Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Omary Tebweta Mgumba (81 total)

MHE. PROF. NORMAN A. SIGALLA KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nina swali moja tu la nyongeza.
Kwa kuwa maeneo yote yaliyotajwa kwa ajili ya ujenzi wa maghala hazijatajwa sehemu zile ambazo tunajua zinazalisha mahindi kwa wingi ikiwemo Wilaya ya Makete, nini kauli ya Serikali juu ya ujenzi wa ghala Makete?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kuwatetea wananchi wake na kunihimiza kufika Makambako tarehe 3 mwezi huu kwenda kuangalia hali ya ununuzi wa mahindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizingatia jibu langu la msingi niliyataja maeneo mbalimbali ambayo Serikali inakwenda kujenga maghala ya kuhifadhia mahindi kuanzia ya Halmashauri mpaka ya wakala wetu wa hifadhi. Moja ya sehemu hiyo ni Makambako; Makambako ni Makao Makuu ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambayo inajumuisha Mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya pamoja na Songwe. Eneo analotoka Mheshimiwa Mbunge ni Makete, ni eneo la Mkoa wa Njombe na ni sehemu ya hii Makambako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili eneo la Makambako ndiyo tunakwenda kujenga ghala kubwa kuliko sehemu yoyote Tanzania; maghala haya matatu tunayoenda kujenga yatakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 60,000 kwa mwaka. Maana yake tukiongeza na uwezo wa sasa wa ghala lile tani 39,000 tutakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 99,000. Hii maana yake maeneo ya mikoa yote hiyo miwili hususani Mkoa wa Njombe ambako lipo Makao Makuu na Wilaya ya Makete tutakuwa na uwezo mkubwa wa kuhifadhi mahindi kwa mwaka ujao Desemba. (Makofi)
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Spika, kwanza niishukuru Serikali kwa kutoa tozo karibu 20 kwenye tasnia ya kahawa. Hata hivyo, pamoja na shukrani hizo sehemu ya jibu inasema kwamba bei ya kahawa inakuwa ndogo kwa sababu ya kutoeleweka vizuri kwa maelekezo ya Serikali kuhusu uuzaji wa kahawa kwenye soko la moja kwa moja (direct exports) kahawa hai organic coffee na kahawa haki (fair trade coffee) miongoni mwa wanunuzi na viongozi wa ushirika, kutoeleweka vizuri kwa maelezo ya Serikali.
Je, Serikali imechukua hatua gani ili hii ieleweke vizuri na wakulima wapate bei nzuri?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, bei ya kahawa ni ndogo kama anavyojua Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini pia Serikali imeuzia wanunuzi binafsi wote, walikuwepo wengi Olam, Kagira na wengine imewazuia sasa hivi hawaruhusiwi kununua kahawa kwa wakulima. Hawa walikuwa na bei nzuri kidogo na msimu ulikuwa unawahi hauchelewi kama ilivyo sasa na mkulima alikuwa anapata nafuu. Kwa nini Serikali imezuia wanunuzi binafsi na inawatesa wakulima? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA):
Mheshimiwa Spika, ni kweli maelekezo ya Serikali yalikuwa kwamba mnunuzi yoyote mwenye soko la moja kwa moja nje ya nchi kwa kahawa hai na kahawa iliyozalishwa kwa kutumia haki anaruhusiwa kuuza kahawa hiyo ili mradi wakulima wale kwa sababu wanatambulika, wapitie kwenye vyama vyetu vya ushirika. Agizo hilo halikueleweka vizuri kwa wanunuzi wala kwa vyama vya ushirika wakadhani kwamba Serikali tumepiga marufuku kwa ajili ya direct export.
Mheshimiwa Spika, hatua gani Serikali imechukua, kwanza tuliwaita wanunuzi wote walifika pale Wizarani wiki moja iliyopita na wadau wengine kwa ajili ya kuwapa ufafanuzi huo na kwa sasa wanunuzi wote wamelielewa hilo na wameshachukua maelekezo ya Serikali. Mnunuzi yoyote mwenye soko la moja kwa moja ambaye anawafahamu wakulima wake anaruhusiwa kukusanya kahawa hiyo na kutuonesha hicho kibali chake kinachoonesha bei aliyouzia ili kwamba tozo na ushuru mwingine wa Serikali tuupate kama inavyostahili.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa nini kama Serikali tumekataza wanunuzi binafsi wasinunue kahawa kwa wakulima. Kama Serikali hatujakataza wanunuzi binafsi kununua kahawa kutoka kwa wakulima. Tulichoelekeza Serikali kwa ajili ya kulinda ubora wa kahawa, lakini pia kupata takwimu sahihi tulizielekeza Halmashauri zetu Serikali za Mikoa na Wilaya pamoja na Vyama vya Ushirika, lakini hasa Vyama vya Msingi vya ushirika ndio wenye jukumu la kukusanya kahawa ile kutoka kwa wakulima na kuipeleka wenyewe Moshi na wale wanunuzi watakuja kununua kahawa pale Moshi. Hili tumelifanya kwa ajili ya kudhibiti ubora na pia kwa ajili ya kupata takwimu sahihi.
Mheshimiwa Spika, nimueleze Mheshimiwa Rweikiza, uzalishaji wa kahawa mwaka jana ulikuwa ni tani 50,000 tu lakini kwa mfumo huu mpaka sasa tulishafikia, kwa kahawa ya maganda, zaidi ya tani 80,000. Mpaka msimu ukiisha tunatumaini tutafikisha zaidi ya tani 100,000.
Mheshimiwa Spika, Kwa hiyo lengo lilikuwa kuwawezesha hawa wakulima wauze wenyewe soko la Moshi; lakini kwenye jibu langu la msingi nimeeleza sababu zilizosababisha bei kushuka. Pia kulikuwa na ukiukaji, maelekezo ya Serikali yalikuwa kwamba vyama vya msingi ndivyo vikusanye kahawa ile, lakini…
… baadae kahawa ile ikachukuliwa na vyama vikuu. Nataka nimuhaidi Mheshimiwa Rweikiza mwakani haitokuwa hivyo hivi vyama vyetu vikuu vya ushirika vyenye madeni ya kutupwa havitoweza kuruhusi wa tena kukusanya kahawa kutoka kwa wakulima bali ni vyama vyao vya msingi wakulima wenyewe ndio watakusanya kahawa na kuiuza katika masoko yetu. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa fursa ya kuulizwa maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, pamoja na umuhimu wa huduma za ugani na upatikanaji wa pembejeo lakini bado huduma hizi haziwafikii wananchi kwenye maeneo ya chini kule ambako ndiko kwenye uzalishaji. Nini sasa mkakati wa Serikali ili kuondoa tatizo hili?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kama ilivyo kwa zao la pamba, zao la muhogo ambalo limekuwa muhimu sana kwa wananchi wa Visiwa vya Ukerewe kiuchumi, lakini hata kwa chakula limekuwa linakabiliwa na matatizo mengi sana ya magonjwa, lakini hata tatizo la ardhi kwenye eneo la Visiwa vya Ukerewe. Je, Serikali ina mkakati wowote wa kutuma timu ya wataalam kufanya utafiti ili basi Visiwa vya Ukerewe vitumie ardhi yake hii ndogo kwa tija zaidi katika kuzalisha zao hili la muhogo? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA):
Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi kujibu maswali la Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kuhusu mikakati ya Serikali tuliyo nayo kwa ajili ya pembejeo na Maafisa Ugani. Kwanza tumezielekeza Halmashauri zote nchi ni kutenga asilimia 20 ya mapato yao ya ndani kwa maagizo ya Serikali kupitia Waziri Mkuu kwa ajili ya kupeleka kwenye sekta ya kilimo ili Maafisa Ugani hawa waweze kuwezeshwa kwa ajili ya kuwafikia wakulia kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, lakini pili, viongozi wote wa Serikali katika ngazi mbalimbali, hasa wale wanaosimamia sekta ya kilimo tumewaambia lazima washiriki katika kilimo ili mashamba yao pia yaweze kuwa mfano kwa wakulima wale ambao wapo wanazunguka. Tunafahamu pia kwamba tuna upungufu mkubwa wa Maafisa Ugani nchini, mahitaji ni zaidi ya 20,000 lakini tulio nao ni 6,800. Tunaendelea kuongea na wenzetu wa Wizara ya Utumishi kwa ajili ya kuongeza Maafisa Ugani nchi nzima ili wawafikie wakulima wetu kwa ajili ya kanuni bora za kilimo.
Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusu zao la muhogo kukubali kule Ukerewe pamoja na vituo vyetu vya utafiti, tuko tayari kama Serikali na tunawaagiza kituo chetu cha utafiti cha pale Ukiruguru, Mwanza pamoja na Ilonga kufika maeneo hayo ya Ukerewe kwa ajili ya kufanya utafiti wa udongo kuona namna gani zao hili linaweza kulimwa katika Visiwa Vya Ukerewe.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, Serikali imekiri kabisa katika majibu haya kwamba sheria iliyopo sasa hivi ni ya mwaka 2001 na kanuni za mwaka 2012. Ni ya zamani kweli kweli, lakini vilevile mwaka 2006 Serikali ilisaini Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kudhibiti Matumizi ya Tumbaku na mwaka 2008 Bunge lako liliridhia mkataba huo. Sasa hivi ni ziadi ya miaka 10, mkataba huo bado haujawa domesticated ndio maana nasema sheria hii haijaletwa hapa Bungeni ili iweze kurekebishwa.
Je, majibu haya ya Serikali ni kweli mwaka huu wataleta sheria hiyo Bungeni hapa sio kuniridhisha mimi? La kwanza hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kwa bahati mbaya sana zao la tumbaku uzalishaji wake unashuka kila mwaka badala ya kupanda bahati mbaya sana na mwaka huu imekuwa mbaya zaidi kwamba hivi ninavyoonge viko vyama vya msingi vya wakulima ambavyo havijapata makisio. Kwa hiyo hawajui kwamba mwaka huu watalima tumbaku au hawatalima na mwezi huu wa tisa ni wa mwisho wa matayarisho.Kwa mfano, Jimboni kwangu kuna Chama cha Msingi cha Upendo...
... na Kikola. Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusu jambo hili?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA):
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na namshukuru Mheshimiwa Mwambalaswa kwa swali nzuri. Ni kweli kama Serikali tuliridhia mkataba huo tamko hilo kwa ajili ya kupunguza matumizi ya tumbaku duniani ikiwemo Tanzania na ni kweli kwamba Serikali kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi kwamba tuko kwenye mchakato wa kufanya marekebisho mbalimbali na tumedhamiria mchakato huu ukikamilika tutaileta haraka iwezekanavyo katika Bunge lako hili tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kwamba ni kweli matumizi ya tumbaku au mahitaji ya tumbaku kila mwaka yanaendelea kupungua kutokana na hili hili azimio ambalo tulilisaini na nchi nyingi ambao wamelisaini pia. Kwa hiyo, zao la tumbaku lina masharti mengi sana sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mwaka jana tulitakiwa kwamba Tanzania kuzalisha tani 72,000 lakini mwaka huu ni tani 55,000 tu kwa sababu tumepata masharti mapya, sasa hivi uzalishaji wa tumbaku kwamba sharti mojawapo kwamba yale mabani yatumie muda miti iliyopandwa na mzalishaji mwenyewe. Na wameshatoa notice ikifika mwaka 2020 kama bado tumbaku yetu tunakausha kwa kutumia miti ya asili maana yake tunaharibu mazingira hawatanunua tumbaku yetu hata kilo moja.
Kwa hiyo, nitoe wito kwa wakulima wote tuzingatie sheria hii kwa sababu tumesharidhia, tuanze kupanda miti yetu ya kisasa kwa ajili ya kufanya ukaushaji wa tumbaku hiyo, la sivyo, soko hilo tutakuwa tumelipoteza kabisa na kilimo hichi kitakuwa kimekwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la mwisho ni vizuri tukafanya diversification of crops yaani tukaangalia na mazao mengine kulima. Kwa sababu zao hili kila siku linaendelea kupigwa vita na wahitaji wenyewe, ahsante.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Naibu Waziri kwa kuteuliwa lakini pia nimpongeze kwa majibu mazuri aliyonipatia. Pamoja na majibu hayo mazuri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Taifa hili hutumia fedha nyingi sana kuagiza mafuta ya kula ukiachilia mafuta ya petroli, lakini nchi hii ina uwezo wa kuzalisha mafuta ya kutosha ya kula na tukaacha kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi. Katika nchi yetu kuna viwanda vingi vinavyokamua mafuta kwa mfano, Kiwanda cha Mount Meru ambacho kina uwezo wa kukamua mafuta tani 400,000 lakini kwa sasa wanapata tani 40,000 tu ukiachilia viwanda vingine.
Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuhakikisha kwamba Mikoa ya Dodoma, Singida na Manyara wanawekwa kwenye mkakati maalum wa kuzalisha mazao ya mafuta na hata Mkoa wa Kigoma unaozalisha mafuta ya mawese, kwamba sasa mkakati uwekwe kwa kupata mbegu bora kwa ajili ya kuzalisha mazao yanayozalisha mafuta, ni mkakati gani umewekwa na Serikali? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, sisi wananchi wa Dodoma ni wakulima wazuri sana wa zabibu na tunazalisha mara mbili kwa mwaka lakini hatuna soko. Zabibu zinaoza mashambani kwa sababu wakulima wamekosa masoko. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba zabibu zote zinazozalishwa na wakulima zinapata soko? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA):
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi ya kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bura, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ni kutaka kujua mkakati wa Serikali kwa ajili ya kuweza kuzalisha mazao ya mbegu ya mafuta hapa nchini ili kumaliza tatizo la mafuta hapa nchini ili kuokoa fedha za kigeni. Serikali ya Awamu ya Tano ikiongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 4 Juni, 2018 ilizindua Programu Maalum ya Kuendeleza Kilimo, kwa Kiluguru tunaita ASDP II ambapo lengo lake ni kuongeza uzalishaji na tija kwa ajili ya mazao ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na mpango huo Mheshimiwa Waziri Mkuu alianza utekelezaji huo tukaenda Mkoa wa Kigoma kwa ajili ya kuzindua na kuendeleza kilimo cha mchikichi, ikafuatiwa na kikao cha wadau kilichofanyika tarehe 24/05 pale Morogoro kwa maana ya kampuni yetu ya uzalishaji mbegu ya ASA, Kampuni ya Utafiti wa Mbegu (TARI) pamoja na Kampuni ya Udhibiti wa Mbegu (TOSCI) wamepanga mikakati na tumekubaliana kama Serikali kuanza kufufua zao la mchikichi kwa ajili ya kuzalisha ndani ya miaka minne miche milioni 20 ili kumaliza tatizo hilo sambamba na kuongeza mbegu bora katika zao la alizeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu zabibu, kwanza nimpongeze Mheshmiwa Mbunge kwa kuwatetea watu wake wa Dodoma ambao ni maarufu kwa kilimo cha zabibu hapa nchini lakini ni kweli bei ya wine inayotokana na zabibu ya Tanzania ipo juu kuliko ya wine zinazotoka nje ya nchi. Hii inatokana na sababu ya gharama kubwa za uzalishaji hapa nchini na tija ndogo wanayopata wakulima, wanatumia gharama kubwa lakini wanapata faida ndogo. Serikali tumeliona hilo na kwa sasa tunapitia na wenzetu wa Wizara ya Fedha kuangalia mfumo wa kodi zetu na ushuru ili kupunguza gharama za uzalishaji kuwezesha wine hii kuuzwa kwa bei nafuu ili soko liwe la uhakika. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mazingira ya Mkoa wa Simiyu yanafanana na mazingira ya Mikoa ya Kati kwa zao la alizeti lakini wakulima wa Simiyu wamekuwa wakilima zao hili kwa kubahatisha mbegu za alizeti zisizo na tija ukilinganisha na Mikoa ya Kati. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuleta mbegu zenye tija ikiwemo na kutoa elimu kwa wakulima wa Mkoa wa Simiyu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa majibu yangu ya swali la msingi nilizungumzia mikakati iliyopo kwa Shirika letu la ASA, TOSKI na TARI. Mbegu zipo na nawaelekeza watu wa ASA wapeleke mbegu kule kwa Mheshimiwa Mbunge ili mbegu hizi zipatikane kwa gharama nafuu kwa hii mbegu aina ya Record. Pia kuna makampuni binafsi ambayo yamethibitishwa na Taasisi yetu ya Kudhibiti Ubora ya TOSCI yanauza mbegu kihalali nayo nayaomba yapeleke mbegu katika Jimbo la Mheshimiwa Mbunge ili wananchi wapate mbegu kwa urahisi zaidi.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi wa Mkoa wa Singida ni wakulima wazuri wa zao la alizeti, je, Serikali haioni umefika wakati sasa wa kulifanya zao hili la alizeti kuwa ni zao la kimkakati ili kuongeza tija na kipato kwa wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA):
Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la alizeti ni moja ya zao la kimkakati. Kama unavyofahamu kipaumbele cha kwanza cha Serikali ni mazao ya chakula na alizeti ni moja ya mazao ya chakula. Kwa hiyo, lipo kwenye zao la kimkakati na ndiyo maana lipo chini ya Bodi ya Mazao Mchanganyiko.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wanasayansi wamefanya utafiti na wanasema kwamba vyombo vya plastiki vikikutana na joto kali vinasababisha madhara makubwa sana kwa afya ya binadamu kwa sababu yanatoa kemikali fulani inayoitwa BPA. Je, Serikali inalitambua hili na kama inalitambua inachukua hatua gani kuwasaidia wakulima hawa wa alizeti ambao wanauza mafuta yao barabarani na yanapigwa jua kali sana? Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba wanahifadhi mafuta hayo ipasavyo ili wananchi wetu wasipate madhara hasa ya kansa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli bidhaa za plastiki kuwekea vyakula hasa vya moto kuna madhara yake lakini kwa haya ya baridi bado tunafanyia utafiti katika Serikali na tumeshaagiza taasisi zetu za utafiti wafanye utafiti kujua madhara yanayopatikana kwa mafuta kuwekwa kwenye vyombo vya plastiki ili wakituletea majibu tutakuja kumpa Mheshimiwa Mbunge.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Licha ya majibu mazuri ya Naibu Waziri nina maswali mawili mafupi ya kuuliza. Swali la kwanza; kwa kuwa tafiti bado zinaendelea kwenye Taasisi zetu hapa nchini na mara kwa mara tafiti hizi huchukua muda mrefu ili mbegu ziweze kutolewa na kuthibitishwa na kuanza kutumika kwa wakulima. Je, kwa msimu huu kuna mkakati gani wa Serikali wa kuwawezesha wakulima kupata mbegu hizi ambazo hazipatikani mara kwa mara?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa viwanda vyetu vinakabiliwa sana na tatizo hili la malighafi ya alizeti ili viweze kuzalisha mafuta ya kutosha ya alizeti ambayo ni mazuri sana kwa upande wa lishe. Je, kuna mkakati gani wa kuhamasisha wakulima katika mikoa mbalimbali hapa nchini ili waweze kulima zao hili la alizeti ili tuweze kupata mafuta ya kutosha hapa nchini?
Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA):
Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kama nilivyotangulia kujibu kwenye swali la msingi, kuna mbegu zaidi ya aina tano mpya zimeshasajiliwa na vituo vyetu ambavyo nimevitaja. Kwa hiyo lile tatizo la zamani, kwamba mbegu ya record ilikuwa haizalishwi vizuri na haitoi mafuta vizuri lilishamalizika kwa sababu vituo vyetu hivi vya utafiti vimefanya utafiti na vimeshaiboresha. Kwa hiyo sasa hivi inazalisha zaidi ya asilimia 48 mpaka 50.
Mheshimiwa Spika, kuanzia sasa ni kwamba mbegu hizi zinapatikana, tuna mawakala tumewaongeza kwa hiyo sasa upungufu huo hautakuwepo. Pia tumeweza kuendeleza shamba letu la Msimba. Tumeshapata wafadhili, wadau wa maendeleo na Serikali, tumeongeza bajeti kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji kwenye shamba la Msimba kule Kilosa ili kuongeza uzalishaji wa mbegu na kumaliza tatizo hili.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuhusu mikakati ya kuhamasisha wananchi. Mikakati hiyo kama Serikali tumeshaianza.
Mheshimiwa Spika, mkakati wa kwanza ni kuingiza mazao yote yanayotakana na mbegu za mafuta kwenye zao la kimkakati, mbegu za mafuta kwa maana ya alizeti, michikichi, nazi, karanga, ufuta, soya na mengineyo, yote sasa tutayaundia bodi kwa ajili ya usimamizi wa kuzalisha mbegu hizi na kumaliza tatizo la upatikanaji wa mazao ya mbegu ya mafuta nchini na kuongeza uzalishaji wa mafuta wa hapa hapa nchini badala ya kuagiza nje ya nchi .
Mheshimiwa Spika, lakini pia katika hamasa hiyo tumeanza kama miezi miwili iliyopita Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa pamoja na Wizara ya Kilimo tulikwenda Mkoani Kigoma kwa ajili ya kufua na kuhamasisha uzalishaji wa mazao ya mbegu mafuta nchi nzima kwa kuanzia na zao la michikichi. Kwa hiyo mikakati hiyo ndani ya Serikali tumeshaianza na hivyo nimwondoe hofu tu Mheshimiwa Mbunge; Serikali tunalitambua hilo. Lengo letu kubwa ni kuanza kujitosheleza kuzalisha mafuta ndani ya nchi ili tuweze kuokoa fedha za kigeni .
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, asante, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini bado kuna changamoto moja ameiacha katika Korosho ambayo ni changamoto ya malipo kwamba mpaka leo Serikali inasuasua kuwalipa Wakulima waliouza Korosho zao. Wapo Wakulima ambao wamepeleka Korosho zao ghalani lakini wamelipwa pesa ambayo haikidhi au hailingani na kiwango walichopeleka. Lakini pia wapo Wakulima ambao mabodi display zinaonesha kwamba wamelipwa tayari lakini wakienda benki pesa hizo hazipo, kwa hiyo kuna malipo hewa. Kwa hiyo, nilikuwa naomba kujua Serikali kwa nini haielezi ukweli juu ya malipo ya Korosho kwa Wakulima wa Korosho.

