Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mwita Mwikwabe Waitara (56 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naomba nimshukuru sana Mungu, ameniwezesha kupitia wananchi wa Jimbo la Ukonga kuingia kwenye jengo hili na naomba nitoe mchango wangu. Naomba Waheshimiwa Mawaziri wanisikilize vizuri kwa sababu Wabunge hawa wa CCM hawatawasaidia sana kwenye utendaji wa kazi, kwa hiyo, ni muhimu sana. Wanasifia yote, halafu wanalalamika mwanzo mwisho, kwa hiyo mimi utaratibu huo siupendi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kaulimbiu ya Serikali hii ni Hapa Kazi Tu maana yake inaonesha hawa watu walikuwa wazembe muda wote tangu mwaka 1961. Wazembe tu ndio maana nasema wamezinduka sasa, eti hapa kazi. Kwa hiyo, mnapokuwa mnapendekeza kauli hizi ni muhimu mkachunguza kama zina mwitikio chanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Serikali inatumbua majipu, maana yake kuna wagonjwa wengi na ugonjwa huu umesababishwa na wenyewe CCM. Halafu Serikali ya CCM waoga sana. Ndio maana kuna polisi huku, wamezunguka jengo la Bunge, wanajaza askari humu ndani watu waogope kutoa hoja, maana yake ni waoga kweli kweli. Wangekuwa sio waoga wangetulia tushughulikiane kwa hoja na kwa vyovyote itakavyokuwa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine waongo, Serikali hii inawaambia watu utawala bora, tena utawala wa kisheria, lakini ukiangalia kauli hii na yote yametajwa kwenye mapendekezo, mmetaja, nilikuwa nasoma hapa.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mmesema utawala bora, mimi naenda kwenye hoja. Hamjasoma vizuri, utawala bora. Naamini kikwazo cha maendeleo ya Tanzania ni CCM wenyewe.
Kwa hiyo, tukipanga mipango tukajadiliana, siku CCM ikitoka madarakani, nchi hii itapata maendeleo makubwa sana. Kwa hiyo, nawaambia Watanzania wajipange kuiondoa CCM madarakani ili wapate maendeleo kwa sababu shida ni CCM, mipango hakuna shida, rasilimali zipo, wataalam wapo, ardhi ipo, kila kitu kipo, shida ni hao wenyewe tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo yangu mawili ya msingi. Moja ni elimu. Nashangaa sana Waziri, kaka yangu Simbachawene wakati anachangia, akawa anakataa tusiseme elimu ya bure haipo. Jambo la kawaida kabisa, kwamba unalipa ada ya shilingi 20,000/= kwa shule za kutwa na shilingi 70,000/= shule za boarding, gharama zingine wazazi wanaingia halafu unasema eti elimu hii ni ya bure, lugha ya kawaida ya Kiswahili tu. Wekeni lugha hii ili msiwachanganye wananchi, elimu ni ya kuchangia, Watanzania wajue na wajue majukumu yao, wafanye kazi ya kusomesha watoto wao, kwamba Serikali ilichofanya imepunguza gharama, very simple ili watu waelewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu mnapowaambia watu elimu ni bure, akienda pale anadaiwa mahindi, apeleke maharage, halafu michango mbalimbali, wanaambiwa walipie mlinzi, semeni ili jambo lieleweke vizuri, kwani siyo dhambi. Hapa hakuna elimu ya bure, ni elimu ya kuchangia na Watanzania wajue. Kwa hiyo, nadhani ni muhimu sana hili jambo likawekwa wazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika hizi shule, kwa mfano, nina madai hapa ya waraka uliotolewa ili wale walimu, wanasema Waraka kwa Watumishi wa Serikali Namba 3 wa mwaka 2014 kuhusu mishahara na posho ya madaraka kwa viongozi wa elimu. Hawa ni wakuu wa shule za sekondari na msingi na vyuo. Maana yake mpaka leo hawa watu wanadai, wametengewa tu shilingi 250,000/-, kwa hiyo maana yake hawa hawawezi kuwa na moyo wa kuendeleza elimu vizuri kama wenyewe wana madai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani Mkuu wa Chuo analalamika, Mwalimu Mkuu analalamika, na wazazi wanalalamika, wanafunzi wanalalamika, kwa hiyo mkitaka mambo yaende sawa, nilimsikia Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini amesema, yeye hataenda kwenye mpango wa tatu wa REA, mpaka makando kando ya mpango wa kwanza…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri hii kauli ikifanyika itasaidia sana. Miradi yote ambayo Wabunge wanataja hapa, barabara ambazo zilipangwa, kama ile ya kutoka Kitunda kwenda Msongora, tangu wakati Mheshimiwa Magufuli akiwa Waziri awamu ya kwanza, awamu ya pili mpaka leo Rais, ni wimbo. Mvua ikinyesha watu hawawezi kwenda mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda hivyo katika miradi mbalimbali ya maji kule Chanika, Msongora, Kidole, Mgeule, ikakamilika, maana yake watu wale ukizungumza habari ya maendeleo na uchumi wa kati watakuelewa. Kwa hiyo, mambo haya ni muhimu sana mkayakamilisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja ya msingi sana ambayo mambo haya hamjayafanyia kazi na nimwombe Mheshimiwa Waziri anisaidie. Kwa mfano, kwenye upande wa elimu, Mawaziri, kila mtu anaibuka na jambo lake katika nchi hii. Tuliwahi kuwa na Mungai akaja hapa na unified science, mimi bahati nzuri ni mwalimu wa hesabu na kemia, akachanganya masomo watoto wakaogopa sana masomo ya sayansi, kwa hiyo watu wakarudi nyuma sana, Waziri akawa na mamlaka hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeenda hapa, akawepo Kawambwa, akaibuka na GPA na nampongeza Mheshimiwa Waziri Profesa Ndalichako amefuta ile, namuunga mkono, turudi kwenye division. Kwenye Sheria za Baraza la Mitihani, kifungu namba 20, kinasema, The Minister may give the Council directions of a general or specific character and the Council shall give effect to every direction. Kumbe hiki kifungu ndiyo kifungu ambacho Waziri anaibuka asubuhi, anaenda anatoa maelekezo Baraza la Mitihani, wanaambiwa sasa hivi ni GPA, ni Division, hiki kifungu kiondolewe. Hata kama Waziri ana mamlaka ashauriane na wataalam wenzake, ili mambo haya yasiwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake mnawayumbisha Watanzania, watoto hawa mnawayumbsha, mara division, yaani mnachofanya nyie ni kwamba kuna golikipa yupo mlangoni pale, anachofanya ameshindwa kiutaalam, kimpira, anaamua aongeze tu ukubwa wa goli, ili ionekane kwamba wamefunga. Hiyo maana yake ni failure, haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mpango wa elimu hapa, hatuna vile vitu vya kitaalam kwa mfano Teachers’ Profession Board, haipo, Quality Assurance Board, haipo. Kama ambavyo kuna Wanasheria wana Chama cha Wanasheria, Walimu wana chama ambacho kinaelekea kuwa chama cha kisiasa siku hizi. Sasa hawa watu lazima wawezeshwe ili waweze kusimamia, lakini ni muhimu sana mkaangalia mambo ya maslahi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi unaleta mpango wa kipato cha kati unazungumza habari ya viwanda, halafu shuleni hata matundu ya choo hamna, hivi kweli hayo ni maendeleo? Yaani uzungumze upate mainjinia wakaendeshe viwanda, matundu ya choo tu ni shida. Yaani madawati ni shida, mnazungumza vitu vikubwa, vidogo tu vimeshindikana hapa. Wewe unazungumza habari hii wakati hata choo hakipo shuleni. Sasa hivi watoto wameandikishwa katika shule hizi, kuna shule ina watoto 617, ina madarasa mawili ya darasa la kwanza. Sasa huu uchumi wa kati nataka nione miujiza, hapa kazi tu na jipu, tuone mambo yatakavyokuwa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya mwisho, utawala bora. Zamani niliwahi kumuunga mkono Mheshimiwa Nape, wakati nilipokuwa kule chama cha zamani, lakini nikagundua Mheshimiwa Nchimbi aliwahi kufuta kanuni ili Nape asigombee Uenyekiti, naona alikuwa sahihi.
Huyu jamaa amekuja hapa, anaondoa hoja, unawaambia watu utawala bora, wana haki ya kupata taarifa kwa mujibu wa Ibara ya 18, Waziri anakaa chumbani, tumelalamika jana yake, kesho yake amekuja hapa akatuambia kuna utafiti wa Uingereza, yaani unawezaje Waziri kujifunza kuzuia taarifa, usijifunze demokrasia ya Uingereza, miundombinu na vitu vingine vikubwa, wewe ukajifunza kuzuia taarifa tu. Unatuambia, kuna utawala bora hapa? Yaani, unazuia Watanzania wasijue tunazungumza kitu gani humu kwenye hili Bunge. Halafu Waziri Mkuu na Mawaziri, wengine ni wataalam na wasomi, wanaunga mkono na kupiga makofi. Ndiyo maana nikawaambia Waheshimiwa Mawaziri, Wabunge wa CCM hawawezi kuwasaidia sana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo mambo kwa kweli ni muhimu mkayatafakari upya. Haiwezekani mkazuia taarifa ya kile kinachoendelea, unatuambia suala la muda wa kazi, sasa, hivi asubuhi na jioni, upi ni muda wa kazi mzuri? Kwa hiyo, asubuhi mnaonesha, jioni mnazima. Yaani jioni saa tisa na nusu, ndiyo muda sasa umekwisha, halafu asubuhi mnaonesha. Unarekodi masaa saba, halafu mna-edit mnatoa kwa saa moja, mnatoa mnayotaka wenyewe muone.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Zanzibar itakuwa hoja yangu ya mwisho. Mimi najua na CCM wanajua kwamba Zanzibar uchaguzi ulikwenda vizuri na Maalim Seif alishinda. Huo ndio ukweli, hata kama hamtaki. Dunia inajua, Afrika inajua, Tanzania inajua, CCM mnajua na Taifa hili mnajua na Mwenyekiti unajua. Uchaguzi wa Zanzibar ulikwisha. Kwa hiyo, mnachofanya ni magumashi na sisi kama watoto wa Tanzania hii hatuwezi kuunga mkono mambo haya. Nchi hii ni ya demokrasia kila mtu ana haki ya kuongoza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tukienda kwenye uchaguzi watu wakapiga kura, hakuna malalamiko, aliyeshinda apewe haki yake, ndiyo mpango mzuri wa maendeleo utakavyokwenda. Twende kwa amani kwa kuheshimiana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, sijaunga mkono hoja mpaka kwanza Mpango wa Maendeleo uje, ndio nitaunga mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)
TAARIFA
MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa.
MBUNGE FULANI: Mwenyekiti, kuhusu utaratibu, kanuni ya 63, ile ile inayotumika. Mimi ninao ushahidi ya kwamba...
MBUNGE FULANI: Kanuni ya 63 ngapi?
MBUNGE FULANI: Kanuni ya 63(3)
MBUNGE FULANI: Mbunge mwingine yeyote anaweza kusimama mahali pake na kutamka kuhusu utaratibu na baada ya kuruhusiwa na Spika kudai kwamba, imetosha. Mbunge aliyezungumza kuhusiana na kwamba Maalim Seif ameshinda, amesema uongo.
WABUNGE FULANI: Kweli!
MBUNGE FULANI: Kwa mujibu, nathibitisha sasa, Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, kifungu cha 42 kutoka (i) mpaka (v) kinazungumzia Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar pekee ndiyo yenye mamlaka ya kumtangaza na kujumuisha kura za ushindi.
(Hapa baadhi ya Wabunge walimzomea Mzungumzaji)
MBUNGE FULANI: Kama Mheshimiwa Mbunge amezungumza, maelezo hayo, kama ameeleza maelezo hayo, kwamba uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa una mshindi, naomba atoe uthibitisho.
WABUNGE FULANI: Aaaa, hakuna.
MHE. MWITA M. WAITARA: Kuhusu utaratibu Mwenyekiti.
MBUNGE FULANI: Aah, atoe.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waitara, unaipokea hiyo taarifa?
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikuhakikishie na Kamati hii kwamba sipokei na yeye yupo humu baada ya uchaguzi wa Zanzibar, uchaguzi ulikuwa na karatasi tano, kwa nini wamehesabu moja ni halali nyingine zote nne sio halali?
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ili na mimi nichangie, lakini kabla sijachangia naipongeza Ofisi ya Bunge kupitia Katibu wa Bunge kwa kitendo cha kuiwezesha Ofisi ya Mbunge wa Ukonga kuwa na fenicha. Kwanza ameonesha uzalendo kwa kuwa fenicha zenyewe zinatengezwa pale Ukonga kwenye Jimbo langu, vilevile kwa kutengeneza mahusiano akaanzia kwangu, hivyo nawapongeza sana waendelee na moyo huo. Nawashukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, sitaunga hoja kama CCM, kwa sababu wanaunga mapema halafu asilimia 95.5 wanalalamika! Huu mtindo haupaswi kuwa entertained kwenye Bunge, mimi nitaenda tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshauri Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana, taarifa ya Upinzani Bungeni imempa maswali wala asiyabeze ni mambo ya msingi kweli, kwa rekodi tu nataka nikumbushe mambo machache ambayo nataka ayazingatie kama atapenda, maana yake anaweza akakaidi tu.
Kwa mfano, nchi hii inataka kuwa nchi ya viwanda, lakini Watanzania wanataka kuhakikishiwa na Serikali hii, mimi siiti Serikali Tukufu sasa Mungu atakuwa nani! Wanasema hivi viwanda vilikuwepo……
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MBUNGE FULANI: Hiyo kengele ni ya mtu mwingine wewe endelea tu.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mwongozo wako hivi vitu vinachanganya hapa.
MWENYEKITI: Endelea.
MHE. MWITA M. WAITARA: Naomba unilinde, hizi kengele na kelele uzuie kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa inaonesha kwamba viwanda viliuzwa, sasa wakati tunaenda kuleta huu Mpango ambao ni mzuri sana kwa Watanzania, lazima Watanzania wahakikishiwe tukianzisha havitauzwa tena, kutolewa bure au kugawanywa kama shamba la bibi? Hilo ni jambo la msingi kabla ya kwenda kwenye mpango wenyewe, hatuwezi kuweka hela mahali ambapo anaweza akaja mtu mwingine hapa, hapa Mheshimiwa Magufuli amekuja na habari ya viwanda, anaweza akaja mwingine na ajenda zake akaanza kuvigawa tena bure, unakuta nchi inapiga marktime. Sheria inasema nini juu ya hayo mambo ambayo yamefanyika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumelalamika sana, watu waligawana viwanda, waliovunja utaratibu hawajashughulikiwa, hawajawajibishwa, hakuna mtu yupo Mahakamani, tunaleta mpango mwingine! Sasa nadhani hili jambo ni muhimu sana likazingatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, kwenye ukurasa wa tatu, napitia ile taarifa ya Upinzani, wamesema fedha zilizotolewa ni asilimia 26, ni muhimu Waziri akatuonesha kama mipango iliyopangwa ilikamilika kwa asilimia 26 kwa eneo hili, hivi hizi zilizobaki asilimia takriban 74 amekuja na miujiza gani tena mingine mipya ambayo itawasaidia ili iweze kuwa sustainable, ni muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi yote iliyopangwa haikuzidi nusu tangu imeanza kuzungumza Serikali hii mpya ya CCM sababu haya ni majina tu, alikuwepo Mheshimiwa Nyerere, amekuja Mheshimiwa Mwinyi amekuja Mheshimiwa Kikwete, sasa ni Mheshimiwa Magufuli. Sasa haya ni majina tu lakini Serikali ya Chama kilekile asilimia 60 ya mipango ya maendeleo haijawahi kufikiwa nchi hii .
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nadhani mambo haya yangetusaidia kwa mfano, yametajwa hapa mambo ya msingi kabisa kwamba Deni la Taifa limeongezeka, nimejaribu kugawa hapa hizi trillion 41536.6 ni kama takriban 923,000 kwa kila Mtanzania hata aliyezaliwa leo, ambazo kama Taifa tunadaiwa katika nchi hii. Sasa nataka kujua, deni likiwa kubwa namna hii athari yake kiuchumi ikoje na watu wategemee nini? Maana tunadaiwa hapa tulipo kila mtu sh. 923,000 kwa mahesabu yaliyotajwa hapa, sasa nikasema haya mambo ni muhimu sana kuyazingatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye rasimu ya Mheshimiwa Warioba haya mambo yangeweza kujibiwa, sasa mkachakachua Waheshimiwa ndugu zangu CCM mkaleta mambo yenu, figisu figisu nyingi, mkapindisha haya mambo. Ile rasimu ilikuwa inaelekeza ili Taifa likope, ili hiyo hoja ije Bunge lijadili, liruhusu ili tuelezwe unakopa, haya maswali ambayo Mheshimiwa Silinde kwa niaba yetu, anauliza, uliweka dhamana ya nini, mlifanyia kitu gani, mipango ikoje, nani alikopa, vitu vya namna hiyo vingeweza kujibiwa sasa ile rasimu mmeichakachua, sisi Katiba hatuna, haya mambo yangeweza kujibiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nirudi kwenye hoja hizi ambazo zimezungumzwa. Miundombinu; tumezungumza hapa, mimi nilipo ni karibu na uwanja wa ndege, nitaomba Waziri mwenye dhamana na eneo hili anisaidie, uwanja wa ndege unajengwa terminal III, lakini taarifa ambazo ninazo phase one walikuwa na mkataba, phase two wanaendelea hawana mkataba eneo lile, lakini unazungumza kutengeneza miundombinu, tuimarishe uwanja wa ndege, lakini wako wananchi pale Kipawa walihamishwa kutoka pale wakapelekwa Kata ya Buyuni na Chanika, kuna ugomvi mkubwa wananchi wale hawajawahi kulipwa mpaka leo. Serikali imechukua watu imewahamisha kutoka eneo la Kipawa ikawapeleka Buyuni wakaenda kuwakabidhi maeneo ya watu, hakuna fidia. Kwa hiyo, aliyekabidhiwa eneo hawezi kujenga kwa sababu mwenye eneo hajalipwa, hivyo kuna mgogoro mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tunapoandaa mipango hii tusitengeneze matatizo kwa wananchi. Unawekeza eneo, unaweka watu pale wanafanya biashara zao lakini wananchi wako wanaishia kulia na kulalamika watu wana makabrasha mezani yamejaa, kesi nyingi na hawajui wazipeleke sehemu gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyekiti Lukuvi amelipokea hili, nadhani na yeye kama ataendelea hivi atakuwa mzuri, angalau amesikiliza, ametoa taarifa ameleta ramani ya maeneo yale angalau uweze kuonesha maeneo ya wazi na maendeleo yaweze kwenda vizuri. Sasa hilo ni kwenye uwanja wa ndege, lakini kuna Mheshimiwa mmoja hapa amezungumza habari ya Dar es Salaam kwamba hakuna wakulima, siyo kweli! Zile hela zije.
Mimi ni Mbunge wa Jimbo la Ukonga nawakilisha Kata ya Kivule, Kata ya Kitunda, kata ya Mzinga, Msongola, Uwanja wa Nyani, Ukwende, Zingiziwa kuna maeneo watu wana mashamba makubwa wanalima mihogo na hata Wabunge wote mnaokaa Dar es Salaam mboga nyingi zinatoka Jimbo la Ukonga ziko safi kabisa. Kwa hiyo kuboresha huduma hii siyo dhambi watu wasibeze hapa, kama mtu anaomba huduma kwenye Jimbo lake asibeze Majimbo ya watu wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la umeme. Ni kweli kwamba tunahitaji viwanda lakini Dar es Salaam pale maeneo mengi ni giza. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana anachukua hatua lakini kama hata Dar es Salalam ambako hawa Wawekezaji wanapita watu wetu ni giza, umeme ni wa kusuasua mpaka leo tunapozungumza, yaani kuna watu wanakaa pale kama wanakaa kijijini halafu unazungumza habari ya viwanda, umeme wa kawaida wa majumbani hautoshelezi, viwanda itakuwaje? Yaani umeme wa kawaida tu haujitoshelezi viwanda inakuwaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini huwezi kuwa na viwanda, huna umeme, mazao ya kilimo na mifugo. Kuna watu wamekataa tamaa, wamezungumza wenzangu wa Mtwara, hata kule Tarime ukienda watu wa kahawa, wananchi wamefyeka mashamba, wengine wanaenda kulima zile bangi ambazo mmesikia watu wamesema na mirungi, wameweka tumbaku haina kiwanda, hamna usaidizi sasa lazima mje na mbinu Mheshimiwa Waziri ya kuonesha watu waliokata tamaa kulima mazao ya biashara kwamba soko lipo na bei itakuwa ni nzuri na makato na manyanyaso mengi ambayo yapo yataondolewa, maeneo yale hata ile kahawa na mahindi, wapo watu ma-settler wachache ambao ndiyo wanamiliki soko pale. Wanapanga bei, pembejeo zile zikienda kwenye Halmashauri wanagawana, kwa hiyo, kuna ulanguzi wa hali ya juu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makandokando haya yangeweza kurekebishwa, angalau Watanzania mnapozungumza habari ya viwanda, watu wanakwenda njia imenyooka, vizingiti vimeondoka, ubaguzi pale hakuna, mambo ya namna hiyo yangetakiwa yafanyike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mbunge wa Ukonga, Ukonga kuna viwanda vya chakula cha kuku, lakini mayai yanapatikana na kuku wa nyama wa kisasa, lakini kule hakuna kiwanda cha kutotoa vifaranga rasmi. Vifaranga vingi vinatoka nje ya nchi na baadhi ya material inatoka nje ya nchi. Sasa wananchi wale wanachukua vifaranga wanawekeza, mtu amedunduliza, mama lishe, kijana wa boda boda pamoja na kupata shida mjini hapa, kukamatwa kamatwa sana, lakini akipata kidogo anawekeza kuku wake 200, 500, wakikua baada ya miezi miwili, mitatu, minne kuku wote wanakufa, ukienda kuulizia unaambiwa kwamba shida ilikuwa ni kiwandani vifaranga vilikuwa na shida ambavyo hatuna viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani mambo kama haya pamoja na kwamba tunawekeza tuone ubora wa mali ambayo inaletwa ili watu wetu wasiingizwe kwenye umaskini ambao kwa kweli tunajitengenezea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Dar es Salaam kwenye biashara kuna habari inaitwa DECI na Malingumu, kwamba watu walikuwa wanapanda pesa. Nimesikia Watanzania wote hapa na Wabunge mnafahamu, yaani pesa ikawa miujiza ya Mungu kwamba pesa unaweza ukapanda ikaota kama uyoga, ikazaa mara mbili, tatu na watu wakavuna na Mawaziri wa Serikali hii ya CCM walishiriki zoezi hili na wakataja maeneo kesi ikaenda Mahakamani. Mpaka leo wananchi wale wanasubiri malipo wamekuwa maskini, wameuziwa nyumba zao. Kwa kweli mnapozungumzia Mpango Mheshimiwa Waziri ungejua hali iliyoko hiyo ungeenda sijui kujifungia wapi kama ni Mungu akutembelee upate miujiza uje na mipango ambayo inatekelezeka. Hizi ni kero ambazo zinaumiza wananchi wale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Afya; sasa mmetangaza kwamba kuna, kwa mfano, mimi kule Ukonga, jana nimejibiwa swali langu na Mheshimiwa nimesikitika majibu, Jimbo la Ukonga na Segerea tunategemea hospitali ya Amana. Tumesema tujenge pale hospitali, Halmashauri imetenga kwa mwaka bilioni moja au milioni 900, hiyo hospitali itagharimu zaidi ya bilioni 600 kwa mpango uliopo, maana Waziri alisoma alichofanya hapa na ndicho mmefanya kuzuia TBC isioneshe na TV zingine watu wasione, watu wa Ukonga walikuwa wanalia. Waziri ametuma mtu hapa ameenda akachukua ame-copy na ku-paste ambacho tulipitisha Manispaa ya Ilala hakuongeza kutoka Serikali Kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ina maana kwa mpango ule ile hospitali itajengwa kwa miaka 26, nimewaambia ile Wilaya kama mpango wenyewe ni ule, ile fedha tuifanyie reallocation, utajenga magofu fedha itapotea haiwezi kusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unakuwa na viwanda, watumishi wetu hawa ni maskini hawana afya, unafanyaje? Mkienda kwenye viwanda vyenyewe, malipo pale pale Gongo la Mboto kuna Kiwanda cha Namela, mwenye kiwanda anawalipa watu wale sh. 4,000/= ambayo imetajwa hapa ndiyo posho ya kufanya kazi. Katika hali ya kawaida Mheshimiwa Waziri, wewe ni mtaalam wa mambo ya finance, hivi sh. 4,000/= Dar es Salaam utaishi kweli? Ndiyo mpango uliopo na Sheria imesema l50,000/= kwenye viwanda. Kwa hiyo, kuna mianya mnatoa wale wawekezaji wakija kwa nia njema tunawapa support, wamechukua ardhi yetu, nguvu kazi ya kwetu, tuna wataalam wanalipwa kidogo sana, lakini mwisho wa siku watatunyonya kweli kweli, sasa mikakati kama hii na mambo haya yangetakiwa yapangiliwe vizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, reli litakuwa jambo langu la mwisho. Reli inayozungumzwa hapa tunahitaji pale Ukonga, huduma ya TAZARA na reli ya Kati kwa maana ya kusafirisha kupunguza misongamano, sasa hili jambo likifanyika itatusaidia.
Nimeona kwenye Mpango imeonekana, sasa shida ni kwamba na kwa ujumla haya makaratasi ukisoma uko chumbani unafurahi kweli kweli, nendeni mahali sasa myaondoe yaende kwenye vitendo ndiyo mahitaji! Shida ya nchi hii siyo mipango, shida ni kwamba mlichokiandika kiwe transformed kwenye actions, watu waone actions zote zimefanyika, barabara za lami zimetajwa, Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Rais ametaja barabara ya Kitunda – Kivule - Msongola mara nne zote akiwa Bungeni hapa sasa imetajwa tena akiwa Rais nataka nishuhudie kama Rais atakuwa mwongo tena, maana yake kama alikuwa ananyimwa hela kugawiwa sasa hivi anagawa mwenyewe, anatumbua majipu na anafanya reallocation nataka tushuhudie mambo haya, ni matarajio ya Wabunge wengi kwamba mipango mliyoileta hapa inatekelezeka.
Halafu Wabunge wa CCM muache kupiga makofi sana huku, mnaunga mkono mwanzo halafu mnalalamika mwanzo mwisho hivi utawala bora unakujaje? Hivi ninyi Viongozi, Mheshimiwa Waziri, Waheshimiwa mnazima TV, mpango mzuri, maneno mengi na majibu mazuri ya Upinzani ya Mheshimwa Silinde hayajaonwa na Watanzania, hoja zetu hazisikilizwi, tuko hapa gizani kama wachawi humu ndani. Watu wamenywea humu ndani, humu ndani hamtaki watu waone kwa nini? Hivi ninyi nani amewaroga! Nani amewaroga? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, dunia hii ya sasa hivi Serikali inakaa kabisa inafunga Vyombo vya Habari, mlisema TV yenu ni gharama siyo? Hizi za watu binafsi zinawahusu nini? Mmeombwa hela? Haki ya Mungu nimesikitika sana, yaani watu wazima, Mawaziri kabisa mnakubali kwenda kuwazuia Watanzania, Ibara ya ndani ya Katiba ya nchi mnaivunja hivi ya haki ya kupata taarifa. Gharama mmesema ni bilioni…! hiyo TBC fungeni ni chombo chenu cha uenezi, endeleeni na mambo yenu, watu binafsi waruhusiwe humu ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nchi imekuwa giza tunaongea hapa yaani mwende mchuje, mrekodi muweke mnayotaka ninyi halafu mtuletee tufurahie, halafu mnatuambia habari ya elimu hapa, mnatuambia mambo ya TEHAMA, humu mmeweka mambo ya TEHAMA, sasa TEHAMA maana yake nini? TEHAMA maana yake ni eti watu wafanye kazi, yaani mchukue viboko muwapige watu ambao hawaendi shamba sasa, kawatandike watu ambao hawaendi shambani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna mtu amemwajiri mtu mzembe anaangalia TV ofisini kwake amfukuze kazi.
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. MWITA M. WAITARA: Nataka nipate majibu.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
eze hotuba nzuri ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwenye idara hii ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru kwa kupata nafasi hii nichangie. Nikupongeze sana wewe binafsi, kulikuwa na maneno sana, sasa najaribu kulinganisha maneno yale juu yako na uongozi wako, wewe ni Mwenyekiti smart kweli kweli, hongera sana Mheshimiwa. Nitakuomba kwa umri wako na uzoefu umsaidia Naibu Spika asiharibu hili Bunge, kwa kweli nasema haya ni muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana Mheshimiwa maana msema ukweli ni mpenzi wa Mungu kama unafanya vizuri tukupongeze, ukifanya vibaya tunakusema lakini sitarajii kwamba wewe utafanya vibaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni Wizara ya Viwanda na Biashara na nina hoja hapa ambazo ningeomba Mheshimiwa Waziri mhusika asikilize. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Waziri kwamba hoja za msingi sehemu kubwa ya hoja hizo zinatoka Upinzani naomba utusikilize vizuri, yale mambo mengine wayapuuze. Kwa sababu kwa mfano mtu akikusikiliza vizuri Mheshimiwa Waziri na akatafakari na mimi nimekusikiliza hapa mara kadhaa nikaenda nikakaa, nikarudi hapa nikaona maneno yako yale kama utaweza kuyatekeleza utakuwa ni Waziri wa kwanza ndani ya CCM kufanya kazi kubwa sana na mimi nakutakia kila la kheri. Siyo kwa sababu ni mtani wangu umekula senene hapana, lakini unavyozungumza nitaomba hayo mazungumzo ya-reflect actions pamoja kwamba kuna kazi kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atusaidie, CBE ipo chini ya Wizara yake na Mheshimiwa Waziri wa Elimu asikilize hapa. Nimepata taarifa kwamba CBE pale kuna majipu, ninazo document hapa ambazo Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana anazo, Mheshimiwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anazo tena ni Profesa, Mheshimiwa Mwenyekiti wa Bodi ambaye ni Profesa wangu wakati nikiwa Chuo Kikuu Dar es Salaam nikiwa Rais wa Chuo kile alikuwa anaendesha Baraza la Chuo nikiwepo, Mheshimiwa Profesa Luhanga na wadau wengine. Wameleta malalamiko wanadai kwamba katika kile chuo, Mkuu wa Chuo pamoja na Mkurugenzi wa Fedha, chini ya Idara yako na hii sasa inaweza ikapunguza maneno yako haya nikatafsiri tofauti, kwamba kuna Mkurugenzi wa Fedha amekusanya zaidi ya shilingi milioni 400 bila kutoa stakabadhi anatoa risiti za karatasi zile baadaye hazionekani, vielelezo hivi hapa vipo, hii ni Idara yako na ulipopata taarifa hapa, wale watu ambao wameleta document hapa wakapigiwa simu wanatishiwa kwa nini wameleta taarifa kwako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hizi tuhuma Katibu Mkuu alipoandikiwa, yaani shilingi milioni 400 zimekusanywa, CBE pale kuna campus nne, nazungumzia Dar es Salaam wamekusanya fedha zaidi shilingi milioni 400 kwa utaratibu ambao kimsingi ni kinyume na utaratibu. Wanasema kuna wanafunzi ambao hawalipi ada wakiongea na Mkurugenzi wa Fedha wanamkatia kidogo anaenda anafuta zile kumbukumbu, wale wataalam wa fedha wanasema bad debtors kwa maana ya kupoteza ushahidi, pia haya ni malalamiko ambayo yapo kule. Kwa maelezo yao inaonesha kwamba Mkuu wa Chuo anaelekeza alama 50 ziongezwe kwa wanafunzi ambao wamefeli ambao yeye ana maslahi nao. Hii inaingia kwenye standard ya elimu na hivi vyuo vimekuwa na malalamiko muda mrefu kwamba wanafanya kazi pale kuonesha urembo CBE almost zote wanashiriki sana haya mambo yako.
Kwa hiyo, ina maana hapa inahusu vilevile na Waziri wa Elimu atambue kwamba ni suala la Wizara ya Biashara lakini pia kuna jambo hilo linazungumzwa. Kuna Mkaguzi wa Nje alipelekwa pale alikuwa hired na chuo, akaahidiwa kupewa shilingi milioni 13 akakubali kufanya forgery kwenye ukaguzi wake, aka-abuse profession lakini badaye akapewa shilingi milioni 3.5 sasa hivi analalamika mtaani kwamba amedhulumiwa, huyu naye ni jipu. Nilipoleta malalamiko kwamba kile chuo kichunguzwe, Mkuu wa Chuo kwa kuzungumza na Mkurugenzi wake wakazunguka hilo zoezi halijafanyika kufanya ukaguzi wa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, CBE ya Mwanza na yenyewe ina malalamiko, kuna mtu pale anaitwa Rose yupo Gerezani Segerea tangu mwaka 2011 lakini kapandishwa mshahara analipwa mshahara. Sasa unatafuta wafanyakazi hewa kumbe wapo, document hizi zipo, Waziri anazo, Katibu Mkuu anayo, Bodi inajua na Mkuu wa Chuo anafahamu. Sasa haya mambo Mheshimiwa Mwijage yatapunguza kasi na maneno yako yanaweza yakatia wasiwasi katika mazungumzo. Vielelezo hapa vipo mpaka risiti, mpaka bank statement hizi hapa zimetolewa. Kwa hiyo, ni muhimu sana haya mambo unapopanga uyaangalie, haya makandokando tunaposema wala siyo kuzomea huu ni ukweli mambo yapo, yafanyieni kazi haya, nendeni mkapeleke special audit, CAG akague hivi vyuo alete taarifa, hilo ni la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, mimi ni Mbunge wa Jimbo la Ukonga. Kule Ukonga tunayo shida ya sehemu ya kupata vifaranga, vingi vinatoka nje ya Jimbo na vingine hata nje ya nchi. Wananchi wengi wanafuga kuku, akina mama, vijana wa bodaboda, wauza maandazi wamekopa VICOBA wanafanya biashara ile kwa maana ya kujikimu. Mtu analisha almost miezi miwili, mitatu kwa gharama kubwa vinakufa vyote na hakuna fidia. Unakuja kutafuta unaambiwa eti havikuchanjwa, nani alipaswa kuchanja, nani ana-control standard, bidhaa inatoka wapi, kiwanda kinalipaje, hayo mambo yote wananchi wangu wanapata shida sana. Kwa hiyo, nitaomba unapokuja hapa pia ni muhimu tukapata majibu hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunajua kwamba kulikuwa na mpango hapa unazungumzia habari ya biashara lakini Serikali hii ya chama changu cha zamani na mimi huwa nazungumza nawashangaa ambao wanapiga humu. Mimi nilikuwa kada wa hicho chama yalinishinda nikabwaga manyanga, lakini niko vizuri kweli kweli. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa namwambia Mheshimiwa Nape kama wakiruhusu kuongea pumba sisi tunaweza kutengeneza pumba tukaitumia vizuri kuliko mtu anayeokota pumba. Kwa hiyo, ni muhimu sana tukazungumza mambo serious. Kule kuna kitu kinaitwa DECI na MALINGUMU, fedha zinapandwa, Serikali ilisajili watu wakawa wanalipa kodi, wakafungua na ofisi, hili jambo na lenyewe mpaka leo wananchi wangu wamepata shida. Watu wa Dar es Salaam wamedhulumiwa fedha kesi imeenda Mahakamani inaendelea au haiendelei haijulikani. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ulivyozungumzia wafanyabiashara wadogo wasaidie hawa watu, hii DECI na MALINGUMU uje na majibu nani alisajili na Mawaziri wastaafu walihusika na fedha zilikusanywa zikaenda Hazina mpaka leo hawajarudishiwa mitaji yao, hawajalipwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo ndiyo maana tukasema viwanda vilikufa watu wakauziana, leo mnakiri wenyewe na mnajua kwamba viwanda vingi vimekuwa scraper. Sasa watu hawa watengenezee matumaini waone hali sasa ni nzuri, makandokando yameondoka, viwanda vikianzishwa vitaendelea kudumu, vitazalisha, watapata ajira, ni muhimu sana kujua hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimeenda kwenye kiwanda cha Mbagala kule, kuna kiwanda pale Ukonga cha Nguo kinaitwa Namel, hivi viwanda mmepitisha mshahara wa wafanyakazi maskini wetu wale wanalipwa shilingi laki moja kwa mwezi, nataka utuambie hivi unavyoanzisha sasa na vyenyewe mshahara shilingi laki moja inasaidia kitu gani. Wanafanya overtime wanalipwa shilingi elfu mbili, hawana gumboot, hakuna usalama mle ndani, wanafanya kazi zaidi ya masaa ya kazi, mikataba hawapewi, kwa hiyo ina maana watu wanaonewa. Kwa hiyo, viwanda vinaweza vikaja mkafurahi kupata kodi, hii milolongo ambayo hamjarekibisha wananchi wakaendelea kuumia na hiyo ni shida tutaomba pia uoneshe kama kuna mazingira rafiki ambayo yametengenezwa ili watu wetu waweze kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, chakula cha kuku Dar es Salaam ni shida sana, bei ni kubwa, kilikuwa kinauzwa shilingi 36,000 kimepanda mpaka shilingi 60,000. Nimejaribu kuuliza wananiambia mahindi, pamba na alizeti zinapelekwa nje bila kuwa processed na wafanyabiashara wakubwa wanaificha kwa hiyo inavyorudi bei inakuwa ni kubwa sana, hatuwezi ku-control.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeuliza kwa mfano dawa zikoje, zile dawa za chanjo za kuku hata ng‟ombe nyingi hazina TBS, nendeni pale Ukonga mkague maduka yale hakuna TBS, hawalipii, kwa hiyo bei wanajipangia wenyewe. Kuna biashara holela na hili linaweza kuhatarisha maisha yetu kwa sababu tunakula mayai ya kuku hawa kumbe yako below standard tunapata magonjwa mengine ya kutisha. Kwa hiyo, Mheshimiwa naomba utusaidie pia katika hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nataka unisaidie ni kuhusu mifuko ile ya kijamii. Kumekuwa na malalamiko hapa kwamba wafanyakazi wale michango yao haipelekwi kwenye mifuko hii ya jamii. Sasa lazima uweke mazingira rafiki kwamba hili nalo ikitokea unafanyaje…
MHE. MWITA M. WAITARA: Dah, ahsante sana, siungi mkono hoja, ila nawasilisha.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kupata fursa hii ili niweze kutoa maoni yangu. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Joseph Mbilinyi Msemaji wa Kambi ya Upinzani, juu ya habari lakini niwapongeze sana pia wale ambao walishirikiana nao kuandaa mambo mazito namna hiyo, nafikiri Mheshimiwa Nape atakuwa amesikiliza hiyo misumari na ataifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nachangia kwenye Wizara ya mtu ambaye ninamfahamu vizuri na imetangazwa hapa kwamba ni shemeji yangu kwa sababu mke wake anatwa Rhobi na Mheshimiwa Nape hatukukutana barabarani, ni kweli kwamba ni shemeji yangu sasa nitaomba Dada yangu Rhobi ninapochangia kwenye hotuba ya mume wake Mheshimiwa Waziri kwa sababu tupo kazini na tumeshachukua mahari, biashara ya ushemeji itakaa pembeni kidogo, hapa kazi tu, kwa hiyo tunaenda na kauli mbiu ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilisema nitakuwa mkweli sana, nimejaribu kutafakari kitu gani nichangie kwenye hotuba hii nikapanga haya yafuatayo niyaseme.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza Mheshimiwa Nape akiwa Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi aliwaita wenzake ni mizigo akiwepo Mheshimiwa Profesa Maghembe, Mawaziri wenzake wale aliowaita, kwa hiyo nilipoona amepewa Wizara ya Habari nikatarajia kwamba ataruhusu mijadala ya wazi ili tumuone kwamba yeye hatakuwa mzigo lakini anaweza kwa lumbesa ili tumjadili na wananchi wamuone. (Makofi)
Sasa hilo amelizuia kwa hiyo tunashindwa kumpima yeye na wenzake nani mzigo zaidi, nani lumbesa hilo na lenyewe kidogo linaleta shida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili Mheshimiwa Nape atakumbuka kwamba wakati nilipokuwa nimeminywa sana kutoa maoni yangu kama kijana msomi kutoka Chuo cha Dar es Salaam, nikapingana na viongozi wa CCM nilipofikiria kuhama CCM Mheshimiwa Nape nilimshirikisha akiwa na Mheshimiwa Kubenea, tulienda kule Kitunda nikamwambia hawa watu ndugu zako, hawa viongozi wa CCM hawa wamenikwaza kwa sababu wamezuia uhuru wa kuzungumza, kutumia akili zangu kitaaluma kama mwalimu tena mwalimu wa Hesabu na Kemia. Kwa hiyo nikamwambia mimi nahama akaniambia safari njema.
Kwa hiyo, anajua wakati nahama Mheshimiwa Nape alikuwa anafahamu. Kwa sababu msimamo ule ule ambao tulitofautiana kule na wenzake yeye ameurejea tena, kwamba hatuwezi kuwa na uhuru wa kutoa maoni hapa na yeye ndiyo msemaji. Nimepitia taarifa yake hapa ameeleza vizuri kwamba yeye ndiyo anasimamia vizuri Wizara hii na kusema akifanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi mojawapo ambayo Mheshimiwa Waziri anasimamia moja, alikiri hapa kwamba hiki kinachoendelea hapa Bungeni cha waandishi wa habari wa TBC kufanya kazi hapa Bungeni alikiri kwamba ni kweli wametoka TBC maana yake kwenye Bunge hili hao wanaozuia taarifa na ku-censor tunachozungumza Mheshimiwa Nape ana mkono wake, kwa hiyo hawezi kukataa na alikiri kwamba hawa watu wapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimefuatilia mara tatu usiku, mara ya kwanza niliamka saa 7.42 usiku na juzi ile nikakuta ndiyo TBC inaonyesha taarifa ambayo imerekodiwa. Siku iliyofuata niliamka saa 8.15 usiku nikakuta tena wanaonesha, juzi nimeamka saa 9.40 usiku maana yake saa kumi kasoro dakika ishirini nikakuta ndiyo wanaonesha taarifa, nikaenda mpaka saa kumi ilikuwa inaendelea. Usiku wa kuamkia leo niliamka saa 7. 17 usiku nikakuta wanaonesha ile taarifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni nini! Mheshimiwa Nape ni muongo na huenda naye vilevile ni jipu humu ndani, anapaswa kutumbuliwa, kwa sababu Mheshimiwa Nape amedanganya hili Bunge. Alipokuja kutoa tamko la Serikali alisema kwamba hoja mojawapo muhimu ni kwa nini taarifa isirushwe na TBC ni gharama. Akaeleza wametafuta muda mzuri wa kuonesha ufanisi wa watu waangalie taarifa ya habari lakini waende kazini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama mwalimu, kama mtu mzima, kama mzalendo nikajaribu kufanya assessment ya kawaida kwamba kama unaonyesha kipindi cha Bunge saa kumi kasoro dakika ishirini na unataka kwa watu wa Dar es Salaam kwa mfano kule Ukonga, Msongola, Mbondole, Kibanda cha Maiti kule au Uwanja wa Nyani atoke ili awahi mjini kati ni lazima aamke saa kumi na moja, maana yake baada ya kumaliza kuangalia taarifa ya habari ambayo imeanza saa tano au saa nne ataoga saa kumi na moja anaanza safari huyu mtu lazima asinzie. Nikajiuliza hapa kuna kuna ufanisi! Hapa kuna ufanisi wa kazi? Nikalijua jibu hapana siyo kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ninyi viongozi wa Bunge hili mmebariki hicho kitu kifanyike, ninyi mnakubali tuzunfumze hapa, mtu akiongea hapa leo, kuna miongozo imetolewa watu wathibitishe tunataka uongo wa Mheshimiwa Nape athibitishe kabla ya kuhitimisha hoja yake hapa, kwa nini amedanganya Bunge, kwa nini amedanganya Watanzania! Hoja ambazo wametoa siyo za kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mmemwambia Mheshimiwa Kubenea athibitishe mambo aliyozungumza, sasa ufanisi wa kazi unaoonekana hapa ni nini! Haya mambo lazima tuyajadili. Mimi ningekuwa na uwezo hii hotuba isingejadiliwa kwa sababu hili jambo tungekuwa na watu ambao hili Bunge siyo CCM wengi, hii Serikali tungeiangusha leo, tungepiga vote of no confidence. Kwa sababu jambo hili siyo jambo la Waitara, siyo jambo la UKAWA, siyo jambo la CHADEMA au la CCM ni jambo la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yupo Mwanasheria hapa na wapo wataalam mbalimbali wamebobea. Ukisoma Ibara ya 18 ni haki ya Watanzania, tukisema mmevunja Katiba mnakataa kwa nini? Mnataka tusemeje sasa? Kama kweli mna nia njema ya kufanya kazi Serikali hii hapa kazi tu tena kwa mara ya kwanza tumepata Rais ambaye ni mwanasayansi, mwalimu, mtaalam maana yake masomo yangu na Magufuli sawa sawa, kwa sababau yeye ameongezeka cheo amekuwa Rais, mimi Mbunge! (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunafanana. Ameongeza degree ya pili ni mwalimu wa Hesabu na Kemia, ndiyo Rais wa kwanza wa Tanzania msomi, mwanasayansi, mwalimu. Walimu hatuongopi challenges, tutasema chochote ili mradi kuna fact. Kama kuna kazi inafanyika kwa nini mnaficha, kwa hiyo hilo jambo kwa kweli nimeumia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine kitendo cha Mheshimiwa Nape kuja hapa jana wametangaza anasema kuna Diamond ataburudisha sijui wapi, kutakuwa na mwanamuziki King Kiki jioni ya leo maana yake ni rushwa, hiyo ni rushwa! (Makofi)
Kwanza mnaposema mnabana matumizi mnaondoa starehe. Huyu King Kiki na wenzake gharama za nani zimemleta hapa, anapiga pale nani analipia hizo gharama? Wabunge wote ambao wataenda kwenye hiyo miziki ili kuunga mkono habari ya Mheshimiwa Nape maana yake mtakuwa mmekula rushwa na wote mlaaniwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ninataka mnisaidie, Mheshimiwa Nape amezungumza, mimi nimesikia story, amezungumza habari ya ngoma na nini, nimeangalia kwenye matumizi. Tulimuita Mheshimiwa Naibu Waziri Mheshimiwa Anastazia Wambura, alikuja Dada yangu kwenye Kamati ya UKIMWI na masuala ya dawa ya kulevya. Ikaonyesha kwamba hawakutenga fedha kwa ajili ya michezo kwa maana ile UMISHUMTA, UMISETA hawakutenga fedha na wanasema hawana mpango huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia hapa wanapozungumza, wamezungumza habari ya Samatta, hawa ni watu ambao wamejikuza wenyewe kama kuku wa kienyeji, mkakuta wamefanikiwa mnawapongeza sana, mnawapa sifa kubwa. Wapi mpango wa Serikali ya kuendeleza vijana, wapi mpango wa kuendeleza michezo shuleni? Kuna vipaji vinakufa pale! Hapa nimeona kwenye vote 6002 Youth Development Program ni zero zero tu! Nimeona kwenye vote 6004 kwenye Sports Youth Development, hakuna fedha ambayo imetengwa pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, wenyewe wanasema fedha ambazo zinatengwa na Kamati imezungumza ukweli hakuna kilichopelekwa sasa unazungumza habari gani hapa? Kwa hiyo sisi tukae hapa Bunge kila mwaka bajeti ikija, King Kiki, Diamond biashara inaisha si ndiyo? Hiyo biashara mtafanya wenyewe watu wa CCM sisi hatufanyi biashara hiyo bwana.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nataka mnisaidie hapa iwe very clear. Wako Wabunge wa CCM humu ambao wanapiga makofi sana, wanafikiri hii hoja ya habari ni ya kwetu. Mimi nitaomba leo Watanzania wajue wale ambao wanapiga makofi kwamba tv isioneshwe waonekane halafu muwe tayari twende kwenye Majimbo tukawaambie kwamba hiyo ndiyo biashara mnayoifanya humu ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunawaambia Rais amehasisha vizuri anawaambia Watanzania kila ukinunua kitu ulipe kodi, kama umelipa kodi upewe risiti, kama hujapewa udai. Hizo fedha zilizokusanywa hapa ndipo mahala pake kwa kuzipanga matumizi yake, hamtaki waone! Wananchi walipwe kodi, lakini mipango wasione! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa mmepunguza bajeti, leo tumejadili hapa bajeti ya Afya imepunguzwa kwa shilingi bilioni 18. Mimi naomba wako wataalam pale, yupo ndugu yangu Ayoub Ryoba amepewa TBC, hii TBC ambayo Mheshimiwa Nape amezungumza alifanya kazi nzuri amesema sehemu kubwa ilikuwa inaisemea Serikali, lakini taarifa rasmi ni kwamba TBC ilifanya kazi ya CCM katika Uchaguzi Mkuu uliopita hiyo ndiyo bottom line.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mimi siungi mkono.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwapongeza viongozi wote wa Wizara ya Nishati na Madini kwa:-
(i) Kupunguza urasimu wa wateja na kutembelea wahitaji wa umeme;
(ii) Kusambaza nguzo kwa sehemu kubwa; na
(iii) Kutenga 94% bajeti ya maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja juu ya mradi wa Kinyerezi II. Mradi huu unagusa mitaa 40 lakini hadi sasa ni mitaa nane tu imefanyiwa tathmini na mitatu tu ndiyo wamepewa cheque ambazo hadi sasa hakuna pesa kwa wananchi. Fidia kwa wananchi hawa imechukua zaidi ya miaka mitano (5) sasa na hivyo hata malipo yake hayatakuwa halisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mitaa inapewa pesa za kulinda mabomba ya gesi. Naomba pesa za ulinzi ziangaliwe upya ili kuboresha malipo haya kwa mazingira ya sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, umeme wa Kinyerezi II unapitia Kata za Kivule, Kipunguni, Gongo la Mboto, Majohe na Kinyerezi. Hata hivyo, Jimbo la Ukonga lina ukosefu wa umeme katika Kata za Pugu, Buyuni, Chanika, Msongola na Zingiziwa. Naomba Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini pamoja na kupeleka umeme mijini na vijijini, ni muhimu kipaumbele kiwe kwenye maeneo ya shule, vituo vya polisi, zahanati na visima vya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Ukonga lina changamoto ya kuhudumiwa na sehemu mbili yaani Kituo cha Gongo la Mboto na Kisarawe. Suala hili linasumbua wananchi, naomba uwekwe utaratibu wa kupunguza hiyo kero.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana aangalie kwenye migodi hasa huduma za jamii kwa wanaozunguka mgodi na mrahaba wa 0.3% namna unavyokokotolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwapongeza Wizara ya Ardhi ikiongozwa na Waziri Mheshimiwa William Lukuvi kwa kuonyesha nia ya kutatua migogoro ya ardhi kwa kushirikisha wadau wa ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumshukuru Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri wa Ardhi na Waziri wa Maliasili kwa kuonyesha uongozi na nia ya kumaliza mgogoro wa ardhi katika msitu wa Kazimzumbwi uliopo katika Kata za Chanika, Zingizwa, Buyuni na sehemu ya Pugu ambao umedumu tangu mwaka 1994 kutokana na kupunguza mipaka mwaka 1954.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu kumaliza mgogoro wa Bonde Msimbazi hasa maeneo ya Kinondoni, Segerea na Ukonga ambapo nyumba za wananchi zimewekwa alama ya “X” na zingine kubomolewa, huko ni kuwarudisha nyuma wananchi wa nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu Mheshimiwa Waziri kumaliza mgogoro wa Kipawa Kipunguni, eneo la Uwanja wa Ndege. Pia mgogoro wa ardhi kati ya watu wa kutoka Kipawa na Kipunguni waliopelekwa Kinyerezi Pugu na Buyuni katika Jimbo la Ukonga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kulinda maeneo ya umma kama vile shule, zahanati, masoko na polisi; ni muhimu upimaji na kulinda maeneo ya huduma za jamii liwe shirikishi kwa viongozi wa mtaa, kata, Wabunge na wananchi ili kuondoa mianya ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama za upimaji ni kubwa sana kiasi kwamba wananchi wengi wanashindwa hivyo kuishi bila kupima maeneo yao. Ni vema Wizara ikaangalia namna ya kupunguza kero hizo ili wananchi walio wengi au wote wapime ardhi yao ili kujipatia manufaa ikiwemo uwezekano wa kukopesheka katika vyombo vya fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ya Ardhi iongeze kasi ya kuondoa migogoro ya ardhi na hasa maeneo ya maliasili ili watu wetu waishi kwa amani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwapongeza Wizara ya Ardhi walau kwa kuweka mipango shirikishi na kuanza kumaliza baadhi ya migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nianze kwenye kitabu hiki cha Mpango, ukurasa wa saba ambapo anasema, mwenendo wa uchumi unaashiria kuendelea kuimarika kwa uchumi na utoaji wa huduma za jamii unaboreka. Ndiyo maana kukawa na hoja kwamba ingelazimika tukapata tathmini ya kipindi kilichopita kwa muda huu tulionao ili tuweze kujua mwelekeo. Hii kauli inachanganya sana wananchi wa kawaida na hata mimi mwenyewe. Ukiangalia hali halisi ya kiuchumi ilivyo, ukitembelea maduka mitaani, wafanyabiashara mbalimbali wanalalamika na hata sisi wenyewe Wabunge tunalalamika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana imeelezwa kwamba imefikia hatua hata kwenye Kamati za Bunge unapewa maji moja ndogo kuanzia asubuhi mpaka jioni. Pia ukipewa chakula kimepangwa unasimamiwa usije ukazidisha vipande vitatu ni viwili tu, maana yake inawezekana ukizidisha utashikwa mkono. Hiyo maana yake inaashiria hali ya kiuchumi ni ngumu lakini kwenye vitabu wataalam wetu Mheshimiwa Dkt. Mpango na wenzake wanasema hali inaimarika na huduma za kijamii zinaboreshwa. Kwa hiyo, naomba hata atakapokuja kuhitimisha hoja ambayo mimi siungi mkono, basi atueleze angalau kinaga ubaga na kwa lugha ambayo tutaweza kuelewa anamaanisha kitu gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niunge mkono hotuba nzuri sana ambayo imetolewa na Kambi ya Upinzani Bungeni. Niseme Waziri yeyote makini tukitoa hotuba hapa ni muhimu akapitia kile tunachokisema kwa sababu takwimu ambazo zinatolewa na sisi upande wa Upinzani hatuzipiki sisi bali zinatoka kwenye nyaraka mbalimbali Serikalini humohumo. Kwa hiyo, tunapotoa hotuba hapa siyo kuibeza na mimi ningekuwa ninyi ningekuwa mjanja sana kwa sababu mngekuwa mkisema naenda kuyafanyia kazi ili next time mkose hoja. Badala yake mnaweza kukaa hapa miaka mitano mnaambiwa mambo yaleyale ukirudi unatoa siasa, unapiga story, unapiga porojo, miaka inaenda na huboreshi. Kwa hiyo, kimsingi unakuwa hufanyi lolote lile. Hoja ikitolewa iangalie na kama ina ukweli ifanyie kazi na kwa kufanya hivyo utakuwa unalisaidia Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kupitia hiki kitabu, mimi nitajikita kwenye kitabu hiki kilichoandikwa, ukurasa wa 66 – 67, Waziri mwenye dhamana amezungumzia utawala bora na utawala wa sheria, lakini nilipoangalia utawala bora alioandika hapa alikuwa anaandika kuboresha majengo na kuongeza polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyoelewa utawala bora angeeleza hapa kwamba mpango wa Serikali ni pia kuheshimiana katika maeneo yetu ya kazi. Kwa sababu kwa utawala huu ambao mnauita utawala wa Awamu ya Tano na mnakwepa kusema utawala wa Chama cha Mapinduzi mnataka watu waamini kwamba miaka inatofautisha matendo yenu, ndiyo maana mnahimiza sana utawala wa Awamu ya Tano, sema Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Watanzania wajue ni ileile hakuna jipya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika hali ya sasa ambayo unataka kuboresha elimu lakini Mwalimu huyu ambaye anadai na hapa katika kuboresha elimu sikuona unaboresha namna gani, wapo Walimu ambao wanadai madai yao tangu mwaka 2012 mpaka leo. Ili uboreshe elimu lazima Walimu walipwe madai yao, wapandishwe vyeo, walipwe likizo na malimbikizo yao ili migogoro iishe. Huwezi kuboresha elimu kwa maana ya majengo wakati Walimu wanadai na Walimu haohao Wakurugenzi ambao mnawateua makada wa CCM wanawaambia wapige deki mbele ya wanafunzi halafu unasema unataka kuboresha elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unazungumzia utawala bora mahali ambapo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu anaagiza eti kuanzia leo Walimu wote nimewashusha vyeo, huo ndiyo utawala bora kweli? Sasa hapa hamzungumzi, mnazungumza habari ya kujenga majengo, haya mambo lazima tuzungumze ukweli. Sasa mnapotuandikia, sisi siyo wajinga, tunaweza kusoma mnachoandika na kuchanganua, lazima mtueleze utawala bora maana yake ni nini? Sasa hivi hali iliyofikia watu hawaheshimiani yaani unakuta Rais ameagiza kwamba Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya watumie ile Sheria ya saa 48, kwa hiyo, Mbunge kwenye eneo lake, Diwani kwenye eneo lake, Mwenyekiti wa Halmashauri au Mstahiki Meya anaweza akaambiwa kamata weka ndani, unasema huu ndiyo utawala bora halafu unataka upewe ushirikiano katika eneo hilo. Kwa hiyo, nashauri wahusika wa haya mambo lazima waangalie vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile kuhusu utawala wa sheria, sasa hivi kinachotawala Tanzania wala siyo sheria ni amri mbalimbali, sheria wala haifuatwi. Bahati nzuri Waziri wa Utawala Bora ndiyo alikuwa mpiga kura kule Kinondoni kwenye uchaguzi wa Meya, walikuwepo hawa. Katika hali ya kawaida inawezekanaje unafanya uchaguzi ambapo unajua idadi ya UKAWA ni nyingi kuliko Chama cha Mapinduzi na Naibu Spika ambaye ni mwanasheria tena alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amehusika kuchakachua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria inasema wateule wa Rais hawatazidi watatu katika Halmashauri lakini mlichokifanya mlipeleka watu wanne pale Kinondoni. Sheria inasema ni lazima mahudhurio yaandikwe, akidi ni mbili ya tatu (2/3), haikutimia hakuna mahudhurio. Watu wa CCM mlikuwa 18, tena viongozi mmekaa pale mkapiga kura mkajiapisha halafu unaandika makaratasi hapa utawala bora wa kitu gani, unamdanganya nani hapa? Huu ndiyo utawala bora kweli, huu ndiyo utawala wa sheria? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi wasomi, Mawaziri, Maprofesa, Wanasheria, Naibu Spika na wenzenu, Mawaziri wazima hata aibu hawana, tena Waziri wa Elimu ambapo Waziri wa Elimu alikuja kupiga kura Ilala. Mimi ni Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Mheshimiwa Profesa Ndalichako mama yangu na mtani wangu ambaye namheshimu sana alikuwepo ameletwa kujiandikisha kupiga kura Ilala halafu tena akakubali kubebwa mzobemzobe anashinikizwa kuja kupiga tena kura Kinondoni, wewe unafanya kitu gani kweli? Hata aibu hamuoni?
Aibu sana kwa Chama cha Mapinduzi, chama kongwe, ndiyo maana mnaitwa chama kizee.
Hata busara na hekima inapotea. Sasa hapa utawala bora mnaozungumzia ni kitu gani? Tangu mmeanza kufanya uhuni katika nchi hii mimi kwa kweli nimekuwa confused.
Ndiyo maana mnachofanya hata hapa kwenye elimu ni maigizo, tumegundua mtaji wenu katika nchi hii ni ujinga.
Ndiyo maana mnavuruga elimu makusudi. Rais amewaambia Watanzania yeye hatakubali mtoto wa maskini asiende chuo kikuu atawakopesha, Waziri anasema ataangalia bajeti ilivyo sasa nani mwenye kauli?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza habari ya afya hapa, Makamu wa Rais anasema dawa hakuna Waziri anasema dawa zipo tele na jana Naibu Waziri amethibitisha, akasema tumwonyeshe, tumemwambia tumpelekee nyumbani kwake akakataa. Sasa haya mambo ukisoma kwa kweli, mimi vitabu vyenu huwa navisoma sana, nipo tayari nisilale usiku lakini navisoma sana, lakini mnatuchanganya sana, kwa nini msiandike ukweli? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, akija hapa Waziri wa Viwanda atapiga ngonjera zake utamwona huyu ndiyo mwanaume ametoka Bukoba wengine hawapo kabisa. Akiimba hapa ngonjera zake utashangaa, sasa nenda kwenye hali halisi, yote haya hamna. Anafukuzwa na Kamati yake kwamba mzee umeandika makabrasha mengi, pesa hakuna, Kamati ya Viwanda inasema hujafanya lolote, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda acha kuimbia watu ngonjera. General tyre mpaka leo haijaanza, watu wanataka kuona mnaleta tena story zilezile. Kwa kweli hii habari inatusumbua sana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme kuhusu hii habari ya mifugo, Wabunge wengi wanakaa Jimbo la Ukonga na Dar es Salaam kwa ujumla, hata kama mtu hakai ana kibanda pale lakini Dar es Salaam hakuna machinjio ya kisasa. Kuna machinjio ndogo kweli kweli pale Vingunguti na yale mazizi ni ya mtu binafsi siyo ya Serikali. Pale Zingiziwa kuna ekari zaidi ya 120, kama mkiweka mifugo pale na kuna mnada wa Kimataifa wa Pugu ambao kimsingi na wenyewe ni jina, ni mnada lakini ni kijiwe cha ng‟ombe, hakuna maji, hakuna chochote pale, ukiboreshwa utasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam ndiyo kuna Mawaziri, ndiyo ipo Ikulu lakini hakuna nyama safi, watu wanaweza kuchinjia vichochoroni wakauza mitaani, sijui kwa nini hampangi haya na maeneo yapo, hapa sikuona chochote kwamba mnaboreshaje suala hili. Dar es Salaam kuna watu wengi na wageni pia lakini suala hili haliwekewi mipango. Mbona mmesema tupande miti ili Jiji lipendeze Wazungu wafurahi, tengenezeni basi na mazingira mazuri ya kuchinjia nyama kwa afya zao. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme habari ya maji. Watu mikoani wanalia, lakini nawaambia hata Dar es Salaam kule Jimbo la Ukonga katika kata 13 ni kata moja au mbili zinaweza zikawa na uhakika wa maji na visima vingi zaidi ya asilimia 90 ni watu wamechimba wenyewe. Mheshimiwa Dkt. Mpango anakaa Zingiziwa pale Nzasa, yeye ni mpiga kura wangu kule, tupange siku moja aende Zingiziwa aone wale watoto na wazazi wa pale maji ambayo wanakunywa, Dar es Salaam acha kule kwao Kigoma, Dar es Salaam, maana anavyoandika hivi vitu twende kwa ushahidi aende aone, hajaandika chochote hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, afya; Jimbo la Ukonga lina wapiga kura zaidi ya laki sita na kata 13. Watu wote wale kutoka Zingiziwa, Chanika, Msongola, Mvuti, Uwanja wa Nyani wanakuja Amana. Tuna eneo kubwa ekari 45 kwa ajili ya kujenga hospitali na tangu mwaka jana niliwaambia kwamba ile hospitali ikijengwa itasaidia mpaka na Kisarawe mpaka Mkuranga. Halmashauri ina uwezo wa kutenga shilingi milioni moja kwa mwaka na gharama yake ni shilingi milioni 26 maana yake Halmashauri ikiachiwa ijenge itatumia miaka 26 watu wanasubiri huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda anapopanga zahanati, kituo cha afya na hospitali ataje majina ili Mbunge ajue zamu hii ni ya Msigwa, zamu ijayo itaenda labda Kwimba na sehemu nyingine, tuwatajie, asiweke kwenye bracket hapa. Aseme anataka kujenga hospitali ipi, zahanati ipi ili tujue kama siyo zamu yangu nisubiri mwaka ujao na akiandika atekeleze, aache kutuimbia ngonjera hapa. Mlishatuambia tutaisoma namba, tutaisoma wote pamoja, bahati nzuri hatuisomi wenyewe na nyie mnaisoma sana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Shirika la Ndege amelizungumzia, nataka nihoji hapa, tuna taarifa kwamba Chato kwa Mheshimiwa Magufuli pale nyumbani kwao Chato unajengwa uwanja wa ndege, mbona kwenye mipango hapa hiyo hela haipo? Bajeti iliyopita haikutajwa na hii hapa haijatajwa lakini unajengwa uwanja wa ndege kule Chato. Tunaomba tujue hiyo bajeti ya kujenga uwanja huo iko wapi mbona hapa kwenye mipango hamuutaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu mtuambie, hivi Chato kujenga uwanja wa ndege, sawa kweli wale ni watani na wakwe zangu, hivi kule Chato mtafanya biashara gani, projection ni nini pale? Yaani mnataka mjenge uwanja wa ndege ili Mheshimiwa Magufuli akitaka kupumzika aende na ndege nyumbani kwao? Kujenga uwanja wa ndege ni lazima kuangalia economic zone kwamba biashara itafanyika kwa sababu population ni kubwa na vitu vya namna hiyo. Haya hata hapa hamuonyeshi, sasa hiyo siyo siri tunajua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile kumekuwa na malalamiko ya ndege mlizonunua, mimi siyo mtaalam, ndege zenyewe ni Bombardier?
Wanasema mikataba duniani mnalipa kwa advance nyie mmeenda kulipa kwa bei ya jumla. Mmechukua hela zote mkaenda kununua ndege kwa mbwembwe, eti mnazindua kununua ndege, hivi kweli nyie mnaumwa, unazindua kununua ndege? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, karne ya 21, Serikali ya Chama cha Mapinduzi zaidi ya miaka 50, umri wa mtu mzima yaani miaka ya chama chenu inanizidi mimi Waitara, Mbunge wa Ukonga hebu niangalie halafu mnasherehekea kununua ndege. Muangalieni mwenzenu Kagame, ndege ya kwanza aliyonunua na mambo anayofanya. Ameleta ndege ambayo inaendesha kwa mitambo, shabash, nyie mnapiga makofi hapa! Wabunge wanasimama hapa hoja ambazo hazina maana eti anaunga mkono ili asisahau maana wamezeeka halafu wanalalamika, mambo gani haya bwana? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme. Mimi ni Mbunge wa Ukonga, ukienda Kata ya Msongola, robo tatu ya kata hakuna umeme. Kivule ina mitaa minne, mitaa miwili ndiyo ina umeme. Ukienda Zingiziwa kuna mitaa nane ni mtaa mmoja tu wa Mheshimiwa Waziri wa Fedha ndiyo kuna umeme. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Chanika kuna mitaa nane, miwili ndiyo ina umeme. Ukienda Pugu kuna mitaa mitano, mitatu ndiyo ina umeme miwili haina umeme. Ni Dar es Salaam hiyo sikutaja majimbo mengine ya Kigamboni na kadhalika na mnasema ule ndiyo mji ambao una population kubwa, ndiyo mji wa kibiashara, ndiyo Rais yuko pale lakini umeme ni shida. Kule mnatoa matamko kushughulikia watu kwenye vikao, kupindishapindisha na kuiba kura za Kinondoni, mnatangaza Meya hewa, mmeleta Meya hewa pale wakati nyie mnatafuta wafanyakazi hewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu Waziri anayehusika ashughulikie suala hili ili umeme isiwe wimbo Dar es Salaam. Watu wanakaa Dar es Salaam kwa maana ya majina lakini akimwambia mtu amtembelee anamzungusha mjini anamkimbia kwa sababu akienda nyumbani kwake hatafanana na mbwembwe alizokuwa anasema. Kwa hiyo, tunahitaji suala hilo lishughulikiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waitara muda wako umeisha tafadhali naomba tu ukae.
Haya basi siungi mkono hoja mimi.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza niseme tu kwamba mimi ni Mjumbe wa Kamati hii ya Utawala na Serikali za Mitaa, kwa hiyo naunga mkono maoni yote ambayo yamewasilishwa na Kamati yangu hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipata fursa ya kushiriki Kamati kwenye ziara na kuangalia miradi na kwenye mawasilisho mbalimbali ambayo yalifanyika kwenye Kamati yetu, yapo maeneo muhimu ambayo nataka kuchangia hapa. Jambo la kwanza; tulizungumza hii Kamati inahusika na mambo ya utawala na tukaangalia eneo la kero kwa wananchi, rushwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, rushwa imekuwa ni kubwa ingawa upande wa Serikali ukizungumza nao watakwambia rushwa imepungua kwelikweli, si kweli. Jambo hili limechagizwa sana na kauli ya Mheshimiwa Rais kwamba maaskari wanaruhusiwa kuchukua rushwa ndogondogo, 5,000 hela ya sabuni na kubrashia viatu. Bahati mbaya sana kwa sababu ya hofu na woga uliopo hakuna mtu ambaye alienda front kumshauri ama kubadilisha ile kauli na imekuwa ni kero kwa wananchi na hasa vijana wa bodaboda ambao wanajitafutia maisha katika jua kali, wanaombwa sana hizi fedha mnaita ndogondogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni maoni yangu kwamba ni muhimu upande wa Serikali wakaliangalia jambo hili upya na ni muhimu kuangalia pia kauli za viongozi wetu na hasa Mheshimiwa Rais. Haiwezekani kiongozi ambaye ameapa kuitii Katiba ya nchi na sheria na kanuni anasimama hadharani bila hofu wala woga anasema askari wakipewa sh. 5,000 ya kiwi ya viatu ni sawasawa kabisa na anasema ni hela ya kiwi, lakini hili jambo limekuwa ni kero kwa wananchi wetu ambao kimsingi maisha ni magumu na kipato ni kidogo na unapokosa sh. 5,000 inaweza kupelekea hata kung‟oa matairi na mambo mengine chungu nzima ambayo yanafanyika, hilo ni eneo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo tuliliona ni eneo la TASAF. Mimi ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, kwa hiyo nafahamu vizuri namna ambavyo watu wetu wamepata msaada mkubwa kupitia fedha hizi na ni mpango mzuri pamoja na kwamba zipo changamoto mbalimbali ambazo inabidi zifanyiwe kazi kwa maana ya kuboresha ili hii fedha iendelee kupatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia wapo wananchi wengi sana ambao hawana uwezo na michakato haikuwapitia, wakazikosa. Kwa hiyo, niishauri Serikali, ni muhimu yale maeneo ambayo watu walikuwa wanakidhi vigezo, wana uwezo mdogo na hawakupata zile fedha, basi maeneo hayo yaangaliwe upya ili watu hao waweze kupata msaada wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni yangu ni kwamba ni muhimu hizi fedha pamoja na kuwapa watu wetu ili kuwasaidia wapo wachache, kama tulipokwenda Zanzibar, Pemba na Unguja ikaonekana baadhi ya maeneo ya Tanzania Bara yamefanya hivyo, wale wazazi wanapewa zile fedha wanatumia wanabakisha kidogo wanaweka miradi midogomidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri tuwekeze kwenye miradi midogo midogo kwa sababu mpango huu sio mpango wa miaka yote, maisha yao yote, kama wakijifunza ku-save kidogo wanatumia na wakaanzisha miradi midogomidogo hata akili zao zinachangamka katika kujipangia mapato na matumizi yao. Kwa hiyo tungependekeza jambo hili muhimu likachukuliwa kwa uzito. Wawezeshwe fedha lakini pia waelekezwe namna ya kuwekeza kwenye miradi midogo midogo ili iwasaidie huko baadaye. Hata kama fungu hili likiondolewa watakuwa wamejipanga vizuri juu ya namna ya kupata huduma kwa sababu lengo ni kuwasaidia hapa walipo na waweze kujiinua kimaisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wamepata msaada, wengine wamesomesha watoto, wengine wamejenga hata vibanda hata kama ni vibovu lakini imesaidia kwa kweli. Kwa hiyo, ile kauli ambayo inaonekana kwamba kuna taarifa huu mpango haujasaidia; leo wale wazazi ambao hawana uwezo, watu wetu wale, badala ya kwenda kupanga foleni kwa Diwani au kwa Mbunge kuomba hela ndogondogo wanakwenda kupanga foleni kwa Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo cha muhimu hapa fedha ni muhimu, ni kuboresha mazingira ambayo yana changamoto mbalimbali na uwazi uwepo, wale wahusika wapewe, hilo ndilo jambo la msingi sana. Mtu ambaye anashauri kwamba hii fedha iondolewe, kwa kweli huyu mtu ni wa kulaani sana, hawatakii mema watu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la watumishi hewa. Ni kweli kwamba Serikali imechukua hatua ya kuangalia watumishi hewa, lakini jambo hili linachukua muda mrefu sana. Wapo watu ambao maslahi yao yamezuiliwa kwa sababu ya hoja ya watumishi hewa na hasa ajira mpya kwa vijana wetu. Sasa ni muhimu jambo hili kuwe na deadline, kwamba mnafanya kwa muda wa mwezi mmoja, miwili, mitatu au minne, jambo limalizike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu watumishi hewa; kwanza watu wanataka kujua nani ni mtumishi hewa ajulikane na hawa ndio wanaotakiwa wawajibishwe; wale waliopokea fedha na wale viongozi ambao ni wa Utumishi waliotengeneza miundombinu ya kupata watumishi hewa, wasiwawajibishe watumishi wasiokuwemo. Kwa sababu kama kuna fedha inalipwa kutoka kwenye akaunti, wale wakubwa wawajibishwe. Hata hivyo, jambo hili liishe ili watu wetu wapate ajira na waweze kutumikia Watanzania kwa ubora zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la utawala bora. Leo asubuhi nilisikitika sana Mheshimiwa Simbachawene. Kwanza anajua hapa karibuni umetengenezwa mgogoro mkubwa sana Serikali za Mitaa. Lilizuka jambo la mihuri hapa mpaka wenyeviti wenzangu wa mitaa wakafikia hatua ya kuandamana, kuunda Kamati mbalimbali na kuanza kufanya zile kazi. Sasa hapa ni muhimu tukajua, zipo kazi za Wenyeviti wa Mitaa, zielekezwe vizuri. Mtendaji anapoajiriwa anajua kazi zake na Wenyeviti wa Mitaa waelekezwe. Sasa kutujumlisha kwamba wote tunapiga maeneo ya umma si kweli, mimi ni Mwenyekiti wa Mtaa, sina kesi ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni muhimu maelekezo yaende kwamba kama kuna Mwenyekiti ambaye kwa kweli ametumia nafasi yake vibaya huyo awajibishwe. Wale ambao wamepewa, kwa mfano Mheshimiwa Waziri ukiulizwa tangu uchaguzi umefanyika mwaka 2014 ni mpango gani mmefanya kutoa semina kwa Wenyeviti wa Mitaa, Madiwani na hata watendaji? Mtu amekuja hapa Hombolo kapata mafunzo yake, kapata ajira akifanya makosa sio fault yake ni fault ya Wizara, kwa hiyo naomba Wizara itimize wajibu wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, nimesikitika sana leo asubuhi, sisi tunasema Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wanajiita Marais; wewe umeunga mkono hiyo hoja kama ni kweli eti kwa sababu madaraka yanashuka kutoka kwa Mheshimiwa Rais, kwa hiyo nchi hii kila mtu ni Mheshimiwa Rais! Sisi tulichouliza ni kwamba, Wakuu wa Wilaya wanahujumu mpaka Waheshimiwa Wabunge, hatuheshimiani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amefanya ziara Dar es Salaam pale Ukonga, kwa heshima nimetoka nyumbani kwangu nimekwenda kwenye eneo lile, nikakuta, Mkuu wa Mkoa anatukana watumishi kwamba ninyi ni mizigo, ninyi ni misumari. Mwanamke, yule mama wa Kinondoni, ninyi wanawake mnasema hapa wanawake wapewe fursa wafanye kazi! Afisa Utumishi wa Kinondoni Makonda anamwambia wewe ni mzigo, hivi nani amekuweka hapa! Toka hapa potea pale mbele!
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkuu wa Mkoa, kwenye public, kwenye mkutano wa hadhara, yule mama ameshindwa hata kutembea miguu imekuwa mizito, hayo ndiyo mambo tunayokataa hapa. Mkuu wa Mkoa yupo kwenye mkutano eneo la mgogoro, limeunda Kamati pale, Diwani amefanya kazi yake, Afisa Utumishi amekwenda, Afisa Mipango ya Maendeleo wa eneo lile, Mkuu wa Mkoa anakuja pale kwa sababu ana polisi anamwambia Diwani apate fursa ya kutoa taarifa, mimi hata kusalimia alinizuia, akasema hiki kikao ni cha Mkuu wa Mkoa, halafu tuheshimiane namna gani? Hayo ndiyo mambo ya msingi ya kuzungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani shule zinafelisha; mwaka jana Mkuu wa Mkoa wa Simiyu ameagiza mkoa mzima, eti wakuu wa shule amewatumbua, halafu mnataka matokeo yawe mazuri yataanzia wapi, hatuheshimiani kwenye kazi. Kwa nini Mkuu wa Mkoa asione kuna shida? Tumesoma ile sheria vizuri, kama kuna shida, kama kuna mkuu ninayempongeza sana ni Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, nilimwona kwenye TV, naomba mumpigie makofi basi hata huyu amefanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu amekwenda anajadili matokeo ya form four, ameita watumishi kwenye idara husika, anasema tulifanya kikao tukasema atakayezembea eneo lake atawajibishwa, anasema naomba idara husika ya elimu iwajibishe wahusika, simple. Kwa hiyo, ukishasema hivyo watafanya utafiti, watafanya enquiry fulani, itakuja taarifa anayehusika na mambo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, haya mambo ndiyo tunataka yafanyike. Hatutaki watu wazembe ila hatutaki watu waonewe tunataka mtu akiwajibishwa; na Waziri ni Mwanasheria wa eneo hili, wote wawili, Waziri wa Utumishi na Waziri wa TAMISEMI na nawaheshimu sana ndugu zangu, lakini tunataka utaratibu tu. Hivi Mkuu wa Mkoa kweli ni rais kwenye mkoa wake! Ni rais kwenye wilaya yake! Kwa hiyo kuna vitu ambavyo mnadanganya watu hapa, naomba tuheshimu hiki chombo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachosema sisi ni kwamba hatupingi kila kitu, yapo mambo yanafanyika mazuri tunaunga mkono. Tunapiga kelele sana kwa mambo mabaya, kukatisha watu tamaa na matumizi mabaya ya madaraka. Hivi inawezekana Mheshimiwa DC amekwenda kwenye mkutano, anamwambia Diwani kamata weka ndani halafu tupige makofi? Ni kiongozi mwenzake halafu anataka ampe ushirikiano, hizo taarifa anazipataje na hao ni watu ambao kwa kweli wameletwa kwenye maeneo yale na kuna mtu amepigiwa kura na watu wake, kwa hiyo mnajenga chuki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Nkamia amesema hapa leo asubuhi, kwamba inawezekanaje DC anatukana wananchi halafu huyu anasema eti ndiyo Rais wa eneo lile…
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kupata nafasi hii. Nianze kwa kutoa pole sana kwa wananchi wangu wa Jimbo la Ukonga kwa mafuriko ambayo yametokea kwenye kata za Msongola, Chanika, Zingizingiwa, Gongo la Mboto, Pugu, Buyuni na Majohe ikiwepo na Kivule. Hali ya usafiri ni mbaya sana lakini wavumilie kwa sababu tumeshachukua hatua kwamba baada ya mvua hizi tutafanya ukarabati ili barabara zirudi katika hali yake ya kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nitoe pole kwa kufariki Mchumi wa Manispaa ya Ilala ambaye alikuwa pia Katibu wa Mfuko wa Jimbo la Ukonga. Nampa pole sana Mheshimiwa Mkurugenzi na watumishi wote wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala akiwepo Mstahiki Meya tupo pamoja nao na tunamtakia Mungu ampe pumziko la amani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mwalimu wa masomo ya hesabu na chemistry na leo nimekusudia kuchangia kitaaluma zaidi. Ningeanza kwa kusema huwa napata shida sana, yako mambo Waheshimiwa Wabunge wanachangia humu ndani, wanazungumzia habari ya elimu lakini inabidi urudi kule kwenye TAMISEMI. Kwa nini Wizara isingeitwa Wizara ya Elimu na mambo yote yanaendana na elimu ili tumuulize yeye, ingekuwa ni rahisi sana. Kama tunazungumza habari ya shule, miundombinu, mahitaji maalum iwe yeye Waziri wa Elimu ndiyo unahusika. Kwa sababu tunazungumza habari ya matundu ya vyoo mpaka tukamuulize TAMISEMI, kwa hiyo, kidogo inaleta shida naomba mliangalie hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na hoja ya madai ya walimu. Mheshimiwa Waziri kama ana nia ya kutaka kufanya kazi ambapo mimi sina shaka na uwezo wake, yeye siyo mwanasiasa labda aanze kujingiza kwenye siasa ambayo kimsingi siyo fani yake. Kama anataka kufanya kazi vizuri hebu achukue kitabu cha Maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani, achukue kitabu cha Maoni ya Kamati ajifungie avipitie atamaliza matatizo yaliyopo hapa. Wala ahitaji kuzunguka sana humu, achukue Maoni Kambi Rasmi ya Upinzani na Maoni ya Kamati akiyafanyia kazi mwaka ujao ataonekana Waziri bora kabisa wa Elimu katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa walimu wanadai shilingi trilioni 1.6 mpaka sasa wamelipwa asilimia mbili tu. Kwa hiyo, unapozungumzia kuboresha elimu lazima uzungumze kuondoa kesho na malalamiko ya walimu katika nchi hii. Kwa kweli imekuwa ni fedhea sana, ni kwa nini wataalam wa kada zingine hawalalamiki sana. Ukienda kwa madaktari wanalipwa, wanasheria wako vizuri sana, kwa nini kuna shida sana kwa walimu? Kwa hiyo, nadhani hili jambo kwa kweli ingefika mahali mkalimaliza mtamaliza shida ya walimu na walimu watafundisha vizuri kwa kupata stahiki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wamesahihisha mtihani wa form two tangu mwaka jana mpaka leo hawajalipwa. Kuna walimu wameenda likizo, madaraja wanalalamika sana tumekutana nao Mheshimiwa Waziri na hivi vitu ni vitu genuine. Kwa hiyo, ni muhimu mkayafanyia kazi, akija kwa Waziri anarudishwa TAMISEMI, TAMISEMI inaenda kwa Mkurugenzi. Wakati mwingine mwalimu anadai madai yake anafunga safari kutoka sehemu ya mbali anakuja Halmashauri anaambiwa faili limepotea na huyu ni mtumishi wa umma. Nadhani mngepunguza kero kwa walimu hawa mgetusaidia sana sisi ili mambo shule yaende vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna hoja hapa ya Bodi ya Mikopo. Nilikuwa nataka niseme lakini yupo Mheshimiwa Ester Mmasi, Wabunge wa Chama cha Mapinduzi mna shida, ilipokuja hoja hapa ya Bodi ya Mikopo, Waziri mlipambana na Mheshimiwa Mwenyekiti ulikalia Kiti mkatupa maoni yetu kabisa. Wanafunzi hao ambao wengine wanasoma na wengine wanaendelea kufanya kazi wanatakiwa kulipa fedha ya mikopo walikubaliana na Serikali kulipa asilimia nane, imetungwa sheria hapa ambayo inafanya kazi kisengere nyuma wanakatwa asilimia 15 na wameshaanza kukatwa wanalalamika. Kuna mwalimu ambaye anakatwa mpaka mwisho wa mwezi anaondoka nyumbani na shilingi 80,000 au shilingi 100,000 sasa unamfanyeje? Hakuna usafiri, nyumba za walimu, inabidi akodi wakati mwingine bodaboda au taxi aende shuleni. Kwa hiyo, ninyi mmetengeneza mazingira magumu sana kwa kuwahukumu walimu ambao humu Bungeni hawamo na tulipinga mkapitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya bure, juzi Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI alisema kwamba mpango huu ni nzuri, hatukatai mpango ni mzuri, kweli idadi ya wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza wameongezeka sana. Sasa shida inakuja nataka mnisaidie, kuna shule moja ya kule Dar es Salaam katika mtihani wa form four waliopata division one walikuwa zero, division two walikuwa watano, division three walikuwa 17, division four walikuwa 70 na division zero walikuwa 105. Kwa hiyo, asilimia 11 ndiyo ilipata daraja la kwanza na la pili, asilimia 88.8 walipata zero na four. Sasa naomba mnijibu, hawa division four na zero wako wapi? Wameenda shuleni miaka minne badala ya kwenda kupata uelewa, wameenda kukua kimwili, wako wapi hawa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule ya pili, division one hakuna, division two wanne, division three wapo 11, division four ni 69 na zero 35. Wanafunzi 15 ndiyo waliopata daraja la kwanza na la pili na daraja la tatu na la nne 104, hawa wako wapi? Shule nyingine division one wapo wawili, division two wapo wawili, division three wapo 18, division four wapo 57, division zero wapo zero 97, wanafunzi154 ni four na zero hawa wako wapi? Ukifanya utafiti taarifa hii inasema asilimia 88 wamepata division zero na division four. Mtusaidie hawa Watanzania walio wengi wameenda wapi. Kwa hiyo hoja inazungumzwa ni kweli kwamba watu wameongezeka lakini kimsingi ubora wa elimu ambayo wanaipata siyo sawa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii elimu ya bure, mimi sijui kiswahili labda kwa sababu ni Mkurya, Waziri wa TAMISEMI juzi kasema walichofanya Serikali ni kuleta elimu ya msingi bila malipo. Hivi elimu ya bure na elimu bila malipo kuna tofauti gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kitendo hicho kimekwaza wazazi wengi sana, wamekubali hawachangii chochote lakini mashuleni kuna tuition zinaendelea, kuna remidial classes na kuna mitihani inafanywa. Kwa hiyo, kuna ubaguzi, wale wazazi wanaoweza kuchangia wanachangia wale ambao ni wenzangu na mimi watoto wao hawasomi. Kwa hiyo, tayari mashuleni kuna matabaka. Ni muhimu mkaja na mpango, kama wazazi wanatakiwa kuchangia msizungukezunguke kutafuta lugha ya kudanganya. Waambieni Serikali imeondoa ada, michango mingine ni
halali, mshiriki kuboresha elimu ili watoto wasome vizuri kwa standard ambayo inaeleweka. Mtakuwa mmetibu tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu heshima ya walimu, kumekuwa na tabia, sasa hivi kidogo imetulia tuliisemea sana kwenye Kamati ya TAMISEMI, kitendo cha walimu matokeo yakiwa mabaya wanawajibishwa wao. Kitendo hicho kimewakwaza walimu sana tungependa waheshimiwe kama wataalam wengine. Kama kuna makosa wapelekwe kwenye vyombo vinavyohusika ili wachukuliwe hatua ambazo zinazotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtihani wa darasa la saba. Maswali ambayo yanatungwa katika mtihani wa darasa la saba ni ya kuchagua. Nimewauliza walimu kwa nini matokeo ni mabaya, wanasema Serikali imeleta asilimia 20 ya pass wakati wa Kikwete, kwa Magufuli wamesema ni asilimia 30, watoto hawa wanapewa maswali ya kuchagua, ana ana doo. Ndiyo maana shuleni kweli kuna watoto ambao ni form two hawajui kusoma na kuandika kwa sababu ameandika jibu ni “A” lakini ukimuuliza “A” umeipataje hawezi kukueleza.

