Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Richard Mganga Ndassa (44 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Naunga mkono, pongezi kwa Wizara kwa maandalizi ya hotuba. Naomba kutoa ushauri katika mazao ya biashara.
Zao la katani; leo hii pamba bei yake ilikuwa imedorora, tulikuwa tunaiita dhahabu nyeupe, katani leo White Gold. Miaka ya 70 katani katika soko la dunia, Tanzania tulikuwa tunaongoza, katani bora ilikuwa inatoka Tanzania. Soko la zao la katani limebadilika na kupanda bei ya katani (fibre), kwa tani ni dola 2,200 - 2,500. Serikali iangalie uwezekano wa kuliibua upya zao la katani.
Zao la pamba, nataka Serikali iwaambie wakulima wa pamba kuhusu mbegu zao (Kyuton) ambazo zimeua kabisa zao la pamba kutokana na wauzaji wa mbegu hizo zilizochakachuliwa kwa sababu ya rushwa. Leo naomba nipate maelezo ni nani hasa wamiliki wa kiwanda cha mbegu ziliozokuwa na manyoya. Hawa wameua kilimo cha pamba. Mbegu hizo zilipigiwa kampeni kubwa na viongozi kuanzia ngazi ya Taifa - Wizara na Wilaya, lakini tungependa kujua ni nani aliyewapeleka nje ya nchi Viongozi wa Juu wa Wilaya na Mkoa? Hii ni rushwa, sheria ishike mkondo wake kwa sababu kwa kufanya hivyo wamelizika zao la pamba kisa rushwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu usindikaji; Tume ya Mazao Mbalimbali tuliyozalisha; tuombe Serikali iangalie utaratibu wa kusindika na kuyaongezea mazao thamani. Mfano: mahindi, hakuna sababu ya kusafirisha mahindi, watumiaji wametaka unga siyo mahindi. Mpunga, watumiaji wanahitaji mchele na siyo mpunga, hapa naomba kwenye maeneo husika, kuwe na mashine za kusaga na kukoboa, lakini mazao haya yaani unga na mchele uwekwe kwenye mifuko ili kila mtu aweze kununua kufuatana na uwezo wake kilo 1, 2, 3 na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ng‟ombe, Watanzania wanataka nyama siyo ng‟ombe. Ng‟ombe wanakunya hovyo njiani, test ya nyama haipo. Kuku, Watanzania wanataka nyama ya kuku, unabeba kuku mzima na manyoya yake kwenda Dar es Salaam, kwa nini wasichinje hao kuku huko huko, nyama ikapelekwe kwenye supermarket na kadhalika.
Narudia tena, napenda na ningependa kujua ni hatua gani zilizochukuliwa kwa wale waliowatapeli wakulima wa pamba kwa kuwauzia mbegu za pamba zisizokuwa na manyoya zisizobeba, zilizosababisha kutoota vizuri tangu zilipotangazwa kwa mbwembwe sana na Viongozi wa Wizara yako. Ningependa kupata majibu yako.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono na ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa utaratibu mzuri alionao wa kuwa msikivu, mtu mnyenyekevu na mwenye mahusiano mazuri sana hasa kwa vyombo vya habari wakiwemo wamiliki na waandishi wa habari. Nakuomba PR hiyo uiendeleze ili tasnia ya habari iweze kuwa nguzo kuu katika ustawi wa Taifa letu. Nakuomba uendelee kuvishauri vyombo vya habari na waandishi wa habari kwamba kalamu zao ziangalie na kuzingatia uzalendo kwa nchi yao Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Michezo Malya kina upungufu mkubwa, lakini kubwa ni kukiboresha chuo hiki ili kiweze kutoa degree ya michezo. Chuo cha Malya ni kiwanda cha kuzalisha walimu wa kufundisha michezo mbalimbali katika shule za msingi, sekondari na vyuo. Michezo ikifundishwa vizuri shuleni, vijana wetu wajipe ajira hasa katika sanaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TFF haisimamii vyema uendelezaji wa mpira wa miguu badala yake imekuwa ni chama cha kukuza vurugu badala ya mchezo wenyewe. TFF imekuwa chanzo cha migogoro kati ya vilabu na vilabu, tofauti na matarajio ya wengi. Ikumbukwe mpira wa miguu ni mchezo unaopendwa na watu wengi lakini Watanzania hawafurahishwi na uongozi wa TFF.
Mheshimiwa Mwenyekiti, programu ya timu ya under 15, 17, 21 haionekani kusimamiwa vizuri. Michezo ni furaha, ajira, utalii, afya na kadhalika, tofauti na kwetu hasa TFF imekuwa ikilalamikiwa kuhusu matumizi mabaya ya fedha.
Naomba Mheshimiwa Waziri akihitimisha majumuisho aniambie fedha zinatolewa na FIFA kwa miaka mitatu ya nyuma yaani mwaka 2013 - 2015 zililetwa na zilitumikaje? Tujue fedha za wafadhili mbalimbali walioichangia timu yetu ya Taifa ya mpira wa miguu kwa wanaume na wanawake, tujue pesa za ligi kuu (VPL) mkataba ukoje hasa upande wa timu shiriki? Yapo malalamiko mengi kwa washiriki wa ligi ya VPL.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ligi daraja la kwanza iliyomalizika hivi karibuni imemalizika kwa migogoro ndiyo maana nimesema kuwa TFF badala ya kuendeleza soka inaendeleza migogoro na upendeleo wa dhati kwa baadhi ya timu. Naomba Mheshimiwa Waziri atueleze ni namna gani atakiendeleza Chuo hicho cha Malya? Pamoja na kutopatiwa pesa zake za OC, ni vyema wazabuni wakalipwa madai yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Baraza la Michezo Tanzania (BMT) hivi kazi yake ni nini? Sioni wanachokifanya, wapo wapo tu. Sioni maendeleo katika michezo mbalimbali iliyo chini ya Baraza. Kila chama ni vurugu, siyo kwenye riadha, ngumi, wavu na kadhalika. Je, ni busara kuendelea na hilo Baraza hilo? Kama ni jipu, litumbuliwe. Naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana lakini ni kweli kama ulivyosema kwamba baadhi yetu ni wakongwe kidogo humu ndani. Kwa sababu ya ukongwe wetu nikuombe sana wewe mwenyewe lakini nimwombe pia Waziri Mkuu wetu, Mkuu wa Kambi ya Upinzani na Wabunge wote, nimesikiliza michango kuanzia mwanzo siku ya kwanza mpaka jana, siyo kawaida ya Bunge letu hata siku moja, tunatoka kujadili Mpango tunajadili ukanda. Bunge lako sasa limeshapelekwa lipande basi la ukanda kwamba kanda fulani, Kanda ya Kusini, Kanda ya Kati na Kanda ya Kaskazini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tukishatoka kwenye ukanda tunaenda wapi? Tutakuja kwenye ukabila, tukitoka kwenye ukabila tunakuja kwenye rangi na dini zetu. Ningeomba sana Waheshimiwa Wabunge kwa sababu sisi ni wawakilishi wa wananchi na kwa sababu tukisema jambo humu ndani, wananchi wetu wanatusikiliza vizuri, tusifike mahali tukawagawa wananchi wetu kwa maana ya ukanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yamesemwa mambo mengi sana kuhusu Rais sijui amefanya nini Kanda ya Ziwa, lakini ukitazama kwa nchi nzima na bahati nzuri Kanda ya Ziwa ni moja ya sehemu ya Tanzania. Rudi uangalie maeneo mbalimbali kwa mfano hata hapa Dodoma, uamuzi mzito alioutoa Mheshimiwa Rais wa kuamua kuhamishia Makao Makuu Dodoma, hakusema kuhamia Mwanza hapana.

Uamuzi mkubwa na mzito wa kuihamishia Serikali Dodoma ni uamuzi mzito, sasa tusije tukafika hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana chonde chonde Waheshimiwa Wabunge! Kwa sababu jana nimeona yale mashambulizi, watu wanatokwa mapovu kwa sababu ya ukanda. Hivi Mwalimu Nyerere ndivyo alivyotuachia maneno hayo? Tukitoka kwenye ukanda tutakwenda kwenye udini na ukabila, hatuwezi kufika. Ili tujenge nchi yetu, Wabunge lazima maneno yetu yanayotoka kwenye vinywa vyetu lazima tuyachuje kabla hatujayatoa. Naomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya mshikamano kama mnakumbuka, mwaka 1979 kwenye vita vya Kagera tulimpiga Idd Amin kwa sababu ya mshikamano na umoja. Mwalimu alitumia maneno matatu, uwezo wa kumpiga tunao, sababu ya kumpiga tunayo na nia ya kumpiga tunayo. Sababu ya umoja ule Watanzania wote Tanzania nzima mwenye kuku, mbuzi, trekta, basi na mwenye lori tukashikamana pamoja ndiyo maana ile vita tukashinda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo vita yetu kuu siyo ya Kagera, vita yetu kuu kwa sasa ni ya kiuchumi. Vita ya uchumi tutaishinda kama tutakuwa pamoja tukaachana na mambo ya ukanda, tukawa Watanzania wamoja tukaungana kumuunga mkono Mheshimiwa Rais wetu, anatuonyesha njia kama alivyotuonesha Baba wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Baba wa Taifa alituunganisha pamoja akasema kwa sababu huyu jamaa ametuchokoza na tunao maadui wengi wa kiuchumi Mheshimiwa Rais wetu Magufuli anatuonesha njia, ni lazima tumuunge mkono sio kwa kumbeza kwa kazi nzuri anazofanya jamani. Niwasihi sana Waheshimiwa Wabunge tumuunge mkono Mheshimiwa Rais, lakini kama Wabunge lazima tuwe wamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba nakujua ni mtu makini, endapo itatokea mimi Mbunge na mwingine labda akasimama humu ndani na kuzungumzia ukanda, mamlaka unayo ili kulinda heshima ya Bunge na nchi yetu. Tukianza kuzungumzia ukanda tutakwenda mbali sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu jirani tu hapa kama mmesikia baada ya uchaguzi kwa sababu ya kabila hili na kabila hili, wanasema wanataka kujitenga kila mtu awe na nchi yake. Tukiruhusu kwa sababu mambo haya huwa yanamea polepole, tunaweza tukaruhusu tukafika huko. Hili ilikuwa ni ombi langu kwako na kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani na Wabunge wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye mpango, nitasema kidogo tu. Nimwombe sana Mheshimiwa Dkt. Mpango, Mheshimiwa Rais anazungumzia kuhusu uchumi wa viwanda, yeye na kila mtu anajua. Katika mpango wake humu ndani sijaona sababu za makusudi hasa upande wa umeme, hivi viwanda anavyotaka kuvianzisha anakwenda kuweka ma-generator au anaweka nini.

Mheshimiwa Spika, viwanda hivi ili viende na vizalishe lazima viwe na umeme wa kutosha na siyo vinginevyo, vinginevyo labda kama tunataka kupiga sound, well, lakini kama tunataka tutoke hapa tulipo, leo tuna megawatts 1,437, au 1,400, lakini tunasema okay, Stiegler’s Gorge mwaka 2021 tunategemea itazalisha megawatts 2,100, hivi leo tukijiuliza kwa sababu ya umeme huu tulionao tunataka viwanda vichipuke kwa haraka kwa umeme upi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge, lakini achilia mbali viwanda, tumeanzisha REA III, ambayo ipo inakwenda Kongwa. Sasa kwa utaratibu huu wa umeme wenye mashaka hata hiyo REA III nafikiri itaishia njiani tu. Sasa ni lazima Mheshimiwa Dkt. Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango, kwanza nimwombe, bahati nzuri Waheshimiwa Wabunge wa CCM wanamheshimu sana, lakini ana ka- arrogance fulani hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia lugha nyepesi ya kidiplomasia, sasa hiyo arrogance hebu ajaribu kuiondoa, kwanza haisaidii Bunge, lakini haisaidii sana Serikali. Kwa sababu naweza nikaja na hoja ya msingi ya kutaka kuisaidia Serikali na nikwenda kwake mara chungu nzima, nikamwambia kuna mwanya hapa tunaweza tukapata pesa, lakini namna ya kumpata utafikiri unataka kumpata nani sijui. Sina uhakika kama hata simu za Waheshimiwa Wabunge huwa anapokea, sina uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ni Wabunge wenzake, wote humu ndani, wa upande ule kule na upande huu, sisi ni Wabunge wenzake. Tunataka tuisaidie Serikali kwa sababu yeye ndiyo amekamata mfuko wa pesa. Sasa mfuko wa pesa hawezi kwenda kutafuta pesa peke yako. Sisi ndiyo wasaidizi wa kumsaidia, mipango ambayo tunamshauri na yeye angekuwa na uwezo wa kupokea basi angalau kama siyo asilimia 75 basi hata asilimia 50, basi hata 25. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitabu hiki nimekisoma, Mdogo wangu Peter hapa tumesoma pamoja, unajua wengine hatuna zile lugha kali, tuna lugha za kidiplomasia. Namwomba sana Mheshimiwa Dkt. Mpango wa Mipango, hebu ajitahidi kwanza kusikiliza Kamati ya Bajeti, aisikilize mipango yake, ushauri wao, ajaribu kuusikiliza pamoja na wataalam wake. Kwa sababu ilishafikia mahali wanakwenda kwenye Kamati ya Bajeti, mnakaa mnazungumza, mnaishauri Serikali, lakini hakuna kinachochukuliwa, as if Kamati ya Bajeti haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ile maana ya kuwa na Kamati ya Bajeti inakuwa haipo kwa sababu yote tunayoshauri kwenye Kamati ya Bajeti yakichukuliwa sana labda ni mawili. Sasa nini maana ya kuwa na Kamati ya Bajeti ya kuishauri Serikali? Maana yake inakuwa haipo.

Mheshimiwa Spika, sasa nimwombe sana Mheshimiwa Dkt. Mpango wa Mipango, mipango yake ili iende vizuri ni lazima awasikilize Waheshimiwa Wabunge.

Peke yake na Wataalam wake watafika mahali ipo siku watakwama, watatuomba tuwasaidie kuwakwamua lakini tutafika mahali tutasema hapana na tutamwambia Mheshimiwa Spika kwa utaratibu huu hatuwezi kwenda hata siku moja kwa sababu sisi ushauri wetu tunashauri lakini hatusikilizwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umesema vizuri sana wakati Mheshimiwa Peter Serukamba akizungumza hapa, kwamba wasikie. Sasa nafikiri na mimi nimemwambia Mheshimiwa Dkt. Mpango asikie. Wenzake wote wanasikia isipokuwa Dkt. Mpango wa Mipango, hasikii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, narudia tena na ukiona Seneta anasema ameshasikiliza mengi huko nje. Dkt. Mpango wa Mipango yeye siyo msikivu kwa Waheshimiwa Wabunge, ajaribu kubadilika kwa sababu wote tuko kwenye boti moja, tunataka tuifikishe hii boti yetu mahali pema, hakuna mtu hata mmoja anayetaka kutoboa mtumbwi hata mmoja, wote tunakwenda katika mtumbwi mmoja, twende salama salmini ili tuifikishe salama nchi yetu mahali ambapo patakuwa na neema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nisisitize tena umeme, lakini pili suala la ukanda. Baada ya maneno hayo, nikushukuru sana kwa nafasi lakini kama nilivyoshauri na nilivyokuomba, suala la ukanda litatufikisha mahali pabaya sana endapo tutaliendekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa ushauri kwa Tume ya Madini kuhusu Maafisa wa Madini wa Mikoa au Wilaya ili kulinda heshima lakini pia mali wanazosimamia, rasilimali ya madini, nashauri, ma- RMO, wote kabla ya kupewa ajira wafanyiwe vetting, lakini waapishwe (wale kiapo cha uaminifu), wajaze fomu za maadili ili kujua mali wanazomiliki. Mheshimiwa Rais wetu amewapa heshima kubwa Tume ya Madini kwa kutambua kuwa sekta ya madini itatoa mchango mkubwa katika mfuko wa Taifa.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa nafasi hii ili nichanguie mpango ambao umeletwa kwetu kwa mujibu wa Ibara ya 94 kama ilivyo kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nauunga mkono sana mpango huu, kwa sababu ndiyo utaratibu wetu humu Bungeni, kwamba mara bajeti inayofuata, lazima kuwe na mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitabu cha Mheshimiwa Dkt. Mpango, ameeleza vizuri sana naomba nisome kidogo tu. Katika mwaka 2021, Serikali itasimamia vipaumbele vifuatavyo; kuimarisha na kusimamia mfumo wa ukusanyaji wa mapato, lakini akaenda mbali zaidi, akasema, malengo ya mpango wa bajeti yanalenga kuimarisha makusanyo kwa kutekeleza hatua za kiutawala zikiwemo kuboresha mazingira ya kufanya biashara kwa wawekezaji kuimarisha uzimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi, lakini akaendelea akasema, usimamizi wa sheria ya kodi, kupunguza upotevu wa mapato na kuyaanisha na kupunguza tozo ya ada mbalimbali zikiwemo za wakala wa Serikali ya matumizi ya fedha za umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la nidhamu ya matumizi ya umma ya fedha za Serikali, nianze kwanza kukupongeza sana sana Mheshimiwa Spika wetu ambaye ni Mwenyekiti wetu kwa kikao cha leo, kwa mambo matatu ambayo wewe umeonyesha kwa dhahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, jambo la kutuletea hizi tabulates hizi ndani ya Bunge, umepunguza sana sana matumizi ya karatasi ambayo yalikuwa yanatumia fedha nyingi sana za Serikali, ilielezwa kwamba matumizi yake kwa mwaka ni karibu bilioni 1.2. Sasa bilioni
1. 2 kama fedha hizi leo hatutumii tena, zitakwenda kwenye mipango mingine, kwa hiyo, nikushukuru sana pamoja na Ofisi yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, hapo awali, Serikali tukiwa Bungeni, Wabunge wako, tulikuwa tunafanya vikao vyetu wakati wa kamati, tunafanya vikao vyetu nje ya maeneo ya Bunge, tulikuwa tunafanya UDOM, wengine wanakwenda Hazina, wengine sijui wanakwenda Mipango, wengine wapi, hiyo yote ilikuwa ni kutumia fedha visivyo, fedha za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa busara zako, ukaamua kwamba kuanzia sasa Kamati zote za Bunge, shughuli zake za kibunge zitafanyika katika majengo ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakushukuru sana, huwezi ukajua, kwa sababu huwezi kuiona moja kwa moja, fedha ambazo tulikuwa tunazitumia, hata sisi wenyewe Wabunge, tulikuwa tunatoka huko tuliko, tunakwenda UDOM, mara unapotea mara unarudi, unakuja tena hapa, mara unakwenda, matumizi yale tulikuwa tunatumia fedha lakini tunatumia na muda, kwa sasa, muda wetu ni mfupi sana unaotumika, tunatumia muda mwingi lakini tunatumia vizuri, kwa sababu shughuli za kamati za Bunge zinafanyika ndani ya eneo la Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, mtu mwingine anaweza akaona ni kitu cha kawaida, lakini siyo cha kawaida, ukiwa na miaka 10, miaka 20, umri unakwenda, kupanda zile ngazi za kwenda ghorofa ya nne, hasa mzee wangu Mheshimiwa Lubeleje, bahati nzuri sijui leo hayupo, kupanda zile ngazi kwenda ghorofa ya nne, iikuwa ni issue. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa busara zako na ofisi yako, hivi sasa leo kwenye jengo la utawala, lakini pia hata kwenye eneo ambalo kamati za Bunge zinafanyika, kote kuna lift, tunakushukuru sana sana kwa kuboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niishauri Serikali, kama tunataka tukusanye mapato yetu vizuri, yapo maeneo ambayo Serikali imeyaacha. Kwa mfano, ukipita hii njia ya kwenda Dar es Salaam, utakuna na malori ya mafuta, utakutana na malori ya mizigo, yenye namba, siyo za Tanzania, yenye namba za nchi za jirani, lakini ukienda kwenye ule mlango wa hicho kichwa cha gari, mmiliki wa hilo gari, tuna jina la mtanzania!

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali inapoteza mapato mengi kweli kweli na hili eneo hili, ukienda kwa wale wenywe wanakwambia kwamba malori haya yanaposajiliwa nje, Serikali inakosa mapato ya ndani, Serikali inakosa fedha ambazo malori hayo yangeweza kununua mafuta hapa Tanzania, tunakosa ajira na vitu vingine vingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali, tunajiuliza tu, hivi kwanini haya malori, kama lori hili lilikuwa la Mheshimiwa Ndassa, au lori hili lilikuwa la Mheshimiwa Ndugai la mafuta, badala ya kulisajili Tanzania nakwenda kulisajili nchi za nje, lazima kutakuwa na tatizo tu, lakini nyumbani kwangu ni Dar es Salaam, lakini lori lakwangu, ambalo nikilisajili kwa Tanzania, Tanzania itapata mapato. Mafuta yale, maana yake sasa hivi utaratibu wanaofanya, yale mafuta, hawachukui tena hapa, wanachukua hokohuko, wanakuja wamejaza, kama lita 400, wanakuja kuchukua mizigo na kurudi, mafuta hayo lita 400, ambayo sisi tunatumia kama kwenye road tall, sasa mapato hayo yanapotea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali, hebu turudi nyuma, ili tushauriane vizuri zaidi, ili malori haya ya mafuta na malori ya mizigo, yaweze kusajiliwa hapa, kama kuna tatizo sehemu fulani, basi turekebishe, kwa sababu hicho ni moja ya chanzo cha mapato ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, ili twende vizuri zaidi, katika kusimamia nidhamu na matumizi ya Serikali na haya mapato ili lazima yapatikane, lazima kuna mambo ya kufanya, ya kusimamia. Suala zima la rushwa, rushwa bado ipo, kuna mianya mingi ya rushwa ambayo inasababisha mapato yetu kupotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali, suala zima la ruswa, lakini pia uaminifu kwa wafanyanyazi, uzalendo kwa wafanyakazi wa Serikali, kwa sababu tunataka mapato yetu yaende mbele zaidi, lakini tukitazama kwa miradi ambayo tumeiainisha miradi mikubwa hii, reli, bwawa, ndege na mengine, bila kuwa na vyanzo imara vya mapato, hatuwezi kufikia ile target ambayo tunataka ifikie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe sana Serikali, wale watu wote ambao wanasimamia maeneo hayo, lazima nidhamu ya matumizi iwepo, wizi, rushwa usipatikane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la mwisho, kwa sababu kengele imelia, nikuombe sana na Bunge letu Tukufu, TRA huwa tunawapa malengo, kwamba lengo lenu kwa mwezi huu ni kiasi fulani, halamshauri zetu lengo lenu ni kiasi fulani, sijui, sina uhakika, kama maeneo mengine yana utaratibu wa kuwekewa malengo. Sasa ombi langu, kwa sababu tunazo taasisi za Serikali, kama TANAPA, Ngorongoro na mengine, hebu, lazima tuwe na kautaratibu kazuri ka kuweka, siyo kuweka wao, kwa sababu taasisi hizi tunategemea ili ziongeze pato letu, tunategemea zitoe gawio, sasa kama watakuwa wanajipangia wao bajeti yao, target yao kwamba wakati wanaweza wakaenda mbele zaidi, kama walivyofanya TCRA Septemba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walikuwa wamejipangia chini lakini wakakusanya trioni 1.8, au 1.7. Kwa hiyo, hata mashirika haya ya umma, ambayo tunategemea tupate gawio kutoka kwa hizi taasisi, bado malengo yao yanaweza Serikali ikayapitia kupita kwa TR, akapitia akasema, hapa wewe hapana umedanganya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lazima pia, hilo gawio, siyo wao ndiyo waseme kwamba sisi tutatoa gawio hili, hapana, Serikali iseme! Kwa kufanya hivyo, mtakuwa mmewasaidia kupunguza matumizi yasiyokuwa na utaratibu tukiaacha wakajiendea tu yale matarajio yetu hatuwezi kuyafikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vinginevyo, naipongeza sana Serikali ya Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri sana anayofanya. Nje na ndani sisi sote tunakubali kwamba hili ni jembe la Tanzania, siyo vinginevyo. Nawaomba hata ndugu zetu, hata kama hutaki kukubali, Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni Rais wa nchi hii, anafanya kazi nzuri, kla mtu anaona na kusikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama watu wa nje wanasifia, wewe uliyeko ndani utashindwa kusifia? Basi hata kama hutaki kusema, hata ukiwa nje sema basi kwamba Mheshimiwa Dkt. John Magufuli Pombe hoyee! Hata ukiwa nje!

