Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Maftaha Abdallah Nachuma (16 total)

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:-

Serikali kwa miaka mingi imekuwa na mpango wa kujenga Hospitali za Rufaa za Kanda; na tayari Kanda zote zina hospitali hizo isipokuwa Kanda ya Kusini tu:-

(a) Je, ni lini Serikali itaanza kujenga hospitali hiyo ya Kanda ya Kusini ambapo tayari eneo la Mitengo Mikindani limetengwa kwa zaidi ya miaka saba na hakuna kinachoendelea?

(b) Je, ni Serikali haioni kama hawatendei haki wananchi wa maeneo ya Kanda ya Kusini kama wananchi wa maeneo mengine?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maftaha Abdallah Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Spika, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Maftaha Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini ningependa kutoa maelezo ya awali kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mpango wa Serikali kila Kanda inatakiwa kuwa na Hospitali ya Rufaa ya Kanda, katika Kanda saba zilizopo ni Kanda nne tu ambazo zina hospitali za Rufaa za Kanda.

Kwa Kanda ya Mashariki Serikali iliipandisha hadhi Hospitali ya Lugalo ya Jeshi kuwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda. Kanda ya Ziwa kuna Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando ambayo ilijengwa na taasisi ya hiari. Kanda ya Kaskazini kuna Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCMC inayomilikiwa na Taasisi ya hiari. Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kuna Hospitali ya Rufaa ya Mbeya inayomilikiwa na Serikali. Kanda tatu ndizo bado hazijapata Hospitali za Rufaa za Kanda ambazo ikijumuisha kanda ya Kati yenye Mikoa ya Dodoma Singida ambapo ni Makao Mkuu ya Serikali. Kanda ya Magharibi ikijumuisha Mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi na Kanda ya Kusini yenye mikoa ya Mtwara na Lindi.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo ya awali sasa napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maftaha A. Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Serikali tayari ilikwishaanza ujenzi wa hospitali ya Kanda ya Kusini katika eneo la Mitengo Mikindani na hatua zifuatazo zimetekelezwa na zinaendelea kutekelezwa kwa awamu. Maandalizi ya mpango kamambe yaani masterplan na michoro pamoja na makabrasha ya zabuni kwa ajili ya mradi yalikamilika tangu mwaka 2009. Awamu ya kwanza ya utekelezaji ilikuwa kujenga uzio kuzunguka eneo lote la hospitali na tayari ujenzi wake umekamilika. Awamu ya pili ilikuwa kujenga jengo la wagonjwa wa nje ambalo hadi Disemba, 2015 ujenzi wake ulikuwa umefikia asilimia 85. Serikali inatoa kipaumbele cha kipekee katika ujenzi wa hospitali hiyo na uongozi wa juu wa Wizara umekuwa ukitembelea na kukagua maendeleo yake mara kwa mara.
(b) Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa si kweli kwamba Serikali haiwatendei haki wananchi wa maeneo ya Kanda ya Kusini na pia Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo haibagui Kanda au eneo lolote. Vilevile usanifu wa hospitali hii ya Kanda ya Kusini ulizingatia mahitaji ya sasa katika hospitali ya ngazi ya Kanda. Hospitali hii itakapokamilika itakuwa ya kisasa zaidi ikilinganishwa na Hospitali za Kanda zilizopo, na itakuwa ni ya pili ya Kanda kujengwa na Serikali yetu. Ya kwanza ikiwa ni ile ya nyanda za Juu Kusini ya Mbeya.