Kwa hiyo, walimu wanalalamika wanasema maswali yasiwe ya kuchagua, wapewe maswali ya kuandika, watoto wapimwe uwezo, yule ambaye anaenda sekondari aende ambaye haendi mpeleke VETA wasipoteze gharama na muda. Katika jambo hili Mheshimiwa Waziri naomba isifanyike siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nizungumze hapa ni kwamba kuna upungufu wa walimu wengi sana hasa wa masomo ya sayansi na hisabati. Hata kwenye Lab. Technician kwa mfano Dar es Salaam, Lab. Technician wanaotakiwa ni 67 waliopo ni 7. Kwa hiyo, mwalimu anafundisha biology, chemistry au physics inabidi aende kwenye Lab. Shule ina wanafunzi 640 mwalimu mmoja wa physics awafundishe wote maana yake unamwambia kwa wiki atasahihisha madaftari 600 mzigo ni mkubwa kweli kweli.

Mheheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba nah ii kazi ya kuhakiki vyeti Mheshimiwa Waziri ambapo mmesema Wabunge, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya hawakikiwi siyo sawasawa sana. Mimi siungi mkono kwa sababu hawa ni watu ambao wanaendesha Mikoa na Wilaya ambapo kuna vyuo vikuu, kuna wataalam, wanaenda kwenye mahafali wanapaswa kuhamasisha vijana wasome. Sasa kama wewe ni Bashite namna gani utamhamasisha mtoto asome shule. Kwa hiyo, ni muhimu kila mtumishi wa umma ahakikiwe na vyeti vithibitike na walio-forge washughulikiwe, ndiyo tutajenga nidhamu ya taaluma ya nchi hii. Profesa hataweza kukubaliana na vitu vinavyofanyika ambavyo siyo sawa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka nilizungumze ambalo mtanisaidia hapa ni uhamisho wa walimu. Ni kweli mnahamasisha mambo ya mahusiano, kuepuka UKIMWI na magonjwa mengine lakini kumekuwa na shida mwalimu kuhama kutoka eneo moja kwenda eneo lingine aidha mwanamke kumfuata mwanamume au mwanaume kumfuata mwanamke, anapewa masharti kwamba atafute mwalimu mbadilishane. Hiki kitu siyo sawasawa na yenyewe ina-discourage walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mwanamke anafundisha Kagera, mwanaume yuko Katavi, hayo mahusiano ya hii familia yanajengwa namna gani na tunataka kuwa na malezi bora?

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyo mtu kila siku anafanya kazi anamfikiria mwenzake, mke anamfikiria mume na mume anamfikiria mke na matokeo yake hajiandai, hapitii vitabu mbalimbali, hafanyi andalio la somo na kusababisha matokeo kuwa siyo mazuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ile ya Maoni ya Upinzani.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, na mimi niungane na wenzangu wote ambao wanamshukuru Mungu kwa kuponywa kwa Mheshimiwa Tundu Lissu na anaendelea vizuri na afya yake inazidi kuimarika. Lakini nianze na mambo machache ya jumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza kwenye vipaumbele hivi vilivyopangwa, nimeona vipaumbele vipo kumi, ile kaulimbiu ya Serikali ya Tanznaia ya viwanda hai- reflect kwenye vipaumbele. Kwenye mpangilio huu viwanda ni kipaumbele cha kumi, maana yake kwenye mpangilio ni cha mwisho kwa hiyo maana yake ni kwamba inawezekana tunaendelea kuibadilisha hiyo kaulimbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo jinginela jumla ambalo nadhani ningemshauri Mheshimiwa Waziri Mpango alipokee ni kwamba mwaka wa jana mpango ulikuja wa mwaka mmoja, na vipaumbele vilikuwepo na mwaka huu vimekuja tena. Tulishauri na mimi ningeomba nirudie tena, kwamba Mheshimiwa Waziri ni muhimu tukubaliane kwamba hivi sisi kama Watanzania, kama Taifa tunaweza kupata kiasi gani kwa ajili ya miradi yetu ya maendeleo? Ukishapata kiwango ambacho unaweza kupata kutoka whatever the sources kama ni nje, ndani, vyovyote vile tukubaliane ni mambo gani machache ambayo yanaweza kutekelezwa yakakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na utakumbuka kwenye bajeti ile ilikuwa shilingi trilioni 29.5 lakini haikufika hata asilimia 70 katika utekelezaji wake. Mwaka wa jana tena imekuja shilingi trilioni 31.4 hatutafika asilimia 70 mpaka 80 kwa mwenendo ulivyo mpaka sasa. Sasa maana yake ni kwamba mipango mingi tuliyopitisha itakwama na hiyo kimsingi ndiyo inazua malalamiko mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu la jumla ambao nashauri hapa, inawezekana watu wanapotoa maoni kuna tafsiri tofauti, watu wanaleta hisia za ukanda na nini, lakini ukweli ni kwamba kama kuna mipango, miradi mbalimbali inatekelezwa ambayo miradi hiyo haikujadiliwa kinagaubaga kwa uwazi Bungeni hapa watu watalalmika hakuna namna, yaani hiyo msikwepe. Mwambieni Mheshimiwa Rais wazi kama analazimisha mipango tunayotaka itekelezwe ni hii mliyoleta hapa tukapitisha, mkitekeleza hii hakuna atakayelalamika. Kwa hiyo, watu wasikwepe wasikimbie kivuli chao. Ni kwamba mipango iliyopangwa itekelezwe, kama kuna mapungufu sheria inaruhusu na Katiba inaruhusu tuje tubadilishe mlete maombi inaruhusuiwa. Fedha kama ikipungua usitumie kinyemela, rudini Bungeni hapa, lete mapendekezo tutaridhia hicho ndicho ambacho Wabunge wanasema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kumekuwa na kauli mkanganyiko sana na hizo kauli ni jambo la jumla sana.

Kwenye miradi mbalimbali, Mheshimiwa Rais akisema kauli maeneo mbalimbali watu wanashituka kwa sababu Watanzania wanajua kwa mujibu wa Katiba hii Rais anapatikana kwa kura nchi nzima na kanda zote zimemchangua. Kwa hiyo, unapoona kiongozi mkuu wa nchi anakwenda mahali anatamka kauli ya kiupendeleo hiyo watu hawawezi kuishangilia, wataipinga, watalalamika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninyi cha muhimu ni kupokea mambo, mwambieni Mheshimiwa Rais kwamba huyu ni kiongozi wa nchi akizungumza tunataka atoe suluhu na tiba kwa kero za Watanzania hayo mahitaji ya Watanzania, kwa hiyo msikimbie kivuli chenu na wala msilalamike hapa kuna mjadala wa ukanda hakuna ukanda. Maneno yanayozungumzwa aidha na Mawaziri na viongozi mbalimbali na Mheshimiwa Rais yanawagawa Watanzania. Kwa hiyo, mkifuta hiyo kauli, mshaurini kimya kimya ni muhimu abadilishe kauli za namna hiyo, azungumze kama Rais wa nchi. Hayo ni mambo ambayo kimsingi hayana upendeleo wowote myapokee na kuyafanyia kazi ni ushauri tu
nilisema natoa ushauri wa mambo ya jumla sasa nakwenda kwenye Mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, habari ya umeme kipaumbele cha kwanza, mimi Mheshimiwa Mpango nakushauri, kwa sababu kumekuwa na mpango wa umeme wa REA na Watanzania wote na Wabunge wote wanasubiri umeme utekelezwe; umeona kuna malalamiko hapa wanasema wakandarasi walitangazwa lakini baadhi ya maeneo hawaonekani tena, walizindua miradi haijatekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni muhimu litekelezwe likamilike kila mahali, kwa maana ya nchi nzima. Hauwezi kuzungumza habari ya viwanda; yaani umeme kwa matumizi ya kawaida haujakamilika, haupo maeneo mengi ni giza, kwenye shule ni giza. Kuna visima vya maji vimechimbwa maeneo mbalimbali hauwezi kutumia maji kwa sabbau hakuna umeme na hakuna uwezo wa kununua jenereta. Pelekeni umeme wa kawaida kwanza halafu hiyo ziada iende kwenye viwanda, watu watakuelewa Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni ujenzi wa miundombinu. Hawa Wabunge wanasema kuna maeneo ambayo mpaka leo Mkoa kwa Mkoa haujaunganishwa, Wilaya kwa Wilaya haijaunganishwa, hilo jambo limezungumzwa mara nyingi. Kama unazungumza habari ya ujenzi wa miundombinu nendeni mkamilishe uhakikishe kwamba Mkoa kwa Mkoa kuna mawasiliano ya kutosha, Wilaya kwa Wilaya halafu uhamie kwenye ajenda nyingine msiguse guse hapa na pale mnahama mnaacha viporo vingi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la mifugo. Kumekuwa na malalamiko, kwa kweli hii ni lana kubwa katika Taifa hili. Watu wote hapa mnategemea kula nyama na mifugo kwa kweli ni mali kubwa sana. Viatu ni humo humo, ni kila kitu lakini inawezekanaje sasa hivi mtu akiwa na mifugo inaonekana kama ni uadui? Yaani kuna ugomvi mkubwa kati ya wakulima na wafugaji. Hakuna malisho ya wanyama, hakuna mahitaji muhimu katika maeneo yale, mifugo inakufa, mifugo inachomwa na hili jambo mnalifahamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa mfano pale Dar es Salaam kuna mnada mkubwa sana wa Pugu ambao unaitwa mnada wa kimataifa, lakini ukienda katika eneo hili ukimwambia mtu wa kawaida kwamba ni mnada wa kimataifa hawezi kukuelewa. Hata kama lile ndilo eneo pekee ambalo Dar es Salaam wanalitumia kwa nyama lakini ni eneo la hovyo. Hakuna josho, hakuna mabwawa, hakuna vyoo, hakuna uzio, ratiba haijulikani, rushwa nje nje! Sasa mambo haya ukiyazungumza watu wanasema kwamba labda ni kuituhumu Serikali, si kuituhumu Serikali tunasema ili mkayafanyie kazi, mkarekebishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna ugomvi mkubwa kati ya wafugaji na wakulima, ugomvi kati ya wafugaji na hifadhi za wanyama. Wale watu wa hifadhi wanachukua mifugo ya wananchi, wanaitoa nchi kavu wanapeleka kwenye mapori, wanawatoza fedha nyingi kweli kweli. Kwa hiyo, mpaka wale wananchi wanaofuga wanaona kwamba kufuga ni laana wanaamua kuachana na ile biashara lakini watu wa vijijini ng’ombe ndiyo benki yao. Ukitaka kuzungumza hapa elimu mtoto asomeshwe hawa ambao wamekosa mikopo ya Bodi ya Mikopo maana yake mtu kama ana ng’ombe wake atauza ili asomeshe mtoto. Sasa ng’ombe mmechukua, mmewatelekeza, wamekufa, wanachomwa na wananyang’anywa. Kwa hiyo nadhani jambo hili lazima pia lifanyiwe kazi vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nimeliona hapa ni miradi ya maji. Mheshimiwa Kiwanga amesema hapa kwamba Mheshimiwa Waziri unatakiwa uwe na akili ya kawaida, yakiulizwa maswali hapa na wewe Mwenyekiti asubuhi umesaidia maswali mengi kwenye upande wa maji ni kwamba kama watu wanahoji sana maana yake maji ni shida karibu kila kona. Ukisema hivi Mbunge wa Dar es Salaam Ukonga utafikiri kuna maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kuna watu mpaka leo wanachota maji kwa kutumia zile kata, mvua ikinyesha ndiyo maji wanayokunywa. Sasa jambo hili limekuwa wimbo wa kila siku. Mheshimiwa Mpango wewe kama Waziri legacy yako itakuwa ni nini? Tuambie basi angalau katika mpango huu umeweka miradi ile yote ya maji ambayo imeanzishwa ikamilike, uibue miradi mingine mipya, Wabunge wakija hapa tuache kupiga story ya maji kila siku kama watu ambao hatuna uelewa, tuzungumze jambo lingine. Ile miradi mliyoanzisha kamilisheni, ile miradi mikubwa angalau basi mwaka ukiisha utuambie mimi kama Waziri wa Mipango na timu yangu nimetekeleza mpango huu umekamilika tukose maswali. Hilo nafikiri ukilifanya utakuwa umetenda haki sana kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani kila mwaka, kila Mbunge hapa, hakuna Mbunge ambaye halilii maji katika eneo lake, umekuwani wimbo wa Taifa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mpango utusaidie, pangeni vipaumbele, kilio cha Wabunge kipokee, tekeleza ili maneno humu ndani yaweze kupungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, susla la utawala bora. Mimi nilikuwa nataka nishauri, maendeleo haya hayawezi kuja kama kuna hofu katika Taifa, kama watu hawana amani katika shughuli zao, kama mtu anafunga duka. Hivi ni mfanyabiashara gani mjinga ambae atakwenda kukopa mkopo wa Benki, afungue biashara halafu mwanaume mmoja anasema kuanzia leo funga maana yake ukifunga duka lake akafungwa na yeye hawatawekeza Mheshimiwa Mpango, na wewe unajua ni mtaalam, hawatawekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna watu ambao ni very sensitive kama matajiri ambao wana fedha zao. Anataka mahali ambapo kuna amani, utulivu na kuaminiana, anakuwa confortable na anawekeza katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika Taifa hili utawala bora na demokrasia imekuwa ni shida. Sisi hata haya mambo tunayozungumza hapa tukitaka kukosoa tu kwamba data hizi si za kweli, Pato la Taifa figure hizi si za kweli unaambiwa ukamatwe uwekwe ndani. Sasa lazima tujadili, maendeleo ni pamoja na demokrasia, maendeleo maana yake ni uhuru wa kuzungumza, kupokea maoni. Kama mnafanya kazi nzuri kwa nini mnakamata watu? Kwa nini watu watishiwe maisha? Kwa nini watu wapigwe risasi? Kama kunafanywa maendeleo, sisi tuacheni tuseme tunavyosema bila kuvunja sheria, bila ku-personalize mambo halafu ninyi mtende kazi. Muwaambie ninyi CHADEMA, CUF mlikuwa mnapiga kelele sisi tulitekeleza hiki na hiki, tushindane kwa namna hiyo. Fanyeni kazi tukose hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hoja zipo nyingi kweli kweli tunazoweza kuzijibu. Hoja zipo na hazina majibu, ni kwa sababu ninyi mna-concentrate kutushughulikia hapa, ni muhimu huu utaratibu uishe. Wekeni uhuru wa kutoa maoni, tuikosoe Serikali, tukosoe mipango ya Mheshimiwa Mpango halafu mkatekeleze mtuambie ninyi mlipiga kelele sasa sisi tumefanya moja, mbili, tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya bure, bahati nzuri mimi ni mwalimu kitaaluma. Hili jambo ni jema, wanafunzi wameandikishwa darasa la kwanza wengi sana. Sasa shida iliyopo umezuka ugomvi sasa kati ya wazazi na walimu.
Serikali ilisema elimu ni ya bure sasa…

(Hapa kkengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia na namshukuru Waziri Mkuu kwa sababu kimsingi anatimiza wajibu wake kama nafasi yake inavyosema. Nitaanza na eneo muhimu sana la ukurasa wa saba kwenye hotuba yake amezungumzia habari ya kudumisha amani na utulivu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba amani huwa hailazimishwi na utulivu wa Taifa hauwezi kulazimishwa kutumia mtutu wa bunduki. Jambo hili ili lifanyike vizuri ni lazima liwe ni zoezi shirikishi. Katika maeneo haya ndiyo maeneo ambayo sisi kama viongozi wa upande wa Upinzani tunalalamikia sana kwamba kwa sasa hali ilivyo ni kama tumesahau kwamba Rwanda nini kilitokea baada ya chokochoko nyingi; ni kama tumesahau nini kilitokea Algeria na tunazungumza kana kwamba haya mambo hayapo katika mataifa mbalimbali baada ya maoni ya Upinzani na viongozi mbalimbali kupuuzwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi tunaona kitendo cha kusema tunakuwa tunadumisha amani na utulivu katika nchi, lakini wakati huo huo viongozi ambao tunakaa katika Bunge hili tunajadiliana mambo ya kitaifa kwa upendo kabisa lakini tunawakamata kwa hila, chuki na tunawasweka ndani, tunawanyima dhamana na watu wengine kadha wa kadha wameumizwa katika maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka nitoe wito kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye mimi namheshimu sana, kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu ukiangalia picha ya yule Diwani wa Kilombero alivyokatwa mapanga kama una moyo wa nyama lazima ushtuke sana. Ukiangalia watu wanavyookotwa katika fukwe mbalimbali. Kwa hiyo, mambo haya tungeomba kwa moyo wa dhati kabisa, kama tunalipenda Taifa letu la Tanzania ambalo tunalipenda sana ni muhimu mambo haya yachukuliwe hatua. Msione kwamba sauti za watu wanaolalamika ni kwamba ni watu ambao hawana maana, hapana!

