Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Pascal Yohana Haonga (50 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisahihishe kidogo jina langu naitwa Mwalimu Pascal Yohana Haonga, Mbunge wa Mbozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie na mimi kwenye Wizara hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na ninaomba nianze kwa kusema kwamba kwa muda mrefu sana wakulima Watanzania wamesahaulika sana. Takwimu zilizoonyeshwa hapa kwenye hotuba hii, wote nadhani tumesoma, tumeona kwamba sekta ya kilimo imeendelea kushuka mwaka hadi mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona kwa mfano mwaka 2015 tumeambiwa kwamba kilimo kilikua kwa asilimi 3.1, lakini mwaka 2014 tunaambiwa kilikua kwa asilimia 3.4. Ikumbukwe kwamba siku za nyuma huko mwaka 2009, kilimo kimeshawahi kukua kwa asilimia hadi 5.1. Hivyo ni dhahiri kwamba wakulima wamesahaulika, japokuwa sasa Sekta hii ya Kilimo inaajiri Watanzania walio wengi, lakini wamesahaulika sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaambiwa kwamba uzalishaji wa mazao ya nafaka, hivyo hivyo umeendelea kushuka mwaka hadi mwaka kama tulivyoambiwa kwamba mwaka 2015 mazao ya nafaka uzalishaji ulikuwa tani milioni 9.8, lakini hivyo hivyo tunaambiwa kwamba mwaka 2015 umeendelea kushuka.
Kwa hiyo, naomba niseme tu kwamba wakulima wamesahaulika na zaidi kwa nini tumefikia mahali hapa? Tumefikia hapa kwa sababu Serikali haijachukua hatua ambazo zinaweza kuwasadia wakulima wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Serikali imeshindwa kuwapunguzia wakulima wetu mbolea, wananunua mbole kwa bei kubwa sana na imefika mahali mkulima mwingine anaamua kuahirisha kulima kwa sababu mbolea ipo juu sana. Hali hii ikiendelea, wakulima ambao ndio wengi zaidi katika Taifa hili, siku moja wataungana na kusema sasa basi, inatosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Waziri wa Kilimo yuko hapa Mheshimiwa Mwigulu Nchemba na Naibu wake, naomba wakumbuke kwamba wako waliowatangulia mbele akiwepo ndugu yangu Mheshimiwa Wassira, lakini yuko aliyekuwepo Naibu Waziri Mheshimiwa Godfrey Zambi na mwingine Mheshimiwa Chiza; leo hawapo kwenye Bunge hili kwa sababu ya ugumu wa kilimo katika Taifa hili.
Mheshimiwa Waziri, kama hamtakuwa makini katika suala hili, kama hamtakuwa tayari kuwasaidia wakulima wa Tanzania, kupunguza bei ya mbolea, kutafuta masoko kwa wakulima wetu ni dhahiri kwamba hali itakuwa ni mbaya kweli kweli, na ninyi nadhani mpaka mwaka 2020, mnaweza mkafuata nyao za akina Mheshimiwa Wassira, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba nchi ndogo kama ya Malawi, imefika mahali inauza mbolea kwa bei ndogo sana; inauza mbegu kwa bei ndogo sana kwa wakulima wake, lakini mbolea hiyo inapita kwenye Bandari ya Dar es Salaam. Ingekuwa ni jambo la busara sana kwenda kuiga kwa wenzetu wanafanya nini hadi mbolea yao wanauza kwa bei ndogo wakati wanaipitisha kwenye bandari yetu, wanatoa na ushuru wa bandari, leo wao wanauza kwa bei ndogo. Nadhani suala hili tungeweza kufanya utafiti tujue ni kwa nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa sana, ninaambiwa kwamba mwaka 2014 pesa kwenye mbolea zilitengwa shilingi bilioni 96, tukaambiwa mwaka 2015 zilitengwa shilingi bilioni 78 kwa ajili ya mbolea, lakini mwaka huu pesa zilizotengwa kwenye mbolea tunaambiwa ni shilingi bilioni 20.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna hii hatuwezi kusonga mbele! Hali ni mbaya kweli kweli na ni dhahiri Serikali hii haitaweza kwa kweli kuwasaidia wakulima na haina nia njema na wakulima wetu. Huyu Rais wetu anayesema kwamba mniombee Watanzania, ajue kwamba wengi wao ni wakulima. Sidhani kama wanaweza wakamwombea kama hatawasaidia kwenda kupunguza kodi katika mbolea na kuongeza fedha katika Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosikitika kingine ni kwamba tunaambiwa wenzetu zao lao la korosho wamepunguza ushuru; ushuru wa Chama Kikuu cha Ushirika, lakini kuna ushuru wa usafirishaji, ushuru wa mnyaufu, ushuru wa Bodi ya Korosho, ushuru wa Mrajisi wa Vyama vya Ushirika; kwenye korosho wamepunguza ushuru huu na tozo hizi.
Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kwenye majumuisho atuambie na sisi wakulima wa kahawa kama mna mkakati wa kupunguza ushuru kwenye kahawa. Kwa sababu kumekuwa na mzigo mzito sana, imefika mahali mkulima wa kahawa anatozwa ushuru wa Bodi ya Kahawa, ushuru wa utafiti (TACRI) kule mkulima analipia, wakati Serikali ingeweza kabisa kuwasaidia wakulima hawa. Vile vile kwenye Halmashauri, wakulima wa Kahawa pia wanatozwa ushuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kabisa Mheshimiwa Waziri atakapokuja kwenye majumuisho, atawatangazia neema wakulima wa kahawa nchi nzima kwamba tumeamua tupunguze ushuru kwenye mazao haya, maana huu utakuwa ni ubaguzi wa hali ya juu sana kama utapunguza kwenye korosho halafu kwenye kahawa ukaacha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze suala linguine. Wakulima wa kahawa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wanaomba Serikali ianzishe mnada kuliko ilivyo leo ambapo wanapeleka kahawa yao Moshi ambapo kuna mnada, wakati asilimia 90 ya kahawa inayouzwa kwenye mnada wa Moshi, inazalishwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo wakulima hawa wamenituma, wanaomba tuwe na mnada wa kahawa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, watu wa Ruvuma na Mkoa mpya wa Songwe ikiwezekana waje Mbeya wauze kahawa yao pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nakumbusha tu kwamba Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, hili ni eneo la muhimu sana. Siku hizi tuna uwanja wa ndege pale Songwe. Kwa hiyo, mazingira yanaruhusu kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kabisa Mheshimiwa Waziri atakapokuja kwenye majumuisho atatuambia kwamba suala hili atakubaliana na wakulima wa kahawa wa Kanda za Juu Kusini kuweza kuanzisha mnada wa kahawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la NFRA kutenga fedha za kununua mazao ya nafaka. Msimu uliopita wakulima wetu wamekopwa mahnidi na wengi hadi sasa walilipwa nusu imefika mahali hawawezi tena kununua mahindi, wamekosa mtaji kwa sababu Serikali kwa jitihada za makusudi kabisa imeamua kuwafilisi wajasiriamali.
Msimu huu tunapokwenda kununua mahindi, naomba Serikali isiwakope wananchi. Ikiwezekana itenge fedha kabisa ya kwa ajili ya kwenda kununua mahindi ya wananchi bila kuwakopa. Wakiendelea kuwakopa wananchi ambao ni maskini na wengi wao pesa wanakopa benki, tunawalipa nusu nusu, hatutafika na mwisho wa siku tutakuwa hatuwasaidii wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ni la msingi zaidi japokuwa wengine wameshaligusia sana, ni mfumo wa kugawa voucher. Mfumo wa usambazaji wa voucher siyo rafiki kwa wakulima wetu. Imefika mahali watu wanagawa voucher wanaangalia, huyu ni ndugu yangu, huyu ni shemeji yangu, huyu ni nani! Leo Wenyeviti wa Vijiji, Madiwani wamekosana na wananchi kwa sababu pia nao wanaambiwa kwamba mnapendelea na mnabagua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mfumo huu wa voucher ikiwezekana tuufute kabisa na badala yake mbolea iweze kupunguzwa bei, tupunguze ushuru kwenye mbolea na baada ya hapo mbolea ipatikane nchi nzima kwa bei nafuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kabisa tukifanya hivi wakulima wetu itafika mahali watafarijika na wataendelea vizuri kabisa, watalima, tutapata mazao ya biashara na chakula; lakini mambo yatakwenda vizuri kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia naomba niseme kwamba leo tuko mahali hapa, lakini nasikitika sana, kuna watu ambao bado hawajalipwa fedha zao za mahindi waliyopima.
Naomba kwa sababu Waziri yuko mahali hapa, ikiwezekana aonane na Mbunge wa Jimbo la Mbozi ili nimwambie ni akina nani hawajalipwa mahindi yao na ni kwanini Serikali inakopa wananchi mahindi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini inafika mahali inawadhulumu na wengine masikini? Hatuwezi kukubali kabisa! Tumesema kwamba sasa inatosha, lakini tukiendelea na utaratibu huu tutakuwa tunawaumiza wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nami sasa niweze kuchangia Wizara hii muhimu ambayo kwa kweli na mimi naomba ku-declare interest kwamba mimi pia ni Mwalimu kama ambavyo wengine wame-declare interest. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunajadili bajeti ya Wizara ya Elimu, wanafunzi ambao wako Vyuo vya Elimu ya Juu, tangu wamefungua chuo hawajapata mkopo; na hili ni jambo la kusikitisha sana. Imefika mahali wanafunzi wetu wanacheleweshewa mikopo na mikopo ambayo mwisho wa siku watakuja kuirejesha, lakini wanapokuwa sasa wanadai hizo fedha, tunaenda kuwapiga mabomu, tunawapelekea Polisi jambo ambalo linasikitisha sana. Kiukweli kabisa kama mikopo inakuwa inacheleweshwa, nadhani mtu wa kwanza kupigwa bomu inatakiwa awe Waziri wa Elimu na Watendaji wake lakini siyo wanafunzi wetu. Tunawaonea sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba japokuwa pia wenzangu amegusia sana kwenye suala hili la Bodi ya Mikopo, naomba nami niguse baadhi ya vitu pia. Kuna kitu fulani kinaitwa Quality Assurance Fee kwenye elimu ya juu. Mwanafunzi anaambiwa alipie shilingi 20,000/= kwa ajili ya kudhibiti ubora wa elimu. Kimsingi jukumu hili la kudhibiti ubora wa elimu ambalo linafanywa na TCU ni jukumu la Serikali. Hivyo, kumbebesha mwanachuo mzigo, ni suala ambalo kwa kweli haliruhusiwi hata kidogo! Kwasababu TCU ni sehemu ya majukumu, inakuwaje tunakwenda kumbebesha mzigo mwanafunzi masikini? Kwa kweli hali hii inasikitisha sana na sidhani kama inatakiwa tuendelee kuivumilia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri, pamoja na sifa ambazo amepewa mimi sitaki kumsifia, kwasababu siwezi kumsifia mtu wakati ni majukumu yake. Naomba suala hili ukaliangalie sana Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nizungumzie suala linguine, kwenye elimu ya juu. Leo wanafunzi hakuna mawasiliano kati ya Wizara ya Ulinzi pamoja na Wizara ya Elimu. Wametangaza kwamba wanafunzi waliomaliza Form Six waende JKT kuanzia tarehe 1 mwezi wa Sita hadi tarehe 6 walipoti JKT. Wakati wowote kuanzia sasa wanafunzi watahitajika kuomba mkopo waliomaliza Form Six. Tafsili yake ni nini? Tafsiri yake ni kwamba wanafunzi wanaoenda JKT wengi wanakosa fursa ya kuomba mkopo. Mwaka 2015 wanafunzi 80 waliokwenda JKT walikosa mkopo Chuo Kikuu cha Dar es salaam peke yake sehemu ya Mlimani. Kwenda JKT imekuwa dhambi leo hii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba suala hili Mheshimiwa Waziri aliangalie sana, kuwe na utaratibu maalum; kabla hawajaenda JKT, waombe mkopo mapema ili wanapomaliza pale waende chuo tayari wakiwa wameshaomba mkopo. Kama tatizo ndiyo hilo, mwisho wa siku watu watasema kwamba JKT hatuendi kwasababu tukitoka JKT tutakosa mkopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine ambalo limekuwa ni tatizo kubwa sana. Hakuna mawasiliano kati ya TCU na Bodi ya Mikopo. Kwanini nasema hakuna mawasiliano? Leo ukisoma kitabu cha TCU kinakuonesha kozi ambazo ukienda kusoma utapata mkopo (priority course), lakini wakati huo huo anapoomba mwanafunzi kozi hizo kwenda kusoma Bodi ya Mikopo inasema kwamba hizi kozi siyo za mkopo. Hakuna mawasiliano kati ya Bodi ya Mikopo pamoja na TCU. Alishaongea Mheshimiwa Godbless Lema kwamba hii nchi imekuwa kama ghetto, hamna utaratibu, nami nadiriki kusema kwamba nchi hii ni kweli hakuna utaratibu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme maneno makali, tunaendesha nchi utafikiri ile nchi ya kijuha, kwasababu kama Bodi ya Mikopo ni chombo cha Serikali, TCU ni chombo cha Serikali hawa wanakwambia hii kozi inakopesheka, ukienda kule wanakwambia hii kozi haina mkopo. Maana yake ni nini? Mheshimiwa Waziri, naomba ukaliangalie hili. Kama Taifa tunaaibika sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninaomba nizungumze suala linguine. Leo kuna changamoto nyingi sana katika elimu ya juu. Ukienda katika hostel za wanafunzi wetu; kwa mfano pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tu sehemu ya Mlimani, wanafunzi ambao hostel inaweza ku-accommodate ni wanafunzi 6,500, lakini idadi ya wanafunzi ni 18,000. Wanafunzi wengi wanabebana, wanalala wawili kwenye kitanda kimoja. Hali ambayo ni mbaya sana! Leo hii kama kuna fedha inatakiwa zipelekwe basi zinatakiwa zipelekwe kwenye elimu ya juu za kutosha. Kama Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli alipeleka pesa kwa Mahakimu akasema hakuna pesa, kesho kutwa kapeleka; baada ya siku mbili akapeleka, leo mnaonaje kupeleka pesa elimu ya juu? Pesa zipo. Tatizo la nchi hii siyo pesa, tatizo la nchi hii ni uongozi mbovu ambao nadhani kwa muda mrefu sana tumekuwa tukilia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nizungumze suala lingine kuhusu mfumo wa uandaaji wa vitabu vya kufundishia na kujifunzia. Leo kutokana na elimu yetu jinsi ilivyo, kila mtu anapanga la kwake. Akilala Mheshimiwa Waziri anaamka asubuhi anasema, leo tunachanganya Physics na Chemistry, wanafunzi wanaanza kusoma. Kesho mwingine anarudi anasema hapana ulikosea. Hii hali ni kwasababu ya kukosa uongozi bora. Tatizo ni Uongozi katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongezee, leo tunataka elimu yetu iwe bora, kuna tatizo la kutowalipa Walimu wetu wanaoidai Serikali. Nataka nitoe mfano mdogo tu. Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Walimu wanainaidai Serikali zaidi ya shilingi milioni 800 na kitu, hawajalipwa. Watoto wetu watafaulu vipi kwa namna kama hii ambapo Walimu waliokata tamaa wanaidai Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Momba wanaidai Serikali zaidi ya shilingi milioni 600. Walimu hawajalipwa hizo fedha! Ileje Walimu wanaidai Serikali zaidi ya shilingi milioni 400, hawajalipwa. Unataka watoto wafaulu vipi? Suala hili halihitaji kufunga kwa maombi wala kupiga ramli, tatizo ni Serikali! Walimu wengi wameshakata tamaa. Suala hili lisiposhughulikiwa kwa kweli tutaendelea kulia na vilio vyetu havitaisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongezee, kuna Walimu wamesimamia mtihani a Kidato cha Nne mwaka 2015 hawajalipwa fedha zao, karibu shilingi milioni 118 Halmashauri ya Mbozi; leo ni nani Mbunge hapa, ni nani Waziri hapa ambaye posho yake ya mwaka 2015 hajaichukua? Posho yake ya mwaka 2014 hajaichukua! Mshahara wake wa mwezi uliopita hajachukua? Ni nani Waziri hapa au Mbunge? Tuwaonee huruma Walimu! Walimu hawa waliokata tamaa mwisho wa siku wakianza kuandamana, msije mkaanza kutafuta mchawi ni nani. Mchawi ni Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu hawa walipwe fedha hizo na wasipolipwa fedha hizo kwasababu sisi ni Wawakilishi wao, nimechangia hata mara ya kwanza nilizungumzia suala hili; tuataenda kukaa nao, ikiwezekana tuingie barabarani. Muwe tayari kutupiga na mabomu! Sawasawa! Kwasababu hatuwezi kuvumilia Walimu wetu wanateseka! Hata mimi pia ni Mwalimu, nina uchungu sana! Naomba kama kweli tunawapenda Walimu wetu, tukalipe fedha hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo, bado kuna suala la makazi bora ya Walimu, ni tatizo! Ameongea mwenzangu pale kwamba ametokea mahali, kwa mfano wanasema hii ni TAMISEMI, hii ni wapi; lakini makazi bora kwa Walimu ni tatizo. Kuna shule moja ambayo nilikuwa nafundisha kabla sijawa Mbunge, shule hiyo ina nyumba moja tu ya mwalimu. Walimu wanalala nane kwenye nyumba moja. Unaweka kitanda, unaweka godoro chini, this is shameful! Kwa kweli suala hili ni aibu sana, Serikali hii lazima ifike mahali iangalie sana kwenye suala la elimu, ahsante.
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Yohana. Tunaendelea na..
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, naomba nisiunge mkono hoja na nimshukuru sana Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa kazi nzuri ambayo anaendelea kuichapa; tunamuunga mkono, Mungu ibariki UKAWA. Ahsante sana.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nichangie ukurasa ule wa nane na wa 17 wa hotuba ya Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa ule wa nane hotuba ya Mhesimiwa Rais imegusa suala la walimu pamoja na malalamiko yao kwamba wana malalamiko. Ni kweli kabisa kwamba suala hili ni suala ambalo lipo. Walimu wana malalamiko kwamba hawana nyumba, lakini pia imefika mahali wana madai ya muda mrefu sana. Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali ya awamu ya tano ambayo ina slogan ya Hapa Kazi Tu; kama kweli itakwenda kujenga nyumba za walimu, italipa madeni sugu ya walimu ya muda mrefu sana, nadhani nchi hii kweli itakwenda, kwa sababu awamu zote zilizopita wote hawakuona umuhimu wa kuwalipa walimu madeni na kuwajengea nyumba bora. Kwa hiyo, nadhani Serikali hii ikifanya hivyo mambo yatakwenda vizuri kabisa. Mheshimiwa Naibu Spika, natoa mfano mdogo. Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi hivi ninavyozungumza inaonekana kwamba walimu waliosimamia mtihani wa kidato wa cha nne mwaka 2014 hawajalipwa fedha zao; na sio walimu tu lakini pia na Watumishi mbalimbali wa Halmashauri wakiwepo askari na madereva. Kwa hiyo, naomba katika haya maneno aliyoyazungumza Mheshimiwa Rais muweze pia kuliangalia hili. Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani kabisa kwamba Serikali yoyote ambayo iko makini inafika mahali deni la mwaka wa jana halijalipwa, lakini leo sina uhakika sana kama sisi Wabunge kuna Mbunge ambaye anaweza akawa anadai deni la mwaka wa jana au mwaka wa juzi. Inawezekana walimu wamesahaulika sana katika Taifa hili, ndiyo maana tunafikia hali kama hii. Mheshimiwa Naibu Spika, naomba walimu wakumbukwe na deni hili lilipwe kwa kweli;
walimu wa Halmashauri ya Mbozi na walimu wengine wowote wanaoidai Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nichangie ukurasa ule wa 17. Wakulima imefika mahali wana malalamiko makubwa sana. Mheshimiwa Rais alipokuwa akilihutubia Bunge, alisema atawasaidia wakulima, ataondoa ushuru wa kwenye mazao. Kwa mfano, Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi tunalima sana kahawa, wakulima wana shida kubwa sana, wanatozwa ushuru wa kahawa 5%, ambayo ni sawasawa na shilingi 175/= kwa kilo moja; lakini pia wanatozwa ushuru wa Bodi ya Kahawa; ushuru wa utafiti; wakulima wamebebeshwa mzigo mkubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali hii ya awamu ya tano iweze kuliangalia hili. alichokuwa anakizungumza Mheshimiwa Rais naomba akifanyie kazi kweli kweli na isiwe maneno tu. Ninaamini kabisa kwamba Mungu atambariki na atakwenda kuwasaidia wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, imekuwa ni mzigo, inafika mahali mkulima wa kahawa licha ya kwamba anatozwa ushuru huo ambao nimesema ni 5%, pamoja na matatizo mengine lakini mkulima huyu wa kahawa na mazao mengine ameshindwa kutafutiwa somo zuri na mwisho wa
siku inaonekana kwamba anauza kwa bei ndogo sana. Kwa mfano, msimu uliopita wakulima wa Kahawa wameuza kahawa yao kwa bei ndogo sana. Naomba Serikali iangalie suala hili maana bila kuwasaidia wakulima kwa kweli tutakuwa tunarudi nyuma, maana tunajua kabisa kwamba kilimo kinachangia zaidi ya asilimia 70 ya pato la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niweze kuzungumza kwa ufupi sana ukurasa wa nne wa hotuba ya Rais. Alizungumzia suala la siku ya uchaguzi kwamba ilikuwa na utulivu na amani. Naomba nizungumze tu kwamba katika hili nadhani Rais wetu atakuwa kidogo aliteleza.
Siku ya uchaguzi tarehe 25 Oktoba, 2015 ilikuwa na amani na utulivu; hayo maneno sijajua vizuri kwamba labda alikosea au aliteleza.
Ni kwamba kuna maeneo mengi sana vurugu zilifanyika, kuna watu walipigwa, watu waliwekwa ndani, watu wamebambikiziwa kesi, watu hadi leo wengine wamekimbia maeneo yao, halafu Rais anasema eti siku hiyo ilikuwa ya amani na utulivu. Mimi nadhani kuna watu
labda walimpotosha Mheshimiwa Rais kwenye hili, nami naomba tu Mheshimiwa Rais inabidi kidogo afuatilie hili vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano natoa mfano mdogo wa Jimboni kwangu Mbozi.
Jimbo la Mbozi uchaguzi siku ya Jumapili, tarehe 25 Oktoba, 2015 watu waliwekwa ndani wakiwa wanadai matokeo. Wamefunguliwa kesi hadi leo! Wengine wameshakimbia, hivi ninavyozungumza hawapo kwenye Jimbo langu. Mheshimiwa Rais anakuja anasema kwamba
Uchaguzi ulikuwa wa amani na huru.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu kwamba siku nyingine Serikali tujipange vizuri. Kunapokuwa na uchaguzi tujaribu kutumia Jeshi la Polisi vizuri na yule aliyeshinda kihalali atangazwe haraka sana. Kwa sababu mambo yote haya yanajitokeza pale mtu ameshinda wanashindwa kutangaza matokeo mapema, inafika mahali watu wanadai matokeo wanaanza kupigwa, wanapelekwa ndani, wanafunguliwa kesi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili kwa kweli linasikitisha sana na machafuko mengi tu yametokea katika sehemu mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mwingine mdogo tu naweza nikatoa. Hata ndugu zetu kule Zanzibar hali kwa kweli haiko shwari kabisa hadi hivi ninavyozungumza. Hali haiko shwari! Hili limejitokeza! Mwenyekiti wa ZEC amekaa peke yake anatangaza kwamba tunarudia uchaguzi
wakati huo unaona kabisa kwamba hawajakubaliana na Tume.
Mheshimiwa Naibu Spika, imefika mahali na ushahidi upo, tutajaribu kuuwasilisha kama utahitajika kwa muda ambao tutapangiwa, Makamu Mwenyekiti wa ZEC alikamatwa akawekwa ndani.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Haonga naomba umalize!
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Kwa hiyo, hali haikuwa nzuri, hapakuwa na utulivu wowote ule. Naomba tunapoelekea huko siku za usoni kweli kabisa tuishauri Serikali isimamie uchaguzi vizuri, aliyeshinda awe ameshinda na mambo yaweze kwenda vizuri kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nichangie suala lingine. Kwenye kilimo kuna suala dogo nilikuwa nimelisahau, kuhusu mfumo wa vocha ambao Serikali inautumia kuweza kuwapa wakulima. Mfumo wa vocha kusema ukweli siyo mzuri kabisa. Vocha hizi zinawanufaisha wale watendaji wachache, Watendaji wa Vijiji, Watendaji wa Kata na watu wachache, mara nyingi sana wanazigawa kwa kufuata itikadi ya Vyama vya Siasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hizi vocha za pembejeo zinazotolewa kuna mtu akiwa chama fulani cha upinzani vocha hizi hazimhusu, hata kama ni mnufaika, hapewi. Vocha hizi zinawanufaisha watu wachache sana. Natoa mfano mdogo tu, Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, msimu wa kilimo huu uliokwisha vocha zilikuja 13,000 kwa Wilaya nzima ya Mbozi. Wilaya ina wakazi zaidi ya 500,000 vocha zimekuja 13,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani kwamba mfumo huu siyo mzuri kabisa, ni mfumo wa ubaguzi, hauwezi kuwasaidia wakulima wetu. Nasema kabisa kwamba kuna namna ambayo inatakiwa tuifanye ili kubadilisha mfumo huu wa kugawa vocha hizi za kilimo. Kama kuna
uwezekano Serikali itafute utaratibu mzuri kwamba mbolea inapoingizwa nchini, kama Serikali inaweza ikatoa ruzuku moja kwa moja kwa ile mbolea inapoingizwa nchi nzima, inapouzwa basi iwe imeshalipiwa ruzuku na kila kitu, angalau sasa ionekane ni ya ruzuku nchi nzima, hata kama ni pesa kiasi kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama mfuko wa mbolea leo unauzwa shilingi 70,000/=. Labda mfuko wa mbolea Dar es Salaam hapo unauzwa shilingi 70,000/=. Kama Serikali inaweza ikaweka pesa yake ya ruzuku kidogo pale, ikalipa kwa mfano hata 40% au 50%, maana yake
shilingi 70,000/= inaweza ikashuka hadi kufikia shilingi 35,000/=hadi shilingi 40,000/=. Hiyo ni nchi nzima, maana yake watu wa Mbozi wanunue kwa bei hiyo, lakini pia watu wa Kigoma wanunue kwa bei hiyo kuliko mfumo wa sasa ambao unawanufaisha wafanyabiashara
wachache, lakini pia ni mfumo wa kibaguzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba suala hili tuliangalie sana kwa sababu Tanzania bila kilimo haiwezekani, ninaamini Kilimo kinachangia asilimia kubwa sana katika pato la Taifa.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Haonga, muda wako umekwisha.
MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kidogo.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Haonga muda wako umekwisha tafadhali! Mheshimiwa Haji Khatib Kai! Mheshimiwa Abdallah Mtolea.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, nchi hii ina matunda mengi kama vile maembe, mananasi, machungwa, zabibu na mengineyo, Serikali haina sababu ya kuagiza juice na wine nje ya nchi kwa kuwa uwezekano wa kuanzisha viwanda vya juice na wine hapa nchini ni mkubwa, kuagiza juice nje ya nchi ni upotevu wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mafuta ya kupikia ambayo ni ya pili kuingizwa nchini yakitangulia mafuta ya magari, Serikali ipige marufuku uingizaji wa mafuta ya kupikia kwa kuwa mazao ya kutengenezea mafuta kama vile karanga, alizeti na mawese vinapatikana hapa nchini. Alizeti inalimwa katika Mikoa ya Singida, Iringa, Mbeya, Rukwa, pamoja na Mikoa mingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo, uagizaji wa toothpick ungepigwa marufuku kwa kuwa tuna miti mingi inayoweza kutengenezea toothpick. Serikali ikizingatia haya yote tutaokoa fedha nyingi sana, lakini pia tutatengeneza ajira kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nawasilisha kwa Waziri wa Nishati na Madini vijiji ambavyo havipo kabisa kwenye mpango wa umeme wa REA Jimbo la Mbozi. Vijiji hivi ni pamoja na:-
Ikonga, Maninga, Iporoto, Twinzi, Halambo, Shasya, Mbuga, Rungwa, Hamwelo, Insani, Itentula, Mboji, Iyenga, Nsega, Ileya, Igaya, Magamba, Mtunduru, Naulongo, Iwalanje, Nambala, Mbulu, Myovizi, Ivufula, Isenzanya na Manyara.
Mheshimiwa Naibu Spika, niaba ya wananchi wa Mbozi naomba Mheshimiwa Waziri awasaidie ili waingizwe katika REA phase III.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia makaa ya mawe yanayochimbwa Kijiji cha Magamba na Kampuni ya Wagamba Coal Company katika Jimbo la Mbozi kuna changamoto zinajitokeza. Kampuni hii haijawahi kulipa service levy katika Halmashauri ya Mbozi tangu uchimbaji wa makaa ya mawe uanzishwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kampuni hii iagizwe kulipa service levy katika Halmashauri ya Mbozi ili kuchochea maendeleo. Pia kampuni hii ielekezwe kutengeneza barabara ya kutoka Magamba-Isansa-Shiwinga-Mlowo katika Jimbo la Mbozi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji anayemiliki shamba kubwa Kijiji cha Senzaya amewakosesha wananchi maeneo ya kulima. Eneo analomiliki ni kubwa na ameshindwa kuliendeleza kwa miaka mingi sana. Naomba Mheshimiwa Waziri aingilie kati ili wananchi waweze kurejeshewa eneo la kulima. Jambo baya zaidi ni kwamba sehemu ya eneo hilo lilichukuliwa kinyemela bila kufuata taratibu/sheria za umiliki wa ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia shamba kubwa na NAFCO - Magamba zaidi ekari 12,000 limechukuliwa hivyo wananchi hawana maeneo ya kulima. Ni vyema Serikali ikarejesha sehemu ya shamba hilo ili kuwasaidia wananchi wa maeneo yanayozunguka mashamba hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mashamba yote mawili (Isenzanya na NAFCO) yapo Wilaya ya Mbozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti naomba kuwasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kilimo halijapewa kipaumbele, limezungumzwa kidogo sana katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/2018. Ni vema kilimo kikapewa kipaumbele ili pia kufikia nchi yenye viwanda tunayoiota. Karne ya 18 na 19 mwanzoni, nchi ya Uingereza ilifanya mapinduzi makubwa sana ya kilimo (Agrarian Revolution) na ndiyo matokeo ya viwanda vya Uingereza vilivyopo hadi leo. Vivyo hivyo nchi za China na India zote zilifanya mapinduzi ya kilimo (Agricultural Revolution) na hatimaye zikafikia hatua ya kuwa na viwanda ambavyo vipo hadi leo. Hivyo hakuna nchi yoyote duniani inayoweza kufikia mapinduzi ya viwanda bila kuboresha kilimo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kuchangia hii hotuba ya Waziri Mkuu. Awali ya yote niweze kwanza kumpongeza Rais mpya wa TLS ndugu yangu Mheshimiwa Tundu Antipas Lissu kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi sana. Kwa hiyo, pongezi sana japokuwa mchakato huu ndugu yangu Mwakyembe alitaka kuingilia, bahati mbaya akawa amelemewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza hayo naomba sasa niweze kujikita kwenye hotuba ya Waziri Mkuu na naomba nianze na suala moja la wakulima wa zao la kahawa. Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati yupo kule kusini alifanya mambo mazuri sana kwenye suala la watu wa korosho akapunguza tozo kwenye korosho na mambo mengi sana, lakini kiukweli kabisa amewasahau wakulima wa zao la kahawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Mbozi pamoja na Mkoa wa Songwe na Mikoa yote ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wanaolima kahawa wana maeneo mengine wanasema kwamba kama Waziri Mkuu hatapunguza tozo na kodi kwenye zao la kahawa maana yake Waziri Mkuu
atakuwa ameonesha upendeleo wa hali ya juu sana na atakuwa amefanya ubaguzi ambao kwa kweli hatutegemei kuuona. Wao pia wanasema kwamba amefanya hivyo kwa sababu kule ni nyumbani kwao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wakulima wa zao la kahawa wanasema kwamba wanategemea kusikia atakapokuwa anahitimisha na hapa nimepokea meseji kama 200 hivi kutoka Jimboni kwangu; wanategemea kusikia anapunguza kodi na tozo mbalimbali kwenye zao la kahawa.
Zipo tozo nyingi sana; kuna ushuru Bodi ya Kahawa, iko tozo kwenye TaCRI na iko tozo kwenye Halmashauri kule asilimia 0.5.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wanaomba tafadhali suala hili Mheshimiwa Waziri Mkuu aweze kulichukulia kwa umakini sana maana kule kwake nadhani ameshamaliza sijui ndio alikuwa anatengeneza mazingira lakini kwa kusema ule ukweli kwenye mazao mengine kama kahawa nahitaji kuona anapunguza tozo na kodi mbalimbali kwenye zao la kahawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kwetu Mbozi kahawa ndio dhahabu yetu; kahawa ndio kila kitu, mtoto anapokwenda shule lazima unaangalia kwenye kahawa na mtoto anapotaka kuoa unaangalia kwenye shamba la kahawa, kila kitu kahawa. Kwa hiyo, tafadhali suala hili ajaribu kuliangalia Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu wakulima wetu wa kahawa sasa wamefika mahali wamekata tamaa na wameanza kung’oa miche ya kahawa kwa sababu bei kwanza ni ndogo na hizo tozo na kodi zimekuwa nyingi hivyo wanategemea atatoa majibu mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu kama hatozungumza lolote kuhusu kahawa mimi na Wabunge wengine tunaotoka kwenye Majimbo na maeneo wanayolima kahawa tutahamasishana kuwaleta wote hapa Dodoma ili waje kupewa majibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba kuzungumzia kidogo suala la maafa amegusa kwenye ukurasa wa 48. Suala la maafa tunajua ndugu zetu wa pale Bukoba tetemeko lilitokea wakapata matatizo makubwa sana. Cha kusikitisha Rais wa nchi hii amechukua muda mrefu
kwenda pale kuwafariji wananchi wale. Kibaya zaidi zipo fedha ambazo zilichangwa bilioni sita kutoka EU na lakini ziko pesa ambazo tulikatwa hapa Bungeni kwa ajili ya ndugu zetu wa Bukoba, hizi pesa zimeliwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatujui hatujaambiwa hadi leo lakini inaonekana fedha hizi zimepigwa. Tulifanya mechi pale Dar es Salaam uwanja wa Taifa; Wabunge tumecheza mechi hadi miguu imeuma, tumepata zaidi ya milioni mia mbili na kitu pesa hizi zinaonekana kama mmeshazipiga. Sasa hatujui kwa nini watu wanapata matatizo badala ya Serikali kuchukua fedha zile kuwasaidia, mnaamua kuzitumia kinyume na matarajio, kinyume na ile kazi ambayo tulikuwa tunategemea zifanye. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunategemea kabisa kwamba pale wananchi wanapopata matatizo, Rais wa nchi, Serikali iweze kutoa lugha nzuri. Leo kama Rais wa nchi anasema mimi sikuleta tetemeko, hatutawasaidia chakula ina maana kwamba Taifa hili tumekosa Rais. Nadhani suala
hili tujaribu kuliangalia sana. Naomba niwe muwazi kabisa kwamba Rais wetu lugha anazozitoa watu wanapopata matatizo…
KUHUSU UTARATIBU.....
MHE.PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme tu kwamba, mara ya kwanza ulisema kuwa hutatoa taarifa yoyote ila nasikitika umetoa taarifa kwa huyo bwana. Labda inawezekana ilikuwa kasoro kwa Simbachawene tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo nililokuwa nalizungumza hapa ni kwamba watu wanapopata matatizo wananchi wakipata maafa, Serikali inatakiwa ikae karibu na wananchi. Sasa kama Serikali fedha zinachangwa inafika mahali fedha zile zinatumika kinyume ni lazima tuhoji, lazima
tuulize. Sasa leo hii tusipouliza unategemea nani atauliza suala hili sisi ndio tunaowakilisha wananchi; tumekaa hapa huu ni mkutano wa hadhara wa wananchi nchi nzima hawawezi kukusanyika wote hapa.
TAARIFA....
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba uweze kulinda muda wangu na najua bado nina dakika kama saba hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niende kuzungumzia suala lingine, suala ambalo Waziri Mkuu amelizungumzia kwenye ukurasa ule wa 11 kuhusu kufanya siasa za kutuunganisha badala ya kufanya siasa za kutugawa. Naomba sitanukuu sana kile alichokisoma pale Waziri Mkuu,
naomba niseme tu kwamba nchi yetu ilipofikia siasa za kuwagawa Watanzania zimeasisiwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siasa hizi zimeasisiwa juzijuzi hapa kwenye vyombo vya habari, imeripotiwa tu Mwenyekiti wa CCM Taifa anasema kwamba Wabunge wa Chama cha Mapinduzi ni marufuku kwenda kumwona Mbunge mwenzao Mheshimiwa Godbless Lema aliyekuwa amewekwa ndani. Siasa hizi za kutugawa Watanzania…
TAARIFA....
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ulinde muda wangu na naomba niseme kwamba ninachochangia hapa sichangii kitu ambacho hakipo, nachangia Hotuba ya Waziri Mkuu ukurasa wa 11.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wale ambao labda hawajasoma hotuba hii vizuri wangepata muda waweze kusoma vizuri, hapa kwenye ukurasa wa 11 amezungumza vizuri sana Waziri Mkuu, kwamba tufanye siasa za kutuunganisha badala ya kufanya siasa za kutugawa na
nilichokizungumza mimi, siku ambayo Mwenyekiti wa CCM Taifa amewaasa baadhi ya Wabunge wasiende kumtembelea Mbunge mwenzao vyombo vya habari vilitangaza, magazeti yaliandika, Kituo cha Utangazaji cha TBC kilitangaza, ITV walitangaza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sasa nashangaa sana, labda inawezekana kuna wengine ambao inawezekana hawafuatilii vyombo vya habari, labda hawajasoma na Hotuba ya Waziri Mkuu. Kwa hiyo, naomba tafadhali usiingie kwenye mtego, hii Hotuba ya Waziri Mkuu naichangia vizuri sana, hii ninayo hapa, ni ukurasa ule wa 11. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba nizungumze; wapo ndugu zetu wengi ambao walifukuzwa siku za hivi karibuni Msumbiji, Mheshimiwa Waziri Mkuu nadhani anakumbuka na Wabunge wote mnakumbuka kwenye Bunge hili. Wale Watanzania wamefukuzwa Msumbiji wamepelekwa mpakani pale wengine wamepoteza maisha, wengine wamebakwa. Rais wa nchi, naomba niseme tu kwamba kiongozi mkuu wa nchi, maana yake mmesema tusimtajetaje, sijajua tatizo ni nini, anasema kwamba walikwenda kwa njia za panya warudi kwa njia za panya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunategemea viongozi wetu, watu wetu wanapopata matatizo tuwe wa kwanza kwenda kuwasaidia, tuwe wa kwanza kwenda kuwatia moyo. Watanzania wengi wanaoondoka nchini hawaendi nchi za huko mbali kwa ajili ya kwenda kutalii, wanatafuta
maisha, wanatafuta fursa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkuu wa mkoa alipojaribu kupeleka hata gari lile la jeshi kwenda kuwabeba wale watu alikatazwa akaambiwa kwamba usiwabebe, waache kama walivyo, walikwenda kwa njia za panya warudi kwa njia za panya. Suala hili kwa kweli linasikitisha sana na kwa jinsi hali ilivyo kwenye nchi yetu kama tutaendelea kwenda hivi, mimi naamini kabisa kwamba tutakuwa hatuwatendei haki Watanzania ambao wametuchagua sisi Wabunge na ambao wamemchagua Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na ambao wametuchagua sisi wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba tu kwamba ifike mahali sisi viongozi ambao ndio tumaini la Watanzania tufanye kazi ya kuwawakilisha wananchi wetu vizuri na tufanye kazi ya kuwatetea, tufanye kazi ya kuwasemea, lakini inapofika mahali unasema kwamba
sikuwatuma mimi kwa kweli hatuwatendei haki hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze suala lingine ambalo linapatikana ukurasa ule wa 21 wa Hotuba ya Waziri Mkuu kuhusu ziada ya chakula ambayo ameizungumza kwenye hotuba hii. Mheshimiwa Waziri Mkuu anafahamu yeye na Wabunge wote wanafahamu kwamba
takribani halmashauri 55 zina tatizo la njaa japokuwa sasa hatujaambiwa, hatujaletewa taarifa rasmi Bungeni kwamba kwa sasa tumefikia wapi, lakini taarifa iliyokuwepo siku za nyuma ni kwamba halmashauri 55 zina njaa. Imefika mahali tunaambiwa kwamba chakula hakitapelekwa, sasa watu waliotuchagua leo tu…
MWENYEKITI: Nakuongeza dakika moja!
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, dakika zangu nadhani umenipunja kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka nizungumze tu kwamba sasa tuulize, wakati Watanzania wanapata njaa kipindi cha Nyerere alikipata wapi chakula cha kuwapelekea, wakati Watanzania wamepata njaa kipindi cha Mkapa, kipindi cha Mwinyi, kipindi cha Kikwete, chakula kilitoka wapi na hii Serikali leo kwa nini inashindwa kuwapelekea Watanzania chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili la njaa halina baunsa, mtu yeyote anaweza akapata njaa kutokana na kwamba inaweza kuwa mvua labda haijanyesha, kumetokea ukame, kumetokea matatizo mbalimbali, sasa leo Serikali inasema kwamba sisi hatutapeleka chakula kwenye maeneo ya njaa, hii ni fedheha kubwa sana kwa Taifa letu na nina… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Maliasili na Utalii idhibiti mauaji ya tembo ambao wapo mbioni kupotea kabisa. Tembo wameendelea kuuawa mwaka hadi mwaka hivyo tutapoteza watalii wengi kutokana na suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wizara ya Maliasili na Utalii iwazuie askari wake kuwapiga risasi na kuwaua wananchi wanaoingia maeneo ya hifadhi. Kuwaua wananchi ni kosa kubwa sana, ni bora hatua kali zichukuliwe kwa askari hawa watovu wa nidhamu. Naomba kuwasilisha.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuchangia naomba nimshauri Mheshimiwa Rais kwamba afanye uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini pamoja na hii nafasi ya Mheshimiwa Dkt. Possi, kwa sababu nimeona kuna baadhi ya Wabunge wa Chama cha Mapinduzi wanashindana kutafuta nafasi hizo kwa kushambulia upande huu. Kwa hiyo, naomba niseme tu kwamba afanye uteuzi huo haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya ushauri huo, naomba niendelee sasa kuchangia bajeti ambayo iko mbele yetu. Naomba niseme tu kwamba katika bajeti hii, yako baadhi ya mambo ambayo nimeyaona kwa kweli hayatawasaidia Watanzania, naona tunaenda kuwaongezea Watanzania mzigo wa umaskini. Kwa mfano, liko jambo hili la ada ya leseni ya magari. Ada ya leseni ya magari kwenda kuihamisha kupeleka kwa wale watu wanaotumia mafuta ya taa, kupeleka kwa wanaotumia petrol na diesel, hapa hatujatatua tatizo tumeruka majivu na kukanyaga moto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme tu kwamba Watanzania walio wengi wanaoishi mijini na vijijini, wanatumia mafuta ya taa na ndio wengi hao maskini. Leo tumeamua kuwatwisha magunia ya mawe kwa kuwaongezea bei kwenye nishati hii ya mafuta ya taa. Umeme mmewanyima, hali ni mbaya kweli kweli! Hali ni ngumu huko vijijini, lakini leo unaenda kumpandishia Sh.40/
= kwenye mafuta ya taa. Hii siyo sahihi hata kidogo! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii alipokuwa anaingia madarakani Mheshimiwa Rais alisema kwamba yeye anawaonea huruma maskini. Alizungumza akasema yeye ni rafiki wa maskini. Sasa urafiki na maskini, huyu unayemtwisha mzigo huu wa kumwongezea Sh.40/= kwenye mafuta ya taa, ni masikini wa namna gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake ni nini? Tafsiri ni kwamba leo Tanzania wanaotumia magari hata asilimia 20 hawafiki. Unachukua asilimia 20 ya Watanzania wanaotumia magari unaenda kuwatwisha mzigo Watanzania zaidi ya asilimia 80 ambao hawana magari eti walipie hii motor vehicle. Hii siyo sahihi hata kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu niwaambie Watanzania, najua tu japokuwa hawanisikilizi, lakini najua tu watasikia hata kwa njia nyingine, kwamba ile Serikali ya Awamu ya Tano waliyotegemea kwamba ingeweza kuwasaidia sasa imeshawasaliti haina msaada tena kwao na hapo waangalie mbadala mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni jambo la ushuru wa Sh.10,000/= kwa nyumba ambazo hazifanyiwa uthamini. Yaani leo Watanzania walio wengi wanaoishi kwenye nyumba ambazo siyo bora, ukienda Mkoa huu wa Dodoma, ukienda huko Mtera kwa Mheshimiwa Lusinde, ukienda huko Chemba na maeneo mengine; na mikoa mingine; nimetoa mfano Dodoma tu, lakini yako na maeneo mengine pia, utakuta nyumba ni ya nyasi, juu wameweka udongo, wamejengea miti, leo huyu mwananchi eti unamwambia eti akatoe Sh.10,000/=, kwa kweli naomba tafadhali atakapokuwa anahitimisha, Mheshimiwa Waziri naomba mwombe Watanzania msamaha kwamba tulikosea, tuliteleza kidogo tulikuwa hatumaanishi hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unaposema walipe Sh.10,000/= kwa kila nyumba, ni kuwatwisha mzigo mzito sana maskini hawa. Hofu yangu kubwa sana ni kwamba ipo siku tutaambiwa tuanze kulipia pumzi tunayoivuta. Kama leo mnasema tuanze kulipia vibanda vyetu vidogo vidogo ambavyo tunavyo, leo vifaa vya ujenzi ni gharama, kila kitu ni gharama, lakini wanaopata shida zaidi ni watu maskini zaidi hawa wa vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafadhali naomba kama mimi labda sikuelewa vizuri, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha, atoe tamko kwamba hatukumaanisha tuichokiandika hapa, au wafute kabisa hiki kitu, kwa kweli watakuwa wamefanya jambo baya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la ukuaji wa uchumi usiopunguza umaskini. Leo tunasema kwamba uchumi wa Taifa letu unakuwa kwa asilimia saba. Uchumi huu ambao tunasema unakuwa kwa asilimia saba, lakini uchumi huu haupunguzi umaskini wa Watanzania wetu. Ni kwa nini uchumi haupunguzi umaskini wa Watanzania? Uchumi umebaki kukua kwenye makaratasi kwa sababu sekta ambazo zinachangia katika ukuaji wa uchumi ni sekta zile za utalii, sekta za mawasiliano, madini na fedha. Kwa hiyo, sekta hizi haziwagusi Watanzania walio wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungekuza uchumi wetu kupitia kilimo, naamini Watanzania wengi tungekuwa tumewasaidia kwa kiasi kikubwa sana. Mheshimiwa Waziri ninakuomba hii hotuba ya Upinzani tafadhali naomba uisome vizuri. Siku za nyuma mlikuwa mnasema hawa Wapinzani wanakuja na vihotuba vyao vidogo vidogo, makaratasi mawili, matatu; wengine wakaiita toilet paper, wengine wakafanya mambo ya ajabu ajabu; leo tumekuja na hii bajeti ya Upinzani mbadala. Mnasema mbona mmeweka kubwa sana? Mnaandika thesis, sijui mnafanya nini? Ninyi watu hamwaminiki! Naomba Waziri tafadhali, tumia hii hotuba ya Upinzani, hii ina vitu vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamechukua takwimu; kwa mfano takwimu zile za utafiti uliofanywa na REPOA. Ule utafiti unasema kwamba tukikuza kilimo kuanzia asilimia nane hadi kumi tutakuwa tumekata umaskini kwa asilimia 50 ndani ya miaka mitatu. Yaani ndani ya miaka mitatu tukikuza Sekta ya Kilimo kwa asilimia nane hadi asilimia kumi, ndani ya miaka mitatu tutakuwa tumeondoa umaskini kwa Tanzania zaidi ya asilimia 50. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli Serikali hii ina nia njema naomba tafadhali chukueni bajeti hii ya Upinzani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, naomba kwa kuwa kuna watu wamezungumza, nami naomba nichangie kidogo kuhusu suala hili la makinikia suala la madini. Naomba tujiulize adui yetu ni nani? Adui yetu ni mwekezaji? Adui yetu ni sheria zetu? Adui yetu ni nani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, adui yetu ni sheria tulizozitunga; Sheria za Madini na Sheria za raslimali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, adui namba mbili ni yule aliyetunga sheria hizi ambaye ni Serikali yetu hii ya Chama cha Mapinduzi. Hii ndiyo iliyotunga sheria hizi. Huyu ndiyo adui. Leo ziko sheria mbalimbali na kuna watu hawasomi!

