Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Omary Tebweta Mgumba (30 total)

MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini napata mashaka na majibu yake, kwa sababu hivyo vikao vyote vya ushauri vya DCC na RCC vimeshafanyika na nina uhakika kabisa Serikali hii ina taarifa ya maombi ya watu wa Morogoro Vijijini kuhamia kule Mvuha.
(a) Mheshimiwa Spika, swali langu ni kwamba kwa sababu mchakato huu ulianza tangu mwaka 2009 wakati huo Mbunge akiwa Mheshimiwa Hamza Mwenegoha na Serikali hii imeshaleta shilingi milioni 500 kwa ajili ya maandalizi ya kuhamia Mvuha; hizo hela zimetumika kwa ajili ya udongo na kupima viwanja. Sasa leo Serikali inapokuja kusema haina taarifa, napata mshangao kidogo.
Mheshimiwa Spika, swali langu, sipendi kuidhalilisha Serikali yangu, namwomba Mheshimiwa Waziri arudi akatafute majibu sahihi ili aniletee kwa ajili ya maendeleo ya watu wa Morogoro Vijijini.
(b) Ni lini Serikali italeta majibu hayo sahihi ili tuweze kuwapelekea watu wa Morogoro Vijijini?
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE - WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAMISEMI): Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri yaliyotolewa na Naibu Waziri, Mheshimiwa Jafo, naomba kujibu swali ambalo hakupenda lijibiwe la Mheshimiwa Mgumba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli wanaweza wakawa wamefanya huo mchakato wote; lakini kama wameufanya na ukawa na dosari kama hizi zilizoelezwa kwa vigezo hivi, haukuweza kupita na kufika katika hatua zilizofuata. Nafahamu walikwama wapi, ndio maana hakijaanza kitu chochote.
Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kumwagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro waanzie pale walipoishia ili watuletee kwa sababu walipokwamia nafahamu siyo mahali pagumu sana. Wakirekebisha yale ya kwao, watuletee sisi tuone ili tuendelee na hatua zinazofuata. (Makofi)
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa, matatizo yaliyopo Nzega yanafanana kabisa na Halmashauri ya Morogoro hatuna high school hata moja katika Halmashauri yetu ya Morogoro Vijijini.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutusaidia ambao ukizingatia juhudi za wananchi tumejitahidi tumejenga ile Sekondari ya Nelson Mandela. Je, Serikali ina mpango gani wa kutuongezea nguvu ili kuimalizie shule ile angalau Halmashauri hii iwe na shule hata moja ya sekondari?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nilifika kwa Mheshimiwa Mbunge, ukitoka pale Morogoro Mjini pale kwa mfano unatoka Ngerengere pale, ukienda mpaka kule mwisho unaenda Kidunda halafu mpaka kule mbali zaidi wananchi wanapata shida.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mtoto akitoka pale maana yake changamoto yake ni kubwa. Ni vizuri zaidi tungepata shule moja ya form five pale, kwa hiyo naomba nikuambie kwa mwaka huu kwa sababu bajeti imeshapita, imani yangu ni kwamba kwa mwaka wa fedha unaokuja 2017/2018 anzeni kuweka maoteo ya bajeti zenu katika Halmashauri, then na sisi huko Ofisi ya Rais TAMISEMI tutaona hicho ni kipaumbele kikubwa ili eneo lile sasa la Mandela tuweze kupata shule ya form five na form six angalau tupate high school moja katika maeneo hayo na Wizara ya Elimu ikija ikiona kwamba, vigezo vimefikiwa basi shule ile itapandishwa kuwa ya form five na form six.
Mheshimiwa Mbunge, naomba nikupongeze kwa juhudi kubwa tutashirikiana kwa pamoja, naomba lianze hilo wazo kwenu then Ofisi ya Rais TAMISEMI katika mchakato wa bajeti itaona siyo mbaya sasa kuipa kipaumbele eneo hili kupata shule ya form five na form six kwa ajili ya vijana wetu.
MHE. OMAR T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa matatizo yaliyoko Tabora Kaskazini ya kukosa soko la tumbaku na bei zake kushuka yanafanana kabisa na matatizo yaliyopo katika jimbo langu la Morogoro Kusini Mashariki hususan katika zao la bei ya ufuta, ukizingatia kwa mfano mwaka jana bei ya ufuta ilifika mpaka shilingi 2500 mpaka 3000 lakini mwaka huu 1500, 1600 mpaka 2000. Na kwa kuwa mazao haya yanategemea soko la dunia na soko la dunia kila siku bei zinashuka kama alivyosema Mheshimiwa Waziri katika jibu lake la msingi kwenye tumbaku na mazao mengine. Je, Serikali ina mpango mkakati gani wa kuwafidia wakulima kwa kutoa ruzuku hasa pale bei zinaposhuka katika soko la dunia ndogo kulinganisha na gharama za uzalishaji wa mazao hayo hususan ufuta katika vijiji vyangu na jimbo langu na Tanzania kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba zao la ufuta nalo lina changamoto zinazofanana na ile ya tumbaku pamoja na kwamba kuna baadhi ya maeneo tunafahamu ambayo zao la ufuta ni kama sasa ndiyo tegemeo. Tutajaribu kuangalia ni nini hasa kinatokea katika wakulima wa ufuta Morogoro Kusini ili tuweze kuangalia namna ya kuwasaidia wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali haijaweza kuja na mkakati wa kufidia wakulima pale soko la dunia la ufuta linapotetereka lakini tumekuwa tukiangalia uwezekano wa kuwasaidia wananchi kuweza kupata mikopo na ndiyo maana tumeanzisha Benki ya Kilimo, lakini vilevile tuna mfuko wa pembejeo tunaamini haya yote pamoja na ruzuku tunayotoa kwenye mazao inamsaidia mkulima pale wanapopata mtikiso wa bei katika soko la dunia. Kwa hiyo, niko tayari kulichukua hili na tutaenda kulifanyia kazi.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo la ufidiaji liko pia katika Jimbo langu la Morogoro Kusini hasa kwenye Kijiji cha Kivuma. Kuna mwekezaji amekuja pale ameanza kuchimba mawe bila kulipa fidia kwa wahusika. Je, nini kauli ya Serikali kwa mwekezaji huyu ambaye hajalipa fidia kwa wahusika wenye umiliki wa ardhi wa pale Kivuma?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Omary Mgumba amesema kwamba kuna mtu ameanza kuchimba mawe katika eneo ambalo wananchi wake hawajalipwa fidia. Kwa sababu hatuhitaji kuendelea kuwa na migogoro isiyo na msingi na kama hajalipa fidia na huu ni mgogoro mpya pengine ambao umeanza siyo siku nyingi kwa sababu sina uhakika kama uko kwenye ile orodha ya migogoro, nimtake Mkurugenzi wa Halmashauri husika afike kwenye hilo eneo aweze kuangalia mgogoro uliopo na kutoa ufumbuzi wa mara moja kwa sababu ni suala ambalo linahitaji sheria ikamilike katika utekelezaji wake ndipo huyu aendelee na kazi yake ya uchimbaji. Kama hajakamilisha, basi ni lazima Mkurugenzi asimamie hilo kuhakikisha wale watu wanapata haki yao na huyu aweze kuendelea na shughuli yake.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mazao mengi ya biashara tunategemea sana soko la nje ambalo lina ushindani mkubwa kuzingatia nchi nyingi zinalima mazao hayo na wakati mwingine wakulima wanalima kutokana na mazoea. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Kitengo cha Utafiti wa Masoko hayo ili kujua mahitaji halisi ya soko la dunia kuliko kama sasa ufuta umeshuka mpaka Sh.1,500 kutoka bei ya mwaka jana ya Sh. 3,000? Nataka kujua tu Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Kitengo hicho cha Utafiti wa Masoko Ulimwenguni ili kutoa habari nchini kwa wakulima kulima mazao kutokana mahitaji ya soko badala ya kulima mazao kwa mazoea.
