Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Peter Ambrose Lijualikali (11 total)

MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika, naomba niseme kwamba taarifa nilizokuwanazo na ambazo ni sahihi ni kwamba daraja la Mto Kilombero lilipaswa kuwa limekamilika mwezi wa 10, 2015. Kutokana na Serikali ya CCM kushindwa kumlipa Mkandarasi kwa wakati, ameshindwa kufanya kazi hii kwa wakati.
Sasa naomba nijue ni lini Serikali ya CCM itaweza kumlipa Mkandarasi huyu ili aweze kufanya kazi yake vizuri? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lingine. Nataka nijue ni kwa nini Mkandarasi huyu amechukua mchanga kama sehemu ya material katika maeneo ya Lipangalala bila kuwalipa fidia yoyote wananchi wa Lipangalala. Nataka nijue, kama amelipa, kamlipa nani na kiasi gani? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, fedha za daraja zinagharamiwa na fedha za Serikali kwa 100%, hizo fedha zinatokana na kodi zetu. Sasa uwezo wa Serikali na miradi yote tuliyonayo, hatuwezi kuikamilisha kwa wakati mmoja. Ndiyo maana muda wa kumaliza umebadilishwa kutoka wa kwanza wa mwaka 2015, sasa tunaongelea Desemba, 2016. Ni kutokana na uwezo wetu wa ukusanyaji wa mapato yetu ya ndani.
Mheshimiwa Spika, kama ulivyosema awali, swali lake kuhusu fidia ya eneo ambalo mchanga unachukuliwa, naomba tuwasiliane Wizarani tumpe takwimu sahihi, kwa kuwa linahitaji takwimu.
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu haya mazuri ya Mheshimiwa Waziri na kwa namna ambavyo wafadhili wetu wameonesha nia ya kuweza kusaidia, lakini kwenye majibu ya Waziri ameonesha mradi utaanza kwenye robo ya tatu, lakini sijaona mradi unakamilika lini? Kimsingi, kwa Kilombero hii imekuwa ni kero. Tumechoka kuzika ndugu zetu, tumechoka kuharibu magari yetu, mazao yanakuwa na bei kubwa kwa sababu ya usafirishaji; kwa kweli imekuwa ni kero kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri sasa aniambie kwamba huu mradi unaisha lini ili hii kero iweze kwisha nasi tujione ni sehemu ya Tanzania? Kwa sababu imefika hatua sasa ukiwa unakwenda Ifakara unasema sasa naingia Tanganyika, maana kule ni vumbi! Hii imekuwa ni kero, kwa hiyo, naomba atuambie sasa huu mradi unakamilika lini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lingine tunaomba atusaidie kwa sababu pale Ifakara na hii Wizara kwa sababu ni ya Uchukuzi na Mawasiliano, pale kuna daraja la Mto Lumemo, kutokana na mafuriko linakwenda katika muda wowote. Kwa hiyo, atuambie kama wako tayari kwenda kuangalia lile daraja na athari za mafuriko waweze kusaidia ili haya mafuriko yatoweke na daraja lipone. Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wananchi wa Ifakara, Mlimba na maeneo yote mpaka kule Mahenge ambapo daraja la Kilombero linawahusu; kazi ambayo Serikali imeifanya ni kubwa na kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi, ujenzi utaanza kipindi cha robo ya tatu. Utakwisha lini? Nadhani kwa sasa ni mapema mno kwa sababu kuna baadhi ya makubaliano katika hawa wafadhili yanatarajia kukamilika hivi karibuni. Tutakapokamilisha na mazungumzo yakikamilika na Mkandarasi tutaweza kuwa na majibu sahihi. Kwa sasa naomba Mheshimiwa Mbunge akubali na wananchi waelewe kwamba Serikali imeji-commit kujenga hiyo barabara na itakapofika robo ya tatu ya mwaka huu wa fedha kazi hiyo itaanza na baada ya hapo, tutajua kadri tutakavyoendelea, lini kazi hiyo itakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la pili, nikubaliane naye na bahati nzuri nina ratiba ya kwenda huko, nitamjulisha siku ambayo nitakuwa huko ili nitakapokuwa huko akanionyeshe hilo daraja tuangalie nini kinaweza kufanyika.
MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
Suala hili la maji kwenye Kijiji changu na Kata ya
Zinginari kuna mradi wa maji ambao unagharimu shilingi milioni 400 umefanywa, muda umeisha lakini mpaka leo maji hayatoki, kimekuwa ni kilio kikubwa sana.