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba kuna watu ambao hawasomi. Ziko Sheria za Madini; ninayo Sheria ya Madini hapa ya mwaka 1997. Mwaka 1997 kulikuwa na sheria mbili ambazo zilifanyiwa marekebisho. Iko Sheria ya mwaka 1997 ya Madini ambayo ni ya Uwekezaji kwenye Madini, lakini kuna Sheria nyingine ya Madini ya mwaka 1997 ambayo hii Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za Fedha ambayo ilifuta kodi kwa wawekezaji wa madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Serikali imeamua kufuta kodi kwa wawekezaji wa madini inawatwisha mzigo Watanzania maskini. Hii siyo sahihi kabisa. Leo madini yetu tunapata mrabaha wa asilimia nne, kuna watu walishangilia Sheria hizi mbaya zinapotungwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa hata kuona Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wale aliowaita wezi, anawaita Ikulu, anasema hawa jamaa ni jasiri sana. Leo wale wezi wamekuwa jasiri, anasema ni wanaume, lakini kuna wenzetu Wabunge wako humu ndani akina Mheshimiwa Ngeleja na wengine akina Chenge na wengine amesema wasisafiri, hawa watu wamezuiliwa passport zao kusafiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo anakuja mtu ambaye ulisema ni mwizi, unasema ni mwanaume. Kumbe ukiliibia Taifa hili kama wewe ni Mwekezaji kutoka nje wewe ni mwanaume. Naomba niseme tu kwamba...

TAARIFA . . .

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme tu kwamba huyu bwana nadhani mara nyingi sana vyombo vya habari hafuatilii; taarifa ya habari hasikilizi, magazeti hasomi, WhatsApp haangalii. Kwa hiyo, naikataa taarifa yake ambayo ni ya kijinga kabisa na ya kitoto. Siwezi kuipokea taarifa kama hiyo. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme tu kwamba nchi yetu ilipofika...

TAARIFA . . .

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia tujaribu kupitia Dispensary wote hata ambao hawajui kwamba Acacia na Barrick wame-share hisa. Naomba niendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hili niliache niendelee sasa kwenye mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako Watanzania wengi waliofungwa kwa kuiba kuku, ng’ombe na vitu vingine, tukawaite wale tufanye nao negotiation pia basi. Tuwaite Watanzania walioba tufanye nao negotiation. Kama tunasema huyu ni mwizi ,tukae mezani tufanye negotiation, tuwachukue na walioiba na wengine. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tu, kwamba haya mambo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze suala la mwisho; hilo la madini nadhani na wengine pia wamezungumza nitazungumza baadaye. Niseme tu kwamba kwa kweli bajeti hii imewasahau wafanyakazi wa Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Utumishi alisema kwamba mwaka huu anaajiri 56,000 lakini hatujaambiwa tarehe ya kuajiri ni lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, akiwa Mtumishi namba moja, leo hajaajiri, watu wamehitimu vyuo, hawaajiri kwa nini?
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba sasa na mimi niweze kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2019/2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na suala la watumishi wa umma. Watumishi wa umma katika mpango huu naona kabisa kwamba wamesahaulika na kama si kipaumbele. Nimeangalia karibu kurasa nyingi sijaona mpango wa kuwaongeza watumishi wa umma mishahara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo kwa kweli limetengeneza vidonda vikubwa sana mioyoni mwa watumishi wa umma katika Taifa letu. Watumishi wanalalamika tangu Serikali hii ya Awamu ya Tano iingie madarakani haijawahi kuwaza wala kufikiria kuwapandishia watumishi wa umma mishahara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukiangalia kwa mfano kwenye kitabu hiki cha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ukurasa wa 85 wanasema ujenzi wa nyumba za walimu katika shule za sekondari na ujenzi wa mabweni.

Pia ukienda kwenye kitabu hiki cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri, wanazungumzia ujenzi wa nyumba za watumishi wa afya, nyumba takriban 306. Hata tukiwajengea maghorofa watumishi wa umma, kwa maana ya watumishi wa umma kwenye afya, idara ya elimu na kilimo, kama hawakuongezewa mishahara tutakuwa tunafanya kazi bure. Watumishi wengi wamekata tamaa, walimu wamekata tamaa na hali ni mbaya kwa sababu Serikali hii haijawahi hata mara moja kuwaongezea mishahara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani inawezekana kuna tatizo aidha mmeshindwa kumshauri Rais afanye hivi au mnamuogopa. Sasa sijui, lakini kama mnamuogopa mtakuwa mmetenda dhambi sana kwa watumishi wa umma ambao tunawafanyisha kazi nzito lakini hali ni mbaya kuliko kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, wapo watumishi waliostaafu wana miaka mingi hawajawahi kulipwa mafao yao lakini sioni kwenye mpango huu kama kuna jambo hilo ambalo limeeleza hawa watumishi wanalipwa lini. Watu wanastaafu na wengine wanafariki kwa sababu ya stress za maisha lakini mafao yao hawajalipwa. Nadhani sisi kama Taifa bila ya kujali itikadi za vyama vyetu kuna jambo sasa la kufikiria namna gani hawa watu wanaweza kulipwa ili mambo yaweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu ni kuhusu mazao yote ya wakulima. Nimesoma kwenye hii hotuba ya Waziri amezungumza kwenye zile changamoto za utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Bajeti wa mwaka 2017/2018, ukisoma changamoto namba sita, anasema changamoto ya masoko na bei ndogo za mazao kwa wakulima. Hii imeelezwa kama changamoto lakini nimekuja kuangalia nikadhani kwamba unapoeleza kama changamoto lazima utuambie kwamba sasa suluhisho la masoko itakuwa ni ipi ili wakulima wetu waweze kupatiwa bei nzuri ya mazao yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo zao la kahawa hali ni mbaya bei ipo chini na mahindi hali ni mbaya. Wamezungumza baadhi ya Wabunge waliochangia humu ndani asubuhi, leo mkulima kwa mfano ukienda Mikoa ya Songwe, Mbeya, Ruvuma na Rukwa debe la mahindi linauzwa shilingi 2,500 na gunia moja linauzwa shilingi 15,000. Ili uweze kununua mfuko mmoja wa mbolea ya kupandia DAP ambao unauzwa shilingi 70,000 na ukisafirisha kutoka mjini kwenda kijijini kwenye mashamba ni shilingi 75,000, kwa hali kama hiyo unaona mkulima anauza bei ndogo mazao yake lakini wakati huo huo pembejeo zipo juu.

Sasa ndiyo hayo mambo ambayo Mheshimiwa Dkt. Mpango ulitakiwa utuambie namna gani mnaenda kushusha bei ya pembejeo kama mbolea lakini pia mnaenda kutafuta masoko ya mazao ya wakulima. Mazao yote nchi nzima, mahindi, kahawa, mbaazi ambayo ilikuwa shilingi 2,000 sasa hivi wanauza shilingi 80.

Mheshimiwa Mwenyekiti, korosho ambalo ndiyo tulisema ni zao pekee lililokuwa limebaki angalau lilikuwa linatuingizia fedha za kigeni nyingi sana katika Taifa letu, leo korosho hali ni mbaya, wakulima wanalia na viongozi wanakuja na matamko wanasema kesho Serikali inaenda kununua korosho kama hazikununuliwa na wafanyabiashara. Sisi tunaomba mkanunue kweli kwa sababu mmeshaahidi kwa wananchi kwenda kununua. Soko huwezi ukatumia mabavu, soko lina principle zake siyo suala la kutumia mabavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niseme tu kwamba, kama alivyochangia ndugu yangu hapo, Mheshimiwa Kanyasu, leo asilimia zaidi ya 70 ya Watanzania ni wakulima, mazao yote bei iko chini tafsiri yake ni kwamba hawa wakulima hata uwezo wa kununua bidhaa utakuwa ni mdogo sana na bidhaa zote zimepanda bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumza hapa kuhusu vifaa vya ujenzi; saruji, bati, mafuta, hali ni mbaya, lakini mazao ndiyo kama hivyo hali imekuwa hivyo. Sasa hapa haitakiwi Wabunge walalamike halafu na Mheshimiwa Dkt. Mpango ambaye aliaminiwa na Rais na yeye analalamika kwenye hotuba yake ule ukurasa wa 35, analamika changamoto ya masoko, bei ndogo za mazao kwa wakulima, anatakiwa atuambie kwamba atafanya nini kutafuta masoko kwa wakulima, siyo suala la kulalamika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake kama Mheshimiwa Waziri analalamika anatakiwa apishe kiti hicho ampe mwingine mwenye uwezo wa kufanya kazi hiyo, mwenye uwezo wa kutafuta masoko ya wakulima. Kwa hiyo, nadhani hilo ndiyo jambo kubwa zaidi, atuambie kwamba utafanya nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapokuwa unalalamika kiongozi, Waziri, kwamba ni changamoto umeitaja, utuambie na way forward, utafanya nini kama changamoto ni soko, utatafutaje masoko sasa. Hapo hajatueleza vizuri, ameeleza changamoto page mbili lakini pale kwenye way forward, namna gani anakwenda kutatua hizo changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto inapojirudia mara kwa mara maana yake imeshindwa kutatuliwa, ni malalamiko tayari hayo, kwa hiyo niseme tu kwamba hili ni vizuri akalipokea akaangalia namna ya kulifanyia kazi. Sisi kazi yetu kama Bunge ni kuishauri na kuisimamia Serikali, ndiyo kazi yetu hiyo. Hayo masoko wakayatafute…

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi natoa suggestion wakatafute masoko ya mazao ya wakulima, hiyo ndiyo solution ninayotoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba nizungumzie kidogo suala la kuhusu hizi changamoto zilizoelezwa hapa. Nadhani kuna changamoto moja kubwa sana imesahaulika na hii changamoto Mheshimiwa Dkt. Mpango naomba akafanye utafiti na Serikali hii ya Awamu ya Tano ikafanye utafiti na hii changamoto isipofanyiwa kazi itaenda kulimaliza Taifa; hili suala la kufanya chaguzi za marudio, pesa nyingi tunapeleka kwenye chaguzi za marudio, sasa hii lazima tuitafutie ufumbuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mbunge alikuwa chama fulani anasema leo naamua kuhamia chama kingine na kuna mmoja nimemsikia asubuhi anazungumza anasema kwamba eti niliondoka huko sasa niko huru, niliondoka CHADEMA niko huru upande wa pili, lakini alizungumza kwamba mimi nimekimbia kwa sababu nilitaka nigombee Uenyekiti na Mbowe halafu nikaona Mbowe amekataa, sasa leo ameingia CCM, tuone kama atakwenda kugombea Uenyekiti na Rais Dkt. Magufuli, tuone, kama ninyi mnaruhusu namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tunahitaji kwamba viongozi ukichaguliwa na wananchi umalize miaka yako mitano, hizi fedha za uchaguzi wa marudio ni fedha nyingi sana. Ni sehemu ya changamoto, angeiweka, kutumia fedha za Watanzania, fedha za wavuja jasho kwenda kwenye chaguzi za marudio, hizi fedha tungeweza kuwasaidia wakulima wetu, tungeweza kulipa mishahara kwa watumishi, tungeweza kufanya mazingira mazuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku zote kama mtu ulikuwa kwenye chama ambacho watu walikuamini na wakakuchagua kwenye chama hicho ukahamia Chama cha Mapinduzi, lazima hata uwezo wako wa kufikiri huweza kupungua, ndiyo unachokiona, ndiyo madhara yake hayo. Kuna sentensi moja ya Kizungu inasema an empty stomach is not a good advisor, kwa hiyo, mimi niseme tu kwamba wakati mwingine tumbo likiwa wazi linaweza likakushauri vibaya, ngoja tuwaache tu mwisho wa siku…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Naomba kuchangia hizi Kamati mbili, lakini nitajikita zaidi kwenye Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji. Naomba nianze kwa kusema kwamba Sekta ya Kilimo imeajiri zaidi Watanzania kwa asilimia 70, lakini pia inachangia zaidi ya asilimia 30 ya GDP, lakini sekta hii pia inachangia chakula kwa nchi yetu kwa zaidi ya asilimia 100, lakini pia Sekta ya Kilimo inatoa malighafi za viwandani kwa zaidi ya asilimia 65.

Mheshimiwa Spika, pamoja na umuhimu wa Sekta ya Kilimo lakini imesahauliwa na Serikali hii ya Awamu ya Tano, leo hakuna masoko ya mazao ya wakulima. Leo Serikali inakwenda kununua kwa mfano, korosho. Badala ya kutafuta masoko ya mazao, kama masoko ya korosho, mahindi, pamba, mbaazi, tumbaku na kahawa, leo Serikali inakwenda kununua mazao. Haitaweza kununua mazao yote kwa sababu nchi hii tuna mazao mengi sana ambayo kwa kweli bei yake iko chini sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme tu kwamba mimi naishauri Serikali ijikite kutafuta masoko ya mazao. Huu ndiyo utakuwa mwarobaini kuliko kwenda kununua mazao, haitaweza, zoezi hili ni gumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunafahamu kwamba mahindi tuna miaka miwili sasa hali siyo nzuri, bei iko chini; tumbaku iko kwenye maghala kwa mura mrefu hainunuliwi; mbazi kutoka kilo shilingi 2,000/= tunafahamu kwamba shilingi 80/= hadi shilingi 100/= hali ni mbaya. Leo wakulima nchi nzima wanalia. Kwa hiyo, Serikali imejikita zaidi kwenda kutafuta masoko ya mazao kuliko kwenda kununua mazao kwa sababu haitaweza.

T A A R I F A

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, ngoja nimwache nisimjibu, kwa sababu wakati mwingine unaacha wafu wazikane wao wenyewe. Kwa hiyo, naomba nisimjibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimekuja kuzungumzia maslahi ya Watanzania. Leo ninavyozungumza nawe kwa mfano kwenye zao la kahawa, nami nilileta hoja binafsi japokuwa haikupata kibali cha kuingia Bungeni, lakini nilileta hoja binafsi ya kuhusu zao la kahawa. Kinachoendelea kwenye kahawa, hali ni mbaya kuliko kawaida.

KUHUSU UTARATIBU

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba kuna watu wengine hawafahamu misemo na methali na kadhalika. Kwa hiyo, naomba niendelee. Labda ni vizuri tu kwa sababu nafahamu yeye alikuwa ni Mtangazaji, nadhani vitu hivyo anavifahamu vizuri sana. Haitakiwi tupoteze muda mwingi sana kwenye hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kungumza hivyo, naomba niendelee sasa kwa ruhusa yako.

SPIKA: Tuvumilie.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Naomba niendelee kwa sababu alikuwa wanatupiga, sisi hatuwapigi, tumeamua kuwasemehe.

SPIKA: Endelea, ila kuna neno moja umesema ulileta hoja binafsi.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, ndiyo.

SPIKA: Halafu ikakataliwa. Nikuhakikishie mezani kwangu sijawahi kuona hoja binafsi kutoka kwako.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, nita…

SPIKA: Endelea tu kuchangia, lakini sijawahi kuiona.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Ahsante. Nikimaliza nitakuletea zile nakala ambazo nilikuwa najibiwa kutoka kwenye Ofisi ya Katibu wa Bunge. Nitakuletea Ofisini kwako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo kwa mfano kwenye zao la kahawa, Serikali imeamua kuyakataza Makampuni yaliyokuwa yananunua kahawa yote, yamezuliwa, badala ya kuruhusu soko huria; kwa sababu tunaamini kwamba soko huria ndilo ambalo linaleta bei nzuri kwa wakulima. Tungeruhusu Makampuni yanunue, yashindane na hivyo Vyama vya Msingi vya Ushirika vilivyoanzishwa ili mwisho wa siku mkulima aweze kunufaika na bei nzuri ya kahawa.

Mheshimiwa Spika, kabla hatujawa na AMCOS (Vyama vya Msingi vya Ushirika) bei ya kahawa mwaka 2017 tuliuza shilingi 4,000/= na kitu, hadi shilingi 5,000/= kwa kilo moja, lakini baada ya kuanzisha, tumeuza kilo moja ya kahawa hadi shilingi 1,800/=. Kwa hiyo, nashauri, ni vizuri Serikali ikaruhusu soko huria kwenye zao la kahawa na wakati mwingine kwa sababu pembejeo ziko juu, mkulima analima kwa jasho sana, anapouza ndipo Serikali inapojitokeza inasema usipeleke kahawa yako Uganda, sijui usipeleke wapi. Nchi hii kuna matatizo makubwa sana ya kilimo. Naiomba Serikali kwa sababu tayari ndiyo inayoongoza, ijitahidi kutatua matatizo ya Watanzania. Kama haiwezi, basi iwaachie wengine ambao wako tayari kuongoza nchi hii. (Makofi)

Mheshimia Spika, jambo lingine, ili tuweze kuondokana na bei ndogo; badala ya Serikali kwenda kununua mazao ambayo haitaweza, ni vizuri Serikali ikatengeneza utaratibu wa kuweka ruzuku kwenye mazao ya mkakati yale ambayo yako matano. Mazao ya mkakati kuna kahawa, pamba, chai, tumbaku na mazao mengine yale matano ya mkakati, Serikali ingeweza kuweka utaratibu kwamba bei inaposhuka, Serikali iweze kuongeza kile kiasi ambacho inaamini kwamba itamparia faida mkulima na siyo kwenda kununua. Kununua, hawataweza kutoa fedha za namna hiyo, lakini kuweka ruzuku inawezekana kabisa. Baadhi ya nchi zimefanikiwa, Indonesia wamefanikiwa na maeneo mengine mbalimbali wamefanikiwa kwenye suala hili la kuweka ruzuku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusu kujenga viwanda vya mbolea. Nataka kuuliza, hii ilikuwa kwenye mpango mkakati wa viwanda wa 2025, lakini pia hata kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi hili lipo. Ujenzi wa viwanda, kiwanda kile cha mbolea kule Kilwa Masoko tumefikia wapi? Pale hamna tofali hata moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashauri, Serikali ambayo tunasema kwamba Watanzania asilimia 70 wanategemea kilimo, hawa watu wanahitaji kuwa na kiwanda. Sasa mpango wa Kiwanda cha Mbolea pale Kilwa Masoko tumefikia hatua gani? Mbolea tunayoagiza nje ya nchi ni zaidi ya asilimia 95.

Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha Minjingu ameongea Mheshimiwa Jitu Soni pale. kinazalisha asilimia tano tu. Sasa Serikali iangalie namna ya kuweza kujenga kiwanda cha mbolea na mbolea itashuka bei na baada ya hapo mwisho wa siku tutazalisha chakula cha kutosha, tutazalisha mazao ya kutosha na wakulima wetu watakuwa na hali nzuri kuliko wakati mwingine wowote ule. Kwa hali jinsi ilivyo sasa, tukiendelea kuagiza mbolea, hatutafika popote pale.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, naomba nizungumzie suala la kupeleka fedha kidogo za miradi hasa kwenye miradi ya maji. Kuna fedha zilikuwa zimetengwa, shilingi bilioni 299.9 zilitakiwa zipelekwe kwenye miradi ya maji. Hadi sasa zimepelekwa shilingi bilioni 1.67 sawa na asilimia 0.6 kutoka Hazina kwenda kwenye miradi ya maji. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Du!

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Kutekeleza kwa asilimia 0.6 hili ni anguko kubwa sana kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Niseme tu kwamba, ni vizuri Serikali iangalie yale mambo ya muhimu, ione namna ya kuweza kupeleka fedha. Kwa mfano, kulikuwa na…

SPIKA: Mheshimiwa Pascal huwa ni vizuri sana ukitumia data ukaweka na reference yako, yaani umezitoa wapi. Itasaidia sana. Endelea tu kuchangia, lakini huwa ni vizuri ukisema reference yako.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Hizi ni takwimu kutoka Kwenye Kamati ya Bajeti na zimetolewa Bungeni hapa na Wajumbe wa Kamati ya Bajeti wapo, nataka kwenye hilo nikuondolee hofu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwenye mambo ya muhimu kama haya, kama tunaweza kutenga shilingi bilioni 299.9 kulepeka shilingi bilioni 1.67 sawa na asilimia 0.6 huku ni kuwachezea Watanzania na mchezo huu wa kuwachezea Watanzania ni vizuri tukaacha. Kuna haja gani ya kuhangaika na SGR Watanzania hawana maji? Kuna haja gani ya kuhangaika na Stiegler’s Gorge Watanzania hawana maji?

Mheshimiwa Spika, ni vizuri tukaanza kugusa maisha ya Watanzania moja kwa moja kwa sababu kama mtu hana maji, huyo mtu leo unamwambia apande ndege inakuwa ni vigumu sana.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Pascal, hiyo ni kengele ya pili.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie dakika moja kwa sababu nimeingiliwa sana, naomba kwa hekima yako, kwa kiti chako…

SPIKA: Ni kengele ya pili Mheshimiwa, muda hauko upande wako tunashukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hotuba hii ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na barabara zangu za Jimboni lakini na zile zinazounganisha mkoa na mkoa. Barabara inayounganisha mkoa mmoja na mwingine hili ni suala la kisera ambapo sera inataka zitengenezwe kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko makubwa sana na Mheshimiwa Silinde amezungumza lakini pia yuko Mbunge hapa wa Kwela amezungumza na nimekuwa nikizungumza mara kwa mara, kuna barabara hii ya kutoka pale Mloo - Kamsamba, Mloo kwa maana Jimbo la Mbozi, Mkoa wa Songwe kwenda Kamsamba, Wilaya ya Momba lakini pia kwenda Kwela, Mkoa wa Rukwa lakini pia kwenda sehemu moja hivi inaitwa Kasansa hadi Kibaoni kwa maana ya Mkoa wa Katavi. Barabara hii inaunganisha karibu mikoa mitatu ya Songwe, Rukwa na Katavi na ni muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti iliyopita walitenga fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu naona safari hii tena wametenga fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu, sasa huu upembuzi yakinifu hatujui mwisho ni lini kwa sababu miaka yote sasa wanatenga fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu. Barabara hii kwa sababu ya umuhimu wake, tulitegemea kwamba Serikali ingekuwa sasa imeshaanza kujenga hii barabara kwa kiwango cha lami kwa sababu tayari Daraja la Kamsamba lilishaisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili ambalo nalizungumza mazao yote yanayoingizia pato kubwa Taifa kama kahawa, mpunga, kwa maana ya mchele lakini pia ujumlishe mazao kama ufuta, alizeti na mazao mengine mengi sana ya misitu na kadhalika yanatoka kwenye eneo hilo. Kwa hiyo, kutengeneza barabara hii kwa kiwango cha lami maana yake inaenda kuongeza kipato cha Mikoa ya Songwe, Rukwa, Katavi lakini pia pato la Taifa kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ili Mheshimiwa Waziri kuacha alama Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, nadhani ni kuhakikisha kwamba barabara hii inatengenezwa kwa kiwango cha lami. Hakuna namna nyingine unaweza ukafanya kuwaaminisha watu wa Kanda za Nyanda za Juu Kusini kwamba kuna kazi imefanyika kama hii barabara itabaki kama ilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Pinda alijitahidi sana barabara kutoka pale Tunduma - Sumbawanga, nadhani anaweza akajivunia. Sasa Mheshimiwa Waziri wewe unatoka Katavi sijui utawaambia nini watu wa Katavi, Rukwa na Songwe kwa sababu barabara hii ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kuna barabara inayotoka Jimbo la Songwe kule kwa Mheshimiwa Mulugo kuna Kata inaitwa Magamba kuja Magamba ya Mbozi, kwa sababu kuna Kata mbili za Magamba, Mbozi kuna Magamba lakini pia Songwe kuna Magamba, watu kutoka Jimbo la Mheshimiwa Mulugo wanalazimika kupita Mbalizi kwa maana Mkoa mwingine wa Mbeya wakati Makao Makuu yako Mbozi pale ndani ya mkoa mmoja hakuna barabara inayounganisha kati ya wilaya ya Mbozi na wilaya ya Songwe. Kwa hiyo, hili ni jambo ambalo kwa kweli Waziri atakapokuja hapa atuambie wanafanya nini kushughulikia changamoto hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine naomba nizungumze kuhusu suala la Wakala wa Ndege za Serikali kuhamishiwa Ofisi ya Rais Ikulu, Fungu 20. Naomba hapa Serikali iweze kuwa makini kusikiliza vizuri sana. Wakala huyu wa Ndege za Serikali kuhamishiwa Vote 20, ukiangalia majukumu ya Wakala wa Ndege za Serikali, moja ni kusimamia mikataba ya ukodishwaji wa ndege kwa kampuni ya ndege ya Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbili, kufanya matengenezo na ununuzi wa vipuli vya ndege za Serikali. Leo Ikulu inaenda kusimamia ununuzi wa vipuli vya ndege halafu haitakaguliwa imenunua vipuli wapi na kwa gharama gani hamna atakayekagua kwa sababu Vote 20 haikaguliwi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kufanya matengenezo kwa maana kufanya ukarabati wa karakana ya ndege za Serikali. Yaani leo watafanya ukarabati wa karakana za Serikali maana yake hawatakaguliwa…

T A A R I F A

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, anaposema Fungu 20 linakaguliwa, Wabunge mara kadhaa hapa tumetaka watuambie, kwa mfano Vote 20 inahusu pia suala la bajeti yao ya Usalama wa Taifa, mbona Bungeni hapa hatujawahi kuambiwa kwamba Usalama wa Taifa wanakaguliwa kwa sababu nayo iko kwenye Vote 20. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Fungu 20 maana yake hata CAG mwenyewe hatakagua na hatutajua nini kinafanyika. Bunge lako Tukufu halitajua fedha za walipa kodi, za wavuja jasho, wauza michicha, wauza nyanya zinazoenda pale kwenye ndege hamna atakayejua kwamba ni shilingi ngapi zinaenda pale na zinafanya kazi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia Waziri atuambie kwa sababu wanasema jukumu lingine la kitengo hicho ni kulipia gharama za bima za ndege, hakuna atakayejua kwa sababu ni kwenye Vote 20 ambayo haikaguliwi. Kwa hiyo, niseme tu kwamba Serikali katika vitu ambavyo wamebugi, kwa mfano, tunasema Serikali hii inafanya kazi na inajali kweli kodi za Watanzania hii Wakala wa Ndege za Serikali wasiipeleke kwenye Vote 20 ili Wabunge tuwe na uwezo wa kuhoji, Watanzania wajue fedha zao zinafanya nini na mwisho wa siku tujue kwamba tunasonga vipi mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ni kuhusu suala la TBA. TBA wanapewa miradi mingi sana.

T A A R I F A

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niseme tu kwamba suala hili la Fungu 20 tunapozungumza kwamba halikaguliwi kwa mfano nisaidie kitu kimoja umeshawahi kusikia matumizi kwa mfano fedha zinazonda TIC kwa maana usalama wa taifa zikajadiliwa hapa Bungeni.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kaboyoka ngoja tulinyoshe hili tunakupa fursa. Mheshimiwa Heche naomba unyamaze nazungumza. Mheshimiwa Heche naomba ukae nazungumza, nazungumza naomba unyamaze Mheshimiwa Heche, toka nje Mheshimiwa Heche naomba utoke nje Mheshimiwa Haonga ongea halafu nitampa yeye fursa ongea ulichokuwa unataka kuongea. Mheshimiwa Heche naomba utoke nje ukiwa umeshapewa hiyo taarifa ya kutoka nje usiende kuzungumza ukiwa humu ndani funga mlango nyuma yako ondoka. Mheshimiwa Haonga. (Makofi)

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kanuni zetu, kwa kanuni zetu tulizonazo Bungeni hapa mtu anayesema anapotosha Mbunge ndio anayomamlaka kwa maana ya nafasi yakuweza kuweza ukutuambia kwamba ushaidi ni huu kwa maana haikaguliwi. Ninajua kwamba hapa Bungeni haijawahi kuna kuba baadhi ya vifungu havijawahi kuletwa hapa Bungeni kwa mfano kama suala la taarifa hizi za TIC kwa maana ya usalama wa Taifa hazijawahi kujadiliwa Bungeni hapa.

NAIBU SPIKA: Basi Mheshimiwa Kaboyoka.

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kama mwenyekiti wa PAC niweke taarifa vizuri, kwamba Fungu namba 20 linakaguliwa lakini hatujawahi kulikagua halijawahi kaguliwa.(Makofi)

NAIBU SPIKA: Waheshimwa Wabunge tusikilizane Mheshimiwa Haonga ulikuwa unapewa taarifa na Mhehimiwa Kaboyoka unaipokea taarifa hiyo.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niipokee taarifa ya Mheshimiwa Kaboyoka hapa na ninaomba niendelee baada ya kupokea.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utaratibu.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Jenista naomba ukae kidogo, naomba ukae kidogo nakupa fursa. Mheshimiwa Haonga umesema unaipokea taarifa ya Mheshimiwa Kaboyoka?

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema kwamba baada ya Mheshimwa Kaboyoka kunipa taarifa nimeipokea na taarifa ya Waziri pia nimeipokea lakini kwamba haijawahi kuletwa hapa kwa maana ya haijakaguliwa muda mrefu.

NAIBU SPIKA: Sawa naomba ukae tusikie kanuni inayovunjwa. Mheshimiwa Jenista Mhagama.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utaratibu nikwenda kanuni ya 64(1) ambayo inaenda sambamba na kanuni hiyo ndogo ya (1)(a) inayokwenda sambamba na kanuni ya 63. Unapotaka kuzungumza Bungeni lazima uwe unasema ukweli na unakuwa na uhakika na kile unachokisema. Mheshimiwa Waziri wa Fedha ametoa maelezo fasaha hapa, Vote 20 inakaguliwa, na Vote 20 sio Vote ya Usalama wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mbunge ameendelea kusisitiza kwamba wakala wa ndege za Serikali kuwekwa kwenye vote 20 tunakwenda kuficha jambo kwa sababu vote hiyo haikaguliwi. Jambo ambalo si kweli kwa maelekezo ambayo tumepewa na Waziri wa Fedha. Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya PAC anasema vote inakaguliwa halafu akasema wao hawajawahi kukagua lakini wao hawana mamlaka ya ukaguzi wa vote hizo kwa mujibu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Mheshimiwa Haonga Mbunge anayechangia hoja hii afute kauli yake, na kama hataki kufuta kauli yake tunaomba alithibitishie Bunge hili kama kweli ana ushahidi. Suala ukaguzi ni kazi ya CAG sio suala la Mbunge kuthibitisha kwama vote imekaguliwa au haijakaguliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika naomba kutoa hoja. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Taarifa.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge naomba tusikilizane, Mheshimiwa Jenista Mhagama amesimama kwa mujibu wa Kanuni 64 ambayo inazungumza kuhusu mambo yasiyoruhusiwa Bungeni. Mheshimiwa Jenista ametoa hoja yake akieleza kwamba mchango wa Mheshimiwa Haonga kuhusu ukaguzi wa vote namba 20 namna alivyozungumza kwenye hoja yake ametoa taarifa ambayo haina ukweli. Lakini pia amezungumza kuhusu matakwa ya kanuni ya 63 inayozungumza kuhusu kutokusema uwongo Bungeni.

Waheshimiwa Wabunge nadhani wote tumeona mjadala namna ulivyoenda kwanza Mheshimiwa Haonga alikuwa anasema wakala kuhamishiwa pale hataweza kukaguliwa na kwa hivyo Bunge halitaweza kupata taarifa yoyote kuhusu jambo hilo.

Mheshimiwa Waziri wa Fedha akasimama kumpa taarifa kwamba vote namba 20 inakaguliwa na yeye akaulizwa kama anaipokea na yote yaliyofutwa baada ya hapo nadhani sote tunafahamu alijibu vipi mwanzoni na baadaye akapewa tena taarifa na Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali. Baada ya mwenyekiti wa Kamati Hesabu za Serikali kumpa taarifa Mheshimiwa Haonga kwamba vote 20 inakaguliwa isipokuwa Bunge halijawahi kukagua ndio maneno Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali.

Mheshimiwa haonga akasema anaipokea alipoulizwa kwa mujibu wa kanuni zetu alisema anapokea taarifa hiyo ya Mheshimiwa Mwenyekiti wa kamati ya PAC. Lakini wakati huo huo akiwa anatoa maelezo yake kabla sijampa fursa ya kuzungumza Mheshimiwa Jenista akasema pia anaipokea taarifa ya Mheshimiwa Waziri kuhusu kukaguliwa kwa vote 20.

Mheshimiwa Jenista amesimama kuomba ufafanuzi kwa sababu anaona kanuni ya 64 lakini pia kanuni ya 63 imetumika katika matumizi ya maneno ya kutokukaguliwa kwa vote 20 na kwa hiyo, Mheshimiwa Jenista anataka tutumie kanuni ya 64 na 63 tukimtaka Mheshimiwa Mbunge atumie uhuru wake uliyowekwa katika kanuni hizi mbili kufuta kauli yake kuhusu kutokukaguliwa kwa vote namba 20 na katika maelezo yake amesema kwamba kuhusu kukagua hiyo ni kazi ya Mkaguzi wetu wa Hesabu za Serikali na si Bunge. Kwa sababu Mbunge huletewa taarifa na CAG. Kwa muktadha huo na kwa kuwa Mheshimiwa Haonga alishaipokea taarifa ya Mheshimiwa Naghenjwa Kaboyoka kwamba Vote 20 hata kama mwanzo alisema hakaguliwa sasa kwa kuwa alipokea taarifa amekiri inakaguliwa na pia akakubali maelezo ya Mheshimiwa Waziri kuhusu kukaguliwa. Sasa kuhusu mambo yanayofuata baada ya hapa yale yanayoletwa huku Bungeni PAC na LAAC inafanya kazi baada CAG kuwaletea kinachokuwa kimeshakaguliwa. Kwa hiyo jambo lolote ambalo CAG hakulileta maana yake yeye ameona halipaswi kuletwa, kwa muktadha huo maneno aliyoyazungumza Mheshimiwa Haonga kuhusu kukaguliwa ama kutokukaguliwa kwa Vote namba 20 ameyanyosha hapa mwishoni kwamba anaikubali taarifa ya Mheshimiwa Waziri lakini pia Mheshimiwa Mwenyekiti wa kamati ya PAC. (Makofi)

Wakati huo huo nitamtaka sasa kwa mujibu wa kanuni zetu kuhusu hayo maelezo mengine ya taarifa kuweza kufika ama kutokufika yale sasa sio ya Bunge hili yale anatakiwa ayafute kwa sababu hayakuwa sehemu ya taarifa aliyokuwa akipewa. Nadhani utakuwa umeelewa vizuri Mheshimiwa Haonga. La kwanza la kuhusu ukaguzi ulilimaliza kwa maelezo yako ya mwisho, lakini lile la taarifa kufika hapa au kutokufika hilo ndio unatakiwa kuliondoa ili umalizie mchango wako.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kwanza nishukuru sana kwa kuweka vizuri nione kwamba umesimamia kanuni vizuri na umeenda vizuri. Niseme kwamba cha msingi ni kwamba hapa nilijaribu kuliweka sawasawa kwamba hii inakaguliwa lakini tangu nimekuwa Mbunge kwa miaka hii mingapi hii taarifa haijaletwa hapa Bungeni kuhusu Vote 20 nadhani haijaletwa hapa kukaguliwa. Lakini hili lingine ulivyoelekeza naona maagizo yako yachukuliwe kama yalivyo kwamba maagizo yako tumeshaweka sawasawa na ninaomba nichangie kitu kingine kwenye hilo tumeshamaliza na ninaomba unisaide muda wangu.

NAIBU SPIKA: Ngoja sasa nitakupa muda wako umalizie. Kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge kwa ajili ya kuliweka sawasawa hili la Mheshimiwa haonga hoja ya kwanza alishaikubali kwamba Vote namba 20 inakaguliwa ile sehemu ya pili kuhusu kuleta taarifa hapa au kutokuletwa taarifa huletwa na CAG, kama CAG hakuleta basi hakuona umuhimu ama hatakiwi kuleta hilo. Na yeye kwa ajili ya kupunguza matumizi ya muda amesema maelezo haya ndio ambayo yanachukuliwa. Kwa hiyo, sehemu hiyo ya mchango wake inakuwa imeondolewa Mheshimiwa Haonga malizia muda wako.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana naomba niendelee kama ambavyo umetaka niendelee. Kuhusu suala la TBA, mheshimiwa TBA wana miradi mingi ambayo wanapewa, wanamiradi mingi karibu miradi 90 wanapewa. Lakini cha ajabu TBA wanaopewa mradi mingi ya ujenzi, miradi mingi haikamiliki kwa wakati. Na kama miradi haikamili kwa wakati tafsiri yake ni kwamba fedha za walipa kodi maana yake mwisho wa siku inakuwa zinatumika nyingi sana maana yake unapochelewesha mradi gharama za mradi zinaongezeka, gharama ya mradi ikiongezeka anayeingia hasara ni watanzania wanaolipa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa naomba niseme tu kwamba hata kule kwetu Mkoa wa Songwe tuna ofisi ya Mkoa wa Songwe zimeanza kujengwa muda mrefu sana ni kama miaka minne sasa hizo ofisi zinajengwa na TBA hazijawahi kukamilika na ni muda mrefu mno.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atuambie ana mkakati gani wa kuwapunguzia TBA miradi. Kusudi hii miradi wapewa wengine na kuwe na ufanisi wa miradi wanapomrundikia mtu mmoja miradi hii miradi, miradi haiwezi kufanyika kwa ufanisi. Na wakati huohuo fedha za watanzani zitakuwa zinapotea kwa hiyo niombe Mheshimiwa Waziri utakapkuja hapa utuambie mna mikakati wa kuwapunguzia TBA miradi ili sasa na wengine waweze kupata miradi na mwisho wa siku iweze kufanyika kwa ufanisi na tuweze kupata ile value for money.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na mimi nichangie Kamati hii ya Kilimo, Mifugo na Maji na ninaomba ku-declare interest kwamba mimi ni mjumbe wa Kamati hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kusema kwamba kwa bahati mbaya sana tunadhani kwamba tunaweza kuwasaidia Watanzania angalau kuondokana na umaskini kupitia kilimo; jambo ambalo kwa kusema ule ukweli kwa haya yanayofanyika imekuwa ni vigumu sana na sidhani kama kweli tupo serious. Unaona leo kwenye ruzuku ya pembejeo za kilimo wamepeleka bilioni 20 kwenye bajeti, na bilioni 20 yenyewe hii, hizi fedha bado inaonekana hali ni mbaya na hizi fedha bilioni 20 haziwezi kuwatosha wakulima wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti tulishapendekeza siku za nyuma kwamba ikiwezekana huu mfumo wa kuweka ruzuku kwenye pembejeo za kilimo, Serikali iachane nao kabisa kwa sababu hauwasaidii wakulima wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukitaka kumsaidia mkulima ni mara mia ukapunguza kodi kwenye mbolea, kwa sababu kinachopandisha bei ya mbolea tunajua kabisa ni kodi; hii kodi ambayo ipo kwenye mbolea. Bahati nzuri hata Waziri amewahi kuzungumza kwamba kwenye mbolea kule kuna tatizo moja, kuna kitu kinaitwa udalali. Tukitaka kuwasaidia wakulima twendeni tukapunguze kodi kwenye mbolea na kwenye pembejeo nyingine ili wakulima wetu waipate dukani kwa bei ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ajabu sana leo nchi kama Malawi inatumia Bandari ya Dar es Salaam na inapofikisha mbolea nchini kwake bei ni ndogo sana mfuko hata shilingi elfu 20 haufiki; unapokwenda Zambia vivyo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wetu tumewachezea vya kutosha na Mheshimiwa Waziri, naomba niwe muwazi kabisa, msema mkweli ni mpenzi wa Mungu, tutakapokuwa tunaenda kwenye Bunge la Bajeti kabisa kama mchezo tunaoenda nao ndio huu, nitashika Shilingi ya Mheshimiwa Waziri na nitaomba huko mbele ikiwezekana uweze kuachia Wizara hiyo kwa sababu naona kama ina changamoto nyingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema ule ukweli kabisa hali jinsi ilivyo hata kwa wafugaji wetu; leo mifugo inakufa. Ukimuuliza Waziri hapa ndugu yangu mifugo iliyokufa; karibu nchi nzima mifugo inakufa kwa sababu ya ukame; hata takwimu hana. Hajui mifugo mingapi, ng’ombe wangapi wamekufa na mbuzi wangapi wamekufa. Sasa kwa hali kama hii, huu ni uzembe na udhaifu mkubwa sana kwa Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wamekuwa wakijipendekeza wanazungumza na uongo hadi wanadanganya wanasema kwamba njaa hakuna kwa sababu Mtukufu Rais amesema njaa hakuna na wao wanafuata hivyo hivyo. Kwa hiyo, inapofika mahali Rais akisema hii ni nyekundu si nyeupe, Waziri nae anasema hii ni nyekundu kwa sababu Rais kazungumza, huko sio kuwasaidia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwe muwazi kabisa nchi nyingine, kwa mfano nchi kama Kenya mifugo ikifa Serikali inaamua kwenda kufidia, inawapa wananchi angalau mifugo kidogo kwa ajili ya kufidia kidogo wananchi wasiingie hasara. Sasa nashauri ikiwezekana na sisi Serikali yetu tuweze kuiga kwa majirani wa zetu hapa Kenya na nchi nyingine tuweze kuiga mfumo wanaoutumia. Mifugo inapokufa angalau tuweze kuwafidia kidogo wafugaji wetu, maana leo katika Taifa letu mifugo imekufa hatujui sasa ukame huu ukiendelea itakuwaje, maeneo mengine; hali ni mbaya zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya ziara maeneo mbalimbali, Kamati yetu tumekwenda Simanjiro na Kiteto, hali ni mbaya kweli kweli tunakutana na mifugo mingi, mizoga ng’ombe wamekufa njiani. Leo Serikali yetu kama haitachukua hatua za kuwafidia wale wafugaji hakika hali itakuwa ni mbaya zaidi kuliko wakati mwingine wowote ule katika Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme; kusema ule ukweli kabisa yapo maeneo mengine mengi tu ambayo bado Wizara hii ina matatizo. Alikuwa anaongea Mwigulu Nchemba hapa akiwa Waziri. Kuna matumaini fulani fulani hivi ambayo kidogo alitaka kuonesha. Anasema mbolea itapatikana madukani kama coca cola; Mheshimiwa Waziri amewasiliana na Mwigulu hiyo mbolea kama coca cola madukani ime… (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa barabara ya kutoka Mlowo (Mbezi) kwenda Kamsamba (Momba) kuelekea Kilyamatundu (Kwela) hadi Kasansa na hatimaye Kibaoni (Katavi). Ni vyema Serikali itengeneze barabara hii kwa kiwango cha lami. Mosi, hii barabara inaunganisha Mikoa mitatu ya Songwe, Rukwa na Katavi na kwa kuwa ni Sera ya Serikali kutengeneza kwa kiwango cha lami barabara zinazounganisha mikoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wananchi wanaoishi maeneo yanayopitiwa na njia hii wanalima mazao ya kahawa, mpunga, mahindi, ufuta, alizeti, mtama, maharage na mazao mengineyo. Naishauri Serikali itengeneze barabara hii kwa kiwango cha lami ili wananchi waweze kusafirisha mazao yao kupeleka sokoni kirahisi. Soko kuu la mazao katika ukanda huu linapatikana Mlowo – Mbozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na barabara hiyo hapo juu, pia kuna barabara ya kutoka Mji Mdogo wa Mlowo, Wilaya ya Mbozi kupitia Vijiji vya Shiwinga – Isansa - Magamba na kuelekea Kata ya Magamba, Wilaya ya Songwe. Hii barabara ni ya muhimu kwa sababu inaunganisha Halmashauri ya Mbozi na Songwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mazao mbalimbali kama vile kahawa, mahindi, maharage, alizeti, ufuta na mengineyo yatasafirishwa kirahisi. Pia makaa ya mawe yanayochimbwa Kijiji cha Magamba yatasafirishwa kirahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na hoja kwanza hii ya kutotekeleza bajeti ya miradi ya maendeleo. Ni kwa muda mrefu sasa Serikali imekuwa haitekelezi ipasavyo bajeti ya miradi ya maendeleo kama ambavyo tunaidhinisha hapa Bungeni. Kama Wabunge tutakuja hapa Bungeni, tutapitisha bajeti, tutapitisha Mipango ya Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka Mmoja au Miaka Mitano, halafu ile bajeti kama haiwezi kutekelezwa, maana yake mwisho wa siku ni kuendelea kumpigia mbuzi gitaa ambapo kwa namna yoyote ile hawezi kucheza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mfano mdogo. Kwa mfano, bajeti ya kilimo ya mwaka 2017/2018, fedha za maendeleo zilizokuwa zimetengwa au zilizoidhinishwa hapa Bungeni, ni shilingi bilioni 150.253 lakini zilizotolewa ni shilingi bilioni 16.5 sawa na asilimia 11 tu. Kutekeleza bajeti kwa asilimia 11 hii kwa kweli siyo sahihi na hatuwatendei haki Watanzania kabisa. Kwa hiyo, ukienda mwaka mwingine 2018/2019 tulitenga shilingi bilioni 98.119 lakini fedha iliyotolewa ni shilingi bilioni 41.22 ambapo ni sawa na asilimia 42. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016/2017 fedha za maendeleo zilizoidhinishwa hapa Bungeni na Bunge hili Tukufu ni shilingi bilioni 100.527, lakini fedha zilizotolewa ni shilingi bilioni 2.25 sawa na asilimia 2.2. Kwa kweli miaka yote mitatu hii niliyotoa mifano kwenye kilimo hatujawahi kufikisha asilimia 50. Sasa sijui tunafanya nini!

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kama hatuwezi kuweka kilimo kama ndiyo kipaumbele namba moja ambapo tunajua wote kwamba ndiko Watanzania wengi wamejiajiri, zaidi ya asilimia 70, tunajua kabisa huko ndiko ambako hata pato la Taifa mchango ni mkubwa, lakini inaonekana kilimo siyo kipaumbele tena katika Taifa hili. Bajeti zenyewe ndiyo hizo tunatenga, lakini pesa za maendeleo hazipelekwi. Kwa kweli jambo hili linasikitisha sana na hatuwatendei haki Watanzania ambao kwa kweli wengi wapo katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, tunafahamu wote kwamba Watumishi wa Umma kwa muda mrefu sasa hawajaongezwa mishahara. Serikali ya Awamu ya Tano haijawahi kupandisha mshahara kwa Watumishi wa Umma. Mheshimiwa Dkt. Mpango anafahamu unapozungumzia Mpango wa Maendeleo wa Taifa, watekelezaji wa Mpango huu ni Watumishi wa Umma. Kwa mfano, unapozungumza leo watu wanaofanya kazi TARURA, au wanaofanya kazi TANROADs au wanaofanya kazi ya kufundisha Walimu au TRA na kwingineko, hawa watu ndiyo wataenda kuteleleza Mpango huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu wamekata tamaa, kwa sababu gharama za maisha zinazidi kuongezeka, hawajawahi kuongezwa mshahara hata shilingi 100/=, hali ni mbaya, halafu tunataka wakatekeleze Mpango wa Maendeleo wa Taifa. Hili jambo Serikali lazima itafakari vizuri. Haiwezekani! Kuna muda fulani kiongozi anasema kwamba kupanga ni kuchagua, tumeamua kuanza na SGR, tumeamua kuanza sijui na kununua ndege na vitu vingine, sasa hivi vitu hata wewe kwenye nyumba yako, unapojenga nyumba, huwezi ukaacha kuwanunulia watoto chakula eti kwa sababu unajenga, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watumishi wa Umma wamekata tamaa na hawa ndio watekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa. Sasa hawa wameshakata tamaa, mwisho wa siku tutakachopanga hapa Bungeni hakitatekelezeka kwa sababu watu wamekata tamaa na hili jambo Serikali lazima ijitafakari vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Awamu ya Tano, ndiyo muda sasa, bado mwaka mmoja. Sasa sijui hili jambo Serikali inaonaje, lakini kwa kweli jambo hili lazima atakapokuja ku- wind up Mheshimiwa Dkt. Mpango atuambie Serikali inafikiria nini kuhusu Watumishi wa Umma ambao hawajapandishwa mishahara kwa muda mrefu na ndio watekelezaji wa Mpango? Kwa kweli wanachozungumza kitu kibaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu au Watumishi wengine wa Umma wana maandamano au mgomo wa chini chini. Huu mgomo hawawezi kusema hadharani. Siyo rahisi, hawawezi kusema hadharani, lakini mwisho wa siku matokeo yake tunaweza tukayaona miaka inayokuja huko baadaye ambayo siyo mazuri hata kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, nimejaribu kuangalia, ni kweli kupanga ni kuchagua, siyo jambo baya. Alipokuja Mheshimiwa Rais Mkoa wa Songwe, alikuja pale kwangu Mbozi, ameenda pale Jimbo la Vwawa, ameenda Tunduma, ameenda Momba, kote alikopita kero namba moja ilikuwa ni maji; kero ilikuwa ni barabara pamoja na mambo mengine. Wananchi wale hamna hata mmoja aliyesema Mheshimiwa Rais sisi tunafurahishwa sana na ununuzi wa ndege. Hamna aliyesema tunafurahishwa sana na ununuzi wa ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kero za wananchi ni maji na ndiyo kipaumbele namba moja ambacho ukienda huko kwa wananchi wanalia. Hata wewe mwenye ni Mbunge, ukienda kule kwako, wananchi wanalia na maji; wanauliza kuhusu Vituo vya Afya, kuhusu Zahanati, kuhusu barabara. Sasa Serikali inaweza ikawa imeamua yenyewe kufanya kitu ambacho hawajafanya tathmini vizuri kwamba je, ndiyo mahitaji halisi ya wananchi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri jambo moja. Nimeona kwenye Mpango hapa, nimesoma, Serikali inasema kwamba imenunua ndege nane na ndege nyingine kabla ya mwaka kwisha...

MHE. RICHARD P. MBOGO: Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Haonga, hebu sikiliza taarifa. Mheshimiwa Richard Mbogo.

T A A R I F A

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa ndugu yangu Mheshimiwa Haonga. Ununuzi wa ndege ni moja ya mikakati ya kuweza kuongeza mapato ambayo yataenda kutekeleza miradi mbalimbali ya huduma za jamii ikiwepo maji ambayo ameyasema. Katika Mpango huu, maji yametengewa shilingi bilioni 686 ili kuweza kutekeleza miradi mbalimbali na Halmashauri yake inapokea zaidi ya shilingi milioni 800 kwa ajili ya miradi ya maji.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Haonga, unasemaje kuhusiana na taarifa hiyo?

MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee. Taarifa yake naona siyo msaada kwenye ninachotaka kuzungumza. Kwa hiyo, sijaipokea kwa sababu hajui hata Halmashauri yangu napokea shilingi ngapi, anabumbabumba maneno tu. Ni vizuri akafanya utafiti kabla ya kuzungumza. Namheshimu sana, lakini ajaribu kuangalia namna tunavyopoteza muda Watanzania. Huu muda siyo wa Haonga, ni muda wa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani hapa niseme tu kwamba ni kweli Serikali imesema inataka kununua ndege 11 na imetumia zaidi ya shilingi bilioni 700 na kitu. Kwa hiyo, maana yake ndege 11 zitakapokuja, kwa taarifa ni kwamba itakuwa ni zaidi ya trilioni moja na kitu. Hizi fedha zingeweza kupelekwa kwenye miradi ya maji, kwenye miundombinu ya barabara au kwenye vitu vyote vinavyowagusa wananchi, tungekuwa mbali sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri, kwa mfano, kwenye Jimbo langu, hata wananchi wa Mkoa wa Songwe wanafahamu, wananchi wa Rukwa wanafahamu, wananchi wa Mkoa wa Katavi wanafahamu…

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitoka pale Mbozi eneo linaitwa Mloo, Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Songwe, kuna barabara kutoka pale kwenda Kamsamba inayoenda…

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. PASCHAL Y. HAONGA: …Rukwa hadi kwenda Kibaoni. Hii barabara Serikali iliahidi kwamba ingeweza kuItengeneza kwa kiwango cha lami. Sasa daraja wanasema imeKwisha lakini ile barabara haijatengenezwa kwa muda mrefu sana. Kwa hiyo, tunaamini fedha nyingi zingekuwa zinapelekwa kwenye maeneo kama haya, lile eneo ni eneo la mkakati.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa rafiki yangu Mheshimiwa Haong kwamba tunavyoongea sasa hivi tunatoka naye kwenye kikao kule Ashera, tumeitwa na Wizara ya Kilimo kusikia maoni ya wadau mbalimbali. Yeye mwenyewe kwa kinywa chake amemshauri Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Serikali inunue ndege ya mizigo (cargo) kwa ajili ya kusafirisha mazao ya horticulture. Sasa namshangaa anafika hapa tena, anageuka. (Makofi)

Mheshimiwa Haonga, si tulikuwa na wewe pale, umesahau tena!

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Haonga.

MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wote duniani wanaoyumba kwanza kwa mitazamo ya vyama, wanahamahama hawawezi kuwa na akili sawasawa.

MWENYEKITI: Hapana.

MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu tumsamehe tu, tumeshamsamehe, hajui alitendalo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Haonga, nakusihi sana, tutumie lugha ya kibunge. Huyu ni Mbunge kama wewe, amechaguliwa na wananchi wa Tanzania kwa eneo lake. Wewe sema tu, unaikubali taarifa hiyo au unaikataa?

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naikataa taarifa yake na asiwe anahama hama vyama, maana yake Watanzania hawatamwamini tena.

MWENYEKITI: Haya endelea kuchangia.

MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

MBUNGE FULANI: Kigeugeu! (KIcheko)

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii barabara ya kutoka Mloo, Mbozi pale, Mkoa wa Songwe kwenda Kamsamba, nadhani wewe unaifahamu hii, kwenda Kamsamba, kwenda Kinyamatundu kule Rukwa kwenda Kibaoni, Katavi, hii barabara…

MWENYEKITI: Sawa, lakini daraja je? Sema na daraja basi.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nazungumzia barabara, kama wewe umeliona daraja, nakushukuru, mimi nazungumzia barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii barabara ni muhimu sana ambapo kule wanalima ufuta, mpunga, kahawa, mahindi, maharage, alizeti na wanalima mazao mengi sana. Barabara hii ingeweza kutengenezwa kwa kiwango cha lami uchumi wa Mkoa wa Songwe, Rukwa na Katavi ungeweza kupaa. Sasa leo barabara hii imeachwa, tunafanya vitu vingine ambavyo kwa kweli kwa Watanzania wala siyo kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani hii barabara ni vizuri Waziri Mpango utu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana kwa mchango wako. Ahsante sana, lakini na daraja ni muhimu sana na ndiyo maana Serikali imeona ianze na daraja hilo na baadaye ina mpango wa lami, utafika tu.

MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia ambacho hakipo. Huwezi ukazungumzia kitu ambacho kipo.

MWENYEKITI: Ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Nami nitachangia Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji na nitaanza na utekelezaji wa kusuasua wa bajeti ya maendeleo ya Wizara ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, sasa imekuwa ni kama mazoea Serikali kutekeleza bajeti ya kilimo kwa kusuasua. Hivi navyozungumza kwa taarifa ambazo ninazo kwa sababu mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Kilimo Mifugo na Maji, kwa taarifa ambazo zilitolewa kwenye Kamati yetu ni kwamba kati ya pesa za maendeleo ambazo zilikuwa zimetengwa karibu shilingi bilioni 143.57 hadi sasa fedha ambazo zimeshapokelewa ni kidogo tu, ni kama shilingi bilioni 21.4 tu sawa na 14.9%. Kama tutaenda hivi tafsiri yake ni kwamba mpaka tunafika mwezi wa sita mwishoni kwa kweli sidhani kama tutafika asilimia 40. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama hatuwezi leo kutekeleza bajeti ya maendeleo kwa kupeleka fedha tafsiri yake ni kwamba Wizara hii kuna shida na shida hii ni kubwa siyo ndogo. Kama shida hii ipo ni vizuri Serikali ituambie tatizo liko wapi? Kama Bunge tunaidhinisha fedha lakini fedha ambazo zinatolewa ni asilimia kidogo tu ambayo ni asilimia 14. Katika asilimia 14 hii fedha za ndani zilizotolewa ni kama shilingi bilioni 5 tu lakini fedha za nje ni bilioni 15. Yaani leo fedha za kutoka nje zinakuwa nyingi kuliko fedha za ndani. Hivi uzalendo uko wapi kati ya hao watu wan je wanaotupatia pesa nyingi na fedha zetu za ndani ambazo zinakuja kidogo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hapa kuna tatizo hatuwezi tukaendelea kuendesha nchi kwa kutumia fedha za nje tu. Kama zitaendelea kutokuja fedha za nje, kwamba, kama zisingekuja Bilioni 15 maana yake tungekuwa na Bilioni 5 tu ambazo ni fedha za ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa mimi nataka nijue, kwa sababu Serikali imekuwa ikijinasibu kwamba makusanyo yanazidi kuongezeka kila mwezi, lakini leo utekelezaji wa Bajeti ya maendeleo, sekta ambayo inaajiri Watanzania zaidi ya asilimia 70 utekelezaji wa Bajeti yake ndiyo namna kama hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli ni vizuri Wizara hii wajipime waone kama wanatosha, na kama hawatoshi siyo dhambi kuwapisha wale ambao wanadhani kwamba wanaweza wakafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili jambo si la kwanza na huu mwaka si wa kwanza maana yake mwaka jana mwaka wa fedha ilikuwa hata asilimia 50 hawakufika. Mwaka uliotangulia, nyuma kidogo, ilikuwa asilimia 16, na miaka ya nyuma ilikuwa asilimia tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tukienda kwa trend kama hii kwa sekta inayoajiri Watanzania walio wengi tutakuwa hatuwatendei Watanzania haki. Ni vizuri tuangalie namna ya kuweza kufanya, na Serikali ione kwamba Watanzania hawatendewi haki hata kidogo.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusu pembejeo. Hivi ninavyozungumza hapa mbolea aina ya UREA kwa Mikoa inayozalisha chakula; wanaozalisha mahindi kwa wingi, Mikoa ya Songwe, Rukwa, Ruvuma, Iringa na maeneo mengine, mbolea aina ya UREA imeadimika; yaani mbolea kuipata ni shida kweli.

Mheshimiwa Spika, sasa Serikali ituambie, kwamba kwa kutumia mfumo wa kununua mbolea kwa pamoja (bulk procurement) tutaweza kutatua tatizo hili la upatikanaji na bei? Leo mbolea aina ya UREA imeadimika, na kipindi hiki msimu huu, kwa maana ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, ndio muda ambao wakulima wanatakiwa waweke mbolea ya kukuzia mahindi.

Mheshimiwa Spika, inawezekana msimu unaokuja kukawa na tatizo la chakula kwa sababu wananchi hawana mbolea ua kukuzia aina ya UREA. Hata hivyo hata hiyo kidogo ikipatikana bado bei elekezi haifuatwi. Kwa mfano kutoka shilingi 54,000 kwa mfuko wa UREA leo umefika shilingi elfu 68. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa Serikali hii ni Serikali ya wanyonge gani?, kama mbolea inapanda kutoka 54,000 kwenda 68,000 ni mnyonge yupi anayesaidiwa hapa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nadhani Wizara hii ya Kilimo kuna tatizo. Bila kujali Itikadi ya Vyama vyetu ni vizuri Wabunge wote tuangalie namna ya kuweza kuiwajibisha Serikali ya namna hii. (Makofi).

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusu suala la kulipa mawakala walio-supply pembejeo mwaka 2015. Mawakala walikopa pesa Benki wakapeleka vocha kwa maana ya ku– supply zile pembejeo kama mbolea pamoja na mbegu hawajalipwa pesa zao ninavyoongea hadi leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wako Mawakala hawa waliokopa pesa Benki wameuziwa nyumba zao na wengine wamefariki kwa sababu ya pressure kwa sababu anauziwa nyumba hana mahali pa kukaa lakini hadi sasa Serikali imejificha kwa mwamvuli wa kwamba tuko kwenye uhakiki; hivi ni uhakiki gani ambao hauishi? Mbona Serikali haituambii? Hata kama wamehakikiwa watu wako watano iwalipe hao watano waliohakikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo watu wanafariki kwa sababu ya pressure ya kuuziwa nyumba Serikali haijatuambia itawalipa lini watu hawa ambao wamehakikiwa, na ni watu wangapi?

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha atuambie wangapi wamehakikiwa hadi leo. Vilevile watuambie mpango wa kuwalipa; kwamba watawalipa lini? Kwa sababu wanaendelea kupotea hawa. Wanasomesha wana watoto na wana ndugu wanaowategemea, leo hawajalipwa. Hawa ndio wanyonge ambao waliisaidia CCM hata kuipa kura. sasa hili jambo Mheshimiwa Waziri aangalie kama Serikali imeshindwa kuwalipa iwaambie kwamba tumewadhulumu, hatutawalipa; kwa sababu kama ni tangu 2015 hadi leo tafsiri yake ni kwamba Serikali haina dhamira njema ya kuweza kuwalipa Mawakala hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lambo lingine kuhusu suala Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kutoa gawio Serikali Kuu. Jambo la kustaajabisha, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko hivi karibuni ilitoa gawio Serikali Kuu, takriban mlioni karibu milioni mia tano. Jambo la kusikitisha ni kwamba leo Wizara inazungumza hapa utekelezaji wa Bajeti wa kusuasua lakini Serikali Wizara ya Kilimo kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko wanatoa gawio Serikali Kuu milioni mia tano.

Mheshimiwa Spika, sasa sijui inakuwaje, yaani mgonjwa ambaye inatakiwa uongezewe damu inafika mahali nawe unataka kumtoa damu, hili ni jambo la ajabu sana. (Makofi)

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, yaani mgonjwa unatakiwa uongezewe damu na wewe unaamua ku toa damu kwa mwingine.

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

T A A R I F A

SPIKA: Mheshimiwa Haonga kuna taarifa unapewa subiri kidogo. Naomba umpe taarifa, ndiyo endelea.

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Spika, naomba tu nimpe taarifa Mheshimiwa anayezungumza, kwamba kuna suala la mchanganyo wanaposema gawio watu wengi wana confuse. Nadhani Mheshimiwa Haonga hajaweza kutofautisha kati ya gawio na mchango.

Mheshimiwa Spika, tunaposema gawio ina mambo matano ndani yake. Kuna suala la dividend, kwa maana ya gawio. Kwa mashirika na taasisi ambazo zinafanya biashara per se inaitwa dividend, ndiyo maana ya gawio. Kuna asilimia 15 ya pato ghafi ambayo ni mchango wa Taasisi kwa Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo naomba nimpe Mheshimiwa Haonga taarifa kwamba hiyo iliyotolewa si gawio ni mchango wa Taasisi kwa Mfuko Mkuu wa Serikali. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Haonga unapokea taarifa hiyo ya Mheshimia Chegeni?

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, mimi naomba niendelee. Huyu bwana wananchi wake wakulima wa pamba kule wanadai Serikali takriban Bilioni 4.4, sasa nadhani angepata nafasi ya kuweza kuchangia angeweza kuzungumzia mambo ya pamba ili kule kidogo aweze kuwasaidia wakulima wa pamba. Naomba nimuache, nimempuuza tu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninachozungumza hapa ni kwamba, leo kama Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko hizo fedha kama zilikuwepo nyingi kwa nini wasingepeleka kwenye angalau wangepeleka NFRA basi wakanunue hata mahindi; kwa sababu bado zinazunguka kwenye Wizara hiyo hiyo. Leo wanatoa pesa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko unapeleka Serikali Kuu halafu mwisho wa siku….

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

T A A R I F A

SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Haonga unapewa. Mheshimiwa Getere.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, ahsante; naomba nimpe taarifa. Tufike wakati sasa humu tuangaliane kwamba tunafikiri kwa kiasi gani. Kama Wabunge humu ndani tunatunga sheria za mashirika kwenda kutoa dividend kwenye maeneo mbalimbali na mambo mengine ya kisheria. Tumetunga sheria humu ndani sisi wenyewe; kwamba kila wewe ukiwa Spika hapo ulipe hiki, ukiwa Shirika ulipe hiki. Sasa inakuwaje leo Mbunge aliyetunga sheria anasema hili ni la hovyo? Tunamuambia Mheshimiwa Haonga alete sheria humu Bungeni ya kuahirisha haya mambo aliyoyasema yeye.

MBUNGE FULANI: hayo yakwake.

SPIKA: Mheshimiwa Haonga pokea taarifa hiyo.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, nadhani watu wengine kama hawa itabidi tuwasamehe tu kwa sababu hawafahamu vitu vingi. Atuambie ni sheria namba ngapi, lakini pia nadhani tu ni vizuri afuatilie mambo mengine. Nadhani ameamua kunipotezea muda tu, tumsamehe tu anapoteza muda wa walipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hapa ninachoshauri, ni vizuri Serikali iangalie, isiwe inakunywa uji wa mgonjwa kwa sababu kufanya namna hii huku ni kunywa uji wa mgonjwa; kwa sababu Wizara hii inachechemea, inatakiwa isaidiwe na si Wizara tena ianze kutoa gawio huku inafanya hivi. Sasa mambo kama haya ni mambo ambayo kwa kweli hii Wizara inatakiwa isaidiwe. Tunayazungumza haya si kwamba labda tunaichukia sana Wizara, tunapenda kuisaidia Wizara, lakini inaonekana kwamba Serikali haiko tayari, Wizara hii iweze kusaidiwa, Wizara ambayo inaajiri Watanzania zaidi ya asilimia 70. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusu suala la Serikali kutoangalia vipaumbele vya wananchi; na hapa nazungumzia suala la maji.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais alipozunguka kwenye ziara mbalimbali nchini maeneo mengi wananchi wetu walizungumzia kuhusu maji. Alikuja Mbozi wananchi walizungumzia kuhusu maji, wanataka maji amekwenda Momba wanataka maji, amekwenda Tunduma wanataka maji, amekwenda Rukwa nai maeneo mbalimbali wananchi wanataka maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nashauri, ni vizuri Serikali ikaangalia vipaumbele vya wananchi badala ya kwenda kwenye vipaumbele ambavyo si vya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo ukienda nchi nzima hakuna sehemu ambayo wananchi wamesema wanahitaji ndege, wanasema wanataka maji. Kwa hiyo mimi nashauri, kama Bunge lako hili Tukufu ambalo unaliongoza wewe; ninashauri kwamba ni vizuri Serikali…

T A A R I F A

SPIKA: Mheshimiwa Haonga kuna taarifa sijui wapi! Kuna taarifa pale!

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge. Pamoja na kazi kubwa ambayo inayofanywa na Mheshimiwa Rais lakini hata katika Jimbo lake kuna Miradi dhahiri shahiri ya maji inayotekelezwa katika kuhakikisha wananchi wa Mbozi wanapata maji. Hata hivyo kikubwa nataka nimwambie kwamba ukisoma maandiko ya dini yanasema yapaswa kushukuru kwa kila jambo ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Haonga utakataa na hilo nalo la kwamba maandiko yanasema kushukuru kwa kila jambo.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, mdogo wangu Aweso afahamu kwamba zile fedha si fedha za msaada, ni fedha za walipa kodi wa Tanzania na watu wa Mbozi pia wanalipa kodi; afahamu siyo msaada. Ndiyo maana hata maeneo mengine ambayo hakuna Madiwani bado pesa zinakwenda kwa sababu ni kodi za Watanzania; kwa hiyo afahamu hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia afahamu kwamba pamoja na kodi zetu kulipa vizuri aelewe kwamba kwenye Jimbo langu pamoja na Miradi ya maji ambayo ilitakiwa imalizike imechelewa kumalizika, kwa maana hiyo hizi kodi zetu hazitendewi haki vizuri, maana wakandarasi wame- raise certificates ili waweze kulipwa hawajalipwa, na Mradi wangu wa maji pale Itewe wa Bilioni 1.5 Wakandarasi wame-raise certificates hazijalipwa hadi sasa; Aweso anafahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata pia visima vinne ambavyo Mheshimiwa Waziri aliahidi alipokuja Mheshimiwa Rais pale Mloo bado hujakamilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunapokuja hapa tunashauri ni vizuri Serikali ikaangalia vipaumbele vya wananchi.

Mheshimiwa Spika, tuangalie; nina uhakika hata ukienda Jimboni kwako wewe kule wale wananchi wanahitaji maji zaidi kuliko ndege. (Makofi/Kicheko)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hii bajeti ya Wizara ya TAMISEMI. Awali ya yote naomba kwanza kuwashukuru viongozi wangu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo ngazi ya Taifa, kwa kuendelea kuwa imara licha ya changamoto mbalimbali ambazo wameendelea kupitia na wafahamu kwamba, siku zote ili dhahabu ing’ae lazima ipite kwenye moto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hilo, naomba niende moja kwa moja kwenye hoja ambazo nimezipanga kuzizungumza siku ya leo na hoja ya kwanza naomba nianze kwenye eneo lile la TARURA:-

Mheshimiwa Naibu Spika, TARURA ni chombo ambacho kiliundwa, lakini chombo hiki kimekuwa sasa ni kama pambo tu kwa sababu, chombo hiki hakipewi fedha. Nchi hii ina vijiji zaidi ya elfu 12, leo TARURA inayosimamia barabara zote za vijiji zaidi ya elfu 12, barabara zote za mijini, eti inapewa fedha 30% tu, lakini fedha hizo nazo wakati mwingine haziendi kama ambavyo tumeziidhinisha kwenye Bunge hili. Kwa hiyo, nashauri kwamba kwenye TARURA hapa yafanyike mabadiliko kidogo kwenye sheria, angalau iwe asilimia 50 kwa 50 ili mwisho wa siku TARURA iweze kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzisha TARURA bila kuwapa fedha maana yake hamna kitu ambacho tumekifanya. Watu wanalipwa mishahara pale TARURA, lakini fedha haziendi kama ambavyo zimeidhinishwa na Bunge. Kwa hiyo, nishauri tu kwamba, licha ya fedha kidogo hizo ambazo hazipelekwi kwanza ziwe zinapelekwa, lakini zaidi ili kuweza kwenda vizuri ni jambo jema kama tutaenda kubadilisha sheria ili iwe asilimia 50 kwa 50 ili mwisho wa siku TARURA iweze kuwa na fungu la kutosha, vijiji zaidi ya elfu 12 ni vingi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, hii mvua iliyonyesha kuanzia mwaka jana na inaendelea, katika maeneo mengi nchini karibu barabara nyingi za vijijini na za mijini zimekatika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Jimbo langu kuna barabara ya kutoka pale Kijiji cha Ivwanga kwenda Mbozi Mission, Mbozi Mission kule kuna hospitali kubwa ya mission, lakini pia kuna Chuo cha Nursing pale cha Serikali, lakini kuna soko kubwa, lakini barabara hiyo pia inaenda hadi Jimbo la Mheshimiwa Hasunga, Kijiji cha Iganduka. Sasa barabara hii ina hali mbaya sana kuliko Waziri anavyofikiria.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna barabara nyingine ya kutoka Mloo kwenda Isansa Kituo cha Afya, imekatika, ina hali mbaya kwelikweli, lakini yote haya ni kwa sababu hizi barabara zinasimamiwa na TARURA na TARURA inapewa pesa kidogo, kwa hiyo, mambo yamekuwa ni mabaya kweli na yamekuwa ni magumu. Madaraja mengi yameharibika kwa hiyo, nashauri sheria hapo iweze kurekebishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine nadhani pamoja na mapambano ambayo yanaendelea kuhusu ugonjwa wa corona nashauri kwamba, pia Serikali ingeangalia kutenga fedha kama dharura kwa ajili ya kuweza kurudisha hali ya miundombinu ya barabara ambayo imeharibika.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine naomba nizungumze suala la kuhusu vituo vya afya. Ukurasa ule wa 54 limezungumzwa suala la vituo vya afya na tumeambiwa kwamba, vituo vya afya vimefikia sasa 968; unapozungumza kutoka mwaka 1961 tangu nchi hii ipate uhuru unazungumza vituo vya afya 968 na kata ambazo tunazo kwenye nchi hii ni zaidi ya kata elfu nne na kitu, maana yake tuna upungufu; ukienda kwenye Sera ya Afya, tuna upungufu wa vituo vya afya zaidi ya elfu tatu na kitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Afya inasema kituo kimoja cha afya kwenye kila kata, leo unazungumza vituo 968. Yaani leo tukisema tuongeze miaka mingine ya Serikali hii ya CCM kukaa madarakani miaka mingine 59 kwa speed hii ambayo inaenda, maana yake unazungumza kutakuwa na vituo elfu moja mia nane na kitu vya afya, kama ndio watakuwa wanaenda hivi, ambapo maana yake miaka 59 ni mingi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi vituo vya afya ni vichache kweli, wakati mwingine watu wanakaa wanampongeza Mheshimiwa Jafo tunakupongeza unafanya nini, wakati mwingine mnamharibia Mheshimiwa Jafo kwa sababu mnatakiwa mmwambie kwamba, kosa liko hapa, ili Mheshimiwa Jafo aweze kusonga mbele. Leo vituo 968 ni vichache mno, yaani tuwaongeze miaka mingine 59 au 60 ndio muwe na 1800, bado hamuwezi kukamilisha vituo vyote kwenye kata zote zaidi ya elfu nne na kitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, huu ni mwendo wa kinyonga, siwezi nikaendelea kumdanganya rafiki yangu Mheshimiwa Jafo, kaka yangu kwamba, anafanya kazi nzuri wakati naona speed ni ndogo. Kwa hiyo, niseme tu kwamba, ni vizuri Sera ya Afya iweze kutekelezwa, kituo kimoja cha afya kwenye kila kata ili mwisho wa siku nchi hii tuweze kuwa na vituo vya afya kwenye kila kata.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili ni jambo ambalo linashangaza sana. Mimi kwangu pale nina kata moja inaitwa Mlowo. Hii kata ina wakazi karibu laki moja, kuna zahanati ya kijiji kwenye kata hiyo; zahanati ya kijiji tu, wakazi zaidi ya laki moja.

Sasa kwa mazingira kama haya unaweza ukawa ni Mbunge mwendawazimu pekee ambaye unaweza ukaanza kupongeza mambo kama haya, wakati watu zaidi ya laki moja hawana kituo cha afya wana zahanati; kwa hiyo, nishauri jambo, Sera ya Afya itekelezwe, kituo cha afya kwenye kila kata, hapo nadhani tutakuwa tumetatua tatizo la vituo vya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa ule wa 141 wa hotuba ya Waziri amezungumza kuhusu kwamba, mwaka huu wa fedha 2020/2021 TAMISEMI imepanga kusimamia shughuli za utawala bora, kukuza demokrasia, ushirikishwaji wa wananchi na kadhalika. Kwenye nchi hii kumetokea tatizo kubwa sana, leo wale Mameya au Wenyeviti wa Halmashauri waliochaguliwa kidemokrasia kabisa hasa kupitia Vyama vya Upinzani wanaondolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Meya mmoja wa Iringa pale anaitwa Alex Kimbe ameondolewa kinyume kabisa na utaratibu. Sheria inasema ili kumwondoa huyu Meya inatakiwa angalao 2/3 ya kura iweze kupigwa; Manispaa ya Iringa yenye Madiwani wote kama 24 ilitakiwa wafikie angalau Madiwani 17 kumwondoa Meya wa Iringa. Wameingia madiwani wa CCM 14, walihitajika Madiwani angalao wafike 17 ndio waweze kumuondoa Meya, leo Madiwani 14 wamevunja sheria, wamemwondoa meya kisa anatoka CHADEMA, hilo tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini tu kwamba, yote haya, huu mpango wa Serikali kwamba, wanataka kusimamia shughuli za utawala bora, hilo jambo haliwezekani. Nimwambie jambo Mheshimiwa Jafo rafiki yangu kwamba, ameshawahi kuongea Desmond Tutu, ameshawahi kusema naomba nimnukuu: “if you are neutral in situation of injustice you have chosen the side of the opressor.”

