Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mary Deo Muro (60 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia hoja zilizoko mezani juu ya Mpango wa Miaka Mitano. Kwanza namshukuru Mungu kuniwezesha kufika katika Bunge lako Tukufu. Pia nashukuru chama changu kuniona nafaa kuiwakilisha jamii. (Makofi)
Awali ya yote, napenda kuungana na wale wote ambao wamechangia hoja inayohusu Tanzania ya viwanda kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kabisa kwamba Tanzania ya viwanda lazima iendane na afya ya wananchi, elimu, utawala bora, miundombinu, maji na ardhi. Nafahamu kabisa kwamba nia na madhumuni ya mpango huu ni kuleta ustawi wa jamii kwa wananchi wa Tanzania ndiyo maana Upinzani na Chama Tawala tunachangia kwa hoja nzito ili tuweze kuleta ustawi wa jamii kwa Watanzania wote. Lengo letu siyo malumbano, lengo letu ni kuhakikisha kwamba Watanzania ambao wanatumia pesa zao kwa ajili ya kutuweka hapa wanapata haki stahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze sasa kwenye mada halisi. Ningependa kuongelea afya kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kabisa kwamba hakuna ufanisi katika Tanzana ya viwanda bila wananchi kuwa na afya bora. Tukiangalia maeneo mengi ya Tanzania tunakuta kwamba huduma za afya ziko hafifu. Kwanza nakumbuka asubuhi ya leo kulikuwa na msemaji mmoja ambae alitoa haja yake kuhusu hali halisi ya afya ya Watanzania na mazingira wanayoishi. Waziri husika alijibu kwamba Serikali siyo sababu ya wananchi kupata matatizo ya afya, isipokuwa wananchi wenyewe ndiyo sababu ya kupata matatizo ya afya au magonjwa ya kipindupindu na magonjwa ya mlipuko. Mimi napenda niulize Serikali iliyoko madarakani kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kabisa kwamba kuna sekta zinazoshughulikia afya na kama kuna tatizo la kipindupindu ina maana kwamba sekta inayohusika haijawajibika. Nataka nijielekeze kwa mfano, natoka Mkoa wa Pwani Wilaya ya Kibaha, ilitokea mlipuko wa kipindupindu na sababu kubwa ni kwamba, Wizara ya Maji kwa Pwani haina mamlaka isipokuwa tunatumia DAWASCO ambayo kwa Pwani hakuna miundombinu ya kutoa maji machafu. Ina maana utiririshaji wa maji machafu ni lazima kwa sababu DAWASCO haijawajibika na watu wa Pwani wanahitaji mamlaka yao ili waweze kuiwajibisha pale inapokuwa haiwezi kufanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi, narudi kwa Waziri aliposema kwamba siyo wao wanaosababisha, yeye kama Waziri anafahamu kabisa ni nani ambaye hakuwajibika mpaka mlipuko wa magonjwa utokee. Kwa hiyo, hawezi kusema kwamba yeye siyo sababu. Napenda kumwambia kwamba yeye na Watendaji wenzake hawakuwajibika. Walitakiwa wawajibike ili ugonjwa wa kipindupindu usitokee kwa sababu wapo ambao wako kwa ajili ya kazi hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kwenda kwenye sekta ya elimu, tunaangalia Tanzania ya viwanda ambayo inatakiwa iende na elimu. Ni kweli tumedahili watu wengi kwa ajili ya sekta mbalimbali, lakini tuangalie sheria zinazo-govern uanzishwaji wa viwanda. Tunafahamu kabisa uanzishwaji wa viwanda siyo ufufuaji wa viwanda pengine ni uanzishaji wa viwanda kwa mashirika yanayotoka nje, wawekezaji kutoka nje. Hautaondoa umaskini Watanzania kama waanzishaji wa viwanda wanakuja wa watu wao kutoka nje, kama sheria za nchi haziwezi kusimamia kuhakikisha kwamba rasilimali watu iliyopo hapa ambayo ni watoto wetu ambao wamesomeshwa kwa pesa za Watanzania wanaajiriwa katika viwanda hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeiomba au niishauri Serikali kwamba, itakapoanzisha mpango huo ihakikishe kwamba inatunga sheria ambazo wawekezaji watakuwa nazo wakiangalia kwamba Tanzania ina watu ambao wanaweza kufanya kazi ambazo wanaleta watu wao kuja kufanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mfano, kuna bomba sasa hivi linatoka Ruvu chini kupeleka maji Dar es Salaam. Nimeshuhudia kwa macho yangu, mpaka yule wa kufukua udongo, yule mtu wa kufanya kazi za welding ni Mhindi wakati tuna Watanzania tunawasomesha VETA hizo mnazosema zimeanzishwa wamekaa mitaani hawana kazi. Sasa unajiuliza je, huu umaskini tunaouimba hapa utaondolewaje kwa kiasi hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiachana na hapo naomba niende kwenye kilimo, nimesoma, nimeangalia jinsi Waziri wa kilimo alivyojipanga, lakini naomba niongee machache juu ya hilo. Nimeona kilimo kina ufugaji, kina kilimo yenyewe, lakini nikiangalia kuna ufugaji, naomba ni-declare interest mimi ni mfugaji wa kuku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona mara nyingi sana kuku wakitoka Kenya wanajazwa pale Dar es Salaam kiasi kwamba wafugaji wa Tanzania tunashindwa, wajasiriamali wa Tanzania tunashindwa kuweza kufanya biashara. Sasa ningeomba Wizara katika Mpango huu wa Tanzania ya viwanda basi wahakikishe kwamba Wizara husika inasimamia kidete hali hii ili Watanzania wajasiriamali waweze kufaidika na kilimo chao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningeomba upangaji wa bei, mkulima amelima kwa shida zote, Serikali inakuwa mpangaji wa bei. Serikali inapanga bei wakati mkulima amelima kwa gharama zake. Anapokosa mapato mkulima anashindwa kuendeleza kilimo. Kwa hiyo, umaskini hatuwezi kuondoa kama Serikali haiwezi kusimamia kilimo ipasavyo, kutafuta masoko ambayo yana tija na kuhakikisha kwamba mkulima anapata faida ili kujikimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miundombinu. Nimeangalia miundombinu nikaona kwamba kwa usafiri kwa mfano wa Dar es Salaam, msongamano wa Dar es Salaam nilivyouangalia, sisi sote tunafahamu kwamba time ni factor ya production, kama hatuwezi ku-save time tuna-consume time kwenye kutembea kwenye barabara masaa manne kutoka Kibaha mpaka ufike Dar es Salaam, masaa manne kutoka Mbagala mpaka city center ukafanye kazi, ina maana muda mwingi unapotea hapo katikati bila kutumika. Hii ina maana kwamba Tanzania ya viwanda watu watakuwa wanatembea kwenye magari masaa manne hawajafika kiwandani ina maana utekelezaji wake utakuwa mgumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuende kwenye miundombinu ya maji. Nimesoma na nimesikiliza lakini nimeshangaa kusikia kwamba asilimia 68 ya Watanzania wanapata maji. Jamani mimi natoka kijijini kwetu Makambako chini kule hawajawahi kuona maji ya bomba hata siku moja. Nimekuja huku Kisarawe Mkoa wa Pwani wanachota maji ya visima, hiyo asilimia 68 ambayo wamei-calculate wakapata hapa sijaweza kuelewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kama kweli tuna nia ya dhati ya kuhakikisha wananchi wetu wanakuwa na afya bora, hebu Serikali ijipange kuhakikisha maji ya uhakika yanapatikana kwa ajili ya kuwapa afya bora Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye ardhi. Ni kweli kabisa ardhi ndiyo mpango mzima wa Tanzania ya viwanda ya Mheshimiwa Magufuli, lakini naomba nitoe ushauri...
MWENYEKITI: Muda wako umekwisha mchangiaji.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia Wizara hii kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la wavuvi wa Mafia ni kule kuambiwa wahame eneo wanalovulia miaka mingi na kufanywa Hifadhi ya Taifa, hivyo wananchi kukosa eneo la uvuvi. Naishauri Serikali kuangalia upya jinsi ya kuwatafutia wananchi eneo la uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la majosho kwa ajili ya wafugaji wa Mkoa wa Pwani, Wilaya ya Kibaha, eneo la Kwala ambako wafugaji wengi Wakwavi, Wamasai wanapoteza mifugo yao mingi na ECF (Ndigana Baridi) kutokana na kukosa majosho na dawa za mifugo kuwa juu. Nashauri Serikali irudishe mpango wa ujenzi wa majosho ili kusaidia wananchi. Pia kuwepo punguzo la bei ya dawa ili kusaidia wananchi kumudu gharama.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nashauri kusaidia udhibiti wa soko la mazao yatokanayo na mifugo, mfano, kuku wa nyama kuletwa kutoka nchi za jirani hivyo kuua soko la ndani la wafugaji. Mfano, wafugaji wa kuku wa mayai wanakosa soko la mayai kutokana na mayai toka nchi za jirani kuingia nchini.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kusaidia Wizara kuwa na vyuo vikuu vya uhakika ili kukuza sanaa na michezo nchini. Naomba Wizara ijikite katika kuibua vipaji kwa kuendeleza michezo shuleni ikiwa ni pamoja na kutoa motisha kwa walimu wa michezo, pia kwa wanafunzi wanaoshinda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kuwepo uhuru wa vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na Televisheni ya Taifa kubaki ya Taifa na siyo kwa ajili ku-report taarifa za chama chochote bali itumike kama chombo huru kwa ajili ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kuunga mkono vyombo vya binafsi kwa mchango mkubwa vinaotoa kwa Taifa. Naishauri TBC kuongezwa mtaji ili iweze kuwafikia watu wengi katika jamii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na ninayo machache ya kuchangia kwenye Wizara hii. Kwanza namshukuru Mungu kuwa na afya njema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kuchangia eneo la mwanamke na nishati; nimeamua kuchangia eneo hili kwa sababu nimeona ni jinsi gani mwanamke anahangaika na nishati kuanzia asubuhi mpaka jioni na saa nyingine ashindwe hata kutayarisha chakula kwa kukosa nishati. Nafahamu kabisa kwamba, ndani ya jengo hili wanaume wengi wanakuta chakula kiko mezani, hawajui mwanamke amehangaika kiasi gani mpaka akifikishe mezani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia safu ya uongozi kwenye nishati naona ni wanaume wawili wamekaa pale, lakini hakuna mwanamke ambaye angesimama kwa niaba ya wanawake wa Tanzania ambao wanahangaika siku nzima kutafuta kuni ili waweze kutayarisha chakula kwa ajili ya familia zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku za katikati hapo nyuma, kulikuwa na mradi unaitwa biofuel ambao tulitarajia kabisa ungeweza kutumia gharama ndogo ya kumfikia kila mwanamke alipo, akapata moto poa, ambao ungeweza kumrahisishia kupika na kufanya kazi za upishi kwa urahisi, lakini mpaka sasa hivi hatuoni dalili zozote za ule mradi wa mibono ambao ungeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kueneza vijiji vingi nishati mbadala. Tunaona kuna biogas na zimetengewa pesa hapa bilioni 3.2, lakini ukiangalia kwa Tanzania ilivyo kubwa, mpaka akafikiwe mwanamke aliyeko kule kijijini pembezoni, akapate biogas itakuwa ni karne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi mwanamke ataendelea kulia machozi jikoni huku akichochea vyungu, akichochea sufuria, ili mwanaume akae ale mezani, ambaye haingii jikoni na mwanaume hapati uchungu kwa sababu siye anayepika! Mwanamke ndiye anayehangaika, apike, atafute wapi kuni, atatafuta mkaa, atatafuta chochote kile, lakini chakula kiive! Namwomba Waziri anapokuja angalau atuambie amemuangaliaje mwanamke wa Kitanzania? Jinsi gani anaweza akasaidika na bajeti hii ambayo ameileta mezani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, atakapokuja kujibu, naomba Waziri aje na majibu sahihi, sana sana atuambie labda ule mradi wa biofuel umeishia wapi? Watu walishaanza kulima na mibono ilishaletwa mpaka majiko, umeishia wapi? Leo ukija kwenye bajeti hii ya 3.2 billion kwa Tanzania nzima wakati unaweza ukatumia biofuel ikaenda kwa haraka na kwa nafuu zaidi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye Mkoa wangu wa Pwani. Mkoa wangu wa Pwani, Wilaya ya Kibaha, kuna mradi ambao ulikuwa unaendelea wa TANESCO wa Gridi ya Taifa, walitathminiwa wakaambiwa kwamba watalipwa. Ni Vijiji vya Kiluvya, Mwanalugali na Mikongeni, lakini tangu wametathminiwa kwenye mpango wa miaka mitano ilielezwa kwamba, wamelipwa lakini mpaka sasa hivi hawajalipwa na kinachoendelea hatuelewi! Wananipigia simu kila siku wanasema utakaposimama, tuulizie kwa Waziri, Je, hela zetu tutalipwa? Kama hatulipwi, tuendeleze maeneo yetu? Kwa hiyo, Waziri atakapokuja kujibu, ningependa kupata majibu ya maswali ya Wanakibaha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kuchangia yafuatayo. Kwa mfano, tunaona TANESCO imebeba mzigo mzito sana, inazalisha umeme, inasambaza, inauza! Hivi kweli, hili shirika binafsi litaweza kufanya kazi zote hizo? Kwa nini Serikali isije na mpango mwingine ambao uta-faster maendeleo ya Tanzania tunapoelekea kwenye Tanzania ya viwanda? Nadhani kungekuwa na mpango wa ziada wa kuisaidia TANESCO isifanye kazi zote peke yake; kuzalisha, kusambaza, kuuza, ndiyo maana unakuta saa nyingine…
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nakishukuru chama changu kwa kunipa nafasi ya kuingia Bungeni na kuwa sehemu ya Bunge kwa ajili ya mustakabali wa nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda nianze kuchangia kuwa mimi ni mmoja kati ya Wajumbe wa Kamati ya Miundombinu ambayo ilikuwa inatembea nchi nzima kuangalia uhalisia wa mambo yanavyoendelea katika Kamati hiyo. Nilichokiona ni kwamba nchi yetu ya Tanzania, kama tuna nia ya dhati, kwa sababu niliangalia Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/2017 – 2020/2021) ambao uliletwa hapa Bungeni. Nikaangalia na Pato la Taifa linakotoka, vyanzo vya Pato la Taifa la kuendeleza mpango huo, nimekuta kuna tofauti kubwa sana kwa sababu vyanzo kama bandari ambayo tulitarajia ilete pato ambalo litaweza kuendesha shughuli za nchi inadidimia na inazama kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo? Bandari ya Dar es Salaam kama ungewapa waendeshaji wengine ingeweza kutumika kama chanzo kikubwa ambacho kingeweza kuinusuru Tanzania kuishia kuwa na wakopaji wa kila siku, kwa sababu tumefika pale bandarini tumekuta kuna vitu viwili, kuna kitu kinaitwa MCL, tumekuta kuna TPA ambayo ndiyo mama. Katika kuangalia hali ile tumekuta kwamba watu wawili hamuwezi kuendesha kitu kimoja kwa nia tofauti. Kwa hiyo, unakuta kwamba bandari badala ya kupata mapato, ikafanya kazi vizuri, yeye anakuwa mwangalizi wakati MCL ambaye hana kipato anashindwa kufanya kazi vizuri. Na sehemu zote hizi kuna watumishi ambao wako pale wanafaidika na hamna kitu kinachotokea ambacho kinarudi kwenye Serikali kama mapato ambayo yanaweza kuendeleza nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza malalamiko ya watu wengi mikoani wanataka maji, barabara, n.k., lakini nimeangalia mapato ya Tanzania kupitia vyanzo halisi, hakuna. Kwasababu kama ni bandari, nimeenda bandarini nimekuta kuna migogoro na migongano ya kimaslahi. Kuna watu wamefika pale wamefanya ni mahali pa kuchukulia hela wakati nchi haipati pato lolote. Unakuta kuna migongano ya kimaslahi, kuna TRA inafanya yake, kuna TPA wanafanya yao, yaani kuna migongano ya kimaslahi imefikia mahali ambapo hatuwezi kupata kitu chochote. Tumefukuza wadau ambao walikuwa wanaleta hela pale bandarini kwasababu ya migongano ya kimaslahi. TRA anataka vyake, TPA anataka vyake sasa wamefika mahali hakuna kinachoendelea ni wawekezaji kuondoka na kutuacha tukiwa watupu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia tulivyofika airport kwenye viwanja vya ndege, nimefika Mwanza; kile kiwanja cha Mwanza nimeona kwenye majedwali inaonesha kwamba wanapewa shilingi bilioni 30, ni kweli tulikuwa Mwanza, tumekuta kuna uendelezaji wa jengo la kuongozea ndege ambalo limejengwa vizuri kwa East Africa nafikiri linaongoza, lakini ukiangalia lile jengo limesimama kwa muda karibu mwaka haliendelezwi kwa sababu halina hela. Na nimeangalia kwenye hotuba ya Waziri inaonesha kwamba anatoa shilingi bilioni 30. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipofika pale tulikuta kwamba kuna shilingi bilioni 20 ambazo Serikali ilitakiwa itoe haikutoa, leo hii unampa shilingi bilioni 30 wakati ana deni halafu mradi ulishasimama. Mobilization ya material mpaka ifike kuanza tena ina maana ni hela zaidi ya hiyo, na hivyo ndivyo vyanzo vya mapato ambavyo Serikali kama ingejikita kwenye vile vyanzo ambavyo ni deal tungeweza tukapata mapato na tukaendesha hizo shughuli zote tunazosema, za maji, za barabara na kadhalika. Hapa hata tupige kelele kama vyanzo hivi tumeshavikalia haiwezekani hata siku moja kutoka hapo!
T A A R I F A...
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante siipokei, naomba akae nayo kwa sababu mimi naelezea kile nilichokiona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hayo kwa sababu kama tutaendelea kupanga bajeti ambazo hazitekelezeki ina maana wananchi wetu tutakuwa tumewatenga mbali sana. Hapa UKAWA na CCM wote tumetoka kwa wananchi, tunahitaji kuwafanyia wananchi ili wapate neema, lakini kama tunafika hapa halafu tunaulizana taarifa wakati mimi nina taarifa sahihi na mimi ndiye niliyezunguka nikaona reality, ninasema haya kwa sababu niliyashuhudia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tungekitengeneza vizuri na tukawekeza vizuri kwa hizo hela zilizotengwa siku tulipokwenda Mwanza tungekuta kwamba lile jengo kwenye kiwanja kile liko mbali sana na umaliziaji. Kiwanja cha Mwanza kinajaa maji, ndege kubwa zinashindwa kutua kwa sababu wakati mwingine kunakuwa na ukungu, hamna viongozea ndege ambavyo wakati wa ukungu ndege zinaweza zikatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vitu vyote hivyo kwa shilingi bilioni 30 haiwezekani. Nimesema hayo kwasababu kama tunaimarisha bandari, viwanja vya ndege tunaweza kuwa na pato ambalo tunaweza kuendesha nchi na tunaweza kupata hayo yote ambayo mmeomba, barabara, maji, afya na kadhalika. Fahamu kwamba afya, maji, elimu hivi vyote ni consumer wa mapato kutoka vyanzo kama bandari na viwanja vya ndege. Viwanja vya ndege vikizalisha vizuri ndipo tunaweza tukapata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa niunge mkono msemaji aliyepita. Tumepita mawasiliano, tumekuta kweli wanasema kwamba watazima huo mtambo, lakini tukajiuliza nchi yetu ya Tanzania ambayo ina wataalam ambao wanawezakugundua, wapo kwa ajili ya kujua kwamba hizi ni bidhaa fake na hizi ni bidhaa ambazo sio fake. Kama wapo na wanalipwa na wanaruhusu vitu viingie, halafu wateja wanunue, hawa maskini wa kule kwetu, halafu waambiwe mitambo ile inazimwa kwa simu zao fake halafu wakose simu, hivi tunawezaje kulifanya hili Taifa liingie katika uchumi wa kati kama sasa hivi bibi yangu na mama yangu kule kijijini aliyenunua simu fake hatakuwa na simu kuanzia mwezi wa sita? Tunatakiwa tufike mahali tuangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilikuwa wapi wakati simu fake zinaletwa hapa nchini? Kile chombo ambacho kinadhibiti uingizaji wa simu fake kilikuwa wapi? Hao ndio waliotakiwa washughulikiwe, kwamba kwa nini mmeruhusu simu fake zikaingia lakini si yule bibi yangu kule nyumbani ambaye hajui na simu nilimpelekea tu mimi na mimi nikiwa najua nimempelekea simu nzuri. Mnafahamu kabisa simu ndiyo mawasiliano ambayo kila mmoja anaweza akawasiliana na mwenzake. Leo hii tunapowazimia watu karibia milioni 20 hawatakuwa na simu, Taifa tunalipeleka wapi? Na kama Taifa litakosa mapato hayo maji mnayoyaomba humu ndani mtayapata wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba jamani kama kweli tuna nia ya dhati tuhakikishe kabisa Serikali inafuatilia. niishauri Serikali fuatilieni vitu, kama kweli mlikuwepo wakati simu zinaingizwa fake mna kitu cha kujibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninarudi kwenye mawasiliano. Nimeona kwamba kuna watu wanachota hela pale. Kuna makampuni yanachota hela pale kwenye mfuko wa uendelezaji minara…
MWENYEKITI: Ahsante!
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mabaraza ya Ardhi yanachelewesha kesi hivyo kuchochea migogoro ya ardhi. Kesi inachukua miaka kumi; nini matokeo yake kama siyo kukuza migogoro?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro kati ya wananchi wa Mwanalugali - Kibaha Mjini na Halmashauri Kibaha Mjini ambao wameporwa ardhi tangu mwaka 2004 kwa madai ya kufidiwa mpaka leo, nini maana yake? Mgogoro kati ya wananchi wa Bagamoyo na EPZ katika shamba ardhi ya Bagamoyo; mgogoro wa ardhi kati ya wafugaji na Vigwaza na wakulima, nashauri wafugaji watengewe maeneo ya mifugo ili kupunguza migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la CDA ni kubwa. Wafanyakazi wa CDA kupora ardhi za wananchi na kujimilikisha. Mhudumu ana viwanja kumi eti kwa sababu wanapopima wanajipa viwanja na kuviuza kwa bei nafuu. Ushauri wangu ni kwamba mambo ya ardhi yarudi mamlaka ya Mji wa Dodoma. Wananchi wamechoshwa na CDA kwa jinsi inavyofanya kazi kwa maslahi ya wafanyakazi wenyewe.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali ifute hifadhi ambazo hazina wanyama tena na maeneo hayo yagawiwe kwa wananchi wanaoishi karibu na maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali isisitize kwa mabalozi walioko nchi za nje kufanya kazi kwa ukamilifu kutangaza vivutio vyetu na kuwe na library zao za maliasili yao katika ofisi zao zinazoelezea jinsi Tanzania ilivyo ikiwa ni pamoja na tamaduni zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoteli za Tanzania ziboreshwe, pia kuwepo na vyuo vikuu vya kufundishia wahudumu wa hoteli hizo Kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, misitu ni mali, Serikali ijipange kupanda miti, pia kutoa zawadi kwa kushindanisha wapandaji bora, waweza kuwa ni Taasisi kwa Taasisi au Wilaya kwa Wilaya.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Umaskini na Athari Zake; kukithiri kwa umaskini kunazalisha uhalifu na ndio unaoondoa amani katika Taifa. Hivyo basi nashauri hatua za kuondoa umaskini zifanye jitihada za haraka ili kunusuru nchi na majanga ya uvunjifu wa amani kunakopelekea magereza kujaa wahalifu na kupelekea Taifa kubeba mzigo mkubwa wa kuwatunza wafungwa badala ya kuelekeza fedha hizo kwenye maendeleo ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ongezeko la Watu. Ifikapo 2020/2026 idadi ya watu itafikia milioni 63 ambayo kama utekelezaji wa mpango wa miaka mitano hauwiani na ongezeko hilo italeta shida kwenye huduma za jamii wakati huo, hivyo ndoa za utotoni zithibitiwe kupunguza ongezeko.
Mheshimiwa Naibu Spika, Elimu. Bila elimu yenye tija Taifa haliwezi kufika kwenye uchumi wa kati. Elimu yetu haisaidii kijana kujiajiri, ni vyema kila Mkoa kukawa na scheme for irrigation ili kumeza ombwe kubwa la vijana wanaomaliza shule ili kuwafanya wasigeuke kuwa wahalifu katika Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, madhara ya ukosefu wa ajira kwa vijana kunasababisha uhalifu kuongezeka hivyo kusababisha ongezeko la ajira za Polisi na Magereza na hivyo kuongezeka kwa matumizi kwa Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kukosa ajira kunasababisha utumiaji madawa ya kulevya hivyo kuligharimu Taifa kuwatibu kwa gharama kubwa na pia kutokana na hali ngumu ya maisha na utumiaji madawa ya kulevya, UKIMWI umeanza kushika kasi sehemu nyingi katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Taifa tuangalie nguvukazi ya Tanzania ambayo iko asilimia 60 ya wananchi wa Tanzania kuwa mzigo kwa nchi, hivyo Taifa lijipange kunusuru tatizo hili ambalo miaka ijayo Taifa halitaweza kulimudu, hilo ni kundi la vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kilimo ni uti wa mgongo, naomba iainishwe vijana wametengewa ekari ngapi ili waweze kujiajiri, pia njia ambazo Taifa litawawezesha.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie kuhusu suala zima la uteketezaji misitu na usababishaji wa mabadiliko ya tabianchi ambalo ndiyo tatizo sugu duniani na kwa Tanzania kupelekea kwa sasa mvua kukosekana. Naishauri Serikali kuanzisha njia mbadala ya mkaa tutapunguza ukataji miti, huko nyuma kulikuwa na mpango wa kupunguza ukataji wa mkaa kwa kuanzisha kilimo cha mibono inayotoa moto poa ambayo ingesaidia kuleta chanzo kipya cha moto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi na kilimo kwenye vyanzo vya maji; elimu kwa wananchi ni ndogo kuhusu suala hilo. Niishauri Serikali yangu kuongeza juhudi ya kuelimisha wananchi, pia Serikali iangalie uvuvi haramu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ufugaji mifugo mingi na hatari mijini; niishauri Serikali yangu kuhakikisha elimu kwa wafugaji mifugo inatolewa, upunguzaji mifugo ili kupunguza uharibifu wa mazingira kupitia mifugo mingi kuchungwa kwenye maeneo madogo. Mfano halisi ni ng’ombe wanaochungwa katika Mji wa Dodoma ambao ni Mji Mkuu wa nchi. Niishauri Serikali kuhakikisha inatoa elimu ya kutumia vinyesi vya ng’ombe hao kutengeneza gesi ili kupunguza ukataji miti kwa ajii ya Mkaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muungano; niishauri Serikali iendelee kuondoa kero za Muungano kadri zinavyozinduliwa. Niishauri Serikali kuhakikisha inajenga dhana za kujitegemea kwa kutenga fedha za ndani za kutosha kuliko kutegemea wafadhili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali iongeze fedha za bajeti kwa ajili ya kufanikisha utendaji wa Wizara hii ili kuleta afya kwa wananchi kwani haiwezi kufanya kazi zenye ufanisi bila kuwa na bajeti timilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kama ifuatavyo:-
Nishauri Serikali kuweka bayana mambo ya kisheria na kuyatendea haki mfano haki ya kujieleza, haki ya kupata habari, haki ya kuishi, ni vizuri Serikali ikatendea haki maeneo hayo ili taifa liwe na Amani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali itambue kuwa amani haiwezi kuwepo bila haki ambayo inatokana na utawala wa Sheria. Sheria za Ndoa na mirathi zipo lakini wananchi wa kawaida hawana elimu ya sheria. Pia nashauri Serikali kufanya juhudi ili kutoa elimu ya sheria kama ilivyo kwa matangazo mengine ya UKIMWI na madawa ya kulevya.
Nashauri Serikali kutembelea mahakama zetu zilivyo na wafanyakazi wanaoishi na kufanya kazi katika wakati mgumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nishauri kuhusu upelekaji wa wafungwa kutoka mahabusu imekuwa shida, hivyo Serikali iangalie kwa nini kutokana na ukosefu wa usafiri, kesi zao huahirishwa mara kwa mara hivyo kusababisha mahabusu kutumikia vifungo vyao kabla ya hukumu. Mfano halisi mtuhumiwa anakaa mahabusu miaka minne kabla ya hukumu, hivyo Serikali inaingia hasara ya kulisha mahabusu. Pia kupunguza nguvu kazi ya Taifa kwa kuwaweka gerezani. Nashauri Serikali iongeze fedha kwa mahakama ili kuongeza utendaji.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mweyekiti, naomba kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali kuongeza watendaji kazi wa maendeleo ya jamii ili kutoa ushauri kwa jamii kuacha tabia za wanandoa kutengana na kusababisha malezi ya watoto kuwa shida, hali inayosababisha kuwepo watoto wengi wa mtaani. Tatizo la watoto hawa linapelekea kuwepo kwa watoto wanaozaa kabla ya wakati jambo ambalo linaendelea kuzalisha watoto wa mtaani. Nashauri Serikali ili kupunguza ongezeko la kasi la watu wanaolitegemea taifa moja kwa moja liongeze watoa elimu kwa jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kuzungumzia juu ya uhaba wa dawa za kutibu na kuzuia magonjwa nyemelezi ya watu walioathirika na UKIMWI ambayo yanasabisha vifo vingi. Nishauri hospitali kugawa dawa za kufubaa na ziambatane na dawa za magonjwa nyemelezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kushauri kwamba vitendea kazi viongezwe katika hospitali, katika maeneo mengine hawana vifaa vya kuhifadhia watoto njiti. Niishauri Serikali kuweka zahanati kila kata ili kurahisisha ufikaji wa wagonjwa kwenye huduma. Pia niishauri Serikali kuhakikisha inaongeza dawa ya kuwezesha kupima UKIMWI kwani mara nyingi zimekuwa adimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba matengenezo katika Chuo cha Maendeleo Kibaha na Shirika la Elimu FDC ili kuweza kutekeleza malengo ya kuanzishwa kwake. Majengo yamechakaa sana na hakuna majiko, wanapika kwenye majiko yaliyochakaa na finyu, pia yanahatarisha afya za wapishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali kukiangalia kwani kilikuwa kinatoa wahitimu ambao wanasaidia sana kuleta mabadiliko kwa jamii. Niombe mortuary ya Kibaha iongezwe kwani ajali zote zinapotokea Morogoro majeruhi na maiti huletwa Tumbi Kibaha pia tuongezewe na dawa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kama ifuatavyo:-

