Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Oran Manase Njeza (37 total)

MHE. ORAN M. NJENZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, kwanza napenda kumshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na vilevile kuipongeza Wizara hii kwa kazi nzuri inayoifanya kwa kusambaza umeme karibu vijiji vyote vya Tanzania hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuwapongeza Mainjinia wa TANESCO waliopo pale Mbeya akiwemo Engineer Maze na Engineer Kiduko pamoja na Engineer Mbalamwezi. Pamoja na hayo, napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Wizara ina mpango gani wa kusambaza umeme pamoja na hii REA kwenye vitongoji vilivyobaki katika vijiji hivyo vilivyotajwa? (Makofi)
Swali la pili, kutokana na ongezeko la usambazaji wa umeme vijijini, inaelekea capacity ya watumishi wa TANESCO ikiwemo vifaa, haitoshelezi tena.
Je, Wizara ina mkakati wa kuhakikisha kuwa inaongeza capacity ya watumishi ili iendane pamoja na usambazaji wa umeme vijijini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na Mheshimiwa Mbunge, ni kweli kabisa, pamoja na mradi huu kabambe wa REA kuendelea kufanya kazi yake, lakini bado kuna miradi mingine itaendelea kwa ajili ya kukamilisha shughuli zinazoachwa na REA. Baadhi ya kazi zinazoendelea hapa sambamba na miradi ya REA ni pamoja na mradi wa Underline. Mradi wa Underline unaendelea kupita kukamilisha maeneo ambayo yanaachwa na TANESCO pamoja na REA.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusiana na uwezo na capacity pamoja na management, ni kweli kabisa, kama mnavyojua, TANESCO ni shirika la zamani, lakini tuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge pamoja Serikali ya Awamu ya Tano, ni kwamba tunapata uwezo wa kuongezewa nguvu. Kwa sasa hivi tunaongezewa nguvu Shirika letu la TANESCO kwa maana ya kulinunulia vifaa vya kutosha kama transfoma pamoja na generetors ambako tunatumia mafuta. Kwahiyo, Mheshimiwa Mbunge nimhakikishie kwamba Shirika la TANESCO pamoja na REA pamoja na miradi mingine, itaendelea kuimarishwa ili ifanye kazi zake vizuri.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana Mwenyekiti, na pia nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini nina maswali madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mradi wa haya madini adimu duniani pamoja na joto ardhi ni muhimu sana kwa uchumi wa viwanda, naomba commitment ya Serikali, moja, je, ni lini wataanza uchimbaji wa joto ardhi ili tuweze kutumia kwenye viwanda vyetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, na pili, naomba pia commitment ya Serikali pamoja na mradi wa Ziwa Ngozi, je, Serikali imetoa leseni ngapi za uchimbaji na uzalishaji wa madini na nishati ya joto ardhi katika sehemu zingine hapa kwetu Tanzania? Ahsante.
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya ni lini tunaanza, utafiti umeshafanyika, unaonesha kwamba ili upate umeme wa joto ardhi unahitaji kuwa na temperature ambayo iko katikati ya nyuzi 180 mpaka 240 celsius. Sasa bahati nzuri hii ya Ngozi iko zaidi ya 240. Kwa hiyo, kinachofuata sasa kwa miezi michache ni kwamba inabidi tuchoronge miamba pale chini tuweze kujua kuna mvuke kiasi gani ambao utaendesha mashine ya kuzalisha umeme wa kiasi gani. Kwa hiyo, tutatoa hiyo tarehe baada ya kujua tuna mvuke wa chini kiasi gani yaani steam.