Mheshimiwa Naibu Spika, hiki kinachofanyika kwenye nchi hii hawa watu wanaondoolewa kinyume na utaratibu kwa kweli, huku ni kunyanyaswa na huo ni uonevu na Mheshimiwa Jafo kama amenyamazia uonevu huu, maana yake na yeye anaungana na Wakuu wa Mikoa wote wanaosababisha uonevu uendelee kwenye nchi hii. Ninapozungumza hapa Meya wa Dar es Salaam, Isaya Mwita, aliondolewa kinyume na utaratibu. Kabisa wanaingia kupiga kura hawana 2/3 wamemwondoa kinyume kabisa, kihuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwambieni ukweli kabisa mambo haya yanaumiza na Mheshimiwa Jafo kunyamazia mambo haya maana yake naye anaungana na yule ambaye anaenda kufanya matendo ya uovu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niseme tu kwamba, haya mambo yanaumiza sana. Nchi hii hata siku moja haitakaa kikae Chama cha Mapinduzi peke yake, lazima vyama vya upinzani viwepo na vitaendelea kuwepo tu. Sasa mazingira kama haya ni mazingira ambayo yanatia hofu sana na utawala bora kwenye nchi hii umeingia katika majaribu makubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo lingine pia, hapa ambalo naomba nizungumze kidogo kuhusu suala la ahadi ya milioni 50 kwenye kila kijiji. Nawakumbusha tuambieni kijiji gani ambacho milioni 50 imepelekwa? Kwa sababu, hapa tumeona watu wanajigamba, wametekeleza, vituo vya afya, sijui vitu gani, lakini milioni 50 iliyokuwa imeahidiwa kwenye kila kijiji wamepeleka shilingi ngapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwangu nina vijiji karibu 121 na nahitaji bilioni sita karibu na milioni 50, maana katika vijiji 121 vya Halmashauri ya Mbozi hawajapeleka kwenye kijiji hata kimoja. Watekeleze ahadi hiyo na ahadi ya laptop kwa kila Mwalimu; wamepeleka laptop ngapi kwa Walimu wa… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, wa Mwaka 2016
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nami niweze kuchangia juu ya Miswada hii miwili ambayo wenzangu tayari wameshaanza kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo. Nimesoma Muswada huo nimeupitia vizuri, lakini tatizo ninaloliona ni kwamba sijaona eneo ambalo ni specific kabisa linalohusu namna ya upatikanaji wa fedha za kwenye hii taasisi ya utafiti ambayo tunakwenda kuipitisha. Tatizo hili tusipoweza kujadiliana kwa makini sisi kwa pamoja leo kwamba fedha zinapatikana wapi, tutarudi kwenye kutelekeza hizi Taasisi za utafiti ambazo nyingi tumeshazianza tayari na nyingine nyingi tulishazitelekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, wapo hawa jamaa tunawaita TaCRI, hawa wanaofanya utafiti wa zao la kahawa. Tunafahamu kabisa na Mheshimiwa Waziri anajua kabisa hili kwamba waliokuwa wanafadhili TaCRI ni European Union ambao hadi sasa hajawahi kupeleka fedha, tunajua kwa nini hajapeleka fedha kwa sababu tunajua European Union iko miradi mbalimbali ambayo walikuwa wanaendesha, lakini baada ya kutokea mgogoro wa kisiasa kule Zanzibar wameamua kujiondoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, leo bado tunaona kuna wadau wengine, kwa mfano mkulima wa kahawa alikuwa anakatwa karibu asilimia 0.75 anapouza kahawa yake ili aweze kuichangia TaCRI, lakini leo tutakwenda kuwabebesha wakulima wetu mzigo mzito sana tusipokuwa makini namna ya kuweza kupata fedha za kugharamia utafiti huu. Tunajua kabisa kwamba wakulima wetu kila tunapoanzisha utafiti wa aina yoyote ile tunaangalia wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii ni sawa na mzazi unakwenda kuzaa watoto halafu unapanga gharama kwamba bajeti ya chai atakunywa kwa jirani, chakula atakula kwa mtu fulani. Kwa hiyo, tusipokuwa makini tutatelekeza hata hii Taasisi ya Utafiti wa Kilimo. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up labda kesho hiyo, naomba atuambie hizi fedha zinatoka wapi na nimepitia sijaona ni maeneo gani wanapata hizi fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu huyu Mkurugenzi Mkuu wa Utafiti, wanasema awe na ujuzi uliothibitika na uzoefu usiopungua miaka 10 katika masuala ya sayansi na utafiti wa kilimo. Ukisoma ukurasa wa 41 na 42. Huyu Mkurugenzi unayeniambia kwamba awe na uzoefu usiopungua miaka 10, hili litakuwa kama ni eneo ambalo watu wetu wenye uwezo mzuri tutawanyima nafasi kama hizi. Leo unaweka miaka 10 uzoefu, kwa hali ya kawaida miaka 10 ni mingi sana, kama amezaa mtoto maana yake yuko darasa la nne au la tano. Sasa hii nadhani tungepunguza kidogo hapa, kwa nia njema, siyo kwa nia mbaya, angalau tuweke hata miaka mitatu, siyo dhambi, tuweke miaka mitatu, naamini tutapata watu wazuri kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hii ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo naomba niondoke kidogo niingie kwenye huu Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania. Amezungumza Mbunge mwenzangu aliyekaa, kuna tatizo moja ambalo linaonekana lazima tulijadili mapema kwa mfano suala la utafiti wa masoko ya samaki ili kuongeza pato la wavuvi na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima hapa tujaribu pia kuzingatia haya, tueleze vizuri kwamba utafiti huu utasaidiaje kutafuta masoko kwa sababu shida katika Taifa letu ni kwamba tunao samaki wa kutosha na mazao mengine ya baharini, tatizo kubwa ni masoko na nadhani kwa sababu sheria hii tunakwenda kuipitisha, naamini kabisa hili suala la masoko pia tulizingatie tuweze kuangalia ni namna gani tutatafuta masoko kwa ajili ya samaki wetu na mazao mengine ya baharini, tutakuwa tumeongeza pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyojua baadhi ya nchi duniani zinazotegemea zao la samaki kuendesha uchumi wa nchi zao, kwa mfano, zipo nchi kama Mauritius, nchi kama Seychelles, nchi kama Phillipines, Norway, Australia na nchi nyingine nyingi ambazo zinategemea samaki kwa ajili ya kuendesha uchumi wa nchi zao. Sasa na sisi hapa lazima tuangalie tunafanyaje kwenye huu utafiti, tunaingiza wapi angalau eneo la kuweza kutafuta masoko kwa ajili ya samaki wetu na mazao mengine ya baharini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo dagaa wengi sana wanavuliwa kwa mfano Ziwa Victoria wanapelekwa Congo, lakini hatujui nchi inapata shilingi ngapi, kwa sababu soko kubwa la samaki na dagaa tunajua kabisa ni Congo. Sasa leo tunapeleka kule, wenzetu wanapeleka kuchakata viwandani, wanatoa ajira lakini sisi Taifa hatunufaiki na chochote na kama ni kunufaika basi itakuwa ni kidogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine naomba nizungumzie ni kwenye suala la udhaifu wa sheria za utafiti. Kumekuwa na tatizo kwa muda mrefu sana, leo wanakuja wageni katika Taifa letu, kwa mfano mdogo walipokuja wale jamaa wa China wamevua samaki kwa muda wa wiki tatu wamepata samaki wengi sana. Wale samaki wamepatikana wengi, lakini wale jamaa walikuja kwa njia za ujanja ujanja, sasa sijui kama walikuja kufanya utafiti au walikuja kufanya uhuni wale samaki jina maarufu samaki wa Magufuli nadhani mnakumbuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa kwa sababu ama kwa kukosa sheria ambazo haziwabani vizuri watu wa namna hii tukajikuta kwamba wale watu wamevua samaki wengi kwa muda wa wiki tatu wamepata samaki wengi na mwisho wa siku tukawakamata tukachukua na ile meli tuka- seeze lakini bahati mbaya sana ile kesi walitushinda Mahakamani, hadi leo hii tumeingia hasara kama Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mambo yote hayo naomba tu tujaribu kuangalia tuweke sheria ambazo zitawabana wale watu wanaokuja kufanya utafiti kutoka nje ya nchi, zitakazowabana wale wezi wanaotuibia samaki wetu. Tunaamini kabisa kwamba tukiwabana samaki tunao wa kutosha, tutauza nje ya nchi tutatengeneza ajira kwa watu wetu, lakini tukikaa kimya na sheria tusipoziweka vizuri itakuwa ni business as usual, tutaibiwa sana na tutaendelea kulalamika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme tu kwamba suala hili tujaribu kuliangalia kama Taifa kwa pamoja. Kwa mfano hizi tafiti tunazozianzisha zote kwa maana ya hizi sheria, hii Miswada tunayoipitia, yote miwili inafika mahali kama alivyoongea Mbunge mwenzangu, tumepitisha sheria, ukiangalia unaona kama nzuri kwenye maandishi lakini hizi tafiti zinaishia kwenye makaratasi, haziwasaidii wananchi wetu, hatuzifikishi kule chini ili watu wetu waweze kujua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa mfano leo bado kama tunazo hizi sheria za utafiti ambazo tumeshazipitia siku nyingi, bado kwenye mazao mbalimbali hapa nchini tumeona kuna ugonjwa wa mihogo, kuna ugonjwa wa kahawa. Kwa mfano, kwenye kahawa kuna ugonjwa fulani unaitwa CBD (Coffee Berry Disease) leo ukimuuliza hata Mheshimiwa Waziri anajua kwamba hadi leo ukiuliza ugonjwa huu wa Coffee Berry Disease, hadi leo hauna dawa zaidi ya kusema kwamba unatakiwa uzuie. Sasa tujue je, hizi taasisi za utafiti ambazo tunazo, tumezianzisha zimetusaidia kwa kiwango gani na tunapoenda kuanzisha nyingine zitatusaidia kwa kiwango gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba mwisho wa siku tutaishia kuanzisha hizi taasisi za utafiti, hazitatusaidia lakini tukiwa makini naamini kabisa kwamba zitatusaidia. Shida kubwa katika Taifa hili, ameongea Mbunge mwenzangu, ni kwenye suala la implementation. Tumekuwa na Taasisi nyingi, tumekuwa na tafiti nyingi, tumezipaki kwenye makabati, tumezipaki huko hatuzifanyii kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kwa pamoja bila kujali itikadi ya Vyama vyetu, tunapokwenda kujadili haya mambo yakafanye kazi kwa wananchi wote kule chini. Taifa lolote lile duniani ambalo halifanyi tafiti, Taifa hili limekufa na mwisho wa siku haliwezi kuwasaidia wananchi wake. Kwa hiyo, naomba kwa nia njema hizi tafiti ziwafikie wananchi wetu na ziweze kuwanufaisha, hatutaki ziishie kwenye makabrasha kama ilivyokuwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kuna Sheria hii ya Uvuvi ambayo ilianzishwa siku za nyuma huko, tujue je, upungufu ambao yalikuwepo siku za nyuma, je tunaweza kuyarekebisha kiasi gani kwa kuanzisha sheria nyingine hii ya uvuvi. Kama kuna upungufu ulikuwepo, tumekwenda kuanzisha sheria nyingine tafsiri yake ni kwamba hii sheria pia itaishia kwenye makabrasha humu, tutaiacha hapa na mwisho wa siku tutakuja miaka mingine mbele kuanzisha sheria nyingine.
MWENYEKITI: Ahsante.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti na mimi naomba nichangie, lakini naomba nianze kwa kusema kwamba taarifa hii ya Kamati, vitu vingi wamezungumza kusema ule ukweli kabisa vitu ambavyo ni vya ukweli japo kuna baadhi ya vitu naona kwamba kidogo kuna shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika taarifa hii ukurasa wa nane, wamegusia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu na Waziri wa Elimu yuko hapa. Miongoni mwa vitu ambavyo Mheshimiwa Waziri vitakuja kukuondoa siku za hivi karibuni nadhani ni Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Mheshimiwa Waziri kusema ule ukweli kabisa ameshawahi kuzungumza na ndugu yangu Heche hapa Bungeni, ulipokuwa Baraza la mitihani pale ulikuwa na heshima kubwa sana Mheshimiwa Waziri lakini leo umeletwa kuwa Waziri wa Elimu kwa kweli to be honestly heshima yako imeshuka sana kutokana na yale ambayo yanaendelea katika Taifa hili hasa kwenye elimu yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wale watoto wetu ambao walikuwa wanadahiliwa siku za nyuma kwa mfano mwaka 2014/2015 walidahiliwa wanafunzi 58,000 na TCU; lakini waliopata mikopo ni zaidi ya 40,000 zaidi ya nusu ya wanafunzi walipata mikopo. 2016/2017, wamedahiliwa wanafunzi 58,000 waliopata mkopo ni wanafunzi 20,000. Ukiangalia Awamu ya Nne walifanya vizuri zaidi katika suala hili la kutoa mikopo kwenye elimu ya juu lakini Awamu ya Tano ime-prove failure kabisa na Mheshimiwa Ndalichako hili unatakiwa ujipime, ujitathmini uone kama unatosha kuendelea kuiongoza Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema ule ukweli wako wanafunzi ambao walikuwa wanaendelea na masomo, wameshakopeshwa, yupo mwaka wa pili, mwaka wa tatu leo unasema kwamba hana sifa, unamuondoa kwenye mkopo. Sijajua vizuri kama hizi ni akili au ni matope lakini najua kabisa kwamba ni Serikali ambayo haipo makini kabisa katika kuhakikisha kwamba wanaboresha elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema ukweli kabisa kwenye hii mikopo wapo wanafunzi ambao wanadai haki baada ya kuona mikopo imecheleweshwa, wanapokuwa wanadai haki wanafunzi hawa wanafukuzwa chuo, wanaonekana kwamba ni wakorofi, hawafai kuendelea kusoma. Kuna mwanafunzi mmoja anaitwa Alphonce Lusako, huyu kijana amefukuzwa chuo mwaka 2011 kwa sababu alikuwa anadai fedha za wale ambao wamecheleweshewa mkopo mwaka 2011, kijana huyu amerudishwa chuoni mwaka jana 2016, lakini mwaka huu 2017 amefukuzwa tena kwa sababu ya kudai haki ya wanafunzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri leo ulitakiwa uwe wa kwanza kuondolewa kwenye nafasi yako kuliko kusimamisha wanafunzi wanaodai mkopo, chanzo cha kudai mkopo ni kwa sababu ninyi mnachelewesha, mikopo yenyewe haitoshi, wanapokuwa wanadai haki mnawafukuza badala ya kwamba Serikali iweze kuwajibika.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Elimu ya Juu kwa kweli hapa lazima iondoke na watu, kama Taifa tuweze kujitathmini upya tuangalie ni akina nani wanaweza wakaongoza. Naomba niseme tu kwamba yapo mambo mengi na madudu mengi sana kwenye Bodi ya Elimu ya Juu wamezungumza wengi sitaki nirudie sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala lingine japokuwa kuna mmoja amesema suala hili la TAMISEMI ni kweli kabisa. Kuna mambo ya TAMISEMI na kuna mambo mengine ya Wizara ya Elimu, lakini mambo haya ni kama mapacha yanaenda pamoja. Leo watoto wetu wanafeli kwa sababu walimu walishakata tamaa. Leo walimu wanaidai Serikali fedha nyingi sana. Serikali inawaambia walimu kwamba asiyetaka kazi aache. Ni kweli walimu wengi leo wameacha kazi wamebaki na utumishi. Kilichotufikisha leo hapa ni kwa sababu ya walimu kukata tamaa na ndiyo maana mmoja ametoa takwimu hapa shule za binafsi zinafanya vizuri kwa sababu kule hakuna madai. Shule zetu za Serikali, hizi za umma zinafanya hovyo kwa sababu walimu wetu tunawakatisha tamaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukiangalia kwa mfano Mkoa wa Songwe madai zaidi ya shilingi bilioni mbili hayajalipwa kwa walimu wetu, Wilaya ya Momba, Wilaya ya Mbozi na Wilaya ya Ileje, shilingi bilioni mbili hawajalipwa. Waziri ninaomba katika hili tafadhali muweze kuliangalia muone kama mnaenda sawasawa.
MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa Haonga muda wako umeisha.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni kuhusu TBC..
Mheshimiwa Mwenyekiti, TBC tunailipia kodi zetu lakini inatangaza habari za Chama cha Mapinduzi.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hongera na utekelezaji wa majukumu ya Wizara. Ili kuwasaidia Watanzania walio wengi wanaosumbuliwa na magonjwa makubwa, mfano magonjwa ya moyo, ni vema Serikali iwekeze sana kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete inayoshughulika na magonjwa ya moyo. Vifaa vyote vinavyotakiwa kwa ajili ya matibabu ya moyo vinunuliwe kwani kuwa na Madaktari Bingwa peke yake bila vitendea kazi haitasaidia. Kwa kuboresha Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Serikali itaokoa fedha nyingi sana ambazo zingetumika kuwatibu wagonjwa wetu nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iwe na mikakati kabambe ya kuimarisha michezo ili kuibua vipaji vya wanasoka nchini. Academics za mpira zianzishwe katika maeneo mbalimbali nchini kwa ushirikiano wa Serikali na wadau mbalimbali wa soka. Vijana wakijifunza mpira katika academy zitakazoanzishwa watajifunza soka na michezo mingine wakiwa bado wadogo. Kujifunza soka ukiwa mdogo unapata uzoefu wa kutosha na hivyo kuna uwezekano wa kucheza soka la kulipwa baadaye. Hivi ndivyo nchi nyingi zenye mafanikio makubwa ya soka duniani zinavyofanya.

Mheshimiwa Spika, pia Shirika la Utangazaji la TBC lizingatie weledi katika ufanyaji kazi. Mfano, kuna muda Shirika hili linajisahau na kutangaza habari za Serikali na Chama cha Mapinduzi na kupuuza habari za Vyama vya Upinzani. Kwa kuwa Shirika hili linaendeshwa kwa kodi za Watanzania wote hivyo ni jambo jema Shirika hili likaacha ubaguzi katika kutoa na kutangaza habari.

Mheshimiwa Spika, uhuru wa vyombo vya habari Tanzania umeendelea kupotea siku hadi siku. Yapo baadhi ya matukio ya hivi karibuni yamethibitisha kupotea kwa uhuru wa vyombo vya habari mfano; kuvamiwa kwa studio za clouds TV na Radio siku za hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Tukio hilo limeishusha sana nchi yetu katika utekelezaji wa uhuru wa vyombo vya habari, pia limeichafua sana nchi yetu duniani kote. Serikali ichukue hatua thabiti katika kushughulikia suala hili.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata fursa ya kuchangia Wizara hii. Nitachangia maeneo makuu mawili, nitaanza na madai ya walimu lakini pia nitazungumzia Bodi ya Mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na suala la madai ya Walimu. Mwaka 2016 Walimu zaidi ya 80,000 wamepandishwa madaraja lakini wanaidai Serikali zaidi ya shilingi bilioni 200, fedha hizi hadi leo hazijalipwa. Tunajua kabisa kwamba haya madai ambayo ni shilingi bilioni 200 ni
fedha ambazo Serikali ingekuwa makini na inawajali Walimu ingekuwa imeshalipa. Leo tutaanza kutafuta mchawi ni nani, kwa nini watoto wetu wanafeli wakati tunajua kabisa kwamba Walimu wetu wana madai makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali iweze kulipa madeni haya kwa sababu Walimu wetu wengi wanakata tamaa sana. Walimu wakiendelea kukata tamaa matokeo tutayaona muda si mrefu na tusianze kutafuta mchawi ni nani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu fedha za Walimu wa maeneo mbalimbali nchini waliosimamia mitihani ya kidato cha nne mwaka 2015. Mheshimiwa Naibu Waziri nimewahi kumwona na kuwambia Wilaya ya Mbozi Walimu wanadai Serikali zaidi shilingi milioni 170, walisimamia mitihani ya kidato cha nne, 2015 akasema atashughulikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika kusema kwamba Walimu hao hadi leo hii hawajalipwa hizo fedha za kusimamia mtihani wa kidato cha nne mwaka 2015. Naomba niulize, ni nani Mbunge humu au Waziri hapa ndani ambaye anaidai fedha Serikali za mwaka 2015 ambazo hajalipwa hadi leo hii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwa masikitiko makubwa kabisa wale Walimu wanasema kwamba wameshakata tamaa. Ukisikia Mwalimu anazungumza kwamba amekata tamaa, hili jambo kwa kweli madhara yake ni makubwa sana na haya mambo yatasababisha watoto wetu wafeli. Mheshimiwa Waziri naomba tafadhali Bunge litakapokuwa limeahirishwa mwezi Juni achukue angalau muda akaonane na wale Walimu wa Mbozi. Walimu hawa wanadai Serikali zaidi ya shilingi milioni 170 walisimamia mitihani hawajalipwa fedha zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya madai ni vizuri wakayalipa kwa sababu Walimu wetu kuendelea kudai nadhani sio afya na haitaleta picha nzuri katika matokeo yanayokuja. Kama wanataka kusubiri majuto tutayapata ila majuto ni mjukuu. Namwomba Mheshimiwa Waziri chonde- chonde katika hili afike Mbozi akawasikilize Walimu wanaoidai Serikali fedha hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu Bodi ya Mikopo. Bodi ya Mikopo leo hii inafanya mambo ya ajabu sana Mheshimiwa Waziri na kama inawezekana ivunjwe. Maana kinachotokea wale watoto yatima ambao hawana baba wala mama wananyimwa mikopo. Mheshimiwa Waziri nimemwona juzi, nimemletea mwanafunzi ambaye baba na mama yake amekufa na nimempelekea na Death Certificates za wazazi wote wawili hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu mwanafunzi alinyimwa mkopo na yuko CBE mwaka wa kwanza. Mwanafunzi huyu niliyempelekea hivyo viambatanisho vyote alishawahi kuomba apatiwe mkopo kwa sababu hiyo na hadi ame- appeal bado amenyimwa. Tunao watu wa aina hii wengi sana katika Taifa hili ambao wamepoteza wazazi na wamenyimwa mikopo. Kama huwezi ukampa yatima mkopo unampa nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazo taarifa kwamba watoto wa Mawaziri ndio hao wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu wanapewa 100%. Mheshimiwa Waziri, kwa kweli suala hili tafadhali naomba mlichukulie kwa umakini sana, kuwanyima watoto wa maskini mikopo hii ni hatari sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine mikopo hii ukiangalia wako wengine waliosoma…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kabla sijaanza kuchangia Wizara hii, naomba niungane na mchangiaji mmoja aliyetangulia, anaitwa Profesa Jay. Mheshimiwa Waziri naomba nimpe ushauri kidogo, kabla sijaendelea kuchangia, anapokuja kwenye Majimbo yetua jaribu kutushirikisha Wabunge wenye Majimbo.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwambia hili kwa sababu mimi huwa sitaki nikae na kinyongo na huwa sitaki tufanye kazi kwa kinyongo na Waziri wangu. Alikuja Jimboni kwangu, ameenda kufanya mkutano na wananchi, anawaambia wananchi Mbunge wenu yuko wapi? Ameanza kuruka sarakasi kama za Bungeni? Mheshimiwa Waziri hii haifai hata kidogo na kwa wananchi wangu hii siyo haki hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri amefanya hivi pia kule kwa Profesa Jay na Majimbo mengine. Alikuja Mheshimiwa Mwigulu Nchemba Jimboni kwangu, ameniandikia message, amenipigia simu nimempa ushirikiano mzuri. Kwa hiyo, naomba wakati mwingine ajaribu kuwa na ushirikiano na mahusiano mazuri na Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kwamba ukuaji wa Sekta ya Kilimo umeendelea kushuka mwaka hadi mwaka. Ukuaji wa Sekta ya Kilimo, tunaambiwa kwamba ni asilimia 1.7 kwa takwimu za NBS na hii unakuja kuona sasa hata bajeti ambayo imetengwa kuanzia mwaka 2010/2011 tuliona asilimia 7.8 ambayo ndiyo ilikuwa bajeti kubwa kwa mara ya mwisho. Tumekuja kuona mwaka 2011/2012, ikawa asilimia 6.9 mwaka jana, 2016/2017 ni asilimia 4.9.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kuwasaidia wakulima wa Tanzania kwa kuendelea kutenga bajeti ya kilimo kidogo kiasi hiki. Naomba niseme tu kwamba Maputo Declaration walipendekeza kwamba angalau nchi wanachama wa AU wajaribu angalau kutenga asilimia 10 kwenye bajeti za kilimo. Hii Maputo Declaration kwa Tanzania tutakuja kuitekeleza lini? Kwa hiyo, naomba niseme kwamba ili kuwasaidia Watanzania hebu tujaribu kutenga bajeti ya kutosha. Kwa mazingira haya, hatuwezi kupata viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, jana nimemwona ndugu yangu hapo Waziri wa Viwanda amebeba makabrasha mengi sana, lakini kwa bajeti hii ya kilimo, kwa kweli naamini kabisa hata Waziri wa Viwanda asitegemee kuwa na viwanda kwa sababu hawezi kuwa na viwanda bila kuboresha kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, historia inatuonesha duniani popote pale, walifanya mapinduzi kwenye kilimo. Tunajua ile Agrarian Revolution iliyofanyika kule Britain, tunajua Agrarian Revolution iliyofanyika kule Marekani, tunajua Indian Green Revolution, tunajua ile China Green Revolution ndipo tukaona sasa wenzetu viwanda vinakuja. Viwanda ni matokeo ya kuboresha kilimo na kupeleka fedha nyingi na kuhakikisha kwamba wakulima mambo yao yanakwenda vizuri kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano viwanda vya nguo, wanategemea pamba; bila kuwekeza kwenye pamba hatuwezi kuwa na viwanda. Bila kuwekeza kwenye mbegu kwa mfano kama alizeti na ufuta hatuwezi kuwa na viwanda vya mafuta. Kwa hiyo, niseme tu kwamba Mheshimiwa Waziri naomba tafadhali, ajaribu kushauri. Najua tu tatizo la viongozi wetu walio wengi hasa Mawaziri mnamwogopa Bwana mkubwa. Hii ndiyo shida kubwa! Mwambieni ukweli, msiogope! Ukweli ndiyo utakaokuweka huru. Kwa bajeti hii, hatuwezi kufika popote na mwakani tutarudi kuja kupiga kelele tena hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo ambalo Mheshimiwa Waziri amezungumza kwenye hotuba yake kuhusu suala la bulk procurement ya mbolea. Siyo jambo baya, lakini naomba tungekuwa tuna-focus zaidi kwenda kujenga viwanda vya mbolea nchini kote.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukijenga viwanda kwa mfano ukajenga Kiwanda cha Mbolea kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambao ni wazalishaji wakubwa sana, ukijenga kiwanda kwa mfano Kanda ya Kaskazini, ukajenga Kiwanda cha Mbolea Kanda ya Magharibi, Kanda ya Kati, Mheshimiwa Waziri mbolea itashuka bei. Kwa sababu tunajua kabisa, kwa mfano, hili suala la saruji, leo kidogo bei ni nafuu kwa sababu viwanda vya saruji viko vingi. Watafanya biashara ya ushindani na mwisho wa siku mbolea itashuka bei. Kwa hiyo bulk procurement ni jambo moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, hili la kujenga viwanda. Tungeendelea kabisa kufikiria hili zaidi kuliko tukawa na hizi kuzibaziba tu angalau kwa muda mfupi, haliwezi kutusaidia sana. Kwa hiyo, naomba niseme tu kwamba alikuja hapa Mfalme wa Morocco, Mohamed wa Sita, tukamwomba atujengee uwanja wa mpira Dodoma. Nadhani wanapokuja watu wetu, kama hawa wadau wa maendeleo, tungekuwa tunawaomba wawekeze kwenye viwanda vya mbolea. Wakiwekeza kwenye viwanda vya mbolea, wakulima wetu watanufaika. Mbolea itashuka bei.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nchi yetu zaidi ya miaka 50 baada ya uhuru tunamwomba mtu uwanja wa mpira badala ya kumwomba viwanda vya mbolea! Mheshimiwa Waziri kwa kweli mimi hili naona siyo sahihi kabisa. Naona leo tumeomba viwanja vya mpira, kesho tutaomba jezi, kesho kutwa tutaomba mipira. Hili jambo halitatufikisha popote pale. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niweze kuzungumzia jambo lingine kwenye bei ya zao la kahawa. Zao la kahawa limeendelea kushuka bei miaka yote. Wenzetu wa korosho mmerekebisha mambo vizuri kabisa kule, leo korosho wananufaika kweli kule Kusini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kahawa imeendelea kushuka bei mwaka hadi mwaka. Ndugu zetu wa jirani tu hapa wa Kenya wanauza kahawa bei nzuri, Uganda wanauza kwa bei nzuri, Tanzania ni nani aliyeturoga? Tatizo liko wapi, Tanzania kahawa yetu tunauza kwa bei ndogo? Leo wakulima wangu Mbozi kule wameamua kuanza kung’oa miche ya kahawa kwa sababu wameona hailipi. Wanaamua walime mazao mengine kwa sababu ya bei ndogo ya kahawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuwasaidie wakulima hawa wa Kahawa, tupandishe bei na ikiwezekana kabisa tuweze kuangalia namna gani ya kuweza kupandisha bei. Kwa nini tusiende kujifunza kwa majirani zetu? Mbona Kenya siyo mbali, hata kwa pikipiki unafika hapa jirani Kenya! Mbona Uganda siyo mbali, kwa nini tusiende kuwauliza ninyi mnauzaje kahawa yenu kwa bei nzuri? Kwa nini Tanzania sisi hatuuzi kahawa yetu kwa bei nzuri?

Mheshimiwa Waziri kwenda kujifunza kwa ndugu yako siyo dhambi hata kidogo! Naomba sasa tukajifunze tuangalie wenzetu, kwa nini wanauza kahawa yao kwa bei nzuri, tuone sisi tuliteleza wapi, tuweze kuwasaidia wakulima wa kahawa, zao ambalo linaelekea kwenda kufa siku za hivi karibuni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, naomba nizungumzie suala la kuanzisha Mnada wa Kahawa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini. Leo nchi nzima, Watanzania wanaolima kahawa wanaenda Moshi kwenye Mnada wa Kahawa. Tukianzisha Mnada wa Kahawa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, kwa mfano, tukaweka Kiwanda cha Kahawa pale Songwe au tukaweka Mbeya, wakulima wetu wataenda kushiriki moja kwa moja kwenye Mnada wa Kahawa pale. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, Vijiji vya Jimbo la Mbozi vinakabiliwa na tatizo kubwa sana la maji. Baadhi ya Vijiji hivyo ni Iyenga, Ilea, Itumpi, Magamba, Mtunduru, Utambalila, Maninga, Mahenje na vijiji vinginevyo. Hivyo katika miradi ya maji vijijini ni vizuri Serikali ikavikumbuka na vijiji hivi vya Jimbo la Mbozi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji Mdogo wa Mlowo wenye idadi ya watu wasiopungua 60,000 unakabiliwa na tatizo sugu na la muda mrefu sana la maji. Bajeti ya mwaka uliopita 2016/2017, Mji Mdogo wa Mlowo ulitenga fedha kwa ajili ya maji. Kwa bahati mbaya na masikitiko makubwa sana, hadi sasa hakuna shughuli yoyote inayoendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atatue tatizo la maji Mji Mdogo wa Mlowo kwani wananchi wanateseka sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, vipo vyanzo vingi vya maji Wilaya ya Mbozi mfano, Mto Lukululu, Mto Mkama na mito mingine. Ni vyema Serikali ijikite kuwapatia maji wananchi wa Mbozi kutoka katika vyanzo hivi. Pia maji ya ardhini hayapo mbali, maeneo mengi yanapatikana mita 75 kuelekea ardhini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na mimi niweze kuchangia, lakini naomba niseme kwamba nitachangia hii kamati Utawala na Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita sana kwenye suala la utawala bora. Taifa letu kwa mara ya kwanza tumeshuhudia kwamba hakuna Utawala Bora katika Taifa letu. Wapo viongozi walipandishwa vyeo baada ya kutuhumia na rushwa, kwa mfano aliyekuwa DC pale Arumeru na leo ni RC Mkoa wa Manyara, amepandishwa cheo licha ya kwamba alituhumiwa kwa rushwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushahidi ulipelekwa TAKUKURU, viongozi wetu...

T A A R I F A . . .

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine kulumbana na watu ambao kwanza hawajui mambo ya nchi yanavyokwenda, siwezi kulumbana naye ngoja nimuache tu, wakati mwingine acha wafu wazikane wao wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiongozi anatuhumiwa kwa rushwa, ushahidi umeshapelekwa, Mbunge Nassari amepeleka ushahidi pale TAKUKURU, TAKUKURU wanachunguza anakuja kupandishwa cheo anakuwa RC. Hiki ni kitu kibaya sana katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala bora katika taifa letu umekuwa ni msiba mkubwa sana. Leo tutakumbuka aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe alituhumiwa tena jukwaani na Paul Makonda ,Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, yule bwana kaachishwa kazi, kwa sababu ya kutuhumiwa tu. Leo mtu alikuwa DC ushahidi upo umepelekwa TAKUKURU muda haujafika si mrefu anapandishwa kuwa Mkuu wa Mkoa. Taifa hili hakuna utawala bora na awamu hii utawala bora uko likizo na jambo hili hatuwezi kulivumilia hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu bomoa bomoa isiyofuta sheria. Leo wote tunafahamu kwamba kaya zaidi ya 1000 zilibomolewa pale Dar es Salaam, lakini kaya hizi zimebomolewa wakati kesi iko mahakamani. Leo mahakama inadharauliwa na mhimili mwingine, huu hauwezi kuwa ni utawala bora na tuheshimu mihimili hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wamekopa fedha benki, kuna watu ambao wamefariki kwa sababu nyumba zao zimesha bomolewa, hawana mahali pa kuishi, Taifa hili linaenaelekea wapi? Awamu ya Tano imetufikisha pabaya sana kwenye utawala bora, hatujawahi kushuhudia haya siku za nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nikuhusu kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa. Unapozuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na nikopongeze sana Mwenyekiti, hii katiba, wewe Mwenyekiti kipindi hicho ulikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali hii; ukisoma Ibara ya Tatu ya katiba yetu Ibara ya Tatu Ibara Ndogo ya Kwanza inasema; “3.-(1) Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa, isiyokuwa na dini, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.” (Makofi)

Mheshimiwa mwenyekiti, ukisoma pia Sheria Namba Tano ya mwaka 1992 ya vyama vya siasa inazungumzia shughuli ya vyama vya siasa ni pamoja na kufanya mikutano ya hadhara. Leo Rais wa nchi amezuia mikutano ya hadhara, ameikanyaga kanyaga Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameiweka pembeni. Hakuna utawala bora, kama unaweza leo ukaweka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania pembeni. Hali hii ni mbaya sana hatuwezi kuivumilia. Na niombe viongozi tulio…

T A A R I F A . . .

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kufungia vyombo vya habari vinavyoikosoa Serikali. Leo vyombo vya habari vinafungiwa, tumeona magazeti yanafungiwa, gazeti la Mwanahalisi limefungiwa, Raia Mwema imefunguwa, Tanzania Daima ilifungiwa, utawala bora uko wapi? Kama leo vyombo vya habari vinavyoikosoa Serikali, vinavyoishauri Serikali, vinafungiwa, Taifa hili liko pabaya zaidi kwenye suala la utawa bora. Leo Bunge Live limefungiwa, hakuna Bunge live wote tunafahamu kwamba Bunge ni mkutano wa hadhara.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na mimi naomba niweze kuchangia mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote na mimi naomba niungane na Watanzania wenzangu kutoa pole kwa Ndugu yangu Tundu Lissu kwa yale ambayo yalimkuta na nitoe pole na niseme tu kwamba hata niliposikia jana kuna baadhi ya Wabunge wenzetu wachahe wanaanza kuleta vijembe kwenye suala kama hili kwa kweli liliniumiza sana. Lakini niseme tu kwamba siku zote matatizo hayana itikadi na matatizo yanaweza kumkuta mtu yeyote yule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niingie kwenye Mapendekezo ya Mpango, tunafahamu wote kwamba kwenye hili kablasha tuliopewa na ndugu hapa Dkt. Mpango ukweli ni kwamba amezungumza vitu vingi sana kuhusu viwanda, kilimo na mambo mengine, lakini hatuwezi kupata viwanda bila kujali kilimo. Wenzangu wamezungumza mengi sana na jana niwapongeze waliotangulia kuzungumza kuhusu kilimo, lakini ukweli unapozungumza habari ya viwanda huwezi kuacha kilimo na ukakiweka pembeni, historia inaonesha nchi zote ambazo leo zina viwanda, nchi kama China na nchi nyingine nyingi ambazo leo zimeendelea ni kwa sababu walifanya mapinduzi katika kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Tanzania tunafahamu kwamba tunapotaka kufika mwaka 2020/2025 tunasema kwamba nataka Serikali hii iwe angalau wananchi wake wale na uchumi wa kati, uchumi ambao utaendeshwa kwa kutegemea viwanda. Lakini ukweli je, ni kwa sasa? Kwa sababu kwa muda huu ukiangalia kama lengo ni kupata malighafi kwa mfano kwenye viwanda vyetu ni kweli lazima tuangalie kilimo, lakini kwa sasa hali ilivyo wananchi wetu wamezalisha sana na wanalia kila kona hawana masoko ya mazao yao na viwanda vya kuweza kuwa-accomodate hayo mazao, kuweza kusindika mazao hayo hazipo. Kwenye hili tumebugi sana na hili niweze kusema kwamba tumerudi nyuma na wanachi wetu wanateseka sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wakulima wote waliolima tumbaku wanalia, wanalia wote waliolima mahindi na hivi ninavyozungumza Kanda za Nyanda za Juu Kusini katika Mkoa wa Songwe, Mkoa Mbeya, Mkoa wa Rukwa, Mkoa wa Ruvuma na mikoa mingine wanalia sana, mahindi yamekaa ndani, hakuna ayenunua yale mahindi, hivyo viwanda mlivyosemakwamba tupate malighafi kwa ajili ya kusindika mazao yetu tuonyesheni basi viwanda hivyo wakulima wetu wakauze mazao hayo kwenye hivyo viwanda basi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ni mbaya kwelikweli amezungumza vizuri ndugu yangu jana mmoja, leo mkulima anayelima ananunua mbolea bei kubwa, anakodi shamba bei kubwa, ananunua mbegu bei kubwa, lakini mwisho wa siku tunakuja kumfungia mipaka eti asiuze mahindi nje ya nchi lakini pa kuuza wakati huo Serikali haitoonyeshi tukauze wapi. Dhambi hii ambayo inatendwa na Serikali yetu na viongozi wa Chama cha Mapinduzi lazima niwe muwazi hapa jambo hili kama hamuwezi mkajadili kwenye caucus zenu mnajadili mambo mengine wananchi wetu msimu wa kulima ndio huu hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili ni baya sana na mwaka 2019/2020 hili jambo litawaghalimu na mjiandae kuondoka, kwaheri Chama cha Mapinduzi kwa sababu suala hili wameshindwa kujadili mambo ya msingi, wanajadili mambo mengine wanaacha suala hili la wakulima wetu. Mimi niseme kwamba leo tunazungumza 60% ya chakula kinachozalishwa nchini kinatoka Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, mkulima huyo hawezi kununua mbolea bila kuuza mahindi, hawezi kusomesha watoto bila kuuza mahindi, hawezi kufanya jambo lolote lile bila kuuza mahindi, leo wakulima hawa wanalalamika mimi naamini hasira hizi na machozi haya mwaka 2019/2020 wajiandae hao waliosababisha na Serikali hii na Chama cha Mapinduzi wala sio Serikali ya CHADEMA, wala sio ya CUF. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajua wako wakulima pia wa tumbaku wanalalamika, wako wakulima wa mbaazi wanalalamika, wakulima wa korosho wenyewe wanasema bei imekuwa nzuri, lakini kiukweli bado hata wa korosho hao pia wamekopwa, bado hawajalipwa. Kiukweli kabisa tusipokuwa makini kwenye suala la kilimo mimi naamni kabisa Watanzania wengi watarudi nyuma kwasababu kilimo ndo kinaajiri 70% na kuendelea ya Watanzania walio wengi.

