Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Jesca David Kishoa (27 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa yote, nikishukuru Chama changu kwa yote, lakini pia nimshukuru mume wangu David Kafulila ambaye pamoja na mimi kuwa mama ametambua ninayo nafasi ya kulitumikia Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye mjadala. Tunajadili Mpango, lakini niseme kwamba mipango siyo tatizo katika Taifa, Taifa hili hatuna umaskini wa mipango, ila tuna tatizo la utekelezaji wa mipango. Tumeshakuwa na mipango mingi, ukiangalia kuanzia mwaka 1981 mpaka 1986 tumekuwa na Mpango mwingine kuanzia mwaka 1987 mpaka mwaka 2002, huu ulikuwa ni Mpango wa kumi na miaka mitano ambao ulikuwa umelenga kwamba mpaka kufikia mwaka 2002 Tanzania iwe nchi ambayo itakuwa ina mfumo wa ujamaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukaja kuwa na Mpango mwingine wa miaka 25 kuanzia mwaka 2000 mpaka mwaka 2025 ambao lengo lake lilikuwa ikifika mwaka 2025, Tanzania iwe ni nchi yenye uchumi wa kati na mipango mingine mingi iliyofuata. Hata hivyo, hii mipango haitekelezeki na haitekelezeki kwa sababu kubwa mbili. Sababu ya kwanza, ni mfumo mbovu tulionao katika Taifa hili na sababu ya pili ni ufisadi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia nchi zote ambazo tumeshafatana nazo katika masuala ya maendeleo kuanzia mwaka 1963; Malaysia, Singapore, Korea Kusini, nchi zote hizi mpaka hivi sasa zimeshakuwa wahisani wetu na zimekuwa wahisani wetu kwa sababu mipango yetu inashindwa kutekelezeka. Nimetangulia kwa kusema kwamba sababu kubwa ni mfumo mbovu, lakini pia na ufisadi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo mbovu kwa maana gani? Kwa sababu ya muda nitazungumzia kwenye suala la elimu kwenye suala la mfumo mbovu. Leo hii tunazungumzia elimu bure, ni suala ambalo naamini kabisa kwamba Watanzania na wazazi wote wa nchi hii wamelifurahia, lakini tunazungumzia elimu bure wakati huo huo kuna changamoto nyingi. Nilimsikia Mheshimiwa Waziri anasema hivi bado zimebaki changamoto ndogo ndogo pamoja na elimu bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi changamoto ndogo ndogo zina uhusiano mkubwa na performance ya wanafunzi. Niseme hivi ni bora mngehakikisha mnaondoa hizi changamoto, halafu mkasema elimu bure. Mfano, mwaka 2015, Taasisi ya Haki Elimu ilitoa ripoti ikasema hivi; katika Taifa letu kuna upungufu wa madawati 1,170,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hesabu ya haraka haraka kama kwenye dawati moja wanakaa wanafunzi watatu watatu, inamaanisha Taifa letu kuna wanafunzi milioni tatu na ushee wanakalia mawe, kwenye nchi ambayo ni ya tano kwa idadi ya misitu Afrika nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwanafunzi anakaa kwenye mawe, mwalimu anakuja darasani kufundisha somo la historia, anaandika zama za kale za mawe, anajiuliza hizi ni za kale au ni za sasa? Ningeomba kwanza waelekeze kwenda kutatuta changamoto zilizopo kwenye mashule, halafu wakaja wakatuambia elimu bure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwenye suala la utawala bora, muundo wa suala la utawala bora kwa ujumla. Mfano mzuri ni hapa Zanzibar wala siyo mbali, unapuzungumzia Zanzibar leo hii ni aibu, hivi karibuni nilimsika Donald Champ, mgombea wa Republican Marekani, anasema Afrika wanahitaji miaka 100 kuendelea kutawaliwa kwa sababu hawajajitambua. Mpaka anafikia hatua ya kusema hivyo ni kwa sababu ya mambo kama yanayoendelea Zanzibar, tunadhalilisha Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu, mnaweza mkasema kwamba labda kwa sababu mpo madarakani, lakini ni hivi Marekani wamesema uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa fair and free, Ulaya wakasema uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa fair and free, mtasema aaa! Hao ni wa mbali, SADC hapa Kusini kwetu wamesema uchaguzi wamesema ulikuwa fair and free, AU wamesema ulikuwa fair and free. Tatizo ni nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1992 nikiwa na miaka mitatu, mlianzisha kitu kinaitwa multipartism mkimaanisha mfumo wa vyama vingi ambao mlikubaliana kwamba kila baada ya miaka mitano kutakuwa kuna utaratibu vyama vinagombea mbalimbali kinachochukua nafasi kinashika dola. Sasa niseme tu kwamba, kinachoendelea Zanzibar ni suala la kukosa ustaarabu tu na siyo vinginevyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Rais Mafuguli aweke mkono wake Zanzibar. Nasema hivi kwa sababu gani? Hata awe mzuri kiasi gani Zanzibar akiharibu hawatamwelewa, kuna msemo unasema hivi: “You cannot stand for something you don’t know and likewise it doesn’t matter how much you know about something, if you cannot stand up on it. Kinachoendelea Zanzibar kama Magufuli hataingia, maana yake ni kwamba Wazanzibari hawatamwelewa, maana ingekuwa Kilimanjaro angeingilia halafu ninyi mnahubiri kwamba hii ni nchi moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Magufuli, suala la Zanzibar alitazame kwa jicho la kipekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ufisadi unaturudisha nyuma sana, namwomba Mheshimiwa Magufuli, kwa sababu ninaposema ufisadi namaanisha ni miongoni mwa sababu inayopelekea hii mipango tunayoijadili hapa isitekelezeke. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ufisadi unaoendelea sasa Mheshimiwa Magufuli anatakiwa auone na auangalie kwa ukamilifu kwa sababu huu ni muda sasa amemaliza kutumbua vipele, atumbue majibu makubwa mengine anakaa nayo mezani. Imefika wakati ni lazima tuseme, kwa sababu kinachoendelea katika Taifa hili tukikaa kimya, tutakuwa hatuwatendei haki wananchi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mwaka jana, kuna ripoti ililetwa hapa, tulieni siyo ESCROW, kuna mjadala ulikuja hapa ukiachana na ESCROW, lilikuwa ni suala la mabehewa. Mwaka jana Taifa letu limeingia hasara ya bilioni 238, hizi zilikuwa ni fedha za wananchi ambao zilikwenda kununua mabehewa, matokeo yake, mabehewa yalikuwa fake. Haya siyo maneno yangu, hii ni ripoti PPRA ambayo ilileta ripoti kwenye Kamati ambayo nipo mimi. Mabehewa yanaonekana kwanza ni fake, lakini cha ajabu hata kampuni iliyopewa tenda ni kampuni ambayo haikufanyiwa due diligence kwa maana ya ukaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa limeingia hasara ya bilioni 238 kwa sababu ya mtu tu kuwa mzembe kuwajibika, halafu leo jipu linahamishwa mkono wa kushoto, linapelekwa mkono wa kulia. Mheshimiwa Magufuli alitumbue na jipu hili liko humu ndani, tunaye Mheshimiwa Mwakyembe, leta ripoti hapa, ripoti kuhusiana na masuala ya mabehewa, mlikataa kuileta hapa kwa nini mnaficha, kama ni safi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwakyembe umeaminiwa na Serikali na Magufuli lete ripoti hapa, tusijisahaulishe haya mambo tunayakumbuka tuliona hata tukiwa nje. Tunaomba tutendeeni haki wananchi wa Tanzania kwa sababu Bunge liliazimia ripoti iletwe Bungeni, naomba ripoti iletwe hapa Bungeni na tuweze kuifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na hiyo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuchukua fursa hii kukishukuru Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ngazi ya Kamati Kuu kwa kuniteua kuwa mgombea wa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Baraza la Wanawake upande wa Bara. Pia nitumie nafasi hii kuwashukuru Kamati Tendaji ya Baraza Taifa ambao wamenipa ushindi wa kishindo wa asilimia 84 kwa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu upande wa Bara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie, na nijikite upande wa Wizara ya Nishati. Nitazungumzia upande wa TPDC hoja ambayo kwenye hotuba ya kamati imezungumzwa.

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada ambazo zinaonekana kufanywa na TPDC bado kuna changamoto kubwa ambayo inaendelea kwenye Kampuni hii ya mafuta na gesi ya Taifa hili; na changamoto hii ni kukosa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa. Ni bahati mbaya sana tumekuwa na changamoto kubwa ya viongozi ambao wamekuwa wakitoa kauli za mazoea. Kuna kauli mbili ambazo zimekuwa zikitamkwa na viongozi pale ambapo wanakuwa wanaona joto la wananchi wa Tanzania lipo juu kuhusiana na utekelezaji wa miradi.

Mheshimiwa Spika, moja ya kauli ambayo wamekuwa wakiisema, wamekuwa wakisema kwamba mradi huu haujatekelezeka kwa sababu majadiliano yanaendelea, hiyo ni kauli namba moja. Kauli namba mbili wamekuwa wakisema mradi huu haujatekelezeka kwa sababu majadiliano kuchukua muda mrefu ni jambo la kawaida sana.

Mheshimiwa Spika, naomba niseme jambo moja. Si kawaida kabisa majadiliano kuchukua muda mrefu, this is very primitive thinking, haya ni mawazo mgando, ni lazima tuseme. Nilisoma jarida la The East African la mwaka jana mwezi wa 5 tarehe 15 kuna kampuni moja kubwa sana inaitwa Delloite; kati ya makampuni 4 makubwa, Delloitte ni mojawapo ambayo imeeleza specifically Tanzania imepoteza sifa ya kuwa nchi yenye vivutio vya kuwekeza kwa sababu tu ya kuchelewa (delays), kuwa na mawazo mgando, mawazo ya kujadiliana muda mrefu, majadiliano yasiyokwisha, miradi isiyotekelezeka; tumeingia kwenye rekodi kama taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mradi wa LNG ni moja ya mradi ambao unaonesha namna ambavyo Serikali inashindwa kuchukua maamuzi kwenye mambo mazito na makubwa kwa maslahi ya taifa. Serikali kwenye mradi wa LNG umekuwa ukitoa kauli za mara kwa mara kwamba majadiliano yanaendelea. Ni mwendo wa konokono, kwa maana ya kwamba hakuna kinachoeleweka mpaka dakika hii, miaka na miaka hakuna kinachofanyika, investment ya over 30 billion dollars katika Taifa letu, investment ambayo ni kuwa East Africa nzima hakuna lakini Serikali inashindwa kufanya maamuzi sahihi, wanakimbilia kusema kwamba kuna migogoro kwa wawekezaji.

Mheshimiwa Spika, let me ask you something. Kwa muda gani tunakwenda kusubiri kuona migogoro ya wawekezaji inakwisha, what if kama migogoro yao ikichukua miaka 50? Tunakwenda kuwasubiri kwa muda kwa kiasi gani? Mlitafuta kampuni kwa ajili ya ku-negotiate on behalf of the Government kwenye mradi huu wa LNG kwa sababu ya ukubwa wake. Mmeshindwa kweli kuibana/ku-deal na kampuni hii ikaja na majibu ya uhakika ya namna gani mnavuka /mnakwenda kutekeleza mradi wa LNG kwa kuwepo na huu mgogoro ambao ni wa wawekezaji?

Mheshimiwa Spika, mambo kama haya, mradi mkubwa kama huu ambao unaangaliwa kwenye mataifa mengi ndivyo hivi vitu vinavyo-test credibility ya Serikali katika Taifa letu. Sasa ni vema Serikali ikatuambia kwenye mradi wa LNG, mradi ambao ni mkubwa sana na unakwenda kusaidia wananchi wengi sana katika Taifa letu; kampuni hii imeshindwa kweli kutekeleza/kutusaidia kuvuka hapa na tukahakikisha kwamba tunaweza kutekeleza mradi huu?

Mheshimiwa Spika, bado kuna suala la mwendo wa konokono kwenye mradi wa Bomba la Mafuta la Hoima. Nimemsikiliza Mkurugenzi wa TPDC mwaka jana mwezi wa tisa anasema mradi huu utatekelezeka lakini bado majadiliano yanaendelea; bado tupo palepale mwendo wa konokono, haya majadiliano yanakwenda mpaka lini? Haya majadiliano yanakwenda kwisha lini? Dunia inakwenda speed sana, lazima tu-cope na speed ambayo dunia inakwenda.

Mheshimiwa Spika, kuna mradi wa kiwanda cha mbolea kule Lindi (Fertilizer Plant). Kuna makampuni matatu makubwa kutoka Ujerumani ambayo yameomba kujenga kiwanda cha mbolea Mkoani Lindi na kiwanda hiki kinakwenda kutumia gesi, lakini cha kusikitisha ni kwamba pamoja na kwamba kiwanda hiki kinakwenda kuwa kikubwa Afrika nzima lakini Serikali kupitia TPDC bado inakwenda mwendo wa konokono. Ni vema tukaelewana hapa vizuri sana. Kupitia vyombo vya habari nilishuhudia Mheshimiwa Rais akiongea na Chancellor wa Ujerumani wakizungumza namna gani wanakwenda kutekeleza mradi huu lakini mpaka sasa hivi ni story tupu, hakuna kinachofanyika.

Mheshimiwa Spika, labda nizungumze kidogo kuhusiana na mradi labda mnaweza mkaelewa kuanzia hapo. Kama tunataka ku-transform Taifa hili kwenye sekta ya agriculture, hiki kiwanda hakiepukiki kwa namna yoyote ile. Hakiepukiki kwa sababu wote tunajua kwamba 75 percent ya wananchi wa Tanzania wanashiriki kwenye Sekta ya Kilimo. Serikali imekuwa ikiagiza mbolea kutoka nje; asilimia 90 inayotumika Tanzania inatoka nje.

Mheshimiwa Spika, takwimu za mwaka 2016/2017 zinaonesha Serikali iliagiza tani za mbolea takribani 150,000, lakini kama ikitokea tukakubali mradi huu/kiwanda hiki kikajengwa, tunakwenda kutengeneza tani 1,300,000 za mbolea kwa mwaka. Kwa hesabu za haraka haraka ni kwamba nchi hii ili iweze kupata mbolea ya kutosha inahitaji mbolea zaidi ya tani 580,000, kwa hiyo tukipata tani 1,300,000 tuna uhakika wa kupata mbolea ndani na tuna uhakika wa kuuza mbolea nje, tunasubiri nini? What are waiting for? Hiki kiwanda kinakwenda kutengeneza zaidi ya ajira 500,000 kwa wananchi wa Tanzania lakini shida inabaki palepale, ukiuliza unaambiwa majadiliano bado yanaendelea yaani ni mwendo wa konokono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na mimi nafikiri huu mwendo wa konokono tukawa na jambo moja, unatokana na hofu ya viongozi kwenye sekta husika, wanahofu ya kutumbuliwa. Kumekuwa kuna shida hii kubwa, maamuzi magumu ambayo yanatakiwa yafanywe kwa maslahi ya Taifa, viongozi wa Serikali wameingiwa na hofu wanashindwa kuyafanya kwa kuhofu kutumbuliwa na Mheshimiwa John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kutumia fursa hii kuiomba Serikali iipe nguvu TPDC, TPDC haiwezi kufanya kazi kama hamuwezi kuipatia fedha kwa namna yoyote ile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie na hoja ya TEITI; nilizungumza hapa mwaka jana kwamba na kwenye taarifa ya kamati imezungumzwa. TEITI iligundua kuna ubadhilifu wa zaidi ya bilioni 30 kwenye sekta ya madini; lakini tangu mwaka jana mpaka hivi ninavyozungumza hatujaona taarifa yoyote ambayo inaweza kuelezea na kudadavua suala hili. Nilipozungumza suala hili mwaka jana, Waziri wa Madini wa wakati huo Mheshimiwa Angella Kairuki alisimama na kusema suala hili lipo kwa CAG na litafanyiwa kazi mpaka kufikia mwezi wa 12... (Makofi)

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. JESCA D. KISHOA:… lakini mpaka hivi ninavyozungumza hakuna tatizo…

T A A R I F A

SPIKA: Mheshimiwa Kishoa kuna taarifa unataka upewe.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, nataka nimpe tu taarifa mchangiaji anayechangia sasa kwamba viongozi wa Serikali wakiwemo Mawaziri, Wabunge, RAS pamoja na RAS wa Mkoa wa Songwe Mheshimiwa Kafulila wapo vizuri hawa hofu yoyote na ndio maana nchi yetu ya Tanzania inaendelea kupaa, miradi mbalimbali inaendelea kutekelezwa. Sasa kama anachangia aende kwenye hoja za msingi asizungumzie suala la viongozi wana hofu, wapo vizuri, imara na wanatekeleza majukumu yao ipasavyo, ahsante. (Makofi)

SPIKA: Shemeji umepewa taarifa hiyo, unasemaje? (Kicheko/Makofi)

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, kunaona kuna taarifa kupokea hapo? Kwanza nimuulize TEITI ni kitu gani, do you know what is TEITI, unajua TEITI ni kitu gani? Tunazungumzia issues, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tunazungumzia issues, we are not doing politics here tena cheap politics; tunazungumzia masuala kwa maslahi ya Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka wakati Waziri wa Madini au Waziri wa Nishati, maana TEITI bado haijajulikana iko Wizara gani, anapokuja kuhitimisha hapa atuambie fedha zetu bilioni 30 ambazo zimeonekana zimepotea kwenye Wizara ya Madini zimekwenda wapi, kwa sababu ni taarifa ya kutoka TEITI na TEITI ni shirika la Serikali.

Mheshimiwa Spika…

SPIKA: Ngoja upokee taarifa Mheshimiwa Jesca.

T A A R I F A

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, ili tumsaidie mtoa hoja, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakati anahitimisha hoja yake, awe focused, ninataka tu nimpe taarifa msemaji na kwa kweli Mheshimiwa Angellah Kairuki wakati akiwa Waziri alilieleza vizuri sana; hakuna fedha iliyopotea. TEITI kinachotokea ni kwamba makampuni yanapeleka hesabu na wao wanakwenda kuangalia kule mnakopeleka fedha kwa ajili ya kufanya reconciliation.

Mheshimiwa Spika, kilichotokea ni kwamba yule mtu aliyekwenda kufanya reconciliation alivyokwenda kwenye source akakuta kilichoripotiwa na makampuni na kile kilicholipwa kuna difference ya hizo fedha. Na sasa kinachotokea ni kwamba kuna mahali pengine ambapo wameripoti wamelipa shilingi kumi halafu kuna mahali hiyo shilingi kumi imeripotiwa mara mbili. Kwa hiyo CAG anachokwenda kufanya ni verification ya hiyo reporting, huo sio wizi. Na kwenye ripoti hiyo imeelezwa sio wizi, ni reconciliation. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba kumpa taarifa hiyo.

SPIKA: Mheshimiwa Kishoa, malizia maana yake muda hauko upande wako.

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru sana, napokea taarifa yake kwa sababu amekiri kwamba kuna fedha bilioni 30 hazionekani. Lakini pia kuna shida gani kumpa CAG akakagua hizi bilioni 30 zimekwenda wapi? Kwa nini suala hili limepigwa danadana toka mwaka jana, shida iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nafikiri hakuna sababu ya Waheshimiwa Mawaziri kuendelea kujitetea kwenye hili, ni suala la mambo kuwekwa wazi kuonekana kwamba, okay reconciliation inatakiwa ifanyike; imefanyika? Hizo fedha ambazo zimepotea zimekwenda wapi? Kwa nini maswali haya yanakosa majibu? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante, ni kengele ya pili.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa nashukuru kwa kupata fursa hii kuchangia kwenye hii Wizara ambayo ina uhusiano mkubwa sana na mkoa ambao nauwakilisha kwa maana ya Mkoa wa Singida. Mkoa wa Singida ni miongoni mikoa ambayo inafanya vibaya sana katika suala la taaluma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuendelea, naomba mama yangu, Mheshimiwa Waziri Ndalichako, wakati unakuja kuhitimisha nakuomba uje na majibu ya kwanini Walimu takriban 366 wanaotokea Mkoa wa Singida Wilaya ya Iramba hawajapandishwa madaraja toka mwaka 2013 na wakati katika mkoa huu Wilaya nyingine zote Walimu wao wamepandishwa madaraja, lakini kasoro Wilaya ya Iramba peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wote humu ndani tunatambua kwamba dunia ya sasa ni dunia ya ushindani, silaha pekee kwenye dunia ya ushindani ni elimu; lakini cha kusikitisha ni kwamba elimu inayotolewa katika Taifa letu ni elimu duni kabisa. Ni elimu ambayo haijakidhi vigezo. Nasema hata kwa sababu hapa nina taarifa ya USAID ya mwaka huu ambayo inaonyesha kwamba asilimia 70 ya wanafunzi hawajui kusoma Kiswahili, Shule ya Msingi na wakati huo huo asilimia 90 ya wanafunzi hawajui kusoma Kiingereza. Kwa tafsiri nyingine ya watu, hata kuandika barua ya kuomba kazi hawawezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Vyuo Vikuu vilivyopo katika Taifa letu, kuna baadhi ya Vyuo Vikuu kwa sasa vimeamua kupanua magori kuhakikisha kwamba wanaanza kusajili wanafunzi kutoka Form Four kwa sababu kuna wanafunzi wa Form Six hawajakidhi vigezo kuingia Vyuo Vikuu. Takwimu ya TCU ya mwaka 2015 inaonyesha kwamba kuna nafasi 25,000 zimeshindwa kuwa fulfilled kwa sababu wanafunzi hawajakidhi vigezo vya kwenda University. Hii inasikitisha sana na ni aibu! (Makofi)
Sasa katika kutafakari, nikaangalia, msingi wa haya ni nini? Sababu kubwa, kwanza ni kwa sababu hakuna mkazo kwenye suala la elimu. Hakuna mkazo ambao Serikali imepelekea kwenye suala zima la elimu. Niseme tu, nafikiri hii ni kwa sababu anguko la elimu katika Taifa hili haliwahusu Mawaziri, wala haliwahusu vigogo katika Taifa hili. Ila kwa sababu hiyo hapa we are not talking the same language! Hatuongei lugha moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna msemo mmoja wa Kiswahili unasema hivi: “kilio na mwenyewe.” Katika hali ya kawaida katika cabinet hii, msiba wa elimu, hamna member hapa kwenye cabinet ambayo inamhusu kwa namna yoyote ile. Kwa sababu asilimia kubwa watoto wao wanasoma nje na wengine wanasoma shule za private. (Makofi)
Kwa hiyo, ifike mahali tulitazame hili kwa sura nyingine. Mfano mzuri ni UK. Uingereza, Waziri kumpeleka mtoto wake kusoma shule ya private ni kashfa kubwa sana. Naomba kupitia Bunge hili Tukufu nimwombe Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli atangaze rasmi Mawaziri wote wa Taifa hili, watoto wao wasome shule za government. Wasome shule za Serikali! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye suala la madawati, ni aibu! Eti wanafunzi milioni tatu na nusu, wingi wote huo wa wanafunzi, wanakaa chini. Upungufu wa madawati ni karibia 1,174,000. Ukiangalia gharama zinazoweza madawati haya, siyo chini ya shilingi ya bilioni 90 mpaka 100.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, ni vema wakaona kwamba kuna umuhimu hata suala hilo wakalipeleka kwenye jeshi, jeshi likatutengenezea madawati wakawa wanalipa taratibu; au wakatumia mifuko ya hifadhi kuhakikisha kwamba mifuko ya hifadhi inakopesha wanajeshi halafu Serikali inakuwa inailipa taratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la ukaguzi. Unapozungumzia ukaguzi, ukaguzi una uhusiano mkubwa sana na performance ya mwanafunzi, kwasababu ukaguzi unapelekea kumtambua Mwalimu bora na ubora wa elimu wanayoitoa. Kwa Taifa letu ni aibu!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia Best Education Statistics za mwaka 2015, zinaonesha karibia asilimia 81 ya shule zote za Msingi hazijafanyiwa ukaguzi, lakini wakati huo huo asilimia 76 ya Shule za Sekondari hazijafanyiwa ukaguzi. Halafu mwaka 2015 mkatenga fedha shilingi bilioni 22.4 kwa ajili ya kupeleka kwenye ukaguzi, mkachukua shilingi bilioni 20 mkawalipa wakaguzi kama mshahara, halafu shilingi bilioni 2.4 ikatumika kwa ajili ya ukaguzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni sawasawa na Mbunge hapa amlipe dereva wake mshahara kila mwezi, halafu asiwe anamwendesha, awe anaendesha mwenyewe. Naona huu ni ubadhirifu wa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtu mmoja anaitwa Aristotle aliwahi kusema hivi: “mizizi ya elimu ni michungu, lakini matunda ya elimu ni matamu.” Mimi nabadilisha kwa Taifa letu, “mizizi ya elimu ni michungu na hata matunda ya elimu ni machungu vile vile.” Tafsiri halisi ya elimu ni ili mtu atoe ujinga awe na uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazomzunguka. Kwa Taifa letu, watoto wetu wanakwenda shuleni ili mradi wavae uniform wafanane na wengine. Ni masuala ya aibu, ambayo ni lazima tuyafanyie kazi haraka iwezekananyo, maana tunachekwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, naomba Waziri, mama yangu Mheshimiwa Profesa Ndalichako kama itakupendeza, muda wowote nikupatie majina haya ya Walimu wote ambao wana madai yao kwa ajili ya kuweza kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siungi mkono hoja, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mimi ninakwenda kujikita kwenye eneo moja tu, eneo la utawala bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, wote tunafahamu na tunatambua kwamba utawala bora ndiyo nguzo muhimu sana kwenye mipango yoyote. Ukiangalia kwenye sustainable development goals, utawala bora ni nguzo muhimu. Ukiangalia kwenye Dira ya Taifa, utawala bora ni nguzo muhimu lakini hata ukiangalia kwenye mipango ambayo tunakuwa tunajadiliana humu ndani, haiwezi kutekelezeka kama eneo la utawala bora haliwezi kuwekewa nguvu inayostahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni lazima ili kuweza kuboresha eneo la utawala bora tutafute vichocheo vikubwa ambavyo vinachochea na kuhamasisha utawala bora katika Taifa letu. Katika tafiti zangu ambazo nimekuwa nikizifanya na tafiti mbalimbali ambazo nimekuwa nikizisoma nimegundua kitu ambacho ni very interesting. Nimekuja kuona suala la utawala bora, tafiti nyingi zinaonesha wanawake wana mchango mkubwa sana kwenye good governance na sehemu hii napenda kuchukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa Rais mwanamke wa kwanza katika Taifa letu, lakini kwa kuwa Rais wa kwanza mwanamke East Africa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, rekodi tuliyoiweka kama Taifa, tumeithibitishia dunia ya kwamba Taifa letu hatuna doubt wala dispute ya uwezo na umahiri wa mwanamke katika masuala ya uongozi. Ni ukweli usiopingika kwamba mama ameanza vizuri. Nampongeza na namuunga mkono kwenye jambo ambalo amelizungumzia jana la kuunga jitihada zake za nguvu kabisa kuwapa vipaumbele wanawake. (Makofi)

Mimi nina ombi moja kubwa sana kwa Mheshimiwa Rais, ukisoma Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Ilani ambayo ilitumika kwenye kampeni 2020, ukiangalia ukurasa wa 281 Ibara ya 231(j) inasema hivi; Serikali ya CCM itabaini na kutekeleza mikakati ya kuongeza ushiriki wa wanawake katika maamuzi na uongozi kwenye nyanja za kisiasa na kiuchumi hadi kufikia 50 kwa 50. Na bold hadi kufikia 50 kwa 50.

