Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Gimbi Dotto Masaba (23 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Wizara ya Mazingira na Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, naomba niwape pole wananchi wa Wilaya ya Itilima kwa kupatwa na msiba wa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji uliotokea hivi karibuni kwa kuvamiwa nyumbani kwake na kupigwa hadi kuuawa. Nawapa pole sana na ni pole kwa Chama. Pia nichukue nafasi hii kukishukuru Chama changu ambacho kimeona umuhimu wa mimi kuwa Mwakilishi wa Mkoa wa Simiyu hasa kwa upande wa UKAWA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niende moja kwa moja kwenye Wizara ya Mazingira. Tunapozungumza suala la mazingira kwa uhalisia ni kwamba tunapaswa kuzungumza kwa mapana zaidi kwa sababu wananchi tulio wengi tumekuwa tukiamini kabisa kwamba mazingira ni kufagia tu. Naamini mazingira tunapaswa kuyatafakari kwa upana zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimemsikiliza Mheshimiwa Waziri wakati anawasilisha taarifa yake, anasema anatarajia kuifanya nchi kuwa ya kijani. Sina hakika kama anaweza kuifanya nchi ya kijani ilihali hawaoneshi u-seriuos wa kubadilisha mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hayo kwa sababu, ukiangalia katika bajeti ambayo imetengwa kwa ajili ya kuboresha mazingira, haikidhi kile ambacho wanakizungumza. Tumejifunza pia kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016, fedha iliyokuwa imetolewa pale ya mazingira ni kama shilingi 3.8 bilioni, lakini mpaka mwezi Machi, Wizara ilikuwa imepokea shilingi milioni 338 jambo ambalo linaonesha wazi kwamba hata ile fedha kidogo haitoki kwa wakati na kama ilitoka mwezi Machi tarehe 31, maana yake hata ile mipango iliyopangwa kwa mwaka wa fedha uliopita haijafanya kazi. Kwa hiyo, hata tukisema kwamba bajeti bado haikidhi, bado Serikali haitoi fedha kwa wakati. Nashauri kama kweli tunataka kufanya mabadiliko ya mazingira na Rais amefuta sherehe ya Muungano akimaanisha kwamba tuwe na nguvu ya mazingira Serikali itoe fedha hizo kwa wakati ili tuweze kuimarisha mazingira yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Nne, ilitoa kauli kwamba wafugaji wafuge ng‟ombe kisasa kwa maana ya kwamba ng‟ombe wanaleta uharibifu wa mazingira jambo ambalo siyo kweli. Nilidhani kwamba badala ya Serikali kutamka wazi kwamba wafugaji wapunguze ng‟ombe, ni vema basi ingeweza kutamka kwamba Mkoa wa Dar es salaam uanze kupunguza magari kwa sababu unaonesha wazi kabisa kwamba ni uharibifu wa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, isitoshe kusema hivyo, badala ya kuwaambia wafugaji wapunguze ng‟ombe, Serikali ijipange kwenda kutoa elimu kwa hawa Wasukuma na wafugaji wengine wa mikoa mingine, badala ya kuwaambia wapunguze ng‟ombe, watoe elimu ya kuwafanya watengeneze biogas kama issue ni kwamba kinyesi cha ng‟ombe ndiyo kinacholeta uharibifu wa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuimarisha mazingira, bado minada yetu kwenye mikoa inafanya biashara, minada yote haina uzio, nashindwa kufahamu kwamba ni mazingira yapi ambayo tunayaboresha wakati minada tunayoiendesha tunathamini kukusanya ushuru badala ya kuimarisha minada ambayo haina uzio, haijulikani kinyesi cha ng‟ombe ni kipi na kinyesi cha mwanadamu ni kipi. Siyo hivyo tu bado minada hii haina vyoo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali, tusizungumze mikakati ya kwenye makaratasi, hii mikakati ya kwenye makaratasi imepitwa na wakati. Waziri anasema anakwenda kuifanya nchi ya kijani, nataka anieleze kwamba nchi yetu inatumia usafiri wa meli, wasafiri wote wa meli naamini kabisa wanajisaidia kwenye bahari zetu, sasa nataka alieleze Bunge kwamba hivyo vinyesi vyote vinavyodondokea na mikojo yote kwenye bahari vinaenda wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatujui hivyo vinyesi vinakwenda wapi na baadaye Wabunge tunakuja hapa tunasimama, tunasifia, tunasema namshukuru Waziri wa Maji ameniboreshea kwenye Jimbo langu maji safi na salama, wakati hujui yale maji kama kweli ni salama. Sasa tunataka kujua vile vinyesi vinakwenda wapi na ile mitambo inatumikaje? Naomba kufahamu katika hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kidogo kwenye suala la Muungano. Nina imani kabisa kwa sasa inavyoonekana, kama Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hauko hai. Nasema kwa sababu kwa sasa Zanzibar kwanza ina bendera yake, ina wimbo wake na mbaya zaidi bajeti ya Zanzibar haiji huku Bara. Naishauri Serikali kama inaamini kabisa kwamba Muungano ni salama, niiombe Serikali hii ipitishe maoni, tuone wangapi wanahitaji Mheshimiwa Mwenyekiti, sisomi nina akili. Mimi nilichojifunza humu Bungeni ukiona sindano inaingia utamsikia Mheshimiwa anatetea na hasa suala likitajwa jina la Rais, nashindwa kufahamu kwamba anatetea kwa misingi ipi, yeye ni Waziri hatakiwi kuonyesha itikadi yoyote. Lakini pia najua…….
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kwamba Muungano siyo salama mpaka sasa hivi. Imeonesha wazi pia kwamba, Wazanzibari waliamua kuchagua Rais wao, lakini kwa sababu Serikali ya Chama cha Mapinduzi ina mabomu, ina silaha, imeamua kupora ushindi waziwazi...
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo mchango wangu kwa leo. Ahsante sana
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii, lakini awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu na mimi kwa kunipa nafasi hii kuweza kusimama katika Bunge lako hili ambalo naamini kabisa kwamba tuko katika Bunge la mwisho kwa kipindi hiki na mkataba wetu unakwenda kuisha wa miaka mitano.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, naomba nitumie nafasi hii kumpongeza Mwenyekiti wa Chama cha Upinzani Kikuu hapa Nchini kwa kuchaguliwa kwa mara nyingine kuongoza Chama hiki kwa umakini mzuri sana. Pia nimshukuru yeye pamoja na timu yake kuhakikisha kwamba yote yale ambayo yalikuwa yanapita katika nyuso zao, nawashukuru na kuwapongeza kwamba wameweza kuyashinda yote. Mungu awasimamie, tunaendelea kuwaombea, naamini katika harakati za kutafuta Dola yote hayo lazima tuyapitie.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikiliza hotuba ya Waziri wa TAMISEMI; katika hotuba yake mambo mengi yamejikita sana kwenye kuboresha mambo mazuri, hakuna sehemu ambayo amezungumzia changamoto. Sasa nilikuwa najaribu kupata masikitiko pamoja na kwamba amezungumza kuhusu Halmashauri, makusanyo, mapato na mengine, lakini sikuona popote alikozungumza kwamba Halamshauri zetu ziko taabani. Leo nakwenda kuzungumza kwa mara ya mwisho kutetea Halmashauri hususani Halmashauri ninazotoka mimi. Kwa kweli inaleta masikitiko makubwa sana na nikirejea kauli ya Spika wakati juzi anabariki hotuba ya Waziri wakati anahitimisha Waziri Mkuu alisema; “ifikapo tarehe 30 Juni atahakikisha malipo ya Wabunge yote yako tayari”.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninasikitika kusema Mheshimiwa Jafo anapenda kufunga Halmashauri zake zikiwa zinaongoza kwa madeni makubwa kwenye Halmashauri zake kwa Madiwani kudai posho nyingi. Sasa sijajua wakati anahitimisha hotuba yake, nataka kusikia ni kauli gani ambayo ataitoa kuhusu madai ya Madiwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na Halmashauri ninayotoka Wilaya ya Itilima; Madiwani mpaka sasa hivi wanadai posho milioni 502. Madeni ya Benki hayalipiki, fedha za Bima hazilipiki, Madiwani hawawezi kutibiwa na Bima zao hakuna malipo yanayofanyika. Sasa ni ishara tosha kwamba Mheshimiwa Jafo anaongoza idadi kubwa ya Watanzania waishio bila furaha yoyote katika Taifa hili. Haiwezekani Diwani akaitwa Diwani hana chochote, madai ya kuanzia Mwaka 2016 mpaka leo ninavyoongea madeni ni makubwa, ni makubwa. Sasa sijui tunakwenda wapi.

MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Masaba kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mwanne Mchemba.

MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa mchangiaji; ni kwamba juzi tu tumetoka kumaliza kukagua hesabu za mikoa yote na halmashauri zote nchi nzima. Kamati yangu asilimia 96 ya madeni ya Waheshimiwa Madiwani wamekamilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kumpa taarifa. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gimbi Dotto Masaba umeipokea taarifa hiyo?

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei na ndiyo maana sikutaka kurejea kwenye halmashauri yoyote, zaidi ya halmashauri ninayoingia mimi, umenielewa? Kwa hiyo nimeongea hivyo nikiwa na uhakika na ukitaka documents za madai naweza kukabidhi kwenye meza yako. Hili jambo siyo ndiyo naanza kuliongea, nilishamfuata Naibu Waziri zaidi ya mara moja.

MHE. DKT. SAADA MKUYA. SALUM: Taarifa

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Masaba kuna taarifa nyingine kutoka kwa Mheshimiwa Saada Mkuya Salum.

MHE. DKT. SAADA MKUYA SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Tunamsikia mzungumzaji anavyosema na Makamu Mwenyekiti ambaye tuko Kamati moja ameelezea situation ilivyo. Sasa ikiwa anachukua sehemu ndogo ya jambo lililokuwepo halafu analitapakanya inaonekana ndiyo situation ilivyo huo ni upotoshaji. Kwa hivyo, tunaomba wakati anachangia aji-confine katika sehemu ambayo yeye yupo na aweke specific area ya kile anachokizungumza kwa sababu sisi tuko kwenye Kamati na situation iko vizuri kama ambavyo Makamu Mwenyekiti ameelezea. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gimbi Dotto Masaba uneipokea taarifa hiyo?

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei. Itilima siyo Zanzibar, kwa hiyo mimi nazungumza hapa kama Mwakilishi wa Itilima

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge tusikilizane kidogo, Waheshimiwa Wabunge tusikilizane kidogo. Naomba make, lakini Mheshimiwa Gimbi Masaba Wabunge wote humu ndani ni Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo nadhani hilo tulimalize kwa namna hiyo, kwa hiyo wewe endelea na mchango wako lakini Mheshimiwa Saada Mkuya Salum ni Mbunge wa Bunge hili kama wewe, kama Mbunge mwingine yoyote.

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani ninachokizungumza Kiti chako kinanielewa vizuri sana. Sauti niliyosimama hapa ndiyo sauti ya ninapotoka, sasa nisipozungumza matatizo ya maeneo niliyotoka nani azungumze? Mimi ndiyo Mwakilishi yeye kama ana mambo mazuri kule aendelee, naomba niendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Waziri nimepitia kwa ufupi kabisa, lakini sikuona mahali popote ambapo kuna ugatuzi wa Majimbo au Mamlaka ya Miji Midogo, sijaona popote pale. Hii ndiyo bajeti ya mwisho, tulitarajia hivi vitu tuvisikie lakini sijaona popote pale; na ni kwa nini nilikuwa nafuatilia? Nilikuwa nafuatilia kule Mkoani Simiyu kuna Jimbo la Bariadi Mjini. Jimbo la Bariadi Mjini lina Halmashauri mbili, lakini Jimbo hili lina Mbunge mmoja. Sheria inamtaka Mbunge ahudumu Halmashauri moja sasa kama hili Jimbo lina Halmashauri mbili, lina Wakurugenzi wawili, lina Wenyeviti wa Halmashauri, lina Mabaraza ya Madiwani wote na haya Mabaraza lazima kuwe na Kamati za fedha. Mbunge anapaswa kuingia kwenye Kamati moja tu ya fedha, lakini sisi pale Bariadi kuna Mbunge ambaye ana ratibu Kamati mbili za Fedha ilihali wakijua kabisa kwamba Kamati ya fedha ni siri.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka kujua kwamba kwa nini ajenda ya ugatuzi wa madaraka haijaletwa wakati kuna Majimbo ambayo yana sifa kabisa ya mgawanyo. Ni nini kinachofanyika pale Bariadi, kuna siri gani katika Jimbo hili kutogawanywa? Kwa hiyo, nataka kauli ya Waziri atuambie ni kwa nini Jimbo hili haligawanywi wakati mamlaka zote linazo, kwa nini? Jimbo hili ni kubwa, lina Kata 31, kwa nini Mzee wangu anateseka na mamlaka mbili ambazo hazina sababu yoyote ya msingi? Kwa hiyo, naomba tafadhali sana watuambie siri ya kutogawanywa Jimbo hili, hilo ni la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, nina ombi; hapo Mji wa Bariadi katika Mji wa Lamadi, huu mji unahitaji kufanywa kuwa mamlaka ya mji mdogo kutokana na kwamba sifa zote zipo za kufanywa kuwa Mji Mdogo wa Lamadi pale kwa sababu mapato yote yapo, sifa zote zipo, tuna kila kitu, tuna sekondari tatu, tuna shule za msingi saba, tuna vituo vya Polisi, tuna njia kama tatu zinazoingiza mapato katika Mji ule.

Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri anapokuja hapa atuambie solution ya Mji wa Lamadi kwa sababu yeye mwenyewe unafahamu ule mji ukifanywa kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo utaleta manufaa makubwa sana. Pia utaleta shule kwa watu wengine kuhakikisha kwamba miji mingine inakua, sasa tunavyoendelea kuona miji inakua halafu tunaendelea kuifunga inakuwa siyo sawa. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri anapokuja kuhitimisha atueleze ni nini hatima ya Jimbo la Bariadi Mjini na Mji wa Lamadi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ninalotaka kuzungumzia ni kuhusu elimu bure; ni kweli kwamba Mbunge ambaye alisimama hapa akasema kwamba yapo mambo mengi waliyoyachukua yaliyotoka upinzani, nakubaliana naye kwa kauli hiyo, lakini namna yalivyochukuliwa sasa na elimu bure.

Waheshimiwa Wabunge hebu tujiulize hivi elimu bure ni nini? Elimu bure tafsiri yake ni nini? Ni kitu gani tulichokuwa tunalipa kikubwa kwenye shule za msingi. Kama leo mwanafunzi anaenda shule amebeba rim, amebeba sijui nini, mita moja ya kitambaa cha skirt ni Sh.10,000 ili aweze kuvaa ni Sh.20,000 mita mbili, yaani yale mahitaji yote yako kwa mzazi. Nilitarajia kwamba, kama ni elimu bure haya majukumu makubwa yaondolewe kwa mzazi, lakini leo haya majukumu makubwa yote yamebaki kwa mzazi.

MBUNGE FULANI: Ream.

MHE. GIMBI D. MASABA: Ream, mlinzi na kila kitu kwa mzazi sasa tafsiri ya elimu bure ni ipi wakati gharama zote ziko kwa mzazi?

T A A R I F A

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. GIMBI D. MASABA: Mimi nilidhani kwamba mzazi huyu apunguziwe majukumu ili anavyotafuta fedha hizi zikasaidie maendeleo mengine. Sasa ni kitu gani tunachozungumza nafikiri hili limebaba ajenda nyingine ambayo ni ya uwongo kabisa jamani.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Masaba kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha.

