Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dua William Nkurua (6 total)

MHE. DUA W. NKURUA aliuliza:-
Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alitoa ahadi Mkoani Mtwara ya kumaliza tatizo la maji katika Mji wa Mangaka kwa kuchukua maji kutoka Mto Ruvuma, mradi ambao pia ungeweza kutatua tatizo la maji katika vijiji zaidi ya 12 vitakavyopitiwa na bomba kuu la mradi huo:-
Je, utekelezaji wa ahadi hiyo umefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dua William Nkurua, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne aliyoitoa Mkoani Mtwara ya kumaliza tatizo la maji katika Mji wa Mangaka pamoja na vijiji zaidi ya 12 kwa kuchukua maji kutoka Mto Ruvuma. Wizara imeajiri Mhandisi Mshauri na anaendelea na kazi za kufanya upembuzi yakinifu, usanifu na kuandaa makabrasha ya zabuni ambayo kazi hiyo inategemewa kukamilika mwezi Julai, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hiyo itakapokamilika itatoa idadi halisi ya vijiji ambavyo viko ndani ya kilomita kumi na mbili kila upande wa bomba litakapopita na gharama ya utekelezaji wa mradi huo. Ujenzi wa mradi unaanza mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. DUA W. NKURUA aliuliza:-
Katika ujenzi wa barabara ya Mangaka - Mtambaswala na Mangaka - Nakapanya, wapo wananchi ambao walishafanyiwa tathmini ya fidia ya kupisha ujenzi huo hawajalipwa na wengine wamepunjwa.
Je, Serikali italeta lini wataalamu wa kuhakiki fidia hizo ili kila mwananchi apate haki yake?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Dua William Nkurua, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ujenzi wa barabara ya Mangaka – Mtambaswala na Mangaka - Nakapanya, Serikali ilitenga fedha shilingi milioni 3,023.528 kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi waliokwisha fanyiwa tathmini ya mazao yao kati ya mwaka 2009 na 2012. Aidha, baada ya uthamini kuidhinishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali mwaka 2013, fidia ililipwa mwaka 2014 kwa kufuata taratibu na sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya wananchi ambao mali zao hazikufanyiwa tathmini katika kipindi hicho hawakulipwa fidia. Tathmini ya fidia kwa mali za wananchi hao imefanyika mwezi Oktoba 2015 na taarifa ya uthamini imekamilika na imewasilishwa kwa Mthamini Mkuu wa Serikali kwa hatua ya kuidhinishwa ili malipo yaweze kufanyika.
MHE. CECILIA D. PARESSO (K.n.y. MHE. WILLIAM D. NKURUA) aliuliza:-
Wilaya ya Nanyumbu ilianzishwa mwaka 2005 lakini mpaka sasa haina Hospitali ya Wilaya hivyo kuwalazimu wananchi kufuata huduma hiyo katika Hospitali ya Wilaya ya Masasi lakini pia kumekuwa na jitihada za kuomba kukipandisha hadhi Kituo cha Mangaka kuwa Hospitali ya Wilaya ya Nanyumbu lakini mpaka sasa hakuna mafanikio yoyote.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kukipandisha hadhi kituo hicho ili kuwa Hospitali ya Wilaya na kunusuru afya za wananchi wa Nanyumbu hasa akina mama wajawazito kwa kulazimika kupelekwa Wilaya jirani ya Masasi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa William Dua Nkurua, Mbunge wa Nanyumbu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha Wilaya ya Nanyumbu inakuwa na Hospitali ya Wilaya, tayari Serikali imetoa kibali na kupandisha hadhi Kituo cha Afya cha Mangaka kuwa Hospitali ya Wilaya baada ya kukidhi vigezo na taratibu zilizowekwa. Kibali hicho kimetolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia barua ya tarehe 27 Februari, 2016.
MHE. WILLIAM D. NKURUA aliuliza:-
Ujenzi wa barabara za lami hufuata Ilani ya Chama Tawala na matamko ya viongozi. Katika ziara yake Wilayani Nanyumbu, Rais wa Awamu ya Nne aliahidi ujenzi wa barabara ya Nangomba hadi Nanyumbu kwa kiwango cha lami.
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa William Dua Nkurua, Mbunge wa Nanyumbu, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Nangomba – Nanyumbu uliofanywa na Kampuni za UWP – Consulting PTY kutoka Afrika Kusini na UWP Consulting Company Limited ya Tanzania ili kuijenga kwa kiwango cha lami. Kwa sasa Serikali inatafuta fedha ili kuanza ujenzi wa barabara hii. Aidha, TANROADS Mkoa wa Mtwara inaendelea na itaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili iweze kupitika majira yote ya mwaka.
MHE. DUA W. NKURUA aliuliza:-
Kuna tatizo la usikivu wa simu za mkononi katika Kata za Napacho na
baadhi ya maeneo ya Kata ya Maratani na Kata ya Mnauje:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya utafiti na hatimaye kuweka
minara ya simu katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dua William Nkurua, Mbunge
wa Nanyumbu kama ifuatavyo:-
Vijiji vyote katika Kata za Napacho, Maratani na Mnauje viliiingizwa katika
awamu ya pili na awamu ya tatu ya utekelezaji wa mradi wa mawasiliano vijijini
wa kampuni ya simu ya Vietel(Halotel). Mpaka sasa Vijiji vya Kazamoyo na
Nakopi Kata ya Napacho na Kijiji cha Mchangani Kata ya Maratani
vimekwishapatiwa huduma ya mawasiliano kupitia kampuni ya Vietel(Halotel).
Aidha, vijiji vilivyobaki vitafikishiwa huduma ya mawasiliano kupitia utekelezaji wa
mradi awamu ya tatu ambao unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba, 2017.
MHE. WILLIAM D. NKURUA aliuliza:-

Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Nanyumbu kinatumia majengo ya nyumba za kuishi Askari Polisi:-

Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Nanyumbu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa William Dua Nkurua, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Nanyumbu ni miongoni mwa wilaya mpya ambayo ilianzishwa mwaka 2007 hivyo baada ya mabadiliko haya ililazimu jengo ambalo lilikuwa likitumika kama Kituo kidogo cha Polisi kata kuanza kutumika kama Kituo cha Polisi Wilaya.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi inatambua changamoto za ukosefu wa vituo vya polisi na ofisi katika wilaya mpya zilizoanzishwa hivi karibuni ikiwemo Wilaya ya Nanyumbu. Jitihada zinaendelea kufanyika za ujenzi wa vituo vya polisi na ofisi za wakuu wa polisi wa wilaya hizo kadiri fedha kutoka kwenye bajeti ya maendeleo na vyanzo vingine vinavyopatikana.