Mheshimiwa MWenyekiti, na leseni ngapi zimetolewa, ni kwamba tumeshatengeneza ramani ya nchi nzima ambayo inaonesha maeneo yote ambayo tunaweza kuendeleza joto ardhi. Kwa sasa hivi ukiacha ya Ngozi, Mbeya eneo lingine ni la Luhoi kilometa kama 70 Kusini Mashariki mwa Dar es Salaam, halafu na lingine liko sehemu za Kusini mwa Morogoro na Ziwa Natroni kwa hiyo maeneo ni mengi lakini tunaenda hatua kwa hatua.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
Kwa kuwa Waziri amepotoshwa kwenye jibu (b) sehemu ya kwanza ya swali langu na hivyo kuwapotosha wananchi wa Mji Mdogo wa Mbalizi na pia kulipotosha Bunge; je, Waziri atachukua hatua gani kwa Afisa huyo aliyempotosha?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ndani ya Mji Mdogo wa Mbalizi kuna ardhi ya zaidi ya ekari 5,000 iliyokuwa Tanganyika Packers, na haijaendelezwa kwa zaidi ya miaka 30 sasa na kwa kuwa Halmashauri ya Mbeya imetenga eneo mahsusi kwa kunenepesha mfugo na kwa ajili ya kiwanda cha nyama, je, ni lini Serikali itarudisha ardhi hiyo kwa Halmasahuri ya Mbeya kwa madhumuni ya makazi bora na huduma za jamii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Sasa naomba nitoe msisitizo katika eneo la kwanza ni kwamba Ofisi ya Rais - TAMISEMI tunapofanya hizi kazi tunahakikisha kwamba coordination inakamilika vizuri. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge kama unaona kwamba kuna mapungufu, naomba u-clarify ni eneo gani ambalo linaonekana halijakuwa sawasawa, ili mimi kama Naibu Waziri, Ofisi ya Rais TAMISEMI nijue kwamba eneo gani ambalo halikukaa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la opotoshaji limekuwa la jumla, lakini hili tulilielekeza katika ofisi zote za mikoa, kwamba ma-RAS wote wako responsible katika majibu yote yanayojibiwa na TAMISEMI. Kwa hiyo, nilitaka angalau ungenipa ufafanuzi ni eneo gani uliona kwamba lilikuwa na mapungufu tuweze kulifanyia kazi kubwa, kwa sababu lengo kubwa ni kujenga, kwamba ni jinsi gani majibu yawe sawasawa kwa ajili ya kuboresha mahitaji ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika eneo la pili…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri amesema hivi swali lake kipengele (b) hakijajibiwa kabisa kwa maana hiyo, kwa sababu umepotoshwa majibu ya kipengele chote.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kuhusu swali la ni lini Serikali itarudisha eneo hili kwa ajili ya wananchi, mimi nilifika pale Mbeya nilipokwenda kutembelea Iyunga lakini nikafika katika Jimbo la Mheshimiwa. Mimi naipongeza Serikali kwa sababu kuna juhudi kubwa imefanyika, sasa pale kuna machinjio ya kisasa kwa ajili ya uchinjaji wa nyama tena wa kisasa katika eneo hilo la Mbeya. Lakini kwamba kuna eneo kubwa sasa eneo hili jinsi gani litafanyiwa kutwaliwa kurudishwa kwa wananchi kwa ajili ya makazi, nadhani sasa jambo hili ni jambo la mchakato, si jambo la kutoa maelekezo tu hapa, nini kifanyike haraka haraka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu lazima tufanye tathimini ni kitu gani kilichokuwepo hapo, kwa sababu inawezekana ukienda ndani kuna migogoro mingine ya ziada. Kwa hiyo, naomba niseme kwamba hilo ni suala zima la mchakato, naamini kwamba Baraza la Madiwani likikaa litafanya maamuzi litapeleka mapendekezo halafu vyombo husika vitakuja kufanya tathimini. Vitakaporidhika TAMISEMI - Ofisi ya Ardhi tutafanya tathimini ya kinakuona kama eneo hilo linaweza likarudishwa kwa ajili ya maslahi ya wananchi ili wananchi wapate huduma ambayo inahitajika katika maeneo yao.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Nashukuru pia kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na pia nashukuru kwa juhudi za misaada ya UNICEF kwa kuboresha elimu kwenye Halmashauri ya Mbeya na sehemu nyingine za nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi hizo, changamoto nyingi, hasa kwa shule za vijijini ni miundombinu. Ukichukulia mfano wa Jimbo langu la Mbeya Vijijini, Shule ya Msingi Ipwizi ya ina walimu wawili na wanafunzi wanaozidi 200; Shule za Iyanga, Shule za Ivwanga hazina hata mwalimu na hizo ziko karibu sana na Jiji la Mbeya.
Mheshimiwa Spika, shule nyingine kama za Kitusi na Ivwanga wanafunzi wanatembea zaidi ya kilometakumi kwenda Mkoa mpya wa Songwe kwa ajili ya kujipatia elimu.