Naomba nizungumzie jambo lingine linalohusu utawala bora. Leo tumezungumza kuhusu utawala bora lakini ukweli ni kwamba viongozi wengi wanaotuhumiwa na rushwa kama ma-DC leo wanapandishwa vyeo wanakuwa Wakuu wa Mikoa. Hivi unawezaje kumpandisha cheo mtu ambaye alikuwa DC unampa Ukuu wa Mkoa anathumiwa kwa rushwa na ushahidi upo, TAKUKURU wameenda wamnachunguza kila kitu, kila mtu ameona kabla TAKUKURU hawatoa majibu leo Rais anaenda kumpa DC kuwa Mkuu wa Mkoa anayetuhumiwa kwa rushwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa hakuna utawala bora na hapa hali ni mbaya kweli kweli kama tutakuwa tuna- promote wanaoharibu nchi yetu, kwa kweli najua kabisa kwamba utawala bora, dhana ya utawala bora tuiondoe kabisa kwenye awamu hii ya tano. Lakini leo tunafahamu wote wanapozungumzia utawala bora tunafahamu misingi ya utawala bora ni pamoja na uwazi, leo Ndugu yangu Mpango hapo tumeambiwa Serkali imeokota vichwa vya treni pale Dar es Salaam bandarini, hivi ni kweli Serikali haijui ni kwamba vile vichwa vya treni vimetoka wapi. Uwazi uko wapi kwenye utawala bora lazima kuna uwazi, uwazi uko wapi, halafu vile vichwa vya treni vinajulikana vimeandikwa kabisa na majina. Sasa haya mambo leo Serikali inataka kununua vile vichwa vya treni, inanunua kutoka kwa nani inafanya biashara na nani, ni suala ambalo lazima tujue kabisa kwamba utawala bora ni tatizo ni janga kubwa nana na Dkt. Mpango ulichokizungumza kwenye ile kablasha kuhusu utawala bora, umezungumza tu kidogo tu mahakama sijui kujenga kufanya nini vitu vingi sana vya msingi ilitakiwa tuwaeleze Watanzania vinakaa vipi. Kwa hiyo kiukweli kwenye hili ni tatizo kubwa sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Waziri Mkuu ukurasa wa 10 limezungumzwa suala la chaguzi ndogo za Wabunge zilizofanyika katika majimbo matano na Madiwani katika kata 59. Chaguzi hizi zilitawaliwa na vurugu, dhuluma, pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu. Viongozi na wanachama wa chama cha CHADEMA walikamatwa na kubambikiwa kesi, wengine waliumizwa kwa kukatwa mapanga na wengine kupoteza maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano Katibu wa CHADEMA, Kata ya Hananasifu Kinondoni aitwaye Daniel aliuawa wakati wa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kinondoni. Hadi sasa hakuna taarifa zozote za kukamatwa kwa wauaji. Kitendo hiki kinalifanya Taifa letu kuwa siyo sehemu salama tena kama zamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mauaji ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Usafirishaji, Akwilina Akwilin. Pia, nchi yetu imeonesha kwamba, siyo sehemu salama tena. Mambo haya yasipodhibitiwa yanajenga chuki na visasi katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, Serikali iliahidi milioni 50 kila kijiji, suala ambalo halijatekelezwa hadi sasa. Huu ni mwaka wa tatu tangu Serikali itoe ahadi, lakini jambo hili halizungumzwi tena. Siyo jambo jema Serikali kuahidi halafu ikashindwa kutekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingi ya maji nchini imesimama kwa sababu ya kutopeleka fedha. Mfano Mji Mdogo wa Mlowo uliopo Jimbo la Mbozi, kuna mradi wa maji wa milioni 400 na certificates zilishatumwa Wizarani, lakini fedha hazijatolewa na kusababisha mradi kusimama
kwa muda mrefu sasa. Naikumbusha Serikali kupeleka fedha za mradi huu ili ukamilike na wananchi wapate huduma ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, alipokuja Halmashauri ya Mbozi alielezwa changamoto nyingi za Wizara hii. Mojawapo ya changamoto hizo ni ukosefu wa magari ya wagonjwa katika vituo vya afya na hospitali; Kituo cha Afya cha Itaka kinahudumia Kata nne za Itaka, Nambinzo, Bara na Halungu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri alipofanya ziara Mkoa wa Songwe aliahidi kuwapatia gari la wagonjwa wananchi wa Mbozi ili lisaidie Kituo cha Afya cha Itaka kutokana na kituo hiki kuhudumia wagonjwa wengi. Litakuwa jambo jema endapo Waziri wa Afya atatimiza ahadi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali ya Awamu ya Nne ilijenga Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo Hospitali ya Muhimbili, sio jambo baya, ni jema, ila tatizo ni kwamba taasisi hii muhimu haina baadhi ya vitendea kazi. Serikali inunue vitendea kazi (vifaatiba) ili kuendelea kupunguza tatizo la wagonjwa, hasa wenye magonjwa makubwa kama ya moyo kwenda kutibiwa nje ya nchi. Fedha zote zinazoidhinishwa wakati wa bajeti kwa ajili ya taasisi hii muhimu ni vema zitolewe zote na kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Wilaya ya Mbozi ina changamoto nyingi zinazohitaji utatuzi, mfano, kuna OPD ndogo, hakuna wodi ya wazazi, hakuna maji hivyo ni vema Serikali ikatatua kero hizi ili wananchi wanufaike.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu upungufu wa watumishi wa afya; Wilaya ya Mbozi ina upungufu wa watumishi wa Idara ya Afya; zaidi ya watumishi 600 wanahitajika. Upungufu huu unazikabili hospitali zote mbili, Hospitali ya Wilaya ya Mbozi na Hospitali ya Mbozi Mission. Hospitali ya Mbozi Mission inaendeshwa kwa PPP hivyo watumishi wanaotakiwa kuajiriwa na Serikali ni wachache sana. Naishauri Serikali kuajiri watumishi katika hospitali hii, pia Vituo vya Afya vya Isanga, Itaka, Iyula na zahanati havina watumishi wa kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kukumbushia ahadi ya Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa alipokuja Mkoa wa Songwe mwaka 2017 ambapo aliahidi mbele ya Wanambozi kwamba bararaba ya kutoka Mlowo - Kamsamba - Kilyamatundu (Rukwa) itatengenezwa kwa kiwango cha lami. Ukisoma ukurasa wa 222 wa hotuba ya Waziri barabara ya Mlowo – Kamsamba yenye urefu wa kilometa 130 imetengewa shilingi milioni 120 tu, je, fedha hizi zitatengeneza lami ya kilometa 200 kweli?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima na taadhima, naiomba Serikali itekeleze ahadi yake ya kutengeneza barabara hii kwa kiwango cha lami kama ilivyoahidi kwa wananchi. Barabara hii inaunganisha Mkoa wa Songwe na Rukwa na ni suala la kisera kuunganisha barabara zote ambazo zinaunganisha mikoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia barabara inayounganisha Wilaya ya Mbozi na Songwe kupitia Kata ya Magamba (Songwe) na Kata ya Mgamba (Mbozi) haijatengenezwa hata kwa kiwango cha changarawe jambo ambalo linawanyima fursa wananchi wa Wilaya ya Songwe kufika Makao Makuu ya Mkoa wa Songwe ambayo yapo Wilaya ya Mbozi. Wananchi wa Wilaya ya Songwe hulazimika kupitia Mbalizi, Mkoa wa Mbeya ili kufika Makao Makuu ya Mkoa. Naishauri Serikali itengeneze barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni zamu yangu na mimi kuweza kuchangia kwenye Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na hoja ya kwanza ambayo ni walimu wa shule za sekondari kuhamishiwa shule za msingi bila kupewa haki zao kisheria.

Mjeshimiwa Mwenyekiti, hata kwenye kitabu hiki cha hotuba ya Waziri wa TAMISEMI ukiangalia ukurasa wa 40 wameeleza pale kwamba walimu 8,834 walihamishwa kutoka shule za sekondari kupelekwa shule za msingi ili kupunguza tatizo la walimu shule za msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza kabisa, kumtoa mwalimu kutoka shule ya sekondari kwenda shule ya msingi hii si sahihi hata kidogo. Kwa sababu huyu mwalimu amejifuza saikolojia ya kufundisha watoto wa sekondari wenye umri mkubwa kuliko wale wa shule ya msingi, leo unapomtoa sekondari kumpeleka shule ya msingi tunakwenda ku-prove failure na hauwezei kupata efficiency hata kidogo na matokeo yatakuwa ni mabaya kweli kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huku ni kukwepa majukumu, Serikali inafika mahali inakwepa majukumu, badala ya kuajiri inafika mahali inaanza kuhamisha walimu wa sekondari kupeleka shule za msingi. Mheshimiwa Waziri, naomba nikuhakikishie kwamba huko sekondari mnakosema walimu wanatosha, sekondari, walimu hawatoshi kwasababau unavyozidi kuongeza idadi huku shule za msingi hata kule sekondari idadi ya wanafunzi inakuwani kubwa sana. Kwa hiyo, mnachokifanya Mheshimiwa Waziri kabisa hamuwatendei Watanzania haki hata kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo lakini bado walimu hawa 8,834 wamehamishwa, lakini hawajalipwa fedha zao. Hawajalipwa disturbance allowance, subsistence allowance, wala transport allowance.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi walimu 117 waliohamishwa kutoka shule za sekondari kwenda shule za msingi wanadai zaidi ya shilingi milioni 300 hawajalipwa hadi leo. Serikali hii ambayo inasema ni Serikali ya wanyonge, wanyonge gani ambao hawajalipwa mpaka leo? Wanyonge ni akina nani kama leo walimu 117 wanadai shilingi milioni 300 na kitu hawajalipwa? Huyu anayejiita kiongozi wa wanyonge ni wanyonge wapi? Hii hali ni mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi juzi mmefuatilia maandamano yamefanyika kule Mbozi na walimu hawa 117, Rungwe walimu zaidi ya 80 wameandamana wanadai fedha hazijalipwa. Waziri wa TAMISEMI uko hapo, ukweli ni kwamba Waziri wa TAMISEMI katika hili mme-prove failure kabisa na mlishaizungumzia siku za nyuma wkamba watumishi wasihamishwe bila kulipwa lakini leo mmeshindwa kufayakazi hiyo ya kuwalipa hawa watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niende kwenye suala lingine la ajira za watumishi. Leo Serikali inakwepa kuajiri watumishi, Awamu hii ya Tano haiajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mfano mdogo tu, ukisoma ukurasa wa 40 wa hotuba hii ya Waziri wa TAMISEMI wanasema, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imefanikiwa kuajiri walimu wapya 2,767. Unapoajiri walimu 2,767 wakati kwenye ukurasa huo huo tumeambiwa kwamba upungufu wa walimu kwenye shule za msingi ni walimu 97,517 unaajiri 2,767 tafsiri yake ni kwamba kama tutakuwa hatuzaliani unahitaji miaka 35 ili kuweza kumaliza tatizo la walimu shule za msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Serikali ya Awamu ya Tano ukilinganisha na awamu nyingine ndiyo Serikali ambayo naona mimi ime-prove failure hamna kilichofanyika kabisa imeshindwa bora hata Serikali ya Jakaya Mrisho Kikwete tunaikumbuka kuna mambo alifanya mazuri, lakini hii ya wanyonge sidhani ni wanyonge gani anaozungumzia

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kufuta, lakini nasema ujumbe hapa ni kwamba Awamu ya Tano haijaajiri, haitoi ajira.

Kwa hiyo, ukichukua hawa walimu, ukichukua miaka 35 tafsiri yake ni kwamba kama Watanzania hatuongezeki, kwa maana hatuzaliani kuanzia leo tunahitaji kuwa na miaka 35 mingine mbele. Ukijumlisha leo ni mwaka 2018 maana yake ni mwaka 2053 ndipo tatizo la walimu litakuwa limekwisha nchini. Kwa muda huo sidhani kama sisi tutakuwepo kwa sababu kutakuwa na chama kingine kinanachoongoza nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine ni mishara kwa watumishi wa umma. Mishahara haiongezwi, Awamu hii ya Tano haijawahi kuongeza mshahara hata mara moja. Gharama za maisha zinapanda, hali ya uchumi inazidi kuwa mbaya, leo watumishi wanapokuwa wanajaza mikataba wanaanza kazi maana yake pale, pamoja na mikataba yao ni kwamba wanasaini kwamba watakuwa wanaongezewa mshahara annual increment kila mwaka, watakuwa wanaongezewa mishahara, wakipandishwa mishahara. Leo hawapandishwi madaraja, hawajaongezwa mishahara ndiyo awamu pekee ambayo haijawahi kuongeza mishahara, na ndiyo Serikali ambayo inajiita Serikali ya wanyonge, sijui wanyonge wapi hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongeze jambo lingine, shilingi milioni 50 za kila kijiji. Usiku wa deni haukawii kuisha; na mimi nawakumbusha amezungumza Mheshimiwa Heche vizuri sana asubuhi. Usiku wa deni ni mwaka kesho kutwa 2020. Kwanza kuanzia mwakani Serikali za Mitaa tutakwenda kuwakumbusha Watanzania shilingi milioni 50 mlizowaahidi hadi leo hamjatoa na muda unazidi kuisha. Kwa hiyo ndugu yangu Mheshimiwa Jafo, Waziri wa TAMISEMI utatuambia hizi shilingi milioni 50 kwenye bajeti hii zipo au hazipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la ubaguzi wa Watanzania. Kuna watu wanaohojiwa uraia wao, viongozi wa dini maaskofu, Askofu Kakobe, Askofu mmoja anaitwa Severine Niwemugizi wa Kanisa la RC hawa watu pamoja na viongozi wengine mbalimbali, wanafunzi Abdul Nondo. Watu leo hii wameanza kubaguliwa uraia wao, wanahojiwa uraia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inafika mahali kama yule askofu kule Bukoba anasema kwamba kiongozi akatubu, tunataka Katiba mpya. Mtu anapotoa maoni yake ambayo amepewa uhuru wa maoni na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unakwenda kumhoji uraia, kwa nini kabla hajatoa maoni yake msingemhoji uraia? Kiongozi asiyekubali kukosolewa hawezi kuwa kiongozi, lindeni uhuru wa maoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, amezungumza ndugu yangu Zitto Zuberi Kabwe, mkitaka basi Mkoa wa Kigoma kama kuna uwezekano basi upelekeni Burundi. Kwa sababu leo inaonekana tatizo kubwa la kuhoji uraia wa watu mnahoji sana watu wa Kigoma. Abdul Nondo mwanafunzi wa chuo kikuu ni mtu wa Kigoma, Askofu Kakobe ni mtu wa Kigoma, wako na wengine n mifano mingine. Leo kukaa mipakani imekuwa ni dhambi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na wewe mimi naamini kama unakaa karibu na mpakani kule si ajabu ukaja kutoa ushauri wako au maoni yako watakuja kukuhoji sijui uko jirani na nchi gani. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee. Wanasema wamba kama umezoea kula nyama ya binadamu huwezi kuacha, ndugu yangu Hussein Bashe amewahi kuhojiwa uraia wake eti kwa sababu kaingia kwenye kura za maoni na ndugu yangu huyu Waziri wa Maliasili amehojiwa akaambiwa si raia wa Tanzania.

Leo dhambi hiyo ya kuhoji watu haijaisha, kuwabugua watu kura za maoni zimekwisha leo Bashe amekuwa raia wa Tanzania ni kwa sababau kura za maoni zimekwisha na leo ni Mbunge mwenzetu kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kumbe hiyo tabia haikwisha imeendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii ni mbaya sana na tunaomba tuikemee kwa pamoja sisi wote kwa sababu leo hii kwa kuwa mtu mwingine, kwa Kakobe leo imetokea kwa Bashe na kwa wengine imetokea kwa Nondo kesho na kesho kutwa ni dhamu yako, kwa kumalizia naomba nizungumze suala… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, lakini kabla sijaendelea, naomba nitoe pole kwa familia ya Mheshimiwa Sugu ambaye yuko ndani kwa sababu ya uonevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa pole hiyo, pia akitoka Mheshimiwa Sugu nitakuja kumpa pongezi kwa sababu tunajua hata Mandela naye amewahi kupitia hatua kama hiyo na naamini kwamba yeye ndio atakuwa Mandela wa Tanzania huko mbeleni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nianze kuchangia Wizara hii ya Mambo ya ndani na naomba nianze na kusoma Ibara ya (14) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. “Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake kwa mujibu wa sheria.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumetokea mauaji yanayofanywa na baadhi ya Maaskari wetu, Maaskari ambao tumewasomesha kwa kodi zetu, Maaskari ambao hatujui kitu gani, either kwa maagizo kama wanavyosema yametoka juu. Mauaji haya yanasikitisha sana na yanavunja Ibara ya (14) Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dada yangu, Mheshimiwa Anatropia amezungumza vizuri sana. Ameuawa ndugu yetu Suguta Chacha Heche; amekamatwa, amepigwa pingu, anachomwa kisu na Askari. Inasikitisha sana na inatia huzuni sana. Ameuawa Aqualina, lakini kuna Maaskari walikamatwa kama sita hivi. Hao Maaskari wako wapi? Leo anakuja DPP anasema kwamba hao Maaskari; yaani leo tunaambiwa kwamba hilo shauri limeshafungwa wakati Maaskari sita walikuwa wamekamatwa tangu awali, hatujui Maaskari hao wamepelekwa wapi; na hatujui kesi imekuwaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wanampongeza Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya ndani, Mheshimiwa Comredi Mwigulu Nchemba. Nimwambie ukweli wanaompongeza wanamharibu na wanaompongeza hawamtakii mema. Namshauri jambo moja tu, kujiuzulu Uwaziri wa Mambo ya Ndani. Namshauri pia IGP pia aweze kujiuzulu. Siyo dhambi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikumbushe kitu kimoja. Kuna watu hawakumbuki historia ya Taifa letu. Mheshimiwa Mwinyi, Rais Mstaafu amewahi kujiuzulu miaka ya 70 kwa sababu ya wale wafungwa kule Shinyanga walifariki gerezani akajiuzulu na baadaye akaja kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kujiuzulu haimaanishi kwamba wewe umetenda dhambi, lakini watu wa chini yako maana yake hawaendi sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtu mwingine inaitwa Meja Jenerali Abddallah Said Natepe, ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani. Alijiuzulu kwa sababu kuna watu walikuwa Magerezani, walikuwa wanatuhumiwa; walifungwa kwa kesi ya uhaini, wakatoroka. Walipotoroka, akaamua kujiuzulu kulinda heshima yake, lakini pia kuchukua hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mheshimiwa Comredi Mwigulu Nchemba amekaa hapo kwenye kiti hicho, sikutegemea kama angeweza kuwepo hata dakika tano hadi sasa kwa sababu kilichotokea kwenye Wizara yake ni madudu; ni takataka. Anachong’ang’ania sijajua ni kitu gani!

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu leo kama kuna watu wanauawa, kuna watu leo wanatekwa, kuna watu wamepotea kwenye nchi hii, Beni Saanane hatui yuko wapi hadi leo, ni mwaka mmoja na nusu; Azori Gwanda. Nasi hatuwatetei CHADEMA tu, tunawatetea na wengine. Azori Gwanda alikuwa ni Mwandishi wa Habari. Yule Diwani wa Kibondo kule alikuwa ni mtu wa CCM. Sisi tunawatetea wote ndugu zangu, hatuwatetei CHADEMA tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba hiyo nafasi, hicho kiatu kimempwaya. Nadhani angeweza kuondoka kwa sababu nafasi haiwezi hata kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua yeye alikuwa ni miongoni mwa watia nia kwenye Chama chake kwa nafasi ya Urais, nadhani ndoto za Urais zitakuwa zimeshaanza kuota mbawa kwa sababu madudu aliyofanya kwenye Wizara hii hayajawahi kufanywa hata mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye hoja nyingine. Leo Magereza zinajaa, Mahabusu wako Magerezani, wafungwa wako Magerezani, siyo kwa sababu labda uovu umeongezeka.

Hapana ni kwa sababu kulikuwa na uonevu wa hali ya juu sana. Mheshimiwa Mwenyekiti, leo watu wanaonewa. Mheshimiwa Sugu kawekwa ndani kwa sababu ana uhuru wa kutoa maoni, ametoa maoni yake, leo amefungwa ndani miezi mitano. Uonevu wa namna hiyo hauwezi kuvumilika hata kidogo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasikitika kuona hadi sasa Serikali haijapeleka vitabu vya kiada vya darasa la nne licha ya kwamba wanafunzi hawa wanajiandaa na mitihani ya Taifa ya darasa la nne. Je, Serikali haioni kama inatengeneza mazingira ya kuwafelisha wanafunzi kwa kutopeleka vitabu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtihani wa kidato cha nne mwaka 2017 shule zilizoibuka bora 100 za Serikali ni sita tu kati ya hizo. Kwa miaka mingi sasa shule za watu binafsi zimekuwa zikifanya vizuri ukilinganisha na shule za Serikali. Utafiti unaonesha kwamba matokeo mazuri ya shule binafsi unatokana na motisha kwa walimu, mishahara mizuri kuliko ile ya Serikali na mazingira bora ya kufanyia kazi. Tangu mwaka 2014 Serikali haijawahi kupandisha mishahara kwa watumishi wakiwepo walimu. Hivyo walimu wengi wa shule za umma wamekosa moral ya kufanya kazi kwa bidii. Litakuwa jambo jema kama Serikali itajifunza mbinu za kufundishia na kujifunzia kutoka shule binafsi. Pia mishahara ingeboreshwa kwa watumishi wa umma ili walimu waliokata tamaa warudishe moral.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Songwe hauna chuo cha VETA hivyo naishauri Serikali ijenge chuo katika mkoa huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu Kambi ya JKT iliyopo katika Kata ya Itaka Wilaya ya Mbozi, kuna migogoro ya mipaka ya ardhi na wananchi wa Vijiji vya Sasenga, Itewe na Mboji. Ramani ya vijiji hivi pamoja na GN vinaonesha kuwepo kwa vijiji hivyo miaka mingi kabla ya kuanzishwa kwa kambi ya JKT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali ishughulikie migogoro ya mipaka kati ya JKT na vijiji hivi kwani kuchelewesha utatuzi wa migogoro kutasababisha uadui mkubwa kati ya wananchi na JKT jambo ambalo siyo jema. Kijiji cha Sasenga wananchi wameamuliwa wote kuhama ili kupisha maeneo ya jeshi bila kuwaonesha kwa kwenda ni uonevu mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Kujenga Taifa JKT liboreshe na kusimamia kwa ufanisi zoezi la kuwapata wananchi wa kujiunga na JKT kupitia wilaya zao. Mwaka jana Wilaya ya Mbozi wananchi walioomba kujiunga na JKT waliachwa wote na badala yake wakachukuliwa watu wa kutoka nje ya Mbozi na nje ya Mkoa wa Songwe. Naomba viongozi wa JKT toka Makao Makuu washuke hadi kwenye Wilaya kusimamia zoezi hili vizuri na wasiachiwe Wakuu wa Wilaya maana ndiyo chanzo cha migogoro na upendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mishahara iongezwe kwa wanajeshi wetu maana wanafanya kazi nzuri ya kulinda mipaka ya nchi yetu. Makazi yao pia yaboreshwe maana hali ni mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, nasikitika kuona vyanzo vya utalii vilivyopo Wilaya ya Mbozi zimesahauliwa kuwekwa kwenye kumbukumbu ya Wizara, pia havijatangazwa mfano katika Kata ya Nanyara Wilaya ya Mbozi kuna vivutio vya utalii vya maji moto na mapango ya popo. Vyanzo hivi havitajwi popote pale wala havipo kwenye kumbukumbu za Wizara. Wizara ichukue hatua thabiti za kuvitambua vyazo hivi na kuvitangaza ili kuongeza mapato ya Halmashauri ya Mbozi na Serikali Kuu.

Mheshimiwa Spika, pia askari wa wanyama pori waepukane na mauaji ya raia wanaoingia kwenye maeneo ya hifadhi badala yake wachuke hatua za kisheria na siyo kuua. Mfano wapo wananchi wasiokuwa na hatia waliuawa mwaka jana Arumeru, Arusha na maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mbozi lenye vijiji 63 na kata 11 lina Mahakama mbili tu za Mwanzo. Naomba kwa niaba ya Wananchi wa Mbozi Serikali iweze kukarabati jengo la Kijiji cha Igamba, Jimbo la Mbozi ili lianze kutumika. Miaka ya nyuma jengo hili lilitumika kama Mahakama ya Mwanzo, Igamba. Jengo hili likikarabatiwa litafanya Jimbo la Mbozi kuwa na Mahakama tatu za Mwanzo za Itaka, Mlowo na Igamba. Hivyo, ni vema Serikali ikawasaidia wananchi wa Igamba ili kuwaepusha na safari ndefu ya kwenda kutafuta huduma hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, Mahakama ya Mwanzo Itaka licha ya kwamba inatumika lakini imechakaa sana hivyo, Serikali ichukue hatua za haraka ili kulinusuru jengo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama ya Wilaya Mbozi iliyopo Mji wa Vwawa ipo katika hali mbaya sana. Ukumbi wa Mahakama ni mdogo sana na miundombinu mbalimbali kama vile vyoo vipo katika hali mbaya sana. Mahakama ya Wilaya ya Mbozi kwa sasa ndiyo Mahakama ya Mkoa wa Songwe. Naishauri Serikali ikarabati Mahakama hiiili iweze kuwahudumia wananchi wa Mkoa wa Songwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, Mahakimu waongezwe mishahara ili wafanye kazi wakiwa na ari nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, Serikali ilitangaza hapa Bungeni kwamba local channels za TV zitaoneshwa kwenye ving’amuzi bure bila kulipia lakini hadi sasa zoezi hilo limeshindikana. Serikali haioni kwamba huku ni kuwanyima wananchi wa Tanzania kupata habari? Hivyo, ni vyema Serikali ikaweka msisitizo kuhusu jambo hili ambalo ni haki ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, pia, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ijenge vizuri uwanja wa mpira uliopo Mji mdogo wa Mlowo ambao ulizinduliwa na Mwenge tarehe 2 Aprili, 2019. Uwanja huu ujengwe vizuri ili kuruhusu michezo mingine iwe na miundombinu mizuri. Mfano michezo ya mpira wa pete, volleyball na michezo mingine.

Mheshimiwa Spika, ili kuboresha mpira wa miguu nchini, Serikali iangalie namna ya kuanzisha academy katika kanda mbalimbali nchini. Leo nchi nyingi zilizoendelea duniani kisoka zilianza na academy na sasa zimefikia hatua kubwa ya kisoka.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nami niweze kuchangia Wizara hii ya kilimo, lakini naomba niseme tu kwamba Waheshimiwa Wabunge wengi hatujajua tatizo liko wapi na ndiyo maana wakati mwingine tunamlalamikia Mheshimiwa Tizeba. Hiyo Wizara tukimweka hata Waziri Mkuu ndiyo awe Waziri wa Kilimo kesho tu mtamuondoa kwenye Wizara hiyo kwa sababu tatizo kubwa ninaloliona ni mtiririko wa fedha usioridhisha. Suala la mtiririko wa fedha usioridhisha si la kumlaumu mtu mmoja, mimi nailaumu Serikali ya Awamu ya Tano (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii ya Awamu ya Tano, ukiangalia kuanzia bajeti ya mwaka 2015/2016 fedha za maendeleo zilizokuwa zimetengwa ni shilingi bilioni 32.7 lakini zilizotolewa ni shilingi bilioni 5.1 sawa na asilimia 16. Mwaka 2015/2016 aliyekuwa Waziri ni Mheshimiwa Mwigulu Nchemba. Bajeti ya mwaka 2016/2017, fedha za maendeleo zilizokuwa zimeidhinishwa na Bunge ni shilingi bilioni 101.5 lakini fedha zilizotolewa ni shilingi bilioni 3.3, sawa na asilimia 3.3. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2017/2018, bajeti hii ambayo tunaimalizia sasa, zilitengwa shilingi bilioni 150.2 zilizotolewa ni shilingi bilioni 27, sawa na asilimia 18. Hapa ndipo naposema kwamba hoja hapa si suala la mtu mmoja ni Serikali ya Awamu ya Tano tangu imeingia madarakani haina mpango, haina mkakati wa kuwasaidia wakulima wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize, tumesema kwamba mapato yanaongezeka, makusanyo yanaongezeka, haya makusanyo yanayoongezeka kwa nini hampeleki kwenye Wizara ya Kilimo? Makusanyo yanaongezeka hatuoni lakini kila siku tunaambiwa makusanyo yameongezeka. Serikali ya Awamu ya Tano naona ni tatizo kubwa na lazima tuchukue hatua sisi Waheshimiwa Wabunge wote bila kujali itikadi ya vyama vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niweze kuzungumzia hoja ya pili ambayo ni kununua kahawa kupitia vyama vya ushirika na nimesikia tunaanza msimu huu kwa kahawa, pamba pamoja na mazao mengine. Suala hapa ni kwamba vyama vya ushirika vilishakuwepo siku za nyuma, kulikuwa na ubadhirifu wa hali ya juu sana na kulikuwa na wizi, je, Serikali imewakamata wale wezi walioiba siku za nyuma? Je, hawa wezi kwa sasa hawapo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kwenye zao la kahawa kulitokea jambo moja ambalo ni la ajabu sana. Wakulima wanauza kahawa mwezi wa saba wanakuja kupewa fedha baada ya miezi sita wakati mwingine baada ya mwaka mmoja, malipo yanacheleweshwa. Je muarobaini wa matatizo haya umeshapatikana? Kulikuwa na mambo mengi sana ya ajabu. Watu waliuza majengo ya vyama vya ushirika, waliuza mali za vyama vya ushirika, kwa sababu Serikali hii ya Awamu ya Tano imekuwa ni Serikali ya mizuka, imekuja bila kufanya angalau tathmini, tumekimbilia jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na vikundi vya wakulima ambavyo vilikopa fedha Benki, wakanunua CPU kwa ajili ya kuboreshea zao la kahawa, hizi fedha atakayelipa ni nani leo tunakwenda kwenye vyama vya ushirika? Hizi CPU watapeleka wapi? Tusipochukua hatua makini kwenye hili tutakwenda kuangukia pua muda si mrefu. Nachoshauri katika hili, hivi vyama vya ushirika vinavyoanzishwa kwenye kahawa, pamba na mazao mengine tungesitisha kwanza, tuweke kipindi cha mpito, tuweze kufanya tathmini vizuri baada ya hapo tuvianzishe tukiwa tayari tumeshatafuta muarobaini wa matatizo ambayo yamewahi kujitokeza siku za nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu masoko ya mazao. Nimesikia Waheshimiwa Wabunge hapa wanalalamika sana mahindi, mahindi; ndipo sasa msingi wa ile hoja yangu ya kwanza kwamba shida ni Serikali ya Awamu ya Tano inapokuja. Ni kwamba, tatizo si mahindi peke yake, angalia kwenye suala la mbaazi. Mbaazi ilikuwa inauzwa kilo Sh.2,000, leo inauzwa Sh.150, Sh.120 hadi Sh.80 naambiwa hapa. Mbaazi inalimwa Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Lindi, Mtwara, Morogoro na maeneo mengine ya nchi, watu wengi wameshindwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao lingine lenye changamoto ni tumbaku. Leo navyozungumza msimu wa tumbaku unakwenda mwingine lakini tumbaku iko kwenye maghala haijanunuliwa, hali ni mbaya sana. Tumbaku inalimwa Katavi, Tabora, Ruvuma pamoja na maeneo mengine mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao lingine ndiyo hili la mahindi. Kule kwetu Mkoa wa Songwe mwaka mmoja na nusu uliopita tuliuza debe moja la mahindi Sh.20,000. Hivi navyozungumza na wewe debe la mahindi linauzwa Sh.3,000, kutoka Sh.20,000 limefika Sh.3,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazao ni mengi yenye changamoto, nenda kwenye kahawa hali ni mbaya, nenda kwenye ufuta, tuliuza Sh.3,000 leo ni Sh.1,000 na kitu . Kwa hiyo, hapa Serikali ya Awamu ya Tano ndiyo mliosababisha matatizo haya na mimi naamini mwarobaini wa haya ni
Serikali hii kuweza kupisha ili Serikali mbadala iweze kuingia na iweze kushika dola kuwatumikia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la pembejeo. Bei ya pembejeo ya mbolea imekuwa ghali sana. Hivi navyozungumza, Mkoa wa Songwe DAP inauzwa Sh.59,000, Urea inauzwa Sh.55,000 lakini bei elekezi ya Serikali mwaka jana, tuliambiwa Mkoa wa Songwe tungeuza Urea kwa Sh.41,500. Kutoka Sh.41,500 leo ni Sh.55,000.

TAARIFA . . .