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba hakuna sehemu yoyote palipotamkwa elimu bure inaitwa elimu bila malipo. Miongozo ya Serikali ilikwishatoka kwamba wazazi watafanya hiki na Serikali itafanya hiki, hiyo elimu bure ilikuwa ya upande wa kule. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gimbi Dotto Masaba, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kuna wakati napata masikitiko sana hata Mbunge anavyosimama anapongeza kila kila kitu hii tuamini ni dhambi, kabisa! Huwezi kupongeza wananchi wako kule wanateseka, dakika saba zote unapongeza. Haiwezekani binadamu akakosa changamoto, kwa nini Serikali hii ina mambo mazuri tu? Huyo huyo Mbunge anayenipa taarifa mimi barabara zote hazipitiki, Serengeti haipitiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimesema lazima tuijue tafsiri ya elimu bure; madawati mzazi, kila kitu mzazi halafu na sisi tumebeba kiholela hoja hii tunasema elimu bure, elimu bure tulikuwa tunalipa nini? Hata kipindi cha Kikwete ada ya sekondari tulikuwa tunalipa Sh.40,000, nani mzazi hana 40,000? Halafu mnaleta hapa slogan ya elimu bure, elimu bure, acheni utani jamani kwenye maisha ya Watanzania, siyo sawa. Eti elimu bure, elimu bure, ipi? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze na mifugo. Hoja kutoka Mkoa wa Simiyu, kwanza kwa kutozwa ushuru mara mbili aidha wauze au wasiuze, analipa ushuru shilingi 6,000/= ilhali wanaopelekea ng‟ombe Mnadani sio wote ni wafanyabiashara, bali wanapeleka ili wauze wapate mahitaji yao kama vile kununua chakula cha familia zao. Sasa unapomwambia auze au asiuze huu ni uonevu wa hali ya juu sana. Kwa maana nyingine ni wizi. Naomba Halmashauri ya Bariadi Mjini itazamwe katika hili na Mnada wa Dutwa Bariadi Vijijini kwani ni tatizo kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata Waziri Mkuu alipokuja kwenye ziara yake Mkoa wa Simiyu alikutana na kero hii na alitoa ufafanuzi kwenye mkutano wa hadhara akisema mauzo yanafanyika mara tu biashara inapokuwa imefanyika. Alisema ni marufuku mwananchi kutozwa ushuru mara mbili, lakini kauli yake imepuuzwa, kwani bado wananchi wanaendelea kutozwa kila kichwa ng‟ombe sh. 6,000/= auze au asiuze, analipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, majosho mengi ya kuoshea mifugo yalishakufa kutokana na kukosekana fedha za kuendeleza majosho kutokana na ufisadi. Wananchi wa Maswa Meatu baadhi yao hawana mahali na kuchungia mifugo yao. Naomba Serikali irudishe pori la Maswa, lirejeshwe kwao ili liwasaidie kuondoa mgogoro wa wakulima na wafugaji, kwa sababu pori hilo limekosa sifa ya kuwa Hifadhi ya Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Simiyu, wananchi wa Simiyu wengi wao ni wakulima wa pamba; wamekata tamaa kulima zao hili kutokana kuuzwa kwa bei ya hasara. Kwa muda mrefu hivyo wamekata tamaa na badala yake kulima zao la choroko kama sehemu ya zao la biashara. Kwa hiyo, naomba Serikali ilitazame kwa umakini zaidi kwani zao hilo limepotea kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Serikali irudishe mbegu za pamba ambazo zilikuwa zinatumiwa zamani, zile zenye manyoya, kwani hizi nazo hazioti kabisa. Serikali ipandishe bei ya pamba badala ya kununua pamba kwa sh. 650/= mpaka sh. 750/= iuzwe sh. 1,500/=. Kwani mbona soda ambayo akina Mengi wanakologa maji na kuweka sukari wanafunika, lakini wanauza sh. 1,000/=? Iweje wananchi ambao ameiandaa pamba yake kwa muda wa miezi sita mpaka saba anauza sh. 650/=. Naomba zao hili liangaliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, njaa Mkoa wa Simiyu haikuwepo kwa miaka mingi sana, lakini Mkoa wa Simiyu kwa sasa unaongoza kwa janga la njaa. Hiyo ni kutokana na wananchi hawa kulima na baadaye kuuza mazao yao kwa hasara kabla ya wakati, baadaye kujikuta hawana chakula. Hivyo ,naomba Serikali iwape elimu kuhusu utunzaji wa chakula chao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mageti ya mazao kila kona na bila hata ya utaratibu maalum. Mageti haya yamesababisha vifo; nashauri wayawekee taa, kama hawawezi kuweka taa na hawalindi usiku, basi wayatoe kwa wakati wa jioni wayarejeshe asubuhi, kwani ni hatari sana. Serikali itoe maelekezo kwa Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha mchango wangu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kama ilivyowasilishwa hapo mbele. Miaka ya hivi karibuni Tanzania imewahi kuingia kwenye mgogoro na nchi jirani ya Malawi kuhusu mpaka ndani ya Ziwa Nyasa. Mgogoro huo ulitaka kufifisha mahusiano mema ya kidiplomasia baina ya Malawi na nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa mahusiano ya nchi, namwomba Mheshimiwa Waziri alieleze Bunge, mgogoro huu umepatiwa ufumbuzi au bado? Kama bado, Waziri aje hapa atueleze, nini kinaendelea? Je, huo mpaka ndani ya Ziwa Nyasa, nchi yetu ina eneo la ukubwa gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Umoja wa Mataifa (UN) umetutaka mataifa yote yapige vita Mataifa yanayotuhumiwa kuzalisha makombora ya nyuklia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kuna taarifa zinaeleza kwamba baadhi ya Balozi za nchi yetu huko ng‟ambo zipo taabani kifedha. Namwomba Mheshimiwa Waziri alieleze Bunge hili hali halisi ya kifedha kwa ofisi za Balozi za Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia Mpango wa Maendeleo wa Taifa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira ilikutana na wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara wakubwa wanaotumia Bandari ya Dar es Salaam ambapo walieleza kwamba mizigo imepungua kwa kiasi cha asilimia 42 na mingi ni ile inayopita kwenda nje ya nchi hususan Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maelezo ya wadau kupungua kwa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam kumesababishwa na kutozwa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa huduma zinazotolewa katika mizigo au bidhaa inayopitia bandari hiyo kwenda nchi jirani (VAT on auxiliary services on transit goods) za Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Zambia, Malawi, Burundi, Rwanda na Uganda. Kutozwa Kodi ya Ongezeko la Thamani katika tozo mbalimbali za bandari kunaongeza gharama ya huduma na biashara katika Bandari ya Dar es Salaam na kupunguza ushindani na bandari nyingine kama zile za Nacala, Beira, Mombasa na Durban. Hivyo basi, ili tuweze kufikia uchumi wa kati, ifikapo mwaka 2025 ni lazima tuiangalie bandari yetu na pia tupunguze ushuru ili tuweze kuzalisha mapato mengi katika Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hii Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Kabla sijaanza kuchangia naomba nijikite moja kwa moja, kwenye Mkoa wetu wa Simiyu, ukiwemo na wewe mwenyewe Mwenyekiti, nadhani nikiutaja Mkoa wa Simiyu hata nisipozungumza chochote naamini roho yako inakuwa burudani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Simiyu ni miongoni mwa mikoa ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikiongoza kupata chakula kwa wingi, lakini kwa kipindi hiki mkoa huu umekuwa ukiongoza kwa janga la njaa. Unaongoza kwa janga la njaa kutokana na kwamba wananchi wa Mkoa wa Simiyu wamekuwa wakitegemea kilimo cha msimu badala ya kutegemea kilimo cha umwagiliaji. Hivyo basi, kuliko wananchi hawa waendelee kutegemea kilimo cha msimu, naomba wananchi hawa wategemee kilimo cha umwagiliaji ili waondokane na janga la njaa ambalo linatukabili kila mwaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili wananchi hawa waondokane na njaa ni lazima Serikali itengeneze miundombinu ya kututengenezea mabwawa kwa maana ya kuendesha kilimo cha umwagiliaji. Baada ya kututengenezea mabwawa hayo, naamini kabisa kwamba Mkoa wa Simiyu utakuwa umekidhi matatizo ya njaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Simiyu ni miongoni mwa mikoa ambayo imezungukwa na Ziwa Victoria, lakini ni Mkoa ambao ndiyo unaoongoza kwa ukosekanaji wa maji. Naomba nizungumzie kwa mfano Wilaya ya Busega Jimbo la Mheshimiwa Chegeni. Wananchi wa Wilaya ya Busega, walio wengi wanaoga maji ya kutoka Ziwa Victoria. Cha kushangaza wananchi hawa wanakunywa maji ya chumvi ya visima, ni jambo ambalo ni la kusikitisha na ni la aibu kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka kwa Bunge lililopita niliuliza swali kuhusiana na suala la utekelezaji wa mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kuwapatia maji safi na salama wananchi wa Mkoa wa Simiyu. Nilijibiwa kuwa mpango huu, unaendelea na hivi punde mradi utakamilika, lakini mpaka ninavyoongea hakuna kinachoendelea tunaendelea kupata takwimu tu na taarifa za kwamba mradi huu utakamilika jambo ambalo naona kwamba siyo sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Simiyu kuna Idara za Maji, siku zote nimekuwa najiuliza kwamba hivi Idara za Maji zinafanya kazi gani, ilihali wananchi wa Mkoa wa Simiyu hawana maji, maji ambayo tumekuwa tukiyatumia wananchi wanatengeneza makazi yao na wanachimba visima kwenye majumba yao na wanakuwa wanatumia na walio wengi unakuta wanafanya biashara ndoo moja shilingi mia mbili, lakini unakuta kuna Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kupata majibu kwamba hii Wizara ya Maji inafanya kazi gani, ambapo wananchi wa Mkoa wa Simiyu hatuna maji. Kiukweli tunapozungumza kuhusu maji ni dhahiri kweli tunapata uchungu kutokana na kwamba Mkoa huu wa Simiyu ni miongoni mwa mikoa ambayo ni mipya, lakini kiukweli mara nyingi umekuwa unasahaulika hata kutajwa kwenye Wizara zingine. Sijajua kwamba hatima ya Mkoa huu wa Simiyu ni nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia hapa kwenye kitabu chake ametutengea fedha Wilaya ya Itilima ambayo mimi natoka na ni Mwenyekiti wa chama katika Wilaya hiyo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), nimekuta wametenga shilingi milioni 200 ni sawa, lakini nimeona Wilaya ya Busega hakuna fedha ambazo zimetengwa kutekeleza mradi huu wa maji. Pia katika Jimbo la Mheshimiwa Mwenyekiti pale Bariadi sijaona fedha ambayo imetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa maji, nimeona Jimbo la Maswa hakuna fedha yoyote ambayo imetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sijajua huu mpango unakwenda vipi, kwa sababu fedha nilizoziona pale Wilaya ya Itilima inayo, Wilaya ya Mwanuzi ipo, ni wilaya kama mbili hivi. Kwa hiyo, sasa nashindwa kuelewa kwamba huu mradi unakwenda kutekelezwa vipi? Hii inaonesha wazi kwamba jinsi ambavyo pamoja na kwamba tunatoa hizi taarifa, ijulikane kabisa kwamba sidhani kama kuna mpango wowote unakwenda kutekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna mpango unakwenda kutekelezwa, ni dhahiri basi tuanzie pale kwenye vyanzo vya maji, kwa mfano Wilaya ya Busega, ndiyo iko karibu sana na ziwa, kwa nini hatujaona mpango wowote wa kutoka pale Busega, lakini pia Bariadi ndiyo inayofuata hatujaona mpango wowote ambao unaelekea pale, kwa maana kwamba kuna fedha yoyote ambayo inakwenda kutimiza huu mpango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisisitize kwenye suala la upatikanaji wa mabwawa katika mkoa huu. Mkoa wa Simiyu una maeneo makubwa sana ya kilimo cha umwagiliaji. Kwa mfano, kama maeneo ya Matongo, Mwamtani, Meatu, Malampaka, Malampaka ni walimaji wazuri wa mipunga na mazao mengine. Kwa hiyo, ni vyema Serikali hii ikajikita sana kututengenezea mabwawa ili Wasukuma waendelee kulima kilimo cha umwagiliaji. Tumechoka kuletewa chakula cha msaada kutoka Serikalini ambacho tukiletewa tunapewa kilo tatu.
Ndugu zangu Wasukuma tunazaa mpaka Mungu aseme wametosha, ukiniletea kilo tatu, kwa kweli hiyo mimi naona siyo sahihi. Kwa hiyo, niombe sana kwamba ifike mwisho, mkoa wetu usiwe tegemezi kwenye chakula cha msaada na badala yake tujisimamie na tuweze kuendana na kasi hii ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, masikitiko yangu makubwa ni kwamba, ziwa linatuzunguka, lakini hatupati maji safi na salama. Kwa mfano, Mikoa kama ya Mara, Mji wa Tarime hauna maji, kuna bwawa moja tu la wakoloni ambalo hata usafi halifanyiwi la miaka nenda rudi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana Mkoa wa Mara, Mkoa wa Simiyu, Mikoa hiyo ipate maji safi na salama ili tuendane na kasi ya Serikali hii ya Awamu ya Tano. Kwa hiyo, niombe sana na Wabunge wenzangu tunaotoka Mkoa wa Simiyu tusichoke kupiga kelele kuhusu mkoa wetu angalau tuone ni jinsi gani Serikali yetu itaweza kutusaidia ili tupate angalau hata robo tatu ya mafanikio ambayo tunayatarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kabisa Mheshimiwa Waziri, Wabunge waliokuja Awamu hii ya Tano tusipopeleka maji Mkoa wa Simiyu nawahakikishia 2020, hakuna Mbunge atakayekuja hapa, hakika wananchi wamechoka kunywa maji ya chumvi. Sasa hivi tumeanza kupata matusi kutoka kwa Wabunge wenzetu kwamba tumeoza meno, si kwamba tumeoza meno kwa sababu hatupigi miswaki, hapana tumeoza meno kwa sababu tunatumia maji ambayo yana chumvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sana Mheshimiwa Waziri, badala ya kuendelea kupata matusi haya basi ifike mahali…
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa mchango wangu katika bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu na hususani kuhusu maendeleo ya vijana nchini ofisi ya Waziri Mkuu imepewa jukumu la kusimamia maendeleo na ustawi wa vijana lakini kundi hili la vijana
halipewi kipaumbele na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa randama ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 20017/2018 Serikali imefanya shughuli tatu tu ambazo inadai kuwa ndizo shughuli za kusimamia na kuratibu maendeleo ya vijana, hizo ni za mbio za mwenge, mafunzo na kutoa mikopo katika mifuko ya vijana na wanawake katika Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika randama hiyo, Serikali imekiri kuwa kwa upande wa mfuko wa maendeleo ya vijana hakuna fedha yoyote iliyotolewa hadi kufikia 31 Februari, 2017. Hii inadhihirisha kuwa Serikali haina mpango wala mkakati wa maendeleo ya vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Taifa ambalo kiwango cha ukosefu wa ajira ni asilimia 11.7 lakini leo hii Ofisi ya Waziri Mkuu inakuja kusema maendeleo ya vijana ni kusimamia mbio za mwenge na uzinduzi wa miradi 1,387 yenye thamani ya shilingi 498,892,879,808 bila kutoa
mchanganuo wa fedha hizo na kuonyesha ni vijana wa ngapi kutoka mikoa ipi walifanikiwa na miradi ya mbio za mwenge. Aidha, Serikali imesema kuwa inaratibu mafunzo ya vijana hao wametoka mkoa gani na wamepatiwa mafunzo gani na mafunzo hayo yamewasaidiaje kupata
ajira na kujikwamua na umaskini.
Mheshimu Mwenyekiti, ni aibu kubwa kwa Taifa letu kukosa kabisa dira mahsusi ya maendeleo ya vijana na kudhani kuwa miradi ya mbio za mwenge ndio maendeleo ya vijana, kitendo hiki ni kuwahadaa vijana na kuwapa matumaini hewa juu ya uwezeshwaji wa kimitaji kwa ajili ya
shughuli zao za kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri Serikali kuacha mara moja kuwahadaa vijana kuwa inawajali wakati vijana wa nchi hii wako hoi hawana ajira na ndio wahanga wakubwa wa dawa za kulevya, UKIMWI na kila aina ya jambo baya. Serikali ichukue suala la vijana kwa uzito
unaostaahili kwa kubuni mpango mahsusi wa kushughulikia utekelezaji wa sera ya maendeleo ya vijana na kuweka mkakati wa kuongeza ajira miongoni mwa kundi hili kwani kuendelea kuwabagua vijana kunawezaa kuliingiza Taifa katika machafuko kutokana na vijana kukata tama ya
maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kuwasilisha mchango wangu wa maandishi kuhusu Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria. Ningependa kuzungumzia kuhusu suala la uwazi katika mchakato wa utoaji haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ni nchi mwanachama wa OGP Open Government Partnership ambapo mojawapo ya misingi muhimu ni Serikali za nchi husika kutekeleza majukumu yao kwa uwazi wa hali ya juu ili wananchi wajue Serikali zao zinavyofanya kazi. Hata hivyo kwa Tanzania hali ni tofauti kwa kuwa uhuru wa habari umeminywa kwa kiwango cha juu kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na usiri mkubwa sana katika mchakato wa utoaji haki Mahakamani. Vyombo vya habari vinazuiwa kuingia Mahakamani kuona mwenendo wa kesi, jambo ambalo limesababisha kushamiri kwa vitendo vya rushwa na wanyonge kudhulumiwa haki zao kutokana na usiri uliogubika Mhimili wa Mahakama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi jirani ya Kenya, kesi zote zenye maslahi kwa Taifa huwa zinarushwa moja kwa moja kwenye Televisheni na wananchi wanaona mwenendo wa mchakato wa utoaji haki. Kesi za uchaguzi na katiba katika nchi ya Kenya zilirushwa moja kwa moja na Citizen TV. Aidha, kuhusu kesi ya BREXIT ya Uingereza juu ya nani kati ya Bunge na Serikali ya Uingereza anatakiwa kuanzisha mchakato wa kujitoa katika umoja wa Ulaya ilirushwa live moja kwa moja na BBC na dunia nzima ilishuhudia na kuona mwenendo wa utoaji haki. Kwa kutumia mifano ya Kenya na Uingereza, nadhani Tanzania sasa inatakiwa kwenda level nyingine kwa kuruhusu uwazi zaidi katika mchakato wa utoaji haki Mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na vyombo vya habari kuruhusiwa kuingia katika vyumba vya Mahakama ili kuripoti mwenendo wa mchakato wa utoaji haki, vyombo hivyo pia viruhusiwe kuwatembelea wafungwa Magerezani ili wafungwa wapate haki ya kueleza fikra na mtazamo wao kuhusu maisha yao Magerezani. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumepiga hatua kubwa ya kudumisha uwazi katika utendaji wa Mahakama, lakini pia tutakuwa tumepiga hatua kubwa katika kujali haki za wafungwa ambazo ni miongoni mwa haki za binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kutoa mchango wangu wa maandishi, juu ya mwingiliano kati ya Serikali za Mitaa, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na Wizara ya Maliasili na Utalii katika utunzaji wa mazingira.
Mheshimwa Mwenyekiti, kuna mwingiliano unaokinzana kati ya Taasisi za Serikali nilizozitaja, katika utunzaji wa mazingira jambo ambalo limefanya zoezi la utunzaji wa mazingira kuwa gumu. Ugumu huo

unasababishwa na kukosekana kwa Sera moja au Sheria moja inayoweka uturatibu wa kuhifadhi mazingira.


Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Halmashauri za Wilaya zina Sheria ndogo zinazoruhusu, mathalani, kuvuna baadhi ya maliasili kama vile madini na magogo kwa ajili ya mbao ili kuongeza mapato ya Halmashauri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) inakataza shughuli kama hizo kwa kuwa dira na malengo ya Wizara hiyo; shughuli hizo zinaharibu mazingira. Wakati Wizara ya Maliasili na Utalii inatenga maeneo ya Hifadhi na Mapori Tengefu na hivyo kukataza wananchi wasitumie maeneo hayo kwa shughuli zao za kiuchumi. Halmashauri zinakuwa na uwezo wa kutoa vibali vya matumizi ya maeneo hayo au Wizara ya Ardhi nayo inaweza kutoa maelekezo tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mkanganyiko huo, utunzaji wa mazingira unaweza kuwa mgumu kutokana na kuwa na vyombo zaidi ya kimoja, vinavyoshughulika na mazingira kwa namna moja au nyingine. Kwa sababu hiyo, napendekeza na kushauri kwamba, Serikali iwe na Sera moja ya mazingira, Sheria moja ya mazingira na chombo kimoja chenye mamlaka na masuala ya mazingira. Kwa mantiki hiyo, Wizara yoyote au Halmashauri yoyote ambayo itakuwa na shughuli ambayo itaathiri mazingira, basi Wizara au Halmashauri hiyo ilazimike kuomba kibali cha kuendesha shughuli hiyo kutoka katika Wizara au Taasisi itakayokuwa imepewa mamlaka ya kusimamia mazingira.


Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kutumia nafasi hii kuzungumzia utunzaji wa mazingira usio na tija. Katika taaluma ya uhifadhi wa mazingira, uhifadhi wenye tija ni ule ambao unafanyika, lakini wakati huo huo kunafanyika pia uvunaji wa mazao yanayotokana na uhifadhi huo, kwa matumizi ya binadamu. Dhana hii ya uhifadhi na matumizi ya rasilimali zinazotokana na uhifadhi huo, ndiyo inayoitwa utunzaji endelevu wa mazingira (Sustainable Environmental Management).


Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu ipo misitu mingi ambayo imetangazwa na Serikali kuwa ni sehemu ya Hifadhi za Taifa na kwa sababu hiyo, Serikali imepiga marufuku uvunaji wa aina yoyote katika misitu hiyo. Matokeo yake ni kwamba, yapo magogo mengi yanaoza katika misitu hiyo na Taifa halipati faida yoyote kutokana na uhifadhi huo. Kwa mfano, Msitu wa Shengena katika Wilaya ya Same, umetangazwa kuwa ni Hifadhi na kwa sababu hiyo wananchi wa maeneo hayo hawaruhusiwi kufanya lolote katika msitu huo. Matokeo yake, miti mingi katika msitu huo imezeeka, magogo yanaoza, wananchi hawapati faida na wala Serikali haipati faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mazingira kama hayo, halmashauri zenye mazingira yanayofanana na yale ya Wilaya ya Same zipewe mamlaka ya kutoa vibali vya uvunaji wa mazao ya misitu kwa usimamizi wa Maafisa Misitu wa Wilaya husika na watakaopata vibali hivyo vya uvunaji waelekezwe pia namna ya kupanda miti ili misitu hiyo iwe endelevu na hatimaye kuwa na utunzaji wa mazingira ambao una faida kwa wananchi na kwa Serikali pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri TARURA kwa kushirikiana na Halmashauri zetu wanunuliwe mitambo ya utengenezaji na kukarabati barabara zetu za vumbi. Mambo haya yamefanywa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kahama na Ushetu kwa udhamini wa Benki ya CRDB. Kama Wizara haina pesa, basi Wakurugenzi waruhusiwe kukopa Benki kwa masharti ya kibiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa data nilizonazo seti nzima ya vyombo hivi ikiwa ni pamoja na malori, bulldozer, kijiko haizidi shilingi bilioni moja. Kwa kufanya hivi tutapunguza gharama za TARURA kwani hata hivyo haina pesa. Kwa asilimia 30 hii, haitoshi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2014/2015 ATCL ilipata hasara ya shilingi bilioni 943 na mwaka 2015/2016 ilipata hasara ya shilingi bilioni 109.2 na mwaka 2016/2017 ilipata hasara ya shilingi bilioni 113.7

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi majuzi tumepokea ndege nyingine ya tatu. Naomba kuishauri Serikali iongeze bajeti kwa ATCL kwani kila mwaka hasara yake inaongezeka kwa asilimia 4.4. Hii shilingi bilioni 3.9 haitatosha kulipia gharama ya hasara ya mwaka wa fedha 2018/2019.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Awali ya yote napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema kwa siku ya leo ili niweze kutekeleza majukumu yangu kwa ajili ya wananchi wa Mkoa wa Simiyu. Vilevile nishukuru Mwenyenzi Mungu; amsaidie mwenyekiti wangu wa Kanda ya Ziwa Serengeti Mheshimiwa Heche aweze kupata nafuu ili aweze kuja kutekeleza majukumu yake. Nimeona jinsi ambavyo ameanza kunyemelewa na kashfa na kwa jinsi ambavyo namfahamu mimi siyo muumini wa kupinga maendeleo. Nafahamu hilo yeye ni Mwenyekiti na mimi ni Makamu wake kwa hiyo tunafanya kazi ofisi moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba tu nizungumze kwamba tunapozungumza Tanzania ya viwanda naamini kabisa hakuna Mtanzania anayepinga Tanzania ya viwanda. Hata hivyo ninachokiona ni kwamba hatuendani na kauli ya Tanzania ya viwanda. Ninasema haya kwa sababu katika taarifa ya Waziri amezungumza mambo mengi sana na mimi kama Mbunge ninayetoka katika Mkoa wa Simiyu tunapozungumza viwanda maana yake tunagusa malighafi za maeneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Simiyu tunalima kila kitu, lakini cha kushangaza sijaona mahali popote ambapo Mkoa wa Simiyu unazungumziwa kuhusu kupata kiwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi niliuliza swali ambalo linahusiana na viwanda ambavyo vilikuwepo kwa muda mrefu, viwanda ginnery na nilivitaja kama viwanda vitano, Nasa Ginnery, Ngasamo Ginnery, Maswa na Malampaka, viwanda vyote hivi vimekufa na nikahoji Serikali inampango gani kuvifufua viwanda ambavyo vimekufa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri alisema mkakati wa Serikali na jukumu alilopewa ni kuhakikisha viwanda vyote vilivyokufa vinafanya kazi. Sasa ninataka kujua kauli ya Serikali, hivyo viwanda ni lini vitaanza kufanyakazi ili wananchi wa Mkoa wa Simiyu waanze kunufanikana na viwanda hivyo vya kuchambua pamba?

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia viwanda lazima tulipe kipaumbele zao la pamba. Mkoa wa Simiyu zao la pamba limekufa, wakulima hawalimi tena zao la pamba kutokana na kwamba soko hili la pamba halipo. Wananchi wanatumia gharama kubwa kuandaa mashamba ya pamba kama vile palizi pamoja na vitu vingine lakini cha ajabu wanakwenda kuuza kilo ya pamba shilingi 1,000; jambo ambalo siyo zuri hata kidogo kwa Watanzania wa Mkoa wa Simiyu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninachotaka kuomba kama kweli Serikali inadhamira ya dhati na kwa kutambua Mkoa wa Simiyu kwamba ni wa wakulima wakubwa sana, ninaomba ipewe kipaumbele kikubwa sana ili kuhakikisha kwamba tunapata viwanda vya kila aina.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumza wakulima na wafugaji, Mkoa wa Simiyu tuna wakulima na wafugaji. Lakini pamoja na malighafi zote hizi hakuna kinachofanyika kule Mkoa wa Simiyu. Sisi ni wafugaji lakini cha kushangaza hakuna hata kiwanda cha kusindika nyama, hakuna. Wafugaji anapakia ng’ombe kwenye malori kupeleka Dar es Salaam. Mmewahi kuona wapi sisi binadamu tunakwenda Jiji la Dar es Salaam kutalii ng’ombe nao wanakwenda kuangalia jiji la Dar es Salaam? Ni aibu kwa Taifa hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini Serikali isitengeneze viwanda ili wananchi hawa waweze kunufaika? Mimi niombe sana, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda niko kwenye kamati yako. Kilio changu kikubwa sijawahi kuchangia nikizungumza suala la kimataifa. Mara nyingi nazungumzia Mkoa wa Simiyu na Wabunge wenzangu wanaotoka Mkoa wa Simiyu kila siku tunapiga kelele kuhusiana na suala ya Mkoa wa Simiyu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunalima choroko, tunalima zao la alzeti, tunafuga, bado ndani ya mifugo tunazalisha mbolea, kwa nini sasa tusiwe hata na kiwanda cha kutengeneza biogas inatokana na vinyesi vya ng’ombe? Kwa nini kila kitu hakuna? Halafu tunakuja tunasema Tanzania ya viwanda! Sipingani na kauli ya Tanzania viwanda lakini matendo yetu hayaendani na Tanzania ya viwanda. Mimi niombe sana kwamba tuangalie ni namna gani tunaweza kuusaidia mkoa huu wa Simiyu ili tuweze kuendena na kasi ya Tanzania ya viwanda ambayo mnaizungumza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda wewe unatoka Mkoa wa Kagera. Mkoa wa Kagera unazalisha ndizi, lakini cha kushangaza sisi unatudanganya unatuambia una viwanda una nini, kwako hakuna hata kiwanda cha kuchakata ndizi, hakipo. Naomba uoneshe mfano sasa wewe vinginevyo utaingia kwenye mkumbo wa Mawaziri hewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika tumekuwa na changamoto katika historia ya Tanzania. Historia ya Tanzania tumeshuhudia kwamba Serikali imekuwa ikiyakopesha mabenki kutoka Benki Kuu kwenda kwenye benki ndogo ndogo wamekuwa wakiwakopesha. Wakikopesha fedha zile benki wananchi wetu wananufaika kukopa hususan akina mama ntilie.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ni kwa mara ya kwanza Serikali ya Awamu ya Tano kunyang’anya fedha kwenye mabenki na kuzirudisha Benki Kuu; jambo ambalo limesababisha sana kuyumba kwa uchumi. Lakini hizi fedha zingekuwa kwenye mabenki ya kawaida mama zetu wangeweza kukopa, lakini sasa hivi wamefungia kule benki tumebaki tunalia; mama analia, baba analia kila mtu analia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wabunge form one tuliambiwa kwamba ukiwa Mbunge unakuwa na fedha nyingi sana. Lakini sasa hivi tunalia hata kuliko mwananchi wa kawaida. Jambo ambalo ni aibu kwa Taifa hili. Hata hivyo naamini kabisa kwamba Wabunge tuna hali mbaya lakini tunashindwa kulia kwa sababu ya utu uzima wetu, kwamba unawezaje kulia wakati na mtoto kule analia; kwa hiyo inabidi mama unyamaze kimpya uendelee kuumia polepole. Lakini mimi ninachokiamini kabisa ni kwamba baada ya miaka kadhaa tutajikuta tumepata maradhi ambayo yametokana na stress zilizosababishwa na ugumu wa maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoomba kusema sasa ni kwamba Mheshimiwa Waziri wa Viwanda atakapokuja kuhitimisha hapa nitahitaji kufahamu suala la viwanda vya ginnery vilivyokufa, ni lini vile viwanda vitafufuliwa, la pilli, nini tamko la Serikali itakapofika msimu wa kuuza pamba wananchi wauze kwa shilingi ngapi ili tuweze kuendana na kasi ya Tanzania ya viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo ninakushukuru sana Mungu akubariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante Kiwanda ambacho Mheshimiwa Waziri wa Viwanda anajifunia nacho ni kwamba kilianzishwa na kikundi cha
vijana kwa ajili ya kutengeneza chaki na Halmashauri ikaingia ikachukua hicho kiwanda. Kwa hiyo, ndicho tunachojivunia nacho. Lakini sisi tunadai viwanda vinavyotokana na pembe za ng’ombe tunaka tutengeneze hata vifungo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi na leo nisimame mbele ya Bunge lako kuchangia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kutambua hatua iliyoanza au aliyoifanya Waziri wa Kilimo; kwa sababu nilivyokuwa najaza hii nafasi kwa maana ya kuja kuchangia Wizara ya Kilimo na Mifugo, nilidhamiria kuwa mtu mwenye hasira sana, lakini kuna jambo ambalo nimeliona humu, kitendo cha kujaribu kufuta ushuru mdogo mdogo kwa maana ya ushuru wa mazao pamoja na mifugo, nimetambua hatua hiyo. Naomba niseme kwa nini nilidhamiria kuwa na hasira? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wangu wa Simiyu kulikuwa na changamoto moja kubwa sana ambayo ilikuwa inafanyika kwa wafugaji kila wanapokwenda kuuza ngombe kwenye minada kulikuwa na utaratibu anaingiza ngombe kwenye mnada bure. Wakati wa kutoa ngombe anatozwa ushuru wa Sh.1,000/= kila kichwa cha ngombe, awe ameuza au hajauza ushuru lazima atoe. Jambo hili lilipelekea kuleta matatizo makubwa sana kwa wananchi wa Mkoa wa Simiyu. Kwa kutambua hili kwamba wamefuta ushuru huu, ndiyo maana nikajikuta hasira yangu kidogo imepungua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe ushauri, pamoja na kutoa kodi hizi, naomba basi Mheshimiwa Waziri apeleke waraka haraka sana kwenye Halmashauri zetu, ili jambo hili lianze kutekelezwa kwa haraka na wananchi waweze kunufaika na mifugo yao ambayo wanaitunza kwa muda mrefu, wanatumia gharama kubwa ili waweze kunufaika nayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, masikitiko yangu yalikuwa kwamba sisi Wasukuma ng’ombe ni ATM yetu. Ukipatwa na janga la njaa kwenye familia, unachagua ngombe wawili, watatu unapeleka mnadani, unauza unanunua chakula. Sasa walivyokuwa wanaambiwa wauze, wasiuze, lazima walipe ushuru, nilikuwa napata masikitiko makubwa sana, kwa sababu huyu mtu ana njaa halafu unamwambia atoe ushuru wakati ng’ombe hajauzika, ilikuwa ni jambo la aibu sana katika mkoa wetu. Kwa hiyo nashukuru katika hilo kwamba limeonekana na naomba nisisitize waraka upelekwe haraka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jana nilisimama hapa nikichangia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji; nilijaribu kugusia suala la pamba, lakini leo nataka nimtafute mchawi wa pamba. Zao la pamba tunamtafuta ni nani aliyesababisha zao hili lipotee? Kumekuwa na historia ya wakulima wa pamba, zamani tumekuwa tukipewa mbegu ambayo ilikuwa na manyoya kidogo, ile mbegu walikuwa wananunua wazazi wetu, tunalima tunazalisha. Mbegu ile ikibaki, ninachokikumbuka tulikuwa tunakwenda tunatengeneza magodoro, tunaendelea kulalia mbegu ambayo ilikuwa inabaki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini cha kushangaza sasa hivi, nataka kujua, ni nani aliyeshauri mbegu hii ya pamba ipelekwe saluni, halafu iletwe sisi tuanze kupanda? Nataka kujua, maana tumeletewa mbegu ambayo ni ya kisasa na mbegu hii haioti na ikiota inaota mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta mwananchi ametumia gharama kubwa kuandaa shamba la pamba matokeo yake anavuna kidogo. Heka moja inatoa kilo 30, anakwenda kuuza kilo ya pamba Sh.1,000/=, halafu tunasema kwamba leo tunamtafuta mchawi ni nani? Mchawi wa pamba ni Serikali yenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukiambiwa pamba ya Tanzania ni chafu…

