Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Peter Ambrose Lijualikali (9 total)

MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI aliuliza:-
Wilaya ya Kilombero ni moja kati ya Wilaya zinazozalisha kwa wingi mazao mbalimbali ya kilimo hususan zao la mpunga:-
(a) Je, ni nini kauli rasmi ya Serikali juu ya kuanza na kumalizika kwa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Kidatu - Ifakara na Ifakara - Mlimba?
(b) Je, ni lini Daraja la Mto Kilombero linalounganisha Wilaya za Kilombero, Malinyi na Ulanga litaanza kujengwa na kuanza kutumika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Peter Lijualikali, Mbunge wa Kilombero, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Kidatu – Ifakara yenye urefu wa kilometa 73.26 ni sehemu ya barabara kuu ya Mikumi – Kidatu – Ifakara – Mahenge yenye urefu wa kilometa 178.08 na barabara ya Ifakara – Mlimba ni sehemu ya barabara ya Mkoa ya Ifakara – Taveta – Madeke yenye urefu wa kilometa 231.53
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara kwa kiwango cha lami umekuwa ukitekelezwa kwa awamu kati ya Ifakara na Kidatu kulingana na upatikanaji wa fedha. Katika awamu ya kwanza na ya pili, ujumla ya kilometa 16.17 zilijengwa na kukamilika kwa kiwango cha lami kuanzia Kijiji cha Kiberege hadi kijiji cha Ziginali na kutoka eneo la Kibaoni (Ifakara) hadi Ifakara Mjini.
Awamu ya tatu ya utekelezaji ilihusisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa sehemu ya barabara kutoka Kibaoni (Ifakara) hadi Ziginali kilometa 16.8; na sehemu ya barabara ya Mikumi – Kidatu – Ifakara kilometa103.3 ambao umekamilika. Usanifu wa barabara umegharamiwa na Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) na Umoja wa nchi za Ulaya (EU) umeonesha nia ya kutoa fedha za ujenzi. Zabuni za kuanza ujenzi zinasubiri uthibitisho wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) kuhusu uwepo wa fedha za kutosha kugharamia mradi huo.
Aidha, upembuzi yakinifu na usanifu wa barabara ya Ifakara – Taveta – Madeke kupitia Mlimba upo katika hatua za mwisho na ujenzi wake utaanza baada ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kukamilika na fedha za ujenzi kupatikana.
Mheshimiwa Spika, Ujenzi wa Daraja la Kilombero ulianza kutekelezwa mwezi Januari, 2013 chini ya Mkandarasi M/S China Railway 15 Bureau Group Corpration wa kutoka China kwa gharama ya Shilingi bilioni 53.214. Mradi huu unasimamiwa na Mhandisi Mshauri M/S AARVE Assiociate Architects Engineering and Consultants Pvt kutoka India akishirikiana na Advanced Engineering Solutions (T) LTD wa Tanzania kwa gharama ya Shilingi milioni 2,759.225.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi huu unagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 na maendeleo ya jumla ya mradi huu yamefika asilimia 42. Ujenzi wa daraja la Kilombero unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2016.
MHE. SUSAN L. KIWANGA (K.n.y. MHE PETER A. LIJUALIKALI) aliuliza:-
Wilaya ya Kilombero ni moja kati ya Wilaya zinazozalisha kwa wingi mazao ya chakula lakini barabara zake nyingi ni mbovu na hivyo kushindwa kusafirisha mazao kwa urahisi.
(a) Je, ni lini barabra ya Kidatu - Ifakara na Ifakara - Mlimba zitajengwa kwa kiwango cha lami?
