Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Grace Sindato Kiwelu (17 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia Wizara hii muhimu sana katika Taifa letu. Nichukue nafasi hii kuwashukuru walimu wangu wote walionisaidia kufika mahali hapa leo, ninawashukuru sana, lakini niwapongeze walimu wote nchini kwa kazi nzuri wanayoifanya pamoja na mazingira magumu waliyonayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, urithi pekee tunaoweza kuutoa kwa watoto wetu ni elimu, na kwa maana hiyo ni lazima elimu hiyo iwe bora na isiwe bora elimu. Na ili elimu hiyo iwe bora ni lazima tuhakikishe tunatatua matatizo ya walimu, wamesema Waheshimiwa Wabunge hapa, matatizo waliyonayo walimu wetu, liko tatizo la upandishwaji wa madaraja, tatizo hili limekuwa ni tatizo sugu, walimu wetu kila mwaka Wabunge wakija hapa wanalisemea hilo lakini bado tatizo hili linaendelea kuwepo.
Nikuombe dada yangu Mheshimiwa Waziri wa Elimu, ninamba tuangalie walimu hao, lakini wanadai kwamba pamoja na hao wanaobahatika kupandishwa hawaangalii umri wa mtu kuuingia kazini, anaweza akaingia wa mwaka huu akampita daraja aliyefanyakazi zaidi ya miaka kumi, sasa yapo malalamiko hayo ninaomba myatazame.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwingine ni tatizo la ucheleweshwaji wa mishahara. Walimu hawa kwanza nimesema wanakaa kwenye mazingira magumu, mazingira hayo yanawasababishia kushindwa hata kuzihudumia famila zao. Mshahara mnawacheleweshea, walimu wanaokaa mbali na miji wanafunga safari kufuata mishahara, wanatumia muda mirefu kufuatilia mishahara yao na watoto wetu wanakosa vipindi. Nikuombe Mheshimiwa Waziri, akikisheni mishahara ya walimu hawa inafika kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine Mheshimiwa Waziri ni unyanyaswaji wa walimu. Wamesema wenzangu hapa, walimu wanapigwa makofi na Maafisa Elimu, wananyanyasika sana walimu hawa. Lakini lingine wako walimu wanaoonekana kuwa upande wa pili wakionekana na upinzani wanaandikiwa barua za onyo, lakini wale wanokuwa upande wa wapinzani wetu wao wanaonekana wanafanya sahihi. (Makofi)
Ninaomba sana Mheshimiwa Waziri, angalieni masuala haya tusiwagawe watanzania kwa itikadi za kisiasa, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ni suala la nyumba. Suala la nyumba maeneo mengi bado ni tatizo hasa wale wanaokwenda maeneo yenye mazingira magumu amesema mchangiaji aliyemaliza hakuna hata nyumba za kupangisha. Na hili ni tatizo kubwa sana hasa kwa watoto wetu wa kike, unajikuta wanapewa nyumba na Wenyeviti wa Vijiji mwisho wanakuwa wake zao. (Makofi)
Ninaomba sana Mheshimiwa Waziri hakikisheni suala la nyumba kwa walimu wetu mnalifanyia kazi haraka ili waweze kupata hizo nyumba za kuishi na hao wanaokaa mbali tuwape basi transport allowance, wanakaa mbali sana na maeneo ya vituo vyao vya kazi. Lakini na posho ya pango, watumishi wa Wizara nyingine wanapata, kwa nini walimu? Walimu wametufikisha hapa ndugu zangu tuwekeze kwa walimu kama kweli tunataka kuboresha elimu ya Taifa letu. Tutafanya mengine yote lakini tusipowekeza kwa walimu wetu kuhakikisha wanapata maisha mazuri, fedha zao wanapata kwa wakati itakuwa ni kazi bure.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee suala la elimu bure. Waraka Namba 6 ulieleza yake mambo mliyoyaeleza pale, lakini niseme kwa kifupi, wamesema pia wenzangu, wakuu wa shule mnawapa wakati mgumu sana, ile fedha ya OC mnayotuma kwanza ni fedha kidogo, haitoshelezi, leo shule nyingi zina madeni ya umeme, maji, walinzi wanadai, leo tumechongesha madawati tumesaidiwa na TANAPA, tuna vifaa ambavyo vinahitaji vilindwe na walinzi. Leo walinzi hawajalipwa mishahara wanaondoka kwenye mashule yetu, viti vikiibiwa tutakuwa wageni wa nani.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia shule nyinge wamekatiwa maji, Mheshimiwa Waziri wewe ni Mwanamke wamesema Wabunge wenzangu mtoto wa kike bila maji hawezi kusoma. Leo shule zimekatiwa maji, watoto hawa wa kike tunawasaidiaje, watakimbia shule mwisho mnakwenda kuwakamata wazazi wao kuwaweka ndani, lakini Serikali ya Chama cha Mapinduzi mmeshindwa kutimiza wajibu wenu kwenye hizi shule. Hakikisheni mnapeleka fedha za kutosha, leo chakula kipatikane mashuleni hasa yale maeneo yenye mazingira magumu. Watoto hawaendi shule kwa sababu hakuna chakula na hata wanakwenda wanasinzia madarasani, walimu wanashindwa kufundisha kwa sababu watoto wetu wana njaa. Wazazi wameshindwa kuchangia kwa sababu hawana kipato cha kuchangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, wengi walipelekwa shule kwa sababu walijua chakula kinapatikana hasa yale maeneo ya wafugaji, leo chakula hakuna watoto wemeondoka mashuleni, lakini hata wale wanao-supply chakula kwenye mashule yetu hawajalipwa mpaka leo wanadai na wengi wao wamechukua mikopo kwenye mabenki, leo tunataka kuwatafutia vifo watu hawa kwa sababu mabenki yatakwenda kutaifisha mali zao. Niombe sana Mheshimiwa Waziri hakikisheni suala hili mnalifanyia kazi, walipeni wazabuni ili waweze kutimiza wajibu wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nisemehe shule zenye mahitaji maalum. Kwa hapa nimshukuru sana Waziri wa TAMISEMI nililisema hili kwenye Wizara yake na tuliwasiliana, niwaombeni sana shule hizi zina mahitaji mengi muhimu. Tunawahitaji watoto wetu hawa wenye ulemavu, tunajua wanao uwezo lakini miundombinu ya shule hizo bado ni tatizo, ukiingia kwenye vyoo ni tatizo, vifaa vya kujisomea bado ni tatizo. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri fuatilieni watoto hawa wenye ulemavu, wanaouwezo wa kuwa viongozi katika Taifa hili. Ni jana tu nimetoka kutuma dawa katika ile shule ya watoto wenye ulemavu Njia Panda, hawana hata fedha za dawa, kwa hiyo niombe sana akikisheni shule hizi mnaziangalia kwa jicho la kipekee.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine ni suala la Ujenzi wa maabara. Tatizo la Serikali hii badala ya kuanza jambo la kwanza tunaanza la mwisho kwenda la kwanza. Maabara hizi zilijengwa, wananchi walipata wakati mgumu sana, walinyang‟anywa mbuzi, walinyang‟anywa kuku, maabara hizi zimekamilika leo, hakuna walimu, hakuna vifaa, tuwaeleweje Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Ninaomba sana na kwenye hotuba yako umesema vifaa vitaanza kununuliwa 2018 kama sikosei, sasa ni kwa nini tusingeanza kuandaa walimu, tukaviandaa vifaa alafu tukajenga hizo maabara. Leo watoto wetu wanakosa walimu, wanasayansi tutawapata wapi, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri ulifanyie kazi suala hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine ni ombi kutoka kwa mdogo wangu hapa ameniomba, wana Chuo cha Maendeleo ya Jamii kule Tarime, anaomba sana chuo kile mkibadilishe kiwe chuo cha VETA. Kwa sababu kama tumeshindwa kuvijenga bora tukatumia vyuo hivi au majengo haya yaliyopo kufungua vyuo vya VETA ili watoto wetu hawa wakaendelee kupata elimu hii ya ufundi kupitia vyuo hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine ni suala la polisi Wilaya ya Siha walisimamia mtihani wa kidato cha nne mwaka jana. Lakini mpaka leo hawajalipwa fedha zao. Nikuuombe sana Mheshimiwa Waziri na ni Wizara yako ilitakiwa iwalipe, tunaomba mkawalipe polisi wale fedha zao na ukizingatia nao bado wako kwenye mazingira magumu fedha zao hawazipatai kwa wakati, kazi hii walishaifanya, ninaomba sana Mheshimiwa Waziri mkalifanyie kazi suala hili ili polisi hao waweze kupata fedha zao.