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba umeniamuru nifute, nitafuta kwa sababu umeniamba nifute. Hata hivyo, naomba nimwambie tu ndugu yangu Mheshimiwa Mapunda kwamba kuna kitu kinaitwa Tatu Mzuka. Sasa ikiwezekana kama ingeweza kumpendeza waambie hata Vodacom wakafute neno Tatu Mzuka na inawezekana hajajua maana ya neno hili. Kwa hiyo, nimeshafuta kwa sababu umeniambia nifute lakini akaangalie maana ya neno hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumzia bei ya pembejeo, kwa mfano, mbolea kuwa ghali sana. Serikali imeweza kutoa bei elekezi kwenye mbolea ya Urea na DAP lakini bei hiyo elekezi haijafuatwa. Tunasema kwamba DAP kwa Mkoa wa Songwe na maeneo mengine iuzwe Sh.54,000 leo inauzwa Sh.59,000. Mbolea ya Urea kutoka Sh.41,500 leo inauzwa Sh.55,000. Mimi naona muarobaini wa suala hili ni kujenga viwanda vyetu, tuache sasa kuagiza mbolea na hapa ndipo tutakapoepukana na matatizo hayo. Tutakuja na mambo mengi sana, tutakuja na mikakati mingi sana lakini bila kujenga viwanda vyetu vya mbolea; kulikuwa na mkakati wa kujenga Kiwanda cha Mbolea kule Lindi kule Kuisni, kiwanda kile kimefikia wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la Taifa letu ni vipaumbele. Tunasema kwamba tunataka kuboresha kilimo tunapeleka pesa kwenda kununua Bombardier, fedha hizi tungeweza kuwekeza kwenye viwanda vya mbolea. Tunajua kwamba bila kuanzisha viwanda vya mbolea, bila kuboresha kilimo hata viwanda vingine vitayumba kwa sababu malighafi ya viwanda vingine zaidi ya asilimia 70 inategemea kwenye kilimo. Nashauri tuanzishe viwanda vyetu vya mbolea kama nchi nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu uchache au uhaba wa rasilimali watu kwenye sekta ya kilimo. Kwa utafiti walioufaya ANSAF mwaka 2013 watumishi wanaohitajika kwenye sekta ya kilimo ni 19,228, watumishi waliopo ni 8,756.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba sasa nami niweze kuchangia Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na hoja ya kwanza ambayo wapo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wameigusia kidogo nami naomba nianze nayo hiyo, kuhusu hii bajeti ya mwaka 2018/2019 ambayo naona kwangu imepuuza sana maslahi ya watumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi wa umma katika Taifa hili tangu Serikali hii ya Awamu ya Tano imeingia madarakani bajeti zake zote, kuanzia bajeti ya mwaka 2015/2016 ambayo ilikuwa bajeti ya kwanza, bajeti ya 2016/ 2017, bajeti ya 2017/2018 ambayo ndiyo inaisha siku chache zijazo, imepuuza maslahi ya watumishi wa umma. Hakuna nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma. Mishahara ambayo watumishi wa umma wanapokea kwa mara ya mwisho iliongezwa mwaka 2014, ni mishahara ambayo Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliiacha hadi watumishi wa umma wanapokea mishahara hiyo, hapajawahi kuwa na nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunafahamu kwamba gharama za maisha zinazidi kupanda, zinazidi kuongezeka. Mwaka 2015 ukiuliza bei ya sukari ilikuwa shilingi ngapi ilikuwa bei ya chini Sh.2,000, lakini leo maeneo mengine hadi zaidi ya shilingi elfu tatu na kitu. Huku ni kuwakosea sana watumishi wa umma kwa sababu gharama za maisha zinaongezeka lakini mishahara yao ni ileile ambayo Awamu ya Nne iliiacha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti haijapunguza kodi kwa watumishi wa umma. Tulitegemea kwamba bajeti hii ingekuwa ni msaada kwa watumishi wa umma ingeweza kupunguza kodi, haijazungumza lolote lile, huku ni kuwapuuza watumishi wa umma. Ikumbukwe kwamba wakati wa kampeni viongozi mbalimbali walikuwa wanaomba kura na Viongozi wa Serikali hii ya Awamu ya Tano na wengine walikuwa wanapiga push up majukwaani wakiomba kura, leo watumishi wa umma wamepuuzwa, wamesahaulika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nasikia ilipokuwa siku ya Mei Mosi pale Iringa, Mheshimiwa Rais anasema hajawahi kuzungumzia popote pale kuhusu kuongeza mishahara kwa watumishi wa umma wakati mwaka jana Mei Mosi kule Moshi - Kilimanjaro alisema mwaka unaofuata kwa maana ya mwaka huu, angeweza kuongeza mishahara kwa watumishi wa umma lakini mwaka huu akiwa Mei Mosi amesema kwamba hakuwahi kuzungumza popote pale kuhusu kuongeza mishahara. Hii siyo sahihi, huku ni kuwapuuza watumishi wa umma...

T A A R I F A . . .

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki nibishane sana na Kiti chako, lakini ukweli unajulikana, Watanzania wanajua ukweli jinsi ulivyo au uko wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe Mosi Februari, 2016, watumishi waliandikiwa barua za kupandishwa vyeo au kupandishwa madaraja, tarehe Mosi Februari, 2016. Tarehe Mosi Novemba, 2017 barua hizi zikafutwa, yaani mwaka moja baadaye barua za watumishi kupandishwa madaraja au vyeo zikafutwa. Hili jambo ni kuwaumiza watumishi kweli, hili jambo halikubaliki hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtumishi ameandikiwa barua ya kupandishwa cheo au kupandishwa daraja, mwaka mmoja baadaye barua inaandikwa nyingine ya kufuta cheo chake. Mwaka huo 2016 kuna watumishi walistaafu na waliondoka na barua ambayo imeshaandikwa mwaka huo na tunajua kabisa kwamba pensheni ya mtumishi wa umma wanai-calculate kulingana na mshahara wake wa mwisho au daraja lake la mwisho, leo huyo mtumishi ameshastaafu yuko nyumbani inakuja kuandikwa barua nyuma kwamba tumeshafuta. Hii siyo sahihi kabisa na haikubaliki kabisa kuwafanyia Watanzania ambao ni wazalendo katika Taifa hili na wanaofanya kazi ngumu sana katika mazingira magumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo watumishi ambao wamestaafu tangu mwaka 2015 hawajalipwa mafao yao hadi leo tunavyozungumza. Mwaka 2015 hawajalipwa pensheni yao, mwaka 2016 hawajalipwa, mwaka 2017 hawajalipwa, hii ni 2018 bado sioni kwenye bajeti hii kama kuna matumaini kwa watumishi hawa ambao wamelitumikia Taifa hili kwa uzalendo na kwa uadilifu wa hali ya juu sana. Namshauri Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mpango, Watumishi wa Umma ni vizuri wale waliostaafu walipwe sasa mafao yao, walipwe fedha zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu kilimo. Bajeti hii ni ndogo, lakini bajeti ya Wizara ya Kilimo imetengewa asilimia 0.52 ya bajeti yote. Tukumbuke Maputo Declaration na baadaye Malabo Declaration, viongozi wa Afrika wote walishauriwa kwamba angalau bajeti zao asilimia 10 iende kwenye bajeti ya kilimo, leo Bunge letu hili Serikali imekuja na 0.52 tunakwenda kwenye nchi ya viwanda ambayo naona haitawezekana kwa sababu bajeti ya kilimo imekuwa ni ndogo mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mazingira haya hata kufikia nchi ya uchumi wa kati na nchi ya viwanda naona ni ndoto za Alinacha, ni ndoto za mchana kweupe. Hatutaweza kufikia kwa sababu siku njema inaonekana tangu asubuhi. Kama tumetenga asilimia 0.52 maana yake viwanda itakuwa ni ndoto, tunazungumza tusiyoweza kuyatenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la masoko ya mazao, juzi nimesikia Serikali inasema sasa tumesharuhusu mazao yauzwe popote pale. Ukweli ni kwamba wananchi wetu wengi wanaolima mazao mbalimbali, kwa mfano wakulima wanaolima mahindi, Mkoa wa Songwe wananchi waliuza debe la mahindi mwaka mmoja na nusu Sh.20,000 kwa debe moja, leo wanauza Sh.3,500 na maeneo mengine na mikoa inayolima mahindi ni mingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipata soko la mahindi nchini Kenya, baada ya kufunga mipaka kuzia mahindi yasipelekwe nje, Kenya wakaenda kununua mahindi Zambia, wameenda kununua Uganda, wananchi wetu wakakosa masoko ya mahindi. Wamenunua pembejeo kwa bei kubwa sana, hali ni mbaya kwelikweli, Serikali lazima ioneshe commitment kwamba masoko ya mazao trip hii hawatazuia tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la Serikali ya Awamu hii ya Tano imetia fora kwa kuleta Bungeni bajeti isiyotekelezeka.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba na mimi niweze kuchangia kidogo, lakini naomba nianze na suala la vitambulisho vya ujasiliamali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka labda nijue kwa sababu Serikali iko hapa, kwa sababu mchakato wa vitambulisho vya wajasiliamali halikuletwa Bungeni, tumeona Mkuu wa Nchi, Rais amewaita Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya Dar es Salaam amewapatia vitambulisho na kwenda kuvipeleka kwenye Mikoa au kwenye Wilaya ili waende kuuza shilingi 20,000/=. Sasa swali langu ambalo naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha atuambie, kitambulisho kimoja kilitengenezwa kwa shilingi ngapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ambalo nitaomba anijibu baadaye atakapokuwa anahitimisha, atuambie Mheshimiwa Rais alipokuwa anasema kuanzia wajasiliamali wa mtaji wa shilingi milioni nne kushuka chini, alikuwa anamaanisha kwamba kushuka chini hadi shilingi ngapi? Je, hata mwenye mtaji wa shilingi 500/= naye anahusika? Kwa sababu kuna akina mama ambao wanauza nyanya mafungu mawili; ana mtaji wa shilingi 1,000/= leo anaambiwa akalipe kitambulisho cha shilingi 20,000. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mama mwingine anauza nyanya chungu, ana mtaji wa shilingi 500 anaambiwa naye alipe kitambulisho cha shilingi 20,000/=. Sasa je, ilikuwa shilingi milioni nne hadi shilingi ngapi? Hapa Mheshimiwa Waziri atatuambia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ambalo naomba Mheshimiwa Waziri atuambie, je, tenda ilitangazwa ili kupata yule atakayetengeneza vitambulisho? Kama tenda hii ilitangazwa, ni nani aliyeshinda? Kama tenda haikutangazwa, tafsiri yake ni kwamba kuna makosa yanayofanyika inawezekana vitambulisho vya ujasiliamali likawa ni dili la mtu na Bunge sisi tusijetukatumika kama rubber stamp kupitisha mambo ya mtu binafsi. Kwa hiyo, tenda ilitangazwa? Nani aliyeshinda kwenye tenda hii? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine niseme tu kwamba ukweli ni kwamba sisi wote tunafahamu ukienda leo kule Mbozi kwa mfano pale Mlowo au ukaenda kule Kijijini Igambo au Hampangala akina mama wanahangaika sana. Hii imekuwa kama ni kodi ya kichwa imerudishwa. Leo mama mmoja anauza nyanya kwenye nyumba moja, anaambiwa alipe shilingi 20,000/=; baba anauza miwa, anaambiwa alipe shilingi 20,000/=, mtoto mwingine anauza bamia, alipe shilingi 20,000/=, mtoto mwingine anauza nyanya chungu shilingi 20,000/=. Nyumba moja shilingi 80,000/=. Sasa hii ni zaidi ya kodi ya kichwa. Kama Serikali imeleta kodi ya kichwa, wawaambie Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najua wewe unatoka kule Rungwe, wapo akina mama wanaohangaika. Kama leo wamerudisha kodi ya kichwa Bunge hili liwaambie kwamba kodi ya kichwa imesharudishwa na hii Wabunge hatutakuwa tayari kukubali suala hili la kodi ya kichwa kurudishwa kwa mara nyingine tena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, leo Serikali ilisema kwamba itapeleka shilingi milioni 50 kila kijiji. Badala ya kupeleka shilingi milioni 50 ya kila kijiji, imeenda kuwadai watanzania wote shilingi 20,000/=. Kwa sababu kama Serikali iliahidi shilingi milioni 50, kwa nini hazijapelekwa? Badala ya kuzipeleka, imeanza kuchukua shilingi 20,000/= kwa kila Mtanzania, kwa sababu nchi hii imewaambia hadi wapiga debe, makonda, wanaoziba pancha za baiskeli, kila mtu. Sasa hali hii ni mbaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, amezungumza dada yangu hapa Mheshimiwa Suzan Kiwanga, naomba haya maneno ya kuhusu ndugu yangu Jenerali Mabeyo Mkuu wa Majeshi, nimeyanukuu hapa; ili mkisema kwamba kama kuna ushahidi, nimeyanukuu yapo hapa na ushahidi upo. Katika baadhi ya maneno yake alisema kwamba, “ndani ya nchi yetu kwa kushirikiana na vyombo vingine, tutawalinda wananchi na mali zao, tutakabiliana na matishio ndani ya nchi yetu na sasa hivi tunaendelea kufuatilia kauli tata zinazoashiria uchochezi na machafuko ndani ya nchi yetu.” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kulinda wananchi na mali zao ni kazi ya Jeshi la Polisi, siyo kazi ya Jenerali Mabeyo. Siyo kazi yake hii. Maana yake kama anataka uteuzi kuwa IGP, atuambie ili Rais amwondoe kwenye nafasi yake… (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: …ya Mkuu wa Majeshi ampeleke kuwa IGP. Maana yake hii siyo kazi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yeye kazi yake ni kulinda mipaka ya nchi hii. Siyo kazi hii… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikikumbusha mara nyingi sana hapa Bungeni kwa njia ya maandishi na kuhutubia kwa mdomo suala la migogoro ya mipaka kati ya Kambi ya Jeshi ya JKT iliyopo Itaka, Mbozi na wananchi wanaozunguka maeneo ya Jeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vilivyoathirika na mgogoro huu ni Itewe, Sasenga na Mboje, zaidi ya kaya 800 zimeathirika kwa kuwa wameambiwa waache maeneo yao ambayo wamekuwa wakiyatumia tangu uhuru. GN na ramani zote zinaonesha kwamba wananchi wa vijiji nilivyovitaja awali kwamba maeneo hayo ni mali yao. Naomba Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na JKT ashughulikie jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba nami niweze kuchangia kwenye hii Wizara ya Mambo ya Ndani. Nimesikiliza karibu wazungumzaji wote, Wabunge wote wa pande zote mbili kwa maana ya Wabunge wa Chama cha Mapinduzi ambao ndiyo wengi, lakini pia na Wabunge wa CHADEMA na CUF na wengine waliochangia wanazungumzia sana suala la maslahi kwa maaskari wetu kwa maana ya Polisi, Zima Moto, Magereza na Uhamiaji, wamezungumza vizuri sana.

Mheshimiwa Spika, niwapongeze Wabunge wote kwa jinsi walivyowapigania maaskari wetu kwa maana ya kutaka kuongeza mishahara. Siyo jambo baya, lakini nakuwa na hofu kidogo na hofu yangu hii labda naomba inawezekana ikaondolewa na Bunge hili kupitia kiti chako kwa sababu wakati mwingine haitakiwi tuwapende maaskari kwa maneno tu, kwa kuzungumza tu, leo ndiyo siku tunayojadili bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani, na leo hapa inaonekana fedha zinazoombwa ni bilioni 921.2.

Mheshimiwa Spika, wakati wa kujadili bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani, pamoja na mambo mengine Wabunge kazi kubwa inatakiwa pia tujadili namna ya kuongeza mishahara ya maaskari wetu. Nashauri, kama kweli tunayozungumza kwamba tunawapenda maaskari na Wabunge wa Chama cha Mapinduzi ndiyo wengi zaidi na ndiyo wanaweza wakapitisha akidi, hebu tufanye maamuzi hapa leo hii kwamba maaskari wetu waongezwe mishahara leo na mishahara hiyo angalau ianzie shilingi milioni mbili kwa askari mmoja na kuendelea kima cha chini na baada ya hapo kila askari apewe angalau gari nzuri ya kutembelea, kila askari apewe nyumba bora na baada ya hapo mambo yaweze kwenda vizuri kwa Jeshi la Polisi.(Makofi)

MBUNGE FULANI: Siyo kwa maneno.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, tusiende kwa maneno.

SPIKA: Mheshimiwa Haonga, kama kweli husemi uongo kwa nini hukuleta hoja mahsusi kwa ajili hiyo. Unajua kabisa kwamba hayo unayoyasema Kanuni hatuwezi kuyafanyia kazi, unajua kabisa. Kwa hiyo kwa nini hukuleta hoja mahsusi ukajenga hoja kwa ajili ya jambo hilo.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, mimi najua, wewe ni mzoefu sana na Bunge hili unaweza ukatuongoza vizuri, kwa sababu jambo lenyewe lina maslahi mapana ya maaskari wetu tukalijadili hapa, kwa sababu CCM ni wengi tuongeze maaskari wetu mishahara milioni mbili mbili wapate magari, wapate fedha kwa sababu wao ni wengi zaidi. Kwa hiyo naomba… (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa cheap politics haikusaidii, lazima ufuate Kanuni za Bunge. Haya nipe Kanuni ya kuweza kufanya hilo unalolisema maana yake unawadanganya askari nchi nzima kwamba Bunge hili linaweza hilo unalolisema, instantly nipe kuhusu utaratibu sasa. Nifungulie ni mahali gani!

MBUNGE FULANI: Ipo, kuna page inayozungumzia mishahara.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, with due respect, naomba niseme kwamba, tunapokuwa tunaijadili bajeti, bajeti hii hapa tunaweza tunakafanya…

SPIKA: Nimekwambia nipe Kanuni gani.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Tunaweza tukafumua bajeti, tukaifumua then baada ya hapo tukajadili kuboresha maslahi ya maaskari wetu.

SPIKA: Mheshimiwa Haonga kaa chini! Kaa chini, unachofanya ni uchochezi tu. Taratibu za Kibunge zinafahamika, kama kweli una nia hiyo ungeleta katika utaratibu wa kawaida. Tunazungumza habari ya jeshi hapa, unachochea wanajeshi, ilete katika utaratibu wa kawaida, kama kweli wewe ni Mbunge serious ili lifanyiwe kazi. Pita kwenye Kamati ya Bajeti kule na kadhalika, maana yake mnavyosema namna hii mnawafanya watu waamini kwamba Wabunge hawa hawawatakii mema askari, hivi na hivi, kitu ambacho si kweli hata kidogo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia hotuba ya Wizara ya Nishati. Awali ya yote nitambue changamoto nyingi zinazoikabili Wizara hii ya Nishati japo Serikali kupitia Waziri na Naibu Waziri watazipunguza kama siyo kuzimaliza kabisa. Vivyo hivyo naamini document niliyompatia Waziri wa Nishati juzi tarehe 27 Mei, 2019 inayohusu tatizo la umeme Mtaa wa Shanko, Kata ya Vwawa itapatiwa ufumbuzi kwa kuwa eneo hili la Shanko limekuwa kama Kisiwa maana limezungukwa na umeme lakini lenyewe halina umeme.

Mheshimiwa Spika, eneo hili upande mmoja kuna kilomita mbili tu toka sehemu ya umeme na upande mwingine kilomita nne, hivyo Serikali ione namna ya kuwasaidia wananchi hawa.

Mheshimiwa Spika, mwisho japo siyo kwa umuhimu, naomba Serikali iwakumbuke wananchi wa Kata za Mara na Magamba Jimbo la Mbozi, kata hizi hazina umeme kabisa kijiji hata kimoja.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. nami naomba kuchangia hii Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Leo nitakuwa nachangia pole pole sana lakini nitamwomba pia Mawaziri watakapokuwa wanahitimisha, nao wajibu pole pole wala wasi-panic na wala wasiwe na mpango wa kuvua nguo kama Waziri mmoja alivyosema atavua nguo. Naamini watajibu vizuri. Nataka twende vizuri kabisa. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na hoja ya kwanza kamba wanafunzi wanaohitimu darasa la saba kila mwaka, kwa takwimu ambazo tunazo wanakadiriwa kuwa milioni moja, lakini wanaojiunga kidato cha kwanza kwa maana ya shule za Serikali na shule za private wanakadiriwa kuwa 300,000 tu. Wanafunzi 700,000 na kitu inaonekana wanabaki nje, hawako private wala Government.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapozungumzia wanafunzi 700,000 ni wengi sana na kwa lugha nyepesi uchukulie ule uwanja wa Taifa ambao unajaa watu 60,000 mara 12 hawa watu wote wanabaki nje, hatujui wanakokwenda ni wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo inawezekana na inajulikana kabisa kwamba watoto wanaohitimu darasa la saba wengi wao wana umri mdogo sana. Wengi ni chini ya miaka 14, wengine 12, 13 wakizidi sana ni miaka 14, lakini hawa wengi wanabaki nje kama 700,000 na kitu hivi. Sasa kwa nini Serikali isitafute utaratibu wa hawa angalau waanze kurudia mtihani kwa utaratibu maalum tu, ambao ni maalum kabisa, kwamba waruhusiwe kurudia mtihani wa darasa la saba?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini hata hapa wako Wabunge wengi, hata baadhi ya Mawaziri ambao walirudia mtihani wa darasa la saba kwa majina ya watu wengine. Hatuwezi kuwataja majina, lakini wapo kwa utaratibu ambao siyo maalum. Sasa kwa nini Serikali isihalalishe suala hili liwe ni suala ambalo ni maalum kabisa kabisa ili kusudi wanafunzi hawa wengi wasibaki mtaani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunahangaika, kwa mfano, wapo baadhi ya makundi yanaibuka nchini tunasikia panya road, sijui nani; ni watoto wadogo sana hawa. Sasa kwa nini Serikali isianzishe utaratibu ambao ni maalum waweze kurudia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, kwa sababu idadi hii ni kubwa sana, kwa nini Serikali isianzishe utaratibu waende kwenye Vyuo vya VETA kupata mafunzo ya ufundi umeme, ushonaji na mafunzo mengine ili Serikali iweze kutoa mikopo kwa wanafunzi hawa kama ambavyo inatoa mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu? Kwa nini wasifanye hivyo? Kwa sababu tunaamini kwamba vyuo vyetu vya VETA viko vingi sana nchini, kwa hiyo, wanafunzi hawa wanaomaliza darasa la saba wanaweza wakapelekwa huko VETA Serikali ikawapa mikopo na wakalipa, kwa sababu mkopo unalipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iweze kuliangalia hili. Mheshimiwa Ndalichako nimekwambia kwamba leo nitakushauri polepole na baadaye ujibu vizuri polepole kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu mishahara pamoja na motisha kwa Wahadhiri pamoja na Wakufunzi wa Vyuo. Juzi wakati nachangia Wizara ya Mambo ya Ndani nilizungumza na leo pia naomba niseme tu kwamba bado Waheshimiwa Wabunge tusiwe na utamaduni wa kulalamika. Yaani wananchi wametupa kura, hiki ndiyo chombo kinachofanya maamuzi, linapokuja suala la kujadili bajeti ya Wizara fulani Wabunge huwa tunajifanya wazalendo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa nini Wizara hii ya Elimu pamoja na kwamba Wabunge wengine wamechangia na Wabunge wa Chama cha Mapinduzi na ninyi mko wengi sana, anzisheni utaratibu mzuri tu tuweze kuongeza mishahara kwa Wahadhiri wetu. Sisi upande huu tutawaunga mkono. Ninyi ndio wengi. Utaratibu, wakati mwingine Mabunge huko nyuma wamewahi kurudisha bajeti isipitishwe. Bunge limewahi kuamua miaka ya nyuma huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unafahamu wakati huu tunapozungumzia bajeti ya Wizara ya Elimu tunazungumzia makusanyo pamoja na matumizi. Kwa hiyo, tunaweza ndio wakati muafaka huu. Wabunge wa Chama cha Mapinduzi mko wengi sana, ninyi ndio mnaopitisha akidi ya kila kitu. Kwa hiyo, hili pia tunaweza tukalijadili, sisi wa upande huu hatuna shida. Hata nikiwauliza Wabunge wa upande huu nyoosheni mikono ambao mnasema tuongeze mishahara kwa Wahadhiri; wengi sana.

(Hapa baadhi ya Wabunge walinyoosha mikono)

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Unaona! Wako wengi sana; lakini nikisema nyoosheni kule, hata mmoja hatanyoosha. Kwa hiyo, niseme tu kwamba hili liko mikononi mwa Wabunge wa CCM na mishahara ya Wahadhiri iweze kuongezwa pamoja na stahiki zao mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ninapozungumza na wewe Wahadhiri kwa taarifa tulizozipata, wameanzisha mgomo wa chini chini, kwa sababu hata zile fedha za nyumba ambayo ni stahiki yao hazipelekwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tutaenda kupata wanafunzi wa aina gani? Mhadhiri anaamua kumkamata mwanafunzi...

MWENYEKITI: Acha uchochezi wewe, Mheshimiwa! (Kicheko)

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mhadhiri wa leo anaenda kumkamata mwanafunzi wakati mwingine kwa sababu tu yule mtu ana stress, ana msongo wa mawazo kwa sababu hela za nyumba zao hizo hajapewa na ni stahiki yao. Sasa mambo kama hayo Serikali iweze kuangalia. Shida ni nini? Wapeni hela zao, waongezeni mishahara, boresheni mambo yao yaweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni suala la utegemezi wa miradi ya maendeleo kwenye fedha za wahisani. Imekuwa ni kawaida, Wizara hii ya Elimu kuomba fedha nyingi kutoka kwa wahisani kuliko fedha zaa ndani. Natoa mfano mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2018/2019 bajeti hii ambayo tunaimaliza sasa, yaani fedha za maendeleo kati ya shilingi bilioni 502 fedha ambazo tulikuwa tumeomba kwa wahisani ni shilingi bilioni 311 sawa na asilimia 62. Hizo zilikuwa ni fedha za nje. Fedha za ndani zilikuwa ni asilimia 38 tu, ndio zilikuwa za kwetu za ndani. Fedha hizo za wahisani ambazo zilikuja hadi sasa ni shilingi bilioni 111 kati ya shilingi bilioni 311.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niulize. Kwa mfano, unapoenda kuomba fedha aidha kwa mtu mwingine, unataka labda kujenga nyumba au kufanya jambo lolote la maendeleo, unaomba nyingi au unaomba kidogo, au wewe unazo nyingi unatakiwa uongezewe? Sasa Serikali yetu tunaomba kwa wahisani shlingi bilioni 311 sawa na asilimia 62, halafu sisi eti asilimia 38. Hii ni aibu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu ndiyo tunaenda kuonesha utegemezi wa hali ya juu sana. Mwaka huu katika fedha za maendeleo shilingi bilioni 413, tunaomba kwa wahisani shilingi bilioni 279 sawa na asilimia 68. Fedha za ndani mwaka huu ni asilimia 32 tu, lakini wakati huo huo hawa wahisani ndio mmekuwa mkiwaita mabeberu. Yaani mnapoomba fedha mnasema ni wahisani, wanapowashauri namna ya kuendesha nchi na mambo kwenda vizuri, mambo demokrasia, mnasema mabeberu. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri, ukiangalia kule nyuma kabisa ukurasa wa mwisho kabisa kule amewashukuru hawa ambao tunawaita wahisani hawa, lakini wakati mwingine mnawaita mabeberu. Inabidi mwaombe msamaha. Kwa mfano, Mheshimiwa Waziri anasema, napenda pia kushukuru baadhi ya mashirika yaliyochangia kufanikisha Programu za Elimu, Sayansi na Teknolojia ambayo ni pamoja na Benki ya Dunia, DFID, SIDA, Umoja wa Nchi za Ulaya, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Jumuiya ya Madola, Global Partnership in education, United Nations, International children’s, (UNICEF)...

WABUNGE FULANI: Mabeberu.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani pale mmetaja wengi, UNESCO, USAID...

WABUNGE FULANI: Mabeberu.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Sasa wote hawa wanapokuwa wanatuchangia tunasema ni wahisani…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, bado dakika mbili.

MWENYEKITI: Hapana. Ahsante sana.
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya pamoja ya ziada ya Nagoya – Kuala Lumpur kuhusu Uwajibikaji Kisheria na Fidia kwa Madhara yanayoweza kutokea kutokana na matumizi ya Bioteknolojia ya Kisasa katika Kutekeleza Itifaki ya Cartagena (Nagoya – Kuala Lumpur Supplementary Protocol on Liability and Redress on Cartagena Protocol on Biosafety) pamoja na Azimio la Kuridhia Itifaki ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika kuhusu Kulinda Haki Miliki za Wagunduzi wa aina mpya za Mbegu za Mimea. (Protocal for Protection of New Varieties of Plants (Plant Breeder’s Rights) in The Southern African Development Community – SADC) pamoja na Azimio la Kuridhia Mkataba wa Marrakesh wa mwaka 2013 unaowezesha upatikanaji wa kazi zilizochapishwa kwa watu wasioona, wenye uoni hafifu au ulemavu unaomfanya mtu kushindwa kusoma (The Marrakesh Treaty to Facilitate Access to Published Work For Persons Who Are Blind, Visually Impaired or Otherwise Print Disabled)
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami naomba kuchangia na nitajikita zaidi kwenye hii Itifaki ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za SADC kuhusu Kulinda Hakimiliki za Wagunduzi wa aina mpya za Mbegu za Mimea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni kuhusu asilimia moja ya pato ghafi la Taifa kutopelekwa kwenye utafiti. Ni kwa muda mrefu sana Serikali yetu haipeleki asilimia moja ya pato ghafi la Taifa kwenye mambo ya utafiti na leo tunaenda kuridhia Itifaki hii, kama fedha hazitapelekwa tafsiri yake ni kwamba tunaenda kuwanufaisha wale ambao watakuwa tayari kupeleka fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba nchi kama Afrika Kusini imeendelea sana na iko serious sana kwenye mambo ya utafiti, leo tunaenda kushindana nao hao kwenye suala hili lakini kwa sababu wao wako serious na sisi hatujawahi kupelekea fedha huko, Serikali ituambie baada ya kupitisha Itifaki hii watakuwa tayari sasa kuanza kupeleka fedha za utafiti ili tutakachopitisha leo hapa au tutaporidhia Itifaki hii isije mwisho wa siku tukashindwa kuwasaidia watafiti wetu. Kwa hiyo, nadhani hili ni jambo muhimu sana isije kuwa tunasindika wenzetu ambao tuko nao lakini wao wamejiandaa kuliko sisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusu fedha za maendeleo ambazo mara nyingi hapa Bungeni tumekuwa tukizipitisha au kuidhinisha lakini fedha hizi hazitolewi. Kwa mfano, leo tunapozungumzia suala hili la Hakimiliki za Wagunduzi wa aina mpya za mbegu maana yake hizi ni fedha za maendeleo na tunajua kwenye fedha za maendeleo Serikali hii ya Awamu ya Tano naona haijajipanga kabisa kwa sababu mara nyingi sana imekuwa ikisuasua kupeleka fedha kama Bunge linavyoidhinisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mwaka 2016/ 2017, zile fedha za maendeleo zilizokuwa zimeidhinishwa na Bunge hili shilingi bilioni 100.527 zilipelekwa shilingi bilioni 2.2. Sasa kama zilipelekwa fedha hizo na hapa tunapitisha Itifaki hii, je, utekelezaji wa haya mambo inakuwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2017/2018 tulipeleka asilimia 11 tu ya fedha za maendeleo ambazo ziliidhinishwa na Bunge hili. Sasa leo tunapitisha Itifaki hii na kwenye Itifaki hapa tunaambiwa bajeti lazima itatumika, sasa inakuwaje kama hatutatenga fedha za maendeleo kwa ajili ya kwenda kutekeleza mambo haya ambayo tunaenda kuyapanga leo? Kwa hiyo, niseme tu kwamba kama Serikali haijajipanga kwenye mambo kama haya ni bora tukawa na subira ili mwisho wa siku tujipange vizuri na baadaye tuangalie namna ya kuweza kufanya lakini kama watatuhakikishia na Mheshimiwa Waziri yuko hapa kwamba fedha za maendeleo zitatolewa vizuri basi hii Itifaki itatekelezwa lakini kama hazitatolewa kama ambavyo miaka ya nyuma zimekuwa hazitolewi, nadhani tutaenda kugonga mwamba na hatutafanikiwa kwenye suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni suala la mbegu za asili. Serikali ituambie wamepanga utaratibu gani kuweza kulinda mbegu za asili. Nafahamu kwamba nchi yetu tumekuwa na mbegu za asili nyingi sana na nyingine zimeanza kupotea polepole. Tulikuwa na mchele mzuri kule Kyela na zamani mnakumbuka ulikuwa unanukia, ule wa Kamsamba leo Serikali imejipangaje kutunza mbegu hizi maana zinaingia mbegu hizo mpya na za kwetu za asili zinapotea.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia nitagusa baadhi ya maeneo kwa mfano nitagusa eneo la kwanza linalohusu zao la Kahawa, pia eneo la pili nitagusa Korosho na kama muda utaruhusu pia nitazungumzia suala la Maafisa Ugani.

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie kwanza suala la zao la Kahawa, ni kwa muda mrefu sasa bei ya kahawa imekuwa ikishuka miaka hadi miaka na msimu huu kahawa ndio imeendelea kushuka imekuwa bei ndogo kuliko wakati mwingine wowote ule.

Mheshimiwa Spika, jambo ambalo naomba nijiulize kidogo na naomba labda tusaidiane kidogo Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atusaidie, kwa nini nchi ambazo zinatuzunguka wanaolima kahawa sawa na sisi kwa mfano nchi kama Uganda pamoja na nchi nyingine ambazo zinalima kahawa Kenya na nyingine kwa nini hawalalamiki sana kuhusu suala la bei ndogo ya kahawa? Na ushahidi unaonyesha kwamba hata kahawa ya Tanzania inatoroshwa kupeleka Uganda kwa maana ya Kahawa ya Kagera inapelekwa Uganda, lakini pia kahawa kutoka Kigoma inatoroshwa na maeneo mengine ya mpakani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kwamba hawa wenzetu kwa sababu tunaamini kahawa inauzwa tuna soko la dunia je wao soko lao liko wapi? Kwa nini kahawa yetu sisi imeendelea kushuka wakati soko la dunia ni moja? Kwa kweli nadhani shida kubwa hapa nayoiona shida kubwa sio soko la dunia hiyo sio shida kubwa, shida kubwa ni utashi wa viongozi wa Serikali hii ya Awamu ya Tano ambao wamepewa dhamana kutuongoza ndio tatizo linaanzia hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo kwa mfano ukiangalia kuna suala la Uganda pale wao hawana kitu kinaitwa vyama vya msingi vya ushirika hawana lakini bei ya kahawa ni nzuri, hawana kitu kinachoitwa hizi tozo karibu zote zimeshaondolewa imebaki tozo moja tu yule anayekuja kununua kahawa analipa ile tozo ya mwisho anapokuwa anasafirisha kahawa anapoondoka, sasa sisi bado kwenye kahawa kuna tozo nyingi sana hili ni tatizo kubwa sana, sasa huyu mkulima wa kahawa kama angeweza kuachwa kwa mfano tukamfutia tozo zote alipe kodi anaponunua saruji kwa sababu ataenda kujenga, alipe kodi anapoenda kununua bati kwa sababu ataenda kujenga, huko ndiko ambako sasa tungeweza kupata kodi kwa njia kama hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nashauri Wizara iangalie namna ya kuondoa tozo na kodi zote kwenye zao la kahawa kama wanavyofanya nchi ya jirani ya Uganda ili mwisho wa siku nchi yetu tuweze kuwasaidia wakulima wa kahawa. Hata eneo tunalolima kahawa ni eneo kubwa sana lakini tija ni kidogo, leo tunaambiwa kwenye takwimu hapa kwamba msimu tulipata zaidi ya tani 60,000 na miaka ya nyuma ilikuwa tani 40 na kidogo 40,000 nakadhalika.

