Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Jesca David Kishoa (16 total)

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa kutoka Benki Kuu inaonesha kwamba kuanzia mwaka 2006 mpaka 2015 takribani miaka kumi kila mwaka nchi imekuwa ikitumia gharama ya takribani wastani wa dola milioni 900 ambayo ni sawa sawa na shilingi trilioni mbili katika fedha hizi zinatumika kwa ajili ya kununulia bidhaa kutoka nje. Katika fedha hizi, fedha dola milioni 120…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Jesca uliza swali.
MHE. JESCA D. KISHOA: Nauliza swali Mheshimiwa Mwenyekiti, dola milioni 120 zinatumika kununulia mafuta ambayo ni sawa na takribani shilingi bilioni 250.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali iliyoko madarakani itawakumbuka wananchi wa Singida ambao wamepuuzwa wametelekezwa, lakini wamesahaulika hata katika hili la mafuta? Ninaomba Waziri aje anipe majibu.
MHE. JESCA D. KISHOA: Ni lini bodi itaundwa kwa ajili ya mafuta?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitambue umuhimu wa maswali haya kwa logic, kwa maana ya kwamba Wizara na Serikali, tukishirikiana na Wizara ya Viwanda, tumedhamiria kwa dhati kabisa kuhakikisha kwamba tunajitegemea kwenye sekta hii ya mafuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Mheshimiwa Mwijage, ameshazindua mkakati ambao utatuondoa katika tatizo hilo. Mheshimiwa Jesca mdogo wangu ambaye tuligombea naye Jimbo moja, wananchi wa Mkoa wa Singida hawajapuuzwa, isipokuwa tunalotaka kufanya kama Serikali na Wabunge wote wanaotokea mikoa hii tuwahamasishe na sisi tulisema kwenye hotuba yetu kila familia iwe angalau na ekari moja ya alizeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Kigoma na Mheshimiwa Jesca amewagusa watu wake wote, kaanzia Singida kwa wazazi wake halafu kaenda swali la michikichi kwa wakwe zake alipoolewa kule na Mheshimiwa Kafulila. Tuwahamasishe, hamasa hii ambayo inatoka kwenye alizeti ambayo Mheshimiwa Allan Kiula, Mheshimiwa Kingu na Mheshimiwa Mlata na Aisharose wanafanya pamoja na akina Mheshimiwa Nkamia na Mheshimiwa Ashatu, tuhamasishe walime alizeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kule Kigoma, kama Mheshimiwa Naibu Waziri alivyojibu ya michikichi 137 kwa kila ekari tuwahamasishe walime, baada ya hapo hatua zitakazofuata za Serikali zitakuwa zile za kisera za kuhakikisha kwamba tuna-discourage mafuta kutoka nje na yatumike yale yanayotoka ndani. Tukianza kwanza kwa ku-discourage mafuta ya nje kabla hatujahamasisha watu kulima kitakachofuata bei zitapanda na watu watakosa hiyo bidhaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili linalohusu bodi na lenyewe sasa hivi alizeti itakuwepo kwenye Bodi ya Mazao Mchanganyiko kwa sababu uzalishaji wake haujawa mkubwa, wananchi hawa tusije tukawawekea mzigo ambao wamekuwa wakibeba wengine kwa ajili ya kuhudumia bodi hizi ile hali wao hawajajitosheleza na kuvutiwa zaidi kwa ajili ya zao hilo.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa mujibu wa jarida la The Citizen la tarehe 23, Oktoba mwaka huu, 2016, imeonyesha kwamba miongoni mwa mikopo iliyokopwa kutoka China mwaka 2015 ni pamoja na Dola za Kimarekani milioni 132 ambazo ni sawa na Shilingi bilioni 300 za Kitanzania kwa ajili ya mradi wa umeme wa upepo Singida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iwaeleze wananchi wa Singida fedha hizi zimekwenda wapi? Kwa sababu mpaka hivi sasa hakuna kinachoendelea, hakuna hata nguzo moja halafu tunaambiwa bado majadiliano yanaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa sababu mazingira kama haya ambapo mikopo inaombwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, lakini fedha zinaelekezwa maeneo yasiyohusika. Ni lini Serikali itaona kuna umuhimu wa kumwagiza CAG akague mikopo inayoagizwa katika nchi hii? Kwa sababu katika deni la Taifa, inawezekana kuna ujanja ujanja unafanyika kwenye suala zima la mikopo. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa mradi wa upepo wa Singida ambao unazalisha Megawatt 100 hautokani na fedha za mkopo, ni wawekezaji binafsi, niweke wazi. Kadhalika, kuhusiana na masharti ya mikopo, ni Makampuni yenyewe yanakopa na kuja kuwekeza kwa ajili ya kufanya biashara na TANESCO inanunua umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la CAG, ni taratibu za Kiserikali. CAG ana utaratibu wa kukagua na Mashirika na ofisi za Serikali zina utaratibu wa kuwasilisha taarifa za kukaguliwa. Tutaendelea kupeleka taarifa kwa mujibu wa CAG ili hesabu zote zikaguliwe. Kwa hiyo, hakuna suala la kuficha kwenye ukaguzi; CAG ana ratiba ya kukagua na Serikali tuna wajibu wa kupeleka takwimu ili zikaguliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea kupeleka takwimu zikaguliwe.