Je, ni kwa nini misaada hii haijalenga kwenye changamoto muhimu za miundombinu katika shule zetu za vijijini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni kweli hili jambo analolisema Mheshimiwa Mbunge lipo na juzi tarehe tano tulipokuwa katika Mkutano wa Programu ya Walimu ya Mpango wa KKK pale Rungwe miongoni mwa changamoto ambayo niliiona ni kwamba kuna mshiriki mmoja alishindwa kuhudhuria mafunzo yale kwa sababu idadi ya walimu ni chache katika shule yao. Na ndiyo maana juzi tulikubaliana kwamba RAS Mkoa wa Mbeya anaweza kupitia michakato ya mgawanyo wa walimu katika shule zote kwa sababu imebainika kwamba kuna baadhi ya walimu wamelundikwa katika baadhi ya maeneo na maeneo mengine wamekosa walimu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa hili jambo unalosema sio jambo la uongo.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwa Mkoa wa Mbeya jambo hilo lipo na RAS Mkoa wa Mbeya Mama yangu Mariam Mtunguja, amelibeba hili na tumekubaliana ndani ya mwezi huu atafanya reallocation vizuri ya walimu katika Mkoa wake wa Mbeya.
Mheshimiwa Spika, lakini suala zima la ajenda ya miundombinu ni kweli naomba tuendelee kushirikiana. Lakini wakati mwingine hii misaada inayotoka kwa wafadhili, inawezekana wao wana malengo yao maalum katika eneo lao.
Mheshimiwa Spika sisi kwanza tunapenda kuwashukuru sana wenzetu wa UNICEF kwa kazi kubwa wanayofanya, na tutajitahidi vile vile kuwashawishi wadau mbalimbali katika baadhi ya misaada, japokuwa itakuwa na capacity building, basi tutatafuta wengine ambao wataweza kutusaidia katika suala zima la infrastructure, jinsi gani tutawekeza miundombinu katika maeneo yetu, lengo kubwa ni kupunguza kero kwa wananchi wetu na hasa watoto wetu wanaotembea umbali mrefu.
MHE ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyo kwenye Mji mdogo wa Maswa tuna tatizo kama hilo kwa Mji wetu Mdogo wa Mbalizi, ambapo Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliahidi kumalizia kipande kidogo cha barabara ya kilometa moja na pia aliahidi kumalizia ujenzi wa stand pale Mbalizi lakini mpaka leo hakuna chochote kinachofanyika labda ningepena Waziri ajaribu kutoa ufafanuzi ni lini ujenzi huo utaanza? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI YA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Ujenzi kwanza naomba tukiri wazi kwamba bajeti katika kipindi ambacho Dkt. John Pombe Magufuli anaahidi bajeti yake ndio kwanza hii tunaanza bajeti ya kwanza na baadaye tuna miaka mitano. Lakini ameahidi stand na amewaahidi barabara ya kilomita moja. Mheshimiwa Mbunge, naomba nikwambie kwamba, ahadi ya Rais itakuwepo palepale na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu kazi hii na sisi tuliopewa dhamana ya kuisimamia, tutaisimamia kwa karibu zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutaisimamia kwa karibu zaidi, lengo ni kwamba, ahadi ya Rais aliyoitoa, ujenzi wa stand, ujenzi wa barabara ya kilometa moja itafanyika na muweze kuona kwamba, maeneo mbalimbali sasa hivi stand zinajengwa kupitia miradi yetu sio stand tu, kuna ma-dampo, kuna barabara. Kwa hiyo, nikwambie Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, katika maeneo ya Mbalizi ni kwamba, watu wawe na subira hii ndio bajeti yetu ya kwanza imeanza. Imani yangu ni kwamba, maeneo ya Mbalizi, kama Mheshimiwa Rais alivyoahidi, suala lile litatekelezwa.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Napenda na mimi kuuliza swali dogo la nyongeza. Pamoja na Jimbo la Mbeya Vijijini kuwa na vyanzo vya uhakika wa maji kutoka Mlima Mbeya, lakini maji yamekuwa yakipelekwa Jijini Mbeya badala ya kupelekwa kwenye sehemu zenye uhaba mkubwa wa maji kwenye vijiji vya kata ya Mjele na Utengule Usongwe. Je, ni lini Wizara itapeleka maji safi kwenye vijiji vya kata za Mjele na Utengule Usongwe?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru ameuliza swali zuri sana, ni swali la kisera. Nimhakikishie kwamba tayari tumeshatoa maelekezo eneo lolote ambalo chanzo cha maji kinaanzia pale, vijiji vilivyo karibu na chanzo ndiyo viwe vya kwanza kupata maji.