Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Maftaha Abdallah Nachuma (60 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia katika Mpango huu wa Maendeleo wa mwaka mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuzungumza lolote, naomba kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kuwa Mbunge …
MWENYEKITI: Nataka tu Jimbo Mheshimiwa.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mtwara Mjini.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru kwa kunibariki kuwa Mbunge wao. Pili, naomba niwashukuru wananchi wangu wa Mtwara Mjini kwa kuniamini na nawaambia waendelee kuniamini nitawawakilisha vyema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuchangia hoja, naomba niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Mtwara Mjini kumetokea maafa, mvua imenyesha, kuna mafuriko na jana nilitoa taarifa hii kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba Waziri husika ashughulikie suala hili, kuna nyumba zaidi ya 500 zimeharibika. Nachukua fursa hii pia kuwapa pole wananchi wote walioathirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kuchangia kama ifuatavyo. Mpango huu umezungumzia suala zima la viwanda na Mheshimiwa Waziri wakati anatoa hoja alisema kuna utaratibu wa kuhakikisha inatawanya viwanda kila eneo la nchi. Pia alisema kuna maeneo ni special investment zone kwa maana kwamba ni ukanda maalumu wa uwekezaji na akataja Mtwara, Bagamoyo na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Mtwara Mjini kuna Kiwanda cha Dangote. Kiwanda hiki kina wafanyakazi wengi lakini kwa masikitiko makubwa kabisa mle ndani kuna kampuni tatu za Wahindi na Wachina, kuna AYOK, UCC na CYNOMA. Naomba nimpe taarifa Waziri husika kwamba kampuni hizi zilizopo mle ndani zinanyanyasa wafanyakazi. Sijui ni utaratibu gani huu wa kwamba tunajenga viwanda badala ya kuwanufaisha Watanzania vinawanyanyasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine katika Kiwanda hiki cha Dangote, lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba inaondoa umaskini kwa wananchi wa maeneo husika. Kwa kiasi kikubwa kiwanda hiki kinaajiri watu lakini wenyeji wa Mtwara wengi hawapati nafasi. Mimi kama Mbunge nimejaribu kutembelea kiwanda hiki zaidi ya mara mbili kwenda kuzungumza na Maafisa Masuuli lakini kuna manyanyaso makubwa ya wafanyakazi mle ndani. Mishahara inatoka kiasi kikubwa lakini wale vibarua na wafanyakazi wanapewa pesa ndogo sana. Nimuombe Waziri husika atembelee Kiwanda cha Dangote - Mtwara kuona manyanyaso yanayofanywa na Wahindi pamoja na Wachina lakini manyanyaso yanayofanywa kwa wananchi wa Mtwara Mjini, Mtwara Vijijini na maeneo ya Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia suala zima la bandari. Katika hoja hii limeelezwa suala zima la kuboresha bandari, lakini Bandari ya Mtwara imetajwa tu kwamba kuna mpango na mkakati wa kujenga magati. Mimi kama Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini nimetembelea Bandari ile ya Mtwara. Pale kuna gati moja limechukuliwa na watu wa gesi wanaitwa BG, lakini ile gati kwa muda mrefu zile meli za BG hazipo. Sasa hivi tumebakiwa na gati mbili tu ambapo tunataka tusafirishe korosho lakini ile gati iko empty na wanasema kwamba pale meli nyingine yoyote hairuhusiwi kutia nanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba katika mpango huu wa kuendeleza bandari wahakikishe Bandari ya Mtwara ambayo ina kina kirefu Afrika Mashariki na Kati, wala haihitaji kutumia gharama kubwa kama ilivyo ujenzi wa Bandari mpya ya Bagamoyo, Wizara husika irekebishe Bandari ya Mtwara na ijenge yale magati manne. Sambamba na hilo ihakikishe inamwezesha yule mwekezaji ambaye ameomba eneo, Mheshimiwa Aliko Dangote kuweza kumaliza mchakato wake ili tuweze kuongeza magati kwa ajili ya Bandari ile ya Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nazungumzie suala zima la miundombinu. Kule Mtwara tuna barabara inaitwa barabara ya Ulinzi, ni miaka mingi barabara hii haizungumziwi kabisa. Naomba Wizara husika ihakishe inashughulikia barabara ya kutoka Mtwara Mjini – Kitaya - Newala na maeneo mengine kwani ni barabara ya Ulinzi ambapo mwaka 1972, mashujaa wetu au wanajeshi wetu walikuwa wanaitumia barabara ile kulinda mipaka ya Tanzania Ukanda huu wa Kusini lakini imesahaulika kabisa. Kwa hiyo, naomba Mpango huu uhakikishe barabara hii ya Ulinzi inajengwa kwa kiwango cha lami, inapita Kitaya - Mahulunga na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine naomba barabara hii ambayo ni kitovu kikubwa cha uchumi wa korosho inayoanzia Mtwara Mjini kuelekea Majimbo yote ya Mkoa wa Mtwara kwa maana ya Mtwara Vijijini, Nanyamba, Newala, Tandahimba hadi Masasi iwekwe kwenye Mpango ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Mimi kabla sijazaliwa naisikia barabara hii inazungumziwa kila siku. Mheshimiwa Nandonde alishawahi kuzungumza kwa miaka mingi sana katika Bunge hili lakini mpaka leo bado barabara hii inasahaulika, kwa hiyo, tunaomba iwekwe kwenye Mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala zima la utalii. Pale Mtwara Mikindani kuna magofu ya kihistoria lakini Serikali imeyaacha na haina mkakati wowote wa kuhakikisha kwamba tunatangaza vivutio vile ili viweze kutoa ajira na kuingiza kipato kwa Serikali hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Maeneo yale ya Mikindani kuna vivutio kuliko hata maeneo mengine ya Tanzania, naomba Serikali ianze kuyatangaza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa kusema mambo machache. Ilizungumzwa hapa kwamba amani na utulivu ndiyo chachu ya maendeleo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ndiyo chachu itakayowavutia wawekezaji kuja kuwekeza Tanzania. Kila mmoja ni shahidi, hata Waheshimiwa wazee wetu wa Chama cha Mapinduzi wanafahamu kabisa tarehe 25 Oktoba, 2015 kule Zanzibar chama kilichoshinda ni Chama cha Wananchi - CUF lakini Tume ya Uchaguzi na yule aliyeshindwa hawakutaka kumtangaza aliyeshinda. Kwa hiyo, niombe tu mshindi wa Zanzibar atangazwe ili nchi yetu iendelee kuwa na amani na utulivu na ili wawekezaji waweze kuja kuwekeza Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema kwamba usafirishaji wa reli ni muhimu sana. Kama ilivyokuwa kwenye reli ya kati na kule Kusini pia kuna reli, lakini kwenye Mpango huu sijaona sehemu yoyote iliyoandikwa kwamba reli hii ya kutoka Mtwara – Liganga - Mchuchuma itajengwa lini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la usafiri wa ndege, niungane na wenzangu kusema kwamba ATC ina ndege moja tu tena ni ya kukodi, tuna ubia na wale watu wa South Africa. Naomba ndege ziongezwe kwa sababu ni za Serikali lakini pili gharama yake ni nafuu sana. Nilienda kuulizia tiketi ya ndege kutoka Dar es Salaam kwenda Mtwara...
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru sana. (Makofi)
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. ABDALLAH N. MAFTAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia mpango huu kwa niaba ya wananchi wa Mtwara Mjini. Nianze tu moja kwa moja kuangazia huu Mpango kwa sababu Mpango kwa kiasi kikubwa unaonesha namna gani nchi yetu sasa hivi inaingia katika uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la msingi sana ambalo sijaliona katika Mpango huu, ni usimamizi wa hivyo viwanda. Kwa masikitiko makubwa kabisa, hivi sasa tuna baadhi ya viwanda ambavyo vimejengwa katika nchi yetu na wawekezaji mbalimbali kutoka nje ya nchi. Kwa mfano, ukija pale Mtwara Vijijini kuna Kiwanda kinaitwa Kiwanda cha Dangote, lakini ukiangalia katika kiwanda hiki unaweza kuona kuna changamoto nyingi sana ambazo Serikali imeshindwa kuzisimamia na kuzitatua, lakini tunaleta Mpango ambao unasema kwamba Tanzania itaondoa umaskini kupitia Sekta hii ya Viwanda wakati hivyo viwanda vichache tunashindwa kuvisimamia na kuleta tija kwa wananchi wetu ili kuondoa umaskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa sana, niliweza kuzungumza suala hili katika mwelekeo wa Mpango kwamba Kiwanda cha Dangote kilichopo Mtwara kimeajiri Watanzania ambao wanatoka sehemu mbalimbali ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini kuna Makampuni mle matatu ambayo ni ya kigeni yanayosimamia uendeshaji. Ipo Kampuni ya Kichina, kuna Kampuni kutoka India na Kampuni nyingine kutoka kule Nigeria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi kampuni zilizopo katika Kiwanda hiki cha Dangote zinanyanyasa kwa kiasi kikubwa sana wananchi wa Tanzania. Sasa swali langu katika Mpango huu ni kwamba, kama tumetengeneza utaratibu wa kuhakikisha kwamba viwanda vinatatua changamoto za umaskini wakati tunashindwa kusimamia viwanda hivi; na pale nilizungumza katika mwelekeo wa Mpango huu kwamba malipo ya mishahara ya wafanyakazi wa Tanzania ambao ni wazalendo ni midogo na hata hiyo midogo yenyewe wanapunjwa. Badala ya kulipwa Sh. 12,000/= kwa siku ambazo zinaandikwa kwenye makaratasi, wanapewa Sh. 7,000/=.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nilizungumza katika mwelekeo wa Mpango hapa Bungeni lakini mpaka leo hii tunapotaka kupitisha huu Mpango, bado marekebisho hayajafanyika katika Kiwanda cha Dangote. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara aunde Tume Maalum iweze kutembelea Kiwanda hiki cha Dangote kwa sababu kinanyanyasa Watanzania walioajiriwa pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze suala zima la bandari. Kwa mujibu wa mwelekeo wa Mpango huu, umesema tutaboresha uchumi wa nchi kwa kujenga bandari mbalimbali na Mheshimiwa Profesa Maji Marefu kazungumza hapa kwamba, bandari siku zote tunaangalia Bandari ya Dar es Salaam na sasa hivi tunaenda kujenga Bandari mpya ya Bagamoyo wakati Mwenyezi Mungu ametubariki, Mtwara tuna bandari ambayo ina kina kirefu Afrika Mashariki na Kati, Bandari ambayo Mwenyezi Mungu ametujaalia wala haihitaji kuchimba, lakini tunaenda kujenga bandari mpya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nashangaa, wakati Serikali hii ina mpango wa kuhakikisha kwamba inabana matumizi, lakini tunaenda kujenga bandari mpya ambayo itatumia Dola za Marekani bilioni karibu 22.5, wakati Bandari ya Mtwara ambayo Mwenyezi Mungu ametubariki ilikuwa ni kuboresha tu kidogo na iweze kutumika kuinua uchumi wa nchi hii. Sasa mipango hii, ni kweli lengo letu ni kuhakikisha kwamba tunaondoka hapa tulipo ili kuwa na maendeleo ya nchi hii wakati tunatumia pesa bila mpango ambao kimsingi unastahiki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu, kama kweli tunahitaji kuboresha uchumi wa nchi hii, tuboreshe Bandari za Mtwara, tuboreshe Mtwara Corridor, tuboreshe Tanga na maeneo mengine. Tusifikirie tu Dar es Salaam, Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala zima la elimu. Sasa hivi tunasema kwamba Serikali imeweka sera ya kutoa elimu bure, lakini kwa masikitiko makubwa kabisa, ukitembelea mashuleni huko, hii sera ya elimu bure imekuja kudumaza usimamizi wa elimu. Tunaangalia fedha za uendeshaji wa hizi shule, kwa mfano, Shule za Msingi; nilitembelea baadhi ya shule kama tano, sita pale Mtwara Mjini katika Jimbo langu, ukipitia fedha zilizoingia shuleni kwa miezi hii mitatu, ni jambo la kusikitisha sana. Kwa mwezi Sh. 27,000/= pesa za maendeleo halafu tunasema kwamba tunahitaji kuinua elimu kwa Sera ya Elimu Bure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba kwa namna ya kipekee kabisa, Serikali iweke utaratibu wa kupeleka fedha mashuleni kama kweli tunahitaji kusimamia elimu na elimu ndiyo chachu ya maendeleo katika dira ya nchi yoyote duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kwa kifupi kilimo na uvuvi. Mpango huu umeelekeza kwamba tutainua kilimo kwa kuboresha mazao ya biashara na mazao ya chakula kwa wakulima, lakini nikizungumzia kwa mfano suala zima la zao la korosho Tanzania, tuna Bodi ya Korosho Tanzania, Bodi ambayo inasimamia Sekta hii ya Korosho Tanzania, lakini kwa masikitiko makubwa kabisa, hawana mkakati hata mmoja kuhakikisha kwamba huyu mkulima anayelima zao la korosho anapewa pesa ambazo zinastahiki pale anapouza mazao yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha ajabu kabisa, ukiangalia katika uuzaji wa mazao haya, zao la korosho kwa mfano, mkulima amewekewa tozo nyingi sana, mpaka tozo ya gunia ambalo Mhindi anakuja kusafirishia korosho kutoka Tanzania kwenda India anabebeshwa mkulima, halafu tunasema tunahitaji kuinua kilimo wakati mpaka leo tunavyozungumza bado bei ya korosho iko chini sana. Korosho inauzwa Sh. 1,800/= hadi Sh. 2,000/=. Ni jambo la kusikitisha kwamba Serikali inashindwa kumtafutia mkulima masoko ya zao la korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, korosho ni zao ambalo mwaka 2015 na mwaka 2014 limeingiza pesa nyingi Serikalini. Ukiondoa tumbaku, zao linalofuata ni korosho, lakini tunashindwa kuweka mikakati ya uhakikisha kwamba tunainua zao hili na mkulima anaweza kunufaika na kilimo hiki cha korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Mungu ametubariki Tanzania tuna Bahari ya Hindi kuanzia kule Mtwara mpaka Tanga, lakini cha ajabu ni kwamba Serikali katika Mpango huu sijaona kwamba imeweka utaratibu kuona inaboresha namna gani Wavuvi wetu wa Tanzania ili waweze kununuliwa vifaa, kupewa vifaa vya kisasa vya uvuvi ili waweze kuwa na uvuvi wenye tija na mwisho wa siku waweze kuondokana na umaskini. Leo tunakuja tunasema tunataka kuboresha kilimo na uvuvi wakati mipango yetu haioneshi namna gani tunaweza kuondoa umaskini kupitia Sekta hii ya Uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wazungu wanasema kwamba Tanzania Mungu ametubariki na hasa upande huu wa Kusini, tunasema ni vision sea, ni bahari ambayo ina samaki kedekede huko chini lakini Serikali haina mpango wowote wa kuinua Sekta hii ya Uvuvi ili Watanzania tuweze kuondokana na umaskini. Tunapiga danadana tu! Ooh, tutajenga Chuo cha Mikindani, wakati hatuna utaratibu, hatujaweka mkakati wowote wa kuhakikisha kwamba tunanunua maboti na vifaa vya uvuvi ili tuweze kuwasaidia wavuvi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kidogo suala zima la maendeleo. Maendeleo yoyote yanategemea amani na utulivu wa nchi, lakini kwa masikitiko makubwa kabisa, kwa mfano ukija Mtwara Mjini tangu mwaka 2013, 2014 mpaka leo hii 2015, Serikali iliweza kuchukua ardhi ya wananchi, maeneo ya Tanga na maeneo ya Mji mwema. Nimezungumza hili jana hapa kwenye briefing na hii ni mara yangu ya tatu nazungumza; Mtwara kuna mgogoro mkubwa sana wa ardhi. Wananchi wamenyang‟anywa ardhi zao na Serikali wakasema kwamba wataenda kulipa fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu mwaka 2013 mpaka leo hii, hakuna senti yoyote iliyotolewa na Serikali. Cha ajabu Serikali ukiiuliza, inasema tutafanya, tutafanya. Wananchi hawana sehemu za kulima, halafu tunakuja na Mpango wa kusema kwamba eti tunataka kuondoa umaskini Tanzania, wakati wananchi wananyang‟anywa ardhi na hawapewi fidia zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu, kwa sababu Waziri wa Ardhi, Mheshimiwa Lukuvi yupo hapa, atembelee Mtwara, akaangalie changamoto za ardhi ambazo zinaelekea sasa kuleta mpasuko wa Kitaifa na mtengamano wa Kitaifa kwa sababu wananchi wanasema tutafika wakati tumechoka na mwelekeo huu utakuwa hauna maana, Mheshimiwa Mwenyekiti, suala zima la amani na utulivu ni jambo la msingi sana. Kama tunahitaji kweli kuhakikisha tunaleta tija katika Taifa hili, umaskini unaondoka, ni lazima tuvutie uwekezaji. Huwezi kuvutia uwekezaji kama hakuna amani na utulivu. Issue ya Zanzibar nayo ni ya msingi sana, siyo issue ya kubeza. Tunahitaji kukaa pamoja ili kujadiliana namna gani tunaweza kuleta amani na utulivu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma Mikataba ya Tanzania, kwa mfano Mikataba ya Uwekezaji, mingi haina tija katika Taifa hili. Kwa mfano, kuna Mkataba wa Mlimani City, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kiliingia mkataba na Mwekezaji kutoka Botswana, Mkataba ambao kimsingi Serikali ya Tanzania inakusanya kwa mwaka asilimia 10% tu ya mapato yanayopatikana pale, wakati kuna mamilioni mengi ya pesa yanakwenda kwa Mwekezaji. Kwa hiyo, tunahitaji sasa kama Taifa tuingie kwenye Mikataba na huu Mpango uoneshe ni namna gani Bunge linaweza kupitisha Mikataba yote ya Tanzania ili tuweze kuwa na uwekezaji wenye tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze angalau kwa kifupi suala zima la afya. Afya ni jambo la msingi sana. Hatuwezi kusema kwamba tunahitaji maendeleo kama Watanzania wengi wanakufa kwa sababu ya afya. Ukija Mikoa ya Kusini, nilizungumza hili wakati wa kikao cha pili kwamba Kanda zote Tanzania tayari zimekamilika kuwa na Hospitali za Rufaa. Kanda ya Kusini mpaka hivi sasa, ujenzi wa Hospitali hii, jengo moja tu, unasuasua ambalo Mheshimiwa Waziri hapa alizungumza kwenye Bunge lako Tukufu kwamba iko katika hatua za umaliziaji ujenzi wa OPD, lakini mpaka hivi sasa ujenzi huo unasuasua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Hospitali ya Mkoa ya Mtwara hakuna X-Ray, Hospitali ya Wilaya hakuna X-Ray, halafu leo tunasema tunataka kuondoa umaskini, tunapitisha Mpango huu. Naomba kwa namna ya kipekee kabisa, kama kweli tunahitaji kuondoa umaskini Tanzania, ni lazima tujali afya za Watanzania, ni lazima tuboreshe afya za Watanzania, tuhakikishe kwamba vifaa tiba vinapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo, naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia hoja iliyopo Mezani leo hii ya Viwanda, Uwekezaji na Biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kusema lolote, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunibariki kuwa na afya njema. Kwa kuwa katika kuchangia Wizara hizi, hii ni mara yangu ya kwanza nitumie fursa hii pia kuwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Mtwara Mjini na niwaeleze kwamba naendelea kupambana vizuri na nitawawakilisha vyema kwa kipindi chote cha miaka mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hotuba hii ambayo imetolewa na Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara, nianze tu kwa kusema kwamba mkakati wa Wizara hii wa kuhakikisha kwamba nchi ya Tanzania inakuwa ni nchi yenye uchumi wa viwanda kupitia bajeti yake hii, kimkakati ni jambo zuri sana. Wenzetu nchi nyingi duniani, ukisoma historia, nchi za Ulaya ziliweza kuendelea kwa kiasi kikubwa kupitia sekta hii ya viwanda. Tangu karne ya 15 kule nchi zote za Ulaya ziliweza kufanya mapinduzi ya viwanda na kuweza kuondoa umaskini na hata kuitawala dunia kwa kutegemea sekta hii ya viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu ya Tanzania, baada ya uhuru, Mwalimu Julis K. Nyerere alijitahidi kwa kiasi kikubwa sana, aliweza kuanzisha viwanda vingi sana. Wakati huo ikumbukwe kwamba tulikuwa katika mfumo wa ujamaa na kujitegemea, uchumi wetu ulitegemea kwa kiasi kikubwa sekta hii ya viwanda, lakini kwa bahati mbaya kabisa, Serikali ya Chama cha Mapinduzi mwaka 1995-1996 iliweza kuingia katika mfumo wa uwekezaji, mfumo ambao haukufuata kanuni, sheria na taratibu za kiuwekezaji na hatimaye zaidi ya viwanda 446 viliweza kuuawa kwa kupewa wawekezaji ambao hawana sifa ya kuwekeza Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze tu angalau kwa kifupi sababu zilizopelekea kuuawa kwa viwanda ikiwa ni kwamba tuliwapa wawekezaji ambao they were not credible buyers katika nchi yetu ya Tanzania, walikuwa hawana uwezo na ujuzi. Jambo lingine lilikuwa ni mazingira yenyewe ambayo tuliyatengeneza hayakuwa rafiki kwa kuweza kuuza viwanda vyetu. Mwisho wa siku leo hii tunasema tunahitaji kufufua uchumi wa viwanda, wakati hatuna utaratibu, hatuna mkakati wowote ili Taifa kama Taifa liweze kuwekeza katika sekta hii ya viwanda kwa kuwapata wawekezaji ambao tunasema ni credible buyers. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Viwanda, Uwekezaji na Biashara amewasilisha bajeti yake hapa lakini nimepitia hii bajeti takribani kitabu chote hiki sijaona hata sehemu moja ambapo ameeleza ni utaratibu gani ambao utatumika katika kuhakikisha kwamba uwekezaji wa ndani ya nchi unakuwa ni uwekezaji wenye tija. Ameeleza tu kwamba tutahakikisha kwamba wawekezaji wa ndani na viwanda vidogo wanapewa kipaumbele lakini sijaona utaratibu wowote ambao wameuweka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, nizungumzie suala zima hili la mashirika ya umma na hasa mashirika ya hifadhi za jamii. Kuna mashirika ambayo yana mkakati wa kuwekeza ndani ya nchi lakini katika uwekezaji wao wanatumia mamilioni ya fedha kinyume na utaratibu. Wizara kama Wizara sijaona mkakati wowote ambao wameueleza ni namna gani watadhibiti mashirika haya kutumia fedha za umma hovyo hovyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Shirika la GEPF wakati tunapitia mpango wao ule wa uwekezaji katika Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma unaweza ukashangaa kuona kwamba wameweka mkakati wamenunua viwanja kwa mfano kule Mtwara wamenunua square meter moja kwa shilingi laki moja na elfu arobaini na nne na something, ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kiwanja hiki sijui wamenunua mbinguni au wamenunua wapi, ni uwekezaji ambao hauna tija. Nazungumzia suala hili la uwekezaji kwamba lazima kama Wizara wahakikishe kwamba wanaweka mechanism iliyokuwa bora kabisa ili waweze kuhimiza uwekezaji wenye tija na Taifa letu liweze kuwa na manufaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia pia kuna kiwanja kimenunuliwa Mwanza ambapo GEPF wanaenda kujenga shopping mall lakini ukiangalia square meter moja wamenunua shilingi laki moja na elfu kumi na tano kana kwamba hicho kiwanja kina dhahabu. Hapa nazungumzia suala zima la uwekezaji wenye tija kwa sababu Wizara hii kazi yake ni kuhakikisha kwamba inachochea Watanzania na mashirika ya ndani ya nchi yaweze kuwekeza uwekezaji wenye tija na siyo uwekezaji wa kifisadi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo suala zima la viwanda. Waziri hapa kazungumzia kwa kiasi kikubwa sana na alikuwa anaruka sana wakati anazungumzia kwamba sasa hivi Taifa letu litajenga viwanda vya kutosha na nchi yetu itaondokana na umaskini kupitia sekta hii ya viwanda. Nizungumza hapa wakati ule tunachangia Mpango wa Serikali kwamba viwanda hivi lazima viwekewe utaratibu maalum wa kuhakikisha kwamba Watanzania walioajiriwa wanafanya kazi kwa tija ili waweze kuondokana na umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia Kiwanda cha Dangote, nimekuwa nikilia sana kwenye Bunge lako hili, ambacho kipo Mtwara Mjini pale, kile kiwanda kimewekezwa na wawekezaji kutoka nje, mwekezaji kutoka Nigeria anaitwa Aliko Dangote, lakini mashirika yaliyopo mle ndani ambayo yanaajiri Watanzania ambao ndio leo hii tunawazungumzia hapa kwamba waondokane na umaskini kile kiwanda kinanyanyasa kwa kiasi kikubwa Watanzania waliopo mle ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia hata namna ya upataji wa kazi, wananchi wa Mikoa ya Kusini wa Mtwara na Lindi ili wapate kazi mle ndani lazima watoe rushwa kuanzia shilingi laki tatu na elfu hamsini. Nilizungumza hapa na nilimwomba Mheshimiwa Waziri ahakikishe kwamba anaunda Tume Maalum ije Mtwara ifanye ukaguzi wa haya ninayozungumza na mwisho wa siku waweze kuwachukulia hatua wale watu, lakini kama Waziri anarukaruka na kusema kwamba tunawekeza katika viwanda wakati hivyo viwanda vichache vilivyopo, watu wananyanyaswa, wanapewa mshahara mdogo, wanapewa shilingi elfu sita kwa siku badala ya shilingi elfu kumi na mbili halafu tunasema kwamba tunataka tuondoe umaskini kupitia viwanda! Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri ahakikishe kwamba anatembelea kiwanda hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la ajabu kabisa kwa wananchi wa Mikoa ya Kusini, hiki Kiwanda cha Dangote kimeanza kuzalisha cement, cement inazalishwa kwa wingi sana. Cha ajabu ni kwamba, bei ya cement Mtwara na Lindi ambako ndiko cement yenyewe inatoka ni shilingi elfu kumi na tatu na mia tano ukija Dar es Salaam, cement ile ile inayotoka Mtwara mpaka Dar es Salaam kilomita zaidi ya mia tano inauzwa shilingi elfu kumi na mbili, huku sio kuwadharau wananchi wa Kusini?
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tunazungumza sana kwamba, tumenyanyasika sana Wanakusini lakini tukizungumza mnatupiga mabomu, mnatuletea Wanajeshi. Haiwezekani na haikubaliki hata kidogo na wala haingii akilini kwa watu wenye akili, kiwanda kiko Mtwara, halafu kinazalisha cement, pale pale Mtwara shilingi elfu kumi na tatu na mia tano, ikisafirishwa kwenda Dar es Salaam na maeneo mengine shilingi elfu kumi na mbili na mia tano, huku ni kuwadharau wananchi wa Kusini na wananchi wa Kusini tunasema tutachoka hivi sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze kidogo suala zima la Viwanda vya Korosho. Viwanda vya Korosho kwa mfano pale Mtwara, kulikuwa na kiwanda kidogo kinaitwa Kiwanda cha OLAM, lakini kwa usimamizi mbovu wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi kile kiwanda kimeachwa kinahamishwa badala ya kutengeneza mazingira rafiki, hiki kiwanda niseme tu kwamba kilikuwa kinaajri takribani akinamama 6,000 ambao walikuwa wanabangua korosho, lakini hakikutengenezewa mazingira rafiki, kikafanyiwa hujuma, mwisho wa siku yule mwekezaji amekihamisha hiki kiwanda na kukipeleka Mozambique. Halafu tunasema kwamba tunataka tuweke mazingira rafiki!
Mheshimiwa Naibu Spika, kila mmoja anafahamu kwamba kama kweli Serikali ingekuwa makini ikajikita katika kuwekeza na kufungua viwanda vidogo vidogo vya korosho, tunaamini kabisa umaskini ungeweza kuondoka katika Mikoa yetu hii ya Kusini na Tanzania kiujumla. Tunasema tu kwenye makaratasi, mikakati yetu haioneshi kwamba kweli tuna nia ya dhati ya kuhakikisha tunajenga viwanda hivi ili tuweze kuwakomboa wananchi wetu ambao ni maskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana, kama kweli tunahitaji kufufua viwanda ili viweze kuleta tija kwa Watanzania, tujenge Viwanda vya Korosho. Korosho yenyewe, kama unavyojua kwamba, kila kitu kinachotoka kwenye korosho ni thamani. Maganda yenyewe ni thamani, mafuta ni thamani, korosho zenyewe ni thamani! Tuhakikishe kwamba tunayenga viwanda vya korosho maeneo ya Kusini na Tanzania kiujumla ili tuweze kuondokana na umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimalizie kwa kusema kwa mfano tuna madini ya Tanzanite, nilikuwa nafanya utafiti mdogo tu, nilikuwa naingia kwenye maduka kuangalia ni madini gani sasa hivi yana thamani. Ukiingia dukani ukakuta Tanzanite unaona ni miongoni mwa madini ambayo yana thamani kuliko madini mengine sasa hivi. Nashauri tujenge viwanda vya kufanya processing.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru sana kwa
kunipa nafasi hii niweze kuchangia taarifa hizi mbili za Kamati ya Nishati na Kamati ya
Miundombinu. Lakini kabla ya yote naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye
ameendelea kunipa afya njema na leo hii nimesimama hapa katika upande huu nikiwa peke
yangu kabisa na afya njema kuwawakilisha wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini ambao
wamenituma nije nieleze haya ambayo nakusudia kuyaeleza hivi sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze Wenyeviti wote wa Kamati zote mbili kwa
mawasilisho yao mazuri kabisa. Niungane na wenzangu kutoa vipengele kadhaa ambavyo
wameweza kuvionesha katika taarifa zao zote mbili.
Nianze na Wizara hii ama taarifa hii ya Miundombinu, moja kwa moja sehemu moja
wamezungumza kwamba, Serikali imeweka ama imeanza mkakati wa kupanua viwanja vya
ndege na mimi ni-declare interest ni Mjumbe wa Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma,
tuliweza kutembelea pale Dar es Salaam, Terminal III kuangalia upanuzi wa ule uwanja.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo ambalo naweza kulizungumza kwamba, tulipata
maelezo pale kwa yule mkandarasi kuna suala hili ambalo Mwenyekiti wa Kamati kaeleza
kwamba ucheleweshwaji wa kupewa pesa ili waweze kuendelea na ule ujenzi na ule ujenzi
uweze kukamilika kwa wakati. Hili suala kwa kweli, Serikali inatakiwa iliangalie kwa jicho la
kipekee kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka hivi sasa tunavyozungumza ni kwamba ujenzi wa
utanuzi ule unasuasua kwa sababu yule mkandarasi hajamaliziwa pesa zake. Kwa hiyo, tulikuwa
tunaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja atueleze kwa nini anachelewesha
kumpa mkandarasi pesa ili utanuzi wa ile Terminal III uweze kwisha kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nizungumzie utanuzi huu uendane sambamba na
utanuzi wa viwanja vile tunaita viwanja vya kanda, kwa mfano Kanda ya Kusini kiwanja kikuu
kiko Mtwara Mjini na pale Mtwara Mjini tulizungumza wakati wa bajeti mwaka uliopita kwamba
ule uwanja hauna taa, ule uwanja unatakiwa utanuliwe! Ule uwanja safari moja tulishindwa
kutua pale tukalazimika kurudi Dar es Salaam kwa sababu ya ukosefu wa taa na taa zilikuwepo
huko miaka ya nyuma, lakini ziliweza kuondolewa hatujui zilipelekwa wapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri
atakapohitimisha hoja hii atueleze ya kwamba mkakati upoje wa kutanua ule uwanja wa
Mtwara ikiwemo sambamba na kuweka taa za ule uwanja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine nizungumzie suala hili la utanuzi wa bandari,
wenzangu wamezungumza sana hapa kwamba kuna mkakati huu kwa mujibu wa Kamati wa
kutanua Bandari za Mtwara na Tanga. Lakini katika utanuzi wa bandari hizi, Mtwara haikutajwa
kinaga ubaga kama ilivyotajwa bandari zingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri atakavyokuja
kuhitimisha hoja atueleze kwa sababu mwaka jana tulipitisha bajeti hapa kwamba kuna utanuzi
wa gati moja Mtwara Mjini ambapo Bandari ya Mtwara tunasema ni bandari yenye kina kirefu
kuliko bandari zote Afrika Mashariki na kati lakini bado nimezungumza na Meneja wa ile bandari
pale Mtwara anasema bado mkataba ule haujasainiwa; pesa zilitengwa sasa tunataka kujua
kwamba tatizo ni nini mpaka leo hawajasaini ule mkataba wa kutanua gati la Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nizungumze suala hili la meli ambalo limetajwa katika
Kamati kwamba inaipongeza Serikali kununua meli na wanataka kukarabati meli za Ziwa
Victoria lakini niombe kwamba isiwe tu katika Ziwa Victoria; tuna Bahari ya Hindi kwa mfano
Mtwara miaka ya nyuma tulikuwa tunasafiri kwa usafiri wa meli kwa kiasi kikubwa na niseme tu
kwamba sasa hivi pale kuna kiwanda ambacho kinazalisha cement kwa kiasi kikubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Dangote anasafirisha anasafirisha cement yake kwa
barabara na barabara inaharibika sana wakati Mtwara tuna bandari yenye kina kirefu
angeweza kununua meli mzigo wake ukawa unapitia katika Bandari ya Mtwara kuelekea Dar es Salaam na kwingineko duniani. Lakini tunaacha hatuboreshi, hatununui meli kwa ajili ya
usafirishaji wa mizigo kwa kupitia Bandari ya Mtwara - Dar es Salaam na kipindi kile tulikuwa
tunaafiri kutoka Mtwara mpaka Zanzibar kwa kupitia Bahari ya Hindi; sasa hivi haya mambo
hayapo kabisa na wala hayatajwi kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe sana kwamba Serikali ihakikishe ya kwamba
inavyoboresha ununuzi wa meli katika Ziwa Victoria wahakikishe na Bahari ya Hindi pia kuwe na
ununuzi wa hizi meli, lakini hata kule Ziwa Victoria, ukienda kule Ziwa Tanganyika pia kule
Kigoma wana shida sana ya usafiri wa meli kuelekea nchi zile za jirani. Nilikuwa naomba kuwe
na uunganishaji wa aina hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala hili la barabara ambalo Kamati imezungumza kwa
kiasi kikubwa kwamba kuna ucheleweshwaji wa pesa za ujenzi wa barabara na niseme tu hata
barabara ile ya kutoka Mtwara Mjini kwenda Mivata ambayo inaunganisha Wilaya zote za
Mtwara Mjini na Mheshimiwa Ghasia juzi aliuliza swali hapa ndani kwamba mkataba ule
unasubiri nini kusainiwa? Na ukimuuliza Meneja wa TANROADS anasema tayari umesainiwa lakini
Waziri anasema bado haujasainiwa kuna mambo wanayashughulikia; sasa sijui imekwama wapi
kusaini ujenzi ule wa kilometa 50 kutoka Mtwara Mjini mpaka Mivata; tunaomba tupate taarifa
kutoka kwa Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika nishati na madini; hivi sasa ninavyozungumza
Mtwara na Lindi takribani miezi zaidi ya mitatu hivi sasa umeme unakatika sana; kila sekunde
umeme unakata. Tunashukuru sana Serikali kwamba imeweza kutanua wigo wa umeme kutoka
Mtwara Mjini kuelekea Lindi na Wilaya zake zote. Sasa tunashangaa kwamba utanuzi huu
hauendani sambamba na kuhakikisha kwamba nishati ile inapatikana na ufanisi. Mtwara Mjini,
Lindi na Wilaya zake zote umeme unakatika sana, tunaomba maelezo ya kina kutoka kwa
Mheshimiwa Waziri hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nizungumze kidogo ambalo Kamati pia imegusia suala la
madini Tanzanite One. Hili suala mimi nikiwa chuoni mwaka 2008 alitembelea Rais wa Afrika
Kusini wakati ule Mheshimiwa Thabo Mbeki alikuwa na article yake aliandika inaitwa “African
Renaissance” yaani kwamba Waafrika tunatakiwa tufufuke tena upya na alikuwa ametueleza
sana kwamba watanzania nyie sisi tuna madini haya ya Tanzanite ambayo yanapatikana
Tanzania tu; dunia nzima wanategemea Tanzania lakini wanufaikaji wa kwanza ni Wamarekani,
wanufaika namba mbili ni Wahindi, watatu ni Waafrika Kusini, wanne ni Wakenya na watano ni
sisi wenyewe Watanzania; yaani sisi wenyewe ni wa mwisho. Alitueleza haya Mheshimiwa Rais
Thabo Mbeki pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Nkurumah Hall. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tangu mwaka 2008 yule ametufungua masikio lakini
mpaka leo bado tuaambiwa kwamba kampuni ama taasisi hii ya madini ya Serikali (STAMICO)
inajiendesha kihasara; tunashangaa hasara hizi zinatoka wapi? Wakati madini tunayo yamejaa
kweli kweli na haya yapo Tanzania tu hata tungeamua wenyewe kuuza bei yoyote tunayohitaji.
Kwa nini tusiende kujifunza kwa wenzetu ambao wameendelea kupitia sekta hii ya madini kwa
mfano Botswana kanchi kidogo tu, tunashindwa nini na Wizara ipo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nieleze kwamba hii STAMICO kampuni ama taasisi hii ya
madini imeshindwa kufanya kazi zake, wakati tunahoji kwenye Kamati ya PIC juzi tu hapa
hawana hata mtaji, wanadaiwa kwelikweli wakati tuna madini yamejaa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana kama Serikali imeshindwa kuziwezesha hizi
taasisi zake ikiwemo STAMICO basi ni vyema ingeifuta kwamba kusiwe na hii taasisi kwasababu
tunaendelea kutumia resources nyingi za Kiserikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimalizie suala hili la kusambaza gesi ambalo Kamati
imezungumza pia kwamba kuna ucheleweshwaji wa kusambaza gesi ambayo tulipitisha
kwenye bajeti hapa katika Bunge lako hili Tukufu lakini nieleze na niombe sana kwamba
usambazaji huu uanzie kule inakotoka gesi Mtwara na Lindi ili iweze kutunufaisha sisi na
baadaye kunufaisha Watanzania wote kama ilivyokuwa kwenye korosho. Ahsante sana kwa
kunipa nafasi hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ABDALLAH N. MAFTAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii nami niweze kuchangia mjadala huu jioni hii ya leo inayohusu Wizara ya Elimu. Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunipa afya njema na leo hii niweze kuchangia Wizara hii ipasavyo. Niseme tu kwamba ninayezungumza hapa pia ni Mwalimu, lakini bahati nzuri nimekuwa kwenye sekta hii ya elimu kama Mkuu wa Shuke kwa miaka mitano, kwa hiyo, nitakachozungumza hapa naomba kitiliwe maanani sana na Waheshimiwa Mawaziri wote wanaonisikiliza; Waziri wa TAMISEMI na Waziri wa Elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kauli ya Mwalimu Nyerere mwaka 1968 kwenye kitabu chake cha Education and Self Reliance, naomba nimnukuu, alisema hivi: “an antithesis of education is a kind of learning that enables an individual a learner to attain skills and knowledge and use that skill and knowledge to liberate himself and society in which he or she lives by participating in doing developmental actions.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Mwalimu Nyerere mwaka 1968 alizungumza maneno haya, akiwa na maana ya kwamba, kinyume kabisa na mambo mengine yote, elimu ni jambo la msingi sana; na yule aliyeenda shule, lazima miaka yake yote anayosoma darasani aweze ku-acqure skills, ujuzi na knowledge ile lakini aweze kuitumia ile knowledge kujikomboa mwenyewe lakini kuikomboa jamii inayimzunguka kwa maana ya kwamba kulikomboa Taifa hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza haya kwa masikitiko makubwa sana. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikileta danadana katika suala hili la elimu kwa miaka mingi sana. Kila Waziri anayeingia anakuja na mitaala yake, anabadilisha system ya elimu; kila Waziri anayekuja anakuja kutunga Sera za Elimu. Mwisho wa siku Taifa kama Taifa hatuna sera, hatuna mtaala mmoja; kila siku tunayumba na hatuwezi kufikia malengo haya ambayo Mwalimu Nyerere aliyazungumza ya kwamba lengo la elimu ni kumfanya aliyesoma aweze kujikomboa mwenyewe na kuikomboa jamii yake inayomzunguka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawezi kuikomboa wala kujikomboa mwenyewe kwasababu elimu yenyewe anayoipata kwasababu inakuwa haina dira, haina mwelekeo kwa maana kwamba hapati elimu ile tunasema quality education, elimu bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nalizungumza hili kwasababu leo hii tunavyozungumza kuna Wizara mbili, zote zinashughulikia elimu. Ipo Wizara ya TAMISEMI na ipo Wizara ya Elimu. Cha ajabu kabisa, nimesikia hapa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wakizungumza wakisema hiki usizungumze kwenye Wizara hii ya leo kwasababu hili lipo ndani ya TAMISEMI, wakati sisi Wabunge tunafahamu ya kuwa wakati Waziri Mkuu alivyowasilisha kwa kiasi kikubwa hatuweza kujadili mambo ya elimu. Kwa hiyo, leo ni siku yetu kama Wabunge tuweze kuwaeleza Waheshimiwa Mawaziri wote wawili kwasababu nchi hii, mitaala yake na mfumo wake unayumbayumba katika elimu, lazima tuwaeleze. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika hili kwa mtazamo wangu na kwa uelewa wangu na kama Mwalimu mzoefu, siwezi kutofautisha kati ya Wizara ya Elimu ya Waziri Mheshimiwa Ndalichako na Wizara ya TAMISEMI inayoshughulikia elimu. Wote ni kitu kimoja!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala hili la elimu; ili tuweze kuwa na elimu bora ni lazima tuanze katika ngazi zote za elimu. Leo hatuwezi kuzungumzia suala zima la vocational training; elimu ya ufundi ambayo Mheshimiwa Profesa Ndalichako anaishughulikia na elimu ya juu kama hatujaweka misingi imara kuanzia pre-primary education. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kuwa na wanafunzi wazuri ambao wakifundishwa vocational skills katika vyuo mbalimbali vya VETA Tanzania, ambao wataweza kufundishwa elimu ya juu, lazima wawe wamefundishwa vizuri kuanzia chekechea. Kwa hiyo, Serikali lazima ihakikishe kwamba inawekeza Elimu ya Msingi kuanzia pre-primary school education. Nazungumza haya kwasababu tumezungumza sana kuhusu elimu ya juu kana kwamba hii elimu ya juu inaanzia elimu ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2015 na mwaka 2014 nilikuwa nimefanya utafiti mmoja nikiwa Mwalimu; Mwenyekiti wa Wakuu wa Shule Wilaya ya Lindi, nilipewa paper ya ku-present mbele ya Mheshimiwa Kassim Majaliwa inayohusu matokeo makubwa katika elimu. Katika conclusion yangu niliweza kuzungumza baada ya utafiti wangu nilioufanya kwamba huwezi kuzungumia matokeo makubwa katika elimu and then ukaweka neno sasa hivi, kitu ambacho hakiwezekani kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwasababu elimu kama elimu ni mchakato ambao ni endelevu. Mwanafunzi anatakiwa afundishwe kwa muda wa miaka miwili au miaka mitatu elimu ya awali. Afundishwe vizuri! Afundishwe vizuri elimu ya msingi lakini akifika sekondari afundishwe vizuri, ndiyo mwanafunzi huyu atakuwa na uwezo wa kufundishwa elimu ya ufundi kwa kufundishwa masomo ya Form Five na Six na masomo ya degree yake, ataweza kufanya vizuri na ataweza kuwa mwanafunzi ambaye atajikomboa yeye mwenyewe na kuikomboa jamii yake inayomzunguka, lakini siyo danadana na mzaha tunaoufanya leo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwakuwa hili haliwezi kuepukika kama nilivyoeleza hatuwezi kufanya separation kati ya Elimu ya Msingi, Sekondari na Elimu ya Vyuo. Naomba nizungumzie suala zima ambalo Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza, kuhusu elimu bure. Wizara kama Wizara imetoa Waraka Na. 6 na hapa Mheshimiwa Waziri amezungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ule waraka kuna maelekezo Waheshimiwa Wabunge naomba myasikilize ambayo yanaeleza, nami hapa waraka wenyewe ninao hapa, huu hapa Waraka Na. 6. Imeelezwa mle ndani kwamba katika mgawanyo wa pesa zinazopelekwa shuleni inatakiwa zitumike katika muktadha ufuatao: Matumizi ya kwanza ni matumizi ya jumla ya ofisi. Hapa tunamaanisha vitambulisho, shajara, maandalio, ulinzi, umeme, maji na fedha za kujikimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine (b), kuna suala zima la uendeshaji wa taaluma, kuna suala zima la mitihani endelezi, kuna suala zima la madawa baridi ya binadamu, mahitaji ya wasichana na kadhalika na matengenezo madogo madogo. Sasa jambo la kusikitisha, ukija katika utekelezaji wa hiyo sera, nilikuwa nafanya utafiti tu kwenye shule zangu kule Jimbo la Mtwara Mjini, ni jambo la ajabu sana. Shule imepelekewa shilingi 27,000/= halafu inaambiwa ifanye mgawanyo huo wote.
MHE. ABDALLAH N. MAFTAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siungi mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia makadirio haya ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenijalia kuwa na afya njema na leo hii naweza kuchangia bajeti hii ipasavyo na siyo matusi kama wanavyofanya wachangiaji wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza moja kwa moja na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa…
Taarifa...
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeipokea taarifa, wasubiri, wasikilize kwa sababu sichomi sindano nazungumza maneno tu ya kawaida. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati niko mwaka wa kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nilikuwa napitia kitabu kimoja kimeandikwa na Ishumi na Nyirenda cha saikolojia. Kuna kipengele kimoja amekieleza kwa kiasi kikubwa sana, kwamba philosophy is the study of fundamental
questions. Wakati anaeleza Mheshimiwa huyu Ishumi na Nyirenda akaliweka neno moja kwamba falsafa maana yake wewe unayesoma lazima uweze kujiuliza swali kwamba hiki unachoelezwa maana yake ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lazima uweke swali, why, kwamba umeelezwa nenda Bungeni, kamtukane Mheshimiwa Sakaya, Mheshimiwa Profesa Lipumba, Mheshimiwa Maftaha na Msajili wa Vyama vya Siasa halafu unabeba kama mbuzi, umebeba kama mzigo kwenye gunia unakuja Bungeni na wewe unakuja kutukana. Hii ni kukosa weledi na kukosa ufahamu wa kielimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi kama nimesoma shule nimeelimishwa, siwezi kufanya haya. Kila unalotumwa na mtu kwamba kalifanye hili, lazima nijiulize kwa nini eti unanituma niende nikamtukane Mwenyekiti wa Chama Taifa, siwezi kufanya haya kwa sababu nina uelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna suala hapa limepotoshwa kwa kiasi kikubwa sana. Waheshimiwa Wabunge hapa wamekuwa wakizungumza na hawapo wamekimbia nje, kwamba eti Msajili wa Vyama vya Siasa amemrudisha Mwenyekiti wa Chama Taifa, Profesa Ibarahim Lipumba kuwa Mwenyekiti wa Chama, hili naomba nikanushe na Watanzania na Bunge hili liweze kufahamu sio kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chama cha Wananchi CUF mwaka jana 2016 mwezi Agosti, tarehe 21, tulikuwa na Mkutano Mkuu wa Chama Taifa. Naomba nizungumze haya ili Watanzania waweze kufahamu kwamba ni nini kinaendelea ndani ya Chama cha Wananchi CUF badala ya kumbebesha mzigo Msajili wa Vyama vya Siasa. Tarehe 21 Agosti 2016 tulipofanya Mkutano Mkuu Chama cha Wananchi CUF kulikuwa na mambo ambayo hayakufanywa sawasawa na Katibu wa Chama kwa makusudi kabisa eti kwa sababu hamuhitaji Profesa Lipumba kuwa Mwenyekiti wa Chama wakati Katiba ya Chama cha Wananchi CUF, Ibara ya 117(1)(2) kinaonesha kabisa kwamba Mwenyekiti wa Chama
cha Wananchi CUF ni Profesa Ibrahim Haruna Lipumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa katika mkutano wetu wa ndani ya chama tuliweza kuona mambo ambayo kimsingi siyo mambo ambayo yanaweza yakafanywa na kiongozi mkubwa kama Katibu Mkuu wetu wa Chama cha Wananchi CUF. Mambo yaliyotokea, kwa sababu
tunazungumza suala la utawala bora hapa na utawala bora pamoja na vyama viendeshe taratibu zao sawasawa. Naipongeza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kusimamia vyama vyetu vya siasa sawasawa kwa sababu watu wanatumia kama SACCOS zao binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulivyoingia kwenye ukumbi wa mkutano upande wa Katibu Mkuu wa Chama, Maalim Seif Shariff Hamad alileta wajumbe 116 kutoka Zanzibar kinyume na taratibu za Katiba ya CUF eti waje kupiga kura ya hapana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa miongoni mwa watu waliouliza maswali ndani ya ukumbi ule, nikahoji kwamba hawa wajumbe 116 ambao wameongezwa kutoka upande wa Zanzibar wapo kwa mujibu wa Katiba na kama wameongezwa mbona upande wa Bara hawapo? Majibu yalikuwa ni kwamba hao wameongezwa ni wajumbe maalum. Tukamuuliza wajumbe maalum mbona huku Bara haukuwateua wajumbe maalum, wakawa hawana majibu wakasema tutawafukuzeni chama, hivi vyama lazima viangaliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kusema kwamba eti Msajili kazi yake ni kusajili tu vyama vya siasa na baadaye kuvifuta, Sheria Na. 5 ya mwaka 1992 ilivyoanzisha vyama vya siasa inampa mamlaka Msajili wa Vyama vya Siasa kusajili pamoja na kuvilea. Naomba niulize swali, hivi unavyosema kuvilea maana yake ni nini, ni kwamba kumchukua mtoto kumweka pale na wewe ukatembea zako, si lazima umwangalie mwenendo wake na takwimu zake ziko vipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wajumbe wa Mkutano Mkuu Taifa wa Chama cha Wananchi CUF tarehe 21, Agosti, 2016 tulivyoona kwamba yanafanyika mambo ambayo ni kinyume na taratibu za uendeshaji wa vikao vyote duniani tukasema kwamba hatuwezi kukubaliana na haya. Wajumbe asilimia 99 kutoka upande wa Tanzania Bara tulikuwa tunataka marekebisho na utaratibu uendeshwe sawasawa likiwemo suala la kuondolewa wajumbe 116 walioletwa kinyume na taratibu za Katiba ya CUF. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulivyomueleza Mheshimiwa Katibu akasema hapana hatutakubaliana na hilo. Pia tukamhoji kwamba kuna watu wameongezwa tunaambiwa wanatoka vyama vingine wameongezwa kama wajumbe waje kupiga kura humu ndani tunaomba tufanye uhakiki wa kila wilaya, akakataa akasema hatufanyi uhakiki, mimi ndio Katibu Mkuu, mimi ndiyo mwenye chama. Sisi tulichofanya tukasema hatuwezi kuendelea na mjadala huu mpaka haya yarekebishwe, kama Wajumbe wa Mkutano Mkuu Taifa tuna uhalali wa kuyarekebisha haya. Wakaenda juu wakaleta vyombo vya habari wakasema kwamba tunakwenda kulazimisha kupiga kura wakati wajumbe zaidi ya 400 tulikataa kwamba tusipige kura kwa sababu hoja ya Kujiuzulu kwa Mwenyekiti ni lazima sisi Wajumbe wa Mkutano Mkuu tukubali sasa Mheshimiwa umejaza wajumbe kutoka Zanzibar ambao sio halali ili kuongeza namba, hatuwezi kukubaliana na hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mengi sana, wakaingia wakaita vyombo vya habari wakasema Mkutano Mkuu umeridhia kujiuzulu kwake kitu ambacho siyo sahihi kabisa. Sisi ndani ya ukumbi tukasajili majina yetu, zaidi ya 324 tukaenda kwa Msajili wa Vyama vya Siasa tukilalamika
kwamba taratibu za uendeshaji wa vikao vya Chama hiki cha Siasa cha CUF zimekiukwa kwa makusudi, tunaomba utupe tafsiri. Msajili wa Vyama vya Siasa alituita sisi wote, upande wa walalamikaji sisi Wajumbe wa Mkutano Mkuu zaidi ya 320, upande wa Katibu Mkuu, tukaitwa tukakaa wote tukawa tumepewa miongozo zaidi ya mara nne, mara tano na mwisho wa siku Msajili wa Vyama vya Siasa akatoa mwongozo kwamba kwa mujibu wa Katiba ya CUF Profesa Ibrahim Lipumba ndio Mwenyekiti halali wa Chama cha Wananchi CUF Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nazungumza haya kwa sababu yameelezwa sana, kuna upotoshwaji unaofanywa kwa makusudi eti kwa sababu ya kuwahadaa Watanzania kwa sababu ya kutafuta huruma kupitia Bunge hili wanakuja wanasema uongo eti kwa sababu wametumwa na mtu mmoja. Chama ni taasisi, chama sio mtu mmoja, chama ni uamuzi wa wanachama ndugu zangu na tunasema tutasimamia hili mpaka mwisho wetu na Profesa Lipumba ndiyo Mwenyekiti halali wa Chama cha Wananchi CUF. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala hapa limezungumzwa kwamba Msajili wa Vyama vya Siasa eti ametoa ruzuku akishirikiana na wahuni wake. Naomba nizungumze tu kwamba ruzuku ya Chama cha Wananchi CUF imeletwa kwa mujibu wa Sheria ya Ruzuku za Vyama vya Siasa na hivi ninavyozungumza baada ya ruzuku kuletwa kwenye chama, Mheshimiwa Mwenyekiti na Kamati Tendaji Taifa, hata mimi ni mjumbe pia, ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje ya Chama cha Wananchi CUF, tulikaa tukapeleka ruzuku wilayani. Tulivyopeleka ruzuku Wilayani ili ziweze
kujenga chama na kulipia posho, Mheshimiwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF akaandika barua kwa Meneja wa Benki Kuu kwamba afungie ruzuku akaunti za wilaya ambazo hata yeye hana mamlaka nazo na tunashangaa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Ofisi ya Waziri Mkuu ilishughulikie hili suala kwamba kwa nini Meneja wa NMB Tanzania ameandikia barua akaunti zote za wilaya za Chama cha Wananchi CUF ambazo wao ndiyo wamefungua akaunti, hazikufunguliwa na Katibu Mkuu Maalim Seif Shariff Hamad lakini hivi ninavyozungumza zimefungiwa na zile pesa hazifanyi kazi ya chama, ziko kwenye akaunti za NMB Tanzania nzima. Tunaomba sana huyu Meneja wa NMB Taifa achukuliwe hatua kwa nini anaingilia akaunti za Chama cha Wananchi CUF ngazi ya wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nizungumze ni suala hili la viwanda ambalo limeelezwa kwa kiasi kikubwa sana. Miaka ya karibuni Serikali iliweza kupitisha sera kwamba ajira zote hivi sasa ziweze kusimamiwa na wamiliki wa viwanda na taasisi husika. Hata hivyo, pale Mtwara katika kiwanda cha… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na niseme tu kwamba naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia mwelekeo huu wa mpango asubuhi hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuchangia mwelekeo huu wa mpango, naomba Nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu-Wataala ambaye ameendelea kunijalia afya njema leo hii, lakini pia niweze kumshukuru Mwenyekiti wa chama changu, Chama cha Wananchi (CUF), full-bright Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, kwa kuendelea kushirikiana vizuri kutetea maslahi ya Watanzania na hasa katika rasilimali zetu za madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niweze kuzungumza kidogo kwamba sisi Chama cha Wananchi (CUF) ilani zetu zote za uchaguzi kuanzia mwaka 1995, mwaka 2000, mpaka mwaka 2010 tulikuwa tunazunguka Tanzania nzima kuwaeleza Watanzania ya kwamba rasilimali za madini ya nchi hii zinatumiwa kwa kiasi kikubwa na wageni wa nje na sisi wenyewe kila shilingi 100 tunapata shilingi tatu tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii nizungumze katika Bunge lako hili kwa namna ya kipekee kabisa niweze kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu huyu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba anasimamia Ilani ya Chama cha Wananchi (CUF), anasimamia itikaChama cha Wananchi (CUF), Sera ya Utajirisho kwamba madini yetu yaweze kuwanufaisha Watanzania na sisi lazima tuunge mkono kama chama imara cha siasa, CUF - Chama cha Wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kuchangia mwelekeo huu wa mpango kwa kusema ya kwamba viwanda kwa kiasi kikubwa sana, nilikuwa nasikiliza hotuba zote mbili, hotuba ya Mheshimiwa Waziri na hotuba ya Kamati ambazo zimezungumzia suala zima la viwanda, na tumekuwa tunazungumza sana kwamba sehemu hii ya viwanda ni sehemu muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishawahi kusema katika Bunge hili wakati nachangia mpango mwaka wa jana na mwaka wa juzi, kwamba nchi nyingi duniani ziliweza kuendelea kupitia sekta ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, karne ya 15, ukisoma historia, sisi tuliosoma historia tunaambiwa ya kwamba nchi zote za Ulaya ziliweza kufanya mapinduzi ya viwanda na hatimaye wakaweza kuwa matajiri mpaka leo hii tunasema wao ndio wanaotusaidia sisi nchi za ulimwengu wa tatu. Kwa hiyo, kwa umuhimu wake hili suala ni suala nyeti sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la ajabu, tulikuwa tumezungumza wakati wa bajeti hapa kwamba wapo wawekezaji wengi wanaohitaji kuwekeza Tanzania. Kule Mtwara kuna wawekezaji wa Kijerumani na Kamati hapa imeeleza ambao wanataka kujenga viwanda vya mbolea, pale Mtwara Msangamkuu. Kule Kilwa pia kuna mwekezaji ameamua kuwekeza kwa kujenga kiwanda cha mbolea, lakini bado Serikali tunaona inasuasua kuwapa rasilimali ya gesi wale wawekezaji ili waweze kujenga vile viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini viwanda vikijengwa pale Mtwara Msangamkuu wananchi wengi wa Mtwara watapata ajira, wananchi wa Kilwa kule kikiwepo kiwanda watapata ajira na umaskini utaweza kuondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana katika mwelekeo huu wa mpango kwamba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hotuba yake atueleze kwa nini mpaka leo wale wawekezaji wanaotaka kuwekeza viwanda vya mbolea pale Msangamkuu, Mtwara Vijijini ambapo ni karibu kabisa yaani ni pua na mdomo katika Jimbo langu la Mtwara Mjini, lakini pia kule Kilwa bado mpaka leo Serikali inasuasua kuwapa wale wawekezaji gesi waweze kujenga viwanda vya mbolea ili kuweza kuondokana na umaskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuzungumzia suala la umeme REA. Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mpango, amezungumza hapa kwa kiasi kikubwa kwamba umeme unaotumika mikoa ya kusini unatoka Mtwara Mjini, viwanda vya kusindika ile mitambo vimejengwa Mtwara Mjini, lakini jambo la ajabu nimekuwa ninazungumza sana, kwenye Mabunge yako yote nimekuwa nazungumza hili; kwamba pale Mtwara Mjini kwenyewe ambapo ndipo mitambo yote ya kusindika umeme ipo, bado kuna maeneo mengi haujapelekwa mtandao wa umeme ikiwemo kule Mbawala Chini, Naulongo, Mkunjanguo na maeneo mengine ambamo pia tulisema kwamba mule mnapita kitu kinachoitwa mkuza wa gesi, lile bomba la gesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tumelia sana kwa muda mrefu katika Bunge hili na Mheshimiwa Waziri akiwa anaahidi kwamba atapeleka umeme kule kote. Sasa ni jambo la ajabu sana kwamba kila mwaka tuwe tunarudia na kurudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaomba katika Mpango huu ambao unaandaliwa, hili suala la kuhakikisha ya kwamba umeme wa REA unasambazwa basi usambazwe kwenye maeneo yote kwa sababu wananchi wa maeneo yale ambapo ni vijiji ambavyo viko mjini lakini bado tunaita ni vijiji kwa sababu vinahitaji kupita umeme wa REA uweze kwenda kule; Tunaomba Serikali ihakikishe ya kwamba inapeleka na sio kila mwaka kupiga dana dana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vipo vijiji vingi pia kule Mtwara na Lindi, bado, na wakandarasi wenyewe waliopewa ukiwauliza wanatuambiwa huko sisi hatuna bajeti, bajeti yetu sisi ni kutoka kijiji hiki tunaingia vijiji vya Tandahimba, Newala na wapi, lakini bado tunahitaji wananchi wale waweze kupelekewa umeme. Ili tuweze kuondokana na umaskini lazima kila kijiji, hata kama kipo mjini, basi umeme uweze kufika. Tunaomba sana hili Mheshimiwa Waziri aje atueleze mpango huu wa maendeleo ameliwekaje mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninataka nilizungumze hapa ni suala la kilimo. Katika Mkutano wa Bunge wa bajeti, wakati tunapitisha Bajeti ya Wizara ya Kilimo nilizungumzia suala zima la korosho. Kulikuwa na suala la mboleo, nilieleza wakati ule na nilimnukuu mtaalam mmoja anaitwa Kunz, mwaka 1988/1989 katika kitabu chake cha Managerial, alisema kwamba failure to plan is planning to fail, kwamba ukifeli kupanga maana yake unapanga kufeli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilizungumza suala la mbolea, kwamba walisema kwamba watagawa mbolea bure kwa wakulima wetu wa korosho lakini halikupangwa lile; na hapa leo kwenye mwelekeo huu wa Mpango bado sijaona pia kama limepangwa. Kilichotokea wakulima wamelanguliwa mbolea badala ya kuuziwa shilingi 20,000 wakanunua mbolea mfuko mmoja shilingi 100,000, 150,000 wengine mpaka shilingi 200,000 baadhi ya maeneo, ni kwa sababu Serikali ilishindwa kupanga sawasawa suala hili la kugawa mbolea bure kwa wakulima wa korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na korosho ndilo zao ambalo linaingiza pesa nyingi Serikalini kuliko zao lolote. Linaanza zao la korosho then inakuja tumbaku. Kwa hiyo, ninaomba kwamba mpango wetu wa safari hii upange sawa sawa, kwamba ni kiasi gani cha mbolea kitapelekwa kwa wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la ajabu katika korosho pia, nilikuwa napitia taarifa za masoko ya dunia; bei ya korosho soko la dunia, kilo moja ni dola 29. Ukijumuisha, ukigawa kwa pesa yetu ya Kitanzania ni sawa sawa na almost kama shilingi 49,000; shilingi 50,000 hivi kwa kilo moja, katika soko la dunia. Kama Bandari ya Mtwara itatumika sawa sawa, ukisafirisha korosho kutoka Bandari ya Mtwara mpaka soko la dunia, bei ya korosho haizidi kilo moja shilingi 2,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba sana, pamoja na kwamba tunajigamba, na tunashukuru kwa kweli kwamba Serikali imejitahidi kuongeza bei ya korosho kwa wakulima, hivi sasa ni shilingi 3,800 mpaka 3,850, lakini bado mkulima angeweza kupata bei kubwa zaidi ya hii kutokana na umuhimu na unyeti wa zao la korosho duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana Serikali ihakikishe inatafuta wanunuzi wa korosho ili korosho yetu hii iweze kuingiza pesa nyingi zaidi ya hizi ambazo tunazipata Hazina, lakini kwa wananchi wetu waweze kuondokana na umasikini, hasa maeneo ya Mtwara na Lindi pamoja na Pwani na maeneo mengine wanayolima korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la ajabu sana nilikuwa napitia taarifa pia za kimtandao kwamba hata katika zile nchi ambazo zinalima korosho duniani, Tanzania haipo. Afrika kuna Côte d’Ivoire, imewekwa Afrika Kusini, imewekwa Thailand na nchi nyingine, Tanzania sisi tunajulikana kwamba hatulimi korosho wakati wanunuzi waliopo Thailand, wanunuzi waliopo India wanakuja kununua korosho Tanzania. Hili linapoteza pia thamani na pato zaidi. Kwa sababu hawa wanunuzi wa kule nchi za nje wanakwenda kununua kule kwenye nchi ambazo zimewekwa kwenye taarifa mbalimbali za kidunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba hili mlizingatie, ni jambo la muhimu sana ambalo ninaomba kuchangia katika huu Mpango ni sekta ya utalii nchini. Ninaomba kuzungumzia suala zima la sekta ya utalii nchini…