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunao upungufu mkubwa sana wa walimu wa Sayansi katika Wilaya yetu ya Siha. Ninaomba sana tuhakikishe tunawekeza kwa walimu hawa, kuna hiyo taarifa tuliyoipata ya mgomo wa UDOM. Walimu hawa hawafundishwi, zaidi ya wiki mbili sasa, walimu hawa wangetusaidia kuziba hilo pengo la walimu wa sayansi. Ninaomba sana Mheshimiwa Waziri fanyia kazi suala hili watoto wetu warudi darasani wakafundishwe ili wakafundishe watoto wetu. Nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kidogo katika hoja hii muhimu katika kujenga Taifa letu. Ili nchi iendelee ni lazima iwe na viwanda vinavyozalisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoka Mkoa wa Kilimanjaro ambao ulikuwa na viwanda kadhaa ambavyo vilichangia pato la Taifa, lakini kwa bahati mbaya hakuna kiwanda kinachofanya kazi kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisemee Kiwanda cha Magunia Moshi. Kiwanda hiki kimeshindwa kwa sababu kumekuwa na uingizaji mkubwa wa magunia toka nje na bei ya magunia hayo iko chini kuliko haya magunia yanayotengenezwa nchini kwetu na sababu kubwa ni kodi nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni kwanini nchi yetu kupitia Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki hamkai na kukubaliana kuzuia uingizaji wa magunia toka nje ili viwanda vilivyo ndani ya nchi zetu hizi viweze kufanya kazi na kuzalisha na kutoa ajira kwa wananchi wa nchi hizi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, kuna umuhimu wa Serikali kukaa na wawezeshaji ili kujua matatizo waliyonayo ili kuondoa matatizo hayo waweze kuzalisha na hata kuuza bidhaa zao wanazozalisha toka kwenye viwanda vyao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, namwomba Mheshimiwa Waziri atusaidie Mkoa wetu wa Kilimanjaro, tuna tatizo la ardhi. Je, Wizara ina mpango gani wa kututafutia wawekezaji wa viwanda vidogo vidogo kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa wetu pamoja na Wabunge tunaotoka kwenye Mkoa huo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ndiyo niliyotaka kuchangia kuhusu Mkoa wangu. Nategemea Mheshimiwa Waziri na wataalam wake wanafanyia kazi mambo hayo ili Mkoa wetu uweze kurudi kwenye hali yake ya zamani ya kiuchumi na kutoa ajira kwa wananchi wa Mkoa wetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la wafugaji na wakulima na hifadhi zetu. Tatizo hili ni kubwa sana katika nchi yetu na kama hatua za dharura hazitachukuliwa tutapeleka nchi yetu kwenye umwagaji damu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hayo baada ya kusikiliza michango ya Waheshimiwa Wabunge humu ukumbini. Jana michango hiyo inaligawa Taifa letu katika makundi makubwa ambao wote ni Watanzania. Mimi niiombe Serikali ichukue hatua za haraka kukaa na Wizara zake TAMISEMI, Ardhi na Maliasili kupanga maeneo kwa ajili ya wafugaji na wakulima, hii itaondoa tatizo hili kubwa, tumechoka kuona damu za Watanzania zikimwagika kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunakumbuka Operesheni Tokomeza iliyofanyika katika nchi yetu na madhara yaliyopatikana katika zoezi hilo. Serikali iliunda Tume ili kuchunguza athari na Tume hii imemaliza kazi yake, je, ni lini taarifa hiyo itatoka ili Bunge lako lipate kujua Tume imebuni nini. Lakini pia liko suala la fidia kwa wananchi walioathirika katika operesheni hiyo, je, ni lini sasa fidia hiyo itatoka?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuishauri Wizara kutoa elimu kwa wananchi ili wajue umuhimu wa hifadhi zetu. Naamini elimu ikitolewa wananchi wetu wataelewa na watakuwa walinzi katika hifadhi zinazozunguka. Pia nitoe ushauri mwingine ili kuondoa tatizo la mipaka na vijiji vinavyozunguka hifadhi zetu ni muhimu sana wataalam wetu wanapokwenda huko kwenye maeneo washirikishe wananchi hii itaondoa migogoro iliyopo huko nimesema hayo kwa sababu wananchi wanalalamika hawashirikishwi wakati wao ni wenyeji wa maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lililopita tulijadili sana suala la Halmashauri zinazozunguka Mlima Kilimanjaro ambao wananchi wake pale ambapo likitokea tatizo hao ndiyo wanakuwa wa kwanza kushirikiana na hifadhi kutatua tatizo hilo. Sasa ningependa kujua ni lini Halmashauri hizo zitaanza kupokea mrabaha unaotokana na mapato ya mlima huo mzuri na wa kwanza Afrika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo mchango wangu kwa leo naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia machache katika Wizara hii. Nianze kwa kutoa pole kwa msiba mkubwa tulioupata katika nchi yetu kwa ajali iliyotokea katika Mkoa wa Arusha.

Mheshimiwa Spika, utamaduni; nchi yetu imebarikiwa kuwa na makabila 126 na kila kabila lina mila na desturi zake na kwa pamoja ndiyo zinatengeneza utamaduni wetu. Ila bado vipo baadhi ya vitu katika tamaduni hizo ambavyo vinadhalilisha wanawake. Kwa mfano, ukeketaji, kutokutoa umiliki kwa wanawake na kurithi wanawake wanaofiwa na waume zao hata kama wanawake hao hawataki. Katika jambo hili la ukeketaji ngariba wameanza kutumia mbinu mpya ya kukeketa watoto wachanga, hili jambo ni baya sana. Mambo haya bado yanaendelea pamoja na kuwa na jitihada za kupiga vita mambo haya.

Mheshimiwa Spika, napenda kujua katika bajeti hii Serikali ioneshe wazi itafanya nini kukomesha tamaduni na desturi hizi mbovu zinazomdhalilisha mwanamke na mtoto wa kike. Ufike wakati wa kuzirasimisha baadhi ya tamaduni katika mfumo rasmi ili kuziondoa zisizofaa.

Mheshimiwa Spika, michezo; kumekuwa na jitihada za kuhamasisha mpira wa miguu kwa vijana walio chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, lakini hakuna nguvu ya kutosha kuhamasisha uwekezaji kwenye mpira wa miguu na michezo mingine. Pamoja na timu hizi za Serengeti Boys na Kilimanjaro Queens kufanya vizuri, bado hazipewi kipaumbele cha kutosha wakati vipo vipaji na wana uwezo wa kufanya vizuri kimataifa na kwa sasa timu hizo zimeweza kufanya vizuri katika michezo yao. Kwa mfano Kilimanjaro Queens, hawa ni wanawake, walichukua Kombe la Afrika Mashariki na Kati mwaka jana.

Mheshimiwa Spika, ili timu zetu zifanye vizuri ni lazima tuwekeze tuwe na chanzo cha kuaminika cha kuwekeza pesa kwenye michezo na lazima kuwekeza na kuupa mwamko wa kutosha mpira wa miguu kwa akinamama. Umefika wakati sasa kuwe na chanzo cha kuaminika cha kuwekeza pesa kwenye michezo na njia rahisi wanayofanya duniani kote ni kupitia Bahati Nasibu ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, hapa kwetu Serikali haitengi pesa kwenye bajeti na hakuna njia ya kuupa pesa mchezo na mchezo wa bahati nasibu unasimamiwa na Wizara ya Fedha badala ya Wizara inayohusika na michezo. Nashauri bahati Nasibu ya Taifa iwe chini ya Wizara hii ili kiwe chanzo cha upatikanaji wa fedha katika michezo na kuwezesha timu zetu kushiriki katika mashindano.

Mheshimiwa Spika, habari, uhuru wa vyombo vya habari; sheria tuliyopitisha hapa Bungeni ina vipengele vinavyolalamika na ni vizuri Serikali ione haya na kuvipitia na ikaangalia namna ya kuvibadilisha ili kuweka uhuru wa vyombo vya habari wa kweli. Tumeona hivi karibuni vyombo vya habari vikivamiwa na viongozi wakiwa kwenye maeneo yao ya kazi, tumeona kwenye vyombo vya habari wanahabari wamepigwa wakiwa wanatekeleza wajibu wao.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha mchango wangu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nimshukuru pia Mheshimiwa Kubenea kwa kunipa dakika zake tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuunga mkono maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, lakini na yale maoni yaliyotolewa na Kamati yetu ya Ardhi, Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na upatikanaji wa fedha katika Wizara hii muhimu sana katika Taifa letu. Kumekuwa na ucheleweshwaji au kutokupelekwa kabisa kwa fedha za maendeleo katika Wizara hii. Wachangiaji wengi wameonesha umuhimu wa Wizara hii, lakini Wizara ya Fedha imekuwa haipeleki fedha za maendeleo na kufanya miradi mingi ya Wizara hii kushindwa kutekelezeka kwa wakati. Pia miradi mingi imekuwa ikitegemea wafadhili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tumwombe Waziri wa Fedha kuhakikisha kabisa zile fedha tunazozitenga hapa ndani ya Bunge ziwe zinapelekwa kwa wakati ili kuisaidia Wizara hii iweze kufanya vizuri zaidi. Amesema kaka yangu, Mheshimiwa Mbatia hapa kwamba ili ng’ombe aendelee kutoa maziwa mengi ni lazima alishwe vizuri. Kwa hiyo tunaomba fedha hizo ziwe zinakwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, Kamati yetu imekuwa ikifanya ziara mbalimbali katika taasisi zilizoko chini ya Wizara hii, kwenye hifadhi zetu na hata misitu. Tumekutana na changamoto mbalimbali, mojawapo ni uhaba wa watumishi katika taasisi hizo na hasa kubwa ni askari wale wa wanyamapori. Tunajua ukubwa wa hifadhi zetu na misitu, hivyo, tuiombe Wizara sasa ihakikishe kwamba inaajiri askari wengi ambao watakwenda kuhakikisha wanalinda mali zetu, wanyama wetu na rasilimali zote zilizomo ndani ya misitu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo malalamiko ambayo tumepata kutoka kwa askari hawa wa Jeshi Usu kwamba kumekuwa na utofauti wa malipo kutoka kwa askari hawa wa Jeshi Usu wa TAWA, TANAPA, Ngorongoro na TFS. Wamekuwa wanalipwa pungufu, posho na wengine mishahara. Tunajua kazi wanazofanya ni kubwa na wanafanya kwenye mazingira magumu wote, kwa hiyo tunaomba sana Wizara ihakikishe askari wetu hawa wote wanalipwa sawasawa, yaani kusiwe na tofauti za mishahara wala posho kwa sababu kazi wanayoifanya ya kulinda rasilimali zetu ni kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, upo upungufu wa magari; tunajua mbuga zetu zilivyo kubwa, lakini pia miundombinu yake si mizuri, magari yaliyopo kule ni machakavu, yanafanya