Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Mary Machuche Mwanjelwa (19 total)

MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona. Katika Jiji la Mbeya tumekuwa na tatizo sugu sana la foleni katika barabara inayotoka Uyole hadi pale kwangu Mwanjelwa, ikifika saa 10 magari hayaendi kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bunge lililopita, Bunge la Kumi hiki kilikuwa ni kilio changu cha muda mrefu kwamba kwa nini tusifanye bypass kutoka barabara ya Uyole hadi uwanja wa ndege wa Songwe, lakini mpaka leo hii hili jambo halijafanikiwa kwenye vikao vyetu vya Road Board nimekwenda mpaka kumwona Meneja wa TANROAD bila mafanikio. Namuomba Mheshimiwa Waziri husika hapa atoe tamko ni lini barabara hii ya bypass kutoka Uyole hadi Uwanja wa Ndege wa Songwe itakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taratibu za ujenzi wa barabara zote huwa tunaanzia kwenye vikao vya Road Board vya Mkoa ambavyo Waheshimiwa Wabunge ni wajumbe. Alichokizungumzia ni kwamba inaonekana Road Board ya Mkoa wa Mbeya bado haijaridhia ujenzi wa Bypass hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nitawasiliana na Road Board Taifa pamoja na Road Board Mkoa wa Mbeya kujua sababu halisi, kwa nini bypass hii bado haijakubalika kitaalam. Siwezi kutoa commitment inayoombwa kabla sijajua sababu za kitaalamu za kutokubalika hiyo bypass.
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kuniona na mimi naomba niulize swali moja tu dogo la nyongeza;
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Wilaya hii ya Chunya ni mojawapo ya Wilaya kongwe sana Tanzania, lakini hospitali hii haina vifaa tiba wala matibabu ni kweli. Pia akina mama kwenye wodi ya wazazi wanapata shida mpaka wanajifungulia chini, naomba kujua Serikali ina mkakati gani kuiangalia jicho la ziada Wilaya hii kongwe nchini
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya vifaa tiba na siyo vifaa tiba tu maana yake kuna changamoto nyingi, ukienda kwenye vifaa tiba utakuta changamoto ya madawa, ndiyo maana katika mpango wetu wa sasa ninawashukuru sana wenzetu wa Wizara ya Afya ukiangalia mpango mkubwa tunaondoka nao, suala zima la vifaa tiba, madawa katika bajeti ya mwaka huu imeji-reflect kabisa ni jinsi gani tutafanya hasa hospitali zetu za Wilaya ziweze kuwezeshwa. Maelekezo makubwa tumeona hospitali nyingi sana mara nyingi zinasuasua katika suala la madawa na vifaa tiba na ndiyo maana mpango wetu mkakati sasa hivi ni kuhakikisha kwamba tunafanya collection ya kutosha, mara nyingi pesa zilikuwa zinakusanywa lakini siyo zile zinakusanywa zinaingia katika Halmashauri na hospitali, nyingi zilikuwa zinapotea.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana tumeasisi hii mifumo ya ki-electronic, hata mwanzo pesa zikikusanywa zilikuwa hazitumiki zote kwa matumizi ya hospitali, mengine watu walikuwa wanatumia kwa ajili ya kulipana per diem mwisho wa siku ni kwamba hata dawa na vifaa tiba vinakosekana. Kwa hiyo kutokana na mwongozo tumesema kwamba pesa zote zinazokusanywa katika hospitali za Wilaya ukiachia na mafungu mengine, lengo letu kubwa kwamba hii mifumo ya electronic tutakusanya fedha lakini lazima mwongozo ufuatwe. Je, asilimia ngapi inaenda katika vifaa tiba na asilimia ngapi inaenda katika dawa, mwisho wa siku tuweze kutatua tatizo la dawa na vifaa tiba katika hospitali zetu.
Hili Mheshimiwa Mwanjelwa tutaenda kulisimamia katika mwaka huu wa fedha ili kuongeze ufanisi katika hospitali zetu za Wilaya na hospitali zetu mbalimbali wananchi waweze kupata huduma.
MHE.DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kuniona.