Nawapongeza Mawaziri na watendaji kwa juhudi wanazochukua, ushauri kwa Serikali itoe fedha kwa wakati na za kutosha ili kupunguzia Wizara hii shida inayoendelea sasa hivi inayopelekea elimu kushuka.

Ninashauri juu ya ndoa za utotoni na mimba za utotoni, ninaiomba Serikali itoe elimu ya kutosha ili watoto wajue mabadiliko ya maumbile yao. Hivyo basi, naishauri Serikali kuridhia sheria ya watoto wanaopata mimba warejeshwe shuleni kwa masharti ambayo hayatafanya wanafunzi hao kurudia kosa hilo.

Pia ninaishauri Serikai iendelee kuandaa mazingira rafiki kwa watoto wa kike kupata elimu bila vikwazo vya kumrudisha nyuma. NIishauri Serikali kuimarisha vyuo vya FDC nchini ambavyo vitasaidia kuelimisha vijana wetu na kujiajiri mfano, FDC Kibaha ina mapungufu mengi sana. Niishauri pia Serikali kukagua shule binafsi nyingine ni za ovyo hazina vigezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ijitahidi kulipa madai ya walimu ili kuwatia moyo, hivyo BRN kufikiwa kwani huwezi kupata matokeo makubwa bila kuwekeza kwa walimu. Mikopo ya elimu ya juu iangaliwe kwani hakuna haki na weledi kwa watoaji wanaotakiwa kupewa wanakosa na wasiostahili ndio wanapata, Serikali iangalie hilo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuchangia mada iliyopo mezani. Kwanza namshukuru Mungu kwa kuwa na afya njema. Napenda kuchangia kwa ujumla na sehemu nyingine kutoa ushauri kwa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kuchangia juu ya ucheleweshaji wa pesa kutoka Serikalini kwenda kwenye Wizara na madhara yanayopatikana kwa ucheleweshaji huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunatembelea miradi, tumekuta kwamba kutokana na ucheleweshaji wa fedha hizo, madhara yaliyojitokeza ni gharama za ujenzi kuongezeka mara mbili. Mfano, barabara iliyojengwa kutoka Dumila kuelekea Ludewa, badala ya kujengwa kwa shilingi bilioni 42 imejengwa kwa shilingi bilioni 42 plus variation ya shilingi bilioni 22. Unaangalia, unasikitika na kukuta kwamba hali hii itasababisha ujenzi wa kilometa chache mahali ambapo ingeweza kujengwa kilometa nyingi kutokana na hizo variations.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukumbuke kwamba kunapotokea variations kubwa kama hizo, kuna negotiation, ndipo loophole zile za ufisadi zinapoingia. Kwa hiyo, naishauri Serikali kama ina nia ya dhati ya kuhakikisha kilometa nyingi
zinajengwa kama walivyojipangia, wapeleke fedha kwa wakati ili kutokuruhusu hizo variations ambazo zina mianya ya ufisadi.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia kwenye viwanja vya ndege. Kwenye viwanja wa ndege tumetembelea; nimekuta kwamba vingi viko chini ya viwango, kiasi kwamba pamoja na ununuaji wa ndege zilizonunuliwa, lakini viwanja vya ndege bado vingi ni vibovu. viwanja vya Shinyanga, viwanja vya Moshi. Moshi, kiwanja ambacho kina mlima wa Kilimanjaro ambapo ungeweza kuleta mapato makubwa, unavitegemea viwanja vitatu ambavyo vinazalisha. Sasa ukiwa na viwanja ambao vinazalisha na viwanja vinavyo-consume, ujue bado hujafanya kazi ya faida.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naishauri Serikali, kama ina nia ya dhati ya kutengeneza pato kwa Taifa, ihakikishe kabisa viwanja hivi vinavyo-consume faida inayotoka kwenye viwanja vile vinavyozalisha, inavitengeneza na viweze kufanya kazi na viweze kuleta faida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuchangia sehemu ya bandari. Bandari yetu ya Tanzania tofauti yake na bandari nyingine za wenzetu ni kwamba bandari ya Tanzania kwa mfano, kwenye ushushaji wa mafuta.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi za wenzetu mafuta yanashushwa kwenye matenki ya Taifa na flow meter inakuwepo tanki la Taifa, ndilo linalogawanya mafuta yale kwenye matenki ya watu binafsi. Sisi kama Tanzania unakuta kwamba matenki ni ya watu binafsi. Kwa hiyo, sisi tunahangaika na flow meter kugawanyia kwenye matenki ambayo siyo ya kwetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali ijitahidi kuhakikisha kwamba manteki ya Taifa yanakuwepo ili tunapopata mafuta tuweze kugawa kwenye mantaki ya wafanyabiashara ili Taifa liweze kupata faida.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nichangie miundombinu na mwanamke. Napenda hii lugha kwa sababu nafahamu kabisa mwanamke wa Tanzania ndiye anayezaa watu wote tulioko hapa; ametuzaa mwanamke, lakini hakuna hata mtu mmoja hajui kama huyu mwanamke alizalia wapi, alisafiri kwa usafiri gani mpaka akafika sehemu aliyojifungulia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiliangalia hilo kwa jicho la uchungu, tutafikiria barabara za vijijini ziboreshwe, mgao ule inaogawa Serikali ihakikishe kwamba inagawa mgao ambao utasababisha barabara za vijijini kujengwa kwa viwango ambavyo mama mjamzito akiwa anaenda kujifungua, hataweza kufia njiani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mfano hai kabisa, nina ndugu yangu ambaye alibebwa kwa toroli, akawa anatembezwa kupelekwa hospitali. Zile kukuru kakara zote, akapata rupture njiani na akafia njiani. Yote hiyo ni kwa sababu tu barabara zile zilikuwa ni mbovu na hakuna njia nyingine, ilikuwa ni kumbeba aidha kwa mzega ama kwa toroli. Sasa tufikirie kama Serikali, huyu mwanamke ambaye ndiye anayezalisha mashambani huko, akitaka kupeleka mazao sokoni anashindwa apitishe wapi ili akafikishe sokoni? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwanamke huyo ndiye ambaye anazaa; anapohitaji kujifungua, hajui apite njia gani mpaka afike hospitali, ukuzingatia kwamba Tanzania sasa hivi bado hatujafika sehemu kila kijiji kuwa na hospitali.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali iliangalie hilo na ichukue umuhimu kuhakikisha kwamba mafungu yale yanawafikia na uwezekano wa kupata barabara ambazo zinapitika ili kurahisisha hawa wanawake waweze kujifungua vizuri na uzazi salama uweze kupatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia eneo la DARTS. Nimeangalia Dar es Salaam mradi wa DARTS, ni mpango mzuri kabisa. Pia kuna treni ile (commuter), naomba basi, kwa sababu tulitembelea na nikaona jinsi gani kama ile commuter itapata vichwa ambavyo siyo long safari, inaweza kuleta faida kubwa kabisa, tena faida ya wazi kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulifanya calculations tukakuta kwamba kwa kupata short safari, vichwa na mabehewa yake tunaweza tukatengeneza faida na Wizara hii ikaweza kuleta faida kubwa kuliko inavyotegemea. Kwa sababu sasa hivi treni ile ya pale Dar es Salaam inayoenda Pugu inatumia vichwa vya long safari, kwa hiyo, mafuta yanayotumika ni mengi. Kwa hiyo, inashindwa kuleta faida tarajiwa. Natamani kuona ile treni inapata vichwa na mabehewa ya short safari ili iweze kutengeneza faida iliyotarajiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie upande wa TCRA; napenda kupongeza TCRA kwa kazi nzuri wanayofanya ambayo ina faida kubwa, lakini pia naomba Serikali iangalie TCRA kwa macho ya huruma kwa sababu maduhuli inayokusanya inapeleka Serikalini hela nyingi, lakini mrejesho wake unakuwa ni wa shida sana kwa ajili ya urasimu wa kurejesha zile hela ili TCRA waweze kufanikisha utendaji wao. Hivyo naishauri Serikali kwamba kwa kuwa TRCA wanafanya kazi nzuri, basi ni vizuri wanapoomba pesa ili waweze kuleta utendaji mzuri, waweze kurejeshewa kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba kuchangia kuhusu Data Center ya Taifa ambayo iko chini ya Wizara hii. Naishauri Serikali kuhakikisha kwamba taasisi zote za Serikali zinatumia Data Center ile iweze kufanya kazi iliyotarajiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kusema hayo, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kuimarisha Jeshi la Kujenga Taifa ili liweze kuwa na tija kama miaka ya zamani lilipojenga uchumi badala ya kuwa consumer wa Pato la Taifa. Miaka hiyo Mlale ilitoa mahindi mengi, Mafinga pia, Ruvu ilikuwa wazalisha mpunga na ufugaji ambao ulileta faida kwa jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali kuweka uwazi katika ajira zinazotolewa ili kuondoa minong’ono iliyopo ya kuwa rushwa inatolewa ili vijana wetu kupata ajira bila usumbufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, nashauri Kiwanda cha Nyumbu kifufuliwe ili watendaji walioajiriwa kwa ajili ya kiwanda wasiligharimu Taifa bila kazi yoyote. Serikali iweze kuona kiwanda hiki kilikuwa na uwezo wa kuongeza ajira na Pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kwamba Vituo vya Jeshi viwekwe mbali na mazingira ya wananchi ili kutoleta migongano na mazoea yaliyopitiliza kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nashauri Serikali iwapatie posho na vitendea kazi askari wetu ili kufanya kazi zao kwa urahisi zaidi.