Je, Waziri anafahamu kwamba kuna hii shida na
kama afahamu atakuwa tayari kwenda na mimi kwenye Jimbo langu ili ashuhudie namna ambavyo shilingi milioni 400 hizi zimeliwa na maji hakuna? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, tuna kesi mbalimbali na kuna baadhi ya maeneo mengine kwamba miradi imetekelezwa lakini wakati mwingine maji hayajapatikana na hii ina maana kwamba inatofautiana kutokana na mazingira. Mengine ni suala zima wakati mwingine zimechimbwa borehole ambapo zile borehole wakati mwingine zinakosa maji, lakini sehemu zingine ni suala
zima la usimamizi na uzembe katika usimamizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa kulijua kwa kuona jambo hilo kwasababu ni maeneo ya Kilombero peke yake ambayo nilikuwa bado sijafika katika Mkoa wa Morogoro na ni imani yangu hata katika Bunge hili la Bajeti nitafika kule Kilombero. Basi naomba nikifika kule tuweze
kuangalia jinsi gani tatizo lililoko pale halafu tulipatie tiba halisia kutokana na jinsi tutakavyoliona lengo kubwa ni kwamba Wananchi wa eneo lako waweze kupata huduma ya maji.
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Juzi hapa tumetoka kwenye Uchaguzi Mdogo Ifakara tarehe 23 ambapo kwanza Mwandishi wa Mwananchi Juma Mtanda alitekwa na wanachama na wafuasi wa CCM, wakampora iPad, simu na Kamera, akaenda Polisi akalalamika. Matokeo yake Polisi wakawatafuta watu wa CCM na wakamrudishia. Maana yake ni kwamba Polisi wanawajua wanaofanya uhalifu huu, mpaka leo hakuna ambacho kimefanyika, hakuna kesi wala chochote, hiyo ni moja. (Makofi)
Pili, kwenye uchaguzi ule kuna Askari WP Huruma alipigwa na jiwe na tofali akapasuka, ameshonwa nyuzi tano na amepigwa na wanachama wa CCM, lakini Polisi wanamuachia anatembea, anafanya chochote taarifa ipo. Namwomba Mheshimiwa Waziri anaiambie kama CCM wanaruhusiwa kufanya vurugu mpaka kujeruhi Askari wetu halafu wakaachiwa huru?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Lijualikali anazungumzia tuhuma za wanachama wa CCM kuwajeruhi Askari Polisi, pia kupora Waandishi wa Habari. Kwanza kabisa nashindwa kulijibu swali hili moja kwa moja kwa sababu unapozungumzia tuhuma kwamba hawa ni wafuasi wa chama fulani inahitaji uthibitisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoweza kusema…

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Naibu Spika, ninachoweza kusema ni kwamba uhalifu wa aina yoyote utakaofanywa na mtu yoyote wa chama chochote, dhidi ya raia yoyote ikiwemo Waandishi wa Habari na Jeshi la Polisi ndiyo kabisa. Jeshi la Polisi liko hapa kwa ajili ya kulinda usalama wetu, hatutakubali kamwe mtu yeyote acheze na Jeshi la Polisi na siyo tu Jeshi la Polisi hata Waandishi wa Habari wamekuwa wakifanya kazi vizuri sana ya kuelimisha jamii na kutoa taarifa nzuri kwa umma. Hatuwezi kukubali Waandishi wa Habari au Jeshi la Polisi kufanyiwa matukio yoyote ya kihalifu na raia mwingine yeyote, tutachukua hatua kali za kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Mbunge kama ana ushahidi wa hilo jambo alete, lakini siwezi nikasema hapa kwamba chama fulani kimefanya jambo fulani bila uthibitisho.