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa rasilimali tulizonazo za watu, mazao ya biashara tukiamua kwa dhati, tunaweza tukapiga hatua kubwa hasa tukijipanga vizuri. Ndani ya miaka mitano tuliyofunga mkataba na waliotuchagua, fursa zipo tukiamua hasa kwa kuanza na viwanda vidogovidogo ambavyo tunaweza kuanza navyo. Ili kuvilisha viwanda vya kati na baadaye viwanda vikubwa, kinachotakiwa ni kuundwa kwa mazingira mazuri ya uwekezaji, katika miradi mbalimbali kutokana na jiografia ya nchi yetu. Miradi hiyo ndiyo itakayounda ajira kwa Watanzania walio wengi na hao ndiyo watakaokuza uchumi wetu.
Kama nilivyoanza hapo juu kuwa tunayo rasilimali yetu ardhi, siasa safi na wajasiliamali. Hivyo tukiwatumia vizuri wajasiliamali, tukawawezesha tukawawekea mazingira mazuri kwa kila eneo, kufuatana na uzalishaji wao hasa katika mazao yanayotokana na ardhi, mito, maziwa, miti, mifugo na kadhalika huko waliko, ile idadi ya vijana kukimbilia mijini itapungua. Hebu tuisome ile Sera ya Taifa ya Biashara ndogo, na viwanda vidogo na tuitekeleze kwa kuisimamia. Sote twajua kilimo ndiyo kinachotoa, mapato kwa watu waishio vijijini, tukiamua kuanzisha viwanda vidogo vijijini vitaleta mabadiliko chanya, katika uchumi wa nchi yetu. Hasa vijijini kwa mazao yetu kuongezewa thamani, badala ya mkulima kuuza mazao yao kama yalivyo, viwanda vidogovidogo vitatumika kuyasindika mazao hayo. Mfano badala ya kuuza mahindi vijijini viwe na mashine za kusaga na kukoboa unga badala ya kuuza mpunga wauze mchele uliofungwa katika pakiti ndogo za kilo moja, mbili au tano huko huko vijijini tayari kupelekwa mjini kwa walaji, badala ya kuuza karanga na alizeti kama zilivyokuwepo, na viwanda vya kukamua mafuta, badala ya kuuza matunda kama yalivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kujengwe viwanda vya kukamulia juisi, viwanda hivi mbali na kuongeza thamani katika mazao hayo, vitaongeza ajira huko huko vijijini na itasaidia vijana kubaki vijijini. Serikali itambue uongozi katika ngazi za Wilaya, na Mikoa kushawishi wawekezaji katika maeneo yao kufuatia fursa zilizoko zitenge maeneo kwa wawekezaji kwa kuondoa urasimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili ile dhana ya kujitegemea ya ki-ujasiriamali nashauri Waziri wa Viwanda, awasiliane na Waziri wa Elimu ili kuingiza somo la ujasiriamali katika mitaala ya shule. Kuanzia ngazi ya elimu ya msingi, sekondari, na katika mafunzo ya ufundi stadi, hii itasaidia kupanua elimu na matayarisho ya kazi ili kuongeza hali ya kupenda kuanzisha na kuendeleza ujasiliamali, ili kuwafanya vijana kubaki vijijini. Vijana wakifundishwa ujasiriamali kuanzia msingi, sekondari na katika mafunzo ya ufundi stadi, watabadili mitazamo yao watapenda kujiajiri tofauti na ilivyo sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona nijikite hasa katika suala zima la ujasiliamali, huko vijijini ili kupunguza idadi kubwa ya vijana kuja mijini kutafuta kazi (ajira) ambazo nazo hapo naomba tujipange vizuri. EPZ tutazipata katika Wilaya zetu na Mikoa yetu, fursa zipo tukiamua na kila mtu akatekeleza na kutimiza wajibu wake ndani ya muda mfupi tutapata matokeo chanya na tutabadilisha maisha ya vijana na kuinua uchumi wa nchi yetu Tanzania. Naomba niwaombe wataalam wote wa Wizara na taasisi zilizo chini ya Wizara yako wafanye kazi kwa kuzingatia weledi wao, tuangalie wapi tulikosea na tuparekebishe na tusonge mbele kwa ari mpya. Ili ile ndoto ya Mheshimiwa John Pombe Magufuli na Watanzania kwa ujumla, Tanzania iwe nchi ya viwanda ili tuweze kuzalisha kwa matumizi ya ndani na baadaye tusafirishe nje ya nchi ili tupate pesa za kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuongeza ajira na vijana wetu waweze kubaki katika maeneo yao ya uzalishaji, Mheshimiwa Waziri tulikuwa na viwanda vingi sana kabla ya kubinafsishwa ningependa kujua ni jinsi gani agizo la Mheshimiwa Rais umelitekeleza. Hasa kwa wale waliojitwalia viwanda na kuvitelekeza mbali na kwamba hadi leo hawajalipa pesa zote kufuatia na mkataba wa mauziano (MOU), ni hatua gani umezichukua?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda cha nguo, kiwanda cha zana za kilimo asilimia 70 ya Watanzania ni wakulima wa pamba, nyuzi, matairi, korosho, kahawa, asali, nyama na kadhalika, ni kichocheo cha upatikanaji wa ajira fedha za kigeni lakini nchi yetu itaitwa nchi ya viwanda. Nchi haiwezi kuitwa nchi ya viwanda wakati viwanda vilivyopo havizalishi katika uwezo wake na havizidi 200-500 tunakuamini Mheshimiwa Waziri, lakini tunakuomba ukaze buti wewe na Wataalam wako, ndiyo mtaifanya nchi hii kuitwa nchi ya viwanda. Ushirikiano na Wizara zingine nchini hii ni kutokana na kutegemeana. Pia chuo chako cha CBE Dar es Salaam nilichosoma mimi kitazamwe upya, elimu inayotolewa pale ni tofauti na zamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi ya kwanza asubuhi hii, nijaribu kujadili hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi. La kwanza, naomba tumwombee Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi nzuri sana anayoifanya, lakini naye pia amekuwa akituomba sisi Watanzania wote kwa dini zetu zote, tumwombee sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, hili ni ombi, sisi kama Wabunge tumekuwa na maneno mengi sana humu ndani ambayo kwa kweli hayana tija sana kwa Watanzania. Nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge wa pande zote mbili; upande wa CCM lakini na upande wa wenzetu; Watanzania wanaotusikiliza na kutuona, wanategemea tutoe michango ili kusudi wataalam walioko hapa waweze upata ushauri mzuri zaidi. Hili kwa kweli naomba sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongezee hapo kwamba, ni vizuri kwa sababu tunazo Kanuni zetu, zituongoze katika kuendesha Bunge letu. Endapo limetokea tatizo, Kiti chako kisisite kuita Kamati ya Uongozi, kwa sababu tukienda na utaratibu huu kama ilivyo sasa, juzi kuna wanafunzi kutoka Msalato walikuwa wamekaa pale, lakini baada ya kuanza kurushiana maneno na kutupa vitabu, wale wanafunzi ambao walikuwa wamekuja kwa ajili ya mafunzo, waliondoka humu ndani. Sasa kwa utaratibu huo, wanapotoka Walimu wao na wao wenyewe wanatuelewaje sisi kama Wabunge? Kwa hiyo, nashauri sana hili tulizingatie kwa sababu sisi ni jicho la Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Mheshimiwa Waziri nataka aniambie, kupitia hotuba yake hasa ujenzi wa Mwanza Airport, imetengwa shilingi bilioni 30. Ni za nini? Ni za kujenga uwanja au ni za kukarabati? Kwa sababu tumekuwa tukisema mara kwa mara, jinsi mnavyotenga pesa kidogo kidogo hizi, hazitoshelezi hata kidogo. Ujenzi wa Mwanza Airport gharama yake ili ikamilike, siyo chini ya Dola bilioni 60 mpaka 90. Sasa leo mkitoa shilingi bilioni 30, pesa hizi hazitoshi. Nashauri Mheshimiwa Waziri, hebu suala hili alitazame upya.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, nizungumzie reli ya kati. Namshauri Mheshimiwa Waziri, nimeongea na Naibu wake, mabehewa wanayopeleka kutoka Mwanza…
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, mabehewa wanayopeleka Mwanza kuja Dodoma au Tabora ni machache mno. Unapeleka mabehewa matatu ya abiria kutoka Tabora kwenda Mwanza; kuna msongamano wa abiria kule, lakini watu weo Mheshimiwa Waziri wanawadanganya eti kwamba abiria ni wachache, siyo kweli. Inawezekanaje eneo lingine wakapeleka mabehewa 15 lakini Tabora - Mwanza, mabehewa matatu; wanasababisha watu walanguliwe. Nashauri suala hili litazamwe kwa mara ya pili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, zipo ahadi za Mheshimiwa Rais mbili; ya kwanza ni ujenzi wa barabara ya lami kutoka Magu mpaka Hungumalwa, sijaiona humu ndani. Ahadi ya pili, wataalam nafikiri walikuwepo siku ya uzinduzi wa Daraja la Mto Simiyu pale Marigisu. Mheshimiwa Rais aliahidi kuweka mita hamsini hamsini kwa kiwango cha lami, lakini sijaona humu. Nashauri hiyo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri, barabara ya kutoka Nyanguge kwenda Musoma na barabara ya kutoka Mwanza - Shinyanga Border barabara hizi zimekuwa zikitengewa pesa mara kwa mara; hivi kwa nini tusiangalie namna nyingine nzuri zaidi ili kusudi barabara hizi zikwanguliwe zote kwa mara moja, halafu ijengwe upya kuliko hivi ilivyo sasa? Tutakuwa tunatenga pesa mara kwa mara lakini pesa hizo hazina maana. Kwa hiyo, nashauri wajaribu kubadilika kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, siku ile niliuliza swali hapa na kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri amesifia hizi ndege zinazotoa huduma humu ndani kwa maana ya kwenda Mwanza na Mbeya. Pamoja na kusifia, lakini ndege hizi zinaumiza sana wasafiri wetu. Bei ni kubwa mno! Kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya, sh. 700,000/=, ukienda na kurudi sh. 1,400,000/=; kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam, sh. 800,000/=; kwenda na kurudi ni shilingi milioni moja na kitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano ukichukua ndege kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam, siyo chini ya sh. 800,000/=. Hebu tuangalie, ndiyo tunataka huu usafiri, lakini basi usafiri huu usije ukawa kama ni adhabu kwa Watanzania. Nashauri chombo ambacho kipo chini ya Mheshimiwa Waziri kisimamie vizuri ili kusudi wananchi wetu wengi wapande usafiri huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, nawapongeza sana Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa taarifa nzuri ambazo wanatupa sisi Watanzania. Ombi langu kwa upande huu, kama vifaa vyao ni vichache kwa sasa na wanafanya kazi katika mazingira magumu, hebu waongezewe vifaa ili kusudi mamlaka hii iweze kufanya kazi yake vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, tunazo taasisi zetu mbili; TPA kuna Kaimu, hakuna Bodi. Kuna maamuzi mazito yapo pale yanatakiwa yatolewe na Bodi. Nataka uniambie, Bodi ile itaundwa lini? ATCL kuna Kaimu, hakuna Bodi na bahati nzuri unasema unataka kupeleka ndege pale. Hivi utaamua mwenyewe pale au itaamua Bodi? Vyombo vile Mheshimiwa Waziri, ni lazima kuwe na Bodi ili iweze kusimamia majukumu yote yaliyopo pale kwa sababu yapo kwa mujibu wa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Waziri, najua mengine hayapo chini yake, lakini bado ana uwezo wa kumwomba Mheshimiwa Rais ili kusudi taasisi hizi hasa TPA kwa sababu kuna mambo mengi mazuri pale, sasa nani anayasimamia? Nani anaamua? Namwomba sana, Mheshimiwa Waziri, hayo nayo ayachukue.
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi naomba Mwanza Airport Mheshimiwa Waziri asipoleta majibu ya kutosha humu ndani nitakamata shilingi. Namwambia mapema kabisa! Shilingi nitaondoka nayo mpaka nipate majibu kwa sababu kila mwaka wanasema watatenga fedha. Mwaka 2015 ilikuwa ni hivyo hivyo, tukatenga fedha nyingi chini ya Mheshimiwa Mtemi Chenge, tukaahidiwa, lakini hakuna fedha iliyotoka. Safari hii namwambia Mheshimiwa Waziri tutaungana watu wote wa Kanda ya Ziwa ili tupate majibu ya kutosha kuhusu Mwanza Airport. Wamesema wengi sana humu ndani na jana Mheshimiwa Maige alisema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi Mheshimiwa Waziri akilinganisha viwanja vya ndege, sikatai maeneo mengine, kwa ajili ya uchumi wa nchi yetu. Mwanza Airport, hivi hawaijui kwamba ina faida gani kwa nchi hii? Nashauri sana. Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujibu alete majibu ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, reli ya kati na yenyewe ina maneno. Standard gauge wanayosema sijui, lakini bado nasema viwanja vya ndege Mwanza Airport na reli ya kati. Vitu hivi viwili wakisimamia vizuri, nina uhakika tutasonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana. Nianze moja kwa moja, sitaki nipongeze, niende Ukurasa wa 78 wa Kitabu cha Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana kwa sababu, ametenga asilimia 94 kwa ajili ya maendeleo, lakini hasa kwenye Sekta ya Nishati. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, lakini ili tuipate hiyo trilioni moja nashukuru kwa sababu, bahati nzuri nyuma yangu hapa kuna Waziri Mkuu na ningemwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu anisikilize vizuri, naomba mumshtue hapo! Hili Jimbo la Ruangwa kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Shabiby, hili Jimbo la Ruangwa kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, eneo lote lile lipate umeme, lakini na maeneo mengine ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge tuliomo humu ndani tunaiomba sana Serikali hii, asilimia 94 ambayo ni sawa sawa na trilioni moja; Mheshimiwa Waziri wa Fedha tumekuwa tukisema mara nyingi sana humu ndani kwamba, pesa hizi zitoke, lakini bahati nzuri au mbaya pesa hizi hazitoki! Hata zile fedha ambazo tumeziwekea uzio na zenyewe mnazipeleka sehemu nyingine, lakini ili nchi hii iendelee na ili iwe ya viwanda lazima tuwe na umeme wa kutosha. Tutaimba nyimbo hapa, lakini kama hatuna umeme wa kutosha, umeme wenye uhakika, hatuwezi tukafikia yale malengo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana hapa, Serikali kupitia Waziri Mkuu, mtakapokaa kwenye vikao vyenu huko hii trilioni moja iliyoombwa na Wizara ya Nishati na Madini itoke ili kusudi huyu Waziri wa Viwanda anapozungumzia viwanda, lazima apate umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukipata umeme wenye uhakika REA wakasambaza umeme vijijini wale vijana wanaokuja mjini hawatakuja mjini tena kwa sababu kuna umeme vijijini. Naomba sana Serikali zile pesa ambazo tulikuwa tumetenga kwa ajili ya umeme Tanzania, tozo, pamoja na zile ambazo zilibaki mwaka jana, lazima wapelekewe wenzetu wa TANESCO ili kusudi waweze kufanya kazi yao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili na hili nimekuwa nikilisema mara kwa mara, Serikali imeshindwa kulipa TANESCO madeni yake, sijui tatizo ni nini! Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri wa Nishati, hii si Serikali kwa Serikali, hivi hawawezi kukaa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha wakaondoa hili deni ili kusudi vitabu vya TANESCO viwe visafi! Maana kila siku tunakuta madeni, madeni, madeni! Hebu wakae chini hili tatizo walimalize.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie bomba la gesi; huu ni ushauri kwa Mheshimiwa Waziri wa Nishati. Bomba hili lina gharama kubwa, linatakiwa liwe na ulinzi wa kutosha na wasiweke pale Waswahili, waweke Jeshi la Ulinzi liende lisimamie ulinzi wa bomba lile kwa sababu, gharama yake ni kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la tatu, mitambo ya kusindika gesi, LNG; bado hatujachelewa, tuongeze speed kwa sababu, huwezi ukazungumzia trillion cubic meters za gesi tuliyonayo, wamesema 57 trillion, halafu huna mtambo wa kusindika hiyo gesi! Lazima tuwe na mtambo wa kusindika hiyo gesi, vinginevyo tutabaki hapa, hata manufaa yatakuwa hayapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bomba la mafuta la kutoka Uganda kuja Tanzania, Tanga. Nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuchangamkia, sasa nimwombe Mheshimiwa Waziri, hii ndiyo fursa yenyewe, tusiiachie hata kidogo, lakini lazima kuwe na ulinzi wa kutosha katika usimamizi wa ujenzi wa bomba hili la mafuta kutoka Uganda kuja Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, REA. Niwapongeze sana REA kwa kazi nzuri sana wanayofanya na niwaombe Waheshimiwa Wabunge, kwa umoja wetu, kwa kazi nzuri sana aliyofanya REA, hata kama huwapendi kwa sura zao, basi wapende kwa matendo yao, wamefanya kazi nzuri mno. Cha msingi hapa, sisi kama Wabunge, ni kuibana Serikali, ili itoe pesa za kutosha ili miradi iliyobaki ya REA II na REA III tunayokwenda kuanza, iweze kukamilika ndani ya muda unaotakiwa. Lazima tuibane Serikali humu ndani na tuishauri Serikali kwamba, kwa sababu, tunakwenda kwenye REA III tuibane Serikali ili kusudi iweze kutoa pesa za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo dogo upande wa REA, lakini ni vizuri wakarudi nyuma ili wajifunze kwamba, tulifanikiwa REA I, kulikuwa na matatizo gani? Changamoto zilizopo, tumekwenda kwenye REA II changamoto ni zipi tulizoziona? Sasa tunakwenda kwenye REA III zipo changamoto nyingi, hasa urukaji wa vijiji na vitongoji; wanaweka umeme hapa, wanaruka, wanakwenda wanaruka, wanaruka, wanaruka!
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri kwa sababu, wanapita kuangalia ni wapi wameweka umeme, ni vizuri kama ni kijiji kimoja basi kijiji chote kiweze kupata umeme. Si vizuri sana wanaweka umeme kwenye nyumba, wanaruka wanakwenda kuweka kwenye nyumba hii, wanaruka! Si vizuri sana, tungependa sana umeme kwenye kijiji X umeme uwepo. Kwenye maeneo ya Jimbo langu, nilishawasilisha kwa Ndugu Msofe maombi, sitaki niseme hapa, lakini nimwombe sana, maeneo ambayo yamerukwa, vijiji ambavyo vimerukwa, naomba katika awamu ya III umeme uweze kupatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho. Naomba kusisitiza tena, najua Waziri wa Fedha hayupo, lakini najua Waziri wa Nishati yupo na Waziri Mkuu ananisikiliza. Pesa tunazokubaliana humu kwamba, pesa hizi zinatakiwa zitumike kwa kazi fulani, naomba zitumike kwa kazi hiyo hiyo, zisitumike kwa kazi nyingine na haya ni makubaliano ya Bunge. Nasisitiza tena, tukikubaliana kwamba, pesa hizi zinakwenda kwa ajili ya umeme, kama ni tozo za mafuta ziende zikasaidie kule, kusaidia wananchi wetu ili waweze kupata umeme wenye uhakika, basi ziende.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila umeme wenye uhakika hakuna maendeleo, bila umeme wa uhakika hakuna viwanda. Mheshimiwa Mwijage, ni vizuri wakakaa kwa sababu huko mbele bila umeme wa uhakika, viwanda tunavyozungumza Dar-es-Salaam au maeneo mengine vijijini, havitapatikana! Ni lazima tupate umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kupata nafasi ya kuchangia katika hotuba ya Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni bajeti ya Serikali wala siyo ya Dkt. Mpango. Wapo watu wengine wanalaumu kama vile Dkt. Mpango hii bajeti ni ya kwake, hii ni bajeti ya Serikali inayosomwa na Waziri wa Fedha Dkt. Mpango. Kwa hiyo niwaombe sana tunapojadili tujadili bajeti, tusijadili mtu alivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina ushauri kwa Dkt. Mpango kwa sababu yeye ndiye Waziri wa Fedha, yapo mawazo mazuri sana ya Kamati, nashauri kwa mfano suala zima la maji ile tozo kutoka sh. 50/= kwenda sh. 100/= Wabunge wote, Watanzania wote, kama itaongezwa iwe sh. 100 kwa ajili ya maji, nina uhakika Watanzania watanufaika, naomba suala hili ulitazame kwa jicho jema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maji ni uhai, mtoto mdogo anategemea maji, akinamama kule wanategemea maji, maji yakiwa mengi vijijini kero kwa chama changu itapungua. Nakuomba sana juu ya hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, imependekezwa, Mheshimiwa Waziri najua yeye ni muungwana sana, chombo chetu kikuu, kisemeo cha Serikali ni TBC, TBC ndiyo mdomo wa Serikali, TBC ndicho chombo ambacho kinaweza kusema kwamba hapa sasa Serikali ifanye hivi, namwomba hebu atumie busara na watalaam wake, hili nalo alione. Mheshimiwa Waziri tukifanya hivyo kwa kweli tutakuwa tumefanya jambo jema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nimelifurahia sana na niipongeze sana Serikali, nimekuwa Mbunge wa siku nyingi kidogo humu ndani, Wabunge wote wa Vyama vyote tulitakiwa tuipongeze sana Serikali kwa kutenga asilimia 40 ya pesa ya bajeti kwenda kwenye maendeleo, haijawahi kutokea. Nilitegemea Wabunge wote watapongeza kwa sababu pesa hizi asilimia 40 ya bajeti ya trilioni 29 inakwenda kwenye shughuli za maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninashauri kwamba, ingekuwa ni amri yangu kwa sababu kweli tumetoka kwenye asilimia 23 tumekwenda sasa kwenye asilimia 40 lazima tuipongeze sana Serikali. Mbali na hilo katika ukurasa wa 98 wa kitabu chako, ninakushauri ile aya ya 102 unapoanza kwanza mpaka namba kumi nishauri hii ndiyo iwe kama ndiyo amri kumi kwa sababu yako maagizo kumi, hii ndiyo iwe amri kumi, sitaki kusema kwa sababu ya muda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri maelezo aliyoyaeleza hapa kuanzia kipengele cha Kwanza, Pili, Tatu, Nne, Tano, Sita, Saba, Nane, Tisa na Kumi, iwe ndiyo mwongozo kwa Maafisa Masuuli wote Tanzania. Atakayekiuka haya wala tusimwonee aibu, kwa sababu ili pesa hizi ziende kufanya kazi yake vizuri, hii asilimia 40 ya bajeti yote kama hizi amri kumi alizoziorodhesha zikisimamiwa vizuri, nina uhakika tutasonga mbele, tukifanya hivyo na naomba nirudie kusema tena hapa, Maafisa Masuuli wote waandikiwe secular kuhusu hizi amri kumi wazitekeleze. Mimi naziita amri kumi kwa sababu kwa jinsi alivyozipanga na kama kila mtu akifuata moja baada ya nyingine, nina uhakika tutafika mbali sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine naunga mkono, kwanza niipongeze sana TRA kwa kufanya kazi vizuri sana. Tunawaamini, mmepewa jukumu zito, lakini niwaombe hasa kwa upande wa kodi za majengo, tukisimamia vizuri kodi za majengo, Dar es Salaam tukafanya tathmini ya kutosha, Mwanza tukafanya tathmini ya kutosha, Arusha na maeneo mengine tukafanya tathmini ya kutosha, Mheshimiwa Waziri wa Fedha kuna pesa nyingi sana pale, tutaboresha miji yetu, tutaboresha miundombinu yetu, kwa sababu pesa zilizoko pale zilikuwa zinapotea bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri mwingine kwa Waziri wa Fedha na Wabunge wenzangu, naomba kuhusu misamaha ya kodi, sikubaliani nayo, lakini hebu mkae vizuri na Wataalam wako mwangalie hasa upande wa madhehebu ya dini, tusiwahukumu kiujumla tukae, tufanye tathmini ya kina, najua mmeshafanya, kwa sababu madhehebu ya dini mengine yanatoa huduma upande wa hospitali, upande wa shule. Kwa hiyo, naomba sana kuhusu hili, mkae mfanye tathmini ya kutosha ili tusilete mgogoro na madhehebu ya dini. Najua Serikali yangu ni sikivu hili italifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine niipongeze Serikali na niweke tu msisitizo, nimesema leo kazi yangu ni kushauri bajeti ijayo ndiyo tutakwenda kwa detail. Kuhusu ujenzi wa reli naipongeza sana Serikali, ununuaji wa ndege hili wala msichelewe, msisikilize yale maneno ya kule, kwa sababu najua Serikali imekaa. Nawashangaa watu wengine tulikuwa tukisimama humu tunasema Tanzania hatuna ndege sasa Serikali imekuja na mpango mzuri wa kununua ndege tatu, watu wengine wanaanza kuhoji! Jamani hivi tunataka Serikali ifanye nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Fedha, nashauri asiwe na kigugumizi kununua hizi ndege tatu, atwange mzigo, alete ndege tatu hizo ili kusudi Watanzania watumie ndege zao, siyo ndege zile zingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni ununuzi wa meli, chonde chonde! Meli hizi kwa jinsi ambavyo mmejipanga kama Serikali zinunuliwe bila kusuasua, hivyo maeneo ambayo tumeshaahidi kuwa tutanunua meli au kukarabati tufanye bila kuchelewa. Ili tufanye hivyo niwaombe sana wenzetu wa TRA kwa sababu tunawategemea. TRA ni kama mshipa kwenye mwili wa binadamu, ukikatika mshipa mmoja au ukisimama mshipa mmoja, ina maana eneo moja lita-paralise, kwa hiyo ili tutekeleze haya ambayo Dkt. Mpango Waziri wa Fedha ameyaainisha humu ndani ni lazima makusanyo yakusanywe na yasimamiwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kukusanya matumizi yetu yawe na nidhamu, tukifanya hivyo tutakwenda vizuri. Kwa kweli naunga mkono sana bajeti hii kwa sababu ina mambo mengi sana mazuri na imegusa wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo Waziri wa Kilimo ni muhimu kuliangalia, hebu tazama kwenye tozo za mazao, tumeyasema mwanzo tozo ni nyingi, ni kero, hebu ziondoeni kwa sababu zinawapa matatizo watu wetu, kwa kufanya hivyo tutakuwa tumefanya kazi nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho Waziri wa Ardhi, Waziri wa Kilimo, Waziri wa Maliasili wakae pamoja waangalie namna ya kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji, yale maeneo ambayo sasa hayana sifa tena ya kuwa mapori ya hifadhi, wakae na waangalie namna nzuri wayagawe ili watu wetu, wakulima na wafugaji waweze kuyatumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, lakini naomba niwashauri katika maeneo mbalimbali ili kuboresha na kustawisha Wizara ambayo ni nyeti katika kuongeza Pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri sana inayofanywa na Mheshimiwa Waziri na viongozi wenzako nashauri kuchukua mapendekezo mazuri yaliyotolewa na Kamati pamoja na ushauri mzuri unaotolewa na Waheshimiwa Wabunge kwa mustakabali wa nchi.
Pia katika kutatua migogoro ndani ya hifadhi Waziri kupitia wataalam wake watatue migogoro kwa kuzingatia hekima, busara na taratibu za kisheria zilizopo, wasitumie mabavu, tunajua sheria zipo lakini tatizo ni ushirikishwaji hafifu au elimu duni ya uhifadhi ikichangiwa na rushwa.
Mheshimiwa Waziri, Shirika la Hifadhi za Taifa linalosimamia Hifadhi za Taifa 16 hadi leo halina bodi kwa mujibu wa Sheria Sura 282 ya mwaka 2002 na kama ilivyorejewa kwa Sheria ya Hifadhi za Taifa ya mwaka1959 Sehemu ya II inayoanzisha Hifadhi ya Taifa na Bodi ya Wadhamini. Nashauri kufuatana na uzito na umuhimu wa taasisi hii Waziri umwombe Mheshimiwa Rais ateue Mwenyekiti wa Bodi na wewe uteue Wajumbe wa Bodi haingii akilini taasisi kubwa kama hii kukaa miaka zaidi ya minne bila Bodi ya Wadhamini.
Naomba niulize, TANAPA kutokuwa na bodi ni nani anaamua maamuzi ambayo uamuzi wake unatakiwa uamuliwe na bodi. Mheshimiwa Waziri Chuo cha Mweka nikiwa Mjumbe wa Bodi kwa wakati huo Rais wa Awamu ya Nne alitamka kwa kumwambia Waziri wa wakati huo Mheshimiwa Mwangunga kuwa chuo hicho kiwe chuo cha mfano (center of excellence) lakini hayo hatuyaoni, kumbuka chuo hicho ndicho kiwanda cha kuzalisha wataalamu katika tasnia ya wanyamapori hasa katika hifadhi zetu zote nchini. Nashauri chuo hicho pamoja na kile cha Pasiansi visimamiwe vizuri ili kutoa wataalam na askari wanaoweza kwenda kusimamia vizuri maeneo ya uhifadhi.
Nimalize kwa kuwaomba viongozi wote walio chini ya Wizara hii kumsaidia Waziri ili yaliyoainishwa ndani ya kitabu hiki yaweze kutekelezwa. Lakini kwa pekee nimpongeze CEO wa TANAPA kwa kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa pamoja na kutokuwa na Bodi ya Wadhamini.
Mheshimiwa Waziri moja ya changamoto kubwa ni kutopata takwimu sahihi za watalii hasa katika eneo la Selous, Serikali iangaie njia nzuri zaidi hasa kwa hawa wenye hoteli ziwe na takwimu sahihi ili kudhibiti mapato ya Serikali lakini kuwe na motisha kwa wafanyakazi na Selous iimarishe usimamizi kwa kila hoteli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika pori la akiba la Selous lina jumla ya kambi za kuweka wageni (camp sites) nane na zisizopewa wawekezaji hadi leo hawajaendeleza, nashauri wanyang‟anywe ili wapewe wengine na kuendelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuondokana na uvamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa kwa ajili ya makazi, kilimo, ufugaji na matumizi endelevu nashauri kuainisha na kuhakiki mipaka ya mapori ya akiba kwa mujibu wa GN kupitia Wizara ya Ardhi, kutoa elimu ya uhifadhi na kufanya tathmini ya mapori tengefu. Pia nashauri kuzishirikisha Wizara na taasisi zingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Utalii (TTB) na TANAPA kwa pamoja na NCCA hawajaonyesha jitihada za kutangaza utalii nje na ndani ya nchi. Je, ni kwa nini taasisi hizo ikiwemo Bodi ya Utalii hawatilii mkazo suala zima la kutangaza na kuondoa vikwazo vinavyokwamisha watalii hasa wa Marekani na Wafaransa ili ile idadi ya watalii iongezeke na nchi ifaidike na utalii kwa kuongeza mapato zaidi.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono na nawapongeza sana hasa kwa kuamua kulisimamia suala la upandaji na utunzaji wa miti. Kwimba tulipata ugeni wa Makamu wa Rais ambapo tulimweleza mipango yetu ya kupanda na kuitunza ambapo tunaanzia kwenye shule za msingi na sekondari. Tumekubaliana kila mwanafunzi anayeanza shule awe na mti wake ambao utapewa jina lake ambapo atautunza hadi amalize darasa la saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, mwanafunzi huyo huyo akiingia darasa la pili, tatu, nne, tano, sita na saba kila darasa atakuwa na mti wake, kwa hiyo akimaliza darasa la saba mwanafunzi mmoja atakuwa na miti saba. Mfano
Shule ya Msingi Kadashi ina wanafunzi 1000, kwa utaratibu huo kutakuwa na upandaji na utunzaji wa miti 1000, hii ni kwenye eneo moja la Shule ya Msingi Kadashi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Askofu Mayala aliyotembelea Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu, kuna wanafunzi zaidi ya 200, hivyo kila mwanafunzi anapoanza kidato cha kwanza hadi cha nne akimaliza form four atakuwa ameacha miti iliyopandwa na kutunzwa miti 800 ikiwa na majina yao. Upandaji wa miti na utunzaji wa miti kwa ajili ya mbao, kivuli, matunda na utunzaji mazingira. Naomba Wizara yako endapo kuna fungu lolote Kwimba iwe pilot area katika suala zima la upandaji na utunzaji wa miti. Kauli mbiu yetu ni ‘upandaji na utunzaji wa miti kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na vijavyo’.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwe kama vichaa katika kupanda na kutunza miti.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami naomba nichangie kuhusu taarifa ya Kamati ya Bajeti. Nakushukuru kwa nafasi hii, lakini nisingependa kurudiarudia yale ambayo yamesemwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niipongeze sana Serikali kwa kweli kwa kazi nzuri lakini kwa nidhamu ya matumizi ya fedha inazokusanya. Nidhamu ya matumizi ya fedha kwa kweli imeongezeka sana. Kwa hiyo, naomba Serikali iendelee na utaratibu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita sana kama ulivyoshauri kwenye maoni na mapendekezo ya Kamati. Maoni ya Kamati hasa ukusanyaji wa ulipaji wa deni la TANESCO. Deni hili limekuwa likikua siku hadi siku. Mwaka 2014/2015 deni la TANESCO lilikuwa shilingi bilioni 186.4. Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati, inasema deni hili sasa hadi Agosti, 2016 limefikia shilingi bilioni 794.9. Kutoka shilingi bilioni 186 kwenda shilingi bilioni 794. Kwa hiyo, limeongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukijipa mwaka mmoja mbele, usishangae likafikia shilingi trilioni moja, sasa ni kwa nini deni hili linakuwa siku hadi siku? Nani halipi deni hili la TANESCO? Ni kwa nini halipi? Kama ni Taasisi za Serikali, nina uhakika zinapata kasma ya kulipa umeme. Taasisi hizi; watu binafsi na mashirika ya umma, kwa nini hawailipi TANESCO pesa zake ambapo yenyewe inatoa huduma ya umeme? Ni lazima ilipwe, kwa sababu ni azimio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kupitia Bunge lako, deni hili ni kubwa; ndiyo maana TANESCO kwa sababu ya madeni makubwa inatumia nguvu nyingi lakini hailipwi na ndio maana wanafika mahali TANESCO wanataka kupandisha bei ya umeme. Inawezekana sababu mojawapo ni hii. Kama hili deni la shilingi bilioni 794 lingelipwa hata robo tatu, nina uhakika TANESCO ingeweza kujiendesha. Vinginevyo, TANESCO itakufa, itashindwa kufanya kazi yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia viwanda, kama hatuna umeme wa uhakika na wenzangu wamesema kwamba umeme unakatikakatika, lakini kama TANESCO haipewi fedha zake, viwanda hivi vitakufa kwa sababu hakuna umeme wa kutosha. Naomba sana Serikali iangalie na tulishauri mwaka 2014 - 2016 kwenye taarifa ya nishati na madini, wakati deni lilikuwa shilingi bilioni 186, lakini nashangaa kwa nini Serikali haitaki kulipa deni hili, mpaka limefikia shilingi bilioni 794. Naomba sana Serikali deni hili lilipwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunahitimisha hapa, mhusika mwenye taarifa hii alisema, hasa kuhusu deni la TANESCO, shilingi bilioni 794 lazima lilipwe vinginevyo TANESCO itakufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tulipitisha vizuri kabisa hapa, sheria nzuri kuhusu gesi na mafuta. Sheria ile tukakubaliana kwamba kwa sababu tumepitisha sheria hii, ambayo na kwenye mapendekezo ya Kamati imo, kwamba kukamilisha kwa kanuni ya sheria ya kusimamia, mapato ya mafuta na gesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa tulipitisha mwaka juzi, 2015 nami nilikuwa Mwenyekiti, tukapitisha hapa, tukategemea kwamba Serikali sasa, kwa mfano mwaka jana, 2016 kanuni hizo zingekuwa zimeshakamilika. Mpaka leo kanuni hizo hazijatekelezwa. Hivi tatizo hasa ni nini? Hizi shughuli za gesi na mafuta zinafanyikaje kama kanuni hazipo? Naishauri Serikali itekeleze agizo la Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekubaliana na Kamati imesisitiza, sijui Serikali inapata kigugumizi kwenye eneo gani? Kwa sababu tunategemea umeme wetu kupitia maji kwa maana ya hydro, gesi; lakini tukasema twende mbali zaidi, kwenye umeme wa joto ardhi (geothermal), tutoke hapo twende kwenye solar power.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukitazama, tumekubaliana humu humu kwenye Bunge suala la umeme wa upepo pale Singida; sasa nauliza, hivi tatizo hasa ni nini? Tukitegemea chanzo kimoja au vyanzo viwili; hydro pamoja na gesi, lakini tunataka tusonge mbele zaidi umeme wetu huu tuuze nje, tupate pesa nyingi za kigeni, lakini tuweze kujitosheleza kwenye umeme wetu wa ndani hasa tunapotaka kwenda kwenye uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda hivi tunavyovisemea, bila kuwa na umeme wa uhakika wa bei nafuu usiokatikakatika, hatuwezi kufika. Itakuwa ni hadithi tu! Ni lazima tujitosheleze na umeme wa kwetu kwa sababu tuna vyanzo vingi, Mungu ametujalia, vyanzo vingi tunavyo isipokuwa ni kuvisimamia na kuvitekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kama tumekubaliana jambo fulani litekelezwe, kwenye eneo fulani, hivi tunashindwa nini kulitekeleza? Leo tuambiane, kwenye geothermal tumesikia asilimia ngapi? Tukubaliane kwenye umeme wa jua, asilimia ngapi? Tutoke hapo twende kwenye umeme wa upepo, asilimia ngapi? Ukitoka hapo, kule Liganga na Mchuchuma ni maneno tu, yanasemwa kila siku; Liganga, Mchuchuma; Liganga, Mchuchuma; hata tutakapokuja tena kesho kutwa, Liganga, Mchuchuma! Ni history tu! Tufike mahali tuseme hili linawezekana, tunaliacha. Nafikiri hata huku kwenye taarifa ya Kamati, limesemwa hili la Liganga na Mchuchuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe umekuwa muda mrefu huku ndani, inawezekana tangu umeanza U-AG Liganga Mchuchuma umeisikia, lakini imefikia wapi? Sijui kuna mgonjwa gani huku anayezuia kila siku! Liganga Mchuchuma kila siku, lakini kama kweli tungeamua tukawekeza pale Liganga Mchuchuma, tungepata umeme wa uhakika, tungepunguza matatizo. Ukiwa na vyanzo vizuri vya umeme nina uhakika hata bei ya umeme itashuka. Ukiwa na vyanzo vingi vya umeme, utauza nje ya umeme wako huu, utapata fedha za kigeni, lakini ni mizunguko tu, tunazunguka lakini hatufiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema mambo matatu haya, kukamilishwa kwa kanuni na sheria za kusimamia mapato ya mafuta na gesi, lakini kuilipa TANESCO deni lake, shilingi bilioni 790, pia kukamilisha kwa miradi mbalimbali ya vyanzo vya umeme, tufike mahali tumalize tuhamie kitu kingine. Mengine najua yamesemwa sana, sitaki kurudia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu kuhusu taarifa hii, ni hayo. Nashukuru sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijadili taarifa hizi mbili
lakini nitajikita sana kwenye Taarifa ya Nishati na Madini. La kwanza, kwa sababu Kamati zetu
hizi zinatoa mapendekezo na maoni mbalimbali; tunatumia karibu siku tano, sita kutoa
mapendekezo; tulishawahi kufanya hivyo siku za nyuma, lakini tukijiuliza: Je, haya mapendekezo
mwisho wa siku nani anakuja kuyajadili?
Taarifa hizi tunazopendekeza, zinaletwa Bungeni lini na kujua kwamba kweli haya
tuliyopendekeza yametekelezwa? Kama yametekelezwa, ni kwa kiasi gani? Nani anajua? Au
kazi yetu sisi ni kutoa mapendekezo, yanakwenda Serikalini halafu basi yanaishia hapo hapo?
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kwamba ule utaratibu wa zamani kweli kwenye enzi za
akina Mheshimiwa Shelukindo, taarifa zilikuwa zinasomwa, mapendekezo yanatolewa,
baadaye Serikali inakuja inajibu pale ambapo imetekeleza; kwa nini imeshindwa na kwa nini
imefanikiwa, ili kusudi kuweza kujua haya yote ambayo sisi Waheshimiwa Wabunge tunakaa siku
mbili tatu humu ndani tunayasema. (Makofi)
Waheshimiwa Wabunge, hili wala siyo la Serikali hata kidogo, ni letu sisi Waheshimiwa
Wabunge. Kwa sababu tukisema kwamba tunataka kufanya jambo hili, lakini lazima tujue
kwamba mambo haya yanatekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, naomba unikubalie niipongeze Serikali kupitia Shirika la
Umeme (TANESCO); sijui wamefanya miujiza gani. Siku hizi sijasikia kukatika katika kwa umeme,
lakini mgao wa umeme; hata kama unakatika labda ni bahati mbaya. Lazima niseme ukweli, ni
tofauti na siku za nyuma. Sasa hivi kukatika kwa umeme kumepungua sana, lakini hata mgao
wa umeme nchini sasa hivi hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaiomba Serikali kupitia TANESCO waongeze ile kasi
ya kulisimamia Shirika hili la TANESCO, kwa sababu yapo mambo mengi. Jambo la kwanza
ambalo naiomba Serikali, tulikubaliana katika kutekeleza kwamba ipunguze gharama za pale
tunaponunua huu umeme. Kwa mfano, Symbion, Aggreko na Songas ambayo kwa taarifa ya
Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, mpaka sasa TANESCO
inadaiwa shilingi bilioni 63. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini, hapa
kuna mkanganyiko wa madeni ya TANESCO. TANESCO inadaiwa kiasi gani na TANESCO inadai
kiasi gani? Mfano, kwa mujibu wa taarifa ambayo imesomwa sasa hivi na Mwenyekiti wa
Kamati, wanasema kwamba TANESCO inadaiwa shilingi bilioni 822, lakini kwa mujibu wa taarifa
ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, wanasema TANESCO inadai shilingi bilioni 796. Sasa ipi ni ipi?
TANESCO inadaiwa au TANESCO inadai?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni vizuri tukapata mchanganuo vizuri ili sisi
Waheshimiwa Wabunge tuweze kujua, kwa sababu hii inachanganya. Kwa mujibu wa taarifa
ambayo imesomwa sasa hivi hapa, wanasema Serikali na taasisi inaidai TANESCO shilingi milioni
269. Sasa hii inachanganya. Tunaomba Serikali, itakapokuja kujibu au Mheshimiwa Mwenyekiti
wa Kamati mtusaidie kujua hasa. Mtupe mchanganuo halisi TANESCO inadai kiasi gani na
TANESCO inadaiwa kiasi gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo naomba tusaidiwe tu, ni haya katika utekelezaji.
Lipo suala la Sera ya Gesi na Mafuta kutafsiriwa katika lugha ya Kiswahili. Tulikubaliana kwenye
Kamati na tukaleta mapendekezo ndani ya Bunge, ndiyo maana nikasema mambo haya kama
hatufuatilii utekelezaji wake, inaweza ikawa ni tatizo. Jambo hili tumelisema humu ndani lakini
imekuwa halieleweki.
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, mpango maalum kuhusu mageuzi katika Sekta ya
Madini; tulikubaliana na hili nafikiri hata Mheshimiwa Rais alilisemea siku moja, kuhusu kuweka
uzio. Hili lilikuwa ni pendekezo la Kamati ya Nishati na Madini, ndani ya Bunge na tukaazimia
kwamba uwekwe utaratibu sasa wa kulinda madini yetu ya Tanzanite huko Mererani; na bahati
nzuri na Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati amelisema hili kwamba hatuoni tija ya uzalishaji
katika eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge lako tulikubaliana kwamba iangaliwe namna nzuri zaidi
ya kuweka uzio, tanzanite inapatikana Tanzania peke yake, hakuna sehemu nyingine. Sasa
kama hatuweki utaratibu mzuri wa kuweka uzio kwenye eneo hilo, itasaidia mambo mawili;
wale walanguzi; kutorosha madini; lakini na kutokujua uhalisia wa madini yenyewe. Kwa hiyo,
bado Serikali ituletee majibu. Je, suala zima la uzio, ni lini litakamilika?
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, kabla kengele haijalia, Waheshimiwa Wabunge,
suala zima la ruzuku kwa ajili ya wachimbaji wadogo wadogo; wiki mbili au tatu zilizopita,
baadhi ya Wajumbe wa Kamati walikwenda Nkasi ili wachimbaji hawa wadogo wadogo
waende kupata hela yao ya ruzuku. Inasikitisha kwamba walikwenda Mpanda, kwamba hawa
wachimbaji wadogo wapate hela ya ruzuku. Wamefika kule, hela ya ruzuku haipo. Kwa hiyo,
hawa waliokwenda kule wakatumia hela za Serikali bila manufaa yoyote yale.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba suala hili la ruzuku ya Serikali lisitumike kisiasa kwa
sababu hawa wachimbaji wadogo wadogo wangependa zaidi wanufaike kama
tulivyokubaliana. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali, mnapozungumzia kwamba mnakwenda
kutoa ruzuku kwa ajili ya wachimbaji wadogo, basi iwe kwenda kutoa ruzuku kweli kweli, lakini
siyo kuwabeba kutoka maeneo ya huku na huko, halafu wanakwenda kwenye eneo husika
wasikute chochote kile. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali iyatekeleze haya, lakini tunapenda zaidi
tuwe tunapata mrisho nyuma kwa yale ambayo Bunge linapitisha ndani ya Bunge, kwamba hili
limetekelezeka, hili halijatekelezeka; ili tuweze kuishauri vizuri Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Naunga mkono taarifa zote
mbili.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nianze kwa kukushukuru wewe kwa nafasi hii, lakini namshukuru sana Mheshimiwa Waziri na timu yake yote pamoja na taasisi chini ya Wizara kwa kweli kwa kazi nzuri sana wanayoifanya. Kuna msemo mmoja wa Kiswahili unasema ukiona adui yako anakupongeza kwa jambo lako, achana nalo; lakini ukiona adui yako kwa jambo lako anakupigia makofi, jitazame mara mbili. Kwa hiyo, wenzetu kila jambo jema linalofanywa wao hawakubali. Namwomba Mheshimiwa Waziri, kwa yale mazuri ambayo mnayafanya na ni mengi tu, kazeni buti, endeleeni, wala msitishwe na hizo kelele ambazo zinatokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Waziri, najua amevaa kiatu cha Mheshimiwa Rais kwa sababu Mheshimiwa Rais ndiye alikuwa Waziri wa Ujenzi; na kiatu hicho naona kinakufaa sana. Naomba, ipo barabara ambayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kutoka Isandula - Magu inakwenda Bukwimba - Ngudu kwenda Hungumarwa. Ni ahadi! Mwaka 2016 mlisema kwamba mmetenga pesa kwa ajili ya usanifu, sasa leo sijaona humu, nami kama Senator hatupendi sana kupiga makelele na hasa ukizingatia kwamba Mheshimiwa Waziri wa Wizara ni mtu msikivu na mwelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne akiwa na Rais wa Awamu ya Tano, walikuja kufungua Daraja la Mto Simiyu, Maligisu. Vingunge wote wa Wizara walifika pale Maligisu na Mheshimiwa Rais aliahidi