Vilevile naishauri Serikali kulipa madeni kwa Jeshi linayodaiwa kwa kuwapa fedha zile zilizopitishwa na Bunge badala ya kusitishwa huduma muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itoe ushawishi wa Watanzania kutumia bidhaa zao ili kuweza kuwaongezea pato.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kuangalia kilimo na elimu kuwa kipaumbele cha kwanza ili viwanda vyetu viweze kupata malighafi kutoka kwa wakulima wetu ili kukuza uchumi wa kaya. Nishauri Serikali kupitia sera zake za viwanda kuzihuisha ili ziendane na wakati wa sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nashauri Serikali itunge sheria na adhabu kali zinazotokana na uharibifu wa mazingira, hasa utiririshaji maji ya viwandani ambayo yamekuwa kero kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri Serikali kurejesha viwanda vyote vilivyobinafsishwa kutumika kinyume na mkataba wa awali. Mfano, Kiwanda cha Korosho Kibaha kimegeuzwa mahali pa kutunzia bidhaa, hivyo matumizi yaliyoainishwa wakati wa mkataba kukiukwa. Naishauri Serikali kupunguza urasimu katika kusajili biashara na kupelekea wawekezaji kushindwa kuwekeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu viwanda na wanawake, naishauri Serikali kuwaangalia kwa jicho la huruma wasaidiwe ili kuweza kupata mikopo ya kuanzisha viwanda vidogo vidogo. Mfano, viwanda vya vyakula vya kuku na mashine za kutotolea vifaranga ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kama ifuatavyo:-

(i) Naishauri Serikali kuangalia upya kuhusu pembejeo kwa ajili ya kilimo kufika mapema kulingana na misimu na pia mbegu ziboreshwe;
(ii) Serikali ijitahidi kuwajali wagani tulionao kwa kuwapa vitendea kazi, usafiri wa kuwafikia wakulima wetu;

(iii) Nashauri Serikali itoe elimu ya ufungashaji ambayo imegharimu mazao yetu yanafungashwa Kenya na kusafirishwa hivyo kupata fedha nyingi kuliko wakulima;

(iv) Nashauri Serikali kuangallia jinsi dawa zinavyohifadhiwa kwani kuna nyingi ni sumu na zinaharibu afya za wananchi;

(v) Nishauri Serikali kuhakikisha wanashughulikia miundombinu ya kutoa mazao mashambani;

(vi) Nishauri Serikali kuelimisha wananchi juu ya uuzaji mazao siyo kuzuia tu kwani mwananchi anatakiwa kuuza ili kununua mahitaji mengine.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kupongeza kwa uwasilishaji wote mzuri. Naishauri Serikali kupeleka fedha zote zilizoidhinishwa na Bunge kwa wakati ili kukidhi matumizi ya balozi zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali kukarabati au kujenga ofisi zake za balozi nchi husika ili kuondokana na upangaji aghali. Naishauri pia Serikali kufuatilia urasimu unafanywa na Mabalozi kuhusu wawekezaji wanaotaka kuwekeza Tanzania, wafungue milango ya Tanzania ya uwekezaji badala ya kuwapa masharti makubwa ambayo yanawakatisha tamaa wawekezaji.

Pia niishauri Serikali kufuatilia balozi zetu katika utendaji kwani vimekuwepo vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu kwa watu wetu wanaokwenda nje hali balozi zikishindwa kuwasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri pia Serikali kuangalia juu ya mipaka, mfano mpaka wa Tanzania na Malawi ambao una utata mpaka sasa hivi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni haki yangu dakika kumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nina machache ya kuchangia hoja iliyoko mezani. Kwanza ningependa kuungana na wengine wote waliosema Serikali iimarishe utafiti kwa sababu utafiti ndiyo utafanya zile tafiti zifike kwa wananchi waweze kulima kilimo bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongolea kuhusu ushirika. Tunafahamu kabisa ushirika ulikuwa ndiyo Sera ya Mwalimu Nyerere ambayo iliwaunganisha wananchi kufikia malengo kwa pamoja. Ushirika huu kwa sasa hivi umeyumba baada ya wafanyakazi wengi kupunguzwa na ukaguzi wa Vyama vya Ushirika kuwa mgumu. Kwa hiyo, ningeishauri Serikali iangalie kwa upya kuongeza wafanyakazi watakaokagua Vyama vya Ushirika kuanzia kwenye Vyama vya Msingi mpaka Vyama Vikuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongelea kuhusu mifugo. Wananchi wa Pwani wanaomba Waziri anapo-wind up awaeleze shamba letu la majani la Vikuge linayumba, lina shida, hakuna majani. Wananchi walikuwa wamezoea kununua majani kwa ajili ya mifugo, ile zero grazing lakini shamba la Vikuge halina majani, ukifika pale limeota miti, Waziri aeleze kuna nini hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia wananchi wa Pwani wanauliza, je, Bonde la Rufiji kilimo kile kimeishia wapi na ile RUBADA imeishia wapi. Waziri tunaomba atueleze ili waweze kujua kwamba labda ipo siku watafikia yale malengo yaliyokuwa yametarajiwa na waanzilishi ya RUBADA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuchangia kwenye eneo la uvuvi. Kwenye uvuvi kuna matatizo ya nyavu na makokoro kama wanavyoita wavuvi. Hata hivyo, mara nyingi unakuta kwamba wananchi wanachomewa nyavu zao shida unaambiwa kwamba kwa sababu wanavua samaki wadogo lakini sijaona mkakakati wa makusudi wa kuzuia watengenezaji wa nyavu au waingizaji wanyavu bali wanawachomea wale ambao wananunua.

Mimi napenda Serikali iweke mkakati wa kuhakikisha kwamba nyavu ambazo hazihitajiki haziingii hapa nchini kwa sababu sio kosa la mvuvi. Mnamuonea mvuvi ambaye anakwenda dukani ananunua zile nyavu kwa sababu yeye siyo muagizaji. Serikali inatakiwa iangalie suala hilo kwamba mvuvi apate haki yake, amenunua zile nyavu kwa sababu ziliingizwa na kuna watu ambao wapo kwa ajili kufanya kazi ya kuhakikisha kwamba nyavu hizo haziingii hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia kuhusu kilimo na niungane na wale wote waliosema kwamba Wagani wamekosa vitendea kazi. Ni kweli kabisa tusitarajie kwamba Mgani huyu yuko ofisini anatakiwa kuwafikia wananchi, aende kwa mshahara wake huo mdogo, hana posho wala kitu chochote akafanye kazi arudi na watoto wake wale nini? Hebu Serikali iangalie hapo kwamba tukitaka Mgani aweze kufanya kazi yake ni lazima tumjali kama tunavyojali wafanyakazi wengine. Hata sisi wenyewe leo hapa tungekuwa hakupati posho leo hakuna mtu angekuwepo hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kuzungumzia kuhusu mgogoro wa wakulima na wafugaji. Mgogoro huu ni wa siku nyingi na kila siku maelezo na majibu ni yale yale. Hivi kwa nini tusifanye research ili kujua ardhi ya Tanzania ni kiasi gani na matumizi ya ardhi ya hiyo ni yapi, tukayapanga kwa vipaumbele ili tujue kwamba mfugaji atakuwa na eneo lake la kufuga na mkulima atakuwa na eneo lake la kulima ili tusilete migongano. Nashauri Wizara mbili hizi zikae zikatathimini, ardhi ipi itumike kwa ajili ya ufugaji, kilimo na reserve kwa ajili ya wanyamapori. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika mifugo hiyo hiyo na napenda kuzungumzia kuhusu walaji wa nyama itokanayo na mifugo. Watanzania wengi au wenzetu anaokuja kutoka nchi za nje wanaogopa kula nyama ya Tanzania kwa sababu moja tu. Sababu ni kwamba nyama ya Tanzania ni hatari kwa sababu machinjio ni mabovu na machafu, hakuna machinjio ya kisasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali iliangalie hili kwamba kama tunaamua kuwalisha Watanzania nyama basi tuangalie hao ng’ombe wananchinjiwa wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefika hapa Dodoma nimekuta kuna machinjio ya kisasa lakini kule kwangu nakotoka Kibaha, Pwani yote ile haina machinjio ya kisasa. Wizara hakikisheni kwamba mnaboresha machinjio ili wananchi Watanzania wasije wakapata maafa kwa kula nyama chafu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kilimo pia napenda kuzungunzia suala la uingizaji wa mazao ya mifugo kutoka nchi jirani. Ni kweli kabisa tuna nia ya dhati na mimi ni mfugaji vilevile, lakini kuna kitu ambacho wafugaji wa Tanzania wanapata shida ni pale ambapo unakuta tunashindana na Kenya au na Uganda kuingiza mazao ya mifugo au mazao ya kilimo bila Serikali kujali angalau wafugaji au wakulima wa ndani. Naishauri Serikali iangalie kwa sababu wananchi wanakuwa wame-invest fedha nyingi kwenye kilimo au kwenye mifugo, mtu anafuga kuku anaenda sokoni anakosa pa kuuza mayai kwa sababu mayai ya Kenya yamejaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kilimo tumeona sehemu nyingi sana wananchi wanalima kwa kujitegemea. Wanajitegemea kwa sababu yeye ndiyo atatafuta mbegu na kila kitu, lakini Serikali inataka kupanga bei au inamzuia kwamba asiuze mazao yake au auze kwa wakati fulani. Tunatakiwa tufahamu kwamba kama unamwambia mwananchi asiuze mazao yake na ana watoto wanatakiwa kwenda shule na anatakiwa kwenda kwenye matibabu bila kuuza mazao yake atategemea nini na yeye anategemea mazao yake ndio ATM yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali itoe elimu kwamba mkulima atalima lakini auze kwa namna moja, mbili tatu lakini isizuie kabisa kwamba wakulima hakuna kusafirisha kwenda kuuza wapi kwa sababu sometimes anakwenda labda kuuza Uganda kwa sababu anajua kabisa Uganda kuna bei nzuri. Kama Serikali inanunua kwa bei ndogo, kwa nini asiuze sehemu nyingine ili aweze kurudisha gharama zake alizotumia wakati wa kilimo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia kuhusu maghala na ununuzi wa Serikali wa mazao ya wakulima. Mazao mengi yanabaki bila kununuliwa na Serikali inanunua mazao machache, kwa mfano tuchukulie mikoa ambayo ni big five unakuta mara nyingi wana mazao mengi kuliko uwezo wa Serikali wa kununua. Kwa nini Serikali isiongeze uwezo wa kununua mazao ili wananchi wasiweze kupoteza mazao yao kwa sababu unakuta hakuna maghala ya kuhifadhia na hakuna ununuzi, watu wameweka mazao yao nje yananyeshewa na mvua, nguvu za wananchi zinapotea bure. Naishauri Serikali iliangalie hilo na ilitendee kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MH. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze uwasilishaji wa Kamati ya Bunge na Kambi ya Upinzani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali kuwaangalia kwa jicho la huruma wajasiriamali wadogo kama wasindikaji ambao wanakutana na pingamizi kubwa na kukatishwa tamaa na Taasisi za Serikali za Udhibiti. Mfano, TFDA imekuwa chanzo cha wajasiriamali kukata tamaa kwani TFDA wanatoza fedha nyingi sana kwa kila product/ bidhaa inayotengenezwa. Pia suala la TFDA kutoza kwa dola imekuwa kikwazo kikubwa na inarudisha nyuma zoezi zima la wajasiriamali kukua. TFDA inatoza dola 2.5 mpaka 500 kwa bidhaa ambayo mtengenezaji anaiuza kwa shilingi za Kitanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iangalie jinsi ya kupunguza urasimu kwenye usajili wa biashara kwani urasimu ni mkubwa unapelekea watu wengi kukata tamaa kwa mfano wawekezaji toka nje wanalalamikia sana kuhusu usajili hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali juu ya kodi kwa wafanyabiashara wanaoanza biashara kutozwa kodi kabla ya biashara kuanza. Sheria ya mlipa kodi inatozwa kwa kuangalia pato la biashara na si mtaji hivyo inasababisha watu wengi kushindwa biashara kwani hawana grace period ya biashara kama wageni wanavyopewa fursa hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kuwa na vipaumbele kwenye mipango yake kwani Serikali ikiwa na vipaumbele vichache vinavyotekelezeka itasaidia kuwezesha nchi kuondokana na utegemezi au kuongeza Pato la Taifa kuliko ilivyo sasa ambapo vipaumbele ni vingi kiasi kwamba utekelezaji unashindikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali katika Mpango wake wa viwanda iimarishe kilimo ambako malighafi zitatoka. Serikali iboreshe tafiti za kilimo na watoe elimu ya kilimo ili wananchi wajue kilimo cha kisasa chenye tija na si kilimo cha mlo tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kuangalia hili suala la masoko kwa mazao, soko la ndani na la nje. Mpaka sasa wananchi wamekata tamaa ya kilimo baada ya Serikali kushindwa kununua mazao yao pia sheria ya kukataza wakulima kujitafutia masoko. Wakulima wengi wamekata mitaji baada ya kulima na kukosa masoko na mazao yao kuishia kuharibika. Pembejeo nazo ni tatizo, hazifiki kwa wakati hivyo kupishana na msimu wa kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali kuweka viwanda vya kuchakata bidhaa zitokanazo na mifugo ikiwa ni pamoja na ngozi, maziwa, nyama kwani Tanzania ina mifugo mingi.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kupongeza Kamati ya Uwekezaji Mitaji kwa taarifa ambayo inaeleza hali halisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuchangia juu ya Shirika la Elimu Kibaha (KEC) ambalo lilianzishwa kwa ajili ya shamba darasa kwa ajili ya wananchi kujifunza maendeleo mahali pale. Ningependa kusema kuwa tunapoangalia Shirika la Elimu Kibaha tulishuhudia uendelezaji wa shirika hilo huko nyuma miaka ya themanini lilikuwa na viwanda vya kutotolesha vifaranga na ufugaji wa ng’ombe ambao sasa hivi haliko hivyo na limekufa kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali kuangalia taasisi hii ambayo ilikuwa na shule, Chuo cha Maendeleo kilichokuwa kinafanya shamba darasa na kutoa vijana kwenda kujiajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kushauri Serikali kuharakisha uundaji wa Bodi ya Wakurugenzi wa RAHCO, kampuni hodhi ya rasiliamli za reli. Nimeona niseme hivi kwani ni wakati ambao sasa tunatengeneza Reli ya Standard Gauge na kampuni hii haina bodi ya rasilimali hiyo itakuwa shida. Niishauri Serikali iharakishe uundaji wa bodi hii ili iweze kusimamia rasilimali za reli kuweza kuleta ufanisi wa uendelezaji wa reli nchini.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kupongeza Kamati ya Nishati na Madini kwa taarifa na kwa utendaji ambao umepelekea kudhibiti mianya ya utoroshaji wa rasilimali yetu ya madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kuiomba Serikali kuharakisha uchakataji wa gesi yetu ili iweze kupunguza shida ya nishati hii ambayo inasababisha ukataji miti holela na hivyo kusabisha uharibifu wa mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika,nishauri Serikali kuharakisha ulipaji fidia kwa wananchi mahali ambako miradi ya umeme inapita kwani imesababisha umaskini kwa jamii pale ambapo wameweka X na kushindwa kulipa hivyo kusababisha wananchi kushindwa kuendeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri Serikali kupunguza urasimu kwa wawekezaji wa miradi ya madini kwani kunawakatisha tamaa wawekezaji hao.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nishauri Serikali kuwawezesha wachimbaji wadogo wadogo kwa kuwapa hitaji la muda mrefu kwani wameshindwa kupata pato kubwa kutokana na vifaa duni wanavyotumia katika uchimbaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri Serikali kuangalia kwa upya juu ya Shirika la TANESCO kwa kulipunguzia mzigo wa kufufua umeme, kusafirisha na kuuza kunakopelekea utendaji ambao ni mgumu na usiokuwa mzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri elimu kwa wachimbaji wadogo ili kusaidia kuwezesha kuchimba kwa tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri Serikali kulipa malipo ya TANESCO kwani inapunguza utendaji wa TANESCO.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri Serikali kujenga matenki ya Serikali ya kupokelea mafuta ili kudhibiti kwa urahisi upotevu wa mafuta unaopelekea Serikali kukosa kodi halisi ya mafuta hayo.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze uwasilishaji wa taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii. Napenda kuishauri Serikali kama ifutavyo:-

(i) Ipunguze mlolongo wa tozo kwenye utalii kwani umesababisha watalii wengi kushindwa kuja Tanzania hivyo kupunguza pato la Tanzania;

(ii) Iboreshe hoteli zetu za kitalii na huduma ziwe za kisasa na pia kutoa elimu kwa wahudumu wetu jinsi ya kuwahudumia watalii wetu. Vilevile iboreshe mitaala ya ufundishaji wahudumu wetu kwani wamekuwa hawakidhi kiwango cha kimataifa hivyo watalii wengi kutofurahia huduma zetu wawapo nchini.

(iii) Ishughulikie migogoro ya ardhi ambayo mingi inasababishwa na Maafisa Ardhi katika Halmashauri kwa kupima maeneo ya wananchi na kushindwa kulipa fidia na kuuza viwanja hivyo kama vyanzo vya mapato ya Halmashauri wananchi wakiachwa bila kipato chochote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri kuwa wanapogawa viwanja vilivyopimwa wazingatie kaya au nyumba husika ina vijana wangapi wenye uwezo wa kujiajiri ili kuondoa tatizo la vijana kukosa ardhi kwa ajili ya kujiajiri.

(iv) Iwakemee viongozi ambao ni Watendaji wa Kata na Vijiji wanaouza ardhi za vijiji bila kushirikisha wananchi.

(v) Itoe elimu kwa wananchi juu ya haki ya msingi ya ardhi na jinsi ya kumiliki ardhi. Niombe pia kuondoa urasimu wa upatikanaji hati miliki kwenye ofisi za ardhi.

(vi) Iharakishe urasimishaji wa ardhi ili wananchi waweze kutumia ardhi hiyo kwa ajili ya kujipatia mikopo ya kilimo.

(vii) Ishughulikie mgogoro uliopo kati ya Halmashauri ya Kibaha na wananchi wa Lumumba na Mwanangali ambao umepelekea wananchi kuwa maskini na kushindwa kuendeleza maeneo yao kwa miaka kumi.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze taarifa ya Kamati, Mifugo na Maji. Napenda kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo ningeshauri Serikali kusaidia wananchi kupata soko au masoko ya mazao yao.