utendaji kazi wao kuwa mgumu sana. Kwa hiyo tunaomba wapate magari ya kutosha na vifaa vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile wana uhaba wa nyumba za kukaa, wanafanya kazi lakini nyumba za kukaa hawana na wanakwenda kupanga mbali na maeneo yao ya kazi. Tunaomba basi nyumba wajengewe na kama inashindikana basi wapewe housing allowances ambazo zinaweza kuwasaidia wao kutekeleza majukumu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nisemee suala la migogoro ya mipaka; suala hili limechukua muda mrefu sana na migogoro bado tunaendelea kuiona. Jana Mheshimiwa Waziri Mkuu amejibu swali kwamba ile taarifa ya zile Wizara nane imeshapelekwa kwa Mheshimiwa Rais, tunashukuru kwa hilo, lakini tunaomba taarifa hii basi itakapofanyiwa kazi na kurejeshwa kwa ajili ya kuanza kutekelezwa wawashirikishe wawakilishi wa wananchi; Wabunge pamoja na Madiwani wa maeneo yale ili kuondoa migogoro hiyo, kwa sababu ikifanywa kimyakimya migogoro hii haitaisha na itaendelea kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tumekuwa tukiona kauli nyingi nzuri na matamko mazuri yanatolewa kwa wananchi, tunaomba yakatekelezeke yasije yakawa ni ya kisiasa kwa sababu tunakwenda kwenye uchaguzi. Tunaomba haya yakafanyike, yafanyiwe kazi vizuri, wananchi wetu waondokane na hii migogoro ya mipaka kila wakati, tupunguze vifo kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pale kwa askari niongeze jambo moja; tulikwenda kwenye mahafali ya hawa askari wa Jeshi Usu, tuliwaomba kwamba pamoja na mafunzo yote wanayopewa lakini wawe wanatimiza wajibu wao wasionee raia, kupiga raia bila sababu. Kwa sababu kumekuwa na malalamiko ya maaskari hawa kupiga wananchi wetu bila sababu, niwaombe sana wasimamie maadili ya kazi zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo tuliliona na imesemwa kwenye Taarifa yetu ya Kamati na ya Kambi ya Upinzani, ni kuhusu migongano ya sheria zilizopo. Mfano ni Sheria ya Ardhi Na.4 ya mwaka 1999, Sheria ya Vijiji Na.5 ya 1999, Sheria ya Wanyamapori na ile Sheria ya Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati yetu tumefanya ziara mbalimbali kwenye hifadhi zetu na tumeona Sheria ya Madini inaweza kutoa kibali cha kuchimba madini kwenye eneo lolote. Tulipita kwenye Hifadhi ya Manyara Bunge lililopita, tulikuta yapo machimbo watu wanachimba kule na hii ni hatari sana kwa watumishi wetu wanaofanya kazi kwenye hifadhi hizo, lakini pia kwa wanyama wetu. Mashimo yale ni makubwa sana yanaweza kuleta athari kwa wanyama wetu. Kwa hiyo niiombe Serikali, Serikali hii ni moja, sheria hizi zimetungwa ndani ya nchi hii, basi ikae kwa pamoja kuhakikisha wanapitia sheria hizi ili kuondoa huo mgongano uliopo katika sheria hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee suala la biashara ya viumbe hai; suala hili limechukua muda mrefu sana, toka 2016, huu ni mwaka wa nne sasa. Wafanyabiashara hawa walizuiwa wakasema wanaweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba wataweza kupangiwa ili kufanya biashara zao vizuri, lakini juzi Naibu Waziri alipokuja kwenye Kamati yetu alituambia kwamba biashara hii imepigwa marufuku.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuiomba na kuishauri Serikali kwamba wafanyabiashara hawa walifuata taratibu zote zinazohusika, walikata leseni, wamelipa kodi na walishakamata wanyama hawa, wameingia gharama ya kuwatunza. Niombe, inawezekana wapo wahalifu wachache walioingilia biashara hii na kufanya wengine kuzuiliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanyama ambao tunawazungumzia siyo wale wanyama wakubwa kama tembo, twiga na swala kama wale waliosafirishwa kwenye Uwanja wa KIA wakati ule; ninaowazungumza na waliokuwa wanasafirishwa ni nyoka, mijusi, ngedere, kenge na vipepeo. Wanyama hawa kama hawatavunwa itakuwa ni hatari sana hapo baadaye kwa Taifa letu kwa sababu hawa watatuletea athari kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimuombe Mheshimiwa Waziri kubadilisha maamuzi ambayo wameyafikia na kuruhusu wafanyabiashara hawa kuendelea na biashara hiyo. Wale waliokosea basi wachukuliwe hatua za kisheria, hakuna anayekubaliana na kusafirisha wanyama hao wakubwa nje ya nchi lakini hawa wengine wadogowadogo ambao wanaweza kuleta madhara hapo baadaye waweze kuruhusiwa kuendelea na hiyo biashara. Kwa sababu tunajua hawa walilipa kodi na walifanya taratibu zingine zote na haya ndiyo maisha yao. Wengine wamekopa wanasomeshea watoto kwa hiyo kuwafungia tu hivihivi siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ninalotaka kulisemea ni lile ambalo limezungumziwa kwenye Kamati yetu kuhusu TANAPA, tozo nyingi sana. Tunaiomba Serikali kuliangalia Shirika hili la TANAPA, limekuwa likifanya kazi nzuri kusaidia wananchi wetu lakini limekuwa likirundikiwa kodi nyingi na juzi zimeongezewa tena hifadhi nyingine tano, kwa hiyo kuziendesha itakuwa ni gharama kubwa sana. Kwa hiyo tuiombe Serikali, tuiombe Wizara ya Fedha kuhakikisha kwamba wanaliangalia Shirika hili la TANAPA ambalo limekuwa likifanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni lile la TFS kuwa mamlaka; wamesema wenzangu, jukumu la TFS tunalijua, inalinda misitu yetu, lakini ni vizuri sasa kuifanya iwe mamlaka ili iweze kusimamia sheria zake na kufanya maamuzi kama linavyofanya Shirika la TANAPA ili nalo liweze kufanya vizuri, tunaomba ikafanyike hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Waziri pia na Naibu wake, wamesema Wajumbe wenzangu kwamba mwanzo Wizara hii ilikuwa ikija mbele ya Kamati ilikuwa ina mambo mengi, lakini wameweza kutekeleza maagizo ya Kamati, wanakwenda vizuri. Niwapongeze sana, lakini yale yote tuliyoyasema kwenye Kambi ya Upinzani na yale ya kwenye Kamati yetu, tunaomba wahakikishe wanayafanya vizuri na hususan posho kwa maaskari wetu pamoja na mishahara yao mkaiboreshe kwa sababu hawa wanalinda rasilimali zetu, ni vizuri wote wakalingana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia bajeti hii ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Utawala Bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, Utawala Bora ni pamoja na watu kupata habari na kujua wawakilishi wao waliowachagua wanawawakilisha vipi ndani ya Bunge, lakini Bunge letu leo limekuwa ni Bunge la kujifungia ndani, tumefunga milango, tumefunga madirisha, hatutaki wananchi ambao tuliwaomba kura kwa unyenyekevu mkubwa, wengine walipiga magoti, wengine walipiga pushapu, ili mradi tupate kura, lakini leo hamtaki kuwapa nafasi wananchi wasikie mnachokisema.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuomba sana, Bunge letu liendelee na ule utaratibu wa zamani. Huko nje wananchi wanalalamika kwa sababu bajeti tunayoipitisha hapa ni kodi zao, lakini leo tunajifungia hatutaki wasikie, ni aibu!
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo kuhusu mwenge. Kama kuna kitu kinachonikera ni suala la kukimbiza mwenge mchana. Wabunge wa Upinzani tulishasema, kuhusu sherehe zinazoadhimishwa na Serikali, lakini mlitucheka, leo zipo baadhi zimesitishwa. Namwomba Mheshimiwa Rais kama alivyoacha kusherehekea hizo sherehe nyingine ambazo ni za muhimu kama Uhuru na Muungano, tuachane na biashara ya kukimbiza mwenge mchana.
Mheshimiwa Naibu Spika, zinatengwa bajeti kwenye Halmashauri zetu, leo kila Mbunge analalamika mafuriko kwenye maeneo yake watu wanakimbiza mwenge, watu wetu wanakufa hawana maji safi na salama, hawana dawa, madaraja yamebebwa na maji, hakuna barabara, tunakimbizana na mwenge, hii ni aibu! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana kama ni kazi ya mwenge naamini imetosha, maana yake siamini kama hata hao mafisadi, hauna tija kwa sasa pamoja na kumulikwa kila mwaka, lakini ufisadi bado upo pale pale. Naomba sana hizi fedha zinazotengwa kwa ajili ya kukimbiza mwenge tuzipeleke kwenye shughuli za maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee suala la upotevu wa pesa katika Halmashauri zetu. Katika Manispaa ya Moshi Mjini kulitokea ubadhirifu wa shilingi milioni 90 kutoka kwenye Basket Fund na suala hili TAKUKURU waliliingilia, wakachunguza na wakagundua baadhi ya watumishi waliziiba fedha hizi na wakawashauri wale watumishi warudishe fedha hizi na mpaka sasa inasemekana zimesharudishwa shilingi milioni 70.
Swali langu ni kwa nini TAKUKURU pamoja na nia njema waliyoonyesha na kazi nzuri waliyofanya, maana wamewaomba warudishe fedha na zimerudi, ni kwa nini sasa TAKUKURU hailipeleki suala hili mahakamani ili wale wote walioshiriki kwenye suala hili wakachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu zetu za nchi?
