Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Bernadeta Kasabago Mushashu (13 total)

MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka nenda, miaka rudi tofauti na kada nyingine za watumishi, kero imekuwa madeni ya walimu, madeni ya walimu. Leo hii mnatuambia kwamba madeni ya walimu yamefikia takribani shilingi bilioni 34 plus. Walimu hawa wanaidai Serikali wengine kama matibabu, likizo, kwa miaka zaidi ya mmoja hadi miwili. Walimu waliopandishwa mishahara miezi 12 iliyopita hadi leo hawajalipwa huo mshahara wanausikia harufu tu. Walimu wengine wamestaafu zaidi ya miezi sita hawajapata mafao yao.
Ningependa kujua kwa kuwa sasa hivi Serikali mnasema mmeshahakiki ni lini, na mnipe tarehe na mwezi hawa walimu watakuwa wamelipwa haya madeni kwa sababu wamechoka kila siku madeni ya walimu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna walimu waliosimamia mitihani mwaka 2015. Leo hii tunazungumza mwaka 2017, kwa nini hadi leo hawajalipwa na ni lini Serikali itakuwa imewalipa hiyo stahili yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema awali, kwanza tuweke kumbukumbu vizuri. Katika kada ambayo Serikali katika njia moja ua nyingine imekuwa ikishiriki vizuri sana katika ulipaji wa madeni ni kada ya walimu. Ukiangalia miaka mitatu mfululizo, trend ya malipo ya madeni ya walimu ambayo tulikuwa tumezungumza hapa katika Bunge kila wakati, kwa kweli Serikali inajitahidi sana. Na ndio maana katika kipindi cha sasa hata ukiangalia katika mwezi wa 11 uliopita huu kuna baadhi ya madeni ya walimu especially katika baadhi ya Wilaya, Halmashauri, kwa mfano kuna Temeke na Halmashauri zingine kulikuwa na outstanding deni karibuni ya shilingi bilioni moja nayo ililipwa vilevile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio maana katika ulipaji wa madeni mapya mengine; ndio maana Serikali ilikuwa inafanya zoezi zima la uhakiki. Na bahati nzuri, ofisi yetu ya TAMISEMI pamoja na Ofisi ya Hazina ndio ilishiriki, na jambo hili sasa hivi limekamilika. Na ndio maana nimesema hapa siwezi kutoa deadline ni lini, deni hilo litalipwa lakini kwa sababu mchakato wa uhakika umekamilika, hili deni la shilingi bilioni 26 ninaamini sasa hazina si muda mrefu mchakato wa malipo utaanza kuanza.
Naomba Mheshimiwa Mbunge, najua uko makini katika hili lakini amini Serikali yako kwa vile zoezi la uhakiki ambalo lilikuwa ni changamoto limekamilika basi walimu hawa si muda mrefu wataweza kulipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala zima la deni la kusimamia mitihani na ndio maana nilisema deni hili lilikuwa ni miongoni mwa madeni haya ambayo yaliyohakikiwa ambayo takribani ilikuwa ni shilingi bilioni sita.
Naomba tuondoe hofu walimu wangu katika mchakato wa sasa walimu hawa wote wataendelea kulipwa ili mradi kila mtu haki yake iweze kulipwa, na Serikali haitosita kuhakikisha inawahudumia vyema walimu wake kwa sababu italeta tija kubwa sana katika sekta ya elimu.
MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na mikakati mizuri na mingi ya Serikali, lakini bei ya kahawa ya mkulima Mkoani Kagera bado ni Sh.1,000 kitu ambacho kinamuumiza mkulima. Kwa kuwa soko la kahawa linategemea soko la dunia, linategemea mauzo nje ya nchi, mahali ambapo mkulima wa kawaida au Vyama vyetu vya Ushirika hivi vya Msingi hawana uwezo wa kuyafikia hayo masoko. Pia kwa kuwa msimu unaofuata wa kahawa unaanza hivi keshokutwa mwezi wa Tano, ili makosa yasijirudie mkulima akaendelea kulipwa 1,000, je, Taasisi za Serikali ambazo zinahusika na utafutaji wa masoko wana mipango gani ya kwenda kule nje ya nchi wakawatafutia Watanzania masoko ikiwezekana wakaingia na mikataba na nchi hizo ili Watanzania wauze kahawa zao na waweze kupata bei nzuri? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwenye baadhi ya super market huko China imeonekana kahawa ambayo inaonekana imetoka Uganda imekaangwa tu haijasindikwa zaidi ya hapo na ikawekwa kwenye kifungashio kizuri, robo kilo inauzwa kwa dola 40 ambayo ni zaidi ya Tanzanian Shillings 88,000 wakati sisi mkulima anapata 1,000 kwa kilo. Je, Wizara zinazohusika kama Wizara ya Kilimo, Wizara ya Viwanda na Biashara, wanawaandaaje Watanzania kwa maana ya wakulima na wafanya biashara wasindike kahawa badala tu ya wakulima kuuza zile zilizo ghafi kusudi Mtanzania aweze kupata bei nzuri na hasa hasa mkulima kutoka Mkoa wa Kagera?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata nafasi hii. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mushashu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza anataka kujua mikakati iliyopo kwa ajili ya kuongeza bei ya mkulima kutoka Sh.1,000 wanayolipwa sasa mpaka ile ambayo itaridhisha na kukidhi gharama za uzalishaji. Kwanza kwa niaba ya Serikali, Wizara ya Kilimo, baada ya kuona changamoto hiyo ya zao la kahawa, bei yake na mazao mengine, tumeanzisha Kitengo cha Utafiti wa Biashara na Masoko ambacho kimeanza kazi tangu tarehe Mosi Julai, 2018. Lengo la kitengo hiki ni kuratibu na kufuatilia mwenendo wa masoko duniani na kutoa taarifa sahihi kwa wakulima wetu wakishirikiana na wenzetu wa Wizara ya Viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa pili tunashirikiana kwa karibu sana na Balozi zetu zilizokuwa nje. Hapa nichukue nafasi kumpongeza sana Balozi wetu wa China, Ndugu Kairuki kwa kazi kubwa anayoifanya na ameweza kutupatia soko jipya la kahawa nchini China lakini pia na Mabalozi wa nchi nyingine kama za Japan, Ujerumani, wote hawa wamekuja na mikakati mizuri na kupanua soko la kahawa yetu inayotoka hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili anataka kujua kwamba mikakati ya kuongeza thamani ya mazao yetu ikiwemo kahawa ili kahawa hii badala ya kuuzwa ghafi tuweze kuiuza wakati imechakatwa. Kwanza niendelee kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa muono huu, lakini nataka nimwambie kwamba Serikali tulishaanza muda mrefu mipango hii na ndiyo maana siyo kwa zao tu la kahawa, hata korosho umeona mwaka huu tumeanza kubangua na mwakani Insha Allah tutabangua zaidi ya asilimia 50 kwenda juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali lake la msingi la kahawa; pia tulishaanza kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vyetu na kiwanda kimojawapo cha Amir Hamza kimeshaanza kuchakata kahawa ya Mkoani Kagera kwa ajili ya kuiuza kahawa iliyokuwa imeshachakatwa badala ya kuuza kahawa ghafi. Pia kwa wakulima hawa tunaendelea kuwasisitiza wajiunge kwenye vikundi vyao vya ushirika ili Serikali tuweze kuwasaidia kwa ukaribu kwenye umoja wao kuongeza mitaji na kununua mashine ndogo ndogo za kuchakata mazao yao, kuuza mazao ya kahawa iliyosagwa badala ya kuuza kahawa ghafi.
