Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Haji Hussein Mponda (12 total)

MHE. DKT. HADJI H. MPONDA aliuliza:-
Mwaka 2012 Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya China, Railway Bureau 15 Group Corporation, waliingia mkataba wa miaka miwili wa ujenzi wa Daraja la Kilombero na barabara zake za maingiliano kwa gharama ya Sh.53.2 bilioni lakini mpaka sasa ujenzi huo bado haujakamilika:-
(a) Je, ni kiasi gani cha fedha kimetengwa na kutolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo tangu mkataba huo uanze?
(b) Je, ni lini daraja hilo litakamilika na kuanza kutumika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Hadji Hussein Mponda, Mbunge wa Malinyi, jirani yangu, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka wa fedha 2010/2011 hadi mwaka huu wa fedha 2015/2016, Serikali imekwishatenga jumla ya shilingi bilioni 25.59913 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Kilombero na gharama za Mhandisi Msimamizi anayesimamia ujenzi wa daraja hilo ni shilingi bilioni 2.75 bila ya Kodi ya Ongezeko la Thamani.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu ulipangwa kukamilika tarehe 20 Januari, 2015. Hata hivyo, haukuweza kukamilika katika muda uliopangwa kutokana na ufinyu wa fedha uliosababisha kuchelewa kulipwa kwa madai ya malipo ya mkandarasi kwa kazi zilizofanyika. Kutokana na tatizo hilo, mkandarasi alikosa mtiririko mzuri wa fedha za kufanya kazi na hivyo kupunguza kasi ya utekelezaji wa mradi.
Hata hivyo, hadi Februari, 2016 Serikali imeweza kulipa madeni yote ya mkandarasi aliyokuwa anadai. Aidha, Serikali itaendelea kumlipa mkandarasi kulingana na kazi atakazozifanya. Kwa sasa kazi ya ujenzi wa daraja imesimama kutokana na Bonde la Mto kilombero kujaa maji. Kazi ya ujenzi wa daraja itaanza mara maji yatakapopungua katika Bonde la Mto Kilombero.
MHE. OMARY T. MGUMBA (K.n.y. MHE. DKT. HADJI H. MPONDA) aliuliza:-
Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini iliahidi kupeleka huduma za umeme katika Hospitali ya Lugala ambayo ni hospitali pekee na tegemezi katika Wilaya nzima ya Malinyi. Katika kutekeleza agizo hili, Oktoba, 2014, TANESCO Mkoa wa Morogoro ilitengewa fedha kwa kuanza ujenzi huo wa 33KV, HT line ya kilometa 3.5 na kuunganisha umeme katika hospitali hiyo na Kijiji cha Lugala lakini hadi leo agizo hilo halijatekelezwa:-
(a) Je, sababu gani zilifanya mradi huo usitekelezeke licha ya kutengewa fedha?
(b) Je, ni lini hospitali hiyo muhimu kwa wakazi wa Wilaya ya Malinyi itapatiwa huduma ya umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Hadji Hussein Mponda, Mbunge wa Malinyi, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa kupeleka umeme katika Hospitali ya Lugala, Wilayani Malinyi haukuweza kutekelezwa kwa sababu fedha iliyotarajiwa kutengwa kutoka kwenye bajeti ya TANESCO ya mwaka 2014/2015 haikutengwa kutokana na ufinyu wa bajeti ya TANESCO. Hata hivyo, Hospitali hiyo pamoja na Kijiji cha Lugala vitapatiwa umeme mwaka huu kupitia bajeti ya TANESCO. Kazi hii itajumuisha sasa ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa tatu, ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa tano pamoja na ufungaji wa transfoma mbili za kVA 100 na kVA 200.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na utekelezaji huo, kazi nyingine itakayofanyika ni kuwaunganishia umeme wateja wapatao 116 katika maeneo hayo. Kazi hii inatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Juni, 2016 na itakamilika mwezi Julai, 2016 kwa gharama ya shilingi milioni 329.27.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA aliuliza:-
Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Mitambo wameahidi kuhamishia kivuko cha MV Kilombero II kwenda katika kivuko cha Kikove katika Mto Kilombero Juu (Mnyera) baada ya kukamilika kwa ujenzi wa daraja la Kilombero.