Kwa kuwa, tatizo la Tabora linafanana sana na tatizo la Mbeya, mojawapo ya Sera ya Awamu ya Tano ni kufufua na kuimarisha viwanda vya ndani katika kukuza uchumi wa ndani, lakini vilevile kuongeza soko la ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mbeya tuna kiwanda cha Mbeya Textile ambacho kimetelekezwa kwa muda mrefu sana, ninaomba Mheshimiwa Waziri atuambie nini mkakati wa kiwanda kile cha Mbeyatex ambacho kimetelekezwa kwa miaka mingi sana? Ahsante sana.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kufufua viwanda hasa viwanda vya nguo, siwezi kutoa jibu moja likawaridhisha Watanzania au Waheshimiwa Wabunge, ni mapana ambayo siwezi kuyakumbatia, kufufua viwanda hivi lazima vifufuke. Ukisoma mkakati wa (C to C) Cotton to Clothing, unaelezea tutakavyofanya, inaanzia kwa wananchi kulima na Serikali kuwawezesha wananchi kulima. Lakini unakwenda zaidi mpaka kwa kudhibiti wananchi wanaoagiza nguo kutoka nje ya nchi ambazo ni dhaifu lakini wengine hawalipi ushuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nimeletewa ripoti, TRA kuanzia mwezi Januari mpaka mwezi wa Mei, walikuwa wameshindwa kuwakamata watu waliopitisha nguo ambazo hazikulipa bilioni 133. Natoka hapa nakwenda kuripoti kwa Waziri wa Fedha, bilioni 133, nguo zilikuwa under-valued, nguo moja nimeoneshwa na wataalam, kilo moja ya nguo ilikuwa imeingizwa nchini kwa kadirio la bei ambayo ni ndogo kuliko pamba, finishing cloth, nguo iliyokwisha tengenezwa kilo moja yake ilikuwa imeingizwa nchini kwa thamani ambayo ni ndogo kuliko bei ya pamba ya Mwanza. Sasa mazingira yote kwa ujumla ndiyo yanafanya ufufuaji wa viwanda hivi iwe vigumu, lakini yote hayo tunayamudu, tutayafanyia kazi, Mbeyatex na yenyewe itafanya kazi.
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Pamoja na hawa professional staff kutofanya kazi zinazopaswa katika Balozi zetu, mimi nilitaka kujua tu effectiveness ya commercial attaché wetu katika balozi hizo kwa sababu wako dormant. Kiujumla nataka kujua suala zima la utalii pamoja na uwekezaji katika kuongeza pato la Taifa na vilevile kuitangaza nchi linashughulikiwa vipi na Balozi zetu? Naomba majibu.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza za Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, amelisema kwa ujumla kwamba kama kuna watu wanapelekwa ambao siyo taaluma yao wanafanya hawafanyi kazi vizuri lakini vilevile amesema kwamba baadhi ya Maafisa huwa hawatekelezi kazi zao vizuri. Kama anavyojua hii ni Wizara mpya, sasa hivi kuna mpango wa kuwaangalia hawa Maafisa wote na kupima utendaji kazi wao na wale ambao wataonekana hawatekelezi kazi zao vizuri tutawarudisha na kuwapeleka wale ambao wanastahiki.
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa Serikali ilianzisha mpango huu wa MMAM miaka kadhaa iliyopita na ukizingatia kwamba wanawake wajawazito na watoto ndio waathirika wakubwa; nataka kujua, nini mkakati wa Serikali katika kutoa vifaa tiba kwa akinamama wajawazito na watoto hususan katika suala zima la misoprostol wakati wa PPH? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikifahamu Mheshimiwa Mary Mwanjelwa ni Daktari, kwa hiyo, najua anaguswa sana katika hilo. Vile vile mkakati uliopo, kwanza niseme lazima sisi Watanzania tujipe faraja wenyewe, kwa sababu jana kama wale watu walikuwa wanafuatilia katika mitandao ya kijamii, walimwona Rais Mstaafu Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akiwa katika harakati mbalimbali za watu wanaomtunuku kwamba ameshughulikia suala kubwa sana la vifo vya akinamama na watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama Watanzania lazima tujivunie kwa kazi kubwa aliyoifanya Rais wetu mstaafu. Harakati za sasa ni nini? Maana yake ni kujielekeza katika kila eneo katika kuboresha Sekta ya Afya. Ndiyo maana hapa nimezungumza mara kadhaa, kwamba sasa hivi tunakwenda kuhakikisha tunatekeleza mradi mkubwa na wenzetu wa kutoka Uholanzi, kuhakikisha mradi karibuni wa shilingi bilioni zipatazo 46. Katika hili maana yake nini? Tutakwenda kufanya mapinduzi makubwa katika Sekta ya Afya, hasa katika Hospitali yetu ya Kanda kuipatia vifaa tiba, lengo kubwa ni kupunguza vifo vya akinamama na watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mkakati wa Serikali ni huo kwa upana, kushirikisha the own source, kushirikisha income ambazo ziko ndani ya nchi, lakini halikadhalika fursa kutoka maeneo mbalimbali. Lengo kubwa ni kwamba Tanzania iwe ni icon kuhakikisha tunapambana na vifo vya akinamama na watoto katika Bara la Afrika.
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nilikuwa na maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
La kwanza, mwanamke ni tunu katika uumbaji wa maisha ya mwanadamu na kwa kuzingatia mila na desturi zetu za Tanzania nilikuwa nataka kujua Serikali inawashirikisha vipi viongozi hawa wa dini wakishirikiana na wasanii hao pamoja na majibu yake aliyotoa juu ya elimu kwa umma na umuhimu wake?