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo ambayo yanaendelea tunaanza kuonesha picha mbalimbali za watu wamepigwa risasi, wengine wamepigwa visu, wengine wametupwa kwenye fukwe za bahari maana yake tunawafanya watu wetu wazoee hii hali na huko mbele hata kama hatutakuwepo, makaburi yetu yataulizwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuombe kama Serikali iliyoko madarakani, Chama cha Mapinduzi mchukue hatua ili Watanzania waishi kwa amani na amani ambayo inazungumzwa ionekane ikitendeka kwa maana kwamba tuheshimiane. Kama kiongozi na Mtendaji Mkuu wa Serikali ukusara wa kumi Mheshimiwa Waziri Mkuu amenukuu maneno mazuri sana, anasema; kuna uhuru wa wananchi kujiunga katika vyama vya siasa, kuna chaguzi mbalimbali zimefanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yetu Mheshimiwa Waziri Mkuu ni kwamba tunapoitisha uchaguzi, yule kiongozi ambaye wananchi walio wengi wamesema ndiyo wanamtaka ndiyo chaguo lao, huyo atangazwe aapishwe na awe kiongozi na mwakilishi wa eneo lile ili kupeleka maendeleo na isiwe vinginevyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanataka Sheria za Uchaguzi zifuatwe, wananchi hawataki polisi wengi katika vituo vya kupigia kura. Hilo tunatoa rai lishughulikiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 33 wa hotuba ya Waziri Mkuu, kwenye eneo hili amezungumzia habari ya mifugo na minada na ukurasa huo huo wa 34 amezungumzia mambo ya utalii. Naomba nitoe taarifa kwamba kule katika Jimbo la Ukonga kuna mnada mkubwa sana wa Pugu unaitwa Mnada wa Kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti,Namshukuru Mheshimiwa Waziri wa Mifugo alikuja katika eneo lile. Lakini mnada ule pale ukifika, jina ambalo linazungumzwa kwamba ni Mnada wa Kimataifa haufanani na hali yenyewe ya mnada ule. Pale hakuna maji ya kutosha, hakuna sehemu ya malisho, hakuna uzio, hakuna huduma ya vyoo vya kisasa, ni vurugu match katika maeneo yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tungeomba kama tunataka kupata mapato mengi ya Serikali na ule ndiyo mnada ambao unatoa huduma kubwa katika Mji wa Dar es Salaam basi mnada ule uboreshwe. Lakini sasa imeibuka hoja eneo lile kuna mgogoro unaibuka kati ya mnada na wananchi wa kijiji/Kata ya Pugu Station Mtaa wa Banguro. Hawa watu walipewa hati ya kuwa kijiji na kufanya shughuli zao mwaka 1976 na Mwalimu Nyerere, lakini sasa wameshaishi zaidi ya robo tatu ya eneo lile lote, lakini inaonekana kwamba Wizara ya Mifugo wanasema ni eneo lao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunomba ili kupunguza migogoro, Serikali itumie akili ya ziada, ikae na wananchi wale, tukubaliane. Kama kuna haja ya kuhamisha mnada kutoka eneo lile kwa sababu sehemu ndogo tu chini ya robo ndiyo unatumika kwa ajili ya mnada na sehemu nyingine zaidi ya robo tatu ndiyo wananchi wanaishi basi hiyo kazi ifanyike mapema ili watu waendeshe shughuli zao. Kwanza ilitangazwa kama kijiji, wana hatimiliki lakini Wizara wanasema ni eneo lao pia. Kwa hiyo, huo nao ni mgogoro ambao naamini kwamba ukianza kujadiliwa ilileta shida katika kukwaza shughuli za kimaendeleo, lakini pia kupoteza mwngi sana wa viongozi kwenda kujadiliana katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 44 na 45 inazungumza habari ya barabara. Ninapozungumza sasa maeneo mengi sana ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam na hasa Jimbo la Ukonga Mwenyekiti unafahamu, unatoka Ilala. Sasa hivi Dar es Salaam ile wakati wa mvua haipitiki na bahati mbaya ile mvua ikinyesha kwa muda mchache sana maana yake inaonesha ama miundombinu imechakaa au kazi haikufanyika vizuri. Lakini tunazo barabara kutoka Kitunda - Kivule - Msongola ambapo mkandarasi yupo zaidi ya miezi kumi amechimba mashimo pale. Nimemwambia Waziri anayehusika, nimewaambia watu wa TANROADS pale. Huyu mtu amekaa miezi kumi, amesababisha kero kubwa katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI, kuna hoja inazungumzwa hapa ya TARURA, mimi kwa maana ya Manispaa ya Ilala, hawa watu walipokuja wamefanya kazi kubwa sana pamoja na kwamba kuna ugumu wa fedha. Kwa hiyo, nilikuwa naomba na maoni yetu ni kwamba ingewezekana hii fedha ya TARURA ya TANROADS ikawekwa asilimia 50 kwa 50 kwa sabau barabara nyingi ziko vijijini. Ili barabara zetu zitengenezwe na wakati wa mvua kuwe na mawasiliano iweze kupitika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nikumbushe tu kumekuwa na mambo mengi sana hapa lakini mimi ni Mjumbe wa Kamati hii ya TAMISEMI na Utawala. Tumepata taabu ya kujadili hii habari ya Tunduma. Ningemuomba Waziri Mkuu na Mawaziri wanaohusika kitendo cha ile Halmashauri kukaa zaidi ya miezi kadhaa kutokuwa na vikao hata bajeti ambayo imeletwa maana yake bajeti ile haikujadiliwa na Baraza la Madiwani na Mbunge na wananchi wamelalamika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitokea kuna uharibifu wa mali maana yake Madiwani wanajitoa, watumishi ndiyo wanapata lawama katika utendaji. Hili ni jambo ambalo halikubaliki, lifanyiwe kazi, hatua zichukuliwe. Wawakilishi wa wananchi wafanye maamuzi kwa kodi ya Watanzania wao ili waweze kujipelekea maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Bajeti ya Serikali, maji yamepata asilimia 25.32, afya ilipata asilimia 25, kilimo ni asilimia 18, TAMISEMI yenyewe ni asilimia 31. Katika mazingira hayo ndiyo maana Wabunge wanasema ni muhimu fedha ya maendeleo iliyotengwa mwaka wa fedha 2017/2018 ipelekwe ikamilishe Miradi ya Maendeleo vinginevyo tutakuwa tunapoteza muda hapa. Tunajadili bajeti ya muda huu lakini bajeti iliyopita haijatekelezwa. Mheshimiwa Waziri Mkuu atakaposimama awaambie Wabunge na Watanzania mpaka sasa fedha ya maendeleo imepelekwa kiasi gani katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 48 unazungumzia habari ya elimu. Mimi nimpe ujumbe Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana katika eneo hili kwamba kwanza hatuwezi kuboresha elimu kama tunatunga maswali ya kuchagua mpaka hata maswali ya hesabu kwenye mitihani ye sekondari na kisingizio kikubwa ni kwamba hakuna muda. Haiwezekani tukapunguza uelewa kwa sababu ya kusingizia muda. Tupunguze maswali lakini wanafunzi wetu wapimwe uelewa. Kwa mfano, katika shule zetu za msingi na sekondari, tuna upungufu mkubwa sana wa matundu ya vyoo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kweli inatakiwa Serikali ije na mkakati. Kwa sababu kwa karne hii, Taifa la Tanzania kuzungumzia habari ya matundu ya vyoo kwamba kuna upungufu mkubwa maana yake unawaambia watu kwamba watu wetu wengi, wanafunzi na walimu wanaenda kujisaidia porini na kwa hiyo, wanachafua mazingira, walete kipindupindu na magonjwa mengine ya kuhara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zinaonesha tuna upungufu wa matundu ya vyoo, shule za msingi 239,716; sekondari 19,122, madarasa maana yake watoto wanakaa chini, tuna upungufu wa madarasa 107,547, nyumba za walimu shule ya msingi peke yake ni upungufu wa nyumba 178,435; sekondari 69,816.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inamaanisha bado tunayo safari ndefu sana ya kuboresha elimu. Ukizingatia Sera ya Elimu ni kama kuna mkanganyiko mkubwa sana lakini ningeomba ili tuboreshe elimu mi lazima tunzingatie mambo ya msingi ya mahitaji. Upungufu wa walimu wa sayansi, vitabu, maabara na vitu vingine kama hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwa dhati kabisa, kuna hoja imeletwa nzuri sana ya elimu bila malipo lakini jambo hili limekuwa na mkanganyiko. Tukubaliane, kwa mazingira yaliyopo Serikali haitaweza kujenga madarasa yote yaishe, huo ndiyo ukweli! Serikali haiwezi kutoa chakula kwa wanafunzi wote mashuleni kwao, lakini ni lazima tukubaliane tuwe na lugha nzuri. Tushirikishe wadau mbalimbali ili tuboreshe elimu ya Tanzania. Kumekuwa na hoja hapa ya shule za private na shule za sekondari. Ningeishauri Serikali iweke msimamo kuboresha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha muda wa Mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nimepiga kelele sana humu ndani, nachangia kwa nguvu mno lakini mambo ni yale yale mpaka koo limeharibika sasa, leo nitachangia taratibu sitapiga kelele sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye taarifa ya Mheshimiwa ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Mipango, ukurasa wa 81 alikuwa anamlinganisha Mheshimiwa Magufuli na watu maarufu waliofanya mambo makubwa duniani. Sasa na mimi nimeingia kwenye Google hapa nikajaribu kuangalia, amemtaja mtu anaitwa Park Chung Hee, huyu amezaliwa mwaka 1917 na amekufa mwaka 1979 lakini alikuwa assassinated maana yake aliuwawa. Alikuwa mwanajeshi tangu mwaka 1944 mpaka 1945 na alikuwa cheo cha Jenerali halafu alikuwa ni Dikteta. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mtoto wake pia wa kwanza alikuja akawa mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Korea. Kwenye historia inaonyesha tarehe 10 Machi, 2017 aliondolewa madarakani kwa kupinduliwa kwa tuhuma za rushwa. Historia inaonesha pia tarehe 6 Aprili, 2018, huyu mwana mama aliyekuwa Rais wa Korea (South Korea) amefungwa jela miaka 24 kwa tuhuma za rushwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilipoangalia historia hii nikasema haya maneno inabidi Mheshimiwa Dkt. Mpango ayafute kwa sababu Mheshimiwa Rais wetu hafanani na mambo ya namna hii. Afute maneno haya sio sawasawa. Nadhani Mheshimiwa Dkt. Mpango atakuwa labda ame-quote vibaya lakini hii uindoe historia imekaa vibaya, nilikuwa nataka nianze hapo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitatumia kitabu cha Mheshimiwa Mpango, ukiacha hilo andishi moja tu ambalo nimeona lina shida, ameandika maneno mazuri kwa sababu amekiri vizuri na nitapitia maeneo machache aliyosema ukweli. Nampongeza sana Mheshimiwa Mpango kwa kusema ukweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mpango yeye ni msomi mchumi, mimi ni mwalimu sielewi, ni mwanasayansi tu wa kawaida lakini 2016 uchumi ulikua kwa asilimia 7, mwaka 2017 ulikua kwa asilimia 7.1, mwaka2018 ulikua kwa asilimia 7.2. Mimi naomba Mheshimiwa Dkt. Mpango atusaidie hivi ukimueleza mtu wa kawaida yaani miezi hii kwa mwaka huu kwamba uchumi umekua ataelewa yaani Mbunge wake sielewi, atusaidie Watanzania waelewe, yaani hii ina-reflect vipi maisha ya kawaida ya wananchi? Kwa kweli hii napata nayo shida sana, unaweza ukaeleza hapa na fomula umeandika, wananchi wa kawaida wanataka kuona kama unasema uchumi unakua, mzunguko wa fedha mtaani uwe mkubwa uonekane, bidhaa ipatikane, watu wapate mahitaji ya kawaida. Sasa hiyo lugha hapa mimi siioni kwa kweli unisaidie Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa utalaam wako.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Bajeti ya Serikali 2016/2017 zilitengwa shilingi trilioni 29.5 hazikufika asilimia 80 katika utekelezaji wake. Mwaka 2017/2018 tulipitisha bajeti ya shilingi trilioni 31.7 sasa hivi taarifa inaonyesha ni asilimia 69 labda imeongezeka kabla ripoti haijaandaliwa. Hii bajeti ya sasa hivi ni shilingi trilioni 32.5, naomba unisaidie ni kwa nini tusiende na bajeti halisi? Tumeshatenga bajeti miaka kadhaa iliyopita tumeona fedha yetu ya ndani ni kiasi gani, tumeona misaada ikoje na mingine inakwama halafu tuseme hapa sisi uwezo wetu ni shilingi trilioni 20, tupange mipango ya shilingi trilioni 20. Hapa ndipo malalamiko yanapokuja kwamba tunawapa watu matumaini makubwa, bajeti kubwa, mambo mengi lakini hayafanyiki, inaonekana tunadanganya, nadhani hili pia lifanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine ni kwenye ukurasa wa 14, Mheshimiwa Mpango amesema kiwango kikubwa cha umaskini kimekuwepo kwa Watanzania, ni maneno kwenye kitabu hiki cha hotuba. Anasema ukosefu wa ajira, sasa naomba unisaidie kwa hapa Mheshimiwa Dkt. Mpango. Maduka mengi yamefungwa huo ndio ukweli, watu wamefungwa biashara zao. Kama biashara zinafungwa maana yake mzunguko wa fedha unapungua, wananchi wa kawaida wale ambao waliokuwa wamepata ajira hawana ajira tena, uchumi unakuwaje hapa? Kwa hiyo, katika hili pia mliangalie.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna usafi wa kila Jumamosi, nimeona tu mahesabu ya kawaida, Watanzania wanaambiwa wafunge biashara zao kila Jumamosi asubuhi wanafungua saa nne haijalishi kama kuna famasi, kuna wagonjwa lakini wale mama lishe ambao wanapika chapati, wanaopika supu, huo ndiyo muda wa kupata hiyo huduma na hao wamejiajiri, sasa tunafanyaje hapa. Kwa hiyo, naomba mtuambie hii ratibu ya kila Jumamosi kufanya usafi tumepata faida kiasi gani na hasara kiasi gani ili tuweze kuamua maamuzi mengine tofauti na haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine bar za Tanzania zinafunguliwa saa kumi zinafungwa saa tano usiku. Kule kuna Ma-barmaid walikopata ajira zao lakini kuna biashara zinafanyika wanalipa kodi. Kwa mfano, Dar es Salaam kuna foleni kweli kweli kama wewe umetoka mjini unafika nyumbani saa tatu, yaani unafika mtaani kwetu Kivule, Gongo la Mboto ni saa tatu usiku kwa mazingira ya Dar es Salaam, mwendo kasi haijafika. Maana yake hawa watakaa pale saa mawili wanazungumza bar inafugwa na ma- defender yanakamata watu kweli kweli, hawa watu wanalalamika. Kama kuna sheria ilikuwepo siku nyingi kwa nini isibadilishwe twende na wakati? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu Kenya hapa hao Usalama wa Taifa, Polisi wanatakiwa kuhangaika na watu ambao vipato vyao havijulikani wamepataje. Kama kuna mtu anakunywa, anakula, anavaa vizuri, ana magari mazuri hatujui kazi yake, hiyo ndiyo kazi ya Usalama wa Taifa kuwatafuta watu ambao wana vipato ambavyo havieleweki. Kenya hapo Nairobi huduma ni saa 24, biashara inazunguka, kila mtu anafanya kazi yake, watu wawajibike. Kwa hiyo, tusitengeneze mazingira ya kutisha watu, wafundishwe ustaarabu na wajitegemee na wafanye maamuzi sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 15 amezungumza habari ya kilimo, mifugo na uvuvi na amesema mwenyewe hizi sekta tatu zinawaajiri Watanzania asilimia 66. Sasa nimuulize Mheshimiwa Dkt. Mpango kwenye bajeti hii malalamiko yote ambayo Wabunge wamesema kwenye kilimo watu wamelima mazao ya pamba, tumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu amechukua hatua lakini hata mahindi mpaka unaenda kwenye msimu mwingine haya mazao bado yapo mtaani. Mifugo imepigwa, imeteswa hakuna malisho, hakuna sehemu ya kuchungia, ugomvi na wakulima, Operesheni Sangara, leo mmezungumza habari ya samaki, haya mambo Mheshimiwa Mpango mngeyachukua mkakae pamoja mkayafanyia kazi mkatengeneza Taifa ambalo tunataka kwenda mbele badala ya kurudi nyuma tusirudie mambo yaleyale ya kila siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, iko hoja hapa Mheshimiwa Jenista ametoka nje, tulipokuwa tunajadili habari ya kuunganisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii tulilalamika hapa kwamba ile formula iingizwe kwenye sheria. Waheshimiwa Wabunge ile formula haijaingizwa, sasa hivi kuna ugomvi mkubwa kati TUCTA na Serikali na wameshusha, ilikuwa 1/540 sasa imeenda 1/ 580. Mafao kwa mkupuo ilikuwa asilimia 50 kwa formula hii ambayo inalazimishwa wataalipwa asilimia 25,. Kwa mkupuo walikuwa wanalipwa asilimia 50 imeshuka zaidi ya nusu kwa yale mafao na kuna ugomvi mkubwa. Tulilalamika sheria iingizwe haijaingizwa wametunga kanuni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ina madhara kwa sababu hawa watumishi ambao, kwa mfano watu wa LAPF, PSPF wanaidai Serikali siyo chini ya shilingi bilioni 600 za madeni hayajalipwa na huu mzigo ni wa Serikali, hawa wastaafu wanachama wa vyama hivi ndiyo wataingia kwenye mzigo huu na hili ni janga la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama hauongezi mshahara Mheshimiwa Dkt. Mpango hawa wakienda kustaafu calculation ya mafao yao mwishoni inategemea increment ya kila mwezi. Ndiyo maana tunasema fuateni taratibu watu waongezwe pesa zao zitawasaidia siku za mbele katika maisha yao. Watu wanakufa haraka kwa sababu ya kukosa huduma nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nishauri jambo muhimu sana hapa, kwa mfano, kwenye Wizara ya Elimu ametaja data ndugu yangu Mheshimiwa Paresso sitaki kurudia yaani ukiangalia figure ya matundu ya vyoo, madarasa, nyumba za walimu, upungufu wa walimu, mimi nadhani Mheshimiwa Dkt. Mpango akija atuambie kwenye bajeti hii haya mambo yatatekelezwa kwa kiasi gani. Wabunge wamelalamika mmechukua kodi ya majengo, kodi ya mabango kwenye maeneo mbalimbali tumeathirika, haujarudisha asilimia Mheshimiwa Mpango, ungetuambia fedha hii imerudishwa kwa kiasi gani, haya mambo yangefanyika ingetusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nishauri jambo muhimu sana, kuna maneno mengi sana yanaendelea na kwa sababu mambo yanafanyika kwa haraka haraka sana kwa mazingira fulani hisia zinakuwa nyingi sana mtaani. Kwa mfano, mimi nimesoma ule Waraka wa Watumishi wa Mungu wa Waislam na Wakristu, mambo ambayo yametajwa, wanashauri hivi, tuwe na utawala bora, tufuate sheria, hii nchi haiongozwi kwa Ilani za vyama na matumizi mabaya ya dola. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, hivi haya mambo ya kutishiana, haya mambo ya kufuata utaratibu kuna kosa gani, Taifa hili humu ndani tumebaguana sana kivyama. Wabunge wa CCM, Wabunge wapinzani wakijadili wanadhani wengine wana haki zaidi kuliko wenzao kumbe Taifa ni la kwetu sisi wote. Tungeona tu kwamba hawa watu wanashauri, mimi nikitoa hoja ingepokelewa kwa nia njema kabisa kwa kujenga Taifa. Hii bajeti ni ya kwetu na ikipita siyo ya CCM ni bajeti ya Watanzania, iwe tumeunga mkono au hatujaunga, tusaidieni kupeleka Taifa mbele kwa kutuunganisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Naomba niseme tu kwamba kwa mara ya kwanza nasimama kwenye Bunge lako Tukufu kuchangia nikiwa mtu huru sana. I will speak out my mind. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, neno la kwanza ni kwamba unajua life is real, kuna maisha halisi na kuna maisha ya kuigiza. Kwa hiyo, kwenye mijadala humu Bunge, Mheshimiwa Mpango na Serikali wajue kwamba kuna watu wanazungumzia maisha ya watu na kuna watu wanazungumzia maisha yao. Wale waliopewa dhamana hiyo ya kuzungumza mambo ya Watanzania, wanyonge, maskini wafanye hivyo, wasikilize kidogo wa-base kwenye mambo ambayo wameamua wao ambao ndiyo mkataba kati yao na Watanzania walio wengi, hili ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hiyo naunga mkono miradi yote ambayo imetajwa hapo ya kimkakati, ujenzi wa reli, Shirika la Ndege na umeme wa maji wa Rufiji. Ni muhimu watu wajue kwamba haya yote, kujenga reli, kuliboresha shirika la ndege na umeme wa maji ya Rufiji wala hauhitaji Katiba Mpya. Kwa hiyo, haya yatekelezwe mapema, wale ambao wanasubiri Katiba Mpya watafanya watakapopata Katiba Mpya, kwa sasa haya yafanyike, huhitaji Katiba Mpya katika kutekeleza haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini liko suala la maji. Wenzangu walipokuwa wanazungumza, maana leo nimepata uzoefu mpya kabisa, mimi ni Mwalimu, yaani ni kama ulikuwa unawafundisha wanafunzi halafu unampa mmojawapo swali halafu unakaa unamsikiliza, nimewa-enjoy sana ndugu zangu wale watasubiri kweli, watasubiri sana. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mchangiaji mmoja anasema kuna mradi wa maji kule Njombe haujakamilika au umekamilika lakini hautoi maji lakini anasema hatua hazikuchuliwa. Mwingine anasema watu hawana amani, watu wana vinyongo yaani wana hofu hofu. Kwa nini mtumishi wa umma, kama ni Mkuu wa Idara ya Maji, Injinia wa Maji una hofu wakati ni mtaalam na umepewa dhamana katika eneo lako? Unasema mradi umekamilika lakini hautoi maji, huyo ambaye amekula pesa awajibishwe na hapo ndiyo inakuja dhana ya kutumbuana, hHuyu hawezi kuonewa huruma. Kama tunazungumza habari ya maji hayapatikani lazima miradi ya maji ikamilike na wale ambao hawakutimiza wajibu wao wawajibishwe na hiyo ndiyo kazi ya Serikali ya Awamu ya Tano, naunga mkono jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo la maji likifanyika nchi nzima, kila jimbo, kila wilaya, kila mkoa maana yake habari ya upinzani haitasikika, watu wataimba CCM wataimba Magufuli, wataimba Majaliwa, wataimba Ndugai, hakuna mjadala, watu wanataka maji hawataki Katiba Mpya. Nani ameitisha mkutano watu wakawaambia alete Bungeni suala la Katiba Mpya, watu wanataka maji, barabara, hayo maneno ya Katiba Mpya ni yao, wananchi kule mtaani wanataka waondolewe kero zao. Hiyo ndiyo kazi Mheshimiwa Magufuli anayoifanya na sisi tunamuunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwamba kule Ukonga kuna shida ya majia miradi inaendelea na kwenye mpango huu imetajwa katika Mkoa wa Dar es Salaam kuondoa kero ya maji ikiwepo Jimbo la Ukonga, Temeke, Kigamboni na Ubungo. Hata na Majimbo mengine kule ambayo wenzangu wapo, akina Mheshimiwa Mnyika na wengine na CCM kwa kweli pale haijabagua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu. Kuna mwenzangu mmoja hapa amesimama akasema hakuna ajira, mimi nilikuwa naangalia kwenye mtandao wa ajira. Kwa mfano Serikali imekarabati Shule Kongwe za Jangwani, Azania, Pugu, Kilakala, Vyuo vya Ualimu, Tarime TCC, Mbeya kule Mpuguso, hii kazi imefanyika na mabilioni ya fedha zimetumika. Tunapozungumza kuna walimu wapya wa sekondari wameajiriwa zaidi ya 4,800 wa hesabu na masomo ya sayansi. Kuna nyumba za walimu zimejengwa, maabara, hosteli za wasichana, kule kwangu Mbondole imejengwa. Haya mambo lazima ukubali na upongeze kidogo. Sisi wengi hapa ni Wakristo hasa upande ule unatakiwa ushukuru hata kwa kidogo. Kuipongeza Serikali ni kuipa moyo kwamba hapa umetatua kero hii lakini bado kuna hili na lile si dhambi. Sasa ukikaa hapa unajadili habari ya kupongeza inaonekana siyo sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la elimu. Elimu, kwa maana ya shule ya elimu ya awali, shule za msingi na sekondari Serikali imefanya vizuri sana baada ya kuondoa ada na kutoa ile elimu bure. Sasa kuna vyuo vya ufundi na teknolojia, kuna vyuo vya elimu ya juu, hapa inabidi Serikali iweke nguzo. Unapozungumza habari ya ajira, ukiwa na vyuo maana yake ni kwamba utapata vijana wengi wakimaliza form four, form six, watakuwa na ujuzi watajiajiri hawatasubiri ajira ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile lazima Serikali ichukue hatua. Kuna mchingiaji mmoja jana amesema kwamba mikopo ya elimu ya juu itolewe na benki, benki haiwezi, hawa ni vijana wamemaliza shule hawana kazi, wanakaa mtaani muda mrefu. Kwa hiyo, lazima Serikali yenyewe ichukue wajibu wa kusomesha Watanzania watoto wa maskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vigezo vya mikopo ya elimu ya juu, naipongeza sana Serikali kwa sababu wakati nikiwa Rais wa Mlimani 2005/2006 tulikuwa tunagoma ndipo unapata mkopo. This time around vijana wanakaa kwenye mabweni yao, fedha zinaingia, wanaenda kwenye mitandao Serikali imefanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, cha muhimu vigezo viangaliwe habari ya kuambiwa tu kwama baba yake alikuwa mtumishi amestaafu amesoma private sasa hawezi kupata mkopo siyo sawasawa. Mimi hapa ni Mbunge na wenzangu kesho nikistaafu maana yake kipato hiki hakipo, mwanangu atakosa mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani vigezo viangaliwe na hali halisi ya mazingira kulingana na wakati. Suala la kuwasomesha vijana wa Tanzania, ni jambo mahsusi, ni jambo maalum lisimamiwe na litekelezwe. Watoto ambao wamefaulu kwenda vyuo vikuu wasibaki mitaani hawasomi itakuwa si sawa, hilo tunaliunga mkono lifanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, afya. Kuna mtu jana anasema kwa nini mnazungumza habari ya vifaa tiba. Tukubaliane kuwa wakati tunapanga kupunguza maradhi ya aina mbalimbali katika hii nchi ni lazima pia haya yaliyopo tuyatibu na kujipanga vizuri, hili jambo ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia takwimu, kwa mfano wamejenga nyumba za madaktari 313, vituo vya afya 350, zahanati mpya 38, hospitali za wilaya 221 na Kivule Ukonga ipo na Bunda kule kwa Mheshimiwa Ester Bulaya ipo, imetajwa hapa na fedha zimepelekwa. Sasa katika eneo hili lazima tukubali kwamba kazi inafanyika kubwa, tuunge mkono wenzetu lakini tuboreshe namna ya kwenda mbele, hilo ni jambo la msingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo la vijana, wanawake na walemavu...

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema kwamba life is real na niko kwenye maisha halisi, nimerudi kwenye enzi zangu na I will speak out my mind throughout this Bunge, kwa hiyo hakuna shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali itajitahidi, kuna suala la vijana, akina mama na walemavu, zile asilimia nne kwa akina mama, nne kwa vijana na mbili kwa walemavu, changamoto kubwa ni kwamba mahitaji ni makubwa kuliko uwezo uliopo na halmashauri zetu hazina uwezo kwa kuwa zina shughuli nyingi sana. Serikali iangalie namna ya kupata fedha iwezeshe makundi haya maalum, hawa ndiyo wapiga kura na ndiyo Watanzania. Hawa akina mama, vijana na walemavu wakiwezeshwa watapungaza utegemezi, wakienda kupiga kura wataiunga mkono Serikali kwani imewawezesha. Hili lifanyiwe kazi haraka sana na halihitaji Katiba Mpya, linahitaji utashi na maamuzi na fedha itafutwe ifanye kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala bora, hapa nina maneno kidogo. Kuna watu hapa wamesimama mtu anaita mkutano wa hadhara anatukana mwanzo mpaka mwisho, akikamatwa anasema ameonewa, nani kamtuma akatukane watu kwenye mkutano wa hadhara? Ameita waandishi wa habari anasema watu wameuawa, sisi tunakwambia tusaidie uthibitishe waliouawa unasema unaonewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wanazungumza utawala bora, tarehe 4 Novemba, Kambi Rasmi ya Upinzani ya CHADEMA walikutana maana wana urafiki wa mashaka kati yao na CUF walikutana. Yuko Mheshimiwa Zitto, Mheshimiwa Mbowe, Mheshimiwa Nyarandu, yuko na mwingine wanapanga namna ambavyo Bunge hili, yaani kikao chako hiki Mheshimiwa Mwenyekiti kitavurugwa na maazimio yao wanapanga hata kwenda nje.Sasa kama mnakubaliana, mnapanga namna ya kuvuruga mahusiano ya kimataifa na mnamtuma Nyalandu aende, halafu hapa mnatuambia habari za utawala bora, mnataka mwongozo wa Spika; nakushukuru Mwenyekiti kwa kupiga chini taarifa zisizo na maana hawawezi kutuingiza huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nashukuru. Unapozungumza habari utawala bora ni lazima uanzie ndani. Ni muhimu sana na lazima tukubaliane. Hatuwezi kuwa na Watanzania wanakutana kwenye magenge yao, wanapanga kuvuruga amani ya nchi, wanapanga kuvuruga mahusiano, halafu wanakuja Bungeni ili tupoteza muda kujadili mambo yao. Wamepanga wao, wamejadili wao, watupoteze muda, hatuwezi kuruhusu mjadala ukafanyika humu ndani. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mambo ambayo tunamuunga mkono Mheshimiwa Dkt. Magufuli ni namna ambavyo anaweza kuchukua hatua kwa watu ambao wamefuja mali za nchi.

Kama kuna watu wanafanya biashara hawafuati utaratibu, hawalipi kodi wamevuruga miradi wakikamatwa wanasema hawana amani, wahalifu lazima washughulikiwe, hata Mwalimu Nyerere alifanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Azimio la Arusha lilikuja kuwawajibisha watu ambao ni wazembe, sasa Mheshimiwa Dkt. Magufuli amewaelekeza watendaji wenzake na hili linahusu ma-DC na Wakuu wa Mikoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya Mbunge ni tofauti na kazi ya DC na RC, wale ni executive, kama kuna mahali kuna mradi haujafanyika mtu amesimamia jengo limekuwa hovyo hovyo anakamatwa anaisaidia Serikali ili kazi ifanyike.

Kwa hiyo, nidhamu ni muhimu sana.

Naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais amefanya ziara kule Nyamongo, amesema wananchi watalipwa fedha zao za muda mrefu. (Makofi)

Sasa yameshughulikiwa wananchi wanaishi kwa amani. Mheshimiwa Dkt. Kigwangala nenda ukashughulikie mambo haya msingi yaishe. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na kwa mara ya kwanza katika historia ya Bunge, naomba niunge mkono hoja kwa nguvu zote asilimia mia moja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naunga mkono hotuba ya Kiongozi wa Upinzani Bungeni; naunga mkono pia hotuba mbili za Utumishi na mambo ya TAMISEMI kwa Wasemaji wa Upinzani Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo kadhaa hapa ya kuzungumza. Kuna hoja hapa ya ndugu yangu, Mheshimiwa Angellah Kairuki aliyowasilisha, ya Utawala Bora; ndiyo nataka nianze nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala bora ambao unazungumziwa ni muhimu tungeanzia hata humu ndani kwenye Bunge hili kama kweli kuna utawala bora. Bunge limengolewa meno, limekuwa butu kweli kweli!
Bunge limekuwa kibogoyo! Bunge limekuwa na watu waoga kweli kweli! Wabunge hawana uhuru wa kuzungumza na kutoa maoni yao! Hili Bunge ni aina ya Mabunge ambayo hayajawahi kutokea, labda hii ndio kazi tu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya masuala ya UKIMWI na Dawa za Kulevya. Nimesikiliza Wabunge wa CCM wengi waliopangwa kwenye Kamati ile. Inaonekana walipangwa na Mheshimiwa Spika kwa maelekezo na naambiwa kwamba kikao kilikaa, wale wengi ambao walikuwa wanamuunga mkono Mheshimiwa Lowassa walitupwa kwenye Kamati yangu na mimi naipenda sana, kama sehemu ya kuwaadhibisha. Maana yake hiyo kazi Spika aliifanya kwa maelekezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Naibu Spika mwenyewe ningependa awe hapa. Jana alimwita Mheshimiwa Mbunge mwenzetu hapa bwege. Akamwambia aache ubwege! Yaani bwege asionyeshe ubwege!
Kwenye kikao cha Bunge jana! Ilizungumzwa, wala siongei uongo. Hapa nitaongea mambo ya ukweli tupu. Alisema Mheshimiwa Bwege, naomba uache ubwege. Sasa wataalam wa Kiswalihi wanaweza wakasaidia.
KUHUSU UTARATIBU......
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuelewa na nitazingatia ushauri wako. Kwa hiyo, maneno yote yale yameondolewa eeh! Mnapenda sana hiyo eeh!
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba muda wangu ulindwe.
Hoja yangu tu ni kwamba, Bunge hili Waheshimiwa Wabunge hawana uhuru, wanapigiwa pigiwa simu, haijalishi nani amepiga lakini wanapigiwa na watu wa ngazi ya juu kwa kuwatishatisha ili wasiwe na uhuru wa kutoa maoni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye taarifa mbalimbali za ukaguzi inaonyesha kwamba hata Ikulu yenyewe kunakuwa na rushwa. Taarifa mbalimbali zipo, wala hili huwezi kupinga. Sasa kama Mheshimiwa Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba Ikulu ni mahali patakatifu, kama kuna chembe chembe za rushwa kwa nyakati mbalimbali, sasa huo utawala bora utawaelezaje watu wa kawaida kama kule jikoni kwenyewe chakula kinaibiwa, watu wananyofoa minofu jikoni...
Tutafanyaje katika mazingira hayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ulizikataa, nakushukuru sana.
MHE. MWITA M.WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nashauri pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kaka yangu, sisi watu wa kule kwetu huwa hatuogopi kusema ukweli. Namshauri Mwanasheri Mkuu wa Serikali, asiwe anatoa tafsiri za sheria za ki-CCM atoe tafsiri za kisheria za sheria in profession. Namshauri sana maana yake nimevumilia imebidi niseme tu hadharani kwamba ni muhimu Mwanasheria aseme sheria za kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, hapa kuna mambo yanaelezwa, sisi tulichosema ni kushauri kwamba katika mambo kadhaa yaliyofanyika, Mheshimiwa Rais hajafuata utaratibu kwa maana ya kutumia mamlaka yake vibaya, kwa maana ya kufanya reallocation ya fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ushauri na sheria hizi zipo, utakuja na tafsiri nyingi sana kwa maana ya kuficha mambo, lakini ukweli unabaki pale pale. Naomba nitaje kwa mfano, Katiba ya Nchi Ibara 18(a), (b) na (c) kinaeleza uhuru wa kupata habari; tena unasema hata nje ya mipaka ya nchi. Hili jambo huhitaji kupata mkalimani, inaeleweka tu, kwamba Watanzania wamenyimwa fursa ya kupata taarifa ya Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapanga wananchi hawa walipe kodi, tunawashawishi namna gani? Hawa jamaa wa CCM wameenda wamekaa kwenye mkutano wao, wanaaminisha watu kwamba ooh, watu wa Upinzani tutaonekana. Hii siyo hoja! Ni hoja ya kitoto kabisa! Hoja hapa ni kwamba ni kwa nini kama kweli mnafanya kazi vizuri, wananchi wasiwe na uwezo wa kujadili na kuona tunachokiona? Nawa…
MWENYEKITI: Ahsante, muda wako… Aalah! (Kicheko)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kengele ya kwanza. Nakushukuru! Naona sasa unaanza kunitania! Aisee! (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Hoja nyingine, ukisoma Ibara ya Katiba ya 135, mambo yale ya Hazina inaeleza, Katiba ya Ibara ya 146(1) inaeleza, vitu vingi vimezungumzwa.
Niende kwenye hoja ya TAMISEMI; kuna jambo la bodaboda hapa; hawa vijana na hasa Dar es Salaam. Sasa hivi kuna uhalifu mkubwa, vijana wetu walishawishika, wengine wamechukua mikopo, wanajikopeshea fedha zao kwa watu binafsi na wengine VICOBAvile wanapata fedha ya kujiendeshea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na mitindo wa kusumbuliwa sana Dar es Salaam pale! Kuna watu wameitwa Askari wa Jiji, nadhani wale tutawashughulikia kwa sababu Jiji la Dar es Salaam tunaongoza sisi, nami ndio Mwenyekiti wa Mkoa, naelekeza sasa, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, hili jambo alifanyie haraka mapema sana. Hawa vijana wanapata shida kule Dar es Salaam, wanakamatwa hovyo, wanasumbuliwa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameenda kuteua hawa Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa, Ma-RAS waliostaafu Majenerali. Sasa hawa vijana ambao wanahitaji hapa ajira, si angewapa kazi hao vijana! Humu ndani kuna Wabunge wana vyeo viwili viwili; yaani mtu ni Mbunge halafu ni DC, halafu ajira ni shida! Hivi huyu mwenye vyeo viwili ana nini? Ana pembe kichwani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wanyang’anywe vyeo, tugawane kilichopo. Mtu amefanya kazi, amestaafu, anapewa kazi nyingine tena, halafu mnataka ufanisi! Watu wameshachoka, wanasinzia ofisini mnawapa kazi nyingine. Hii kitu kwa kweli vijana hawa msiwanyanyase na utaratibu uwekwe sawa sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti ya Manispaa ya Ilala tumekadiria kukusanya shilingi bilioni 85 ikiwepo kodi ya majengo na mabango lakini shilingi bilioni 28; Shilingi bilioni 18 majengo na Shilingi bilioni kumi ni mabango. Maana yake huu mpango, kwenye hotuba ya Waziri wa TAMISEMI inaeleza kwamba Halmashauri itasimamia, kwenye Mpango wa Waziri wa Fedha inaonyesha vinginevyo. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind-up hapa aeleze kipi ni kipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Manispaa ya Ilala ilifanyiwa ukaguzi mwaka 2011/2012 - 2012/2013 lakini na hii ya leo nimeisoma, Manispaa ile inaonekana ni miongoni mwa hati isiyoridhisha. Sasa haya mambo, walikaguliwa watu 2011, Mkaguzi Mkuu alikagua, akaleta taarifa; lakini ninavyozungumza hapa, tuna vitengo na idara zaidi ya 18 lakini viongozi wale watano tu ndio wamethibitishwa, wengine wote wanakaimu. Nimejaribu kuhesabu hapa, karibu 13! Sasa katika mazingira hayo, tunafanyaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, siungi mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayofanya pamoja na Waziri Mheshimiwa Angellah Kairuki, Mheshimiwa Jenista Mhagama; Manaibu, ndugu yangu Mheshimiwa Mavunde na Mheshimiwa Stella Ikupa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Mheshimiwa Rais, Mawaziri wote na Wabunge wote wa Chama cha Mapinduzi kwa kuendelea kusaidia kusimamia utekelezaji mzuri na murua wa Ilani ya Uchaguzi wa mwaka 2015 - 2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajibu yale maswali ya jumla sana kwa sababu ya muda, yako mengi lakini nitajitahidi. La kwanza, imezungumzwa hoja hapa ya TARURA. Tumefurahi sana kama Wizara kwamba kila Mbunge aliyesimama kuchangia humu alipongeza kazi kubwa na nzuri ambayo inafanywa na Wakala wa Barabara wa Mjini na Vijijini ya TARURA. Ila changamoto iliyokuwepo ni upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe tu taarifa kwamba tayari imeshaundwa timu ya Kitaifa ya kutambua barabara, itafanya kazi yake baada ya kuleta mrejesho wa kitaalamu. Sasa tutapitia upya kuangalia mgao ule wa asilimia 70 ya TANROADS na asilimia 30 ya TARURA ili hawa watu waweze kuongezewa fedha na waendelee kuimarisha barabara zetu za mjini na vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo limezungumzwa ilikuwa ni hoja juu ya maboma ya afya. Kwenye bajeti ya mwaka 2017/2018 tulikamilisha maboma 207 na vituo 552 vimeendelea kuimarishwa. Kwenye bajeti hii ambayo imeletwa, nadhani kuanzia kesho, tumetenga fedha zaidi ya shilingi bilioni 10 kujenga Vituo vya Afya vingine vipya 52, lakini mbali na hizo hospitali 67 za mwanzo za mwaka huu ambazo tunamalizia, hapa pia tumetenga bajeti ya hospitali nyingine mpya 27. Kwa hiyo, kazi ile inaendelea kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu leo swali la msingi hapa ni kwamba kuna maboma mengine ambayo wananchi wameendelea kujenga bado Serikali hii ya Awamu ya Tano ina nia njema kabisa kuendelea kusaidia kuyakamilsha ili huduma ya afya iendelee kuimarika katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, amejibu Mheshimiwa Waziri wa Elimu kwamba kuna maboma ambayo yamekamilishwa lakini ile ni bajeti ya 2016/2017. 2018/2019 tunapeleka vifaa vya maabara kwenye Shule za Sekondari 1,250; lakini kama ambavyo inajulikana pia mwezi wa Kwanza Wizara ya TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia mradi wa EPFR tumeshapeleka fedha, shilingi bilioni 56 kwenye Elimu ya Msingi na Sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi wa Pili pia tumepeleka fedha shilingi bilioni 29.9 ili kukamilisha maboma. Hapa ninapozungumza tupo kwenye mchakato pia kupeleka fedha nyingine kumalizia maboma ya Shule za Msingi, Walimu na watumishi wengine wa Serikali. Kazi kubwa inaendelea kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja ya asilimia 10. Naomba nitumie nafasi hii kuwapongeza sana Kamati ya Utawala na TAMISEMI ya Bunge hili Tukufu. Katika bajeti hii ambayo imewasilishwa ya mafungu ya Wizara ya TAMISEMI kila Mkoa Wakurugenzi wote walilazimika kutoa maelezo ya ziada, kila mtu aeleze mpango aliyonao wa kukusanya asilimia 10 kwa vijana, akina mama na watu wenye elemavu, pia kuonyesha ameshafikisha asilimia ngapi na adhabu mbalimbali zimetolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nilitaarifu Bunge kwamba katika kipindi hiki baada ya Bunge hili Tukufu kufanya mabadiliko makubwa ya sheria kifungu Na. 35, kwa kweli usimamizi umeimarika zaidi. Mwaka 2016/2017 fedha za mikopo zilizoenda kwenye makundi haya matatu maalum, tulipeleka shilingi 8,917,700,164/=.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2017/2018 ile asilimia 10 ilipelekwa kwenye vikundi, shilingi 27,402,737.81. Kwenye vikundi 10,000 imeenda 72, lakini niseme tu, bahati nzuri sana naomba niwapongeze akina mama wa Taifa hili wamekuwa waaminifu sana na wamekopa sana kuliko vijana na watu wengine wote. Namba yao ilikuwa kubwa. Pia hata kwenye marejesho akina mama wamekuwa waaminifu, wamerejesha sehemu kubwa. Tunaomba waendelee kuhimizwa, waelimishwe kwa weledi, wakope ili waweze kujikwamua kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka mwezi Februari mwaka huu, 2019 tumeshakusanya fedha, zinapelekwa kwenye vikundi, shilingi 21,423,619,000/= zimeshaenda kwenye makundi hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru sana kwamba sasa, baada ya maelekezo ya Kamati ya Utawala na Bunge hili Tukufu, kanuni za kazi hii zimeshaandaliwa, zipo kwenye hatua ya mwisho, lakini maelekezo yametoka kwamba sasa kutakuwa na akaunti maalum ambayo fedha hizi zikikusanywa ni lazima ziingizwe pale. Kwa hiyo, kuna ujanja unafanyika wakipeleka fedha kwenye vikundi, fedha za marejesho wanajumlisha wanakwambia ni asilimia zaidi ya 100. Tukasema hapana, ili tutenganishe, kutakuwa na akaunti mahususi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zinazokusanywa ziingizwe kwenye akaunti hiyo, zikipelekwa kwenye vikundi zipelekwe hivyo na zikirejeshwa zionekane ili tuweze ku- control. Kwa hiyo, kazi inamalizika na watapewa maelekezo mahususi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja hapa ya posho ya Wenyeviti wa Mitaa na Madiwani. Naomba nijibu hoja hizo mbili kwa mkupuo. Juzi niliulizwa swali hapa, nirudie kwamba Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji na Wajumbe wao, kabla ya kufanya uamuzi wa kugombea ni lazima wakidhi sifa na vigezo vilivyo kwenye kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inaelekezwa kwamba mgombea au Mwenyekiti wa Kijiji, Mwenyekiti wa Kitongoji, Wajumbe wa Serikali za Mitaa na Wahumbe wa Halmashauri za Vijiji ni lazima wawe na kipato ambacho kinawawezesha kuishi. Kwa hiyo, ni lazima mtu apime uwezo wa kuhudumia. Kazi hii kimsingi ni kazi ya kuijtolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunatarajia pamoja na hoja mbalimbali zilizopo kwamba waongezwe posho, cha kwanza ajue kwamba ni kazi ya kujitolea na apimwe kwa uwezo wake wa kusimamia ili pia kuepuka hata ubadhirifu mbalimbali ambao unaendelea kwenye maeneo yetu ya Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya posho ya Madiwani ni kweli. Posho ya Diwani kwa mwezi ni shilingi 350,000/=. Kwa Wenyeviti na Mameya ni mpaka Shilingi 400,000/= ukomo. Kila Halmashauri imejipangia utaratibu wa posho mbalimbali kwenye vikao vyao. Tumetoa maelekezo kwamba imeonekana kwamba kuna Halmashauri nyingine wanalipa fedha kubwa sana, nyingine ndogo, kama ilivyo kwa Wabunge. Hata kama utaenda mahali gani, lakini ile per- diem unayolipwa na sitting inatambulika. Kwa hiyo, ikawekwa flat rate. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ni maelekezo ya Mheshimiwa Waziri kwamba kuwe na flat rate kwenye Halmashauri zetu. Kuna malalamiko, kuna barua tumepata, lakini ni kwamba ile posho ya kawaida Diwani atapewa; hizi posho za vikao na kulala, iwe standard. Kwa sababu kikao wanachokaa Dar es Salaam na sehemu nyingine ni ile ile, ukumbi ni ule ule. Kwa hiyo, kumekuwa na double standard ile. Kwa hiyo ndiyo maelekezo. Haki zao nyingine zile zipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, posho za Wenyeviti wa Mitaa zinatofautiana. Kwa mfano, mimi ni Mbunge wa Ukonga, Ilala. Kule tulikuwa tunalipwa posho shilingi 40,000/=, lakini kwa sababu ya mapato ya Halmashauri ya Ilala tumepandisha mpaka shilingi 100,000/=. Kwa hiyo, kuwalipa Wenyeviti wa Mitaa inategemea na Halmashauri inapata kiasi gani? Hao hao inabidi wasaidie pia katika kukusanya kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo mengine wakitumwa kusimamia kodi hawasimamii, lakini ukweli ni kwamba Watanzania wote wanapaswa kulipa kodi ili miradi ya maendeleo iweze kukamilishwa. Hawa nao wasaidie kukusanya kodi, kuibua vyanzo, wakaangalie watu walinde miundombinu, fedha zitapatikana, watalipwa zaidi ya hiyo ambayo ipo katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo imezungumzwa hapa, kulikuwa na hoja ya nyumba za wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa. Kwenye bajeti ya mwaka 2019/2020 tumetenga zaidi ya shilingi 4,626,000,000/= kwa ajili ya kujenga nyumba mpya na kukarabati. Kulikuwa na hoja hapa nadhani eneo la Liwale, wametengewa fedha zaidi ya shilingi milioni 330 kwa kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna hoja ya magari ya Ma-DC, Wakurugenzi na Wakuu wa Mikoa. Naomba nitoe taarifa kwamba jambo hili tunalitambua na Serikali inaendelea kuhimiza, tutakuwa tunanunua magari kulingana na uwezo Serikali kadri muda unavyoenda. Vile vile viongozi hawa wamepewa dhamana kubwa katika maeneo yote ya Serikali za Mitaa, hawatakwama kufanya kazi zao. Tutafanya kila linalowezekana ili waweze kufanya kazi na waweze kufika maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetoa ushauri, kuna Wilaya nyingine ni kubwa sana kulingana na jiografia yake na mazingira ya miundombinu ile. Kwa hiyo, tunatakiwa tuangalie vipaumbele kulingana na uwezo kadri ambavyo itakuwa inawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo ilijtokeza hapa walizungumzia ahadi za viongozi mbalimbali. Naomba tuwahakikishie kwa kasi hii ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali ya Awamu ya Tano na ushirikiano mzuri wa Wabunge wa Chama cha Mapinduzi ahadi zote za viongozi na Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Mawaziri wote zitatekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nilikuwa nataka nizungumzie hoja ambayo imejitokeza hapa. Kumekuwa na hoja kwamba nikiwa nazungumza wananiambia ongea kama Naibu Waziri, lakini nimeambiwa hapa kwamba inawezekana nafasi hizi tumehongwa. Nadhani nijibu hii hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri nina uzoefu wa pande zote mbili; upande wa Upinzani na upande wa Chama cha Mapinduzi. Naomba niwapongeze Wabunge wa Chama cha Mapinduzi kwa kazi kubwa mnayofanya. Naomba niwaambie, kwa uzoefu ambao nimekaa miaka kumi upande huo, upinzani wa nchi hii bado sana. Bado sana kwa kweli wanapaswa kujipanga. Kwa kasi hii iliyoko sasa ya kuweka miradi kila mahali, hii kasi nadhani wanatakiwa kujipanga zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba ni kweli, kunaweza kuwa na hoja pinzani lakini wali wa kushiba unaonekana kwenye sahani. Nani hamjui Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli? Nani anaweza kupambana naye? (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mazingira haya, sisi tuchape kazi.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie Wabunge wa Viti Maalum wa Chama cha Mapinduzi. Nilikuwa nafuatilia trend ya Wabunge wa Upinzani hasa wa CHADEMA wale na Wabunge wa CCM, big up sana Wabunge wa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila Mbunge wa CCM akienda kwenye mkoa, mara amechangia cement, amepeleka mabati, amewezesha vikundi, ametoa elimu ya uraia, akisimama hapa anachangia vizuri. Kwa hiyo, hii ndiyo tofauti kubwa kati ya nyie akina mama wa hapa na Wabunge wa Viti Maalum kule. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, unajua wale watu wana msongo wa mawazo, siyo mikopo tu, hatima yao ya mwaka kesho. Hali ni mbaya! Kwa sababu kuna Wabunge hapa walishaanza kuaga kwenye Majimbo yao. Mbunge wa Tanga alizungumza juzi kwamba ni Mbunge wa kwanza wa Upinzani, akashindwa kumalizia kwamba Mbunge wa kwanza wa Upinzani na wa mwisho anaaga pale Tanga. Kwa sababu tunafanya replacement, wala siyo kunyang’anywa. Hawatanyang’anywa Ubunge, lakini watu wanaangalia, Watanzania wanaona kwa kazi ya Mheshimiwa Rais, miradi mikubwa inayofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nani anaweza akasimama akaponda ndege kweli? Nani anaweza akaponda? Unaponda ndege halafu unaenda unapiga selfie unaturushia tuangalie. Unaponda reli, Mbunge unatoka Morogoro pale, ikianza ile maana yake hata mabasi yale na nini havitakuwepo. Speed ndogo, unalala Morogoro, unafanya kazi Dar es Salaam. Ikianza Dodoma, unalala Dodoma unafanya kazi mahali popote pale. Haya ni mambo ambayo yanapaswa kuungwa mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwangu tu ni kumwambia Mheshimiwa Rais aendelee na kazi hii, Waheshimiwa Mawaziri na Waziri Mkuu, Makamu wa Rais, Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, nyie ndio wenye dhamana ya nchi hii, Watanzania wamewaamini, wamewapa kura za kutosha. Kelele za chura hazimzuii ng’ombe kunywa maji na kelele za mlango hazimzuii mwenye mji kulala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri muwe na amani sana. Sisi tunazunguka, tumeenda. Leo wanasema ooh, sisi tunapishana kila mahali.

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Tunafanya ziara kila mahali, lakini haya ni maelekezo, kama Rais halali, Waziri atalalaje? Mbunge wa CCM analalaje na watanzania wanataka maendeleo?

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Fedha zinakuja na zinasimamiwa. Watanzania nawaomba sana chonde chonde lipeni kodi. Fuata utaratibu, tii sheria bila shuruti, maandamano hayatakiwi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, maandamano kama unataka, chumbani kwako, hutaki utachakazwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana (Makofi/ Kicheko/Vigelegele)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye hoja, lakini pia namshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan kwamba, sasahivi fedha nyingi sana zinaenda katika Halmashauri katika miradi mbalimbali. Takriban kila Mbunge hapa ana jambo la kusimama na kusema juu ya Mheshimiwa Rais na juu ya Serikali ya Awamu ya Sita, tunamshukuru sana kwa hatua hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais alitoa muelekezo kwa wewe Mheshimiwa Spika na Wabunge ambao mlisaidia kusema; wananchi wa Tarime Vijijini wanashukuru sana kwamba, ile fedha ya CSR imetoka na miradi sasa inaendelea; hali ya kisiasa itakuwa tulivu jimboni.

Mheshimiwa Spika, pia Mheshimiwa Rais ametoa fedha ambazo kwa sasa vijana wa darasa la saba wakimaliza mitihani yao mwakani wataingia form one kwa kuwa madarasa yamejengwa na kazi inaenda mchakamchaka sana.

Mheshimiwa Spika, nampongeza CAG kwa kazi ambayo anaifanya. Ametoa taarifa ambayo kila Mbunge akisoma baadhi ya mambo ambayo yapo kwenye majimbo yetu tunayaona kwenye ripoti hii. Tunamshukuru na tunaomba aendelee hivyo.

Mheshimiwa Spika, lakini ziko changamoto nyingi sana. Na ukitaka kusaidia Watanzania wakati ukiwa umekalia hicho Kiti kwa muda ambao Mungu atakupa na sisi kukujalia kuendelea kukaa hapo ni kuangalia namna ambayo tutapitia mfumo wa Serikali za Mitaa Tanzania. Mfumo huu umeanza tangu mwaka 61, ukashindwa 71, ukawa resumed mwaka 82, tukaanza operation mwaka 84; ni miaka 38 mpaka sasa tunao mfumo huu. Kunakuwa na changes ndogondogo sana.

Mheshimiwa Spika, mazungumzo yote humu Wabunge wakisimama tunazungumza fedha ambazo zikienda kwenye majimbo yetu zitaondoa kero za Watanzania ambao wametuchagua sisi kuja kukaa kuzungumza. Tunazungumza hoja ambazo kila Mbunge angetamani fedha zinazotajwa hapa, haya mabilioni yanayotajwa kwa namna mbalimbali kwamba, yamepotea tungetamani yaende yakaondoe changamoto za barabara, maji, afya, shule, mikopo watu wawasomeshe Watanzania wapate elimu na huduma bora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hili jambo ni muhimu sana kwa sababu tunazungumza hapa fedha nyingi katika halmashauri. Tuchukue mfano rahisi, tulipata fedha za Uviko zikaja kwenye majimbo. Mheshimiwa Rais akatoa maelekezo, Wakuu wa Mikoa na Ma-DC wakafanye special operation, yale madarasa yakajengwa ndani ya muda mfupi yakakamilika. Malalamiko ni machache, lakini fedha hizi za Serikali, za wananchi kule, hili ni shamba la bibi, ndiyo fedha ambazo zimeibwa sana na zimeliwa. Miradi mingi katika maeneo haya haijakamilika, na hoja nyingi ukisoma zinajirudia.

Mheshimiwa Spika, CAG miaka miwili mpaka mitatu nyuma alisema hoja ile ile. Sasa kama kuna mtu yupo mahali alipewa hoja mwaka uliopita, mwaka wa kwanza, mwaka wa pili na mwaka huu imejirudia, mwakani ataleta story hiyo hiyo, kwa nini watu hawa wasiwajibishwe? Kwa nini wasichukuliwe hatua? Hawa ni watumishi, CAG na watu wake, wanalipwa posho, wanatumia muda, akili na damu, wanasafiri wanaumia, hawa wakienda wakaleta ripoti tunatarajia mabadiliko.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia michango ya Wabunge humu ndani, watu wanaumia sana, kwamba tunazungumza kwamba kwenye majimbo yetu kuna changamoto, tuna shida na watu wetu, lakini tunaambiwa fedha zimekusanywa, zimepotea. Ripoti hii imetoa tathmini ya ukaguzi wa fedha. Tungetaka tupate ripoti nyingine sambamba na hii ambayo inaonesha, watumishi ambao wamekula fedha za Umma ni akina nani; na wapo wapi; wanafanya nini kwa sasa? Lazima watuoneshe.

Mheshimiwa Spika, CAG ameonesha fedha ambazo zimepotea, tupate ripoti ya wale ambao wamehusika. Yaani haiwezekani watu hapa watoe mishipa kujadili fedha imepotea, halafu kuna mtu anakula kiyoyozi tu, au mwingine amehamishwa kutoka point A kwenda point B. Hii haikubaliki.

Mheshimiwa Spika, tukitaka kupiga hatua; tena Mheshimiwa Rais wetu yuko China, ningeomba akope sheria za Wachina kidogo tu, siyo zote, watu wa namna hiyo kule China hawawezi ku-survive. Umefanya kosa, imethibitika, hujaonewa, unawajibishwa, anakaa mtu mwingine. Wapewe nafasi watu wenye uwezo huo. Kama mtu amekaa mahali kwa bahati mbaya, atoke. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huu mjadalla wa sasa hapa, hata huko mtaani watu wanatushangaa. Tulikuwa tupewe hapa ripoti wahusika wote wakiwa korokoroni, ndiyo tunazungumza hapa. Anaitwa mmoja mmoja, anaulizwa fedha ziko wapi? Rudisha, kama umemeza, tapika fedha ili zirudi katika eneo lake. Ndiyo hoja ya msingi hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ni mjadala hapa wa maneno mengi; kwa mfano, unaposema MSD wanaidai Serikali Shilingi bilioni 250, halmashauri tumekabana mashati, mia mbili mia mbili; mia tano, mia tano; buku buku; tumepeleka fedha pale kuomba dawa. Dawa hazijaja, kumbe hawa wanaidai Serikali hawajalipwa fedha. Sasa Mbunge unasema nini kwenye jimbo lako? Yaani wananchi wametoa kodi wamelipa kutoka mazao yao na shughuli mbalimbali, fedha imepatikana, tumepeleka pale MSD, dawa hazipo. Kwa hiyo, mzigo huo siyo wa kwetu. Tunaomba hao watu walipwe fedha ili wananchi wapate dawa na huduma kama ambavyo wamechangia.

Mheshimiwa Spika, hizo fedha wamepeleka miaka miwili mpaka mitatu hawajarejesha, dawa hazipo, fedha wamechukua na maelezo hamna, na watu wapo ofisini. Mimi naona hii siyo sawa.

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine nataka nizungumze, kwenye halmashauri zetu na ndiyo maana naomba tupitie huu mfumo wa Serikali za Mitaa. Halmashauri zile, Mbunge anazungumza hapa, ikitokea kuna shida kwenye jimbo, Mbunge utaulizwa, hujasemea watu wako, hufanyi kazi nzuri, lakini twende kwenye maeneo yetu, kuna maagizo ambayo Katibu Mkuu TAMISEMI anamwagiza Mkurugenzi. Mkurugenzi anaitwa Dodoma halafu anapewa maagizo, na halmashauri Madiwani wamepitisha mipango yao. Sasa wanasigana; Mkurugenzi ameambiwa lazima nitekeleze hili. Fedha nifanye re-allocation ifanye mradi fulani, na mradi huo haukupendekezwa, mradi wa Madiwani ni tofauti na ule pale. Kwa hiyo, Mkurugenzi anasimama kwamba bosi amesema lazima lazima nitekeleze; Madiwani wanasema, hiki siyo kipaumbele chetu; Mbunge anasema yuko kwake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimekusikia umesema mara kadhaa kwamba kama Bunge likiisha kwa mfano 2025, wengi hapa asilimia 60 mpaka 70 hatutakuwepo. Sababu mojawapo ni miradi kwenye halmashauri na maagizo mbalimbali. Wapo Wakurugenzi kwenye halmashauri zetu hawafanyi kazi. Anaitwa mkoani asubuhi mpaka jioni, kaenda na gari, kaenda na dereva, kapewa maagizo; maagizo hayo, Mbunge hajui, Mwenyekiti wa Halmashauri hajui. Kwa hiyo, kuna shida. Kwa hiyo tuangalie hata mfumo wetu unavyofanya kazi.

Mheshimiwa Spika, hawa wakurugenzi pia wapewe watu wenye uwezo. Zamani walikuwa wanateuliwa miongoni mwa Watumishi wa Umma. Wanafanyiwa vetting, wana uzoefu. Leo kwa mfano ukimwuliza CAG, kwenye halmashuri hizi atuambie maeneo ambayo watu wameshindwa kuandaa ripoti ni wangapi? Pale Tarime ili wafunge mahesabu walikuwa wanaenda kuazima watu Serengeti. Wataalamu hawapo. Kwa hiyo, tunazo hoja nyingi sana za kuangalia.

Mheshimwa Spika, naomba kwamba fedha ambazo zimepotea, wamezungumza, sitaki kusema kwa sababu nilikuwa kule Tanga, lakini nimefurahi kuiona kwenye ripoti hii. Haya mambo yapo, yamefanywa, na wahusika wapo, peleka ukaguzi maalumu Bandari ya Tanga, watu wawajibishwe, tupone. Ukitaka kutengeneza taswira nzuri, kama kuna mtu amepoteza fedha ya Serikali, halafu amewajibishwa, hata kizazi kingine kitajifunza. Kama kuna mtu amepoteza fedha na hakuwajibishwa kwa sababu ni mjomba, shangazi, mnafahamiana, ni ukanda, kabila moja, hili Taifa litakufa.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. WAITARA M. MWIKWABE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa maoni yangu katika suala la mazingira. Ni muhimu Wizara ya Mazingira na Muungano ibainishe na kutambua maeneo ambayo watu wamejenga katika kingo za mito na mabonde.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba maeneo hayo yatambuliwe na kuagiza wahusika wote wahame kwa mujibu wa Sheria na hili lisimamiwe wakati wote sio wakati wa mvua tu na kila mtu ajue kwamba maeneo hayo hayajengwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri sheria itekelezwe wakati wowote na Viongozi wa Serikali ambao watahusika kuuza au kushawishi watu kujenga au kuwaandikia vibali ili waishi kwenye kingo na mabondeni washughulikiwe kisheria ili kuondoa malalamiko na usumbufu wakati wa mvua.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi; katika Mkoa wa Dar es Salaam na hasa Jimbo la Ukonga kuna mnada wa Kimataifa wa Pugu. Barabara ya kwenda mnadani ni mbovu na mwaka 2016/2017 ilipangwa kujengwa lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika, naomba Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana azingatie barabara hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Ukonga kuna shida ya mawasiliano hasa Kata za Msongola, Zingiriwa, Chanika, Kivule, Mzinga, Buyuni, Pugu, Pugu Station na Majohe, je, kwa nini Mheshimiwa Waziri asihimize uwekaji wa mitandao ya simu ili Kata hizo zipate mawasiliano ya uhakika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna malalamiko mengi ya wananchi waliohamishwa kutoka Kipawa na kupelekwa Buyuni, Zavala na Kipawa Mpya. Naomba kujua mipango ya Serikali kulipa fidia wahanga na kupeleka miundombinu kama walivyokubaliana na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kwa maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Wizara kuboresha mnada wa Pugu ambao unaitwa mnada wa kimataifa ili kufanana na jina lenyewe kwa kupeleka maji na kuboresha barabara inayoenda mnadani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba kuna mnada wa kimataifa Pugu, bado hakuna machinjio ya kisasa ila kuna machinjio ya mtu binafsi Mazizini, Ukonga, lakini katika kata ya Zingiziwa Ukonga kuna eneo la wazi la kujenga machinjio ya kisasa na kuongeza mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe maoni yangu kwa maandishi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 72 unataja miradi ya visima katika Kata za Gongolamboto, Chanika, Pugu Mpera, Kitunda na Ukonga. Kata hizi pia zilitajwa mwaka wa fedha 2016/2017 na hadi sasa visima hivyo havijakamilika. Naomba kujua ukweli wa miradi hii kama kweli ipo. Nashukuru Waziri na Naibu wake kwa ushirikiano wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 73 ametaja miradi tarajiwa katika Kata za Msongola, Chanika, Gongolamboto, Pugu na Kitunda. Kata hizi nazo zimekuwa zikitajwa kila mwaka bila mafanikio. Kwa uhakika kuna shida kubwa ya maji katika Jimbo la Ukonga na hasa kwenye maeneo ya huduma za umma kama shule, zahanati, Polisi, Ofisi za Mitaa na Kata.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya upatikanaji wa maji ni mbaya katika maeneo ya Msongola-Mpera, Msongola- Mvuti, Msongola-Mbondou, Msongola-Uwanja wa Nyani, Buyuni-Zavala, Buyuni, Buyuni-Kigezi, Zingiziwa-Nzasa, Chanika, Pugu Station, Kivule-Bombambili, Pugu, Ukonga, Gongolamboto na Msongola-Yangeyange. Naomba kujua kwa uhakika utekelezaji wa miradi ya maji Ukonga na Kata zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa maoni yangu juu ya hoja ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna upungufu mkubwa wa wataalam wa sekta ya afya karibu zahanati, vituo vya afya na hata hospitali za mjini na vijijini. Hili jambo ni kubwa naomba Serikali ilifanyie kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mahusiano makubwa ya TAMISEMI na Wizara ya Afya hivyo ni maoni yangu kuwa kuwe na chombo cha pamoja kushughulikia allocation ya watumishi wa afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shida ya wazee kupata matibabu kwa kutumia bima au utambulisho kwa wazee.

