Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Maftaha Abdallah Nachuma (39 total)

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza;

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini ujenzi ule kimsingi umesimama na hakuna kinachoendelea pale Hospitali ya Mitengo.

(a) Je, ni lini sasa Serikali itaanza kuendeleza ule ujenzi wa Hospitali ya Kanda pale Mitengo?

(b) Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ujenzi wa hospitali hii bado umesimama na wananchi wa Kanda ya Kusini na hasa wale wa Mtwara Mjini wana changamoto za kupata matibabu bora ya tiba, lakini kimsingi kwamba Hospitali ya Ligula, hospitali ambayo ni Hospitali ya Mkoa hakuna x-ray, x-ray zimeharibika na ni muda mrefu hivi sasa wananchi wanahangaika kutembea umbali mrefu kwenda kufuata x-ray Mkoa wa Lindi na Dar es Salaam. Je, Serikali ipo tayari hivi sasa kuleta x- ray mpya ambazo zitaweza kutumika kwa ajili ya kuboresha tiba za wananchi wa Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA AFYA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwanza, kwamba ujenzi umesimama siyo kweli, kwa sababu mara tu baada ya mimi kupewa heshima hii ya kuhudumu kwenye Wizara hii kama Naibu Waziri nilipoanza kazi tarehe 19 Disemba, 2015 nilifika mimi mwenyewe binafsi kwenye Hospitali hii ya Kanda ya Kusini kwenye eneo la Mikindani.

Nilifika na nilijionea mimi mwenyewe na nilifanya ziara ya kushtukiza kwa maana hiyo hakuna hata mtu mmoja Mkoani Mtwara ama Lindi aliyekuwa anafahamu kwamba siku hiyo kuna Naibu Waziri wa Afya angefika, na wala hata Mkuu wa Mkoa hata RMO hawakujua. Nilifika na nikapitiliza mpaka site na nilikuta kuna mafundi wapo site wanaendelea na ujenzi. Kwa maana hiyo siyo siasa tu na ndiyo maana tukisema hapa kazi tu, tunamaanisha tupo kazini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusu x-ray nimpongeze Mheshimiwa Nachuma kwa jitihada zake anazozifanya kufuatilia uwepo wa vifaa tiba, vifaa na vitendanishi kwenye hospitali hii. Alifika kwenye ofisi zetu akiulizia lakini pia Mbunge mwingine wa Nachingwea naye alifika mpaka ofisini kwangu na bahati nzuri alinikuta na tukazungumza, labda niseme tu kwamba kuna matatizo ya hapa na pale kwenye vifaa vya imagine, x-ray, Ct-Scanner, MRI na vitu vingine kama hivyo.

Mheshimiwa Spika, lakini tupo kazini tunayafanyia kazi, tunabuni mbinu mbadala za namna ya kuziwezesha hospitali zote nchini kuwa na vifaa vya uhakika kupitia mipango mbalimbali na muda si mrefu mikakati yetu ikiiva nchi hii, matatizo ya Ct scanner, matatizo ya MRI, matatizo ya x-ray yatakuwa historia.