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna wakati mwingine sahihi ambao kama wanawake wa Taifa hili tunautegemea kama kipindi ambacho mama Samia Suluhu Hassan atakuwa madarakani kwa ajili ya kutekeleza jambo hili. Suala hili tusilitazame katika sura ya kisiasa, suala hili tulitazame katika sura ya usimamizi wa masuala ya kiuchumi na masuala ya utawala bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, wanawake wamepimwa na wamethibitika kuonekana kuwa ni waadilifu na wana uwezo mkubwa sana kusimamia masuala mbalimbali katika Taifa letu. Lakini pia sisi hatutakuwa wa kwanza kufanya hivyo, nimesoma miaka mitano iliyopita Germany, nimeangalia sheria yao na ninayo hapa, Germany wametunga sheria, yaani kwa upande wao hilo suala halina mjadala. Uwakilishi wa wanawake not less than 30 percent kwenye mashirika yote ya umma, pamoja na private sector. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hapa kwetu Tanzania wanawake wameonesha jitihada kubwa sana katika kufanya shughuli zao. Nimesoma taarifa ya utafiti uliofanywa na Tanzania Chamber of Commerce, industry and Agriculture (TCCIA); wanasema hivi, wanawake wa Tanzania ndiyo lion share, I mean ndiyo majority share, I mean ndio wamiliki wakuu wa biashara ndogo ndogo na biashara za kati. Wanawake hawa wanasimamia zaidi ya asilimia 95 ya idadi ya biashara zote Tanzania. Wanachangia zaidi ya asilimia 35 ya uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Naomba nitumie jukwa hili la Bunge lako Tukufu kumuomba Mheshimiwa Rais apambane huko aliko na sisi kama Wabunge kwa nafasi yetu tutamsaidia. Ninaomba kutoa taarifa, ninakusudia kuleta Muswada Binafsi Bungeni wa kutaka not less than 30 percent ya viongozi wa mashirika ya umma wawe wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba taasisi zote zinazo-deal na masuala haya waweze kunisaidia kwa ajili ya kupata information za kuweza ku-package hoja yangu ambayo nitakuja kuleta Muswada Binafsi. Lakini pia niwaombe na Waheshimiwa Wabunge wanaume watuunge mkono sana katika hili. (Makofi)

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Jesca Kishoa kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Engineer Manyanya.

T A A R I F A

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, napenda kumpa taarifa ndogo tu Mheshimiwa Jesca kwamba kwa jinsi ambavyo ameweza kuinukuu Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, kwa jinsi ambavyo ameweza kusikiliza vizuri hotuba ya Mheshimiwa Rais ya jana na kwa jinsi ambavyo anaendelea na mchango wake, kwa kweli naamini kama Kambi ya Upinzani itakuwa inaendelea kutoa michango positive na kuwa pamoja katika timu moja katika Bunge, mambo mengi ambayo tulikuwa tunayapanga yataendelea vizuri. (Makofi)

Kwa hiyo mimi nampongeza kwa positivity, uchanya wake katika mchango huu. Ahsante. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Jesca Kishoa, hiyo sio taarifa. Malizia mchango wako. (Kicheko)

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba niendelee kwenye eneo lingine dogo la transparency. Unapozungumzia utawala bora suala la transparency haliepukiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up anisaidie. Sitaki sana kujua sababu gani iliwafanya mkajiondoa kwenye OGP (Open Government Partnership). Wote tunajua hii Open Government Partnership wakati mmejiunga mwaka 2011 na bahati mbaya au nzuri sijajua ni kwa kusudi gani mkaja mkajitoa, mmepeleka barua yenu kule kwenye committee tarehe 29 Juni, 2017. Mmetaka kujiondoa na mmejiondoa kwenye umoja huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la sisi kujiunga kwenye Open Government Partnership lilikuwa linawasaidia sana watafiti wa Taifa hili, lilikuwa linawasaidia sana NGO’s, wasomi wa Taifa hili. Walikuwa wana uwezo wa kupata taarifa mbalimbali ambazo wanazihitaji kwa ajili ya kusaidia hata katika masuala haya ya kujadili bajeti, tulikuwa tuna uwezo wa kupata references ambazo zimefanywa na researchers, lakini pia hata wanafunzi wetu ambao wako shuleni OGP imekuwa ikiwasaidia sana wao kupata taarifa na kuwasaidia katika masuala yao mbalimbali ya kitaaluma.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Rais hebu turudi kwenye OGP, kuna tetesi ambazo nimezisikia kwamba mmejiondoa kwenye Open Governance Partnership kwa sababu kuna namna nyingine mmetafuta ya kutaka kutoa information zenu kupitia umoja fulani ambao uko Afrika, lakini it’s kind of kutaka kufunika funika vitu hivi. Mimi ninaomba sana Serikali, turudi kwenye OGP. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie na suala la uhuru wa vyama vya siasa. Katika Taifa letu mara nyingi sana tumekuwa tukishuhudia vyama vya siasa hususan vyama vya upinzani vimekuwa vikikosa fursa ya kufanya mikusanyiko ambayo kikatiba ipo kihalali kabisa.

Ninataka nimuombe Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Rais katika suala hili hebu rekebisheni hapa. Hivi vyama vina haki kabisa ya kikatiba ya kufanya mikutano ya hadhara. Vina haki ya kikatiba ya kukutana na wananchi na kueleza sera zao. (Makofi)

MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Jesca Kishoa kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete.

T A A R I F A

MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu muongeaji asipotoshe, Mheshimiwa Rais jana amezungumza, anataka kukutana na vyama vyote vya siasa, wazungumze waone nini sasa wanaweza wakaendesha nchi yao pamoja. Haya masuala ya kwamba sijui vyama vimezuiwa kupiga nini, sijui kufanya mikutano, yanatokea wapi? Naomba nitoe Taarifa. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Jesca Kishoa.

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nasikitika sana kusema kwamba sijajua kama Mheshimiwa Mbunge ni kweli hafahamu au laa! Suala la kufanya mikutano ya siasa sio suala la Mheshimiwa Rais kutuambia, ni suala la Kikatiba ambalo linatakiwa lifanyike katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii tukianza kuiendesha kwa matamko na sio kwa kufuata misingi ya Kikatiba tutapotea. Ni muhimu sana ili Serikali iweze kuwa ni Serikali ambayo inazingatia utawala bora basi itoe fursa kwa vyama vya kisiasa kufanya mikutano yao.

WABUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, kwa muda tulionao hiyo itakuwa Taarifa ya mwisho.

T A A R I F A

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Musukuma, taarifa inatokea upande ule. Mheshimiwa jitambulishe.

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naitwa Francis Isack Mtinga.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe Taarifa mzungumzaji kwamba nchi yetu haijawahi kuzuia mikutano ya vyama, kilichokuwa kinatakiwa ni kwamba kila mtu kwenye Jimbo lake akafanye mkutano. Kwa hiyo, anaposema kwamba tumewahi kuzuia mikutano, anapotosha. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa Jesca Kishoa, unaipokea Taarifa hiyo?

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei lakini niseme tu kwamba mimi nazungumzia vyama vya siasa sio mkutano wa Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sijajua kwa upande wenu hili ninyi mnalifanyaje, lakini sisi wa vyama vya upinzani tunakuwa tuna mikutano ya hadhara ambayo ni kama chama ambacho kinajumuisha viongozi wa chama wanakwenda kutangaza sera ya chama chao na wananchi wanapata elimu ili kuweza kupima chama gani ambacho kinafaa kushika madaraka.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bil akufuata utaratibu)

WABUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa. Asipotoshe, aseme ukweli.

NAIBU SPIKA: Subiri, subiri.

Waheshimiwa Wabunge, tusikilizane, mikutano ya vyama vya siasa huwa ni mikutano ambayo iko kwenye katiba zao. (Makofi)

Hiyo mikutano hufanyika kwa vipindi fulani na hiyo mikutano hata Chama cha Mapinduzi huwa ile mikutano sio ya hadhara. Kwa mfano tarehe 30 Aprili, 2021 Chama cha Mapinduzi kimetangaza kitakuwa na Mkutano Mkuu, Mkutano Mkuu unaenda kufanyika pale JK Convention Centre. Ule niyo utaweza kuita ni Mkutano wa CCM, lakini ameenda Rais mahali unasema huo ni Mkutano wa CCM, ule sio mkutano wa CCM, ni mkutano wa Rais. Mkutano wa Chama cha Mapinduzi ni kama huo tunaoenda kesho kutwa. Sasa ukisema mikutano ya vyama vya siasa imekatazwa, kuna chama kiliitisha mkutano halafu ukakatazwa?

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Ngoja, tuelewane vizuri. Hata Katiba tuwe tunaisoma vizuri, leo naongea nikiwa nimekataa. Hata Katiba tuisome vizuri. Katiba ikishaweka zile haki kule, imeweka na mipaka yake na usisome kifungu kimoja ukata kukisimamia hicho ukasahau kingine. Katiba yetu inazungumza haki nyingi sana. Ile haki ya kwako wewe haitakiwi kuzidi pua yako ili usiisumbue haki ya mtu mwingine.

Kwa hiyo lazima utaratibu ufuatwe na ndiyo maana Bunge letu hutunga sheria ili kuvikazia vile vifungu vya Katiba. Kwa hiyo, ukizungumza tu hivi jumla mtu anawaza kuna katazo labda liko mahali, hapana, tuelezane vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Jesca Kishoa malizia mchango wako.

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, sitaki sana kubishana na Kiti chako, lakini niseme tu mimi ni miongoni mwa wahanga wakubwa sana kwenye suala hili la mikutano ya hadhara.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie hoja yangu.

NAIBU SPIKA: Haya, malizia sekunde 30. Naambiwa hapa muda wako umekwisha.

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kusisitiza vyama vya siasa tunahitaji kupata uhuru wa kikatiba wa kufanya mikutano ya hadhara. Ni kwa muda mrefu sana na mimi nimekuwa ni muhanga katika eneo ambalo nilikuwa nikiwakilisha kama Mbunge wa Mkoa wa Singida kuanzia term ya Bunge lililopita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa nikizuiliwa kufanya mikutano yangu ya hadhara na wananchi kwa sababu ambazo hazieleweki. Kuna wakati mwingine wamekuwa wakitoa sababu za kusema kwamba hali ya…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa ahsante sana. Muda wako umekwisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuweza kuchangia kwenye Wizara hii muhimu sana, Wizara ya kimkakati, Wizara ambayo ina mchango mkubwa sana kwenye pato la uchumi wa nchi yetu. Mimi nitajikita kwenye maeneo matatu na eneo langu la kwanza, linakwenda kujikita kwenye eneo la bomba la mafuta ghafi la EACOP. Naomba nichukue fursa hii kwa moyo wa dhati kabisa kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukamilisha Host Government Agreement na kwa namna ambavyo anakuwa proactive katika kufanikisha masuala haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia nimefurahishwa na shareholding structure iliyopo kwenye mradi huu. Ukiachana na masuala mazima ya namna ambavyo mgawanyo ulivyo, lakini pia mradi huu unakwenda kutunufaisha sana ukiangalia kwamba, unakwenda kupita kwenye mikoa 8, lakini wilaya ziko 24, kata 134, vijiji 257 na vitongoji 527. Ni kwa uhakika kwamba, watu wa maeneo haya ambao bomba hili linapita wanakwenda kunufaika, lakini mradi huu unakwenda kutengeneza ajira zaidi ya 10,000. Nilikuwa ninatazama taarifa mbalimbali za Wizara, ninaona vitabu vya Wizara viko silent kueleza suala la wafanyakazi ambao watakuwa skilled na unskilled. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ipo changamoto nyingine kubwa sana pamoja na yote ambayo nimeyazungumza juu. Kuna changamoto kubwa ambayo nitaomba Mheshimiwa Waziri utakapokuja kuhitimisha hapa, utoe ufafanuzi kwenye Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa sababu, utata huu kwa kweli unazidi kuwapa watu sintofahamu. Nina swali la kuuliza, mradi huu wa EACOP ni nani anakwenda ku-finance mradi huu? Ninajua kwamba Serikali inatenga bilioni 2.6 kwa ajili ya kulipa fidia lakini mradi huu wenye thamani ya USD bilioni 2.5, ni nani anakwenda kuilipa? Kwa sababu, mtu ambaye mlikuwa mnamtegemea ambaye ni Kampuni ya TOTAL, ambaye ni majority share kwenye mkataba huu, hana uwezo wa kulipa fedha hizo mpaka hivi ninavyozungumza sasa nitatoa sababu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mezani kwangu nina jarida la UK ambalo ni very prominent magazine la energy voice. Mapema sana mwezi wa 5 hata kabla ya mkataba huu kuingiwa, mabenki ya UK, mabenki ya Ufaransa ambayo yalikuwa yametoa ahadi kutoa fedha kwa Kampuni ya TOTAL, kwa ajili ya ku-facilitate mradi, ujenzi huu wa bomba la mafuta, mabenki yametangaza kwamba, hayatatoa fedha hata senti tano tena. Sababu ya mabenki haya kutoa tangazo hili, mabenki yamegoma kwa sababu, wamesema wanakwenda kuunga mkono kampeni ya ku-burn emission masuala ya carbon dioxide. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na naomba nirejee kwa ufupi sana eneo ambalo la magazine hii imeripoti wanasema hivi: “French banks have committed not to provide projects financing for the TOTAL East African Crude Oil Pipe Line – EACOP”. Ukiangalia kwamba kwenye makubaliano yetu, tumekubaliana kwamba mradi huu ujengwe mpaka kufikia 2024 uwe umekwisha kamilika. Lakini kampeni ambayo mabenki haya yanasema yanai-support, kampeni hii inakwenda mpaka kufika mwaka 2050. Ninaomba Mheshimiwa Waziri atusaidie kutuambia, kama hafahamu basi ninamuomba awatafute watu wa TOTAL wamuambie fedha hii au mradi huu nani anakwenda kuu-finance? Kwa sababu wao fedha waliyokuwa wanategemea kutoka kwenye mabenki ya Ufaransa, mabenki yamesema hayatoi fedha tena.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, lakini ninaomba.

SPIKA: Taarifa Mheshimiwa, nakukubalia tuendelee.

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, ahsante nilitaka kumpa taarifa mzungumzaji, inawezekana kweli anachokizungumza anakijua, lakini sisi hatufungi mkataba na mabenki ya Ufaransa. Tunafunga mkataba na mkandarasi ambaye ni TOTAL, ambaye tayari kwenye mkataba alikuwepo anaweka. Yeye ana uhakika gani kwamba, mkandarasi ana fedha kiasi gani za kuweka hapo? Kwa sababu sisi hatufungi mkataba na yale mabenki, kama ameona hiyo document ni ya kwake na yeye, sisi tunakubaliana na mkataba unaoendelea sasa hivi. Mpaka siku mkandarasi atakapoamua kwamba, hana uwezo wa namna hiyo ndio tutaelewa jambo hilo. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa unapokea taarifa hiyo.

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, siwezi kuipokea taarifa hii, labda nimuelimishe kidogo Mheshimiwa Mbunge. Mkandarasi na TOTAL ni watu wawili tofauti. Mkandarasi anayehusika kwenye ujenzi wa mradi wa EACOP sio huyo TOTAL unayemsema wewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba niipe challenge Economic Intelligence System ya Taifa letu. Haya ndio mambo ambayo ni very sensitive katika Taifa hili ambayo tunategemea hawa watu watusaidie. Kwa maana taarifa kama hizi kama zimetokea toka Mwezi Mei mwanzoni kabla ya mkataba huu kuingia hizi nchi mbili ilikuwa ni vyema Wizara wakakaa chini na TOTAL wakakubaliana kwamba hizi fedha zinakwenda kutolewa wapi kwa sababu kimsingi toka mwanzo TOTAL walikwishaeleza kwamba fedha wanapata kutoka kwenye Mabenki ya Ufaransa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee, suala jingine ambalo ninaomba leo kauli ya mwisho kutoka Serikalini. Hivi hii itakuwa mara yangu nne ndani ya Bunge lako Tukufu kuzungumzia suala hili kwasababu nimelishazungumza Bunge lililopita na sasa nalizungumza kwa mara ya kwanza katika Bunge la Awamu hii. Suala la Mkataba wa SONGAS, nimelizungumza suala hili mara nyingi sana na nakumbuka hata Mheshimiwa AG amekuwa akisimama humu ndani akitoa ahadi kwamba wanafanyia review mikataba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumebakiza miaka miwili tu ili mkataba wa SONGAS uweze kuendelezwa na nina taarifa, nina taarifa watu wa SONGAS wameshaanza kufanya robbing hata kwa wabunge kutaka mkataba wao uendelee kuwepo. Ninaomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu pamoja na Bunge lako Tukufu tuungane kwa pamoja tupinge mkataba huo kuendelea kama mkataba huu haujafanyiwa review. Kwa sababu kama Taifa hatunufaiki kwa namna yoyote na masuala haya yameanza kuzungumzwa toka mwaka 2009 na CAG; mwaka 2018 na CAG, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge mwaka 2005 wakati huo alikuwa Mheshimiwa Shelukindo amezungumza suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapoteza kila mwezi zaidi ya Dola milioni 5 kwa sababu ya mkataba huu mbovu. Ninaelewa, ninaelewa huenda wakati huo walikuwa wanataka ku-rescue nchi, kuitoa nchi kwenye giza lakini tunapokwenda sasa mwaka 2024 wakati mkataba huu unakwenda kuendelezwa, kukubaliwa kuendelezwa. Namuomba Mheshimiwa Rais, nakuomba na wewe kupitia Bunge lako Tukufu, tupinge mkataba huu kuendelea kama haujafanyiwa review ya aina yoyote ili wananchi wetu waweze kunufaika kwa kiwango kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kama sisi tuliwekeza kwa sehemu kubwa kwasababu sisi tuliwekeza 73% kwenye Capital Structure halafu SONGAS waka-invest kwa 27% kwenye investment structure lakini kwenye shareholding structure SONGAS wao ndio majority kwa kumiliki 54% haiwezekani. Ninaomba suala hili litazamwe upya na tuangalie na tulitazame kwa namna ya kipekee.

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa jambo dogo sana kwa ufupi najua dakika zangu zimekwisha, suala la umeme wa upepo. Leo tunazungumzia suala la energy mixing. Unazungumzia suala la energy mixing, tunajua kuna vyanzo mbalimbali; lakini ni kwa nini upepo umesahaulika?

Mheshimiwa Spika, natoka Mkoa wa Singida; Mkoa wa Singida ni miongoni mwa maeneo ambayo yanaongoza kwa upepo mkali East Africa nzima na inauwezo wa kuzalisha Megawatts za kutosha kutokana na umeme wa upepo. Lakini suala hili limekuwa likipigwa danadana miaka nenda miaka rudi na ninakumbuka mwaka 2017 nilisimama humu Bungeni nikamuomba Mheshimiwa Waziri na ninashukuru huyu huyu ambaye aliyepo sasa, nikamuhoji kuhusiana na suala hili na akasema ndani ya miaka miwili umeme wa upepo Singida mradi utanzaanza kutekelezeka. Lakini mpaka ninavyozungumza hapa hata nguzo hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba suala hili mkumbuke basi na chanzo hiki muhimu sana cha upepo ili kuweza kutusaidia wananchi wa Singida lakini pia na Taifa kwa ujumla kwa kuzalisha Megawatts za kutosha. Baada ya kusema hayo, nashukuru sana na Mwenyezi Mungu awabariki Wabunge wote Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naomba nitumie nafasi hii kukutakia kila kheri kwenye uchaguzi wa nafasi ya Urais Bunge la Dunia, wengine wanakusikia lakini sisi tumekuona na tunajua utendaji wako na competence yako kwenye nafasi hii ya Uspika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa namna ambavyo wameendelea kufanya kazi kwa umahiri mkubwa, lakini pia Viongozi mbalimbali wa Taasisi za Wizara ya Nishati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita zaidi kwenye eneo moja na kutokana na umuhimu wake ndiyo maana nahitaji muda wa kutosha sana kuchangia eneo hili. Nitajikita zaidi kwenye eneo due diligence (Uchunguzi wa Kina).

