Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Haji Hussein Mponda (29 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu katika Bajeti hii ya Wizara lakini naomba nianze kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu aliyenipa afya ya kuniwezesha kutoa mchango katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uungwana hata ukipewa kidogo inabidi ushukuru. Nianze kwa kupongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri ambayo wanaianza ndani ya miaka miwili na nusu tunaona matokeo na tuna imani dhamira ya Serikali na mwelekeo wa Tanzania ya Viwanda mwaka 2025 tutakuwa tumeifikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Morogoro ni mojawapo ya mikoa miwili ambayo ina eneo kubwa. Mkoa huu wa Morogoro umepakana na Lindi, Pwani, Ruvuma, Iringa, Dodoma, Njombe, Tanga kwa maana tuna kilometa za barabara zipatazo 2,017. Katika kilometa hizo kilometa 538 za lami na kilometa 1497 ni za changarawe na vumbi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia bajeti iliyowekwa ambayo tunaizungumzia naomba kidogo Serikali, Wizara Mheshimiwa Mbarawa na Naibu Waziri wako na watendaji wengine hebu muiangalie kwa kina sana. Mkoa tumeomba ili tuhudumuie barabara hii yenye urefu wa kilometa 2,017 yenye madaraja 938, tumeomba bilioni 61, lakini tulizopewa ni bilioni 21 maana yake ni asilimia 43 tu ya tulichoomba. Nini Tafsiri yake? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa huu wa Morogoro una mikakati na miradi inayofahamika kuiokoa nchi hii kwenye janga la njaa. Kuna mkakati wa Fanya Mkoa wa Morogoro Kuwa Ghala la Taifa (FAMOGATA). Kuna miradi ambayo inafadhiliwa na marafiki zetu Wamarekani na wadau wengine wa maendeleo mradi wa SAGCOT na kuna mradi mwingine Feed the Future. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii ili iwezeshe nchi hii ijitegemee kwa chakula ni kwamba lazima kuwe na kilimo cha biashara. Sifa ya kilimo cha biashara kuwe na mambo matatu; mosi, kuwa na miundombinu ya uhakika; pili, kuwa na nishati na nishati tayari tunayo na maji, maji tunayo Mkoa wa Morogoro. Tulichopungukiwa ni barabara za uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira yetu ya Mkoa wa Morogoro, hizi kilometa 1,497 zinapita katika maeneo ya bonde na mvua inanyesha karibu miezi saba. Hali yake ni kwamba itakapokarabatiwa tu baada ya miezi mitatu imeharibika. Sasa nauliza hizi bilioni 21 sijui kama zitatuwezesha na hiyo dhamira ambayo tunakwenda ndani ya Mkoa wa Morogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili nifafanue zaidi nirudi kwenye barabara ambayo tutaizungumzia muda mrefu, barabara ya Ifakara – Lupilo – Malinyi – Londo – Lumecha mpaka Songea. Barabara hii ina kilometa 396, barabara hii inapita katika ardhi kama nilivyosema ni bonde lakini ardhi yenyewe ni tifu tifu, kwa hiyo inahitaji hela ya kutosha. Nimekwenda kwa Mheshimiwa Profesa Mbarawa mara mbili, nimeandika na barua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Engineer Mfugale, wanamuumiza bure huyu dada TANROADS Manager wa Morogoro, Engineer Dorothy Ntenga, anajitahidi lakini kwa hicho wanachompelekea wanamuumiza. Nami nimpongeze yeye na kundi lake zima pale TANROADS Morogoro wanajitahidi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekwenda ofisi kwa Mhandisi Mfugale zaidi ya mara mbili…

T A A R I F A . . .

MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea Taarifa yake na ndiyo maana nilikuwa nataka kuishinikiza huko huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ina mambo mawili ambayo inabidi Waziri ayaelewe. Tarehe 5 Septemba, 2015, wakati tunatafuta kutengeneza Serikali, tulimnadi Dkt. John Pombe Magufuli na tulimwambia moja ya shida ya wakazi wa Wilaya ya Malinyi ni miundombinu ya hii barabara. Pale pale alisema nimefanya kwenye hii Wizara, sasa nipeni nafasi kwa nchi nitaweza niikamilishe, maana yake ni kwamba hii ni ahadi ya Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni sera. Sera zinazungumza wazi kuunganisha barabara zinazounganisha mikoa ziwe za lami. Hii barabara ninayozungumzia hawa TANROADS wanaijua, inaitwa T16 na upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umeshakamilika miaka miwili iliyopita. Sasa inabaki kuanza kujenga hiyo barabara. Habari njema tayari wadau wameshajitokeza, ADB Bank, wao wako tayari kufadhili hii barabara. Sasa niwaulize namna gani wataweza kusogeza speed maana hii barabara sasa hivi imebaki miaka miwili na Rais hapa ameshaahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mawasiliano. Wilaya ya Malinyi kuna Kata mbili ndani ya Tarafa moja ya Ngoilanga Kata ya Kilosa Mpepo na Kata ya Biro. Kata hizi hazina kabisa mawasiliano. Nimeomba sana, habari njema ni kwamba wameniletea kupitia UCSAF ule Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, tumepata minara miwili mmoja Ngoilanga na mwingine Kiswago pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa Serikali wamewekeza kila mnara dola la Marekani 30,000, minara hii haifanyi kazi, hii minara ya Tigo, tumeeleza mara nyingi hebu tuone hii value for money, kwa nini hawa wanatuchezea kiasi hicho mbona minara yao ambayo haina ufadhili wa Serikali inafanya kazi? Kwa nini hii minara ambayo wanatengeneza sub-standard? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na minara hiyo lakini bado Kata yangu ya Ngoilanga iko kwenye giza, haina mawasiliano na vilevile Kata ya Biro bado hawana mawasiliano kabisa. Nimwomba Mheshimiwa Waziri, wakati anajumuisha awahakikishie maana ilikuwa ni mojawapo ya ahadi ambayo wameahidi. Mheshimiwa Profesa Mbarawa wewe ni rafiki yangu toka 2015 ulikuwa unasema mimi nitamaliza hii lakini mpaka leo hii hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba ya Wizara wameelezea ujenzi wa vivuko, kuna kivuko pale cha Kikove kinaunganisha Jimbo la Mlimba na Jimbo la Malinyi. Kivuko kile wameweka milioni 400 kwa ajili ya kumalizia ujenzi. Niwaombe, hata wakimalizia ujenzi, kile kivuko bado kuna changamoto, hakuna barabara ya kufika pale kutoka Ngoilanga. Niwaombe, kwenye hii bajeti watafute na mifumo mingine au vyanzo vingine wakimaliza kile kivuko cha Kikove basi ili kitumie barabara ile sasa kutoka kwenye Kijiji cha Ngoilanga iweze kufika pale kwenye kivuko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema, kuniwezesha kusimama leo na kutoa mchango wangu katika mada iliyoko mezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuongoea katika Bunge hili, naomba pia nichukue fursa hii kuwashukuru wapiga kura wa Jimbo la Malinyi, Jimbo hili siyo jipya tumebadilisha jina zamani lilikuwa linaitwa Ulanga Magharibi. Nawashukuru sana kwa kunirudisha kwa awamu ya pili najua wana imani kubwa kwangu na naomba niwaahidi kwamba, sitawaangusha, nitawatetea, tutafanya kazi pamoja kuleta maendeleo katika Jimbo na Wilaya yetu mpya ya Malinyi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwetu Malinyi na Wilaya ya Ulanga. Mvua zinaendelea kunyesha, mvua hizi zimeleta madhara makubwa, zimeharibu miundombinu, zimeharibu na mashamba. Sasa hivi ninavyozungumza maeneo mengine hayafikiki kabisa, kutokana na uharibifu wa barabara uliosababishwa na hizo mvua. Kama mtakumbuka siku ya Jumanne, nimetumia Kivuko kile kilichozama Kivuko cha Kilombero, saa kumi na mbili jioni nimetoka Jimboni nimetumia kile Kivuko, lakini saa moja na nusu Kivuko kilekile kimezama na kimepoteza ndugu zetu pamoja na mali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Serikali wamekuwa karibu sana na wananchi na wamekuwa wasikivu mara moja, siku ya pili asubuhi tulikuwa na Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Profesa Mbarawa, ameahidi na nawaomba tafadhali Serikali ahadi ambazo mmeziahidi naomba niwakumbushe maana muda unakwenda. Ahadi ya kwanza ya kurudisha haraka mawasiliano, Ulanga na Malinyi wako kwenye Kisiwa, kwa hiyo tumeahidiwa mawasiliano yatarudishwa, pamoja na ngalawa zilizoletwa, au boti zile za Wanajeshi hazitoshelezi. Tuliomba na tunaendea kuomba, warudishe kivuko kingine pale, maana bila kivuko pale jamani wale watu wanaishi katika maisha hatari na wale watu wanaishi katika maisha magumu gharama za bidhaa zinazidi kuongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inayotishia nyingine stock za dawa zinakaribia kuisha mwishoni mwa wiki hii, hatujui baada ya wiki hii tutaishije kwa wale ambao watapata bahati mbaya ya kuugua. Pamoja na maombi hayo na kwa kuwa Serikali imeahidi, tunaomba ahadi ile itimizwe, umaliziaji wa ujenzi wa lile daraja la Kilombero. Serikali wameahidi kwamba kabla ya mwezi wa 12 mwaka huu daraja lile litakuwa limekamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, sasa naomba nijikite mchango wangu katika mada iliyokuwa mezani kwetu na nitajikita katika maeneo matatu, mawili hasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kuhusu ugharamiaji wa Mpango huu. Tumeshuhudia na taarifa ambayo tumeipokea bado miradi mingi kutegemea na Mpango wa mwaka jana, haikuweza kutimizwa. Changamoto kubwa hatuna fedha ya kutosha, wenzangu wameshauri, na mimi ninashauri ile ripoti ya Chenge one, ripoti ya Chenge two ifike muda sasa Serikali mtusikie, muanze kutekeleza hasa ninyi wataalamu ripoti ile imechimba kwa kina zaidi na wataalam hao kwenye Kamati ile tunaendelea kuishauri mtekeleze angalau machache muone namna gani mnaweza mkaongeza pato la nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutegemea na taarifa ya ripoti ya tafiti iliyofanywa na Dkt. Ngowi na wenzake wa Chuo Kikuu cha Mzumbe wakishirikiana na Norwegian Church Aids imebainika kuna upungufu mkubwa, watu hawalipi kodi. Wale wanaostahili kulipa kodi karibu milioni 15 nchi hii hawalipi kodi na asilimia ambayo imetoa ile ripoti ni asilimia 12 tu ndiyo wanaolipa kodi, maana yake nini asilimia 88 nchi hii tunakosa mapato. Kwa hiyo, kama Serikali wakija na mfumo mwingine na wigo wakiupanua zaidi, haya mambo tunayozungumza hapa, miradi inashindwa kukamilika itakuwa imefikia mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashauri Wizara hii ya Fedha na Mipango, hebu wasilianeni, muungane na watu wa NIDA, iwapo kama wenzetu wa NIDA watamaliza zoezi la Utambulisho wa Kitaifa, ni rahisi kuoanisha zile nationa ID na kumbukumbu za watu hao ambao wanakwepa siku zote kulipa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili, utahusu maeneo wezeshi kwa viwanda, na nitayabainisha maeneo kama matatu ama manne. Tunazungumzia viwanda ambavyo tunavyovilenga ni vile viwanda vitatumia malighafi ya kilimo, mifugo na uvuvi. Nikitoa mfano katika maeneo ambayo ninatoka maeneo ya Wilaya ya Malinyi, Kilombero na Maeneo ya Wilaya ya Ulanga. Maeneo haya yamebainishwa katika Mpango wa SAGCOT lakini kwenye Mpango huu wa mwaka huu, hakuna chochote kinachozungumzia SAGCOT. Jamani mpango ule ni kuwawezesha wakulima kulima kilimo cha biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kilimo cha biashara kitoe tija kuna mambo manne tu, kuna suala la nishati, miundombinu, maji na masoko. Suala la nishati Jimbo letu la Malinyi, ni vijiji 20 tu ndio vimeunganishwa na ule mradi wa REA kwa umeme. Kama vijiji vyote vingepata umeme hii ingekuwa na tija sana kwa wakulima kuongeza thamani ya mazao yao na upande wa pili kuongeza ajira kwa watu wanaojihusisha na kilimo, sasa niiombe basi Serikali wamalizie ile miradi ya REA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema kwamba ili kilimo kiwe na tija kuwe na barabara. Barabara zetu Wilaya ya Malinyi, Ulanga ni aibu, sasa hivi huwezi kufika maeneo mengine kwenye Wilaya ya Malinyi, kama ile Tarafa ya Ngoilanga ina watu 60,000 lakini leo hawafikiki kabisa sababu ya ubovu wa barabara. Mkandarasi yuko site, lakini amekimbia kwa sababu Serikali wenyewe wanajua, kwa hiyo naomba nisisitize katika mpango huu.
La kwanza, malizieni ile barabara ambayo tunaizungumizia, kuanzia Kidatu, Ifakara, Lupilo kwenda Mahenge, kutoka Lupilo kwenda Malinyi Kilosa kwa Mpepo, Londolumecha - Namtumbo. Barabara hii yenye kilometa 396 ni muhimu sana. Maana siku zote mnaendelea na mchakato. Hata kwenye taarifa hii mliyoiandika watu wa mipango bado mmeweka barabara hii inaendelea na mchakato ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina mpaka lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashauri, kwa sababu Mkandarasi yuko site, mumuongezee spidi amalizie huo mchakato wa upembuzi yakinifu. Baadaye tuzungumzie mwaka kesho tuanze kujenga hii barabara. Haitakuwa na tija tu peke yake kwa wakazi wa maeneo haya, barabara hii ni shortcut ya kutoka Mikoa ya Kusini kuja Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nimalizie ya mwisho kuhusu Utawala Bora. Wilaya ya Malinyi ni mpya na Wilaya hii ipo pembezoni, tunaomba mtuwezeshe ujenzi wa majengo ya Wilaya hii.
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako tayari umekwisha.
MHE. DKT. HADJI HUSSEIN MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wa Wizara kwa kufanikisha majukumu yao katika kiwango cha kuridhisha. Naomba nijikite mchango wangu katika sehemu zifuatazo:-
(a) Kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya kilimo; usambazaji wa pembejeo nashauri uende sambamba na mahitaji halisi kwa eneo husika na muda muafaka, mfano wakulima wa Bonde la Kilombero hususan Wilaya ya Malinyi na Ulanga hawahitaji sana mbolea, ni vema Serikali ikatoa pembejeo za mbegu bora za mpunga badala ya mbolea ambayo haitumiki au kuhitajika sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima wa zao la mpunga bado wana changamoto kubwa ya soko la uhakika. Naiomba Serikali waendelee kununua mpunga kupitia Mfuko au Wakala wa Hifadhi ya Chakula (NFRA). Katika mwaka huu, Wakala waweke utaratibu wa kuja kununua mpunga katika Wilaya za Malinyi, Ulanga na Kilombero badala ya kujikita zaidi maeneo ya Mbeya na Sumbawanga peke yake.
(b) Utatuzi wa migogoro ya wakulima na wafugaji; naipongeza Serikali katika kuanzisha na kutekeleza zoezi la mpango wa matumizi bora ya ardhi na upimaji wa ardhi. Mkakati huu peke yake hautamaliza kutatua migogoro inayoendelea bila ya kujenga miundombinu rafiki kwa mifugo ikiwemo kujenga visima vya maji, malambo, majosho katika maeneo tengwa kwa ufugaji. Serikali inaweza kuwawezesha wafugaji kupitia SACCOS zao kujenga miundombinu hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nashauri Serikali kuelimisha na kuwezesha utaratibu wa kudumu wa uvunaji wa mifugo kwa kuwezesha upatikanaji wa soko la mifugo.
(c) Uvuvi; uwezeshaji wavuvi; katika bajeti hii Serikali imejikita zaidi katika uvuvi wa bahari au ziwa na kuwawekea taratibu za uwezeshaji wake. Nashauri Serikali pia kuangalia uwezeshaji kwa wavuvi katika mito mikubwa kama vile Kilombero, Rufiji na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Shukurani.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kunipa wingi wa afya ambayo inaniwezesha leo kusimama hapa na kutoa mchango katika mada ambayo tunaizungumzia. Vile vile naomba nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi leo ya upendeleo ili nami nitoe mchango wangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na pongezi za dhati kabisa, nimpongeze Mheshimiwa Waziri Profesa Ndalichako na timu yako, mmeanza vizuri. Mmeanza vizuri wala msitikisike, mikakati mnayoweka tuna imani mnaweza mkatutoa hapa tulipo. Pia, niipongeze Kamati mahiri, Kamati ya Huduma za Jamii; Kamati hii mchango wao na upembuzi waliofanya kwa kweli umesaidia, pengine utaboresha zaidi hii sekta ya elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wengi wamelalamika, wametoa maoni yao na ushauri; kwa kifupi picha iliyojitokeza hapa, hali ya elimu sio nzuri. Mchango wangu utajikita huko huko na kutoa mfano wa hali halisi. Mheshimiwa Waziri matokeo ya mwaka jana ya vijana wetu wa Kidato cha IV, Wilaya yangu ya Malinyi ni miongoni mwa zile shule 10 ambazo hazikufanya vizuri, Wilaya yangu imetoa shule tatu, zile shule ambazo zimeshika mkia. Matokeo haya yalitusikitisha, yalitushtua, kama wadau wa elimu tulirudi tukakaa chini, kulikoni? Tulijua, lakini imebidi kama wanasayansi twende kwa kina zaidi. Tumeongea na Bodi za shule, tumeongea na Walimu, tumeongea na wananchi, baadaye tumebaini yafuatayo ambayo yanalinganalingana na wenzangu, lakini yangu ni mabaya zaidi na ndiyo maana yamekuja kutokea matokeo yale. Tuna upungufu mkubwa wa Walimu, hususan Walimu wa Masomo ya Sayansi. Tunahitaji Walimu 72, lakini hali ilivyo sasa hivi kule hata kama walimu hawa wakija changamoto nyingine nitazieleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la mabweni; hizi Shule za Sekondari za Kata ambazo ndiyo nyingi katika Jimbo langu, katika Wilaya hii Mpya ya Malinyi zinachachukua wanafunzi kutoka vijiji mbalimbali. Shule nyingine ya Kata kati ya vijiji vitano mpaka kumi, lakini vijiji hivi viko mbali na hizo shule.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Shule ya Sekondari Ngoeranga, wanafunzi wengine wanatoka Kijiji cha Kilosampepo, kilometa 22! Kwenda na kurudi mtoto huyu maana yake kwa siku atembee kilometa 44! Kwa hiyo, kulikuwa na dhana pale na ingeweza kuleta jibu hilo, mabweni. Hata hivyo, nimeona azimio la Mheshimiwa Waziri la uboreshaji wa mazingira ya kufundishia na mazingira ya kujifundishia, lakini mmeelekeza mboreshe hizo shule kongwe.
Nashauri waanze kule kwenye matatizo kweli kweli ambapo kama wanaweza wakayarekebisha matatizo haya, hizo shule kongwe tayari wako pazuri! Mheshimiwa Waziri tumeongea, ameonesha dhamira, naomba asirudi nyuma kwamba, baada ya Bunge hili, pamoja na Mkurugenzi wa TEA watakwenda Wilaya ya Malinyi, waje wayaone haya mambo ambayo mtayazungumza, yamechangia sisi kuwa wa mwisho katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana. Hawa walimu niliosema hata kama wakiletwa, nyumba ni changamoto. Shule nyingine hazina kabisa nyumba ya Mwalimu na shule hizi ziko vijijini wakati mwingine hata hizo nyumba za kupanga, aghalabu, hazipatikani kirahisi. Shule hizi kwa mazingira yalivyo kule tunapakana na mito mingi, tunahitaji madaraja, tunahitaji na barabara, navyo ni kikwazo, Walimu na wanafunzi hawa kufika kwa wakati hasa kipindi cha masika.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliliona tena tatizo lingine, mfumo wetu huu wa elimu, mtoto huyu anaanza darasa la kwanza mpaka la saba anajifunza Kiswahili, anapoingia form one Kiingereza, hapo ndio shughuli. Masomo yote ni ya Kiingereza, kwa hiyo ukiangalia ufaulu wao form two wanakwenda vizuri lakini wanapoingia form three, form four ni hatari.
Mheshimwa Naibu Spika, sasa mimi nashauri, kwa nini sasa kama hizi shule binafsi wanaweka pre-form one mwaka mzima ni bora tuchelewe lakini tufike. Kwa hiyo, vyema watoto hawa kabla hawajaendelea kuanza form one walio-pass darasa la saba waanze pre-form one kwa mwaka mzima, wawezeshwe masomo ambayo yanawasumbua, masoma haya ni kiingereza masomo ya hisabati na sayansi. Baada ya hapo ndio waingie kidato cha kwanza mpaka la nne. Hili linawezekana, nimeongea na Mheshimiwa Waziri ukawa unasitasita ukasema sijui kama itawezekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba Wabunge wenzangu tukubaliane, ndio maana nimesema chelewa lakini ufike, hawa tunawawahisha wa miaka minne matokeo yake wanakuja kuishia wengi wao asilimia karibu 30 ya watoto wetu mitihani ya form four wanapata division zero.
Mheshimwia Naibu Spika, haya tuliweza kuwezesha sasa tunapitisha hii bajeti, naona wengine mtakwenda mtafika hatua hii mtaigomea, hamtaki kupitisha hii bajeti. Lakini mimi nawashauri na kwanza naomba nishauri Kamati ya Bajeti hii fedha iliyotengwa ni ndogo sana katika Wizara hii, hii sekta ya elimu ni nyeti, ni muhimu sana, tunaomba ile wiki ya kujadili na Serikali Kamati ya Bajeti makae muongeze fedha hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata ukiangalia bajeti hii muundo wake yaani ile structure asilimia 17 ndio inazungumzia elimu ya msingi na elimu ya sekondari, asilimia 48 elimu ya vyuo vikuu, wapi na wapi! Kama kweli tunataka twende uchumi huu wa viwanda wafanyakazi wengi watatakiwa ni hawa wa elimu ya kawaida, elimu hii ya form four, kwa hiyo ingekuwa vyema zaidi tungeboresha hii bajeti, hiyostructure tuweke fedha nyingi zaidi tuziwekeze kwenye elimu ya misingi na elimu ya sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wamelalamikia, wamechangia wameonesha hoja yao, na mimi naungana nao sula la maslahi ya walimu. Wala nisitafune tafune kwa kwali walimu wanaonewa, mafao yao yanasua sua.
Kwa nini wafanyakazi wengine malipo yao pamoja na sisi Wabunge yanaenda chapu chapu kwa nini hawa walimu bado kilia siku sauti ni hiyo hiyo, kila siku wanalalamika lakini kama ni kusikilizwa kidogo kidogo.
Mheshimwa Naibu Spika, naomba nimalizie kuhusu COSTECH (Taasisi ya Sayansi na Teknolojia). Tunasema tunataka tuipeleke nchi hii kuwa ya viwanda, uchumi wa kati, kuwa nchi ya teknolojia ya kisasa, lakini hatufiki huko kama hatuwezi tukawezesha taasisi hii kufanya kazi zake kikamilifu. Maana wao ndio wanatengeneza, wanasimamia suala zima la utafiti na utafiti majibu yake ndio yanatoa ushuhuda au evidence, ushuhuda huu ndio unaotufanya sisi watunga sera, sisi wasimamizi wa hii Serikali namna gani unaweza kuishauri vizuri kwa kutegemea matokeo ya utafiti.
