Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. David Ernest Silinde (17 total)

MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:-
Wilaya ya Momba ni moja kati ya Wilaya mpya zilizoanzishwa hivi karibuni ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi:-
Je, kwa nini Serikali imekuwa ikisuasua kutoa fedha ili ziweze kujenga ofisi na nyumba za watumishi katika Makao Makuu ya Wilaya ya Momba eneo la Chitete?
NAIBU WAZIRI WA TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika mwaka wa fedha 2013/2014, ilifanikiwa kupeleka fedha shilingi milioni 250; ambazo zimetumika kuanza ujenzi wa nyumba ya Mkuu wa Wilaya na ujenzi wa nyumba mbili za Viongozi waandamizi ambao umefikia hatua ya msingi. Katika mwaka wa fedha 2014/2015 fedha zilizotengwa kwa kazi hizo hazikupelekwa. Aidha, katika mwaka 2015/2016, Serikali imetenga shilingi milioni 282.7 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa nyumba hizo na shilingi milioni 200 zimetengwa kuanza ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa ujenzi wa Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Momba, Serikali katika mwaka wa fedha 2014/2015, ilitoa shilingi milioni 450; kwa ajili ya kuanza ujenzi wa ofisi hizo. Katika jitihada za kuhakikisha Halmashauri inawapatia watumishi wake nyumba bora, Serikali imezielekeza Halmashauri kutumia mapato ya ndani, kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi. Aidha, Halmashauri imeingia mkata wa ujenzi wa nyumba 20 kwa gharama ya shilingi bilioni 2.1 na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ili kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kujenga nyumba na Ofisi za Viongozi katika Wilaya mpya kwa kadri upatikanaji wa fedha utakavyoruhusu.
MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:-
Wakati wa Kampeni za Urais mwaka 2015 wananchi wa Momba walipewa ahadi ya kutatuliwa kero ya ushuru wa mazao na mifugo kwenye vizuizi na minada:-
(a) Je, mpaka sasa Serikali imefikia hatua gani katika kushughulikia kero hii?
(b) Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya mwenendo mbovu wa ukusanyaji wa ushuru huo?
NAIBU WAZIRI (TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ushuru wa mazao hutozwa kwa mujibu wa sheria ya fedha za Serikali za Mitaa Sura Na. 290 kwenye eneo ambalo zao hilo huzalishwa na kuuzwa. Kwa mujibu wa sheria hii ushuru unatozwa kwa mnunuzi wa mazao kutoka kwa mkulima asilimia tatu hadi asilimia tano ya bei ya gharama (farm gate price). Aidha, kwa upande wa ushuru wa Mifugo, ushuru huu hutozwa mnadani au sokoni baada ya mifugo kununuliwa.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inasisitiza na kuwataka Wakurugenzi wote wa Halmashauri kuhakikisha kuwa wanazingatia sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia utaratibu wa utozaji na ulipaji wa kodi katika ushuru husikia.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA (K.n.y. MHE. DAVID E. SILINDE) aliuliza:-
Ili kurahisisha msukumo wa kimaendeleo na kukuza uchumi katika Bonde la Ziwa Rukwa, Serikali iliahidi kujenga daraja linalopita katika Mto Momba kati ya Kata ya Kamsamba (Jimbo la Momba) na Kata ya Kipera (Jimbo la Kwela) mwaka 2009. Je, ni lini ahadi hiyo ya Serikali itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, jitihada za Serikali kuhusiana na ujenzi wa daraja la Momba lililoko kwenye barabara ya Sitalike hadi Kilyamatundu, Mkoa wa Rukwa katika Jimbo la Kwela na vile vile Kamsamba hadi Mlowa, Mkoa wa Songwe, zinaendelea, ambapo kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ikiwa ni pamoja na kuandaa na nyaraka za zabuni imekamilika mwaka 2015. Kazi ya Ujenzi wa daraja la Momba imepangwa kuanza katika mwaka wa fedha 2016/2017 kama ambavyo Waziri wangu wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano alivyomwahidi Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha, Mbunge wa Kwela.
MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:-
Barabara ya kutoka Kakuzi - Kapele mpaka Ilonga ina kilometa 50.6, pia inaunganisha Mkoa wa Songwe na Rukwa bado ipo chini ya Halmashauri pamoja na maombi ya kuipandisha hadhi kupitia vikao vyote ikiwemo Road Board kukubali.
Je, ni kwa nini Serikali inachelewa sana kuipandisha hadhi barabara hiyo ili ihudumiwe na TANROADS kutokana na umuhimu wake.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kupandishwa hadhi barabara unafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007 na Kanuni zake za mwaka 2009. Aidha, maombi ya kupandisha hadhi barabara ya Wilaya ya Kakozi - Kapele hadi Ilonga kuwa ya Mkoa yamepokelewa na yatafanyiwa kazi na Wizara sambamba na maombi kutoka Mikoa mingine. Mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo taarifa itatolewa na Serikali kupitia kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Songwe.
MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:-
Ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete ya ujenzi wa daraja la Kamsamba–Kilyamatundu bado haijatekelezwa tangu mwaka 2009.