Mheshimiwa Spika, swali la pili nilikuwa naomba kujua kwamba Serikali imekusanya Korosho hizi zikawekwa kwenye maghala Mtwara na Lindi na maeneo mengine na Korosho zinahifadhiwa haizidi miezi mitatu, Korosho zimeanza kuota hivi sasa zingine. Je, Serikali haioni kwamba inalitia hasara Taifa hili kwa kuziweka Korosho hizi bila kuzibangua?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kujibu swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Nachuma. Kwanza sisi kama Serikali au Taasisi ya Serikali iliyopewa jukumu hili bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko tunalipa pesa kwa wakulima, na mpaka jana kiasi cha Korosho tulizokusanya ni zaidi ya tani laki mbili kumi na tatu na tumeshafanya uhakiki zaidi ya tani laki moja na ishirini na tisa na tani laki moja na kumi na sita ndizo tulizozilipa.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu Mheshimiwa Mbunge ajue kufahamu kwamba malipo hatuwezi kuanza kulipa kabla ya kujiridhisha katika uhakiki na pesa hii niwahakikishie kwamba pesa zipo na mimi mwenyewe na Mheshimiwa Waziri Mkuu tumetoka juzi huko ambao kulikuwa kweli na changamoto hasa kwenye malipo ya daraja la pili ambao mwanzo pale tuliona mkazo kuanza daraja la kwanza lakini kuanzia jana wameanza kulipwa pia na Korosho daraja la pili hasa Mikoa ya Pwani na Mikoa ya Tanga.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anazungumzia kuhusu hasara ambayo kwa kuweka Korosho muda mrefu, kwanza ni kweli Korosho sio kama zabibu kwa sababu zabibu ukiiweka muda mrefu ndio ukali wake unaongezeka lakini Korosho kila unavyoiweka ubora wake unazidi kushuka. Hilo tunalifahamu na ndio maana tumeshaingia mikataba na wabanguaji wa ndani wameshaanza kubangua na sasa hivi tuko kwenye mazungumzo ya mwisho kwa ajili ya kuuza tani zaidi ya laki mbili kwenye masoko ya Kimataifa muda sio mrefu Korosho zitaanza kusafirishwa nje ya nchi.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, asante nilitaka kuuliza swali la nyongeza, suala la ununuzi wa Korosho unaendana sambasamba na ulipaji wa wadau wanaoshiriki katika suala zima la Korosho, ununuzi unaoendelea mpaka sasa hivi halmashauri hazijapewa pesa yao ya ushuru hata senti tano. Nilitaka kuiuliza Serikali yangu, kwa kuwa Serikali imeamua kununua Korosho ni lini italipa ushuru wa halmashauri ili Bajeti zetu ziende kama tulivyozipanga?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hawa Ghasia Mbunge wa Mtwara Vijijini, kwanza ni kweli kuna watoa huduma mbalimbali katika zao la Korosho, na sisi kama Serikali tuliona mwanzoni kutokana na mkanganyiko uliokuwepo tuliweka mkazo zaidi kulipa kwamba wakulima kabla ya watoa huduma.

Mheshimiwa Spika, na mpaka sasa tulishalipa wakulima zaidi ya asilimia 59 sasa hivi tumeshaanza kulipa na watoa hudma wengine wakiwemo hao watu wa halmashauri, mpaka jana tulishalipa zaidi ya bilioni nne kwa wasafirishaji lakini tumeshalipa watunza maghala zaidi bilioni sita na tushalipa pia watoa huduma wengine wasambazaji wa magunia zaidi ya bilioni nne nukta nane.

Kwa hiyo na hiyo ya Halmashauri tunaifahamu tushawaambia watu wa vyama vikuu na vyama vya msingi watunze rekodi zao vizuri wote tutawalipa kwa sababu halmashauri na Serikali kuu wote ni wadau katika hili, Serikali kuu export levy na hawa hizo fedha za halmashauri zote Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi zipo kwenye mikakati na tutazilipa. Lakini la mwisho, nitoe ufafanuzi katika hili, ni kweli Serikali tunanunua Korosho lakini sio kwamba Serikali yenyewe ndio inanunua Korosho ni Taasisi ya Serikali ya Bodi ile ya nafaka ya mazao mchanganyiko ndio inayonunua Korosho, kama zinavyofanya biashara Taasisi zingine kama TTCL na zingine sio Serikali kuu.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru.

Kwanza nishukuru kwa majibu yenye kutia matumaini ya Serikali kupitia kwa Naibu Waziri. Lakini kwa kuwa usanifu wa awali ulionesha chanzo cha maji kwa ajili ya miradi hii ambacho sasa si cha kuaminika, Serikali sasa iko tayari kupitia usanifu ule ili chanzo cha maji kwa ajili ya mradi huu ukiwa ni Ziwa Victoria?

Swali la pili, kwa sababu mbali na Bonde hili la Miyogwezi, kuna Bonde la Bugolola lakini na maeneo mengine ambayo ni potential kwa ajili ya uzalishaji wa chakula kwenye Visiwa vya Ukerewe. Lakini yote haya tunaweza tukayatumia kwa ufanisi kama Mheshimiwa Waziri anaweza kufika pale akapitia na tukaweza kufanya maamuzi yenye maslahi.

Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari baada ya Bunge hili kuandamana na mimi ili tuweze kufika katika Visiwa vya Ukerewe tuweze kupitia mambo haya? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi anavyotumia muda mwingi kufuatilia na kuwapigania watu wake wa Ukerewe.

Pili, nimesikiliza ushauri wake na kwa niaba ya Serikali tunauchukua ushauri huo na nichukue nafasi hii kuwaelekeza Wahandisi wetu wa Kanda ya Umwaliaji, Kanda ya Mwanza kufika Ukerewe kuanza uchambuzi wa awali kuangalia hiko chanzo kipya na cha zamani ili kuja kutushauri kitaalam kuutekeleza mradi huo upya.

Swali lake la pili, kutaka kwamba kwenda kuambatana na mimi kufika katika eneo hili, Mheshimiwa Mbunge niko tayari baada ya Bunge hili likimalizika tarehe 8 Februari tuoanane ili tupange siku gani tunaweza kutembelea huko maeneo yake.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri sana ya Serikali ya kwamba katika Bajeti ya mwaka 2019/2020 mabwawa haya mawili sasa yatatengewa fedha kwa ajili ya ukarabati. Naamini kabisa hata wananchi huko waliko wanasikiliza, watakuwa wamefurahia sana haya majibu. Wako tayari kufuata maelekezo yoyote ya kiutaalamu yatakayotolewa na Serikali kuhakikisha kwamba mabwawa haya yatakapokuwa yametengenezwa na kukarabatiwa, yasije kupambana na tatizo hili tena.

Mheshimiwa Spika, nina ombi moja tu kwa Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba tuongozane naye, tuambatane naye, twende tukayatembelee haya mabwawa mawili kwenye Kata hizi, ili kwa pamoja tuwe na uelewa wa pamoja nini hasa kinatakiwa kufanyika kwenye haya mabwawa. Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru, nimekubali ombi lake. Nataka nimuahidi hapa kwa sababu Bunge lako tukufu litaahirishwa tarehe 8 Februari, basi tarehe 9 niko tayari kuambatana naye kufika Jimboni kwake, siyo kuangalia bwawa tu, ni pamoja na kuangalia kilimo cha zabibu.
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza. Kule Moshi kuna scheme ya umwagiliaji inaitwa Moshi Lower inayohudumia Kata za Mabogini, Arusha Chini na Kahe kwa wakulima wa mpunga na vitunguu. Wakati wa kiangazi, kutokana na uchakavu wa miundombinu na mabadiliko ya tabia ya nchi, kunakuwa na mgogoro mkubwa sana wa maji kwa sababu hayatoshi, lakini wakati wa mvua kunakuwepo na mafuriko ambayo yanaharibu vilevile miundombinu na hata hicho kilimo chenyewe. Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga kitu kama bwawa au miundombinu yoyote ya kuvuna hayo maji ili yaweze kutumika wakati wa kiangazi na kutatua mgogoro unaojitokeza wakati huu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Serikali kwanza tunaona umuhimu wa ujenzi wa bwawa hilo kwa ajili ya kuvuna maji ya mvua. Kwa hiyo, kwa niaba ya Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, tutatuma timu yetu ya Kanda ya Kilimanjaro kufika katika bwawa hilo kufanya tathmini ya awali, baadaye tutapanga pesa kutokana na uwezo wa kibajeti na upatikanaji wa fedha, ili kuweza kujenga bwawa hilo kwa ajili ya kuvuna maji ili yaweze kutumika wakati wa kiangazi.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza wakati Mheshimiwa Rais anasema kwamba Serikali itanunua korosho yote kutoka kwa wakulima na aliwatangizia wakulima wote wa Watanzania kwamba korosho kilo moja itanunuliwa Sh.3,300 kwa maana ya kutaka kuwasaidia wakulima wanyonge. Pia hivi karibuni tumeshuhudia Serikali hiyo hiyo inawalipa wakulima chini ya bei ya Sh.3,300 maeneo mengine Sh.2,600 na maeneo mengine chini hapo ikiwemo Mikoa ya Pwani, Mtwara pamoja na Lindi. Sasa nataka kufahamu kauli ya Serikali, Mheshimiwa Waziri hapa atuambie, je, ni kwa nini wanakiuka maagizo yaliyotolewa na Mheshimiwa Rais kwa ajili ya kuwalipa wakulima hao korosho zao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili kwenye majibu ya msingi ya swali (a) anaongelea suala la Bodi ya Mazao Mchanganyiko na kwamba ni ya wao kukusanya korosho ni pamoja na kuzuia biashara ya kangomba, lakini hapa kwenye majibu yake na tumeona karibuni kampuni ya INDO, kutoka Nairobi imepewa kazi ya kuuza korosho kwa niaba ya Serikali. Sasa nataka anitofautishie kangomba hii inayofanywa na Serikali kupitia INDO pamoja na Bodi ya Mazao Mchanganyiko kwa sababu wamesema wanaziuza korosho zile kwa faida, kuna tofauti gani na wale kangomba wadogo wadogo waliokuwa wanakusanya korosho kwa wakulima na kuzipelekwa kwenye Vyama vya Msingi?
NAIBU WAZIRI KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo ningependa kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mbunge wa Ndanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli, Serikali kupitia Mheshimiwa Rais aliutangazia umma wa Tanzania na ulimwengu kwamba korosho mwaka huu 2019 tutanunua kwa Sh.3,300 na ni kweli sasa tunanunua na tunalipa hivyo kwa korosho daraja la kwanza.

Mheshimiwa Spika, niendelee kuongeza jibu hilo Mheshimiwa Mwambe anafahamu, tunapozungumza korosho ina madaraja mawili makubwa; daraja la kwanza yaani standard grade na daraja la pili maana yake under grade, Mheshimiwa Rais alipokuwa anazungumza tunakwenda kununua korosho kwa Sh.3,300 maana yake ni kuhamasisha ubora katika nchi hii, kwamba hiyo ni bei ya daraja la kwanza. Kwa hiyo inafahamika kisheria na kikanuni mahali popote pale.

Mheshimiwa Spika, korosho daraja ya pili bei yake ni asimilia 80 ya bei ya daraja la kwanza. Ndiyo maana nilikwishawatangazia wakulima na wanafahamu wenyewe, daraja la pili litanunuliwa kwa asilimia 80 ya bei ya daraja la kwanza, maana yake inakwenda kununuliwa kwa Sh.2,640 na korosho hapo hapo ikizidi chini ya daraja la pili, haitanunuliwa, atarudishiwa mkulima akaichague ili ailete ama iwe daraja la pili au daraja la kwanza.

Mheshimiwa Spika, tulipomaanisha tunanunua korosho hatumaanishi tunanunua mpaka vigawe au mawe, mnafahamu mwaka jana 2019 nchi hii iliharibika duniani kwa kupata sifa potofu na mbovu, tumepeleka matofali badala ya korosho kwenye soko la kimataifa. Kama Serikali hatuwezi kurudia hilo na mtu yeyote hawezi kuchafua jina la nchi yetu na kuharibu ubora wa korosho yetu ikakosa soko katika soko la kimataifa.

Mheshimiwa Spika, swali la pili anataka kufahamu kati ya kampuni iliyonunua korosho kutoka Bodi ya Nafaka ya Mazao mchanganyiko na kangomba. Kwanza Mheshimiwa kuna mambo ya msingi tuyaweke kwenye mambo ya msingi kama nchi, siyo kila jambo linahitaji siasa, korosho ni uchumi, nilitarajia Waheshimiwa Wabunge tuwe pamoja katika hili kwa nia nzuri ya Serikali kupitia Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipoamua kununua korosho hizi kwa bei ya Sh.3,300 badala ya ile wakulima walikuwa wanakwenda kulipwa Sh.2,700 ambayo wameikataa wakulima wenyewe.

Mheshimiwa Spika, sisi kama Serikali tusingeweza kukaa kuona wakulima wanagoma, bei ni ndogo hailipi gharama zao, Serikali ndiyo imechukua jukumu hilo kuhakikisha kwamba tunanunua kwa Sh.3,300. Leo tunapopata wanunuzi ambao wananunua zaidi hilo, siyo kubeza, mlipaswa kupongeza la sivyo sasa hivi wakulima wote wangelipwa Sh.2,700.

Mheshimiwa Spika, anasema tofauti ni nini, katika biashara ya korosho kuna watu kwenye mnyororo wa thamani kuanzia mzalishaji, kuna mawakala, kuna madalali, kuna wafanyabiashara wadogo na kuna wanunuzi wakubwa, tofauti kati ya kangomba na yule, yule ni mnunuzi, hizi korosho tumezinunua au kuzikusanya kwa mkulima siyo kuzila ila kuziuza.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo yule ni mnunuzi kwenye soko la kimataifa, tofauti ya yule na kangomba, yule ananunua kwenye mfumo rasmi unaotambulika kisheria. Kangomba ni watu ambao wananunua korosho kinyume cha sharia. Kama tunavyofahamu korosho ni moja ya zao la kimkakati ambalo tumeliweka ununuzi wake kwenye mfumo rasmi tunanunua na tunakusanya kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani na kwa maana hiyo haruhusiwi mtu yoyote kwenda kununua ila ni Vyama vya Msingi na Ushirika..

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri ameelewa, yanatosha usiongeze, Mheshimiwa Naibu Waziri inatosha…

NAIBU WAZIRI KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba niongezee kidogo…

SPIKA: Inatosha kabisa.

NAIBU WAZIRI KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali, hata hivyo ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; je, ni kwa kiasi gani Serikali imesambaza tafiti hizo za gharama za uzalishaji kwa wakulima wa kahawa ili kuwawezesha kufahamu msimu hadi msimu kama wanauza kwa faida ama hasara?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; wakulima wengi wamekuwa wakilalamika juu ya bei duni ya mazao yao mwaka hadi mwaka; je, Serikali ina mkakati gani wa kufanya tafiti za gharama za uzalishaji kwenye mazao mengine ya kipaumbele kama pamba, tumbaku, chai, korosho yakiwemo mahindi ili kuwawezesha wakulima hao kufahamu gharama zao za uzalishaji na hivyo kufahamu kama wanauza kwa hasara au kwa faida mwaka hadi mwaka? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Msuha kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza anataka kujua matokeo ya tafiti hizi zimewafikia namna gani wakulima wa Tanzania; nataka nimueleze Mheshimiwa Mbunge, matokeo yote ya tafiti hizi tumeyifikisha kwa wakulima kwa njia mbalimbali; kwa njia ya mawasiliano ya television, radio na magazeti na vipeperushi vingine, lakini pia kwa kushiriki Taasisi zetu za TACRI na zingine zinazofanya utafiti wa kahawa na mazao mengine kwenye Maonyesho kama Nane Nane na maonyesho mengine ili wakulima na watu wengine wapate elimu ile pale. Pia zaidi, tuna mpango ambao ni endelevu ulioanza tangu SDP I wa kujenga kila kata vituo vya elimu kwa wakulima ili kutoa elimu kwa wakulima muda wote.


Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, anataka kujua kwamba, je, tafiti hizi za kujua gharama ya mazao mengine hasa mazao yale ya kimkakati na mazao ya mahindi ikoje. Kwanza nataka nimpe uelewa vizuri Mheshimiwa Mbunge na nimpongeze kwa kazi kubwa anayoifanya. Zao la mahindi ni moja ya zao la kimkakati. Labda Waheshimiwa wengi hapa wanashindwa kutambua kwamba kipaumbele cha kwanza cha Taifa ni mazao yale zamani tulikuwa tunaita mazao ya chakula. Kwa sasa hivi hatujaweka hiyo demarcation kwamba kuna mazao ya chakula na mazao yote ya biashara. Sasa hivi mazao yote ni ya biashara ila kipaumbele tumeyapa haya mazao nane ya mwanzo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kujua tumefanya tafiti ngapi; tumefanya kila zao na kila mwaka kupitia ikutano yetu yote ya wadau. Kwa mfano, nimpe kwenye zao la korosho, kilo moja ya kuzalisha korosho ni Sh.1,350 na kwenye kilo moja ya kuzalisha mahindi, heka moja inatumia Sh.740,000. Kwa hiyo, kila mwaka tunafanya na kupeleka elimu hii kwa wakulima.
MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini tunakubaliana kwamba masuala ya utafiti kwa ujumla nchini yamedorora sana. Hii ni kwa sababu vituo vya utafiti kikiwemo Kituo cha Utafiti Uyole - Mbeya viko hoi. Uyole iko hoi kimiundombinu na hata kibajeti. Sasa ni lini Serikali itatambua umuhimu wa vituo hivi kama zamani ili kuvipelekea bajeti stahiki tupate kuboresha kilimo nchini na hasa kituo cha Uyole Jijini Mbeya . Miundombinu iko hovyo, hata hali za wafanyakazi ziko hovyo. Before wakati tuko…

NAIBU SPIKA: Umeshauliza swali Mheshimiwa. Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo, majibu kwa swali hilo.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbilinyi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze kwa ajili ya kuviona vituo hivyo, lakini nataka nimhakikishie kwamba, kama Serikali hatujawahi kuviacha nyuma vituo hivi kama anavyodai na ndiyo maana mwaka juzi 2017, tulileta Muswada wa Sheria na Bunge hili likaridhia. Kwa ajili ya kuviboresha vituo vile, tuliweza kuunda Sheria maalum ile Sheria hatari na kuunda vituo vyetu nane vikuu na nane vidogo, jumla vituo 16 na kuvipangia majukumu mahususi kwa kila kituo mazao mawili mawili ili kuyapunguzia mzigo.

Mheshimiwa Naibu Spika, yote haya ni katika kuweka juhudi za msingi ili vituo hivi viwe na mazao machache ya ku-focus badala ya kubeba mazao yote na sasa hivi tuko kwenye mchakato wa bajeti na miongoni mwa vipaumbele tulivyovipa na katika hivi vituo vya utafiti kwenda kuviongezea uwezo pia kuviboresha miundombinu yake ili viweze kukidhi matarajio ya wakulima wa nchi hii.
MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na mikakati mizuri na mingi ya Serikali, lakini bei ya kahawa ya mkulima Mkoani Kagera bado ni Sh.1,000 kitu ambacho kinamuumiza mkulima. Kwa kuwa soko la kahawa linategemea soko la dunia, linategemea mauzo nje ya nchi, mahali ambapo mkulima wa kawaida au Vyama vyetu vya Ushirika hivi vya Msingi hawana uwezo wa kuyafikia hayo masoko. Pia kwa kuwa msimu unaofuata wa kahawa unaanza hivi keshokutwa mwezi wa Tano, ili makosa yasijirudie mkulima akaendelea kulipwa 1,000, je, Taasisi za Serikali ambazo zinahusika na utafutaji wa masoko wana mipango gani ya kwenda kule nje ya nchi wakawatafutia Watanzania masoko ikiwezekana wakaingia na mikataba na nchi hizo ili Watanzania wauze kahawa zao na waweze kupata bei nzuri? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwenye baadhi ya super market huko China imeonekana kahawa ambayo inaonekana imetoka Uganda imekaangwa tu haijasindikwa zaidi ya hapo na ikawekwa kwenye kifungashio kizuri, robo kilo inauzwa kwa dola 40 ambayo ni zaidi ya Tanzanian Shillings 88,000 wakati sisi mkulima anapata 1,000 kwa kilo. Je, Wizara zinazohusika kama Wizara ya Kilimo, Wizara ya Viwanda na Biashara, wanawaandaaje Watanzania kwa maana ya wakulima na wafanya biashara wasindike kahawa badala tu ya wakulima kuuza zile zilizo ghafi kusudi Mtanzania aweze kupata bei nzuri na hasa hasa mkulima kutoka Mkoa wa Kagera?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata nafasi hii. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mushashu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza anataka kujua mikakati iliyopo kwa ajili ya kuongeza bei ya mkulima kutoka Sh.1,000 wanayolipwa sasa mpaka ile ambayo itaridhisha na kukidhi gharama za uzalishaji. Kwanza kwa niaba ya Serikali, Wizara ya Kilimo, baada ya kuona changamoto hiyo ya zao la kahawa, bei yake na mazao mengine, tumeanzisha Kitengo cha Utafiti wa Biashara na Masoko ambacho kimeanza kazi tangu tarehe Mosi Julai, 2018. Lengo la kitengo hiki ni kuratibu na kufuatilia mwenendo wa masoko duniani na kutoa taarifa sahihi kwa wakulima wetu wakishirikiana na wenzetu wa Wizara ya Viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa pili tunashirikiana kwa karibu sana na Balozi zetu zilizokuwa nje. Hapa nichukue nafasi kumpongeza sana Balozi wetu wa China, Ndugu Kairuki kwa kazi kubwa anayoifanya na ameweza kutupatia soko jipya la kahawa nchini China lakini pia na Mabalozi wa nchi nyingine kama za Japan, Ujerumani, wote hawa wamekuja na mikakati mizuri na kupanua soko la kahawa yetu inayotoka hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili anataka kujua kwamba mikakati ya kuongeza thamani ya mazao yetu ikiwemo kahawa ili kahawa hii badala ya kuuzwa ghafi tuweze kuiuza wakati imechakatwa. Kwanza niendelee kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa muono huu, lakini nataka nimwambie kwamba Serikali tulishaanza muda mrefu mipango hii na ndiyo maana siyo kwa zao tu la kahawa, hata korosho umeona mwaka huu tumeanza kubangua na mwakani Insha Allah tutabangua zaidi ya asilimia 50 kwenda juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali lake la msingi la kahawa; pia tulishaanza kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vyetu na kiwanda kimojawapo cha Amir Hamza kimeshaanza kuchakata kahawa ya Mkoani Kagera kwa ajili ya kuiuza kahawa iliyokuwa imeshachakatwa badala ya kuuza kahawa ghafi. Pia kwa wakulima hawa tunaendelea kuwasisitiza wajiunge kwenye vikundi vyao vya ushirika ili Serikali tuweze kuwasaidia kwa ukaribu kwenye umoja wao kuongeza mitaji na kununua mashine ndogo ndogo za kuchakata mazao yao, kuuza mazao ya kahawa iliyosagwa badala ya kuuza kahawa ghafi.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mwaka jana kwenye msimu wa kahawa, Serikali ilitangaza bei elekezi Sh.1,400 lakini wakulima wamelipwa Sh.1,106. Ni kwa nini wamelipwa hiyo badala ya bei elekezi iliyoelekezwa na Serikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafsi hii. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bilakwate kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kupitia Bodi ya Kahawa, mwezi Julai mwaka jana ilitangaza bei elekezi ya Sh.1,400 ya kahawa. Bei elekezi ni bei ya chini anayotakiwa kulipa mkulima maana yake kama tungeruhusu wafanyabiashara binafsi kununua, lakini kahawa hii haikununuliwa na wafanyabiashara binafsi, ni wakulima wenyewe kupitia Vyama vyao vya Msingi na Vyama Vikuu vya Ushirika waliamua kwenda kuuza kahawa yao kule mnadani Moshi. Kwa hiyo kama wakulima wenyewe kupitia vyama vyao ndiyo waliamua kwenda kuuza kule baada ya kukusanya kahawa yao, kwa hiyo wanakwenda kulipwa kutokana na bei waliyouza kwenye mnada, siyo bei iliyotangazwa ile elekezi kwa sababu hakuna mfanyabiashara binafsi aliyenunua kwa wakulima kule Moshi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hivi Vyama vya Ushirika siyo wafanyabiashara bali wanakusanya kwa niaba ya wanachama wenzao, kwa niaba ya wakulima wenzao baadaye wanakwenda kuuza kwa pamoja kule Moshi na ndiyo maana kwamba sasa hivi kutokana na myumbo wa bei mwaka jana, bei ilishuka kwenye soko la dunia na ikaathiri mnadani pale Moshi na ndiyo maana sasa bei hiyo wanakwenda kulipwa kwa kuzingatia bei iliyouzwa hiyo kahawa.
MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu na Naibu Waziri anayejibu maswali kule Kagera walifika na wakafanya mambo lakini nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kutoa bei elekezi kama alivyouliza Mheshimiwa Bilakwate kahawa ikauzwa kwa Sh.1,000, huku Karagwe hamna shida lakini ukija Muleba, Bukoba Vijijini, Misenyi bei ya Sh.1,000 watu hawajalipwa mpaka leo, mnasubiri nini? Si muende kama milivyoenda kwenye korosho watu wapate haki zao? Kahawa ipo kwenye maghala lakini mpaka leo watu hawajalipwa na ninyi Wizara ya Kilimo mmenyamaza. Nataka nipate majibu, ukienda Muleba, Chama cha Msingi Magata, Misenyi, Katoro, Kaibanja, Kazinga watu wana shida na kahawa mmeshachukua na hela hawajalipwa, ni lini watalipwa hela zao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Alhaj Abdallah Bulembo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la nyongeza la Mheshimiwa Bilakwate, sisi Serikali hatujanunua kahawa ya wakulima wa Tanzania popote pale. Wakulima hawa kwa kupitia vyama vyao vya msingi na vyama vikuu waliamua kwa hiari yao kwenda kuuza kahawa wenyewe kule mnadani Moshi. Kilichotokea kwenye Wilaya hizi alizozitaja Muleba, Bukoba na Bukoba Vijijini na sehemu nyingine ni kwamba kahawa yao wameshakoboa, wamefika pale Kilimanjaro Moshi kama nilivyosema kutokana na kuyumba kwa bei kwenye soko la dunia na uzalishaji mkubwa uliotokea kwa nchi ya Brazil kuingiza sokoni zaidi ya magunia milioni saba mwaka jana ikaathiri bei nzima ya kahawa na kusababisha bei kushuka chini mno.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa sababu walienda kuuza wenyewe maana yake ile bei imewakuta wao moja kwa moja. Kilicholewesha mpaka sasa kutolipwa fedha zao ni hiki Chama cha KCU hakijauza kahawa yote. Kwa hiyo, sehemu nyingine hawajalipwa kwa sababu wenyewe hawajauza kahawa hiyo. (Makofi)
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza niishukuru Serikali kwa majibu yake mazuri, lakini sasa naomba nimuulize Naibu Waziri maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, Serikali ipo tayari sasa kuipa kipaumbele Skimu ya Umwagiliaji ya Ishololo ili iweze kuleta tija kwa wakulima wetu mara itakapokuwa imepata fedha?

Mhesimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni lini Serikali itachimba bwawa katika Skimu ya Umwagiliaji ya Nyida ambayo imekuwa ikitegemea maji ya mto ambao ni wa muda?

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Azza Hillal Hamad, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Azza Hillal kwa kuonesha uongozi kwa mfano. Tunamfahamu ni mdau wetu mzuri katika sekta ya kilimo, ni mkulima mkubwa wa mpunga, anawaongoza watu wake wa Shinyanga yeye mwenyewe kwa kuwa mbele na wale wanaoongozwa kuwa nyuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza kujibu swali lake la nyongeza la kwanza, nimhakikishie kwamba Serikali ipo tayari kuipa kipaumbele hii Skimu ya Ishololo pale ambapo tutaanza kupata pesa. Kama nilivyosema kwenye majibu yetu ya awali, tumeshaanza mazungumzo na wadau wetu mbalimbali ikiwemo Serikali bya Japan kupitia Shirika lake la JICA.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili kuhusu suala la ujenzi wa bwawa katika hii Skimu ya Nyida, nimhakikishie Mheshimiwa Azza Hillal Serikali inafahamu na ipo katika mipango mikakati yetu kwa miradi yote ile inayotumia maji katika mito ambayo ni ya msimu kuijengea mabwawa ukiwemo huu wa Nyida ili tuweze kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuleta kilimo chenye tija, chenye manufaa kwa wakulima wetu.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu ya Serikali lakini pia
nichukue fursa hii kuishukuru Serikali kwa kupeleka mnada wa kahawa Wilayani Mbinga kuanzia msimu ujao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kumetokea changamoto kadhaa katika mfumo huu mpya ikiwemo kuchelewesha malipo kwa wakulima, wakulima kulipwa bei tofauti lakini pia kukosekana kwa uaminifu kwa baadhi ya watendaji wa AMCOS. Je, Serikali imejipangaje kutatua kero hizi kwenye msimu ujao wa kahawa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kumekuwepo mabadiliko ya bei msimu kwa msimu, je, Serikali inajipangaje ama ina mpango gani wa kuanzisha Mfuko wa Kuimarisha Bei ya Kahawa (Price Stabilization Fund) ili kuondokana na tatizo hili la mabadiliko ya mara kwa mara ya bei ya kahawa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Martin Msuha, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anataka kujua changamoto zilizojitokeza katika msimu uliopita hasa ya kuchelewesha malipo kwa wakulima pamoja na wakulima kulipwa bei tofauti na bei ambayo ilitangazwa na Serikali ama iliyouzwa mnadani. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Msuha kwa ufuatiliaji wa wakulima wa kahawa nchi nzima kupitia wakulima hawa wa Mbinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kujibu swali lake napenda kusema kwamba madai yake ni ya kweli, mimi mwenyewe nilifika katika Mkoa wa Ruvuma na tuliongea na wakulima walithibitisha hilo. Kilichotokea mwaka jana kama unavyokumbuka, ndiyo ulikuwa mwaka wa kwanza kutumia mfumo huu wakulima wenyewe kwenda kuuza kahawa yao Moshi kupitia vyama vyao vya ushirika. Kwa hiyo, kahawa ile walivyokoboa na kuipeleka mnadani ilichelewa sana kuuzika kutokana na anguko kubwa la bei katika soko la dunia na katika soko la mnada hapa nchini. Kwa sababu walienda kuuza wenyewe, ilikuwa hamna namna nyingine lazima wasubiri mpaka kahawa iuzwe ndipo walipwe. Hata hivyo, kadiri watakavyoendelea kuuza kwenye mnada ndivyo hivyo wakulima wataweza kulipwa pesa zao kwa kuzingatia na mauzo kwenye mnada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili amesema kwamba tumejipangaje. Mwaka huu tumejipanga kupeleka minada hiyo katika kanda zao lakini pili ni kuruhusu wakulima wenyewe kupitia vyama vyao vya ushirika kama wakipata soko la moja kwa moja kuuza nje ya nchi tutatoa vibali hivyo ili wauze moja kwa moja. Kwa taarifa tu ni kwamba mpaka sasa tumeshapata wanunuzi ambao wapo tayari kuingia mkataba na Serikali kwa ajili ya kuuza kahawa hiyo kupitia mnada wa moja kwa moja (direct export market) kwa ajili ya kahawa hiyo na tayari mahitaji ya wanunuzi wale ni makubwa kuliko uzalishaji uliopo nchini.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Zao la kahawa lina matatizo makubwa sana nchi nzima na matatizo yanayolikabili ni pamoja na pembejeo na bei yenyewe ya kahawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi hapa Dodoma tulikuwa na kikao cha wadau na Mheshimiwa Waziri uliongea vizuri sana, uzalishaji unapungua kila mara na maeneo mengine kwa mfano kwangu kule Rombo wanaamua kung’oa kahawa ile ya zamani wanapanda ndizi na kabichi. Je, ni mkakati gani ambao Serikali inao kuwasaidia wakulima ili kunyanyua kiwango cha uzalishaji wa kahawa yetu ambayo katika soko la dunia inasemekana ni kahawa tamu sana ukilinganisha na kahawa kutoka maeneo mengine?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Selasini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, anataka kujua Serikali tuna mkakati gani wa kuongeza tija na uzalishaji wa zao la kahawa ili kuvutia bei nzuri kwa wakulima. Mkakati wa kwanza ni kwamba sasa hivi tupo kwenye mazungumzo ya makampuni ambayo yanatengeneza mbolea kama OCP kutoka Morocco ili kujenga kiwanda kikubwa cha mbolea hapa nchini ili kurahisisha upatikanaji wa mbolea na pembejeo zingine kwa ajili ya kupunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kupitia Shirika letu la Maendeleo la Taifa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo, tunawawezesha wakulima kwa kuwapa mikopo na Serikali inadhamini zaidi ya asilimia 80 ya matrekta na nyenzo zingine za kilimo kwa ajili ya kupunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima. Lengo ni kuongeza tija na uzalishaji, kama alivyosema tuna miaka zaidi ya kumi hatujaweza kuongeza uzalishaji wa kahawa.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Pamoja na kupongeza ziara nzuri ya Mheshimiwa Rais Magufuli kwa baadhi ya Mikoa ya Kusini ambayo inalima korosho, Serikali itakubaliana na mimi kama ilivyotokea kwenye kahawa mabadiliko ya mfumo wa ununuzi wa korosho yameathiri mapato ya Halmashauri ambazo zilikuwa zinategemea ushuru wa korosho. Halmashauri nyingi kwa asilimia 70 mpaka 80 zilikuwa zinategemea mapato haya. Serikali ipo tayari kufanya tathmini ya madhara yatakayojitokeza baada ya maagizo ya Mheshimiwa Rais kwamba pesa hizi zisidaiwe na hivyo kuangalia namna ya kufidia ili hizi Halmashauri zisiathirike zaidi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Nape, Mbunge wa Mtama, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la msingi anasema kwamba, je, Serikali ipo tayari kufanya tathmini ya athari zilizopatikana kwa kushuka mapato ya Serikali ya Halmashauri? Kwanza nichukue nafasi hii kusema kwamba Serikali haijabadili mfumo wa ununuzi wa korosho hapa nchi. Kama mnavyofahamu tuliingia kwenye mfumo huo baada ya wakulima wenyewe kukataa kuuza katika mnada uliokuwa halali kwa wanunuzi wale kutokana na bei ambayo haikuwavutia zaidi ya minada mitatu minne. Kama Serikali tusingeweza kuangalia hali ile iendelee ndiyo maana tuli- intervene ili kuhakikisha wakulima hawa wanapata bei nzuri wanayostahili. Wakati ule tunaingia tulikuwa tunafahamu bei ni ndogo lakini tulienda kuwalipa wakulima bei ya Sh.3,300 ambayo ilikuwa huwezi kuipata mahali popote duniani zaidi ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, swali lake la kama tupo tayari kufanya tathmini, napenda kusema kwamba tupo tayari na tumeshaanza kufanya tathmini hiyo lakini mapato yale ya Halmashauri ni ya Serikali na iliyolipa ni Serikali, kwa hiyo, Serikali haiwezi kumlipa Serikali mwenzie. Msimu ujao tutajipanga vizuri na mfumo utakuwa kama ulivyokuwa, mapato ya Halmashauri watayapata kupitia mfumo utakaokuwepo.
MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kutokana na swali la msingi, niipongeze Wizara ya Kilimo na Waziri Mkuu kwa kazi waliyoifanya Kagera. Wakulima wa kahawa Mkoa wa Kagera wa Muleba, Misenyi na Bukoba Vijijini kupitia KDCU na KCU mpaka leo kuna ambao hawajalipwa malipo yao ya kupeleka kahawa KDCU na KCU. La pili, bado kuna wakulima ndani wana kahawa…

MWENYEKITI: Swali ni moja tu Mheshimiwa.

MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itoe tamko kwa wale wakulima ambao hawajalipwa haki yao, ni lini watalipwa haki yao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Alhaj Abdallah Bulembo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna baadhi ya wakulima waliouza kupitia Vyama vya Ushirika vya KCU na KDCU hawajalipwa malipo yao mpaka sasa hata wale wa Tarime Vijijini katika Mkoa wa Musoma. Kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, walioenda kuuza kahawa ile ni wakulima wenyewe kupitia vyama vyao vya ushirika kwenye mnada wa Moshi, kwa hiyo watalipwa baada ya kahawa yao kuuzwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichotokea katika msimu wa mwaka jana kahawa ilianguka sana sokoni kwa hiyo wakulima wale waliona siyo busara kuuza kwa bei ya chini kuliko gharama za uzalishaji walizoingia. Pia, kahawa hii ambayo ikikobolewa inatoka madaraja zaidi ya matano, wakati mwingine inachelewa kwa sababu imeuzwa daraja moja, madaraja mengine hayajauzwa. Kwa hiyo, wanasubiri ili kuuza kahawa yote na kwenda kuwalipa wakulima na wanachama wao. Kwa hiyo, naomba waendelee kuwa na subira kwa sababu kahawa hiyo wameuza wenyewe kila wanapouza watalipwa.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kumekuwa na utaratibu wa hizi AMCOS zetu kuajiri ama kutokuwa na vigezo vya wale ambao wanaajiriwa kwamba hawawekewi elimu ni kiwango gani na kwa kiasi kikubwa wahasibu ndiyo wanakuwa ni watu pekee wenye elimu kiasi ambacho kinapeleka kufanya hujuma nyingi sana kwenye hizi AMCOS. Naomba kujua Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba wale ambao wanafanyia kazi hizi AMCOS wanawekewa vigezo vya kielimu ili wakulima wasiweze kuibiwa kama ilivyo hivi sasa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maftaha, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Serikali tulishaanza mpango huo tangu msimu uliopita kwa mfano Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru tulianza kuajiri Wahasibu wenye degree moja na kuendelea kwa ajili ya kuongoza vile vyama vya ushirika. Utaratibu ule tutaendeleza nchi nzima kupitia vyama vyote vya ushirika ili tupate Wahasibu wenye weledi ili kuweza kuwahudumia wakulima wetu.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Mhandisi aliyekuwa anasimamia kujenga Soko la Nkwenda alikuja na Fuso mbili akahamisha nondo, mabati na saruji akidai anapeleka vifaa hivyo vya ujenzi katika Soko la Sirari katika Mkoa wa Mara na Serikali ina taarifa ya tuhuma za huyu Mhandishi. Je, ni hatua zipi zilichukuliwa dhidi ya Mhandisi huyu ambaye kwa kweli alikuwa kikwazo katika ukamilishaji wa soko hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa katika majibu ya Serikali imesemwa kwamba masoko haya yalijengwa kimkakati ili kuweza kusaidia wananchi kufanya biashara na nchi zilizo jirani na maeneo ambayo yamejengwa masoko hayo. Je, sasa ni lini Serikali itayakamilisha?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Conchesta Rwamlaza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anasema kwamba huyu Mhandisi alipeleka magari kuhamisha vitu hivyo na kwamba Serikali tunayo taarifa na anataka kujua kwamba tumechukua hatua gani. Mpaka sasa tulishavielekeza vyombo vyetu vya ulinzi na kiuchunguzi kuendelea kuchunguza tuhuma na jinai hiyo ili ikithibitika amefanya jambo hili hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ni lini masoko hayo yatakamilika, kama nilivyojibu kwenye swali lake la msingi, kwenye bajeti hii tumetenga zaidi ya shilingi bilioni 2.9, Waheshimiwa Wabunge mkitupitishia haraka iwezekanavyo kuanzia Julai 1, tutaanza kutekeleza ujenzi wa masoko hayo yote.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niipongeze Serikali na niishukuru kwa moyo wa dhati kwa kutusaidia kutujengea jengo kubwa la NFRA pale Babati kwa ajili ya kununua mahindi na kuyachakata. Bahati mbaya mwaka huu tangu Januari mvua hazinyeshi Kanda ya Kaskazini na hali si nzuri, hatuna maharage wala mahindi. Naomba nifahamu Serikali imejipanga vipi kwa ajili ya kukabiliana na hali hii ambayo wananchi wanakwenda kukabiliana nayo ya ukosefu wa mahindi na maharage ili wananchi wetu wapate mazao hayo kwa bei rahisi na wasiingie katika baa la njaa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Mheshimiwa Gekul anataka kujua kwamba Serikali tumejipanga vipi katika kukabiliana na tishio la upungufu wa chakula nchini kutokana na ukame uliopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwanza tumetenga shilingi bilioni 15 kupitia Wakala wetu wa Taifa (NFRA) kwa kuendelea kununua mahindi kwa ajili ya kuyahifadhi kwa ajili ya kuja kuyasambaza au kupeleka sehemu ambazo zitakuwa na mahitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia sasa hivi tumeshawaelekeza wataalam wetu wamesambaa nchi nzima kufanya tathmini ya kina kujua athari iliyoletwa na mabadiliko ya tabianchi hususan huu ukame ili kujua athari iko kiasi gani ili tuweze kuongeza mikakati mingine. Pia tumetenga zaidi ya shilingi bilioni tisa kupitia Bodi yetu ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kuendelea kununua mahindi na mazao mengine kukabiliana na hali hiyo.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo kwa majibu yake mazuri, lakini napenda niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tabora ni miongoni mwa mikoa ambayo imepata athari kubwa sana ya uharibifu wa mazingira kutokana na ukataji wa miti ambayo inatumika zaidi kwa ajili ya mkaa na kuni. Hali hiyo
imepelekea Mkoa wa Tabora na maeneo ya jirani kupata mvua ya kusuasua ambayo ndio inatumika zaidi kwa kilimo. Sasa swali langu, je, Serikali ina mkakati gani wa haraka wa kuhakikisha kwamba pamoja na athari zote hizo zilizopatikana wananchi wataendelea na shughuli za kilimo kama kawaida?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, pamoja na Serikali kuyaingiza maeneo ya Imalamihayo, Inala, Bonde la Kakulungu na Magoweko katika mpango wa umwagiliaji, lakini mpaka leo maeneo haya bado hayajaanza kufanya kazi. Sasa tunataka tupate majibu ya Serikali ni lini maeneo haya na skimu hizi zitaanza kufanya kazi kwani mpango huu unaonesha umeanza kazi tangu mwaka 2018?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekit, nashukuru. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rehema Juma Migilla kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza anataka kujua mikakati ya Serikali kwa ajili ya kuendeleza kilimokwa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hapo Tabora. Sisi kama Serikali cha kwanza tulichokifanya, mkakati mkubwa tuliokuwa nao ambao badala ya kutegemea fedha za kibajeti, lakini pia badala ya kusubiri fedha za washirika wa maendeleo kutoka nje ya nchi tumeielekeza Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo kuja kwenye halmashauri mbalimbali nchini kukaa nao na kubainisha yale maeneo yanayofaa kwa kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kubainisha kujua mahitaji yenu wataenda kuingia mikopo kwa dhamana ya halmashauri na sisi Serikali tutawadhamini zaidi ya asilimia 80 ili kujenga miundombinu ya umwagiliaji ikiwemo huu Mkoa wa Tabora ili wakulima waendelee kulima cha kisasa cha uhakika na chenye tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili anasema, ni lini kwamba miradi hi tuliyiotaja kwenye jibu letu la msingi kwamba itaanza kufanya kazi. Hii miradi itaanza kufanya kazi muda mfupi ujao baada ya upatikanaji wa fedha za kibajeti na kama nilivyosema kwenye jibu la awali chanzo kingine cha pesa ni kupitia mikopo kupitia Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa mwaka 2018 kwa maana ya mwaka uliopita Serikali ilipora fedha za wakulima wa korosho zaidi ya bilioni 300 ambazo zilikuwa ni za export levy na kusababisha wakulima wa korosho kushindwa kununua sulphur. Mwaka huu tumeona uzalishaji wa korosho ulikuwa wa chini sana kwa sababu wakulima wanashindwa kununua sulphur.

Je, Serikali ipo tayari sasa msimu huu wa korosho unaokuja kuweza kugawa sulphur bure kwa wakulima wa korosho ili tija iweze kuongezeka katika uzalishaji wa korosho?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa bei ya kahawa imeendelea kuwa chini mwaka hadi mwaka na hali hii imetokana na suala la pembejeo kuwa juu sana wakati bei ya kahawa imeendelea kuwa chini kabisa. Je, Serikali iko tayari sasa kuanzisha mfuko wa kuimarisha bei kwenye zao la kahawa yaani Price Stabilization Fund ili pale kahawa inaposhuka bei Serikali iweze kufidia kupitia mfuko huo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anataka kujua kuhusu suala la export levy, kwanza sio kweli, Serikali haijapora pesa za wakulima wa export levy, wakulima wa korosho kule Mtwara. Haya yalikuwa ni mapato ya Serikali kama mapato mengine na tulileta mapendekezo hapa na yalipitishwa na Waheshimiwa Wabunge. Kwa hiyo, Serikali ilichofanya ni utekelezaji wa sheria ile ambayo ilipitishwa na Wabunge akiwepo Mheshimiwa Haonga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusu kahawa kwamba tuanzishe mfumo wa price stabilization kwa ajili ya kufidia pale bei zinapoanguka. Kwanza, ni wazo zuri ambalo na sisi Serikali tunalipokea. Lakini katika mazao sio la kahawa peke yake ambayo yanaanguka katika masoko ya dunia, ni suala la msingi, sio bei. Hatuna uwezo wowote wa ku-control bei katika soko la Kimataifa. Uwezo wetu sisi ambao tumegundua kama Serikali ni tija ndogo wanayoipata wakulima katika mazao kwamba wanatumia gharama kubwa lakini wanachokipata ni kidogo na ndiyo maana sasa hivi tunaimarisha mfumo wa upatikanaji pembejeo ili kuongeza tija kwa wakulima, watumie gharama ndogo wapate mavuno vizuri ili tuweze kushindana katika masoko ya ndani na ya nje ambayo hatuna uwezo wa kupanga bei.
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza swali kuhusu kilimo cha korosho. Juzi wakulima wa korosho wamelipwa fedha chini ya kiwango ni theluthi moja ya haki yao. Je, Mheshimiwa Waziri unawaambia nini wakulima hawa, hizi fedha ndiyo basi au watalipwa zingine na sababu gani ambazo zimefanywa hawakuweza kulipwa hela zote?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunafahamu malipo yote wanayopaswa kulipwa wakulima wa korosho ni zaidi ya bilioni 723 na mpaka sasa tumelipa zaidi ya bilioni 633. Bado kuna wakulima ambao wanadai Serikali bilioni 100 hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka wiki iliyopita tulipeleka zaidi ya bilioni 50 na malipo yanaendelea mpaka sasa hivi na kama anachokizungumza, kama tunavyofahamu, wanunuzi wa korosho kabla Serikali hatujaweza kuokoa hali ilivyokuwa, walikuwa zaidi ya 100. Lakini mwaka huu mnunuzi ni mmoja tu na ukizingatia kwamba hii benki ya maendeleo ya kilimo na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ilikuwa haijajiandaa katika ununuzi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilipaswa mjue kwamba Mbunge ungeipongeza Serikali na Bodi ya Nafaka na Mazao mchanganyiko kwa hatua ilizochukua mpaka leo tumeweza kulipa zaidi ya bilioni 633 na mnunuzi akiwepo mmoja kitu ambacho kilikuwa hakuna kwenye bajeti badala ya kusema kwenda kwenye…

MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa RUBADA kwa muda mrefu imeshindwa kuyaendeleza haya mashamba, je, haioni sasa ni wakati muafaka Serikali iyachie maeneo haya kwa ajili ya matumizi ya wananchi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili Bonde la Mto Karema kuna mradi wa umwagiliaji ambapo Serikali imetoa fedha nyingi lakini mradi huo haujawahi kukamilika na una muda mrefu sana. Ni lini Serikali itakamilisha mradi wa irrigation uliopo pale Karema?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kakoso, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza amependekeza kwamba kwa sababu RUBADA imeshindwa kuendeleza mabonde haya basi yarudishwe mikononi mwa wakulima. Kwanza, nataka nimueleze Mheshimiwa Mbunge RUBADA haijawahi kumiliki ardhi kama jibu langu la msingi lilivyokuwa, muda wote wa uhai wa RUBADA ardhi hii ilikuwa inamilikiwa na Serikali za Vijiji na vijiji husika na watu binafsi.