Hili jambo naomba lifanyiwe kazi ili wazee wasipate shida pindi wanapougua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shida kubwa ya gari la wagonjwa katika hospitali, vituo vya afya Ilala na hasa Jimbo la Ukonga. Naomba nipate gari la wagonjwa walau lihudumie Ukonga tu ili kuwa na uharaka wa usafiri pindi tupatapo wagonjwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia. Kwanza namshukuru Mungu kupata fursa ya kusimama kwenye hili Bunge Tukufu kuchangia hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu; na kuna mambo mawili yawekwe mstari vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, unapokuwa kiongozi wa Serikali unaisemea Serikali, unapokuwa Mbunge unasemea wananchi wako. Haya mambo mawili lazima yapigiwe mstari vizuri, la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, ninaomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo ameifanya, hasa katika Mkoa wa Mara, ndio mkoa ambao hauna Hospitali ya Rufaa sasa kwangu inaendelea kujengwa, watu wetu wataishia pale Musoma hawataenda Bugando. Vilevile Musoma kulikuwa na shida ya uwanja wa ndege kwa muda mrefu, ametoa fedha nyingi mkandarasi yupo site, tutapata huduma ya ndege pale katika Mkoa wa Mara. Mheshimiwa Rais pia ametoa fedha katika majengo yetu ya mkoa, na tunamshukuru sana tunaomba aendelee kufanya hivyo kwa sababu Mkoa wa Mara kwa kweli kwa hadhi yake na heshima kubwa ungeweza ufanane na hadhi ya Mwalimu Nyerere, lakini kuna mapungufu ya hapa na pale ambayo naamini kwamba yataendelea kutekelezwa kadri ambavyo Wabunge wenzangu wataendelea kuleta maoni ndani ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mimi namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwamba, kule Tarime tuna barabara yetu ya Tarime - Mugumu - Serengeti yenye urefu kilometa 86; nimeambiwa hivi asubuhi kwamba kuna mkataba angalau kilometa 25 kutoka pale Mgabili mpaka Nyamongo watajenga. Huu utakuwa ni mkombozi mkubwa sana katika eneo hili. Tuombe aendelee kutoa fedha ili tuweze kupata miundombinu watu wetu waweze kufanya kazi ya kuhudumiwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumze mambo maalum katika Jimbo la Tarime Vijijini, na hili ni jimbo maalum ndiyo maana kuna kanda maalum. Sasa ondoa mawazo ya polisi, tuje kwenye huduma za kijamii, maliasili na ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilimuomba Waziri akiwepo Mheshimiwa Ndumbaro tangu mwaka 2020 aende kule Tarime kwenye kata ya Nyanungu, Kwihancha, Korongo na Nyarugoba hakwenda; lakini namshukuru Mheshimiwa Rais aliunda kamati ya Mawaziri wanane wakazunguka walienda wakaishia Musoma Mjini pale kwangu hawakufika, lakini wakanipa idadi na orodha ya vijiji ambavyo Mheshimiwa Rais ametoa kibali kwamba wananchi wale watapata eneo angalau la kuchunga na kutoa huduma kwa mifugo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niliomba kwamba mambo haya, na nimewasiliana na wenzangu wa Mkoa wa Mara, watu wa Serengeti, Mbunge wa Serengeti, Mbunge wa Bunda na mimi Tarime Vijijini; kwamba maeneo haya kuna malalamiko ya wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo GN ya mwaka 1968 ambayo wananchi wenyewe wanajua wapi kuna beacon na wapi hakuna beacon; na kumekuwa na ugomvi wa muda mrefu katika eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Mheshimiwa Rais ametoa maamuzi ya kutoa baadhi ya maeneo yaende kwa wananchi, lakini bahati mbaya; mimi ninapozungumza hapa nimeona juzi Mheshimiwa Waziri wa Ardhi na Naibu Waziri wa Maliasili walikuwa Musoma na wakatoa tamko, nikauliza wenzangu kikao kinachoendelea mmeshirikishwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, niliposema kwamba nendeni kule site na nikatoa hoja kwa Mheshimiwa Rais alipokuja tarehe tano Februari kule Musoma nikazungumza habari hii ya hifadhi ya Serengeti na malalamiko yaliyopo ya muda mrefu yaondolewe ili sisi Wabunge tupate amani na kuwa na mahusiano kati ya wananchi na Hifadhi ya Serengeti; kwa sababu pia inalazimika kutoa huduma kwa watu ambao wanazunguka pale kwenye mambo ya usalama na kwa ajili ya rasilimali za taifa na yeyote anayekwenda katika eneo lile. Kazi hiyo haikufanyika.

Sasa badala yake wametoka watu hapa Wizara hizi mbili wameenda kule Tarime, Serengeti, Nyamongo, Kwihancha, Gorong’a pamoja na Nyanungu; na wananchi wamenipigia simu kwamba sasa wanakagua mipaka ile. Kule Kwihancha ambako tulisema waende hakuna shida kwa sababu wananchi wameonesha beacon na wamekubaliana na wapimaji na watu wa hifadhi ya Serengeti. Lakini Gorong’a na Nyanungu wameenda kuonesha beacon juu ya mlima ambako kuna vijiji ambako kuna vijiji vya watu. Sasa wananchi wanauliza Mbunge anajua? Mbunge sijui.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kilichoniuma ni kwamba wamekwenda Nyanungu ambako mimi ndiyo Mbunge, watu wamenipigia kura, nikawaahidi wakati wa uchaguzi kwamba nitawatetea na Mheshimiwa Rais amekubali kutenga eneo mchunge. Sasa wale watu wameambiwa kwamba Mbunge wenu ameshirikishwa ingawa hapa hayupo; na ni uongo.

Sasa imagine; pale Ilala pale kwenye Bonde la mto Msimbazi wanaenda kuhamisha watu unaambiwa umeshirikishwa na hukushirikishwa. Kwa nini Waheshimiwa viongozi tunategeana mabomu njiani? Hizi ni ajali! Kwa sababu unaweza kutoa taarifa za uongo kabisa katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Waziri wa Ardhi twende na Wabunge wa Mkoa wa Mara wenye migogoro, twende tukae na wananchi wetu. Hamuwezi kwenda peke yenu kule mnawapa taarifa za uongo, halafu nikitoka Bungeni nikafanye kesi. Mimi si dhaifu kiasi hicho; sitafanya biashara hiyo, tutagombana. Tunataka twende sawasawa pamoja. Kama kuna jambo lipo, Mbunge ameleta Bungeni Waziri amshirikishe Mbunge ampe na background, wapange ratiba waende, kuna haraka gani katika jambo hili? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba, na hili uwe ni ujumbe kwa Waheshimiwa Mawaziri, sina ugomvi nao mimi, ninachosema, Mawaziri hawa tunaweza kuwatengenezea shughuli nzuri Wabunge wakashinda wakae hapa comfortably, lakini kwenda kutoa taarifa ya uongo halafu unasema Mkoa wa Mara unaongoza kuvamia maeneo; sasa hiyo taarifa mmejadili na nani? Unakuta Mwenyekiti wa Kijiji ambaye hawezi ku-argue, unaongea naye halafu unauliza Mbunge niambie, mimi nipo Dodoma nyie mpo huko Tarime Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba hili kweli lifanyiwe kazi vizuri, na iwe ni maeneo yote tushirikishane tu kuna ugomvi gani? Bora nialikwe hata nisihudhurie; lakini sijashirikishwa, watu wanaambiwa Mbunge wenu ameambiwa mnaniwekea bomu hilo ambalo nitakubali tulipukiwe wote siyo mimi peke yangu…

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wa madini na mazingira, na hapa naomba Waziri wa Madini na Waziri wa Ardhi na Mazingira wanisikilize vizuri. Katika Jimbo la Tarime Vijijini eneo la Nyamongo kuna malalamiko ya muda mrefu sana, na ni malalamiko ambayo ni very genuine, yanaonekana kwa macho. Nataka nisema, tunayo changamoto ya maji machafu, ni malalamiko ya muda mrefu, tunayo changamoto miradi ya maendeleo, tuna changanoto ya fidia katika eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la Murwambe, Kumalela, Nyamichele tangu mwaka 2012 watu waliahidiwa hawajalipwa nitaomba watu hawa, mgodi umeagiza kulipa tumeongea na Rais wa Barrick duniani wamekubali kulipa naomba haya mambo yafanyiwe kazi.

Lakini ningetaka nisema kwenye miradi hii ya CSR, kengele imegonga ya kwanza. Miradi ya CSR nataka niulize Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI anisaidie. Hivi, mimi ni Mbunge, nilikuwa Naibu Waziri wa TAMISEMI, Naibu Waziri wa Muungano na Mazingira, Naibu Waziri Ujenzi na Uchukuzi, Mbunge wa kipindi cha pili, mwanasiasa wa siku nyingi, nimekaa na Halmashauri yangu, tumejadili mipango ambayo ninayo hapa, ambayo inatoa kero Nyamwaga hospitali, maji Nyamongo na vituo vya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeuandikia na mgodi correspondences nyingi tukajibiwa, tumeandika tumepeleka TAMISEMI tukajibizana na Profesa Shemdoe, tukajibiwa, barua imetoka imeenda Wizara ya Fedha tukajibizana Tutuba tukakubaliana. Tunataka fedha iende kwenye miradi ya maendeleo. Wako akinamama pale Nyamwaga wanajifungulia barabarani kwa sababu wodi haijakamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo kule Nyamongo hii ripoti ya Jafo ya maji machafu imeharibu hali ya hewa kwa sababu watu wanaogopa kunywa maji na kula Samaki, lakini kwenye fedha hiyo ya CSR kuna fedha milioni 900 mgodi wamekubali kutoa maji kwenye chanzo chao, maji yaende pale Kewanja na Nyangoto ili wapate maji. Hizo fedha Mkuu wa Mkoa peke yake ambaye ni mgeni Mkoa wa Mara amekuja ameandika barua kwenda Wizara ya Fedha amezuia fedha zote. Angalia, Mbunge amekaa Halmashauri imekaa, TAMISEMI imeandika, Fedha imeandikwa, Mkuu wa Mkoa bosi mkubwa ameandika barua peke yake miradi sasa imerudishwa Tarime wakajadili.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Serikali za Mitaa ninayo hapa inaeleza Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya wata-facilitate na watengeneze mazingira mazuri kuboresha miradi ya wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mbunge nimekuja hapa nazungumza habari ya fedha iende kule yeye amezuia. Nataka niambiwe utaratibu ukoje? Yaani Baraza la Madiwani limepitisha, sasa huyu mtu mmoja anazuiaje? After all fedha ya CSR hii fedha wala hatupewi cash, tunakaa kwenye vijiji. Kwa mara ya kwanza Tarime baada ya kuwa Mbunge fedha hii ilikuwa inasaidia vijiji 11 tu kati ya vijiji 88; tumekaa na Wenyeviti wa Vijiji, Madiwani wa Kata 26 bila kubaguana vyama, tukakubaliana sisi tufanye kazi ya Tarime Vijijini tupunguze malalamiko na kero, wakaridhia kila kijiji, kila kata ina mradi huu. Ningeomba nielezwe tukileta mipango kwenye halmashauri yetu inakuwa kuwaje tunakwamishana njiani.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante, kengele ya pili hiyo.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Rais anafanyakazi nzuri naomba viongozi wengine aliowateua wamsaidie, Wabunge mliopo humu mtarudi hapa Bungeni kama kazi nzuri inafanyika kwenye majimbo yenu tushirikishane baada ya kuyasema hayo…. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi. Naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, pia na mapendekezo kwamba ataendelea kumalizia miradi ile ya kimkakati kama SGR, Bwawa la Mwalimu Nyerere na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mipango ya maendeleo ya nchi yetu, ni vizuri tukatumia fursa pia ya kuwa na watu wengi. Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 inaonesha kwamba tuna Watanzania milioni 61.34 ambao wanawake ni milioni 31.24 sawa na asilimia 50.9 na wanaume tupo milioni 30.1 sawa na asilimia 49. 1; na nguvu kazi ya Taifa ni asilimia 55.9; na ndiyo maana tunazungumza hapa, kuna njaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kwamba ukifuatilia hata katika familia zetu, jamii zetu za kawaida, ni watu wachache sana wanafanya kazi. Kama kuna mtu ni mtumishi au mfanyabiashara, unakuta watu wengi wanamtegemea. Sasa hao watu ambao wameongeza ni vizuri ukawatumia kama fursa pia. Maana yake tuwekeze kwao kwa kuwawezesha kufanya kazi ambazo angalau hata pato la mtu mmoja mmoja ataweza kujitegemea na kuchangia kidogo katika pato la Taifa ili kupunguza mzigo kwa watu. Hatuwezi kuona watu wameongezeka, watu milioni 61 halafu tunapata njaa na watu wapo mtaani wanazurura tu. Watu wanakaa vijiweni tu, wanataka tu kupiga mzinga, nipe mia tano, nipe buku, na maisha yanaenda. Sasa nadhani ni muhimu tuangalie jambo hili na kujua kwa nini watu hawafanyi kazi? Nini kifanyike ili watu waweze kufanya kazi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna watu wa kutosha, wana nguvu, wala hata siyo wagonjwa; wagonjwa ni wachache, lakini kwanini kuna njaa? Nadhani jambo hili lichukuliwe hata nje ya mpango huu lijadiliwe. Ukitembea mtaani watu wapo saa mbili asubuhi wanazurura, hawafanya kazi, tunagombana bure tu. Hata ukienda ukaombwa hela usipotoa maana yake ni adui yako. Sasa hili siyo jambo ambalo kwa kweli tunaweza tukalifanya liendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata watu wa kutosha, wafanye kazi, wajilishe wenyewe, wachangie, na walipe kodi. Ndiyo maana watu hawalipi kodi, kwa sababu kama mtu hafanyi kazi, ukimdai kodi atalipa nini? Wanakamatwa vijana wenye nguvu, wenye utashi, eti ni wazururaji; kwanini? Hana kazi ya kufanya? Nadhani hili jambo lifanyiwe kazi vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, kuna Watu wa TASAF. Mpango wa Serikali ulikuwa ni kuwawezesha watu ambao ni kaya masikini, wanawezeshwa fedha kidogo kila mwezi, lakini wa-graduate kutoka hatua ya kuwa masikini zaidi. Kulikuwa na miradi midogo midogo; miradi ya kilimo cha umwagiliaji, ili mwisho wa siku hii tabia iishe. Siyo sawa, ukienda kwenye kata zetu, kwenye vijiji siku ambazo zimepangwa akina mama, vijana, wazee vikongwe wanakaa wanasubiri fedha, shilingi 30,000 mpaka shilingi 35,000 kwa mwezi mzima. Ukikaa pale ukaangalia, yaani Tanzania hili jambo lifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale watu ambao wana uwezo wawezeshwe watoke kwenye hiyo hali, tusaidie watu ambao kweli wana uwezo mdogo na tuweze kuwa- monitor. Kuna mchezo ambao wale ambao hawana uwezo hawapewi fedha, wale wenye uwezo wanapewa pesa. Majina yamegeuzwa chini juu. Hili nalo lifanyiwe kazi vizuri sana. Huwezi kuwa na Taifa ambalo watu wao wanasubiri mwezi mzima waende kupiga foleni eti wapewe shilingi 30,000, inatosha kitu gani? Hivi kwa mfano kiroba shilingi ngapi unanunua? Zaidi ya shilingi 50,000! Haisadii! Ni hela kidogo sana, lakini udhalilishaji ule; kwa sababu mtu anakaa pale; kwa kweli hili tuliangalie, lifanyiwe kazi. Taifa ili liweze kuendelea ni lazima watu wafanye kazi na mtu wa kusaidiwa kweli atambulike na anayepaswa kupewa msaada, apewe msaada. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Mbunge mchangiaji. Nadhani jambo analolisema Serikali imekusudia kufanya hivyo hivyo. Naomba tu nimpe taarifa kwamba Mpango huu wa Kaya Masikini lengo lake ni hilo hilo, kwamba ni kuziwezesha zile kaya masikini, lakini baada ya muda zina- graduate; na zikisha-graduate zinatoa fursa kwa wengine ili waingie na mwisho wa siku wengi watakuwa wameboresha hali zao za maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Ushahidi, nataka tu nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika kufanya utafiti na kufanya tathmini ya Mpango wa TASAF mpaka sasa tayari tunazo kaya zaidi ya 1,000 zinazoanza kuandaliwa ku-graduate kutoka katika Mpango wa TASAF kwenda kujitegemea hili kaya nyingine zisizokuwa na uwezo ziingie na mwisho wa siku ziweze kujitegemea. Hizi kaya zinazopewa hizo shilingi 30,000, shilingi 12,000, shilingi 22,000, upo uthibitisho wa wanakaya wameweza kuanzisha miradi ya kimaendeleo na ya kiuchumi ambayo imeweza pia kusaidia kwenye jamii.

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Waitara, muda wako umelindwa.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Mheshimiwa Waziri nimekusikia, naomba uchukue mawazo yangu yafanyiwe kazi. Bado kazi iliyofanyika ni ndogo sana sehemu kubwa watu wetu kuna hiyo hali ambayo nimeizungumza. Sitaki kubishana na Serikali, nakubaliana kwamba tuendelee kufanya kazi na ni- recognize kwamba kuna maeneo wame-graduate na kuna watoto wamesaidiwa na wamesoma. Nikasema ukienda kuangalia namna ambavyo wamekaa pale, wanasubiri hicho kiasi kwa kweli, bado inabidi tufanye kazi zaidi na Serikali itoe ushirikiano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kwenye mpango zimetajwa baraba za vijijini na mijini kwa maana ya TANROADS na TARURA. Nilikuwa nataka nishauri kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha, ukienda kwenye Majimbo yetu Vijijini, Barabara za Vijijini nyingi hazihitaji hata kuwekwa lami. Unakuta Mbunge anakosa hata grader aweke mafuta hata Mfuko wa Jimbo au dau aweze kulima barabara, lakini barabara moja kila mwaka inatengewa fedha nyingi sana shilingi milioni 500, shilingi milioni 300 au shilingi milioni 700 wanalima, kila mwaka au kila baada ya miezi sita, na malalamiko ni mengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini msitenge fedha hiyo mnunue magreda na ma-compacter mgawe kwa kila Jimbo ili wale ma-engineer wa TARURA walime barabara kwa bei nafuu, unaweza ukapata mdau ukajaza mafuta kwenye grader badala ya kukodi. Hapa tunapiga mark time, nunua magreda mpe kila Mbunge kwenye Jimbo aajiri ma-engineer walime barabara kwa gharama ndogo. Halafu kama ni mpango mkubwa wa kuweka lami au changalawe, tangaza mkandarasi afanye kazi hiyo. Utaokoa fedha nyingi sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na pia huduma itapatikana katika Majimbo yetu na malalamiko mengi ya Wabunge yatapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, katika hotuba ya Mheshimiwa ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 27 amezungumzia uchumi shindani na shirikishi. Mheshimiwa Waziri, kwa mfano ukienda kule Sirari, tuna eneo tumetenga muda mrefu kwa ajili ya Soko la Kimataifa la Mabwe. Huduma zote kutoka Kanda wa Ziwa zinatoka katika mpaka wa Sirari. Ukijenga pale soko, bidhaa zote kutoka Kenya utapata mapato na fedha hiyo itaraudi haraka sana na uchumi utapanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nilikuomba ukienda kule Nyamuhonda, mpaka Sirari, na Itiru kumtoa mwananchi wa kawaida ambaye anataka mifuko miwili ya cement au mabati aende kulipa ushuru Sirari ni mbali sana. Tuwee fedha ndogo ili watu waweze kulipa kodi, tuweze kupata fedha katika maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nizungumze katika huu uchumi shirikishi, nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge, Watanzania na Serikali, ni kwamba Wizara ya Maliasili ina lugha yake, Wizara ya Maji ina lugha yake, Wizara ya Kilimo wana lugha yao, Wizara ya Ardhi wana lugha yao. Tunazungumza uchumi shirikishi; mimi nina mfano, halafu tunajadili hapa mambo ya Watanzania watu wanaongea Kichina, Kihindi, kama Wamarekani au Wacanada, kama wamezuka leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie, mfugaji ukienda ukachukue ng’ombe zake 30 ambapo ng’ombe mmoja ni Shilingi milioni tatu, unazungumza karibu Shilingi milioni 90 umemnyang’anya, halafu umeenda umetaifisha, na eneo hilo huyu mtu hana sehemu ya kunywesha maji ng’ombe zake, hana sehemu ya malisho, hana sehemu ya soko, mifugo hiyo ndiyo benki yake. Huu uchumi unaozungumzwa shirikishi siyo sawa. Hapa kila Mbunge ana malalamiko. Nimefuatilia sana ziara za Waheshimiwa Viongozi wetu, wanatoa maamuzi kana kwamba wao sio Watanzania. Hivi unafuta Kijiji, halafu wale wananchi wanaenda wapi? Huyu Mbunge aliyempigiwa kura wanakwambia tulikuchagua wewe halafu tumefutwa, turudishie kura zetu; unafanyaje? Hili jambo naomba Serikali ilichukue very serious.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapozungumza mwezi wa Tisa uliopita, kule katika Jimbo langu wamekusanya ng’ombe kutoka Nyanungu, Nyarokoba, Kuyancha wameenda wametaifisha ng’ombe, wanasema hazina mwenyewe, watu wangu wanalia; halafu tena tarehe 15 mwezi wa Kumi wamekusanya nyingine, na ninapozungumza ziko hifadhini. Jua limekausha maji, only source ya maji ni Mto Mara, hakuna sehemu ya kunywesha wale ng’ombe, wamewekwa pale ndani; kuna maji ya chumvi, hawasikilizwi, hawaendi. Sasa huyu mwananchi wa kawaida ambaye mtoto wake yupo sekondari, yupo chuo, angeuza mfugo amsaidie, sasa hawezi; chakula hana, angeuza ng’ombe apate chakula; anaishije ndugu zangu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Viongozi na Mawaziri mtusikilize. Mnaenda kwenye Majimbo, sikilizeni watu. Hawa sio Wanyama, tuzungumze na Watanzania wenzetu, haitafurahisha; kuna watu hapa wanaitwa chawa, ukichangia jambo hapa badala yakujadili hoja, wanakujadili wewe. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Waitara.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaombe, mlinde uchumi wa Watanzania, halafu…
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi. Naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwa kazi nzuri ambayo anafanya kwa ujumla wake lakini pia kwa kuchukua hatua na kutoa maelekezo kwa Waziri wa Madini Dkt. Biteko na wenzake kutanzua mgogoro mkubwa ambao ulikuwa pale Tarime wa mambo ya miradi ya CSR. Kwa hiyo, tunamshukuru sana kwa sasa kwa kweli siyo kama hali ilivyokuwa hapo awali, kuna mabadiliko makubwa sana katika miradi hii ya CSR. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana niseme tu kwamba ule Mgodi unaitwa Barrick North Mara na mgodi huo ume-take over kutoka Acacia tangu mwaka 1995/1996. Kwa hiyo, ilirithi madeni pamoja na mkataba na uchimbaji na kila kitu. Kile ambacho wananchi walikuwa wanadai kutoka nyuma maana yake Barrick kwa sasa wanawajibika kulipa kwa sababu ilikuwa kwenye mkataba na walikubaliana. Nilitaka niweke maelezo very clear. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaipongeza Barrick pamoja na mvutano ambao ulikuwepo tangu nimekuwa Mbunge katika jimbo lile 2020 mpaka leo kuna mabadiliko makubwa sana. Barrick zile ajira 46% wanatoa katika vijiji 11 pale pale kwenye Mgodi wa Barrick North Mara. Vilevile hata bidhaa ilikuwa inatoka nje ya hata ya nchi. 80% ya bidhaa pale mgodini inatoka ndani ya nchi na wengi akina mama na vijana wana-supply katika Mgodi wa Barrick North Mara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile walikuwa wanamsikia Rais wa Barrick, leo navyozungumza anakaa na wale wananchi wanazungumza na viongozi wa vijiji wanapanga mipango pale mtaani kabisa katika jengo la sekondari na wanazungumza na wanapeleka maombi kadhaa ambayo mgodi umepokea na wanaendelea kuyafanyia kazi. Hayo ni maendeleo makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba kwenye miradi ya CSR kuna mambo mawili hapa; la kwanza kuna fedha ya kwanza ambayo ilienda Barrick wameweza kutoa fedha mara mbili tu. Mara ya kwanza ni mwaka 2019/2020 wakati huo nilikuwa Mbunge wa Ukonga. Katika fedha hiyo ililipwa shilingi bilioni 5.7. Nimelalamika hapa Bungeni na ningeomba Mheshimiwa Waziri hili jambo la miradi ambayo fedha ilipelekwa kwenye miradi mbalimbali. Miradi mingi imekuwa viporo, nondo zimekuwa stranded, ma-cement yameharibika mpaka leo. Ripoti ya CAG haijatoa taarifa nani mhusika, hiki kitendo kimekwaza Wananchi wa Tarime na kama Mbunge sifurahii. Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri asimamie jambo hili ile ripoti itoke fedha hazikutumika vizuri miradi haikukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha ya awamu ya pili ambayo tumepokea mwaka jana yaani 2022/2023 navyozungumza shilingi bilioni 7.3 ipo kwenye miradi mbalimbali ya Halmashauri ya Tarime Vijijini na tumebadilisha utaratibu, hii miradi ipo kwenye kata 26. Mheshimiwa Naibu Waziri amekuja tulizungumza vikao mbalimbali tunamshukuru mabadiliko ni makubwa sana. Kilichotokea kwamba fedha hii Kamati ya TAMISEMI ambayo ni mjumbe ilikwenda pale ni kwamba kwa kuwa kuna changamoto nyingi hakuna madawati, hakuna visima vya maji, hakuna zahanati, watoto wanakaa chini. Kwa hiyo, tulikubaliana kwamba fedha ile ukiipeleka kwenye kata, Diwani wa kata husika kupitia WDC wanaangalia wenye kipaumbele ni kitu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini baada ya batch hii kwenda tumejenga madarasa ya kutosha, tukaweka madawati, tukachimba visima, tukajenga majengo ya mama na mtoto, tukapeleka hata vitanda tu vya kina mama kujifungulia, ina maana awamu nyingine ijayo tunaenda kuteua miradi ya kimkakati ambayo sasa itaonekana kwa macho na kwa sababu Barrick wamekubaliana kuwachukua baadhi ya viongozi kutoka Nyamongo, kutoka katika Halmashauri yetu ya Tarime DC wataenda kujifunza wenzetu wa Msalala kazi ambayo imefanyika na pale Kahama. Tunaamini kwamba tunaendelea vizuri kwa maana ya Mgodi wanafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wameahidi kujenga uwanja wa mpira pale, wana-supply maji katika vijiji 11 kwenye kata tano kutoka kwenye chanzo chao ili kuondoa sintofahamu kwamba maji yale ni ya sumu walikuwa hawawezi kuyaamini kuyatumia lakini Mheshimiwa Waziri yako mambo ya Wizara kufanya katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano amezungumza mwenzangu kwamba kuna watu wana dai. Kule kulikuwa na vijiji vitano ambavyo viliingia mkataba na Mgodi wa Barrick kutoka Acacia kwamba katika uzalishaji watapata 1%. Hiyo fedha mara ya mwisho wamelipwa mwaka 2012. Mpaka leo fedha haijwahi kulipwa, ni mgogoro mkubwa kwa sababu kila wakikutana wanajadiliana walipwe fedha zao. Hili ni Wizara isimamie lipo kwenye mkataba na hiyo fedha walilipwa dola milioni mbili mpaka walienda mahakamani na jalada lipo. Waliambiwa msiende mahakamani, msigombane na mgodi mulipwe fedha. Kwa hiyo, naomba jambo hili litekelezwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha ile ikienda kuna wananchi wanadai maduara 360 mpaka leo. Wamezunguka sana wamesaga lami. Wameenda kila mahali mpaka kwa Rais na Mheshimiwa Naibu Waziri ulikuja pale. Kama vijiji vile vitano vikilipwa 1% ndiyo watalipwa wenye maduara. Hawawezi wenye maduara yakalipwa fedha ambayo haifiki. Kwa hiyo, kama kweli tunataka kuwasaidia wale watu.

TAARIFA

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita kuna taarifa.

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa muongeaji taarifa kwamba tena kati ya hao ambao hawajalipwa mpaka sasa hivi kuna baadhi yao wengi wao wamekwisha fariki. Ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita unapokea taarifa?

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ni wengi wamefariki dunia na wameacha haki zao zinapotea. Kwa hiyo, nasema kwamba wale watu wakilipwa vijiji vile vitano vikilipwa 1%, watafanya miradi ya maendeleo lakini watu wa maduara watalipwa lakini kwa sasa ilivyo wale watu wanagombana wenye maduara ndiyo fedha yao kwa sababu waliwekeza hawajalipwa, vijiji vinasema hatuwezi kulipa kwa sababu hatujalipwa. Mgodi unasema kwamba wao hawajaendeleza maeneo yale, kama hawajaendeleza maeneo warudishe kwenye vijiji, vijiji vitafute muwekezaji mwingine watachimba ili kazi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi lingine ambalo nataka niseme hapa. Kuna mgogoro mkubwa katika eneo langu na hili jambo mlisikilize vizuri. Mgogoro uliopo ni kwamba mgodi unafanya evaluation ya kutoa maeneo ya watu. Tuna maeneo kama Nyamichere tangu mwaka 2012 maeneo kama Murwambe yamekuwa mabovu majengo ya watu, maeneo kama Kewanja, Komalela, Nyabichune. Hapa tunazungumza kata tano zinazozunguka ule mgodi. Watu hawa wamefanyiwa tathmini lakini mpaka leo hawajalipwa. Sasa kuna ugomvi pale, ukienda kwenye mgodi wanasema sisi tunalipa tulichoambiwa tulipe, mdhamini mkuu yupo Wizara ya Ardhi kwa Mheshimiwa Angeline Mabula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wanavutana, ningeomba Mheshimiwa Waziri wa Madini usimame katikati. Kitendo cha watu wale kutolipwa fedha zao na tena wanalipwa kiasi kidogo, ekari moja ya ardhi ambayo ina dhahabu chini wanalipwa shilingi milioni tano tu. Ndiyo maana umasikini hauwezi kwisha, unachukua ardhi, ulipe shilingi milioni tano aende atafute eneo lingine ajenge, aanze kuwekeza, na ana familia kubwa, extended family pale. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili jambo limeleta taharuki. Kuna ugomvi ambao siyo wa lazima. Kama Wizara ya Ardhi itafanya tathmini vizuri, ikapandisha bei ya ardhi, ikafanya tathmini kwa wakati, mgodi wanasema tukiambiwa na Serikali lipa shilingi milini 10 tutalipa. Tumeambiwa tulipe shilingi milioni tano ndiyo tulichoambiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba mtanzue huu mgogoro ili wale watu wafanye kazi ya uwekezaji wapate ushirikiano na wananchi wale, wafanye kazi nzuri. Mgodi wa Barrick ndiyo walipaji wakubwa wa kodi kuliko migodi yote hapa Tanzania. Lakini malalamiko ni mengi kwa sababu wale watu wanatambua haki zao. Wanajua chini ya ardhi kuna dhahabu, kuna matrilioni lakini hizo fedha hazilipwi zinalipwa kidogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mgogoro ule kati ya Barrick na wananchi niutanzue, na hii ni kwa Wizara ya Madini na Wizara ya Ardhi kufanya kazi pamoja ili watatue jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi lingine, migogoro mingi iliyopo katika maeneo yetu ni kwa sababu kwa kweli ukiangalia hali za watu katika maeneo ya migodi, ikiwepo Nyamongo, hasa wale wananchi wa kawaida maisha yao hayafanani. Sasa hivi Nyamongo imechangamka sana, mgodi umetengeneza mahusiano, umewekeza, watu wamepata kazi, lakini wengi ni wageni ambao wamekaa pale. Wananchi wa kawaida wenye ardhi wanalipwa kidogo sana. Kwa hiyo ningeomba jambo hili Mheshimiwa Dotto Biteko…

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. MWITA M. WAITARA:…umesifiwa sana kwa kuwawezesha wachimbaji wadogo kuendesha maisha yao. Sasa njoo Nyamongo nenda maeneo ya machimbo, wezesha wananchi wa kawaida, wale wanaozunguka migodi wapate maisha mazuri, wafanane. Ametuleza Mheshimiwa Salome Makamba, ni kweli kwamba ukimlipa fedha kidogo…

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. MWITA M. WAITARA: … anaenda kuanza maisha, lakini akipata hisa, akapata share kidogo maana yake atakula yeye na kizazi chake na ndugu zake na mahusiano
yataimarika. Vilvile nikiangalia bei ya mazao na bei ya ardhi…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita Waitara muda wako umekwisha nakuongeza dakika moja nyingine malizia hoja yako.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nakushukuru sana, niombe Mheshimiwa Waziri wa Madini ufanye tathmini nzuri sana…

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. MWITA M. WAITARA:…, je wananchi wale ambao wanalipwa fedha wanaboreshewa maisha au fedha inapita mlango mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho nilitaka nikuombe, fanya tathmini, uchunguzi wa kimadini ya Locoba, Kuihanchat, Koronga, Nanungu na Hifadhi ya Serengeti. Migogoro mingi iliyopo pale watu wanaamini pale kuna dhahabu na inafichwa haijulikani. Nenda ufanye uchunguzi mtangaze kuna dhahabu ufanyike uchimbaji halali ili kuondoa migogoro iliyopo katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima kubwa naomba niunge mkono Bajeti ya Mheshimiwa Dotto Biteko ameiheshimisha amekuja na mambo wakati wa shida, watu wanakusikiliza lakini lile Bwawa la Nyamongo la maji machafu Mheshimiwa Rais aliagiza akiwa Makamu wa Rais kwamba lichimbwe jipya mpaka leo halijachimbwa, tunaomba utekelezaji, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba nimshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka fedha kujenga VETA Tarime, shilingi bilioni 1.4. Pia nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kulipa baadhi ya madai ya watumishi wakiwemo walimu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kupeleka vishikwambi ambavyo vimesaidia pia kupeleka teknolojia na kurahisisha mawasiliano. Nampongeza Mheshimiwa Rais kwa jambo kubwa hili ambalo ameruhusu tufanye mjadala wa kupitia mitaala ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu katika eneo hili, hili ni jambo muhimu sana, tunazungumzia Watanzania wa leo na kesho na vizazi vijavyo, tujipe muda wa kutosha wa kutafakari jambo hili. Tunahitaji kupata muda wa kujadiliana. Yako maswali yanahitaji kuwa na majibu. Kwa mfano, Mheshimiwa Waziri amesema, Januari mwakani 2024 wanaweza wakaanza utekelezaji. Tungependa Mheshimiwa Adolf Mkenda atuambie mkakati wa utekelezaji huu ukoje? Zile shule za zamani za ufundi wamekarabati lini? Vitendea kazi vya kisasa umepeleka lini, kwa maana ya ukarabati wa karakana na kadhalika? Vyuo vya ufundi vimesimama kwa muda mrefu. Walimu wabobevu wenye taaluma hiyo wameandaliwa lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, haya mambo ni muhimu. Unaona watu wanauliza, Zanzibar kule Darasa la Kwanza mpaka la Saba hapa mnapendekeza Tanzania Bara, Darasa la Kwanza mpaka la Sita. Tumetajiwa mifano ya nchi nyingine ambazo zimefanikiwa, mnafanya reference wapi? Mambo haya yote yanapaswa kujadiliwa kwa kina ili tupate kitu cha maana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamependekeza hapa pia, ni vizuri tukapitia Sheria ya Elimu, twende kwenye sera, twende kwenye mitaala na tutengeneze kitu ambacho kitadumu kwa miaka 100 ijayo, tutengeneze Tanzania ambayo inaonekana kwa macho tuchore roadmap ya nchi yetu kwa upande wa taaluma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile watu wanahoji hata lugha ya mawasiliano. Hili ni muhimu pia tutakubaliana kama Taifa, tunatoka hapa tunaenda wapi? Kila mtu aweze kuridhika na tuweze kwenda mbele. Pia maeneo yetu kwa mfano, mimi maeneo yetu watu ni wakulima kule, mitaala ambayo inatengenezwa, tungetarajia kuwe na fani ya uchimbaji, kuanzia level ya chini kabisa. Mahali ambapo kuna kilimo, kuwe na fani ya kilimo proper na vifaa viende vya kisasa. Mahali ambapo kuna uvuvi, kwenye maziwa na Bahari, lazima mitaala ya kisasa ya kuvua iwepo ili tukimaliza jambo hili, tuwe tumefanya once and for all na watu waweze kunufaika tupunguze shida kubwa ya ajira katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni ubora wa elimu. Nimeangalia matokeo ya Kidato cha Nne, ni kwa miaka mitatu. Kwa mfano, 2020 waliopata Division One mpaka Division Three walikuwa 152,909. Division Four mpaka Zero ni 318,148. Hao waliofeli ni asilimia 65. Mwaka 2021 waliofanya Form Four, waliopata Division One mpaka Three ni 173,422; Division Four mpaka Zero 310,398. Asilimia 62 hawa walifeli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2022 waliofanya mitihani darasa la kwanza mpaka la tatu ni 192,348, lakini daraja la nne na zero 328,000, kwa ujumla wake, kwa miaka mitatu hii. Maana yake waliopata Division One mpaka Four ni asilimia 34, zilizobaki walifeli kwa lugha nyingine. Hawa wako mtaani. Hii nime-sight miaka mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sura moja nimeona hapa, mwaka huu wa 2022 kwa mfano, division one walipata wawili, division two wakapata sijui sita, wengine wote katika watoto 200 walipata four na zero. Hii maana yake ni dalili mbaya kwenye ubora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nini kinachangia hapo? Mimi nazungumza kama mwalimu na Mbunge wa Vijijini. Tusijifiche ukaweka kichwa chini kwenye katani, halafu huku nje ukasema umejificha, lazima tuambiane ukweli. Tuna upungufu mkubwa kwa mahitaji ya elimu kwa walimu wenyewe. Ukiacha upungufu kwa maana ya idadi, hawa walimu wanaweza kufundisha? Unaposema anafundisha hesabu, anaijua? Kiingereza anafundisha anakijua? Kiswahili hicho anakijua? Kifaransa anakijua? Au ni walimu ambao wanafundisha Kiswa-Kinge shuleni! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuna shida, Mheshimiwa Profesa Mkenda kuna kazi ya kufanya ya ziada. Hawa walimu wetu, hii performance ndiyo maana unakuta kuna ukinzani kati ya shule za watu binafsi na shule za Serikali. Hawa watu binafsi wana walimu wa kutosha kila somo. Shule za Serikali hakuna walimu wa kutosha. Shule za private kuna wanafunzi idadi ndogo darasani, shule zetu kuna 100,000 mpaka 200,000 kwenye darasa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa private wana motisha A moja kwa shilingi 100,000, hawa wa Serikali hawana motisha. Hawa wa private wana usafiri, wana chakula shuleni, wa Serikali hatuna. Hawa walimu wetu vijijini hawana nyumba. Leo tunazungumza matundu ya vyoo hayatoshi, lazima tukae kama Wabunge tuzungumze hali halisi. Hii imesababisha Profesa kwa kweli katika sehemu ambayo mimi mlinikwaza sana Wizara ya Elimu ni kitendo cha kundoa ranking. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani shule tunajua kabisa kwamba kama mwalimu analipwa vizuri, kama mwalimu ana usafiri, maeneo mengine wana ratiba ya chakula, halafu ana wanafunzi wachache, anaweza akamfuatilia mwanafunzi mmoja mmoja, obvious performance ya huyu wa wanafunzi wachache itatofautina na performance ya mwalimu ambaye ana wanafunzi wengi na hana sehemu ya kufikia na ana madeni na mshahara ni mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo lazima tulizungumze. Unapotaja shule imefanya vizuri, hivyo ni vigezo. Tunazo maabara ambazo ni mbovu hazijakamilika. Wenzetu wana maabara na vifaa. Tuna walimu wachache wa hesabu. Hivi kama una shule ambayo ni form one mpaka form four, hakuna mwalimu wa hesabu, mnatarajia apate A kwenye mtihani? Hiyo miujiza inatokea wapi? Sasa Profesa ungetuonesha mpango wa Serikali kupata walimu wa hesabu wa kutosha nchi hii, mpango wa Serikali wa kuleta walimu wa sayansi wa kutosha, mpango wa kuajiri walimu wa Tanzania ambao wako mtaani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa yako, Profesa sasa hivi vijana wetu wamekata tamaa kwenda kusoma masomo ya ualimu. Wanaona kama ni fani ambayo hawapati ajira huko mitaani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa yako Profesa sasa hivi vijana wetu wamekata tamaa kwenda kusoma masomo ya ualimu, wanaona kama ni fani ambayo hawapati ajira huko mitaani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe jambo hili pia liangaliwe upya, tupeleke walimu, tuboreshe mazingira ya kazi watoto wetu wasome vinginevyo kuzuia ranking eti wanafanyabiashara unajidanganya tu. Walimu wana magrupu, wanafunzi wana magrupu, wazazi wana magrupu, wanafunzi tunawasiliana na ukweli hata mimi watoto wangu wanasoma private.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtoto wangu wa form two anaweza akamshinda mwanafunzi wa kawaida wa form four mimi naangalia mimi ni mwalimu naangalia hata wanacho kifundisha, mazingira ya kufundishia na kujifunzia lazima yaboreshwe. Kwa hiyo, hilo lifanyike vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mimi ni Mbunge wa Tarime Vijijini jirani na Kenya. Kenya walimu wa Serikali ndiyo wanalipwa vizuri zaidi kuliko private, nenda ufanye research. Kwa hiyo, inamaana Kenya unapoenda kuomba kazi walikosa kazi za Serikalini ndiyo wanaenda private, kwanini? Wanalipwa vizuri zaidi na motisha ni kubwa. Tunaweza kuiga jambo zuri si vibaya tukaiga na kwa maana ya kuanza kuboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, muingiliano na usimamizi wa elimu ni kweli kuna mapungufu kwenye private, wana michango mingi, wana masharti mengi lakini tuwe na chombo huru cha kuwasimamia. Hivi nimeamua kupeleka mtoto wangu private kwa kipato changu alafu unakuja kuniwekea masharti, tuboreshe shule za Serikali ambazo wananchi wengi masikini wanapeleka watoto wao. Watu walipeka Kenya, walipeleka Uganda, walikuwa wamerudisha, kwa mtindo wa sasa hivi tena watu wameanza kwenda Kenya na Uganda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuboreshe shule za Serikali, tuajiri walimu, tujenge maabara, tuboreshe huduma motisha alafu tushindane. Ila kwenye level ile ya chuo kikuu mimi natofautiana na wenzangu, kwamba mtoto wa waziri akope sawa sawa na mkulima kule Kangeliani, kule Nyabitucho, mimi nadhani tuliangalie. Vigezo vya mikopo ya elimu ya juu vinaweza kuangaliwa visiwe fixed. Mtu alikuwa ni mtumishi angeweza kusomesha mtoto, sasa amestaafu awe anaumwa, au mtu siyo Mbunge tuangalie vigezo hali halisi ya maisha ikoje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusikalili mambo, maombi yangu Mheshimiwa Waziri nina shule zangu sita nguvu za wananchi, shule ya Kubiterere, Kimusi, Nyagisya, Barata halafu Inchugu, Nyanungu hizi shule mpeleke wakaguzi kule zifunguliwe. Wananchi wangu wamechanga pesa wenyewe, wamejenga shule, wanataka watoto wao wasome ili tushindane na watu, kwetu tulichelewa sana kwenda shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba hiyo Mheshimiwa Waziri hilo lifanyiwe kazi lakini wale wakaguzi wa udhibiti ubora wale hawana hata magari, posho zenyewe wanaenda kukagua huku awajalipwa wamekopwa, wanatangulia kazini halafu unataka akakague shule nzuri aridhike. Unakuta wanaficha ficha hata wamepokelewa wakapewa tu chakula, akapewa sehemu ya kulala, akahifadhiwa wanakaguaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, equip hiyo department ya udhibiti ubora watu wawe fame wawe sawa sawa wakague na vigezo tuvijue na kusiwe na meanders. Hata mkifungia shule kwenye matokeo, watoto wanaumia sana. Watoto wametoa hela mamilioni unafuta matokeo, unaadhibu watoto na wazazi, adhibu shule, adhibu wale wataalamu wetu msiumize wazazi wanaumia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho niunge mkono hoja ya Mheshimiwa Profesa Palamagamba Kabudi, mwalimu wangu nilitaka niwaombe Waheshimiwa Wabunge. Mkiangalia kwenye uchaguzi ukitaka kujua anachozungumza Mheshimiwa Profesa Palamagamba ni kwamba wakati wa uchaguzi hivi ni wananchi wangapi ambao walishindwa kupiga kura? wanaandikiwa ni wazi kwamba ni wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tupeleke mfumo elimu ya watu wazima kwa kila kijiji wale ambao wapo tayari kusoma, wasome kuna wengine hawasomi kwa sababu hawana nafasi, kuna wengine wamesoma hakusoma sana malezi, tutoe fursa kwa wote kama ambavyo tumetoa fursa kwa wale ambao wamepata ujauzito na changamoto mbalimbali ya kurudi shuleni basi na hawa ambao hawakusoma vijijini wasome kwa hiyari na walimu wapo na vijana wetu wawepo. Pendekezo muhimu la mwisho kwenye ualimu… (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita, ahsante sana. Kengele yako imelia.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hii hoja ni muhimu niunge mkono kwa nguvu zote tupate mjadala wa kutosha kwenye mitaala ya elimu. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi. Kwa niaba ya Wananchi wa Tarime Vijijini, Wananchi wa Tarime na Wananchi wa Mkoa wa Mara tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka shangwe kubwa katika Mkoa wa Mara, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na Mungu ambariki sana aendelee kuwa na sikio la kusikia kilio cha wanyonge na hasa kutoka Mkoa wa Mara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Wizara ya Ardhi ina changamoto nyingi na niwe mkweli, mimi ni miongoni mwa watu ambao wana migogoro mingi yaani kule Mkoa wa Mara lakini na mikoa mingine. Kwa hiyo la kwanza nimwombe Mheshimiwa Waziri awe na ngozi ngumu katika eneo hili. Ameshikilia kura za Chama cha Mapinduzi, ameshikilia kura za Mheshimiwa Rais, ameshikilia kura za sisi Wabunge kurudi hapa Dodoma kuendelea kukalia kwenye viti hivi. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri ni lazima ajipange vizuri katika eneo hili. Huo ndiyo ukweli wa Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Katiba yetu ya Mwaka 1977, Toleo la Mwaka 2005 Ibara ya 8 naomba ninukuu Ibara ya 8(1).

“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, na kwa hiyo:-

(a) wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata mamlaka na madaraka yake toka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii;

(b) lengo kuu la Serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi;

(c) Serikali itawajibika kwa wananchi;

(d) wananchi watashiriki katika shughuli za Serikali yao kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma hii ibara kuonyesha kwamba kitendo cha kutotatua migogoro vizuri ya ardhi kinawakwaza wananchi walio wengi na hao wananchi wanaipenda Serikali yao. Maendeleo yote ambayo yanafanyika na Mheshimiwa Mama Samia ni kwa ajili ya wananchi. Mheshimiwa Waziri katika eneo hili, lazima ibara ya 8 hii niliyosoma izingatiwe sana. Maana yake katika mipango yote ya Serikali ya ardhi lazima tuangalie haki za watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika maeneo mengi kule Tarime, Wizara ya Ardhi ndiyo inamiliki Mthamini Mkuu wa Ardhi. Akishafanya tathmini ya ardhi, wanawasiliana na Wizara ya Madini, halafu mgodi unaambiwa kwamba ulipe. Nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri kwamba, kitendo cha watu wa Tarime maeneo ya mgodi chini ya ardhi kuna dhahabu, wanalipwa ekari moja shilingi milioni tano, bei ambayo hata ukienda mtaani Tarime huwezi kununua ardhi ekari moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo hicho kinafanya tufikirie zaidi, kwa nini eneo ambalo chini kuna dhahabu unalipa ekari moja shilingi milioni tano sawasawa na ardhi ambayo unaweza kufidia ujenge choo au ujenge zahanati? Wizara haioni kuna sababu ya msingi sana kuangalia viwango vipya vya bei ya ardhi na hivyo ndiyo vinapelekea migogogro mingi kwa sababu wananchi wanajua ukishatoa ardhi yetu unaenda kuchimba dhahabu au vito vingine na unapata fedha nyingi zaidi. Hili ni vizuri pia likaangaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile migogoro ya ardhi, Waheshimiwa Wabunge nataka nishauri, ukisikiliza vizuri Hotuba ya Kamati yetu wanasema fedha zilizotengwa kwenda kutatua migogoro ni kidogo ukilinganisha na fedha ambayo imepelekwa kwenda kulipana posho, allowance, mafuta na vitu vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwashawishi Waheshimiwa Wabunge, katika eneo hilo Mheshimiwa Waziri lazima atuambie tubadilishe sisi hapa ndiyo Watanzania. Fedha nyingi iende kutatua migogoro ili uchaguzi ujao Chama Cha Mapinduzi kisiadhibiwe ili uchaguzi wa Mama Samia 2025 tupate ushindi wa kishindo. Hatuwezi kushinda vizuri uchaguzi kama watu wanaenda kwenye uchaguzi na vinyongo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna taarifa, Kamati ilimwita Mheshimiwa Waziri na Mwenyekiti hapo yupo, wametusomea Waheshimiwa Wabunge, tusome Taarifa ya Kamati, tuunge mkono Waziri atueleze, kwa nini aliamua kupanga fedha kidogo ya kwenda kutatua migogoro kwenye majimbo yetu na fedha nyingi kwenye safari na posho? Hilo ni muhimu sana tukaambizana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme hii migogoro kwa mfano kule kwangu, leo tunapozungumza ukizungumza habari ya Komarela, Kewanja na Nyamichere, Mthamini Mkuu wa Serikali ameenda ametoa notisi kwamba watu eneo hili msiendeleze, halafu baada ya muda fulani anaambiwa kwamba usilipe. Wakati fulani wanafanya tathmini ambayo wanalalamikiana. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri akijipanga vizuri maana yake kwangu na Wabunge wengine migogoro ya fidia itakwisha. Kwa sababu watu wake ndiyo wanafanya kazi ya uthamini katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina migogoro ya ardhi ile ya Komarela na mgodi, nina mgogoro wa ardhi Mheshimiwa Waziri wa siku nyingi kwa Korutambe na Remagwe, nina mgogoro wa ardhi pale Kebweye na Kyoruba, nina mgogoro wa ardhi Mwito na Msege, nina mgogoro wa ardhi Mwito na Gibaso, nina migogoro mingi ambayo hii inapelekea amani isiwepo na watu wanapoteza imani. Mheshimiwa Waziri anayo kazi hiyo, Mheshimiwa Rais amempa kipande muhimu kweli kweli, awe mpole apokee maoni, awe humble, asikilize na atatue migogoro na timu yake aiambie kwamba kule kuna wananchi ambao lazima wasikilizwe vizuri ili kuondoa changamoto tulizonazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimshauri Mheshimiwa Waziri, katika utatuzi wa migogoro wamesema kamati hapa, tunajua kuna Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999, lakini vile vile tuna Sheria ya Fidia ya Ardhi ya mwaka 2016 na Kanuni zake za mwaka 2018, lakini ushirikishwaji. Wasiende kusoma document kama zilivyo kwa wananchi wa kawaida, wanawaamrisha. Waende kwenye vijiji, waite Viongozi wa Vijiji, Wabunge na Madiwani watushirikishe tuwape maoni. Tukienda kutatua mgogoro hatumwachii Waziri peke yake, tunataka mgogoro ukitatulika, Serikali inufaike na wananchi wanufaike na amani itawale na maendeleo yapatikane katika eneo husika, tusiamrishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Kamati kwamba jambo hili wameliona na ndicho kilichofanyika katika maeneo mengi sana, lakini pia kamati imeomba kwa kuwa na mimi naunga mkono, Taarifa hiyo ya Mawaziri nane ije hapa Bungeni, kila mtu aone eneo lake walipitia wapi, GN inasema nini, tusome tuweze kuwashauri. Hatuwezi kuwa Wabunge tena sehemu ya kulalamika, wakati sisi ndiyo wasemaji kwa niaba ya Watanzania ambao walituamini kuja hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwombe Mheshimiwa Waziri, walipokuja Tarime kule, msoma ramani wake alisema ile GN ya mwaka 1968 ina ramani (surveyed map) ya mwaka 1968. Wakasema hii ramani kwa haraka haraka tumeacha kwenye gari, tukienda kwenye mkutano tutawapa. Inaombwa tangu siku ile mpaka juzi, mpaka jana, mpaka leo haipo. Tunahitaji Tarime pale kwenye ile migogoro ya ardhi tupate GN ile tunayo ya mwaka 1968, tupate ramani, (surveyed map) ya mwaka 1968 mjadala uanzie hapo ili kuweza kuondoa mzizi wa fitina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mapendekezo hapa kwa Mheshimiwa Waziri. Migogoro ya ardhi iliyopo, ukienda Nanyumbu kuna mgogoro, ukienda Kiteto kuna mgogoro, ukienda sijui wapi kuna mgogoro. Mkoa wa Mara kuna mgogoro wa ardhi pale Rorya, Serengeti, Bunda pale Nyatwali, Tarime Mjini na Vijijini. Hii migogoro huu ni Mkoa mmoja wa Mara. Sina taarifa nzuri ya mikoa mingine. Nataka nimwombe tena Mheshimiwa Waziri, shemeji yangu, mke wangu ni Msukuma, Waziri mwenye nguvu kubwa tunaomba sasa aonyeshe Udaktari wako kwenye kazi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatamani tunapoenda kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa atumalizie migogoro ya ardhi kwa watu wetu. Tunatamani uchaguzi wa mwakani tusihukumiwe kwa sababu ya migogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuombe pia kwenye kiti hicho, ni vizuri Wabunge tusome Ripoti ya Kamati hii, tuisimamie Serikali, tuishauri vizuri. Mheshimiwa Rais ameshampa dhamana Mheshimiwa Angeline Mabula kutatua migogoro ya ardhi.Naomba Mheshimiwa Waziri avae kiatu kimtoshe afanye kazi ya kutatua migogoro hii. Tumechoka kulalamikiana na kuja kulia katika Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja hasa Ripoti ya Kamati ije Bungeni tujadili ili Watanzania wapate amani ya kwao. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Tangu asubuhi jina langu linakosewa. Ninaitwa Mwita Mwikwabe Waitara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kwa nafasi ya kuchangia Wizara ya Maliasili na Utalii, na nataka nitumie nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Tarime Vijijini, kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwa sababu ya maelekezo yake mazuri ambayo angalau hali ya utulivu imerejea kule jimboni kwangu. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kauli yake ambayo aliitoa hapa Bungeni amabyo pia iliendelea kupooza watu wa Tarime. Nimshukuru pia Mheshimiwa Spika, alitoa mwongozo mzuri mara kadhaa. Lakini pia nimshukuru sana Mheshimiwa Comrade Mohamed Mchengerwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huyu Waheshimiwa Wabunge ndiye Waziri wa Maliasili wa kwanza kufanya mkutano Tarime na ukaisha kwa amani watu wakacheka wakaondoka. Na Mheshimiwa Mchengerwa Wazee wa Tarime wamekuandalia zawadi, siku ukirudi Mheshimiwa Waziri wa Kilimo kama ulivyoahidi kabla ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenda pale utapata kitu kinaitwa kichuli ya kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru pia Mheshimiwa Mchengerwa, anajua kutibu makovu. Mheshimiwa Mchengerwa namna ambavyo uliingia Tarime uliacha hawa wanaitwa Majeshi ya Uhifadhi pembeni ukaenda kiraia ukaingia moja kwa moja kwenye mkutano, walijenga imani kuanzia muda ule mpaka unaondoka Tarime, nakushukuru sana. Na ile, walisema tu kuwa Mheshimiwa Mbunge tukipata watu kama akina Mheshimiwa Mchengerwa kwenye migogoro, hata kama mgogoro hauishi watu wanapona bila kupata matibabu, hongera sana Mheshimiwa Mchengerwa. Ndiyo maana unasifiwa namna ambavyo uli-handle mambo ya Michezo. Hii ni Wizara ambayo ilikuwa haina jina kubwa lakini ameipa heshima kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaturajia sisi ambao tunakaa karibu na Hifadhi ya Serengeti Mheshimiwa Mchengerwa ufanye mambo makubwa zaidi yale ya Wizara ya Michezo, na usuluhishe migogoro kwa sababu asilimia 50 ya nchi hii ni hifadhi za Taifa. Kwa hiyo ukiweza kuleta amani na mahusiano mazuri kati ya wananchi na hifadhi zetu maana yake kura za Mama Samia, kura za Wabunge, kura za Madiwani na kura za Chama cha Mapinduzi ziko kwenye mikono salama. Tunakutakia kila la kheri katika jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Mhcengerwa alipokuja kule alipewa ujumbe, kwamba pamoja na kwamba yamefanyika mambo mazuri sana lakini kauli ya Mheshimiwa Naibu Waziri watu wa Tarime wanahitaji waombe radhi kwa kauli ile. Kwamba yeye ametumwa na Serikali ni kauli ya Mama na kwa hiyo kule si chooni. Watu tisa walikufa wakapotea mpaka leo; aliulizwa na akina mama wenzake. Mheshimiwa Rais ndiye mfariji namba moja wa Taifa kwa mujibu wa Katiba. Viongozi lazima mkinge kumuongelesha Mheshimiwa Rais mambo maovu ambayo hayana maana sana, lakini pia kutoa matumaini pasipokuwa na matumaini, kupeleka amani mahali ambapo hakuna amani. Kauli ile tu Mheshimiwa Waziri ndiyo imebaki kwenye Wizara yako; mengine yote Mungu akubariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa humu Bungeni ilisheheni vitu vingi sana, alizungumza namna ambavyo ng’ombe wa watu wanataifishwa, alionyesha mahusiano mabovu yaliyopo, aliangalia shida ya malisho, akaangalia shida za kilimo, akaangalia kila kitu. Mimi ningekushauri, pamoja na Waziri wa Ardhi, ile hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ya hali ya migogoro nchini ichukuliwe, kila Waziri achukue kipande chake atengeneze mpango kazi wa utekelezaji, mtakuwa mmetibu sehemu kubwa sana ya migogoro ya ardhi na mahusiano katika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, amesema jambo zuri na wenzangu wamezungumza. Kwamba, migogoro hii huwezi kufanya peke yako, kuna viongozi kule. Kuwa kiongozi, kwamba umekuwa Waziri au umekuwa si kwamba umekuwa na akili nyingi kuliko wote, shirikisha. Kuna watu wana utashi pale na kuna watu wana uelewa. Timu uliyosema utaunda tushirikishe tukushauri ni jambo jema, utapata mambo mengi sana na utamsaidia Mheshimiwa Rais na migogoro; tunaamini kwamba bajeti ijayo malalamiko ya Mbuga kuwalipa wananchi itapaungua humu Bungeni. Kwa hiyo tunakushukuru kwa hatua hiyo ambayo umeona. Mimi namfuatilia; hata kama amekaa Wizara tatu kwa miaka mitatu, ni kwamba Mheshimiwa Rais anamtumia vizuri, kuna vitu vya msingi sana kwake na ndiyo maana watu wote wanamuunga mkono katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo migogoro kule Mkoa wa Mara. Hifadhi ya Serengeti asilimia 75 iko katika Mkoa wa Mara. Lakini mgogoro huu utaukuta Bunda, Tarime, Serengeti, na unakwenda mpaka kule Arusha, mgogoro unaenda mpaka Simiyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba, ni vizuri ukae vizuri na watu hawa ili uweze kutatua. Mnapokwenda kujadili migogoro ya hifadhi msione kuwa wanyama ni bora kuliko watu. Kuona kwamba wanyama ni bora lakini pia na watu ni bora pia tuna wahitaji. Kama tunafanya uhifadhi tunufaike ni kwa ajili ya watu wetu. Ni vizuri watu wasilie wanyama wanacheka, watoto wafurahie matunda ya nchi hii. Kazi hiyo umepewa Mheshimiwa Mchengerwa, na tunaamini kwamba unaweza ukaifanya vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano tunayo barabara ya kutoka Serengeti kule inaenda mpaka Ngorongoro, imeahidiwa ijengwe kwa kiwango cha lami lakini hijajengwa. Pale Serengeti hakuna hata uwanja wa ndege. Ukiuliza inakotoka bidhaa inayotumika pale hifadhini inatoka nje ya Mkoa wa Mara. Hakuna ajira, hakuna kazi kwa akina mama, vijana wetu wanazurura pale mtaani wanakutana hawapati ajira, mahusiano mema hayapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hata mazungumzo yanakuwa ya uadui mkubwa kwa sababu wanaona kwamba wanufaika ni watu wengine ilhali Hifadhi ipo kwetu. Kwa mfano Tarime, mimi nalalamika hapa kila siku lakini hakuna hata senti moja kama service levy kutoka Hifadhi ya Serengeti kuja Tarime pale. Sisi tunaambulia tembo kuua watu, tembo kula mazao, ng’ombe kupotea, watu kupotea, watu kufirisika na uhasama. Pia hata hiyo CSR hakuna mpango mkakati, ukiuliza hawezi kukuambia ni kitu gani hasa wanataka kufanya. Wanaweza wakachimba kisima leo kesho wakakuambia kisima kipo hifadhini. Tunaomba hii mipango pia iwekwe sawasawa ili watu waweze kunufaika vizuri, tunahitaji pale uwanja wa ndege ili tuweze kufanya kazi ya kitalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mheshimiwa Mchengerwa amekuja kule Kuhancha Golong’a na Nyanungu, yote tutazungumza lakini watu wangu pale ambao ninawawakilisha hapa Bungeni wanahitaji sehemu ya kuchungia mifugo yao, wanahitaji sehemu ya kulima, wanahitaji sehemu ya kuishi. Wale ni wakulima na wafugaji wala si wafanyabiashara. hata ukiwapelekea fedha wakila ikiisha watarudi palepale, na ndiyo maana walikwa na hasira kubwa. Lakini maneno yako yana matumaini, kwamba tulieni Mama anawasikiliza na utarudi mgogoro utaisha, na kwamba waendelee kulima. Kauli hiyo imeponya makovu yote ambayo ambayo yalikuwa yanakwamisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimuombe Mheshimiwa Waziri. Tulimpa risala Kalikatonga, alipata risala Nyanungu na Gorong’a, yale ndiyo maombi ya watu wa Tarime na mimi ndiye Mbunge wao; naomba ayafanyie kazi tutampa heko sana kwa kufanya kazi hiyo. Wale watu wana makovu tangu wakati wa uhuru. Ni wakati huu wa Mama Samia, kama Mama, mzazi, mlezi na mwenye huruma wapete unafuu wa maisha yao. Wao wana matumaini, wajenge nyumba za kudumu, mifugo yao iishi wasomeshe watoto ili wapate maisha bora sawa na Watanzania wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile hakuna namna ya kupata maji kule tofauti na kuchota maji ya Mto Mara. Kama mtaweka miundombinu pale kwa teknolojia ya kupata maji wakati wote tutawashukuru sana. Maji ya chumvi hata mimi nimekulia pale wote wamepeleka katika Hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuambie Mheshimiwa Mchengerwa jambo ambalo linajadiliwa sana kule Bunda. Habari ya Nyatwali imeleta taharuki kubwa na kwa kweli wanaona kama watu hawa wanabaguliwa. Tusifanye double standard, watu wale wa Ngorongoro wamepelekwa kule Kilindi wale wamepewa usafiri watu wa Tarime na Bunda waliona. Wamewezeshwa kwa miundombinu, kuna huduma za kijamii, kuna maji, kuna shule, kuna huduma za afya zinapatikana, wakapata pia na fedha ya kuanzia maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watu wa Nyatwali wakipewa milioni mbili hauwapi eneo la kwenda kuishi, wana makaburi yao, wana familia kubwa, wana watoto, wanasomesha, wakaanze maisha lakini mambo haya Mheshimiwa Waziri hebu jiweke ungekuwa ni wewe ungefanyaje? Ni very unfair. Hapa mimi naona ni kama kuna watu wengine wanapendwa zaidi wengine hawapendwi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mngetaka kutatua migogoro hii ni vizuri mkaangalia as whole, kwa ujumla wake. Wote ni Watanzania tunapenda hifadhi ziwepo, nchi ni ya kwetu lakini watu wasiishe kulalamika na kulialia kama wanabaguliwa. Kazi hiyo Mheshimiwa Waziri umepewa, mimi naamini unaweza kuifanya kazi hiyo, na nitakupa ushirikiano na Mheshimiwa Rais amekuamini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi hapa nilipo leo naweza nikaenda Nyanungu nikatembea mtaani kwa sababu Mheshimiwa Waziri ametoa kauli nzuri sana. Naweza nikaenda Kuyanja nikapokelewa nikapewa uji na Kichuli kwa sababu umetoa kauli nzuri. Nikienda Nyakatonga nitalala, nilikuwa siwezi kwenda kulala. Na kwa taarifa yako Mheshimiwa Waziri nilikuwa nimeamua nisiende maeneo yale mpaka mtakapo toa kauli. Kwa hiyo sasa Bunge likiisha nimeshapanga ratiba ya kwenda kuongea na watu wangu kwa kuwa Mama amesema mgogoro utaisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wote hawa wanampongeza sana Mheshimiwa Mchengerwa, wanampa ushirikiano na wanamuunga mkono Mheshimiwa Rais. Tunachotaka ni kutatua migogoro hii ya hifadhi na wananchi. Hifadhi iwepo, watu wawepo, maendeleo yawepo, watu wasome, watu wajenge na siasa iendelee, na 2025 tunataka Chama cha Mapinduzi kishinde kila kona kupitia kwako kwa kuondoa migogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo sishiki shilingi ninafuraha kubwa kwa kweli kwa Mheshimiwa Waziri nakuunga mkono kwa asilimia 100. Ahsante sana kwa nafasi.
Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kupata nafasi.