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mazao yetu mengi kwa sasa bado yanategemea masoko ya nchi za nje, lakini naomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba takribani kila zao kubwa la biashara linalo Bodi na hizo zina Vitengo vya Utafiti wa Masoko. Kwa hivyo, labda tu tutumie nafasi hii kuvikumbusha hivyo vitengo kwamba wanao wajibu wa kufanya huo utafiti na kufikisha habari wanayoipata kwa wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo hapa ninaloliona ni pale ambapo bodi na hivyo vitengo wanapokuwa na habari kuhusu soko kuanguka au kupanda wakaacha kufikisha habari hiyo kwa wadau wao ambao ni wakulima. Kwa hivyo, niwakumbushe tu katika bodi na taasisi hizi zinazohusika na utafiti wahakikishe kwamba hicho wanachokibaini na kukijua kuhusu masoko ya haya mazao basi kwa haraka iwezekanavyo wafikishe habari hiyo kwa wahusika kwa maana ya wakulima na wafanyabiashara wa mazao hayo.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Sheria ya Mipango Miji Namba Nane ya Mwaka 2007 inasema mashamba ya kilimo na mifugo kwa mijini na mamlaka za miji yasizidi ukubwa wa heka tatu. Ukizingatia Ngerengere sasa hivi ni mamlaka ya mji mdogo na shamba lile lina ukubwa wa zaidi ya hekta 4,562 ambazo ni sawa na heka 10,036, ambapo ni kinyume na sheria hii namba nane ya mwaka 2007. Je, Serikali haioni uwepo wa shamba hili katika Mamlaka ya Mji wa Ngerengere inakiuka sheria hii namba Nane na ukizingatia Serikali inafuta mashamba mengi sasa hivi kwa kuzingatia shabaha hii kwa wananchi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Halmashauri ya Morogoro ina ardhi kubwa nje ya Mamlaka ya Mji wa Ngerengere, je, Serikali iko tayari wakatupa ardhi hiyo kwa ajili ya maendeleo ya Mji wa Ngerengere na Serikali tukawapa ardhi nyingine kwa ajili ya kuendeleza shamba la mifugo, kwa kuzingatia Sheria ile Namba Nane ili iwe nje ya hapo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama alivyosema kwamba Sheria Namba Nane ya Mipango Miji ya mwaka 2007 pamoja na mambo mengine inakataza kuwepo na mashamba yanayozidi heka tatu ndani ya maeneo ya mji. Nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na kwamba shamba la Ngerengere mipaka yake iko karibu na mjini lakini eneo linalotumika hasa kama shamba ni mbali kidogo na mji. Pale karibu na Ngerengere eneo kubwa la shamba hilo ni makazi ya wafanyakazi, kwa hiyo shamba lenyewe liko mbali na mji, kwa hiyo haivunji hasa Sheria Namba Nane kwa sababu shughuli zenyewe za kufuga ng’ombe hazipo karibu na hapo, ziko nje kidogo ya mipaka ya Mji Mdogo wa Ngerengere.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, kwamba kwa nini Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini isifikirie kutoa ardhi mbadala? Nafikiri anachosema Mheshimiwa Mbunge kina mantiki, kwa hiyo, ni suala la taasisi husika za Kiserikali ikiwa ni pamoja na halmashauri pamoja na Wizara ya Ardhi kujadiliana na kuangalia uwezekano wa kupata ardhi nyingine ili kuliondoa shamba hili ili labda liweze kutumika kwa ajili ya matumizi mengine ya mji. Kwa hiyo, ni suala ambalo linazungumzika, nafikiri ni kitu ambacho kinaweza kikafanyika. Nimshauri Mheshimiwa kwamba mjadala huu alifuatilie na aanzishe katika mamlaka husika ili utatuzi uweze kupatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo nimweleze vile vile Mheshimiwa Mbunge kwamba mashamba ya mifugo kuwepo karibu na mijini mara nyingine inasaidia kwa sababu inawasaidia wananchi walioko karibu na maeneo yale kuweza kupata ajira, wanaweza vile vile wakapata maziwa na nyama kwa bei rahisi zaidi. Kwa hiyo, ni suala la kuangalia ni nini kinafaa katika mazingira yale.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, je, Serikali ina mpango gani kupeleka umeme kwenye huduma zingine za jamii kama vile zahanati, Vituo vya Polisi na Ofisi za Serikali ya Kijiji katika Kijiji hicho cha Lugala?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa sababu matatizo yaliyopo Malinyi yanafanana kabisa na matatizo yaliyoko katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, je, Serikali ina mpango gani kupeleka umeme katika Vijiji vya Luholole, Misala, Mmalazi, Kivuma, Ludewa na Amini kule kwenye Kata ya Kinole?
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali wa kupeleka umeme kwenye maeneo aliyoyataja hasa ya huduma za jamii uko pale pale. Kama nilivyosema mara nyingi kazi kubwa ya mradi wa REA awamu ya tatu, inakusudia kupeleka umeme kwa vipaumbele vya zahanati, shule za sekondari na shule za msingi lakini pamoja na taasisi nyingine za Serikali ikiwa ni pamoja na Magereza. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba maeneo yote ya vituo vya afya, zahanati, shule pamoja na taasisi nyingine yatapelekewa umeme wa uhakiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusiana na vijiji alivyovitaja, kama nilivyosema REA awamu ya tatu itapeleka umeme kwenye vijiji vyote ikiwa ni pamoja na vijiji vya Mheshimiwa Mbunge Omary kama alivyovitaja bila kubakiza kijiji chochote.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa matatizo yaliyopo katika Mkoa wa Lindi yanafanana kabisa na yaliyopo katika Mkoa wa Morogoro kwenye Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki hasa kwenye Kata za Maturi, Mkulazi, Seregeti na Tununguo. Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka minara katika kata hizi na Vijiji vyake vile vya Usungura, Kidunda na vinginevyo ili kuimarisha mawasiliano katika vijiji hivyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tena kuchukua fursa hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kama nilivyotoa maelezo katika jibu la swali la msingi kwamba tuna dhamira ya kuhakikisha kwamba vijiji vyote vinapata mawasiliano. Kwa hiyo, naomba kuchukua fursa hii kumhakikishia kwamba tutafuatilia kuhakikisha katika Jimbo lake na hizo kata alizozitaja, mawasiliano ya simu yanapatikana kupitia Mic, Airtel, Tigo, Vodacom, Viettel pamoja na wengine ambao wanakuja karibuni tutakapotoa tenda ya masafa ya mawasiliano.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa matatizo yaliyopo katika Mkoa wa Lindi yanafanana kabisa na yaliyopo katika Mkoa wa Morogoro kwenye Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki hasa kwenye Kata za Maturi, Mkulazi, Seregeti na Tununguo. Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka minara katika kata hizi na Vijiji vyake vile vya Usungura, Kidunda na vinginevyo ili kuimarisha mawasiliano katika vijiji hivyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tena kuchukua fursa hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kama nilivyotoa maelezo katika jibu la swali la msingi kwamba tuna dhamira ya kuhakikisha kwamba vijiji vyote vinapata mawasiliano. Kwa hiyo, naomba kuchukua fursa hii kumhakikishia kwamba tutafuatilia kuhakikisha katika Jimbo lake na hizo kata alizozitaja, mawasiliano ya simu yanapatikana kupitia Mic, Airtel, Tigo, Vodacom, Viettel pamoja na wengine ambao wanakuja karibuni tutakapotoa tenda ya masafa ya mawasiliano.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, pamoja na majibu mazuri ya Serikali kupitia Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji, lakini swali langu la msingi lililenga mahsusi vyanzo vya maji vilivyopo katika