Mheshimiwa Spika, kwa kifupi ni kwamba Bunge lako hili Tukufu mwaka 2017 lilipitisha sheria hapa tulishaifuta RUBADA sasa hivi haipo, mali zote za RUBADA zimerudi Serikalini na ziko chini ya Msajili wa Hazina. Sasa hivi tuko kwenye mchakato wa kuona nani apewe ardhi hiyo kwa ajili ya kuiendeleza. Hilo wazo lake tunalichukua kwamba kama itarudishwa tena kwa wananchi kwa sababu iko kwa wananchi basi itakuwa hivyo na wataendelea kuilima.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu Bonde la Mto Karema, anataka kujua lini mradi huu utakamilika. Ni kweli kwamba miradi mingi ya umwagiliaji katika nchi hii ama ilitekelezwa chini ya kiwango au ilitekelezwa pasipo ufanisi uliokusudiwa. Kama Serikali baada ya kuliona hilo wataalam wanapitia kufanya tathmini ya kina tuone athari tuliyoipata ili kutumia tathmini ile tuweze kuyaendeleza mabonde haya. Kutegemea na upatikanaji wa fedha tutapanga jinsi ya kwenda kumalizia mradi huu.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, kasi ya uzalishaji wa kilimo cha viungo kama vile hiliki, mdalasini, pilipili manga, binzari nyembamba kwa nyumbani Zanzibar tunaita uzile, imekuwa bado ni ndogo sana na kuna maeneo mengi ambayo yanaweza yakastawi mazao haya.

Mheshimiwa Spika, Serikali ituambie katika kuhakikisha kwamba kwa hali ya hewa na udongo, mahitaji ya mazao haya bila mbolea, ina mkakati gani wa ziada kuona kwamba mazao haya yanalimwa na wakulima wakapata faida na Serikali inapata tija kubwa?

Mheshimiwa Spika, la pili, kuna malalamiko makubwa kwa baadhi ya wakulima kwamba Maafisa Ugani hawatoi elimu inayostahili katika maeneo ambayo wakulima wangeweza kulima kilimo cha aina yoyote bila kutumia mbolea: Serikali ituambie ina mkakati gani katika kuwawezesha Maafisa Ugani ili waweze kuwafikia wakulima walio wengi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru. Swali la kwanza la Mheshimiwa Masoud anataka kujua mkakati wa Serikali ambao tunaweza kuwawesha wakulima ili waweze kuongeza uzalishaji na tija.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, yaani kilimo tulichokuwa tunalima, kilikuwa cha kubahatisha; mkakati mkubwa wa Serikali uliopo sasa kwanza ni kufanya utafiti wa afya ya udongo ili kubaini asili na kuangalia aina ya udongo iliyoko pale ili kuwashauri wakulima ni zao gani ambalo linakubali kwa udogo wa ikolojia eneo walipo? Kwa hiyo, huo mkakati ambao utakamalizika muda mfupi ili kwamba tutoe elimu sahihi na kuwashauri wakulima aina gani ya zao walime? Mbolea gani watumie? Namna gani ambayo wanaweza kufaidika kwa kuongeza uzalishaji na tija?

Mheshimiwa Spika, katika swali la pili, anazungumzia kuhusu Maafisa Ugani kwamba wapo lakini hawawafikii wakulima kutoa elimu sahihi. Kwanza, nichukue nafasi hii kueleza kwamba Maafisa Ugani ni kweli anachosema Mheshimiwa Mbunge kwamba wako wachache. Mahitaji Maafisa Ugani ni zaidi ya 20,000 nchini hii, tuliokuwa nao ni 8,600. Kwa hiyo, tuna upungufu zaidi ya 11,400.

Mheshimiwa Spika, kama Serikali, kwa kujua hilo kwa sasa hivi ni kwamba Serikali imeshaanza kutoa vibali kwa ajili ya kuajiri watumishi na mkazo mmoja utaelekezwa huko ili tupate Maafisa Ugani kwa ajili ya kwenda kutoa elimu.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, kama Serikali tuna mkakati ambao ulikuwepo tangu katika ASDP I wa kujenga vituo vya elimu kwa wakulima kila Kata, mkakati huo utaendelea, lengo ni kuwakusanya wakulima kutoka katika vijiji mbalimbali kukutana pale kunapokuwepo na mashamba darasa ya mazao yanayokubali katika maeneo yao ili wapate elimu ya pamoja kwa ajili ya kuwasaidia katika kuongeza tija na uzalishaji.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Awali ya yote, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na nimeyapokea.

Swali la kwanza; kwa kuwa Benki ya Kilimo mpaka sasa haijaweza kuwa katika Mikoa yote na hizo benki nyingine alizozizungumzia kama NMB na alitaja benki mbili zote hizo ni Commercial na zinahitaji wewe unayekwenda kukopa lazima uwe na dhamana na wanawake wengi hawana nyumba wala hawana dhamana ambazo zinatambulika kibenki: Je, Serikali iko tayari ku-guarantee mikopo hiyo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Tatizo katika kilimo ni pamoja na mbegu bora na mara nyingi unakuta kwamba mbegu hizo ni ghari na pia siyo rahisi kumfikia mkulima. Ni lini sasa mbegu hizo zitagaiwa kwa wanawake hao kupitia katika Kata zao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru. Swali la kwanza la Mheshimiwa Shally Rymond anataka kujua kwamba kwa sababu benki ya Maendeleo ya Kilimo haipo kila Mkoa na kwamba hizi benki nyingine ni za kibiashara, anataka kujua mikakati ya Serikali kama iko tayari kudhamini mikopo hii.

Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali tupo tayari na tulishaanza na ndiyo maana kama alivyosema Benki ya Maendeleo ya Kilimo haipo kila Mkoa, ni kwa sababu hii ni Benki ya Maendeleo, ni benki ya kimkakati na lengo lake ni kuwasaidia wakulima kupitia madirisha mbalimbali ya Taasisi za Fedha. Moja, tulichokifanya, Serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo tumedhamini mikopo yote ambayo inayotolewa na Benki ya NMB ili kwenda kwenye Sekta ya Kilimo hususan pamoja na akina mama.

Mheshimiwa Spika, swali la pili kwamba ni lini Serikali itatengeneza mazingira ya mbegu hizi zikapatikana katika ngazi za Kata ili wanawake wazipate kiurahisi?

Mheshimiwa Spika na Mheshimiwa Mbunge, ni kwamba Serikali siku zote kwamba tuko tayari. Mbegu hizi kupitia Shirika letu la Mbegu (ASA) na Taasisi nyingine binafsi na mawakala mbalimbali, tumeweka mazingira mazuri kwamba mbegu hizi zinapatikana Tanzania kote, siyo kwa kwenye Kata tu, mpaka ngazi za vijiji kwa kuzingatia mahitaji. Kama kuna mahitaji maalum katika eneo unalotoka, baada ya Bunge hili tuone ili tuwaelekeze wenzetu wa ASA ili waweze kupeleka mbegu haraka iwezekanavyo ziwafikie wakulima.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ukiacha Taasisi nyingi kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake lakini Benki ya Kilimo ndiyo yenye dhamana ya kutoa mikopo. Benki ya Kilimo imekuwa na tabia ya ubaguzi, inatoa mikopo kwa wale wanawake ambao wana uwezo au wake za vigogo, lakini wale wanawake ambao wana uwezo mdogo na wamejiunga kwenye vikundi wamekuwa wakipewa masharti magumu.

Je, Serikali inatoa kauli gani hususan kwa wanawake wa Ulanga, Kilimanjaro na juzi nilikuwa Mbeya kule, hamna hata mmoja aliyepata mkopo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru. Napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mlinga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza siyo kweli kama Serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo tunatoa mikopo kwa kibaguzi. Hii kama nilivyosema ni benki ya maendeleo, ni benki ya kimakakati na tumeianzisha maalum kwa ajili ya kuendeleza sekta ya kilimo hapa nchini. Kwa hiyo hizi ni pesa za umma, kama pesa za umma lazima zina taratibu zake na zina masharti. Labda hao wanaoona wanapata maana yake ni wanawake waliotimiza vigezo vinavyohitajika na benki ili waweze kupata mikopo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niendelee kumshauri kama nilivyosema kwenye jibu letu la msingi, tumewaelekeza wanawake hao hususani wale wa vijijini wajiunge kwenye vikundi, vile vikundi vyao ndiyo vitatumika kama dhamana na benki hii itaendelea kutoa mikopo. Hivi ninavyozungumza, pamoja na maelekezo ya Serikali tuliwaambia kwamba mikopo wanayotoa asilimia 20 watoe kwa akinamama, lakini benki hii imeweza kutoa mpaka leo tunavyozungumzia zaidi ya asilimia 33 ya mikopo yote waliyotoa imekwenda kwa akinamama.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwenye Wizara ya Kilimo. Serikali kupitia Wizara ya Kilimo mwaka juzi walianzisha utaratibu wa kwamba zao la korosho lilimwe katika kila mkoa hapa Tanzania kwenye mikoa 17. Wakati wa uhamasishaji huo, wakawahamasisha pia akinamama wengi sana kwenye Wilaya ya Masasi, Wilaya ya Tandahimba ikiwemo pamoja na Newala, Lulindi pamoja na Ruangwa wakope pesa kwenye mabenki lakini pia walikopeshwa pesa pamoja na Halmashauri. Sasa bahati mbya sana mpaka sasa hivi Serikali haijalipa pesa hizo za hao akinamama na wameanza kutaifishwa, kufilisiwa na wanashindwa kufanya shughuli zao na hapa tunasema tunataka tuwawezeshe akinamama. Sasa nataka tusikie kauli ya Serikali, je, ni lini watawalipa akinamama hao waliozalisha miche iliyopelekwa mikoa mingine 17 pesa zao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru. Napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mwambe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli Serikali miaka yote tuna mradi wa kuongeza uzalishaji wa korosho hapa nchini kutoka tani 300,000 za sasa kwenda tani milioni moja ndani ya miaka mitano ijayo. Kwa hiyo miongoni mwa miradi hiyo lazima tulikuwa tuongeze eneo la uzalishaji na moja ya mikakati ilikuwa kwamba kuzalisha miche zaidi ya milioni 10 kwa kila mwaka kwa muda wa miaka hiyo mitatu. Pia ni kweli kwamba miche hii ilizalishwa kwa vikundi mbalimbali vya akinamama na vijana, lakini baada ya kupitia yale madeni, tumegundua kwamba kuna kasoro nyingi katika yale madeni.

Mheshimiwa Spika, kama ninavyosema siku zote kwamba hizi ni pesa za umma, kama Serikali tuliona ni busara kwamba tufanye uhakiki wa kina ili tujue, tubainishe na kutambua yapi madai halali na yapi madai yaliyopikwa ili wale halali waweze kulipwa. Niendelee kumsihi tu Mheshimiwa Mwambe na wengine wote waendelee kuvuta subira, jambo hili karibu linafika mwisho, timu ya uchunguzi iko katika hatua za mwisho kumaliza, tukimaliza hela zipo na tutawalipa wote waliozalisha miche hii.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, moja ya changamoto wanayoipata wakulima wakiwemo Wanawake hasa wanaolima tumbaku ni upatikanaji wa pembejeo kwa wakati hususan mbolea aina ya NPK.

Je, Serikali inawahakikishiaje wakulima wa tumbaku kwamba watapata mbolea ya NPK kabla ya mwezi wa Nane mwaka huu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru. Napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Sitta kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli yaani mwaka jana mbolea zilichelewa kufika kwa wakulima na sababu ndiyo mwaka wa kwanza ambao tulikuwa tunatekeleza ule mfumo wa bulk procurement (uagizaji wa mbolea kwa pamoja) na kitu chochote kikiwa cha kwanza lazima kina changamoto zake. Tumeona hizo changamoto, lakini mwaka huu ambao mchakato wa kufahamu kiwango cha uzalishaji na mahitaji ya mbolea tumeshakifanya mapema na tayari sasa hivi watu tuko kwenye mchakato wa kupata Mawakala wa kuagiza hizo mbolea na vyama vyenyewe tumevipa ruhusa ya kuagiza. Kwa hiyo, hilo tatizo mwaka huu halitakuwepo na mbolea zitafika kwa wakati kwa wakulima wa tumbaku na hasa akinamama wa Tabora.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri wa Kilimo, ninayo maswali maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Mfumo wa Uagizaji wa Mbolea kwa pamoja unatumika tu kwa mbolea za DAP na UREA. Je, ni kwa nini sasa Serikali isitumie mfumo huu kwa kuagiza mbolea nyingine za NPK, CAN, SA na pembejeo nyingine?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Mkoa wa Katavi ni umbali wa kama kilimita 1,500 kutoka Dar es Salaam, kwa hiyo, mbolea inaposafirishwa na magari inakuwa na bei juu zaidi.

Ni kwa nini sasa Serikali isiweke utaratibu wa kusafirisha mbolea hiyo kwa njia ya treni ili mkulima wa Mkoa wa Katavi apate bei nafuu ya mbolea?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Taska Mbogo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Taska Mbogo alitaka kujua kwa nini Serikali tusitumie Mfumo huu wa Uagizaji wa Mbolea kwa Pamoja (BPS) kwa mbolea zingine kama NPK, CAN na SA. Kwanza, mfumo huu tumeanza kuutumia mwaka jana na umeonyesha matokeo mazuri. Tusingeweza kuingiza mbolea zote kwa wakati mmoja lakini baada ya mafanikio tuliyoyaona katika mfumo huu, mwaka huu tumeshaanza kuutumia mfumo huu kwa ajili ya mbolea ya NPK kwa wakulima wa tumbaku na sasa tutaendelea na utaratibu ili kuingiza mbolea tajwa, viuatilifu na pembejeo zingine katika mfumo wa BPS ili kurahisisha upatikanaji wa mbolea kwa haraka na bei nafuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, anasema kwa sababu Mkoa wa Katavi uko mbali na Dar es Salaam, ni vizuri tungesafirisha mbolea hizi kwa njia ya treni ili kupunguza gharama za usafiri. Tunachukua mawazo haya na tulishayafanyia kazi, tangu mwaka jana kama nilivyosema hii mbolea ya NPK tuliisafirisha kwa kutumia treni na gharama za usafiri zilishuka na mbolea hii kufika kwa wakulima kwa wakati. Mawazo yake tunayachukua ili tuyahamishie katika mazao mengine. Kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi, tayari tumeshalielekeza Shirika letu la Reli Tanzania ili kutoa kipaumbele kwenye kusafirisha bidhaa ya mbolea ili kushusha gharama za usafiri.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya asilimia 75 ya wananchi wa Tanzania ni wakulima na wanaishi maeneo ya vijijini. Hawa wafanyabiashara aliowataja Mheshimiwa Naibu Waziri wenye makampuni wanaonunua mbolea hizi, wamekuwa wakinunua na kuziweka mjini na inawapasa wakulima sasa watoke vijijini kwenda kununua hizo mbolea mjini kitu ambacho kimekuwa kikiwasababishia gharama za mbolea kupanda sana? Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba mbolea hizi zinapatikana kwenya Kata au Tarafa?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe tuna maghala na maeneo mengi ya Njombe kuna maghala kwenye Kata hizi. Je, Serikali ina mpango gani ili kuhakikisha hawa wafanyabiashara wanapeleka mbolea hizi kwenye Kata ili gharama za usafirishaji ziweze kupungua kwa wakulima? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joram Hongoli, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli wakulima wengi wanaishi vijijini na kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, tumeshayaelekeza makampuni yote yanayoingiza mbolea hapa nchini na wasambazaji wawe na mawakala kila Mkoa
na Wilaya na pia wawe maghala ili kuwezesha mbolea hizi zinapoingia Dar es Salaam kufika kwenye mikoa yote inayotumia mbolea kwa wingi. Pia tumevielekeza Vyama vya Msingi vya Ushirika na Vyama Vikuu, kuwa mawakala kwa ajili ya usambazaji wa mbolea kwenye Kata na Vijiji katika Mikoa na Wilaya zinazolima mazao mbalimbali.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri kabisa na pili nimefurahi kusikia Mheshimiwa Waziri ametambua kuwa Mkoa wa Kagera ndiyo mkoa pekee nchini unaopakana na nchi nyingi za Afrika Mashariki. Mkoa wa Kagera unapakana na nchi nne za Afrika Mashariki kati ya tano kwa maana ya Burundi, Rwanda, Uganda, Tanzania yenyewe ambayo Kagera imo na hata Kagera inaifikia Kenya kwa kupitia Ziwa Victoria.

Ni kwa nini sasa Serikali isione kuna umuhimu wa kuufanya Mkoa wa Kagera kuwa kituo kikubwa cha biashara Afrika Mashariki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa hivi sasa Mkoa wa Kagera ndiyo mkoa pekee unaolima na kuzalisha kahawa nyingi nchini na hata tafiti zimeonesha hivyo kwamba Mkoa wa Kagera unazalisha asilimia 65.6 mpaka sasa, lakini kumekuwepo na malalamiko mengi ya utoroshwaji wa kahawa kutoka Mkoa wa Kagera kwenda Uganda.

Ni lini sasa Serikali itajenga mnada wa kimataifa Mjini Bukoba ili kahawa zote za maeneo ya Maziwa Makuu ziuzwe Mjini Bukoba? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la pili la nyongeza la Mheshimiwa Halima Abdallah Bulembo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge jinsi anavyowapigania wakulima wa kahawa wa Mkoa wa Kagera, hii inaonesha namna gani alivyokuwa jirani na watu wa Kagera.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali kwa kutambua umuhimu wa Mkoa wa Kagera kwenye uchumi wa Taifa hili na hasa uzalishaji wa kahawa kama alivyosema, inazalisha zaidi ya asilimia 40 ya kahawa yote nchini, lakini ndiyo mkoa unaoongoza kwa kilimo cha kahawa aina ya Robusta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tumeshapanga sisi kama Serikali kwamba kuanzia msimu wa mwaka huu tutakuwa na minada ya kanda kwenye kanda zote nne za uzalishaji wa kahawa hapa nchini; kwamba tutakuwa na mnada wa Kanda Kagera, Kilimanjaro, Nyanda za Juu na kule Ruvuma. Pia nimtoe wasiwasi kwa mujibu wa takwimu na hali halisi ilivyo, kahawa yote ya Mkoa wa Kagera asilimia zaidi ya 90 inauzwa katika soko la moja la moja (direct export) na mpaka sasa tunapoongea, wakulima hasa Chama Kikuu cha Ngara kimeshaanza kuleta makubaliano hayo, kahawa yote imeshauzwa imebaki tu asilimia 10 ambayo ndiyo itaenda kwenye mnada. Ahsante sana.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri alifanya ziara kwenye hili na anazungumza eneo ambalo analifahamu. Pamoja na majibu yake mazuri ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza mradi huu ulibuniwa muda mrefu sana na ni mradi ambao una uwezo wa kuhudumia eneo kwa maana hekta karibu zaidi ya hekta 5000 na tathmini ambayo unasema ilifanyika ya usanifu uliofanyika ulifanyika muda mrefu.

Je, Serikali iko tayari sasa kuharakisha mapitio ya usanifu upya ili kujua gharama halisi kwa mazingira tuliyokuwanayo sasa na kwa namna ya kutekeleza mradi huu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili tunayo Skimu ya Songea na Makalala kule Magoma, lakini pia skimu ya Kwamkumbo pale Mombo ambapo wananchi wamekuwa wakiathirika wakati mvua maji yakiwa mengi yanaenda kwenye mashamba ya wakulima na kuharibu mazao na kusababisha hasara kubwa.

Je, Mheshimiwa Waziri uko tayari, kuwatuma wataalam wa umwagiliaji waende kwenye maeneo haya na kuona namna ya kutatua changamoto hizi za wananchi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anataka kufahamu Serikali kuharakisha mchakato wa kuweza kupitia upya tathmini ya mradii huu. Kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tangu siku zile nilivyofika mimi katika bonde hili na kufika bwawa lile tayari tushawaelekeza viongozi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Kanda ya Kilimanjaro wanalifanyia tathmini upya bwawa lile ili kujua gharama halisi na kuanza utekelezaji kwa mipango ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu athari ya mafuriko katika skimu hizi tatu alizozitaja za Skimu ya Songea na Makalala, kwamba nitumie nafasi hii kwanza kuwaelekeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Kanda ya Kilimanjaro kwenda haraka katika mabwawa haya kufanya tathmini na kuona namna gani tunaweza kujenga miundombinu ile yamatuta kwa ajili ya kukinga mafuriko ya athari ya mabwawa haya.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Spika, ahsante, bonde la Mto Manonga kama lilivyo bonde la mto Mkomazi kuna Skimu ya Umwagiliaji ya Igurubi, ambayo ilijengwa miaka ya 1980 lakini sasa hivi ilibebwa na maji wakati wa msimu wa mvua uliopita. Naiomba Serikali basi kama inaweza kwenda kuifufua hiyo skimu ili wananchi wa eneo hilo waendelee na kilimo cha mpunga, lakini pia skimu zingine ambazo za namna hiyo zilizoachwa kama kule Kibaha Vijijini na sehemu zingine ziangaliwe zote ili ziweze kufufuliwa, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru, kwanza ombi lake la kwenda kufanya ukarabati mkubwa kwenye skimu hii ya Igurubi kwanza tunalipokea, lakini nichukue nafasi hii kuwaeleza Wabunge wote skimu ziko nyingi sana katika Taifa hili, tuna eneo zaidi la hekta milioni 29 zinafaa kwa umwagiliaji na mpaka sasa miaka 58 tumeendeleza hekta 4,75,000 tu. Kwa hiyo, tukitumia au tukitegemea skimu hizi zote kuendeleza kwa kupata pesa za kibajeti tutachelewa sana, sisi kama Serikali na ndiyo maana tulianzisha benki ya mkakati ya Maendeleo Benki ya Kilimo kwa ajili ya kuendeleza miradi mikubwa hii.