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Singida Jimbo la Iramba Magharibi kuna Mradi wa World Bank ambao ulijengwa mwaka 1978 wa matenki ya maji ambayo mpaka leo yamekaa kama sanamu. Naomba Mheshimiwa Waziri aseme ni lini au Serikali ina mkakati gani wa kumalizia mradi huu kwa sababu ni muda mrefu sana?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, tumetoa maelekezo, tumeandaa bajeti ya mwaka uliopita kwamba katika bajeti hiyo tuhakikishe kwamba tunatekeleza miradi ile ambayo bado haijakamilika; na tunaendelea hivyo na mwaka huu pia tumeandaa bajeti. Kwa hiyo katika halmashauri yake kama kuna miradi ambayo ilikuwa haijakamilika basi fedha katika mpango kazi wao wahakikishe kwamba wanaielekeza kwenda kukamilisha miradi ambayo haijakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano anaouzungumzia Mheshimiwa Mbunge nimeukuta Nanyamba ambapo Mheshimiwa Mbunge alinifuata na tukaenda kukaa na halmashauri. Kulikuwa na matenki yamejengwa lakini hayana maji. Sasa hivi Nanyamba tayari wananchi ile fedha ya mwaka jana wameshaitumia vizuri, wameelekeza kwenye miradi ambayo ilikuwa haijakamilika, wananchi wanapata maji. Naomba na Mheshimiwa Mbunge afanye hivyo.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa mikopo isiyolipika (non performing loans) imekuwa kwa kikubwa sana tangu miaka 1990, na sababu kubwa ni mbili, ya kwanza ni mazingira magumu ya biashara na ya pili ni riba kuwa juu.
Swali, ni kwanini, Serikali haioni haja ya kuwasaidia wafanyabiashara kwa kuwapa riba yenye mikopo nafuu kama njia ya stimulus package?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa muda mrefu Serikali yetu imekuwa ikijinadi kuwa yenyewe ni Serikali ya Kijamaa, na misingi na Sera ya Serikali ya Kijamaa ni pamoja na kuwa ukomo wa riba. Je, ni lini Serikali itaweka ukomo wa riba kama ambavyo nchi ya kibepari ya Kenya imeweka ukomo wa riba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, kutokana na mfumo wa mwaka 1991 na Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha, Benki Kuu au Serikali haiwezi kutoa mwelekeo au ukomo wa riba kwa ajili ya benki na taasisi za kifedha. Nchi yetu ni nchi huru inayofuata liberalization of the economy na hilo haliwezi kufanyika kwa sababu nimesema ni sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, nchi ya Kenya iliweka ukomo huo lakini imeingia katika matatizo makubwa ya kiuchumi kwa benki na taasisi za kifedha. Hivyo nchi yetu kama nchi huru inayofuata liberalization of the economy hatuwezi kufanya hivyo kwa sababu ni sheria iliyopanga hivyo.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashindwa kuelewa wananchi wa Mkoa wa Singida tumeikosea nini Serikali hii. Toka miaka ya 1970 uwanja huu ulipojengwa, haujawahi kufanyiwa maintenance ya aina yoyote, uwanja ni pori, hauna fence, imefikia hatua wananchi wameanza kupima viwanja na kujenga nyumba zao. Nataka commitment ya Serikali very seriously, ni lini mnakwenda kujenga uwanja wa ndege Mkoa wa Singida? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa umeme wa upepo Singida umewashinda, treni inayokwenda Singida kwa sasa hivi imeshakufa, ujenzi wa vyuo vikuu Singida umeshawashinda, aiport Singida imeshawashinda. Je, hii ndiyo fadhila mnayowalipa wananchi wa Mkoa wa Singida pamoja na wao kuwa champions kutoa kura kwa Chama cha Mapinduzi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, utakubaliana na mimi kwamba kwa commitment hii Serikali iliyoifanya kwa ajili ya ujenzi wa viwanja mbalimbali kama nilivyojibu katika swali la msingi ni kuonesha namna Serikali hii ilivyo serious kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa viwanja mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii tu kuwaonya wananchi ambao wanakwenda kujichukulia maeneo hayo na kujipimia viwanja, kwa sababu sio sahihi, wanavunja sheria na sheria itachukua nafasi yake. Kwa hiyo, waache uwanja huu wazi ili taratibu zikamilike tujenge uwanja huu, wananchi wa Singida na Watanzania kwa ujumla waweze kupata huduma kupitia uwanja huu.