Aidha, napenda kutumia fursa hii kuyapongeza mashirika ya dini na taasisi binafsi kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuanzisha Hospitali za Rufaa za Kanda.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:-
Mafuriko yanayotokea Mtwara Mjini kila mwaka hasa katika Kata ya Shangani, Cuono, Magomeni na Ufukoni yanasababishwa namiundombinu mibovu ambayo imejengwa chini ya kiwango katika maeneo mengi ya Mji wa Mtwara:-
(a) Je, Serikali iko tayari sasa kujenga upya mitaro, madaraja pamoja na miundombinu mingine ili maji yaweze kusafiri kuelekea baharini wakati wa masika?
(b) Je, ni lini Serikali itaanza kujenga barabara ya Mikindani - Lwelu ufukweni mwa bahari kwa kiwango cha lami ikizingatiwa kuwa barabara hiyo iko ndani ya Manispaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maftaha Abdallah Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika mwaka wa fedha 2015/2016 imetenga Dola za Kimarekani 540,000 kupitia mradi wa Tanzania Strategic Cities Project (TSCP) kwa ajili ya upembuzi yakinifu, usanifu na ujenzi wa mradi wa barabara ambao utahusisha ujenzi wa mitaro na madaraja ambao utahusisha uboreshaji wa miundombinu iliyoharibika na mvua. Utekelezaji wake upo katika kukamilisha hadidu rejea ili utaratibu wa manunuzi ya kupata Mkandarasi Mshauri ziweze kufikika.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshaanza matengenezo ya barabara ya Mikindani- Mchuchu- Lwelu kwa kiwango cha lami, ambapo katika mwaka wa fedha 2013/14 kilometa moja ilitengenezwa kwa kiwango cha lami. Aidha, ili kuhakikisha barabara hiyo inapitika wakati wote, Serikali katika Bajeti ya mwaka 2016/2017 imetenga shilingi 89,000,000 kwa ajili ya kuifanyia matengenezo. Azma ya Serikali ni kuijenga barabara hiyo yote ya kilometa 11 zilizobaki kwa kiwango cha lami kadri upatikanaji wa fedha utakavyoruhusu.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:-
Miundombinu ya maji Mtwara na mikoa yote ya Kusini mwa Tanzania ni hafifu na wakazi wengi wa miji ya Kusini na vijijini hawapati maji safi na salama.
Je, Serikali iko tayari kujenga bomba la kuvuta maji toka Mto Ruvuma ambalo limekuwa likizungumzwa kwa muda mrefu bila mafanikio?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maftaha Abdallah Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na uandaaji wa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya mradi wa kutoa maji kutoka Mto Ruvuma kupeleka Manispaa ya Mtwara pamoja na vijiji 25 vitakavyopitiwa na bomba kuu ndani ya kilometa 12 kila upande, kazi hiyo imekamilika mwezi Julai, 2015.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inaendelea na majadilinao na Serikali ya China kwa ajili ya kupata mkopo nafuu wa utekelezaji wa mradi huo. Ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2016/2017. Kazi zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa chanzo, mtambo wa kutibu maji, bomba kuu la kupeleka maji Mtwara Mikindani, matanaki pamoja na mabomba ya kusambazia maji.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:-
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa Mwanza alipiga marufuku na kuziagiza mamlaka zinazohusika kuacha kuwasumbua wafanyabiashara wadogo wadogo maarufu kama Wamachinga:-
Je, Serikali inatekeleza agizo hilo kwa kiwango gani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maftaha Abdallah Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mantiki ya agizo la Mheshimiwa Rais akiwa Mwanza ilikuwa ni kutowahamisha wafanyabiashara wadogo katika maeneo walipo endapo hakuna maeneo mbadala yaliyotengwa kwa ajili ya biashara zao. Mikoa na Halmashauri zimeendelea kutimiza malengo ya kuweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara wadogo kwa kutenga maeneo rasmi ya kufanyia biashara na kuboresha yaliyopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo yaliyotengwa rasmi kwa wafanyabiashara wadogo katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara ni Likonde, Mbae na Mjimwema. Vilevile, Halmashauri inaboresha Soko la Skoya ambalo halitumiki kwa muda mrefu kutokana na kujaa maji wakati wa mvua. Kazi zinazofanyika ni kurekebisha mitaro ya kupitisha maji ili eneo hilo liweze kutumika kama ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutumia fursa hii kuzikumbusha Halmashauri zote nchini kutenga maeneo kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo kutokana na umuhimu wao katika kukuza kipato na ajira. Aidha, wafanyabiashara wadogo wanatakiwa kuzingatia sheria na kuhakikisha wanaendesha biashara katika maeneo yaliyotengwa rasmi ili kuepuka usumbufu.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA Aliuliza:-
Gesi inayochakatwa Mtwara huweza kuzalisha viwanda vidogo vidogo ikiwemo mbolea na kwa miaka mingi wananchi wa Mtwara wamekosa fursa ya ajira ukilinganisha na maeneo mengine ya Tanzania kama vile Arusha, Mwanza, Kilimanjaro na kadhalika.