Kwa hiyo sasa hivi Benki ya Maendeleo ya Kilimo itapita kila Halmashauri ambayo iliyokuwa na eneo hili la umwagiliaji kwa ajili ya skimu zingine tuziendeleze kwenye kilimo cha kibiashara kwa ajili ya kupata mikopo yenye riba nafuu ili badala ya kusubiri hela za kibajeti ili tuweze kuendeleze skimu hizi kwa muda mfupi Tanzania nzima.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nitumie fursa hii kushukuru majibu ya Serikali sambamba na hayo nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, namba moja, ni miaka tisa sasa toka tumeingiza zaidi ya milioni 143 kwenye mradi huu na hakuna ambacho kimeweza kuwa realized mpaka leo. Ukichukua faida ambazo tungezipata kwa mradi ule watu 12,000 kunufaika tungekuwa tu kwa mwaka tunapata zaidi ya bilioni 50; mpaka leo tunazungumzia miaka tisa tungekuwa tumetengeneza zaidi ya bilioni 500, ukiangalia hii opportunity cost peke yake acha multiplier effect kipindi cha uchumi wa viwanda na mazao ambayo yangetokana na matokeo yale ya pale kwenye mradi ule tungekuwa tumepiga hatua kubwa sana kwa wananchi wa Kondoa.

Je, ni lini sasa Serikali itafikia hatua ya kuweza kufanya hii tathmini ya kina na hatimaye kufanya hii tathmini ya kina na hatimaye kukamilisha mchakato mradi huu utekelezwe? la kwanza.

Mheshimiwa Spika, swali la pili ili Mheshimiwa Naibu Waziri uweze kujiridhisha na fursa iliyoko kule fursa kubwa sana.

Ni lini sasa mimi na wewe na pamoja na wataalam wako tutaongozana tuende pale Mongoroma tukaone nini kinaweza kikafanyika kwa haraka zaidi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anataka kujua kwamba huu mradi umechukua muda mrefu zaidi ya miaka tisa na hela pale tumeshawekeza ni lini sasa kwamba tumeanza kuuharakisha huu mchakato.

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kwanza kumhakikisha Mheshimiwa Mbunge pamoja na kwamba sijafika katika mradi huu, lakini viongozi wetu, Wahandisi wetu wa Kanda ya Umwagiliaji Kanda ya Dodoma tayari wako kwenye mchakato wa kuufanyia tathmini ya kina ili kubaini gharama halisi za sasa badala hizi za miaka kumi iliyopita ili kuingiza katika mpango kabambe wa umwagiliaji ambao tumeuhaulisha ile Sera ya mwaka 2013 kwa hii ambayo Sera Mpya ya mwaka 2018 mradi huu pia tunaenda kuutekeleza na tathmini itafanyika haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Spika, pili kama nilivyojibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kafumu kwamba mradi mbadala au njia mbadala ya kutekeleza miradi hii mikubwa ni kutumia Benki ya Maendeleo ya Kilimo kwa sasa hivi kwa sababu tunaondoka kwenye kilimo kile cha kujikimu tuko kwenye kilimo cha kibiashara. Kwa hiyo, lazima sasa tuwekeze ndiyo maana tumewaletea benki hii yenye riba rafiki kwa wakulima ili kuenda kuendeleza miradi mikubwa kama hii kwa sababu ile ni benki ya kimkakati.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili niko tayari baada ya bajeti yetu inayoanza kesho tarehe 17 Mei na kumalizika tarehe 20 Mei tuonane tupange ikiwezekana tarehe 21 na 22 Mei mimi na wataalam wangu tuko tayari kufika Kondoa ili kuliangalia.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na yenye kuleta matumaini kuhusiana na miradi hii ya umwagiliaji. Lakini pamoja na pongezi hizo mimi naomba niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, iko miradi ya kilimo cha umwagiliaji ambayo ilikuwa inaendelea katika Mkoa wetu wa Ruvuma ikiwemo mradi wa kilimo cha umwagiliaji uliopo Legezamwendo, Misyaje na baadhi ya vijiji vingine. Miradi hii imesimama kwa ajili ya kukosa pesa na nina uhakika tayari miradi hii ilishaanza. Kuendelea kuchelewa kupeleka pesa maana yake ni kuongeza gharama za mradi.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha tunapeleka pesa katika miradi hii ili kukamilisha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru, ni kweli kwamba kuna miradi mingi ambayo imeanza kujengwa na haijamalizika mpaka sasa na labda nilitaarifu Bunge lako rasmi; baada ya Tume hii ya Taifa ya Umwagiliaji kurudi Wizara ya Kilimo tuliweza kupita katika scheme karibuni zote nchini ili kuzingalia na namna gani na wataalam wetu na hiyo pia ndani ya Serikali kama mnakumbuka siku tatu zilizopita Mheshimiwa Waziri Mkuu amewasimamisha zaidi ya Wakurugenzi saba kwa ajili ya kupisha uchunguzi tufanye tathmini ya kina kuangalia matumizi ya fedha kwa sababu pesa zilikwenda nyingi, lakini matumizi yalikuwa ni mabovu sana.

Kwa hiyo siyo kila mradi ukikwama kumalizika ni kwa sababu kwamba pesa zilikosekana, lakini baada ya hiki chombo tulichounda sasa hivi, Tume tuliyounda sasa hivi kwenda kuchunguza mapungufu hayo ya ubora wa miradi, thamani ya miradi baadae tutakuja na taarifa rasmi na kujipanga namna gani tutakwenda kumaliza mradi huu.
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza, lakini pia nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amezungumza habari ya tathmini na mimi nashukuru kwa kuniahidi kwamba kabla ya Desemba tathimini hizo zitakuwa zimefanyika ili waweze kujua fedha ngapi zinahitajika ili kumalizia na kukarabati miradi hiyo. Hata hivyo, kwa kuwa tayari tuna miradi ambayo fedha zake zinajulikana kwamba zikipatikana miradi hiyo inaweza kukamilika kwa mfano Mradi wa Umwagiliaji katika Kijiji cha Kongogo ambao umekuwa ni wa muda mrefu. Swali la kwanza, je, Serikali sasa iko tayari kupeleka fedha kabla ya hiyo tathmini kwa sababu tayari tathmini yake inajulikana ili mradi ule uweze kukamilika? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amehusisha kwamba wako washirika mbalimbali ambao wanaweza kutusaidia katika suala zima la miradi yetu ya umwagiliaji na sisi Bahi tayari tunao wafadhili ambao wanatusaidia hususan Shirika la LIC ambalo nataka nichukue nafasi hii kuwashukuru sana kwa namna ambavyo wamesaidiana na kushirikiana vizuri na wananchi wa Bahi katika miradi hii ya umwagiliaji. Tayari wameshatuandikia andiko na michoro mizuri kabisa ya utengenezaji wa bwawa katika Kijiji cha Chikopelo lakini bado hatujapata fedha. Je, Serikali sasa itakuwa tayari kupokea andiko hili kutoka wenzetu hawa Shirika la LIC ili kama alivyoahidi Mheshimiwa Waziri waweze kututafutia fedha katika mashirika haya mbalimbali ya wadau wetu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Omary Ahmed Badwel, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anataka kujua kama Serikali iko tayari kwa ajili ya kupeleka fedha kwa mradi huu wa skimu ya Kongogo ambayo ni ya muda mrefu. Kwanza, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Badwel kwa ufuatiliaji wa karibu sana na ushirikiano anaowapa watu wake wa Bahi. Sisi kama Serikali kwanza tuko tayari kwenda kupeleka fedha na ndiyo maana kwenye bajeti ya mwaka huu, mwaka 2019/2020 tumetenga zaidi ya shilingi milioni 217 kwa ajili ya kufanya tathmini ya miradi hiyo ukiwemo huu wa Kongogo.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili, anataka kujua pia kama Serikali tuko tayari kuchukua andiko walilofadhiliwa na wadau hao wa maendeleo. Serikali iko tayari na sisi binafsi tulishaanza lakini baada ya Bunge hili kwisha tunaomba atupe hilo andiko tulifanyie kazi. Kama tulivyosema hela tulishatenga tutafanya kila liwezekanavyo ili na hili andiko tulitekeleze haraka iwezekanavyo.
MHE. FLATEY G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa majibu ya Mheshimiwa Waziri yanasema fedha hazipatikani na zitengwe kwenye mapato ya ndani ya Halmashauri ya Karatu; na kwa sababu ukiangalia mapato ya Halmashauri hayana uwezo wa kujenga hata bwawa: Je, Serikali haioni sasa itumie namna mbadala kutokana na hali hii ili kusaidia watu wa Bonde la Eyasi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Wilaya ya Karatu na Wilaya ya Mbulu zilikuwa Wilaya moja na Bonde la Eyasi ni sawasawa na Bonde la Bashai: Je, kuna mpango gani pia wa kusaidia Bonde la Bashai kulipatia fedha ili skimu hii ipate kuendelea?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru. Swali la kwanza la Mheshimiwa Flatey Massay anasema kwamba Serikali ya Halmashauri ya Wilaya haina fedha ya kuweza kujenga hili bwawa wala miundombinu mingine mbadala wa vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli, lakini kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, Serikali tutaendelea kutenga bajeti ile ya kiserikali kutoka Serikali Kuu kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, lakini kama tulivyoelekeza, naye mwenyewe anajua. Hili Bonde la Eyasi kwenye kilimo tu cha vitunguu ndiyo linachangia mapato zaidi ya asilimia 33 ya Halmashauri hiyo ya Karatu, lakini haipeleki Halmashauri hiyo ya Karatu hata senti tano kuendeleza kilimo cha umwagiliaji na kilimo cha vitunguu katika bonde hilo.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana kama Serikali tumeelekeza watenge kwenye mapato yao ya ndani asilimia 20 ili kwenda kunenepesha ng’ombe yule wanayemkamua kwenye vitunguu ili waweze kukamua zaidi siku zijazo. Hatujasema kwanza hicho ni chanzo pekee cha kuendeleza huko, hapana. Hicho ni kimojawapo, ndio maana nimesema kwenye ile programu ya Jenga, Endesha na Kabidhi kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo na Benki ya Rasilimali pia wanaruhusiwa kwenda kuchukua mkopo. Tutaenda kujenga hiyo miundombinu baada ya kuiendesha halafu baadaye tutakabidhi baada ya mapato hayo kuisha. Pia tutaendelea kutenga kwenye bajeti kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili, skimu hii iliyokuwa katika Wilaya ya Jimbo la Mbulu pia utaratibu utakuwa ni huo huo na ombi lake nimelipokea, ni vizuri alete sasa hilo andiko na tutatuma Tume ya Taifa ya Umwagiliaji waende huko wakafanye tathmini na kuangalia mahitaji, baadaye tutaingiza kwenye bajeti kupeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa skimu hiyo.
MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Hata hivyo, ikumbukwe kwamba, Skimu ya Muo ilipitishwa kwenye bajeti ya mwaka 2009 na mwaka 2010, lakini ni kweli mpaka mwaka 2018 shilingi milioni 261 zilikuwa zimekwishatolewa, lakini haitoshi tunaambiwa kwamba, katika kilometa nane za mraba kilometa sita tayari zilikuwa zimeshasambazwa mabomba yenye mioundombinu ya kiumwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwenye ile tume waliyoituma Septemba, 2019 ubadhirifu katika mradi ule ulionekana. Nasema hivi kwa sababu moja, watakumbuka kwenye ule mradi mabomba yalitakiwa kufukiwa chini kwa nchi mbili kwenda chini, lakini ukienda kwenye mradi mabomba asilimia 90 yaliyolazwa pale yako juu kabisa yanaonekana na yanapasuliwa na wanyama, yanavuja ni kwamba, umepoteza tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, haitoshi. Katika Mradi wa Muo Skimu fedha za Serikali zimetolewa, lakini pia ile Kamati ya Kusimamia Maji ya Kata haikuwahi kuidhinisha mkandarasi alipwe, lakini pamoja na kwamba, Vijiji vyote Suduni, Kikarara, Mahoma na Kidia hawajapata maji hata kijiji kimoja, lakini mkandarasi alilipwa maji mpaka leo hayajatoka. Swali langu kwa Serikali kwa kuwa, baadhi ya mikoa tumeona wakandarasi wakiwajibishwa, je, ni kwa nini hatuoni umuhimu wa kumwajibisha mkandarasi huyu ambaye mpaka leo ameshindwa kukaa kwenye matakwa ya kimkataba?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa majibu haya ya Serikali na hasa nikianza kusoma statement ya kwanza, opening statement ya Mheshimiwa Naibu Waziri anasema, “Serikali inatambua umuhimu wa uendelezaji wa Skimu ya Umwagiliaji wa Muo”, lakini huku chini tunaambiwa Serikali imefika mahali inaona kuna kila sababu sasa ya ku-divert mradi badala ya Muo Scheme iende kukidhi haja ya wakulima wa mazao ya migomba wakulima wetu kule Moshi, lakini pia na wale wamama wanaolima mbogamboga tunaona leo tubadilishe mradi tukafanye ni mradi wa kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya maji kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke huu mradi hasa tulipotaka sisi ni kwa ajili ya umwagiliaji, ili kipato cha watu wetu kiweze kuinuka, lakini sasa kwa majibu haya ya Serikali, swali, je, Serikali inataka kutuambia kwa kuwa sisi watu wa Kilimanjaro tumekuwa na meneo madogo basi ni hatupaswi kushiriki kwenye masuala mazima ya kilimo? Kama ni hivyo basi naomba leo tusimame pale mbele tuwambie wananchi wa Old Moshi Mashariki kwamba, Serikali imekataa msishiriki kwenye masuala ya kilimo kwa kuwa ardhi yenu ni ndogo. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ester Mmasi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza la kujua kwamba, ni kwa nini Serikali hatuchukui hatua stahiki kwa mkandarasi ambaye amefanya kazi chini ya kiwango; kwanza nataka nimhakikishie kwamba, Serikali tulishaanza kuchukua hatua ya kwanza kubadilisha huo muundo kwa ajili ya kuweka wakandarasi wa umwagiliaji katika ngazi ya wilaya, lakini pia tulituma tume maalum kwa ajili ya kufanya tathmini ya miradi yote ya umwagiliaji nchini pamoja na mradi huu. Taarifa tayari tunazo na taarifa tumeshazifikisha kwa TAKUKURU kuanza kuchukua hatua kwa wakandarasi wote waliofuja fedha za umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili anataka kusema kwamba, kwa nini Serikali sasa tunataka tubadilishe matumizi ya mradi ule kutoka mradi wa umwagiliaji kwenda mradi wa maji ya kunywa. Kwanza nataka nimwambie Mheshimiwa Mbunge sio Serikali wenye nia hiyo, baada ya Serikali kutuma timu ya wataalam kwenda kubainisha mahitaji ya sasa ya ule mradi, hili hitaji limetoka kwa watumiaji wenyewe, watu wa Moshi. Wakasema sasa kwa sasa hivi eneo limepungua sana na nyumba wamejenga mpaka wengine wanakaribia kwenye chanzo ndio maana wanataka kwamba, kubadilisha matumizi badala ya kutumia kilimo cha umwagiliaji wafanye ule mradi kwa ajili ya maji ya kunywa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndio maana kwa hekima ya Serikali tumeamua badala ya kuliamulia tuandae mkutano wa wadau wote ili tukutane kwa pamoja ili tuone sasa kipaumbele cha watu wa hapo ni nini, bado wana nia ya mradi wa umwagiliaji au wanataka maji ya kunywa. Baada ya mkutano ule ndio tutapanga nini cha kufanya kutokana na kipaumbele cha wananchi wenyewe kwa sababu, Serikali hii ni shirikishi, lazima tuwashirikishe wananchi wenyewe katika maamuzi sahihi ya maendeleo yao.
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nina kila sababu za kuishukuru Serikali si kwa majibu tu, lakini kwa utekelezaji wa vitendo. Kwa mfano katika Skimu ya Itumbiko, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Kakonko, Ndugu Masumbuko, ameshirikiana sana na wananchi na mimi mwenyewe na tayari maji yameanza sasa kuingia katika mfereji mkuu na banio limetengenezwa, lakini bado tunahitaji miundombinu mingine ikiwemo barabara za kutoa mazao mashambani zitengenezwe.

Pia nashukuru Tume ya Umwagiliaji imenipa taarifa kwamba, shilingi milioni 109 kutoka Food Aid Counterpart Fund zimepatikana kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Umwagiliaji wa Gwanumpu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa hiyo, nina swali moja tu la nyongeza; kwa kuwa, wakati tunaanzisha miradi hii ya Itumbiko na Gwanumpu kwenye package hiyo tulikuwa na Mradi wa Umwagiliaji wa Nyamtukuza ambao uko katika mpaka wa Wilaya ya Kakonko na Ngara na mradi huu ulitarajiwa kunufaisha Kata za Kumbuga katika Wilaya ya Ngara na Kata ya Nyamtukuza katika Wilaya ya Kakonko na tayari Serikali imeshaweka fedha nyingi, lakini mradi umetelekezwa hautekelezwi na sababu zinazotolewa hazitoshelezi kwa sababu ni zile za mabishano tu kwamba, nani autekeleze, ni Ngara au Kakonko? Ni Kagera au ni Kigoma? Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari sasa kuingilia kati ili mradi huu nao utengewe fedha ili utekelezwe na wananchi wa Ngara na wa Kakonko waweze kunufaika na mradi huu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Christopher Chiza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kwa niaba ya Serikali, tunampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa juhudi zake kutekeleza miradi hii. Alitenga fedha za Jimbo kwa ajili ya kushirikiana na wananchi wake kusaidiana na Serikali kuendeleza skimu hii aliyoisema.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili kwenye swali lake la msingi nataka nimweleze kwamba, niko tayari kuingilia kati kwa sababu, nia ya Serikali ni kupeleka maendeleo kwa wananchi wake, mradi cha muhimu kwamba, watu wa Kagera ni Watanzania, watu wa Kigoma ni Watanzania, ilimradi mradi huu tuumalize kwa wakati upeleke maendeleo kwa wananchi wetu na waweze kunufaika na Serikali yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la mwisho, sio kwa umuhimu, nataka nimwombe Mheshimiwa Mbunge, hela kama alivyosema ziko tayari, lakini kuna changamoto ndogo tu kutoka wale viongozi wa skimu, waharakishe mchakato ule wa kupata watia saini, ili hela zile ziweze kuingizwa kwenye akaunti yao haraka iwezekanavyo.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pia nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali yaliyotolewa hivi punde, lakini pamoja na majibu hayo mazuri naomba niwe na maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri amesema Serikali itapeleka wataalam kwa ajili ya kuyachunguza mabwawa hayo waone nini cha kufanya. Je, ni lini Serikali itapeleka wataalam hawa ili wakafanye kazi hiyo ikizingatiwa kwamba, mabwawa haya ni muhimu sana katika kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na uchumi wa Taifa kwa jumla?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, baada ya bwawa la Izava kubomoka mwaka 2017/2018, inaonekana baada ya maji kupita kwa misimu miwili ule mchanga na tope lote lililokuwa limejaa pale chini limeondoka. Je, Serikali haioni pengine hii inaweza kuwa ni muarobaini kwa maana ya dawa ya kuyasafisha mabwawa yetu yaliyojaa tope wakafanya hivyo kwa mabwawa yote ambayo yana matatizo ya tope hapa nchini? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Joel Mwaka, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza kwa umuhimu wa kilimo na umuhimu wa wananchi wa Chilonwa, Serikali kwamba, inachukua nafasi hii kuwaelekeza wataalam wa umwagiliaji Kanda ya Dodoma, hususan wa Halmashauri ya Chamwino waende kuanzia kesho kufanya tathmini na kuangalia uharibifu wa mabwawa hayo, ili kuishauri Serikali na kuanza haraka sana kuyaboresha mabwawa hayo ili kuimarisha kilimo cha uhakika katika wilaya hiyo.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anasema kwamba, bwawa hili la Izava lilipobomoka maji kwa miaka hii mitatu yamesafisha tope lote. Nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge awe na subira, kwa sababu tunapeleka wataalam hivi karibuni kuanzia kesho. Acha waende watathmini halafu watuletee majibu sahihi ya kitaalam, baada ya hapo Serikali itaona ni njia gani nzuri ya kufanya, kwa sababu hii njia ni kutokana na ajali ya mafuriko hatuwezi kusema ikawa ndio njia mbadala sasa ya kusafisha mabwawa yetu yote nchini.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwanza kabisa ninaomba niipongeze sana Serikali kwa hatua yake ya kuamua sasa kutuma timu ya Wataalamu kufanya tathmini ili kuweza kuendeleza Bwawa hili lakini nilikuwa naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hawa Wakandarasi katika nchi nzima wako Wakandarasi ambao wamekuwa wakijenga Mabwawa na wengine wamekuwa wakitudhalilisha na kutusababishia matatizo na kusababisha pesa nyingi za Wananchi na pia vilevile pesa kutoka kwa Wafadhili kuonekana kwamba ni nchi ambayo ni kama vile kuidhalilisha nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wamekuwa wanajenga vitu ambavyo haviko katika viwango na wengine wamekuwa wakishindwa kumaliza,

Je, Serikali iko tayari sasa kufanya tathmini nyingine upya ili hawa Wakandarasi ambao baadhi yao wakiharibu Mkoa mmoja anaenda kwenye Mkoa mwingine waweze kuchukuliwa hatua ikiwemo kushindwa kabisa kupewa kazi na ikiwezekana kutokupewa kazi kabisa katika nchi ya Tanzania ili kuendeleza heshima tuliyonayo kama nchi na kuweza kulinda pesa za wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Waziri nilikuwa naomba kabla ya tathmini je Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuambatana na mimi kuweza kujionea kwa macho yake athari zilizoko pale katika eneo lile ambalo limesababisha kwa kiwango kikubwa wakinamama wanapata shida walikuwa wanalima lakini sasa hivi hawalimi maji walikuwa wanapata eneo la karibu lakini sasa imekuwa wanapata eneo la mbali, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) Mheshimiwa Spika, kwanza naomba unipe nafasi nimpongeze Mheshimiwa Lucy kwa jinsi anavyowapigania Wakulima wote wa Mkoa wa Shinyanga na akishirikiana na Mbunge wa Jimbo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza, kwanza Serikali tuko tayari na tulishaanza kufanya tathmini ya kina na ndiyo maana tuwaarifu Waheshimiwa Wabunge wanaona Miradi mingi ya Umwagiliaji imechelewa kupelekewa fedha kwa sababu Serikali tumejipa jukumu la kupitia Miradi yote ili kubaini ubadhirifu na jinsi ya kutathmini thamani ya fedha ya Miradi hiyo kabla hatujaanza kupangia fedha nyingine kwa ajili ya kuendelea.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, zoezi hilo la kudumu na tutaendelea na Miradi yote Tanzania kabla hatujaanza kuipatia fedha nyingine. Swali lake la pili, niko tayari kuambatana na yeye baada ya Bunge hili nitaanzia Mkoa wa Shinyanga kwenda kutembelea Mradi huo ili kubaini changamoto hizo tuweze kutafutia ufumbuzi.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi nzuri za Serikali kutaka kuhakikisha wananchi wanapata mazao yao pindi wanapokuwa wamelima vizuri lakini napenda kujua, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba inafanya utafiti wa kutosha kuhusiana na aina ya mbegu na aina ya mbolea pamoja na aina ya udongo wa sehemu husika ili wananchi waweze kulima vizuri na wasiweze kupata hasara? Katika Mkoa wangu wa Katavi, Jimbo la Kavuu mahindi yameenda vizuri na mvua hizi lakini bado kuna mdudu ambaye amekuwa akishambulia mahindi na hivyo kusababisha hasara.