Ningependa kuishauri Serikali juu ya uwahishaji wa pembejeo kwa ajili ya kuendana na wakati wa uhitaji. Tunaposema tutaondoa umaskini pamoja na kuwapa uhuru wa kuzalisha na kuuza kwa faida ili kurudisha gharama zilizotumika wakati wa kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kupata matrekta badala ya kilimo cha mkono kisicho na tija kwa jamii kinachosababisha vijana wengi kukata tamaa na kukimbilia mijini kutafuta fursa na wanapozikosa hugeuka wahalifu. Ningeshauri Serikali kuangali upya juu ya Mto Ruvu kutumika kikamilifu katika umwagiliaji ili kuwakwamua wananchi hao kuondokana na lindi la umaskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali juu ya upigaji chapa mifugo kwani zoezi hili limeharibu soko la ngozi ambalo lilikuwa limeshamili sasa hivi limeporomoka ghafla badala ya ngozi za Tanzania kukosa ubora kutokana na chapa hizo. Nashauri Serikali kusaidia vijiji kuwa na majosho ya ng’ombe kama hapo awali miaka ya sabini ambapo uogeshaji ulifanyika kwenye majosho ya Serikali kwa kulipia ili kusaidia kupunguza vifo vya mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali juu ya tatizo la maji ambalo ni lengo la Taifa kwani maeneo mengi ya Tanzania yana shida ya maji, hata yale ambayo vyanzo vyake viko bayana, ukiangalia utaona jinsi ambavyo wananchi wengi wanashirikiana na mifugo. Nashauri Serikali ifuatilie kwa karibu sana juu ya miradi ya maji ambayo inaendeshwa kwani inajengwa chini ya kiwango. Hivyo Serikali ifuatilie kwa karibu ili kuondoa pesa inayopotea. Nishauri kuwahisha fedha kwenye Halmashauri zetu ili ziweze kutumika kwa wakati.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze na kuunga mkono hoja iliyopo mezani juu ya Taarifa ya Kamati ya Sheria Ndogo iliyowasilishwa vizuri na Mwenyekiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Bunge liwe macho juu ya sheria zozote inapotokea zinakinzana na Katiba ya nchi au inapokinzana na uhalisia wakati wa utekelezaji nikimaanisha sheria inapokuwa haina maslahi kwa jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeshauri sheria ya umri wa mtoto wa kike kuolewa itoe uangalizi wa sheria hii kwani watoto wa kike sasa hivi wanabalehe mapema, hivyo, naishauri Serikali iangalie kwani sasa hivi ina mchanganyiko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kuleta muswada wa sheria kuhusu mwanamke kuwa na haki ya kumiliki ardhi ya familia, sio kama ilivyo sasa ambapo haiko hivyo.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, niunge mkono taarifa ya UKIMWI na nipongeze uwasilishaji mzuri. Nipende kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali kuiwezesha Mamlaka ya Udhibiti wa Madawa ya Kulevya kupata vitendea kazi vya kisasa ili kuweza kuenda sambamba na vitendea kazi vinavyotumiwa na wahalifu. Serikali iwe sober house zake za binafsi ni ghali mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri Serikali kuipa meno Mamlaka ya Kudhibiti UKIMWI, kuwapa nguvu na mamlaka ya kufanya kulingana na uwezo wao. Serikali iwaongezee rasilimali watu ili kuwezesha utekelezaji wa kazi au majukumu yao kwa urahisi na kwa ufanisi. Nipende kuishauri Serikali kutoa waraka maalum ili kuwezesha halmashauri zote kuunganisha shughuli za UKIMWI kuunganishwa na madawa ya kulevya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, UKIMWI una vyanzo vingi vya kupata hasahasa wanaojidunga wamekuwa chanzo kikuu na hivyo suala hili linatakiwa kuangaliwa kwa makini ili kutoa elimu kwa vijana wetu jinsi ya kuishi maisha ambayo yatawaweka mbali na magonjwa hayo ambayo yana punguza nguvu kazi ya Taifa. Nishauri Serikali kuongeza bajeti ya UKIMWI na madawa ya kulevya. Niiombe Serikali kuwezesha waathirika wa UKIMWI kupata lishe kwani waathirika wanashindwa kupata lishe ili waweze kumeza dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali kuweka mpango maalum wa utoaji dawa za magonjwa nyemelezi yanayotibiwa na septrin na dawa hii haijaambatanishwa kwenye dawa za kufubaza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo dume ni sababu mojawapo kwani mwanamke hana mamlaka juu ya mwili wao na pia wanawake wengi waume wao wengi hutumia dawa za UKIMWI kwa siri na huzihifadhi ofisini. Niishauri Serikali kuanzisha au kuendeleza taaluma, mitaala ya kujifunza jinsi gani UKIMWI unavyoenezwa na pia kupunguza uwepo wa night clubs kwenye makazi ya watu.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze na kuunga mkono hoja ya Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali kuhusu wazee wa Tanzania walio wengi wako katika hali mbaya sana. Hawana chakula, hawana dawa na hawana kadi za bima, Serikali iliangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe mikopo ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu Serikali iangalie kwani inatolewa kwa upendeleo, wale wenye haki ya kupewa hawapewi na kupewa wasiostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, si kweli kwamba hospitali zina dawa za kutosha kwani ni mara nyingi nimefika Hospitali ya Tumbi kupeleka wagonjwa hakuna hata panadol; niiulize Serikali ni vipi dawa ziwepo na mgonjwa aambiwe hakuna?

Mheshimia Mwenyekiti, nipende kushauri kuhusu TFDA, tozo za TFDA ni kubwa mno tena kutozwa kwa dola tena hata kwa product ambazo ni ndogo. Hii imesababisha wajasiriamali kupata shida sana wanapokwenda kusajili product zao. Mfano beer 1H (200C) $ 10 kwa nini kwa dola na si kwa Tanzanian shillings?

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule nyingi hazina vyoo na madarasa ya kutosha. Walimu hawatoshelezi wakati mitaani walimu wamejaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali kuboresha Hospitali ya Milembe iongezewe mgao wa fedha na kuboreshwa.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza na naunga mkono taarifa ya Kamati. Ningependa kuongelea juu ya msongamano wa wafungwa na mahabusu magerezani yamefikia mahali pa kuvunja haki za binadamu kwani inafikia mahali wafungwa na mahabusu kushonana kama vijiti vya kiberiti, kitu ambacho hukupelekea wafungwa kukosa haki ya msingi ya kulala na pia kuambukizana magonjwa. Msongamano huu pia umesababisha Serikali kutumia fedha nyingi kuwahudumia. Ningeshauri ugeuzwe kuwa nguvu kazi ya uzalishaji hivyo kuzalisha vyakula au huduma itakayoongeza pato la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nishauri Serikali inapopeleka mabalozi nje iangalie uwakilishi bora wenye tija wa kutangaza na kutafuta fursa za kiuchumi, kwani Mabalozi ndio wanaotarajiwa kuiuza nchi yetu kimataifa. Nishauri Serikali kufanya upimaji wa kazi zilizofanywa na balozi ili kutathimini iwapo kuna haja ya balozi huyo kuwepo huko kwenye uwakilishi wa Serikali katika nchi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri Serikali kuangalia pya juu ya watoto wanaozaliwa magerezani, wasiishi maisha ya ufungwa ya mzazi. Serikali itafute njia ya kuwalea watoto hao na kuwapa haki za msingi za watoto ili wasijione nao kama wafungwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri Serikali kuwajali wafungwa wenye ulemavu na wenye maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa kuwapa lishe bora pia kuwakinga na magonjwa nyemelezi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri Serikali kuangalia upya mpango wa ulinzi wa Wabunge ambao wamekuwa wakikamatwa kwenye maeneo ya Bunge kinyume na kanuni za Bunge, hivyo suala hili limekuwa kero sana kwa Wabunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri Serikali kuwahisha fedha zinazoidhinishwa na Bunge kwa wakati, nashauri Serikali itambue uhitaji wa Wizara hii kwani ni nyeti sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri Serikali kuboresha nyumba za askari magereza kwani zina hali mbaya sana, zinapunguza morali ya kazi kwa askari hao.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri kwamba Uongozi wa Bunge uendelee kutoa elimu na maelekezo juu ya taratibu za Bunge ambazo zitasaidia Wabunge kutambua wajibu wao. Pia nishauri Uongozi wa Bunge kuweka Semina zitakazowaelimisha Wabunge kujua ni yapi mambo ambayo hayatakiwi Mbunge kufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri vilevile uongozi wa Bunge kabla ya Mbunge kupewa adhabu aitwe aonywe na apate muda wa kujieleza ili haki ipate kutendeka.