Mheshimiwa Spika, leo Waheshimiwa Wabunge wanafanya kazi ya Kikatiba, lakini vilevile nimepata meseji nyingi kutoka kwa watu wa Tarime na Mkoa wa Mara naomba sasa wasikilize maelezo ya chifu. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, la kwanza ni kwamba haya ni makubaliano kati ya Tanzania na Dubai kwenye mambo ya kiuchumi na mambo ya kijamii, jambo la pili kutakuwa na nafasi ya Serikali kutengeneza mikataba midogo midogo kulingana na eneo mahsusi na masharti yake, hili ni vizuri likaeleweka sana, lakini waswahili wanasema wasiwasi ndio akili. Kitendo cha Watanzania kuwa na wasiwasi na hofu ni jambo la kawaida. Mheshimiwa Rais amesikia, Serikali imesikia, Wabunge wamesikia, chama kimesikia, wataalam wamesikiana, watazingatia yote ili katika utekelezaji wa mikataba hiyo hofu ya Watanzania ikapate matibabu ya kudumu na mwisho wa siku nchi iweze kupata manufaa ambayo tunatarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile yako mambo ya msingi tu, mtu mmoja akaniambia mnauza bandari, hata ardhi watachukua. Kwenye Ibara ya 8 imezungumza namna ambavyo ardhi itatumika, imejibiwa hiyo hoja, lakini pia amezungumza habari ya ajira, imezungumzwa kwenye Ibara ya 13, local content, wazawa watapata ajira, maboresho, mafundisho na huyu mwekezaji akitoka lazima aache utaalam katika nchi yetu, lakini pia wamezungumza hoja ya kwamba mikataba haivunjwi, Ibara ya 23(4) unarudi Ibara ya 20 inaeleza utaratibu utakaotumika namna ya kuondoa migogoro hiyo.

Mheshimiwa Spika, lakini mimi hii ni awamu ya pili Bungeni hapa sijawahi kujadili azimio lolote hapa likiwa na mkataba wa wazi kama hivi. Nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya. Leo kila Mbunge anasimama hapa anachangia akiwa na mkataba kifungu kwa kifungu tunajiridhisha haikuwahi kutokea, sasa nauliza ambao wanalalamika hapa, hivi nani amewahi kuona mkataba wa ujenzi wa SGR kutoka Dar es Salaam - Morogoro mmeona? Kutoka Morogoro - Dodoma, mmeona? Kwa nini hamjaona? Nani ameona mkataba ule wa Daraja la Tanzanite, Dar es Salaam, mmeona? Mmeona mkataba wa Kigongo – Busisi mmeona? Mmeona mkataba wa Bwawa la Mwalimu Nyerere? Maana yake Mheshimiwa Rais anataka uwazi katika jambo hili, ameruhusu Watanzania wajadili, watoe maoni na yupo tayari kufanya maboresho hata hapa tulipo anaangalia mijadala ya Wabunge wake, anasoma kwenye mitandao ataifanyia kazi vizuri ili Watanzania waweze kunufaika kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kwa mara ya kwanza kupata nafasi nzuri sana ya kujadiliana, lakini mimi nimekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi hakuna Mtanzania mwenye akili timamu ambaye atapinga uwekezaji katika bandari zetu zote hakuna atakayepinga, cha muhimu ni kwamba kama tunawekeza tunawekeza wapi, kitu gani, tunapata nini, maslahi mapana ya nchi yetu? Hiyo ni muhimu sana na ni ukweli kwamba tumezidiwa sana na wenzetu kwenye taaluma na teknolojia. Tunataka wenye uwezo waje kuwekeza ili sisi Watanzania na wataalam wenye nafasi wahakikishe kwamba maslahi ya nchi yanazingatiwa.

Mheshimiwa Spika, lakini pia kwenye kitabu chetu cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania ukurasa wa tatu, tarehe 26 Aprili, 1964 Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Watu wa Tanganyika waliungana na kuwa nchi moja na kwa hiyo, ni Taifa moja, lakini pia kwenye kitabu cha historia, sisi ni wajukuu wa Mwalimu Nyerere hebu tuwakumbushe watu mambo haya.

Mheshimiwa Spika, ukisoma kitabu cha Mwalimu Nyerere historia yake, wakati anazungumza anataja misingi ya Chama cha Mapinduzi, CCM ni chama cha wanyonge chenye kupigania vita ya ubepari na unyonyaji, lakini binadamu ni sawa, hakuna ubaguzi wa kidini, kikabila na kijinsia, lakini pia kudumisha na kutetea Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na Mwalimu alisema kwamba yeyote atakayetaka kuvunja Muungano hatakomea hapo, ataendaelea kuwagawanya watu kwa misingi ya Ubara na Uzanzibari; Uzanzibari na Upemba na kuendelea unaweza ukasema Ukurya na Uchaga; Umakonde na Umatengo na kuendelea.

Mheshimiwa Spika, ni kwamba Mheshimiwa Rais Mama Samia, ni Rais wa kwanza mwanamke katika nchi hii. Tulimpa heshima Baba wa Taifa akaitwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ninapendekeza huyu aitwe Mama wa Taifa kama ambavyo tulimpa Mwalimu Nyerere hiyo heshima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la pili ni mama ambaye alipoingia madarakani aliahidi kwamba kazi itaendelea na kazi inaendelea; lakini Mheshimiwa Rais aliahidi kwamba hakuna kitakachosimama na hakuna kilichosimama, lakini Mheshimiwa Rais huyu kwa huruma yake alimkuta mtu yuko gerezani akamtoa, akaenda akala pale Ikulu akakaa naye, lakini huyu ameruhusu mikutano ya vyama vya siasa, mama huyu pia ametoa hata ruzuku wanafanya siasa leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ningekubaliana na ndugu yangu yule kama angekosoa vifungu kwenye muswada huo au kwenye makubaliano hayo. Kitendo cha kusema kwamba Mheshimiwa Rais kwa sababu ni Mzanzibari anauza Bandari ya Dar es Salaam na Ndugu Profesa Makame Mnyaa Mbarawa kwa sababu ni Mpemba, ni Mzanzibari anauza Bandari ya Watanganyika, Mheshimiwa Mbowe amemkosea sana Mheshimiwa Rais, amewakosea sana Watanzania na Mheshimiwa Mbowe anapaswa kumwomba radhi Mheshimiwa Rais kwa kumdhalilisha, lakini kuleta dalili mbaya za kuligawa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatuwezi kujadili hoja za msingi za Watanzania kwa misingi ya tulipotokea. Profesa Kitila amesema amekuwa Mbunge wa Ubungo, mimi nimekuwa Mwenyekiti wa Mtaa pale Kivule, Dar es Salaam, nimekuwa Mbunge wa Dar es Salaam hata Mlimani nilikuwa Rais wa Serikali ya Wanafunzi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kina Watanzania wote na watu kutoka nje wangeniuliza mimi ni Mkurya kutoka Kanganiani nisingepata fursa hiyo.

Mheshimiwa Spika, nataka nikwambie kitendo hiki viongozi wa nchi hii lazima tukichukulie hatua. Kwenye Vyama vya Siasa, kwenye sheria yetu Political Parties, inataja mahsusi kwamba Chama cha Siasa lazima kioneshe Ibara mahsusi ambayo italinda Muungano wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama tutaruhusu mijadala ya design hii ya kuanza kubagua ukimsema Rais wa nchi umemsema Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, nataka niwambie Watanzania, wanachama, viongozi, wafuasi wa Chama cha Mapinduzi hatuwezi kukaa kimya kwa mambo kama haya. Tunataka watu walete hoja za msingi, watujengee hoja, watukosoe na Rais mwenyewe amekwishasema akosolewe kwa hoja. Tena amesema wakifanya vikao vyao wakisema ya kwao, Rais ametuzuia amesemea tutoe hoja tusitukane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niwaombe Wabunge wa Chama cha Mapinduzi hii ni dalili nzuri kwamba watu hawa hawawezi kupewa nchi, wametuonesha wenyewe. Mheshimiwa Rais ajiandae 2025/2030 njia iko wazi, abebe msalaba huu, sisi tumemuamini na wanawake wanaweza na chenji inabaki. Tunataka tumpe heshima Mheshimiwa Rais ili atoe nafasi kwa wakina mama wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wewe ni mwanamama Watanzania tunakuamini, Wabunge tunakuamini, hauwezi kuleta hapa mkataba ambao ni wa hovyo. Wewe ni Wakili Msomi, Daktari wa Falsafam PhD ya Sheria, haiwezekani. Kwa hiyo, wasituone kwamba sisi Wabunge wa CCM hatuna akili sio kweli, tunajua sana. Hiyo kazi ambayo wanafanya kwenye mitandao, hayo mambo ambayo wanapotosha tuna uwezo mkubwa kuliko wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais katika jambo hili atuache tushughulike na watu kidogo, tulikuwa tumepoa. Tunaweza kufanya ambayo wanafanya zaidi yao. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Waitara, sekunde 30 malizia.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nataka niwambie watu wa Tarime, huyu mama Mheshimiwa Rais ndiye aliyesema mgogoro wa hifadhi kule utakwisha; fidia ya Nyamongo; mama huyu ndiye amesema; kulikuwa na viongozi wa ajabu ajabu ametuondolea; mama huyu ameahidi miradi mikubwa ya nchi; mama huyu ndiye amepeleka VETA Nyamongo; na mama huyu ndio ameahidi zile ambulance. Tunapoongeza mapato ya bandati maana yake madarasa yatajengwa, vijana watapata ajira na mradi wa maji kutoka Rorya – Tarime – Nyamwaga – Nyamongo utakamilika, hizi ndizo fedha ambazo zimekuja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo watu wa Tarime, watu wa Mara na Watanzania waelewe Wabunge wa CCM wanaunga mkono mambo ya msingi na hapa tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho nataka niwambie Watanzania...

SPIKA: Mheshimiwa Waitara, ahsante sana.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, haiwezekani Mbunge wa Chama cha Mapinduzi uje ukae humu ndani uje upinge hoja ya Mama Samia utakuwa hujitaki. Ukitaka kutupinga toka nje, tafuta chama kingine, hii ni hoja ya Chama cha Mapinduzi, ni hoja ya Mama Samia lazima tumuunge mkono iwe jua, iwe mvua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono azimio kwa nguvu zote na Watanzania watuelewe, watuunge mkono, tukachape kazi. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaomba nijibu hoja ambayo imejitokeza hapa inasema kwa nini hatupongezi.

Kwenye hesabu ya form five na six au wale ambao mmesoma Additional Mathematics kuna topic inaitwa Logic, yaani kama una true/false maana yake ni false, kama una false/ true unapata ni false, kama una true/true ni true. Sasa sisi hatupongezi wala hatuungi mkono hii bajeti kwa sababu nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, kwenye bajeti ya mwaka 2016/2017 Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ilipata fedha asilimia 18 tu, tunapongezaje hapa? Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ni asilimia 3.31, unapongeza nini? Wizara ya Maji na Umwagiliaji ni asilimia 8.4, unapongeza nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mmezungumza habari ya madini hapa mnataka sisi tupongeze lakini mikataba hatujaiona, misamaha mliyotoa hatujui, wahusika hawajashughulikiwa, mchanga ndiyo umezuiliwa, dhahabu inaendelea kuzolewa, Wanyamongo pale Tarime wanapigwa wapo ndani wamevunjwavunjwa, tuna makaburi mengi, tuna makovu, kuna watu ambao hawawezi kuzaa kwa sababu wamekunywa sumu madini ya zebaki, tunapongezaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja wapo ya sababu ambazo Mheshimiwa Waziri ametaja ya bajeti kutotekelezwa, ametaja Afrika kwamba uchumi haujakua kwa sababu ya utawala bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kule Mawazo Katoro amenyongwa mchana kweupe, alikuwa kijana wetu wa Upinzani, wa CHADEMA, ameuawa katika utawala huu, tunapongeza nini? Tunapozungumza, Ben Saanane hayupo na Serikali haitoi majibu, huyu ni kijana Mtanzania mzalendo, tunapongeza nini?

T A A R I F A .....

HE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, imepita kama upepo, yaani siipokei, siikubali, ndiyo utaratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee. Viongozi wa Serikali na Chama Tawala ni muhimu mkawa makini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nasema tu kwamba naomba muda wangu ulindwe. Mnapotaka tujadili kama Taifa, kama Bunge moja ni muhimu pia tukaangalia vipande vipande vya matukio mbalimbali. Kwa mfano mmeteua watu ambao wanaiwakilisha Serikali katika maeneo mbalimbali, lakini tunapozungumza hapa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hai anazuiliwa kufanya kikao cha halmashauri, Mstahiki Meya wa Ubungo yupo ndani, amewekwa lock up. Tunapozungumza Mkuu wa Wilaya anaongoza wenzake na Jeshi la Polisi ambalo tunalipa kodi kuwapa mishahara na nguo na kila kitu, wanakwenda kuharibu shamba la Mtanzania mmoja amewekeza, Mheshimiwa Mbowe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wakati mwingine mnaposema tuungane mkono kwa kweli tunashindwa kuwaelewa, haya mambo tunayounganisha, connectivity, inakuwaje? Kwa sababu kama mnataka tuungane katika mambo ya msingi, humu ndani kwenye Bunge hili wenzetu akina Mheshimiwa Halima Mdee, Mheshimiwa Ester Bulaya wamewajibishwa hapa kwa adhabu kubwa kubwa. Juzi umeombwa mwongozo mtu anaomba mwongozo, Mwenyekiti anasimama anasoma mpaka vifungu, maana yake hilo jambo limeandaliwa limeandikwa. Sasa mnaposema tuunge mkono ni muhimu sana tukubaliane tunataka tufanye kitu gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa nini hatuungi mkono, kwa mfano Mheshimiwa Dkt. Mpango; mjukuu wangu wala sina shida na yeye; Mheshimiwa Dokta Mpango kwenye ukurasa wa 19, watu 7,277 wamefunga biashara zao. Hawa walikuwa wanasomesha, wana wagonjwa, wana watoto, wana kodi wanalipa maana yake zote zime-paralyze sasa unaungaje mkono, hili ni jambo kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kodi ya majengo, sisi kule Dar es Salaam pamoja na kwamba kuna ufugaji mdogo mdogo, kodi ya majengo tulikuwa tunapata shilingi bilioni 18 kwa mwaka kwenye taarifa hapa, Serikali kupitia TRA imekusanya shilingi bilioni 15, Mkoa wa Dar es Salaam peke yake ni shilingi bilioni tisa, unapigaje makofi katika eneo hili? Halmashauri imeondolewa kukusanya kodi, Halmashauri imenyang’anywa… (Makofi)

T A A R I F A

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Huyu ni Mbunge wa kule Tabora, Wilaya yake ni maskini kweli kweli, kwa hiyo nadhani tutafute hela hapa, yule nimefika kwake Sikonge haki ya Mungu hana hata lami yule, acheni kupiga makofi ya kishamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nasema, mimi naangalia upande wa negative, kwamba hawa watu walivyoacha biashara, imewa-affect, hii kama wamefungua au wamenufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine, nimesema kule kwenye halmashauri hizi Wabunge wanapiga makofi sana lakini najua hii bajeti ikiisha mwaka ujao kila mtu atakuwa analia na kusaga meno hapa kwa sababu Halmashauri nyingi zinatumia kodi ya majengo, imenyang’anywa ilikuwa hata mabango, yamechuliwa asilimia tano akina mama na asilimia tano vijana, tunakwenda kuwakopesha nini? Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Mpango lazima aje na utaratibu wa kufanya replacement ya fedha ambayo imeondolewa halmashauri ili Halmashauri iweze kujiendesha. Mvua ikinyesha kidogo tu Halmashauri nyingi hazipitiki, hakuna miradi ya maji, tunasema halmashauri. Mheshimiwa Waziri alipoulizwa swali hapa anasema Mbunge ni Diwani aende kwenye Halmashauri wakae wajadiliane, mnajadili nini kama fedha hazipo? Mnajadili nini kama vyanzo vya fedha vimeshanyang’anywa? Kwa hiyo, haya ni mambo ambayo ni muhimu mkaangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amekuja na hoja, kwenye halmashauri zetu ilikuwa mtu akifanya kosa dogo anapigwa faini shilingi 50,000, imepanda mpaka shilingi 200,000 mpaka 1,000,000, mwaka mmoja mpaka miaka miwili, sasa hawa wananchi wa kawaida ambao ni maskini tunaowatetea tunawatengenezea adhabu kubwa na vifungo. Badala ya kuwaelekeza na kuwafundisha namna ya kufuata sheria tunatunga sheria za kwenda kuwakandamiza wakafungwe zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema Machinga waende wakajiandikishe, ni jambo zuri zaidi, lakini eti ambaye hakujiandikisha atafungwa sasa mechanism ikoje kuwatambua hawa watu? Nani anafanya utaratibu huo ili akwame? Nadhani tungeelekeza nguvu kufundisha watu wetu na kuwaelekeza kufuata sheria, tusiende sana kwenye adhabu mbalimbali ambazo zinakwenda kuumiza watu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii bajeti Mheshimiwa Waziri hatuungi mkono kwa sababu gani, mlikujaa na bajeti ya shilingi trilioni 29 ya mwaka jana imekamilika kwa asilimia 38 tu. Umeongeza sasa unazungumza shilingi trilioni 31.4 haujaeleza ni miujiza gani itatumika fedha hii ipatikane. (Makofi)



Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri anakaa kule Zingiziwa kwangu kule Ukonga, unafahamu mvua imenyesha kwako huwezi kwenda kuna mahandaki, hakuna maji, nimenunua mpaka jenereta kule Zingiziwa shule ya Msingi kule ni Dar es salaam sasa kule kwenu kule Buyungu, Kakonko ikoje hali hiyo? Haya mambo ukiyalinganisha huwezi kupiga makofi humu ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnataka tujadili kama Taifa ni muhimu sana tukubaliane, mnavyotenda mtende kwa Watanzania wenzenu sawa sawa mnavyotendewa nyie, tuheshimiane. Kwanza utaratibu wa kuonyesha kwamba eti mtu akishakuwa mpinzani siyo Mtanzania sio sawa sawa. Hauwezi kutudharau kwenye mikutano, mkatunyima nafasi, tv mnatumia mnavyotaka nyie, inakua Chama tawala halafu tukija hapa tupige makofi. Mkiboresha mambo hayo sisi hatuna shida na ninyi na hakuna mtu ambaye anasema tuibiwe, sisi huwa tunapinga kuliko ninyi kwamba wizi mwiko. Leteni mikataba, Twiga walioibiwa, tubadilishe sheria, watu wanyongwe, watu wafilisiwe; na uzuri wa Mungu wote watakuwa Chama cha Mapinduzi hakuna mpinzani hata mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo vipi? Nakushukuru sana, siungi mkono hoja, ahsanteni sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri kwa sababu nilikuwa na mgogoro wa Kazimzumbwi kwa kweli yeye na Mheshimiwa Waziri Mkuu waliingilia kati. Nawashukuru sana Waheshimiwa hawa, kwani walifunga safari kutoka hapa mpaka Ukonga na wakahakikisha kwamba jambo hilo linajadiliwa kwa manufaa ya watu wa Ukonga. Kwa hiyo, nawashukuru sana, nawatakia kazi njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani Waheshimiwa Mawaziri wapo humu. Hizi pongezi ambazo Mheshimiwa Lukuvi anapewa na wengine, nadhani Mawaziri wangefanya kazi kama hiyo tungekuwa hatuna mgogoro mkubwa. Kwa hiyo, ni muhimu wakajifunza mambo mazuri kama haya. Anapokea simu na Naibu wake, wanakusikiliza, wanakupa majibu, wanatembelea Majimbo; na kama jambo haliwezekani, anakwambia hili kwa mujibu wa sheria haliwezekani. Mheshimiwa Lukuvi nafikiri kwa sababu ya uzoefu wake, anaweza akatoa tuition kwa wenzake ili tukaenda vizuri. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, Mheshimiwa Lukuvi naomba anisaidie kumaliza migogoro maeneo yafuatayo Ukonga. Moja, kuna mgogoro wa UVIKIUTA, nyumba zimevunjwa zaidi ya mara tatu, anaufahamu vizuri. Tunahitaji watu wale wapate amani, wapate maelekezo ya kisheria waishi kwa amani katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mgogoro upo pale Pugu Kajiungeni. Ni eneo la wazi, hakuna eneo lingine, vijana walikuwa wanacheza mpira, akinamama wanafanya kazi zao; nyumba zilivunjwa usiku wa saa 9.00. Ofisi ya Mkoa tumeenda mara nyingi sana, lakini hatuna majibu mpaka leo. Kwa hiyo, tunaomba atusaidie tupate majibu katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Kipunguni haina Shule ya Sekondari, haina huduma za kijamii, ni kata mpya. Eneo pekee ambalo lilikuwa limebaki, limevamiwa na watu, hawana documents zozote zile, lakini majibu hayapatikani mpaka sasa. Kwa hiyo, tunaomba atusaidie pia, kupata majibu katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro mwingine mkubwa wa ardhi ni wananchi ambao walihamishwa kutoka eneo la Uwanja wa Ndege wakapelekwa maeneo ya Buyuni, Zavala na maeneo mengine kule. Wale watu wameondolewa kutoka hapa Uwanja wa Ndege Kipawa, kule hawakupewa ardhi, lakini bahati mbaya pia wakapewa maeneo ya watu. Kwa hiyo, kuna ugomvi kati ya watu ambao wametoka Kipawa na wale ambao ni wenyeji waliokutwa katika eneo lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Lukuvi kwa sababu yupo tayari, akutane na watu hao awasikilize, kwani ni kilio cha muda mrefu na kweli wana shida kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni bomoa bomoa. Eneo la Kata ya Pugu Station, Kata ya Ukonga na Kata ya Gongo la Mboto, maeneo yaliyobomolewa kupisha ujenzi wa reli kwa kiwango cha standard gauge; hatupingi, lakini wale watu wengine walikuwa na hati, wamechanganywa kule kule na hakuna fidia yoyote ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mambo kama haya wakiyafanya ni muhimu watu wafahamu sheria zinasema nini? Haki zao ni zipi? Wakati mwingine kutoa taarifa in advance ili kama kuna mtu ana-vacate, aweze ku-vacate ili asipoteze mali zake zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, neno la mwisho ni upimaji wa maeneo ya umma. Migogoro mingi iliyopo katika maeneo yetu hayapimwi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Lukuvi, achukue hatua mahususi kupima maeneo haya ili kuondoa migogoro kati ya wananchi na maeneo ya umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa mchango wangu wa maandishi. Naomba kusema mkakati wa makundi uliochukuliwa na Wizara hii ya Ujenzi ili kuondo kero ya mafuriko katika jiji la Dar es Salaam. Nakushukuru kwa Wizara kuanza ujenzi wa barabara ya Kitunda, Kivule kilometa 3.2 kwa kiwango cha lami. Barabara hii huyu mkandarasi amegeuka kero kwa kwenda taratibu sana tena wakati huu na mvua hali ni mbaya sana. Pamoja na kazi nzuri ya Meneja wa TANROADS naomba Wizara iingilie kati ili kuondoa kero ya barabara hii ili kuleta ufanisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuipongeza Wizara kwa kuongeza kilometa tano za Kivule - Msongola ila naomba huyu mkandarasi asipate tena kazi kwa sababu ni mharibifu na anaichafua Serikali (SAI na TANG Co.)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Pugu inahitaji mipango mikubwa ya kuipanua ili ikidhi kiwango na wakati kwa idadi ya watu waliopo. Barabara ya Chanika - Mbande ni kero kubwa hasa kwa daraja lilikatika na mashimo makubwa barabarani. Naomba Wizara iharakishe ujenzi wa barabara ya Pugu - Kinyerezi - Kifuru ili kupunguza mzunguko wa wananchi wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi. Ninazo salamu kutoka Jimbo la Tarime Vijijini kwa Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan wakimpongeza kupata tuzo na kutambulika kama kiongozi mashuhuri duniani katika viongozi 100, na bahati nzuri amepeleka fedha za miundombinu barabara ya kutoka Tarime – Mugumu na Mkandarasi yuko site, watalii wataongezeka, watapeleka ujumbe kwa Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii kama ambavyo wenzangu wamezungumza ni Wizara ambayo ingeweza kutuvusha sana na kuwafanya watu wakaendelea, lakini kwa kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwamba kuna mambo manne ili nchi iendelee, eneo la ardhi bado kuna shida kubwa sana. Mheshimiwa Waziri lazima ajipange na wenzake Naibu Waziri kufanya kazi hiyo kwa kweli. Karibu kila jimbo kila mahali kuna migogoro mingi ambayo imedumu kwa muda mrefu zaidi na palipo na migogoro maana yake hakuna maelewano, hakuna maendeleo, ni ugomvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kwangu kule Tarime Vijijini, tunayo madai ya wananchi wangu ya kulipwa fidia, ukienda eneo la Nyamichele tangu 2019. Nenda pale Murwambe, Matongo na Komarera kule kuna shida. Haya mambo ni muhimu yakafanyiwa kazi, kwa sababu eneo la Tarime kwa asili sisi watu ni wengi, ardhi ni kidogo sana haitoshi. Hata vita ya koo ambayo ilikuwa inapigana kule Tarime mnasema Warenchoka na Wanchali mpaka mkatubatiza majina kwa sababu shida kubwa ni ardhi, watu hawana sehemu ya kulima. Sasa kule Tarime ardhi ni finyu, haitoshi lakini wananchi wanajua kwa uhakika kwamba ndani ya ardhi yao kuna dhahabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fidia ambayo inalipwa, eti hekari moja Serikali inalipa Shilingi Milioni tano. Hata Waziri akipewa fedha hiyo akatafute ardhi hawezi kununua kwa kiasi hicho. Bahati mbaya wametengeneza migogoro wenyewe, wanachukua tangazo wanabandika kwamba ardhi hii tutaihitaji, yaani mwananchi akiona umebandika tangazo aache kulima, kujenga au kuendeleza chochote kile kwa sababu utamlipa. Hakuna mkataba, hakuna makubaliano, hivi ikitokea mwekezaji hataki eneo la mtu na hakuna makubaliano, unafanyaje? Hayo ndiyo madai yaliyopo pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Nyamichele waliwaambia wasubiri watawalipa, hawakulipwa mpaka leo. Matokeo yake wale Wazungu wa Mgodi wa Barrick wamechimba underground. Watu mazao yao yalikatwa, nyumba zilibomolewa, watu wana shida muda mrefu sana. Katibu Mkuu Kijazi alipita kule Nyamichele, akanikuta Tarime, nikamwambia watu wa Nyamichele wanataka kauli ya kiongozi, tathmini inafanyika lini? Unajua walimsimamisha hata hakusalimia kabisa akafunga vioo akaondoka, nikapata wakati mgumu kwelikweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, waambie viongozi kazi mojawapo ya Mheshimiwa Rais kumsaidia ni kutatua kero za wananchi, hata kama huna majibu. Wananchi wanalalamika, simama uwasikilize, utapokea hoja zao, utasema nimezibeba, naenda kuzifanyia kazi. Hayo maeneo ni vizuri fidia ikalipwa, Nyamichele, Komarera na Murwambe. Katika maeneo haya kuna mazao ya watu mengine nimeambiwa yalikatwa, kuna majina pale yapo. Mheshimiwa Waziri alikuwa Naibu Waziri kwenye Wizara hiyo, walikuwa na Mheshimiwa Lukuvi, walifanya kazi nzuri sana, siyo vibaya akiiga au akaendeleza walikoishia, kwa sababu anajua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inapendeza sana wananchi wakilalamika, kiongozi aende awasikilize. Asiende Musoma Mjini, aenda awasikilize, kuna malalamiko mengi ambayo wananchi hawana majibu. Sasa kuna uchonganishi unafanyika pale Tarime kwenye eneo la mgodi. Wale valuers wanaowatuma, wanawaambia gharama ni ndogo imepangwa. Ukienda kwenye mgodi wanasema fedha zipo za kuwalipa, wanatuchelewesha. Wanaona viongozi wa Serikali hatuwasaidii, Wabunge hatuwasemei, mgodi una fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara waende ili waondoe changamoto hiyo, waongee lugha moja. Kile ambacho mgodi unasema lazima pia kauli hiyohiyo iende kwa wananchi. Wasiamini kwamba hatuwezi kuwasaidia ili waweze kulipwa fedha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni muhimu sana kama kuna makubaliano wanataka waingie na wananchi wenye maeneo yao na kumekuwa na tabia ya kuchelewa kuwalipa, kuwe na mkataba kwamba kama unachukua eneo langu unakaa nao miaka miwili, miaka mitatu, ikitokea wewe hujanilipa fidia na mimi sikujiendeleza unalipa compensation ya kuchelewesha muda. Mtu anakaa miaka 10, enelo lake hajawahi kulipwa mpaka leo na hakuna chochote kile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wanalalamika sana wananchi, ni muhimu kuwa na makubaliano. Nchi hii inaongozwa kwa sheria, tufuate sheria za ardhi. Kama unataka eneo langu tukubaliane, unalipa fidia, hulipi fidia, unipe muda ambao umenichelewesha kufanya kazi za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, mipaka ya hifadhi. Katika watu ambao kwa kweli wana mambo mengi ya kulalamikia ni pamoja na Tarime Vijijini. Eneo la Kata ya Nyanungu, Kata ya Gorong’a, Kata ya Nyarokoba, Kata ya Kwihancha ni maeneo ambayo kumsikia mtu amepotea, siyo ajabu. Kwamba watu wamechukua ng’ombe za watu wameenda kupiga mnada mchana kweupe, siyo ajabu, kwamba mtu ameliwa na fisi, siyo ajabu, kwamba Kamati imeundwa na hakuna majibu, siyo ajabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Hayati Magufuli alikuwa na nia njema na Mheshimiwa Rais Mama Samia ameunga palepale, ametoa maelekezo akafanya maamuzi. Yaani Mawaziri Nane wanashindwa kwenda kusikiliza wananchi wenye migogoro, wanaenda kukaa Musoma kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, kweli? Wanashindwa kwenda site, wanasoma beacon ambazo yaani wamepokea taarifa ya SANAPA. Yaani mimi Waitara namlalamikia hapa Amar, halafu wewe unakuja unachukua taarifa za Amar, unanihukumu nazo. This is not fair, siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitarajia kwamba katika kutatua hii migogoro, viongozi waende wakae chini, Mbunge, Diwani, Mkuu wa Mkoa, DC na wananchi wote wawepo ndiyo watu waseme migogoro na tutatue hizo changamoto. Hii habari ya kujifungia na kutuandikia taarifa siyo sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wemekwenda Musona na Mheshimiwa Waziri alikuwepo, lakini hawakwenda Nyamungo, Gorong’a, Kwihancha au Nyarukoba, lakini wataalam wake wamewaambiwa wananchi Mbunge wenu alikuwepo, alishirikishwa, je, Mheshimiwa Waziri anataka nyumbani kwangu wachome moto? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wakienda wakaweka beacon, wakahamisha watu, Mbunge maana yake ameridhia watu wahamishwe, lakini kama ningekuwepo na wananchi wakawepo, wale wananchi wamezaliwa pale miaka ya 1980, miaka 1970 wanajua mipaka yao, wangesaidia maelezo kwa Mheshimiwa Rais kwa nia njema ili afanye maamuzi, watu waishi. Kwa kweli hakuna maendeleo kule, sasa kumekuwa na chuki kati ya watu wa hifadhi, wananchi, viongozi, hapaeleweki, duniani hatupo, ahera hatupo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima watusaidie vizuri, siyo sawasawa kwa kweli na migogoro imekaa muda mrefu sana. Ukiona kila Mbunge hapa analalamika kila kona, hawa Mawaziri ni muhimu sana. Pia ni muhimu hili Bunge, mambo yote ambayo yamekaa muda mrefu, malalamiko ya majimbo mengi, ya wananchi wengi, Bunge litoe muda maalum wa changamoto hizo kutatuliwa. Tusiwe hewani hewani, kama tunawapa miezi sita, Mheshimiwa Waziri akafanye kazi na wenzake, alete majibu kwenye Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ilivyo kila mtu anajisikia. Nilisikia wanasema eti hawana hela ya mafuta kwenda kule Nyamongo, eti mtaalam hana hela ya kwenda kule kuangalia migogoro ya wananchi. Wananchi hawa ili tuwaongoze vizuri lazima tuwasikilize, lazima tutatue changamoto zao, usipofanya hivyo itakuwa siyo sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne, migogoro ya wakulima na wafugaji. Hii Wizara kama nilivyosema Mheshimiwa Waziri akifanya kazi vizuri na wenzake na uwezo huo anao labda maamuzi tu, ni muhimu sana kwa sababu haiwezekani Wabunge wa Bunge hili, unajua watu wanauana kule, mwenye ng’ombe ni adui wa mkulima, mkulima ni adui wa mfugaji na sisi ni viongozi, Serikali ipo, sheria ipo, ardhi haipangwi, hii haikubaliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima watu wetu waishi kwa ustaarabu. Kama kuna mtu anafuga tujue wapi wanafuga ng’ombe, mbuzi, kondoo, maeneo yatengwe. Kama kuna sehemu watu wanalima tujue wanalima sehemu hiyo, iende, ndiyo uongozi wa nchi. Haitakuwa sawa kama tunakaa hapa watu wanauana, Watanzania wenyewe kwa wenyewe wanauana. Watu walewale, jamii ile ile halafu kuna Mbunge, kuna Diwani, kuna Viongozi, siyo sawasawa. Lazima tukubaliane, maeneo yapimwe, wale wafugaji wale siyo maadui wa wakulima, ila viongozi hatujachukua nafasi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inabidi tupange mpango vizuri, watu wanaofuga ng’ombe wafuge, au mfugo wa aina fulani wafuge, anayelima alime ili tuuziane. Hawa wanahitaji nyama, huyu anahitaji chakula, kuna shida gani? Tupangeni, jambo hili ni muhimu sana. Mbunge kusimama hapa anakutajia watu waliouwawa, hawajaugua, siyo bahati mbaya, kwa mapanga na sisi viongozi tupo, hilo lazima lifanyiwe kazi na Bunge hili kwani kazi yake ni hiyo kulinda watu wake, kuwasimamia Watanzania waishi kwa ustaarabu mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne, Mheshimiwa Naibu Waziri anafahamu, yeye alikuwa Naibu Waziri na ameenda kutatua mgogoro pale Mlitolegebasi. Watu walipigana mishale, wakapigana mapanga kwa sababu ya ule mgogoro, mpaka leo Mheshimiwa Waziri hajawahi kwenda pale na ule mgogoro upo. Kwa hiyo, wakati wa uchaguzi tunafanya kazi ya kugombea na kusuluhisha migogoro. Tumalize migogoro sasa kabla ya uchaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda wakati wa uchaguzi unaambiwa wewe umekuja kwa sababu unataka kula, Hapana. Tumesema mara kadhaa, tunawakumbusha tena, mahali popote katika majimbo yetu, kwenye mikoa yetu, kwenye wilaya yetu, kwenye vijiji vyetu, vitongoji vyetu, tarafa zetu, Waziri aainishe migogoro hiyo waifanyie kazi, tusifanye kazi ya kuzima moto, muda wanao, nafasi wanazo, dhamana wamepewa, watatue changamoto za wananchi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Kengele ya pili, Mheshimiwa Mwita.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Katika eneo hili ningependa nijue Mheshimiwa Waziri fidia ya Nyamichele, Komarera, Murwambe ni lini? Nitashika shilingi na nitakatalia mpaka Tarime Vijijini aifuate kule Nyanungu kwenye mgogoro wa ardhi, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi nimefika na mambo mawili tu ya kuzungumza leo; jambo la kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa Royal Tour ambayo imefanyika Tanzania, kazi ambayo ameifanya Mheshimiwa Rais ni ya kuitangaza nchi, lakini pia kuisemea, lakini amefanya kazi kubwa sana ya kuutangaza Mlima Kilimanjaro kwa sababu kuna watu waliaminishwa kwamba Mlima Kilimanjaro hauko Tanzania upo Kenya lakini kwenye kupanda mlima ule ameitangaza nchi, lakini vilevile sisi watu wa Serengeti wakati ule wa nyumbu anapokuwa anavuka Wakenya wanapanga ratiba wanasema nyumbu ni wa Kenya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Rais alienda Serengeti na akaonesha kwamba ile ni sehemu ya Tanzania na Mbuga ya Serengeti inaendelea kushamiri. Lakini vilevile ni muhimu watu wakajua kwamba kitendo cha Mheshimiwa Rais pia kuweka wazi mikakati ya kupambana na Covid-19 ilisaidia sana kufungua nchi, lakini pia na watalii kuongezeka. Wenzetu wanataka kujua kama kuna tatizo namna ya kuweza kuliondoa na kupambana nalo, hiyo pia ilisaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini zipo faida mbalimbali ambazo pia tumepata kama nchi na Mheshimiwa Rais amesaidia ndege nyingi za kitalii na za kimataifa kuongezeka kuja hapa Tanzania kwa mfano tarehe 4 Juni yaani kesho Eurowings Discovering wataanza kutoka moja kwa moja Ujerumani kuja hapa KIA na watabeba watalii 300 kwa wakati mmoja watakuja mara mbili kwa wiki, lakini tarehe 20 Juni, 2022 Dutch Airlines watatoka direct kule na kuja moja kwa moja KIA na kuongeza idadi ya watalii, kwa hiyo ni faida ambazo zinapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, abiria wameongezeka lakini pia miruko ya ndege imeongezeka katika eneo hili, lakini vilevile mashirika mapya yameongezeka kuleta ndege zao pale, lakini mapato ya Serikali yameongezeka katika eneo hili na ajira rasmi na ambazo sio rasmi zimeongezeka, hiyo ni baadhi tu ya faida ambazo tumepata kutoka kwa hao watalii. Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana tunaomba aendelee nayo.

Mheshimiwa Spika, lakini sisi watu wa Tarime tunamshukuru Mheshimiwa Rais ametoa fedha kujenga kilometa 89 kutoka Tarime mpaka Mugumu Serengeti, kwa hiyo hata kama kuna watalii kutoka Kenya kule watavuka pale wataenda pale Kibaso na Marariet na kuweza kutoa huduma na fedha itaongezeka na uchumi utaongezeka katika eneo lile.

Mheshimiwa Spika, ninachoomba katika eneo hilo la Royal Tour Wizara iongeze package ya Kiswahili kama sehemu ya utalii, kama inawezekana wale wenzetu wakija hapa kwetu tu wapate crash program ya kufundishwa Kiswahili ili wakienda wajue kwamba Kiswahili kipo Tanzania na sisi ndio wataalam wa Kiswahili, kwa sasa ilivyo katika somo huko duniani Wakenya wanapata ajira kubwa sana ya Kiswahili kana kwamba wanakijua kuliko Watanzania, kwa hiyo tutumie fursa hiyo kutangaza Kiswahili chetu, vijana wapate ajira lakini pia ipatikane ajira ya ukalimani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo kwa kweli mambo yote mazuri hayo ya Royal Tour yanaharibiwa na migogoro iliyopo katika maeneo yetu. Kule kwangu Tarime Vijijini Mheshimiwa Rais alikuta Tume ambayo ilikuwa imeundwa na mtangulizi wake Mheshimiwa Magufuli akafanya maamuzi akaelekeza Mawaziri nane waende kwenye maeneo yetu kutatua changamoto. Nasikitika kusema mpaka leo tangu nimezungumza hapa hotuba ya Waziri Mkuu, Wizara hatujawasiliana wala wahusika na kule katika eneo la mgogoro hawajafika kwa hiyo, watu wangu wanalalamika, lakini vilevile kuna vijiji 975 ambavyo vinahusika katika maeneo mbalimbali zaidi ya mikoa 10 na kitu ambayo ina mgogoro wa ardhi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni jambo kubwa ambalo Wizara lazima ilibebe na ilifanye, kama Mheshimiwa Rais amesimamia Royal Tour imeanza inafanya kazi, watalii wanakuja, ndege zinaongezeka, lazima tutatue migogoro ya wananchi wetu, itakuwa haina maana sana kama tunapata faida ya watalii kuongezeka halafu migogoro ipo katika maeneo yetu, inatia doa katika kazi nzuri ambayo Mheshimiwa Rais amefanya, hivyo Mheshimiwa Waziri unayo kazi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo ningechangia tofauti sana kama mwenzako mtangulizi angekuwa amekaa hapo, nilimuomba mara kadhaa tangu mwaka 2020 aende pale Tarime aende pale Nyanungu, aende Gorong’a aende Kwihancha, hawajawahi kwenda kuwasilikiza wananchi wangu na wanalalamika katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Tarime ina kata tatu ambazo zina mgogoro na Hifadhi ya Serengeti na tuna vijiji saba, huu mgogoro pia unagusa watu wa Bunda, inagusa watu wa Serengeti, inagusa watu wa Butiama inaenda mpaka Rorya utaona ni sehemu kubwa sana ambapo tungepanga haya mambo…., ukienda Kijiji cha Masanga, Kenyamosabi, Kegonga, Nyandage, Karekatonga, Kibaso, Nyabirungo huku kote kuna migogoro mikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini hawaishii hapo, nataka niseme tu kwamba yapo mambo ambayo yamefanyika katika eneo la Tarime yametesa sana watu wangu, kwa mfano kuna maeneo ambayo watu wameuawa, unashangaa mtu analishwa mizoga, watu wanalishwa pilipili mpaka wengine wamekuwa vipofu, lakini pia wanachoma nyumba wa watu, wanaharibu mazao ya watu. Hili jambo sio jambo zuri. Kwa mfano ukienda Kata ya Gorong’a kuna watu 10 wameuawa, Wanene Masyaga, Chacha Nyahiyo, Nchakwa Chacha Mahanga, Chacha Mwita Magori, Lucas Gasaya Marwa, Manga Wankyo, Wambura Chacha Mwaisori, Mwita Ryoki, Woryo na Manga Karumanga hii ni kata moja tu watu 10 wameshauawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kata ya Nyanungu kuna watu watano; Nyang’anyi Chacha, Mwita Nyangaya, John Sensema, Marwa Sasi, Mwita Chacha Mugesi hii miili mingine ilipotea ili kupoteza ushahidi, na Tume zimeundwa nyingi sana hapa sio sawa waliokufa, waliopigwa risasi, tunao watu hapa saba Chacha Magalya, Woryo, Seerya Magaiwa, Matiko Gesabo, Emaru Moseti, Boke Waisiko, Chacha Mwiniko hawa wamepigwa risasi wapo ni walemavu.

Mheshimiwa Spika, Tume zimeundwa nyingi, bahati mbaya katika eneo hilli unaunda Tume ambayo gari lenyewe tunawalalamikia watu wa TANAPA Serengeti wanatoa gari, wanatoa posho, wanatoa hoteli, wanaandaa chakula, ripoti zote hazijawahi kutoka, nikisema hayo mambo utafikiri natunga. Ningeomba Mheshimiwa Waziri baada ya Bunge hili aende katika Jimbo la Tarime Vijijini aone kwamba mambo haya ni ya uongo au ni ya ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya ninayoyazungumza yapo na nimewaandikia barua wahusika wa Wizara hii kwamba nendeni mkawasikilize, ukienda kwenye mipaka ya hifadhi nililalamika kwamba mmechukua greda, mmelima barabara katikati ya mashamba ya watu, lakini mashamba yale…

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Mwita kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

T A A R I F A

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza nimshukuru mchangiaji anayechangia, naomba tuweke kumbukumbu sawa, nampa taarifa kwamba anaposema Mawaziri hawajafika katika mikoa iliyotembelewa mara mbili kwa ile timu ya Mawaziri Wanane mkoa wake ni mmojawapo ambao tumeenda mara mbili, timu ya kwanza ilienda ikiongozwa na Mheshimiwa Lukuvi walienda mpaka vijijini, ile ya pili tumeenda tumeongea na ule uongozi wa mkoa na maelekezo yote yametoka. (Makofi)

Kwa hiyo, anaposema hawajaenda aweke kumbukumbu vizuri kwa sababu tunaweza tukapotosha kwa kitu ambacho sio sahihi sana. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ahsante sina nia ya kutaka kubishana na Mheshimiwa Waziri dada yangu Dkt. Mabula, ninachosema kwamba walienda Musoma wakaishia Musoma Mjini hawakwenda Nyanungu, hawakwenda Gorong’a, hawakwenda kwa wananchi, na mgogoro uliopo ni kwamba beacon ambazo zinatangazwa GN 235 ya mwaka 1968 wananchi wanabishania kwamba siyo kweli. Kwihanja walipokwenda wataalam wakakutana na viongozi wa wananchi wale wazee, wakawaonesha na beacon, leo mgogoro umekwisha pale Kwihancha, hapa sehemu ya Gorong’a na Nyanungu ni kwamba beacon wanasema ni za kwao, ni eneo la hifadhi, wananchi wanasema hapana tunakaa hapa, watu wamezaliwa pale miaka 80 unaishi hapo, ukienda ukakaa nao watakuonesha document zipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri eneo hili kuna watu ambao wamezaliwa wameongoza miaka 20 Udiwani wapo hadi leo. Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri na wenzake wa Maliasili na Utalii watume watu waende waongee na wale wazee au niwalete hapa uwasikilize ndio hoja iliyopo.

Mheshimiwa Spika, lakini ipo mifugo imekamatwa, kwa mfano Nyangage watu 20 wameathirika na kukamatwa mifugo yao…

SPIKA: Mheshimiwa Waitara ngoja, kabla haujahamia kwenye mifugo unajua nilikuwa naisikiliza hoja yako ili nielewe unaelekea wapi, umetaja hapo watu waliouawa, umetaja hapo watu waliopigwa risasi kwa maana ya kwamba wameumizwa. Huyo anayeyafanya hayo ni nani maana hayo mambo ni mazito sana, anayeyafanya hayo ni nani?

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, mambo yote hayo ya risasi na mauaji watuhumiwa wanaolalamikiwa ni wa Hifadhi ya Serengeti kwa sababu watu wanapotea kwamba wameenda kuchunga halafu hawaonekani na ilikuwa ng’ombe wamekamatwa, lakini mtu haonekani, kwa hiyo wanaotuhumiwa hapa ni Hifadhi ya Serengeti, sasa nani specific kwa maana ya majina…

SPIKA: Ngoja, ngoja, kama hizo ni tuhuma mbona wewe umezisema kana kwamba inajulikana kabisa kwamba ni nani aliyefanya hayo mauaji na ni nani aliyepiga hizo risasi.

Kwa sababu hili ni Bunge, ukisema mambo mazito kama hayo na kwamba kuna Tume hazijawahi kufanya chochote na hayo mambo hayajatokea jana wala leo, sasa hebu liweke vizuri ili mimi nijue nini cha kuiagiza Serikali hapa.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sijataja majina ya watu hapa, ninachoomba hapa ni kwamba haya ni malalamiko ya wananchi na majina yapo na Tume zimeundwa kwa mfano huyo Manga Kahurumanga ni mwaka jana, Mkuu wa Mkoa aliunda Tume na mimi nilikuwepo, ripoti mpaka leo hayajatoka. Kwa hiyo, hayo yote yamefanyiwa kazi majibu kwa wananchi pale hakuna.

Kwa hiyo, nitaomba utusaidie kwamba viongozi wa Serikali na hasa wa Hifadhi ya Serengeti haya malalamiko wayafanyie kazi yakome yasiendelee, yaani watu wasipotee katika mazingira ya kutatanisha, ndio ombi langu.

Mheshimiwa Spika,...

SPIKA: Ngoja, ngoja.

Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu tuhuma hizo ni nzito sana na tuhuma zinaelekezwa kwa chombo cha Serikali.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, tuhuma anazozitoa Mheshimiwa Mbunge katika kuchangia ni nzito kwa kweli na mimi nakuelewa kwa nini unataka upate angalau nini ambacho Serikali inasema.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ni kiongozi tena wa muda mrefu na uwakilishi wetu sisi kama Wabunge sio kusema tu ndani ya Bunge, ipo mifumo mbalimbali ambayo tunakutana na Wabunge na Serikali. Sasa kulileta hapa jambo zito kwa maelezo ya namna hiyo mauaji, risasi, hakuna kinachofanyika ni tuhuma nzito ambazo kwa kweli pengine zinahitaji tafakari, lakini pia kwa nafasi ya humu niseme tu kama anazo tuhuma mahsusi si vizuri kuzisema kwenye chombo hiki kikubwa badala ya kuwa tumekutana na tukapata hizi information na utafiti ukafanyika, tukajua kweli ni vipi.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu mtu akipotea haina maana mtu ameuwawa kuna watu chungu mzima hapa wana ndugu zao wamepotea. Hata mimi mwenyewe kwetu kuna watu wamepotea, sasa sio akipotea ameuawa na mtu fulani au na watu fulani.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nadhani ama atuhakikishe hilo analolisema na kama anaweza kuonesha ushirikiano na Serikali katika kueleza hayo yote anayoyasema au afute maelezo haya yasiwe sehemu ya mchango wake. (Makofi)

SPIKA: Sawa, sasa Mheshimiwa Mbunge yeye ameeleza kwa kirefu na mimi nilikuwa ninamsikiliza ili nielewe hoja yake inaelekea wapi na kabla hajahamia kwenye mifugo kuna hoja nzito ya watu waliopigwa risasi ambao maana yake kwa maelezo yake yeye na amewasoma hapo majina maana yake wapo waliopigwa hizo risasi kwa maelezo aliyoyatoa yeye, lakini pia amesoma hapo majina akisema hawa watu wameuawa. Maana yake kwa maelezo yake yeye anao ushahidi kwamba wameuawa kwa sababu hauwezi kusema mtu ameuawa kama amefariki, wanaofariki wapo wengi watu wanaumwa malaria na nini ukisema mtu ameuawa maana yake lazima kuna ushahidi unaoashiria kwamba kuna mtu amemuua mtu mwingine.

Sasa kwa sababu hili jambo ni zito kwa kweli na tupo kwenye Wizara hapa wakiwa wameleta hoja hapa ili tuwapitishie jambo lao, sasa Mheshimiwa Waitara huo ushahidi ulionao kuhusu mambo haya, wewe niletee mimi huo ushahidi ulionao, halafu huo ushahidi ulionao ukishaniletea mimi nitaiagiza Serikali kwa sababu siko nao huo ushahidi hapa. (Makofi)

Kwa hiyo, niletee ushahidi ili mimi niiagize Serikali kuhusu jambo hili kwa sababu tuhuma hizi ni nzito sana ulizozitoa hapa ndani. Malizia mchango wako. (Makofi)

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na nitafanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa ninasema kuna mifugo ya watu inakamatwa kwa mfano nimesema Kata ya Nyandege watu wameathirika mifugo yao, Tyegonga watu 18; Korong’a watu 17; na hayo yote ya mifugo kuna malalamiko makubwa sana, jambo baya lililofanyika pale ni kwamba wanakamata mifugo ya watu hawa ni jamii moja; mjomba, shangazi, sisi ni wale wale, halafu wanapeleka pale Kibaso kwenye uwanja wa wazi wanapiga mnada ng’ombe za watu.

Mheshimiwa Spika, unajua katika maisha yetu kama mtu alikuwa analimia ng’ombe zake halafu wamekamatwa wakaenda wakauzwa, mwenzake akachukua unatangaza watu waanze kuuwana.

Mheshimiwa Spika, ningeomba pia hata kama ni faini au hata kama ni kuuza wasiuzie pale pale katika maeneo yale yale ya jirani wapeleke sehemu nyingine kama ni lazima wauze mifugo ya watu. Nitaomba sana hapa kwamba watu wa Hifadhi ya Serengeti wanatakiwa watoe huduma na ushirikiano kwa watu wale wanaokaa karibu na Hifadhi ya Serengeti, waliahidi CSR lakini maeneo haya hakuna maji, hakuna malambo hakuna zahanati...

(Hapa kengele ililia kuahsiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Mwita Waitara kengele ya pili imegonga, nakupa dakika mbili umalizie mchango wako.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba kwamba kwa kuwa hawa watu wa hifadhi wanafanya shughuli pale, ugomvi ulipo kwenye kata yangu na ni ugomvi mkubwa ni kwamba pale wakati wa kiangazi hakuna malambo, yamekauka, hakuna mito tofauti na Mto Mara, hawa wa hifadhi waliahidi kwamba wangechimba malambo katika eneo lile ili wakati wa kiangazi mifugo ipate maji, wasiende kwenye Mto Mara, katika hali ya kawaida kama hakuna alternative wakati wa kiangazi watu wataenda kwenye Mto Mara, wataenda kulisha ng’ombe na kuchota maji, ugomvi unaanzia pale, wanakamatwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho ningeomba kwamba yapo mambo mengi katika Hifadhi ya Serengeti, tunapenda kuunga mkono Serikali kwa kazi nzuri, lakini naomba Mheshimiwa Waziri kwa dhati kabisa ni mpya kwenye Wizara hii, lakini ningeomba jambo la kwanza twende pale mambo ninayozungumza hapa siyo kwa kwangu, wanipe nafasi ya kwenda kukaa na wananchi, awasikilize, aone hata hizo familia azitembelee, utagundua kwamba kuna shida kubwa pale Tarime na kwa kweli naomba msaada wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba ulibebe jambo hili kama mzazi. Kule kuna kilio kikubwa sana, migogoro ya ardhi hapa ni karibu kila Mkoa, Waziri lazima ajipange. Kazi nzuri ya utalii ili ifanyike vizuri lazima migogoro kwenye majimbo itatuliwe, twende tuwasikilize watu, kama ni kusogeza mipaka bahati nzuri Mheshimiwa Rais ameonesha njia jambo hili siyo jema, tunataka mapato ya utalii, lakini watu wetu pia waendelee kuishi kwa amani na kupata maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mimi sijaku-miss ila nimefurahi wewe angalau kupata fursa ya kuongoza Bunge baada ya muda kidogo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo yamezungumzwa hapa, wapo Wabunge wanasema Tanzania kupitisha sheria hii itakuwa nchi ya 67 kwa dunia na wengine wakasema ni nchi ya tano Afrika na story nyingi sana za mataifa mengine. Nikawa najiuliza tu kwamba hivi tunahitaji sheria nzuri au tunahitaji idadi ya nchi ambazo zimetunga sheria mbovu yaani tunataka tuige kitu gani hapa, ina add value gani kwenye sheria hii? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Sheria amenisaidia jambo muhimu sana ambalo lilikuwa kwenye mchakato wa Katiba Mpya. Alipoanza Ibara ya 2 anasema, sheria hii itatumika Tanzania Bara. Huyu ametukumbusha kwamba kumbe bado tunahitaji Serikali tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Waziri wa Sheria amekaa maana ni Ofisi ya Wanasheria wa nchi hii wamekaa wakaona hii sheria itumike Tanzania Bara peke yake na Bunge hili lina Wabunge kutoka Zanzibar wanawakilisha maslahi ya Zanzibar na kumbe tulikuwa na hoja ya akina Jaji Warioba ya Serikali tatu, mimi nadhani hiki kipengele kimewaumbua kweli kweli. Unajua njia ya muongo huwa ni fupi, mmetusaidia.
Kwa hiyo, Watanzania wajue na dunia inajua kwamba tunalazimika kuwa na Serikali tatu kwa sababu hata nyie wenyewe hamuitambui Zanzibar ila wakati wa kuchakachua matokeo mnafanyaga kwamba ni kwenu ila kwenye sheria mbalimbali wala hamhusiki.
TAARIFA...
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza sipokei taarifa za design hiyo, mimi napeleka wapi hizi? Hili ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunazungumza mambo ya Tanzania ya wote, hili siyo Baraza la Wawakilishi. Kwa hiyo, naomba niendelee, hawa watu wana copy na ku-paste lazima tuwape habari zao. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mapendekezo yangu baada ya kupitia muswada huu vizuri, nimeusomasoma sana, kama Waziri angekuwa ana nia njema sina shida na jina lililotajwa kwamba ni kupata taarifa ambayo of course inatumika interchangeably mara taarifa, mara habari maana na hiyo pia inabidi uweke very clear unamaanisha kitu gani hapa. Ndiyo maana watu wakahoji leo asubuhi jina likabadilika ghafla kwa hiyo ikazungumzwa kitu kingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukizungumzia taarifa na ukasoma ile Ibara ya 18 maana yake jambo lote hili lina expire, halina maana. Kwa sababu mmesema kwamba mnataka kuwasaidia wananchi wapate taarifa lakini umeweka masharti mengi kweli kweli na adhabu mbalimbali ambazo taarifa ikitoka zinatumika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, leo nilikuwa nasoma Gazeti la Habari Leo linaandika sana habari zenu hili, ukurasa wa pili, nasoma kidogo kwa ruhusa yako, anasema, watoa taarifa fake za uhalifu kutupwa jela, faini ya shilingi milioni tatu au mwaka mmoja au vyote kwa pamoja. Sheria ya Kuwalinda Watoa Taarifa za Uhalifu na Mashahidi ya mwaka 2017, huyu ni mwandishi wa habari ameandika wa gazeti la leo, hivi sheria hii ipo kweli? Kwa hiyo, huyu naye anatakiwa afungwe miaka kumi si ndiyo maana katoa taarifa ambayo sio sahihi. Si ndiyo maana yake? (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mwandishi ukimuuliza amekosea kidogo tu kwamba hii sheria haipo, alikuwa anamaanisha kitu kingine lakini kalamu ikateleza na kwenye printing hakusoma vizuri ikatoka. Sasa adhabu imeshatolewa kwenye sheria ambayo mnazungumza leo. Nilikuwa nawaonesha haya mnayozungumza hapa yanawahusu na ninyi wenyewe pia huenda hata huyu mwandishi ni mtoto wa kada wa CCM halafu ndiyo anawajibishwa na wewe unapiga makofi hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ni muhimu sana awasaidie Watanzania na mimi pia sielewi, hii Ibara ya 6 yote ilipaswa iondoke kama ambavyo Kambi ya Upinzani ilipendekeza kama kweli nia ni kusaidia watu wapate taarifa mbalimbali zinazohusu maisha yao ya kila siku kwa mujibu wa Ibara ya 18. Kwa mfano, unazungumziaje habari ya mtu anamiliki biashara yake nikitoa taarifa eti ataathirika, mliongea naye lini, yaani wewe una share kwenye hiyo kampuni? Kwa nini usipokee taarifa yangu halafu uifanyie utafiti, kwa sababu kuna zile sheria za defamation na Waziri anafahamu, kama taarifa inatolewa ambayo inamhusu mtu itatumika hiyo lakini siyo kunihukumu mimi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge lazima wajue ilivyo mpaka sasa hivi watu wengi ambao wamewajibishwa ni wale wakuu wa taasisi. Hawa Maafisa wa Habari watakuwa wanateuliwa na wakuu wa taasisi. Hivi Mkuu wa NIDA yuko wapi, naona wanasema anasota mahakamani si ndiyo? Hiyo ilikuwa NIDA maana yake huyo ndiyo bosi wa NIDA, anamteua Afisa Habari ambaye kabla hajatoa habari inabidi aende kwake aka-confirm atampa atoe taarifa za kuficha madhambi yake halafu huyu unaenda kumuuliza asipokupa taarifa. Kwa hiyo, kama kuna mfanyakazi mwingine kwenye Idara ile akinipa taarifa waandishi wakiitoa nje Watanzania wakajua hawa ndiyo wanatakiwa kuwajibishwa ila huyu ambaye ametoa taarifa ya uongo hatakiwi kuwajibishwa. Ndiyo maana mnaambiwa hayo mnayozungumza humu ni mambo ambayo mnatengeneza mazingira ya kujificha kwenye mgongo wa nyuma, lakini ukweli wa mambo ni kwamba mnaficha ukweli. Hilo ndiyo lengo la sheria hii ambayo mmeileta hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Ibara ya 6(5), hapa imezungumzwa miaka thelathini, kwanza Waziri hapa ametaja kijiji, bahati nzuri mimi ni Mbunge wa Ukonga inawezekana wajanja wajanja ni wengi pale kuna mwingiliano mkubwa sasa, mimi nipo Tarime nyumbani, kule Kegonga, Masanga, kutoka Nyanungu aje Tarime Mjini ili akamuone Afisa Habari wa Manispaa inabidi kwanza awe na nauli ya shilingi 15,000 kwenda na shilingi 15,000 kurudi yaani akitaka taarifa ya Serikali ni mpaka awe na shilingi 30,000. Halafu hawezi kufika akarudi siku hiyo hiyo, mvua kwa mfano imenyesha itabidi alale mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, anayetaka taarifa hapa inabidi kwanza awe na nauli ya kwenda na kurudi, apate hela ya kulala gesti, apate hela ya chakula, kwa hiyo, lazima uwe na bajeti ya kutafuta taarifa ya Serikali. Hivi mnadhani Waziri hii kweli ni haki? Hiki kitu kinachofanyika hakikubaliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu mnasema taarifa ikiombwa huyu atazungukazunguka siku thelathini. Ikitokea sikupata taarifa, maana anaweza akaamua kunipa au asinipe halafu aende kwa bosi wake, bosi wake anaweza akahamisha akasema hili halinihusu na ndiyo tabia yao, apeleke kwa mtu mwingine tena, sheria hapa inasema utaanza upya tena. Imagine umechukua siku 30 wakikusikiliza ndiyo wanakujibu siku ya mwisho ndiyo wanakujibu siku ya mwisho kwamba hii taarifa haiko kwangu nenda kwa Waziri Mwakyembe. Anakaa nayo tena siku nyingine zile ishirini na tisa anahamisha anasema kwamba hili jambo liko kwa Mheshimiwa Maghembe angalia mchezo unaofanyika hapa na hiyo ipo all over.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ile Ibara ya 6 ametoa adhabu miaka 15 na isiyozidi 20. Niliona mapendekezo ya Sheria ya Dawa za Kulevya wametoa adhabu mpaka ya miaka mitano, hivi kweli Bunge hili, ndiyo maana huwa sisemi Tukufu ila tuseme kwa sababu imeandikwa, Bunge hili kweli hivi mtu anayeuza dawa za kulevya, anaharibu vijana wa Tanzania, anaharibu nguvukazi ya Watanzania ni sawa na mtu ambaye amepotosha taarifa tu au kwa sababu hakupewa taarifa na mhusika katika Idara husika, inaweza kuwa sawasawa kweli? Hebu tuwe makini katika mambo haya tunayoleta kama viongozi na watu wazima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye Ibara ya 12, nilitaka nijue, kama nimeenda kwenye Idara fulani, nikaomba taarifa, wakanipa taarifa ambayo naona ni ya uongo, kuna mtumishi mle ndani akanipa taarifa sahihi, kwa sababu tu mimi ninayo ya kweli ambayo nimetoa kwenye source halisi kwa watu ambao wako jikoni, lakini nimepewa iliyopotoshwa hapa napewa adhabu kwa taarifa hizi. Kwa nini sheria isiseme unaweza ukapewa taarifa mahali popote ila ikichunguzwa ikaonekana kwamba kweli haina ukweli huyu mhusika ndiyo ashughulikiwe lakini hapa inabana kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 10 ameelezea namna ya kupata taarifa, hajaruhusu kupiga simu ambayo ni njia rahisi kwamba mtu kama hana nauli, anataka taarifa akapiga simu, anajieleza, anajitambulisha, anahojiwa apate taarifa. Hapa mmeorodhesha kwamba unaweza ukaandika barua, njia ya elektroniki lakini simu hazipo. Maana yake ni lazima mtu asafiri akapate taarifa, kwa hiyo mnaingiza watu kwenye gharama ya kutafuta taarifa hizi katika maeneo ambayo ni mbali na wanapokaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni Ibara ya 21, kinasema:-
“Mmiliki wa taarifa ambaye maombi ya kupata taarifa yatatumwa kwake anaweza kutoza ada iliyowekwa kwa ajili ya kutoa taarifa hiyo.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaona sasa? Kwa hiyo, sasa mnaanza kufanya biashara ya kuuza habari, mnaanza kuwauzia wananchi taarifa, ndiyo mmesema hapa kwenye Ibara ya 21 na huyu atakuwa na discretion ya kupanga ada awadai kiasi gani kwamba mwananchi anahitaji taarifa fulani inabidi alipie kiasi hicho. Kwa hiyo, kama huna hiyo ada iliyowekwa na mwenye chombo chake ambaye ana taarifa hiyo ina maana hiyo taarifa hautapata na biashara yako itakuwa imeishia hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo nilitaka niseme la jumla, hii sheria kwa namna mlivyoileta ukiisoma vizuri maelezo ya Waziri mdomoni anamaanisha kitu kingine, alichokiandika ni kitu kingine. Kwa sababu ni Mwanasheria anajua akiandika hivyo watu wa kawaida hawatajua.
Waheshimiwa Wabunge hiki kinacholetwa kimsingi kinaenda kuumiza watu wetu na sisi wenyewe tukiwa miongoni mwao. Wakati Mheshimiwa Bashe anazungumza hapa watu wa CCM wamekaa kimya kama wamelowa, hawasemi ili baadaye wampeleke kwenye vikao vyao wakamtishe sio, hawakumpigia makofi. Hata hivyo, ukweli ni kwamba hii habari ya kutoa taarifa mbalimbali, hili Bunge lilikuwa linajadili habari ya Lugumi, Lugumi ilianza kwenye vyombo vya habari hakuna afisa aliyetoa taarifa, hiyo habari mmeizugazuga hapa imeisha. Mambo ya IPTL ni waandishi wa habari waliibua mijadala mbalimbali, Balozi Ole alikuwa Italia mpaka anashtakiwa ni waandishi wa habari waliandika habari za kiuchunguzi. Yako mambo mengi ambayo yameibuliwa na vyanzo ambavyo sio rasmi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ningewashauri kama kweli mna nia njema mngekubali taarifa ipatikane kwa mujibu wa Ibara ya 18, mtu yeyote anaweza atakayetoa taarifa ahojiwe, iwe verified halafu kama kuna mtu ambaye atakuwa amekiuka misingi ya utaratibu katoa taarifa ya uongo, zipo sheria zile za forgery, defamation na mambo mengine yasaidie. Hilo ndiyo lingekuwa jambo la msingi sana lakini unaleta sheria ambayo inataka kuwatisha kwanza watu yaani hapa itakuwa ukitaka taarifa unaulizwa nani amekuambia, upelelezi haujakamilika, wewe siyo mhusika, nani amekupa mamlaka maana yake tunajenga nchi ya uoga. Waziri wa Sheria wewe umri wako siyo mkubwa sana siyo kwamba utaendelea kuwa Waziri kila siku, angalia wenzako wapo mtaani, wengine wameenda lupango, hizi sheria ambazo unaleta hapa kwa kweli lazima mziangalie mara mbili mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, lakini siungi mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa Mwaka 2016
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naomba nianze tu na hii ya Chemistry Professional Act maelezo ya jumla tu kwamba nimejaribu kuusoma huu muswada nia ni njema ya Serikali na mimi ni mwana chemist pia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama alivyosema Mheshimiwa Susan Lyimo hapa ukiangalia ile composition ya namna ya kuwapata hawa wanataaluma ni kama huu muswada hautoi uhuru wa wao wenyewe kupatikana. Nadhani Mheshimiwa Waziri ambacho ungefanya ilitakiwa hao watu iwekwe utaratibu ambao wanakutana na wanachaguana halafu Wizara iwe ni kusimamia na kuondoa kero mbalimbali, ku-facilitate utendaji wao ingekuwa jambo jema sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na hata mimi ningependa nipate maelezo sikuona sababu ya kuingiza polisi katika eneo hilo kwa sababu hawa watu kimsingi au kumpa Waziri mamlaka makubwa sana kuwadhibiti kwa sababu wao ni wataalamu kama umeingia kwenye maabara kuna jambo linazungumzwa ni professional yaani huwezi kuingiza siasa katika eneo lile. Kwa hiyo, sioni kuna sababu yoyote ya msingi ya kuwa na hofu kwamba lazima wabanwe sana waminywe mamlaka yao na lengo ni jema kwamba tuwe na watu hawa na Bodi yao na Baraza lao ambalo wanaweza kufanya maamuzi yao kitaalamu halafu Serikali inayachukua inayafanyia kazi mwisho wa siku hawa watu kazi wanayofanya itakuja Serikalini tu. Kwa hiyo, nadhani muangalie utaratibu wa kuwapa uhuru wakufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nije sasa kwenye hii ya Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Kwanza nilisikitika sana, katika mawasilisho ya Kamati ile wanaonyesha kwamba hawakukutana na wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alitaja kama nakumbuka vizuri hawakukutana. Lakini wataalam kutoka SUA hawakuwepo na wataalam kutoka Muhimbili, sasa kwa kadri ninavyofahamu hivi ni vyuo vikubwa na vya muda mrefu na vina wataalam wa waliobobea hata vinavyoanzishwa wanakuwepo na wataalam kutoka maeneo haya na ninyi wenyewe mnafahamu kama Naibu Spika na wataalam wengine mnafahamu hili.
Sasa ningeomba nielezwe aliandika kupewa maandishi kutoka Mlimani uje kusoma unless huyu mtu ametuma mtu ambaye ni professional afanye interpretation alimaanisha kitu gani kwa hiyo ina maana Kamati haikupa fursa ya kukutana wataalam wenyewe ipendekeze.
Mheshimiwa Naibu Spika, na ninaamini kwamba ilipotengenezwa huu muswada mpaka unakuja hawakuwa tena wameshirikishwa, sasa kwa kweli ni jambo ambalo sikuona kama ni sawa sawa yaani huwezi kuwa unazungumza habari ya Ofisi ya Mkemia Mkuu na Mamlaka yake na Bodi unaunda halafu Muhimbili ambao unapozungumza haya mambo biologist na nini ndio wataalamu wetu pale.
Kwa hiyo, nadhani mngesaidia maelezo mwanzoni mtusaidie kama kulikuwa na shida gani yaaani wali-divert, hawakutoa ushirikiano au ilikuwaje.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya nne, kifungu kidogo cha (4) anasema; “bila kujali masharti yaliyotangulia katika kifungu hiki, Mwanasheria Mkuu wa Serikali atakuwa na haki ya kuingilia kati katika kesi au shauri lolote lililofunguliwa dhidi ya mamalaka.”
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake huyu anakwenda kwenye government interest ya kuwa-defend. Lakini ningetaka hapa niliposoma hapa tafsiri ya Kiswahili kwenye Kiingereza pale inaeleweka vizuri lakini hapa ilivyowekwa ni kana kwamba anaingilia kusimamia shitaka ambalo dhidi ya mamlaka lakini anaweza kaathiri upande mwingine usipate haki vizuri, kwa hiyo, naomba lugha hapa ieleweke. Kwamba huyu anaweza akingilia kwa maslahi ya Serikali na maslahi ya mamalaka hii, lakini vilevile bila kuathiri au kuminya haki ya upande mwingine katika zile pande mbili zinazokuwa zinasigana. Kwa hiyo, ni muhimu sana nimeona hiyo lugha haijakaa sawasawa Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya tano, (section 5) ile mamalaka itakuwa maabara ya rufaa na matokeo yake ya uchunguzi itakuwa ni ya mwisho kuhusiana na masuala yanayohusu uchunguzi wa kimaabara.
Sasa kwenye kipengele (a) itafanya shughuli za kitafiti, uchunguzi na kimaabara na kuishauri Serikali na taasisi nyingine kuhusu masuala yanayohusu uchunguzi wa sumu, kibaiolojia, vinasaba na dawa za kulevya. Sasa hapa hoja yangu ilikuwa ni kwamba kwanza niipongeze Serikali kwa sababu tulipokutana mimi ni Mjumbe wa Kamati ya UKIMWI na Dawa za Kulevya, kwa hiyo, ninapoona maeneo ya madawa ya kulevya nina interest nayo. Lakini hii tulipokutana na Mkemia Mkuu mojawapo ya mapungufu ya utendaji ilikuwa ni haya mamlaka ya kukamata, kuchunguza na kushitaki.
Kwa hiyo, nadhani hili neno lote kwa pamoja nikupongeze kwamba angalau umei-capture hii hoja ambayo tulipokutana na Ofisi ya Mkemia Mkuu walitoa hiyo kwa hiyo hilo nashukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kipengele cha 7 kina shida pale, hii sehemu kwa mfano ndio inatoa composition hivi sasa ya Wajumbe wa Mamlaka hii kwenye Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Wametajwa hapa kwanza (c) anasema mwakilishi kutoka taasisi za elimu ya juu au utafiti wenye utaalamu katika masuala yafuatayo....
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hii nilikuwa nashauri, ametaja hapa pathologia, kemia na madini. Hapa mimi naona kulikuwa na sehemu mbili muhimu sana, ningedhani katika composition ya member hawa ni muhimu kuwe na mtu ambaye ni professional chemist ili a-deal moja kwa moja na mambo ya kemia na nini, lakini pia kuwe na biologist katika eneo hili.
Kwa hiyo, ningependekeza kwamba, hapa ni muhimu hawa watu wawili wawepo bila kusema either of these two, angalau wawili hawa kwa sababu, kama ni chemist mambo anayojua ni tofauti na biologist na Dkt. anafahamu. Kwa hiyo, nadhani mngesaidia ile ili at least kama hoja inaingia pale kila mtu yupo kwenye reli yake ambayo ni professional na itakuwa haina shida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine kuna hii hoja ya (e) hapa sikuona imetajwa kwamba, kuna watu ambao ni ma-chemist, lakini hawapo Serikalini ni binafsi. Sasa na yenyewe hapa hii hoja haijawa captured hapa. Hata vyuo binafsi, kule kwenye professionals ndio mmetaja, lakini hapa kwenye hawa Wajumbe hamkutaja kama kuna uwakilishi wa taasisi binafsi, kama kuna uwakilishi wa vyuo binafsi, kama kuna watu kwa mfano TBS maana wenyewe ndio wanapima viwango na nini, kwa mfano kuna Wizara ya Kilimo hapa. Sasa nadhani hayo mambo ni muhimu mkayaangalia kwa maana hiyo, sasa hii namba haipaswi kuwa fixed kama ilivyo sasa inabidi iwe iwe ziada kulingana na maeneo ambayo na mimi naona ni muhimu sana mkayazingatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, kuna tafsiri ya Kiswahili hapa ni tofauti kule. Nilipoona kwamba, mwakilishi wa Wizara haikuwa imetaja Wizara gani, lakini kule kwenye ile sehemu ya Kiingereza imetaja Minister responsible for Health kwa hiyo, nadhani hapo pia katika maeneo ya nyongeza hiyo (b) inabidi useme ni mwakilishi wa Wizara ipi. Haukuwa umetaja.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pale kwenye hiyo hiyo 7(5) muda wa kuwa madarakani Wajumbe, mwenendo wa Bodi pamoja na masuala mengine yanayohusiana na Bodi yatakuwa kama yalivyoainishwa kwenye jedwali. Kwenye jedwali nimesoma ile sehemu ya miaka mitatu, sasa mimi nikawa nashauri kwa nini isiwe miaka mitano kwa sababu, hawa watu ukiwa na muda mfupi sana wa kufanya kazi ina maana unaweza ukawa umeanza labda ndio una-take off halafu muda unaisha. Kwa hiyo, mtu mwingine anakuja tena mpaka uchukue mazoea ya nini, unaanza upya; nikaona kwamba, ingependeza kama ungempa miaka mitano anakuwa angalao na muda wakutosha ku-perform. Hata kama atateuliwa term ya pili mtu aki-serve miaka 10 inakuwa ni rahisi kupima mabadiliko yake na kazi ambayo imefanyika na watu hao kwa wakati huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingine ambayo nimeiona ni kifungu cha 10. Kwenye kifungu cha 10 pale hasa (a) atakuwepo Mkemia Mkuu wa Serikali atakayeteuliwa na Rais. Sasa (a) anasema angalau na sifa ya Shahada ya Uzamili ya Kemia au na taaluma zingine, sasa ukishasema ni Mkemia Mkuu wa Serikali maana yake unatakiwa uwe ni Mkemia yaani hutakiwi kuwa na taaluma nyingine. Kwa hiyo, ningeshauri kama wanamaanisha Mkemia huyu mtu lazima awe professional chemist, lakini wanaposema awe na level nyingine maana yake nini sasa? Maana yake hapo unatoa room kwamba unaweza kuletewa mtu mwingine yoyote halafu ukasema huyu ni Mkemia Mkuu kumbe sio mwana-chemistry. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani mtakuwa hamjatendea hata hilo jina lenyewe wala huhitaji Mheshimiwa Waziri na mwenzako kuzunguka, yani huyu mtu awe professional chemist. Labda uongeze kwamba, awe m-chemist angalau na taaluma nyingine inayofanana na hiyo, hiyo itakuwa imeenda vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye kifungu cha 3 kuna sehemu hapo unazungumza tu kwamba, awe ni Mtumishi wa Serikali.
Sisi tunapendekeza na mimi, kama walivyosema wenzangu wa upande wa Upinzani, ni muhimu tusiwe na limitation hata kama mtamteua huyu mnayemtaka wa Serikalini, lakini kwenye sheria ionekane kwamba mtu yeyote ambaye anaweza kuwa mkemia ili mradi anakidhi hizi sifa atateuliwa. Sasa kama ni Mtumishi wa Serikali, kama ni private sector, kama taasisi yoyote, lakini angalau kusiwe na ubaguzi, huyu awe ni mtu Mtanzania ambaye ana sifa za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye kipengele cha 16ambacho kinahusu usimamizi, sasa pale imezungumzwa na wenzetu na Kambi Rasmi ya Upinzani hapa, inaweza kuwa hapa inasema hii nia njema, ile habari ya nia njema ile ina shida, yaani maana yake kwamba kwa mfano mabadiliko yakitokea hawa watu hawahusiki, lakini kama mtu amekula deal amepiga hela mahali anaweza aka-delay tu halafu akasema mimi nilifanya hiki kitu kwa nia njema kumbe ni makusudi na kuna kitu anakificha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya 17(3) pale (a) kulipa faini isiyopungua shilingi 5,000,000 au kifungo kisichopungua mwaka mmoja au vyote kwa pamoja iwapo mkosaji ni mtu binafsi; hapo maana yake una-deal na mtu ambaye ni tofauti na, ingiza hapo na hata kama ni mtumishi, hata kama ni Afisa wa Serikali anafanya kazi lakini amefanya hili kosa hii adhabu iende pande zote. Kama ni mtu wa kawaida amefanya kosa awajibishwe kama ni mtumishi wa Serikali awajibishwe pia, maana yake utawatisha watasimamia utaratibu wa kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha 26. Hii naona nimeifuta kwa sababu, niliangalia 11 haikuwa sehemu ya rufaa, lakini 26 ime-capture ya kwamba kama kuna maamuzi yametoka na mtu hajaridhika basi anaweza akakata rufaa kwa Waziri au kwenye Bodi na kwa Waziri na kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niseme mambo ya jumla pamoja na ile sehemu ya 45 ambayo wenzangu wamesema ile nia njema. Sisi tungeshauri hii habari ya nia njema kuwa na mipaka, ukiiacha hivi ilivyo watu watafanya makosa kwa kusingizia kwamba unajua niliamua haya maamuzi kwa sababu ya nia njema, kumbe yeye alikuwa na mambo yake tu. Sasa mambo ya jumla ni kwamba ningedhani, nimesoma sana huu muswada ambao kimsingi nauunga mkono, lakini inaonekana sehemu kubwa yaani ni kupimapima tu DNA na nini, yaani haioneshwi kwamba watafanya hata utafiti, watafanya hata uchambuzi kama ufumbuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano hapa Tanzania gongo inapatikana na gongo watu wanakunywa na ipo, sasa hawa kwa nini wasisaidie kwenda hata kuboresha vitu vya namna hiyo? Yaani haiwezi kwenda kuzuia uvumbuzi, kama mtu anaweza kutengeneza gongo hawa wakaboreshe ili isiweze kudhuru, kama ilivyo konyagi na vinywaji vingine, watapata kipato na watakuwa wamechangia katika ufumbuzi wa kisayansi. Mimi nilikuwa nashauri hilo liangaliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile naamini kwamba hii miswada yote miwili itasaidia. Kwa mfano, wapo akinamama na akinadada ambao wanajichubua na nini kwa hiyo, na hili lenyewe litasaidia kudhibiti hivi vipodozi vya design mbalimbali na matumizi yake, hata wanaume kama wapo, mimi si miongoni mwao. Lakini hiyo ni muhimu kwamba ikaangaliwa hata kwa mfano dawa mbalimbali; yaani hii inatakiwa kitu kikubwa ambacho ambacho tutakuwa tunapata products mbalimbali za kisayansi katika eneo hili. Kwa wale wanamaabara, lakini pia na hii Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata vilevile utafiti, kwa mfano kuna mbolea zipo hapa zinaharibu ardhi yetu, hazizalishi vizuri. Hao pia watasimamia kudhibiti vitu vya namna hiyo na matokeo yake tutakuwa na heshima kubwa kwa sababu tutakuwa tumepanua. Kwa namna ilivyo hapa ni kama tunasubiri tu uende upime kama DNA, ukague kama labda kuna sumu, kuna poison na nini, lakini niwapongeze kwa mara nyingine kwamba angalau changamoto ambayo Mkemia Mkuu alikuwa anasema ya kwamba wanashindwa kufanya kazi kwa sababu ya ukosefu wa fedha; sasa angalao hapo kutakuwa na vote itakuja kwenye Bunge litapitisha, kutakuwa na bajeti ambayo itakuwa allocataed, hili jambo zuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia pale walituambia mitambo ni mibovu, lakini kwa sababu, shida ilikuwa ni pesa. Sasa with this maana yake anaweza akanunua mitambo na iwe ya kisasa, lakini pia, kama atafungua kwa mfano kwenye Kanda mbalimbali, sikuona mahali popote kama kutakuwa na Kanda, walikuwa wanadai unaweza ukaona dawa zimekamatwa kwa mfano Tabora halafu inabidi zije hapa Dar es Salaam; sasa inategemea expire date ikoje na hiyo bajeti haikuwepo, hii shughuli ikachelewa. Sasa kwa muswada huu ina maana uta-facilitate kazi iweze kufanyika vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mkemia alisema kwa mfano, kulikuwa na shida ya upungufu wa watumishi, sasa kwa hili maana yake ni lazima kuajiri, kwa hiyo, kutakuwa na uwezekano mkubwa sana wa kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili la DNA kwanza gharama ilionekana ni kubwa sana, kwanza ilikuwa ni moja mashine au mbili halafu gharama ni kubwa, lakini sasa kama wana bajeti watafanya hii kazi, kutakuwa na mashine kila eneo nah ii habari kwamba 60% angalau ya watoto hawajulikani baba na mama wanatofautiana, lakini wote ni wazazi nah ii itasaidia kidogo, ili kila mtu ajue mtoto wake ni yupi na aweze kumhuduamia vizuri na kweli hata itapunguza ugomvi katika familia zetu. Maana sasa kama mtoto hafanani fanani hivi unajihisihisi, hata kutoa matumizi kidogo inakuwa ngumu. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo naomba niwasilishe. Ahsanteni sana.
Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, wa Mwaka 2016
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Utafiti wowote, ukitaja tu neno utafiti kwa lugha ya kawaida mtu anategemea kwamba ni kazi ambayo inafanyika kujibu baadhi ya matatizo au kuleta mafanikio au kuboresha. Kwa namna yoyote ile lazima kuwe na kitu kinafanya utafiti ufanyike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia tu uanzishwaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na sitaenda sehemu nyingine ile. Pamoja na kwamba nimepata marekebisho ya Serikali, lakini nina shida ya mwanzoni kabisa hapo anapozungumzia hii section ya kwanza tu, mwanzoni walikuwa wamesema kwamba sheria hii itatumika Tanzania, lakini baadaye wameandika kwenye Ibara ya kwanza wanasema ni Tanzania Bara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanzoni walikuwa hawajasema inatumika wapi ndiyo wamefanya marekebisho kwenye schedule of amendment ambayo ninayo hapa wakasema itafanya kazi Tanzania Bara. Ukisoma Katiba ya Tanzania Nyongeza ya Kwanza katika mambo ya Muungano neno la 18 inaonesha kwamba utafiti ni jambo la Muungano. Ikishakuwa jambo la Muungano sasa vinginevyo Waziri aje anieleze au alieleze Bunge na Watanzania waelewe wanapozungumza hili jambo ni miongoni mwa mambo ya Muungano halafu baadaye unaleta sheria ambayo inasema itatumika Tanzania Bara, unataka kuniambia kwamba ni kauli ya Waziri alichokiandika hapa ndiyo inafanya kazi au ni Katiba ndiyo inafanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wakati gani neno utafiti linakuwa jambo la Muungano na ni wakati gani neno hili linakuwa siyo la Muungano. Tukisema ni jambo la Muungano maana yake inabidi uende kwenye Katiba Ibara 98 ambayo inaeleza namna ambavyo sheria hii inapaswa kupitishwa. Sasa kama ni jambo la Muungano kwenye Ibara ya 98 ya Katiba ya nchi inaeleza kwamba jambo hili litapitishwa kwa 2/3 ya Wabunge wa Tanzania Zanzibar na kwa 2/3 ya Bunge hili la Tanzania kama hivi tulivyo humu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mambo haya yameshafanyika maana yake vinginevyo maelezo yaletwe kwa nini inageuzwa hapa, kama wenzetu wa Zanzibar waliwahi kujadili jambo hili kama ambavyo imefanyika katika maeneo mengine kwenye Ibara hizi basi ni muhimu. Vinginevyo huu Muswada maana yake utakuwa haujatimiza vigezo ilibidi uahirishwe ili Katiba ifuatwe na uletwe hapa pia. Sasa nitategemea kwamba kabla ya kwenda mbele haya mambo inabidi yatolewe ufafanuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwenye huu Muswada wa Sheria ukisoma hapa sijajua Waziri anamaanisha nini, nimejaribu kuangalia hivi nini malengo yake! nimesoma mwanzo mpaka mwisho haya mapendekezo ya Muswada wa Sheria hii inaonesha kwamba bado mambo ya msingi hayatajibiwa. Kwa mfano, wakulima wa kawaida wa Tanzania hata kama ni wa mahindi, korosho wanatarajia ukitaja tu, kwamba sasa Tanzania inakuwa na Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo yaani waone sasa shida ya mbegu mbovu haitakuwepo, hilo jibu kama Watanzania kupata sijaliona hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale watumia mbolea wanataka waone kwamba taasisi hii ikiwa imeimarika sasa itasaidia kuboresha kwamba mbolea itakayotumika haitaharibu ardhi yao, yaani kuchujuka kwa muda fulani baada ya kutumia mbolea zetu za kawaida, hayo majibu inabidi yawepo. Sheria inabidi pia itaje kwamba hivi uchumi wa Tanzania economic growth itakuwaje kama kuna taasisi ambazo zita-control mambo hayo, mambo ya msingi mimi sikuyaona hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji, (productivity) kwamba hii sheria inawezaje kusaidia Watanzania kuboresha mazao yao wazalishe kwa faida na walime kilimo cha kisasa hayo mambo hapa sikuyaona. Kilimo cha kisasa kwamba angalau ipendekeze kusimamia mambo gani kufanya watu wasilime kutegemea mvua ya kawaida baada ya utafiti wa tasnia ya kilimo hii watu watalima kwa kutumia mvua ya kawaida au umwagiliaji au nini, hayo mambo yote ya msingi hapa hayajajibiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine tulitegemea malengo ya sheria hii lazima yaoneshe kwamba contributional agriculture research kuleta kilimo cha kisasa itasaidia nini hii taasisi. Mambo haya ni mambo ya kawaida kabisa kwamba angalau katika malengo ya sheria Mtanzania wa kawaida bila kuwa Mtaalam, bila kuwa Mbunge, mkulima wa kawaida huko aliko awe na matumaini na atamani kwamba sheria ikipitishwa moja kwa moja ananufaika bila kumuuliza Waziri, bila kumuuliza Mbunge, kwa maneno tu ya mazungumzo humu ndani, mambo hayo sikuyaona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile sheria hii itawasaidia nini wakulima wa Tanzania kwa kuanzishwa kwa mambo ya soko (market economy) inawajibika vipi kutafuta soko la wakulima wetu, hilo pia katika mazingira hayo sikuona chochote hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile usalama wa mbegu zetu na mazao wamesema wenzangum wamelalamika kwamba nchi hii kumekuwa watu wanalima mazao kwa sababu hatusindiki mazao yetu yanaharibika, thamani yake inashuka, haya mambo yote yalipaswa yawepo maana yake inapendekezwa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Tanzania, sasa haya mambo yote ya usalama sikuyaona mahali popote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cost effectiveness sijaona teknolojia itasaidia vipi kwenye teknolojia ya kisasa wakulima walime; teknolojia gani itumike ku-control bei yake na vitu vingine vya namna hiyo, hayo mambo yote sijayaona. Mamlaka ya Taasisi ya Utafiti itakuwaje coordinating ata-oversee namna gani au atatoa guidance namna gani katika taasisi zingine za utafiti wa mambo ya kilimo hilo sikuliona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilivyozungumza hapa sikuona mahali ambapo inaonesha kwamba kuna mambo ya ku-control mbegu kama nilivyosema. Wenzetu kama Waganda wana taasisi wanayo National Crop Resource Research Institution. Hapa tunazungumza lakini ukiangalia kwa namna yeyote ile inabidi ihusiane na mambo ya mifugo hivi kwa sababu huwezi kuzungumza habari ya kilimo bila kuzungumza habari ya mifugo, maana yake ndiyo chakula chao, hivi vitu vinategemeana sana. Leo kuna ugomvi katika maeneo mbalimbali sasa utasaidiaje katika mazingira hayo. Hayo mambo mengine nimeona nizungumze.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo pili ambalo nataka nilizungumze hapa sijaliona kwenye haya mapendekezo usalama wa chakula chetu nimesema, lakini vilevile hii sheria lazima ionyeshe kwamba taasisi itasaidia kupunguza umaskini wa Watanzania uliokithiri, tumeona mashahidi hapa juzi kama hii taasisi ikiwepo je, wale watu ambao wanalima nyanya hapa Kilosa hivi halafu ngombe wanakula, hivi hii itasaidia nini katika mambo hayo. Walime mazao gani kwa wakati gani na soko likoje na hao wana-link, maana yake kwenye sheria hapo wameonesha tu kwamba anaweza mtu akafanya utafiti kutoka nje, lakini hawaoneshi kwamba tunaweza tukafanya utafiti Tanzania tukaunganisha na sehemu nyingine tukaboresha kilimo chetu kiwe cha kisasa. Hiyo na yenyewe haipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria inasema tu kwamba wanaweza wakaruhusu mtu ambaye siyo Mtanzania akaja akafanya utafiti na akishafanya utafiti; je, wenzetu mbona hamsemi sheria itaruhusu hawa na wenyewe wafanye utafiti mahali popote, waende wakope teknolojia ya kisasa waboreshe kilimo chetu ili tuweze kushindana na nchi zingine, hilo jambo pia silioni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile sheria haisemi hapa kuna adhabu nyingi sana zimeoneshwa, kwa mfano haioneshi kwamba hii sheria itaifanya Taasisi ya Kilimo iwe ni kitu shirikishi, haioneshi kwamba kama kutakuwa na transparency, haioneshi kwamba mwananchi wa kawaida, mkulima wa kawaida kama ana malalamiko!
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnajua mbolea zinaletwa hapa wenzetu wakulima wa pamba wamesema, wanapewa mbegu za pamba zinaharibu ardhi yao, zingine hata hazioti, hiyo transparency, uwezo wa mkulima wa kawaida kuhoji na kupata taarifa kwenye taasisi ya utafiti wa kilimo nakulalamika, hapa vilevile sioni jambo hilo. Integrity ya hii italindwa namna gani, accountability ya hawa watu wote wanaohusika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshangaa sana nchi hii ina Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, chuo ambacho ni chuo kikongwe katika Afrika Mashariki na Kati, lakini hii sheria inaletwa hapa ya kuunda Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ambayo haigusi au haitaji kabisa kwamba SUA ina mchango wowote, nimeshangaa sana! Maana yake wanataka kutuambia hawa wataalam wetu ambao wapo siku zote hamtambui mchango wao, najua hawa ndiyo benki yetu ya mawazo, hawa wana uzoefu wa muda mrefu sana, wangeweza kutushauri namna ya kwenda mbele, mambo gani yamekosewa na hawa ndiyo tumewapa task hiyo kwa muda mrefu na Wakufunzi wengi nchi hii wametoka pale. Mambo haya ningeomba nimshauri Mheshimiwa Waziri mnapoleta sheria kama hizi, haya mnazungumzia maisha ya wakulima wa Tanzania, wafanyabiashara na watu mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine wamependekeza maneno mengi, sikuona wanasema hawa kama watafanya utafiti kwenye taasisi ya kilimo, kilimo ni chakula, hawaoneshi kwamba watashirikiana namna gani hata na hii Mamlaka ya Chakula Tanzania, hawatajwi katika hii sheria mahali popote, nimesoma sikuona. Sasa mambo kama haya nadhani na wengine watakaofuata hata hiyo Miswada inayofuata ya kesho ule wa Fisheries, ni lazima mkileta Muswada hapa hata kama mmeandika Kiswahili/Kingereza mwananchi wa kawaida aweze kuona, hivi ananufaika namna gani bila kuhoji bila kuuliza, kukusikiliza tu ataona kwamba hii kitu kweli ni ukombozi.
MWENYEKITI: Ahsante.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 3 wa Mwaka 2017
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi na naomba niungane na Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani upande wa Katiba na Sheria kwa kutoa pole sana kwa Mheshimiwa Tundu Lissu kwa sababu alipaswa kuwa hapa, hili ni eneo lake la kitaaluma, lakini kwa sababu ya mipango ya watu wabaya katika Taifa hili hayupo pamoja nasi. Mungu aendelee kumpa nguvu apate nafuu na kupona haraka ili aweze kuchukua jukumu lake muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema, wale ambao wamemuumiza Mheshimiwa Lissu kwa kiwango kile kama ni kijana ambaye hajapata mtOto asipate kabisa na kama ni mtu ambaye ana familia asiisaidie familia yake, a-paralyse kila mahali na apate mauti makubwa sana.

T A A R I F A . . .

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naomba muda wangu ulindwe na naomba niendelee kwenye hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi hoja yangu ya kwanza iko pale kwenye mabadiliko katika Sheria ya Elimu. Nataka nitoe tu ushauri kwamba ni kweli kwamba kama sasa hivi kabla haya marekebisho hayajaja Bungeni kumekuwa na malalamiko mengi sana ya wamiliki wa shule na vituo vya kulelea watoto hata vile vya watu binafsi, kuna masharti mengi sana na mzunguko mrefu kwelikweli ambayo vilevile yanapelekea sura kama kuna mazingira ya rushwa hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, masharti yaliyopo kwa watu kumiliki shule binafsi ni makubwa kuliko shule za Serikali. Kwa hiyo nashauri Wizara hii ya Elimu na Waziri mwenye dhamana ajielekeze kusimamia shule za Serikali ziwe bora zaidi, hizi za private zinakufa zenyewe tu kwa sababu wananchi walio wengi, maskini, wanategemea shule za Serikali kwa sababu ni bei nafuu zaidi. Hilo ni jambo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili; masharti yale yaliyotolewa, ni lazima masharti ya kuanzisha vituo vya kulea watoto wadogo na wale wenye miaka miwili mpaka mitano vizingatie pia maeneo ya wamiliki kwa sababu unategemea kuna mtu ana eneo dogo unamtaka awe na ekari saba ndipo awe na kituo hicho, kitu ambacho kwa kweli hakiwezekani. Sheria zifuatwe, mazingira yatofautiane kutoka eneo na eneo kulingana na upatikanaji pia wa ardhi. Hilo ni jambo la pili.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ni hii habari ya DAWASA. Bahati nzuri mimi ni Mbunge kutoka Ukonga - Dar es Salaam, ni waathirika wakubwa wa eneo hili. Kwanza kuna mkanganyiko mkubwa kati ya DAWASA, DAWASCO na halmashauri zetu. Nadhani hata kabla ya kuleta hii sheria ni muhimu mkaangalia, isssue hapa sio kuongeza majukumu ya DAWASA, suala la msingi ni kwamba miradi ambayo DAWASA wameanzisha mingi haijakamilika, shughuli ambazo wamepewa hazijakamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kuna mwingiliano mkubwa wa mamlaka hizi tatu, kwamba kuna miradi ipo ya DAWASA, kuna miradi ipo ya DAWASCO na kuna shughuli ambazo zinafanya halmashauri zetu. Kwa hiyo ni lazima kuwe na utaratibu mzuri ambao kimsingi jambo likianzishwa liwe linamalizika.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni hili la miradi mbalimbali iliyopo ambayo watu wameshakula fedha. Kuna miradi mingi sana imeanzishwa imekufa watu wanakula fedha hawawajibishwi, hawachukuliwi hatua mbalimbali. Maana yake ni kwamba tunaendelea kukosa maji katika Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini imetolewa hoja hapa ya Kambi ya Upinzani kwamba majitaka Dar es Salaam ni shida kubwa, mvua ikinyesha dakika mbili tu kila mahali panafurika na wananchi ambao si wastaarabu ndio wanatumia muda huo kwenda kufungulia maji machafu kuingia mtaani. Kwa hiyo tunaugua sio kwa sababu kila Jumamosi ufunge maduka na labda niseme vizuri, sijui kama hata Waziri wa Fedha ameshafuatilia, hii jambo la kufunga maduka Dar es Salaam kwa kweli kwetu ni shida kubwa kweli kweli. Hivi unatumia akili gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu mwananchi, mama lishe au baba lishe anafungua asubuhi, ana dustbin pembeni amepika chapati, ni siku ya Jumamosi watu wanaweza wakanunua maandazi yao, chapati zao muda ule unamwambia afunge mpaka saa nne na hawa watu hawafanyi usafi. Kwa hiyo wanafunga maduka hata ya dawa, sasa kama umepata shida usiku umeugua unahitaji huduma ya dawa unaambiwa duka lazima lifungwe, hilo duka si chafu. Kwa nini asiangalie mtu ambaye kwa kweli ni mchafu ndiye awajibishwe? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hii ni amri ambayo tumejaribu kuangalia sijui imeandikwa kwenye sheria gani. Sasa Mwanasheria Mkuu wa Serikali utusaidie mambo kama haya, unapoleta mabadiliko hata kauli za viongozi ambazo hazipo kwenye sheria yoyote katika nchi hii leta tuingize kwenye sheria kama ni lazima. Ili basi mtu akisoma, wananchi wanaenda wanaangalia hivi imeandikwa wapi, Rais amesema wafanye usafi kila siku ya Jumamosi ya mwisho wa mwezi, amekuja Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akaongeza ya kwake, Mkuu wa Wilaya ataongeza ya kwake, sasa hii nchi inaendaje kweli. Kila mtu ni amri tu kweli? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mnavyozungumza habari ya maji Dar es Salaam kuna shida kubwa pia hii ambayo inasababishwa mwende muifayie marekebisho, muhimu zaidi. Kwa hiyo cha muhimu hapa ni kuiwezesha hii DAWASA ifanywe wajibu wake; kwamba mvua ikinyesha miundombinu iwe imetengenezwa, imerekebishwa, maji yana maelekezo yake; hicho kitu kwa kweli hakijafanyika na imekuwa ni sehemu ya shida.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naangalia hapa, hii Sheria ya Petroli hakuna sehemu hapa imetajwa gesi, labda mtanisaidia baadaye, hivi ukizungumza maliasili, gesi haimo? Maana umezungumza hapa madini na petrol, gesi ni sehemu ya maliasili pia, lakini hapa naona kwamba haijazungumzwa. Hata hivyo, imeelezwa jambo ambalo itabidi mtujibu, kwamba juzi na amesema Mheshimiwa Tundu Lissu wakati akiwa mzima wa afya hapa ndani, kwamba hizi sheria ambazo zinakuja kwa speed kubwa na ukiona Kamati hii, si kwamba naituhumu, Kamati imesema inaunga mkono hata mambo mengine haitaki kuangalia kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, yule Mheshimiwa Mwenyekiti ameenda ameandika maelezo yake kuhusu fidia, kuteuliwa kwenye Kamati, mambo ya msingi hawajaangalia, wangetueleza wao kama Kamati ya Sheria hii ilikuja juzi hapa tukasema imekuja kwa dharura. Kuna mambo mengi nchi hii ambayo tunafanya sasa yaani nguvu kubwa inayotumika leo ya makinikia na vitu vingine vyote ni dharura hii hii imetufikisha hapa tulipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hii Kamati imeshauri nini Serikali kwamba kipindi kijacho hii habari ya dharura tuache, tuzingatie utaratibu tupokee ushauri wa Waheshimiwa Wabunge, usiangalie chama chake, sura yake, uwezo wake, angalia hoja Mezani. Dharura imetuumiza, imeligharimu Taifa hili na hii tabia inaendelea kujirudia, lakini Kamati wameona muhimu kuandika kujisifia kwenye taarifa yake pale mwanzoni. Naomba ushauri muhimu ukazingatiwe, kwamba ni muhimu waangalie, mambo ya msingi ambayo tumesema yazingatiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nimeliona hapa ambalo Msemaji wa Kambi Rasmi amelizungumza ni kitendo cha kuondoa nguvu ya Bunge. Tuliomba kwamba kama sheria; hata mambo ya msamaha wa kodi; kama sheria inarekebishwa, basi Bunge, kwa sababu mikataba hii ambayo mingi imeingiwa katika Taifa hili mikubwa ya mabilioni ya fedha, Bunge limekuwa likinyimwa haki ya kuipitia na kuishauri Serikali vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tukaona kuingiza kipengele hiki cha kulazimisha mkataba huo mkubwa uletwe humu Bungeni ili tupate fursa ya kuona sheria hiyo na mikataba mbalimbali. Sasa tena ndugu zangu mnaleta hoja ya kusema muondoe Bunge lisiwe na uwezo wa kuweza kuhoji, hii na yenyewe ni sehemu ya tatizo kubwa zaidi. Ninyi

wenyewe mnasema tunamuunga mkono Rais ili sasa Bunge liwe na meno, Bunge liwe na nguvu kumbe ilikuwa ni kanyaboya, ilikuwa ni uongo tu, mmezunguka miezi miwili, mmerudi mnafuta tena fursa ya Bunge kupata sheria mbalimbali na kupata fursa ya kuweza kujadili vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la msingi tukubali, nimeona kuna maneno kuondoa msamaha wa kodi, ni kweli kwamba kuna baadhi ya miradi; hata kule Dar es Salaam tumeathirika; miradi mingi imekwama kwa sababu kuna fedha ya ziada inatakiwa ilipwe ili fedha zitoke kuja kwenye miradi ya maendeleo, lakini shida kubwa iliyopo ni ustaarabu wa Mawaziri hawa ambao tunawateua katika Taifa hili, kwamba wakipata fursa ya kutoa msamaha wa kodi; hatujamsahau Daniel Yona hapa na mmemfunga sijui kifungo cha aina gani kile, yupo; lakini na yeye alitoa msamaha na wengine juzi wamewajibishwa; kwamba wamepuuzia hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninachoomba ni kwamba, unaposema Waziri apewe nafasi ya kutoa dhamana, hata kama ataunda Kamati; yaani Waziri ndiye anayepaswa kushauriwa, lakini Waziri huyo huyo ndiye anayepaswa aunde Kamati ambayo itamshauri. Yaani mimi Waitara nataka ushauri sasa, halafu Waitara anatafuta watu wake wanaunda Kamati ya kwake Waitara, ndio wanamshauri, halafu Waitara akipewa ushauri na watu wa Kamati aliyounda anaamua kutoa msamaha wa kodi, sijui hiyo imekaaje.

