Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Prosper Joseph Mbena (13 total)

Watoto wengi nchini wameendelea kudhalilishwa kwa kukosa malezi bora ya wazazi wao hali inayosababisha waishi maisha ya kuombaomba na kwa kuwa baadhi ya wazazi wanaosababisha hali hiyo ni wanaume wanaoharibu maisha ya wasichana kwa kuwapa mimba na kukwepa jukumu la kulea watoto wanapozaliwa.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwabaini wanaume hawa na kuwafikisha mahakamani kwa kosa la kuwatelekeza watoto na kuwasababishia mateso na kuwanyima haki zao za msingi?
(b) Je, ni lini Serikali italeta Bungeni muswada wa kufanya marekebisho katika sheria husika ili kuwashughulikia wazazi wanaowatelekeza watoto wao kwa kutowahudumia ipasavyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prosper Joseph Mbena, Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini, lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mipango mbalimbali ya kuwababini wanaume wanaotelekeza familia na vitendo vingine vya unyanyasaji. Mipango hiyo ni pamoja na Mpango wa Muitikio wa Kitaifa wa Kuzuia Ukatili Dhidi ya Watoto wa mwaka 2013 hadi 2016 na Mpango wa Kuzuia Ukatili Dhidi ya Wanawake wa mwaka 2005 – 2015. Mipango hiyo hivi sasa inaunganishwa kuwa mpango mmoja wa Kitaifa ili uweze kukidhi haja za upatikanaji wa taarifa zinazohusu ukatili dhidi ya watoto na wanawake ikiwemo utelekezaji wa familia. Kupitia mpango huu, Serikali itahamasisha jamii kuibua vitendo vya ukatili ikiwa ni pamoja na kuwabaini wahusika na vitendo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara yangu imeanzisha mtandao maalum wa mawasiliano kwa ajili ya kutoa taarifa mbalimbali za ukatili dhidi ya watoto (the child helpline number 116) ambapo mtoto mwenyewe au mtu mwingine kwa niaba ya mtoto huweza kuripoti tukio lolote la ukatili dhidi ya watoto. Vilevile, Wizara inatekeleza Mpango wa Ulinzi na Usalama wa Mtoto wa mwaka 2013 – 2017 na kupitia mipango hii jamii zimekuwa zikielimishwa masuala mbalimbali yanayohusu ukatili, unyanyasaji na mazingira hatarishi kwa watoto na wanawake ili waweze kutoa taarifa ya matukio hayo yanapotokea na kuwabaini wahusika ili kuchukuliwa hatua stahiki.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009 imezingatia suala zima la utoaji wa malezi, matunzo na ulinzi kwa kutoa majukumu kwa wazazi, walezi, jamii pamoja na Serikali. Aidha, kifungu cha 14 cha sheria hiyo kimeweka adhabu kwa wazazi au walezi watakaokiuka kutoa malezi bora kwa kulipa faini ya shilingi milioni tano za kitanzania au kifungo cha miezi sita au vyote kwa pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haijapokea changamoto yoyote inayohitaji marekebisho kuhusu utekelezaji wa kifungu hiki cha sheria.
MHE. PROSPER J. MBENA aliuliza:-
Ujenzi wa barabara ya kutoka Bigwa - Kisaki upo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM na fedha za ujenzi zitatoka kwenye mpango wa MCC II au Serikalini na nyumba zote zilizomo ndani ya mita 60 zimewekwa alama „X’ tayari kubomolewa katika maeneo ya Ruvu, Kibangile, Kisemu, Mtamba, Nzasa, Kangazi, Kisanzela, Tambau, Mvuha na Magazi hadi Kisaki:-
(a) Je, Serikali itakuwa tayari kuwawekea wananchi hao utaratibu wa kuwajengea nyumba bora ili kuachana na utaratibu wa kuwalipa fidia kidogo isiyolingana na mali zao wanazoziacha?
(b) Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza ili wananchi waliowekewa alama ya kubomolewa nyumba zao waanze maandalizi ya maeneo ya kuhamia?