Mheshimiwa Spika, mtupe muda kidogo tu mkakati huu utakapo kamilika Tanzania mpya mtaiona ikiwa imefika na mtaanza kufaidi matunda ya uwepo wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. ABDALLAH N. MAFTAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Naomba niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kwa muda mrefu Serikali ilikuwa na mpango wa kuhakikisha inatoa huduma za afya bure kwa wazee, lakini kumekuwa na mkakati na utaratibu wa kutoa bima ama kadi za matibabu kwa wazee ambazo zina mipaka. Kwa mfano, mzee wa Mtwara Mjini akienda Mtwara Vijijini kule hana nafasi ya kutibiwa japokuwa ana zile kadi. Je, Serikali ina mkakati gani sasa hivi wa kuondoa mipaka ya kadi za matibabu za wazee? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kuuliza swali hili la muhimu sana. Takribani mwezi mmoja umepita Mheshimiwa Waziri wa Afya alinipa jukumu la kutengeneza Kikosi Kazi ambacho kitawashirikisha wadau mbalimbali kwenye Mfuko wa Afya kwa Umma (CHF) na Bima ya Afya kwa ujumla wake. Kikosi Kazi kimeshakaa na tumepanga mpango kazi wa namna mpya ya kuboresha huduma za afya kutokana na kadi ya CHF.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo tutakayoyafanya ni pamoja na kuweka utaratibu mzuri wa cross subsidization, dhana unayoisema Mheshimiwa inaitwa cross subsidization. Pia tutashughulikia suala la portability ya kadi kwa maana ya kutoka kwenye level moja kwenda kwenye level nyingine kwa maana ya kutoka kwenye level pengine ya wilaya kwenda kwenye level ya rufaa ya mkoa ama kutoka wilaya moja kwenda wilaya nyingine ama kutoka zahanati kwenda kituo cha afya, hiyo inaitwa portability ya hiyo kadi. Hili ni jambo mojawapo ambalo tunalifanyia kazi na tutaliwekea mkakati mahususi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ni lazima kutakuwa na ongezeko la uchangiaji kwa sababu unapotoka level ya chini kwenda level ya juu gharama za huduma pia zinaongezeka. Tutakapoleta mpango huu tutawashirikisha Wajumbe wa Kamati yetu na Wabunge wote kwa ujumla ili kwa pamoja twende kuwahamasisha wananchi wakubaliane na mpango huu mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu utakuja sambamba na kutafuta namna bora zaidi kwa kulekule kwenye halmashauri kutenga fedha mahsusi kwa ajili ya kulipia Bima ya Afya kwa wazee ili waweze kupewa Kadi za Bima za Afya bure kama ambavyo sera inasema. Kwa maana ya kwamba ni lazima tuwabane walionacho ili tuweze kuwahudumia ambao hawana uwezo wakujihudumia, hiyo ndiyo mikakati ya Serikali. (Makofi)
MHE ABDALLAH N. MAFTAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
(a) Kwa kuwa Mtwara Mjini kila kipindi cha masika maji huwa yanajaa na mafuriko yanatokea na Serikali inatoa kilo 16 za unga, je, Serikali iko tayari hivi sasa kusema tarehe ngapi itaanza ujenzi wa miundombinu Mtwara Mjini?
(b) Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri kadanganywa katika jibu lake nililiouliza kwamba Barabara ya Mikindani- Lwelu itajengwa lini kwa kiwango cha lami, yuko tayari hivi sasa kufuatana na mimi kama Mbunge ili aweze kujionea mwenyewe kwamba kadanganywa? Ahsante
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la lini barabara hii itajengwa nadhani katika jibu langu la msingi nimesema. Katika Mradi ule wa Strategic City ambapo lengo lake kubwa ni kuhakikisha kwamba tuna maeneo mbalimbali ya miji ambayo imejengwa miradi hii, hata ukiangalia pale Tanga, ukiangalia Mbeya ukiangalia Arusha, huu ndiyo mpango mkakati, hivi sasa tunakwenda hata katika Jiji la Dar es Salaam. Eneo hili nimesema kwamba mchakato wake sasa uko katika hali ya manunuzi, lengo ni kwamba bajeti hii sasa mchakato utakapokamilika maana yake miundombinu inakwenda kujengwa. Lakini kusema kwamba nimedanganywa au vipi nitafika kule Mtwara, naomba nikwambie Mheshimiwa Mbunge, siyo Mtwara peke yake, nitahakikisha maeneo yote, ikiwemo na Mtwara niende nikakague maeneo ya field, hii ndiyo kazi kubwa tumekuwa tukiifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo letu ni kuweza kufika kila maeneo kubaini changamoto mbalimbali na hasa katika kipindi hiki mvua inanyesha, maeneo mengi sasa hivi yameharibika. Taarifa ya habari pale ukiangalia jana Kyela, ukiangalia Morogoro na maeneo mbalimbali yameharibika. Kwa hiyo, ni jukumu la Ofisi hii, kufika kila mahali kubaini uhalisia wa eneo lile wananchi waweze kupata huduma inayokusudiwa na Serikali yao.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Nashukuru Mheshimiwa Spika, kwa kiasi kikubwa swali langu lilikuwa na sehemu mbili hivi, lakini limejibiwa swali moja tu.
Nilikuwa nimezungumza kwamba tatizo la maji kwa Mikoa hii ya Kusini na hasa miundombinu yake ambayo imejengwa tangu ukoloni ni miundombinu hafifu sana. Kwa mfano, mradi ule wa maji wa Makonde umejengwa mwaka 1953 na mpaka hivi sasa navyozungumza unatoa maji kwa asilimia 30 tu kwa sababu ya miundombinu yake ni hafifu. Naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwa kuwa katika majibu yake ya msingi Mheshimiwa Waziri amezungumzia suala zima la mradi wa maji wa Mto Ruvuma na akasema kwamba upembuzi yakinifu umekamilika na wananchi watapata maji na vijiji takribani 25 vinavyopitia lile bomba ambalo linatarajiwa kujengwa wataweza kunufaika na mradi huu wa maji.
Mheshimiwa Spika, swali tangu mwaka 2015 mpaka hivi sasa navyozungumza wale wananchi wameambiwa maeneo yale ambayo maji yatapita au ule mradi utapita wasiendeleze yale maeneo na hawajalipwa fidia hata senti moja mpaka hivi sasa, je, ni lini wale wananchi watapewa fidia ili waweze kutumia zile fedha kwenda kununua maeneo mengine waweze kuendeleza kilimo?
Mheshimiwa Spika, imekuwa ni kilio kikubwa sana Mtwara Mjini na maeneo mengine ya Kusini, kwamba watendaji wa Idara za Maji wanavyokuja kusoma mita hawasomi zile mita na wamekuwa wakikadiria malipo ya mita kila mwezi, wanaona usumbufu kwenda kuzipitia mita wakati mwingine na kuleta usumbufu mkubwa kwa wananchi na kuwabambikia fedha nyingi za kodi ya maji kinyume na taratibu na kanuni. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri kwamba mwaka huu mwezi wa pili Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji alitembelea kule Mtwara na wananchi waliandamana kwa ajili ya tatizo hili, naomba atoe majibu ya uhakika kwamba ni lini sasa Serikali itakoma kukadiria mita za maji...
SPIKA: Mheshimiwa Nachuma yaani umehutubia.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: ...na badala yake waende kusoma mita?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nitoe majibu ya nyongeza kwa maswali mawili aliyouliza Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mradi huu wa kutoa maji kutoka Mto Ruvuma mpaka Mtwara ni kweli tumeuzungumza kwa muda lakini Serikali imedhamiria kuujega mradi huu kwa kutumia utaratibu wa PPP, imeshapata mbia ambaye atatafuta fedha kwa maana building and finance, Serikali yenyewe itachangia kwa kuweka msimamizi atakayesimia. Kazi ambazo tunafanya sasa ni kufanya due diligence ya ile kampuni kama ina uwezo wa kufanya kazi hii na tuko kwenye hatua ya mwisho na ndio maana tumesema kuanzia mwaka wa fedha huu unaoanza mwezi wa saba tunaweza kuanza kujenga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa tutakapokuwa tumekamilisha hatua zote hizi ndio tutakapolipa fidia ya wale wananchi ambao mradi utapita hatutaweza kulipa fidia kabla hatujakamilisha majadiliano na ile kampuni ambayo itajenga ili kusudi tuwe na uhakika kwamba wale wanaohusika wote na watakaoathirika na mradi huu wataweza kulipwa. Lakini katika swali lake la pili la kwamba ni lini Serikali itaacha kukadiria, ninafikiri suala la kukadiria mita siyo utaratibu tunasema kila mtu atalipa maji kulingana na namna anavyoyatumia. Kwa hiyo, kuna maeneo ambayo bado yana utata kuhusu ukadiriaji hili mtuachie tutalifanyia kazi ili tuhakikishe kwamba kila mmoja alipe maji kwa kadri anavyokuwa ameyatumia, ahsante.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa shule hii ni siku nyingi sana imezungumzwa na Serikali kwamba itapandishwa hadhi kuwa shule ya Kidato cha Tano na Kidato cha Sita, lakini siyo kweli kwamba hii shule ina upungufu wa matundu ya vyoo, mimi shule hii naifahamu sana. Mwaka jana yamejengwa matundu 16, tatizo ni mabweni.
Swali langu la kwanza; je, Serikali ipo tayari hivi sasa kutenga bajeti ya kutosha ili shule hii ya Mchinga Sekondari waweze kujenga mabweni kwa ajili ya kupokea wanafunzi wa Kidato cha Tano na cha Sita? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, amezungumza hapa Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba shule ya Kidato cha Tano na cha Sita, mwanafunzi kutoka Lindi na maeneo mengine anaweza kupangiwa mkoa wowote, lakini shule hizi za Kidato cha Tano na cha Sita Tanzania zina matatizo mengi ya chakula na wanafunzi wanakula milo ambayo siyo kamili, wanakula maharage ya kuoza maeneo mengi. Swali langu; Serikali iko tayari hivi sasa kuhakikisha kwamba inapeleka bajeti ya kutosha ili wanafunzi wa Kidato cha Tano na cha Sita Tanzania waweze kupata milo kamili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza suala la kutenga fedha za kutosha, naomba nikiri kwamba katika mchakato wetu wa bajeti tulivyokuwa tunazungumza hapa, nilitaja miongoni mwa vipaumbele katika bajeti zetu. Vipaumbele vile viliji-reflect katika kila Halmashauri ilitenga nini. Tulikuwa na mpango mkakati mkubwa wa kuhudumia shule kongwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, jambo hili nadhani mchakato wake tulishaupitisha katika suala zima la mchakato wa bajeti. Halikadhalika Mkoa wa Lindi na vipaumbele vyake vimewekwa. Lengo kubwa ni nini? Kwa sababu ilikuwa ni maelekezo na Halmashauri ya Lindi ilishatenga baadhi ya fedha kwa ajili ya ku-facilitate hilo jambo. Lengo kubwa ni fedha zipatikane ziweze kupelekwa ilimradi kazi ile iweze kukamilika vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala la kwamba shule hizi chakula chake, mgao wake hauendi vizuri; naomba niwaambie ndugu zangu, ni kwamba hili kama Serikali tumeliona na ndiyo maana kila wakati sasa hivi tunafanya rejea hata ya viwango vya posho ya kila siku ya chakula. Lengo letu ni kwamba, tufike muda tu-realize kwamba unit cost ya mwanafunzi kwa sasa ni kiasi gani, ili tunapokwenda katika mpango mpana kabisa wa kuhakikisha tunaboresha elimu Tanzania tuboreshe kwa ukubwa wake.
Naomba nikiri wazi kwamba Serikali inafanya kila liwezekanalo sasa hivi ili kutatua na kuongeza kiwango cha Walimu. Najua mpango huu mpana unapouanzisha ni lazima una changamoto yake kubwa. Sasa zile changamoto zinatupa sisi jinsi gani tutafanya tuweze kwenda vizuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nimesema katika majibu yangu ya kwanza katika lile swali lake la kwanza la nyongeza kwamba ukiangalia sasa, zile shule kongwe tunaanza kuzibadilisha, tunakwenda kuziwekea miundombinu, lakini kuangalia ni jinsi gani watoto watakapokuwa katika mazingira ya shule waweze kupata elimu bora. Sambamba na hilo upatikanaji wa elimu bora unatokana na jinsi gani mtoto anapata lishe ya kutosha pale shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali inafanya utaratibu wote wa kina ili mwisho wa siku tuone elimu yetu Tanzania tunaipeleka wapi ilimradi tuweze ku-compete katika nchi nyingine za wenzetu za East Africa.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Nimesikitishwa sana na maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri pale alivyoeleza kwamba Manispaa ya Mtwara Mikindani imetenga maeneo kama vile Likonde, Mbae na Mjimwema.
Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe maeneo haya ni Tarafa mbili tofauti; na siku ya tarehe 21 mwezi wa Nane, Serikali iliweza kubomoa vibanda vidogo vidogo ambavyo vimejengwa katika Kata ya Jangwani, Tarafa ya Mikindani ambapo ni kilometa takribani 10 kwa maeneo aliyoyataja ambapo kuna akinamama wafanyabiashara wadogo wadogo wanauza samaki kihalali kabisa katika maeneo yale. Cha ajabu wale samaki wao wamevunjwavunjwa na kumwagwa. Akinamama wale walikopa pesa kutoka katika mabenki na taasisi mbalimbali za kifedha na mpaka hivi sasa ninavyozungumza hawana uwezo wa kulipa mikopo ambayo wamekopa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari hivi sasa afuatane na Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini ambaye anazungumza, aje kuangalia mazingira yale ambayo wale akinamama wamebomolewa maeneo yao ya kuuza samaki ambapo ni mbali takriban kilometa 10 kutoka eneo ambalo amelitaja yeye?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
himiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Maftaha yuko pale site; na hapa nimesema majibu ya msingi ya Serikali ni kwamba lazima Halmashauri zitenge maeneo. Hata hivyo, tumezielekeza Halmashauri kwamba, maeneo watakayotenga lazima waangalie kile kitu kinaitwa accessibility, yaani ni jinsi gani yatafikika? Ndiyo maana Halmashauri mbalimbali tumezielekeza kwamba ziwasiliane na SUMATRA katika maeneo hayo kwamba kuwe na uwezekano hata wa daladala ziweze kufika kwa sababu maeneo mengine unakuta watu wanashindwa kwenda kwa sababu daladala hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba, jana nilipokuwa nikijibu hapa maswali mbalimbali nikasema Mkoa wa Mtwara ni mkoa wangu wa kipaumbele, ni mkoa wa kwanza. Naomba niseme kwamba nimekubali ombi lake, tutakwenda site, lengo kubwa ni kuwasaidia hawa Watanzania wadogo wanaotaka kujikomboa katika suala la uchumi. Kwa hiyo, hilo, aondoe shaka ndugu yangu, mimi nitafika site, tutakwenda pamoja katika hilo.
MHE. MAFTAH A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru niweze kuuliza swali la nyongeza. Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kabisa kwamba Serikali iliweka mkakati wa kuhakikisha ya kwamba maeneo yote ambayo limepita bomba la gesi kitaalam wanaita mkuza wa gesi, kwamba vijiji vile na mitaa ile itakuwa imepatiwa umeme kupitia REA Awamu ya Kwanza, Pili na ya Tatu. Lakini mpaka sasa hivi ninavyozungumza maeneo mengi ya vijiji na vitongoji vya Mtwara Mjini na Lindi kwa mfano Dimbozi, Mbawala Chini, Mkunjanguo na Naulongo kule kote bado hakujapelekewa umeme. Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali ukoje kuhakikisha kwamba wanamaliza tatizo hili katika ule mkuza wa gesi kwamba wapate umeme wale wananchi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Maftaha kwamba tunapotekeleza Mradi wa REA Awamu ya Tatu, awali ya yote tunaanzia kwenye vijiji ambavyo viko kwenye mkuza wa bomba la gesi. Kwa hiyo, nikuhakishie Mheshimiwa Maftaha na niombe tu kwamba tutakapomaliza Bunge kama una fursa basi tutapanga siku tupitie kijiji hadi kijiji ili kuhakikisha wananchi wako wanapata umeme.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante, nishukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2013 wananchi wa Mtwara waliweza kuandamana kwa kiasi kikubwa sana Mtwara na Lindi wakidai namna gani kwamba rasilimali hii gesi inaweza kuwanufaisha na tunashukuru hivi sasa manufaa
hayo yanaanza kuonekana. Nilikuwa naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba ule mpango wa kuwapa wawekezaji ambao wana nia ya kuwekeza Mtwara gesi waweze kutengeneza ama wajenge viwanda vya mbolea umefikia wapi mpaka hivi sasa?
(b)Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba kujua, kulikuwa na mkakati na mwaka jana tulielezwa ndani ya Bunge hili kwamba kuna usambazaji wa gesi asilia kwenda majumbani kwa mana kwamba mikoa ya Dar es Salaam na maeneo mengine. Nilikuwa naomba kujua mkakati huu kwa Mkoa wa Mtwara na Lindi upoje kwa sababu tulipewa tu taarifa kwamba upembuzi yakinifu umeshaanza nataka kujua mimi kama Mbunge sina taarifa nao. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Maftaha kwa kweli kati ya Wabunge ambao wanahangaikia sana maslahi ya wananchi wake ni pamoja na Mheshimiwa Maftaha. Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusuaiana na maswali yake ya msingi kabisa, kwanza kabisa ujenzi wa kiwanda cha mbolea Mtwara; nataka tu nimwambie Mheshimiwa Maftaha pamoja na wananchi wa Mtwara na Lindi kwamba hatu ailiyofikiwa sasa hivi; kwanza kuna
Kampuni ya HELM kutoka Ujerumini imeshapata eneo kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanda cha mbolea na makadirio ya kukamilisha ujenzi huo ni mwaka 2020 lakini hata hivyo nimwambie tu hatua ambazo zinafanywa na Serikali. La kwanza kabisa; Serikali kupitia TPDC wanafanya majadiliano sasa ya kuelewana sasa bei ya kununua gesi kati ya TPDC pamoja na Kampuni ya HELM itakayojenga kiwanda hicho na kwa sasa wameshaonesha kutenga jumla ya dola za Kimarekani milioni 200 kwa kampuni hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini taratibu za kuuziana gesi wakishamaliza kujenga ujenzi huo 2020 wataweza kupewa gesi na mahitaji ya kiwanda hicho cha mbolea inafikia milioni 80 futi za ujazo mpaka 104; kwa hiyo matarajio yapo na wananchi wa Mtwara watanufaika na kiwanda
hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la pili; ni kweli kabisa tulitarajia sana tuanze usambazaji wa gesi majumbani katika mji wa Mtwara na Lindi na Dar es Salaam pia, lakini tumefikia hatua nzuri. Upembuzi yakinifu umekamilika, matarajio yameshapatikana na kwa sasa Mtwara na Lindi wanahitaji milioni tano za gesi hadi kumi futi za ujazo ambazo zinagharimu shilingi bilioni mbili, Kwa hiyo kuanzia Julai mwaka huu, Wananchi wa Mtwara, Lindi na Dar es Salaam wataanza sasa kupata gesi ya majumbani. Na Mheshimiwa Maftaha wale wananchi wako wale wa Mbawala chini pamoja na Mtajitambua wataanza kupata gesi asilia.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Ahsante Mheshimiwa Mwenyekiti naomba kwa namna ya kipekee nishukuru kwa sababu suala hili la ulipaji wa maeneo haya fidia hii ni suala la muda mrefu sana kwa kuwa Wizara hii ya TAMISEMI na Wizara ya Ardhi imekubali sasa kulimaliza suala hili tunashukuru kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini, lakini hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, nilikuwa naomba kujua sheria inatueleza kwamba kwa kuwa maeneo haya yamechukuliwa mwaka 2012/2013 ni muda mrefu hivi sasa wananchi wale wamekosa maeneo ya kulima na kufanya shughuli zao za kimaendeleo, je, Serikali ipo tayari kulipa pamoja na fidia ya nyongeza?
Swali la pili, kwa kuwa ahadi hii ya kuwalipa wananchi hawa Jimbo la Mtwara Mjini ni la muda mrefu, je Mheshimiwa Waziri yupo tayari kulithibitishia Bunge hili kwamba wananchi wa Mtwara Mjini wa maeneo haya ya Mji mwema na Tangira kwamba tarehe hizo walizotaja ni kweli wataenda kulipa fidia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kulifuatilia hili jambo kwa sababu ni haki za wananchi wako kwa hiyo commitment yako kwa wananchi wako imekuwa vizuri, lakini jambo la pili, utaratibu wa malipo ya fidia ni kwamba mara baada ya tathimini ikishafanyika ikipita miezi sita maana yake malipo yanatakiwa yalipwe ndani ya miezi sita; ikipita miezi sita lazima kuna malipo ya nyongeza yatafanyika. Kwa hiyo, naomba nikuhakikishie kwamba Wananchi haki zao zitalindwa kulingana na muda uliocheleweshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la pili kwamba commitment ya Serikali sasa itaenda kulipa hili nimezungumza hapo awali kwamba kilicho chelewesha mwanzo kutokana na Bodi ilikuwa haijaundwa na bahati nzuri sasa bodi imeshaundwa na ndio maana sisi ofisi yetu ina jukumu la kutoa kibali tumeshatoa kibali. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba uondoe hofu kwamba wananchi wa Mtwara leo hii wananisikiliza live kupitia vyombo vya habari kwamba Serikali imejipanga katika hili na itaenda kutekeleza kwa kadri mipango yote ilivyowekwa vizuri kupitia Halmashauri yenyewe.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo hili la kutokuwa na mawasiliano katika jimbo hilo la Momba linafanana kabisa na barabara ya ulinzi ambayo inaanzia Mtwara Mjini na kuzunguka Mikoa yote ya Kusini kwamba mvua zilizonyeesha hivi sasa barabara hii haipitiki na hasa katika maeneo ya kijiji cha Kivava na Mahurunga mvua imeweza kukata madaraja na barabara hii hivi sasa haipitiki. Je, Serikali hivi sasa ipo tayari kuharakisha ujenzi wa barabara hii ya ulinzi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba sasa hivi mkandarasi yuko site kwa ajili ya ujenzi wa kipande cha kutoka Mtwara hadi Mnivata na baada ya hapo tunaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuendelea kujenga barabara hiyo mpaka Newala na baadaye tunaendelea na ile barabara inayoambaa kwenye Mto Ruvuma ambayo tunasema ni barabara ya ulinzi, nadhani hilo analifahamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu madaraja yaliyobomoko, bahati nzuri Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mtwara ni kati ya Mamaneja ambao ni wepesi sana na alishatujulisha hayo na tumempa maelekezo ya kufanya huku akiwasiliana na Road Board kwa ajili ya kutumia fedha za emergency kurekebisha zile barabara zilizokatika.
MHE. MAFTAH A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kabla sijauliza swali la nyongeza, naomba nifanye masahihisho kidogo. Mheshimiwa Naibu Waziri kasema eneo la Libya ni shamba la chumvi.
Mheshimiwa Spika, mgogoro huu siyo shamba la chumvi ni makazi ya watu ambao nilizungumza wakati wa bajeti hapa kwamba waliamka asubuhi wakakuta wamewekewa beacon kwamba eneo lao limeuza. Siyo shamba la chumvi. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri afanye masahihisho.
Mheshimiwa Spika, sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, Machi 5 mwaka huu wa 2017, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikuwa Mtwara, pamoja na mambo mengine Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alikuwepo Mtwara Mjini na alilalamikiwa kuhusu suala la mgogoro wa ulipaji wa fidia katika maeneo ambayo yamechukuliwa mwaka 2013; Mji Mwema. Akaahidi kwamba wananchi wale watalipwa pesa zao mwishoni mwa mwezi Julai, lakini mpaka leo tunapewa taarifa kwamba yule CEO wa UTT amesema hawezi kuwalipa wale watu.
Mheshimiwa Spika, naomba kujua majibu ya Wizara hii kwamba ni kweli inawatendea wananchi hawa wa Mtwara Mjini haki? Kwa sababu tangu mwaka 2013 wamechukuliwa maeneo yao, halafu leo Serikali inasema haiwezi kulipa zile pesa. Naomba tupate ufafanuzi.

