Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Omary Tebweta Mgumba (12 total)

MHE. OMARY T. MGUMBA aliuliza:-
Wilaya ya Morogoro ina Halmashauri mbili; Makao Makuu ya Wilaya yapo mjini na huduma zote kuu za Kiwilaya kama vile hospitali, polisi, mahakama na kadhalika zinapatikana Morogoro Mjini, hivyo kuwalazimu wananchi wa Morogoro Vijijini kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 150 kufuata huduma hizo:-
(a) Je, ni lini Serikali itaifanya Halmashauri ya Morogoro Vijijini kuwa Wilaya kamili na kuhamishia Makao Makuu ya Wilaya katika Kijiji cha Mvuha na kuwaondolea adha wananchi?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhamasisha taasisi za fedha kama vile benki kufungua matawi na huduma ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini ili kuweza kuvutia kampuni mbalimbali ya kibiashara na wawekezaji na kuinua maisha ya wananchi hao?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omary Tebweta Mgumba, Mbunge wa Morogoro Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Morogoro ina Halmashauri mbili. Makao Makuu ya Wilaya yapo Mjini na huduma zote za Kiwilaya kama vile hospitali, polisi, mahakama na kadhalika zinapatikana Morogoro Mjini na kuwalazimu wananchi wa Morogoro Vijijini kutembea umbali wa zaidi ya Kilometa 150 kufuata huduma hizo.
(a) Wilaya ya Morogoro inaundwa na Halmashauri mbili ambazo ni Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro. Uanzishwaji wa Wilaya unazingatia Sheria ya Uanzishwaji wa Mikoa na Wilaya Sura Na. 397 ya mwaka 2002 ambayo pia imeainisha vigezo na taratibu zinazopaswa kuzingatia.
Mheshimiwa Spika, taratibu zinazopaswa kuzingatiwa ni pamoja na maombi ya kujadiliwa kwenye Serikali za Vijiji ili kupata ridhaa ya wananchi wenyewe, maombi kujadiliwa kwenye Baraza la Madiwani, vikao vya Kamati ya Ushauri vya Wilaya yaani DCC na Kamati ya Ushauri ya Mkoa yaani RCC. Maamuzi ya vikao hivyo huwasilishwa Ofisi ya Rais - TAMISEMI kwa ajili ya uratibu na uhakiki.
Aidha, vigezo vinavyozingatiwa katika kuanzisha Wilaya mpya ni pamoja na ukubwa wa eneo usiopungua kilometa za mraba 5,000. Idadi ya watu wasiopungua kati ya 250,000 hadi 300,000, idadi ya Tarafa zisizopungua tano, idadi ya Kata zisizopungua 15 na idadi ya vijiji visivyopungua 50.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa Ofisi ya Rais (TAMISEMI) haijapokea maombi haya ya kuifanya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kuwa Wilaya ya kiutawala. Halmashauri inashauriwa kuwasilisha ombi hili na kujadiliwa katika vikao vilivyopo kwa mujibu wa sheria ili kupata ridhaa.
(b) Mheshimiwa Spika, zipo taasisi za kibenki ambazo zimeonyesha nia ya kufungua matawi katika kijiji cha Mvuha kunapotarajiwa kujengwa Makao Makuu ya Wilaya zikewemo NMB na CRDB kwa lengo la kutoa huduma. Majadiliano yanaendela ikiwa ni pamoja na kuharakisha na kugawa viwanja katika eneo hilo.
MHE. SUSAN L. A. KIWANGA (K.n.y. MHE. OMARY T. MGUMBA) aliuliza:-
Vijana ndio nguvu kazi kubwa katika Taifa letu na Serikali haina uwezo wa kutoa ajira kwa vijana wote kwa sasa:-
(a) Je, Serikali itawawezesha kifedha vijana wa vijiji vyote 64 vya Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki katika makundi ili waweze kujiajiri wenyewe na kupunguza tatizo la ajira na umasikini wa vijana na akina mama?
(b) Je, ni lini Serikali itaanzisha kituo maalum cha kuwawezesha vijana kupata sehemu ya kujifunzia kwa vitendo shughuli mbalimbali za ujasiriamali na kupata taarifa mbalimbali za maendeleo?