kwamba ile approach ya mita 50 upande huu na mita 50 upande huu itajengwa kwa kiwango cha lami. Tena kama natania, ili na fisi nao waje wapite kwenye lami. Hiyo ilikuwa mwaka 2015. Mheshimiwa Waziri, maagizo ya Mheshimiwa Rais, mita hamsini hamsini, hebu tusimwangushe Mheshimiwa Rais. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kubwa, Mheshimiwa Waziri, anazo taasisi zaidi ya 30 zilizo chini yake. Taasisi hizi ni kioo kwa nchi yetu na Taasisi hizi ni uchumi kwa nchi yetu. Nawaomba kwa sababu bahati nzuri ma-CEO wapo hapa, Wakurugenzi wapo kwa maana ya Wenyeviti. Kwa taasisi hizi, kila CEO, Mwenyekiti kwenye eneo lake kwa ajili ya kuisaidia Serikali na kwa sababu tunaomba pesa nyingi, pesa hizi tunazitegemea kutoka kwenye hizi taasisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba sana viongozi hawa, yale makubaliano ambayo inawezekana Mheshimiwa Waziri tutaweka na utaratibu mmoja mzuri, nafikiri wa kupimana, kwa sababu ile business as usual, tukienda na utaratibu huo kwa taasisi zetu hizi, tunaweza tukafika mahali tukashindwa kufikia yale malengo. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, pamoja na viongozi wa taasisi zilizo chini yako, zifanye kazi ili kusudi matokeo makubwa tuyaone kwa kuisaidia nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, namwomba Mheshimiwa Waziri upande wa Wakala kwa Mama Kijazi pale, TMA. Eneo hili ni eneo zuri sana kama watapatiwa vifaa na wataalam wa kutosha. TMA hii igawanyike kikanda; Kanda ya Ziwa, (mimi nazungumzia Kanda ya Ziwa, huku kwingine baadaye) ili kusudi waweze kutambua na kuwashauri wakulima, maana yake sasa hivi kuna ubashiri, lakini tutoke kwenye ubashiri tusogee kwenye uhalisia kwamba mvua zitanyesha kesho saa fulani. Jamani wale wavuvi kesho kutwa msiende ziwani kwa sababu kuna


upepo mkali. Sasa ili wafanye hivyo ni lazima wawe na vifaa vya kutosha vinavyoweza kuhimili badala ya kwenda kupiga ramli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, barabara ya Nyanguge - Musoma, Mwanza -Shinyanga Boarder tumekuwa tukizitengea pesa nyingi kila mwaka. Hivi hakuna utaratibu mzuri wa kuzifumua hizo barabara zikajengwa upya? Maana yake kila mwaka fedha inatengwa. Namshauri Mheshimiwa Waziri, hebu walitazame hili kusudi barabara zetu hizi ambazo kiuchumi na kijamii zina faida kubwa sana kwa Kanda ya Ziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, nashukuru tunatengeneza hii reli ya kati. Sasa nasikia na namwomba CEO wa TRL, kama treni itatoka Dar es Salaam lakini inakuja Shinyanga, inafika Malampaka, halafu haisimami katikati hapa pote inakwenda kusimama Mwanza; nashauri treni hii isimame Bukwimba Stesheni, panajulikana! Panaeleweka! Kadogosa; siwezi kusema Kisukuma lakini nakuomba treni isimame Bukwimba Stesheni, miundombinu ipo ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, kumekuwa na malalamiko mengi sana kuhusu upoteaji wa makontena. Hebu wataalam wako wakae waangalie namna nzuri zaidi; hivi NASACO, Wakala wa Meli, nasema mkae mwangalie; Wakala wa Meli wa wakati ule NASACO, tulikosea wapi? Kwa nini tuliwaondoa? Kwa sababu haiwezekani mizigo ikawa inapotea, makontena hayajulikani, yanaingia makontena na taarifa hatuna. Naomba kama inawezekana NASACO iangaliwe upya ili kusudi tuweze kurejesha heshima ya nchi yetu hasa upande wa mizigo inayokwenda nje na ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru tena lakini naomba kusisitiza, taasisi hizi ni kioo cha nchi yetu; TPA ni kioo na uchumi, ATCL, TRL na mengine, ni kioo kwa uchumi wa nchi yetu. Toeni huduma, fanyeni biashara lakini kwa manufaa ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii na naunga mkono hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapa hongera sana kwa kazi nzuri sana wanayoifanya chini ya usimamizi wa Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa ujumla. Mheshimiwa Waziri Ummy naomba kukumbushia vitanda vitano na magodoro yake, ahadi uliyoniahidi na mimi nikaenda kutoa ahadi ya vitanda vitano, magodoro na mashuka yake katika Kituo cha Afya cha Malya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi hiyo imekuwa ya siku nyingi, naonekana muongo kwa sababu ya kutotekeleza ahadi iliyopitia kwangu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri. Mimi naheshimika kwa kutosema uongo kwa wananchi wangu ambao nawaamini na wao wananiamini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri naomba utekelezwaji wa ahadi hiyo ya vitanda vitano katika Kituo cha Afya cha Malya, Jimbo la Sumve. Nawatakia kila la kheri katika utekelezaji wa majukumu yaliyo mbele yenu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, niruhusu na mimi niungane na wale waliompongeza Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji mzuri, lakini nimewasikiliza Wabunge wenzangu kwa umakini sana tangu jana na leo, tatizo hapa ni rasilimali fedha. Hakuna zaidi ya hapo kwa sababu hata tukipiga kelele namna gani, tukiimba namna gani kama hakuna pesa hata hii miradi tunayoiombea saa hizi haiwezi kutekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitoe ombi kama alivyotoa Mheshimiwa Kangi Lugola pale, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu, wa vyama vyote tukubaliane kimsingi, yale mapendekezo ya mwaka jana ya tozo ya shilingi 50 yaongezeke sasa yaende shilingi 100. Yakiwa shilingi 100 yatatupa shilingi bilioni 316. Hizi ukizijumlisha na fedha za ndani ambazo ni shilingi bilioni 408 ukajumlisha na fedha za nje ambazo ni shilingi bilioni 214 unapata jumla ya shilingi bilioni 940 na zaidi. Fedha hizi shilingi bilioni 940 inazidi hata ile bajeti ya mwaka jana. Sasa ili tufike huko, tukubaliane tu kimsingi tutoke kwenye 50 ya tozo twende shilingi 100.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunataka kweli miradi yetu hii ambayo tunaizungumzia humu ndani iende ikatekelezwe, tukubaliane kwamba shilingi bilioni 316 kila mwaka ziende kwenye miradi ya maji. Tukijipa miaka mitatu, tutakuwa na karibu shilingi trilioni moja, zote hizi zinakwenda kwenye maji. Najua matatizo ya maji kuanzia 2018, 2019 na 2020, kama tutakuwa na pesa hizo shilingi trilioni moja na zaidi, nina uhakika matatizo ya maji yanaweza kupungua.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili matatizo ya maji yapungue, ni lazima tuamue kwamba sh.50 itoke huku iende sh.100. Lazima tuamue! Bila kuamua kwa sababu hakuna sehemu nyingine, tukitegemea bajeti ya Serikali ya shilingi milioni 408 na pesa za nje shilingi milioni 214, fedha za nje zinaweza zikaja kidogo au zisije. Sasa ili tuondoke huko, ni lazima Bunge lako liamue, kwamba shilingi 50 tuachane nayo, twende kwenye shilingi 100 itakayotuzalishia shilingi bilioni 316 kila mwaka na hizi zinakwenda kwenye maji. Bila kufanya hivyo, tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tuamue sisi Wabunge wote. Naomba Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Mheshimiwa Mama Hawa Ghasia, naomba mwende mlisimamie hili. Mwaka 2016 tulikubaliana humu ndani, lakini halikutekelezwa, tunaomba mwaka huu, mlibebe kama lenu, lakini ni la Bunge zima. Yale maneno kwamba itashusha inflation, inflation hii itashuka lakini in multiple effect itakuwa ni kubwa zaidi, kwa sababu matokeo ya kuongeza sh.100/= multiple effect yake itakuwa ni kubwa zaidi tofauti na tunavyofikiria. Naomba sana Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Mama Hawa Ghasia hili walibebe ili kusudi waende kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali angalau kwa kuanza mradi wa maji wa Ziwa Victoria. Naomba process zilizoanza ziharakishwe. Mwaka 2016 tulitenga shilingi bilioni moja, hakuna kilichofanyika; mwaka huu imetengwa shilingi bilioni mbili, najua yupo hapa Mheshimiwa Lwenge, hili suala nafikiri ni la kusukuma haraka haraka ili kusudi mradi huu ukamilike.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Kwimba, tayari nimeshamwandikia Mheshimiwa Waziri kwamba kuna visima vya maji 188 Wilaya nzima, havifanyi kazi, vimezeeka, maji hayatoki na pampu zimeibiwa. Visima 188 kwa Wilaya nzima ya Kwimba, Majimbo mawili Sumve na Kwimba, maana yake mimi ndio Mbunge ninayejumuisha Majimbo yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, hii dhana ya kuwatua ndoo akinamama ili ikamilike na iwe na uhalisia visima hivi 188 tuangalie namna ya kusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna miradi mingine minne ya maji ya World Bank imekuwa ya muda mrefu sana, leo ni zaidi ya miaka 10 na kila siku nimekuwa nikiuliza swali humu ndani. Mheshimiwa Lwenge, matatizo yaliyoko kule hayasemeki! Watu wana urasimu wa kumwaga. Ukiuliza hiki, unaambiwa Mkandarasi; ukiuliza hivi, utaambiwa Wizara.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba Mheshimiwa Waziri anisaidie kuondoa kero iliyopo kwenye maeneo hayo. Kadashi na Isunga tatizo ni kubwa, nimemwandikia, mengine yako chini ya asilimia 45 mengine 50, tatizo wanasema hela mnazo ninyi, wengine wanasema hela ziko huku. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri hili alisimamie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, narudia kuomba tena, hata ukitaka maji kule Tukuyu, najua kuna mvua nyingi tu huko, kwa Mheshimiwa Spika pia anataka maji,; bila kukubaliana hapa ongezeko la shilingi 50 kutoka kwenye shilingi 50 kwenda kwenye shilingi 100 tutakuwa tunasema hapa, tutaimba umwagiliaji sijui vitu gani; tutazame REA! Tulivyoanza REA, tulikubaliana humu ndani; leo tazama vijiji karibu vyote vinakwenda kupata umeme kwa sababu ya makubaliano ya humu ndani. Pesa za Mfuko wa Barabara sabini kwa thelathini, tazama barabara zetu leo ni sababu ya kukubaliana. Naomba na hili sasa na lenyewe tukubaliane tutoke kwenye shilingi 50 twende kwenye shilingi 100 ili tupate shilingi bilioni 316 kila mwaka ili tuweze kujenga visima na vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mimi niungane na wenzangu katika kuwapongeza Mawaziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwangu la kwanza, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri wa Michezo, tunacho kiwanda cha kuzalisha wataalam wa michezo nchini, Chuo cha Michezo Malya. Wataalam hao ni walimu wanaotoka kwenye shule za misingi wanakwenda kujifunza namna ya kufundisha michezo mbalimbali kwenye shule zetu za misingi na sekondari, ndiyo maana nakiita ni kiwanda. Ili upate wachezaji wazuri wa fani zote, huwezi ukaanza na vijana wa sekondari wala vyuo, lazima uanze na shule za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, chuo hiki malengo yake nafikiri anayafahamu na bahati nzuri juzi alifika akaona miundombinu yake, jinsi tulivyo-invest siku zote.