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiliacha hivi TAKUKURU wakiendelea kumalizana ofisini fedha za walipa kodi zitaendelea kupotea na tukizingatia zaidi ya 70% ya fedha tunazopitisha hapa zinakwenda kwenye Halmashauri. Fedha hizo zingekuwa zinafanya kazi inayotakiwa leo wananchi wetu vilio walivyonavyo vingepungua. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Simbachawene, Waziri wa TAMISEMI, suala hili mlifuatilie na wale watumishi mhakikishe wanafikishwa mahakamani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala lingine niungane na Mheshimiwa Waziri (TAMISEMI) kuhusu uongezaji wa mapato katika Halmashauri zetu. Halmashauri zetu hasa mapato ya ndani yamekuwa ni kidogo sana na hii inatokana na wale wazabuni tunaowapa tender hawawi wa kweli, wanaziibia Halmashauri zetu. Wengi wamekuwa wakitumia vitabu viwili na kuleta yale mapato madogo katika Halmashauri zetu na kusababishia Halmashauri zetu kushindwa kujiendesha na kukosa yale mapato ya ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitolee mfano Halmashauri yetu ya Siha, yupo mzabuni mmoja, niiseme hii kwa sababu watumishi wamekuwa wakianzisha kampuni zao na wamekuwa wakijipa tender wenyewe na suala hili linasababisha sana Halmashauri zetu kushindwa kuendelea. Halmashauri yetu ya Siha yupo mzabuni mmoja amepewa zaidi ya zabuni tano na mpaka sasa anadaiwa zaidi ya shilingi milioni 56 hajaweza kuzileta katika Halmashauri yetu. Nimeona kwenye magazeti juzi wanasema Halmashauri ya Siha tusipoweza kukusanya itafutwa, lakini wanaoturudisha nyuma ni wazabuni kama hawa. Niombe Mheshimiwa Waziri tufuatilie na wale watumishi wote watakaogundulika kwamba wana kampuni ambazo wamejipa bila kufuata taratibu waweze kuchukuliwa hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la elimu. Mzungumzaji aliyemaliza kuongea alisema siku ya wanawake duniani tulitembelea maeneo mbalimbali kwenda kusherehekea sikukuu ya wanawake duniani. Mimi nilibahatika kwenda katika shule ya watoto wenye ulemavu iliyopo Njia Panda, Jimbo la Vunjo. Shule ile ina wanafunzi 69 wasiosikia, wana matatizo makubwa sana, ina walimu 11 lakini ina watumishi watatu, matroni na mlinzi hawa bado hawajaajiriwa. Ukizingatia kauli ya elimu bure, awali wazazi walikuwa wanachangia kwa kuwaandikia lakini leo mwalimu mkuu wa shule ile hawezi kuandika kwa sababu anaogopa kufukuzwa kazi. Matroni na mlinzi hawajalipwa mshahara huu ni mwezi wa nne. Hata kutoa huduma ndogo ndogo kama matengenezo ya vitasa, kununua vitabu, toka Januari mpaka sasa wamepata capitation shilingi 25,000 tu, hii ni aibu. Mheshimiwa Waziri umeonesha hapa shule tulizonazo, nilitegemea ungetuonesha tuna shule ngapi za watoto wenye ulemavu kwa sababu tunahitaji watoto wetu wapate elimu na najua shule za watoto wenye ulemavu zina mahitaji zaidi ya hawa watoto wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, shule ile inahitaji mambo mengi mfano na pia ukarabati haina uzio. Pia walikuwa na kilio kwamba wanahitaji kupata shule ya sekondari kwa sababu watoto wanaotoka pale wakifaulu, wakipelekwa kwenye shule hizi nyingine kuendelea na masomo hawapati walimu wenye lugha ya alama. Kwa hiyo, uelewa wao unakuwa ni mdogo wakifika form two wanarudi nyumbani. Wanasema wanalo eneo kubwa pale, wanaomba sana ile shule iendelezwe mpaka sekondari ili watoto wetu pamoja na ulemavu lakini akili wanazo, wanao uwezo wa kusoma, tukiwapa mahitaji yao na tukatekeleza mahitaji yao, naamini watakwenda kuwa viongozi wazuri katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine nizungumzie suala la posho za Madiwani, Wenyeviti wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji. Leo tuko Bungeni tunayo maafa kwenye maeneo tunayotoka lakini wanaowajibika ni hawa Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa. Tunaiomba sana Serikali hii ya Hapa Kazi Tu basi watazameni hawa, wanafanya kazi ngumu. Likitokea janga wa kwanza kugongewa ni Diwani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa niunge mkono taarifa zote mbili zilizowasilishwa na Wenyeviti wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuanza kutoa mchango wangu ningependa kuiambia Serikali, Bunge huwa linakutana hapa kupitisha bajeti ya Wizara na huwa wanatuambia wameweka cealing kwa hiyo, tunafuata cealing waliyotupa, lakini toka taarifa hizi zimeanza kuwasilishwa hapa ndani ya Bunge, hakuna Kamati hata moja ambayo imesema kuna Wizara ambayo imepata fedha zote walizozihitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti,sasa niiombe Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwamba, Bunge likishapitisha bajeti ihakikishe bajeti inafika kwa wakati kwenye zile Wizara, ili ile mipango iliyopangwa kwa ajili ya hizo Wizara iweze kutekelezeka, bila hivyo tutakuwa tunapiga kelele tu na kazi hazifanyiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la migogoro ya wakulima na wafugaji. Tumekuwa tukiona katika vyombo vya habari kwamba wakulima na wafugaji wamekuwa wakigombana kila siku. Ningependa kujua ile Kamati iliyoundwa ya pamoja ya kutatua migogoro imefikia wapi? Amesema msemaji aliyepita, tungetaka kujua wamefikia wapi ili kupunguza mauaji ya wakulima na wafugaji ambayo yanaendelea kutokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ni ya wakulima, wafugaji na wafanyakazi, haipendezi kuona wakulima wetu au wafugaji wakiendelea kuuana kila siku. Ifike wakati sasa Serikali ije na mpango madhubuti wa kutuonesha kwamba wanamalizaje tatizo hili la wafugaji na wakulima. Ili liishe ni lazima tuwe na matumizi bora ya ardhi na ndiyo maana nimeanza kwa kusema kwamba, ni lazima Wizara hii ya ardhi iweze kupatiwa pesa kwa wakati, iweze kupima na kuondoa migogoro hii. Tukiweza kupima na kuwapa wakulima maeneo yao na wafugaji, naamini kabisa tutakwenda kuondoa vifo vya wakulima na wafugaji kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisemee TANAPA. Niipongeze TANAPA imekuwa ikifanya kazi nzuri sana, lakini yapo matatizo yanayoendelea kujitokeza kwa maaskari wa TANAPA. Ni juzi tu hapa Mbunge alinyanyuka na kusema kwamba kuna mwananchi amepigwa risasi ya jicho na ikatokea kisogoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuwaomba ndugu zetu wa TANAPA na Wizara kwa ujumla wawe wanafanya utafiti ambao unaweza kujua kwamba askari wanaowaajiri wanao uzalendo wa kweli; kwa sababu kila siku Wizara imekuwa tukikaa nao na wanasema wanatoa mafunzo lakini mafunzo haya naona bado hayasaidii. Ndugu zetu, watoto wetu wameendelea kuuawa na sisi hatupendi kuleta migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa sana TANAPA ichukulie suala hili kwa umakini sana na kufuatilia ili kuondoa tatizo la vifo kwenye mbuga zetu, mapori ya akiba na hifadhi. Naamini tukifanya hivyo tutakwenda kupunguza suala la vifo kwa watu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la njaa. Juzi tulikuwa tumekwenda Karatu kwenye msiba, kwa bahati nzuri tuliona mizoga ya ng’ombe, mbuzi katika makundi makubwa imetapakaa, imekufa. Sasa ningependa kujua Wizara husika inachukua tahadhari gani kunusuru mifugo hii? Pia si kwa mifugo tu, hata kwa wananchi. Wameanza kufa ng’ombe, lakini itakuwa ni aibu kubwa sana Watanzania wakifa kwa njaa. Ilitolewa taarifa hapa na siamini kama iko sahihi kwa sababu, ma-DC na Wakuu wa Mikoa wamekuwa waoga sana kutoa taarifa sahihi. Ningependa Serikali ihakikishe kwamba, hakuna Mtanzania yeyote atakayekufa kwa njaa katika kipindi hiki cha ukame.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kuzungumzia suala lililosemwa kwenye taarifa yetu; tulikutana na wasafirishaji wa nyama, wafanyabiashara wanaosafirisha wanyama-hai. Walitueleza matatizo yaliyowakumba, walipewa leseni lakini walisitishiwa biashara hiyo; na kibaya zaidi walipositishiwa tayari walikuwa wameshakamata wanyama kwa ajili ya kuwasafirisha. Sasa ningependa kujua ni sababu gani za msingi zilizosababisha watu hawa kusitishiwa biashara yao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tuna taarifa zinazodai kwamba wako watu ambao si Watanzania wamepewa vibali kwa ajili ya kusafirisha wanyama hawa. Ningependa kujua ni sababu gani za msingi zilizosababisha Watanzania hawa ambao rasilimali hizi ziko ndani ya nchi yao, wao wananyimwa, lakini wanapewa wengine. Tungependa waziri anapokuja kujibu atuambie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lile suala nililokuwa nalisemea la kuhusu migogoro ya mipaka; Serikali inachangia sana na hii inaonesha kwamba Wizara zile husika huwa hazitoi ushirikiano, hazishirikishani na hii ndiyo inayoleta shida, kwa sababu unakuta kimeanzishwa Kijiji, Kata, Wilaya au Mkoa lakini hawashirikishi hata haya Mashirika ya TANAPA pale wanapoweka ile mipaka kujua kwamba hili ni eneo la hifadhi. Kwa hiyo, ningeomba sana Wizara zile husika waweze kushirikisha mashirika yetu haya pale