Mheshimiwa Spika, tunajua ya kwamba hili ni eneo muhimu sana pale inapokuja wakati anatafutwa Mzabuni au Mkandarasi wa kutekeleza miradi ya maendeleo. Kuna Mwandishi mmoja wa vitabu anaitwa George Richard aliwahi kusema “No man can find out the truth of something without doing investigation” akimaanisha ya kwamba hakuna mtu yeyote anayeweza kugundua ukweli bila kufanya uchunguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wote tunajua madhara ya kutofanya due diligence ya uhakika kwenye sekta au wakati unahitaji mkandarasi wa kutekeleza miradi ya Serikali. Moja ya madhara makubwa ni lazima utapa mkandarasi wa mchango kwa maana ya kwamba utapata Mkandarasi ambaye hana sifa, lakini cha pili endapo utafanya due diligence ambayo haina umahiri, utapata changamoto ya ucheleweshwaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na la tatu hata kama miradi hiyo itatekelezeka basi itatekelezeka chini ya kiwango. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunatambua worldwide yapo maeneo ambayo ni key areas kwa ajili ya kufanya investigation kwenye kuchagua Mkandarasi. Kwanza kabisa, huwezi kumchagua Mkandarasi au mzabuni bila kufanya financial due diligence. Nikisema financial due diligence nina maana kwamba unakagua financial muscles, misuli ya kifedha ya kampuni. Utaangalia masuala ya cash flow, utaangalia masuala ya tax record, utaangalia masuala ya historical financial statements za kampuni. Pia ni lazima utaangalia masuala ya legal and regulatory compliances, lazima ujithibitishie kwamba kampuni hiyo imekidhi matakwa ya kisheria. Utaangalia masuala ya leseni, utaangalia masuala ya vibali kama vimethibitishwa ili usije ukachukua kampuni ambayo iko kinyume na utaratibu na lazima pia uangalie masuala ya legal disputes, kama kampuni hiyo imeshapata pingamizi maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lazima uangalie masuala ya operational due diligence, ujithibitishie uwezo wa kampuni wa kutekeleza miradi. Utaangalia masuala ya technology lakini pia utaangalia masuala ya products zinazotakana na kampuni hizo na mambo mengine mengi sababu ya muda siwezi kusema yote, lakini kuna masuala ya risk assessment lazima wafanye, lazima ufanye due diligence kwenye management profile, lazima uangalie timu ya kwenye kampuni wale wahusika wa management team kama una profile nzuri unaweza ukachukua kampuni kumbe ni wala rushwa watupu, kwa hiyo lazima ujiridhishe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini, ni bahati nzuri sana nimeshiriki ziara zote za Kamati hii. Umetutuma tukaenda kukagua miradi ya Serikali, mambo ambayo tumeyakuta kule mengine yanatia kichefuchefu kwelikweli ni lazima tuseme. Tumekwenda Korogwe tukakagua miradi ya REA. Miradi ya REA kuna changamoto kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, tumefika Korogwe tumekutana na Mkandarasi anaitwa Tontan, Mkandarasi huyu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amemkabidhi bilioni 3.9 kama malipo ya awali kwa ajili ya kutekeleza mradi wa Vijiji vya REA vijiji 54, kwenye Wilaya ya Korogwe lakini Mkandarasi huyu tulipombana akathibitisha mbele ya Kamati ya kwamba fedha zile amezipiga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, amethibitisha mwenyewe kwamba fedha zile ambazo amepewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bilioni 3.9 kwamba amezila kinyume na utaratibu. Tukauliza kuhusiana na masharti ya kimkataba, tulichoona mpaka leo ninavyozungumza hapa yule Mkandarasi hajachukuliwa hatua yoyote baada ya ubadhirifu mkubwa alioufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kibaya zaidi Tarehe 14 Februari, mwaka huu Mkandarasi huyo huyo aliyefanya ubadhirifu mwaka jana, ndiyo huyo huyo kapewa tena tender kwenye gridi imara mwaka huu. Wote humu ndani tumekuwa tukizungumza kwamba Mama yetu anazunguka usiku na mchana kutafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Ni wajibu wetu kama Serikali na kama Bunge kuhakikisha kwamba fedha hizi zinatumika ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niwaambie wananchi wa Korogwe popote walipo kwamba Rais wao alitenga shilingi bilioni 3.9 kwa ajili ya watu hao kupelekewa umeme, kwenye vijiji vyao 54 lakini wameponzwa na Mkandarasi asiyekuwa na maadili, wameponzwa na baadhi ya watendaji kwenye Wizara ikiwepo watendaji wa REA kutopeleka fedha hizo mahali panapohusika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, umeisikiliza vizuri sana hotuba ya Kamati imeeleza vizuri suala hili na imeomba kwamba hatua kali zichukuliwe kwa kampuni hii na wahusika wote. Mambo haya yameendelea siyo tu Korogwe peke yake. Tumeona hata maeneo mengine kuna mradi wa Kinyerezi One extension wa megawatt 185. Alikuwepo Mkandarasi wa kwanza ambaye Serikali ikatenga fedha dola milioni 133, kati ya dola milioni 188 akatangazwa kufilisika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najiuliza hichi ni kitu gani? Tunakwenda wapi? Hii due diligence inafanyika kwa kiwango gani? Kama tuna kitengo ambacho kinaweza kuwapa nafasi wakandarasi kutekeleza miradi halafu wakawa wanatabia ya kutangaza kufilisika, halafu wakawa wana tabia ya kutafuna fedha za wananchi wa Tanzania hatuwezi kukubaliana na suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninao ushauri, kwanza ushauri wangu wa kwanza ninaliomba Bunge lako Tukufu ikikupendeza iiunde Tume ambayo itakwenda kukagua vitengo vyote vinavyo- deal na due diligence kwenye Taasisi ya Wizara ya Nishati. Yaani kwa maana ya kwamba due diligence na wenyewe ifanyiwe due diligence. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ninaomba baada ya kubainika taarifa ya kutoka kwenye ukaguzi huo iletwe Bungeni na Bunge liweze kuchukua hatua, wale wote wanaohusika kwenye masuala ya ten percent wachukuliwe hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ningependa kuomba sana. Mheshimiwa Waziri pelekeni hawa watu wapate taaluma, vitengo hivi wapate taaluma. Wahusika waendelezwe. Ipo mifano mingi duniani ambayo imepitia changamoto kama hizi, ambapo Wakandarasi wakipewa tender wanatangaza kufilisika. Maeneo mengi Wakandarasi wanafuja fedha ya Serikali, kuna maeneo mengi ya kujifunza.

Mheshimiwa Spika, maeneo machache ambayo nimeweza kuyaangalia na ninaweza nika-share hapa Bungeni, kuna mradi wa Solyndra Project huko California, wali-face the same coincidence kama ya kwetu, nendeni kajifunzeni kule. Kuna Bwawa la Bakun ni project iko kule Malyasia wali-face changamoto kama ya kwetu, nendeni mkajifunze kule. Kuna Bujagali Project iko Uganda hapo, nendeni mkajifunze kule, kuna Fukushima Power Plant Japan wali-face masuala tunayoya-face sisi Wakandarasi kutangaza kufilisika, Wakandarasi kutafuna fedha za Serikali, nendeni mkajifunze kule walichukua hatua gani, mkiwa hamna ninazo hapa naweza nikawapatia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niseme hivi, tusiwe na haraka sana ya kuona matokeo ya mambo makubwa na wakati tuna mengine ya kawaida ambayo bado hatujayakamilisha. Nimesikiliza taarifa nzuri sana ya Mheshimiwa Waziri lengo lake ni zuri sana, lakini napenda nishauri kwamba kama kuna vijiji 12,000 ambavyo bado havijapatiwa umeme, hakuna sababu ya kwenda kukimbilia vitongoji 36,000 kuvipatia umeme kabla ya kukamilisha vijiji hivi 12,000. Tuende tumalize hatua ya kwanza ya vijiji vyote, vikamilishiwe umeme, tuende hatua ya vitongoji. Lengo ni kuona kwamba watu wote kwa wakati sahihi wanapata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba nikushukuru sana, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza kabisa niuelekeze mchango wangu katika Shirika letu la TPDC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna msemo unasema hivi, to realize the value of what you have imagine you have lost it. Ili tuweze kujua mchango wa TPDC kwenye sekta ya nishati tufikirie kuipoteza TPDC kwenye sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vyovyote vile tusitegemee TPDC inaweza kufanya vitu vikubwa na vizuri kama haijawezeshwa vya kutosha. TPDC leo hii inadai TANESCO zaidi ya bilioni 500, hizi ni fedha nyingi sana. Wakati inadai TANESCO deni la bilioni karibu 600 wanamchukua TPDC kupitia kampuni tanzu ya TANOIL wanamwingiza kwenye market sharing kwenye biashara ya mafuta. Tafsiri yake ni kwamba, ni kama unamchukua mtoto wako unamfunga miguu na mikono, halafu unampeleka kwenye ulingo akapambane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, TPDC kupitia kampuni tanzu ya TANOIL inaagiza only 2% ya mafuta yote yanayoletwa nchini kila mwezi, yaani katika tani laki tatu zinazokuja kwenye nchi kila mwezi TPDC wanaingiza tani elfu ishirini peke yake. Huyu TPDC kupitia kampuni tanzu ya TANOIL anawezaje kupata muscles kwenye negotiation ya price kama asilimia ya kuingiza mafuta ni only 2%? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri mambo kadhaa; kwanza ni muhimu sana Serikali ikaingilia kati deni hili la TPDC kudai TANESCO. Wanaweza wakatenga kiasi kidogo cha ruzuku wakaweza kupunguza ukubwa wa deni hili. Pia kuna haja ya kubadili sheria zetu kwenye Petroleum Act tukaona kwamba, badala ya fedha yote inayopatikana TPDC kupelekwa Hazina, basi ikishafika Hazina irudi kwa ajili ya kusaidia shughuli za TPDC. Ni muhimu sana kwa sababu TPDC ikiwezeshwa ndio muarobaini wa kudumu wa changamoto ya mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa mwisho kwa upande wa TPDC, ni muhimu sasa ule ujenzi wa vituo vya uhifadhi wa mafuta ukamilishwe kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kwa ufupi ucheleweshwaji wa Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere. Taarifa ya Kamati iko very clear, sababu zinazotolewa na Serikali ambazo zinaonesha ucheleweshwaji wa Mradi wa Julius Nyerere, sababu hizi hazitoshi. Sababu hizi hazitoshi kwa sababu leo tunaambiwa Mradi wa Julius Nyerere umechelewa kukamilika eti kwa sababu za kimazingira. Ninavyofahamu hakuna mradi wowote ambao unaweza ukatekelezeka bila kufanyika feasibility study, lakini pia najua hakuna mradi wowote ambao unaweza ukakamilika bila kufanya environment impact assessment. Haiwezekani mradi wa over six trillion uwe na kikwazo cha kimazingira, kwanza ni aibu hata taarifa hii kuwepo kwenye documents za Serikali kwa sababu, inaonesha namna ambavyo hatuko smart. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaambiwa sababu nyingine ni Covid-19. Leo naomba niseme Covid-19 imekuwa ikitumika mara nyingi kama kichaka cha kuficha uovu ambao unaendelea kushindwa kutekeleza miradi mbalimbali ya Serikali. Kama kweli sababu ni Covid-19 basi tuambiwe, ile scope time kwa sababu, inaonekana ule muda ambao wanasema umesababishwa na Covid-19 hauendani kabisa na uchelewaji, tumechelewa zaidi ya mwaka mzima. Tunahitaji tuambiwe very specifically, hiyo mitambo wanayosema kwamba, imeagizwa na ikachelewa kuja kwa sababu ya Covid-19 kwanza ni mitambo gani na evidence tupewe kwa sababu, inasikitisha sana miradi mikubwa kama hii ambayo ina nia ya kutaka kututoa kwenye changamoto ya umeme kushindwa kutekelezeka kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa haraka haraka nijielekeze sasa kuchangia eneo la global agenda kubwa ya duniani kwa sasa inayohusiana na masuala ya energy transition. Wote tunajua katika hii dunia tumekuwa tukiishi na kunakuwa na vipindi vinapita; kulikuwepo mwanzoni kuna kipindi cha renaissance, wanaojua historia karne ya 14, kikaja kipindi cha enlightment karne ya 17, kikaja kipindi cha industrial revolution, kikaja kipindi cha globalization, kimekuja kipindi sasa cha fourth industrialization ambapo hapa tunazungumzia masuala ya artificial intelligence, tunazungumzia masuala ya internet na tunazungumzia masuala ya energy transition. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika kipindi hiki unapozungumza energy transition haya ni makubaliano ambayo yamefanywa na Wakuu wa Nchi mbalimbali duniani kutaka kuangalia njia mbadala ya kuweza kuokoa dunia na athari hasi za tabianchi na mazingira na ndio maana kumekuwa kukifanyika mikutano mikubwa duniani. Umefanyika mkutano wa Paris Agreement mwaka 2016, lakini pia kuna Mkutano wa Scotland Cop26 wa mwaka 2021 ambao lengo kubwa la mikutano hii na huu Mkutano wa Scotland Cop wa 26 alihudhuria Mheshimiwa Rais mwaka jana, lengo kubwa la makubaliano haya wamesema kwamba, wanataka sasa dunia iwe na joto lisilozidi 1.5 centigrade. Njia wanayoitumia wanasema wanataka kutumia njia ya kusitisha matumizi ya nishati chafu ambayo ni fossil.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nina vitu nataka nishauri hapa. Kama kuna kipindi tunatakiwa kuipa kipaumbele kwa nguvu zote taasisi ya Serikali ya GST ni sasa. Nasema hivyo kwa sababu gani; sisi tuna critical minerals, hizi critical minerals ndio zinazohitajika sana kwenye soko la dunia sasa hivi kwenye madini, kwa sababu moja, ndio madini yanayotakiwa kutumika kutengeneza miundombinu ya nishati safi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia umeme wa upepo unatengenezwa kwa kutumia turbines. Turbines inatumia madini ya copper, ukiangalia mabetri ya magari yanatengenezwa kwa kutumia madini ambayo yanaitwa graphite, kwa hiyo, haya madini yote na mengi sana yapo nchini Tanzania, lakini tuna changamoto kubwa moja, GST ambao ndio watafiti wakubwa wa madini katika nchi yetu hawawezeshwi. Ndio kwanza bajeti yao wametengewa bilioni 3.5 na hii ni OC peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri, ile helicopter iliyokuwa inazurura majuzi hapa kwenye mikoa mbalimbali ipelekeni GST ikafanye kazi kwa ajili ya kuchunguza madini haya yanapatikana wapi. Itakuwa sio mara ya kwanza, tuliwahi kuwa na helicopter sisi 1990 huko miaka ya nyuma na ilifanya kazi kubwa. Ni vizuri sasa hivi tunapotaka kutafuta madini haya ambayo yanaweza kutunufaisha kwenye nchi yetu, vitu kama hivi vitumike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Tanzania ni watano duniani kwa madini ya graphite ambayo ndio yanahitajika sana kwa sasa, lakini yako wapi? Ni jitihada gani Serikali imefanya kuyatafuta? Tunategemea taarifa kutoka kwenye kampuni za madini, haiwezekani. Tutafute madini haya ili yaweze kutusaidia kwenye kutengeneza miundombinu ya nishati safi ambayo ndio agenda kubwa duniani kwa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuna changamoto GST hakuna watumishi. Ni vema idadi ya watumishi ikaongezeka ili wafanye kazi kwa uhakika zaidi. Itakuwa ni aibu sana pamoja na rasilimali kubwa hii ambayo Mwenyezi Mungu ametupa ya kuwa na madini ambayo ndio yanahitajika kwa sasa, critical minerals, halafu bado tukaendelea kuyakalia, tukaendelea kuyafunika na tusijue namna ya kutumia na wakati kufikia mwaka 2025 kama tutakuwa vizuri kwenye kuyatafuta, nchi ya Tanzania ndio inakwenda kuongoza dunia nzima kwa kutoa madini ya graphite, hizi ni tafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, naomba nigusie umeme wa upepo Mkoa wa Singida. Tumekuwa tukiimba wimbo huu kwa muda mrefu sana. Naomba tu ku-declare, pamoja na kwamba, duniani kwa sasa agenda ya matumizi ya nishati safi ni pamoja na nishati ya umeme wa upepo, lakini nashindwa kuelewa ni kwa nini Serikali imekuwa na kigugumizi kwenye utekelezaji wa Mradi huu wa Umeme wa Upepo Singida? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka nenda miaka rudi tumezungumza, toka miaka ya 2011/2012 mpaka leo hakuna kitu kilichofanyika hata nguzo moja hakuna. Tunaahidiwa miaka yote umeme wa upepo, umeme wa upepo, hakuna kilichofanyika. Watafiti wametafiti wakaona kwamba, umeme wa upepo wa uhakika katika ukanda wa East Africa unapatikana Singida na Makambako na una uwezo wa kuzalisha nishati ya kutosha, kwa nini kunakuwa na kigugumizi kwenye utekelezaji wa nishati ya umeme wa upepo Mkoa wa Singida? Wananchi wa Singida tumewakosea nini Serikali hii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inazungumza vyanzo vingine vya umeme wa upepo inaacha kutaja Singida kwenye umeme wa upepo na wakati inajua kuna umuhimu wa kuwa na energy mixing kwenye uzalishaji wa umeme. Naomba Serikali kwa dhati kabisa na Mheshimiwa Januari Makamba aji-commit kwenye hili, wenzake wengi waliji-commit kwenye hili, lakini hakuna utekelezaji wowote. Do your part Mheshimiwa Waziri kwenye hili, afanye hili ili wananchi wa Singida wamkumbuke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa nianze kwa kusema kwamba suala la bajeti ni moja ya jukumu muhimu sana la Kibunge ambapo linapima uwezo wa Bunge katika kushiriki kupanga na kupitisha matumizi ya Serikali na baadaye kuhoji matumizi ya bajeti tengwa.

Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu huo ni muhimu tukajikumbusha kwamba nchi yetu imepata makusanyo makubwa kutoka kwenye sekta mbalimbali. Moja ya sekta muhimu sana ambayo nchi imekuwa ikikusanya mapato hayo makubwa ni Sekta ya Utalii. Tuna taarifa kwamba kabla ya COVID - 19 sekta hii ilikuwa inakusanya takribani asilimia 17.9 na baada ya COVID-19 inafanya vizuri kuelekea kufikia kiwango kilekile ambacho kilikuwepo awali.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya mchanganuo huo na mchango huo wa sekta hii kwa pato la Taifa, ni muhimu sasa Serikali na wananchi tunapaswa kujua tuna wajibu wa kulinda vya kutosha sekta hii kwa wivu mkubwa. Ni wakati muafaka nafikiri wa Serikali kuweka wazi na kuwaeleza wananchi wa Tanzania kujua vita kubwa inayoendelea kiuchumi hasa hasa kwenye sekta hii upande wa East Africa. Tusidanganyane hapa, kumekuwa kuna maneno mengi sana na kuna watu wamekuwa wakizungumza mambo mengi wakijinasibu kwamba wao ni wazalendo, mimi nasema hivi hakuna mahali popote katika dunia hii anakuwepo mzalendo wa Taifa lake anakuwa na guts za kwenda kwenye public na ku- damage nchi yake kwenye ajenda ambayo inahusiana na masuala ya kimataifa. Ni wakati wa kuwaeleza wananchi wa Tanzania ukweli, wajue ukweli ili tuweze kushikamana sana kwenye vita hii ya kiuchumi inayoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaenda kwenye mjadala unaoendelea sasa, mjadala wa National Cake Ngorongoro; yanasemwa mambo mengi sana na mambo haya yanayosemwa na yana pollute mind za Watanzania, ni vema tukaweka mambo sawasawa hapa mezani kwangu na ukihitaji nitakupatia hapo nina ripoti ya TAWIRI, TAWIRI ni Tanzania Wildlife Research Institute ya mwaka 2020 ambayo inaonyesha kwamba idadi ya watu Hifadhi ya Ngorongoro kwa miaka 30 mfululizo kuanzia mwaka 1970 na kuendelea mpaka 2018 imeongezeka mara tano zaidi hii ni ripoti ya utafiti. Ukiangalia the citizen gazeti lilinukuu takwimu ya sensa maalum ya Ngorongoro mwaka 2017 ilikuwa ni sensa maalum kabisa kwa ajili ya National Park ya Ngorongoro inaonyesha idadi ya wananchi kwenye Hifadhi ya Ngorongoro ilifika 98,183 kutoka wananchi 8,000 mwaka 1959. Ukiangalia upande wa mifugo ilitoka mifugo 16,100 mpaka mifugo 805,000 kwa muda huo huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwa hesabu ndogo tu ambayo haihitaji records science, ukiangalia eneo la Ngorongoro ni kilometa za mraba 8,292 kwa mwaka 1959 uwiano wa mtu mmoja na eneo ilikuwa hivi; mtu mmoja anakaa kilometa za mraba moja lakini kufikia mwaka 2019 uwiano ukabadilika mtu mmoja anakaa kilometa za mraba 0.084 sawasawa na hivi watu 11 wanakaa kilometa za mraba moja. Hapo bado sijataja nafasi ya wanyama katika eneo hilo. Naomba niseme hivi, hesabu hazijawahi kudanganya, nimejaribu kuyasema haya yote kwanza ili kuthibitisha hoja ya msingi ya idadi ya watu kuwa kubwa kwenye hifadhi na ndiyo maana Serikali ikaona umuhimu wa kupunguza idadi ya wananchi na wanyama katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wanasiasa na wanaharakati waache kupotosha wananchi kwa kutumia kiraka cha haki za binadamu. Kwenye vita hii naomba nitangaze, naungana na Mkuu wa Nchi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kulinda urithi wa Tanzania, naungana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kulinda Taifa na urithi wa Taifa letu, naungana na wananchi wote wa Tanzania wanaosimama na kulinda Taifa letu na urithi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namwomba sana Mkuu wa Nchi, Mheshimiwa Rais kwenye hili asirudi nyuma, vizazi na vizazi vitamkumbuka katika hili, hili suala limekuwa likijaribiwa kwa muda mrefu bila mafanikio. Tunahitaji rasilimali hii I mean tunahitaji keki hii ya Taifa ambayo Mwenyezi Mungu ametupa, inufaishe vizazi na vizazi. Pia tuambiane ukweli hivi ni wapi katika Taifa hili kimewahi kufanyika kilichofanyika kule Msimiro? Ni wapi acha Tanzania, East Africa ni wapi kimewahi kufanyika kilichofanyika Msimiro, leo wananchi wanahamishwa Msamiro I think… (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, Handeni.

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, Handeni huko. Leo wananchi wanahamishwa unapelekwa eneo unajengewa nyumba, unakuta hospitali, unakuta shule, unapewa hati kama una wanawake watatu unapewa hati za nyumba tatu, naomba leo nitangaze rasmi mimi naitwa Ole-Kishoa ili nipelekwe kule Msamiro na mimi nikapewe nyumba ya bure kabisa. Na wanao pinga hili wanatakiwa ku-declare interest, tuna taarifa kuna wabunge wengine humu ndani wanatetea haya kwa maslahi ya mashemeji zao huko, tunajua. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kuna wanaosema kwamba wananchi wa Loliondo na Ngorongoro hasa hasa wananchi wa Ngorongoro kuhamishwa eneo lile ni makosa kwa sababu maeneo yale wameshayazoea. Nataka niseme jambo moja tunatengeneza double standard ya hali ya juu sana katika Taifa letu, kwa sababu kama hili likisikilizwa maeneo mengine watu watakapokuja kuhamishwa kwa kupisha miradi ya maendeleo watajenga experience ya Ngorongoro, watakataa watasema mbona Ngorongoro hawakuhama kwa sababu walikuwa wamezoea maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nina mambo manne ya kushauri; la kwanza, ni muhimu sasa Serikali ikaweka wazi ime-target kiwango kiasi gani cha wananchi wanaotakiwa kubaki pale katika Hifadhi ya Ngorongoro. Pili; Wizara iongezewe bajeti kwa ajili ya kuhakikisha kwamba zoezi hili linafanyika ufanisi mkubwa sana. Tatu; mbinu rafiki za kuhamisha wananchi hawa ziendelee kufanyika kwa sababu tunahitaji wananchi hawa wahamishwe kama ambavyo inafanyika sasa, wamehamishwa kwa hiari kabisa, hakuna ambaye amelazimishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho; tunahitaji kwenye yale maeneo ambayo wamepeleka vituo vya afya wapeleke Madaktari wa kutosha. Eneo ambalo wamepeleka shule wapeleke Walimu wa kutosha ili wananchi wa Ngorongoro ambao wamehamia maeneo hayo waweze kupata haki zao stahiki.

Mheshimiwa Spika, nakusihi sana kupitia Bunge lako hili Tukufu liendelee kuwasihi wananchi wa Tanzania, ni vema tukalitazama suala hili kwa sura ya kizalendo katika nchi yetu, ni vema ifike mahali tujue kwamba hakuna mtu mwenye nia ovu katika suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wapo watu wanaoaminishwa kwamba eneo hili kuna sijui mwarabu anataka kulichukua, yaani kuna propaganda za ovyo, watu wanatafuta kiki. Wanasiasa wanatafuta kiki. Tusiruhusu mambo haya. Najisikia vibaya sana kuona kwamba leo niko kwenye nchi ambayo kuna mwananchi from know where yuko nchi nyingine anamtukana Rais wa Tanzania. Hili suala haliwezi kukubalika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kwa kumalizia nigusie jambo moja linalohusiana na Jimbo la Mkalama, Singida. Nimekuwa nikisikiliza sana watu wengi sana humu ndani wakiwa wanachangia, wanazungumzia kwenye suala la miundombinu, wanazungumzia ukubwa wa barabara zao kutokuwa na lami, mtu anazungumzia kilomita mbili, mwingine anazungumzia kilomita tatu na mwingine anazungumzia kilomita tano.

Mheshimiwa Spika, kuna Wilaya moja Mkalama ipo Singida kule pacha na Wilaya ya Mheshimiwa Waziri alikotoka, Wilaya ya Iramba. Hii Wilaya ya Mkalama kuna kilomita zaidi ya 42 kutoka barabara kuu mpaka kufika Halmashauri. Barabara ni ya vumbi, barabara ni rough road, ni mbaya, madaraja hayafai, hayapitiki mvua ikinyesha. Wananchi wa kule wanajishughulisha sana na suala la kilimo cha vitunguu. Ikifika wakati wa mavuno wanapata taabu sana.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, namwomba kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, kama kuna jambo ataliacha kuwa na alama kwenye Wilaya ya Mkalama ambalo ni pacha na Jimbo lako la Iramba, fanya jambo kwa ajili ya Wilaya hii Mheshimiwa Waziri. Inasikitisha sana kuona kwamba Iramba... (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza kabisa, napenda kutoa pongezi kwa Kamati ambayo imewasilisha muda siyo mrefu, kwa sababu kuna mambo ya msingi wameweza kuyaweka bayana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukianza na suala la Serikali kuchelewa kupeleka fedha za miradi katika maeneo husika, hasa katika eneo la umeme; mimi ni miongoni mwa wahanga katika tatizo hili. Umeme wa upepo Singida, kwa muda mrefu, toka miaka ya 1990 mpaka
Bunge lililopita, Serikali imekuwa ikipiga danadana kuhusiana na suala hili. Majibu ni yale yale! Kila siku Mheshimiwa Waziri husika anapokuja kuzungumzia suala hili, analeta majibu yale yale ambayo anayazungumza toka Bunge lililopita na bahati nzuri ni Waziri yule yule kutoka Bunge
lililopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri Serikali, kama wameshindwa kupata fedha kutoka nje ambazo wanazitegemea, basi ni heri atumie fedha za ndani kutekeleza mradi huu, kwa sababu ni muda mrefu sana. Tumepewa majibu haya haya kila siku, wananchi wa Mkoa
wa Singida wamechoka na Wabunge wa Singida naamini hapa wataniunga mkono katika hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba katika suala hili la umeme wa upepo wa Singida, Serikali, kama kuna uwezekano wa kuchukua fedha kutoka ndani, ichukue na itekeleze mradi ule kwa sababu kiukweli tumechoka. Upepo wenyewe labda tungekuwa tumepewa na mtu;
tumepewa na Mwenyezi Mungu, ilikuwa ni suala la Serikali kutekeleza mradi huu na kuweza kutimiza ahadi ambazo wanazitoa kwa wananchi wa Mkoa wa Singida.
Mheshimiwa Naibu Spika, Singida ninyi Chama cha Mapinduzi mnajua ni champion wa kutoa kura kwa Chama cha Mapinduzi mfululizo miaka yote, lakini ni miongoni mwa watu ambao kwenye miradi mmewasahau. Naomba suala la umeme wa upepo wa Singida, Serikali ilichukulie kwa uzito wa kipekee, kwa sababu ni ahadi za muda mrefu sana ambazo zimekuwa hazitekelezeki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuachana na hayo, naomba pia nizungumzie suala ambalo limekuwa likizungumzwa miaka nenda miaka rudi karibu Mabunge yote; ni suala la mikataba kuwekwa wazi. Namaanisha mikataba ya gesi pamoja na mikataba ya madini specific. Suala hili la mikataba kuwekwa wazi limeshazungumzwa kwa muda mrefu sana. Wamezungumza Awamu ya Nne, wamezungumza Awamu ya Tatu na Awamu ya Tano tena tunalizungumza suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Serikali yoyote ambayo inajipambanua kwamba yenyewe ni ya uwajibikaji, uwazi na ya kutumbua majipu, suala la mikataba kuwekwa wazi lilikuwa siyo suala la kuanza kuihoji, lilikuwa ni suala ambalo lilipaswa kutekelezeka tu. Miongoni mwa vitu ambavyo tulipaswa tuvizingatie ni pamoja na sisi kuwa Wajumbe kwenye organizations ambazo zinazungumzia masuala ya mikataba kuwa wazi. Mfano, sisi ni member kwenye OGP (Open Governance Partnership), lakini toka mwaka 2011 tumekuwa member katika organization hii,
bado vitu vyetu tunafanya kwa mazingira ya usiku usiku; Bunge usiku, mikataba usiku.
Mheshimiwa Naibu Spika, bado sisi toka mwaka 2009 ni member kwenye Shirika la EITI (Extractive Industry Transparency Initiative). Hii ni aibu. Ukiachana na sisi kuwa member katika hizi taasisi, lakini bado Awamu ya Nne Bunge hili lilipitisha sheria ya kutaka mikataba kuwa wazi na
Mheshimiwa Rais, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akasaini, lakini danadana zikaanza kupigwa baada ya kufika kwa Waziri husika kwa maana ya kutunga kanuni ambazo zinaweza zikasababisha sheria hiyo kutekelezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda tu ni kutofahamu, linapokuja suala la sheria ambazo zina maslahi kwa umma, kwa mfano, mwaka 2016 tulipitisha sheria ambazo zinafunga vyombo vya habari, zinafunga demokrasia, zimepitishwa Rais akasaini immediately na Waziri husika
akatunga kanuni na zikaanza kutekelezwa, lakini zinapokuja sheria kama hizi ambazo zina maslahi kwa umma, kwamba mikataba iwe wazi, sheria hizi zinakaa muda mrefu sana. Mfano, toka Awamu ya Nne mpaka sasa, bado Mheshimiwa Waziri hajatunga kanuni na mpaka dakika
hii hajasema sababu ni nini. Labda ni kutofahamu, au ni kufahamu lakini ni kiburi tu kwamba mikataba ikiwa wazi kuna faida gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, mikataba inapokuwa wazi, kwanza wananchi wanakuwa na confidence na Serikali yao. Pia mikataba inapokuwa wazi, wale wawekezaji katika eneo husika wanakuwa na mahusiano mazuri na watu wa eneo lilo ambalo linawazunguka kwa kuamini
kwamba wanayoyafanya ni mambo ambayo wanayajua kwa maana yako wazi. Lingine, mikataba kuwa wazi inasaidia sana zile organisations na NGOs ambazo zinafanya tafiti mbalimbali kuwa na correct details, figures ambazo ni sahihi kuhusiana na mkataba husika au investment husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna nchi mbalimbali ambazo unaweza ukafikiri labda ni Tanzania tu tutakuwa wa ajabu sana, lakini zipo nchi nyingi sana ambazo zimeweka mikataba wazi; na kwa sababu ya muda nashindwa kuzitaja lakini nitazitaja chache, ninazo hapa zote.
Nchi ya Liberia, Ghana, Congo, USA, Colombia, Canada; nchi karibu zote zimeweka mikataba wazi. Kwa nini Tanzania tunaendelea kuweka mikataba hii katika hali ya usiku? Naomba kama Bunge, ikiwezekana tutunge sheria ambayo itambana Waziri, kwamba ndani ya miezi sita
atunge kanuni ambazo sheria itaanza kutekelezeka, lakini siyo afanye anavyotaka yeye.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo lingine ambalo limenishtua kidogo na napenda kushare na Wabunge wenzangu humu ndani. Naomba Waziri atakapokuja kuhitimisha alielezee kwa ufasaha kabisa, kwa sababu siyo vyema kuliona linaandikwa kwenye majadala ya Kimataifa halafu kama Wabunge humu ndani hatuna information sahihi. Kuna kampuni inaitwa BG Group ya Uingereza ambayo inamiliki vitalu vya gesi Tanzania. Ilifanya transfer share kwenda Kampuni ya Shell ambayo ni kampuni kutoka Uholanzi. Kisheria na kiutaratibu wakati kampuni inafanya transfer shares, ni lazima kama Serikali tupate kitu kinaitwa Capital Gain Tax, lakini ni aibu kwa Serikali hii, transfer share imefanyika lakini Serikali haijapewa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri anapokuja kuhitimisha hapa aseme kama kodi hii imelipwa au kama suala hili lina ukweli kiasi gani? Siyo vyema kuona linazungumzwa na kama Wabunge hatulifahamu lakini pia kama Serikali haiji kutoa maelezo
yoyote kwa maana ya Wizara. FCC hawana majibu, nimewauliza na wakasema watatoa kwa maandishi, mpaka leo hawajanipa; TRA hawana majibu, lakini pia Wizara tunaomba majibu leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala lingine la uwekezaji katika gesi asilia.
Unapozungumzia…
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza kabla ya kuendelea nianze na quotation moja aliitoa mtaalam mmoja wa masuala ya uongozi anaitwa John Maxwell, anasema hivi:- “If you want to recognize the intelligence of the leader look people around him.”
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mkuu wetu wa Nchi amezungukwa na watu aina ya Goodluck amezungukwa na watu aina ya Bashite what do we expect. (Kicheko/ Mheshimiwa Naibu Spika, sikutegemea kama tunaweza kuwa na aina ya viongozi ambao wanaweza kuja Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kuchangia katika suala zima la utawala bora baadaye nitamalizia na utumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu kwa sasa hivi imekumbwa na tatizo kubwa sana katika suala la uchumi na tatizo hili linatokana na ukosefu wa utawala bora katika Taifa letu. Leo hii nchi yetu tumekosa fedha za MCC takriban Dola 463,000,000 kutoka Marekani kwa sababu ya ukosefu wa utawala bora. Leo hii tumekosa mikopo kutoka nje.
Mheshimiwa shemeji yangu naona hayupo hapa leo, Mheshimiwa Waziri wa Fedha, amekwenda Ulaya, amezunguka nchi zote, amekosa mikopo kwa sababu kigezo namba moja cha mkopo ni lazima kuwe na good governance katika Taifa, lakini tunakosa fursa hizi kwa
kutokuwepo na utawala bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka leo Bajeti ya Mwaka 2016/2017, imetekelezeka kwa asilimia 34 tu kwa sababu kubwa ya ukosefu wa utawala bora. Wakati huo huo tunakosa misaada kutokana na ukosefu wa utawala bora katika Taifa hili. Wawekezaji wanakimbia, wafanyabiashara wanakimbia; kwa sababu hakuna mwekezaji ambaye ana akili timamu anaweza kuwekeza kwenye nchi ambayo muda wowote mkataba unaweza ukavunjwa kwenye majukwaa. Hakuna mwekezaji ambaye anaweza kuwekeza kwenye nchi ambayo haifuati misingi ya utawala wa Sheria , hakuna.
Mheshimiwa Naibu Spika yapo mambo humu ndani tunaweza kutofautiana kwa sababu ya itikadi zetu, lakini yapo mambo ambayo lazima tuungane kwa ajili ya maslahi ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, utawala wa sasa unaendeshwa kwa double standard, Serikali haina consistency. Kwa mfano unaweza kukuta kwamba watu ambao wako ngazi ya chini wanavunja Sheria na wanachukuliwa hatua kali, lakini wapo watu ambao wapo kwenye mamlaka kubwa wanavunja sheria na wakati mwingine wanalindwa mpaka na mitutu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi binafsi ni mdau mkubwa sana wa vita juu ya ufisadi, lakini jitihada za Mheshimiwa Rais wetu zinakosa uhalali kwa sababu ya kuwa na double standard. Kuna maeneo anaonekana anachukua hatua na kuna maeneo anaonekana hachukui hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkutano uliopita kuna suala nililizungumza humu ndani, nilizungumzia suala la uvunjaji wa Sheria ya Finance Act ambayo iliundwa mwaka 2012 section namba 29 inasema kwamba hakuna transfer share yoyote ambayo itafanyika bila kulipwa Capital Gain Tax.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kampuni inaitwa Shell ilifanya transfer share kutoka kampuni ya BG. Shell ilinunua vitalu vya gesi kutoka kampuni ya BG, lakini hakuna Capital Gain Tax ambayo imelipwa. Cha kusikitisha sana wakati tupo kwenye Kamati, Mkutano uliopita niliuliza viongozi wa FCC wakasema kwamba swali lako tutajibu kwa maandishi mpaka leo hawajajibu. Nika-take trouble kupitia Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge, section namba 29 nikasema kwamba, toeni sababu kwa nini mpaka leo Capital gain tax haijalipwa lakini mpaka leo, toka tarehe nne TRA nao hawajajibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Muhongo alijaribu kupiga bla bla, lakini nashukuru alikiri kwamba kuna wizi unafanyika kwenye makampuni haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii kampuni ya Shell, hii ni kampuni ambayo wiki mbili zilizopita, nina ushahidi hapa, imekuwa reported kwenye vyombo vyote duniani kwamba imetoa rushwa ya trilioni mbili kwa ajili ya kukidhi maslahi yake kwenye Serikali ya Nigeria. Baada ya kugundulika ndipo wakaamua kuitumbua.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sisi kwenye Serikali yetu kampuni hii lazima tuone kwamba kuna harufu ya rushwa hapa. Haiwezekani fedha za wananchi takribani dola milioni 500, takribani kama trilioni moja na ushee, ni hela nyingi sana, zinaweza kutengeneza hiyo standard gauge ambayo Mheshimiwa Rais anataka kuitengeneza kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro; lakini imepotea katika mazingira hayo na hakuna ambaye amechukuliwa hatua na vitu vinafunikwa funikwa na hakuna ambaye anahoji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kweli Mheshimiwa Rais wetu anataka tutengeneza imani na yeye, aanze kuchukua hatua ambazo zinalenga kote kote, achukue hatua kwa watu wake, achukue hatua kwa watu ambao anafikiri kwamba hawamuhusu, wote kwa pande zote mbili
achukue hatua kwa sababu mnatupotezea imani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haraka haraka naomba pia nichangie upande wa utumishi. Kuna uhusiano mkubwa sana kwenye suala la uwajibikaji na maslahi, hivi vitu viwili vinakwenda sambamba. Hapa nilipo nina chati kutoka Chuo cha Walimu, Kanda ya kati lakini nitaongelea
specifically Singida. Walimu wa Mkoa wa Singida toka mwaka 2013 mpaka leo hawajapa stahiki zao, takribani bilioni 2.4.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kutegemea matokeo makubwa Singida na ndiyo maana elimu imekuwa ikianguka kila siku, tumegundua miongoni mwa sababu ni pamoja na hii. Naomba niishauri Serikali jambo moja; kama ambavyo wanafanya kwa wakandarasi, mkandarasi anapokuja kulipwa fidia zake, anapokuja kulipwa malipo yake analipwa kwa riba. Vivyo hivyo tupeleke utaratibu huu kwa upande wa watumishi wa Serikali, specifically Walimu pale mnapokuja kuwalipa muwalipe kwa riba kwa sababu fedha zile kwa wakati ule value yake ni tofauti na wakati huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Mheshimiwa Waziri atutazame upya kwa sababu inasikitisha sana elimu yetu imekuwa ikisuasua kwa muda mrefu sana na Walimu wamekuwa wakilalamika sana, wanaishi maisha magumu, wanakosa stahiki zao. Moja kwa moja hiyo automatically inapelekea utendaji mbovu kwenye elimu wanayoitoa kwa wanafunzi wetu. Tutaendelea kuzalisha watoto ambao hawana vigezo, hawana sifa, kwa sababu tunashindwa kuwasaidia Walimu kupata stahiki zao.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nitaanza kwa kuzungumzia suala zima la ripoti ya madini kwa ufupi, ili kuweka rekodi sawa.

Suala la wizi kwenye sekta ya madini ni suala ambalo wapinzani kwa muda mrefu sana wamekuwa wakilizungumza na endapo kama tungesikilizwa leo hii tusingekuwa tunazungumzia wizi wa takribani miaka 19 iliyopita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkutano wa Bunge uliopita, niligusia pia suala hili kwa maana ya umuhimu wa kuweka mikataba wazi na pamoja na sababu nyingine nyingi nilizozitaja pia nilisema kuna umuhimu kwa sababu sisi ni member kwenye organizations ambazo zina-deal na masuala ya Open Governance mfano EITI, lakini pia na OGP yaani Open Governance Partnership.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mheshimiwa Rais ameagiza wale walio-initiate wizi huu kwenye makinikia wafikishwe kwenye vyombo vya sheria lakini pia wachukuliwe hatua, lipo jambo la msingi sana ambalo naomba nimshauri kwa upendo kabisa. Experience is the best teacher. Kwa sababu kuna uzoefu ambao umewahi kujitokeza mwaka 2012 ambapo kulikuwa kuna Balozi mmoja anaitwa Mahalu alipelekwa kizimbani kwa kosa la ufisadi wa bilioni 2.5 na alipofika kizimbani akajitetea kwa kusema kwamba yale yote ya ununuzi wa jengo lile ambalo alikuwa amelinunua yalikuwa ni maelekezo kutoka kwa mwajiri wake, na kesi ikawa imeishia hapo. Sasa huu ni uzoefu tu ambao umewahi kujitokeza. Napenda nimshauri Mheshimiwa Rais kwamba ili kuweza kuweka mbivu na mbichi hadharani ni bora atoe immunity kwa mapapa ili suala hili liweze kutendeka kwa haki, siyo kuonea vidagaa kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la IPTL. Pamoja na kuwepo na ufisadi mkubwa sana kwenye madini na gesi, lakini bado kuna ufisadi mwingine mkubwa kwenye umeme. Wabunge wa awamu iliyopita watakuwa mashahidi na watakuwa wana kumbukumbu nzuri kwamba miongoni mwa maazimio ambayo waliwahi kuyaweka wakiwa kwenye awamu ile ni pamoja na mtambo huu wa IPTL kutaifishwa. Nasikitika sana mpaka hivi sasa mtambo huu wa IPTL bado Serikali inapiga danadana kuutaifisha.

Mheshimiwa Mwneyekiti, nataka Serikali itoe majibu ni kwa nini mnapiga danadana katika hili wakati mna baraka zote kutoka kwa Bunge, wakati mna baraka zote kutoka kwa Mahakama ya Kimataifa ambayo imehukumu kesi na tunadaiwa takribani bilioni 400 na huu ni mzigo wanaenda kuulipa walipa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ni vema mkatambua kwamba Bunge ndiyo Supreme organ of the State. Pale Bunge linapofanya maamuzi au maazimio ni vema mkayatekeleza kwa sababu mnatengeneza mazingira ambayo tunashindwa kuelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna swali la kujiuliza hapa, hivi mnashindwa kutaifisha mtambo wa IPTL kwa sababu gani? Je, ni kwa sababu huyu mmiliki wa IPTL singasinga anawachangia kwenye kampeni zenu au ni kwa sababu gani? Ni huyu Singasinga amewaweka mfukoni? Ni sababu ipi inasababisha mtambo huu wa IPTL ambao unatupa wakati mgumu wananchi wa Tanzania, walipa kodi wananyanyasika kwa ajili ya mtambo huu na Serikali mnaendelea kupiga danadana kwenye mtambo huu? Kuna kitu gani ambacho kimejificha?

Mheshimiwa Rais kama ameweza kuzuia makontena ya mchanga, siamini kama anaweza akashindwa kuzuia IPTL au kuifungia IPTL, labda kuwe kuna sababu ambayo imejificha. Ninaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha aseme sababu ni nini? Kwa nini IPTL mnashindwa kuifungia na wakati inatupa mzigo mkubwa sana? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nigusie suala la benki ya FBME, nimeona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri amezungumzia ukurasa wa 15. Ni mambo ya aibu sana, nimeona sababu kubwa ya benki hii kufungwa ni uchunguzi uliofanyika kutoka Marekani. Karne hii unazungumzia uchunguzi kutoka Marekani toka mwaka 2012 benki hii imekuwa reported kwamba inatakatisha fedha, lakini mnakuja mnasubiri uchunguzi kutoka Marekani, Financial Intelligence Unit wako wapi? PCCB wako wapi?

Usalama wa Taifa na wengine mko humu ndani mko wapi? Kama mnashindwa ku-deal kwenye vitu sensitive kama hivi tunaachaje kuamini kwamba kazi yenu kubwa Usalama wa Taifa ni kuudhoofisha upinzani? Tunaachaje kuamini kama kazi kubwa ya Usalama wa Taifa ni kufanya mambo ya ajabu ajabu ambayo yanaendelea kwenye Taifa letu. Haya mambo ni ya aibu sana na si mazuri sana kuyazungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe ushauri kwa Serikali kuhusiana na suala hili, kama tatizo lipo kwenye hii kikundi cha Financial Intelligence Unit kuna mambo mawili ya kufanya, moja ni kukiondoa kikundi hiki na kukiweka kingine, kama hiyo haiwezekani basi muandae programu maalum kwa ajili ya kuwapa watu wetu hawa mafundisho waweze kuwa na uwezo mkubwa wa ku-deal na vitu kama hivi ambavyo ni muhimu sana. Ni aibu sana kwa Taifa letu leo hii tunakaa tunasubiri uchunguzi kutoka Marekani, karne hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na FBME, hivi mnasubiri nini kufungia Benki ya Stanbic? Nini kinawafanya mchelewe kuifungia Benki ya Stanbic au mnasubiri pia uchunguzi kutoka Marekani? Wakati PCCB wame-prove kwamba Benki ya Stanbic ilifanya miamala ambayo ni ovu, na wakati CAG ripoti yake ime-prove kwamba Stanbic ilifanya miamala ambayo ni haramu. Serikali inasubiri nini? Kwa nini msichukue hatua? Kwa nini mnakuwa mnategemea tafiti na uchunguzi kutoka sehemu nyingine? Kuna mambo ambayo kwa kweli hata ukiyazungumza yanatia aibu, ni vema tukajitathmini upya, tunakosea wapi? Tunakwama wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka sana nimalizie kwenye suala la kodi. Nimemsikia Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake kuna page fulani amezungumzia kuhusiana na easy of doing business kwamba Tanzania tumefanya vizuri sana, your right, uko sahihi, lakini unaangalia tumefanya vizuri ukilinganisha na akina nani? Ukiangalia kwenye nchi washindani mwekezaji anapokuja au mfanyabiashara kuna vitu anavizingatia anapokuja kuwekeza. Tanzania ndio nchi inayofanya vibaya katika nchi za East Africa kwenye suala la access of financing na kwenye suala la tax rates, viwango vya kodi ni vikubwa. Haya ndiyo mambo ambayo mfanyabiashara Mwekezaji akija kuwekeza kwenye Taifa ni mambo makubwa anayoyazingatia na ndio mambo ambayo tunayafanya vibaya kuliko mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Mheshimiwa Waziri pale mnapokuwa mnajidai na kujitutumua kwamba tumefanya vizuri, ukilinganisha na mataifa mengine, kwa kweli sisi siyo Taifa la kuendelea kujilinganisha na Mataifa kama ya Burundi, tunafanya vibaya kweli na nina taarifa hapa kutoka PriceWaterHouseCoopers ndio takwimu hizi zinaonyesha tunafanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vema sasa Serikali kupitia hotuba yake nzima na mambo ambayo imepanga ikajitathmini upya. Hivi ni vitu gani ambavyo nyie mnavipa kipaumbele? Ni vitu gani ambavyo hamvipi vipaumbele? Kile ambacho mnakihubiri kila siku, kile ambacho mnakisema kila siku, siyo kitu ambacho mnakipa kipaumbele. Ukiangalia kila siku mnahubiri uchumi wa viwanda lakini mnaelekea kwenye maeneo mengine ambayo hayana uhusiano wa moja kwa moja na uchumi wa viwanda ambao mnaouhubiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo ni msingi na ni muhimu sana katika kwenye uchumi wa viwanda ni pamoja na umeme. Tuna megawati 1,051 ni aibu, tuna makaa ya mawe yamerundikana Liganga na Mchuchuma takribani milioni 480 lakini hakuna kinachofanyika hapa, mnahubiri viwanda, viwanda vinatoka wapi?(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo yanasikitisha sana, naomba nimalize kwa kukushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nitazungumzia suala zima la gesi na baadaye nitajielekeza kwenye suala la umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda mrefu katika taifa letu wananchi wa Tanzania wemekuwa na matumaini makubwa sana kuhusiana na suala la gesi ya Mtwara. Matumaini haya yametokana na sababu nyingi mbalimbali ikiwa ni pamoja na sababu ya miradi miwili mikubwa. Mradi namba moja ni mradi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam ambalo limechukua takriban shilingi trilioni 2.5 katika utekelezaji wake na mradi wa pili ni mradi wa LNG (Liquefied Natural Gase) ambayo kama ingekuwa imetekelezeka kwa sasa ingekuwa imetumia Dola za Kimarekani bilioni 30.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda mrefu sana Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi imekuwa ikitumia akili ndogo sana kupanga mipango na kutekeleza miradi mikubwa na mambo makubwa. Bomba la gesi la Mtwara kwenda Dar es Salaam limetumia pesa nyingi sana, lakini kwenye ripoti ya CAG anaonesha bomba hili la gesi lina uwezo wa kufanya kazi kwa asilimia sita tu. Tafsiri yake ni kwamba hata hilo deni ambalo tumelikopa China la trilioni 2.5 hatuwezi kulilipa kwa sababu bomba hili halifanyi kazi vizuri; matokeo yake tutaanza kuchukua fedha kutoka kwenye madawa; tutaanza kuwabana wafanyabiashara kwa ajili ya kulipa deni hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tatizo lingine ambalo ni kubwa sana. Naomba Mheshimiwa Waziri husika atakapokuja kuhitimisha atoe majibu ni ni kwa nini wanakuwa wana poor project plan ambayo inapelekea miradi mikubwa kama hii inashindwa kutekelezeka kwa ufanisi?