Je, ni upi mpango wa Serikali ya Awamu ya Tano kukamilisha ujenzi wa daraja hilo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Daraja la Momba lililopangwa kujengwa katika barabara ya Mkoa ya Kibaoni - Muze - Ilemba - Kilyamatundu na barabara ya Mkoa ya Kamsamba hadi Mlowo ni kiunganishi muhimu cha Mkoa wa Rukwa katika eneo la Kilyamatundu na Mkoa wa Songwe katika eneo la Kamsamba. Kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo kutarahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo kutoka sehemu moja kwenda nyingine, kuimarisha shughuli za kijamii na kiuchumi katika Bonde la Ziwa Rukwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza azma hiyo, Serikali ya Awamu ya Tano imepanga kuanza ujenzi wa daraja hilo katika mwaka huu wa fedha 2016/2017. Zabuni za ujenzi wa daraja la Momba ziliitishwa tarehe 11 Januari, 2017 kwa ajili ya kumpata Mkandarasi. Mara baada ya hatua hii ya zabuni na tathmini kukamilika, mkataba kwa ajili ya kuanza ujenzi utasainiwa. Aidha, katika mwaka wa fedha 2016/2017 kiasi cha shilingi bilioni 2.935 zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa daraja hilo.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA (K.n.y. MHE. DAVID E. SILINDE) aliuliza:-
Ili kurahisisha mfumo wa kimaendeleo na kukuza uchumi katika Bonde la Ziwa Rukwa, Serikali iliahidi kujenga daraja linalopita katika Mto Momba kati ya Kata ya Kamsamba (Jimbo la Momba) na Kata ya Kipeta (Jimbo la Kwela) mwaka 2009.
Je, ni lini ahadi hiyo ya Serikali itakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, daraja la Momba ni kiungo muhimu katika barabara ya Kibaoni - Kasansa - Muze - Ilemba - Kilyamatundu - Kamsamba hadi Mlowo ambayo inaunganisha mikoa mitatu ya Katavi, Rukwa na Songwe. Barabara hii ni kiungo muhimu sana kati ya mikoa hii mitatu ya Katavi, Rukwa na Songwe kwani inapita katika Bonde la Ziwa Rukwa ambalo ni maarufu sana kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo. Hali ya barabara ni nzuri kwa wastani ila inapitika kwa shida wakati wa masika katika baadhi ya maeneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kufahamu umuhimu huo itaanza ujenzi wa daraja la Momba ambalo ni kiungo muhimu katika barabara hiyo katika mwaka wa fedha 2016/2017. Serikali imetenga shilingi milioni 2,935 kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 na kwa sasa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) upo katika hatua za mwisho za kumpata mkandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika mwaka wa fedha 2017/2018 zimetengwa shilingi milioni 3,000 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa daraja hilo.
MHE. CECILIA D. PARESSO (K.n.y. MHE. DAVID E. SILINDE) aliuliza:-
Katika Tarafa ya Kamsamba kuna Shule ya Sekondari ya Wazazi inayomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya CCM ni muda mrefu sasa shule hiyo haitumiki na haina mwanafunzi hata mmoja na hivyo kufanya majengo yake kuharibika.
Je, kwa nini Serikali ya Awamu ya Tano isirudishe shule hiyo kwa wananchi ili waweze kuitumikia au kubadili matumizi na kuwa Chuo cha Ufundi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ernest David Silinde, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Shule ya Sekondari ya Wazazi ya Kamsamba, iliyoko katika Tarafa ya Kamsamba, Wilaya ya Momba ambayo inamilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya CCM haitumiki na haina wanafunzi. Shule hii ni ya kutwa kwa wavulana na wasichana, kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha nne na ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 225 iwapo miundombinu yake yote itakamilika na kutumika.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Halmashauri itafanya mazungumzo na mmiliki wa shule ili kuona uwezekano wa kurejesha majengo hayo Serikalini ili shule ianze kupokea wanafunzi.
MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itakamilisha miradi ya umeme katika vijiji ambavyo havijafikiwa katika Halmashauri ya Momba?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ni kufikisha umeme katika vijiji vyote visivyo na umeme nchini ikiwemo vijiji vya Wilaya ya Momba ifikapo Juni, 2021. Katika Wilaya ya Momba jumla ya vijiji 27 vitapatiwa umeme kupitia mzunguko wa kwanza wa awamu ya tatu ya miradi ya kusambaza umeme vijijini. Vijiji hivyo ni pamoja na Ikana, Nakawale, Ipanga, Mpui, Mfuto, Machindo, Muungano, Samang’ombe, Tundumakati, Unyamwanga, Nello, Tukuyu, Mlimani, Majengo Mapya, Ihanda na Migombani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi za mradi zinazotekelezwa na Kampuni ya STEG International ambazo zinahusisha ujenzi wa kilometa 60 za umeme msongo wa kilovoti 33 na kilometa 108 za njia za umeme msongo kilovoti, kufunga transfoma 54 na kuunganisha wateja 1,773. Gharama ya mradi inakadiriwa kuwa shilingi 6,607,000,000 na mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Aprili, 2019.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vitakavyobakia katika mzunguko wa kwanza wa REA III vitapatiwa umeme katika mzunguko wa pili wa REA-III iunaotarajiwa kuanza mwezi Aprili, 2019 na kukamilika mwezi Juni, 2021.
MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:-
Katika kutekeleza azma ya Tanzania ya viwanda.
Je, Halmashauri ya Momba inatarajiwa lini kujengewa kiwanda na cha aina gani?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa uchumi wa viwanda umeainishwa katika Mpango wa pili wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/2017-2020/2021). Lengo kuu la Mpango huo ni kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Katika ujenzi wa uchumi wa viwanda, jukumu la Serikali ni kuweka mazingira wezeshi ikijumuisha sera na mikakati rafiki kwa wawekezaji pamoja na miundombinu wezeshi na miundombinu saidizi wakati shughuli za biashara na ujenzi wa viwanda zikiwa ni jukumu la sekta binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza hili Serikali imeendelea kuhamasisha ujenzi wa uchumi wa viwanda kwa kuelekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia Mikoa na Wilaya kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda ikiwemo Halmashauri ya Momba ambao wametenga ekari
• kwa ajili ya viwanda. Lengo la mpango huo ni kuwa na maeneo ya kutosha kujenga viwanda sasa na baadaye. Kuelimisha wananchi juu ya ujenzi wa uchumi wa viwanda, kuvutia wawekezaji na kuboresha mazingira ya kufanya biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Halmashauri ya Momba na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) itaongeza juhudi ya kuhamasisha wawekezaji wa ndani na wa nje kujenga viwanda Wilayani Momba kutegemeana na fursa za uwekezaji zilizopo.
MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza ajira kwa Watanzania waliohitimu Vyuo bila kujali kada walizosomea ambao mpaka sasa wapo mitaani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha wahitimu wa vyuo wanapata ajira za kuajiriwa na kujiajiri Serikali imeendelea na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuongeza fursa za ajira kama ifuatavyo:-
(a) Kusimamia utekelezaji wa sera ya uchumi wa viwanda kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji katika viwanda nchini kupitia sekta binafsi kwa lengo la kutengeneza nafasi nyingi za ajira.
(b) Utekelezaji wa miradi mikubwa nchini, ikiwemo mradi wa bomba la mafuta, ujenzi wa reli ya kisasa na ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa nishati kupitia miradi mbalimbali ambayo yote kwa ujumla itasaidia kupanua wigo wa nafasi za ajira.
(c) Kutoa elimu kwa vijana kuhusiana na masuala ya ajira kwa lengo la kuongezea ufahamu mpana katika masuala ya ajira na kuongeza uwezo wa kujiamini katika kujiajiri kupitia sekta mbalimbali za kilimo, ufugaji, uvuvi na ujasiliamali.
(d) Kuandaa na kusimamia utekelezaji wa programu ya Taifa kukuza ujuzi nchini ambayo ina lengo ya kutoa mafunzo kwa vitendo sehemu ya kazi kwa wahitimu wa vyuo. Mafunzo haya yatawapatia wahitimu wa vyuo ujuzi unaohitajiwa na waajiri, hivyo kuwawezesha kuajirika.
(e) Kuendelea kuwezesha vijana kujiajiri kwa kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu kupitia Mfuko Maendeleo ya Vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji programu ya Taifa kukuza ujuzi ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuwezesha vijana kuajirika na kupunguza tofauti ya ujuzi uliopo katika nguvu kazi na mahitaji ya soko la ajira.
MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:-
Tatizo la maji Wilaya ya Momba halijapatiwa ufumbuzi wa kudumu mpaka sasa.
Je, ni lini Serikali ya Awamu ya Tano itamaliza tatizo hilo katika Wilaya ya Momba?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI aliuliza:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua tatizo la maji katika Wilaya ya Momba katika utekelezaji wa Awamu ya Kwanza ya Programu ya Maendeleo ya Maji yaani WSDP, Serikali imekamilisha ujenzi wa miradi sita katika Vijiji vya Namtambalala, Iyendwe, Itumbula, Mnyuzi, Chilulumo na Kamsamba katika Jimbo la Momba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Awamu ya Pili ya Utekelezaji ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, jumla ya vijiji 10 vimependekezwa ili kuendelea kuboresha huduma ya maji katika Halmashauri ya Momba. Vijiji vilivyopendekezwa ni pamoja na Vijiji vya Ikana, Namsinde, Nkangamo, Mpapa, Chole, Itelefya, Chitete, Tindingoma, Kasinde na Samang’ombe. Serikali itaendelea kutatua tatizo la majisafi na salama kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kubaini vyanzo vipya vya maji na kujenga miundombinu ya maji katika Halmashauri ya Momba kwa kadri fedha zitakavyopatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Serikali imechimba visima virefu viwili katika vijiji vya Chitete na Tindingoma. Usanifu wa miradi hiyo miwili upo katika hatua za mwisho za kutangaza zabuni kwa ajili ya kuwapata wakandarasi wa ujenzi. Uchimbaji wa kisima kingine katika kijiji cha Ikan
MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:-