Mkoa wa Morogoro hususan katika Milima ya Uluguru katika Vijiji vya Tegetero, Kinole, Mgeta na

Hewe lakini majibu yamekuwa ya jumla mno. Sasa nataka
kujua katika pesa hizi zilizotengwa shilingi 2.1 bilioni kwa ajili ya utunzaji wa maji ni kiasi
gani kimetengwa kwa ajili ya kutunza vyanzo vya maji katika Mkoa wa Morogoro ambao ndiyo chanzo cha
Mto Ruvu ambao unategemewa kwa ajili ya maji ya Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na kadhalika?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika Mkoa wa Morogoro tuna Chuo cha cha Kilimo cha Sokoine
ambacho kina wataalam waliobobea katika masuala haya ya utunzaji wa mazingira hususan katika kilimo na wako tayari kutumika kama muda wote wanavyojitolea lakini tatizo ni uwezeshaji. Je, Serikali ina mpango mkakati gani wa kuwawezesha wataalam hawa ili washiriki katika utunzaji huu wa mazingira kwa weledi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anasema alitaka kusikia kuhusu Milima ya Uluguru na ni kweli Mto Ruvu unatokea milima hiyo na katika ziara yangu nimekwenda kuona kule unakotokea. Kwanza kabisa, ni kiasi gani cha fedha kimetengwa, Mheshimiwa Mgumba kwa vile maji
yanatumika Mkoa wa Dar es Salaam zaidi, DAWASA peke yake wanatoa shilingi bilioni 1 kwenye Bonde la Wami Ruvu kwa ajili ya kushughulikia Mto Ruvu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika kiasi hiki cha shilingi bilioni 2.1 kilichotengwa siwezi kusema ni kiasi gani kimetengwa kwa ajili hiyo lakini ni fedha nyingi sana ambayo inapelekwa kwenye Bonde letu la Wami Ruvu kwa sababu hii Taasisi ya Bonde la Wami Ruvu iko moja kwa moja chini ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Hata hivyo, upo ushirikiano mzuri na Mkoa wa Morogoro kuhakikisha kwamba rasilimali hii inatunzwa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu wataalam wa Chuo cha Sokoine, kama nilivyosema ushirikiano upo, kwa hiyo wote tunashirikiana, tunapata utaalamu wa wasomi wetu wa Chuo cha Sokoine na wanajadili na ndio maana utaona kwamba Bwawa la Mindu limewekewa mipaka na tayari kuna miti inapandwa kwa ajili ya kulinda bwawa lile. Utaalamu wote huo tunaupata kutoka Chuo cha Sokoine. Kwa hiyo, tunawashirikisha hawa watu ili kuweza kuwa na makubaliano ya pamoja kuhakikisha kwamba tunatunza rasilimali hizi.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.Kwa kuwa matatizo yanayowakabili watu wa Kwera yanafanana kabisa na matatizo yanayotukabili watu wa Morogoro Kusini Mashariki na Morogoro Vijijini kwa ujumla, kuna Barabara ya Bingwa – Mkuyuni – Kisaki mpaka kuelekea Rufiji kule Mloka kuelekea Mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara na pia kuelekea katika Mbuga ya Selous.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii iliahidiwa kuwekwa kiwango cha lami tangu Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne na Waziri wa Ujenzi aliyekuwa katika Serikali ya Awamu ya Nne ambaye sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli; na kwa kuwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umeshamalizika, je, Mheshimiwa Waziri, ni lini barabara hii itaanza kutengenezwa kwa kiwango cha lami ili kuinua hali ya kiuchumi ya wananchi hawa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba hii barabara baada ya kukamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, anafahamu kwamba tumeanza kujenga. Hata hivyo, nakubaliana naye kwamba kipande ambacho tumeanza kujenga mpaka sasa ni kifupi. Nimhakikishie, tutaendelea kuongeza kasi ili hatimaye barabara hii ifike Kisaki kama ilivyokusudiwa.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali kupitia Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kuna mradi mwingine unaofadhiliwa na Benki ya Dunia katika Mji Mdogo wa Malinyi unaosuasua toka mwaka 2013. Kwa sasa mabomba ya usambaji maji ya mradi huo yamekwama katika Bandari ya Dar es Salaam kwa sababu ya tozo ya storage. Halmashauri tumeomba kuondolewa kwa tozo hiyo lakini mpaka sasa hatujafanikiwa. Je, Serikali inatusaidiaje katika ombi hilo ili kukamilisha mradi huu ili wananchi wapate maji safi na salama?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa matatizo ya maji yanayowakabili wananchi wa Malinyi yanafanana na matatizo yanayotukabili wananchi wa Morogoro Kusini Mashariki; na kwa kuwa vijiji vya Mtego wa Simba na Newland vilikuwa ni vitongoji wakati wa mradi wa maji Fulwe - Mikese unafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina mwaka 2006; na kwa kuwa mradi huo sasa unatekelezwa tangu mwaka 2016 na vitongoji hivi viwili vya Newland na Mtego wa Simba sasa ni vijiji kamili.
Je, Serikali inavisaidiaje vijiji hivi vya Mtego wa Simbana Newland kupata maji safi na salama ukizingatia vilikuwa ni sehemu ya mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mradi wa Malinyi, kwa bahati nzuri nimeshatembelea kule na niliyakuta mabomba yapo na mkandarasi alikuwa anaendelea kufanya kazi. Kama kuna mabomba ambayo yamesalia, yako bandarini na yanaendelea kuongeza storage, kwangu hii ni taarifa mpya lakini hili ni suala la kiutawala, tupate taarifa ni kwa nini mabomba hayo yamekwama, tutasaidiana ili yaweze kutoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kuhusu kupeleka maji Mtego wa Simba na Newland. Tunaendelea na Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Kama alivyosema mwenyewe kwamba kuna mradi unaendelea tutahakikisha kwamba mradi huu unakamilika ili na hayo maeneo mawili yaweze kupata maji ama ya mabomba au kwa kutumia visima ili mradi wananchi hao wapate maji safi na salama.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serilkali kupitia Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Serikali imetenga shilingi milioni 368.5 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya maji katika vijiji vya Mkuyuni na Madam. Na kwa kuwa mwaka wa fedha 2016/2017 umebaki mwezi mmoja tu kumalizika, lakini mpaka sasa pesa hizi hazijafika; na kwa kuwa bajeti ya maji kwa ajili ya Morogoro imepunguzwa kutoka shilingi bilioni 4.2 ya mwaka jana mwaka huu imekuwa ni shilingi bilioni 1.5.