T A A R I F A

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei taarifa kwa sababu kadandia gari kwa mbele. Nilichozungumza ni kwamba katika orodha ya nchi zinazouza korosho duniani Tanzania haipo, ndiyo taarifa iliyopo pale. Sasa yeye anazungumza yawezekana kwamba hajasoma sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kwa sababu kanipotezea muda bure tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninaomba kuchangia katika huu mwelekeo wa mpango ni sekta ya utalii nchini. Sekta hii ya utalii nchini ni sekta muhimu sana na taarifa ambayo tulipewa hapa Bungeni, tulielezwa ya kwamba Tanzania ina vivutio vingi sana, ukiondoa Brazili inayofuata ni Tanzania. Hata hivyo nikapitia mpango wa Wizara ya Maliasili na Utalii, kuna pesa ambazo wameziweka zinaitwa pesa za REGROW, wamekopa Benki ya Dunia kwa ajili ya kuendeleza sekta ya utalii kule Nyanda za Juu Kusini. Sasa ninaomba sana zile pesa dola milioni moja ambazo zimekopwa Benki ya Dunia kwa ajili ya kuendeleza utalii Nyanda za Juu Kusini basi zifike kule Kusini pia ili sekta hii ya utalii iweze kutangazwa sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na katika hili, pale Mtwara Mjini tuna eneo la Mikindani. Mikindani kuna majengo ya kale sana. Sasa nimeangalia taarifa hapa sijaona mpango uliowekwa sawasawa juu ya sekta ya mambokale katika utalii kwamba Serikali imejipangaje kutangaza mambokale ili iweze kuwaingizia pesa Serikali ya Tanzania, lakini wananchi kwa ujumla kwa kupata ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mikindani kuna majengo na vivutio vingine vingi vya kale, lakini vivutio vile vimeachwa kwa wazungu, watu wanaoitwa Trade Aid ndio wanaokarabati, ndio wanaotangaza na kukusanya pesa wakati Serikali hii ina shida ya pesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba sana kwamba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha mpango sekta hii ya utalii iangalie sekta ya mambo kale na hasa hasa utalii katika maeneo haya ya Mikoa ya Kusini ya Mtwara na Lindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninataka kulizungumza ni suala hili la miundombinu. Tunaishukuru Serikali kwa kiasi kikubwa imekuwa ikijenga miundombinu, imekuwa ikijenga barabara lakini pia imeweza kuleta pesa za kutosha pale Mtwara Mjini na linajengwa gati linajengwa la mita 300.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana, sambamba na upanuzi wa Bandari uliopo Mtwara Mjini hivi sasa tunaomba swala la reli hili ambalo imekuwa Serikali imekuwa ikizungumza kila mwaka, kila siku, reli ya Kusini, ili Mtwara corridor iweze kufunguka, iweze kufungua uchumi wa ukanda ule wa Kusini lazima hili suala la kujenga reli kutoka bandari ya Mtwara kwenda Mchuchuma na Liganga kule kwenye makaa ya mawe iweze kuwekwa kwenye bajeti ya mwaka huu, pesa ziweze kutengwa ili sasa uchumi wa Kusini na Watanzania uweze kusheheni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, reli hii ilikuwepo miaka ya nyuma lakini iliondolewa, sijui iliondolewa kwa sababu gani. Sasa tunaomba sana, kwa sababu kuna mkakati unaitwa Mtwara corridor wa kufungua Kusini mwa Tanzania ili Tanzania yetu sasa iweze kweli kuwa ni Tanzania ya uchumi. Bandari yetu inavyojengwa kama reli ikijengwa mizigo ikiletwa pale tunaamini ya kwamba bandari itaingiza pesa nyingi na bajeti yetu itakuwa haisuisui tena kwa sababu ya makusanyo. Tusiangalie sana Bandari ya Dar es Salaam, tutanue Kusini, tutanue Mtwara corridor kama tulivyokuwa tunaahaidi siku zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, naomba nizungumze suala zima la ardhi. Wakati tunapitia bajeti hapa, Mheshimiwa Waziri wa Ardhi alizungumzia mipango mikakati, na tunashukuru kwa kweli pale Mtwara Mjini tumezindua mpango kabambe wa ardhi. Hata hivyo kuna mambo ambayo yalizungumzwa na kuahaidiwa katika Bunge lako hili Tukufu, suala la kulipa fidia kwa maeneo ambayo Serikali ilichukua. Kwa mfano, Mtwara Mjini eneo la Mji Mwema, Serikali ilihaidi kwamba mpaka mwezi wa nane mwaka huu itakuwa tayari imelipa fidia. Jambo la ajabu wanaleta taarifa kwamba Serikali imeshindwa kuwalipa wale watu wa Mji Mwema wakati wale watu wamechukuliwa ardhi tangu mwaka 2013, ni jambo la ajabu sana. Tunazungumza ndani ya Bunge, tunapanga ndani ya Bunge wananchi wanasikia halafu baadaye Serikali inasema haina pesa kupitia UTT, UTT wameghairi kulipa. Ni jambo la ajabu kwa kuwa tunazungumza, tunapitisha kwenye bajeti lakini utekelezaji wa haya mambo ya msingi unakuwa hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri atakavyokuja atueleze kwamba mkakati upoje kuhusiana na sekta hii ya ardhi ambayo bado ina changamoto nyingi; Tanzania pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wa Mbingu na Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nasoma degree ya kwanza pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nilisoma course moja, African Political Thought. Wakati ule napitia kile kitabu, kuna Mwanazuoni mmoja anaitwa Okodiba Noli, aliwahi kusema kwamba “a state is political organization with territoriality recognize boundaries and independent government.” Akiwa na maana ya kwamba nchi yoyote ni taasisi ya kisiasa ambayo ina watu wake, ina mipaka yake lakini kubwa zaidi, ina Serikali ambayo ni independent.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipitia mafuhumu zaidi ya maelezo ya Mwanazuoni huyu, anamaanisha kwamba katika nchi yoyote lazima kuwe na Serikali ambayo kazi yake kubwa ni kulinda rasilimali na kulinda watu wake. Naomba nitumie fursa hii kulipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri inayofanya ya kuhakikisha kwamba inalinda amani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na leo hii sisi kama Wabunge tuko katika Bunge hili tukishiriki mijadala hii ya Bunge kwa amani na utulivu kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza pia Jeshi la Ulinzi na Usalama na Jeshi la Polisi kwa kuweza kudhibiti hali mbaya ambayo imetokea miezi kadhaa iliyopita pale Kibiti. Sasa hivi sisi wananchi wa Kusini tunapita kwa amani kabisa. Hii ndiyo dhana ya kwamba nchi yoyote iliyokuwa huru lazima iweze kujilinda na iweze kulinda mipaka yake pamoja na raia wake, nalipongeza sana Jeshi la Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi, naomba nichukue fursa hii pia kueleza baadhi ya mambo ambayo kimsingi yanapaswa kufanywa sawasawa wakati tunalinda rasilimali na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 25 mwezi wa Tatu pale Mtwara Mjini, kijana mmoja ambaye anajulikana kwa Abdillah Abdulahman, alikuwa katika ufukwe wa bahari wa maeneo ya Kianga akiwa anajitafutia kitoweo, sisi watu wa Pwani tunaita kumbwa, wale wadudu wa sea shells; wakati anajitafutia kitoweo hiki, ghafla wakatokea Jeshi la Polisi ambao tunasema ni kikosi kazi ambacho kimeundwa na Wizara ya Uvuvi na Maliasili, wakawa wamemwita yule kijana. Kijana kwa kawaida, kwa sababu Jeshi letu la Polisi linaogopeka kidogo, alivyoona anaitwa akakimbia. Askari wakaamua kumpiga risasi kisogoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi, wahakikishe ya kwamba wanafanya uchunguzi sawasawa kabla ya kuweza kuchukua hatua hizi za kuweza kuwamiminia watu risasi pale wanapofanya operation maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze suala la Mahakama ambapo tulipitisha katika Bunge hili tarehe moja mwezi wa Saba mwaka 2017, tulipitisha sheria hapa ya Mahakama ya Mafisadi Tanzania. Jambo la kusikitisha kabisa, ukipitia kwenye Halmashauri zetu, kwa mfano, pale Mtwara Mjini, wafanyakazi wa Halmashauri waliweza kutafuna zaidi ya shilingi milioni 800.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewasilisha taarifa hizi Serikalini kwa muda mrefu sana, lakini jambo la ajabu ni kwamba wanaotafuna hizi shilingi milioni 800 mpaka shilingi milioni 900 hawapaswi kushtakiwa kwenye Mahakama ya Mafisadi. Sasa ni jambo la ajabu sana! Halmashauri kutafuna pesa zaidi ya shilingi milioni 800, ni pesa nyingi sana, pesa ambazo zingeweza kujenga shule, zingeweza kujenga miundombinu, zingeweza kununua dawa, lakini zinatafunwa na wale waliotafuna hawaitwi mafisadi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kwamba iletwe sheria Bungeni tuipitishe kwamba pesa za Serikali zikitafunwa kuanzia shilingi milioni 200, 300, 400 mpaka 600 bado wapelekwe kwenye Mahakama ile ya Ufisadi. Kuweka shilingi bilioni moja, ni nyingi sana, Halmashauri zetu zinatafunwa sana, tunaomba sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama yanavyofukuliwa makaburi katika maeneo mengine; makaburi yanafukuliwa kwenye vyeti, kwenye taasisi za kiserikali, lakini tulikuwa tunaomba sana wale waliotafuna pesa, mabilioni mengi miaka miwili, miaka mitatu, miaka mitano iliyopita, wachukuliwe hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mahakama hii ya Mafisadi iweze kuwachukuliwa hatua. Kwa sababu Wanasheria wanasema kwamba sheria haiendi retrospective, lakini kwa sababu Taifa hili limetafunwa sana, Taifa hili tumekuwa masikini hapa kwa sababu ya watu wachache, wajanja wachache ambao tuliwapa dhamana ya kusimamia rasilimali zetu, lakini wamechukua pesa zetu na mwisho wa siku Tanzania tunasema ni maskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukipitia kwenye sekta mbalimbali, kwa mfano, Sekta ya Utalii, mabilioni ya pesa yameweza kutafunwa sana. Jambo la ajabu sana, niliwahi kuzungumza wakati nachangia mjadala wa taarifa za Kamati hapa; Taarifa ya Kamati ya Maliasili na Utalii, ukipitia Olduvai Gorge ni eneo pekee ambalo binadamu wa kale alipatikana duniani, liko Tanzania, ni Olduvai Gorge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya nyuma ukipitia taarifa za Serikali, Olduvai Gorge ilikuwa inakusanya karibu shilingi 1,700,000,000 kwa mwaka. Sasa hivi wajanja wachache wakahakikisha kwamba Olduvai Gorge wanaitoa kwenye eneo la malikale na kulipeleka kwenye Taasisi ya Ngorongoro na badala yake sasa hivi linakusanya shilingi milioni 700.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni ufisadi. Watendaji wana under estimate pale kwa ajili ya kujinufaisha wao binafsi. Tunaomba Mahakama hii ya Ufisadi Tanzania, ifanye kazi yake ipasavyo. Tusiseme kwamba eti mpaka pesa ifike shilingi bilioni moja, basi mtu aweze kushtakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo hapa nimezungumza pia wakati naanza utangulizi wangu kwamba mtengano wowote wa Kitaifa unataegemea na kugawana fursa hizi sawasawa kama Taifa. Leo hii Tanzania kila kanda ina hospitali ya kanda, isipokuwa kanda ya Kusini pekee, jengo linaanza kujengwa takribani miaka 10 iliyopita hivi sasa, mpaka leo halijakamilika pale Mtwara Mitengo. Mpaka leo jengo la Hospitali ya Kanda ya Kusini limejengwa zaidi ya miaka 10 halijakamilika, lakini maeneo yote kuna Hospitali za Kanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshindwa kuzungumza maeneno haya kwa muda mrefu sana. Tumekuwa tukiongea kwa muda mrefu sana kwamba rasilimali hizi za Taifa zigawanywe sawasawa ili kanda nyingine na Kanda ya Kusini pia tuweze kupata Hospitali hii ya Rufaa, pesa ziweze kutengwa kwenye bajeti zinazokuja, nasi Wanakusini tuweze kunufaika na rasilimali hizi za Kitaifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tunazungumza kwa muda mrefu sana; na ikumbukwe mwaka 2013 wananchi wa Mikoa ya Kusini waliandamana sana wakidai rasilimali ziweze kuwanufaisha kama Watanzania wengine. Wapo watu waliokuja kupotosha Watanzania, wakasema kwamba Wanakusini wanahitaji gesi watumie peke yao, kitu ambacho hakikuwa sahihi kabisa. Tulichokuwa tunasema ni kama ilivyo kwenye korosho kwamba korosho zimekusanya mabilioni ya pesa, pesa zote zinapelekwa katika Mfuko wa Hazina na zinatumika kwa ajili ya Watanzania wote kununua dawa, kujenga barabara na miundombinu mingine ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nasema suala la umeme Kusini limekuwa ni kizungumkuti sana. Tunaipongeza Serikali kwamba imenunua mashine mbili ambazo zinaenda kutoa megawati nane; bado tatizo la umeme litakuwa ni endelevu, ni miezi zaidi ya saba hivi sasa, Mtwara na Lindi hatuna umeme wa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jambo hili linapelekea viwanda kutojengwa Mtwara. Pia limepelekea wawekezaji kukimbia Mtwara. Tunaiomba Serikali, naomba Ofisi ya Waziri Mkuu ije na mpango wa kudumu wa kuhakikisha kwamba Mikoa hii ya Kusini tunakuwa na umeme wa uhakika ili wawekezaji waweze kuja Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kama Serikali ingeamua kuondoa tatizo la umeme Kusini ingenunua mashine moja tu ambayo inatoa megawati 20; na tulikuwa tunapitia taarifa mbalimbali, Wizara ikaenda wataalam wakaenda kuangalia Ujerumani, kuna mashine moja ambayo itaweza kutoa megawati 20 za umeme ambazo zitaweza kusambaza umeme Mtwara na Lindi, inauzwa shilingi bilioni 50 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali kweli ingekuwa na nia ya dhati ya kuhakikisha kwamba inataka kuondoa tatizo la umeme Kusini, basi ingeweza kununua mashine moja ya megawati 20, inauzwa shilingi bilioni 50, siyo nyingi. Kwenye korosho tunakusanya billions of money ambazo zinasaidia Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba sana Serikali iangalie kwa jicho la kipekee kabisa, suala hili la umeme Kusini liweze kwisha. Hatutaki kurudi kule tulikotoka, wananchi wanadai sana. Ukifanya mikutano hadhara, kila mwananchi anazungumza suala la umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Serikali iliyopita iliweka utaratibu kwamba pale kunapotoka rasilimali yenyewe, hii gesi basi wananchi wapate unafuu. Ikaweka punguzo la kuunganisha umeme, badala ya kuunganisha umeme kwa Sh.370,000/= ikawa Sh.190,000/= hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kila mwananchi anakuja kwenye mikutano ya hadhara anauliza kwani hili punguzo ambalo Serikali liliweka kwa nini mmeliondoa wakati gesi ipo? Nami nauliza, gesi bado ipo, kwa nini punguzo ambalo Serikali iliweka kwenye umeme, leo hii Serikali inasema imeondoa punguzo hili? Naomba sana kwamba sekta hii isaidie Wanakusini ili Serikali iweze kusemwa sawasawa na wananchi hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, kuna suala hili la dawa za kulevya. Tunaipongeza Serikali, imeweza kuzuia dawa za kulevya nchini, ni jambo zuri sana, kwa sababu vijana wetu walikuwa hawaeleweki; ilikuwa inapoteza nguvu kazi. Serikali lazima iwekeze vya kutosha kudhibiti uvutaji na uenezaji wa dawa za kulevya Tanzania. Naiomba Serikali, pale inapofikia kuangamiza madawa ya kulevya, kama inavyochoma moto mashamba ya bangi, basi hata tukikamata Cocaine na Heroin tushuhudie zikiwa zinachomwa hadharani kama zinavyochoma bangi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila siku Serikali imekuwa inatuambia kwamba imekamata kilo 10 kilo 20, gramu sijui ngapi za Heroin au Cocaine, lakini hatuoni zinaangamizwa au zinachomwa moto. Tunataka Serikali iangamize tukiwa tunaona kama tunavyoona kwenye bangi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu, pia hotuba ya Waziri Mkuu imezungumza kwamba inatenga zaidi ya shilingi bilioni 20.8 kila mwezi kupeleka shule za msingi na sekondari kwa maana ya kugharamia elimu ya msingi. Ni jambo jema sana. Wakati huo wa nyuma kulikuwa na michango mingi katika shule ambayo ilikuwa inachangishwa na wazazi. Leo hii ukipita maeneo ya kusini, mzazi ukimwambia achangie hata chakula cha mtoto wake ili mtoto aweze kusoma akiwa ameshiba, kile anachofundishwa aweze kukielewa sawasawa, anasema na Serikali imesema elimu bure. Nani amekwambia uchangie? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetamka hapa kwamba michango yote ipitie kwa Mkurugenzi. Mkurugenzi huyu mnamtwisha mzigo mkubwa sana. Haiwezekani leo mpaka mchango wa Sh.5,000/= wa shule ya msingi, shule zote zilizopo za msingi na sekondari akusanye Mkurugenzi. Tunarudisha nyuma elimu yetu bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mkurugenzi huyu apunguziwe mzigo na Serikali itoe tamko kwamba suala la chakula cha mchana shuleni kuanzia shule za msingi mpaka sekondari ni jambo la lazima na wazazi lazima wahusike kuchangia chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala hili limezungumzwa na wenzangu hapa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumzia suala la migogoro ya ardhi, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeliona hili kwamba kuna migogoro mingi ya ardhi, ni kweli kabisa. Naitaka Serikali pale ambapo iliahidi kwamba italipa fidia, kwa mfano pale Mtwara Mjini, Mji Mwema, basi ahakikishe kwamba inalipa fidia za wananchi wale siyo Serikali inakuwa na kauli mbili mbili kwamba, leo wanasema tutatoa fidia maeneo tuliyoyachukua, baadaye inasema Serikali haiwezi kutoa. Tutazungumza haya katika Wizara ya Nyumba, Ardhi na Maendeleo ya Makaazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia bajeti hii ya Nishati na Madini. Kabla sijaanza kutoa salamu za Wanamtwara na maagizo ya Wanamtwara kwa Wizara hii, naomba kwanza nitoe masikitiko yangu kwa kiasi kikubwa sana. Mheshimiwa Waziri hapa wakati anawasilisha hotuba yake kazungumzia mambo mengi yanayohusu gesi, mambo mengi yanayohusu petroli na mambo mengi yanayohusu mafuta ambayo ndiyo chachu ya uchumi wetu wa sasa hivi hapa nchini Tanzania.
Mheshimiwa Spika, masikitiko yangu, nilikuwa napitia gazeti leo hii, gazeiti la The Citizen, CAG ameeleza masikitiko yake makubwa kabisa na naomba ninukuu, halafu nimuulize Mheshimiwa Waziri swali langu. Amesema hivi:
“It was unfortunate that NAOT does not have a single expert in auditing accounts related to oil and gas despite trillions of cubic feet of fossil fuel reserves having been discovered in Tanzania”.
Mheshimiwa Spika, gazeti la leo, kwamba anasikitika na anaeleza, analiambia Taifa hili kwamba pamoja na umuhimu wa gesi na mafuta tuliokuwa nayo na wingi wake wote, lakini hana mamlaka ya kwenda kukagua, sasa sijui tatizo ni nini? Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kutoa majibu atueleze kwa nini account zile zinazotokana na visima vya mafuta na gesi havikaguliwi na CAG.
Mheshimiwa Spika, naomba nianze kuzungumzia suala zima hili la umeme vijijini. Ile Mikoa ya Kusini tuna bomba la gesi na kwa bahati nzuri Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini alizungumza katika mihadhara yake mingi sana kwamba Wanamtwara na Lindi watakuwa wananufaika na gesi kupitia mle lilimopita bomba la gesi kupitia Sekta ya Umeme.
Mheshimiwa Spika, mpaka hivi sasa ninavyozungumza ule unaitwa mkuza wa bomba la gesi ambalo Serikali imekuwa inaahidi kupitia miradi yake ya REA Awamu ya Kwanza, REA Awamu ya pili, mpaka hivi sasa tunakwenda kwenye REA Awamu ya tatu bado vijiji vile vyote havijapata umeme huu pamoja na ahadi nyingi na majigambo makubwa ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri ya kwamba, ni lini sasa atahakikisha kwamba maeneo yote yanayopita bomba la gesi, mkuza wa gesi, anatekeleza ahadi yake ya kupeleka umeme? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna suala hili la wananchi wa mikoa ya kusini kunufaika na gesi. Hata hivyo, nitoe masikitiko yangu makubwa sana, kwamba tumekuwa tunazungumza sana, tumekuwa tukiahidi sana, tukieleza sana, kuliko kutekeleza.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa napitia mpango wa TPDC wakati tuko kwenye Kamati, lakini juzi taarifa yao tumekuwa tunapitia. Kuna mkakati ambao Serikali wameweka wa kuhakikisha kwamba gesi inayotoka mikoa ya kusini, Mtwara na Lindi inafika Dar es Salaam, baadaye itapelekwa mikoa mingine ya kaskazini kwa mfano Tanga, Mwanza na maeneo mengine. Katika mkakati ule pia wameeleza kwamba hii gesi itakuwa inapelekwa kwa ajili ya matumizi ya majumbani kuanzia Dar es Salaam, lakini cha ajabu ukipitia taarifa ile ya TPDC mikoa ya kusini, Mtwara na Lindi haipo.
Mheshimiwa Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri atakapokuja na majibu yake atueleze wananchi wa Mtwara na Lindi mkakati ukoje. Kwa sababu niliuliza swali hili wakati tunasikiliza taarifa ya Kamati ya Nishati na Madini tulivyowaita kwenye Kamati yetu hii ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma na wakasema kwamba watakwenda kulishughulikia. Naomba majibu ya Mheshimiwa Waziri kwamba asije akawa anazungumza tu wakati kwenye maandishi kule hakuna na Wanamtwara na Wanalindi pia wanasubiri majibu stahiki kutoka kwa Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Spika, nizungumzie pia suala zima ambalo Mheshimiwa Silinde ameligusia hapa, la kuwapa wawekezaji ambao wapo mikoa hii ya kusini nishati hii ya gesi waweze kutumia kama nishati. Leo hii tuna kiwanda ambacho kilitarajiwa kujengwa Mtwara maeneo ya Msangamkuu, ni kwa miaka minne hivi sasa yule mwekezaji anaomba apewe gesi ili aweze kujenga kiwanda cha saruji, mpaka leo tunavyozungumza ni danadana tu kwenye Wizara hii ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Spika, niombe sana Mheshimiwa Waziri ahakikishe kwamba wawekezaji hawa ambao wana nia ya kuwekeza Mikoa ya Kusini wanapewa nishati hii ya gesi ili waweze kuondoa umaskini ambao wananchi wa mikoa hii ya kusini umekuwa unatutawala kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kama hiyo haitoshi, Mheshimiwa Silinde kazungumza, mwekezaji Aliko Dangote, kwa muda mrefu sana amekuwa akiomba gesi ili aweze kuitumia kama nishati. Mheshimiwa Silinde kazungumza kwamba ananunua makaa ya mawe kutoka Msumbiji, sio Msumbiji Mheshimiwa Silinde, ananunua makaa ya mawe kutoka South Africa. Meli inakuja Mtwara ku-gati kutoka South Africa ambayo mwekezaji huyu Aliko Dangote anatumia kama nishati wakati Mtwara tuna gesi iko kedekede, cubic meter za kutosha, kwa nini asipewe hizi gesi sambamba na kwamba yuko tayari kuuziwa, lakini Wizara mpaka leo inaleta danadana? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwaka 2012, wananchi wa Mtwara na Lindi waliandamana kwa kiasi kikubwa sana wakidai manufaa ya gesi, kwamba kwa namna gani hii gesi itaanza kuwanufaisha wananchi wa mikoa ile. Na madai yetu yale yalipotoshwa sana, watu walifikia wakati, wengine viongozi kabisa wa Kitaifa wakiwabeza wananchi wa kusini kwamba wao wanahitaji kutumia gesi peke yao. Madai yetu yalikuwa ni kwamba gesi inayotoka mikoa hii, kwa sababu inaanzia pale, kwanza tunufaike kwa kupata mrabaha. Nimepitia na nimesikiliza hotuba ya Mheshimiwa Waziri, wakati anawasilisha sijaona hata sehemu moja na sijamsikia anasema kwamba mrabaha kiasi gani utabakizwa Mtwara na mikoa ile ya kusini ya Mtwara na Lindi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini cha ajabu kabisa kule kwenyewe inakotoka hii gesi, Msimbati, hata barabara ya kufika Msimbati ni kizungumkuti. Kwa nini Wizara na Serikali isitenge bajeti ya kujenga angalau barabara ile kiwango cha lami kutoka Mtwara Mjini mpaka kule Msimbati? Wananchi wa kusini wakidai haki hizi mnawapiga mabomu, mnatuletea Wanajeshi na kwamba sisi hatuipendi Serikali. Tunachosema ni kwamba, Serikali ihakikishe kwamba manufaa yanayotokana na gesi hii na sisi wananchi wa kusini tuweze kunufaika nayo.
Mheshimiwa Spika, upotoshwaji unaofanywa wa kwamba tunataka tuitumie gesi peke yetu si kweli. Nazungumza haya kwa sababu tuna ushahidi wa kutosha sana, tuna ushahidi wa kutosha. Sisi wote ni mashahidi, kwa kiasi kikubwa Korosho inazalishwa Mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani, lakini korosho ile kwa taarifa za mwaka jana na miaka mingi mfululizo limekuwa ni zao ambalo linaingizia Taifa pesa nyingi sana. Mwaka jana, 2014/2015 limekuwa ni zao la pili, lakini zile pesa zinazokusanywa na mapato ya korosho zote zinapelekwa Hazina zinanufaisha Watanzania wote.
Mheshimiwa Spika, tunachosema Wanakusini, tunachosema Wanamtwara na Lindi ni kwamba tunufaike na fursa za ajira na isiwe Serikali na Wizara inaondoa fursa hizi. Kwa sababu unapomnyima mwekezaji huyu kutumia gesi, kwa mfano, Aliko Dangote akiagiza makaa yake ya mawe kutoka South Africa anakodi meli, gharama zinakuwa ni kubwa, mwisho wa siku simenti inakuwa bei mbaya. Tunaomba sana wananchi wa Mtwara na Lindi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini jambo la ajabu sana, Serikali hii imekuwa ni sharp sana katika kuondoa rasilimali za kimaendeleo Mikoa ya Kusini kuliko kupeleka kwingine. Nimekuwa nazungumza hili kwa muda mrefu sana. Bomba la gesi limejengwa kwa miezi 18 tu. Kwa miezi 18 pesa zilizotumika zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni mia mbili kama na hamsini na tano, lakini tunavyosema kwamba, tunahitaji maendeleo yaletwe kusini yanachukua muda mrefu sana. Suala la kufanya negotiation ya mkataba tu kwamba huyu mwekezaji wa Kiwanda cha Mbolea Mtwara, Dangote na yeye mwekezaji wa simenti inachukua muda mrefu, kwa nini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, siungi mkono hoja mpaka haya maswali yangu yaweze kupatiwa majibu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MAFTAH A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nguvu, uzima na afya njema ili niweze kuchangia hotuba ya Waziri wa Nishati na Madini kwa maandishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka Waziri wa Nishati na Madini afahamu kuwa mwaka 2012 Mtwara na viunga vyake kulitokea vuguvugu la gesi na wananchi wakidai haki ya ajira kupitia sekta hii muhimu, lakini kwa makusudi kabisa Serikali ilitumia nguvu kubwa kuwapiga wana Mtwara na hata kuwaua kwa risasi akiwemo mama mjamzito eneo la Mkanaled. Wapo waliovunjwa viungo vya miili yao na wapo waliochomewa nyumba moto na wapo waliopoteza mali na rasilimali ambako kulifanywa na vyombo vya dola.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali baadaye iliunda tume ya kuchunguza athari za vurugu hizo ambayo iliongozwa na Chara Mwijage, lakini cha ajabu mpaka leo hawajaleta mrejesho na wananchi pamoja na askari kadhaa pia wameathirika sana. Je, ni lini Serikali italipa athari hizi kama ilivyoahidi?
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa kutumia gesi majumbani ambao utaanza Dar es Salaam, Mwanza, Tanga na maeneo mengine, tayari mchakato wake umekamilika maeneo hayo isipokuwa Lindi na Mtwara ambako gesi yenyewe inatoka, wanasema watafanya upembuzi yakinifu. Ni jambo la ajabu sana Bomba la gesi limejengwa kwa miezi 18 tu limekamilika ila kuleta maendeleo Kusini Serikali inaleta kigugumizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri aseme ni tarehe ngapi huo upembuzi umefanyika maana mimi ni Mbunge wa Jimbo sina taarifa yoyote Mtwara? Je, ni lini gesi itasambazwa majumbani Mtwara na Lindi na ni kwa nini Waziri asianze Mtwara na Lindi ambako gesi inatoka na ipo karibu?
Mheshimiwa Naibu Spika, Mtwara mjini kuna mitaa mingi sana kama vile Chipuputa, Kihoro, Komoro, Mbawala Chini, Lwelu, Dimbuzi, Kata ya Mtawanya, Likombe, Mitengo na Naliendele maeneo mengi nguzo za umeme hazijafika.
Mheshimiwa Naibu Spika, umeme unatoka Mtwara mjini ambapo kuna plant ya kufua umeme, Makao Makuu ya TANESCO Mkoa umeme hakuna. Wananchi wanauziwa nguzo kwa pesa nyingi ambayo hawana uwezo kutokana na hali ngumu kiuchumi kwa kuwa fursa za ajira hakuna.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara kwa niaba ya wananchi wa Mtwara, kupeleka nguzo kata zote za Mtwara mjini na wasiwape wananchi mzigo wa kulipia nguzo kwa kuwa wanatakiwa kunufaika na rasilimali ya gesi ikizingatiwa ndiyo waangalizi wa miradi yote ya gesi ambayo ni muhimu kwa Taifa hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia pesa ya kuunganisha umeme hii iliyosemwa imepunguzwa hadi 99,000, bado ni nyingi, wananchi wengi hali zao ni mbaya kiuchumi, hivyo wanashindwa kumudu gharama hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba gharama hii ya 99,000 iondolewe kwa wananchi wa Mtwara na Lindi kwa kuwa rasilimali hii muhimu inalindwa na wananchi hawa, hivyo ni vyema wakalipa gharama za umeme na siyo kupewa mzigo mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, bomba la gesi liko nje sana, mimi kama Mbunge nimekuwa nawaasa wananchi walinde rasilimali hii muhimu kila siku, hivyo Wizara ihakikishe inafunika Bomba hili na hasa maeneo yaliyoathirika na mvua. Nimeeleza hili kwenye Kamati (TPDC) na leo naiomba Wizara bomba lipo nje sana Mtwara.
Mheshimiwa Naibu Spika, Msimbati inakotoka gesi yenyewe Serikali inashindwa kujenga barabara ya lami ya kutoka mjini. Ni jambo la ajabu sana hakuna kituo cha afya, maana ni kata kwa mujibu wa maeneo ya kiutawala, kwa nini Serikali isijenge kituo cha afya? Jengeni tafadhali.
Sambamba na hilo, Mtwara nzima hakuna hata shule moja au hospitali ambayo imejengwa kwa rasilimali hii inayotoka mkoani humo. Hivi naomba kuuliza, wananchi wa Mtwara wakidai haki hii ni dhambi?
Mheshimiwa Naibu Spika, namsihi sana Waziri katika hotuba yake kueleza asilimia 94 ni maendeleo, basi aiangalie Mtwara kwa namna ya kipekee kabisa ili malalamiko yaweze kwisha na Watanzania wanufaike na rasilimali hii muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mrabaha ni muhimu sana kwa wana Mtwara, mwekezaji wa kiwanda cha Mbolea anaomba gesi kwa kununua Msanga Mkuu apewe ili wana Mtwara wapate ajira, Dangote apewe gesi maana anaagiza makaa ya mawe Afrika Kusini. Pia Wizara ijenge shule ya gesi Mtwara ili kuondoa malalamiko.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuendelea kunipa uzima na afya njema, na leo naomba nichangie hoja hii ya maliasili na utalii kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Mikindani upo Manispaa ya Mtwara Mikindani ambalo ni jimbo langu. Mji huu ni mji wa asili ambao una magofu na vivutio vingi vya utalii ikiwemo Old Boma ambayo ilijengwa na Mjerumani kama ngome yake kuu ya ulinzi karne ya 19. Cha ajabu, mji huu umesahaulika, umeachwa na jambo la ajabu kabisa yanatangazwa maeneo ambayo hayana vivutio kama Mikindani. Namuomba Waziri aje na majibu juu ya kuutangaza mji huu kuwa ni mji wa kitalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtwara kuna fukwe nyingi nzuri sana ambazo kama Serikali ikitangaza watalii wengi wanaweza kuja Mtwara na hatimaye Taifa hili kupata kipato kikubwa kupitia sekta hii. Nimeuliza swali la utalii Mtwara tangu kipindi cha Kikao cha Kwanza katika Bunge lako hili mpaka leo sijapata majibu. Namtaka Waziri akija anieleze, yupo tayari hivi sasa kutangaza fukwe za Mtwara sambamba na kuzitambua katika Wizara yake kuwa kitovu kikuu cha utalii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Msimbati, Mnazibay kuna fukwe ambayo haipo duniani na kuna maua ambayo hayapo na hayaoti popote duniani isipokuwa Mnazibay tu. Nimuombe Waziri aje Mtwara nifuatane naye kama Mbunge, na asije kimya kimya ili nimuoneshe vivutio hivi vya utalii Mtwara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Lindi eneo la Mipingo, Kata ya Nangaru alichukuliwa mjusi na Wajerumani ambaye mabaki yake yapo Ujerumani. Tangu mwaka 1907 mpaka leo Wajerumani wanapata pesa nyingi kupitia mjusi huyu
mkubwa kuliko mijusi yote duniani. Serikali hii ya CCM ni lini itaenda kumrudisha mjusi huyu na kumleta Tanzania ili tunufaike na pesa za utalii?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nashukuru Mwenyezi Mungu Subhuhana Wataala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri hapa amezungumza kwa kiasi kikubwa sana na amejaribu kueleza kwamba Tanzania ni nchi ya nne Afrika kwa upatikanaji wa maji ambayo yapo chini ya ardhi ikitanguliwa na nchi ya Zambia, Mozambique, Sudan ya Kusini na ya nne ni Tanzania. Kwa hiyo, Mwenyezi Mungu ametujalia maji mengi sana Tanzania, suala lililopo ni Wizara husika kuhakikisha kwamba wanaweka mikakati ambayo inatekelezeka, mikakati ambayo mwisho wa siku itakuja kuzalisha maji na wananchi waweze kuyapata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Chikota amezungmza mradi ambao amezungumza zaidi ya miaka mitatu hivi sasa pale Mtwara, mradi ambao unatoka katika Jimbo la Nanyamba kule eneo la Mayembe Chini unakuja mpaka Mtwara Mjini. Huu mradi hivi sasa ni zaidi ya miaka minne haujakamilika na kila mwaka tunavyokuja ndani ya Bunge tukija kuhoji tunaambiwa watu wa Benki ya Exim ya China hawajatoa pesa na Serikali ipo kwenye majadiliano, tumefikisha suala hili katika Wizara ya Fedha, kwa muda mrefu na huu ni mwaka wangu wa tatu nazungumza ndani ya Bunge hili kwamba ule mradi vijiji vimechukuliwa zaidi ya vijiji 26, wananchi wamechukuliwa maeneo kutoka Jimbo la Nanyamba, Mtwara Vijijini mpaka baadhi ya mitaa ya Mtwara Mjini wamechukuliwa maeneo zaidi ya miaka mitatu hivi sasa, hawajapewa fidia kwa kigezo kwamba Exim Bank ya watu wa China haijatoa pesa za mradi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba sana Wizara ya Fedha, inavyopanga mikakati yake kwa sababu hili ni jambo la pili kwa Mtwara, liko jambo la ardhi pia Wizara ya Fedha iliahidi itatoa pesa kwa ajili kulipa fidia kupitia UTT lakini hawatoa pesa, mwisho wa siku wananchi wamechukuliwa maeneo yao. Kwa hiyo, hata hapa pia kwamba pamechukuliwa zaidi ya miaka mitatu wananchi hawa wanapaswa kulipwa fidia ili sasa na wao waweze kufanya shughuli zingine kwa sababu mashamba yao yamesitishwa kupisha mradi huu. Kwa hiyo, naomba sana Wizara ihakikishe Wizara ya Fedha inapeleka fedha kwenye miradi ya maji ili kuondoa matatizo ambayo tumezungumza kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nilizungumza hapa mwaka jana na mwaka juzi kwamba Mtwara Mjini hatuna tatizo la maji pale chini, kuna mradi ambao Serikali ilitenga bilioni tano ambapo mkandarasi alikuwa site, mkandarasi tayari ameshatafuta maji, maji yamepatikana, tumefanya pump test na maji yalikuwa ni mengi sana. Maji mengine ile clip niliichukua nikamrushia Mheshimiwa Waziri kumjulisha kwamba maji yamepatikana Mtwara Mjini katika eneo la Lwelu tunachohitaji sasa ni Wizara kutoa pesa ziweze kujenga visima, ziweze kujenga mtaro, ziweze kusambaza maji kuna maeneo zaidi ya kata tano Mtwara Mjini tuna tatizo la maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kwamba hawa wakandarasi tunaowapa miradi hii kuweza kutekeleza kwa sababu yule mkandarasi alishasema kwamba tayari amesha-raise certificate ameshapeleka Wizarani suala lililobaki ni yeye kulipwa zile pesa ili aweze kuchimba visima aweze kusambaza maji katika kata za Mtwara Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo naomba nimtajie Mheshimiwa Waziri maeneo ambayo Mtwara Mjini tunashida ya maji ziko kata zaidi ya nne hapa, katika Kata ya Mitengo pekee eneo la Mitengo Juu hatuna maji, wananchi hawana maji, eneo la Mji Mwema, Vitengo hakuna maji, Kilima Hewa hatuna maji, maji hayapo kabisa Kata ya Ufukoni, Kihole hakuna maji, Comoro ambako hata mimi mwenyewe ndiyo naishi huko hakuna maji, yaani anapoishi Mbunge maji hakuna. Lakini Soko Jinga hakuna maji, Kwa Selemu hakuna maji, Mbaye Juu hatuna majina, Mtwara Mjini na maji chini yako mengi na mkandarasi yuko site, pesa hapewi kwa ajili ya kusambaza maji. Kwa hiyo, naomba sana huyo mkandarasi certificate ameshatoa, kazi ya Wizara ni kutoa pesa ili huyu jamaa aweze kuchimba visima na aweze kusambaza mabomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengine ni pamoja na eneo la Chipuputa nalo pia liko Mtwara Mjini maji hatuna, tuna eneo la upande wa Magereza hakuna maji, kuna Mbawala Chini ile mitaa ambayo inatoka nje ya mji kidogo ambayo mwanzo ilikuwa vijiji kote hakuna maji Mbawala Chini, Naulongo, Dimbuzi, Mkunja Nguo, Mwenge, Naliendele Mikoroshoni kote hatuna maji wakati maji Mtwara yapo kedekede, suala lililobaki ni Wizara kutoa pesa kumpa mkandarasi ili aweze kusambaza haya maji na wananchi wa Mtwara Mjini waweze kupata maji kwa sababu tuna maji baridi kweli pale chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilikuwa naomba sana Wizara ihakikishe mwaka huu huyu mkandarasi anapewa fedha ili aweze kusambaza haya maji wananchi wangu wa Jimbo la Mtwara Mjini wanahitaji maji kwa kiasi kikubwa sana. Pale ambapo kuna miradi hii ya visima ambavyo vimejengwa kuna wakati fulani tulitembelea maeneo ya Ruvu Juu, Ruvu Chini kupitia Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, utakuta vyanzo vimejengwa vizuri sana pesa zimetumika nyingi sana kujenga hii miradi, lakini vile visima havijafunikwa yaani siku moja anaweza akatoa mtu tu huko chizi chizi akaja akaingia pale akamwaga uchafu akamwaga nini wananchi wanaweza kupoteza maisha, kwa sababu ya ulinzi wa visima vya maji Tanzania miradi hii mikubwa ya maji lazima ifunikwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipitia taarifa za nchi zingine maeneo mengi visima vya maji vimefunika, Tanzania visima vya maji viko naked na ulinzi wenyewe ukiangalia hakuna ulinzi wa kutosha, wakati maji ndiyo maisha ya Watanzania. Naomba sana hii miradi inavyotekelezwa kutengewe pesa maalumu, bajeti ya kufunika visima Ruvu Chini, Ruvu Juu visima vifunikwe Mtwara Mjini pale Mangamba visima vifunikwe (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati fulani taarifa zinasema wakati wa kampeni mgombea mmoja alienda akawatumia wale watumishi wa pale, akamwaga uchafu ndani ya maji, wananchi wa Mtwara tukanywa kwa sababu ulinzi wenyewe hautoshi. Sasa hii siyo Mtwara ni Tanzania nzima. Kwa hiyo, naomba sana kwamba Wizara itenge bajeti ya kuhakikisha kwamba vyanzo vya maji hivi visima hivi vya maji, mabirika haya ya maji yanafunikwa kunakuwa na ulinzi kwa ajili kuwafanya Watanzania waweze kuwa salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni mtu wa Mtwara, lakini nilikuwa naishi Lindi kama mwalimu, kuna Mradi wa Ng’apa ambao umeanza kujengwa zaidi ya miaka saba hivi sasa pale Lindi, mradi ambao ulitakiwa uende kuwanufaisha wananchi wa Lindi Mjini, wananchi wa Mitwelo pale lakini huu mradi unasuasua sana zaidi ya miaka saba sasa, mkandarasi aliyepo pale yupo taratibu sana, tunashangaa tatizo ni nini? Kwa nini maeneo mengine ya nchi hii wakandarasi wanakuwa wanakimbia kimbia hivi lakini ukija maeneo ya Kusini wakandarasi wapo taratibu na hawachukuliwi hatua yoyote. Tuna mradi huu wa Ng’apa ni wa muda mrefu wananchi wa Lindi wana matatizo kuliko maeneo yote ya Kusini mwa Tanzania hawana maji ya kutosha, maji pale Ng’apa yapo na ule mradi utatoa maji mengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa sababu kila mwaka tunaambiwa hapa mkandarasi atamaliza mwaka huu naomba usimamizi uwe wa kina yule mkandarasi amalize mradi wa Lindi Mjini ili wananchi wa Lindi Mjini waweze kupata maji na wananchi wa Mitwelo kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala hili la bill za maji, kumekuwa na malalamiko makubwa sana Tanzania, kumekuwa na malalamiko Mtwara Mjini kumekuwa na malalamiko Mikoa ya Kusini Lindi kumekuwa na malalamiko mpaka Dar es Salaam, kwamba watu wanakadiria tu bill za maji yaani wale wanaokuja kuchukua bill za maji kusoma mita hawasomi mita wanakadiria tu unaambiwa mwezi huu unalipa shilingi 40,000 mwezi huu unalipa shilingi 50,000 wakati hawajasoma exactly ni cubic meter ngapi zimeweza kutumika kwa mwezi husika, kwa hiyo, naomba Wizara iangalie hili suala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2017 nilizungumza kuhusiana na Mtwara Mjini lakini hili suala haliko Mtwara Mjini ni Tanzania mzima, wasomaji wa mita hawasomi mita wanakadiria na kuwabambikiza wananchi bill za maji kubwa ambazo ni kinyume kabisa na uhalisia wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la upotevu wa maji ni jambo ambalo limekuwa ni chronic hivi sasa, sisi tunaishi Dodoma hapa, ukipita mitaani huko maji mabomba yanapasuka sana, mabomba yanavuja sana kuna sehemu zingine barabarani kumetengeneza mpaka mabwawa, ukienda hapa Dodoma hapa njini tu eneo la Chadulu ukifika pale kila siku maji yanavuja na unatoa taarifa kwa watu wa maji hawaji kurekebisha. Tanzania nzima iko hivyo Dar es Salaam napo hivyo, leo mbona likipasuka unaweza ukatoa taarifa kwa watu wa Idara ya Maji wanachukua muda mrefu sana kuja kurekebisha. Tunaomba sana maji yanapotea kwa sababu haya maji yanatumia gharama sana kuyachimba kupatikana kwake na kuyasambaza yasiachwe yanamwagiga yanapotea.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati
MHE. MAFTAH A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Mwenyezi Mungu, Subhanahu wa taala, Mwenyezi Mungu ambaye ameendelea kunipa afya njema. Asiyeshukuru kidogo basi hata akipewa kingi hawezi kushukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tulikuwa Mtwara na Lindi tukiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa Dkt. Kalemani tumeenda kuzindua umeme, sasa hivi Mtwara na Lindi tumeunganishwa kwenye Gridi ya Taifa, tunashukuru sana. Tunashukuru sana kwa sababu na sisi sasa tumewekwa miongoni mwa Watanzania maana kwa miaka mingi tumekuwa tukililia suala la Mikoa ya Kusini kuunganishwa na Gridi ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru kwamba Mtwara Mjini hivi sasa tumezindua pia mashine mbili mpya ambazo zitaenda kutoa megawati nne za umeme lakini bado mpaka leo hazijaunganishwa sawasawa, tumeenda kuzindua tu. Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri kwamba zile mashine sasa zianze kufanya kazi kwa sababu ile juzi tukiwa pale Mtwara bado umeme usiku ulikatika kwa sababu zile mashine bado hazijaanza kufanya kazi. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri Dkt. Kalemani mashine hizi sasa ziunganishwe na mashine zingine zile tisa tuweze kuondoa tatizo la kukatika kwa umeme mikoa hii ya Mtwara na Lindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze suala hili ambalo nimekuwa nazungumza kwa muda mrefu ndani ya Bunge hili na huu ni mwaka wangu wa tatu nazungumza haya. Kumekuwa na eneo ambalo tunasema ni mkuza wa gesi ambapo bomba la gesi limepita na ikumbukwe Mikoa ya Mtwara na Lindi na hasa Jimbo la Mtwara Mjini, wananchi waliandamana wakapigwa risasi wengine wakauwawa wakidai kujua namna gani hii gesi itaweza kuwanufaisha, tukawa tumeahidiwa sana. Miongoni mwa ahadi za Serikali zilikuwa ni kupewa umeme wa uhakika. Kwa hiyo, tunashukuru sasa hivi hili linakuja kutekelezwa lakini tunaomba kuwe na kasi ya kusimika zile mashine umeme usikatikekatike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwenye haya maeneo ni ule mpango wa Serikali, waliambiwa wawapelekee wananchi nguzo za umeme lakini walichofanya ni kupeleka nguzo chache sana kwenye huo mkuza wa gesi kwa maana ya maeneo lilipopita bomba la gesi ambapo Serikali ilisema lazima wale wananchi wapate umeme. Maeneo ya Mtwara Mjini, Lindi na maeneo mengine lakini kilichofanyika Serikali imepeleka nguzo chache sana, wananchi wengi katika maeneo yale hawajapata umeme. Wakitaka kulipia umeme wanalipa kwa bei kubwa sana, nguzo wanunue kwa Sh.500,000, kitu ambacho Serikali ilishasema kwamba wale watu watapelekewa nguzo kwa sababu bomba la gesi limepita mule waweze kuunganisha umeme kwa Sh.27,000 lakini kinachotokea ni kinyume kabisa nguzo zimeenda chache sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo ya Jimbo la Mtwara Mjini, kwa mfano, Mtawanya bomba la gesi limepita mule nguzo za umeme hazijaenda kabisa, maeneo ya Magomeni, pale pale Mtwara Mjini baadhi ya maeneo nguzo hazipo. Kuna maeneo ya Chipuputa hakuna nguzo za umeme, kuna maeneo ya Kiholo, Komoro pale Mtwara Mjini, Mbaye na Mitengo, kote huko bomba la gesi limepita na Serikali iliahidi itapeleka umeme maeneo yale lakini nguzo zimeenda chache sana na wananchi wa wakienda kuomba TANESCO wanaambiwa hapa nyie ni mjini, kwa hiyo, mnalipia Sh.500,000 nguzo na ukilipa hiyo Sh.500,000 ndiyo tutakupelekea umeme. Sasa tunaenda kinyume kidogo na ahadi na nia ya Serikali. Yawezekana wakati mwingine Mheshimiwa Waziri hayajui haya lakini watendaji kule wanafanya haya, wananchi wananiagiza mimi kila siku na ndani ya Bunge hili nimekuwa nazungumza sana. Naomba sana Wizara iangalie maeneo haya ambayo yalikuwa ni ahadi ya Serikali kupeleka umeme kutokana na kupatikana kwa gesi hasa katika maeneo ya ule mkuza wa gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna maeneo pia ya pembezoni kwenye miji hii iliyopo Mtwara na Lindi, maeneo yale ambayo mwanzo kabla mji haujatangazwa kuwa Manispaa yalikuwa ni maeneo ya vijijini lakini yale maeneo yakaingizwa kwenye Manispaa lakini kumekuwa na tatizo sana la umeme na tumekuwa tunaongea sana. Ndani ya Bunge hili nimeongea sana yale maeneo ya pembezoni ambayo sasa hivi ni mitaa mwanzoni yalikuwa ni vijiji wapelekewe huu mpango wa umeme ambao Serikali inasema imeweka mkakati wa kusambaza umeme, tunasema diversification of electricity yaani yale maeneo yapelekewe isije ikawa tunatumia sana vyombo vya habari kuzungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwenye hii hotuba leo imetaja sana Mtwara na Kusini, nimekusikia sana Mheshimiwa Waziri Kalemani lakini sasa tunaomba haya maeneo umeme upelekwe kwa sababu unaambiwa na watendaji kwamba huku tunafanya kila nikikuuliza Waziri unaitikia sana unasema bwana nimepewa taarifa kwamba tunapeleka na mwaka jana uliniahidi Mheshimiwa Waziri kwamba utakuja Mtwara nikupeleke kwenye maeneo niende kukuonesha haya ninayozungumza lakini haujafika. Nikuombe mwaka huu baada ya bajeti mguu kwa mguu wewe na Naibu Waziri wako Mheshimiwa Subira anaijua sana Mtwara, kakaa sana Mtwara huyo, tunatembea mguu kwa mguu, niite mkutano wa hadhara wananchi wakupe kero hizi ambazo wananiagiza kila siku wananchi wa jimbo la Mtwara Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, safari hii kama Waziri hautaniahidi kwamba utapeleka umeme nang’ang’ania shilingi yako. Maeneo haya ni maeneo ya Mbawala Chini narudia tena Bunge hili limekuwa linanisikia sana nikiyataja, Mbawala Chini uende umeme, mfanye diversification kwenye maeneo haya. Kuna maeneo ya Kijiji Naulongo au Mtaa wa Naulongo pelekeni umeme, kuna eneo la Mkunjanguo mpaka watu sasa wananitania ndani ya Bunge wananiita Mkunjanguo kwa sababu nilikuwa nazungumza sana . (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri haya maeneo yazingatie peleka nguzo za umeme wananchi wanataka umeme, ndio manufaa yenyewe ambayo mmetuambia wananchi wa Mtwara. Kuna maeneo ya Namayanga, Dimbuzi, Mkangala tunaomba umeme muupeleke kwenye maeneo haya. Nimekuwa nalia sana, naagizwa sana, kila siku nikifanya mkutano wa hadhara wananchi wanalia sana kwenye haya maeneo. Kwa hiyo, niombe sana mlishughulikie suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala hili la punguzo la umeme. Tuliahidiwa kwamba pamoja na mambo mengine manufaa ya umeme Mikoa hii ya Kusini Mtwara na Lindi kwamba kuna gesi tutapunguziwa umeme, wananchi wakaacha kuandamana. Wananchi wamenituma kwa mara nyingine nije kuzungumza ndani ya Bunge, kwa kuwa gesi bado ipo Mtwara na Lindi, lile punguzo tunaomba liendelee kuwepo msiliondoe. Kwa sababu sasa hivi wananchi wanavyoenda kuomba kuunganishiwa umeme wanaambiwa walipe Sh.390,000 wakati pale gesi bado ipo na punguzo lilikuwepo. Naomba hili punguzo wananchi wapewe, walikuwa wanaunganisha umeme kwa Sh.97,000 kwenye yale maeneo ambayo sio mkuza wa gesi tunaomba liendelee kwa sababu gesi bado Mtwara na Lindi ipo haijaondolewa katika mikoa hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuunganisha gesi majumbani tunashukuru kwamba Serikali imezungumza kwenye hotuba hapa kwamba Mtwara nayo ipo. Majaribio ya kuunganisha gesi majumbani yameanza Masaki Dar es Salaam wakati gesi yenyewe iko Mtwara, tunashangaa sana gesi imetokea Mtwara kwa nini wasingeanza pale kwanza au sisi wana Mtwara hatuna majumba ya kutumia gesi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana isije ikawa inazungumzwa sana kwa sababu nilishaliona suala hili kwenye Kamati wakati tunapitia taarifa ya TPDC mwaka juzi ndiyo nikaliibua nikawaambia Mikoa ya Kusini ambako inatoka gesi yenyewe kumesahaulika kabisa, ilikuwa haipo kabisa. Tunashukuru safari hii mmeweka na unatuambia kwamba tunaenda kupewa hii gesi tuweze kutumia kama nishati. Hii itapunguza matumizi ya mkaa na ukataji wa misitu kule. Kwa hiyo, tunaomba suala hili Mtwara Mjini, Lindi Mheshimiwa Waziri alizingatie kwamba wananchi wanahitaji gesi majumbani isiwe inazungumzwa tu halafu mnaanza Dar es Salaam, kule kwenyewe inapotoka gesi kunakuwa ni kizungumkuti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba kuzungumzia suala la viwanda. Serikali ya Awamu ya Tano inasema kwamba ni Serikali ya viwanda. Kusini kuna wawekezaji wanahitaji kujenga viwanda vya mbolea, Petrochemical, wanataka kujenga viwanda vya mbolea Mtwara na Lindi mpaka leo bado wanapigwa danadana tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri mwaka huu hawa watu wape gesi waweze kujenga viwanda vya mbolea kwa sababu viwanda vitatoa ajira kwa wananchi wa Mtwara na Lindi na sisi tutaondokana na umaskini kwa sababu gesi hii Mwenyezi Mungu ametupatia imeanzia pale. Wenzetu maeneo mengi ya Tanzania viwanda vimejengwa siku nyingi sisi tuna kiwanda kimoja tu cha Dangote nacho kinasuasua.

Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri safari hii unitekelezee mambo haya, ahsante sana.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Namshukuru Mwenyezi Mungu, Subhannah-Wataalah.

Nianze kuuliza maswali kwa Wizara hii ya Fedha na swali langu la kwanza nilikuwa naomba kujua, kwa sababu Wizara hii ndiyo Wizara mama; na wakati tunachangia Wizara mbalimbali ambapo Wizara hii inaenda kutoa fedha; mara nyingi Mheshimiwa Waziri Mpango anakuwa hayupo ndani ya Bunge. Naomba kujua kwa nini Mheshimiwa Waziri Mpango huwa mara nyingi tukiwa tunachangia bajeti mbalimbali hizi ambazo yeye ndio kikwazo cha kutoa fedha kwenye miradi mbalimbali, ndani ya Bunge anakuwa hayupo? Hilo ni jambo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo naomba kujua kutoka kwenye Wizara hii, kuna suala hili la kutopeleka fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo. Hili limekuwa ni tatizo sana. Tulikuwa tunasikiliza taarifa ya Kamati hapa, ni asilimia tano tu ndiyo zimeweza kupelekwa mwaka 2017 kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo. Sasa tatizo nini? Tunaomba Mheshimiwa Mpango atueleze.

Mheshimiwa Spika, hapa naomba niongee kwa mifano kwamba miradi mbalimbali na hasa iliyopo maeneo ya Kusini mwa Tanzania, Mtwara na Lindi, Wizara ya Fedha imekuwa na kigugumizi kikubwa sana cha kupeleka fedha za maendeleo kwenye Mikoa hii ya Kusini.

Mheshimiwa Spika, mradi wa kwanza ambao naomba nizungumzie hapa ni mradi mkubwa ambao Serikali imekuwa inazungumzwa kabla hata hatujaingia kwenye mpango wa kujenga reli ya kati hii ambayo inaenda kujenga kwa kiwango cha standard gauge. Kusini kumekuwa kunazungumzwa mradi wa reli kutoka Bandari ya Mtwara kuelekea Mchuchuma, Liganga na Mbambabay na kule Kusini ili kuweze sasa kufunguka. Imekuwa inazungumzwa kwa muda mrefu sana na Mheshimiwa Waziri Mpango amekuwa anazungumza kila mwaka feasibility study na hizo pesa hajawahi kuzipeleka.

Mheshimiwa Spika, tunaomba atakapokuja kuhitimisha hapa, atueleze, kwa nini hataki kupeleka fedha za feasibility study ambazo kila mwaka wanaweka kwenye bajeti, wanaweka kwenye Mpango lakini hataki kuleta fedha hizi ili sasa ile Reli ya Kusini ambayo mwaka 1963 iling’olewa kwa makusudi kabisa na Serikali hii, ikapelekwa maeneo mengine, lakini hata kuirudisha mnakuwa na kigugumizi sana. Hata ile feasibility study hataki kuleta pesa. Mwaka 2017 tuliambiwa shilingi bilioni mbili zimetengwa kwamba Mchina sijui nani ameshapatikana, lakini mpaka leo zile fedha hazijaletwa na Mheshimiwa Mpango. Tunaomba atueleze wakati wa kuhitimisha bajeti, miradi hii ya Kusini anakuwa na kigugumizi sana kuleta fedha kwa ajili ya kufanya feasibility study.

Mheshimiwa Spika, mradi mwingine ambao naomba Mheshimiwa Mpango akija hapa atueleze, ni mradi wa maji ambao unatoka Mto Ruvuma. Hii ni bajeti ya tatu tunazungumza suala hili; na tatizo tunaambiwa ni Wizara ya Fedha haijapeleka fedha. Mradi wa Maji wa Mto Ruvuma, vimechukuliwa zaidi ya vijiji 26 vya wananchi; wananchi wamechukuliwa maeneo yao, mashamba yao kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, Serikali inasema itakuja kulipa fidia, lakini inasema Wizara ya Fedha haipeleki fedha kila mwaka. Sasa tunaomba akija hapa atueleze, kwa nini mradi ule mkubwa wa maji kutoka Mto Ruvuma kuja Mtwara Mjini hataki kutoa fedha na kila mwaka anatenga Bajeti?

Mheshimiwa Spika, mradi mwingine ambao naomba Mheshimiwa Mpango aje atueleze hapa wakati wa kuhitimisha hii hoja, atueleze UTT PID ambayo ilichukua maeneo ya wananchi Mtwara, katika Mtaa wa Mji Mwema, mashamba yamechukuliwa pale, tangu mwaka 2013. Serikali ilikuja ndani ya Bunge hili ikasema kwamba inaenda kutoa fidia. Nina Hansard zaidi ya mbili ambazo Wizara iliahidi hapa kwamba itaenda kutoa fidia.

Mheshimiwa Spika, wananchi wamechukuliwa mashamba, wamechukuliwa maeneo yao ambayo walikuwa wanaendeleza kiuchumi, lakini mpaka leo tunavyozungumza, Wizara ya Mheshimiwa Mpango haitaki kupeleka fedha. Niliuliza kwenye Wizara ya Ardhi, nikauliza kwenye Wizara ya TAMISEMI nikaambiwa tatizo ni UTT PID ambayo ipo chini ya Wizara ya Fedha haitaki kupeleka fidia kwa wananchi hawa wa Jimbo la Mtwara Mjini. Naomba uje utueleze kwa nini hutaki kuleta fedha Mheshimiwa Mpango kwenye miradi hii iliyopo Mtwara na Lindi?

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumze pia suala hili la EFD machines. Kuna hawa ambao wamepewa Uwakala (authorized dealers) ambao ndio wanaosambaza hizi mashine na wamechukua fedha kwa wananchi ambao ni wafanyabiashara wadogo wadogo maeneo ya Lindi na Mtwara hasa pale Mji wa Lindi. Wamelipa shilingi 690,000 lakini zile mashine hawazipeleki kwa wananchi. Wale mliowapa uwakala wa kusambaza EFD machines wanachelewesha kuzipeleka kwa wananchi, lakini kinachotokea sasa, TRA inaingia kwenye maduka yale na kufunga maduka na kuwabambikizia kodi wale wananchi, wakati Serikali haitaki kupeleka zile mashine kupitia dealers ambao mmewaweka ninyi Wizara ya Fedha. Tunaomba mkija mtupe maelekezo, kwa nini wananchi wanatoa fedha na wanakaa muda mrefu sana bila ya kuzipeleka zile mashine za EFD kwa wananchi, wafanyabiashara hawa wadogo wadogo?

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nilikuwa naomba, Mheshimiwa Mpango hapa atakapokuja ku-wind up atueleze, ukija Mji wa Lindi na Mtwara miezi miwili iliyopita kulikuwa na hali ya ajabu sana.

Mheshimiwa Spika, naamini wakati nasoma historia niliweza kusoma kwamba wakoloni walivyokuja Tanzania, walikuwa wanakusanya capital kwa kutumia njia za ajabu sana. Walikuwa wanatumia njia inaitwa plundering, nyingine ni looting, grabbing and Kidnapping. Kitu hiki ndiyo kinachofanyika kwenye ukusanyaji wa kodi maeneo ya Mtwara na Lindi.

Mheshimiwa Spika, pale Lindi Mjini TRA wameweza kuwabambikia kodi wananchi, muuza matunda, ambaye anauza matunda, ndizi, nyanya, anauza embe akapelekewa kodi shilingi 700,000, anauza matunda ya shilingi 100,000 au shilingi 200,000 tu. Hili ni jambo la ajabu sana, akaambiwa afunge kibanda chake, asiuze, akapelekewa makadirio ya kodi shilingi 700,000; anauza matunda. Ni primitive accumulation of capital ambayo Watanganyika tulipigana kuondoa ukoloni huu kwa sababu ya kodi kandamizi.

Mheshimiwa Spika, kuna mtu mwingine ambaye alikuwa anauza vipodozi, akapelekewa makadirio ya kodi shilingi 8,000,000. Duka lake likafungiwa Lindi Mjini. Hata majina hapa ninayo, Mheshimiwa Mpango akiyataka nitampelekea. Ni jambo la ajabu sana. Tunaipeleka wapi nchi hii?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilikuwa naomba Mheshimiwa Mpango atakapokuja atueleze, ni kwa nini wafanyakazi wake katika maeneo ya Mtwara na Lindi wanatumia njia za kikoloni na kandamizi katika kukusanya kodi kitu ambacho ni kinyume kabisa na wananchi tulipigana na ukoloni kupinga mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mtu mwingine ni muuza chakula pale Lindi Mjini, stendi, anauza chakula (food vendor) akapelekewa kodi shilingi 4,000,000. Kama hatoi fedha hizo TRA mgahawa wake ulifungiwa, ni jambo la ajabu sana. Kwa hiyo, naomba sana kwamba hizi taratibu za kodi hakuna anayekataa kodi, watu wote sisi tuko entitled kulipa kodi, wananchi wako entitled kulipa kodi, lakini kodi ziendane kabisa na kipato. Tunasema pay as you earn; kadri mtu anavyopata ndivyo alipe kutokana na kipato chake na siyo kubambikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba Mheshimiwa Mpango atakapokuja atueleze kwa nini maeneo haya ya Mtwara na Lindi kodi kandamizi zinakuwa ni kubwa? Maduka yamefungwa Mtwara, Lindi yamefungwa kwa kiasi kikubwa sana kuliko maeneo mengine ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie pia suala la miradi ya maendeleo. Taarifa ya Kamati imezungumza hapa, ni asilimia tano tu ya pesa za miradi ya maendeleo zimepelekwa mwaka 2017.

Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba maelezo ya kina, kwa nini? Kwa sababu tunahitaji pesa ziende ili maendeleo yaweze kuonekana na nchi yetu iweze kuwa na mapato. Waheshimiwa Wabunge wamezungumza hapa. kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Mpango atueleze kwa nini fedha za maendeleo zinapelekwa chache sana? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nilikuwa naomba nizungumze hapa na Mheshimiwa Mpango anipe maelezo, mwaka 2016 nilizungumza suala la ukaguzi wa CAG, ndani ya Bunge hili kwamba CAG amekuwa hakagui Taasisi fulani hivi za fedha. Kwa mfano, vile visima vile vya makusanyo ya gesi na mafuta CAG haendi kukagua na nikaomba kwamba uletwe muswada hapa kubadilisha zile sheria. Mwaka huu nashukuru Waheshimiwa Wabunge wenzangu wameniunga mkono, wamezungumza hilo, nami naomba nipate maelezo kwa sababu hata zile Taasisi za Kijeshi tunaona CAG anaenda kukagua, lakini taasisi hizi za fedha ambazo tunahitaji fedha zikusanywe….

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nakushukuru sana, naomba Mheshimiwa Mpango atupe maelezo.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Bismillah Rahmani Rahim .

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhannah Wataalah naomba nianze kuchangia hotuba hizi mbili, hotuba inayozungumzia Hali ya Uchumi wa Taifa na Mpango pamoja na Bajeti ya Serikali kwa kuanza na maneno yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waingereza wanasema: “an old is wise, the more it hears, the less it speaks.” Waswahili wanasema kwamba, ndege huyu anayeitwa bundi ni ndege ambaye ana busara sana, lakini ukisikia bundi anazungumza, basi ujue kuna uchuro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara ya kwanza nitaongea maneno mazito kwenye Bunge hili katika hotuba hizi mbili ambapo sijawahi kuzungumza ambayo ni maagizo ya Wanamtwara. Jambo la kwanza, ili nchi yoyote iweze kuendelea, lazima kuwe na hali ya amani na utulivu. Hali ya amani inatengenezwa na Serikali iliyoko madarakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nazungumza ndani ya Bunge hili kwa muda mrefu sana, kwamba Serikali kwa mwaka 2012/2013, ilitengeneza mazingira ambayo hivi sasa nami nimechaguliwa kama Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini, ambalo ni Jimbo mama Kanda ya Kusini na Waheshimiwa Wabunge wote wa Mikoa ya Kusini wana majumba ama wana viwanja vyao Jimbo la Mtwara Mjini. Hii inadhihirisha kwamba Mtwara Mjini ndiyo Jimbo mama Kanda ya Kusini. Wananchi wakanichagua mimi Maftaha Nachuma kuwa Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini, nije kuwakilisha kero za wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kero ya kwanza ambayo walinipa wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini ni kuja kuzungumza ndani ya Bunge hili kuiambia Serikali iliyoko madarakani suala zima la maslahi ya gesi. Jambo la pili, ambalo walinituma wananchi wananchi wa Mtwara kuja kuzungumza ndani ya Bunge hili, kufikisha kilio chao, ni suala zima la migogoro ya ardhi ambayo Serikali ya Awamu ya Nne na Serikali zilizopita huko nyuma zilidhulumu wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini kwa kiasi kikubwa sana. Hali ilikuwa ni tete kweli kweli, wananchi wakanituma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro wa kwanza mkubwa ni mgogoro ambao Serikali ilichukua maeneo mwaka 2012/2013. Maeneo ya wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini, panaitwa Mji mwema, Serikali iliahidi kulipa fidia. Eneo la Mji Mwema, limekuwa linazungumzwa suala hili, nimeleta swali siku ya pili, baada ya kufika Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wakati anaomba kura Mtwara Mjini, alielezwa kero hii na wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini. Mwaka 2017 alipokuja Mtwara alielezwa jambo hili na wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini pale kwenye Uwanja wa Mashujaa. Nikazungumza ndani ya Bunge hili zaidi ya mara tatu. Nimefikisha, nikapewa Hansard mbili ndani ya Bunge hili, kwamba Serikali iko tayari kulipa fidia ya wananchi hawa, wananchi 2,200. Hapa naomba nilithibitiishie Bunge hili, kwa sababu hili limekuwa ni kero kubwa sana kwa wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezuia maandamano zaidi ya mara 10, wananchi wanataka kuandamana kwa sababu wamechukuliwa maeneo yao, wakaambiwa wasiyaendeleze. Nilipewa Hansard hapa na Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kwamba wanaenda kulipa. Mwisho wa siku wanakuja ndani ya Bunge hili, wanasema hatuwezi tena kulipa kama Serikali. Nikiuliza upande wa pili naambiwa, Waziri Mheshimiwa Dkt. Mpango hataki kupeleka fedha kupitia Taasisi ya UTTPID ambayo ilichukua maeneo haya ya Jimbo la Mtwara Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme Wanamtwara wanisikie. Kilio chao walichoniagiza nije kueleza ndani ya Bunge hili, wakaandamana kwa kiasi kikubwa ili niweze kutangazwa tarehe 26, nilivyoshinda zaidi ya vyama vitano pale Mtwara Mjini. Naomba nisome hii Hansard na Mwenyezi Mungu aweze kunishuhudia leo kwamba leo kilio cha Wanamtwara nimefikisha kwa mara nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hansard ya mwaka 2017 anasema: “Mheshimiwa Spika, fidia stahiki itaanza kulipwa kwa wananchi 2020 kuanzia mwezi Juni, 2017 hadi robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2017/2018. Taasisi ya UTTPID (narudia tena Taasisi ya UTTPID) ambayo iko chini ya Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Halmashauri, inatarajia kutumia shilingi bilioni 7,523 kwa ajili ya malipo ya fidia kabla ya kuanza kwa kazi ya upimaji wa viwanja. Ofisi ya Rais TAMISEMI, ilitoa kibali cha kuendelea na utekelezaji wa mradi kupitia barua yenye kumbukumbu Namba GB203/234/01/117 ya tarehe 2 Septemba, 2016.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ulipaji wa fidia haukuanza mapema kutokana na Kampuni husika ya UTTPID, kutokuwa na Bodi. Bodi imeshaundwa na makubaliano ya pamoja yamefanyika katika Kikao cha tarehe 2 Mei, 2017 baina ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, UTTPID na Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina Hansard mbili ndani ya Bunge hili, Serikali ikiahidi kulipa fidia hizi pesa, shilingi bilioni saba kwa wananchi hawa wa Jimbo la Mtwara Mjini. Katika Mtaa wa Mji Mwema. Jambo hili limekuwa tete sana Mtwara. Nimezuia maandamano zaidi ya 10. Narudia tena, sasa nazungumza ndani ya hili Bunge lako Tukufu, safari hii nikiondoka hapa kwenda kwenye Jimbo la Mtwara Mjini, kwa sababu wananchi wamenituma kwa mara nyingine tena, naenda kutangaza maandamano makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba maandamano hayo, aje kuyapokea Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu kaambiwa maneno haya ndani ya Jimbo la Mtwara Mjini zaidi ya mara mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo wamenituma wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini nizungumze hapa, ni suala hili, wenzangu wamezungumza; suala la pesa za korosho ambazo zilikusanywa, kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha korosho Mtwara na maeneo mengine. Kwa sababu Jimbo la Mtwara Mjini pia nina AMCOS zaidi ya mbili pale; nina AMCOS ya Mikindani na ya Naliendele. Zimekusanywa pesa za Export Levy. Pesa zilizokusanywa ni zaidi ya shilingi bilioni 210 ambazo zilitakiwa ziende kununua sulphur kuendeleza kilimo cha korosho. Zile pesa hazijaletwa Kusini kwa ajili ya kuendeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana sana na hoja na mwelekeo wa Serikali hivi sasa, kwa sababu nchi zote zilizoendelea duniani walikuwa na sera tunasema, Strong State Intervention, kwamba lazima Serikali iwe na meno katika kusimamia uchumi. Napongeza hilo kwa sababu Serikali dira yake ni hiyo. Wenzangu wamezungumza kwamba tunahitaji kuwa decentralization sasa hivi inakufa, hapana. Ili nchi iweze kuendelea, lazima kuwe na Strong State Intervention.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza kwa kununua ndege ambazo zinaenda kuchochea Utalii hivi sasa Tanzania nzima. Ndege ni kielelezo kwamba ili nchi iweze kuendelea wageni waweze kuja ndani ya nchi kuleta pesa za kigeni, lazima tuwe na usafiri. Katika hilo niwashauri sana kwamba lazima tutoke na sisi kwenda kujenga mahusiano nje ya nchi ili tuweze kushawishi wawekezaji, kama Wabunge, kama Serikali, kama wananchi, Watanzania waweze kuja kuwekeza Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nayazungumza haya kwamba zile fedha za korosho ambazo Serikali ilikusanya shilingi bilioni 210 tunaomba zirudi. Mheshimiwa Dkt. Mpango, kazungumza hapa kwamba mwaka huu anapendekeza sheria kwamba pesa zote zinazokusanywa kupitia Bodi za Mazao zipelekwe katika Mfuko Mkuu wa Serikali, zikusanywe na TRA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema sheria haiendi retrospective. Sheria hairudi nyuma. Zile pesa zilikusanywa kabla ya hii sheria, shilingi bilioni 210. Wananchi wa Mikoa ya Kusini, Mtwara na Lindi ambao ndio walimaji wakubwa wa korosho, mwaka huu wamekosa sulphur kwa sababu hizi pesa hazijaenda. Wanasema katufikishie kilio hiki Mbunge wetu, kwamba tunataka zile pesa ziweze kuletwa ziendeleze hata kwa mwakani. Vinginevyo watafanya maandamano makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza maneno haya, sijawahi kuzungumza ndani ya Bunge hili. Hiki ni kilio cha wananchi wa Kusini, ni kilio cha wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini. Nimekuwa natumia busara nyingi sana, kila mtu anafahamu ndani ya Bunge hili kwamba ukisikia maandamano yameanza Kusini, yameanzia Mtwara Mjini. Nimekuwa natumia busara nyingi sana kuongea na vyombo vya Serikali, kuongea na vyombo vya Dola na kuwashawishi wananchi kuleta amani na utulivu ndani ya Majimbo ya Kusini kwa kuanzia na Mtwara Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika hili namwomba sana Mheshimiwa Dkt. Mpango, amekuwa hajibu maswali yangu, amekuwa hajibu hoja zangu; nimezungumza maneno haya wakati amewasilisha Bajeti yake, hakujibu hata moja. Hajajibu hata hoja moja na anazungumza kwamba ni maneno ya wananchi wa Mtwara. Mheshimiwa Dkt. Mpango amekuwa hajibu hoja za wananchi wa Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamwomba Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ananisikia ninavyozungumza maneno haya, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, aje kupokea maandamano makubwa kwa wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini na Mikoa ya Kusini kwa kupokwa haki zetu hizi. Wananchi hawawezi kuchukuliwa maeneo zaidi ya miaka mitano mpaka hivi sasa hawajalipwa fidia zao na wala Serikali haisemi chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri sana Mheshimiwa Dkt. Mpango atakapokuja kuhitimisha hoja yake, mwaka 2017 niliunga mkono Bajeti hapa, nikasema ndiyo. Kama hatatoa hizi pesa shilingi bilioni nane hata kwa kunyang’anya, kwa kukopa na kufanyaje, waleteni. Wachukue kwenye korosho walipe wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini, yale maeneo ya Mji Mwema, wanalalamika sana, wameambiwa kwamba eti wapimiwe tena viwanja, wamechukuliwa zaidi ya miaka mitano, halafu virudi tena. Haiwezekani, huku ni kuwadharau wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyenzi Mungu, kwa kunijaalia uzima na afya njema na leo naomba kuchangia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa maandishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi ya Mtwara Mjini hayapapimwa. Katika kikao cha kwanza Bunge lako hili la Kumi na Moja nimeuliza maswali juu ya upimaji na urasimishaji wa ardhi Mtwara Mjini ambalo mpaka sasa halijajibiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri atakapokuja kujumuisha hoja yake aje na majibu stahiki, ni lini maeneo mengi ya Mtwara Mjini yatapimwa na kurasimishwa? Swali hili ni muhimu sana kwa kuwa mtu akimiliki kipande chake cha ardhi kisheria anaweza kukopa benki kwa kutumia dhamana ile na kuweza kumsaidia kujikwamua kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtwara Mjini kuna migogoro ya ardhi mingi sana. Nashangaa Mheshimiwa Waziri ameweka/ametaja mgogoro mmoja tu ambao ni wa Libya. Siyo kweli kwamba Mtwara Mjini kuna mgogoro huu tu. Ipo mingi sana ambayo Serikali inakwepa kwa makusudi kabisa kupitia Maafisa wake wa Ardhi Mtwara Mjini wakiongozwa na Afisa Mipango Miji. Kuna eneo la Mji Mwema na Tangla, maeneo ambayo yalikuwa ya wananchi Serikali, imechukua tangu mwaka 2013 mpaka leo Serikali haijalipa fidia kwa wananchi wale. Wananchi hawana sehemu ya kulima na wengine wamebomolewa makazi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tathmini iliyofanyika kila squire meter moja walilipia shilingi 250 tu. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri kwa nini Serikali hii inawadhulumu na kuwanyanyasa wananchi wa Mtwara?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua kwa kuwa ni miaka mitatu sasa tangu wananchi wamenyang‟anywa maeneo yao na hawajapewa fidia, je, Serikali ipo tayari kulipa fidia ya miaka mitatu ili ilingane na thamani ya ardhi ya sasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi wameibiwa katika tathmini iliyofanywa na watendaji wa Halmashauri na kupewa shilingi 250 - 450 kwa square meter moja, Serikali ipo tayari hivi sasa kufuta bei hii na kufanya tathmini upya kwa maeneo hayo ya Mji Mwema na Libya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mgogoro huu ni mkubwa sana Mtwara Mjini na wananchi wamemwelezea mpaka Waziri Mkuu na kuahidi kuutatua, Mheshimiwa Waziri Lukuvi lini atakuja Mtwara Mjini ajionee mwenyewe kuliko kutegemea taarifa za uongo za Maafisa Ardhi ambao ndio wahusika wakuu wa utapeli huu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Plot Na. 99 ya Mzee Mayunga ekari 15 ambazo amenunua tangu miaka ya 1980 na amekuwa akilipia kila mwaka, leo Maafisa Ardhi wameshirikiana kuficha file la huyu mzee na wamemwambia kiwanja hicho hakitambuliki ili wauze eneo hilo kwa mtu mwingine. Plot hii Na. 99 anayonyang‟anywa ili wauze na wamethubutu mpaka kuficha file la mzee huyu ambalo lilikuwa Halmashauri, hii ni dhuluma ya hali ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Mheshimiwa Waziri Lukuvi ahakikishe anamrudishia mzee huyu plot yake Na. 99 ambayo wameitisha watendaji wa Halmashauri na Mkoa wa Mtwara. Watendaji wa Ardhi Mtwara Mjini ni majipu makubwa yaliyoiva, tafadhali uje Mtwara kuyatumbua au mnasubiri mpaka watu waandamane na Mheshimiwa Rais aje kutumbua?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna msemo unaosemwa sana Mtwara kuwa kutokana na sakata la gesi Mtwara, viongozi wengi wamenunua viwanja kupitia hawa Maafisa wa Ardhi. Naomba sana msipokuja kuwatumbua watu hawa, usemi huu tutauamini sana kwamba mnawalinda kwa kuwa mnawatumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba zinazoitwa za bei nafuu siyo kweli kwani bei yake ni ya juu sana. Mwalimu mwenye mshahara wa shilingi 100,000 kwa mwezi kama basic salary hawezi kununua nyumba hizi kwa shilingi milioni 40, shilingi milioni 50 na kuendelea, mnasema ni za bei nafuu? Hapana, hizi ni nyumba za wale wale wenye fedha nyingi ambazo sitaki kutumia jina maarufu sana lililopita mtaani kuwa ni nyumba za mafisadi. NHC iwezeshwe kujenga nyumba za bei nafuu.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujua katika mwelekeo wa Mpango huu, juu ya hoja ambayo tulijadili sana mwaka jana wakati wa Mpango wa Serikali 2016/2017, nayo ni kuhusu Mahakama ya Mafisadi. Suala hili limekuwa kimya nashangaa kwa nini wakati mafisadi wapo, wengine wamestaafu, ni kwa nini kwenye mwelekeo wa Mpango huu wa 2017 suala hili la Mahakama ya Mafisadi halipo?
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka kujua juu ya mwelekeo wa Mpango huu kuhusu ujenzi na ukarabati wa Mahakama Tanzania na hasa katika Jimbo langu la Mtwara Mjini Mahakama ni chakavu sana na hazikidhi haja. Je, ni lini suala hili litatatuliwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda vya korosho ni muhimu sana katika kuinua uchumi wa nchi hii hasa Mikoa ya Kusini. Naomba kujua ni lini Serikali itafufua Viwanda vya Korosho, Mikoa ya Kusini ili kuinua uchumi kwa kuongeza thamani ya korosho na bei?
Mheshimiwa Naibu Spika, mikataba ya gesi na mafuta ni muhimu sana kuletwa Bungeni ili ijadiliwe kabla ya kuingia kwenye mikataba hii. Kwa muda mrefu mikataba imekuwa haina tija kwa Taifa hili na mapendekezo ya Mpango huu suala hili halipo, naomba majibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ardhi ni muhimu sana maana kumekuwa na migogoro mingi ya ardhi hapa nchini. Kwa mfano, kumekuwa na utaratibu wa Serikali kuchukua ardhi kwa wananchi na kukaa muda mrefu bila kulipa fidia kwa mfano Mtwara Mjini tangu mwaka 2012 mpaka leo UTT ilipima viwanja Mji Mwema ambako ni mashamba ya wananchi hawajalipwa. Hili ni jambo la hatari sana, naomba majibu tafadhali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia elimu ndiyo msingi wa maendeleo wa nchi yoyote ile duniani. Sera ya Elimu bure iangaliwe upya ili shule ziweze kujiendesha. Shule zinapata OC ya Sh. 27,000/= tu kwa mwezi itaweza kuendesha ofisi na shule kweli? Ni jambo la ajabu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo ya elimu ya juu iangaliwe upya ili kila Mtanzania mwenye sifa ya kusoma elimu ya juu apate mkopo kama Mheshimiwa Rais alivyoahidi. Kunyima mikopo watoto maskini kama ilivyo kwa mwaka huu ni jambo hatari sana kwa mustakabali wa Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana miundombinu ya barabara kama vile reli kutoka Mtwara Mjini hadi Mchuchuma na Liganga kwenye chuma na makaa ya mawe iwekwe kwenye Mpango wa mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, utanuzi wa Bandari ya Mtwara ufanyike kwa haraka ili kuinua uchumi wa nchi yetu. Bandari hii haihitaji gharama sana kwa kuwa ni natural harbour, Serikali itenge fedha haraka kwa ajili ya utanuzi wa bandari hii. Sijaona suala hili kwenye mapendekezo ya Mpango huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo barabara ya Mtwara - Newala imetengewa fedha lakini mpaka sasa hata robo kilomita haijatengenezwa, ni jambo la ajabu sana. Naomba barabara hii ianze kujengwa tafadhali.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hotuba hizi mbili za Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia, kunipa afya njema na leo hii niweze kuchangia Wizara hizi ipasavyo. Naomba nianze moja kwa moja na Wizara hii ya TAMISEMI na hasa katika eneo hili la Mipango Miji, kumekuwa na matatizo makubwa sana kwenye suala la upangaji miji. Leo hii tunapopita kwenye Halmashauri zetu na hasa kwenye miji midogo na miji mikubwa katika suala la kupanga ardhi ni changamoto kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo baya ambalo naweza kulisema hapa, watu ambao wanashughulika na upangaji wa ardhi, wanafanya mambo ya ajabu sana kwa wananchi wetu wa Tanzania. Unaweza ukakuta wakati wanaenda kupima ardhi, wanapima kwa bei kubwa sana, wananchi wa kawaida hawapati ahueni ya kupimiwa viwanja vyao mpaka uweze kuwa na pesa za kutosha. Hii ni kwa sababu gharama zimekuwa kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri Mheshimiwa Jafo kwa kazi nzuri anayoifanya, ahakikishe kwamba Halmashauri zetu hizi zinapewa vifaa vya kupima ardhi na maeneo yaweze kupimwa kwa viwango ambavyo vinastahiki, lakini mwisho wa siku, kiwango kinachotumika kupimia ardhi, basi hata unapotoa fidia, iweze kulingana na viwango halisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine kuna maeneo yanaweza yakapimwa, lakini kukawa na double allocation yaani leo hii kiwanja kimoja kinapewa watu zaidi ya watatu, maeneo mengine kiwanja kimoja watu wanne. Hili ni jambo kubwa sana na kuna changamoto kubwa na migogoro mingi ya ardhi kwenye miji yetu kutokana na sekta hii ya ardhi kwenye Halmashauri, lakini hasa kwenye miji yetu midogo na mikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kidogo suala la elimu. Elimu ni jambo ambalo tumekuwa tunazunguza sana kwenye bajeti zetu zote hapa, kwamba maeneo mengi, shule nyingi za mijini na vijijini hazina madarasa ya kutosha. Mheshimiwa Waziri amezungumza hapa kwamba enrolment ya wanafunzi wa darasa la kwanza sasa hivi imefikia asilimia 101. Enrolment imekuwa ni kubwa sana, kwa hiyo, madarasa hayatoshi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukifika Mtwara Mjini unaweza ukashangaa sana. Shule ina wanafunzi zaidi ya 660, madarasa yaliyopo ni matatu. Shule ya msingi Mbae, watoto 650, madarasa matatu. Kwa hiyo, naomba sana, Wizara ya TAMISEMI ihakikishe inajenga madarasa, inapeleka fedha za maendeleo katika Halmashauri zetu ili madarasa yaweze kujengwa ili tuweze kuendana na kasi hii ya enrolment ya wanafunzi iende sambasamba na idadi ya madarasa tuliyokuwa nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wakati tunasoma wakati ule miaka ya 1990 kule mwanzoni, ilikuwa ukifika shuleni asubuhi ni lazima ukimbie mchakamchaka. Leo hii mchakamchaka haupo, watoto hawafanyi mazoezi. Hata michezo mashuleni imedorora sana. Nalizungumza hili kwa sababu, wakati fulani nilikuwa Mkuu wa Shule Mchinga sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna michango mingi sana, inapofika suala la UMISETA na suala la UMITASHUMTA, yaani badala ya Serikali kutenga fedha kwa ajili ya michezo, wanawabebesha Wakuu wa Shule pesa zile ndogo ambazo ni za maendeleo, wanaambiwa wachangie kwa ajili ya michezo ya UMISETA na UMITASHUMTA. Mkuu wa Shule anakuwa kama kaibeba shule kichwani kama shule yake mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana, TAMISEMI itenge pesa za kutosha, zipelekwe mashuleni kwa ajili ya kugharamia michezo. Tunaamnini watoto wakifanya michezo, wakikimbia mchakamchaka asubuhi, wakicheza mpira, brain zao zinakuwa na uwezo wa kufikiri sawa kuliko hali ilivyo hivi sasa. Suala la michezo ni suala muhimu sana. Michezo ni afya, michezo ni burudani, michezo ni furaha, michezo ni ajira. Vipaji vingi vinapotea kwa sababu hatuwekezi vya kutosha katika ngazi za Shule za Msingi na Sekondari. Uhakikishe Mheshimiwa Jafo unatenga pesa za kutosha kupeleka mashuleni kwa ajili ya kugharamia UMISETA na UMITASHUMTA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia suala ambalo Waheshimiwa Wabunge wenzangu wamezungumza sana kuhusu posho za Madiwani kwamba hazitoshi. Nami naungana nao. Vilevile posho za Wenyeviti wa Mitaa, unaweza ukashangaa Halmashauri nyingine hizo posho hazipo kabisa. Wenyeviti wa Mitaa wanafanya kazi kubwa sana. Wenyeviti wa Mitaa wanahudumia wananchi sana. Tunaomba sana kwamba posho za Wenyeviti wa Mitaa zipelekwe, ziongezwe, iwekwe sheria maalum, waweze kupewa posho ambayo angalau inafanana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii hali iliyopo Wenyeviti hawa wanapata posho kulingana na maeneo na makusanyo ya Halmashauri. Ukija kwa mfano pale Mtwara, Mwenyekiti wa Mtaa mwezi mzima analipwa shilingi 20,000 tu, ni jambo la ajabu sana. Huyu Mwenyekiti wa Mtaa anahudumia wananchi usiku na mchana, halafu mwisho wa siku, mwezi mzima analipwa shilingi 20,000 kwa hisani ya Halmashauri. Naomba sana tuweke utaratibu wa kutosha kabisa, Wizara ipeleke fedha iweze kuwahudumia Wenyeviti hawa wa Halmashauri kwa sababu wanafanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la miradi ni jambo ambalo linashangaza sana. Pesa za kuendeleza miradi haziendi katika Halmashauri zetu. Unaweza ukaangalia ukipitia randama hapa kwa mwaka mzima zimeenda 15% au 16%, ni jambo la ajabu sana. Miradi yetu haiendi kwa sababu pesa hazipelekwi kule kwenye Halmashauri. Nilikuwa naomba sana Mheshimiwa Waziri Jafo kwa sababu tunakufahamu sana, ni katapila, utenge pesa za kutosha zifike Halmashauri ili miradi yetu hii iweze kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine, kwa mfano pale kwangu Mtwara, siku moja DC alimuuliza Mkurugenzi kwamba tunataka tukakague miradi ya Halmashauri. Mkurugenzi hana miradi, pesa hazijaenda, anamwambia miradi iliyopo hapa ni Miradi ya Mfuko wa Jimbo tu, ya Mbunge. Twende tu ukakague ujenzi wa kupumzikia wagonjwa pale zahanati na maeneo mengine, lakini Halmashauri miradi imesimama kwa sababu pesa hazifiki. Ni jambo la ajabu sana, tulikuwa tunaomba pesa zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya Halmashauri pesa ziweze kufika na kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni afya. Hili ni jambo muhimu sana, kwamba tunaekelezwa sasa hivi kwamba dawa zile tunaita tresa medicines zinafika asilimia 94 kwa taarifa za Waziri anavyosema. Bado ukiingia kwenye hospitali na zahanati zetu, tunaambiwa dawa hazitoshi ama dawa hazipo. Leo mgonjwa anatoka huko anaenda
hospitali anaambiwa dawa zimeisha. Bado tatizo lipo sana, tunaomba Mheshimiwa Waziri kama ni tatizo la watendaji basi tunaomba lichukuliwe hatua ipasayo, lakini kama ni tatizo kwamba tunaambiwa pesa zipo, dawa zipo kumbe kule pesa hazijafika, hili nalo ni tatizo lingine. Tunaomba sana kwamba dawa ziweze kupatikana kama taarifa zinavyoelezwa kwamba iwe kweli aslimia 94.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala hili la dawa zile maalum ambazo ni za kifua kikuu, ziko dawa za HIV na kisukari. Hizi dawa zinatolewa kwenye Hospitali za Mikoa tu, hospitali ambazo zina specialists. Ukipita kwenye vituo vyetu vya afya au kwenye zahanati zetu hakuna hawa specialists na zile dawa hazitolewi na mtu mwingine, hata yule Medical Assistant haruhusiwi kutoa zile dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba sana, kwa sababu wagonjwa hawa wako wengi sana, wako huko vijijini mbali, wanatembea umbali mrefu sana tunaomba hizi dawa zipatikane kwenye zahanati zetu, zipatikane kwenye vituo vya afya. Kama issue ni mafunzo, basi hata wale medical assistant kwa sababu wanaokoa maisha ya Watanzania sana, wapewe mafunzo ya kutoa hizi dawa, isiwe tu pale kwenye specialist kwenye Hospitali za Mikoa ambazo ziko mbali sana na wananchi. Tulikuwa tunaomba sana hili liweze kupewa upekee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la barabara kwenye miji yetu imekuwa changamoto sana. Watu wa TARURA wamekuwa ni Mungu watu. Leo ukienda kumwuliza mtaalam wa TARURA, ukimwomba mtaalam wa TARURA aje kutoa ufafanuzi kwa wananchi ambao anawatumikia, anakuwa hawataki, yaani wako pale kama Miungu watu.