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti iliyowekwa hapa ni 0.04% ni kidogo mno na mimi nakumbuka utaratibu wetu tulikubaliana COSTECH itengewe bajeti ya asilimia moja ya bajeti ya Serikali. Sasa leo kiko wapi? Tunawashauri Serikali na Kamati hii ya Bajeti mrudi mpitie bajeti ya COSTECH kama kwa fedha hii hawawzi wakafanya chochote matokeo yake tunalaumu ndio tunaruka ruka kwa sababu wakati mwingine tunakosa vigezo, ushahidi kwenye mipango yetu na sera tunazozipanga. Nakushukuru kwa kunipa nafasi tena na naunga mkono hoja asate.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wa Wizara kwa utekelezaji wa majukumu yao kwa kiwango. Mchango wangu utajikita katika sehemu zifuatazo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, sekta ya masoko. Wakulima wa mazao ya nafaka wanakabiliwa na changamoto kubwa ya masoko ya uhakika kwa mazao mfano soko la mpunga na mahindi kila mwaka yanakabiliwa na kutokuwa na soko la uhakika. Nashauri Serikali kupitia Wizara ichukue hatua katika kutafuta masoko ya mazao haya katika nchi jirani kama Sudan ya Kusini, Kenya, Zambia na nchi jirani ambazo zina uhaba wa mazao haya badala ya wafanyabiashara binafsi kusimamia na utafutaji wa masoko kwa mazao hayo makuu ya nafaka. Aidha, Serikali kwa kupitia vyombo vya habari watangaze taarifa za masoko kwa wakulima ili wawe na uwezo katika kujadili (debate) vyema bei inayolipa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni kuhusu Bodi ya Leseni za Maghala. Naipongeza Wizara kwa mpango wake katika kuboresha na kuongeza wigo wa mkopo kwa wakulima vijijini ili kuongeza bidhaa za kilimo. Kwa kuwa Mkoa wa Morogoro ni ghala ya chakula la Taifa na moja ya Mikoa yenye viwanda vingi, naishauri Wizara ianzishe Ofisi ya Leseni ya Kodi za Maghala katika mkoa wa Morogoro ili kusogeza huduma zaidi na karibu ya wakulima ili kuongeza uwezo wao wa kuzalisha mazao kwa wingi/ufanisi kwa kuwezesha Mkoa wa Morogoro kutekeleza majukumu yake kiukamilifu kuwa ghala la chakula la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hotuba ya Wizara hii, lakini kabla sijaanza hivyo naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa neema, ameniwezesha leo kwa afya njema kusimama mbele yako na kuweza kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali yangu, Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya uongozi wa Dkt. John Pombe Magufuli kwa mwanzo mzuri aliouanza. Tunaiomba Tanzania na Watanzania wengine wote bila kujali vyama, tumuunge mkono kiongozi huyu, ana dhamira ya kweli na tukimuunga mkono tutafika mbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mchango wangu nitajikita zaidi kwenye sekta ndogo ya wanyamapori na migogoro inayoendelea baina ya mapori haya tengevu au mapori ya akiba na vijiji ambavyo vinapakana. Wenzangu wameongea sana, nitaongea kwa vielelezo zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mtakumbuka mwaka 2009 wakati tunarejea Sheria ya Wanyamapori, Bunge hili lilitoa maelekezo kwa Serikali na yalikuwa mawili, kwamba, kwa kuwa sheria zamani ilikuwa inaruhusu matumizi ya binadamu katika mapori haya ya akiba, mapori tengevu, lakini sheria ile baada ya kurejewa hairuhusu tena. Kwa hiyo, lilikuwa la maangalizo mawili, Serikali ilipewa kazi wakaifanye, lakini mpaka leo bado linasuasua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ya kwanza waangalie umuhimu wa uendelezaji wa mapori tengevu hayo na mapori ya akiba. La pili, urekebishaji wa mipaka, lakini naweza kusema na wote tunashuhudia mpaka leo Serikali hawajafanya. Naomba nimwombe ndugu yangu, Profesa Kaka yangu, yeye amebobea kwenye mambo haya na hapa kama upele umepata mkunaji, hembu athubutu kufanya haya mawili. Kwa kuwa mazingira haya wananchi tunalalamika, Serikali wanashindwa kuchukua hatua, nitatoa mfano kwanye pori tengevu la Kilombero. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2012 baada ya kusisitiza kusukuma sana ndiyo kidogo walijaribu kuweka mipaka, kurejea ile mipaka ya pori tengevu baada ya marekebisho ya ile Sheria ya Wanyamapori 2009, lakini walichofanya wamemega ardhi ya vijiji na ndiyo maana mgogoro kule bado unaendelea. Maeneo ya Vijiji vya Igawa, Kiwale, Lupemenda na vijiji vingine eneo lile wamekuja kurekebisha ile mipaka wamemega ardhi yao, wananchi wale wanapotumia ardhi yao kiuhalali, ndiyo migogoro kila siku inaendelea na wananchi wale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama haitoshi, badala ya kurekebisha mipaka mrudishe ardhi ile sasa kwa Serikali ya vijiji eneo lile mkatengeneza kitu kinaitwa buffer zone. Buffer zone kwenye eneo lile la bonde la Mto Kilombero kwenye Wilaya zile mbili; Malinyi na Ulanga ina range inatoka kilomita moja, maeneo mengine mpaka kilomita 12. Ukubwa wote huo wanaita buffer zone, matokeo yake sasa mmeingiza vijiji 18 na vitongoji karibu 22, vijiji na vitongoji hivyo vimesajiliwa, watu wanaishi kihalali, kuna shule za msingi, kuna mashamba, wananchi wanaishi kule kihalali, lakini wanaishi kila siku kwa hofu. Hawana amani, wanashindwa kujiendeleza kwa sababu hawajui hatima yao ni nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Kijiji cha Kiswago, kuna Kitongoji cha Salamiti, kitongoji kile kinashindwa kuendeleza shule ya msingi, watoto inabidi watoke kule kilomita 18, mtoto huyu wa shule ya msingi miaka saba aende mpaka shule ya msingi Kiswago kwenda na kurudi kilomita 36 kwa siku. Matatizo yote haya ni kwa sababu bado wameng‟ang‟ania, bado hawataki kutoa uamuzi ili maeneo ambayo wametenga kama buffer zone watayarejesha kwenye ardhi ya kijiji ili wananchi waendeleze pale kwa maendeleo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nimesema na mara ya mwisho na mpaka Bunge lililopita watani zangu majirani walikuwa wananiita mzee wa buffer zone na nitaendelea kwa sababu Serikali bado kila wakiambiwa hawasikii. Mara ya mwisho kuuliza swali hapa Bungeni 2015 mwezi wa Nne, niliuliza swali hapa nikitaka majibu ya Serikali kuhusu suala la buffer zone ndani ya pori tengevu la Kilombero.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu ya Serikali walisema Serikali tayari kupitia Waziri Mkuu, wakati huo Mheshimiwa Mizengo Pinda alitoa agizo kwamba Wizara hizi tatu,Wizara ya Maliasili,Wizara ya Mazingira, Wizara ya Ardhi na TAMISEMI pamoja na Ofisi ya Mkoa Morogoro, wakae pamoja na walisema tayari wameshakaa na wataalam wameshapendekeza na taarifa njema kwamba tayari hata tafiti za TAWIRI zimeelekeza maeneo yale ya buffer zone maeneo mengi siyo rafiki tena kwa wanyama wanatakiwa wayarudishe kwa matumizi ya binadamu, matumizi ya wananchi kwa ajili ya kilimo na mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ilikuwa 2015 mwezi wa Nne, wamesema tayari wataalam wameshakaa wamependekeza. Namwomba Mheshimiwa Waziri Profesa, leo atakapohitimisha hapa, wananchi wa Malinyi, wananchi wa Ulanga wanataka wasikie nini hatima ya hii buffer zone.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake wanaishi kule kwenye buffer zone kila siku wanawasumbua, hiyo mifugo kila siku wanawapiga faini, wengine wamefika hatua mpaka wamekata tamaa, wakienda Lindi wanafukuzwa, wakienda maeneo mengine wanafukuzwa, hawa Watanzania wana haki ndani ya Katiba na sheria zinawalinda, mpaka lini wataendelea kuwanyanyasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali ndiyo inayosema nawashauri tena, habari njema Sheria ile ile ya 2009 ya Wanyamapori, ukiangalia kifungu cha 21 imempa mamlaka Waziri, wakati huo kabla hawajafanya maamuzi yao, lakini eneo lile la buffer zone Waziri ana mamlaka ya kutoa matumizi ya eneo lile. Sasa namwomba Profesa leo anapohitimisha atuambie kwa kutumia mamlaka aliyokuwa nayo, ni lini sasa hiyo buffer zone ndani ya pori tengefu la Kilombero inarejeshwa kwa wananchi kwa ajili ya maendelezo ya kilimo na mifugo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo naona nisichanganye mada, nataka nimalizie hapo lakini naomba unipe nafasi wakati tunapopitisha bajeti hii nataka nishike shilingi ya kaka yangu. Kama hatakuwa na kauli thabiti juu ya suala hili la kuondoa migogoro kati ya Pori Tengefu la Kilombero na wananchi wanaoishi vijiji jirani na pori hilo, basi nitakuwa tayari ndugu yangu hata kama hatutaelewana siku nyingine leo nitatoa shilingi yake na naomba nitendewe hiyo haki, nataka nikamate mshahara wa Waziri leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa ujumla kwa utekelezaji wa majukumu yake kwa ufanisi. Mchango wangu utajikita katika mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sekta ndogo ya wanyamapori/migogoro ya mipaka katika marejeo ya Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 2009; Serikali ilielekezwa kutathmini juu ya uendelezaji wa mapori ya akiba na mapori tengefu yote yaliyoko nchini ili kubaini uendelezaji wake, aidha, marekebisho ya mipaka yake ili kuondoa migogoro ya ardhi baina ya mapori hayo na ardhi ya vijiji vinavyopakana navyo, hadi leo maelekezo hayo ya Bunge bado hayajatekelezwa na Serikali na badala yake ni kuendelea kwa migogoro katika mapori hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la migogoro ya aina hii hususan kwa pori tengefu la Kilombero na vijiji jirani, nimeliongelea sana na mara ya mwisho Serikali kupitia Mheshimiwa Mizengo Pinda, Waziri Mkuu Mstaafu, Aprili, 2014 alitoa agizo kwa Wizara ya Maliasili kuweka utatuzi wa kudumu katika mgogoro wa ardhi kwa pori hilo na mengine lakini hadi leo agizo hili halijatekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja yake atoe kauli ya wazi, ni lini ardhi iliyoko katika eneo la buffer zone katika pori tengefu la Kilombero itarejeshwa katika ardhi ya vijiji ili iweze kutumika kwa matumizi ya kilimo na mifugo ambayo ndio uhai wa wananchi hao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani na nitaunga mkono kama Waziri atatoa majibu ya kuridhisha katika ombi la wananchi wa Ulanga na Malinyi.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu katika mada iliyopo mbele yetu. Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kunipa uwezo wa afya leo kusimama hapa mbele na mimi nitoe mchango katika mada hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wamekupongeza na mimi nitakuwa mchoyo wa fadhila. Pongezi hizo ni kweli unastahili, za haki na za dhati kabisa kwamba nafasi uliyokalia hapa unaiweza. Sisi tuko pamoja nawe, tunakuomba usiyumbe, endelea kurekebisha Bunge hili kama mhimili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu katika bajeti hii nitajikita zaidi kwa mambo yafuatayo na nitaanza na mambo ya mapato. Changamoto kubwa ni kwamba bajeti tunapitisha lakini inafika wakati tunashindwa kutekeleza bajeti hii kwa sababu ya mapato. Kamati ya Bajeti toka kipindi cha Mwenyekiti Chenge wametoa maelekezo, wametoa ushauri lakini Serikali ni muda sasa bado hawatilii maanani vyanzo vipya vya mapato ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachofanyika Serikali yetu inaendelea na vile vyanzo vya kawaida na matokeo yake yanatupelekea tunapofika nusu ya mwaka wa kifedha tunarudi tena tunakaa chini tunaanza kupitisha bajeti na matokeo yake tunashindwa kutekeleza miradi mingi ambayo tumeiweka kwenye bajeti. Kwa kuwa kipindi hiki tunaweza tukajifunza, basi muanze kutekeleza angalau yale ambayo Kamati wamependekeza, ndani ya miezi sita pengine mnaweza mkaleta matokeo mapya zaidi mkayafanyia kazi katika bajeti ijayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kingine hapa nimekiona kidogo, natoa angalizo kwamba, wanataka waongeze wigo wa walipa kodi. Angalizo langu wigo huo wanapotaka kuupanua wasije wakagusa hawa wananchi wa kawaidam maana wanasema wanataka wachukue sekta zisizokuwa rasmi, kwa mfano wenye maduka madogo madogo ambao wengi wako vijijini, wenye miradi ya Sh. 70,000 mpaka Sh. 100,000 kama watawaingiza hawa kwamba ndiyo wanaongeza wigo wa walipa kodi, hili ni angalizo, Serikali watakuwa wanawaonea kwa kuwa hawa kwa lugha nyingine ni wajasiriamali ambao wanajitahidi na tunatakiwa Serikali tuwaunge mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii imeleta neema na imeleta matumaini katika kutatua kero za wananchi. Bunge hili toka tunaanza kikao hiki cha bajeti watu wanazungumzia kero mbalimbali kama migogoro ya ardhi, miundombinu, sekta ya afya na sekta ya maji. Nitatoa mfano katika Jimbo la Malinyi, tuna migogoro ya ardhi ambayo inatokana na matumizi ya ardhi ile kati ya watumiaji wake (wafugaji na wakulima).
Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro mingine Serikali wenzetu ndiyo wameitengeneza. Kwa mfano, mgogoro ule wa Pori Tengefu la Bonde la Mto Kilombero. Ile hifadhi ya Pori Tengefu la Mto Kilombero ndiyo chanzo kimojawapo cha migogoro kati ya wakulima na wafugaji katika maeneo ya Wilaya ya Ulanga na Wilaya ya Malinyi. Tumewaomba na wamekubali lakini ni muda mrefu sasa bado hawajaanza kutekeleza ombi letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi ombi letu ni rahisi sana kwamba lile Pori Tengefu la Bonde la Kilombero kuna ile buffer zone, eneo lile lina range, linatoka kutoka kilomita moja mpaka 12, eneo lile ni pana sana. Matokeo yake wamekuja kuingiza mpaka vijiji 18 na vitongoji 22, wananchi wale wanaishi kihalali katika maeneo yale, wanashindwa kujiendeleza na matokeo yake kwa sababu ya uhaba wa ardhi tunaingia kwenye migogoro kati ya wakulima na wafugaji. Kwa kuwa tayari wameshakubali, naomba basi katika bajeti hii na naiona kweli wametekeleza basi migogoro hii ifikie mwisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, mvua ya mwaka huu imekuwa nyingi na imeathiri sana miundombinu. Mojawapo ya miundombinu ni barabara zetu ambazo wananchi wengi wanazitumia. Nikitolea mfano ni barabara ya kuanzia Ifakara – Lupilo - Malinyi, Kilosa Mpepo - Namtumbo - Songea. Kwa kuwa barabara hii sehemu kubwa ni vumbi au barabara ya kawaida mvua zimeathiri sana. Naomba bajeti hii kama tutaipitisha, najua barabara sehemu nyingi zimeharibika lakini tunaomba kipaumbele kipelekwe kwenye barabara ambazo zimeathirika sana ikiwepo hiyo ambayo nimeitaja.
Mheshimiwa Naibu Spika, angalizo lingine naiomba Serikali kwamba, hii bajeti tunapoipitisha basi fedha hizi zipelekwe katika muda muafaka. Maana tumeshuhudia bajeti zilizopita kwamba tunapitisha bajeti lakini uwasilishwaji au upelekaji wa fedha umekuwa unasuasua. Kama tutapitisha halafu fedha haziendi kwenye bajeti impact yake itakuwa ni ndogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wamegusia suala la bajeti finyu au fedha chache zilizotengwa kwa ajili ya Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali. Waheshimiwa Wabunge, sasa tuko kwenye mchakato wa kupitisha bajeti na kazi yetu nyingine inayofuata ni kuangalia ni namna gani fedha hizi za wananchi ambazo tumepitisha zinatumika na taasisi ambayo itatusaidia sana, jicho letu ni hili moja tu, ni jicho la CAG. Kwa bajeti ambayo wameitenga au fedha ambazo zimewekwa hapa ni kidogo sana. Naomba nimkumbushe Mheshimiwa Waziri wa Fedha wakati anaomba bajeti yake ya fedha, kitabu chake kile cha hotuba ukurasa wake ule wa 94, naomba ninukuu, alisema:-
“Wizara hii ya Fedha itaendelea kuimarisha uwezo wa kitaalam kwa wakaguzi wake, maana yake hawa CAG, na kuendelea na ujenzi wa majengo ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ili kuimarisha uhuru wa wakaguzi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na tija zaidi ili kukidhi matakwa ya viwango vya kimataifa vya taasisi za ukaguzi pamoja na maazimio ya kimataifa ya Lima na Mexico ambayo Tanzania imeridhia”.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wapi na wapi, walichotenga kinatofautiana na kile walichokisema, hakuna reflection na alichosema Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake. Nitoe mfano, bajeti ya mwaka huu ambayo wametengewa shilingi bilioni 32, ukiangalia mwaka wa fedha uliopita walitengewa shilingi bilioni 63, sasa wapi wanakoelekea wakati taasisi hii CAG wetu ana ithibati katika uwanja wa kimataifa. Kwa mgao huo maana yake tunamrudisha nyuma. Hiyo fedha niliyosema shilingi bilioni 32 ni matumizi ya kawaida lakini matumizi ya maendeleo ukijumlisha na matumizi ya kawaida yanafikia shilingi bilioni 44.7 ambapo mwaka jana wa kifedha CAG alipewa shilingi bilioni 74.2.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali wametoa maelezo hapa kwamba watakapofikia mwisho wa miezi sita (mid year review) mwaaangalia kama CAG fedha haitoshi wataweza kumwongezea. Mimi kwa uzoefu mdogo niliokuwa nao Serikali inaongea kwa maandishi. Tunaomba Serikali ili kweli tumpe nguvu CAG hapa watakapoishia watoe maandishi kama ni kweli wako committed, watakapofanya mid year review watajazia hii fedha ambayo imetengwa kwa ajili ya CAG ili aweze kukamilisha majukumu yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie, wenzangu wamechangia kuhusu kodi…
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na kuunga mkono hoja na nachangia katika masuala yafuatayo:-
Kilimo, umuhimu wa Sekta ya Kilimo katika uchumi uko wazi; naishauri Serikali kuweka dhamira na mikakati kuongeza uzalishaji tija kuwa kilimo chetu kiwe cha kibiashara. Hivyo yafuatayo yazingatiwe.
(a) Kilimo cha umwagiliaji kwa kuongeza mabanio yaliyopo sasa hususan katika maeneo ambayo yana fursa za uhakika wa mito ya kudumu kwa Mkoa wa Morogoro, Wilaya za Malinyi, Ulanga na Kilombero.
(b) Uwepo wa Soko la kuhakikiwa kwa mazao ya kilimo. Wakulima katika kero kuu zinazowakabili wakulima ni soko la uhakika kwa mazao hususan mazao ya nafaka kama mpunga au mahindi. Mifugo; mwendelezo/ongezeko kubwa la mifugo na ufugaji kiholela wa mifugo aina ya ng’ombe nchini inahatarisha uchumi wa nchi huko siku za usoni. Nashauri Serikali kusimamia na kutekeleza zoezi la matumizi bora ya ardhi ili yatengewe maeneo mahsusi kwa malisho ya mifugo. Aidha, Serikali kuweka miundombinu rafiki wa mifugo kama marambo ya maji na visima katika maeneo ya malisho ya mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa hili utasaidia kwa kiasi kikubwa sana kumaliza changamoto katika mifugo, migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji. Aidha, itainusuru nchi katika kuelekea nchi kuwa jangwa kama tutaendeleza ufugaji/uchungaji wa ng’ombe kiholela.
Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. DKT. HAJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kuunga mkono Hoja. Wilaya ya Malinyi ni miongoni mwa wilaya mpya na zilizoko katika mazingira magumu (pembezoni). Hivyo, wahitaji kupewa kipaumbele na jicho la kipekee. Wilaya ya Malinyi haina Mahakama ya Wilaya hivyo, hutegemea Wilaya jirani (mama) Ulanga. Tumepeleka maombi ya kuanzisha au kujengewa majengo ya Mahakama ya Wilaya ya Malinyi. Tunaomba Serikali kulipa kipaumbele ombi hili la ujenzi wa Mahakama ya Wilaya kwa kuwa huduma hiyo inapatikana mbali sana kilomita 200 hadi 300 toka Wilayani Malinyi kwenda Ulanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Malinyi ina Mahakama za Mwanzo mbili tu kuhudumia wilaya nzima yenye ukubwa wa kilomita za mraba 10,576 na idadi ya watu karibu 250,000. Hivyo tunaomba tuongezewe Mahakama za Mwanzo. Aidha, Mahakimu waliopo wa Mahakama za Mwanzo wamekuwepo muda mrefu katika vituo vyao vya kazi; hivyo kuathiri sana utendaji/ufanisi wa majukumu yao ya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara iweke na kumwezesha Hakimu wa Wilaya ya Ulanga ambaye pia anahudumia Wilaya ya Malinyi kuja kusikiliza mashtaka (kesi) katika Wilaya ya Malinyi ili kuepusha au kupunguza usumbufu kwa watuhumiwa kwani wanapata adha kubwa sana kwenda na kurudi Mahenge (Ulanga). Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Naipongeza Serikali katika ukamilishaji wa daraja la Mto Kilombero. Hakika daraja hili ni ukombozi mkubwa sana kwa wakazi wa Wilaya ya Malinyi, Ulanga na Kilombero.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliahidi kujenga na kumaliza barabara ya Ifakara – Lupiro – Malinyi – Kilosa Mpepo – Londo –Namtumbo (TI6) katika kiwango cha lami. Naiomba Serikali kutekeleza ahadi hii ya ujenzi wa kiwango cha lami kwa kuwa kuwa barabara hii inahudumia maeneo muhimu ya uzalishaji wa mazao ya nafaka (mpunga). Ni eneo ambalo Taifa linategemea chakula (mpunga). Hivyo kuwepo kwa barabara ya lami itaongeza tija sana kwa kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii, aidha itakuwa ni njia ya mkato, hivyo kuokoa muda na fedha kwa wakazi wa Mikoa ya Ruvuma na Njombe kuja Dar es Salaam na Dodoma (HQ). Wakati mchakato wa ujenzi wa barabara ya lami (TI6) unaendelea, naiomba Serikali kutoa kipaumbele na kuongeza bajeti ya ukarabati ya maeneo korofi, kwani fedha iliyotengwa haitoshi kabisa. Ni kipande cha kilomita 25 tu za changarawe, zimetengwa kwa urefu wa barabara yenye urefu zaidi ya kilomita 300.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado Wilaya ya Malinyi ina changamoto ya mawasiliano ya simu katika Kata za Ngoheranga, Kilosa Mpepo, Biro na Sofi. Aidha, minara iliyotengwa na TiGO kupitia ruzuku ya UCAF haifanyi kazi kwa kiwango cha kuridhisha na baadhi ya minara hiyo haifanyi kazi kabisa kutokana na hitilafu/upungufu wa kiufundi. Ahsante.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara kwa kutekeleza majukumu yao vizuri pamoja na changamoto mbalimbali zinazoikabili Wizara na Serikali kwa ujumla. Hakika mimi binafsi naridhika sana na utendaji wao na nawaomba waendeleze ubunifu, uadilifu na kujituma katika kuwahudumia Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nitauelekeza zaidi kwenye changamoto ya uhaba wa vituo vya tiba katika Wilaya ya Malinyi (Morogoro). Wilaya ya Malinyi ina Kituo kimoja tu cha Afya cha Mtimbira na haina Hospitali ya Wilaya. Halmashauri imependekeza kukipandisha hadhi Kituo cha Afya cha Mtimbira ili kiwe na hadhi kama ya hospitali ili kiweza kuhudumia wananchi wengi wanaohudumiwa na kituo hicho lakini majibu ya Serikali bado hayakubaliani na ombi hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto za Kituo hicho cha Afya cha Mtimbira, tunaiomba Wizara kuona namna mbadala au kutoa upendeleo wa kipekee kwa kuongeza mgao wa dawa, watumishi, vitendanishi na kadhalika ili kukidhi mahitaji halisi ya wagonjwa wanaohudumiwa na kituo hicho cha afya. Halmashauri kwa kushirikiana na TAMISEMI, tutajitahidi kujenga vituo vingine vya afya katika Halmashauri ya Malinyi lakini katika kipindi hiki cha mpito, tunaiomba Wizara ya Afya kuliangalia ombi letu la Kituo cha Mtimbira kupata hadhi ya hospitali. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE.DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia sisi wote kuwa wazima wa afya ili kukabiliana na majukumu yetu pamoja na kazi zetu za Ubunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili naomba nichukue fursa hii kukushukuru wewe mwenyewe binafsi kunipa nafasi angalau nitoe mchango wangu katika Wizara hii muhimu sana katika Wilaya zetu za Malinyi, Ulanga na Kilombero.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nafasi hii niitumie kutoa shukrani kwa Wabunge, wakazi wa Malinyi, wakazi wa Morogoro na Watanzania nzima kwa ujumla, ndugu, marafiki na majirani kwa pole, salaam za rambimbi na dua kuhusu kifo cha mzazi wangu Mzee Hussein Mustafa Mponda lakini tunajua fika sisi wote ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea. Innalillahi Wainna Ilayhi Rajuun.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu leo utajikita kwenye eneo moja tu kubwa ambalo kutegemea hotuba ya Waziri imezungumzia Idara ya Wanyamapori na dhana ya ushirikishaji jamii katika uhifdhi wa wanyamapori na ardhi oevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ambayo inajikuta na migogoro inayojitokeza baina ya Hifadhi, Mapori Tengefu na Mapori ya Akiba na Vijiji vinavyopakana ni hasa imetokana na mabadiliko ya Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 2009 ambapo kwa mabadiliko hayo yalivyofanyika, Serikali walipewa maelekezo wafanye mambo mawili:-

