Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Kiswaga Boniventura Destery (20 total)

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA aliuliza:-
Kituo cha afya Kisesa kiliombewa kibali ili kipandishwe hadhi kuwa Hospitali kamili:-
Je, ni lini Serikali itatoa kibali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniventura Destery Kiswaga, Mbunge wa Magu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007, kila Wilaya inatakiwa kuwa na hospitali moja ya Wilaya na tayari hospitali hiyo ipo katika Wilaya ya Magu. Kituo cha Afya cha Kisesa kiliombewa kuboreshwa ili kiweze kutoa huduma za upasuaji mdogo kukidhi mahitaji hayo kwa wagonjwa badala ya kutegemea hospitali ya Wilaya pekee.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kituo hicho kianze kutoa huduma za upasuaji, Serikali iko katika hatua za mwisho za umaliziaji wa ujenzi wa jengo la upasuaji, jengo la kuhifadhia maiti pamoja na chumba cha X-ray. Aidha, tayari X-ray machine imeshapatikana, inasubiri tu kufungwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa chumba cha X-ray.
MHE. KISWAGA B. DESTERY aliuliza:-
Nyumba za kuishi walimu ni chache katika maeneo yao ya kazi na
mishahara yao pia ni midogo kuweza kumudu upangaji wa nyumba mitaani.
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga nyumba za walimu na
kuboresha mishahara yao?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kiswaga Boniventura Destery, Mbunge wa Magu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mahitaji ya nyumba za walimu wa Shule za Msingi katika Halmashauri ya Magu ni 1,447, zilizopo ni nyumba 284 na upungufu ni nyumba 1,183. Aidha, Shule za Sekondari zina mahitaji ya nyumba 396, zilizopo ni nyumba 53 na upungufu ni nyumba 343.
Mheshimiwa Spika, kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari ya Awamu ya Pili (MMES II), Halmashauri imepokea shilingi milioni 326.8 ambazo zitatumika kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya nyumba za walimu. Kwa upande wa Shule za Msingi, Serikali katika mwaka wa fedha 2015/2016 imetenga shilingi milioni 100 kutokana na mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa nyumba tano na shilingi milioni 127 zimetengwa kupitia ruzuku ya maendeleo (CDG) kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa nyumba sita za walimu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kuboresha mishahara ya walimu, Serikali imekuwa ikitoa nyongeza za mishahara kila mwaka kadiri uchumi unavyoruhusu. Kwa mfano, mwaka 2007/2008 hadi mwaka 2015/2016 mshahara wa mwalimu mwenye cheti yaani astashahada, uliongezeka kwa asilimia 156.28 kutoka shilingi 163,490/= hadi shilingi 419,000/= kwa mwezi. Mshahara wa mwalimu mwenye stashahada uliongezeka kwa asilimia 160.2 kutoka shilingi 203,690/= hadi shilingi 500,030/=; na kwa mwalimu mwenye shahada kwa asilimia 121.05 kutoka shilingi 323,900/= hadi shilingi 716,000/= kwa mwezi. Serikali imekuwa ikiboresha mishahara hiyo kwa kuzingatia umuhimu wa kazi wanayofanya walimu. Hata hivyo, Serikali inaendelea kuboresha mishahara ya walimu na watumishi wengine kwa kadiri hali ya kifedha inavyoruhusu.