MHE. BERNADETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Bukoba Sekondari ina umri wa miaka 80, Rugambwa Sekondari ina umri wa miaka 55 lakini pamoja na uzee shule zote zilipitiwa na tetemeko na Bukoba Sekondari ikaja vilevile ikaezuliwa na kimbunga. Kwa niaba ya Mkoa wa Kagera na wanafunzi wanaosoma katika shule hizo, naipongeza sana Serikali kwa kutoa Sh.1,481,000,000 kwa ajili ya kukarabati Bukoba Sekondari na kuahidi kukarabati Rugambwa mwaka huu kuanzia mwezi huu wa Aprili. Kwa kuwa Rugambwa wakati wa tetemeko nyumba za walimu na zenyewe zilianguka na nyingine zikaathirika sana, hadi leo Mkuu wa Shule hana mahali pa kuishi, je, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea nyumba za kuishi walimu wa Shule ya Sekondari Rugambwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, shule zote mbili, Bukoba Sekondari na Rugambwa zinahitaji kumbi za mikutano. Bukoba Sekondari haina ukumbi kabisa, Rugambwa ukumbi wake ni mdogo sana unachukua watoto 300 wakati wako wanafunzi karibu 700/800. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea kumbi za mikutano ili wanafunzi wapate mahali pa kufanyia mitihani na kufanyia mikutano?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kwa dhati kabisa na kwa furaha kubwa nipokee shukrani na pongezi za Mheshimiwa Mbunge kwa kazi ambayo Serikali imefanya katika shule zake. Lazima niseme kwamba Mheshimiwa Mushashu ni moja kati ya Wabunge makini sana katika Sekta ya Elimu na tumeendelea kufarijika na uzoefu wake mkubwa kama Mwalimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maswali yake, kwanza kuhusiana na nyumba za Walimu katika Shule ya Rugambwa, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunavyozungumza tayari Serikali inafikiria kujenga nyumba nane za Walimu katika shule ya Rugambwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na kumbi za mikutano katika shule zote mbili, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia ikiwa ni pamoja na miundombinu katika shule zake kadiri uwezo wa fedha utakavyoruhusu.
MHE. BERNADETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mto wa Kanoni kwa sasa umejaa sana mchanga na kina kimepungua sana, kwa watu wenyewe itakuwa si kazi rahisi kuondoa mchanga na zitahitajika fedha nyingi sana; pamoja na hatua zilizoainishwa kwenye jibu la swali ambazo ni za muda mrefu:-

Je, ni kwa nini Serikali isiwasaidie sasa hawa watu wanaohangaika na mafuriko kila mwaka kwa kutoa fedha kiasi za kuanza kusafisha mto huu angalau mara moja kwa mwaka?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Spika, awali yote napenda kumshukuru Mheshimiwa Benadetha kwa kufuatilia kwa kina suala hili na kutupatia taarifa za kina kuhusu changamoto hii.

Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikiashia Mheshimiwa kuwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi ni sikivu na inajali wananchi wake. Hivyo, Serikali inalichukulia kwa uzito suala hili na tunawasiliana na mamlaka husika ikiwemo Halmashauri ya Bukoba Mjini kuona namna bora na ya kudumu ya kutatua changamoto ya kujaa mchanga katika Mto Kanoni ili kuondoa kero ya mafuriko ya mara kwa mara.
MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, ninayo maswali mawili.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Kagera ni mkoa mkubwa, una watu zaidi ya 3,000,000 lakini hadi leo hauna Chuo kikuu hata kimoja. Vipo vyuo vikuu vilikuwa vimeanzishwa na Mashirika ya Dini, moja ni Lutheran, walianzisha kile cha Joshua Kibira; Roman Catholic walianzisha branch ya Saint Augustine lakini vyote Serikali ilivifunga: Kwa kuwa Serikali inasema kuanzisha Vyuo Vikuu ni gharama, badala ya Serikali kuvifunga, haioni ingekuwa ni vizuri wakaendelea kuvijenga, kuvipa miongozo na kuviwezesha hivi vilivyoanzishwa badala ya kuvifunga? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; miaka ya nyuma huko Mkoa wa Kagera ulikuwa unawika kwenye elimu, uko katika the best three, lakini sasa hivi haiko hivyo: Je, Serikali haioni kwamba sasa wakati umefika, angalau waanzishe tawi moja la Chuo Kikuu cha Serikali kama Sokoine, kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mkoa wa Kagera ili kuchochea maendeleo ya Mkoa huo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Benardetha Mushashu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Kagera tulikuwa na vyuo vikuu binafsi viwil,i hivyo alivyovizungumza Mheshimiwa Mushashu; hicho cha Kadinali Rugambwa na kile cha Kibira alichokizungumza. Nikuthibitishie mbele ya Bunge lako Tukufu, Chuo hiki cha Kadinali Rugambwa hakikufungwa, badala yake walihamisha usajili kutoka ule wa TCU kwenda ule wa NACTE. Kwa hiyo, chuo hiki kipo, kinaendelea kutoa huduma pale, ingawa hazitoi zile kozi za degree, badala yake zinatoa zile kozi za kawaida, za chini, lakini bado kinaendelea kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, kwenye hiki chuo cha pili cha Kibira, wenyewe wamiliki wa chuo hiki waliomba kifungwe kutokana na kushindwa wao wenyewe kuendesha chuo hiki. Kwa hiyo, nimshawishi tu Mheshimiwa Mbunge aweze kuwasiliana na wamiliki wa chuo hiki waweze kujipanga vizuri ili sasa waje kufanya maombi upya kama upo uhitaji wa kukifungua chuo hiki kama wataona inafaa, nasi tuko tayari kupokea maombi yao.