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa LNG (Liquefied Natural Gas) haijawahi kutokea katika Taifa hili kuwa na mradi mkubwa kama huu. Huu ni mradi wa kihistoria, lakini cha kushangaza mradi huu umeshindwa kutekelezaka kwa sababu Serikali mmeshindwa ku-deal na investors.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa kwenye meza yangu nina taarifa kutoka kwenye jarida kubwa kabisa la kimataifa la Reuters la Uingereza ambalo nimem-quote meneja wa Statoil anaeleza kwamba mradi huu umeshindwa kutekelezeka kwa sababu ya kusuasua kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Kama utahitaji taarifa hii naomba umtume mhudumu aje aichukue copy yako nimekutolea. (Makofi,)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha aseme tatizo ni nini? Nimesikia kwenye hotuba asubuhi anasema kwamba majadiliano bado yanaendelea. Wawekezaji wanalalamika, tatizo ni nini? Ni hivi, hawa investors ambao anawapiga danadana wamehamisha mradi huu wa LNG wameupeleka Msumbiji.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu kupelekwa Msumbiji tafsiri yake ni kwamba kufikia mwaka 2021 ambapo mradi huu unakwenda kutekelezeka maana yake ni kwamba Msumbiji watateka soko la gesi katika Afrika Mashariki pamoja na Kusini mwa Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri labda sijui ni kutofahamu, mimi nashindwa kuelewa! Unapozungumzia uwekezaji wa takriban dola za Kimarekani bilioni 60, bilioni 30 unakuwa unazungumzia uchumi wa Uganda. Uchumi wa Uganda ni takrban dola la Kimarekani bilioni 60. Unapozungumzia investment ya dola za Kimarekani bilioni 30 unazungumzia robo tatu ya uchumi wa Tanzania ambao ni dola za Kimarekani bilioni 45. Unapokuwa unazunguzia uwekezaji wa takriban dola bilioni 30 unakuwa unazungumzia mara kumi ya uchumi wa Rwanda. Uwekezaji huu ni mkubwa sana. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atupe sababu kwa nini mradi huu unashindwa kutekelezeka kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala zima la umeme. Taifa hili lina vyanzo vingi vya umeme. Tuna maporomoko ya mito, tuna upepo, kwa mfano mimi mkoa wangu wa Singida kuna upepo wa kumwaga. Pia tuna makaa ya mawe ukienda kule Liganga na Mchuchuma takrban tani milioni 480 zimejaa kule, lakini bado umeme ni wa kusuasua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia mpango wa miaka mitano uliotolewa na Waziri wa mwaka 2016 - 2021 ukurasa wa 12 unaonyesha kwamba mwaka 2011 Serikali ilidhamiria kuongeza megawatt kutoka 900 mpaka 2,700 kufikia mwaka 2011, lakini cha kusikitisha mpaka inafika mwaka 2016 megawatt zilizoongezeka 1,246 na kwa bahati mbaya sana nimemsikia na Mheshimiwa Waziri asubuhi kwenye hotuba yake na nimeipitia kumbe zimeshuka tena mwaka huu zimekuwa Megawatt 1,051.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kama kuna Waziri yeyote hapa asimame aniambie kama kuna nchi yoyote imewahi kufanya mapinduzi ya viwanda kwa megawatt 2,000. Mnampa Mheshimiwa Rais mizuka ya uchumi wa viwanda na wakati mmeshindwa na mnajua haiwezekani.

Mheshimiwa Naibu Spika, mnapowaita wawekezaji waje kuweze katika taifa letu na wakati umeme uliopo ni wa kukatika…

TAARIFA ....

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, yaani katika taifa letu ikitokea mvua hata ya saa moja tu, umeme unakatika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mnapowaita wawekezaji waje kuwekeza na wakati umeme wenu ni wa kukatika na kuwaka, mnataka kuwaharibia mitambo yao?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Serikali inayojipambanua kwamba ni Serikali ya viwanda kuna mambo ambayo yalipaswa kupewa kipaumbele. Mimi binafsi nimeunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais za kununua ndege pamoja na kujenga reli ya standard gauge, lakini katika Serikali inayojipambanua kwamba yenyewe ni ya viwanda hii haikuwa kipaumbele. Kipaumbele namba moja kilipaswa kuwa ni umeme, kilimo na mambo mengine lakini kukimbilia kufanya mengine ndiyo maana mambo yanakuwa hayaendi. Niwashauri Waheshimiwa Mawaziri wamsaidie Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijielekeze kwenye skendo (scandal) kubwa sana ambayo nimewahi kuizungumza humu ndani na leo nairudia na nitairudia kwa ufupi tu. Nataka nijue kauli ya mwisho ya Serikali kuhusiana na capital gain tax ambayo haijalipwa kwenye transfer of shares kutoka kampuni ya BG kwenda kanuni ya Shell. Hii nchi si shamba la bibi, hii nchi ina wananchi na hii nchi ni ya wananchi. Nataka kauli ya mwisho kutoka Serikalini, hizi fedha ambazo mpaka dakika hii hazijalipwa. Tatizo ni nini? Akina nani walihusika? Ni nani alivunja sheria hii na amechukuliwa hatua gani? Mheshimiwa Waziri na Naibu wake naomba majibu hapa kesho atakapohitimisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Kwanza kabisa nitoe pongezi kwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa hotuba nzuri ambayo imegusa maeneo strategic kwa ajili ya kulisaidia Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongea kwa ufupi sana kwasababu haya yaliyoandikwa kwenye Mpango ambayo tumeelezewa na Mheshimiwa Mpango ni masuala ambayo yamekuwa yakijirudia, kwa hivyo tusipoteze muda kuendelea kurudia mambo ambayo tumekuwa tukiyarudia mara kwa mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala moja la msingi sana Mheshimiwa Mpango naomba utakapokuja kuhitimisha unisaidie kulijibu nalo ni kuhusu umakini wa uandaaji wa Mpango. Huu Mpango unalenga kutekeleza Dira ya Taifa 2020/2025. Nilichokuwa nakitegemea ni Mpango huu kuonesha una lengo la kutekeleza Dira ya Taifa ya 2020/2025 kwa asilimia ngapi ili ije kuwa rahisi kuhoji.

Mheshimiwa Mpango wewe unajua, Mpango unapokuja kuleta humu Bungeni ni lazima uwe smart kwa maana aya lazima uwe specific, measurable, uwe realistic, uwe attained na uwe frame timed. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri ni Kenya. Kenya wanapokuja kuanda Mpango wanakuwa very serious. Unakuta wanaadika kwamba Mpango huu umelenga inapofikia wakati fulani ajira mpya zitazaliwa kwa asilimia kadhaa, hiyo inakuwa inasaidia tunapokuja kurudi humu ndani kuangalia tumefikia wapi na tumetokea wapi, nafikiri hili litakuwa ni tatizo la uhaba wa wataalam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mpango ambao unakuwa wanaleta Bungeni kuwa na mapungufu kama haya ndiyo maana mambo mengi yanakuwa hayaendi sawa sawa, ndiyo maana Taifa hili bado linaendelea kuwa katika mazingira magumu, wananchi wanakuwa wanaishi maisha ya kimasikini, maisha ya mateso, ukata ni mkubwa kweli kweli na hili mnaweza mkalikataa lakini ni kitu ambacho kimekuwa proved. Mna mamlaka kubwa ambazo zinahusika na tafiti mbalimbali, mfano, nimeona katika ripoti ya BOT Juni, 2017 na Juni, 2015 inaonesha mzunguko wa fedha umeporomoka kutoka asilimia 15 mpaka negative three percent ambacho hiki ni kiwango kikubwa cha run rate.

Mheshimiwa Mwenyekiti, BOT pia wanaonesha kwamba mikopo isiyolipika yaani non-performing loans imengonezeka kutoka asilimia tano mpaka tisa na hii ndiyo sababu kubwa ya mabenki yetu ku-collapse.

Mheshimiwa Mwenyekiti, World Bank Report ya mwezi huu imeonesha pia kwamba urahisi wa kufanya biashara yaani easy of doing business, Tanzania tumeporomoka kutoka nafasi ya 132 ya mwezi huu mpaka 137. Deni la Taifa ambalo linapaa kwa kasi ya ajabu linaongezeka kwa asilimia 17. Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa hesabu ya kawaida tu kama deni linakuwa kwa asilimia 17 na uchumi unakua kwa asilimia 6 katika hali ya kawaida ni vigumu kulipa deni hili kwasababu huwezi kushindanisha baiskeli na bodaboda. Deni linakwenda kwa speed kubwa sana ambayo inakuwa siyo ya kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali na viongozi wake mmekuwa mkijinasibu mara kwa mara kwamba nyie ni Serikali ya watu wanyonge, ninyi ni Serikali ya watu mnaojali maslahi ya watu maskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 70 ya wakulima wa Kitanzania asilimia 75 ni wanawake, sijaona effort zozote za Serikali za kuweza kusaidia hawa wakulima wa Taifa hili hasa katika suala kubwa la mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa napitia report ya Poverty and Human Development ambayo imeonyesha kwamba kwa wastani, mwananchi/mkulima wa Tanzania anatumia kilo tisa kwenye ekari moja ya shamba lake, lakini kwa nchi ndogo kama Malawi, mwananchi wa kawaida kwa wastani anatumia kilo 27 kwa ekari moja. Sasa ninashindwa kuelewa na natafuta reflection ya Serikali ambayo inajinasibu kwamba yenyewe ni Serikali ya wanyonge, natafuta reflection ya matendo yake na hawa wanyonge. Reflection ya Serikali ya wanyonge haipo kwenye kujenga kiwanja cha ndege wapi kule?

Chato! Reflection ya Serikali ya wanyonge haipo kwenye kununua bombadier ambazo hata uwezo wa kusimamia bado ni mdogo zaidi ya kuingiza hasara tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, reflection ya Serikali ambayo inajinasibu kwamba ni ya wanyonge sitegemei kama inaweza ikawaumiza sekta binafsi kwa sababu wote humu ndani tutajua umuhimu wa sekta binafsi katika maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hebu tujaribu kuwa wakweli, hebu tuwasaidie hawa Watanzania, ninyi mnafahamu namna ambavyo mambo yanakwenda ambavyo siyo vizuri, lakini mnashindwa kusema hapa. Mshaurini Mheshimiwa Rais vizuri na nimefurahi kuona baadhi ya Wabunge wa CCM wamefunguka na wameonyesha concern yako ka Mheshimiwa Dkt. Mpango. (Makofi)

Mheshimiwa Dkt. Mpango, ukweli ni kwamba kama haya unayoambiwa hautayazingatia huko mbele ya safari kila kitu kitakuja kukurudia wewe, kwa sababu nchi inaporomoka. Ukiangalia Mheshimiwa Mkapa alivyokuja alikuta deni ni kubwa sana akalishusha mpaka ikawa trilioni 10, akaja Mheshimiwa Kikwete akaacha deni la trilioni 45 sasa kipindi kile kama mnakumbuka vizuri mwaka jana nilitoa maelezo binafsi kuhusiana na Deni la Taifa kutoa angalizo kwa Serikali na ninsahukuru na wewe ulikuja ukatoa maelezo kwa kuonesha concern yako kwamba umeyakubali na unayafanyia kazi, lakini cha kusikitisha ni kwamba ile concern ambayo uliionesha. Mheshimiwa Mpango unakataa, lakini tulizungumza na uliniambia. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natamani kuona Taifa la Tanzania ambalo kwa muda mrefu sana limekuwa ni Taifa la kimasikini tunaliangalia kwa jicho la tofauti katika kuleta maendeleo. Kama nilivyotangulia kusema kwamba sitakuwa na mengi ya kusema maana mengi tumeshayasema kwenye Mipango mingine iliyopita kwahiyo haya hata nikiendelea kuongea tutaendelea kurudia tu mambo ni yale yale hakuna kinachobadilika, hakuna kinachofanyika, kinachopangwa hapa sicho kinachofanyika, tunajadiliana mengine, yanafanyika mengine. Ukifuatilia matumizi ya pesa nyingi nyingine hazipitishwi na bajeti ambazo tunakuwa tunazipanga hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa nianze kwa kusema jambo moja, hatuwezi kufanya mapinduzi ya viwanda kabla hatujafanya mapinduzi ya nguvukazi iliyo bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo mengi sana ambayo ni muhimu kwenye mapinduzi ya viwanda. Ukiachana na habari ya umeme na raw materials, lakini jambo lingine ambalo ni la msingi na ni nguzo kwenye mapinduzi ya viwanda ni pamoja na nguvukazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipata fursa ya kumsikia Mama Christina Lagade ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa la IMF alipokuwa Ethiopia mwaka 2017 mwishoni, anasema nchi kama Tanzania, Kenya, Nigeria na Ethiopia yenyewe, pamoja na fursa zilizonazo za kupelekea uchumi wa viwanda, haziwezi kufikia huko kama hawatawekeza kwenye nguvukazi (competitive labour force).

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuwa na nguvukazi kama mfumo wa elimu hau-reflect dira ya Taifa. Hivyo vitu vitatu vinategemeana; nguvukazi, mfumo wa elimu na dira ya Taifa ni vitu ambavyo vinategemeana kweli kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu awamu ya pili ianze mpaka sasa hivi, kiwango cha elimu yetu kinashuka kwa speed iliyopindukia. Sizungumzii idadi ya wanafunzi mashuleni, nazungumzia kiwango cha ubora wa elimu inayotolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia ripoti ya Shirika moja la viwanda la Kimataifa la UNIDO ambalo linaonesha kwamba asilimia 80 ya labor force katika Taifa letu ni unskilled. Mheshimiwa Waziri wa Elimu haya mambo unapaswa kuja na majibu, kwa sababu hatuwezi ku-invest, hatuwezi kuandaa kizazi kupeleka watu shuleni wakasoma halafu wakawa unskilled.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ATE (Association of Tanzania Employers), Shirikisho la Waajiri na wenyewe wamekuja na taarifa yao, wanasema 30% to 40% ya ajira wanazozitangaza watu wanakosa vigezo/sifa. Tafsiri yake hapa kuna mismatch, mismatch kwa namna gani, kwa maana ya kwamba watu tunaowazalisha wanapishana na mahitaji ya soko la ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema suala hili likaangaliwa kwa umakini mkubwa kwa sababu tunaweza tukawa tunahubiri kwamba ajira hakuna na wakati sababu kubwa inaweza ikawa ni tunapishana na mazingira ya sasa na uhitaji wa elimu tunaotakiwa kuupata kutokana na ushindani uliopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kusikitisha zaidi ni kwamba elimu hii inashuka kwa kasi kipindi ambacho tunaihitaji kutokana na ushindani ambao tunao. Wakati huo huo, nchi zote ambazo zimefanikiwa katika mapinduzi ya viwanda zime-invest sana kwenye nguvu kazi. Zime-invest kwenye nguvu kazi kwa namna gani? Zime-invest kupitia elimu ya kati. Tunachemka kweli kweli, tumeshindwa kutengeneza uwiano sahihi wa nguvu kazi kupitia elimu ya kati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi ambazo zimefanikiwa kwenye mapinduzi ya viwanda kupitia nguvu kazi ya elimu ya kati wanafanya hivi; uwiano wa elimu ya kati na elimu ya juu ni moja ya ishirini mpaka moja ya hamsini kwa maana ya kwamba, kama kwa elimu ya juu kuna mtu mmoja basi elimu ya kati kuna watu ishirini au kama elimu ya juu kuna mtu mmoja basi elimu ya kati kuna watu hamsini lakini sisi ni vice versa. Kama elimu ya juu kuna watu watatu eti nguvu kazi kuna mtu mmoja ambaye ni elimu ya kati. Tume-invest sana kutengeneza managers tunaacha kutengeneza watendaji ambao ni watu wa elimu ya kati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka, nimepitia kitabu cha Ally Mafuruki ambacho amekizindua mwaka jana Mheshimiwa Rais mwenyewe, ningeomba au ningependekeza kama Mheshimiwa Rais alikipeleka akakiweka kwenye draw, akifungue akisome kina majibu mengi sana ya matatizo yetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza kabisa nianze kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi, lakini pia nitachangia dakika hizi tano specifically katika Mkoa wangu wa Singida, sitazungumzia masuala ya kitaifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumze kwa masikitiko makubwa sana, inaaminika na kwa uzoefu kwamba maeneo ambayo yanakuwa karibu na miji mikuu katika nchi mara nyingi huwa yananufaika kwa kiwango kikubwa sana na fursa ambazo zinakuwepo katika mji mkuu. Singida ni eneo ambalo liko pua na mdogo na mji mkuu wa Tanzania, lakini kuna mambo ambayo yanaonesha dhahiri shahiri kwamba Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi inashindwa kuwatendea haki wananchi wa Singida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, treni ya kutoka Dodoma kwenda Singida imeshakufa toka mwaka 2009. Uchumi wa wananchi wa Singida kwa sehemu kubwa ni wafugaji, inaonesha kwamba kuna mifugo milioni moja na laki nne. Hawa wafugaji wanapotaka kutafuta masoko usafiri ambao ni bora na wa uhakika walikuwa wanatumia treni kwa ajili ya kusafirisha mifugo yao. Wakulima wa Singida walikuwa wanatumia usafiri wa treni kwa ajili ya kusafirisha mazao yao. Gharama za bidhaa kutoka maeneo mengine kuja Singida na kutoka Singida kwenda maeneo mengine zilikuwa za kiwango cha chini kwa sababu gharama za usafirishaji zilikuwa za kiwango cha chini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna ajira nyingi zimepotea kutokana na treni hii kutoonekana tena Singida pamoja na mama ntilie ambao walikuwa wanapika pale station, kulikuwa na vijana waliokuwa wanafanya biashara ndogo ndogo pale mpaka sasa hivi watu wale hawana uhakika wa maisha yao yanakwendaje. Nataka Waziri husika ajue kwamba wananchi wa Singida wanataka treni yao. Wananchi wa Singida tunataka treni yetu Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, airport ya Singida; huu ni mwaka wa 30 toka eneo kutengwa. Baada ya eneo kutengwa Naibu Spika nikikupeleka Singida sasa hivi huwezi kujua kama uko airport kwa sababu hata fence hakuna ni pori tupu liko pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, najiuliza and I want government kunijibu hapa, hivi mnapata hisia gani ambapo mnaona kwamba eneo ambalo mwaka 2010, mwaka 2015 wamekuwa champion kuwaweka kwenye viti hapa mnazunguka halafu leo ni mkoa ambao hata uki-google kwenye Wikipedia wanasema ni mkoa wa kimaskini Tanzania. Wananchi wa Singida siyo wajinga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, this is not fair. Wanakwenda kujenga International Airport Chato kwenye watu 365,000 mnaacha Singida ambako kuna watu 1,300,000. This is not fair at all, tumewakosea nini ninyi. Linapokuja suala la sikukuu ya Chama cha Mapinduzi miaka 30 ndio mnakuja mnatuletea ubwabwa, hatutaki ubwabwa tunataka maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, this is not fair, hii haikubaliki. Inaumiza sana karne hii eneo lenye hadhi ya mkoa ambalo lipo karibu na makao makuu ya nchi halina airport? Mambo mengine yote yamewashinda, hakuna hata chuo kikuu kimoja, hakuna treni, umeme wa upepo umewashinda, kila kitu kimewashinda Singida tumewakosea nini sisi? (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nafikiri niendelee tu na kuchangia kwa sababu nilipokuwa nazungumzia Chato sikusema Geita nimesema Chato kuna wananchi 365,000 asome ataona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Iramba mpaka sasa hivi kwa muda…

T A A R I F A . . .

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei kwa sababu hata Singida kuna utalii vilevile.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Iramba kwa muda mrefu sana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.

Kwanza nianze kwa kusema kwamba kama Taifa tunahitaji mjadala mkubwa sana kwenye sekta ya elimu. Elimu yetu inapitia kipindi kigumu sana, elimu ya Tanzania inapitia kipindi kigumu na hili limethibitishwa hata na Rais wa awamu iliyopita Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete; na hili pia limethibitishwa na Rais ya awamu ya nyuma Mheshimiwa Benjamin William Mkapa. Tusiitazame elimu katika sura ya kutoa ajira peke yake ni vyema tukaitazama elimu katika sura pana hasa sura ya kichumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi zote ambazo ni magwiji kiuchumi siri kubwa wali-invest kwanza kwenye sekta ya elimu. Taasisi zote, mamlaka zote za kiuchumi na za kifedha zinathibitisha kwamba elimu ndiyo sarafu ya dunia. Kwa sasa tafsiri yake ni kwamba elimu ndiyo inayoshikilia uchumi wa dunia kwa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi nchi ambazo zimeshaendelea ambazo siri yao kubwa ni kwenye sekta ya elimu, wali-invest kwa kiwango kikubwa mfano ni China. Mwaka 1970 alikuwepo Rais mmoja anaitwa Deng aliwahi kupiga simu saa tisa usiku akampigia Rais wa Marekani Jimmy Carter akimuomba apelike wanafunzi 5,000 kwa ajili ya kupata mafunzo kwenye teknolojia kwenye vyuo vya teknolojia. Jimmy Carter kwa kuona umuhimu wa simu ile usiku akamwambia badala ya wanafunzi 5000 lete wanafunzi 1,00,000. Alifanya vile kwa sababu pia kwanza alihisi huenda kuna uvamizi kwenye nchi yake, lakini kwa umuhimu wa muda ule kupigiwa simu ile akaona yule mtu amethamini sana suala hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Trump analalamika kwamba China wanaiba teknolojia, anashindwa kujua kwamba ilikuwa ni mpango wa China wa miaka mingi baada ya wanafunzi kupelekwa Marekani kupata elimu. Dunia inakwenda kwa kasi sana, ni lazima tuende na kasi hiyo kwa sababu bila kufanya hivyo tutaendelea kuwa wasindikizaji. Nimesoma moja ya jarida la Harvard Business la Mei 2017 linaonesha kwamba kwa miaka 10 mfululizo kuanzia mwaka jana kutakuwa na capital flight ambayo imeanzia Marekani ikaenda China sasa inatoka China inakuja Afrika, inakwenda kutengeneza ajira takribani milioni 85 mpaka milioni 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri kama Taifa tumeandaaje vijana wetu kwa ajili ya fursa kama hii? Kwa sababu hii capital flight kwenye manufacturing sectors ambayo itakuja Afrika kama vijana wetu wangekuwa na uwezo ambao wakiwa skilled wakiweza ku-compete kwenye sekta ya ajira miongoni mwa vigezo vikubwa ambavyo vitaweza kutumika kwenye mitaji hii ambayo itakuja Afrika ni pamoja na wafanyakazi kwenye nchi husika wakiwa na wafanyakazi ambao watakuwa ni skilled. Ninasikitika kwamba kwa Tanzania tunaweza kukosa fursa hii kwa sababu ya kuendelea kupuuza sekta ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Serikali inapambana kutengeneza Stiegler’s Gorge, wakati Serikali inapambana kutengeneza standard gauge kama njia za ku-influence investment, don’t forget about education. Hii ni sifa mojawapo kubwa ambayo wawekezaji wengi wanaitumia wanapokwenda kuwekeza. Nisikitike zaidi kwamba elimu yetu imefikia hatua kwamba unaweza ukakuta kwamba graduate anashindwa kuandika hata sentensi moja kwa lugha ya kiingereza. Unaweza ukakuta graduate anashindwa kuandika barua ya kuomba kazi kwa Kiswahili anashindwa kuandika format haya ni majanga ambayo kama taifa tunaendelea kutia aibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo kadhaa ya kuishauri Serikali. Moja Serikali ni lazima muongeze juhudi za kufanya auditing kwenye education, mfanye ukaguzi wa kina, na uwe katika international standard kwa sababu kunaonekana kuna kizungumkuti sana kwa wakaguzi wetu hata hawa wakaguzi wanaofanya ukaguzi wanapashwa kufanyiwa ukaguzi pia, hii ni kwa sababu inaonesha kuna mapungufu makubwa sana katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo nataka kuishauri Serikali ni kwamba mchujo wa ufaulu wa wanafunzi ni lazima uzingatie uwezo wa wanafunzi, msifanye siasa kwenye hili. Leo division kesho GPA sijui kesho kutwa kitu gani!