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili tunalielekeza kwa Wakurugenzi wa mamlaka ambao wanahusika na huo mradi, wahakikishe katika eneo hilo kwanza wanawapa maji wananchi waliopo pale baadaye sasa ndiyo wanapeleka maeneo mengine ya mjini. Kwa hili, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nitalifuatilia mimi mwenyewe.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kama ilivyo kwenye Jimbo la Busokelo kuna barabara ya Mbalizi kwenda Makongorosi ambayo inapitia kwenye Bonde la Ziwa Rukwa ambayo tumegundua neema ya gesi nyingi sana. Sasa ni lini Serikali itajenga barabara hiyo ya Mbalizi - Makongorosi kwa kiwango cha lami ambayo ni ya Mkoa wa Mbeya na Mkoa wa Songwe? Ahsante.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali tunaifahamu barabara hiyo na tuna mpango thabiti wa kuijenga. Lakini kwanza tupo katika mchakato wa awali hapo utakapo kamilika tutamtafuta mkandarasi ili tuweze kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
MHE. ORAN M. NJENZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, suala la Mji Mdogo wa Mbalizi kuna changamoto kubwa za maji kama iliyokuwa kwa Mji wa Mikumi. Je, ni lini mtatatua changamoto kubwa ya maji kwenye Mji Mdogo wa Mbalizi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya tuliwasiliana nae nikiwa kwenye ziara Mbeya na tukawa tumekubaliana kwamba tufanye mapendekezo, Wizara imeshaagiza tayari kwamba Mamlaka ya Maji ya Mkoa wa Mbeya ijipanue ili iweze kuhudumia mpaka eneo la Mbalizi. Tayari wanaendelea na utaratibu huo wameshafanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbalizi na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbalizi ameonekana kuridhia ili Mamlaka ya Maji ya Mbeya iweze kupeleka miundombinu mpaka Halmashauri ya Mbalizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niahidi kwamba taratibu hizi zitakamilishwa na wananchi wa Mbalizi watapata huduma ya maji kutokana na Mamlaka ya Maji ya Mji wa Mbeya.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kupewa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kumshukuru Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo kwa mkutano tuliofanya na wakulima na wawakilishi wa Wanunuzi mwishoni mwa mwaka 2016.
Mheshimiwa Spika, katika mkutano huo tulikubaliana kuwa wanunuzi wadogo wapewe leseni ya muda na vile vile wajiunge kwenye vikundi na pia hii Kampuni ya pareto ambayo ilikuwa imebinafsishwa kutoka Serikalini kulikuwa na asilimia 10 ambazo walipewa wakulima. Vilevile katika hicho kikao tulikubaliana kuwa zichunguzwe hizo asilimia kumi ziko kwa nani kwa vile wakulima hawakupewa hizo asilimia kumi.
Mheshimiwa Spika, pamoja na makubaliano yote hayo, hakuna hata kimoja kilichozingatiwa na leo hii kuna kampuni mpya mbayo imejenga kiwanda eneo la Inyara, Mbeya ambayo imezingatia vigezo vyote na ilipewa leseni ya kununua pareto kwenye vijiji viwili tu kati ya vijiji zaidi ya 20 vinavyolima pareto. Sasa ni kwa nini Serikali isiboreshe hii Bodi ya Pareto ili tuweze kuboresha kiwango cha zao la pareto?
Mheshimiwa Spika, nashukuru.
La pili vilevile nilitaka kupata uhakika wa Serikali, kwa sababu inavyoelekea hakuna ushindani sasa hivi, watatuhakikishia vipi ya kwamba hawa ambao wametimiza vigezo vyote wanaruhusiwa kununua pareto ili inunuliwe kwa ushindani? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwanza nikiri kwamba Mheshimiwa Njeza amekuwa akifuatilia sana maslahi ya wakulima wake wa pareto, kahawa na mahindi. Kwa hiyo, tumekuwa naye karibu sana. Vilevile nikiri kwamba tulifanya kikao na wakulima, mkutano ambao ulitusaidia sana kupata makubaliano kuhusu namna bora ya kuendesha zao la pareto.
Mheshimiwa Spika, kutokana na mazungumzo yetu, baadhi ya masharti ambayo wakulima na wawakilishi wao tulikubaliana watekeleze, bado wako mbioni kutekeleza na hivyo bado tunasubiri kutoka kwao.
