Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Omary Tebweta Mgumba (48 total)

MHE. PROF. NORMAN A. SIGALLA KING aliuliza:-
Mwaka 2016 - 2018 bei ya zao la mahindi ambayo ndiyo nguvu ya uchumi kwa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini imeshuka sana hadi kufikia shilingi 2000 kwa debe kwenye baadhi ya Wilaya kama Ludewa na Makete.
• Je, ni lini Serikali itaongeza fedha NFRA ili mahindi yanayozalishwa yanunuliwe na kuwapa ahueni wananchi?
• Je, ni lini Serikali kupitia NFRA itajenga maghala katika kila Halmashauri ili kurahishisha uhifadhi wa mahindi na mazao mengine?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge na kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama naomba nilitumie Bunge lako tukufu kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa imani kubwa aliyoionesha kwangu kuniamini kama naweza kutoa mchango wangu kumsaidia katika sekta hii ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimshukuru Mheshimiwa Spika kwa miaka mitatu niliyokaa hapa Bungeni jinsi alivyonihamisha kwenye Kamati tatu kuanzia Kamati ya Sheria Ndogo, Kamati ya PAC na Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii imenipa uzoefu wa kutosha kufahamu shughuli za Serikali na Bunge kwa ujumla. Pia niwashukuru wajumbe wa Kamati hizo zote wakiongozwa na wenyeviti na makamu Wenyeviti hasa nikianza na ile ya Kamati ya Sheria Ndogo Mzee wangu Chenge nimekuja PAC Mama Kaboyoka na Kamati ya Ardhi ndugu yangu Nape na Wabunge wote wa Kamati hizo walinipa ushirikiano wa kutosha katika majukumu yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho lakini siyo kwa umuhimu niwashukuru sana wapiga kura wangu wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki kwa uvumilivu na ushirikiano wanaonipa hasa kwa wakati huu niliokuwa mbali nao kwenye kutimiza majukumu yangu ya kitaifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nimshukuru mke wangu mpenzi na familia yangu, Bi. Husna Abbas Mgumba kwa uvumilivu na ushirikiano wa karibu sana wanaonipa na ushauri wake kuwatumikia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo na shukrani hizo, nianze kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge na kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Norman Adamson Sigalla King, Mbunge wa Jimbo la Makete lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa nafaka hususan mahindi ili kuiwezesha NFRA kutekeleza jukumu la kununua na kuhifadhi akiba ya chakula. Pamoja na ruzuku ya Serikali, wakala hutumia vyanzo vyake vingine vya mapato kugharamia ununuzi wa nafaka ambazo hununuliwa kutoka kwenye maeneo yenye ziada katika uzalishaji wa chakula kupitia vikundi au vyama vya wakulima. Aidha, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) hauna uwezo wa kununua mahindi yote yanayozalishwa nchini bali inatekeleza na jukumu la kununua na kuhifadhi akiba ya chakula cha taifa kwa kuzingatia bajeti inayototengwa na Serikali na vyanzo vingine vya mapato kwa lengo la kuhakikisha usalama wa chakula ili kukubaliana na upungufu wa chakula unaoweza kujitokeza nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na mikakati ya kutafuta masoko kwa ajili ya mazao ya wakulima ikiwemo mahindi kwa kuondoa zuio la kuuza mahindi nje ya nchi, kuongeza bajeti ya Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kwa ajili ya ununuzi wa mazao na kuongeza uwezo wa Wakala wa Kuhifadhi Nafaka kutoka tani 251,000 hadi kufikia tani 501,000 ifikapo mwaka 2019/2020. Aidha, mikakati mingine ni kuongeza matumizi ya mahindi kwa kuyaongezea thamani ili kuuza unga na pumba pamoja na kuliingiza zao la mahindi katika mfumo wa stakabadhi ghalani ili kuongeza wigo wa masoko ya mazao ya kilimo nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Wizara imetenga jumla ya shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa maghala 15 katika Halmashauri za mikoa ya Mwaza, Manyara, Singida, Kigoma, Simiyu, Tanga na Tabora. Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) unajenga maghala na vihenge vya kisasa katika Halmashauri za Shinyanga, Babati, Makambako, Sumbawanga, Mpanda, Mbozi, Dodoma na Songea ambayo ni makao makuu ya kanda zetu saba yenye uwezo wa kuhifadhi nafaka tani 250,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, katika mradi wa kudhibiti sumukuvu jumla ya maghala 14 yatajengwa katika Mikoa ya Songwe, Dodoma, Manyara, Tabora, Kigoma, Mtwara, Ruvuma, Mwanza, Geita na Simiyu. Aidha, Wizara itakamilisha ukarabati wa maghala 33 kwa ajili ya hifadhi ya mahindi katika Halmashauri za Wilaya za Mlele, Nsimbo, Songea na Njombe pamoja na kuandaa mpango wa ukarabati na ujenzi wa maghala kwa nchi nzima. (Makofi)
MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-
Serikali ilifuta tozo na kodi kadhaa katika kilimo na biashara ya kahawa, lakini bado bei anayopata mkulima ni ndogo.
Je, ni kwa nini tangu kufutwa kwa tozo na kodi hizo bei kwa mkulima haijapanda?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi hii kujibu swali la Mheshimiwa Mheshimiwa Rweikiza. Kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, bei ya kahawa duniani inapangwa kwa kuzingatia masoko mawili makuu ya rejea duniani ambayo ni Soko la Bidhaa la New York, Marekani (New York Commodity Market) kwa kahawa za arabika na Soko la London, Uingereza (LIFE) kahawa ya aina ya Robusta. Mwenendo wa bei katika masoko hayo una athari za moja kwa moja kwenye soko la kahawa na bei anayopata mkulima. Aidha, bei ya kahawa katika masoko hayo pia huathiriwa na ugavi na mahitaji (demand and supply) ya kiasi cha kahawa kinachozalishwa duniani kwa wakati husika ambapo uzalishaji wa kahawa nchini ni wastani wa tani 50,000 za kahawa safi sawa na asilimia 0.6 ya kahawa yote duniani na hivyo kutokuwa na ushawishi katika bei ya kahawa.
Mheshimiwa Spika, pamoja na Serikali kufuta tozo na kodi katika zao la kahawa, bei ya mkulima imeshuka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mzalishaji mkuu wa kahawa duniani, nchi ya Brazil kushusha thamani ya fedha yake (devaluation of currecy) na hivyo kahawa yao kuuzwa kwa bei ndogo ili kuvutia wanununuzi wengi. Pia kuongezeka kwa uzalishaji ambapo msimu wa 2018/2019 nchi ya Brazil na nchi nyingine duniani zimeongeza uzalishaji na kua na ziada ya tani 420,000 na kutoeleweka vizuri kwa maelekezo ya Serikali kuhusu uuzaji wa kahawa kwenye soko la moja kwa moja (direct exports), kwa kahawa hai (organic coffee) na kahawa haki (tair trade coffee) miongoni mwa wanunuzi na viongozi wa ushirika.
Mheshimiwa Spika, pamoja na bei ya kahawa katika soko la dunia kushuka kutoka USD 87.4/50kg za kahawa mwaka 2016/2017 hadi dola 79.8 kwa gunia la kilo 50 la kahawa safi mwaka 2017/2018 bei ya kahawa ya mkulima wa kahawa imeimarika kwa kahawa ya robusta kutoka shilingi 1,400 kwa kilo mwaka 2016/2017 hadi shilingi 1,600 kwa kilo mwaka 2017/2018; na bei ya arabika kupungua kwa kiasi kidogo kutoka shilingi 4,000 kwa kilo mwaka 2016/2017 hadi shilingi 3,800 kwa kilo mwaka 2017/2018. Aidha, bei ya arabika kwa mkulima ingeweza kupungua zaidi kama Serikali isingeondoa tozo katika tasnia ya kahawa.
Mheshimiwa Spika, katika mwa 2017/2018 Serikali ilifuta jumla ya tozo 17 na tozo mbili mwaka 2018/2019 katika tasnia ya kahawa ambazo zimesaidia kuimarisha bei ya mkulima. Aidha, kupungua kwa kodi na tozo hizo kumesaidia bei ya kahawa kuwa nzuri ambapo kwa mara ya kwanza katika msimu wa 2017/2018 kahawa ilitoka nchi ya Uganda na kuletwa Tanzania kutokana na wakulima wa Uganda kuvutiwa na bei iliyokuwa inapatikana Tanzania. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI (K.n.y. MHE. JOYCE B. SOKOMBI) aliuliza:-
Zao la pamba ambalo lililimwa kwa wingi Mkoani Mara na pia ilisaidia sana kuwainua wananchi kimapato.
Je, Serikali inachukua hatua gani za kimkakati za kulifufua zao hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge na kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joyce Bitta Sokombi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa zao la pamba kwa uchumi wa taifa na wakulima wa pamba nchini. Kutokana na umuhimu huo Serikali imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali inayolenga kuongeza uzalishaji, tija, ubora na masoko ya uhakika kwa kuimarisha usimamizi katika mnyororo wa thamani wa zao hilo ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi. Aidha, huduma za ugani, upatikanaji wa pembejeo na mifumo ya masoko imeendelea kuboreshwa ili kuwanufaisha wakulima wa pamba nchini.
Mheshimiwa Spika, mikakati hiyo ni pamoja na kurahisisha upatikanaji wa pembejeo ambapo katika msimu wa 2018/2019 wakulima watapatiwa pembejeo kupitia Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS), kuimarisha huduma za ugani ambapo wakuli wawezeshi (leader farmers) wapatao 4,532 wawili kutoka kila kijiji kinacholima pamba katika Kanda ya Magharibi wameainishwa na kupewa mafunzo ya kanuni za kilimo bora cha pamba ili wafikishe huduma za ugani kwa wakulima wenzao kikamilifu.
Mheshimiwa Spika, mikakati mingine kuongeza matumizi ya dhana za kilimo ambapo takribani vyama vya ushirika zaidi ya 300 vitapatiwa mikopo ya matrekta kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo. Kueneza teknolojia ya kilimo, hifadhi ardhi katika maeneo yanalima pamba nchini na kuboresha mfumo wa masoko ya pamba kwa kuimarisha Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) ili viweze kunua pamba inayozalishwa na wakulima na hivyo kuimarisha ubora na usafi wa pamba.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeanza kurekebisha mfumo wa uzalishaji wa mbegu bora za pamba kwa kufuata vigezo vyote vya ubora kwa mujibu wa Sheria ya Mbegu Na. 18 ya mwaka 2003. Aidha, juhudi zinazofanyika sasa ni kuzalisha kwa wingi mbegu ya aina ya UKM08 chini ya uratibu wa Kituo cha Utafiti cha Ukiriguru Mwanza kwa kushirikiana na sekta binafsi na Bodi ya Pamba. Vilevile aina mbili za mbegu mpya za UK171 na UK173 zitaanza kupatikana kwa wakulima kuanzia msimu wa 2018/2019.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali italeta Bungeni muswada wa kurekebisha Sheria ya Tumbaku ya mwaka 2004 ambayo imepitwa na wakati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA):
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Jimbo la Lupa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la tumbaku hapa nchini husimamiwa na Sheria ya Tumbaku Na. 24 ya mwaka 2001, Sura ya 202 ya Sheria za Tanzania (Tangazo la Serikali Na. 296 la mwaka 2000) pamoja na Kanuni za Sheria ya Tumbaku za mwaka 2012 (Tangazo la Serikali Na. 392 la mwaka 2012). Kabla ya Sheria ya mwaka 2001 zao la Tumbaku lilikuwa likisimamiwa na Sheria ya Bodi ya Tumbaku ya mwaka 1984 yaani The Tobacco Processing Marketing Board, pamoja na kanuni zake za mwaka 1997 ambazo zilifutwa kwa Sheria ya Tumbaku ya mwaka 2001 na kanuni zake za mwaka 2012.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mabadiliko ya urazinishaji wa bodi za mazao, Sheria ya Sekta ya Tumbaku ilifanyiwa marekebisho na Bunge mwaka 2009 kupitia Sheria Na. 20 ya Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Mazao ya mwaka 2009. Pamoja na mambo mengine, Sheria ya Tumbaku iliweka majukumu ya pamoja, majukumu ya usimamizi, ugharamiaji wa majukumu pamoa na mkutano wa wadau.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, sheria na kanuni hizo zinaweka masharti ya msingi kwa ajili ya kuzingatiwa na mkulima, mnunuzi na msindikaji wa tumbaku ili kuhakikisha kuwa tumbaku inayozalishwa na kusindikwa hapa nchini inakidhi ubora unaokubalika kimataifa na hivyo kuwezesha kupata soko la uhakika pamoja na kumlinda mlaji au mtumiaji wa bidhaa ya tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2018/2019 Wizara inatarajiwa kufanya marekebisho kwenye sheria mbalimbali za mazao ikiwemo Sheria ya Tasnia ya Tumbaku. Kwa sasa Wizara inaendelea kupitia sheria zinazosimamia sekta ya kilimo ili kuimarisha na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mazao mbalimbali hususani mazao ya biashara.
Kuhusu Sheria ya Tumbaku Wizara kwa kushirikianna wadau inaendelea kupitia na kuainisha changamoto zilizopo katika sheria hiyo na baada ya zoezi hilo kukamilika, marekebisho ya sheria hii yatawasilishwa Bungeni kwa mujibu wa Kanuni na taratibu zilizopo. Aidha, sheria hiyo haijapitwa na wakati, bali marekebisho yanayokusudiwa kufanyika ni kwa ajili ya kuboresha sheria hiyo ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa zao la tumbaku.
MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:-
Wananchi wa Kanda ya Kati ni wakulima wazuri wa zao la alizeti:-
Je, Serikali haioni ni muda muafaka sasa wa Bodi ya Mazao Mchanganyiko kuanzisha Mfuko mahsusi wa uendelezaji wa zao la alizeti?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na jitihada mahsusi za kuendeleza zao la alizeti ambazo ni pamoja na kuwa na Mfuko wa kuendeleza zao hilo. Kutokana na umuhimu huo, Serikali kwa kushirikiana na wadau, imeandaa Mkakati wa Kuendeleza zao la Alizeti nchini (Sunflower Development Strategy 2016 – 2020) ambapo unalenga kuongeza uzalishaji na tija; kuboresha ubora wa mbegu za alizeti; kuimarisha tasnia ya alizeti kwa kuboresha uratibu miongoni mwa wadau; kuchochea ukuaji wa tasnia ya alizeti kwa kuweka sera wezeshi; na kuhakikisha uwepo wa masoko ya uhakika kwa mazao ya alizeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ilianzishwa ili kufanya biashara na pia kushirikiana na wadau wengine katika kuendeleza mazao mchanganyiko. Hivyo, Bodi hiyo haiwezi kuanzisha Mfuko wa kuendeleza zao la alizeti peke yake bali kwa kushirikiana na wadau wengine wa zao la alizeti. Aidha, pale itakapokubalika, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko itakuwa ni miongoni mwa wadau muhimu wa kuanzisha Mfuko huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka mitatu (3) mfululizo wadau wa alizeti wamekuwa wakikutana kujadili changamoto mbalimbali ya zao hilo na kuzitafutia ufumbuzi. Katika kurasimisha jitihada hizo na kuwa na Jukwaa la Wadau, Wizara iliitisha kikao cha wadau kwa ajili ya kujadili namna bora ya kuendeleza zao la alizeti hususan katika upatikanaji wa mbegu bora, huduma za ugani na teknolojia bora za usindikaji wa alizeti. Aidha, katika ushirikishwaji huo wa wadau, suala la Mfuko wa Kuendeleza zao la Alizeti litajadiliwa kwa kina na kama inaonekana ni muda muafaka wa kuanzisha Mfuko huo, wadau watakubaliana kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uanzishwaji wa mifuko zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Wizara tayari zipo jitihada za kuimarisha utafiti wa mazao ya mbegu za mafuta ambapo kwa zao la alizeti Taasisi ya Utafiti wa Kilimo TARI imejipanga kuendeleza kusafisha mbegu za awali aina ya “Record” kwa ajili ya kuzalisha madaraja ya msingi na hatimaye daraja la kuthibitishwa. Kuimarisha upatikanaji na usambazaji wa mbegu bora za alizeti kupitia Wakala wa Mbegu wa Taifa (Agricultural Seed Agency-ASA) na kuhamasisha makampuni binafsi ya kuzalisha mbegu bora za alizeti.
Aidha, katika jitihada hizo, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko inashirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Muungano wa Wazalishaji wa Zao la Alizeti Tanzania (Tanzania Sunflower Processors Association – TASUPA) na Mfuko wa Kuendeleza Masoko ya Mazao ya Kilimo (Agricultural Market Development Trust-AMDT) katika kuhakikisha wakulima wa alizeti wanapata mbegu bora na huduma za kilimo bora cha alizeti.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza:-
Wakulima wengi wamehamasika katika kilimo cha alizeti lakini alizeti inayolimwa haitoi mafuta kwa wingi:-
Je, Serikali ina mkakati gani katika kuimarisha utafiti wa mbegu ya alizeti inayotoa mafuta mengi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto za uzalishaji wa mazao ya mbegu za mafuta ikiwemo alizeti Serikali inatekeleza mkakati wa miaka mitano, yaani 2016/2020 wa kuendeleza zao la alizeti ambao unalenga kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima, kuhamasisha matumizi ya kanuni bora za kilimo, kujenga uwezo wa vyama vya wakulima kuzalisha mbegu bora za daraja la kuazimiwa yaani QDS na kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika viwanda vya usindikaji.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Vituo vya Utafiti vya Ilonga (Morogoro), Makutupora (Dodoma), Tumbi (Tabora), Uyole (Mbeya), Ukiriguru (Mwanza) na Naliendele (Mtwara) inaendelea kufanya utafiti wa mbegu bora za alizeti ambapo mbegu tano aina ya record, hysun 33, agura 4, NSFH 145 na NSFH 36 zimesajiliwa.
Mheshimiwa Spika, kati ya mbegu hizo, mbegu aina ya record inayozalishwa nchini tangu mwaka 1985 imefanyiwa maboresho na kuiwezesha kuwa na tija ya uzalishaji wa tani 1.5 mpaka tani mbili kwa hekta; ukinzani dhidi ya magonjwa, kuhimili mabadiliko ya tabianchi na kutoa mafuta mengi kwa asilimia 48 mpaka 50. Aidha, mbegu ya record ni open pollinated variety (OPV) inayoweza kutumiwa na wakulima kwa misimu miwili hadi mitatu ukilinganisha na mbegu aina ya chotara ambazo zinaingizwa kutoka nje ya nchi na kutumika kwa msimu mmoja tu.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha mbegu nyingi zaidi zinazalishwa na kuwafikia wakulima, Kituo cha Utafiti Naliendele kinakamilisha utafiti wa aina tatu mpya za mbegu ya alizeti katika msimu wa 2018/2019. Aidha, Serikali imeingia ubia na sekta binafsi kufanya utafiti na kuongeza uzalishaji wa mbegu nchini badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi ambapo Kampuni ya Silver Land na Quality Food Product zipo katika hatua ya majaribio ya aina mpya ya mbegu za chotara za alizeti ambazo zitazalishwa nchini.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:-