wanapokwenda kuanzisha either ni Kijiji au Kata kwenye yale maeneo ambayo yanazunguka hifadhi zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini tukifanya hivi tutaendelea kuondoa malalamiko ya wananchi na nchi yetu itakuwa na amani. Hatuwezi kuona Watanzania wanaendelea kufa kila siku kwa sababu ya sisi tuliopewa nafasi tumeshindwa kuzitumia nafasi zetu kuwaweka waweze kuishi vizuri katika nchi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, amesema Mwenyekiti katika taarifa yetu, utalii wetu bado hatujaweza kuutangaza vizuri. Tulibahatika sisi Kamati Bunge lililopita kutembelea Afrika Kusini tuliona wenzetu wanavyotumia utalii wa fukwe, lakini nchi yetu tumeshindwa kutumia fukwe tulizonazo na tunazo fukwe nzuri sana; lakini za kwetu ukipita ni harufu tu, utasikia harufu zinazonuka huko tumeshindwa kuzitumia vizuri. Niiombe sasa Wizara itumie utalii wa fukwe lakini pia na yale maeneo ambayo kwenye kamati tumeonesha tuweze kuyatangaza vizuri na kupata watalii wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo maeneo mengi sana ya utalii, lakini kama nchi tumeshindwa kutumia na wale wenzetu wa kusini wanayo maeneo na tumeomba kabisa kwamba ile Bodi ya Utalii iweze kupata fedha za kutosha kuweza kutangaza maeneo yale ili tuweze kupata pato kubwa sana la fedha za kigeni kutoka nje kama mataifa mengine ambayo wameweza kupata kupitia maeneo ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie machache katika Bajeti hii ya Ofisi ya Rais. Nianze kwa kuziunga mkono hotuba zote mbili za Kambi ya Upinzani na niishauri Serikali isijisikie vibaya wala kuona aibu kuchukua yale mazuri yaliyomo katika hotuba zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la utawala bora. Utawala bora ni pamoja na kuviruhusu vyama vya siasa kutimiza wajibu wake kwa kufanya mikutano ya hadhara, lakini toka imeanza Serikali hii ya Awamu ya Tano, imekuwa na uoga na sijui ni kwa sababu gani wakati mnatamba kwamba mnafanya kazi zenu vizuri na hapa ni kazi tu, lakini mmekuwa mkivipiga marufuku vyama vya upinzani kufanya mikutano na kutoa ruhusa kwa Madiwani na Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkumbuke kuwa katika vyama vyetu tuna viongozi wa vyama wa Kitaifa, tunao Wajumbe wa Kamati Kuu ambao sio Wabunge na siyo Madiwani, je, hawa watafanyia wapi kazi zao. Kwa hiyo, nataka kuiambia Serikali ya Chama cha Mapinduzi waache kunyima haki kwa vyama vingine vya upinzani wakati wao wanapokuwa kwenye maeneo ambayo sio ya kwao wanahutubia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mgombea wetu wa Urais alipata kura zaidi ya milioni sita na wa Chama cha Mapinduzi alipata kura milioni nane, tofauti ya kura milioni mbili. Yeye anapita kuwashukuru Watanzania, lakini huyu wa kwetu aliyepata kura milioni sita mnakataa asiende kuwashukuru wananchi ambao walimuunga mkono, hii siyo haki kabisa! Tunaomba Katiba iheshimiwe kwa sababu ninyi ndio mmekuwa mkivunja Katiba wakati vyama vya siasa vipo kihalali, vya upinzani na hata hicho cha CCM, kwa hiyo, tupewe haki sawa kuhakikisha tunazungumza na Watanzania. Kutuambia tusubiri mpaka 2020 hamtutendei haki. Chama chochote cha siasa mtaji wake ni watu. Kwa hiyo, tunapokwenda kufanya mikutano, tunakwenda kuzieneza sera zetu na kupata wanachama wa kujiunga na chama chetu, lakini nashindwa kuelewa sijui uoga wenu ni nini. Niwaambie tu, huko nje Watanzania wameshakata tamaa na Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala la afya. Kumekuwa na tatizo ndani ya nchi yetu la vifo vya akina mama na watoto. Naliomba Bunge na Serikali, ifike wakati tuhakikishe kwamba tunakwenda kupunguza vifo hivi kwa kuhakikisha tunatenga bajeti ya kutosha kwa akina mama ili waweze kupata huduma bora wanapofika kwenye vituo vya afya ikiwemo huduma ya upasuaji, kwa sababu akina mama wengi wamepoteza maisha kutokana na vituo vyetu kutokuwa na vifaa na hasa madaktari na wahudumu wa afya pamoja na dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba sana Serikali na sisi kama Bunge tulisemee hili ili kuhakikisha vifo vya akina mama na watoto katika nchi yetu vinapungua. Nawaomba Wabunge wenzangu tukatoe elimu kwenye maeneo yetu tunayotoka na kuwaomba akina mama pindi wanapokuwa wajawazito waweze kuhudhuria kiliniki, hii itasaidia sana kupunguza vifo vya akina mama na watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni Bima ya Afya. Suala hili limekuwa ni tatizo kubwa sana, hata Waheshimiwa Wabunge wenyewe humu ndani ni mashahidi. Zipo hospitali ambazo zinakataa kupokea Bima ya Afya hata kwa Waheshimiwa Wabunge, sembuse huko kwa wananchi wetu ambao ni wengi. Yapo maduka ya dawa yanakataa kupokea kadi hizi.

Kwa hiyo, naiomba Serikali kwanza itoe elimu kwa wadau wote wahusika umuhimu wa hii Bima ya Afya ili wananchi wengi waweze kujiunga katika bima hii waweze kupata huduma nzuri ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la elimu. Hapa kwanza naomba nimpongeze na kumshukuru Mheshimiwa Simbachawene. Katika bajeti iliyopita nilizungumzia shule ya watoto walemavu Njiapanda. Kulikuwa kuna baadhi ya watumishi walikuwa hawajalipwa, nakushukuru kwamba watumishi wale wamelipwa, lakini pia namshukuru Waziri wa Elimu Mheshimiwa Mama Ndalichako, alikwenda kutembelea shule ile na niliongea na Mwalimu Mkuu akaniambia kwamba yale niliyoyasema yakiwemo shule ya sekondari ya watoto wenye ulemavu, mchakato umeanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, lakini naomba mchakato uende haraka kwa sababu watoto wale mwaka huu wanakwenda kufanya mtihani wa darasa la saba. Tunaomba sana ili mwakani nao waweze kujiunga kidato cha kwanza, tusiwaache watoto hawa nyuma kwa sababu wanao uwezo na hawa ndio viongozi wetu wa baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nizungumzie shule za Kata. Mkoa wetu wa Kilimanjaro hasa kule Uchagani waliitikia vizuri sana ujenzi wa shule za Kata na kuna baadhi ya vijiji vina shule mbili mpaka tatu za sekondari na hii sasa imeleta upungufu wa wanafunzi; kwa mfano, katika kijiji cha Kitandu katika Kata ya Uru Mashariki tunazo shule mbili na katika shule moja ya Mawela tuna madarasa zaidi ya manne hayana wanafunzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, pamoja na kuwa shule hizi zilijengwa na nguvu za wananchi, mngewashauri waweze kutumia shule moja aidha, kwa kufanya hostel, kuhamisha shule moja kwenda kwenye shule nyingine ili ile shule nyingine iweze kutumika hostel au tukaweza kuifanya o-level ili wale watakaomaliza pale waweze kuingia kwenye hii shule nyingine kuliko kuacha madarasa wazi, inakuwa haina faida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine elimu yetu tumeona inaendelea kushuka na hii ni kwa sababu Wakaguzi hatujawatengea fedha za kutosha za kuweza kukagua shule zetu. Naiomba sana Serikali iweze kutenga fedha za kutosha ili Wakaguzi hawa waweze kufanya kazi zao ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la posho za Madiwani. Wabunge wenzangu wamesemea sana posho za Madiwani. Tunajua Waheshimiwa Wabunge wanapokuwa hawapo, Madiwani wamekuwa wanafanya kazi kubwa sana. Naiomba Serikali, kwenye hotuba yetu ya Upinzani kwa upande wa TAMISEMI tumeomba kuongeza posho zao. Najua Madiwani wako kwenye ile Sheria ya Mafao, lakini mafao yao mwishoni yanakuwa ni madogo kwa sababau ya posho wanazozipata. Kwa hiyo, naomba posho zao ziongezwe na hii ni pamoja na Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa. Halmashauri nyingi zimekuwa haziwapi fedha. Naiomba TAMISEMI, aidha, itoe mwongozo au itunge sheria ya kuzielekeza Halmashauri zetu kuhakikisha Wenyeviti hawa wanalipwa fedha zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho nizungumzie ujenzi wa stand ya Ngangamfumuni. Mheshimiwa Simbachawene tunakuomba sana, mchakato huu ulishakamilika na TIB tayari walishakubali kutoa fedha, kujenga na kusimamia ndani ya miaka 15 wakisharejesha fedha zao watukabidhi stand. Kwa hiyo, nakuomba sana Mheshimiwa Waziri utukubalie kusaini ili tuweze kupata fedha hizo kwa maendeleo ya wananchi wetu wa Manispaa ya Moshi na kwa Taifa zima. Sioni ni kwa sababu gani unapata kigugumizi. Sitaki kuamini zile sababu zilizosemwa juzi kwa sababu yapo niliyokuomba na ukayafanya, kwa hiyo, nikuomba tena kwa mara hii stand ya Ngangamfumuni muweze kutupatia kibali na ujenzi huo uweze kuanza mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni suala la Ben Saanane. Mimi ninatoka Mkoa wa Kilimanjaro na ni Mbunge wa Viti Maalum, akina mama wa mkoa ule wanaulizia Ben Saanane yupo wapi na leo Kiongozi wa Upinzani ameuliza swali hapa, tungependa kujua Ben Saanane alipo, na kwa taarifa walizosema ambazo sina hakika nazo tunataka taarifa sahihi, kama kweli Ben yupo basi tumpate na kama hayupo ni vizuri mkatuambia ili familia yake ijue kama wameshampoteza Ben kama alivyosema Mbunge wa Rombo walie.




Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. GRACE S. KIWELU: Naomba kuchangia machache katika taarifa ya Mjumbe wa Kamati hii. Naomba kuongeza machache katika katika maoni yetu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya ardhi katika maeneo ya Hifadhi ni tatizo kubwa sana katika vijiji vinavyozunguka hifadhi zetu. Hivyo ni jukumu la Serikali kuhakikisha migogoro hiyo inamalizika na kuleta uelewano kati ya wananchi na watumishi wa Hifadhi (Askari) zetu. Kama Serikali haitachukua hatua za haraka, migogoro hii itasababisha vurugu na hata kusababisha majeraha hata vifo kwa wananchi wetu. Hivyo, ni muhimu sana wananchi kushirikishwa na Wizara husika kwenye zoezi hili ili kufikia muafaka kwenye suala hili la mipaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafugaji wamekuwa na malalamiko mengi kuwa Askari wa Wanyamapori wamekuwa wakiwanyanyasa sana kwa kuswaga ng’ombe zao kwa nguvu na kuziingiza kwenye hifadhi na kulazimishwa kutoa rushwa na wakishindwa kutoa rushwa hiyo mifugo yao hupigwa mnada. Ziko taarifa kuwa Askari hao kutumia ndugu zao kununua ng’ombe hao. Kama Kamati tumeliomba Bunge liunde Kamati Maalum kuchunguza tuhuma hizo ili ukweli ujulikane na sheria ichukue mkondo wake kwa wale watakaokutwa na hatia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uvamizi wa mifugo katika hifadhi; katika ziara zetu tumeona jinsi vyanzo vya maji vikiharibiwa na mifugo na kukosekana kwa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya mabwawa, malambo kwa ajili ya mifugo. Hivyo, tunaishauri Wizara husika kuweka malambo na mabwawa katika maeneo hayo ili kupungua au kumaliza kabisa suala hilo la uvamizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuweka msisitizo kwenye ushauri wa Kamati yetu kuhusu uundaji wa Kamati kujua ni kwa nini mapato ya Sekta hiyo ya Uwindaji yameshuka? Siyo Mheshimiwa Waziri kukimbilia kufuta leseni za vitalu ambazo tayari wawekezaji wameshalipia na kupata booking za wageni; leo ukiwaambia unawapunguzia muda wa leseni zao, itakuwa siyo sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ziara zetu tumeona mapitio ya wanyama yamezibwa kwa shughuli za kibinadamu na hii imesababishwa na kutokuwepo kwa vibao vya kuonesha kuwa eneo hilo ni shoroba. Hivyo, tunashauri hifadhi zishirikiane na Halmashauri na Wizara zinazohusika kuweka mipaka na mabango kuonesha maeneo hayo ya shoroba ili kupunguza na kumaliza kabisa tatizo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo niliyochangia hapo juu na tukizingatia maoni yote ya Kamati, naamini migogoro inayoikabili sekta hii ya utalii itapungua na kwisha kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, naomba kuwasilisha mchango wangu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi hii kuchangia machache katika bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukizungumzia suala la amani kila siku, inawezekana sielewi amani inayozungumziwa ni ipi katika Taifa letu, kwani yameendelea kutokea matukio mbalimbali ya kutisha, watu wamekuwa wakiokotwa kwenye fukwe zetu za bahari wakiwa wamekufa; wengine wamepotea katika mazingira ya kutatanisha, wengine wamekuwa wakitekwa na watu wasiojulikana; pia waandishi wa habari wamekuwa wakipigwa na kutekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, habari zilizoko mitaani zinadai kuwa Waandishi hao hufanyiwa hivyo kwa sababu ya kuandika mambo yasiyofurahisha wakubwa. Naomba kujua Serikali inachukua hatua gani kwa haya mambo yanayoendelea katika nchi yetu ambayo tunadai nchi yetu ni ya amani na utulivu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza viongozi wa dini; Maskofu kwa waraka wao waliotoa kuonesha hali ya nchi ilivyo kwa sasa. Naishauri Serikali badala ya kuubeza waraka huu tukae chini kama Taifa, tujadiliane haya kwa maslahi ya Taifa letu. Viongozi hawa wa dini wamekuwa wakituombea katika shughuli zetu za kila siku. Hivyo tusiwapuuze tu kwa sababu wamesema ukweli kuhusu hali ya nchi ilivyo, kwa sababu tusiombe tu kuombewa lakini pale wanapoona nchi haiendi vizuri wakisema, mnasema wametumwa na Wapinzani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba kama Taifa, kuna kila sababu ya kuzungumza kuhusu Taifa letu linavyokwenda kwa maslahi ya nchi yetu ya Tanzania, tusitengeneze Taifa la chuki na visasi. Naomba sana Serikali itutafutie hawa watu wasiojulikana ni akina nani na wako wapi? Tusiache hali hii ya wasiojulikana kuendelea kutesa na kuwa hakuna aliye salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mipaka ya nchi yetu haiko salama sana. Naishauri Serikali kuhakikisha tunafanya mazungumzo na nchi tunazopakana nazo ili kukabiliana na uwekaji wa mipaka hiyo. Kamati yetu ilitembelea mpaka wa Uganda na Tanzania, hali siyo nzuri. Wananchi wa Uganda wameingia ndani ya nchi yetu kwa kuvuka alama za mipaka iliyoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nampongeza DC wa Wilaya ya Misenyi kwa kazi nzuri anayoifanya pamoja na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama ya kuhakikisha wananchi na mali zao ziko salama, ingawa wako baadhi ya wananchi wetu waliokufa, waliopigwa na kunyang’anywa mali zao. Naishauri Serikali kuweka barabara katika maeneo ya mipaka yetu ili kuweza kuwarahisishia Watendaji wetu kufika kwenye maeneo hayo pale yanapotokea matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la barabara ni kubwa sana. Hivyo ni muhimu tukachukua hatua za haraka kuondoa kero hiyo. Wenzetu upande wa pili; Uganda, wana barabara inayopitika vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ndiyo machache niliyokuwa nayo kwa leo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa mchango wangu kidogo katika Wizara hii muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunamshukuru Mungu kwa mvua zinazoendelea katika nchi yetu pamoja na kuwa zimeleta madhara makubwa sana. Mfano, vifo kwa ndugu zetu na uharibifu mkubwa sana wa miundombinu ya barabara na madaraja. Ninapenda kujua Serikali ina mpango gani wa haraka kuhakikisha miundombinu hiyo niliyoitaja inatengenezwa ili kuondoa usumbufu mkubwa wanaoupata wananchi wetu kwa sasa uweze kuisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu nyumba za TBA Dodoma, mimi ni mmoja kati ya wapangaji wa nyumba hizo ila nyumba hizo kwa sasa ziko kwenye hali mbaya, zinavuja, matengenezo hayafanyiki kabisa, tunafanya wenyewe, kibaya zaidi hali iliyopo sasa hivi mazingira yanayozunguka nyumba zetu ni mabaya sana, majani yamekuwa marefu sana yanahatarisha usalama wa maisha yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kutokuzolewa kwa takataka kwenye maeneo yetu na hii kunaweza kuibua magonjwa ya kuambukiza mfano kipindupindu. Tunaomba sana usafi na matengenezo hayo niliyoonesha hapo juu yafanyiwe kazi ili kulinda afya za wapangaji wa nyumba hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ya kutoa mchango wangu huo, naamini niliyoyasema yatafanyiwa kazi kwa haraka hali ni mbaya, hasa nyumba zilizoko Area D Site Two, uchafu umezidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa mchango wangu kidogo katika Wizara hii muhimu katika kuendeleza michezo na utamaduni katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, Sera ya Sheria ya Utamaduni inayotumika nchini kwa sasa imepitwa na wakati ndiyo maana tunashuhudia migongano na mivutano hasa katika tasnia zingine sanaa zikifungiwa kwa maelezo ya kufanyika kinyume na maadili tuliyokubaliana ambavyo vinatumika kuamua huyu kakiuka maadili na huyu hajakiuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tumeona hata baada ya baadhi ya kazi za sanaa kufungiwa kumekuwa na malalamiko kuwa mbona baadhi ya kazi za sanaa ambazo zinaonekana kuwa na migogoro kuliko zilizofungiwa bado zipo na zinatumika. Hii inaonesha upo umuhimu wa kupitia upya sheria na sera za utamaduni nchini ili kulinda na kutunza utamaduni wetu na kazi zetu za sanaa bila uonevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili, ipo haja ya kupitia upya sheria na taratibu zinazotumia mwenendo wa vyombo vya habari vya ki-electronic yaani TV na Radio katika mazingira ya teknolojia ya leo unapofungia TV na Radio za nchini kwetu kwa sababu ya kupiga muziki fulani (kutumia kazi fulani za sanaa) wakati huo huo ving’amuzi vyetu nchini vinaonesha channels za nje ya nchi ambazo hatuna uwezo wa kuzuia uoneshwaji wake nchini ni sawa na kuvinyima vituo vyetu vya TV hapa nchini vishindwe kushindana kwenye ushindani wa soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, kama kweli tunataka nchi yetu tusomeke kwenye dunia kwenye michezo ni lazima Serikali ikubali kuwekeza katika michezo, tusipofanya hivyo tutaendelea kuwa wasindikizaji katika michezo tutakayokuwa tunashiriki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali lazima tukubali kushirikiana na Wafadhili wanaofadhili timu zetu kuhakikisha timu zetu zinapata muda mrefu wa kukaa kambini ili waweze kufanya mazoezi ya pamoja. Tusipofanya hivyo tutaendelea kuwa wasindikizaji kwenye kila mashindano. Pia tuwatie moyo wachezaji na wasanii wetu tusiwakatishe tamaa maana wengi wamefika hapo kwa juhudi zao wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia katika Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la upungufu wa walimu wa shule za msingi; hakuna elimu bila walimu, elimu bure bila walimu haitasaidia kama hakutakuwa na idadi ya kutosha ya walimu wenye weledi na motisha ya kufanya kazi ya kufundisha. Ningependa kujua Serikali imeajiri walimu wangapi mpaka sasa ili kukabiliana na upungufu huo? Serikali ina mkakati gani endelevu wa kuhakikisha tatizo la upungufu wa walimu linatoweka kabisa? Serikali imepanga kuajiri walimu wangapi katika mwaka wa fedha 2018/2019?