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Mimi naomba nifahamu, Jimbo la Kilombero lina Halmashauri mbili, Halmashauri ya Mji wa Ifakara wenye kata tisa na Halmashauri ya Kilombero yenye kata kumi. Kama ambavyo Jimbo la Bariadi ambalo lina Halmashauri mbili, Bariadi Vijijini kuna kata ishirini na moja na Bariadi Mjini kuna kata kumi. Hata hivyo, Mbunge wa Kilombero amezuiliwa na alizuiliwa kushiriki vikao vya Halmashauri ya Kilombero. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipotaka kushiriki nimefungwa miezi sita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mwenzangu anashiriki mwanzo mwisho sehemu zote mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nifahamu, ni
kwa nini mimi wa Kilombero siyo tu kwamba nimezuiliwa kushiriki vikao hata kufanya maamuzi kwenye hizi kata zangu kumi sishiriki, lakini mwenzangu wa CCM anashiriki? Sasa naomba Waziri aniambie ni kwa nini ubaguzi huu unafanyika dhidi yangu halafu mwenzangu wa CCM anaachiwa afanye kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nifahamu inawezekana vipi Mbunge wa Kilombero nazuiliwa kushiriki vikao…
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Mheshimiwa Lijualikali ni Mbunge ambaye ana Halmashauri mbili. Kama zilizovyo haki za Wabunge wengine katika majimbo yao na katika Halmashauri zao wanapaswa kuwa wajumbe wa vikao mbalimbali ikiwepo Kamati ya Mipango na Fedha lakini pia na Baraza la Madiwani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inakuwa vigumu sana kulisema jambo hili kwa sababu mhusika angepaswa tu ku-balance interest za maeneo yote na akaweza kufanya Ubunge wake. Kinachotokea ni pale ambapo mhusika pia ni Diwani na Diwani wa upande mmoja wa Jimbo. Kwa hiyo, scenario yake haiwezi ika-fall in all four angles kama ilivyo scenario ya Bariadi. Kwa sababu hiyo Mheshimiwa Mbunge anayo maelekezo yangu ambapo mimi na yeye tulizungumza sana jambo hili tukiwa pamoja na Mheshimiwa Kiwanga ambayo hayo hayatekelezi. Hivyo, kwa sababu ameleta jambo hili hapa Mheshimiwa Lijualikali ofisi yangu ipo, njoo tuzungumze tuone huo ugumu unaoupata na kwa nini haitokei hivyo, tutalimaliza jambo hili, nakukaribisha sana ofisini.
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Mheshimiwa Waziri Mji wa Ifakara ni Halmashauri mpya, kutokana na upya wake bado ni changa. Barabara zetu bado ziko katika level ya tope, kutokana na mvua hizi ambazo kule zinanyesha barabara zinaharibika sana. Sisi kama Halmashauri tunajaribu kuziwekea vifusi lakini kwa sababu ni Halmashauri mpya, hatuna fedha za kutosha kuweza kujenga lami.
Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Halmashauri ambayo ni mpya ili iweze kuboresha barabara zake, ziweze kuwa katika kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nafahamu Kilombero na maeneo mengine, naomba niwape pole Wabunge wote kwa sababu nikijua wazi kwamba kipindi hiki mvua zinanyesha, barabara nyingi sana katika maeneo yetu zimeharibika vya kutosha. Ndiyo maana katika bajeti yetu ya mwaka huu, tuliyoipitisha tumetenga karibuni shilingi milioni 247 mwaka huu wa fedha 2017/2018 ili kuhakikisha tunafikia maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa sitaki kutoa commitment ya uwongo kusema kesho Kilombero pale Ifakara tutakuja kujenga barabara za lami, itakuwa ni uwongo. Kikubwa zaidi tutaangalia jinsi gani tutafanya kwa bajeti iliyopo sasa, kwa sababu tunakwenda awamu kwa awamu. Tulikuwa na miji mikuu, tumeenda na manispaa, tunaenda katika halmashauri za miji, tunaangalia jinsi gani tutafanya kwa sababu kila barabara zingine zinawekewa kifusi ili barabara iweze kupitika.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba commitment ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wake wanaweza kufikiwa, wanaweza kusafirisha mazao yao na hata kusafiri sehemu zingine, hii ni commitment ya Serikali. Hivyo, tutajitahidi kufanya kila liwezekanalo bajeti iliyotengwa katika eneo hilo tutaisimamia vizuri, kwa sababu changamoto kubwa ni usimamizi wa bajeti katika maeneo yetu wakati mwingine.