Hata hivyo, naomba nishauri kuwa Uongozi ujaribu kufuatilia tabia za Waheshimiwa Wabunge ili kutambua tabia zilizojificha kwa Wabunge hao ili wapate kusaidiwa mapema kabla hawajatenda makosa ambayo yanaweza kuathiri utendaji wa kazi zao za Kibunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nishauri Kamati ya Maadili inaposhughulikia masuala ya Wabunge iweke weledi mbele na iwachukulie wakosaji wote sawa bila kuweka upendeleo wa aina yoyote. Pia nashauri adhabu zinazotolewa ziangaliwe zisiwe zile ambazo zinadhalilisha au kuathiri utendaji wa Wabunge husika kwani wametumwa na wananchi kuwawakilisha hivyo adhabu yoyote ile isiathiri uwakilishi wao.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona niishauri Serikali kuhusu ng’ombe kupigwa kuchapwa na kuwekewa namba. Jambo hili limesababisha mazao ya ng’ombe kukosa soko kwani ngozi nyingi za Tanzania zimeendelea kukosa soko. Nishauri Serikali kutafuta njia nyingine ya kutambua mifugo badala ya alama hizi kwenye ngozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri Serikali kuongeza juhudi za kuwawezesha wajasiriamali. Kwa mfano, walioamua kufuga nyuki wanapata shida sana ya kupata vifungashio hivyo wanauza asali zao kwa shida sana na kwa hasara. Niishauri Serikali kuwasaidia wajasiriamali hao kupunguziwa bei ya mizinga badala ya mzinga mmoja kuuzwa kwa shilingi elfu themanini, hali hiyo inasababisha ugumu kwao kumudu bei hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri Serikali inapotaka kukopesha mikopo kwa wajasiriamali isiache mbali utafutaji wa masoko ya uhakika kuliko ambavyo wajasiriamali wengi wamekuwa wakitengeneza bidhaa kisha kukosa masoko, hali ambayo imesababisha kushindwa kurejesha mikopo hiyo na hivyo kusababisha fedha hiyo kushindwa kwenda kwenye mizunguko ya ukopeshaji kwa wajasiriamali wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri Serikali juu ya ulipaji watumishi waliostaafu uwe wa haraka na umakini mkubwa kwani wastaafu wanapata shida sana kulipwa. Wapo waliostaafu tangu mwezi Julai, 2017 mpaka leo hii hawajalipwa. Niiombe Serikali kuliangalia kwani watumishi hao wamekata tamaa na wengine kupata magonjwa ya msongo wa mawazo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na uwanja wa ndege Songwe. Nimetembelea uwanja wa ndege wa Songwe na kuona jinsi ambavyo hauna taa za usiku kwa ajili ya kufanya ndege zitue vizuri na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uwanja wa Mwanza, nashauri kwamba Serikali iboreshe uwanja huo kwani unahitajika sana. Pia nishauri jengo la kuongozea ndege ambalo limesuasua kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu barabara za mwendokasi, ni wazi wananchi walifurahia ujio wa mwendo kasi, lakini Serikali imeshindwa kusimamia vizuri ili kuondoa kero zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, jamii iliamini kuwa mwendokasi itakuwa suluhisho, lakini kero zake ni kubwa, magari ni machache hivyo watu hukata tiketi na kukaa muda mrefu pia kujazana kama njiti za viberiti. Hali hii inaondoa dhana ya usafiri salama Dar es Salaam. Niishauri Serikali mwekezaji kuongeza magari.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nishauri Serikali kuangalia jinsi gani inaweza kwenda na mwendokasi wa ujenzi wa reli hiyo hiyo ya Kenya ambayo inatoka Mombasa na inakaribia Nairobi na wote tunawahi soko la mizigo ya Congo. Iwapo sisi tutatumia umeme kwenye reli yetu wakati Kenya wanatumia mafuta, je, gharama zitalingana za kuchukua mzigo huo Congo? Kama sivyo Serikali itaenda kupata hasara.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mlandizi Chalinze, nashauri kwamba barabara hii Serikali iamue kufanya matengenezo ya kudumu badala ya jinsi ilivyo sasa ambapo inatengenezwa na kuweka matuta muda mfupi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua Mlandizi ni bonde la mpunga hivyo ni bora kuinyanyua ili kuzuia ile hali ya sasa ambayo kila inapotengenezwa inatitia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii iwe na vipaumbele kwani imebeba miradi mingi kwa wakati mmoja kiasi imepelekea kushindwa kutekeleza mipango yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, bandari, niishauri Serikali kuwa kazi ya kuanzisha bandari kila kona wakati kuna Bandari ya Dar es Salaam ambayo ina miundombinu mingi iboreshwe ili kuweza kukidhi matarajio ya uendelezaji wa bandari yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzisha bandari nyingine Bagamoyo tukijua kabisa bandari nyingine na zenye tija mfano Mtwara kubaki ikifanya kazi chini ya kiwango kitu ambacho si sahihi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali juu ya ufungaji flow meter bandarini kuokoa ufisadi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu viwanja vya ndege, nashauri viwanja vya Taifa letu kumilikishwa. Nimesema hivyo kwani mashirika ya mafuta yanayoendesha biashara ndani ya viwanja hivyo yanamilikiwa wakati viwanja vyenyewe havina hatimiliki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Nami nina machache, najua mengi sana wameongea wenzangu lakini kuna machache ambayo ningependa kuongezea. Nafahamu kwamba kazi ya Bunge ni kuwatumikia wananchi na ni kwa ajili ya ustawi wa wananchi. Kama hivyo ndivyo basi, ina maana kwamba wananchi wangefurahi sana kuona kwamba tunawatetea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu moja tu. Huko mitaani sasa hivi wastaafu wana shida kubwa sana. Wastaafu waliostaafu tangu mwaka jana mwezi wa Julai hawajalipwa mafao yao mpaka sasa hivi. Nyumba hiyo unakuta baba na mama wamestaafu, nyumba hiyo hiyo ina vijana ambao wamesoma mpaka chuo kikuu lakini hawajaajiriwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema kwamba Serikali inashughulikia ustawi wa wananchi lakini tuangalie jinsi ambavyo wastaafu hawa hawatendewi haki. Mstaafu anaenda kwenye Ofisi za Serikali kufuatilia mafao yake anaambiwa tunalipa waliostaafu mwezi wa Aprili, ni lini Serikali imeanza kuweka foleni ya wastaafu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema haya kwa sababu nina watu ambao ni jamaa zangu, majirani, wanajamii na wapiga kura wangu ambao wamestaafu mwezi wa saba mpaka sasa hivi ninavyoongea hawajalipwa mafao yao, wataishije? Januari wameshindwa kupeleka watoto shule sababu ni kwamba hawajapewa mafao. Je, Serikali ina mpango gani wa kulipa mafao kwa wakati na sheria za ajira zinasema nini juu ya mfanyakazi anapomaliza kipindi chake cha kutumikia Serikali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tuna nia ya dhati ya kuinua uchumi huyu mtu ambaye tangu Julai mwaka jana hajapewa mafao yake, angekuwa amepewa angekuwa amejiendeleza kiasi gani? Tuna nia kweli ya kupunguza umaskini, hivi kweli Serikai itapunguza umaskini kwa njia hii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kabisa sisi ni Wabunge, hivi leo hii kama tungefika 2020 halafu tuambiwe kwamba mafao yetu tutalipwa 2021 tungekubali? Nauliza Wabunge ambao tupo kwenye Bunge hili, tungekubali 2021 ndiyo tulipwe mafao yetu? Kwa nini tunawafanya hivi wananchi ambao wametutuma mahali hapa kuwatumikia? Kwa nini hatuwasemei na kwa nini Mawaziri wanaohusika wanajua kabisa kwamba wafanyakazi hawa ambao wamelitumikia Taifa hili wameweza kutoa nguvu zao na muda wao, wamemaliza vyema lakini wanashindwa kuwapa stahili zao. Mtu anastaafu mwezi wa Julai, huu ni mwezi wa Aprili, hajapewa hata mafao yake, anaishije? Wanapata depression, wanakufa vifo ambavyo havitegemewi. Kwa nini lakini Serikali inafanya hivi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri atakapokuja ku-wind up atuambie sheria zinasema nini na kinachofanyika ni nini? Je, hizi foleni ni mpango wa Serikali, ni Serikali haina fedha za kuwalipa au vinginevyo vyovyote vile atuambie ili tuweze kuelewa na tukawaambie kwamba Serikali sasa hivi inapangisha foleni wastaafu kwa sababu haina hela na kama hela zipo za kufanya mambo mengine kwa nini hazipo za kuwalipa wastaafu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo naomba niongee kuhusu elimu. Watu wote wameongelea kuhusu elimu lakini nilisikia siku moja Mheshimiwa Mkapa anasema kwamba tukae tuzungumze elimu inaenda wapi, tunaelekea wapi na elimu. Nami nataka niulize swali kwa sababu najua kabisa Waziri wa Elimu yupo hapa, atuambie, kuna kitu nilikisikia mijadala ikiendelea juu ya wanafunzi kukariri, tunaambiwa kwamba wasirudie madarasa. Naomba nipate ufafanuzi, hivi kama mwanafunzi amefika darasa la nne amefeli halafu anaendelea la tano huyo tunazalisha wasomi wa aina gani miaka ijayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutaendelea kujadili mjadala ambao uwazi kabisa na nini hasara ya kumfanya mwanafunzi akariri? Kama akirudia darasa Serikali inapata hasara gani badala ya kupata faida kupata mtu ambaye ni bora? Ni kwa sababu ya elimu bure tunataka wasiendelee kuwa wengi kwenye madarasa hayohayo wakati wengine wanaingia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali itoe jibu ambalo litakuwa makini tuelewe kabisa kwamba Serikali inasema wanafunzi wasikariri kwa sababu inaogopa gharama itakayoingia kwa sababu itakuwa na wanafunzi wengi au sababu yoyote ya msingi ambayo itaonesha kwamba ni kweli Serikali imesema hivi kwa sababu hizi na hizi, vinginevyo tunaomba wakati ana-wind up atuambie ni nini kinataka kufanyika kwa Serikali na hii elimu kweli tuna nia ya dhati na elimu yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tulisoma, tulikuwa tunarudia mpaka mara sita, tuko hapa leo hii tunasema watoto wasirudie, darasa la nne aende mpaka la saba. Halafu akishafika la saba hajui kusoma na kuandika, akishakuwa hajui kusoma na kuandika anafanya nini au anakuwa wa kitu gani? Ningependa kusisitiza Serikali ipambanue huo mjadala unaoendelea. Kama kweli ni kutokukariri watupe sababu, kama kuna kukariri tutashukuru kwa sababu ndivyo tunavyohitaji iwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ningependa kuongelea ni kwamba, bajeti ya mwaka jana tuliongelea kwamba tunahitaji tozo ile ya mafuta iende kwenye maji. Ni jambo jema na tuliona ni jema kweli, lakini kama imeshaenda tangu wakati huo, hatujui kwamba ilienda ngapi kwa sababu hatujaona imeenda ngapi lakini cha muhimu ni kwamba ikienda kule inafanya yale matarajio na kama haifanyi yale matarajio sababu ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano wa kwangu mimi kule Kibaha, niliandika swali kuuliza kwamba miradi ya Kibaha inajengwa chini ya kiwango, wananchi wa Kibaha wanakosa maji siyo kwa sababu hela hazijatolewa. Ilitolewa shilingi milioni 531 mradi wa maji, vikao, imepotelea yote porini kwa sababu mabomba yamewekwa mabovu na hayako kwenye viwango, badala ya kuweka connector kachomelea moto, sehemu nyingine kafunga mipira ikawa maji yanamwagika, mradi ukakataliwa na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukataliwa na wananchi ukarudishwa Halmashauri, wana miezi nane mpaka sasa hivi watu wa Vikawe hawapati maji, lakini Serikali ilishatoa shilingi milioni 530 lakini zimepotea kwa sababu watendaji wamekula zile hela. Tangu siku ile niliyosema Serikali haikufanya kitu chochote mpaka sasa hivi ninaposema ni miezi nane, ukienda Vikawe hakuna maji na shilingi milioni 531 zilishaliwa, tunaelekea wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala la wajasiriamali wadogo wadogo wanaoinua maisha yao. Kwa kweli Waziri wa Viwanda alisema kwamba tuanzishe viwanda vidogo vidogo, wanawake wajasiriamali wameanzisha, wengine wanasindika spices lakini tatizo ambalo limetokea ni kwamba tozo ndogo ndogo kwenye viwanda vidogo vya wajasiriamali ni nyingi mno. Mtu anatengeneza spice anaambiwa anatakiwa apate usajili TFDA, anatakiwa aende OSHA, anatakiwa aende TBS, wote hao wanachukua hela za huyu huyu mjasiriamali mdogo ambaye ndiyo kwanza anahangaikia maisha yake tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini hivi vitu vyote visiwekwe pamoja gharama zipunguzwe ili hawa wajasiriamali waweze kupata faida. Inafikia mahali wajasiriamali wanakata tamaa, wanaona kwamba hawapati kitu chochote. Tutaendelea kuzalisha maskini kwa sababu tu Serikali imeweka mlolongo wa tozo ambazo zingeweza zikawekwa pamoja na zikaleta faida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ningependa kuzungumzia jinsi ambavyo viwanda tumevipokea sawa, kuna mwenzangu mmoja ameongelea, lakini kuna tatizo ukaguzi wa viwanda na shughuli zinazofanywa katika viwanda hivyo. Hawa vijana wetu tumesema watapata ajira, sawa, lakini mwisho wa siku tunazalisha magonjwa ambayo Serikali itaingia tena hasara ya kutibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina kiwanda pale Kibaha kinazalisha sabuni, vijana wameajiriwa lakini hamna vitendea kazi, hamna mask, wanafanya kazi vumbi za sabuni zote zinaishia kwa vijana hawa. Vijana hawa wanaishia kuwa na TB… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishauri Serikali kuwa watoto wasio na uelewa wa haraka kukaririshwa hakuepukiki kwa ajili ya ustawi wa Taifa letu. Ni ukweli usiopingika kuwa wapo ambao wanaingia kidato cha kwanza kupitia maswali ya kuchagua ambayo hata mwanafunzi akifumba macho ana uwezo wa kupasi. Katika hili, naomba tufike mahali tubadili mtindo wa maswali tuwe na mtindo wa kupima uelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili niongelee kuhusu motisha kwa walimu. Naishauri Serikali kuwatia moyo walimu badala ya kuwavunja moyo kwani wanafanya kazi katika mazingira magumu. Inapotokea kupewa majibu yasiyostahili kutoka kwa viongozi wa Serikali au mfano Wakuu wa Wilaya kuwapa adhabu, hekima ingeweza kutumika kutatua matatizo yanayojitokeza. Nashauri Serikali kuweka mazingira rafiki ya kufundishia mfano walimu kuwa na nyumba karibu na mahali wanapofundisha. Niishauri Serikali kuhakikisha inaongeza fedha kwenye eneo la vifaa vya kufundishia mfano karatasi za kutungia mitihani ili kutoa mitihani ya mwezi kiurahisi kwa ajili ya kupima maendeleo ya wanafunzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, napenda kuongelea kuhusu ukaguzi. Niishauri Serikali kujipanga kwa ajili ya kuhakikisha vifaa vinakuwepo kama magari ya kuwapeleka wakaguzi kwenye shule mbalimbali kwa ajili ya kufanya ukaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, niishauri Serikali kuwekeza katika kumkomboa mtoto wa kike kwa kuwajengea mabweni ili kuwaondoa katika shida hii ya kupata ujauzito wakiwa shuleni. Watoto wa kike wameshindwa kufikia malengo yao ya baadae kutokana na mazingira yasiyo rafiki katika kujifunzia, mfano umbali mrefu na mapori kwa ajili ya kuzifikia shule hizo hivyo humo njiani kukutana na majanga ya kubakwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano ni ucheleweshaji wa fedha. Serikali inachelewesha fedha hivyo mipango mingi kushindwa kutekelezeka kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sita, nishauri juu ya chakula shuleni. Mpango wa chakula shuleni unasaidia wanafunzi kuwa na utulivu na kujifunza kwa urahisi. Niishauri Serikali kuweka utaratibu mzuri wa kuwepo chakula shuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, saba ni uhaba wa walimu. Niishauri Serikali kuliangalia hili kwani mwalimu kufundisha watoto mia moja darasa moja na ana vipindi vinne kwa siku na hivyo kuwa na madaftari 400 ya kusahihisha kitu ambacho hawezi mwalimu kufanya kwa usahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, niishauri Serikali kuweka utaratibu wa kukariri ili kuboresha elimu ya Tanzania.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kuchangia na kuzungumzia yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu miradi kujengwa chini ya kiwango; miradi mingi nchini inajengwa chini ya kiwango hivyo kutumia fedha nyingi za Serikali na kuleta hasara kwa Serikali, huku ikiachwa miradi hiyo itakuwa haitoi maji kama ilivyotegemewa. Mfano, Mradi wa Maji wa Vikawe wenye gharama ya shilingi milioni 531 ambao hautoi maji baada ya wananchi kuukataa kutokana na mabomba kuvuja na kuongeza gharama za maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu umwagikaji maji hovyo (upotevu wa maji), nashauri Serikali kuliangalia suala hili la maji kwa wananchi imekuwa kawaida kwa mamlaka kurudisha hasara kwa wananchi. Mamlaka zimekuwa zikifanya uzembe wa kufanya matengenezo ya mara kwa mara ili kudhibiti upotevu wa maji unaondelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, uhaba wa wahandisi wa maji, maeneo mengi hapa nchini hakuna wahandisi wa maji, wanatumiwa wale ambao hawana ujuzi na hivyo kusababisha miradi mingi kujengwa chini ya kiwango. Mfano, Mhandisi wa Halmashauri ya Kibaha ambaye ni wa mazingira hivyo kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi. Naishauri Serikali kuendelea kuwaandaa wahandisi katika vyuo vyetu ili kupata wahandisi bora ili kulinda fedha za Serikali zinazopotea bila sababu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira ya uwekezaji; niishauri Serikali kuangalia jinsi Serikali na watendaji kupunguza urasimu kwa wawekezaji kwani imefikia watu/wawekezaji wanahofia kuwekeza kutokana na sera zetu zinazobadilika mara kwa mara, hivyo kuhofia kupoteza mitaji yao. Pia nizungumzie tozo zilizopita kiasi mfano TBS, TFDA, OSHA vitu vyote hivyo badala iwe inalipiwa mahali pamoja na kuhakikisha kodi yake inakuwa ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu leseni la biashara; niishauri Serikali kuangalia mlolongo wa upatikanaji wa leseni. Unatakiwa kulipa TRA baada ya kukadiriwa kwa mteja ambaye ndio kwanza anaanza biashara atakadiriwa kwa mteja badala kwa faida baada ya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, masoko ya uhakika; nizungumzie masuala ya masoko nishauri Serikali kuhakikisha inatafuta soko la bidhaa za watanzania kwani wanazalisha bidhaa lakini hakuna soko la uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali ijitahidi kutafuta masoko hata kwa bidhaa za viwandani kwani kuanzisha viwanda bila soko la bidhaa hizo itakuwa kama viuatilifu vya Kibaha ambavyo hakuna soko na uzalishaji imebidi kupunguzwa. Kutokana na kupungua uzalishaji kiwanda kimeshindwa kuajiri vijana wa Kibaha wa kutosha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuchangia machache. Kwanza ningependa kusema kwamba Serikali kama ina mpango mkakati wa kuhakikisha sekta hii ya viwanda inafanya kazi vizuri, ningependa ifahamu kwamba kilimo kiwe ni kipaumbele kwa ajili ya kulisha viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ningependa kuzungumzia kwa vile nina muda mchache ningependa kuzungumzia biashara kwa ujumla nikianzia na TRA. TRA imekuwa ni tatizo kwa sababu unapotaka kupata TIN kwa mfano TRA, utaenda kama unatafuta kazi, kwanza wafanyakazi wa TRA ni wachache, ilitokea tangazo hapa wafanyakazi wanaotakiwa kuajiriwa 400 na zikatokea nafasi 56 wakaomba. Wale 400 hatujui kama wameajiriwa au hawajaajiriwa. Wengine wanasema mpaka sasa hivi hawajaajiriwa. Imesababisha TRA kuwa na upungufu wa wafanyakazi na hivyo wananchi kupata shida sana kupata mahitaji yao pale TRA. Kwa hiyo, TRA imekuwa na usumbufu mkubwa sana. Kwa hiyo, naomba Serikali ifanye mchakato wa kuongeza wafanyakazi ili TRA iweze kufanya kazi kama inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kusema kwamba biashara ni matangazo. Nimeona viwanda kwa mfano kuna Kiwanda pale Kibaha cha Viuatilifu. Tangu uzinduzi umefanyika hamna mtu hata wa Kibaha anayejua kiwanda kile kinafanya kazi gani, kwa sababu hamna uzalishaji, hamna biashara kimekaa kama pambo. Tulitarajia watu wa Kibaha kwamba kiwanda kile kikiwepo vijana wetu watapata kazi, lakini kinyume cha hapo ni kwamba kile kiwanda hakifanyi kazi inayotakiwa na biashara ya viuatilifu hatuioni. Na matangazo ya kuonesha kwamba labda kiwanda kile kipo pale kwa sababu kina faida fulani hamna, hamna matangazo yanayoonesha kwamba wananchi wanaweza wakapata hizo dawa labda hata za majumbani kuondoa mazalia ya mbu, hatuoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ningependa kumwambia Waziri hivi viwanda vinavyoaanzishwa basi na matangazo yawepo. Viwanda visaidiwe kufanya matangazo, viwanda vimekaa kama picha hamna kinachoendelea. Pale Kibaha kuna matrekta tunayaona hatujui yapo pale kwa ajili ya nini kwa sababu wananchi hawajatangazia kwamba aidha yale yanauzwa au chochote, sasa biashara za viwanda kama hazitaenda na matangazo ina maana ni sawa sawa na kutwanga maji kwenye kinu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kusema kwamba Tanzania tunashindwa kufanya biashara ya ku- export, wananchi wengi wanashindwa kwa sababu Serikali haijatoa elimu juu ya ufungashaji. Unakuta kwamba mazao yanazalishwa hapa halafu yanachukuliwa yanapelekwa Kenya, wanafanya ufungashaji kupeleka nje na yanakuwa labeled kwamba mazao haya yanazalishwa Kenya. Sasa kama Tanzania tunataka kufanya biashara basi eneo la ufungashaji liboreshwe ili wananchi wajue akiwa na bidhaa yake anaifungasha vipi ili aweze kuipeleka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia eneo la biashara za nje kuna usumbufu na urasimu mkubwa sana kiasi kwamba watu wakitaka kuuza bidhaa zao nje wanapata usumbufu kiasi kwamba wanakata tamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuuongelea juu ya wasindikaji wadogo, wamekata tamaa walio wengi kwa sababu kwa ajili ya zile tozo ambazo ni msululu. Unakuta kuna TFDA, kuna OSHA, kuna TBS kibiashara chenyewe ni kidogo production ni ndogo product moja unavyotaka kwa mfano ya spice anataka kutengeneza viungo unakuta kwamba msululu wa kodi zenyewe zilizoko pale zinamfanya huyu mjasiriamali mdogo ashindwe kufanya uzalishaji. Kama tunataka viwanda vidogo kama tulivyosema kwamba hata anayetwanga tangawizi yake akai-pack anaweza kuwa ni kiwanda basi hizo kodi tupunguze ili viwanda vidogo hivi viweze kumudu gharama hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti ningependa kuongelea juu ya ukaguzi wa Idara ya Viwandani. Tumefurahi kweli viwanda vimekuja watoto wetu waweze kupata kazi lakini wanapata magonjwa kuliko hata kazi wanayofanya. Kwa sababu unakuta kwamba viwanda havina vitendea kazi mtu anafungasha pale Kibaha kuna Kiwanda cha Sabuni. Siku nzima anabeba sabuni zile, anahamisha, anafungasha lakini hata kinga yake hana. Hana hata ile mask ili ya kufunga puani ili angalau asivute yale mavumbi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, karakana za jeshi; nipende kushauri Serikali kuhakikisha kufufua karakana za nyumbu ambazo wakati wa Mwalimu Nyerere Nyumbu ilishaanza kuunda mpaka magari yake ukiacha matengenezo ya kawaida na uchongaji wa vyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Nyumbu Kibaha ilisaidia kuajiri vijana wetu wengi ambapo kwa sasa hali ya karakana haiko sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuongeza ajira kwa vijana wetu kupitia JKT. Nashauri Serikali kuangalia kwa upya juu ya wale vijana 2000 ambao walichukuliwa operation Kikwete kwa ahadi ya kuajiriwa. Mbaya zaidi walipomaliza na kuingia utawala mwingine wale wote waliokuwa nyuma, utawala huu haukujali kuwaajiri, walianzisha operation nyingine ambayo imemaliza mkataba wake wa kujenga Mererani na kuahidiwa kuajiriwa mara moja kwa kauli ya Rais. Je, wale walioko mitaani na ujuzi wa silaha hatuji kuleta hatari pale ambapo watashindwa maisha na kuamua kuingia katika uhalifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za fidia, nashauri Serikali kulipa fidia kwa wananchi ili kuweza kukidhi mahitaji yao ili kupunguza minong’ono iliyojaa uraiani inayopunguza mshikamano na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zabuni na ulipaji wa zabuni. Nashauri Serikali kuhakikisha wazabuni waliohudumia majeshi yetu kulipwa kwa wakati ili kutowapelekea wazabuni hao kuuziwa dhamana zao na mabenki kwa kushindwa kulipa mikopo yao.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iweke kipaumbele juu ya ulipaji wa mawakala na kuwaokoa na udhalilishaji unaofanywa na mabenki. Nashauri Serikali kuhakikisha haizuii uuzaji wa mazao ya kilimo bali itoe maelekezo ya kuhifadhi baadhi ya chakula ili kutoangukia kwenye njaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali kuongeza fedha za utafiti wa vituo vyetu, kwa mfano Vituo vya Utafiti vya Mlingano, Ukiriguru na Naliendele ili itoe matokeo yatakayoleta ufanisi katika kilimo. Pia niishauri Serikali kuhakikisha inaangalia zaidi katika suala zima la ushirika nchini kwani hakuna watumishi wa kutosha tangu walipostaafisha watumishi kwa manufaa ya umma hawakuajiri watumishi wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali kuangalia umwagiliaji kwenye mashamba yetu, kwenye mito yetu mfano Mwalimu Nyerere alianzisha shamba la mpunga Ruvu ambalo sasa hivi linapimwa viwanja tu na umwagiliaji uko mahututi. Niishauri Serikali kufufua mashamba haya badala ya kufanya maji haya kupotelea baharini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia, kama ifuatavyo:-

Kwanza napenda kuishauri Serikali kuangalia upya juu ya suala zima la upigaji chapa mifugo ambao unaharibu uzuri wa ngozi hivyo ngozi zetu kukosa soko katika soko la dunia.

Pili, napenda kushauri Serikali kujenga majosho ambayo miaka ya 1970 ilijenga majosho hayo na kusaidia wafugaji kuoshea ng’ombe au mifugo kwa kulipia kidogo hivyo kunusuru mifugo yao na magonjwa. Nashauri jambo hili lifanyike ili kusaidia wafugaji.

Tatu, nizungumzie suala zima la usalama wa nyama tunayotumia pamoja na machinjio yetu. Machinjio mengi nchini ni machafu, miundombinu yake ni mibovu na hatarishi kwa afya ya jamii. Nimetembelea machinjio ya Dodoma ni ya kisasa na safi. Je, kwa nini Serikali isiziagize Halmashauri zote nchini kujenga machinjio ya kisasa?

Nne, uchomaji nyavu za wavuvi si jambo la hekima bali kinachotakiwa ni kuzuia uingizaji au utengenezaji wa nyavu zisizofaa kufika kwa watumiaji.

Tano, operation ya uvuvi haramu iwe na weledi na si ya kuonea watu kwani tunajenga uhasama na jamii. Mfano, mwananchi ajue ni kiasi gani cha samaki anaruhusiwa kuwa nacho ili asiweze kushikwa siyo kama ilivyo sasa.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Spika, hoteli za kitalii na uhudumiaji wageni, ningependa kushauri Serikali kuanzisha vyuo maalum kwa ajili ya vyuo vya kuelimisha wahudumu wa kuhudumia watalii. Imekuwa watalii wengi wakilalamikia huduma zinazotolewa hapa nchini kuwa ni za chini sana.

Mheshimiwa Spika, hata waongozaji wa watalii ni kwamba hawana mafunzo maalum hivyo kuwa shida kwa watalii wetu. Gharama za juu kwa watalii hivyo kupunguza ujio wa watalii, mfano watalii kulipia huduma moja mara mbili kuliko ilivyo sasa ambapo mtalii analipia hoteli, analipia usafiri halafu anapofika kwenye eneo la mbuga anakutana na tozo ya kuingiza chombo hicho kwenye mbuga hii inakatisha tamaa kwa watalii.

Mheshimiwa Spika, nishauri gharama zinazolipwa wenye mahoteli hata kama watalii hawajalala hivyo kukatisha tamaa kwa wamiliki wa mahoteli ya kitalii.

Mheshimiwa Spika, vitalu vya uwindaji; nashauri Serikali kugawa vitalu kwa kuzingatia wazawa pia ugawaji wa vitalu uende kwa wakati. Pia nashauri kuwawekea mazingira mazuri ya uwekezaji katika utalii. Pia niishauri Serikali kuangalia upya juu ya mipaka ya kuhifadhi maliasili na mbuga kwa ujumla. Pia Serikali ihakikishe maeneo hayo ili yale ambayo hayatumiki yarudi kwa wananchi na yabadilishwe matumizi.

Mheshimiwa Spika, niishauri Serikali kuhakikisha inaongeza fidia kwa wananchi wanaopata madhara ya kuvamiwa na wanyama hivyo kuleta hasara kwa wananchi. Vikundi vya wanawake, wanawake wachonga vinyago mfano pale Mwenge. Niishauri Serikali kuyaangalia makundi haya ya wanawake wanaojishughulisha na vinyago wanawauzia watalii wetu wapewe mikopo ya kuwawezesha kutoka maliasili kuwasaida. Pia Serikali isaidie masoko ya vinyago.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Ofisi za Balozi zetu, nashauri Serikali kujenga Ofisi zake katika Balozi zetu kwani fedha nyingi zinatumika kugharamia Ofisi hizi wakati kuna viwanja. Mfano, Msumbiji kuna eneo la kujenga na tunashindwa kujenga. Tukope hata mikopo ya masharti nafuu ili ije ilipwe kwa fedha zile ambazo tungelipa kodi ya majengo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, uteuzi wa Mabalozi; nashauri Serikali kuangalia uteuzi unaofanyika kama unaendana na faida tunazopata kutokana na uwekezaji huo katika Balozi hizo. Ni kwa kiasi gani upimaji wa utendaji wa Balozi zetu ukichukulia kuwa kuna malengo mahususi ya uanzishaji Balozi hizo ikiwa ni pamoja na kutangaza vivutio vya Tanzania ili kuwezesha Tanzania kupata wawekezaji.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Spika, nipende kupongeza uwasilishaji wa Wizara na Kamati ya Bajeti. Napenda kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu Deni la Taifa, nipende kuishauri Serikali kuangalia juu ya madeni haya ambayo yamesababisha mpaka vifo vya Watanzania wenzetu waliotoa huduma kwa Serikali kwa sababu ya kuchelewa kulipwa hivyo kushindwa kulipa mikopo na mabenki kuchukua mali zao. Ningependa kushauri Serikali kukopa mikopo yenye riba nafuu na kuwekeza kwenye miradi yenye kurudisha faida haraka ili mzunguko wa fedha hizo kuwa mizuri na kulipia madeni kwa wakati ili kuepuka riba kubwa.