Sasa ni vizuri zaidi pale walipoishia wenzake hebu na yeye akanyage sasa huo moto ile accelerator asitoe mguu wake ili ipae zaidi, chuo kile ikiwezekana kiondoke na kutoa certificate, diploma kiende kwenye degree ya michezo. Tukifanya hivyo Mheshimiwa Waziri chuo kile tutakuwa tumekisaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nimuombe Katibu Mkuu, tuna upungufu kadhaa hasa upande wa maji, kipo kisima kikubwa tulitumia pesa zaidi ya shilingi milioni 230 kwa ajili ya kujenga kisima cha maji kwa ajili ya Malya ambayo mnufaika mmoja wapo ni Chuo cha Michezo Malya, tumepungukiwa mambo madogo madogo. Bahati nzuri kama sikosei Mkuu wa Chuo cha Malya yupo, nafikiri anaweza akamweleza Katibu Mkuu, hili tatizo la upungufu wa maji linaweza likaondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niruhusu kwa sababu vinginevyo sitajitendea haki nimpongeze sana Naibu Spika kwa kuweza kuchukua baadhi ya wachezaji wa michezo ya ngoma za asili kwenda kupata mafunzo ya ziada kwenye chuo chetu cha Bagamoyo. Ni chuo kizuri na sisi Waheshimiwa Wabunge nafikiri si vibaya tukaiga utaratibu huo mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, Baraza la Michezo la Taifa. Mimi sijui Bwana Malinzi ni Malinzi yupi sasa, Baraza hili ndilo linalosimamia michezo yote. Sijaona wala kusikia Baraza limekwenda limekemea eneo fulani penye mgogoro, lipo lipo tu. Nilisema kipindi kile na leo nasema tena kwa sababu Baraza hili ndiyo mlezi wa vyama hivi vya michezo. Sina uhakika kama Baraza hili linafanya kazi yake ile ambayo tuliitunga humu Bungeni. Mimi nasema kama upo upungufu kwenye utaratibu wetu hebu tuje hapa tubadilishe. Kwa sababu haiwezekani leo hii Baraza kila mnapoenda iwe kwenye vilabu, iwe kwenye riadha, kuna migogoro. Sasa kazi ya Baraza hili ni nini? Naomba Baraza hili hebu lijipange vizuri kwa sababu michezo hii ni mingi kama walivyosema wenzangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Uwanja wetu wa Taifa tubadilike sasa tuache kuutumia kwa ajili ya mechi za Simba na Yanga na hizi mechi la ligi. Uwanja ule tunaweza tukaugeuza ukawa ni uwanja wa kibiashara na ukawa ni uwanja wa kuleta watalii kutoka nje hasa michezo ya kimataifa. Nilisikia juzi juzi hapa Mheshimiwa Waziri sijui timu gani inakuja utasema, tuna uwanja mzuri, tuna mbuga za

wanyama, wachezaji hawa wa kigeni wakija kucheza michezo ya kimataifa Tanzania kwenye uwanja wetu wa Taifa baada au kabla ya michezo ile wanatembelea mbuga zetu za wanyama, tunapata watalii kupitia michezo na kupitia uwanja ule, ni jambo linalowezekana. Naomba Mheshimiwa Waziri akae na Katibu Mkuu wake na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii ili kusudi uwanja ule unufaishe pande zote mbili, kwenye upande wa michezo na kwa upande wa utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije upande wa timu zetu hasa hizi timu kubwa za Simba na Yanga lakini kuna mtu mmoja amechangia hapa anauliza kuhusu waamuzi. Mimi nishauri, tuwe wanasiasa au tuwe watu gani, tukitaka mpira wetu uendelee kwa timu zetu hizi Simba, Yanga na timu zingine sisi wanasiasa hebu tukae pembeni kidogo. Kwa sababu kama sisi wanasiasa tutaingia ndani tukajifanya sisi ndiyo waamuzi namba 12 au 13 kinachofuata ni kuharibu ile test ya mpira wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tunavurunda humu ndani kwa kutumia urafiki na wanasiasa tukienda huko nje hatufanikiwi. Watani zangu Yanga ndani humu wanacheza vizuri sana, lakini wakienda huko nje na bendera yetu ya Taifa wanarudi na rundo la magoli. (Makofi)

Sasa tujiulize hivi kwa nini humu wanaweza na kwa nini nje hawawezi? Ni kwa sababu ya mambo yetu ya siasa. Tukiacha siasa tukafanya mpira uwe mpira, wakacheza mpira bila kupendelewa na watu fulani fulani whether ni viongozi wa kisiasa au linesman, nina uhakika hata huku nje watashinda kwa sababu kule nje hamna kubebwa, mbeleko kule nje hakuna, ziko hapa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Baraza la Michezo tukiendelea kwa utaratibu huu wa kuzibeba timu zetu, tukienda nje ni aibu, tutaendelea kuwa wasindikizaji. Nirudie Baraza la Michezo hebu fanyeni kazi yenu. Hivi sisi kweli maandalizi yote hayo kwa timu zetu, tuna wachezaji wazuri lakini tukitoka hapa tukienda nje tunafungwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata timu yetu hii ya vijana nina uhakika kama haitaingiliwa na wanasiasa kwenda kuwa-lobby wale wachezaji wazuri waliomo mle ndani, maana yake tutaanza wewe ni wa kwangu, wewe ni kwangu tutawapa vichwa watashindwa kufanya kazi yao ya kuchezea mpira uwanjani. Tuwaache wao na makocha wao na wataalam wao ili kusudi wacheze mpira, watuletee sifa Tanzania, kwamba Tanzania sasa sio Tanzania kama ile ya zamani. Tukianza sasa sisi wanasiasa kuingia ndani nina uhakika timu ile itarudia njiani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, wewe najua ni mpenzi mzuri wa mpira hasa wa miguu na ni kiongozi na humu tuko wapenzi wengi wa mpira wa miguu na michezo mingine, niwashauri sana Wabunge wenzangu pamoja na ushabiki wetu, pamoja na Mzee Mkuchika pale na Yanga yake tuache ushabiki usiokuwa na utaratibu kwa manufaa ya timu zetu. Nina uhakika hata timu ya sasa inayokuja kwenye ligi kuu ya Singida United mtakuja kuniambia na kukumbuka maneno yangu kwa sababu wanasiasa wanaingia kutafuta umaarufu, pesa zikishawaishia wanakaa pembeni ile timu inabaki peke yake. (Makofi)

Wameshaanza kuingia wanasiasa kujipendekeza. Muda utakapofika wakikaa pembeni ile timu itabaki peke yake. Naomba Singida United ibaki kama ilivyoanzishwa kwa mapenzi yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na nawatakia Mawaziri kila kheri katika kusimamia sera, sheria na kanuni za sekta hii muhimu ya elimu. Nina mambo muhimu katika maeneo matano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, uboreshwaji wa miundombinu katika Shule ya Wasichana ya Sekondari ya Sumve. Shule hii Serikali imeisahau kama vile ni private secondary school. Shule hii inachukua wanafunzi toka maeneo mbalimbali ya nchi yetu wa kidato cha tano, lakini haina walimu wa kutosha, vitanda, magodoro hayafanani na jina la shule na mengine mengi. Naomba shule hii Wizara iithamini kama ilivyokuwa zamani hasa ikizingatiwa kuwa ni shule ya wasichana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Wilaya ya Kwimba leo ni zaidi ya miaka kumi tumetenga eneo la kujenga Chuo cha VETA lakini Wizara imekuwa ikiahidi kila mwaka kuwa kitajengwa lakini imekuwa ni hadithi isiyoisha. Naomba katika bajeti hii nipate ufumbuzi wa ahadi ya siku nyingi ya Wizara ya ujenzi wa VETA Kwimba au niambiwe nitumie mbinu gani ili ujenzi huo uanze. Chuo hicho kinahitajika sana, mimi kama Mbunge kwa zaidi ya miaka 20 nimekuwa nikiomba ujenzi wa Chuo cha VETA Kwimba, nimekuwa nikitumia lugha ya kiungwana, naomba na Wizara nao wawe waungwana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, FDC Malya. Tunacho Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Malya ambacho ni kama Wizara imekitelekeza, kinaendeshwa isivyo au kama siyo cha Serikali. Chuo hiki nilipendekeza kama Serikali inaona imeshindwa kukihudumia kupitia Wizara ikifanye kiwe Chuo cha VETA kwani shughuli inazozifanya zinafanana na za Chuo cha VETA. Huo ni ushauri wangu endapo Wizara haijajipanga kujenga chuo, miundombinu iliyopo Malya inajitosheleza, inachotakiwa ni uboreshaji, lipo eneo kubwa la kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, hayo niliyoyaomba ya shule ya wasichana ya Sumve, VETA na FDC Malya yatazamwe kwa jicho la huruma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, katika jimbo langu tunayo shule ya sekondari ya wasichana ya waliokosa fursa baada ya kupata mimba, kuishia kidato cha kwanza au cha pili inayojulikana kama Arch Bishop Mayala iliyosajiliwa. Mwaka jana Makamu wa Rais alipata nafasi ya kuitembelea ambapo alivutiwa sana na uamuzi huo wa kuanzisha shule hiyo. Nimuombe Mheshimiwa Waziri katika ratiba zake Mkoani Mwanza aitembelee shule hiyo ili ajionee mwenyewe na kutoa ushauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, suala la ugawaji wa vitabu katika shule zetu za sekondari ni vizuri ukafuata uwiano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na naomba kuongeza michango yangu baada ya kuchangia kwa kuongea.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo linalosumbua katika miradi ya maji inayoendelea kwani imeshindwa kukamilika, miradi ya maji inayoendelea katika Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba ni minne, hali ya ujenzi hadi sasa ni kama ifuatavyo:-

(i) Isunga hadi Kadashi asilimia 50, kazi kubwa iliyobaki ni ulazaji wa bomba ambapo bomba linalohitajika ni kilometa 22.

(ii) Igunguya hadi Nyanhiga mpaka Igunguya asilimia 95, mradi upo katika majaribio na Nyanhiga amebakiza kulaza bomba kilometa 11.

(iii) Igumangobo asilimia asilimia 75, amebakiza kulaza bomba mita 150 na kukamilisha ujenzi wa tenki.

(iv) Mhande hadi Shirima mpaka Izizimba ‘A’ asilimia 45 kazi kubwa iliyobaki kutandaza bomba kuu kilometa 40 na mtandao wa bomba vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu kubwa ni kuwa wakandarasi kutoiamini Serikali kuhusiana na malipo yao kutokana na ucheleweshaji uliojitokeza huko nyuma. Serikali inasema nini katika kujenga imani kwa Wakandarasi ili waweze kufanya kazi kwa haraka na wakandarasi kushindwa kujituma au kuwa wazalendo kwa kufanya kazi kwa kasi na kwa ubora tarajiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba visima vingapi ni vibovu na viko maeneo gani na sababu ya ubovu, tuna visima 188 vibovu na sababu ya ubovu kunaibiwa kwa pampu, kuharibika kutokana na umri mkubwa na kuishiwa maji kutokana na mabadiliko ya tabianchi kutokana na Sera ya Maji ya mwaka 2002, uendeshaji na matengenezo kwa maji vijijini asilimia 100 ni wananchi kupitia Jumuiya za Watumiaji Maji (COWSO) wakati kwa Mamlaka za Maji za Wilaya na Mikoa Serikali inasaidia kutoa ruzuku.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali haioni imefika wakati Kamati za Maji au Jumuiya za Maji Vijijini kusaidiwa hasa kwa kukarabati visima vilivyopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, visima hivi vibovu viko katika maeneo yafuatayo; Bungulwa (5), Bupamwa (3), Fukalo (4), Hungumalwa (4), Malya (12), Mantare (8), Bungando (2),
Igongwa (4), Ilula (4), Iseni (1), Kikubiji (5), Maligisu (3), Malya
(13), Mhande (5), Mwabomba (9), Mwagi (7), Mwakilyambiti(
7), Ng’hundi (6), Ngudu (6), Nkalalo (2), Nyambiti (11), Sumve
(17) na Walla (18).

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kata ambazo hazina kabisa huduma ya maji safi na salama ni kata ya Shilembo ambapo kuna kisima kimoja tu vijiji vyote, vijiji ambavyo havina kabisa huduma ya maji ni Mantare (Mwampuru) na Ngulla (Nyambuyi).

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami niungane na wachangiaji waliopita kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri, nipongeze pia timu yake kwa pamoja kwa kazi nzuri ambayo wameifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wakati anaomba kura alizungumzia sana hasa katika suala zima la kuondoa tozo katika mazao mbalimbali na hili ameshaanza nalo, Mheshimiwa mchangiaji aliyepita anasema tozo, jamani ni hatua kwa hatua. Ameanza na tozo sasa baadaye itakwenda kwenye kutafuta masoko, ni hatua kwa hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo sitasema sana kuhusu pamba kwa sababu wewe Mtemi ni shahidi, tumezungumzia sana kuhusu zao la pamba, bei na mambo mengine. Najua Serikali ya Chama cha Mapinduzi ni sikivu, sasa yale ambayo tutakuwa tunayasema humu ni vizuri Serikali ikayachukua na kuyafanyia kazi. Si jambo jema sana Waheshimiwa Wabunge wanasema jambo hilo hilo lakini tukumbuke zao la pamba kwa Kanda ya Ziwa ndiyo baba na ndiyo mama, ndiyo kila kitu. Uchumi wa Kanda ya Ziwa unategemea zao la pamba, bila pamba kwa kweli katika Kanda ya Ziwa sijui kama wengine tungekuwemo humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kwa sababu hata tukiulizana humu ndani ikifika pahali tunabeza pamba, sijaona humu Mbunge aliyevaa nguo ya ngozi ya ng’ombe au ya punda; wote tumevaa nguo zinazotokana na zao la pamba. Sasa kama mahitaji ya pamba ni makubwa, leo hatutaki kuzingatia na kuona kwamba zao hili ni zao la biashara na linasaidia nchi hii, kwa kweli tutakuwa hatujitendei haki. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali ilione hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kuangalia kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri kuhusu kilimo cha kutumia matrekta. Mwaka jana kama unakumbuka wakati Waziri anawasilisha taarifa yake hapa alisema kwamba kuanzia sasa na kuendelea tunataka tuanze kununua matrekta ya kutosha ili kusudi jembe la mkono tukutane nalo makumbusho au sehemu nyingine. Sasa nimejaribu kuangalia kupitia Mfuko wa Pembejeo, wali-project kununua matrekta 79 lakini yaliyonunuliwa ni matrekta 43, matrekta ya mikono power tiller 10, hakuna hata moja lililonunuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka huu wa fedha wamekisia kununua matrekta mapya 71. Sasa sioni kwamba hivi kweli nia ni kununua matrekta nchi hii ipate matrekta ya kutosha. Hata hivyo, tukitaka kulima kisasa, kilimo kipana, mashamba makubwa ni lazima tutumie matrekta; hatuwezi tukaendelea kutumia jembe la mkono halafu ukawa na kilimo kikubwa. Lazima matrekta yatumike, kama hukumwezesha yule mtu mdogo kule chini kumkopesha kupitia huu Mfuko wa Pembejeo matrekta yatakuwa labda ni ya mjini tu lakini wakulima wakubwa wapo vijijini na bila kuwakopesha wakulima kule vijijini hawawezi kulima kwa kujitosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Mheshimiwa Tizeba yeye ni mtoto wa mkulima pamoja na kwamba ametoka kwenye wafugaji, yeye ni mtoto wa mkulima anaifahamu Mwanza, hebu atusaidie hasa upande wa matrekta ili kusudi matrekta yaende yakafanye kazi yake kule yalime kwa kilimo siyo cha kujikimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kwenye mazao kujitosheleza hasa kwa chakula. Inashangaza kuona kwamba eti nchi hii, nitoe tu mfano Mkoa wa Morogoro tulikubaliana hapo mwanzo kwamba kuwe na ghala la chakula la Taifa, lakini sioni jitihada zozote zile kuonesha kwamba ni kweli pale ni ghala la chakula. Tulisafiri juzi kwenda Mlimba, mito tuliyokutana nayo, nikauliza hivi Mkoa wa Morogoro una jumla ya mito mingapi? Nikaambiwa Mkoa wa Morogoro una jumla ya mito zaidi ya 1000 na inafaa kwa umwagiliaji. Sasa unajiuliza hivi tatizo letu ni akili zetu au kutokutekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mkoa huu una mito zaidi ya 1000 na inatiririsha maji mwaka mzima, hivi kilimo cha kumwagilia kinatushinda nini? Una mito zaidi ya 1000 huwezi kumwagilia, maji unayaacha tu yanatiririka yanakwenda baharini; kwa nini maji yale tusiyatumie kwa ajili ya umwagiliaji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, hivi inawezekana kweli Tanzania tukawa tuna njaa? Hivi mwanzo wakati wa Baba wa Taifa, kuna mikoa minne ilichaguliwa, the big four ikawa inazalisha chakula cha kutosha kwa makusudi. Tukawa na siasa ni kilimo, kilimo cha kufa na kupona lakini hiki kilimo cha kufa na kupona sasa hivi sijui kimefia wapi, siasa ni kilimo nayo imefariki dunia, hakuna. Sasa hii mikoa mitano au minne, leo tukisema kwamba hebu tuiwezeshe hii mikoa iliyokuwa inazalisha kwa wingi chakula, chakula hicho kiweze kusaidia maeneo mengine yenye ukame lakini mikoa hiyo na yenyewe tumeiacha, hatupeleki mbolea na tukipeleka mbolea ni ya shida.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali kwa hii mikoa mitano au minne hebu turudi nyuma tuagalie ni wapi tumekosea na wapi sasa tufanye nini. Nashauri, siyo jambo jema sana kukaa tunalia hapa kwamba chakula hakuna, lakini lazima tulie kwa sababu inawezekana wenzetu wataalam mnataka kutusaidia lakini hamtaki kutusaidia. Ukitazama ile timu ya Mheshimiwa Waziri ina Maprofesa na Madaktari waliosomea mambo ya umwagiliaji lakini umwagiliaji sasa unaonekana na wenyewe hauna tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye suala la pembejeo kwa mfano upande wa zao la pamba inasikitisha tu, imesemwa jana hapa. Pembejeo zinaenda kwa wakati ambao haufanani na majira yanafahamika kwamba majira ya kulima pamba ni mwezi fulani, kupeleka dawa ya kupulizia wadudu ni mwezi fulani na kupeleka mbegu ni mwezi fulani lakini inapelekwa tofauti. Kwa utaratibu huu mazao yetu yanakwenda kufa. Tulikuwa tunaongoza kwa mazao mengi tu si katani, pamba, korosho wala kahawa lakini leo mazao yote haya yameshuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji ukitazama kwenye majedwali huku unashuka, mfano zao la pamba mwaka jana ilikuwa tani 122; mmekisia tani laki moja na nusu, hamuwezi kufika pamba haipo msijidanganye. Hii tani laki moja na nusu hamuwezi kupata hata siku moja, mmetoka kwenye tani 122 mnataka kwenye 150 mtaipata wapi? Pia hawa wakulima wa pamba mnawasaidia nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri na kumwomba sana Mheshimiwa Tizeba najua changamoto ziko nyingi kwenye Wizara yake, lakini hebu wakae na wataalam hasa kwenye suala la chakula kwa sababu hata Mheshimiwa Rais amesema jamani tunalia njaa, tunasema hatuna chakula, Masanja yeye analima anavuna, Athumani kwa sababu ni mvivu halimi, anakaa anasema kwamba tunaomba chakula cha njaa, lakini kama tuki…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nami niungane na wachangiaji wenzangu waliopita kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake kwa kazi nzuri sana wanayofanya katika Wizara hii ya Ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Lukuvi ni Waziri wa mfano na hili wala halina kificho, kwa hiyo nimwombe tu Waziri Mheshimiwa Lukuvi pamoja na timu yake basi ile speed ambayo wanayo ikiwezekana waongeze kwa sababu ardhi ndiyo kila kitu, maeneo mengi inatakiwa watu wapimiwe ili wakae kwenye makazi salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba uniruhusu nimshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais. Kitendo alichokifanya jana cha kuwaonesha Watanzania na dunia kwa ujumla katika sakata kubwa la usafirishaji wa mchanga. Kazi ile imefanywa kitaalam na niwaombe Waheshimiwa Wabunge wote, wa vyama vyote, hata mdogo wangu pale Mheshimiwa Ester Bulaya, kwa sababu bahati nzuri wenzetu upande wa kule mlikuwa kila siku mkisema kwamba tunaibiwa sasa ule ni mwarobaini, sasa tumuunge mkono Mheshimiwa Rais kwa hatua hii ambayo ameichukua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nimpongeze pia Mheshimiwa Rais kuhusu kuivunja CDA. Mheshimiwa Lukuvi mimi ni mmoja wa wahanga niliyedhulumiwa kiwanja changu na bahati nzuri Mheshimiwa Naibu Waziri anafahamu, nafikiri kwa hali ya sasa tutakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara mwaka huu imepanga kukusanya maduhuli, tozo shilingi bilioni 112, nilikuwa najaribu kuangalia ile trend, mwaka 2015/2016 Mheshimiwa Waziri alipanga kukusanya bilioni 70, akakusanya bilioni 74, mwaka uliopita 2016/2017 alipanga kukusanya milioni 111.7 mpaka Mei ana bilioni 80.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri kwa sababu najua yeye pamoja na timu yake ni wachapakazi wazuri na mimi kama Mjumbe wa Kamati hiyo tungependa zaidi ile bajeti ambayo wameipanga wakaitekeleze, kwa sababu ili apate fedha za kuweza kufanyia kazi kwenye maeneo ambayo ameyapanga lazima makusanyo, ikiwemo na tozo ziweze kupatikana. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake speed iongezeke, lakini pia kuzuia mianya ya pesa zinazotumika vibaya kwa sababu bila kuzuia mianya hawezi akakusanya vizuri. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri aliangalie hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nimwombe, Halmashauri zetu huko tuliko bila kuficha Mheshimiwa Waziri hatuna uwezo wa pesa wa kupima kila kitu, tunayo Miji, lakini nianzie upande wa taasisi za Serikali, shule za msingi, shule za sekondari, zahanati, vituo vya afya, tukiacha kwa jinsi ilivyo sasa taasisi za Serikali zinavamiwa, inawezekana hata kwa Mheshimiwa Waziri zipo shule za msingi na shule za sekondari zinavamiwa na watu, wanajenga karibu na shule. Unakwenda kujenga karibu na shule ya sekondari pale kuna wasichana, kuna vijana, kuna nyumba ya makazi pale, kwa hiyo mtajikuta kwamba hakuna kitakachokuwa kinaendelea kwa sababu mji na shule ni vitu viwili tofauti. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri hili alitazame vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, nimejaribu kuangalia kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri mipaka ya Kimataifa na anasema kwa mwaka 2017/2018 Wizara itaendelea na uimarishaji wa mpaka wa Tanzania na Kenya ikiwa ni pamoja na utengenezaji wa ramani za msingi pamoja na kupima kipande cha mpaka kuanzia Ziwa Victoria hadi ziwa Natron. Akaendelea, Majadiliano kati ya Tanzania na Zambia, Tanzania na Uganda kwa ajili ya uimarishaji wa mipaka yanaendelea.