Kwa hiyo, naomba kuwe na usimamizi, sheria hizi ziweze kurekebishwa sawasawa. Hawa watu wa TARURA kwa sababu wanawahudumia wananchi wa kawaida, wanahudumia Watanzania, basi waweze kusimamiwa na Madiwani, waweze kusimamiwa na Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi wakati nafanya mikutano ya hadhara pale Mtwara, utamaduni wangu ni kuhakikisha kwamba Wakuu wa Idara wanakuja kutoa ufafanuzi kwa sababu wanawatumikia wananchi, wapo kwa ajili ya wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini. Wote wanakuja, lakini Wakuu wa Idara wa TARURA hawataki kuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana, kama wapo kwa ajili ya wananchi, basi wahakikishe ya kwamba wanawatumikia wale wananchi. Madiwani na Wabunge ndio wawakilishi wa wananchi. Sasa leo tunashangaa sana kusikia kwamba eti Diwani haruhusiwi kumuuliza mtu wa TARURA nini kinaendelea. Mtu wa TARURA akiulizwa, anasema mimi sisimamiwi na Diwani wala na Mbunge. Sasa wanafanya kazi kwa ajili ya nani? Tulikuwa tunaomba sana, hawa watu wa TARURA wawajibike kwa ajili ya wananchi.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika mwelekeo wa mpango huu wa mwaka 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na suala hili la mashirika ya umma, Mama Lulida alikuwa kazungumza hapa siku ya jana akieleza kwa masikitiko makubwa sana. Alikuwa amezungumza kwamba baadhi ya mashirika ambayo takribani tuko nayo Tanzania kwa kiasi kikubwa mashirika ya umma yanaendeshwa kihasara. Yapo mashirika mpaka hivi sasa ninavyozungumza, miradi na mali walizokuwa nazo takribani na madeni yote madeni waliyokuwa nayo inazidi mali walizokuwa nazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa mfano Shirika la Mbolea Tanzania (TFC), wakati tunapitia mpango wao katika Kamati ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma, unaweza ukashangaa sana kwamba deni walilokuwa nalo ni takribani shilingi bilioni 66. Lakini madeni, mali waliyokuwa nayo, mali nzima ukiuza majengo na kila kitu wana mali zenye thamani ya shilingi bilioni 23.8. Kwa hiyo, unaweza ukaona ni jambo la ajabu sana kwamba haya mashirika yamefilisika, Serikali, Waziri wa Fedha na Mipango, sijaona wakati napitia taarifa yake hapa na mwelekeo wa mpango hajaeleza kinaga ubaga kwamba kuna mkakati gani wa kuhakikisha kwamba anafufua mashirika haya ya umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tumeona hapa na Wabunge wengi wamezungumza kwa kiasi kikubwa sana kwamba Serikali imekuwa ikikopa kwenye mashirika haya, mashirika ya fedha na mashirika ya umma ya ndani ya nchi. Tuhakikishe kwamba tunaweka mikakati kabambe ili haya mashirika yaweze kufufuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia uendeshaji wa haya mashirika, yanaendeshwa kinyume na taratibu za kimaadili. Kwa mfano, mwaka jana tuliweza kuzungumza katika mpango hapa kwamba yapo baadhi ya mashirika yanatumia madaraka yao vibaya. Kwa mfano, Shirika la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kiliweza kuingia mkataba na mwekezaji kotoka Botswana, mkataba ambao haunufaishi Serikali. Lakini jabo la ajabu tuliweza kuzungumza katika mpango tukaongea kwenye bajeti hapa, lakini kwenye mpango aliokuja nao Mheshimiwa Mpango hapa hakuna mwelekeo wowote kwamba kuna nini kitafanyika ili kuhakikisha ya kwamba haya mashirika ambayo yanawekeza kinyume na taratibu na sera za uwekezaji Tanzania na kwamba hayaingizi kipato katika Serikali yetu yanachukuliwa hatua stahiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ukisoma mkataba wa Mlimani City ambao Mbotswana aliingia kwa kiasi kikubwa yule jamaa anakusanya pesa nyingi sana. Lakini jambo la ajabu Serikali inakusanya asilimia 10 tu ya mapato yote na hakuna uhakiki wowote ambao unafanyika wa kuhakikisha kwamba kile anachokusanya kinafanyiwa mahesabu sawasawa ili ile asilimia 10 ama anapata zaidi ya ile asilimia 10 anayotoa Serikali ya Tanzania iweze kunufaika. Ni kwa sababu mipango yetu haioneshi namna gani tunaweza kuweka mazingira ya kiuwekezaji ambayo hawa wawekezaji kutoka nje wanaweza kuliingizia Taifa hili pato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia suala zima ambalo niliweza kuzungumza katika mpango uliopita, kwamba mashirika haya kwa mfano PSPF, wamekuwa wakiwekeza kwenye viwanja kwa kiasi kikubwa sana na wakati wananunua hivi viwanja wananunua square meter moja kwa pesa nyingi sana kinyume kabisa na bei halisi na halali katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, niliweza kueleza hapa, na leo naomba nilizungumze tena, Shirika la PSPF waliweza kununua kiwanja Mjini Mwanza square meter moja walinunua shilingi 250,000, ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lakini ukija kule Mtwara pia, wamenunua square meter moja shilingi155,000, maeneo ambayo bei hiyo haijafika, ni kwa sababu mashirika haya yanawekeza kiufisadi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana katika mpango huu tuhakikishe ya kwamba haya mashirika yanapitiwa upya na waweze kuja na mpango kabambe ambao utaweza kuinua uchumi wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze pia suala zima la PPP (sekta binafsi). Tumeweza kuzungumza kwa muda mrefu katika Bunge hili kwamba hawa wawekezaji kutoka nje ya nchi ndio ambao wanategemewa sana na Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi, ambao tunawategemea wajenge viwanda na vile viwanda viweze kutoa ajira. Lakini cha ajabu mazingira mpaka leo tunavyozungumza sio rafiki kwao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilizungumza hapa wakati wa mpango uliopita na nikazungumza wakati wa bajeti pia, kwamba tunao wawekezaji wamejenga viwanda, kwa mfano mwekezaji huyu Aliko Dangote kule kiwanda cha saruji Mtwara, lakini mpaka leo huyu mwekezaji ananyimwa kupewa gesi ambayo anaweza kuitumia kama nishati ili sasa bei ya saruji iweze kushuka na saruji iweze kuzalishwa kwa wingi Tanzania na watu wengi waweze kujenga, ni jambo la ajabu sana. Tunaomba sana hawa wawekezaji wapewe gesi, mwekezaji huyu wa saruji apewe gesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuna mwekezaji wa mbolea ambayo ni kwa muda mrefu hivi sasa, tuliongea wakati wa mpango, wakati wa bajeti pia tulizungumza, ambaye anaomba apewe gesi aweze kujenga kiwanda cha mbolea Msangamkuu pale Mtwara Vijijini. Mpaka leo yule mwekezaji hajapewa hiyo gesi. Tunaomba Waziri Mpango atakapokuja kuhitimisha atupe maelezo kwamba mpango ukoje wa mwakani wa kuhakikisha kwamba hawa watu, hawa wawekezaji wanapewa hii gesi ili iweze kunufaisha katika sekta hii ya viwanda na kweli iweze kuinua uchumi wa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nizungumze suala zima la miundombinu ambalo tumezungumza kwa kiasi kikubwa sana, lakini sijaona mkazo katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mpango hapa wakati anazungumza. Tulizungumza sana kwamba uchumi wowote hauwezi kuimarika popote duniani kama miundombinu ni hafifu. Tunayo miundombinu ya barabara ambayo imesimama hivi sasa na tuliweza kuzungumza, kwa mfano barabara kadhaa za hapa nchini kama ile barabara ya Ulinzi kule Mtwara ambayo sijaona kwenye mwelekeo wa mpango wapi imewekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliweza kuzungumza pia reli ya kutoka Mtwara kuelekea Liganga na Mchuchuma ambayo Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza. Kwa hiyo, niombe sana kwamba kama kweli tunahitaji kufufua uchumi tuhakikishe kwamba tunajenga miundombinu imara ili kweli Watanzania waweze kuondokana na umaskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa sababu ya muda.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu wataala kwa sababu tangu tumemaliza kufanya Uchaguzi Mkuu ndani ya chama, uchaguzi ambao ulimweka Prof. Ibrahim Lipumba kuwa Mwenyekiti wa Chama Taifa, lakini mimi ninayezungumza hapa Maftah Nachuma kuwa Makamu Mwenyekiti Bara. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kutusimamia na sasa chama chetu kimesimama imara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa maneno ambayo alisema Mwanafalsafa Mtume Muhammad (S.A.W.) karne ya sita alizungumza maneno yafuatayo, kwamba man laa yashkur kaliila, laa yashkur kathiira. Kwamba yeyote ambaye hashukuru kidogo alichopewa, basi hata akipewa kingi hawezi kushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa dhati kabisa nishukuru Wizara hii ya TAMISEMI kwa bajeti ambayo mwaka 2018 tulipigania sana zikaletwa Mtwara shilingi bilioni 21 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu pale Mtwara Mjini, kujenga mifereji, kujenga shopping mall. Tunaishukuru sana TAMISEMI kwa sababu imeweza kutusikiliza kilio cha wana Mtwara na sasa tunajenga mifereji ya kupeleka maji baharini ili Mtwara sasa tuondokane na mafuriko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na shukrani hizo, bado kuna makandokando mengi katika zile fedha ambazo zimeletwa shilingi bilioni 21. Wale ambao walipewa dhamana ya kupitia na kusaini mikataba, kuna makandokando mengi sana. Mikataba ile ilisainiwa kwa namna ambayo haieleweki, haikuwa na uwazi. Kwamba watu waliitwa kutoka Mtwara Mjini, akaitwa Mkurugenzi, akaitwa aliyekuwa Meya kwenda Dar es Salaam, baadaye wakarudishwa pale Mtwara wakiwa wamesaini mikataba. Kwa hiyo, kuna malalamiko mengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Madiwani ambao wanazungumza mambo mazito sana, kwamba mikataba yule Mkandarasi aliyepewa ule mradi wa kujenga miundombinu Mtwara Mjini mkataba wake umesainiwa kimazingara mazingara. Tunaomba Wizara ya TAMISEMI ifanye uchunguzi haraka iwezekanavyo, wale wote waliohusika kwamba wamepewa kiasi kidogo ili wampe yule Mkandarasi kutoka China, kufanyike uchunguzi wa kina, waweze kuchukuliwa hatua. Kwa sababu kiasi kinachotajwa kwamba kimetolewa ni kiasi kingi sana kitu ambacho zile fedha zingeweza kusaidia kuboresha miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza ni kwamba mpaka hivi sasa ule mradi unasuasua. Fedha zipo, Mkandarasi anasuasua kwa sababu mazingira ya ule mkataba ni mazingira ya ajabu ajabu. Tunaomba uchunguzi ufanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nizungumzie suala la Hospitali ya Mtwara. Hospitali zetu za Mtwara hasa ile Hospitali ya Wilaya lakini pia ni ya Mkoa ya Mtwara, tunaomba ipelekewe vifaa. Hospitali ile haina X-Ray, haina vifaa vya kupimia, haina CIT-Scan. Wananchi pale wanapotaka kupimiwa au wanavyotaka kupimwa, pale ambapo wanaambiwa waende waende Hospitali ya Mkoa ambapo imezukuwa Hospitali ya Rufaa hivi sasa, wakifika pale vile vipimo vyote havipo, wanaambiwa waende Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba sana, tumekuwa tunazungumza kwa muda mrefu sana kwamba hospitali hii ipelekewe vifaa, vifaa tiba, hata dawa nayo pia hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine la ajabu sana. Ukienda kwenye hospitali hii hivi sasa kuna walinzi ambao wamewekwa wa SUMA JKT wanaoangalia wagonjwa wanavyoenda pale kutibiwa. Nimepata malalamiko mengi kama Mbunge kwamba walinzi wanawapiga wagonjwa wanavyoenda kuingia hospitali pale eti kwa sababu wanapita mlango ambao hauko sawa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekit, sasa naiomba Serikali, pamoja na kwamba tunahitaji ulinzi uwepo katika hospitali zetu, lakini lazima wagonjwa waweze kuheshimiwa, Wana- Mtwara waweze kuheshimiwa, wasipigwe na hapa Mapolisi na SUMA JKT ambao wamewekwa pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo naomba kuzungumza ni suala hili la demokrasia; Katiba katikaIbara ya 146 inaeleza kwamba: TAMISEMI imepewa mamlaka ya kusimamia chaguzi. Mheshimiwa Waziri hapa kazungumza kwamba mwaka huu tutakuwa na uchaguzi wa mitaa, lakini kuna mambo ya ajabu sana tumekuwa tuna- experience ndani ya nchi yetu tangu chaguzi hizi zinafanyika hasa hasa hizi chaguzi za marudio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachoomba kuelekea katika uchaguzi huu jambo la kwanza kuwe na Tume Huru ya Uchaguzi; tunahitaji kuwe na Tume Huru ya Uchaguzi ili iweze kusimamia sawasawa kwa sababu kuna mambo mengi ambayo yamekuwa yakijitokeza katika usimamizi wa hizi chaguzi. Kwa mfano, suala hili la kutafuta wagombea vyama vya siasa vinateua wagombeakwa mujibu wa sheria lakini wakipelekwa kwa wale wanaosimamia, wale wanaoteua, wale watendaji wakata wanawaengua wagombea kutoka upinzani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza haya tuna ushahidi sana, kwa mfano, pale Kata ya Nanguruwe kuna wagombea walishawishiwa wakahamia Chama cha Mapinduzi, lakini sisi Chama cha Wananchi - CUFtukasimamia uchaguzi na mchakato ndani ya chama. Wagombea wetu walivyokwenda kutakana kuteuliwa wakaenguliwa bila sababu za msingi, wakaenguliwa bila utaratibu, wakati tunasema nchi yetu niya kidemokrasia na ni nchi ya vyama vingi. Nami nilienda pale Nanguruwe kuzungumza naMtendaji wa Kata nikamwambia kwa nini unamwengua mgombea wa CUF akanieleza kwamba hajatimiza vigezo, hali ya kuwa kila ya kitu tumefanya,form kajaza sawasawa na alivyojaza mgombea wa CUF, ndivyo alivyojaza mgombe wa CCM lakini mgombe wa CUF amaenguliwa. Sasa haya ni mambo ya ajabu sana, kwa hiyo tunaiomba TAMISEMI tunavyokwenda kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa, haya mambo yaweze kufanyika sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine pia pale Kata ya Tangazo, Mtwara Vijijini napo, pia kulikuwa na mazingira hayo hayo kwamba wagombea wa Chama cha Wananchi - CUF wanaenguliwa bila kufuata taratibu za kisheria na Watendaji Kata na ukimuuliza Mtendaji Kata anasema nimepata maelekezo kwamba huyu mtu hafai na kweli tumemwondoa. Kwa hiyo, mazingira hayo tunanyima demokrasia ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwenye hizi chaguzi, sisi tumeshiriki chaguzi zote za marudio Chama cha Wananchi - CUF,hasa kule kwetu Kusini kwa mfano,kuna kata moja, Kata ya Nalingu pale Mtwara Vijijini chama cha Wananchi - CUF kilipambana, mgombea wetu alikuwa makini, wananchi wakampenda, wananchi wakamchagua, tulivyokuja kwenye kuhesabu kura chama tawala kinaleta polisi ndani ya masanduku na wakawaambia kwamba bwana tunachotaka hapa sisi kama polisi, sisi ndio tunahesabu hizi kura. Kwa hiyo hiki ni kinyume kabisa cha demokrasia nchini, kwamba tunapoingia kwenye chaguzi tusiruhusu Jeshi Polisi kwenda kuhesabu, kwenda kung’ang’ania masanduku ya watu waliofanya maamuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sanakwamba, kama kweli tunahitaji amani ya kweli, ni lazima chaguzi hizi tuzisimie sawasawa tufuate sheria, tufuate Katiba namna inavyosema,Tume ya Uchaguzi iweze kuwa huru, wale askari wakae mbali kwa mujibu wa sheria inavyosema, lakini hivi sasa chaguzi zote za marudio tumeona, tumeweza kujiridhisha kabisa kwamba polisi wanaingia ndani kwenda kuhesabu kura. Je hii ni kazi ya polisi? Tunaomba sana haya mambo yaweze kuzingatiwa.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Mheshimiwa Nkamia hapa ameezungumza mambo mengi yanayohusu Chemba, lakini sisi pia kama Chama cha Wananchi - CUF kule Chemba yule DC wake niliwahi kuzungumza kwenye Bunge hili, niliwahi kuzungumza hapa kwamba, balada ya kusimamia miongozo ya Serikali, badala ya kusimamia taratibu za nchi hii,yeye kazi yake kubwa amekuwa anafanya kazi ya kuwafukuza Wenyeviti wa Mitaa wa Chama cha Wananchi - CUF. Hivi ninavyozungumza zaidi ya Wenyeviti tisa amewafukuza, yaani anaeenda sehemu anaitisha mkutano, anawaambia hawa mimi nawafukuza. Hafukuzi Wenyeviti wa CCM, hafukuzi Wenyeviti wa chama kingine, yeye anafukuza Wenyeviti wa Chama cha Wananchi - CUF.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili naomba kujua,utawala bora tunaozunguza hapa ni utawala bora wa aina gani, demokrasi tunayozungumza ni demokrasia ipi, kama DC yupo pale kuangalia upinzani, pale waliposhinda anawafukuzafukuza. Wakati tunasema kwamba demokrasia uwaache wananchi wafanye wanayotaka, wamchague kiongozi wanayemtaka, wananchi wamechagua viongozi, wamechagua Wenyeviti waCUF,DC anaenda anawafukuza Wenyeviti tisa, ni mambo ya ajabu sana. Tunaomba sana Serikali kwa kweli kama tunahitaji tuwe na amani na utulivu ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunahitaji hawa Ma-DC wafanye kazi zao walizopangiwa na mteule wao.

T A A R I F A

MWENYEKITI: Mheshimiwa Agnes, taarifa.

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampataarifa mzungumzaji kwa kifungu cha 68(7), yeye angelikuwa anaona Tanzania haina demokrasia, leo hii imekuaje yeye kutoka upinzani amekuwa Mbunge?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Maftaha.

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namheshimusana kwa sababu anachokizungumza hakifahamu. Hapa tunachozungumza,ni kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa, na ipo kwenye taarifa ya Waziri wa TAMISEMI ukurasa wa 12kwamba, mwaka huu kuna uchaguzi wa Serikali za mitaa tunazungumza yanayojiri, yanayojitokeza katika chaguzi hizi ambazo tumekuwa tukizifanya kwa muda wa miaka mitatuhivi sasa, kwamba Wapinzani wanaong’olewa, wapinzani wanaondolewa lakini Ma-DC waliochaguliwa kusimamia maendeleo ya wananchi wao wanafanya kazi ya kuhujumu upinzani na kuwafukuza Wenyeviti waliochaguliwa wa Chama cha Wananchi - CUF na wa vyama vingine, sasa hapa tunasema hakuna demokrasia ya kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nizungumze jambo moja hawa Ma-DC na Ma-RC kwa sababu wamekuwa na utamaduni, kwa mfano, pale kwangu Mtwara,juzi Mheshimiwa Rais kaja Mtwara, katika jimbo la Maftaha Nachuma ambaye ndiye, Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini, RC tunamuuliza kwamba katika ratiba umemweka Mbunge wa jimbo ili aweze kusalimia wananchi wake. RC anasema wewe hatuwezi kukuweka kwa sababu wewe ni mpinzani. Sasa haya ni mambo ya ajabu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo,kule kote alikopita ambapo Wabunge ni wa Chama cha Mapinduzi wamepewa nafasi Mkoa ule ule lakini mimiwa Mtwara Mjini nauliza pale mbona hujaniweka kwenye ratiba, ananijibu wewe ni mpinzani. Sasa hii ni demokrasia ya wapi, lakini niwaambie, naomba niwaambie kwamba hawa Ma-DC na Ma-RCna viongozi wengine wanapimwa na Mheshimiwa Rais kwa kazi wanazofanya, sio kazi ya kuwahujumu wapinzani ndani ya nchi hii. Mheshimiwa Rais atawapima atawapandisha vyeo kwa kazi wanazozifanya.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaomba sana Serikali, kwa sababu hawa watu wanafahamika, nilishawahi kuzungumza hapa ndani ya Bunge hili kwenye Briefingnikamweleza Waziri Mkuu wakati Fulani, akasema hakuna maagizo yoyote wanayotuma hawa Ma-DC na Ma- RC waweze kuwahujumu upinzani na hasa pale ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au Kiongozi yoyote wa Kiserikali anavyokwenda kutembelea kwenye maeneo yetu kwamba ni Mbunge lazima upewe nafasi. RC anayetoka Mtwara Mjini anamnyima nafasi Maftaha eti kwa sababu ametokea Chama cha Wananchi CUF, anaenda Nanyumbu, anaenda kule wapi, anaenda kuwapa wale Wabunge wa CCM, Mkoa mmoja ule ni ubaguzi na sisi tunasema kwamba kama tunahitaji nchi hii iwe na amani ili amani yetu iweze kuendelezwa tuheshimu msingi ya kidemokrasia, ni lazima tuheshimu misingi ya utawala bora hatuwezi kuwa na ubaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii tunasema inafuata good governance kwamba utawala bora na utawala wa kisheria na miongoni mwa misingi ya utawala bora ni kuwa na inclusive, watu lazima tushirikishwe, nilichaguliwa na wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini na kwa kuthibisha hilo juzi Mheshimiwa Rais ameondoka, lakini nilivyoitisha mkutano wa hadhara mafuriko yamekuwa ni makubwa kweli kweli kwa sababu wananchi wanamwamini Mbunge wao waliyemchagua. Serikali lazima ishirikiane na Mbunge husika sio kumtenga Mbunge, sio misingi ya kidemokrasia. Kwa hiyo kwa sababu Waziri ananisikia Mheshimiwa Mkuchika alikuwepo ameshuhudia hilo na Waheshimiwa Mawaziri walikuwepo wameshuhudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti,jambo lingine la ajabu ambalo nasikitika sana baadhi ya Wabunge wenzetu wanashadidia Wabunge wa Chama cha Mapinduzi wanashadidia kwamba Mbunge wa CUF amenyimwa nafasi halafu. Naomba haya mambo yaweze kurekebishwa ilituweze kuwa na maendeleo sawasawa ya nchi hii. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nashukuru Mwenyezi Mungu kunijalia afya njema niweze kuzungumza machache yanayohusu maji hasa katika jimbo langu la Mtwara mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni nchi ya tano kwa kuwa na maji mengi ardhini leo hii, ni jambo la ajabu sana mpaka leo tunazungumza suala la maji, maji, maji, Tanzania kwamba tuna maji wakati ukichimba hata chini ya Bunge ndani yake huko kuna maji mengi kabisa maji baridi kabisa.

Mhrdhimies Mwenyekiti, kwa miaka mitatu hivi sasa kuna miradi mingi tumekuwa tunaizungumza miradi ya maji ya maji kwa mfano; mradi wa kwanza ambao ni mradi mkubwa sana tulielezwa ndani ya Bunge mwaka 2016 kwamba Serikali inataka kujenga Mradi mkubwa wa maji ambao utatatua kero ya maji katika majimbo ya Mtwara mjini, Jimbo la Mtwara vijijini na Jimbo la Nanyamba na huu mradi ni mradi wa kutoa maji mto Ruvuma kule Kitaya wenye gharama shilingi bilioni 200, mpaka leo huu mradi aujahanza na tulielezwa wakati ule kwamba huu mradi ni fedha za kutoka Benki ya Watu wa India Exim Benki ni mkopo lakini mpaka leo hatuelewe huu mradi umefikia wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kila mwaka unawekwa kwenye bajeti, kila mwaka unaelezwa kwenye vitabu vya bajeti kwamba kuna mradi mkubwa wa kuboresha majiji ikiwemo mji wa Mtwara, Mtwara Mjini lakini pia wilaya zile zingine ambazo nimeweza kuzitaja. Sasa tulikuwa tunaomba sana kwamba wakati huu mwaka huu ni mwaka wa nne sasa tunaenda tunahitaji miradi hii mikubwa iweze kutekeleza fedha zake ziweze kuletwa kwa ajili ya kuweza wananchi wetu kuondokana na tatizo la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine tulikuwa na mradi wa maji pale Mtwara mwaka jana zilipelekwa bilioni tano kasoro hivi huu mradi, ni mradi wa kutoa maji kutoka kule Kata ya Jangwani eneo la Lwelu na lengo lake ni kusambaza maji maeneo yale ambako mtandao wa Bomba haujafika. Sasa huu mradi nataka kumueleza Mheshimiwa Waziri hapa kwa sababu, Waziri hakuwepo wakati huu mradi tunaanza lakini Naibu Waziri alikuwe kwamba huu mradi wale wahusika wa maeneo yale ambapo visima vimechimbwa na tunashukuru kwamba tulifanya pump test maeneo yale maji yakapatikana mengi sana pale Lwelu, lakini kuna maeneo ambapo lile bomba limeweza kupitishwa lile bomba limepita mule wale wananchi wa maeneo yale mashamba yale hawajapewa hata senti tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepigiwa simu sana wananchi wa maeneo yale wameniijia nyumbani zaidi ya mara kumi mara ngapi wakakaa wananiambia kwamba Mheshimiwa Mbunge tunataka utufikishie kilio chetu kwamba tunahitaji maji kweli wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini, lakini huu mradi wa bilioni tano inakuwaje kwamba Serikali imeleta huu mradi wamechukuwa mashamba ya watu wamechimba visima wamepitisha bomba lakini hawajapewa hata senti tano wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakaniambia Mheshimiwa Mbunge utufikishie kwa Mheshimiwa Waziri na nikaongea na Mheshimiwa Prof. Mbalawa nikamueleza Mheshimiwa Waziri tunakufahamu kwa utendaji wako mzuri ukiwa kwenye Wizara ile ya Mawasiliano ulikuwa unafanya kazi nzuri sana nilikueleza suala hili kwamba wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini ambapo huu mradi umepita hawajapewa hata senti tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kujuwa naomba kuuliza hivi ni kweli kwamba wananchi wakipelekewa mradi eti kwa sababu wanashida ya maji hawa watu hawapewi fidia japo mashamba yao yamechukuliwa maeneo yale yamechukuliwa siyo kweli Mheshimiwa Waziri tunaomba Mheshimiwa Waziri ule mradi wa Lwelu ambapo unaenda kupeleka maji kwenye maeneo ya Kiolo maeneo ya Mbalawa chini kule, Magomeni, Chipuputa, Mitembo na maeneo yote ya Jimbo la Mtwara mjini hawa wananchi lile pomba lilipita wananchi walipwe fidia yao kwa sababu ni haki kulipwa fidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nilikuwa ninaomba kuzungumza siku nyingi tuna pitia taarifa kwamba Serikali imedhamiria kuondoa tatizo la maji katika jiji la Dar es Salaam na nizungumze tu kwamba sisi Wabunge wote ni wadau wa mji wa Dar es Salaam na sisi Wabunge la Kusini hasa hasa ni wadau wa maeneo ya Mbagala, maeneo yale ya Chamazi kule ndiko tunakoishi tukifika Dar es Salaam. Sasa haya maeneo yanatatizo la maji sana na kila mwaka inawekwa kwenye mpango kwamba tuna visima vya borehole ambayo vinachimbwa kule kibiji na maeneo mengi lakini inazungumzwa tu kila mwaka kuna visima visima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mtandao wa maji haujengwi kupelekwa maeneo ya Rangi Tatu, kupeleka maeneo ya Chamazi, kupeleka maeneo ya Mbagala kiujumla wake tunahitaji watu wale wa Dar es Salaam wapate kweli maji kwa sababu pale Kimbiji kuna maji mengi sana sana huu ni mwaka wa tatu tunapitia taarifa kwamba visima vimeandaliwa, visima vitapeleka maji lakini utekelezaji haupo Mheshimiwa Waziri tunaomba kwamba maeneo haya yapelekewe maji safari hii, hii miradi isiwe kizungumkutu kwamba inazungumzwa inatajwa inatajwa kila mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nilikuwa naomba kuzungumza hapa ni mradi wa Makonde, huu mradi ulijengwa na wakoloni mwaka 1953 na wananchi wa Wilaya ya Tandahimba, Jimbo la Nanyamba, Newala Kiujumla wake, wanashida ya maji sana, sana, pale Mtwara na huu mradi ndiyo suluhisho lakini kila mwaka inazungumzwa fedha zinazopelekwa ni fedha chache kila mwaka inaelezwa hapa kwamba tumetenga fedha kwa ajili ya kurekebisha mtandao maji yapo pale Makonde yapo mengi sana, lakini tatizo ni serikali kupeleka fedha ili yale Mabomba ili yaweze kurekebishwa na mashine iweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na tunaambiwa mashine iliamishwa kwenye mradi huu miaka hiyo ya nyuma iliamishwa mashine na kupeleka maeneo mengine sasa naomba kujuwa sisi wananchi wa kule wananchi wa Mtwara hatupaswi kutumia mashine ile ili tuweze kupata maji kwa hiyo, tunaomba Serikali kwa sababu Serikali ndiyo yenyewe ilifanya blunder ya kuondoa mashine ya mradi wa Makonde watenge fedha za kutosha ili wananchi wa Tandahimba, Newala, Nanyamba na Mtwara Vijijini wapate maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni mfumo wa maji taka kwamba kumekuwa na baadhi tu ya miji hapa Tanzania ndipo huu mfumo umeweza kurekebishwa au umeweza kutengenezwa. Lakini maeneo mengi ya mijini Tanzania huu mfumo wa maji taka ni mfumo muhimu sana kwa sababu, mfumo wenyewe wa watu wanavyoenda kuchimba vyoo vyao vile halafu hali inakuwa ni mbaya vikijaa inakuwa hali mbaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wananchi hawana fedha ya kukodi maboza kila siku kwenda kuondoa maji taka tunaomba sasa Serikali kuanzia Mji wa Mtwara Mjini hakuna kabisa huo mkakati yaani Serikali haituelezi. Nimekuwa nauliza kila mwaka hapa kwamba kwanini Serikali haiweki mfumo wa maji taka katika Mji wa Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sisi pale Mtwara Mjini tuko karibu na bahari sana gharama yake inakuwa ni ndogo na tunavyojuwa mfumo wa maji taka kwenye maeneo yenye vyazo maji vikubwa kama Bahari ya Hindi mifumo inaelekea huko baharini, kwahiyo tunaomba Serikali safari hii itenge kiasi cha fedha Mheshimiwa Waziri unanisikia Mheshimiwa Naibu Waziri unapiga kazi sana tunakusikia tunaomba mfumo wa maji taka Jimbo la Mtwara Mjini kwa sababu sisi tumekuwa tukipata shida sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilikuwa naomba kuzungumza ni hili suala la wakala, wa wachimbaji wa visima wa ujenzi wa mabwawa. Mheshimiwa Waziri amezungumza vizuri sana hapa kwamba kuna huyu wakala, lakini jambo la ajabu huyu wakala ukitaka kuchimba kisima chochote kile hata ukiwa wewe ni Mbunge ukaenda ukawaeleza kwamba tunahitaji kuchimba kisima gharama wanazokupa ni kubwa sana na wananchi wa kawaida wanakuwa hawawezi kuwa-ford, kchukua hizi gari ambazo ni wakala wa Serikali gharama zake zimekuwa ni kumbwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati fulani nilikuwa natafuta maji Mtwara Mjini nikaenda kuwaeleza hawa mawakala lakini gharama walizonipa ilikuwa ni kubwa sana hata kama ni Mbunge niliweza, yaani sikuweza kuwa-ford zile gharama kwa hiyo watu wa kawaida, inakuwa ni hatari zaidi. Kwa hiyo, naomba kwa sababu lengo la Serikali ni kuwasaidia wananchi wa Tanzania, wananchi wa vijijini waweze kupata maji maeneo ambako hakuna vyanzo vya maji, lakini hizi gari za wakala zinaweza zikachimba visima virefu na visima vifupi gharama ziwe nafuu ili wananchi waweze kuwa-ford. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu na nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ya kwanza niweze kuchangia Wizara hii muhimu sana kwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wizara ya Afya kwa sababu bila afya njema hakuna Taifa la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati fulani hivi nilizungumza tukiwa katika Vikao vyetu vya Briefing nikamweleza Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu, kwamba kuna tatizo kubwa la Ugonjwa wa Malaria Tanzania na hasa ukiangalia maeneo yetu ya Pwani, kwa mfano, Jimbo la Mtwara Mjini, pale Mikindani na ukanda mzima wa Pwani kwa sababu kuna mazalia mengi ya mbu kutokana na chaneli za bahari ambazo zinaingia nchi kavi zinazalisha mbu wengi sana na Malaria umekuwa ni ugonjwa ambao unaua sana Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti nilimweleza Mheshimiwa Waziri wa Afya kwamba, wakati nasoma kidato cha kwanza mwaka 2000, niliweza kusikia taarifa za nchi mbalimbali duniani wamedhibiti ugonjwa huu wa malaria kwa kutoa chanjo ya malaria, nilipewa majibu ambayo sikuridhika nayo sana, lakini baada ya juzi Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutembelea nchi ya Malawi tukasikia kule Malawi kwamba wameingiza mpango wa kutoa chanjo ya malaria ikiwa ni nchi ya kwanza barani Afrika. Niwapongeze sana, hawa watu wa Malawi na jambo hili nimwombe Mheshimiwa Ummy Mwalimu, kama kweli tuna nia ya dhati ya kudhibiti tatizo la malaria Tanzania, basi tutoe chanjo ya malaria kwa wananchi wa ukanda huu wa pwani ambapo kuna mazalia mengi ya mbu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linawezekana, Mheshimiwa Waziri atuletee mpango wa kuleta chanjo ya malaria hapa Tanzania kwa sababu ni ugonjwa ambao unaua sana sana na wazungu wanasema failure to plan is plan to fail kama Wizara haina mkakati wa kuweka utaratibu wa kuwa na chanjo ya malaria maana yake malaria haiwezi kuondoka Tanzania. Tunaomba Watanzania wapewe chanjo ya ugonjwa huu malaria na hii inawezekana, kama wenzetu wa Malawi wameweza kanchi kadogo tu haka inakuwaje sisi Watanzania wenye resources nyingi kwenye bahari hii kubwa sana ambayo imeleta channel nyingi za kusababisha mazalia ya mbu kuwa mengi hapa nchini Tanzania. Tunaomba Watanzania wapewe chanjo ya malaria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine pale Kibaha kuna Kiwanda cha Viuadudu, kiwanda ambacho kwa muda mrefu hivi sasa, Serikali ama Wizara haijaweka mpango mzuri wa kuhakikisha kwamba zile dawa zinazotengenezwa hapa Tanzania zinapelekwa kwenye halmashauri zote nchini ili ziweze kupulizia kwenye mazalia ya mbu. Kiwanda kinazalisha dawa nyingi sana, tulitembelea pale kama Kamati, cha ajabu, wale wataalam wanasema zile dawa soko lao kubwa liko nje ya nchi wakati Tanzania hapa watu wanaugua malaria, watu wanakufa kwa malaria kuliko ugonjwa hata wa UKIMWI, malaria inaua kuliko hata UKIMWI, Kiwanda cha dawa za kuondoa mazalia ya mbu kipo Kibaha Tanzania, lakini soko lake lipo nje, wakati huku watu wanakufa kwa malaria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ije na mkakati na mpango maalum kwamba zile dawa za kuondoa mazalia ya mbu hasa kwenye miji ya pwani kwa mfano Mji wa Mikindani, Tarafa ya Mikindani pale Mtwara Mjini, watu wanakufa sana kwa malaria, kwa sababu kuna channel nyingi za mbu. Tunaomba hii Wizara iweke mikakati wa kuleta dawa katika halmashauri zote na kuanzia Mtwara Mjini ili wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini wasife kwa malaria kwa sababu dawa zinapatikana hapa nchini Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zikipulizwa kwenye channels zote, kwenye vile vyanzo vya maji tukapuliza hii dawa ambayo inazalishwa pale Kibaha, ugonjwa wa malaria utaondoka Tanzania, tudhibiti kwanza kwa sababu watu wanasema vaccination is better than cure, kwamba kinga ni bora kuliko kutibu sasa tusisubiri, tusisubiri watu wanaugua malaria then sisi tuweze kuomba misaada kwa hisani ya wananchi wa nchi za Ulaya ama nchi ya Marekani, tunaomba Serikali iweke kwenye bajeti Wizara hii, ije na mpango maalum wa kuhakikisha kwamba dawa zinazozalishwa pale Kibaha zinaenda kuondoa mazalia ya mbu Tanzania nzima na hii inawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo naomba kuzungumzia ni hospitali za wilaya; Mheshimiwa Waziri amezungumza hapa kwamba tuna mpango wa kujenga hospitali za wilaya Tanzania, lakini ukiangalia kwenye mpango huu, Mtwara Mjini sisi hatuna hospitali ya Wilaya na kila mwaka nimekuwa nazungumza kwa nini wasiweke kwenye bajeti kwamba kama yale maeneo yote ambayo tunahitaji kujenga hospitali za wilaya, basi yapewe kipaumbele yale ambayo hayana hospitali za Wilaya. Kwa hiyo naomba sana Mtwara Mjini, Manispaa ya Mtwara hatuna hospitali ya wilaya, tunaomba Mheshimiwa Ummy Mwalimu atuletee hospitali ya wilaya, wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini wanataka watibiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo naomba kuzungumza hapa ni kwamba, tumezungumza kwa muda mrefu kuhusu Hospitali ya Mkoa wa Mtwara na hii hospitali Mheshimiwa Ummy Mwalimu amekuwa akiizungumza kwa muda mrefu kwamba imepandishwa hadhi na kuwa hospitali ya rufaa. Jambo la ajabu, hii hospitali hata specialist hakuna, nimekuwa nazungumza miaka yote hapa ndani ya Bunge hili, kwamba tunahitaji specialist hakuna. Nimetembelea pale, kila siku nakuwepo pale, naongea na Madaktari wananiambia Mheshimiwa Mbunge katufikishie kilio chetu hiki, hatuna specialist hapa na hii hospitali inasaidia mkoa mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo namwomba sana Mheshimiwa Ummy Mwalimu, hii hospitali nimezungumza sana na wanasema kwamba wameipandisha hadhi kuwa ni hospitali ya rufaa, haina vifaa tiba pia, hata x-ray ni mbovu. Mwaka jana nimezungumza hapa x-ray ya hosptali ya Ligula ya Mkoa ambayo inahudumia mkoa mzima ni mbovu, kwa maana hiyo hatuna x- ray, hatuna vifaa tiba, ukienda pale dawa zenyewe hakuna dawa, yaani unatibiwa lakini hakuna dawa, unaambiwa uende ukanunue. Kila siku tunazungumza maneno haya, naomba Wizara iiangalie hii hospitali ya mkoa ambayo inahudumia wananchi wote wa Mkoa wa Mtwara na wananchi wengine kutoka nchi za jirani kama Mozambique.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwenye hospitali hii, nimekuwa nazungumza sana, niliongea wakati nachangia Wizara ya TAMISEMI hapa kwamba, sasa hivi hospitali zote zimewekwa utaratibu wa kulindwa na watu wa Suma JKT, lakini hawa Suma JKT hawapewi utaratibu mzuri za kuweza kuwapokea wagonjwa kama walinzi pale magetini, wakati mwingine wanawapiga wagonjwa, wanawadhalilisha wagonjwa, eti kwa sababu wamepita milango ambayo siyo sahihi. Mfano mzuri ni hii Hospitali ya Ligula, kuna walinzi wa Suma JKT, wananchi wameniletea malalamiko haya mengi sana, wameniambia kwenye mikutano ya hadhara, wameniambia nyumbani kwangu, Ofisini kwangu, wameniletea kwamba wanapigwa wanapoenda kutibiwa pale Hospitali ya Ligula na walinzi waliowekwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri kwa sababu tatizo hili siyo la Mtwara tu, siyo Ligula tu ni katika maeneo mengi, hawa walinzi awaangalie kwa sababu mtu anakwenda hospitali akiwa anaumwa, halafu anaenda kusumbuliwa, anapigwa ni jambo la ajabu sana, tunaomba Mheshimiwa Waziri aliangalie hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tumezungumza hapa kwamba Serikali imeweka mkakati ya kuwa na hospitali za kanda Tanzania na kila mwaka tunazungumza Kanda ya Kusini hatuna hospitali ya kanda ya rufaa. Katika maeneo mengi ya Tanzania kuna hospitali za kanda, maeneo haya yote na Serikali inapeleka fedha nyingi na mwaka jana hapa Mheshimiwa Waziri alituambia kwenye bajeti kwamba ametenga bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa OPD pale Mtwara. Hiyo bilioni moja haijaletwa Mtwara, bilioni moja hiyo haijaletwa kwa ajili ya kujenga hospitali ya kanda ambayo inatakiwa ijengwe pale Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni jambo la ajabu sana, tumekuwa tukizungumza kwa muda mrefu, kila mwaka Mheshimiwa anatenga bajeti, anatuambia tunapeleka bilioni moja na bilioni moja hata kama ingepelekwa bado haiwezi kukidhi haja. Tunaomba kama kweli tuna nia ya dhati ya kuboresha hospitali hizi za kanda au kujenga hospitali ya kanda, basi kule Mtwara ambako ndiko kunatakiwa kuwe na hospitali ya kanda kusini walete fedha ya kutosha kama wanavyopeleka maeneo mengine ili na sisi wananchi wa Mikoa ya Kusini tuwe na hospitali ya kanda ambayo tutaweza kuitumia kwa ajili ya kujitibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana safari hii, Mheshimiwa Ummy Mwalimu namweleza kabisa, kama hatatenga na kuleta fedha hii nang’ang’ania shilingi yake atatoka bila mshahara kwenye Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza hayo kwa niaba ya wananchi wa Mtwara kwa sababu wamenituma nije kuwaeleza wana tatizo la afya na Wanamtwara mnanisikia nazungumza ndani ya Bunge tukufu, Mheshimiwa Waziri ananisikia ninavyozungumza kwamba yale maneno mliyoniambia nije kumwambia Mheshimiwa Waziri aboreshe afya Mtwara, leo hii nazungumza na Mwenyezi Mungu ananisikia, ni siku ya kwanza ya Ramadhani nimefikisha kilio chenu wananchi wa Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri Ummy arekebishe mambo ya afya, amebaki yeye tu, mambo mengine yote Mtwara yako safi isipokuwa kwenye afya. Mheshimiwa Ummy Mwalimu namwaminia sana dada yangu, aje atuboreshee afya Mtwara. Ahsante sana kwa kunisikiliza. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na pia nitoe shukrani zangu za dhati kwa Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kusaini ujenzi wa gati moja la Bandari ya Mtwara ambayo ndiyo chachu ya uchumi Kanda yote ya Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Mtwara Corridor inategemea kwa kiasi kikubwa ujenzi huu wa bandari ulioanza kwa kusafisha maeneo ya ujenzi huo. Ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri ni kwamba, ahakikishe mara tu baada ya kumalizika ujenzi huo, basi magati mengine yawekwe kwenye orodha ya kujengwa ambayo ni matatu. Gati moja halitoshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba utanuzi wa bandari uendane na ujenzi wa reli ya Kusini ambayo itaanzia Mtwara – Liganga – Mchuchuma – Mbamba Bay na nchi nyingine za Kusini mwa Afrika. Ujenzi wa reli hii utasaidia sana kufungua uchumi na Bandari yetu ya Mtwara itapata mizigo ya kutosha, hivyo kuliingizia Taifa pato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mitandao ya simu kwa baadhi ya maeneo ya Mtwara Mjini haipo. Mfano, Mbawala Chini, Mkangala, Naulongo, Namayanga, Dimbuzi; maeneo haya network hakuna kabisa na yapo Mtwara Mjini. Sambamba na hilo, Mtwara Mjini hakuna network ya TBC kabisa. Hii inafanya Wanamtwara wakose huduma ya taarifa mbalimbali hivyo kuwa nyuma ya wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Ulinzi; mwaka 2016 tuliongea sana juu ya umuhimu wa barabara hii ambayo inaanzia Mtwara Mjini mpaka Ruvuma. Tunaomba iwekwe kwenye bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Viwanja vya Ndege ambavyo havimilikiwi na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, naomba kujua, kwa nini Serikali imeruhusu hili? Haioni kama ni hatari kwa Taifa letu na uchumi? Naomba Wizara itoe tamko juu ya hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna eneo ambalo hivi sasa Jijini Dar es Salaam ambalo lina msongamano mkubwa kama Mbagala hasa njia panda ya Charambe. Hapa kuna ulazima wa kujenga flyover haraka sana. Naomba bajeti ieleze, ujenzi wake utaanza lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kilwa Road hasa eneo la Somanga - Nangurukuru imeharibika sana na ina mashimo na mabonde makubwa na sioni ujenzi au ukarabati kabambe unafanyika hasa eneo hili. Tunaomba majibu ya Waziri ili nayo ianze kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya uchumi imesainiwa kwa kilomita 50. Tunaomba Mkandarasi asimamiwe kama alivyosema Mheshimiwa Rais alipokuja Mtwara Machi, 2017 na kusema kuwa Mkandarasi hayuko sharp, tunaomba asimamiwe barabara hii ijengwe haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa sasa kuna utanuzi wa bandari unaanza, tunaomba Wanamtwara Kusini tupatiwe usafiri wa meli hasa kwa ajili ya mizigo, kwa kuwa barabara inaharibika kwa cement kupitia barabara ya lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Uwanja wa Ndege wa Mtwara ni mbovu, hauna taa za kuongozea ndege; ndege hazitui usiku na inaleta usumbufu sana sambamba na kudumaza uchumi. Naomba bajeti hii ianze kukarabati na kuweka taa katika bajeti hii.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Afya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Mtwara ya Mkoa haina X-Ray na iliyopo ni mbovu. Naomba kuuliza, kwa nini hospitali hii ya Mkoa wa Mtwara haipelekewi X-Ray ya uhakika wakati kila mwaka tunaongea hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali inayotumika kama ya Wilaya inaitwa Hospitali ya Likombe iliyopo Mtwara Mjini, kwa nini haina X-Ray mpaka leo? Bajeti ya mwaka 2016/ 2017 Mheshimiwa Waziri alisema hospital hizi za Mtwara Mjini zitapelekewa X-Ray, mpaka leo bado. Kwa nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Waheshimiwa Wabunge wamepewa Ambulance: kwa nini Mtwara Mjini Wizara haijatuletea Ambulance hizo? Naomba Wizara itueleze Wanamtwara Mjini, juu ya Ambulance kwa ajili ya Tarafa ya Mikindani na Tarafa ya Mjini ili kuondoa kero na adha kubwa wanayopata wagonjwa wa Mtwara Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wodi ni chache katika Hospitali ya Likombe ambayo ndiyo Hospitali ya Wilaya, Mtwara Mjini. Naomba kujua, ni lini wodi zitaongezwa, nyumba za Madaktari na Wauguzi wa Hospitali ya Likombe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mazingira ya Wodi za Hospitali ya Mkoa (Ligula) siyo nzuri kabisa, naomba hospitali ipakwe rangi, vyoo vitengenezwe na huduma ya maji katika Hospitali ya Ligula yarekebishwe haraka iwezekanavyo, maana hali ya vyoo ni mbaya sana katika hospitali hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye taarifa ya Waziri katika kitabu chake kinaonesha Mtwara Mjini dawa zinapatikana kwa asilimia 92% kitu ambacho ukienda Hospitali ya Ligula ya Mkoa na Wilaya hali ni tofauti kabisa. Wagonjwa wanaambiwa baada ya siku mbili tu dawa zimekwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ufafanuzi, kwa nini tunaambiwa dawa zinapatikana kwa asilimia kubwa, lakini hospitali dawa hakuna na zikiwepo zinakwisha kwa siku mbili tu?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mwenyezi Mungu. Pia nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii. Naomba nami nichangie mchango wangu kwenye Wizara hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, mwaka 2017 uliunda Kamati ya Kuchunguza Madini ya Tanzanite na Madini ya Almasi na nilikuwa miongoni mwa wajumbe kwenye Kamati ile. Naomba nizungumze yale mapendekezo ambayo Kamati ilipendekeza utekelezaji wake umekuwa kwa kiasi gani. Nimshukuru Mheshimiwa Dotto Biteko, Waziri wa Wizara hii kwa sababu ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa ile Kamati ya Tanzanite na kwa kiasi kikubwa hotuba yake imegusagusa mambo hapa nimeweza kuyasikia, lakini nataka niweze kufahamu utekelezaji hasa ukoje.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, jambo la kwanza, tuliona pale Mererani pale ambapo kuna Mgodi wa Tanzanite kwamba kumekuwa na mrundikano wa leseni nyingi sana za wachimbaji hawa wadogowadogo ambao amewataja na tuliweza kubaini kwamba kuna leseni zaidi ya 900 pale ambazo zimetolewa na Serikali na Wizara na kukawa na changamoto kubwa kule chini, wale wachimbaji wadogowadogo wanavyochimba, kwamba wanafikia sehemu inaitwa mtobozano, wanatobozana kule chini wanakutana wanauana huko chini, watanzania wengi wanakufa.