Zao la Korosho pamoja na kuingiza mapato makubwa Serikalini bado lina changamoto nyingi sana katika uuzaji wake kwa upande wa Wakulima:-

Je, Serikali ipo tayari kuondoa changamoto hizo ili kuleta tija kwa Wakulima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maftah Abdallah Nachuma Mbunge wa Jimbo la Mtwara mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli zao la Korosho ni mojawapo ya mazao ya Kilimo yanayoliingizia Taifa mapato ambapo katika kipindi kilichoishia Oktoba, 2018, zao la Korosho liliingizia Taifa fedha za kigeni za Kimarekani zaidi ya dola milioni mia tano sabini na tano pointi sita sawa na zaidi fedha za Kitanzania trilioni moja nukta tatu ikilinganishwa na mazao mengine ya biashara. Aidha, pamoja na mchango wa zao hilo katika uchumi wa Taifa, zao la Korosho limekuwa likikabiliwa na changamoto mbalimbali ambapo Serikali imekuwa ikizitafutia ufumbuzi.

Mheshimiwa Spika, changamoto hizo ni pamoja na kuyumba kwa bei ya zao la Korosho katika soko la dunia kutokana na Korosho kuuzwa ikiwa ghafi bila kuongezewa thamani; Tija ndogo katika uzalishaji wa wakulima; baadhi ya wakulima kutotumia miche bora na matumizi hafifu ya pembejeo ikiwemo viuadudu kama sulphur; wakulima kutozingatia Kanuni bora za Kilimo katika uzalishaji, uvunaji na uhifadhi hafifu wa Korosho; uwezo mdogo wa maghala ya kuhifadhia Korosho na baadhi ya wakulima kuchanganya Korosho na mawe na mchanga kwa ajili ya kuongeza uzito wakati wa mavuno ambao unashushia ubora.

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imeboresha mfumo wa uuzaji wa Korosho kwa kuimarisha usimamizi na ukaguzi kuanzia ngazi ya vyama vya msingi, maghala makuu, maghala ya hifadhi na kutoa elimu kwa wakulima; kurejesha Kiwanda cha BUCCO cha Mkoani Lindi cha kubangua Korosho ujenzi wa maghala matatu ya kuhifadhia Korosho katika Mikoa ya Ruvuma, Pwani na Tanga ili kuongeza Kiwango cha kuhifadhi na ubora wa Korosho pamoja na kuzalisha miche bora zaidi ya milioni kumi na kuisambaza kwa wakulima.

Mheshimiwa Spika, mikakati mingine ni pamoja na kuimarisha mnyororo wa thamani katika zao la Korosho ili kuongeza uzalishaji, kuimarisha usambazaji wa pembejeo za Kilimo kwa wakati, kutoa huduma za ugani pamoja na kuweka mazingira wezeshi na kuwajengea uwezo wabanguaji wa ndani wa Korosho kwa lengo la kuongeza thamani ya Korosho inayozalishwa nchini.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji wa Miyogwezi uliopo katika Kijiji cha Igongo, Ukerewe ni tarajio kubwa la suluhu ya upungufu wa chakula, zaidi ya miaka mitano sasa toka kufanyika uwekezaji wa zaidi ya shilingi milioni 700 bado mradi huo umetelekezwa:-

(a) Je, kwa nini Serikali imetelekeza mradi huo?

(b) Je, nini kauli ya Serikali kuhusu uendelezwaji wa mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Serikali haijautelekeza Mradi wa Kilimo cha Umwagilia wa Miyogwezi, bali mradi huo umesimama kutokana na muda wa utekelezaji wa mradi wa DASIP uliokuwa unafadhili mradi huo kumalizika kabla ya Mradi wa Miyogwezi haujakamilika. Mradi wa Miyogwezi ulitekelezwa kupitia mradi wa District Agriculture Sector Investment Project yaani (DASIP) ambao jumla ya shilingi 695,784,852.50 zilitumika. Utekelezaji wa mradi huo ulihusisha ujenzi wa mabanio mawili na mifereji mikuu yenye urefu wa kilometa 3.15 ambapo kilometa 1.1 zilisakafiwa. Ujenzi wa mabanio mawili katika mto wa kudumu yaani perennial river wa Miyogwezi na katika mto wa msimu wa Mriti. Hadi kukamilika kwa muda wa Mradi wa DASIP mwezi Disemba, 2013 ujenzi wa mradi huo ulikuwa umefikia asilimia 76. Aidha, uendelezaji wa mradi huo umechelewa kutokana na Serikali kujipa muda wa kufanya tathmini ya kina ya utekelezaji wa miradi yote ya DASIP ili kupima ufanisi wake ulivyotekelezwa.

(b) Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha mradi wa Miyogwezi na miradi mingine ya umwagiliaji nchini inakamilika, Serikali imekamilisha mapitio ya mpango kabambe wa umwagiliaji wa mwaka 2002 kwa kuzingatia mipango shirikishi ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali maji yaani (Integrated Water Resource Management) ili kubaini maeneo yanayofaa kwa uendelezaji wa miundombinu ya umwagiliaji yakiwemo mabwawa, visima vifupi na virefu vya chini vya ardhini, pamoja na hali ya skimu zote za umwagiliaji nchini.

Mheshimiwa Spika, mapitio ya mpango huo pia yamebaini miradi yote ya umwagiliaji ambayo haifanyi kazi na ambayo ujenzi wake haujakamilika katika kipindi kilichopita ikiwemo Mradi wa Miyogwezi. Aidha, Mradi wa Umwagiliaji wa Miyogwezi ni miongoni mwa miradi ya umwagiliaji itakayotekelezwa katika Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) kuanzia mwaka 2018 hadi mwaka 2023.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati Bwawa la Ikowa linalohudumia Skimu ya Umwagiliaji ya Chalinze iliyopo Kata ya Manchali na Bwawa la Buigiri iliyopo Kata ya Buigiri?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joel Mwaka Makanyaga, Mbunge wa Chilonwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Bwawa la Ikowa lililopo Wilayani Chamwino, Kata ya Manchali lilijengwa mwaka 1959 kwa ajili ya kupata maji ya mifugo na kumwagilia, jumla ya hekta 300 katika Skimu ya Chalinze. Kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na shughuli za kibinadamu katika maeneo hayo, bwawa lilijaa mchanga, magogo ya miti pamoja na tope kutoka katika korongo la Mjenjeule na hivyo kusababisha kupungua kwa kina cha maji katika bwawa hilo.

Mheshimiwa Spika, kufuatia hali hiyo Serikali ilifanya ukarabati mkubwa wa bwawa hilo mwaka 2009 kwa kunyanyua kingo na tuta za bwawa na hivyo kuliwezesha kumwagilia eneo la hekta 50 tu kati ya hekta 300 zilizokuwa zinatumika katika kipindi hicho. Aidha, tathmini iliyofanyika mwaka 2012 ilibaini kuwa zinahitajika shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya ukarabati wa bwawa na kunyanyua tuta ili kuongeza kina cha hilo bwawa ili kuwezesha kumwagiliwa hekta 300 katika Skimu ya Chalinze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bwawa la Buigiri ambalo liko katika Kata ya Buigiri lilijengwa 1960 ikiwa na uwezo wa kumwagiliwa hekta 40 na kunyeshea mifugo. Kufuatiwa bwawa kuvuna maji ya mvua ya mafuriko, lilijaa mchanga na kupungua kina cha maji. Pamoja na Serikali kurikarabati bwawa hilo, katika kipindi cha mwaka 2005 na mwaka 2009 bado bwawa hilo liliendelea kujaa mchanga na tope kutokana na shughuli za kibinadamu zinazosababisha uharibifu wa mazingira katika vyanzo vya maji. Aidha, tathmini iliyofanyika mwaka 2012 ilionesha kuwa bwawa hilo linahitaji ukarabati wa sehemu ya kutoroshea maji (slipway) na kunyanyua tuta ili kuongeza kina kwa gharama ya shilingi milioni 475.

Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa bwawa hilo kwa wananchi wa Wilaya ya Chamwino, Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, itatenga fedha katika bajeti ya mwaka 2019/2020 kwa ajili ya kuyafanyia tathmini ya kina na usanifu kuandaa nyaraka za zabuni kwa ajili ya kutangaza na ukarabati. Aidha, Serikali inashauri wananchi wanaoishi kwenye maeneo ya vyanzo vya maji na kufanya shughuli za kibinadamu kushiriki katika kuboresha mazingira yao ili changamoto za kujaa mchanga na tope, iweze kupata ufumbuzi wa kudumu.
MHE. CECIL D. MWAMBE (K.n.y. MHE. HALIMA J. MDEE) aliuliza:-

Mwezi Novemba, 2018, Rais aliutangaza ulimwengu kwamba Serikali yake itanunua korosho zote kwa bei isiyopungua shilingi 3,000/= kwa kilo.

(a) Je, mpaka sasa ni kiasi gani kimetumika na kimetoa chanzo kipi na je, tani ngapi zimenunuliwa?

(b) Je, Wakulima/Vyama vya Msingi vingapi vimelipwa na vingapi bado havijalipwa?

(c) Je, zoezi hilo linatarajiwa kukamilika lini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Jimbo la Kawe lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, makadirio ya uzalishaji wa korosho msimu wa 2018/2019 ni zaidi ya tani 240,000 za korosho ghafi. Hadi kufikia tarehe tarehe 30 Januari, 2019, Serikali imekusanya jumla ya tani 214,269.684 za korosho ghafi zenye thamani ya Sh.707,089,957,200 sawa na asilimia 89.3 ya lengo la uzalishaji.

Mheshimiwa Spika, ununuzi wa korosho unafanywa na Taasisi ya Serikali ya Bodi ya Nafaka na mazao mchanganyiko ambapo malipo yaliyolipwa na kuingizwa kwenye akaunti za wakulima hadi tarehe 30 Januari, 2019 ni kiasi cha Sh.424,849,405,110 zilizotokana na korosho za wakulima kiasi cha tani 134,535,904. Aidha Bodi ya Nafaka na Mazao mchanganyiko ni Taasisi ya kibiashara yenye lengo la kupata faida na mtaji wake unatokana na ruzuku kutoka Serikali na mikopo kutoka Taasisi kama Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), NMB, CRDB na Benki zinginezo.

(b) Mheshimiwa Spika, jumla ya wakulima laki 390,466 wamekwishalipwa hadi kufikia tarehe 30 Januari 2019. Aidha Vyama vya Msingi 603 vimelipwa kati ya Vyama vya Msingi 605 vilivyohakikiwa.

(c) Mheshimiwa Spika, zoezi la operesheni korosho linaendelea vizuri na linatarajia kukamilika ifikapo tarehe 15 Februari, 2019.
MHE. MARTIN M. MSUHA aliuliza:-

(a) Je, ni lini Serikali itafanya utafiti wa gharama za uzalishaji wa kahawa Wilayani Mbinga kwa mara ya mwisho?

(b) Je, utafiti huo ulibaini kilo moja ya kahawa kavu inazalishwa kwa gharama gani?

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Martin Mtonda Msuha, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2015/ 2016, Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TACRI) imefanya utafiti wa gharama za uzalishaji wa kahawa katika Wilaya saba za Mbinga, Mbozi, Tarime, Rombo, Muleba, Karagwe na Buhigwe ambazo ni miongoni mwa Wilaya zinazozalisha zao la kahawa hapa Nchini.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, utafiti uliofanywa na Kituo cha Utafiti cha TACRI kwa wakulima wa kahawa aina ya arabica umeonesha kuwa gharama za uzalishaji wa aina bora ya kahawa zenye ukinzani wa magonjwa ni shilingi Sh.2,192,000 kwa hekta sawa na wastani wa Sh.825.44 kwa kilo zenye tija ya wastani wa kilo 2,662 kwa hekta. Aidha, gharama za uzalishaji wa kahawa zisizo na ukinzani wa magonjwa ni Sh.2,571,200 kwa hekta sawa na wastani wa kilo 1,931.78 kwa kilo zenye tija za wastani wa kilo 1.331 kwa hekta. Aidha, gharama za uzalishaji wa kahawa wa aina hiyo zimeongezeka kutokana na matumizi makubwa ya viuatilifu vya kuzuia kutu ya majani (Coffee Leaf Rust) na Chulebuni ambayo Coffee berry disease yaani CBD.

