Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Susan Limbweni Kiwanga (17 total)

MHE. SUSAN L. KIWANGA aliuliza:-
Licha ya Jimbo la Mlimba kuwa na uzalishaji wa mazao ya kilimo, linakumbwa na ukosefu mkubwa wa miundombinu ya barabara zinazopitika na madaraja, jambo linalosababisha wakulima kushindwa kusafirisha mazao yao kwenda kwenye masoko na hivyo kuendelea kuwa maskini licha ya kuwa na utajiri wa mazao ya kilimo:-
(a) Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Ifakara - Mlimba, Mlimba - Madeke na Mlimba - Uchindile?
(b) Je, ni lini Serikali itajenga madaraja ya kudumu katika Mito ya Mtunji, Chiwachiwa, Mngeta na Londo kwa kuwa yaliyopo sasa ni ya miti?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mbunge wa Mlimba, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Ifakara - Mlimba - Madeke yenye urefu wa kilometa 231.53 inahudumiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS) na barabara ya Mlimba - Uchindile inahudumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero. Serikali imeanza maandalizi ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Ifakara - Mlimba kwa kuanza na upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa sehemu ya barabara ya kutoka Ifakara – Kihansi yenye urefu wa kilometa 126 kwa lengo la kuunganisha kipande cha barabara ya lami chenye urefu wa kilometa 24 kati ya Kihansi – Mlimba. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina inaendelea na inatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa ujenzi wa madaraja ya kudumu katika Mito ya Mtunji, Chiwachiwa na Londo utatekelezwa na Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Aidha, katika mwaka wa fedha 2015/2016, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS), inaendelea na maandalizi ya ujenzi wa daraja la Mngeta. Hadi sasa ukaguzi wa eneo la kujenga daraja umefanyika na taratibu za ununuzi ili kumpata mkandarasi wa kujenga daraja hilo ziko katika hatua za mwisho.
MHE. MARTIN M. MSUHA (K.n.y. MHE. SUSAN L. KIWANGA) aliuliza:-
Pamoja na Jimbo la Mlimba kuwa na vyanzo vingi vya maji ikiwemo mito mikubwa, wananchi bado wanakumbwa na uhaba mkubwa na maji safi na salama.
(a) Je, ni lini Serikali itaanzisha mpango wa usambazaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa Mlimba?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha skimu za umwagiliaji ili kuvipa tija vyanzo vya maji vilivyopo katika Jimbo la Mlimba?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mbunge wa Mlimba, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji katika Halmashauri zote nchini. Katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa programu, Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero inatekeleza miradi 14, kati ya miradi hiyo miradi nane ipo katika Jimbo la Mlimba. Ujenzi wa miradi mitano katika vijiji vya Mlimba A, Mlimba B, Viwanja Sitini, Kamwene na Masagati umekamilika na inatoa huduma ya maji kwa wananchi wapatao 24,632. Miradi mitatu ya Idete, Namwawala na Matema ipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji. Lengo la Serikali ni kukamilisha ujenzi wa miradi hiyo ili wananchi waweze kupata huduma ya maji kama ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza kutekeleza Skimu ya Umwagiliaji ya Njage yenye eneo la hekta 325 kupitia Mfuko wa Wilaya wa Kuendeleza Umwagiliaji (DIDF) na hivi sasa skimu hii imeingizwa katika mradi wa Expanded Rice Production Project ili kukamilisha ujenzi wa skimu hiyo.
Aidha, Serikali kupitia Gereza la Idete, inajenga skimu ya umwagiliaji yenye jumla ya eneo la hekta 1,000. Vilevile shamba la Kilombero Plantation Limited (KPL) lenye eneo la hekta 4,000 litaendelea kuzalisha mazao na liko katika hatua ya uendelezwaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Marekani, kupitia Mfuko wa Feed the Future inafanya upembuzi yakinifu katika maeneo yaliyoainishwa katika mpango kabambe wa umwagiliaji wa mwaka 2002 ya Kisegese, Udagaji na Mpanga – Ngalimila. Maeneo yatakayofaa yataingizwa kwenye hatua ya usanifu wa kina.
MHE. SUSAN L. KIWANGA aliuliza:-
Serikali imetwaa maeneo ya vijiji katika Kata za Idete, Namwala, Mofu, Mbinga, Igima, Mchombe, Mngeta, Kalengakelu, Mlimba, Kamwene, Chita na Utengule kwa madai kwamba ni maeneo ya hifadhi bila kuwashirikisha wananchi, jambo ambalo limefanya wananchi kushindwa kuendeleza shughuli zao za kilimo na ufugaji na hivyo kuendelea kuwa maskini.
Je, Serikali itakuwa tayari kushirikisha wananchi ili kuweka mipaka kati ya maeneo ya kilimo na ufugaji na yale ya Hifadhi ya Taifa ili kuondoa mgogoro wa ardhi uliopo hivi sasa kwa wananchi kukosa maeneo ya kilimo na malisho ya mifugo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu haijawahi kutwaa na haina utaratibu wa kutwaa maeneo ya vijiji na kuyafanya kuwa maeneo ya hifadhi bila ya kuwashirikisha wananchi. Aidha, sehemu ya maeneo ya vijiji vilivyoko ndani ya kata 12 zilizotajwa yamo ndani ya eneo la Hifadhi ya Ramsar ya Bonde la Kilombero iliyotambulika na kuorodheshwa mwaka 2002.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Ramsar la Bonde la Kilombero ni muendelezo wa hifadhi ulioanza na Pori Tengefu la Kilombero lililoanzishwa kwa Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori, Sura ya 302 ya mwaka 1952 kupitia Tangazo la Serikali Namba107. Pori hili lilirithiwa na Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Namba12 ya mwaka 1974 na kuboreshwa na Sheria Namba 459 ya mwaka 1977 baada ya taratibu zote za kisheria kukamilika ikiwemo ushirikishaji wananchi. Aidha, eneo hili ambalo ni chanzo kikubwa cha maji na lenye uwepo wa viumbe adimu duniani lina ukubwa wa kilometa za mraba 7,967.35 sawa na hekta 795,735 sifa ambazo zinalifanya kuwa eneo la tatu kwa ukubwa lenye umuhimu wa Kimataifa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya ardhi liliyopo baina ya wananchi na vijiji katika kata zilizotajwa ambavyo vilianzishwa baada ya kuanzishwa kwa Pori Tengefu la Kilombero imetokana na hatua mbalimbali za ukiukaji wa sheria, kanuni na taratibu. Aidha, katika kutatua migogoro hiyo, Serikali inaendelea kutekeleza yafuatayo:-
(a)Kupitia Mradi wa KILORWEMP unaotekelzwa chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii; kupitia upya mipaka, kuweka alama, kuchora ramani na kutunza kumbukumbu kwa njia za kawaida na kielektroniki.
(b)Kupitia mpango wa upimaji ardhi za vijiji vya Wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi unaosimamiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; kukamilisha upimaji na urasimishaji wa ardhi ambapo mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji itaandaliwa na wananchi na watamilikishwa ardhi kisheria.
(c)Kupitia Kamati Maalum ya Kitaifa iliyoundwa kushughulikia migogoro ya rdhi nchini; kufika katika maeneo ya Ramsar na Pori Tengefu la Kilombero na kutekeleza majukumu yake katika kutatua migogoro kwa kuwashirikisha wananchi kama ilivyo kwa utekelezaji wa hatua zingine nilizozitaja hapo juu.
MHE. SUSAN L. KIWANGA aliuliza:-
Katika Jimbo zima la Mlimba kuna kituo kimoja tu cha polisi cha Mngeta jambo linalofanya hali ya usalama kwa wananchi kuwa duni.
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga vituo vya polisi katika Jimbo la Mlimba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mbunge wa Mlimba kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uhaba wa vituo vya polisi nchini na ili kuimarisha usalama nchini Serikali ina mpango wa kujenga vituo vya polisi hadi ngazi ya kata na tarafa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira hadi hapo hali ya fedha itakapokuwa nzuri na kutuwezesha kutekeleza mpango huo.
MHE. SUSAN L. KIWANGA aliuliza:-
Serikali inafanya zoezi la kimya kimya la utafutaji wa mafuta na gesi katika Jimbo la Mlimba bila kutoa taarifa rasmi kwa wananchi juu ya zoezi hilo:-
Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya mchakato huo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika Kitalu cha Kilosa Kilombero unaofanywa na Kampuni ya Swala Energy ulianza mwezi Februari, 2012. Kampuni hiyo ilianza kufanya utafiti wa awali wa kijiolojia kwa ajili ya kutambua aina na sifa za miamba iliyopo na kutoa taarifa ya mitetemo (seismic data).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na tafiti hizo, kampuni ilionesha uwezekano wa kuwepo kwa mafuta na gesi asilia katika eneo hilo. Eneo lililoainishwa kwa ajili ya uchimbaji wa kisima hicho lipo katika Kijiji cha Ipera Asilia katika Hifadhi Tengefu ya Bonde la Kilombero. Uchimbaji unatarajiwa kuanza mwezi Septemba, mwaka 2017 baada ya utafiti kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Februari, 2017, Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ilianza kutoa elimu kuhusu utafiti wa mafuta na gesi asilia na fursa zitakazopatikana kwa wananchi wa Mlimba hasa katika maeneo yanayozunguka mradi huo. Elimu hiyo itahusu pia athari za mazingira na ushiriki wa wananchi katika miradi mbalimbali kwa manufaa ya wananchi pamoja na Taifa kwa ujumla.
MHE. SUSAN L. KIWANGA aliuliza:-
Katika Jimbo zima la Mlimba hakuna Mahakama hata moja, jambo linalosababisha mahabusu kupelekwa Jimbo la Kilombero umbali wa takriban kilometa 260 kuhudhuria mahakama:-
Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama katika Jimbo la Mlimba ili kuwaondolea wananchi adha ya kusafiri umbali mrefu katafuta huduma ya Mahakama?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Suzan Limbweni Kiwanga, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, uanzishaji wa Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo nchini unaongozwa na Sheria ya Mahakimu, Sura 11 ya Sheria za Tanzania (The Magistrate Courts Act, Cap. 11) of the laws of Tanzania. Kifungu cha 3(1) kinaeleza kuwa katika kila Wilaya kutaanzishwa Mahakama za Mwanzo; Kifungu cha 4(1) kinaeleza kuwa kutaanzishwa Mahakama za Wilaya katika kila Wilaya na Kifungu cha 5(1) kinampa mamlaka Jaji Mkuu kutoa amri ya kuanzisha Mahakama za Hakimu Mkazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Mlimba, Tarafa ya Mlimba ipo Mahakama ya Mwanzo inayoendelea kutoa huduma hadi hivi sasa. Serikali inatambua kuwa miundombinu ya Mahakama hiyo hairidhishi na hivyo katika mwaka wa fedha 2017/2018 tumepanga kujenga Mahakama ya Mwanzo mpya katika Tarafa ya Mlimba.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umbali na ukubwa wa Wilaya ya Kilombero yenye Majimbo ya Kilombero na Mlimba na itajitahidi kuhakikisha kwa kadri ya uwezo utakavyokuwa kujenga Mahakama za Mwanzo za kutosha katika Wilaya nzima ya Kilombero ili kusogeza huduma za Mahakama na utoaji haki karibu zaidi na wananchi.
MHE. SUSAN L. KIWANGA aliuliza:-
Jimbo la Mlimba linakabiliwa na miundombinu mibovu ya barabara na kushindwa kupitika kipindi chote cha mwaka na hivyo kusababisha adha kubwa kwa wanawake, watoto, wagonjwa na pia wananchi kwa ujumla wanaosafirisha mazao kufuata wanunuzi na huduma za Serikali kama vile kwa Mkurugenzi wa Halmashauri, Mkuu wa Wilaya, Hospitali ya Wilaya, Mahakama na Polisi Wilayani Ifakara.
(a) Je, ni lini barabara ya Ifakara - Mlimba - Madeke - Njombe itajengwa kwa kiwango cha lami kwa kuwa upembuzi wa barabara hiyo ulishafanyika?
(b) Wakati tunasubiri barabara ya lami, je, Serikali ina mpango gani wa kuitengea fedha za kutosha barabara hiyo ili kuifanya ipitike kwa kipindi chote cha mvua na kiangazi?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mbunge wa Mlimba, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Ifakara – Mlimba – Madeke yenye urefu wa kilometa 231.53 inahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Morogoro. Barabara hii inaunganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Njombe katika Kijiji cha Madeke. Barabara hii inapitika kwa kipindi kirefu cha mwaka ingawa kuna maeneo machache bado yanapitika kwa shida wakati wa majira ya mvua.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilishaanza maandalizi ya ujenzi kwa kiwango cha lami barabara hii ya Ifakara - Mlimba
- Madeke ambapo imeshakamilisha kazi ya usanifu wa kina wa sehemu ya barabara kati ya Ifakara na Kihansi yenye urefu wa kilometa 126 ili kuunganisha na kipande cha barabara ya lami chenye urefu kilometa 24 kilichojengwa kwa kiwango cha lami hapo awali kati ya Kihansi na Mlimba. Ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu hiyo iliyofanyiwa usanifu wa kina utaanza pindi fedha zitakapopatikana.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii kiuchumi na kijamii, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga shilingi bilioni 2.52 kwa ajili ya matengenezo ya aina mbalimbali ya barabara na madaraja ili barabara ipitike majira yote ya mwaka mpaka hapo itakapojengwa kwa kiwango cha lami.
MHE. SUSAN L. KIWANGA aliuliza:-
Jimbo la Mlimba lina mito mikubwa inayotiririka mwaka mzima kwa miaka mingi, lakini Jimbo limekuwa na tatizo kubwa la kupata maji safi na salama.
(a) Je, ni lini Serikali itatumia uwepo wa mito hiyo kama fursa ya kuwapatia maji safi na salama wananchi wa Mlimba hasa Mji Mdogo wa Mlimba?
