Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula (19 total)

MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-
Je, Serikali haioni umuhimu wa kumaliza ujenzi wa nyumba za kambi ya Polisi Mabatini zilizoanza kujengwa tangu mwaka 2012 na sasa zinazidi kuwa magofu ili zisaidie hizo familia chache zipatazo 13?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing‟oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nyumba za kambi ya Polisi Mabatini zilianza kujengwa mwaka 2012. Kutokana na ufinyu wa bajeti nyumba hizo hazikuweza kukamilika kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetenga fedha katika mwaka wa Fedha 2016/2017 ili kukamilisha ujenzi wa nyumba hizo.
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-
Jimbo la Nyamagana ni jimbo pekee lililochangia mradi wa ujenzi wa nyasi bandia kupitia TFF shilingi 160,000,000.
Je, ni lini Serikali itawasisitiza TFF kuhakikisha kuwa uwanja huu unakamilika kwa wakati na kuendeleza malengo yaliyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing‟oma Mabula, Mbunge wa Nyamangana kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, uboreshaji wa uwanja wa Nyamagana wa kuweka nyasi bandia ulianza mwaka 2014 ukiwa na thamani ya dola za Kimarekani 737,886 sawa na shilingi za Kitanzania 1,193,161,662. Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) lilitoa msaada kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kiasi cha dola za Kimarekani 618,946 sawa na shilingi za Kitanzania 1,000,835,682 na Halmashauri ya Nyamangana ilichangia dola za Kimarekani 118,943 sawa na shilingi za Kitanzania 192,330,831.
Mheshimiwa Naibu Spika, nyasi hizo bandia zimegharimu tozo kiasi cha dola za Kimarekani 100,121.93, sawa na shilingi za Kitanzania 220,268,400 ikujumuisha import duty na VAT. TFF kama msimamizi wa mpira wa miguu kwa niaba ya Halmashauri ya Nyamangana na Serikali, wameshughulikia mchakato wa kutoa msamaha wa tozo hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nyasi bandi tayari zimewasili Dar es Salaam tangu tarehe 17 Aprili, 2016. Baadhi ya vifaa tayari vimeshafika katika Uwanja wa Nyamagana na mkandarasi amekwishaanza kazi ya ukarabati wa uwanja huo. TFF sasa wako katika mchakato wa kumalizia kusafirisha vifaa vilivyobaki.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ukweli kwamba ukarabati wa uwanja wa Nyamagana kuufanya uwe wa nyasi bandia unahitaji umakini mkubwa ili uwe mzuri, imara na wenye hadhi ya Kimataifa ni lazima mkandarasi ahakikishe kuwa ubora wa viwango vinazingatiwa. Kwa vile mpango wa ukarabati huo ulitakiwa ukamilike mwishoni mwa mwezi huu, natoa wito kwa mkadarasi huyo kuhakikisha kwamba ukarabati huo unakamilika haraka iwezekanavyo ili uweze kutumika.
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-
Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu aliahidi ujenzi wa barabara ya lami kutoka Igoma – Kishiri – Kanindo kupitia Kata za Lwanhima na Bulongwa.
Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza kutekelezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Igoma – Kishiri – Kanindo ina urefu wa kilometa 15 ikiwa ni mzunguko kupitia Kata za Igoma, Lwanhima na Buhongwa katika Jiji la Mwanza. Ili kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais, Serikali imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali katika bajeti ijayo ya mwaka 2017/2018 ikiwa ni hatua muhimu katika kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua hiyo itawezesha Serikali kujua gharama za mradi na kutenga bajeti kwa ajili ya kuanza ujenzi. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa ahadi hii ya Mheshimiwa Rais itatekelezwa kama ilivyoahidiwa.
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-
Fedha zinazotengwa na Halmashauri kutokana na mapato ya ndani; asilimia 10 ya fedha hizo zinatakiwa kwenda kwa vijana na wanawake na zinatakiwa ziwafikie walengwa kila mwaka bila kukosa.
Je, Serikali iko tayari kutoa agizo la msisitizo kwa Halmashauri zote nchini kutenga fedha hizo na wala wasichukulie kama ni hisani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Halmashauri zote zinatakiwa kutekeleza agizo la kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya Mfuko wa Vijana na Wanawake. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri zilitengewa jumla ya shilingi bilioni 56.8 ambapo hadi Machi, 2017 kiasi kilichopelekwa kwenye mifuko kilikuwa ni shilingi bilioni 16.05. Halmashauri ya Jiji la Mwanza pekee imeshapeleka shilingi milioni 147.0.
Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa Halmashauri zote nchini kuanza kutenga maeneo rafiki ya kufanyia biashara kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo wadogo, kupeleka fedha kwenye mifuko na kusimamia marejesho ili ziweze kunufaisha makundi mengine. Utekelezaji wa maagizo haya ya Serikali ni kipimo cha utendaji kwa Wakurugenzi wote nchini na kushindwa kutekeleza, sio vyema kabisa. Aidha, hatua zitachukuliwa kwa kuzingatia taratibu zilizopo.
STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-
Rais wa Awamu ya Nne alipofanya ziara katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana mwaka 2014 aliahidi kupatia x-ray.