La pili katika Serikali ya Awamu ya Nne iliyopita Waziri husika alikuwa ameunda Kamati ya Vazi la Taifa ambalo nchi zawenzetu wengine wa hapa Afrika, ndio kutambulisha Utaifa wao nilikuwa nataka Mheshimiwa Waziri atueleze jambo hili limefikia hatua gani na mikakati yake endelevu? Ahsante.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, la kwanza juu ya ushiriki wa viongozi wa dini na makundi mengine katika jamii katika kuhakikisha sanaa yetu inatumika vizuri na haimdhalilishi mwanamke.
Mheshimiwa Spika, nikiri kwamba kwanza ni kweli kwamba mwanamke ni ana hadhi yake katika jamii na hasa katika jamii zetu za Kiafrika na nimpongeze sana Mheshimiwa Mary Mwanjelwa kwa namna anavyopigania hadhi ya mwanamke katika Taifa letu. (Makofi)
Wizara yangu inatoa wito si tu kwa viongozi wa dini hawa wasanii wetu wamo katikakati ya jamii zetu, hawa wasanii ni watoto wetu, ni ndugu zetu na wanaingia kwenye nyumba mbalimbali za ibada na kukutana na viongozi wetu wa dini, natoa wito kila mmoja wetu aone kwamba kuna umuhimu wa kila mmoja kushiriki na kuwahamasisha wahakikishe wanazingatia maadili ya Mtanzania katika shughuli zao za sanaa.
Mheshimiwa Spika, nataka nilihakikishie Bunge lako ikiwa jamii itayakataa matendo yanayofanywa na wasanii, wasanii hawa wataacha kufanya hayo matendo, lakini ikiwa jamii inayashabikia na kuyapenda, wasanii hao wataona ndio fashion na wataendelea kufanya. Kwa hiyo, hata kama sisi tukihamasisha namna gani kama jamii haitayakataa na kuyaona hayafai, kila Mtanzania akaona mwanamke akidhalilishwa amedhalilishwa mzazi wake, amedhalilishwa ndugu yake, haya matendo yatakoma katika jamii yetu.
Kwa hiyo nadhani ni suala la jamii yetu zaidi kuyakataa na kuwatenga kijamii wale ambao wanafanya shughuli za kuwadhalilisha akina mama wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili la Vazi la Taifa na wakati wa bajeti niliulizwa hili swali na nililitolea ufafanuzi, ni kweli ulifanyika mchakato wa kutafuta Vazi la Taifa hapa lakini tulikuja kugundua kwamba ule mchakato tukiendelea nao mpaka mwisho tunaweza tukajikuta tumetoka na vazi la viongozi na sio Vazi la Taifa. Jamii yetu Watanzania tuna makabila 126 kila kabila lina aina yake ya kuvaa, mnaweza mkaendeleza mkafanya mchakato mkafika mwisho halafu mnakwenda mnawaambia Wamasai waache mavazi yao wachukue hili la kwenu, iko hatari ya kuwa na vazi la viongozi na badala ya kutengeneza Vazi la Taifa. Sasa tukatoa wito kwamba kwa ule mchakato ulipofikia ulipendekeza vazi la kanga kuwa ndio vazi preferable ambalo kwa kweli watu wanaweza wakalitumia. Lakini tunaogopa kufikia mahali pa kutengeneza vazi tukalilazimisha na likabaki kuwa vazi la viongozi.
Mheshimiwa Spika, lakini hata hayo mataifa mengine ambayo yana mavazi ambayo yanaonekana yanawakilisha Utaifa wao hawakufanya mchakato wa kufikia Vazi la Taifa. Ilikwenda ikatokea wakajikuta wana vazi, likapendwa na walio wengi na likarasimishwa. Hapa tukiendelea na mchakato huu tutatengeneza vazi la viongozi na halitakuwa Vazi la Taifa letu.
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja dogo la nyongeza. Nikija katika swali la msingi ambalo limeulizwa na Mbunge wa Mbeya Mjini ambalo mimi nimeletewa majibu yake hapa, naomba kuuliza swali dogo moja tu la nyongeza kwa sababu sikuuliza swali la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake ya matumaini ambayo ametupatia sisi Wana-Mbeya kwamba mwakani suala hili litakuwa limekamilika katika suala la msingi la Mbunge wa Mbeya Mjini. Nilitaka kujua tu Hospitali hii ya Rufaa ya Mbeya kwa sababu ndiyo inayohudumia Ukanda mzima wa Nyanda za Juu Kusini, congestion ya wagonjwa ni kubwa sana, Serikali ina mkakati gani katika kuongeza majengo ili kupata bed capacity? Ahsante.
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa kwa kupigania maendeleo ya Mkoa wa Mbeya na maendeleo ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini. Nimetembelea Mbeya na nimemwona Mheshimiwa Dkt. Mary akishiriki katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo, za afya, elimu na za kuwawezesha wanawake kiuchumi. Nakupongeza sana kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nikijibu swali lake, ni kweli Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya inahudumia mikoa takriban minne; Mikoa ya Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa, Ruvuma, Rukwa na Katavi. Kwa hiyo, kwetu sisi ni hospitali ambayo tunaipa kipaumbele cha kutosha. Katika kumthibitishia hili, tunafanya mipango ya kuongeza kujenga jengo kwa ajili ya kuhudumia wanawake wajawazito katika kile Kitengo cha Hospitali ya Wanawake cha Meta.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutaanza kwanza kuongeza jengo kwa ajili ya akina mama wajawazito halafu tutapanua miundombinu, tunataka pia Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya itoe huduma pia ya matibabu ya saratani badala ya wananchi kuhangaika kwenda Dar es Salaam. Tunataka huduma kama hizo za saratani pia ziweze kupatikana na Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumthibitishia Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa, kwa sababu makusanyo ya Serikali ya Awamu ya Tano ni makubwa sana, tuna matumaini kwamba tutapata hela kama tulivyoweka katika bajeti yetu ili tuweze kutekeleza mipango hiyo ya miradi ya maendeleo ambayo tumeipanga.
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali moja tu dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninaipongeza sana Serikali kwa kutenga asilimia kumi kwa ajili ya wanawake na vijana. Serikali sasa hivi haioni kwamba kuna umuhimu kuhakikisha inawashirikisha Wabunge wa Viti Maalum katika Halmashauri zetu, kwa kuzingatia kwamba mara nyingi pesa hizi haziwafikii walengwa. Washirikishwe kisheria na ikiwezekana washirikiane na Maofisa Maendeleo wa Miji pamoja na Kamati ya Fedha, naomba Serikali itoe tamko. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani tukifanya reference wiki hii nilijibu swali hili siku ya Jumatatu, ushiriki wa Wabunge wa Viti Maalum katika Kamati ya Fedha, na nilizungumza kwa upana kwa ku-qoute sheria na vifungu vya kanuni. Nilitoa mifano mbalimbali katika maeneo hayo nikasema wadau watakaa wataona kama inafaa basi tuboreshe sheria zetu na kanuni zetu, hili jambo nililiongelea juzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine kwa sababu nimejua kwamba Mheshimwa Waziri wangu wa Afya alitaka ku-top up katika eneo hilo nadhani aongezee katika kipande hicho.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nataka tu kuongeza majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba sambamba na Halmashauri kutakiwa kutenga asilimia tano kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake; Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imetenga shilingi bilioni moja katika bajeti ya 2016/2017 kwa ajili pia ya kuwakopesha wanawake. Kwa hiyo, fedha hizi tutazipeleka katika zile Halmashauri ambazo kwanza zimefanya vizuri, kwa hiyo kigezo ni Halmashauri kutenga za kwako, halafu Wizara yangu itaongeza zaidi ya zile ambazo zimetengwa na Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kupitia Benki ya Wanawake Wizara pia imetenga shilingi milioni 900 ambazo tutazikopesha kwa wanawake wajasiriamali katika Halmashauri mbalimbali nchini
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. La kwanza, katika mgodi wa JPM ambao uko katika Kata ya Mpanda Hoteli ilikuwa ni sehemu ambayo imewekwa mizinga ile ya kijeshi; lakini hapo hapo katika mgodi huo wa JPM kwa sababu wengi ni wawekezaji wageni, lakini wananchi wa mahali pale wanapata shida sana. Naomba Serikali iweze kutoa tamko kwa sababu wananchi hao wananyanyaswa.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, mimi natoka Mbeya, lakini pale Mbeya sehemu ya Mbalizi kuna Jeshi la Wananchi ambao wako pale na liko jirani sana na wananchi hususan Kata ya Iwindi na Utengule, Usongwe. Sasa nina wasiwasi kwamba lisije likatokea jambo ambalo lilitokea Mbagala. Serikali inatoa tamko gani kwa wananchi hawa ambao wanaweza wakapata madhara kama ya Mbagala? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI (K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mary Mwanjelwa anazungumzia unyanyasaji aliouita unyanyasaji ambao unafanywa na Jeshi la Wananchi kwenye mgodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe hili jambo tulifanyie utafiti na tulichunguze uhalisia wake. Baada ya hapo ndiyo tutakapoweza kutoa tamko la Serikali. Sehemu ya pili, swali lake la pili kuhusiana na Mbeya ni kweli, baada ya kutokea matatizo yale ambayo yalitokea Mbagala, Serikali ilichukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kwamba inadhibiti matatizo kama yale yasijitokeze. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nichukue nafasi hii kuwahakikishia tu Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla kwamba hatutarajii matatizo kama haya yajitokeze kwa sababu Serikali imechukua hatua madhubuti. Hata hivyo, hatutalidharau jambo hili ambalo amelizungumza Mheshimiwa Mbunge nalo pia tutalichukua, tulifuatilie kwa kina tuone kama kuna kasoro tuweze kuzifanyia kazi na kuzirekebisha.
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali
moja dogo la nyongeza.
Ni kweli kabisa hili suala nimekuwa nikilifuatilia na kuliulizia kwa miaka mingi. Nakumbuka hata Mheshimiwa
Rais alipokuwa Waziri wa Ujenzi, hili suala nimekuwa nikilizungumza hususan katika barabara ya mchepuko wa
Uyole hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kama ifuatavyo; pamoja na maswali mazuri ya Mheshimiwa Mbilinyi,
nilitaka kujua ni lini barabara ya mchepuko kutoka Uyole hadi Uwanja wa Ndege itakamalika pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri? Kwa sababu kwenye kikao chetu cha Road Board tulikubaliana kwa pamoja kwamba barabara ya mchepuko lazima itiliwe mkazo, vinginevyo nitakamata shilingi kwenye bajeti yake. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali Mheshimiwa Mary Machuche Mwanjelwa, Mbunge wa Viti Maalum, swali ambalo huwa linafuatiliwa sana na
Mheshimiwa Mbilinyi, Mbunge wa Mbeya Mjini kama ifuatavyo:- (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mwanjelwa kwamba kazi hii inayofanyika sasa
ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina inafanyika kwa umakini na watu makini. Nikuhakikishie, mara itakapokamilika mchepuko huu tutaujenga.
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Swali langu ni dogo tu, majanga ya moto katika Jiji la Mbeya yamekuwa yanajitokeza mara kwa mara hususan Soko la SIDO Mwanjelwa, Uhindini na sababu kubwa ni uchakavu na ubovu wa miundombinu. Naomba Serikali iniambie ina mkakati gani katika kuondoa tatizo hili kwa kushirikiana na Halmashauri?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, emphasis ya swali lake ipo katika miundombinu na ndiyo maana nilikuwa nadhani nilijibu na kama kutahitajika maelezo ya ziada yataweza kutolewa, emphasis yake ameitoa kwenye miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie muda si mrefu hapa tutasoma bajeti yetu ataona ni kwa namna gani Wizara yetu imezingatia haya ambayo ameyauliza, vilevile wakati tunapitisha Bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI unafahamu kuna baadhi ya fedha zimetengwa kwa ajili ya kushughulikia miundombinu katika Jiji la Mbeya.

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ameyatoa kuhusiana na vifaa vya Zimamoto siyo tu kwa Mkoa wa Mbeya lakini nchi yetu kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa Mbeya binafsi nilifanya ziara katika Mkoa wa Mbeya na nataka nipongeze sana uongozi wa Jeshi la Zimamoto, Mkoa wa Mbeya kwamba umefanya ubunifu wa hali ya juu kwa kuhakikisha kwamba unapanua huduma za zimamoto katika Wilaya nyingine za Mkoa wa Mbeya.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuwaunga mkono tuliweza kuhakikisha kwamba tunafanya mambo makubwa matatu. Moja, tumewapatia gari ambayo itakuwepo katika Wilaya ya Rungwe, pili kulikuwa kuna changamoto ya gari ya zimamoto ya Mkoa wa Mbeya ambayo tumefanya jitihada ya kukamilisha matengenezo yake na sasa inaendelea kutoa huduma katika Mkoa wa Mbeya, pamoja na mambo mengine ambayo zaidi yanalenga katika kuongeza utoaji wa elimu ya uokoaji katika Mkoa mzima wa Mbeya na Wilaya nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba katika bajeti inayofuata na katika bajeti zilizopita tumetoa kipaumbele sana katika kuhakikisha kwamba tunatenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa magari ya ziada ya zimamoto. Hizo ni kati ya jitihada ambazo tunachukua ukiachilia mbali mchakato ambao unaendelea sasa hivi wa mazungumzo na kampuni ya Ubelgiji pamoja na Austria kuweza kupata mkopo wa vifaa vya zimamoto na uokoaji kwa Tanzania nzima.
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la Korogwe Vijijini linafanana sana na Jiji la Mbeya ambalo linapanuka kwa kasi, jiji hili kwenye kata za pembezoni ambazo ni Tangano, Iduda, Itezi, Iganjo, Nsomwa, Sanga, Mwasekwa na Msalaga hazina kabisa umeme na ni kwa muda mrefu sana. Kata hizi mazingira yake yamekaa kwa mfumo wa REA na tunashukuru kwamba REA Awamu ya Tatu ilishazinduliwa katika Mkoa wa Mbeya. Swali langu ni kwamba Serikali ina mkakati gani wa kuvipatia umeme vijiji hivi ambavyo kwa TANESCO inaelekea imeshindikana?Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Mwanjelwa kwamba hata TANESCO bado inapeleka umeme katika maeneo mbalimbali kufuatana na bajeti zake. Tumeshakaa na Mheshimiwa Mbunge na ni kweli kabisa yako maeneo yenye utata kidogo kama eneo la Uyole.