(b) Je, ni lini daraja la Mto Kilombero linalounganisha Wilaya za Kilombero, Malinyi na Ulanga litamalizika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Peter Lijualikali, Mbunge wa Kilombero, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa barabara ya Kidatu hadi Ifakara kwa kiwango cha lami umekuwa ukitekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Katika awamu ya kwanza Serikali ilijenga kilometa 10 kutoka Kijiji cha Kiberege hadi Ziginali ambapo kazi hii ilikamilika mwaka 2006. Katika awamu ya pili, Serikali ilijenga kilometa 6.17 kutoka Kibaoni hadi Ifakara Mjini ambapo kazi ilikamilika mwaka 2008.
Aidha, katika mwaka wa fedha 2012/2013, Serikali ilipata msaada kutoka Serikali ya Marekani kupitia Shirika lake la Maendeleo la Kimataifa la USAID kwa ajili ya kugharamia kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara yote. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina imekamilika. Kazi ya kuandaa nyaraka za zabuni na kutafuta Mhandisi Mshauri atakayesimamia ujenzi wa barabara inaendelea. Kazi ya ujenzi wa barabara ya Mikumi - Kidatu -Ifakara itaanza mara baada ya kukamilika taratibu za ununuzi ili kumpata mkandarasi wa kujenga barabara hii.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeanza maandalizi ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Ifakara - Mlimba kwa kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa sehemu ya barabara kutoka Ifakara hadi Kihansi kilometa 126 ili kuunganisha na sehemu ya barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 24 iliyojengwa hapo awali kati ya Kihansi na Mlimba. Kazi ya upembuzi yakinifu ipo katika hatua za mwisho na inatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2016. Kazi ya usanifu wa kina inatarajiwa kuanza mara baada ya upembuzi yakinifu kukamilika.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa daraja la Kilombero ulianza tarehe 21 Januari, 2013 ambapo gharama za ujenzi ni shilingi bilioni 55.97. Utekelezaji wa kazi ya ujenzi wa daraja la Kilombero umefikia 50% ambapo kazi inaendelea vizuri na inategemewa kukamilika mwezi Disemba, 2016.
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI aliuliza:-
Tangu awamu zilizopita hadi Serikali ya Awamu ya Tano, wananchi wa Kilombero wamekuwa wanapewa ahadi za ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Kidatu hadi Ifakara na kutoka Ifakara hadi Mlimba:-
(a) Je, Serikali haitambui mchango wa Wilaya ya Kilombero katika nchi wa kulisha Taifa?
(b) Kitendo cha Serikali ya awamu hii kuahidi ujenzi wa viwanda wakati eneo muhimu kwa uchumi wa nchi kama Kilombero likiachwa bila barabara inayosafirisha wakulima na mazao; je, maana yake ni nini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Peter Lijualikali, Mbunge wa Kilombero, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua mchango wa Wilaya ya Kilombero katika uzalishaji wa mazao ya chakula kwa wingi kwa ajili ya matumizi yao na Taifa kwa ujumla hivyo kulifanya eneo hilo kuwa miongoni mwa maeneo ya ghala la Taifa.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano, pamoja na kuahidi ujenzi wa viwanda imeweka pia katika kuimarisha miundombinu ya barabara kuelekea kwenye maeneo yenye umuhimu wa kiuchumi kama Kilombero.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutekeleza azma hiyo, Serikali katika eneo la Kilombero, pamoja na ujenzi wa Daraja la Kilombero unaoendelea, imekamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami kilometa 16.17 katika Barabara ya Kidatu hadi Ifakara kati ya Kiberege na Ziginali na Kibaoni hadi Ifakara. Aidha, katika barabara ya Ifakara hadi Mlimba zimejengwa kwa kiwango cha lami kilometa 24 kati ya Mlimba hadi Kihansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutimiza ahadi ya Serikali ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Mikumi – Kidatu – Ifakari, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Mikumi – Kidatu – Ifakara (kilometa 103.3) umekamilika. Usanifu huo umejumuisha upanuzi na ukarabati wa barabara ya lami iliyopo na madaraja sehemu ya Mikumi hadi Kidatu kilometa 35.2 na Kidatu hadi Ifakara kilometa 74.4. Ujenzi wa kiwango cha lami wa sehemu ya Kidatu hadi Ifakara pamoja na madaraja umepangwa kuanza katika robo ya tatu ya Mwaka wa Fedha 2016/2017 chini ya ufadhili wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU), Serikali ya Marekani kupitia USAID na Serikali ya Uingereza kupitia DFID.
Usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara kutoka Ifakara hadi Kihansi (kilometa 126) ili kuunganisha na kipande cha barabara ya lami (kilometa 24) kilichojengwa awali kati ya Ifakara na Mlimba unaendelea na umepangwa kukamilika mwishoni mwa Oktoba, 2016.
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI aliuliza:-
Serikali ilibinafsisha viwanda mbalimbali nchini ili kuongeza tija katika uzalishaji na kutengeneza ajira kwa Watanzania:-
(a) Je, Serikali ina mpango wowote wa kuvirudisha Serikalini viwanda vyake vilivyobinafsishwa kwa wawekezaji na wakashindwa kuviendeleza hususan viwanda vya MMMT - NDC na UWOP vilivyopo Mang’ula/Mwaya?
(b) Je, Serikali haioni kama kuendelea kuviacha viwanda hivi kwa wawekezaji walioshindwa kuviendeleza na kuamua kukata mashine za viwanda na kuuza kama chuma chakavu ni uhujumu wa uchumi wa Taifa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Peter Ambrose Lijualikali, Mbunge wa Kilombero, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha viwanda vyote vilivyobinafsishwa vinafanya kazi. Tunataka viwanda vyote vifanye kazi ili rasilimali zile zitumike kikamilifu na kwa tija, tupate ajira kwa wananchi wetu, tuzalishe bidhaa na kuongeza wigo wa kulipa kodi. Kama kasi ndogo ya kurejesha viwanda inavyomsikitisha Mheshimiwa Lijualikali, nasi upande wa Serikali hatufurahiii hali hiyo. Tarehe 22 Juni, 2017 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa mwongozo maalum kwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji juu ya kuharakisha ufufuaji wa viwanda hivi. Kabla ya mwezi Septemba, 2017 tutatoa taarifa ya kwanza kuhusu uboreshaji wa viwanda hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda vya MMMT - NDC ni moja ya rasilimali ambazo tumeanza nazo kufuatia agizo tajwa hapo juu. Kiwanda cha Ushirika Wood Products Ltd (UWOP) kama vilivyo viwanda vingi vilisimamisha uzalishaji kimekumbwa na matatizo ya mashauri mahakamani na madeni ya benki. Hilo ni moja ya mambo ambayo yamepelekea viwanda viwanda vingi visiendelee, kwani wale waliopewa kwa bei ya hamasa waliuliza rasilimali zile au kuweka dhamana benki na fedha waliyopata kufanyia shughuli tofauti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza kwenye sehemu ya kwanza ya swali, umetoka mwongozo maalum juu ya kushughulikia viwanda vya aina hii. Viwanda vilivyobinafsishwa lazima vifanye kazi, yeyote mwenye kiwanda cha aina hiyo awasiliane na Msajili wa Hazina ili apate mwongozo utakaomsaidia kuendesha kiwanda au kuwapa walio tayari ili wakirekebishe.
MHE. PETER A. LIJUALIKALI aliuliza:-
Wakulima wa miwa kata za Sanje, Msolwa Station, Kidatu na Mkula wanaouza miwa kwa Kiwanda cha Sukari Illovo wamekuwa wakilalamika kuhusu upimaji wa uzito wa miwa na kiwango cha sukari katika muwa.
Aidha, Kiwanda cha Illovo kimehodhi upimaji wa uzito wa kiwango cha sukari na kisha kuwashurutisha wakulima kuamini kuwa vipimo vyao ni sahihi.
(a)Je, Serikali haioni kuwa utaratibu huu unatoa mwanya kwa wakulima kunyonywa na kupewa vipimo batili?