MHE. KISWAGA B. DESTERY aliuliza:-
Pamoja na kwamba polisi ni walinzi wa raia na mali zao, ila wanakabiliwa na changamoto za nyumba za kuishi, maslahi duni na ukosefu wa vitendea kazi:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha vitendea kazi kama magari na mafuta?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga nyumba za askari polisi na kuboresha mishahara yao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kiswaga Boniventura Destery, Mbunge wa Magu lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikiboresha hali ya vitendea kazi kwa Jeshi la Polisi ikiwemo vyombo vya usafiri, mawasiliano na zana nyingine za kazi. Mathalani kwa mwaka wa fedha 2015/2016, Serikali ililipatia Jeshi la Polisi jumla ya magari 387 kati ya magari 777 yanayotarajiwa kununuliwa. Aidha, Serikali inatarajia kuongeza fedha ya mafuta na vilainishi katika bajeti ya mwaka wa fedha ya 2016/2017. Ni kweli kuwa Jeshi la Polisi, linakabiliwa na changamoto ya uhaba wa nyumba za makazi ya Askari. Kupitia Mpango Shirikishi wa wadau mbalimbali na mikopo yenye riba nafuu, Serikali inakusudia kujenga nyumba jumla yake ni kama 4,136 katika mikoa 15 pamoja na Mikoa mitano ya Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika kulipatia ufumbuzi wa kudumu tatizo la makazi kwa askari. Serikali inaandaa mpango mkakati wa kujenga nyumba zaidi ya 35,000 kufikia mwaka 2025, ikiwa ni wastani wa takriban nyumba 3,500 wa kila mwaka.
Aidha, Serikali itaendelea kuliwezesha Jeshi la Polisi kutatua changamoto za makazi ya askari kwa kudhamini mikopo nafuu kutoka Taasisi ya kifedha na kuchangia ujenzi wa nyumba pale bajeti inaporuhusu. Kama ilivyo kwa watumishi wengine wa Umma, Serikali imekuwa ikiongeza viwango vya mishahara, kwa Askari wa Jeshi la Polisi kila mwaka.
MHE. KISWAGA B. DESTERY aliuliza:-
Serikali imeweka mpango wa umeme vijijini ambapo kwa Jimbo la Magu ni asilimia 20 tu ya vijiji ndivyo vimepata umeme ambalo ni hitaji muhimu kwa kila Mtanzania:-
(a) Je, asilimia 80 ya vijiji vilivyobaki vitapata lini umeme?
(b) Je, Serikali imejipangaje kukabiliana na tatizo la kukatikakatika kwa umeme nchini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniventura Desdery Kiswaga, Mbunge wa Magu, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kutambua juhudi za Serikali za kusambaza umeme katika Jimbo lake la Magu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji 39 kati ya 142 vilivyoko kwenye Jimbo la Mheshimiwa sawa na 27% tayari vimepatiwa umeme. Hata hivyo, vijiji 18 sawa na 13% viko katika utekelezaji wa awamu ya pili na hivyo kufanya jumla ya vijiji 57% sawa na 40% kuwa vimepatiwa umeme mara baada ya awamu ya pili kukamilika Juni, 2016. Vijiji 34 kati ya 85 vilivyosalia vitajumuishwa kwenye mpango wa usambazaji umeme awamu ya tatu utakaoanza Juni, 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la kukatikakatika kwa umeme nchini inatokana na sababu za uchakavu na kuzidiwa kwa miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme na vituo vya kupoza umeme. Sababu nyingine ni pamoja na matukio ya kulipuka kwa transfoma yanayosababishwa na radi hasa kipindi cha mvua pamoja na wizi wa mafuta ya transfoma unaofanywa na wananchi wasiokuwa waaminifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na tatizo la kukatikakatika kwa umeme nchini, TANESCO inachukua hatua za kujenga mifumo ya njia kubwa za umeme wa msongo wa kilovoti 400 za backbone unaoanzia Iringa – Dodoma - Singida - Shinyanga. Kadhalika kuanzisha mradi wa North East Grid unaoanzia Dar es Salaam – Chalinze - Tanga - Arusha. Sambamba na miradi hiyo, upo mradi wa North West Grid unaoanzia Geita – Chalinze – Katavi – Kigoma - Rukwa - Mbeya. Hali kadhalika na mradi wa Makambako - Songea wenye kilovoti 220.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kukamilika kwa miradi hii, kutaimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika maeneo mengi nchini. TANESCO inakamilisha upanuzi wa mifumo ya usambazaji wa umeme katika Majiji makubwa ya Arusha, Dar es Salaam pamoja na Mwanza. Kazi zinazohusika ni pamoja na ujenzi wa njia mpya za umeme na kupanua vituo vya kupoza umeme (substations). Kukamilika kwa kituo cha kupoza umeme cha KIA Mkoani Kilimanjaro kutaimarisha sana upatikanaji wa umeme maeneo ya Mererani pamoja na uwanja wa ndege wa KIA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vituo vya kupoza umeme katika Jiji la Dar es Salaam vya Gongolamboto, Kipawa, Mbagala na Kurasini vitaunganishwa kwa njia ya sakiti mizunguko (ring circuits) kutoka Ubungo, Kinyerezi kuanzia Machi, 2016. Kukamilika kwa mradi huu kutaimarisha upatikanaji wa umeme katika maeneo yanayohudumiwa na vituo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingine ni ule wa ujenzi wa kituo cha kupoza umeme katikati ya Jiji la Dar es Salaam ukijumuisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 chini ya ardhi kwenda kituo cha Sokoine pamoja Kariakoo. Aidha, ifikapo Machi, 2016, TANESCO itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Udhibiti wa Mfumo wa Usambazaji wa Umeme kwa Jiji la Dar es Salaam (Dar es Salaam Distribution Management System).
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na tatizo la umeme hasa kuungua kwa transfoma, TANESCO imeendelea kufunga mifumo ya kudhibiti radi (lightning arrestors) nchi nzima na kuachana na transfoma za mafuta hasa maeneo yaliyokithiri kwa wizi wa mafuta.
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA aliuliza:-
Serikali ilitenga eneo la Sayaka Salama Bugatu kuwa hifadhi ya msitu, lakini msitu wenyewe haukui huku wananchi, wafugaji na wakulima wakikosa maeneo ya mifugo yao na kilimo.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwarudishia wananchi maeneo hayo ili waweze kuyatumia kwa kilimo na mifugo.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniventura Desdery Kiswaga, Mbunge wa Magu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, msitu na hifadhi Sayaka ulitangazwa rasmi kuwa Msitu wa Hifadhi chini ya Serikali Kuu kwa Tangazo la Serikali namba 90 la tarehe 19 Juni 1996. Katika siku za nyuma Halmashauri ya Wilaya ya Magu iliomba kubadilishwa kwa matumizi ya msitu huu wenye ukubwa wa hekta 5421, lakini kwa kuzingatia sababu za msingi za kiuhifadhi, Wizara kupitia barua kumbukumbu namba JA/66/298/02/33 ya tarehe 19 Desemba, 2001 ilikataa ombi hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hifadhi ya msitu wa Sayaka ni sehemu muhimu sana inayochuja na kudhibiti taka nyingi kutoka mto Duma unaopita katika hifadhi hii. Uwezo huu wa kudhibiti na kuchuja taka ambazo ni pamoja na tope na viuatilifu vinavyotoka mashambani unatokana na uoto wa asili uliopo ambao unahitaji kuboreshwa zaidi ili uendelee kupunguza athari za tope na viuatilifu katika Ziwa Victoria.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, hatua ya kubadilisha msitu huu na kuwa mashamba eneo la kuchungia mifugo au shughuli nyingine za kibinadamu zisizo za uhifadhi itasababisha kupotea kwa uoto wa asili na kusababisha mmomonyoko mkubwa wa udongo ndani ya hifadhi na hivyo kuruhusu taka nyingi kuingia ziwani jambo ambalo litapunguza uhifadhi wa mazingira ya Ziwa Victoria ambalo ni muhimu kwa Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu mkubwa wa msitu wa Sayaka, Serikali haina mpango wa kubadilisha matumizi yake kinyume na malengo ya kuanzishwa kwake, kwani hatua hiyo itasababisha athari kubwa na nyingi za kimazingira na kiuchumi. Aidha, wananchi wanaoishi vijiji vinavyozunguka Msitu wa Hifadhi ya Sayaka ndiyo watakaokuwa waathirika wa kwanza kwa upepo mkali, upungufu wa mvua utakaoathiri mifugo na kilimo na athari nyinginezo kwa siku zijazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuanzishwa kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania mnamo mwaka 2011, usimamizi na ulinzi wa misitu huu umeimarishwa na kufanya uoto wa asili kurejea kwa kufanya marejeo ya soroveya, kuimarisha mipaka na kuweka vigingi 65 katika mipaka. Aidha, Kamati za Maliasili za Vijiji Kumi ndani ya Halmashauri ya Magu zimeanzishwa kwa ajili ya kushirikiana na wataalam katika ulinzi wa msitu huu.
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA aliuliza:-
Zahanati za Nyang‟hanga, Salongwe, Nsola, Bundilya, Nyamahanga, Nyashingwe, Chabula, Ikengele, Isangijo, Langi na Lutale ziko kwenye hatua za ukamilishaji.
Je, ni lini Serikali itazikamilisha zahanati hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniventura Destery Kiswaga Mbunge wa Magu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016 Halmashauri ya Wilaya ya Magu imetengewa shilingi milioni 160 kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa zahanati kumi na tano ambazo ziko katika hatua mbalimbali. Vilevile katika mwaka 2016/2017 zimetengwa shilingi milioni 212.7 kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, azma ya Serikali ni kuhakikisha tunakamilisha majengo hayo ili huduma zianze kutolewa. Kama nilivyoeleza hapa Bungeni mara kadhaa, hivi sasa tunakamilisha tathmini ya ujenzi wa miundombinu ya zahanati na vituo vya afya ili kuandaa mpango wa haraka utakaosaidia kukamilisha ujenzi wa majengo hayo muhimu kwa nchi nzima.
MHE. KISWAGA B. DESTERY aliuliza:-
Wazee wa nchi hii walilitumikia Taifa na kuchangia Pato la Taifa:-
Je, ni lini Serikali itaanza kuwapatia kiinua mgongo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kiswaga Boniventura Destery, Mbunge wa Magu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Namba 6 ya mwaka 2004, kiinua mgongo ni malipo yanayolipwa na mwajiri kama mkono wa ahsante kwa mfanyakazi wake baada ya kumaliza mkataba wa kazi. Hata hivyo, katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 na kuwalinda wazee wa nchi hii na umasikini wa kipato, Serikali inaandaa mpango wa pensheni kwa wazee nchini. Aidha, hadi sasa Serikali imetekeleza mambo yafuatayo:-
(i) Kuainisha idadi ya wazee wote nchini;
(ii) Kuainisha viwango vya pensheni;
(iii) Kuandaa utaratibu utakaotumika kulipa pensheni;
(iv) Kuandaa taratibu za kiutawala za kusimamia utoaji wa pensheni kwa wazee; na
(v) Kushirikisha wadau mbalimbali katika kuandaa Mpango wa Pensheni kwa Wazee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itakapojiridhisha kuwa taratibu zote ziko sawa itatoa taarifa ya kuanza kwa malipo.
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA aliuliza:-
Serikali kwa sasa ina Sera ya Elimu Bure kuanzia chekechea hadi kidato cha nne:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu bure kwa kidato cha tano na sita?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniventura Destery Kiswaga, Mbunge wa Magu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali haina mpango wa kutoa elimu bila malipo kwa wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita na badala yake imejikita zaidi katika kuboresha miundombinu ambayo ni pamoja na upungufu wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, majengo ya utawala pamoja na kumalizia changamoto za uhaba wa Walimu wa sayansi na vifaa vya kufundishia na kujifunzia ikiwa ni pamoja na masuala ya TEHAMA.
Mheshimiwa Naibu Spika, kukamilika kwa miundombinu hiyo itasaidia kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wenye sifa ya kuingia kidato cha tano wanapata fursa ya kuendelea na masomo yao.
MHE. KISWAGA B. DESTERY aliuliza:-
Serikali iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Magu fedha za ujenzi wa ofisi za halmashauri, lakini ujenzi huo haujakamilika:-
Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kiswaga Boniventura Desdery, Mbunge wa Magu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, awamu ya kwanza ya ujenzi wa Jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Magu ilianza tarehe 12 Januari, 2013 kwa kutumia Mkandarasi Beijing Construction Engineering Group wa Dar-es-Salaam. Ujenzi wa Jengo hilo unatarajia kugharimu jumla ya Sh.6,765,596,533.05 hadi kukamilika kulingana na usanifu uliofanyika. Kati ya fedha hizo Sh.2,744,537,216.94 zimeshapokelewa na kutumika tangu mwaka 2013 ujenzi ulipoanza.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2017/ 2018, Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 600 kuendelea na ujenzi. Katika robo ya kwanza ya Mwaka wa Fedha 2017/ 2018 Serikali imetoa jumla ya shilingi milioni 200 ambazo zimepokelewa na halmashauri na mkandarasi anaendelea na ujenzi katika jengo hilo la halmashauri yake.
MHE. KISWAGA B. DESTERY aliuliza:-
Madiwani ni wasimamizi wakuu wa rasilimali za halmashauri na wakati wa uchaguzi wa Madiwani, Wabunge na Rais ni mafiga matatu:-
• Je, ni lini Serikali itawaongezea posho ya mwezi Madiwani hao?
• Je, ni lini Serikali itawapa usafiri na msamaha wa kodi Madiwani katika vyombo vya usafiri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniventura Destery Kiswaga, Mbunge wa Magu, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Waheshimiwa Madiwani katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kwa Mwaka wa Fedha 2012/2013 Serikali ilipandisha posho za Madiwani kwa mwezi kutoka Sh.120,000/= hadi Sh.250,000 kupitia Waraka Maalum wa tarehe 16 Agosti, 2012. Vile vile katika Mwaka wa Fedha 2014/2015 posho hiyo iliongezwa kutoka Sh.250,000/= hadi Sh.350,000/= kwa mwezi kwa Madiwani na Sh.400,000/= kwa mwezi kwa Mwenyekiti au Meya. Serikali itaendelea kuboresha maslahi ya Waheshimiwa Madiwani kadri hali ya uchumi wa nchi inavyoruhusu.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Waheshimiwa Madiwani kupewa vyombo vya usafiri na msamaha wa kodi, kwa sasa Serikali imeridhia Waheshimiwa Madiwani wakopeshwe na Mabenki kwa masharti nafuu kutokana na posho zao. Tayari mabenki yameanza kutoa mikopo kwa Waheshimwa Madiwani zikiwemo Benki za NMB na CRDB.
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA aliuliza:-
Mwaka wa 2014/2015, Jimbo la Magu halikupatiwa Walimu wa shule za msingi na bado kuna uhaba wa Walimu:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta Walimu Magu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniventura Desderius Kiswaga, Mbunge wa Magu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Magu inao Walimu wa shule za msingi 1,281 kati ya Walimu 2,002 wanaohitajika, hivyo kuna upungufu wa Walimu 821. Kati ya Walimu 1,276 wa shule za msingi walioajiriwa mwezi Disemba, 2017, Halmashauri ya Wilaya ya Magu ilipangiwa Walimu 56 ambao wameripoti kwenye shule zilizokuwa na uhitaji mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Walimu 77 ambao ni miongoni mwa Walimu wa ziada wa masomo ya sanaa katika shule za sekondari za Halmashauri ya Wilaya ya Magu wamehamishiwa shule za msingi. Vile vile katika Mwaka wa Fedha 2017/2018, Serikali imepanga kuajiri Walimu 10,130 wa shule za msingi nchi nzima ili kukabiliana na uhaba wa Walimu katika maeneo mbalimbali; na Halmashauri ya Magu nayo itapangiwa Walimu hao. (Makofi)
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA aliuliza:-
Serikali inaanzia katika ngazi ya kitongoji, mtaa na kijiji:-
Je, ni lini viongozi na Wenyeviti wa Vitongoji, Mtaa na Kijiji watalipwa mishahara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniventura Destery Kiswaga, Mbunge wa Magu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa sifa zinazomwezesha Mtanzania kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kijiji, Kitongoji au Mtaa ni pamoja na kuwa na shughuli halali inayomwingizia kipato. Kwa muktadha huo, utaratibu wa viongozi kwa ngazi hiyo kulipwa mishahara kama ilivyoulizwa katika swali la msingi haujawahi kuwekwa kwenye sheria yoyote.
MHE. KISWAGA B. DESTERY aliuliza:-

Serikali ilikuwa na mpango wa kupeleka maji katika Mji wa Kisesa - Bujora na Kata ya Bukandwe:-

Je, ni lini Serikali itaanza kujenga na kupeleka maji katika miji hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kiswaga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya na Shirika la Maendeleo la Ufaransa inatekeleza Programu ya Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Jiji la Mwanza na Miji ya Magu, Lamadi na Misungwi na miradi ya Majitaka katika Miji ya Bukoba na Musoma kwa gharama ya EURO million 104.5.

Aidha, kupitia programu hii, AFD imeridhia kutoa fedha ya nyongeza (additional financing) kiasi cha EURO milioni 30 sawa na shilingi bilioni 75 kwa masharti ya mkopo nafuu. Kwa sasa mchakato wa kutia saini Mkataba wa Makubaliano ya Kifedha (Financing Agreement) kati ya AFD na Wizara ya Fedha na Mipango unaendelea.

Mheshimiwa Spika, kulingana na andiko la mradi, fedha hizo za nyongeza zitatumika kutekeleza mradi wa kupeleka maji katika maeneo ya Usagara, Buhongwa, Busweru na Mji mdogo wa Kisesa - Bujora na Kata ya Bukandwe pamoja na Vijiji vya Igetimaji, Kitumba, Mwahuli, Busekwa na Ihayabuyaga. Mradi huu unategemewa kuanza katika mwaka wa fedha 2019/2020.

Hivyo, nawaomba wananchi wa Kisesa, Bujora na Kata ya Bukandwe wawe na subira kwa kuwa mpango wa kuwapelekea maji uko katika hatua nzuri.
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa fedha ili kukamilisha ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Magu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniventura Destery Kiswaga, Mbunge wa Jimbo la Magu kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Serikali imeendelea na ujenzi wa majengo ya utawala katika Halmashauri 100 ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Magu ambazo kwa ujumla zimegharimu kiasi cha shilingi bilioni 147.33.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na ujenzi wa jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Magu ambalo litagharimu shilingi bilioni tano hadi kukamilika. Hadi mwezi Februari 2021, Serikali ilikuwa imekwishatoa shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo ambalo tayari limeezekwa. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 750 kwa ajili ya kuendelea na hatua ya ukamilishaji wa jengo hilo.
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA aliuliza:-

Je, ni lini barabara ya Kisamba – Sayaka hadi Salama inayounganisha Mkoa wa Mwanza na Simiyu itaanza kuhudumiwa na TANROADS?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniventura Destery Kiswaga, Mbunge wa Magu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Kisamba – Sayaka hadi Salama ni barabara ya Wilaya inayohudumiwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).

Mheshimiwa Spika, ili barabara yoyote iweze kuhudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) zipo taratibu ambazo lazima zifuatwe ikiwa ni pamoja na maombi ya kupandishwa hadhi ya kuwa barabara kuu ama ya mkoa kuwasilishwa kwenye mamlaka zinazohusika kwa kuzingatia utaratibu ulioainishwa kwenye Sheria ya Barabara ya mwaka 2007 na Kanuni zake za mwaka 2009 ambayo imeainisha pia vigezo vinavyohitajika katika kupandisha hadhi barabara. Ahsante.
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Magu –Ng’hungumalwa kwa kiwango cha lami utaanza baada ya upembuzi yakinifu kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniventura Destery Kiswaga, Mbunge wa Magu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami, barabara ya Magu – Bukwimba - Ngudu – Ng’hungumalwa yenye urefu wa kilometa 71 ilikamilika mwaka 2019.

Katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali imetenga shilingi milioni 1,500 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kilometa 10 kwa kiwango cha lami barabara hii. Serikali itaendelea na ujenzi wa barabara hii kadri ya upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya kuanzisha Wilaya mpya ya Kisesa Mkoani Mwanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniventura Destery Kiswaga, Mbunge wa Jimbo la Magu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mwanza uliwasilisha mapendekezo ya kuanzisha Wilaya ya Bujora (Kisesa) kupitia barua ya tarehe 15 Machi, 2021 na tarehe 10 Mei, 2021. Ofisi ya Rais – TAMISEMI inaendelea na uchambuzi wa mapendekezo ya kuanzisha wilaya hiyo na maeneo mengine ya utawala yaliyowasilishwa. Uchambuzi wa taarifa hizo utakapokamilika timu ya wataalam itatumwa kufanya uhakiki na baadae kuishauri mamlaka ipasavyo juu ya suala hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshauri Mheshimiwa Mbunge na wananchi wawe na subira katika kipindi ambacho Serikali inaendelea na uchambuzi na tathmini ya taarifa zilizowasilishwa.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE K.n.y. MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuweka taa za barabarani katika Miji ya Magu, Kisesa, Nyanguge, Lugeye na Ilungu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniventura Destery Kiswaga, Mbunge wa Magu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Wakala wa Barabara Tanzania Mkoa wa Mwanza umepanga kuweka taa katika Miji ya Magu, Kisesa, Nyanguge, Lugeye na Illungu. Uchambuzi wa zabuni kwa ajili ya kumpata mkandarasi unaendelea na unatarajiwa kukamilika tarehe 15 mwezi Februari mwaka huu wa 2023 na kazi inatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu wa 2023, ahsante.
MHE. STANSLAUS S. MABULA - K.n.y MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA katika Wilaya ya Magu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Bonivetura Destery Kiswaga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nia ya Serikali ni kuwezesha upatikanaji wa fursa za ujuzi na stadi mbalimbali za maisha kupitia elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi katika Mikoa na Wilaya zote nchini. Kutokana na nia hiyo, Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa ujenzi wa Vyuo vya VETA kwa awamu katika Mikoa na Wilaya mbalimbali ikiwemo Wilaya ya Magu kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi ambacho Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA katika Wilaya ya Magu na maeneo mengine, wananchi wa Magu wanashauriwa kutumia Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Mwanza pamoja na Vyuo vingine vya VETA na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vilivyopo jirani kwa ajili ya kupata elimu na mafunzo ya ufundi. Ninakushukuru sana.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE K.n.y. MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali italipa kiinua mgongo kwa wazee ambao hawajawahi kuajiriwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniventura Destery Kiswaga, Mbunge wa Magu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kiinua mgongo ni malipo ambayo hulipwa na mwajiri pindi mfanyakazi wake anapostaafu kufanya kazi. Hata hivyo, kutokana na kuwepo kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambapo mwajiriwa na mwajiri huchangia, mfanyakazi hulipwa pensheni badala ya kiinua mgongo na hupokea mafao ya mkupuo mara anapostaafu na badaye kuendelea kulipwa pensheni ya kila mwezi kwa maisha yake yote. Hivyo, kwa sasa hakuna mfumo wa kulipa kiinua mgongo kwa mzee ambaye hajawahi kuajiriwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.