NAIBU WAZIRI (TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mgumba Tebweta Omary, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, lenye Sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, vijana katika Halmashauri ya Morogoro Kusini Mashariki, wamekuwa wakiwezeshwa kiuchumi kupitia fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambapo kila Halmashauri hupaswa kutenga 5% ya mapato yake yandani kila mwaka wa fedha kwa ajili ya vijana. Katika bajeti ya mwaka 2014/2015 Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ilifanikiwa kutenga shilingi 10,300,000/= kwa vikundi vya vijana 19 kwa ajili ya kutekeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi. Aidha, katika bajeti ya mwaka 2015/2016 vikundi vya vijana vimetengewa Shilingi milioni 87,500,000 ili kuviwezesha kiuchumi na kujiajiri.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro imejenga Vituo viwili vya Mafunzo (Agricultural Resource Centres) katika Kata za Ngerengere na Mvuha kwa madhumuni ya kutoa elimu na mafunzo ya ujasiriamali ili kuwajengea vijana dhana ya uthubutu katika kufanya shughuli za kiuchumi.
Halmashauri imetoa mafunzo ya ufyatuaji wa matofali ya interlock kwa vikundi vya vijana katika Kata nne za Kinohe, Kisemu, Ngerengere na Mvuha, ambapo jumla ya vijana 40 wamewezeshwa kupata elimu hiyo ya ujasiriamali. Mpango huu ni endelevu na Halmashauri inakusudia kutenga fedha katika bajeti ya mwaka 2016/2017 kwa ajili ya ununuzi wa mashine ya kufyatulia tofali ili ziwezeshe kuwanufaisha vijana wengi zaidi kiuchumi na kuboresha maisha na makazi ya wananchi wa Wilaya hiyo.
MHE. OMARY T. MGUMBA aliuliza:-
Sera ya Serikali ni kuzitaka Halmashauri zote nchini kutenga fedha kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Akina Mama kwa mujibu wa sheria ili kuwezesha upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu; lakini Halmashauri nyingi ikiwemo Morogoro Vijijini haitoi mikopo hiyo kwa makundi hayo kama ilivyokusudiwa:-
Je, Serikali ina mpango gani mahsusi wa kuzibana na kuziamuru Halmashauri zote ikiwemo ya Morogoro Vijijini kutenga asilimia tano ya fedha za mapato ya ndani kwa vijana na asilimia tano kwa ajili ya akina mama ili waweze kupata mikopo yenye riba nafuu na kutimiza lengo lililokusudiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omary Tebweta Mgumba, Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro imewezesha vikundi 39 vya wanawake na vijana vyenye wanachama 295 ambavyo vimepata mikopo ya shilingi milioni 23.8 kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Wanawake. Katika mwaka wa fedha 2015/2016, zimetengwa shilingi milioni 175, kwa ajili ya wanawake na vijana kutokana na mapato ya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mkakati wa Serikali hivi sasa ni kuimarisha makusanyo ya mapato ili kujenga uwezo wa kutenga fedha zaidi.
Aidha, katika bajeti ya mwaka 2016/2017, sharti la kupitisha makisio ya bajeti ya kila Halmashauri lilikuwa ni kuonesha asilimia kumi zilizotengwa kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Wanawake. Kutokana na mapato ya ndani Halmashauri zote zimeagizwa kuhakikisha fedha hizo zilizopelekwa kwenye vikundi husika ikijumuisha walemavu na kusimamia marejesho yake ili vikundi vingine viweze kunufaika.