Mheshimiwa Spika, napenda kujua je, pendekezo lile Mheshimiwa Waziri limetekelezwa kwa kiasi gani kwamba, wale Watanzania wanaokufa kutokana na idadi kubwa ya leseni ndogondogo zilizotolewa pale Mererani na kule chini wanauana kwa sababu wanakutana kule chini na wakati mwingine wanakutana na ule mgodi wa TML na wanauawa kule chini, Watanzania wengi sana. Suala hili limefikia wapi na utekelezaji wake ukoje? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine naomba kujua kutoka kwa Mheshimiwa Waziri hapa, kwamba amezungumza suala la one stop center kwamba itajengwa katika ule ukuta wa Mererani pake Arusha. Utaratibu wa hii one stop center ukoje, unakwenda kujenga kwa ajili ya kuuza yale madini yetu kwa sababu ya wanunuzi ambao wanakuja kununua kutoka nje ya nchi au tunakwenda kujenga zile smelters za kuchenjua yale madini. Kwa sababu tatizo limekuwa ni kubwa sana kwamba uchenjuaji unafanyika India kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Spika, hili jambo Kamati ilizungumza sana, kwamba Watanzania wanakosa ajira sana kwa sababu yake madini yetu hayachenjuliwi hapa Tanzania, hasa madini ya Tanzanite na kwa kiasi kikubwa yanachenjuliwa kule India na taarifa zinaeleza kwamba India kuna watu zaidi ya laki sita wamepata ajira kutokana na uchenjuaji wa madini ya Tanzanite ambayo yanatoka Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa naomba kujua seriousness ya Serikali juu ya kuchenjua madini haya pale Mererani Arusha. Kwa hiyo, hiyo smelter one stop center inakwenda kutoa suruhisho la kudumu, kwamba Watanzania sasa tuweze kuchenjua wenyewe na kule India kuwe hakuna tena ajira ya kuchenjua haya madini ya tanzanite.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine naomba kufahamu, Mheshimiwa Waziri atueleze, wakati tunapitia zile taarifa mbalimbali za watoa taarifa mbalimbali tulielezwa kwamba kutokana na utoroshwaji wa madini ya tanzanite ambao unafanyika kwenye Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, kuna njia za panya zaidi ya 400 ambazo madini haya yanapita kuelekea kule Kenya na hili limepelekea Watanzania wenyewe tuwe ni watu wa mwisho kunufaika na madini haya ambayo yanapatikana Tanzania tu duniani, sisi wenyewe tukawa watu wa mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wa kwanza ni kule yanakokwenda Marekani, ambako ni Tucson kule Marekani ndiko yanakouzwa na wanaopeleka kule ni Wahindi, ambao wanakwenda kuuza kwa kiasi kikubwa sana haya madini! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hao ndiyo wanufaikaji wa pili, wanufaikaji wa tatu ni watu wa Afrika Kusini, ambako hii kampuni ya TML ndiyo inaonyesha kwamba uhusiano wake mkubwa na nchi ya South Africa ndiko wanakotoka kule, lakini wengine ni Wakenya, wa nne, na sisi wenyewe ni wa mwisho watu Watanzania. Sasa hili limepelekea kwa sababu kuna njia nyingi za panya, haya madini yanatoroshwa katika nchi ya Tanzania kuelekea nchi ya Kenya na taarifa zinasema, Kenya imeendelea baadhi ya miji imekuwa ni mikubwa, imekuwa na maendeleo ukiwemo Mji wa Naivasha kwa sababu ya madini ya tanzanite yanayotoroshwa kutoka Mererani Arusha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa naomba kujua, hizi njia 400, kwa sababu imeelezwa hapa kwenye na taarifa ya Kamati na ya Upinzani imezungumzwa pia kwamba personnels wenyewe hawatoshi. Mpango wa Wizara ukoje wa kuajiri personnel ya kuweza kuhakikisha kwamba tunadhibiti hizi njia za panya, njia 400 zilizopo pale Arusha na kule Mkoa wa Kilimanjaro. Mheshimiwa Waziri naomba atupe maelezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, kulikuwa na suala hili la STAMICO, kwamba, STAMICO tumekuwa tunazungumza kwa muda mrefu sana, kwamba ni taasisi ya Serikali ambayo imekosa nguvu, aidha nguvu ya kifedha ama nguvu ya kiusimamizi, kwamba hata wale watendaji wake wamekuwa ni watu ambao tulivyoenda kuangalia wizi ambao ulikuwa unafanywa na watu wa TML, pale Mererani Arusha, yaani zinaibiwa ndoo sita za madini, yule mtu wa STAMICO yuko palepale ndani, ukiangalia ile clip inaonesha kabisa mtu wa STAMICO amewekwa pembeni kule, watu wanafanya sorting ya madini, ndoo sita zinaibiwa, yeye yuko palepale, ambaye ndiyo tegemeo la Serikali, tegemeo la Watanzania kwamba aweze kusimamia madini yetu pale ili Serikali iweze kupaya gawio, iweze kupata tozo, iweze kupata kila kitu, yeye yuko palepale, ndoo sita za madini zinaibiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atuambie, kwamba Watanzania hawa tunaowapeleka kwenye kampuni hii ya Serikali, ambayo sisi tunaitegemea, sasa hivi wameweka mkakati gani wa kuweka personnel ambao wana uwezo wa kusimamia madini yetu ili Serikali isikose mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi STAMICO tuna asilimia pale 49 katika ile kampuni ya TML, kwamba ushirikiano wa Serikali tunategemea kampuni hiyo, kwa hiyo ni lazima tuwe na watendaji ambao wana capacity kubwa ya kuweza kuwazuia wale wageni, wale akina Riziwani Ulaa,na wengine wale wenzao ambao walikuwa wanaiba yale madini yetu takribani ndoo sita na Serikali kukosa kabisa gawio na kukosa kabisa mapato.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, kuna hisa moja ambayo ilikuwa imezungumzwa sana katika ile kampuni ya TML, tunaita hisa kivuli, ya mtu mmoja anaitwa Amy Mpungwe, hii hisa imekuwa haielewekieleweki, kwamba hiyo hisa hata gawio nalo halipatikani kwa huyo Amy Mpungwe, ambaye ni Mtanzania, aliingia kwenye ile TML. Sasa Mheshimiwa Waziri tunaomba atupe taarifa, tumezungumza suala la local content hapa, kwamba kuwawezesha watanzania waweze kujihusisha na rasilimali za Tanzania na sheria hii inaeleza asilimia 25 Watanzania waweze kuhusishwa katika ajira na katika kumiliki rasilimali za Watanzania. Ile hisa moja iliyopo kwenye kampuni hii ya TML, ya Amy Mpungwe ambaye ni Mtanzania, bado inaendelea kuwa hisa kivuli, hisa hewa au namna gani. Tunaomba atupe maelezo Mheshimiwa Dotto Biteko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, naomba kuzungumza, mwaka jana nilieleza hapa suala la madini ya blue sapphire, ambayo kwa kiasi kikubwa duniani sasa hivi yanaonekana kwamba yanazalishwa kutoka nchi ya Sri Lanka, lakini ukija kule kusini, Ruvuma pale Tunduru, madini ya blue sapphire yanapatikana kwa kiasi kikubwa sana na wanunuzi wa madini haya hapa Tanzania ni watu wa Sri Lanka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa niiombe Serikali, kwa sababu haijaweka utaratibu mzuri, haijaweka utaratibu wa kuwa wa certificate of orgin, yaani kuoesha kwamba madini haya yanatoka Tanzania, kwa sababu yakinunuliwa na wale wa Siri Lanka, wanapeleka kule Sri Lanka, wanajumuisha na ya kwao, halafu ni madini yenye thamani sana duniani, blue sapphire, halafu wanasema haya madini yote yanatoka Sri Lanka, wakati mengi yake yanatoka kwetu Tanzania na haijulikani kama yanatoka Tanzania na yanatoka Tunduru Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri, mwaka jana nilizungumza hapa hili suala kwamba aende Tunduru akaweke utaratibu mzuri, yale madini yetu yanayotoka pale Tunduru, yaweze kuonyeshwa kweli yanatoka Tanzania na yanatoka Tunduru badala ya kwamba yanajumuishwa kule dunia nzima inafahamu blue sapphire inatoka Sri Lanka pekee, kumbe siyo kweli. Namwomba Mheshimiwa Waziri na Wizara, hili suala waliangalie kwa jicho la kipekee kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, kuna suala hili Mheshimiwa Waziri amezungumza hapa, kwamba tunahitaji kuwasaidia wachimbaji wadogo wadogo waweze kupata manufaa na hawa ni Watanzania na hawa ndiyo maskini ambao tunawazungumzia hapa, lakini ukienda Tanga leo hii hawa wachimbaji wadogo wamepewa leseni, lakini bado wanasumbuliwa sana na Askari wetu. Yaani wale wachimbaji wakubwa kwa mfano, ukienda kwenye maeneo ya Umba River, eneo la Kalalani, Mgombeni, Kigwase, Mwakijembe, wanatumwa wale watu polisi Askari wa….

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Maftah, nakushukuru sana.

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie, kidogo tu.

SPIKA: Haya haya.

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, nilichokuwa nasema, kwamba ukienda kule Tanga kwenye maeneo hayo niliyoyataja, wale wachimbaji wakubwa, wanawatuma Askari, kwenda kuwabugudha hawa wachimbaji wadogo ambao ni Watanzania kwenye maeneo yetu hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sana Serikali kwamba hawa watu wana haki na wamepewa leseni zile za kisheria kabisa, waachiwe ili tuweze kuondokana na umaskini hapa nchini Tanzania. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami nichangie bajeti hii ya Wizara hii muhimu ya TAMISEMI kwa kuanza na maneno yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwenyezi Mungu Subhanahu-Wataala anasema kwenye kitabu chake kitakatifu cha Quran, “antum shuadaau fil-ardhwi.” Kwamba wenyewe nyie binadamu hapa hapa duniani mnajuana na mnafahamiana kwamba huyu anafanya nini na huyu yupo vipi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kila anayesimama ndani ya Bunge hili anaanza kwa kupongeza. Sisi Wabunge tunafahamiana, nani anayepongeza kwa dhati na nani anayepongeza kwa ajili ya kutaka kuonekana kwamba naye anaiunga mkono Serikali, lakini kinafsi tunafahamiana sisi binadamu wenyewe humu ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuzungumza kwa dhati kabisa kwamba Mheshimiwa Jafo mimi ninampongeza. Pongezi zangu hizi ni za dhati kabisa kwa sababu sinaga unafiki siku zote. Ninalozungumza, kama kuna ukweli nazungumza ukweli kwamba hapa natakiwa nizungumze ukweli, kama kwenye kukosoa ninakosoa ukweli. Mimi ni miongoni mwa watu ndani ya Bunge hili ambao tunazungumza ukweli panapotakiwa kuzungumza ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Jafo tunakushukuru sana kwamba uliweza kuleta fedha pale Mtwara shilingi bilioni 21 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Mtwara ikiwemo ujenzi wa baadhi ya barabara pale Manispaa ya Mtwara Mikindani ambapo Mbunge wake ndio mimi ninayezungumza, Mbunge wa Mjini Kanda ya Kusini pale. Zile fedha zimefanya kazi ile ambayo Mheshimiwa Jafo ulikusudia iweze kufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, niliwahi kuzungumza ndani ya Bunge hili kwamba wakati tunapitisha wale Waheshimiwa Madiwani, wameenda kusaini ule mkataba, walienda kusainia Dar es Salaam na yule Mkandarasi ambaye anafanya kazi ya ujenzi wa ule mkataba. Sasa sijui kulikuwa na nini? Niliwahi kuuliza hapa ndani ya Bunge Mheshimiwa Jafo nikamweleza kwamba kwa nini wale wahusika walikwenda kusainia ule mkataba Dar es Salaam? Kwa sababu taarifa tulizokuwa nazo ni kwamba kulikuwa na ujanja ujanja kidogo ulifanyika ili baadhi ya fedha ziweze kuchotwa na kutumika kwa maslahi mengine ambayo siyo ya ule ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, kwenye hizi fedha, ujenzi unaendelea vizuri, lakini unachelewa kukamilika, sasa hatujui tatizo ni nini? Tatizo ni wewe TAMISEMI au tatizo ni yule Mkandarasi ambaye ni Kampuni ya Kichina? Barabara kadhaa zimejengwa, nyingi bado hazijakamilika pale Mtwara Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba msukumo wako Mheshimiwa Jafo, kwa sababu ni mtu ambaye unasikia tukikueleza, tunaomba umsukume yule Mkandarasi, barabara zile za Mtwara Mjini eneo la kupumzikia wananchi wa Mtwara pale Mashujaa, tunajenga pale Hide Park, eneo la kupumzika lile, paishe, pakamilike kwa wakati ili vijana wetu waweze kupumzika siku za weekend na sisi wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini. Kwa hiyo, tunaomba huu mradi uufuatilie uweze kukamilika kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni hili suala la ugonjwa huu ambao Mheshimiwa Jafo ameugusia, ugonjwa wa Corona, ni ugonjwa ambao ni hatari sana. Ugonjwa huu hasa kwenye Halmashauri hizi ambazo zipo pembezoni huko kwa mfano Mtwara, kule Kitaya maeneo ya Masasi, Nanyumbu na wapi ambapo tumepakana na nchi ya Mozambique wananchi wanaingiliana sana na sijaona utaratibu wa Serikali kwamba inawapima wale watu wanaokuja kupitia zile njia za panya. Kwa sababu maeneo yale ya Kitaya, Mahurunga na Kivava watu wanapita usiku na mchana kutoka Msumbiji kuja Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nashauri Wizara ya TAMISEMI iweke mpango maalum wa kuhakikisha kwamba mipaka ile (njia zote za panya) zinazibwa na wale watu wanaoingia wanapimwa sawa sawa. Hiki kitendo ambacho kinafanywa na Serikali kwa kumulika tu, unachukua kitu kama tunavyofika hapa Bungeni unamulikwa usoni, halafu joto lako sijui likiwa 32 wewe hauna Corona. Wenzetu nchi za nje ukienda Kenya hawapimi kwa kipimo hicho tu kimoja wakaweza kugundua kwamba huyu mtu anaumwa Corona, wanapima damu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tulikuwa tunaomba sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, weka fedha za dharura kwa ajili ya kushughulikia watu wote wanaoingia Tanzania na Watanzania kila Halmashauri waweze kupimwa damu tuweze kugundua ugonjwa huu wa Corona.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipimo cha kumulika joto tu kwamba joto limepanda au halijapanda, mtu mwingine anaweza akapanda joto lake kwa sababu ya mazoezi, ametembea sana kwenye jua, joto lake likapanda. Ili tuweze kugundua kweli kuna wagonjwa wa Corona Tanzania, tufuate nchi za wenzetu; majirani zetu hapa Kenya na Uganda wanatumia vipimo maalum, kila mwananchi anapimwa kipimo cha damu ili aweze kugundulika kama ana Corona au hana vimelea hivi vya Corona. Tunaiomba Serikali ichuke suala hili seriously. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, kuna suala hili la Hospitali za Wilaya. Niliwahi kusema mwaka 2019 kwamba maeneo mengi wenzetu wamepewa Hospitali za Wilaya, Manispaa ya Mtwara Mikindani sina Hospitali ya Wilaya na niliongea na Mheshimiwa Jafo tukakubaliana kwamba atatenga fedha kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Mtwara Mikindani, lakini mpaka leo zile fedha hazijaletwa na tulishatenga eneo pale Kata ya Ufukoni ambapo kuna wakazi wengi sana, nikazungumza na Mheshimiwa Waziri Kata ya Ufukoni ina wakazi wengi sana, hatuna Kituo cha Afya lakini pia Manispaa nzima haina Hospitali ya Wilaya. Tunaomba itengwe fedha tujengewe Hospitali za Wilaya, pale Mtwara Mikindani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana, hii ni bajeti yangu ya mwisho kuzungumzia suala la TAMISEMI mwaka huu 2020. Mheshimiwa Waziri kwa kuwa uliniahidi kwamba Mtwara Mjini utaleta fedha tujenge Hospitali ya Wilaya, naomba basi mwaka huu utuletee zile fedha, wananchi wa Mtwara nilishawaeleza kwamba tayari Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI ameahidi na ameiandika kwenye diary yake kwamba miongoni mwa maeneo ambayo Hospitali za Kanda zitapelekewa fedha kujengwa ikiwemo ni Manispaa ya Mtwara Mikindani, mwaka huu tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, tulipata zile fedha kwa ajili ya kuboresha Kituo cha Afya cha Likombe. Tulipata shilingi milioni 500 pale Mtwara. Sasa kituo kile kinatumika sasa kama Hospitali ya Wilaya kwa sababu hatuna Hospitali ya Wilaya. Wananchi wa maeneo mengi hata maeneo ya vijijini kule Mtwara Vijijini, Jimbo la Nanyamba na wengine wanatoka Mozambique wanakuja kujitibu kwenye Hospitali ile ya Likombe, lakini ile hospitali haina capacity kubwa ya kuweza kupokea wagonjwa wengi kwa kiasi hicho ambacho wanafika pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, bado tunaomba kile kituo kama mpango wa Hospitali ya Wilaya bado unachelewa, basi kipewe vitendea kazi maalum; kiwekewe X-Ray, kiongezewe watabibu na kipelekewe madaktari bingwa kwa sababu kile kituo kinafanya kazi kama Hospitali ya Wilaya. Mheshimiwa Jafo kwa kuwa ni msikivu sana tunaamini na wananchi wa Mtwara wanaamini kwamba haya yote ambayo wamenituma kuja kukueleza utayafanyia kazi mwaka huu 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala hili la fedha, Kamati ya TAMISEMI imezungumza na imeshauri Serikali kwamba fedha ambazo zinatengwa na Halmashauri ambazo sisi wabunge tulipitisha hapa kwenye Bunge hili ikawa ni sheria sasa kwamba ile asilimia 10 ni lazima iende kwa wahusika; walemavu na vijana waweze kupata ile fedha, lakini Kamati imeeleza hapa kwamba zipo baadhi ya Halmashauri hazipeleki zile fedha. Nyingine zinapeleka 3% tu. Imetajwa hapa Halmashauri ya Simiyu na Halmashauri nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa huku ni kulidharau Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo ndiyo tulipitisha hii sheria kwamba ile asilimia 10 itengwe na kila Halmashauri itenge kwa mapato ya ndani kwa ajili ya kuhudumia hawa watu wenye ulemavu na vijana. Tunaomba sana Halmashauri ambazo hazitengi hizi fedha, Serikali, Mheshimiwa Jafo aje atueleze anazichukulia hatua gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inachukua hatua gani kwa Halmashauri ambazo hazitengi fedha hizi asilimia 10 kwa ajili ya kuwagharamia, kuwapa hawa vijana na watu wenye ulemavu kwa sababu ni sheria ambayo tulipitisha sisi kama Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Kutokuitekeleza hii sheria maana yake ni kulidharau Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii mtaani kuna walimu wengi sana ambao wame-graduate takribani miaka mitatu, minne hivi sasa na hawana ajira. Ukipitia shule za sekondari na msingi ambazo Serikali inajinasibu kwamba tumeweka elimu bure, wanafunzi wamekuwa ni wengi, ikama ya walimu imekuwa ni ndogo. Yaani ukilinganisha walimu na masomo, walimu ni wachache masomo yaliyoko na pia wanafunzi ni wengi kuliko walimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba ile ratio sasa ya walimu kwa masomo iweze kuzingatiwa. Hili haliwezi kupatikana kama Serikali inawaacha walimu mtaani wanahangaika, hawana ajira. Shule hazina walimu, lakini walimu wanahangaika, wanatembea mitaani, Serikali haitaki kuwaajiri. Tunaomba kasi ya kuajiri ambayo Serikali imekuwa inadonoadonoa iweke utaratibu maalum wa kuwaajiri hawa walimu ambao wapo mitaani, shule zetu ziondokane na upungufu wa walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, walimu wapo wengi sana Mheshimiwa Jafo unawajua huko mitaani. Ukitembelea shule hata hapa Dodoma, nenda kaangalie ikama ya walimu kwa masomo, bado walimu hawatoshi wakati Serikali imesomesha walimu wengi wapo mitaani. Shule za private huko, nazo zimejaa. Kwa hiyo, hawa walimu tumewafundisha kwa kazi gani? Wamesoma kwa gharama kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri kwenye ule mkopo wa Serikali hawa walimu wote wanasomeshwa na wanakopeshwa, wengine wanapewa grant, walimu wa sayansi wanasomeshwa bure na Serikali. Leo tunawasomesha, tunaenda kuwaacha mtaani. naomba Wizara ya TAMISEMI, kwa sababu tuna uhitaji wa walimu, shule zetu za msingi na sekondari hazina walimu, tuongeze walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, nizungumze kidogo suala hili la TARURA. Wenzangu wamezungumza kwamba TARURA ina maeneo mengi ya kufanyia kazi ikiwezekana kuliko hata TANROADS kwa sababu miji yote, vijijini huko na mijini wamepewa usimamizi wa TARURA. Fedha wanazopewa ni asilimia 30, TANROADS wanapewa asilimia 70. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tunaomba atleast iweze kuongezwa hii fedha asilimia 30 ifike asilimia 50 angalau iwe nusu kwa nusu kati ya TANROADS na watu wa TARURA ili hawa watu wa TARURA waweze kujenga barabara zetu. Barabara zetu ni mbovu na mafuriko ndiyo hivyo kama unavyoona tena na ofisi ambayo inashughulikia suala la maafa mwaka 2019 haijapewa hata senti tano. Ofisi ya Mheshimiwa Jenista hapa haijapewa hata senti tano kwenye suala la maafa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tulikuwa tunaomba, ili kuokoa barabara zetu, maafa haya ambayo yanatokea mijini na vijijini, TARURA ipewe fedha itasaidiana na Wizara ya Mheshimiwa Jenista ili kujenga barabara ambazo zimebomoka huko mijini na vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, michezo na hasa mpira wa miguu ni mchezo unaotoa ajira ya pesa nyingi kwa wiki au mwezi. Wapo wachezaji wengi duniani kutoka Afrika ambao wanalipwa mabilioni ya fedha kwa wiki mfano Samweli Eto wa Cameron na Didie Drogba wa Ivory Coast. Wizara ihakikishe inainua michezo kwa kuanzisha timu za vijana kila wilaya ili kutengeneza vipaji ambavyo vitaweza kupata ajira ya kucheza mpira wa kitaaluma ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, Viwanja wa Michezo; ili michezo ikue lazima kuwe na viwanja vizuri vyenye ubora.

Mheshimiwa Spika, Viwanja vya Michezo vya Kikanda; viwanja hivi ni muhimu kujengwa ili kuwe na uwiano katika nchi. Kanda ya Kusini ikiwa na uwanja pale Mtwara itachochea wananchi kupenda michezo na kuinua uchumi wa vijana na Watanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, michezo mashuleni ndio chachu ya kuinua vipaji vya Watanzania. UMISETA na UMITASHUMTA iwekezwe ipasavyo. Wizara itenge pesa zipelekwe mashuleni badala ya kuwabebesha mzigo huu TAMISEMI peke yake na hata TAMISEMI hawapati pesa mashuleni kwa ajili ya michezo badala yake wanabebeshwa mizigo Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu mzigo ambao hawajatengewa bajeti yake.

Mheshimiwa Spika, ili timu ya shule iende katika kituo cha tarafa au cha wilaya kilichotengwa kwa ajili ya michezo kuna gharama kubwa mfano chakula na gharama za wasimamizi. Wizara itenge pesa za UMISETA na UMITASHUMTA ili iweze kufanyika effectively maana kinachofanyika hivi sasa ni kuondoa lawama tu na sio effective kwa sababu haifanyiki kwa siku zinazotakiwa kwa kukwepa gharama.

Mheshimiwa Spika, Wizara iweke siku maalum ya maonyesho ya ngoma za asili ambayo itafanyika kikata, wilaya, mkoa na kitaifa hii itasaidia kufufua utamaduni wetu nchini na pia kujitangaza kwa mataifa na baadaye kuingiza pato la Taifa kupitia utamaduni wetu.

Mheshimiwa Spika, Mtwara na Lindi hakuna frequency za TBC (television) na zinapatikana kwa taabu sana. Naomba Wizara iweke mawimbi ya Television hizi Mtwara (TBC1 na TBC2). Mimi tangu TBC2 imewekwa binafsi sijawahi kuiona na wala sijui inafananaje. Katika maeneo yote imefungwa isipokuwa Mtwara na Lindi tu.

Mheshimiwa Spika, si kweli, kwamba waandishi wanavamiwa nchini, isipokuwa waandishi wa habari wanapokuwa kazini wanaweza kupata ajali kama mfanyakazi yeyote yule na sio kama inavyodaiwa na baadhi ya Wabunge kwamba waandishi wanavamiwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu na Kiti chako, napenda kuchangia Wizara hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kuhusu Mji wa Mikindani. Mji huu ni wa kale wenye majengo mengi na historia kubwa ya asili tangu wakati wa miaka 200 BC. Mji huu umeachwa na historia hii ya pekee nchini inatoweka bila sababu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni kuhusu Trade Aid. Kuna taasisi ya Kiingereza inaitwa Trade Aid ambayo ni charity group inayofanya kazi ya kuangalia baadhi ya majengo kwa maslahi yao binafsi na sio Taifa kama Taifa. Kampuni hii ya Kiingereza wanakarabati baadhi tu ya majengo na kutangaza nje ya nchi, kwa bahati mbaya kila kinachokusanywa ni chao kwa kigezo kuwa wanasaidia jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kusaidia jamii ni jambo jema, lakini Serikali lazima ikarabati majengo ya kale ya Mikindani sambamba na kujenga kituo cha watalii Mtwara ili kuvutia watalii kufika Mtwara Mjini eneo la Mikindani. Ukikarabati majengo haya na kujenga vivutio vingi ni wazi kwamba vijana wetu watapata ajira kwa kuhudumia wageni mbalimbali na hivyo kuondoa umaskini Mtwara Mjini na Tanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu ni kuhusu ukarabati wa jengo la miaka 100. Kuna jengo ambalo linasemwa limekarabatiwa lakini jengo hili kubwa na muhimu halijakarabatiwa bali limezibwa milango tu. Wito wangu kwa Serikali, Waziri aje Mtwara – Mikindani kujionea hali; jengo hili muhimu likarabatiwe na Serikali siyo kuiachia Trade Aid na Mikindani Tourist Center ijengwe Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, utalii wa Kituo cha Mikutano Arusha (AICC). AICC Arusha ni nguzo muhimu ya watalii wanaokuja kwa ajili ya mikutano nchini. Kupitia kituo hiki cha AICC, Serikali inakusanya pesa nyingi sana bahati mbaya pesa hizi zinarudishwa kwa Mkurugenzi wa AICC na kufanya ukarabati ambao hauko sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, AICC wamekarabati Ukumbi wa Simba kwa shilingi bilioni 3.5 lakini wamejenga majengo marefu yenye ghorofa sita kwa shilingi 1.8. Ukarabati wa Ukumbi wa Simba umetumia pesa vibaya kuliko kujenga jengo kubwa jipya. Wito wangu CAG aende akakague ukarabati huu wa AICC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema haya kwa sababu sheria iliyoanzisha Shirika hili la AICC ni kuendeleza ujenzi wa kumbi nyingine za mikutano nchini. Kama ukarabati tu unazidi ujenzi, sidhani kama tunaweza kujitanua katika utalii wa mikutano. Naomba CAG akakague ukarabati wa AICC Ukumbi wa Simba. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia dakika hizo tano ulizonipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwamba ili tuweze kuwa na wanafunzi ambao wanafundishika vizuri level zote za elimu, iwe sekondari kwa maana ya kwamba O-level na A-level lakini Vyuo vya Ufundi, Universities ni lazima tuanze na uwekezaji katika elimu, pale tunasema Pre–Primary Education yaani Elimu ya Msingi na Elimu ya Chekechea kabisa kule chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanafunzi yeyote ambaye amefundishwa vizuri, akiwa chekechea, elimu ya awali, mtoto huyu atakuwa na uwezo mzuri wa kuweza kufundishika vizuri atakapokuwa Shule ya Msingi. Akifundishwa vizuri shule ya msingi, atafundishika vizuri sekondari, elimu ya kidato cha nne lakini pia kidato cha tano na kidato cha sita, hata anapofika level ya elimu ya juu, kwa maana ya Chuo Kikuu, atafundishika vizuri na mwisho wa siku tutaweza kuwa na wasomi wazuri katika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa sana kwa kuona kwamba sasa hivi katika nchi yetu kuna mkanganyiko wa usimamizi wa elimu. Tuna Wizara ya Elimu, tuna Wizara ya TAMISEMI, mimi nashangaa sana na nazungumza haya nikiwa Mwalimu, lakini pia nikiwa Msimamizi wa Elimu, kwamba tunavyoangalia Wizara ya Elimu, kwamba imepewa kusimamia miongozo, ni jambo la ajabu sana. Tunataka Wizara ya Elimu isimamie elimu, tunataka Wizara ya Elimu isimamie miundombinu ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ninavyozungumza, ukija Mtwara Mjini pale kwa mfano, tuna Shule ya Msingi Mbae, ina madarasa mawili; haina vyoo, lakini ina wanafunzi zaidi ya 630 halafu leo hii tunasema kwamba eti wanafunzi Mtwara na Lindi hawafanyi vizuri katika mitihani yao. Hatufanyi vizuri kwa sababu hatuna miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Mikoa ya Mtwara na Lindi hatufanyi vizuri katika elimu kwa sababu pia Walimu hawatoshi. Shule za Msingi, Shule za Sekondari hatuna Walimu wa kutosha. Tunaomba Wizara itusaidie hili. Mkoa mzima wa Mtwara tuna upungufu wa Walimu, hawatoshi, watuletee Walimu tuweze kufanya vizuri kama ilivyo katika mikoa mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa dakika zangu ni chache, naomba nizungumze suala hili ambalo Serikali ya Awamu ya Nne ililianzisha. Mimi nilikuwa Msimamizi wa elimu wakati huo, nilikuwa Mkuu wa Shule, Mchinga Sekondari kwa miaka mitano. Tulipewa miongozo ya kusimamia elimu kupitia BRN, lakini tangu mwaka 2016 hatuoni kuna nini? Kwa nini huu mpango unaoitwa BRN (Big Result Now) ambao Serikali iliiga kutoka nchi ya Malaysia. Ule mpango ulikuwa ni mzuri kwa sababu ule mpango ulikuwa unaleta usimamizi katika elimu kwamba Mwalimu anapofanya vizuri, anapofundisha vizuri, mwisho wa siku anakuja kupewa motivation kupitia Wizara ya Elimu na TAMISEMI, lakini sasa hivi BRN haitajwi kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwamba kama kweli tunahitaji matokeo mazuri katika elimu, turudishe huu mpango wa BRN katika elimu, ulikuwa unasaidia sana kuchochea Walimu kuweza kufanya kazi, Walimu kuweza kufundisha kwa sababu walikuwa wanapewa motisha pale ambapo wanafaulisha vizuri masomo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la kuboresha elimu linaendana sambamba na kuboresha maabara. Kulikuwa na mpango wa kujenga maabara, nami kipindi kile nikiwa Mkuu wa Shule, tuliweza kujenga maabara nyingi sana, lakini mpaka leo tunavyozungumza zile maabara hazina vifaa, hazina kemikali, hazina Walimu wa sayansi ambao watakuja kufundisha yale masomo ya sayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama kweli tunahitaji kuipeleka elimu yetu mbele, lazima Wizara ya Elimu iliangalie suala hili la maabara tupeleke kemikali mashuleni. Jambo la umuhimu zaidi ni usimamizi wa elimu kwa Wakuu wa Shule. Wakuu wa Shule ndiyo nyenzo pekee ambapo tukiwatumia ipasavyo, hawa Walimu wanaweza kusimamia elimu yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango huu wa elimu bure hivi sasa hasa katika Shule za Mikoa ya Lindi na Mtwara, hakuna michango inayokusanywa, hakuna pesa za ulinzi wala taaluma na hizi shule maeneo mengi ziko vijijini, ziko maeneo ya vijiji na Halmashauri zenyewe…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu na Kiti chako, napenda kuchangia Wizara hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, korosho wakulima hawajalipwa; kutokana na taarifa za TAKUKURU mwaka 2015/ 2016 wakulima wa Mkoa wa Mtwara wa zao la korosho hawajalipwa bilioni thelathini na vyama vya msingi. Hali hii imekuwa inawavunja nguvu sana wakulima kwa kuwa Serikali ilijigamba kwa kiasi kikubwa kuwa Mfumo wa Stakabadhi Ghalani unamsaidia mkulima. Hata hivyo, pamoja na wizi wote huu kwa wakulima wanyonge, hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa kwa wahusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Malipo ya Korosho 2016 Mtwara Mkindani; Mtwara Mjini kuna AMCOS mbili, moja ya Naliendele na nyingine ya Mikindani. Wananchi wameniambia wamepeleka korosho zao kwenye vyama hivi vya msingi lakini cha ajabu;

(a) Baadhi yao mpaka sasa hawajalipwa.

(b) Kuna minada mine ambayo ilifanyika mfululizo lakini vyama hivi vimelipwa minada ya tatu na nne (ya mwisho na kuacha ya kwanza ambayo ilikuwa na bei kubwa).

(c) Korosho kuuza kwenye mnada Sh.4,000/= lakini wananchi wamelipwa Sh.3,100/= (elfu tatu na mia moja) tu au chini ya hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wakulima hawa walipwe pesa zao haraka iwezekanavyo na wahusika wote wachukuliwe hatua stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Pembejeo ya Salfa (sulfur). Naomba sana Serikali inunue pembejeo na kugawa bure kama ilivyoahidi. Kuna wakulima ambao wanahitaji salfa ya maji ambayo wanadai ni nzuri kuliko ya unga, hivyo, wasikilizwe wakulima hawa juu ya salfa hii ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Uvuvi Mtwara. Mtwara kuna Bahari ya Hindi yenye samaki wengi sana. Naomba Wizara ijenge viwanda vya samaki kama ilivyo Mwanza. Viwanda vya samaki vikijengwa itasaidia watu wetu kupata ajira na kuondokana na umaskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Zana za Kisasa za Uvuvi; Wizara hii kazi zake ni pamoja na kuhakikisha inawasaidia Watanzania wavuvi waweze kuvua uvuvi wa kisasa. Naomba Wizara itenge pesa ya kutosha ili kununua zana za uvuvi, mfano boti za kisasa na mashine za boti hasa kwa wavuvi wa Mikindani, Misete na Kianga ambako wanavua uvuvi ambao hauna tija kwa sababu hawana vifaa vya kisasa. Serikali itenge pesa za kutosha kwa ajili hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Cooperate Social Responsibility. Wizara kwa mwaka 2016/2017 imekusanya pesa nyingi sana za mapato ya korosho, lakini jambo la ajabu hivi vyama vya msingi havina mchango wowote kwenye kusaidia jamii. Hakuna shule hata moja kupitia fedha nyingi zinazokusanywa katika korosho, Bodi ipo, vyama vya ushirika vipo wanakusanya pesa nyingi sana, kwa nini hawasaidii katika elimu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara itoe miongozo ili pesa za korosho Kusini zitumike kuinua kiwango cha elimu Kusini. Serikali inakusanya pesa nyingi kwenye korosho kuliko zao lolote lile nchini, vyama vya ushirika vya korosho viwe vinasaidia elimu kwa lazima Mtwara.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu na kiti chako, napenda kuchangia Wizara hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii inahusisha pia uwekezaji ambao kwa kiasi kikubwa uwekezaji bado haujapewa kipaumbele. Kwa kiasi kikubwa hotuba ya Waziri Mheshimiwa Mwijage imejikita katika kuzungumzia viwanda ambavyo kwa kiasi kikubwa ni mbwembwe kuliko uhalisia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Taasisi zote za Umma zenye mitaji ya umma ilitakiwa tuelezwe, kwa kuwa taasisi hizi, mfano Mifuko ya Hifadhi yote inajikita katika uwekezaji. Kwa kiasi kikubwa uwekezaji huu hauna tija. Nilitegemea hotuba ya Mheshimiwa Waziri ieleze juu ya uwekezaji butu unaofanywa na Mifuko ya Hifadhi za Jamii pamoja na Taasisi za Serikali kama vile Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, ununuzi wa viwanja bei ni za juu, hifadhi za Jamii kama LAPF wamenunua Kiwanja Mwanza Square metre moja kwa Sh.255,000/= kitu ambacho siyo kweli. Kuna harufu ya matumizi mabaya ya Ofisi. Mtwara wamenunua kiwanja eneo la Rahaleo Square metre moja ni Sh.155,000/= eneo ambalo mimi nalijua. Niliwaambia haya, wakasema valuer ameruhusu. Valuers wanacheza deal na wahusika. Tunataka uwekezaji wenye tija kama Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimeingia mkataba wa miaka 50 na mwekezaji kutoka Botswana. Huu mkataba unampa mamlaka ya kukusanya kila anachokipata na kuipa Serikali asilimia 10% tu. Hali hii haikubaliki. Kibaya zaidi, anajenga vibanda na anakusanya billions of money. Hivi baada ya miaka 50 vibanda vile vitakuwa na thamani kweli?

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri apitie uwekezaji unaofanywa na Taasisi za Umma sio kuwaza viwanda vya watu ambao yawezekana wasije kabisa kujenga. Hivi vilivyopo vifanyiwe uhakiki wa kina.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumuuliza Waziri, Mheshimiwa Mwijage, Kiwanda cha Mbolea Mtwara kina tatizo gani? Kwa nini hakijengwi wakati mwekezaji yupo tayari? Kwa nini hawawezeshwi kujenga kiwanda hicho? Kwa nini hawampi rasilimali anazotaka ili ajenge kiwanda Mtwara? Kila kitu kipo mpaka kwenye eneo, kigugumizi cha nini au Mheshimiwa Waziri hataki maendeleo ya Mtwara?

Mheshimiwa Naibu Spika, Mtwara Mjini kulikuwa na Viwanda vingi vya Korosho, vyote sasa hivi havipo. Baya zaidi kilikuwepo kiwanda cha OLAM, mwekezaji aliwekeza Mtwara Mjini na kiwanda hiki kilikuwa kinaajiri wananchi wengi sana, lakini Serikali ilimwekea mazingira mabaya ya kodi; huyu mwekezaji, amehamisha kiwanda na kukipeleka Msumbiji. Kwani kuna nini wawekezaji wa Mtwara hamwataki wawekeze Mtwara? Au Wizara inataka Mheshimiwa Rais aje tena Mtwara atamke aliyotamka tarehe 4 Machi, 2017? Naomba wawekezaji wenye nia ya kuwekeza Mtwara wapewe mazingira rafiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu third party katika ajira, UCC Dangote Mtwara; kuna usumbufu mkubwa kiwanda cha Dangote kwa kuwa kuna mtu kati anaitwa UCC ndio anayesimamia na kuajiri watu, baadaye anampa mahindi na mahindi anampeleka Dangote. Hawa watu wakati wanapokonya haki za waajiriwa kiwandani, wananyanyasika sana, wafanyakazi hawana utaratibu, wanadhulumiwa haki zao wakidai mwajiri anasema hawamhusu na anamwambia UCC wafanyakazi kadhaa hawatakiwi na wanafukuzwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza, Serikali ilitoa waraka mwaka 2014 wa kuzuia mtu kati kutoa ajira ya mawakala, umefikia wapi?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MAFTAH A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, nashukuru ofisi na kiti chako kwa kuendelea kutenda haki juu ya mijadala ya Bunge. Katika Wizara hii ya Maji na Umwagiliaji naomba kuchangia mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji Mtwara Mjini umekwama kwa nini? Ni muda mrefu hivi sasa Mtwara Manispaa haina maji ya kutosha na Serikali ilianzisha mradi wa kutoa maji Mto Ruvuma hadi Mtwara Mjini ili kuondoa tatizo la maji. Bajeti ya 2016/2017 Mheshimiwa Waziri alisema tayari fedha zimetengwa, usanifu umekamilika na taratibu za kutafuta mkandarasi zinafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kushangaza ni kwamba mpaka leo ukiuliza unapata majibu ya Mheshimiwa Waziri kuwa hakuna pesa na pesa zilitarajiwa kutoka Exim Bank ya China. Kwa nini tunadanganya umma wakati pesa hakuna? Kwa nini tumechukua maeneo ya wananchi kwa miaka mitatu hivi sasa bila kuwalipa fidia juu ya mradi huu? Kwa nini mpaka leo Serikali haina majibu ya kina juu ya suala hili?

Mheshimiwa Naibu Spika, kila siku wananchi ambao maeneo yao yamechukuliwa wanapiga simu na wanasema wamechoka, Serikali haioni kama wananchi huwa wamechukuliwa maeneo yao na kuwazuia kufanya shughuli za kimaendeleo kama vile kilimo na hatimaye kuwadumaza wananchi wa Mtwara? Mradi huu unapelekea wananchi wa Mtwara waone kuwa wanaonewa kwa kutowalipa fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Miradi ya Maji Nchini; Mheshimiwa Waziri kwenye kitabu chake cha bajeti ametaja miradi mingi itakayotekelezwa kupitia bajeti hii lakini cha ajabu mradi wa kutoa maji Mto Ruvuma/Mtwara haupo kwenye orodha hii, huku ni kututenga wana Mtwara.

Mheshimiwa Naibu Spika, Maji Mbagala. Mkoa wa Dar es Salaam upande wote wa Mbagala ambako kuna watu wengi kuliko maeneo yote hakuna mtandao wa DUWASA/ DAWASCO, hali hii haikubaliki. Watu wa Mbagala wanahitaji maji safi na salama. Jambo la ajabu kuna bore holes Kimbiji ambako ni karibu na Mbagala lakini mtandao hakuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, majadiliano na China (Exim) yanaendelea mpaka lini? Mheshimiwa Waziri anasema ili mradi wa Mtwara uanze majadiliano yanaendelea, kila mwaka anatoa kauli hii. Naomba kuuliza majadiliano haya yatakwisha lini? Kuendelea huku hakuna mwisho ili tuwapatie maji safi na salama kutoka Mto Ruvuma? Sisi Waheshimiwa Wabunge wa Mtwara Mjini na Nanyamba tumeongelea sana suala hili na Serikali haitoi majibu ya kina badala yake inasema tu fedha hakuna. Haya ni majibu rahisi wakati wananchi wamezuiwa maeneo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Pesa Ndogo Zilizotengwa kwa ajili ya Mtwara Manispaa. Kutokana na mradi wa kuleta maji kutoka Mto Ruvuma kukwama mwaka 2015/2016 na 2016/2017, nilitarajia mwaka huu wa fedha Wizara ingetenga fedha kwa ajili ya mradi huu. Hata hivyo nasoma bajeti ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 147 pesa zilizotengwa hazihusishi fidia na gharama za mradi huu mkubwa, bado Wizara haioneshi kama Wanamtwara wana umuhimu wa kupata maji safi na salama.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia Wizara hii. Kabla ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kuendelea kunipa afya njema, lakini kwa namna ya pekee kabisa, nashukuru kiti chako kwa kuendelea kutenda haki hasa katika upande wetu huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtaalam mmoja anaitwa Kunzi mwaka 1988/1989 aliandika kitabu chake cha Managerial and Planning ambacho aliweza kueleza kwamba “failure to plan is planning to fail,” yaani siku zote wewe ukishindwa kupanga jambo maana yake ni kwamba unapanga kufeli. Alizungumza Kunzi maneno haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma kitabu hiki cha hotuba hapa, kwa kiasi kikubwa naomba niishukuru Wizara hii kwamba imeweza kuondoa tozo nyingi sana katika zao ambalo kwa kiasi kikubwa linalimwa Mikoa ya Mtwara na Lindi; zao la korosho. Tozo nyingi sana zimeondolewa. Tunashukuru sana Wizara hii kwa sababu kupitia kuondoka ama kuondolewa kwa hizo tozo, hivi sasa bei ya korosho iko juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru pia Wizara hii kwa kuhamasisha wanunuzi wengine kwamba mwaka wa 2016/2017 wanunuzi wa korosho waliweza kuongezeka. Miaka yote tulikuwa na Wahindi tu, lakini mwaka 2016 tumeweza kuona Vietnam na watu kutoka Uturuki wamekuja kununua korosho Mikoa hii ya Mtwara na Lindi na Tanzania kiujumla; na bei sasa imekuwa kubwa kwa sababu kuna ushindani huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo yote, naomba nizungumzie changamoto kadhaa ambazo zipo katika zao hili la korosho hasa mwaka 2016 kwa maana kwamba msimu wa mwaka 2016/2017.