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo ya Rais hasa ikizingatiwa kuwa hospitali hiyo kwa sasa haina kifaa hata kimoja katika kitengo cha mionzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ahadi hiyo ilitolewa na Mheshimiwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne mwaka 2014 wakati wa ufunguzi wa jengo la upasuaji katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana. Katika mwaka wa fedha 2017/ 2018, Serikali imetenga jumla ya shilingi 133,136,000 kwa ajili ya kununua mashine ya x-ray mpya ikiwa ni utekelezaji wa ahadi hiy iliyotolewa na Mheshimiwa Rais inayolenga kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-
Tatizo la watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu linaendelea kuwa kubwa.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto hii kubwa hasa katika Jiji la Mwanza?
(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kukijengea uwezo Kitengo cha Ustawi wa Jamii kukabiliana na changamoto hii?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kabla sijajibu swali hili la msingi kwanza nikushukuru sana na kukupongeza na wewe kwa kushirikiana pamoja na Serikali katika kuhakikisha kwamba tunarudisha ule uzuri wa asili, nakushukuru na kukupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009, kifungu cha 16, msamiati unaotumika katika kubainisha watoto hao ni watoto walio katika mazingira hatarishi na si watoto wanaoishi katika mazingira magumu. Katika kukabiliana na changamoto hii, Serikali inatekeleza Mpango wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto wa mwaka 2017/2018 ambao utaisha 2021/2022, ambapo umebainisha majukumu mbalimbali ya wadau katika kuondoa changamoto hiyo. Moja ya shabaha ya mpango huo ni kupunguza idadi ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2021/2022 ikiwemo katika Jiji la Mwanza.
Mheshimiwa Spika, katika kupambana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto, Jiji la Mwanza limeunda kamati 11 za ulinzi na usalama kwa wanawake na watoto katika mitaa 11; makao ya watoto manne yamesajiliwa; jumla ya watoto walio katika mazingira magumu (hatarishi) 5,843 walibainishwa, wakike wakiwa 3,337 na wanaume, 2,506. Kati ya watoto hao, jumla ya watoto 2,381 walitengenezewa kadi za bima ya TIKA, watoto 27 walipelekwa katika Vyuo vya VETA na watoto 741 wanasomeshwa katika shule za sekondari. Aidha, zoezi la utambuzi wa watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani katika kata zote 18 umefanyika mwaka 2018. Jumla ya watoto 426 wanawake wakiwa ni 21 na wanaume 405 walitambuliwa. Kati yao watoto 135 walipelekwa kwenye makao ya watoto ya muda, watoto 120 waliunganishwa na familia zao, watoto 165 walirejeshwa kuendelea na masomo na watoto 323 walipata huduma za matibabu.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kuona umuhimu wa huduma za ustawi wa jamii, imeanzisha Kitengo cha Ustawi wa Jamii katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI, lengo likiwa ni kuboresha huduma hizi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, Serikali imeendelea kuwajengea uwezo Maafisa Ustawi wa Jamii katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na ulinzi na usalama wa mtoto, haki za mtoto na uendeshaji wa mashauri ya watoto. Serikali pia imeimarisha mipango ya bajeti katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuanzisha kifungu cha malipo (cost center) na kuingiza huduma za ustawi wa jamii katika mfumo ulioboreshwa wa mipango na bajeti katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa (Improved Plan Rep.). (Makofi)
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-
Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Nyamagana linalojengwa katika Kata ya Mkolani limechukua zaidi ya
miaka minne sasa bila kukamilika:-
(a) Je, Serikali haioni kuwa na miradi isiyokamilika kwa wakati kunarudisha nyuma maendeleo;
(b) Je, ni lini sasa Serikali itapeleka fedha za kukamilsha jengo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana, lenye vipengele (a) na (b), kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba ujenzi wa jengo la Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana ulioanza mwaka wa fedha 2008/2009 umechukua muda mrefu. Sababu kubwa ya kuchelewa kukamilika kwa ujenzi huo ni changamoto ya upatikanaji wa fedha za ruzuku ya maendeleo. Hadi sasa kiasi cha shilingi bilioni 1.34 kati ya shilingi bilioni 1.84 zilizokuwa zinahitajika zimetolewa na kutumika katika kujenga boma lenye vyumba 23 vya ofisi, kumbi mbili, mgahawa, chumba cha kuhifadhia nyaraka, vyoo, kuezeka jengo lote, kupiga plasta, kuweka milango, vigae, kupaka rangi, kuweka dari, kufunga milango na madirisha na mfumo wa maji safi na maji taka.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa kumaliza jengo hilo, jumla ya shilingi milioni 420 zimetengwa katika mwaka wa fedha 2018/2019 ili kumalizia mfumo wa usalama wa jengo ikiwemo zimamoto, mfumo wa umeme, tanki la maji na uzio. Kwa maana hiyo, ujenzi wa jengo hilo unatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha 2018/2019.
MHE. RASHID A. SHANGAZI (K.n.y. MHE. STANSLAUS S. MABULA) aliuliza:-