Swali lake la pili, Serikali haijashindwa, kwa fedha ambazo ziko committed kwa viwanja vyote ambavyo tunaendelea kufanya matengenezo ni kuonesha Serikali ya Awamu ya Tano iko serious. Kuna fedha karibu shilingi trilioni moja imetumika kwa ajili ya marekebisho ya viwanja vikubwa na niwaalike Waheshimiwa Wabunge wanavyopita maeneo kama ya KIA waone matengenezo yanayoendelea, wanavyopita Dar es Salaam waone namna tunavyouboresha uwanja ule na maeneo mengine, wakienda Shinyanga waone shughuli zinavyoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu kwamba Serikali iko serious, hatujashindwa, tunaenda kutengeneza viwanja, tunakwenda kuwahudumia wananchi na Mheshimiwa Kishoa asiwe na wasiwasi.
Suala hili nimuombe tu awe mvumilivu kwa sababu wapo Mheshimiwa Mlata, Mheshimiwa Kingu, wamekuwa wakija kuulizia juu ya uwanja huu kuonesha namna Serikali ya Chama cha Mapinduzi imejipanga kisawasawa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Pamoja na kuwepo kwa changamoto kubwa ya uhaba wa maji katika Mji wa Singida, lakini pia kuna changamoto kubwa ya miundombinu mibovu kwa maana miundombinu yake ni ya muda mrefu sana. Ni lini sasa Serikali itatatua changamoto hii kwa sababu ni ya muda mrefu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunatakiwa kutenga fedha za maintenance. Mnapoleta bajeti Waheshimiwa Wabunge kupitia kwenye Halmashauri zenu kama ambavyo wamefanya watu wa Rungwe, tunatakiwa pia kutenga bajeti kwa ajili ya matengenezo ili hii miundombinu ifike mahali kwamba isichakae kabla hatujafanya ukarabati. Pia sasa hivi kama miundombinu imeshachakaa, basi tunaomba muainishe kwenye Halmashauri mtuletee ili tutenge fedha kwa ajili ya ukarabati.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatumia fedha nyingi sana za kigeni kuagiza chuma kutoka nje kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa reli ya kati.