Mheshimiwa Spika, vile vile kuhusiana na leseni ya kampuni za kununua pareto; nilieleze tu Bunge lako Tukufu kwamba zao la pareto ni zao lenye masharti tofauti kidogo na mazao mengine kwa sababu tunachoruhusu kipelekwe nje siyo pareto ghafi, siyo maua, bali ni sumu ghafi. Katika maana hiyo, ili uweze kupeleka nje lile zao ni lazima uwe na kiwanda.
Mheshimiwa Spika, tunafanya hivyo kwa sababu huko nyuma wakati tulikuwa tunaruhusu kupeleka maua nje, kiwango cha pareto yetu kilishuka sana kwa sababu hatukuwa tunaweza kudhibiti ubora wa sumu inayopelekwa nje, ndiyo maana tukaleta ili kunusuru zao lisije likaanguka nchini. Tukaleta kigezo kwamba ni lazima uweze kuwa na kiwanda ili uweze kuzidua au kuchakata na kuwa sumu ghafi.
Kwa hiyo, kampuni yoyote ambayo imekidhi masharti hayo, katika hali ya kawaida tunaruhusu inunue pareto. Kampuni ambayo anaizungumzia ya TAN Extract ya Mbeya ambayo ndiyo imeingia tu sokoni na kutimiza masharti, tutaendelea kutoa leseni ili waweze kununua pareto maeneo mengine zaidi ya vijiji ambavyo wanatoa sasa.
Vilevile nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa hatujaona kwamba tatizo ni Bodi ya Pareto lakini ni kanuni na sheria ambayo tumewekeana wenyewe kama wadau na Serikali iko tayari kuirejea na kuangalia upya sheria na kanuni hizo kama itaonekana inafaa.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Kama ilivyo kwa Jimbo la Kwela, kuna barabara mbili ambazo ziliahidiwa na Mheshimiwa Rais; Barabara ya Mbalizi kwenda Makongorosi ambayo inaunganisha Mbeya na Mkoa mpya wa Songwe. Pia kuna barabara ya Isyonje – Kikondo – Makete mpaka Njombe ambayo vile vile inaunganisha Mikoa ya Mbeya na Njombe ziliahidiwa na Rais kwamba zitajengwa kwa kiwango cha lami. Je, ni lini hizi barabara zitajengwa kwa kiwango cha lami pamoja na kulipa fidia wale wote ambao ni waathirika.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba serikali imeshaanza kuchukua hatua za dhati kabisa za kujenga barabara ya kutoka Isyonje – Makete na hiyo barabara yote tumeshaanza hatua na kwamba wakandarasi wameshatafutwa na nadhani anafahamu Mheshimiwa Mbunge na hasa nikijua amemuulizia vile vile Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Miundombinu ambaye naye yupo katika barabara hiyo. Nimhakikishie Serikali itatekeleza kile ambacho imekusudia na imeanza kukitekeleza.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa ajili ya matatizo ya migogoro ya wafugaji na wakulima, maeneo mengi yanahitaji sasa hivi kuwe na vituo vidogo vya Polisi. Je, Serikali au Wizara inatupa commitment gani kuwa kutakuwa na vituo vya Polisi katika maeneo hayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa wananchi wamekuwa wakijitolea kujenga vituo vya Polisi kama ilivyokuwa kwa kituo cha Polisi cha Wilaya ya Mbeya ambao wamejenga kwa asilimia karibu zaidi ya 50. Je, Serikali inawaahidi nini wale wananchi wa Mbalizi kuwaunga mkono kuwamalizia kile kituo chao cha Polisi? Ahsante.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpe pole Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete kwa kupatwa na msiba na ndiyo maana hajaweza kuwepo kuuliza swali. Mungu ampe moyo wa ustahimilivu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la nyongeza alilouliza Mheshimiwa Oran; moja kituo cha Mbeya ambacho wameshafanya kazi kubwa sana nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amefanya hamasa kubwa sana na najivunia kwamba nilikwenda kumuunga mkono wakati wa kampeni. Kwa kuwa amefanya kazi kubwa sana na sisi kama Wizara tuna bajeti ambayo tumetenga kwa ajili ya umaliziaji wa majengo ambayo yameshafikia hatua kubwa. Hivyo, tutafanya ziara, tutajionea na tutaweka wataalam ili waweze kukadiria na kwenda kwenye utekelezaji wa umaliziaji ili nguvu ya wananchi isiweze kupotea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ujenzi wa vituo karibu na maeneo ambayo yanakuwa na migogoro ya mara kwa mara, Serikali inaendelea kufanya utaratibu wa kuweza kuwepo vituo hivyo lakini pale ambapo vituo hivyo havipo tutaendelea kufanya doria ili kuweza kuhakikisha kwamba tunawahakikishia wananchi usalama wao punde panapokuwepo na migongano ya aina hiyo hata kama bado hatujaweka vituo vya Polisi.