Je, ni lini Serikali itasitisha usafirishaji wa gesi kutoka Mtwara kwenda Kinyerezi ili wana Mtwara waweze kunufaika na ajira zinazotokana na uchakataji wa gesi hiyo asilia kufanyika Mtwara na Seriakli kujenga viwanda vitokanavyo na gesi Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maftaha Abdallah Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Sera mpya ya Nishati ya mwaka 2015 na Sera ya Gesi Asilia ya mwaka 2013 zinalenga kutoa fursa ya rasilimali ya gesi asilia kuwanufaisha Watanzania wote wakiwemo wananchi inapopatikana rasilimali hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika hadi sasa kuna miradi miwili inayosafirisha gesi asilia kutoka Mtwara na Lindi hadi Dar es Salaam. Miradi hiyo ni mradi wa kusafirisha gesi kutoka Mtwara na Lindi hadi Dar es Salaam uliokamilika mwaka 2015 na mradi wa Songas uliokamilika mwaka 2004. Gesi inayochakatwa inasafirishwa kwa bomba kwa maeneo mbalimbali nchini yakiwemo kwa ajili ya maeneo ya Mtwara, Lindi, Mkuranga na Dar es Salaam. Visima viwili vya gesi asilia katika eneo la Mnazi bay vimetengwa rasmi kwa ajili ya wananchi wa Mkoa wa Lindi na Mtwara.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na gesi asilia kutoka Lindi na Mtwara kutumika kuzalisha umeme kwa asilimia 50 pia gesi hiyo inatumika katika kusambaza gesi majumbani na viwandani katika maeneo mbalimbali. Kwa sasa Serikali kupitia Shirika la Maendeleo la Taifa (TPDC) inatekeleza mradi wa kuunganisha gesi hiyo katika Kiwanda cha Dangote kilichipo Mtwara ambacho kinahitaji futi za ujazo milioni 45. Pia shirika hilo liko kwenye majadiliano na kiwanda cha URANEX kinachotarajia kujengwa Mkoani Lindi ili kuweza kuunganisha gesi asilia hiyo.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:-
Mwaka 2012/2013 Serikali ilichukua ardhi ya wananchi wa Mtwara Mjini eneo la Mji Mwema na Tangira. Aidha, Serikali imewazuia wananchi hao kufanya shughuli za maendeleo katika maeneo hayo. Serikali iliahidi kuwalipa wananchi hao fidia lakini hadi sasa fidia hiyo haijalipwa.
Je, ni lini Serikali italipa fidia kwa wananchi wao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maaftaha Abdallah Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, fidia stahiki itaanza kulipwa kwa wananchi 2,020 kuanzia mwezi Juni, 2017 hadi robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2017/2018. Taasisi ya UTT - PID kwa kushirikiana na Halmashauri inatarajia kutumia shilingi 7,523,000,000 kwa ajili ya malipo ya fidia kabla ya kuanza kwa kazi ya upimaji wa viwanja. Ofisi ya Rais - TAMISEMI ilitoa kibali cha kuendelea na utekelezaji wa mradi kupitia barua yenye Kumb. Na. GB. 203/234/01/117 ya tarehe 02/09/2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ulipaji wa fidia haukuanza mapema kutokana na kampuni husika ya UTT -PID kutokuwa na Bodi. Bodi imeshaundwa na makubaliano ya pamoja yamefanyika katika kikao cha tarehe 02/05/2017 baina ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, UTT – PID na Halmashauri.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:-
Manispaa ya Mtwara Mikindani ina migogoro mikubwa ya ardhi inayokaribia kusababisha uvunjifu wa amani:-
Je, Serikali ipo tayari hivi sasa kutatua migogoro hiyo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali Na. 50 la Mheshimiwa Mftaha Abdallah Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifutavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa kumekuwepo changamoto ya kuibuka kwa migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara. Hata hivyo, Serikali imekuwa ikichukua hatua na jitihada mbalimbali ili kuhakikisha kuwa migogoro hiyo inapungua au inamalizika kabisa.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azma hiyo, Wizara iliwataarifu Waheshimiwa Wabunge kuwasilisha taarifa za migogoro iliyopo katika maeneo yao. Aidha, Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya waliombwa kuwasilisha taarifa za mashamba makubwa yaliyotelekezwa na migogoro iliyopo katika mikoa yao kupitia barua yenye Kumb. Na. EA 171/438/01 ya tarehe 21 Desemba, 2015.
Mheshimiwa Spika, baada ya kupokea taarifa za migogoro kutoka katika maeneo mbalimbali, Wizara imekuwa ikiyapitia hayo na kutatua migogoro kama ilivyowasilishwa kutoka kwa viongozi wa maeneo husika.