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la pili la vyuo vyetu hivi vikuu kuanzisha matawi kwenye eno hilo, ni suala ambalo linakubalika, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, lakini inatakiwa sasa ifanyike ile needs assessment kwa vyuo hivi vyenyewe kwa sababu wana mamlaka ya kufanya hivyo kama wanaona uhitaji huo wa kuanzisha branch hizo uko katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutawafikishia ujumbe huu waweze kuja Kagera wafanye market analysis pamoja na needs assessment ili kuona kweli kama upo uhitaji wa kuanzisha branch kwenye maeneo hayo, waweze kufanya hivyo. Ahsante. (Makofi)
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza. Ufungaji wa Benki ya Wakulima ya Kagera iliyopo pale Manispaa ya Bukoba, iliwaumiza watu wengi ambao hawakuwa na hatia wakiwepo vikundi vya akinamama, SACCOS za akinamama, wakulima, wajasiriamali na hata wale wastaafu waliokuwa wameweka akiba zao. Serikali iliwalipa Sh.1,500,000/= pekee hata kama mtu alikuwa na akiba ya shilingi milioni 40. Sasa hivi anatuambia kwamba Serikali imekuwa ikikusanya madeni, pamoja na kuuza mali za Benki hiyo tangu mwaka 2018. Je, ni lini sasa Serikali itakamilisha hilo zoezi la kuwalipa hiyo Sh.1,500,000/= pamoja na akiba zote walizokuwa wameweka kwenye hiyo benki? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa nini Serikali isione umuhimu sasa badala ya kuzifunga, ikaziunganisha hizi Benki ndogo ndogo, kama ilivyofanya ikaunganisha Benki ya Wanawake, Benki ya Posta, Benki ya Twiga, TIB wakatengeneza Tanzania Commercial Bank kwa hiyo, mtaji ukawa umeongezeka kuliko kungoja sasa hizi Benki wakazifilisi na wakawaumiza wananchi ambao wanakuwa wameweka akiba zao kwenye hizo Benki? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kasabago Mushashu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kujibu awali ya yote napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Mushashu, kwa juhudi yake ya kuwatetea wananchi hao ambao walipata hasara hiyo katika benki iliyohusika, pamoja na Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini ndugu yangu Byabato, kwa kuwa wanafuatilia kwa karibu suala hili lililojitokeza katika Benki hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi la ulipaji wa fidia ya amana linaendelea mpaka hivi sasa tunavyozungumza. Wale wote ambao hawajajitokeza kwenda kuchukua amana hiyo, basi tunamwomba Mheshimiwa Mbunge, awashajihishe watu hao waende kupata fidia hiyo isiyozidi Sh.1,500,000/=. Wale ambao amana yao ni zaidi ya Sh.1,500,000/= waendelee kuwa na subira, mpaka zoezi la ufilisi wa benki hiyo utakapokamilika na watalipwa kwa mujibu wa taratibu za ufilisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili. Serikali tayari imeshaanza zoezi kwa upande wake kuziunganisha Benki, ambazo zilipata changamoto mbalimbali zikiwemo mitaji. Tayari Serikali yetu imeshaziunganisha Benki ya Posta, Benki ya Wanawake, Benki ya TWIGA na Benki ya TIB na kuunda Benki inayojulikana kwa jina la Benki ya Biashara Tanzania (TCB). Ahsante sana.