(b)Je, Serikali haioni kuwa hali hii ya kumuachia mwekezaji kuhodhi upimaji wa uzito na kiwango cha sukari katika muwa hutoa mwanya kwa mwekezaji kumnyonya mkulima?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali ya Mheshimiwa Peter Lijualikali, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, upimaji wa uzito wa miwa ya wakulima unaotumiwa na wakulima wa Kiwanda cha Kilombero unatumia mizani maalum (weighbridge) ambayo inaratibiwa kwa mfumo wa computer. Mizani hiyo huhakikiwa na Wakala wa Vipimo kabla ya msimu wa uzalishaji wa sukari kuanza. Hivyo, kutokana na taratibu hizo hatutarajii mizani hiyo kutoa vipimo batili.
(b) Mheshimiwa Spika, upimaji wa kiasi cha sukari katika miwa hufanyika katika maabara zilizopo kiwandani. Kiwanda cha Kilombero kinafanya upimaji huo kwa uwazi na kimewaruhusu wakulima kuweka wawakilishi wao katika maabara hizo ili kuona na kuhakiki namna ambavyo upimaji unafanyika. Wakulima pia wamewekewa wawakilishi wao katika eneo la kupokelea miwa kabla ya kupimwa na kuingizwa kiwandani ili kuhakikisha kuwa miwa yao inaingia kiwandani na miwa ya kiwanda kwa uwiano ulio sawa.
Mheshimiwa Spika, katika kushughulikia changamoto ya kutokuaminiana baina ya pande hizo mbili, Serikali kupitia Bodi ya Sukari Tanzania inafanya ufuatiliaji katika viwanda ikiwemo Kiwanda cha Kilombero ili kuona namna ya miwa ya wakulima na ya kiwanda inavyopimwa katika mizani na upimaji wa kiasi cha sukari katika maabara. Katika msimu wa mwaka 2016/2017 zoezi hilo limefanyika katika Kiwanda cha Kilombero na kuonyesha kuwa upimaji wa miwa pamoja na kiasi cha sukari katika miwa unafanyika kwa uwazi na kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
MHE. PETER A. LIJUALIKALI aliuliza:-
(a) Je, ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara umefikia hatua gani?
(b) Je, barabara hii inatarajiwa kukamilika lini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA), alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Peter Ambrose Lijualikali, Mbunge wa Kilombero lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Kidatu-Ifakara yenye urefu wa kilometa 66.9 ni sehemu ya barabara ya Mikumi – Ifakara – Mahenge/Lupiro – Kilosa kwa Mpepo – Londo Lumecha yenye urefu wa Kilometa 534.4 inayounganisha Mkoa wa Morogoro na Ruvuma katika Mto Londo.
Mheshimiwa Spika, mkataba wa ujenzi wa barabara hii seuemu ya Kidatu – Ifakara (kilomita 66.9) na daraja la Ruaha Mkuu (mita 130) ulisainiwa tarehe 24 Julai, 2017 kati ya Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango na mkandarasi aitwaye Reynolds Construction Company kutoka nchini Nigeria kwa gharama ya Euro 40,441,890.81 bila VAT na inasimamiwa na Mhandisi Mshauri aitwaye Nicholas O,Dwyer Company Limited kutoka Ireland kwa gharama ya Euro 1,648,310.00 ambapo ujenzi wake unatarajiwa kukamilika tarehe 2 Aprili, 2020.
Mheshimiwa Spika, hadi sasa mkandarasi ameleta mitambo eneo la kazi kwa asilimia 90 na amekamilisha ujenzi wa kambi na maabara ya vifaa vya ujenzi kwa asilimia 100. Aidha, mkandarasi anaendelea na upimaji wa barabara, uhamishaji wa nguzo za umeme, simu na mabomba ya maji na kusafisha eneo la barabara pamoja na kujenga njia za mchepuo. Maandalizi ya eneo la kusaga kokoto na kufanya matengenezo ya kawaida ya barabara ya kutoka Kidatu hadi Ifakara ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka.