Mheshimiwa Naibu Spika, utafiti pia umeonesha, wakulima wanaolima kilimo cha mseto yaani intercropping kwa kuchanganya zao la kahawa na migomba, gharama za uzalishaji ni wastani wa Sh.1,557,683 kwa hekta kwa kahawa bora na Sh.2,157,967 kwa kahawa isiyo na ukinzani kwa magonjwa. Aidha, kupitia tafiti hizo, Serikali imekuwa ikishauri wakulima kutumia aina bora za kahawa ili kuwa na kilimo chenye tija, faida na endelevu.
MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU aliuliza:-

Kahawa ni zao la biashara na la kimkakati ingawa kwa miaka kadhaa bei ya zao hilo imeendelea kuwa chini:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuinua zao hilo Mkoani Kagera ikiwemo kupandisha bei ili kumnufaisha mkulima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Benardetha Kasabago Mushashu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, zao la kahawa ni miongoni mwa mazao ya kimkakati ambalo Serikali imeamua kuboresha mazingira ya uzalishaji pamoja na masoko ili kumnufaisha mkulima. Ili kufikia lengo hilo, Serikali imeimarisha usimamizi katika uzalishaji na kuboresha mifumo ya masoko. Bei ya mazao ya kilimo ikiwemo kahawa inategemea nguvu ya soko kwa kuzingatia mahitaji na ugavi wa uzalishaji duniani. Aidha, Serikali kupitia Bodi ya Kahawa imeruhusu na kuratibu uuzwaji wa kahawa moja kwa moja yaani direct export kwenye masoko ya Kimataifa yenye bei nzuri kuliko mnadani kwa kufuata Sheria na Kanuni zilizopo kwa kahawa maalum yaani Kahawa ya Haki yaani fair and organic coffee na kahawa zingine zenye mahitaji na masoko maalum.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuboresha mazingira ya biashara ya zao la kahawa, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pomoja na kuamua kuanzisha minada ya kahawa kwenye maeneo ya uzalishaji kuanzia msimu wa mwaka 2019/2020. Lengo la utaratibu huo ni kuharakisha malipo na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa minada na kuwashirikisha wakulima wengi zaidi katika mikoa inayozalisha zao la kahawa ukiwemo Mkoa wa Kagera.

Mheshimiwa naibu Spika, Serikali pia imedhibiti makato yasiyo na tija kwa wakulima na yanayokatwa kwenye Vyama Vikuu vya Ushirika na Vyama vya Msingi ili kubaki na makato yanayolenga kuendeleza zao la kahawa. Aidha, kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Serikali imewezesha Vyama vya Ushirika vya Kahawa vikiwemo Vyama vya Mkoa wa Kagera kupata mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kufanikisha shughuli za ukusanyaji na uuzaji wa kahawa ya wakulima, hivyo kumpunguzia mkulima mzigo wa riba uliokuwa unatozwa na mabenki ya kibiashara kwani TADB inatoza riba ya kiwango cha asilimia nane ukilinganisha na benki za kibiashara zilizokuwa zinatoza na zinazotoza riba ya asilimia 18 hadi 22.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na mikakati hiyo, Serikali imefuta tozo na kupunguza viwango vya makato mbalimbali vilivyokuwa vinatozwa kwa wakulima ikiwemo pamoja na kupunguza tozo zinazotozwa katika biashara ya kahawa pamoja na kupunguza viwango vya makato mbalimbali vilivyokuwa vinakusanywa kwa mkulima. Aidha, Serikali pia imepunguza kiwango cha ushguru wa mazao unaotozwa na mamlaka za Serikali za Mitaa kutoka asilimia tano hadi asilimia tatu ya bei ya kahawa ya shambani. Kwa kufanya hivyo, wakulima wa kahawa Mkoani Kagera na mikoa mingine watapata bei nzuri na hivyo kuongeza mapato yao na kuinua uchumi wa Taifa letu.
MHE. AZZA H. HAMAD aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha mradi wa ujenzi wa Bwawa la Umwagiliaji katika Kijiji cha Ishilolo, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Azza Hilal Hamad, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa ujenzi wa Bwawa la Ishololo uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini ni moja kati ya miradi iliyokuwa ikitekelezwa kupitia Mradi wa Uwekezaji katika Kilimo katika Wilaya (DASIP) chini ya iliyokuwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika. Utekelezaji wa mradi huo ulifikia ukomo wake mwezi Desemba, 2013 ambapo Benki ya Maendeleo ya Afrika ilisitisha kutoa fedha za utekelezaji wa miradi wakati utekelezaji wake ukiwa haujakamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inayo dhamira ya kukamilisha skimu zote za umwagiliaji ambazo utekelezaji wake haujakamilika kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa fedha. Skimu hii ipo miongoni mwa skimu za umwagiliaji zitakazopewa kipaumbele katika kutekeleza Mpango Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji (Irrigation Master Plan 2018 - 2025) ambapo kwa sasa umeanza kutekelezwa. Kwa kuzingatia umuhimu wa miradi hii ukiwemo mradi wa umwagiliaji wa Ishololo, tayari Serikali imekwishaanza mazungumzo na wadau mbalimbali, ikiwemo Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo la JICA kwa lengo la kuboresha miradi yote ambayo haijakamilika na ile inayofanya kazi chini ya ufanisi uliokusudiwa.
MHE. MARTIN M. MSUHA aliuliza:-

Hivi karibuni Serikali ilibadilisha mfumo wa ununuzi na uuzaji kahawa kwamba ni lazima kupitia Vyama vya Ushirika vya Msingi:-

Je, ni Vyama vingapi vya Msingi vya Ushirika (AMCOs) vimeundwa Wilayani Mbinga kufuatia kubadilishwa kwa mfumo huo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Martin Msuha, Mbunge wa Mbinga Vijijini, naomba kutoa maelezo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Vyama vya Ushirika huanzishwa na wananchi kutokana na mahitaji yao, hivyo, kupelekea kuwepo kwa aina mbalimbali za Vyama vya Ushirika kama vile vyama vya ushirika vya mazao ya kilimo na masoko, mifugo, uvuvi, viwanda, nyumba, fedha na madini kwa mujibu wa Sheria ya Ushirika Na. 6 ya mwaka 2013.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali imeelekeza biashara ya zao la kahawa na mazao mengine ya biashara kufanyika kupitia Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) badala ya wanunuzi binafsi kwenda kwa wakulima moja kwa moja. Utaratibu huu utawawezesha wakulima kunufaika na kilimo cha kahawa kwa kuzalisha kahawa yenye ubora na kuzwa kupitia minada ambapo wanunuzi watashindanishwa na hivyo kupelekea mkulima kupata bei nzuri na yenye tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa Mkoa wa Ruvuma una jumla ya Vyama vya Ushirika vya Msingi vya Kahawa 67 na Chama Kikuu cha Ushirika kimoja (MBIFACU) ambavyo vimeansihwa na wakulima wa kahawa katika Mkoa wa Ruvuma. Aidha, Wilaya ya Mbinga ina jumla ya Vyama vya Ushirika vya Msingi vya Kahawa 58 ambavyo ndivyo vitasimamia na kuendesha biashara ya kahawa katika Wilaya ya Mbinga.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza:-

Serikali ilikuwa na mradi wa kujenga masoko katika eneo la Nkwenda na Murongo katika Wilaya ya Kyerwa lakini masoko hayo hayajakamilika na yametelekezwa. Je, Serikali ilikuwa na malengo gani kujenga masoko hayo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, masoko ya Nkwenda na Murongo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa ni kati ya masoko matano ya kimkakati yaliyopangwa kujengwa kupitia Mradi wa Uwekezaji katika Sekta ya Kilimo Wilayani (District Agricultural Sector Investment Project – DASIP) na ujenzi ulianza kutekelezwa mwaka 2006/2007 hadi mwaka Desemba, 2013. Masoko mengine yapo katika Halmashauri za Busoka (Kahama), Kabanga (Ngara) na Sirari (Tarime). Mradi huo uligharamiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika na Serikali ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la ujenzi wa masoko hayo ya kimkakati ilikuwa ni kuanzisha mfumo thabiti wa masoko utakaoongeza tija na pato kwa wakulima ndani ya Wilaya husika. Mfumo huu ulijenga mazingira wezeshi kibiashara katika maeneo ya mpakani ili kurahisisha biashara na majirani zetu na kuinua hali za kiuchumi za wananchi wa maeneo hayo na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi mradi wa DASIP unafungwa Desemba 2013/2014, kazi ya ujenzi wa masoko hayo ilikuwa haijakamilika na yalikuwa katika hatua mbalimbali za ujenzi. Kwa kuzingatia umuhimu wa masoko hayo ya kimkakati katika Halmashauri husika, Serikali imepanga kukamilisha ujenzi wa masoko hayo na mengine nchini kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II). Katika bajeti ya mwaka 2019/2020 Serikali imetenga shilingi bilioni 2.9 kuendelea na ujenzi wa masoko hayo.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:-

Manispaa ya Tabora ipo kwenye mradi mkubwa wa maji toka Ziwa Victoria na Bwawa kubwa la Igombe linalotumika kuhudumia Wakazi wa Tabora Manispaa litakuwa halina matumizi tena.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuliweka Bwawa la Igombe kwenye scheme za umwagiliaji ili wakazi wa Tabora waendeshe Kilimo cha umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Viti maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa kupanga matumizi ya maji kutoka katika chanzo, utunzaji wa mazingira na matumizi ya kijamii hupewa umuhimu zaidi kabla ya matumizi mengine. Ujenzi wa miundombinu ya kutoa maji kutoka Ziwa Victoria umelenga zaidi katika kupunguza upungufu wa maji uliopo kwenye Manispaa ya Tabora ambayo kwa sasa inahudumiwa na Bwawa la Igombe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji hayo ni kwa ajili ya matumizi ya kijamii tu kwani hayatatosha kwa Kilimo cha umwagiliaji. Kwa kutambua umuhimu wa kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa tija na kukabiliana na mabadiliko tabianchi, Wizara yetu kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, ina mpango kabambe wa Taifa wa umwagiliaji unaotekelezwa kuanzia 2018/2019 hadi mwaka 2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo katika Manispaa ya Tabora, mpango huu umejumuisha uboreshaji na ujenzi wa skimu za umwagiliaji za Imalamihayo, Inala, Magoweko na Bonde la Kakulungu.
MHE. PASCAL Y. HAONGA (K.n.y. MHE. CECIL D. MWAMBE) aliuliza:-

Pembejeo za kilimo ni ghali sana, hivyo wakulima wengi hushindwa kununua na kusababisha kupata mavuno haba. Je, Serikali ipo tayari kupunguza au kuweka bei elekezi iliyo nafuu kwa mkulima ili aweze kupata pembejeo za dawa, mbolea na zana za kilimo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Ndanda kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha pembejeo za kilimo yaani mbegu, mbolea, viwatilifu na zana za kilimo zinapatikana kwa wakati na kwa bei nafuu. Hatua hizo ni pamoja na uagizaji wa pamoja, utoaji wa ruzuku, kufuta au kupunguza tozo na kodi zinazochangia kuongezeka kwa bei ya pembejeo na kufanya tafiti katika mnyororo wa thamani wa mazao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina utaratibu wa kuweka bei elekezi ya mbolea kupitia mfumo wa ununuzi wa pamoja nchini kwa mbolea za kupandia aina ya DAP na kukuzia aina ya Urea. Utaratibu huu ulilenga kuhakikisha upatikanaji wa mbolea kwa wakati na kwa bei nafuu kwa wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jitihada za kuongeza uzalishaji wa kipato cha mkulima, Serikali hununua na kusimamia udhibiti na usambazaji wa viuatilifu vya kupambana na milipuko ya visumbufu vya mazao na mimea kama vile kweleakwelea, viwavijeshi, viwavijeshi vamizi, panya, nzige wekundu na nzi wa matunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kumpunguzia mkulima harubu katika uzalishaji na uongezaji thamani ya mazao, Serikali imeendelea kutoa kutoa mikopo nafuu ya zana za kilimo kupitia Mfuko wa Taifa wa Pembejeo za kilimo, Benki ya Maendeleo ya Kilimo na Shirika la Maendeleo la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa mbegu na viuatilifu, Serikali inafanya utafiti wa kubaini gharama za uzalishaji wa mbegu kwa kulinganisha na bei za mbegu zilizopo sasa ambazo utaiwezesha Serikali kuamua endapo kuna ulazima wa kuweka bei elekezi katika viuatilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hatua hizo, Serikali inahamasisha ujenzi wa viwanda vya mbolea, viwatilifu, zana za kilimo na uwekezaji katika mashamba ya mbegu ili kupunguza gharama za pembejeo kwa wakulima.
MHE. MOSHI S. KAKOSO (K.n.y. MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA) aliuliza:-

Bonde la Mto Rufiji lina eneo kubwa lenye rutuba ambalo lingetumika vizuri lingeweza kulisha Mji wa Dar es Salam na viwanda vyote nchini, RUBADA imechukua maeneo hayo ambayo inakadiriwa kuwa na ukubwa wa hekta 500,000 na kuwapa baadhi ya wawekezaji ambao wengi wao ni matapeli na madalali wa viwanja/mashamba:-

Je, lini Serikali itamua kunyang’anya maeneo yote ambayo wawekezaji wameshindwa kuwekeza kwa kadri walivyoomba ili Sera ya Serikali ya Viwanda iweze kutimia?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Jimbo la Rufiji, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Uendeshaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) ilianzishwa na Sheria ya Bunge Namba 5 ya mwaka 1975 na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali Namba.146 tarehe 1 Julai 1976. Mojawapo ya majukumu ya RUBADA ilikuwa kusimamia matumizi ya ardhi ya kilimo kwenye Bonde la Mto Rufiji ikiwemo kuratibu upatikanaji wa ardhi kwa wawekezaji kwa ajili ya shughuli za kilimo.

Mheshimiwa Spika, kwa kumbukumbu zilizopo, RUBADA haikuwahi kuchukua eneo la ardhi lenye ukubwa wa hekta 500,000 na kuwapa wawekezaji. RUBADA ilikuwa inamiliki hekta 21 katika Kituo cha Ikwiriri, hekta 12.675 katika Kambi ya Vijana Mkongo, hekta 1.15 katika Kambi ya Utete, hekta 5,128 katika Shamba la Ngalimila Kilombero, Mkoani Morogoro, hekta 5,800 katika Shamba la Mngeta, Kilombero, Mkoani Morogoro na eneo la kilometa za mraba 13,907 kwa ajili ya majengo na viwanja Jijini Dar es Salaam. Aidha, ardhi yote nyingine kwenye eneo la Bonde la Mto Rufiji lilikuwa linamilikiwa na Halmashauri 29 za Wilaya, Vijiji na wananchi mbalimbali.