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, eneo hili la Libya ambalo ni maarufu kama Mangowela, lakini wale waliochukua lile eneo kwa kuwanyang’anya wananchi eti wanawaeleza wawahamishe, wamebatiza jina wakaita Libya, lakini asili yake ni Mangowela. Sasa naomba kujua, yule mtu ambaye amewanyang’anya wananchi wale ni taasisi inaitwa Azimio na Serikali imemchukulia hatua maeneo mengi. Je, Serikali iko tayari hivi sasa kumnyang’anya ardhi ile ambayo ameidhulumu kwa wananchi na badala yake wananchi wale wameambiwa waende Mahakamani wakati wanajua kabisa kwamba anafanya ujanja kule Mahakamani? Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwanza niseme tu nilikuwepo huko mwezi uliopita na bahati nzuri nilionana na uongozi wa mkoa pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtwara- Mikindani.
Mheshimiwa Spika, sasa wale kama wameshindwa kulipa au wameshindwa kuchukua, hatuwezi kuendelea kuwalazimisha kwa sababu ile ardhi ni mali. Kama wameshindwa, maana yake ni kwamba mnunuzi yeyote ambaye anataka kuwekeza pale, anaruhusiwa kuja. Wale wamesha-declare kwamba hawawezi na hatuwezi kuwalazimisha. Kama wame-declare hawawezi, maana yake ni kwamba tunaangalia utaratibu mwingine na hili liko chini ya Mkuu wa Mkoa analisimamia.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Wizara yangu inasubiri wao wenyewe wahusika kwa maana ya Manispaa pamoja na Mkoa husika kwamba watakuja na mpango upi au watakuja na utaratibu upi ambao watakuwa wamejiwekea? Kwa maana ya UTT, hawawezi tena na wamesha-declare kwamba hawawezi kuchukua.
Mheshimiwa Spika, suala la pili analolizungumzia, lipo Mahakamani na siwezi kulijadili hapa na ndiyo maana nimetaja na namba ya shauri lilipo Mahakamani. Tusubiri shauri hilo liishe ndiyo waweze kulileta hapa.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo hili la Morogoro Kusini linafanana kabisa na Jimbo la Mtwara Mjini ambako umeme unatoka pale lakini bado kuna vijiji vingi kwa mfano Naulongo, Mkunjanguo, Namayanga na Mawala Chini kule kote mtandao wa umeme haujafika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nimemweleza Mheshimiwa Waziri mara nyingi sana, je, yupo tayari hivii sasa kutoa kauli ya mwisho kwamba ni lini mtandao wa umeme utapita kwenye vijiji hivi nilivyovitaja? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kama alivyosema, wiki mbili zilizopita nilikuwa Mtwara kushughulikia tatizo la umeme kukatika katika. Nilipita katika vijiji 16 na bahati nzuri vijiji vingine alivyosema Mheshimiwa Maftaha hivi leo mkandarasi yupo kule. Kwa hiyo, wakandarasi wameshaanza kazi Mheshimiwa Mbunge, asante sana. (Makofi)
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Kakunda, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kumekuwa na malalamiko mengi sana kwa Wakazi wa Dodoma wakiwemo Wabunge na Taasisi mbalimbali za Kiserikali kwamba ili waweze kupata huduma ya ardhi Manispaa ya Dodoma, basi kuna mzunguko mkubwa sana na mlolongo mkubwa sana.
Je, Serikali ipo tayari hivi sasa kufanya uchunguzi maalum na kuchukua hatua kwa kuwa, sasa Manispaa ya Dodoma ni Mji Mkuu kwamba tunahitaji huduma hizi ziende kwa haraka? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, zipo Taasisi za Serikali ambazo zinahamia Dodoma hivi sasa, zinataka kujenga ofisi zao hapa Dodoma, lakini bado kumekuwa na urasimu mkubwa sana taasisi hizo kupewa ardhi pale Manispaa.
Je, Serikali ipo tayari hivi sasa kuweka utaratibu maalum ili Taasisi hizi za Kiserikali ama Taasisi za Umma ziweze kupewa maeneo ya kuweza kujenga ofisi zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Maftaha Abdallah Nachuma na ndiyo maana wakazi wa Kusini wanamwita mashine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mlundikano wa kazi uliokuwepo katika kipindi hiki cha awali cha utekelezaji wa majukumu mapya ya kuunganisha majukumu ya iliyokuwa Manispaa ya Dodoma na ile iliyokuwa CDA ndio umefanya kuwe na baadhi ya malalmiko katika hatua za awali za utekelezaji wa kazi, kwa sababu kulikuwa na migogoro mingi sana ya viwanja, mahitaji ya kubadilisha mikataba mingi sana na hapo hapo kuna mahitaji ya kuendelea kupima maeneo mapya. Kwa hiyo, haya matatizo ambayo Mheshimiwa Maftaha ameyataja ni matatizo ya mpito tu ambayo yatarekebishwa hivi karibuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la pili, hadi sasa Manispaa imepima viwanja 1,288 na ambavyo tayari hati zake zimetayarishwa. Maeneo ambayo ni Mji Maalum wa Serikali yamepimwa viwanja 147, ikiwemo Ikulu, Wizara zote zimepatiwa hati na vilevile taasisi za umma na viwanja vya mabalozi 64.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nakuonesha hati ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI ni hii hapa, tayari imepatikana na ipo Ofisini. Wizara zote zina hati kama hii. Taasisi zote za umma ambazo zinahitaji ardhi, waende Manispaa pale watapewa hati zao ambazo zitawawezesha kupata maeneo ya kuweza kujenga ofisi zao haraka sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile katika maeneo ya Nala wamepima viwanja 922 na kiwanja cha michezo cha Nzuguni kimepimwa, kile ambacho tulipata msaada kutoka Morocco na viwanja 218 katika maeneo mengine.
Waheshimwa Wabunge na wananchi kwa ujumla wanakaribishwa waombe viwanja Manispaa na mimi kama msimamizi wa Manispaa hiyo, nawaahidi kwamba watakuwa wamepata hati kabla ya mwisho wa mwezi huu wa pili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo ambalo limepimwa viwanja vya Serikali ni hili hapa na naweza nikalionyesha Waheshimiwa Wabunge waweze kuliona. Kazi imefanyika vizuri. (Makofi)
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana nilikuwa naomba kuuliza swali la nyongeza kwamba sasa hivi Tanzania kuna dawa hizi ambazo zinaitwa tressa medicines ambazo zinatolewa kwenye Hospitali za Rufaa ama Hospitali za Mikoa tu na kwamba kule vijijini kwenye Zahanati na Vituo vya Afya hizi dawa hazitolewi za magonjwa kama BP, magonjwa HIV, Kifua Kikuu sasa swali langu; nilikuwa naomba kujua kwa sababu wananchi wanapata tabu sana kusafiri umbali mrefu kwenda kutafuta dawa hizi kwenye Hospitali za Mikoa na Hospitali za Rufaa.
Je, Serikali ipo tayari hivi sasa kufundisha wale Medical Assistant’s kule vijijini ili dawa hizi ziweze kutolewa kule vijijini? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kutoa ufafanuzi, tumapoongelea suala la tressa medicines tuna maanisha kwamba ni dawa zile muhimu na ambazo sisi zina tusaidia katika sekta ya afya kubaini na kuangalia kwamba zile dawa muhimu zipo. Tressa medicines sio dawa ambazo unasemasijui kwa lugha ya kitaalam mnasemaje kwamba ni dawa ambazo ni muhimu ambazo zilikuwa zinatakiwa kutotolewa katika sehemu fulani tressa medicine ni general term ambayo sisi tunaitumia kuhakikisha kwamba tunazibaini na kuzipatia zile dawa muhimu kule ambapo tunazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa labda niendelee kwa kusema kwamba sasa hivi ndani ya Serikali na mwanzoni mwa mwezi huu tumetoa mwongozo wa utoaji wa dawa katika ngazi mbalimbali. Mwongozo huu kwa jina la kitaalam tunaitwa standard treatment guedline hapo siku za nyuma kila ngazi ilikuwa inajitolea dawa holela na kadri walivyokuwa wanaiona. Na hii changamoto tulikuwa tunaipata sana katika Hospitali kubwa makampuni ya dawa yana kuja yanamwambia mtoa huduma andika dawa hii wakiwa wanampa na yeye motisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati sisi Serikali tunaagiza dawa nyingi kwa pamoja unakuta sasa mgonjwa anaandikiwa dawa anaambiwa dawa hazipo. Serikali imeongeza sana bajeti ya dawa kutoka bilioni 30 mwaka 2015/2016 kufikia bilioni takribani 270 katika mwaka wa 2017/ 2018 ni zaidi ya mara tisa ndani ya miaka miwili. Kwa hiyo, hali ya upatikanaji wadawa sasa hivi nchini ni nzuri sana pamoja na hizi tressa medicines.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lako lingine la nyongeza ilikuwa sasa kutokana na mwongozo huu, umeweka utaratibu dawa gani kwa ugonjwa gani zitakuwa zinapatikana na kwamba hivyo vituo vya afya vitatakiwa kuzingitia dawa gani na kutoa matibabu kwa kulingana na ule mwongozo wa utoaji dawa ambao kama na sisi Serikali tumetoa. Tunatambua kwamba baadhi ya maeneo ambayo tunachangamoto ya watumishi tunaendelea kutoa mafunzo ili na wale watumishi waweze kutoa tiba kwa wale wagonjwa wanaofika pale ambapo hamna madaktari kwa kuzingatia miongozo ambayo na sisi tutakuwa tumewapa.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa tatizo la maji la Mji wa Tukuyu linafanana kabisa na Manispaa ya Mtwara Mjini, ambako kwa muda mrefu Serikali imekuwa na mpango wa kutoa maji kutoka Mto Ruvuma, lakini ule mradi mpaka hivi sasa umekwama kwa sababu kibali bado hakijasainiwa na Waziri husika. Je, ni lini Serikali itatoa kibali hiki ili zile pesa ziweze kutoka Exim Benki ya China na ule mradi uweze kutekelezwa mara moja Mtwara Mjini, kwa sababu kuna tatizo kubwa la maji? Ahsante
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iko kwenye hatua za mwisho kukubaliana na Benki ya Exim kwa ajili ya kutoa fedha ya ujenzi wa mradi huo na siyo kwamba kibali hakijatolewa na Waziri, tuko katika hatua nzuri. Mwezi uliopita mimi mwenyewe nimeenda mpaka kwenye chanzo pale Ruvuma nimeenda kutembelea pale na sasa hivi hatua inaendelea vizuri kabisa, wakati wowote huo mradi utaanza utekelezaji. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, hakuna wasiwasi mradi upo na hiyo fedha imeshapatikana tunakamilisha taratibu ndogondogo tu ili uweze kuanza. (Makofi)
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, uwanja wa ndege wa Kanda ya Kusini ni uwanja ambao upo Mtwara Mjini na ule uwanja wa Mtwara Mjini nimekuwa nazungumza sana kwenye Bunge hili kwamba ni uwanja ambao hauruhusu ndege kuweza kutua wakati wa usiku, miaka ya nyuma huko taa zilikuwepo zikaondolewa. Je, mpango wa Serikali wa ahadi inazotoa kila mwaka wa kukarabati na kuweka taa za kuongozea ndege Mtwara Mjini kiwanja hiki cha Kanda ya Kusini utaanza lini.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Maftaha kwa kuendelea kufuatilia ujenzi huu wa uwanja wa ndege wa Mtwara. Kikubwa tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ni kwamba katika Bajeti ya fedha ya mwaka uliopita kulikuwa kumetengwa fedha, pia katika mwaka huu unaokuja kwa ajili ya kuongeza zile huduma ambazo zilikuwa zimepungua katika uwanja huu tumeweka fedha za kutosha. Kwa hiyo, avute tu subira, nimefika uwanja wa ndege wa Mtwara nimeuona kwanza sasa hivi huduma zinaendelea vizuri, hili zoezi la taa litakamilika tu Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi.
MHE. MAFTAH A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri, tatizo hili la maji katika Wilaya ya Nyang’hwale linafanana kabisa na tatizo la maji Mtwara Mjini na kwa kiasi kikubwa Mtwara Mjini kuna mradi ambao ulipangwa kutekelezwa kwa kupata pesa kutoka Benki ya Uchina ambapo mpaka sasa bado hizp pesa hazijapatikana.
Juzi nilikuwa namuuliza Mheshimiwa Waziri akaniambia kuna pesa zingine zimesainiwa maji yatoke Bonde la Ziwa Kitele mpaka Mtwara Mjini.
Je, Serikali iko tayari hivi sasa kutekeleza mpango wa muda mfupi wa kuchimba visima kwa kutumia gari za Idara ya Maji ambazo zipo pale Mtwara katika maeneo ambayo maji hakuna kama Kata ya Ufukoni na Likombe?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali inaendelea kuhakikisha kwamba Mji wa Mtwara unapata maji safi na salama. Mwezi uliopita tumesaini mkataba wa shilingi bilioni tano ambao utatoa maji Mbuo kwenye Bonde la Kitele kupeleka mjini. Kwa bahati nzuri Mheshimiwa Mbunge wewe ni Mbunge wa Mji wa Mtwara, kwa hiyo, maeneo yote ambayo yalikuwa hayajapata maji safi tunahakikisha kwamba yanapata hata kabla ya huo mradi mkubwa wa kutoa maji Mto Ruvuma kuleta Mtwara Mikindani.
Mheshimiwa Spika, pia kuhusiana na huu mradi mkubwa wa kutoa maji Ruvuma, tayari Serikali iko kwenye hatua za mwisho kukamilisha mazungumzo na Exim Bank ya China ili sasa utekelezaji uanze. Kwa hiyo, nikuombe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba uvute subira Serikali yako kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji inaendelea kuzungumza na hawa wafadhili kwa maana ya Waziri wa Fedha (Hazina) wanaendelea kuzungumza na mfadhili ili mambo yakikamilika tuanze utekelezaji.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pia nashukuru kwa majibu sahihi ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri kazungumza hapa kwamba Bandari hiyo ya Mtwara ndiyo itakuwa chanzo cha ufunguzi wa kitu tunachoita Mtwara Corridor, maendeleo ya Kusini mwa Tanzania na Afrika kwa ujumla. Naomba kujua kwamba hili gati linajengwa hivi sasa ni gati moja tu. Mkakati wa Serikali ukoje kuhakikisha kwamba wanamaliza ujenzi wa magati matatu yaliyobaki ili yaweze kukamilika magati manne?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, naomba kujua kwa kuwa Bandari ya Dar es Salaam hivi sasa ina msongamano mkubwa sana na Mtwara sasa hivi hii bandari inajengwa. Je, Serikali ipo tayari hivi sasa kuhakikisha kwamba inapunguza cargo on transit kutoka Bandari ya Dar es Salaam waweze kuruhusu Bandari ya Mtwara ili kuweza kuondoa msongamano hivi sasa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, magati matatu yaliyobakia mpango wake wa kujengwa kwanza tunataka kushirikisha Sekta Binafsi lakini vile vile kwanza tunataka tuhakikishe kwamba gati hili moja na kwa namna mizigo ilivyo kwa sasa tunadhani kwamba linatosha kwa muda mfupi na wa kati. Baada ya hapo ikishafunguliwa ile reli ya kutoka Mtwara mpaka Mbamba Bay kwa vyovyote vile gati hizi nne lazima ziongezeke. Kwa hiyo, nimshukuru kwa swali hilo, nimepata fursa ya kutoa ufafanuzi zaidi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Bandari ya Mtwara kutumika kama mbadala wa Bandari ya Dar es Salaam; sababu mojawapo ya kupanua hii gati kama tulivyosema hili gati ni la urefu wa mita 350, ni kubwa sana ili liweze kuruhusu meli kubwa sana ziweze kutia nanga Mtwara. Moja kati ya sababu ni hiyo, kwamba meli zingine kubwa ziweze kutua Mtwara badala ya muda wote kufikiria kuingia Dar es Salaam.