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kuna shule Shikizi nyingi ambazo zina Walimu wa kujitolea na hawapati posho. Je, ni lini Serikali itaanza kuwalipa posho hawa Walimu wanaofundisha kwenye Shule Shikizi? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, katika jambo hili nadhani kila Halmashauri ina mkakati wake ku-address matatizo ya watumishi katika maeneo mbalimbali; na kuna baadhi ya maeneo mengine utakuta watu wanatumia own source kuonesha jinsi gani wana-address hili jambo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kuna mambo specific katika eneo la Mheshimiwa Njeza, tutalichukua halafu tuangalie jinsi gani tutafanya kuona nini kimetokea huko ilimradi tuliweke sawa ili kila mtu apate stahiki yake. Kama kuna maeneo mahususi katika Halmashauri husika, basi tutayatoa kwa lengo la kuweka mustakabali mzuri katika maeneo yetu hayo.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kupata tafsiri ya jina langu.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali yanayotia moyo, pamoja na kuwepo na jitihada za kuweka mfumo mzuri wa masoko, bado mfumo wa masoko umedhoofishwa na kuwepo kwa wanunuzi wachache ambao wamekuwa wakiwadidimiza wakulima kwa bei isiyokuwa ya ushindani.
Swali la kwanza, je, ni kwa nini zao la pareto lina mnunuzi mmoja ambaye anajipangia bei anavyotaka mwenyewe?
Swali la pili, je, ni kwa nini tumeshindwa kuanzisha soko la bidhaa (commodity exchange) ambayo imekuwepo toka mwaka 2014?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, kwa nini soko la pareto lina mnunuzi mmoja. Naomba nimueleze Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kipindi kirefu pareto imekuwa inanunuliwa na mtu kwa sababu masharti yaliyopo katika ununuzi wa zao la pareto ni kwamba ni lazima mnunuzi awe na kiwanda kwa sababu kinachouzwa kwenye pareto siyo maua ni ile sumu. Sasa kama hatujui kiwango cha sumu kilichopo kwenye maua ni vigumu sisi kujua bei ambayo wakulima wetu wanapata vilevile ni vigumu hata kukokotoa kodi ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, naomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa kuna kiwanda cha pili kimejengwa Mbeya, kwa hiyo tunaamini kwamba kitaongeza ushindani. Nafahamu ameshaniletea malalamiko mara nyingi sana kwamba pamoja na kuja na hichi kiwanda bado kuna vizingiti vya kuhakikisha kwamba kiwanda cha pili nacho kinaruhusiwa kununua pareto, naomba tu nimhakikishie yeye pamoja na wakulima wake kwamba mimi mwenye nitafuatilia kuhakikisha kwamba huyu mnunuzi mpya aliyeingia sokoni anaruhusiwa kununua bila vizingiti vyovyote.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili la commodity exchange. Ni kweli kwamba kwa muda sasa Serikali imekuwa ikifikiria kuanzisha mfumo wa commodity exchange kama namna mojawapo ya kutafuta masoko kwa ajili ya mazao yetu. Ili tuweze kuanzisha mfumo wa commodity exchange ambayo kimsingi ni mfumo wa kisasa zaidi wa stakabadhi ghalani unaotumia teknolojia kubwa zaidi na unaoweza kuunganisha mazao yetu katika soko la dunia tunahitaji vitu vingi sana ikiwa ni pamoja na teknolojia yenyewe ni lazima tuwe na maghala ambayo yanakidhi sifa za Kimataifa, vilevile lazima tuweze kufanya na uzalishaji ule wa bidhaa ambao unapatikana kwa quality ile ambayo inahitajika na kwa viwango ambavyo soko la dunia linahitaji.