Mheshimiwa Spika, lakini ukiangalia Uganda wanalima zaidi ya tani wananapata zaidi ya tani 300,000 wanapolima mara moja zaidi ya 300,000 tunaingia mara sita kwa Uganda, kwa hiyo tija kwenye zao la kahawa pia hapa kuna shida, tuna mashamba makubwa lakini tija ni ndogo. Kwa hiyo, ni vizuri tukatafuta muarobaini kwa nini wenzetu ambao wanalima kahawa wana mashamba madogo kuliko ya kwetu lakini wanapata kahawa nyingi kuliko sisi shida iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba nizungume jambo la pili ambalo ni jambo la kuhusu suala la korosho. Aliyevuruga suala la korosho au biashara ya korosho huyu tumchukulie kama alivyokuwa wahujumu uchumi wengine, kwa sababu leo ukiangalia zao la korosho kwa takwimu ambazo tunazo mwaka jana korosho fedha za kigeni tuliingiza dola za Marekani milioni 367 ukichukua zao lililofuatia lilikuwa ni Tumbaku ambalo lilikuwa ni dola za Marekani milioni 222, na kahawa ilikuwa dola za Marekani milioni 134, lakini ukichukua mazao yote kama Karafuu, Katani, Chai, Pamba unaona mazao yote haya ukijumlisha bado hayawezi kufikia kwenye zao la korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa leo tunaweka watu kwenye magereza zetu tumewajaza watu ambao wanasema ni wahujumu uchumi kwa vitu vidogo lakini kuna watu waliochezea zao la korosho tunacheka nao, tunakula nao, tunakunywa nao, tunawaangalia. Leo tulitegemea kwamba watu hawa wangekuwa magereza lakini tunacheka nao tunawaangalia tu. Sio mtabiri wala sio Nabii kama Mbunge wa Arusha Mjini Mheshimiwa Lema lakini Rais ajaye sijui atakuwa nani aidha upande wa CCM au CHADEMA au CUF ninaamini atakuja kufanya jambo kwa sababu naamini kwa upande huu kipindi hiki ni kwamba ni nani amfunge paka kengele inawezekana ndio shida inaanzia hapo. Lakini kwa hawa wanaotuingizia hasara Taifa letu kwa kweli lazima wachukuliwe hatua kama wahujumu uchumi wengine ambavyo wamekuwa wakifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo zao hili tumepoteza export levy mwaka jana ilikuwa zaidi ya bilioni 300 export levy leo hatujapata hata shilingi hatujapata kwenye export levy kwa sababu ya watu wachache tu walioamua kutufanyia mambo ambayo kwa kweli sio mazuri hata kidogo. Leo halmashauri zinazolima korosho Tandahimba maeneo yote yanayolima korosho hawajapata ushuru unaotokana na zao la korosho. Leo halmashauri hizi zinaendaje kuendesha mambo yao? Kwa sababu kuna watumishi ambao wanaajiriwa na halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo tunaambiwa kwamba hawatapewa fedha kwa maana ya ushuru wa korosho maana yake hawa watu wameporwa ushuru wa mabango, wameporwa ushuru wa majengo, leo unaenda kuwapora na ushuru wa korosho tafsiri yake ni kwamba hizi halmashauri zinaenda kufa, sasa kama zinaenda kufa mwisho wa siku itakuwa sasa mwisho wataenda kuzifuta tu kwa sababu sasa hivi shida kuendesha mambo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo bado nisisitize kuna hana najua Mheshimiwa Waziri wewe ni mgeni lakini kuna haja ya waliohusika wote waweze kufunguliwa kesi za uhujumu uchumi ili mwisho wa siku tuweze kupeana adabu na mwisho wa siku mambo yaweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ambalo noamba nizungumzie kidogo ni suala la kuhusu Maafisa Ugani, kwa takwimu tulizo nazo Tanzania tuna vijiji zaidi ya 15,000 vijiji tulivyokuwa navyo lakini Maafisa Ugani ambao tunao ni 7,974. Juzi hapa uliongea kwamba unapozungumzia kwa mfano suala la uchumi wa viwanda huwezi ukaiacha kwa mfano Bandari ile ya Bagamoyo ukaiacha ni sawa na ng’ombe anakuwa nyuma halafu mkokoteni unakuwa mbele, wakati ng’ombe anatakiwa akae mbele avute mkokoteni. (Makofi)

Sasa leo kama inafika mahali Maafisa Ugani wako wachache namna hii ambao ni 7,964 tu, lakini na vijiji zaidi ya elfu 15 ni sawasawa na mfano uliotoa ule kwamba, unapeleka mkokoteni mbele halafu ng’ombe wanaovuta wanakaa nyuma. Sasa jambo hili Mheshimiwa Waziri atueleze wakati atakapokuwa anahitimisha, je, wana mpango gani kuhusu kuajiri Maafisa Ugani? Kwa sababu, hatuwezi Maafisa Ugani ni wachache. Hata hawa waliopo utakuta yuko mmoja, huyohuyo wanampa kazi ya utendaji, mara watampa sijui kazi ya nini; hawa ni wacache, lakini wanapewa na majukumu mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, hawa Maafisa Ugani waliopo tunaomba waweze kuajiriwa na wengine ili wawe wengi zaidi, lakini pia waweze kupewa motisha. Leo maeneo mengine ya nchi ambazo zimeendelea huko ambazo ziko serious kwenye masuala ya kilimo Maafisa Ugani hawa amepewa angalau mtu anapewa, hata kama hawezi kupewa gari, basi mpe hata pikipiki ili aweze kufanya kazi kwenye mazingira mazuri. Maana kilimo chetu sasa tunakitegemea kwamba, inapofika mwaka 2025 twende kwenye uchumi wa kati, hatuwezi kuwa na uchumi wa kati ikiwa Maafisa Ugani ni wachache namna hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine kwenye kilimo ambalo naomba nigusie, ni kilimo cha umwagiliaji. Mwaka jana, bajeti ambayo tunaenda kuimalizia sasa kwenye suala la umwagiliaji, tulitenga kama bilioni 24 hivi, lakini mwaka huu tumetenga bilioni nane tu; tunawezaje kuwa na nchi ya viwanda kama tumetenga bilioni nane kwenye umwagiliaji? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumza)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Haonga.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kuunga mkono hoja ya Upinzani.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2017.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Naomba niseme tu kwamba kuna usemi unaosema if we fail to plan then we plan to fail.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ambalo kwa kweli limeendelea kupigiwa kelele sana siyo tu kwamba ni Wabunge wa upande fulani, bali hata wadau ambao mmewaona tangu wamekuja ile siku ya kwanza wamepigia kelele sana kuhusu suala hili la muda mdogo kwenye hili jambo la muhimu sana katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kabisa kwamba hili jambo la Hati za Dharura ambalo hata miaka ya nyuma pia limewahi kulalamikiwa kwa muda mrefu sana na limekuja kuleta madhara, hasara zake ni kubwa mno kuliko faida ambazo tutaweza kuzipata. Kwa mfano, leo hii tungeweza tukasema kwamba tutafute case study nchi gani ambazo zimefanikiwa katika mikataba ya madini tungeenda kufanya, labda katika nchi kama Ghana, ziko nchi mbali mbali South Africa, Botswana na nchi nyingine tungetumia muda mrefu, tutume watu wetu kule waweze kuangalia namna gani nchi hizi zimeweza kunufaika hili suala halikuwa suala la muda mfupi, halikuwa ni suala la dakika mbili wala dakika tatu kama ambavyo tunakimbia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi Profesa Luoga alisema kwamba tumepewa siku Sita tu, tungekuwa tumepewa Mwezi hata mmoja, yaani walipewa siku sita kuandaa Miswada hii, wangepewa mwezi mmoja wangefanya vizuri sana, huyu ni Profesa Luoga. Alizungumza maneno haya alipokuwa anajaribu kutoa ufafanuzi kuhusu Miswada hii ambayo imeletwa. Kwa hiyo, naomba suala hili la kuharakisha mambo haya utafikiri nchi iko kwenye vita, utafikiri ni vita ya Iddi Amini na Tanzania, utafikiri ni sijui ni vita ya nini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tafadhali tujaribu kuangalia, tunazungumzia maisha ya watoto wa watoto wetu, tunazungumzia miaka 100 ijayo, miaka 200 ijayo, hatuwezi tukajadili suala la mustakabali wa Taifa letu ndani ya siku mbili, tatu tu. Leo unasema kuna wachangiaji nane na wengine wanagawana dakika mbili mbili, halafu huku wako watatu tunajadili suala kubwa kama hili. Naamini mwakani hili suala linaweza kurudi tena, kama siyo mwakani basi miaka ya hivi karibuni. Kwa hiyo, naomba tu mambo ya muhimu kama haya tujaribu angalau kuweka muda wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ziko changamoto nyingi sana za madini, kwa mfano Sheria ya Madini ya 1998 ilitamka kwamba mwenye miliki ya madini na fedha yote itokanayo na mauzo ya madini ni mwenye leseni ya kuchimba madini. Mambo yote haya unaweza ukaona kwamba changamoto zote hizi pamoja na nyingine za kutorosha madini yetu, pamoja na mrabaha kidogo yote haya tungekuwa tumepata muda mwingi wa kutosha zaidi, naamini tunaweza kuyashughulikia vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, hili suala amezungumza na mwenzangu na wengine wameongea juzi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumiliki madini kwa niaba ya Watanzania wote, amezungumza jana Mheshimiwa Lema, wamezungumza na wengine suala hili naona tu kwamba kuna sehemu tumeteleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha naamini yeye ni msomi mzuri sana, naamini kabisa kama mnakumbuka wakati wa Tume ya Warioba ile ya Katiba, Mheshimiwa Waziri yeye mwenyewe ni miongoni mwa watu waliosema kwamba Rais apunguziwe majukumu, Rais apunguziwe madaraka, Mheshimiwa Waziri leo anasema Rais amiliki madini yote ya nchi hii kwa niaba ya Watanzania wote, wakati naamini kabisa kwamba ni miongoni mwa watu waliotoa ushauri tumpunguzie Rais mamlaka kama hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ardhi inatosha, lakini ya madini tuangalie utaratibu mwingine, naamini yeye ni msomi, ni mtaalam mzuri, lakini kwenye hili Mheshimiwa Waziri

ameteleza kabisa. Najua kabisa Mheshimiwa Waziri alipokuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amefanya mambo mazuri mengi tu, lakini baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria naona kuna vitu vinaanza kupungua.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi mle ndani Mheshimiwa Waziri anatuambia kwamba stupid, anatukana Wabunge stupid, lakini naamini kabisa mambo yote haya tukijaribu kwenda mbele yanaweza kidogo yakawa yanapunguza hata ile sifa yake nzuri tunayoijua akiwa Mwalimu wetu. Yeye ni Mwalimu wangu mimi nimesoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tunamjua uwezo wake, kwa hiyo naomba tu ajaribu kuisaidia Serikali….

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2017.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nami niweze kuchangia Muswada huu. Awali ya yote naomba niseme kwamba kumetokea sintofahamu tangu siku ya kupitisha bajeti hadi leo, jana nimesikia baadhi ya Manaibu Waziri wakiwa wanajibu maswali ya Wabunge wanasema kwamba “wewe unauliza swali na wewe, au unahitaji mradi fulani kwako? Kwa sababu ulikataa kupitisha bajeti hatutakuletea.” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lile onyo ambalo ulilitoa nadhani unavyoahirisha Bunge mchana nadhani pia ungewapelekea baadhi ya Manaibu Waziri pia maana inawahusu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kupeleka maendeleo kwenye Jimbo fulani hivi sio hisani. Kupeleka maendeleo kwenye Jimbo ni lazima, kodi zinalipwa wananchi wa Majimbo husika wanalipa kodi lazima wapelekewe huduma. Mwananchi anapokuwa ananunua sabuni, anapokuwa ananunua nguo, anapokuwa ananua bidhaa mbalimbali analipa kodi. Anapolipa kodi anategemea kodi hiyo iweze kurudi kutengeneza barabara, kodi hiyo iweze kuleta dawa hospitali, kodi hiyo iweze kufanya shughuli mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba ili mambo haya yaweze kwenda vizuri ili siku nyingine basi hizi kura tatu hii kura ya ndiyo, hapana na abstain ondoeni zote basi ibaki ya ndiyo ili muweze kwenda vizuri kama mnadhani kwamba itasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, upotoshaji huu tukiuruhusu ukaendelea, naamini kwamba kama alivyoongea Mheshimiwa Silinde tutakuwa tunaligawa Taifa, hatuwezi kufika popote pale tutaligawa Taifa hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba baada ya kuzungumza hayo wako baadhi ya Mawaziri au Manaibu Waziri kwa mfano, yuko ndugu yangu hapa Naibu Waziri kutoka kule Katavi, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji unapotoka hapa unaenda Katavi lazima upitie kwangu pale Mlowo, kama utapitia Mlowo pale kwangu maana yake mkisema kama hayo yanayozungumzwa kwamba hayatafanywa kwenye Majimbo yetu, maana yake na wewe Naibu Waziri tukuzuie usipite pale kwa sababu hiyo barabara hawatumii wa Mbozi tu, wanatumia hata ninyi Mawaziri mnapopita maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee marekebisho katika…

T A A R I F A ...

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ya ndugu yangu hapa naipokea kwa mikono yote kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sidhani kama amewatuma hao watu kuzungumza hayo maneno kwamba hawatapeleka bajeti huko, kwa sababu alichaguliwa na wananchi wa maeneo mbalimbali, hata kama kuna maeneo mengine kura hazikutosha, lakini walimchagua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuzungumza hayo, naomba niende sasa katika maeneo mengine kuhusu marekebisho katika Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura 290.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushuru wa mabango na kodi ya majengo kuchukuliwa na Serikali Kuu huku ni kwenda kuziua Halmashauri zetu. Tunaenda leo kukusanya ushuru wa majengo, tunaenda kukusanya ushuru wa mabango, leo Halmashauri zetu zitakufa kwa sababu hivi ndivyo vyanzo vya mapato kwenye Halmashauri zetu hapa nchini. Sasa kama leo tunakusanya ushuru huu Serikali Kuu inaenda kuhodhi, Halmashauri zetu kwa kweli zitakuwa katika hali mbaya sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, atakapokuwa anahitimisha Waziri wa Fedha naomba haya mambo ujaribu kuyaangalia, leo tupo hapa ndani wako wachache ambao wao wenyewe jambo likizungumzwa hata kama ni baya kwa wananchi wanapiga makofi, kesho litakapokuwa limeharibika hao hao wanakuruka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba tafadhali akili za kuambiwa changanya na za kwako, kama ni wataalam wako walikupotosha tafadhali katika hili jaribu kurekebisha, kwa sababu leo huwezi ukaenda kupora vile vyanzo vya mapato kwenye Halmashauri zetu, kwa sababu ndivyo tunavyovitegemea huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine naomba pia nizungumzie suala la kuwatambua wafanyabiashara wadogo, kuna jambo moja mmelizungumza hapa na kuna mtu mmoja hapa alikuwa anasema hapana, eti Machinga hawatalipa kodi, mnapotosha. Naomba hii hotuba ya Waziri msome ukurasa ule wa 47 inawezekana kuna wengine hawasomi . Ukurasa ule wa 47 unasema naomba nisome kidogo kwamba:

“Hatua za mapato na maboresho ya mfumo wa kodi, ada na tozo mbalimbali, hatua za kisera na kiutawala.”

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa pale kwenye hatua za kisera na kiutawala wameweka baadhi ya mambo pale kwa mfano jambo mojawapo ni kwamba kukusanya kodi kwa kutumia machine zetu (electronic machine) lakini ukisoma kipengele cha nne kinasema kwamba:

“Kuwatambua rasmi wafanyabiashara wadogo wadogo wasio rasmi na wanaofanyia biashara katika maeneo yasiyo rasmi.”

Mfano, Mama Lishe, wauzaji mitumba wadogo, wauza mazao ya kilimo wadogo kama mbogamboga, ndizi, matunda na na kadhalika, kwa kuwapatia vitambulisho maalum kwa kazi wanazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hapa tunazungumza haya mambo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapohitimisha aweze kulitolea maelezo vizuri, huu ni uwongo mchana kweupe, mnataka hawa wafanyabiashara mkishawatambua ili muweze kuanza kuwatoza kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka Mbunge mmoja wa Mwanza alikuwa analalamika, anasema kwamba Machinga wanafukuzwa na Rais akaagiza kwamba Machinga wasionewe popote pale wala wasifukuzwe, leo mnasema Machinga wasifukuzwe, mnataka muanze kuwatoza kodi. Hii ni aibu kubwa sana kwa Taifa letu ambalo lina rasilimali za kila aina, Taifa ambalo lina madini, lina Tanzanite, lina dhahabu, lina gesi, lina kila kitu, kwenda kukimbizana na ushuru wa Mama Lishe…..

T A A R I F A ...

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, huyu bwana nadhani inawezekana kabisa kwamba hayuko makini na taarifa yake naomba sasa rasmi niikate kwa sababu kuna vitu ambavyo nadhani havielewi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachokizungumza hapa ni kwamba, unapoenda kuwatoza wa machinga kodi, unapoenda kuwatoza mama lishe kodi, leo tuna madini; dhahabu, Tanzanite na juzi mmesema kuna trilioni 108, mnataka kudai hizo ndiyo sasa ziongezwe kwenye bajeti hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme badala ya kuwatoza hawa Mama Lishe, kuwatoza hawa wauza mboga mboga na matunda nendeni mkawatoze wale wanaochimba madini katika nchi yetu, wanaotorosha madini, nendeni mkawatoze wawekezaji wakubwa kwenye vitalu vya uwindaji, nendeni mkawatoze wale wakubwa ambao wamewekeza kwenye miradi mikubwa mikubwa. Naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, kama Chama cha Mapinduzi kimechoka kutawala nchi hii na mnataka 2020 muambulie zero, nendeni kwenye hili ambalo mnataka kulianzisha hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakuhakikishia kabisa Mheshimiwa Waziri kwa sababu najua na wewe pia inawezekana ni mgombea mwenzangu kwa sababu nimesikia juzi unawapongeza wananchi wa Jimbo la Buhigwe, unasema unawashukuru wananchi wa Buhigwe wakati wewe ulichaguliwa na Rais, wale wananchi unakutana nao maeneo gani mpaka unaenda kuwapongeza? Kwa hiyo, inawezekana ukawa ni mgombea na wewe kama ulivyokuwa wagombea wengine, sikukatazi wewe nenda, lakini wale wananchi kule utakachokutana nacho utakutana na wamachinga hao hao ambao umewatoza kodi, utakutana na mama lishe, utakutana na wauza mboga mboga, ndiyo wapiga kura wetu kule.

Naomba kwenye hili kama Serikali haitachukua hatua Mheshimiwa Waziri imekula kwako, hii na nina amini kabisa usifanye mchezo Jimbo si mchezo, na nina amini lakini Obama yupo makini sidhani kama ataruhusu hali hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye jambo lingine, yuko Mbunge mwenzetu humu ndani amezungumza jambo, amesema mimi nilidhani kumbe hizi kodi zitakusanywa kwenye Majiji, sijui kwenye Miji, kwenye Halmashauri haihusiki, amedanganya na kama hajadanganya basi hakuelewa vizuri, kwa sababu..

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma wa Mwaka 2017
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ninaomba na mimi niweze kuchangia muswada wa kuunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshauri Mheshimiwa Waziri, yale yote ambayo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imewasilisha ni vizuri akayachukua na akayafanyia kazi kwa sababu yana faida kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine kama ulivyotangulia kuzungumza tunapokuwa tunatunga sheria za nchi yetu, ni vizuri basi hata yale ambayo yanatoka kwa mtu ambaye ni wa upande mwingine, ili mradi tu kama yana maslahi mapana kwa Taifa letu, ni vyema tukayafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba niungane na mchangiaji Mwalimu Kasuku Bilago kuhusu ile formula kutokuwekwa kwenye muswada huu. Mara nyingi sana wote tunajua kwamba mara nyingi sana kanuni zimekuwa ni kichaka cha Serikali kujifichia. Mara nyingi sana zimekuwa ni kanuni ambazo Waziri peke yake anaenda kujifungia, anaangalia nifanye nini, nadhani siyo sahihi hata kidogo. Kwa hiyo, nashauri kama alivyotangulia kuongea mzungumzaji wa kwanza kwamba jambo hili ni vema basi, kwa maana ya formula ingeweza kuweka kwenye muswada na badala ya Waziri kwenda mwenyewe kupeleka kwenye kanuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna Mbunge ambaye anashiriki kwenye kutunga hizo kanuni. Sasa Waziri anapokuwa amekosea na yuko peke yake na ukiwa peke yako ni rahisi kukosea, kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba tu ni vizuri ingeweza kuletwa formula hapa tukajadili kwa pamoja, tujue sasa hawa wastaafu wetu watanufaika vipi tuweze kujadiliana kwa maslahi mapana ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme tu jambo lingine kwamba hata ile denominator ambayo inatumika kwa sasa ile 540 kwa 580 bado unaweza ukaona kwamba siyo nzuri kwa wastaafu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo 540 ipo tangu kipindi cha ukoloni, ni ya muda mrefu sana. Kwa hiyo, kama lengo ni kui-merge mifuko hii ili kuboresha mafao ya wastaafu, basi ingekuwa ni vema tungeboresha hata tuweke denominator ya 520. Tukiweka denominator ya 520 wastaafu wetu watanufaika vizuri, watapata pension ya kutosha na mwisho wa siku tutakuwa angalau na sisi tumeingia historia ya kutengeneza ya kwetu kuliko ile ambayo tulitengenezewa na Wakoloni miaka hiyo ambayo ni 540 ambayo siyo nzuri, inawanyonya watumishi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo, nashauri hapa Mheshimiwa Waziri katika jambo ambalo ukilifanya naamini utakuwa umetendea haki Watanzania ni pamoja na kuweka hii denominator 520 ambayo itakuwa ni jambo jema na wastaafu wetu wataenda kupata pension ya kutosha na mwisho wa siku wataishi bila stress hapo watakapokuwa wamestaafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni jambo ambalo linahusu wale watumishi ambao wako kwenye mifuko mbalimbali ya hifadhi ya jamii. Huyu Mheshimiwa Waziri anahusika na mambo ya kazi na ajira, siyo ajabu kesho na keshokutwa akaleta tatizo lingine la ajira. Kwa sababu hawa watu wameajiriwa kwenye mifuko mbalimbali, atakapokuwa ana-windup atuhakikishie hapa kwamba je, wale ambao wameajiriwa kwenye mifuko mbalimbali watachukuliwa kupelekwa kwenye mfuko mpya, hii mifuko ambayo itakuwa imeunganishwa? Kwa sababu tusipolichukulia vizuri hili, mwisho wa siku wale wote walioajiliwa watakuwa wamepoteza ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kwenye kupoteza ajira, tunaweza tukapoteza watu wengi sana. Kwa mfano, ukichukua PSPF, iko karibu kila mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ngazi ya mkoa kuna mtu mmoja anaitwa Afisa Mfawidhi, pia kuna kuna mwingine anaitwa Afisa Mfawidhi Msaidizi na kuna madereva. Sasa hawa wapo kwenye kila ngazi ya mkoa, je, watawachukua wote hawa kwenda kuwapeleka kenye mifuko mingine hii au ndiyo watakuwa wameshawatelekeza?
Unapowatelekeza maana tafsiri yake ni kwamba badala ya kutatua tatizo, unakuwa umesababisha tatizo kubwa la ukosefu wa ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba baada ya mwanachama kufariki wategemezi watanufaika kwa miezi 36 tu. Sasa jambo hili labda naomba Mheshimiwa Waziri atusaidia mwishoni hapa, criteria ipi ilitumika kusema kwamba hawa wategemezi anufaike kwa miezi 36? Kwa nini isiwe miaka mitano? Kwa nini isiwe miaka 10? Kwa nini isiwe miaka nane? Maana yake hii miezi 36 ni sawa na miaka mitatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri atuambie ni criteria ipi ilitumika kuweka miezi 36 na siyo miaka mitano au 10 na kadhalika? Atuambie aliangalia kitu gani? Kwa sababu siku moja nimewahi kumsikia akisema mifuko yetu itafika mahali itakosa fedha za kujiendesha. Sasa kama itakosa fedha na kuna mtu alikuwa anachangia, tusije tukawatesa wategemezi ambao mara nyingi unajua kabisa wengi wanakuwa wanateseka kwa sababu tu watu wao waliokuwa wanafanya kazi wamefariki, tunakuja kuacha miezi 36 tu. Kwa kweli hii naomba tu watusaidie, kwa nini isiwe miaka mitano au 10?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu madeni makubwa ambayo mifuko hii inaidai Serikali. Kwenye hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani tumesikia wote kwamba kwa mfano PSPF waidai Serikali karibu shilingi trilioni tatu. Sasa kama hili jambo ndivyo ilivyo, hebu tuambiwe vizuri: Je, hii mifuko italipwa hizi fedha kabla ya kwenda kuiunganisha au yale madeni yatahamishwa kutoka kwenye mifuko tuliyokuwa nayo sasa kwenda kwenye ile mifuko mingine ambayo sasa tutakuwa tumeshaipata ile miwili kwa maana ya PSSF na ile mingine ya NSSF? Kwa hiyo, kama tutahamisha madeni, hiyo pia tutataka tuambiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kama hayo madeni yakihamishiwa kule kwenye mifuko mingine hii mipya, kama
Serikali itaendela kukopa mifuko hii, hii mifuko haita-survive kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri Serikali ikaangalia utaratibu mwingine wa kutafuta fedha kuliko kwenda kukopa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii. Inafika muda watumishi wengi wanataka kustaafu, Serikali imeshakopa fedha wanahangaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Serikali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania wa Mwaka 2018
MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba kuunga mkono mapendekezo ya Kambi Rasmi ya Upinzani ambayo yametolewa hapa na Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kuanzishwa kwa Bodi hii itakuwa ni tatizo la unyonyaji kwa walimu wetu. Leo tunasema kwamba walimu watakatwa ada ya cheti cha usajili, lakini pia watakatwa ada ya leseni ya kufundishia kila mwaka, huu naona ni unyonyaji mkubwa sana kwa walimu ambao unaenda kufanyika kama tutaenda kukubali kupitisha suala hili bila kulifanyia marekebisho na bila Serikali kuzingatia ushauri wa Kambi Rasmi ya Upinzani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo walimu wanakatwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, waliosomeshwa au walionufaika na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, leo walimu wamekopa kwenye taasisi zetu za fedha ikiwepo benki na taasisi mbalimbali, wapo walimu leo wanapokea mshahara mdogo sana, wengine wanapokea hadi Sh.50,000. Kuna mjumbe mmoja kazungumza humu ndani amesema Sh.100,000 lakini kuna wengine wanapokea Sh.50,000 na wengine hawana kitu. Sasa leo tunaenda kuwaongezea hizi ada kulipia leseni kila mwaka na kulipia ada ya cheti kila mwaka, tafsiri yake ni kwamba tunaenda kuwaongezea mzigo mkubwa sana. Nadhani kama alivyoongea Mbunge mmoja humu ndani ni vizuri hizi ada za leseni zikaondolewa ili sasa waweze kusajiliwa bure na inawezekana kabisa. Kama mnasema kwamba kwenye elimu bure mmefanikiwa sasa hili kwa nini dogo msiliweze? Unawezaje kufanya kubwa bure na hili dogo ukashindwa kufanya bure? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la mkanganyiko wa majukumu yanayomhusu mwalimu. Wamezungumza Wabunge wengi humu ndani, leo mwalimu anaajiriwa na Utumishi, mwalimu analipwa na TAMISEMI, mwalimu anaanza kupandishwa daraja na TSC, naona kwamba kinachofanyika hapa ni kuwachezea walimu wa nchi hii, ni kufanya mzaha kwa walimu wetu. Mkanganyiko huu wa majukumu tunaweza kuuondoa tukawa na chombo kimoja tu cha kuhangaikia matatizo ya walimu au mambo ya walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, nchi kama ya Kenya nao wana TSC na siyo dhambi Watanzania kwenda kujifunza Kenya, hii Bodi ya Taaluma ya Ualimu Kenya wanayo lakini iko chini ya TSC. TSC ya Kenya inaajiri mwalimu, inampandisha daraja mwalimu, inamlipa mwalimu, inafanya kila kitu. Tanzania tunafanya vitu vya ajabu sana na hii ni aibu kubwa sana na kwenda kujifunza kwa mtu aliyefanikiwa sio dhambi. Jambo la muhimu tujifunze Wakenya wamefanyaje na baada ya hapo naamini sasa tutakuja na Bodi nzuri yenye maslahi kwa Watanzania na ambayo mwisho wa siku itamsaidia mwalimu badala ya kwenda kuwachanganya walimu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu Mwenyekiti wa Bodi ya Taaluma ya Ualimu anavyopatikana. Mnasema leo Waziri ateue Mwenyekiti wa Bodi, tutaenda kupata akina Kailima wengine. Tunajua Waziri ni kada wa Chama cha Mapinduzi, hata kama kesho CHADEMA itaongoza nchi hii bado huyo Waziri atakuwa ni kada wa Chama cha CHADEMA, hata kama ni CUF wataongoza nchi hii, lakini huyo bado atakuwa ni kada wa chama. Mwisho wa siku tutapata Mwenyekiti wa Bodi ambaye ni kada wa chama cha siasa, tutaenda kuzalisha akina Kailima wengine kwenye ualimu na mwisho wa siku matatizo yatakuwa makubwa zaidi ya kuyapunguza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba tutafute utaratibu mwingine ambao ni mzuri, huyu Mwenyekiti wa Bodi tumtafute kwa njia nyingine ambayo ni bora zaidi ambayo haitakuwa kumteua, ikiwezekana wafanyishwe hata mitihani hawa watu waweze kupatikana na sifa nyingine. Tukienda kuteua, Waziri ataenda kuteua mtu ambaye ni wa chama chake, hatutapata Mwenyekiti wa Bodi hapa tutapata kada wa Chama cha Mapinduzi na mwisho wa siku hii Bodi ya Taaluma ya Walimu itakuwa ni Bodi ya CCM, haitakuwa ni Bodi ya Walimu katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma vizuri kwenye Muswada huu, Bodi ina uwezo wa kukataa kumsajili mtu na sababu za kukataa zikaambatanishwa ndani ya mwezi mmoja. Tunafahamu kwamba watumishi wa umma wanaruhusiwa kuwa kwenye vyama vya siasa ili mradi wasifanye siasa mahali pa kazi na muda wa kazi. Kama wanasema Bodi ina uwezo wa kukataa kumsajili mtu na sababu za kukataa kuambatanishwa tafsiri yake ni kwamba ikionekana kwamba yule mwalimu ana mtazamo au ni mwanachama wa chama kingine uwezekano mkubwa wa kumpiga chini unaweza ukajitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitengeneza msingi msingi mzuri wa nyumba ndipo utakapopata nyumba ambayo ni imara na bora lakini tukianza kwa msingi mbovu tutaenda kupata Bodi ambayo ni mbovu sana ambayo haijawahi kutokea katika Taifa letu. Kwa hiyo, niombe tu ni vizuri tukaa vizuri, tukatulia na tusiwe na papara ili mwisho wa siku tuweze kupata sasa Bodi nzuri na haina matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema mamlaka ya Bodi pia ni pamoja na kutoa onyo, hoja ya kufukuzwa au kuondolewa kabisa kwenye orodha ya usajili kwa mwalimu atakayefanya kosa na kuhukumiwa kifungo cha zaidi ya miezi sita. Bado naona wapo watu wanaweza wakaa tu kwenye ile Bodi kwa sababu wapo chama fulani wakaamua tu kumshughulikia mtu mwingine kwa sababu ya mtazamo tofauti wa kisiasa. Ni vizuri mambo haya tukatengeneza vizuri ili tuweze kutengeneza chombo kizuri kwa walimu na mwisho wa siku mambo yaweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza maneno hayo naomba nikazie zaidi hasa hili la ada na makato ya leseni, hapa ni vizuri ikawa bure kabisa. Mishahara kwa walimu haijawahi kuongezwa, mishahara ambayo walimu wanapokea leo ni mishahara aliyoiacha Rais wa Awamu ya Nne Kikwete, Rais wa sasa hajawahi kuongeza mishahara kwa walimu. Leo mnaongeza makato, tukisema muongeze mishahara mnasema kwamba hadi mmalize Stiegler’s Gorge na Standard Gauge ndiyo mtaongeza mishahara kwa watumishi wa umma. Sasa Rais huyu wa wanyonge, kwa kweli ni vizuri mkaangalia mambo haya tusijetukayapeleka vibaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ipo hapa na ni Serikali ambayo imejinasibu kwamba ni sikivu, naamini kwenye hili itasikia. Kwa mtazamo wangu kama haya hayatachukuliwa maana yake Serikali itakuwa mmeweka pamba masikioni, mambo yatakuwa ni yaleyale na business itakuwa ni as usual. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na Mungu akubariki sana.