T A A R I F A . . .

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na kumheshimu dada yangu, ingekuwa sheria inaruhusu ningemjibu kwa kinyumbani, lakini taarifa yake siipokei, kwa sababu amekubali kwamba tatizo ni kwamba wananchi hawakuelewa matumizi ya ile pamba. Ilikuwa ni jukumu la nani kuwaelimisha hao wananchi kama siyo Serikali? Kama Serikali haikuwajibika kuwaelimisha namna ya matumizi ya hii mbegu, maana yake bado mchawi ni Serikali yenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitoka kwenye suala la mbegu hii kumekuwa na changamoto ya kuchelewesha mbolea. Tunategemea sana kilimo cha msimu. Mvua zetu ni za msimu; kuna mvua za kulimia, kuna mvua za kuoteshea, kuna mvua za mwisho. Sasa wananchi wamekuwa wakiletewa mbolea kwenye mvua ya kuvunia.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama tatizo ni kuleta mbolea, naomba Mkoa wa Simiyu, jana nilizungumza kwamba sisi tunazalisha mbolea. Kama tunazalisha mbolea, naomba basi wananchi wapewe elimu waweze kuitumia mbolea ambayo wao wanaizalisha kule, ambayo ni mbolea ya ngombe, kuliko kusubiri mbolea ambayo haijulikani itakuja wakati gani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kabisa kwamba wananchi wale wakifundishwa matumizi ya mbolea wanayoizalisha, hakuna ngombe atakayedondosha kinyesi chochote, watatamani hata kuwafungia maliboro kwenye nanii ili kuhakikisha ile mbolea haipotei. Ni kwa sababu hawajui matumizi yake, ndiyo maana ile mbolea inapotea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumze kuhusu suala la mifugo. Tumekuwa na changamoto sana kuhusiana na suala la malisho. Mwaka 2016 niliuliza swali hapa, kuhusu kutenga maeneo ya kuchungia. Nikadai eneo la Maswa Reserve kwamba limekosa sifa, kwa nini lisirudishwe kwa wananchi ili waweze kuchungia ngombe zao? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa na changamoto kwenye maeneo ambayo yako karibu na hifadhi…

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, basi naomba niunge mkono hoja ya Upinzani. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuweka mchango wangu.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata fursa hii, pia nimpe pole Mheshimiwa Freeman Mbowe, Mwenyekiti wangu na viongozi wengine waandamizi wanaopitia changamoto zinazoendelea katika Taifa hili. Naamini kabisa kwamba nguvu ya umma iko siku itashinda dola. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kumrudisha Mheshimiwa Spika wetu na kwa uhai ambao anao kwa sasa Mungu aendelee kumjalia na kumpa afya njema ili aweze kuliongoza Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja kwa moja naomba niende kwenye Mkoa wangu wa Simiyu nikianza na changamoto ambazo zinaendelea katika Wilaya ya Itilima tarehe 30 Machi, kuna watu ambao wanaishi kandokando ya hifadhi waliuawa na tembo ambao wanazunguka kwenye mashamba ya wananchi. Naomba nitoe masikitiko yangu kwamba Serikali imekuwa ikikaa mbali sana na hawa wananchi ambao wanapata madhara haya na nisikitike kwamba hata kwenye misiba ya haya majanga yanayotokea Serikali haifiki. Mfano ninao kwa hawa wananchi waliofariki tarehe 30 katika kijiji cha Nyantugutu na kijiji cha Longalombogo, hata Mkuu wa Wilaya hakufika kwenye huo msiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sana tunapozungumza kwamba kuna kifuta machozi kwa hawa wananchi mfuko wa maafa ambao uko kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu uhakikishe kwamba hawa watu wanapopata madhara kama haya na familia zao Serikali iweze kufumbua macho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa pili naomba nijielekeze kwenye mradi wa maji wa kutoka Ziwa Victoria kwenda Mkoa wa Simiyu.

Waheshimiwa Wabunge walionitangulia kuchangia Mheshimiwa Raphael Chegeni na Mheshimiwa Mashimba Ndaki wamegusia sana kuhusu suala la huu mradi. Mradi huu umekuwa ni kizungumkuti katika Mkoa wetu na nasikitika kwamba naamini kabisa toka uhuru au toka dunia iumbwe wananchi wa Mkoa wa Simiyu hawajawahi kuonja maji ya Ziwa Victoria licha ya kwamba kuna wengine wanaoga kwenye Ziwa Victoria lakini hawajawahi kunywa maji yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ieleweke kabisa kwamba mnamuaibisha Mheshimiwia Rais, tunapozungumza kwamba Mheshimiwa Rais anatoka maeneo hayo ya Kanda ya Ziwa Victoria halafu kwenye maeneno yake hakuna maji ni jambo ambalo tunasikitika sana. Kwa hiyo, ninaomba sana mradi huu uharakishwe kwenye bajeti hii ya Serikali muone umuhimu wa kuhakikisha kwamba mradi huo unawafikia, kwani kuwafikia mradi huu haitoshi tu kwamba watanufaika kunywa maji hayo, inatosha pia kuchochea maendeleo ya kilimo cha umwagiliaji katika mkoa huu. Kwa hiyo, niombe sana Serikali ione umuhimu wa kupeleka mradi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia bado narudi kule kuhusu barabara ya kutoka Bariadi kupitia Makao Meatu kwenda Karatu, Arusha; Serikali ihakikishe kwamba ule ujenzi unakamilishwa kwa wakati muafaka ili kuweza kuchochea maendeleo kwenye Mkoa wetu wa Simiyu kwa lengo la kupeleka maendeleo kwa kasi licha ya kuwa kwamba Mkuu wa Mkoa anapambana kadri Mungu ambavyo anamjaalia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukisoma kitabu cha Mheshimiwa Waziri Mkuu amezungumzia sana kuhusu suala la kilimo, naomba nijikite kwenye suala la zao la pamba, kwenye zao la pamba lazima tukubaliane kwamba wananchi wamehamasika sana kulima zao la pamba sasa isitoshe tu kuhamasika kulima zao hili la pamba. Naiomba Ofisi ya Waziri Mkuu itoe bei elekezi mapema ili wananchi hawa wajue kabisa kwamba mwaka 2018 watauza kwa bei ya shilingi ngapi katika zao lao la pamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema kwa nini watoe bei elekezi kuna watu kwa sasa wanapita kwenye mashamba ya wakulima na kuwalaghai wananchi kwa bei ambazo wanaziona wao bila kujua kwamba wananchi hawa kuna muda itafika watauza kwa bei stahiki na watapata faida watanufaika na zao lao. Kwa hiyo, ninaomba mtoe kauli ya Serikali kwamba mwaka huu 2018 bei ya pamba ni kiasi gani lakini pia itoe kauli kwa wananchi ambao wanapita kwenye mashamba kwa ajili ya kuwalaghai wananchi hawa na matokeo yake wanashindwa kunufaika na pamba hiyo.

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ambalo nataka nichangie ni kuhusu Wilaya ya Itilima, Mheshimiwa Leah Komanya alisimama akauliza kuhusu swali la Hospitali ya Rufaa; mimi naomba nitoe masikitiko kwamba pamoja na kwamba Mheshimiwa mwenzangu anadai kwamba tupate Hospitali ya Rufaa, Mkoa wa Simiyu una Wilaya kama mbili mpya lakini nasikitika kwamba Wilaya hizi hazina hata Hospitali ya Wilaya, hazina Mahakama za Wilaya, hazina Vituo vya Polisi hususani Wilaya ya Itilima ambayo ni miongoni mwa Wilaya kubwa. Wilaya ina kata 22, ina vijiji 102, ina vitongoji 446, imegawanyika katika tarafa nne lakini cha kusikitisha Wilaya ya Itilima haina Hospitali ya Wilaya, haina Mahakama ya Wilaya na tatu, haina Kituo cha Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Polisi kilichopo kiko nje na Makao Makuu ya Wilaya kwa maana ya kata jirani na hata tarafa jirani. Kwa hiyo, ninaomba sana kwamba angalau kwenye bajeti ya 2018/2019 basi Serikali ione umuhimu angalau kutupatia kimojawapo kati hivi ambavyo nimevitaja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia kwa umakini sana ni suala la viwanda. Ukisoma kwenye mpango wa bajeti wa mwaka 2018/2019 katika ukurasa wa 12, kifungu cha (8), Waziri wa Fedha Mheshimiwa Mpango ametueleza kwamba mpaka sasa Serikali ina viwanda 3,600. Pia ukisoma kwenye ripoti ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda ametueleza kwamba tuna viwanda 3,060 ukisoma kwenye ripoti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu yeye anasema tuna viwanda 3,306. Sasa wapo watu wanahoji kwamba tunataka kujua viwanda vidogo ni vingapi na viwanda vikubwa ni vingapi, mimi nomba muhoji kwamba hii ni Serikali moja lakini kila mtu ana takwimu za kwake. Kwa hiyo, ni namna gani ambavyo huhitaji kuhoji maswali mengi unahitaji kupata majibu kupitia document na data zao ambazo wanazitoa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imeongoza Taifa hili kwa miaka miwili na zaidi lakini naomba niseme kwamba kwa lugha nyepesi ni kwamba tumefanikiwa kuwa na hivi viwanda ambavyo tayari vina takwimu hizi ambazo ninyi mnaweza mkajumlisha mkaona kwamba Waziri wa Fedha Mheshimiwa Mpango ame-miss vingapi na Mheshimiwa Waziri Mkuu ame-miss vingapi.

Mheshimiwa Spika, turudi kwenye historia ya Mwalimu Nyerere, Mwalimu Nyerere alitawala miaka 24 kwa taarifa ya Dkt. Neville Reuben katika Kigoda cha Mwalimu 2016 amesema kwamba Mwalimu Nyerere alifanikiwa kuwa na viwanda 414 kwa kipindi cha miaka 24 aliyotawala.

Ndugu zangu mnaweza mkaona kwamba hawa ndugu zangu wao wametawala miaka miwili na zaidi wako hapo kwenye hivi viwanda.