(b) Je, ni lini Serikali itatumia uwepo wa mito hiyo kujenga mabwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwajiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mbunge wa Jimbo la Mlimba, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari imeanza kutumia fursa ya mito iliyopo katika Jimbo la Mlimba kuwapatia maji safi na salama wananchi wa Jimbo hilo. Mpaka sasa kuna miradi minne ya Tanganyika Masagati, Chita/Ching’anda, Mngeta/Mchombe na Mkangawalo/ Kidete/Itongowa. Vyanzo vyake ni mito.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika bajeti ya mwaka 2017/2018 Serikali imepanga kujenga mradi wa maji Mbingu/Vigaeni ambao chanzo chake ni Mto Ifumbo. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero imepanga kufanya usanifu wa kupeleka maji katika Kata ya Mlimba kwa kutumia Mito ya Mgugwe na Mpanga, kwa sasa mji mdogo wa Mlimba unapata huduma ya maji kupitia visima virefu.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa ujenzi wa mabwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Kuanzia mwaka 2013/2014 hadi 2015/2016, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Marekani kupitia Shirika lake la Maendeleo (USAID) ilifanya upembuzi yakinifu katika Bonde la Mto Kilombero ikiwemo maeneo ya Jimbo la Mlimba kwa ajili ya kubainisha maeneo ya kujenga skimu za umwailiaji na mabwawa ambapo takribani hekta 43,000 zilibainishwa. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya uendelezaji maeneo hayo.
MHE. SUSAN L. KIWANGA aliuliza:-
Katika Jimbo zima la Mlimba hakuna Mahakama hata moja, jambo linalosababisha mahabusu kupelekwa Jimbo la Kilombero umbali wa takriban kilometa 260 kuhudhuria mahakama:-
Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama katika Jimbo la Mlimba ili kuwaondolea wananchi adha ya kusafiri umbali mrefu katafuta huduma ya Mahakama?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Suzan Limbweni Kiwanga, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, uanzishaji wa Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo nchini unaongozwa na Sheria ya Mahakimu, Sura 11 ya Sheria za Tanzania (The Magistrate Courts Act, Cap. 11) of the laws of Tanzania. Kifungu cha 3(1) kinaeleza kuwa katika kila Wilaya kutaanzishwa Mahakama za Mwanzo; Kifungu cha 4(1) kinaeleza kuwa kutaanzishwa Mahakama za Wilaya katika kila Wilaya na Kifungu cha 5(1) kinampa mamlaka Jaji Mkuu kutoa amri ya kuanzisha Mahakama za Hakimu Mkazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Mlimba, Tarafa ya Mlimba ipo Mahakama ya Mwanzo inayoendelea kutoa huduma hadi hivi sasa. Serikali inatambua kuwa miundombinu ya Mahakama hiyo hairidhishi na hivyo katika mwaka wa fedha 2017/2018 tumepanga kujenga Mahakama ya Mwanzo mpya katika Tarafa ya Mlimba.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umbali na ukubwa wa Wilaya ya Kilombero yenye Majimbo ya Kilombero na Mlimba na itajitahidi kuhakikisha kwa kadri ya uwezo utakavyokuwa kujenga Mahakama za Mwanzo za kutosha katika Wilaya nzima ya Kilombero ili kusogeza huduma za Mahakama na utoaji haki karibu zaidi na wananchi.
MHE. SUSAN L. KIWANGA aliuliza:-
Jimbo la Mlimba lina mito mingi inayotiririka mwaka mzima ambayo inaweza kutumika kujenga malambo kwa ajili ya mifugo:-
Je, ni lini Serikali itajenga Malambo kwa ajili ya kunyweshea mifugo katika Jimbo la Mlimba?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mbunge wa Mlimba, kama ifauatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba uwepo wa mito mingi katika Jimbo la Mlimba ni fursa kwa ajili ya upatikanaji wa maji kwa matumizi mbalimbali ikiwemo mifugo.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Wizara yangu imepokea ombi la Mheshimiwa Susan Kiwanga na litazingatiwa katika bajeti ya mwaka 2018/2019. Pia nitoe wito kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuendelea kuhamasisha sekta binafsi, wafugaji pamoja na wadau wa maendeleo kuibua miradi ya ujenzi wa malambo, mabwawa, majosho na visima virefu kwa lengo la kuboresha shughuli za ufugaji ili kuleta tija.
MHE. SUSAN L. KIWANGA aliuliza:-
Serikali iliahidi kuweka mipaka ya kutenganisha Vijiji vya Jimbo la Mlimba na RAMSAR SITE kwa kuwashirikisha wanavijiji wa maeneo husika lakini kazi hiyo haikufanyika badala yake wakulima waliambiwa mwisho wao kwenye maeneo hayo ni mwezi Agosti na wafugaji mwisho wao kwenye maeneo yao ni Julai:-
• Je, kwa nini Serikali haikutekeleza jukumu lake la kuweka mipaka badala yake wakulima na wafugaji wamepewa barua ya kusitisha kutumia maeneo hayo na kusababisha taharuki kubwa kwa wananchi?