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa Mkoa wa Katavi na Mikoa mingi ya Kusini Magharibi imekuwa ikitajwa kama ni mikoa ya uzalishaji wa mazao ya chakula yakiwemo mahindi, mpunga na maharagwe.

Je, Serikali ina mkakati gani hususan katika Mkoa wa Katavi kuhakikisha kwamba inafanya utafiti na ku-introduce zao la biashara kwa wakulima wa Mkoa wa Katavi ili waweze nao kutoka kwenye masuala ya mazao ya chakula waende sasa kufanya biashara katika mkoa huo? Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba watu wao wanapata mazao ya kibiashara?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Pudenciana Wilfred Kikwembe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Serikali kwanza tuna Kituo chetu cha Utafiti cha Mlingano Tanga ambacho tumekipa jukumu mahsusi kwa ajili ya utafiti wa udongo kuangalia afya ya udongo na tabaka la udongo ili kufahamu kwamba udongo wa sehemu husika unakubali mazao gani, una upungufu wa virutubisho vya ardhi vya mbolea kiasi gani ili sasa kumwelekeza mkulima kulima kulingana na ikolojia ya eneo lake na mazao yanayokubali kutokana na ardhi ile.

Mheshimiwa Spika, kazi hiyo ya awali tumeshamaliza kwenye mikoa zaidi ya 16 na sasa hizi pia tumetambulisha maabara yetu kama pale SUA na Chuo cha Kibaha (TARI) kwa ajili ya kazi hiyo. Kwa hiyo, niwahamasishe wakulima wote kuchukua nafasi hasa kwenye kilimo cha biashara ni vizuri kufanya utafiti wa udongo kabla ya kulima kwa sababu ardhi imeshachakaa sana.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu mkakati wa Serikali tuliokuwa nao kwa ajili ya kutambulisha mazao ya biashara katika mikoa ya Nyanda za Juu hususan katika Mkoa huu wa Katavi. Kwanza hili ni swali zuri sana na ni mkakati wa Serikali sasa hivi kuwatengenezea wakulima kuwa na kiiunua mgongo wakati wanapofikisha miaka zaidi ya 60 kwa sababu kuendelea kulima mazao muda mfupi mahindi na mpunga maana yake ni kuwalazimisha wakulima kulima mpaka kufa. Katika mipango hii ya Serikali katika Mkoa wake wa Katavi, mwaka huu tumeshaanza kuzalisha miche zaidi ya 600,000 ya korosho na tumeshagawa sasa hivi katika Wilaya ya Tanganyika miche zaidi ya 250,000 na tarehe 8 mwezi huu tunakwenda kugawa miche iliyobaki ya korosho zaidi ya 350,000 katika Wilaya zote za Mkoa wa Katavi ili sasa kutambulisha na kuhamasisha wakulima hawa wakalima mazao muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, vilevile mwaka huu temegawa zaidi ya miche 800,000 ya kahawa katika Mkoa huo huo wa Katavi na mwaka huu unaokuja katika bajeti tumepanga kuzalisha miche 1,000,000 ya kahawa, miche 1,000,000 ya korosho na miche 1,000,000 ya maparachichi ili kwenda kuipanda katika Mkoa huo wa Katavi. Nakushukuru sana.
MHE. ANTHONY C. KOMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika majibu ya Serikali skimu za asili ile mifereji ya asili haikutajwa hata moja na katika Jimbo la Moshi Vijijini ambalo lina Kata 16, Kata 14 zote za Kibosho, Uru, Old Moshi, Mbokomu na Kimochi zote zinategemea hizi skimu za asili; Je, mko tayari kutuma wataalamu katika Jimbo la Moshi Vijijini kwenda kuona hizo skimu ambazo nazizungumzia na kubainisha changamoto zilizopo na kupendekeza utatuzi mahsusi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; katika Kata ya Old Moshi Magharibi upo mfereji unaoitwa Makupa ambao kwa sasa hivi wananchi wanaoishi nje ya Moshi Vijijini wanachangisha fedha ili kuukarabati na fedha zinazohitajika ni kidogo sana. Upo mfereji mwingine unaoitwa mfereji wa Muo ambao uko katika Kata ya Old Moshi Mashariki na unahudumia Vijiji Nne, Kijiji cha Suduni, Kikarara na Tela.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kufahamu kutoka Serikalini, mtakuwa tayari kuwaunga mkono wananchi wa Kata hizi mbili ili kukamilisha haya malengo ambayo kwa kweli ile mifereji pamoja na jitihada kubwa sana zilizokuwa zimeshafanywa na Serikali huko nyuma, sasa hivi hiyo mifereji haitumiki kabisa kutokana na kubomokabomoka.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, swali lake la kwanza anataka kujua kama Serikali tupo tayari kutuma wataalam kwenda katika Jimbo la Moshi Vijijini, ili kwenda kuangalia jitihada zilizofanywa na wakulima wa huko; Serikali tupo tayari na nichuku nafasi hii kuwaelekeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Kanda ya Kilimanjaro kutuma timu pale, ili iende kuangalia uhakiki na kufanya tathmini tuone hitaji mahususi ni nini, ili tuweze kuwaunga mkono.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa taarifa tu Mheshimiwa Mbunge kwa sasa tumeshapitia muundo wote wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, sasahivi inaanzia mpaka ngazi ya wilaya, palepale kuna wataalam wa Tume ya Umwagiliaji Ngazi ya Mkoa wapo na Ngazi ya Kanda. Kwa hiyo, pia nichukue nafasi hii baada ya Bunge hili waone wale watu wa kanda ya umwagiliaji katika wilaya yako, ili watatoa ushirikiano mkubwa, ili kufanya tathmini ya kina.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili pia anataka kujua kama Serikali tuko tayari kuwaunga mkono kwa kiasi hiki kidogo ambacho kinahitajika kwenda kuwaunga mkono kuboresha miundombinu ya umwagiliaji katika skimu hizi za Makupa na Muo; Serikali tuko tayari, lakini kwanza hatuwezi kujua pamoja na kiasi hiki kidogo kinachohitajika ni vizuri kwanza tusubiri taarifa hawa wataalam waende wakajionee na kufanya tathmini tuone hitaji hasa linahitajika kiasi gani, baadaye tutapeleka fedha kama ulivyoomba Mheshimiwa Mbunge.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, pamoja na mifereji hii ya asili maji mengi sana ya mvua yanapotea kwa mfano katika Jimbo la Rombo wenzetu jirani Kenya wanachukua maji ya kwetu huku Tanzania ya mvua wanalimia halafu wanakuja kutuuzia tena mazao. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba, maji haya ambayo ni mengi sana yanapotea bure yanawekewa utaratibu ili yatumike kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli maji mengi yanapotea kutokana na hii mifereji haijaboreshwa, yanapotea mengi sana. Kama sisi Serikali mipango tuliyokuwanayo, moja ni kujenga mabwawa kwa ajili ya kuhifadhi maji na kuvuna maji wakati wa mvua, ili tuyatumie wakati wa kiangazi. Na moja ya ambayo tulishaifanya katika Mkoa huu wa Kilimanjaro katika Wilaya ya Moshi tumeshachimba mabwawa manne na visima kwa ajili ya kuhifadhia hayo maji, lakini pia katika Wilaya ya Siha, tumechimba pia mabwawa matatu kwa ajili ya kuhifadhia maji. Kwa hiyo, mipango tuliyokuwanayo ni ujenzi wa mabwawa kwa ajili ya kuhifadhi maji wakati wa mvua na kuyatumia wakati wa kiangazi.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, katika skimu aliyoitaja Mheshimiwa Waziri, skimu ya umwagiliaji wa Kijiji cha Soko na Mawala vilivyoko Kahe katika Jimbo la vunjo pamoja na vile vya Lowa Moshi kwa ujumla vilivyoko kata ya Mogiri, Moshi Vijijini Serikali ina mpango gani endelevu na shirikishi katika kuyavuna maji haya, kuyatawala maji haya na kuyatumia maji haya, ili jamii nzima iweze ikapata elimu endelevu, ili yaweze kutumika kitaalam na kisayansi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, anapenda kujua mipango ya Serikali tuliyokuwanayo ya endelevu kwa ajili ya kutunza upotevu wa maji katika Mkoa huu wa Kilimanjaro, hususan katika Wilaya hii ya Moshi Vijijini. Mipango ya kwanza ni kutoa elimu kupitia kwenye vile vyama vyao vya wakulima wamwagiliaji. Tumewahamasisha wakulima wale wajiunge katika vyama vya watumia maji ya umwagiliaji, ili iwe rahisi sisi kama Serikali na wadau wengine kuwafikia wengi zaidi na kwa wakati kuendelea kuwapa elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia sasa hivi kama tulivyosema programu ya sekta ya kilimo onaongozwa na SDP II na asilimia zaidi ya 59 ya bajeti yake itatekelezwa na sekta binafsi. Tunawahamasisha sekta binafsi zote na kupitia benki yetu ya maendeleo ya kilimo kwa ajili ya kwenda kufanya tathmini na kuainisha fursa zilizopo kwenye kilimo cha umwagiliaji kwa kushirikiana na sekta binafsi hizi zitaendelea kujenga hizo skimu, baadaye wataziendesha na kukabidhi baada ya kurudisha gharama zao walizozitumia.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, miradi mingi ya umwagiliaji imetumia fedha nyingi sana hapa nchini na miradi hiyo haijakamilika ukiwemo mradi wa Skimu ya Karema. Nilikuwa nataka kujua Serikali ina mpango gani wa kukamilisha Skimu hiyo ya Karema?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, huu mradi umechukua takribani miaka 10 haujakamilika na kusababisha hasara kwa wakulima baada ya mifumo ya maji iliyotengenezwa kusababisha mafuriko makubwa kwenye maeneo ya uzalishaji. Serikali kupitia kwa Waziri je, yuko tayari kwenda pamoja kushuhudia ile miradi na kubomoa ule mradi ili uweze kuwasaidia Wananchi ambao kimsingi wanakula hasara?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza anatambua kwamba, juhudi za Serikali ambazo tumezifanya tumetumia fedha nyingi sana katika miradi mingi ya umwagiliaji, ukiwepo huu wa Karema na fedha zote zilizohitajika tulipeleka, lakini tukiwa wakweli miongoni mwa miradi mingi ambayo pesa zake hazikutumika kwa mujibu wa malengo ya Serikali na kuwanufaisha wakulima ni pamoja na miradi ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya Serikali kulitambua hilo nduo maana kwamba, kabla ya kuanza kupeleka pesa nyingine wala kuomba hapa kwenye Bunge lako utuidhinishie pesa nyingine nyingi zaidi tuliona kwanza tufanya tathmini ya kina, ili tubaini kasoro na tubaini ufanisi na changamoto ambazo tumezipitia kwenye miradi ile kabla ya kutenga fedha hizo. Na nimuarifu Mheshimiwa Kakoso kwamba, tathmini hiyo tumeshaimaliza na tumebaini mapungufu yalikuwa wapi na ni namna gani kwamba, tulifanya vizuri na vibaya; sasa ndio maana nimemuahidi kwamba, tutatenga fedha katika bajeti ijayo ya mwaka 2020/2021 baada ya kumaliza tathmini hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili anasema kwamba, kama Serikali niko tayari kuambatana naye kwenda katika mradi huu wa Karema, ili kwenda kuubomoa miundombinu, ili Wananchi hawa waweze kupata maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuko hapa kwa ajili ya kujenga, dhamira ya Serikali ilikuwa ni kusogeza na kuwaletea maendeleo Wananchi wale wa Karema, ili wawe na kilimo cha uhakika cha umwagiliaji na kuweza kulima zaidi ya mara mbilil kwa mwaka. Kwa hiyo, hatuko tayari kwenda kuiobomoa, ila niko tayari kuambana naye kwenda hapo Karema na timu yangu ya wataalam ili kwenda kuangalia kasoro hizo ili tuweze kutafuta ufumbuzi wa kuziboresha zaidi tuwaletee maendeleo Wananchi wa Karema.
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya serikali. Sasa naomba niulize maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya miradi ya umwagiliaji imekuwa haina tija kwa wakulima wetu, na hii ni kutokana na kwamba inategemea maji ya mvua za msimu.

(i) Je, serikali haioni sasa ni muda muafaka wa kuanza kujenga mabwawa badala ya kuanza kujenga mitaro ili tuweze kuvuna kwanza maji na baadaye kuweza kuyasambaza katika mashamba yetu?

(ii) Je, serikali imechukua hatua gani kwa miradi ya umwagiliaji ambayo imejengwa chini ya kiwango na imekuwa haina tija kwa wakulima wetu ukiwepo Mradi wa Masengwa na Mradi wa Ichololo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Azza Hilaly Hamad kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza anataka kujua je hatuoni umuhimu wa kuanza kabla ya miundo mbinu ya umwagiliaji. Nitake kwanza kuchukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Azza Hilaly kwa uongozi wake kwa mfano, kwa sababu anatuunga mkono kwenye kilimo na amejenga bwawa la umwagiliaji eneo lake kwa kilimo cha mpunga.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kama nilivyojibu swali la msingi, kwamba Serikali tupo tayari na tulishaanza kupitia Mpango Kabambe wa Umwagiliaji wa Mwaka 2012 tangu mwaka 2018. Kwa ajili sasa kwenda kuanza ujenzi wa miundo mbinu ya bwawa kabla ya hii miundo mbinu ya uwagiliaji kwa sababu tumeeona kwamba maji mengi wakati wa mvua yanakwenda baharini na kwenye mito na baadaye tunashindwa kupata maji ya umwagiliaji.

Kwa hiyo serikali tumeshaaza mpango huo na huo mpango umeshakamilikia ambao tumeugawa katika awamu mbili. Awamu ya kwanza miaka mitano kuanzia mwaka huu mpaka mwaka 2025 na awamu ya pili itakuwa kuanzia mwaka 2025 mpaka mwaka 2035.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili; kwamba je, Serikali tumechukua hatua gani kwa miradi iliyojengwa chini ya kiwango. Kwanza, hatua tuliyoichukua kama Serikali ni kuhamisha Tume yenyewe ya Umwagiliaji kutoka kwenye Wizara ya Maji kuja Wizara ya Kilimo ili kukiweka pamoja kilimo pamoja na umwagiliaji. Pili ni kuimarisha Muundo wa Tume ya Umwagiliaji; kwamba badala ya kuwa na watalamu kwa ngazi ya kanda tu sasa tuna wataalamu kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa na kanda ili kuwe na usimaizi wa karibu sana katika miradi hii ya umwagiliaji siku hadi siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, tuko kwenye hatua za kufanya tathmini ya kina ili kujua mapungufu ya msingi yaliyosambisha miradi hiyo kujengwa chini ya kiwango na baada ya hapo hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wote ambao walitufikisha hapa ili tupate majibu sahihi ya nini cha kufanya kuendeleza miradi hiyo.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika. Mradi wa Ruafi Katongoro Irrigation skimu serikali imetumia zaidi ya bilioni 1.8; Lakini hauna faida yoyote kwa wakulima zaidi ya 2000 wa Kata za Kilando, Kipili pamoja na Itete.

Je, ni lini Wizara kilimo na umwagiliaji itaenda kuimarisha mradi wa skim ya katongoro na ruafi ili wakulima wanufaike na kilimo cha mpunga?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali moja la Mheshimiwa Ally Keissy kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokuwa najibu swali la msingi, kwamba kuna miradi mingi ambayo imejengwa chini ya kiwango pamoja na Serikali kupeleka kiasi kikubwa sana cha fedha kwa ajili ya mahitaji ya wakati huo. Kwa sasa hivi serikali tutatuma timu ya wataalam kwenda kuangalia mapungufu yaliyofanyika katika mradi huo; na haraka iwezekanavyo baada tathimini hiyo tutaanza kupanga fedha kwa mujibu wa bajeti kwenda kuwahudumia watu hawa zaidi ya 2000 kwenye kilimo cha kisasa.
MHE. RHODA E: KUNCHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mkoa wa Katavi bado una changamoto kubwa ya miradi ya umwagiliaji kuchukua muda mrefu na bila sababu ya msingi. Mradi wa mamba katika Jimbo la Kavuu ni miongoni mwa miradi, ambao imechukua muda mrefu na kuleta usumbufu mkubwa sana kwa wananchi wa jimbo la kavuu. Serikali inasema nini kuhusiana na mradi huu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rhoda Kunchela kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli miradi hii mingi ya umwagiliaji imechukua muda mrefu kumaliziwa. Kama nilivyozungumza hapo awali, ni kwamba changamoto kubwa ilikuwa ni kwamba miradi hii haikuleta gharama halisi wakati wa ujenzi wake. Kama tunavyofahamu wakati ule kulikuwa na miradi tuliyokuwa tunaitekeleza kwa ngazi mbili. Kuna miradi ambayo ilikuwa inatekelezwa kwenye ngazi ya wilaya ambao ni ya DIDF miradi ambayo ilikuwa inatekelezwa ngazi ya taifa. Miradi yote ambayo ilikuwa chini ya thamani ya milioni 500 ilikuwa ni ngazi ya wilaya na miradi ambayo ilikuwa ni zaidi ya milioni 500 tunatekeleza ngazi ya taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kuna baadhi ya halmashauri, mojawapo ikiwa yakwako, ilileta mradi huo chini ya thamani ya mradi ili kwamba wapate kigezo hela hizo ziende kwenye wilaya yako wakatekeleza wao ilhali mradi ulikuwa unahitaji fedha nyingi. Sasa baada ya mapungufu hayo tumesema kwamba tunaunda kikosi kazi ili kupitia kujua gharama halisi ya kiasi gani kinachohitajika; na baada ya gharama hizo ndio tutaanza ujenzi wa mradi huo.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafsi hii. Mvua zinazoendelea kunyesha katika Wilaya ya Lushoto zimefanya uharibifu mkubwa sana wa miundo mbinu ya skimu za umwagiliaji, Skimu ya Mng‟alo Kitivo pamoja na skimu kiwani mwezae kwa Mgiriki Kata ya Lunguza nakufanya sasa kilimo cha mpunga kiwe shakani.

Je, serikali ina mpango gani mahususi wa haraka kwenda kuondoa mawe ambayo yamenasa katika kingo za mto umba ambao ndio unapeleka maji katika skimu hizi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Rashid Shangazi Mbunge wa Mlalo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kwamba tumepata taarifa; kwanza kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge mwenyewe kwamba alishatuambua, lakini pia kutoka kwa katibu Mkuu wa Chama Chama Mapinduzi, anayesimamia ilani, Dkt. Bashiru Ally. Alifika mwenyewe kwenye skimu hiyo na alitupigia simu kujua namna gani tunakwenda kusimamia utekelezaji wa ilani katika Jimbo hilo la Mlalo huko Lushoto.

Mheshimiwa Spika, Serikali tupo tayari, na nichukue nafasi hii kuwaelekeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kanda ya Kilimanjoro, viongozi wa mkoa na wilaya kwenda haraka iwezekanavyo katika skimu hii katika banio la Ng‟alo Kitivo pamoja na Skimu ya Lunguza ili kuangalia mapungufu haya na uharibifu mkubwa wa mawe tuone namna gani tunaweza kuondoa haraka iwezekanavyo. Nami nikuahidi pia baada ya Bunge hili, kwa sababu nilishafika miezi miwili iliyopita, nitarudi tena huko ili kuona namna gani tunaweza kuwaidia watu wa Mlalo.
MHE. ZAINABU MUSSA BAKARI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Baada ya majibu ya Serikali napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, baada ya kufanya utafiti na kugundua ugonjwa huo ni kwa kiasi gani Serikali imewafikia wakulima kuwapa elimu pamoja na kuwafahamisha dawa muhimu za mipapai hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kiasi kikubwa Watanzania wamejikita katika kilimo cha mapapai na vilevile inaonekana kwamba wakulima wakinunua mbegu za mipapai, mipapai mingi inakuwa haizai. Je Serikali ina mkakati gani wa kuwapatia wakulima pembejeo na kuhakikisha mbegu wanazonunua zinazaa ili kukiimarisha kilimo hicho?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zainabu Bakari, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anataka kujua Serikali tumewafikiaje wakulima baada ya kugundua matatizo hayo ya magonjwa ya mapapai. La kwanza tumewafikia kwa ajili ya kwenda kuwapa elimu moja kupitia kituo chetu cha TPRI ambao ndiyo wadhibiti wa magonjwa haya mbalimbali kupitia viuatilifu. Kwa hiyo wao kwanza wanapita sehemu mbalimbali kukagua maduka yanayouza viuatilifu hivyo ili kubaini kama viuatilifu vile vinaubora na vinakidhi vigezo kwa ajili ya kupambana na ugonjwa huu.