Mheshimiwa Spika, kuna Waheshimiwa Wabunge wanahoji kwamba viwanda vidogo ni vingapi na vikubwa vingapi! Waheshimiwa Wabunge nataka niwaambie mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Mazingira, hivi viwanda mnavyovihoji mimi Mjumbe sijawahi kuviona. Sijawahi kuviona kwa sababu hata kwenye ziara ya Kamati ilifaninkiwa kwenda kutembelea SIDO kwenye karakana za SIDO ambazo hata mashine zake zilizoko kule hata watumishi majina yake walishasahau zinaitwaje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni namna gani Kamati haishirikishwi ipasavyo kwenye jambo la kufika kwenye hivi viwanda ingawa hivi viwanda ukimsikiliza Mheshimiwa Waziri wa Viwanda anavijua kwa ufasaha mkubwa, hali kadhalika tumeona namna ambavyo Mheshimiwa Rais kuna maeneo anasema viwanda hivi vipo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia Wizara hii ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda nimpongeze Mheshimiwa Joseph Mbilinyi na nimpe hongera kwa kuongeza CV ya siasa katika Taifa hili. Tunamwambia karibu tuendelee na kulijenga Taifa hili, mapambano yanaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mengi ya kuzungumza kutokana na kwamba mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira, yapo mengi nayofahamu na Waziri wa Viwanda anafahamu nini ambacho nimekuwa nikikidai katika Kamati hiyo. Kwa leo nataka nibebe angalau hoja moja au mbili kutokana na muda na naomba nizungumzie kuhusu uhaba wa sukari nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hitaji la sukari kwa mwaka ni tani 440,000, uwezo wa viwanda vyetu ni kuzalisha tani 3,000 pekee. Hivi navyozungumza bei ya sukari kwa mfuko wa kilo 50 ni Sh.110,000 lakini kila mwaka tunakuwa na upungufu wa sukari karibia tani 140,000 sawa na asilimia 32.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilitoa vibali kwa ajili ya kuagiza sukari kwa wafanyabiashara kwa lengo la kukidhi mahitaji ya Taifa letu au kwa maana nyingine kwa walaji. Nikizungumzia suala la bei ya Brazil, sukari kwa bei ya Brazil ni sawa na dola 3,090 sawa na Sh.860,000 na hiyo ni pamoja na kodi asilimia 25 na VAT asilimia 18. Kwa bei hii sukari ilipaswa kuuzwa Sh.65,000 na siyo Sh.110,000 au ingeweza kuuzwa Sh.80,000 maana wao kule wananunua kilo 50 Sh.65,000 maana yake wangeweza kuuza hapa Sh.80,000 na isiwe Sh.110,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza haya kwa masikitiko kwa sababu kila kukicha tunaisikia Serikali inasema ni Serikali ya wanyonge. Kama Serikali ni ya wanyonge ni kwa nini Serikali inawauzia wananchi sukari kwa bei ya juu kiasi hiki? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ina maana ukigawanya hapa ni kama wanauza kwa kilo Sh.3,000. Kama Serikali ni ya wanyonge, kwa nini basi Watanzania wasipate sukari kwa Sh.1,500 kwa kilo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilitoa vibali watu waagize sukari kwa lengo la kuleta ushindani wa soko. Cha kushangaza ni kwamba sukari ile ile ya ndani na nje inauzwa bei moja. Sukari kwa bei ya ndani inauzwa Sh.110,000 na sukari ya nje inauzwa bei ileile. Sasa najiuliza, ni kwa nini Serikali ilitoa vibali kwa walewale wenye viwanda badala ya wafanyabiashara wengine ili kuleta ushindani wa soko na kuleta tija kwa walaji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja anipe majibu, kwa nini Serikali haikutoa vibali kwa wafanyabiashara wengine na ni kwa nini imetoa kwa wafanyabiashara walewale ambao sisi tunasema sukari ambayo wanazalisha wao haikidhi na ndiyo maana Serikali iliamua kutoa vibali ili tukidhi hitaji la Watanzania? Kwa hiyo, naomba majibu atakapokuja Mheshimiwa Waziri wa Viwanda. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri inayofanya Jeshi la Polisi, lakini kwa muda mrefu jeshi hili lina upungufu wa vituo vya Polisi kwenye maeneo yetu pamoja na vitendea kazi. Naomba Serikali itenge fedha za kutosha kwenye maeneo yetu na kuongeza vitendea kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kumekuwa na upungufu wa nyumba za Askari. Kila mmoja wetu anafahamu mazingira wanayoishi Askari hawa. Ni muda muafaka kwa Serikali kuja na mkakati kabambe wa kujenga nyumba za kutosha kwa ajili ya Askari wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka ya hivi karibuni kumeripotiwa mauaji na kupotea kwa raia hapa nchini. Kuna maiti zinaokotwa kwenye fukwe za bahari, watu wanapotea na kutekwa, lakini kwa bahati mbaya mpaka sasa Jeshi la Polisi halijawakamata na kuwapeleka wahusika wa matukio haya Mahakamani. Ukimya huu unawatia wasiwasi wananchi, maana hawaoni hatua zozote zikichukuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Nne ilihamasisha sana dhana ya Polisi Jamii na ulinzi shirikishi kwa maana kwamba suala la usalama ni suala la kushirikiana kati ya jamii na Jeshi la Polisi. Kwa siku za hivi karibuni, tumeshuhudia dhana hii kuanza kupoteza maana kutokana na matendo yanayofanywa na baadhi ya Askari Polisi yanawakatisha tamaa wananchi. Naomba Wizara iangalie upya mahusiano ya Jeshi la Polisi na wananchi ili kuhakikisha usalama wa raia wetu na mali zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016 kulikuwa na kampeni kali ya kupambana na dawa za kulevya iliyoendeshwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Wote tulishuhudia orodha ndefu ya wafanyabiashara na watumiaji wa dawa za kulevya na wengine kuitwa Polisi kuhojiwa na kupimwa mikojo. Nataka kujua katika ile orodha, ni wangapi wamefikishwa Mahakamani? Utumiaji wa dawa za kulevya umepungua kwa kiasi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Zimamoto halina magari na vifaa vya kutosha kukabiliana na majanga yanayotokea kwenye jamii yetu. Serikali ijitahidi kulipangia fedha za kutosha ili liwe na magari na vifaa vya kutosha vya uokozi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa ya kuchangia Wizara hii ya Kilimo. Wizara hii ni muhimu sana hususani kwa sisi Wabunge ambao tunatoka kwa waathirika wakubwa wa kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siko mbali na wale waliozungumzia bei ya pamba. Kama umesikiliza Wabunge wengi wanazungumzia bei ya pamba, mwaka jana tuliuzia shilingi 1,200 na mwaka huu ni shilingi 1,100. Ikumbukwe kwamba wakati tunauza pamba shilingi 1,200 bei ya nondo ilikuwa ni shilingi 9,000 leo tunauza pamba shilingi 1,100 bei ya nondo ni shilingi 22,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kuonesha namna ambavyo mkulima huyu anaendelea kudidimizwa kana kwamba analima kwa ajili ya chakula cha dagaa. Sisi tulitamani kwamba wakulima wanaolima zao la pamba lengo lao ni kubadilisha maisha ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba nzuri. Cha kushangaza Serikali ndiyo imekuwa muumini mkubwa wa kuhakikisha kwamba wakulima hawasongi mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niungane pia na Wabunge waliosema kwamba suala la ushirika halina tija yoyote kwa wakulima. Serikali imetangaza kufufua ushirika lakini haina mtaji wowote wa kuendesha ushirika. Wakati Waziri Mkuu amekwenda Mwanza alikutana na wafanyabiashara, masikitiko yangu ni kwamba nilitarajia badala ya kukutana na wafanyabiashara angekutana na wakulima wenyewe ambao ndiyo wahanga wakubwa wa tatizo hili la kilimo cha pamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetangaza ushirika, mnaagiza kwamba yale mashirika yanayonunua pamba eti ndiyo yapeleke fedha kwenye huo ushirika halafu ndiyo yanunulie pamba za makampuni yale yanayonunua pamba, hili ni jambo ambalo halikubaliki. Wakati tunazungumzia historia ya kuua ushirika maana yake ni kwamba walioua ushirika hawajachukuliwa hatua yoyote ile, lakini leo mnataka tena kuchukua fedha za wafanyabiashara wa haya makampuni wanaonunua pamba maana yake ni kwamba muwaangamize hawa wafanyabiashara kwa lengo la kuua mitaji yao, hii haikubaliki hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Bunge lililopita tulipitisha hapa kwamba msimu wa pamba uanze tarehe 1 na ndivyo ilivyokuwa, lakini mpaka hivi ninavyozungumza hakuna pamba yoyote iliyoanza kununuliwa. Hainunuliwi kwa sababu ya hili suala la ushirika la kutaka kupeleka fedha kwenye ushirika ili waweze kununua hizo pamba sasa wafanyabiashara wamegoma kupeleka fedha zao. Nachotaka kusema sasa, Serikali kama inataka suala la ushirika liendelee pelekeni fedha zenu ili muendelee kununua kwa njia ya ushirika na siyo fedha za makampuni yaliyoko kule Mkoani Simiyu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe masikitiko yangu, kuna watu wamechangia hapa kuhusu zao la mihogo na kuna taarifa kwamba Serikali hii imeingia mkataba na Wachina kwa ajili ya kupeleka mihogo lakini utashangaa hakuna sehemu kwenye hiki kitabu cha Waziri pameandikwa kitu kinaitwa muhogo. Ukitoka hapo nje kuna watu wamekuja kwa ajili ya kutetea kilimo cha muhogo. Hii ni aibu ndugu zangu kwamba watu wametoka mbali kwa ajili ya kuja kutetea zao lao la mihogo, halafu halimo hata kwenye kitabu hiki, ni mambo ya kusikitisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe kwamba kama Serikali inataka suala la ushirika liendelee pelekeni fedha zenu kuliko kutumia fedha za wakulima na kitendo cha kuwagombanisha makampuni ya pamba na wakulima kwamba wasionane nao na badala yake wakauze kwenye ushirika hilo halikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, mnamo tarehe 27 Kamati ya Viwanda ilikutana na wafanyabiashara wa makampuni kama zaidi ya 23. Katika kikao hicho, changamoto za mlundikano wa kodi zilitawala sana ila naomba nibebe haya machache kuhusiana na viwanda vya ndani vya kuyeyusha chuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, uwekezaji wa viwanda 16 vya chuma nchini ni dola milioni 170.3 ambayo ni takribani shilingi bilioni 392 na vinatoa ajira kwa Watanzania 25,913. Uwezo wa viwanda hivi kuzalisha kwa mwaka ni tani 1,082,700. Uzalishaji wa sasa ni tani 240,336 sawa na 22% tu na shida kubwa imeelezwa ni uhaba wa chuma nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, akiba ya chuma tuliyonayo kama nchi ni tani milioni 126 ambazo zinaweza kuchimbwa metric ton milioni tatu kwa zaidi ya miaka 100 ambapo uhitaji wa chuma wa Taifa ni metric ton 440,336 ukiondoa chuma kwa ajili ya SGR ambapo hata nati moja inatoka Uturuki ambapo Afrika Mashariki pekee kwa mwaka inaingiza chuma chenye thamani ya dola bilioni 1.5 sawa na trilioni 3.3 thamani ya kiwanda cha makaa ya mawe na chuma cha Liganga na Mchuchuma ni dola bilioni 2.9 sawa na shilingi trilioni 6.38 fedha ambayo tunairudisha kwa miaka miwili tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania kwa mwaka inaingiza chuma zaidi ya metric ton 200,000 sawa na 45% tu mahitaji ya chuma. Tena chuma hiki kinaingizwa kwa kodi kidogo au bila kodi kabisa huku tukijua tunadhoofisha sana viwanda vingi kujiandaa kufungwa. Hivyo, naomba kodi ya dola 400 kwa metric ton iongezwe ili kufidia gap kwa wafanyabiashara wa ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mambo matatu kwa Waziri wa Viwanda na Biashara. Naomba chuma kinachotoka nje kiongezwe ushuru hadi kufikia dola 400 kwa metric ton ili kulinda viwanda vya ndani. Kwa nini tunashindwa kuanzisha kiwanda chetu kwa ajili ya kuyeyusha chuma hapa nchini ili hata SGR ijengwe kwa chuma chetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, ile kampuni SHGL iliyokuwa inataka kununua migodi ya Liganga na Mchuchuma kwa miaka 100 ili wao wachukuwe 80% na Tanzania 20% makubaliano yamefikia wapi? Naomba kufahamu kuhusu wafanyabiashara kumi wa mji wa Kahama ambao walikamatwa toka mwezi wa 10 mwaka 2018 mpaka leo wana miezi saba wako ndani na hawajui hatima yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri afike katika Gereza la Shinyanga Mjini kujua hatima ya wafanyabiashara hao. Nini hatima yao? Naomba kama wamebainika na kosa wapigwe faini na waachwe waendelee na biashara zao. Ili kuweza kufikia uchumi wa viwanda ni lazima wafanyabiashara wetu tuwaone kwa jicho la huruma zaidi, kwani ndio nguzo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nakushukuru nami kwa kunipatia nafasi ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Naomba nianze kwa kumpongeza Mwenyekiti wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman Mbowe kwa kazi anayoifanya, lakini pia nimpe pole kwa changamoto anazopitia. Sisi kama Wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) bado tunaendelea kumtia moyo na tunamshukuru kwa kuijenga CHADEMA kama taasisi. Hata kipindi anachopitia changamoto taasisi inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na changamoto ambayo naona nisipoisema kidogo nitapata shida sana. Nianze na Mkoa wa Simiyu kabla sijaingia kwenye mambo mengine. Mkoa wa Simiyu umekumbwa na changamoto kwenye Halmashauri zake kwenye suala la uchumi. Halmashauri za Mkoa wa Simiyu zinakabiliwa na uhaba wa fedha, hususan Wilaya ya Itilima. Wilaya ya Itilima ni Wilaya ambayo imeshindwa kujiendesha kutokana na kwamba Wilaya ile ni mpya na haina mapato yoyote ya kuendelea kujiendesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu Serikali ianze kuchukua mapato kutoka kwenye Halmashauri zetu kumekuwepo na changamoto nyingi sana. Madiwani wanakopwa, hawalipwi posho zao, magari ya Halmashauri hayana service hakuna fedha, Wakurugenzi wanashindwa kusafiri kutoka sehemu nyingine kwenda sehemu nyingine kwa sababu hakuna fedha. Historia inaongea ni namna gani Serikali Kuu imeshindwa kukusanya mapato vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2017/2018 tulikusanya shilingi bilioni 11.172 na katika mwaka wa fedha 2018/2019 tumekusanya shilingi bilioni 8.434, sawa na upungufu wa negative 44.5. Hapa tutaona ni namna gani ambavyo tumeshindwa kukusanya mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema haya kwa masikitiko makubwa sana kwa sababu, wakati mapato yanakusanywa na Halmashauri zenyewe zilikuwa zina uwezo wa kujiendesha, lakini leo zimeshindwa kujiendesha kwa sababu kwanza wao wenyewe wameingiza hasara kwenye ukusanyaji wa napato takribani bilioni 6.8. Haya kwa nini tunayahitaji kuyaingiza kwenye Taifa letu? Nasisitiza na kuomba sana Serikali warudishe makusanyo kwenye Halmashauri zetu ili ziweze kujiendesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, naomba nizungumzie kuhusu bajeti ya maji. Mheshimiwa Waziri Mkuu amezungumza kwenye kitabu chake katika ukurasa wa 55, amesema upatikanaji wa maji umefanikiwa kwa asilimia 85. Historia inaongea, kwenye bajeti ya maji, Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge naomba tuipongeze Serikali ya Awamu ya Nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya Serikali ya Awamu ya Nne, nimechukua mfano mdogo tu. Bajeti ya mwaka 2012/ 2013, zilitengwa shilingi bilioni 466, zikatolewa shilingi bilioni 303, sawa na asilimia 65, hii sio mbaya ndio maana nimesema tuna kila sababu ya kuipongeza Serikali ya Awamu ya Nne. Mwaka 2013/2014 zilitengwa shilingi bilioni 553, zikapelekwa shilingi bilioni 353 sawa na asilimia 64. Mwaka 2014/2015 zilitengwa bilioni 485, zikatolewa shilingi bilioni 249 sawa na asilimia 50; akaja baba yangu, mwaka 2016/2017, zilitengwa shilingi bilioni 915.1, zikatolewa shilingi bilioni 350.99 tu sawa na asilimia 23. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati kiongozi pale Mheshimiwa John Mnyika ameuliza swali lake akajibiwa kwa kejeli na Serikali ikijinasua kwamba, imetekeleza jukumu la maji kana kwamba, asilimia zote imemaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi takwimu tunazotenga zenye namba nyingi…