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Taarifa za Polisi na mambo tunayoyaona kila siku kwenye jamii yanaonesha kwamba ukatili wa kijinsia unaendelea kuongezeka; je, nini sababu ya ongezeko hilo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imeweka mikakati mingi ya kudhibiti ukatili wa kijinsia ikiwemo Mabaraza ya Watoto, Madawati ya Jinsia, Kamati za Ulinzi, nani anaratibu afua hizi zote? Kwa nini basi tunapata taarifa tu kutoka kwenye Dawati la Polisi, lakini kwenye hizi afua mlizoweka hatupati taarifa zake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bernadeta, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli taarifa za Jeshi la Polisi zinaonesha kwamba ukatili umeongezeka. Sababu ya kuongezeka vitendo vya ukatili ni mmomonyoko wa maadili wa malezi na makuzi kwa Watoto; wazazi na walezi kutowajibika kumlinda mtoto; matumizi mabaya ya kieletroniki, na pia kuiga maadili ambayo siyo utamaduni wa Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wanapokuwa katika majukwaa yao kutoa elimu hii ya kutokomeza ukatili wa jinsia kwa wananchi wao. Vilevile tunaambiwa mtoto wa mwenzio ni wako, kwa hivyo tuwajibike sote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Swali lake la pili, afua zote zinatekelezwa na Wizara tukishirikiana na wadau mbalimbali hasa Jeshi la Polisi ambalo lina mamlaka ya kutoa taarifa zote za ukatili wa kijinsia katika nchi yetu, ahsante. (Makofi)
MHE. BERNADETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza. Hadi sasa maeneo mengi katika Mkoa wa Kagera ambayo yamesambaziwa umeme wa REA umeme umefika tu kwenye ngazi ya vijiji haukuteremka chini. Swali la kwanza, je, ni lini sasa madi wa ujazilizi densification itaweza kuanza Mkoani Kagera ili vijiji vyote sasa na maeneo yote yaliyorukwa na vitongoji yaweze kupatiwa umeme?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; katika Mkoa wa Kagera kwenye Manispaa ya Bukoba tunazo Kata kama Kahororo, Buhembe, Nshambya, Nyanga, Kagondo, Kibeta, Kitendaguro na Ijuganyondo ambavyo pamoja na kwamba kata hizo ziko kwenye Manispaa ya Bukoba lakini zimekaa kama vijiji. Je, ni lini sasa Serikali itaanzisha mradi wa Peri- Urban ili sasa vijiji hivi au mitaa hii inayofanana na vijiji iweze kupata umeme wa REA kwa bei nafuu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bernadeta Kasasabago Mushashu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kwenye awamu ya kwanza upelekaji wa umeme vijijini tumefika hasa kwenye centres za yale maeneo na ni kwa sababu ya fedha iliyokuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, REA III round II peke yake ina shilingi trilioni moja na bilioni mia mbili na hamsini kwa ajili ya kufikisha umeme kwenye vile vijiji vyote ambavyo havikuwa na umeme. Azma na nia ya Serikali ni kuhakikisha kila mtu anapata umeme kwenye eneo lake na tayari nia hiyo imeanza. Tayari uko mradi wa ujazilizi tunaita Densification One ambao unaendelea katika baadhi ya maeneo yetu, lakini tumemaliza tayari upembuzi na kupata wakandarasi, tunaamini kufikia Julai densification 2(b) itaanza, lakini kufikia kwenye Oktoba densification 2(c) itaanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado hii haitaweza kumaliza kwa sababu katika hizi densification tuna vitongoji karibu 5,000 na zaidi kidogo. Mnakumbuka hapa tayari Bungeni Mheshimiwa Waziri amesema kwamba tunatafuta mkakati mkubwa wa kuweza kupata fedha nyingi karibia trilioni sita kwa ajili ya kupeleka sasa umeme kwenye vitongoji vyote vilivyobaki nchini ambavyo havina umeme. Kwa hiyo kadri pesa inavyopatikana vitongoji vitazidi kupelekewa umeme kwa kadri Serikali inavyozidi kujipanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la pili la Peri- Urban, nimshukuru Mheshimiwa Bernadetha kwa kuulizia kuhusu Jimbo la Bukoba Mjini, makofi yalikuwa mengi, swali sikulisikia vizuri, lakini naamini alichokizungumzia ni peri-urban na tayari Serikali imeshatangaza na imefikia hatua za mwisho za kupata wakandarasi wa kupeleka umeme katika maeneo ya mijini lakini yenye uso wa vijiji kama alivyozitaja hizo kata saba za Jimbo la Bukoba Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna mikoa mingine kama tisa katika awamu hii ya peri-urban nayo kufikia Julai tunaamini mradi huu utaanza kwa ajili ya kufikisha umeme katika maeneo haya kwa ajili ya kupata umeme kwa gharama nafuu.
