Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Ester Alexander Mahawe (15 total)

MHE. FLATEI G. MASSAY (K.n.y MHE. ESTER A. MAHAWE) aliuliza:-
Serikali kupitia mpango mkakati wa kuwawezesha wananchi wa vijijini iliahidi kutoa shilingi 50,000,000 kwa kila kijiji na mtaa:-
(a) Je, ni lini fedha hizo zitatolewa?
(b) Je, Serikali imejipanga vipi kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wananchi juu ya njia bora ya kutumia fedha hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ester Alexander Mahawe, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali imetenga shilingi bilioni 59.5 katika Bajeti ya mwaka 2016/2017 chini ya Fungu 21 kwa ajili ya kuwawezesha wananchi vijijini kwa kutoa shilingi milioni 50 kwa kila kijiji. Fedha hizo zitatolewa mara baada ya kuidhinishwa na Bunge lako Tukufu na baada ya kukamilisha taratibu mbalimbali zinazolenga kuhakikisha uwepo wa tija katika matumizi ya fedha hizo.
(b) Mheshimiwa Spika, kuhusu mpango bora wa elimu ya ujasiriamali kwa wananchi, ili kuhakikisha matumizi bora ya fedha hizo Serikali inaendelea kukamilisha maandalizi ya utaratibu maalumu wa utoaji wa fedha hizo, ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu ya ujasiriamali. Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI imepewa kazi ya kuratibu utekelezaji wa mpango huo.
MHE. ESTER A. MAHAWE aliuliza:-
Bajeti ya mpango wa barabara inayopelekwa katika Halmashauri zetu ni ndogo na haikidhi mahitaji:-
Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa kuongeza bajeti hiyo ili Halmashauri nchini ziweze kununua vifaa vya kutengenezea barabara zao za ndani ili kuondoa kero isiyokuwa ya lazima?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester Alexander Mahawe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za matengenezo ya barabara katika Mamlaka za Serikali za Mitaa hutengwa kulingana na Sheria ya Mfuko wa Barabara ikiwa ni asilimia 30 ya fedha za mfuko. Fedha za Mfuko zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 23.8 mwaka 2005/2006 hadi shilingi bilioni 249.8 mwaka 2016/2017. Hata hivyo, kulingana na mtandao wa barabara unaohudumiwa na mamlaka za Serikali za Mitaa, unaofikia kilomita 108,946 fedha hizo ni kidogo ukilinganisha na mahitaji halisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za Mfuko wa barabara zinahitajika kutumika kwa ajili ya matengenezo ya barabara pekee. Aidha, Halmashauri zinaruhusiwa kukopa fedha kwa ajili ya ununuzi wa mitambo katika taasisi za kifedha na kurejesha mikopo hiyo kupitia makusanyo yake ya ndani. Hata hivyo, Halmashauri itatakiwa kwanza kupata kibali kutoka kwa Waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, suluhisho la kudumu la matengenezo ya barabara zinazohudumiwa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa ni kuanzisha wakala ambao utafanya kazi kama vile TANROADS inavyofanya. Tayari Ofisi ya Rais, TAMISEMI inaanda rasimu ya nyaraka muhimu ambazo zitaanzisha wakala huo
MHE. ESTER A. MAHAWE aliuliza:-
Wilaya ya Simanjiro haina Hospitali ya Wilaya na hivyo kusababisha mateso kwa wakazi wa maeneo mbalimbali ya Wilaya hiyo hususan wanawake ambao wanakosa huduma za kujifungua lakini pia kutokana na uchache wa vituo vya afya na zahanati.
(a) Je, ni lini Serikali itavipa hadhi vituo vya afya vya Mererani na Orkesment ili kupunguza tatizo?
(b) Wilaya ya Simanjiro ina gari moja tu la wagonjwa; je, ni lini Serikali itapeleka gari lingine kwenye Kituo cha Afya Mererani ili kuokoa maisha ya akina mama wajawazito?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester Alexander Mahawe, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, maombi ya kupandisha hadhi Kituo cha Afya Orkesment kinachomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kuwa Hospitali Teule ya Wilaya tayari yamewasilishwa katika Wiazara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto mwezi Oktoba, 2016 kwa uamuzi, baada ya kujadiliwa na kukubalika katika vikao ngazi ya Halmashauri na Mkoa. Kibali kikipatikana Serikali itaingia mkataba rasmi wa utoaji huduma na mmiliki wa kituo hicho ili kuainisha majukumu ya kila mdau. Aidha, Halmashauri imepokea shilingi milioni 80.0 zilizotengwa katika bajeti ya mwaka 2016/2017 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya wazazi katika kituo cha afya cha Urban Orkesment kinachomilikiwa na Serikali. Taratibu za kumpa Mkandarasi zinaendelea.
