Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Charles Muhangwa Kitwanga (11 total)

MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Wananchi wa Jimbo la Igalula hususani Kata ya Loya na Halmashauri yetu imefanya kazi kubwa sana kujenga kituo hicho cha polisi na nguvu kwa sasa imetuishia na kazi kubwa imefanyika. Serikali kupitia Wizara haioni umuhimu wa kusaidia nguvu hizi za wananchi katika kumalizia kituo hiki cha polisi na kiweze kuanza kufanya kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kata ya Igalula na Kata ya Kigwa kuna vituo vya polisi ambavyo vingeweza kutoa huduma katika Kata ya Loya kipindi hiki hatuna kituo kituo cha polisi katika Kata ya Loya. Tatizo letu kubwa lililopo pale katika vituo hivi viwili vya polisi havina usafiri. Je, Wizara haioni umuhimu wa kuvipa usafiri vituo hivi vya polisi ili viweze kuendelea kutoa huduma katika maeneo ambayo hayana vituo vya polisi?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali bado inaendelea na juhudi zake za kuhakikisha kwamba inajenga vituo mbalimbali katika nchi yetu. Kwa hiyo basi, pamoja na juhudi zilizofanywa na wananchi, nimwombe Mheshimiwa Mbunge ashirikiane na Serikali na kuona kwa namna gani tunaweza tukakamilisha kituo hiki. Nina uhakika kabisa wananchi kwa juhudi walizozifanya bado kuna nafasi ya kuendelea kushirikiana na Serikali ili kukamilisha ujenzi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili amezungumzia tatizo la usafiri. Ni kweli vituo vingi havina usafiri lakini Serikali katika bajeti yake ya mwaka huu inajipanga kuhakikisha kwamba inanunua magari mengi ili kuweza kuvipatia vituo mbalimbali usafiri na tutaangalia kituo kimojawapo kati ya alivyovisema tutaweza kukipatia usafiri.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa kituo cha Chalinze ni kituo ambacho kiko kwenye barabara kuu ya kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma na kituo hicho hakina computer hata photocopy hakuna.
Kwa hiyo, ukipata tatizo wanaenda kutoa photocopy nje kwenye stationery. Ni lini Serikali itaona umuhimu wa kuwawekea photocopy machine ya kuwa wanatumia kuliko kusambaza nje siri za kituo hicho?
WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, juzi tu Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo hilo alinipigia simu, tuliongea naye na hayo anayosema Mheshimiwa Mbunge tuliyazungumza. Kwa hiyo, asiwe na wasiwasi ajue kwamba na Mbunge wa Jimbo hilo ameshanieleza tatizo hilo na tutalitatua.
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ingawaje dah, Waziri kajibu kwa pozi kweli kweli mistari michache tu. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, anasema kwamba wanaendelea kujenga, hivi miaka 51 ya Uhuru upungufu nyumba 10,000 wapewe miaka mingapi ili wamalize hili tatizo katika nchi yetu? Magereza nimeshuhudia mwenyewe kwa mfano katika Wilaya yetu ya Kilombero kuna magereza mawili ya Idete na Kiberege wafungwa wanaenda kujenga nyumba za watu binafsi kwa nini msitumie nguvu kazi ya wafungwa hawa ili kwenda kujenga nyumba na Serikali muongeze hela kule juu kumalizia majengo haya? Hiyo nguvu kazi ya hawa wafungwa walioko magerezani mtafanya lini huo mpango? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la Polisi yaani kama kuna tatizo kubwa ndani ya Mkoa wa Morogoro ni suala la nyumba za Polisi hasa Wilaya ya Kilombero likiwemo na Jimbo la Mlimba. Kwanza Wilaya ya Kilombero pale Ifakara kulikuwa na majengo ya Kituo cha Polisi, Mlimba hakuna kabisa wanategemea TAZARA…
MWENYEKITI: Mheshimiwa naomba uulize swali tafadhali.
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Na zile nyumba zimeuzwa ule mwaka zilizouzwa nyumba za Serikali.
MWENYEKITI: Mheshimiwa naomba uulize swali kwa ufupi.