Mheshimiwa Spika, wakandarasi wengi wanapata hasara kwani Serikali haiwalipi riba kwa pesa ambayo inacheleweshwa katika malipo ukizingatia wakandarasi hawa wanakopa kwenye mabenki hayo na wakichelewesha wanatozwa penalty.

Mheshimiwa Spika, kuhusu vipaumbele kuwa vingi, ningeshauri Serikali kuwa na vipaumbele vichache ili kuweza kuvitekeleza kwa wakati hivyo kuokoa fedha badala ya kuwa na vipaumbele vingi ambavyo havitekelezwi kwa wakati. Mfano, tuna ujenzi wa Bwawa la Rufiji, reli, viwanja vya ndege, flyovers huku kuna huduma za jamii zinabaki zikisua sua.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mikopo mabenki ya ndani, niishauri Serikali kukopa mikopo nje badala ya sasa ambapo Serikali inanyang’anyana na sekta binafsi mikopo katika benki hizo hivyo sekta binafsi kukosa mikopo na kushindwa kujiendesha na kufunga biashara nyingi hivyo Serikali kukosa kodi ya kuendesa Serikali.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kodi ya mapato, nashauri Serikali kuangalia upya juu ya kodi hizo kwani zimekuwa sababu ya wafanyabiashara wengi kuhama na kuhamia nchi jirani kama wafanyabiashara wa Tunduma waliomua kuhamia Zambia kutokana na kodi zilizo msururu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mashine za EFD, nipende kuishauri Serikali kuliangalia kwani mashine hizi nyingi ni mbovu, lakini pia upatikanaji wake ni wa shida, unalipia kisha unasubiri muda mrefu sana mpaka kupata. Pia bei zake ziko juu kiasi ambacho wenye mitaji midogo ni ngumu kulipa kwa mara moja. Serikali ingeanzisha ulipiaji mashine hizi kidogo kidogo.

Mheshimiwa Spika, kodi kabla ya biashara, niishauri Serikali kuondoa mpango wa Serikali wa kuwatoza kodi wateja wapya kabla ya biashara na kuwa-charge kwenye mitaji badala ya kuwa-charge katika faida ya biashara.

Mheshimiwa Spika, wawekezaji kutoka nje wamepewa muda wa matazamio, baada ya hapo ndiyo wanatozwa tofauti na sisi wazawa tunatozwa kabla ya biashara.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kuhusu hali ya amani nchini. Nashauri Serikali kuangalia upya juu ya suala zima la chanzo cha amani kama kipo vizuri. Chanzo cha amani ni haki. Haki ni tunda la amani, bila haki haitatokea hata siku moja amani ikawepo. Kamata kamata ambayo inaendelea hapa nchini na mauaji yanayoendelea yanachochea uvunjifu wa amani. Niishauri Serikali kuangalia kuna shida gani inayosababisha watu kuuliwa katika mazingira ya kutatanisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee juu ya polisi kubambikia kesi wananchi na kuwafanya kukaa mahabusu kwa miaka sita bila kesi zao kumalizwa mapema. Niishauri Serikali kuangalia juu ya mahabusu hawa kwani huongeza msongamano magerezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali juu ya polisi kutumia nguvu nyingi kwenye mambo ya kawaida, mfano, unapozuia au kutawanya waandamanaji wasio na silaha kwa bunduki na risasi za moto mpaka kufikia kuua kama alivyouwa Ndugu Akwilina. Maandamano ya CHADEMA yalikuwa ya amani, hayakutakiwa kufyatuliwa risasi za moto. Polisi wameshindwa kufanya kazi ambayo wana wajibu nayo wanafanya kazi ya siasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee juu ya polisi wanavyowachukua watuhumiwa ndivyo sivyo, ni hatari sana kwani huwapiga watuhumiwa ambao hawajahukumiwa, hivyo kupewa hukumu na polisi kitu ambacho si haki. Je, kama haki haikutendeka, amani itatoka wapi? Hawa polisi wanaishi na wananchi huko kwenye jamii, hivyo itafika siku ambapo jamii itachoka na kupambana na polisi huko huko kwenye jamii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishauri Serikali kuharakisha urasimishaji wa hati za maeneo ya wananchi ili kuwezesha kupata mikopo kiurahisi na kupunguza umaskini. Nashauri zoezi la utoaji huduma kwa wahitaji kupitia TASAF kuchunguzwa, kwani wataalam wengi hawana weledi katika utendaji. Watendaji wamesababisha misaada hiyo kuwaacha walengwa na kupewa wenye uwezo na hivyo zoezi hilo kukosa maana ya kuanzishwa kwake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali kuwalipa watumishi waliostaafu stahiki zao kwani ajira inapokoma ni dhahiri mtumishi anakuwa na mipango yake ya kujikimu baada ya kustaafu. Hivyo, nishauri Serikali kuliona hilo kwani inaharibu taswira ya utumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri Serikali kufungua milango ya uhamisho kwa watumishi wale ambao wanahitaji kuungana na familia pale mwenza mmoja anapohamishwa hivyo kuleta usumbufu kwa watoto ambao hawaelewi wabaki na mzazi yupi. Kumekuwa na usumbufu mkubwa kwa mtumishi anapotaka kuhama, kuambiwa atafute mtu wa kubadilishana naye, je asipopatikana huyo mtu hivyo mtumishi anakosa haki ya kuhama? Je, huo ni wajibu wa mtumishi au Serikali kutafuta jinsi ya kujua ni wapi mtumishi huyo atapangwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia watumishi wapate kozi fupi za kujengewa uwezo ili wapate uelewa mpana katika sehemu zao za kazi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze nami kuchangia mada iliyoko mezani. Kwanza ningependa kusema amani ni tunda la haki, mahali popote pale ambapo haki haitatendeka ni kwamba amani haiwezi kupatikana. Tutacheza, tutasema, tutachangia, tutafanya tufanyavyo lakini kama watendaji hawatatenda haki hakuna amani itakayopatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hayo kwa sababu kumekuwepo na kamata kamata, mauaji na hao wasiojulikana na vyovyote vile na wale wanaouawa mikononi mwa polisi. Hivi kama ungeweza kufikiria mtu anauawa mikononi mwa polisi, halafu useme kwamba kuna amani hao waliopata huo msiba wa kuuawa huyo ndugu yao mikononi mwa polisi wawachukulieje polisi hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vema kabisa tutakaa tukafikiria hivi kama kweli tunataka kuzungumzia habari ya amani, tuangalie haki inatendeka kwa kiasi gani, ndipo tutaweza kusema kwamba sasa hivi Tanzania tuna amani ya kutosha kwa sababu haki inaenda sambamba na amani. Huwezi kupata amani kama hutendi haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kama inataka kuhubiri amani tuone haki ikitendeka kwa watu wote na vyombo vyetu vya ulinzi vitende haki kwa wananchi ndipo tutasema kwamba Tanzania sasa hivi ina amani. Hatuwezi kusema theory wakati practical hazipo. Niishauri Serikali kama kweli Mheshimiwa Waziri wetu ana nia ya dhati ya kurejesha amani ile tuliyokulia sisi kwa umri huu, haki itendeke kwa wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshuhudia ubambikaji wa kesi, kijana anashikwa, kwanza utaratibu wa polisi kuwakamata wahalifu ni mbovu, kwa sababu sheria zinasema kabisa kwamba utamkamata, utamfikisha mahali akajieleze halafu kesi iende mahakamani, lakini mtu anampiga mhalifu, anageuka yeye kuwa ndio mahakama na kumsababishia maumivu na wakati mwingine kumsababishia kifo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sehemu zingine polisi wamempiga mpaka kijana mmoja anafika hospitalini anakufa, kwa sababu tu polisi hawajui kazi yao kwamba akishamshika mtuhumiwa huyo sio mhalifu tayari, mahakama ndio itakayosema kwamba yeye ana uhalifu na aingie jela. Hata hivyo, unakuta kwamba polisi anachukua hatua ya kumwadhibu wakati yeye siyo mahakama, tutasemaje kuna amani kama kuna mambo haya yanatendeka? Hiyo amani ambayo tunaihubiri ni ipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuzungumzia upekuzi. Jamani hivi kweli unapoenda kumpekua mtu kuna sheria, tuna vitambulisho, unatakiwa kama ni kwenye mtaa kuna Serikali ya Mtaa, inatakiwa ishuhudie mtu anapekuliwa, lakini mtu anaingia yeye kama ni polisi anaanza pekupeku anaingia chooni, anaingia chumbani, anaingia huku, sehemu zote anaingia kwenye nyumba ya mtu. Hivi huyo mtu anajisikiaje, maana yake hata ile diginity yake inapotea. Kwa nini tufanyiwe hivi wananchi wa Tanzania, huko tulikotoka hatukushuhudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina miaka yote hii sijawahi kuona Serikali ambayo inaruhusu mtu apekuliwe, ukiuliza unaambiwa nimeambiwa kutoka juu, huko juu ambako kupo juu sana, tunajua kabisa juu anakaa Mungu peke yake. Siku hizi anashusha directive kwamba sasa utafanya hivi na hivi ni kweli au huko juu anakoeleza kila siku ni wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda Mheshimiwa Waziri akija hapa atuambie huko juu wanakosema kila siku juu ni wapi huko tukakujue. Kama ni mbinguni tujue kitabu kinasema nini, Mungu alishusha biblia, alishusha maelekezo kwamba taratibu za kidini zitaenda hivyo. Huko juu sasa hivi ambako kila kitu juu, juu, ni wapi? Maana yake tumekuwa hatuelewi huko juu ni wapi? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho ningependa kusema ni upepelezi wa kesi. Mahabusu anakaa miaka sita kwa sababu upelelezi haujatimia, huyo mahabusu akishakaa miaka sita aje ahukumiwe anakuwa na miaka mingapi au akutwe hana kosa analipwa fidia? Kama sio uonezi. Tunataka kuchambua kwa sababu nimesema kabisa amani ni tunda la haki, kama watu hawa hawatendewi haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naapa hakutakuwepo na amani katika nchi hii mpaka tufike hapo, kwa sababu haki isipotendeka, amani natokea wapi wakati watu wanalalamika kila kona kwamba nimefanyiwa hivi, mimi unajua ilikuwa iwe hivi, nimefanyiwa hiki, kwa nini ifike mahali hapo, kwa nini tusione kwamba nchi ya amani haina migogoro, haina mambo ya kubambikiziwa, haina mambo ambayo ukiangalia kwa macho hata hivi unaona kabisa kwamba hii sio haki mtu kutendewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuongelea kuhusu watoto magerezani. Tunafahamu kabisa kwamba magereza yetu yanafanya kazi lakini Serikali ina mpango gani juu ya watoto wale walioko magerezani ambao wanazaliwa magerezani. Hivi kweli mtoto afungwe pamoja na mzazi wake kwa kosa ambalo hakufanya. Kwa nini isitokee kwamba mtu akishajifungua apewe kifungo cha nje ili yule mtoto aweze kupata haki za msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefika pale Ruanda nimekuta mtoto amefungwa na mzazi wake, akipita pale mlangoni kuingia na mtoto ananyoosha mikono hivi kuingia kama mfungwa, ametoka shule anaingia na yeye kama mfungwa, huyu mtoto anajifunza nini labda katika maisha yake atakuwa amejifunza nini? Serikali jamani tunaenda wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutasema kwamba kuna amani, huyu mtoto anayejifunza mambo mabaya ya gerezani atakapokuwa atakuwa mbaya kuliko baba yake au mama yake aliyeingia gerezani, kwa sababu atakuwa amejifunza ukatili. Kwa nini ifike mahali tumfunge mtoto yule ambaye hajafanya kosa? Kwa nini tusichukue hatua zingine za kum-rescue yule mtoto ili aje awe kijana mzuri au kijana bora katika maisha yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri anapo-windup atuambie hawa watoto watafungwa magerezani mpaka lini? Kwa sababu kama ni makosa walifanya wazazi wao na wakati mwingine mimba zenyewe zinapatikana humo humo magerezani, sasa yeye amekosa nini? Hajaingia jela yeye na wala mahakama haikumhusu yeye, kwa nini afungwe kama mfungwa wa kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuzungumzia kuhusu matumizi mabaya ya silaha au nguvu inayotumika na polisi katika kukamata mtu. Ifike mahali Serikali watueleze vizuri hivi anaponikamata mimi na begi langu kwa kunikwida na kunipiga na kunifanyaje wakati sina silaha, sina nguvu kama yeye ambaye amejifunza nguvu za kumkamata, mtu ni nini hiki kinatendeka jamani? Tunatambua amani huyu mtu anayefanyiwa haya ndani ya moyo wake anafurahi au ndugu zake wanaoona anatendewa hayo wanafurahi? Kama hawafurahi, hawana amani hawa watu, hawana furaha na Serikali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tufike hapo, kwa nini tusifike mahali pa kufanya yale tuliyokuwa tunafanya enzi zetu miaka hiyo. Serikali zilikuwa zinafanya mambo haya haya na watu hawa hawa tuliopo tumeshuhudia mengi, haya tunayoona ni mageni. Mtu anakuja anakamatwa au polisi wanatawanya maandamano au wanatawanya watu ambao wako mikusanyiko. Hii mikusanyiko haina silaha, haina chochote unaamua kutumia risasi ambazo tunazinunua kwa pesa nyingi kufyatua na kuumiza watu ambao ni nguvu kazi. Hivi tunaenda wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ukiuliza hivi kwa nini mnafanya hivi? Eti kutoka juu, mbinguni? Yaani iwe ndio kinga tunataka kujua kutoka juu, huko juu kuna nini? Tunajua huko juu anakaa Mungu peke yake, Mheshimiwa Waziri atueleze huko juu kuna nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ukamataji holela nimeshangaa kitu kimoja jamani. Sisi tulikuwepo hapa Bungeni siku moja tunashangaa watu wanakamatwa, Wabunge wanakamatwa wanaambiwa kwamba sijui wamempiga Shonza tulishangaa na ile immunity iko wapi?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wapima Ardhi Binafsi. Nipende kushauri Serikali kutambua kazi kubwa inayofanywa na sekta binafsi ya uendelezaji wa ardhi kwa kupima na kusaidia uendelezaji wa ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali kuwaondolea VAT katika malipo yao au kodi ambayo itafanya kuongeza gharama kwa wananchi wanaohitaji kupimiwa ili kufanya kazi ya kupanga miji yetu na vijiji kufanyika kwa haraka ili kuokoa janga la ujenzi holela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapimaji binafsi wameongeza kasi ya upangaji miji kutokana na Serikali kutokuwa na wafanyakazi wataalam wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mgawanyo wa Ardhi. Nishauri Serikali kuhakikisha kuwa inatenga ardhi kutokana na uhitaji mbalimbali. Kwa mfano, ardhi kwa ajili ya wafugaji; ieleweke kwamba kila mkoa, wilaya, kata zinatenga maeneo ya wafugaji na wakulima ili kuondoa migogoro inayopelekea wananchi kuuana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri Serikali kuangalia upya juu ya hifadhi za wanyama au maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya misitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali ifuatilie migogoro inayoendelea kati ya wananchi na Hifadhi za Taifa ili kujiridhisha mipaka ya awali badala ya kuwachomea wananchi nyumba zao na kuwanyang’anya mifugo yao au kupiga risasi mifugo ya wananchi, jambo ambalo limezalisha chuki baina ya wananchi na wahifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Gharama za Upangaji Ardhi na Malipo ya Majengo. Niishauri Serikali kuliangalia hili kwani limekuwa kikwazo kikubwa kwa wananchi. Mwananchi analipia ada ya kiwanja kila mwaka halafu analipia kodi ya jengo ambapo pia amelipa kodi wakati wa kununua vifaa vya ujenzi, hivyo mwananchi kuona kuwa na ardhi au kujenga nyumba ni kosa kwani kodi nyingi zinamfuata mwananchi huyu. Naishauri Serikali kuchagua kodi mojawapo ilipwe ili kuwapunguzia misururu ya kodi iliyopo sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hati za Kimila Kutotambuliwa Kisheria. Niishauri Serikali kuliangalia hili kwani hati za kimila hazitambuliwi mara mwananchi ahitajipo mkopo benki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maeneo yasiyoendelezwa yarudishwe kwa wananchi au kupangiwa matumizi mengine. Nishauri Serikali maeneo ambayo hayatumiki mfano eneo kubwa la Shirika la Elimu Kibaha ambalo limekuwa pori na kusababisha mauaji na ubakaji mkubwa. Niombe Shirika la Elimu Kibaha kuchunguzwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni ulinzi wa madini yetu. Kutokana na Serikali kuona ni vyema kulinda madini yetu kwa faida ya wananchi wa Tanzania imeweza kujenga ukuta huko Mererani. Napenda kujua, katika uchimbaji wa madini haiwezekani kutokea mtu kuruka ukuta huo huo chini kwa chini? Kuna mkakati gani wa kuhakikisha wachimbaji hao hawatokezi mbali nje ya ukuta huo? Kama ulinzi huo kwa tanzanite unafaa, je, Serikali ina mpango gani kuhusu migodi mingine ya dhahabu, kwa mfano Buzwagi na kwingineko?

Mheshimiwa Naibu Spika, madini ya ujenzi kodi zake ni za juu kiasi cha kusababisha wananchi kushindwa kugharamia ununuzi wa madini hayo kwa ajili ya ujenzi wa makazi bora na salama kwa wananchi. Napenda kuishauri Serikali kuliangalia hilo kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu madini ya Liganga na Mchuchuma, napenda kushauri Serikali kuharakisha mchakato wa uchimbaji kwani chuma au nondo tunazojengea sasa hivi siyo imara, zinatokana na vipande chakavu vinavyookotwa na kuyeyushwa, hivyo vinasababisha nyumba nyingi za kawaida kuporomoka na maghorofa pia. Naishauri Serikali kulishughulikia hili kwa ukaribu kwani nondo za nje ni ghali sana na za hapa ni dhaifu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu fidia kwa wananchi wanaopisha wawekezaji, natambua kwamba madini mengi huvumbuliwa na wananchi, hivyo badala ya kuwaondoa wazawa wangeongezewa uwezo kwa kukopeshwa vifaa vya uchimbaji ili waweze kujiongezea pato kwani wawekezaji wanapopewa uwekezaji hawataki kuwashirikisha wazawa wanawafanya vibarua na kuwanyanyasa. Niishauri Serikali iliangalie hili kwa faida ya wachimbaji wadogo wadogo kwani wanasaidia mzunguko wa fedha hapa nchini na kukuza uchumi wa nchi tofauti na wawekezaji wanatorosha fedha hii kwa manufaa ya nchi zao.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Spika, ningependa kuchangia kama ifuatavyo. Nashauri Serikali kuhakikisha haki na amani inalindwa na itambue amani ni tunda la haki. Pale tu ambapo Polisi watatenda haki ndipo amani itashamiri Tanzania. Mfano, Polisi wanapozuia vikao vya ndani kwa Upinzani wakati Chama Tawala wakifanya vikao, hiyo siyo haki. Nimeshuhudia kwa macho yangu nikiwa kwenye kikao cha ndani Kibaha, nikiambiwa kuvunja kikao hicho eti kutatokea vurugu wakati ni kikao cha Kikatiba cha chama.