Je, ni lini matayarisho ya uhamisho wa Kivuko hicho yataanza rasmi kwa kuwa ujenzi huo wa daraja la Kilombero unatarajia kukamilika hivi karibuni?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Hadji Hussein Mponda, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), imeanza maandalizi ya kuhamisha vivuko vya MV Kilombero I na MV Kilombero II kuvipeleka eneo la Kikove katika Mto Kilombero kwenye barabara inayounganisha Mlimba na Malinyi. Wakala wa Barabara kwa kushirikiana na Wakala wa Ufundi na Umeme umefanya ukaguzi wa barabara ya Mlimba hadi Malinyi ili kubaini mahitaji ya miundombinu itakayowezesha kivuko hicho kufanya kazi katika eneo hilo la Kikove. Miundombinu hiyo ni pamoja na maegesho na barabara unganishi katika kila upande wa mto.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali ni kuhamisha vivuko vilivyopo eneo la Ifakara kwenda eneo la Kikove katika barabara ya Mlimba – Malinyi mara tu baada ya mradi wa ujenzi wa daraja la Mto Kilombero na barabara za maingilio kukamilika. Hivi sasa ujenzi wa daraja la Mto Kilombero umekamilika na Mkandarasi anakamilisha ujenzi wa barabara za maingilio ili daraja lianze kutumika.
MHE. OMARY T. MGUMBA (K.n.y. MHE. DKT. HADJI H. MPONDA) aliuliza:-
Vijiji vya Ngoheranga na Tanga katika miradi ya maji inayofadhiliwa na Benki ya Dunia (Phase II World Bank Project), vimepangiwa kufanyiwa upembuzi yakinifu, usanifu wa kina, uchimbaji wa visima na ujenzi wa miundombinu ya maji; zoezi hili limeishia tu kwa uchimbaji wa visima virefu nane na mradi kusitishwa.
(a) Je, ni lini Serikali itakamilisha utekelezaji wa miundombinu ya usambazaji wa maji ya bomba kama ilivyo katika vijiji vingine vinavyofadhiliwa na Benki ya Dunia?
(b) Je, ni lini Serikali itapelekea maji katika vijiji vilivyosahaulika vya Mtimbira, Majiji, Kiswago na Ihowanja?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali Mheshimiwa Dkt. Hussein Mponda, Mbunge wa Malinyi, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vya Ngoheranga na Tanga ni kati ya vijiji kumi ambavyo vilifanyiwa usanifu mwaka 2008 na mwaka 2010 vilichimbwa visima vitatu ili vitumike kwa ajili ya usambazaji wa maji ya bomba. Kati ya visima hivyo visima viwili vilikosa maji kabisa na kitongoji kimoja cha Mkanga kilipata maji kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2015 wataalam wa Halmashauri ya Wilaya kwa kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge walishauri vichimbwe visima virefu na kufungwa pampu za mkono kwa kila kitongoji ikiwa ni mbadala wa maji ya bomba. Ushauri huu ulizingatiwa na visima 13 vilichimbwa ambapo visima vinane vilipata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itakamilisha uwekaji wa miundombinu ya usambazaji wa maji ya bomba katika visima vinane vilivyopata maji kupitia Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ambayo imeanza kutekelezwa mwezi Julai, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, vijiji vya Mtimbira, Majiji, Kiswago na Ihowanja havijasahaulika kwani Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya maji katika vijiji hivyo kupitia Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Halmashauri inaendelea kukamilisha taratibu za utekelezaji wa miradi katika vijiji hivyo ili wananchi waweze kunufaika na huduma ya maji.
MHE. DKT. HAJI H. MPONDA aliuliza:-
Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo (SAGCOT) imekamilisha ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji, Itete ambapo imehusisha ujenzi wa miundombinu ya banio na mfereji mkuu wa kilometa 6.6, lakini katika kipindi kifupi cha matumizi ya skimu hii mfereji huo mkubwa umeshaanza kuharibika kutokana na kiwango duni cha ujenzi:-
(a) Je, ni lini Serikali itamalizia ujenzi wa mfereji mkuu na mifereji ya kati, ili kuendeleza kilimo katika hekta 7,000 zilizobaki katika skimu hiyo?