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. GIMBI D. MASABA: …halafu utekelezaji wake unakuwa mdogo, nataka kuuliza ni nani wanayemdanganya? Kwa faida ya nani?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Gimbi kuna Taarifa.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimpe Taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba, utekelezaji wa miradi ya maji si kama kilimo cha matikiti kwamba, mwezi mmoja, mwezi wa tatu unavuna. Utekelezaji unaweza ukawekwa mwaka huu, ukavuka hadi miaka miwili, lakini atambue tu katika Mfuko wa Maji tumetengewa shilingi bilioni 158, mpaka mwezi Februari tumeshapokea zaidi ya shilingi bilioni 93. Pia tuna mitadi mikubwa ambayo inatekelezwa maeneo mbalimbali zaidi ya bilioni 54, milioni 154 zimeshatoka. Kwa hiyo, atambue hilo, nampa taarifa. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Gimbi, Taarifa hiyo.

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa siipokei. Kama ana majibu ya kwangu asubiri atanijibu wakati Mawaziri watakapokuwa wana-wind up. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeyasema haya nikisisitiza kwamba, kama Serikali ya nne ilitenga bajeti kidogo, wameona ni namna gani iliweza kutekeleza kwa asilimia ambayo inazungumzika. Hawa wanatenga kwa namba kubwa, matokeo yake utekelezaji ni hakuna, hiyo ndio hoja yangu ya msingi. Sasa nikahoji nani wanamdanganya na ni kwa faida ya nani, kwamba tukiongea namba kubwa, hii itawadanganya wananchi, sasa hali kadhalika hata sisi wenyewe humu Bungeni tunadanganywa. Nawashauri Waheshimiwa Wabunge tusomeni historia ya Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kuhusu suala la fedha za maendeleo. Hivyo hivyo historia inazungumza na kabla sijazungumza historia ya Serikali ya Awamu ya Nne nizungumze tu ni kwa mara ya kwanza bajeti ya Serikali ya Awamu ya Tano kutekelezwa kwa asilimia ishirini na… (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante, muda wetu ndio huo.
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya SADC ya Usimamizi wa Mazingira kwa ajili ya Maendeleo Endelevu (The Southern African Development Community SADC – Protocol on Environmental Management for Sustainable Development)
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nakushukuru, nami naomba kuchangia. Napenda tu niseme kwamba Itifaki hii kimsingi imekuja wakati ambao asilimia 80 za maambukizi ya magonjwa yanatokana na kemikali zinazotokana na madawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazungumza kuridhia Itifaki ya SADC, ni sawa, lakini natoa masikitiko yangu kwamba, pamoja na kwamba tunaridhia Itifaki hii lakini kumekuwa na utaratibu wa kutozingatia umuhimu wa mazingira ya Taifa letu. Ukiangalia bajeti ya mazingira iliyopita ni 0.0. Sasa nilikuwa najiuliza, tunavyozungumza kuridhia Itifaki hii, wakati huo huo Serikali haioni umuhimu wa kuboresha mazingira yetu kupitia bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba tunakwenda kuridhia vitu kama hivi, bado kwenye taarifa ya Makamu wa Rais imezungumzia asilimia 61 ya ukataji wa miti nchi yetu iko hatarini. Kwa hiyo, pamoja na kwamba Serikali imeleta Azimio hili na huku ukizingatia karibu dawa zote zinatumia kemikali, hata ukiangalia kwenye kilimo chetu, dawa tunazotumia kwenye mahindi zote zinatumia kemikali; ukienda kwenye mboga mboga zote zinatumia kemikali; nataka niiulize Serikali, imejipangaje kuhakikisha kwamba inakuja na utaratibu ambao utawezesha kkutupatia dawa ambazo hazina kemikali? Kwa sababu dawa karibu zote zina kemikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuzungumzia, kuhusu suala la ozone layer, bado narudi kule kule kwenye bajeti. Kwenye Bajeti Kuu ya fedha za Maendeleo kulikuwa na sifuri, lakini bado fedha za nje tulipata kiasi cha shilingi milioni 500. Sasa najiuliza, Wazungu wanaona umuhimu wa mazingira wa Taifa letu, lakini sisi hata huu mradi wa Ozone Layer hatuoni umuhimu wa kuzuia hili joto ambalo ni hatari kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza suala la mazingira ni lazima turudi kwenye Sheria Na. 20 ya mwaka 2004 kuhakikisha kwamba inatumika vizuri ipasavyo kuliko ambavyo tunavyozungumza kinagaubaga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mchango wangu niuelekeze kwenye Sheria ya Fidia kwa Wananchi kipindi anapopata madhara ya kujeruhiwa na wanyama hususani mnyama aina ya tembo. Kwamba mwananchi akijeruhiwa na tembo analipwa fidia shilingi laki tano mpaka milioni na fidia hizo zinatolewa kwa wakati, jambo ambalo linasababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi hawa. Hali kadhalika fidia ya mazao kwa wananchi kipindi mazao yao yanapoharibiwa wanarudishiwa fidia kidogo, ekari moja shilingi laki moja ilhali ekari moja ya kulima inakadiriwa kuwa laki moja, jambo ambalo si sawa, tunawapunja sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo ninaomba hii sheria ya fidia ibadilishwe kwani si rafiki tena kwa mazingira ya sasa kwani gharama za kilimo zinaongezeka kila siku na pia binadamu wanaongezeka lakini pia kutokana na kuwa na changamoto ya uharibifu wa tembo kuwa umekithiri, ni vizuri Serikali ikalitazama suala hili kwa undani zaidi ikiwa ni pamoja na kuchukua tahadhali zifuatazo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, inasadikiwa miti ya pareto ni adui wa tembo , sasa kwa nini Serikali isianzishe kampeni ya upandaji wa miti ya pareto kwenye maeneo ya pembezoni mwa hifadhi ikiwemo na upandaji wa pilipili kwani pia pilipili ni adui wa tembo?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha, ahsante.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada huu ni hatari kwa Wanahabari na maendeleo kwa ujumla, umelenga kuondoa kabisa uhuru wa habari. Muswada unasema Mwandishi wa habari akipewa taarifa na Afisa wa Serikali kuhusu jambo fulani anaweza kushtakiwa Mwandishi pekee na si aliyetoa habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, jambo la kutaifisha mitambo ya kutangazia au kuchapisha magazeti halipaswi kuungwa mkono. Waziri amepewa mamlaka ya kuelekeza nini chombo cha habari ki-report kwa wakati huo, hii itavinyima vyombo vya habari kukosa uhuru wa wake. Waziri au Serikali anaweza kuelekeza waandishi wote waandike habari hata za CCM pekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria za Tanzania zinamzuia Mwandishi wa habari kupiga picha au kuandika chochote wanapokuwa gerezani. Pia wanazuiwa ku-record au kutangaza live wakati Mahakama inaendesha kesi. Sasa Je, kwa namna hii, Tanzania kuna uhuru wa vyombo vya habari? Tunataka sheria hizi kandamizi zifutwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia sheria hii mpya imwondolee madaraka makubwa Waziri wa Habari. Kwa mfano kifungu cha 54 - 55 amepewa mamlaka makubwa sana, hivyo nashauri badala yake Baraza la Habari ndilo liwe na mamlaka ya kuvionya na kukemea vyombo vya habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania si yetu sisi wana UKAWA tu bali ni ya watu wote, hivyo Chama Tawala wakilazimisha kupitisha Muswada huu wajue wazi hawatukomoi sisi wana UKAWA tu bali wanaukomoa umma wa Watanzania na wao pia, siku moja utawageukia tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wa CCM kama kweli wapo hapa kwa ajili ya kula posho za vikao hata kama tungeandika mpaka tukatokwa na povu Muswada lazima upite tu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi nichangie Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi. Naomba nianze kwa kuunga mkono hoja ya Kambi ya Upinzani Bungeni. Hotuba yetu ina vitu vizuri, tumeshauri vizuri, naiomba Serikali ichukue ushauri huo utawasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite moja kwa moja kwenye Operesheni Nzagamba. Naenda moja kwa moja kwenye Operesheni Nzagamba kwa sababu ninafahamu ni nini ambacho ninakwenda kukizungumza na nini matokeo ya Operesheni Nzagamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposimama hapa, hususan mimi nikisimama ni kwamba si mgeni kwenye suala la ufugaji, hata uvuvi. Operesheni hii naomba niwaeleze Waheshimiwa Wabunge, kwamba tunapozungumza hii operesheni inawezekana wapo wachache ambao wanaielewa kwa udogo sana, lakini niwaambie kwamba jambo hili la Operesheni Nzagamba limesababisha matatizo makubwa sana. Limesababisha vifo, watu kufilisiwa ng’ombe wao; limesababisha matatizo mengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lililopita hapa tulipitisha Sheria ya Mahakama za Kutembea, tukazibariki. Sasa hiyo sheria tuliyoipitisha mimi nasema imekwenda kutumika kwa wafugaji. Imetumikaje; hawa waliokuwa wanatekeleza Operesheni Nzagamba walikuwa wanakwenda wakiwa na timu nzima; wakiwa na mnunuzi wa ng’ombe, wakiwa na dalali, wakiwa na Mwanasheria, wakiwa na mgambo. Sasa kama ng’ombe wanapigwa Itilima atakayenunua wale ng’ombe si wa Itilima, unakuta ametoka Katavi, unakuta ametoka mikoa mingine. Sasa najiuliza kwamba, hawa waliokuwa wanaenda kununua hawa ng’ombe walikuwa wanajuaje kwamba kuna mnada wa ng’ombe Itilima? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni changamoto ambayo ni kubwa. Kilichokuwa kinafanyika, wanakwenda na mgambo wakiwakuta wale wachungajhi wale, wanakimbia wanawaacha, wanawakimbia wale ng’mbe wao. Mgambo wanawazingira wale ng’ombe, wakishawazingira wale ng’ombe dalali anaanza kazi yake. Anaanza kufanya hivi, analeta ng’ombe mmoja-mmoja anasema ng’ombe huyu laki nne, anakosekana mnunuzi, laki tatu, anakosekana, laki mbili, anakosekana, laki moja, anakosekana. Anaweka pembeni analeta tena ng’ombe mwingine, laki nne, anakosekana, wakifika ng’ombe wanne anawaambia laki tatu kwa pamoja, mununuzi anapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alipoteuliwa, Wasukuma wote tulifurahi katika uteuzi wa Rais, tulishangilia kwa sababu anafahamu jiografia ya wafugaji, lakini umekwenda kututelekeza. Leo wafugaji wanalia anajifanya kwamba hajui umuhimu wa wafugaji, jambo ambalo linasikitisha sana. Naomba wanisamehe kaka zangu wote wanaotoka Mkoa wa Simiyu, Mheshimiwa Mpina ametutelekeza, haendani na kile tulichokuwa tunakitegemea sisi. Haiwezekani leo Mheshimiwa Waziri asisahau… (Makofi) [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Gimbi, Mheshimiwa Jenista kuhusu utaratibu.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ni jambo la kiutaratibu na watu wanaweza wakaliona ni jambo ambalo halina maana, lakini naomba niseme Kanuni ya 64(1)(b) inampasa kila Mbunge anayechangia humu ndani kuchangia hoja kwa kuzingatia hoja ambayo imewasilishwa ndani ya Bunge. Hoja inayochangiwa inahusu Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Waziri mwenye dhamana ya Mifugo na Uvuvi alipoteuliwa hakuteuliwa kwa muktadha wa kutazama kabila la Wasukuma, aliteuliwa ili kuwa na fairness, kusimamia sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza Sekta nzima ya Uvuvi na Mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, si sahihi sana kusema kwamba alipoteuliwa Waziri huyu, Wasukuma walifurahi lakini sasa Wasukuma wanasikitika amewatelekeza, siyo fair. Ni lazima tuseme siyo fair, tuchangie kwa kuzingatia utaratibu ambao… (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Jenista. Mheshimiwa Gimbi maneno hayo ni ya maudhi kwa hiyo naomba uyaondoe.

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siamini kama nimezungumza kitu ambacho ni cha ajabu sana, siamini. Nasema hivyo kwa kutumia lugha ya Wasukuma nikiamini kabisa kwamba Wasukuma ndiyo wafugaji wakubwa wakifuatiwa na Wamasai, nimezungumza hivyo. (Makofi)

MHE. AMINA S. MOLLEL: Taarifa.

MHE. GIMBI D. MASABA: Nimezungumza kwa uhalisia huo.

MHE. AMINA S. MOLLEL: Taarifa.

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo...

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge naona muda umeisha, hamna taarifa wala nini, Mheshimiwa Gimbi endelea.

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Gimbi naomba uendelee kutoa mchango wako kwa lugha iliyokuwa inastahiki Bungeni.

MHE. GIMBI D. MASABA: Nimezungumza haya kwa uchungu, sikutaka kwenda kwenye kitabu cha Waziri hata kidogo. Mara nyingi kwenye michango yangu nimekuwa nikisimama nazungumzia kuongezewa kwa bajeti…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Selasini kuna nini tena. Mheshimiwa Gimbi kidogo, Mheshimiwa Chief Whip wa upande wa Upinzani.

T A A R I F A

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepaswa nitoe taarifa hii kwamba hata wafanyabiashara wanafurahi kama Waziri mfanyabiashara ameteuliwa kwa sababu anaifahamu sekta. Kwa hiyo, Gimbi hakuwa na maana ya ukabila ila alikuwa ana maana kwamba kwa sababu Mheshimiwa Mpina ni mfugaji, basi wafugaji watafurahi kwa sababu anaifahamu sekta. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Gimbi naomba uendelee.

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza uhalisia wa mazingira yenyewe, Mheshimiwa Waziri anajua, pamoja na kwamba wananchi walitaifisha hizo ng’ombe, kuna wananchi walikwenda mahakamani na walishinda kesi.

Sasa anataka kuniambia kwamba wananchi walioshinda kesi Mkoa wa Simiyu, hajui kama wanatakiwa kurudishiwa ng’ombe wao? Mpaka leo hawajawahi kurudishiwa ng’ombe, halafu leo wanataka tuzungumze maneno ya upole, kwa vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la uvuvi, sawa Mheshimiwa Mpina amekulia dagaa lakini leo dagaa kwa wavuvi imegeuka almasi. Mkoa wa Simiyu tuna minada, leo ukienda kwenye mnada unatafuta dagaa huwaoni, lakini muuzaji wa dagaa yupo, maana yake ni kwamba dagaa ameficha guest, kwa hiyo ukimuuliza dagaa wapo wapi, zipo guest unataka? Huko ndiyo anatupeleka Mheshimiwa Mpina, dagaa wanauziwa guest halafu wanataka tuzungumze lugha ya kipole hapa, haiwezekani. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini ambacho hakifahamu Mheshimiwa Mpina kwa wafugaji na wavuvi, hapana haiwezekani…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Gimbi malizia sentensi yako.

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kidogo sekunde tu. Huu uanzishaji wa hifadhi za wanyamapori za jamii zimeleta changamoto kubwa sana. Mwaka jana nilizungumzia kuhusu suala la Hifadhi ya Maswa Reserve kuhusu kuongeza mipaka, wananchi wanakosa malisho na kila kitu, lakini wametanguliza watu wanakwenda kulaghai viongozi halafu wanachukua maeneo wananchi wanashindwa kupata machungio. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo yanaudhi sana, nakushukuru sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Kulitangaza Jiji la Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi wa Mwaka 2018
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru nami kwa kupata nafasi ili niweze kuchangia Muswada huu. Naomba niungane na wale wanaosema kwamba Kambi ya Upizani Bungeni hatupingani na hoja ya kwamba kufanya Mji wa Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi. Tatizo hapa ni taratibu ambazo tunazitumia, ukisoma kwenye huu Muswada hata ule ujanja ujanja unaotumika kupitisha Muswada huu utaelewa kabisa hata kama umesoma ukaacha vyeti shuleni, utajua kabisa kwamba kuna njia ambazo zinatumika ambazo siyo sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunajadili sheria ya kufanya iwe Makao Makuu ambapo masikitiko yangu ni kwamba kwa nini sheria hii haikuja kabla ya kuhamia hapa Makao Makuu. Mheshimiwa Rais alitoa tamko kwamba tunahamia Makao Makuu na ameshafanya utekelezaji, watu wote wamehamia hapa na tamko amelitamka Mheshimiwa Rais na akatekeleza. Leo Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI ameleta tupitishe sheria, sasa nataka nitoe masikitiko yangu kwamba kwa nini kwamba sheria hii haikuja kabla ya kuhamia hapa Makao Makuu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba Mwalimu Nyerere alitamka hapa patakuwa Makao Makuu ya Nchi, lakini kuna maswali tujiulize kwa nini Mwalimu Nyerere hakuhamia? Hakuhamia kwa sababu alikuwa hajaleta Muswada Bungeni wa kutunga Sheria ya Makao Makuu. Leo Rais wa Awamu ya Tano ametamka na kuhamia, hivi vitu hata ungemweleza nani unaona namna gani Serikali ya Awamu ya Tano wanavyokosea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu hata kama hutaki kuzungumza unazungumza, kuna vitu ambavyo vipo tofauti sana. Leo kuna Wabunge walijaribu kuzungumzia kuhusu suala la taratibu za kufanya kuwa Jiji, lakini kuna watu waliwapinga wakasema hapa tunachodiri sio Sheria ya jiji, bali tunajadili kupitisha sheria ya kufanya iwe Makao Makuu ya Nchi. Sasa najiuliza unawezaje kujadili suala la kupitisha Makao Makuu ya Nchi ukashindwa kujadili umuhimu wa Manispaa ya Mji kuwa Jiji unashindwaje? Kwa sababu hivi vitu viko wazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na Mheshimiwa Halima Mdee bosi wangu aliyezungumza kwamba, ukisoma kwa mujibu wa Sheria Na.8 ya mwaka 2007, kifungu cha tano
(5) kwamba Bunge ndio lenye Mamlaka ya kupitisha kuangalia hadhi ya namna ya jiji ndio lenye Mamlaka, kwa kujiridhisha kwa mambo matatu. Kuangalia idadi ya watu angalau ifikie laki tano, lakini pia kuangalia mapato angalau yawe yamefikia asilimia tisini na tano, lakini pia kuangalia miundombinu yenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo sisi tunatangaza kuhamia Makao Makuu ya Nchi ili hali miundombinu bado sio. Barabara kuu ni moja tu hiyo ndio inayosomeka lakini mbwembwe nyingi tunazungumza kuhamia Makao Makuu kufanyaje, jamani kwani ukienda pale airport sisi kila siku tunasafiri jamani, tunakwenda kwenye nchi zingine hata ukienda hapo China wenzetu wamepanga miji, sisi tukitaka kupanga miji tunabomolea watu. Serikali inashindwa nini kutenga maeneo mazuri halafu ikaanzisha miundombinu mizuri, kupanga miji mizuri, halafu ndiyo baadaye tunakuja kutangaza jiji mahali hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunatagaza jiji halafu tunawaambia wanachi waondoke, tunawabomolea, hii sio sawa jamani, tunalazimisha kitu ambacho bado hakijawa vizuri. Pia tukigusa maslahi ya Watumishi sijui nini na nini taarifa zinaanza, kwa nini hatutaki kuuona ukweli kwamba tumekosea. Leo tunapitisha hii sheria halafu tafsiri yake ni nini? Ni kwamba mtasema Bunge limetunga Sheria ya Kuhamia Makao Makuu au Rais ndio ametunga sheria ya kuhamia Makao Makuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vitu ambavyo tunatakiwa kujiuliza. Kwa hiyo, hivi vitu pamoja na kwamba wengine hatujui sheria hivi vitu viko wazi. Tumeona utaratibu wa Majiji, tumeona utaratibu wa Makao Makuu upo wazi. Hii ni nini? Sawa labda kama wameamua kuwafuta Wagogo watani zangu, kuwasuuza maana kipindi kile Obama anakuja hapa waliwasomba kutoka Dar es Salama kuwaleta hapa. Sasa yawezekana wameamua kuwafurahisha ili kuondoa ile dhana. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.