Mheshimiwa mwenyekiti, niongelee tatizo la uhaba wa vitabu katika shule zetu za msingi, unakuta kitabu kimoja kinasomwa na watoto watano mpaka sita, hii inaleta usumbufu mkubwa kwa watoto wetu na uelewa kuwa mdogo. Je, ni lini Serikali itahakikisha tatizo hili la upatikanaji wa vitabu linakwisha katika shule zetu? Mbali na upatikanaji mdogo wa vitabu bado vitabu hivyo vina mapungufu makubwa ndani na tatizo hili limekuwa likijirudiarudia pamoja na Wabunge kulisemea humu ndani. Je, tatizo ni nini? Ni akina nani wanafanya uhakiki huo wa vitabu? Kwa sasa hivi tunategemea nini kwenye uelewa wa watoto wetu? Itakuwaje kama vitabu vina makosa kwa watoto wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya mwaka juzi nilimuomba Mheshimiwa Waziri kulifanyia kazi kwa haraka suala la wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi waweze kupelekwa kwenye shule za sekondari za wanafunzi walio na ulemavu, lakini hilo halikufanyika. Wanafunzi hawa wamechanganywa na wanafunzi wasio na ulemavu, hii hatuwatendei haki watoto hawa. Kwa mfano shule ya watoto wenye ulemavu Njia Panda darasa lilikuwa na watoto 20 na wote wamefaulu, nimpongeze mwalimu mkuu na walimu wote wa shule hiyo kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa watoto hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu hapa ni kwamba kwa sababu uelewa wao ni wa taratibu, hivyo wanatakiwa kuwa na walimu wanaowafundisha na kuwafuatilia kwa karibu. Si kwamba watoto hawa hawana akili ila wanahitaji ufuatiliaji. Hawa watoto kumi waliofaulu wamepelekwa shule ya ufundi Moshi wanane na wanafunzi wawili wamepelekwa shule ya sekondari Mbulu. Niombe kujua, Serikali ina mpango gani na watoto hawa? Ni lini shule za sekondari za watoto wenye ulemavu zitajengwa za kutosha ili watoto wetu wapelekwe huko ambapo watapata walimu na vifaa kwa ajili ya aina ya ulemavu walio nao? Tusipofanya hivyo watoto hawa watafeli wengi na maisha yao hayatakuwa na mwisho mwema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Nami nianzie alipomalizia mwenzangu, nitaanza kuzungumzia kwenye migogoro ya mipaka kati ya hifadhi za vijiji pamoja na mapori yetu ya akiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekaji wa vigingi limekuwa ni tatizo kubwa sana kwa wananchi wetu lakini kibaya zaidi suala la ushirikishwaji halipo. Wananchi wamekuwa wakipigwa lakini cha kushangaza ni kwa nini Serikali haitaki kushirikisha wananchi. Kingine nachojiuliza ni kwamba uanzishwaji wa vijiji inashirikisha Wizara ambayo inatokana na Serikali hii. Ni kwa nini sasa wanapoanzisha vijiji wasingeshirikisha Wizara zinazohusika mfano TAMISEMI, Maliasili na Ardhi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili tatizo limekuwa kubwa sana na ni mmoja wa Wajumbe wa Kamati na naunga mkono taarifa ya Kamati yetu kwamba ni vizuri zoezi hili likasimamishwa ili utaratibu wa ushirikishwaji wa wananchi ukafanyika. Kutumia bunduki na risasi siyo suluhisho la kumaliza migogoro. Wananchi wamekuwa wakipigwa na hii imesababisha maumivu makubwa sana kwa wafugaji wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafugaji wa nchi hii wamekuwa wakilia kila siku, mifugo yao imekuwa ikiuwawa na hii inasababishwa na askari wale ambao si waaminifu wamekuwa wakiswaga mifugo na kuiingiza kwenye hifadhi zetu za Taifa. Sisemi kwamba askari wote ni wabaya lakini wapo baadhi yao hawana utu, wamekuwa wakidai rushwa kwa wananchi wetu na ukishindwa kutoa rushwa mifugo yako wanaiingiza kwenye hifadhi lakini mingine inapigwa risasi na mingine inakufa kwa kukosa matunzo. Kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri na Waziri alieleza kwenye Kamati yetu kwamba wako ng’ombe waliokamatwa na kuingizwa kwenye hifadhi na alitoa amri ng’ombe hao waachiwe lakini mpaka leo kuna baadhi ya ng’ombe hawajaachiwa. Sasa huu ni ukiukwaji wa taratibu na sheria kwa wafugaji wetu na tuelewe kabisa kwamba mifugo kwa wafugaji ndiyo maisha yao. Mifugo hiyo ndiyo wanayosomeshea watoto wao, wanalisha familia zao na hata kupata afya bora wanaotumia fedha zinazotokana na mifugo. Kwa hiyo, ni lazima tuwafanyie haki wafugaji hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamesema wenzangu nchi hii wafugaji wanalia, wakulima wanalia, wafanyabiashara wanalia usalama unatoka wapi. Kama watu wote tunalia kwa sababu ya ukiukaji wa sheria, hii siyo sawa, tumwombe Waziri ahakikishe kwamba haki inatendeka ili wananchi wetu waweze kuishi kwa amani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la wafanyabiashara ya wanyama hai. Mwaka 2016 wafanyabiashara hawa walizuiliwa kufanya biashara hii. Wafanyabiashara hawa walikuwa wamekata leseni, wamelipia ada wanazostahili kulipia lakini pia walikuwa walishatafuta usafiri wa kusafirisha wanyama hao. Likatolewa agizo la kusitisha usafirishaji wa wanyama hawa. Waziri alikuja mbele ya Kamati lakini alisema ndani ya Bunge hili kwamba mnaanza mchakato wa kuwarudishia fedha za leseni lakini pia na kupanga utaratibu mzuri wa kuweza kuwaruhusu waendelee na biashara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanyama wanaokamatwa ni wale ambao wanasumbua sana katika jamii yetu mfano, kweleakwelea, tandu, ngedere, lakini badala ya kuwashukuru wafanyabiashara hawa imekuwa ni tatizo kwako. Ni muda mrefu sasa umepita wafanyabiashara hawa walikopa fedha benki, wengine wameuziwa nyumba zao, maisha yao ni magumu sana kwa sasa. Kwa hiyo, niombe sana Wizara ichukue hatua za haraka kuhakikisha wafanyabiashara hawa wanaruhusiwa kufanya biashara hiyo ya usafirishaji wa wanyama hai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ni suala la biashara ya uwindaji. Biashara hii imeshuka na sababu za kushuka tumeelezea kwenye taarifa yetu ya Kamati ni baada ya matamko ya Mheshimiwa Waziri ambapo alisitisha biashara hii na ikasababisha vitalu vingi kurudishwa zaidi ya vitalu 18 vimerejeshwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia machache katika Wizara hii muhimu kwa afya ya Watanzania. Nianze kwa kuunga mkono hotuba ya Kambi ya Upinzani ambayo imesheheni ushauri na mambo mazuri kwa sekta yetu ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuipongeza Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete chini ya uongozi mzuri wa Profesa Janabi na pongezi hizi ziende kwa madaktari wote, wauguzi na watumishi wote wa taasisi hiyo. Taasisi hii imekuwa ikifanya kazi nzuri na imesaidia sana kupunguza gharama za matibabu nje ya nchi, lakini bado kuna mtatizo ya vitendea kazi ambavyo vitarahisisha matibabu kwa wagonjwa na hata kwa watoa huduma. Mfano, kuwa na mashine zote kwa ajili ya vipimo hapo hapo hospitali kuzuia kwenda kufanya vipimo nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, Taasisi hii imekuwa inakusanya fedha nyingi, lakini pale inapoomba tena fedha ambazo walikusanya wao hawapati. Mfano, mwaka jana waliomba bilioni nne, hawakupata wakati waliweza ku-save zaidi ya shilingi bilioni 12 za kwenda kutibu wagonjwa nje ya nchi. Nashauri Serikali itenge 30% ya mapato hayo ili kuwawezesha kuboresha huduma kwa wagonjwa na kurahisisha kazi kwa madaktari wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, udhaifu wa vipimo vya tiba katika hospitali zetu, kumekuwa na tatizo hili kwa wagonjwa kupewa majibu tofauti na maradhi waliyonayo na hii husababisha wagonjwa kutopona maradhi waliyonayo pamoja na kupewa dawa ambazo si sahihi kwa magonjwa hayo na kufanya dawa hizo kuwa sumu mwilini, badala ya kuwa tiba na hata kusababisha vifo kwa wagonjwa wetu. Wanaopona ni wale wenye uwezo wa kwenda hospitali nyingi kwa ajili ya kupima upya au kwenda nje ya nchi. Je, ni wangapi ambao hawana uwezo huo wanapoteza maisha. Nashauri Serikali kuchukua hatua kwenye suala hili ili kunusuru maisha ya Watanzania na kuhakikisha umakini unakuwepo.