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Mkoani Kagera kilimo cha vanila kilianza kwenye miaka ya tisini lakini hadi leo hakuna mfumo unaoeleweka wa kilimo cha vanila nchini. Je, ni lini Serikali sasa italeta mwongozo juu ya namna ya kulima, wakatoa huduma za ugani na wakaelekeza juu ya masoko?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa huko ulimwenguni katika nchi nyingine kilo ya vanilla inanunuliwa kati ya 800,000 mpaka 1,000,000 wakati mkulima wa Kagera anauza vanilla kwa 20,000, 15,000 mpaka 30,000 tu. Je, ni lini sasa Serikali kwa kutumia balozi zetu za nje wataweza kututafutia masoko yanayoeleweka ili kuweza kumnufaisha huyu mkulima kupata bei nzuri ya vanilla?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Benardeta Kasabago Mushashu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, wiki mbili zilizopita Wizara ya Kilimo pamoja na wadau wa zao la vanilla tulikutana tukafanya mkutano wa pamoja hapa Dodoma kwa lengo la kuandaa na kutengeneza mwongozo.

Mheshimiwa Spika, nilihakikishie Bunge lako kwamba tuko katika hatua za kuanza kuandaa mwongozo huo ambao utajumuisha masuala ya utafiti, kalenda ya mazao, mfumo wa bei, masoko na uzalishaji bora wa vanilla ambao unakidhi mahitaji ya soko la dunia, hasa ile ambayo ina vanillin na moisture content ambayo inahitajika kimataifa.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu masoko; baada ya mkutano huo wa wadau, sisi kama Wizara ya Kilimo tumeshawaandikia Ubalozi wa Tanzania Nchini China ikiwa ni moja ya sehemu ya masoko makubwa ya vanilla kuanza mazungumzo na ufunguzi wa soko hilo na tutafanya katika maeneo mengine ili kumsaidia mkulima wa vanilla aweze kupata soko la uhakika.
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza. Bukoba Government Referral Hospital haijafikia hadhi ya kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera. Hata Mheshimiwa Waziri wa Afya alisimama hapa na yeye mwenyewe akakiri kwamba ile hospitali bado haijafikia ile hadhi, na mkatuahidi kwamba mtatuletea fedha kusudi tuweze kujenga hospitali nyingine au kukarabati ile ifikie hadhi hiyo: Je, ni lini Serikali italeta fedha za kutosha kuweza kutuhakikishia kwamba wanatujengea hospitali yenye hadhi ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Mkoa wa Kagera uko mpakani na unapakana na nchi kadhaa. Kwa hiyo, yakitokea magonjwa ya mlipuko ni rahisi kuingia Mkoa wa Kagera kwa sababu magonjwa hayana mipaka. Kwa kuwa juzi juzi uliingia mgonjwa mbaya sana wa Marburg na mkaona Wizara na Mkoa walivyokuwa wanahangaika kutafuta mahali pa kuweka wale watu waliokuwa wamechangamana na wagonjwa, kwa sababu hakuna isolation centers ikabidi wawaweke mpaka kwenye mahoteli na hayo mahoteli yakafungwa yakawa hayatoi huduma kwa wakati huo: Je, ni lini sasa Serikali itaujengea Mkoa wa Kagera Isolation center? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ufatiliaje wake makini wa masuala ya afya ya Mkoa wake wa Kagera. Pia nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea, hata mwaka huu inatarajia kupeleka zaidi ya shilingi bilioni nne kwa ajili ya kuendelea kuboresha hospitali yao ya Mkoa. Vile vile nimhakikishie kwamba hospitali ya Mkoa wa Kagera ni sawa na Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, level yake ni moja, lakini tutaendelea kuwaongezea wataalam na vitu vingine ambavyo vimepungua kwenye hospitali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, Mheshimiwa Mushashu anazungumzia suala la ugonjwa wa Marburg. Nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tumeshapata heka 90 ndani ya Mkoa wa Kagera kwa ajili ya kujenga hiyo isolation center. Wakati huo tunapojenga isolation center tunahitaji tafakuri ya kina, kwa sababu ninyi Wabunge wa Mkoa wa Kagera mnajua kuna mwenzetu, Dkt. Mahona Ndulu wakati akihudumia wagonjwa wa Marburg alipata matatizo ya figo na moyo ambapo ilihitaji awepo kwenye sehemu ambazo hizo huduma zitakuwepo. Wakati tunatafakari hayo, tutaendelea kuona namna gani tutaitumia hiyo sehemu ya heka 90.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Wabunge wa Mkoa wa Kagera kwa nia yao ya kwenda kumpongeza daktari huyo.