Katika kipindi cha hivi karibuni wananchi wamekuwa wakilalamikia mzunguko wa fedha kuwa mdogo:-

Je, hali hiyo imesababishwa na nani?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania inatekeleza Sera ya Fedha inayolenga kusimamia mzunguko wa fedha unaoendeana na mahitaji halisi ya uchumi kwa lengo la kudumisha utulivu wa mfumuko wa bei na hivyo kuweka mazingira mazuri ya ukuaji wa uchumi.

Mheshimiwa Spika, kabla ya mwaka 2017 kulitokea changamoto ya kuongezeka kwa mikopo chechefu ambayo kwa sehemu kubwa ilisababishwa na baadhi ya taasisi za fedha kutoa mikopo bila kuzingatia Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na Kanuni zake za mwaka 2008. Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali ilichukua hatua ya kusimamia kwa karibu Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 pamoja na Kanuni zake ikiwa ni pamoja na kuhamisha fedha za taasisi za umma kutoka kwenye mabenki ya biashara kwenda Benki Kuu ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kufuatia hali hiyo, kuanzia Januari, 2017, Serikali kupitia Benki Kuu ilichukua hatua za kuongeza ukwasi kwenye uchumi ili kutatua changamoto ya kupungua kwa mzunguko wa fedha katika soko. Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kushusha riba ya Benki Kuu (discount rate) kutoka asilimia 16 Machi, 2017 hadi asilimia 7 Agosti, 2018. Pili, Benki Kuu ilipunguza kiwango cha kisheria cha sehemu amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu na mabenki ya biashara (Statutory Miminimum Reserve Requirement, SMR) kutoka asilimia 10 hadi asilimia 8 mwezi Aprili, 2017. Tatu, kuruhusu mabenki kutumia asilimia 10.0 ya sehemu ya SMR kama chanzo kimojawapo cha kusaidia hali ya ukwasi kwenye uchumi. Mwisho, Benki Kuu ilianzisha utaratibu wa kutoa mikopo ya muda maalumu kwa mabenki pamoja na kununua fedha za kigeni kutoka kwenye soko la jumla la mabenki ili kuongeza ukwasi kwenye uchumi.