Hata hivyo, vijiji anavyotaja vya Idunda, Kasilanda pamoja na vingine baadhi yake vipo kwenye miradi ya REA. Kwa hiyo, tutakaa na Mheshimiwa Mbunge tuone vijiji vinavyoingia mijini vitabaki TANESCO na vile ambavyo viko kwenye vijiji vitapelekewa umeme kupitia miradi ya REA.
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Naibu Waziri kwanza naishukuru sana Serikali yangu kwa maana ya kwamba iliweza kutatua tatizo la walimu waliokuwa wanapandishwa madaraja lakini hawapati mshahara. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, kwa kuwa taarifa ya uhakiki wa vyeti imeshatolewa na katika Jiji la Mbeya kuna walimu zaidi ya 200 waliobaki. Je, ni lini sasa Serikali itaruhusu marekebisho ya mishahara kwa walimu hao waliokwishapandishwa vyeo vyao kufanyika? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, kumekuwa na tatizo la watumishi kukaa katika kituo kimoja kwa muda mrefu sana na hivyo kushindwa kuleta changamoto mpya katika kipindi hiki cha Hapa Kazi Tu na kufanya kazi zao kwa mazoea. Nilitaka kujua nini mkakati wa Serikali katika hilo?Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli alichosema Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa, alitaka time frame ni kwamba katika mwaka ujao wa fedha zoezi hili litaanza. Mheshimiwa Mwanjelwa asihofu watumishi wake watapata hiyo stahiki yao inayotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala la watumishi wengi kukaa kituo kimoja muda mrefu, ni kweli tunafahamu kwamba mtumishi anapokaa miaka 15, 20 hana changamoto mpya ambayo anaweza akaileta katika eneo hilo. Ndiyo maana Ofisi yetu kila mwaka tumekuwa tukifanya utaratibu huo katika maeneo mbalimbali, lengo kubwa ikiwa ni kuleta hii changamoto mpya na tunaendelea kufanya zoezi hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, tuko makini
sana katika kuhamisha watumishi. Kwa mfano, tumetoa maelekezo kwa Wakurugenzi wetu kwamba waangalie jambo hilo, lakini wasihamishe watumishi hivi hivi bila kuwa na pesa yao kuweza kuwalipa. Jambo hili tumelielekeza na bahati nzuri Mheshimiwa Rais siku ya Mei Mosi alilitolea maelekezo maalum kwamba sasa hakuna utaratibu wa kumhamisha mtu kabla ya pesa yake kuwa tayari.
Naomba nimhakikishie kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutahakikisha tunakuza utendaji wa kazi na kuangalia mtu kama ame-over stay kwa muda mrefu tutaona namna ya kumhamishia sehemu nyingine ili kuleta changamoto mpya.
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, la kwanza, maji yanapokuwa ni adha kubwa waathirika wakubwa kwa kiwango kikubwa wanakuwa ni wanawake. Katika Wilaya hii mpya ya Songwe iliyoko Mkwajuni ni kilometa kumi tu kutoka katika Ziwa Rukwa, sasa nataka kujua, nini mpango wa Serikali katika kuvuta maji kutoka Ziwa Rukwa ambalo Mheshimiwa Mulugo amekuwa akililia kwa muda mrefu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Wilaya hii mpya ya Songwe, matatizo yake yanafanana sana na Wilaya ya Chunya ambayo ilikuwa ni Wilaya moja katika Mkoa wa Songwe. Katika Wilaya hii ya Chunya kuna Kata za Makongolosi, Matundasi na Bwawani hazina maji kwa muda mrefu sana. Nini mkakati wa Serikali katika hilo? Nashukuru.(Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze kwa swali zuri ambalo ameliuliza kwa niaba ya Mulugo. Kuhusu kwamba Mkwajuni iko kilometa kumi kutoka Ziwa Rukwa na angependelea kwamba maji yale yangepelekwa kwenye Mji wa Mkwajuni, jibu ni kwamba, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi kwamba tumetenga milioni 100 kwa ajili ya kufanya usanifu. Sasa usanifu ndiyo utaelekeza ni wapi tuchukue maji. Kama tutaona maji ya Ziwa Rukwa yanafaa basi tutachukua hapo na kuweza kupeleka maji katika Mji wa Mkwajuni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu mkakati wa hizo
Kata za Makongolosi na zingine katika Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, mkakati wa Serikali ni kwamba katika bajeti kila Halmashauri tumeitengea fedha na tumetoa mwongozo kwamba wao watoe vipaumbele kulingana na zile bajeti. Inasikitisha kwamba unaweza kufika mahali kwenye Halmashauri ikiwepo hata hii ya Songwe, katika bajeti ya mwaka uliotangulia walitengewa milioni 752, lakini mpaka leo tunamaliza mwaka fedha zipo lakini hakuna kazi iliyofanyika.
Mheshimiwa Spika, nitakwenda kule kuangalia matatizo yao ni yapi ili tuweze kuwasaidia tuweze kutatua matatizo ya wananchi. (Makofi)
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ninakushukuru. Katika Wilaya ya Mbeya tumekuwa na viwanda vingi sana kama Kiwanda cha Mbeya Textile, Hill Soap, Tanganyika Packers, Zana za Kilimo na kadhalika na viwanda hivi ni vya muda mrefu sana vimekufa. Namuomba Mheshimiwa Waziri kwa kushirikiana na Msajili wa Hazina, anieleze ni lini na nini mkakati wa Serikali katika ufufuaji wa viwanda? Siyo ujenzi wa viwanda. Ahsante.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio. Natambua na kumbukumbu zinaonesha kwamba viwanda vingi vilivyopo Mbeya vilikufa na vilipokufa vilibinafsishwa na kupeleka miliki kwa watu wengine, watu binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa taarifa ya awali kwamba Treasury Registrar kwa kushirikiana na Wizara za kisekta wanafuatilia ikihusisha uhamishaji wa miliki ambayo ni masuala ya kisheria kusudi waweze kuvirudisha hivyo viwanda kwenye wamiliki wapya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niwaeleze Waheshimiwa Wabunge, mtu aliyeuziwa kitu kwa mkataba huwezi kumnyang’anya hivi hivi, labda tubadilishe matumzi ya sheria, siyo kitu rahisi.
Ningependa tuwanyang’anye mara moja, lakini siyo kitu rahisi. Tunachofanya zaidi pamoja na kuwanyang’anya, tunajaribu kuangalia namna gani rasilimali zile zinaweza kutumika kuzalisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, kwa uelewa zaidi, someni vision 2025 mjue kwa nini viwanda vilikufa? Vingine vilikufa kwa sababu pale vilipojengwa, havikustahili kujengwa.
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja dongo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilio changu cha zaidi ya miaka minne katika Bunge hili ni kuhusu barabara ya mchepuko kutoka Uyole - Songwe Airport kupitia Mbalizi kimekuwa kirefu na nimekuwa nikielezea ni kwa nini. Naishukuru Serikali kwenye bajeti yake Mheshimiwa Waziri amesema kwa kilometa 40 hizi upembuzi yakinifu utaanza. Nilitaka Mheshimiwa Waziri atoe tamko hapa upembuzi yakinifu huu utaanza lini kutokana na adha hii ya Wanambeya ambayo tumekuwa tukiipata kwa muda mrefu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Mwanjelwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Mwanjelwa anafahamu kwamba hilo eneo analoliongelea ndilo eneo ambalo na mimi kila wakati napita nikienda kuwatembelea wakwe zangu. Nakuomba sana Mheshimiwa Dkt. Mwanjelwa, utuamini siyo kwa sababu hiyo, utuamini kwa sababu tumedhamiria na ndiyo dhamana yetu ya kutekeleza ahadi zote za Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne ambaye aliitolea ahadi barabara hii na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano ambaye naye aliitolea ahadi. Mimi nakuomba utuamini mwaka huu wa fedha unaokuja kuanzia Julai, 2016 mpaka Juni, 2017 kama huo upembuzi yakinifu hautafanyika, ninakuhakikishia dada yako atarudi.
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasimama kwa niaba ya Mheshimiwa Oran ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mbeya kijiografia imekaa vibaya sana, vituo vingi zaidi hasa katika Kata ya Igoma Tarafa ya Tembela pamoja na kule Isangati hakuna vituo vya polisi kabisa na jiografia yake kama nilivyosema ni mbaya. Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alikuwa ameahidi kabisa kwamba vituo hivi vijengwe, lakini mpaka leo hakuna. Nataka kujua majibu ya Serikali ni lini itajenga Vituo vya Polisi huko Igoma pamoja na Ilembo katika Tarafa ya Isangati?
Swali la pili, Wabunge wa Mkoa wa Mbeya wote kwa pamoja tunachanga kwa juhudi zetu na wananchi kujenga Kituo cha Polisi cha Mbalizi. Ninataka kujua ni nini mkakati wa Serikali katika kuongeza nguvu katika kituo hiki cha Polisi Mbalizi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Mary Mwanjelwa, Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo hili na Wabunge wa Mkoa wa Mbeya ambao wameshirikiana katika kujenga kituo hiki. Binafsi nilikwenda pale kuzindua ujenzi huo na sisi vilevile tulichangia, lakini niwapongeze pia, wananchi wa Mbeya kwa kuweza kujitolea kukijenga kituo hiki katika hatua ambayo sehemu iliyofikia ni karibu asilimia 50 ya ujenzi imekamilika na huu ni mfano wa kuigwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, changamoto ambayo ameizungumza katika maeneo mengine ya Isangati, nitoe changamoto kwamba wakiendelea na jitihada kama hizi itasaidia kuharakisha ukamilishaji wa ujenzi wa vituo katika maeneo mengine kwa haraka ili kusaidia kukamilisha dhamira njema ya Serikali ya kukamilisha ujenzi wa vituo 65 nchi nzima vyenye mapungufu katika maeneo mbalimbali nchini.
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira kule Mbeya umekuwa static kwa muda mrefu sana na Mgodi huu mimi naweza nikasema sasa wananchi wa Mkoa wa Mbeya na mikoa ya jirani tumekuwa yatima. Nini tamko la Serikali, nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana nae kwanza Mwanjelwa hongera sana. Hata mwaka jana amehangaika sana kuhakikisha kwamba mgodi huu unafanya kazi. Nimpe taarifa tu, mwaka 2017/2018 Shirika la STAMICO limeanza uchimbaji, na hivi sasa limeishachimba tani 500 ya makaa ya mawe na wataendelea na uchimbaji. Kadhalika kuna makampuni mawili yataingia ubia ili kuwezesha uchimbaji kuwa wa manufaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mgodi wa Kiwira umeishaanza shughuli na kufika mwaka 2018/2019 tunatarajia tani 100,000 zitakuwa zimezalishwa katika mgodi ule. (Makofi)
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Jiji la Mbeya halina master plan, general plan scheme na limekuwa katika data collection ya almost bilioni1.5. Swali langu ni kwamba je, Serikali haioni kwamba sasa ni wakati muafaka wa ku-push hili jambo lifike mwisho?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Waziri walishatembelea katika Jiji la Mbeya na nilikuwa bega kwa bega, mguu kwa mguu na Mheshimiwa Naibu Waziri yeye mwenyewe amejionea ni jinsi gani Jiji la Mbeya limekuwa ni la squatter kwa muda mrefu sana, hususan katika maeneo ya Isanga, Ilemi, Nzovwe, Iyunga, Kalobe, Nonde, Mwakibete, Sinde, Soweto; yote haya na mengineyo mengi ni Squatter kwa muda mrefu sana. Swali langu kwa Serikali, haioni kuwa sasa ni wakati muafaka tena wa kusaidia up grading katika maeneo hayo? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI:Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Mwanjelwa kwa sababu mara nyingi katika Bunge hili kama tutakumbuka kila akileta swali la Makazi mara nyingi anapenda kutolea mfano wa Mbeya ambao unakuwa pengine haujawa na master plan mpaka dakika hii, lakini ni mji ambao unakuwa kwa kasi kubwa. Sasa hivi Wizara yangu inayo miji karibu 28 ambayo tayari michakato yake ya master plan inaendelea.
Mheshimiwa Spika, Jiji la Mbeya bado halijawa, mimi niwaombe sana watu wa Mbeya tuanze maandalizi ya kuwa na master plan kwa sababu mchakato mzima lazima uanzie kwenye eneo husika. Ni wazi kama wataanzisha kama ambavyo miji mingine imeanza kama Arusha, Dar es Salaam na Mwanza ambayo imeishaanza, sasa mimi niseme tu kwamba Jiji la Mbeya nalo sasa linatakiwa lianze mchakato huo kwa sababu ni suala ambalo litafanya libadilishe kabisa mandhari ya mji wenyewe.
Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la pili, ni kweli nikiri kwamba nilikwenda Mbeya na tuliongozana naye, na maeneo anayoyataja ni kweli hayavutii kwa kasi ya namna ambavyo ilivyo. Mimi nimpongeze kwa sababu pia, amekuwa na kiu ya kutaka kuona mabadiliko yanakuwepo.
Mheshimiwa Mwanjelwa naomba nikuhakikishie kwamba kwenye maeneo ya Iyunga, Kalobe, Uyoe, Nonde, Mwakibete, Sinde, Isanga, Soweto na kadhalika, kweli nilijionea maeneo hayako katika hali nzuri.
Mheshimiwa Spika, sasa mimi niseme pale ambapo mtaanza master plan, basi tutawekeza pia katika maeneo hayo kuhakikisha kwamba yanabadilika ikiwa ni pamoja na kubadili mandhari kama ambavyo ulivyoomba kuweza kufanya ile pulling ya land kuweza kuleta pamoja na kuweza kujenga majengo ambayo pengine yatapendeza zaidi au kuweka mandhari ambazo zitafanya ule mji kweli uonekane kweli ni Jiji.