Je, Serikali inanipa commitment gani ya kuleta hela hizi shilingi milioni 368.5 kabla ya mwaka wa fedha uliobaki mwezi mmoja kuisha?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa katika mpango wa muda wa kati, Serikali imetenga shilingi milioni 150 kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya kupeleka maji katika Vijiji vya Lolole, Madam, Mwalazi, Kibuko na kitongoji cha Misala katika Kijiji cha Mkuyuni. Na kwa kuwa huu mradi wenyewe kwamba…
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kuna mradi wa maji katika kijiji cha Kibwaya ambao unakamilika muda si mrefu, je, Serikali badala ya kutafuta chanzo kingine cha maji, kwa nini isiongeze pesa katika mradi huu ili kupeleka maji katika vijiji hivi ambavyo nimevitaja vya Lolole, Misala, Madam na Kibuko?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli, mwaka huu wa fedha tulionao tulitenga zaidi ya shilingi bilioni 4 na kwamba mwaka unaokuja fedha hiyo imepungau kidogo. Lakini ni kwamba hivi sasa tunavyoongea tayari tumempatia shilingi milioni 976 na kwamba fedha hivyo wiki ijayo itatumwa kwa ajili ya kwenda kuendelea na utekelezaji wa miradi. Kutenga fedha kidogo ni kwa sababu wakati tunatenga shilingi bilioni nne kulikuwa na miradi inayoendelea na baadhi imekamilika. Ndio maana mwaka huu tumepunguza kidogo kwa sababu ya miradi iliyopo sasa ambayo imeelekea kukamilika haitakuwa na thamani kubwa zaidi.
Mheshimiwa Spika, lakini pili kuhusu usanifu, tumetenga fedha kwa ajili ya usanifu wa miradi katika kijiji ambacho kinahitaji kupata maji, ameshauri kwamba tutumie chanzo kilichopo, tunaweka consultant, consultant ndiye atakayebainisha kama tutumie chanzo hicho au kingine kitakachokuwa kimepatikana.
Kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inafanyia kazi kuhakikisha maeneo yake yote yanapata maji safi na salama. Na bahati nzuri nilishatembelea kwake na tulienda kuzindua miradi ambayo tayari mingine imeshakamilika. Utekelezaji utaendelea na katika Jimbo lake Fulwe itapata maji ya kutoka Chalinze mara baada ya mradi wa Chalinze kukamilika.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa matatizo yanayowakabili wananchi wa Bagamoyo yanafanana kabisa na ya Morogoro Kusini Mashariki. Kwenye mipango ya Serikali ya REA awamu ya tatu, Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki tumepata vijiji saba tu na kuacha vijiji 47 kati ya vijiji 64 ambavyo vyote havina umeme katika Kata za Tegetero, Kibuko, Tomondo, Maturi, Mkulazi na Seregeti. Je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka umeme katika huu mradi wa REA awamu ya tatu, katika Kata hizo na vijiji vyake vyote?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa Mheshimiwa Mbunge anavyosema. Kwanza nimpongeze, nilipokuja kuzindua Morogoro tulishirikiana na Mheshimiwa Omary na nilimwambia alete vijiji vyake tuviboreshe.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, tumeshafanya mapitio siyo vijiji saba vinavyopelekewa umeme raundi ya kwanza bali ni vijiji 14. Hata hivyo, vile vijiji vingine 47 alivyotaja basi tutakaa tuvipitie, lakini vyote vitapatiwa umeme kwenye raundi inayofuata itakayoishia mwaka 2021.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa gharamba za uzalishaji wa korosho za wabanguaji wa ndani wadogo na wakubwa ni kubwa pamoja na korosho yenyewe kuzalisha, na kwa kuwa wabanguaji wadogo na wakubwa wanashindanishwa kupata korosho kama malighafi katika mnada wa stakabadhi ghalani pamoja na wabanguaji kutoka nchi za nje kutoka India na Vietinam ambao wanapata ruzuku.
Je, Serikali ina mpango gani mahsusi wa kuwawezesha wabanguaji wadogo na wakubwa waliowekeza nchini, kupata korosho kama malighafi katika minada hapa nchini ili kutoa ajira na kuongeza thamani korosho zetu. (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, swali alilouliza Mheshimiwa Mbunge ndilo eneo mojawapo ambalo Serikali inalifanyia kazi kwa umakini sana, kwa sababu ni katika eneo hili ambako au tutaendelea kusafirisha korosho ghafi kwenda nje au tutatengeneza utaratibu ambao korosho itabanguliwa nchini na kusafirishwa ikiwa imebanguliwa.
Mheshimiwa Spika, suala la soko, ndio msingi wa kwanza wa kujua, mbangue muuze iliyobanguliwa au muuze ambayo haijabanguliwa. Kwa sababu soko la korosho liko sensitive sana na ubora wa korosho yenyewe, mnaweza mkatumbukia kwenye ubanguaji, halafu mkaishia kukaa na korosho yenu mkakosa mnunuzi na wakulima wataathirika zaidi ama mkabangua nchini kwa utaratibu ambao unawezekana mkashindana kwenye soko, kwa hivyo mkatengeneza hizo ajira anazozisema hapa nchini na mkauza korosho mkapata soko kuuza korosho nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, ziko nchi ambazo wameweka utaratibu wa upendeleo, kwanza, kwa kuwaruhusu wabanguaji wa ndani wanunue katika masoko na baada ya kununua ndio wanaruhusu wanunuzi kutoka nje waingie na wao kununua, yote haya tunayatafakari na tutakuja na jawabu ambalo litakuwa kwa vyovyote haliwaweki katika uwezekano wa kukosa soko wakulima, pia tuwe na uwezo wa kubangua korosho wenyewe hapa nchini ili twende na yote mawili bila kuathiri jambo moja au lingine. (Makofi)
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Matatizo yaliyopo katika Jimbo la Mufindi Kusini yanafanana kabisa na matatizo yaliyoko katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki. Tuna mradi wa maji katika vijiji vitano una miaka zaidi ya tisa. Serikali imejitahidi kujenga miundominu yote ya kuhifadhi na kusambaza maji kwa kutegemea chanzo cha Mto Ruvu katika mradi wa Chalinze III lakini mpaka leo maji hayatoki. Nataka kujua ni lini Vijiji hivi vitano vya Maseyu, Kinonko, Kidugalo, Ngerengere, Sinyaulime pamoja na kambi mbili zetu za Jeshi za Kizuka na Sangasanga vitapata maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kaka yangu Mheshimiwa Mgumba kwa namna ya kipekee anavyowapigania wananchi wake. Kwa kuwa suala la maji ni maisha ya watu, labda nimwombe Mheshimiwa Mbunge baada ya Bunge na mimi nipate nafasi ya kuweza kufika Morogoro Kusini Mashariki ili tuweze kuzungumza na wananchi na kuangalia namna gani tunaweza kuchukua hatua za haraka ili kuweza kuwasaidia wananchi wale kuondokana na adha ya maji. Ahsante sana.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Kutokana na Sera nzuri ya Serikali ya CCM ya Elimu Bila Malipo imesababisha mwamko wa elimu na wanafunzi kufauli kwa kiasi kikubwa na kusababisha upungufu wa madarasa zaidi ya vyumba 45 katika Jimbo langu. Je, Serikali imejipangaje katika kutatua tatizo hili la ujenzi wa vyumba 45 ukizingatia kipindi hiki wananchi wengi wako kwenye kilimo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, upungufu wa vyumba vya madarasa ambavyo vipo kwenye jimbo lake, hakika upungufu huu upo kwenye majimbo mengi. Katika moja ya maswali ambayo nilijibu wakati ameuliza Mheshimiwa Esther Matiko akiwa anaongelea juu ya uhaba wa vyumba vya madarasa, nika- refer kwamba, ni wajibu wetu sisi wananchi kwa kushirikiana na sisi viongozi pamoja na Serikali, kwanza kwa kutazama idadi ya vijana ambao wanajiunga na shule zetu na hasa baada ya mwitikio mkubwa baada ya Elimu Bila Malipo, Sera ambayo inatekelezwa vizuri sana na CCM.