Mheshimiwa Waziri, Watanzania tunaweza sisi tukawa watulivu lakini huwezi ukajua nchi zingine kwenye mipaka yetu hiyo, nakumbuka vizuri kwenye mpaka wetu wa Zambia lakini bado tuna tatizo na Kenya na Uganda. Nashauri kwamba, najua kuna kazi nzuri inafanywa tusiishie tu kwenye maneno, twende kwenye vitendo zaidi, ni vizuri tukaainisha mipaka yetu inaishia hapa. Tukiacha wenzetu wanaweza kwa sababu huwezi kujua anaweza akaja Rais mwenye mfano huo unaofanana na wengine huko, akasema hili ni eneo la kwangu akalazimisha, kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri hili alitazame vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni huduma za upangaji Miji. Tuna utaratibu wa kujisahau tunaacha miji inajengwa, inakua bila kupimwa na baadaye ndiyo tunakwenda kupima, kinachofanyika ni kwenda kuweka “X” kwenye nyumba za wananchi, kitendo hiki sio kizuri sana. Kwa nini sasa kusiwe na uratibu mzuri wa kupima na kuweka mipango miji ikakaa vizuri iliyopimwa ili kusudi watu waweze kukaa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Malya, Sumve, Kabila, Nyambiti, Nhungumalwa, Mvomero, maeneo haya Mheshimiwa Waziri ni maeneo yanayokua. Mheshimiwa Naibu Waziri wewe anafahamu pale Sumve ni Mji unaokua, sasa tusipoupima leo na tukisema tutegemee Halmashauri, Halmashauri hazina kitu, nafikiri zote ukiachia labda zile za mjini, lakini ukisema Magu iende ikapime yenyewe, Kwimba, Mvomero hatuwezi kutimiza yale ambayo Mheshimiwa Waziri ameandika humu. Kwa hiyo, nimwombe sana kwenye maeneo mengine kule kama Halmashauri zenye uwezo zikafanye lakini Halmashauri ambazo hazina uwezo kwa kweli nimwombe sana Mheshimiwa Waziri ziweze kusaidiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nipongeze utendaji kazi mzuri wa Shirika letu la Nyumba National Housing, niwaombe sana kwa sababu wanafanya kazi nzuri na mimi kama Mjumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili kwa kweli kazi yao ni nzuri sana, tuwatie moyo, kazi wanayofanya ni nzuri sana, bahati nzuri na mimi niliishawahi kuwa Mjumbe wa Bodi wa Shirika la Nyumba kazi tuliyoiacha sisi ndiyo wanayoiendeleza, naomba moto tuliouacha basi mwendeleze lakini niwatakie kila la kheri katika shughuli zenu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri upande wa mipaka ya Tanzania nimelisema hili nalirudia tena, tunaweza tukaliona kama ni jambo dogo, lakini mbele ya safari lina athari kubwa tukiliacha. Nasema tena tukiacha tukasema kwamba kwa sababu majirani zetu ni wazuri mno wanaweza wakafika mahali wakatugeuka. Nimshauri sana Mheshimiwa Waziri hili kwa sababu ameshalianza, naomba waendelee nalo, nawatakia kila la kheri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa nafasi hii. Nianze kwa kuiunga mkono bajeti ya Serikali, lakini pia niunge mkono taarifa ya Kamati ya Bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikiliza sana mwasilishaji wa upande wa pili, anasema bajeti ni mbaya sana haijawahi kutokea, lakini humu mimi ni wa muda mrefu kidogo bajeti hii ni bajeti ya karne haijawahi kutokea, bajeti ni nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashauri tu wenzangu, tunaweza tukawa wavivu wa kusoma, ni vizuri twende tusome ukurasa kwa ukurasa mtari kwa mstari kwa mstari. Tusirukie kusema kwamba bajeti hii ni mbaya, siyo mbaya hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna msemo wa kiswahili unasema ukiwaona adui zako wanachukia jambo lako endelea nalo, lakini ukimwona analifurahia liache haraka iwezekanavyo. Kwa hiyo, hii ni jambo jema sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na timu yako. Bajeti hii haijawahi kutokea, ni bajeti nzuri nzuri nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini waswahili wanasema kama una shughuli mahali, kuna harusi au kuna jambo fulani unaalika akina mama kwenda kuchambua mchele. Katika kuchambua mchele unaondoa zile chuya na michanga midogo midogo unabakiza mchele. Sasa wenzangu wanachagua mpaka na mchele badala ya kuchagua mchanga na chuya. Ni vizuri tukajitahidi kwenye bajeti hii tukachagua yale mabaya ambayo ndiyo yanatakiwa yaboreshwe lakini ninyi mnachukua yote kwa pamoja. Tujifunze hii ni bajeti ya Serikali yetu na ninyi mmekuja na mbadala yetu lakini hizo figure mlizotaja hazina uhalisia hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri nikuombe labda safari nyingine vitabu hivi tuwe tunavipata mapema kidogo kwa sasa hatuwezi kulinganisha kwa sababu imesomwa pale lakini hatuwezi kuona popote pale. Kwa hiyo, niombe sana bajeti hii Waziri wa Mipango sisi kama CCM ni bajeti yetu, lazima tuiunge mkono kwa sababu ina mambo mengi sana kuhusu wananchi wetu na hata wananchi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanakimbilia kusema unajua hii tozo ya shilingi 40 kwenye magari, nilikuwa naongea na Mheshimiwa Shabiby hapa kuna mama mmoja ametoka kumtaja Mheshimiwa Shabiby, anasema katika ongezeko hili la shilingi 40 kwa lita moja, yeye ndiyo mwenye mabasi, hakuna hata senti tano itakayoongezeka. Sasa wewe humiliki hata bajaj au baiskeli unasema itaongezeka, itaongezeka wapi? Mwenye mabasi yake anasema hakuna senti tano itakayoongezeka. Kwa utaratibu wa Chama cha Mapinduzi, bajeti iliyopikwa vizuri ongezeko la shilingi 40 kwa lita moja ingekuwa ni vizuri zaidi tungeshauri badala ya kulalamika kama ambavyo sasa mimi nashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu liko suala la kuwatua ndoo akina mama kuhusu suala la maji, nishauri na nikuombe kwenye tozo tuna shilingi 50 tuchukue hii shilingi 40 tuiongeze kwenye shilingi 50 ili tupate shilingi 90 ziende zikahudumie maji vijijini. Hii shilingi 50 tayari ipo na sababu kuna ongezeko hili la Sh.40 kwa lita moja, shilingi 50 na shilingi 40 unapata shilingi 90, tuziweke pamoja hizi ziende zikahudumie maji vijijini na hiyo ndiyo itakuwa suluhisho la kuwatua ndoo akina mama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye maeneo mengi, nakumbuka asubuhi katika swali namba 368, 369, 370, haya maswali yalikuwa yanahusu maji, kila Mbunge alisimama mpaka ukawa unatuhesabu lakini ukashindwa kutuchukua wote kwa sababu wengi tulikuwa tunataka kuuliza kuhusu swali la maji. Kwa hiyo, niombe sana Waziri wa Fedha, Waziri wa Maji, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti mtakapokwenda kule kwenye Finance Bill tafadhalini sana sana muangalie suala hili kwa sababu bila maji tutakuwa hatujawasaidia akina mama. Nikushauri sana sana na naomba nirudie hii, kwetu sisi kama wana CCM na hili nalisema wazi kwa sababu maji vijijini kwa akina mama ndiyo kete yetu ya CCM lazima tuibebe. Hamsini, arobaini, tisini naomba tuziunganishe tuzipeleke kwenye maji ili kusudi tupate maji kwa ajili vijiji vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyo vijiji vingi kule kwangu vinahitaji maji na suluhisho kubwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha haipendezi sana tunalo Ziwa Tanganyika, Nyasa, Victoria lakini ukienda Kigoma na wilaya zake zingine hazina maji lakini maji yako Ziwa Tanganyika, ni wakati sasa tuamue. Vivyo hivyo kwa Ziwa Nyasa, Victoria lazima tuweke nguvu. Vilevile tunayo mito mingi imetuzunguka, naomba tuamue sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini Serikali ya Chama cha Mapunduzi chini ya Jemedari Mkuu, John Pombe Magufuli ambaye leo amewaonesha Watanzania, wapo watu walikuwa wanadhani kwamba anatania, sasa leo wamesikia na wameona kwa macho yao kwamba watalishughulikia suala hili. Sisi kama Watanzania, Waheshimiwa Wabunge hapa nafikiri kitu ambacho tungefanya ni kuomba Serikali kama navyoiomba sasa kama kuna mikataba ambayo haitunufaishi sisi tuilete hapa haraka iwezekanavyo ili tuirekebishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kwa mapato yale kwa kiasi kile kilichotajwa na kama sikosei Waziri wa Fedha sijui ndiyo yule pale Dkt. Mpango nafikiri ulikuwepo umesikia wale wataalam wanasheria wamesema kwamba hapa tunapunjwa badala ya kumi tunachukua mbili. Kama mikataba hii ina matatizo, mimi nashauri tena Waheshimiwa Wabunge wa itikadi zote na vyama vyote tumuunge mkono Mheshimiwa Rais kwa sababu pesa zile zikipatikana, matrilioni yale yanayotajwa ambayo yanaweza kusaidia bajeti tano mara moja mbali ya hizi, miundombinu ya barabara, maji, reli, vitu vyote nafikiri vitakamilika kwa sababu tunaweza hata kukopesha nje. Niombe sana Waheshimiwa Wabunge…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii. Naomba kuunga mkono taarifa za Kamati zote mbili, iliyosomwa na dada yangu, Mheshimiwa Kemilembe pamoja na mama Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita sana kwenye ile Sehemu ya Tatu yenye maelezo ya ushauri, maoni na mapendekezo. Kabla ya hapo naomba nikuombe wewe kwa niaba ya Mheshimiwa Spika kwa sababu Mwenyekiti wa Kamati anapomaliza kutoa taarifa yake anasema naomba kutoa hoja na sisi hoja hiyo tunaiunga mkono lakini baada ya hapo tunachangia anakwenda anafanya winding up akishamaliza unatuuliza tunasema ndiyo. Kwa hiyo, unasimama unasema kwamba mapendekezo, maoni na ushauri tunaupeleka Serikalini na Serikali iuchukue. Sasa mimi swali langu, inapochukua ushauri, mapendekezo na maoni haya, hivi Bunge lako Tukufu kwa kila Kamati linapata feedback wapi na wakati gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu upo utaratibu baada ya kumaliza kwa mfano Kamati zote hizi kutoa taarifa zake, siku ya Ijumaa Ofisi ya Bunge inachukua mapendekezo, maoni na ushauri wa kila taarifa ya Kamati inatengeneza kitabu, hiyo ni Ofisi ya Spika, anakabidhiwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, Waziri Mkuu anatawanya yale mapendekezo kwa kila Wizara husika ili baadaye waje walete taarifa Bungeni, sasa sikumbuki mara ya mwisho ni lini ilifanyika hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili sisi Wabunge tujitendee haki ni vizuri kwa yale mapendekezo tunayopendekeza ushauri na maoni yetu, tuwe tunapata feedback. Kama utakuwa ni utaratibu huu wa business as usual, tunatoa mapendekezo, ushauri, halafu hatupati mrejesho, hakuna kitu ambacho tutakuwa tunafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe tukianza kwa mfano na Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, kwenye yale maoni na mapendekezo yaliyotolewa na Mwenyekiti wangu wakati anasoma pale ambayo tuliyaridhia, lakini kwa yale maoni na mapendekezo yaliyotolewa na Mheshimiwa Mama Mary Nagu, hebu tujipe kwa mfano mwezi Machi, tuwe tunapewa taarifa na Wizara husika kwa yale ambayo tuliyopendekeza kwamba yametekelezwa kwa asilimia ngapi lakini kwa nini hatukuyatekeleza ili tuone namna nzuri zaidi ya kuishauri tena Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu nakumbuka mwaka 2016 tulifanya hivihivi; mwaka 2017 tulifanya hivihivi; 2018 tunafanya hivihivi. Je, ule ushauri wetu, sisi kama Bunge linalotoa mamlaka na sisi kazi zetu kama sikosei kupitia Ibara ya 65 ya Katiba, kazi yetu ni kuishauri Serikali, sasa tunapoishauri, je, tunapata mrejesho kutoka wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuombe sana uielekeze Serikali huu ushauri wetu ikiwezekana tutakaporudi kwenye Bunge la Machi kama siyo maoni, mapendekezo au ushauri wote angalau tupate ili tuweze kuisadia Serikali zaidi. Huo ndiyo ulikuwa ushauri wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niombe sana Serikali kwa sababu kila taarifa iliyosomwa na Mwenyekiti wa Kamati humu ndani niliisikiliza. Taarifa nyingi au miradi mingi au utekelezaji wa shughuli nyingi umekwama kwa sababu ya upelekwaji au kutokupelekwa kwa pesa kwenye maeneo husika. Nimwombe sana ndugu yangu Waziri wa Fedha kwa sababu tunataka tutekeleze yale ambayo tunataka yatekelezwe lakini mengine yanashindwa kufanyika kwa sababu hakuna pesa, yale maeneo ambayo yanakulenga wewe moja kwa moja kuhusu upelekwaji wa pesa basi pesa hizo zipelekwe ili kusudi zikatekeleze haya maazimio au mapendekezo ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo, kwa sababu mimi ni senior senator si jambo jema kupigiwa kengele ya pili. Nakushukuru lakini kama nilivyoomba tafadhali mapendekezo haya Serikali iwe na utaratibu wa kutupa mrejesho ili tuweze kujua kwamba limetekelezwa kwa kiasi gani. Nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono, nawatakia kila la kheri katika utendaji mzuri uliotukuka. Naomba sana na kwa mara nyingine ulinusuru zao la pamba tumkomboe mkulima wa pamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la pamba linaonekana kama zao lisilokuwa na maana, ili kuwakomboa wakulima wa pamba, naomba Nyambiti Ginnery ifufuliwe ili ianze kazi ya kuchambua pamba kama ilivyokuwa zamani. Tathmini tayari imeshafanyika kupitia mifuko ya kijamii kupitia Ndugu Bandawe (PPF), kinachochelewesha ni uamuzi toka Ofisi ya Waziri Mkuu. Nashauri maamuzi yafanyike ili ginnery hiyo ianze kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili Mheshimiwa Mwijage unalifahamu, naomba uwasiliane na Mheshimiwa Mhagama ili uamuzi utolewe. Uwepo wa kiwanda hicho utachochea upatikanaji wa ajira za kudumu na muda. Ajira kwa akina mama lishe na kadhalika.

Mheshimiwa Mwijage, najua ukiamua suala hili utalimaliza haraka. Nawasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii, lakini naomba uniruhusu nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Profesa Kabudi kwa taarifa yake nzuri sana na mimi nitatoa ushauri, lakini pia nitakuwa na maombi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika watu ambao nawaamini sana ni pamoja na Profesa Kabudi ambaye ni mbobezi wa mambo ya sheria kama ulivyo wewe Mwenyekiti wetu Mtemi Andrew John Chenge na ndiyo maana wamekuweka leo makusudi ili utusaidie baadhi ya mambo fulani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri kwenye maeneo mawili. Ushauri wangu wa kwanza, namwomba sana Mheshimiwa Waziri aongeze pesa kwa ajili ya kugharamia mashahidi ili kusudi mashahidi hawa wanapokwenda kutoa ushahidi wao, waweze kuukamilisha mapema kwa sababu pesa hizi zinapochelewa au zinapokuwa kidogo, mashahidi hawaendi na kesi zinachelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili, naomba sana Ofisi ya Mwanasheria Mkuu (AG) iangalie namna nzuri zaidi ya kuwa na wataalam kwa maana ya makada ambao wataweza kusaidia hasa katika masuala ya kesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, inaweza ikatokea kesi ya mambo ya fedha, lazima kuwe na mtaalam wa mambo ya fedha, lazima kuwe na mtaalam kwa kesi hizi, lazima kuwe na mtaalam wa mambo ya ujenzi, mambo ya benki lakini la lazima kuwa na mtaalamu wa mambo ya IT. Kwa sababu kwa kufanya hivyo, kesi hizi wakati mwingine zinachelewa kwa sababu wataalam kutoka Ofisi ya AG katika fani hizi ni wachache. Huo ndiyo ulikuwa ushauri wangu ili kesi hizi ziweze kwenda haraka daima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, kama nilivyotangulia kusema kwamba namwamini sana Profesa Kabudi, naomba nilete ombi kwako Mheshimiwa Waziri. Wilaya ya Kwimba tunazo Mahakama za Mwanzo kumi. Tunayo Buyogo, Nyambiti, Nyamikoma, Ngula, Bungulwa, Malya, Nyamikoma na Kikubiti. Mahakama hizi hazina Mahakimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mahakama za Mwanzo kumi zilizoko Wilaya ya Kwimba na jiografia ya Kwimba inajulikana, tuna Mahakimu wanne tu wa Mahakama za Mwanzo. Wanne tu kati ya Mahakama kumi. Sasa hili ni tatizo kubwa, kwa kufanya hivyo, hao Mahakimu hao huwa wanazunguka, lakini katika kuzunguka wakati mwingine wanachelewa kwa sababu hawana usafiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali kupitia kwa Mheshimiwa Waziri ninayemwamini na ninazungumza kwa upole kabisa. Kwa sababu suala hili tumekuwa nalo kwa muda mrefu. Nakuomba sana Mheshimiwa Profesa Kabudi, Mahakama kumi hizi bila kuwa na Mahakimu, ni kesi ngapi mnasema kwamba kesi ndani ya muda fulani ziwe zimeshapitiwa na kutolewa maamuzi, lakini Mahakimu wanne kwa Mahakama kumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine namwomba Mheshimiwa Waziri, kulikuwa na ahadi ya muda mrefu sana, tangu enzi za Mheshimiwa Waziri Mwapachu, akaja Mheshimiwa Migiro, akaja Mheshimiwa Nagu, Marehemu Mheshimiwa Kombani, Mheshimiwa Chikawe One na Chikawe Two, leo upo wewe kuhusu ukarabati wa Mahakama za Mwanzo katika Mahakama ya Nyamikoma na Kikubiji. Mahakama hizi ni za siku nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri na tumeshaandika kwa maandishi. Pia Mahakimu hawa, hawana hata karatasi kabisa za kuandikia. Pia pamoja na upungufu wa Mahakimu, makarani hawapo, waliopo ni wahudumu. Sasa angalia, Mahakimu hawapo, makarani hawapo, sasa hebu niambie maana ya kuwa na Mahakama pale ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri kwa unyenyekevu mkubwa, sitaki kusema kwamba Mahakama hizo amezitelekeza kwa sababu siyo tabia yake. Sitaki kusema kwamba Mahakama hizo hazipendi au hazitaki, siyo tabia yake.

Namsihi sana mwana wa Singida, hebu Mahakama hizi sasa ambazo zilipangiwa kukarabatiwa muda mrefu kama ilivyoandikwa kwenye vitabu hivi, Mahakimu basi wapatikane, nyumba na majengo hayo yakarabatiwe na watu walioko kule ambao ni watumishi walioko chini yake, basi vifaa ambavyo wanavihitaji viweze kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mimi nimwombe sana Waziri wa Fedha pamoja na Waziri Mpina waangalie suala la usindikaji wa ngozi.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2016/2017 tulisindika jumla ya ngozi 1,000,215 ambazo ziliipatia Serikali shilingi bilioni 34.7; mwaka 2017/2018 ikashuka ikaenda mpaka vipande 292 iliyozalishia shilingi bilioni 3.2. Kutoka kwenye shilingi bilioni 34 mpaka shilingi bilioni tatu, sasa tatizo ni nini? Hebu Serikali mkae kwa sababu ng’ombe ni haohao, tatizo ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kutoka shilingi bilioni 34 mpaka shilingi bilioni 3 kwa mwaka mmoja na sisi Serikali tunatafuta pesa ili zikafanye kazi nyingine. Niiombe sana Wizara ya Fedha kama liko tatizo la tozo au export levy, hebu mkae na mtazame kwa sababu tunapoteza mapato mengi sana. Inawezekana ngozi hizi badala ya kupitia kwenye utaratibu wetu mzuri zinapitia Kenya na Uganda, hebu litazameni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini la pili, nishauri sana, ukitazama kelele zote hizi zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge wanaosababisha hasa ni wataalam wetu, wanatuangisha mno. Bajeti zote ukisikiliza, kwa sababu wana tabia nzuri sana ya kusema kwamba aah, Mawaziri si wa kupita tu, walishapita wangapi hapa bwana, hawa ni wapitaji tu hawa, kwa hiyo, wanafanya mambo yao. Sasa kwenye haya ndugu zangu naomba tubadilike kwa sababu kelele hizi siyo zetu sisi peke yetu humu, ni mpaka na wapiga kura wetu huko. Kwa hiyo, niombe sana wataalam wetu maana hata ukitazama hiki kitabu, kimesemwa na wenzangu hapa, Mheshimiwa Ulega kakamata lile chuma anachoma ng’ombe ambaye hajawahi kufuga ng’ombe hata mbuzi. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, lakini ukija ukurasa wa mwisho wa kitabu chao, mtaalam ambaye ni daktari wa mifugo, Dkt. Maria na yeye kakamata chuma anambabua huyo ng’ombe. Tunataka kuuza ngozi, sasa mnaharibu ngozi. Kwa nini usitumie utaratibu wa kuchukua tag mkatoboa sikio, ndio utaratibu wa nchi zote duniani, mimi sijaona duniani wanachukua chuma wanamtoboa ng’ombe kwenye mapaja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi niombe sana wataalam wetu mliangalie hili. Mheshimiwa Mpina, tunajua wewe ni mchapa kazi mzuri sana, mdogo wangu, fuata mambo mawili katika maamuzi yako, pamoja na sheria, tumia busara na hekima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili nami nichangie katika hotuba mbili za Mawaziri wawili wa TAMISEMI pamoja na Utawala Bora. Naomba uniruhusu niwashukuru sana Viongozi wangu wakiongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Waziri Mkuu, Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunipa salaam za pole baada ya kupata msiba wa marehemu mama yangu, nawashukuru sana kwa pole hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, niruhusu niwapongeze sana Mawaziri hawa wawili kwa maana ya Mheshimiwa Selemani Jafo pamoja na Mheshimiwa Kapt. Mst. George Mkuchika ni Mawaziri wanaochapa kazi zao vizuri na hotuba zao kwa kweli zinajielekeza wazi. Mchango wangu nitajikita sana katika kushauri na kuomba, lakini namwomba Mwenyezi Mungu anijaalie ili niishauri vizuri Serikali nisiende kwenye mkumbo ule mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa kwanza, nivipongeze sana vyombo vya usalama, vyombo vyetu hivi vinafanya kazi nzuri sana Usalama wa Taifa, pia TAKUKURU wanafanyakazi nzuri sana na niwaombe viongozi wao wakuu tunapoambiwa kwa mfano, makusanyo kuanzia Julai mpaka Machi kupitia TRA tumeweza kukusanya shilingi trilioni 11.78, nina uhakika kwamba TAKUKURU, Usalama wa Taifa wao ni wadau wakubwa sana kwa sababu mianya mingi ambayo imekuwa ikijitokeza wao wamekuwa jicho la kwanza kuiona na kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili twende mbele zaidi, nawaomba sana wenzetu hawa wa Vyombo vya Usalama na TAKUKURU, katika nchi yetu hii ninyi ni watu muhimu kweli hasa kwenye suala zima la uchumi wa nchi yetu na usalama wa nchi yetu. Kwa hiyo, ombi langu kwenu ni kwamba endeleeni kuwa wazalendo kwa nchi hii ili kuweza kuokoa rasilimali za nchi yetu. Mkiwa wazalendo hata haya tunayoyazungumza humu ya mapato, upungufu huu, nafikiri mtatusaidia kabla hatujaenda kwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, narudia tena, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, TIS nawashauri sana kwa sababu ninyi ni watalaam, mnajua mambo mengi, tunaweza tukakusanya pesa nyingi zaidi mkiamua kutusaidia, tunaweza tukazuia mambo mengi mkiweza kutusaidia kwa kutumia vizuri weledi wenu, nafahamu ni watalaam. Hebu ongezeni weledi wenu najua ni wazalendo sana sina shaka na hilo, lakini ongezeni jitihada ili kusudi nchi yetu iweze kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la TARURA. Chombo hiki tumekianzisha juzi ni chombo kizuri sana. Nina ushauri kwamba tulipoanzisha Mfuko wa Barabara tulikubaliana kwamba tuweke asilimia 70 kwa 30 ili asilimia 30 hii iende kwenye barabara za vijijini kwa maana ya Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kwa sababu nia ni njema sana, tunaambiwa kuna kilometa zaidi ya laki moja, kwa pesa hii ya asilimia 30, naona kama vile haitoshi. Naomba kwa sababu tulianzisha Mfuko huu kwa Sheria ya Mfuko wa Barabara, niiombe Serikali ilete amendments ili tujaribu kubadilisha kwa jinsi tutakavyoona inafaa, kwa sababu hatuwezi tu kuamua hapa sasa hivi, ni lazima tulete mabadiliko ya sheria kwa sababu Mfuko huu tulianzisha kwa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo ambayo napendekeza kwa kuanzia na Wabunge tunaweza tukaridhia, tutoke kwenye asilimia 70 twende kwenye asilimia 65, twende taratibu ili tusiathiri upande mwingine, tufanye 35 kwa 65. Nafikiri kwa kufanya hivyo tutakuwa tumesaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI kwa sababu ya pesa hizi kidogo na makusanyo yetu hayajatengemaa vizuri na jambo hili nililisema huko nyuma wakati Waziri wa TAMISEMI akiwa marehemu Kingunge Ngombale Mwiru. Lazima tufike mahali tuzisaidie Halmashauri zetu, kwa sababu ya pesa hizi kidogo tukiamua kama ni mwakani au lini, tukiamua kila Halmashauri ikawa na grader lake kwa ajili ya kutengeneza barabara zinazoharibika, ni uamuzi tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila Halmashauri ikawa na Grader hizi pesa kidogo kidogo hizi tunazokusanya, barabara inapoharibika mara moja mnaweka mafuta, grader inakwenda kutengeneza barabara inapitika asubuhi na mchana lakini inapitika masika na kiangazi ni suala la uamuzi. Kwa zile Halmashauri ambazo zina grader nafikiri barabara zao huwa haziharibiki mara kwa mara. Huo ulikuwa ni ushauri wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye suala la Jimbo. Naomba Mheshimiwa Jafo nilishakwenda kwake, Waziri wa Elimu anisaidie shule zangu mbili za sekondari na huwa napata tabu wanapogawa pesa wanasema shule kongwe, lakini kuna shule moja kongwe, shule ya wasichana, Sumve Girls ya A-Level. Inachukua wasichana kutoka nchi nzima wanachaguliwa wa Lindi wapo, kutoka Mtwara wapo, wanakwenda Sumve kusoma pale, ni shule ya siku nyingi. Shule hiyo amesoma Mama Maria Nyerere.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali mahitaji yao wanayo, upanuzi wao wanahitaji mabweni mawili, madarasa manne, bwalo moja na jengo la utawala moja, kiasi cha shilingi kama zaidi ya milioni 400. Naomba sana Serikali shule hii ya wasichana waiangalie kwa jicho la huruma. (Makofi)

Pia kuna shule ya Taro. Kuna pesa zilitolewa mwanzo milioni 206 cha kushangaza Serikali kwa makusudi ikaja ikazibeba zile pesa zote, baadaye ikarudisha milioni 80. Nakuomba sana Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Jafo, nilishakwenda ofisini tukazungumza na watu wake, nikaenda kwa Mama Ndalichako, Waziri wa Elimu, nikazungumza naye, pesa hizo mpaka leo hazijarudi. Naomba ili tukamilishe mabweni mawili, madarasa manne, maabara mbili, tunahitaji milioni 168 ili kukamilisha kazi iliyobaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kushauri pia hivi sasa kuna ongezeko kubwa la wanafunzi kuanzia ngazi ya chekechea, shule ya msingi mpaka sekondari, sina uhakika tumejiandaa namna gani. Kwa ongezeko hili kufuatana na maelezo ya kitabu chako, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, ni lazima tuangalie sasa miundombinu ya madarasa, vyumba vya Walimu, vyoo pamoja na Walimu...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyotangulia kusema, ni kazi kubwa inayofanywa na Rais wetu ambaye ni mzalendo namba one katika kuvifufua vyombo vyetu vya usafiri kama ndege, meli na ujenzi wa reli (SGR). Niliwahi kusema na kuomba kuhusu TRL mara itakapokamilika naomba treni hiyo katika safari zake isimame katika kituo (station) ya Bukwimba, kwa kuwa jiografia ya Bukwimba ni eneo linalofaa kuwa na bandari kavu. Hii itasaidia kwa station ya Fela na Mwanza South kupumua. Stesheni ya Mwanza pamejaa, ukiweka bandari kavu Bukwimba itasaidia kwa wafanyabiashara wenye mizigo yao kuichukulia Bukwimba badala ya Fela au Malampaka. Miundombinu ya Bukwimba inajitosheleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri naomba nipate majibu hii railway levy ambayo ni tozo ya 1.5% kwa mizigo inayopitia bandarini (magari, container na kadhalika) kutozwa hiyo asilimia, mfuko huu ulianza mwaka 2015/2016 na mara ya mwisho Serikali ililipa shilingi bilioni 38.41 kama advance kwa mkandarasi Dar es Salaam – Morogoro na hizo pesa tulikubaliana ziwe refenced kwa matumizi yaliyokusudiwa. Naomba kujua mambo mawili; je, hadi sasa ni kiasi gani cha pesa kimeshakusanywa kufuatia tozo hiyo? Ni kwa nini kiasi hicho hakipelekwi moja kwa moja kunakokusudiwa kama Bunge lilivyopitisha mwaka 2015/ 2016? Naomba kupata majibu kutoka Serikalini kuhusu mambo hayo mawili na ombi la bandari kavu Bukwimba station.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono na kuwapongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake yote na Wizara yake. Mheshimiwa Waziri naomba kutoa ushauri katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, TCRA ni moja ya taasisi muhimu sana katika uchumi wa nchi yetu. Yapo makampuni ya simu ambayo baada ya agizo la Mheshimiwa Rais alipozindua National Data Center na kuyataka makampuni ya simu kujiunga ili kubaini kama makampuni hayo yanalipa VAT inayotakiwa; lakini hadi leo baadhi yao hayaja-comply. Naomba kujua kwa nini makampuni hayo yameshindwa kutekeleza agizo la Rais wetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara na madaraja; mwaka 2017 Serikali ilitenga zaidi kilometa 200 za kufanya upembuzi yakinifu kwa barabara ya Ilungu(Magu) Bukwimba – Ngudu – hadi Hungumalwa. Katika kitabu chake cha bajeti sijaona popote pesa zilizotengewa kwa ajili ya barabara hiyo. Naomba kujua ni kwa nini barabara hiyo haijatengewa pesa?