Pili, Benki Kuu ilipunguza kiwango cha kisheria cha sehemu ya amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu na Benki ya Biashara (Statutory Minimum Reserve Requirement) kutoka 10% hadi 8% mwezi Aprili, 2017.

Tatu, kuruhusu mabenki kutumia 10% ya sehemu ya Statutory Minimum Reserve Requirement kama chanzo kimojawapo cha kusaidia hali ya ukwasi katika uchumi.

Mwisho, Benki Kuu ilianzisha utaratibu wa kutoa mikopo ya muda maalum kwa mabenki pamoja na kununua fedha za kigeni kutoka kwenye soko la jumla la mabenki ili kuongeza ukwasi kwenye uchumi.

Mheshimiwa Spika, hatua hizi za Sera ya Fedha zimesaidia kuboresha hali ya ukwasi kwenye Benki za Biashara na kupunguza riba katika Soko la Fedha baina ya mabenki kutoka wastani wa asilimia 4.6 kwa mwaka unaoishia Februari, 2018 hadi asilimia 2.3 kwa mwaka unaoishia Februari, 2019. Kuongeza kwa mikopo ya sekta binafsi kutoka wastani wa asilimia 1.7 mwaka 2017 hadi asilimia 7.3 Januari, 2019 na kupungua kwa riba ya mikopo kutoka wastani wa asilimia 21 mwaka 2016 hadi wastani wa asilimia 17 mwaka 2018.

Hivyo basi, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba kwa sasa hakuna tatizo la mzunguko mdogo wa fedha katika soko baada ya Serikali kuchukua hatua hizi. Pia mzunguko wa fedha katika uchumi unaendana na malengo na mahitaji halisi ya shughuli za kiuchumi zilizopo.
MHE. CECIL D. MWAMBE (K.n.y. MHE. DAVID E. SILINDE) aliuliza:-

Zoezi la usambazaji wa umeme wa REA katika Wilaya ya Momba bado haujakamilika hadi sasa:-

(a) Je, ni lini Serikali itaanza mchakato wa kupeleka umeme katika kata ambazo hazijafikiwa na miradi hiyo katika Jimbo la Momba?