Mheshimiwa Spika, nishauri Serikali ifuatilie rushwa zinazoendelea kwa Askari wa Usalama Barabarani. Mfano, magari yanayotoka Saba Saba kuelekea Nane Nane, siku moja kwa macho yangu nimeona Polisi wanasimama Kilimo Kwanza kila daladala wanatoa Sh.2,000, hivyo halikaguliwi linaendelea na safari hata kama kuna shida kwenye gari.

Mheshimiwa Spika, Serikali iangalie kwa upya maisha ya Askari Magereza na Polisi, makazi yao siyo rafiki. Hawawezi kufanya kazi zao kwa weledi kama Serikali haitawaangalia kwa jicho la ziada.

Mheshimiwa Spika, niombe Serikali iangalie ajira za Polisi kwani zinatolewa kwa upendeleo bila kujali sifa tarajiwa za Polisi zilizoainishwa katika ajira hizo.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Najua kabisa dakika zangu ni chache, nina mambo machache sana ya kushauri kwa ajili ya mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza natambua kabisa kwamba enzi za Mwalimu Nyerere alipotoa ile kauli mbiu ya Kilimo ni Uti wa Mgongo, alimaanisha kwamba binadamu huwezi kutembea bila uti wa mgongo na ukawa hai. Kwa maana hiyo kama tunafahamu kabisa kwamba kilimo ni uti wa mgongo, ningemshauri Waziri wa Fedha Mheshimiwa Dkt. Mpango yafuatayo na inatokana na kile ambacho nakiona kwenye kilimo kwa wakati huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Mwalimu Nyerere aliposema Kilimo ni Uti wa Mgongo, alihakikisha katika maeneo mbalimbali anawasaidia wananchi kulima kisasa. Kwa mfano, natoka Pwani, alihakikisha Bonde la Ruvu linatoa mpunga wa kulisha karibu Dar es Salaam nzima na Tanzania kwa ujumla. Leo hii ukipita Kibaha ukafika Ruvu, utakuta lile bonde limegeuzwa kuwa viwanja vya kujenga nyumba. Nataka kujua hivi tumeshabadilisha lile shamba la Ruvu kuwa la ujenzi? Wakati Waziri ana windup atujulishe basi kama lile bonde ambalo tulikuwa tunapata mpunga na tunanunua chakula kwa bei nafuu kama limebadilishiwa matumizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye viwanda nimeona Pwani tunaongoza kwa viwanda, lakini kinachonishangaza pale Kibaha kuna matrekta, wananchi wa Tanzania ili tuweze kuondokana na kilimo cha jembe, tulitarajia kwamba Serikali itakuja na mpango angalau wa kuanzisha hata SACCOS wakopeshwe yale matrekta waweze kulima kilimo cha kisasa ili tuendane na ule mpango wa Rais wa Awamu ya Kwanza wa kauli ya mbiu ya kusema kwamba kilimo ni uti wa mgongo. Matrekta yale yanaoza pale Kibaha hayajulikani yatapaki kwa muda gani na wananchi wanalima kwa jembe la mkono na ni wa Kibaha pale pale. Hakuna maelezo yale matrekta yametengenezwa halafu yanaenda wapi, mwaka juzi yalikuwepo pale pale, mwaka jana yako pale pale lakini tuna Tanzania ya viwanda. Sasa ukianza kujiuliza nini maana ya Tanzania ya viwanda, kama ni Tanzania ya viwanda…

T A A R I F A . . .

MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sikubaliani na hiyo taarifa kwa sababu mimi nimesema hivi, sasa hivi ni Tanzania ya viwanda na kile Kiwanda cha pale Kibaha hakijaanza enzi hizo za Wabunge walipokopa, yale matrekta yametengenezwa siku za karibuni, tunahitaji yatumike ili uti wa mgongo uwe ni kilimo. Hatuwezi kuwa na vijana ambao hawana kazi, Bonde la Ruvu limechukuliwa linajengwa nyumba, matrekta ambayo tulitarajia yagawiwe kwa wananchi yamepaki pale, halafu tuseme kuna Tanzania ya viwanda na kwamba tutawakwamua wananchi kwenye umaskini? Hicho ndicho nilichokuwa nakizungumzia.

T A A R I F A . . .

MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, siwezi kukubali ile taarifa, mimi naongelea mpango ambao una mambo mengi, kwake kwenyewe hata maji hamna, sasa tunataka mwananchi ajikwamue ili hizi rasilimali nyingine ziende mahali kwingine zikafanye kazi. Kwa hiyo, mtani wangu siwezi kumkubalia hilo. Mimi nilikuwa naelezea kwamba tuko vizuri katika kupanga mipango lakini katika kutekeleza lazima tuchukue hatua za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naongelea kuhusu PPP. Nafahamu kabisa kama tungetumia PPP ina maana tungeweza kubakiza akiba ya pesa tukafanya mambo mengine kulikoni kila kitu kufanya sisi kama Serikali. Tunachukulia mfano kwamba mpaka sasa hivi haijajulikana kama reli na Stiegler’s Gorge vinajengwa kwa pesa za ndani au kwa mkopo? Hata tunapoulizwa na wanachi tunashindwa kujibu kwa sababu, mara tuambiwe inajengwa kwa mkopo, mara tuambiwe inajengwa kwa pesa za ndani, kipi ni kipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda Mheshimiwa Dkt. Mpango ukija ku-windup utuambie kabisa hii miradi ya kimkakati inafanywa kwa pesa za ndani au kwa pesa za mkopo au kwa pesa za ndani pamoja na pesa za mkopo? Hilo tutaelewa ili tuweze kuwaelimisha wananchi kwamba jamani tunafanya hili kwa pesa za mkopo na kwa hili tunafanya kwa pesa za ndani. Hii itasaidia suala hili kueleweka kuliko kufanya propaganda kwamba tuna hela nyingi sana wakati wananchi wanaishi kwa shida, tuna hela nyingi sana wakati tungeweza kufanya kwa PPP tukaokoa hela.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo ya wanafunzi bado ni tatizo, kwanza inachelewa na pili inatolewa bila kufuata taratibu. Mfano, kuna yatima ambao wamejaza vizuri pamoja na yote hayo bado hawapewi mkopo wanapewa ambao wana uwezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, motisha kwa walimu. Hakuna elimu bora bila walimu kupewa motisha. Hata kama mna madarasa mazuri kiasi gani au miundombinu yote iwepo bila kuhakikisha walimu wana ari ya kufundisha ni kazi bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukataji mikopo kwa asilimia 15. Tukumbuke kuwa wapo pia walimu ambao wanakatwa mikopo na mshahara yao ni midogo. Ukikata mkopo kwa asilimia hizo unamwacha hana chochote na kushindwa kuwajibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu bure. Changamoto za elimu bure ni kubwa mno, watoto ni wengi, hakuna madarasa, walimu, vifaa vya kufundishia na maabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria za uanzishaji shule. Shule za Serikali zinaanzishwa hata kama hakuna vyoo, madarasa machache ukilinganisha na za binafsi ambazo unakuta hazipati usajili wakati pengine hawana baadhi ya mahitaji madogo tu. Tuangalie na kuwatia moyo wenye shule binafsi kwani wanaisaidia Serikali kielimu hivyo inatakiwa sekta binafsi hii isaidiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti kushuka. Naomba tuangalie suala hili maana watoto ni wengi madarasani wakati fedha zao haziongezeki, mishahara haiongezwi, hakuna mafunzo ya ziada ya mitaala na sera zinabadilishwa lakini walimu hawapati mafunzo juu ya mabadiliko hayo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kupata nafasi ya kuchangia hotuba iliyopo mezani. Kwanza namshukuru Mungu kwamba nina afya njema, kwa hiyo nitakuwa niko vizuri kuweza kuchangia yale ambayo naona ni muhimu kwa ajili ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuanza na suala la hifadhi ya jamii. Hifadhi ya jamii mifuko iliunganishwa ya LAPF, GEPF na PPF ikaunda PSSSF. Kwenye kitabu chao ukurasa wa 70 wanahitimisha kwa kusema hatua hii imewezesha kutatua kero za wastaafu ambazo zilidumu kwa muda mrefu lakini ukiangalia kwenye uhalisia ni kwamba wastaafu wengi wanahangaika sana kupata mafao yao. Nina ndugu zangu ambao mpaka leo hii wana mwaka mzima hawajapata mafao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Ukiachia hao wastaafu, kuna watoto ambao waliachwa na hao ambao walikuwa ni wafanyakazi na walijiunga katika mifuko hii. Nina watoto yatima ambao ninaishi nao kuanzia Januari mpaka sasa hivi ni mwezi Aprili hajalipiwa ada ya shule. Wakati nafuatilia nimekuta na akina mama wengi sana ambao wanalalamikia suala la watoto wao kutolipiwa ada na sasa watoto wako majumbani hawaendelei na shule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukiangalia wanavyohitimisha kwamba eti kero zimepungua, sijaona kwamba kero zimepungua kwa mifuko hii kuunganishwa labda Serikali ijipange upya kuhakikisha kwamba tatizo hili linapungua. Nafahamu kabisa hii Wizara ina wanawake wengi, Makatibu Wakuu watatu kama sio wawili ni wanawake, Mheshimiwa Waziri wa Nchi ni mwanamke, kwa kiasi nilichokutana na wale wanawake wanahangaika na watoto mitaani huko hawasomi kwa sababu waume zao wamefariki na mifuko hii tangu imeunganishwa watoto hao wanapata shida kulipiwa mafao yao ya elimu, kwa kweli naomba Serikali mkajipange vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najua kabisa Mheshimiwa Jenista unasikia na unafahamu jinsi gani akina mama wanateseka katika kuhangaika na hawa watoto. Nakupa mifano hiyo miwili kwamba nina watoto wa ndugu zangu tena kaka yangu ambaye ananiachia ziwa, mpaka sasa hivi tangu mwezi Januari hawajalipiwa ada. Nimejaribu kulipa na mimi napokea posho kama watu wengine nimeshindwa, ina maana hao ambao hawana hata ndugu wa kuwalipia hali yao ikoje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuhamia sehemu ya Mahakama. Napenda kusema kwamba Mahakama ni mahali ambapo tunatakiwa tupate haki na kama haki na kwa wakati. Ukiangalia jinsi kesi zinavyocheleweshwa Mahakamani imesababisha msongamano mkubwa sana wa mahabusu na ukienda magerezani unakuta hali ni mbaya sana ambayo imesababishwa na ucheleshwaji wa kesi ambazo zingeamuliwa kwa haraka ina maana mahabusu kule magerezani wangepungua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tunapanga bajeti ya kulisha watu magerezani ni kwa sababu tumeshindwa kuwa na kesi zinazoenda haraka ili kupunguza mahabusu, ukipunguza wafungwa maana yake umepunguza na bajeti ya Serikali. napenda kuwaambia Serikali kama tunataka kupunguza gharama za kuendesha baadhi ya mambo ni pamoja na kuhakikisha kwamba kesi zinaendeshwa haraka. Kwa kufanya hivyo, tunapunguza gharama za uendeshaji wa Serikali na pia tunaongeza pato kwa sababu kesi zikiisha haraka watu wanaenda kufanya kazi zao walizozizoea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ambacho nakishangaa sijajua kama msongamano ulioko magerezani na ile mito ndoo ambayo inawekwa kule zote hizo ni adhabu za huyo mtu ambaye amefungwa au ni nini? Haki za binadamu ziko wapi kumfanya mtu aishi na kinyesi? Kwa nini Serikali isitengeneze vyoo hata kama maeneo ya kulala ni finyu lakini vyoo vingetengenezwa kulikoni watu wanalala na vinyesi, haki ya binadamu inakuwa wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuzungumzia habari za UKIMWI. Tunafahamu kabisa UKIMWI ni janga la Taifa na Serikali inajitahidi kuhakikisha kwamba dawa za kufubaza ugonjwa wa UKIMWI zinapatikana lakini watu hawafi kwa sababu ya wadudu wale wa UKIMWI wananchi wengi wanakufa kwa sababu ya magonjwa nyemelezi magonjwa kama Kifua Kikuu, kuharisha na kadhalika ambayo tumekuwa tukisema humu ndani mara nyingi kwamba kama ARV ingekuwa na package ya Septrin, it means wananchi wenye magonjwa nyemelezi wangeweza kupata dawa hizo na wakapona. Kama tunawapa dawa za UKIMWI hatuwapi dawa za magonjwa nyemelezi wagonjwa wengi wanakufa kwa magonjwa nyemelezi na wala sio kwa ugonjwa wa UKIMWI wenyewe. Kwa hiyo, naiomba Serikali ifanye mkakati wa kuweka Septrin kwenye package ya ARV ili mtu anapopewa dawa za ARV apewe na zile za Septrin zitasaidia anapopata magonjwa nyemelezi anatumia zile dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ni tatizo la vituo vya kupimia UKIMWI.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mary Muro kuna taarifa.

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu kumpa taarifa Mheshimiwa anayechangia hivi sasa kwamba si kila mgonjwa anayepewa dawa za ARV anahitaji kupewa Septrin. Tunachotaka kushauri wagonjwa wote au watu wote wanaopata huduma ya ARV ni vizuri wanapojisikia tofauti waende kwenye vituo vyao kwa ajili ya kutibiwa, watapewa dawa zingine kwa sababu watakuwa wanapewa zile kule lakini sio lazima package ya ARV apewe na Septrin.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa hiyo. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mary Muro, unaipokea taarifa hiyo.

MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ningeomba wasubiri baadae watajibu, lingine ni kwamba vituo vilivyo vingi watu wanapewa sawa dawa za ARV lakini wanapokuwa na magonjwa ya nyemelezi hakuna Septrin. Sasa tunaweza tukawauwa hawa watu kwa kukosa Septrin na sio ARV. ARV zinapatikana na ugonjwa wa UKIMWI shida ni magonjwa nyemelezi na wala sio ugonjwa wa UKIMWI wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuongea vituo vya kupimia UKIMWI. Kuna vituo vichache vya kupimia UKIMWI halafu viko mbali kwa hiyo havifikiki. Nashauri Serikali ijitahidi kuongeza vituo vya kupimia UKIMWI. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna tatizo la viral load mashine, nashauri Serikali ijipange at least kila mkoa uwe na viral load mashine kwa sababu unakuta vipimo vile vinapelekwa mbali njiani vinakutana na shida kadha wa kadha tunaweza tusipate really matokeo kwa sababu ya ule ubebaji labda unatoka Njombe kwenda Mbeya au utoke sehemu moja na kupeleka sehemu nyingine ambayo ni mbali. Sehemu fulani Serikali imesema imejitahidi kununua dawa na kujenga vituo basi ijitahidi kuongeza na hizo viral load mashine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuongelea suala la kodi ya mapato. Ni kweli Watanzania wanaishi kwenye wakati mgumu sana kwa sababu ukienda ofisi za Kodi ya Mapato unaweza ukashinda siku nzima unahangaikia kitu kimoja. Haijulikani kama wafanyakazi ni wachache au ndiyo system ilivyo? I ile hali ambayo inaonekana katika Ofisi za Kodi ya Mapato inasababisha watu wengine kukata tama. Kama Serikali ina nia ya kukusanya mapato iongeze watendaji ili kurahisisha kazi. Ni mara nyingi sana mimi nimefika pale nimekuta watu wanagongana tu kwenye corridor, kila sehemu kumejaa. Sasa watu hawa wanatuletea pesa na wao wanaisaidia Serikali kukusanya mapato, kama watendaji ni wachache ina maana wanahangaika siku nzima na wanapoteza muda wa kufanya kazi zingine na Serikali inakosa mapato. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili ilishagonga Mheshimiwa, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kuongeza watendaji katika Sekta ya Afya, kwani Madaktari ni wachache, hivyo wanazidiwa na kazi, wanachoka na hivyo kufanya kazi chini ya kiwango.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Wizara hii kuhakikisha inatoa elimu juu ya afya za Watanzania badala ya kusubiri waugue ndipo wawaelimishe. Pia Wizara ya Afya itoe kinga nyingi ili kupunguza gharama za matibabu. Naishauri Serikali kutoa ufadhili kwenye magonjwa yasiyoambukiza, kwa mfano, kisukari kinawapata watu ambao uwezo wao wa kutafuta fedha za kujitibia hawana, hivyo, wazee hawa wanakufa kabla ya muda.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaendelea kuishauri serikali kuwa wagonjwa wa UKIMWI hawafi kwa kutotumia ARV bali wanakufa kwa magonjwa kama Kifua Kikuu, kuharisha na typhoid. Hivyo tunashauri kwenye ARV ziwepo ceptrine ili pale mgonjwa anapopata magonjwa nyemelezi waweze kupewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nyongeza ya Madaktari wa upasuaji katika Hospitali ya Tumbi kwani hospitali hii inapokea wagonjwa wa ajali za barabara ya Morogoro. Wawili waliopo hawatoshi, tuongezewe, kwani hospitali hii imepandishwa hadhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bima ya Afya imeonesha kasoro nyingi ikiwepo usumbufu wa kutopata huduma stahiki, mfano dawa mara nyingine uambiwe ukanunue au mara nyingine uambiwe ni kwa magonjwa baadhi tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba wahudumu wa afya msingi waajiriwe ili kusaidia huduma za vijijini. Wahudumu hawa walikuwa msaada sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, matibabu kwa wazee ni shida. Bima walizoahidiwa hawajapewa na waliopewa hawapati huduma hizo hospitalini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Spika, nipende kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Jangwani; nipende kujua nini sababu ya ujaaji wa maji, baada ya matengenezo ya mwendokasi ndiyo imekuwa mbaya kuliko. Swali; je, upembuzi yakinifu haukufanyika au ilikuwaje, kila ikinyesha mvua lazima watu washindwe kupita barabara hii? Leo hii tunavyoongea Jangwani hakupitiki; je, hivi kweli wananchi wanazunguka na kupoteza muda mwingi kutafuta jinsi ya kufika kazini kwao?

Mheshimiwa Spika, barabara na fidia kwa wananchi wa Kibaha wanaopisha upanuzi wa barabara TAMCO – Mapinga. Wananchi wanashindwa kujua hatma ya maisha yao kufuatia tathmini iliyofanywa na malipo kukwama, hivyo kusababisha wananchi kuwa na umaskini uliokithiri. Serikali irudi kwa wananchi iwaambie wamekwama wapi kulipa fidia iliyowaahidi miaka minne iliyopita.

Mheshimiwa Spika, magari ya mwendokasi; najua kuwa SUMATRA ambao wanatetea pia wasafiri ambao ni idara katika Wizara hii. Usafiri wa mwendokasi ni shida sana, magari ni machache sana na wasafiri ni wengi, hivyo kupelekea wasafiri kujazana sana mpaka kukosa hewa na kusababisha wengine ku-faint kwa kukosa hewa. Nini maana ya kugharamia mradi huu na kuondoa mabasi ya kawaida, wananchi hawaielewi nia ya Serikali kuondoa magari ya kawaida, Serikali imewapa mateso makubwa kwa kuleta mradi huu.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa majengo kwa ajili ya kuuza. Ujenzi unaojengwa na TBA usiangalie upana wa viwanja na ubora wa majengo wanayoyajenga ambayo inapelekea wananchi kushindwa kununua kutokana na udhaifu unaopelekea wanunuzi kuona nyumba hizi sio rafiki kwa maisha yao.