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwanza nashukuru kwamba Serikali inajua hivi viwanda vimehujumiwa. Tuna viwanda ambavyo vilikuwa vinafanya kazi nzuri sana, lakini hao ambao tumewapa wamekata mashine na kuziuza kama scrapers, hasa kule kwangu MMMT imefanyika hivyo na Serikali inajua. Kitu kinachonishangaza ni huu upole wa Serikali kwenye kuwashughulikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, watu waliotuhujumu, walioharibu mali zetu wameharibu vitu vyote, halafu tunawabembeleza! Kwenye jibu la msingi hapa, Serikali inasema kwamba imewaambia hawa waliowekeza waje ofisini wapate mwongozo namna ya kuendesha au kuwapa walio tayari, yaani watu hawa wanabembelezwa. Sasa Serikali hii sijui, naomba nipate majibu, kwa nini watu hawa wanabembelezwa kiasi hiki wakati wameharibu rasilimali zetu? Hilo ni swali la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwenye kiwanda changu cha MMMT kule kuna shida kubwa. Mwekezaji amepewa, amekata mashine, lakini bado ameongeza eneo la kiwanda, amenyang’anya ardhi karibu robo tatu ya kijiji. Serikali kama hamjui, naomba mjue na ninamwomba Waziri twende Ifakara, Mang’ula aende ashuhudie wananchi wa Mang’ula ambao wameporwa kiwanda na pia wameporwa na ardhi yao…
Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba Mheshimiwa Waziri twende Ifakara. Je, yuko tayari kwenda au hayuko tayari kwenda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI): Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la kwanza kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi, Serikali imeanza kuchukua hatua kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina pamoja na Taasisi ya TIRDO. Sasa hatua ya kwanza tuliyoanza, kwanza inafanyika technical audit katika viwanda hivi vingi sana, maana yake idadi ya viwanda vilivyobinafsishwa ni takriban viwanda 153. Kwa hiyo, tumeanza kufanya uhakiki na tayari tumeshapitia viwanda 110 kwa ajili ya kuvipitia na kupata taarifa zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyozungumza hivi sasa, Serikali hii haifanyi kazi kwa upole, tarehe 26 Januari, 2016 baada ya Msajili wa Hazina kutoa kusudio la kuvitwaa baadhi ya viwanda, alikitwaa Kiwanda cha Chai cha Mponde kwa sababu mwekezaji alikiuka masharti na tarehe 15 Machi, 2017 pia tumetoa Kiwanda cha Nyama Shinyanga ambacho kilikuwa kinamilikiwa na Triple S na sasa tunaangalia utaratibu wa kuweza kukamilisha taratibu za kumpata mwekezaji mwingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali hii haifanyi kazi kwa upole. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea kuchukua hatua stahiki na ninavyozungmza hivi sasa tayari viwanda nane vimeshakuwa kusudio la kuweza kuchukuliwa hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la lake la pili, ananiuliza kama kweli niko tayari kuongozana naye kwenda kwenye kiwanda hiki kule Kilombero kuona namna ambavyo jambo hili linavyofanyika kwa mwekezaji kunyang’anya ardhi. Kwa sababu ni ombi maalum la Mheshimiwa Lijualikali, niko tayari kuongozana naye kwenda Kilombero kwa ajili ya kazi hii. (Makofi)
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri ni kwa nini ujenzi wa barabara ya Ifakara-Kidatu unasuasua?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia naomba nifahamu ni lini yupo tayari twende wote kwenye hii barabara tukakague tuone shida?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, kama ulivyoelekeza tutaongea na Mheshimiwa Mbunge ili baada ya Bunge tutembelee eneo hili.
MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba hii barabara inasuasua sana na ilisimama kwa takriban miezi minne mpaka mitano. Ikumbukwe kwamba Serikai iliingia mkataba wa ujenzi na wahisani wa EU na USAID kwa masharti kwamba Serikali italipia gharama za fidia pamoja na kuruhusu mashine na vifaa vingine viingie nchini bila VAT wala ushuru mwingine.
Mheshimiwa Spika, lakini hivi ninavyokwambia tayari mashine zimeingia lakini zimeshikiliwa na TRA. TRA wanadai kwamba hawatambui mkataba kati ya Serikali na Hazina, wao wanataka fedha zao tu na hii imesababisha hii barabara iende kwa kususasua sana. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri aniambie ni kwa nini TRA wanazishikilia mashine hizi wakati mkataba unaruhusu mashine ziingie bure? Hali hii inasababisha barabara iende kwa kususasua. Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, la pili, naomba nijue kama itawezekana kwa yale madaraja ambayo yapo sasa hivi kama tunaweza tukayachukua tukayapeleka sehemu zingine zenye uhitaji hasa Mlimba na Kilombero kwa sababu sasa hivi huku kwetu barabara zile za mitaa ni mbovu sana. Kwa hiyo tunaomba baadhi ya haya madaraja yafanye kazi kwenye mitaa mingine. Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na barabara ya Ifakara kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa mgogoro uliokuwepo wa interpretation ya mikataba ukiwepo mkataba wa European Union, lakini pia Bunge hili lilipitisha msamaha wa VAT mwaka jana, kwa hiyo zile taratibu za Kanuni zilikuwa hazijakamilika. Kwa sasa tumeshamaliza kuchambua ule mkataba wa European Union pia na taratibu za VAT nazo zimekamilika. Kwa hiyo mgogoro huo Mheshimiwa Mbunge haupo tena ndiyo maana vile vifaa sasa vimetoka na mkandarasi anaanza kazi. Hilo tumelimaliza, hiyo sasa ni historia.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kwa yale madaraja ambayo yalikuwa yanatumika, baada ya kukamilisha sasa lile daraja kubwa la zege kiutaratibu yale madaraja huwa tunayapangia kwenda kujenga maeneo mengine kulingana na uhitaji. Kwa hiyo kama uhitaji utakuwepo na kwenye maeneo aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge, nayo yatakuwa considered kwa ajili ya kupeleka hayo madaraja ili pia yakatumike eneo hilo.