• Kwa kuwa wananchi hao walifungua kesi kupinga maonevu hayo mwaka 2015 kesi Na. 161 kuhusu mgogoro huo na bado kesi hiyo haijakwisha, kwa nini Serikali imewasitisha wananchi hao kuendelea kutumia maeneo hayo kabla ya kesi haijakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mbunge wa Mlimba, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekaji wa alama za mipaka kwenye maeneo yaliyohifadhiwa kisheria hufanyika kwa kuwashirikisha wananchi wa maeneo husika. Katika Pori Tengefu la Kilombero, zoezi la uwekaji wa alama za mipaka (vigingi) limefanyika kwa kuwashirikisha wananchi ambapo hadi kufikia Agosti, 2018, jumla ya vigingi 143 vimesimikwa kwa upande wa Wilaya za Malinyi na Ulanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, katika Wilaya ya Kilombero zoezi la uelimishaji wananchi limefanyika katika vijiji saba vya Miwangani, Namwawala, Idandu, Mofu, Ikwambi, Miomboni na Kalenga. Baada ya hatua hiyo, uwekaji wa alama ya mipaka utaendelea na utashirikisha wananchi wa maeneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba wananchi walifungua Kesi ya Ardhi Na.161 ya mwaka 2015 kupinga zoezi la Operesheni Okoa Bonde la Kilombero iliyofanyika mwaka 2012 kwa madai ya kuwa watu wanaofanya shughuli katika bonde hilo walipwe stahiki zao na kupewa muda muafaka wa kuondoka. Hoja ya wananchi hao ililenga kuiomba Mahakama izuie Serikali katika kuendesha operesheni tajwa kupitia Shauri Na.357 la Mwaka 2017 yaani Miscellaneous Land Application No.357 of 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Mahakama kusikiliza ombi la wananchi hao ilionekana kutokuwa na tija hivyo ikaamua kutokukubaliana na shauri hilo na badala yake ikaelekeza kesi ya msingi Na. 161 ya mwaka 2015 iendelee kusikilizwa, kesi hiyo itatajwa tena tarehe 19/9/2018. Hata hivyo, kesi iliyopo mahakamani kwa sasa haizuii Serikali kuendelea na operesheni itakayosaidia kuokoa Bonde la Kilombero ambalo ni muhimu sana katika kulinda ardhi oevu na ni chanzo kikubwa cha maji ya Mto Rufiji unaotegemewa kwa uzalishaji wa umeme kupitia mradi wa Rufiji.
MHE. SUSAN L. KIWANGA aliuliza:-
Jimbo la Mlimba lina vijana wengi wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari na vyuo lakini wanashindwa kujiajiri kwa kukosa elimu ya ufundi kutokana na jimbo kuwa na kituo kimoja cha ufundi stadi kilichopo Shule ya Msingi Mchombe. Hata hivyo, kituo hicho chenye mahitaji ya walimu sita kina walimu wawili pekee na hakina vifaa. Aidha, kituo kilichopo Shule ya Msingi Mpanga hakina walimu wala vifaa:-
(a) Je, ni lini Serikali itaboresha vituo hivyo vya Mchombe na Mpanga kwa kuwapelekea walimu na vifaa?
(b) Vijana wachache wanaomaliza Kituo cha Mchombe na kufanya mitihani ya NECTA hawapewi vyeti. Je, ni lini Serikali itaweka utaratibu mzuri katika vituo hivyo ili wawe wanapewa vyeti ili waweze kujiendeleza katika vyuo vya Serikali na kupata madaraja?
(c) Kwa kuwa mitaala ya vyuo vingi imepitwa na wakati, je, Serikali haioni haja ya kuboresha mitaala ya vituo hivyo ili iendane na wakati uliopo kama vyuo vya VETA?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mbunge wa Mlimba lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2018/2019, Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero imetenga shilingi milioni 10 kwa ajili ya kununulia vifaa na ukarabati wa Kituo cha Ufundi Stadi Mchombe na shilingi milioni 15 kwa ajili ya kufufua Kituo cha Ufundi Stadi Mpanga. Aidha, Serikali inaendelea kubaini walimu waliosomea fani mbalimbali za ufundi ili wahamishiwe kwenye vituo hivi vya ufundi stadi vikiwemo vituo vya Mchombe na Mpanga.
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba wanafunzi wanaohitimu mitihani ya NECTA katika vituo vya ufundi vilivyoko kwenye shule za msingi hawajapatiwa vyeti vya kuhitimu mafunzo hayo tangu mwaka 2015. Aidha, mitaala inayotumika kutoa mafunzo katika vituo vyote 208 ambavyo kwa mwaka 2018 vina wanafunzi 3,000 na walimu 557 ni ya muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo, Serikali inaupokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge wa kuhakikisha kuwa wanafunzi wanaohitimu mafunzo hayo wanapatiwa vyeti ili wavitumie katika michakato ya kujiendeleza au kazi kwani vijana hao ni sehemu ya nguvukazi katika ujenzi wa uchumi wa viwanda. Kwa kutumia uzoefu uliopatikana hadi sasa, Serikali itaifanyia mapitio mitalaa ya mafunzo hayo ili iendane na mahitaji sasa.
MHE. SUSAN L. KIWANGA aliuliza:-