MHE. OMARY T. MGUMBA aliuliza:-
Wananchi wa Ngerengere wamezungukwa na kambi za Jeshi zaidi ya tatu na kwa upande mwingine shamba la mifugo;
Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza sehemu ya Shamba la Mifugo Ngerengere na kuwapa wananchi, hasa ikizingatiwa kuwa watu wameongezeka sana na ardhi ni ndogo kwa huduma za kijamii?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omary Tebwete Mgumba, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, shamba la mifugo Ngerengere lililopo Wilaya ya Morogoro Vijijini lina ukubwa wa hekta 4,562, lenye uwezo wa kutunza ng’ombe 1,650 hadi 2,000. Aidha, shamba limegawanywa katika vitengo viwili vya Kiwege na Makao Makuu ambako kundi la ng’ombe wa aina ya Boran hufugwa. Rasilimali zilizopo na miundombinu ya huduma za maji ni pamoja na mabwawa matatu, josho, barabara, mazizi, mabirika ya kunyweshea mifugo, nyumba za watumishi, malisho ya wanyama ikijumlisha idadi ya ng’ombe 827, mbuzi 196 na nguruwe 25.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa ardhi kwa wananchi wa Ngerengere na kwa kuzingatia hilo mwaka 1991 kiasi cha hekta 528 zilipunguzwa kwenye eneo la shamba lililokuwa na hekta 5,090 na kupewa Kijiji cha Ngerengere ili wananchi waweze kugawiwa kwa matumizi yao na shamba kubakiwa na hekta 4,562, ambalo limepimwa na kuwekewa alama na wataalam wa ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa na programu na mikakati mbalimbali ya kuendeleza sekta ya kilimo hususan mifugo. Kutokana na umuhimu wa shamba la Ngerengere kwa wananchi wa eneo hilo Kanda ya Mashariki na Taifa, Wizara katika mipango yake inaendelea kuliimarisha shamba hili na mashamba mengine kwa ajili ya upatikanaji wa mifugo bora na yenye tija kwa ajili ya kukidhi soko la ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, napenda kuwashauri na kuwahimiza wananchi na wafugaji kutumia fursa za uwepo wa shamba la Ngerengere katika kuboresha mifugo na malisho, kufuga kulingana na uwezo wa ardhi, kufuga mifugo yenye tija, pia kutumia mbegu bora za ng’ombe, mbuzi na nguruwe zinazopatikana katika shamba la mifugo la Ngerengere.
MHE. OMARY T. MGUMBA Aliuliza:
Mto Ruvu ndiyo chanzo kikuu cha maji katika Mkoa wa Dar es Salaam.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kutenga fedha za kutunza mazingira katika vyanzo vya maji ambavyo viko katika hatari ya kukauka kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na shughuli za kibinadamu?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwashirikisha wataalam wa SUA katika utunzaji wa mazingira katika vyanzo vya maji katika Mkoa wa Morogoro?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI Alijibu:
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omary Tebweta Mgumba, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango wa miaka mitano wa kutunza na kuhifadhi vyanzo vya maji ambao utekelezaji wake ulianza mwaka wa fedha 2014/2015. Wizara yangu inatenga fedha za utekelezaji wa mpango huu katika bajeti yake kila mwaka. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 kiasi cha shilingi bilioni 2.1 kilitengwa kwa ajili ya mpango huo.
Mheshimiwa Spika, suala la utunzaji wa vyanzo vya maji ni mtambuka, ambalo linahitaji ushirikishwaji wa wadau ikiwa ni pamoja na wataalam kutoka sekta mbalimbali zikiwemo sekta za kilimo, madini, viwanda, mazingira na misitu. Mkoa wa Morogoro uko kwenye Bonde la Wami/Ruvu na wataalam na wadau wengine wanashirikishwa katika utekelezaji wake. Mpango huu pamoja na mambo mengine umeainisha maeneo ya vyanzo vya maji na kuweka mikakati ya jinsi ya kutunza na kuhifadhi maeneo hayo ili vyanzo hivyo visiharibike. Aidha, kupitia Bodi ya Maji ya Bonde la Wami/Ruvu wataalam wamekuwa wakishirikishwa katika kufanya utafiti na ukusanyaji wa takwimu na taarifa mbalimbali muhimu ili zitumike katika kutoa maamuzi sahihi ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji.
MHE. OMARY T. MGUMBA aliuliza:-
Kuna vyanzo vingine mbadala ya maji katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki kama vile Mto Mbezi, Mto Ruvu na chanzo cha maji katika Kijiji cha Bamba Kiloka.
Je, Serikali ina mpango gani wa muda mfupi, kati na muda mrefu wa kutatua changamoto ya maji safi na salama katika vijiji vya Mkuyuni, Madam, Luholole, Kibuko, Mwalazi, Kibuko na Mfumbwe katika kupanua na kuongeza uwezo wa tanki la Mto Mbezi ili liweze kukidhi mahitaji ya sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omary Tebweta Mgumba, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji vya Fulwe unaogharimu shilingi bilioni 2.2; Gwata unaogharimu shilingi milioni 440.6; Chanyumbu unaogharimu shilingi milioni 785.7; Mkulazi unaogharimu shilingi milioni 216.7; Kibwaya unaogharimu shilingi milioni 627.2 na Kiziwa unaogharimu shilingi milioni 785.8. Aidha, halmashauri imepanga kutumia shilingi milioni 368.5 kwa ajili kufanya ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya mradi wa maji katika kijiji cha Mkuyuni na Kivuma ambao unatumia chanzo cha maji cha Mto Mbezi.