(b) Je, ni lini Serikali itafanya ukarabati wa mfereji mkuu uliobomoka katika kipindi hiki cha uangalizi?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Hadji Hussein Mponda, Mbunge wa Jimbo la Malinyi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa mradi wa umwagiliaji katika Skimu ya Itete ulianza mwezi Mei, 2013 na kukamilika mwezi Oktoba, 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, upanuzi wa mradi huu unategemea kwa kiwango kikubwa kiasi cha maji katika Mto Mchilipa, kwani usanifu wa awali ulibainisha hekta 1,000 ambazo ndizo zilizoendelezwa. Ili kuweza kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji katika eneo lililobaki Serikali inajipanga kufanya upembuzi yakinifu kuona kama kuna uwezekano wa kujenga bwawa ili kutunza maji ya mvua ya Mto Mchilipa, ambayo yatatumika katika kuendeleza eneo lililobaki.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ndogo iliyobomoka ya mfereji, Wizara yangu kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Kanda ya Morogoro imeshafanya mawasiliano na Mkandarasi aliyejenga skimu hiyo na amekubali kufanya marekebisho katika sehemu hiyo katika kipindi cha uangalizi.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA aliuliza:-
Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) iliingia mkataba wa utafiti wa uchimbaji wa gesi na mafuta na Kampuni ya Mafuta ya Swala (SOGTP). Katika utekelezaji wa mpango huo wamegundua kuwepo kwa wingi mafuta ya petroli na gesi katika vijiji vya Kipenyo na Mtimbira Wilayani Malinyi katika Mkoa wa Morogoro.
(a) Je, ni lini uchimbaji wa visima na uvunaji wa mafuta utaanza rasmi katika maeneo hayo?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwatayarishia wananchi wa maeneo hayo ili kuondoa migogoro inayoweza kujitokeza baina yao na Serikali kama vile gesi ya Mtwara?
WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Hadji Hussein Mponda, Mbunge wa Malinyi, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti wa mafuta katika kitalu cha Kilosa – Kilombero unafanywa na Kampuni ya Swala Oil Gas Tanzania ulianza mwezi Februari, 2012. Utafiti huo ulianza baada ya kusainiwa kwa Mkataba wautafutaji kati ya Serikali kupitia TPDC na Swala mwezi Februari, 2012.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo ambalo limeainishwa kwa ajili ya uchimbaji wa kisima hicho lipo katika Kijiji cha Ipera Asilia katika Hifadhi Tengefu ya Bonde la Kilombero.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kisima hicho kinatarajiwa kuanza kuchimbwa mwezi Septemba, 2018 kutegemea matokeo ya utafiti huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TPDC imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi wa maeneo kunakofanyika utafiti huo. Tarehe 06 hadi 17 Februari, 2017 TPDC kwa kushirikiana na Kampuni ya Swala ilitoa elimu ya masuala ya gesi na mafuta katika maeneo ya Halmashauri ya Mji huo ikiwa Mji Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Wilaya za Kilombero pamoja na Malinyi. Aidha, wananchi wa Kata ya Mtimbira, Njiwa pamoja na Kitete katika maeneo vijiji vya Mtimbira, Kipenyo, Ipera Asilia na Warama pia walipata elimu ya hifadhi ya mazingira pamoja na manufaa ya mradi huo.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA aliuliza:-
Wilaya ya Malinyi haina kabisa huduma za Kibenki ambapo wananchi hufuata huduma hizi katika Wilaya jirani ya Kilombero au Ulanga. Serikali kupitia taasisi za kibenki zikiwemo CRDB na NMB zimeahidi kuanza kutoa huduma toka mwaka 2015, lakini hadi leo hakuna utekelezaji wowote:-
• Je, ni lini huduma hizi zitaanzishwa rasmi katika Wilaya ya Malinyi?
• Wakati benki zikisubiri ujenzi wa Matawi yao; Je, kwa nini wasianze kutoa huduma hizo kwa kutumia matawi yanayohamishika (Mobile Service)?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dokta Hadji Hussein Mponda, Mbunge wa Malinyi, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko ya mfumo wa fedha nchini ya mwaka 1991, yaliitoa Serikali katika uendeshaji wa moja kwa moja wa shughuli za mabenki nchini. Hii ilifanyika ili kuruhusu ushindani huru na kuwezesha kuboresha huduma katika sekta ya fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua mchango mkubwa unaotolewa na taasisi za fedha katika maendeleo ya kiuchumimi, Serikali inatambua umuhimu wa wananchi wa Tanzania kupata huduma za kibenki karibu na maeneo yao. Aidha, Serikali inatambua pia kuwa huduma hizo za benki kwa wananchi lazima ziwe na faida kwa pande zote mbili yaani kwa mabenki na wateja pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua ukweli huo faida kwa pande zote na kwa kutilia maanani gharama za kuanzisha na kuendesha tawi kuwa kubwa, NMB na CRDB zinaendelea na upembuzi yakinifu kwa ajili ya kufungua tawi katika Wilaya ya Malinyi. Upembuzi huo ndiyo utakaotoa mwelekeo wa kufungua tawi au la, kwani tawi linatakiwa liwe endelevu kwa kujiendesha kwa faida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Malinyi ni moja ya Wilaya ambazo zinanufaika na mfumo wa utoaji huduma kupitia mawakala wa Fahari Huduma (Malinyi SACCOS na Zidua Waziri Shop) zinazoendeshwa na benki ya CRDB ambapo wateja wanapata huduma za kibenki ikiwemo kufungua akaunti, kuweka na kuchukua fedha, kuomba mikopo na kupata ushauri wa huduma za kifedha. Aidha, wananchi wa Wilaya ya Malinyi wanashauriwa kutumia njia mbadala kupata huduma za kibenki ikiwemo kupitia simu za mkononi yaani (Sim banking) ya CRDB na Banking on the Wheel ya NMB iliyoko Mlimba kwa kipindi hiki ambacho mchakato wa kufungua tawi unaendelea.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA aliuliza:-
Mkoa wa Morogoro umechaguliwa kuwa ni Ghala la Chakula la Taifa hususani katika mazao ya mpunga na miwa. Katika kutaekeleza hili Serikali imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ujenzi wa skimu za umwagiliaji katika Vijiji/Kata za Usangule – Mto Lwasesa, Igawa – Mto Furua, Lupunga – Mto Mwalisi na Kilosa – Mto Mwalisi.
• Je, ni lini kazi hiyo ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina itakamilika?
• Katika kipindi hiki cha maandalizi ya ujenzi wa mabanio haya ya kilimo cha umwagiliaji, je, Serikali ina utaratibu gani wa usimamizi wa ardhi husika ili kuepuka migogoro ya watumiaji wa mabanio hayo siku za usoni?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa maji na umwagiliaji naomba kijibu swali la Mheshimiwa Dkt. Hadji Hussein Mponda, Mbunge wa Malinyi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa Serikali imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu kwa ajili ya kuongeza wigo wa kilimo cha umwagiliaji katika maeneo mengi hapa nchini yakiwemo maeneo yaliyotajwa. Utekelezaji wa shughuli hizo unategemea upatikanaji wa fedha. Katika mwaka huu wa fedha 2017 Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kukamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika Vijiji/Kata za Usengule Mto Lwasesa, Igawa Mto Puma, Lupunga Mto Mwalisi na Kilosa Mto Mwalisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa lengo la kuepuka migogoro ya watumiaji wa mabanio ya maji kwa siku za usoni, Halmashauri ya Malinyi inashauriwa kuandaamipango ya matumizi bora ya ardhi ambapo ardhi inayofaha kwa matumizi ya kilimo cha umwagiliaji itabainishwa na kutengwa rasmi kwa matumizi hayo. Mipango hii itawezesha usimamizi wa kisheria wa ardhi inayofaa kwa umwagiliaji katika maeneo ya vijiji hivyo. Aidha, wakati wa kuanza ujenzi wa mabanio hayo kutaundwa vyama vya umwagiliaji kulingana na sheria ya umwagiliaji ya mwaka 2013. Vyama hivyo vitakuwa na jukumu la kusimamia maeneo hayo na uendeshaji wa skimu za umwagiliaji katika maeneo hayo.
MHE. HADJI H. MPONDA aliuliza:-
Serikali kupitia aliyekuwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda alitoa agizo la kuweka utatuzi wa kudumu katika migogoro ya ardhi iliyopo baina ya wananchi na Serikali katika maeneo ya vijiji na mapori tengefu. Aidha, katika kampeni zake Wilayani Malinyi Mheshimiwa Rais aliahidi uhaulishwaji wa Buffer Zone ya pPori Tengefu la Kilombero kwa vijiji vinavyopakana ili wawe huru katika shughuli zao, lakini hadi leo hakuna utekelezaji wowote.
(a) Je, utekelezaji wa ahadi na agizo hili umefikia wapi?