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Sasa hivi hawana nyumba kabisa. Je, Serikali katika huo mpango wao wana mpango gani wa kujenga nyumba na Vituo vya Polisi ndani ya Wilaya ya Kilombero, Ifakara na Jimbo la Mlimba ambapo wanakaa kwenye vituo vya TAZARA?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu ni rafiki yangu sana. Ananiuliza tupewe miaka mingapi, yeye ana miaka mingapi? (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeeleza na nirudie tena tunafanya kila linalowezekana tuhakikishe askari wetu wanakuwa na mahali pazuri pa kukaa. Ndiyo jibu sahihi, tunafanya kila linalowezekana askari wetu wawe na mahali pazuri pa kukaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili nalo ni kwa sababu yeye ni rafiki yangu namjibu, mpango gani? Mpango nimeueleza kwenye jibu langu la msingi na nimhakikishie tu kwamba tutafanya kwa jinsi tulivyoeleza katika mpango wetu kuhakikisha kwamba askari wote wanapata nyumba nzuri na mahali pazuri pa kukaa.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri lakini naomba, kwa sababu Singida ni center ambapo watu wengi wanaosafiri wanapita mkoa ule na unaona kabisa zile nyumba za maaskari pale kushoto baada ya uwanja wa Namfua. Sasa yuko tayari kuanzia pale kabla hajaenda mikoa mingine ili zile nyumba zikatengeneze sura ya Mkoa wa Singida?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Martha Mlata, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Singida na Tabora siyo mbali basi tutazingatia pendekezo lake.
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza. Kwa kuwa wananchi wengi wameitikia wito wa kusaidiana na Serikali katika kujenga Vituo vya Polisi hususani katika Wilaya yangu Bahi, wananchi wa Kijiji cha Chipanga A, kwa miaka mitano iliyopita wamejenga kituo cha kisasa, kikubwa na kwa asilimia 100 wamejenga wao wenyewe. Licha ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani aliyekuwepo Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha na Naibu Waziri wa baadaye Mheshimiwa Silima kutembelea kituo kile na kumuomba kifunguliwe na wao wakaahidi kitapokelewa na Serikali na kufunguliwa lakini hadi sasa ni miaka mitano mpaka kituo kile kinachakaa hakijafunguliwa. Je, ni lini Serikali sasa itakipokea kituo hicho na kukifungua kabla hatujaamua kukitumia kwa matumizi mengine?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Bahi, kwa jinsi ambayo wameweza kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa kituo hicho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nichukue fursa hii kuwaelekeza Jeshi la Polisi nitakapotoka hapa wanipatie taarifa ni kwa nini mpaka leo kituo hiki hakijafunguliwa. Baada ya kupata taarifa hiyo tutakaa na Mheshimiwa Mbunge tuone utaratibu wa kuweza kukifungua.
MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kanuni ya 145(a) na (b), yeyote ambaye anaingia katika maeneo ya Bunge au ukumbini ni lazima akaguliwe. Kwa utaratibu huo huo, magari ya Mawaziri na ya Wabunge wakati mwingine hukaguliwa kwa kutumia mbwa. Unapotumia mbwa kukagua magari wakati mwingine hudondosha mate na yale mate ni najisi tunaita muhalladha na najisi ile haiondoki mpaka uoshe mara saba na mara moja uhakikishe unatia mchanga. Je, hakuna utaratibu mwingine mzuri wa ku-check magari haya hasa kwa wale waislamu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Bunge lililopita tulishuhudia Mbunge mwenzetu akivamiwa katika maeneo anayoishi na kuharibiwa gari lake. Je, Bunge lina utaratibu gani kuhakikisha kwamba Wabunge hawa wanapata ulinzi au usalama wao unalindwaje kwenye maeneo yao wakiwa katika Bunge hili?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rashid Abdallah kwa observation yake ya msingi kabisa ambayo ni ya kiimani. Kwa kuwa ameuliza hakuna utaratibu mwingine na sisi kama Serikali pamoja na Bunge tuseme tumepokea ushauri ili tuli-digest jambo hilo huku tukiangalia maslahi mapana kwani imani inatuhusu na ulinzi unatuhusu. Kwa hiyo, ni jambo ambalo sote tutaliangalia tufikie muafaka mzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la pili kuhusu Mbunge kuvamiwa, taarifa zake tunazo na tunachofanya ni kuimarisha ulinzi katika mazingira ya Wabunge wetu ili kuhakikisha kwamba wako katika maeneo salama. Niwahakikishie tu Wabunge kwamba wako mikono salama na kwa kuwa mnafanya kazi vizuri na sisi tunahakikisha kwamba wanakuwa salama. Niwatangazie tu Watanzania kwamba Wabunge hawa wanachapa kazi na jana wamechapa kazi mpaka saa sita usiku, wameunganisha kikao hiki. Kwa hiyo, wanapokutana nao huko uraiani watambue kwamba Wabunge hawa ni wachapakazi. Niwaambie vijana wangu kwamba hata wanapokuwa barabarani hawa Wabunge wakiona wako speed wawaambieni tu tunawahitaji lakini watambue ni kutokana na uchapakazi wao wanawahi mikutano.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa katika suala zima la ulinzi tunategemea sana askari wetu, lakini tumekuwa tukishuhudia askari wetu wakipoteza maisha wakiwa kazini wakati mwingine kwa kupambana na majambazi au wakipata ajali kwenye misafara mbalimbali. Nataka kufahamu Serikali ina utaratibu gani wa kuhudumia familia za askari hawa wanaopoteza maisha wakiwa kazini kama kusomesha watoto na huduma na huduma nyingine muhimu?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Catherine kwa kulileta jambo hilo. Ni kweli kumekuwepo na matatizo hayo na sisi kama Wizara niliwaelekeza wataalam wangu kuangalia maeneo ambayo yanahusu sheria na yale yanayohusu sehemu ya bima kwa ajili ya askari wetu ili kuweza kusaidia askari kwanza akiwa bado yuko kazini, pale anapopata ajali kazini kuweza kuhudumiwa katika maumivu anayoyapata. Nilipozunguka nilipata taarifa kwamba kuna askari wanaumia kazini wanaambiwa bima haiingii kwenye baadhi ya vipimo ama katika baadhi ya dawa wanazotaka.