Je, Serikali haioni haja ya kutumia fedha hizo kununua chuma kutoka Liganga na Mchuchuma badala ya kuendelea kupoteza fedha za kigeni kutoka nje? Na kama alivyoelezea…
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa reli unaoendelea sasa ni kwamba upo katika kuanza, lakini hatua za kujenga kiwanda kwa ajili ya kutegemea chuma cha Liganga ni kazi ambayo inahitaji hatua katika vipindi mbalimbali na chuma kile ni tofauti na vyuma vingine, pale tuna tinanium, tuna vanadium zote ni madini ambazo ni aghali sana na muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachofanyika ni upembuzi yakinifu katika kuwapata wataalam watakaoweza kuifanya kazi hiyo kwa utaalam wa hali ya juu unaowezekana na hivyo lazima tufate taratibu zote. Kwa hiyo, hatuwezi kusimamisha miradi mingine wakati tukisubiri mradi wa Liganga na Mchuchuma.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Tanzania ndiyo nchi ambayo inaongoza kwa viwango vya juu vya kodi ukilinganisha na nchi ya Kenya, Rwanda na Uganda. Serikali ina mkakati gani wa kupunguza viwango hivi kwa sababu vinaathiri sana wafanyabiashara hasa wadogo wadogo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi kodi za forodha ambazo zinatozwa huwa tunafuata mfumo wa kodi wa Afrika Mashariki. Kwa hiyo, si sahihi kusema Tanzania tunaongoza kwa viwango vikubwa vya kodi. Jana tu tumepitisha bajeti kuu ya Serikali, tumeona ni kwa kiwango gani tumeweza kupunguza na kuondoa kodi ambazo zimekuwa ni kero kwa wafanyabiashara wetu hasa wafanyabiashara ndogondogo.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Serikali imekuwa na utaratibu wa kupeleka wanafunzi katika vyuo vya nchi za nje kwa ajili ya kupata utaalam kwenye masuala ya gesi na mafuta. Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba wanafunzi hawa baada ya masomo wanapata ajira kwenye makampuni haya ambayo yanafanya tafiti kwenye Taifa letu ili waweze kuonyesha uwezo wao, experience yao na uzalendo wao katika makampuni ya utafiti? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kujibu swali la nyongeza. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Kishoa linalohusu masuala ya namna gani Serikali imejipanga kutumia utaalam wa vijana ambao wamekuwa wakipelekwa nchi mbalimbali kupata mafunzo katika eneo la mafuta na gesi. Ni kweli kwamba utaratibu huo upo na hata mwaka huu wa fedha unaoendelea tumepokea nafasi 20 kutoka katika nchi ya China kwa ajili ya kupeleka vijana wetu.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa utelekezaji wa miradi ya gesi na mafuta unayoendana na ubia baina ya Taasisi yetu ya TPDC na kampuni hizo ya kimataifa, ni wazi kabisa kwamba mpango wa Serikali ni kuona vijana wale wakihitimu wanafanya kazi katika maeneo haya. Kwa vyovyote vile, kwa kuwa baada ya kuhitimu wanakuwa wamepata teknolojia na wanatosha katika mazingira hayo, wengi wamekuwa wakipata ajira katika kampuni hizi za kimataifa zinazofanya utafiti ndani ya nchi yetu lakini Serikali itaendelea na utaratibu huo. Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Spika, naomba niongeze majibu kidogo kwenye suala hili la msingi sana la kuweza kuwawezesha Watanzania kushiriki katika uchumi unaojengwa kwenye nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika, baada ya kuona kwamba mageuzi makubwa ya kiuchumi yanafanyika na hasa uwepo wa miradi mikubwa ya kimkakati katika nchi yetu, Serikali imefanya kwa makusudi marekebisho ya sheria mbalimbali, lakini vilevile imetunga kanuni mbalimbali za kuhakikisha Watanzania ambao wana uwezo na weledi katika sekta hizo wanapewa kipaumbele cha ajira kwenye maeneo husika.
Mheshimiwa Spika, suala hili limeshafanikiwa, kanuni zimeshatengenezwa kwenye suala la mafuta na gesi na wenzetu wa Wizara ya Madini wameshatengeneza kanuni za kuhakikisha Watanzania wanaajirika kwenye maeneo hayo. Vilevile Ofisi ya Waziri Mkuu inatengeneza sasa mfumo mzuri wa local content wa kuhakikisha bidhaa na huduma za Watanzania zinaweza kutumika na zikashiriki katika ujenzi wa uchumi wetu kupitia miradi mikubwa ya kimkakati katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa barabara hii imechukua muda mrefu sana kukamilika kwa kiwango cha lami, na kwa kuwa tunayo Sheria ya PPP, ili kuacha kuendelea kutegemea zaidi bajeti, kwa nini Serikali imeshindwa