Barabara kutoka Ifakara hadi Mlimba mpakani mwa Mkoa wa Njombe (Madeke) ni kero kubwa kwa wananchi wa Jimbo la Mlimba:-

Je, ni lini Serikali itajenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Ifakara – Mlimba – Taweta - Madeke yenye urefu wa kilometa 220.22 inaunganisha Mkoa wa Morogoro na Njombe katika Kijiji cha Madeke. Barabara hii ni ya changarawe na udongo ambapo sehemu kubwa inapitika vizuri isipokuwa maeneo yanayohitaji kuimarishwa ili nayo yapitike wakati wote wa mwaka.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, Serikali imeshakamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa sehemu ya barabara kutoka Ifakara Kihansi (km 126) ikiwa ni hatua ya awali ya kuanza mipango ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. Hatua hiyo itawezesha kuunganisha sehemu ya barabara hiyo na kipande cha barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 24 kilichojengwa hapo awali kati ya Kihansi na Mlimba. Kufuatia kukamilika kwa hatua hiyo, Serikali imeanza kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, aidha, katika mwaka wa fedha wa 2019/2020 kipande kilichobaki kati ya Mlimba hadi Taweta kimewekwa kwenye mpango ili kufanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Serikali itaendelea kutenga fedha za matengenezo ili barabara hii iweze kupitika wakati wote wa mwaka wakati fedha za ujenzi kwa kiwango cha lami zinatafutwa.
MHE. DEVOTHA M. MINJA (K.n.y. MHE. SUSAN L. KIWANGA) aliuliza:-

Mji Mdogo wa Mlimba unazungukwa na Kata za Chisano, Kalengakelo na Kamwene na zina jumla ya wakazi wasioupungua elfu hamsini na nane ambapo hawana maji kwa matumizi ya nyumbani na kunywa; na kwa kuwa kuna chanzo kikubwa cha maji na Mhandisi wa Halmashauri ameshaleta andiko la mradi wa maji:-

Je, ni lini Serikali itapeleka fedha za mradi huo ili wananchi hao wapate maji ya kunywa safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mbunge wa Mlimba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto ya maji kutotosheleza wakazi wa Kata za Mlimba, Chisano, Kalengakelo na Kamwene waliopo katika Jimbo la Mlimba, Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero kwa kushirikiana na Wizara ya Maji imesanifu mradi mkubwa wa maji ambao utahudumia wakazi zaidi ya 29,713. Mradi huu utakapokamilika utatatua kero ya maji katika kata zilizotajwa hapo juu ikiwemo Mlimba kwa kuondoa mgao wa maji kabisa.

Andiko la mradi huu linafanyiwa kazi na Wizara ya Maji ili Serikali iweze kutafuta fedha zaidi ya shilingi bilioni 4.5 kuweza kufanikisha ujenzi wa mradi huu ambao umeonekana kuwa suluhisho la maji katika Jimbo la Mlimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, katika jitihada hizo za kuwapatia wananchi wa Jimbo la Mlimba huduma ya maji safi na salama, Serikali kupitia program ya maji inaendelelea na ujenzi wa mradi wa maji wa Kata za Chita/ Ching’anda a Mbingu/Vigaeni. Pia imekamilisha ujenzi wa miradi ya maji saba katika Vijiji vya Tangamyika, Masagati, Matema, Kamwene, Viwanja Sitini, Mlimba A na B, Namwawala na Idete.
MHE. SUSAN L. KIWANGA aliuliza:-

Jimbo la Mlimba lina wahitimu wengi wa Shule za Msingi na Sekondari ambao wanabaki majumbani kila mwaka:-

Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha Ufundi ili vijana hao waweze kupata Ufundi Stadi ili wajiajiri?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga Mbunge wa Mlimba kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uhitaji wa Vyuo vya Ufundi Stadi katika kuendeleza vijana wake ili waweze kushiriki kikamilifu katika harakati za maendeleo ya nchi yao. Katika kutimiza lengo hili, Serikali imejiwekea mkakati madhubuti wa kuendeleza elimu ya ufundi katika ngazi mbalimbali. Hivyo, Serikali inaendelea na juhudi za kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga Vyuo hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza mkakati huu wa kuendeleza elimu ya ufundi, Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa kila wilaya na mkoa unakuwa na chuo cha ufundi stadi ili kupanua fursa kwa vijana wetu. Kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali kwa kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatumia shilingi bilioni 40 kujenga vyuo 25 vya VETA katika ngazi ya Wilaya ambapo sasa hivi vipo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Aidha, kwa Jimbo la Mlimba na wilaya nyingine, Serikali inafanya juhudi ya kutafuta fedha kwa ajili ya kuhakikisha mkakati wa kuwa na VETA kila Wilaya unakamilika.
MHE. SUSAN L. KIWANGA Aliuliza:-

Jimbo la Mlimba lina mito mingi mikubwa inayotenganisha kata pamoja na vijiji.