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza swali langu halijajibiwa. Niliuliza kwa nini Serikali haisemi ukweli ndani ya Bunge? Kwa sababu hapa nina Hansard mbili Serikali ikiahidi kulipa fidia wananchi hawa, lakini pia kuna maelezo ambayo siyo sahihi sana kwenye maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Serikali hii ya Awamu ya Tano inafanya mambo makubwa sana, imeweza kununua ndege, imeweza kuwa na mkakati wa kujenga standard gauge, lakini pia imeweza kuweka mkakati wa kujenga Stiegler’s Gorge, inashindwaje kulipa fidia ya shilingi bilioni nane kwa wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini maeneo ya Mjimwema? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, naomba kujua, katika kuilazimisha Halmashauri sasa kuwaeleza wananchi waweze kupimiwa viwanja, wapo wananchi waliokubali na wengine hawajakubali. Je, kwa kuwa hili suala la Taasisi ya UTT-PID ipo ya chini ya Serikali Kuu, Serikali iko tayari hivi sasa kuja Mtwara Mjini na kuweza kutoa elimu kwa wananchi hao wa Mjimwema na Tangira ili waweze kukubaliana na maamuzi ya Serikali? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kutokana na swali lake jinsi alivyouliza, majibu ya Serikali ni sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, alitaka kujua kwa nini Serikali haisemi ukweli Bungeni juu ya fidia ya wananchi wa Mtwara? Na sisi tumeongelea habari ya fidia aliyoitaka ya UTT. Mpaka sasa hivi anavyozungumza UTT haidaiwi kulipa fidia yoyote kwa wananchi wale kwa sababu tayari Manispaa imeshachukua mradi ule na zoezi limeshaanza na wananchi wanapimiwa na kuna makubaliano ambayo wameingia kati ya wananchi na Manispaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kule hakuna anayedai fidia, kwa maana hiyo, kwa sababu tayari baada ya UTT kujitoa wananchi kupitia Halmashauri yao wameamua kuchukua eneo lile na kuanza kupimiwa na viwanja wanapewa kama sheria inavyosema. Kwa hiyo, Serikali imejibu kulingana na swali lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili analotaka habari ya kutoa elimu, sisi tuko tayari wakati wowote tunatoa elimu, tuna vipindi mbalimbali na hata wakitaka twende kule tutakwenda kwa sababu ndiyo kazi yetu kuelimisha wananchi ili waweze kuelewa haki zao za msingi na waweze kufanya mambo yao pasipo kubughudhiwa.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kumekuwa na ahadi nyingi sana na za muda mrefu kwenye mitaa ya pembezoni mwa Manispaa ya Mtwara Mikindani ambayo hakuna mawasiliano maeneo hayo na nimekuwa nikichangia ndani ya Bunge hili na kuyataja maeneo hayo kwa muda mrefu kwamba maeneo ya Namayanga, maeneo ya Naulongo, Mkunjanguo, Mbawala Chini na Mkangara, mawasiliano hayapo kabisa ya simu. Je, ni nlini Serikali hii itapeleka mawasiliano kwenye mitaa hii ambayo ni muhimu ndani ya Manispaa ya Mtwara Mikindani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli mahitaji ni mengi ni kweli ahadi ni nyingi, lakini ni ukweli pia kwamba ahadi nyingi tunaendelea kuzitekeleza kadri tunavyokwenda.
Nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla, kadri tunavyoweka minara katika maeneo mbalimbali na baada ya minara kuwashwa bado tunahitaji kuona changamoto ambazo zitakuwa zimejitokeza baada ya hii minara kuwashwa kwa sababu suala la mawasiliano ni suala ambalo baada ya kuwasha minara inaweza ikajitokeza baadhi ya maeneo yakawa na uhafifu wa mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niwaomba tu tuendelee kuwasiliana pamoja tunavyoendelea kutekeleza ahadi hizi. Lakini pia tuendelee kupata feedback baada ya minara kuwashwa ili tuhakikishe kwamba maeneo yote yanafikiwa na mawasiliano haya kupitia minara yetu.
MHE. MAFTAH A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mtwara Mjini kuna Mradi wa Maji ambao unatekelezwa na Serikali kutoa maji Kijiji cha Lwelu kuelekea Kata za Ufukoni, Magomeni na maeneo mengine ya Mtwara Mjini lakini mkandarasi yule anasuasua sana na tayari kasha-rise certificate Wizara bado haijamlipa na mradi umesimama. Je, Serikali inatoa kauli gani ili kuhakikisha mkandarasi yule analipwa na mradi ule unaendelea haraka ili wananchi wa Mtwara Mjini wapate maji? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tuna miradi mingi hapa nchini inaendelea na huu mradi wa Mtwara tunaufahamu vizuri na kila mwezi sisi tunaendelea kulipa, hata leo tunafanya malipo kwa wakandarasi. Tutahakikisha kwamba na mkandarasi huyo tunamlipa ili aweze kuendelea kumaliza kazi hiyo ili wananchi wa Mtwara Mjini waweze kupata maji safi na salama. (Makofi)
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Serikali ina wajibu wa kulinda mipaka yake yote ya nchi hii kwa ajili ya kujilinda na maadui mbalimbali wanaovamia ndani ya nchi yetu na ili uweze kulinda mipaka ni lazima kuwe na barabara kwenye mipaka yote, barabara ambazo zinapitika kwa muda wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka wa kusini unaoanzia Mtwara Mjini kupita Mahurunga – Kitaya – Tandahimba – Newala mpaka Ruvuma, hii barabara ilipandishwa hadhi kwa muda mrefu sasa na inaitwa Barabara ya Ulinzi. Mpaka leo Serikali inasuasua kujenga. Naomba kujua ni lini barabara hii ya ulinzi ambayo nimeitaja itajengwa kwa kiwango cha lami ili kulinda mpaka wa kusini sawasawa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba barabara zote za mipakani ndani ya nchi yetu ziko kwenye mpango wa kutengenezwa kwa kiwango cha lami na barabara hiyo aliyoitaja Mheshimiwa Maftaha ikiwemo. Nimhakikishie Mheshimiwa Maftaha kwamba upembuzi yakinifu umeshafanyika na usanifu wa kina tayari umekwishafanyika. Sasa hivi tuko kwenye taratibu za kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara husika.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa sababu Serikali imeweza kutambua angalau kwamba kuna shilingi milioni 92.4 ambazo Manispaa ya Mtwara Mikindani inadaiwa, kwa maana ya shule za msingi na shule za sekondari. Naomba kuuliza maswali yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Shule ya Sekondari Sabasaba, Raha Leo, Chikongola na Shule zote za Msingi za Manispaa ya Mtwara Mikindani zinadaiwa hizi stationery kabla Serikali haijaanza utaratibu wa kupeleka elimu bure. Siku za nyuma ilikuwa michango inakusanywa kupitia kwa wazazi then zinalipwa stationery hizi ambazo zinatumika katika shule za msingi na sekondari. Ni lini Serikali italeta hizi shilingi bilioni 92.4 kwa ajili ya kulipa kwenye hizi shule ambazo zinadaiwa pale Mtwara Mjini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Mkuu wa Shule ya Sekondari na Mwalimu Mkuu wa Shule za Msingi ndiyo wanaobeba haya madeni kama yao, ni declare tu interest nilikuwa Mkuu wa Shule, nafahamu kila Mkuu wa Shule anavyotembea anadaiwa yeye. Je, Serikali inawasaidiaje hawa Wakuu wa Shule za Sekondari na Walimu wa Shule za Msingi ili haya madeni yasionekane kama ni ya kwao yawe ni madeni ya Serikali na Serikali iweze kulipa kwa wakati? Ahsante (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tumekiri kwamba Serikali kweli inadaiwa madeni hayo lakini utaratibu wake bado una mchakato ambapo tunahitaji kuyaangalia kwa undani zaidi madeni hayo. Ndiyo maana tumesema kwanza kuanzia Mwalimu Mkuu ajiridhishe na hayo madeni aandike barua kwa Mkurugenzi wa Halmashauri kwamba nimeridhika kwamba madeni haya ni halali. Mkurugenzi wa Halmashauri alete tena kwetu tuyaangalie tena baadaye tutapeleka Wizara ya Fedha madeni ambayo tulishajiridhasha tena kwa mara nyingine sisi kwamba hayo ni halali halafu Serikali itaweka utaratibu wake vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili kwamba tunawasaidiaje Wakuu wa Shule, wao wenyewe hasa wale waliokuwepo na Mheshimiwa Nachuma ulikuwepo na wewe umezalisha kumbe hayo madeni. Sasa wewe utakuwa shahidi mzuri vilevile katika kutuhakikishia kwamba madeni hayo ni halali. Kweli kama waajiriwa wetu Walimu Wakuu tumewakabidhi dhamana kubwa kwanza hatutaki waendelee kuzalisha madeni mengine kwa sababu sasa hivi tunapeleka fedha. Atakayezalisha deni lolote kuanzia sasa hivi itakuwa ni wajibu wake kulilipa kwa sababu tunapeleka hela sasa hivi. Kwa hiyo, kwa yale ya zamani tunaandaa huo mchakato kama nilivyokueleza katika swali la kwanza ili kusudi tuweze kuwaondolea huo mzigo wa madai.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Manispaa ya Mtwara Mikindani ina mitaa mingi ambazo nguzo za umeme hazijafika na nimekuwa nikiitaja hapa Bungeni kwa muda mrefu sana, kwa mfano, Kijiji cha Mbwala Chini, Mtaa wa Naulongo, Mkunja Nguo, Kata ya Magomeni, Kata ya Ufukoni na Kata ya Mitengo maeneo mengi hayana nguzo za umeme. Nilikuwa naomba kujua kwa sababu nimeongea kwa muda mrefu ndani ya Bunge hili, kwa nini Serikali haitaki kuwapatia wananchi hawa umeme? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Maftaha, lakini kusema kwamba Serikali haitaki, siyo kweli, ukweli ni kwamba Serikali inataka kuwapelekea umeme wananchi wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Mbunge, wiki iliyopita niliongea naye, Kijiji cha Mkunja Nguo tayari mkandarasi tumeshamtuma na ameshafanya survey. Maeneo mengine ya Mbwala Chini bado wanafanya survey. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge maeneo yote ya Mtwara Mjini ambayo ameyataja yatapelekewa umeme na mara baada ya Bunge hili tutakwenda kukagua. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge vijiji 12 na mitaa nane ya Mtwara Mjini tutaipelekea umeme kupitia mradi huo unaoendelea.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Wakati tunapitisha bajeti hapa nilizungumza juu ya barabara muhimu sana Kanda ya Kusini inayopita mikoa yote ya Kusini, kwa maana ya Lindi, Mtwara na Ruvuma, barabara ya Ulinzi. Kwa kuwa bajeti haijasema chochote juu ya barabara hii kwamba imetengewa kiasi gani, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara hii ili huu mpaka wa Kusini unaoanzia Mtwara Mjini maeneo ya Mahurunga, Kitaya, Tangazo, Tandahimba, Newala mpaka kule Ruvuma uweze kulindwa sawasawa pale ambapo maadui wa nchi hii wanaweza wakatokea? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maftaha, Mbunge wa Mtwara Mjini maarufu kama Gas City, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua umuhimu wa barabara hii ya ulinzi. Sisi kama Serikali ambacho tunakifanya kabla hatujaja kuboresha barabara iwe kiwango cha lami, tunahakikisha inapitika muda wote. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Mtwara kwa ujumla tunahakikisha kwanza barabara hii inapitika lakini kwenye strategic plan zetu za Wizara tumeitazama. Labda tu akipata nafasi tuzungumze ili tuangalie tumeipanga lini tutakuwa kwenye hatua ya lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi msukumo mkubwa ilikuwa ni kuhakikisha hii barabara inayotoka Mtwara Mjini - Mnivata - Tandahimba - Newala - Masasi inakamilika kwa kiwango cha lami. Ukiwa Tandahimba iko barabara inakwenda kuungana na barabara hii ya msingi, lakini kama alivyosema ukiwa Newala kiko kipande kinakwenda kuungana na barabara hii, kwa hiyo, barabara hii kubwa ikikamilika basi tutaweza kuzingatia na hii barabara ya msingi kuhakikisha inajengwa kwa kiwango cha lami. Tuonane tuangalie kwenye mipango ya Wizara ni lini tutakwenda kwenye hatua ya lami.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, asante. Nashukuru kwa majibu mafupi na precise ya Mheshimiwa Naibu Waziri, hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa utaratibu wa manunuzi ni mchakato na majibu yake hayajaeleza kwamba exactly timeframe ni lini Serikali imempa huyu mkandarasi kukamilisha mchakato wake ili ujenzi na ukarabati uanze mara moja.
Sasa nilikuwa naomba kupata majibu kwamba ni lini hasa, ni baada ya miezi mingapi huyu mkandarasi atakuwa amemaliza?
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na utaratibu huko miaka ya nyuma kwamba baadhi ya vitu vinahamishwa mikoa ya Kusini na baada ya uhuru tu mapema ilihamishwa reli lakini pia na taa za Uwanja wa Ndege wa Mtwara. Sasa nilikuwa naomba kujua kwamba ukarabati ambao unatarajiwa kufanyika katika uwanja huu utahusisha pamoja na uwekaji wa taa za kuongozea ndege ambazo zilizoondolewa miaka ya nyuma? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza niseme ujenzi umeshaanza kwa sababu ujenzi una hatua mbalimbali, kwenye hatua hii mpaka mkataba umesainiwa na tumepata fedha nyingi. Kwa taarifa tu Mheshimiwa Nachuma awali tulikuwa tunakadiria tufanye matengenezo kwa shilingi zipatazo bilioni 39 lakini kwa kuzingatia maboresho na kufanya uwanja uwe na uwezo wa kupokea hata ndege Airbus aina ya A340-200 kwa hiyo, tumezingatia, huwezi kupokea ndege hii bila kuwa na taa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kutakuwa na barabara na kutua na kurukia zenye urefu wa mita 3,000, kutakuwa na maegesho ya ndege, kutakuwa na barabara za kuingilia katika uwanja na jengo la abiria lakini kuweza kutua ndege kubwa kama nilivyosema lakini pia taa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Nachuma usiwe na wasiwasi kwamba ule uwanja nafikiri miezi 20 ijayo utaona huduma zimeongezeka na utaendelea ku-enjoy huduma za ndege.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, asante, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini bado kuna changamoto moja ameiacha katika Korosho ambayo ni changamoto ya malipo kwamba mpaka leo Serikali inasuasua kuwalipa Wakulima waliouza Korosho zao. Wapo Wakulima ambao wamepeleka Korosho zao ghalani lakini wamelipwa pesa ambayo haikidhi au hailingani na kiwango walichopeleka. Lakini pia wapo Wakulima ambao mabodi display zinaonesha kwamba wamelipwa tayari lakini wakienda benki pesa hizo hazipo, kwa hiyo kuna malipo hewa. Kwa hiyo, nilikuwa naomba kujua Serikali kwa nini haielezi ukweli juu ya malipo ya Korosho kwa Wakulima wa Korosho.