Katika kipindi chote ilipokuwepo RUBADA imewezesha upatikanaji wa Hati Miliki usio wa moja kwa moja yaani (Derivative Right of Occupancy) wa eneo la hekta 2,000 katika eneo la Nyumbunda, Nyambili na Bungu, Wilaya ya Kibiti kwa mwekezaji FJS African Starch Development kwa ajili ya kilimo na ujenzi wa kiwanda cha kuchakata mihogo. Aidha, Serikali haitasita kuchukua ardhi hiyo ya kilimo iwapo itathibitika kuwa mwekezaji ameshindwa kuendeleza kwa shughuli za kilimo na uzalishaji wa mazao ya kilimo.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM (K.n.y. MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN) aliuliza:-

Tanzania ina ardhi kubwa yenye rutuba ya kutosha na inawezekana kabisa kulima mazao yasiyotumia mbolea za viwanda ambayo bei zake ni kubwa sana katika Soko la Dunia:-

(a) Je, Serikali imeweka mikakati gani ya kutoa elimu hiyo kwa wakulima?

(b) Je, Serikali inachukua hatua gani kuona kuwa Tanzania ni nchi inayoongoza kwa kuzalisha mazao yasiyokuzwa kwa kutumia mbolea za viwandani?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf Salim Hussein, Mbunge wa Chambani, lenye sehemu (a)na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Taasisi za Sekta Binafsi imeendelea kutoa elimu ya kilimo bora inayojumuisha matumizi sahihi ya mbolea za asili, viuatilifu vya asili, mbegu bora na hifadhi ya mazingira ili kuzalisha mazao kwa tija na kuwa na kilimo endelevu.

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza mpango wa muda mrefu wa matumizi sahihi ya virutubisho vya udongo, Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania yaani (TARI) inafanya utafiti wa afya ya udongo katika Kanda zote saba za kiikolojia za kilimo nchini. Utafiti huo unalenga kubaini aina za virutubisho na tabia za udongo katika maeneo mbalimbali nchini ili kuweza kutoa elimu kwa wakulima kuhusu kiasi, aina na matumizi sahihi ya mbolea za viwandani na asili. Utafiti huo umeanza kwa kuchukua sampuli za udongo katika Kanda za Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kati, Kanda ya Kaskazini na sehemu ya Kanda ya Mashariki na utaendelea katika maeneo mengine nchini na utakamilika Juni 2020.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua ongezeko la mahitaji ya mazao na bidhaa za kilimo zinazozalishwa kwa kutumia mbolea za asili na viuatilifu vya asili, Serikali imeboresha mtaala wa mafunzo katika Vyuo vya Kilimo ambapo mada za kilimo hai na hifadhi ya mazingira zimejumuishwa ili kuwawezesha Maafisa Ugani na wakulima kupata elimu hiyo.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Tanzania Organic Agriculture Movement, Sustainable Agriculture Tanzania, Ecology Agriculture chini ya SWISSAID, Zanzibar Organic Producers, Tanzania Alliance for Biodiversity na TANCERT inatoa elimu ya kilimo hai kwa wakulima na kutoa vyeti vya ubora wa mazao kwa ajili ya masoko maalum. Baadhi ya mazao ambayo yanazalishwa katika mfumo wa kilimo hai hapa nchini ni pamoja na kakao, kahawa, pamba na viungo.
MHE. SHALLY J. RAYMOND (K.n.y. MHE. ESTER M. MMASI) aliuliza:-

Changamoto kubwa inayowafanya wanawake wa Tanzania wasishiriki kwenye Sekta ya Kilimo na ufinyu wa Bajeti na mitaji kutoka kwenye Taasisi za Kifedha:-

Je, ni nini kauli ya Serikali juu ya ushiriki wa wanawake kwenye Sekta ya Kilimo ukizingatia changamoto hizo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ester Michael Mmasi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Sekta ya Kilimo inajumuisha sekta ndogo za kilimo mazao, mifugo, uvuvi na misitu. Bajeti ya Wizara za Sekta ya Kilimo zinajumuisha bajeti ya Wizara za sekta husika, Bodi za mazao na Taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara hizo za Kisekta. Utekelezaji wa bajeti hizo huwawezesha wanaume na wanawake katika shughuli za kilimo. Wanawake wanachangia asilimia 90.4 ya nguvukazi ya wanawake inayotumika katika shughuli za kilimo na huchangia wastani wa asilimia 70 ya mahitaji ya chakula nchini.

Mheshimiwa Spika, katika kutatua changamoto hizo, Serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004 kupitia mifuko ya uwezeshaji ikiwemo Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake ambao huchangia 4% ya mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kila mwaka. Kwa mfano, katika mwaka 2017/2018, jumla ya shilingi 15,633,312,764.91 zimetolewa kwa vikundi 2,919 vya wanawake na vijana vyenye jumla ya wanawake wajasiriamali 29,190 katika Halmashauri mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa wanawake katika kilimo Serikali, imeilekeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) katika mikopo inayotoa yote isipungue asilimia 20, mikopo hiyo itolewe kwa vikundi vya wanawake na miradi inayoongozwa na akina mama. Hadi Januari, 2019, asilimia 33 ya mikopo iliyotolewa katika vikundi vya wanawake na Benki ya Maendeleo ya Kilimo ilienda kwa wanawake.

Mheshimiwa Spika, vilevile, benki za NMB na Azania zimeanzisha madirisha maalum ya kutoa mikopo kwa vikundi vinavyojishughulisha na kilimo na miradi mbalimbali. Pia Serikali imehamisisha wanawake kujiunga kwenye vikundi vya ushirika wa akiba na mikopo kama SACCOS, VICOBA ili kupata huduma za kifedha na mikopo kwa urahisi ili kuongeza mitaji yao katika kilimo.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeuelekeza Mfuko wa Pembejeo za kilimo kutoa kipaumbele kwa vikundi vya wanawake vinavyoomba mikopo ya kuendeleza kilimo. Vilevile, Serikali imeendelea kutoa hatimiliki za ardhi za kimila na hatimiliki za ardhi za muda mrefu kwa ajili ya kuwawezesha wanawake kumiliki ardhi na kuzitumia hati hizo kama dhamana, kukopa katika Taasisi mbalimbali za kifedha ili waweze kupata mitaji ya kununua pembejeo na zana bora za kilimo ili kuongeza uzalishaji, tija na kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya usindikaji wa mazao kwa kuongeza tija na vipato vyao.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:-

Mkoa wa Katavi unapata mvua za masika kuanzia mwezi Septemba na Oktoba lakini mara nyingi pembejeo zimekuwa zikichelewa kupelekwa wakati mwingine hadi mwezi Novemba:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka kwa wakati pembejeo Mkoani Katavi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatumia Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja (Bulk Procurement System – BPS) kuagiza mbolea ya kupandia (DAP) na mbolea ya kukuzia (UREA). Mfumo huo unawezesha upatikanaji wa mbolea kwa wakati na kwa bei nafuu na kudhibiti upandishaji wa bei za mbolea kiholela.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inakamilisha zabuni ya kuagiza mbolea tani 280,000 ambapo tani 170,000 ni mbolea ya kupandia na tani 110,000 ni mbolea ya kukuzia kwa ajili ya msimu wa 2019/2020 kupitia mfumo wa BPS. Mbolea hiyo inatarajiwa kufikishwa hapa nchini mwezi Agosti, 2019 na kusambazwa kwa wakulima wa Mkoa wa Katavi na Mikoa mingine nchini kabla ya mwezi Septemba.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, ziada ya mbolea iliyopo nchini inaendelea kusambazwa katika maeneo mbalimbali kulingana na msimu wa kilimo, ambapo hadi tarehe 30 Machi, 2019 kulikuwa na mbolea tani 147,913 za mbolea zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeyaelekeza makampuni yanayoingiza na kusambaza mbolea ya Premium Agrochem, OCP na Export Trading Group kuhakikisha kwamba ifikapo Julai, 2019 kampuni hizo ziwe na maghala ya kuhifadhia mbolea na mawakala wa kusambaza mbolea katika mikoa inayotumia mbolea kwa wingi ukiwemo Mkoa wa Katavi ili kuondoa changamoto ya upungufu wa mbolea kwa wakulima katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imelielekeza Shirika la Reli Tanzania kutoa kipaumbele cha kusafirisha mbolea ili kusafirisha mbolea nyingi kwa wakati mmoja na gharama nafuu ili kumfikia mkulima kwa wakati na bei nafuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inakusanya mahitaji ya mbegu bora na viuatilifu katika mikoa mbalimbali ili kuhamasisha kampuni na wafanyabiashara kupeleka pembejeo hizo kwa wakulima kabla ya msimu wa kilimo kuanza na wakati na kwa kuuza kwa bei ya mauzo na bei nafuu.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza:-

Wananchi wa Tarafa ya Mombo wamekuwa na hitaji la kuwa na skimu kubwa ya umwagiliaji katika Bonde la Mto Mkomazi na mara kadhaa viongozi wa Serikali wamekuwa wakitoa ahadi ya kukamilisha jambo hilo.

Je, ni lini Serikali itatekeleza mradi wa umwagiliaji katika Bonde la Mto Mkomazi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Timotheo Mnzava Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijiji kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 1980 Serikali kupitia na washirika wa maendeleo, yaani Wakala wa Ushirikiano wa Kitaalam wa kimataifa wa Serikali ya Ujerumani (Germany) Agency for Technical Cooperation Limited) ulifanya upembuzi yakinifukwa ajili ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji katika Bonde la Mkomazi katika tarafa ya Mombo, Halmashauri ya Korogwe. Hata hivyo taarifa ya upembuzi yakinifu na usanifu zilibaini kuwa ujenzi wa bwawa hilo ungesababisha kuongezeka kwa maji katika Ziwa Manga na kupelekea kuzama kwa Kijiji cha Manga Mikocheni pamoja na mashamba ya wakulima.

Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto hiyo katika mwaka 2014/2015 wataalam wa Ofisi ya Kanda ya Umwagiliaji ya Kilimanjaro walifanya mapitio ya upembuzi yakinifu upya na usanifu wa kina uliofanywa katika eneo hilo kwa lengo la kuepusha uwezekano wa kufurika kwa Ziwa Manga, kuzama kwa Kijiji ca Manga Mikocheni na mashamba ya wakulima kutokana na ujenzi wa bwawa hilo. Mapitio hayo yalibaini uwezekano wa ujenzi wa bwawa na mradi wa umwagiiaji katika eneo hilo bila kuathiri wakazi wa eneo hilo. Mapitio ya usanifu huo yalibaini kuwa ujenzi wa bwawa pekee utagharimu shilingi bilioni 1,543,736,877.

Mheshimiwa Spika, Serikali iko katika mchakato wa kufanya ukaguzi na tathmini ya kina ya miradi yote ya umwagiliaji nchini ili kufanya uhakiki wa eneo la umwagiliaji kwa lengo la kubaini ubora wa miradi, thamani ya fedha, gharama za miradi na mahitaji halisi ya sasa ya kuboresha, kuendeleza na kuongeza miradi mipya ya umwagiliaji. Aidha, baada ya tathmini hiyo Serikali itaendelea kutafuta fedha ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha mabwawa na skimu za umwagiliaji nchini ikiwemo mradi wa umwagiliaji katika Bonde la Mkomazi zinaendelezwa na kuwanufaisha wananchi wa Mombo na taifa kwa ujumla.
MHE. EDWIN M. SANNDA aliuliza:-

Halmashauri ya Mji wa Kondoa imewasilisha andiko la Mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji katika Kijiji cha Mongoroma, Kata ya Serya takribani miaka mitatu sasa, eneo la ekari 3,000 limetengwa kwa ajili ya mradi huo utakaonufaisha takribani wananchi 12,000.

Je, ni lini Serikali italeta fedha hizo ili mradi huo uanze?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika,kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Mgante Sannda, Mbunge wa Jimbo la Kondoa Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2010/2011 Serikali kupitia Idara iliyokuwa ya Umwagiliaji chini ya Wizara ya Kilimo ilitumia shilingi milioni 300 kwa ajili ya kuendeleza miradi ya umwagiliaji ya Kisese, Kidoka na Mongoroma Serya katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa wakati huo. Kati ya fedha hizo shilingi 143,265,000 zilitumika kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika mradi wa Mongoroma Serya uliopo katika Kata ya Serya. Kazi zilizofanyika ni pamoja na upimaji wa sura ya ardhi, usanifu wa kina matayarisho ya gharama za ujenzi, tathmini ya rasilimali maji, tathmini ya awali ya mazingira, utafiti wa udongo na masuala ya jamii.

Mheshimiwa Spika, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa bwawa la Mongoroma Serya ulibaini kuwa bwawa hilo lingegharimu shilingi bilioni nne kwa wakati huo. Aidha, bwawa hilo lingekuwa na uwezo wa kumwagilia zaidi ya hekta 3,000 na kunufaisha zaidi ya wakulima 12,000 kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, matumizi ya binadamu, unyweshaji wa mifugo na wanyamapori pamoja na ufugaji wa samaki katika vijiji vya Mongoroma, Serya na Munguri.

Mheshimiwa Spika, Serikali iko katika mchakato wa kufanya tathmini ya kina kwa miradi yote ya umwagiliaji nchini ili kubaini thamani ya fedha, ubora wa miradi na mahitaji halisi ya uboreshwaji, uendelezwaji na kuchagua miradi michache kwa utekelezaji wa ujenzi kwa miradi yenye tija, matokeo na manufaa makubwa kwa wakulima na Taifa kwa ujumla. Aidha, baada ya tathmini hii na kutegemea upatikanaji wa fedha Serikali itahakikisha bwawa hilo na skimu zingine zitajengwa.
MHE. OMARY A. BADWEL aliuliza:-

Kwa sasa Dodoma ni Makao Makuu ya nchi yetu na kwa sababu hiyo idadi ya watu pamoja na mahitaji ya huduma mbalimbali ikiwemo chakula vitaongezeka. Wilaya ya Bahi ambayo ni miongoni mwa Wilaya za Dodoma ina fursa muhimu za uzalishaji mchele kutokana na jiografia yake lakini inakwamishwa na miundombinu chakavu na isiyokamilika katika skimu zake za umwagiliaji wa zao la mpunga:-

Je, Serikali imejiandaa kuchukua hatua gani kutoa fedha za ukarabati na umaliziaji wa miradi hiyo ya umwagiliaji ili Wilaya ya Bahi ipate fursa ya uzalishaji mchele kwa wingi na kukidhi mahitaji ya chakula katika Mji wa Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omary Ahmad Badwel, Mbunge wa Jimbo la Bahi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika kukamilisha na kukarabati miundombimu ya umwagiliaji chakavu iliyopo Wilaya ya Bahi, Serikali itafanya tathmini ya miradi hiyo kabla ya mwezi Desemba, 2019 na utekelezaji wake utahusisha wadau mbalimbali wa miradi ya umwagiliaji wakiwemo washirika wa maendeleo, wawekezaji binafsi na ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi. Lengo ni kuhakikisha kuwa, kilimo cha umwagiliaji kinakuwa cha uhakika na kuongeza upatikanaji wa chakula nchini.