La kwanza, watafiti kama kuna ulazima wa uendelevu Mapori Tengefu kwa wakati huo ilikuwa 42; na la pili, ni kurejea mipaka ya Mapori Tengefu au Hifadhi kwa sababu sheria ya zamani ilikuwa inawaruhusu wakazi wa maeneo yale kutumia mapori yale lakini Sheria ilivyobadilika 2009 ikakataza. Niipongeze Serikali wameanza kutekeleza kwa ukanda wa kwetu kule Malinyi, Kilombero na Ulanga kwenye lile bonde la Kilombero, ardhi oevu yake na Pori Tengefu la Bonde la Kilombero. Walichofanya mwaka 2012 walirejea wakaangalia ile mipaka, wakaweka mpaka kati ya kiini cha Pori Tengefu la Kilombero na ardhi ya kijiji, ule mpaka wakauita buffer zone.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lile ni panasana lina- range wakati mwingine kilometa mbili mpaka kilometa 25 ambayo imesababisha vijiji karibuni 23 na vitongoji vyake 18 wananchi wanaishi kihalali maeneo yale. Vijiji vile vimesajiliwa, sasa hii ni changamoto ambayo Serikali waliiona pale na baada ya kupigia kelele, kuishauri Serikali nishukuru tena wamekubali kurejea upya mipaka ile na nawashukuru uongozi wa Menejimenti ya Bonde la Kilombero walitushirikisha wadau ngazi ya Halmashauri walituita Mikumi nakumbuka ilikuwa tarehe 20.10.2016, tumewekwa semina ya siku mbili kuonyeshwa umuhimu wa lile bonde na kuonyesha namna gani bonde na namna linavyoathiriwa na nini hatima yake. Kulikuwa na option tatu:-