Kwa hiyo, hili la kuzihudumia familia wanapokuwa wamepata ajali tunaliangalia kwa mapana kisheria ili familia hizo zisiyumbe baada ya kuwa askari wetu amepata ajali.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kabla sijauliza swali langu, naomba kuwashukuru wale wote ambao wanatoa misaada kwa Wilaya yangu ya Bukoba Mjini na naomba Watanzania wote na wasio Watanzania waangalie kwa jicho la huruma Bukoba Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kumuuuliza Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa Wizara yake inalinda raia na mali zao, hivi sasa Wilaya ya Bukoba Mjini watu wote wanalala nje na matatizo wanayoyapata ni kuibiwa mali zao na askari wanakwenda na kukamata wale watu ambao wanawasaidia wale wahanga. Je, Wizara yake imejipangaje kwenda kukabiliana na janga hili Bukuba Mjini kwa kuwalinda raia?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge wa jambo alilolileta ambalo liko muda huu. Niseme tu tangu tukio limetokea Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kushirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama Mkoa na Wilaya wameimarisha ulinzi katika maeneo husika. Kwa kuwa watu ni wengi inatokea katika kutafuta namna ya kujiridhisha kujua yupi anayeenda kwa ajili ya kutoa huduma na yupi anayeenda kwa ajili ya kukwapua ama kuchukua vile ambavyo vimezagaazagaa, kwa hiyo, ndiyo maana utaona kuna mwingiliano wa aina hiyo, lakini nia ya Wizara pamoja na Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya ni kuhakikisha kwamba watu hawa ambao wamepata matatizo wao pamoja na mali zao wanakuwa katika hali ya usalama.
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ieleweke kuwa wananchi wa Siha siyo kwamba wanachukia polisi kuwepo katika eneo hilo lakini kilichoonekana ni kwamba watu wameongezeka sana katika eneo hili na ushahidi upo kwamba wameshakufa watoto wanne na tarehe 18/08/2016 kuna mtoto ambaye risasi ilimfuata nyumbani na mpaka sasa ana ulemavu. Maswali yangu mawili ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Serikali isione ni busara sasa na ni wakati muafaka ikafuata ushauri wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Siha ya kwamba mazoezi ya polisi yapelekwe katika eneo la heka 500 ndani ya NARCO lakini hilo eneo likagawanywa katika sehemu tatu? Sehemu ya kwanza ni kutoa eneo ambalo litasaidia kupunguza ukata wa ardhi kwa wananchi wa Siha hasa walioko upande wa milimani, sehemu ya pili ikatolewa kwa ajili ya kufanya utalii wa kimila. Kama mnavyokumbuka mwaka huu Waziri wa Utamadumi alikuja pale na alifanya tukio kubwa ambalo linafanyika East Africa yote kwa ajili ya utalii. Kwa hiyo, Wizara ya Utamaduni na Idara ya Mambo ya Kale ikakabidhiwa chini ya Halmashauri eneo lingine kwa ajili ya kufanya utalii wa kimila. Eneo linalobaki tukajenga Chuo Kikuu cha Polisi badala ya kufanyia mazoezi yanayowaathiri wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni kwamba…
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Huwa sichanganyikiwi mkiongea sana. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, wananchi walioumia na huyu mtoto aliyepata ulemavu Serikali iko tayari kutoa fidia lakini vilevile Waziri kutembelea kuwaona waathirika?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo alilopendekeza ametaja kwamba ni eneo la NARCO na NARCO iko chini ya Wizara nyingine na Wizara husika wana mpango wa matumizi wa eneo hilo. Ninachotambua ni kwamba ni kweli Wilaya ya Siha pamoja na Mkoa mzima wa Kilimanjaro una matatizo makubwa ya ardhi. Mkoa pamoja na Wilaya kwa kushirikisha Wizara ya Ardhi mara kwa mara wamekuwa wakiangalia mpango bora wa matumizi ya ardhi na sisi kama Wizara ya Mambo ya Ndani ni sehemu ya Serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata eneo. Hata hivyo, kwa sasa yale niliyoyasema kwenye jibu la msingi yanasimama kwa maana tunatarajia kupima eneo lile ambalo linatumika kwa ajili ya mafunzo, kuweka alama na wananchi hawa waweze kutafutiwa maeneo mbadala ambapo mazungumzo yameendelea katika maeneo tofauti na Waziri wa Ardhi alishafika kule kuweza kuangalia njia bora ya kuwapatia vijana maeneo ya ardhi kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hili ambalo amelisemea la kijana aliyeumia, kwa niaba ya Wizara na Serikali nitoe pole na tumepokea hayo ambayo ameyasema kama mapendekezo. Tutaongea na wataalam tuone ni kitu gani wamekuwa wakifanya punde yanapotokea mambo ya aina hiyo.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja dogo la nyongeza.
Kwa kuwa suala la usalama ni jambo la msingi sana kwa raia wa Tanzania, kumekuwa na matukio mengi sana ya watu kupigwa na wengine kuuawa katika mpaka wa Kiteto na Chemba. Polisi wa eneo hili hasa wale wa Wilaya ya Chemba walioko Mrijo wanashindwa kufuatilia matukio haya kutokana na ukosefu wa vifaa ikiwemo magari, wengi wanaazima pikipiki na wakati mwingine baiskeli. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba vifaa vinapatikana katika maeneo ambayo kuna matatizo kama haya ili kunusuru wananchi na mali zao?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Nkamia kwa kulisema jambo hili na niwahakikishie tu wananchi wa Chemba kwamba Mheshimiwa Nkamia amekuwa akifuatilia sana suala hili. Ameshakuja mara kadhaa ofisini na mimi nimemuahidi kwamba tutakapopata magari kwa ajili ya Wilaya mpya na Wilaya Chemba tutaipa kipaumbele zikiwepo na Wilaya nyingine kama Mkalama ambapo Mheshimiwa Allan Kiula naye amekuwa akisumbua mara kwa mara. (Makofi)
Kwa hiyo, napenda kumwambia Mheshimiwa Nkamia suala la magari pamoja na nyumba za askari katika Wilaya yake mpya tutalipa kipaumbele kwa kutambua mazingira tete ya eneo hilo ambapo pana changamoto za kugombania matumizi ya ardhi ambayo yanahitaji sana askari kuwepo katika maeneo hayo. Nitoe rai kwa wananchi wa maeneo husika watoe ushirikiano kwa Jeshi la Polisi punde mtu mmoja anapokuwa amekiuka sheria katika maeneo husika ili aweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Na mimi naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa zama hizi tumeona askari wakifanya mazoezi katika barabara wakiwa na silaha za moto na kwa mujibu wa sheria vikosi vyote vya ulinzi na usalama wana maeneo yao maalum ya kufanyia mazoezi. Je, Serikali haioni kwamba wanawapa maadui nafasi kuona udhaifu wa askari wetu na kuingiza maadui kupambana na vyombo vya ulinzi na usalama? Ni kwa nini vyombo hivi visibaki sehemu zao za kufanyia mazoezi huko huko vilikopangiwa?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza vikosi vya ulinzi na usalama kufanya mazoezi ni sehemu ya maisha yao…
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Na kila siku kwao ni mazoezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili alilosema kwamba kufanya mazoezi barabarani wanawafanya maadui wajue udhaifu wao, nimwambie tu mazoezi yale wanayofanyia barabarani ni ya viuongo na ni sehemu tu ndogo kati ya yale mazoezi makubwa wanayofanya ya kukabiliana na wahalifu. Na mimi niseme tu kwamba kwa mwananchi yeyote ambaye havunji sheria hana haja ya kushtuka anapoona askari wanafanya mazoezi. Wanafanya mazoezi hayo kwa ajili ya wahalifu, kwa hiyo, kama siyo mhalifu huna haja ya kuwa na mashaka.