Kwa hiyo, tunafikiri kwamba wakati tunaendelea kuboresha mazingira yetu ya ndani tutaendelea kwa sasa kutumia utaratibu wa stakabadhi ghalani na tumeona mafanikio makubwa sana kwenye korosho na tayari tunaelekea kutaka kuuza mazao mengine kama mbaazi, ufuta kwa kutumia utaratibu huo. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba hatujalitupa lakini bado tunaboresha mazingira ili iweze kufanikiwa kwa urahisi zaidi.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana vilevile nishukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kazi zilizokuwa zinaendelea zilizokuwa zinafanywa na Halmashauri na hizo zimehamishiwa kwenye TARURA sasa hivi. Je, ni lini TARURA wataanza na kuendeleza hizo kazi?
Swali la pili, kama ilivyo katika Mji Mdogo wa Rujewa vilevile Mheshimiwa Rais aliahidi kumalizia ujenzi wa kituo cha mabasi cha Mbalizi katika Mji Mdogo wa Mbalizi.
Je, ni lini kazi hiyo ya kujenga kituo cha mabasi cha Mji Mdogo wa Mbalizi kitaanza? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tumekuwa na kipindi cha mpito ambapo kazi za ujenzi wa barabara katika Halmashauri zilikuwa zikisimamiwa ndani ya Halmashauri zetu, lakini chini ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Sasa hivi tumeunda Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini ambao unaitwa TARURA sasa umeshaanza kuchukua majukumu hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, tunafahamu wazi kwamba kulikuwa na mikataba mingine na kazi mbalimbali zilikuwa zinaendelea na tulitoa maelekezo katika ofisi yetu kwamba zile kazi zote kutokana na mikataba iliyokuwa inaendelea ambazo ziliingiliwa na Halmashauri kazi zile zilipaswa kuendelea, isipokuwa taratibu za malipo ndio zilikuwa zinafanyiwa utaratibu maalum. Tulitoa maelekezo haya kwa Mameneja wa TARURA katika nchi nzima katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hata hivyo, wakati mwingine kulikuwa na uelewa tofauti katika baadhi ya maeneo, baadhi ya maeneo kazi zilikuwa zinaendelea vizuri lakini sehemu zingine kazi zilisimama, kazi kubwa iliyofanyika ni kuhamisha zile akaunti ziweze kufanya kazi vizuri ili utaratibu uendelee kufanyika kama ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na concern yako Mheshimiwa Oran naomba niiagize Halmashauri yako Meneja kama kuna changamoto ambayo ameipata katika ofisi yake tuwasiliane na ofisi na hasa na Mtendaji Mkuu wa TARURA ampe maelekezo ya kutosha nini kifanyike, ili kazi kule site isiendelee kukwama, ziendelee kufanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala zima la ujenzi wa stendi hii ya Mbarali, naomba nilichukue hili halafu nijue kwamba kuna kitu gani kilichokubaliwa na imefikia hatua gani? Changamoto iko wapi? Hili naomba niwahakikishie ofisi yangu itasimamia kwa sababu ahadi ya Mheshimiwa Rais lazima itekelezwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilichukue jambo hili tutaenda kulifanyia kazi haraka iwezekanavyo, kuangalia nini tufanye ili kuhakikisha ile stendi inatengenezwa.(Makofi)
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza nianze kwa kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kufanya ziara katika Halmashauri ya Mbeya na katika ziara yake tuliahidi kuwa mradi wa Iwindi wananchi wangeanza kupata maji kabla ya Desemba mwaka 2017, je, ni lini mradi wa maji kwa Vijiji vya Izumbwe, Iwindi, Mwashiwawala na Mbalizi utakamilika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge wa Mbalizi, Mzee Njeza kwa kazi kubwa anayoifanya katika suala zima la kuhakikisha wananchi wake wanapata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa nilishafanya ziara kule lakini ipo changamoto baadhi yetu wataalam kushindwa kusimamia miradi. Moja, nataka nimhakikishie tu, katika hali niliyoiona nipo tayari kushirikiana naye lakini pia na watalaam wetu kwenda katika kusukuma miradi ile ili wananchi wake waweze kupata maji kwa wakati. Ahsante sana.