Mheshimiwa Naibu Spika, wapo wakulima wameweza kutueleza Wawakilishi wao, sisi Wabunge; kwa mfano, pale kwangu Mtwara Mjini tuna AMCOS mbili; kuna AMCOS ya Mikindani na kuna AMCOS ya Naliendele. Hivi Vyama vya Msingi vimechukua korosho za wakulima lakini kwa bahati mbaya wameweza kuchukua hizo korosho kupitia minada. Imefanyika, minada zaidi ya minne; mnada wa kwanza mpaka wa nne.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la ajabu sana, la kushangaza ambalo naomba Mheshimiwa Waziri akija atuletee majibu ya kina kwa wananchi hawa, kwamba hizi AMCOS zimeweza kulipa minada miwili ya mwisho, yaani mnada wa tatu na mnada wa nne na wakaacha mnada wa kwanza na wa pili, ambao bei zake zilikuwa ni kubwa kuliko hii minada miwili ya mwisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba akija Mheshimiwa Waziri atupe taarifa, kwa nini hawa wanunuzi wa korosho kupitia hivi vyama vya msingi? Wameruka bei zile kubwa ambazo zilikuwa ni Shi.4,000/= na ilitangazwa kupitia vyombo vya habari kwamba korosho sasa mwaka huu zimepanda, zinauzwa Sh.4,000/= kwa kilo, lakini hawakulipa bei hiyo ya Sh.4,000/= wakaja kulipa minada ya mwisho ambayo imekuja kununuliwa na Wahindi kwa bei ya Sh.3,700/= na Sh.3,600/=.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa anipe maelezo ya kina katika hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo naishukuru Wizara hii, imeelezwa hapa kwamba mwaka huu 2017/2018 kutatolewa pembejeo za sulphur bure kwa wakulima wa Korosho. Nimesoma kitabu chote hiki mpaka kwenye bajeti yenyewe ambayo ni shilingi bilioni 266, sijaona hata eneo moja hilo ambapo wameweza kueleza kwamba pesa hiyo ya kununua sulphur ambayo itaenda kugawiwa bure kwa wakulima wa korosho, imekuwa indicated kwenye hiki Kitabu cha bajeti. Sasa isije ikawa tunazungumza tu lakini kwenye bajeti humu hakuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala la kugawa pembejeo bure, ni suala kubwa sana kwa sababu wakulima wa korosho ni wengi; na kama likifanikiwa hili kwa kweli Wizara hii itakuwa imefanya jambo kubwa sana. Kwa hiyo, naomba maelezo ya kina, hizi pesa zimewekwa katika fungu gani? Kama hazijawekwa zinapatikana sehemu gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala hili la Taasisi ya TFC, Taasisi hii ya kushughulikia pembejeo na mbolea Tanzania. Ni Taasisi ambayo wakati tunapitia kwenye Kamati yetu ya PIC ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, tuliweza kupitia documents zake. Ni Taasisi mfu, yaani wanapewa ruzuku kila mwaka, wanapewa pesa nyingi na Serikali, lakini wana madeni kweli kweli! Hawana hata kiwanda kimoja cha kuzalisha mbolea Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashangaa sana, kwa nini tunaendelea kuienzi na kuilea TFC? Kwa nini isifutwe? Naomba Mheshimiwa Waziri aje atueleze, kwa nini hili Shirika linaendeshwa kihasara? Halileti tija kwa Taifa letu, halisaidii wakulima lakini bado tunaendelea kulilea. Naomba maelezo ya kina kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na Mifugo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze pia suala hili la uvuvi. Tunashukuru hivi sasa pale Mtwara Mjini kuna jengo lile ambalo inasemekana kwamba litakuwa ni Chuo cha Uvuvi. Ni muda mrefu hivi sasa, lile jengo limejengwa, hakuna vifaa, hatuoni mkakati wowote wa kuhakikisha kwamba kile chuo kweli kinaanza, wanafunzi wanaanza kusoma pale. Mwaka 2016, tuliongea kwenye bajeti hapa, walieleza katika bajeti yao pia kwamba hiki Chuo kitaanza. Sasa naomba kujua hiki Chuo cha Uvuvi Mikindani pale kitaanza lini?

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, maeneo yale ya Kusini mwa Tanzania lakini maeneo yale ya Magharibi kule, tuna bahari hii ambayo ni bahari ya Hindi ambayo ina samaki wengi sana. Nilieleza hapa mwaka 2016 kwamba Waingereza wanasema maeneo yale ya Kusini yanaitwa, tunasema it is just virgin sea; yaani ni bahari bikira ambayo ina samaki ambao hawajawahi kuvuliwa tangu tupate uhuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujua kwamba Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba inanunua vifaa vya uvuvi kwa wavuvi wa maeneo haya ya Kusini? Pia hata kule Ziwa Tanganyika kuna samaki wa kila aina; kule Kigoma ukienda kuna samaki wa kila aina, lakini hawana vifaa vya kisasa vya uvuvi. Naomba Wizara itueleze kwamba mkakati wao wa kusaidia wavuvi ukoje katika kuwasaidia kununua zana za kisasa za uvuvi?

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema kwamba wakati tupo katika RCC pale Mtwara tuliweza kupewa taarifa na TAKUKURU kwamba mwaka 2015/2016 wakulima wa Kkrosho wa maeneo ya Mtwara wanadai vyama vya msingi shilingi bilioni 30. Yaani vyama vya msingi vimechukua korosho kwa wakulima, wameenda kuuza, lakini hawajawapa pesa wananchi wale. Shilingi bilioni 30 hazijalipwa, kwa taarifa ya TAKUKURU.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Kiti chako kiamrishe hii Wizara ipeleke TAKUKURU waende kukagua kwenye Vyama hivi vya Msingi kwa sababu wanawaibiwa wakulima sana. Tulivyohoji, tulivyowauliza, wakatuambia siyo shilingi bilioni 30 ni shilingi bilioni 11, lakini taarifa zinasema
na chombo cha uhakika kabisa, TAKUKURU kwamba wakulima wameibiwa shilingi bilioni 30. Tunaomba CAG aende akakague Vyama hivi vya Msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, kuna taarifa ambazo siyo rasmi sana, lakini zinazungumzwa na wafanyabiashara wa korosho. Naomba Mheshimiwa Waziri hapa akija atupe majibu kwamba mwaka 2016 kulikuwa na fraudulent iliyofanyika bandari ya Mtwara ili iweze kuzuiwa kusafirisha Korosho kupitia bandari ya Mtwara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na wajanja inasemekana ndani ya Wizara yake ambao walikuwa wanaweka vingingi; na inasemekana kwamba ilikuwa kusafirisha korosho kutoka Mtwara tani moja kuelekea Soko la Dunia, ilikuwa ni dola karibu 14,000; lakini kutoa mzigo kutoka bandari ya Dar es Salaam ilikuwa ni dola 400.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba tupate ufafanuzi, kama hilo ni kweli kwa nini iwe hivyo? Lengo ni nini? Kuzuia bandari ya Mtwara isiweze kusafirisha korosho au tatizo ni nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atuletee majibu ya kina atakapokuja kuhitimisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haya, naomba kushukuru sana kwa kunipa nafasi. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kwamba, Mtume Muhammad Karne ya sita alishawahi kusema kwamba “Manla-yashkurunnasa la-yashkurullah” yaani yule ambae hawezi kumshukuru binadamu mwenzake basi hata Mwenyezi Mungu kwa neema alizompa hawezi kumshukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti naomba nichukue fursa hii kukushukuru wewe na kiti chako, lakini kwa namna ya kipekee kabisa kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuja Mtwara kuzindua mradi mkubwa wa utanuzi wa Bandari ya Mtwara Mjini, ninamshukuru sana na nimuombee tu Mwenyezi Mungu aendelee kutusainia mikataba mingine magati yale matatu yaliyobaki yaendelee kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikichangia moja kwa moja kwenye Wizara hii ya maji, mwaka jana niliuliza swali hapa namba 197 ambalo niliulizia suala zima la ujenzo wa maji kutoka Mto Ruvuma kuja Manispaa ya Mtwara. Majibu ya Mheshimiwa Waziri, alieleza Bunge lako hili Tukufu kwamba kwa sasa Serikali inaendelea na majadiliano na Serikali ya China kwa ajili ya kupata mkopo nafuu wa utekelezaji wa mradi huo. Ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2016/2017 na kazi zitakazofanyika ni pamoja ujenzi wa chanzo, mtambo wa kutibu maji, bomba kuu la kupeleka maji Mtwara Mikindani pamoja na kujenga matenki lakini pia na usambazaji wa maji hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikiangalia katika kitabu hiki, Mheshimiwa Waziri amepanga vizuri sana, ameweka na ameeleza kwamba mradi huu bado mpaka leo haujapata pesa wakati mwaka jana walitueleza kwamba mradi huu wa kutoa maji Mto Ruvuma na kusambaza maji Mtwara Mjini ungeweza kuanza katika bajeti iliyopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba atueleze Mheshimiwa waziri kwamba tunavyoelezwa hapa ndani ya Bunge hili na kwenye Hansard inaeleza kwamba pesa zimetengwa, lakini huu mradi mpaka leo naambiwa majibu yale yale ya mwaka jana mabyo alitueleza, aje na majibu ambayo kimsingi yatawaridhisha wananchi wa Mtwara Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nieleze tu kwamba baadhi ya maeneo ya Mtwara Mjini na hasa kata ya Ufukoni na kata ya Mitengo maji hatuna kabisa na mimi kama Mbunge niliweza kutenga pesa zangu baada ya kuona kwamba huu mradi ni mradi wa muda mrefu na utachukua muda mrefu kuweza kuanza, lakini pia kumalizika, nikapeleka pesa zangu milioni 10 kwa ajili ya kichimba kisima pale. Hata hivyo niliweza kuomba Idara ya Maji, kuna gari pale wanalo la Wizara ambalo linafanya utafiti na kuchimba maji lakini pesa alizonieleza ni pesa nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwambiwa kwamba tutashirikiana na Mbunge tuweze kuchimba kisima maeneo ya Comoro ambako utafiti tayari nilishatoa pesa yangu ya mfukoni tukafanya utafiti, lakini mpaka leo wananinyima gari la kwenda kuchimba kisima pale ili wananchi waweze kupata maji ni jambo la ajabu sana. Nilikuwa namuomba Mheshimiwa Waziri aliangalie hili, atusaidie gari kwa sababu huu mradi bado haueleweki kwa sababu kila siku tunapewa dana dana kwamba watu wa Benki ya China hawajatoa pesa; kila nikiuliza naambiwa watu wa Benki ya China hawajatoa pesa na wananchi kule wanapiga simu sana na wanadai sana maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, mle ambamo tathmini imeweza kufanyika kutoka Kitaya, Jimbo la Nanyamba mpaka Mtwara Vijijini, vijiji vile 26 wote wanahitaji fidia lakini mpaka leo, miaka zaidi ya mitatu hivi sasa wale wananchi wamechukuliwa maeneo yao na fidia hawajalipwa, wanasumbua kweli kweli Wabunge wote wa Mtwata Mjini na Mtwara Vijijini wanatusmbua sana. Kwa hiyo, nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri anisaidie hilo, atupatie gari tuweze kuchimba kata hizi ambazo Mtwara mjini hatuna maji, nitasaidia na mimi Mbunge ili tuweze kuondoa tatizo hli la maji. Pia nizungumzie…………..

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru, muda wenyewe ndiyo hivyo tena, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu na kiti chako na katika Wizara hii ya fedha naomba kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kodi ya Majengo (Property Tax), naomba sana irudishwe kwenye mamlaka ya mwanzo ambayo ni Halmashauri ili ziweze kukusanya ipasavyo. Tangu Serikali Kuu ichukue kodi hii ya majengo, Halmashauri zimekosa mapato na kodi hii haikusanywi tena. Serikali Kuu irudishe kodi hii Halmashauri kwa maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti iliyopita, kuna fedha nyingi sana hazijapelekwa Halmashauri ili miradi mingi iende kama ilivyopangwa. Ucheleweshaji wa fedha za maendeleo kama ilivyopangwa ni kurudisha nyuma kasi ya maendeleo nchini. Naomba suala hili liangaliwe ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kitendo cha Serikali kukopa ndani ya nchi na hasa mashirika ya Hifadhi za Jamii kama vile PSPF, LAPF, NSSF na nyingine, kunaleta ushindani na wananchi wa kawaida ambao huweka fedha zao huko kwa wakati maalum hivyo wanapotaka kujitoa huwekewa vigingi vingi kwa kuwa mifuko hii inakosa fedha. Pia Serikali inachukua muda mrefu sana kulipa madeni ya mifuko ya Hifadhi ya Jamii, hivyo mifuko hii hudumaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali ni kwamba, kwa kuwa inakopesheka nje ya nchi, basi ifanye hivyo ili mzunguko wa fedha ndani ya nchi kupitia mifuko hii ya Hifadhi za Jamii na mabenki yetu ziendelee kutoa mikopo kwa wananchi wa kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mabenki hutoa riba kubwa sana kwa wananchi wanaowakopesha. Wananchi hawa hushindwa kulipa mikopo hiyo na hatimaye kufilisiwa mali zao na vitu vyao vya ndani, hivyo kuwafanya kuwa maskini zaidi badala ya kuwainua kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbunge kila mwezi analipa fedha nyingi sana ya VAT na kodi ya mapato kupitia mshahara wake kila mwezi. Kitu cha ajabu, Wizara imeweka kodi nyingine kwenye kiinua mgongo kilicholipiwa kodi kabla hakijawekwa kutunzwa. Hali hii ni mbaya sana na siyo ya kuvumilika kuweka kodi juu ya kodi kwenye gratuity ya Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Mashirika ya Umma yakaguliwe na CAG kwani matumizi yao, mfano kuna taasisi ya AICC iliyopo Arusha ambayo kazi yake kubwa ni kujenga Vituo vya Mikutano kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha Sheria ya Taasisi hii ya AICC. Bahati mbaya badala ya kufanya kazi yao, wanatumia shilingi bilioni 3.5 kwa kukarabati ukumbi wa Simba na huku wakijenga nyumba kubwa yenye ghorofa sita kwa shilingi bilioni 1.8 tu. Haiwezekani ukarabati uzidi majengo makubwa. CAG akague Arusha AICC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vema Wizara ikaweka katika bajeti zake shilingi milioni 50 za kila Kijiji ambazo ziliwekwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Kwa nini haziwekwi kwenye bajeti?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri fedha za Mfuko wa Jimbo ziongezwe Mtwara Mjini, watu ni wengi, hazitoshi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia. Kwanza kabisa naomba nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhanah Wataala ambaye ameendelea kunijalia afya njema na leo hii niweze kuzungumza machache niliyokuwa nayo, pili nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi asubuhi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kwamba wakati nachangia bajeti ya Wizara ya Maji, nilizungumza hapa kwamba Mtume Mohammed alisema Karne ya Sita kwamba Man laa yashkur nnasa,laa yashkur Allah, kwamba mtu yeyote ambaye hashukuru binadamu wenzake kwa wema wanaofanya basi hata Mwenyezi Mungu kwa neema alizompa hawezi kumshukuru pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee kabisa naomba nikiwa kama mzalendo wa Taifa hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kitendo kikubwa alichokifanya jana, kwa maamuzi magumu aliyoyafanya jana, kuhakikisha kwamba wale wanaotorosha madini yetu kwenda nje ya nchi wanachukuliwa hatua kwa kunyang’anywa yale madini. Tunampongeza kweli na ni kitendo cha kishujaa kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nieleze tu kwamba nchi hii kama hatuchukui maamuzi magumu tutaendelea kuwa maskini mpaka kiama. Wenzetu walioendelea duniani kupitia sekta hii ya madini, nchi ndogo kama Botswana ni kwa sababu wanachukua maamuzi magumu. Nimwombee Mwenyezi Mungu aendelee kumpa afya njema Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania achukue maamuzi magumu zaidi, Tanzania tuondokane na umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mimi ninayezungumza hapa kama siyo kufanya maamuzi magumu nisingekuwa Mbunge leo hii, mimi nilikuwa Mwalimu, nikaandika barua kuomba likizo isiyokuwa na malipo ili niweze kugombea Jimbo la Mtwara Mjini, lakini kulikuwa na ujanja ujanja ulifanyika wakaninyima ruhusa nikamua kuacha kazi masaa 24 ili niweze kugombea Ubunge na leo hii nazungumza ni Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Jimbo la Mtwara Mjini ni kwa sababu ya maamuzi magumu. Kwa hiyo, hii nchi kama tunahitaji maendeleo lazima tuwe na Viongozi wanaochukua maamuzi magumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwa namna ya kipekee kabisa, niishukuru Wizara hii ya Ardhi, siku kadhaa zilizopita nilikuwa Mtwara nikiwa na Mheshimiwa Waziri hapa tulienda kuzindua mpango kabambe ambao unaitwa master plan kwa mara ya kwanza tangia Serikali hii ya Awamu ya Tano mpango wa kwanza kuzindua ni mpango wa master plan wa Mtwara Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kufanya kazi kubwa sana na wananchi wa Mtwara sasa kwa sababu hii master plan ambayo tumeizindua juzi ndiyo mwarobaini ya migogoro yote ya ardhi pale Manispaa ya Mtwara Mikindani. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na namshukuru sana, Mungu ambariki aendelee kutatua migogoro mingine ambayo ipo katika maeneo mbalimbali ya nchi hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, wakati nafanya kampeni 2015 niliweza kuzungumza mambo mengi sana yanayohusu ardhi, kwa sababu Mtwara Mjini kulikuwa na changamoto nyingi sana za ardhi. Miongoni mwa mambo mengi ambayo nilikuwa nayahutubia na wananchi wangu wakanituma nije kueleza katika Bunge hili, ilikuwa ni suala la urasimishaji wa ardhi. Mheshimiwa Waziri hapa wakati anazungumza kwamba maeneo kadhaa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi sasa urasimishaji unaendelea ikiwemo Jimbo la Mtwara Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara hii na namshukuru Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kwa kubariki Mtwara Mjini, lakini pia kutuletea Wataalam ambao tunashirikiana nao katika suala hili la urasimishaji wa ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wito wangu kwa Madiwani wa Jimbo la Mtwara Mjini, wahamasishe wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini ili zoezi hili liweze kukamilika kwa wakati. Kwa namna ya kipekee kabisa nawashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Mtwara Mjini kwa kuendelea kuwa na imani na Mbunge wao na nawaambia kwamba naendelea kupambana, nitawatetea kipindi chote cha miaka yote iliyobaki na Mtwara Mjini sasa ni Mtwara kuchele kweli kweli, siyo kama kauli za kubeza za miaka ya nyuma kulivyokuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukrani hizo za dhati kabisa naomba nizungumze suala moja ambalo hivi sasa pale Mtwara Mjini, nimwombe Mheshimiwa Waziri atusaidie katika hili. Mtwara Mjini kuna eneo linaitwa Mangowela, sasa hivi wamebatiza jina panaitwa Libya, hili eneo lilikuwa linamilikiwa na Wazee Nane wa Mji wa Mtwara, na hapa nina majina yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niyasome haya mbele ya Bunge lako hili Tukufu, wamiliki wa eneo hili ni Mzee Mohammed Saidi Mussa, Mussa Ismail Selemani, Ndugu Karama Akidi Ismail, Ndugu Abdallah Mfaume Mkulima, Ndugu Fatu Mchimwamba, Ndugu Abubakari Zarali Mohammed, Ndugu Musa Saidi na Ndugu Ashiraf Makuti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wazee hawa ni wazee ambao wamezaliwa miaka 1920 huko nyuma, walikuwa wanamiliki eneo hili la Mangowela, lakini hivi sasa linaitwa eneo la Libya, lakini jambo la ajabu sana ambalo lilifanyika miaka ya 2000 wameamka asubuhi wakakuta beacon zimewekwa, walivyoulizwa hizi beacon zilizowekwa katika eno hili la Libya ni za nini, wanaambiwa kuwa hili eneo limeuzwa na wamiliki wa eneo hili. Wakashangaa sana, kwamba wamiliki wa eneo hili ni watu wa aina gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, huu mgogoro ni mgogoro ambao ni mkubwa sana hivi sasa Mtwara, naipongeza Wizara hii kwamba jana niliuliza swali hapa juu ya mgogoro wa Mji Mwema na kwamba tayari wameshamaliza na fidia ile inaenda kulipwa mwisho wa mwezi huu, tunashukuru sana kwa hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri mgogoro huu wa Mji wa Libya, naomba sana wananchi hawa wamekuja Ofisini kwangu zaidi ya mara nne, wametembea maeneo yote kudai haki yao, lakini mpaka leo wanaambiwa lile eneo limeuzwa na wao wameuzwa bila wao kuelezwa. Hata hao waliouza wanasema kwamba walipewa na watu fulani, lakini hakuna documents zozote kwamba lile eneo lilikuwa ni la kwao, wamiliki wa eneo hili la Libya ni hawa wazee ambao nimewasoma hapa, kwa hiyo tunaomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja atusaidie katika hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuzungumza Mbunge mmoja kaongea hapa kuhusu shirika la NHC (Shirika la Nyumba Tanzania), kwa kweli linafanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha wanaboresha makazi ya Watanzania, wanajenga majumba maeneo mengi, lakini nyumba hizi ambazo zinajengwa kwamba eti ni nyumba za maskini, kimsingi siyo nyumba za maskini. Mfano tu hata nikiwa Mwalimu pale Lindi, mwaka 2007, kuna nyumba zilijengwa pale Lindi, lakini zile nyumba mimi nilienda kuomba kama Mwalimu, Mwalimu ambaye nilikuwa nachukua mshahara 940,000 wakati ule, nikaambiwa kwamba zile nyumba wewe kama Mwalimu huwezi kuzinunua ni nyumba ambazo zinaanzia Sh.50,000,000/= na Sh.60,000,000/= huko na kuendelea. Sasa hizi kweli ni nyumba za bei nafuu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba Waziri ahakikishe kwamba hii NHC kweli ijenge nyumba za bei nafuu ili Watanzania wengi maskini waweze kupata hizi nyumba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze pia suala hili la kucheleweshwa hati, Mheshimiwa Waziri ana mpango mzuri sana hapa, kazungumza vizuri sana, kwamba ametoa maagizo kwa Taasisi zote, kwa Halamshauri zote, wahakikishe kwamba tunaenda kama Wabunge kukagua Masjala za Halmashari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe atoe agizo lingine kwamba ucheleweshaji wa hizi Hati unafanywa na Watendaji wa Halmashauri na watu wa ardhi wa Halmashauri na wale ambao wataendelea kukiuka agizo lako Mheshimiwa Waziri, basi hawa watu aweke hatua za kuchukuliwa mara moja ili sasa tatizo hili la kuchelewesha Hati Tanzania liweze kwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja hizi za Kamati zote mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nianze kwa kuunga mkono hoja za Kamati lakini nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhanah-Wataala na kwa namna ya kipekee kabisa niweze kukushukuru wewe kwa kuweza kunipa hii nafasi kwa wakati huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo kadhaa ya kuweza kuchangia kwenye Kamati hizi zote mbili. Jambo la kwanza Mtume Muhammad Swalallah-Alay-Wasallama karne ya sita (AD) alisema kullil-hakka laukana murra kwamba sema ukweli japokuwa unauma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitakuwa mkweli sana katika maelezo yangu haya machache. La kwanza, nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri mpya wa Wizara hii ya Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Kigwangalla kwa maamuzi yake magumu anayochukua usiku na mchana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa wakweli, sisi kama Wabunge ni mapema sana leo hii kuanza kum-judge Mheshimiwa Kigwangalla kwamba eti anaipotosha Wizara, Wizara haiendi sawa, atakaa kwa muda mfupi. Naomba nizungumze jambo moja tu ambalo kimsingi namuomba Mheshimiwa Waziri Kigwangalla achukue maamuzi magumu, kwa sababu nilishawahi kusema ndani ya Bunge hili kwamba kama nchi haichukui maamuzi magumu, tutarudi kule tulikotoka. Ni lazima tutoke tulipo, tuelekee mbele ili tuweze kuwa na maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunapitia taarifa ya AICC mwaka 2017 tukiwa kwenye Kamati yetu pale Arusha, kwamba wale mkakati wao na strategic plan zao zote wamepewa tangu mwaka 1978 waendeleze utalii Tanzania na siyo kung’ang’ania pale Arusha kwenye yale majengo. Tukawa tumewaeleza, kwa nini mpaka leo hii Tanzania ina ardhi kubwa sana, hamjajitanua? Wakawa hawana majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tukiwa tunapitia taarifa za AICC tuliweza kugundua ukarabati wa Jengo la Simba, ule ukumbi wa Simba hawa AICC, wamekarabati kwa shilingi bilioni 3.5. Tukiangalia nyumba walizojenga, wamejenga nyumba zaidi ya sita pale zenye ghorofa zaidi ya sita kila moja na zile nyumba zimegharimu shilingi bilioni 1.8. Kuna ubadhirifu mkubwa wa fedha unaofanyika na Idara hizi za Utalii Tanzania na lazima Mheshimiwa Waziri asimame imara kufufua makaburi haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine taarifa ya Kamati imezungumza suala la Olduvai Gorge kwamba ni sehemu ambayo binadamu wa mwanzo Tanzania kwa taarifa za kihistoria amegundulika Olduvai Gorge. Taarifa za mapato ya Serikali kuanzia mwaka 2012/2013 Olduvai Gorge kwa mwaka ilikuwa inaliingizia Taifa hili shilingi bilioni 1.7. Baadae akatokea kidudu mtu pale, Wizarani Idara ile ya Olduvai Gorge ikaondolewa kwenye Idara ya Mambo Kale na ikapelekwa kwenye Shirika la Umma la Ngorongoro na hivi sasa Olduvai Gorge kwa mwaka inakusanya shilingi milioni 700 pekee badala ya shilingi bilioni 1.7. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni ufisadi watu wame- under estimate pale. Serikali lazima ifanye upembuzi yakinifu, ihakikishe ya kwamba Mheshimiwa Waziri anaunda Tume Maalum, anafukua makaburi ili tuweze kutoka hapa tulipo na nchi yetu iweze kupata mapato. Kwa hiyo, kusema kwamba eti Mheshimiwa Waziri anafanya maamuzi haraka haraka, hili siyo kweli na mimi siungi mkono hoja. Nampongeza na kumwombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kufufua makaburi ili sekta hii ya utalii iweze kuingiza pato kubwa kwenye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine mizungumzie kidogo, kuna pesa ambazo Serikali imekopa, pesa za REGRO ni pesa zilizokopwa Benki ya Dunia, dola milioni moja sawa sawa na shilingi 1,800,000,000 hivi za Kitanzania hivi sasa, ambazo zimepangwa kuendeleza utalii Southern Circuit.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipitia taarifa za TTB, zile pesa zimepangwa kuendeleza Southern Circuit, wanazungumzia Mkoa wa Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyozungumza Kusini, tunazungumza Mtwara na Lindi, Morogoro siyo Kusini, Kusini ni Mtwara na Lindi. Kwa hiyo, naomba sana zile shilingi bilioni mbili kasoro ambazo zimepangwa kwa ajili ya kuendeleza utalii Kusini ziletwe Mtwara na Lindi watangaze vivutio vilivyopo Mikindani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mikindani kuna vivutio vingi sana, tuna soko la watumwa pale, tuna custom pale ya zamani, tuna majengo ya karne ya saba mpaka leo yapo Mikindani, kuna maeneo ambayo Vasco Da Gama alipita akaweka mahema na ndala pale Mikindani, lakini yameachwa. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali, Idara hii ya mambo ya kale ipewe pesa na hasa Mtwara Mikindani kule Kilwa Masoko, Kilwa Kisiwani, kuna mambo mengi ya kitalii ambayo Serikali hii inatakiwa iyaone na hasa kupitia idara hii ya mambo ya kale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba Serikali imekuwa ikiangalia sana Northen Circuit, yaani unavyozungumzia utalii, tunazungumzia sana Arusha, Ngorongoro na maeneo mengine kule, lakini huku Kusini kumesahaulika sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naitaka Serikali kwamba bajeti inayokuja hizi shilingi bilioni mbili ambazo zimetengwa, basi ziletwe kule Kusini zitangaze vivutio hivi vya utalii kule Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kidogo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. MAFTAH A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, namshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu-Wataala,lakini nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi jioni hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu hapa wamezungumza mambo mengi sana na hasa hasa suala zima la uzalendo la Daktari Janabi, nami niungane nao kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha kwamba anajitoa na haya maendeleo tunayoyaona kwenye upasuaji wa moyo ni kwa sababu ya jitihada binafsi za Daktari Janabi ambaye ameamua kutumikia Taifa letu hili la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kuna suala limeleezwa na Waheshimiwa Wabunge hapa, suala la delivery kits wale akinamama wanavyokwenda kijifungua katika hospitali zetu wanakuwa na changamoto kubwa sana juu ya vifaa vya kujifungulia. Suala hili limekuwa ni tatizo kubwa sana, tumekuwa tunaongea kwa muda mrefu sana ndani ya Bunge hili kwamba vifaa hivi viweze kutolewa katika hospitali zetu za Serikali, lakini jambo la kusikitisha sana mpaka leo hivi vifaa havitolewi kwa ajili ya akinamama wanapokwenda kujifungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kwangu Mtwara Mjini nilipochukua pesa zangu nilinunua vifaa hivi vya milioni 30 zaidi ya akinamama 5,000 nimeweza kuwagawia, kila mmoja ujauzito ukifika miezi nane au miezi tisa anafika Ofisi ya Mbunge, nimeweza kuwagawia bure kabisa hizi delivery kits. Naomba sana Serikali iweze kuendeleza zoezi hili katika Majimbo yetu yote ye Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia suala hili la hospitali za Kanda. Tumekuwa tunazungumza sana ndani ya Bunge hili kwamba Kanda zote Tanzania zina hospitali za Kanda isipokuwa Kanda ya Kusini pekee mpaka leo bado hatuna hospitali ya Kanda. Tumekuwa tunaongea sana kila Bunge, hii ni mara yangu ya tatu nazungumza ndani ya Bunge hili na Serikali inaahidi kwamba tunajenga lile jengo. Mpaka leo jengo la OPD limejengwa kwa muda wa zaidi ya miaka 10, utafikiri hili jengo unajengwa mnara wa Babeli ambao ndiyo haujakwisha mpaka leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kwamba hospitali ya Kanda ya Kusini tunamaanisha Mtwara, tunamaanisha Lindi, tunamaanisha pia kule Ruvuma mpaka leo hatuna hospitali ya Kanda, bajeti inayotengwa kwa ajili ya hospitali ya Kanda ya Kusini kila mwaka ni bajeti ambayo haitoshi hata lile jengo mpaka leo halijakamilika na tunaambiwa kila mwaka tutatenga pesa. (Makofi)

Mheshmiwa Mwenyekiti, jambo la kusikitisha sana, unaweza ukaangalia kuna hospitali zingine za Wilaya tu, hospitali za maeneo mengine zimetengewa zaidi ya bilioni nne, zingine bilioni tano, lakini hospitali ya Kanda ya Kusini, taarifa nikipitia kwenye randama hapa naambiwa bilioni mia moja lakini mpaka leo hizo bilioni 100 zenyewe inakuwa ni kizungumkuti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa dada yangu Ummy Mwalimu tunamheshimu sana, hiyo hospitali ya Kanda ya Kusini, Mtwara, Lindi na Ruvuma tunaomba atenge pesa katika Bunge hili katika bajeti hii ili hospitali iweze kwisha, tumechoka kuzungumza neno moja kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine naomba sana hospitali ya Mkoa wa Mtwara, hospitali ya Ligula X-Ray hakuna. Nimezungumza sana ndani ya Bunge hili, nimepiga kelele sana, nimeandika sana, hii ni bajeti yangu ya tatu nazungumzia suala hili kwamba hospitali ya Mkoa wa Mtwara haina X-Ray iliyoko yenyewe ni mbovu na hawa watu wa Ligula hospitali walifanya jitihada kuiomba NHIF waweze kuwanunulia kwa mkopo lakini hawataki na hili ni kwa sababu Wizara haiko serious. Tunaomba sana vifaa tiba hivi, x-ray ya hospitali ya Mkoa wa Mtwara iweze kununuliwa na isiwe ahadi kila siku, tulikuwa tunaomba sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia CT Scanner hatuna kwenye hospitali ya Mkoa, CT Scanner haipo sasa ni jambo la ajabu sana. Tumekuwa tunaomba sana, tunazungumza sana, tunaandika sana, namwomba dada yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu safari hii aweze kuiangalia kwa namna ya kipekee kabisa hospitali ya Mkoa wa Mtwara hospitali hii ya Ligula juu ya vifaa tiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze pia suala la watumishi. Ukija hospitali ya Mkoa wa Mtwara watumishi wanaohitajika ni watumishi 681, watumishi waliopo Madaktari, Wauguzi na wengine wote ni 255 pekee, upungufu ni zaidi ya watumishi 455. Tunaomba sana Wizara hii ilete watumishi katika hospitali ya Mkoa wa Mtwara, hospitali ya Ligula ili sasa tuweze kupata huduma hizi za afya kama maeneo mengine ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la ajabu sana kwenye hospitali hii, tunaye Specialist mmoja pekee, hospitali ya Mkoa inayohudumia Majimbo 10 ya Mkoa wa Mtwara lakini ina Specialist mmoja tu. Naomba Wizara watuletee Specialist hospitali ya Ligula, hospitali ya Mkoa ili na sisi tuweze kupata tiba hizi kama maeneo mengine ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze pia suala hili la dawa ambalo limesemwa hapa na hotuba ya Mheshimiwa Waziri amesema kwamba sasa hivi upatikanaji wa dawa ni asilimia 85. Pia katika upatikanaji huo amezungumza suala la watu ambao wamepewa misamaha ya dawa, kwa mfano, watoto chini ya miaka mitano, lakini pia watu wenye magonjwa maalum kama vile pressure na kisukari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali halisi iliyopo kule ukipitia, ukienda hospitali, ukienda katika zahanati zetu, dawa zikishafika ndani ya muda mfupi tu wagonjwa wanaambiwa dawa zimekwisha waende wakanunue kwenye pharmacy. Sasa unashangaa hii misamaha, mtoto kapewa msamaha, mzee kapewa msamaha, lakini mwisho wa siku wanaambiwa kwamba eti zile dawa hazipo waende wakanunue kwenye pharmacy wakati tumempa msamaha wakati hana uwezo wa kujiendesha, hana uwezo wa kujihudumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera inasema wazee kuanzia miaka 60 wapate zile card za matibabu bure, lakini kuna jambo ambalo linatendeka huko wilayani, huko mikoani ambalo naomba usimamizi sana wa Mheshimiwa Waziri kwamba hizi card zitolewe sawasawa na takwimu
zinazotolewa hapa, kwa mfano, pale kwangu takwimu zinasema wazee 1,500 ndiyo wamepewa zile card za matibabu bure, lakini ukienda huko mitaani hata hao wazee kiuhalisia 1000 hawafiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana kwamba suala la kupewa takwimu ambazo siyo sahihi na Watendaji wa Serikali huko Halmashauri na huko Mikoani Mheshimiwa Ummy Mwalimu uweze kuzipitia na uweze kuhakikisha kwamba takwimu unazopewa kweli ni takwimu za ukweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala hili la dawa hizi ambazo ni dawa maalum, dawa za kisukari, dawa za UKIMWI na dawa zingine ambazo ni dawa maalum ambazo zinatolewa na Specialist tu. Hapa nimeeleza kwamba Mtwara hospitali ya Mkoa ina Specialist mmoja tu sasa wagonjwa wanatoka wilayani huko, wanatoka kwenye Kata za mbali huko wanakwenda kuchukua dawa hizi kwenye hospitali ya Mkoa. Naomba sana hawa wanaoitwa Medical Assistance hawa wapewe mafunzo na Serikali huko huko waliko hizi dawa ziweze kupatikana, wagonjwa wasiwe wanatembea umbali wa kilomita 80 kuja kufutilia dawa za UKIMWI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mhesimiwa Ummy Mwalimu kwa sababu tunamfahamu, uwezo huo anao, ahakikishe kwamba analeta mafunzo maalum kwa hawa Specialist kwenye hospitali zetu za Kata, vituo vyetu vya afya ili dawa hizi maalum ziweze kupatikana huko ili wagonjwa wetu wasitembee kwa umbali mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuweza kunipa nafasi niwe mchangiaji wa kwanza kwenye Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii pia kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wa Ta’ala ambaye ameweza kunipa afya njema na leo hii niweze kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii ili tuweze na sisi kunufaika na rasilimali za Tanzania hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze moja kwa moja suala hili; hotuba ya Mheshimiwa Waziri imezungumza kwa kiasi kikubwa sana ujenzi wa barabara, na nichukue fursa hii kushukuru na kuishukuru Wizara kwa kuanza utekelezaji wa ujenzi wa Barabara ya Uchumi ambayo inajengwa kuanzia Mtwara Mjini mpaka Mnivata kule kwenye Jimbo la Nanyamba na baadaye itafika mpaka Masasi. Nichukue fursa hii kuishukuru Wizara kwa kuanza kutekeleza kilometa hizi 50 kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nizungumze kwamba wakati barabara hii inazinduliwa na Mheshimiwa Rais alivyokuja Mtwara mwaka jana kuja kuzindua ujenzi wa barabara hii na miundombinu mingine, alitoa wasiwasi wake juu ya mkandarasi ambaye amepewa ujenzi wa barabara hii; kwamba kuna wakati fulani akiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi aliwahi kumsimamisha kazi, akawa amemuagiza Mheshimiwa Profesa Mbarawa kwamba awe makini sana; pale Mtwara tukiwa bandarini tunazindua ujenzi wa lile gati, na akasema kwamba atakuwa makini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nisikitike tu, yule mkandarasi bado yuko slow sana. Nimuombe Waziri, Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa, akaze buti huyu mkandarasi aendane na kasi ya ujenzi lakini pia aendane na muda ambao umewekwa; yuko slow sana yule mkandarasi anayejenga barabara ya Uchumi kutoka Mtwara Mjini mpaka Mnivata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nizungumze suala zima la barabara ya ulinzi; tulikuwa tumezungumza hapa kwa muda wa miaka miwili na huu ni mwaka wa tatu hivi sasa, kwamba kuna barabara ya ulinzi ambayo ilitumika kulinda mpaka wetu wa kusini, barabara inayoanzia Mtwara Mjini, inapita Jimbo la Mtwara Vijijini, inafika kule Kitaya Jimbo la Nanyamba, inafika Tandahimba, Newala mpaka kule Ruvuma. Hii ni barabara muhimu sana, ni barabara ambayo makamanda wetu walikuwa wanaitumia kumdhibiti Mreno ambaye alikuwa anakuja kutuchokoza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mwaka 1972 ndege ya Mreno ambayo ilikuja kuvamia Tanzania iliweza kudunguliwa Kijiji cha Kitaya pale Jimbo la Nanyamba, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Vijijini. Lakini baada ya kuidondosha ile ndege ya Mreno yule kamanda wetu aliuawa pale, pamejengwa mnara mdogo sana. Mimi naomba sana na naishauri Wizara hii, hii barabara ijengwe na pale pajengwe mnara wa kumbukumbu ambao utaonesha kweli kwamba shujaa wetu pale Kijiji cha Kitaya ndipo alipouawa akiwa analinda mpaka wa Tanzania ambao uko huku maeneo ya kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii imekuwa ikizungumza sana, imekuwa ikiongea sana kwamba tutatenga bajeti, niombe sana kwamba mwaka huu barabara hii ya ulinzi ambayo inalinda mpaka wa kusini itengewe pesa ili iweze kuanza kutengenezwa, kwa sababu hatuwezi jua huko mbeleni kwamba kitu gani kinakuja juu ya mipaka yetu ya Tanzania. Mpaka huu ni mpaka muhimu sana, barabara hii ni barabara muhimu sana, inaanzia Mtwara mpaka Ruvuma kule. Ninaomba sana Wizara iangalie kwa jicho la kipekee mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala hili ambalo tumekuwa tunazungumza la maendeleo ya Ukanda wa Kusini (Southern Development Corridor) ambalo limekuwa likizungumzwa kwa muda mrefu hivi sasa na maendeleo ya Ukanda wa Kusini inaanzia katika ujenzi wa bandari. Tunashukuru kwamba Gati la Bandari la Mtwara linajengwa kwa mita 350, lakini ujenzi wa gati ya bandari unaendana sambamba na barabara ya reli. Miaka ya 1963 huko Mtwara, kule kusini kulikuwa na reli na ile reli ikaondolewa, hatujui ilipelekwa wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ili kuweza kufungua uchumi wa Kanda ya Kusini kuna ulazima Serikali ihakikishe kwamba huu ujenzi wa reli ambao umekuwa ukizungumzwa kila mwaka kwamba reli inayotoka Mtwara kuelekea Liganga na Mchuchuma kule kupitia kule Mbambabay ni muhimu mwaka huu sasa tuweze kutengewa pesa ile pesa iweze kupelekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana ilizungumzwa hapa kwamba imetengwa pesa kwa ajili ya upembuzi yakinifu karibu shilingi bilioni mbili, sijaona upembuzi yakinifu uliofanyika mpaka leo hii. Kwa hiyo tunaomba sana, ili tuweze kufufua uchumi wa kusini (Southern Corridor) ambapo itaunganisha Mikoa ya Kusini – Mtwara, Lindi, Ruvuma lakini kule maeneo ya Malawi na nchi nyingine za Kusini, tujenge hii barabara ya reli ya Ukanda wa Kusini. Itengewe pesa mwaka huu na pesa ziweze kutolewa kwa ajili ya upembuzi yakinifu lakini na ujenzi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala hili la utanuzi wa bandari; lengo la kujenga bandari hizi; Bandari ya Mtwara, Bandari ya Tanga, Bandari ya Mafia, Bandari ya Kilwa ni kuhakikisha ya kwamba tunafanya decentralization of the economy, hatuwezi kutegemea Bandari moja ya Dar es Salaam. Leo hii ukifika Bandari ya Dar es Salaam, mizigo yote ambayo inatakiwa kushuka Tanzania inashukia Bandari ya Dar es Salaam wakati Bandari za Mtwara, Tanga pamoja na Kilwa ni bandari zenye vina virefu, meli ya aina yoyote inaweza ikagati katika maeneo haya. Bandari ya Mtwara Wazungu wanasema ni natural habour, ni bandari ambayo ina kina kirefu kuliko bandari zote za Afrika Mashariki na Kati. Kuna meli nyingine, kama sio ukarabati wa Bandari ya Dar es Salaam, haziwezi kugati Dar es Salaam, lakini Mtwara zinaweza kugati kwa sababu ya kina kirefu cha maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nashangaa sana kwamba tunatumia Bandari ya Dar es Salaam tu. Leo hii ukiamua kuagiza gari kutoka Japan/kutoka nje ya nchi, katika East Africa kwa nchi yetu ya Tanzania iko Bandari ya Dar es Salaam pekee na Bandari ya Mombasa, wakati tungeweza kuongeza Bandari za Mtwara na Tanga ili tuweze kuuondoa msongamano Dar es Salaam. Mimi naiomba sana Wizara hii kwamba upanuzi wa bandari ambao tayari gati limeanza kujengwa pale Mtwara, kwanza uweze kukamilika kwa wakati, lijengwe kwa kasi lakini pia tuitumie Bandari ya Mtwara ili kuondoa msongamano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naamini Bandari ya Mtwara ikitumika sawasawa hii barabara yetu ya Morogoro haitaharibika hivi kwa sababu barabara inayotengenezwa Tanzania kila siku ni barabara ya Morogoro kwa sababu mizigo inakuwa mingi sana. Magari ya Zambia, magari ya Burundi, magari ya Tanzania, on transit zote zinatokea Dar es Salaam. Tupanue Bandari ya Mtwara, tutumie Bandari ya Mtwara ili kuondoa uharibifu wa barabara moja hii ambayo inatengenezwa kila wakati.

Jambo lingine ni suala hili la meli; usafiri wa meli wakati fulani hivi nilitembelea Comoro pale, ukifika Comoro, Comoro ilipigwa volcano, yaani Comoro hata nyanya hazistawi, kila kitu wananunua kutoka nje, wanategemea kutoka Tanzania. Sasa hatuna usafiri wa meli ambapo wafanyabiashara wa Tanzania wangeweza kutokea Mtwara; Mtwara na Comoro karibu sana; wangeweza kutokea Dar es Salaam kwa kutumia meli, wangeweza kutokea Pemba kuelekea Comoro kupeleka mizigo kule na Watanzania tungekuwa na manufaa, wafanyabiashara wetu wangeweza kuinuka kiuchumi kwa usafiri wa meli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pale Mtwara tuna Kiwanda cha Dangote ambacho ana magari zaidi ya 1,000 yanayosafirisha cement kutoka Mtwara kuelekea kwenye soko kuu ambako ni huku Dar es Salaam na maeneo mengine. Kama tungeweza kumruhusu huyu Dangote akajenga ile bandari yake ndogo, lakini pia akalazimishwa kununua meli ili simenti yake aweze kusafirisha kwa njia ya meli, barabara hii isingeharibika, angeweza kuleta mzigo wake Dar es Salaam kupitia kwenye Bahari ya Hindi… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia Wizara tajwa hapo juu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, uwanja wa ndege wa Kanda ya Kusini ulikuwa na taa kabla ya uhuru. Baada ya uhuru taa ziliondolewa na kupelekwa Arusha. Kutokana na mahitaji, sasa hivi Uwanja wa Mtwara ni uwanja wa Kanda lakini hauna taa. Ni lini kwenye bajeti hii taa zitawekwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais alisema akiwa Bukoba kuwa zimetengwa pesa shilingi bilioni 41 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mtwara. Mheshimiwa Waziri anasema shilingi bilioni 54 zimetengwa. Ni lini ukarabati utaanza? Kila mwaka yamekuwa yakisemwa haya na hamna utekelezaji, kwa nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna taarifa za chini chini kuwa ATC Bombardier wanataka kusitisha safari za Mtwara kwa kigezo kuwa abiria hawatoshi. Yapo mashirika binafsi mengi kwa mfano Precision Air wanaenda Mtwara kila siku asubuhi na wanapata abiria, iweje Shirika la umma lenye bei nafuu likose abiria?

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Kusini tunahitaji fursa ya Bombardier (ATC) tufaidi kama maeneo mengine. Naomba maelezo ya Mheshimiwa Waziri, kwa nini Bombardier inataka kuacha kuja Mtwara?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Wizara hii iweke minara ya simu kwenye maeneo ambayo haipatikani mitandao hasa maeneo ya mjini pembezoni mwa Mtwara na mtandao hakuna kabisa; maeneo hayo ni Mbawala Chini, Mkangala, Mkunjanguo, Naulongo na Dimbizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujua ni lini maeneo haya ya Mtwara Mjini mtaweka minara ili mawasiliano yanapatikane?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala kwa kunijalia afya njema. Pia nikushukuru wewe kuweza kunipa nafasi niweze kuchangia kwa dakika hizi tano kwenye Wizara hii ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtaalam mmoja anaitwa Kunzi alisema mwaka 1988/1989 alipomaliza kuandika kitabu chake akasema kwamba failure to plan is planning to fail (ukishindwa kupanga maana yake umepanga kufeli). Nilikuwa nasikiliza hotuba ya Mheshimiwa Waziri hapa, maneno yake mengi amezungumza, lakini sijaona hata mstari mmoja kwenye kitabu chake hiki ameeleza ana mkakati gani juu ya elimu ya watu wazima Tanzania. (Makofi)

Mheshmiwa Mwenyekiti, elimu ya watu wazima taarifa ya Kamati imeeleza hapa kwamba wako vijana wengi, wapo Watanzania wengi sana hawajui kusoma na kuandika. Hawa wawekewe mkakati maalum, wapewe masomo maalum na watengewe bajeti kwenye Wizara hii. Elimu ya watu wazima imekufa, tunaomba sana Wizara mwaka huu iweze kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kugharamia elimu ya watu wazima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Nne ilinikuta mimi nikiwa mwalimu na nilikuwa Headmaster wa Mchinga Sekondari, shule ambayo Mheshimiwa Bobali kaizungumza hapa, nimekaa pale kwa miaka mitano kama Mkuu wa Shule. Tulikuwa na mpango huu kwa muda mrefu sana wa kuipandisha hadhi ile shule iweze kuwa ni kidato cha tano na sita, miundombinu yote tulikamilisha, mimi naungana mkono na Mheshimiwa Bobali hii shule iweze kupanda kuwa ya kidato cha tano na sita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo lilikuwa ni zuri sana ni suala la BRN, mpango ambao Serikali waliuiga kutoka Malaysia na kule Malaysia walikuwa wanaita The Big Fast Result. Serikali ya Awamu ya Nne ikasema tuige mpango huu wa kuinua kiwango cha elimu na sekta nyingine tano ili tuweze kuwa na matokeo makubwa. Mimi nashangaa sana kwamba hivi sasa huu mpango wa BRN (Big Results Now) wameuacha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu ulikuwa una tija sana katika shule zetu za msingi na sekondari. Walimu walikuwa wanafanya kazi kwa bidii sana kwa sababu walikuwa wanaahidiwa kwamba somo lako wakifaulu wanafunzi kwa kiasi hiki utakuwa motivated kwa kiasi hiki cha pesa, kwa kiasi hiki cha tour lakini na mambo mengine.

Kuuondoa Mpango wa Big Results Now kwenye Wizara hii ya Elimu maana yake tunarudisha nyuma elimu yetu. Tunaomba sana Serikali irudi kwenye BRN, ilikuwa inafanya vizuri sana, ilikuwa inachochea sana elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mwaka 2014, shule yangu ya Mchinga sekondari pale ilikuwa ni shule ya kwanza katika shule za Serikali, Kanda ya Kusini kupitia mpango huu wa BRN. Tuliweza kusimamia vizuri sana, tulipeleka vijana wengi, takribani 21 kwenda form five na six. Naomba sana mpango huu tuweze kuuresheja ili kuweza kurudisha morali katika shule zetu za sekondari na za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni hili suala la uhaba wa madarasa. Ni kweli kabisa kwamba shule zetu zina enrollment kubwa sana, kutokana na Mpango wa Elimu Bure wanafunzi wengi wanaingia darasa la kwanza madarasa hayatoshi. Shule ya Msingi Mbae, Mtwara Mjini hii ni mara yangu ya tatu nazungumza hapa, ina wanafunzi zaidi ya 600, madarasa yaliyopo ni mawili pekee. Wanafunzi 600 madarasa mawili, ni jambo la ajabu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Wizara ipeleke pesa Shule ya Msingi Mbae iliyopo Mtwara Mjini tuweze kujenga madarasa na vyoo, hata vyoo pale hakuna, naomba sana Wizara iangalie suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la upungufu wa walimu wa sayansi pia ni jambo muhimu sana. Nashauri kwamba vyuo vyetu ambavyo vilikuwa vinafundisha walimu wa masomo ya sayansi viwekewe msisitizo, vitengewe bajeti ya kutosha na walimu wafundishwe masomo ya sayansi sawasawa. Hivi sasa imekuwa walimu wengi wanakimbia kwa sababu hakuna motivation. Walimu wengi wa sayansi waliofundishwa na Serikali wanakwenda katika shule za private kwa sababu kule kuna malipo ya kutosha, incentives za kutosha, motivation ya kutosha, shule zetu za sekondari za Serikali zinakosa walimu wa sayansi kwa sababu hatuna vivutio. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati fulani ilielezwa sana hii sera kwamba tunahitaji walimu wa sayansi waweze kubaki katika hizi shule za Serikali, tutawapa motivation maalum, lakini mpaka leo hakuna wanachopata cha ziada walimu wa sayansi katika shule zetu za Serikali. Tunaomba yale yanayozungumzwa yaweze kutekelezwa ili elimu yetu iweze kuwa kama maeneo mengine.