MHE. UPENDO F. PENEZA (K.n.y. MHE. PETER A. LIJUALIKALI) aliuliza:-

Je, ni lini programu ya REA III itaanza kutekelezwa katika vijiji ndani ya Wilaya ya Kilombero?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Peter Ambrose Lijualikali, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ilianza kutekeleza Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini ikiwemo vijiji vya Wilaya ya Kilombero Julai, 2018.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kampuni ya State Grid Electrical and Technical Works Ltd Novemba, 2018 ilikamilisha upimaji na usanifu katika vijiji 21 vya REA III, Mzunguko wa Kwanza. Kwa sasa mkandarasi anaendelea na kazi ya ujenzi wa miundombinu katika Vijiji vya Kirama, Mbasa, Michenga, Mautanga, Ihanga na Miwangani. Kazi za ujenzi wa mradi huu zitakamilka mwezi Juni, 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi za mradi wa Jimbo la Kilombero zinahusisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa Kilovoti 33 umbali wa kilomita 16.5, njia ya umeme wa msongo wa Kilovoti 04 urefu wa kilomita 28, ufungaji wa transformer 14 za KVA 50 na 100, pamoja na kuunganisha umeme wateja wa awali 497 na gharama ya mradi ni shilingi 1,700,060,000/=. Ahsante sana.
MHE. PETER A. LIJUALIKALI aliuliza:-

Je, kwa nini Serikali isifute kodi kwenye vifaa vya kusambazia maji kutokana na matatizo ya maji tuliyonayo katika Taifa letu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Peter Ambrose Lijualikali, Mbunge wa Jimbo la Kilombero, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tarehe 12 Septemba, 2017, Bunge lako Tukufu lilipitisha marekebisho ya Sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura ya 148. Marekebisho ya Sheria hiyo ya VAT yalihusisha vifungu vya 6 na 7 pamoja na aya ya 9 ya sehemu ya pili ya Jedwali la Sheria ya VAT ambayo vina lengo la kupunguza gharama za utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kuongeza tija ya matumizi ya fedha za umma na kuhakikisha miradi inayotekelezwa kwa fedha za Serikali na za washirika wa maendeleo inakamilika kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Maji tayari imeshasambaza Waraka wa Hazina namba sita uliotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango kuhusu utaratibu wa kutoa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa miradi ya maji itakayotekelezwa kote nchini. Ni wajibu kwa Maafisa Masuuli wote kuzingatia utaratibu ulioainishwa na Serikali katika misamaha ya kodi kwa vifaa vya kusambazia maji ili miradi yetu ya maji ikamilike kwa wakati.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA (K.n.y. MHE. PETER A. LIJUALIKALI) Aliuliza:-

Jeshi la Magereza lilikuwa na mpango wa ujenzi wa Gereza Kitongoji cha Nakato na Kijiji cha Kibaoni, Wilaya ya Kilombero.

Je, mpango huu umefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Peter Ambrose Lijualikali, Mbunge wa Kilombero kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kilombero ni miongoni mwa Wilaya 51 nchini ambazo hazina magereza. Mpango wa kuwa na magereza katika kila Wilaya una lengo la kupunguza tatizo la msongamano kwenye baadhi ya magereza yanayopokea wahalifu kutoka Wilaya zisizokuwa na magereza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa kuwa na magereza kila Wilaya utarahisisha usikilizwaji wa kesi, wafungwa na mahabusu wataweza kupata huduma kwa urahisi kutoka kwa mawakili wao na pia kupunguza gharama za usafiri kwa ndugu zao wanapowatembelea magerezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Magareza ina mpango wa kujenga magereza kwa Wilaya ambazo hazina magereza nchini ikiwemo Wilaya ya Kilombero. Aidha, mpango huu utatekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa rasilimali fedha.