatao 155,253.
Mheshimiwa Spika, Serikali imepata fedha za kutekeleza mradi huo kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya India wa Dola za Marekani milioni 500 zitakazotumika kutekeleza miradi ya maji katika Miji mbalimbali ukiwemo Mji wa Makambako. Tayari Serikali imesaini Mkataba wa Kifedha na Serikali ya India na ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2018/2019.
MHE. DEO K. SANGA aliuza:-

Serikali ilichukua eneo la Idofu kwa ajili ya kujenga One Stop Center lakini hadi leo wananchi hawajalipwa fidia:-

(a) Je, ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi hao?

(b) Je, ni lini Serikali itaanza kujenga One Stop Center kama ilivyokudia?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Makambako, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilifanya uthamini wa eneo kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Ukaguzi wa Pamoja (One Stop Inspection Station – OSIS) cha Makamboko katika eneo la Idofu Makambako. Tayari kazi ya uthamini wa mali na mazao yatakayoathiriwa na mradi huo imekamika. Wananchi ambapo mali zao zimeathirika na maradi watalipwa fidia kwa kuzingatia Sheria Na.4 ya Ardhi ya mwaka 2001 kabla ya ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa kuanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari imeanza hatua za maandalizi ya awali wa ujenzi wa Kituo cha Ukaguzi wa pamoja kwa kusaini mkataba na Mhandisi Mshauri UWP Consulting (T) Limited akishirikiana na UWP Consulting ya Afrika kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na uandaaji wa nyaraka za zabuni kwa vituo vya Ukaguzi wa Pamoja vya Mikumi, Makambako na Mpemba. Mhandisi Mshauri amekamilisha kazi ya awamu ya kwanza ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali mwezi Juni, 2018. Kazi ya usanifu wa kina itakamilika mwishoni mwa mwezi Februari, 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hizi zinatekelezwa kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia. Malipo ya fidia yakikamilika na Serikali kupata fedha ndipo ujenzi kwa Kituo cha Ukaguzi wa Pamoja cha Makambako utaanza.
MHE. DEO K. SANGA Aliuliza:-

Serikali ilikopa fedha za mkopo nafuu kutoka Serikali ya India kwa ajili ya miradi 26 ya maji ikiwemo Mji wa Makambako.

Je, ni lini mradi huo wa maji utaanza na kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI Alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Makambako kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepata mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 500 kutoka Serikali ya India kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika miji 28 kwa upande wa Tanzania Bara na mradi mmoja upande wa Zanzibar. Utekelezaji wa miradi hiyo umegawanyika katika awamu mbili; awamu ya kwanza ni usanifu na awamu ya pili ni ujenzi wa miradi husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Wizara imefikia katika hatua za mwisho za kumpata mtaalam mshauri kwa ajili ya kuandaa ripoti (detailed project report). Baada ya ripoti ya mradi kukamilika, Wizara itaendelea na hatua ya kutafuta wakandarasi kwa ajili ya ujenzi wa miradi. Ujenzi wa miradi hiyo unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2019/ 2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wa kukamilika miradi hiyo utajulikana mara baada ya usanifu kukamilika.
MHE. NEEMA W. MGAYA (K.n.y. MHE. DEO K. SANGA) aliuliza:-

Askari wa Kituo cha Polisi katika Mji wa Makambako hawana gari la doria wala nyumba za kuishi:-

(a) Je, ni lini Serikali itajenga nyumba za kuishi Askari hao?

(b) Je, ni lini Serikali itatoa gari la doria kwa Kituo cha Polisi Makambako?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Makambako, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Makambako ina askari wapatao 111 na kuna jumla ya nyumba 12 tu katika Mji wa Makambako. Nyumba hizo ni takribani asilimia 11 ya mahitaji halisi ya nyumba za makazi na askari katika mji huo. Hata hivyo, katika jitahada za kutatua changamoto hiyo, mwezi Oktoba, 2018 Serikali imeanzisha ujenzi wa nyumba 20 katika Mji wa Makambako ambapo nyumba hizi kwa sasa zimeshakamilika na askari wameshahamia.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Makambako kwa sasa ina magari matatu; magari mawili ya zamani ambapo moja ni PT. 0766 Landrover inayohitaji matengezo makubwa ili liweze kufanya kazi; na nyingine ni aina ya PT.1912 Toyota Land Cruiser ambayo ndiyo inatumika ingawa inafanyiwa matengenezo ya hapa na pale. Gari hili ndiyo inalotumika kwenye doria na operesheni mbalimbali pamoja na kupeleka askari kwenye matukio makubwa yanayotokea sehemu za mbali. Doria katika Mji wa Makambako hufanyika kwa kutumia gari, miguu pamoja pikipiki.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, mwezi Septemba mwaka 2018 Wilaya ya Makambako imepata mgao wa gari jipya moja aina ya Ashok Leyland kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Jeshi la Polisi katika wilaya hiyo. (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-

Mradi wa Maji wa Bwawani umekuwa ukisuasua kujengwa ikiwemo kuzungushiwa uzio:-

Je, ni lini mradi huo utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Jimbo la Makambako, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mkataba wa ujenzi wa mradi wa kuboresha huduma ya maji kwenye Mji wa Makambako ulisainiwa tarehe 23/05/2017 kati ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Iringa (IRUWASA) na Kampuni ya Ujenzi inayoitwa Building Water and Earth Works Ltd ya Jijini Dar es Salaam kwa gharama ya shilingi bilioni 1,568 ikiwa ni pamoja na kodi ya ongezeko la thamani (VAT). Kazi ya ujenzi ilianza tarehe 08/06/2017 na kwa mujibu wa mkataba, kazi hii ilitakiwa kukamilika tarehe 08/02/2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa utekelezaji wa mradi huu kulijitokeza kazi ya ziada ya ujenzi wa uzio kuzunguka chanzo cha maji cha bwawani ili kuzuia uchafuzi unaofanyika kwenye chanzo hicho. Kazi hii imeongeza muda wa kukamilisha kazi zilizopangwa kwa mujibu wa mkataba hadi tarehe 30/06/2019. Kwa sasa uzalishaji wa maji katika chanzo hicho unaendelea na tayari mradi huo unatoa huduma kwa wananchi. Kazi zilizobaki zitaendelea kukamlishwa huku wananchi wakiendelea kupata huduma ya maji.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza: -

Je, ni lini Mradi wa Kusambaza Maji Mji wa Makambako utaanza?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Makambako, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ilipata mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya India kupitia Benki ya Exim India jumla ya Dola za Marekani milioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika miji 28. Utekelezaji unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Aprili, 2021. Ujenzi wa mradi unatarajiwa kuchukua miezi 24.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-

Je, ni lini Wananchi wa Idofi watalipwa fidia baada ya maeneo yao kuchukuliwa na Serikali kwa ajili ya kujenga Mradi wa Idofi One Stop Centre?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Makambako, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza miradi ya ujenzi wa vituo vya pamoja vya ukaguzi wa magari ya mizigo (One Stop Inspection Station) katika shoroba mbalimbali za barabara nchini, ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Ukaguzi Makambako katika eneo la Idofi.

Lengo la ujenzi wa vituo hivyo ni kupunguza vikwazo visivyo vya kiforodha kwa wasafirishaji wa nchi za SADC na EAC wanaotumia barabara zetu. Vituo hivyo vitakapokamilika vitakuwa na Ofisi ya Polisi, TRA, Afya, Uhamiaji na Vituo vya Mizani katika eneo moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Kituo cha Makambako hadi kufikia Aprili, 2021 jumla ya shilingi 870,182,049 zimelipwa kwa wananchi 39 kati ya 275 wanaopisha ujenzi wa mradi huo. Aidha, Serikali inaendelea kutafuta jumla ya shilingi 3,758,635,767 ili kukamilisha malipo ya fidia kwa wananchi 236 waliosalia. Ahsante.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-

Je, ni lini wananchi wa Makambako watalipwa fidia baada ya maeneo yao kuchukuliwa na Serikali kwa ajili yakuzalisha umeme wa upepo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Makambako, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika juhudi za kuongeza upatikanaji wa umeme nchini kupitia vyanzo mbalimbali, eneo la Kijiji cha Majengo Jijini Makambako, limebainika kuwa na uwezo wa kuwekewa miundombinu ya kuzalisha umeme kupitia nishati ya upepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inakamilisha taratibu za kuingia Mkataba wa uzalishaji wa umeme wa upepo na Mwekezaji Binafsi aitwaye Sin Tan. Kwa mujibu wa Mkataba huo, fidia kwa wananchi wa maeneo yatakayotumika kuzalisha umeme huo, italipwa na mwekezaji huyo, katika kipindi cha kuanzia mwezi Agosti, 2021 na Julai, 2022 ambacho ni kipindi kinachotarajiwa kutekelezwa kwa mradi huo.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha Mradi wa Maji katika Vijiji vya Ikelu, Ibatu, Mtulingala, Nyamande, Usetule Mahongole Wilayani Makambako?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda, Mbunge wa Jimbo la Makambako, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji vya Ikelu, Ibatu, Mtulingala, Nyamande, Usetule na Mahongole. Utekelezaji wa mradi wa maji katika Kijiji cha Ikelu umefikia asilimia 98 na umeanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi wa kijiji husika. Kazi zilizobaki ni ulazaji wa bomba umbali wa kilometa 29.8, ujenzi wa tanki la maji lenye ujazo wa lita 25,000 na ufungaji wa pampu unatarajiwa kukamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi Desemba, 2021.

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi wa maji katika Kijiji cha Ibatu umefikia asilimia 56 ambapo kazi zilizobaki ni ukamilishaji wa ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 100,000, ufungaji wa pampu ya kusukuma maji pamoja na uunganishaji wa umeme. Mradi huo umepangwa kukamilika mwezi Machi, 2022. Aidha, utekelezaji wa miradi katika Vijiji vya Mtulingala - Nyamande - Mbugani na Usetule – Mahongole kwa pamoja umefikia asilimia 67 na inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Machi, 2022.

Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa utekelezaji wa miradi hiyo kutaboresha huduma ya upatikanaji wa maji na kunufaisha wananchi wapatao 18,000 wa vijiji hivyo.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kujenga kilomita sita ya barabara kwa kiwango cha lami katika Mji wa Makambako?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Jimbo la Makambako, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara zilizoahidiwa zinasimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini kwa maana ya TARURA. Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano aliahidi kujenga kilomita sita za barabara kwa kiwango cha lami katika Halmashauri ya Mji wa Makambako ambapo Wakala wa Barabara TANROADS alikasimiwa kutekeleza ujenzi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia mwaka wa fedha 2020/2021, jumla ya kilomita 3.5 zimejengwa kwa kiwango cha lami ambapo jumla ya Shilingi bilioni 1.97 zilitumika katika ujenzi huo. Aidha, Serikali itaendelea kutenga fedha ili kukamilisha ujenzi wa kilomita sita kwa kiwango cha lami kwa kadri fedha zitakavyopatikana. Ahsante sana.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza: -

Je, ni lini Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Makambako wataongezewa posho kama ilivyo katika Halmashauri nyingine nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga Mbunge wa Jimbo la Makambako kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikiwalipa Madiwani wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ikiwemo Halmashauri ya Mji Makambako posho kwa mujibu wa Sheria za Serikali za Mitaa Sura 287 na 288 na kwa kuzingatia Kanuni za Kudumu za Halmashauri husika.

Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka 2019 Halmashauri ya Mji Makambako imekuwa ikilipa posho ya vikao ya Shilingi 50,000 ikiwa ni Shilingi 10,000 zaidi ya kiwango kilichopendekezwa. Aidha, hivi sasa viwango vya posho za safari kwa Halmashauri hiyo vinalipwa kwa kuzingatia waraka wa zamani kwa sababu viwango vya posho mpya havikutengewa bajeti ya mwaka 2022/2023, kwa kuwa wakati maelekezo ya mabadiliko ya posho hizo yanatoka tayari Bajeti ya Halmashauri ilikuwa imeandaliwa na kupitishwa kwenye vikao vya Kisheria vya Maamuzi.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Mji wa Makambako inashauriwa kufanya mapitio ya bajeti au izingatie maelekezo ya Waraka Na. 1 wa Utumishi wa Umma wenye Kumb. Na. CAC.17/228/01/A/176 wa Tarehe 10 Juni, 2022 kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza: -

Je ni lini Serikali itaangalia upya mipaka ya kiutawala katika Jimbo la Makambako?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, URATIBU NA BUNGE (MHE. UMMY H. NDERIANANGA) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kesenyenda Sanga Mbunge wa Makambako kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Ibara ya 74(6)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ndiyo yenye dhamana ya kuchunguza mipaka na kuigawa nchi katika majimbo ya uchaguzi kwa ajili ya uchaguzi wa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, Katika maandalizi ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, Tume kwa kuzingatia matakwa ya Katiba itatangaza utaratibu na sifa za kugawa maeneo mbalimbali kwa ajili ya uchaguzi. Hivyo, Mheshimiwa Mbunge anashauriwa kuwa pindi Tume itakapotoa tangazo la kuanzisha maeneo mapya ya kiutawala, ashirikiane na Mamlaka za kiutawala katika Wilaya na Mkoa kuandaa na kuwasilisha mapendekezo kwa kuzingatia vigezo vitakavyokuwa vimewekwa na Tume. Ahsante.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaangalia upya mipaka ya kiutawala ikiwemo na Halmashauri ya Mji wa Makambako?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Jimbo la Makambako, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikizingatia suala la maendeleo ya mipaka ya maeneo ya utawala ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na kusogeza huduma karibu na wananchi.

Mheshimiwa Spika, mabadiliko ya mipaka ya maeneo ya utawala kwa mujibu wa mwongozo wa uanzishaji wa maeneo ya utawala katika mamlaka za Serikali za Mitaa wa mwaka 2014 huanza na kusudio ambalo hupaswa kujadiliwa katika vikao vya Ngazi ya Halmashauri, Wilaya na Mkoa. Kusudio hilo huwasilishwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia Katibu Tawala wa Mkoa.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI bado haijapokea kusudio la kubadili mipaka kutoka Halmashauri ya Mji wa Makambako. Hivyo, endapo kuna uhitaji wa kubadili mipaka, inashauriwa kuanzisha kusudio na kuliwasilisha katika vikao vya Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango, Baraza la Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) na hatimaye katika Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC).
MHE. NJALU D. SILANGA K.n.y. MHE. DEO K. SANGA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Stendi na Soko la kisasa katika Mji wa Makambako?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Jimbo la Makambako, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Mji wa Makambako ipo kwenye Mradi wa kupendezesha Majiji, Manispaa na Miji (Tanzania Cities Transformation Infrastructures and Competitiveness – TACTIC) ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia. Kupitia mradi huo, Mji wa Makambako utajengewa Stendi na Soko la Kisasa.
MHE. BONIPHACE M. GETERE K.n.y. DEO K. SANGA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaowaongezea posho Madiwani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Makambako, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iliongeza posho za Madiwani ambapo mwaka 2012 posho hizo ziliongezwa kutoka shilingi 120,000 hadi shilingi 250,000 kwa mwezi sawa na ongezeko la asilimia 108.3. Aidha, katika mwaka wa fedha 2014/2015, Serikali ilipandisha tena posho za Madiwani kupitia waraka wa mwaka 2014 kutoka shilingi 250,000 hadi shilingi 350,000 kwa mwezi sawa na ongezeko la asilimia 40 na shilingi 400,000 kwa Meya na Mwenyekiti wa Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuzijengea uwezo Mamlaka za Serikali za Mitaa ili ziweze kubuni na kuimarisha vyanzo vya mapato pamoja na kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha kwa kutumia mifumo ya kieletroniki ya kukusanya na kutumia fedha katika kutekeleza miradi ya maendeleo pamoja na matumizi mengineyo.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapitia upya uhalisia wa malipo ya umeme kwa Vijiji vya Mkolango, Kiumba, Ikwete na Malombwe ambapo walilipia kwa bei ya Mjini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Makambako, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Vijiji vya Ikwete na Mkolango, wananchi wote wa maeneo hayo wanalipia gharama ya shilingi 27,000 kwa ajili ya kuunganishiwa umeme. Aidha, Vijiji vya Malombwe na Kihumba ni miongoni mwa vijiji vyenye sura ya Vijiji-Miji ambavyo kwa tathmini ya awali, vilionekana vinastahili kulipia shilinigi 320,960 kama garama ya kuunganishiwa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kubaini changamoto katika tathmini ya awali, Serikali kupitia TANESCO inaendelea kufanya tathmini ya maeneo yote yenye sura ya Vijiji-Miji yakiwemo maeneo ya Malombwe na Kiumba ili kuyapatia suluhisho la gharama za kuunganishiwa umeme. Serikali inaendelea kuomba wananchi wa maeneo hayo wawe na subira wakati suala hili linashughulikiwa.
MHE. FESTO R. SANGA K.n.y. MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka fedha za ujenzi wa Shule ya Sekondari katika Kata ya Mjimwema Makambako?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Jimbo la Makambako, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI inatekeleza mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ambapo ujenzi wa shule mpya unafanyika katika Kata ambazo hazina shule. Katika awamu ya kwanza shule 231 zimejengwa.

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi unaendelea ambapo jumla ya shule 1,000 zitajengwa na mchakato wa kupeleka fedha kwa Halmshauri utakapokamilika fedha hizo zitapelekwa. Hivyo, Halmashauri iweke kipaumbele cha ujenzi wa shule hii kwenye mpango wake kwa awamu zijazo katika Kata ambazo hazina shule ikiwemo Kata ya Mjimwema Makambako.
MHE. BONIPHACE M. GETERE K.n.y. MHE. DEO K. SANGA aliuliza: -

Je, ni lini Kituo cha Afya Makambako kitapata mashine ya X-ray na Ultra Sound?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Jimbo la Makambako, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekwishapeleka mashine ya X-ray kwenye Kituo cha Afya Makambako ambayo ilisimikwa kituoni hapo mwezi Machi, 2021 na inatumika.

Mheshimiwa Spika, mwezi Septemba 2021 Serikali ilipeleka mashine ya Ultrasound katika Kituo cha Afya cha Makambako na inatumika, ahsante.
MHE. BONIPHACE M. GETERE K.n.y. MHE. DEO K. SANGA aliuliza: -

Je, ni lini Kituo cha Afya Makambako kitapata mashine ya X-ray na Ultra Sound?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Jimbo la Makambako, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekwishapeleka mashine ya X-ray kwenye Kituo cha Afya Makambako ambayo ilisimikwa kituoni hapo mwezi Machi, 2021 na inatumika.

Mheshimiwa Spika, mwezi Septemba 2021 Serikali ilipeleka mashine ya Ultrasound katika Kituo cha Afya cha Makambako na inatumika, ahsante.