Mheshimiwa Spika, katika mpango wa muda wa kati, Halmashauri imetenga shilingi milioni 150 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa miradi ya maji ya mtiririko (gravity water schemes) ambao utahudumia vijiji vya Mwalazi, Luholole, Kibuko na Madam, Lubungo na Maseyu.
Mheshimiwa Spika, mpango wa maji wa muda mrefu utahusisha ujenzi wa miradi ya maji katika vijiji 19 vikiwemo vijiji kumi vya Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki. Miradi hiyo itagharamu shilingi bilioni 8.62 kuanzia mwaka 2017 mpaka 2021.
MHE. OMARY T. MGUMBA aliuliza:-
Vijiji 17 pekee kati ya vijiji 64 ndivyo vilivyopata umeme katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki na ni vijiji saba tu vya Ludewa, Mtego wa Simba, Kidugaro, Lung’ala, Mangala na Kinonko vilivyo katika orodha ya kupatiwa umeme katika REA III awamu ya kwanza ya mwaka 2017/2018.
Je, ni lini Serikali itapeleka umeme katika vijiji 47 vilivyosalia?
WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omary Tebweta Mgumba, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa vijiji 17 kati ya vijiji 64 ndio vilipatiwa umeme katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki. Vijiji vingine saba vitapatiwa umeme katika mzunguko wa kwanza wa mpango wa tatu wa REA ulioanza hivi karibuni. Kampuni ya State Grid ya Tanzania ambayo ndio mkandarasi wa eneo hilo tayari ameshaanza kazi katika vijiji hivyo saba ambavyo tumeviongeza. Katika eneo hilo kazi inajumuisha ujenzi wa njia ya kilometa 16.5 ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 pamoja na kilometa 16 za njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4. Kazi nyingine ni ufungaji wa transformer nane pamoja na kuunganisha wateja 256. Gharama ya mradi huu ni shilingi bilioni 1.2 na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2019.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vingine vilivyobaki vitapatiwa umeme katika mzunguko wa pili wa REA Awamu ya Tatu unaoendelea ambapo kwa pamoja utakamilika mwezi Julai, 2019 baada ya mzunguko kukamilika. Mradi huu utakamilika, kama nilivyosema mwaka 2020/2021.
MHE. OMARY T. MGUMBA aliuliza:-
Kata sita za Tegetelo, Kibuko, Tomondo, Tununguo, Seregete, Matuli na Mkulazi katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki hazijafikiwa na miundombinu ya umeme mpaka sasa. Je, ni lini Serikali itapeleka umeme katika kata hizo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omary Tebweta Mgumba, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ni kufikisha umeme katika vijiji vyote visivyo na umeme nchini ikiwemo vijiji vya Wilaya ya Morogoro ifikapo mwezi Juni, 2019. Kupitia mzunguko wa kwanza wa awamu ya tatu ya miradi ya kusambaza umeme vijijini katika Wilaya ya Morogoro vijiji 14 vitapatiwa umeme ifikapo mwezi Aprili, 2019. Vijiji hivyo ni pamoja na Tununguo, Kibwege, Lung’ala, Kidugalo, Kinonko, Vihengele, Konde, Vigolegole, Singisa, Rudewa, Bonye, Mtego wa Simba, Muungano na Mangala.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi za kupeleka umeme katika vijiji hivyo, zinajumuisha ujenzi wa kilometa 16.5 za njia za umeme msongo wa kilovolti 33 na kilometa 16 za njia za umeme msongo kilovolti 0.4, kufunga transfomer nane na kuunganisha wateja 258. Gharama ya mradi inakadiriwa kuwa shilingi bilioni 1.3. Kazi hii itatekelezwa na Mkandarasi Kampuni ya State Grid Electrical and Technical Works.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vitakavyobaki katika mzunguko wa kwanza wa REA Awamu ya Tatu vitapatiwa umeme katika mzunguko wa pili wa REA Awamu ya Tatu ambapo mradi unategemewa kuanza mwezi Julai, 2019 na kukamilika mwezi Juni, 2021.