Mheshimiwa Naibu Spika, Daraja la Mto Simiyu (barabaraya Magu - Mara); daraja hilo ni muhimu sana. Ikumbukwe kuwa daraja hilo limecheza, hivi sasa kwenye daraja hilo magari hayaruhusiwi kupita nyakati za usiku kutokana na mvua. Lakini ukweli na watalam wako wanajua kuwa daraja hilo limechoka, ipo haja ya daraja hilo kujengewa upya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu TTCL huyu ni mtoto wetu lazima tumbebe kwa mbeleko ya Taifa. TTCL ni Shirika linalotoa huduma, lakini pia kupitia Mkongo wa Taifa tuutegemee kiuchumi na kiusalama, Serikali lazima tulilinde.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu DMI na NIT; vyuoni hivi viwanda vya kuzalisha wataalam wa kwenye maji na barabarani, Serikali iviimarishe vyuo vyetu kwa kuzipa hela za kutosha kutokana na bajeti yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa ATCL, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa upendo mkubwa sana kwa Taifa. Rais Magufuli ni mzalendo number one kwa nchi yake, hasa katika kulifufua shirika. Ushauri wangu kwa Bodi ya Wakurugenzi katika kulisimamia vizuri shirika kwa kushirikiana na uongozi wote wa shirika. Hii ni katika kumuunga mkono Mheshimiwa Rais. Tuachanena wanaobeza jitihada za shirika, tunalitaka shirika letu la ATCL lisiwasikilize wapinga kila kitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. RICHARD M. NDASSA:Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuchika namheshimu na kumwamini sana. Hoja yangu niviporo vya TASAF II, Kata ya Bungulwa kuhusu ujenzi wa barabara ya Bungulwa Nhundya; yapo makalvati zaidi ya 50 kwa zaidi ya miaka 10 lakini hakuna kinachoendelea. Nataka majibu ni nini hatma ya kiporo hicho au ndiyo imeshindikana? Hii si mara ya kwanza kuuliza swali hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba majibu wakati wa kuhitimisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa pongezi kwa kazi nzuri zinazofanywa na Serikali kupitia Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaunga mkono hotuba endapo nitapata jibu sahihi na nitashika shilingi ya mshahara endapo sitapata majibu sahihi ya kujengewa Chuo cha VETA Kwimba ambapo ni ahadi ya Serikali. Waziri na watendaji ni waungwana sana lakini cha kushangaza kwa zaidi ya miaka 15 kumekuwa na ahadi ndani ya Bunge na kwenye vitabu lakini utekelezaji ni zero. Mimi ni Seneta humu Bungeni siyo vizuri sana kukaa naulizia suala hilo hilo kila Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kwimba ilikuwa moja ya wilaya iliyokuwa imepangiwa kujengewa Chuo cha Ufundi miaka 10 iliyopita. Wilaya ya Kwimba kutokana na agizo la Wizara tuliambiwa tutafute eneo ambapo tayari eneo lipo la ekari 60 na lina hati ya umiliki chini ya Halmashauri ya Kwimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua kutoka kwa Mkurugenzi wa VETA, ni nani aliyefuta Wilaya ya Kwimba kwenye orodha ya wilaya zilizopitishwa kujengewa chuo cha VETA? Mkurugenzi wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, naomba kupitia Wizara ya Elimu nipate ahadi, dhamira, kukiri, kutimiza ahadi (commitment) ya kujengewa Chuo cha VETA ambapo ni ahadi ya Serikali kwa zaidi ya miaka 10.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri arejee andiko langu hapo juu kuwa sitaunga mkono na nitashika shilingi endapo sitapata commitment ya Serikali. Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako namheshimu sana, naomba yeye na viongozi wenzake hiki kilio cha VETA kifikie ukingoni.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamba ni siasa lakini pamba ni uchumi. Nitamke wazi kuwa siungi mkono bajeti hii kwa sababu moja kubwa. Mheshimiwa Waziri Mkuu alihamasisha sana Wakuu wa Mikoa, mikoa 10 na wilaya 46 zinazolima pamba, wananchi wakajitokeza kwa wingi wakalima kweli, kitu cha kushangaza ni kwamba matarajio ya wakulima hawa kwa bei ya mwaka jana kwa kilo moja ilikuwa Sh.1,200, lakini bila aibu mkulima huyu amejitolea kweli kweli, bei ya sasa kwa kilo moja ni Sh.1,100. Hivi mkulima huyu tunamsaidia namna gani? Kila mwaka msimu unapoanza, kelele ya bei ni kwa zao la pamba peke yake, hivi tatizo huwa ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kupitia bei ya soko. Bei ya soko ni senti 76, ukikokotoa utakuta thamani ya pamba nyuzi ni Sh.1,357 thamani ya mbegu ni Sh.281, ukijumlisha kwa kilo moja unapata Sh.1,638. Gharama za uendeshaji na uchambuaji kwa yote hayo ni Sh.405, ukitoa kwenye hiyo Sh.1,600 utabaki na Sh.1,233. Ni bora basi huyu mkulima ambaye amehangaika usiku na mchana kulima mngemuachia bei yake iwe kwa kilo Sh.1,200, Sh.100 mnamnyang’anya, kwa nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, eti wanasema hiyo ni kwa sababu mkulima huyu anatakiwa kulipia deni la viuadudu la shilingi bilioni 29, mkulima huyu alipie mabomba ya kupulizia shilingi milioni 525 lakini mkulima huyu alipie deni la mbegu shilingi bilioni 1.2, mkulima huyu alipie deni la shilingi bilioni 27.7, mkulima huyu huyu, lakini alipie na deni la miaka ya nyuma shilingi bilioni 3. Hivi wakati haya madeni mnayatengeneza mkulima huyu alikuwepo? Hakuwepo! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi jinsi mkulima huyu wa pamba anavyoonewa, analazimishwa kukatwa ile Sh.100 ili kusudi alipie mbegu kabla hata ya kulima, akatwe shilingi bilioni 16 lakini anunue chupa milioni tano shilingi bilioni 20, pia alipie mabomba shilingi bilioni 2. Hivi mkulima huyu hata kabla hajalima mnaanza kumkata kwenye hii Sh.100, huyu mkulima amekosea nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri, kwenye kitabu chake ukurasa wa 148, kwenye pamba, unasema kwamba mchango kwa ajili ya maendeleo ya zao la pamba fedha ambazo huwekwa kwenye Mfuko wa Pembejeo wa Zao la Pamba kwa ajili ya kusaidia kutoa mbegu na dawa za pamba, Sh.30 kwa kilo zinaondolewa. Unasema unaondoa Sh.30, unamuongezea Sh.100 utakuwa umepunguza au umeongeza? Kwa sababu huku unasema umeondoa Sh.30 lakini unakwenda unamuongezea Sh.100 huko, utakuwa umepunguza au umeongeza matatizo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mfuko kwa jinsi ulivyo, tunaiomba Serikali ukafanyiwe ukaguzi na CAG kwa sababu hiki ni kichaka cha watu kupata fedha za wakulima. Siku zote mifuko hii imekuwa ikiwanufaisha wao wala siyo wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina ugomvi hata kidogo na Mheshimiwa Waziri Tizeba, hata kidogo, ni mdogo wangu, ugomvi wangu uko kwa wakulima wa bei ya Sh.1,200, hii Sh.100 irudisheni kwa wakulima. Mnataka tutoke tani 122,000 twende kwenye tani 1,000,000 za pamba, mtafikaje huko kama mnawanyima incentive hawa wakulima? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wale wote wanaotoka kwenye mikoa wanayolima pamba, tusiunge mkono mpaka tupate maelezo ya kina kuhusu hii Sh.100. Sisi tunakubali kama ni Sh.1,200 lakini siyo kwa Sh.1,100. Mheshimiwa Tizeba mwakani kuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa, tutawaambia nini wale wananchi? Kama nilivyosema, pamba ni uchumi, pamba ni siasa, lazima tufike mahali tuwasaidie wananchi wetu, wamejitolea mno kulima na Waziri anafahamu jinsi walivyohangaika, kuna wadudu na matatizo mengine yamejitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi na hili naomba Waziri aje alifafanue vizuri zaidi, anasema ushirika kazi yake ni kukusanya, sijui unakusanya kutoka kwa nani? Yaani huyu mkulima achukue pamba yake ampelekee huyu ushirika, ushirika ambao tunaujua sote pamoja na Waziri, hii pamba yangu au yake? Halafu baada ya hapo aje mnunuzi, pamba yangu iende ikakae siku tatu, nimezoea nikuchukua pamba yangu naipeleka sokoni, napima kilo shilingi ngapi, nachukua hela yangu, sasa mkulima huyu aende akakopwe? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo jema kuimarisha ushirika lakini twende basi taratibu. Ukishasema kwamba kazi yao hawa ni kukusanya, je, anakusanya kwa siku ngapi? Kwa siku nne au tano yaani huyu mkulima apeleke pamba yake ikasubirie pale, Mheshimiwa Tizeba mdogo wangu nawe unatoka kwenye pamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siungi mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji mzuri sana na nimtakie mfungo mtukufu wa Ramadhani (Ramadhan Kareem).

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishukuru sana Serikali kwa kutuboreshea Kituo cha Afya cha Malya, kwa niaba ya wananchi wanaozunguka kituo hicho pamoja na wa Jimbo la Maswa, tunaomba kutupatia watalaam hasa daktari, aliyepo ni clinical officer, Wauguzi na wahudumu pamoja na watalaam wa maabara, Wafamasia na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumkumbusha Mheshimiwa Waziri ombi la gari kwa ajili ya hospitali ya Sumve kama barua yetu kwako tuliyowasilisha kutokana na jiografia ya eneo. Gari hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa sana kuokoa maisha ya wazazi na watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitangulize ombi la kukiboresha Kituo cha Afya cha Nyambiti. Nyambiti ni Mji unaokuwa kwa kasi na kwa haraka sana kutokana na kuwa na viwanda viwili vya kuchambua pamba. Kuna kituo cha treni (railway station), sekondari mbili, shule za msingi nne na jamii inayoendelea kukua. Naomba katika mpango wa uboreshaji wa vituo vya afya, Kituo cha Afya cha Nyambiti kiwe kimojawapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimtakie Mheshimiwa Waziri Ummy kila la kheri katika njozi zake na Mungu atamsimamia.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii nami niweze kuchangia mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kusema kwamba naunga mkono mapendekezo haya ya Serikali kwa asilimia mia moja, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na wafanyakazi wake kwa maandalizi mazuri kwa kweli ya hotuba hii. Nina ushauri ambao ningependa kuutoa, lakini kwa sababu tukienda kwa wenzetu hawa wa TRA kwa sababu yote tunayozungumza humu ndani lazima pesa zipatikane, wala siyo vinginevyo, wala sio maneno. Sasa ni namna gani ofisi yako Mheshimiwa Waziri wa Fedha inaweza ikapata hizi shilingi trilioni 18 ambazo tumeipa jukumu la kuzitafuta TRA. Sasa ni lazima kwanza ile mianya ya upotevu lazima tuizibe. Lakini wafanyakazi wenyewe wa TRA ambao wanafanya kazi nzuri sana, sina mashaka na TRA wanafanya kazi nzuri sana na ndiyo maana mapato kila mwaka kila mwezi yanaongezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni wajibu wetu sasa, Mheshimiwa Waziri hakikisha hakuna shilingi hata moja inayolala nje, pesa ya Serikali hata senti moja inayolala nje, hakikisha kwamba kila shilingi inayokusanywa lazima iingie ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukija kwenye nidhamu ya matumizi ya fedha, yapo matumizi mengine kwa kweli hayafanani, hayafai. Ili tuwe na pesa nyingi za kutosha ni lazima tunapozipokea, tunapozikusanya, lazima tuwe na nidhamu ya kuzitunza na kuzitumia. Ipo miradi mikubwa, naomba kwa sababu tunacho Kitengo chetu cha TISS kwenye ile miradi mikubwa ili kwenda kui-verify kama kweli hiyo pesa imetumika kama inavyotakiwa. Nashauri Mheshimiwa Waziri wa Fedha watu hawa kwa sababu wapo na kazi yao ni moja ni kuangalia upande wa pili, je, pesa hii imetumika vizuri?

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha, moja ya eneo ambalo mapato ya Serikali huwezi kuyapima, kuyaona vizuri na eneo hilo kila mwaka tumekuwa tukilalamika na ukiuliza watu wanatupiana mpira ni pale bandarini.

Mheshimiwa Naibu Spika, floor meter watakwambia imepona, lakini ukienda kwenye uhalisia Mheshimiwa Waziri wa Fedha eneo lile ni eneo muhimu kweli kweli kama litasimamiwa, kwa sababu mimi nia yangu ni kupata mapato mengi siyo vinginevyo, tupate mapato mengi ili kusudi pesa hizo ziweze kwenda kusaidia mambo mengine huko.

Sasa pale kwenye floor meter Mheshimiwa Waziri wa Fedha hebu pelekeni timu pale, TISS waingilie kati liko tatizo. Watakwambia wamechelewesha kushusha sijui, kuna linkage sijui, kuna temperature sijui, maneno matupu yale, liko tatizo kubwa sana pesa nyingi zinapotea pale. Ni lazima tufanye utaratibu Mheshimiwa Waziri wa Fedha, pesa hizi ziweze kukusanywa kama inavyotakiwa. Lakini ili tukusanye kama inavyotakiwa lazima pale watu wa TISS waende wakaangalie upya.

Mheshimiwa Naibu Spika, jamb la pili nikushukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, mwaka jana tulileta mapendekezo kwako kuhusu hii michezo ya kubahatisha.

Mwanzo nafikiri hukuwa unanielewa vizuri, kama nilivyosema mimi nia yangu kwa kweli ni kutafuta namna ya kukusaidia wewe kutafuta vyanzo vingine vya mapato. Hata ukipata shilingi mbili, shilingi tatu, shilingi nne, ukiziongezea kwenye zingine ukakusanya huku na huku chungu chako kitajaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha mwaka jana ulikubali, na nimeambiwa kwamba kutoka kwenye bilioni 27 ambayo zilikuwa zimekadiriwa mpaka juzi hapa mmeweza kupata shilingi bilioni 64. Sasa kama tukisimamia vizuri na yale mapendekezo niliyokuletea kwa nia njema kabisa wala siyo vinginevyo, nia ni kukusanya lile eneo likisimamiwa vizuri eneo lile utatoka kwenye shilingi bilioni 64, shilingi bilioni 70 utakwenda mpaka kwenye shilingi bilioni 100 au zaidi. Lakini ni lazima hayo mapendekezo uyapitie vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili ni technical kidogo na mtu anaweza akafikiri kwamba hivi hii Gaming Board ni nini, hivi nayo ina hela? Lakini ukienda Marekani, Las Vegas pale wanaishi lile Jimbo ni kwa sababu ya casino tu. Kwa hiyo, eneo hili Mheshimiwa Waziri wa Fedha nikuombe sana yale mapendekezo ambayo tumekuletea, uyaainishe vizuri ili yaje kwenye Finance Bill. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe tena hapo, michezo hii ili wote tupate kwa maana ya mchezaji, Serikali na Mwekezaji lazima zile asilimia uziweke vizuri. Kwa sababu utakuta kwa mfano, BIKO, TatuMzuka na mwingine Bet hawako kwenye Gross Gaming kwenye GGR, sasa kwa nini unawatenganisha wakati wao wote wanafanya mchezo mmoja. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri ili tupate pesa nyingi za kutosha na ziende zikafanye kazi kwenye maeneo yetu hili eneo nalo nafikiri ungelitazama vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye suala la mwisho kabla kengele haijalia. Naunga mkono mapendekezo ya Kamati ya Bajeti, lakini mimi hasa kwenye hii skipper hii siyo mbaya sana kwa sababu itatupeleka kuzuri. Lakini liko tatizo hebu litazameni vizuri tusije tukafika pahala Mheshimiwa Waziri wa Fedha tukaanza kuulizana maswali kwa sababu tender yake ilitangazwa mwaka 2016, ikagota pahali ikapelekwa kwa AG ndiyo sasa imekuja tena sina tatizo nao, lakini kwa nini ilipelekwa kwa AG, AG alishauri nini lakini uwekezaji wao nani anaujua kweli kama ni shilingi bilioni 44 nani anaujua. Maana yake mtu anaweza akasema mimi niwekeza shilingi bilioni 44 na hapa nikikaa nitakusanya 66 nani anajua kwamba ni kweli uwekezaji wake ni shilingi bilioni 44. Ni jambo jema lakini ni vizuri Mheshimiwa Waziri wa Fedha ukajiridhisha zaidi ili kusudi yasije yakajitokeza kama yale ya EFDs.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, naunga mkono. Huo ndiyo ulikuwa ushauri wangu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Niunge mkono hotuba zote mbili kwa maana ya hotuba ya Waziri pamoja na hotuba ya Kamati ya Madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita sana katika kushauri na moja litakuwa ni ombi na baadaye Mheshimiwa Waziri atakaposimama kesho basi anisaidie kupata majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa jana kuizinduzia rasmi Tume ya Madini chini ya Prof. Kikula pamoja na wenzake akiwepo pia Prof. Mruma. Sina wasiwasi na watendaji hawa kwa sababu nawafahamu ni wazuri. Mheshimiwa Rais amewaamini na kwa sababu ni watu wenye weledi mkubwa Tume hii ya Madini sasa wataibadilisha italeta taswira ambayo itaakisi matokeo mazuri kwa rasilimali zetu ambazo Mungu Mwenyezi ametujalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine niishauri Serikali, nimejaribu kupitia kitabu naangalia zile takwimu, madini yanayosafirishwa nje au yale yanayouzwa ndani ukiangalia rasilimali zote tulizonazo, takwimu hizi kama vile zimepikwa, lakini hata kama zimetengenezwa kwa uhakika zitakuwa ni za uwongo kwa sababu madini tuliyonayo na takwimu tulizoonyeshwa hapa hazifanani hata kidogo. Mimi naomba sana Tume hii nategemea mwakani utakapokuja Mheshimiwa Waziri atatuletea takwimu za madini yote, siyo almasi peke yake, dhahabu peke yake, atuletee takwimu za madini yote kokote yanakochimbwa. Kwa mfano, hapa ametulea takwimu za madini yanayouzwa ndani, yanayouzwa nje, ametaja Chunya na Mwanza peke yake, sasa nikawa najiuliza hivi madini yako Chunya na Mwanza peke yake, kwa maana ya Kanda, hizo Kanda zingine kwa nini hawakuonesha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa sababu ofisi hii ni mpya kwa maana ya Wizara iwe inatupa taarifa kamili za kila Kanda ni kiasi gani imekusanya na hili liwe jukumu lao. Nimwombe Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati, najua atatoa taarifa yake Machi mwakani, napenda tupate taarifa kamili kwa kila Kanda imefanya nini na imekusanya nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba Tume hii iongeze ukusanyaji wa maduhuli. Kwa sasa wanasema mpaka Machi wamekusanya shilingi bilioni 310 ni ongezeko la asilimia 59 lakini inawezekana walikisia makisio ya chini, haiwezekani mka-surpass kwa asilimia 59 hata kidogo. Tunaomba makisio yafanane na hali halisi ya kile ambacho kinavunwa, makisio hayo ni madogo mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Tume hii wasiwe na urasimu wa kutoa leseni. Nimwombe Mheshimiwa Waziri anisaidie, kuna machimbo ya dhahabu ya kule Muheza, machimbo yapo sehemu moja inaitwa Magambazi kupitia kampuni ya CANACO, Mheshimiwa Doto mdogo wangu alienda pale akapaona, akazungumza na Mkuu wa Mkoa, mwekezaji yule amewekeza pesa zake nyingi, hebu lisuluhisheni hili ili huyu mwekezaji aweze kufanya kazi zake lakini pia Serikali kupita machimbo yale tuweze kupata mrabaha wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tuna GST, najua Profesa Mruma alikuwa kiongozi pale, anajua matatizo ya GST, kazi zao zinajulikana lakini huyu mtoto GST hatumtendei haki kwa sababu hatumpi pesa za kutosha za kwenda kufanya utafiti wa maeneo ambayo kuna madini. Tunampa pesa kidogo lakini tunamwambia akafanye utafiti, hawezi kwenda kufanya utafiti kwa sababu hana pesa za kutosha. Kwa hiyo, niombe sana ili GST ifanye utafiti na moyo wa kujitolea ni lazima watu hawa wapewe pesa za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwa hayo makampuni ya wawekezaji wanapokuja nishauri sana Mheshimiwa Waziri ushirikishwaji wa wananchi kule kunakochimbwa madini ni wa muhimu. Ni lazima kuwe na sheria inayomtaka mwananchi kushiriki, kwamba wewe mwekezaji wetu, tunashukuru umekuja lakini ni lazima kuwe na clause inayosema ni lazima uchangie au ufanye moja, mbili, tatu. Ukimwachia huyu mwekezaji peke yake aamue yeye kwa jinsi anavyotaka na ataamua, anaweza akatoa au asitoe, lakini kama kutakuwa na clause inayosema kwamba lazima utatoa hiki na hiki na hiki hii itasaidia, huo ndiyo utakuwa ushirikishwaji mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri anazungumzia mambo ya sera na sheria. Wizara imetengeneza Kanuni saba za Madini ambazo sitaki nizitaje kwa sababu ya muda, siyo vibaya kwa sababu hizi Kanuni nafikiri Waheshimiwa Wabunge, najua kwenye mfuko mmetupa zile sheria, tunamwomba sasa Mheshimiwa Waziri hizo Kanuni saba hizo, siyo vibaya akazileta Bungeni hapa na siyo tu kwetu hapa ni vizuri akazishusha mpaka chini kwa DC na RC kule ambako madini yanachimbwa ili kusudi wajue hizo kanuni zinasemaje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu Mthamini wa Madini hasa Almasi yupo mmoja tu kama siyo wawili. Sasa Mthamini wa Madini ya Almasi akiwa mmoja au wawili unategemea nini? Anaweza akashirikiana na wale watu wa upande mwingine kuidanganya Serikali. Tuwe na
utaratibu mzuri wa kuwasomesha na siyo madini ya almasi peke yake nafikiri na madini mengine, tuwe na utaratibu wa kuwasomesha hawa wataalam wetu waje wafanye kazi ambayo tunaitaka ili mapato ya Serikali yaongezeke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni kuhusu utoaji wa leseni kwenye maeneo mbalimbali yale ambayo hayaendelezwi. Ndugu yangu amesema hapa Mheshimiwa Mwenyekiti wa Wazazi Mstaafu, yale maeneo ambayo yamechukuliwa na watu ambao hawayaendelezi, zaidi ya miaka 10, 20, 30, hivi tunasubiri nini kuwanyang’anya? Nashauri kwenye zile leseni muangalie namna nzuri zaidi, mbali ya kuandika jina na anuani muweke na picha ya huyo mwekezaji tuione, hii itasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tena kwamba naunga mkono shughuli za Serikali lakini niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu na taasisi zote zilizo chini ya Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii niunge mkono Mapendekezo ya Mpango wa mwaka 2019/2020 pia naunga mkono mapendekezo na maoni ya Kamati ya Bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, binadamu na wanyama kimahitaji tunafanana ila tofauti binadamu anaufahamu na kujitambua; mnyama ajitambui lakini binadamu anaufahamu wa kujitambua, inapotokea binadamu akajitoa ufahamu wa kujitambua huo ni uvivu wa kufikiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inapotokea Mheshimiwa Mbunge aliyekaa miaka mitatu ndani ya Bunge aliyekaa miaka mitano ya nyuma ndani ya Bunge asitambue yote yanayofanyika huo ni uvivu wa kufikiri kutokuona yote hayo hata huu mpanga bahati nzuri Mheshimiwa Mpango umetuambia vizuri sana jamani eeee naomba tujikite kwenye mpango ili kusudi maoni, ushauri na mapendekezo yenu baadaye sasa iwe mpango sasa wa maendeleo uwigizwe kwenye Mpango wa Maendeleo wa 2019/2020 ulitushauri hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa inasikitisha badala ya kuzungumzia mpango wenyewe kwa mfano mimi nitashauri tukiachana na haya mengine Mheshimiwa Mpango nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wa kuthubutu wala kutokuogopa mtu wala nchi yoyote ile kuhusu mradi wa Stiegler’s Gorge na hili Mheshimiwa Mpango, Waziri wa Mipango sisi hapa kama mradi huu ukikamilika tutapata megawatts 2,100 ni tija kwa Taifa hawa wanaosema eti watu wa nje wakichukia, sisi tulikuwa tunaitaji kilometa za mraba 100 wala siyo zaidi ya hapo kilometa 50 urefu na kilometa mbili upana ili tupate megawatts 2,100 hivi kweli hii ni rasilimali ya Taifa rasilimali ya nchi hii tumepewa na Mungu hivi unapoogopa kutumia cha kwako utumie cha nani? Eti kwa sababu watu wa nje watanuna wache wanune hili ni Taifa huru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Mpango katika mpango wako kuna mradi wa makaa ya mawe Mchuchuma ili nafikiri tangu ukiwa Katibu wa Mipango limekuwepo, tumelisema, tumelisema sasa tuondoe kwenye story sasa tuweke kwenye uhalisia ebu tufike mahala sasa tuamue kwamba je? Huu mradi wa makaa ya mawe Liganga na Mchuchuma bahati nzuri mmewakabidhi NDC hebu sasa tufikie pahala tumalize hili suala baada ya kukaa kila mwaka inakuja, lakini ili tuendane na sekta ya viwanda ni lazima Mheshimiwa Mpango kuna maeneo mawili/kuna viwanda viwili; Kilimanjaro Tools na Mang’ula Tools hizi kama zitaimarishwa zitaenda kulisha mitambo ya viwanda vyetu, naomba hili tusilionee aibu lazima tulitekeleze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ushauri katika kuboresha shirika letu la ndege la Air Tanzania tunategemea ikifika Oktoba 2019 tutakuwa na ndege nane, lakini tatizo kubwa ambalo lipo ni upungufu wa marubani. Marubani waliopo leo ni 33, marubani 16 wameenda mafunzoni na ndege hizi nane zinahitaji jumla ya marubani 70; marubani hao 70 ni lazima wawe wazalendo. Na wewe kwenye kitabu Mheshimiwa Dkt. Mpango umeandika kwamba kusomesha kwa wingi katika fani na ujuzi adimu na maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii fani ya urubani ni fani maalum na adimu na lazima tupate marubani wetu wazalendo ili waje waendeshe ndege zetu hizi ili kupunguza gharama. Tukitegemea marubani wa nje gharama itakuwa kubwa zaidi.