(i) Aidha, kisiwepo nabuffer zone;

(ii) Iwepo na buffer zone lakini kuwe na masharti maalum; na

(iii) Imeridhiwa wadau wote wa mipaka ya buffer zone ile irejewe isiwe mipana kama kiasi kile ili kuokoa vijiji vile ambavyo viko kihalali na kuokoa maeneo ambayo wananchi tayari wameshaanza kutumia ambayo sasa itatusaidia kupunguza migogoro ya ardhi na pori tengefu lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushahidi ulikuwepo; ukirejea matokeo ya utafiti wa wanyamapori (TAWIRI 2009, 2010, 2011) na mtafiti mmoja ambaye ni mtaalam wa wanyamapori katika Mkoa wa Morogoro ni Ndugu Joseph Joachim Chuwa alifanya utafiti kwa kushirikiana na SUA waliangalia changamoto, waliangalia masuala ya kijamii na uchumi yanayosukuma uhitaji wa ardhi na uendelevu wa lile bonde na baadae tafiti ile ilihitimisha kwamba ni vyema wadau, ni vyema wananchi wahusishwe ili kulilinda lile bonde na mimi nasema wananchi wa Malinyi, Ulanga na Kilombero ndiyo tunanufaika na lile bonde, tuko tayari na tunalipenda sana maisha yetu tunategemea lile bonde.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotokea, hao hao Serikali wenyewe hawasimamii ipasavyo bonde lile kwa sababu sisi hatuwezi kulima ndani ya bonde lile karibu na ule mto ambao unakuwa protected, ni watu wanatoka mbali na Serikali wanawatazama siku zote matokeo yake wanatuathiri sisi ambao wanasema hawa wakazi wa Wilaya hizi tatu wao ndiyo waharibifu wa lile bonde owevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali kipindi hiki wamerejea tena kuweka mipaka. Niwashukuru wamechukua dhana kweli shirikishi lakini ajabu yake na hii naomba heshimiwa Waziri unisikie kwa makini sana; kwamba wataalam wale kutoka Wizara ya Ardhi, TAMISEMI na Maliasili na Utalii wanakwenda kila kijiji, wanaongea na wananchi, wanaongea na viongozi, tunafikia muafaka kwamba mpaka wa lile buffer zone uwe wapi. Tunaelewana kabisa, tunakubaliana lakini sasa kinachofanyika wanapokwenda kuweka mipaka ile kwenye beacon wanatofautiana makubaliano ya awali na wananchi wale. Sasa mimi niwahoji; mnasema shirikishi mnawashirikisha wananchi, wananchi wamechukua muda wao, wameeleza matatizo yao, wataalam wenu mumewatuma kule lakini hamtaki kusikia mnakwenda kuweka beacon kama mnavyotaka, kwa kusema hapo hamtatatua tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri niwaombe, nimeongea na wataalam hawa wanawanyooshea vidole ninyi viongozi wa Wizara. Wansema tumeongea na wananchi na tumekubaliana lakini tunapokwenda kule wanatu-monitor, wanatufuatilia kwa njia ya TEHAMA, wanasema lazima mpaka uwe hapa. Kama ni hilo ni kweli hamtutendei haki kabisa wananchi wa Wilaya hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwakumbushe Mheshimiwa Maghembe najua bado utarudi mwaka 2020 na najua bado una sifa na utapenda kuwa Waziri, sasa hapa changamoto iliyopo 2020 Mheshimiwa Rais wakati tunamnadi kwenye Jimbo la Malinyi tarehe 05.09.2015 alisimama kwenye jukwaa baada ya kuelezwa changamoto hii, aliahidi ataongeza ardhi ya kutosha, ataongeza maeneo yale ambayo wananchi wapate kuendesha shughuli zao za kila siku. Labda mimi niseme tu, hapa changamoto kubwa siyo kwamba hatutaki bonde lile tusililinde, hapana, changamoto kubwa lile buffer zone ni pana mno; wewe umeona wapi buffer zone kilometa 25? Kawaida ya buffer zone ni kilometa angalau mita 500, angalau kilometa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe basi mtusikilize buffer zone ile muipunguze badala ya kuwa na kilometa 25, kilometa 8, kilometa 12 iweke ile standard yenu kama ilivyokuwa buffer zone kwenye maeneo mengine ya kilometa mbili ambayo itatuwezesha sasa kwanza, kutekeleza ahadi
ya Mheshimiwa Rais na hiyo itakuwa njia rahisi Mheshimiwa Rais atapita tu kama barabara imewezeshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo zoezi linaendelea tuna ombi maalum watu wa Malinyi; kwamba kwa kuwa wanaweka hiyo mipaka kwahiyo watu wanaoishi kule siyo kihalali kwenye ile kiini cha pori wataondolewa na wakiondolewa kule kuna mifugo itahamia kwenye milima.

Tunaomba mtusaidie Halmashauri hawana uwezo wa kulinda ile milima na ile milima ndiyo vyanzo vya maji yanayotiririka katika lile Bonde la Kilombero na hatimae unakuwa mto unaelekea mpaka unakuwa Mto Rufiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara kwa utekelezaji wa majukumu yao kwa kiwango na cha kuridhisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali katika kukubali ombi la wakazi wa Wilaya ya Malinyi, Ulanga na Kilombero katika kufanya marekebisho ya mipaka ya Pori Tengefu la Kilombero kwa kushirikisha wananchi. Wakazi wa Wilaya hizo tatu tunafahamu umuhimu wa kuhifadhi Bonde la Kilombero na ardhi yake. Ushirikiano wanaopewa wananchi na wataalam wa wanyamapori katika kurekebisha mipaka sio rafiki kabisa kwani wanayokubaliana au kujadiliana na viongozi wa vijiji na kata au wananchi hayatekelezwi. Wananchi bado wana mahitaji ya kutengewa (kupewa) ardhi ya nyongeza kutokana na hali halisi ya kuongezeka kwa matumizi ya ardhi kwa kilimo, mifugo na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja kubwa ya wananchi hao ni kwamba ile ardhi ya buffer zone ni kubwa (pana sana) kwani kuna maeneo yana upana wa kilometa 8 -12. Ombi letu wakazi wa Malinyi, Ulanga na Kilombero upana wa eneo (ardhi) hiyo ya buffer zone ungepunguzwa iwe na upana wa angalau kilometa 1 au 2 tu kati ya ardhi za vijiji na kiini cha Pori Tengefu la Kilombero. Ardhi hiyo itakapoongezeka kwa wakazi itatupunguzia kwa kiasi kikubwa migogoro baina ya hifadhi, wafugaji na wakulima. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mojawapo ya malalamiko katika nchi hii ni mipaka na migogoro ambayo inaendelea katika vijiji vinavyopakana na hifadhi au mapori tengefu au mapori ya akiba. Naomba nianze kwa kumpongeza Waziri Mkuu kwa busara zake na kuwa msikivu zoezi hili katika bonde la Kilombero limekamilika Wilaya ya Malinyi na zoezi hili lilifanywa kwa kuwashirikisha wananchi. Pamoja na kukamilika zoezi hili yameacha kilio, imeacha kero, imeacha malalamiko kwa wananchi hawa. Naomba ieleweke zoezi hili limefanyika baada ya mabadiliko ya Sheria ya Wanyamapori ambayo yalifanyika mwaka 2009.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hiyo ya wanyamapori kabla ya 2009 wananchi walikuwa wanaruhusu matumizi ya binadamu katika mapori tengefu likiwemo Bonde la Kilombero. Sasa ilivyobadilika sheria ile wananchi hawa kihalali kabasa vijiji karibuni 16 na vitongoji vyake kama 25 vinaishi kihalali kule katika maeneo yale. Sasa sheria imebadilika inawakataza, sasa hapo ndio umeanza mgogoro, lakini busara ambazo ametumia Waziri Mkuu ni kwamba ametuma wataalam, wajadili na wapitie mipaka ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lile zoezi limekamilika kama ninavyosema bado malalamiko yako pale kwa sababu pamoja imetambulika ile mipaka, lakini mashamba ya wananchi, wananchi wa Wilaya ya Malinyi na Wilaya ya Ulanga kilio chao kikubwa mashamba walikuwa wanalima maeneo yale hasa maeneo ya buffer zone sasa wamezuiliwa hawawezi kulima tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nini maana yake? Kwa hiyo, kuwazuia kulima maeneo yale tayari tunatengeneza mazingira magumu na tujue kwamba mpunga ambao unapatikana Ifakara au mchele unaitwa Kilombero asilimia 80 ya mchele ule unatoka Malinyi. Sasa kitendo cha kuwazuia wananchi hawa wasilime maeneo yale tayari tumetengeneza mazingira ambayo ni njaa ambayo itatokana na kukataza kulima maeneo yale.

Nikuombe Mheshimiwa Waziri Mkuu ulimtuma Waziri wako wa Maliasili na Utalii amekuja maeneo yale, ameona na mimi namshukuru Waziri Dkt. Kiwangalla ametumia busara zake, ameona hali halisi ameunda tume ya watu 21 ambayo itafanya kazi ndani ya mwezi mmoja kuona nini changamoto wananchi wale ili kama mazingira yanaruhusu basi maeneo yale waruhusiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo letu lenyewe tunaliomba wala sio kubwa sana ni katikati ya kilometa mbili mpaka kilometa tano kutoka nje ya mipaka ya kijiji, vinginevyo kama atazuia wananchi wale basi kilio kitakuwa kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili Serikali imeeleza hapa ukosefu wa pembejeo kuna changamoto mbalimbali zimesababisha na ukosefu huu. Naomba nielezee kwenye Wilaya ya Malinyi. Mwaka huu wananchi Wilaya ya Malinyi wameshindwa kulima mahindi kwa sababu ya sumu ya panya haikupatikana kwa wakati muafaka na taarifa tayari ilishatolewa kwa sababu tataizo hili limejitokeza miaka mitatu mfululizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali unapofikia wakati wa kuweka hizi bajeti waangalie msimu upi ambao unatakiwa kupeleka hizi pembejeo, vinginevyo kilio hiki kitaendelea. Kwa mfano, mwaka huu watu hawatalima mahindi kwa sababu ya hizo sumu za panya hazikufika kwa wakati muafaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho Serikali mwaka 2010 waliingia mkataba wa mkopo na Serikali ya India wamekopa karibuni milioni 40 za Kimarekani toka Serikali ya India na mradi huo ulikuwa kuwezesha matrekta ya SUMA JKT, lakini mpaka ilivyofikia mwaka 2015 matrekta yale yalikuwa na matatizo ya urejeshaji wa mikopo ile na ndani ya miaka mitano ni asilimia 40 tu ya madeni 46 ndio yamerejeshwa. Sasa mwaka 2017 Serikali mmeanza mradi mwingine tena mradi mwingine wa kuunganisha matrekta pale Kibaha, matrekta aina ya…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kutoa mchango wa sekta muhimu sana katika maisha yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kutoa mchango wangu, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia sisi sote na mimi mwenyewe binafsi angalau leo natoa mchango katika sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi wamezungumzia umuhimu wa sekta hii, ni kwamba asilimia 75 ya Watanzania tuko vijijini na wengi walioko vijijini shughuli kubwa kule ni kilimo. Ukiangalia uchambuzi wa Kamati ya Kilimo, imebainisha wazi kabisa kwamba kasi ya sekta ya kilimo inazidi kuanguka mwaka hadi mwaka. Tunaiomba Serikali na maelekezo ambayo wametoa Wabunge waliotangulia, hebu muangalie changamoto hasa na baadaye mzipatie ufumbuzi wa kudumu katika kuendeleza hii sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana mkono na Kamati ya Kilimo ambayo wameitaka Serikali kutambua fursa zilizoko na hizo fursa ambazo zinatambuliwa ndiyo mkakati hasa ufanyike. Mimi nitatoa mfano Mkoa wa Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi tunafahamu Mkoa wa Morogoro ni mkoa ambao tayari kuna miradi ambayo inaendelezwa pale. Naomba Serikali itupe mrejesho, kuna Mradi wa SAGCOT, kuna Mradi wa Feed the Future ambao unafadhiliwa na Wamarekani na vilevile kuna mkakati wa Fanya Mkoa wa Morogoro kuwa Ghala la Chakula lakini sii tunaotoka Mkoa wa Morogoro hatuoni jitihada za dhati kabisa juu ya miradi hiyo. Ukienda pale Morogoro, ukiuliza mtu wa kawaida tu SAGCOT unaijua, hawaelewi hali kadhalika hata huo mradi ambao unafadhiliwa na Marekani. Picha ya hapa ni nini? Kama kweli fursa zilizopo katika Mkoa wa Morogoro Serikali inawekeza pale, tunaweza tukatoa matokeo makubwa sana katika suala hili hasa la vyakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite zaidi ili unielewe, mfano nitautolea Wilaya ya Malinyi. Wilaya ya Malinyi kama itawezeshwa kilimo cha umwagiliaji tayari pale kuna mito zaidi ya 30 inamiminika kuanzia masika na kiangazi, lakini wilaya yote ile kuna banio moja tu liko Itete.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeeleza mara nyingi na kuishauri Serikali, mnaonaje sasa mito mingine kwa mfano, Rasesa, Furua na Sofi, kama itatumika na kuweka scheme za umwagiliaji, nina uhakika tatizo la chakula litakuwa limetoweka kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wa maeneo yale, wengi tunalima kilimo cha zao la mpunga na mahindi. Katika msimu wa mwaka uliopita tumechelewa kuanza kilimo cha mahindi kwa sababu ya shambulio la panya. Nilichogundua kwamba hakuna mawasiliano kati ya Wizara na watendaji walioko kule wilayani hawa Maafisa Ugani, vilevile kati ya Wizara na wananchi. Wadudu/panya hawa kumbe dawa yake ipo na dawa zinafanyiwa utafiti mara kwa mara kwenye Chuo cha SUA, SUA ndiyo center ya panya katika nchi hii. SUA iko Mkoa wa Morogoro, ni karibu sana na Malinyi, sasa kwa nini ndani ya miaka miwili mfululizo Wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi tumekuwa na tatizo la panya lakini majibu hakuna! Kama mwenendo huu utaendelea, wananchi hawa wataendelea kuteseka zaidi na zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mbegu; wananchi Mkoa wa Morogoro pamoja na SUA tuna Kituo cha Utafiti cha KATRIN Ifakara, pale wanatengeneza mbegu ya kisasa ya SARO 5 lakini usambazaji wake wananchi mpaka leo hawaelewi. Kwa hiyo, hoja yangu hapa, namshauri Waziri, hebu uweke mikakati ya mawasiliano, mnafanya kazi nzuri pamoja na vyuo vyenu vya utafiti, lakini hakuna mrejesho kwa wananchi. Wananchi mpaka leo hawajui ni mbegu gani bora ya kutumia katika zao la mpunga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara kadhaa nimeiomba Serikali kwamba wakulima wa mpunga wanasumbuliwa na ugonjwa ambao wa virusi. Ugonjwa huu kule tunaita kimyanga kwa lugha ya nyumbani, lakini lugha ya kitaalam unaitwa rice yellow mottle virus. Ugonjwa huu sio mgeni sana kwa nchi za Afrika, unapatikana sana West Africa. Niwaombe mara nyingine, kwa nini msipeleke wataalam waende wajifunze kule West Africa, wenzetu wameutatuaje ugonjwa huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa mwisho niongelee suala la masoko, wengi wameeleza, kama hatuna uhakika wa masoko kwa wakulima wetu kwa kweli tunapoteza nguvu za wakulima hawa. Niombe hasa soko la mpunga, mwaka wa fedha uliopita Serikali walitenga
angalau fedha za kuanza kununua karibuni tani 100,000 kupitia NFRA lakini naona kwenye bajeti hii wamesahau kabisa. Kwa hiyo, mtakapoweka soko hili la kupitia NFRA tayari itakuwa mmewatengenezea mazingira ya kuwa na soko la uhakika la zao la mpunga wananchi wale wa Malinyi, Kilombero na Ulanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie la mwisho na niendelee kusisitiza tu, kama tunataka tutoke na kilimo chenye tija, twende na kilimo cha kibiashara ambapo sifa kubwa ya kilimo cha biashara inahitaji maji. Maji yapo, ni utaratibu namna gani tunaweza tukayatengenezea skimu tukayapata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine tunataka miundombinu, kwa mfano kule Malinyi inafikia wakati bei ya mpunga inateremka na wananchi wanaumia kwa sababu miundombinu hali siyo nzuri sana. Mtu utoe gunia la mpunga pale upeleke kwenye soko Ifakara toka Malinyi ni kilometa 150 lakini gunia lile linagharimu shilingi 10,000 kwa gunia moja la kilo 100. Kwa hiyo, hii linampunguzia mapato huyu mkulima na matokeo yake hata soko sasa linapungua kwa sababu ya bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wengine wamekuwa wanaeleza hawana imani na Waziri, mimi binafsi Mheshimiwa Tizeba namfahamu, uwezo wake ni mkubwa, naomba tumuunge mkono, tumtengenezee mazingira hata sisi Wabunge, huu ndiyo wakati wetu kutengeneza bajeti hii, kama ina upungufu, Kamati ya Bajeti ikae…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi kwanza kukushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba muhimu sana katika kipindi hiki cha bajeti. Naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu ndiye aliyetuwezesha leo kutupa mazingira haya leo tunachangia hii bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nianze na pongezi za dhati kabisa, kwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dkt. John Pombe Magufuli, jamani kazi inafanya. Pongezi pia kwa Waziri Mkuu na Mawaziri walioko katika Wizara yake, lakini vilevile na Manaibu Waziri, pongezi za dhati vilevile ziwafikie Wakurugenzi, Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) na Mamlaka ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya. Kamishna Siang’i anafanya kazi ya kujituma sana, mpaka tumefikia hali tulivyo hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, michango yangu itakuwa mifupi sana leo, nitazungumzia hotuba hii ya Waziri Mkuu, kipengele cha 87 na 88 kinazungumzia huduma za kiuchumi. Wote tunajua humu tunapozungumzia uchumi, tunazungumzia Watanzania ambao wengi wako vijijini na wanategemea ardhi. Niipongeze Serikali hii kwa mara nyingine tena, katika Wilaya ya Malinyi, Wilaya ya Kilombero na Ulanga, tuna mradi wa urasimishaji wa ardhi ambao unatuwezesha kupima, kupanga namna gani tutatumia ardhi yetu na mwishoni kuwakabidhi wananchi hati za umiliki. Hili limesaidia kwa kiasi kikubwa sana kuondoa migogoro ya ardhi ambayo inatuweka sasa kwa msingi wa ardhi namna gani tunaweza kuwekeza kuunga mkono jitihada za Dkt. John Pombe Magufuli katika suala la uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo kwenye ardhi kwenye kipengele cha 89, Serikali imeeleza wanatekeleza agizo la Mheshimiwa Rais, tarehe 15 Januari mwaka huu Mheshimiwa Rais kama alivyo kwa tabia yake mjasiri, anathubutu ni kweli, amethubutu kusimamisha zoezi la kufuta vijiji 364 katika nchi hii. Wananchi hawa, miongoni mwa hivyo vijiji 364, vingine vipo katika Wilaya ya Malinyi, wamejikuta wao ni wahanga wa mabadiliko ya Sheria ya Wanyamapori ya 2009. Sheria ya zamani ilikuwa imenyamaza haikusema lolote hasa katika mapori tengefu na ndio matokeo yake kwamba vijiji vimesajiliwa ndani ya mapori tengefu na wananchi wameruhusiwa shughuli za kawaida za maisha yao, pamoja na kilimo, uvuvi na ufugaji, sasa 2009, tukabadilisha ile Sheria, imekataza, lakini wananchi hao tayari wako ndani ya hifadhi na wako ndani ya yale mapori tengefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa Watendaji wa Serikali hasa hawa wa Wanyamapori wamekuwa too machinery, wamekuwa wanafanya kazi kimashine mno, huwezi kuangalia mazingira yale unawaambia wananchi wale watoke vile vijiji 364. Huu msiba kwa kweli ungekuwa mkubwa sana. Bado migogoro inaendelea, pamoja na Rais ametumia busara ameonyesha ujasiri wake, ameunda Tume ya Mawaziri nane, wamezunguka Mawaziri wale watachukua na michango ya wataalamu, rai yangu ya mwisho kwa suala hili, upande wa kule Malinyi lile Bonde la Kilombero, tuna dhamira ya kweli na tunataka kulilinda, wananchi wale wanachogombania ni kiasi kidogo sana, ile buffer zone, eneo lile la Pori Tengefu la Kilombero ni ina range kati ya kilomita nane mpaka kilomita 23, wananchi hao wanataka kidogo tu wapewe angalau kilomita tatu ndiyo mashamba yao yamo mle. Ndiyo maana nasisitiza nashauri tena Serikali, hili zoezi wanaloendelea nalo la kurejea mipaka wawaachie mashamba yale wananchi, hayo ndiyo maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uchumi, vilevile linaendana na suala la barabara, Serikali imeonesha dhamira yake na tumeiona barabara inayounganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Ruvuma. Hii barabara inaanzia Mikumi, Ifakara, Lupilo, Malinyi, Kilosa Mpepo, Londo, Lumecha mpaka inaingia Songea. Barabara hii sasa imetoboka toka 2017, lakini ombi langu toka itoboke ile barabara haiwezi kutumika kwa sababu bado ina maeneo korofi katika bajeti hii, sijaona dhamira ya kweli kabisa kurekebisha ile barabara ili yale maeneo korofi angalau ipitike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiikamilisha barabara hii sasa tutakuwa tumekamilisha dhana na Sera ya barabara kwamba iunganishe Mkoa kwa Mkoa, nitachangia zaidi itakapofika kwenye Wizara ya Ujenzi. Kwa hiyo hapa ninachoomba, Mheshimiwa Waziri Mkuu, hili suala la barabara ya kuunganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Ruvuma ni muhimu sana kwa maendeleo sio tu hii Mikoa miwili, lakini kwa nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, kama nilivyosema nitachangia ni suala la Tume ya Udhibiti UKIMWI. Ndugu yangu hapa Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya UKIMWI ameshagusia, lakini naomba nisisitize zaidi, jamani, suala la UKIMWI, takwimu zinatuonesha kwamba linapungua, lakini kihali halisi bado tatizo ni kubwa. Sasa naomba tuungane wote kwa pamoja na ule mkakati ambao unasema 90 kwa 90 kwa 90, nini maana yake 90 kwa 90 kwa 90? Ni kwamba asilimia 90 wanaokadiriwa wanaishi na Virusi vya UKIMWI wao wamepima na 90 ya pili ni kwamba wale ambao wamegundulika wanaishi na Virusi vya UKIMWI baada ya kupimwa, waingie kwenye matibabu na asilimia 90 yao wanaendelea na matibabu na 90 ya tatu wale ambao wanaendelea na matibabu ya ARV’s asilimia 90 yao wao wamefubaza Virusi vya UKIMWI. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo mkakati ambao unaweza ukatokomeza suala la UKIMWI, nini maana yake, ile 90 ya mwisho maana yake ni kwamba kama mtu umefubaza Virusi vya UKIMWI unakuwekea mazingira wewe huwezi kumwambukiza mwenza wako unayeshea naye kama yeye hajaambukizwa na halikadhalika na yeye hawezi kuambukizwa na Virusi vya UKIMWI kama yule mwenza anatumia ARV’s. Sasa changamoto iliyopo Tanzania hatuna rekodi nzuri katika ile 90, 90, 90 na mkakati huu mwisho 2020 ni mwaka kesho. Sasa hii 90 ya kwanza ndio tuko asilimia 61, najiuliza asilimia 61 leo, 2019 mkakati unasema 2020 tuwe
tumefikia asilimia 90.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa kuna changamoto, tunaiomba Serikali, Kamati ya UKIMWI wamependekeza mara nyingi, tunaiomba Serikali labda isikie kwamba vitu ambavyo vinachangia navyo hii 90 ya kwanza ni suala la Sheria ya UKIMWI. Sheria ya UKIMWI haimruhusu mtoto chini ya miaka 18 kwenda kupima bila ridhaa ya mzazi au mlezi ambapo hawa watoto wa miaka 18 na takwimu zinaonesha waathirika wengi, survey iliyofanywa mwaka 2017 ilionyesha asilimia 40 ya waathirika wa Virusi vya UKIMWI ni vijana wenye umri kuanzia miaka 15 mpaka miaka 24, ndiyo hao tunazungumza wengi wao hawaruhusiwi kwenda kupima kwa hiari yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama mtu ataenda kupima yeye mwenyewe, kwa hiyo tukiongeza idadi ya watu kupima Virusi vya UKIMWI, tunaongeza ile 90 ya kwanza. Sasa hili suala ni la kisheria tumeiomba mara nyingi Kamati ya Masuala ya UKIMWI, Serikali wamekuwa wana-dill dull suala hili hawalileti...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi ili nipate kutoa mchango wangu. Kabla ya hapa naomba tumshukuru Mwenyenzi Mungu aliyetujalia uhai mpaka tunakuwa na mazingira ya kukusanyika hapa pamoja na majanga mbalimbali tunawatumikia wananchi.

Mheshimiwa Spika, niungane mkono na wenzangu walioanza na nakumbuka mwezi Novemba, 2015 Mheshimiwa Rais alikuja humu na wengine waliondoka. Hotuba ya Mheshimiwa Rais ilikuwa so impressive, ilikuwa na matumani makubwa sana na tunaona kwa miaka mitano yametekelezwa. Kwa hili tunampongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli na kundi lake la Baraza la Mawaziri kwa kweli wametutendea haki, sina haja kutamka wametekelezaje ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo sisi tulienda kuahidi Watanzania tutawafanyia nini kwa miaka mitano, kwa kweli kwa kiasi kukubwa yamefanyika, pongezi sana kwa Serikali waetutendea haki. Sasa sisi wengine wa CCM tunatembea kifua mbele, maana yake sisi wa Morogoro tunasema manta hofu maana yake tunatembea bila wasiwasi, tunaenda Oktoba hii tuna hakika tunawafyeka tena.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita zaidi kwenye hotuba hii ibara ya 43 mpaka 45, ni kwamba tumeendelezwa kupitia Dira ya Taifa kwamba ifikapo 2015 tutaingia uchumi wa kati, uchumi unaowezeshwa na viwanda. Hotuba aliyoitoa Mheshimiwa Waziri Mkuu imeleeza, imenyooka moja kwa moja na hata ukiangalia Mpango wa Maendeleo wa 2020/2021 na hata bajeti imesisitiza na imetengeza vile vipaumbele vinne mojawapo ni kuwezesha uchumi wa viwanda ili twende huko katika Dira ya 2025.

Mheshimiwa Spika, hivi viwanda tunavyovizungumzia vikubwa vingi vinatokana na mazao ya kilimo na mifugo. Hali ilivyo kama tunataka twende huko kuwezesha hivyo viwanda ni lazima tuwe kilimo cha biashara na mojawapo ya sifa za kilimo cha biashara ni lazima muwe na miundombinu ya uhakika na usafiri na usafirishaji. Ni lazima muwe na maji, maji haya kilimo kinahitaji maji, tusitegemee ya mvua za Mwenyenzi Mungu, maji ya skimu za umwagiliaji. Tatu, tunahitaji nishati ili kuchakata mazao yetu, kuongeza thamani, na la nne ni soko la uhakika. Serikali naona wanatupeleka huko, lakini balaa la mwaka huu, maana mwaka huu ni changamoto kidogo, maradhi upande wa pili tuna mvua nyingi sana ambayo imeharibu miundombinu ya barabara na madaraja.

Mheshimiwa Spika, mfano tu ni barabara ambayo inapita katika ukanda mkubwa wa uzalishaji ambapo Serikali wamepeleka Mradi wa SAGCOT ambayo inaanzia Mikum – Ifakara – Lupilo – Malinyi - Kilosa Mpepo – Londo – Lumecha - Kitanga - Songea. Barabara hii ikiwezeshwa itatufikisha tunakokwenda kwenye uchumi wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuja na ameona barabara hiyo, naipongeza Serikali wameanza hatua ya kuifanyia kazi kwa vitendo maana CCM inafanya kazi kwa vitendo. Mmeweka mkandarasi kile kipande cha kilometa 70 kuanzia Mkamba - Ifakara, sasa ni mwaka wa pili, wa tatu mkandarasi yule anasuasua. Kila tukijiuliza hatupati majibu, Serikali tuambieni tatizo liko wapi, anatuchelewesha huyu na ndiyo maana upande wa pili wanapata ajenda. Tunakwenda kwenye uchaguzi, Mheshimiwa Waziri Mkuu hebu mwangalieni huyu mkandarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mkimaliza kipande cha kuanzia Ifakara mmeahidi mnakwenda kipande cha Ifakara – Lupilo - Malinyi - Songea, barabara hii ni muhimu sana. Kama tunataka kilimo cha biashara barabara hii ndiyo itawezesha kupeleka mazao haya kwenye soko na vilevile ndiyo itakuwa kivutio. Kilimo cha biashara tusitegemee hawa wakulima wetu wa kawaida wadogo wadogo, tunahitaji wawekezaji na mwekezaji hawezi kuja kwenye maeneo ambayo hakuna usafiri wa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeahidi mara nyingi sasa ni wakati muafaka muanze kujenga barabara hiyo nayoizungumzia ambayo ina tija kwenye mwelekeo wa kumfanya Mtanzania aingie kwenye uchumi wa kati ifikapo 2025 na wala siyo mbali. Habari njema bado tunaye Jemedari, mtu anayethubutu, Dkt. John Pombe Magufuli ndani ya miaka mitano atatufikisha huko kwenye uchumi wa kati 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, sipendi kuzungumzia huu ugonjwa mpya ulioingia ambao unasababishwa na Virusi vya Corona. Mimi ni mjumbe wa Kamati ya UKIMWI na Madawa ya Kulevya. Tunaipongeza Serikali wamepokea ushauri wetu, wameufanyia kazi lakini kuna mambo mawili, haya naendelea kusisitiza kama wajumbe wenzangu walivyosisitiza tusije tukachanganywa na huu ugonjwa mpya, bado UKIMWI ni tishio.

Mheshimiwa Spika, kwa miaka iliyopita bajeti ya kudhibiti ugonjwa wa UKIMWI tunategemea fedha kubwa kutoka kwa wafadhili, karibu mpaka asilimia 98. Sasa ifike wakati pamoja na changamoto hizo, tena habari ambayo siyo njema tayari baadhi ya wafadhili wamepunguza msaada huo wao kwa asilimia 23.

Mheshimiwa Spika, niombe kwenye bajeti hii tuanze kuwekeza kwenye vita dhidi ya UKIMWI kwa fedha zetu za ndani angaliu asilimia 75. Tumelizungumza sana suala hili sasa tumefikia mwisho na Kamati inavunjwa lakini mtakuja mtukumbuke. Kama tusipowekeza kwenye vita dhidi ya UKIMWI kwa pato la ndani na huyu adui mwingine wa Corona aliyeingia ndiyo tutazidi kuchanganyikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine kwenye UKIMWI ni Mfuko wa UKIMWI (ATF). Mfuko huu tunauzungumzia lakini bado una changamoto na sisi tumependekeza ikiwezekana wekeni tozo au kwa sababu ninyi mna wataalam tafuteni vyanzo vingine, vinginevyo huu Mfuko utabaki kuitwa Mfuko lakini hauna fedha, Mfuko maana yake ni fedha.

Mheshimiwa Spika, nakupongeza sana kwa kunipa nafasi hii na naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. DKT. HAJDI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya uzalishaji (kilimo); Serikali ilichukua mkopo wa Dola za Kimarekani milioni 40 kwa kununua na kusambaza matrekta na zana zake mwaka 2010. Hadi ilipofika mwaka 2015 ni asilimia 46 tu madeni ya mauzo ya matrekta hayo yalikusanywa. Mradi huu umekumbwa na changamoto nyingi pamoja na SUMA JKT kukosa uzoefu katika masuala ya biashara hivyo kusababisha mradi huo kuwa na hasara kubwa kwa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi kifupi sana kimepita katika mradi huu wa SUMA JKT wa matrekta kuonesha hasara, Serikali 2017 imechukua mkopo mwingine wa matrekta ya aina ya Ursus yanaunganishwa na kampuni ya Kibaha chini ya NDC. Watekelezaji wa mradi huu wa matrekta ya Ursus wanaonesha toka Mwanza na hawana uzoefu kabisa katika masuala ya biashara ya matrekta na zana za kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali itoe maelezo na kutuhakikishia Watanzania kwanza fedha zetu za SUMA JKT, tractors zitarudishwa au tayari tumeshapata hasara. Pili; nashauri Serikali kuwawezesha NDC wajiendeshe kibiashara katika kutekeleza mradi wa Ursus tractors pamoja na kutumia mikakati/mbinu zote za masoko yaani marketing strategies za (1) Promotion (2)Price (3) Place (4) Production vinginevyo nao Ursus tractors project unaweza ukaishia hasara kama ule wa SUMA JKT (tractors project)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Nampongeza Mheshimiwa Waziri Profesa Mbarawa, Naibu Mawaziri wote na timu nzima ya utendaji wa Wizara kwa kazi nzuri wanayotekeleza katika kutimiza majukumu ya Wizara. Pongezi pia kwa TANROADS Manager wa Morogoro, Engineer Doroth Mtenga na timu yake kutekeleza majukumu yao katika mazingira magumu na ufinyu wa bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, sera ya barabara ni kuunganisha barabara za kuunganisha Mikoa ziwe za lami. Ni lini barabara ya Ifakara – Lupilo – Malinyi - Kilosa Mpepo – Londo – Lumecha – Songea itaanza ujenzi wa lami? Barabara hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli na muda umebakia kidogo na utekelezaji wa ahadi ya Rais mwaka 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Barabara inaelekeza kujenga barabara za Makao Makuu kwa kiwango cha lami. Wilaya ya Malinyi tunapendekeza/kuomba kuanza ujenzi wa barabara ya lami kwa kilomita mbili katika Mji wa malinyi. Ombi letu halitekelezwi. Tunaomba kauli ya Waziri, atueleze ni lini ataanza kutenga bajeti ya kuanza kujenga barabara ya lami katika Mji wa Malinyi (Makao Makuu ya Wilaya)?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Nampongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na timu yote ya Wizara kwa utekelezaji wa majukumu yao ya Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya sababu ya kutofanya vizuri kwa vijana wetu katika mitihani ya kidato cha nne na sita ni lugha ya kiingereza. Lugha hii ndiyo inatumika katika kufundishia vijana wengi lakini hawaelewi kiingereza. Napendekeza kwamba vijana baada ya kumaliza darasa la saba kabla ya kuanza masomo ya sekondari watumie mwaka mmoja wa matayarisho na kuwaweka katika kukielewa kiingereza, yaani tuwe na utaratibu wa pre- form one kwa mwaka kwa kuwawezesha katika kukielewa kiingereza na hisabati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Malinyi tunaomba Mheshimiwa Waziri kupitia TEA juu ya ukamilishaji wa bweni la wasichana katika shule ya sekondari ya Kipingo Malinyi. Ombi lilikubaliwa lakini hadi leo hakuna utekelezaji. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri atupatie kipaumbele, ombi la Malinyi Wilaya ambayo haina kabisa shule ya sekondari ya bweni wala hakuna high school kwa Wilaya yote ya Malinyi. Ahsante.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na maoni ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwamba kumekuwa na ushirikishwaji mdogo sana na wananchi katika uwekaji wa vigingi vya mipaka ya hifadhi/vijiji.

Mheshimiwa Spika, zoezi la utambuzi wa mipaka katika Wilaya ya Malinyi katika Pori Tengefu la Kilombero limekamilika lakini limeacha changamoto/lawama kwa Serikali kwamba wananchi hawakushirikishwa kwa mapana. Matokeo ya zoezi hili limesababisha wananchi kukosa mashamba na baadhi ya vitongoji kuwa katika miliki ya pori tengefu. Hii imeleta taharuki kubwa kwa wananchi kukosa ardhi kwa maendeleo ya kilimo na kiujumla ustawi wao.

Mheshimiwa Spika, katika kampeni zake Mheshimiwa Rais mwaka 2015 aliwaahidi wananchi wa Malinyi kuongezea ardhi kutoka katika kingo (buffer zone) ya Pori la Kilombero. Kingo hii bado ni pana sana (kilometa 5 -12) hivyo kuwaongezea wananchi angalau kilometa tatu tu hakutoathiri kwa vyovyote ustawi au uendelevu wa Pori Tengefu la Kilombero. Hali hii kwa ukosefu wa mashamba kwa wananchi wengi wa Malinyi kutakuwa na athari kubwa kimaendeleo, ustawi wa uhai kiujumla kwa wananchi wa Malinyi.

Mheshimiwa Spika, ninaiomba Wizara ya Maliasili na Utalii iridhie maoni/ushauri wa Kamati hususan kurejea upya mipaka ya Pori Tengefu la Kilombero kunusuru mashamba na baadhi ya vitongoji na kuondoa migogoro katika maeneo hayo. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. DKT. HAJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa ujumla katika utekelezaji wa majukumu yake katika kipindi hiki cha miaka mitatu yanaridhisha sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu unajikita katika kifungu 8.7, ukurasa 41 wa kitabu cha hotuba ya Waziri Mkuu, kuhusu huduma za uchumi; suala la migogoro ya ardhi kati ya wananchi na hifadhi/mapori tengefu. Katika Wilaya ya Malinyi/Morogoro wakazi wa vijiji karibu 18 vinavyopakana na Pori Tengefu la Kilombero wana mgogoro mkubwa wa marekebisho ya mipaka bado sio rafiki kwa wananchi. Sehemu kubwa ya mashamba yao yanayotumika kwa kilimo/ ufugaji yamechukuliwa na buffer zone ya Pori Tengefu la Kilombero.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hawa ni waathirika wa mabadiliko ya Sheria ya Wanyamapori ya 2009 ambapo sasa mashamba yao hayo ambayo walikuwa wakiyatumia hapo kabla ya 2009 yamenyang’amywa hivyo kusababisha kuwa na uhaba wa mashamba kwa shughuli zao za kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali warejee tena upya zoezi la kurekebisha mipaka ya Pori Tengefu la Kilombero ili kupunguza upana wa buffer zone kwa kuyaachia mashamba hayo yarudishwe kaika ardhi ya vijiji kwa faida ya maendeleo na ustawi ya wakazi wa Wilaya ya Malinyi, karibu watu 92,000 wameathirika na mgogoro huu wa mipaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja ya Waziri, lakini pia naipongeza Wizara yote kwa ujumla kwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi pamoja na changamoto ya ufinyu wa Bajeti (fedha) zinazowakabili.

Mheshimiwa Naibu Spika, huduma za kinga hususan chanjo ni muhimu sana katika suala la afya za watoto miaka walio na umri wa chini ya miaka mitano na wanawake wajawazito. Ili Wizara iweze kutekeleza kwa ukamilifu huduma hii inahitaji uwepo wa dawa, chanjo na vifaa vya kutolea chanjo pamoja na usafiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Malinyi inatekeleza huduma za chanjo kwa ugumu sana kwa kutokuwepo na gari la chanjo. Kubwa zaidi wilaya inakabiliwa na uhaba mkubwa na magari, hivyo kusababisha Idara yote ya Afya katika Wilaya ya Malinyi haina kabisa gari la kuhudumia shughuli za afya ikiwemo huduma za utoaji chanjo.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kutokuwepo na gari la chanjo au gari maalum kwa huduma za afya katika Wilaya ya Malinyi; nimemtaarifu Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu naye aliahidi kutupatia gari moja zitakapowasili gari maalum za chanjo mwishoni kwa 2018. Gari hizo za chanjo zimefika, lakini Wilaya ya Malinyi haijatengewa gari hata moja, tunaomba gari moja toka Wizara ya Afya kwa huduma za afya katika Wilaya ya Malinyi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Aidha, nawapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri na timu yote ya Wizara katika utekelezaji wa majukumu yao kwa ufanisi pamoja na changamoto za ufinyu wa fedha (bajeti).

Mheshimiwa Spika, katika mradi na ujenzi na reli ya SGR ni muhimu katika vituo vikubwa kama vile Morogoro, Dar es Salaam na Dodoma kungejengwa maeneo makubwa ya kuegesha magari (car parking) ili kuwezesha abiria wanaotoka Dodoma kwenda Dar es Salaam kwa usafiri binafsi, wanapofika Morogoro wanaweza kuegesha magari yao kwenye maengesho hayo, kisha kupanda SGR kwa safari ya Dar es Salaam na hivyo hivyo wanaporudi.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Kidatu – Ifakara – Lupiro – Malinyi – Londo – Lumecha – Songea inapitia katika maeneo muhimu kwa uchumi wa nchi pamoja na mradi SAGCOT (kilimo cha biashara) lakini barabara hii bado haijapewa kipaumbele.

Mheshimiwa Spika, barabara kipande ya Kidatu – Ifakara, ujenzi wa kiwango cha lami unasuasua sana. Sababu ni uzembe wa Mkandarasi. Tunaiomba Serikali itafakari kama kweli Mkandarasi anao uwezo wa kumaliza kazi katika muda muafaka. Aidha, Serikali ilete taarifa ni mkakati gani utafanya katika kumsukuma Mkandarasi kumaliza kazi ndani ya muda.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Ifakara – Lupiro – Malinyi – Londo –Lumecha – Songea imefunguka toka mwaka 2017, lakini haipitiki kabisa kipande cha Mpepo - Londo kutokana na milima haijachongwa. Tunaiomba Serikali irekebishe maeneo korofi yote ili barabara hii itumike kwa kuwaunganisha wakazi wa Mikoa ya Morogoro na Ruvuma.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Ifaka – Lupiro – Malinyi – Londo imetolewa ahadi na Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli katika kampeni zake za uchaguzi mwaka 2015, lakini pia alirudia ahadi hiyo katika ziara yake mkoani Morogoro Mei, 2018 kuanza kujenga kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, Serikali katika majumuisho, naomba itoe maelezo katika kutekeleza ahadi hiyo ya Mheshimiwa Rais kwa wakazi wa Morogoro/Ruvuma. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. DKT. HAJI H. MPONDA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na naipongeza Wizara kwa ujumla katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara pamoja na changamoto ya ufinyu wa bajeti.

Mheshimiwa Spika, Serikali imejenga skimu ya umwagiliaji ya Itete katika Wilaya ya Malinyi (2011-2013). Toka skimu hiyo kukamilika na kukabidhiwa kwa wananchi katika Vijiji vya Minazini, Alabama na Itete, skimu hiyo haitumiki kwa kikamilifu kutokana na changamoto za upungufu wa maji, mitaro mibovu na ukosefu wa barabara kuelekea katika mashamba ya skimu hiyo.

Mheshimiwa Spika, Serikali mwaka 2015 na 2016 ilikiri kabisa kwamba skimu hiyo imejengwa chini ya kiwango stahiki na kuahidi kuifanyia marekebisho upya ili skimu itumike kikamilifu. Naiomba Serikali itekeleze ahadi ya ukarabati au marekebisho ya skimu hiyo katika bajeti ya mwaka huu 2019/ 2020 kama ilivyoahidi.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Malinyi bado ina fursa kubwa ya ujenzi wa skimu zingine katika Mito ya Lwasesa, Sofi, Furua, Mwatisi na mingineyo. Je, ni lini Serikali itafanya utaratibu wa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika mito hiyo minne ili ititirishe maji ya uhakika masika na kiangazi ili ujenzi wa skimu za umwagiliaji uanze. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja ya Waziri na niwapongeze Mawaziri pamoja na timu yao yote ya Wizara katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Wizara katika kupanua wigo wa mazao ya utalii kwa kutumia Mto wa Kilombero kwa utalii wa kuvua samaki wakubwa aina ya Mjongwa n.k.; yaani king fish touring katika Mto Kilombero. Utalii huu ulikuwepo hapo mwanzo lakini hivi sasa umesimama kwa muda mrefu, inahitajika promotion kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la utatuzi wa mgogoro wa matumizi ya ardhi kati ya hifadhi/vijiji. Napongeza Serikali katika jitihada zake kwa kukabiliana na migogoro hii; shukrani za pekee kwa Mheshimiwa Rais kwa hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na utoaji wa elimu ya uhifadhi, uhakiki wa mipaka katika Pori Tengefu la Kilombero, nashauri Serikali, katika vijiji 16 ndani ya Wilaya ya Malinyi zoezi hili la uwekaji alama za kudumu/uhakiki wa mipaka irudiwe tena kwa kuwa mashamba mengi ya wanachi wa Malinyi kwa sasa yapo katika ardhi ya Pori Tengefu la Kilombero. Hivyo, kusababisha uendelezaji wa mgogoro wa wananchi wa vijiji hivyo na pori tengefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishauri tena Serikali, kwamba ingerejea upya zoezi la utambuzi wa mipaka/ uwekaji wa alama za kudumu ili kuyanusuru mashamba ya wananchi kwa maendeleo na ustawi wa wananchi lakini pia uendelezaji wa uhifadhi. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na kuwapongeza Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na team yote ya Wizara kwa utekelezaji wa majukumu yao pamoja na changamoto ya ufinyu wa bajeti. Pongezi pia kwa TANESCO kwa uendelezaji mzuri wa taasisi kufikia matokeo chanya hadi 2019 kutoa gawio kwa Serikali.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Morogoro kama hatua za dharura hazitachukuliwa dhidi ya mkandarasi wa REA III, M/S State Grid mradi huu hautokamilika kutokana na uwezo hafifu wa mkandarasi huyo Mkoani Morogoro katika REA III.

Mheshimiwa Spika, mkandarasi huyu State Grid alishindwa kumaliza mradi wa REA II katika Mkoa wa Lindi (2012 - 2016). Hata hivyo la ajabu bado mkandarasi huyu anaendelea kupewa kazi tena katika Mkoa huohuo wa Lindi na Morogoro, licha ya mapungufu makubwa katika utendaji kazi katika miradi ya umeme.

Mheshimiwa Spika, Mkandarasi ameonesha waziwazi kushindwa kazi kwa sababu zifuatazo; uwezo finyu kiufundi, fedha, vifaa vya kufabyia kazi na usafiri.

Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali aidha itengue mkataba au wamlazimishe mkandarasi aweke wakandarasi wadogo (sub- contracting) au wasaidiane na timu ya ufundi TANESCO Mkoa wa Morogoro.

Mheshimiwa Spika, mradi wa kuzalisha umeme wa Stiegler’s Gorge Power Project katika kutengeneza masuala ya mazingira/huduma kwa jamii imeelekeza zaidi katika upande wa Lower Rufiji kwa kuweka miradi kama ya mabwawa, skimu za umwagiliaji n.k. Mradi huu umesahau/ umeacha kabisa upande wa Upper Rufiji ambapo ndiko kunakozalisha maji kwa kuendesha mradi wote mfano Mto Kilombero na bonde lake linazalisha adilimia 65 ya maji yote ya mradi.

Mheshimiwa Spika, Serikali ni muhimu wangepima upya mradi na kuona namna gani wanaweka miradi ya kijamii na mazingira katika maeneo ya Upper Rufiji (Wilaya ya Malinyi, Ulanga, Kilombero) kutekeleza miradi ya skimu za umwagiliaji n.k ili kuwezesha kulinda mazingira wezeshi kuweka uendelevu wa Mto Kilombero.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja ya bajeti 2019/2020 na naipongeza Serikali katika utekelezaji wa Ilani ya CCM, 2015 kwa kiwango kinachoridhisha. Katika uboreshaji wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji katika Wilaya ya Malinyi kuna fursa kubwa za uwezeshaji wa biashara ya kilimo cha mazao ya nafaka (mpunga, ufuta, mahindi) kupitia miradi ya SACGOT, FEED THE FUTURE, FOMAGATA (Miradi ya Kitaifa). Miradi hii ya kilimo cha biashara ili iweze kufanikisha ni muhimu kuwepo na uboreshaji wa miundombinu ya barabara kuu inayopita katika Ukanda huo wa SACGOT.

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Mikumi – Ifaraka – Malinyi – Londo – Songea. Barabara hiyo ni muhimu sana kujengwa katika kiwango cha lami. Ujenzi wa barabara hii utatengeneza mazingira ya kushawishi na kuvutia wawekezaji kwa kuwa, eneo hilo linalopita katika Bonde la Mto Kilombero ambalo linafaa sana kama litatumika kikamilifu linaweza kutatua tatizo lote la upungufu wa chakula katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa muda mrefu imekuwa ikitoa ahadi ya ujenzi wa barabara hivyo, kiwango cha lami (Mikumi – Ifakara – Malawi – Londo – Songea), lakini ahadi hizo hazitekelezwi hivyo, kuathiri sana ushawishi na kuvutia wawekezaji wa kilimo cha biashara na viwanda katika maeneo ya Bonde la Kilombero kutokana na changamoto ya ubovu mkubwa wa barabara hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja.