Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Joyce Bitta Sokombi (15 total)

MHE. JOYCE B. SOKOMBI aliuliza:-
Ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Musoma kuwa kwenye hadhi ya Kitaifa kama siyo Kimataifa ni wazo la siku nyingi.
(a) Je, ni lini uwanja huo utajengwa katika hadhi stahiki?
(b) Je, Serikali ina mpango gani mahususi wa kuwa na ndege zake ili Mbuga yetu ya Serengeti iweze kufikiwa na watalii kwa urahisi kutoka nje moja kwa moja kuliko kupokea watalii wanaofikia Kenya na kuishi Kenya?
(c) Je, ni kiasi gani cha fedha tunachopoteza kwa kutokuwa na ndege zetu wenyewe kuleta watalii hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI (K.n.y. WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joyce Bitta Sokombi, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikifanya matengenezo ya miundombinu ya Kiwanja cha Ndege cha Musoma ili kiendelee kutoa huduma kama ilivyokusudiwa. Katika mpango wa muda mrefu, Serikali inaendelea na maandalizi ya uboreshaji wa miundombinu ya kiwanja hicho ambapo upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa kutumia fedha za mkopo toka Benki ya Dunia unaendelea.
Mheshimiwa Spika, kazi hii ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina unahusisha pia viwanja vya ndege vya Iringa, Njombe, Songea, Lindi, Kilwa Masoko, Tanga, Moshi, Lake Manyara, Singida na Kiwanja kipya katika Mkoa wa Simiyu ambapo viko katika hatua za mwisho na inatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka huu wa 2015/2016.
(b) Mheshimiwa Spika, mpango mahususi wa Serikali kuimarisha Shirika la Ndege la Tanzania yaani ATCL katika siku za hivi karibuni ni kununua ndege mbili mpya zenye uwezo wa kubeba abiria 78 kila moja ili kuimarisha huduma ya usafiri wa ndege hapa nchini hiyo ikiwa ni pamoja na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika, mpango mwingine ni kununua ndege nyingine mbili mpya zenye uwezo wa kubeba abiria 120 na 155 ambazo zinatarajiwa kufika hapa nchini mwanzoni mwa mwaka 2017 na 2018. Ndege hizo zikifika, zitaliwezesha Shirika la Ndege ATCL kurejesha safari zake za Afrika Kusini, Afrika ya Magharibi, Uarabuni pamoja na India. Idadi hii itafuatiwa na ununuzi wa ndege za ziada katika kuimarisha soko hilo. Hatua ya tatu ni kununua ndege ya masafa marefu kuelekea China, Mashariki ya Mbali, Jumuiya ya Ulaya na kadhalika. Hatua hii itakaribisha pia wawekezaji wa ndani na nje.
Mheshimiwa spika, pia kuchukuliwa kwa hatua hizi kutawawezesha watalii wengi kufika Tanzania moja kwa moja kwa kutumia Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) wakiwemo watalii wa Mbuga ya Wanyama ya Serengeti.
(c) Mheshimiwa Spika, ni vigumu sana suala hili kulitolea takwimu sahihi kwakuwa linahitaji kufanyiwa utafiti wa kina zaidi. Aidha, faida ambazo nchi zenye Mashirika ya Ndege ya Taifa yenye nguvu huzipata ni kuimarika kwa uchumi wa Kimataifa pamoja na kuharakisha maendeleo zaidi. Watalii, wawekezaji na watu wa kawaida hupenda kuwa sehemu ya mataifa yenye usafiri wenye hakika wa ndege, hivyo kujengeka kwa uchumi wa nchi hizo.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI aliuliza:-
Mafuriko na uharibifu wa mazingira umewafanya wahanga wa matukio haya kukosa mahitaji muhimu:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti mafuriko na uharibifu wa mazingira katika Mkoa wa Mara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joyce Bitta Sokombi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imechukua hatua kadhaa za kukabiliana na tatizo la mafuriko na uharibifu wa mazingira Mkoani Mara. Hatua hizo ni kama ifutayo:-
Moja, kuelimisha wananchi kuhusu utunzaji wa hifadhi ya mazingira na madhara yatokanayo na kujenga kwenye mikondo ya maji na mabondeni ili kuepukana na athari za mafuriko na uharibifu wa vyanzo vya maji. Aidha, Kamati ya maafa ya Mkoa wa Mara, huratibu matukio ya maafa yatokanayo na mafuriko pale yanapojitokeza ikiwa ni sehemu mojawapo ya kupambana na athari ya mafuriko katika maeneo husika.