(c) Je, ni lini Serikali itatengeneza upya madaraja ya Ruvu, Mvuha na Dutuni yaliyomo kwenye barabara hiyo hasa ikizingatiwa kuwa madaraja hayo ni mabovu sana na yamedidimia na yanaweza kusababisha ajali kwa wanaopita hapo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Prosper Joseph Mbena, Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza utekelezaji wa mradi huu wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Bigwa hadi Kisaki kwa kuanza na kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa sehemu ya barabara ya Bigwa hadi Mvuha ambapo ni kilomita 78 uliokwishaanza baada ya kusaini mkataba wa Mhandisi Mshauri, Unitec Civil Consultants Ltd. wa Dar es Salaam akishirikiana na Mult-Tech Consultant (Pty) Ltd. wa Gaberone Botswana kwa gharama ya Sh. 713,471,140,000/=. Mkataba wa kazi hii ulisainiwa tarehe 9 Septemba, 2014 na utatarajia kukamilika tarehe 30 Juni, 2016. Aidha, upembuzi yakinifu na usanifu huo utajumuisha pia madaraja ya Ruvu, Mvuha na madaraja mengine yote yaliyoko kwenye sehemu ya barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, mara baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, ujenzi wa sehemu ya barabara ukijumuisha madaraja ya Ruvu na Mvuha yaliyoko katika sehemu ya barabara hii yatajengwa kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, usanifu wa daraja la Dutuni ulikishwafanyika na kukamilika mnamo Septemba, 2014. Hata hivyo, ujenzi wa daraja jipya haujaanza kutokana na ufinyu wa bajeti. Wakala wa Barabara Mkoa wa Morogoro utaendelea kuyafanyia matengenezo stahiki madaraja haya ili yaendelee kutumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu fidia, Serikali haina mpango wa kuwajengea nyumba wananchi waliowekewa alama ya „X’ na ambao nyumba zao zitahitajika kubomolewa ili kupisha ujenzi wa barabara mpya. Fidia ya fedha italipwa moja kwa moja kwa kila mwananchi anayestahili fidia kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Na.13 ya mwaka 2007 na Kanuni zake za mwaka 2009.
MHE. PROSPER J. MBENA aliuliza:-
Wananchi wa Wilaya ya Morogoro Vijijini kwa muda mrefu wamekuwa wakikosa huduma nzuri za matibabu katika hospitali ya Wilaya kama vile X-Ray, MRI, TSCAN dawa za kutosha, Madaktari Bingwa na Wauguzi kwa sababu tu Wilaya na Halmashauri yake zimechelewa kuhamia Mvuha suala ambalo Ofisi ya Rais, TAMISEMI inalishughulikia:-
(a) Je, Serikali itakuwa tayari kuanza kujenga Hospitali ya Wilaya Mvuha mahali ambapo ndipo patakapojengwa Makao Makuu ya Wilaya?
(b) Je, Serikali kwa sasa iko tayari kukiteua Kituo cha Afya cha Lukange ambacho ni bora sana kimejengwa na Kanisa Katoliki na kukikabidhi kitoe huduma kwa wananchi kama Hospitali Teule ya Wilaya ya Morogoro Kusini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prosper Joseph Mbena, Mbunge wa Morogoro Kusini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, tayari Halmashauri imetenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya katika eneo la Mvuha yatakapohamia Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro. Halmashauri inashauriwa kuweka katika vipaumbele vyake na kutenga bajeti katika mwaka wa fedha 2017/2018 ili kuanza ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inakubaliana na wazo la kukifanya Kituo cha Afya Lukange kuwa Hospitali Teule ya Wilaya kwa kipindi cha mpito. Hata hivyo, suala hili linahitaji makubaliano baina ya Serikali na mmiliki wa kituo ambaye ni Kanisa Katoliki. Hivyo, tunashauri vikao vya maamuzi vya ngazi husika vya Mkoa na Wilaya, vikiona inafaa vianze mchakato huo mapema. Vikao hivyo, vikikaa na kuridhia pendekezo hilo, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto haitasita kuteua kituo hicho kuwa Hospitali Teule ya Wilaya.