kuweka msisitizo kwenye PPP ili kuhakikisha kwamba miradi hii pamoja na miradi ya ujenzi wa barabara inatekelezeka kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jesca Kishoa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifahamishe tu Bunge lako Tukufu kwamba harakati za ujenzi wa barabara hii zimeshaanza, kwa sababu ujenzi wa barabara unaanza kwenye hatua ya usanifu, kupata michoro na tuko kwenye hatua ya kutafuta fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu katika bajeti hii tutakayoanza mwezi wa Julai ya 2018/2019 tumetenga shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kuanza ujenzi. Vilevile yapo mazungumzo ambayo yanaendelea ili kuweza kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua umuhimu wa hii barabara kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, Serikali imetupia macho na kwa kweli imeonyesha commitment ya hali ya juu kuhakikisha kwamba barabara hii inakamilishwa. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Jesca Kishoa pamoja na hii concept ya PPP, tunakaribisha wadau wa PPP kama watajitokeza na kama mradi wao hautakuwa mzigo kwa wananchi Serikali iko tayari kuchukua mawazo yake hayo.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha uhalali wa magawio ambayo tunapewa kutoka kwenye makampuni haya Serikali haioni kama kuna haja ya ku-list share zake kwenye stock market ambako kule wanafanya scrutiny ya hali ya juu pamoja na kuweka hesabu wazi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa maslahi mapana ya umma ni lini Serikali itaona ipo haja ya CAG kupewa mamlaka kisheria ya kuweza kufanya ukaguzi kwenye mashirika na makampuni hayo? (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa maswali mazuri ambayo yanaelezea mpango mbadala wa kuona namna gani CAG anaweza akakagua mashirika haya ambayo Serikali ina hisa chache.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na la kwanza la listing of shares nadhani kuna taratibu tu ambazo huwa tunafanya uchambuzi hata kwa mashirika haya ambayo Serikali ina hisa kubwa tunaangalia namna ambavyo yanaweza yakastahimili kwenye ushindani ule punde watakapokuwa wameshaweka hesabu zao zote zikiwa sawa, kwa sababu kuna implication zingine za viashiria vya performance za mashirika ambavyo vinatumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili la pili la CAG kuweza kukagua hata kwenye maeneo ambayo Serikali ina hisa chache nikiri tu kwamba hilo ni wazo jema na sisi kama Serikali tunaona tunapokwenda huenda kukawa na uhitaji huo kwa sababu utakubaliana na mimi kwamba hata juzi juzi tulibadilisha sheria kuweza kuiruhusu Serikali kuweka guarantee hata katika maeneo ambayo Serikali ina hisa chache, tukiwa tumeenda kwenye uchumi wa kisasa ama kwenye uwekezaji wa kisasa wa maeneo ambayo ni miradi mikubwa kama ilivyo kwenye bomba la mafuta.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo kwenye bomba la mafuta hata kama Serikali ina hisa chache lakini uwekezaji wake ambao Serikali inaweka unaweza ukawa mkubwa kuliko eneo ambalo Serikali ina hisa chache kwa maana hiyo kutakuwepo na justification ya kuona kwamba CAG anaenda kufanya ukaguzi kwenye maeneo ambayo Serikali imeweka uwekezaji na ni uwekezaji mkubwa licha ya kwamba inaweza ikawa na hisa chache.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, kwanza niseme tu kwamba nasikitishwa na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Spika, mradi huu toka mwaka 2016 Mheshimiwa Waziri aliekuwepo alisema 2017 utekelezaji utaanza na utakamilika 2019 leo tunaambiwa mpaka 2027, nataka kujua sababu kubwa ya mradi huu kusuasua na hizi danadana inatokana na nini?

Swali la pili, najua kwamba kulikuwa kuna majadiliano kati ya Serikali na Benki ya Exim ya China kwa ajili ya mkopo wa Dola Milioni 132. Nataka kujua majadiliano haya yamefikia wapi ili mradi huu uweze kutekelezwa na wananchi wa Mkoa wa Singida tumechoka kudanganywa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Jesca kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimetaja miradi mitatu iliyopo katika Mkoa wa Singida sasa sijui alitaka kujua upi kati ya hiyo lakini kwa swali la pili ninaamini alitaka kujua mradi ambao unatekelezwa kati ya Mkandarasi anayeitwa GEO Wind ambaye kwa sasa financier wake ni Green Climate Fund.