(b) Je, Serikali ina mpango mbadala kwa wananchi wanaoishi kihalali katika maeneo hayo ya Buffer Zone ya Pori Tengefu la Kilombero?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Hadji Hussein Mponda Mbunge wa Malinyi lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilianza kutekeleza agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu mstaafu mwezi Februari, 2016 wakati ilipozindua programu maalum ya upimaji wa vijiji na urasimishaji wa ardhi (Land Tenure Support Programme) vya Wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi unaosimamiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Programu hiyo ya miaka mitatu inafadhiliwa na DFID, DANIDA na SIDA kwa jumla ya dola za Kimarekani milioni 15.2.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi mwezi Mei, 2018 jumla ya vijiji 12 kati ya vijiji 14 vinavyopakana na hifadhi katika Wilaya ya Malinyi vimepimwa. Hii ni sawa na asilimia 85.71 ya vijiji vinavyotarajiwa kupimwa. Aidha, katika Wilaya ya Ulanga jumla ya vijiji saba vimepimwa na kati ya hivyo vijiji vitano alama za mipaka zimeshawekwa. Katika Wilaya ya Kilombero jumla ya vijiji 22 vinavyopakana na hifadhi vinatarajiwa kupimwa. Elimu na uhamasishaji umefanyika katika vijiji saba vya Wilaya hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia mpango huu, Serikali inaamini kwamba matumizi ya ardhi katika maeneo yanayozunguka Pori Tengefu la Kilimanjaro yakiwemo maeneo ya Wilaya ya Malinyi yatawekwa bayana na hivyo kupatikana kwa utatuzi wa kudumu wa migogoro ya ardhi iliyopo baina ya wananchi na Pori Tengefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizo, Serikali imeunda Kamati Maalum kwa ajili ya kuongea na wadau mbalimbali kwa lengo la kupata picha halisi ya mgogoro ili kutoa ushauri na mapendekezo yatakayowezesha kupata suluhu ya kudumu ya mgogoro wa matumizi ya ardhi katika Bonde la Kilombero. (Makofi)
MHE.DKT. HADJI HUSSEIN MPONDA aliuliza:-
Serikali imekuwa akiahidi kufungua barabara ya Miku1mi – Ifakara –Lupiro - Kilosa kwa Mpepo – Londo – Namtumbo (T16) yenye urefu wa kilomita 396 inayounganisha Mikoa ya Morogoro na Ruvuma:-
(i) Je, ni lini barabara hii itafunguliwa ili ianze kutumika kwa kuwaunganisha wakazi wa mikoa hii miwili?
(ii) Je, ni lini kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii ya T16 utakamilika na kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Hadji Hussein Mponda, Mbunge wa Malinyi, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa Serikali imepanga kuunganisha mikoa yote nchini kwa barabara za lami ikiwa ni pamoja na barabara ya kuunganisha Mikoa ya Morogoro na Ruvuma, kwa kupitia Barabara Kuu ya Mikumi – Kidatu- Ifakara – Mahenge/Lupiro – Londo hadi Lumecha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa barabara hii imekwishafunguliwa na inapitika wakati wa kiangazi tu kutokana na baadhi ya maeneo kutopitika wakati wa masika. Kazi ya kuimarisha sehemu zisizopitika inaendelea kadri Serikali inavyopata fedha. Serikali imeanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami kwa awamu na itaendelea kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Awamu ya Kwanza, Serikali ilijenga sehemu ya barabara kutoka Mikumi hadi Kidatu (kilomita 35.2); Awamu ya Pili, Serikali imekamilisha ujenzi wa Daraja la Kilombero lenye urefu wa mita mia tatu na themanini na nne pamoja na barabara unganishi yenye urefu wa (kilomita 9.142) inayoishia kwenye Kijiji cha Kivukoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza utekelezaji wa awamu ya tatu inayojumuisha ujenzi kwa kiwango cha Lami sehemu ya barabara kutoka Kidatu hadi Ifakara yenye urefu wa kilomita 66.9 ambapo Mkandarasi Reynolds Construction amekabidhiwa site ya kazi na kazi hii imepangwa kukamilika ifikapo tarehe 4 April, 2020.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu barabara ya Ifakara Mjini – Mahenge/Lupiro-Kilosa kwa Mpepo – Londo – Lumecha (kilomita 426,) usanifu wa kina ulikamilika mwezi Juni, 2017. Serikali inaendelea kutafuta fedha za ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA aliuliza:-

Wilaya ya Malinyi tangu mwaka 2014 mpaka sasa inakabiliwa na mlipuko wa panya wanaoshambulia mbegu za mazao ya Mpunga na Mahindi katika kipindi cha upandaji:-

(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kusambaza sumu maalum ya kuua panya hao?