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika, nafahamu Serikali imetoa msamaha wa kodi kwenye miradi yake lakini natamani nifahamu ni kwa nini sasa miradi ya watu binafsi wanaofanya kazi hii wenyewe hawapati misamaha? Maana yangu ni kwa nini kwenye vifaa vingine watu wanaofanya kazi hizi hawapati misamaha ya kodi ili kusaidia Serikali kupeleka huduma hii? Msamaha huu ungekuwa inclusive yaani usiwe tu kwa watu wanaofanya kazi Serikali peke yake. Kwa hiyo, napenda kufahamu ni kwa nini watu wengine pia hawapati misamaha huo?

Mheshimiwa Spika, pia naomba nifahamu kama Mheshimiwa Waziri atakubali kwenda nami sambamba kwenye Jimbo langu hasa kwenye Kata za Kipangalala na Kibaoni ambako kuna miradi mikubwa ya maji ya takribani shilingi milioni 600 lakini ni kama vile imesimama na fedha hizi ni kama zimelala. Kwa hiyo, naomba nifahamu commitment ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwa sababu anafahamu haya mambo nilishakaa naye ofisini kwake na kuzungumza kwa kirefu.

Kwa hiyo, naomba nijue kama yuko tayari twende Jimboni kwangu ili tukaone nini shida na tupate majibu kwenye mambo haya. Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri lakini kubwa sisi kama Wizara ya Maji lengo letu na nia ya Mheshimiwa Rais ni kumtua mwana mama ndoo kichwani na kuhakikisha Watanzania waishio mijini na vijijini wanapata maji safi salama na yenye kuwatosheleza. Kwa mazingatio na ushauri wako niseme tu kwamba tumepokea ushauri na tutaufanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la commitment ya mimi kuongozana naye katika Jimbo lake, Mheshimiwa Lijualikali mimi sina kikwazo chochote, nipo tayari kuhakikisha tunakagua miradi ya maji. Ahsante sana.
MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kule kwenye Jimbo langu kuna ujenzi wa barabara ya Ifakara – Kidatu. Barabara hii ilizinduliwa na Mheshimiwa Rais mwaka 2018 na akatoa ahadi kwamba mpaka mwaka huu mwezi wa Nne itakuwa imeshakamilika. Barabara hii mpaka hivi sasa imekamilika kwa asilimia takribani tano tu na bado mwezi mmoja mradi uweze kufungwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kauli ya Serikali, ni kwa nini barabara hii imechukua muda mrefu hivi na ni lini itakamilika ili adha ya watu wa Kilombero iweze kwisha?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli barabara ya Kidatu - Ifakara ilianza kujengwa kwa kiwango cha lami na katika hatua za awali kumekuwa na kusuasua. Nami nimetembelea eneo hili, hata juzi RAS alitembelea eneo hili na kutoa maagizo makali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunafahamu changamoto zilizopo lakini hapo awali kulikuwa na changamoto ya masuala ya vifaa kwa maana ya zile excemptions. Tatizo hili lilishaisha na tumetoa maelekezo mkandarasi afanye kazi usiku na mchana ili kuweza kufidia muda ambao ulipotea wakati ule wa malumbano wa masuala ya VAT Excemption.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge wewe vuta subira, sisi tunaendelea kuisimamia kwa nguvu na utaona kwamba sasa kutakuwa na uhai mkubwa wa kuhakikisha barabara hii inajengwa na inakamilika na wananchi wanapata manufaa ya kuitumia barabara hii ikiwa katika kiwango cha lami. (Makofi)