Kwa hiyo hapa ndipo mahali ambapo kuna mianaya ya rushwa, ndiyo watu wanapitisha deal zao, anatengeneza watu ambao anawajua; kwa hiyo lazima kiwe chombo kingine ambacho hiyo Kamati ya kumshauri Waziri ikishaundwa nani ana-cross check? Maana yake haioneshi kwamba itakuja kwenye Kamati yoyote wala itakuja kwenye Bunge hili. Ili sasa umdhibiti Waziri kwamba kutoa msamaha iwe kweli kuna ulazima na mradi ambao ni mkubwa ambao una maslahi makubwa katika Taifa hili ndipo nafasi itolewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, ikigundulika kwamba Waziri ametoa msamaha kijanja kijanja ambapo yeye mwenyewe ananufaika Sheria iwepo ya kumwajibisha huyu Waziri Waziri kwa mujibu wa Sheria zilizopo, ndipo itamdhibiti; ili ifike mahali mtu akipewa hii nafasi aogope. Kwamba ni kweli mimi nataka nitoe msamaha, huu msamaha ni genuine? Una maslahi mapana ya Taifa langu? Je, yeye ni nani ambaye anaweza kumhoji. Haya ni mambo ya masingi sana ambayo yanaweza kuzingatiwa ili haki iweze kutendeka
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MWITA C. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Polisi wamefanya kazi sana, ila wamefanya kazi vibaya sana. Kazi wamefanya, lakini wanafanya mbaya, ndiyo maana watu wanalalamika. Ni muda tu mfupi lakini kwa kweli Wizara hii mambo ambayo yamefanyika ni mengi sana na mengi yake ni mabaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Mwigulu Nchemba ndugu yangu, asikilize tunachokizungumza hapa. Inawezekana watu wanaingiza siasa katika mambo ya msingi katika maisha ya watu, ni bahati mbaya sana. Tunatarajia Mheshimiwa Mwigulu Nchemba atakapokuja hapa kuhitimisha hoja, aje atueleze zile CCTV Camera ambazo zilikuwa kwenye nyumba ambayo ndugu yake Mheshimiwa Lissu wa Singida alikuwa anaishi, nani aliziondoa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia aeleze upelelezi umefika wapi? Muhimu sana. Hili jambo halihitaji siasa. Huyu mtu amelalamika kwamba anafuatiliwa na magari, akataja mpaka namba ya simu, akataja hata namba ya gari. Mheshimiwa Mwigulu Nchemba hajawahi kusimama hadharani na akawaeleza Watanzania, nani alikuwa na gari ile? Wale ni akina nani mpaka leo! Sidhani hata ndugu yake Mheshimiwa Lissu kama pole alimpa. Sina hakika kama ametoa hiyo pole kwake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, yako mambo yanazungumzwa hapa; tumezungumza juzi, Mheshimiwa Heche amezungumza akaomba Mwongozo hapa kwenye Bunge hili, kwamba Mbunge anasema ametishiwa maisha. Hawa watu wanapiga simu, wakati mwingine wanaandika message.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa Polisi ukiandika maneno yenye ukakasi kwenye mitandao, unafuatiliwa popote ulipo, unawekwa ndani, kizuizini. Hawa ambao wanatuma message za kwamba “nitakushughulikia;” “nitakuonyesha;” “utanikoma;” kwa nini hawashughulikiwi? Mheshimiwa Heche alilalamika hapa Bungeni, lakini bahati mbaya naona haya mambo yamebadilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Mwigulu Nchemba aseme, yule ndugu yake John Heche, Ndgu Chacha Suguta ambaye amezikwa leo, yule bwana amekamatwa na Polisi akapigwa pingu. Hapo ndipo watu wanahoji maadili ya Polisi. Hata kama sio wote, watu wanahoji inakuwaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Polisi aliyefundishwa, ameenda Chuo cha Mafunzo kule Moshi au elsewhere, anamkamata mtuhumiwa aidha ana makosa au hana makosa; wala hata hakuua; au hata kama ni muuaji, Mahakama ndiyo ina wajibu wa kusema huyu ahukumiwe kiasi fulani au apewe adhabu gani. Anapigwaje kisu? Hiyo kauli ni lazima ichukuliwe kwa uzito wake katika Taifa hili na iwe fundisho na matukio mengine ambayo yanafafana na hayo. Hayo ni mambo ambayo kwa kweli yanahitaji kuangaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba alizungumza kwamba kuna watu wanaokotwa kama jambo la kawaida. Hii hali ya watu kuamka asubuhi amekatwa mapanga kama yule wa Kilombero, kama dude la mgomba, halafu watu wanaona, watu wanaokotwa kwenye mifuko ya sulphate kwenye kingo za bahari kama mambo ya kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo haya mnazoeza Watanzania mauaji, itafika mahali kuanza kuona siyo jambo la ajabu ajabu sana. Mwingine anasimama hapa mtu mzima kabisa anatwambia kwamba eti kwa sababu idadi ya Wapinzani ni chache kuliko ya CCM; so what? Yaani unahalalisha uhalifu kwa idadi ya watu, kitu ambacho hakikubaliki. Yaani mtu sikutarajia anaweza kuongea kitu cha namna hiyo ambacho kimsingi ni jambo ambayo haliruhusiwi kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachosema, Polisi wamefundishwa. Polisi wanalipwa kodi ya Watanzania; Polisi viatu wanavyovaa ni kodi yetu, chakula chao ni nguvu yetu; nguo wanazovaa ni sisi; wafanye kazi kwa uadilifu, wafuate maadili yao. Hiyo ndiyo hoja ya msingi hapa. Hatusemi wamfuatilie mtu yeyote yule. Kamata mtu yeyote ambaye ana makosa yaliyothibitishwa apelekwe Mahakamani ahukumiwe. Siyo ku-retain watu katika retention kama ilivyo kwa wale Mashehe. Ni makosa makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, hivi sisi tunachangisha kujenga Vituo vya Polisi; pale Chanika tumejenga. Hawa Polisi tunajenga pamoja nyumba na Vituo vya Polisi, hawana magari. Kwa nini magari ya washa washa yale msiyabadilishe yawe magari ya kufanya patrol kwenye vituo vyetu ambako kuna kuna raia? Ujambazi unafanyika, hawana mafuta ya kufanya patrol, lakini magari ya washa washa yapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, ndugu yangu na mjukuu wangu, nilishangaa sana. Jeshi la Polisi nchi hii, ndugu y angu Sirro, kaka yangu wa kule Musoma, anafanya maandamano ya magari kwenye mikoa nchi nzima kwa Mange Kimambi? (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani they are not serious, yaani mtu yuko Marekani, anaandika maneno kwenye mtandao, tutaandamana tarehe 26. Wamekamata vijana wetu nchi nzima, wanawapiga. Mange Kimbambi, kweli! Haki ya Mungu mimi nisingehangaika naye. Nilikuwa nawashangaa hapa Wabunge wa CCM kuwe na maandamano kwa hoja ipi? Nani anaandamana? Sisi tulikuwa hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitaka kuandamana tutakaa vikao, tutaitishana, hakuna Mbunge wa Upinzani atabaki humu ndani. Tutakwambia weka barabarani majeshi, weka maji ya kuwasha, weka bunduki, piga risasi, ua unayeua, atakayebaki ataandamana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani mnahitaji kutumia akili sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kupata nafasi ya kuchangia katika eneo hili muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze hapa ambapo mwenzangu ameishia. Kumekuwa na mjadala wa muda mrefu sana juu ya ama kutungia kiingerea au kiswahili. Hili ni jambo ambalo kwa kweli Mheshimiwa Waziri, Profesa inatakiwa Serikali ilitolee maamuzi mapema kwa sababu kadri tunavyovuta muda maana yake tunazidi kuchelewa kufanya maamuzi ya mambo yetu na kuweza kuboresha elimu yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nadhani hili ni jambo la muhimu sana kwa sababu wamelifanyia kazi, tafiti zimefanyika, wataalam wameandika na Profesa anajua. Kwa hiyo si jambo la kuvutana tena, aje atueleze nini msimamo wa Serikali, tunafanyaje? Tunaamua kutumia kiingereza kufundisha kutoka chekechea mpaka Chuo Kikuu au tunaamua kutumia kiswahili? Tuamue ili tusiwe na double standard katika elimu yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningeomba Mheshimiwa Waziri atusaidie, nimesoma bajeti yake ambayo ameleta kwenye Bunge hili tukufu ili tuijadili, na bahati nzuri huyu ni mwalimu. Lakini jana wafanyakazi wa nchi hii popote walipokuwa, hata wagonjwa waliamka vitandani wakakaa wakitazama kumsikiliza Mheshimiwa Rais kwamba angalau kwa sababu aliwaahidi kwamba ataongeza mishahara angeweza kusema neno jana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa bahati mbaya sana ameeleza mipango mingi ya Serikali, lakini hakusema ataongeza mishahara kwa watumishi lini na hasa walimu ambao wamekuwa na malalamiko kwa muda mrefu sana. Hili ni jambo ambalo kwa kweli na ile speech ya Rais Mheshimiwa Magufuli Rais wetu wa Tanzania na Rais wa Kenya ziliwekwa pamoja parallel, kwa hiyo, wakawa wanalinganisha kwamba Uhuru Kenyatta yeye ameongeza asilimia tano, lakini sisi tunasema tunaangalia kwanza, tunatoa ahadi mpaka leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu sana kumbukumbu ziwe sawa. Rais aliwaahidi wafanyakazi ataongeza mshahara mwaka jana mwezi wa tano, sasa mwaka huu tena ameenda kuahidi kwa hiyo nadhani mumsahauri vizuri, kama jambo haliwezekani, hilo jambo lisitamkwe, watu wanakuwa na matumaini hewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ina shida kubwa sana ambazo Mheshimiwa Waziri alipaswa atueleze kwenye bajeti hii. Kwa mfano, kumbukumbu zinaonesha kwamba tuna shida mpaka ya matundu ya vyoo katika nchi hii. Kwa mfano shule ya msingi peke yake kuna upungufu wa matundu ya vyoo 239,716, kwenye bajeti ya waziri anaonesha kwamba watajenga matundu ya vyoo ambayo ni asilimia 0.73 ndiyo yatakayojengwa kwa mwaka huu wa fedha. Sasa nimejaribu kupunguza hapa hayo ni matundu 2,000 kwa mwaka wa fedha 2018/2019 lakini ukipunguza hapa kwa matundu 239,000 maana yake tuna upungufu wa matundu ya vyoo 235,000 bado unaweza ukaona shida ni kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la madarasa, kwenye bajeti anaonesha kwamba mwaka huu atajengwa madarasa 2,000, lakini shule za msingi peke yake tuna upungufu wa madarasa 107,000 ukipunguza maana yake tunadaiwa madarasa 107,000. Nyumba za walimu, upungufu uliopo unaonesha shule za misingi 178,435, sekondari 69,816 lakini Mheshimiwa Waziri anasema watajenga nyumba 56. Ukitafuta asilimia ni 0.023, ndiyo asilimia itakayojengwa. Kwa hiyo ningedhani kwamba malalamiko ya wananchi na walimu na wadau ni kwamba inatakiwa tuoneshe hizi kero zilizopo tunapunguza kwa kiwnago gani? Kama unapunguza asilimia 0.02 kwa kweli sio sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine masomo; kwa maana ya upungufu kwa somo. Kama unaambiwa tuna nchi ya viwanda, halafu walimu wa hesabu tuna upungufu wa walimu 7,291, biolojia ni walimu 5,181, kemia 5,377, fizikia ni 6,875; na hapa nichukulie kwa mfano Mkoa wa Dar es Saalam kuna labaratory technicians pale mahitaji ni 67 tulikuwa nao mwaka jana saba tu peke yake maana yake hao walimu pamoja na madai yao na mapungufu, changamoto mbalimbali wanafanya kazi ya kufundisha mara mbili na hakuna malipo ya ziada. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo limechagizwa na Serikali, kuhusu elimu ya bure, na mimi nimekuwa nikipinga mara zote kwamba Tanzania hakuna elimu ya bure, kuna elimu imepunguzwa gharama zake. Serikali ilichofanya imeondoa ada, lakini mambo mengine yatabaki na tukubaliane haiwezekani Taifa hili kila kitu kikatolewa bure bure, watu wote watakuwa wazembe, itakuwa ni ulemavu. Kuna wajibu wa wanafunzi wenyewe wafanye mitihani wafaulu, kuna wajibu wa wazazi na walezi wasimamie na kuna kazi za kufanya, kuna wajibu wa walimu wafanye kazoo yao na kuna wajibu wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini haiwezekani leo kwa mfano shule haina maji wale wazazi wangekaa vizuri pamoja wakajadiliana, wanaweza wakachimba visima shuleni na maji yakaondoka. Kuna upungufu wa madarasa, wangeweza kuchangisha, darasa moja wangechanga bilioni 21, una shule ina wanafunzi 2,000 wale wazazi ambao hawana uwezo wangewekwa pembeni, wale wazazi wenye uwezo wakubaliane, jambo hili linawezekana.

Kwa hiyo, mnapowaaminisha wananchi kwamba elimu ni ya bure watu wanabweteka, inawezekanaje watu wawazae watoto wao, wawapeleke shuleni, wakae miaka minne wasichangie gharama hawawajibiki, hili taifa litakuwa Taifa la wazembe kweli kweli. Huu uzembe, ni ugonjwa ambao unalelewa ambao hatuungi mkono. Kuna watu ambao wanapaswa kusaidiwa na kuna watu ambao wanaweza kufanya kazi hiyo na michango ni ya hiari, wale ambao wanaweza wafanye kazi hiyo, hili jambo si sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti unaonesha asilimia 60 au zaidi ya wanafunzi ambao wanamaliza form four hawa wanapata divison zero, divison four, Wabunge na wananchi wanauliza, hawa watoto baada ya kupata zero na for wanaenda wapi? Ndiyo maana inakuja hoja hapa ya VETA, na mnataka watoto wapate mimba katika umri mdogo. Sasa mtoto anamaliza darasa la saba hakwenda sekondari au kaenda kapata zero, hana ufundi wowote hata kufika hawezi kupika, hata bustani hawezi kulima, hivi vyuo vya ufundi ni muhimu sana. Mheshimiwa Ndalichako haya ndiyo majibu unatakiwa uje hapa utuoneshe, mkakati ukoje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu, shule za sekondari na shule binafsi. Mimi ni mwalimu na nimefanya utafiti mdogo. Shule yangu moja, ni-declare (to declare) ilikuwa ya mwisho lkatika shule za Tanzani form four mwaka jana, inaitwa Nyebulu Sekondari. Nimeenda shuleni pale walimu wanasema na mnawazuia private wasigawanye, lakini kuna shule za vipaji maalum, maana yake tayari huu ni ubaguzi, wamelekwa pale wenye uwezo mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shule za mikoa wamepelekwa, kuna shule za kata, hizi za kata ndizo class c. Mheshimiwa Ndalichako, kwanza mmetunga maswali ya kuchagua mpaka hesabu na mnataka nchi ya viwanda na nilipowauliza mkasema hapa ni muda, suala sio muda! Kama mtu hana uwezo wa kwenda high school, asiende, lakini akibaki mahali uwepo mpango mkakati wa kumsaidia apate uwezo wake wa kuishi. Msipeleke watoto shuleni kisiasa, wazazi wanaamini wameenda shule kumbe kimsingi wamelekwa, unapata asilimia ndogo unaenda sekondari. Miaka minne unakula ugali wa baba na mama, shambani huendi, huchangii Pato la Taifa, unapata zero. Huyu mtoto atajengewa chuki kwenye jamii yake, watu wanatakiwa wajue, kama huna uwezo wa kwenda sekondari usiende ufanye kitu kingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Profesa, unatungaje maswali ya kuchagua ya hesau halafu taifa liendelee? Unatungaje kazi hiyo? Halafu mnachokifanya katika mfumo wa maswali ya mtihani ana ana ana doo, watoto waansinzia, anaangukia hapa nda! Halafu ninyi mmechukua wanafunzi ambao hawana uwezo kwenye shule za kata mmerundika kwenye darasa moja yaani asie na uwezo amekaa na asie na uwezo mwenzake, nani anamuuliza mwenzake swali? Hii ni changamoto, halafu mnataka kutuletea hapa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi ya kuchangia kwenye eneo hili muhimu. Jambo langu la kwanza ni huduma mbalimbali ambazo zilikuwa zinatolewa Jeshini. Jeshini walikuwa wanauza vifaa vya ujenzi ambayo ilikuwa inaleta unafuu kwa Wanajeshi, walikuwa wanapata huduma mbalimbali za vinywaji, hivi vitu vikaondolewa kule Jeshini, nataka tupate kauli ya Mheshimiwa Waziri kwamba, baada ya kuondoa hizi huduma Jeshini nini mbadala wake sasa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa ni watu ambao wanakuwa maeneo yao ya kazi kwa muda mwingi, kwa hiyo ile kupunguza bei ina maana na wenyewe hawafanyi biashara zingine za kuingiza kipato ilikuwa inawasaidia sana, nasikia malalamiko mtaani huko. Kwa hiyo, nadhani Waziri atupe maelezo nini kitu mbadala wa hiyo huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka kuliongelea ni fedha kutotosha, lakini fedha ambazo zinapangwa kwenye Wizara hii pia ambayo ni muhimu sana kwa bahati mbaya sana baadhi ya Mafungu hazipelekwi kabisa. Nimejaribu kuangalia kumbukumbu kwa mfano 2015 kuna fedha hazikwenda, maeneo mengine wamepeleka mpaka asilimia tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano specifically Ngombe Fungu la 38 mwaka 2016 zilitengwa shilingi bilioni nane ambazo zilipaswa kufanya miradi kwa mfano kujenga Uwanja wa Ndege wa Tanga, kujenga maghala ya mlipuko ili kuepuka mambo kama yale ya Mbagala na Gongo la Mboto ambayo yalituathiri, lakini kwa bahati mbaya Fungu hili mwaka 2016 hawakupelekewa hata senti moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unaweza ukaona hali ilivyo katika hili na ni sehemu zipo nyingi sana ambazo zimetajwa, asilimia 1.3, asilimia nane, asilimia 12 na asilimia 13. Kwa hiyo, fedha zinatengwa pamoja na kwamba ni pungufu lakini pia hazipelekwi katika maeneo haya. Tunaomba hiyo fedha iliyotengwa hata kama ni kidogo kiasi gani ipelekwe ili miradi iliyopangwa na Jeshi hili katika maeneo mbalimbali iweze kuzipata fedha kwa wakati ili miradi hiyo ambayo imekusudiwa kufanywa itekelezwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, wenzangu wamependekeza suala la utafiti. Ukienda kwa mfano kama kile kituo cha NASA kule Marekani, nilipata fursa siku moja kukitembelea, wale watu asilimia 95 ni Wanajeshi na ndiyo wagunduzi wakubwa. Sasa kwetu hapa tuna Sheria ya Jeshi tangu mwaka 1966, nadhani sasa ni wakati muafaka hii sheria iletwe hapa Bungeni ibadilishwe ili Jeshi letu liendane na Jeshi la kisasa la sayansi na teknolojia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vyovyote vile hata kibinadamu tangu mwaka 1966 mambo ambayo yamepangwa kwenye hiyo ya sheria kwa kweli yamepitwa na wakati. Kwanza ulikuwa ni wakati wa ukoloni, nchi nyingi zilikuwa hazijapata uhuru, teknolojia haijakua na watu wengi hawajasoma, sasa tunataka Jeshi la kisasa, lenye wataalam waliobobea na wapanue wigo, lakini hawawezi kupanua wigo kama sheria haijafanyiwa marekebisho. Kwa hiyo, tungeomba hiyo sheria iletwe Bungeni, ifanyiwe marekebisho iendane na wakati kwa maana ya Jeshi la kisasa na la kukidhi mahitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo tulizungumza hapa, Jeshi la Wananchi kwa sasa ni chombo ambacho kimebaki Watanzania tunakitegemea wote bila vyama vyetu, lakini tunawashauri Serikali na Mheshimiwa Waziri ni muhimu sana wakati wa uchaguzi 2010 na 2015 kule Zanzibar Jeshi lilihusika kusimamia uchaguzi, kazi ambayo ni ya Mambo ya Ndani. Tunaomba jambo hili lisirudiwe tena kwani ni jambo baya kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji chombo ambacho ni very independent, kifanye kazi iliyokusudiwa, kama kuna mahali kuna hali ya hatari imetangazwa, waingie sababu inaeleweka, haya mambo ya uchaguzi ya siasa humu ndani acha tupambane na Polisi ambao tumezoeana Mheshimiwa Mwigulu anajua hilo, lakini Jeshi wafanye kazi yao, tutawapa ushirikiano, tunawaheshimu sana wabaki. Tusiwe kila mahali tunayogusa tunaingiza siasa kitu ambacho kwa kweli sio sawasawa, itafika mahali tuanze kulalamikiana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine limeulizwa hapa jambo la kuhusu mipaka, nadhani ni muhimu tukapata majibu. Imetajwa kwamba kwa mfano Tarime ambako ni kwetu, kule kuna beacon ziliondolewa maeneo ya Migori na ni muda mrefu, mazungumzo yamefanyika hayajakamilika. Kwa hiyo, tungeomba mambo haya na yenyewe pia yafanyiwe kazi yaishe kwa sababu ni mambo ambayo yana maswali ambayo yanazungumzwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo madai mbalimbali ya Wanajeshi. Mimi ni Mbunge wa Jimbo la Ukonga, tuna Kambi ya Jeshi pale na lile Jimbo vilevile lina wastaafu wengi. Kwa kweli Mheshimiwa Waziri ni aibu, mtu ambaye amekuwa mstari wa mbele aliyeapa kwamba yeye anakufa kwanza ndiyo nchi yake ibaki salama, ana-sacrifice maisha yake, halafu amefanya kazi muda mrefu sana, amestaafu, anaganga njaa mtaani na mkongojo anadai fedha yake ya kustaafu, siyo jambo jema kwa kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwanajeshi anadai uhamisho, kwanza wenzetu hapo ni amri, mnaamrisha nenda kituo, eneo au kambi fulani, anafunga mizigo hata familia hakuiaga, ameacha mke na watoto wanadai fedha za uhamisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu bima za afya. Wanajeshi hawana bima kwa hiyo wakienda kwenye duka la Jeshi akikosa dawa naye hana pesa, mke au mtoto wake, atakufa. Hivi akiwa vitani umemtuma kazi maalum ya nchi atafikiria familia au atafanya mapambano. Kwa hiyo, nadhani wapewe huduma zao, wapewe bima, hii siyo sawa sawa, hawa watu wanasafiri sana ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, JKT wapewe miradi ya ujenzi, wamefanya kazi kubwa sana, tulikwenda juzi kule Nyakato - Bukoba, JKT wanafanya kazi nzuri. Wapewe kazi ya miradi wana uzalendo wana-save hela ya Serikali ili watimize azma, wanafanya kazi nzuri sana nami nawapongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Haya majina ya Waheshimiwa haya yanatuvimbisha vichwa wakati mwingine, kuna watu wakiitwa jina inawezekana ukapata ujumbe vizuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri alikuja Ukonga katika mnada wa Pugu na akajionea hali ya shida iliyopo na ugomvi wa mnada ule na wananchi wanaozunguka eneo lile Mtaa wa Banguro. Nimeona kwenye ukurasa wa 40 amelizungumzia hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri anisikilize. Eneo la Banguro ni kweli kwamba Wizara yake ina hati ya mwaka 1939, lakini vilevile wananchi wenyewe walipewa hati ya Kijiji na Mheshimiwa Rais wa Kwanza wa nchi hii, Julius Kambarage Nyerere ya mwaka 1976 na wamejenga shule, wana zahanati, shughuli za maendeleo zinaendelea katika eneo lile. Kuna hekari 4,800 na wameshachukua hekari hizo zote karibu 4,162 anazo 108. Alipozunguka alikuwa anaoneshwa beacons ambazo ziko kwenye Miji ya watu na huduma za Kijamii.

Mheshimiwa N aibu Spika, ushari wangu ni kwamba, kwa kuwa wananchi walipewa hati na Serikali na hati ya kwanza ni ya mwaka 1939, hati ya pili ya mwaka 1976, automatically hii hati ya mwisho imefuta ile ya kwanza na ndiyo maana wamefanya shughuli za kimaendeleo, kuna zahanati pale wanajenga, shule ipo na watu wanaishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ningeshauri kwa sababu kuna hekari zilizobaki 108, kama alivyosema abaki na hizi kwa maana ya kuimarisha, lakini ikimpendeza sasa hivi ule mnada uko mjini, kuna maeneo hata hapa Ruvu makubwa tu, mapori makubwa ng’ombe wanahitaji maji, wanahitaji majosho, wanahitaji mabwawa, wanahitaji huduma mbalimbali katika eneo hilo, kule Dar es Salaam anapaswa alete tu nyama, hawa ng’ombe wanaweza wakatoka kwingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mheshimiwa Waziri hataki kwenda Ruvu, pale Zingiziwa tuna hekari 70, ni nje ya Mji, anaweza akapeleka hiyo huduma katika eneo lile. Kwa sasa wananchi wale kwa kweli wamepata sintofahamu, hawafanyi shughuli za kimaendeleo, wanaambiwa watafukuzwa kesho, watabomolewa kesho, kwa hiyo, natarajia katika mazungumzo yake na kwa sababu aliunda timu itakuwa imemshauri vizuri kwamba wale wananchi kwa sababu walipewa na Serikali na wana leseni za makazi, wengine wana hati miliki kama alivyojionea. Kwa hiyo, ningeshauri kwamba kauli yake itoke ili wapate amani katika maisha yao, waweze kujiendeleza, wasikae kwa wasiwasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Pugu Station wananchi wamevunjiwa nyumba kutoka Gongo la Mboto, kuja Ukonga, kuja Pugu mpaka Pugu Station. Tena sasa inakuja hofu tena ya mnada wa Pugu, kwa kweli hawawatendei haki wale wananchi. Ni muhimu ili watu wafanye shughuli za kimaendeleo na za kiuchumi wapate fursa na kauli ya Serikali ili waweze ku-settle na wajiendeleze. Hilo ni jambo la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri mradi ule aliuona, katika eneo lile hakuna hata uzio, ndiyo maana kuna ugomvi kati ya wananchi na Wizara ya Mifugo na kuna malalamiko. Pale wanahitaji maji, wanahitaji uzio, ng’ombe wanaokufa juzi ameona wamekamatwa. Nilimwambia siku ile ng’ombe wanaokufa kwanza kuna tundu la kuchomwa ile mifugo ili wateketezwe, lile limeharibika na ile ya kuchimbia ile mifugo haipo, hivyo wanatupwa kule bondeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakitupwa kule bondeni, watu wanazunguka, wanachukua mizoga, wanachinja, wanaingia mtaani, watu wanakula mizoga iliyokufa, ile ambayo wamekamata juzi ni michache. Ukweli ni kwamba ng’ombe wanakufa na watu wanakula vibudu pale kwa sababu hiyo. Kwa hiyo nadhani hilo nalo Mheshimiwa Waziri alishughulikie.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, kule Dar es Salaam tuna machinjio mbili, ile ya Vingunguti lakini na ile ya Mazizini. Mazizini ni machinjio ya mtu binafsi kwa hiyo hata Halmashauri inashindwa kuiboresha. Kwa hiyo, wananchi wa Mazizini wanapata shida, kuna maji machafu nilishamwambia na Mheshimiwa Naibu Waziri anajua. Maji yote ya ng’ombe wanaochinjwa pale, damu zote zinaingia mtaani. Kwa hiyo, ile sehemu wakati wote wa majira ya mwaka ni kipindupindu na magonjwa ya kuhara. Tumewaambia, tumelalamika mara nyingi walishughulikie, kama wanachukua kodi, waboreshe maeneo ya kufanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyabiashara hawa wa ng’ombe wanalalamika wana leseni mbili; kuna leseni ya kutoka kwenye mnada na akifika tena machinjioni analipa tena leseni nyingine. Bahati mbaya wale wafanyabiashara wanazuiliwa kuonana na viongozi yaani umoja wao, viongozi hawakutani nao ili wawaambie kero zao. Wanazuia hata ng’ombe ambao wanachinjwa hawajui idadi, wanadhulumiwa. Wanasema wale Madaktari, machinjio yote hata hii ya Kizota hapa Dodoma na nyingine Dar es Salaam, ng’ombe wanaochinjwa wale jamaa wanasema wanaibiwa nyama kwa sababu hawawezi kuhakiki. Kwa hiyo, hili nalo naomba Mheshimiwa Waziri alishughulikie lipate ufumbuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kumekuwa na shida mwenzangu amezungumza hapa asubuhi kwamba, ukihamisha mfugo kutoka eneo moja kwenda lingine unalipa kodi, hizi kodi si ndiyo Rais alisema kwamba ni Rais wa wanyonge ataziondoa, kulipwe kodi moja ambayo inaeleweka, leseni iwe moja, waiunganishe ili kuondoa usumbufu na kuondoa mianya ya rushwa na kuwasumbuasumbua watu. Vikodi kodi vingi vingi hivi kila mahali watu kwa kuwa wajanja wameingiza mikono yao na wafanyabiashara kimsingi hawanufaiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri kwa kweli ni mtu wa Kanda ya Ziwa na mimi nimeolea kule Nyakabindi kule Bariadi, yeye ni mfugaji, ni mkulima, kwa kweli siyo haki wakulima wa nchi hii, yaani mkulima analia, mvuvi analia na nyama tunaitaka. Haiwezekani wameendesha operesheni nyingi zimewaumiza watu sana. Operesheni Tokomeza walikuwa wanachukua ng’ombe, wanachukua miti wanawachomeka kule nyuma mpaka mtu anatoka utumbo, ni very unfair Mheshimiwa Waziri, siyo sawasawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, wafugaji hawa wanazunguka nchi nzima yaani Mmasai akionekana mahali ni kama mnyama, Msukuma watu wanatuchukia. Wameleta ugomvi kati ya wafugaji na wakulima. Watenge maeneo, ng’ombe apewe heshima yake, watengewe maeneo ya wafugaji ili tuondoe ugomvi kati ya wakulima na wafugaji. Nilitarajia Waziri aje na hiyo suluhu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wote wangetamani kupata nishati ya umeme popote walipo, wawe wa mjini au vijijini. Kwa hiyo, ushauri wangu kwanza ni kwamba, Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Waziri wa Fedha miradi ya umeme popote ilipo, iwe ya TANESCO au REA, fedha itoke ikamilike watu watoke gizani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna faida nyingi sana, kwanza kuna usumbufu mkubwa sana mtaani. Watu wa Dar es Salaam na maeneo mengine wanazuiliwa wasitumie mkaa na wanakamatwa sana, wanapigwa, wanateswa na watu wa Maliasili, lakini gesi ni ghali sana, umeme ni ghali na haupatikani. Kwa hiyo, mkitaka ku-save maliasili yetu kwa maana ya misitu lazima umeme upatikane kwa bei ya chini na gesi kwa bei nafuu, ili wananchi wa-opt waone kwamba, kununua gunia Sh.70,000 ni gharama zaidi kuliko kulipia umeme, kwa hiyo, misitu itabaki salama na hali yetu ya maisha itakuwa nzuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Dar es Salaam hasa Ukonga, kuna mitaa haina umeme kabisa. Sasa watu wakiambiwa waende mjini wanafikiri maana yake umeme upo, unafahamu katika mitaa tisa ya Kata ya Msongora ni mitaa miwili ambayo ina umeme, mitaa mingine haina umeme na hata maeneo ya shule. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri alifika mpaka usiku akaona hakuna umeme pale Ukonga Msongora, Chanika, Kidugalo, Vikongoro, Zavala, mitaa yote sita kati ya mitaa nane, hakuna umeme Buyuni, Kivule, Mvulege, Banguro, tuna mitaa mingi ambayo haina umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu TANESCO na hapa ndiyo nasema inatakiwa itengenezewe utaratibu mwingine, wananchi wana fedha mkononi wanalipia umeme zaidi ya miezi sita unaambiwa nguzo na mita hazipo, hili ni shirika la kibiashara, TANESCO wameshindwa kufanya biashara. Watu wana pesa zao, wanahitaji umeme, wanalipia, TANESCO haipeleki umeme. Ndiyo maana watu wanasema TANESCO hii kunatakiwa kuwe na chombo kingine washindane kama ilivyo kwenye mambo ya simu. Kama tungekuwa na shirika lingine ambalo TANESCO wakiweka bei Sh.320,000 mwingine aweke Sh.270,000, mwingine Sh.250,000, labda hao wangeamka kutoka usingizini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri alipokee hili. Kwenye taarifa mbalimbali inaonesha kwamba TANESCO inajiendesha kwa ma-trilioni ya fedha kwa maana ya hasara. Kwa hiyo, tungependa tupate taarifa halisi kwa nini TANESCO, Shirika la Umma kodi yetu, linajiendesha kihasara na nani anasababisha? Tuone tatizo ni nini? Watu wanahitaji umeme, kila mahali ukisoma taarifa za TANESCO kuna hasara wanaingia. Tungependa tujue kama Taifa na kama Bunge kwa nini kuna hasara TANESCO? Ni muhimu sana hili jambo likafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu gharama ya umeme. Kuna hoja hapa maeneo ya mjini wanalipia Sh.321,000 hata kama huhitaji nguzo, vijijini Sh.170,000. Watu wa mjini siyo kwamba wana uwezo mkubwa, ambacho kingefanyika kuna watu mjini ni maskini kweli, ana kijumba chake anahitaji umeme hapati kwa sababu ya gharama kubwa, kwa hiyo, ninyi mngeangalia watu ambao hawana uwezo, Wenyeviti wa Mitaa, Wabunge, Madiwani wanajua mtu ambaye hana uwezo apewe bei nafuu, wale wenye uwezo wapewe bei ambayo inawezekana, lakini mkisema mjini na vijijini mtaumiza watu wengine. Mjini wengine wanakaa kwa sababu tu ya majina lakini hawana maisha mazuri, ni maskini, hawasomi na ndiyo maana TASAF iko mjini na vijijini na Ukonga kwangu Kivule ipo. Hivyo, hili jambo Mheshimiwa Waziri mliangalie vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengine ni ya umma. Kuna shule hazina umeme, wana visima vya maji, walimu wanahitaji photocopy wachapishe mitihani, hata kufeli mitihani kwa wanafunzi wetu ni mazingira. Kwa hiyo, hili suala la umeme ningekuwa mimi, kama ilivyo Idara ya Maji, Serikali ingekuja na mpango mkakati, wametuambia vijiji vyote watapata umeme, Wabunge wanatarajia, wananchi wanasubiri lakini umeme haupatikani, hili jambo lingeisha. Huwezi kwenda kwenye viwanda kama hata umeme majumbani hauna, haiwezekani. Hauwezi kwenda kwenye viwanda vikubwa umeme wa majumbani hauna, lazima mpango uwekwe mahsusi umeme upatikane mjini na vijijini, anayehitaji umeme awekewe ambaye hahitaji abaki kwenye giza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo mngeyafanya na Serikali ya Chama cha Mapinduzi ndiyo mngepata sifa. Kuna watu wanashauri hapa mahali ambapo kuna hasara watu washughulikiwe. Kuna mafisadi wengi, kuna mikataba mingi IPTL iko miaka nenda miaka rudi, ishughulikiwe, haya ndiyo maeneo Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli amulike atu wenye mikataba mikubwa. Watu wanaacha kutumia umeme wa bei nafuu wanatumia jenereta katika ofisi zao matokeo yake tunashindwa kujiendesha tunapata hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Fedha ni muhimu, hayumo humu Bungeni lakini taarifa anazo. Hii miradi ya REA, miradi ya umeme, Mheshimiwa Mpango kama kuna mahali umekwamisha bajeti yako inakuja hapa watu wanakusubiri. Kwa hiyo, tunaomba fedha itoke, kama fedha haipo mtuambie fedha haipo tupange mipango ya kupata fedha, umeme upatikane, tunataka umeme mjini na vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwenye taarifa hizi mbili, kuna mambo yanayohusu maboma na mimi nimepewa dhamana ya kusimamia elimu upande wa TAMISEMI kama Naibu Waziri, lakini nataka niseme tu kwamba huwezi kuwa unakula keki wakati huo huo tena unataka ibaki kama ilivyo. Kwa hiyo, kama unaamua kufanya miradi mikubwa kama kununua ndege sita, mradi wa umeme wa maji kule Rufiji, reli ya umeme na vitu vingine, lazima kuna baadhi ya mambo yapungue, tukubaliane hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, nilitaka niwaombe Waheshimiwa Wabunge, maboma ni kweli kazi imefanywa na Ofisi ya TAMISEMI, tuna maboma nchi nzima zaidi ya 8,110, ambayo inahitaji takribani shilingi bilioni 140. Kazi imefanyika na mipango ya Serikali sasa ni kupeleka fedha kukamilisha maboma haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, maelekezo yametoka kwenye Halmashauri zote kwamba kila Halmashauri na ndugu yangu Mheshimiwa Silinde alikuwa anazungumza Momba imeelekezwa asilimia 40 ya fedha ya mapato ya ndani ziende kwenye huduma za kijamii ikiwepo elimu. Sasa Mheshimiwa Mbunge angetusaidia yeye amesimamia imeenda asilimia ngapi katika eneo lake. Kwa hisani ya Mheshimiwa Rais Magufuli, Momba imeongezeka uandikishaji darasa la kwanza kutoka asilimia 61 mpaka asilimia 83.1. Analeta fedha nchi nzima kila mwezi, zaidi ya shilingi bilioni 9 shule ya msingi, zaidi ya shilingi bilioni 20 sekondari, shilingi bilioni 5 ni posho ya watendaji kwa maana ya Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na posho ya madaraka kwa watendaji. Serikali hii pia imepeleka pikipiki kila Kata karibu nchi nzima ili wakasimamie elimu na kuboresha ubora wa elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa wanapozungumza habari kwamba kuna miradi imekwema, tumekataa misaada na mikopo ya masharti. Tutapokea mikopo ile ambayo haitutwazi utu wetu na haitudhalilishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunavyozungumza tangu tumeanza Mradi wa EPforR zimeshaenda fedha zaidi ya shilingi bilioni 98. Mwezi huu Waheshimiwa Wabunge mtaangaliaangalia kwenye Majimbo yenu, tumepeleka fedha shilingi bilioni 53.34 kwenye EPforR kujenga madarasa, mabweni, nyumba za walimu na vitu vingine kadha wa kadha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyozungumza tuna miradi mbalimbali nchi nzima inayotekelezwa na wafadhili na mabilioni ya fedha yanakuja mfano Mradi wa Tusome Pamoja na kadhalika. Wafadhili hao ni World Bank, Uingereza na Sweden ambapo wametoa fedha na tunaenda nao sawasawa. Kwa hiyo, miradi iliyopangwa chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe itakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka niseme hapa jambo la msingi sana. Waheshimiwa Wabunge, mimi nimesikiliza michango hapa, hizi ni Kamati za Bunge na niwashauri ndugu zangu wa Upinzani na mnisikilize vizuri yako mambo ambayo ukiyasema vizuri Serikali itapokea lakini ukianza vibaya utamaliza vibaya, ukianza vizuri utamaliza vizuri. Unaweza ukawa na hoja nzuri sana lakini namna ambavyo unai-present kwa kukashfu haitapokelewa, watu wataipinga, ndiyo maana watu wana-react kwa sababu ya hoja ambazo zinakuja upande wa pili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi katika hali ya kawaida kwa Mtanzania yeyote na hii lazima muifanyie kazi, kwa kazi ambazo anafanya Mheshimiwa Magufuli Watanzania wote wameshakubali mmebaki nyie tu na nyie ni wachache. Kwa mfano, alipokuwepo Mheshimiwa Kikwete alisemwa vibaya kama mnavyozungumza leo, leo mnasema Mheshimiwa Magufuli na wenzake wakitoka wataenda mahakamani haya maneno ni maneno ya kawaida, kelele za chura hazimnyimi ng’ombe kunywa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, hoja za upinzani zimeisha nchi hii, sasa hoja ni za kuungaunga, tuchape kazi, tujipange, tujifungie, tupokee maoni ya Kamati tukatekeleze. Tukienda kwenye uchaguzi tunataja hoja mnatoa maneno, Watanzania watapanga wanachagua maneno au wanachagua vitendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naomba niwasilishe. (Makofi/Vigelegele)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kupata nafasi hii na mimi mkono hoja. Nampongeza na Mheshimiwa Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wa Wizara kwa kazi kubwa na nzuri wanayofanya. Nawapongeza sana Jeshi la Wananchi kwa kazi kubwa wanayofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo amesema Mheshimiwa mchangiaji Dkt. Mwakyembe, Jeshi limekuwa sehemu ya kimbilio sana. Tunapokuwa tunapata majanga makubwa katika nchi hao ndiyo watu ambao kwakweli wanakuwa multipurpose wanafanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa, lakini vilevile tunapopata mafuriko maeneo mbalimbali wanashiriki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia hivi karibuni ukiacha shughuli kubwa ambayo wanafanya hata nje ya nchi kujenga heshima na utashi wa Tanzania na uzalendo uliotukuka, wamekuwa wakitumwa katika maeneo mbalimbali kwakweli hatujawahi kupata malalamiko kutoka huko ambako wanafanya kazi, maana yake wanabeba uzalendo, wanawakilisha nchi yetu vizuri sana na kupeleka sura chanya ya Jeshi letu nje ya mipaka ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais pamoja na kwamba Jeshi wanafanya kazi lakini amewapa nafasi kubwa wamefanya kazi kubwa sana ya ujenzi wa nyumba za Serikali, sasahivi wanajenga majengo hapa ya Mji Mpya wa Serikali pale Mtumba, lakini wamekabidhiwa majengo kule kwetu Ukonga, Jimbo la Ukonga pale tunashukuru sana, lakini kubwa zaidi ni kitendo cha ushujaa Mheshimiwa Rais aliona ambacho alikuwa anafanya yule Ndugu Charles Mbuge na akampandisha kuwa Brigadier General jambo kubwa sana kwa kazi kubwa anayofanya. Hii maana yake aatia nguvu wanajeshi ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa sana. Tunawathamini, tunawaheshimu waendelee kufanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema namna hiyo, nashukuru sana naunga mkono hoja. Nawapongeza sana wanajeshi na Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi kwa kazi kubwa na nzuri anayofanya. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza naunga mkono hoja za Kamati zote tatu kama zilivyotolewa. Pia nitajairibu kupitia baadhi ya maeneo machache.

Mheshimiwa Spika, la kwanza, nitoe tu taarifa kwamba kwa sababu mambo yamezungumzwa mengi upande wa elimu, niliarifu Bunge letu kwamba Serikali inapeleka fedha nyingi sana katika kuboresha elimu. Tunachoomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote na hasa Watumishi wa Umma ni kuhakikisha kila shilingi inapopelekwa, inasimamiwa vizuri ili tuangalie value for money. Hilo ni jambo la msingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, ninapozungumza, hii elimu msingi bila malipo, mpaka ninapozungumza hapa, mpaka Desemba, 2018, Serikali ya Awamu ya Tano ya Chama cha Mapinduzi imeshapeleka shilingi bilioni 634,189 ambazo zimeenda kwenye Elimu Msingi bila malipo. Hizo zinakwenda kwenye posho ya madaraka, Maafisa Elimu wale wa Kata, Wakuu wa Shule, motisha na vinginenvyo.

Mheshimiwa Spika, kwenye hoja mbalimbali, imejitokeza hapa hoja ya majengo ambayo yamesimamiwa kwenye ukarabati wa shule kongwe na TBA. Ni kweli, hoja hii ilijitokeza kwenye Kamati ya TAMISEMI ambayo nami nilikuwepo na Mheshimiwa Waziri, Ofisi ya TAMISEMI imeshalipokea hili, inalifanyia kazi, tutapitia mikataba ile na kuchukua hatua maeneo ambayo wameshindwa kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Spika, ziko shule nyingi kama Ihungo, Kigoma Sekondari, Songea Wasichana, Mirambo, Nangwa, Tosamaganga, Malangaze na nyingine ambazo mpaka leo hazijakamilika. Waheshimiwa Wabunge na Kamati ya TAMISEMI naomba niseme kwamba hili jambo linafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, ni elimu ya msingi bila malipo, zimejitokeza hoja hapa na michango mbalimbali; Mheshimiwa Waziri wa Elimu yupo anaweza akatoa ufafanuzi zaidi, lakini tunao Waraka hapa Na.3 wa mwaka 2016 ambao unaonesha zoezi la kuimarisha elimu Tanzania ni zoezi shirikishi, ziko kazi ambazo zinafanywa na Serikali na fedha zinapelekwa kama zilivyotajwa, ziko kazi zinafanywa na wazazi, uko wajibu wa wanafunzi wenyewe na wadau mbalimbali wa elimu.

Mheshimiwa Spika, michango kwa elimu na miundombinu inaruhusiwa kwa utaratibu uliowekwa, Wakuu wa Wilaya wameelekezwa kwa kushirikiana na wazazi waunde Kamati mbalimbali wanachangisha wale wanaoweza, ambacho kimeelekezwa ni kwamba kusiwe na michango ambayo ni gandamizi, akinamama kunyang’anywa meza na mitaji yao midogo midogo, lakini michango ya kuchangia elimu na miundombinu yake inaruhusiwa kwa usimamizi wa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi na kwa vibali maalum, Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge wasaidie hilo, liendelee kufanyika. Hili linaenda sambamba pamoja na zoezi la kumalizia maboma yaliyopo.

Mheshimiwa Spika, juzi niliulizwa swali hapa juu ya maboma; nikawaambia tunahitaji takribani zaidi ya bilioni 417 kumaliza maboma yote nchi nzima, lakini, tutakuwa tunafanya kwa awamu kulingana na uwezo uliopo, mazungumzo yanafanyika na Wizara ya Fedha, kikao kilimeshafanyika chini ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Kwa hiyo ina maana muda sio mrefu sana zoezi hili litapunguza idadi ya maboma ambayo yapo katika eneo hilo. Kwa hiyo, tuna uhakika kwamba ndani ya muda mfupi ujao, madarasa yatajengwa na watoto wetu hawataendelea kukaa chini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia niwatoe wasiwasi, wanafunzi wote ambao wamefaulu kwenda kidato cha kwanza mwaka 2019 wote wataingia darasani na watasoma. Mpaka kufikia mwezi wa Tatu kazi nzuri imefanyika na hili jambo linasimamiwa vizuri sana. Kwa hiyo wananchi na Watanzania wasiendelee kuwa na hofu, hili jambo linasimiwa na Serikali ipo kazini, wasiwe na hofu.

Mheshimiwa Spika, kuna hoja imejitokeza hapa ya kuimarisha usomaji, zile KKK (Kusoma, Kuhesabu na Kuandika). Tuna miradi miwili mikubwa, mradi wa kwanza, unaitwa EMIS na tumeenda mbali zaidi na EQUIP ambao mradi huu una fedha nyingi sana zinaenda. Tunafundisha Walimu wa darasa la kwanza na pili, mpaka la tatu na la nne. Tumejenga shule zinaitwa shikizi, ambazo unapunguza umbali kutoka nyumbani kwa mtoto na shule mama na Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi tumezikagua zinaendelea. Tumefundisha Kamati za Shule, tumefundisha Walimu, tumetoa tablets. Kwa hiyo mambo mengi makubwa sana yanafanyika katika eneo hilo. Naomba mtuunge mkono tuendelee kufanya kazi hiyo na kila mtu ambaye anaweza kuchangia elimu, achangie elimu lakini kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Rais anaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kweli, baada ya elimu msingi bila malipo, changamoto ni kubwa ufaulu wa wanafunzi umeongezeka, watoto wengi wanaenda mashuleni waliokuwa wanashinda kwenye masoko, sasa hawaendi masokoni wanakwenda shuleni, wale ambao walikuwa wanapiga debe, sasa hawaendi, mtaani watoto hawapo, wote wameenda shuleni. Hili ni jambo kubwa, tumpongeze Mheshimiwa Rais na Serikali ya Awamu ya Tano ya Chama cha Mapinduzi kwa maamuzi thabiti kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la kuweka kumbukumbu hapa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa…

NAIBU WAZIRI, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, dakika moja, tu...

SPIKA: Waitara. (Kicheko)

NAIBU WAZIRI, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, jambo la ufaulu ambapo matokeo yametolewa. Maafisa Elimu wameonesha kwamba shule za private zimefaulu zaidi kuliko shule za Serikali. Serikali inasimamia shule za msingi zaidi ya 16,000, shule za private ni shule 1,413 sawa na asilimia nane tu, lakini hawa wenzetu katika shule zao wanachuja watoto, kuna mitihani ya darasa la nne ya Serikali, ya kidato cha pili na cha nne.

Mheshimiwa Spika, kwa maelekezo ya Serikali kwa Waraka nilionao watoto wakifaulu wa darasa la nne, wakifaulu wa kidato cha pili, hawa wanamaliza mtihani darasa la saba, wamalize na kidato cha nne, wenzetu wanawachuja watoto, wanawarudisha nyumbani. Kwa hiyo wale wote ambao wameanza la kwanza mpaka la saba, la sita wamezuiliwa; wale ambao wameenda form one mpaka three wamerudishwa, sisi Serikali ni kokoro, wote tunawapokea, wanafanya mitihani, asilimia nane huwezi kulinganisha na asilimia 92.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa muda ulionipa. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza naunga mkono hoja Kamati zote mbili, Kamati ya Sheria Ndogo ambayo inaongozwa na Mtemi Chenge na Kamati ya Sheria ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Mchengerwa. Kuna hoja zimejitokeza hapa zinazohusiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya kwanza ni ile ambayo Waheshimiwa wa Kamati ya Sheria Ndogo wamepitia na kweli kwamba kulikuwa na upungufu katika Halmashauri zetu umetajwa, sina sababu ya kuutaja hapa. Tunaomba tuseme kwamba tumepokea maoni yenu na mapendekezo yenu tutayafanyia kazi na kuboresha ili sheria ndogo kwenye Halmashauri zetu ziendane sawasawa na sheria mama pamoja na matumizi bora ya kuboresha utawala bora katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ambalo limezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge hapa ni uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Hili jambo bado lipo kwenye mchakato hatujachelewa. Kwa kawaida mambo ya kisheria na Wanasheria wanafahamu, Mheshimiwa Salome Makamba alikuwa anachangia hapa, ni kwamba jambo hili limeanza mchakato wa kuangalia uchaguzi uliopita, upungufu ambao ulijitokeza, malalamiko yaliyotolewa na wananchi na wagombea waliokuwa wanagombea nafasi mbalimbali, wakiwemo wagombea wa Uenyekiti wa Mtaa mwaka 2014.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa yamepokelewa na wataalam wetu katika Ofisi ya TAMISEMI yatarudishwa kwenye Halmashauri zetu, yatakuja kwenye vyama vya siasa, tutapokea maoni, kwa hiyo jambo hili mtashirikishwa vizuri. Tumeanza kufanyia maboresho maoni ya 2014 ambayo pia watu walitoa. Kwa hiyo ni jambo ambalo bado liko kwenye mikono salama, naomba mwendelee kutupa imani yenu, tutatoa ushirikiano hakuna tatizo katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu. Tumezungumza kodi ya majengo, hili jambo ni kweli wakati yametolewa maekelezo ya kukusanya kodi ya majengo, yamekuja maoni mbalimbali ya Waheshimiwa Wabunge, Waheshimiwa Madiwani na Halmashauri na wadau mbalimbali na wananchi wenyewe na hasa wafanyabiashara ambao kimsingi wanalipa kodi kwa Watanzania jambo limechukuliwa na Serikali ambayo ni sikivu ya Chama cha Mapinduzi, limefanyika kwenye mchakato, yatakuja maboresho humu na Waheshimiwa Wabunge mtapata nafasi ya kutoa maoni yenu ili tufanye maboresho ya namna bora ya kusimamia kodi ya majengo bila kuleta kero na malalamiko kwa wananchi wetu. Hili jambo nilitaka niliseme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne ambalo limezungumzwa hapa, kuna Mbunge mmoja amezungumza anasema kuna mjumbe wa NEC alikuwa anasemwa huko mtaani kwamba sijui nilikwenda kwenye Mkutano fulani nikitaka watu wampinge Tundu Lissu. Naomba niseme kwamba, Tundu Lissu mke wake ni Mkurya anaitwa Robi, ameoa Nyarero pale nyumbani, kwa hiyo ni shemeji yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jambo hili, nataka niseme msimamo wangu ni kwamba, Tundu Lissu ana maumivu, alipatwa na tatizo na watu wote walimpa pole na sio kumwambia hadharani, lakini sasa baada ya kupata madhara hayo amegeuza machungu yake yawe machungu ya Watanzania, hatuwezi kukubali. Machungu ya mtu mmoja, hayawezi kugeuzwa machungu ya Taifa. Savimbi sio lazima awe na mandevu, unaweza ukawa Savimbi kwa matendo yako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo yanayofanyika duniani. Huyu ni Mtanzania, angerudi hapa Tanzania aeleze machungu yake, maumivu yake, tumsikilize, tumsaidie kulia. Ameamua kwenda ughaibuni, anamtukana Rais wa nchi, anasema Rais wetu ambaye ni Daktari, ni msomi wa hesabu kama mimi, wa hesabu na kemia, eti Rais Mheshimiwa Dkt. Magufuli hawezi kutunga hata sentensi moja ya Kiingereza, sio kweli this is very unfair, hizo haki mnazozungumza sijui mnatoa wapi? Hamwezi kuwa na haki ya kusema muonewe wenyewe huruma lakini haki ya kutukana wenzenu, kuwadhalilisha watu wazima na familia zao, hilo halikubaliki na haliwezi kuungwa mkono, ni very unfair. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine katika maelezo anasema, anapaka matope Taifa ili Serikali ianguke, amesema wakati anahojiwa Ai…International Study of Africa, nimemsikiliza, anasema yeye anapaka matope Taifa ili akirudi hapa asikilizwe, apate uongozi na Serikali ianguke, huyu atakuwa ni mhaini, anataka kuiangusha Serikali, anaipaka matope Tanzania, misaada ambayo inakuja hapa, Watanzania wa Singida, watu wa Mara, Wagogo, makabila yote, wanawake, wazee na vijana wananufaika, leo mnazungumza habari ya maji hapa.

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ndio mambo ambayo hatuwezi kuyakubali yakafanyike. Tumeshasema kama kuna mtu ameonewa katika Taifa aseme, tutasimama upande wake kumtetea.

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): …lakini
sio anageuza mambo yake binafsi, mtu ambaye anatetea tumbo lake…

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): …halafu anageuza tena tuzungumze kama ya Taifa, haiwezekani…

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Kwa mambo ambayo Mheshimiwa Tundu Lissu anayafanya Watanzania wasimame na watambue…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Msigwa, kaa chini.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA):
Watambue wazalendo ni wapi, wanafiki ni wapi, wasaliti ni wapi. Tanzania ni ya kwetu, una jambo lako rudi Tanzania, tukae pamoja, tujadiliane, tupange mipango yetu, uongozi wa nchi hii utatolewa na Watanzania, uongozi wa nchi hii hutakabidhiwa Ulaya, tutakupa sisi Watanzania kwa muda tutakaotaka. (Makofi/Vigelegele)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Hoja ni nyingi lakini nitajaribu kupitia zile ambazo nitaweza ndani ya muda huo na nyingine kila Mheshimiwa Mbunge ambaye ametoa mchango wake kwenye eneo hili tutampa majibu ikiwezekana kwa maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja katika michango ya Waheshimiwa Wabunge ilikuwa inazungumzia Watumishi wa Umma ambao wanakaimu kwa muda mrefu. Naomba tuwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba hoja hii tumeipokea, tunatoa maelekezo kila ngazi ya Serikali za Mitaa wakusanye taarifa zao wazilete ili wale watu ambao wanakaimu kwa muda mrefu na wanakidhi vigezo, basi waweze kuthibitishwa kazini ili waweze kufanya kazi kwa umakini zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, tunafajamu kwamba tuna upungufu wa wahandisi katika Halmashauri zetu, ni kweli, wahandisi wengi walipelekwa TARURA, lakini jambo hili limeshachukuliwa na Serikali linafanyiwa kazi ili tupate wahandisi hasa wa majengo na waweze kusimamia miradi mbalimbali ambayo kwa kweli kwa awamu hii ya tano miradi mingi Serikali imepeleka fedha ujenzi wa vituo vya afya, nyumba za viongozi wetu wa Wilaya na mikoa. Kwa hiyo, hili jambo limechukuliwa litafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa mchango wa Mheshimiwa Mbunge mmoja, alijaribu kutoa maelezo ya kupotosha ya elimu msingi bila malipo. Naomba niseme tu kwa watanzania wote na Waheshimiwa Wabunge kwamba kwa kweli kama kuna jambo kubwa ambalo Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli amefanya, ni maamuzi thabiti ya kuruhusu elimu msingi bila malipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na wanafunzi wengi waliopata fursa ya kusoma na gharama imekuwa ikiongezeka. Tumepanda kutoka shilingi bilioni 249 sasa mwaka huu wa fedha tunaozungumza ni shilingi bilioni 288 elimu msingi bila malipo. Hili siyo jambo la kubeza, ni jambo la kumpongeza Mheshimiwa Rais na Watanzania wana macho wanaona; na masikio na nina uhakika wataendelea kumuunga mkono katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna madai yamezungumzwa hapa ya Waheshimiwa Madiwani na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa. Jambo hili limesemwa kwa upana na uzito. Tumelichukua Ofisi ya TAMISEMI linafanyiwa kazi na baada ya muda siyo mrefu sana litapata muafaka na naamini kwamba kero hiyo itakuwa imeondoka. Kwa hiyo, linafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchangiajie ambaye amemaliza sasa hivi amezungumza kama wengine ambavyo wamesema habari ya madarasa, nyumba na mambo mbalimbali ya miundombinu ya elimu, lakini ukweli ni kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ya Chama cha Mapinduzi imejitahidi sana kuboresha miundombinu ya elimu. Changamoto nyingi ilikuwa tunajaribu kuboresha maeneo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2019 kwa mfano, tulikuwa na shida ya magari, hapa tunafanya mchakato wa kununua magari 26; kila mkoa Maafisa Elimu wa Mikoa watapata magari mapya kabisa ili waweze ku-move kutoka eneo moja kwenda lingine kusimamia suala zima la elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika bajeti hii ambayo tumezungumza tutanunua magari 40 tena ambayo yataelekezwa kwenye ngazi ya elimu sambamba na kujenga nyumba za Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Makatibu Tarafa. Ukiangalia kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI utaona imezungumzwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumejenga madarasa 4,400, matundu ya vyoo zaidi ya 8,000, maabara 22, tumepeleka fedha mwezi wa Pili hapa shilingi bilioni 29; tupo kwenye mchakato wa kupeleka shilingi bilioni 34 kwenda sasa kukamilisha maboma ya shule za msingi. Zaidi ya maboma 2,000 yatafanyiwa kazi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na hoja hapa ambazo zimezungumzwa, naomba niseme tu, mwingine alisema nitaje uwezo wangu, nisiwe nachangia kama Naibu Waziri. Nijibu na nianzie hapa hapa nazungumza.

