Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Kunti Yusuph Majala (5 total)

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kutokana na majibu ya Mheshimiwa Waziri, ni masuala yale yale kwamba tupo kwenye mchakato. Naomba kupata majibu katika maswali yangu mawili.
(a) Ni lini sasa TAMISEMI itakamilisha mchakato wa marekebisho ya sheria hiyo ili Halmashauri zetu ziweze kujipatia mapato yake stahiki?
(b) Ni lini kikao hicho cha wadau kitakwenda kufanyika ili tuweze kuokoa mapato mengi yanayopotea katika sekta hii? Asante.
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kweli kumekuwa na kero kwa Waheshimiwa Wabunge wote katika Majimbo yote kwa sababu minara imeenea maeneo yote.
Mheshimiwa Spika, kila mtu katika Jimbo lake ana mnara na kila mtu anatarajia kukusanya kodi. Lengo ni kuhakikisha Halmashauri zinapata mapato, ndiyo maana ofisi yetu imeona, kwa sababu suala hili linagusa Halmashauri zote, lazima tuwe na mfumo ambao utakuwa muafaka kuhakikisha kwamba fedha zinakusanywa hali kadhalika Halmashauri zinapata fursa ya kukusanya hayo mapato vizuri na ndiyo maana mchakato huo umeshaenda.
Mheshimiwa Spika, bahati nzuri sana kikao cha wadau kimeshakamilika, na jukumu linalofanyika ni kwamba paper itaondoka katika Baraza za Mawaziri, itajadiliwa na itakuja huko. Hata hivyo, tumeenda mbali katika marekebisho ya sheria hii, tunaenda kuangalia suala zima la crop cess, watu wanajua ushuru wa mazao umekuwa ni changamoto kubwa sana.
Kwa hiyo, sheria hii inakutanisha mambo mengi ili mradi Sheria ya Fedha Sura Namba 290 itakapokuja hapa Bungeni, basi iweze kukidhi mahitaji ya Waheshimiwa Wabunge wote katika Halmashauri zao, fedha ziweze kukusanywa na wananchi wapate huduma bora. Asante.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza kwenye Wizara ya Nishati na Madini. Wilaya ya Chemba ni miongoni mwa Wilaya mpya na upatikanaji wa huduma ya nishati kwa maana ya umeme ni kwa vijiji 60 tu kati ya vijiji 112. Nataka kufahamu ni lini sasa kwa REA Awamu ya Tatu itakwenda kukamilisha vijiji hivi 52 vilivyobaki ili Wilaya yetu na wananchi wale waweze kupata huduma hii ya umeme wa REA Awamu ya Tatu? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa katika Jimbo la Chemba tulipeleka umeme katika vijiji 62 na vikabaki vijiji 52; kwa hiyo viko 124. Niseme tu vijiji 52 vilivyobaki tumeshazindua katika maeneo ya Chemba na Wilaya zote, Mkoa wa Dodoma na tunaelekea katika Mikoa ya Singida na mingine. Upelekaji wa umeme katika REA Awamu ya Tatu umeanza tangu mwezi Machi na utakamilika kwa nchi nzima ikiwemo pamoja na Jimbo la Chemba mwaka 2020. Mradi huu unakwenda kwa awamu, baadhi ya vijiji na vitongoji vitakamilika mwezi Machi, 2019 na baadhi yake kwenye densification ni miezi 15 kuanzia sasa. Kwa hiyo, vijiji vyote 52 kati yake vijiji 12 vitapatiwa umeme 2019 na vilivyobaki vya Chemba mwaka 2020.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Kwa kuwa Serikali inatoza VAT kwenye vifaa vya ujenzi lakini pili tena tuna suala zima la tozo kwenye majengo, je, Serikali haioni sasa kuna sababu ya kumtoza mwananchi huyu kodi moja tukaondoa ya majengo tukabaki na hiyo tozo ya vifaa vya ujenzi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kodi hizi mbili ni kodi tofauti kabisa huku tuna- charge kodi ya VAT kwa mlaji wa mwisho na hasa ambaye yuko registerd kwa VAT, ambaye anavuka mapato yake kwa shilingi milioni 100 na kodi ya majengo hii ni kodi tofauti kabisa wala hazina sababu ya kuunganishwa pamoja. Mheshimiwa this isproperty tax na hii ni kodi ya mlaji, ka hiyo, kodi hizi haziwezi kuunganishwa na ikawa kodi moja.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, Mheshimiwa Waziri, wananchi wa Kata ya Makole, Manispaa ya Dodoma walisitishiwa uendelezaji wa nyumba zao kwa ajili ya upanuzi wa uwanja wa ndege ulioko hapa wakati huo kuna wananchi wa Kata ya Msalato 89 wanaidai Serikali tangu mwaka 2005.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kujua wananchi wa Msalato watalipwa lini lakini pili wananchi wa Makole waliositishiwa uendelezaji wa nyumba zao…
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kumekuwepo na upanuzi wa uwanja wa ndege au tutautumia sasa hivi hapa Dodoma na wananchi wa Makole madai yao ya fidia yanashughulikiwa kupitia Wizara ya Fedha na sasa hivi Wizara ya Fedha wako kwenye uhakiki wa kuhakikisha kwamba wanalipa hayo madai yao wakati watakapomaliza uhakiki.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kituo cha Afya cha Hamai kilichopo Wilayani Chemba kina upungufu mkubwa wa vifaatiba. Kituo hicho ndicho kinachotumika kama hospitali ya wilaya, kinahudumia wananchi wote wa Jimbo la Chemba, lakini pili, majirani zetu kwa maana ya Chilonwa na Jimbo la Kiteto mpakani kule. Sasa nataka kujua Wizara imejipangaje kutupatia vifaatiba zikiwemo x-ray machines pamoja na ultrasound? La pili suala zima la ambulance yetu, imechoka haitamaniki, haithamaniki. Nataka kupata majibu ya Waziri kuhusiana na hicho kituo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kunti, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika jibu lililotangulia, kwamba ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba vituo vyote vya afya vinapelekewa vifaa. Niruhusu nichukue fursa hii kuiagiza MSD kuhakikisha kwamba zile oda zote ambazo zimepelekwa kuwe na msukumo wa kuhakikisha kwamba hivyo vifaa vinapatikana mapema ili viweze kutumika katika vituo vya afya kama Serikali tulivyokusudia. Pia ni ukweli usiopingika kwamba MSD safari hii wanakwenda kuagiza kutoka kwa manufacturer, sio habari ya kuagiza kutoka kwa mtu wa kati na kuna specifications ambazo lazima tuzingatie, lakini ni vizuri tukahakikisha jambo hili linafanyika mapema.