Mheshimiwa Naibu Spika, uwajibikaji wa watumishi wa Sekta ya Afya; zipo taratibu na sheria zilizowekwa kwa ajili ya uwajibishaji wa watumishi wa afya, yapo Mabaraza ya Madaktari na Baraza la Wauguzi; haya ndiyo yenye jukumu la kuwawajibisha na si vinginevyo. Toka Awamu hii ya Tano imeanza tumeona viongozi wa kisiasa na wasiokuwa na mamlaka wala taaluma hiyo kuingilia kuwawajibisha Madaktari na Wauguzi pasipo kufuata taratibu. Tunajua upo upungufu unaofanwa na watumishi hao, lakini ni muhimu kufuata taratibu zilizopo. Tusipofanya hivyo tunapunguza morali wa kufanya kazi kwa watumishi hao muhimu wa sekta ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha mchango wangu huo mdogo wa sekta hii ya afya.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi. Nami niungane na wanachama wenzangu kutoa pole kwa viongozi wetu wa Chama Taifa, Wabunge, kwa wakati mgumu wanaopitia kipindi hiki, najua wako na kesi Mahakamani. Tunaendelea kuwaombea kwa Mungu awape ujasiri na dhahabu ili ing’ae ni lazima ipite kwenye moto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Jafo, kazi yako inaonekana. Nina mambo matatu. Kwanza nizungumzie issue ya Wakurugenzi, naiomba Wizara sasa ifanye tathmini kwa Wakurugenzi ambao wameteuliwa ili wale wenye sifa waweze kubaki na wale ambao hawana sifa tuweze kuwaondoa kwa sababu Wabunge wengi hapa wakichangia wameonesha mambo hayaendi kwenye Halmashauri zao. Wakurugenzi wengi waliteuliwa kisiasa. Wengi waliokosa kura za maoni walipewa kama zawadi na walioshindwa kwenye Uchaguzi Mkuu na hii imesababisha ugomvi mwingi kwenye Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko baadhi ya Halmashauri Wakurugenzi wanashindwa hata kuendesha vikao vya Mabaraza, wanaitisha vikao vya Mabaraza, lakini ikifika wakati wa vikao wanakaimisha Wakuu wa Idara na hii inasababisha maamuzi mengi kutokufikiwa kwa wakati na maendeleo ya Halmashauri hizo yanarudi nyuma. Kwa hiyo, niombe sana wafanye tathmini kwa hawa Wakurugenzi wenye sifa wabaki, wale ambao hawana sifa waondolewe. Pia tufuate utaratibu wa Utumishi wa Umma wanaotoka kwenye utumishi wa umma ndio waajiriwe katika nafasi hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili nizungumzie miradi ya maendeleo kwenye halmashauri zetu; fedha hizi zimekuwa zinachelewa na hazifiki kwa wakati na kibaya zaidi Serikali Kuu ilichukua vyanzo vile vya mapato tena vyenye fedha nyingi wakiahidi kwamba wanakusanya ili waturudishie. Kibaya zaidi fedha hazirudi kwa wakati na zikirudi ni chache, niiombe Wizara sasa kwanza itupe tathmini wakati tulipokuwa tunakusanya wenyewe kama Halmashauri na wao walipoanza kukusanya yale malengo waliyojiwekea yamefikia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hayajafikia ni vizuri sasa vyanzo hivi vya mapato vikarudishwa kwenye Halmashauri zenyewe, ziendelee kukusanya ili kuweza kutekeleza ile miradi ya maendeleo tuliyojiwekea. Serikali Kuu kwa sababu wamechukua vile vyanzo lakini fedha hawazileti. Niishauri Serikali sasa ni wakati muafaka wa kubuni vyanzo vyao vya mapato na kuacha kuchukua vyanzo vya mapato vya Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni upungufu mkubwa wa Watendaji wa Vijiji; kumekuwa na upungufu mkubwa sana, unakuta vijiji viwili, vitatu vinakaimiwa na mtu mmoja. Hili limekuwa ni tatizo kubwa sana kwa wananchi wetu kupata huduma kwa wakati. Kwa hiyo, niiombe Wizara kuhakikisha kwamba Watendaji hawa wanaajiriwa ili wananchi wetu waweze kupata huduma hizi kwa haraka pale wanapofika kwenye hizo ofisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu ofisi za Watendaji hawa, hakuna, hata za kata baadhi ya vijiji hazina ofisi hizo kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la upungufu wa Walimu. Tumekuwa na upungufu mkubwa sana wa Walimu katika Mkoa wetu wa Kilimanjaro na Jimbo la Moshi Vijijini wa shule za msingi. Hii imetokana na kuwa Walimu wengi wamefikia umri wa kustaafu. Tunaomba sana suala la walimu ajira zao zipatikane kwa wakati, pia nyumba za Walimu bado ni tatizo kubwa sana kwa Walimu wetu tuhakikishe nyumba zinajengwa na ajira ipatikane kwa haraka kwa ajili ya watoto wetu hawa ili waweze kupata elimu bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine pia yako matatizo kwa watumishi wetu, wamekuwa wakilalamika hawapati mafao yao kwa wakati, nimwombe Waziri tuhakikishe Walimu wetu tunajua wengi tumefika hapa kwa sababu ya Walimu, kwa hiyo tuhakikishe mafao yao yanapatikana kwa wakati.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuchangia machache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kupongeza hotuba zetu zote mbili za Kambi ya Upinzani. Zimeeleza mambo mengi mazuri na tunaishauri Serikali kuzingatia yale yote yaliyoelezwa na kambi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa pole kwa Wabunge wenzetu, Mheshimiwa Freeman Aikael Mbowe pamoja na Mheshimiwa Esther Matiko ambao walikaa gerezani kwa siku 104 kwa kunyimwa haki yao ya dhamana. Nimpongeze Jaji Rumanyika kwa kuweza kuona hilo na kutoa haki na hata leo wako nje kwa dhamana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumwambia Mwenyekiti wetu wa Chama, Mheshimiwa Freeman Aikael Mbowe, tunakupongeza kwa uimara wako, pamoja na yote ambayo unafanyiwa umeendelea kuwa imara na wewe ndiwe Mwenyekiti wetu…

MBUNGE FULANI: Atabaki kuwa juu.

MHE. GRACE S. KIWELU: Najua wako ambao wanaumia kwa ajili ya wewe kuwa Mwenyekiti lakini utaendelea kuwa juu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia kuhusu Tume huru ya Uchaguzi. Najua wengi watatushangaa ni kwa nini tunazungumzia Tume hii lakini kitanda usichokilalia huwezi kujua kunguni wake. Sisi tunayo maumivu tuliyoyapata kwa sababu ya Tume hii ya Uchaguzi kutokuwa huru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi ambazo mfumo wake ni wa kupata viongozi kwa mujibu wa sheria kwa kupigiwa kura, viongozi wengi wameanza kudharau wapigakura wao na tumeona wakifanya maamuzi bila kujali wanawaathiri vipi wapigakura wao. Tumefanya maamuzi mengi bila kujali waliotupa dhamana ya kutuleta humu ndani wanataka nini. Wanafanya haya kwa sababu wanajua Tume wameimiliki, si huru, wanafanya maamuzi bila kujali mawazo ya wananchi wao ambao ndiyo wamewapa dhamana ya kuwaleta humu. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie akina mama wa Kinondoni kwamba Mbunge wao hana heshima kwa akina mama ambapo mama yake amemzaa yeye na kuweza kuwa kiongozi leo. Wabunge wanawake wa CHADEMA tumechaguliwa kama walivyochaguliwa Wabunge wengine wa Viti Maalum kwa kufuata taratibu na kanuni za chama chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee, tumeshuhudia mabadiliko makubwa sana sasa hivi ya uteuzi wa Wakurugenzi wa Wilaya umeacha kufuata taaluma, taratibu na sheria zilizokuwa zinafanyika hapo awali lakini sasa hivi kigezo namba moja ni kuwa kada wa Chama cha Mapinduzi. Kibaya zaidi tunakwenda kwenye chaguzi za Serikali za Mitaa ambazo tunajua Tume haina muundo mpaka chini, wanakwenda kuchukua watu kutoka TAMISEMI, sasa kwa muundo huu ambao Awamu ya Tano umeanza nao wa kuchagua Wakurugenzi sifa zao wawe makada wa Chama cha Mapinduzi, tunawaambia mapema kwamba, kama walivyosema wenzangu jana kwamba hatutakubali kudhulumiwa, wakatende haki kwa wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua haki hii haitatendeka kwa sababu walishaonywa na Mkuu wa Nchi kuwa wasipomtangaza mgombea anayetokana na chama tawala akatafute kazi nyingine na kauli hii haijawahi kufutwa mpaka leo. Kwa maana hiyo, Wakurugenzi, Maafisa Kata ambao wako kwenye kata zetu zinazokwenda kufanya uchaguzi watakwenda kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunataka TAMISEMI ituambie hawa Maafisa Kata walioletwa pamoja na Wakurugenzi, wana haki kweli ya kuendelea kuwa wasimamizi wa uchaguzi wakati wanakwenda kufuata maelekezo ambayo walishapewa na Mkuu wa Nchi? Ndiyo maana tunaendelea kulalamika na kusema kwamba Tume hii si huru tunataka Tume huru itakayozingatia haki za wapigakura. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona uhuni uliofanyika kwenye chaguzi za marudio, watu wamepora maboksi na kwenda kujaza kura na kurudisha kwenye vituo wakisaidiwa na Polisi. Pia tumeona kwenye vituo vya kupigia kura, mawakala tuko ndani tunaheshabu kura lakini Mapolisi wanabandika matokeo nje, wanaingia kuchukua maboksi ya kura. Halafu mnatuambia hii ni Tume huru, kwa kweli Kambi ya Upinzani na wapinzani wote bado tunaendelea kudai Tume huru ya Uchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la ma- DC na Wakuu wa Mikoa. Mimi ninatoka Mkoa wa Kilimanjaro, sina tatizo na Mkuu wangu wa Mkoa, anafanya kazi zake vizuri, anatimiza wajibu wake kuleta maendeleo kwa wananchi wake. Nina tatizo na Mkuu wa Wilaya ya Hai, DC Sabaya. Huyu kabla ya uteuzi wake alikuwa Diwani Kata ya Sambasha, Halmashauri ya Arusha DC, kwa Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, DC huyu ameletwa Wilaya ya Hai, anasema anakuja kupambana na Mheshimiwa Mbowe. Namwambia hana ubavu wa kupambana na Mheshimiwa Mbowe. Amekuwa akiingilia shughuli za vyama vya siasa, pia mmeona akiwa anawabughudhi wawekezaji. Tunajua Ma-DC na Wakuu wa Mikoa ni wanasiasa, lakini tunajua ziko sheria na taratibu zilizowekwa kwa ajili ya kuwawesha kufanya kazi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Sabaya amekuwa akikamata viongozi wetu wa chama kuzuia wasifanye vikao, tuna chaguzi zinaendelea chini za chama, Mheshimiwa Sabaya hataki vikao vifanyike, lakini amekuwa akimsumbua Mwenyekiti wa Halmashauri kwa kumbambikizia tuhuma za uongo. Nampongeza Mwenyekiti wa Halmashauri, ni mwanamke na yuko imara kweli kweli. Amekuwa akiwalazimisha Wenyeviti wetu wa Vijiji na Vitongoji kusaini barua za kujiuzulu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii siyo haki na siyo kazi aliyotumwa kufanya Hai. Ametumwa akashirikiane na wananchi wa Hai kuleta maenendeleo na siyo vinginevyo. Kama ni mwanasiasa, kwanza atekeleze kazi zake, akimaliza ndiyo akafanye siasa ya chama chake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la kushuka kwa mapato kwa Halmashauri zetu. Halmashauri nyingi nchini zimeshindwa kukusanya mapato kutokana na vyanzo vingi vikubwa vya mapato kuchukuliwa na Serikali Kuu. Hii imesababisha Halmashauri zetu kushindwa kuleta maendeleo na ile mipango waliyokuwa wamepanga kushindwa kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naitaka Serikali, yale mapato ambayo waliyokuwa wanakusanya, ni wakati muafaka sasa kurudisha kwenye Hamashauri zetu ili ziweze kujiendesha, kwa sababu kutakuwa hakuna maana kuanzisha Halmashauri ambazo zinashindwa kujiendesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo madogo madogo ambayo yalikuwa yanafanywa kutokana na hayo mapato ya ndani ikiwemo ujenzi wa vyoo, kulipa bill za maji na umeme, lakini yameshindwa kufanyika mpaka sasa. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)