Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Lathifah Hassan Chande (12 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa maendeleo uweke kipaumbele suala la maji na miundombinu katika Mkoa wa Lindi. Mkoa wa Lindi unakabiliwa na tatizo kubwa la uhaba wa maji safi, takribani asilimia 85 ya wananchi wa Mkoa wa Lindi hawapati maji safi kupelekea kunywa na kutumia maji ya mito na mabwawa pamoja na wanyama. Kitu cha kusikitisha zaidi hospitali ya Mkoa wa Lindi nayo ina tatizo la uhaba wa maji safi kupelekea wagonjwa kuletewa maji ya vidumu kutoka majumbani.
Hii ni hali mbaya inayopelekea wagonjwa kuwa hatarini kupata magonjwa ya mlipuko, nilitegemea mpango wa maendeleo ungekuwa na mipango ya miradi mbalimbali ya maji katika Mkoa wa Lindi na maeneo yote nchini ambako kunakabiliwa na tatizo la maji.
Miundombinu ilipaswa ionekane kwa mapana katika mpango wa maendeleo kati ya mwaka 2012 - 2015 shilingi bilioni 6.4 zilitengwa kwa ajili ya ukarabati wa barabara yenye urefu wa kilomita 230 inayotoka Nangurukuru kuelekea Liwale. Hali ni hiyo hiyo katika barabara ya Nachingwea – Liwale. Serikali iweke mpango wa kuzijenga hizi barabara katika kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu elimu; Serikali haijaainisha ina mpango gani juu ya wanafunzi waliofaulu kwenda Vyuo Vikuu, mpaka dakika hii hakuna kinachoeleweka juu ya wengi na hawa wanafunzi waliofaulu vizuri na kukosa mikopo. Serikali itambue kwamba elimu inaelekea kuanguka kama haitoandaa mpango wa kueleweka juu ya mikopo ya elimu ya juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu afya; nchi nzima inakabiliwa na tatizo kubwa la uhaba wa dawa katika hospitali, vifaa tiba na chanjo. Hii imejikita katika Wilaya zote za Mkoa wa Lindi na maeneo mbalimbali nchini. Huu mpango ulipaswa uoneshe maboresho katika sekta ya afya, akinamama na watoto wanaendelea kupoteza maisha yao wakati wa kujifungua kwa kukosa vifaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kilimo; mpango wa maendeleo umekosa shirikisho la soko la mazao kwa wakulima wa mazao mbalimbali kama ufuta, mbaazi na kadhalika. Ni vema Serikali ingepanua wigo kwa wakulima kwa kuwatafutia masoko.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mawasiliano; mpango wa maendeleo uzingatie suala la kuhakikisha hata maeneo yote nchini yanapata mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la uchumi; uchumi unaendelea kuanguka na matumizi kuongezeka hata baada ya wafanyakazi hewa kutambulika. Watumishi wengi wamesimamishwa kupeleka kila mwezi wanaendelea kupokea mishahara. Halmashauri zifikishiwe pesa kwa wakati kwa kutekeleza maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iliahidi elimu bure kwa wanafunzi, lakini hii haijaainishwa katika mpango wa maendeleo, kwani elimu bure haina maana yoyote kama wazazi bado wanaendelea kutoa michango. Pia kumekuwa na ucheleweshaji wa pembejeo, mpango huu ungeainisha ni kwa kiwango gani Serikali itahakikisha wakulima wanafikishiwa pembejeo kwa wakati.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabla ya yote napenda kutoa pole zangu kwa familia zote zilizokumbwa na msiba huu mkubwa, kwa kweli ni janga kubwa katika Taifa letu. Vilevile ningependa kutoa pole kwa Mbunge wa Mkoa wa Arusha Mheshimmwa Godbless Lema. Mungu azilaze roho za marehemu mahala pema peponi, Amina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuchangia katika Wizara hii hususan juu ya Sera ya Serikali ya 2002 iliyoelekeza kwamba wananchi waweze kupata huduma ya maji ndani ya umbali usiozidi mita 400, lakini ni dhahiri kwamba imeonesha hadi sasa hii sera imeshindikana kutekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunafahamu kwamba maji ni uhai. Mwanadamu akose kila kitu lakini si kukosa maji. Sasa pale ambapo Serikali inaweka mipango ya maendeleo, hata kama ikaweza kufanyia kazi mipango yote isipokuwa hili suala la maji basi nisawa sawa na bure. Kwa sababu mwananchi analazimia kutumia muda mwingi katika kutafuta maji kuliko katika kufanya shughuli za uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inavyosema kwamba uchumi unakua kwa asilimia saba ni bure kama mwananchi analazimika kutembea umbali wa hadi kilometa tano hata kumi kwa ajili ya kutafuta maji. Hii sera imeshindikana si kwa vijijini tu, mfano mkubwa ni mkoa wetu wa Lindi ambako maji ni janga kubwa mno kiasi cha kusababisha maji kuwa yenye thamani kama dhahabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi, Hospitali ya Sokoine hakuna maji, kweli hospitali inakosa maji au kwa kuwa Mawaziri mnapata maji hadi majumbani mwenu? Akina mama wanaenda kujifungua hospitali huku hakuna huduma ya maji wagonjwa wanaenda hospitali wanaolazwa pale wanakosa huduma ya maji, jambo ambalo linasababisha kuwa prone katika kupata magonjwa ya mlipuko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wauguzi wanakosa huduma ya maji, madaktari wanakosa huduma ya maji kweli Serikali inaliona hili tatizo na kukaa kimya bila kukuchua hatua yoyote? Kusema ukweli hili ni suala la kusikitisha mno kwa sababu hadi vyoo navyo vinakosa maji pale hospitalini, naomba mliangalie hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, si hapo tu unapoingia vijijini vile vile hali ni mbaya zaidi katika mkoa wetu wa Lindi. Hatuna maji katika Wilaya za Liwale, Nachingwea, Ruangwa, Mchinga, Mtama pamoja na Kilwa. Ni sawa sawa na kwamba sisi hatustahili kuwa na haya maji, kitu ambacho ni muhimu kuliko vitu vyote ambavyo binadamu anahitaji. Ukienda Liwale si vijijini tu, ukienda Ruangwa siyo vijijini tu bali hata mjini tunakosa maji, naomba mliangalie hili. Wananchi wanalazimika kutembea umbali wa kilometa tatu hadi kilometa kumi kwa ajili tu ya kutafuta maji, na mwisho wa siku hawapati maji safi na salama kwa sababu wanaishia kufuata na kutumia maji ya madimbwi na maji ya mabwawa ambayo pia wanyama wanatumia maji hayo hayo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
HE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote napenda kwanza kuanza kwa kuchangia sekta ya ujenzi hususan barabara. Katika Mkoa wetu wa Lindi tunashukuru barabara imejengwa ambayo tunaunganishwa kutoka Mkoa wa Lindi hadi Mkoa wa Mtwara na kuelekea Ruvuma. Sasa utata unakuwepo katika barabara za kuelekea kwenye Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni suala la kusikitisha sana kwa sababu inafika wakati unaenda kwenye Wilaya ya Liwale na Nachingwea lakini inakuwa kama ile ni barabara ya kuelekea kijijini. Naiomba Serikali iangalie katika kujenga barabara zinazoelekea katika hizo Wilaya ili nazo ziweze kuwa katika kiwango cha lami kuliko kila siku kuendelea kuiboresha katika kiwango cha vumbi. (Makofi)
Mhshimiwa Naibu Spika, hii pia inaleta adha kubwa kwa watumiaji wa hizi barabara hususan Wana-Lindi pale wanapohitaji kutoka Wilaya moja kwenda Wilaya nyingine. Imepelekea hadi akina mama wanapoteza maisha yao pale ambapo wanahitaji kuhamishwa kutoka Hospitali ya Wilaya na kupelekwa kwenye Hospitali Mkoa ya Lindi, kutokana adha hii ya barabara kuwa mbovu.
Mheshimiwa Naibu Spika, upembuzi yakinifu umefanyika kutoka barabara ya Nanganga kuelekea Ruangwa. Sasa sijui ni kwa kuwa kuna Waziri Mkuu ambaye ana interest pale, kwa sababu inawezekanaje kuwe na mpango wa kujenga barabara ya kutoka Nanganga kwenda Ruangwa na iachwe hii inayoelekea Nachingwea na Liwale?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Serikali iweze kuliangalia hilo ili kuwatoa wananchi wa eneo hilo kwenye adha ya tatizo la usafiri, especially kipindi hiki cha masikika, usafiri inakuwa ni shida. Kwa gari dogo unatumia siku mbili kutoka Nangurukuru hadi kufika Liwale kwa kupitia barabara ya Njinjo ambayo ina urefu wa kilometa 230. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile hata wafanyabiashara wanaishia kuharibikiwa na magari njiani na kutoweza kuendelea kutokana na ubovu huu wa barabara na kupelekea hadi kufika siku saba, ambayo ni wiki nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuishauri Serikali iweze kuangalia hili na pia ikiwezekana Waziri husika aweze kutupa jibu; lini atahakikisha kwamba barabara hizi za kutoka Nanganga - Nachingwea hadi Liwale na kutoka Nangurukuru hadi kufika Liwale zitajengwa katika kiwango cha lami? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuchangia katika sekta ya uchukuzi juu ya matumizi ya bandari yetu katika kukuza mapato ya Taifa letu. Hadi sasa hivi shehena zinazopita katika bandari zetu zinaendelea kushuka na zimeshuka kutoka asilimia 5.2 mwaka 2014/2015 hadi kufika asilimia 0.1. Hii ni ishara mbaya sana kwa mapato ya nchi yetu. Maana yake ni kwamba mapato ya bandari yanaendelea kushuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia Machi, 2017 takwimu za TRA zinaonyesha kwamba mapato yaliyotokana na forodha, ikiwemo bandari ni shilingi trilioni 4.3. Sasa kama kusingekuwa na upungufu wa shehena katika Bandari, maana yake haya mapato yangeongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukiangalia bajeti nzima ya mwaka 2016/2017 ni shilingi trilioni 29.54, lakini tumeendelea kushuhudia mapato ya bandari yanavyozidi kushuka kwa kasi. Sasa je, tutaweza vipi kuboresha vyanzo vyetu vya mapato kwa usimamizi mbovu kama huu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania tumebarikiwa kijiografia kuwepo katika Ukanda wa Maziwa Makuu, lakini hii lawama Serikali haiwezi kuikwepa kutokana na kuwa na sera mbovu juu ya uratibu wa shughuli za bandari. Hili ni janga kwa Taifa letu.
Napenda kuishauri Serikali iweze kuboresha sera zake juu ya uratibu wa bandari ili tuweze kutumia vizuri baraka hizi tulizopewa na Mwenyezi Mungu ya kuwa strategically positioned na hatimaye kuweza kuongeza mapato yatokanayo na bandari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuchangia juu ya hii sekta ya uchukuzi kuhusiana na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL). Naungana mkono na juhudi zilizotumika katika kufufua Shirika hili la Ndege la ATCL, lakini siungi mkono njia zinazotumiwa na Serikali katika kusimamia Shirika hili la Ndege. Kwa nini nasema hivyo? Nasema hivyo kwa sababu kitendo cha Serikali kununua ndege kwa gharama ya shilingi bilioni 500 na kuzikodisha hizi ndege kwa Shirika la ATCL naona ni kitu ambacho ni kibaya kwetu sisi kama Taifa ambalo kwa sasa hivi uchumi wetu upo dhaifu na bajeti ikiwa ime-under perform. Kwa nini tumeshindwa kuendelea na mfumo wa Public Private Partnership (PPP) ambapo wenzetu wa Kenya tukiangalia Kenya Airways asilimia 29.7 shares zinamilikiwa na Serikali ya Kenya huku asilimia 26.8 zinamilikiwa na Shirika la Ndege la KLM.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile wamejiingiza katika soko mitaji, soko la hisa Dar es Salaam, Uganda na Nairobi ambapo umma nao umeweza kumiliki hizo shares nyingine zilizobaki. Kwa nini ishindikane kwetu sisi? Tuna mambo mengi ambayo tunahitaji ku-prioritize na siyo kununua ndege. Kwa sababu tungeweza kuendelea huu mfumo wa PPP, japo tulifanya vibaya, hii siyo kwamba tuachane kabisa na huu mfumo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili suala la Serikali kununua ndege kwa gharama hizo za shilingi bilioni 500 kwangu mimi naona siyo sahihi kwa sababu tuna mambo mengi. Vijijini maji hamna, dawa hamna katika sekta ya afya, elimu pia haijaboreshwa kwa kiwango kile inavyotakiwa, lakini tunahangaika kununua hizi ndege. Napenda kupata majibu juu ya kwa nini Serikali imeshindwa kuendelea na huu mfumo wa PPP? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda kuishauri Serikali iweze kusisitiza ATCL iweze kukabidhi mahesabu yake kwa sababu hadi Februari Waziri Mkuu aliagiza CAG iweze kupatiwa mahesabu ya madeni na mali juu ya management nzima ya ATCL tangu waweze kupatiwa hizi ndege mwaka 2016. Nashauri kwamba wakabidhi mahesabu haya ya tangu 2009 ambayo tangu mwaka 2009 walishindwa kuyakabidhi kwa CAG. Kwa sababu kuna poor management ya ATCL inayopelekea kuongezeka kwa madeni na kutokuweza kujua exactly mali zetu za ATCL ziko kiasi gani mpaka dakika hii. Kwa hiyo, kikubwa napenda pia kushauri Serikali iweze kufanya hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, yangu ni hayo. Ahsante, nashukuru.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongelea juu ya sera ya Serikali ya kuhakikisha kila kata nchini inapata kituo cha afya. Mpaka sasa hivi imeonesha hii sera imeshindikana na kupelekea katika kata za nchi nzima 3,959, kata 448 tu ndiyo zimepata vituo vya afya. Sasa tukienda kwenye Mkoa wa Lindi, tuna kata 138 lakini cha kusikitisha sana ni kata 19 tu ambazo zina vituo vya afya. Kibaya zaidi ni kata moja tu yenye kituo cha afya ambacho kinatoa huduma ya dharura ya upasuaji ya mama mjamzito, hii kata iko Kilimalondo - Nachingwea. Hii imepelekea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi kuwa tegemezi kubwa kwa ajili ya kutoa huduma ya afya especially kwa akina mama wajawazito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kibaya zaidi na kutegemewa kote kwa hii hospitali ukiangalia majengo yake tangu mwaka 1954 hayajawahi kufanyiwa ukarabati wowote. Vilevile hakuna nafasi ya kutosha, hata tukisema pawe expanded palepale kibaya zaidi labour ward ina uwezo wa kuhudumia akina mama wajawazito 30 tu kwa wakati mmoja wakati wa kujifungua, hii ni hali mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile vifaa muhimu kama x-ray hakuna, sasa hivi ni miezi mitatu ilikuwepo x-ray moja tu ambayo mpaka sasa hivi haifanyi kazi, kwa hiyo hilo pia liangaliwe. Pia watumishi hawatoshelezi mahitaji ya hospitali ile ya Mkoa. Wauguzi wengi wamestaafu, hakuna specialists wa kutosha na hii tumbua tumbua yenu hii kwa maana hiyo hata hao wachache waliopo tumbua tumbua kwa sababu ya kutuaminisha kwa ajili ya kuwa na vyeti fake, matokeo yake hawa wachache pia wataendelea kupungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa Serikali ihakikishe inatekeleza sera yake ya kuhakikisha kila kata inafikiwa na kupatikana vituo vya afya katika hizo kata, pia kutokana na kwamba tayari kuna eneo limetengwa kwa ajili ya kujenga Hospitali ya Mkoa wa Lindi, basi kwa nini Serikali
isifikirie angalau unit ya labour iweze kuwepo pale, ambayo itakuwa na facilities zote zinazohitajika kwa ajili ya mama anapokuwa anajifungua, hii itasaidia kupunguza hata maternal mortality rate. Pia kuweza kuajiri watumishi zaidi watakaoweza kukidhi mahitaji yaliyopo pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bima ya afya, takwimu zinaonesha kwamba ni asilimia nane tu ya Watanzania ambao wako kwenye mfumo wa bima ya afya, ni dhahiri mnafahamu ni mzigo kiasi gani wa gharama uliyopo kwa wananchi juu ya huduma hii ya afya. Napenda kuishauri Serikali iweze kupunguza tozo zisizokuwa za msingi ili hata private sectors waweze kutoa huduma hii ya afya kwa gharama zilizo nafuu ili wananchi waweze kufikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vifaa tiba na dawa; Serikali imekuja na mfumo ambao uko centralized, ambapo dawa zote zinasambazwa na Medical Stores Departments, ni dhahiri kwamba usambazwaji wa dawa kikamilifu umeshindikana, maeneo yote yanashindikana kufikiwa…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ni mwaka wa pili sasa tangu Serikali ya Awamu ya Tano ijinasibu kuwa hii ni Tanzania ya viwanda. Kwanza kabisa, napenda kuzungumzia juu ya rasilimali tulizonazo. Gesi asilia iligundulika kwa mara ya kwanza katika visiwa vya Songo Songo, Mkoani Lindi mwaka 1974. Ikagunduliwa Mtwara Vijijini (Mnazi Bay mwaka 1982 na Ntorya mwaka 2012), Mkuranga Mkoa wa Pwani mwaka 2007 na Lindi, Kiliwani mwaka 2008.

Mheshimiwa Naibu Spika, kiasi cha gesi asili iliyogunduliwa katika maeneo haya inakadiriwa kuwa futi za ujazo trilioni nane. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kumekuwa na kasi kubwa ya utafutaji mafuta na gesi asilia uliojikita zaidi kwenye maji ya kina kirefu cha bahari na kiasi cha gesi asilia iliyogunduliwa katika kina kirefu cha maji ni takribani futi za ujazo trilioni 33.7. Jumla ya gesi asili iliyogunduliwa nchi kavu na baharini inafika takribani futi za ujazo trilioni 41.7. Rasilimali hii ya gesi asilia inaweza kutumika katika maeneo mbalimbali yakiwemo kuzalisha umeme, malighafi ya kuzalisha mbolea na kemikali, nishati viwandani, majumbani na kwenye taasisi mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa Mkoa wa Lindi hauna hata kiwanda kimoja cha kuzalisha mbolea za viwandani licha ya gesi kuwepo mkoani hapo. Ni wakati sasa wa Serikali kutafuta na kuelekeza wawekezaji wa kuzalisha mbolea katika Mkoa wa Lindi ukizingatia ukamilikaji wa barabara ya Masasi-Ruvuma kupitia Tunduru utafanya usafirishaji uwe rahisi wa mbolea hiyo hasa ukizingatia Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ndiyo watumiaji wakubwa wa mbolea hiyo ya viwandani. Ujenzi huu wa viwanda utasaidia vijana wa Lindi ambao zaidi ya asilimia arobaini (40%) hawana ajira, jambo ambalo litapunguza kama si kuondoa kabisa tatizo la ajira kwa vijana Mkoani Lindi na Kanda ya Kusini kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuzungumzia juu ya usindikaji na kuongeza thamani mazao. Mkoa wa Lindi unazalisha kwa wingi mazao kama korosho, ufuta, muhogo, mbaazi na mengine mengi. Kwa sasa duniani kote faida ya kilimo chochote kiko kwenye usindikaji na uongezaji thamani ya zao husika. Mkulima wa Lindi na Mtwara bado hajanufaika na anachokizalisha kwa kuwa mteja wake mkuu ni mlanguzi ambaye ananunua kwa mkulima na kuuza kwenye masoko na makampuni makubwa kwa bei itakayompa faida.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoani Lindi kulikuwa na viwanda vya korosho ambavyo vilikuwa na mashine za kubangua korosho lakini sasa viwanda hivi havifanyi kazi.

Matokeo yake korosho zinauzwa bila kuongezwa thamani na kupelekea kupunguza kipato. Naiomba Serikali ijikite katika kufufua viwanda hivi Mkoani Lindi na pia katika kujenga viwanda vingine hata kwa kushirikisha private sectors ili kuweza kumnufaisha mkulima, kutoa ajira kwa vijana, kudhibiti walanguzi na hatimaye kuongeza pato la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na viwanda vya nguo hapa nchini, vipo wapi sasa? Mitumba leo inapigwa marufuku huku Serikali haijaleta njia mbadala wa kuleta nguo za bei nafuu kuweza kukidhi mahitaji ya majority. Makubaliano ya East African Common Market ni kwamba mitumba marufuku ikifika 2019. Wenzetu Rwanda wameanza kuwapa mafunzo akinamama kutengeneza nguo za gharama nafuu kwa kutumia materials zinazopatikana kwa wingi. Imebaki miaka miwili tu tutapiga marufuku mitumba ya Ulaya badala yake tutanunua za bei rahisi kutoka Rwanda na China. Sisi tutanufaika na nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kiwanda Morogoro kinaitwa Mazava ambacho kinazalisha sport wear lakini bidhaa zote zinapelekwa Ulaya na Marekani wakati Tanzania hakuna product yoyote sokoni. Tunahitaji kuwa na viwanda vya nguo vitakavyoweza kuzalisha, kujiendesha pia wakati huo huo nguo ziweze kuuzwa kwa bei nafuu. Tukiwa na viwanda vyetu vitakavyozalisha kwa wingi itasaidia kushusha gharama za uzalishaji na bei ya kuuza itakuwa rahisi na mwananchi wa kawaida ataweza kumudu.

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu Kenya wana kitu kinaitwa Vision 2030. Kwenye manufacturing wana-target kutoka kwenye kumiliki soko kwa 7% hadi kufikia 15% ambayo ni zaidi ya mara mbili. Kwa maana hiyo viwanda walivyonavyo sasa wataviongeza mara mbili. Kipaumbele kimoja cha Wizara ya Viwanda na Biashara Kenya ni kutengeneza skilled technical human resources.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja kati ya vitu vinavyoangusha watu wetu hapa hawana uwezo wa kushindana kimataifa, skill level iko chini. Kwa hiyo, hata tukijenga viwanda bila kuwa na programu maalum ya kunyanyua skill za watu wetu, bado effect kwenye uchumi wa viwanda itakuwa ndogo maana kazi zitakuja kuchukuliwa na watu wa mataifa ya jirani ambao wameandaliwa Kenya na Rwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kushauri Serikali ijikite katika kujenga viwanda na vilevile kutayarisha vijana kwa kutengeneza skilled technical human resources ili waweze kupata ajira katika hivi viwanda. Vilevile Serikali iboreshe miundombinu ili kuwezesha movement ya bidhaa zinazotengenezwa, maana kuongelea Tanzania ya Viwanda bila kuwa na uhakika wa miundombinu ya barabara ni sawa na kuongelea mwili wa binadamu bila damu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawasilisha.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia mjadala huu wa bajeti. Kwa kuwa Wabunge wengi hapa wameongea hili suala la makinikia naona ni vema na mimi niweze kuligusia kidogo pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la wizi wa madini ya nchi hii vilevile suala la mikataba mibovu ya madini na suala ya sheria mbovu za madini imekuwa ni kilio cha wapinzani kwa miaka mingi sana na Watanzania kwa ujumla. Na kwa kuwa Serikali hii hii ya CCM ndiyo iliyolea huo wizi kwa kipindi chote hicho kwa kuleta mikataba mibovu ya madini na sheria mbovu za madini, basi Serikali hiyo ya CCM pamoja na Wabunge wake wa CCM wanawajibu wa kuwaomba msamaha na kuwaomba radhi kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba kuchangia mjadala huu wa bajeti iliyoletwa hapa. Naunga mkono maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani na ningependa kuanza kwa kuongelea juu ya miradi ya maendeleo. Serikali inapaswa ielekeze pesa nyingi katika miradi ya maendeleo ambayo ina wananchi wengi (labour intensive), kama vile sekta za uvuvi, kilimo, na sekta za ufugaji. Kwa nini nasema hivyo, nasema hivyo kwa sababu hizi ni sekta ambazo zina shughuli ambazo ni endelevu na haziitaji watu walioandaliwa skilled labour.

Vilevile tofauti na hivyo leo hii Serikali inajinadi kwamba imetoa ajira kwa wananchi wengi lakini hizo walizozitoa siyo ajira bali ni vibarua ambavyo havina mwendelezo wowote. Kwa sababu wameelekeza pesa nyingi kwenye miradi ya maendeleo ambayo ni capital intensive ambapo ili iweze kufanikiwa hiyo miradi lazima itumike mitaji ya kuwezesha kununua mashine na mitambo na pesa nyingi zinaelekezwa kwenye kuwalipa wasimamizi na wataalam ambao wengi wao siyo Watanzania ni wananchi kutoka nchi nyingine tofauti, hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ningependa kuchangia juu ya Sera za kikodi. Sera za kikodi kwa mfano, Serikali ya Awamu ya Tano ilikuwa na nia njema ya kutaka kukusanya madeni ya kodi ambayo yalikuwa yamelimbikizwa kwa muda mrefu, hiyo ni nia njema kabisa ya Serikali ya Awamu Tano. Lakini sasa sera ya kikodi imeonesha mapungufu pale ambapo Serikali ilitaka wadaiwa hawa walipe madeni yote haya ya kodi ndani ya muda maalum bila kuangalia athari za kiuchumi ambazo zingeweza kujitokeza, matokeo yake wanafanyabiashara wengi wao wakiwa wenye makampuni makubwa walilazimika kwenda kwenye taasisi za kifedha na mabenki mbalimbali kukopa pesa ili waweze kulipa hayo madeni ya kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande mmoja walifanikiwa kulipa madeni haya ya kodi lakini kwa upande mwingine walishindwa kurejesha ile mikopo kwenye hizo taasisi za kifedha na kupelekea sekta ya fedha kudorora na hadi baadhi ya mabenki kufungwa. Sasa sera za kikodi zinapaswa zielekeze na ziweze kuzingatia maeneo mengine ya uchumi ambayo yanaweza yakaathiriwa kwa njia moja au nyingine pale ambapo ikiwa njia za kutekeleza hilo, hata kama ni nia njema lakini pia liangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine ni kuhusu sera za kifedha. Sera za kifedha zinatakiwa zielekezwe katika kuhakikisha kwamba ukuaji wa uchumi unakuwa shirikishi yaani inclusive economic growth kwa ajili ya kuweza kutoa ule utata uliko kwamba sasa hivi kwenye makaratasi na takwimu ina……

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii ya kuweza kuchangia katika hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kwanza kuchangia kuhusiana na suala zima la Tume ya Uchaguzi. Katika hotuba ya Waziri Mkuu alisema kwamba Tume ya Uchaguzi imekuwa ikifanya kazi kwa ufanisi, sasa ni ufanisi gani anaouongolea kama Tume hii mpaka sasa tumeiona ikiwa inatenda kazi kinyume na taratibu na kanuni zilizowekwa na sheria ambazo ziko wazi. Jambo la kushangaza zaidi Tume hii ipo chini ya Mwenyekiti ambaye ni Jaji, tulitegemea kwamba mtu kama Jaji angeweza kuisimamia hii Tume iweze kuwajibika na kufanya kazi zake wka kufuata taratibu na sheria na kanuni zilizopo.

KUHUSU UTRATIBU . . .

MHE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuendelea na mchango wangu hapa kwenye suala la Tume ya Uchaguzi kuhusu taratibu ambazo zinatakiwa kufuatwa kila baada ya uchaguzi ni Daftari la Mpiga Kura linatakiwa kuboreshwa mara mbili baada ya uchaguzi kumalizika, mpaka sasa hivi tumeshuhudia kwamba Daftari la Mpiga Kura halijaboreshwa hata mara moja na sasa hivi ni mwaka wa tatu tangia tumalize uchaguzi uliopita. Sasa hii inatuwekea sintofahamu na tunaanza kuingia mashaka kwamba Tume wana mpango gani tunapoelekea kwenye uchaguzi wa mwaka 2020 kama mpaka dakika hii hakujafanyika taratibu za kuhuisha Daftari la Mpiga Kura .

Kwa hiyo, hiki ni kitu ambacho kimetuletea mashaka na tunaomba Serikali iliangalie hili waweze kulichukulia hatua haraka iwezekanavyo ili tunapoelekea kwenye uchaguzi hili zoezi liwe tayari limeshamalizika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine ambalo liko katika uwezeshaji wa uchaguzi (Electoral Support Program) ambao ni mradi kwa ajili ya kuwezesha uchaguzi. Lakini kitu cha kusikitisha kabisa ni kwamba huu mradi haujapatiwa pesa hata kidogo. Katika bajeti ya mwaka 2017/ 2018 bajeti ambayo ilipitishwa ilikuwa ni shilingi bilioni 10 lakini hawakupewa hata senti tano na mwaka huu pia bajeti cha kushangaza bajeti imeenda kupunguzwa by 50% badala ya shilingi bilioni 10 wakati ule sasa hivi wanapewa shilingi bilioni tano, sasa inakuwaje tunakuwa na mradi kama huu halafu hamna pesa yoyote ambayo inaenda kupitishwa, ningeomba hili pia liangaliwe kwa sababu mradi wa uwezeshaji wa uchaguzi ni suala muhimu sana na utahitaji kuwa na funds za kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ningependa kuongelea suala la Commission of Mediation and Arbitration (Tume ya Usuluhishi na Uamuzi). Nimeona katika hii hotuba ya Waziri Mkuu amesema kwamba kumekuwa na ujenzi wa Mahakama na ukarabati wa Mahakama mbalimbali lakini hamna sehemu aliyoongelea kuhusiana na suala hili muhimu la Commission of Mediation and Arbitration, tungeomba hili suala Serikali ilichukulie umaanani na umuhimu kwa sababu mpaka sasa hivi imejitokeza changamoto nyinig sana kuhusiana na suala la Tume hii ya Mediation and Arbitration, kwanza hamna majengo ya kutosha, mpaka sasa hivi tunachokiona ni kwamba unakuta wanakuwa na chumba kimoja ambako ndiyo wanafanya hiyo mediation na zinavyokaa kesi mbili hadi tatu; kwa hiyo, kuna kuwa na muingiliano kunakuwa hamna privacy, huku wanafanya mediation na huku pia yaani kusema kweli tunahitaji sana kuwe kuna majengo ya kutosha. Pia kuwe kuna staffing maana iko understaffed.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachoshangaa ni kwa nini Serikali inashindwa kuleta watumishi au kuajiri watumishi kwa ajili ya hii Tume ukizingatia tuna wanafunzi wengi ambao wana graduate, ishindikane vipi hawa watu washindwe kuajiriwa. Ningeshauri hili suala lingechukuliwa kama suala ambalo ni muhimu sana ikiwa kama kitengo cha kutaka kuhakikisha kwamba tunaimarisha eneo letu la utoaji haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ningependa kuongelea suala la strong institution for sustainable development, tunahitaji kuwa na taasisi imara kwa ajili ya maendeleo endelevu. Nasema hivi ni kwa sababu taasisi zetu zinahitaji kuwa na uwezo wa kujiendesha, uwezo wa kujisimamia katika maamuzi yake, lakini kitu ambacho kinaendelea sasa hivi unakuta kwamba mfano mdogo tu naweza kuutoa ni Jeshi la Polisi. Jeshi la Polisi sasa hivi kinachoendelea ni kwamba mtu anaweza akachukuliwa akawekwa mahabusu kwa muda wa siku 14 pasipo kupewa haki yake ya kufikishwa Mahakamani. Kinachobaki wanakuambia kwamba wanasubiri maelekezo kutoka juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunapokuwa na taasisi kama hizi, zinakosa kujisimamia na kuweza kujiendesha bila kutegemea maamuzi ya mtu huyu mmoja, naomba niwakumbushe kwamba Ujerumani kulikuwa kuna Adolf Hitler, alikuwa anaingilia mifumo ya utoaji haki. Aliingilia hadi Jeshi la Polisi na ilipelekea hadi kukawa na machafuko. Hatutaki kufikia huko, sasa tunaomba ifike wakati taasisi zetu zijengewe uimara, ziweze kujitegemea zenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine la mabadiliko ya tabianchi. Mabadiliko ya tabianchi ndiyo hapo ambapo tunakuta kunaweza kukajitokeza majanga kama mafuriko, lakini sasa kitu cha kushangaza ni kwamba hamna pesa za ndani zinazotengwa kwa ajili ya kitu muhimu kama hiki…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi hii ya kuweza kuchangia kwenye Wizara hii ya Maji.

Awali ya yote napenda kuzungumzia kuhusiana na suala zima la kutunza vyanzo vya maji. Tunatambua kwamba mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la shughuli za kibinadamu linapelekea hali hatarishi kupelekea kwenda kukosa maji katika siku za usoni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikitumia mabilioni ya fedha kwenye miradi ya usambazaji wa maji, lakini imeacha kujiwekeza katika suala zima la kutunza vyanzo vyetu vya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naweza kusema kwamba Serikali imeshiriki katika kuhujumu vyanzo vya maji. Kwa nini nasema hivyo? Ni kwa sababu haijaweka kipaumbele kwenye suala hili hata katika hii bajeti ambayo inaenda kupitishwa hamna fedha zilizotengwa kwa ajili ya kutunza vyanzo vya maji. Miradi hii ambayo ikitumia mabilioni ya fedha sustainability yake itakuwaje, maana yake itakuwa ni miradi isiyo endelevu kama vyanzo vyenyewe vya maji hakuna mkakati wowote wa kuvilinda.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haijaweka mpango wa muda mfupi wala wa muda mrefu katika suala zima la kutunza vyanzo hivi vya maji. Nasema hivyo nikitambua kabisa nchi nzima hili tatizo limejitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa mfano wa Lindi na Kilwa Kusini tangu enzi za wakoloni kuna mto mmoja unaitwa Mto Mavuje ulikuwa una uwezo wa kusambaza maji kwenye kata nne, Kata za Pande, Kilwa Masoko, Limalyao na Kivinje. Enzi za wakoloni walizuia maji kwenye mto ule wakaweka na mageti lakini leo hii mageti yale yameanguka Serikali haijachukua hatua yoyote ya kuweza kwenda kuyarudishia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, Serikali hii hii ilichokifanya imeingia mkataba na mwekezaji wa nje Bio Shape kwa ajili ya kuja kulima mimea ya nishati. Bio Shape alikuja hapa kwa ajili ya mradi huo, cha kushangaza mradi huo ulihitaji awe anakata misitu, kwa hiyo akakata miti katika eneo hilo la mto na mradi huu umeota mabawa. Ameenda kukata miti kwenye mto huo, kumebaki jangwa na mto huo sasa unashindwa hata kuhudumia kata nne kama ilivyokuwa enzi za wakoloni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la maji ni la kidunia siyo kitaifa tu, ndiyo maana unakuta nchi za wenzetu Serikali inachukua hatua katika kudhibiti vyanzo vya maji. Mfano naweza nikatoa Australia, wameweka udhibiti kwa kuhakikisha kwamba wale wanaoingia katika maeneo ya vyanzo vya maji wanatozwa, kwa hiyo inakuwa fundisho kwa watu wengine. Siyo huko tu, South Africa wameanzisha kampeni ya Water Wise, ambayo inahamasisha na kuelimisha wananchi juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji, kwa nini sisi Tanzania tushindwe? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Wizara ya Maliasili na Utalii imeweza kushirikiana na TANAPA katika kudhibiti watu kuingia na kufanya shughuli hovyo katika hifadhi za misitu na maeneo ya mbuga za wanyama, kwa nini ishindikane kuja na mfumo/mpango madhubuti kwa ajili ya kuweza kudhibiti na kutunza vyanzo vyetu hivi vya maji huku tukitambua kabisa kwamba Serikali inatumia pesa na mabilioni ya pesa katika miradi mbalimbali ya maji ambayo haiwi endelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mwingine ni Stiglers Gorge ambao hautokuja…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kati ya tatizo kubwa na sugu linalofanya uzalishaji wa korosho katika Mikoa ya Kusini ni uzee wa miti iliyopo. Kama ilivyo katika mazao mengine kama miembe, michungwa, parachichi, limao na mengine mengi ni wakulima wachache sana wanazalisha mazao hayo kibiashara wanatumia miche au miti ya zamani ya kiasili. Wengi wanatumia ya kisasa (cross breed) ili kuweza kupata mti bora wenye uwezo mkubwa wa kuhimili magonjwa kutoa mazao mengi na kuweza kuzaa ndani ya muda mfupi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango gani ili kuhakikisha kwamba wakulima wa korosho wanapanda kwa wingi miche ya kisasa ya mikorosho inayozozalishwa nchini ukizingatia kwa muda mrefu zao la korosho limekuwa likishika namba mbili nyuma ya tumbaku katika mazao yanayoliingizia Taifa pesa nyingi pamoja na pesa za kigeni, kuna mashamba ambayo yameteuliwa kuzalisha miche ya mikorosho ya kisasa, mashamba hayo yapo Mkoa wa Tanga, Pwani na maeneo machache ya Mkoa wa Lindi na Mtwara. Serikali ina mpango gani wa kuinua uzalishaji wa mashamba haya ili miche inayozalishwa iweze kuwafikia wakulima wengi zaidi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine ni ufisadi uliokithiri, wawakilishi wa wanunuzi huhongwa katika minada badala ya kuwa upande wa wakulima wanakuwa upande wa wanunuzi pamoja na viongozi wa vyama vya msingi. Hii hupelekea wote kwa pamoja kushirikiana katika kumkandamiza mkulima na kumfanya mnunuzi anaeshinda kununua sio anayetoa bei ya kumnufaisha mkulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine lipo katika mfumo na mlolongo mzima wa malipo kuwa mlolongo mrefu sana kupelekea pesa kuchelewa kumfikia mkulima na kupelekea wakulima waone bora kuuza korosho kwa njia ya kangoma kuliko kupeleka korosho zao kwenye utaratibu wa stakabadhi ghalani. Malipo hupitia process ambazo ni manual na taratibu za kibenki kuchukua muda mrefu kiasi cha kwamba hadi pesa inamfikia mkulima inakua tayari imeshuka kwa mfumo thamani. Serikali ijitahidi kuhakikisha kuwa mfumo huo unafupishwa ili kuweza kutoa nafasi kwa mkulima kupata pesa zake kwa wakati na kufanya maandalizi ya msimu unaofuata mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuzungumzia suala la utawala mbovu katika Wizara ya Kilimo. Wafanyakazi wengi wamesimamishwa kwa muda hadi kufika mwaka mmoja na zaidi bila kupewa nafasi ya kusikilizwa wala kuchunguzwa jambo ambalo liko kinyume na taratibu za kisheria. Wengine walisimamishwa kwa kosa la kile tunachoita kutekeleza majukumu yao ya kazi mfano, TPRA ambao walileta taarifa kuwa mbolea iliyoingizwa nchini ilikuwa mbovu, iliamuliwa kwamba mbolea ikakaguliwe na Mkemia Mkuu ambaye alithibitisha kuwa mbolea haina matatizo lakini katika hali ya kushangaza mbolea hiyo hiyo ilipoingia kwa ajili ya matumizi ikaonekana na ikathibitika kuwa mbovu. Sasa
hao waliosimamishwa baada ya Mkemia Mkuu kuthibitisha kuwa mbolea ni nzima kwa nini baadae ilipothibitika kuwa kweli mbolea mbovu kwa nini hawajarudishwa kazini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni mfano mmoja tu lakini wafanyakazi wa vitengo mbalimbali wamesimamishwa kwa kipindi kirefu bila kujua hatma yao. Huu ni utawala mbovu ambapo haki za wafanyakazi hazisimamiwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa napenda kuzungumza juu ya makampuni na mawakala kuna madai ya mwaka 2014/2015, 2015/2016 hali kadhalika, lakini cha kushangaza kila siku Wizara inafanya ukaguzi na uhakiki wa madai hayo. Ifike wakati sasa watu walipwe madai yao. Wizara itueleza ni lini watalipwa madai yao.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati
MHE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii ya kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri wote tunatambua kwamba kwa muda mrefu sana nchi yetu ilisemekana kukosa chanzo cha uhakika cha kuzalisha umeme baada ya mabwawa ya Kidatu na Mtera kupungukiwa na maji mara kwa mara, hali iliyosababisha kukosa umeme wa kutosha nchini. Kutokana na hali hii, Serikali iliyokuwa madarakani kwa kipindi hicho iliwekeza nguvu nyingi sana kwenye mradi wa gesi ambao ndiyo tulitegemea uweze kutuzalishia umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ya Nishati ilituhakikishia kwamba mradi huo ungeweza kutupatia umeme wa kutosha nchi nzima na hata tungeweza kuuza umeme kwenye nchi za jirani. Mradi huu wa gesi uligharimu takribani dola bilioni 1.225, katika dola hizo dola milioni 875.7 zilitumika katika ujenzi wa bomba la gesi ambapo takribani dola milioni 300 zilitumika katika ujenzi wa vinu kwa ajili ya kuchakata gesi. Leo hii Serikali inakuja na mradi mpya wa Stiegler’s Gorge. Mbali na kwamba mradi huu una madhara mengi yakiwemo yanayoweza kujitokeza kwenye mazingira yetu, lakini Serikali imeendelea kupigia debe huu mradi uweze kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wa CCM siyo kwamba sisi tuna akili mgando, Wabunge hatukatai maendeleo, miradi ya maendeleo tunaikubali, lakini ikumbukwe kwamba muda mfupi uliopita Serikali iligharamia mabilioni ya fedha ambazo ni fedha za walipa kodi wa Tanzania. Leo hii huu mradi unaenda kutelekezwa tunaingia kwenye mradi mwingine, tunaelekea wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia katika mwaka wa fedha 2018/2019, pesa ambayo inaombwa kwa ajili ya Wizara ya Nishati ni Sh.1,665,141,000,000. Katika pesa hizi ambazo zinaelekezwa katika huo mradi ni shilingi bilioni 700 ambayo ni sawa na asilimia 42 ya fedha za miradi ya maendeleo katika Wizara hiyo ya Nishati. Vilevile pesa nyingine inayoenda ambayo ni Sh.112,083,000,000 zinzelekezwa katika mrai wa REA, ni asilimia 6 tu ndiyo iliyotengwa kwa ajili ya mradi huu wa gesi ambao tayari ulishagharimu pesa nyingi za nchi hii, hii maana yake nini? Mnataka kutuaminisha kwamba Serikali ina fedha nyingi au ni misuse ya zile resources chache tulizonazo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Stiegler’s Gorge itaenda kugharimu fedha hizi zote, wapi tunapoelekea? Tunawaambia nini wananchi wa Lingoko, Mkoa wa Lindi, wananchi wa Songosongo Kilwa, wananchi wa Mtwara Vijijini ambao wameacha makazi yao, wameacha mashamba yao kwa ajili ya kupisha mradi huo wa gesi ambao sasa hivi umeenda kupewa asilimia 6 tu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni suala ambalo kusema ukweli naishauri Serikali kuliko kuelekeza hii pesa katika mradi mpya huu wa Stiegler’s Gorge bora hiyo pesa ielekezwe katika mradi ambao tayari umeshaligharimu Taifa mabilioni ya fedha, haiwezekani kila siku tukawa tunaanzisha miradi mipya ambayo haitekelezeki. Mpaka leo hii fedha zilizotumika hatujaona returns zozote, leo hii tunaingia kwenye mradi mwingine? Waziri wa Nishati tunaomba mliangalie tena hili suala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kuliongelea ni juu ya usambazaji wa gesi.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kitu kinachoonyesha Serikali hii kwa kupanga tuu inajua kupanga, lakini kwenye kutekeleza, ipo shida, mipango ipo mingi lakini utekelezaji ni shida sana sana. (Makofi)

Kwanza ningeanza kuongelea suala la nishati. Tulikuwa na mradi wa nishati kwa kutumia gesi, mradi huo ambao bahadhi ya ndugu zetu ndugu zangu wa Kusini (Mtwara na Lindi) waliandamana na hata tulipoteza baadhi ya ndugu zetu na wengine walifunguliwa kesi, wengine walikimbia nchi kwa ajili ya huo mradi. Mradi huu ulitumia takribani hata zaidi ya trilion 1.2; lakini pia wananchi walilazimika kuacha makazi yao, mashamba yao na kushindwa kuendelea na kazi kwa ajili ya kujiinua kiuchumi na mpaka leo hii baadhi yao hawajalipwa fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunaona Serikali ya Awamu ya Tano inaenda kuua ule mradi wa gesi, imekuja na mradi mpya wa Stieger’s Gorge. Mradi huu ambao kwanza kwa taarifa tuliyopewa utaenda kugharimu pesa nyingi zaidi kuliko ule mradi wa gesi, tumeambiwa mpaka kumalizika huo mradi inaweza ikatumika takribani trilioni saba na hadi sasa zimetengwa, bilioni 700 kwa maana hiyo hadi kuja kumalizika itakuwa ni ndani ya miaka kumi, kwenye hatua za awali tu tayari imetumika bilioni 700.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi najiuliza, huu mradi kuna kitu gani mpaka tunalazimishia uendelee pamoja na kwamba wataalam wametuambia kuna athari nyingi zitakazoenda kujitokeza kwenye mazingira, lakini bado tunataka kuendeleza na huu mradi, tuna option nyingi za kuweza kwenda nazo, kwanza kuna hiyo gesi ambayo tayari tumeshatumia fedha, lakini pia vilevile kuna upepo, kwa sababu huu mradi wa Stieger’s Gorge kama ni megawatts umeme utakaoweza kuzalishwa ni megawatts 2,100 ukiangalia mradi wa upepo unauwezo wa kuzalisha umeme wa megawatts mara nne na zaidi wa huu hapa wa Stieger’s Gorge kwani kuna kitu gani hasa kwenye huu mradi wa Stieger’s Gorge tunahitaji kujua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakumbuka vizuri kabisa, wakati tupo kwenye kipindi cha Bunge la Bajeti, Waziri wa Mazingira, Mheshimiwa Januari Makamba, Serikali itakuja kufanya tafiti kujua hizo athari, lakini cha kushangaza wenye hili hapa huu mpango tunachokiona hakuna pesa yoyote iliyotengwa kwa ajili ya kufanya hizo tafiti juu ya hizo athari zinazoweza kujitokeza. (Makofi)

Sasa na juzi tumemsikia kabisa Rais Magufuli akisema kwamba huu mradi utaendelea kufanyika na ametupilia mbali zile information ambazo zipo bian stone research. Sasa tunataka kujua tunaendea na huu mradi kwa research gani ilifanyika na Serikali? Kama kuna research imefanyika basi tulitewa tuweze kujadili hapa ndani Bungeni. Kwa sababu sielewi kwa nini tunaendeleza kitu ambacho kwa asilimia kubwa itatuletea sisi wenyewe athari nyingi, na ukikaa ukiangalia huu mradi there is no sustainability kwa sababu kama ni maji, maji yatafika wakati yatakwenda kuisha, kwa sababu maji yanatumika na wanyama, mimea, binadamu wote tunategemea kutumia haya maji. Kwa hiyo ikifika sehemu maji yameisha tunafanyaje?
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.4) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza)
MHE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote ningependa kuzungumzia juu ya marekabisho ya Sheria ya Proceeds of Crime, yaani mali zinazotokana na uhalifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 37 ambayo inaenda kufanya marekebisho ya sheria mama ya Kifungu cha 22 ambacho kinaenda kufuta kabisa kifungu Kidogo cha (4) na kuleta Kifungu Kipya cha 4C ambacho kinasema, mtu akikutwa na mashitaka ambayo yapo katika serious offences ikiwemo utakatishaji fedha na uhujumu uchumi, basi mali aliyoipata ndani ya miaka mitano iliyopita itashikiliwa na kuchukuliwa kama mali iliyopatikana kutokana na uhalifu huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu hiki kiko kinyume na sheria kwani inawezekana kabisa ikawa mapendekezo haya ya sheria yana nia ovu ya kuwakamata watu na kuwabambikiza na kesi za uhalifu kwa nia tu ya kuweza kukamata mali zao ambazo inawezekana kabisa mali hizi walizipata kihalali kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu, inawezekana kabisa mtu akawa amepata mali kihalali, baada ya miaka mitano akaja kutenda lile kosa. Sasa kushikilia baadhi ya hizi mali ni kinyume na sheria ya umiliki wa mali kwa sababu, zitenda kuguswa hata mali ambazo hazihusiani na mtuhumiwa. Mfano, mali ambazo zimechumwa na mke na mume, lakini pia zitaenda kugusa hata mali ambazo zimetokana na mirathi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza Serikali ifute kabisa Kifungu cha 4C kuepusha kuleta shida na kwenda kutekeleza sheria hii ambayo mimi naiona ina nia ovu. Watu watakuja kukamatwa kwa makosa ambayo wanafanya leo mali zao zichukuliwe walizozimiliki miaka mitano iliyopita, haiko sahihi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kushauri kwamba, pamoja na haya, tuangalie kwamba kila mali kabla haijawa seized kuwe kuna hearing ya uthibitisho wa mali hii ilipatikana vipi? Yaani kuwe kuna separate hearing ya kila mali ambayo itachukuliwa na kuunganishwa na huo uhalifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo sasa ningependa kuzungumzia juu ya marekebisho ya Sheria ya Mawakili. Ibara ya 5 inazuia Mawakili kupewa vibali vya kufanya shughuli za kiuwakili wa Kiserikali kwa muda wote wa utumishi wao katika Serikali. Ibara hii inaenda kinyume na Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ndogo ya (2) inayosema, naomba nisome, “Ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote katika Jamhuri ya Muungano kuweka sharti lolote ambalo ni la kibaguzi ama kwa dhahiri au kwa taathira yake.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa hiyo Ibara ya 5 ya Marekebisho ya Sheria ya Mawakili tunavyoiona inalenga kubagua taaluma ya sheria ikiwa kama taaluma ya sheria ni taaluma kama ilivyo taaluma nyingine. Kwa mfano, daktari ambaye ni Mtumishi wa Umma anaruhusiwa ku-practice taaluma yake nje ya utumishi wake wa Umma. Ikiwa kama Mhasibu anaruhusiwa ku-practice taaluma yake nje ya utumishi wa Umma kwamba anaweza hata akafanya shughuli za financial consultancy, na kadhalika, vilevile lecturer anaruhusiwa ku-practise taaluma yake nje ya Utumishi wa Umma, sasa iweje Mwanasheria azuiliwe ku-practice taaluma yake nje ya Utumishi wa Umma? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni suala ambalo haliko sahihi hata kidogo. Ikumbukwe kwamba baadhi ya hawa Mawakili wa Serikali wengine wamesomeshwa kwa pesa binafsi, vilevile kuna ambao wamesomeshwa kupitia mikopo ya elimu, mwisho wa siku wanahitaji kulipa mikopo hii. Isitoshe wanahitaji kukidhi maisha yao na wana majukumu katika familia zao. Sasa unapowakatalia hili maana yake ni kwamba unawaambia wategemee kipato kinachotokana na Utumishi wa Umma na wakati ni dhahiri wote tunatambua kwamba kipato kinachotokana na Utumishi wa Umma hakitoshelezi kukidhi mahitaji haya yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo tu kwamba kumnyima Wakili wa Serikali kwenda kufanya shughuli hizi za kiuwakili kunaenda kumkata miguu, lakini pia vilevile jamii inaenda kunyimwa fursa ya kuweza kupata service kutoka kwa Mawakili hawa wa Serikali. Mfano mkubwa ni sisi wenyewe, siyo kwamba Mawakili wale binafsi hawana uwezo wa kufanya hizi shughuli, lakini kuna wakati mtu ambaye ni wakaribu kabisa anakuwa ni yule Wakili wa Serikali, tunategemea kupewa huduma kutoka huko. Mfano, tumekuta sisi wenyewe Wabunge humu ndani, mara ngapi tunahitaji affidavits ziwe signed? Mara ngapi tunahitaji forms za maadili zikasainiwe ambapo watu hawa wamekuwa wakitufanyia stamping muhuri, tunaupata kutoka kwa hao hao Mawakili wa Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufanya hivi ni kwenda kufanya kitu ambacho siyo kwamba kitamnyima tu haki yake yule Wakili wa Serikali, lakini hata na jamii nzima ambayo inawategemea. Hii pia, itaenda kudhoofisha taaluma nzima ya sheria, kwa sababu watu watakosa interest ya kwenda kwenye taaluma ya sheria. Sio hivyo tu, watu watakuwa hawataki wajiriwe wawe watumishi wa Umma na kusababisha Serikali kukosa Mawakili wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza kwamba Ibara hii ya 5 iondolewe na badala yake pamoja na kwamba dhamira ilikuwa ni nzuri, lakini badala yake ili kuepusha Wakili wa Serikali kwenda kufanya shughuli za kiiwakili ambazo zitakuwa na conflict of interest na Serikali, basi kwa kuwa haya ni masuala ambayo yana mwelekeo wa kinidhamu na kiutendaji, kwa nini Serikali isije na utaratibu wa kuweka mwongozo ambao utakuwa wa kiutumishi, aidha kwa kupitia Utumishi au kwa kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo yote, napenda kuzungumzia suala la Serikali kutuletea Miswada ya mabadiliko ya sheria kwa kupitia Hati ya Dharura. Hili suala haliko sawa hata kidogo kwa sababu, ukiangalia hata hizi sheria ambazo zimeenda kurekebishwa, mnataka kuniambia kuna udharura gani wa kufanya marekebisho ya Sheria ya Mawakili? Kuna udharura gani wa kufanya marekebisho ya Sheria za Usajili wa Vizazi na Vifo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda Serikali iangalie hili kwa umakini zaidi kwa sababu, tunavyoendelea kuletewa haya marekebisho ya sheria kwa Hati ya Dharura matokeo yake kunakuwa kuna ushirikishwaji finyu sana wa hao wadau ambao ndio wadau wakuu wa hizi sheria na kuwanyima haki wadau hawa kuweza kushiriki kikamilifu kwa kutupatia sisi maoni ya kutosheleza kwa sababu, mwisho wa siku tunaishia kutunga sheria na baada ya miaka michache tu mbele, hizi sheria zinaenda kuonekana kuwa na upungufu. Kwa hiyo, nasi kama Bunge mwisho wa siku tunakuwa tunatunga sheria mara kwa mara kutokana na upungufu huo ambao usikute kungekuwa kuna ushirikishwaji wa ukamilifu wa wadau hawa tungeweza kutunga sheria ambazo zinaweza zikawa everlasting. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, basi baada ya kusema haya yote, naomba nikushukuru, ahsante. (Makofi)