Wale wanaostahili kufaulu wafaulishwe wale wanaofeli wafelishwe, tusianze kufanya siasa kwenye elimu. (Makofi)

Suala la tatu, Serikali lazima mu-invest kwa nguvu kubwa kwenye elimu ya kati, ile fedha ya skills development levy ambayo mmeitoa na kuipeleka kwenye mkopo wa elimu ya juu irudisheni VETA. Hii elimu ya kati inakufa, huu uchumi wa viwanda nani anaenda kufanya kazi hapo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu Serikali mnapaswa muwakumbuke. Moja ya vitu ambavyo Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi ya Awamu ya Tano mnakosea ni kusahau walimu wetu. Serikali hii imepuuza walimu, Serikali hii inanyanyasa walimu, Serikali hii haioni mchango wa walimu, Serikali hii haioni kama kuna umuhimu wowote wa kuwasaidia walimu. Kenyatta hapa ameongeza asilimia tano mishahara ya walimu, ninyi mnaona walimu kama using machine, I don’t know mnawaonaje walimu wetu wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba muwakumbuke walimu wetu hawa, muwakumbuke na muwathamni kweli kwa sababu wao ndio chanzo cha maendeleo yoyote ya kiuchumi kwa sababu kupitia elimu wanayoitoa tunaenda kupata watu ambao ni productive. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende sasa kwenye Chuo cha UDOM na na-decraire interest mimi ni mwanafunzi wa pale namalizia masters yangu pale. Hiki chuo kilikuwa kina mpango wa kusajili wanafunzi mpaka 40,000; lakini mpaka sasa wamesajiri wanafunzi 25,000 tu, na wanashindwa kufanya mwendelezo kwa sababu ya ninyi kwenda pale kuweka Wizara zenu sita. Haijulikani mnaondoka lini haijulikani mko pale, yaani hamjielewi. Chuo cha UDOM wakati kinajengwa planning yake haikuzingatia kwamba kuna Wizara sita zinakwenda kukaa pale, barabara ambazo ziko UDOM ninyi mnajua wanafunzi wanakoishi na madarasa yalipo kuna umbali wa kilometers… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwanza kabisa, nianze kwa kusema yapo mambo katika Taifa letu ambayo kiukweli yanatia kichefuchefu sana. Kama Taifa na Bunge endapo mambo haya hayatachukuliwa hatua yoyote sisi Wabunge humu ndani tunakosa sababu ya kuendelea kuwa humu ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie picha halisi ya ufisadi mkubwa unaofanyika kwenye mradi wa Songas. Kwenye mradi wa Songas kuna ufisadi mkubwa sana. Ukiangalia investment ya mradi wa Songas kwenye upande wa capital structure, Songas wali-invest karibu Euro milioni 392. Katika Euro 392, Serikali ilitoa Euro milioni 285 ambayo ni sawasawa na asilimia 73 na Songas wenyewe walitoa karibia asilimia 27 peke yake, shikilia hapo kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye shareholding structure umiliki kwenye mradi wa Songas, Serikali inamiliki only 46 percent na Songas inamiliki 54 percent ya mradi mzima. Swali kwa Serikali ambalo ningependa Mheshimiwa Waziri anapokuja kesho ku-wind up hapa aseme. Kama Serikali kwenye capital structure ime-invest kwa asilimia 73 kwa nini kwenye shareholding structure inamiliki asilimia 46 peke yake? Serikali kwenye shareholding structure inakuwa minority wakati kwenye investment imekuwa majority kwa ku-invest 73 percent. Swali la kwanza hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kila mwezi TANESCO inalipa Dola milioni tano kwenye mradi wa Songas kama capacity charges. Capacity charges ni kitu gani? Capacity charges ni fidia anayopewa mwekezaji kufidia gharama alizowekeza na lengo kubwa ni kutaka baada ya mkataba kuisha ile mali inakuwa chini ya Serikali. Sasa Serikali kupitia TANESCO inalipa Songas Dola milioni tano kila mwezi kila mwezi, katika Dola milioni tano kila mwezi wanaacha kutoa Dola milioni 3.6 kwa ajili ya Serikali kama Serikali ambayo imetoa 73 percent kwenye uwekezekaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipiga mahesabu ya toka mradi huu ulipoanzishwa mwaka 2004 mpaka sasa ni 14 years, Dola milioni 3.6 kwa miaka 14 tumepoteza zaidi ya trilioni 1.3. Mkataba huu wa Songas ni wa miaka 20, tafsiri yake ni kwamba huu mkataba unakwenda mpaka mwaka 2024, kama mtapuuza tunakwenda kupoteza zaidi ya trilioni mbili kwenye mradi mmoja peke yake wa Songas. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo Serikali kuna wakati lazima msikilize na mtii. Mamlaka kubwa kama Bunge inaposhauri ni lazima msikilize, mamlaka kubwa kama CAG inaposhauri lazima msikilize. Suala hili la ufisadi kwenye Songas limezungumzwa kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge mwaka 2005, ninayo hapa na mwaka 2006 chini ya Mwenyekiti wake, kipindi hicho alikuwa Mheshimiwa William Shelukindo, katika ukurasa wa 8, anaeleza namna ambavyo mkataba huu una ubadhirifu mkubwa na Serikali inaibiwa pesa nyingi sana, lakini Serikali ikauchuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, CAG akaja mwaka 2009 ninayo hapa taarifa, akaelezea vizuri kupitia ukurasa wa 135 namna ambavyo Serikali inapoteza pesa na mkataba ulivyokuwa umekaa kijizi-jizi. CAG ameeleza vizuri sana, kwa sababu ya muda nashindwa kusoma, lakini Waheshimiwa Wabunge wakipata nafasi wapitie hii ripoti ya CAG ya mwaka 2009, ameeleza vizuri sana. Ufisadi huu Ndugu Ludovick Utouh ameupambanua vizuri sana na huyu ni CAG mwingine tofauti na wa sasa hivi lakini mpaka hapo Serikali bado ikaendelea kuuchuna. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, akaja CAG mwingine Profesa Mussa Assad mwaka 2018 na ninyi mnajua ni juzi tu hapa. Ukiangalia ukurasa wa 131 ameeleza vizuri namna gani na amechambua kwa mahesabu, tunapoteza fedha kiasi gani kwenye mkataba wa kijizi ambao tumeingia mwaka 2004, lakini mpaka sasa Serikali hii bado mnauchuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naongea hapa, hasira za Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwenye mkataba wa IPTL nategemea kuziona kwenye mkataba wa Songas kwa sababu hawa ni Kulwa na Doto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naliomba Bunge lako Tukufu liunde Kamati. Kama hili jambo limekuwa likipigwa danadana toka mwaka 2004 mpaka sasa na tumeshapoteza trillions of money, naomba Kamati iundwe iweze kuchunguza jambo hili. Tetesi zilizopo ni kwamba suala hili limefunikwa na kigogo mkubwa ambaye hagusiki kwa namna yoyote ile na ndiyo maana Serikali inakuwa inasuasua katika kuchukua hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kauli ya Serikali itakuwa haijanyooka vizuri, naahidi kuleta Hoja Binafsi humu ndani, mbivu na mbichi zijulikane. Haiwezekani tukaendelea kuibiwa namna hii. Naomba nitangaze rasmi, mwenye masikio asikie, mradi wa Songas ni mali ya Serikali, Songas ni mali ya wananchi na Songas ni mali ya Taifa. Naongea kwa ujasiri huu kwa sababu naamini kwamba Serikali ili-invest pesa nyingi sana kwenye mradi huu lakini haipokei chochote kutokana na mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa tabia hizo hizo za kuendelea kupuuza hivyo hivyo, kuna mambo ambayo niliyazungumza hapa mwaka 2016/2017 lakini mpaka leo Serikali haijachukua hatua yoyote. Hizi sheria tumezitunga wenyewe, tumezipitisha wenyewe, pale ambapo tunaona sheria zinavunjwa ni vema hatua ikachukuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye transfer of shares ambayo hata kwenye Kamati Mheshimiwa Waziri nilihoji lakini majibu hamkunipa, nikahoji FTC majibu hawakunipa, nikamfuata Mkurugenzi wa TPDC personally majibu hakunipa, alikuwa anababaika tu. Kulikuwa kuna transfer of shares kutoka vitalu vya gesi kutoka Kampuni ya BG kwenda Kampuni ya Shell. Utaratibu uliopo ni kwamba, kama kuna transfer of shares yoyote, ukiangalia Financial Act ya mwaka 2012, kipengele cha 29 kinaeleza kwamba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda za mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ni bahati mbaya sana huu ni mwaka wa tatu nikiwa humu Bungeni kama Mbunge, kwenye Mabunge ya Bajeti, Bunge linakuwa linajikita zaidi kujadili ni namna gani Serikali itumie fedha badala kwa sehemu kubwa kujadili ni namna gani Serikali ikusanye fedha. Nitakwenda kujikita kwenye eneo la ukusanyaji wa fedha. Kuna eneo moja ambalo ni very strategic napenda Mheshimiwa Mpango alizingatie kwa umuhimu mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunajua kwamba Serikali inamiliki shares kwenye makampuni mbalimbali, yapo makampuni ambayo Serikali ina total ownership lakini pia yapo makampuni ambayo Serikali inamiliki asilimia fulani ya shares. Kuna changamoto kubwa sana hapa, haya makampuni ambayo Serikali inamiliki share kadhaa yamekuwa yana tabia ya kutoa taarifa ambazo siyo sahihi. Haya makampuni yanatoa taarifa ambazo siyo sahihi kwenye mitaji yake, faida inayoingiza na usahihi wa gawio ambalo linatolewa Serikalini. Sababu kubwa ya Serikali kushindwa kukagua gawio ambalo inapata kutoka kwenye makampuni haya ni kwa sababu kuna sheria ambayo ipo inambana/inamzuia CAG kufanya uchunguzi kwenye makampuni ambayo Serikali inamiliki shares chini ya asilimia 50. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Dkt. Mpango hauoni kwamba kuna haja kubwa sana ya Serikali kuchukua shares zake kuzihamisha kutoka kwenye haya makampuni na kuzipeleka kwenye Soko la Mitaji (Stock Market)? Tunajua kwamba kwenye Stock Market kuna very serious scrutiny, wanafanya ukaguzi wa kina na mahesabu yanawekwa wazi. Napenda kutumia fursa hii kumwomba sana kuchukua shares kutoka kwenye makampuni mhamishie kwenye Soko la Mitaji ili muweze kujua haya makampuni yanaingiza mtaji na faida kiasi gani na mwisho mjue usahihi wa gawio ambalo Serikali inapata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mifano mizuri sana. Makampuni yote ambayo yako listed kwenye soko la mitaji mfano NMB na TBL wanafanya vizuri sana, wanatoa gawio kubwa kwa Serikali lakini pia wanatoa kodi kubwa sana kwa Serikali. Ni kwa sababu kuna uwazi mkubwa ambao unatokana na Stock Market. Hata humu Bungeni tulipitisha sheria ya kuyataka makampuni ya mawasiliano na makampuni ya madini kuwa registered kwenye Soko la Mitaji purposely kutaka yawe wazi. Sasa unajiuliza kwa nini hamuoni umuhimu kwenye eneo ambalo mna-interest kwa sababu mna shares kwenye haya makampuni, mkachukua shares mkazipeleka kwenye Soko la Mitaji ili muwe na uhakika wa gawio ambalo Serikali inaingiza? Naomba atakapokuja ku-wind up hapa ajaribu kuligusia hili kwa umuhimu wake mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Dkt. Mpango vizuri sana; kuna eneo nimeona amefuta kodi kwa ajili ya ku-influence the investors, well and good, hilo nampongeza sana. Kuna jambo moja ambalo napenda kumshauri, kuna kodi ambayo ina utata mkubwa sana, nashauri ipitiwe upya ikiwezekana na yenyewe iondolewe kwa sababu ina-discourage sana investors.

Mheshimiwa Mwenyekiti, investor anaweza akaja aka- invest kupitia viwanda moja kwa moja na yupo mwingine anaweza akaja aka-invest kupitia kununua shares kwenye Soko la Mitaji. Sasa unakuta mwekezaji ameweka shares zake kwenye Soko la Mitaji, zimekaa kule labda takribani miaka mitatu akaona hakuna kinachoongezeka akaamua kutaka kuziuza, anapokwenda kuziuza muda aliotumia kununua labda ni miaka mitatu iliyopita, let’s say labda alinunua dola 1,000 kwa miaka mitatu iliyopita wakati huo exchange rate ikiwa ni Sh.2,000 akaja labda akauza baada ya miaka mitatu shares zile zile dola 1,000 kwa exchange rate ya Sh.2,200, mnakuja kumtoza Capital Gain Tax kwenye ongezeko la exchange rate. Hii kodi ina-discourage sana investors, nashauri hii kodi iondolewe kwa sababu mnapokuja kukata Capital Gain Tax kwenye ongezeko la exchange rate mnakuwa hamuwatendei haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine ambalo napenda pia kuligusia kwenye sekta ya mifugo. Haya ni maajabu ya dunia, Tanzania tunazalisha maziwa kwa mwaka takribani lita bilioni 2.4, Kenya hapo majirani zetu wanazalisha kwa mwaka lita takribani bilioni 5.4, tuna difference karibu ya lita bilioni 3. Kinachonishangaza zaidi ni kwamba wakati Kenya wanazalisha lita za maziwa bilioni 5.4 Tanzania tunazalisha lita bilioni 2.4 wakati tuna ardhi kubwa sana, mito mingi sana, maziwa na mifugo mingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo, Mheshimiwa Mpina na nashukuru yupo hapa, hakuna sehemu yoyote nimeona amegusia suala hili na ameeleza ana mkakati gani kuifanya Tanzania kuwa champion kwenye uzalishaji wa maziwa. Kama Taifa tuna kila sababu ya kuwa maridadi kwenye uzalishaji wa maziwa kutokana na namna ambavyo tumebarikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na suala la LNG. Hili suala la LNG nililizungumza toka mwaka 2015 naingia humu Bungeni. Limekuwa ni suala ambalo limepigwa danadana miaka nenda miaka rudi. Nilipitia jarida moja la Reuters mwezi Machi, 2018, TPDC wananukuliwa wanasema kwamba makubaliano ya LNG pamoja na haya makampuni mjadala wake kwa sababu umeshakuwa mzito na wameushindwa, Serikali imetangaza sasa apatikane Mshauri Mwelekezi aweze kutoa mawazo yake aisaidie Serikali kuweza kuingia makubaliano sahihi na haya makampuni. Mkurugenzi wa TPDC akanukuliwa akisema kwamba toka mwezi Machi mpaka kufikia mwezi wa Mei, suala hili litakuwa
limekwishatekelezeka, lakini mpaka sasa hivi tunaenda mwezi Agosti hakuna kunachoeleweka wala kinachofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya sana kwa sababu huu ni mradi ambao unakwenda kutengeneza historia mpya ya Taifa letu katika ukanda wa Afrika Mashariki, hakuna mradi mkubwa kama huu Ukanda wa Afrika Mashariki nzima. Ni mradi mkubwa sana. Ni investment kubwa sana ambapo kama Serikali nilitegemea hata kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri angeielezea kwa mapana yake, kwa uzuri na kwa kuifafanua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyoendelea kuchelewa hivi Msumbiji wameshateka soko lote la East Africa. Ni vema tukatumia nafasi hii vizuri, kama huyo mtaalam mnamtafuta wa kuja kusaidia ku-negotiate kwenye masuala ya kisheria na kuhakikisha kwamba kunakuwa na win-win situation do that, kwa nini mnachelewa? Kwa nini suala hili mnakuwa mnalipiga danadana miaka nenda miaka rudi? Inasikitisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nigusie Deni la Taifa. Deni la Taifa linazidi kukua kwa kasi ya ajabu na linazidi kukua kwa sababu kuna mambo mengine ambayo tunayaona kama ni madogo lakini yanachangia kwa kiwango kikubwa sana ukuaji wa deni hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kumsikia Mheshimiwa Rais hata Mheshimiwa Waziri kipindi fulani akisema kwamba Serikali iko pia busy kulipa madeni ya kipindi cha nyuma sana. Kwa kufanya hivyo, tafsiri yake ni kwamba kuna fedha ambazo Serikali inalipa madeni ya nyuma ambayo yalikopwa kwa exchange rate ya kiwango hicho kwa wakati huo. Mnapokuwa mnalipa wakati huu mnalipa kwa exchange rate ya wakati huu kwa maana hiyo mnakuwa mnalipa fedha nyingi zaidi ukilinganisha na kama madeni hayo yangelipwa wakati huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna njia ambayo niliisoma ambayo Uganda wanai-apply katika kukopa na kulipa. Kuna mfumo ambao…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kujadili kwenye hotuba hii muhimu ya mpango wa maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapojadili mpango wa maendeleo kimsingi tunajikita kwenye mambo matatu makubwa, jambo la kwanza tunajadili ni namna gani tunakwenda kuongeza mapato; jambo la pili, tunajadili ni namna gani tunakwenda kupunguza gharama ambazo sio muhimu kwa maana ya kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, lakini jambo la tatu tunazungumza namna ya kutekeleza vipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nitakwenda kugusia upande wa ni namna gani tunaweza kuongeza mapato. Nitajikita kwenye eneo ambalo ninaamini kwa sehemu kubwa sana tunapoteza mapato; tunapoteza mapato mengi kwenye eneo la mikataba mibovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni bahati mbaya sana na ninashindwa kuilewa commitment ya Serikali katika hili. Kwamba, ni kwa nini mnashindwa kufanya review kwenye mikataba mibovu ambayo tunapoteza mapato mengi Serikalini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 5 mwezi Mei mwaka huu alisimama AG humu ndani, kipindi cha Bunge la Bajeti akiwa anajibu hoja yangu ya mikataba mibovu, specifically kwenye Mkataba wa SONGAS. Ali-declare na akakubali kwamba, mkataba wa SONGAS ni mkataba ambao uko very complicated na Hansard ninayo hapa ya siku nzima ya tarehe 5, kwa sababu ya muda siwezi kumnukuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliahidi kwamba, mikataba mibovu ukiwepo mkataba wa SONGAS utakwenda kufanyiwa marekebisho ndani ya miezi miwili kuanzia mwezi wa tano, lakini mpaka hivi ninavyoongea leo huu ni mwezi wa 11 hakuna mrejesho wowote, hakuna chochote ambacho kumefanyika na kila mwezi kuanzia mwezi wa 05 mpaka sasahivi mwezi wa 11
tunapoteza dola milioni tano kila mwezi kutokana na mkataba huu mbovu for 14 years, kwa miaka 14 tumekuwa tukipoteza mapato kutokana na mkataba huu. Hapa ndio ambapo naweka kigugumizi ni kwa nini Serikali inashindwa kurekebisha kufanya review kwenye mikataba hii ambayo inaingiza hasara kubwa kwenye Taifa letu? Nataka wakati tunahitimisha Mheshimiwa AG aje atupe mrejesho wa wamefikia wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ukienda ukiangalia international standards za contracts kuna kipengele kwenye mikataba ambayo, especially mikataba ya umeme, kuna kipengele kinaitwa despute resolution. Hiki ni kipengele ambacho kama kuna conflict of interest kwenye pande mbili kwenye mkataba basi, wanapata fursa kupitia kipengele hiki kwenda kufungua account ambayo inaitwa ni Escrow Account, wanaweka fedha kule mpaka mgogoro utakapokwisha. Kwa nini kwenye suala la SONGAS kunakuwa kuna kigugumizi cha kuchukua mapato yanayopatikana kupeleka kwenye account ya Escrow mpaka pale tutakapojua mbivu na mbichi ni zipi? That is question number one.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni kwa nini kwenye Mkataba wa SONGAS Serikali mnashindwa kuchukua kesi na kuipeleka arbitration? Who is behind this kiasi kwamba, mnashindwa? Mbona kesi ngapi mnazipeleka arbitration kwa nini kesi ya SONGAS ambayo taarifa mmepoteza pesa nyingi kuliko hata kwenye kipindi cha IPTL?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni hii tunaingia hasara kubwa sana kama Serikali, sijajua ni kwa nini tunasuasua katika kuchukua hatua? Ninashindwa kuelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo kama Taifa tunapoteza mapato, hapa naomba niwazungumzie TEITI na nichukue fursa hii kuwapongeza sana TEITI (Tanzania Extractive Industry Transparency Initiatives). TEITI wote tunajua ni muunganiko wa makundi matatu, kundi la kwanza ni asasi za kiraia wako watano, kundi la pili ni makampuni wawakilishi kutoka kwenye makampuni ambao wako watano, makampuni ya sekta ya uziduaji, na kundi la tatu ni wawakilishi kutoka Serikalini jumla wako 15 ni makundi muhimu sana. TEITI wametoa ripoti mwezi wa nne mwaka huu ambayo inaonesha kwamba Serikali ya Tanzania inakiri kupokea shilingi bilioni 435 kutoka kwenye makampuni yanayo-deal kwenye sekta ya uziduaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo makampuni husika, kwa maana ya makampuni yanayo--deal kwenye oil, gas and mining, yanakiri kwamba yenyewe yamepeleka Serikalini bilioni 465. Sasa na TEITI wanasema kwamba huu utafiti walioufanya uli-deal na makampuni 50 kati ya makampuni 1,287. Unaweza ukajiuliza kama kwenye makampuni 55 peke yake ya sekta hii ya uziduaji wamegundua kuna upotevu wa fedha shilingi bilioni 30 what if wangefanya upekuzi kwenye makampuni 1,287 tungekuwa tumepata hasara kiasi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, well and good Mheshimiwa Waziri ali…

T A A R I F A . . .

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa sababu amezidi kuishindilia hoja yangu na kuthibitisha kwamba kuna sintofahamu ya shilingi bilioni 30. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amesema kwamba wamepeleka taarifa ili CAG aweze kukagua haya makampuni. Swali dogo sana, wote tunajua kwamba, sheria haimruhusu CAG kufanya ukaguzi kwenye makampuni ambayo Serikali inamiliki less than 50% ya shares kwenye makampuni hayo. Sasa anatuthibitishia kwa kiwango gani kwamba CAG atapata mamlaka ya kwenda kufanya upembuzi na ukaguzi ambao ni wa uhakika na wakati bado hana authority ya kufanya hivyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hii niiseme tu, kipindi kijacho tutunge sheria ambayo itampa uwezo CAG aweze kwenda kupenya mpaka kwenye makampuni ambayo Serikali inamiliki less than 50% ili kuweza kuondoa mapato yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tukishindwa kudhibiti mapato yetu yanavyoendelea kupotea hatuwezi kufanya maendeleo yoyote, miradi yoyote haiwezi kufanyika. Natambua zipo njia nyingi ambazo zinatumiwa na makampuni mbalimbali kukwepa kodi na kupoteza mapato yetu. Na moja ya njia hizo, yapo makampuni ambayo yanatumia njia ya transfer pricing, yapo makampuni ambayo yanatumia njia ya thin capitalisation na yapo makampuni ambayo yanatumia njia ya production cost na eneo hili ndio sisi kama Taifa tunapoteza sana.

