Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Saul Henry Amon (3 total)

MHE. SAUL H. AMON: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Rungwe ni moja kati ya Wilaya ambazo zimebarikiwa sana kuwa na vyanzo vingi vya maji. Hata hivyo, kuna baadhi ya maeneo maji yamefungwa yasiendelee kutiririka kwa sababu ya uhaba wa maji, hakuna matenki, miundombinu ni ya kizamani mno na watu wameongezeka.
Je, Serikali ina mpango gani na Wilaya ya Rungwe ili kuisambazia maji ambayo hayana taabu ni maji ya kutega? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli kabisa kwamba Wilaya ya Rungwe kuna maji ya mtiririko/mserereko. Ndiyo maana tumehakikisha kwamba kila Halmashauri inapatiwa fedha na Wizara ya Maji na Umwagiliaji ili sasa hilo suala la miundombinu, matenki na watu wameongezeka, kwa sababu maji yapo tuhakikishe kwamba tunaiboresha na wananchi wanaweza kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshauri Mheshimiwa Mbunge kama anaona wataalam wake kidogo wana upungufu, Wizara ya Maji na Umwagiliaji tuko tayari kusaidiana kutoa wataalam ili kwenda kukamilisha hiyo miradi kwa sababu fedha ipo.
MHE. SAUL H. AMON: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri. Naomba kama Naibu Waziri ana nafasi aone hali ilivyo mbaya, kile kipande cha kata nne hata kwenda kuwasalimia tunaogopa kwa sababu tunatoa ahadi lakini haitimizwi. Je, yuko tayari kuongozana na mimi akaangalie hali ilivyo mbaya ya hicho kipande cha kutoka Njiapanda mpaka Mpakani? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, vilevile barabara hii iko sawa kabisa na barabara ya Igogwe – Mchangani - Mbeye One. Mazao ni mengi lakini wananchi wa eneo hilo wanauza mazao kwa bei ya chini sana kwa sababu hakuna usafiri. Naomba Waziri atakapokuja Rungwe aangalie vipande hivyo viwili na aone ukweli na hali halisi ilivyo kwa wananchi wa Rungwe. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, kubwa ambalo Mheshimiwa Mbunge analitaka kwangu mimi ni suala la kupata fursa ya kwenda kutembelea ili nijionee kwa macho hali halisi ikoje. Mimi niko tayari baada ya kwamba tumehitimisha shughuli za Bunge la Bajeti, nikiamini kwamba bajeti yetu itakuwa imepita salama ili nikajionee na tushauriane.
Mheshimiwa Spika, lakini pia naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwa kupitia chombo chetu cha TARURA ambacho tumekianzisha tutahakikisha tunawaelekeza maeneo yote ambayo ni korofi yaweze kutengenezwa ili yapitike vipindi vyote.
MHE. SAUL H. AMON: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii.

Kwanza nishukuru Serikali kwa kuboresha Vituo vya Afya vya Masukulu na Ikuti, hapo nashukuru sana, kwani sasa hivi vinaonekana kama hospitali, lakini wananchi wa Kata ya Mpuguso na Kata ya Isongole kwa nguvu zao wamejenga vituo vya afya kufikia hatua ya maboma, wengine mpaka kumalizia kwenye ceiling board.

Je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia hivi vituo vya afya kwa hao watu wanaotoka mbali sana ili viweze kwisha kwa haraka na waweze kuvitumia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba nijibu swali la Mheshimiwa Amon la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshaanza kutekeleza kuunga mkono juhudi za wananchi ambapo wameongeza nguvu zao. Tumeshapeleka fedha katika kumalizia maboma ya shule za sekondari, tupo kwenye mchakato wa kupeleka maboma kumalizia maboma ya shule za msingi; awamu ya tatu ni maboma ya zahanati na vituo vya afya na maweneo ambayo tutazingatia ni maeneo ambayo wananchi wameshaonesha juhudi zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba mchakato huu ukikamilika aneo lake pia, ambalo amelitaja tutalizingatia sana. Ahsante.