Mheshimiwa Naibu Spika, demokrasia ambayo inazungumzwa katika nchi hii mimi siielewi. Mheshimiwa Msigwa sijui kama yupo humu ndani. Mheshimiwa Msigwa wakati anagombea Uenyekiti wa Kanda, walienda wakaondoa wagombea wa CHADEMA akabaki peke yake. Pamoja na hayo, walipowaondoa alienda akapata kura asilimia 48 za hapana. Huyo ndio Mheshimiwa Msigwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa mlimsikia Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kambi Rasmi ya Upinzani anazungumza kwamba leo mafisadi ambao wamekamatwa kudhulumu Taifa hili, leo anasema waondolewe wasichukuliwe hatua. Huu ndiyo ulikuwa wimbo wao wa siku zote. Kwa kweli katika mazingira haya hatuwezi kukubaliana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza ukaona, hivi Mkuu wa Majeshi ambaye anaangalia ulinzi wa nchi hii, hutaki atoe kauli juu ya ulinzi wa nchi hii kweli! Kama kuna chokochoko ndani za kichochezi, anaachaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Selasini ni Mjumbe wa Kamati ya Utawala na TAMISEMI, amekuwa kwenye vikao vyote vya Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, naomba nimpongeze Mheshimiwa Selasini, ametoa michango mizuri sana. Wakuu wa Mikoa ambao walikuwa na matatizo ambao hatukatai, tumezungumza nao, tumetoa maelekezo na wamebadilika. Alikuwa na malalamiko ya Mfuko wa Jimbo, tumeongea na Mkurugenzi, imeisha. Haya mambo ya jumla jumla hayatakubalika. Kama kuna mtu ana kesi specific, case by case alete tuchukue tuifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo chetu cha Hombolo kimetoa semina kwa mafunzo mbalimbali. Niseme kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi ipo kazini na kwa kweli siasa ni kupambanisha hoja siyo vioja. Tumeshuhudia kwenye Bunge hili, wenzetu wana vioja, CCM wana hoja, chapeni kazi. Huo ndiyo ukweli na Watanzania wanaona.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, inawezekanaje Mbunge anasema patachimbika. Hivi hao Watanzania mnaowazungumzia, ni hawa tunaokaa nao sisi au nyie ndio mnajua! Kama patachimbika, mtakuwepo, tutakuwepo. Huu mchezo dakika 90 haziishi, hao Watanzania tupo nao wote. Kwa hiyo, maneno kama hayo ya kuchochea watu, kuandaa kifujofujo, Serikali haiwezi kuruhusu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka tupate hoja za wanasiasa makini kama akina Mheshimiwa James Mbatia, wanatoa hoja hapa mtu unafurahi, akina Mheshimiwa Selasini na wengine. Wale ambao hawataki kufanya siasa kwa vyama hivi; leo amekuja Prof. Pierre Lumumba, anasema Magufulification of Africa, yaani Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli anakuwa reffered Afrika nzima. Huyu ni Rais wa mfano. Miradi ambayo ameitoa ni ya kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Chama cha Mapinduzi mna huruma sana. Miradi pale Rombo tumepeleka, Iringa inajengwa lami, Tarime kuna mpango wa kimkakati, soko liko pale zaidi ya shilingi bilioni kadhaa, Majimbo yamepewa fedha mbalimbali, watumishi wamepelewa; mnataka nini ndugu zangu wa upinzani? Mnataka mpewe nini? Gunia la chawa! (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka niwashauri ndugu zangu wa Upinzani kwa kazi hii inayofanyika ya Chama cha Mapinduzi, ilitakiwa tupange vizuri namna ya kutoa hoja. Mahali pa kukosoa ukosoe vizuri, wala siyo kutukana… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, katika michango ya Waheshimiwa Wabunge kuna mambo ambayo yamezungumzwa, ambayo yanahusiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Kuna hoja zimetolewa na nimejaribu kupitia kitabu cha Kambi Rasmi ya Upinzani, wameandika data nyingi humu, lakini nyingi siyo za kweli na nilipojaribu kufuatilia nikagundua kwamba hizi zilikuwa zinaandikiwa pale African Dream, wakishirikiana na wenzao. Hizi data ni za African Dream, kwa hiyo, naomba mnisikilize niwape data za Serikali, ambaye ni custodian wa information hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama walisikiliza vizuri wakati Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Utumishi anazungumza hapa, alitoa tamko la Serikali kwamba madai ya Walimu na madaraja na maslahi mengine yataanza kushughulikiwa kuanzia Mei Mosi, maana yake kesho, lakini pia kuna maelekezo yametolewa kwa vyombo mbalimbali vinavyoshughulika na utumishi wa umma, hiyo kazi itafanyika. Kwa hiyo, kimsingi hili pia halipo kwenye Wizara ya Elimu, lipo utumishi, lakini limeulizwa hapa nikasema nilitolee kauli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna hoja imezungumzwa ya elimu msingi bila malipo na kwa bahati mbaya sana nilimsikia Mheshimiwa Yosepher Komba akizungumza, kwa namna ambayo kwa kweli alikuwa anabeza, lakini kwa kweli ukifuatilia namna ambavyo mpango huu wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Awamu ya Tano umewasaidia Watanzania walio wengi, enrollment imeongezeka, watoto wa shule ya msingi na madarasa ya awali wameongezeka sana. Kila mwezi Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, anapeleka shilingi billioni 23 kwa ajili ya elimu msingi bila malipo. Kwa hiyo, siyo jambo la kubeza kwa kweli ni jambo la kupongeza na Watanzania wengi walio maskini, watoto wao wanaingia shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wamezungumza kwamba watu wanafelifeli, siyo kweli, tunao watoto ambao wamefaulu vizuri sana kutoka shule za kata na wameenda mpaka shule za vipaji na tutawapa taarifa ya majina yao kwa ajili ya kumbukumbu kwa ajili ya muda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mwaka 2016/2017, Serikali iliajiri Walimu wa sayansi 3,081, mwaka 2017/2018, walimu 2,767 wa sekondari na msingi, lakini hapa tunapozungumza, tumesambaza Walimu 4,500, miongoni mwao Walimu 3,088 wote ni Walimu wa sayansi, no, ni Walimu wa shule ya msingi, lakini 1,400 ni Walimu wa sayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge alizungumza, maeneo yale ambayo yalikuwa na upungufu mkubwa sana kwa upande wa masomo ya sayansi tumepeleka. Ni kweli kwamba hawatoshi lakini wameenda. Kumbukumbu ya kitabu chao hili cha African Dream, kinaonesha kwamba ni upungufu karibu Walimu 91,000, siyo kweli. Tuna upungufu wa Walimu ni kweli tunakubali, 66,485 kwa shule za msingi na Walimu 14,080 kwa shule za sekondari. Mpango uliopo, kila mwaka tutakuwa tunaajiri Walimu kupunguza gape hili na hawawezi kuchukua miaka 10 kama walivyosema, siyo kweli, itachukua muda mfupi kwa mpango ambao Mheshimiwa Rais amesharidhia, tunaziba ma-gape ya watu waliofariki dunia, watu waliosimamishwa kazi kwa makosa ya kiutumishi na mambo kadha wa kadha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile madarasa yamejengwa, kwa mfano, mpaka kufikia Februari, 2019 shule za msingi yamekamilishwa madarasa 2,840, tunaendelea kujenga madarasa 2,638, hapo yanaendelea kujengwa. Matundu ya vyoo 76,700 na yanaendelea kujengwa 3,004, nyumba za Walimu 720 na tunatengeneza madawati 135,000. Hii kazi kubwa inafanyika chini ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna mpango wa shule shikizi, tumejenga shule shikizi kupunguza umbali kati ya shule na shule 255,000 kwa kutumia bilioni 18.5 zimefanya kazi kwenye mikoa tisa na halmashauri 63, madarasa 502, 0fisi 251, matundu ya vyoo 1,255, maktaba 34 na maboma 223.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wametoa hoja hapa ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi kwamba aliahidi kutoa fedha za mabona shilingi bilioni 29, naomba nitoe taarifa kwamba juzi tulitoa fedha shilingi bilioni 29.9 kwa kuhusiana na Wizara ya Elimu na tumepeleka kujenga maboma mbalimbali zaidi ya 2,300 yanaendelea kujengwa. Hapa tulipo tunapeleka mpango mwingine wa kukamilisha maboma ya shule za msingi nchi nzima kwenye halmashauri zote na majimbo yote ikiwezekana. Hii ni kazi nzuri ambayo inafanyika ya Awamu ya Tano ya Chama cha Mapinduzi, chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye mpango wa 2019/2020 tutajenga nyumba za Walimu 364 kwa kutumia shilingi bilioni tisa, lakini sekondari maalum 26 kila mkoa kwa ajili ya watoto wa kike, kupitia mradi wa SEP, lakini EP4R tunanunua magari 26 kuratibu elimu kwa ngazi ya mkoa, kila mkoa watapata gari jipya, tunajenga majengo ya utawala 50, nyumba za Walimu 800, mabweni 300, matundu ya vyoo 1000, kumbi za kufundishia kwa maana ya kumbi za wanafunzi zile mbalimbali 2,000 zinajengwa, lakini shule kongwe zinakarabatiwa 15.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ni mambo makubwa ambayo yanafanyika katika nchi hii na ni muhimu sana tukaitia moyo Serikali ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme jambo moja la mwisho, kuna hoja inapotoshwa kwamba Serikali imesema elimu bure, kwa hiyo, michango hairuhusiwi. Umetolewa Waraka wa Wizara ya Elimu ambao umeanza kufanya kazi Januari, 2019, mwongozo umetolewa. Tukubaliane nchi hii kwa ukubwa wa taifa hili na upungufu wa fedha uliopo, haiwezekani tukaishi kama ndege bila kuchangia chochote. Serikali ilitoa fedha, bure, tumeondoa ada na shule za sekondari zingine tumepeleka fedha na mabweni yanajengwa miundombinu inaimarishwa na Walimu wanalipwa na watumishi wengine wa Serikali, lakini wananchi wenye uwezo watachangia kadri ambavyo uwezo wao utaruhusu na Serikali imetoa huo mwongozo, kuanzia ngazi ya kijiji, ngazi ya kitongoji, ngazi ya kata, Waheshimiwa Wabunge, kwenye mikoa. Kilichozuiliwa ni kwamba, asitolewe mtoto darasani eti kwa sababu ya mchango mzazi wake au mlezi hajachanga, hapana. Kama mtoto anadaiwa, mzazi na Walimu wasimamie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tukasema Walimu wasisimamie michango, kwa sababu ilionekana kwamba Mwalimu anapokwenda kudai michango kwa wazazi anajenga chuki na usimamizi unakuwa mgumu. Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi watasimamia zoezi la michango, wenye uwezo wananchi wa kawaida, Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wengine wachangie kile ambacho wanaweza. Ukichimba kisima cha maji sawa, ukijenga darasa sawa, tundu la choo sawa, darasa sawa, nyumba ya mwalimu sawa, hii kazi ni ya Watanzania wote, tushikamane, tuunge mkono kazi nzuri ya Serikali ili mambo yaweze kuboreshwa na Watanzania wote na watoto wetu waweze kusoma vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi na ninaunga mkono hoja za kamati zote tatu. Waheshimiwa Wabunge kupitia Kamati zao walitushauri kama Serikali, tumechukua hatua kwa mambo ambayo walielekeza na tunaendelea kuboresha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajielekeza kwenye hoja zilizozungumzwa na Waheshimiwa Wabunge juu ya elimu, na Waheshimiwa Wabunge wengine wamezungumzia maboma. Niwaambie tu kwamba, tulitoa fedha hapa shilingi bilioni 29.9 ya kupeleka kwenye maboma mbalimbali yakaleta mabadiliko makubwa, lakini pia hapa tulipo tupo kwenye mkakati wakupeleka fedha zaidi ya shilingi bilioni 200, ili kuongeza miundombinu ya elimu. Pia tumetenga fedha zaidi ya bilioni 200 kwa ajili ya kwenda kuimarisha elimu ya shule za msingi, na kazi hiyo inaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu watu wakaelewa kwamba kila mtu akisimama anazungumza miundombinu hapa. Juzi tulizungumza mjadala wa fedha hapa tunatarajia kupata, zingesaidia sana. Tunatafuta vyanzo mbalimbali ili kuhakikisha kwamba tunaboresha elimu yetu. Ufaulu umeongezeka sana. Kwa kauli ya Mheshimiwa Rais na maelekezo yake ni kwamba elimu bure ipatikane kwa watoto wengi wa Tanzania ambao walikosa fursa hiyo imesaidia sana kuwa na watoto wengi shuleni; kwahiyo tunahitaji kuboresha huduma hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi ambzo zinazungumzwsa trilioni 1.5 zingeweza kujenga mabweni zaidi ya 300 Tanzania nzima, madarasa 800 ya sekondari, madarasa 1,200 ya shule za msingi, tungejenga shule 26 mpya za wasichana, tungejenga mabweni maalum mahsusi na shule za msingi, ni mambo makubwa sana. Ukitaka kujua hili tafuta taarifa hizi ili tuweze kuzungumza kwa pamoja, kwamba tunapokuwa tunapanga mipango kuboresha elimu yetu tushirikiane kwa pamoja bila kuleta ubaguzi na ubinafsi uliopitiliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza hoja hapa zimezungumzwa; kwa mfano kuna hoja ya Serikali za mitaa. Uchaguzi huu uliashaisha na wenzetu walisusa wenyewe na maelekezo na msimamo wa Serikali ni kwamba uchaguzi umekwisha. Kama kuna mtu anampinga Mwenyekiti wa Mtaa afuate utaratibu, asipofuata mtakuja hapa tena kulialia na kulalamika. Sheria ndogo zipo kwenye vijiji, kamati za ulinzi na usalama zipo pale watafanya kazi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na si kweli kwamba ukienda kwenye ngazi za vijiji na vitongoji eti wanachama wa upinzani ni wengi kuliko wa CCM, sijapata kuona hali hiyo. Kwa hiyo, ukitaka kuleta, haiwezekani, wanachama wa Chama Cha Mapinduzi ni wengi kuliko wa upinzani; na ndiyo maana hata huko mtaani wala hakuna kelele. Kwa hiyo kama kuna mtu anahamasisha na kutisha watu Wenyeviti waliochaguliwa halali kisheria na kikatiba wafanye kazi zao kama kuna mtu anawabughudhi sheria lazima ichukue mkondo wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja hapa ambayo imetolewa na Mheshimiwa Mbunge wa Tanga Mjini. Mheshimiwa Mbaruku amekuja kutoa hoja kwamba kuna Madiwani wamerudi kutoka CUF wameingia CCM na wamehudhuria vikao vya Halmashauri kule. Nimeongea na Mkurugenzi wa Jiji, Mheshimiwa Mbunge amekaa hapa wiki mbili za kamati hakuleta hoja, hakupiga simu, hakuja Wizarani, hajalalamika na hana barua yoyote ile. Hii wiki ya kwanza ya Bunge imeisha. Kwa hiyo natoa hoja ambayo Mkurugenzi wa Halmashauri wa Jiji la Tanga hawezi kufanyia kazi mambo ya mtaani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu ni kwamba, barua ilipaswa kuandikwa ya kuonesha kama kweli CUF hao madiwani wamehama. Yeye ameona watu wanasema Katibu Mkuu wa CCM ameenda kwenye mkutano, wamevutiwa na mambo yake mazuri na utekelezaji wa ilani, wakaenda kumsalimia, huenda walikuwa wanaweka booking kwamba, hivi karibuni watarudi CCM. Sasa kama CUF wanasema madiwani wamehama…

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): …wampelekee barua Mkurugenzi ili aweze kuchukua hatua hiyo. Kwa hiyo, utaratibu uliopo kama barua haijaenda wale wataenda kupata stahiki zao na huu ndio utaratibu wa kawaida…

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge kama kuna mambo yanatolewa ya mlalamiko ndiyo maana tuko hapa kwenye corridor, tunakunywa pale chai canteen tunazungumza tunawasiliana tunapeana taarifa. Ukileta hapa kama taarifa rasmi tutaku-crush kwa sababu ni taarifa ya uongo; tuwasilisne kama una taarifa za kutosha, barua iandikwe ifanyiwe kazi, haijaandikwa wakurugenzi watafanya kazi na watawatambua hao madiwani wataendelea kuwapa stahiki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, imezungumzwa hapa uchaguzi wa 2020. Niseme tu vizuri bahati nzuri nina uzoefu wa ile kambi na nina uzoefu wa hapa. Waheshimiwa Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi naomba niwaambie ukweli hawa wanaweweseka hali ni mbaya kwelikweli huko majimboni. Hali ni mbaya kwelikweli! Kwa sababu katika awamu za nchi hii, hii ndio awamu pekee kila Mbunge iwe kisirisiri, iwe chumbani kwake akisimama lazima amtaje Rais John Pombe Magufuli kwa kazi aliyoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna jimbo la uchaguzi halina mkono wa Rais Magufuli. Hakuna mkoa hauna mkono wa Waziri, hakuna maeneo hakuna jiwe ambalo limeacha kuguswa. Kwa mazingira hayo Watanzania hawakutaka upinzani walitaka kazi na …

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): ..kiongozi mwenye msimamo, kuondoa rushwa. Upele wa Tanzania umepata mkunaji na 2020 wanatoa zawadi na kura za asante kwa Rais Magufuli ili aweze kusonga mbele na kazi lazima iendelee…

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ni muhimu.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): …Kwa hiyo, wasiwasi wao ni faida kwetu kamba, mchezo umewashinda kabla ya kuingia uwanjani. Asante.

(Hapa, baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Waitara.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Namshukuru Mungu kwa uzima na nafasi. Pia namshukuru Mheshimiwa Waziri, Eng. Dkt. Leonard Chamuriho, kwa ushirikiano; Naibu Waziri mwenzangu; Makatibu Wakuu wote wawili; familia yangu; na wapiga kura wa Jimbo la Tarime Vijijini; pia namshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuniamini katika nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, shikamoo. Tumewasikia. Nimekaa hapa, tumesikiliza maoni. Nimewaamkia Waheshimiwa Wabunge, shikamoo tena Waheshimiwa Wabunge. Nawasalimia kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Kicheko/Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, hii Serikali ni Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, hii ni bajeti yake ya kwanza katika Awamu ya Sita. Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi ndiyo Wizara ambayo alikuwa anaongoza Hayati Dkt. John Pombe Magufili. Kwa hiyo, nilishtuka sana nilipoona Waheshimiwa Wabunge wanataka kupiga sarakasi kwa bajeti ya kwanza ya Mheshimiwa Mama Samia na Wizara ya Hayati Dkt. Magufuli na wengine wakataka kugaragara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaombe, hakuna sababu ya kugaragara, kazi inaendelea. Sisi wasaidizi wa Mheshimiwa Rais kwa niaba ya Serikali hii ya Awamu ya Sita tunafanya kazi hiyo. Ndiyo maana nikasema shikamooni Waheshimiwa Wabunge na tumewasikia vizuri kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Baba wa Taifa aliwahi kusema, ili Taifa liendelee mambo matatu yanahitajika; la kwanza ni watu. Sisi tupo Waheshimiwa Wabunge na ninyi na Watanzania wengine. La pili, akataka tuwe na uongozi bora. Uongozi bora wa Awamu ya Sita upo, mama Samia ameshika usukani. Pia tunatakiwa tuwe na siasa safi, ndiyo maana hata juzi wakati Mheshimiwa Rais Samia anateua Wakuu wa Mikoa, ameteua na mtu aliyekuwa Upinzani, tena alipambana naye kutaka kuwa Rais wa nchi hii; kwa hiyo, hiyo ni siasa safi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile maoni yote ya Waheshimiwa Wabunge wamezungumza hapa, mimi ni Naibu Waziri mzoefu kidogo, hii ni Wizara ya tatu; nilikuwa TAMISEMI, nikaenda Muungano, sasa nimekuja Ujenzi. Ukweli ni kwamba wakati Waheshimiwa Wabunge wanachangia hoja, mimi nilikuwa Mbunge wa Ukonga, Mbunge wa mijini. Sasa ni Mbunge wa Tarime Vijijini. Nilikuwa nawasikiliza vizuri kuanzia kwenye utosi mpaka kwenye unyayo wa mguu. Mnachokizungumza, mnataka barabara za majimbo yenu zipitike na kura zetu ziendelee kuwa salama na hasa kwenye uchaguzi ujao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, tunayo maelekezo ya chama katika maeneo hayo mahususi kabisa, tunayafanyie kazi na yote yanaungana mkono na maoni mliyoyatoa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme kwamba katika michango ya Waheshimiwa Wabunge, kuna Wabunge walijaribu kuhoji hata miradi mingine ya kimkakati. Amiri Jeshi Mkuu, Kiongozi Mkuu wa Serikali, Rais wa Nchi, ameshasema kazi iendelee na amesema ndani ya Ukumbi huu wa Bunge kwamba miradi ya kimkakati, miradi vielelezo ni lazima iendelee. Kwa hiyo, hakuna namna ya kuanza kujadili tena habari ya Daraja la Busisi, habari ya SGR, Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere na miradi mingine ya kimkakati; itaendelea. Rais ameshasema, nani tena apinge katika mazingira hayo? Kwa hiyo, hakuna mjadala mwingine wa hivyo. Sisi kazi yetu ni kutekeleza na kuhakikisha kwamba fedha ya Serikali inasimamiwa vizuri, kazi iende vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja mahususi ambazo zimezungumzwa, nataka nijibu baadhi ya maeneo. Kwa mfano, maboresho ya bandari, imezungumzwa hapa. Hata hivyo, tukumbuke Mheshimiwa Rais juzi tu ameteua Mtendaji Mkuu wa Bandari hii; haya ni maboresho. Tunajua kwamba kuna fedha zimewekezwa kule Tanga, zimewekezwa Bandari ya Mtwara, tumeweka fedha Kigoma; na mabadiliko lazima yafanyike. Mtarajie mabadiliko makubwa katika maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, kuna watu wamezungumza habari ya fidia; Mheshimiwa Kunti Majala amezungumza hapa. Juzi Kamati ya Miundombinu ilikuwa hapa, fedha zimetoka na watu wanalipwa fidia Uwanja wa Ndege wa Msalato, wanalipwa fidia Uwanja wa ring road ya hapa Dodoma, fedha zinatoka na mambo yote yanafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Musoma, tunapozungumza Mheshimiwa Mathayo anajua kabisa, fedha zimetengwa; jana na leo na kesho, watu wote watakuwa wamelipwa fidia. Mkandarasi yupo site. Tarehe 30, Desemba, 2022 Uwanja wa Ndege wa Musoma utaanza kufanya kazi. Sasa kazi hii inafanyika vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, zimezungumzwa hapa barabara. Nataka niwaombe Waheshimiwa Wabunge, kwa kweli Wizara hii inataka kufanya kazi nzuri sana. Wote hapa ni Wanasayansi; Dkt. Chamuriho ni Engineer, mimi ni Mwanasayansi hapa, tunajua barabara ni sayansi pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Kunti Majala ametaja barabara ambayo ina kilometa 20, wametengewa shilingi bilioni tano za kuanzia, anasema yeye hahusiki na fedha hiyo; lakini tunataka tujue kwamba kwa kuwa kuna Wabunge hapa kweli hawakupata mgao, haya ndiyo mambo ambayo Mheshimiwa Waziri ameshatuelekeza, tukimaliza tu bajeti hii kesho, sisi hatulali, ni kupitia maoni na mawazo ya Waheshimiwa Wabunge ili wale waliokosa kipindi hiki, bajeti ijayo uwe mjadala tofauti. Hata sisi tungefurahi sana mambo yakienda sawa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekubaliana na watendaji pia, baada ya bajeti hii kupitishwa leo, mkitupitishia fedha mkatutuma kazi, hata watendaji wenyewe huko waliko wakae mguu sawa. Haya mambo yote mliyojadili tumechukua, tumeyafanyia kazi. Sisi ni wasikivu Waheshimiwa Wabunge, ninaomba mtuelewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalize kwa kusema hivi, yako mambo ambayo sisi tunategemeana sana humu; na hii ni Serikali ya Watanzania; na barabara hizi mnazozungumza; viwanja vya ndege na maeneo mbalimbali ni vitu ambavyo na sisi pia ni wahusika. Tunataka tusaidiane katika jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe mwenyewe umezungumza, nami nimesema nitakwenda kwenye barabara yako kule Mbeya na shida ambayo unazungumza na migomo mbalimbali, Mheshimiwa Waziri ataeleza, tumewasikia vizuri sana. Nataka niwaambie tu kwamba mkipitisha fedha zinazotengwa hapa, sisi bajeti ijayo lazima tuje kuonesha zinafanya kazi zipi na utekelezaji wa miradi. Uzuri ni kwamba miradi yenyewe mtaiona huku.

Mheshimiwa Naibu Spika, mmetupa ushauri, sisi hatutalala. Mimi, Mheshimiwa Waziri, Naibu mwenzangu, watendaji wakuu na kila mtu pale alipo tutafanya kazi ya ziada sana. Tumepewa mfano hapa wakati wa mchango kwamba tuangalie mchango wa Wizara ya Maji, wamefanya kazi nzuri sana. Tumesema na Mheshimiwa Waziri kwamba kipindi kijacho, Wizara ya Ujenzi itakuwa ni Wizara ya kupigiwa mfano kwa sababu ni Wizara ambayo inashikilia uchumi wa nchi hii, inamgusa kila Mbunge, inagusa kila Mtanzania, inagusa kila mkoa, inagusa kila wilaya. Kazi yetu, Mungu ametupa uhai, Mheshimiwa Rais ametuamini; tutachapa kazi kweli kweli. Hapa kazi lazima iendelee.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kwamba Waheshimiwa Wabunge, Waheshimiwa Mawaziri na watendaji wengine wa Serikali, Watanzania wanataka tufanye kazi; na wanataka wafanye kazi ili hotuba ya Mheshimiwa Rais nzuri hapa Bungeni lazima itimie kwa vitendo huko kila mwananchi alipo.

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, baada ya kusema hayo, nawashukuru sana kwa kunisikiliza, naomba niseme naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi.


Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Wakati ukaguzi wa CAG unafanyika mpaka tarehe 30 Juni, 2020/2021 tulikuwa na Halmashauri za mamlaka 185, lakini mpaka tarehe hiyo walikuwa wameshakagua Mamlaka ya Serikali za Mitaa 42 sawa na asilimia 23. Pia walifanya ikaguzi maalum kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa 34. Kamati ya LAAC ilikutana na kuwahoji mamlaka nne, hiyo taarifa yote ambayo imezungumzwa hapa. Sambamba na hilo ni kwamba kulikuwa na shida ya muda na bajeti vile vile.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka Waheshimiwa Wabunge waone huu ukosefu wa muda na bajeti, madhara yake ni nini? Nikijaribu kuangalia, ukiacha mengine ambayo yametajwa hapa kule Ilemela, inawezekanaje watu ambao walikuwa ni watumishi, bado wanaingia kwenye mfumo wa Serikali na wanabadilisha ankara ambazo ni mabilioni kwa mabilioni kwamba hao watu kweli hawajulikani?

Mheshimiwa Naibu Spika, inawezekanaje kwamba kuna stakabdhi 822, yaani hazionekani! Halafu kuna makampuni 270 wanafanya biashara katika Halmashauri ya Ilemela halafu hawalipi kodi. Pia ukiangalia kwa mfano fedha ambazo ile asilimia 10 ambayo inapelekwa, mamlaka 155 fedha haijarejeshwa shilingi bilioni 47.01. Pia mamlaka 83 hawajapeleka fedha katika makundi yale matatu; vijana, wanawake na watu wenye ulemavu shilingi bilioni 6.8.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika ukaguzi maalum uliofanyika, katika mamlaka 37 shilingi bilioni 19.72 hazikupelekwa benki. Hawajaishia hapo, kwenye mashine za POS katika ukaguzi wa CAG yenye ukurasa 308 wanasema kuna shilingi bilioni 18 zilipotea au hazikwenda benki, hawajui ziko wapi. Pia wanatuambia, kuna vyanzo ambavyo ni muhimu hawakukusanya kodi au ushuru wenye jumla ya shilingi bilioni 14.3. Vilevile kuna maeneo ya levy haikukusanywa ambayo ni shilingi bilioni 6.03.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye afya wanatuambia, kwenye mamlaka 46 za Serikali za Mitaa, dawa zili-expire ambazo zilikuwa na gharama ya shilingi bilioni 3.49. Pia wanatuambia kwenye ukaguzi, nimefupisha tu, kwamba kuna fedha ambazo kuna madai mbalimbali ya mishahara na taasisi, amesema Mheshimiwa Waziri, lakini hapa walikuwa wanadai jumla ya shilingi bilioni 160 hazijalipwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia fedha ambazo zilipaswa kwenda Social Security Funds hazikupelekwa. Katika mamlaka 42 ni shilingi bilioni 183.09. Kuna miradi ya maendeleo ya wananchi ilicheleweshwa katika mamlaka 128 yenye jumla ya shilingi bilioni 195.65. Vilevile mamlaka 21, Shilingi bilioni 41.51 Wilaya ya Buhigwe iliachwa iliachwa. Sasa yako mengi ya kutaja.

Mheshimiwa Naibu Spika, walipanga kupeleka vitabu Million 6.3 vilienda vitabu Milioni 1.4 yenye gharama ya Bilioni 5.18. Nachosema ni kwamba ukiangalia kazi ambayo Mheshimiwa Rais Mama Samia anayofanya na kutafuta fedha katika vyanzo mbalimbali, ukasoma ripoti ya CAG yenye kurasa 308, ukaangalia upotevu wa fedha zilizopotea, jambo hili Waheshimiwa Wabunge halipaswi kunyamaziwa. Jambo hili ni lazima Mheshimiwa Rais, achukue hatua, Serikali ichukue hatua na Bunge lazima liwe na meno. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia hata taarifa yenyewe imekuja hapa tunapewa Dakika Tano, unaambiwa ingiza kwenye Hansard hili jambo tulipaswa tujadili siku tatu, kila Kamati na siku zake na tufanye maazimio na Serikali ipewe muda ije itupe majibu. Hatuwezi kuwaambia wananchi wachangie maendeleo wakati kapu limetoba, tenga haliwezi kujaa, kuna matundu kibao. Waheshimiwa Wabunge tumekutana kwenye Bunge hili kwa ajili ya Watanzania maskini, wanatusikiliza lazima tuwe sauti kwa wasiokuwa na sauti, tufanye maamuzi sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge hili lazima kabla ya Bajeti ijao Serikali ije na mpango mkakati vinginevyo ukaguzi wa CAG ni kupoteza fedha. Fedha hizi ni nyingi kwelikweli lazima zisimamiwe. Nilikuwa nasoma ripoti naangalia kule Nyamungo ambapo wananchi wangu hawana maji, hawana barabara, watoto wanakaa chini, nikajiuliza tungeweza kuchimba visima vingapi katika Halmashauri yetu? Tungenunua magreda mangapi katika hizi fedha? Tungetengeneza madawati mangapi watoto wasome? Walimu wangejengewa nyumba ngapi? Hili Waheshimiwa Wabunge ni jambo ambalo ni muhimu, lazima tuchukue hatua na Serikali hapa lazima iwajibike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa walioiba fedha washughulikiwe, tuambiwe kwanini hawapo jela? Wako wapi na wanafanya nini? Nani anawalinda, anawalinda kwa faida ya nani, kwanini wasiwajibishwe? Kama watu wameiba fedha hawajahukumiwa utamkamata nani? Haya ni mambo ya kupendeleana, Bunge msikubali kufanya hivyo, lazima tuwawajibishe watu. Serikali isilete maneno maneno hapa watu wawajibishwe, hawa ni wezi sawa na vibaka wengine mtaani, wawajibishwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaambie ripoti hii iko mtaani, ripoti hii wananchi wanasoma, wanaelewa, wanataka kuwaona Wabunge wao wa Chama Cha Mapinduzi kwa asilimia kubwa mnachukua hatua gani? Tuanze kuchukua hatua sasa kabla ya sisi kwenda kuwajibishwa na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, ahsante. (Makofi)
Hoja ya Dharura (Changamoto ya Kupanda kwa bei za Mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi. Kwanza naomba nikushukuru sana kuruhusu hoja hii ijadiliwe na Bunge, lakini naipongeza Serikali kwa hatua ambayo kupitia Mheshimiwa Waziri Mkuu kufanya kuijadili kuangalia namna ya kupunguza shida ya mafuta Tanzania.

Mheshimiwa Spika, hoja yangu wakati nimesimama hapa naomba mwongozo wako wakati ule ilikuwa ni hoja hii. Kwa hiyo, kwa kunipa nafasi ya kuchangia maana yake sintarudia tena kusimama itakuwa imekufa.

Mheshimiwa Spika, mambo yafuatayo moja ni kwamba bei imepanda ya mafuta na bei hizi kuna mjadala mkubwa sana kwenye mitandao ya kijamii inaendelea, wananchi wamepata mkanganyiko. Kama sisi kwa mfano, nchi kama Zambia ukiangalia bei ambao wanauza kule Zambia diesel kule shilingi 2,470 lakini tunajua wengi mizigo yao wanapitishia kwetu hapa, lakini sisi hapa Tanzania diesel imetangazwa bei ya EWURA ni zaidi ya shilingi 3,000.

Mheshimiwa Spika, watu wameenda mbali zaidi kuangalia mpaka Msumbiji kule Maputo bei ikoje, wamezungumza bei ya mafuta kule Zanzibar na wanajaribu pia kutugawa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni jambo ambalo Serikali lazima ichukue hatua za dharura. Kwa sababu, kwa mfano mimi natoka Tarime Vijijini kuna hoja imezungumzwa kwamba Rais wa Kenya Mheshimiwa Uhuru Kenyatta ameweka ruzuku ya Shilingi Bilioni 850 au Zaidi, lakini Wakenya wakati wa shida ya mafuta kule Kenya walipiga foleni kule Tarime mpaka hapa Kirumi kuja Musoma kuchukua mafuta. Baada ya Mheshimiwa Rais wa Kenya kuweka ruzuku kwenye mafuta yao zile foleni pale Tarime hazipo sasa, maana yake imekuwa na impact, mafuta kule Kenya yameshuka wanapata huduma ndani ya nchi yao.

Mheshimiwa Spika, kwa wale ambao wanabeza kwamba ruzuku haitasaidia kwamba siyo kweli, itasaidia sana kuondoa kero kwa wananchi, itasaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lazima tukubaliana kwamba sasa hivi kwa mfano, nadhani wiki iliyopita walitangaza kupandisha bei ya nauli kwa mabasi, sasa bei imepanda jana tutarajie kwamba kesho keshokutwa wenye mabasi watapandisha bei kwa sababu mafuta yamepanda na wanayo hoja ya kuzungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, jambo hili kwa kweli ni jambo muhimu kweli Serikali kuchukua hatua. Hatua ya kwanza ni kwamba Serikali iangalie namna ya kuongeza ruzuku ili kupunguza bei. Pili ni kupunguza zile tozo ambazo bei zinapanda duniani kote, lakini bei zipo kwenye individual countries kwa sababu ya kodi ambazo wameziweka. Kwa hiyo, sisi kama Serikali, kama nchi tukae chini tuangalie ni kitu gani kifanyike kupunguza ukali wa maisha kwa wananchi wetu na wananchi hawana namna yoyote ile wanaangalia Serikali yao ya Chama cha Mapinduzi, yenye huruma, sikivu iwaondolee uchungu wa maisha ya ukali ule ili waendelee kuishi kwa raha katika Serikali yao ambayo wanaipenda sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaunga mkono hoja tunatarajia kwa hatua ambayo Serikali imechukua jana kukaa pamoja, wasikae vikao virefu, watu wanaendelea kuumia, maneno mengi mtaani, waje na suluhu ya dharura ya kusaidia Watanzania ili maisha yaendelee.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Kigua. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali, 2017
MHE. MWITA M.WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kupata fursa ya kuchangia kwenye hoja hii ambayo imeletwa na Serikali. Nianze tu kwa kusema umeanza mtindo na naona umezoeleka na Wabunge wa


CCM. Tunapokuwa tunatoa hoja zetu kama Kambi ya Upinzani Bungeni tunatarajia aliyetoa hoja wakati wa majumuisho ndiyo azijibu hizo hoja, lakini Wabunge wa CCM muda wote wanajikita sana kupinga kile kilicholetwa hapa mezani. Wamejigeuza kuwa wasemaji wa Serikali na kwa hiyo sasa unashindwa kutenganisha mchango ambao umetolewa na Wabunge wa CCM na majibu ya Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mawaziri wanashindwa kufanya kazi yao vizuri. Tunatarajia, tunaomba Naibu Spika uongoze watu vizuri kwamba kama tumetoa hoja, tusubiri Mheshimiwa Waziri, huyu Mbunge wa CCM aliyepewa fursa kama hana neno la kusema akae kimya au akae chini na asuburi Waziri mwenye dhamana au Mwanasheria Mkuu wa Serikali…

TAARIAFA...

MHE. MWITA M.WAITARA … Mheshimiwa Naibu Spika, nakuheshimu sana na naomba niseme habari ya vyama ianze na Kiti.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waitara naomba ukae chini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi na naomba nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kupeleka fedha nyingi sana katika majimbo yetu. Kwanza anatafuta fedha, anapeleka fedha zikafanye kazi. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI amsaidie Mheshimiwa Rais kusimamia watumishi waliopo katika Serikali za Mitaa lakini pia kusimamia miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TAMISEMI ndiyo nchi, tunamtegemea sana. Ningedhani ungeshona makombati kama wale wenzake wa Kilimo ili ionekane kwamba ni mtu kazi, kwa sababu shughuli iliyopo TAMISEMI ni pevu kwelikweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano nimesoma bajeti hii sijaona mahali popote ambapo Mheshimiwa Waziri amesema kwenye bajeti hii kwamba anakwenda kukomesha shule kufungwa kwa sababu hakuna matundu ya vyoo, kwa watoto kukaa chini hakuna viti, madawati na meza, Walimu wanakaa mbali kwa sababu hakuna nyumba za kutumia watumishi wa kada za elimu na afya. Hii ni changamoto kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli wanavyozungumza kwamba shule fulani imefungwa haina choo, maana yake ni kuonesha kwamba hawa watu siyo wastaarabu na kwa kweli siyo jambo jema sana. Ni ama TAMISEMI wapeleke fedha au yaende maelekezo mahususi kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zetu watenge fedha na jambo hili likomeshwe mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekuwa msikivu. Kulikuwa na makisio ya fedha ya miradi mbalimbali ya maendeleo. Kwenye majengo yetu kuna mabweni hayajakamilika, kuna mabwalo hajayaisha, kuna shule hazijakamilika kwa sababu wali- underestimate makadirio ya matumizi ya fedha katika halmashauri zetu, lakini naona wamegundua kwamba walifanya makosa, wameleta document hapa kuonesha kwamba angalau darasa moja ni shilingi milioni 25 na matundu ya vyoo yameongezeka. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri kilichobaki hapa ni kupeleka maelekezo mahususi kwamba vile viporo vya mabweni, mabwalo, madarasa na nyumba, fedha zitengwe ili zikamilike ili wananchi waweze kutumia katika matumizi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri afanye ukaguzi maalum wa ile asilimia 40 kwa baadhi ya halmashauri na asilimia 60 ya mapato ya ndani. Miradi mingi kwenye majimbo yetu ambayo viongozi wakienda wanaoneshwa kwenda kukagua na Waziri na Naibu Mawaziri, Waziri Mkuu na Makatibu Wakuu, wanapelekwa kwenye miradi ambayo fedha imetoka TAMISEMI kutoka Serikali Kuu. Tunaomba wakague miradi ya mapato ya ndani ya asilimia 40 na asilimia 60 ambako huo ndiyo mwanya wa upigaji mkubwa sana. Fedha nyingi zimepotea, miradi haijakamilika na watu wanagoma kulipa kodi kwa sababu hawaoni tija ya fedha ambazo wanatoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, usimamizi wa miradi; nimeona kwenye andiko Mheshimiwa Waziri ameonesha kwamba zinaundwa Kamati ndogondogo za wananchi kwenye vijiji. Hapa kuna changamoto kubwa sana; zinakwenda fedha za miradi, zinaundwa Kamati za Ujenzi za Wananchi, zinaundwa Kamati z Mapokezi na Manunuzi, wanapewa vifaa kwa kuletewa, hawaendi kununua wenyewe wale wananchi. Hawana uwezo wa kuhoji, hawajui mambo ya manunuzi. Pia bahati mbaya sana katika hiyo shughuli hawana posho yoyote, kwa hiyo wanaishia kubishana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mwananchi ambaye atashinda kwenye kijiji asubuhi mpaka jioni hakuna chai wala chakula, wanagombana na Wakurugenzi, wanagombana na Walimu, wanagombana na Madaktari. Kwa hiyo miradi haikamiliki kwa sababu hakuna fedha ya usimamizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti hapa imeonesha namna ambavyo viongozi wa TAMISEMI watakwenda mikoani, mikoa itakwenda kwenye wilaya, wilaya waende kwenye kata na kata kwenye vijiji, wale wa chini wasimamizi wa kila siku hawapo, lakini kwenye bajeti hii hakuna mahali popote ambapo panaonyesha kwamba kuna posho hata kidogo kwa Wenyeviti wa Vijiji, Wenyeviti wa Mitaa, Madiwani mishahara au posho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zote hizi tirioni 9.1 zitasimamiwa na madiwani katika halmashauri. Wakurugenzi wamewapa mafunzo ya Kutosha, Wakuu wa Mikoa wamefundishwa, Ma DC wamekaa hapa Dodoma. Tunataka kuona semina kwa madiwani wetu wakijengewa uwezo ili waweze kusimamia fedha za halmashauri ili waweze kuhoji. Wanapewa fedha shilingi 40,000 wanapoteza mwelekeo kwa sababu ya mazingira hayo. Ni vizuri fedha itengwe wawezeshwe wawe na uwezo wa kusimamia na kuhoji ili miradi iweze kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia usimamizi Mikoani, Mheshimiwa Waziri ni muhimu sana ukamsaidia Mheshimiwa Rais, kama ambavyo umeangalia pia Baraza la Mawaziri, ni vizuri tukaanzia mikoani, hivi mkoa gani unaongozwa na nani kwa tija ipi. Kuna mwingine unamkuta ni mfanyabiashara unampeleka mkoa ambao ni wakulima au ni wachimbaji, haelewi. Lakini pia badala ya kushirikisha kumekuwa na order na amri mbalimbali. Katika maeneo yetu, amesema Mheshimiwa Jafar; kuna Migogoro pale Bunda ya ardhi haijatatatuliwa, kuna migogoro Rorya haijatatatuliwa, kuna migogoro Serengeti hakuna utatuzi, kuna Tarime hakuna utatuzi, Mkoa mzima ni vurugu match. Ukienda pale kwa Kurutambe na Magwe watu wanauana migogoro ya ardhi, viongozi hawaendi pale. Nenda Mnito Msege juzi wamechinjana, nenda Mnito Kibaso wameuana; hali ya utatuzi wa migogoro lazima…

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waitara kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ester Bulaya.

T A A R I F A

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa taarifa Mheshimiwa Waitara kwamba ni kweli kwa Mkoa wa Mara migogoro ya ardhi imekithiri na Bunda kuna mgogoro mkubwa pale Nyatwali watu wanalazimisha kuhama kwa fidia ndogo na wakidai wanatishwa, kwa hiyo hilo jambo lipo na ni very serious.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waitara taarifa unaipokea.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa muhimu sana kutoka kwa Ester Bulaya wa Bunda. Nilikuwa nasema kwamba hii migogoro isipo tatuliwa, Mheshimiwa Waziri anamsaidia Mheshimiwa Rais kutafuta kura za Wabunge wa CCM, Madiwani wa CCM, Wenyeviti wa CCM wa Mtaa na Madiwani wa Chama Cha Mapinduzi. Ni muhimu sana jambo hili lipewe uzito kwa sababu wale wananchi wasiposikilizwa, wakaamrishwa, wakatishwa maana yake wanaleta hasira kwetu sisi. Kwa hiyo ni muhimu sana hili jambo likafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia usimamizi wa miradi; miradi mingi kwenye halmashauri, amesema Jaffar ukienda pale Bumela fedha imeenda milioni 500 imekwisha, ujenzi umesimama waliokula fedha wapo wanakula Maisha. Ukienda pale Magoma milioni 700 imekwisha kituo cha afya hakijaisha. Nenda Genkuru nenda Nyemwaga ukaguzi huu ni mwaka wa tano, timu zimeenda tisa ya ukaguzi maalumu hakuna ripoti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na Waheshimiwa Wabunge utaratibu wa kula fedha za umma za wananchi wakawaida hao maskini ambao tunawasemea Bungeni hapa halafu tunakaa kimya si sawasawa kwa kweli hawa watu wamejitolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana, Mheshimiwa…

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ningetaka nitoe ombi kwenye Bunge hili ni muhimu sana. Baada ya bajeti hii Bunge lipate muda wa kujadili.

MWENYEKITI: Mheshimiwa, ahsante sana, unga mkono hoja, muda wako umeisha.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyeki, si nitaunga baadaye?

MWENYEKITI: Mheshimiwa maliza, muda wako umeisha.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa mapendekezo ambayo nimetoa. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2017.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, nichangie kwa muda wa dakika tano. Wabunge wa Chama cha Mapinduzi muda wote wanaposimama wanaonesha kwamba suala la muda siyo

jambo kubwa kwao, ni muhimu sana tukubaliane kwamba leo kwa mfano tumeshiriki wadau walioitwa kuja kutoa maoni, lakini wengi waliotajwa ni zile taasisi ambazo ni mahsusi na watu wengi waliokuja ni watu wa hapa Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, ungewaambia watu watoke Geita ambo wameathirika kwa muda mrefu na madini haya na madhara mbalimbali wangekuwa na maoni tofauti na wangeweza kusema hali halisi ya hisia zao kwa kadri yanavyoisha. Kwa sababu ya muda hakuweza kufika, ungewaita watu wa Tarime kule Nyamongo wangekuja hapa wangeonesha namna ambavyo wameathiriwa na uwepo wa madini kwenye maeneo yale, sasa kwa sababu ya muda pia hawakuweza kufika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Ibara ya …..

T A A R I FA...

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo hainisaidii sana, kwa hiyo naachana nayo. (Makofi)

Kwenye Ibara ya 5(1) kumekuwa na mjadala tangu jana na sheria zilizopitishwa juu ya kukabidhi madaraka haya makubwa kwa Rais. Siyo kwamba Rais haaminiki, lakini bahati nzuri Rais tuliye naye Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli matendo yake mengi ambayo anafanya yanaonesha kwamba Marais wanatofautiana sana na ndiyo maana tukasema ni muhimu jambo hili la kukabidhiwa majukumu haya makubwa likawa na upana wake likawa ni Serikali kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, haya maamuzi ya leo ya Muswada wa Mabadiliko Mbalimbali ya Sheria utaona huyu ni wa Chama cha Mapinduzi na amekuwepo Serikalini kwa muda takribani miaka 20, lakini baada tu ya kuwa Rais maamuzi ambayo anayafanya yanatofautiana sana na wenzake wote waliomtangulia. Kwa hiyo, ina maana ukiacha majukumu haya akawa nayo Rais pekee yake anaweza akaja mwingine akafanya mengine mabaya tofauti na hapa tunapofanya leo. Kwa hiyo, ukajikuta kila siku Bunge hili ni kuleta mabadiliko, mabadiliko, mabadiliko kwa sababu mtu ameamua. Napendekeza ni muhimu nguvu hizi kubwa zikapunguzwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la makinikia ambalo limezungumzwa tumesema tu ya kwamba, mlisema tuunge mkono tukasema sisi hatuna taarifa hatuna ile sheria, tumeiona baada ya kuleta Muswada huu. Unaona kuna mabadiliko ya sheria hapa, tungependa kujua wale watu ambao wameshatajwa kwamba walihusika kwenye ufisadi wa madini, akina Mheshimiwa Profesa Muhongo na wenzake, hii sheria inabadilika maana yake kuna maeneo ambayo yalikuwa na ukakasi yaliyopelekea viongozi hao wakafanya maamuzi kutumia sheria na mikataba iliyopo, sasa sheria inabadilika lakini wao wameshapakwa matope, wameshaoneshwa kwamba ni watu ambao siyo waadilifu na wenyewe nafasi yao iko wapi katika jamii hii? Hilo jambo ni muhimu sana likasemwa katika mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la asilima 16 mpaka asilimia 50 ya ushiriki wa Serikali kwa maana ya kupata share, tungependa kujua hii share ya asilimia 16 inahusu wachimbaji wadogo wazawa au wageni, utofauti wake ukoje? Je, hii asilimia ina-apply kwa watu wote wawili wazawa na wageni au kuna asilimia nyingine itatengwa au hawa wazawa wamesamehewa kwa sababu hawana mitaji, hawana teknolojia na mikopo yao huenda huwa ni midogo huenda kuweza ku- facilitate uchimbaji huu ambo unafanyika? Kwa hiyo tungependa pia tukalifahamu hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine muhimu nataka nilizungumze hapa ni fidia; kwenye maeneo ya madini kumekuwa na tatizo kubwa kwamba wananchi wa kawaida wazawa wanagundua au wanakutana na madini katika maeneo yao, lakini anakuja kufidiwa analipwa fedha kidogo na fedha inawachanganya wengine wanahama kwenda maeneo mbalimbali wanajenga nyumba na badaye anauza, lakini anapogundua amemaliza fedha zake na uchimbaji unaendelea katika eneo lake lile, mfano Mheshimiwa Profesa Kabudi amesema kule Mlimani mwananchi aliuza eneo akaiuzia Serikali ikajenga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alipomaliza fedha zake akarudi kuja pale anaona Chuo kipo, watu wananufaika akaamua kuishi kuzunguka eneo lile wakamruhusu akaishi mpaka amekufa ndiyo akawa amepotea.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mfano huo siyo mzuri sana, kwa sababu ni kuudhalilisha utu wa mwanadamu, ni kwa nini kusiwe na utaratibu wa sheria au kifungu ambacho kinaonesha kama mwananchi atakuwa na eneo lake ambalo lina dhahabu asilimia moja au ngapi ipatikane ili na yeye aendelee kufaidi madini yale mpaka mwisho wa uchimbaji wake, kwa maaana ya kizazi na kizazi. Hiyo itaondoa malalamiko na ugomvi kati ya wananchi na wawekezaji katika maeneo husika, huwezi kuwa unashinda njaa wakati kuna madini hapo na wewe huna kitu…

(Hapa kengelele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma wa Mwaka 2017
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Asubuhi wakati unamalizia kipindi cha asubuhi, uliwapongeza Waheshimiwa Wabunge kwa kuchangia vizuri na ukasema katika utungaji wa sheria ni jambo muhimu sana, ni muhimu watu wakajielekeza kwenye hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kujielekeza huko kwenye hoja, ni pale ambapo mimi kama Mbunge nasema yangu. Tukianza kusema Mbunge wa upande huu ametoa hoja wewe unamjibu kama Serikali, kwa kweli hatuendi mbele. Nadhani hilo ni jambo la msingi sana kuzingatia. Tuache Serikali iwajibu hoja ambazo wamepewa ili watusaidie twende mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hii sheria, kimsingi huko mtaani na wananchi wetu na hasa watu ambao wanafanya shughuli za kimikataba wanatarajia kwamba sheria hii inapopitishwa leo wapate ahueni ya kupata tiba ya malalamiko mengi ambayo wanayo mtaani kule. Kuna watu ambao wanafanya kazi migodini, wameachishwa kazi, hawana ajira wamekuwa blacklisted maeneo mengi wanataka hii suluhu wapate wafao yao waanze maisha mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu ambao wameajiriwa wakamaliza mkataba wao, fedha zao wamezuiliwa, wanaambiwa ni baada ya miaka 55, wanatarajia tupate majibu hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naona ni jambo ambalo ni muhimu sana na ndiyo maana Wabunge wakaomba hii sheria ilipaswa ipewe siku mbili mpaka tatu kujadiliwa kwa sababu tunajadili maisha ya watu wetu katika Taifa hili. Hapa ndiyo mahali pekee tunaweza kuwasaidia. Sasa nitashangaa tunaanza kulumbana kwa vitu ambavyo havina maana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 27(b) kama wenzangu walivyozungumza kwamba inatajwa kutakuwa na kulipa mafao ya jumla, lakini hapa ambacho tungeomba, tungetaka formula ambayo itatumika kutengeneza fedha hizi ijulikane kwenye sheria. Tunataka hii iingizwe kwenye sheria tufahamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mtindo wa kumwambia Waziri atakaa peke yake, atengeneze sheria, halafu atatoa kiasi gani kwa kweli ni kama tunawaambia watu kwamba huo utaratibu watapata fedha lakini hawajui kiasi gani na hakuna namna ambayo tutarudi kuja kujadili tena hapa. Kwa hiyo hili jambo lingewekwa kwenye sheria na formula hapa tuzi-testify kwamba kama mtu anapewa milioni kumi, formula hiyo inampa outlet shilingi ngapi, ijulikane hapa! Lakini hili jambo kulificha kwenye kanuni kule, Waziri aende akakae na wenzake atengeneze halafu alete, sisi Wabunge hatutamhoji, hatutaiona ataweka kwenye gazette, wananchi wetu hawataona, wataendelea kupiga kelele na kulalamika mtaani bila majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, jambo hili kwakweli ni kubwa kwelikweli lilipaswa liwekwe wazi kila Mtanzania ajue na Wabunge wajue, tupitishe kitu ambacho tunakijua kwamba hii formula, inawezekana. Kama inashindikana, wataalam wa hesabu tupo hapa, tulete, tusaidiane, tuitoe hadharani ijulikane ili watu wapate majibu, hakuna sababu ya kuficha formula hii ya kupata fedha ya Watanzania wetu ambazo kimsingi ni jasho lao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, niliona kwenye Bodi pale ambayo wameweka kwenye schedule namba moja, provisions relation rating to the Board. Hapa kuna mambo yafuatayo; moja, wametaja Wajumbe wote, sikuona kama watazingatia gender balance katika eneo hili. Wametaja nafasi, lakini kwa sababu kwa namna ya kuboresha kwamba angalau jinsia nyingine ishirikishwe, kwa kulazimisha ilitakiwa itajwe kwamba katika Bodi itakapokuwa ina-appoint hawa wahusika, watazingatia gender. Hilo jambo sikuliona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, wamesema kutakuwa na uwakilishi wa taasisi ambazo zina ajira kubwa, most employee organizations. Hapa unapozungumzia ajira katika nchi hii, kuna watu ambao wana mahitaji maalum, sikuona uwakilishi wao katika eneo hili kwamba angalau wale wenye mahitaji maalum na wenyewe angalau mtu mmoja ambaye atawawakilisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana wasipokuwepo hapa, madai yao mbalimbali hayatazungumzwa. Watazungumza mtu kama mimi ambaye sina mahitaji maalum, nina viungo kamili, sina ulemavu wowote. Hawa watu wanahitaji wapate mtu hapa wa kuwasemea kwenye Bodi hii kwa kuzingatia mahitaji yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, hii sheria ambayo inayojadiliwa leo kwamba inapitishwa, ndiyo sheria ambayo kila Mbunge, message ambazo mnatumiwa kwamba watu wanalalamika mtaani hawana haja, wanataka fedha zao; wale watu wanauliza, kwa nini mimi nifanye kazi, nimemaliza miaka sita au kumi, unaniambia nisubiri miaka 55, nina watoto ninasomesha; na mwingine ni mgonjwa, angefanya biashara aanze maisha yake mengine. Kwa nini unamlazimisha? Yaani kazi ya ajira imekuwa tena ni utumwa kwake, analazimishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, jambo hili nadhani Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla na Wabunge wa Bunge hili Tukufu ni muhimu tujielekeze tukitoka humu ndani, wananchi wanaolalamikia fedha zao ambazo wamefanyia kazi tusiwalazimishe matumizi yao. Tuwa-guide lakini tutoe tiba ya jumla katika jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anajua, mara nyingi tumekwambia sana watu wanalalamika mtaani, tupate majibu! Kwa mtindo ambao nauona huu ambapo watu wanajigeuza kuwa upande wa Serikali, kazi ya Bunge tunatunga sheria, sisi tunaishauri Serikali, tunaiwajibisha. Humu ndani tumejigeuza, tumejipa vyeo, Mawaziri, Kamati, tunazungumza hapa. Ndiyo picha inayoonekana hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani mimi Mbunge hakuna tofauti na Waziri, wala hakuna habari ya chama hapa. Hapa ni kwamba sisi Wabunge tuisimamie Serikali, wananchi wetu wanalalamika, sheria hii inawaumiza, wanataka fedha zao wajenge nyumba, wakopeshwe, watibiwe na wasomeshe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishie hapa.
Ahsanteni sana.