MHE. PROSPER J. MBENA aliuliza:-
Ujenzi wa Bwawa la Maji Kidunda lililopo katika kata ya Serembala, Morogoro Kusini umesababisha matatizo makubwa kwa wananchi wa kata ya Serembala, Magogoni na vijiji jirani kutokana na fidia kidogo kwa kupisha ujenzi wa mradi huo ikilinganishwa na mali walizoziachia yaani mashamba, nyumba zao na mali nyingine zilizo kwenye maeneo makubwa ya ardhi iliyochukuliwa kwa ajili ya mradi huo.
(a) Je, Serikali iko tayari kurudia zoezi la tathmini ya mali za wanavijiji wote walioathirika kwa kutoa nyumba na mashamba yao ili kupisha mradi wa bwawa la Kidunda na kuwalipa fidia wanayostahili?
(b) Je, Serikali iko tayari kwenye bajeti hii kumalizia malipo ya takribani shilingi bilioni 3.7 kuwafidia wananchi hao kulingana na tathmini iliyofanyika?
(c) Je, Serikali itakuwa tayari kuwawekea miundombinu ya uanzishwaji wa mashamba ya umwagiliaji na viwanda vidogo vidogo kwenye kata ya Serembala kwa ajili ya kutoa ajira kwa wananchi Serembala Magogoni, Mvuna na Kkata za jirani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prosper Joseph Mbena, Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaandaa malipo ya fidia kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 ambayo inaelekeza pia kuwa endapo malipo ya fidia yatachelewa kulipwa kwa zaidi ya miezi sita tangu kupitishwa, mlipaji anapaswa kufanya mapitio na kulipa nyongeza kutokana na muda uliozidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshalipa jumla ya shilingi bilioni 7.4 kwa familia 2,603 kama fidia ya kupisha ujenzi wa Bwawa la Kidunda. Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa mwaka wa fedha 2016/2017 na imetenga kiasi cha shilingi bilioni mbili kwa mwaka wa fedha 2017/2018, kwa ajili ya fidia kulingana na tathmini iliyofanyika. Malipo yamekuwa yanafanyika kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Bwawa la Kidunda linajengwa mahsusi kwa ajili ya kuhifadhi maji ya matumizi ya majumbani kwa wakazi wa Kibaha, Bagamoyo na Dar es Salaam. Bwawa hilo halitahusu kilimo kikubwa cha umwagiliaji. Serikali itaangalia uwezekano mwingine wa kuweka miundombinu wezeshi ya kilimo cha umwagiliaji kulingana na maeneo husika.(Makofi)
MHE. PROSPER J. MBENA aliuliza:-
Wakati wa mjadala wa hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi tarehe 22 Mei, 2017, Bungeni, Wabunge wengi walieleza umuhimu wa Serikali kuongeza juhudi za uvuvi kwenye Bahari Kuu na kuitaka Serikali kununua meli kubwa za kuvua samaki kwenye Bahari Kuu:-
(a) Je, Serikali inaweza kueleza sababu zilizofanya Shirika la Uvuvi la Tanzania (Tanzania Fisheries Company-TAFICO) lishindwe kuendelea na biashara ya uvuvi wa Bahari Kuu?
(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kulifufua Shirika hilo la TAFICO?
(c) Je, miundombinu iliyokuwepo ya uvuvi kwa ajili ya TAFICO ikiwa ni pamoja na meli, dry dock na zana nyingi za uvuvi ambazo zilijengwa na kulipiwa na Serikali ya Japan ipo katika hali gani?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prosper Joseph Mbena, Morogoro Kusini, lenye vipengele (a), (b) na (c), Kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, lililokuwa Shirika la Uvuvi Tanzania (Tanzania Fisheries Corporation - TAFICO) lilianzishwa kwa Sheria ya Makampuni ya Umma Na. 17 ya mwaka 1996. Lengo la kuanzishwa kwa TAFICO lilikuwa ni kuendesha shughuli za uvuvi kibiashara katika maji ya ndani na siyo uvuvi wa bahari kuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1996, Serikali ilitoa tangazo Na. 322 kuhusu kurekebisha Mashirika ya Umma ili yaweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na tija zaidi ambapo TAFICO ilikuwa ni miongoni mwa mashirika yaliyotakiwa kubinafsishwa au kufanyiwa marekebisho. Kwa msingi huo, shughuli za Shirika la TAFICO liliwekwa chini ya Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) kwa ajili ya taratibu za ubinafsishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaona umuhimu wa kufufua TAFICO ili Sekta ya Uvuvi iweze kuchangia ipasavyo katika ajenda ya uchumi wa viwanda. Hivyo Wizara imekamilisha waraka wa Baraza la Mawaziri kwa ajili ya mapendekezo ya kutunga Sheria mpya ya Shirika la Uvuvi Tanzania. Suala hili linafanyika kwa kuzingatia ushauri wa kitaalam ili kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali za uvuvi zilizopo ikiwa ni pamoja na uvuvi wa bahari kuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mabadiliko ya sera ambapo Serikali ilijitoa kufanya shughuli za moja kwa moja za uzalishaji na biashara, Serikali kupitia Msajili wa Hazina iliuza mali za TAFICO zinazohamishika zikiwemo meli na mitambo ya barafu mwaka 2008 na kubakiza mali zisizohamishika yakiwemo majengo ambayo yamekarabatiwa na sasa yanatumika kama Ofisi za Serikali na matumizi mengine. Aidha, kutokana na kukaa muda mrefu bila kutumika na athari za mvua za Elnino, Dry Dock imechakaa na imezama upande mmoja.
MHE. PROSPER J. MBENA aliuliza:-
(a) Je, kwa nini Serikali haina utaratibu wa kuwachukua wagonjwa wa akili wanaoranda randa barabarani na mitaani na kuwapeleka kwenye hospitali za wagonjwa wa akili kupatiwa matibabu?
(b) Je, Serikali inafahamu idadi ya wagonjwa wa akili waliopo barabarani na mitaani kwenye wilaya za nchi yetu ambao wanahitaji huduma ya matibabu na inatoa maelekezo gani kwa Waganga Wakuu wa Wilaya kuhusu kuwahudumia wagonjwa hao?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prosper Joseph Mbena, Mbunge wa Morogoro Kusini, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu la kwanza la kulinda afya ya jamii kuanzia katika ngazi ya familia. Aidha, jamii zetu zimekuwa zikiwanyanyapaa, kuwabagua na kuwatenga wagonjwa wa akili kunakopelekea wagonjwa hawa kurandaranda mtaani. Sheria ya Afya ya Akili ya mwaka 2008 inawataka na ndugu na jamii wawaibue wagonjwa wa akili na kuwapeleka kwenye vituo vya kutolea huduma ili wapatiwe matibabu na wakishapata nafuu, huruhusiwa kwenda kukaa na familia zao na kwenye jamii wanazotoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa mujibu wa Sheria ya Afya ya Akili ya mwaka 2008, Sehemu ya Tatu, kifungu cha sheria Namba 9 (1-3) kimeeleza wazi kuwa, Afisa Polisi, Afisa Usalama, Afisa Ustawi wa Jamii ngazi ya Wilaya pamoja na Viongozi wa Dini, Afisa Mtendaji wa Kata na Afisa Mtendaji wa Kijiji, wana jukumu la kubainisha mtu yeyote anayerandaranda na kutishia amani na usalama au vinginevyo kumkamata na kumfikisha katika sehemu ya magonjwa ya akili na ikithibitika taratibu za kumpatia matibabu huanza kama ilivyoainishwa katika Sehemu ya Tatu ya Sheria ya Afya ya Akili ya mwaka 