Mheshimiwa Spika, swali la pili nilikuwa naomba kujua kwamba Serikali imekusanya Korosho hizi zikawekwa kwenye maghala Mtwara na Lindi na maeneo mengine na Korosho zinahifadhiwa haizidi miezi mitatu, Korosho zimeanza kuota hivi sasa zingine. Je, Serikali haioni kwamba inalitia hasara Taifa hili kwa kuziweka Korosho hizi bila kuzibangua?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kujibu swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Nachuma. Kwanza sisi kama Serikali au Taasisi ya Serikali iliyopewa jukumu hili bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko tunalipa pesa kwa wakulima, na mpaka jana kiasi cha Korosho tulizokusanya ni zaidi ya tani laki mbili kumi na tatu na tumeshafanya uhakiki zaidi ya tani laki moja na ishirini na tisa na tani laki moja na kumi na sita ndizo tulizozilipa.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu Mheshimiwa Mbunge ajue kufahamu kwamba malipo hatuwezi kuanza kulipa kabla ya kujiridhisha katika uhakiki na pesa hii niwahakikishie kwamba pesa zipo na mimi mwenyewe na Mheshimiwa Waziri Mkuu tumetoka juzi huko ambao kulikuwa kweli na changamoto hasa kwenye malipo ya daraja la pili ambao mwanzo pale tuliona mkazo kuanza daraja la kwanza lakini kuanzia jana wameanza kulipwa pia na Korosho daraja la pili hasa Mikoa ya Pwani na Mikoa ya Tanga.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anazungumzia kuhusu hasara ambayo kwa kuweka Korosho muda mrefu, kwanza ni kweli Korosho sio kama zabibu kwa sababu zabibu ukiiweka muda mrefu ndio ukali wake unaongezeka lakini Korosho kila unavyoiweka ubora wake unazidi kushuka. Hilo tunalifahamu na ndio maana tumeshaingia mikataba na wabanguaji wa ndani wameshaanza kubangua na sasa hivi tuko kwenye mazungumzo ya mwisho kwa ajili ya kuuza tani zaidi ya laki mbili kwenye masoko ya Kimataifa muda sio mrefu Korosho zitaanza kusafirishwa nje ya nchi.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa kumekuwa na operesheni ambayo inafanywa na Jeshi la Polisi ya kusaka watu ambao wanasema hawana kazi mtaani. Cha ajabu hawa watu wanakamatwa kipindi kile cha jioni tayari wamesharudi makazini wakiwa wamepumzika barazani huko Dar es Salaam na maeneo mengine ya Tanzania hali ambayo inapelekea kujaza mahabusu zetu katika maeneo mengi ya nchi hii. Serikali inatoa tamko gani kuhusu operesheni hii inayofanywa na Jeshi la Polisi ambayo inapelekea kujaza mahabusu bila sababu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maftaha, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina taarifa ya maelezo ambayo ametoa Mheshimiwa Mbunge kwamba Polisi wanachukuwa mtu yeyote. Nachojua katika utaratibu wa kawaida wa Jeshi la Polisi ni kufanya doria na pale wanapoona watu wanaojihusisha na uhalifu ama wana viashiria vya uhalifu kuwachukuwa na kufanya uchunguzi wao ili hatua zaidi zichukuliwe. Taarifa za ziada kwamba kuna watu ambao anadhani yeye hawakupaswa kuchukuliwa na Jeshi la Polisi kutokana na shughuli hiyo, labda angetupatia taarifa mahsusi ili tuweze kuzifanyia kazi.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Naomba kujua mara nyingi nimekuwa naongea Vijiji vya Manispaa ya Mtwara Mjini nimekuwa nikivitaja vijiji hivi katika Bunge hili miaka yote mitatu na Serikali ikiwa inaahidi kwamba, inatekeleza suala la kupeleka umeme. Vijiji hivi ni Mkangara ambako Naibu Waziri alishaenda kule na akaona hali halisi, Naulongo, Mkunjanguo, Namayanga na maeneo…