(b) Je, ni lini mradi wa kuwasha umeme Tarafa ya Kamsamba utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Momba ina jumla ya vijiji 72, kati ya hivyo, Vijiji 13 vya Nkangano, Chiwanda, Isanga, Kakozi, Ndalambo, Chitete, Tindingoma, Ntungwa, Mkonko, Kamsamba, Masanyinta, Itumbula na Mpapa, vimepata umeme kupitia Mradi wa REA II na wateja wa awali 854 wameunganishiwa umeme. Jumla ya Vijiji 15 vya Halmashauri ya Momba vya Nakawale, Ikana, Ivuna, Ipatikana, Muungano, Myunga, Machindo, Mfuto, Isanga, Tindingoma na Kikozi vimepatiwa umeme kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza unaoendelea kutekelezwa na Kampuni ya STEG International Services. Kazi za kupeleka umeme katika vijiji hivi itakamilika ifikapo mwezi Juni, 2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi za mradi zinahusisha ujenzi wa kilometa 168 za njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 na kilometa 109 za njia za umeme msongo kilovoti 0.4, kufunga transfoma 37 na kuunganisha wateja wa awali 1,775. Gharama ya mradi ni shilingi bilioni 11.23. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2019, mkandarasi ameshafunga transfoma 15 kati ya 21 na kuwasha umeme. Jumla ya wateja wa awali 244 wameunganishiwa umeme. Mkandarasi anaendelea na kazi ya kuvuta waya kufunga transfoma katika Vijiji vya Ipata, Mpui, Msungwe na Kapele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tarafa ya Kamsamba ilipatiwa umeme kupitia Mradi wa REA awamu ya pili ambapo kazi ya kusambaza umeme katika baadhi ya vitongoji vya tarafa hiyo inaendelea chini ya TANESCO kwa bei ya shilingi 27,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kukamilika kwa Mradi wa REA awamu ya tatu, mzunguko wa kwanza, jumla ya vijiji 24 vitapatiwa umeme katika Halmashauri ya Momba. Vijiji 44 vilivyosalia vitapatiwa umeme katika Mradi wa REA II, mzunguko wa pili unaotarajia kuanza mwezi Julai, 2020.
MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani kwa sasa kutatua kero ya maji kwa uhakikia katika Jimbo la Momba?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika juhudi za kutatua tatizo la maji katika Jimbo la Momba, Serikali inaendelea kutekekeza miradi mitatu katika Vijiji vya Ndalambo ambapo ujenzi umekamilika kwa asilimia 95, Kijiji cha Chitete ujenzi umekamilika kwa asilimia 12 na Tindingomba ujenzi umekamilika kwa asilimia 80. Miradi hii ikikamilika, itahudumia jumla ya watu wapatao 23,397 na kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi, salama kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali imeanza kutekeleza miradi ya vijiji vitano kupitia Programu ya Malipo kwa Matokeo (PfR) katika Vijiji vya Mkulwe, Chiwanda, Kasinde, Ikana na Namsinde II kwa gharama ya Sh.805,885,340. Kukamilika kwa miradi hii, kutawezesha jumla ya watu 31,984 kupata huduma ya maji.
MHE. PASCAL Y. HAONGA (K.n.y. MHE. DAVID E. SILINDE) Aliuliza:-

Je, ni lini barabara ya Mlowo – Kamsamba – Kiliyamatundu – Kibaoni itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) Alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Mlowo – Kamsamba – Kiliyamatundu – Kibaoni yenye urefu wa kilometa 369 ni barabara ya Mkoa na inahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi. Aidha, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha ujenzi wa Daraja la Momba lenye urefu wa mita 84 na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 1.2.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina inaendelea kwa barabara kuanzia Kamsamba hadi Mlowo, kilometa 130.14 na barabara ya mchepuo kwa kuingia Makao Makuu ya Wilaya ya Momba, kilometa 15, kwa gharama ya shilingi milioni 765.46. Kazi hii imefikia asilimia 75.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 180 kwa ajili ya kufanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara na kuijenga kwa kiwango cha lami sehemu ya barabara hii kuanzia Kiliyamatundu hadi Kasansa (sehemu ya Kilyamatundu – Muze (km 142) na Ntendo – Muze (km 37.04), taratibu za kumpata Mshauri Elekezi wa kufanya kazi hiyo zinaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sehemu ya barabara kutoka Kasansa hadi Kibaoni (km 60), sehemu ya kuanzia Kibaoni hadi Majimoto (km 34) ipo kwenye hatua za manunuzi ya kumpata mshauri elekezi kwa ajili ya kufanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Kibaoni – Majimoto – Inyonga (km 162). Aidha, sehemu iliyobaki kuanzia Muze – Mamba – Majimoto (km 55) Serikali inatafuta fedha ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii kwa ajili ya usafiri wa wananchi na usafirishaji wa mazao ya chakula na biashara yanayozalishwa na wananchi wa maeneo ya Kata za Igamba, Hulungu, Itaka, Nambinzo hadi Kamsamba pamoja na maeneo ya Kiliyamatundu, Muze, Kasansa, Majimoto hadi Kibaoni, Serikali inaendelea kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kuifanyia matengenezo mbalimbali ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka na mara tu usanifu wa kina utakapokamilika, ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara hii utafanyika kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA (K.n.y MHE. DAVID E. SILINDE) aliuliza:-

Je, ni upi mpango wa sasa wa kutatua kero ya maji katika Jimbo la Momba?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Mheshimwa Maziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mpango wa sasa wa Serikali wa kutatua kero ya maji katika Jimbo la Momba ni kupitia utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP) ambayo inatekelezwa pia katika Halmashauri zote nchini. Programu hiyo imelenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na endelevu ya majisafi na salama.