Nimuombe sana Mheshimiwa Dkt. Mpango, hili la marubani nafikiri ni jambo jema tukapata marubani wetu wakaenda wakafanya mafunzo kwa sasa kabla ndege zingine hazijaja hizi maana zingine zikafika mwezi wa kumi na moja nyingine mwakani. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri wa Mpango, ndege hizi zitahitaji marubani wazalendo wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine Mheshimiwa Dkt. Mpango, Kanda ya Ziwa tunalima sana pamba, lakini bahati mbaya hatuna viwanda vya nguo sasa mazao yanayotokana na pamba hivi tunafurahia sisi kusafirisha marobota kutoka Sumve kuyapeleka Dar es Salaam.

Kwa hiyo nikuombe sana Mheshimiwa Dkt. Mpango katika mpango wako kwa sababu hii ni Serikali ya viwanda na mazao yale yapo sasa kama pamba hebu tuwe na utaratibu agalau wa kusimamia Wizara ya Viwanda na Uwekezaji hebu Bwana Mwijage aje na mpango maalum na kamati yake kuhusu mazao ya biashara pamba, korosho, kahawa ili mazao hayo ikiwezekana yawe yanabanguliwa humu ndani na kufanya packing humu ndani ili baadae tuuze sasa badala ya kuuza raw material tuuze bidhaa ambayo imechambuliwa tayari na kwenda nchinje kwa ajili ya kuongeza thamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni kuombe sana suala la Mkoa Mwanza, Simiyu, Mara lazima tuwe na kiwanda kinchotengeza nguo na inawezekana basi angalau kimoja tu Mheshimiwa Mpango kimoja tu kanda ya ziwa angau kwa kuanzia ili zao lile la pamba liweze kutumika badala ya kusafirisha marobota, tupate kiwanda kimoja cha kutengeneza nguo na mahitaji ni makubwa sana ya nguo za aina mbalimbali huo ndio ulikuwa ushauri wangu Mheshimiwa Mpango na nikushukuru sana na nikuombe usiogope hizi kelele za huyo, huyo, huyo, wewe songa mbele tu watu wapige kelele lakini si tunajua tutafika wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa nafasi hii. Kwanza niishukuru sana Serikali, Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake na Katibu Mkuu. Profesa Mbarawa nakuamini sana na nakuheshimu sana. Katibu Mkuu wa Wizara hii namheshimu sana na namwamini sana kwa sababu ya utendaji kazi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitazungumzia Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria peke yake. Tarehe 5 Februari, 2016, niliuliza swali, lilikuwa linasema hivi: “Je, ni lini mradi wa ujenzi wa bomba la maji ya Ziwa Victoria kutoka Magu, Sumve, Malya utaanza?” Tarehe 5 hiyo, Serikali ikasema: “Kazi ya upimaji pamoja na usanifu itakamilika Aprili, 2016 na ujenzi wa mradi unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2016/2017 baada ya usanifu kukamilika”. Kwa maana hiyo, usanifu umeshakamilika, mradi huu ulitakiwa uanze mwaka wa fedha 2016/2017. Cha kushangaza, kama nilivyosema, Profesa Mbarawa nakuheshimu sana, Katibu Mkuu, nakuheshimu sana na hasa tunaposimama sisi Wabunge wakongwe humu ndani na huwa hatupendi kusimama na kuanza kulaumu lakini hii inasikitisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kusikitisha zaidi, kwenye kitabu chako hiki, ukurasa wa 155, umetenga shilingi milioni 200. Unasema, shilingi milioni 200 kwa ajili ya kujenga mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria hadi Mji wa Malampaka, Sumve na Malya. Najiuliza, kwa mtu mwenye akili yake timamu kabisa, maji unayatoa Ziwa Victoria mpaka Malampaka kwa shilingi milioni 200? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi fedha huwezi ukasema ni za usanifu ni za ujenzi. Sasa shilingi milioni 200 unajenga choo au unajenga mtandao wa mabomba kutoka Mwanza, Ihelele, Magu, Sumve, Malya, Malampaka kwa shilingi milioni 200? Mheshimiwa Waziri, with due respect, hebu tuangalie sasa mambo haya mengine jamani haya, hivi hawa wataalam wetu hawa wanatusaidia au hawatusaidii? Unatenga shilingi milioni 200, usanifu umeshakamilika, no doubts, sasa hizi shilingi milioni 200 Mheshimiwa Waziri, Profesa Mbarawa, Katibu Mkuu, Dkt. Mkumbo ni za nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani, niombe sana kwa kweli mliangalie suala hili. Hata kama ungekuwa ni wewe leo, Waziri na Waziri mwingine tu, kwa hali kama hii, hivi unaweza ukasimama ukasema naunga mkono hoja, naunga mkono bajeti, kwa milioni 200 zinakwenda kufanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na wataalamu wako mradi huu ni wa siku nyingi muuangalie. Ukitazama miradi mingine iliyoanza na imekamilika, huu ukaachwa, Maswa, Itilima, Bariadi, Busega imeshakamilika na Magu uko njiani kwenda kukamilika. Huu sasa mmeweka kama kisiwa, Jimbo la Sumve na Malampaka, tumewakosea nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ahadi hii siyo ya leo. Alikuja Rais wa Awamu ya Nne, pale Ngudu, Waziri Mheshimiwa Maghembe alikuwepo na akaambiwa kwamba mradi huu tunataka ukamilike mwaka 2015 lakini haukukamilika. Akaja Waziri Mheshimiwa Lwenge, mradi haukukamilika, akaja Mheshimiwa Kamwelwe na nimekaa naye na nimekwenda mpaka ofisini kwake anasema mradi huu utaanzia Fela - Sumve – Malya - Malampaka, kwenye kitabu hiki mnakuja kutenga shilingi milioni 200!

Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani, hivi mnataka Mbunge kama mimi mzoefu humu ndani nisimame na kupiga kelele kila siku humu ndani? Hata ile heshima tu, Mheshimiwa Mbarawa nakuheshimu sana lakini tutazame basi suala hili. Ni bora kabisa msingetenga hata senti tano, ndiyo maana nauliza hizi shilingi milioni 200 mmezitenga ni kwa ajili ya nini? Kwa sababu siyo za usanifu maana ulishakamilika siku nyingi na maeneo ya kuweka matenki yameshaainishwa, wataalamu wenu wamekwenda kule wakasema tenki litakaa hapa na mtiririko utakuwa hivi, mradi huu utapitiwa na vijiji zaidi ya 40 mpaka Malampaka, kazi imeshafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja yake aje na majibu ya mradi huu. Kwa sababu majibu haya ambayo anasema kazi ya upimaji tayari, ujenzi wa mradi utatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2016/2017, haya ni majibu ya Serikali, lingekuwa ni swali la nyongeza ingekuwa suala lingine. Swali la nyongeza unaweza ukalibabaisha lakini jibu hili ninyi wenyewe mmeandika kwa maana ya kwamba utafiti mmeshafanya na majibu ya wataalam mmeshaletewa na ndiyo maana mkasema mradi huu kwa mwaka wa fedha 2016/2017 utaanza kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo siyo majibu yangu, ni majibu ya Serikali. Majibu haya pia yalitolewa humu Bungeni. Wananchi wote wa Jimbo la Sumve, Wilaya ya Kwimba na Malampaka walisikia majibu haya ya Serikali na wakashangilia, leo ni miaka minne mradi hata kuanza bado leo tunakuja kutenga shilingi milioni 200! Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, tafadhali sana, wataalamu tafadhalini sana, mradi huu ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano lakini na ahadi ya Mawaziri humu Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana, utakapokuja kusimama kuhitimisha Mheshimiwa Waziri, uniambie mradi huu utakamilika lini. Pamoja na kazi nzuri sana unayofanya, basi mradi huu nao uingizwe kwa mwaka huu. Donyoadonyoa kila sehemu mnakoweza ili upate angalau shilingi bilioni 2 au 2.5 ili mradi huu uanze kwa mwaka huu wa fedha. Kwa sababu haiwezekani nitakapotoka hapa nakwenda kule jimboni, tumeshawaambia siku nyingi mradi huu unaanza, nikienda kule nawaambia nini hawa wananchi wa Jimbo la Sumve? Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Profesa Mbarawa nawaambia nini kwamba huu mradi ni kiini macho, mbona hautekelezwi, leo tunatenga shilingi milioni 200?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningekuwa upande mwingine huko labda ningesema lakini niiombe sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Serikali yangu sikivu, kama nilivyosema kwamba nawaheshimu sana Mawaziri na wataalamu, mradi huu naomba upangiwe utaratibu wa kuanza kwenye mwaka huu wa fedha 2019/2020. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, lakini niseme kwa sababu nawaamini, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa nafasi hii lakini niseme tu kwamba naunga mkono bajeti ya Wizara hii nyeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu. Nimpongeze sana Engineer Mfugale kwa kazi nzuri sana anayoifanya. Tunaweza tukamuita huyu ni gwiji wa barabara na madaraja ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niwapongeze sana ma-Engineer wa mikoa yote nchini kwa sababu tumekuwa tukiona Mheshimiwa Rais akipita huko na huko akifungua barabara au akiweka mawe ya msingi. Bila hawa ma- Engineer nafikiri kazi hii isingekuwa inafanyika vizuri. Kwa hiyo, niwapongeze sana sana Mameneja wa TANROADS wa Mikoa yote Tanzania kwa kazi nzuri mnayofanya chini ya gwiji wa barabara ndugu Engineer Mfugale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Engineer wa Mkoa wangu, Engineer Luviga kwa kazi nzuri sana anayoifanya. Nimpongeze pia Kaimu Engineer wa Mkoa wa Dar es Salaam Julius Ngusa kwa kazi nzuri anazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu la kwanza linahusiana na ATCL. Tumwombe CEO wa ATCL, ikiwezekana, tumeshaleta maombi upande wa kwako, tuwe na ndege ya kutoka Dodoma kwenda Mwanza na Mwanza kuja Dodoma itasaidia sana Wabunge na watu wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 28 Januari, 2016 niliuliza swali humu ndani na likajibiwa na Serikali. Swali langu lilikuwa linasema hivi, je, ni lini barabara ya Magu – Bukwimba – Ngudu – Hungumalwa itajengwa kwa kiwango cha lami? Majibu ya Serikali yanasema: “Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/2015 na 2015/2016, Serikali ilitenga jumla ya Sh.200,000,000 kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara yenye urefu wa kilometa 70 na taratibu za kumtafuta Mhandisi Mshauri zinaendelea. Baada ya kukamilika kwa usanifu na gharama za mradi huu kujulikana, Serikali itatafuta fedha za kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami”. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa 2014/2015, 2015/2016, 2016/2017, 2017/2018, 2018/2019 leo ni 2019/2020. Nataka
nipate majibu ya Serikali, nimeona humu mmetenga Sh.440,000,000 kwa kilometa 10 sijui ni za nini, ni za changarawe au za nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Eng. Mfugale najua kabisa barabara hii unaifahamu vizuri sana umuhimu wake. Ili Mji wa Ngudu ufunguke, barabara hii inakwenda kuunga ile barabara ya lami ya kutokea Musoma, barabara hii ukiifungua inakwenda kuunga kwenye barabara inayotokea Mwanza kwenda Shinyanga. Kwa kufanya hivyo, utakuwa unapunguza msongamano wa mabasi ya kwenda Mwanza, mabasi yanayotoka Dar es Salaam kwenda Musoma badala yake yanapitia Hungumalwa kwenda Mara, ili tupunguze huu msongamano barabara hii ni muhimu. Mji huu wa Ngudu umedumaa kwa sababu hakuna miundombinu ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mheshimiwa Mfugale kwa utendaji wako mzuri mpaka unapewa daraja la flyover (Mfugale flyover) sifa zote hizo, unashindwa kweli ka barabara haka ka kilometa 74, kweli? Bwana Mfugale, bee kamwene bee bwana Mfugale, kilometa 74. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri barabara hii iko kwenye Ilani ya Chama chetu. Barabara hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais alipokuja Ngudu wakati wa kampeni. Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alipokuja Ngudu, nafikiri wewe bwana Mfugali ulikuwepo, kama hukuwepo basi msimamizi wako alikuwepo, Mheshimiwa Rais aliahidi lakini wakati huo Rais wetu wa sasa ndiyo alikuwa Waziri wa Ujenzi. Sasa wazee na mimi mzee humu ndani hata ka heshima kadogo tu bwana Mfugale? Barabara hii ni muhimu sana naomba muishughulikie na kwa kufanya hivyo mtakuwa mmefungua…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ndassa, unatakiwa unitazame mimi sio Mfugale. (Kicheko)

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nimekuona. Ni macho tu na unajua macho yana degree 180. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri Engineer Kamwelwe, nilikuja ofisini kwako na kama unakumbuka ukaniambia niandike barua pale Water Front. Nikaandika barua na nikakuletea ya barabara hiyo, sasa leo rafiki yangu Mheshimiwa Engineer Kamwelwe unaniwekea kilometa 10 za changarawe badala ya lami wakati barabara hii imeshafanyiwa upembuzi wa kina? Nikuombe sana Mheshimiwa Kamwelwe na labda sasa nimuombe Mheshimiwa Rais barabara hii wewe unaifahamu vizuri zaidi…

WABUNGE FULANI: Hayupo humu.

MHE. RICHARD M. NDASSA: Nyamazeni ninyi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Rais, barabara hii ni muhimu sana kwa wananchi wa Wilaya ya Kwimba. Barabara hii ikitengenezwa itafungua milango ya uchumi kwenye Wilaya ya Kwimba hasa Ngudu. Barabara hii ni muhimu sana, nikuombe sana Mheshimiwa Kamwelwe, utakaposimama kuja kihitimisha nipate majibu hasa kwa barabara hii muhimu kwa Wilaya ya Kwimba. Barabara hii iko kwenye Ilani ya Chama chetu cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tuangalie uwezekano, Waheshimiwa wakubwa kabisa wa kujenga barabara ya kutoka Fulo – Mantale – Nyambiti Junction. Barabara hii ni muhimu sana inajumuisha Wabunge watatu kwa maana ya Majimbo matatu. Jimbo la Misungwi, Sumve na Kwimba, barabara hii ni muhimu sana ikitengenezwa kwa kiwango cha lami. Nimeshaleta mapendekezo kwenu muangalie angalau muiingize kwa mwaka ujao wa fedha ili barabara hiyo iweze kujengwa kwa kiwango cha lami kwa sababu inatumia pesa nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, barabara ya kutoka Mwanza kwenda Shinyanga border yenye urefu wa kilometa 102 imekuwa ikitumia pesa nyingi sana za matengenezo ya mara kwa mara. Waziri anafahamu na nafikiri Engineer wa mkoa anafahamu na Engineer wetu anafahamu kwa nini barabara hiyo isifumuliwe angalau hata kilometa 10 za kwanza baadaye kilometa 10…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa nafasi hii kwa kuwa mchangiaji wa kwanza katika hotuba ya Waziri wa Ulinzi. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri pamoja na wataalam wote wa Wizara hii, mimi naomba nikuombe pamoja na wenzetu, lakini kwa Wabunge wote haipendezi hata kidogo kuzungumzia kuhusu posho, maslahi ya wanajeshi wetu humu ndani kwa kufanya hivyo kwa sababu hawa nao ni wafanyakazi pamoja na kazi nzuri wanazofanya lakini bado tuna Jeshi la Polisi, tuna Jeshi la Magereza lakini bado kuna wafanyakazi wengine tunapo- side kwamba eti hawa waongezewe posho ni kuwagombanisha hawa wanajeshi na Serikali yao.

Niwaombe sana ndugu zangu tusijipendekeze kwa kusema humu ndani eti waongezewe posho naomba sana. Jeshi hili lina utaratibu wake kuhusu maslahi, Jeshi hili lina utaratibu wake namna ya upandishwaji vyeo, hawapandishwi hivi hivi, tuwaachie wenyewe wafanye kufuatana na utaratibu wa kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo niseme tu kwamba Mheshimiwa Waziri kwasababu ya kazi nzuri sana inayofanywa na Wizara hii kupitia Jeshi letu, kupitia CDF na JKT wanafanyakazi nzuri sana niwape tu assurance kwamba bajeti hii itapita bila matatizo ili muende mkafanye kazi ya kulinda nchi yetu ndani na nje.

Mimi nina maombi mawili; la kwanza ni ushauri lakini pili ni ombi. Ombi langu la kwanza Mheshimiwa Waziri tulipokuwa pale Mlale nilitoa ombi mbele ya Amiri Jeshi Mkuu, mbele ya CDF, lakini na Mkuu wa JKT, nilisema hivi Kanda ya Ziwa kwa maana ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita, Chato na Singida hakuna Kambi ya JKT na hili ni suala la kisera Mheshimiwa Waziri. Tunaomba sana tunaomba sana Kanda hiyo siyo kwamba imesahaulika hapana, nafikiri ni utaratibu na muda ulikuwa bado haujafika nikuombe sasa Mheshimiwa Waziri kwa Kanda hii ya Ziwa hebu tupate Kambi ya JKT. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kwimba, Tarafa ya Mwamashimba tunalo eneo la ekari 3750 nina uhakika eneo lile kwa sababu halitumiki kwa sasa, halitumiki vizuri eneo lile najua litatosha kwa ajili ya Kambi yetu ya JKT. Vijana hawa watakaokwenda pale mbali na Kambi najua watafanyakazi ya kilimo, ufugaji kwa kufanya hivyo watapata ajira kupitia ufugaji na kilimo. Niombe sana Mheshimiwa Waziri hili ulibebe kwa sababu nililisema siku ile na leo narudia tena kusema mbele ya viongozi wakuu, hebu mlibebe hili kwasababu Kanda yetu ya Ziwa kwa kweli haina Kambi ya JKT na nikuombe Mheshimiwa Waziri kama nilivyoomba pale Kwimba Mwamashimba tunalo eneo la ekari 3750. (Makofi)

La pili hili ni ushauri, vijana waliopitia JKT wanasifa kuu kadhaa ni wakakamavu, ni wachapakazi, ni wazalendo, ni watu wanaojituma, ni watu wenye nidhamu na wavumilivu sasa vijana hawa Mheshimiwa Waziri, kwa mwaka 2001 tuliporudisha JKT mpaka 2014 vijana walioenda JKT walikuwa 104,594. Walipomaliza walioajiriwa/waliopata ajira ni asilimia 24 tu kati ya vijana 104,594. Sasa nikuombe Mheshimiwa Waziri hawa vijana hawa wanafundishwa namna ya kutumia silaha za moto kundi kubwa hili la watu/la vijana karibu 76,000 linaenda vijijini, wakija wale ndugu zetu wa nchi zinazotuzunguka wakawashawishi kwa sababu hawana kazi, lakini wamejifunza namna ya kutumia silaha kwa njia moja, sitaki ..., wanaweza kushawishika, lakini nikuombe Mheshimiwa Waziri wanaweza wakashawishika kwenda kujiunga na makundi mengine yaliyoko nje.

Sasa ombi langu tunayo maeneo mazuri ya kilimo, madini, uvuvi, mifugo hebu hawa vijana hawa kwa sababu ni wataalam hebu tuwachukue tuwapeleke kwenye maeneo ya kilimo, mifugo na uvuvi. Kwa mfano ukichukua vijana ukawapeleka Kanda ya Ziwa ile kanda yote ile ni ya uvuvi, ukiwapeleka kule watafanyakazi ya kuvua pamoja na kuchakata samaki. Ukiwapeleka maeneo ya mifugo pale Mpwapwa na maeneo mengine watafanya kazi ya kufuga lakini pamoja na kuchakata mazao ya mifugo, hili ni jambo ambalo kuliko kuwaacha tu hawa vijana hawa ambao ni wengi kila mwaka tunawazalisha, niombe sana Mheshimiwa Waziri vijana hawa wa JKT tunaweza tukawapeleka wakafanyakazi nzuri zaidi kuliko kusubiri ajira, lakini wanaweza wakajiajiri wao wenyewe kutegemea na mafunzo wanayoyapata. Ajira haziwezi kutosha sijui kwenye Mashirika ya Umma wala sio Serikalini, lakini bado wanaweza wakajiajiri kwa kazi ya kulima, kufuga, uvuvi na kwenye madini. Huo ndiyo ulikuwa ushauri wangu.
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa utendaji uliotukuka kwa kipindi cha miaka minne ya Uongozi wake
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Niseme tu kwamba, umetumia Busara sana sana kutujumuisha sisi Wabunge ili tumpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri sana anayofanya. Nimemsikiliza mtoa mada kwa kweli mambo ambayo ameyasema ni mengi sana, sitaki niyarudie, lakini endapo kuna Mtanzania au Mbunge hatayaona haya au hayasikii haya kule porini, kuna mnyama mmoja anaitwa ngiri, ngiri hana kumbukumbu hata kidogo, hata ukimfaa namna gani hana kumbukumbu na ndiyo maaana wawindaji kule porini, anapotoka porini akienda kwenye shamba la mahindi au la mihogo, kuna mwindaji atamkosa kosa risasi lakini speed yake atakayotokanayo hapa ni kama kilomita mia moja kwa saa, atafunga break. Akifungu break atasema hili nilipokoswa koswa ilikuwa jana au juzi. Atasema ilikuwa juzi, anarudi tena kwenye shamba, atakoswakoswa tena atakimbia mbio, atasimama, atasema hii ilikuwa jana au juzi. Ni kwa sababu mnyama huyu ngiri hana kumbukumbu.