Serikali kupitia Mamlaka ya TCRA wamefungia Local Channels kuonekana kwenye baadhi ya ving’amuzi hapa nchini, mfano Azam Tv, DSTV na vinginevyo.

(a) Je, Serikali haioni kwa kufanya hivyo imewanyima wananchi fursa ya kujua mambo yanayoendelea kwenye Taifa lao?

(b) Je, ni lini Serikali itatoa muafaka wa jambo hili?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana, lenye Sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa wananchi kupata fursa ya kujua mambo yanayoendelea kwenye Taifa. Kwa misingi hiyo, imetoa leseni zenye masharti tofauti ikiwemo leseni ya public, yaani utangazaji wa umma ambapo matangazo huruhusiwa kurushwa kwa watoa huduma wenye must carry. Hivi sasa matangazo ya umma ni TBC 1 na TBC 3 maarufu kama Safari Channel.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha makampuni yanayomiliki visimbusi au ving’amuzi vya DSTV, Zuku na Azam hayakustahili kutoa huduma ya kubeba channel za ndani zisizolipiwa, yaani free to air local channels, kutokana na masharti ya leseni zao. Utoaji wa huduma za maudhui kupitia visimbusi vyao uko kwenye mfumo wa kukidhi soko la kimataifa na maudhui yake kuwa ya kulipia. Masharti ya leseni hizo na mfumo mzima wa miundombinu ya utangazaji husika yamelenga soko la kimataifa na hutofautiana na masharti ya leseni za watoa huduma za maudhui ya ndani ya nchi. Kuruhusu channels za ndani kuoneshwa kwa kutumia leseni za matangazo ya kimataifa kutazifanya free to air local channels kuwa za kulipia badala ya kuonekana bure.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TCRA imefanya jitihada ikiwa ni pamoja na kukaribisha maombi ya leseni ya kubeba maudhui ya channels za ndani, yaani multiplex operator, kutoka kwa wanaohitaji kutoa huduma yakiwemo makampuni ya Azam, DSTV na Zuku ili yaweze kupata leseni stahiki na kuweza kutoa huduma za kubeba au kuonesha maudhui ya ndani kupitia visimbusi vyao. Kwa sasa TCRA inashughulikia maombi yaliyopokelewa ili iweze kushauri kuhusu utoaji wa leseni stahiki.
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-

Serikali imeruhusu urasimishaji wa makazi katika maeneo mbalimbali Nchini ikiwemo Jiji la Mwanza isipokuwa maeneo ya Kata ya Isamilo, Mbugani, Mabatini na Igogo.

Je, ni lini Serikali itawamilikisha wananchi hawa maeneo yao kwa kuwa wameishi katika maeneo haya kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendele ya Makazi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na zoezi la urasimishaji wa makaziyasiyopangwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni utekelezaji wa kifungu namba6.4.1(iii) cha Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 ambacho kinatamka kwamba;

“Maeneo ya makazi holela isipokuwa yale yaliyojengwa kwenye maeneo ya hatarishi hayatabomolewa bali yataboreshwa na kuwekewa huduma za msingi”.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Jiji la Mwanza urasimishaji wa makazi unafanyika katika kata mbalimbali zikiwemo Kata za Isamilo na Mbugani. Katika Kata ya Isamilo urasimishaji umefanyika katika Mitaa ya Msikiti, SDA pamoja na National ambapo michoro ya mipangomiji miwili yenye jumla ya viwanja 3,444 imeandaliwa, viwanja 560 vimepimwa na viwanja 101 tayari vimemilikishwa. Aidha, Katika Kata ya Mbugani urasimishaji umefanyika katika Mitaa ya Nyashana na Kasulu ambapo michoro miwili ya mipangomiji yenye jumla ya viwanja 1001 iliandaliwa na viwanja 395 vimepimwa na vipo katika hatua ya umilikishaji.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kufanyika urasimishaji katika mitaa hiyo, maeneo mengine ya kata za Isamilo, Mbugani, Igogo na Mabatini hayajafanyiwa urasimishaji wa makazi kutokana na sehemu kubwa ya maeneo hayo kuwa hatarishi; ambayo yapo kwenye milima yenye miteremko mikali zaidi ya asilimia 15. Hivyo maeneo hayo hayakidhi vigezo vya kurasimishwa kwa kuwa ni hatarishi kwa maisha ya wananchi na mali zao pamoja na ugumu wa kuyafikika kwa barabara.

Mheshimiwa Spika, Mpango Kabambe wa Jiji la Mwanza 2015/2035 umeainishabaadhi ya maeneo ya Kata za Mbugani, Isamilo, Pamba, Nyamagana, Mkuyuni na Igogo kuwa ni maeneo yanayotakiwa kuendelezwa upya (redevelopment) kwa kuzingatia hali halisi ya miinuko na ujenzi hatarishi uliofanyika. Kwa sasa wamiliki wamakazi hayo watatambuliwa na kupatiwa leseni za makazi (formalization)wakati wakisubiri uendelezwaji mpya wa maeneo hayo.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI (K.n.y MHE. STANSLAUS S. MABULA) aliuliza:-

Magari mengi ya Serikali yanafanyiwa service kwenye gereji kubwa hapa nchini hii imekuwa tofauti kwa magari yanayomilikiwa na Jeshi la Polisi:-

Je, Serikali haioni kuwa upo umuhimu wa kuwa na maeneo ya kutengeneza na kurekebisha magari ya Polisi ili kuliimarishia vitendea kazi.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana kama ifutavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi linayo karakana kuu ya kutengeneza na kurekebisha magari yake iliyopo barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam. Karakana hii ina matawi katika kila Mkoa nchini nzima, matawi hayo kufanya kazi kwa utaratibu wa Jeshi la Polisi chini ya Komandi ya karakana kuu iliyopo Dar es Salaam ambako kuna mafundi wenye ujuzi mkubwa. Aidha, Jeshi la Polisi kupitia makubaliano ya kimkataba kuna baadhi ya magari ya Jeshi la Polisi hutengenezwa katika karakana za wazabuni waliokubaliana baada ya kupata kibali cha TEMESA.
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Kinyata kwa njia nne kutoka Mwanza Jiji kuelekea Usagara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ya Nyamagana – Usagara ni sehemu ya barabara Kuu ya Mwanza – Shinyanga Mpakani yenye urefu wa kilometa 104. Barabara hii ni muhimu katika kukuza uchumi wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa na ni kiunganishi kati ya Mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Mara, Geita na nchi jirani.

Mheshimiwa Spika, Serikali tayari imeanza mipango ya kuanza ujenzi wa barabara ya Mwanza hadi Usagara kwa njia nne. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii unaendelea ambapo umezingatia kupanua barabara hii kuwa na njia nne kuanzia Mwanza Mjini hadi Usagara yenye urefu wa km 22. Kazi hii inafanywa na Mhandisi Mshauri M/s NIMETA Consult (T) Ltd ya Tanzania kwa gharama ya Shilingi Milioni 980.84. Aidha, usanifu wa kina unatarajiwa kukamilika Septemba, 2021 na baada ya kukamilika barabara hiyo itaingizwa kwenye mpango wa ujenzi ikiwa ni pamoja na upanuzi wa njia hizo nne kutoka Mwanza Jiji hadi Usagara kutegemea na upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-

Je, ni lini serikali itakuwa tayari kuanza mradi wa TACTIC ili kufikia Malengo Makuu ya Serikali ya mwaka 2020 – 2025 katika kuboresha miundombinu ya barabara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Uendelezaji Miundombinu katika Miji (TACTIC) unatarajiwa kutekelezwa katika Halmashauri za Miji 45 nchini. Mradi unatarajiwa kutekelezwa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa fedha za mkopo wenye masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia. Serikali inaendelea na mazungumzo na Benki ya Dunia kuhusu upatikanaji wa fedha hizo na mradi utaanza kutekelezwa baada ya kukamilika kwa majadiliano na fedha kutolewa.
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutimiza masharti ya ajira kwa watumishi ikiwa ni pamoja na kuwapandisha madaraja na stahiki nyingine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutimiza masharti ya ajira kwa watumishi wake ikiwemo kupandisha vyeo Watumishi, ambapo Serikali ilitoa barua Kumb. Na. BC.46/97/03D/59 ya tarehe 28 Aprili, 2021 iliyoruhusu upandishwaji vyeo kwa Watumishi wa Umma kuanzia tarehe 1 Juni, 2021. Hadi kufikia tarehe 1 Septemba, 2021, jumla ya Watumishi wa Umma 174,222 wamepandishwa vyeo na kubadilishiwa mishahara yao.

Aidha, Serikali itaendelea kuboresha maslahi kwa watumishi wa umma kadri bajeti itakavyoruhusu.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaainisha bei rasmi za kuunganisha umeme maeneo ya kata za mjini zenye sura za vijiji?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na zoezi la utambuzi wa maeneo na wananchi wanaoishi katika maeneo ya Kata za Mjini zenye sura za vijiji.

Mheshimiwa Spika, zoezi hili linatarajiwa kukamilika mnamo mwezi Desemba, 2022 na baada ya zoezi hili Serikali itapanga bei muafaka za kuunganisha umeme kulingana na uhalisia wa maeneo husika.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara kuu ya Mwanza - Shinyanga kwa kiwango cha njia nne kutoka Mwanza Mjini hadi Usagara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza maandalizi kwa ajili ya ukarabati wa barabara kuu ya Mwanza, Shinyanga, yenye urefu wa kilometa 104 ambao utahusisha na upanuzi wa barabara kutoka njia mbili kuwa njia nne kwa sehemu ya kutoka Mwanza Mjini hadi Usagara, kilometa 25. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa barabara hii iko katika hatua za mwisho na inatarajiwa kukamilika tarehe 27 Aprili, 2022.

Mheshimiwa Spika, baada ya usanifu wa kina kukamilika na gharama za ukarabati kujulikana, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ukarabati utakaohusisha upanuzi wa sehemu ya kutoka Mwanza Mjini hadi Usagara, kilometa 25 kutoka njia mbili kuwa njia nne. Ahsante.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutimiza masharti ya ajira kwa Watumishi ikiwemo kuwapandisha madaraja na stahiki zingine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutekeleza matakwa ya kisera, kisheria na miongozo mbalimbali ya kiutawala na kiutumishi inayolenga au inayoelekeza Serikali katika kumtimizia masharti na haki za mtumishi wake. Aidha katika kufanya hivyo Serikali imeendelea na Utaratibu wa kupandisha madaraja watumishi ikiwemo utaratibu wa mpandisho wa mserereko. Pamoja na hilo Serikali imeendelea pia kuongeza kima cha chini cha mshahara na pia kuongeza allowance katika kazi za ziada na posho za muda wa ziada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na hilo pia mwaka 2021/2022, Serikali ililipa shilingi bilioni 124.3 kwa watumishi 75,007 ikiwa ni malimbikizo (arrears) ya mishahara. Vilevile, Serikali iliongeza umri wa watoto wa watumishi wa umma kunufaika na huduma ya bima kutoka miaka 18 hadi miaka 21 ambapo katika kipindi cha mwaka mmoja jumla ya watoto 65,353 wamesajiliwa.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI K.n.y. MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga barabara ya Mkuyuni hadi Mahandu kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing'oma Mabula, Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Mkuyuni hadi Mahandu ina urefu wa kilometa 10.5. Serikali imekamilisha usanifu kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami ambapo kiasi cha shilingi bilioni 20 zinahitajika. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali ilitenga shilingi billioni 5.36 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya urefu wa kilometa 5.04 kiwango cha lami; kilometa 1.725 kiwango cha zege; kilometa 1.8 kiwango cha changarawe; na kilometa 0.7 kiwango cha mawe.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali imetenga shilingi bilioni 3.42 kwa ajili ya ujenzi wa barabara kilometa 2.2 kiwango cha lami; kilometa 1.0 kiwango cha zege; kilometa 6.29 kwa kiwango cha changarawe; na kilometa 2.0 kiwango cha mawe.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuweka kwenye mpango Barabara ya Mkuyuni hadi Mahandu na barabara nyingine katika Jimbo la Nyamagana kwa kutenga bajeti kwa ajili wa ujenzi na matengenezo ya barabara hizo, ahsante. (Makofi)
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA K.n.y. MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza: -

Je, Serikali haioni kutoa fedha za ujenzi wa vituo vya afya kwa kigezo cha idadi ya tarafa ni kuwanyima wananchi vituo vya afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kati ya tarafa 570 zilizopo 211 hazikuwa na kituo cha afya hata kimoja, hivyo Serikali ilitoa kipaumbele cha ujenzi wa vituo vya afya kwenye tarafa ambazo hazina kituo cha afya. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali ilijenga vituo vya afya 234. Kipaumbele cha ujenzi kilizingatia tarafa ambazo kata zake hazikua na kituo cha afya. Aidha, ujenzi wa kituo cha afya ulizingatia kata za kimkakati.
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza: -

Je, ni lini ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa barabara ya Mkuyuni hadi Mhandu itatekelezwa?

NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imeanza kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina barabara ya Mkuyuni hadi Mhandu ili kuijenga kwa kiwango cha lami. Kazi hii ilianza tarehe 6 Juni, 2021 na inatarajiwa kukamilika Julai, 2022. Aidha, baada ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kukamilika, Serikali itatafuta fedha ili kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami. Ahsante.