Mheshimiwa Spika, kupitia pragramu hiyo, tayari katika Wilaya ya Momba Serikali imekamilsha miradi ya maji mitano katika vijiji vya Namtambala, Itumbula, Iyendwe, Mnyuzi na Chilulumo ambapo jumla ya wananchi 20,271 wanapata huduma ya maji.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/ 2019, Halmashauri ya Wilaya ya Momba imetengewa kiasi cha Sh.1,744,000,000 kwa ajili ya uchimbaji wa visima, usanifu na ujenzi wa miundombinu ya maji. Utekelezaji wa miradi hiyo uko katika hatua mbalimbali ambapo mradi wa maji katika Kijiji cha Tindingoma, mkandarasi amesaini mkataba kwa ajili ya ujenzi; Mradi wa maji katika Kijiji cha Kitete upo kwenye hatua za manunuzi; na kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa ujenzi wa mradi katika Kijiji cha Ikana upo kwenye hatua ya usanifu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hatua hizo zilizochukuliwa, Serikali pia ipo katika hatua ya manunuzi ya kumpata makandarasi wa kupima na kuchimba visima katika vijiji saba (7) vya Mpapa, Samang’ombe, Kasinde, Namsinde, Chole, Nkangamo na Itelefya. Vilevile, mkandarasi huyo atafanya usanifu wa mradi wa maji utakaotumia chanzo cha Mto Momba kwa kuhudumia vijiji 21 vya Ivuna, Lwate, Mkomba, Ntungwa, Kalungu, Sante, Tontela, Kaonga, Nsanzya, Chuo, Namsinde I, Kasanu, Masanyinta, Senga, Mweneemba, Makamba, Naming’ongo, Yala, Muuyu, Usoche na Makao Makuu ya Wilaya ya Momba.
MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:-

Nchi Wahisani na Wa shirika wa Maendeleo wamekuwa wakishindwa kuleta misaada na ahadi zao kwenye utekelezaji wa Bajeti ya Maendeleo kwa wakati na nyakati nyingine kushindwa kuleta kabisa katika kipindi cha miaka mitatu ya fedha mfululizo iliyopita ya 2016/2017, 2017/ 2018 na 2018/2019:-

Je, Serikali inatueleza ni kitu gani kinasababisha hali hii?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikishirikiana na nchi Wahisani pamoja na Washirika wa Maendeleo katika kutekeleza Bajeti yake kwa kupokea fedha za Bajeti ya Maendeleo kupitia Misaada na Mikopo nafuu kwa mujibu wa makubaliano ya kimkataba.

Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo kuanzia 2016/2017 hadi 2018/2019 Washirika wa Maendeleo wamekuwa wakitimiza ahadi zao kwa wastani wa zaidi ya asilimia 77 kwa mtiririko ufuatao:-

Mheshimiwa Spika, mw aka 2016/2017 ki asi kilichopokelewa kutoka kwa Washiriki wa Maendeleo kilikuwa ni shilingi bilioni 2,474 sawa na asilimia 69 ya lengo la kipindi hicho la kupokea shilingi bilioni 3,601; mwaka 2017/2018 kiasi kilichopokelewa kilikuwa ni shilingi bilioni 3,351 sawa na asilimia 84 ya lengo la kipindi hicho la kupokea shilingi bilioni 3,971; na mwaka 2018/2019 kiasi kilichopokelewa kilikuwa ni shilingi bilioni 2,082 sawa na asilimia 78 ya lengo la kipindi hicho la kupokea shilingi bilioni 2,676.

Aidha, katika kipindi cha kuanzia Julai, 2019 hadi Februari, 2 020 fe dha za mis aa da na mikop o nafuu zilizopokelewa kutoka kwa Washirika wa Maendeleo zimefikia jumla ya shilingi bilioni 1,631.19 sawa na asilimia 90 ya lengo la kipindi hicho.

Mheshimiwa Spika, kwa takwimu hizi, siyo sahihi hata kidogo kusema kwamba kuna nyakati nyingine Washirika wa Maendeleo wamekuwa hawatimizi ahadi zao kabisa.