(b) Mheshimiwa Spika, Halmashauri imetenga gari moja ambalo linatumika kutoa huduma za dharura kwa wagonjwa wenye rufaa. Gari hilo hutoa huduma kwa wagonjwa katika vituo vyote kikiwemo Mererani pale inapotokea dharura.
Hata hivyo, gari hilo ni chakavu kiasi cha kuhitaji matengenezo ya mara kwa mara. Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro imeshauriwa kuweka kipaumbele na kutenga bajeti katika mwaka 2017/2018 kwa ajili ya ununuzi wa gari la kuhudumia wagonjwa.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY (K.n.y MHE. ESTHER A. MAHAWE) aliuliza:-
Vituo vya Afya na Zahanati zilizo karibu na Hospitali za Wilaya zina changamoto ya utoaji huduma bora kwa sababu ya upungufu wa dawa na watumishi wa kada ya afya hivyo kusababisha kuhudumiwa na Hospitali za Wilaya ambazo bajeti za dawa hazikidhi:-
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuongeza bajeti ya Hospitali za Wilaya zilizoko katika Mkoa wa Manyara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rai, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Alexander Mahawe, Mbunge wa Viti Maalum, kutoka Mkoa wa Manyara kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa 2016/2017, Halmashauri za Mkoa wa Manyara zimetengewa bajeti ya shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya. Kati ya fedha hizo, fedha zilizopokelewa hadi Machi, 2017 ni shilingi bilioni 1.07 sawa na asilimia 75%. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Halmashauri za Mkoa huo zimepanga kutumia shilingi 1.58 kwa ajili ya dawa sawa
na ongezeko la asilimia 9.7 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kuanza kutumia mfumo wa kupeleka fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa moja kwa moja katika vituo vya tiba yaani Direct Facility Financing (DFF), hali itakayosaidia vituo vya kutolea huduma kuboresha upatikanaji wa dawa kwenye hospitali,
vituo vya afya na zahanati. Halmashauri zitabaki na jukumu la kusimamia taratibu zote na kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
MHE. ESTER A. MAHAWE aliuliza:-
Fedha zinazokusanywa za asilimia 0.3 ya service levy zimeshindwa kusaidia Halmashauri nchini kwa uwiano unaolingana.
Je, Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka fedha hizo kukusanywa na TAMISEMI ili kila Halmashauri iweze kupata mgao unaolingana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester Alexander Mahawe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, service levy ni chanzo kinachokusanywa na Halmashauri kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290 kifungu cha 6(1) na 7(1). Ushuru huo unatozwa kutoka kwa makampuni, matawi ya makampuni na mfanyabiashara yeyote mwenye leseni ambaye anafanya shughuli zake katika Halmashauri husika. Hivyo, Halmashauri ndiyo yenye mamlaka ya kukusanya ushuru huo kwa mujibu wa sheria. Ofisi ya Rais, TAMISEMI kazi yake ni kuandaa sera, sheria, kanuni na miongozo na kusimamia utekelezaji wake kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Spika, Serikali imepanga kuboresha utaratibu unaotumika kukusanya ushuru huo kwenye Halmashauri kwa kufanya marekebisho ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa ili kuondoa utata uliokuwepo ambapo makampuni yalikuwa hayalipi ushuru huo kwa kuzingatia kuwa unalipwa Makao Makuu ya Kampuni.
Mheshimiwa Spika, Bunge litapata fursa ya kujadili marekebisho hayo ambayo yanakusudia kuziwezesha Halmashauri kukusanya ushuru wa huduma kwa kiwango cha kuridhisha.
MHE. ESTER A. MAHAWE aliuliza:-
Kadi za kulipia Ngorongoro zimekuwa kero kwa wageni na wahudumu kwani muda mwingi umekuwa ukipotea wakati kufanya malipo.
Je, ni lini Serikali itafanya marekebisho ili kuwe na mfumo wa kadi kama za TANAPA?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester Alexander Mahawe, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Manyara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imebadilisha mfumo wa malipo na utoaji wa vibali vya kuingia katika Hifadhi ya Ngorongoro.