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa duniani kwa sasa, watu zaidi ya 28 wanakufa kila sekunde kwa sababu ya magonjwa yasiyoambukiza na kwa sababu Tanzania kwa sasa kisababishi kikubwa cha vifo Tanzania ni magonjwa yasiyoambukiza. Kwa nini Serikali isitoe fedha za kutosha ili wananchi waweze kupata elimu, wajue visababishi, wajue na namna ya kujikinga kwa sababu haya magonjwa yanaweza kuzuilika?

Mheshimiwa Naibu Spika, tumbaku ni zao la biashara ndani ya Tanzania, lakini tumbaku hiyo hiyo ni kisababishi kikubwa kinacholeta magonjwa yasiyoambukiza kama kansa, stroke, presha na kisukari. Je, ni lini Serikali itawawezesha wakulima wa tumbaku nchini ikawapa mazao mbadala, wakawatafutia na masoko ili kusudi waondokane na hiki kilimo ambacho kinaathiri afya zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kuja na swali hili zuri ambalo ni eneo kwa kweli ambalo Mheshimiwa Waziri wa Afya ameliwekea msisitizo wa nguvu sana kwa sababu ndiyo tatizo kubwa kwa sasa kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza; kwanza Serikali imeweka fedha nyingi kwa sababu ukiona kwenye miundombinu, lakini ukiona manunuzi ya CT scan na mambo mengine, lakini Wabunge wamemwona Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan hapa karibuni alisaini mikataba na Wakuu wa Mikoa kwenye eneo hili la lishe. Pia wameona viongozi mbalimbali wakishiriki katika matamasha makubwa. Kwa hiyo fedha tulizotaja hapa ni fedha tu kwa ajili ya hamasa, lakini hatujazungumzia kwa ujumla dawa na sehemu zingine mtambuka ambazo fedha zimewekezwa kwa ajili ya eneo hilo. Kwa hiyo kuna fedha za kutosha na tutaendelea kuona ni namna gani tutasisitiza eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu tumbaku; kupanga ni kuchagua, ni ukweli kabisa kama ambavyo Mbunge anasema tumbaku ina madhara mengi, siyo tumbaku tu pekeyake pamoja na kelele zinazopigwa mitaani pamoja na mambo mengine mengi ambayo tunayatumia. Sasa Mheshimiwa Mbunge pamoja na ukweli huu wa kwamba tunahitaji kutafuta zao mbadala wa tumbaku, naomba nisiseme lolote hapa kwa sababu linahusu Wizara zote na taratibu zetu na maslahi ya wananchi, tutashirikiana na Wizara husika na tuone ni namna gani tunaweza kufanya, lakini kweli kuna tatizo hili na siyo tumbaku peke yake kuna mambo mengi yanayosababisha tatizo hilo. (Makofi)
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mkoa wa Kagera una maambukizi makubwa ya Malaria, ni namba tatu kwa maambukizi makubwa Kitaifa na kwa kuwa Wilaya ya Ngara ndiyo inayoongoza katika maambukizi ya Malaria Mkoani Kagera. Je, ni lini sasa Serikali itatusaidia kufanya unyunyiziaji wa viuatilifu (Indoor Residual Spraying) katika Wilaya ya Ngara ili kupunguza maambukizi ya Malaria?