T A A R I F A . . .

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Taarifa yake naichua lakini ni kwa sababu PPP tunayozungumza Tanzania siyo kwenye elimu tu, tunazungumza kwenye sekta nyingi kuwe na ushirikiano huu sekta binafsi na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nizungumze suala lingine kwamba elimu yetu wanafunzi wanaishia katika elimu ya juu. Tulitembelea baadhi ya Vyuo Vikuu Tanzania katika Kamati yetu ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, tumefika pale MUCE (Mkwawa University College of Education) kuna ufisadi mkubwa unaofanywa na watendaji ambao Serikali ama sisi Watanzania tumewapa dhamana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kuna jengo la maabara linajengwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu naomba kuhoji Serikali kimaandishi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa maji taka Mtwara Mjini upoje, Mtwara Mjini hakuna mfumo wa maji taka kabisa na bahari ipo karibu kabisa. Nataka kujua kwa nini Serikali haitaki kujenga mfumo wa maji taka Mtwara Mjini? Kuna uchafu mwingi sana majumbani ambao kungekuwa na mfumo wa maji taka magonjwa kama kipindupindu yasingeweza kutokea Mtwara Mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukosefu wa maji taka Dodoma - Chaduru; Dodoma Jijini Mtaa wa Medeli Mashariki eneo la Chaduru hakuna mfumo wa maji taka. Wabunge wengi tunaishi huko, ni karibu na Bunge, ni mjini sana lakini hakuna mfumo wa maji taka. Je, ni lini mfumo huo utafika Dodoma Chaduru?

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya maji Mtwara Mjini kusuasua, naongea tena, miradi ya maji Mtwara Mjini inasuasua sana. Mkandarasi wa mradi wa kutoa maji Lwelu kuja Mitengo, Mbae na Ufukoni anasuasua kwa sababu hapati fedha kwa wakati. Naomba kujua kwa kuwa pump test tayari imefanyika lini ataanza kuchimba matenki na kusambaza maji kwenye kata husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za maji Mtwara Mjini haziji, ukurasa wa 224 wa hotuba ya Waziri wa Wizara ya Maji ametaja maeneo ya Mkoa wa Mtwara ambapo pesa zimepelekwa kwa ajili ya miradi ya maji, cha kushangaza Mtwara Mjini (Manispaa) hakuna hata senti moja iliyopelekwa. Naomba kujua kwa nini wananchi wa Mtwara Mjini hatupewi pesa za Serikali kwa ajili ya maji?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhahuna Wataalah.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Waziri Mheshimiwa Dkt. Charles Tizeba aweze kunisikiliza kwa sababu haya ni maagizo ya wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini na Mikoa ya Kusini. Mwaka jana nilichangia Wizara hii kinatoa wasiwasi wangu juu ya suala la usambaji wa magunia na sulphur bure nikaonyesha wasiwasi wangu na yametokea yale yale, kwamba mwaka huu Wizara imesema haitatoa tena sulphur bure na magunia bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka yote kulikuwa na pesa ambazo zilikuwa zinakusanywa ambapo hizi pesa zilikuwa zinapelekwa kwenye Mfuko wa Wakfu, lakini ule mfuko sasa hivi umefutwa na Serikali kwamba zile pesa za export levy taarifa tulizokuwa nazo za msimu wa mwaka jana tumeweza kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 110 ambazo hizo pesa zilitakiwa ziende zikanunue sulphur kwa wananchi wa Mikoa hii ya Kusini, wananchi wanaolima korosho Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zile pesa wakulima wanauliza sana na wameniagiza nije kuzungumza ndani ya Bunge hili kwamba wamekuwa na matatizo makubwa ya sulphur mwaka jana, sulphur badala ya kuzwa shilingi 25,000 zikalanguliwa mpaka shilingi 110,000 kwa mfuko mmoja. Sasa tulikuwa tunaomba sana pesa za service levy ambazo zimekusanywa kupitia kwa wakulima hawa kila kilo moja ya korosho ziko zaidi ya shilingi bilioni 110, tunaomba zinunue pembejeo wakulima hawa, wananchi wa Kusini waweze kupata pembejeo kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hapa kuna wakulima ambao tayari mpaka leo ninavyozungumza wamepeleka pesa zao kwa vyama vya msingi ili waweze kupewa sulphur wengine wametoa shilingi 400,000 wengine shilingi 500,000 lakini mpaka sulphur maeneo mengi haijaenda. Mheshimiwa Waziri hapa amesema kwamba tayari wameagiza sulphur zipo zitaanza kugaiwa Mtwara na Lindi lakini maeneo mengi wananchi wametoa pesa sulphur mpaka leo bado haijafika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la msingi hapa ni kwamba kupulizia korosho wanaanza kuanzia mwezi wa Aprili maeneo mengine mwezi Mei huu, lakini mpaka mwezi wa Juni maeneo yote yanakuwa tayari yameshakamilika. Sasa unaposema sulphur iko njiani mpaka leo hawa wananchi wanaenda kupuliza muda gani. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana Wizara pesa za service levy, pesa za export levy ambazo zimekusanywa ziende kununua sulphur ziweze kufika kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nimetumwa na wananchi wa Mikoa hii wakulima hawa wa korosho wanauliza suala la CEO ambaye alikuwa anafanya kazi nzuri sana Mheshimiwa Jarufo, tumepata taarifa ambazo siyo rasmi tu kwamba amesimamishwa kazi. Lakini ukaguzi unaonesha huyu jamaa alikuwa anafanya kazi vizuri, anashirikiana na wakulima vizuri, wakulima wanaolima zao hili la korosho, lakini tunaambia tu kwamba ametolewa. Sasa tunaomba majibu ya Mheshimiwa Waziri kwamba kumtoa huyu CEO ni kweli yanayosemwa na wakulima wa korosho kwamba katolewa kwa ajili ya ubaguzi. Tunaomba majibu utakapokuja kutueleza, utueleze kwamba utoaji wa CEO wakulima wa korosho wanasema katolewa kwa ubaguzi, lakini hajafanya jambo lolote baya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nilikuwa naomba kuzungumza hapa ni suala la malipo ya korosho. Maeneo mengi mpaka leo ziko zaidi ya shilingi bilioni nne wakulima wa korosho hawajalipwa. Wakulima wanapeleka kwenye vyama vya msingi korosho zao tangu tarehe 17 Novemba, 2017 na naomba ninukuu hapa baadhi ya maeneo tu, kuanzia pale Mtwara Mjini, Tandahimba na maeneo mengine kuna Kata ya Dinduma wananchi wanadai mnada wa tarehe 17 Novemba, 2017 mpaka leo hawajalipwa, wananchi wa Namnyanga, wananchi wa Mdimba, wananchi wa Tumbwe Tarafa ya Namikupa, Tarafa ya Mahuta, Litehu, maeneo haya yote hawajalipwa pesa zao za korosho tangu mwaka jana tarehe 17 Novemba. Jambo hili linaumiza sana kwa kweli wakulima wanajitahidi kulima kwa muda mrefu, wanalima wanapata changamoto nyingi, lakini pesa zao hawapewi kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala hili la AMCOS, wanaoteuliwa kuingia kwenye AMCOS hizi wanakuwa ni watu ambao hawana uwezo, ni watu ambao wanaenda pale kwa uwakilishi wa wananchi bila kufuata vigezo na wahasibu ambao wanaingia kwenye hivi vyama vya msingi wanakuwa ni wajanja sana, wanapiga mabilioni ya pesa sana wahasibu kwa sababu viongozi wa AMCOS hawana elimu uwezo wao ni mdogo.

Naomba Mheshimiwa Waziri ulete muswada tubadilishe sheria hapa kwamba kila aneyeajiriwa kwenye AMCOS hizi, kila anayegombea kwenye AMCOS kuwe na sifa fulani angalau ya elimu wanapigwa sana, wakulima wanaibiwa sana Wahasibu wa hizi AMCOS zote kwa sababu uwezo wao ni mdogo. Kwa hiyo, naomba tulete Muswada wa Sheria kubadilisha hizi sheria waajiriwa waweze kuwa na uwezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Mheshimiwa Waziri hapa wakati anazungumza ameleza kwamba kuna Tume ya kusimamia kilimo kule maeneo ya Kusini nami nilikuwa naomba sana kwa sababu maeneo ya Kusini ni asilimia 90 ya ardhi ni ardhi ambayo inarutuba sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pia namshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala, lakini niwashukuru vile vile wananchi wangu wa Mtwara ambao leo hii wameniagiza kwa mara nyingine tena nimweleze Mheshimiwa Mpina kwamba kijana aliyeuawa na kikosi kazi chake ambacho alikiunda yeye cha kushughulikia uvuvi haramu katika Operesheni ya MATT ambayo inafanyika kwenye Bahari ya Hindi kuanzia kule Mtwara mpaka kule Tanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawasilisha salamu hizi kwa niaba ya wananchi wa Mtwara, wameniagiza nimweleze Mheshimiwa Waziri ile roho iliyoondoka, iliyopotea, kijana Abdillah Abdulrahman ambaye alipigwa risasi kisogoni kwake akiwa anatafuta kitoweo. Tunaomba kauli ya Serikali kwa sababu mpaka leo Serikali iko kimya na Wizara hii ndiyo iliyounda ile Tume ya Kushughulikia Uvuvi Haramu na huyu kijana alikuwa hafanyi uvuvi haramu. Tunaomba tamko na kauli ya Serikali kutoka Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, nikiwa nasoma, nilisoma jiografia na historia, niliweza kusoma kwamba maelezo ya zamani ya vitabu vyote vimeandika kwamba Miji ya zamani Miji yote Tanzania na duniani kote ilikuwa inaanzishwa kutokana na mambo kadhaa. Jambo la kwanza, ni uwepo wa water bodies yaani vile vyanzo vya maji. Kwa hiyo, wananchi wengi wamejenga katika maeneo mbalimbali ambako maji yanapatikana kwa lengo kuu moja au mawili:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, kutumia yale maji kwa ajili ya kuweza kujipatia chakula chao kwa kufanya uvuvi ambao tunasema subsistence kind of fishing ili waweze kuvua, waweze kutumia wale samaki kwa ajili ya kula. Hawa wananchi wamejenga kwenye vyanzo hivi vya maji waweze kupata wale samaki wanapokwenda kuvua mwisho wa siku waweze kupata pesa, wakiuza waweze kuendesha maisha yao, waweze kujenga nyumba, waweze kusomesha, waweze kufanya mambo mengi ya maendeleo. Nilikuwa nasoma mambo haya wakati nasoma historia wakati nikiwa sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, watu wengine wamejenga maeneo mbalimbali kwa sababu tu ya kufuata barabara. Sasa mimi na wananchi wangu wa Jimbo la Mtwara Mjini ni miongoni mwa wananchi ambao tulijenga Mtwara, tuliamua kuishi Mtwara tangu mababu na mababu kwa sababu ya kufuata bahari ambayo ndiyo ilikuwa inatunufaisha kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunasikitika sana kwamba oparesheni hizi zinazoendesha (Operesheni MATT) na Operesheni Jodari) ambazo zinafanyika kwenye bahari kuu kwamba wananchi wanakatazwa kuvua samaki, wananchi wanakatazwa kwa maana nyingine wasile samaki wao ambao Mwenyezi Mungu amewapa na wao wameenda kujenga kwenye maeneo yale ili waweze kunufaika na samaki kwa kisingizo kwamba ni uvuvi haramu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wote na Wabunge wengine wamezungumza hapa kwamba hakuna anayetaka wanachi wafanye uvuvi haramu, la hasha, hata pale Mtwara mwaka 2008 wananchi walikamatwa wengi sana ambao walikuwa wanatumia uvuvi wa mabomu na sisi tulifurahia sana kwa sababu samaki waliendelea kupatikana na wananchi tulikuwa tuna-enjoy samaki, tuna-enjoy matunda aliyotupa Mwenyezi Mungu. Sasa wanavyosema kwamba eti kila nyavu ni nyavu haramu, hawa wananchi wa kawaida ambao Serikali hii haijawapa vifaa maalum vya kuvulia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka mwaka 2008 tukiwa Chuo Kikuu pale tuliweza kuletewa samaki wa Magufuli wakati ule, tuliweza kula wale samaki zaidi ya mwezi mzima pale Chuo Kikuu kwa sababu walikamata meli moja tu ya Wachina waliokuwa wanavua wale samaki, wakaikamata, wale samaki tuligawiwa Vyuo vyote Dar es Salaam pale. Tuliweza kula mwezi mzima mpaka tukawachoka, hiyo ni meli moja tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, wavuvi wetu Serikali haijawapa vifaa, wanavua kwa nyavu za kawaida halafu wanakwenda kuwakamata, wanawaambia mnavua uvuvi haramu, wakale wapi? Waishi vipi? Wananchi hawa wanaishi kwenye maeneo ya bahari, wafanye kazi gani? Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana Serikali ihakikishe ya kwamba inaleta vifaa vya uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Mtwara nimeshaandika sana, nimezungumza sana ndani ya Bunge hili kwamba wananchi wangu wamejiunga katika vikundi vidogo vidogo wanahitaji boti, wanahitaji zana za kisasa za kuvulia Serikali ituletee waweze kukopa wale wavuvi mwisho wa siku waweze kufanya uvuvi ambao hawaitwi uvuvi haramu, kwa hiyo, tunaomba sana Serikali itekeleze hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, pale Mtwara kuna Chuo cha Uvuvi ambacho kimejengwa, huu ni zaidi ya mwaka wa saba hakijaanza kutumika, wanafunzi hawajaanza kusoma, zaidi ya miaka saba lile jengo lipo tu, lipo baharini kabisa pale Mikindani, ninapoishi mimi, bahari iko hapa kile Chuo kipo pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji sasa hiki Chuo kianze kufanya kazi, wanafunzi wafundishwe, waweze kusoma, mwisho wa siku tusifanye uvuvi haramu lakini Serikali haitekelezi, haitupi haya, mwisho wa siku wanakuja kutukamata kwa yale ambayo tunafanya, wanasema kwamba eti hatuvui sawasawa.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, ni kwa muda mrefu sasa Mikindani Mtwara kuna majengo mengi ya kale ambayo yangeweza kuvutia sana utalii Mtwara na Kusini kwa ujumla wake. Mtwara kwa kushirikiana na Trade Aid – Shirika la Charity kutoka Uingereza tuliweka Siku ya Mikindani ili kuutangaza rasmi Mji wa Mikindani kuwa ni mji wa utalii Tanzania na hasa katika sekta ya mali kale.

Mheshimiwa Spika, tulipanga kila kituo lakini Wizara kwa nini inasuasua kulifanya hili kwa maendeleo ya Mtwara, Kusini na nchi kwa ujumla wake? Naomba Wizara ituambie Wana Mtwara Mikindani lini watazindua Siku ya Mikindani ili kuutangaza utalii?

Mheshimiwa Spika, kuhusu fedha za Regrow; kuna fedha zaidi ya shilingi bilioni mbili za kuendeleza utalii kusini. Fedha hizi zimepelekwa Morogoro, Iringa ambako sio Kusini, Kusini kijiografia na kiutawala ni Mtwara na Lindi pamoja na Ruvuma. Mikoa hii imesahaulika sana pamoja na kuwa vivutio vingi vya kiutalii kwa nini fedha za Regrow Kusini zipelekwe maeneo mengine badala ya Kusini halisi?

Mheshimiwa Spika, kwa nini kila kinachopangwa Kusini kinahamishwa? Tatizo ni nini? Fedha za Regrow ziletwe Kusini Mtwara na Lindi ili ziendeleze Mikindani, Fukwe na Kilwa pamoja na Mbuga ya Selous upande wa Kusini.

Mheshimiwa Spika, Olduvai Gorge irudishiwe mali zake, hii ni mara yangu ya tatu naongelea hili. Eneo hili la mali kale lilikuwa linaingiza fedha sana kabla halijahamishwa kwa maslahi binafsi na kupelekwa Hifadhi ya Ngorongoro ambalo ni Shirika la Umma. Hivi sasa Olduvai Gorge inaingiza fedha ndogo sana kuliko wakati ikiwa mambo kale. Kama lengo ni kuongeza mapato, basi Olduvai Gorge irudishwe kwenye Idara ya Mambo Kale na si Ngorongoro.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu na naomba kuchangia kwa maandishi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuongelea kuhusu mauaji ya raia Abilah Abdureheman wa Mtwara Mjini. Kijana huyu aliuawa na Jeshi la Polisi tangu tarehe 25 Machi, 2018 ufukweni/pwani ya Mtwara Mjini Kianga. Nimeongea sana kuhusu suala hili ila bado sijapata majibu ya Serikali na hatua kwa wahusika ni zipi maana Waziri aliahidi kuunda tume mpaka sasa hakuna majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali (Waziri) atoe majibu stahiki juu ya mauaji haya kwa kijana ambaye hakuwa na hatia kwa kisingizio kuwa alikuwa mvuvi haramu. Suala hili limeleta taharuki kubwa sana Mtwara Mjini, Serikali lazima ifanye uchunguzi wa kweli na wahusika wachukuliwe hatua na mimi kama mwakilishi wa wananchi nipate majibu ya kina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, napenda kuongelea Kituo cha Polisi Mtwara (Wilaya) ambacho kiko mbioni kubomoka. Kituo cha Polisi Wilaya ya Mtwara ni kibovu sana, zege inakatika na siku yoyote itabomoka. Naiomba Serikali ikarabati haraka kituo hiki kwani askari wetu watapoteza maisha muda wowote baada ya kuwabomokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, niongelee kuhusu kukosekana kwa samani katika Kituo cha Wilaya ya Mtwara. Kituo hiki hakina meza na viti ambavyo vinaweza kukidhi mahitaji ya polisi wanapotoa huduma. Polisi wanasimama muda wote wanapohudumia wananchi. Naomba ziletwe meza na viti katika kituo hiki cha Polisi Wilaya kwani hali ni mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne nitaongelea kuhusu nyumba za bati za Polisi wa Mtwara. Nyumba za bati kwa polisi ni hatari sana. Mtwara Mjini zipo nyumba nyingi za bati mpaka leo. Hali hii inatisha sana kwani umeme unaweza kuangamiza maisha ya askari wetu mara moja. Naomba pesa ziletwe Mtwara Mjini kwa ajili ya kujenga nyumba bora za polisi badala ya hizi za bati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, niongelee kuhusu bodaboda na polisi. Mtwara Mjini wahalifu wengi wameingia kwenye kazi ya bodaboda na uhalifu umepungua sana Mtwara Mjini kwa kuwa wahalifu wana kazi ya kufanya. Jambo la ajabu askari wetu ambao hawaitakii mema amani yetu wanawasumbua sana bodaboda tena bila sababu. Askari wanawafukuza kana kwamba wameua, wanakamata pikipiki hovyo na kutoza fine ovyo tena bila sababu. Bodaboda anatakiwa apeleke Sh.40,000 kwa tajiri wake kwa wiki lakini anashikwa na polisi anatozwa Sh.120,000 au Sh.90,000 kwa kisingizio kuwa amefanya makosa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Polisi zimejaa pikipiki nyingi sana. Polisi hawatoi elimu, wananyang’anya pikipiki za maskini, wanaziacha zinaoza katika vituo vya polisi. Hali hii haikubaliki hata kidogo. Naitaka Serikali iangalie suala hili kwa jicho la kipekee kabisa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo kadhaa nataka majibu ya Serikali. Majeshi yetu kupelekwa Darfur na Congo DRC, kwa nini mpaka leo majeshi yetu yanapelekwa Darfur na Congo DRC? Malipo yake kwa Taifa hili kwa sasa ni shilingi ngapi? Fedha za malipo zinachangia bajeti kiasi gani? Ukombozi wa Afrika umekwisha, Watanzania wengi wameuawa sana, hakuna malipo kutoka kwa nchi tulizokomboa mfano South Africa, Namibia, Zimbabwe, Mozambique na nyingine nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeanza kupeleka Watanzania wengi kuuawa bila malipo kwa muda mrefu, sasa hivi imefika wakati wa nchi kuomba malipo kwanza kabla ya kupeleka vijana wetu kuuawa, Congo kwa mfano kuna madini mengi na wanajeshi wetu wanauawa huko kila siku. Naomba watulipe fedha au madini ili tujenge uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, duniani sasa hivi hakuna nchi inapeleka watu wake vitani nchi nyingine bila malipo makubwa. Serikali ituambie wale wanajeshi waliouawa mwaka jana na mwaka juzi Congo DRC fidia imelipwa kiasi gani? Leo kuna wanajeshi wanapelekwa Darfur miaka mitatu wakati Omar Al-Bashir amefukuzwa, hakuna amani, nani anatulipa? Umoja wa Mataifa inalipa kiasi gani kwa thamani ya watu wetu wanaenda kuuawa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka tulienda kumuondoa Mohamed Bakar kule Comoro kwa maslahi ya Wacomoro tulilipwa bei gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Rwanda tunaisifia kuwa iko juu kiuchumi na kwamba Kagame anajenga uchumi wake. Kazi yake amepeleka majeshi Congo DRC anachochea vita, wanateka maeneo ya madini, wanachimba na kuuza then wanajenga uchumi wa Rwanda. Sisi Jeshi letu tunapeleka kuuawa bure bure tu, haikubaliki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumshukuru Mungu kwa kunijalia afya njema. Napenda kuchangia kwa maandishi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu hospitali za wilaya 67; naomba kama hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI ilivyosema juu ya ujenzi wa hospitali za wilaya nchini. Napenda kupongeza mpango huo na sisi Wilaya/Manispaa ya Mtwara mjini hatuna hospitali ya wilaya kabisa. Naomba Mtwara Mjini tupewe hospitali hivyo kwa kuwa tuna shida sana ya hospitali na hasa ukizingatia hata hospitali ya kanda hatuna Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ubovu wa barabara Mtwara Mjini; kuna barabara ambazo hazipitiki kabisa wakati wa masika (kifuku). Barabara hizo ni Mbae –Mbawala chini, Mtawanya- Namayanga na Mikindani – Dimbuzi kupitia Lwelu. Naiomba sana Wizara barabara hizi za mjini Mtwara zijengwe kwa lami ili kuondoa usumbufu wa kukarabati kila mwaka kwa kuwa maji huharibu wakati wa mvua na wananchi wanakosa mawasiliano kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, stendi za kisasa Magomeni na Mikindani Mtwara; kumekuwa na ahadi za muda mrefu sana juu ya ujenzi wa stendi Mtwara Mjini eneo la Magomeni, Mkanaledi na Mikindani Mtonya. Naomba pesa ziletwe mwaka huu wa fedha kwa ajili ya ujenzi huo kwani wananchi wengi wamehamishwa kupisha ujenzi huo eneo la Magomeni lakini Mikindani Mtonya wananchi wanaishi kwa wasiwasi juu ya kupewa fidia majumba yao ili kupisha ujenzi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu TARURA Mtwara Mjini; watu wa TARURA ni viburi sana na hasa Mtwara Mjini. Wakati mwingine wanakaa na fedha kwa mfano Mtwara Mjini walikuwa na Milioni 20 za halmashauri lakini hawachongi barabara na miundombinu ya mjini inaharibika sana wakati wa mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; TARURA wanakataa kutoa taarifa kwa wananchi pamoja na mimi Mbunge kuwaandikia barua kuja kutoa ufafanuzi juu ya ujenzi wa miundombinu ya barabara kwenye mikutano ya hadhara lakini TARURA pekee walikataa kuwapa taarifa wananchi juu ya mpango kazi wao wakati wanafanya kazi na wapo kwa ajili ya wananchi wa Mtwara Mjini. Watendaji wa aina hii hawatufai Mtwara kwani wananchi lazima wapewe taarifa za maendeleo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo ubadhirifu mkubwa wa fedha za halmashauri nchini. Kwa mfano Mtwara Mjini Mwekahazina na syndicate yake walitafuna milioni 800 na ushee. Cha ajabu Mwekahazina kahamishwa lakini hajachukuliwa hatua za kupelekwa kwenye Mahakama ya Mafisadi, pia wenzake waliohusika bado wapo Mtwara Manispaa na wanafanya hujuma juu ya Mkurugenzi kwa kusimamia vema halmashauri ya Mtwara Manispaa. Naomba wahusika wote wachukuliwe hatua stahiki na kuhamishwa mara moja Halmashauri ya Mtwara Mikindani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu dawa; upatikanaji wa dawa bado siyo mzuri sana Mtwara Mjini, wananchi wengi wanaambiwa hamna dawa kwenye zahanati zetu na hospitali ya Mkoa wa Mtwara. Naomba dawa ziongezwe na Mbunge nipewe taarifa juu ya kiwango cha dawa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, nachangia kwa maandishi Wizara ya Nishati kama ifuatavyo na naomba Waziri anipe majibu stahiki:-

Mheshimiwa Spika, bei ya umeme wa REA Mtwara Mjini, hotuba ya Waziri imesema ataweka utaratibu vijijini kote bei ya REA iwe 27,000/=, lakini Mtwara Mjini hii program ilikuwepo lakini ikaondolewa. Sababu za msingi hakuna, naomba Waziri atupe majibu kwa nini bei hii imeondolewa Vijiji vya Mtwara Mjini ambavyo wamebatiza jina la mitaa.

Mheshimiwa Spika, mkuza wa gesi Mtwara-Lindi; ilisemwa mote mlimopita bomba la gesi mngepelekewa umeme kwa gharama ya REA yaani 27,000/=tu, lakini Mtwara Mjini kata takribani nane bomba hili la gesi limepita. Cha ajabu wananchi wa kata hizi watozwa laki tatu mpaka tano kwa ajili ya kuunganisha umeme wakati sera inasema shilingi 27,000 tu kwenye huu mkuza wa gesi. Waziri kwa nini anatukandamiza Wanamtwara Mjini?

Mheshimiwa Spika, usambazaji wa umeme vijijini/ mitaa ya pembezoni mwa Mtwara Mjini; kila siku Waziri nikimuuliza anasema maeneo ya pembezoni mwa Mji wa Mtwara yatapelekewa umeme kwa mfumo wa ujazilizo. Mpaka leo Waziri amepeleka sehemu moja tu ya Mbawala Chini kwenda kulambisha kidogo tu. Maeneo ninayoyalalamikia kila siku ni: Mbae-Mkangala; Lwelu- Dimbuzi na Mkangala - Mkunjanguo mpaka Mwenge na Mtawanya- Namayanga.

Mheshimiwa Spika, maeneo haya ya pembezoni ya Mji wa Mtwara yanaitwa mitaa lakini Wizara haitaki kupeleka umeme kabisa. Waziri atuambie kwa nini anatunyanyasa wana Mtwara Mjini kwa kukataa bila sababu kupeleka umeme mitaa hii wakati umeme wote kusini unatoka Mtwara Mjini? Maeneo haya kila moja haizidi kilomita tatu kutoka vyanzo vya umeme lakini Serikali haitaki kupeleka mtandao wakati gharama ni nafuu sana.

Mheshimiwa Spika, gesi majumbani Mtwara Mjini; imepelekwa majumbani Masaki, Dar es Salaam kwa miaka miwili sasa lakini pale inapotoka hii gesi Wanamtwara tupo tayari kununua hii gesi lakini Serikali haitaki kutuletea. Anachofanya Waziri ni danganya toto tu na kuahidi kuwa mradi wa Mtwara utaanza, lakini hata mimi Mbunge wa Jimbo sina taarifa hata moja juu ya utaratibu wa hiyo gesi majumbani. Nimemuuliza Mheshimiwa Waziri anasema utaratibu bado lakini Masaki anakoishi yeye kapeleka gesi anatumia gesi kupikia, pale Mtwara inapotoka gesi anasema mchakato unaendelea. Hali hii ni uonevu mkubwa na ukandamizaji wa Wanamtwara ambao tumekuwa tunalalamikia kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, ukurasa wa 90 wa hotuba ya Waziri amesema mchakato wa kupeleka gesi Uganda unakamilika. Haiingii akilini hata kidogo gesi iende nje kutumiwa majumbani wakati pale inapotoka Mtwara ni nyumba 300 tu wakati kila nyumba Mtwara inahitaji hii gesi nafuu ya Serikali. Haikubaliki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. MAFTAH A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhanah wataala, naomba nichangie kwa dakika hizi tano kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni suala la fidia ya ardhi. Ndani ya Bunge hili hii ni mara yangu ya nne nasimama nikiwa nazungumza suala zima la eneo la Mjimwema pale Mtwara Mjini. Eneo ambalo lilichukuliwa na Serikali, Serikali iliyopita na Serikali hii ya Awamu ya Tano wakaahidi kulipa fidia, kuwalipa wananchi wa Mjimwema.

Tangu mwaka 2013 walipochukuliwa yale maeneo yao wale wananchi wamekatazwa kulima maeneo yale wala kuendeleza maeneo yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikaleta swali mara mbili ndani ya Bunge hili na Serikali ikaahidi kwamba itaenda kulipa mwaka jana baada ya bajeti tu. Hata hivyo jambo la kusikitisha sana, baada ya kumalizika kwa bajeti naambiwa Serikali haiwezi kulipa. Sasa nashangaa sana, yaani Serikali hii inachukua maeneo ya wananchi zaidi ya miaka mitano sasa tangia mwaka 2013, halafu inaahidi kulipa na hatimaye inakuja inawaacha njiani, inasema haiwezi kulipa fidia Halmashauri wenyewe ndio waende wakalipe fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo sana, wananchi wa Mjimwema, Mtwara Mikindani wanasikitika sana kwa sababu wamekosa kuendeleza yale maeneo kwa ahadi kwamba Serikali itawapa fidia, lakini mpaka leo Serikali inasema haiwezi kufidia wakati ilishaahidi hapa. Mimi nina Hansard mbili; ndani ya Bunge hili Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Ardhi ikisema inaenda kulipa fidia watu wa Mjimwema. Naomba safari hii Mheshimiwa Waziri atupe majibu ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana nilimpongeza sana hapa Mheshimiwa Waziri kwa mpango kabambe wa Mtwara, lakini katika hili Mheshimiwa Waziri Lukuvi ametuangusha wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini. Naomba hizo pesa kama ni Waziri wa Fedha ampatie hizo pesa ili aweze kuwalipa wale wananchi. Wananchi wanalia sana, wananchi wa Mjimwema, Mtwara Mjini hawawezi kuchukuliwa kwa siku zote hayo maeneo yao halafu Serikali inawaacha njiani kwamba haiwezi kulipa, haiwezekani. Serikali hii haisemi uongo na hili ni Bunge, Hansard mbili zimezungumza hapa kwamba tunawalipa lakini wanasema hawawezi kulipa ni jambo la ajabu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, naomba kuzungumzia suala la urasimishaji, tunashukuru kweli mpango huu wa urasimishaji Mtwara ni Mji wa pili na urasimishaji unaendelea pale Mtwara. Hata hivyo, niseme Mheshimiwa Waziri kwamba vifaa hajatusaidia, kwamba wale wanaopima hawana vifaa vya kutosha, kwa hiyo kasi imekuwa ndogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya mwaka hivi sasa na maeneo waliyopima ni machache mno pale Mtwara mjini. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Lukuvi kwa sababu ni msikivu sana tunamwaminia, naomba atupe vifaa Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani ili urasimishaji uende kwa kasi katika maeneo ya Chipuputa, maeneo ya Kiholo, maeneo ya Komoro, maeneo ya Magomeni, Kata ya Ufukoni; tunataka urasimishaji kwa sababu wale wananchi walijenga kiholela holela. Kwa hiyo tunaomba vifaa ili kazi iweze kuendana na maagizo yake ambayo ameyatoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo naomba kuzungumza ni suala la migogoro ya ardhi. Ni kweli kwamba hata pale kwetu Mtwara bado lipo na mwaka jana Mheshimiwa Waziri nilimweleza suala la yule jamaa tapeli, anaitwa siju Azimio, sijui nani sijui, maeneo mengi amefuta hati zake, lakini Mtwara mjini eneo la Libya mpaka leo wale wananchi walinyang’anywa na bado Mheshimiwa Waziri Lukuvi pamoja na usikivu wake Mtwara Mjini amekaa kimya juu ya mgogoro huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yule tapeli naona kaenda mahakamani sasa hivi kwa sababu yale maeneo alichukua kinyume na taratibu. Yaani watu wamelala, wanaamka asubuhi wanakuta beacons zimewekwa pale; mwaka jana nilizungumza hapa. Kwa hiyo hili suala halihitaji mahakama, linahitaji yeye kama Waziri kwa mamlaka yake aliyopewa aende akachukue yale maeneo awarudishie wananchi wa Libya Mtwara Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wananchi wanalia sana na yule ni tapeli na Mheshimiwa Waziri tumeshamsikia anazungumza katika maeneo mengi kwamba huyu tapeli lazima maeneo aliyochukua yarudishwe kwa wananchi. Kwa hiyo, hili suala la mgogoro wa Libya Mtwara Mjini Mheshimiwa Waziri mwaka huu aende akatusaidie wananchi wale wapate lile eneo lao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kuna mgogoro ambao nao nilizungumza mwaka jana, naomba utusaidie Mtwara Mjini juu ya suala hili ili wananchi wapate haki zao, kwa sababu Serikali zilizopita huko nyuma zilikuwa ni Serikali za kudhulumu wananchi, ilikuwa ni udhulumati, wananchi wananyang’anywa maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilikuwa nataka kuzungumza ni suala hili la mashamba ya walowezi. Tanzania hii kuna maeneo mengi ambayo yalikuwa ni mashamba ya walowezi. Hata pale Lindi ukija Kikwetu Estate pale lile shamba ni kubwa sana. Wananchi wanahitaji maeneo waweze kujenga nyumba, wanahitaji kuendeleza pale Kikwetu pale Lindi, lakini wanasema lile lilikuwa ni shamba la mlowezi mmoja kamuuzia Mohammed enterprises.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haliendelezwi na Mheshimiwa Waziri ameshatamka kwamba kisheria kama mtu hajaendeleza kwa muda fulani basi yale maeneo yanarudishwa kwa wananchi. Kikwetu Estate wananchi wanahitaji kujenga pale, wanahitaji kulima pale. Niombe sana kwa sababu yalikuwa ni mashamba ya walowezi huko nyuma tunaomba yarudishwe kwa wananchi ili waweze kuyaendeleza.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami nichangie Wizara hii ya Madini. Nasikitika sana, baada ya kusikia taarifa ya Wizara hapa kwamba bado inazungumza suala la STAMICO kuendelea kuwepo kama Shirika la Serikali la kusimamia madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, STAMICO tumeizungumzia kwa muda mrefu sana ndani ya Bunge hili. Kamati mbalimbali zimezungumza juu ya udhaifu wa STAMICO kwamba imeshindwa kusimamia rasilimali za madini Tanzania. Leo tunasikitika kuona kwamba mpaka leo Serikali bado imeamua kuilea STAMICO kama Shirika la Madini wakati inatuingizia hasara katika nchi hii, imeshindwa kusimamia madini yetu ya vito na madini mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate taarifa kwamba kwa nini Serikali pamoja na STAMICO kuliingizia hasara Taifa hili bado mnaendelea kuibeba STAMICO? Hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nazungumza suala la kuongeza thamani ya madini. Wenzangu wamezungumza hapa kwamba Tanzania tuna tatizo kubwa, madini yetu hayachakatwi hapa Tanzania eti kwa sababu zile mashine zinauzwa bei mbaya; na sababu nyingine inatolewa kwamba zile mashine kidogo zinahitaji utaalam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana na juzi ndani ya viwanja vya Bunge tunayo mashirika mbalimbali, kampuni mbalimbali za watu binafsi wametuonesha mashine hapa. Zile mashine ni bei rahisi sana. Serikali ingeamua kama kweli ingekuwa na nia ya dhati ya kuchakata madini yetu Tanzania ili yaweze kutoa ajira kwa Watanzania, ingeweza kununua zile mashine. Ni bei rahisi sana tumeambiwa hapa nyuma. Kwa hiyo, naiomba Serikali kwamba, iwekeze kwenye kuchakata madini, madini yachakatwe Tanzania; tanzanite ichakatwe Tanzania. (Makofi)


Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati fulani wakati tunapitia taarifa ya tanzanite, tanzanite imetoa ajira kwa kiasi kikubwa sana Mji wa Jaipur kule India. Zaidi ya watu laki sita wameajiriwa katika Mji wa Jaipur kule India kupitia madini ya Tanzanite ambayo yanatoka Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo la ajabu sana, zile ajira zingeweza kutengenezwa hapa Tanzania, Watanzania wetu wakawa wamepata ajira kupitia madini haya ya tanzanite, madini ambayo yanapatikana Tanzania pekee duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, wakati umefika sasa wa kuhakikisha kwamba tunanunua zile mashine za kuchenjua yale madini ya tanzanite, viwanda viwekwe pale Arusha na maeneo mengine ili Watanzania wetu waweze kupata ajira na siyo tunaenda kuwatajirisha watu wa nje zaidi ya ajira 600,000 kule India, Jaipur. Naomba Mheshimiwa Waziri akija hapa atuambie wana mkakati gani wa kuleta zile mashine kwa wingi za kuchenjua madini ya tanzanite ili kudhibiti utoroshaji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo Kamati ya Madini ya Tanzanite ilipendekeza ilikuwa ni ujenzi wa One Stop Centre. Kuwe na eneo moja maalum ambalo madini yetu ya tanzanite yaweze kuuzwa pale, yaweze kuuzwa kupitia mnada, yaweze kuuzwa kwa njia nyingine. Sasa Serikali imejipangaje kutekeleza agizo hili la pendekezo hili la Kamati ya Tanzanite ambayo ililitoa? Mheshimiwa Doto Biteko alikuwa ni Mwenyekiti wa Kamati ile. One Stop Centre Tanzanite wamejipangaje mwaka huu kuijenga hapa Tanzania ili madini yetu haya yasitoroshwe? Kwa sababu, tunaambiwa kwamba, madini ya tanzanite huko nje yamezagaa sana kwa sababu, utoroshwaji ni mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kule Kilimanjaro kuna njia za panya nyingi zaidi ya 300. Sasa hivi tunashukuru kwamba Serikali imeweza kujenga ule ukuta, lakini bado yapo maagizio mengine ya Kamati ambayo yalipendekezwa.

Tunaiomba Serikali, kama kweli tuna nia ya dhati ya kuifanya tanzanite iweze kuwanufaisha Watanzania kwa sababu, ni madini yanayopatikana Tanzania tu duniani, tungeweza kudhibiti zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado utoroshwaji tunaamini upo, kwa sababu wachimbaji wadogo wadogo kule wako wengi, kuna leseni zaidi ya 800 pale zimetolewa na agizo hili pia nalo wamelitekelezaje kama Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Doto Biteko, Mheshimiwa Waziri, kulikuwa na pendekezo la Kamati ya Tanzanite kwamba zile leseni zile ziunganishwe kwa sababu, leseni ziko nyingi, zimetolewa zaidi ya leseni 800, eneo dogo la Mererani pale Arusha. Serikali inatekelezaje agizo hili? Kwamba, zile leseni ziunganishwe na wale watu waweke kwenye vikundi, hasa wale wachimbaji wadogo wadogo, ili kudhibiti utoroshwaji wa tanzanite. Tunaomba Mheshimiwa Waziri akija atueleze kwamba zile leseni 800 wamezi-combine au imekuwaje mpaka leo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la kudhibiti haya madini. Ni jambo muhimu sana kwa sababu haya madini yanapatikana Tanzania tu na eneo dogo tu la Mererani, lakini ukienda huko nje bei zake zimekuwa ni ndogo ukilinganisha na thamani ya madini ya Tanzanite. Ukienda maeneo mengi ya India, South Africa, yamezagaa kweli kweli na bei zimekuwa ni ndogo mpaka kule Tuckson, Marekani bei zimekuwa ni ndogo kwa sababu yamezagaa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaiomba Serikali ili kudhibiti haya madini, iweze ku-declare kwamba atakayepatikana anatorosha madini, basi aweze kuuawa, iwe nyara ya Taifa. Lilikuwa ni miongoni mwa mapendekezo ya Kamati ya Tanzanite, sijui Serikali imejipangaje kutekeleza? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba iwe nyara ya Taifa kwa sababu ni madini ya kipekee, yako Tanzania tu duniani.

Mtu akikamatwa anatorosha ovyo ovyo huko, ili nasi yaweze kutunufaisha, basi ikiwezekana auawe. Naomba Mheshimiwa Waziri atekeleze hili agizo kwamba tanzanite iwe ni nyara ya Taifa kama nyara nyingine. Kwamba, smugglers wachukuliwe hatua kali ili watu wasiweze kutorosha nchi yetu iweze kuwa na manufaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo naomba kuchangia hapa ni suala hili la kampuni hizi ambazo ni kampuni hewa, kuna kampuni nyingi sana za Tanzanite zimeanzishwa. Ukipitia zile taarifa, ile Kampuni ya TML, nayo inamilikiwa na Kampuni ya TML South Africa. Tanzanite South Africa nayo inamilikiwa na kampuni ya Uingereza. Kwa hiyo, yaani tanzanite ina makampuni mengi sana, kampuni mama, kampuni dada hizi kama tatu, lakini wote hawa wanashughulikia suala moja la tanzanite. Sasa Serikali inakosa mapato sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Wizara hii Mheshimiwa Waziri na Manaibu ni watu makini sana. Wachunguze haya makampuni hewa ambayo yapo, yameanzia pale TML, TML Tanzania, kuna TML South Africa, kuna TML England nayo pia ina kampuni mama nyingine huko. Kwa hiyo, hizi kampuni kwa taarifa tulizokuwanazo ni kampuni hewa na zinakwepa kodi kupitia mauzo ya Tanzanite.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba wazipitie hizi kampuni zote ikiwezekana waweze kuzuia wasiziruhusu hizi kampuni kufanya biashara ya madini ya Tanzanite hapa Tanzania. Madini haya ni madini yenye thamani sana. Kwa hiyo, naishauri Serikali ihakikishe ya kwamba, inatekeleza hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala hili la madini ya blue sapphire. Tanzania hii madini ya blue sapphire pale ukienda Tunduru yamejaa sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuchangia mchango huu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najaribu kufikiria na kusoma soma hivi vitabu vya mipango ambavyo tumekuwa tunaletewa hapa kwa muda wa miaka mitatu hivi sasa tangu nimekuwa Mbunge, lakini nimegundua kwamba mipango hi ni mingi sana, lakini siyo tu mingi, mipango hii inahitaji muda sana, lakini mipango hii inahitaji udadavuzi wa kutosha kabisa ili kuweza kutekeleza mipango hii kutokana na intricacies zake zilizopo, Waingereza wanasema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yangu ni nini? Kwa sababu Wizara hii imepewa majukumu mengi sana, Wizara ya Fedha kazi yake ni kuleta mipango yote ya fedha, kutengeneza bajeti ya fedha, kuzipa Wizara zote fedha na utekelezaji wake kufuatilia, lakini tumeipa kazoi nyingine ya kutengeneza mipango na kusimamia mipango. Mimi nilikuwa nashauri kwamba mamlaka zinazohusika Serikali itenganishe kuwe na Wizara ya Mipango na kazi yake iwe ni kutunga mipango na kusimamia mipango pekee, lakini kuwe na Wizara ya Fedha lakini kuichanganisha, kuziunganisha kama ilivyo hivi sasa ndiyo maana tunaona baadhi ya maeneo yanasahaulika, baadhi ya mambo ambayo yamepangwa na Serikali yanashindwa kufuatiliwa kwa sababu Wizara hii imepewa jukumu kubwa sana. Nashauri Serikali itenganishe ziwe Wizara mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na nilikuwa napitia mpango hapa huu muelekeo wa mpango kwenye changamoto hizi amezungumza Mheshimiwa hapa kwamba miongoni mwa changamoto ni uwezo wa wakandarasi wanaopewa zabuni za ujenzi katika miradi inayofuatiliwa kutokuwa na uwezo wa kutekeleza miradi hiyo kwa wakati uliopangwa kwenye mikataba. Sasa ni jambo la kusikitisha sana kwamba Serikali yenyewe ndiyo inachagua hao wakandarasi, Serikali ndiyo inayofuata taratibu za manunuzi na tukachangua wanunuzi ambao hawa wakandarasi ambao ni best kutokana na Sheria ya Manunuzi lakini mwisho wa siku inafuatiliwa, inaonekana kwamba wale wasimamizi au wale watekelezaji au wale waliopewa zabuni hawana uwezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze jambo moja hapa, mwaka jana wakati Mheshimiwa Rais amekuja Mtwara kuja kuzindua pale ujenzi wa bandari lakini pia kuweka jiwe la msingi la barabara kutoka Mtwara Mjini mpaka Mnivata kilometa 50, alizungumza wasiwasi wake huu kwamba kuna mkandarasi yule amepewa ujenzi wa barabara ile kutoka Mtwara Mjini mpaka Mnivata kilometa 50 barabara ya uchumi, yule mkandarasi alisema kwamba hana uwezo wa kutosha. Sasa tunashangaa kwamba mtu hana uwezo wa kutosha na anajulikana na Serikali lakini bado anapewa ule mradi kutekeleza, mpaka leo ule muda ambao alipangiwa kumaliza ule mradi, mradi unasuasua mopaka leo ile barabara kilometa 50 tu sasa ni jambo la ajabu sana.