NAIBU SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa Maftah, uliza swali.

MHE. MAFTAH A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujua kwa nini Serikali haitaki kutenga bajeti ili kupeleka umeme katika vijiji hivi au mitaa hii?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maftaha kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo yeye mwenyewe amekiri kwenye swali lake la nyongeza kwamba, mimi hata pamoja na Waziri wa Nishati tumeshafanya ziara zaidi ya mara mbili katika Mkoa wa Mtwara. Maeneo ambayo ameyataja ikiwemo Mkangara, Chipuputa na Mheshimiwa Mbunge atakubaliana na mimi hata TANESCO Mkoa wa Mtwara imekuwa ikijitahidi kufanya miradi. Nilipofanya ziara mwaka jana zaidi ya mitaa saba TANESCO imefanya miradi, lakini kwa eneo maalum ambalo ni maeneo aliyoyataja yameshaingia kwenye mpango wa utekelezaji wa mradi wa ujazilizi unaoanza Machi, 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, hata alipofanya ziara Mheshimiwa Waziri wa Nishati pia ametoa maelekezo yale ambayo tuliyaelekeza siku za nyuma na kwa kuwa Mtwara imepitiwa na bomba la gesi na Serikali ilitoa punguzo kwa ajili ya kuwasambazia umeme wananchi wa maeneo ya gesi na mitaa mingi ipo katika Mtwara Mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge ambaye amekuwa akifuatilia mara kwa mara kwamba, vijiji, mitaa aliyoitaja na vijiji katika Manispaa ya Mtwara Mikindani na maeneo ya Mtwara vitapatiwa umeme na kazi zinaendelea na mradi wa ujazilizi utaanza mwezi Machi, 2019. Ahsante sana.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kumekuwa na utaratibu wa hizi AMCOS zetu kuajiri ama kutokuwa na vigezo vya wale ambao wanaajiriwa kwamba hawawekewi elimu ni kiwango gani na kwa kiasi kikubwa wahasibu ndiyo wanakuwa ni watu pekee wenye elimu kiasi ambacho kinapeleka kufanya hujuma nyingi sana kwenye hizi AMCOS. Naomba kujua Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba wale ambao wanafanyia kazi hizi AMCOS wanawekewa vigezo vya kielimu ili wakulima wasiweze kuibiwa kama ilivyo hivi sasa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maftaha, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Serikali tulishaanza mpango huo tangu msimu uliopita kwa mfano Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru tulianza kuajiri Wahasibu wenye degree moja na kuendelea kwa ajili ya kuongoza vile vyama vya ushirika. Utaratibu ule tutaendeleza nchi nzima kupitia vyama vyote vya ushirika ili tupate Wahasibu wenye weledi ili kuweza kuwahudumia wakulima wetu.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kuna Wilaya ambazo zina Majimbo mawili na Wilaya hizi ziligawanywa Majimbo kwa sababu ya ukubwa wa zile Wilaya na idadi kubwa ya watu, lakini hivi sasa kuna tetesi ambazo zinatembea chini kwa chini huko Serikalini kwamba yale Majimbo ambayo yaligawanywa kutokana na ukubwa lakini pia na wingi wa watu yanataka kurudishwa kuwa Jimbo moja moja.