Mheshimiwa Spika, ni wajibu wetu sisi kwa kushirikiana na wananchi tuhakikishe kwamba, kwanza halmashauri zetu ndani ya own source zetu tunatenga na tuwashirikishe wananchi na Serikali nayo itaunga mkono.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kama Serikali ilivyosema katika jibu lake la msingi kwamba kuna vijiji saba ambavyo umeniongeza kwa hiyo, je, nataka kuvijua vijiji hivi saba ni vipi na ni lini vitaanza kupatiwa umeme?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa, katika Kata ya Mkulazi kuna miradi miwili nya kielelezo inayofanyiwa kazi sasahivi na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli, Kiwanda cha Mkulazi cha Sukari pia na ujenzi wa Bwawa la Kidunda, je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka umeme katika kata hii yenye vijiji vinne na Kijiji cha Kwaba, ambavyo ni vijiji vya Kwaba, Kidunda pamoja na Usungura?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa Mheshimiwa Mgumba nakupongeza sana unavyoshughulikia masuala ya umeme katika Jimbo lako. Tulipokutana Morogoro ulituomba tukuongezee vijiji na tumekuongezea, lakini vijiji alivyotaka tumuongezee Mheshimiwa Mbunge pamoja na kwamba tumeshapeleka umeme katika vijiji vingine vikiwemo vijiji vya Mtego wa Simba pamoja na Kinonko, tunampelekea kwenye vijiji vingine ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameomba.
Mheshimiwa Naibu Spika, na vijiji ambavyo ameomba tumpelekee ni pamoja na Kibuko, Luhorole, Kizinga, Pangawe pamoja na Usungura. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikupe, kama vijiji ambavyo tumepeleka na vijiji vingine 40 tutakupelekea Mheshimiwa Mbunge, wala hakuna wasiwasi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la pili kwamba ipo miradi ya vielelezo katika maeneo ya Usungura, ni kweli kabisa. Maeneo yale kutajengwa viwana vya sukari, lakini kadhalika kuna bwawa la maj. Kwa hiyo, tumemuongezea mbali na vijiji vingine vile 11 nilivyotaja na wala sio saba, tunaviongezea vijiji vingine vitatu vikijumlisha na Bwawa la Kidunda, ili tupeleke umeme Kidunda, Usungura pamoja na Kwaba. Kwa hiyo, nimpe imani Mheshimiwa Mbunge kwamba vijiji vyote vya Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki vitapatiwa umeme kupitia mradi wa tatu wa REA. (Makofi)
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mkoa wa Morogoro wenye Wilaya saba na Halmashauri tisa ina Hospitali za Wilaya mbili tu ambazo ni Ulanga na Kilosa. Kwa kuwa katika bajeti ya mwaka huu, Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya katika Wilaya ya Morogoro hususani katika Halmashauri ya Morogoro Vijijini katika Kata ya Mvuha.
Je, ni lini Serikali italeta hizi shilingi milioni 500 ili tuanze ujenzi wa Hospitali ya Wilaya katika Halmashauri ya Mvuha?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Naibu Waziri, napenda kujibu swali hili la Mheshimiwa Omary Mgumba, ni kweli na mimi nilipata fursa ya kufika Mvuha nikiwa na Mbunge mwenyewe jiografia na hali ya pale tunatakiwa tufanye kila liwezekanalo kuhakikisha tunaimarisha huduma ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wengine wote ni jukumu la Serikali kuhakikisha kwamba tunaboresha sekta ya afya ndiyo maana leo hii tunaboresha vituo vya afya 212 kwa awamu ya kwanza kihistoria.
Mheshimiwa Mgumba naomba nikuambie, nilifika pale na tumebaini changamoto na Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi itafanya kila liwezekenalo kuwasaidia wananchi wa Morogoro Vijijini na wananchi wengine katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu moja kubwa ni kwamba tunafanya ujenzi wa vituo vya afya 212 then vituo vya afya vingine 70 vipya vitakuja, niwaombe Waheshimiwa Wabunge tushirikiane kusimamia matumizi mazuri ya fedha, lengo kubwa ni kwamba ikifika tarehe 30 Aprili, tuwe tume- launch vituo vya afya visivyopungua 212 katika historia ya nchi yetu hii.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi kuuliza maswali ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki tulipata vijiji 17 kati ya vijiji 64 katika miradi ya umeme ya REA Awamu ya Kwanza na REA Awamu ya Pili, na kwa kuwa katika awamu zote hizo utekelezaji wake wa miradi hiyo kuna taasisi za umma kama vile shule, zahanati, vituo vya afya na nyumba za ibada na vijiji na vitongoji vingi kwa mfano, Kijiji cha Tomondwe, Mfumbwe, vitongoji vya Misala vilirukwa.
Je, Serikali huu mradi wa densification utafika lini Morogoro hususan katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki ili vijiji na vitongoji hivi vilivyorukwa vipatiwe umeme? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, pamoja na majibu hayo nataka niweke kumbukumbu sawa. Swali kama hili niliuliza katika Bunge lililopita katika swali la nyongeza na swali la msingi Bunge lingine lililopita. Serikali ilinipa majibu katika jimbo langu wamenipa vijiji 20 na si 14; mpaka sasa hivi huyo mkandarasi ameshafika na amefanya survey ya vijiji vyote 20. Hata hivyo kwa kuwa amefanya vijiji saba amepata mkataba wa kufanya survey pamoja na kujenga miundombinu ya umeme. Lakini vijiji 13 ameambiwa tu afanye survey ukizingatia ndani ya vijiji hivyo ndiko kunakojengwa kiwanda kikubwa cha sukari ambacho kitaanza ujenzi mwaka huu pamoja na Bwawa la Kidunda.
Je, Serikali imejipanga vipi ili kumalizia na ujenzi katika vijiji hivi 13 na vijiji vile vingine vya Tomondo na sehemu zingine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza Mheshimiwa Mgumba amejielekeza kwenye utekelezaji wa miradi ya REA Awamu ya Kwanza na REA Awamu ya Pili ambako yako maeneo mbalimbali yalirukwa.
