Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Issa Ali Abbas Mangungu (16 total)

MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na ninashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Swali la kwanza, maeneo haya ambayo yanachimbwa madini yako mbali na makazi ya watu mfano Kimbiji na Chamazi, lakini Serikali imezuia. Je, umbali upi unaotakiwa kiasi kwamba mkafikia kufunga yale machimbo ya maeneo yale?
Swali la pili, madini haya sasa hivi yanatoka katika Mkoa wa Pwani hasa Wilaya ya Mkuranga. Je, kuna tathmini gani mmefanya kwamba machimbo haya sasa hivi hayataleta athari katika maeneo mliyoyapeleka?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa maeneo ya Kigamboni kwa sasa yana madini aina ya ujenzi na hasa ya changarawe pamoja na kokoto. Maeneo yanayochimbwa kwa Kigamboni hasa hasa ni maeneo ya Mjimwema pamoja na Kijisu. Hata hivyo, eneo alilotaja la Kimbiji pamoja na Chamazi ni kweli kabisa kuna wachimbaji wadogo wadogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba siyo kweli kwamba tumesimamisha au tumefunga eneo la Kigamboni. Tulipofunga ni eneo la Kunduchi ambapo sasa wachimbaji tena ambao walikuwa kidogo ni haramu wanachimba kuelekea upande wa barabara. Kwa hiyo, pale Kunduchi tulisimamisha tena miaka minne iliyopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimtahadharishe tu Mheshimiwa Mbunge kama nilivyosema, lakini namshukuru kwa kuwaulizia wananchi wa Kigamboni. Taratibu za Sheria ya Madini zinataka uache umbali wa mita 200 kutoka makazi, lakini kadhalika zinataka uache umbali wa mita 100 kutoka vyanzo vya ziwa au bahari kama ferry ya Kigamboni ilivyo na inataka uache umbali wa mita 100 kutoka umbali ambako sasa kiwanja cha ndege kitajengwa au city itajengwa. Sasa kwa Kigamboni kuna eneo kubwa ambalo limeainishwa kwa ajili ya satellite city. Eneo lile tumezingatia Sheria ya Madini kuacha umbali wa mita 100 usiopungua 100 hadi 200.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba taratibu sasa kule kigamboni tunatenga eneo rasmi la Mjimwema pamoja na maeneo ya Mkuranga aliyosema ya Visiwasiwa, pamoja na maeneo mengine ya kule Kibaha kwa Mathias na kwa Mfipa. Maeneo hayo tunayatenga kwa ajili ya wananchi wa Dar es Salaam ili wapate maeneo rasmi sasa ya kuchimba madini ya mchanga kwa ajili ya shughuli za ujenzi.
Kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Mbunge, tutakaa pamoja na utendaji wako ili tubainishe maeneo ambayo tutachimba kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa Kigamboni.
MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Spika, nashukuru, na ninashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri wa Katiba, lakini ningependa kumuuliza maswali mawili.
Swali la kwanza; viwanja katika eneo la Kijichi, Tuangoma na Chamazi vipo na nitampelekea orodha hiyo baada ya kikao hiki, je, yupo tayari sasa kuanza mpango huo wa ujenzi haraka iwezekanavyo ili wananchi waweze kupata huduma hiyo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mahakama ya Kizuiani ambayo iko moja inahudumia zaidi ya watu 800,000, haina choo, haijafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu, ipo karibu na soko, uendeshaji wa kesi pale unakuwa ni mgumu, haki inachelewa kupatikana; je, Serikali ina mpango gani wa kufanya marekebisho na matengenezo ya dharura katika mahakama ile?
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, kwa upungufu wa mahakama 102 kwa Mkoa wa Dar es Salaam, Serikali yenyewe haioni kwamba inachelewesha haki na kusababisha vitendo viovu kama rushwa na mambo mengine?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, kwanza, anasema viwanja vipo, hiyo ni taarifa nzuri sana kwangu, namuomba sasa atuwasilishie rasmi hivyo viwanja ambavyo tayari vina nyaraka zake.
Mheshimiaw Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mangungu kwamba tuna pesa ya kujengea mahakama sasa, mkikumbuka mapema mwaka huu Mheshimiwa Rais aliagiza pesa yote ya maendeleo ya mahakama itolewe, kwa tuna shilingi bilioni 12.3 tayari, lakini vilevile Waheshimiwa Wabunge mmetuidhinishia shilingi bilioni 22 katika mwaka huu wa fedha, tuna jumla ya shilingi bilioni 34.3 na hizo pesa tunajenga Mahakama za Mwanzo 50, anayewahi kwa hoja za msingi tutampa hiyo mahakama, sasa nakuomba Mheshimiwa Mangungu badala ya kuongea jenga hiyo hoja kimaandishi.
Mheshimiwa Spika, tunajenga vilevile Mahakama za Wilaya 20 na tunajenga Mahakama Kuu mpya mbili katika mikoa ya Mara na Kigoma na vilevile Mahakama za Hakimu Mkazi tunajenga saba, tano katika mikoa hii mipya na mahakama nyingine mbili katika mikoa ya Ruvuma na Lindi.
Mheshimiwa Spika, la pili; Mheshimiwa Mangungu anasema mahakama yake haina choo, hilo ungelisema hata bila hapa mbele ya Bunge ningeweza tu kukusaidia naomba tuonane baadaye, ni vitu vidogo sana kuviongelea hapa. Ahsante sana.
MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona, aliyoyazungumza Mheshimiwa Ndassa yanafanana na Jimboni kwangu Mbagala. Kuna mradi ule wa maji, Mpera na Kimbiji, ambao sasa hivi unafika miaka nane, haujatekelezwa na wala maji hakuna. Lakini vilevile kulikuwa na mpango wa kuchimba visima virefu katika Jimbo langu, mpaka leo mpango ule haujatekelezwa kwa kukosa fedha.
Je, Waziri anatupa jibu gani wakazi wa Mbagala, na wananchi wa Mbagala kwa ujumla, lini visima vile vitaanza kuhudumia Jimbo la Mbagala na Dar es Salaam kwa ujumla na je, ule mpango wa visima virefu upo au umekufa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Maji inaendelea na mradi wa kuchimba visima vya Mpera na Kimbiji; na mpaka sasa tunavyoendelea tayari tumeishafikia asilimia 60, na mradi huo unakamilika mwezi Disemba mwaka huu. Baada ya hapo tutaanza na mradi mwingine sasa wa kuweka mabomba, ambayo sasa yatatoa maji kwenye visima na kuyasambaza mpaka kwenye maeneo yake, ya Mheshimiwa Mbunge ya Mbagala. Kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba hakuna wasiwasi ule mradi unaendelea, na mwaka huu unakamilika. Lakini pia ameomba kwamba je, Serikali ina mpango gani wa kuchimba visima virefu? Ni kwamba tunaendelea kulingana na bajeti tunavyotenga, tutaendelea na kama maji yanapatikana tutaendelea kuchimba visima virefu.
MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini swali langu la msingi niliuliza ni utaratibu gani mtaweza kuwasaidia makundi maalum ya wanwake na vijana ili waweze kupata mikopo kwa riba nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili nilitaka kuuliza, kwa kuwa kuna ugumu na sheria zinazoibana Serikali kusimamia riba hizi. Ni lini sasa Serikali itatusaidia kutimiza ile ahadi ya shilingi milioni 50 kila kijiji na mtaa ili tuweze kuwasaidia wananchi wetu na kinamama wa Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi; kwa mujibu wa Sheria Benki Kuu haiwezi kutoa maelekezo ya kuleta riba elekezi ili kuweza kusimamia mabenki haya yaweze kufanya vizuri katika soko letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuhusu shilingi milioni 50 kama ambavyo Serikali imekuwa ikisema; tunaendelea kuandaa utaratibu na kwenye bajeti yetu ya fedha ya mwaka 2016/2017 tumetenga bajeti hii na tutaweza kuitekeleza kabla ya mwaka huu wa fedha haujaisha.
MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kama Serikali inatenga bajeti, je, Mheshimiwa Waziri anajua kwamba Wazee wa Baraza wanakopwa na hawalipwi kwa wakati posho zao na wengine mpaka wanafikia kukutwa na umauti wakiwa wanadai pesa nyingi sana idara ya mahakama, je, hilo analitambua?
Mheshimiwa Spika, lakini la pili, kwa posho ya sh. 5,000
na uzito wa kesi wanazoamua wazee hawa hamuoni kwamba Serikali yenyewe inachochea vitendo viovu vya rushwa na mambo mengine katika mahakama zetu katika kutoa maamuzi? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ni kweli yapo malimbikizo ya posho ya Wazee wa Baraza na mpaka sasa malimbikizo hayo ni sh. 335,479,000; na tunatarajia kwa fedha ambayo imetengwa mwaka huu kuweza kulipa malimbikizo hayo ya fedha hizo wanazodai Wazee Wa Baraza.
Mheshimiwa Spika, pia tunatambua kabisa kwamba kiwango cha sh. 5,000 kwa mazingira ya leo ni kiasi kidogo ndiyo maana Serikali na Mahakama inafanya jitihada ya kuona uwezekano wa kuongeza posho hiyo, sio tu kwa Wazee wa Baraza wa Dar es Salaam bali Wazee wa Baraza wa Mahakama zote nchini.
MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, miradi hii ya World Bank katika Jimbo langu la Mbagala ilikuwepo Kijichi, Kiwika, Kizinga na Bugdadi ambapo visima vimechimbwa, maji yamepatikana lakini mpaka sasa hivi miundombinu ile haijasambazwa, wananchi bado wana kero kubwa. Je, ni lini Serikali sasa itasambaza miundombinu ile ili wananchi waweze kupata maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni hatua nzuri na ndiyo tunavyokwenda, tunachimba tunapata maji, tunafanya test, tunaona kwamba maji haya yanafaa kwa matumizi ya binadamu. Baada ya hapo tunaweka bajeti kwa ajili ya kuweka sasa miundombinu ya kusambaza na kuhifadhi maji ikiwemo na kujenga matanki. Kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 na juzi Mheshimiwa Mbunge umepitisha bajeti basi naomba kwa kutumia Halmashauri yako na fedha mnapanga wenyewe mhakikishe kwamba mnaweka sasa miundombinu ili wananchi waendelee kupata maji.
MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Hali inayojitokeza Mlimba ni sawasawa na inavyojitokeza Jimbo la Mbagala. Niliwahi kuuliza swali la msingi, nikaambiwa kwamba mwaka huu watajenga Mahakama katika Jimbo la Mbagala, lakini tatizo ni viwanja. Tayari tumeshapata viwanja eneo la Kijichi na Chamazi. Je, ni nini tamko la Serikali kuhusu kujenga Mahakama katika Jimbo la Mbagala? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mpango wa kujenga Mahakama ya Mwanzo huko Temeke; na sasa tutahakikisha tunajua Temeke sehemu gani?Hata hivyo, nimelipokea suala la Mbagala, tutalifanyia kazi na kuona hii Mahakama ya Mwanzo ambayo imepangwa kujengwa Temeke mwaka 2017/2018 itakuwa sehemu ipi na kama siyo Mbagala, basi suala la Mbagala tutalichukulia kwa umakini unaostahili.
MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Mheshimiwa Naibu Waziri amesema katika jibu lake hapa kwamba Halmashauri zijitahidi kuweza kuwapa semina au mafunzo Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Maafisa wengine. Hata hivyo, Wizara yake inadaiwa na Halmashauri, kwa mfano, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke tunadai gawiwo la asilimia 30 ya shilingi bilioni moja kutokana na gawiwo la kodi ya ardhi. Tangu mwaka 2014 tunadai na tunauliza hawatujibu, hawaoni kwamba juhudi za Halmashauri kuweza kupanga, kutoa elimu zinakwamishwa na Wizara yenyewe kwa kutokurejesha ile asilimia 30?
Makazi, majibu mafupi.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nimesema hapa kwamba Halmashauri zishiriki katika suala zima la kuwajengea uwezo Wenyeviti hawa lakini kwa kushirikiana pia na Wizara. Maana ya kujenga uwezo ni kwa kutumia mapato ya ndani ya Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la asilimia 30 kutorudi kwenye Halmashauri, naomba niseme tu kwamba, tunapokusanya mapato haya, yanakwenda kwenye kapu moja la Serikali ambapo tunakwenda kugawana keki wote kwa pamoja na pale pesa hizo zinaporudi Wizarani mara moja zinakwenda katika maeneo husika. Tunatambua wazi kwamba Halmashauri nyingi zinadai lakini katika kudai pia kuna Halmashauri nyingi pia Wizara inazidai ambazo walikopeshwa pesa kwa ajili ya kupima viwanja. Kwa hiyo, pesa wakati mwingine inapoingia Wizara inakata katika kufidia madeni ambayo imetoa ili pesa ile iweze ku-generate na kuweza kuwapa Halmashauri nyingine lakini Halmashauri nyingi zaidi zinadai.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwahakikishie tu kwamba tumekwishachukua takwimu sahihi za madai yanayodaiwa kwa asilimia 30. Kwa hiyo, mara tutakapopokea fedha kutoka Hazina na sisi tutazituma moja kwa moja. Nia na dhamira ya Serikali ni nzuri ya kuweza kuhakikisha mpango unakwenda vizuri kwa kushirikisha pande zote. Kwa hiyo, zitakapokuja hizi fedha tutazileta na tunajua zitasaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe tahadhari pia, tuna malalamiko likiwepo lalamiko kutoka Halmashauri ya Magu kwamba pesa hizi zikirudi Wakurugenzi wanazipangia shughuli nyingine na idara husika haipewi. Kwa hiyo, tuseme pesa hizi zikirudi kule zinatakiwa zirudi kwenye idara husika ili zifanye shughuli ya utawala wa ardhi na siyo kuzipangia matumizi mengine. Naomba sana Wakurugenzi ambao wanazitumia ndivyo sivyo, basi tunakwenda kufanya uhakiki ili tuweze kuona ni namna gani pesa hizi zitafanya kazi iliyokusudiwa.
MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Hospitali ya Rangi Tatu, Mbagala ina upungufu mkubwa wa dawa na huwa zinachelewa kuletwa katika hospitali ile. Vilevile tunawadai MSD dawa zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 300. Je, Wizara itatusimamia dawa zile zipatikane ili tuweze kutoa huduma hasa ikizingatiwa tunatoa huduma mpaka maeneo ya Mkoa wa Pwani maeneo ya Mkuranga?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kituo hiki cha Rangi Tatu nakifahamu vizuri kwa sababu mdogo wangu pale ndiyo in charge wa kituo kile, sidhani kama Mheshimiwa Issa anajua, kwa hiyo nafahamu changamoto hiyo na kwamba kina wateja wengi sana, maana yake analalamika halali kwa kufanya kazi kwa bidii kuwahudumia Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakachokifanya, nitafanya kazi kwa ukaribu na Mheshimiwa Mangungu kufuatilia tuone kama kweli wanadai shilingi milioni 300 na kama wanadai basi waweze kupata huduma hiyo ya dawa.
MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Hali inayojitokeza Mlimba ni sawasawa na inavyojitokeza Jimbo la Mbagala. Niliwahi kuuliza swali la msingi, nikaambiwa kwamba mwaka huu watajenga Mahakama katika Jimbo la Mbagala, lakini tatizo ni viwanja. Tayari tumeshapata viwanja eneo la Kijichi na Chamazi. Je, ni nini tamko la Serikali kuhusu kujenga Mahakama katika Jimbo la Mbagala? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mpango wa kujenga Mahakama ya Mwanzo huko Temeke; na sasa tutahakikisha tunajua Temeke sehemu gani? Hata hivyo, nimelipokea suala la Mbagala, tutalifanyia kazi na kuona hii Mahakama ya Mwanzo ambayo imepangwa kujengwa Temeke mwaka 2017/2018 itakuwa sehemu ipi na kama siyo Mbagala, basi suala la Mbagala tutalichukulia kwa umakini unaostahili.
MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Ningeomba Naibu Waziri nami anithibitishie je, ni lini Serikali italeta maji au mtandao wa DAWASA utafika katika Kata za Kiburugwa, Kilungule na Chamazi kwa sababu tangu nchi hii kupata uhuru eneo hilo halijawahi kupata maji na wala hakuna mpango wowote.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, visiwa vya Kimbiji vinakamilika lini? Maana yake...
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nilishatamka katika Mbunge hili kwamba vyanzo tumekamilisha, visima vya Mpera pia vimekamilika, Ruvu Chini imekamilika, Ruvu Juu imekamilika. Kilichobaki sasa hivi tayari tunaendelea sasa na mikataba ya kutengeneza usambazaji wa hayo maji kuyapeleka kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo napenda, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge sasa hivi tuna mkataba mmoja, tumeshapata fedha kutoka Benki ya Dunia dola milioni 50, tunajipanga kuhakikisha maeneo yote ya Dar- es - Salaam yanapata huduma ya maji kwenye vijiji, vitongoji na mitaa yote. Kwa hiyo asiwe na wasiwasi maji yatapatikana. (Makofi)
MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri kwa ushirikiano walioutoa kwa wananchi wa Mbagala mpaka mradi huu kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa kuwa baada ya kukamilika substation ya Mbagala, Mbagala ni eneo ambalo lina viwanda; je, wana mkakati gani sasa kuvishawishi viwanda vilivyopo Mbagala kutumia gesi asilia ili kupunguza low voltage ambayo tunaipata kutokana na matumizi ya viwanda vile?
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Serikali itafanya eneo la Mbagala (District) kuwa Mkoa kwa sababu ina wateja wengi na TANESCO imeelemewa kule Mbagala kiasi kwamba inashindwa kupaleka umeme katika maeneo ya Toangoma, Vigozi, Mponda na maeneo mengine?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri tumepokea pongezi zake, nasi kwa kweli tunamshukuru sana kwa ushirikiano alioufanya kwa kipindi chote cha utekelezaji wa mradi huu Jimboni kwake Mbagala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ameeleza mkakati wa Serikali wa kuvishawishi viwanda kutumia gesi asilia. Naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge Wizara yetu kupitia TPDC tuna mkakati wa kusambaza gesi asilia kwa matumizi ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwa mwaka huu wa fedha ambao utaanza 2018/2019 TPDC imeshaingia makubaliano ya awali ya kusambaza gesi katika maeneo mbalimbali ya viwanda yaliyopo Mkuranga, kwa mfano Kiwanda cha Bakhressa, Loth Steel cha Mkuranga na pia hata Kiwanda cha Biku na Cocacola Kwanza, Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wazo lake hilo linafanyiwa kazi na viwanda tunavihamasisha vitumie gesi kwa sababu gesi ipo na ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, ameuliza ni lini tutaifanya Mbagala kuwa Mkoa? Naomba nilichukue hili suala na linajadilika ndani ya Wizara, tunaweza tukalifanyia kazi. Ni kweli Mbagala ina wateja na watumiaji wengi wa umeme. Naomba hili tulichukue. Ahsante. (Makofi)
MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali ndogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa ziara Naibu Waziri alitoa ahadi ya kusaidia kupatikana kwa mtandao wa maji katika Jimbo la Mbagala. Hata hivyo, katika tenda waliyotangaza mwezi uliopita maeneo yote ya Mbagala hayajatajwa, wameendelea na maeneo yale yale ambayo kila siku wamependelea kupeleka maji. Je, wananchi wa Mbagala tutegemee nini juu ya upatikanaji wa maji safi na salama kutoka katika chanzo cha Ruvu Juu na Ruvu Chini?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwaambie wananchi wake wa Mbagala wakae mkao wa kula. Jumatatu pale Dar es Salaam nakutana na Benki ya Maendeleo ya Ufaransa, walishatuahidi kutoa dola milioni 130 kwa ajili ya mradi wa maji safi na maji taka eneo la Temeke ikiwemo na Mbagala. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba tu asubiri kidogo atapata majibu, wananchi wa Mbagala hawajaachwa. Tunahakikisha Dar es Salaam yote inapata maji safi na salama ikiwemo pamoja na visima vya Kimbiji na Mpera. (Makofi)
MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa Serikali inasema kwamba wameingiza Teaching Allowance katika mishaharana Serikali ilikuwa inafanya uhakiki kwa ajili ya kulipa madeni ya walimu na malimbikizo yao wakati wa kustaafu na wale ambao wako kazini. Je, Serikali imefikia wapi katika kuhakiki madeni hayo na kuyathibitisha ili walimu sasa waanze kulipwa maana wamekuwa wakisumbuka na muda mrefu wamekosa kupata haki zao hasa wale waliostaafu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, anasema kwamba walimu wa mijini wanaweza wakapanga nyumba. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuwaongezea allowance hizi ili waweze kukabiliana na changamoto ya nyumba katika maeneo ya mijini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Issa Ali Mangungu, Mbunge wa Mbagala, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kwamba Serikali imeshakamilisha uhakiki wa madeni na watumishi wengi tu wakiwemo walimu wameshaanza kulipwa. Wale ambao hawajalipwa naomba waendelee kusubiri, muda wao wa kulipwa ukifika watalipwa. Hakuna mtu yeyote ambaye hatalipwa deni ambalo ni halali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili ameuliza kwamba Serikali ina mpango gani wa kuwaongezea allowance walimu? Napenda nimhakikishie kwamba Serikali ni mwajiri wa watumishi wote, siyo walimu peke yake. Kwa hiyo, kama ambavyo tumeweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba tunaweka kipaumbele cha kuwa na nyumba katika maeneo ambayo ni vigumu kupata nyumba kama maeneo ya vijijini ambako hakuna hata nyumba za kupanga kwa watumishi wote; watumishi wa afya, walimu na watumishi wengine, hivyo hivyo hatuwezi kubagua kwamba sababu ni walimu kwa sababu ni walimu, tuwaongezee allowance walimu peke yao watumishi wengine tuwaache gizani, hapana. Nadhani huo utakuwa ni ubaguzi na Serikali haiwezi kufanya hivyo.
MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Spika, nashukuru, lakini ningemuomba Mheshimiwa Waziri kama atakubali ombi langu la kuongozana na mimi ili akaangalie jinsi gani wananchi wanavyokadiriwa makadirio ya juu yasiyokuwa na haki na kuwapa usumbufu mkubwa hasa wale ambao wanaishi katika maeneo ambayo hayajapimwa.

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; je, ni lini Serikali itaifanya sasa Wilaya ya Mbagala kuwa mkoa wa kikodi ili waweze kukusanya vizuri kodi katika maeneo yasiyopimwa, yameachwa kwa asilimia nyingi sana na wanashindwa
kufikia huko kwa sababu TRA hawana man power ya kutosha? Kama hawawezi basi warudishe kwenye halmashauri zetu ili waendelee na zoezi hili.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la kwanza, wananchi kukadiriwa gharama kubwa kwa ajili ya kulipa kodi ya majengo. Naomba niwaambie wananchi wa Tanzania kwamba dhamira njema ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli ya kuhakikisha Watanzania hawaumizwi tena na kodi hizi tayari Bunge hili lilishapitisha sheria.

Mheshimiwa Spika, sasa kila jengo ambalo ni la chini ni shilingi 10,000 kwa hiyo hakuna anayelipa zaidi ya 10,000 kwa kila jengo ambalo ni la chini na kwa majengo ya ghorofa kwa kila ghorofa moja naomba niwaambie Watanzania kwa kila floor ya ghorofa lako ni shilingi 50,000 kwa hiyo hakuna makadirio yoyote ambayo yako juu na Mheshimiwa kaka yangu Issa Ali Mangungu niko tayari kwenda na wewe Mbagala tukaongee na wananchi wetu tuwaeleweshe nini dhamira ya Serikali yao na nini tumeanza kutekeleza.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili; hili ni jambo la kiutaratibu, naomba nilichukue tutakwenda kulifanyia kazi ili tuone ni lini sasa Wilaya ya Mbagala inaweza kuwa sasa ni Mkoa wa Kikodi ili tuweze kushughulikia ukusanyaji wa kodi hii kwa ufanisi.
MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na napenda kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Waziri ulitembelea Jimbo la Mbagala kwenye mradi wa Mgembaki pamoja na Kiwika na ulitoa maagizo kwa sababu miradi hiyo inaendeshwa kiufanisi, wananchi ambao walichangia miradi ile pamoja na Wizara pamoja na watu wa DAWASA wakae pamoja ili waangalie jinsi ya kuiendesha kwa ufanisi, lakini cha ajabu watu wa DAWASA wameingia kule na wanataka kuchukua vyanzo vile bila kushirikisha Kamati zile za wananchi na kuacha kabisa maagizo uliyoyatoa.

Je, utakuwa tayari sasa turudi tena kwa wananchi wale na DAWASA ili tuweze kuangalia jinsi gani ya kuendesha miradi ile kwa maridhiano?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, Mheshimiwa Mbunge unafanyakazi kubwa na sisi kama Wizara ya Maji hatuwezi kuwa kikwazo, nipo tayari kuongozana na wewe. Ahsante sana.