Je, ni lini TARURA itajenga madaraja ya kudumu katika Kata ya Mbingu na Kijiji cha Chiwachiwa, Kata ya Igima na Kijiji cha Mpofu, Kijiji cha Ngajengwa (kwa Mtwanga), Kata ya Mchombe na Kijiji cha Igia, Kata ya Mofu na Kijiji cha Ikwambi, Kata ya Mbingu, Kata ya Utengule na Kijiji cha Ipugasa, Kata ya Kamwene na Kata ya Uchindile, Kata ya Msagati Kijiji cha Taweta na Kijiji cha Tanga, Kata ya Kalengakelu na Merela, Kata ya Mlimba - Sokoni na Kata ya Idete – Barabara ya Itikinyu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mbunge wa Mlimba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeanza kushughulikia ujenzi wa vivuko katika Halmashauri ya Kilombero hususani Jimbo la Mlimba. Katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali ilinunua na kuweka daraja la chuma katika Mto Kihansi linalounganisha Vijiji vya Chita, Idunda na Melera kwa gharama ya shilingi milioni 717.62. Kazi hiyo tayari imekamilika ikiwa ni hatua ya awali ya kuunganisha Kata za Chita na Kalengakele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka 2019/2020 TARURA imetenga kiasi cha shilingi milioni 127.94 kwa ajili ya ujenzi wa madaraja/makalvati katika barabara za Miembeni - Vigaeni, Kichangani katika Kata za Mbingu, Namwawala - Mofu katika Kata ya Mofu, Iduindembo - Utengule katika Kata ya Utengule, Manyasini katika Kata ya Mlimba, Ngwasi - Uga katika Kata ya Kalengakelu na Uchindile.

Aidha, TARURA kwa kushirikiana na Mfuko wa Barabara (Road Fund) imeweza kutenga kiasi cha shilingi milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la mita 25 katika barabara ya Kisegese - Chiwachiwa - Lavena ambapo kwa sasa lipo katika hatua za upembuzi yakinifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga fedha na kujenga barabara, madaraja na makalvati kwa awamu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. DEVOTHA M. MINJA (K.n.y. MHE. SUSAN L. KIWANGA) aliuliza:-

Kata za Mchombe, Igima, Mbingu, Namwawala na Idete katika Jimbo la Mlimba zilipelekewa mradi wa umeme kwa gharama nafuu lakini mradi huo umefanywa vibaya na hivyo kusababisha wananchi wengi kukosa umeme:-

(a) Je, ni lini Serikali itapeleka umeme kwa wananchi hao?

(b) REA ilikabidhiwa mkandarasi kupima maeneo yatakayounganishwa umeme katika vijiji vya Msolwa, Miembeni, Iduimdembo, Ipungusa, Matema, Lumumwe, Uchindile, Kitete na Ngwasi katika Awamu ya Pili; Je, kwa nini kazi hiyo inasuasua?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mbunge wa Mlimba lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa umeme kwa gharama nafuu (Low Cost Design) katika Mkoa wa Morogoro ulitekelezwa katika vijiji 14 vya Wilaya ya Kilombero. Kazi za mradi zilihusisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 35.2; njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilomita 82.6; ufungaji wa transfoma 262 za KVA 15 na 25; pamoja na kuunganisha umeme wateja 4,671. Gharama ya mradi ni shilingi bilioni 6.935.

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia mwezi Desemba, 2018 vijiji vyote 14 vya Mkusi, Njage, Ngajengwa, Igima, Mbingu, Kisegese, Namawala, Idete Magereza, Miwangani, Katurukira, Mihelule, Mikoleko, Msolwa Station na Nyange vilipatiwa umeme na wateja 4,286 waliunganishwa na huduma ya umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mradi huo wa Low Cost Design katika Wilya ya Kilombero hususan Jimbo la Mlimba, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza inapeleka umeme katika Jimbo la Mlimba katika vijiji vya Ipugusa, Msolwa, Kalengakelu, Miembeni, Iduindembo, Ipungusa, Matema, Lumumwe, Uchindile, Kitete, Idandu na Ngwasi. Kazi zinazofanywa kwa sasa ni pamoja na kusimika nguzo, kuvuta nyaya na kufunga transfoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia utekelezaji wa mradi huu, Kijiji cha Kalengakelu kimepatiwa umeme na wateja zaidi ya 20 kutoka Vitongoji vya Usalama na Samora vimeunganishiwa umeme. Kazi ya kupeleka umeme katika vijiji hivi itakamilika mwezi Juni, 2020, ahsante sana.