Mimi niishauri Serikali kwamba yale ambayo tumeyaona kwamba ni mapungufu na wale ambao hawafai, wazabuni ambao tumewapa tender hawawezi kusimamia na kutekeleza sawa sawa kwa wakati basi wasipewe hizi kazi ndiyo lengo la Serikali kuliko kuchelewesha kazi tunawapa wale wale ambao tumeona wana makosa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nilikuwa napitia kitabu cha Mheshimiwa Mpango hapa kana kunavyopanga hii mipango tunatakiwa tuangalie usawa wa nchi yetu kwa sababu lengo la nchi hii ni kuondoa umaskini. Sasa tulikuwa kwenye bajeti tunazungumza suala la ujenzi kwa mfano wa viwanja vya ndege na humu kwenye mpango nimeona pia kwamba Serikali imejipanga kukarabati na kuendeleza viwanja vya ndege, sasa naangalia hapa kwenye ukurasa huu wa 30 sioni kiwanja cha ndege cha Kanda ya Kusini ambacho ndiyo chanzo kikuu cha uchumi kwa ndege zetu za Kanda ya Kusini, uwanja wa ndege wa Mtwara hapa haupo wa Kanda ya Kusini sasa ni jambo la ajabu sana tunazungumza maeneo mengine na Kanda zingine zinaachwa kwa makusudi kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na tulizungumza wakati wa bajeti hapa kwamba kiwanja kile kilitengewa shilingi bilioni 54 kwa ajili ya ujenzi lakini humu kwenye mpango hakipo na miradi ambayo inatekelezwa ambayo imepangiwa bajeti tumeiona humu yote ipo imetajwa na Mheshimiwa Waziri wa Mpango. Sasa tunaomba utuambie Mheshimiwa Waziri wa Mpango kwamba tunavyopanga na maeneo mengine tunasahau ama tunayaacha? Badala ya kwenda mbele tunarudisha nyuma, lengo ni nini Mheshimiwa Waziri Mpango?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine pia ni suala hili la reli ya Ukanda ule wa Kusini wenzangu wamezungumza na ukanda huu wa Kusini Mheshimiwa Akbar kasema kwamba ndiyo ufunguzi wa uchumi na tunapotaka kuondoa umaskini lazima hii nchi tu-decentralise uchumi wetu, tufungue milango yote; reli ya katikati standard gauge ni jambo jema sana, lakini reli ile ya Kusini ambayo iling’olewa miaka ya 1963 na kupelekwa maeneo mengine basi irudishwe sasa ianzie pale Mtwara Mjini, Bandari ya Mtwara ielekee kule isiwe kila mwaka tunaandika kwenye mipango, utekelezaji unakuwa ni mdogo. (Makofi)

Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana kwamba ule tunaoita upembuzi yakinifu ule ambao unataka kuanza kutoka Mtwara Mjini mpaka kule Mbambabay, kule Mchuchuma na Ligfanga basi uweze kupelekewa fedha siyo kila mwaka tunaandika kwenye mipango fedha hazipelekwi na utekelezaji unakuwa ni mdogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine kuna suala la uendelkezaji wa viwanda ili viweze kuleta ajira kubwa sana kwa Watanzania na kuondoa umaskini, lakini jambo la kusikitisha chuma kinapatikana Mchuchuma na Liganga ndipo kwenye chuma pale na chuma ndicho kitatoa material chuma kinapatikana Mchuchuma na Liganga lakini kiwanda cha kutengeneza chuma kinakwenda kuwekwa Moshi, ni jambo la ajabu sana. Serikali hii inatakiwa iangalie kwa sababu tunavyowekeza katika uchumi wetu tunahakikisha ya kwamba tunawekeza kwa gharama nafuu sana sasa unavyotoa chuma kutoka Mchuchuma na Liganga kama huo mradi ukikamilika then ukakipoeleka Moshi kwenye Kiwanda cha Chuma gharama inakuwa ni kubwa sna na inakuwa badala ya kwenda mbele bado utatumia rasilimali kubwa snaa katika kusafirisha material. (Makofi)

Mimi nashauri kwamba kiwanda cha chuma kijengwe kule kule Songea, kule kule Mchuchuma na Liganga ambako ndiko material yale yanatoka kule na tusiende kuweka umbali mrefu kama ilivyokwenye taarifa mbalimbali ambazo tumekuwa tunazisoma za Kamati. Hii itapunguza ile hali ya kuweza kutumia gharama kubwa kwenye kusafirisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nilitaka kuzungumza kwenye mpango hili limezungumzwa suala la afya kwamba Serikali imejipanga na inamkakati wa kurekebisha suala hili la afya nalo pia kama ilivyo kwenye maeneo ya viwanja vya ndege kwamba Mikoa ile ya Kusini ukisoma kwenye taarifa hapa ya Mheshimiwa Mpango kwamba amepanga kuboresha hospitali za rufaa kwenye ukurasa wa 24. Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini haipo, nikiangalia humu hakuna kabisa, haijatengewa hata kuwekwa tu kwenye mpango kwa sababu tunaanza kuweka kwenye mpango halafu tunaingia kwenye bajeti. Sasa Hospitali ya Kanda ya Kusini haipo humu ndani na tumezungumza wakati wa bajeti, tumezungumza miaka yote, kwenye mipango yote iliyopita sasa kama unaondoa kwenye kitabu cha mpango vipi kwenye bajeti inayokuja? Kwahiyo mimi nishauri sana kwenye ukurasa wa 24 ihakikishwe ya kwamba hospitali hizi za Kanda basi ziangaliwe Kanda zote ili Watanzania waweze kuwa na afya bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nakushukuru.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa dakika hizi chache nilizozipata. Kwanza naomba kuunga mkono hoja hizi za Kamati zote mbili lakini nitaongea haraka haraka sana kwa sababu ya muda.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, Kamati ya Nishati na Madini imezungumza mambo mengi sana ya msingi na miongoni mwa mambo ambayo nimeyapenda sana ni suala zima la kudhibiti utoroshwaji wa madini ambapo imeweza kuipongeza Serikali. Nami pia nichukue fursa hii kuipongeza Serikali kwa kitendo cha kujenga ule ukuta wa Mererani ambapo tanzanite ilikuwa inatoroshwa kwa kiasi kikubwa sana. Wakati wa Kamati Maalum tuliweza kupewa taarifa kwamba miji mingi ya Kenya ukiwemo Mji wa Naivasha umeendelea kwa kiasi kikubwa kwa sababu ya madini ya tanzanite yanayotoroshwa kutoka Mererani Tanzania, leo ni mji bora kabisa kule Kenya. Kwa hiyo, naipongeza Serikali kwa kitendo hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizo bado kuna uhafifu katika kudhibiti madini mengine yakiwemo madini ya blue sapphire ambayo yanapatikana kule Tunduru, Mkoani Ruvuma. Kule Tunduru kuna watu wa Sri Lanka wengi sana ambao wananunua madini haya na wanayapeleka kwao wanayaunganisha wanasema haya madini yanatoka Sri Lanka, blue sapphire inatoka Tunduru. Niitake Serikali kama kweli tunahitaji kudhibiti sekta hii ya madini ambayo imenufaisha nchi nyingi duniani basi tudhibiti madini ya blue sapphire kule Tunduru yasiweze kutoroshwa hovyo hovyo na kupelekwa Sri Lanka na zaidi kuweka label ya Sri Lanka kwamba yanatokea pale Sri Lanka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nizungumzie suala la miradi hii ya gesi. Nisikitike kwamba Kamati imesema ni sekta ndogo ya gesi na sekta ndogo ya madini. Nashangaa, kwa nini iitwe sekta ndogo? Kwa sababu kama kweli tunahitaji kuitumia gesi sawasawa, nchi za wenzetu kwa mfano, Qatar na nchi zingine zimeweza kuendelea kwa kutumia uchumi wa gesi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali tuwekeze katika miradi ya gesi ambayo ilianza kuwekezwa miaka sita, saba iliyopita. Kule Mtwara na Lindi kuna ule mradi wa LNG, nashangaa kwamba Serikali iko kimya sana, haiendelezi mradi ule. Ule mradi ulikuja kuleta ajira nyingi sana kwa wananchi wa Mikoa ile ya Kusini, wananchi wa Mkoa wa Lindi. (Makofi)

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Maftaha kuna taarifa, Mheshimiwa Heche.

T A A R I F A

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, sina uhakika sana na maelezo yake na kwa kawaida huwa nazungumza mambo ambayo nina uhakika nayo.

MHE. RICHARD M. NDASSA: Taarifa.

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba unilindie muda wangu.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, taarifa inabidi akishachangia mtu akishapewa taarifa aipokee kwanza ile taarifa aanze kuzungumza ndiyo anapewa taarifa nyingine. Mheshimiwa Ndassa.

T A A R I F A

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kwa sababu muda wangu ni mchache sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilichokuwa nazungumza hapa ni kwamba sekta ya gesi na mafuta ni muhimu sana, haziwezi kuitwa ni sekta ndogo. Naamini kama kweli kwa sababu taarifa ya Kamati imezungumza hapa kwamba Serikali ina mpango wa kuongeza megawatts za umeme na mipango ya Serikali inasema ikifika 2020 basi tuweze kuwa na MW 5,000 lakini taarifa ya Kamati inasema mpaka 2020 tutakuwa na megawatts zisizozidi 2,780. Kwa hiyo, naishauri Serikali kwa sababu tuna sekta ya gesi Mikoa ya Kusini, mpango ule wa kujenga zile plant za Lindi, kuendeleza zile plant za Mtwara, tujenge plant ya umeme Kanda ya Kusini ili tuweze kuziongeza hizi megawatts Taifa hili liweze kuondokana na tatizo hili la umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mipango ya Serikali ya kujenga Stigler’s Gorge, ni mipango mizuri kwa sababu lazima kama Taifa kuwe na miradi ya kielelezo lakini bado ikifika 2020 hatutakuwa na megawatts zile ambazo tunazihitaji. Kwa hiyo, kwa kuwa miradi ya gesi iko tayari maeneo ya Kusini, Serikali ijenga plant za umeme kwa kutumia hii gesi yetu ambayo Mwenyezi Mungu ametubariki. Bahati njema kwamba Mikoa ya Kusini hivi sasa tayari Serikali imeshaiunganisha katika gridi ya Taifa. Tukijenga plant Mtwara na Lindi tutaweza kusafirisha umeme mwingi tukaingiza katika gridi yetu ya Taifa na tukaondokana na tatizo hili la kukosa umeme wa uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine naomba nizungumzie…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la utawala bora ni pamoja na Serikali kushirikisha wananchi. Nchi hii ina mfumo wa ushiriki wa wananchi kupitia wawakilishi wanaochaguliwa na wananchi wenyewe. Wawakilishi hao ni Wenyeviti wa Mitaa, Madiwani, Wabunge pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano na Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kushangaza sana kumekuwepo na mpango wa makusudi wa kuzuia wawakilishi kufikisha kero za wananchi pale viongozi wa Kitaifa wanapotembelea maeneo yetu, kwa mfano Mtwara Mjini, Novemba 6 mwaka jana, mwaka 2018, tulizindua Mji Mkongwe wa Mikindani ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Hasunga, lakini jambo la kushangaza Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara alikataa mimi Mbunge wa Jimbo kusalimia wananchi katika mkutano nilioshiriki kwa kiasi kikubwa kuwaomba wana Mtwara Mjini kushiriki uzinduzi huo, hali iliyosababisha wananchi wengi kuchukia sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilipomuuliza Mkuu wa Mkoa kwa nini hanipi nafasi, alisema kwa mdomo wake kuwa, hivyo ndivyo tulivyopanga kama hujaridhika fanya unavyojua wewe. Kama Mbunge niliumia na kauli ya Mkuu wa Mkoa kwani alitaka mimi nibishane naye ili apate kick ya cheo chake. Niliamua kukaa kimya nikafikisha kwenye kikao na Mheshimiwa Waziri akasema kweli haikuwa sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 2 Aprili, 2019 Mheshimiwa Rais alikuja Mtwara Mjini kufungua miradi kadhaa, siku mbili kabla tulipewa ratiba ya ziara hiyo. Tukiwa kwenye uwanja wa mkutano, Airport Mtwara, nilimuuliza Mkuu wa Mkoa kuhusu utaratibu wa Mbunge wa Jimbo ambaye ni mwenyeji kuhusu ukaaji, kusalimia na kumpokea Mheshimiwa Rais pale aliposhuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitika kusema kuwa, Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya na baadhi ya Wabunge wa chama tawala walikataa mimi Mbunge mwenyeji:-

(a) Walinizuia kwenda kumpokea Mheshimiwa Rais badala yake wakawekwa watu wa CCM na yeye mwenyewe Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya tu wakati mimi ni Mbunge mwenyeji;

(b) Mkuu wa Mkoa wa Mtwara akanizuia hata kukaa viti vya nyuma ya Rais, kama Mbunge mwenyeji, wakasema huruhusiwi kukaa huku hata kama ni Mbunge, viongozi wa CCM wamepewa nafasi; na

(c) Mkuu wa Mkoa akanizuia hata kusalimia wananchi wangu na kumkaribisha Mheshimiwa Rais, kama Mbunge mwenyeji. Mbaya zaidi nilipouliza kwa nini mnamzuia Mbunge aliyechaguliwa na wananchi wengi, wakaniambia ungekuwa CCM ungepewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaomba kujua utawala bora tunaozungumza ni wa aina gani? Kwani huyu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara na DC wa Wilaya ya Mtwara hawajui kama nchi hii ni ya vyama vingi na Mbunge wa Jimbo ni kiongozi halali kikatiba? Naomba kujua kwa nini umlazimishe mtu kuhama chama?

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini nimeamua kufanya siasa safi kwa kuwa, nataka amani na utulivu Mtwara Mjini na Kusini kwa ujumla. Haya yanayofanywa na Mkuu wa Mkoa na DC kwa utashi wake noamba yakomeshwe mara moja maana nguvu ya Mbunge wa Mtwara Mjini kwa wananchi ni kubwa sana, nddio maana nikifanya mikutano Wananchi wananiitika sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata kama humuhitaji Mbunge wa CUF, lakini ndio kawekwa na wananchi wa Mtwara Mjini, lazima apewe heshima na haki yake kama mimi ninavyowaheshimu RC, DC na Wabunge wote wa CCM nawaheshimu sana. Naomba tuendelee kutunza heshima hii na amani ya Mtwara kwa kuheshimiana, kama wote viongozi wa wananchi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Ahsante Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema nami niweze kuchangia Wizara hii ya Uchukuzi na Mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuanza tu kwanza niseme kwa moyo wa dhati kabisa kwamba miundombinu ni jambo ambalo nchi za wenzetu, nchi zote za Ulaya na kule Marekani watumwa walipelekwa nchi hizi kwa ajili ya kwenda kujenga miundombinu. Leo hii nchi za Ulaya na Amerika zimeweza kuendelea kwa sababu ya miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nieleze kwamba kwa kasi hii ambayo tunaiona ya ujenzi wa miundombinu Tanzania, Wizara hii imefanya kazi kubwa sana. Jambo la kipekee ambalo naweza kuzungumza pamoja na kwamba kuna miradi mingi sana sasa hivi imeanzishwa katika baadhi ya maeneo ya nchi yetu na ni imani yangu kwamba baada ya miaka 10, 15 Tanzania tutafikia ule uchumi wa kati 2025 na kuendelea huko kama kasi ya miundombinu itaenda hivi hivi kama ilivyo hivi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala ambalo wenzangu wamezungumza na hasa taarifa ya Kamati imezungumzia kwa kina sana kwamba ili tuweze kuendelea hivi sasa na hata nchi za wenzetu kama nilivyotangulia kusema waliwekeza kwenye miundombinu na hasa miundombinu ya reli. Kwa muda mrefu imekuwa ikizungumzwa takriban miaka mitatu hivi sasa kila mwaka katika vitabu vya bajeti inatajwa Reli ya Kati (Standard Gauge) ambayo hii inajengwa lakini Reli ya Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Kusini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Reli ya Kanda ya Kusini ni muhimu sana kiuchumi kwa sababu reli hii itaanzia Mtwara Mjini kuelekea Mchuchuma na Liganga ambako kuna makaa ya mawe na chuma. Hii reli kwa taarifa tulizokuwa nazo mpaka hivi sasa kwa sababu Serikali imejipanga kwenda kujenga kwa kutumia mfumo wa PPP (Public Private Partnership) na kuna wawekezaji wengi wameamua kujitokeza kuwekeza kwenye hii reli, mimi niishauri Serikali isiwe na kigugumizi cha ujenzi wa hii reli kwa sababu economic viability yake ni kubwa sana kuliko reli zote Tanzania. Tunaomba Serikali itenge fedha za kutosha isiwe kila mwaka tunaelezwa kwamba upembuzi yakinifu umekamilika, pesa tunaenda kuzitoa sijui wapi, wapewe hawa wawekezaji ambao wako tayari kuwekeza katika hii Reli ya Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, reli hii ikijengwa maana yake tunaenda kufufua ule mpango unaoitwa Southern Development Corridor yaani Maendeleo ya ule Ukanda wa Kusini. Tunaamini reli hii ikiisha kutokea Bandari ya Mtwara Mjini tutaenda kufufua uchumi na hata nchi zote za Ukanda wa Kusini watatumia reli hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana kwa sababu Serikali imeweka kwenye mpango kwa muda mrefu kazi iliyobaki ni kutekeleza. Tunahitaji Reli ya Kusini na hata taarifa ya Kamati imeeleza kwa kina sana kwamba reli hii inaenda kuleta uchumi mkubwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wananchi waweze kuondokana na umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo naomba kuzungumza ni suala hili la usafiri katika bahari zetu. Serikali imekuwa na kizungumkuti, siku zote Serikali haiwekezi kwenye uwekezaji wa meli katika Bahari ya Hindi.

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka ya nyuma wakati si tunakua, sisi tunaishi kule Pwani Mtwara, tulikuwa tunatumia sana usafiri wa meli kutoka Mtwara kuelekea Dar es Salaam na maeneo mengine mpaka kule Zanzibar. Kama kweli tunahitaji kufufua uchumi wa Tanzania tusiwekeze kwenye kujenga tu barabara hizi tununue meli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tunazungumzia uwekezaji, kuna ile taasisi ya Serikali inaitwa Marine Service ambayo inajenga meli katika Maziwa Makuu. Neno marine maana yake ni bahari, kwa hiyo, nashauri sana Serikali inunue meli kwa ajili ya kusafirisha cement kutoka pale Mtwara, Mheshimiwa Dangote anatumia magari kusafirisha kwa njia ya barabara ya Kilwa na inaharibika sana. Kama Serikali ingenunua meli au ingewekeza kwenye meli usafiri wa meli ni rahisi kuliko usafiri wowote duniani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kule hakuna kutengeneza barabara, maji Mwenyezi Mungu kayaweka, kazi ya Serikali ni kusafirisha tu. Kwa hiyo, cheapest transport duniani ni usafiri wa meli, kwamba Serikali ikiwekeza kwenye meli tunaamini kabisa barabara zetu za Ukanda ule wa Kusini hazitaharibika kwa malori makubwa makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine naomba sana Mtwara Mjini baadhi ya maeneo hakuna mawasiliano ya simu. Nimekuwa nazungumza kwa muda mrefu na nilimwandikia Naibu Waziri, Mheshimiwa Nditiye ananisikia, nilimweleza kwamba kuna maeneo ya Mtwara Mjini ambapo hakuna mawasiliano ya simu yaani ukifika kule mawasiliano hakuna. Maeneo kama ya Mkunja Nguo, Naulongo, Mkandala, Dimbuzi na Mwenge mawasiliano ya simu kule hayapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilimwambia Mheshimiwa Nditiye kwamba tunahitaji awekeze ili watu wa Mtwara waweze kupata mawasiliano ya simu kwenye maeneo haya. Baadhi ya maeneo ya pembezoni ya Mtwara Mjini tunahitaji minara ya simu ili wananchi waweze kuwasiliana.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, tunahitaji hizi ndege ambazo Serikali imeamua kununua za ATC zifike Mtwara. Taarifa tunazoambiwa kwamba Mtwara hakuna abiria si kweli, Precision kila siku asubuhi wanakuja Mtwara na kurudi na wanajaza iweje leo ATC wanatuambia kwamba eti Mtwara hakuna abiria. Sisi tunahitaji hizi ndege kwa sababu ni za bei nafuu, kazi yake ni kutoa huduma kwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wana- Mtwara tunahitaji ndege hizi tuweze kuzipanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni ucheleweshaji wa miradi. Ni kweli kuna kasi kubwa ya uanzishwaji wa miradi ya barabara lakini wakandarasi wanacheleweshwa sana kupewa fedha zao. Kwa mfano, barabara ile ya uchumi ambayo inaanzia pale Mtwara Mjini – Mnivata - Tandahimba mwaka huu nimeona kwenye kitabu hapa kwamba zimeongezwa kilomita zingine 50 lakini hiyo kilometa 50 kutoka Mtwara Mjini - Mnivata zinasuasua sana kwa sababu yule mkandarasi hapati pesa kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri, alikuwa anafanya kazi kubwa sana akiwa kwenye Wizara ya Maji Mheshimiwa Nditiye, Mheshimiwa Kwandikwa rafiki yangu kabisa na amekitembelea kipande kile cha kutoka Mtwara Mjini – Mnivata mkandarasi anasuasua fedha hapati kwa wakati. Naomba mumpe fedha kile kipande cha barabara kiweze kuisha na kipande kuanzia Mnivata - Tandahimba na maeneo mengine yale tunaomba mwaka huu fedha zitoke kwa wakati yule mkandarasi aweze kumaliza ili na sisi barabara hii tuweze kuitumia. Hii barabara ndiyo chanzo kikuu cha uchumi, korosho zote zinapita kwenye barabara hii kutokea Tandahimba - Mtwara Mjini pale bandarini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara nyingine ni barabara ya ulinzi ambayo nimekuwa naizungumzia kwa muda mrefu ambayo inaanzia Mtwara Mjini – Tangazo – Mahurunga – Kitaya - Kiromba na ukanda ule wote mpaka Mozambique. Barabara hii ni muhimu sana kwa sababu ndiyo chanzo cha ulinzi wa Ukanda ule wa Kusini naomba nayo ipewe kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nianze kwa kuwapongeza Wenyeviti wakamati zote mbili kwa mawasilisho mazuri ambayo wameyaleta leo hii. Nitachangia Kamati zote mbili kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, ni suala hili la makampuni ya simu. Makampuni ya simu yamekuwa yakiwaibia Watanzania kwa kiasi kikubwa sana, leo ukiamua kuweka bando lako kwa mfano kwenye simu kwa mfano TIGO, au AIRTEL au VODA ukajiunga bando la wiki moja baada ya dakika tano au 10 au 20 wakati mwingine unatumiwa meseji kwamba bando lako limekwisha, huu ni wizi mkubwa sana ambao unafanywa na makampuni ya simu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali kwamba ihakikishe ya kwamba makampuni ya simu yanafuatiliwa kwa karibu sana kwa sababu yamekuwa yanatuibia Watanzania, yameachwa hovyo wafanye wanavyotaka. Ukiwauliza wanakwamba vigezo na masharti kuzingatiwa hali ya kuwa bando lako haujatumia hata siku tatu bando la wiki linaisha ndani ya masaa 24, wanakwambia ujiunge tena, wizi huu unafanywa na makamouni ya simu. Serikali kama haipo vile Tanzania tunaomba sana kwa sababu Watanzania wengi ni maskini sana, Watanzania anavyochukua Sh.500 yake akaamua kujiunga bando atumie siku halafu anatumia dakika mbili tatu anaambiwa bando lako limeisha, hakuna ufuatiliaji wowote unaofanyika na Serikali. Tunaomba Serikali ihakikishe kwamba inafanya ufuatiliaji wa karibu. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. JACQULINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mchangiaji anayechangia sasa kwamba ni kweli kabisa anavyosema kwamba haya mashirika ya mawasiliano yamekuwa ni tatizo kubwa kosa mfano shirika la mawasiliano la VODACOM. Mimi nataka nitoe ushuhuda ni jana tu usiku nimenunua kifurushi nikapiga simu nilipopiga simu nikaambiwa kwamba namba unayopiga kwa sasa haipatikani…

MWENYEKITI: Taarifa gani unataka kumpa?

MHE. JACQULINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikazima hiyo simu nikalala asubuhi nachukua simu yangu…

MWENYEKITI: Mheshimiwa…

MHE. JACQULINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naongezea nafafanua

MWENYEKITI: Hapana naomba ukae chini. Mheshimiwa usijibu endelea kuchangia.

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na nakubaliana kabisa na mawazo ya Mheshimiwa Ngonyani kwamba ni kweli kabisa napokea taarifa yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mashirika haya kama ikiwezekana sisi kama Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi ni lazima tuweke utaratibu ikiwezekana kwa sababu kwa kuwa wizi ni dhambi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wizi haufai na ni kosa la jinai, ikiwezekana tuyachukulie hatua mashirika haya Waheshimiwa Wabunge ikiwezekana tuende mahakamani kuyashtaki mashirika haya ya simu kwa kuwaibia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu nyingine ni suala la barabara. Sasa hivi Tanzania kwa kiasi kikubwa miundombinu inajengwa barabara nyingi zinajengwa lakini tatizo la barabara hizi zinazojengwa zinachukua muda mrefu sana kumalizika. Sasa tatizo ni nini tunaomba Serikali itueleze kwa nini barabara nyingi ambazo ni muhimu zimeanzishwa kujengwa Tanzania, lakini barabara ambayo inapaswa ikamilike kwa mwaka mmoja au kwa miezi sita au miaka miwili inachukua miaka minne mpaka miaka mitano barabara hazikamiliki. Kwa hiyo, niiombe Serikali kwamba fedha ambazo zinakusanywa kwa ajili ya barabara zipelekwe kwa wakati kwa wale wakandarasi ambao wamepewa kujenga hizi barabara ili barabara ziweze kukamilika kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano barabara ya Uchumi kule Kusini ambayo inaanzia Mtwara Mijini inafika Tandahimba, Newala mpaka Masasi muda wake umemalizika sasa hivi ni zaidi ya miaka miwili ile barabara haiajakamilika. Ukiwauliza hawa wakandarasi wanasema fedha wanachelewa kupelekewa, waki- raise kitu kinachoitwa certificate wakipeleka Wizarani kwa wahusika, wanachelewa kupata fedha zao ili waweze kuendelea na ule ujenzi. Tunaomba sana barabara hizi kwa sababu Serikali imeamua kujenga barabara, zikamilike kwa wakati, wakandarasi, wazabuni wapewe fedha zao kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilizungumza hapa ndani ya Bunge hili kwamba kuna barabara muhimu sana ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambazo Serikali ni lazima izijenge barabara hizi zikiwemo barabara zile za mipakani. Leo hii mpaka wa Kusini kuna barabara ya Ulinzi ambayo inazunguka Mkoa mzima wa Mtwara inafika Mkoa wa Lindi mpaka Mkoa wa Ruvuma, barabara ambayo ilitumika wakati ule wa kulinda wale ambao walikuwa ni wavamizi wanaotoka Msumbiji, wale Makaburu leo hii ile barabara imesahaulika sana. Tumekuwa tunazungumza ndani ya Bunge hili kwamba barabara za ulinzi ni barabara muhimu sana kwa ulinzi wa Taifa letu hili. Barabara inayotoka Mtwara kuelekea Mikoa hii ya Kusini yote hii inayozunguka Mto Ruvuma, tunataka Serikali kwa kuwa imehaidi ndani ya Bunge hili kwa muda mrefu kwamba itakuja kujenga barabara hii, tunaomba itekelezwe hii ahadi, barabara ile ijengwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara pia ambayo inatoka Dar es Salaam kuelekea Mikoa ya Kusini ni barabara ambayo miaka ya karibuni iliweza kujengwa na Serikali lakini barabara ambayo kutokana na maroli yanayosafirisha cement kutoka Kiwanda cha Dangote kuja Dar es Salaam kwenye soko kuu ile barabara inaharibika sana na inachukua muda mrefu sana kurekebishwa. Barabara ya Kibiti – Lindi, ni barabara ambayo Serikali inarekebisha lakini kwa utaratibu sana, maeneo mengi imebomoka. Tunachoitaka Serikali tuliwahi kuzungumza hapa hivi sasa Serikali imejikita kujenga meli kule kwenye Maziwa Makuu kupitia ile Taasisi za Serikali Marine Service, tunaomba Serikali itanue wigo itengeneze meli ziweze kutumika kwenye bahari ya Hindi kwa ajili ya kusafirishia mizigo ya cement kutoka Mtwara kuelekea Dar es Salaam na kwingineko duniani. Tunavyoendelea kutumia barabara moja barabara ya Kibiti - Lindi barabara inaharibika sana na Serikali inatumia fedha nyingi sana kurekebisha na kuweka viraka viraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Mwenyezi Mungu ametubariki Tanzania tuna Bahari ya Hindi na bahari yenyewe ina kina kirefu kuanzia pale Bandari ya Mtwara, Serikali neno Marine maana yake ni bahari lakini leo hii imejikita kujenga meli katika Maziwa Makuu kana kwamba sisi hatuna bahari hapa Tanzania. Kwa hiyo niiombe Serikali kwamba iweke mpango wa makusudi kabisa wa kununua meli mbalimbali ambazo zitasafirisha mizigo ya cement na mizigo mingine kutoka Ukanda ule wa Kusini kuja Dar es Salaam na kuelekea duniani mpaka huko Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili Bandari ya Mtwara imekuwa inarekebishwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nawapongeza Wenyeviti wa Kamati kwa mawasilisho mazuri, lakini pia nawapongeza baadhi ya Waheshimiwa Mawaziri wanaoshughulika na hizi Kamati za Kisekta.

Mheshimiwa Spika, nitazungumza kwa haraka haraka kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza, nitajikita sana kwenye Sekta hii ya Utalii. Kumekuwa na mpango wa kuboresha utalii Tanzania nzima na hasa ukanda ule wa Kusini; na Serikali imejikita kwenye kukopa fedha Benki ya Dunia. Hizi fedha tumekuwa tunazungumza kwa muda mrefu ndani ya Bunge hili, huu ni mwaka wa tatu hivi sasa, zililetwa fedha za regrow kwa ajili ya kukuza utalii maeneo ya Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hizi fedha mpaka leo hazieleweki kwamba zinapelekwa wapi? Taarifa zinaeleza kwamba wanapeleka mikoa ya kule Iringa na Mkoa wa Morogoro. Wameacha mikoa ya Kusini halisi ambayo ni Mtwara na Lindi. Kwa hiyo, tunaomba Wenyeviti watakapokuja kuhitimisha hizi hoja, hili suala watueleze kinagaubaga kwamba kwa nini mkakati wa fedha za regrow ambazo ni fedha za mkopo wa Serikali na kazi yake ni kuboresha utalii Southern Circuit, tukimaanisha Mikoa ya Kusini ambayo ni Mtwara na Lindi kwa kiasi kikubwa, bado hakuna mpango wa kuboresha miundombinu ya barabara kule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo barabara ya Selous kule kutoka Nachingwea kuelekea Liwale na mvua hizi, haipitiki kabisa, lakini hizi fedha zipo, Waziri anashindwa kuzileta kwa ajili ya kuboresha miundombinu ile ili watalii waweze kupita kuanzia pale Lindi Nachingwea mpaka kule Liwale. Hizo ni fedha za regrow ambazo ni mkopo wa kuboresha miundombinu ya mikoa ya kusini katika Sekta ya Utalii, tunaomba zifike Mtwara na Lindi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, kuna suala hili la utalii wa mambo kale tunaona kama limesahaulika hivi. Pale Mikindani tuna majengo ya mambo kale kule Mtwara ambayo hayapo Tanzania yote hii, yapo Mikoa ya Mtwara hasa hasa Mikindani, Mtwara na Lindi. Pia kuna ule ufukwe wa bahari ambao unaanzia kule Msimbati mpaka kule Kilwa Kisiwani. Tunaomba Serikali itupe mpango maalum wa kuuboresha na kutangaza yale maeneo ili tuweze kuleta watalii wengi kwa ajili ya kuliingizia Taifa hili Pato.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, tuna taasisi ile inaitwa TAWA ambayo iko affiliated katika Wizara. Tulikuwa tunaomba sana, wakati fulani tuliwasikia kwenye Kamati yetu ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma wakaeleza changamoto zao ni nyingi sana, lakini changamoto kubwa ni kwamba ile Taasisi ya TAWA ambayo imepewa mamlaka ya kuweza kutangaza vivutio mbalimbali vya maeneo ya Pwani, kwa mfano ule Kilwa Kisiwani, yale majengo ya kale tunaomba ipewe mamlaka kamili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la ajabu kwenye hii Taasisi ya TAWA, kuna wafanyakazi ambao walipewa training kwa miaka mitatu hivi sasa, wale wafanyakazi ambao walipaswa kuibeba ile Taasisi ili iweze kufanya kazi sawasawa na kuwa na mamlaka kamili, wale wafanyakazi wamehamishiwa Wizarani. Sasa sijui mkakati wa Serikali ukoje wa kuhakikisha ya kwamba TAWA inapewa meno ya kutosha, inakuwa ni taasisi ambayo imesimama yenyewe kama ilivyo Ngorongoro na TANAPA ili iweze kujitangaza na kutangaza maeneo ya kiutalii.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu TAWA imepewa maeneo ya Pwani, sisi tunaamini kwamba ingekuwa na mamlaka kamili, ingeweza kusaidia kutangaza utalii maeneo yale yote ya bahari na fukwe zote na mambo kale. Ilishawahi kusemwa hapo nyuma kwamba wanyama hawa wanaenda wanakufa, mabadiliko ya hali ya nchi, hawa wanyama watapotea, utalii utakaobaki ni utalii wa mambo kale.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali isidharau mambo kale. Tunahitaji miji hii ambayo duniani yamaingiza fedha nyingi sana. Kwa mfano, kuanzia pale Mikindani kwenda kule Kilwa Kisiwani na maeneo yote ya Zanzibar, Serikali iweze kuboresha, tuhakikishe kwamba inaboresha miji hii na inaitangaza ili tuweze kuingia fedha nyingi za utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho, tunaomba sana kwenye Sekta ile ya Uvuvi, basi tumekuwa tunazungumza kwenye Bunge hili kwa muda mrefu iweze kutengwa bahari ya uvuvi. Sasa imekuwa ni historia tu kila siku inazungumzwa kwamba ile bandari ya uvuvi haijengwi. Wizara haitengi fedha, Waziri hatengi fedha.

Mheshimiwa Spika, Tanzania tumebarikiwa, Wazungu wanasema Tanzania ina virgin sea (bahari bikira), ina samaki wengi sana, kuanzia ile strip ya Kusini kule mpaka Zanzibar, hakuna bahari ya uvuvi. Tunaomba Serikali mwaka huu ije na mkakati maalum kuweza kutenga bandari ya uvuvi ili wavuvi wetu waweze kuvua na kuwa na masoko ya uhakika.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa dakika za nyongeza. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu wataala na leo niweze kuongea machache haya kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza naomba nipate ufafanuzi kwa Waziri, Mheshimiwa Zitto kamalizia hapo kusema kwamba, kumekuwa na utaratibu wa Serikali kuchoma nyavu za wavuvi wadogowadogo na hasa maeneo ya ukanda huu wa pwani kutoka Mtwara, pale Mikindani, maeneo ya Kiyanga, lakini pia mpaka kule Kilwa, nyavu zimechomwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kufahamu hapa ni kwamba, wale waliochomewa nyavu zao, wao wanakuwa wamenunua zile nyavu madukani, naomba kujua kutoka kwenye Wizara hii, kwamba Serikali imechukua hatua gani mpaka hivi sasa, ama wanunuzi wangapi walioleta zile nyavu Tanzania wamekamatwa na wameshtakiwa na Wizara hii, badala ya kuwachomea wale wavuvi wadogowadogo ambao wanatafuta fedha kwa shida sana kupata zile fedha za kununua nyavu na mwisho wa siku wameenda kuwachomea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kujua, Mheshimiwa Waziri alipofika Kilwa, amefika Kilwa akawaita wavuvi wa Kilwa wote kwa maneno mazuri sana, akawaambia kwamba tunahitaji hivi sasa tuzungumze na nyinyi kama ndugu, kama rafiki, tunaomba nyavu zenu mzikusanye wenyewe kwa amani. Wale wavuvi wakazikusanya nyavu zao, Mheshimiwa Waziri akasema, nakwenda Dodoma, nakwenda Wizarani halafu nitarudi tena hizi nyavu tumezitunza, lakini anaondoka pale Kilwa, anafika baada ya kilomita tatu, nne, tano, anawaagiza watendaji, chomeni moto hizo nyavu, wakati aliwaahidi kwamba wazitunze! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kujua, kwa nini Mheshimiwa Waziri aliwahadaa wale wananchi akasema zile nyavu za milimita nane zitatunzwa halafu mwisho wa siku akatoka hatua mbili, tatu, akaagiza kwamba zile nyavu zichomwe moto pale Kilwa na wanachi wakawa na majonzi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba kujua, kwamba kulikuwa na hii inaitwa Operation Jodari na Operation Sangala ambayo Wizara imekuwa inafanya kwenye maziwa makuu kule lakini pia kwenye Bahari ya Hindi kutoa Mtwara mpaka kule Kilwa na maeneo mengine yote mpaka kule Tanga na Zanzibar. Naomba kujua kwa sababu mwaka jana kuna kijana aliuawa pale Mtwara Mjini Kiyanga, mtu ambaye anakwenda kutafuta samaki kwa mikono, kwa kutumia mideki, akapigwa risasi ya kisogoni! Nikazungumza ndani ya Bunge hili, anaitwa Abdillah Abdulrahman, mkazi wa Kiyanga Mtwara Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikaeleza kwamba Serikali ichukue hatua juu ya huyu mtu aliyeuawa kwa kisingizio cha Operation Jodari ambacho kinafanyika kwenye Bahari ya Hindi. Mpaka leo sijapata majibu, naomba Mheshimiwa Mpina atupe majibu, kwamba yule kijana, ile roho iliyopotea mpaka leo Serikali imechukua hatua gani, kwa sababu hatujaona tume iliyoundwa, hatujaona chochote, hata kutoa pole Mheshimiwa Waziri, hajaja Mtwara kutoa pole, hata kama mimi nimezungumza humu, zaidi ya mara tatu, mara nne, mara tano ndani ya Bunge hili. Hata nikimsemesha, hata Waziri ukimsalimia, haitikii! Yaani leo ukikutana naye hapo nje, unamsalimia kwa ajili ya kujenga mahusiano, hata kuitikia imekuwa ni shida. Sasa kwa sababu Serikali hii ni sikivu sana, Mheshimiwa Rais anasalimia watu, tunasalimiana naye, Waziri Mkuu anasalimia watu, Mawaziri wengine wanasalimia, lakini Mheshimiwa Waziri Mpina, hata tukimsalimia, mimi mwenyewe zaidi ya mara tatu nimemsalimia anakaa kimya. Sasa, Waziri kama Waziri jambo la kwanza ni kujenga mahusiano na wale ambao unawaongoza, sasa Mheshimiwa Mpina, tunaomba atupe maelezo ya kina kwamba yule kijana aliyeuawa, zimechukuliwa hatua gani mpaka leo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba kujua, kwamba pale Mtwara kuna Chuo cha Uvuvi, chuo ambacho kimekuwa kinazungumzwa kila siku na nilimweleza Mheshimiwa Naibu Waziri hapo juzi, kwamba kile chuo lini kinaanza kazi, Chuo cha Mikindani cha Uvuvi. Pale tunaona kuna madawati yamewekwa, kuna meza zimewekwa lakini hakuna walimu, mpaka leo hawajaletwa walimu, hakuna kifaa chochote, hakuna hata Boti ambayo wale wanafunzi wakidahiliwa wataweza kuzitumia kwa ajili ya kwenda kufanyia mazoezi ya kuvua pale Mikindani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naishi Mikindani hapohapo kwenye chuo, niliambiwa kwamba kimeanza, kile chuo mpaka leo nazungumza na watu wa Mtwara hakijaanza. Sasa tunasema, tunataka tuvue uvuvi wenye tija, uvuvi ambao utapelekea Watanzania kujikomboa na umaskini na sisi wananchi wetu wa Pwani wengi ni wavuvi. Wananchi wangu wa Mtwara Mjini maeneo ya Kiyanga, maeneo ya Mikindani, wote ni wavuvi, wanategemea uvuvi katika Bahari ya Hindi ili waweze kujikwamua. Tunaomba kile chuo kifanye kazi isiwe kila mwaka, tunazungumza, tunaahidi lakini utekelezaji unakuwa haupo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, naiomba sana Wizara hii, kwamba, ili tuweze kuvua uvuvi wenye tija, kama ilivyozungumza kwenye Ilani, kwenye nini, lakini pia Serikali inaahidi kila mwaka, lazima tuwe na vifaa vya kisasa vya kuvulia samaki, lazima tuwe na Boti za kisasa za kuvulia samaki. Wakati tuko Chuo Kikuu, mwaka 2008 pale, tuliweza kula samaki wengi sana, ambao Mheshimiwa Rais kipindi kile akiwa Waziri wa Wizara hii alikamata meli, wakaletwa wale samaki Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pale, tukala bure wiki nzima, kwa sababu tu wamevuliwa kitaalam, wale samaki walikuwa ni wengi. Tunaamini kwamba Serikali ikileta maboti, wananchi wetu wataweza kuvua kitaalam kuanzia Mtwara mpaka kule Kilwa, mpaka Dar es Salaam, Tanga na Zanzibar ili tuweze kuondokana na umasikini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi; nimshukuru Mwenyezi Mungu na niombe kuchangia Wizara hii kwa dakika hizo nilizozipata.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kabisa nikiri kwamba Wizara hii sasa hivi imepata majembe, tunaamini kabisa ni majembe ambao wanaweza wakafanya kazi yao sawasawa. Mheshimiwa Kigwangala kipindi umepata ajali ulikuwa kwenye mihangaiko yako hiyo ya kuhakikisha kwamba Wizara hii inakaa sawa, mwenyezi mungu akubariki sana na Mheshimiwa Naibu Waziri pia nimeshawahi kukuona Mtwara umekuja pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ya kwangu ni machache; jambo la kwanza; kwamba hiki kitabu cha hotuba ya Waziri, hii picha iliyowekwa hapa mbele ni picha ya jengo la kale lililopo mbele ya nyumba yangu pale Mtwara Mikindani. Jengo hili ni miongoni mwa majengo ambayo kimsingi yaani kama kweli Wizara ingekuwa na nia ya dhati ya kuhakikisha kwamba TTB inatangaza, inatangaza sawasawa vivutio hivi ambavyo vipo Mtwara Mikindani mimi naamini kwamba watalii wangemiminika wengi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, jengo hili ni jengo ambalo lilitumiwa na Wakoloni na wakati huo jengo hili lilitumika kama Custom, kama magereza na kama ofisi zote za Serikali; yaani ofisi ya mkoa na ofisi ya wilaya vilevile ofisi. Kila kitu kilikuwepo ndani ya jengo hili ambalo liko kwenye picha hii. Jambo ninaloomba, Wizara ihakikishe kwamba sasa hivi kwasababu; tumekuwa tunaangalia hapa picha kwenye simu jana kuna dereva mmoja kamgonga mnyama twiga; twiga ni mnyama mpole sana. Sasa kwa sababu hawa wanyama wanagongwa gongwa, na pia mazingira na hali ilivyo hivi sasa hawa wanyama wataisha kwahiyo utalii utabaki kwenye mambo kale.

Mimi niiombe Serikali iwekeze kwenye kutangaza mambo kale. Mji wa Mikindani ni mji wa kipekee sana; Mheshimiwa Ngombale ameongea hapa, Mji wa Kilwa ni mji wa kipekee sana, una majengo mengi ya kale. Kama tukiamua kutangaza sawasawa TTB kafanya kazi yake tunaamini kwamba Serikali itaongeza idadi ya watalii. Tuanze na Mji wa Mikindani mji mkongwe wa mikindani ambao uko Mtwara Mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo linguine, kuna fedha zinaitwa fedha za REGROW kazi yake ni kukuza utalii ukanda huu wa Kusini. Nilikuwa naomba kujua, nimekuwa nikizisikia fedha hizi kwa muda wa miaka minne hivi sasa. Hizi fedha zimeletwa ama zipo kwenye makaratasi tu? Kama zimeletwa kule kwetu kusini mkakati upoje? Kwa sababu kuchanganya, yaani leo hii watu wanavyosema kwamba Kusini wanazungumza Mbeya wanavyosema kusini wengine wanazungumza Morogoro. Kusini ni Mtwara na Lindi, kwamba kusini Kiserikali nchi hii ni Mtwara na Lindi. Kwahiyo tunataka Serikali kama fedha zimepatikana fedga za REGROW zije kutangaza utalii kusini Mtwara pale kwenye mji wa Mikindani, kule Kilwa Kaskazini na kule kwenye msitu ule wa Selou uliopo Lindi; tunaomba hizi fedha ziletwe kule. Isiwe inazungumzwa tu Iringa Kusini; watu wanazungumza Iringa wanazungumza Mbeya na Mtwara na Lindi mnaisahau. Kwa hiyo naomba hizi fedha za REGROW ziletwe kweli Kusini kwenyewe, kusini halisi ambako ni Mtwara na Lindi tunashida ya kutangaza vivutio vya kiutalii na kuboresha …

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: …katika mji wa Selous. Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nilikuwa naomba nizungumze kuna hizi fukwe za bahari. Kuna fukwe za bahari kule kusini kuanzia pale Mnazi Bay Mtwara ni fukwe ambazo ni za Kimataifa, Wakoloni wote walipitia kwenye fukwe ya Mnazi Bay wakajenga mahema yao pale akina Vasco Dagama, akina nani na wengine wengi sana; wakaja mpaka Mji wa Mikindani wakajenga mahema yao pale. Hizi fukwe zimesahaulika; ni fukwe nzuri kuliko fukwe zote duniani; fukwe ya Mnazi Bay ipo, Mtwara Vijijini pale na Msimbati. Nilikuwa naomba Serikali kama imeisahau hii fukwe ihakikishe ya kwamba inatangaza hii fukwe; watu wa TTB waje kuiangalia hii fukwe kwa sababu Wajerumani wameweka kwenye page zao zote duniani; kwamba miongoni mwa maeneo ambayo wamepita maeneo muhimu ya fukwe muhimu Tanzania ni fukwe ya Mnazi Bay ambayo iko Mtwara Mikindani; naomba Wizara ije kuiangalia hii fukwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nilikuwa naomba kujua; kuna suala la wauza mikaa. Wauza mikaa imekuwa ni kero sana kule Mtwara, wanakamatwa sana. Yaani mtu akishikwa na gunia moja na mkaa anapigwa sana na watu wa maliasili, ukiwauliza wanasema wanataka walipe ushuru. Sasa hawa wauza mikaa ni watu masikini kabisa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Muswada wa Sheria ya Kulitangaza Jiji la Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi wa Mwaka 2018
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu na nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi niweze kuchangia Muswada huu.

Mheshimiwa Spika, kimsingi kabisa Muswada huu ni muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa letu. Kama walivyotangulia kusema na taarifa ya Kamati imezungumza hapa kwamba nchi nyingi sana zimeweza kuhamisha Makao Makuu ya Serikali kwa sababu ya mambo mbalimbali na sisi Tanzania base yetu ni pale Mwalimu Nyerere alivyo-declare kwamba angeona na angetamani kwamba Makao Makuu yahamie Dodoma ambako ni katikati ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa kuna mambo mawili, nilikuwa nasikiliza Wabunge wenzangu hapa, nimeona majibu ya upande wa Serikali wakati mwingine kuna kujichanganya kidogo. Kwenye preamble ukisoma kipengele cha mwisho kinaeleza kwamba:-

“WHEREAS on the 26th April, 2018 His Excellency JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, the President of United Republic of Tanzania officially declared Dodoma to become the City to become developed and administered by the Dodoma City Council”.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, jambo la kwanza hapa ni Dodoma kutangwaza kuwa Jiji na ilitangazwa na Mheshimiwa Rais tarehe 26 Aprili, 2018 pale Uwanja wa Jamhuri. Alitangaza kwamba Dodoma sasa ni City kwa mamlaka aliyopewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili inasema, naomba kunukuu:-

“AND WHEREAS consequent to the declaration of the City of Dodoma by His Excellency JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, the President of the United Republic of Tanzania, the Government has determined to establish and develop the City of Dodoma as the Capital City of the United Republic of Tanzania”. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hapa kuna mambo mawili, kuna suala la kutangazwa Mji huu wa Dodoma kuwa Jiji na kuna suala la kuhamia Makao Makuu ya Serikali. Kwa hiyo, hatuwezi kukwepa kuzungumzia vinasaba mbalimbali vinavyofanya Makao Makuu ya Serikali kama Jiji viweze kutekelezwa sawasawa na kweli dunia iweze kufahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na kutangazwa kuwa Jiji na Makao Makuu ya Serikali na kama nilivyosema kwamba, naunga mkono hii hoja kwa sababu ya mambo kadhaa. Jambo la kwanza tunafanya decentralization of economy kwa sababu pale Dar es Salaam pamekuwa na maendeleo makubwa kwa sababu Ofisi zote za Serikai zilikuwa pale Dar es Salam. Pia kulikuwa na suala la msongamano mkubwa sana wa magari Dar es Salam, leo hii tunavyoleta huu Muswada na kuunda hii sheria, mimi naamini kwamba sasa msongamano ule wa Dar es Salaam ambako Ofisi zote za Serikali, magari ya wafanyakazi na watumishi wa Serikali yalikuwa yako pale Dar es Salaam sasa hivi yatakuwa Dodoma, tutapunguza msongamano pale Dar es Salam, ni jambo jema sana.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine naomba nizungumze kidogo kwamba tunavyokwenda sasa kuhamia hapa Dodoma rasmi na kwamba tayari imeshatangwaza kuwa ni Jiji kama nilivyosema na kama taarifa hii ilivyoeleza basi tuboreshe miundombinu ya Dodoma. Leo hii ukitembea hapa hapa Dodoma mitaa hii ya Medeli East, Chaduru na sisi kwa sababu Wabunge ni wakazi wa Dodoma kwa muda wa miezi saba kwa mwaka, tunaifahamu hii Dodoma, kwa hiyo, tunaomba Serikali sasa sambamba na kuleta huu Muswada waboreshe miundombinu ya Dodoma. Maeneo ya Chaduru mvua zikinyesha yaani mtu hapiti, gari yake haifiki kule mtaani ni katikati ya mji kabisa. Pia ukija kwenye maeneo yale mengine maeneo ya hapa chini kidogo tu; Waheshimiwa Wabunge wakati ule wa masika gari zao wanaacha karibu mita 200 then wanatembea kwenye maji wanaenda majumbani kwao; ni hapa hapa chini tu hapa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sana kwamba hii sheria ikipita tuboreshe miundombinu ya Dodoma kwa sababu kuna wageni wengi sana. Mimi naamini kwamba sasa Makao Makuu ya Serikali yanavyohamia hapa Dodoma sasa hata Mabalozi wote watahamia Dodoma, ni imani yangu hiyo. Nilishasikia humu ndani ya Bunge kwamba wametengewa maeneo ya kujenga Ofisi za Kibalozi, kwa hiyo, tunaamini kwamba kutakuwa na wageni wengi sana. Kwa hiyo, miundombinu yetu sasa ioneshe kwamba kweli ni Jiji lakini Dodoma ni Makao Makuu ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine naomba nichangie kidogo ni suala hili la Wagogo wanaoishi Dodoma hapa. Wakazi wengi wa Mji wa Dodoma ni Wagogo lakini hawa Wagogo wakati mwingine wamekuwa, sijui nitumie lugha gani hapa kuzungumza, wanavyopita barabarani, wewe ukiwa unaendesha gari, Wagogo wanataka kukatiza kwenye zile zebra, wanatembea kama hawataki. Sasa hili ni jambo la hatari sana kwamba hawa Wagogo kwa sababu tunahamishia Makao Makuu ya Serikali hapa Dodoma wapewe elimu. (Kicheko)

Mheshmiwa Spika, ahsante. Nilikuwa nazungumza hili maana nina ushahidi sana. Tunaendesha gari sisi Wabunge tukiwa hapa, ukikaribia zile zebra, watu wanakatiza pale zebra wanatembea kama wanaingia ndani. Sasa haina maana kwamba kwa sababu ni zebra basi watu watembee kilonyalonya. Inapofika
kwamba Dodoma inakuwa Makao Makuu ya Serikali, Serikali itoe elimu kwa Wagogo kwamba wahakikishe wanakimbia wanavyokatiza maeneo ya zebra. Pia kwa mujibu wa Sheria za Usalama Barabarani zebra mwisho 12 ikifika usiku watu wanatakiwa wakimbie zebra ili kuepuka kugongwagongwa ovyo.

Mheshimiwa Spika, wapo pia waendesha baiskeli hawajali magari, watembea kwa miguu hawajali magari, tunaomba sana Wizara inayohusika, kwa sababu sasa hivi Dodoma ni Makao Makuu ya Serikali basi elimu iweze kutolewa hawa Wagogo ili wasiweze kugongwagongwa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ambalo nilikuwa naomba kumalizia katika kuchangia Muswada huu, kwa sababu Dodoma sasa itakuwa Makao Makuu ya Serikali lakini pia ni Jiji basi tunaomba Idara ile ya Ardhi pale City Council kama Muswada huu unavyosema ichangamke, kwa sababu hawachangamki. Ukipeleka kupitisha ramani kutaka kujenga nyumba kunakuwa na mlolongo mkubwa na urasimu mkubwa. Mimi naamini ni kwa sababu tu pia hata watendaji wenyewe wale wa Idara ile ya Ardhi na Mipango Miji Dodoma wako wachache, waongezewe kwa sababu sasa wajenzi watakuwa ni wengi Mji wa Dodoma na watu wanahitaji kujenga Dodoma, watu wanahitaji kupitisha ramani zao basi kuwe na kuchangamka, waweze kuongezewa vitendea kazi na personnel iweze kuongezeka ili sasa mambo yaende sawasawa kama ilivyokuwa Mji wa Dar es Salam ambako Serikali inahama kuhamia Dodoma.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi.