Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Additional Questions to the Prime Minister from Hon. Omary Tebweta Mgumba (1 total)

MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Kuna swali dogo tu la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa majibu mazuri ambayo kutoka Serikalini.

Swali dogo la tu la nyongeza, kwa kuwa kama ulivyosema kwenye majibu yako ya msingi, kwamba mmegundua kuna watu ambao wameleta madai ambayo si sahihi, lakini naamini pia kuna watu ambao watakuwa madai yao ni sahihi. Sasa nini kauli ya Serikali kwa wale ambao madai yao ni sahihi ambao wamekaa muda mrefu kiasi kwamba imewaongezea gharama kwa maana ya riba sehemu walizokopa, nani atalipa gharama hizi kwa ajili ya usumbufu uliotokea na gharama zilizoongezeka kwenye madeni hayo?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mgumba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimeeleza kwenye jibu la awali kwamba kwanza tunathamini sana kazi waliyoifanya katika kutoa huduma kwenye sekta zetu. Lakini mbili, tumewashukuru kwa uvumilivu kwa kipindi chote hiki ambacho sisi tunafanya uhakiki. Baadhi ya wadai nimepata nafasio ya kukutana nao hapa Dodoma wakati huu wa Bunge na kuzungumza nao na kuwaambia kwa nini tumechelewa kuwapa fedha zao, wale ambao kweli wana madai halali.

Mheshimiwa Spika, lakini bado nirudi tena kusema kwamba, hatuna namna nyingine ya kufanya zaidi ya uchelewaji huu wa kulipa kwa sababu tuko kwenye zoezi la kuhakiki, ili tujiridhishe. Kama ingekuwa tumechelewa tu, kwamba hatuna kazi yoyote, tumeacha tu hapo kungekuwa na swali ambalo naamini unacholenga kingeweza kupata maelezo. Lakini bado niwahakikishie kwamba taratibu zinakamilika na tulisema tunakamilisha tarehe 30 Juni, yaani kesho tu tarehe 30 Juni, tunatarajia Wizara ya Fedha itapewa taarifa kutoka kwenye Wizara mbalimbali, kwamba madai yetu halali ni haya kwa ajili ya watu hawa kwa huduma waliyoitoa, baada ya hapo tunalipa tu na tutaendelea kuwapa nafasi zaidi ya kutoa huduma.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niwahakikishie kwamba wataendelea kutoa huduma, hasa wale ambao ni waaminifu kwenye awamu ijayo hii ya mwaka wa fedha mpya wa mwaka 2017/2018.