MHE. OMAR T. MGUMBA aliuliza:-
Shamba Na. 217 lenye ukubwa wa hekta 63,000 lililopo katika Kata ya Mkulazi, Morogoro Vijijini limepata Mwekezaji Kampuni ya Mkulazi Holding Company Limited kwa ajili ya kuliendeleza kwa Kilimo cha Mazao mbalimbali na uwekezaji wa kiwanda cha sukari. Aidha, wakulima wadogo (out growers) wametengewa eneo la hekta 3,000 tu na Wawekezaji hekta 60,000 kwa ajili ya shughuli zao:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza ardhi ya akiba kwa wakulima wadogo kutoka hekta 3,000 kwenda hekta 23,000;
(b) Je, Serikali haioni kuwa kwa kutenga hekta 3,000 tu itazalisha vibarua wengi wazawa badala ya kuwashirikisha katika uzalishaji ili kuinua hali zao za maisha pamoja na kuongeza Pato la Taifa.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omary Tebweta Mgumba, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa juhudi anazofanya katika kuhakikisha wakulima wanapata maeneo ya kilimo, napenda kutoa taarifa kuwa, hekta 3,000 za wakulima wadogo wadogo zilizoainishwa na Mheshimiwa Mbunge ziko kwenye eneo la Matokeo Makubwa Sasa. Katika mpango huu inakadiriwa kuwa hekta 250,000 kwa ajili ya wakulima wadogo wa kibiashara na hekta 350,000 kwa ajili ya wakulima wakubwa wa kibiashara zitapatikana na zitalimwa zao la miwa na mpunga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili la Mkulazi ambalo liko kwenye Jimbo la Mheshimiwa Mbunge jumla ya hekta 63,000 zimepimwa na kutolewa Hati Miliki ambayo inamilikiwa na Serikali Kituo cha Uwekezaji (TIC), ambapo hekta 60,000 ni kwa ajili ya wakulima wa mashamba makubwa ya kibiashara ya uwekezaji na hekta 3,000 ni kwa ajili ya wakulima wa mashamba madogomadogo ya kibiashara. Wakulima wadogo watatoka kwenye vijiji vinavyozunguka eneo hilo la uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji wa uwekezaji mkubwa utatumia teknolojia ya kisasa na Kanuni bora za kilimo, kwa kufanya hivyo, maeneo ya wakulima wadogo yatachangia kwa kiasi kikubwa ukubwa wa eneo linalozalisha zao hilo, pia wingi wa ubora wa zao ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje na hivyo kuongeza kipato cha mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushirikishwaji huu hautazalisha vibarua bali utazalisha wakulima na wajasiliamali wengi, ambao watashiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani (value chain) wa zao husika.
MHE. OMARY T. MGUMBA aliuliza:-
REA I na II ilikuwa ni kupeleka miundombinu ya umeme vijijini na baadhi ya Makao Makuu ya vijiji tu na kuacha vitongoji vya vijiji husika.
Je, Serikali ina mikakati gani ya kuwapatia umeme vitongoji vyote na vijiji vilivyorukwa katika REA I na II?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omary Tebweta Mgumba, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza mradi wa kupeleka umeme katika vijiji vyote ifikapo mwezi Juni, 2021. Katika kufikia azma hii, Serikali inatekeleza mradi wa REA awamu ya tatu kupitia maeneo yafuatayo: kwanza, grid extension unaohusu kupeleka umeme katika vijiji vyote ambavyo havikufikiwa na miundombinu ya umeme. Mradi huu wa REA III mzunguko wa kwanza umekwishaanza. Mzunguko wa kwanza unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2019 na mzunguko wa pili unatarajiwa kuanza mwezi Julai, 2019 na kukamilka mwezi Juni, 2021.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aina ya pili ya mradi wa REA ni mradi wa densification. Mradi huu umepangwa kutekelezwa katika vijiji ambavyo tayari vimefikiwa na miundombinu ya umeme lakini baadhi ya taasisi za huduma za kijamii na Vitongoji havikupata umeme wakati wa utekelezaji wa REA I na II.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aina ya tatu ni mradi wa kupeleka umeme katika vijiji nje na miundombinu ya umeme wa gridi kwa kutumia nishati jadidifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji na vitongoji vilivyorukwa wakati wa utekelezaji wa miradi ya REA I na II vitapatiwa umeme kupitia miradi ya densification na utekelezaji wa awamu ya kwanza ya miradi ya densification ulikwishaanza katika mikoa nane ya Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa, Pwani, Tanga, Arusha na Mara. Serikali inafanya maandalizi ya densification awamu ya pili unaotarajiwa kuanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2018/2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki jumla ya vitongoji 55 vimeainishwa kwa ajili ya kupatiwa umeme kupitia densification awamu inayofuata. Mkakati wa Serikali ni kuvipatia umeme vitongoji vyote ifikapo mwezi Juni, 2021.
MHE. OMARY T. MGUMBA aliuliza:-
Barabara ya Ubena, Ngerengere hadi Mvuha ina urefu wa zaidi ya kilometa 70 na inaunganisha Wilaya ya Bagamoyo na Halmashauri ya Morogoro ambako Makao Makuu ya Wilaya mpya ya Mvuha yanatarajiwa kujengwa. Aidha, barabara hii inaunganisha Mkoa wa Pwani na Morogoro. Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro haina uwezo wa kuhudumia barabara hiyo:-
(a) Je, ni lini Serikali itakubali ombi la kupandisha barabara hiyo kuwa ya Mkoa?
(b) Je, ni lini Serikali itatengeneza barabara hiyo ya Ubena – Mvuha kwa kiwango cha changarawe ili ipitike mwaka mzima?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omary Tebweta Mgumba, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Ubena Zomozi kwenda Ngerengere hadi Mvuha yenye urefu wa kilomita 105.4 ilipandishwa hadhi na Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano tangu Januari, mwaka 2017 kutoka barabara ya Wilaya na kuwa barabara ya Mkoa baada ya kukidhi vigezo vya Sheria ya Barabara ya mwaka 2007 na Kanuni zake za mwaka 2009. Kwa sasa barabara hii inahudumiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Morogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu kubwa ya barabara hii inapitika kwa shida hasa wakati wa masika hususani kati ya kipande cha Ngerengere na Mvuha ambacho kina urefu wa kilomita 95.4. Sehemu iliyobaki kati ya Ubena Zomozi na Ngerengere inapitika vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Morogoro, inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali katika maeneo korofi ili iweze kupitika majira yote ya mwaka. Aidha, kutokana na umuhimu wa barabara hii ya Ubena Zomozi – Ngerengere – Mvuha – Kisaki – Stiegler’s Gorge inayoelekea katika mradi wa kufua umeme kwa kutumia maporomoko ya Mto Rufiji katika mwaka wa fedha 2018/2019 wizara yangu imetenga jumla ya shilingi bilioni tano kwa ajili ya ukarabati mkubwa.
MHE. OMARY T. MGUMBA aliuliza:-
Barabara ya Bigwa – Kisaki ni muhimu kiutawala na kiuchumi kwa kuwa inaunganisha Mbuga ya Selous, Mkoa wa Pwani, Lindi na Mtwara:-
• Je, ni lini barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami?
• Nyumba za wakazi zilizopo pembezoni mwa barabara hiyo zimewekwa alama ya X kwa muda mrefu lakini wananchi hawajalipwa fidia. Je, ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi hao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omary Tebweta Mgumba, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, lenye sehemu (a) na (b), kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) inaendelea na kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami barabara ya Bigwa – Kisaki kwa kuanza na kipande cha barabara ya kuanzia Bigwa - Mvuha chenye urefu wa kilometa 78. Mhandisi Mshauri alitoa Ripoti ya Awali (Draft Final Report) tangu tarehe 2 Julai, 2017. Kazi hii imefanywa na Kampuni ya Unitec Civil Consultants Limited ya Dar-es- Salaam ikishirikiana na Kampuni ya Mult-Tech Consultant Limited kutoka Gabone, nchini Botswana. Kwa sasa Mhandisi Mshauri anaendelea kufanya marekebisho mbalimbali yaliyoelekezwa na Wakala wa Barabara (TANROADS) ili kukamilisha kazi hiyo ya usanifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara baada ya usanifu wa barabara hii kukamilika na gharama kujulikana, Serikali itatafuta fedha ili ujenzi uanze kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, Serikali italipa fidia kwa wananchi ambao nyumba zao zitaathirika na ujenzi wa barabara ya Bigwa – Mvuha – Kisaki zilizowekwa alama ya X kwa mujibu wa Sheria ya Barabara ya mwaka 2007 na Kanuni zake za mwaka 2009.