Mheshimiwa Spika, miradi hii kama tulivyosema inatekelezwa na wawekezaji binafsi, Serikali tunaweka mazingira ya uwekezaji baada ya hapo yeye anatakiwa atafute mfadhili atakayeweza kumfadhili na kukamilisha eneo lake la uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, mwenzetu wa GEO Wind huyu ni mfadhili wake wa tatu, alienda Exim wakajadiliana lakini hawakukubaliana baadaye akapata mtu mmoja anaitwa Aplonia kutoka Hispania wakajadiliana hawakukubaliana, sasa saa hizi yupo na huyo ambaye tunamuita Green Climate Fund wanaendelea na majadiliano, watakapokamilisha na wakawa tayari kuwekeza upande wetu tumeshakamilisha, tumeshaweka masharti na tuko tayari kumpokea kwa ajili ya uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana tukasema tunatarajia kati ya mwaka 2023 mpaka 2027 miradi hii itakuwa imekamilika baada ya kukamilisha upande wao.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Moja ya changamoto kubwa inayopelekea miradi hii ya REA kutotekelezwa kwa wakati ni pamoja na ukosefu wa nguzo. Nataka kusikia kauli ya Serikali imejipangaje kwa ajili ya kutatua changamoto hii?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa kuna makampuni yasiyo na uaminifu katika kutekeleza miradi hii ya REA jambo ambalo linasababisha kuendelea kuchelewesha utekelezaji wa miradi hii, mfano kampuni ya TONTAN ambayo imetumia zaidi ya bilioni 3.8 kinyume na utaratibu. Nataka kujua kauli ya Serikali imekwishachukua hatua gani mpaka sasa dhidi ya kampuni hii?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la nguzo kwa ajili ya usambazaji wa umeme tunaendelea kuvihamasisha na kuviwezesha viwanda vyetu vya ndani kuhakikisha kwamba vinatosheleza soko. Hata hivyo, ni kwa sababu kazi zimekuwa nyingi na miradi imekuwa mingi na hivyo viwanda vinaonekana kuzidiwa na kazi ambazo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amewezesha zifanyike katika nchi yetu. Hata hivyo, tunajitahidi na viwanda vimekuwa vikizalisha nguzo na kwa sehemu kubwa tatizo huilo limepungua na endapo litakuwa kubwa sana tutahakikisha tunazipata kokote zinakowezekana kupatikana ili hilo tatizo liishe.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali la pili, kuhusiana na wakandarasi ambao wanalegalega katika katika utekelezaji wa kazi zao. Kama ambavyo tumekuwa tukisema tunao wakandarasi wa lot kama saba ambao tumekuwa tukikamatana nao kwa nguvu zaidi kuhakikisha kwamba wanakamilisha kazi zao. Vile vile, tumewekeana malengo na mikakati na muda utakapofika endapo watashindwa kukamilisha, basi tutavunja mikataba hiyo ili tuweze kupata watu wengine wa kukamilisha kazi kwa wakati. Hata hivyo, kwa sasa tunaendelea vema katika ambayo tumeweka utaratibu wa kufuatilia siku kwa siku kwa kuajiri wale vijana wetu ambao tumewapeleka katika maeneo yetu ya majimbo na hivyo tunapata taarifa za mara kwa mara na usimamizi unakuwa wa karibu. Tunaamini kazi zitakamilika kwa wakati.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tunayo Sheria Tanzania Extractive Industry Transparency Initiative Act ya mwaka 2016, Section Number 16 ambayo inataka mikataba yote ya Sekta ya Uziduaji iwekwe wazi na iwekwe wazi kwenye website pamoja na vyombo vya habari media zote Tanzania. Nataka kujua commitment ya Serikali, kwa sababu EITI wanakuja validation Tanzania mwaka huu.

Serikali imejipangaje kuhakikisha kwamba mnalinda reputation ya nchi kwa kuwa na sheria ambayo haitekelezeki kwa muda mrefu toka 2016? (Makofi)

Swali la pili, nataka commitment ya Serikali ni lini suala hili linakwenda kukamilika kwa sababu limekaa kwa muda mrefu sana? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimjibu Mheshimiwa Jesca Kishoa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa swali lake la kwanza, Wizara yetu ya Madini na wakifanya kazi pamoja na TEITI na mamlaka nyingine ya Serikali ikiongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wako katika mchakato ambao unachambua na kufanya kazi kwa kushirikiana na kampuni zote zilizowekeza katika sekta za rasilimali hizi ili kuona namna bora ya kuweka wazi hiyo mikataba kwa mujibu wa matakwa ya Sheria ya Taasisi ya Kimataifa ya EITI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kwamba ni lini? Kwa ratiba tuliyonayo tunategemea kwamba kufika Mwezi wa Kumi mwaka huu taratibu zote zitakuwa zimekamilika na hivyo mikataba hiyo itakuja kuwekwa wazi kwa mujibu wa matakwa ya Taasisi ya