Mheshimiwa Spika, kwa Mkoa wa Mtwara, Wizara ilipokea taarifa za migogoro mbalimbali ikiwemo migogoro mikubwa. Kati ya iliyopokelewa ilikuwa ni mgogoro wa Shamba la Chumvi, maarufu kama Libya; mgogoro wa Mjimwema na Tangila, maarufu kama UTT; mgogoro wa mipaka baina ya wakazi wa Mtepwezi na Jeshi la Magereza Lilungu; mgogoro kati ya wananchi wa Mangamba na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege; na mgogoro baina ya wananchi wa Mbae Mashariki na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Mheshimiwa Spika, kuhusu mgogoro katika eneo la Libya, wananchi walifikisha suala hilo Mahakamani na sasa shauri hilo lipo katika Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara kama Shauri la Madai Na. 7 la mwaka 2014. Kwa upande wa mgogoro wa UTT, mgogoro huu nao ulifikishwa Mahakamani kama Shauri la Madai Na. 8 la mwaka 2015 ambapo wananchi 723 wanadai fidia Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara na wapo tayari kuiondoa kesi hiyo Mahakamani endapo watalipwa fidia hiyo. Aidha, shauri hili litakuja Mahakamani kwa ajili ya usuluhishi wa mwisho tarehe 18, Septemba, 2017.
Mheshimiwa Spika, kwa maeneo mengine nchini ambayo yalitembelewa na timu ya wataalam wa kisekta iliyoundwa kuchunguza vyanzo vya migogoro ya ardhi na kupendekeza namna ya kuzitatua, Serikali itahakikisha kuwa migogoro yote inatatuliwa kwa wakati kwa kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:-
Je, kuvunjwa kwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kuna faida gani kwa wakazi wa Dodoma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maftaha Abdallah Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini, maarufu kama mashine ya Kusini, kama ifuatavyo:- (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilivunja Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) tarehe 15 Mei, 2017 kutokana na muingiliano wa kimamlaka kati yake na Manispaa ya Dodoma ambapo licha ya kuongeza gharama za uendeshaji, ulisababisha migogoro mingi ya kiuendeshaji, ikiwemo vyanzo vya mapato na migogoro ya ardhi, hali iliyosababisha kupungua kwa kasi ya maendeleo ya mji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuvunjwa CDA wananchi wamepata faida nyingi ikiwa ni pamoja na kupungua kwa gharama za uendeshaji ambazo zilibebwa na wananchi kupitia kodi, kuongezeka kwa kasi ya utekelezaji wa kazi, kuongezeka kwa mapato ya Halmashauri ambayo matumizi yake huamuliwa na Wawakilishi wa wananchi (Madiwani), kuongezeka kwa idadi ya watumishi, majengo, maabara na vitendea kazi vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko hilo limewezesha kuongeza ufanisi wa Manispaa katika kuwahudumia wananchi.
Aidha, ubadilishaji wa mikataba ya upangishaji (Ground Lease Agreements) za miaka 33 iliyokuwa ikitolewa na CDA kwa kuwapatia wananchi Hatimiliki za miaka 99 umehamasisha uwekezaji katika kuendeleza kwa kasi zaidi Mji wa Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi kifupi cha kuanzia Mei hadi Desemba, 2017 wananchi wamebadilisha jumla ya mikataba 19,000 kati ya 65,000 iliyotolewa na CDA kuwa kwenye mfumo mpya wa Hatimiliki za miaka 99.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na faida hizo, Manispaa ya Dodoma inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo madeni na migogoro iliyorithiwa kutoka CDA. Manispaa inakabiliana na changamoto hizo kwa kuimarisha makusanyo na kuimarisha usimamizi katika sekta ya ardhi.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:-
Bandari ya Mtwara ni Bandari yenye kina kirefu Afrika Mashariki na Kati na Serikali kwa makusudi imeamua kuitupa na kujenga Bandari katika maeneo mengine ya nchi tena kwa gharama kubwa sana:-
Je, Serikali ipo tayari kukiri makosa na kuiboresha Bandari ya Mtwara ili korosho zote zisafirishwe kupitia Bandari hiyo kwa lengo la kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali lililoulizwa na Mheshimiwa Maftaha Abdallah Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali ni kuendeleza bandari zote nchini kadri uwezo utakavyoruhusu ili kuchochea ukuaji haraka wa uchumi. Hii inatokana na ukweli kwamba bandari ndiyo njia kuu ya kuchochea uchumi katika Taifa lolote lililobahatika kuwa na bahari.
Mheshimiwa Spika, napenda kutoa taarifa kwa Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Mtwara Mjini na Mtwara yote kwa ujumla kuwa Serikali haijawahi na haina nia ya kuitupa Bandari ya Mtwara kwani inafahamu fursa zilizopo katika ukanda wa maendeleo wa Mtwara yaani Mtwara Development Corridor.
Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza azma yake, katika Mwaka wa Fedha wa 2016/2017 Serikali ilitenga shilingi bilioni 59.32 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa gati moja lenye urefu wa mita 350 la kuhudumia shehena mchanganyiko ikiwemo ya korosho. Aidha, Serikali kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania imetenga shilingi bilioni 87.044 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa gati hilo. Gati hili linasanifiwa na kujengwa na Mkandarasi China Railway Construction Company (CRCC Group) kwa kushirikiana na China Railway Major Bridge Engineering Company Limited kwa gharama ya shilingi bilioni 137.39 pamoja na VAT. Mkataba wa ujenzi kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari na kampuni hiyo ulisainiwa tarehe 4 Machi, 2017 na ujenzi wa gati hilo utakamilika ndani ya miezi 21.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:-
Je, kwa nini Serikali haisemi ukweli Bungeni juu ya fidia kwa wananchi wa Mtwara Mjini?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maftaha Abdallah Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro mkubwa wa fidia uliopo sasa katika Manispaa ya Mtwara Mikindani unahusu eneo la Mjimwema na Tangira unaotokana na upimaji wa viwanja 10,000 uliotarajiwa kufanywa kwa njia ya ubia baina ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, pamoja na Taasisi ya UTT- PID mwaka 2003. Upimaji huu haukufanyika kama ilivyopangwa kutokana na amri ya kusitishwa kwa miradi yote ya upimaji wa viwanja ambavyo Halmashauri mbalimbali zilikuwa zikishirikiana na UTT-PID iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI mwaka 2004.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na katazo hilo, Manispaa ya Mtwara Mikindani iliendelea kuomba kibali cha kuendelea na mradi huo, kwa kuwa shughuli mbalimbali tayari zilikuwa zimeshafanyika zikiwemo uthamini kwa ajili ya fidia. Baada ya ufuatiliaji, Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilitoa kibali cha kuendelea na mradi huo kwa barua yenye Kumb. Na. GB.2013/234/01/117 ya tarehe 2/09/2016.
Hata hivyo mwishoni wa mwaka 2017 Taasisi ya UTT- PID ilikiri kutoweza kuendelea na mradi huo kutokana na ukosefu wa fedha uliosababishwa na taratibu za utekelezaji wa mradi huo kuchukua muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Januari, 2018 Baraza la Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani liliamua kuendelea na mradi huo kwa kuwapimia wananchi maeneo yao na kisha kuwapa viwanja kulingana na ukubwa wa maeneo yao na hatimaye kuwamilikisha kisheria badala ya kusubiri fidia ambayo kimsingi haipo. Jumla ya shilingi milioni 170 zilitengwa katika bajeti ya Halmashauri kwa ajili ya kugharamia zoezi la upimaji na ufunguzi wa barabara za msingi katika eneo la mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa eneo la Tangira katika Kata ya Mitengo waliridhia kuendelea na utaratibu wa kupimiwa viwaja katika mashamba yao. Mpaka sasa jumla ya viwanja 1,212 vimepimwa. Aidha, jumla ya viwanja 2,800 vinatarajiwa kupimwa katika eneo la Mjimwema Kata ya Magengeni. Kwa maeneo mengine upimaji wa viwanja utaendelea baada ya kukamilika kwa majadiliano baina ya Serikali na wananchi ambao ni wamiliki wa asili wa mashamba husika.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:-
Serikali imeanzisha utaratibu wa kutoa elimu bure na kuanza kutekeleza utaratibu huo kwa kupeleka fedha shuleni kidogo kidogo kulingana na idadi ya wanafunzi husika tangu Oktoba 25, 2015:-
(a) Je, Serikali inafahamu kwamba shule nyingi za msingi na za sekondari nchini zikiwemo za Mtwara Mjini zilikuwa na madeni mengi ya wazabuni na steshenari?
(b) Je, Serikali inaweza kueleza kuwa madeni hayo yatalipwa kwa utaratibu upi ikiwa fedha zinazotolewa ni kidogo kwa uwiano wa mwezi kwa mwaka husika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maftaha Abdallah Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uwepo wa madeni katika shule za msingi na sekondari ambayo yanaanzia mwaka wa fedha 2008/2009 hadi 2016/2017, ikiwa ni madeni ya wazabuni kwa ajili ya chakula cha wanafunzi shuleni na shajara. Katika ya hayo, Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani inadaiwa shilingi milioni 92.4. Madeni hayo ni yale yalikuwepo kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa Mpango wa Elimu bila Malipo Desemba, 2015. Kwa sasa, Serikali imejizatiti kutozalisha madeni, ambapo fedha za chakula na mahitaji mengi zinapelekwa kwenye kila shule moja kwa moja kila mwezi. (Makofi)
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:-
Je, kwa nini Serikali haitaki kukarabati Uwanja wa Ndege Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maftah Abdallah Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali iko katika hatua za mwisho za kukamilisha taratibu za manunuzi kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Mtwara. Hadi sasa mkandarasi kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa kiwanja hiki amepatikana ambaye ni Beijing Construction Engineer Group Co. Ltd. ya China kwa gharama ya shilingi bilioni 50.366. Hatua iliyobaki ni mkandarasi kukamilisha taratibu za kupata udhamini (bank guarantee) ili aweze kulipwa malipo ya awali (advance payment) na kukabidhiwa eneo la mradi. Hivyo, mradi huu utaanza kutekelezwa mara tu baada ya taratibu za manunuzi kukamilika.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kumsimamia mkandarasi akamilishe jukumu lake ili kazi ya ukarabati wa uwanja uweze kuanza mara moja.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:-

Zao la Korosho pamoja na kuingiza mapato makubwa Serikalini bado lina changamoto nyingi sana katika uuzaji wake kwa upande wa Wakulima:-

Je, Serikali ipo tayari kuondoa changamoto hizo ili kuleta tija kwa Wakulima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maftah Abdallah Nachuma Mbunge wa Jimbo la Mtwara mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli zao la Korosho ni mojawapo ya mazao ya Kilimo yanayoliingizia Taifa mapato ambapo katika kipindi kilichoishia Oktoba, 2018, zao la Korosho liliingizia Taifa fedha za kigeni za Kimarekani zaidi ya dola milioni mia tano sabini na tano pointi sita sawa na zaidi fedha za Kitanzania trilioni moja nukta tatu ikilinganishwa na mazao mengine ya biashara. Aidha, pamoja na mchango wa zao hilo katika uchumi wa Taifa, zao la Korosho limekuwa likikabiliwa na changamoto mbalimbali ambapo Serikali imekuwa ikizitafutia ufumbuzi.

Mheshimiwa Spika, changamoto hizo ni pamoja na kuyumba kwa bei ya zao la Korosho katika soko la dunia kutokana na Korosho kuuzwa ikiwa ghafi bila kuongezewa thamani; Tija ndogo katika uzalishaji wa wakulima; baadhi ya wakulima kutotumia miche bora na matumizi hafifu ya pembejeo ikiwemo viuadudu kama sulphur; wakulima kutozingatia Kanuni bora za Kilimo katika uzalishaji, uvunaji na uhifadhi hafifu wa Korosho; uwezo mdogo wa maghala ya kuhifadhia Korosho na baadhi ya wakulima kuchanganya Korosho na mawe na mchanga kwa ajili ya kuongeza uzito wakati wa mavuno ambao unashushia ubora.

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imeboresha mfumo wa uuzaji wa Korosho kwa kuimarisha usimamizi na ukaguzi kuanzia ngazi ya vyama vya msingi, maghala makuu, maghala ya hifadhi na kutoa elimu kwa wakulima; kurejesha Kiwanda cha BUCCO cha Mkoani Lindi cha kubangua Korosho ujenzi wa maghala matatu ya kuhifadhia Korosho katika Mikoa ya Ruvuma, Pwani na Tanga ili kuongeza Kiwango cha kuhifadhi na ubora wa Korosho pamoja na kuzalisha miche bora zaidi ya milioni kumi na kuisambaza kwa wakulima.

Mheshimiwa Spika, mikakati mingine ni pamoja na kuimarisha mnyororo wa thamani katika zao la Korosho ili kuongeza uzalishaji, kuimarisha usambazaji wa pembejeo za Kilimo kwa wakati, kutoa huduma za ugani pamoja na kuweka mazingira wezeshi na kuwajengea uwezo wabanguaji wa ndani wa Korosho kwa lengo la kuongeza thamani ya Korosho inayozalishwa nchini.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itavunja Bodi za Wahandisi kutokana na kauli ya Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maftaha Abdallah Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Usajili wa Wahandisi ilianzishwa chini ya Sheria ya Usajili wa Wahandisi Na. 15 ya mwaka 1997. Bodi hii inalo jukumu la kusajili wahandisi na makampuni ya kihandisi pamoja na kusimamia shughuli za uhandisi na mwenendo wa wahandisi na makampuni ya ushauri wa kihandisi hapa nchini. Kwa kuzingatia majukumu iliyopewa, Bodi ya Usajili wa Wahandisi tangu kuanzishwa kwake imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa na kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha bodi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa, moja ya Bodi zinazofanya kazi vizuri na kwa weledi wa kutosha ni Bodi ya Usajili wa Wahandisi na baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kutokana na kuanzishwa kwa Bodi hiyo ni kusajili jumla ya wahandisi 25,263 katika madaraja tofauti hadi kufikia Machi, 2019. Sambamba na hilo, makampuni ya ushauri ya kihandisi yapatayo 338 yameweza kusajiliwa katika kipindi hicho zikiwemo maabara za upimaji vifaa vya ujenzi 32.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano haina kumbukumbu zozote zinazoonyesha kuwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwahi kutoa kauli ya kuivunja Bodi ya Usajili wa Wahandisi.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:-

Je, Serikali inahakikishaje amani na utulivu vinakuwepo katika chaguzi mbalimbali nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maftaha Abdallah Nachuma Mbunge wa Mtwara Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwafahamisha wananchi kuwa ni jukumu la Serikali kuhakikisha kuwa amani na utulivu vinatamalaki nchini wakati wote bila kujali nyakati au majira mbalimbali katika mwaka. Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama limejipanga vizuri kudhibiti vitendo mbalimbali vya uvunjaji wa sheria ikiwemo fujo au aina yeyote ya ukosefu wa amani vinavyoweza kusababisha wananchi kushindwa kushiriki katika shughuli zao za kila siku, ikiwemo kushiriki katika michakato ya chaguzi mbalimbali zinazofanyika nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Polisi inaendelea kutoa mafunzo mbalimbali kwa askari wake wa ukakamavu, upelelezi na kuongeza vifaa vya kutenda kazi ili kuwajengea uwezo na weledi mkubwa wa kuweza kuzuia na kukabiliana na vitendo kama hivyo vinavyojitokeza nyakati za uchaguzi.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:-

Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji na Vitongoji wanafanya kazi kubwa na ngumu sana hasa Mtwara Mjini na maeneo mengine ya nchi yetu.

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwalipa mishahara kama ilivyo kwa Watendaji wa Vijiji na Mitaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maftaha Abdallah Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Wenyeviti wa Vijiji, Mitaa na Vitongoji katika shughuli za maendeleo. Hata hivyo, kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Wenyeviti wa Serikali za Vijiji, Mitaa, Vitongoji na Wajumbe wa Serikali za Vijiji pamoja na Wajumbe wa Mitaa za mwaka 2014 zilizotolewa kupitia Tangazo la Serikali Na. 322 na Na. 323, sifa zinazomwezesha mkazi wa Mtaa, Kijiji na Kitongoji kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti au Mjumbe wa Serikali za Mitaa ni pamoja na kuwa na shughuli halali inayomwingizia kipato.

Mheshimiwa Spika, Wenyeviti wa Vijiji, Mitaa na Vitongoji siyo watumishi wa umma na hivyo hawaajiriwi na kulipwa mishahara kama ilivyo kwa Watendaji Vijiji na Mitaa. Hata hivyo, kwa kuzingatia kazi kubwa inayotekelezwa na viongozi hawa katika kusimamia shughuli za maendeleo katika maeneo yao, Serikali inawalipa posho kutokana na asilimia 20 ya mapato ya ndani ya Halmashari kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290. Ulipaji wa posho ya viongozi hao unategemea hali ya makusanyo ya kila Halmashauri. Serikali inatoa wito kwa Halmashauri zote ikiwemo Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani kuthamini mchango mkubwa wa viognozi hao na kuwalipa posho kutokana na mapato ya ndani. Ahsante.