Mheshimiwa Spika, pili, tunapitia, tunatoa elimu mbalimbali kupitia vyombo mbalimbali vya habari kama redio, TV na makongamano na warsha kuwafikia wakulima huko waliko ili kwamba kuwapa elimu kukabiliana na magonjwa hayo mbalimbali ikiwemo hii ya mipapai.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anataka kujua mikakati ya Serikali tuliyokuwa nayo kwa ajili ya kuwapatia mbegu bora za mipapai. Moja kama nilivyosema jibu la msingi kwamba kituo chetu cha utafiti cha TARI - Tengeru, ambacho kiko maalum kwa ajili ya kufanya utafiti wa mazao ya mbogamboga na mazao ya matunda hapa nchini, lengo ni kufanya utafiti wa kina kugundua mbegu bora ambazo zinaendana na hali yetu ya mazingira, lakini pia zenye ubora wa ukinzani wa magonjwa haya pamoja na hali ya mabadiliko ya tabia nchi. Kwa hiyo, atupe nafasi tu kituo hiki kinafanya utafiti huo na wako katika hatua za mwisho kuja na majibu ambayo sahihi kukabiliana na ugonjwa huo.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali langu la nyongeza. Kabla sijauliza swali la nyongeza naomba nitumie fursa hii kuwapongeza na kuwatakia heri wanafunzi wote wa Tanzania kwa kuanza mitihani yao ya kidato cha nne, tunawaombea Mwenyezi Mungu awasimamie, awabariki ili waweze kufanya vizuri mitihani yao.

Mheshimiwa Spika, naomba sasa niulize swali langu la nyongeza, kutokana na swali la msingi namba saba, nami nataka niulize kwamba, kuna suala la sumu kuvu ambalo lipo ndani ya karanga na lipo vile vile ndani ya mahindi na ukizingatia mahindi ni chakula chetu kikubwa na ni chakula cha msingi kutokana na utafiti uliofanyika. Je, wamefikia hatua gani kuhakikisha kwamba mahindi haya hayana sumu kuvu au yamepungua kwa kiasi gani? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mama yetu Salma Kikwete kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli kuna ugonjwa hatari unaosababishwa na huu wa sumu kuvu unaosababishwa na fangasi wakuvu ambao ugonjwa huu umeleta athari kubwa hasa katika mikoa hii ya Kanda ya Kati hususan kwenye kule Wilaya ya Kondoa, Chemba na watu zaidi ya 19 walipoteza maisha.

Mheshimiwa Spika, kama Serikali baada ya kugundua hiyo kwanza sasa hivi tumekuja na programu ambayo imeanza tangu mwaka jana na tumetenga zaidi ya bilioni 35 kwa ajili moja kutoa elimu ya ugonjwa huu kwa umma, lakini pili kujenga miundombinu ya kuhifadhia mazao haya ambayo kama mahindi na karanga ili yasiweze kuathirika na sumu kuvu. Mikoa ambayo tumeilenga ni mikoa 10 na mikoa miwili ya Zanzibar na ikiwepo hii ya Kanda ya Kati.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo moja kabisa ni kuwafikia wakulima kuwapa elimu sababu gani zinasababisha ugonjwa huu, madhara yake ni nini na kinga yake ni nini? Ili kuondokana na tatizo hili lililopo hapa nchini.
MHE. ZAYNAB M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Serikali imebaini kwamba kuna tatizo la soko; na kwa kuwa Serikali imebaini kuna uhaba wa zao lenyewe na watumiaji. Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kuweka mkakati madhubuti wa kuwatafutia wakulima hawa soko la nje waweze kusafirisha nazi zao kwenda nje ya nchi kwani hapa Tanzania kwa mujibu wa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri inaonekana kwamba soko limepungua? Pia wangeweza kutoa elimu ya kutosha watu wakajua matumizi na thamani ya zao la nazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; bila shaka Naibu Waziri anajua thamani ya zao la nazi, zao la nazi lina thamani kubwa sana. Kwanza mti wenyewe unatumika kama mbao, unatumika kwa kutengenezea furniture, mti wenyewe unatoa nazi, nazi inatoa tui ambalo linapikiwa, nazi ina maji ambayo yanatumika kwa afya zetu; nazi machicha yake yanatumika kwa ajili ya kutengenezea kashata na vitu vingine, lakini pia mnazi huohuo unatoa makuti ambayo yana thamani katika utalii wetu wa hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huo huo mnazi huo huo unatoa kitu kinaitwa kitale, kitale kina thamani kubwa sana watu wa afya wanaweza wakajua na watu wa Pwani wanaweza wakaelewa thamani ya kitu kinachoitwa kitale. Sasa ni lini Serikali itaweka mkakati wa kuhakikisha zao hili la nazi halipotei nchini kwetu kwa kurudisha vituo vya utafiti vilivyokuwa Dar es Salaam, Mafia, Bagamoyo na Lindi ili wakulima wale wasiweze kupoteza thamani ya zao la nazi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zaynabu Matitu Vulu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza anataka kujua mikakati ya Serikali kutafuta soko la nazi nje ya nchi; ni kweli kwamba kama Serikali tuna mikakati mbalimbali lakini tufahamu kwamba matatizo makubwa ya soko la nazi sio bei, tatizo kubwa ni kipato kidogo wanachopata wakulima wa nazi na kipato hicho kinaweza kuongezeka kutokana na bei kubwa au tija kuongezeka au kuongeza uzalishaji, lakini pia kupunguza gharama za uzalishaji wakulima hao wa nazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Serikali moja ambalo ndiyo tumeanzisha vituo vya utafiti hivi 16, kimojawapo ni Kituo chetu Cha Utafiti cha pale Mikocheni ambacho kimepewa mahususi kwa ajili ya utafiti wa zao la nazi. Lengo ni kuja kupunguza gharama za uzalishaji, lakini kupata mbegu bora zinazoweza kuhimili ukame na magonjwa kwa ajili ya kuongeza tija na uzalishaji kwa wakulima wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili anataka kujua ni lini Serikali tutaanza kurudisha vile vituo vyetu vya utafiti kama zamani. Kama nilivyosema katika majibu yetu ya msingi, kwanza zamani hatukuwa na vituo vile vya utafiti zaidi ya hiki cha Mikocheni, tulikuwa na vituo vya kuzalisha miche ya minazi na baadaye kuisambaza kwa wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, huo utaratibu mpaka sasa hivi tunao, tunacho kule Zambezi Bagamoyo, tunacho pale Mkuranga na tutaendelea kufungua vituo hivyo Mafia na sehemu zingine kwa wakulima wakubwa wa nazi, lakini hasa baada ya kupata taarifa za utafiti kutoka kwenye kituo chetu hiki cha TARI pale Mikocheni ambacho tumewapa mahususi kwa ajili ya kufanya utafiti wa zao la nazi ili kuja sasa na mbegu ambayo inahimili ukame na magonjwa tuachane na mbegu yetu ile fupi tuliyoletewa kutoka nje ambapo kule ni nchi ambazo ni za baridi, haiwezi kuhimili kutokana na hali ya joto na hali ya mazingira ya nchini kwetu. Kwa hiyo, nitoe wito kwa wakulima wote; sasa hivi tunasisitiza tutumie mbegu yetu ile ya asili ya East African Tall ambayo inahimili ukame, joto na mazingira yetu.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Zao la kahawa ni miongoni mwa mazao ya kimkakati, lakini zao hili limekuwa kila mwaka linapungua uzalishaji. Je, ni nini mkakati wa Serikali kuongeza uzalishaji wa kahawa ili zao hili muhimu lisiweze kufutika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, naamini miongoni mwa sababu zinazosababisha zao za kahawa kushuka ni kwa sababu tunapeleka kahawa ghafi kwenye soko la dunia. Je, ni nini mkakati wa Serikali wa kuanzisha viwanda ili tupeleke kahawa ambayo iko tayari kutumika kuliko kupeleka kahawa ghafi ambayo bei yake inakuwa chini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Innocent Seba Bilakwate, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, anataka kujua mikakati ya Serikali kuhusu kuongeza uzalishaji. Mkakati wetu wa kwanza ni kuendelea kutoa elimu kwa wakulima kuzingatia kanuni bora za kilimo hasa kupitia Maafisa Ugani wetu na Maafisa Kilimo ili watumie mbinu za kisasa kwa ajili ya kuongeza tija ambayo ndio tatizo sugu kwa kilimo cha Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, katika zao la kahawa hilo hilo, ni kuendelea kuzalisha. Tuna mkakati na program ya miaka mitano ya kuzalisha miche milioni 10 na kuisambaza katika mikoa yote inayolima kahawa. Mkakati huo unaanza mwaka huu 2019/2020 na utaisha 2024/2025. Pia tunaendelea kupanua mikoa, tunaendelea kulitambulisha zao hili la kahawa kwa ajili ya kuongeza uzalishaji hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusu mkakati wa Serikali katika uimarishaji wa viwanda kwa ajili ya kuongeza thamani. Sisi kama Serikali tulishaanza kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje kuja kuwekeza kwenye sekta hii ya kahawa. Nichukue nafasi hii kuwapongeza kampuni ya ndani…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, jibu kwa kifupi sana.

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna viwanda viwili mpaka sasa Kiwanda cha Chanika kule Bukoba pamoja na Kiwanda cha Amir Hamza ambavyo vinazalisha zaidi ya tani 6000 za kahawa iliyoongezewa thamani, lakini changamoto kubwa tuliyonayo matumizi ya ndani ni madogo. Nitoe wito kwa sisi Wabunge na wananchi kwa ujumla tuweze kupenda vyetu tutumie bidhaa zinazozalishwa ndani, ili kuunga uchumi wa Taifa letu na kuleta moyo kwa hawa waliowekeza viwanda hapa nchini.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwea kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri zao la kahawa jinisi ambavyo bei yake iko chini zao la chai pia, bei yake iko chini kwa muda mrefu. Je, Serikali ina mkakati gani kuongeza bei ili kuweza kuwasaidia wakulima wa chai kupata kipato kiweze kuwasaidia katika maisha yao ya kila siku? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli kama alivyosema zao la chai bei yake inaendelea kushuka. Ni kutokana na yaleyale ni over supply katika soko la dunia, lakini wanywaji wanabaki ni walewale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyofahamu uzalishaji unaweza kuongezeka ndani ya miaka mitano, lakini wanywaji wa chai na watu wenye uwezo wa kununua hiyo chai kuongezeka kwake mpaka afikishe zaidi ya miaka 18 na kuendelea. Mkakati mmoja wa Serikali ni kuhakikisha kwamba, tunakuwa na mnada kama walivyokuwa wenzetu wa Kenya hapa nchini, ili kuuza chai yetu kwenye mnada hapa nchini, lakini mkakati wa pili tunaendelea kwenye mazungumzo na wenzetu wa China, ili kupata bilateral agreement tuuze moja kwa moja chai yetu kwenye ma-super market ya China badala ya kuuza kwa kutumia…

MWENYEKITI: Asante.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kati ya mambo yaliyoua zao la kahawa ni ushirika kwa sababu, ushirika ndio ulikuwa unatafuta pembejeo, n.k. Sasa chama kikuu cha ushirika pale Kilimanjaro (KNCU) ambacho kilimiliki mali nyingi sana za wakulima wa kahawa bado kinasuasua na mali zile baadhi zilishikiliwa na watu. Sasa je, Serikali ina mpango gani wa kufufua vyama vya ushirika vinavyotoka maeneo yanayozalisha kahawa, ili vyama vile viweze kusimamia zao hili kikamilifu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali kufufua vyama vya ushirika yeye mwenyewe ni shahidi, la kwanza kupitia viongozi wote hao wa vyama vya ushirika kufanya uhakiki kwa ajili ya madeni na mali za ushirika. Hilo tumeshalifanya huko katika Mkoa wa Kilimanjaro na Taifa kwa ujumla, tumeshawachukulia hatua wale wote waliotufikisha hapa mahali ilipo, lakini la pili kuendelea kutoa kuwahamasisha Wananchi wenyewe na wakulima kuchagua viongozi wazalendo waadilifu ambao watawatumikia kwa kuzingatia maslahi yao badala ya kuchagua kwa wale viongozi wanaojua kusema maneno mengi matokeo yake wanakuja kuwakandamiza na kuwaibia washirika kwa kushirikiana na viongozi asiokuwa waaminifu.
MHE. NAPE M. MNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kama ilivyo kahawa, korosho ni zao la mkakati na bila shaka ndio zao linaloongoza kuingiza kipato kwa nchi yetu. Sasa hali toka msimu umeanza hali ya upatikanaji wa magunia ni mbaya sana, hili jambo limezungumzwa na kuzungumzwa. Hivi asubuhi ya leo imefikia mahali kwa sababu ya kukosekana kwa magunia viongozi wa vyama vya msingi wameanza kutishiwa maisha, wengine wanafungiwa ofisini, wakulima wanapewa magunia mawili, gunia moja. Serikali inatoa tamko gani ku-rescue hali hii kwa sababu, ikiachiwa ikaendelea hivi zao hili tunaliua tena?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli kamba, kuna changamoto ya magunia na Serikali tumeiona na yeye anafahamu wenye jukumu la kuagiza magunia walikuwa ni vyama vya ushirika na ndio hao ambao waliagiza magunia. Baadaye tulivyoona kwamba, inasuasua Serikali tumeingilia kati, tumeshaongea na yule msambazaji, mpaka sasa magunia zaidi ya 2,400,000 yako bandarini. Na mpaka hivi tunavyozungumza ameshatoa zaidi ya magunia laki saba, jana amepakia zaidi ya magunia 258,000 kupeleka huko mikoa ya Kusini. Na leo hivi ninavyozungumza tunaendelea kupakia magunia 255,000 na usiwe na wasiwasi na tumeshamuelekeza maalum apeleke zaidi ya magunia 30,000 pale Lindi Mwambao.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mkakati gani wa kuwanusuru wakulima wa tumbaku waliokosa mikataba ya tumbaku baada ya kampuni ya TLTC kufunga shughuli zake hapa nchini na wakulima wanakosa majawabu. Tulikuwa tunaomba Serikali itoe majibu ya msingi wakiwemo wakulima wa Mishamo.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa kwanza wa Serikali ni kuendelea kutoa elimu kwa wakulima. Kilimo, mauzo ya soko la tumbaku ni soko la kimkataba, unatakiwa kuzalisha baada ya kuuza. Kwa hiyo, lazima kwamba, tuendelee wakulima wakaheshimu makubaliano hayo wasiendelee kuzalisha kabla hawajajua mnunuzi ni nani na watauza kwa bei gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mkakati wa pili, tuko kwenye majadiliano tunaongea na kampuni ya BAT ambayo imekubali kununua tumbaku yetu zaidi ya tani 8,000 ambao tukishamaliza majadiliano hayo tutawaleta huko kuja kununua hiyo tumbaku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la tatu tunaendelea na mazungumzo na kampuni ya TLPC ili ambayo ile iliyojitoa ili waendelee kununua tumbaku ya wakulima wetu.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Wazir, licha ya hayo majibu kwamba, vyuo vipo bado hawa wataalam wanaokuwa wanamaliza kwenye vyuo hawapewi ajira na ndio maana tunazidi kuona upungufu wa maafisa ugani kwenye maeneo yetu. Je, nini mkakati wa Serikali kuajiri maafisa ugani wa kutosha kwa ajili ya kusaidia kufundisha wakulima kuzalisha mbegu bora?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Mkoa wa Kagera hususan Wilaya ya Kyerwa ni walimaji wakubwa wa zao la mgomba, kwa maana ya migomba. Nini mkakati wa Serikali kuja na viwanda au kuja na mbinu ya kuongeza thamani katika zao la ndizi kwa kuwa hilo zao au ndizi huwa zinaharibika muda mfupi baada ya kukomaa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza anataka kujua mkakati wa Serikali kutoa ajira kwa maafisa ugani; kwanza niseme ni kweli maafisa ugani hawatoshelezi, lakini kwamba, tutaendelea kuajiri kutokana na vilevile kuzingatia kipato cha Serikali kwa sababu hata tukiwaajiri hawa wana stahiki zao lazima wapewe, badala yake tukija kuwaajiri bila kuwalipa tutaanzisha changamoto nyingine ambayo haiwezekani. Kwa hiyo, tutaendelea kuajiri kwa kuzingatia uwezo wa serikali kuwalipa na kutoa gharama nyingine. Lakini la katika kukabiliana na tatizo lililopo kama Serikali cha kwanza mkakati tuliokuwanao tunaendelea kujenga vituo vya rasilimali kilimo kila kata, ili maafisa ugani wachache hawa waliokuwepo waweze kuwakusanya wakulima na kutoa elimu ya kilimo cha kisasa kwa wakulima walio wengi kwenye kata zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kwenye suala la Kagera kwenye suala la migomba; ni kweli migomba ni zao ambalo linapoteza thamani mapema. Mkakati wa Serikali kama tulivyosema siku zote Serikali ya Awamu ya Tano ya Chama cha Mapinduzi ni Serikali ya Viwanda, tutaendelea kuweka mazingira ya kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ili kuja kuwekeza katika viwanda kuongeza thamani. Na hii tutumieni kama fursa hata wabunge tuna uwezo hapa wa kwenda kuanzisha hivi viwanda vidogovidogo kuongeza thamani kwa sababu Serikali tulishajitoa kwenye suala la kufanya biashara tangu miaka ya 90.
MHE. AIDA J. KHENAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, pamoja na kuwa na vyuo vitatu Nyanda za Juu Kusini, lakini bado tunakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa fedha kwenye chuo cha utafiti. Serikali ina mpango gani wa kupeleka fedha za kutosha ili kuleta tija kwa ajili ya uzalishaji unaoendelea Nyanda za Juu Kusini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, anataka kujua mkakati wa Serikali kupeleka fedha; kwenye bajeti ya mwaka huu tumetenga na tunapeleka fedha zaidi ya bilioni 10 kwenye vyuo vyetu vya utafiti na kilimo kwa ajili ya kwenda kuimarisha utafiti katika vyuo hivyo, ili viweze kuwahudumia wakulima.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kabla sijaenda kwenye maswali, nami niungane na wewe kumpongeza Mheshimiwa Mzindakaya, nami ndio mrithi wake katika Jimbo, naomba wananchi waniunge mkono miaka 45 washuhudie maendeleo. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naenda kwenye swali. Namshukuru sana kwa majibu yenye ufanisi aliyotoa Mheshimiwa Naibu Waziri, japo tatizo hili nimelisema hapa Bungeni mara nyingi sana, sasa ifike wakati Serikali iende kwenye utekelezaji iwasaidie wananchi hao ambao wanajisaidia wenyewe Serikali iwaunge mkono.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, namwomba sasa Mheshimiwa Waziri afike kwenye eneo hili ili aone wananchi hawa wanavyohangaika kujinasua na umasikini. Waswahili wanasema kuona kunaongeza huruma kuliko kuambiwa.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, swali la kwanza la Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha anataka kufahamu hatua za utekelezaji wa mradi huu umefikia wapi kwa sababu ameshasema mara nyingi. Kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi, ni kwamba mradi huu umeibuliwa na nguvu wananchi na Serikali hii inawaunga mkono wananchi na ndiyo maana tumeanza kwanza kuboresha mfumo wa utendaji kazi wa Tume yetu ya Taifa ya Umwagiliaji. Kuanzia sasa tumeanza kujipanga Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ipo katika ngazi ya Wilaya, Mkoa, Kanda na Taifa.

Mheshimiwa Spika la pili, nachukua nafasi hii kuwaelekeza wataalam wa Taifa ya Umwagiliaji kwenda kwenye mradi huu haraka iwezekanavyo kufanya tathmini hiyo ili tuweze kuleta maendeleo kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anataka kufahamu ni lini nitaenda pale kuona? Baada ya Bunge hili nimwahidi Mheshimiwa Mbunge, kuanzia tarehe 22 mwezi wa Tisa, nitakwenda huko kwenye Mikoa ya Rukwa na Katavi kwa ajili ya kufuatilia miradi hii. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Tukitaka kufanya mapinduzi ya kilimo, hakika kilimo cha umwagiliaji ndicho ambacho kinaweza kumsaidia mkulima wa Tanzania. Katika Bonde la Eyasi Wilayani Karatu, wananchi wale wanatumia kilimo cha umwagiliaji lakini hakuna miundombinu ya uhakika. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inawejengea miundombinu ya uhakika ili umwagiliaji wao uwe endelevu na kilimo chao kiweze kuwasaidia?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, ni kweli bonde hili la Eyasi ambalo mimi mwenyewe nilifika, ni bonde muhimu sana kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na ni chanzo kikubwa cha uchumi kwa watu wa Tarafa ile hasa kwenye zao la vitunguu.

Mheshimiwa Spika, katika bonde hili mikakati tuliyokuwa nayo kama Serikali, kwanza kama nilivyosema ni kwamba hatuwezi kusubiri pesa za kibajeti miaka yote hii. Kwa hiyo, sasa hivi kupitia Sheria ile ya PPP tumekuja na mpango kabambe kwa ajili ya kushirikiana na sekta binafsi kuendeleza miundombinu hii kwa utaratibu ule niliosema kwenye jibu la msingi la jenga, endesha na kabidhi baada ya yule mdau anayeendesha ule mradi kurudisha gharama zake.

Mheshimiwa Spika, pili, kupitia Serikai ya Halmashauri, ukizingatia Halmashauri hii ya Karatu zaidi ya 33% mapato yake yanatoka kwenye bonde hili. Kwa hiyo, tukasema zaidi ya mapato hayo ya ndani 20% warudushe kuwekeza katika bonde lile ili liweze kurudisha maendeleo kwa wananchi.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshmiwa Spika, pamoja na majibu marefu sana Mheshimiwa Waziri, lakini kinagaubaga kabisa hajasema wazi ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha sukari pamoja na miwa ya wananchi inapata bei nzuri ukilinganisha na sukari inayoletwa toka nje?

Mheshimiwa Spika, sasa nataka kufahamu kwa Mheshimiwa Waziri, ili kuweza kulinda viwanda vya ndani, anasema nini kuhusu sukari inayoingizwa nchini kwa bei nafuu kuliko sukari inayozalishwa Tanzania?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, utakumbuka mwaka 2018 Serikali ilichukua maamuzi mazuri kabisa ya kuamua kukusanya korosho zote kwa wakulima na baadaye kutangaza bei nzuri na kusema watawalipa wakulima wote. Hivi sasa kumekuwa na sintofahamu kubwa sana kwenye mikoa yote inayolima korosho Tanzania kwa sababu mpaka sasa hivi Serikali haijakamilisha malipo kama ambavyo iliahidi. Utakumbuka maelekezo ya Mheshimiwa Rais na maneno yake alisema kwamba Serikali imeshatenga pesa na sasa hivi pesa hizo zinatakiwa kulipwa kwa wakulima kwa 100%.

Mheshimiwa Spika, sasa swali langu, nataka nipate commitment kutoka wa Serikali, ni lini hasa watakamilisha malipo ya pesa za wakulima wa korosho wa Tanzania kwa sababu walisema pesa hizo wanazo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mwambe anasema katika majibu yetu hakuna mkakati. Angerudia kwenye swali lake la msingi, hilo halikuwa swali la msingi, sisi tumejibu majibu yetu kwa kuzingatia swali la msingi tuliloulizwa.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake hili la nyongeza la kwanza anasema kwamba sukari inatoka nchi na ina bei ndogo kuliko sukari inayoazalishwa hapa nchi. Nini mkakati wa Serikali kulinda viwanda vya ndani? Kwanza ni kweli sukari yote inayotoka nje kuletwa hapa nchini ina bei ndogo kuliko sukari yetu. Ni kwa sababu wenzetu gharama za uzalishaji zipo chini kuliko gharama za hapa ndani kwa sababu wenzetu wanakwenda mpaka kwenye by product nyingine kwa hiyo wanashusha gharama za uzalishaji.

Mheshimiwa Spika, sisi ili kulinda viwanda vya ndani kama tulivyosema, hii Serikali ya Awamu ya Tano ni Serikali ya Viwanda na ndiyo maana mkakati wa kwanza tumewapa ile gap sugar, wenye viwanda vyenyewe ndio waagize sukari ile pungufu ili kuvilinda viwanda vya ndani viweze kuongeza uwezo wa kimtaji na kulinda masoko yako.

Mheshimiwa Spika, hili limetupa manufaa makubwa. Kwa mfano, kiwanda cha sukari cha mtibwa, kabla ya utaratibu huu, uwezo wake wa kuzalisha ni zaidi ya tani 60,000 lakini ulikuwa unazalisha tani 15,000 tu kwa mwaka. Baada ya utaratibu huu, mwaka 2018 kwa mara ya kwanza imefikia kuzalisha tani zaidi ya tani 32,000. Kwa hiyo, hayo ni mafanikio makubwa sana katika kulinda viwanda vyetu vya ndani.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo swali lake la pili anataka kujua malipo ya watu wa korosho. Ni kweli tumesema Serikali fedha tunazo na kweli Serikali fedha tunazo. Ndiyo maana katika hili la utaratibu wa sukari, tulielekeza kampuni yetu au Taasisi ya Serikali ya Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kununua korosho zote kutoka kwa wakulima. Taasisi hii ilienda kukopa kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo.

Mheshimiwa Spika, kilichotokea ni kwamba ile limit ambayo walipangiwa kwamba wameshafikia ukomo ilikuwa lazima kwamba wauze korosho kwanza ili wapunguze lile gap waweze kuuza tena. Sasa tumeshauza korosho hizo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kabda ya msimu huu kuanza wakulima wote watakuwa wamelipwa fedha zao.(Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante pamoja na mazuri ya Serikali ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Bashay tunazalisha vitunguu na tunasindika pale pale kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri tunasindika kwa kutumia mashine ile na kwakuwa tuna rojo na oil na tuna powder; je, Mheshimiwa Naibu Waziri haoni kwamba sasa umefika wakati wewe mwenyewe kuja Bashay kuwasaidia wakulima kwa changamoto hii ya uuzwaji wa vitunguu saumu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili kwa kuwa kuna wanunuzi na walanguzi ambao hawafuati taratibu kama alivyosema kwenye jibu la msingi; je, aoni yeye mwenyewe hataisaidiaje AMCOS ya Bashay kuondokana na uchuuzi huo ambao haufuati vigezo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anataka kwamba Serikali tufike pale ili kuona changamoto hii na kuona namna ya kuwasaidia wakulima hawa, kwamba nikimaliza ziara ya Mikoa ya Katavi na Rukwa basi mkoa utakaofuata ni Mkoa wa Manyara pamoja na kufika Mbulu Vijijini kuangalia hali halisi ya wakulima wetu wa vitunguu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili anataka kujua kwa sababu sasa hivi ni chama kimoja tu cha msingi kinanunua mazao haya ya vitunguu kutoka kwa wakulima na wanapitia watu mbalimbali kwa ajili ya ununuzi huo, nitafika wakati huo huko kwa ajili ya kuona utaratibu huo wa ununuzi unaofanyika, hasa hawa waliosema kwamba ni madalali ambao sisi tunawaita kwamba ni wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo. Lengo kwamba tutaweza kuunganisha na kuweka mfumo rasmi kwamba kila kijiji wafungue vyama vya msingi vya ushirika ili viweze kukusanya mazao kutoka kwa wanachama wao na wakulima, baadae hawa wanunuzi wadogo wa kutoka ndani na nje ya nchi wakija watumie vyama hivi vya msingi kununua mazao kutoka kwa wakulima.
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nauliza maswali mawili ya nyongeza; Je, Serikali ina mkakati gani wa ndani ambao utahakikisha kwamba viuatilifu vyote vinaagizwa kwa mfumo wa bulk procurement ambao sasa hivi haujaanza. Mfumo huu ndiyo ule ambao unasaidia kulifanya zao la korosho ku-stand kwenye uzalishaji mkubwa zaidi kama ulivyofanyika mwaka juzi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa udhibiti wa wafanyabiashara wasio waaminifu pamoja na kutumia watafiti ambao wengine wanashirikiana katika kutengeneza baadhi ya viuatilifu ambavyo wanavichanganya na dawa kama za salfa, dawa kama za pecoxystrobin na proquinazid ambazo zinachangia sana kuweza kusaidia kuongeza uwezo wa kemikali na kuua wadudu lakini vinaharibu mazingira katika maeneo yetu. Je, mkakati gani upo ambao utaweza kuwadhibiti kupitia TPRA hawa wafanya biashara ambao si waaminifu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anataka kujua mkakati wa Serikali kwa ajili ya kuanzisha mfumo wa uagizaji wa viuatilifu kwa pamoja (bulk procurement) ukoje. Nataka nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge, Serikali sasa hivi tuko kwenye hatua za mwisho wa mchakato wa kumalizia ili kwa ajili ya uagizaji wa viuatilifu kwa pamoja. Nataka nimhakikishie msimu ujao wa kilimo cha korosho wa mwaka 2020/2021 kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi, tutaagiza viuatilifu kwa pamoja kwa kutumia Mfumo wa Bulk Procurement.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili anataka kujua mkakati wa Serikali tuliokuwa nao katika kudhibiti uingizaji nchini wa viuatilifu feki. Tulishawaelekeza Taasisi yetu ya TPRA na wako field wanafanya ukaguzi wa mara kwa mara na ukaguzi wa kushtukiza katika maduka yote ili kubaini viuatilifu ambavyo havina sifa na kuvitoa sokoni na kuchukulia hatua kwa wale walioviingiza. Pia, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama pamoja na TRA wanadhibiti mipaka yetu kwa ajili ya kuingiza viuatilifu hivi feki ili kuwalinda wakulima hawa wapate viuatilifu vinavyostahili.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Niipongeze Serikali kwa majibu mazuri katika swali hilo. Pia kwa dhati kabisa nichukue fursa hii kuishukuru Serikali kwa kupeleka Mnada wa Kahawa Wilayani Mbinga kuanzia msimu huu wa mwaka 2019. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa na maswali madogo mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, ni kweli Serikali imepeleka zao la korosho katika Kata za Rwanda na Litumbandyosi. Changamoto ya wakulima hao ni upatikanaji wa miche bora na kwa bei nafuu. Je, Serikali iko tayari kuendelea kutoa miche ya mikorosho bora kwa bei nafuu au bure kwa wananchi wa Kata ya Rwanda na Litumbandyosi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika jibu la msingi, Serikali imekiri kuwa ilitoa mafunzo ya uzalishaji wa miche bora ya mikorosho katika vikundi sita vya Jembe Halimtupi Mtu, Chapakazi, Twiga, Juhudi, Kiboko na Korosho ni Mali lakini vikundi hivi bado vinaidai Bodi ya Korosho. Je, ni lini madeni ya vikundi hivyo yatalipwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tupo tayari kupeleka miche ya mikorosho kwa bei nafuu kwa wakulima wa Wilaya ya Mbinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kama tunavyofahamu deni likivuka mwaka madeni yote haya ya Serikali yanahamia Hazina. Sasa hivi Serikali tuko kwenye hatua za mwisho za kumalizia uhakiki na vikundi vyote ambavyo uhakiki umemalizika vimeshaanza kulipwa na hivi alivyovitaja vitaanza kulipwa baada ya uhakiki kukamilika.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa Serikali imeamua zao la mchikichi lilimwe Kigoma na liweze kuwa zao la biashara na Waziri Mkuu kwa kuweka msisitizo ameenda Kigoma mara tatu kufuatilia zao hili la mchikichi; na kwa kuwa wananchi wameamua kuitikia mwito huo wa kulima zao hilo…

MWENYEKITI: Swali.

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali iko tayari sasa kuhakikisha wananchi wanapata mbegu na kuanza kulima zao hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Genzabuke, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tuko tayari kwa ajili ya uzalishaji wa miche ya michikichi na kuigawa kwa wakulima. Sasa hivi tumeshatenga zaidi ya shilingi bilioni 5 kwa ajili ya kuanza uzalishaji mwaka huu na mwaka huu mwezi Septemba, miche zaidi ya milioni moja itakwenda sokoni. Tumeshaingia mkataba na sekta binafsi kuzalisha miche milioni tano kwa msimu huu unaokuja na ndani ya miaka mitatu tunategemea kuzalisha miche zaidi ya milioni 20 na kuigawa Tanzania nzima.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na nazi kuwa na mandhari nzuri inayovutia inapopandwa, lakini zao lake limekuwa likiporomoka bei mwaka hadi mwaka. Kwa mfano, mwaka jana bei ya jumla ya nazi ilikuwa inauzwa shilingi 400 au zaidi lakini nazi hiyo hiyo mwaka huu inauzwa kwa shilingi 50. Swali la kwanza, je, Serikali ina mkakati gani wa kuweza kumsaidia mkulima kwa kuweza kudhibiti bei na kuweza kupata faida ukizingatia zao la nazi linavunwa mara nne kwa mwaka?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa nazi ina faida nyingi ikiwemo mafuta na nyingine Mheshimiwa Naibu Waziri amezielezea. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweza kuwasaidia wakulima wa zao la nazi kuweza kuanzishiwa viwanda vidogovidogo ikiwemo ya mafuta, tui la nazi au vifuu kutengeneza mkaa mdogo mdogo ili kudhibiti mazingira ya nchi ili na wao wakulima wa zao hilo waweze kupata faida? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, mkakati wa kwanza Serikali kwa ajili ya kuongeza bei pamoja na kutafuta soko kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi. Soko bado lipo kubwa ndani ya nchi na ndio maana tunalazimika wakati mwingine kuagiza tui la nazi kutoka nje ya nchi kuonyesha kwamba bado kuna mahitaji makubwa ya nazi. Lakini tatizo kubwa linalokuja si bei, tatizo kubwa ni tija ndogo wanaipata wakulima kutokana na kipato kidogo wanachokipata kwenye kuchukua nazi.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano mzee Bakhresa yuko tayari kuwekeza na mashine zimeshaingia zina miaka minane lakini anashindwa kupata mali ghafi ya kutosha kuweza kuzalisha tui la nazi hapa nchini kwa muda wote wa mwaka. Kwa sababu kama ulivyosema ni kiasi kidogo kutokana na matatizo unayokumbuka.

Mheshimiwa Spiaka, swali lake la pili kuhusu mkakati wa kuweza kuongeza thamani ni kweli tuna mkakati wa kwanza kama nilivyosema kwenye kuongeza tija na uzalishaji ili kuweza kuwavutia wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani wan je kuja kuweka viwanda vidogo, vya kati na vikubwa baada ya uhakaika wa upatikanaji wa malighafi.

Mheshimiwa Spika, mkakati wa kwanza ni kuendelea kuongeza shughuli za utafiti ili kuja na mbegu ya minazi ambayo itaweza kukinzana na mabadiliko ya tabia nchi na huu ugonjwa uliokuwepo ili wananchi hawa wakazalishe nazi nyingi zaidi.

Mheshimiwa Spika, mkakati wa pili ni kutoa elimu kwa wakulima kwa ajili ya kuchanganya mazao mbalimbali kwenye mashamba ya minazi kama miembe, michungwa na mazao mengine ili kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza kipato kwa wakulima hao.

Mheshimiwa Spika, pia tunaendelea kuwaelimisha wananchi waache kutegemea ile minazi ambayo iliyokuwa walirithi kutoka kwa mababu zao sasa hivi tunawahimiza kupanda mbegu mpya ili wawe na minazi mipya ambayo italeta tija na uzalishaji mkubwa itaenda kuongeza kipato chao.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa moja ya majukumu ya Bodi ya Korosho ni kufanya biashara na kusimamia ubora wa korosho. Katika msimu wa 2018/2019 jukumu la kufanya biashara ya korosho lilifanyika na Bodi ya Mazao Mchanganyiko. Je, Serikali imejipangaje katika kuhakikisha msimu wa 2019/2020 jukumu hili linafanywa na Bodi ya Korosho?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika msimu wa 2017/2018 Bodi ya Korosho iliingia Mkataba na vikundi mbalimbali kuzalisha miche ya korosho na kupitia Bodi ya Korosho walifanya mikataba na vile vikundi. Mpaka hivi ninaposimama hapa, baadhi ya vikundi havijalipwa fedha zao. Je, ni lini sasa Serikali itawalipa wanavikundi wale ambao walizalisha miche ya korosho na miche ilisambazwa katika mikoa mbalimbali ili wapate fedha zao kama sehemu ya wajasiriamali? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, swali lake la kwanza anataka kujua kwamba jukumu mojawapo la Bodi ya Korosho ni kutaka kufanya biashara ya korosho. Nataka nichukue nafasi hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya kuwatetea wakulima wa korosho hususan watu wa Tunduru na Mkoa mzima wa Ruvuma na Watanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jibu lake hili, kwanza nimwambie kwamba majukumu yake kama kwenye jibu langu la msingi nilivyosema hayajaondolewa kwenye Bodi ya Korosho kwa sababu bodi hizi zina majukumu mawili tofauti. Jukumu la kufanya biashara ni jukumu la Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ambalo sasa anaponunua korosho ni jukumu lao la kimsingi la kisheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu la Bodi ya Korosho ni kusimamia, ni waratibu, ni uratibu wa kusimamia biashara ya korosho na hili jukumu wanaendelea nalo kwamba wale waliobaki ambao menejimenti inaendelea kuratibu na mpaka sasa hivi inaratibu katika ubora wa biashara ya korosho pamoja na biashara nzima ya korosho na maandalizi ya msimu ujao wa korosho.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili, anataka kufahamu kwamba ni kweli kwamba mwaka 2017, sisi kama Serikali tuko katika programu ya kuendeleza zao la korosho ya miaka mitatu ya kuzalisha miche milioni 10 na kuigawa kwa mikoa mbalimbali inayolima korosho. Ni kweli Serikali tuliingia mkataba kupitia halmashauri mbalimbali na vikundi mbalimbali kwa ajili ya uzalishaji huo wa miche na mpaka sasa kuna baadhi ya mikoa sita tumeshalipa. Baadhi ya mikoa mingine ipo kwa sababu kwamba ulipaji huu utalipwa baada ya kufanya uhakiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ile mikoa yote ambayo imelipwa, ile mikoa imemaliza uhakika na hii mikoa ambayo bado haijalipwa itamaliza uhakiki haraka iwezekanavyo ili kuweza kuwalipa kuendeleza zao letu la korosho.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Niishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini pamoja na majibu haya mazuri sana ya Serikali nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Itigi ni eneo ambalo lina mbuga na ardhi ni nzuri na kama ilivyoonesha kwenye historia kwamba Serikali imekiri kweli kwamba, maji huwa yanajaa.

Sasa je, Serikali iko tayari sasa pamoja na kutuma Tume ya Umwagiliaji wataalam hawa waangalie namna iliyo bora ya kuyavuna maji haya ili yaje kuwa msaada wakati wa kiangazi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Wananchi wa Itigi na maeneo jirani wanalima sana zao la dengu na kwa kuwa Bodi ya Mazao Mchanganyiko imekuwa haizingatii sana mazao haya ambayo yanapatikana maeneo ambayo ni machache kama Shinyanga na kwetu Itigi na maeneo ya Tabora suala la dengu.

Je, sasa Serikali iko tayari kufanya juhudi za makusudi kusaidia wananchi hawa wanaolima dengu kupata masoko ya uhakika badala ya kupunjwa na walanguzi ambao huwa wanakuja kila mwaka na bei inakwenda chini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anataka kujua kwamba, Serikali kama iko tayari kutuma wataalam wake kwa ajili ya kwenda kufanya tathmini ya kina kule.

Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ipo tayari na ndiyo maana katika jibu langu la msingi nimesema kwamba kupitia swali lako hili, natoa maelekezo kwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Kanda ya Dodoma kwenda haraka iwezekanavyo katika hii mbuga ya Itigi ili kwenda kufanya tathmini ya kina ili tuone namna gani bora ya kuweza kuvuna maji haya ya mvua yanayosababisha hasara kubwa kwenye hili bonde kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anataka kujua Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko. Ni kweli Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kwa mujibu wa sheria ambayo tumeikabidhi kusimamia mazao zaidi ya 35 ikiwemo zao la alizeti na kwamba Serikali tupo tayari kama ulivyoona sasa hivi tupo katika majadiliano ya kina na wenzetu wa India na Vietnam ambao ni wanunuzi wakubwa kwa ajili ya kuingia mkataba maalum wa kuuza mazao haya ya mikundekunde kwa sababu wao ndiyo walaji wakubwa ili tusije kuhangaika na soko huko baadae.

Mheshimiwa Spika, tunafahamu kwa sababu wenzetu wameweka ban kwenye suala hili la kuingiza kiasi cha dengu na mazao haya ya mikundekunde, sasa tunataka tuingie makubaliano hayo ili tutengeneze soko la uhakika na la bei nzuri kwa wakulima wetu.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Bwawa la Mesaga liko Kata ya Kenyamonta na ni kata ambayo inaongoza kwa kuwa na watu wengi katika Wilaya ya Serengeti. Bwawa hili lilianza kutengewa fedha ama kutolewa fedha 2014/2015. Tumeona zimeenda shilingi milioni 200 na zikaenda tena shilingi milioni 198, ni fedha nyingi. Hata hivyo, ukiangalia majibu ya Serikali wanasema sijui kuna fidia na ni kama walipeleka waka-dump zile hela wamezitelekeza mpaka leo. Mimi nilitaka kujua, Serikali mlipeleka fedha kwenye eneo lenye mgogoro ambalo halina andiko mradi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, nashukuru kwamba Wizara imetenga fedha shilingi milioni 217 kwa ajili ya Bwawa la umwagiliaji la Nyamitita, niombe fedha hizi zitoke. Niseme kwamba pamoja na fedha hizi kutengwa, kumekuwa na tendency ya fedha kutokutoka. Naomba fedha hizi zitoke pamoja na za Bwawa la Mesaga, wananchi wanataka kujua ni lini fedha za Bwawa la Mesaga zitatoka?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chacha Ryoba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza anataka kujua kama eneo hilo lina mgogoro kwa nini Serikali ilipeleka fedha? Eneo lile wakati lilifanyika andiko na hitaji la kujengwa mradi ule hakukuwa na mgogoro na hii ni baada ya kupata taarifa ya kimaandishi kutoka kwa wakulima na viongozi wa Wilaya kwamba wakulima wamekubali eneo lile liendelezwe kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, shida kubwa iliyoko pale na Mheshimiwa Mbunge anajua kwa sababu nimeshafika pale ni kwamba wale wakulima ambapo lile bwawa linajengwa, wale wa sehemu ya juu baada ya hela kupelekwa wanataka wafidiwe na wakulima wenzao waliokuwa upande wa chini. Mgogoro ulioko pale ni wale wakulima wa chini hawataki kuwamegea ardhi wale wakulima wenzao waliopisha bwawa lile kujengwa. Baada ya hali hiyo kutokea na hela tulishapeleka ndiyo maana kama Serikali tumewaelekeza kwanza wakulima wenyewe wakae na uongozi wa wilaya watatue mgogoro huo. Baada ya utatuzi huo kukamilika na tukipata taarifa kwamba hakuna mgogoro basi hatua zingine za kupeleka fedha zitaweza kukamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili anataka kujua lini sasa Serikali tutapeleka fedha kwenye Bwawa hilo la Mesaga. Kama nilivyojibu kwenye maelezo yangu ya awali, kutokana na mwongozo tuliokuwa nao sasa hivi wa kuendeleza miradi yote ya umwagiliaji, lazima tupate commitment letter kutoka kwa wanufaika wenyewe kwamba eneo linalojengwa mradi halina matatizo na wamekubaliana ili tusijepeleka fedha halafu kumbe kuna mgogoro. Kama tunavyofahamu tulipitisha wenyewe sheria hapa, ardhi yoyote haiwezi kutwaliwa bila kwanza kulipwa fidia. Kwa hiyo, wale wanaopisha eneo la ujenzi ule wa bwawa lazima kwanza wafidiwe na wenzao kule eneo la chini na baada ya mgogoro huo tutapeleka fedha.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kutokana na utaalam ambao Serikali iliufanya eneo lile halifai kulima miwa lakini haina maana kwamba halifai kwa kilimo cha mazao mengine.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Wilaya ya Moshi Vijiji ni kati ya maeneo yenye uhaba mkubwa sana wa ardhi, je, ni kwa nini Serikali isitoe eneo hili kwa wananchi ili walitumie kwa ajili ya kilimo cha mazao mengine badala ya kuendelea kukaa mikononi mwa TPC kwa sababu TPC wanaonyesha kwamba hawakuwa na programu wala utayari wa kulitumia hili eneo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, wakati eneo hili likitolewa na nakumbuka ilikuwa wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu kulikuwa na pragramu ya kulingawa eneo hili kwa wananchi ili litumike kwa ajili ya makazi. Ni kwa nini Serikali isirejee uamuzi au mipango yake ile ya awali ya kuligawa hili eneo kwa wananchi ili walitumie kwa makazi badala ya TPC kulihodhi tu bila kuwa na jambo lolote ambalo wanalifanya?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Selasini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anasema kwamba lile eneo kwa mujibu wa utafiti na tathmini ya udongo limeonekana halifai kwa kilimo cha miwa lakini linafaa kwa mazoa mengine. Sasa anataka kujua kwa nini Serikali tusiwape wananchi eneo lile ili waweze kulima mazao mengine.

Mheshimiwa Spika, kwanza eneo lile kama nilivyojibu katika majibu yangu ya msingi ni eneo ambalo Serikali tulishalibinafsisha kwa kampuni binafsi, ni eneo la taasisi au kampuni nyingine. Kwa hiyo, kwa mujibu wa sheria na kanuni mbalimbali huwezi kuchukua mali ya mtu mwingine ukaigawa kwa watu wengine. Kwa hiyo, kwa sasa hivi TPC baada ya kuona kwamba hawawezi kulitumia eneo hilo kwa kilimo cha miwa na ni mali yake ameamua kuliendeleza kwa ajili ya hifadhi ya misitu na mbuga ya wanyama na watavutia watalii na kuigiza mapato Serikalini ya kigeni na mapato mengine.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anasema Serikali zamani ilikuwa na malengo kulirudisha lile eneo kwa wananchi ili liwe eneo la makazi kwa ajili ya wananchi wa Moshi. Kama nilivyojibu kwenye swali la msingi lile eneo ni mali ya mtu na tulimpa kwa mujibu wa sheria haiwezekani kumpokonya na kumpa mtu mwingine.