Kimataifa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa kwa dhati ya moyo wangu napenda kuchukua fursa hii kuipongeza Serikali kwa nia yake ya kutaka kusitisha Mkataba huu mwaka 2024 ni jambo ambali nimelipigia kelele kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya nyenzo muhimu sana na mahsusi kwa ajili ya kusaidia kutoingia mikataba ambayo haina tija katika Taifa ni pamoja na utekelezaji wa Sheria ya Tanzania ya Extractive Industry ya mwaka 2015 inayotaka mikataba yote ya sekta ya uzidiwaji kuwekwa wazi. Nataka kujua ni kwa nini kumekuwa kuna kusuasua kwa Sheria hii kutekelezeka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Mkataba kati ya Serikali na Kampuni ya Songas ulioingiwa mwaka 2004 ni mkataba ambao unanyima fursa ya nchi ya Tanzania kunufaika na rasilimali kikamilifu. Nataka kujua Serikali imejipangaje mwaka 2024 kwenye mkataba mpya kuhakikisha kwamba hawafanyi makosa yaleyale kwenye eneo ya Investment cost, shareholding structure agreements na pamoja na eneo la capacity charges?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jesca Kishoa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninapokea pongezi alizozitoa kwa Serikali kwa jitihada ambazo zinafanyika pia ninamshukuru kwa kuuliza maswali ya msingi kabisa yenye ufuatiliaji na tija kwa watu wote wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na swali la pili kwamba Serikali imejipangaje. Kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, tayari imeshaundwa timu ya kuanza kupitia mkataba uliopo sasa na kubaini ni wapi tuliteleza na kutibu hayo maeneo ambayo tuliteleza ili yasijitokeze tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, timu zipo nyingi, ipo timu iliyoundwa na TANESCO inaendelea na upitiaji, ipo timu iliyoundwa na Wizara inaendelea na upitiaji, ipo timu iliyoundwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali inaendelea na upitiaji. Kama tulivyosema kwenye swali la msingi mkataba unaisha Julai, 2024 na hii ni Mei, 2022, kwa hiyo tuna miaka miwili kufikia muda wenyewe wa kuisha kwa mkataba. Tunayo imani kwamba tutakuwa tumeshajipanga vizuri na kuona ni kitu gani tutakifanya kuhakikisha kwamba mikataba tutakayoingia itatupa tija sisi kama Taifa na kuhakikisha kwamba nia na azma ya kupeleka umeme kwa wananchi inafikiwa kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la kwanza la msingi la kwamba uwazi unakuwa guaranteed kiasi gani na Serikali. Niseme kama alivyosema kwenye Sheria ya Transparent Initiative ya Extractive Industry na umoja tuliokuwa taasisi tuliyokuwa nayo ya TEIT ambayo inasimamia uwazi na uwajibikaji katika mikataba hii, imekuwa ni shughuli inayoendelea nasi tunaji-subject kule kuweka mambo yetu wazi, kuonyesha wachimbaji au wadau katika eneo hilo wamekusanya pesa kiasi gani, wamepata faida kiasi gani, wamelipa kodi kiasi gani, tunaweka wazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kupitia Bunge hili Kamati za Kudumu za Bunge zimekuwa zikiitisha mikataba hii, zimekuwa ziikitisha value for money areas, zimekuwa zikiitisha Wizara na maeneo mbalimbali kwenda kueleza kwao na kujua namna gani haya mambo yako wazi. Kupitia Bunge hili tunaamini wananchi wote sasa wanakuwa tayari kuona kwamba Serikali inafanya kitu gani kwa uwazi na uwajibikaji kupitia sisi Wabunge ambao tunakuwa kwenye Kamati mbalimbali. Kwa hiyo, niseme hata yeye Mheshimiwa Mbunge yuko na uhuru kupitia kwenye Kamati kuweza kupata taarifa mbalimbali zilizopo katika maeneo hayo. (Makofi)
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona, ni kwa muda mrefu sana wananchi wa Mkoa wa Singida wameelekezwa kupisha maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha ndege Mkoa wa Singida. Nataka kujua ni lini Serikali itaanza uboreshaji na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege Mkoa wa Singida?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Kishoa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli nimemsikia mara kadhaa Mheshimiwa Mbunge akizungumzia suala la Uwanja wa Ndege wa Singida na sisi kama Serikali kupitia Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi tunasema tuainishe eneo la ujenzi wa Uwanja wa Ndege na kufanya tathmini kwa maana ya kujua gharama halisi. Katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 tumetenga bajeti kwa ajili ya kufanya hizo tathmini kwa ajili ya eneo la ujenzi wa uwanja wa ndege hapa Singida.