Pili, kubaini na kuwataka wakaazi wote wanaoishi mabondeni waliojenga katika maeneo ya mikondo ya maji, kuhama ili kuepuka athari za mafuriko sambamba na kulinda vyanzo vya maji.
Tatu, kuhimiza kampeni ya upandaji miti nchini, ambapo kila wilaya zikiwemo Wilaya za Mkoa wa Mara zinazopaswa kupanda na kutunza miti isiyopungua 1,500,000 kwa mwaka. Aidha, katika kuimarisha zoezi la upandaji miti nchini, Serikali imeandaa Mkakati wa Kitaifa wa Upandaji Miti wa mwaka 2015 mpaka mwaka 2021, utakaotekelezwa kwa kushirikiana na taasisi za Serikali, mashirika binafsi katika maeneo yote nchini.
Nne, kusimamia na kuendeleza hifadhi ya misitu na kuwaondoa wavamizi wote katika hifadhi za misitu zilizoko Mkoani Mara. Mfano msitu wa Kinyanyali, Kalwilwi, Mrima Mkendo na Kalano, ambapo kaya sita zimeshaondolewa kutoka kwenye msitu wa Kinyang‟ali. Serikali itaendelea kuhimiza wananchi Mkoani Mara na nchini kote kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, kwa kutokujenga na kufanya shughuli zisizo rafiki wa mazingira katika maeneo ya mabondeni na kwenye kingo za mito ndani ya mita 60 ili kuepuka uharibifu wa mazingira na athari zitokanazo na mafuriko.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: aliuliza:-
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara inakabiliwa na Matatizo mbalimbali kama vile uhaba wa magari ya kubebea wagonjwa, uhaba wa vitanda hasa kwenye wodi za akinamama, uhaba wa dawa na kadhalika:-
Je, ni lini Serikali itayashughulikia matatizo hayo ili kuboresha huduma zinazotolewa hospitalini hapo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joyce Bitta Sokombi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, inayo magari mawili ya kubebea wagonjwa ambayo ni STK 8368 na STK 7079. Gari namba STK 7079 lilipata ajali, lakini limeshafanyiwa matengenezo kupitia TEMESA Mkoa wa Mwanza ili liendelee kutoa huduma kwa wagonjwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali hiyo ina jumla ya vitanda 240 kati ya 420 vinavyohitajika. Kwa siku inalaza wagonjwa wanaofikia 169 katika wodi tatu za wazazi zilizopo. Mkoa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, wamepanga kujenga wodi (Postnatal Ward) ambayo itawezesha kuongeza idadi ya vitanda 20 kukidhi mahitaji ya sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya dawa katika hospitali imeongezeka kutoka shilingi milioni 710 kwa mwaka wa fedha 2015/2016 hadi shilingi bilioni1.8 kwa mwaka wa 2016/2017 sawa na ongezeko la asilimia 61. Mkakati wa Serikali hivi sasa ni kuimarisha makusanyo ya mapato ya huduma kwa njia ya kielektroniki ili kuongeza uwezo wa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika hospitali zote nchini.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI aliuliza:-
Barabara ya kutoka Tarime kwenda Serengeti ni barabara muhimu sana kwa wakazi wa Wilaya hizo na kwa maisha yao ya kila siku:-
Je, ni lini barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joyce Bitta Sokombi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Tarime – Serengeti ni barabara inayojulikana kwa jina la Tarime – Nyamwaga - Mugumu yenye urefu wa kilometa 87.14 ambayo inaunganisha Wilaya za Tarime na Serengeti.
Mheshimiwa Spika, barabara ya Tarime – Nyamwaga – Mugumu (Serengeti) ni barabara inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mara. Kwa kuzingatia umuhimu wa barabara hii, Wizara kupitia TANROADS imekuwa ikijenga kwa kiwango cha lami kwa awamu kutokea Tarime Mjini hadi Kibumayi ambapo kilometa saba zimekamilika. Vilevile, katika mteremko wa Nyamwaga kuelekea mgodi wa Nyamongo kilometa 0.6 zimekamilika.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa 2016/2017, ujenzi wa kilometa 2.2 unaendelea katika maeneo ya Kibumayi na mteremko wa Nyamwaga. Aidha, ujenzi wa daraja la Mto Mara lenye urefu wa mita 94 na ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara unganishi ya kilometa 1.8 unakaribia kuanza kwa sababu mkandarasi amekwishapatikana na yupo katika maandalizi ya kuanza ujenzi.
Mheshimiwa Spika, sambamba na ujenzi huo unaoendelea, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara yote yenye urefu wa kilometa 87.14 unaendelea na unatarajiwa kukamilika Septemba, 2018. Hivyo, ujenzi wa barabara hii yote kwa kiwango cha lami unatarajiwa kuanza pindi kazi za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina zitakapokamilika.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI aliuliza:-
Katika Mkoa wa Mara kuna usumbufu mkubwa unaosababishwa na tembo. Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti tembo hao?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joyce Bitta Sokombi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na madhara yanayosababishwa na wanyamapori, hususan tembo, Serikali imechukua hatua mbalimbali ili kunusuru maisha na mali za wananchi waishio kando ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Kwanza, Serikali imeunda timu ya udhibiti wa wanyamapori hatari na waharibifu ambayo inajumuisha watumishi 14 kutoka kikosi dhidi ya ujangili kilichopo Bunda, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Pori la Akiba Ikorongo – Gurumeti, Halmashauri ya Wilaya na Gurumeti Reserves. Lengo ni kuhakikisha kwamba tukio lolote la uvamizi wa tembo linashughulikiwa mara moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuweka minara (observations towers) ambayo askari wanyamapori wanatumia kufuatilia mwenendo wa tembo ili pale wanapotoka nje ya hifadhi, hatua za kuwadhibiti zichukuliwe na tatu, kuweka mizinga ya nyuki pembezoni mwa mashamba ili tembo wanapoingia katika mashamba wafukuzwe na nyuki.
Nne, kutumia ndege zisizokuwa na rubani (unmanned aerial vehicles) kwa ajili ya kufukuza tembo. Mafunzo ya kutumia ndege hizo yametolewa kwa watumishi kwa kushirikiana na Shirika la World Animal Protection.Kwa ajili hiyo, Pori la Ikorongo limepewa ndege moja, Halmashauri ya Serengeti imepewa moja na Kikosi Dhidi ya Ujangili Bunda kimepewa ndege moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, tano, kuendelea kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii ili wananchi waepuke kulima katika shoroba za wanyamapori. Sita, kuendelea kufanya utafiti na kushauri wananchi kulima mazao ambayo hayavutii kuliwa na wanyamapori na saba, kuhamasisha Halmashauri ya Wilaya kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na jitihada hizi, matukio ya uvamizi wa tembo yamepungua kutoka 128 mwaka 2015/2016 hadi 105 katika mwaka 2016/2017. Aidha, katika mwaka 2015/2016, tembo waliweza kufanya uharibifu hadi umbali wa kilometa 30 kutoka kwenye hifadhi, lakini kwa mwaka 2016/2017 umbali huo umepungua hadi kilometa 12 tu.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI aliuliza:-
Kumekuwa na tatizo kubwa la maji katika Wilaya ya Musoma Vijijini hasa vijiji vya Kabulabula, Bugoji, Kangetutya na Saragana. Aidha, visima vilivyochimbwa na wanakijiji hao vinakauka wakati wa kiangazi.
Je, ni lini Serikali itahakikisha programu za maji zinapelekwa na zinatekelezwa kwa umakini katika Wilaya ya Musoma Vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joyce Bita Sokombi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli visima vingi hasa vilivyochimbwa na kufungiwa pampu hukauka wakati wa kiangazi na hivyo kuathiri upatikanaji wa huduma katika maeneo husika. Sababu kubwa ni mabadiliko ya tabianchi hali inayosababisha maji kupatikana katika kina kirefu zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua changamoto hiyo, Serikali kupitia Programu ya Uendelezaji wa Sekta ya Maji (WSDP II) imeanza kufanya usanifu wa mradi mpya utakaotumia Ziwa Victoria kama chanzo cha maji cha uhakika. Vijiji vitakavyoingizwa katika mpango huo ni Kabulabula, Bugoji na Saragana.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI aliuliza:-
Kwenye bahari na maziwa yetu kuna samaki wa aina mbalimbali kama vile dagaa, furu, uduvi au dagaa mchele na wengine ambao ni wadogo sana.
(a) Je, ni nyavu zenye ukubwa wa size gani zinahitajika kwa ajili ya uvuvi wa aina hizo ndogo ndogo za samaki?
(b) Je, Serikali inafanya utaratibu gani wa kuwapatia wavuvi wa nyavu ndogo ndogo za samaki nyavu zinazohitajika kwa uvuvi huo?
(c) Je, elimu ya kutosha kwa nyavu husika imefanyika kwa kiwango gani hasa kwa wavuvi wanozunguka Ziwa Victoria?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joyce Bitta Sokombi lenye sehemu (a), (b) na
(c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kila samaki hunaswa kwa kutumia wavu wa aina yake bila kuathiri samaki wengine. Kwa mfano kulingana na kanuni za uvuvi nyavu za kuvulia dagaa baharini zinapaswa kuwa na macho au matundu yenye ukubwa wa milimita 10 na kwa upande wa dagaa wanaovuliwa ziwani ukubwa wa macho au matundu ya milimita nane. Aidha, dagaa huvuliwa nyakati za usiku kwa kutumia mwanga wa taa za karabai.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuwawezesha wavuvi kupata dhana za uvuvi kwa gharama nafuu ikiwa ni pamoja na kuwaondelea kodi katika dhana na malighafi za uvuvi zikiwemo nyuzi za kushonea nyavu vifungashio na injini za kupachika. Aidha, Serikali inaendelea kuwahimiza wavuvi kujiunga katika vikundi na kuanzisha vyama vya ushirika vya msingi, vyama vya akiba na mikopo (SACCOS) na VICOBA ili waweze kukopesheka na kuweza kununua dhana na vyombo bora vya uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kupitia programu ya utoajiwa ruzuku kwa wavuvi Serikali katika awamu ya kwanza ilinunua engine 73 ambapo hadi sasa engine 49 zimelipiwa na kuchukuliwa vikiwemo vikundi 13 kutoka ukanda wa Ziwa Victoria. Vile vile Serikali imeweka mazingira ya kupata mikopo kwa ajili ya kununua dhana bora za uvuvi kwa kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB).
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuwatumia Maafisa wa Idara ya Uvuvi na BMUs imekuwa ikitoa elimu ya kutosha kuhusiana na matumizi endelevu ya nyavu za uvuvi kwa wavuvi wanaozunguka Ziwa Victoria na katika maeneo mengine nchini. Aidha, viongozi wa mikoa na Wilaya wamekuwa wakiongelea suala hili katika hotuba zao wanapofanya ziara za kuwatembelea wavuvi katika maeneo yao.
MHE. MARWA R. CHACHA (K.n.y. MHE. JOYCE B. SOKOMBI) aliuliza:-
Katika Msimu wa mwaka 2017/2018, wananchi wa Wilaya ya Serengeti na Bunda wanaoishi kandokando ya Mbuga ya Serengeti wameathirika sana kwa mashamba yao kushambuliwa na tembo na hivyo kukumbwa na baa la njaa:-
Je, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kuyafanya maeneo hayo kuwa kipaumbele cha kuwapa msaada wa chakula?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joyce Sokombi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) mnamo mwezi Mei, 2017 ilichukua hatua madhubuti ya kupeleka mahindi kiasi cha tani 400 kwa Wilaya ya Serengeti na tani 253.6 kwa Wilaya ya Bunda na kuyauza kwa bei nafuu kwa wananchi walioathiriwa na ukame pamoja na uharibifu wa mazao uliosababishwa na wanyamapori.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua stahiki na za haraka za kukabiliana na upungufu wa chakula katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo Wilaya ya Serengeti na Bunda. Aidha, Wizara ya Kilimo itashirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kuweka mkakati wa pamoja wa kudhibiti tembo wanaoharibu mazao ya wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa Serikali mnamo mwezi Mei, 2018 kupitia Wizara ya Kilimo ikishirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Ofisi ya Taifa ya Takwimu itafanya tathimini ya awali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa mwaka 2017/2018 na upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2018/2019 (Preliminary Food Crop Production Forecast) katika Wilaya zote nchini ikiwemo Wilaya ya Serengeti na Bunda ili kujua hali ya uzalishaji na upatikanaji wa chakula nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande mwingine Wilaya ya Serengeti na Bunda zimekuwa zikifanya tathmini za athari za uharibifu wa mazao unaosababishwa na tembo mara unapojitokeza ili kubaini ukubwa wa tatizo na idadi ya wakulima walioathirika. Taarifa za tathmini hizo huwasilishwa Wizara ya Maliasili na Utalii ambapo wakulima waliobainika kuathiriwa hulipwa kifuta jasho.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mengine matokeo ya tathmini hii yataainisha Wilaya zenye viashiria vinavyopelekea uwepo wa upungufu wa chakula kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya uharibifu wa mazao unaosababishwa na wanyampori.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa upatikanaji wa chakula katika maeneo yatakayobainishwa kuwa na viashiria vya upungufu wa chakula na kuchukua hatua stahiki ikiwamo ya kufanya tathmini ya kina ya chakula na lishe (Comprehensive Food and Nutrition Security Vulnerability Assessment).
Mheshimiwa Naibu Spika, tathmini ya kina itaainisha hali halisi ya upatikanaji wa chakula, idadi ya watu walioathirika, viwango vya athari, kipindi cha athari, sababu zilizosababisha na hatua stahiki za kuchukuliwa na Serikali na wadau wengine katika kipindi cha muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu. Lengo ni kuhakikisha uwepo wa hali endelevu na ya utengemano wa hali ya usalama wa chakula na lishe nchini.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI aliuliza:-
Wafanyakazi katika Mgodi wa Nyamongo hawalipwi mshahara bali posho tu.
(i) Je, Serikali inasema nini juu ya wafanyakazi hao?
(ii) Je, kwa nini wafanyakazi hao hawalipwi mishahara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA, NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joyce Bitta Sokombi, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mgodi wa Dhahabu wa Nyamongo unamilikiwa na Kampuni ya ACACIA. Kwenye mgodi huo kuna makundi ya aina mbili ya wafanyakazi. Kwanza, kuna wafanyakazi walioajiriwa na Kampuni ya ACACIA na pili kuna wafanyakazi walioajiriwa na makampuni yanayopewa kazi na ACACIA (Sub-Contractors).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wafanyakazi walioajiriwa na ACACIA wao hawalipwi posho bali hulipwa mishahara kwa mwezi. Kwa wafanyakazi walioajiriwa na makampuni mengine (Sub-Contractors) wao hulipwa mishahara kwa kuzingatia aina ya mkataba wa ajira na asili ya kazi anayofanya mfanyakazi kwa kuzingatia sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ofisi yangu kupitia Idara ya Kazi itaendelea kufanya kaguzi za kazi katika maeneo mbalimbali ya kazi nchini ikiwemo Kampuni ya ACACIA kwa lengo la kuwatambua waajiri ambao hawazingatii matakwa ya sheria za kazi.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI (K.n.y. MHE. JOYCE B. SOKOMBI) aliuliza:-
Zao la pamba ambalo lililimwa kwa wingi Mkoani Mara na pia ilisaidia sana kuwainua wananchi kimapato.
Je, Serikali inachukua hatua gani za kimkakati za kulifufua zao hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge na kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joyce Bitta Sokombi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa zao la pamba kwa uchumi wa taifa na wakulima wa pamba nchini. Kutokana na umuhimu huo Serikali imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali inayolenga kuongeza uzalishaji, tija, ubora na masoko ya uhakika kwa kuimarisha usimamizi katika mnyororo wa thamani wa zao hilo ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi. Aidha, huduma za ugani, upatikanaji wa pembejeo na mifumo ya masoko imeendelea kuboreshwa ili kuwanufaisha wakulima wa pamba nchini.
Mheshimiwa Spika, mikakati hiyo ni pamoja na kurahisisha upatikanaji wa pembejeo ambapo katika msimu wa 2018/2019 wakulima watapatiwa pembejeo kupitia Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS), kuimarisha huduma za ugani ambapo wakuli wawezeshi (leader farmers) wapatao 4,532 wawili kutoka kila kijiji kinacholima pamba katika Kanda ya Magharibi wameainishwa na kupewa mafunzo ya kanuni za kilimo bora cha pamba ili wafikishe huduma za ugani kwa wakulima wenzao kikamilifu.
Mheshimiwa Spika, mikakati mingine kuongeza matumizi ya dhana za kilimo ambapo takribani vyama vya ushirika zaidi ya 300 vitapatiwa mikopo ya matrekta kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo. Kueneza teknolojia ya kilimo, hifadhi ardhi katika maeneo yanalima pamba nchini na kuboresha mfumo wa masoko ya pamba kwa kuimarisha Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) ili viweze kunua pamba inayozalishwa na wakulima na hivyo kuimarisha ubora na usafi wa pamba.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeanza kurekebisha mfumo wa uzalishaji wa mbegu bora za pamba kwa kufuata vigezo vyote vya ubora kwa mujibu wa Sheria ya Mbegu Na. 18 ya mwaka 2003. Aidha, juhudi zinazofanyika sasa ni kuzalisha kwa wingi mbegu ya aina ya UKM08 chini ya uratibu wa Kituo cha Utafiti cha Ukiriguru Mwanza kwa kushirikiana na sekta binafsi na Bodi ya Pamba. Vilevile aina mbili za mbegu mpya za UK171 na UK173 zitaanza kupatikana kwa wakulima kuanzia msimu wa 2018/2019.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI aliuliza:-

Mara ni mkoa ambao una makundi makubwa ya jamii ya wafugaji, wakulima na wavuvi lakini kwa sasa kuna shida kubwa ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji:-

Je, ni lini wafugaji watapatiwa eneo kwa ajili ya kuendesha shughuli zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joyce Bitta Sokombi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Mara unakadiriwa kuwa na ng’ombe 1,305,075, mbuzi 733,321, kondoo 437,387,
nguruwe 5,802, punda 11,757 na kuku 1,524,653. Upande wa Nyanda za Juu katika Wilaya za Serengeti, Tarime, Rorya, Butiama na Bunda ndizo zenye ufugaji mkubwa wa mifugo ambapo Wilaya za Musoma, Rorya na Bunda kwa kiasi kikubwa zinashughulika na uvuvi hasa kwenye vijiji vya mwambao wa Ziwa Viktoria.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Mara kupitia Halmashauri 9 umeshatenga maeneo yenye jumla ya ukubwa wa hekta 15,588.55 kwa ajili ya malisho ya mifugo kupitia mpango wa matumizi ya ardhi ya vijiji. Mkoa kupitia Halmashauri utaendelea kutekeleza mpango wa matumizi ya ardhi kwa vijiji ili kuainisha matumizi ya ardhi kwa makundi mbalimbali wakiwemo wafugaji na wakulima ili kuepusha migogoro. Ahsante.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itawalipa fedha zao wananchi wa Musoma ambao maeneo yao yapo pembezoni mwa Uwanja wa Musoma na wameshafanyiwa tathmini ili kupisha upanuzi wa ujenzi wa uwanja huo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Joyce Bitta Sokombi, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Musoma ambao uko katika hatua za awali za manunuzi ili kumpata Mkandarasi. Mchakato wa manunuzi unakwenda sambamba na ulipaji wa fidia kwa wananchi watakaoathirika na mradi huu wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Musoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itahakikisha kwamba, wananchi wanaostahili kulipwa fidia wanalipwa kabla ya kuanza utekelezaji wa mradi huu wa upanuzi wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Musoma.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI aliuliza:-

Kutokana na gharama za pango kuwa kubwa na hivyo kuongeza gharama za uendeshaji kwa Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere kilichopo Mkoani Mara:-

Je, ni lini Serikali itakijengea chuo hicho majengo yake na kuanza kuyatumia rasmi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika,kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayani na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joyce Bitta Sokombi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika,Serikali iliamua kuanzisha Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Mwalimu Julius Nyerere Wilayani Butiama kama sehemu ya kumuenzi Baba wa Taifa ambaye aliamini katika umuhimu wa sekta ya kilimo kama uti wa mgongo katika ustawi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia kimeendelea kufanya shughuli zake kwa muda katika majengo ya Shule ya Sekondari ya Oswald Mang’ombe iliyopo Wilaya ya Butiama.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendeleana ujenzi wa majengo ya chuo (Campus Kuu) ambapo kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ujenzi wa jengo la utawala lenye thamani ya shilingi milioni 200 umefikia asilimia 50. Aidha, katika Mwaka wa Fedha 2019/2020 kiasi cha shilingi bilioni moja kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mingine. Vilevile, Serikali inaendelea na juhudi za kupata fedha zaidi kutoka vyanzo vingine kama vile miradi ya Benki ya Dunia.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI aliuliza:-

Wafanyakazi wa Kiwanda cha MUTEX ambacho kilifungwa tangu mwaka 1984, wamekuja kulipwa stahiki zao Disemba, 2018 na badala ya kulipwa shilingi 400,000/= kwa gharama ya kila mwezi wakalipwa shilingi 100,000 tu:-

Je, Serikali haioni kuwa inawakandamiza wastaafu hao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joyce Bitta Sokombi, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ilisimamisha uzalishaji katika kiwanda cha Nguo cha Musoma (Musoma Textile Mills Limited – MUTEX) mwaka 1994 baada ya kukabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mtaji na ongezeko kubwa la madeni kutoka iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC). Kiwanda cha MUTEX kilifilisiwa na hatimaye kuuzwa mwezi Machi, 1998 kwa Kampuni ya LALAGO Cotton Ginnery and Oil Mills Company Limited.

Mheshimiwa Spika, kikao kati ya wadai, Serikali na Mfilisi kilifanyika Septemba 23, 2005 na kuridhia mapendekezo ya kulipa kiasi cha shilingi 161,347,359 kwa wafanyakazi 935 waliokuwepo kiwandani wakati Serikali ilipofanya uamuzi wa kusitisha uzalishaji. Maamuzi ya kulipa kiasi hicho cha fedha yalizingatia sheria, kanuni na taratibu za ufilisi.

Mheshimiwa Spika, baada ya zoezi la ufilisi kukamilika, wafanyakazi 512 pekee ndiyo waliojitokeza kuchukua mafao yao na wafanyakazi 423 waligoma kupokea mafao yao kwa madai kwamba, nauli ya familia na gharama za kusafirisha mizigo ni ndogo. Wafanyakazi hao 423 walifungua kesi katika Mahakama ya Kazi ya Tanzania, shauri la Uchunguzi wa Mgogoro Na. 49 wa mwaka 2007. Mahakama ilitoa tuzo mnamo tarehe 10 Juni, 2008 na kutupilia mbali shauri hilo na kuamuliwa wadai waende kwa Mfilisi kuchukua stahili zao.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, wafanyakazi hao hawakuridhika na uamuzi wa Mahakama na kufungua shauri lingine la kuomba marejeo katika Mahakama ya Kazi Tanzania shauri la Maombi ya Marejeo Na. 77 la Mwaka 2008. Mahakama hiyo ilitoa tuzo tarehe 15 Februari, 2010 na kutupilia mbali shauri la marejeo. Uamuzi ukabaki kuwa wafanyakazi hao 423 waliogoma kuchukua mafao yao waende kwa Mfilisi kuchukua stahili zao kama ilivyokubalika katika kikao cha wadau.

Mheshimiwa Spika, baada ya Serikali kupokea maombi ya malipo kutoka kwa wafanyakazi hao mwaka 2018, Ofisi ya Msajili wa Hazina ilifanya uhakiki wa wafanyakazi hao ili kujiridhisha na hatimaye kufanya malipo. Awali jumla ya wafanyakazi 219 walijitokeza na wasimamizi wa mirathi 14 na hivyo kulipwa jumla ya shilingi 44,591,559. Ofisi ya Msajili wa Hazina ilifanya tena zoezi la uhakiki mwezi Juni, 2019 kwa wafanyakazi ambao hawakujitokeza kwa uhakiki wa awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katika zoezi hilo, jumla ya wafanyakazi 115 walijitokeza tena pamoja na wasimamizi wa mirathi 27 ambao kwa ujumla wanastahili kulipwa shilingi 20,738,863. Ofisi ya Msajili wa Hazina inaendelea na taratibu za kulipa fedha hizo kwa wahusika katika mwaka huu wa Fedha 2019/2020. Aidha, Serikali inafuatilia kwa karibu malalamiko yote yanayohusu tofauti ya kiwango cha malipo yaliyofanyika hivi karibuni ikilinganishwa na kiwango kilichoidhinishwa kwenye kikao cha pamoja kati ya Mfilisi, wadau pamoja na Serikali kuona kama yana msingi na ukweli wowote.
MHE. ESTHER N. MATIKO (K.n.y MHE. JOYCE B. SOKOMBI) aliuliza:-

Mkoa wa Mara unakabiliwa na changamoto za maji safi na salama kwa muda mrefu hasa katika Jimbo la Musoma Vijijini, Wilaya ya Bunda, Jimbo la Serengeti, Butiama na Rorya licha ya kwamba Mkoa huo umezungukwa na Ziwa Victoria:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha inasambaza mabomba ya maji katika maeneo yenye ukosefu wa maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joyce Bitta Sokombi kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na washirika wa Maendeleo wanatekeleza mradi wa majisafi wa Mugango, Kiabakari na Butiama kwa gharama za dola za Kimarekani milioni 30.69. kwa sasa Serikali inakamilisha taratibu za manunuzi za kumpata mkandarasi na ujenzi unatarajiwa kuanza katika mwaka huu wa fedha 2018/2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa chanzo cha maji kutoka Ziwa Victoria, ujenzi wa mtambo wa kutibu maji, ujenzi wa matanki ya kuhifadhi maji, ujenzi wa ofisi ya mamlaka, ujenzi wa vituo vya kuchotea maji na ujenzi wa mabirika ya kunyweshea mifugo. Mradi huu unatarajiwa kujengwa ndani ya kipindi cha miaka miwili hadi kukamilika na utahudumia watu wapatao 164,924 katika Miji ya Mugango, Kiabakari, Butiama pamoja na vijiji 13 vilivyopo katika halmashauri ya Musoma Vijijini pamoja na Butiama.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Maji ina mpango wa muda mrefu kwa wananchi waishio kwenye vijiji arobaini vilivyopo kandokando ya Ziwa Victoria kwenye Mkoa wa Mara ili kuhakikisha wanapata maji safi na salama. Wizara imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na hatua inayofuata ni kukamilisha usanifu wa kina wa miradi ya maji kwa ajili ya vijiji vyote 40.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali imefanya makubaliano na mtaalam mshauri ya kufanya utafiti na usanifu kuangalia uwezekano wa kuwapatia wananchi wengine zaidi huduma hii muhimu ya maji kutoka Ziwa Victoria.