Je, kama hilo ni kweli, hatuoni kwamba Serikali ita-hinder utendaji wa Majimbo hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa
Mwenyekiti, kama Mbunge mwenyewe alivyoli-phrase swali lake kwamba ni tetesi, naomba nami kwa upande wa Serikali tusijibu tetesi, ikiwa rasmi itasemwa kama ni rasmi.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza imeelezwa kwamba TFDA ndiyo Mamlaka ambayo inashughulikia chakula na dawa, lakini kwa hali ya uhalisia TFDA yenyewe capacity yake ni ndogo sana ya kuweza kupima vinasaba vyote Tanzania nzima kwa sababu Ofisi yao Kuu iko pale Dar es Salaam na wana vifaa vichache sana.

MWENYEKITI: Uliza swali.

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, je, ni lini Serikali itaiongezea vifaa TFDA iweze kufanya kazi yake sawasawa nchi nzima?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna dawa pia ambazo inasemekana na wataalam wa afya, kwamba zinapelekea kuharibu miili ya binadamu na hasa zile dawa za kufanya rangi ya watu weusi iweze kuwa nyeupe, je, Serikali imechukua hatua gani mpaka hivi sasa ili kuwafanya Watanzania wengi wanaotumia dawa hizi wasiweze kupata madhara?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA (K.n.y. WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maftaha kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nimhakikishie kwamba uwezo wa TFDA sio mdogo kama anavyodhani, Taasisi hii ni kubwa, ina Maabara ya kisasa sana pale Dar es Salaam lakini pia imeanza kujenga uwezo Kikanda na sio kwamba wanafanya kazi Dar es Salaam peke yake, wako katika Kanda mbalimbali katika nchi yetu, na wana maabara inayotembea, (mobile lab) kwa maana hiyo nadhani uwezo wao ni mzuri na wataendelea kuuboresha ili kuweza kufika nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la dawa ambazo zinasababisha au tunaziita hizi dawa za kujichubua, ili watu wabadilike rangi zao, hili napenda nimwarifu Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu, kwamba TFDA imekuwa ikichukua hatua mara nyingi sana. Dawa nyingi sana zimeshaondolewa kwenye soko zenye madhara haya na hizi mara nyingi ni dawa ambazo zina maada inayoitwa steroid ambazo kwa kweli zinaharibu ngozi na zinaweza kusababisha madhara makubwa, zimekuwa zikiondolewa na wahusika wamekuwa wakipigwa faini na kwa maana hiyo sasa hivi kuna udhibiti mzuri sana wa dawa zinazosababisha madhara haya.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Mtwara kimejengwa enzi ya Mkoloni na hivi sasa ukiingia mle ndani kinakaribia kubomoka, kinauliza kabisa niue nikuache, niue nikuache? Kila mwaka tunazungumza ndani ya Bunge na Serikali inasema imetenga bajeti. Kwa nini mpaka leo Serikali haileti fedha kwa ajili ya kukarabati kituo hiki ambacho hivi sasa kinatarajia kubomoka?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maftaha Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu yatakuwa ni yale yale tu kwamba vituo vinavyohitaji kukarabatiwa ni vingi ikiwemo hiki cha Mtwara Mjini. Hata hivyo, kwa sababu kituo hiki nakifahamu na gharama zake za ukarabati si kubwa sana pengine mimi na Mheshimiwa Mbunge wakati tukisubiri hali ya bajeti ikae vizuri tushauriane ikiwezekana hata kwenda pamoja jinsi ya kutafuta njia zingine mbalimbali za kusaidia kukiweka vizuri kituo hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya hivyo katika maeneo mbalimbali nchini kwa kutumia rasilimali nyingine nje ya kibajeti. Nina hakika kwa gharama ndogo za ujenzi zinazohitajika katika kituo hicho tunaweza tukafanikiwa tukashirikiana. Naamini Mheshimiwa Maftaha ni mchakapazi kwa hiyo, hata nikimshawishi na yeye kupitia fedha za Mfuko wa Jimbo achomoe kidogo halafu tushirikiane kutafuta wadau basi tutaweza kukitendea haki kituo hiki.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; ili haya makampuni ya kihandisi yapate usajili, inasemekana na wahandisi wenyewe kwamba kumewekwa tozo kubwa sana na hii Bodi. Je, Serikali iko tayari hivi sasa kupunguza tozo hizo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ili uweze kujenga nyumba, angalau ghorofa moja Tanzania ni lazima upate vibali vya makampuni ya kihandisi na vibali hivyo ni lazima uwe na kibali cha architect, structure, quantity QS, Contractor na pia ulipe malipo ya halmashauri na TRA. Sasa, je Serikali haioni kwa sababu ili upate vibali hivi, fedha ya tozo ya vibali vya wahandisi inaizidi fedha uliyokuwa nayo ya ujenzi. Je, haioni kwamba Serikali kwa kuruhusu suala hili wananchi wengi wanashindwa kujenga nyumba bora nzuri?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nachuma almaarufu kama Mashine ya Kusini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze tu Mheshimiwa Nachuma kwa kuwa mfuatiliaji mzuri, lakini kwa sababu huyu Mheshimiwa ni Mwalimu niombe tu hata baada ya majibu yangu, baadaye pia nikusheheni documents za kutosha ili kwanza aone kazi nzuri ambayo bodi inafanya, lakini pia aweze kuona umuhimu wa kutumia taaluma hii. Taalum hii ni muhimu sana kwa sababu katika ujenzi lazima weledi uzingatiwe ili kuhakikisha kwamba hizi rasilimali zinazojengwa, majengo na huduma zingine kwa sababu bodi hii inasimamia wahandisi wa aina tofauti; wako wahandisi wa umeme, majengo, wako ma-technician na makundi mbalimbali. Kwa hiyo aone kazi hii kubwa inafanyika na kazi inafanyika vizuri. Pia Bodi hii inafanya kazi ya kusimamia zoezi zima la uadilifu katika sekta hii, lakini vile vile inasimamia kuhakikisha kwamba hata usalama unakuwa wa hali ya juu katika ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kujibu swali lake, anaona kwamba tozo ni kubwa. Ziko bodi m balimbali, kwa ulinganifu naona kwamba tozo ambayo inatozwa na bodi hii ukiwianisha na bodi zingine tofauti, sio ukubwa. Labda Mheshimiwa Mbunge tutaweza kuzungumza tuone ushauri wake unalenga nini ili tuone kama kutakuwa na jambo la kufanya kazi tutafanyia kazi, lakini kimsingi ukilinganisha tozo inayotozwa na huduma inayotolewa na gharama za rasilimali ambazo zinafanyika, kwangu naona kwamba bado ilikuwa ni reasonable na kwa muda mrefu hatujapata malalamiko mbalimbali kutoka kwa wateja ambao wanahudumiwa na bodi hii, lakini nalichukua pia kwa ajili ya kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vibali mbalimbali, kila tozo zinazotozwa kwenye vibali hivi, vingi amevitaja Mheshimiwa Mbunge inakuwa na sababu zake, lakini nijikite tu kwenye eneo hili kama nilivyosema, tutajaribu kuangalia lakini kwa sababu ziko taasisi mbalimbali zinatoza, tunaweza tukaangalia tuone kama kutakuwa na tozo ambayo itakuwa inaleta meaning moja basi hizo tutazifanyia kazi tukishirikiana na wenzetu ili tuhakikishe kwamba kusiwepo na tozo ambayo inafanana na madhumuni ya tozo nyingine ili tuwe na tozo ambazo kimsingi zitakuwa zinalenga kutoa huduma ambayo tumelenga tukusanye ili tuweze kufanya kazi nzuri kuhakikisha kwamba taaluma hii inawatendea haki Watanzania na kuimarisha uchumi na asset ambazo zinajengwa.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; hivi sasa Manispaa ya Mtwara Mikindani kumekuwa na baadhi ya Viongozi wa vyama vya siasa wa wilaya na mkoa ambao wameweza kuratibu vikundi mbalimbali kwa ajili ya kufanya uhalifu kwenye uchaguzi unaotarajia kufanyika mwaka huu 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, je Serikali Mheshimiwa Waziri yuko tayari hivi sasa kuja Mtwara kuweza kuchukua ushahidi ambao nitampatia kwa mikono yangu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili Manispaa ya Mtwara Mikindani kuna baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wanachukua na kuwatumia baadhi ya askari polisi kwenda kuwafanyia hujuma Wapinzani usiku saa nane, saa tisa na kuwagongea majumbani kwao na kuwakamata bila sababu yoyote ya msingi na kwenda kuwaweka ndani eti kwa sababu tu wanafanya kazi ya kunadi Chama cha Wananchi - CUF na vyama vingine vya Upinzani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali iko tayari hivi sasa kuwachukulia hatua Askari wa aina hiyo wanaotumika kwa ajil ya Chama Tawala? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maftaha Nachuma kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza ameuliza kama nipo tayari kwenda kuchukua ushahidil; nimuhakikishie kwamba niko tayari kufanya hivyo kama ushahidi huo ni kweli anao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ametoa tuhuma nzito kwa Jeshi letu la Polisi kwamba linashirikiana na vyama sijui chama gani. Mimi nimuhakikishie Mheshimiwa Maftaha na Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla kwamba tunavyotambua na ilivyo kabisa, si tunavyotambua, na uhalisia ulivyo, Jeshi letu la Polisi kwa kiwango kikubwa wanajitahidi kufanya kazi zake kwa kufuata weledi, sheria na maadili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa kuwa yeye Mheshimiwa Maftaha ambaye mimi ninamheshimu sana kama ni miongoni mwa viongozi wasio wengi sana makini wa upinzani anaweza kusema ana ushahidi wa jambo kama hilo wa tuhuma hizo nzito; imani yangu ni kwamba nitakapokuwa nimeambatana naye kama alivyoomba katika swali lake la msingi basi atatupatia ushahidi huo ili tuweze kuchukua hatua. (Makofi)
MHE. MAFTAH A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nimekuwa nayataja maeneo kadhaa ambayo yapo jimbo la Mtwara mjini kwa muda mrefu ndani ya Bunge hili na maeneo hayo, Naulongo, Mkunjanguo, Namayanga, na Mbawala Chini ambapo hakuna mawasiliano ya simu kabisa. Nilikuwa naomba commitment ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba ni lini atafanya ziara ya Mtwara Mjini kuja kukagua mguu kwa mguu maeneo haya ili aweze kudhibitisha kwamba maeneo haya yanahitaji mawasiliano kwa simu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge anaomba nifanye ziara katika Mkoa wa Mtwara na sisi unafahamu Mheshimiwa Mbunge tuna miradi mingi sana ambayo Wizara yangu inasimamia, nitafanya ziara mapema baada ya Bunge hili katika Mkoa huu wa Mtwara.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri pale Mtwara Mjini Manispaa ya Mtwara mjini nimekuwa naulizia barabara kwa muda mrefu barabara ya kutoka Mikindani, Lwelu mpaka Dimbuzi lakini barabara ya kutoka kata ya ufukoni, Mbaye mpaka Mbawala chini. Lakini barabara ya kutoka Mtawanya mpaka Namayanga. Barabara hizi nimekuwa nikizungumza ndani ya Mbunge hapa kwa muda mrefu na hivi sasa TARURA imekuwa inasuasua kuzitengeneza barabara hizi ambazo ni muhimu kwa wananchi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuzitengeneza barabara hizi kwa kiwango cha lami?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuchukue jambo hili kama ulivyosema Mheshimiwa Mbunge. Lakini naomba kuweka takwimu sawa kwamba katika maeneo ambayo tumeyapa kipaumbele sana ni Mtwara Mikindani. Katika mpango wetu wa miji mikakati, miji ile ambayo nane ambayo inahusisha Tanga, Dar es Salaam, Arusha, Dodoma, Ujiji lakini vilevile Mikindani ipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndio maana leo ukiangalia ya miaka mitano iliyopita na Mtwara ya leo ni vitu tofauti. Lakini huwezi ukafanya mambo yote kwa siku moja, imani yangu Serikali tutaendelea kupambana lengo kubwa ni kuwahudumiwa wananchi hasa wa Mtwara mikindani na maeneo mengine waweze kuhakikisha barabara zao zinapitika kwa wakati wote.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na matengenezo ya mara kwa mara ambayo hayakidhi haja ya barabara kubwa inayotoka Mtwara Mjini mpaka pale Mnazi Mmoja, Manispaa ya Lindi kwa sababu barabara hii imekuwa inaharibika sana kwa magari yanayosafirisha saruji kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam na Serikali inaahidi kutengeneza kwa kiwango kikubwa lakini mpaka leo barabara hii ina mashimo, wanaweka viraka vidogo vidogo lakini hairekebishwi vile ambavyo inatakiwa kujengwa.