Napenda nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba maeneo ambayo yalirukwa katika awamu ya kwanza na ya pili Serikali yetu imekuja na mpango wa densification, kwa maana ya ujazilizi katika maeneo ambayo taasisi za umma, vijiji na kaya mbalimbali. Kwa kuwa densification imetekelezwa katika mikoa nane ya awali kama ambavyo tumepata kusema ndani ya Bunge lako Tukufu, awamu inayofuata sasa Serikali kupitia Wakala wa Umeme Vijijini imeajiri mshauri elekezi ambaye ni Multconsult ASA kutoka Norway pamoja na NORPLAN ya Tanzania kwa ajili ya kufanya verification ya maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia kupitia Wakala wa Umeme Vijijini imeomba ufadhili kutoka Norway, Sweden na Ufaransa kwa ajili ya densification ya awamu ya pili. Nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba maeneo mbalimbali na mikoa mbalimbali yataanza kufikiwa na densification ya awamu ya pili ikiwemo Mkoa wa Morogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili Mheshimiwa Mgumba amejielekeza kwenye maeneo yale ambayo kama ambavyo amerejea jibu letu Bungeni la Mkutano wa Tisa kwamba katika vijiji vyake 20, vijiji saba vimefanyiwa survey na hivyo 13. Kama tunavyotambua jimbo hilo miradi mikubwa ya kimkakati inatekelezwa ikiwemo ujenzi wa Kiwanda cha Sukari pia na ujenzi wa Bwawa la Kidunda. Nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge nia yetu sisi kama Wizara ya Nishati ni kuwezesha sekta zingine. Kwa hiyo ni wazi kabisa kwamba vile vijiji 13 ambavyo vipo katika maeneo ambayo miradi mikubwa inapita tumemuelekeza mkandarasi ambaye ni State Grid maeneo yote ambayo amefanya upembuzi yakinifu amalizie kuendelea na ujenzi wa miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimtoe hofu Mheshimiwa Mgumba kwamba maeneo yote ambayo ameyataja, hivyo vijiji 20 lakini pia kwa kutambua umuhimu wa maeneo hayo pia tumemuongezea vijiji nane vikiwemo vijiji viwili katika Kata ya Mkulazi ambako mradi mkubwa wa ujenzi wa kiwanda cha sukari unafanyika na Bwawa la Kidunda. Pamoja na kwamba maagizo ya Serikali pia yameelekeza kwamba maeneo ambayo kuna miundombinu mikubwa ya umeme iliyopita katika kata yake mojawapo ambayo ameitaja Tomondo pia tumempa vijiji vinne kwa sababu iko karibu na Kata ya Kiloka na Mikese ambako kuna miundombinu ya umeme. Kwa hiyo, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Wizara inafanya kazi pamoja naye. Ahsante sana.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri kwa niaba ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; swali langu kipengele cha (a) lilikuwa liko straight forward niliomba kwamba Serikali iongeze ardhi ya wakulima wadogo toka hekta 3,000 mpaka hekta 23,000, lakini kwenye majibu ya msingi ya Mheshimiwa Waziri bado hakutoa jibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wa swali langu ilikuwa ni ardhi iliyotengwa kwa ajili ya wakulima wadogo ni ndogo, naiomba Serikali iongeze. Je, ni nini kauli ya Serikali katika suala hili kuongeza ardhi hiyo kutoka hekta 3,000 kwenda 23,000? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sSwali la pili; kwa kuwa, katika jibu la Serikali limesema imetenga ardhi ya ukubwa wa hekta 3,000 kwa ajili ya wakulima wadogo wa vijiji vinavyozunguka shamba hili la Mkulazi kwa maana ya Vijiji vya Kidunda, Chanyumbu, Usungura, Mkulazi katika Kata ya Mkulazi na Kijiji cha Kwaba katika Kata ya Matuli; na kwa kuwa, mradi huu ni miongoni mwa miradi mitano ya kielelezo ya Kitaifa, manufaa yake inawanufaisha Watanzania wengi. Je, Serikali itatenga ardhi kiasi gani kwa ajili ya wananchi wengine nje ya vijiji hivi vitano wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki ili washiriki katika mradi huu wa wakulima wadogo. (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na ombi lake la kwamba ardhi ile iongezwe mpaka hekta 23,000 kwa ajili ya wakulima wadogo, naomba nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kweli katika majadiliano ambayo yanaendelea kati ya NSSF na PPF ambao hasa ndio wanaomiliki Mkulazi Holdings tayari kuna mwelekeo kwamba ardhi ile itaongezeka ili wakulima wadogo waweze kuongezeka kwa wingi zaidi. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba tayari hilo linafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuhusiana na swali lake la pili ni kwamba huu ni mradi wa Kitaifa na hivyo ingekuwa vema kama vijana na wananchi wengine Watanzania wakaweza kunufaika. Nimhakikishie kwamba tayari Ofisi ya Waziri Mkuu ya Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu wameweka mkakati wa kuhakikisha kwamba vijana wengi zaidi watanufaika katika mradi huo na watatengewa blocks pamoja na kupatiwa mafunzo ili waweze kushiriki vizuri katika kilimo cha miwa, vijana wale watatoka nchi nzima siyo Morogoro peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tayari kuna huo mpango wa kuhakikisha vijana wengi wanashiriki zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu itashirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha kwamba vijana wanapata elimu nzuri ya namna ya kuotesha miwa na kushiriki katika value chain nzima ya zao la miwa. (Makofi)
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongezaKwa kuwa, matatizo yanayokabili Jimbo la Kibamba yanafanana kabisa na matatizo yanayokabili Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, hususani katika Kata ya Mkambarani katika Vijiji vya Pangawe na Kizinga. Mheshimiwa Mwenyekiti, Pangawe na Kizinga tuna mradi mkubwa wa maji pale, lakini mradi ule maji hayatoki hasa wakati wa kiangazi ambao kunasababishwa na kile kidaka maji ambao sisi ndio watu wa Pangawe tulianza, lakini watu wenzetu wa MORUWASA wakaja kuweka juu yetu, matokeo yake wanatuathiri sisi hatupati maji pale, lakini tumechanga wenyewe pesa tumeweza kujenga lakini tumekatazwa na Mamaka ya Maji ya Bonde la Ruvu. Je, Serikali inatusaidiaje watu wa Pangawe na Kizinga kuzungumza na Mamlaka ya Maji ya Bonde la Ruvu, ili waturuhusu hicho kibali na sisi tuhamishe hicho kidaka maji kwenda kwa wenzetu kule juu cha MORUWASA na Jeshi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri chanzo cha Pangawe nilifanya ziara Mkoa wa Morogoro, nimeenda mpaka pale kwenye chanzo nikakiona. Kipindi cha kiangazi ndio chanzo pekee ukiachana na bwawa la Mindu ambacho kinaleta maji ya mtiririko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kile chanzo Jeshi la Wananchi wa Tanzania wanachukua pale, Mamlaka ya Maji Safi Morogoro nao wanachukua pale, vijiji vingine vilivyo karibu navyo vilikuwa vinahitaji kuchukua pale, sasa hivi tumeelekeza yafanyike mazungumzo ili menejimenti ya chanzo ibaki kwenye eneo moja la Mamlaka ya Maji ya Morogoro, baada ya kuwa kwenye hilo eneo moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutakubaliana, tutawapa assignment hawa watu wa MORUWASA ili wahakikishe wanapeleka maji kwenye maeneo yote, kwa sababu kama chanzo kimoja kimoja kitafanyiwa menejimenti na taasisi nyingi kwa vyovyote vile tutarajie kwamba performance yake haitakuwa nzuri. (Makofi)
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza kuhusu Bwawa la Kidunda.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri kwa sababu mradi huu mpaka sasa accessibility ya kufika sehemu ambayo inajengwa bwawa haifikiki kirahisi ni pamoja na utekelezaji huu, lakini kulikuwa na mpango wa kuiboresha na kuitengeneza barabara hii ili ujenzi huu uweze kuanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujua katika upande wa Serikali, ni lini barabara hii itaanza kujengwa ili kurahisisha ujenzi wa bwawa huu kuanza?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mgumba kwa kuuliza swali ambalo ni la msingi, lakini jibu ni moja dogo kwamba katika mwaka wa fedha unaokuja tumetenga fedha, kwa hiyo utaiona hiyo fedha kwenye wasilisho la bajeti ya Waziri wa Maji ambapo tutaanza na ujenzi wa barabara ili kumwezesha Mkandarasi sasa awe na uwezo kwenda kujenga bwawa.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa matatizo yanayowakabili wananchi wa Mkoa wa Tabora yanafanana kabisa na wananchi wa Mkoa wa Morogoro hususani katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki hasa katika shule ya Mkuyuni ambayo upungufu wa madarasa yanayohitajika ni zaidi ya 18, shule ya msingi Ngerengere Njia Nne madarasa 21 yanahitajika na shule ya msingi Mikese Fulwe madarasa zaidi ya 10.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa kuwa uwezo wa halmashauri yetu ni mdogo na uwezo wa wananchi kujenga madarasa haya yote ni mdogo sana. Je, Serikali kuu ina mpango gani wa kutusaidia kumaliza tatizo hili la vyumba vya madarasa ili kuinua ubora katika shule zetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba sana Mheshimwa Omari Tebweta Mgumba, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki nikutane naye baada tu ya Bunge mchana saa saba na nusu ili tuweze kupanga mikakati pamoja. (Makofi)
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, Mheshimiwa Naibu Waziri katika majibu yake anasema kwamba REA Awamu ya Tatu lengo lake kubwa ni kupeleka umeme katika vijiji ambavyo havina miundombinu ya umeme, lakini kosa lile lile lililofanyika katika REA I na II, kuruka Vitongoji na Vijiji tumeliona tena katika REA hii ambayo inatekelezwa. Kwa mfano, sasa hivi kimepewa Kijiji cha Bagilo ambapo vimerukwa Vijiji vya Hewe, Mgozo na Tegetero, lakini pia...