Mfumo huu mpya kabisa ujulikanao kama Ngorongoro Safari Portal ulianza kutumika tarehe 01 Februari, 2017 na umeonyesha ufanisi mkubwa ikiwa ni pamoja na kuondoa kabisa msongamano wa wageni katika malango ya kuingia kwenye hifadhi na kuongeza ufanisi katika makusanyo ya mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo huu mpya uko kwenye mtandao wa internet na hivyo huwezesha wakala wa utalii kulipa na kupata vibali moja kwa moja kwa njia ya mtandao bila kulazimika kufika katika ofisi, kwenda benki au malango ya kuingia katika Hifadhi za Ngorongoro.
MHE. ESTER A. MAHAWE aliuliza:-
Madini ya Tanzanite yanachimbwa Mkoani Manyara katika Wilaya ya Simanjiro, lakini madini hayo huchakatwa na kuuzwa Mkoani Arusha hali inayosababisha wananchi wa Manyara kutofaidika kiuchumi.
(a) Je, ni nini kauli ya Serikali kuhusu kujenga kiwanda cha kuchakata madini hayo Mkoani Manyara?
(b) Je, ni kiasi gani cha fedha kimeshachangiwa na madini haya katika mapato ya Mkoa wa Manyara?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Madini, naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Ester Alexander Mahawe, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Manyara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha kuwa madini ya Tanzanite yananufaisha wananchi wa Simanjiro, Serikali imetoa tamko la kutaka shughuli zote zinazohusu madini ya Tanzanite ikiwemo uendeshaji wa minada na ujenzi wa viwanda vya uchakataji wa madini hayo zifanyike katika eneo la Mererani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali imetenga eneo katika Kijiji cha Naisinyai, Mererani ili kuwa eneo maalum kiuchumi kwa ajili uanzishaji wa viwanda vya uchakataji (Economic Processing Zone - EPZ) ili kuvutia uwekezaji katika eneo hilo kwa kutoa vivutio mbalimbali kwa wawekezaji. Hivyo Wizara itaendelea kuhamasisha wawekezaji wa viwanda vya kuchakata madini ya Tanzanite kujenga viwanda katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza hilo kwa vitendo, Wizara ya Madini imepata kiwanja katika eneo la EPZ ili kujenga Kituo cha Umahiri (Center of Excellence), sehemu ya jengo hilo itakuwa na taasisi mbalimbali zinazosimamia shughuli za madini ili kutoa huduma kwa wafanyabiashara wa madini ya Tanzanite kwa haraka (One Stop Centre). Pia baadhi ya ofisi katika jengo hilo litatumika kutoa huduma za uthaminishaji wa madini na kuendesha minada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2017 madini ya Tanzanite yamechangia kiasi cha shilingi 140,954,229.37 kutokana na kodi ya tozo ya huduma (Service Levy) inayotozwa mujibu wa Sheria ya Ushuru wa Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, manufaa mengine yaliyopatikana kwa Wilaya ni pamoja na fursa za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kutokana na kuwepo kwa migodi katika eneo husika na huduma za jamii zinazotolewa na mgodi ambapo mgodi umetoa ajira kwa wafanyakazi 674 ambapo asilimia 93 ya walioajiriwa ni Watanzania na asilimia saba iliyobaki ni wageni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya waajiriwa hao, asilimia 21.81 ya wafanyakazi wameajiriwa katika vijiji kutoka vijiji vinavyozunguka mgodi vya Naisinyai na Mererani. Katika kipindi hicho mgodi wa Tanzanite One umefanikiwa kuchangia jumla ya dola za Kimarekani 429,664 katika utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii ukilenga kuimarisha mahusiano na jamii zinazozunguka mgodi pamoja na kuchangia maendeleo ya Taifa kwa ujumla. Huduma hizi zinahusisha masuala ya elimu, afya, lishe, ujenzi na sanaa.
MHE. ESTER A. MAHAWE aliuliza:-
Takwimu zinaonesha upungufu mkubwa wa matundu ya vyoo zaidi ya 200,000 katika shule mbalimbali za sekondari na msingi.
(a) Je, nini mkakati wa Serikali wa kumaliza tatizo hilo?