Je, ni lini Serikali inatekeleza ahadi yake ya kutekeleza na kutanua barabara hii kwa kiwango cha lami kutoka Mtwara Mjini mpaka Mnazi Mmoja na kule Nanganga?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli barabara hii ya kutoka Mtwara kuja Mnazi Mmoja - Mingoyo inatumika sana na magari makubwa ambayo yanabeba mzigo mkubwa hususan saruji, na ni kweli barabara hii nimeipita ina mashimo na tunaendelea kuyaziba hayo mashimo ili huduma iweze kurejea, lakini Mheshimiwa Mbunge utakubaliana na mimi kwamba barabara hii imedumu kwa muda mrefu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara zina umri wake na barabara ndiyo maana zinaendelea kuhudumiwa lakini barabara ukiikuta imekaa zaidi ya miaka 30 inastahili sasa hiyo barabara tuibadilishe kabisa kwa sababu ndiyo maana unaona ukiziba hapa sehemu nyingine inafumuka kwa sababu ule muda wa kuishi wa barabara hii umetimia.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nikuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba uko mpango kabambe ambao tutakuwa na mradi wa World Bank ambao taratibu zinaendelea vizuri kwamba tutaifanyia matengenezo na kuijenga upya barabara hii kutoka Mtwara kuja Mnazi Mmoja kwa maana hiyo na kutoka pia Mnazi Mmoja kwenda mpaka Masasi kwa hiyo upo mradi unaendelea vizuri. Kwa hiyo wewe uwe comfortable hatua zinaenda vizuri. Wakati ukifika utaona tunaenda kufanya maboresho makubwa ya barabara hii muhimu na mahitaji ya matumizi ya barabara hii sasa hivi yameongezeka sana, hali ya Mtwara sio kama zamani, utakubaliana na mimi kwamba tunaitazama kwa macho mawili.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza kwa kuwa hawa Wenyeviti wa Serikali za Vijiji na Mitaa wanafanya kazi inayofanana kabisa na hawa Watendaji wa Vijiji na Mitaa, lakini Serikali inawalipa Watendaji tu. Je, Serikali haioni kwamba inawabagua Wenyeviti hawa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili kwa kuwa Halmashauri nyingi hivi sasa mapato yake yamechukuliwa na Serikali ikiwemo kodi ya majengo pale Mtwara Mjini na nchi nzima kiujumla ambayo ilikuwa inasaidia sana kupata makusanya ili kuweza kuwalipa posho kwa mujibu wa sheria hawa Wenyeviti wa Vijiji Serikali ama Vijiji vingi ama Halmashauri nyingi zinashindwa kutoa hata posho ya shilingi 20,000 kwasababu haina vyanzo vya mapato ikiwemo kodi ya majengo.

Je, Serikali ni lini itarudisha kodi hii ili halmashauri nyingi ziweze kukusanya na kuwapa posho Wenyeviti wa Mitaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge swali lake la kwanza anasema Serikali inawabagua Wenyeviti kwa sababu Watendaji wanalipwa. Suala hili siyo kweli kwa sababu wanapokuwa wanaomba hizi kazi utaratibu unatofautiana, Wenyeviti wa Mitaa wanachaguliwa na wananchi wao na wale Watendaji wanaomba kazi na wanaajiriwa na Serikali na nimeeleza kwenye jibu la msingi ni kwamba malipo ya Wenyeviti wa Mitaa na Wenyeviti wa Vijiji na Wajumbe wao inategemea makusanyo ya mapato ya ndani na tumeshapitisha bajeti, hatujazuia Halmashauri kuwa na uwezo wa kuwalipa Wenyeviti tukazuia, ndiyo maana tukasema tunatambua kazi nzuri inayofanywa kwa sasa utaratibu uliopo Halmashauri yenye uwezo italipa posho kulingana na uwezo ule na Wenyeviti wa Mitaa waendelee kutuvumilia uwezo ukiruhusu hatujakataa kuwalipa ila uwezo ukiruhusu watalipwa.

Kwa hiyo, Halmashauri zetu kama watabuni vyanzo vingine vya mapato wakipata uwezo wa kuwalipa watalipa Serikali haijazuia kabisa. Lakini hakuna ubaguzi na Wenyeviti wanajua kwamba hawa ni waajiriwa, wanaombwa na vyeti, wana-qualify na hawa ni watumishi wa wananchi ambao wamechaguliwa na wananchi wale na wanafanyakazi nzuri sana kama tulivyosema.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anazungumza kurudisha kodi ya majengo, kwa hiyo, kuwezesha Serikali zetu kwenye Halmashauri kuwalipa Wenyeviti wa Mitaa.

Mheshimiwa Spika, baada ya kodi hii kuchukuliwa kodi ya majengo pamoja na mabango pamoja na kodi zingine hii fedha inachukuliwa yote kwa ujumla wake nchi nzima inapelekwa kwenye kapu kuu la Serikali, kwa hiyo, hata miradi ya kimkakati barabara zinazojengwa, miradi ya maji, mishahara ya watumishi hii ni fedha ambayo inatumika kule, kwa hiyo siyo kwamba haina kazi. Lakini tumeelekeza Halmashauri na tumewaambia wabuni miradi mbalimbali ya kimkakati na Wizara ya TAMISEMI, Wizara ya Fedha tunawezesha kuanzisha miradi mikubwa mikubwa na Mtwara nimekuja pale kuna miradi mikubwa inaanzishwa.

Kwa hiyo ukipata uwezo kama huu ukapata fedha katika eneo lile na vyanzo vingine ukibuni bila kunyanyasa wananchi wataongezewa posho zao. Kwa sasa Halmashauri itaendelea kulipa kwa kadri itakavyoweza na pamoja kazi nzuri inayofanyika hatujazuia Halmashauri kulipa kulingana na uwezo wake.