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji itaendelea kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Bahi pamoja na vyama vya wamwagiliaji wa maeneo hayo kuandaa maandiko kuomba mikopo kutoka taasisi za kifedha kama vile Benki ya Maendeleo ya Kilimo kwa lengo la kukamilisha ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji ili wananchi wa maeneo haya waweze kuwa na uhakika wa chakula cha kutosheleza kwenye maeneo yao.
MHE. FLATEY G. MASSAY (K.n.y. MHE. QAMBALO W. QULWI) aliuliza:-

Wakulima wa Bonde la Eyasi wanategemea kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia chemchem za Qangded; na kutokana na kupungua kwa kiasi cha maji katika vyanzo hivyo wakulima wengi wanashindwa kuzalisha:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza vyanzo mbadala kama mabwawa na visima virefu ili kilimo katika bonde hilo kiwe endelevu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Qambalo Willy Qulwi, Mbunge wa Jimbo la Karatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa wakulima wa Bonde la Eyasi wanategemea kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia chemchemi za Qangded. Aidha, kutokana na kupungua kwa kiasi cha maji katika vyanzo hivyo pamoja na kuongezeka kwa mahitaji ya maji kwa matumizi mbalimbali ikiwemo umwagiliaji, wakulima wanashindwa kuzalisha mazao ya kilimo ipasavyo.

Mheshimiwa Spika, ili kuongeza vyanzo mbadala vya maji kama mabwawa na visima virefu, Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Karatu itafanya upembuzi yakinifu kwa lengo la kubaini maeneo yanayofaa kujengwa mabwawa na kuchimbwa visima virefu na hivyo kuongeza vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Spika, ili kuharakisha upembuzi yakinifu, Halmashauri ya Wilaya ya Karatu inashauriwa kutenga fedha zitokanazo na mapato ya ndani kama ilivyoelekezwa kuwa kila Halmashauri itenge asilimia 20 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya Sekta ya Kilimo ikiwemo kuendeleza kilimo cha umwagiliaji. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo itaendelea kutafuta vyanzo mbadala vya fedha ili kuendeleza kilimo cha umwagiliaji katika Bonde la Eyasi.

Mheshimiwa Spika, kupitia Sheria Na. 5 ya Umwagiliaji ya Mwaka 2013 tunatambua kuwa ushiriki wa sekta binafsi katika kuendeleza kilimo cha umwagiliaji. Hivyo, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi itaendelea kutafuta vyanzo vingine vya fedha ili kujenga mabwawa na visima virefu kwa kutumia utaratibu wa Jenga, Endesha na Kabidhi.
MHE. ESTER M. MMASI aliuliza:-

Mfereji wa Muo Irrigation Scheme (MUU) ni mradi wa Umwagiliaji uliopata fedha takribani Shilingi milioni 248 mnamo mwaka 2018.

Je, kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kukamilisha mradi huu kwa faida ya wakazi wa Old Moshi Mashariki?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ester Michael Mmasi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa uendelezaji wa Skimu ya Umwagiliaji Muo kwa ajili ya shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa Old Moshi na Taifa kwa ujumla. Aidha, kwa kuzingatia mahitaji na umuhimu wa uendelezaji wa Skimu ya Umwagiliaji ya Muo Serikali mpaka kufikia mwaka wa fedha 2019/2020 tumeshapeleka jumla ya shilingi milioni 261 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizo zilitokana na Mfuko wa Local Government Capital Development Grant jumla ya Shilingi za Kitanzania milioni 51 kwa ajili ya kusakafia mfereji mkuu umbali wa mita 200. Mfuko wa Umwagiliaji wa Wilaya (District Irrigation Development Fund) jumla ya Shilingi za Kitanzania milioni 200 kwa ajili utandikaji wa mabomba kutoka kwenye chanzo cha maji, progamu ya kuendeleza kilimo wilaya jumla ya shilingi milioni 10 kwa ajili ya kuendeleza utandikaji wa mabomba.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa kazi zifuatazo zilizokwishatekelezwa ni pamoja na ujenzi wa banio kwenye chanzo cha mfereji mkuu umekamilika. Utandikaji na ufungaji wa mabomba class B umbali wa kilometa sita kati ya kilometa nane umekamilika. Ujenzi wa matenki mawili ya kurekebisha msukumo wa maji umekamilika. Ujenzi wa chemba ya kufunika kwenye sehemu ya banio na ujenzi wa mfumo wa hewa katika mabomba umekamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi Septemba, 2019, Serikali ilituma wataalam wake katika skimu ya Muo kwa lengo la kubaini changamoto zilizopo na kuanisha mikakati na mahitaji ya kuendeleza skimu hiyo. Changamoto zilizobainishwa ni pamoja na kuwepo kwa hitaji jipya la kubadilishwa matumizi ya chanzo cha maji kwa matumizi ya maji ya kunywa badala ya maji ya umwagiliaji na kuwepo ongezeko la shughuli za ujenzi katika skimu hiyo kusababisha kupungua kwa eneo la kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia changamoto hizo Serikali imepanga kuitisha mkutano wa wadau kwa ajili ya kujadili na kupata ufumbuzi wa changamoto hizo. Aidha, baada ya makubaliano ya mkutano wa wadau kuhusu kubadilisha matumizi au la ya chanzo cha maji Serikali itaendelea kutafuta fedha za kibajeti kutoka vyanzo mbalimbali kwa ajili ya uendelezaji wa skimu hiyo.
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA aliuliza:-

Mwaka 2005 Serikali ilikamilisha ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Itumbiko, lakini banio lake limeharibika na kusababisha Skimu nzima kushindwa kufanya kazi; aidha, Serikali kupitia Mfuko wa Food Aid Counterpart Fund ilipata shilingi milioni 300 ili kujenga miundombinu ya umwagiliaji katika Kijiji cha Gwanumpu lakini mradi huo hauendelei licha ya kutengenewa fedha za utekelezaji.

(a) Je, lini Serikali itakarabati banio la Skimu ya Umwagiliaji ya Itumbiko ili kuokoa miundombinu inayoendelea kuharibika na kuwasaidia wananchi kuendelea kulima ?

(b) Je, ni kwa nini Serikali imeshindwa kuwasiliana na Mkurungenzi Mtendaji wa Wilaya ya Kakonko ili kufuatilia fedha za Food Aid Counterpart Fund ambazo zimekosa wafuatiliaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Christopher Kajoro Chiza, Mbunge wa Jimbo la Buyungu, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Skimu ya Umwagiliaji ya Itumbiko ina jumla ya hekta 230 na inategemewa na wakazi zaidi ya 339. Skimu hiyo imejengwa mara ya kwanza mwaka 2004 kwa fedha kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Umwagiliaji Wilaya kwa kiasi cha shilingi milioni 340 ambazo zilitolewa kwa awamu mbili. Aidha, kutokana na uharibifu wa miundombinu uliotokana na mafuriko mwaka 2017/2018 Serikali itatuma wataalam wake kufanya tathmini ya kina ili kubaini athari zilizotokea na kuainisha gharama za ukarabati zinazohitajika kwa ajili ya ukarabati na uendelezaji wa Skimu hiyo ya Itumbiko.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Kakonko Serikali inatekeleza ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Gwanumpu iliyopo Kijiji cha Gwanumpu, Kata ya Gwanumpu, yenye hekta 139 kwa kushirikiana na Serikali ya Japan, kupitia shirika lake, kupitia Mradi wa Food Aid Counterpart Fund kwa gharama ya Sh.358,302,000. Aidha, jumla ya Sh.248,570,000 zimetolewa katika awamu ya kwanza na ya pili na Sh.109,732,000 zitatolewa kutegemeana na utekelezaji wa mradi huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inafuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa ujenzi wa Skimu ya Gwanumpu kwa ushirikiano na Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Mwezi Disemba mwaka 2019 wataalam wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji wakishirikiana na wataalam wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko walipitia upya tathmini ya awali iliyofanyika na kubainisha gharama za ujenzi kwa wakati huu na kuziwasilisha katika shirika la Food Aid Counterpart Fund kwa ajili ya kupata fedha za ujenzi huo.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA aliuliza:-

Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya mabwawa ya zamani yanayotumika katika kilimo cha umwagiliaji ambayo yamepungua kina na kushindwa kuwasaidia wananchi hususan Mabwawa ya Kijiji cha Buigiri, Kijiji cha Chalinze na Kijiji cha Izava?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joel Mwaka Makanyaga, Mbunge wa Jimbo la Chilonwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Bwawa la Buigiri ambalo lipo katika Kata ya Buigiri lilijengwa mwaka 1960 likiwa na uwezo wa kumwagilia hekta 40 na kunyweshea mifugo. Bwawa hilo limekuwa likijaa mchanga na tope kutokana na mafuriko na hivyo kupungua kwa kina cha maji. Pamoja na Serikali kukarabati bwawa hilo katika kipindi cha mwaka 2005 na mwaka 2009 kwa kuongeza kina kwa mita moja bado bwawa hilo liliendelea kujaa mchanga na tope kutokana na shughuli za kibinadamu zinazofanyika juu ya bwawa na kusababisha mchanga na tope kujaa bwawani. Tathmini iliyofanyika mwaka 2012 ilionesha kuwa bwawa hilo linahitaji ukarabati wa sehemu ya kutoroshea maji na kunyanyua tuta ili kuongeza kina kwa gharama ya Shilingi milioni 475.

Mheshimiwa Spika, bwawa la pili Bwawa la Ikowa lililopo katika Kijiji cha Chalinze na Ikowa lilijengwa mwaka 1959 kwa ajili ya kupata maji ya mifugo na kumwagilia jumla ya hekta 96 kati ya hekta 220 katika Skimu ya Chalinze. Kutokana na mabadiliko ya tabianchi na shughuli za kibinadamu katika maeneo hayo, bwawa hilo limekuwa likijaa mchanga na tope kila msimu wa mvua na hivyo kusababisha athari katika tuta na kupungua kwa kina cha maji katika bwawa hilo. Tathmini iliyofanyika mwaka 2012 ilibaini kuwa zinahitajika shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya ukarabati wa bwawa na kunyanyua tuta ili kuongeza kina cha bwawa na hivyo kuwezesha kumwagilia hekta 220 katika Skimu ya Chalinze.

Mheshimiwa Spika, bwawa la tatu ni Bwawa la Izava lilijengwa miaka ya 1972/1973 kwa ajili ya mifugo na kilimo cha umwagiliaji. Pamoja na changamoto ya kujaa mchanga na matope bwawa hilo limeendelea kutoa huduma kwa wananchi hadi mwaka 2015 ambapo kupitia Mradi wa TASAF ililikarabati pamoja na kushirikiana na wananchi kupitia utaratibu wa kufanya kazi za kujitolea na kutumia kiasi cha Sh.7,418,000 kuwalipa wananchi hao. Mwaka 2017/2018, wakati wa mvua za msimu, kingo za bwawa hilo zilibomoka na hivyo kushindwa kutunza maji kwa ajili ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, Serikali itatuma timu ya wataalam kwa ajili ya kufanya usanifu wa kina ili kubaini mahitaji halisi ya ujenzi wa mabwawa hayo kwa wakati huu. Aidha, Serikali inashauri wananchi wanaoishi kwenye maeneo ya vyanzo vya maji na na upande wa juu wa bwawa kuacha kufanya shughuli za kibinadamu ili kuboresha mazingira yao na kutatua changamoto za kujaa mchanga na tope ziweze kupata ufumbuzi wa kudumu.
MHE. LUCY T. MAYENGA (K.n.y. MHE. AHMED A. SALUM) aliuliza:-

Bwawa la Ishololo katika Kata ya Usule na Misengwa katika Kata ya Musengwa ni mabwawa ambayo ujenzi wake haujakamilika kwa muda mrefu sasa; na kwa kuwa, tumeshaomba maombi maalum ili tupate fedha za kukamilisha miradi hii miwili:-

Je, Serikali inatoa tamko gani katika kukamilisha miradi hii?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ahmed Ally Salum, Mbunge wa Jimbo la Solwa, lenye sehemu kuu mbili kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Skimu ya Masengwa yenye eneo la ukubwa wa hekta 325 ilijengwa chini ya mradi shirikishi wa kuendeleza kilimo cha umwagiliaji mwaka 2004 kwa ujenzi wa banio na mfereji. Hata hivyo, skimu hiyo inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji ya umwagiliaji hususan kipindi cha kiangazi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto hiyo, katika mwaka 2007/2008, Ofisi ya Umwagiliaji Kanda ya Mwanza ilifanya upembuzi wa awali na kupata sehemu ya kujengea bwawa. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kupitia upya upembuzi wa awali na kufanya upembuzi wa kina wa Mradi wa Umwagiliaji wa Masengwa utakaohusisha ujenzi wa bwawa ili kupata gharama halisi ya ujenzi kwa sasa. Serikali itaendelea kutafuta fedha kutoka vyanzo mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa bwawa mapema iwezekanavyo katika mradi wa umwagiliaji Masengwa baada ya kazi ya upembuzi yakinifu kukamilika.

Mheshimiwa Spika, Mradi wa ujenzi wa Bwawa wa Ishololo uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini ni mojawapo ya miradi iliyokuwa ikitekelezwa kupitia Mradi wa Uwekezaji katika Kilimo katika Wilaya yaani DASIP. Miradi hiyo ilikuwa inagharamiwa kwa pamoja na Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika kuanzia mwaka 2006/2007 hadi mwaka 2013/2014 ambapo jumla ya shilingi Tshs. 572,552,001.79 zilitumika kwa ajili ya ujenzi wa Tuta la Bwawa ambao ulifikia asilimia 26.

Mheshimiwa Spika, kutokana na mradi huo kutokamilika kwa wakati, Wizara katika mwaka 2016 ilipitia upya mpango kabambe wa kuendeleza kilimo cha umwagiliaji ambapo mradi huo ni mojawapo ya miradi kabambe itakayotekelezwa katika Awamu ya Kwanza. Aidha, Serikali itatuma timu ya wataalam kufanya tathmini ya mahitaji na gharama za kuendeleza mradi huo kwa sasa ili kuanza ujenzi wa mradi huo ikiwemo ujenzi wa bwawa.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE aliuliza:-

Je, Serikali inasema nini juu ya ucheleweshwaji wa pembejeo za kilimo hasa mbegu na mbolea ambazo huwasababishia wakulima hasara?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pudenciana Wilfred Kikwembe, Mbunge wa Jimbo la Kavuu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, upungufu wa mbolea nchini umechangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo kuchelewa kupatikana kwa mahitaji kutoka kwa makampuni ya mbolea hapa nchini; kuongezeka kwa matumizi ya mbolea kutokana na bei nzuri ya mazao kwa msimu wa 2018/2019; kuongezeka kwa kilimo cha kibiashara baada ya Serikali kuwahakikishia wakulima kuwa haitafunga mipaka na kuingilia upangaji wa bei za mazao ya kilimo; na kuwepo kwa mvua nyingi ambazo zimesababisha kuongezeka kwa viwango vya matumizi ya mbolea kwa wakulima.

Mheshimiwa Spika, katika msimu wa 2019/2020 upatikanaji wa pembejeo zikiwemo mbegu bora hadi kufikia Desemba, 2019 ni tani 71,155.13. Kati ya hizo, tani 58,509.9 zimezalishwa nchini, tani 5,175.79 zimeingizwa kutoka nje ya nchi na tani 7,469.44 ni bakaa ya msimu 2018/2019. Aidha, upatikanaji wa mbolea hadi kufikia tarehe 30 Januari, 2020 ni tani 410,499 zikijumuisha tani 92,328 za UREA na tani 84,311 za DAP. Kati ya hizo, tani 225,417 zimeingizwa kutoka nje ya nchi, tani 16,685 zimezalishwa ndani ya nchi na tani 168,397 ni bakaa ya msimu wa 2018/2019.