(b) Kwa kuwa upatikanaji wa sumu ya panya una changamoto nyingi: Je, Serikali ina mkakati gani mbadala katika kukabiliana na panya hao waharibifu wa mazao shambani?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kumjibu Mheshimiwa Hadji Hussein Mponda, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, visumbufu vya mazao wakiwemo panya husababisha upotevu wa mazao nchini. Milipuko ya panya imekuwa ikitokea katika Mikoa ya Tanga, Lindi, Mtwara, Mbeya, Songwe, Iringa, Pwani, Shinyanga, Arusha, Kilimanjaro na Morogoro ikiwemo Wilaya ya Malinyi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wana wajibu wa kupambana na panya katika mashamba yao wakati wote kwa kutumia mbinu husishi wakiwa wachache. Aidha, inapotokea panya kuongezeka na kufikia zaidi ya 700 kwa ekari, Serikali huratibu ugawaji wa sumu kali kwa wakulima ambayo ina uwezo wa kudhibiti panya kuanzia dakika 45 hivyo kuzuia ufukuaji wa mbegu.

Serikali kwa kutambua athari za sumu kali kwa binadamu na viumbe wengine, wakati wa mlipuko hutumia wataalam wake kutoka Kituo cha Kudhibiti baa la Panya cha Morogoro kusimamia uchanganyaji wa sumu hiyo na chambo na kuwagawia wakulima ili kuhakikisha kuwa wakulima wanapata huduma hiyo kwa wakati. Wizara ya Kilimo inanunua sumu kabla ya msimu wa kilimo kuanza na kwa kushirikiana na TAMISEMI inahamasisha wananchi kuchangia chambo kwa ajili ya kuchanganya kwenye sumu hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati mingine ni pamoja na kutoa elimu ya udhibiti wa panya kwa Maafisa Ugani na wakulima, kuhamasisha wakulima kufanya usafi wa mashamba, kutumia mitego ya ndoo ya kuchimba ardhini, kuvuna kwa wakati, kutokulundika mazao shambani na kutumia sumu tulivu aina ya tambi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sumu hii ni matokeo ya utafiti uliofanywa na Wizara ili kupunguza matumizi ya sumu kali ambayo hutumika wakati panya wakiwa wachache. Aidha, nashauri Halmashauri ambazo hupata milipuko ya panya mara kwa mara kutenga bajeti kwa ajili ya kushirikiana na Wizara kufanya udhibiti endelevu wa panya mashambani.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA aliuliza:-

Mradi wa Maji unaotekelezwa chini ya Programu ya WSDP katika Vijiji vya Malinyi, Kipingo na Makerere unasuasua sana toka 2015 hadi sasa mradi huo haujakamilika:-

(a) Je, ni lini mradi huo utakamilishwa ili kuwawezesha wakazi wapatao 18,000 wa vijiji hivyo kupata maji safi na salama?

(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapelekea maji wakazi wa Vijiji vya Miembeni, Mchangani na Misegese Kata ya Malinyi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Hadji Hussein Mponda, Mbunge wa Jimbo la Malinyi, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuanzia mwaka 2015, Serikali inatekeleza mradi wa maji wa Malinyi unaotarajia kuhudumia Vijiji vya Kipingo, Makerere na Malinyi ambapo ni Makao Makuu ya Wilaya. Ujenzi wa mradi huo unagharimu shilingi bilioni 3.01. Hadi kufikia mwezi Oktoba, 2019, utekelezaji wake umefikia asilimia 80. Kazi zilizofanyika ni ujenzi wa miundombinu ya chanzo cha maji, ulazaji wa bomba kuu la maji urefu wa kilomita 22, ujenzi wa tanki la lita 150,000, vituo vya kuchotea maji 47 na ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji kwa umbali wa kilomita 14.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kukamilika kwa kazi hizo, miundombinu hiyo imeshindwa kufikisha huduma ya maji kwa wananchi kutokana na upungufu katika usanifu wa mradi. Serikali imemwagiza Mtaalam Mshauri anayesimamia ujenzi wa mradi huo kufanya marekebisho ili wananchi waweze kupata huduma ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Vijiji vya Mwembeni, Misegese na Mchangani kuna visima virefu viwili vyenye maji ya kutosha. Hivyo, kwa mwaka huu wa fedha 2019/2020 Serikali itafanya usanifu ili kuviendeleza visima hivyo ili kuboresha huduma ya maji kwa wananchi wa vijiji hivyo. (Makofi)