Mheshimiwa Spika, haya yote na ndiyo maana Bunge lako Tukufu kwa kazi nzuri sana inayofanywa na Mheshimiwa Rais wetu na kila mtu ana macho na masikio, lakini hata kama hujui kusoma basi hata kuangalia picha inakushinda. Niombe sana Watanzania tumpe moyo Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu, niwaombe watendaji wa Serikali kwamba ni lazima tukimbie na spidi ya Mheshimiwa Rais wetu ili matarajio yake aliyonayo kwa Watanzania yaweze kufikia hapo anapotaka. Haipendezi sana Mheshimiwa Rais mpaka anafikia mahali aseme hivi ninyi haya hamyaoni mpaka mimi niingilie kati? Kwa hiyo, ili tufike huko tunakotaka kwenda, niwaombe sana watendaji, spidi ambayo wewe unayo na Bunge lako, na watendaji wa Serikali nao lazima wafanye hivyo ili tufikie malengo yetu ambayo tunayataka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho; niombe sana wenzangu, Wabunge wa upande wa pili, nchi hii ni yetu sote, na Rais huyu ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hatuna sababu ya kuanza kufika mahali na kuanza labda kumbeza, vinginevyo utakuwa unajibeza wewe mwenyewe uliyeko humu ndani. Lakini wananchi walio wengi wa Tanzania kwa sasa wameshamuelewa Rais wetu kwamba anataka kuwafanya nini, hasa wanyonge wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja azimio hili. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Naungana na walionitangulia kuwapongeza sana Wenyeviti hawa wawili; Mheshimiwa Serukamba pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya UKIMWI. Nimefurahi sana kwa taarifa zao nzuri sana, ushauri wao na maoni yao kuhusu maeneo ambayo wanayasimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze upande wa elimu. Kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Prof. Ndalichako, Waziri wa Elimu kwa kuja Sumve kwenye mahafali. Ujio wake Mheshimiwa Prof. Ndalichako umemuibua kijana mmoja wa kutoka shule zetu za Serikali anayeitwa Mayeka Ndaki aliyepata Division 1.7 shule za Serikali. Ujuo wake Mheshimiwa Waziri kwa kweli tunaufurahia sana; na wameniomba nimletee shukrani hizo ili akipata nafasi siyo vibaya, basi akapita tena kwa sababu aliwatia moyo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Prof. Ndalichako kwa Wilaya yetu ya Kwimba kutupatia Chuo cha VETA. Chuo hicho sasa tayari kimeshaanza kujengwa. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, maana yake siyo Kwimba tu peke yake, ni zaidi ya vyuo karibu 50 vinajengwa nchi nzima kupitia bajeti iliyopita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa huu utaratibu mzuri wa Elimu Bila Malipo kuanzia Chekechea mpaka Kidato cha Nne. Naleta ombi kama Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati itampendeza; kama tumeweza kulipia Chekechea mpaka Kidato cha Nne, wanapofaulu hawa vijana kwenda Kidato cha Tano na Sita, mfuko unaweza ukawa mdogo lakini siku zijazo tunaweza tukawafikiria hawa vijana. Maana yake nao ni Watanzania. Kidato cha Tano na cha Sita, ikiwezekana nao waingie kwenye utaratibu huu wa Elimu Bila Malipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, nakuomba sana, ili tupate wanasayansi wengi na wazuri, tunazo maabara zetu huko kwenye maeneo yetu, tumeanzisha kwa nia nzuri tu. Namshauri Mheshimiwa Mwenyekiti na Waziri wa Elimu, tuone namna nzuri zaidi ya kukamilisha haya maboma ya maabara na kupeleka wataalam pia kwa maana ya Walimu wa Masomo ya Sayansi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri tunatengeneza maabara nzuri, tunapeleka na vifaa labda, lakini Walimu wa Masomo ya Sayansi hawapo, inakuwa ni kazi bure. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati yetu nzuri sana hii ya Maendeleo ya Jamii, angalau alione hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, nafikiri Mheshimiwa Waziri Jafo hayupo, lakini Serikali ipo; Mkoa wa Mwanza wakati wanafanya ukarabati katika ukamilishwaji wa maboma, Wilaya ya Kwimba peke yake ndiyo iliyosahaulika. Sijui ni kwa sababu gani? Hii kila siku nimekuwa nikiisema. Ni Wilaya peke yake iliyosahaulika, wilaya nyingine zote zilipewa fedha hizo kwa ajili ya kukamilisha hayo maboma. Sisi tukaja baadaye tukaomba tupatiwe fedha za maboma 21, lakini mpaka leo, hazijapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije Wizara ya Afya. Nawapongeza wananchi wa Wilaya ya Kwimba na Mkoa wa Mwanza na Watanzania wote kwa ujumla. Wananchi wamejitolea kujenga Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya, cha ajabu ni kwamba hospitali zile ukienda baada ya kufunguliwa utakuta kuna mganga mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tukiziimarisha hizi hospitali zetu kwa maana ya Zahanati, zikaimarika vizuri kukawa na wataalam wa kutosha, tukaviimarisha Vituo vya Afya vikawa na wataalam wa kutosha, madawa, X-Ray, Ultrasound na kadhalika, hutapata wagonjwa wa kwenda kwenye Hospitali ya Wilaya au ya Mkoa, vinginevyo labda mgonjwa awe amezidiwa sana. Tukiwa na Zahanati na Vituo vya Afya vyenye vyombo vya kutibia na waganga wa kutosha, nina uhakika itasaidia sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, inakuwa haina maana, zile nguvu za wananchi tunazipoteza bure. Tumejenga Zahanati, Vituo vya Afya kwa gharama kubwa, ambavyo kwa sasa inakaribia shilingi milioni 900, lakini ukienda unakuta wataalam hawapo. Inakuwa tu kama jitu liko pale, white elephant liko pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, bado wanaweza kutumia utaratibu mzuri ambao naupendekeza kwa upande wa elimu na kwa upande wa afya. Kama hatuna wataalam wa masomo ya sayansi, hatuna waganga wa kutosha, hivi wale wanafunzi wanaomaliza vyuo vikuu katika vyuo vyetu upande wa elimu na afya, wakati tunasubiri ajira, ili kupunguza hii gap iliyopo ya upungufu wa wafanyakazi, ni jambo ambalo linawezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, wale mlioshiriki kwenye Mkutano wa SADC pale Dar es Salaam, Rais wa Afrika Kusini alikuja na familia yake inaitwa YES (Youth Employment Service). Unawachukua hawa vijana waliomaliza vyuo wanakwenda kupata uzoefu kwenye maeneo hao. Wakati huo huo watakuwa wanafundisha au wanatoa huduma kuliko kuwaacha tu, wanapata uzoefu. Namwomba Mheshimiwa Waziri wa Elimu na Waziri wa Afya, hebu tuangalie na hilo nalo mkiona linafaa basi tuweze kufanya hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, nitakuwa simtendei haki Rais wangu kama sitampongeza kwa kazi nzuri sana za kizalendo anazozifanya nchi hii. Nawaomba sana Watanzania wenzangu wote, hata upande wa kule kwa rafiki yangu Mheshimiwa Mbowe, Rais anafanya kazi nzuri sana, nzuri mno na kila mtu anaona. Cha kufanya ni sisi Watanzania tuungane tumwombee ili aendelee na kasi ya kutuletelea maendeleo Watanzania wote. Haya mengine yatafuata baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nami niseme, Mheshimiwa Mbatia alisema maneno mazuri sana jana, nikawa nafikiria, Mwalimu Nyerere alikaribishwa pale New York na Mama Mongella, akamkuta Mganda mmoja, huyo Mganda akamwuliza Mwalimu, Mwalimu siku hizi kwenu sisikii neno ukabila, Mwalimu akamwambia, mama ilikuwa zamani, siyo leo; saa hizi wanasema!

Mheshimiwa Naibu Spika, nami namwambia Mheshimiwa Mbatia, ule utaratibu wa 1995 tulipoingia Bungeni na ustahimilivu wa namna ile na kuitetea Serikali ilikuwa wakati huo baba, siyo leo. Sasa Wabunge wote humu, hasa upande ule kule kuna mhemko! Uchaguzi kesho kutwa, wanafikiria, hivi viti kweli nitavirudia tena mwakani! Hiki ni kionjo tu, itakapofika kwenye Bunge la Bajeti ni mshike mshike! Kwa hiyo, tuvumiliane tu ndugu zangu. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Kufuta Hasara itokanayo na Maduhuli ya Madeni ya Nyuma ya Ada na Leseni za Magari, Riba na Adhabu kwa kipindi kinachoishia tarehe 30 Juni, 2019
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa nafasi hii. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kuleta Azimio hili la kufuta bilioni 398. Hii siyo mara ya kwanza kufuta deni, nimwombe Mheshimiwa Dkt. Mpango aliridhie ombi langu ili kusudi kuondoa haya mawazo ambayo yanawapelekea wenzetu kufikiri kwamba Chama cha Mapinduzi kinategemea hizi pesa ili kusudi kiweze kufanya uchaguzi. Chama cha Mapinduzi kina vyanzo vyake vingine vingi na siyo pesa hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimwombe Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa sababu wenzetu wanafikiri kwamba eti Azimio hili unalolileta la kufuta hizi bilioni eti ni pesa ambazo zitatumika kwenye uchaguzi, la hasha. Sasa nimwombe arudishe nyuma kidogo kwa sababu tumekuwa tukifanya jambo hili ili waone kwamba je, pesa tulizofuta hapo awali zilikuwa za uchaguzi?

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, niwaombe wenzangu wa Chama cha wenzetu kule akina Mheshimiwa Lema na wengine, si vizuri sana kuwa mnasingizia Chama cha Mapinduzi eti pesa hizi wanazichukua kwa ajili ya kazi hii. Tukianza kufanya hivyo hatuwezi kufika mbali, nina uhakika kabisa Ofisi ya Bunge inafanya kazi na Ofisi ya CAG na siku zote PAC na LAAC inafanya kazi na Ofisi ya CAG na siyo mara ya kwanza PAC kupewa taarifa kutoka kwa CAG na siyo mara ya kwanza Kamati ya LAAC kupewa taarifa za baada ya kukagua kwamba pesa hizi zinatakiwa zifanye hivi au kuna upungufu kwenye eneo fulani.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana tuwe na utaratibu wa kuiamini Ofisi ambayo tunafanya nayo kazi kama ilivyo kwa Ofisi ya CAG, LAAC lakini tukianza utaratibu wa kuanza kuhoji chombo ambacho tunafanya nacho kazi nafikiri tutakuwa tunawashusha morari wenzetu wa Ofisi ya CAG.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango nirudie, nimalizie kama atakuwa nafasi yake nzuri tu, hebu alete Maazimio ya nyuma ambayo tumeshawahi kuyafanyia kazi kwa kufuta kiasi cha pesa ambacho siku zote tumekuwa tukifanya hivyo, kwa sababu huu ndiyo utaratibu na tumekuwa tukifanya hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono Azimio lililoletwa na Waziri wa Fedha na nakushukuru sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa nafasi hii, lakini tu niseme kwamba naunga mkono Bajeti Kuu ya Serikali kwa asilimia 100 na nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake yote kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii ni bajeti nzuri sana, na mimi niliyekaa muda mrefu kidogo humu ndani naifananisha bajeti hii na bajeti ya mwaka kama 2005/2006 kama siyo 2004 iliyokuwa chini ya Awamu ya Mzee Mkapa, ilifuta kero zote ambazo zilikuwa zinatatiza kwa nchi yetu na hii imetokea, nikushukuru sana Dkt. Mpango kwa usikivu, nikushukuru sana pamoja na Wataalam wako, naomba tuendelee hivi, kwa sababu kwanza kwa kitendo cha kuondoa hizi ada na tozo 54 ni jambo la kujivunia, ni jambo la kimapinduzi, litainua uchumi na hiyo ni kwa sababu utakuwa umewajali wananchi wa Tanzania, naipongeza sana Serikali na nina ushauri mmoja au miwili katika mapato ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha na wataalam wako hebu tujaribu kuangalia, mimi bado huwa najiuliza kwa nini huu Mpango wa PPP, hatuutumii, una tatizo gani? Hebu tukae tujifikirie mara mbili mbili, tukiutumia na sheria tumeshatunga. Tukiutumia una matatizo gani? Tukae tujipange vizuri, lakini ushauri mwingine, nikushauri Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Serikali inaweza ikaongeza vyanzo vingine kupitia dhamana ya Serikali za Mitaa, municipal bond nafikiri nikisema hivyo unanielewa. Hiyo itasaidia kuongeza vyanzo, mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri sana iliyofanya mimi kama mwananchi, Mbunge wa Jimbo la Sumve, Wilaya ya Kwimba, Mkoa wa Mwanza nikisimama mbele yako Mheshimiwa Waziri wa Fedha Serikali yangu ambayo ninayoiamini sana, naulizwa sawa, mmeondoa tozo na ada 54 mimi mkulima wa zao la pamba nafaidika nini na tozo hiyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi leo wananchi wa Mkoa wa Mwanza, Wilaya ya Kwimba lakini na Wilaya zingine zinazolima zao la pamba, wakulima hawa wanahangaika kama watoto wa bata, zao la pamba sijui lina mkosi gani? Pamba yao wanahangaika hawajui wapi waipeleke, wapi wauze leo msimu wa pamba ulianza tarehe 2 Mei na hili tunalisema, tunalisema, tunalisema. Tarehe 2 Mei mpaka leo hakuna kinachoendelea, zao la pamba hili limekuwa kama vile adhabu kwa mkulima, Mheshimiwa Waziri wa Fedha wewe unajua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mazao haya matano haya, major crops yanakuongezea uchumi kwenye hela za kigeni, lakini wananchi hawa wanajiongezea kipato. Sasa leo mazao haya mojawapo zao la pamba, leo tumelitelekeza wananchi wanahangaika bei leo tena kwa bahati nzuri Waziri wa Kilimo hayupo, lakini wameenda huko wameona hali halisi, leo mimi Mbunge message nilizonazo na simu ninazopigiwa zaidi ya mia moja wanauliza Mheshimiwa Mbunge pamba yetu tutaiuza wapi? Tupeleke wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali naomba hili tuchukue hatua za haraka, kwa sasabu wananchi hawa kama watauza pamba yao, watakwenda dukani watanunua simenti, mabati, mbao na pesa itaingia kwenye circulation, hawa wanaouza vifaa vyao pesa zao watalipa kodi, lakini kama leo pesa zao, pamba yao imekaa nyumbani, imerundikana kwenye maghala, hamna mnunuzi, muathirika namba moja atakuwa ni mkulima, lakini na Serikali itakosa kodi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, halafu mimi niombe sana ikiwezekana Waziri mwenye dhamana ya Kilimo, Waziri mwenye dhamana na Viwanda tuache kufanya siasa kwenye kilimo cha pamba, naona tunafanya siasa, kinachotokea sasa kuna mawakala wako kule ambao wanasema sisi tunazo pesa, tunanunua kwa kilo shilingi 1,200 lakini wanawapa watoe pesa wanakwenda kununua kwa shilingi 500/600/700 lakini huku wanasema tunanunua kwa shilingi 1,200 na hawa ni wafanyabiashara wanunuzi wapo na bahati nzuri Serikali inafahamu tunawachezea wakulima, tunawanyanyasa wakulima wa zao la pamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sana Serikali ya chama changu najua ni sikivu sana kwenye zao la Pamba na imekuwa kila msimu, misimu yote, mara tunapotaka kuanza msimu wa Pamba utasikia mara bei imepanda, mara imeshuka, mara imepanda, mara imeshuka niiombe sana, lakini ukienda kwa umbali zaidi bei ya Pamba unakuta wanauza mpaka shilingi 1,500/ shilingi 1,400 lakini ukija huku, kwa mfano hata leo kama nilivyosema mawakala hawa ambao ndiyo wanunuzi, nafikiri kuna kamgomo baridi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iingilie kati huu mgomo baridi uliopo iutatue, hii siyo bure wanataka wawapandie wakulima wa zao la pamba ili kusudi wawaibie zaidi, kwa kufanya hivyo hata cess ya Halmashauri kwa zile bilioni zako mia saba themanini na ngapi sijui? Huwezi kuzipata kwa sababu sisi Mwanza tunategemea pamba, lakini ili pamba iuzwe na kwa kuona lazima ipitie kwenye Vyama vya Ushirika na kadhalika, sasa kwa kufanya hivyo ile pesa yako Mheshimiwa huwezi kuipata.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, nimeona kwenye Finance Act, nikushukuru sana, safari hii hujagusa suala la gaming board kwa sababu kama ulikuwa unagusa na kuna watu wanapitapita na wameshapita na umeshawasikia wanataka kuondoa ile VAT ya 18% kwenye winning tax.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa tafadhali, tafadhali sana usikubali, kwa sababu pale kuna mapato ya kila mwezi unapata bilioni tatu, shilingi bilioni tatu mara kumi na mbili zaidi ya bilioni thelathini na sita usikubali hata kidogo, fumba macho, nenda hivyo hivyo kama mlivyoanza zamani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, lakini niiombe sana suala la pamba Serikali, Serikali pamba, pamba, pamba burobaa burobaa, pamba naomba sana, sana Serikali iingie kati, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Mimi nitakuwa na masuala mawili. La kwanza ni la Uchaguzi Mkuu.

Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, imetaja kazi nzuri sana alizofanya Mheshimiwa Rais katika nchi yetu na kila mtu anajua kwa sababu kuna uchaguzi, mimi nilikuwa natoa tu mapendekezo; ili kasi hii iendelee, nawaomba Watanzania wote tumpitishe Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli katika uchaguzi ujao ndani ya chama na kwenye Uchaguzi Mkuu ili aweze kugombea peke yake, kwa sababu kazi aliyoifanya ni kubwa, kubwa, kubwa sana na ya kupigiwa mfano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu alikuwa anamsaidia vizuri sana Mheshimiwa Rais, nawaomba wapiga kura wa Jimbo la Ruangwa, pamoja na demokrasia, apite bila kupingwa. Vile vile wa tatu; na hili simung’unyi maneno; katika miaka mitano ndani ya Bunge hili, Mheshimiwa Spika, wetu, Bunge hili umeliongoza vizuri sana, sana, sana na mabadiliko tumeyaona. Nawaomba wapigakura wa Kongwa na wanisikie hao Wagogo watani zangu wakupitishe bila kupingwa ili kusudi kasi hii iliyopo iweze kuendelea. Baada ya huo utangulizi, nilisema nitazungumzia mambo mawili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, wachangiaji wote waliosimama wamezungumzia kuhusu homa kali ya mapafu (Corona Virus); nami nitajikita hapo hapo mwanzo mpaka mwisho, kwa sababu ugonjwa huu unatesa dunia.

Mheshimiwa Spika, naomba tuungane na Mheshimiwa Rais kuliombea Taifa letu ili shetani huyu Corona Virus aweze kuishia huko aliko. Naomba tusilete siasa katika ugonjwa huu. Ugonjwa huu ni mbaya, ni mbaya sana. Kirusi hiki ni tofauti na virusi vingine. Ni kirusi ambacho hakionekani, hakishikiki na wala hakijulikani, kiko kimya, kinaambukizwa kwa mfumo wa hewa. Naomba sana, hili tumwombe Mwenyezi Mungu atusamehe, atuepushe na ugonjwa huu hatari wa Corona Virus.

Mheshimiwa Spika, nimekuwa nikisikiliza mara nyingi katika mitandao na ili tusaidiwe, tuombe wataalamu wetu; najaribu kumtazama hapa Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla ambaye ni mtaalamu wa milipuko, simwoni, wangetusaidia pamoja na Mheshimiwa Dkt. Ndugulile. Tunaambiwa kwamba ugonjwa huu unaambukizwa kwa hewa; mtu anapopiga chafya, anapokohoa. Sasa hizi masks ambazo tunatakiwa tuvae usoni kuziba midomo na pua, lakini hizi masks bei yake ni kubwa sana. Mtanzania wa kawaida wa kule Sumve, Ruangwa na Kongwa hawezi kumudu kuzinunua.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu na ninafikiri unakubalika; nimemsikiliza mtaalamu jana anasema kwamba tunaweza tukatumia vitambaa kama mask. Bahati nzuri kama utaruhusu na kwa sababu shule nyingi zimefungwa sasa na baadaye zitafunguliwa, nina mfano wa mask kwa ajili ya watoto wa shule ambazo ni kitambaa. Bei yake ni chini ya shilingi 500/= kwa mask moja ya kitambaa ambayo inazuia.

Mheshimiwa Spika, pili…

SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Ndassa.

MHE. RICHARD M. NDASSA: Naam.

SPIKA: Eeh, pokea kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa msemaji ambaye anaongea kwa lengo la kumsaidia tu katika mchango wake kwamba kwanza ugonjwa wa COVID 19 hausambazwi kwa njia ya hewa. Ni ugonjwa ambao unasambazwa na kutokana na maji maji ambayo yanatokana na chafya kwenye pua au mdogo wake yanapomfikia mtu mwingine na au akishika maeneo ambayo mtu amepigia chafya au maji maji yale ya kutoka kwenye mdogo yatapokuwa yamedondokea.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika maambukizi haya, yeyote kati yetu akipata maambukizi ni kwamba, moja alikuwa karibu na mtu ambaye alikuwa na ugonjwa huu akampigia chafya au akamkoholea au ameupata kwa kushika sehemu ambazo mtu alipiga chafya au akakohoa naye akashika uso wake, akashika macho, pua au mdomo. Ndiyo maana wakati tunaingia hapa nimewaambia Waheshimiwa Wabunge, ukipata ugonjwa huu, hiyo ni kati ya mikono yako. Usafi wa mikono yako ndiyo inaweza ikakukinga.

Mheshimiwa Spika, la pili ambalo nataka nilitolee ufafanuzi, masks za vitambaa havizuii virusi wala bacteria. Havimkingi mtu kupata virusi vya Corona. Kwa hiyo, tuwe waangalifu sana na aina ya masks tunazozitumia. Kuna masks ambazo ni surgical mask na N95 ambazo zimethibitishwa pasipo shaka kwamba zinaweza zikazuia virusi au kumkinga mtu.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya kwa taarifa hiyo muhimu. Tunakushukuru. Hii taarifa ni kwa wote, wala siyo kwa Mheshimiwa Ndassa peke yake. Mheshimiwa Ndassa endelea.

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Namshukuru Mheshimiwa Dkt. Ndugulile kwa maelezo ya ziada hayo, lakini nilikuwa najaribu tu kuona namna nzuri zaidi ya kuzuia kwa sababu unapozungumzia hizi masks za box, twende kwenye uhalisia, Mheshimiwa Waziri wa Afya na Naibu Waziri wa Afya, kwenye uhalisia hizi masks za box kwanza uwezo wake kwa mujibu wa wataalamu wanasema zinatakiwa zivaliwe ndani ya masaa manne. Zaidi ya hapo, yenyewe inabeba ule uchafu tena na hiyo mask ya box huwezi kuifua ni lazima uitupe.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa huyu mwananchi wa kawaida, mwananchi wa kawaida uwezo wa kununua mask kila siku ni mdogo, tofauti na hizi mask 95 Mheshimiwa Dkt. Ndungulile anaifahamu, najaribu kuzungumzia uhalisia kwamba ili tuwasaidie wananchi wetu hasa waliopo chini ni lazima tuangalie namna nyingine mbadala na namna nyingine mbadala wenzetu wa Wizara ya Afya mnaweza kutasaidia ili tutafute na namna nzuri zaidi ya kuzuia haya maambukizi ya corona virus.

Mheshimiwa Spika, lingine nishauri tu kama nilivyoshauri mwanzo na mimi kwa sababu Mheshimiwa Dkt. Ndungulile amesema hazizuii. Lakini bado Mheshimiwa Dkt. Ndungulile, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya nitakupa hizi sample uende nazo kwa wataalam wako ili wakadhithibitishe kwa sababu nia hapa ni kuzuia, ni kuzuia huko vijijini maambukizi haya leo tunaona kama ni kitu cha kawaida lakini ugonjwa huu ni hatari sana kwa Taifa letu. Haya mafanikio ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu ameyaeleza ya SGR, Reli ya kati hiyo hatuwezi kuyapata kama Watanzania ni wagonjwa niombe sana, niombe sana lazima Serikali yetu ilitazame kwa makini sana suala hili la ugonjwa wa corona.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja ya Waziri Mkuu.
Sheria ya Fedha ya Mwaka 2019
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nimshukuru sana Waziri kwa uwasilishaji wa hii Sheria ya Fedha, lakini pia niunge mkono mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa na ushauri au maombi hasa kwenye hii taarifa ya Waziri wa Fedha, pale kwenye ukurasa wa (v) inayosema kwamba kuandaa kanuni za kuwawezesha, kuwatambua na kuwatoza ada ya mwaka ya vitambulisho wafanyabiashara hawa wadogowadogo. Naomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, suala hili limekuwa kidogo na matatizo mengi huko vijijini na hata mijini kwa sababu sasa umepewa meno ya kwenda kuandaa kanuni basi iwapendeze kanuni hizo ziandaliwe mapema ili iweze kujulikana kwamba nani hasa muhusika na vitambulisho hivi au nani anastahili kupata vitambulisho hivyo.

La pili, nitaomba tu Mheshimiwa Waziri anisaidie pale ukurasa wa 7(iii) inayozungumzia pesa za miradi ambapo wamempa mamlaka Mlipaji Mkuu wa Serikali kuongeza muda wa matumizi ya fedha ya mwaka wa fedha hususan upande wa miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo tatizo ambalo huwa linatukumba mara kwa mara hasa mwaka wa fedha unapokaribia kwisha. Mfano, mwezi huu ni Juni, lakini pesa zinaweza zikatumwa leo, ikafika Agosti. Sasa tungependa kujua huo muda ambao huyu Mlipaji Mkuu wanasema anapewa muda, muda gani? Wanaweza wakasema ni muda gani ambao anatakiwa apewe, hii angalau itasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe tu ushauri, tumepitisha bajeti yetu jana ya trilioni 33. Nawasihi sana wenzangu sina tatizo kwanza na Sheria ya Fedha sababu imeandaliwa vizuri na wataalam. Niombe kwao, TRA ni kama moyo wa binadamu, moyo wa binadamu usipofanya kazi vizuri, baadhi ya eneo au mwili mzima unaweza uka-paralyze, tunawategemea sana, lakini BOT tunawategemea sana, hatuwezi kupata hizi trilioni 33 endapo wafanyakazi wa TRA siyo wazalendo na siyo waaminifu. Ili tufikie huko kwenye trilioni 33 lazima mioyo yenu iwe ya uzalendo hasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huwa naona wafanyakazi wa BOT wao wanavaa mashati meupe, shati jeupe likiwa na doa hutalivaa tena kwa sababu limeshachafuka. Niwaombe wafanyakazi wa TRA na BOT hasa TRA vaeni mashati meupe wawe wasafi na usafi huo uonekane ndani ya mioyo yao, siyo juu juu tu, usafi uonekane ndani ya mioyo yao. Wanayo dhamana kubwa ndiyo maana nimesema TRA ni kama moyo kwa mwili wa binadamu, damu isiposambaa vizuri, wasipokusanya vizuri pesa, ina maana nchi yetu haya yote tuliyopitisha itakuwa ni kazi bure, nawaomba sana TRA.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe TRA, Mheshimiwa Waziri, pesa nyingi/makusanyo mengi iwe ni wilayani na mikoani pesa nyingi zinapotea kwa sababu ya baadhi ya wafanyakazi wetu wa TRA, siyo wote. Hata kwenye kikao cha wafanyabiashara na Mheshimiwa Rais sote tulisikia na tuliona malalamiko mengi yalikuwa ni TRA. Sasa tukijiuliza kwa nini tunashindwa kufikia malengo, lakini tukijiuliza kwa nini eneo lingine linavuka malengo, lazima tujiulize, lakini inawezekana tatizo ni wafanyakazi wa TRA.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado nasisitiza, bila TRA kusimamia vizuri makusanyo na mapato ya Serikali, hizi shilingi trilioni 33 ambazo tutazifanyia kazi kwenye shughuli za maendeleo, recurrent na OC, bila kuzisimamia vizuri tusishangae tutakapokuja mwakani tukiulizana makusanyo yamefikia asilimia ngapi; 45%, 60%, 70%, lakini nafikiri tunao uwezo, TRA wakiamua vizuri tunaweza tukakusanya zaidi. Kwa hiyo, niwaombe sana watu wa TRA, kuweni wazalendo ili pesa hizi shilingi trilioni 33 zipatikane na nchi yetu iweze kuneemeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii asilimia 100. Nakushukuru sana. (Makofi)