Swali la pili, kwa kuwa zipo nchi duniani ambazo tayari zimeshatokomeza kabisa Malaria. Je, ni lini Tanzania tumelenga ni mwaka gani tutakuwa tumefikia zero Malaria, kwa maana ya kutokomeza kabisa Malaria? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ni kuhusu Mkoa wa Kagera. Ni kweli kwamba Mkoa wa Kagera ni Mkoa wa tatu una asilimia 18 ukiongozwa na Tabora wenye asilimia 23 ukifuata Mtwara. Ni kweli Ngara inaongoza na tulikwenda na tunao ushirikiano na wenzetu wa Rwanda katika kutokomeza na tumeshajenga vituo upande wa Tanzania na upande wa Ngara kwa ajili ya kuweka utaratibu.

Mheshimiwa Spika, moja ni huu ambao amesema kunyunyuzia hiyo dawa, lakini tunafikiria kwa sababu Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati anazindua Malaria Council alielekeza kwamba tuandike Wizara ya Fedha tuoneshe tunahitaji shilingi ngapi kwa ajili ya kununua zile dawa za kuua viluilui na tayari tumeshafanya na tumewasilisha Wizara ya Fedha bilioni 22 kwa ajili ya nchi nzima na mojawapo Ngara kwa maana ya Mkoa wa Kagera ikiwepo ni sehemu ya kufanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu ni lini tutaweza kutokomeza Malaria. Kwanza nikuhakikishie kabisa kuna Mikoa zaidi ya tisa sasa ni chini ya asilimia moja Malaria kwenye nchi yetu, na Mikoa mingi sana imeshuka. Kwa hiyo, tunadhani mpaka 202030 nchi yetu nayo itafikia kwenye kiwango cha hizo nchi nyingine. (Makofi)
MHE. BERNADETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, mafuriko katika Mto wa Kanoni ulio katika Manispaa ya Bukoba umewatesa watu kwa miaka mingi na sasa hivi naishukuru Serikali kwa kuweza kukubaliana na ombi la Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba na sasa wanauingiza mto huu katika mradi wa TACTIC.

Je, kuna mvua za vuli zitaanza mwaka huu za mwezi Oktoba mpaka Januari; Serikali inaweza ikaongezea fedha kiasi kwenye ile milioni sita inayotengwa na Halmashauri ili kusudi angalau wakafanya ukarabati wa awali isije ikatokea tena mafuriko mwaka huu?

Swali la pili; ili kuweza kuondoa mafuriko kabisa katika mto huu, inabidi mto upanuliwe, kina kiongezwe, kuta zijengwe za mto huu kutoka kwenye Kata ya Kagondo, Rwamishenye, Amgembe, Gireye, Bakoba hadi kuingia kwenye Ziwa Victoria. Je, katika huu mradi unaokuja wa TACTIC haya maeneo yote yatazingatiwa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la mama yangu Mheshimiwa Mushashu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru sana Mama Mushashu kwa sababu katika kumbukumbu yangu ni Mbunge mwana mazingira muda mrefu sana na hili analozungumza ni utashi kutoka katika moyo wake kabisa na nikiri wazi kwamba Manispaa imeanza kufanya kazi na Serikali kila muda tunafanyakazi, na Mama Mushashu anakumbuka kupitia mradi wa UGLSP pale katika Manispaa ya Bukoba hata mwanzo tulianza kufanya kazi hii kale kamfereji kadogo kalikokuwa kanaenda pale mpaka katika ziwa.

Kwa hiyo, tumetenga milioni sita hata hivyo tutaangalia pale itapobainika kwamba ile milioni sita ina changamoto tutaona nini cha kufanya kwa upande wa Serikali kwa ujumla wake. Lakini katika hizi kata zingine je, zitahusika vipi? Kama nilivyosema ni kwamba lengo letu ni kwamba kuondoa changamoto ya mafuriko na kama ulivyosema kweli katika kata hizi zote zinakabiliwa na mafuriko haya mto unapotokea jambo hili.

Tutaangalia katika ujenzi wa kuta katika mto huu jambo hilo lote litazingatiwa na hata kama kutatakiwa additional financing ya kuhakikisha maeneo mengine yote tuyaboreshe tutalifanya Mheshimiwa Mbunge bila shaka aina yoyote.