2008, Kifungu cha 11(7) na kifungu Namba 12 cha sheria hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, japokuwa idadi kamili ya wagonjwa wa akili haifahamiki nchini, inakadiriwa kwamba wagonjwa wa akili ni asilimia moja tu ya Watanzania wote. Kwa idadi ya Watanzania milioni 50 inafanya wastani wa wagonjwa laki tano. Kati ya hao asilimia 48 ndiyo wanafika katika vituo vya kutolea huduma za afya, asilimia 24 wanakwenda kwa waganga wa kienyeji na asilimia iliyobaki, wanapelekwa kwenye tiba za kiroho kwa maana Makanisani na Misikitini na wachache ndiyo wanarandaranda mitaani bila msaada wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatoa maelekezo kwa Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwahamasisha Jamii, Watendaji Kata na Serikali za Mitaa, wawaibue watu wanaoonekana kuwa na dalili za ungonjwa wa akili na kuwapeleka kwenye vituo vya afya ili wapatiwe matibabu, kwani huduma hii bila gharama yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, nitoe rai kwa jamii waache kuwanyanyapaa wagonjwa wa akili na badala yake wawafikishe kwenye vituo vya tiba mara wanapoona kuwa wana dalili za ugonjwa huo ili wapatiwe matibabu stahiki na waache kuhusisha na imani za kishirikina. (Makofi)
MHE. PROSPER J. MBENA aliuliza:-
Ujenzi wa barabara kutoka Bigwa - Kisaki iko kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa John Pombe Magufuli alitoa ahadi ya kujenga barabara hiyo alipohutubia wananchi wa Morogoro na kwamba fedha za ujenzi zitatoka Serikalini, nyumba zote zilizomo ndani ya mita 60 zimewekwa alama ya ‘X’ tayari kubomolewa katika maeneo ya Ruvu Kibangile, Kisemu, Mtamba, Nzasa, Kangazi, Kisanzala, Tambuu, Mvuha, Mngazi hadi Kisaki:-
• Je, Serikali itakuwa tayari kuwawekea wananchi hao utaratibu wa kuwajengea nyumba bora kwa wanaopenda badala ya kuwalipa fidia kidogo isiyolingana na mali zao wanazoziacha?
• Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza ili wananchi waliowekewa alama ya kubomolewa nyumba zao waanze maandalizi kwenye maeneo watakayohamia?
• Je, ni lini Serikali itatengeneza upya madaraja ya Ruvu, Mvuha na Dutumi yaliyomo kwenye barabara hiyo, hasa ikizingatiwa kuwa madaraja hayo ni mabovu sana na yanaweza kusababisha ajali kwa wanaopita hapo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Prosper Joseph Mbena, Mbunge wa Jimbo la Morogoro lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Bigwa hadi Kisaki kwa kuanza na kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa sehemu ya barabara ya Bigwa hadi Mvuha yenye urefu wa kilometa 78, pamoja na madaraja ya Ruvu na Mvuha kwa gharama ya Sh.713,471,140/=. Usanifu wa barabara ya Bigwa hadi Mvuha unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2017. Aidha, usanifu wa daraja la Dutumi ulishakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina sehemu ya Bigwa hadi Mvuha, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara pamoja na madaraja yaliyopo kwenye barabara hii. Serikali inaendelea kufanya matengenezo ya aina mbalimbali kwa barabara yote ya Bigwa hadi Kisaki ili iendelee kupitika katika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 zimetengwa jumla ya shilingi milioni 807.84 na katika mwaka wa fedha 2017/2018 zimetengwa jumla ya shilingi milioni 1,126.36.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wote ambao nyumba zao zipo kwenye eneo la hifadhi ya barabara kati ya mita 22.5 na mita 30 kutoka katikati ya barabara kwenda kila upande watalipwa fidia wakati Serikali itakapohitaji kuyatumia maeneo hayo kwa ajili ya upanuzi wa barabara. Aidha, wale wote waliopo kwenye eneo la hifadhi ya barabara ndani ya mita 22.5 kutoka katikati ya barabara kwenda kila upande wanatakiwa kuondoa mali zao kwa mujibu wa sheria ya barabara Na. 13 ya mwaka 2017 na hawatalipwa fidia.
MHE. PROSPER J. MBENA aliuliza:-
Kutokana na kuongezeka kwa matangazo ya biashara kwenye vyombo vya habari, upo uwezekano wa baadhi ya matangazo hayo kuwakera na kuleta hisia tofauti kwa baadhi ya watu na hasa watoto kutokana na maudhui mabaya ya baadhi ya matangazo haya.
(a) Je, Serikali haioni kuna umuhimu wa kuunda chombo cha kusimamia maudhui ya matangazo ya kibiashara ili kuweka na kusimamia taratibu na kanuni za matangazo?
(b) Je, ni idara gani ya Serikali inahusika moja kwa moja na malalamiko ya wananchi dhidi ya kampuni na taasisi zinazotoa matangazo yenye athari kwa jamii?
(c) Je, ni hatua gani zinachukuliwa dhidi ya kampuni hizo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prosper Joseph Mbena, Mbunge wa Morogoro Kusini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tayari ina vyombo vya kusimamia maudhui ya vyombo vya habari nchini, yakiwemo maudhui katika matangazo. Vyombo hivyo ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inayoundwa chini ya kifungu cha Sheria Na. 4 cha Mamlaka ya Mawasiliano Na. 12 ya mwaka 2003, ambayo ina Kamati ya Maudhui iliyoundwa chini ya kifungu cha 26 cha sheria hiyo na marekebisho yake katika kifungu cha 173 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroni na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010. Kamati hii ndiyo inayosimamia maudhui ya matangazo ya kielektroniki (redio, television na mitandao ya kijamii).
Mheshimiwa Naibu Spika, chombo cha pili ni Bodi ya Filamu Tanzania ambayo vilevile inasimamia maudhui katika picha jongevu zinazorushwa katika majumba ya sinema, hadharani vilevile katika michezo ya kuigiza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Idara ya Habari Maelezo ni chombo cha tatu ambacho kimehuishwa chini ya kifungu cha Sheria Na. 4 na Sheria Na. 5 vya Sheria ya Huduma ya Habari Namba 12 ya mwaka 2016 kinachosimamia maudhui katika machapisho mbalimbali yakiwemo magazeti, majarida pamoja na vipeperushi.
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali inapobainika bila kutia shaka kuwa kampuni, asasi au taasisi imechapisha ama kutoa tangazo lenye athari kwa jamii. Hatua hizo ni pamoja na kupewa onyo, kufungiwa kutoa huduma kwa kipindi kitakachotajwa au kufungiwa kabisa kutokujihusisha na utangazaji au uchapishaji wa habari pamoja na matangazo. Serikali inaendelea kuhimiza jamii nzima kuendelea kuzingatia sheria na taratibu zilizopo katika kusambaza habari mbalimbali kwa jamii.
MHE. PROSPER J. MBENA aliuliza:-
Nchi nyingi duniani ikiwemo Japan, Uholanzi na Marekani hutumia wataalam wastaafu kwenye sekta mbalimbali za uchumi katika shughuli mbalimbali za kutoa ushauri ndani na nje ya nchi zao. Wataalam hao (volunteers) wanatoa mchango mkubwa kwenye kushauri.
(a) Je, ni lini nchi yetu itaiga utaratibu huo mzuri wa kuwatumia wataalam wake wastaafu ipasavyo badala ya kuwaacha tu mitaani?
(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka kumbukumbu ya taarifa ya wataalam wastaafu wake (directory) kwa kila mmoja kwenye fani yake (profession) ili kuweza kuwatumia wataalam wastaafu hao pale ushauri wao utakapohitajika?
WAZIRI WA MADINI (K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI UMMA NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prosper Joseph Mbena, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali inao utaratibu wa kuwatumia wataalam wastaafu kwa kuwapatia mikataba pale wanapohitajika. Matumizi ya wataalam hao yamefanunuliwa katika aya ya 12.2 ya Waraka wa Rais Namba 1 wa mwaka 1998, pamoja na Kanuni ya D. 28 ya Kanuni za Kudumu (Standing Orders) katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009. Miongozo hii inaelekeza kwamba endapo utaalam wa mtumishi unahitajika sana Serikali inawajibika kumuomba mtumishi kuendelea na kufanya kazi.
(b) Mheshimiwa Spika, Serikali inapokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge wa kuanzisha kanzidata ya wataalam wastaafu ili kuweza kuwatumia pale watakapohitajika.
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO (K.n.y. MHE. PROSPER J. MBENA) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya kutoka Bigwa – Mvuha – Kisaki katika Wilaya ya Morogoro Vijijini kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prosper Joseph Mbena, Mbunge wa Morogoro Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Bigwa – Mvuha – Kisaki (km 133.28) ni barabara ya Mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Morogoro. Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) tayari imeanza maandalizi ya ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara hii ambapo kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa sehemu ya Bigwa – Mvuha (km 78) inayofanywa na Kampuni ya Mhandisi Mshauri M/S Unitech Civil Consultants Limited ya Dar es Salaam imekamilika. Serikali ipo kwenye hatua ya kutafuta fedha za ujenzi.
Mheshimiwa Spika, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Bigwa – Mvuha – Kisaki (km 133.28) utatekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, Serikali inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya matengenezo ya aina mbalimbali kwa barabara hii ili iweze kupitika majira yote ya mwaka ambapo katika mwaka wa fedha wa 2018/ 2019 jumla ya shilingi milioni 1,822.550 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo.
Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali inaendelea na ukarabati kwa kiwango cha changarawe katika sehemu ya Mvuha – Kisaki (km 65.29). Sehemu hiyo ni kipande cha barabara ya Ubena Zomozi – Ngerengere – Mvuha – Kisaki Stiegler’s Gorge inayoelekea katika Mradi wa Kufua Umeme wa Mto Rufiji (Rufiji Hydropower Project). Kazi za ukarabati wa barabara hiyo unaendelea na utekelezaji wake umefikia asilimia 50.
MHE. PROSPER J. MBENA aliuliza:-

Vigezo vilivyotumika kuchagua Vituo vya Afya 100 kupatiwa shilingi milioni 700 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maabara na upasuaji wa akina mama wanaojifungua kwa maana ya shilingi milioni 400 kwa ajili ya maabara na upasuaji na shilingi milioni3 00 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa toka MSD ni vigezo ambavyo pia vipo katika Vituo vya Afya Duthumi, Tawa, Mvula na Mtamba katika Jimbo la Morogoo Kusini.

Je, ni lini Seikali itawatendea haki wananchi wa Morogoro Kusini kwa kuwatengea fedha ili kukamilisha miundombinu ya upasuaji angalau kituo kimoja Kata ya Duthumi, Tawala Mvuha na Mtamba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prosper Joseph Mbena, Mbunge wa Morogoro Kusini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza Mpango wa Kuboresha Vituo vya Afya nchini ambapo hadi sasa Vituo vya Afya 350 vimepatiwa fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati.

Mheshimiwa Naibu Spika, vigezo vilivyotumika kuchagua vituo hivyo vinavyokarabatiwa na kujengwa ni uhitaji mkubwa wa huduma za dharura na upasuaji kwa mama wajawazito, sababu za kijiografia na umbali mrefu ambao wananchi wanatembea kupata huduma za dharura.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali ilitoa kiasi cha shilingi million 500 kwa ajili ya ujenzi na upanuzi wa Kituo cha Afya cha Duthumi kilichopo katika Jimbo la Morogoro Kusini. Vilevile katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilion1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro inayojengwa katika Makao Makuu ya Halmashauri eneo la Mvuha.
MHE. PROSPER J. MBENA aliuliza:-

(a) Je, ni lini Serikali itafanya utafiti wa uhakika katika Vijiji vyote vya Jimbo la Morogoro Kusini ili kubaini madini yaliyopo?

(b) Je, Serikali itawasaidiaje Wachimbaji wadogo wa Rubi, Spinel na Dhahabu ili waweze kuzalisha zaidi na kupata masoko ya uhakika?

(c) Je, ni lini Serikali itatuma Wataalam wa kuthibitisha wingi wa madini ya Graphite na Chokaa katika maeneo ya Jimbo la Morogoro Kusini ili mipango ya kuchimba iweze kuanza?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Prosper Joseph Mbena, Mbunge wa Morogoro Kusini, lenye vipengele (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mwaka 2014, Serikali kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST) ilifanya utafiti wa awali wa kijiolojia katika Jimbo la Morogoro Kusini na kutengeneza ramani ya kijiolojia (Quarter Degree Sheet – QDS) zipatazo tisa.

Mheshimiwa Spika, taasisi kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ikiwemo kampuni ya Beak Consultants ya Ujerumani na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kati ya mwaka 2013 na 2014 walifanya utafiti wa awali na kubainisha uwepo wa madini ya dhahabu katika Kata za Mkuyuni, Mikese, Mazimbu, Kisemu na Tununguo; vilevile madini ya chokaa katika Kata ya Mkuyuni na Kisaki; madini ya Kinywe (graphite) katika Kata za Mvuha, Mkuyuni, Kisemu na Mtombozi.

Mheshimiwa Spika, aidha, utafiti huo ulibainisha pia uwepo wa madini ya ruby katika Kata za Tawa, Mkuyuni na Mkambalani. Vilevile kuna madini ya spinel na barite katika Kata za Mkuyuni.

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali za Madini (SMMRP) imenunua mtambo wa kuchoronga miamba mipya na kuikabidhi katika Shirika la (STAMICO) kwa lengo la kufanya utafiti katika maeneo ya wachimbaji wadogo kwa gharama nafuu.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA (K.n.y. MHE. PROSPER J. MBENA) aliuliza:-

Kumekuwepo na ongezeko la matukio ya ukatili mkubwa kwa wanyama katika nchi yetu hususan kuku, mbuzi na ng’ombe wakati wakisafirishwa kutoka eneo moja kwenda eneo lingine?

(a) Je, Chama cha kuzuia ukatili wa Wanyama nchini yaani Tanzania Society for the Prevention of Cluelty to Animals (TSPCA) kinashirikiana kwa kiasi gani na Serikali katika kudhibiti vitendo hivyo vya kikatili wa Wanyama?

(b) Je, kwa mwaka 2018 na 2019 ni kesi ngapi zinazohusu matukio ya ukatili kwa Wanyama zilifikishwa Mahakamani?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prosper Joseph Mbena Mbunge wa Morogoro Kusini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inashirikiana na Mashirika yasiyo ya Kiserikali kama vile TSPCA katika kudhibiti vitendo vya kikatili kwa Wanyama kwa kuzingatia Sera ya Mifugo ya mwaka 2006 na Sheria ya Ustawi wa Wanyama ya mwaka 2008 kwa kuelimisha jamii kuhusu masuala ya Ustawi wa Wanyama. Pia elimu inayotolewa inalenga kuelimisha jamii kuhusu njia sahihi ya usafirishaji mifugo, matumizi ya Wanyama kazi kama punda na kuzuia ukatili wa Wanyama kwenye minada ya mifugo. Aidha, jumla ya wataalam wa mifugo 25 kwenye minada wamepata mafunzo na pia wafanyabiashara wa mifugo takribani 300. Pia, elimu hutolewa kwa njia ya mabango na vipeperushi kwenye minada mikubwa.

Mheshimiwa Spika, Kwa kuzingatia Kifungu namba 60, wanaokiuka Sheria hiyo wanatozwa faini ya papo kwa papo badala ya kupelekwa Mahakamani. Faini hiyo ni shilingi 50,000 kwa kila anayekiuka Sheria hiyo. Kwa mwaka 2018 jumla ya makosa 3,542 kwa kosa la ukatili wa Wanyama yameripotiwa ambayo yamegawanyika kama ifuatavyo; ng’ombe 847, mbuzi na kondoo 1,578, Nguruwe 85, kuku 539 na punda 490.