Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Mary Machuche Mwanjelwa (3 total)

MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA aliuliza:-
Kila jamii ina mila na desturi zake; hapa nchini wanamuziki wamekuwa hawavai mavazi ya staha au utu wa mwanamke umekuwa ukidhalilishwa kutokana na kuvaa nguo zinazoonesha maungo yao.
Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti mavazi yasiyo na staha kwa wanamuziki wa kike?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Mary Machuche Mwanjelwa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) imekuwa ikitoa elimu kwa wasanii mara kwa mara kupitia vyombo vya habari, makongamano, semina na warsha juu ya umuhimu wa maadili katika sanaa na namna ya kubuni kazi za sanaa zenye ubora na zinazozingatia maadili, elimu imekuwa ikitolewa kupitia vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo E fm Radio, EATV, Magic FM, Azam TV, Channel Ten, Clouds Entertainment na TBC.
Mheshimiwa Spika, kwa wasanii wanaokiuka maadili kwa kuvaa mavazi au kubuni kazi za sanaa zinazomdhalilisha mwanamke hatua za kinidhamu na kisheria kama vile kufungia kazi zao, kuwafungia wao wenyewe na kuwatoza faini zimekuwa zikichukuliwa.
Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka 2014/2015 mpaka sasa wasanii watatu wa kike na msanii mmoja wa kiume na kikundi kimoja cha kanga moko walipewa maonyo na wengine kufungiwa kabisa kwa kudhalilisha utu wa mwanamke. Aidha,kwa mwaka 2016/2017 msanii mmoja wa kiume alipewa onyo na kutozwa faini.
Mheshimiwa Spika, Sera ya Taifa ya Utamaduni ya mwaka 1997 imeeleza wazi kwamba kila Mtanzania ana wajibu wa kulinda mila na desturi zetu sambamba na kuhakikisha maadili yanalindwa na mwanamke hadhalilishwi wakati wa shughuli za sanaa. Wizara yangu inapenda kutoa wito kwa kila Mtanzania kuhakikisha kwa namna moja au nyingine anatunza na kulinda maadili na utamaduni wa Mtanzania.
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA aliuliza:-
Je, nini mkakati na sera ya Serikali kwa wafanyakazi hususani walimu wanaojiendeleza katika kuwapandisha madaraja na kuwaongezea mishahara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Mary Machuche Mwanjelwa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za 2009, watumishi wa umma hupandishwa vyeo kwa kuzingatia sifa na ufanisi na utendaji kazi. Mwalimu anapohitimu mafunzo yake anastahili kubadilishiwa muundo wake wa utumishi mfano, Mwalimu Daraja la III - Stashahada kwenda Daraja la II ngazi ya Shahada. Kupanda daraja kwa mtumishi kunategemea utendaji kazi utakaothibitishwa na matokeo katika Mfumo wa Wazi wa Upimaji Utendaji Kazi wa mtumishi husika yaani OPRAS system. Watumishi wote wanatakiwa kujaza fomu hizo na kupimwa utendaji wao wa kazi kama wanastahili kupandishwa daraja.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kama ilivyoelezwa na Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, walimu wakiwemo watumishi wengine wenye sifa watapandishwa madaraja katika mwaka wa fedha 2017/ 2018 baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki wa watumishi.
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA aliuliza:-
Je, nini sera ya Serikali katika kubadilisha mandhari ya maeneo ambayo ni squatter au ya wazi kwa kuwekeza katika majengo ili kuwa na makazi ya kisasa kwa ajili ya wananchi kwa kutumia ardhi iliyopo katika eneo husika?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali namba 475 la Dkt. Mary Mwanjelwa, Mbunge wa Viti Maalumu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kifungu namba 4.1.4.2 cha Sera ya Taifa ya Makazi ya mwaka 2000 kinaelekeza kuwa maeneo yaliyojengwa bila kupangwa na kuwekewa huduma za msingi yaboreshwe na wananchi wenyewe kwa kushirikiana na asasi za kijamii. Kwa maeneo yaliyojengwa bila kupangwa na kupimwa lakini yapo katikati ya miji (prime areas) hususan katika Jiji la Dar es Salaam, Wizara imeandaa rasimu ya mkakati wa uboreshaji wa maeneo hayo kwa kutumia dhana ya kukusanya ardhi (land pooling). Utekelezaji wa dhana hii utawawezesha wananchi wa maeneo husika kupata makazi bora na pia kupata ardhi kwa ajili ya uwekezaji mpya.
Mheshimiwa Spika, dhana ya kukusanya ardhi inalenga kuboresha maeneo hayo kwa kujenga majengo makubwa ya ghorofa ili kuweza kuwapatia makazi mbadala wakazi wa maeneo husika katika eneo hilo hilo, na pia kupata eneo la uwekezaji utakaojumuisha ujenzi wa majengo ya kibiashara kama vile maduka makubwa (super markets and shopping malls), makazi ya maghorofa ambayo mengi yanakuwa na apartments, hoteli, huduma za kijamii, maeneo ya wazi, maeneo ya burudani na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, rasimu hiyo kwa awamu ya kwanza inapendekeza kufanya ukusanyaji wa ardhi katika maeneo ya Manzese, Vingunguti, Buguruni, Msasani, Keko, Namanga, Mikocheni na Kawe.