Mheshimiwa Spika, TEMESA; matengenezo yanayotokana na TEMESA ukipeleka gari kutengenezwa inatengenezwa kwa muda mrefu kuliko yanayotengenezwa kwa watu binafsi. Hata barabarani taa zote zinapoharibika urekebishaji ni shida.

Mheshimiwa Spika, bandari; nishauri Serikali kujifunza utoaji huduma wa Bandari za Durban, Beira na Mombasa, vinginevyo wateja watatukimbia iwapo urasimu wetu na tozo nyingi utaendelea katika Bandari ya Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, TTCL; tumeimba mara nyingi sana kuwa Serikali ilipe madeni inayodaiwa pia itoe uhuru wa uendeshaji ili ijiendeshe kibiashara, iwe na uwezo wa kukopa na kukopesha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali juu ya mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara ni ndogo jambo linalosababisha mazingira magumu ya utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuishauri Serikali juu ya Mradi wa Bagamoyo Special Economic Zone. Mradi huu umeingiza hasara kwa kutokutekelezwa mpaka sasa. Tukumbuke kuwa fidia kubwa imelipwa ikiwa ni fedha za walipa kodi na ni muda mrefu. Je, hiyo fedha ingeingizwa kwenye mradi mwingine, tungekuwa wapi sasa hivi? Fedha nyingi zimetumika kwenye kuhakikisha kuwa mradi huu unalitoa Taifa letu hapa lilipo kuelekea uchumi wa kati kwa kuifanya reli kupokea mzigo mkubwa toka bandarini kubeba na reli zetu kuelekea kwenye nchi nyingi zisizo na bandari.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Bagamoyo na Mkoa wa Pwani walitoa maeneo yao wakijua kuwa nao vipato vyao vitaongezeka kwa bandari hiyo kujengwa, kwani wangepata ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, tozo za TFDA zinatozwa kwa fedha za kigeni na kwa kila product inayotengenezwa nembo yake na kwa gharama kubwa. Hivyo, tunawavunja moyo wajasiriamali wadogo ambao ndio kwanza wanajikusanya kwa mitaji midogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni TRA. Naomba kuishauri Serikali kuacha kutoza kodi on capital basis kwani unamkadiriaje mteja anayeanzisha biashara wakati hajaanza biashara? Hii imefanya watu wengi kushindwa kuendeleza biashara zao, kwani mitaji yao inakuwa imemezwa kwenye kodi kabla ya biashara kuanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni ufungaji biashara. TRA badala ya kujadili na wafanyabiashara ndipo wafunge au wapewe muda wa kulipa kidogo kidogo wanafunga biashara. Hii ni kuipa hasara Serikali.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Bajeti ya Wizara; ninapenda kuishauri Serikali kuongeza bajeti ya Wizara hii kwani imeshindwa kufanya shughuli zake kwa ufanisi. Mfano, Mkoani Pwani, Wilaya ya Kibaha kuna Kambi ya Nyumbu na Msangani. Matatizo ya Msangani na Nyumbu ni tangu enzi za awamu ya kwanza za mwasisi wa Taifa hili, ndiyo barabara inayoelekea kwenye kambi hizo ilitengenezwa, ni mbovu na ni shida kiasi hata wanaofanya au watoa huduma katika majeshi hayo hupata shida kufika huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Jeshi la Nyumbu; enzi za Mwalimu, Nyumbu iliweza kutengeneza mpaka gari kwani Nyumbu ina mashine na mitambo ambayo iliwezesha kufanya kazi kwa ufanisi lakini leo hii Nyumbu tuliyoitarajia kuleta mapinduzi ya viwanda majeshini imepotea. Hali hii imesababisha wananchi na vijana waliokuwa wamepata vibarua kukosa ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la migogoro ya mipaka na raia; nitoe ushauri Serikalini kuhakikisha inafuatilia mipaka hiyo na maeneo yote ya Jeshi yapimwe na kupata haki za umiliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajira Jeshini ni tatizo, kuna vijana walioahidiwa kuajiriwa baada ya kujenga Mererani na pia wapo wa Operesheni Kikwete waliahidiwa kuajiriwa lakini mpaka sasa wapo mitaani na tunajua wanajua matumizi ya silaha, hivyo kuwaacha mtaani ni hatari. Operesheni Magufuli nao wapo mtaani, je, hii si hatari kubaki na vijana bila kupewa shughuli za kufanya?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Uvuvi; nishauri Serikali kuhakikisha kunakuwepo na meli za uvuvi kwa ajili ya kuvua katika vina virefu. Ilitokea wakati ambapo meli za kigeni zilivua samaki wakubwa katika kina kirefu na kupata samaki wengi na wakubwa. Hii inaonesha tulivyo na utajiri mkubwa katika bahari yetu inayotuzunguka.

Mheshimiwa Spika, nishauri Serikali kuongeza vifaa vya doria kwani maharamia baharini wako wengi hivyo kutushia uhai wa wavuvi katika bahari yetu.

Mheshimiwa Spika, Uhaba wa Viwanda vya Kuchakata Mazao ya Baharini. Ninaishauri Serikali kuhakikisha inawekeza katika viwanda vya kuchakata mazao ya baharini.

Mheshimiwa Spika, Mabwawa ya Kufugia Samaki. Wananchi wengi wanahitaji elimu ya ufugaji samaki katika mabwawa. Watu wengi wamehamasika sana juu ya ufugaji samaki lakini elimu hawana ya jinsi ya kutengeneza mabwawa na jinsi ya kuzalisha wa samaki.

Mheshimiwa Spika, Mifugo. Nipende kuishauri Serikali kuondoa uchapaji ng’ombe ambao unasababisha uharibifu wa ngozi, pia kupunguza thamani ya ngozi hizo na kukosa soko la kimataifa.

Mheshimiwa Spika, nishauri Serikali sehemu zilizo na mifugo kujengwa viwanda ili kuondoa adha hii ambayo inawapata wafugaji kupata masoko bora na rafiki. Usafirishaji kupeleka mbali imekuwa ni shida na ghali, hivyo kuwakatisha tamaa.

Mheshimiwa Spika, ninaishauri Serikali kuhakikisha inasimamia thamani ya nyama inayoliwa; mabucha mengi yanatoa huduma ya nyama isiyo salama kuanzia uchunaji hadi ukataji buchani.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri Serikali kutoa elimu kwa vyombo vya habari na meseji kwenye simu kwa kuwa wananchi wengi wana simu ilikuwaelimisha faida za kupanda miti kwa matumizi ya kuni na mkaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vitalu vile ambavyo vingi vilikuwa kwenye halmashauri zetu vinakufa kwa kukosa fedha za kuviendesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri Serikali kutafuta njia mbadala wa mkaa kwani ukataji wa miti hautasimama mpaka njia mbadala; mfano gesi kuwa bei ya chini ndipo tutaweza kuokoa misitu yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kushauri Serikali kuboresha barabara zinazoingia hifadhini kuliko ilivyo sasa, barabara ni mbovu inatia aibu watalii wanapokuja kutembelea mbuga zetu mfano njia inayoingia mbugani.

Mheshimiwa Naibu Spika, hotel zetu nyingi zilizoko kwenye mbuga zetu haziko katika hali nzuri pia huduma zake si nzuri, Serikali ifuatilie.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri Serikali kufuatilia au kuhakikisha inapunguza utitiri wa tozo uliopo tangu mtalii anapoingia nchini na kuelekea kwenye mbuga zetu ili kuwezesha watalii wetu kuvutiwa kuja nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri vyuo vyetu vya utalii vipitiwe, vingi havina sifa hivyo kutoa wahudumu ambao hawakidhi vigezo vya kimataifa, wengi hawawezi hata kuwasiliana kwa kushindwa lugha ya kiingereza hivyo kushindwa kuhudumia kulingana na mahitaji ya wageni.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Spika, nipende kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nishauri Serikali kushughulikia miradi ambayo ikitekelezwa inachangia pato kubwa kwa Taifa na kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja.

Mheshimiwa Spika, napenda kuishauri Serikali kujizatiti kwenye Mchuchuma na Liganga mahali ambapo tungekuza uchumi wa nchi wa urahisi kuliko miradi ambayo yenyewe inakuwa mlaji na si mtoa faida ya haraka na haitengenezi ajira kwa wananchi wengi kwa wakati mmoja.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Ludewa, mahali ambapo kuna Liganga na Mchuchuma wamechoka kusikia maelezo hayo hayo huku uwekezaji ukiwa sifuri. Waziri anapokuja kuhitimisha aje atueleze Serikali imekwama wapi kwenye Mradi wa Liganga na Mchuchuma.

Mheshimiwa Spika, ningependa kuishauri Serikali kufuatilia migodi inayofungwa na kuacha mashimo makubwa yakiwa wazi na yamekuwa hatari kwa jamii yanapojaa maji. Nishauri Serikali kuhakikisha kuwa kabla migodi haijafungwa wanatakiwa kuhakikisha Mikataba yao inasomeka kutokufunga mpaka mashimo yote yamefunikwa.

Mheshimiwa Spika, ningependa kushauri Serikali kuhakikisha inapiga marufuku Wawekezaji wakubwa kuwakandamiza wachimbaji wadogo pale wanapogundua mahali kuna madini.

Mheshimiwa Spika, niishauri Serikali kuhakikisha wachimbaji wanakuwa na bima za maisha kwani wengi wamekuwa wakipata madhila kwa wachimbaji ambapo huishia kufa na kuacha familia ikiwa haina walezi.

Mheshimiwa Spika, nishauri Wizara kuangalia jinsi uchimbaji wa mchanga pia unaacha mashimo makubwa na kuharibu mazingira.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Spika, ninapenda kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nipende kupongeza juhudi kubwa za Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri na ari mliyonayo katika kuhakikisha nchi yetu inaondokana na giza.

Mheshimiwa Spika, nishauri Serikali ilipe fidia kwa wananchi ambao wanapitiwa na miradi ya umeme ili wawe marafiki wa miradi hiyo na waweze kuilinda.

Mheshimiwa Spika, niongelee suala la fidia kwa wanachi wa Mkoa wa Pwani, Kibaha eneo la Kiluvya, Mpiji, Mikongeni na Chalinze. Niombe Serikali ikutane na wanachi hawa kuwapa moyo na kuwaeleza kinachoendelea. Tathmini imefanyika miaka mingi ikifuatiwa na katazo la kutoendelea na shughuli yoyote katika eneo hilo. Hii imewapa umaskini wananchi hao kwani nyumba zao zimechakaa na kuanguka lakini hawana uwezo wa kujenga kwa hili katazo.

Mheshimiwa Spika, ninajua mpango wa usambazaji na uuzaji wa umeme ni wa TANESCO, naona si vyema kulitwisha hili shirika shughuli zote.

Mheshimiwa Spika, nishauri kupunguza urasimu wa kulipa waathirika wa hitilafu za umeme. Kumekuwa na shida pale iwapo hitilafu inatokea, ulipaji wake umekuwa wa shida.

Mheshimiwa Spika, nishauri Serikali juu ya utaratibu wa kuunga umeme kutoka kwenye nguzo ambayo mtu amenunua bila yule anayeungiwa kurudisha angalau nusu hasara kwa aliyeweka nguzo. Mfano mtu amelipia nguzo tano na kuungiwa umeme, kazi ambayo ingefanywa na TANESCO au mteja huyo ambaye wanaenda kumuungia wanaenda kuchukua kwenye nguzo za mteja ambaye alinunua bila hata ridhaa yake, hii siyo nzuri sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kupongeza bajeti hii kutokana na kuangalia angalau baadhi ya mambo ambayo yamekuwa kero kwa wananchi walio wengi wajasiriamali. Wajasirimali wengi walikata tamaa uanzishaji wa biashara ulioendana na kodi kabla ya biashara kuanza. Wajasiriamali wengi walimalizia mitaji yao kwenye kodi hivyo kuja na punguzo la kodi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kupongeza kauli ya Serikali ya kutowafungia wafanyabiashara kwani imekuwa Serikali ikipata hasara kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kuchangia juu ya hali mbaya ya halmashauri zetu hivyo zimeshindwa kutekeleza utoaji wa asilimia nne za wanawake na mbili za mikopo kwa walemavu pia nne za vijana kutokana na vyanzo vyote vikuu vya halmashauri kuchukuliwa na Serikali Kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, urejeshaji wa fedha kutoka Serikali Kuu ni mdogo hivyo kusababisha halmashauri nyingi kushindwa kujiendesha. Naishauri Wizara ya Fedha kupunguza gharama za uhamasishaji wa uhakiki wa ardhi ambao sasa hivi ni asilimia kumi imekuwa mzigo sana kwa wale ambao wananunua ardhi kutoka kwa mmiliki mmoja kwenda kwa mwingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri TRA kukaa na wadau au wafanyabisahara kujua shida zao badala ya kuonekana kwa walipakodi wakati wa kufuatilia kodi tu.
Muswada wa Sheria ya Wakala wa Meli Tanzania wa Mwaka 2017
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Spika, ahsante nami napenda kuchangia mchango kidogo. Kwanza na- declare interest kwamba mimi ni Mwanakamati, kwa hiyo mchango wangu ni mdogo sana.

Mheshimiwa Spika, kwanza nipende kupongeza Kamati ya Miundombinu kwa kazi kubwa ambayo wameifanya na kwa muda mrefu. Napongeza Serikali pamoja na kwamba imechelewa sana kuleta Muswada huu pengine tungekuwa tumeokoa hela nyingi za Taifa hili lakini pia nimpongeze AG kwa ushirikiano wake pamoja na Kamati kwa sababu yeye nafikiri ndiyo amesababisha leo tumeingia humu kwa sababu baada ya kushindikana ilibidi kukaa naye kwa muda mrefu na kuweza kupata maamuzi ya kuingia nao Muswada ndani humu.

Mheshimiwa Spika, jambo moja tu ambalo ningependa Serikali itambue ni kwamba, Wabunge kazi yao siyo kupitisha Sheria, Bunge kazi yake ni kutunga Sheria, kwa hiyo, serikali inapoleta Miswada isiwe na mategemeo kwamba lazima ipite, ni mpaka pale Kamati zinapojiridhisha kwamba ni hakika Taifa linakwenda kusonga mbele ndipo Miswada hii itapita.

Mheshimiwa Spika, hii imetokana nasema hivi kwasababu gani, tulipata kigugumizi au Serikali ilipata kigugumizi pale ambapo sisi tulisema kwamba tunahitaji jina la NASACO libadilike na Serikali imeendelea kushikilia kwamba ibaki kama NASAC na sio maritime. Tulisema hivyo kwa sababu tulitaka jina libadilike ili libebe maudhuhi ya kibiashara ili kuweka room pana kwa ajili ya agency wengine, tunafahamu kabisa kuna mabadiliko ambayo Serikali imefanya kulingana na ushauri tulioutoa ikiwa ni pamoja na yale ya shirika lenyewe kutokufanya biashara in such lakini kufanya kwa yale mambo ambayo ni ya Kiserikali.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano nyara za Serikali, kushughulikia nyara za Serikali, makilikia na vinginevyo. Lakini mpaka sasa kamati aijaweza kuelewa kwanini Serikali imeng’ang’ania jina na sisi tulikuwa na sababu kubwa ya kusema kwamba jina libadilike lisiitwe NASACO ili tusirudi nyuma kwenye NASACO kwa sababu watu wengi watafikiri kwamba ni NASACO na pia kuwapa assurance agency ambao watafanya biashara wanaofanya biashara ili waweze kushiriki wakiwa huru wakijua kabisa ni shirika jipya na mambo ni mapya na wakijua kwamba sheria zie ambazo zinaenda kuingongoza shirika hili zitawa-favour.

Mheshimiwa Spika, sasa cha kushangaza ni kwamba Serikali imekaa na msimamo uleule wa kwamba lazima iitwe NASAC. Sisi kama wanakamati tunaendelea kusema kwamba tunaiomba Seriakali ikafikiri kwa upya juu ya kubadilisha jina hili liwe maritime kama nchi nyingine zinavyofanya. Jambo lingine ningependa kuchangia kwamba tukiangalia shirika la NASACO lilianza 1973, na leo hii ni 2017 ndio tunaenda kubadilisha sheria ndio tunaangaika na miswada lakini tufikiri kwamba Serikali ilikuwepo na iliona NASACO inakufa na iliona wezi wakiwa wanaendelea kuiba hebu niishauri Serikali kwamba ni kipindi kirefu sana ambacho tumibiwa waatanzania.

Mheshimiwa Spika, nafahamu kabisa wananchi waliko uko nje wanateseka kwa sababu Bandari ya Dar es Salaam imefanya chini ya kiwango, na imefanya chini ya kiwango kwasababu bandari ya Da es Salaam iligeuka shamba la bibi kwa sababu ya sheria ambazo zilikuwa zinawa-favour wezi kuiba. Hatuwezi kuwalaumu wezi kwasababu sheria zilikuwa zinawaruhusu kufanya hivyo. Kwa hiyo ningependa kushauri Serikali isiwe inachelewesha miswada kuileta na pale kamati tunaposhauri kwamba tuleteeni muswada ifanye hivyo kwa sababu sisi tumetumwa na wananchi na tunafanya kazi ya wananchi ili kuwafanya wananchi waweze kupata zile haki zao za msingi.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano pesa nyingi ambayo imepotea bandarini pale au kushuka kwa mizigo, uingizwaji wa mizigo bandarini kule ambako umesababishwa na ma- agency ambao sio waaminifu umesababisha bandari ile kukosa mizigo au kutokupata mizigo iliyotarajiwa na kupunguza mapato ya Serikali na inavyopunguza mapato ya Serikali wanaoumia ni wananchi wetu ndio maana wakati naanza kuchangia nimesema hivi Wabunge kazi yao sio kupitisha sheria ni kutunga sheria inamaana kwamba kazi yao wanafuatilia mpaka wafike kutunga sheria wameshaona kiini na kuona kwamba sasa tumefikia muafaka na Serikali sasa sheria inaweza kuingia Bungeni.

Mheshimiwa Spika, tumeweza kupata majina tofauti wakati tuko kwenye muswada lakini tulivumilia tukasema tutashikilia palepale kwamba sisi hatuko tayari kupitisha muswada, tuko tayari kutunga sheria hatuwezi kupitisha sheria tunatunga sheria Serikali mtungojee tujiridhizishe tukashauri tunaomba hata Bunge muwape semina yakutosha juu ya muswada huu ili tuwe na uelewa wa pamoja, pamoja kwamba na hilo halikufanyika lakini tunahitaji wakati mwingine inapofikia mahali kama hapa Bunge lipate uelewa wa pamoja ili tunapoingia hapa Bungeni tunakuwa na sauti moja ya wananchi ya kuwatetea wananchi.

Mheshimiwa Spika, ningependa kusema kwamba shida ile ambayo tumeipata sisi yakubadilisha majina ni kwa sababu tu tumetaka tunafahamu kabisa kwamba Nasako ilikuwa na matatizo yake na matatizo haya tusingependa yarudi tena kwenye shirika jipya ambalo tunataka lituondoe hapa tulipo. Kwahiyo Serikali tunaomba mtambue kabisa kwamba nia na dhamira ya kamati aua ya Wabunge kusema kwamba irudi isiwe NASACO ni kuhakikisha kwamba haturudi tena kule tulikotoka na zile sifa mbaya ambazo tulizokuwa nazo kule NASACO.

Mheshimiwa Spika, tunaanza upya mambo mapya ili tuweze kwenda na mwendo ambao mwendo kasi ambao Serikali ya awamu ya tano inapenda. Kwa kusema hayo ningependa kwamba sisi kama kamati tunaendelea kudai
ile separation ya regulator na operator na pia tunaendelea kudai jina la NASAC kubadilishwa tunaiomba Serikali ilichukulie hilo kwamba ndio msimamo wa Kamati, ahsante sana.