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Kidunda kimepewa, vimerukwa vijiji vya Mkulazi na Chanyumbu; je, Serikali ina mpango gani wa kuvipatia vijiji hivyo ambavyo vimerukwa katika REA III ili tusirudie kosa lile la REA I na II?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba mradi huu umeanza. Ni kweli umeanza, lakini mkandarasi huyu ana miezi sita sasa tangu alipokuja kufanya tathmini tu, hajarudi site mpaka leo. Baada ya kumfuatilia inaonekana kwamba hajapewa advance wala letter of credit ya kuanza kazi. Katika majibu yake Mheshimiwa Naibu Waziri anasema mradi huu unatakiwa ukamilike Julai, 2019, mpaka leo kazi haijaanza. Je, ni lini Serikali itaweza kutoa letter of credit kwa mkandarasi huyu ili aweze kuanza kupata vifaa na vitendea kazi ili aweze kuanza mradi na kutekeleza ndani ya wakati? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza lazima nimpongeze Mheshimiwa Mgumba kwa kazi anayoifanya. Ndani ya kipindi kifupi amkeshauliza zaidi ya maswali manne ya Sekta ya Nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza alijielekeza kwenye changamoto zilizojitokeza katika REA ya I na REA II ya urukwaji wa vijiji. Naomba nikiri kweli changamoto hiyo ilikuwepo, lakini pia naomba niseme kupitia mradi huu wa REA Awamu ya Tatu, baada ya kupokea maombi mbalimbali ya Waheshimiwa Wabunge, awali mpango ulikuwa ni vijiji 3,559 lakini baada ya kupokea malalamiko ya kurukwa kwa vijiji, vitongoji na taasisi za umma tumefanya tathmini nyingine na upembuzi yakinifu, tumepata vijiji kama 1,541 ambavyo vinatakiwa viongezeke awamu hii tunapoendelea kutekeleza mzunguko huu wa kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge vijiji alivyovitaja ni miongoni mwa vijiji 1,541 ambavyo vitaongezeka kwenye vijiji 3,559 na vitakuwa vijiji 5,100 kwa awamu ya kwanza ambavyo vitapelekewa miundombinu ya umeme. Pamoja na kwamba nakiri, lakini gharama zitaongezeka. Pia kwa kuwa kazi ya Bunge hili ni kuidhinisha bajeti kwa miradi hiyo na uhitaji unaonekana ni mkubwa, sina mashaka kwamba Bunge litatimiza wajibu wake na kwamba vijiji ambayo tumeviona lazima viongezeke ili kutimiza lengo ambalo limekusudiwa kwamba tusirudie makosa ya awamu nyingine, litatimia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, amejielekeza kwamba ni kweli Mkandarasi wa Mkoa huu wa Morogoro, State Grid alifanya tathmini na kwamba hajalipwa advance. Nataka niseme wakati wa malipo ya advance kulikuwa na masharti na sharti mojawapo lilikuwa malipo lazima wa-submit performance bond. Bahati mbaya mkandarasi huyu haku-submit kwa wakati, lakini nakiri mpaka sasa hivi Wakandarasi wote wamesha-submit, utaratibu wa malipo unaendelea kwenye Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, utaratibu wa ufunguaji wa letter of credit, tunashukuru tumepokea barua wiki iliyopita kwamba sasa tunaweza tukaendelea na utaratibu huo. Kwa hiyo, tunajipanga pamoja na Wakala wa Nishati Vijijini ili kuifanya kazi hiyo kwa haraka na miradi hii itekelezeke kwa haraka. Ahsante. (Makofi)
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa umbali wa kutokea Ubena Zomozi mpaka Ngerengere ni kilomita 18 na kati ya hizo kilomita 11 zimetengewa kujengwa kwa kiwango cha lami katika Bajeti ya 2018/2019 na zimebaki kilomita saba tu; na kwa kuwa barabara hiyo inaunganisha majeshi yetu mawili kati ya Kizuka mpaka Sangasanga. Je, Serikali haioni umuhimu wa kumalizia hizo kilomita saba kwa kiwango cha lami ili barabara hii ifike Ngerengere Mjini na kule kwenye Kambi yetu ya Jeshi ya Sangasanga?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ahadi kama hii ilitolewa na Rais wa Awamu ya Nne tangu 2010 na Rais wa Awamu ya Tano 2015 katika barabara ya Bigwa – Mvuha kujengwa kwa kiwango cha lami; na kwa kuwa barabara hii iko kwenye ilani ya Chama cha Mapinduzi na upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ulishamalizika muda mrefu. Ni lini Serikali itaanza kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami ukizingatia tumebakiza miaka miwili kwenda kwenye uchaguzi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kipande cha barabara kati ya Ubena hadi Kizuka chenye urefu wa kilometa 11 kimewekewa lami na kipande cha kilometa saba kati ya Kizuka mpaka Ngerengere bado ni cha vumbi. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mgumba ambaye kwa kweli Mheshimiwa Mwenyekiti nikiri kwamba ni Mbunge ambaye anafuatilia sana suala la barabara hii kwamba tunafahamu umuhimu na unyeti wa kipande cha barabara kutoka Kizuka kwenda Ngerengere cha kilometa saba, lakini vilevile kutoka Ngerengere kwenda Sangasanga cha kilometa sita na kipande cha kutoka Sangasanga kwenda Mdaula, tunajua umuhimu wa eneo hilo na unyeti wa eneo hilo. Namuomba Mheshimiwa Mbunge tutakapotoka hapa twende Wizarani tukamwoneshe taratibu na hatua ambazo tumekwishafikia kuhakikisha kipande hicho chote ambacho kina mzunguko kinawekewa lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili; ni kweli kwamba kuna ahadi mbalimbali zilishatolewa na viongozi wetu wakuu kuweka barabara kwa kiwango cha lami kutoka Bigwa kuja Mvuha mpaka Kisaki. Nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba mipango ipo, bahati nzuri upembuzi yakinifu ulishafanyika na usanifu wa kina tayari, kinachosubiriwa sasa ni upatikanaji wa pesa ili tuweze kutangaza tender, kumpata mkandarasi wa kujenga kwa kiwango cha lami. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa kipaumbele cha watu wa Kinole ni ujenzi wa Kituo cha Polisi ambacho tumeshajenga ambacho kimefikia mtambaa wa panya kinasubiri kuezekwa pamoja na ujenzi wa kituo cha afya; na kwa kuwa katika Kata ya Kinole kuna SACCOSS ya mfano yenye mtaji wa zaidi ya shilingi bilioni mbili na wakulima wakubwa wa matunda na viungo lakini kuna mzunguko mkubwa sana wa pesa lakini usalama ni mdogo na Serikali imepeleka pesa kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Kituo cha Kisimbi.
Je, Serikali iko tayari kuhamisha pesa hizi ilizopeleka katika ujenzi wa Kisimbi ambao ni ujenzi wa kituo cha utalii ambao siyo kipaumbele cha wananchi na kuna tatizo la mgogoro wa fidia na kupeleka kwenye umaliziaji wa Kituo cha Polisi kwenye mapato ya ndani?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo alilolisema Mheshimiwa Mbunge ni pendekezo. Niseme tu kama Serikali tunapokea pendekezo, lakini nimuombe Mheshimiwa Mbunge tupate fursa tuongee kwa undani zaidi ili tuweze kuhusisha na wadau wengine na Wizara zingine ambazo zinahusika.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu ya Mheshimiwa Waziri anasema kwamba kwa mujibu wa sera angalau kila tarafa iwe na shule ya sekondari ya kidato cha tano na sita; na sisi Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki tumeshaanza ujenzi huo katika tarafa zote tatu za Mkuyuni Ngerengere na Nelson Mandela. Shule ya Nelson Mandela tulishamaliza bado bwalo kumalizia juu. Je, Serikali iko tayari kutuunga mkono kumalizia bwalo ili mwezi wa saba wanafunzi waanze, ukizingatia mwaka jana zaidi ya wanafunzi 60 wamekosa kwenda katika hizo shule za kitaifa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mgumba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kama Serikali iko tayari kuwaongezea nguvu kukamilisha bwalo na anataka limalizike mwezi wa saba, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na nia ya Wizara ya kuendelea kusaidia ujenzi wa miundombinu bado muda wa matayarisho utakuwa ni muhimu kwa sababu kipindi cha mwezi mmoja kwa kweli kina changamoto katika taratibu za kawaida za kupata fedha. Hata hivyo, halmashauri yake walete mapendekezo na sisi tutajipanga ili tuweze kuwasaidia katika mipango mingine ijayo. (Makofi)
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa Halmashauri ya Morogoro mpaka sasa haina hospitali ya Wilaya na kwa kuwa Tarafa ya Ngerengere na mahali ambapo panajengwa hospitali ya Wilaya kuna umbali wa zaidi ya kilometa 105.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tarafa ya Ngerengere kuna miradi mitatu mikubwa ya Kitaifa ambayo ni standard gauge pamoja na ujenzi wa kiwanda cha sukari pamoja na Bwawa la Kidunda ambao unasababisha wingi mkubwa wa watu. Je, Serikali haioni umuhimu wa kukarabati Kituo cha Afya Ngerengere ili kiwe na hadhi ya kituo cha afya kuweze kuwa-accommodate watu hawa wote na kujenga Kituo kingine cha Afya katika Kata ya Mkulazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabla ya kujibu naomba nitangulize maneno yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo ambayo tumekuwa tunapata taabu pale ambapo pesa za maendeleo zinapelekwa hazifanyiwi kazi kwa wakati ni pamoja na kwa Mkurugenzi wa Halmashauri anayotoka Mheshimiwa. Kuna pesa zimepelekwa kwa ajili ya kujenga kituo cha afya lakini kasi yake ni mbovu sana. Naomba nichukue fursa hii kwanza kumuagiza Mkurugenzi ahakikishe kwamba pesa iliyopelekwa inatumika kukamilisha ujenzi wa kituo cha afya ili wananchi waweze kupata huduma ya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni azma ya Serikali kuhakikisha maeneo yale yote ambayo iko haja na kama ambavyo ametaja umbali na ni ukweli usiopingika kwamba Ngerengere ina umuhimu wake. Naomba nimhakikishie kwamba baada ya hili zoezi kukamilika na mimi nikapata fursa ya kwenda, tutashauriana namna nzuri ya kuweza kuhakikisha ukarabati unafanyika na huko.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, hayo marekebisho anayoyasema Mheshimiwa Waziri yalishafanyika tangu mwaka jana na sasa hivi tuko kwenye hatua ya kusubiri fedha kama anavyosema. Kwa kuwa barabara hii umuhimu wake umeongezeka kitaifa kwa sababu mradi wa kufua umeme wa Stiegler’s unaojengwa utatumia barabara hii lakini pia mpango wa Serikali wa kufufua utalii katika Ukanda wa Kusini hasa katika Mbuga ya Selous barabara hii itahitajika. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuharakisha ujenzi wa barabara hii ili kufungua utalii katika ukanda wa Kusini katika Mbuga ya Selous ukizingatia zaidi ya 70% ya mbuga hii iko Mkoa wa Morogoro? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa, Sheria Tathmini inasema kwamba mtu akishafanyiwa tathmini alipwe ndani ya miezi sita na Serikali sasa inasema kwamba itajenga barabara hii kwa kutegemea upatikanaji wa fedha. Kwa kuwa malipo ya fidia yanalipwa baada ya fedha kupatikana, je, Serikali inatoa kauli gani kwa watu watakaoathirika na mradi huu ambao hawafanyi maendelezo ya nyumba zao zaidi ya miaka nane sasa ili waweze kuendelea na ujenzi wao mpaka hapo hizo hela zitakapopatikana?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mgumba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba uniruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Mgumba kwa sababu amefuatilia sana barabara hii. Tangu niingie kwenye Bunge hili kila wakati nimemsikia akizungumza juu ya barabara ya Bigwa – Kisaki. Hata Waswahili wanasema baada ya dhiki ni faraja, ni faraja kwamba sasa tunaenda kutengeneza hii barabara na hatua iliyofikia siyo haba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kwanza, amezungumza juu ya umuhimu wa barabara hii kujengwa kwa haraka. Kweli maeneo haya ni muhimu sana kwa sababu barabara ya Bigwa – Kisaki ita-facilitate upitishaji wa mizigo na vitu muhimu kwenda kwenye ujenzi sehemu tunayoenda kufua umeme kule Stiegler’s Gorge, lakini pia nayafahamu maeneo haya yana utalii kama alivyosema na eneo hili pia ni muhimu sana kwa kilimo cha mazao ya chakula na biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeitazama barabara hii tumeitazama na hatua iliyofikiwa siyo hatua mbaya, kipande cha kilometa 78 tutakwenda kuungana na barabara inayotoka Ngerengere ambayo ndiyo tumeipa kipaumbele zaidi ili mizigo ianze kupita Ngerengere kwenda Mvuha mpaka Stiegler’s Gorge. Kwa hiyo, asiwe na wasiwasi barabara zote hizi mbili zitaunganika tu, tukianza na ile ya Ngerengere pamoja na hii aliyozungumza. Barabara zote ziko katika maeneo yake nasi tumejipanga kuhakikisha tunaendelea kujenga kwa kiwango cha lami. Hatua iliyofikiwa ni nzuri ya kutafuta fedha ili tuanze ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa eneo hili la Morogoro kwa ujumla wawe na subira wakati tunaendelea na harakati hizi. Hata kwa mwaka huu tumetenga shilingi bilioni 5 kuanza kujenga barabaa hii ya Ngerengere - Mvuha, kwa hiyo, kuja kuunganisha na barabara hii itakuwa rahisi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu fidia utaratibu na kanuni zipo kwamba tutalipa fedha kulingana na thamani ya fedha kwa wakati huo. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mgumba na wananchi wake ambao wamepisha maeneo kwa muda mrefu, niwapongeze sana, wamevumilia miaka nane, tunaendelea kutafuta fedha ili tulipe fidia hii. Tutalipa fidia hii kulingana na kanuni na sheria zinavyosema ili tuweze kuwa-compensate wananchi hawa kwa sababu wamesubiria fidia yao kwa muda mrefu.