(b) Je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka wa kuja na mkakati mbadala kama ilivyofanya wakati wa kumaliza tatizo la madawati na maabara nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester Alexander Mahawe, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tuna upungufu wa matundu ya vyoo 276,198 kwa shule za msingi na 20,534 kwa shule za sekondari. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 jumla ya matundu ya vyoo 6,708 kwa shule za msingi na 2,071 kwa shule za sekondari yamejengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya tathmini ya kina tumebaini kuwa zinahitajika jumla ya shilingi bilioni 646.822 kumaliza tatizo hilo. Wizara yangu imetoa maelekezo kwa halmashauri zote kwamba katika Bajeti ya mwaka 2018/2019, fedha za ruzuku ya maendeleo ambazo ni jumla ya shilingi bilioni 55.2 endapo zitapitishwa na Bunge, sehemu kubwa ya fedha hizo ielekezwe kwenye kipaumbele cha miundombinu ya elimu ikiwemo vyoo kwenye shule zote ambazo tayari wananchi watakuwa wamechangia nguvu zao.
Uamuzi huo utatoa nyongeza kubwa sana kwenye Bajeti ya shilingi bilioni 19.97 ambayo imetengwa chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mahsusi kwa ajili ya matundu ya vyoo katika shule za msingi na shule za sekondari. Mkakati wa Serikali ni kutumia fedha hizo kumalizia kazi za ujenzi ambazo zitakuwa zimeanzishwa na wananchi.
MHE. ESTHER A. MAHAWE aliuliza:-
Sera ya Elimu ya mwaka 2014 inaelekeza utoaji wa elimu bila malipo kuanzia ngazi ya chekechea hadi kidato cha nne ikiwemo kuondoa gharama za kulipia mitihani ya kitaifa katika shule za msingi na sekondari lakini wanafunzi wanaosoma katika shule zisizo za Serikali wanalipishwa gharama hizo wakati wazazi wao wanalipa kodi inayowezesha kutolewa elimu hiyo bila malipo:-
Je, ni lini Serikali itafuta ada hiyo ya mitihani kwa wanafunzi wanaosoma katika shule binafsi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu swali, naomba nitambue kwamba Mheshimiwa Esther Alexander Mahawe ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Shule Binafsi Nchini. Lazima tu niseme kwamba katika kipindi cha uongozi wake Serikali imenufaika na ushirikiano mkubwa ambao umefanya Serikali iweze kuwahudumia sekta binafsi katika elimu, tunamshukuru sana Mheshimiwa Esther Mahawe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba sasa kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, nijibu swali la Mheshimiwa Esther Alexander Mahawe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa sekta binafsi katika utoaji wa elimu nchini. Aidha, ili kuhakikisha mazingira rafiki katika utoaji wa elimu, Serikali imekuwa ikifanya majadiliano na sekta binafsi kwa lengo la kuondoa changamoto zinazowakabili. Hadi sasa Serikali imeweza kuondoa baadhi ya kodi na tozo mbalimbali ambazo awali walikuwa wakitozwa mawiliki wa shule binafsi. Mfano wa kodi hizo ni Kodi ya Mabango, Kodi ya Kuendeleza Ufundi Stadi (Skills Development Levy), tozo ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi (OSHA) pamoja na tozo ya zimamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utekelezaji wa Mpango wa Elimu bila Malipo, Serikali ilifuta ada na michango ya lazima katika shule za umma ngazi ya elimumsingi yaani elimu ya awali hadi kidato cha nne. Ada na michango hiyo iliyokuwa ikilipwa na wazazi au walezi kwa sasa hugharamiwa na Serikali. Mpango huu haukuzihusu shule binafsi pamoja na shule za umma ngazi za kidato cha tano na sita. Hivyo, shule hizo zitaendelea na utaratibu wa wazazi kuchangia gharama za uendeshaji wa elimu ikiwemo kulipa ada za mitihani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya utoaji elimu nchini kadiri uwezo wa kifedha utakavyoruhusu. (Makofi)
MHE. ESTER M. MMASI (K.n.y. MHE. ESTER A. MAHAWE) aliuliza:-
Gharama za kupanda Mlima Kilimanjaro ni mara mbili ya gharama za kupanda Mlima Kenya; hali hii imesababisha kushuka kwa idadi ya watalii na kuinyima Serikali mapato. Je, ni lini Serikali itafanya marekebisho ya bei hizo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester Alexander Mahawe, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mlima Kilimanjaro ni mlima mrefu kuliko yote Barani Afrika ukiwa na urefu wa mita 5,895 kutoka usawa wa bahari. Mlima huu una sifa nyingi za kipekee ikiwemo ya kuwa mlima mrefu duniani uliosimama peke yake (the only free standing mountain in the world), asilimia 85 ikiwa ni vertical, wenye barafu japo upo katika Ukanda wa Ikweta. Ni moja ya eneo la Urithi wa Dunia na umetunukiwa tuzo ya kuwa kivutio bora (One of the Africa Wonders).
Mheshimiwa Spika, aidha, Mlima Kilimanjaro una aina zaidi ya 200 ya ndege na zaidi ya aina species 140 za mamalia wakiwemo tembo, pofu, pongo, jamii ya swala, minde, twiga, simba, chui na wengineo, sifa ambazo Mlima Kenya hauna.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kununi za kupanda mlima, Mlima Kilimanjaro hupandwa kwa wastani wa siku sita. Safari ya kupanda mlima huu kwa mtalii kutoka nje ya nchi huipatia Serikali mapato ya dola za Kimarekani 684.4 pamoja na kodi ya VAT. Mtalii anayepanda Mlima Kenya kwa siku sita hulipa dola za Marekani 460. Tofauti ya gharama kati ya milima hii zinatokana na umuhimu wa kipekee pamoja na sifa ya Mlima Kilimanjaro ambazo haziwezi kulinganishwa na Mlima Kenya.
Mheshimiwa Spika, njia ya kupanda Mlima Kilimanjaro zimetengenezwa vizuri kiasi cha kuwezesha mtu wa kawaida asiye na utaalam kupanda mlima hadi kileleni wakati kwa Mlima Kenya upandaji unahitaji utalaam (technical climbing). Tofauti hizi husababisha gharama za utalii kati ya milima hii zisifanane.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2017/2018 Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro ilipokea na kuhudumia watalii 51,825 ambao waliingizia Taifa mapato ya shilingi bilioni 76.16. Kwa sasa Serikali imepanga kukutana na wadau wa Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro ili kukubaliana masuala mbalimbali ikiwemo bei ya kupanda Mlima Kilimanjaro.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA (K.n.y. MHE. ESTER A. MAHAWE) aliuliza:-
Sekta ya utalii inachangia pato kubwa la fedha za kigeni katika nchi yetu.
Je, ni lini Serikali itatengeneza barabara ya Serengeti ambayo ni mbovu kiasi cha kufanya watalii kukataa kupita huko?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester Alexander Mahawe, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa naibu Spika, Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ndiyo zinachangia zaidi katika mapato ya fedha za kigeni zitokanazo na shunguli za utalii hapa nchini. Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ina ukubwa wa kilometa za mraba 14,763 na barabara zenye urefu wa kilometa 3,155. Barabara hizo ni pamoja na barabara kuu zinazounganisha Hifadhi na Mikoa ya Arusha, Mara na Simiyu. Barabara nyingine ni zile za mizunguko ya utalii na nyingine ni za utawala na doria. Barabara zote hizo ni za kiwango cha changarawe.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara zenye matumizi makubwa ni zile kuanzia mpaka unaotenganisha Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro hadi Kituo cha Seronera yenye urefu wa kilometa 60 na kilometa 30 kutoka Seronera hadi lango na Ikoma. Barabara hizi wakati wa msimu wa watalii wengi zinatumiwa na magari zaidi ya 300 kwa siku. Kutokana na matumizi makubwa kiasi hicho, barabara hiyo yenye kiwango cha changarawe uchakavu wake huongezeka kwa kasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwezi Agosti, 2016 hifadhi inaendelea kuelekeza nguvu za ziada kuhudumia barabara hizi wakati wote wa msimu wa watalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, juhudi zinazoendelea zinahusisha kufanya matengenezo ya barabara hizo kwa kutumia nyenzo mbalimbali ikiwemo mitambo miwili ya barabara yaani motor graders pamoja na malori. Ili kupata ufumbuzi wa muda mrefu kukabiliana na changamoto hiyo ya ubovu wa barabara, Shirika la Hifadhi za Taifa linaendelea kutafuta teknolojia mbadala ili kuwa na barabara zitakazodumu bila kuathiri ikolojia ya wanyamapori.
MHE. ESTER A. MAHAWE aliuliza:-

Mkoa wa Manyara, hususani Wilaya ya Mbulu, umewahi kutoa wanariadha mahiri ambao walililetea Taifa heshima kubwa, lakini cha kushangaza wanariadha hao wametelekezwa:-

(a) Je, ni lini Serikali sasa itaandaa utaratibu wa kuwaenzi wanariadha hao?

(b) Je, ni lini sasa Serikali itajenga uwanja kwa ajili ya riadha katika Mkoa wa Manyara ili kuwahamasisha wanariadha wapya?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ester Alexander Mahawe, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, picha anayoichora Mheshimiwa Mbunge ya wanamichezo kutothaminiwa haiendani na hali halisi upande wa wanamichezo nchini waliofanya vizuri na kujituma ipasavyo. Naomba nitoe mifano kadhaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanariadha Filbert Bayi aliyevunja rekodi ya dunia ya mbio za mita 1,500 huko New Zealand mwaka 1974 ni Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki ya Tanzania na mmiliki wa Shule za Filbert Bayi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Suleiman Nyambui, mshindi wa medali ya shaba Mashindano ya All African Games mwaka 1978 na medali ya fedha ya Michezo ya Olimpiki 1980 kwa mbio za mita 5,000 sasa ni Kocha wa Riadha wa Taifa wa Brunei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Juma Ikangaa, mshindi wa kwanza wa mbio ndefu za marathon Jijini New York mwaka 1988 na mshindi wa pili mara tatu mfululizo wa marathon Jijini Boston mwaka 1988 – 1990 ni Mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na mratibu wa mashindano ya riadha kwa wanawake (ladies first) yanayodhaminiwa na Shirika la Kimataifa la Ushirikiano la Japan (JICA) pamoja na Wizara yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Samson Ramadhani, mshindi wa marathon medali ya dhahabu Australia mwaka 2006 ni Afisa wa Jeshi;

Mheshimiwa Mwenyekiti, Gidamis Shahanga, mshindi wa medali ya dhahabu mbio za marathon nchini Canada mwaka 1978, Uholanzi 1984, Nairobi 1988 na Vienna, Austria 1990 ni Mwenyekiti Mstaafu wa Halmashauri ya Katesh Manyara; na wengine wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanamichezo, wakiwepo wanariadha walioliletea Taifa hili sifa na heshima kubwa wanatoka sehemu mbalimbali za Tanzania. Wizara imeanza mchakato wa kuanzisha makumbusho maalum Uwanja wa Taifa ambapo picha za wanamichezo wote walioliletea Taifa letu heshima katika vipindi mbalimbali zitawekwa.
MHE. ESTER A. MAHAWE Aliuliza:-

Halmashauri ya Mbulu haina Hospitali ya Wilaya hivyo wananchi wa Kata za Gidhim, Yayeda, Ampatumat hutembea umbali mrefu kufuata huduma katika kituo cha Afya Dongobeshi.

(a) Je, ni lini Serikali itapandisha hadhi Kituo cha Afya Dongobesh ili kiweze kuwahudumia wananchi wa Mbulu Vijijini na kupunguza msongamano katika Hospitali ya Rufaa ya Hydom?

(b) Je, ni lini Serikali itaongeza Watumishi wa Afya, dawa na vifaa tiba katika kituo hicho cha afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Ester Mahawe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwe Mwenyekiti, Kituo cha Afya Dongobeshi kilianzishwa mnamo mwaka 1974 kipo kata ya Dongobeshi, kinahudumia jumla ya wakazi takribani 30,000 wa Tarafa ya Dongobeshi na wakazi wa maeneo jirani wakiwemo wananchi wa Kata za Gidhim, Yaeda na Amputamat.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa kituo hiki, Serikali kwa nyakati tofauti imekuwa ikitoa fedha kwa lengo la kuboresha miundombinu pamoja na huduma za afya zitolewazo kwenye kituo hiki. Mwezi Machi, 2018 Serikali ilitoa kiasi cha shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ambayo ujenzi wake umekamilika hivi karibuni. Majengo hayo ni wodi ya Mama na Mtoto (Maternity and Pediatric Ward), jengo la upasuaji, jengo la maabara, nyumba moja ya mtumishi na jengo la kuhifadhia maiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuongeza idadi ya watumishi katika Kituo cha Afya cha Dongobeshi. Mwaka wa fedha 2017/2018 watumishi sita wapya wameajiriwa na kufanya kituo kuwa na jumla ya watumishi 37. Aidha, Serikali imetuma fedha bohari Kuu ya Dawa (MSD) jumla ya shilingi milioni 320 zikiwa ni kwa ajili ya kunua vifaa tiba, hadi sasa vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 37 vimepelekwa kituoni hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka wa fedha 2018/2019, jumla ya shilingi bilioni 1.5 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu inayojengwa katika Tarafa ya Dongobesh. Kukamilika kwa hospitali hii kutaondoa msongamano kwenye Hospitali ya Hydom. Kwa kuwa, Hospitali ya Wilaya inajengwa katika eneo la Dongobesh hakuna sababu ya Kituo cha Afya kilichopo sasa kupandishwa hadhi kuwa hospitali.
MHE. ESTER A. MAHAWE aliuliza:-

Kata za Naberera, Kitwai, Lorbene, Loibosroit, Norakauwo na Komolo katika Wilaya ya Simanjiro hazina huduma ya mawasiliano ya simu:-

Je,ni lini sasa Serikali itapeleka minara ya simu ili wananchi hao waweze kupata huduma ya mawasiliano ya simu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa, Ester Alexander Mahawe, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Manyara, kama Ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kufikisha huduma za mawasiliano nchi nzima. Kata ya Naberera, ilijumuishwa kwenye zabuni ya mwezi Agosti, 2017 na vijiji vitano vilipata mtoa huduma kampuni ya Vodacom ambayo tayari imefikisha huduma ya mawasiliano katika vijiji hivyo. Aidha, vijiji vingine vitatu katika Kata hiyo ya Naberera vilijumuishwa katika zabuni ya awamu ya tatu mwezi Disemba, 2018 na kupata mtoa huduma kampuni ya mawasiliano Tanzania TTCL ambayo inaendelea na utekelezaji wa mradi wa kufikisha mawasiliano katika vijiji hivyo. Hadi hapo ifikapo tarehe 30 Juni, 2020 tunategemea mradi utakuwa umekamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Kata za Kitwai na Loibosroit zilijumuishwa kwenye zabuni ya awamu ya tatu na kupata watoa huduma kampuni ya Halotel kwa Kata ya Loibosroit na kampuni ya mawasiliano Tanzania kwa Kata ya Kitwai. Zoezi la kusaini mkataba lilifanyika tarehe 13 Desemba, 2018 na fedha za awali tayari zilikwishatolewa kwa watoa huduma ambapo kwa sasa wanaendelea na taratibu za ujenzi wa mnara ili kukamilisha mradi ifikapo Juni, 2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Kata ya Komolo iliingizwa kwenye zabuni ya awamu ya nne ya Julai, 2019, japokuwa haikufanikiwa kupata mtoa huduma hivyo tunategema itajumuishwa tena katika zabuni ya awamu ya tano. Aidha, Vijiji vya Kata za Lorbene na Norakauwo vyote kwa pamoja vitajumuishwa kwenye zabuni ya awamu ya tano ambayo itatangazwa katika mwaka wa fedha 2019/2020.
MHE. ESTER A. MAHAWE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi wa Sinai, Hangoni, Kwere na Mruki waliopitiwa na barabara ya “By Pass” ya magari makubwa yatokayo Dodoma na kutokea stendi mpya ya Babati Mjini?
NAIBU WAZIRI UJENZI (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ester Alexander Mahawe Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa barabara ya mchepuo Babati Bypass katika barabara ya Dodoma Babati, Arusha na Singida Babati unatekelezwa kwa pamoja na mradi wa Mtera Bypass katika barabara ya Iringa Dodoma chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika na uko katika hatua ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na maandalizi ya makablasha ya zabuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya majukumu ya Mhandisi Mshauri ni kutambua sehemu ambamo barabara ya mchepuo itapita yaani alignment. Mara baada ya maeneo itakamopita barabara ya mchepuo kujulikana na kukubaliwa na Serikali kazi itakayofuata ni ya usanifu wa kina ambapo mali zitakazokuwa katika maeneo inamopita barabara ya mchepuo zitatambuliwa na kufanyiwa tathimini kwa ajili ya fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua iliyofikiwa sasa ni kwamba kazi ya upembuzi yakinifu inaendelea lakini bado maeneo na mali zitakazoathiriwa na mradi itakamopita barabara hayajajulikana, hivyo mali na kutathiminiwa na kufidiwa hazijajulikana Serikali italipa fidia kwa mujibu wa sheria.