Mheshimiwa Spika, kutokana na kuwepo kwa upungufu wa pembejeo nchini, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha pembejeo zinapatikana kwa wingi ili kutosheleza mahitaji ya ndani ya nchi. Hatua hizo ni pamoja na kutoa vibali kwa wasambazaji wakubwa wa mbolea kuagiza nje ya mfumo wa BPS kutokana na mahitaji ya wakulima na soko ambapo tani 200,000 zimeagizwa na hadi kufikia tarehe 30 Januari, 2020; kutoa kibali cha kuagiza tani 45,000 kwa Umoja wa wasambazaji na wauzaji wa pembejeo za kilimo; na kuagiza mbolea tani 43,000 kwa kutumia mfumo wa BPS ambapo mbolea hiyo imeanza kuingia nchini na kusambazwa nchini tangu tarehe 28 Januari, 2020. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na wadau inaendelea kuboresha mifumo ya uzalishaji, uthibiti na usambazaji wa pembejeo nchini ambapo sekta ya umma na binafsi zitashirikishwa na kuhamasishwa kuzalisha pembejeo nchini ili kukidhi mahitaji.
MHE. ANTHONY C. KOMU aliuliza:-

Mkoa wa Kilimanjaro unao kilimo cha umwagiliaji kinachotumia vyanzo vya asili kama chemchem za maanguko ya Mlima Kilimanjaro lakini kutokana na sababu mbalimbali ikiwepo mabadiliko ya tabianchi maji yamepungua sana hivyo mifereji ya asili inahitajika kujengwa kwa zege kuhakikisha matumizi mazuri ya maji:-

Je, Serikali inasaidiaje kutatua changamoto hii?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anthony Calist Komu, Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto za kilimo cha umwagiliaji katika Mkoa wa Kilimanjaro ikiwemo upungufu wa maji kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Katika kukabiliana na changamoto hizo Serikali inatekeleza mradi wa kuendeleza skimu za wakulima wadogo (Small Scale Irrigation Development Project) ambapo hadi sasa imefanya ukarabati wa mifereji na miundombinu mingine ya umwagiliaji katika skimu Nane za Mkoa wa Kilimanjaro.

Mheshimiwa Naibu Spika, Skimu hizo ni skimu ya Mawala iliyopo Wilaya ya Moshi kwa gharama ya shilingi milioni 147, skimu ya Kikafuchini shilingi milioni 294, skimu ya Musamwinjanga shilingi milioni 275 na skimu ya Nsanya milioni 275 zilizoko Wilaya ya Hai. Skimu zingine ni skimu ya Mowonjamu Shilingi milioni 165 na skimu ya Kishisha Shilingi milioni 165 zilizoko Wilaya ya Siha, na skimu ya kivulini Shilingi milioni 125 na skimu ya kileo Shilingi milioni 216 zilizoko Wilaya ya Mwanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha kilimo cha umwagiliaji kinakuwa chenye tija Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika mwaka wa Fedha wa 2019/ 2020 imetenga kiasi cha shilingi milioni 412 kwa ajili ya ujenzi wa bwawa dogo la Orumwi lililoko Wilaya ya Siha litakalokuwa na mita za ujazo 58,000 na kutumika kuhifadhi maji ya kilimo cha umwagiliaji. Aidha, Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imekamilisha ukarabati wa miundombinu ya skimu ya umwagiliaji ya Soko iliyoko Wilaya ya Moshi Vijijini. Ukarabati huu ulihusisha kusakafia mifereji ambapo utapunguza upotevu mkubwa wa maji uliokuwa ukitokea kabla ya ukarabati huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kukarabati skimu mbalimbali za umwagiliaji zilizoko nchini kama zilivyoainishwa kwenye mpango kabambe wa umwagiliaji wa mwaka 2018 – 2035, ambapo skimu za umwagiliaji za Mkoa wa Kilimanjaro zitaendelezwa na kukarabatiwa kutokana na mipango hiyo. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-

Mradi wa umwagiliaji wa Karema ni wa muda mrefu toka umeanza:-

Je, ni lini mradi huo utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini, kama ifuayavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2009/2010 na mwaka 2011/2012 kupitia Mpango wa DADP Mradi wa Umwagiliaji wa Karema ulipatiwa fedha kiasi cha shilingi milioni 742,485,000 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya umwagiliaji ambapo fedha hizo zilitumika kwa ajili ya ujenzi wa banio, uchimbaji wa mifereji miwili yenye jumla ya urefu wa kilometa nne, ambapo mfereji namba moja ulichimbwa urefu wa mita 3,800 na mfereji namba mbili ulichimbwa mita 200, ujenzi wa tuta la kuzuia maji ya mafuriko lenye urefu wa mita 280, ujenzi wa Ofisi ya Kamati ya Umwagiliaji ya Mradi, ujenzi wa madaraja matatu ya kuvuka kwa miguu (Foot Bridges), ujenzi wa vivusha maji chini ya ardhi viwili, ujenzi wa mifereji katika mfereji namba mbili kwa mita 25 na ujenzi wa kivusha maji kwa juu chenye urefu wa mita 27.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ujenzi huo bado zilihitajika fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya mradi, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa bwawa, ujenzi wa banio la pili, kusakafia mfereji mkuu, kuchimba mifereji ya matoleo ya maji, kuchimba na kujenga mifereji ya mshambani, ujenzi wa vigawa maji vya mashambani na kujenga barabara za mashambani. Aidha, ujenzi huo ulisimama kutokana na kumalizika kwa programu ya kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya kwanza (ASDP I) iliyotekeleza mradi huo kupitia mipango ya maendeleo kilimo ya wilaya (DADPS) mwaka 2013/2014.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kumalizika kwa SDP I Serikali imefanya tathmini ya utekelezaji wa programu hiyo, ili kubaini ufanisi na changamoto kabla ya kuanza ujenzi wa miradi iliyobaki. Aidha, mradi huo utatekelezwa kupitia bajeti ya Serikali pamoja na ushirikiano wa wadau wa maendeleo na sekta binafsi katika mwaka 2020/2021 kupitia programu ya kuendeleza sekta ya kilimo Awamu ya II (ASDP
II) iliyoanza kutekelezwa tangu mwaka 2018/2019.
MHE. AZZA HILALY HAMAD aliuliza:-

Je, lini Serikali itachimba bwawa kwa ajili ya kuboresha Mradi wa Umwagiliaji Nyida.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Azza Hilaly Hamad Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza Mradi wa Kuendeleza Skimu za Umwagiliaji za Wakulima Wadogo ikiwa ni pamoja na Skimu ya Umwagiliaji ya Nyida. Katika kutekeleza Mradi huo, Kampuni ya Shekemu Construction Ltd. inafanya kazi ya ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya kuboresha mfumo wa usambazaji maji mashambani ambapo utekelezaji wa Mradi huu kulingana na Mkataba umefikia asilimia 68 ya kazi zote za ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia mwezi Disemba 2019 jumla ya Shilingi za Kitanzania 282,154,880.68 zimelipwa kwa Mkandarasi kati ya Shilingi za Kitanzania 466,594,981.81 zilizotengwa kwa ajili ya kuendeleza Skimu ya Nyida. Mradi huo kwa sasa umesimama kupisha msimu wa kilimo kwa wakulima na mvua zinazoendelea kunyesha. Hivyo, Mkandarasi ataendelea na kazi iliyobakia kulingana na Mkataba mara baada wakulima kuvuna mazao yao na msimu wa mvua kumalizika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mabadiliko ya tabianchi na mvua zisizotabirika pamoja na wakulima kuwa na mwamko mkubwa wa kilimo cha umwagiliaji kwa kutaka kuongeza tija na uzalishaji kwa kulima misimu miwili kwa mwaka; na kwa kuzingatia kuwa chanzo cha maji cha skimu hiyo ni Mto Manonga ambao ni wa msimu; na hivyo Serikali iliona umuhimu wa ujenzi wa Bwawa ili kuendeleza skimu hiyo.

Aidha, ili kutekeleza mradi huo, mwaka 2013 Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya ya Shinyanga na Nzega zilifanya Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa awali kwenye eneo linalokusudiwa kujengwa bwawa la Nyida eneo la Lyamalagwa litakalokuwa na uwezo wa kumwagilia maji mita za ujazo 4,167,825 kwa gharama ya shilingi bilioni 3.5 kwa wakati huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kutokana na mabadiliko ya kimuundo ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, na miradi mingi ya umwagiliaji kujengwa chini ya kiwango wakati huo, Serikali haikuweza kutekeleza mradi huo kwa wakati kutokana na kufanya tathmini ya kina ya ufanisi ya miradi hiyo na hivyo kushindwa kutekeleza mradi kwa wakati. Aidha, kwa kuwa muda mrefu umepita tangu tathmini hiyo ifanyike, Serikali itafanya mapitio upya ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili kupata mahitaji na gharama halisi ya ujenzi wa bwawa na athari zake kwa sasa na itaanza kujenga ujenzi wa bwawa hilo baada ya tathmini hiyo kukamilika.
MHE. ZAINABU MUSSA BAKARI aliuliza:-

Yamejitokeza maradhi katika mimea ya mipapai nchini ambayo yanahatarisha kupotea kwa mimea hiyo:-

(a) Je, Serikali imechukua hatua gani ya kuweza kudhibiti maradhi hayo?

(b) Je, kuna utafiti wowote uliofanywa juu ya maradhi hayo ili kugundua yanasababishwa na nini?

(c) Kama bado; je, Serikali haioni kuna hatari ya kupoteza mimea ambao ni muhimu sana?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zainabu Mussa Bakari, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imefanya utafiti na kugundua kuwa ugonjwa wa Ubwili unga ndio unaoathiri mipapai kwa kiwango kikubwa. Baada ya kugundulika ugonjwa huo, Wizara ya kilimo imechukua hatua za kuudhibiti kwa kutumia viuatilifu vyenye viambata vya croripynfos (udhibiti wa kwenye udongo), Profenophos na Dichlorovosch (udhibiti kwenye majani). Aidha, njia nyingine ya uthibiti ni kwa kutumia mbinu bora za kilimo (Cultural Control) kwa kupanda miche wakati wa kiangazi ili mimea isishambuliwe ikiwa michanga, kupalilia shamba kwa wakati na kung’olea miche iliyoathirika na utumiaji wa wadudu marafiki (Biological Control).

Vilevile Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu kufuata kanuni bora za kilimo ili kuepuka magonjwa mbalimbali yanayoweza kuathiri mimea ikiwemo mipapai.

(b) Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Kituo cha Utafiti cha TARI-Horti Tengeru imeendelea kufanya utafiti magonjwa na wadudu wanaoathiri mazao ya bustani ikiwemo mipapai. Utafiti huo umegundua kuwa ugonjwa wa Ubwili unga unaoathiri mipapai unaosababishwa na vimelea vya kuvu (fungus) vijulikanavyo kitaalam kama Oidium caricae papaya.

(c) Mheshimiwa Spika, mipapai haiwezi kupotea nchini kwa kuwa tayari njia za kudhibiti magonjwa na wadudu wanaoshambulia mimea hiyo zipo. Aidha, Wizara itaendelea kuwaelimisha wakulima na wadau mbalimbali juu ya udhibiti wa ugonjwa na wadudu wanaoshambulia mimea na mazao ikiwemo mipapai ili kuongeza uzalishaji na tija ya mazao hayo.
MHE. ZAYNAB M. VULU (K.n.y. MHE. MBARAKA K. DAU) aliuliza: -

Bei ya zao la nazi imekuwa ikishuka kwa kasi kubwa katika miezi ya hivi karibuni: -

(a) Je, ni zipi sababu za kushuka kwa bei ya zao hilo?

(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuokoa zao hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbaraka Kitwana Dau, Mbunge wa Mafia, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu za kushuka kwa bei ya zao la nazi ni pamoja na:-

Uwepo wa wanunuzi wachache wa nazi na hivyo kutokuwepo kwa bei ya ushindani ikilinganishwa na misimu iliyopita; kupanda kwa gharama za usafirishaji wa nazi kutoka Sh.2,800 miaka mitatu iliyopita na kufikia Sh.5,500 kwa gunia lenye nazi 200 mwaka 2019; kupungua kwa wanunuzi wakubwa wa viwanda vya mafuta ya nazi na bidhaa zake; kuongezeka kwa matumizi ya bidhaa mbadala za nazi kama vile mafuta ya kula ya mawese toka nje ya nchi na matumizi ya mafuta ya kupaka yasiyotokana na nazi; kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola na kushuka kwa mfumuko wa bei toka asilimia 11 kwa mwaka 2006 mpaka asilimia nne mwaka 2018/2019; kushuka kwa uzalishaji wa nazi nchini kutokana na magonjwa na mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo yamesababisha kupungua kwa uzalishaji wa nazi na kutowavutia wawekezaji wa ndani na nje kwa sekta ya viwanda vya kuchakata nazi kutokana na hofu ya kukosa malighafi ya kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inafanya jitihada za kuongeza wawekezaji katika zao la nazi kwa lengo la kumpatia mkulima soko la uhakika na bei nzuri. Jitihada hizo ni pamoja na kutoa elimu katika mnyororo wa thamani wa zao la nazi ikiwa ni pamoja na kuwapatia wakulima mashine za kukamua mafuta ya nazi. Hadi kufikia tarehe 30 Septemba, 2019, Vikundi vya Wajasiriamali vya Tujitegemee na Kaza Moyo vimepatiwa mashine zenye uwezo wa kukamua mafuta ya nazi lita 400 kwa siku ambapo lita moja huuzwa kati ya Sh.8,000 hadi Sh.10,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali inaendelea kutafuta masoko ya mazao yote ya kilimo likiwemo zao la nazi kwa kuwaunganisha wakulima na wanunuzi kupitia vikundi na vyama vya ushirika. Vilevile, Serikali inaendelea kuweka miundombinu ya usafiri kwa kuunda kivuko kitakachowezesha kuwaunganisha wananchi wa Mafia na sehemu zingine kwa usafiri kutoka Mafia hadi Nyamisati, Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti na hivyo kuwawezesha wakulima wa Mafia kusafiri na mizigo yao pamoja na nazi kwenda Dar es Salaam ambapo watauza kwa bei nzuri katika masoko makubwa.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:-

Kahawa ni miongoni mwa zao la Mkakati na Biashara lakini bei ya zao hilo imekuwa ya kusuasua:-

Je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha zao hilo linaongeza kipato cha Taifa kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Seba Bilakwate, Mbunge wa Jimbo la Kyerwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mikakati mbalimbali ya kuhakikisha zao la kahawa linapata soko la uhakika na lenye tija kwa wakulima. Mikakati hiyo ni pamoja na kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi bora ya pembejeo; Kuongeza uzalishaji kwa upanuzi wa mashamba ya wakulima; Kuzalisha miche bora ya kahawa yenye kuhimili ukame, magonjwa na wadudu ili kuongeza tija kwa wakulima; na Kuhamasisha matumizi ya kanuni bora za kilimo kupitia Maafisa Ugani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na mikakati hiyo, Serikali inaendelea kuboresha mifumo ya masoko ya mazao ya kilimo ikiwemo zao la kahawa kwa kufanya utafiti wa mahitaji ya soko, kuimarisha Vyama vya Ushirika, kusimamia mikataba baina ya wanunuzi na wakulima na kuhamasisha uzalishaji wa ufanisi wenye tija ili kuweza kupunguza gharama za uzalishaji na hivyo kuongeza kipato cha wakulima na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika msimu wa mwaka 2019/2020, mfumo wa mauzo ya kahawa moja kwa moja (direct export) umetumika katika mauzo ya kahawa katika Mkoa wa Kagera ikiwemo Jimbo la Kyerwa ambapo asilimia 72.92 ya kilo 22,000,000 ya kahawa yote iliyozalishwa katika Mkoa wa Kagera imeuzwa kwa mfumo huo. Aidha, mfumo wa minada katika kanda pia umetumika ikiwa ni pamoja na kuviwezesha Vyama vya Ushirika kuuza kahawa kwa mikataba mapema kabla ya mauzo halisi kufanyika. Hadi kufikia mwisho wa msimu wa 2018/2019 kiasi cha tani 66,646 za kahawa kiliuzwa ikiwa ni asilimia 102.86 ya makisio ya uzalishaji ya tani 65,000 na kuingizia Taifa Dola za Marekani milioni 123. Kati ya tani hizo zilizouzwa, tani 41,971 zimeuzwa kupitia minada ya kahawa na tani 24,575 zimeuzwa katika soko la moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inawahakikishia wakulima wa kahawa nchini kuwa mifumo ya mauzo ya kahawa moja kwa moja na minada ya kahawa katika Kanda za Mbeya na Songwe; Ruvuma na Njombe; Kagera na Moshi iliyotumika msimu wa 2019/2020, itaendelea kutumika nchini. Kutumika kwa mifumo hiyo kutasaidia kuongeza kipato cha wakulima na Taifa kwa ujumla.

Aidha, Serikali inavihimiza Vyama vya Ushirika na wakulima wa kahawa nchini kuzalisha kahawa kwa wingi yenye ubora kwa kuzingatia ubora unaokubalika sokoni ili wapate bei nzuri.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST (K.n.y. MHE. LUCIA M. MLOWE) aliuliza:-

Njombe ni kati ya Mikoa mikubwa ya Kilimo na ina mashamba darasa ambapo wanafunzi wa maeneo mengine wanakuja kujifunza:-

Je, ni lini Serikali itaanzisha Chuo cha Kilimo katika Mkoa wa Njombe?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lucia Michael Mlowe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua mchango wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ikiwemo Mkoa wa Njombe katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara. Kutokana na umuhimu huo Serikali ilianzisha vyuo vitatu vya Kilimo katika Nyanda za Juu Kusini ambayo Mkoa wa Njombe umo, ili kuzalisha wataalamu wa Ugani watakaotoa huduma za ushauri kwa wakulima katika mikoa hiyo. Vyuo hivyo ni MATI Uyole, Igurusi na Inyala vyenye uwezo wa kudahili wanafunzi takribani 700 kwa wakati mmoja. Hata hivyo, vyuo hivyo vinadahili wanafunzi chini ya uwezo kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo uchakavu wa miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilianzisha Chuo cha Wakulima cha Ichenga mkoani Njombe kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wakulima. Kwa sasa Serikali haina nia ya kuanzisha chuo kipya cha kilimo katika Mkoa wa Njombe wala kwenye kanda yoyote ile, badala yake Serikali ina mpango wa kuviboresha vyuo vya kilimo vilivyopo, kikiwemo Chuo cha Wakulima cha Ichenga kwa kuvikarabati na kuviwezesha kifedha, ili viweze kuchukua wanafunzi na wakulima kwa ajili ya mafunzo ya rejea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali itaendelea kushughulikia changamoto katika vyuo vya kilimo ili kufikia lengo la kuwa na wataalamu wa kilimo wa kutosha na hivyo kufanikisha mapinduzi ya kilimo hapa nchini. Vile vile, Serikali inafanya ukarabati kwa chuo cha MATI Inyala kwenye Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambapo Mkoa wa Njombe upo.
MHE. IGNAS A. MALOCHA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga mradi wa umwagiliaji uliopo katika Kata ya Ilemba ambao ulijengwa na wananchi na ukabomolewa na mvua msimu wa 2018/2019?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha, Mbunge wa Jimbo la Kwela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua na kuthamini juhudi zilizofanywa na wananchi kwa kujenga Mradi wa Umwagiliaji Ilemba ambao umekuwa ukibomolewa mara kwa mara na mvua za msimu na kurudisha nyuma jitihada za wananchi kujiletea maendeleo. Aidha, kwa kuzingatia umuhimu wa mradi huo kwa wananchi wa Jimbo la Kwela, Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji itatuma wataalam kufanya tathmini ili kuona sababu zinazosababisha miundombinu kubomolewa na kutafuta njia za kuondoa tatizo hilo.

Mheshimiwa Spika, Serikali itatafuta fedha na kuingiza katika mipango yake ya kibajeti baada ya taarifa ya tathmini ya wataalam hao kukamilika. Aidha, Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji itaendelea kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ili kuandika maandiko mbalimbali ya kuomba fedha kutoka taasisi za fedha, wadau wa maendeleo na Benki za Maendeleo na Biashara kwa ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta ya umma kupitia utaratibu wa Jenga, Endesha na Kabidhi ili kuweza kupata fedha za kukamilisha ujenzi wa Mradi wa Ilemba na hivyo kuwanufaisha wananchi wa Kata ya Ilemba na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla.
MHE. CECIL D. MWAMBE (K.n.y. MHE. SAED A. KUBENEA) aliuliza:-

Ni ukweli kwamba bei ya bidhaa za Viwandani kwa kiwango kikubwa zinatokana na gharama za uzalishaji kama vile maji, umeme, nguvu kazi na kadhalika:-

Je, kitendo cha kutoa kibali kwa Viwanda vya Sukari kuagiza sukari kutoka nje, siyo kuua kabisa Kilimo cha zao la miwa ambacho wakulima wanategemea kuuza kwenye viwanda vya ndani?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, Mbunge wa Jimbo la Ubungo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Bodi ya Sukari imeakuwa ikifanya tathmini ya mahitaji ya sukari nchini kwa mwaka na kwa kuzingatia matumizi ya kawaida na matumizi ya viwandani. Aidha, tathmini hiyo hufanyika sambamba na kujua uwezo wa viwanda vya kuzalisha sukari hapa nchini ambapo nakisi kati ya uzalishaji na mahitaji ndiyo kiasi cha sukari inayohitajika kuagizwa kutoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, tathmini ya mahitaji ya sukari kwa miaka miwili iliyopita, yaani 2017/2018 na 2018/2019 ilibaini kuwepo na utengamano wa soko la ndani kwa bei na upatikanaji wa sukari nchini. Aidha, utengamano huo ni matokeo ya maamuzi ya Serikali ya kutumia mfumo wa kuwapa leseni wazalishaji wa ndani kuagiza sukari kutokana na mahitaji badala ya mfumo wa kutumia wafanyabiashara kuagiza sukari toka nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, mfumo huo umeweza kudhibiti uingizaji wa sukari ya ziada nchini kwani wazalishaji huagiza kuliangana na kiasi kilichoainishwa kwenye leseni husika. Aidha, kabla ya utaratibu wa kuwapata vibali wenye viwanda kuagiza sukari, nakisi ya sukari (Gap Sugar) ilikuwa ni zaidi ya tani 130,000 nchini, lakini baada ya utaratibu wa kuwapa wenye viwanda kuagiza, upungufu umepungua hadi kufikia tani 38,000.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho uzalishaji wa miwa kwa wazalishaji wadogo umeongezeka kutoka tani 568,083 msimu wa 2017/2018 hadi tani 708,460 msimu wa 2018/ 2019. Ongezeko la uzalishaji wa miwa kwa wakulima madogo limekwenda sambamba na ongezeko la kipato cha mkulima ambapo mapato ghafi kwa wakulima wa Kilombero, kwa mfano wakulima wa Kilombero yamefikia thamani ya shilingi bilioni 68.7 msimu wa 2018/2019 kutoka shilingi bilioni 48.1 misimu wa 2017/2018.

Aidha, kutokana na ongezeko la uzalishaji wa miwa kwa wakulima wadogo, uzalishaji wa sukari nchini umeongezeka kwa asilimia 16.8 kutoka wastani wa tani 307,431.26 hadi tani 359,219.25 katika msimu wa 2018/2019 wa kilimo.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-

Wakulima wa vitunguu saumu wanayo changamoto ya soko la kuuzia zao hilo:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutafuta soko la vitunguu saumu nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, vitunguu saumu vinavyozalishwa nchini hutumika ndani ya nchi na vilevile huuzwa nje ya nchi vikiwa ghafi. Aidha, baadhi ya mataifa ambayo hununua vitunguu saumu vinavyozalishwa nchini ni Shelisheli, Visiwa vya Comoro, Msumbiji, Zambia, Mauritania, Kenya, Uganda na Falme za Kiarabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa mazao ya kilimo ikiwemo vitunguu swaumu, Serikali inakamilisha upatikanaji wa simbomilia (barcode) na kiwango cha ubora wa bidhaa zinazotokana na vitunguu saumu kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Aidha, Wizara imeanzisha Kitengo cha Masoko chenye jukumu la kutafuata mahitaji ya masoko ya wakulima ndani na nje ya nchi ikiwemo vitunguu swaumu kwa kufahamu kiwango kinachohitajika, ubora, bei na muda wa unaohitajika sokoni wa mazao na bidhaa hizo sokoni ili kutoa taarifa kwa wakulima na hivyo kuzalisha mazao yanayokidhi mahitaji ya soko.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) ilivijengea uwezo vikundi vya wakulima katika Bonde la Bashay na kuwawezesha kusindika vitunguu saumu na kuwa katika bidhaa mbalimbali zikiwemo mafuta na unga wa vitunguu saumu. Jitihada hizo zimesaidia kuongeza thamani ya zao la vitunguu saumu muda wa kuhifadhi bila kuharibika ubora wake na kuimarisha soko la bidhaa hiyo ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima na wasindikaji wa vitunguu saumu wa Mbulu huwezeshwa kushirki Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam kila mwaka ili kutangaza na kutafuta masoko ya viunguu saumu na bidhaa zake ndani na nje ya nchi. Serikali kwa kushirikiana na Asasi Isiyo ya Kiserikali ya Global Communities iliandaa Kongamano la Vitunguu Saumu lililofanyika katika Bonde la Bashay tarehe 16 Aprili, 2019 katika AMCOS ya DIDIHAMA ambapo wafanyabiashara kutoka sehemu mbalimbali za nchi walialikwa lengo likiwa ni kutafuta soko la vitunguu saumu.

Aidha, Serikali inaendelea kudhibiti uuzaji holela wa vitunguu saumu kwa kutumia magunia ya lumbesa, mabeseni na ndoo ili mizani itumike katika minada ambayo hufanyika katika ghala la vitunguu saumu Bashay Wilayani Mbulu na hivyo kuratibu soko na bei ili kumnufaisha mkulima. (Makofi)
MHE. SALUM MWINYI REHANI Aliuliza:-

Dawa ya Sulphur ndiyo dawa ya udhibiti wa fungue (fangi) kwenye mazao ya korosho na mazao mengine, na Serikali imeunda mfumo wa kuagiza dawa hii ya kupuliza kwa njia bubu procurement; na mwaka jana baadhi ya wakulima waliathirika kwa kuchelewa na kupata dawa feki.

(a) Je, ni lini Serikali itakuwa tayari kuleta dawa mbadala ambazo ni rahisi zaidi?

(b) Je, ni lini Serikali itakaa na Vyama vya Msingi ili kupanga ratiba ya kuagiza na kuleta dawa na kupiga na pia kuzuia dawa za msimu uliopita?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) Alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Salum Mwinyi Rehani, Mbunge wa Uzini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haijaanzisha mfumo bubu wa ununuzi wa Salfa. Zao la korosho huathiriwa na magonjwa aina mbalimbali yakiwemo yale yanayosabishwa na fungue. Miongoni mwa magonjwa tishio kwa zao hili ni Ubwiriunga, Blaiti, Chule na Mnyauko fusari. Hata hivyo, magonjwa hayo yamekwisha kupatiwa tiba isipokuwa mnyauko fusari. Serikali inaendelea na tafiti kupitia taasisi zake ili kupata kinga na tiba stahiki za magonjwa na wadudu wanaoshambulia zao la korosho hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, salfa ni miongoni mwa viuatilifu vinavyotumika kwa kinga na tiba ya ugonjwa wa Ubwiriunga. Serikali inakusudia kuandaa mfumo wa pamoja wa ununuzi wa viuatilifu kwa ajili ya matumizi ya msimu wa 2020/2021 ambapo viuatilifu vingine kwa ugonjwa huo ambavyo ni triadimenol, hexaconazole, tebuconazole na vinginevyo. Hata hivyo, Serikali itaendelea kuhimiza matumizi ya salfa kwa kuwa kiuatilifu hiki hakiitaji ujuzi mwingi wakati wa kukitumia shambani kwa kuwa kimezoeleka na vilevile hakiingii ndani ya mmea na hivyo kufanya korosho inayozalishwa kuwa na sifa ya kilimo hai (Organic Cashew Nut).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Bodi ya Korosho itendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Vyama vya Msingi vya Ushirika katika kutathmini mahitaji ya viuatilifu na ratiba ya uagizaji wa viuatilifu hivyo. Aidha, Serikali kupitia TPRI itaongeza udhibiti katika ukaguzi wa viuatilifu nchini ili kuviondoa sokoni viuatilifu visivyo na sifa.
MHE. MARTIN M. MSUHA aliuliza:-

Tangu uhuru Wilaya ya Mbinga imekuwa ikitegemea zao moja la biashara ambalo ni kahawa:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka zao lingine la biashara Wilayani humo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Martin Mtonda Msuha, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya utafiti wa afya na tabaka la udongo katika kanda saba za kilimo zenye kuwezesha uzalishaji wa mazao mbalimbali kulingana na ikolojia ya kanda husika. Kanda hizo za kiikolojia ni pamoja na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini inayohusisha Wilaya ya Mbinga na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na utafiti huo, Serikali imeandaa mwongozo wa uzalishaji wa mazao kwa kuzingatia ikolojia ambapo Mkoa wa Ruvuma una fursa kubwa ya kuzalisha mazao mengine ya biashara tofauti na kahawa ikiwemo mazao ya korosho, muhogo, alizeti, ufuta na matunda yanayostawi katika ukanda wa baridi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima katika Halmashauri ya Mbinga wamehamasishwa na wameanza uzalishaji wa kibiashara wa mazao ya korosho, alizeti, ufuta, soya, parachichi, miwa, tumbaku pamoja na mazao mapya kama macadamia. Aidha, Serikali inaendelea kusimamia uendelezaji wa mazao kwa kuhamasisha matumizi ya teknolojia bora katika mnyororo wa thamani, kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika kilimo pamoja na kuimarisha ushirika na mifumo ya masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika msimu wa mwaka 2016/2017, Serikali kupitia Bodi ya Korosho ilitoa mafunzo ya uzalishaji wa miche bora ya korosho kwa vikundi sita vya wakulima vya Jembe Halimtupi Mtu group, Chapakazi Group, Twiga Group, Juhudi Group, Kiboko Group na Koroshomali Group ambapo kwa pamoja vilizalisha jumla ya miche bora 111,336 na kuisambaza kwa wakulima kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa zao hilo. Aidha, msimu wa mwaka 2018/2019, jumla ya hekta 29,374.6 zilipandwa mazao ya biashara katika Wilaya ya Mbinga ambapo kati ya hizo, hekta 265 zilitumika kuzalisha zao la korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika msimu wa 2018/2019, eneo la hekta 806 zilitumika kuzalisha zao la soya, hekta 317 zao la alizeti, hekta 240 ufuta, hekta 32 miwa na hekta 89.5 ni parachichi. Uzalishaji wa zao la soya umeongezeka kutoka tani 42.6 msimu wa mwaka 2017/2018 hadi kufikia tani 403 msimu wa mwaka 2018/2019. Aidha, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga inayo ikolojia inayoruhusu uzalishaji wa mazao mengi ya biashara, Serikali itaendelea kuimarisha huduma za ugani ili mazao hayo yazalishwe kwa wingi na tija.
MHE. ZAYNABU M. VULLU aliuliza:-

Zao la nazi ni zao ambalo pia lina faida nyingi sana kuanzia mti, matawi, na nazi yenyewe:-

(a) Je, ni lini Serikali itatafuta soko la kudumu la zao hilo?

(b) Je, Serikali ina mpango wa kuhamasisha kilimo cha zao hilo kama ilivyokuwa zamani?
NAIBU WAZIRI WAKILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zaynabu Matitu Vulu, Mbunge Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, soko la kudumu la zao la nazi lipo nchini kwa sababu kiasi cha nazi kinachozalishwa bado hakikidhi mahitaji ya soko la ndani la nchi kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya zao hilo ikiwemo ulaji wa madafu na watumiaji wa nazi. Aidha, mafuta mwali yanayotokana na nazi yanaendelea kupata umaarufu kutokana na uhitaji wake kuwa mkubwa ndani na nje ya nchi ambayo lita moja inafikia hadi shilingi 40,000. Bidhaa kama fagio, mbao, ka mbao na samani zinazotokana na mti wa mnazi na uwezo wa zao hilo kutunza mazingira huongeza thamani ya zao la minazi.

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha soko la zao la nazi nchini msimu wa mwaka 2018/2019 wakulima wapatao 74 katika Mikoa ya Lindi na Mtwara wamefundishwa namna ya kukamua mafuta mwali. Vilevile, kikundi cha wanachama 50 katika Wilaya ya Bagamoyo kimepewa mashine yenye uwezo wa kukamua lita 500 za mafuta ya mwali kwa mwaka. Aidha, Serikali inaendelea kuimarisha masoko ya mazao yote ya kilimo likiwemo zao la nazi kwa kuwaunganisha wakulima na wanunuzi kupitia vyama vyao ushirika, masoko ya moja kwa moja na viwanda vidogo vya kuongeza thamani ya zao la nazi.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wazalishaji wa zao la nazi kuendelea kupanda mbegu bora zenye ukinzani dhidi ya magonjwa na zenye tija kubwa. Tanzania ni nchi ya 10 Duniani kwa uzalishji wa nazi ikiongozwa na nchi ya Indonesia na kwa Afrika ni nchi ya kwanza ambapo huzalisha wastani wa tani 530,000 za nazi kwa mwaka, ikifuatiwa na Ghana ambayo huzalisha wastani wa tani 366,183.

Mheshimiwa Spika, pia Serikali inaendelea kuhamasisha kilimo cha minazi nchini ambapo imeanzisha shamba lenye ukubwa wa hekta 54 katika kituo kidogo cha utafiti cha Mbezi Wilaya ya Bagamoyo ili kuzalisha miche bora ya minazi yenye ukinzani dhidi ya ugonjwa wa kunyong’onyea kwa minazi (Coconut Lethal Disease) na kuisambaza kwa wakulima kwa gharama nafuu.

Mheshimiwa Spika, Serikali inahamasisha kilimo cha minazi katika maeneo mapya ili kuongeza uzalishaji wa nazi nchini ambapo msimu wa 2018/2019 ilizalisha na kusambaza jumla ya mbegu ya miche 11,000 kwa wakulima katika Mikoa ya Rukwa na Mwanza. Aidha, Serikali inafanya mazungumzo ya Jumuiya ya Asia – Pacific Coconut Community) ambayo hutunza ‘‘germplasm” ya minazi kuwezesha upatikanaji wa mbegu bora za minazi zenye kuongeza tija na uzalishaji mkubwa kwa wakulima. (Makofi)
MHE. PAULINE P. GEKUL aliuliza:-

Je, ni lini Shamba la Singu Estate litarudishwa kwa wananchi wa Kata ya Sigino kama alivyoahidi Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati alipofanya ziara katika Jimbo la Babati Mjini mwaka 2017?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pauline Philipo Gekul, Mbunge wa Babati Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Shamba la Singu namba 679 lenye Hati namba 11837 ambalo ukubwa wake ni hekta 1,260 sawa na ekari 3,080 lipo kilomita tano kutoka Mji wa Babati Mkoani Manyara linamilikiwa na Kampuni ya Agric. Evolution (T) Co. Ltd. Mnamo mwaka 2004 Mji wa Babati ulipandishwa hadhi na kuwa Halmashauri ya Mji, hatua iliyopelekea kubadilika kwa Sheria za uendeshaji wa Mamlaka hiyo na pia kuanzisha mchakato wa kubadilishwa kwa shamba hili kutoka matumizi ya kilimo na kuwa na matumizi mbalimbali ya kimji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria zilizotumika katika mchakato wa kubadilisha matumizi ya shamba la Singu zilimlazimu mmiliki wa shamba hilo kurejesha hati ya umiliki wa shamba ili liweze kubadilishwa kuwa na matumizi mbalimbali ya ardhi ya jumla. Baada ya hati hiyo kurejeshwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi iliridhia mabadiliko hayo na kupitisha rasmi mpango wa kina wa matumizi ya ardhi katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, makubaliano yaliyofanyika kati ya mwenye shamba, Halmashauri ya Mji na wananchi wa kijiji cha Singu ni kama ifuatavyo; kijiji kipatiwe ekari 50 kwa ajili ya huduma za jamii kama vile shule, zahanati na kadhalika ili ziwanufaishe wananchi wa Singu. Wananchi waliokuwa wamejenga ndani ya eneo la ekari 200 kwenye shamba hilo wasitolewe bali wapimiwe na kumilikishwa viwanja katika maeneo waliyojenga.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara aliyoifanya katika Kijiji cha Singu mwezi Agosti mwaka 2017, wananchi na uongozi wa kijiji kwa ujumla wao waliweza kuridhia uendelezaji wa eneo hilo kimji ili waweze kunufaika na huduma zitakazopatikana na kwamba wananchi wa Singu watapewa kipaumbele katika ugawaji wa viwanja hivyo. Kuanzia mwaka 2017 hadi sasa mambo yafuatayo yamefanyika;

(i) Umeandaliwa mpango kabambe wa mji kwa miaka 20 ijayo ambapo Singu ilipangwa kama mji wa pembezoni;

(ii) Umeandaliwa upangaji wa kina;

(iii) Upimaji wa viwanja umefanyika;

(iv) Utengenezaji wa barabara katika eneo la mradi umefanyika na;

(v) Juhudi za usuluhishi wa mgogoro kati ya Mwekezaji na wananchi wa Singu zimefanyika kupitia uongozi wa mkoa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na muafaka kupatikana na wananchi kupewa zaidi ya ekari 800 na kumilikishwa maeneo yao kisheria.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO aliuliza:-

Serikali ilivunja Bodi ya Korosho na majukumu yake sasa yanatekelezwa na Bodi ya Mazao mchanganyiko:-

Je, ni lini Serikali itachukua hatua ya kuunda tena Bodi ya Korosho na kuiwezesha kutekeleza majukumu yake kama ilivyo kwa mazao mengine?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sikudhani Yassini Chikambo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Bodi ya Korosho Tanzania imeanzishwa chini ya Kifungu cha 3(1) cha Sheria ya Tasnia ya Korosho Na. 18 ya Mwaka 2009. Majukumu ya Bodi ya Korosho ni kusimamia na kuratibu uendeshaji wa tasnia ya korosho nchini ikiwa ni pamoja na uzalishaji, usindikaji na biashara ya korosho. Aidha, Serikali kupitia Waziri wa Kilimo kwa mujibu wa Kifungu cha 8 cha Sheria ya Tasnia ya Korosho kutoa maelekezo na mwongozo maalum kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa tasnia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alitengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Korosho na kuivunja Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi tarehe 10 Novemba, 2018 kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho ambaye ndiye Mtendaji Mkuu wa Bodi aliondolewa katika nafasi yake tarehe 26 Oktoba, 2018.

Mheshimiwa Naibu Spika, si kweli kwamba Serikali ilivunja Bodi ya Korosho na majukumu yake kutekelezwa na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko. Bodi ya Nafaka ilianzishwa kwa Sheria Na. 19 ya Mwaka 2009 na inaendelea kutekeleza majukumu yake ya Kisheria ambayo ni pamoja na kufanya biashara ya kununua na kuuza nafaka na mazao mengine ndani na nje ya nchi ambapo imepewa jukumu maalum la kununua korosho. Mnamo tarehe 15 Aprili, 2019 Waziri wa Kilimo alimteua Kaimu Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Korosho na Wajumbe wa Bodi nane (8) wameshateuliwa kwa kipindi cha miaka mitatu. Bodi hiyo, inakamilisha muundo wake baada ya Mwenyekiti wake kuteuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inakamilisha kuunda upya Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania. Uteuzi wa Wajumbe utatangazwa na Mamlaka za uteuzi muda mfupi ujao kwa mujibu wa Katiba, Sheria na Kanuni zilizopo.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-

Eneo la mbuga linalozunguka Mji wa Itigi linafaa sana kwa kilimo cha mazao mbalimbali kama mahindi, alizeti, choroko na dengu, lakini eneo hili linajaa maji na kufanya kilimo kuwa kigumu. Je, Serikali ipo tayari kusaidia wananchi wanaolima katika eneo hilo kwa kuwajengea mifereji ya kuongoza maji yasiingie mashambani?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, eneo la mbuga linalozunguka Mji wa Itigi limekuwa likijaa maji pale mvua zinapokuwa juu ya wastani ambapo historia inaonesha kuwa bonde hili lilijaa maji kipindi cha mwaka 1997/1998 wakati wa mvua za Elnino na katika msimu wa 2015/2016 baada ya miaka tisa tangu wakati wa mvua za Elnino mwaka 1997/1998.

Mheshimiwa Spika, Serikali inalichukua suala la Mheshimiwa Mbunge na itatuma wataalam wa kilimo na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa ajili ya kwenda kufanya utafiti na tathmini ya kina ya maji kujaa kwenye mashamba ya wakulima. Utafiti na tathmini hiyo itakapokamilika tutakuja na mikakati na mapendekezo stahiki yatakayosaidia kutatua changamoto ya kujaa maji mashambani na kuwasaidia wakulima wa eneo la mbuga linalozunguka Mji wa Itigi ili kuongeza uzalishaji na tija kwa wakulima hao.
MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:-

Mabwawa ya Mesaga, Nyamitita na Bugerera katika Wilaya ya Serengeti yalikuwa kwenye mchakato wa kujengwa kwa ajili ya umwagiliaji:-

Je, mchakato umefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha, Mbunge wa Jimbo la Serengeti, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa umwagiliaji Mesaga ulisanifiwa mwaka 2004 kwa ajili ya ujenzi wa bwawa na miundombinu ya shambani. Hata hivyo, fedha za ujenzi zilianza kupatikana mwaka 2014 na 2015 ambapo mradi ulipokea shilingi milioni 200 na shilingi milioni 198 mtawalia. Fedha hizo kwa pamoja zilitumika kuanza ujenzi wa utoro wa maji (spill way) kwa kuwa hazikutosha kuanza ujenzi wa tuta la bwawa na ujenzi wa mifereji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na changamoto ya fidia katika eneo hilo, Serikali imetoa maelekezo kwa uongozi wa wilaya kutatua mgogoro wa fidia kwa kupitia na kuhuisha gharama za mradi huo ili ziendane na wakati. Aidha, Serikali itashirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kuandaa andiko jipya la mradi kwa ajili ya kutafuta fedha za kukamilisha mradi huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa Nyamitita ulitekelezwa mwaka 2013 na unahusisha banio na mifereji ya umwagiliaji. Mradi huo unafanya kazi ingawa haujakamilika kutokana na ufinyu wa bajeti ambapo katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 217 ili kuendeleza ujenzi wa mradi huo na hivyo kuwanufaisha wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa umwagiliaji Bugerera unahusisha bwawa dogo la miundombinu inayoweza kumwagilia hekta 5 tu. Mwaka 2010, Serikali ilifanya upimaji na usanifu kwa ajili ya kuongeza ukubwa wa bwawa na kuongeza shamba la umwagiliaji hadi kufikia hekta 80. Aidha, Serikali itaendelea kutafuta fedha ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha mabwawa ya Mesaga, Nyamitita na Bugerera yanajengwa na kuwanufaisha wananchi wa Serengeti na Taifa kwa ujumla.
MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. ANTONY C. KOMU) aliuliza:-

Shamba la miwa la TPC lina eneo lenye ukubwa wa zaidi ya hekta 6,000 ambalo halifai kwa kilimo cha miwa lakini zipo taarifa kiuwa wawekezaji wanataka kulitumia eneo hilo kuanzisha hifadhi ya wanyamapori:-

(a) Je, ni kwa nini Serikali inaruhusu mwekezaji huyo kuanzisha mradi tofauti kabisa?

(b) Je, ni kwa nini Serikali isitoe eneo hilo kwa wananchi wanaozunguka shamba hilo kwa ajili ya malisho ya mifugo yao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anthony Calist Komu, Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, lenye sehemu (a) na (b), kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kampuni ya TPC ina takribani hekta 13,000 ambapo hekta 8,500 zimeendelezwa kwa kilimo cha miwa na eneo hekta 4,500 ambazo zipo kusini mwa Kiwanda cha TPC katika Vijiji vya Mawala na Mikocheni halina udongo wa kuwezesha kilimo cha miwa ya sukari kutokana na hali ya udongo kuwa na magadi. Tangu mwaka 1936 ambapo shamba hilo lilikuwa linamilikiwa na Serikali kabla ya ubinafsishwaji, eneo hilo la hekta 4,500 halikuwahi kulimwa zao lolote. Aidha, eneo hilo lilikuwa ni korido ya wanyamapori waliokuwa wakihama kutoka Tarangire kupitia Msitu wa Tembo kwenda hadi Ziwa Jipe. Ilipofika mwaka 2014 Serikali iliipatia Kampuni ya TPC leseni Na.1 ya kuanzisha shamba la wanyamapori (Certificate of Game Ranching) baada ya kukubali maoni ya TPC.

Mheshimiwa Spika, kutokana na maendeleo ya kazi za binadamu katika vijiji vilivyopo Kata ya Msitu wa Tembo wilaya ya Simanjiro, Vijiji vya Kahe, Mawala, Chemchem na Mikocheni Wilaya ya Moshi Vijijini vimesababisha korido hizo kuvunjika na wanyama kuendelea kuwepo katika maeneo hayo. Kwa hali hiyo, ili kuzuia uharibifu wa misitu na uwindaji holela wa wanyamapori, kiwanda cha TPC kilipewa leseni ya eneo hilo kwa ajili ya kuendeleza hifadhi ya mazingira ikiwemo misitu pamoja na wanyamapori waliomo katika eneo hilo. Aidha, ikumbukwe kwamba uamuzi huo wa Serikali ulizingatia umuhimu wa hifadhi ya maliasili iliyoko katika eneo hilo, pamoja na ukweli kuwa udongo katika eneo hilo usingeweza kutumika kwa kilimo hata kama sehemu hiyo ingekabidhiwa kwa wenyeji wa vijiji vinavyozunguka eneo hilo.