Kwa hiyo, nilikuwa ninaiomba Serikali kwa unyeyekevu mkubwa sana wala sina nia ya kumkomoa mtu yeyote hapa, ninachojaribu kukifanya ni kutaka kama Bunge, kama Serikali, kama nchi, tuhakikishe tunalinda mapato yetu na hatupotezi mapato yetu kwa namna yoyote ile. Kwa sababu siku ya mwisho wanaokwenda kuumia ni sisi wenyewe. Tunakaa hapa, tunakaa Bungeni tunakula fedha za wananchi kwa njia ya posho tunajadiliana mambo ambayo utekelezaji wake ni mdogo sana kwa sababu kubwa usimamizi wa mapato bado ni mdogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili ni jambo la msingi ambalo nashauri sana na wala nisitafsiriwe tofauti, ni kwa nia ya kutaka kujenga.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza kwa masikitiko makubwa sana nikutaarifu tu kwamba taarifa ambayo umesomewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Wajumbe wa Kamati hatujapata fursa ya kuipitia; na sijajua lengo hasa ni nini, taarifa tumekuja kukutana kama ambavyo wewe umeisikia hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasimama mbele ya kiti chako kwa dakika kumi ambapo dakika zote hizi kumi nakwenda kuzungumzia suala moja tu na suala hili leo ninazungumza ni mara ya tano na sio lingine ni juu ya SONGAS.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashindwa kuelewa ni kwa nini suala hili limekuwa ni gumu sana kuchukuliwa hatua. Nashindwa kuelewa ni kwa sababu gani Serikali imekuwa ikisuasua kuchukua hatua kwenye suala hili la ubadhirifu wa rasilimali za wananchi wa Tanzania. Waheshimiwa Wabunge nafikiri hawajapata fursa ya kuelewa vizuri suala hili ndiyo maana wanashindwa kujua uzito wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ufupi sana, utafutaji wa gesi asilia kwenye visima vya SONGAS ulianza mwaka 1969, mpaka kufikia mwaka 1990 Serikali ilikuwa imeshatumia zaidi ya dola milioni 150. Baada ya tafiti kuonesha kwamba gesi inaweza kutumika kuzalisha umeme, Serikali kwa haraka sana ikatangaza zabuni na wakampata mzabuni ambaye ni SONGAS.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mpaka hatua ya mzabuni kupatikana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia TPDC ilikuwa inamiliki visima vitano vya gesi ikiwepo kisima namba tatu, nne, tano, saba na tisa. Pia TPDC walikuwa wanamiliki mitambo ya kuchakata gesi ambayo pia ilikuwa ni mali ya Serikali. TANESCO walikuwa wanamiliki mitambo ya kuzalisha umeme ambayo yalikuwa ni majenereta manne, yapo pale Ubungo Dar es Salaam. Pia eneo la Songosongo ambapo visima hivi vinapatikana, lilikuwa ni eneo ambalo lipo chini ya TPDC kwa maana hiyo lilikuwa ni eneo la Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi, Serikali ikaona ili mradi uweze kuanza ikaenda kuchukua mkopo kutoka World Bank Dola za Kimarekani milioni 216, sasa viini macho vinaanzia hapo. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliwapa SONGAS visima vyake vyote vitano bure bila gharama yoyote kulipwa! Kiini macho namba mbili, Serikali iliwapatia SONGAS mitambo ya kuchakata gesi bure bila gharama yoyote kulipwa. Kiini macho namba tatu, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliwapatia SONGAS zile jenereta nne za TANESCO ambazo zipo pale Ubungo bure bila gharama yoyote kulipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ile asilimia tisa ambayo kwenye mkataba inaonesha kwamba ndio hisa za TANESCO walikisia tu kwamba tathmini ya eneo zima lile la TANESCO ni dola milioni moja, huu ni wizi wa mchana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hisa ambazo zinamilikiwa na TPDC asilimia 29. Hisa hizi wamefanya makisio bila kuwa na evaluation report. Wanasema eneo la Songosongo na njia yake ya kupitisha bomba la gesi linakadiriwa kuwa na thamani ya dola milioni tatu lakini ukiuliza evaluation report iko wapi, haipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kiini macho cha mwisho, japokuwa mitambo na kila kitu SONGAS walipatiwa na Serikali, lakini bado Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia TANESCO tunawapa fedha za fidia SONGAS na wakati katika uwekezaji Serikali ndiyo imewekeza kwa kuwapa mitambo na kila kitu kwa maana ya capacity charge tunatoa sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa kuliko yote, ningependa Serikali ituambie, kwamba dola milioni 60 za kwenye ESCROW akaunti zimekwenda wapi? Hii ni kwa sababu Serikali pamoja na mbia wakati wanakubaliana kufanya mradi huu, walikubaliana kuweka dola milioni 60 kwenye akaunti ya ESCROW ilikuwa ni kama kinga kwamba ikitokea mradi usipotekelezeka, basi mwekezaji hiyo pesa anaichukua. Hii pesa ilitokana na kodi ambayo walikuwa wanakatwa wananchi wa Tanzania kwenye petroli na dizeli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mpaka hivi ninavyozungumza na wewe hizi fedha kwenye akaunti hazipo na kibaya zaidi unapowauliza wahusika wanasema kwamba zimetumika kununua mtambo namba tano na vielelezo hawana. Sasa unaweza ukaona ni kwa namna gani katika mradi huu wa SONGAS kuna wizi mkubwa kiasi hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Menejimenti ya Songas ilipata fursa ya kukutana na Kamati. Niliona kwenye taarifa ya Gazeti la The Citizen la tarehe 2 ambalo linaonesha Katibu Mkuu wa Nishati na Madini anaelezea kwamba mapendekezo yaliyokuwa yanatolewa na Kamati iliyoundwa na Mheshimiwa Spika, yameshaanza kufanyiwa kazi miezi miwili iliyopita. Huu ni uongo uliopindukia. Kwa sababu baada ya kukutana na wahusika, Menejimenti nzima ya Songas wanakiri, wanasema hata hiyo ripoti hawajawahi kuisikia wala hawaijui. Sasa ni bahati mbaya tunakuwa na aina ya watumishi Serikalini ambao wanakuwa wanatoa taarifa za uongo bila hata kuwa na aibu! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujua ni kitu gani...

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. JESCA D. KISHOA: …ni kitu gani ambacho…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kishoa kuna taarifa. Mheshimiwa Subira Mgalu.

Hii hoja ni ya Kamati, siyo hoja ya Serikali. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge, mnafahamu, atakayehitimisha hoja hapa ni Mwenyekiti wa Kamati na sio Mawaziri. Kwa hiyo, yeye hapo ni kama Mbunge mwingine kwenye hili. Mheshimiwa Subira Mgalu.

TAARIFA

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vyovyote vile siwezi kupokea taarifa hii, maana hata Wabunge humu ni mashahidi. Hakuna mtu mwenye uwezo wa kuwa na access na hiyo taarifa. Uwezekano wa kupata taarifa hiyo na kuipitia ni mgumu kuliko kawaida. Nami niseme tu, kama tutaendelea kuwa humu ndani na kuendelea kudanganyana kwamba taarifa imekabidhiwa kwenye Umma na kwa hiyo, mambo yanaenda sawasawa, tunakuwa hatutendei haki nafasi zetu kama viongozi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee…

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kubenea.

TAARIFA

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea kwa mikono yote miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, udhaifu mkubwa unaoonekana kwenye mikataba ni sawasawa na baba ameshikwa na mtoto wake, amefungwa mikono na miguu, halafu mtoto anamwita jirani amcharaze viboko baba yake.
Hicho ndicho ambacho kimefanyika. Watoto wa Tanzania…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kishoa malizia dakika moja, kengele ya pili imeshagonga.

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, nina jambo moja tu na ninaomba popote pale alipo Mheshimiwa Rais anaposikia sauti hii, achukulie hatua suala hili, kwa sababu Serikali yoyote inayojinasibu kama ni Serikali inayopinga ufisadi, haiwezi kwa namna yoyote ikaruhusu mkataba wa Songas ukaendelea kuwepo. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani. Kabla ya kuendelea na mchango wangu ningependa kuomba kiti chako kutumia kanuni ya 64(1)(a) ambapo ningependa u-set position, kwa maana ya kwamba Kanuni hii imekuwa ikitumika kwa upande wa Waheshimiwa Wabunge ambao imekuwa ikisemakana wanatoa taarifa za uongo Bungeni basi iwe applicable kwa upande wa Waheshimiwa Mawaziri ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitoa taarifa za uongo na hakuna hatua yoyote inayochukuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Wizara ya Nishati peke yake kuna mambo mbalimbali ambayo yakiahidiwa nami nayahesabia kama ni ya uongo kwa sababu yameshindwa kutekelezeka. Mwaka 2016 mwezi 11 Waziri wa Nishati alipokuwa akijibu swali ndani ya Bunge, swali langu ambalo nilikuwa nina hoji kuhusiana na ujenzi wa miradi ya uzalishaji wa umeme wa upepo aliahidi kwamba kufika mwaka 2017 mwezi wa nne miradi hiyo ujenzi wake utaanza na utakamilika mwaka 2019; lakini mpaka hivi ninavyozungumza Mheshimiwa Naibu Spika hakua taarifa yoyote ambao inaonesha wamekwamba wapi. Ni miezi 30 mpaka sasa hakuna kinachoendelea,

Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 25 Mei, 2018 alisimama AG humu ndani akaahidi baada ya hoja yangu ya mikataba mibovu ikiwemo mkataba wa Songas; akasema ndani miezi miwili, kuanzia mwezi wa tano, kwa maana ya mwezi wa saba, mikataba yote itakuwa imeshafanyiwa review, lakini mpaka kufikia hivi sasa ni takribani mwaka mzima hakuna ambacho kinafanyika. Mwaka 2018 mwezi wa 11 Bunge la mwisho aliyekuwa Waziri wa Madini wakati huo alisimama kutoa taarifa Bungeni kwenye hoja yangu ambayo ilikuwa inahusiana na taarifa kutoka TEITI, taarifa ya nane, iliyokuwa inaonyesha kuna upotevu wa fedha bilioni 30.5, akaahidi akasema kwamba ameshapeleka taarifa kwa CAG na kufikia mwezi wa 12 taarifa itakuwa tayari. Hata hivyo mpaka sasa hivi ninavyozungumza hata kwenye Kamati taarifa hii haijapelekwa na hapa Bungeni kwenye hotuba sijasikia taarifa ya namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu gani, ni muhimu tukajenga heshima ya Bunge hili na Mawaziri waanavyokuja humu ndani wajue kabisa wanazungumza na supreme organ of the state. Pia ni vyema tukajua kwamba moja ya vitu ambavyo vina taste credibility ya Bunge hili ni pamoja na masuala kama haya. Kwa sababu hizi ni sensitive issues lakini ni mambo ambayo yanakosa majibu kutoka Serikali. Ninajua na tunatambua kwamba kuna kitengo hapa Bungeni ambacho kinahusisha masuala ya kufuatilia ahadi za Serikali, na wanalipwa mshahara mzuri sana, nashindwa kuelewa wanafanya kazi gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye hoja nyingine kuhusiana na TEITI. Natamani na ninahitaji kujua kwamba Serikali ina mpango gani na TEITI. Wote tunajua kwamba TEITI ni taasisi ambayo inahusiana na masuala ya uwazi na uwajibikaji; Serikali imeifanya TEITI kama mradi wake na wanasahau kwamba TEITI wana wajibu mkubwa sana katika taifa hili ya kuhakikisha kwamba public inakuwa aware na masuala yote yanayohusu matumizi ya makubwa ya rasilimali zao. Ni vyema Serikali ikatuambia kama haioni umuhimu wa TEITI ni muhimu mkajiondoa kwenye umoja huu kitamaifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa ninavyohamu na ninavyoamini kwa Serikali yoyote ambayo ikijipambanua kwamba yenyewe inayopinga ufisadi kwenye mamlaka au taasisi ambazo zinakuwa zina influence transparency zinaunga mkono kwa kiasi kikubwa sana. Nashindwa kuelewa ni kwa nini Serikali inashindwa kuunga mkono suala hili la TEITI na kuisaidia TEITI. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka kufikia Februari, 2019 TEITI hawajapata pesa yoyote. Taatifa ya utekelezaji wa majukumu ya taiti ya mwaka 2016/2017, 2017/2018 zimebaki kwenye droo kwa sababu TEITI haina mratibu. Ni mambo ya aibu kabisa mamlaka kubwa kama hii kukosa mratibu mpaka sasa hivi. Lakini mmewahamisha kutoka Dar es Salaam ambapo walikuwa wanakaa kwenye Ofisi kubwa jengo kubwa mmewahamisha mmewaleta hapa Dodoma wanakaa kwenye vyumba viwili vidogo viniwafinya kiasi kwamba hata taarifa wanashindwa kuziweka kwenye sehemu husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiona haja ya sisi Wabunge wa Serikali kuhakikisha kwamba tunafanya marekebisho kwenye Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji ya Mwaka 2015 ili kuipa TEITI nguvu na mamlaka yakusimama yenyewe kuwa huru kimiundo na kimifumo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia nigusie suala la bomba la gesi la kutoka Mtwara kwenda Dar es Salam. Moja ya sababu kubwa ya watu wengi kushindwa kununua gesi ya TPDC ni gharama za ujazo wa bomba kuwa kubwa sana. Na kwa sababu mambo hayo mnashindwa kuyaweka wazi kuna taarifa, inasemekana kwamba gharama halisi ya bomba la gesi na gharama tunayolipa kuna ziada ya dola kimarekeni milioni 400.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kulipa gharama zote hizi hii ndio inayopelekea gharama ya gesi hii uwa kubwa. Naomba kupitia Bunge hili Tukufu, na hii nitaishikia shilingi, Serikali iunde timu ya watalamu kwenda kuchunguza gharama halisi ya bomba la gesi, lakini pia wachunguze mkopo ambao tumpewa kutoka China Exim Bank.

Mheshimiwa Naibu Spika, na bahati nzuri sana huu mkataba upo very clear mkataba upo clear kwa maana ya kwamba wanasema hivi, ikitokea kwamba Tanzania tumshindwa kulipa hili deni tujue kabisa kwamba gesi yote inayopatika Mtwara inakwenda kuwa controlled na China na bomba la gesi lenyewe. Hii haitakuwa maajabu kwa sababu hili suala limefanyika Srilanka, limefanyika Zambia. Kwa hiyo ni muendelezo wa mambo ambayo kama hatuwezi kuwa makini tunaweza tukajikuta tunapotea rasilimali muhimu sana katika taifa hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, bomba la gesi ambalo linafanya kazi kwa 6% tu na tumetumia mkopo mkubwa kiasi hicho kwa sababu ya kulijenga, inaonesha ni namna gani kama Serikali tunafanya mambo mengi kwa kukurupuka bila kutafakari na kuwa business plan. Baada ya kusema hayo naomba niunge mkono hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni akushukuru sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapokuwa tunazungumzia maendeleo ya kiuchumi hatuwezi kuacha kuzungumzia suala zima la ubora wa watu, yapo matatizo mengi ambayo yamesababishwa kwa kiwango kikubwa siyo na sera au mfumo, lakini yamesababishwa pia na tatizo la ubora wa watu, kwa maana ya maarifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano mdogo sana, ukiangalia Serikali inakusanya kwa mwezi bilioni 1,300. Katika kila bilioni 1,300 bilioni 580 inatumika kulipa wafanyakazi, kama sawasawa na kama asilimia 45. Sasa unaweza ukaona kwamba, asilimia 45 hii ni portion kubwa sana, lakini inaoneka ni kubwa kwa sababu ya uzalishaji ni mdogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunazungumzia uchumi wa viwanda. Kama Taifa tulishapiga hatua kubwa sana kwenye suala la uchumi wa viwanda toka miaka ya sabini, sabini na tano, cha ajabu tukapiga--reverse big time ukilinganisha uchumi wa viwanda wa sasa na uchumi wa viwanda wa miaka ya 1970 ni vitu viwili tofauti. Kwa mambo kama haya, hata ikitokea Baba wa Taifa Julius Kambarage Nyerere akafufuka leo, atakufa kwa stress ambazo zipo katika Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunazungumzia uchumi wa viwanda tunaambiwa vyerehani, tunaambiwa vyanzo vya mapato ni mawigi. Dunia kwenye Force Industrial Revolution, wanazungumzia artificial intelligence, asimame Waziri yeyote hapa aseme kama kwenye Wizara yake ameshafanya research akaangalia ni kwa kiwango gani artificial intelligence inakwenda kuathiri sekta yake au kwa kiwango gani inakwenda kunufaisha sekta yake, hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vema tuka-invest bila kuogopa kwenye ubora wa watu. Ni mambo ya ajabu sana tunazungumzia uchumi wa viwanda na wakati hatu-invest vya kutosha upande wa watu. Ninaomba kipindi cha zamani tulikuwa tunaangalia kwenye soko la ajira tulikuwa tunapambana sana na Wakenya, lakini sasahivi tunakwenda kupambana na ma-robot kwa sababu, ya uwezo tulionao na nguvu tuliyotumia kuwekeza kwenye ubora wa watu wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naangalia Google wamejenga center kubwa sana ya artificial intelligence pale Accra, Ghana, mwaka jana na wamealika nchi tisa kwenye timu hiyo kuhakikisha kwamba wanapata knowledge ya namna gani artificial intelligence inaenda kunufaisha katika Mataifa yao, kwa upande wa East Africa wamechukua Rwanda peke yake. Kwa hiyo, ni bora wakati tunafikiria uchumi wa viwanda, lakini tukawekeza kwa nguvu kubwa sana kwenye ubora wa watu wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nigusie pia suala la Deni la Taifa. Kwa muda mrefu sana tumekuwa tukipigia kelele suala la Deni la Taifa, mwaka 2016 nilileta maelezo binafsi humu ndani kuelezea ni kwa namna gani Deni la Taifa linakua kwa kasi kubwa sana, lakini mpaka leo Deni la Taifa limeendelea kuwa ni habari ambayo haina majibu ya kutosha. Badala ya kuendelea sasa kuangalia ukubwa wa Deni la Taifa ni muhimu sasa tukajielekeza kuangalia uhalali wa deni hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha Dkt. Mpango atakapokuja hapa nimtake wakati anahitimisha kwa kutumia Audit Report ya Madeni kwa sababu najua Serikali mnakagua madeni, atuambie uhalali wa deni ambalo tunalilipa la bomba la gesi ambapo inaonekana kwa kiwango kikubwa deni hili limekuwa na kizungumkuti kikubwa. Tutaendelea kukamata wauza kahawa na wafanyabiashara wadogo kwa ajili ya kulipa madeni ambayo hayaeleweki watu waliingia katika utaratibu gani? Ninaomba Mheshimiwa Mpango afanye hivyo, atuambie gharama halisi ya gharama ambayo ilitumika kujenga bomba la gesi na atuambie tunalipa kiasi gani kila mwezi kufidia gharama hiyo ya bomba la gesi? Na kama hatafanya hivyo, nakusudia kuleta hoja binafsi Bunge lijalo, kutaka Serikali iunde Tume kwa ajili ya kuchunguza suala hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia, nigusie kwenye suala zima la TRA. Imekuwa ni kama utaratibu fulani hivi kwamba nchi nyingi ambazo ni za kimasikini zimekuwa na utaratibu wa kutengeneza muundo mkubwa sana wa Serikali na kuu-feed kwa gharama kubwa sana. Hii inaonesha ni kwa kiwango gani ambavyo tunakuwa tunakosa trust na private sector.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Mataifa ambayo yameonesha trust kwa private sector kiwango cha kuzipa private sector mamlaka ya kutengeneza Mahakama. Kwa mfano kama Marekani, lakini sisi imefikia hatua kwa mfano TRA tunashindwa nini kutengeneza mfumo ambao utatusaidia kukusanya kodi kiurahisi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kupeleka ma- agency maeneo mbalimbali kama ambavyo mabenki yanafanya. Tunakuwa tuna ma-agency mbalimbali maeneo yote nchini ambayo inarahisisha zaidi ukusanyaji wa kodi. Ni vema tukawa tunakuwa innovative kuhakikisha kwamba, tunakusanya mapato na kuhakikisha kwamba tunafanya vizuri kwenye sekta ya uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Natambua tunajadili Mpango huu wakati dunia inapita kwenye mtikisiko mkubwa wa COVID-19. Nimeangalia ripoti ya World Bank, ukuaji wa kibiashara kidunia ulikuwa umeshakua mpaka kufikia asilimia 64 lakini baada ya COVID- 19, biashara ya dunia ime-drop mpaka asilimia 37 ya pato la dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema haya, nataka niiombe Serikali, kwa sababu wataalam wa kiuchumi wamefananisha anguko hili na lililotokea wakati wa Vita ya Pili ya Dunia, nataka tunapojadili hotuba hii ya Mpango basi tuonyeshe reflection kubwa sana na gonjwa hili la COVID-19 ili tuweze kuchangia ndani ya changamoto hii tusiwe tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kutekeleza Mpango tunahitaji fedha ya kutosha. Nimeona Mheshimiwa Mpango na baadhi ya Wabunge wakitoa malalamiko kwa namna ambavyo kumekuwa na malalamiko makubwa sana kwenye ukusanyaji wa kodi, tunahitaji fedha ili kuweza kutekeleza Mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tujiulize ni kwa nini tunakusanya kiasi kidogo cha kodi ukilinganisha na nchi nyingine nyingi lakini pia kuna kilio kikubwa kuhusu mzigo wa kodi. Tanzania tunakusanya kodi asilimia 13 ya pato la Taifa. Nimefanya research kidogo Lesotho wanakusanya asilimia 29 ya pato la Taifa; Kenya wanakusanya asilimia 20 ya pato la Taifa; South Africa wanakusanya asilimia 28 ya pato la Taifa; ukienda Burkina Faso wanakusanya asilimia 18 ya pato la Taifa; Namibia asilimia 30; Zimbabwe asilimia 21.1; Mozambique asilimia 23 na Zambia asilimia 15.2. Tanzania tunakusanya asilimia 13 ya pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini sababu? Hii inathibitisha kuna udhaifu mkubwa sana kwenye sayansi ya kukusanya kodi. Namwomba Mheshimiwa Mpango anapokuja kuhitimisha hapa atuambie ni kwa nini kuna malalamiko na kelele nyingi kwenye ukusanyaji wa kodi na wakati tunakusanya asilimia 13 tu ya pato la Taifa ukilinganisha na nchi nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijielekeze kwenye hoja yangu ya msingi kabisa ya zao la alizeti. Kuhusiana na kilimo cha zao la alizeti kama nchi tunatia kichefuchefu. Naomba niseme hivi, kuna mtu mmoja aliwahi kusema Afrika miujiza haitakuja kufika mwisho na mimi ninaungana naye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia zaidi ya asilimia 60 ya ardhi inayofaa kwa kilimo duniani inapatikana Afrika lakini kila mwaka Afrika tunatoa zaidi ya dola bilioni 27 tunaangiza vyakula kutoka nje. Kwenye muujiza huu, Tanzania hatuko nyuma, kila mwaka nchi ya Tanzania tunaagiza mafuta zaidi ya dola milioni 280. Tunatumia wastani wa dola milioni 280 kuagiza mafuta ya kula kwa pesa za kigeni badala ya pesa za kigeni kuingia ndani kupitia zao la alizeti kwa kuuza mafuta, tunatumia fedha za kigeni kuagiza mafuta kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefanya study ndogo sana kwenye zao la alizeti ambalo limekuwa recognized na WHO kwamba ni zao linalotoa mafuta bora kabisa, inaonyesha kwamba karibu nusu ya eneo la Tanzania linafaa kwa ajili ya zao la alizeti. Mfano, Simiyu, Shinyanga, Singida, Iringa, Morogoro na kwingineko wanaweza kulima alizeti. Cha ajabu tunazalisha tani laki nane peke yake kwenye zao la alizeti, kiasi hiki hakifiki hata 0.1 percent ya kiasi cha mbegu za alizeti kinachozaliwa dunia nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka nitoe mfano wa nchi kama Ukraine, nchi ambayo inaongoza kwa kilimo cha alizeti na uzalishaji wa mafuta. Nchi ya Ukraine inazalisha takribani tani milioni 16.5 kwa mwaka lakini wanalima kwenye square meter za mraba 20,000. Ukisema square meter za mraba 20,000 ni sawasawa na nusu ya Mkoa wa Singida maana Mkoa wa Singida ni square meter za mraba 48,000. Sisi Tanzania tunauza mafuta, kahawa, chai, almasi, tunapata dola bilioni 5 kwa mwaka na wakati Ukraine hiyo dola bilioni tano wameipata kwa kuuza mafuta ya alizeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka nimalizie, kama Ukraine wanafanikiwa, kama Ukraine wanaweza kulima zao hili na kupata manufaa sisi tunashindwa nini? Namwomba Waziri wa Viwanda na Biashara, Waziri wa Uwekezaji, Waziri wa Kilimo hebu wakae chini na kutafakari, umizeni vichwa acheni kumbwelambwela.

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia galoni ya lita tano ya mafuta ya kula inauzwa Sh.28,000, wananchi wanalia, wananchi wanateseka. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MBUNGE FULANI: Taarifa.

