Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Joyce Bitta Sokombi (22 total)

MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, natambua umuhimu wa upembuzi yakinifu na kwamba unaendelea katika ujenzi wa uwanja wa Musoma. Je, ni lini ujenzi wa uwanja wa Musoma utaanza rasmi?
Pili, nimesikitika sana kwa majibu namba (c), nanukuu: “Ni vigumu sana suala hili kulitolea takwimu sahihi kwa kuwa linahitaji kufanyiwa utafiti.”
Mheshimiwa Spika, swali hili tangu nimelipeleka lina miezi mitatu. Je, jibu hili ndilo linaloendana na Hapa Kazi Tu? Ni lini swali hili litapatiwa majibu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI (K.n.y. WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO): Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kuanza kwa uwanja wa ndege, kama nilivyosema ni mara tu baada ya ukamilifu wa upembuzi yakinifu ambao ulitarajiwa kuanza mwezi Februari, 2017.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na takwimu za kina, ni kweli kabisa ili kupata ulinganifu wa hasara unazopata ndani na nje; na unapofanya takwimu za kisayansi, ni lazima uangalie mapato unayopata ndani na mapato unayopata ambayo unayakosa kwa kukosa ndege ambayo inasafiri Kimataifa.
Mheshimiwa Spika, hivyo unavyofanya ulinganisho siyo rahisi ukapata takwimu leo wakati unatakiwa ulinganishe na mataifa mengine pia yanapataje faida kwa matumizi ya ndege za aina hiyo hiyo.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kweli sijaridhishwa na majibu niliyopewa. Ukikaa ukiangalia, kwa mfano kule Kisorya mpaka Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama alikuja, wale watu walipewa amboni tatu tu na hawana makazi. Naomba Mheshimiwa Waziri husika anielezee kwamba atawasaidiaje wananchi wale, kwa sababu hawana sehemu za kukaa? Pia toka walivyopewa chakula na mazao yote yaliharibiwa: Je, Serikali ina mpango gani kuwasaidia wale wananchi pia kupata chakula?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni kwa nini Serikali inasubiri linapotokea janga, ndiyo wanaanza sasa kutuma wataalam wao kwenda kuwapa wananchi elimu ya mazingira? Kwa nini wasiwe wanatoa kabla? Ahsante, naomba majibu.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwa mujibu wa taarifa kutoka kwenye Kamati ya Ulinzi na Usalama, kama nilivyoeleza kwamba tumekuwa tukishirikiana nao na kuona namna majanga haya yanapojitokeza na kuweza kuwahudumia wananchi hawa waliopatwa na majanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa msisitizo ambao Mheshimiwa Mbunge anasema kwamba hawa wananchi sasa hawana makazi kwa muda mrefu na kwamba hawana chakula; nitafanya ziara kwenda kuona eneo analolizungumzia Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kuona namna ya kuwasaidia hawa wananchi ambao wanateseka bila chakula na bila sehemu ya kuishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nijbu hili swali lake analosema kwamba Serikali inasubiri; Serikali hatusubiri, ndiyo maana muda wote, saa zote tumekuwa tukisisitiza wananchi kutokujenga mabondeni, tumekuwa tukisisitiza wananchi kutokujenga kandokando ya mito na tumesisitiza wananchi waliojenga na kuziba mifereji na kusababisha mafuriko kutokufanya hivyo. Kwa hiyo, kila siku tuko katika jambo hili katika kuhakikisha kwamba wananchi hawajengi kwenye mabonde kwenye kingo za mito wala bahari, wala maziwa ili kuepukana na maafa haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, tumekuwa tukiwaondoa wananchi wanaoishi kwenye mabonde na sehemu hizo. Pia tunaweka msisitizo mkubwa wa kuhakikisha kwamba katika miradi yetu ya kimazingira, maeneo mengine ambayo yanatuama maji tunatengeneza mifereji na tunatengeneza mabwawa ya kuweza kuya-contain hayo maji ili sasa tuweze kuyapunguza mafuriko haya katika namna hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, siyo kweli kwamba Serikali inangojea tatizo litokee, Serikali iko makini na tutaendelea kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha kwamba mambo haya hayajitokezi tena.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Majibu ya Naibu Waziri hayajaniridhisha, ukilinganisha na kwamba vifaa tiba na madawa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa havitoshelezi. Je, ni lini atahakikisha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara itakuwa na vifaa ambavyo vitakuwa vinatosheleza kwa asilimia mia moja? (Makofi)
Swali la pili; kwa kuwa gari lililopo ni moja ambalo lina uhakika wa kubeba mgonjwa mahututi kumtoa Hospitali ya Rufaa Musoma kumpeleka Mwanza na ile nyingine ni hizi gari ndogo: Je, ni lini atatuletea ambulance nyingine katika Hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba nikwambie kwamba najua, kwa sababu wakati nakwenda kufunga Mkutano wa ALAT kule Musoma, nilitembelea mpaka Mkoa wa Mara kuona mpango mkakati wa kujenga Hospitali hii ya Rufaa ya Mkoa wa Mara. Nimetembelea pale, nimeona na tumebadilishana mambo mengi sana na Katibu Tawala wa Mkoa ule. Kwa hiyo, najua kuna changamoto, ndiyo maana katika majibu yangu ya msingi nilisema kweli kuna changamoto katika hospitali hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo letu ni nini? Ni kuhakikisha kwamba sasa tunasukuma jambo lile. Naomba tushirikiane na Waheshimiwa Wabunge; kama mnavyojua kwamba commitment za afya zina cross cut maeneo mbalimbali nchini. Kwa hiyo, ni imani yangu kwamba, tutaendelea kushirikiana. Commitment ya Serikali, tukiangalia sasa hivi bajeti ambayo imetoka, shilingi milioni 700 mpaka shilingi bilioni 1.8, ni ongezeko la asilimia 61. Hili ni jambo kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachofanyika sasa hivi ni nini? Ni kusaidia kusukuma nguvu sasa ili fedha zipatikane na wananchi wapate huduma. Katika mchanganuo wa bajeti katika eneo hilo, ndiyo unagusa katika maeneo mbalimbali ya vifaa tiba na madawa kuiwezesha hospitali hii iweze kufanya vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo Mheshimiwa Mbunge amezungumzia suala la ambulance; ni kweli. Najua kwamba ambulance moja inafanya kazi vizuri, lakini na hizi nyingine zina changamoto kubwa. Sasa naomba nimsisitize Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na wadau wengine mbalimbali, katika mchakato huu wa bajeti unaokuja wa 2017/2018, tuweke kipaumbele kinachojiainisha katika upatikanaji wa ambulance. Serikali haitasita kulisukuma hili. Lengo ni kupata ambulance ya maana katika kusaidia wakati wowote emergency inapotokea, wananchi waweze kupata fursa za tiba. Kwa hiyo, nakubali ombi hilo, tutaenda kulifanyia kazi kwa pamoja kama Wabunge na Serikali.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Majibu ya Waziri hayajaniridhisha. Barabara hii ina umuhimu mkubwa kwani hutumiwa na watalii wengi wanaotoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta kuja Serengeti National Park. Je, hamuoni kwamba tunapoteza watalii wengi kutokana na ubovu wa barabara hii?
Mheshimiwa Spika, kwa taarifa niliyoipata ni kwamba barabara hii ilikuwa iishe 2017, lakini nashangaa kwa majibu ya Waziri kwamba barabara hii inaisha 2018. Sasa nataka
nijue barabara hii inaisha 2017 au 2018? Je, upembuzi yakinifu unaisha 2017 au 2018? Je, kwenye bajeti 2017 barabara hii imetengewa bajeti?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA
MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii unaisha mwaka 2018 kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi. Nimhakikishie Mheshimiwa Sokombi kwamba hicho tunachokisema ndicho tutakachokitekeleza na umuhimu wa barabara hii
umetokana na hao watalii wengi ambao wameanza kuonekana. Tunataka barabara hii pamoja na hiyo nyingine, kama unavyofahamu tunajenga barabara nyingine ya kutoka Sanzatu, zote hizi tutazijenga kwa ajili ya kufungua utalii. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge hawa watalii mara baada ya kukamilisha kujenga barabara hizi wataongezeka.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa sababu pia uwanja wa Musoma upo kwenye ajenda hiyo na kwamba upembuzi yakinifu umeshafanywa. Kwa sababu kutengwa fedha ni kitu kingine na ujenzi ni kitu kingine, je, ni lini Serikali itaanza ujenzi katika uwanja wa Musoma?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA
MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Sokombi na wananchi wote wa Mji wa Musoma na viunga vyake ambao kwa kawaida wamezoea kutumia uwanja wa ndege wa Musoma kwa safari zao kwamba Serikali iko makini na katika muda wa
hivi karibuni kama mtakumbuka tuliwaambia katika viwanja vitatu vya mwanzo tutakavyohakikisha kwamba ujenzi wake unaanza haraka ni pamoja na Musoma, Nduli na Mtwara.
Naomba nimhakikishie Serikali ipo mbioni kuhakikisha viwanja hivi vitatu vinapata fedha na uzuri wake fedha za viwanja hivi vitatu vinatarajia ataketupa fedha maana sio mfadhili ni mkopehsaji hivi karibuni.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la
nyongeza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa Mara kulikuwa na takribani viwanda saba, lakini sasa hivi viwanda
vyote vimekufa, kimebakia kiwanda kimoja tu cha samaki cha Mara Fish.
Je, ni lini Serikali itafufua viwanda hivyo kwa sababu sasa hivi ni kipindi cha viwanda tu? Ahsante.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, mojawapo ya maagizo niliyopewa katika Wizara yangu pamoja na Treasurer Registrar ni
kuhakikisha vile viwanda vilivyobinafsishwa au ambavyo havifanyi kazi vinafanya kazi. Zoezi hilo linaendelea.
Mhesimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba nashindwa kusema ni lini kwa tarehe, napenda nimhamasishe
Mbunge na yeye akimbilie kwenye viwanda vidogo, kwa sababu viwanda vidogo kulingana na taratibu za Bunge,
pesa mnazonipa za NEDF, zinaniwezesha mimi kuweza kutoa vile viwanda vya shilingi milioni 10, shilingi milioni 80 na shilingi milioni 200. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge, twende kwenye viwanda vidogo kwa sababu vinaweza kufanya kazi kuanzia ngazi ya familia na vinajenga utamaduni wa Watanzania kumiliki. Hivyo viwanda vingine ni vya watu ambao ni wa kupita.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Ahsante Mwenyekiti, nipende tu kuuliza swali kwamba Wilaya ya Bunda ina hospitali moja ambao ni Hospitali ya Manyamanyama, na ile hospitali ya Manyamanyama inaitwa Hopsitali ya Wilaya, lakini haina hadhi kama Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Waziri, je, ni lini itakuwa na kiwango kama Hospitali ya Wilaya na dawa zipelekwe kama Hospitali ya Wilaya? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli na tulipofika pale Bunda tulitembelea yale maeneo yote tukaona kwamba kuna changamoto kubwa na hili tulitoa maelezo katika maeneo mbalimbali, hata hivyo kwa ajili ya the backup strategy ya kufanya kwa Bunda na kwa sababu ukiangalia kwa ndugu yangu Kangi Lugola wagonjwa wote wanakuja pale, kwa ndugu Boniphace wagonjwa wote wanakuja pale, ndio maana sasa hivi kwa muda unaokuja na si muda mrefu sana japo tunaweka mikakti ya ile sehemu ya Manyamanyama pale lakini katika eneo la Mgeta tunakwenda kutengeneza kituo cha afya tunakwenda kukiimarisha kwa kiwango kikubwa lengo kubwa ni kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokuja pale kuweza kuhakikisha kwamba akina mama na watoto afya zao tunazilinda vizuri.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo la Mbogwe ni sawa na tatizo lililoko katika Mkoa wa Mara hasa Musoma Vijijini. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri atuhakikishie kwamba ni lini wananchi wa Musoma Vijijini watapata umeme wa REA?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa, tulipokwenda katika Mkoa wa Mara wakati tunazindua Mheshimiwa Mbunge alitupa support kubwa sana. Hongera sana pamoja na Wabunge wote wa Mkoa wa Mara; lakini ni lini sasa umeme vijiji hivyo vitapelekewa; tumeshaanza na kuja kufikia mwezi ujao wakandarasi watakuwa wameingia vijiji 42 katika Mkoa wa Mara na vijiji vilivyokuwa vimebaki vitakamilika sasa ifikapo mwaka 2020. Hata hivyo, si kwenye vijiji tu na vitongoji vyote Mheshimiwa Sokombi, Taasisi zote za Umma, Makanisa na Misikiti pamoja na visiwa ambavyo viko Mkoa wa Mara.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitika sana. Majanga ya tembo katika Mkoa wa Mara na Tanzania kwa ujumla ni makubwa sana, lakini majibu ya Waziri yamekuwa ni mepesi sana. Nitanukuu, naambiwa kwamba kuanzia mwaka 2015 mpaka 2016 ni matukio 128 na mwaka 2016 mpaka 2017 wamepunguza hadi 105, kwa maana hiyo matukio waliyoweza kuyapunguza ni 23 tu. Hatuoni kwamba itachukua muda mrefu sana mpaka kuhakikisha kwamba tatizo la tembo hapa Tanzania kwa ujumla litakuwa bado ni tatizo kubwa sana kwa wananchi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine, hawa tembo zamani wananchi walikuwa wanajichukulia wenyewe hatua mikononi na tembo hawa walikuwa hawasumbui wananchi. Lakini kwa sababu Serikali imeona kwamba tembo ni wa thamani kuliko binadamu, na ukiua tembo ni shida unafungwa miaka mingi, na tembo akiua binadamu ni halali. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri aje na majibu mazuri kwa wananchi wa Mkoa wa Mara, je, warudi kule kule wajichukulie hatua mkononi? Kwa sababu ile nyama ya tembo inaliwa na wanasema kwamba aidha…
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, ni kweli kwamba uvamizi wa tembo katika maeneo ya wananchi ni changamoto kubwa katika maeneo ya Bunda, Tarime na Serengeti. Hata hivyo Serikali inachukua kila aina ya hatua kuhakikisha kwamba inapambana na kuzuia hali hii, na orodha ya hatua ambazo zimechukuliwa nimezitaja. Pamoja na hayo, tunaendelea na utafiti wa kuweza kutambua njia nyingine bora zaidi za kukabiliana na jambo hili. Na Mheshimiwa Mbunge atakuwa ni shahidi kwamba wafanyakazi wetu pamoja na wafanyakazi wa Halmashauri wanafanya juhudi kubwa sana ya kusaidia wananchi katika jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, si kweli kabisa kwamba tembo ni bora kuliko wananchi. Lakini ni jambo lisilopingika kwamba wanyamapori ni rasilimali kubwa yetu sisi sote kama wananchi wa Tanzania na tunawashukuru sana wananchi wa Mara kwa juhudi kubwa ambazo wanafanya kusaidia nchi nzima katika kuwahifadhi wanyama hawa.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mweyekiti, ahsante. Nasikitika sana kwa majibu ya Waziri ambayo yamekuwa ni hayo hayo yakijirudia. Tumeona wenzetu wa Kahama na Shinyanga wananufaika kwa kiasi kikubwa sana na mradi huu wa maji kutoka Ziwa Victoria. Ni kwa nini Serikali imeviacha vijiji hivi ambavyo viko karibu kabisa na Ziwa Victoria kuvipatia maji muda mrefu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi la usanifu limekuwa likichukua muda mrefu sana kabla miradi kuanza kutekelezwa. Je, ni lini usanifu wa mradi huu utakamilika? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu concern ya Mheshimiwa Mbunge kwa changamoto hii ya maji na ame-compare na mradi wa maji unaokuja Kahama sasa hivi unakwenda Tabora mpaka Sikonge. Ni kweli, katika nchi yetu na maeneo mbalimbali kuna changamoto ya maji lakini siyo kwamba watu wa vijiji vile wamesahaulika ndiyo maana katika jibu langu nilizungumzia mpango wa maji katika Ziwa Victoria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipofika Musoma jambo ambalo tulielekezana na wataalam ni kwamba siyo vyema watu wa mji kwa mfano ukianzia hapa Bunda mpaka unafika kule Musoma ambako ukiangalia wana utajiri mkubwa wa Ziwa Victoria halafu wakaendelea kupata shida ya maji. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika Programu ya Uendelezaji wa Sekta ya Maji Awamu ya Pili ni commitment ya Serikali katika kipindi hiki cha miaka hii, tutahakikisha usanifu unakamilika lakini siyo usanifu peke yake bali mradi mkubwa huu wa maji lengo ni kuwasaidia wananchi wa eneo lile kwa sababu wakikosa maji hata huduma za uchumi zinakwama.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kupata nafasi hii. Napenda tu kumuuliza Mheshimiwa Waziri ni lini Kituo cha Bunda Mjini kitapewa hadhi ya hospitali ya Wilaya?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS – TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mchakato wa kupandisha kituo cha afya kuwa hospitali ni utaratibu. Mchakato huo unaanzia katika Halmashauri kwenye Baraza la Madiwani linafanya hivyo and then inaenda DCC, RCC, baadaye inafika kwa Waziri mwenye dhamana wa sekta ya afya; atakapoona kwamba kituo hiki kimekidhi na inafaa kufanya hivyo, basi atafanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani kama mchakato huo umeshaanza basi, jukumu hilo litakuwa chini ya Ofisi ya Waziri wa Afya, atakapoona kwamba vigezo vimekamilika na inabidi kufanya hivyo basi atafanya hivyo bila tatizo. (Makofi)
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli inasikitisha kwa Mheshimiwa Naibu Waziri kuleta majibu ambayo hayaridhishi.
Kwanza ni uongo, kokolo la milimita 10 linavua dagaa na wale sangara wadogo ina maana kwamba unapowavua unaenda kuwatupa? Naomba muwe mnakaa mnaleta majibu ambayo ni ya uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakwenda kwenye maswali yangu ya kimsingi. Ziwa Victoria kuna samaki ambao nature yao ni wadogo, kwa mfano furu, gogogo pamoja nembe. Wizara inatenganisha vipi uvuvi huu wa samaki wa aina ya gogogo na sangara? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Ziwa Victoria linatumika na nchi tatu ambayo ni Kenya, Uganda na Tanzania yenyewe; na ndani ya ziwa hakuna ukuta ambao utatenganisha samaki kutoka Tanzania kwenda Uganda au kwenda Kenya, je, Serikali inafahamu kwamba wavuvi wa Tanzania wanapata shida kulinganisha kuliko wavuvi wa Kenya na Uganda? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza nataka nimthibitishie kwamba nyavu za kuvua dagaa za milimita nane zipo kwa mujibu wa Sheria Namba 22 ya mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2009 kanuni namba 58 (1) (a)ukienda kusoma utakuta pale size ya milimita nane kwa ajili ya dagaa wa maji baridi na milimita 10 section hiyo hiyo 58 (1)(b) utakwenda kukuta kwa ajili ya milimita 10 zile za baharini, kwa hivyo si uongo ni mambo ya ukweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa upande wa sangara wadogo anaowazungumzia, ni kweli nyavu hizi za milimita nane zitakapokwenda katika ziwa hazitachagua, tunafahamu hilo jambo. Kwa vyovyote vile sangara wadogowadogo ama sato watavuliwa na hiyo kwa kitaalamu tunaita bycatch kwa maana ya kwamba wale ambao hatukuwatarajia kanuni zetu na sheria zetu ziko wazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mvuvi wa dagaa kama atakwenda kuvua kilo 100 atayoipata kwa ajili ya dagaa kwa vyovyote vile anaweza pia kwenda kupata kiasi cha kuanzia kilo moja hadi kilo 10 ya samaki ambao hawakutarajiwa na hivyo tunafahamu jambo la namna hiyo wala sio jambo geni kwamba samaki anaweza akaenda akanaswa katika mtego ambao si wa kwake.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la lake la pili sasa Mheshimiwa Sokombi ni kuhusuiana na jambo la kuwatesa wavuvi wetu wa Tanzania na wavuvi wa nchi jirani, kwa maana Ziwa Victoria hili ni mali ya nchi tatu sisi Waganda na Wakenya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nilihakikishie Bunge lako kwamba tayari nchi ambazo tuna-share nao Ziwa Victoria wametuletea maombi, na mijadala inaendelea ya kuweza kushirikiana katika ulinzi shirikishi wa Ziwa letu Victoria na module ambayo wao inawavutia sana ni module hii ambayo sisi Watanzania tunaitumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli samaki kama sangara ni samaki wanaosafiri umbali mrefu, lakini nataka nikuhakikishie bado fursa kubwa ya uvuvi katika Ziwa Victoria kwa upande wa Tanzania ambao ndio tunamiliki sehemu kubwa ipo kubwa na wavuvi wamekuwa wakinufaika na sisi wenyewe kama nchi tumekuwa tukinufaika.
Naomba Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote kwa ujumla wake wajue kwamba Ziwa Victoria hili ni mali yetu, ni mgodi wetu, tuulinde kwa ajili ya kizazi chetu cha leo na kizazi kijacho. (Makofi)
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nashukuru pia kupata swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mara umezungukwa na Ziwa Victoria lakini cha ajabu Ziwa hilo hilo lime-supply maji kutoka Ziwa Victoria kuja Shinyanga, Tabora na Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mara hasa Musoma Vijijini na Wilaya ya Bunda haina maji. Je, Mheshimiwa Waziri ni lini Wilaya hizo zitapata maji? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mara ukianzia na Mji wa Mara tumechukua maji kutoka Ziwa Victoria pamoja na vijiji vyote vinavyozunguka ule Mji wa Musoma kwahiyo siyo kwamba hakuna mahali tumechukua maji kutoka kwenye Ziwa Victoria. Pia katika maeneo mengine, unajua hatuwezi kusema tutapeleka maji ya Ziwa kupeleka kila Kijiji katika mradi huu wa WSDP tulikubaliana kwamba ili tuweze kufika maeneo mengi lazima tutafute teknolojia ambayo ni rahisi ili kila Kijiji kiweze kupata maji kwa haraka na ndiyo maana tulianza na concept ya visima. Sasa baada ya kuona kwamba visima maeneo mengine havijakuwa endelevu ndiyo tumeanza kurudi sasa kubuni miradi mikubwa zaidi ambayo teknolojia Wananchi hawawezi kuendesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichukua maji kwenye bahari au kwenye ziwa utahitaji umeme mkubwa, mitambo mikubwa na wananchi hawawezi kuendesha na ndiyo maana sasa tunafikiria kwamba katika awamu inayokuja hii awamu ya tano ili tuwe na uhakika kwamba miradi yetu inakua endelevu tunataka tusimamie chini ya Wakala wa Maji Vijijini, hawa watakuwa na mfumo unaokuwa ni sahihi kwa nchi nzima kuliko sasa kila Halmashauri, unakuta Halmashauri nyingine umewapelekea fedha mpaka inafika mwezi Juni hawajafanya kitu chochote, fedha wanazo lakini hawafanyi chochote sasa nataka tuingize kwenye Wakala wa Maji ambao watasimamia ujengaji wa hii miradi, halafu hawa TAMISEMI, hizi Halmashauri zitakuwa zinaendesha pale ambapo wanaweza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichukua kwa mfano Nansio, tumejenga mradi mkubwa wa maji, Halmashauri haiwezi kuendesha kwahiyo imebidi Wizara tuendelee kuendesha kwahiyo maeneo mengine tutafanya hivyo. Ukichukua mradi mkubwa kutoka kwenye mto ni lazima pia uendeshaji wake uwe sasa chini ya Wizara maana yake Halmashauri haziwezi kuendesha kwahiyo hili jambo tutalifanyia kazi…
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Imekuwa ni kawaida sana kwa migodi mingi na makampuni mengi kukaa na wafanyakazi bila kuwaajiri. Mheshimiwa Waziri umejibu kwamba wale wafanyakazi wameajiriwa, si kweli, wale wafanyakazi hawajaajiriwa. Hii inapelekea wafanyakazi wengi kukosa stahiki zao. Kwa hiyo basi, je, Serikali itaweka mkakati gani madhubuti wa kuhakiki migodi yote na makampuni yote kuhakikisha wafanyakazi hawa wamelipwa stahiki zao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Sheria ya Ajira na kanuni zake ya 2003 inasema kwamba; mfanyakazi yeyote anapokuwa anafanya kazi sehemu yoyote kwa muda wa miezi sita anatakiwa aajiriwe na apewe haki zake za kimsingi.
Sasa swali langu linakuja, ni kwamba, Serikali haioni inapoteza mapato kwa kutowaajiri wafanyakazi hao kwa kuwafanya vibarua muda mrefu. Kwa nini Serikali isiingilie kati kuhakikisha wafanyakazi wa migodi wanapata haki zao za kimsingi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA, NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anasema si kweli kwamba wafanyakazi hao wameajiriwa. Nitamuomba tu Mheshimiwa Mbunge kama anayo taarifa nyingine tofauti atuwasilishie, lakini tarehe 28/4/2018 wakaguzi kutoka Ofisi ya Idara ya Kazi walikwenda kufanya ukaguzi katika Kampuni ya ACACIA na wakagundua idadi ya wafanyakazi na walio na mikataba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama kuna taarifa tofauti Mheshimiwa Mbunge anaweza kutuwasilishia katika ofisi yetu ili tuweze kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni kuhusu lini tutafanya uhakiki katika migodi. Idara ya Kazi mara zote imekuwa ikifanya kaguzi mbalimbali kuhakikisha kwamba waajiri wote nchi wanafuata sheria ya ajira na mahusiano kazini sheria Namba 6 ya mwaka 2004. Ni kazi yetu kama Serikali kuhakikisha kwamba work places zote hizi tunazitembelea…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuiuliza Serikali; ni lini itajenga barabara itokayo Bunda kwenda Musoma Vijijini ili wananchi wa Kangetutya, Saragana, Bugoji na Kandelema wafaidike kwa sababu wakulima wanapolima mazao yao wanapata shida sana kusafiri kutoka Musoma Vijijini kwenda Bunda? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
M NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba barabara zote kubwa zinajengwa; na nimepata fursa ya kwenda Mkoa wa Mara kuna kipande tumeanza kwa ajili ya kujenga daraja pale na yeye mwenyewe ni shuhuda kama atakuwa amepata nafasi ya kwenda hivi karibuni. Naomba nimhakikishie, Serikali ya Awamu ya Tano, suala la miundombinu ni kipaumbele chetu. Avute subira, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba barabara zote zinajengwa.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo la Kilolo halina tofauti na tatizo lililoko katika Mkoa wa Mara. Mkoa wa Mara tuna chanzo cha maji Ziwa Victoria lakini ni Mkoa ambao unaongoza kwa shida ya maji. Wananchi wale wanaenda kuchota maji kwenye Ziwa. Ni lini Serikali itatatua tatizo hili ili wananchi wa Mkoa wa Mara wapate maji safi na salama? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpe taarifa; tayari Mji wa Musoma tumekamilisha Mradi Mkubwa wa Maji ambao unatoa lita milioni thelathini na sita kwa siku na sasa hivi tunafanya kazi ya usambazaji. Vile vile tunaanza utekelezaji wa Mradi wa Mgango Kyabakari, fedha tumepata, tunaanza utekelezaji mwaka ujao wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu; tunaanza utekelezaji wa Mradi Mkubwa wa Maji Rorya ambao utachukua maji kutoka Ziwa Victoria na Mradi huu utapeleka maji mpaka Tarime na Sirari. Kwa hiyo Serikali ya Chama cha Mapinduzi vyote ilishaviona kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais na eneo la Rorya alilitembelea Mheshimiwa Waziri Mkuu na mimi nikafuatilia. Kwa hiyo mama yangu usiwe na wasiwasi, Serikali ya Chama cha Mapinduzi inapenda watu wake, miradi yote ya maji itatekelezwa.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa Mkoa wa Mara ilionekana kwamba mtoto wa kike hana thamani kwa upande wa elimu. Sasa Serikali imeona kabisa kwamba kuna shida ya mabweni ya watoto wa kike. Mtoto wa kike anapotoka shule kwenda nyumbani anakwenda kufanya kazi za nyumbani na anapotoka tena nyumbani kwenda shuleni ni umbali mrefu anafika amechoka sana.
Kwa nini Serikali isichukue hatua ya haraka kuhakikisha inajenga mabweni katika shule za Mkoa wa Mara? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema ni kweli katika baadhi ya mazingira tunaweka kipaumbele kujenga mabweni kwa mfano katika maeneo ya wafugaji na baadhi ya maeneo katika baadhi ya mikoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya kujenga mabweni kwenye kila shule ya sekondari nchini ni kubwa sana, lakini vilevile katika mazingira ambayo shule imesajiliwa kama shule ya kutwa kwa mazingira yake siyo vizuri sana kuweka mabweni wakati mtoto anaweza akatembea umbali wa kilomita mbili, moja ama mita 500 akafika shuleni. Kwa hiyo, ni jambo ambalo tunaliangalia case by case kwa mazingira na tunahimiza kwamba wazazi, wananchi na Halmashauri zijenge dahania (hostel) ambazo zitasaidia hasa watoto wa kike wasitembee umbali mrefu kwenda nyumbani na shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hicho ndicho kitu tunachohimiza na Serikali itawaunga mkono katika kuendesha yale mabweni. Shule ikipandisha hadhi tu ikapata hadhi ya kuchukua wanafunzi kutoka mikoa mingine, Serikali inaingiza mkono moja kwa moja hapo kusaidia, ahsante. (Makofi)
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Mara kuna tatizo kubwa sana la barabara hasa barabara ya Wanyele – Kitario. Barabara hii imekatika, hakuna mawasiliano. Barabara ile inahitaji kujengewa daraja na barabara hiyo pia ilishaua watoto zaidi ya 20:-

Je, ni lini Serikali itaweka mkakati wa kipaumbele kuhakikisha inajenga daraja na tukichukulia kwamba kipindi cha masika kinakaribia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inao utaratibu wa kutenga fedha kushughulikia maeneo korofi kama hayo ambayo Mheshimiwa Mbunge anayataja. Namwomba tu Mheshimiwa Mbunge, labda tuwasiliane baadaye kwa sababu ni eneo limekuwa mahsusi na kwa wakati huu tuone kama lipo tatizo kwa kupitia utaratibu ambao tupo nao wa kushughulikia maeneo korofi na kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya barabara wakati wote, tuweze kushughulikia eneo hili. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge ili niipate sawasawa tuweze kushughulikia eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kupata nafasi hii. Tatizo lililopo Bukoba ni sawa na tatizo lililopo katika Mkoa wa Mara hasa Jimbo la Bunda Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunda Vijijini tuna Shule za Sekondari 12…

MWENYEKITI: Uliza swali Mheshimiwa.

MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naweka hoja vizuri ili swali lieleweke. Ili mtoto awe na usikivu mzuri darasani, mazingira ya shule zile ni mabaya sana, maboma hayajamaliziwa, kwa hiyo, ili mtoto awe na usikivu darasani ni vizuri kuwe na miundombinu mizuri na mazingira mazuri. Je, ni lini Serikali itahakikisha inajenga na kuzimalizia zile Shule za Sekondari katika Jimbo la Bunda Vijijini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule zetu na ndiyo maana Serikali imeendelea kutenga fedha kwa mabilioni kuhakikisha kwamba tunaondoa changamoto ya miundombinu katika shule zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu katika mwezi wa Januari ilitoa shilingi bilioni 56 kwa shule tofauti 500 nchi nzima. Lengo lake ni kuendelea kupunguza changamoto za miundombinu katika shule hizo. Hata Mkoa wa Mara na Bunda anapotoka Mheshimiwa Mbunge nao wamefaidika na mpango ule wa ujenzi kupitia mradi wa kulipa kulingana na matokeo (EP4R).

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wizara ya TAMISEMI hivi karibuni imetoa fedha kwa ajili ya kumalizia maboma nchi nzima. Naomba Mheshimiwa Mbunge awasiliane na Halmashauri yake kupata taarifa sahihi kwa sababu fedha hizo zimeenda nchi nzima. Kama bado kuna upungufu ni nia ya Serikali kuendelea kukabiliana na changamoto hizo kadiri uwezo wa fedha utakavyoruhusu.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nilitegemea swali hili lingejibiwa na Wizara ya Mifugo na Kilimo lakini limejibiwa na TAMISEMI, kwa vile Serikali ni moja naamini tatizo la Mkoa wa Mara linaenda kutatuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu idadi ya ng’ombe nina mashaka nayo, kutokana na mabadiliko ya tabia nchi wafugaji wengi wageni toka sehemu mbalimbali wanaingia mkoani kwa ajili ya malisho kwa kufuata mbuga. Malisho ni shida sana katika Mkoa wa Mara, Mkoa umeelemewa na ndiyo sababu kubwa sana Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na wakulima na wafugaji kuna mgogoro mkubwa sana. Kwa nini Serikali isione umuhimu wa kuweka sheria ya kuwasaidia wafugaji hawa?

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Serengeti, Tarime, Rorya, Butiama, Bunda na Musoma Vijijini zimesahaulika ndio zenye wafugaji wengi sana na hakuna sehemu za malisho. Je, Serikali haioni umuhimu wa kutoa elimu kwa wafugaji hawa ili wafuge ufugaji wa kisasa ili kuweza kujikwamua katika mahitaji yao ya kila siku?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Joyce Sokombi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namuomba Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi kama alivyosema Serikali ni moja, ulipozungumza habari ya Halmashauri na vijiji unazungumza TAMISEMI lakini pia tunafanya kazi pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha kwamba mambo yanaenda sawasawa. Kwa hiyo, swali lipo sehemu sahihi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la msingi anasema idadi ya ng’ombe ina tatizo, sisi tumejiridhisha kwamba idadi hii ni kamili kwa sababu sensa imefanywa na Serikali na ni data kamili labda kama ana taarifa nyingine tofauti na hizi tutamkaribisha tu-compare notes.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli baada ya kuona kwamba kuna shida kubwa ya malisho na migogoro mingi ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima ameunda timu ya Mawaziri wanane wanaendelea na vikao vyao maeneo mahsusi yamependekezwa na wadau wameshirikishwa, Tarime, Serengeti, Bunda na maeneo mengine nchi nzima yatatengewa maeneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mpango huo kukamilika na taarifa kupewa Mheshimiwa Rais ataona itakavyofaa ili kuruhusu baadhi ya maeneo yawe kwa ajili ya wafugaji na wakulima na tunaamini baada ya zoezi hilo migorogoro ya wakulima na wafugaji itakuwa imefikia ukomo wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili anazungumzia kuhusu kutoa elimu, nimemsikiliza mara kadhaa hapa Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Mpina na Mheshimiwa Ulega wametoa taarifa mara nyingi na mipango mbalimbali na ni kweli kwamba wafugaji wetu wanashauriwa kufuga kwa tija, afuge mifugo michache kulingana na eneo lake lakini yenye manufaa ya kusomesha na kupata kipato. Hiyo kazi inafanywa na Serikali na inaendelea kuleta tija kubwa sana. Ahsante.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa majibu ya Waziri anasema kuna mkakati wa kuanzisha vyumba maalum vya matunzo ya watoto na matibabu, yaani neonatal care units kwa maana hiyo, hivi vyumba havipo. Anawaambiaje Watanzania kwa muda huu atawasaidia vipi akinamama wanaopata matatizo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sio kwamba, huduma za neonatal care hazitolewi. Ni baadhi kwamba, kuna baadhi ya hospitali zina vyumba maalum vya neonatal care units na baadhi ya hospitali hazina, watoto wanawekwa katika wodi moja. Kwa hiyo, katika mkakati ambao tunao sasa hivi ni kuhakikisha kwamba, kila hospitali ya rufaa ya mkoa inakuwa na chumba mahususi kwa ajili ya kutoa huduma kwa watoto wachanga, lakini si kwamba, huduma hizi hazitolewi kwa sasa.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililoko Bunda ni la Mkoa mzima. Tumeona ufunguzi wa REA Phase II na Phase III umefanyika lakini kilichofanywa na wakandarasi ni kwenda kumwaga nguzo tu. Naomba kujua ni lini vijiji vya Kabulabula, Bugoji, Mhoji, Komoge na Kabage vitapata umeme?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Sokombi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Kijiji cha Kabulabula kimeshapelekewa umeme isipokuwa vitongoji viwili kati ya vitongoji vinne. Niseme tu mahali ambapo wamemwaga nguzo siyo kwamba wamemwaga bali wameshakamilisha survey. Kijiji cha Kabulabula vitongoji vitatu vilivyobaki vitaanza kupelekewa umeme kuanzia mwezi Julai, 2019.