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kidogo niwape solution, nataka niwasaidie hawa…

MWENYEKTI: Muda wako umeisha, ahsante sana Mheshimiwa Jesca Kishoa. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwanza kabisa naomba kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji wake mzuri lakini kwa namna ambavyo anaendelea kuonesha weledi katika Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitajikita kwenye maeneo mawili, eneo la kwanza ni la mikataba kuwekwa wazi, wote tunajua umuhimu wa mikataba kuwekwa wazi moja ya advantage kubwa ambayo tutaipata ni kutengeneza trust kati ya wananchi na Serikali, lakini advantage ya pili ambayo tutaipata kama tukiwa mikataba wazi ni investars watajenga trust na Serikali na kuepusha migogoro baina yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, advantage nyingine ambayo ni muhimu sana taasisi mbalimbali kama haki rasilimali na nyingine vyombo vya habari, watafiti watatoa mchango mkubwa sana kushauri Serikali namna bora ya kuingia mikataba hii kwasababu watakuwa wanauwezo wa kufanya ulinganifu wa mikataba mbalimbali. (Makofi)

Mheshimimiwa Naibu Spika, jambo moja ambalo Serikali liweke akili ni rasilimali za nchi yetu ya Tanzania, ni rasilimali za wananchi wa Tanzania Serikali ni wasimamizi tu, ukiangalia kwenye Sheria ya Extractive Industry Transparency and Accountability Act ya Mwaka 2015 sheria inaeleza very clearly inataka mikataba iwekwe wazi. Nataka niihoji Serikali leo kupitia kiti chako pia ni kwa nini Serikali mpaka siku ya leo toka mwaka 2015 ukiangalia mwaka 2016, 2017, 2018 mpaka hivi ninavyozungumza hapa hakuna mkataba hata mmoja ambao umekwisha kuwekwa wazi wa kwenye sekta ya uziduaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tusiogope kuweka mikataba wazi, nchi zimekwishafanya hivyo, Ghana wameweka mikataba wazi, Chad wameweka mikataba wazi, Mongolio wameweka wazi Ukraine wameweka mikataba wazi nchi nyingi nikisema nizitaje hapa nitamaliza muda wangu sisi tunafeli wapi? Kwa nini tunashindwa kuweka mikataba yetu wazi! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up atuambie ni lini Taifa letu Nchi yetu itaanza rasmi kutekeleza sheria ambayo tuliitunga wenyewe ya kuweka mikataba wazi, asipofanya hivyo na kama hataeleza na sitaridhishwa nitashika shilingi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nielekee kwenye TEIT bado tunaendelea kuziba mianya inaonyesha uwazi, tumekataa kuweka mikataba wazi tumejiondoa kwenye OGP Open Government partinership tulibakiza TEIT kama kiashiria pekee cha afadhali at-least kutuonyesha mwanga nini kinaendelea kwenye rasilimali zetu. Lakini nasikitika kukuambia kwamba, TEITtoka mwaka 2018 mwaka wa fedha 2018/2019 hawajapewa hata shilingi tano, mwaka wa fedha 1920 awajapewa hata shilingi tano mwaka 2021 awajapewa hata shilingi tano wanafanyaje kazi hawa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna pesa ambayo imetoka kutoka world bank bilioni 1.75, nafikiri ndio hii ambayo Wizara inatazama inakwenda TEIT, lakini wanatakiwa wajue kwamba fedha hii imetengwa na world bank purposely kwa ajili ya mradi wa EGPS, na hii ni extra-resource ni lazima Serikali itenge fedha kwa ajili ya TEIT ili TEIT iweze kujiendesha yenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niipongeze sana TEIT inafanya kazi kubwa sana pamoja na kutokuwana fedha nimepitia ripoti za TEIT 10 toka mwaka 2009 mpaka mwaka 2019, kuna mambo yanasikitisha kwelikweli, TEIT wamelipoti wanasema hivi, kuna risiti za malipo kutoka makampuni ya madini kwenda Serikalini, hazionekani na wanasema zaidi ya fedha bilioni 90 za kitanzania hazina maelezo ziko wapi na vielelezo havipo hizi sio taarifa za Jesca Kishoa ni taarifa kutoka TEIT. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, CAG alipewa kazi maalum ya kuchunguza ripoti ya saba na ya nane kuangalia fedha hizo zimekwenda wapi, nataka nikujulishe leo kwenye Bunge lako Tukufu ripoti hiyo toka CAG ameifanyia kazi imefichwa makwapani hatujaiona na hatujui hiko wapi. Nina jedwali linaonesha fedha ambazo TEIT imeweka wazi ambazo zinaonesha kuna discrapper za hali ya juu sana kwenye ripoti ya kwanza ya TEIT wanaonyesha kuna fedha ambazo risiti zake zina maelezo yake hayaeleweki milioni 24 zaidi ya bilioni 24 ripoti ya pili inaonesha zaidi ya bilioni tano hazina maelezo na risiti zake haziko wazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ripoti ya tatu inaonyesha zaidi bilioni 10 ripoti ya nne zaidi ya bilioni 2 ripoti ya tano zaidi ya bilioni nane ripoti ya sita zaidi ya bilioni 2 ripoti ya saba zaidi ya bilioni 27 ripoti ya nane zaidi ya bilioni 30 ripoti ya tisa zaidi ya bilioni 1, ripoti ya kumi zaidi ya bilioni 3. Takribani zaidi ya bilioni 90 hazina maelezo yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri Serikali kuna kila sababu ya kutunga sheria ya kumpa mamlaka CAG aweze kuwa na mamlaka ya kukagua pesa zinazotoka kwenye makampuni na pesa zinazolipwa Serikalini. Lakini pia ipo haja kupitia kiti chako kama itakupendeza uitake Serikali ripoti ambayo CAG aliipitisha ripoti ya saba na ya nane ambayo aliikagua akairudisha wizarani iletwe hapa Bungeni Wabunge tuihoji na tuipitie kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naushauri wangu wa mwisho kwa Serikali kama itapendeza hebu ipeni mamlaka STAMICO ipeni nguvu kama ambavyo mmeipa nguvu TPDC, ili STAMICO kama itakuwa ina uwezo wakuwa na shares iweze kusajili shares zake kwenye soko la mitaji automatically hesabu zitakazokuwa zinaingia zitakuwa zinaonekana kwasababu ukishaingia kwenye soko la mitaji, ukishapeleka shares zako huko automatically wewe hesabu zako zinakuwa wazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana. Ahsante. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba mimi ni Mbunge wa Kambi ya Wachache lakini pia pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri wa Fedha Mheshimiwa Mwigulu Nchemba amekuwa ni mpinzani wangu kwa term mbili mfululizo Jimboni kwangu Iramba Magharibi na nikiri kwamba tulitifuana kwelikweli, lakini ninaomba nikiri kwamba na bila kigugumizi kwamba bajeti hii ni miongoni mwa bajeti ambazo ni bora sana ambazo tumewahi kuwa nazo katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii ni bora kwa sababu inakwenda kutua mzigo wananchi wetu, tumeona tozo nyingi zimefutwa, kodi, ushuru mbalimbali zimefutwa kama ambavyo zimeonekana kwenye ukurasa wa 28 na 31 wa kitabu cha bajeti. Kwa kusema hivyo ni wazi kwamba kama Serikali inaweza kuwapunguzia mzigo mkubwa wananchi wa tozo hizi, inatakiwa kugombezwa au kupongezwa, inatakiwa kupongezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi yapo mambo ambayo lazima tushauri, nchi yoyote ambayo inaweza ikaonesha ina uwezo wa kujiendesha na kujisimamia kiashiria kikubwa kabisa ni kwenye mapato yake ya ndani, ukiangalia kwa mujibu wa sura ya bajeti yetu utaona kwamba tunatarajia kukusanya trilioni 26.03 mapato ya ndani, ukiangalia matumizi ya kawaida tunatarajia kuwa na trilioni 23 point something, sasa ukichukuwa mapato ya ndani ukatoa matumizi ya kawaida unabaki na trilioni three point something.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tusingekuwa na mikopo na misaada ya kibajeti ni wazi kwamba tulikuwa tunakwenda kutumia trilioni tatu kwa ajili ya miradi ya maendeleo jambo ambalo siyo zuri sana. Mwaka wa Fedha 2021/2022 Serikali inatarajia kukusanya trilioni 36.33 na ukiangalia katika bajeti yetu tunategemea, bajeti yetu inategema takribani asilimia 30 ya mikopo ya kibiashara na misaada kutoka nje na ndani lakini kwa mazingira kama haya na ninaomba hapa Mheshimiwa Waziri anisikilize vizuri kwa mazingira kama haya nina ombi ni vema vyanzo vyote ambavyo zimewekwa kwenye Finance Bill, ambavyo vimetengwa kuwa mahsusi kwa ajili ya kuchangia miradi ya maendeleo, vyanzo hivi viwekewe zuio kuwepo na akaunti ambayo itakuwa ni special kwa ajili ya kutunza vyanzo hivi, kwa mfano tozo ya lane za simu, miamala ya fedha, petrol na tozo nyingine, fedha hizi zipewe akaunti maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nalisema kwa sababu tusipofanya hivyo tutajikuta tunaingia kwenye mtego mbaya sana wa kukusanya tozo hizi tukapeleka kwenye mfuko wa Serikali halafu zikapangiwa matumizi mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili Mheshimiwa Waziri you must be very smart kwa sababu mwisho wa siku utakuja kubeba mzigo ambao utashindwa kuutua, kama tunaona kuna kazi kuweka kwenye akaunti special basi tunaweza tukazipeleka Serikali Kuu lakini tukaweka kwenye special reserve fund kwa ajili ya matumizi ya kutelekeza miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye akaunti hii ambayo itatengezwa kwa ajili ya kutunza fedha hizi, basi CAG apewe mamlaka kamili ya kuweza kukagua na kupitia kwa ajili ya kuhakikisha kwamba fedha ambazo zimekusudiwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinakwenda kuliko kusudiwa, na hii itawapa confidence hata wananchi ambao wanakatwa tozo hizi, kwenye lane za simu na maeneo mengine kwamba watakuwa wanaona moja kwa moja wanachangia fedha na inakwenda kutekeleza miradi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nina hoja yangu nyingine ambayo ningemuomba Mheshimiwa Waziri wakati wa hitimisho, basi ajaribu kutoa ufafanuzi zaidi kwenye tozo hizi, kumekuwa kuna ukakasi na kupindishapindisha na kutokuwa na uelewa wa tozo ambazo zimesoma kwenye bajeti hii. Ukweli ni kwamba bado tozo hizi hajizaeleweka vizuri na nina wasiwasi mkubwa kwamba kuna uwezekano mkubwa wananchi wakaingia kwenye mtafaruku wa namna mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano kwenye hii tozo ya hawa watu wa bodaboda, ukiangalia kwamba Serikali kwenye bajeti imeeleza kwamba imeshusha kutoka elfu thelathini mpaka shililngi elfu kumi, lakini ukiangalia faini hii hiyo shilingi elfu kumi ambayo imeshushwa ni kosa moja, kuna hatari kubwa ya traffic kupambana na bodaboda kwa sababu bodaboda wanaamini kwamba ni kwa makosa yote kama ambavyo ilikuwa awali kwa shilingi elfu thelathini, kwa hiyo ni vizuri vitu hivi mkavitolea ufafanuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka nimalizie na hoja nyingine ambayo inahusiana na namna ya matumizi tumejikita sana kujadili namna ya kutumia fedha, ningependa sasa hivi nijaribu kuelezea kwamba ni namna gani bora tunaweza tukakusanya fedha na tukadhibiti mapato, wote tunajua kwamba Serikali yetu inamiliki shares kwenye makampuni mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo makampuni ambayo Serikali ina total ownership lakini yapo makampuni ambayo Serikali inamiliki kwa asilimia Fulani, lakini kumekuwa kuna tabia ya makampuni haya kuwa yanatoa taarifa ambazo siyo sahihi kwenye mitaji yake, kwenye gawio Serikalini, lakini hata kwenye faida inayoingiza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haikagui, Serikali haina mamlaka ya kukagua makampuni haya kwa sababu ya sheria ambayo inamzuia CAG kukagua makampuni ambayo Serikali inamiliki less than 50 percent. Nina mapendekezo ninaomba Mheshimiwa Waziri Mwigulu Nchemba mnaweza mkapeleka shares zile ambazo Serikali inamiliki less than 50 percent, mkazipeleka kwenye stock market mkizipeleka kwenye stock market automatically share hizi makampuni haya yatafanyiwa ukaguzi na zile fedha zitakuwa wazi kwa sababu kule kwenye stock market wanafanya scrutiny ya hali ya juu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo tutakuwa tuna nafasi ya kujua kile ambacho tumeingiza kina uhalali kiasi gani. Pia nina pendekezo lingine tunaweza tukabadilisha sheria yetu tukampa mamlaka CAG akafanya ukaguzi hata kwenye makampuni yote ambayo Serikali inamiliki less than 50 percent bila kujali shares zetu ziko kiasi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo la mwisho ambalo ni muhimu sana ni muhimu tunaweza tukaunda PIC (Public Investimate Company) ambayo kampuni hii itakuwa ni kampuni inayomiliki hisa ambazo Serikali inamiliki minority shares, tukiwa na hii kampuni, itatusaidia kuhakikisha kwamba hesabu zote zinakuwa wazi, zitalazimika kukaguliwa kwa sababu inakuwa ni kampuni tanzu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nielekee moja kwa moja kwenye mchango wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunafahamu kwamba ili kupata umeme wa uhakika ni muhimu sana kuwekeza kwenye energy mixing. Mwenyezi Mungu ametubariki, kwamba tuna vyanzo vingi sana vya umeme ambavyo vinaweza vikatuwezesha tukapata umeme wa uhakiki ikiwa ni pamoja na umeme wa upepo ambao unapatikana Mkoani Singida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote humu ndani tunafahamu kwamba kumekuwa na changamoto kubwa sana ya mwenendo wa hali ya umeme katika Taifa letu. Hata ile target ambayo Wizara wanayo, ya kufikia mwaka 2025 kuwa na megawatt 5,000 litakuwa ni jambo ambalo haliwezekani kwa sababu ya namna tunavyokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme ni kivutio kikubwa sana kwa wawekezaji, lakini kwa namna tunavyokwenda tunapoteza wawekezaji wengi sana kwa sababu hakuna mwekezaji ambaye anaweza kuwekeza kwenye nchi ambayo umeme unakuwa ni wakusua sua na kukatikakatika na kuwaharibia mitambo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu tunazopewa, kimsingi si sababu tunazotakiwa kuambiwa. Tunaambiwa kwamba mindombinu imechoka. Tuna engineers, tuna graduates wanazunguka wanatafuta ajira, kwa nini mitambo hii inashindwa kufanyiwa maintenance? Hata hivyo, swali lingine la kujiuliza, kama sasa hivi tuna megawatts 1,600 halatu tunashindwa kuifanyia maintenance, vipi lile dude la kule Rufiji la megawatts 2115 likikamilika? Si tutailipua nchi hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaambiwa mitambo imezidiwa, kwamba unakuta transformer moja inahudumia watu zaidi ya 130; swali la kujiuliza, wakati vitu hivi vinaagizwa, hivi huko Wizarani hakuna zile specifications kwenye procurement? Kwa sababu kinachofanyika ni kama unachukua mgonjwa ambaye anahitaji oxygen anakuja mgonjwa mwingine unatoa kwa huyu uliyeweka kwanza unaweka kwa mwingine ili kuokoa maisha yake, huyo mwingine, lakini matokeo yake unaweza ukakuta unawapoteza wote kwa wakati mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya masuala ni muhimu yakafanyiwa kazi. Ni aibu sana; wakati wenzetu, kwa mfano China leo wanajadili, wanahangaika kupambana ili wapate jua ambalo ni artificial,l sisi bado leo tunazungumzia masuala ya transformer kulipuka, hili si sawa. Labda nafikiri hatuoni ukubwa wa tatizo kwa sababu tumekuwa hatufanyi tafiti za mara kwa mara ili kujua ukubwa wa tatizo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitakwenda kukuonesha ni kwa namna gani kukatikatika kwa umeme kunaathiri sana Taifa letu kiuchumi. Suala hili la kukatika kwa umeme, kwanza ni suala ambalo si la ajabu sana kwa sababu linatokea nchi nyingi sana na maeneo mbalimbali, tunatofautiana viwango. Kwa nchi za Afrika, nimesoma taarifa za Statistica za mwaka 2018 wamefanya tafiti kwenye nchi 15 wakagundua kwamba Tanzania imeshika nafasi ya tisa kwa mwaka huo, kwamba umeme umekatika mara 670. Nchi inayoongoza ni nchi ya Nigeria, umeme ulikatika mara 4,600, ikifuatiwa na nchi ya Niger 1,400 na nchi ya Congo mara 830. Nchini ambayo inafanya vizuri ni South Africa, ambapo kwa mwaka huo umeme ulikatika mara 50, ikifuatiwa na nchi ya Msumbiji, hapa jirani zetu, umeme ulikatika mara 80, na mwisho Nchi ya Senegal ambayo umeme ulikatika mara 130. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikajaribu kufuatilia, ni kwa nini South Africa wanafanya vizuri, nilichokuja kugundua, na ninaomba hapo Wizara wanisikilize vizuri ili wajue ni nini cha kufanya. Kule South Africa kuna kitu kina ESKOM ambayo ni sawa na TANESCO ya hapa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ESKOM kwa kipindi kile cha mwaka 2019 waliangalia kwa takriban miaka 10 mfululizo, Nchi ya South Africa ilikuwa inakua kiuchumi chini ya asilimia moja na wakagundua kwamba sababu kubwa ilikuwa ni kukatikatika kwa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma report ya Council for Scientific and Industrial Research, inaonesha South Africa kwa kipindi kile chote imepoteza takriban Rand bilioni 338. Sasa, kwa Taifa letu hili lazima tujifunze. Ni makosa makubwa sana kufanya makosa ambayo mwenzako alishayafanya nawe ukayarudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nijielekeze kukuonesha ni namna gani tunapoteza kama Taifa. Hapa mezani kwangu nina report ya EWURA ya mwaka 2018. Report hii inatoa taarifa za mwaka 2017. Inaonesha hivi: “kwa kipindi cha mwaka 2017 umeme wa Tanzania umekatika mara 2,844”.

Ukichukua takwimu hiyo hapo ni umeme ambao ni planned na unplanned kukatika. Kwa maana nyingine ni kwamba kuna wakati umeme unakatika TANESCO wamepanga na kuna wakati umeme unakatika hata wenyewe TANESCO hawajui. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukichukua mara 2,844 kule kukatikatika kwa umeme maana yake ni siku 118 umeme ulikatika. Tukienda kwenye hesabu za kawaida kabisa kwenye uchumi unaweza ukaona kwamba ukimchukua mfanyabiashara wa kawaida tu ambaye labda anaingiza laki mbili na kitu kwa siku; yaani let us say kwamba umefanya annual turnover, labda anapata milioni mia moja, ukichukua siku hizi ambazo alikuwa hafanyi kazi maana yake amepoteza takriban milioni 32. Huyo ni mfanyabiashara mmoja. Chukua wafanyabiashara wa Tanzania 100,000 ambao kipato chao ni cha kawaida kabisa. Maana yake kwa mwaka 2017, umepoteza zaidi ya trilioni 3.2. Hii ni mara tatu ya fedha ambazo tumekopeshwa na IMF kwa ajili ya COVID, hiyo trilioni 1.3.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo kadhaa ya kushauri hapa. Jambo la kwanza, ni muhimu sasa Serikali itenge fedha ya kutosha kwa ajili ya kufanya maintenance kwenye mitambo ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, kwa sababu ya muda, nahitaji Serikali kupitia Wizara waweke specifications zinazoeleweka kwenye procurements zenu ili wanapokuwa mnaagiza vifaa vya mitambo ya umeme muwe mnaagiza kulingana na uhitaji uliopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, wataalam wetu waliopo Wizarani wapelekeni wakajifunze. Wanakaa humu ndani wanafanya nini kama mambo haya kuna maeneo mengine wameshafanya makosa haya na wakajifunza? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wa mwisho. Ni muda sasa Shirika hili la TANESCO likagawanywa mara tatu, ligawanywe liwe lina kitengo cha kuzalisha, kusafirisha na kitengo cha kusambaza…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. JESCA D. KISHOA: …na nakumbushia ile precaution aliyoitoa Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati anajibu maswali, ya kwamba kama TANESCO itagawanywa mara tatu, kuna uwezekano wa kila kampuni kutofanya vizuri na ikasababishia wengine kuharibikiwa; lakini lazima hayo yote yazingatiwe kwa sababu tunaamini kwamba tuna wataalam wa kutosha kwenye nchi hii, watekeleze wajibu wao. Ahsante. (Makofi)
THE WRITTEN LAWS (MISCELLANEOUS AMENDMENTS) (NO. 4) ACT, 2021
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ukiangalia sehemu ya Muswada inafanya mabadiliko kwenye extractive industry transparency and accountability Act ambapo ukiangalia Kifungu cha 51 kinapunguza idadi ya board member wa TEITI kutoka 15 mpaka nane.

Mheshimiwa Spika, sasa napenda kwanza tungeelewana jambo moja humu dani. Nadhani upo umuhimu mkubwa sana wa sisi Wabunge kuelewa kazi kubwa ya TEITI na TEITI ni kitu gani. Kwanza nianze kwa kusema kwamba TEITI ni Kamati muhimu sana, ni whistleblowers, ni wapiga filimbi, TEITI ni CAG wa Sekta ya Uziduaji. TEITI ni watchdog wa Sekta ya Mafuta, Oil and gas. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ukiangalia kwenye kifungu hiki ni kama vile tunakwenda kumkata mikono. Tunafanya makosa makubwa sana kwa sababu mbali na sababu ambazo zimetolewa hazina mantiki sana lakini tunakwenda kuvunja Global Aids Standards, tunakwenda kutia aibu kama Bunge kama tukikubaliana na suala hili kwa sababu, Global Aids Standards wanataka uwiano ulio sawa kwenye ile committee member ya Bodi ya TEITI. Lakini pia ukiangalia sababu ambazo Serikali imetoa ya kwanini wanapunguza idadi kutoka 15 mpaka nane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sababu ya kwanza wanasema kwamba wanataka kuongeza ufanisi. Hivi kweli, kama una watendaji 10, ukipunguza watano unaongeza ufanisi au unapunguza ufanisi? Wanasema sababu ya pili ni kupunguza gharama. Hivi kweli kwa watchdog wako, kwa mpiga filimbi wako, kwa whistleblower wako unaweza kuona kwamba unapunguza gharama kweli? Kwa hii Kamati ambayo inakagua na kuangalia uhalali wa tunachokipata kutoka kwenye rasilimali zetu? Nadhani tungeangalia upya kwa upana na umuhimu wa TEITI katika Taifa hili.

SPIKA: Hii ni Bodi, ni Kamati au ni kitu gani?

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, ni Board Member ya TAIT ni Kamati ambayo inasimamia/inakagua mapato yanayotoka kwenye Sekta ya Mafuta, gesi na madini…

SPIKA: Hiki chombo chombo kinaitwaje? Yaani hiki tunachokiongelea?

MHE. JESCA D. KISHOA: TEITI!

SPIKA: No! no! no! yaani ni Bodi, Kamati? What is it?

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, kirefu chake wanasema ni Tanzania Extractive Industry Transparency Initiative.

SPIKA: Naelewa. Hawa 8,15 ni kitu gani hiki?

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, hawa 15 waliokuwepo na sasa hivi wanapunguzwa walikuwa ni wawakilishi kutoka kwenye maeneo matatu. Wawakilishi kutoka Serikalini wako watano…

SPIKA: Kuunda nini?

MHE. JESCA D. KISHOA: Kuunda Bodi.

SPIKA: Ni Board Members hao?

MHE. JESCA D. KISHOA: Yes! Yes! Wako 15.

SPIKA: Board Member ya watu 15 ya nini? Iko wapi mahali pengine? (Makofi)

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, hii ina sababu moja, kwa sababu ina wawakilishi kutoka maeneo matatu muhimu. Ina wawakilishi kutoka Serikalini. Ina wawakilishi kutoka kwenye Asasi za kiraia na ina wawakilishi kwenye makampuni.

SPIKA: Bado katika nane unaweza ukawapata hao hao pia, si Bodi? (Makofi)

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, lakini pia ni International Standards. Ni suala mbalo lilipitishwa toka mwaka 2012.

Mheshimiwa Spika,…

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Ngoja upokee Taarifa. Nani mwenye Taarifa aendelee.

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, Msekwa.

SPIKA: Aaah! Samahani, samahani endelea Mheshimiwa Mbunge.

T A A R I F A

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nilikuwa napenda kumpa Taarifa Mheshimiwa ambaye anazungumza hiyo inaitwa Kamati sio Board Members.

SPIKA: Unapokea Taarifa hiyo?

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, naomba niendelee.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia kazi kubwa ambazo TEITI imekuwa ikifanya mfano TEITI imekuwa ikitoa ripoti kila mwaka ya kuonesha…

SPIKA: Ooh, dakika zako zimeisha!