MHE. ORAN M. NJENZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, napenda vile vile kushukuru majibu ya Serikali na pia nipende kutambua jitihada zinazofanywa na Serikali ya mkoa na TANAPA vile vile kwa kushiriki katika ujenzi wa kituo cha afya pale Ilungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza kwa vile hii fidia ni ya muda mrefu 1965; je, Serikali inathibitisha kuwa hii fidia itakayolipwa mwaka huu itazingatia thamani na sheria zilizopo sasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa vile Mji wa Mdogo wa Igoma unakua kwa haraka sana na pale kuna eneo la hifadhi ambalo limezungukwa na mji; je, Serikali itakuwa tayari kuliachia lile ili liweze kutumiwa na shule pamoja na huduma zingine za kijamii? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu hilo swali, kwanza naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akifanya katika kufuatilia fidia hii ya wananchi wake na amefuatilia kwa muda mrefu na taarifa ziko nyingi sana na wananchi wajue kwamba Mheshimiwa Mbunge anafanya kazi nzuri sana hongera sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu fidia, kama nilivyosema kwenye swali la msingi tunafanya tathimini upya mwezi Februari mwaka huu. Kwa hiyo, baada ya tathimini hiyo ni wazi kabisa kwamba tutabaini kwamba mahitaji au fidia inayotakiwa italingana na hali halisi ya leo na si ya mwaka 1965. Kwa hiyo wananchi watapata nafasi nzuri kabisa ya kupata fidia inayostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maombi yanayohusu hapa kujenga makao makuu kutokana na ongezeko la watu. Naomba nitoe maelezo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza maeneo mengi yameleta maombi ya namna hiyo yanayofanana, lakini hili ombi ambalo amelileta Mheshimiwa Mbunge nimhakikishie tu nitachukua jukumu la kwenda kwanza kukutana na wananchi wenyewe ili niangalie hilo eneo kama kweli linafaa kutolewa kwa ajili ya huduma za jamii. Hata hivyo, mkazo zaidi utaendelea kusisitizwa kwamba hifadhi ni muhimu kuliko vitu vingine vyote.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Pamoja na Jimbo la Mbeya Vijijini kuzungukwa na milima inayotiririsha maji mwaka mzima, lakini wananchi katika vijiji vingi hawana maji salama.
Je, ni lini Serikali itajenga miundombinu kwa kuwapatia maji salama wananchi wa vijiji vya Mbeya Vijijini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tunaendelea na usanifu na baadhi tumeshasaini mikataba kwenye Jimbo lake kuhakikisha kwamba wananchi wote wa Mbeya Vijijini, Jimbo la Mheshimiwa Mbunge wanapata maji safi na salama. Tulikuwa tumebuni miradi kwenye vijiji kadhaa lakini baadae tukagundua kwamba yale maji yatakwenda kwenye kijiji cha mwisho na kuacha vijiji vya katikati, tumechelewa kwa sababu ya kuhakikisha kwamba tunaainisha na vijiji vya katikati. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mwaka ujao wa fedha mapema kabisa tutasaini mikataba, na mimi Mheshimiwa Waziri ameshanipangia ratiba, katika ratiba Mikoa nitakayoizungukia ni pamoja na Mkoa wa Mbeya. Kwa hiyo ntahakikisha tunaambatana na wewe kwenda kwako ili tuweze kuona hivyo vijiji vyenye uhaba mkubwa wa maji.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nashukuru. Katika milima ya Panda Hill Wilaya ya Mbeya kuna madini ya niobium ambayo yanatarajiwa kuchimbwa hivi karibuni. Je, Serikali imechukua hatua gani na tahadhari gani ili yasije yakatokea yale yaliyotokea kwenye Acacia na Barrick Gold Cooperation?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru sana, Mgodi wa Niobium hapa Tanzania ni mgodi pekee ambao unapatikana katika eneo la Songwe. Kinachofanyika sasa ni majadiliano kati ya Magereza ambako eneo la mgodi litachukua ili kuona kama kutakuwa na re-settlement na majadiliano kama yakikamilika.
Kwa hiyo, nimpe taarifa tu, taratibu zinazofanyika sasa ni majadiliano kati ya Kampuni pamoja na Magereza, taratibu zikishakamilika basi uwekezaji utaendelea.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kuna shule Shikizi nyingi ambazo zina Walimu wa kujitolea na hawapati posho. Je, ni lini Serikali itaanza kuwalipa posho hawa Walimu wanaofundisha kwenye Shule Shikizi? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, katika jambo hili nadhani kila Halmashauri ina mkakati wake ku-address matatizo ya watumishi katika maeneo mbalimbali; na kuna baadhi ya maeneo mengine utakuta watu wanatumia own source kuonesha jinsi gani wana-address hili jambo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kuna mambo specific katika eneo la Mheshimiwa Njeza, tutalichukua halafu tuangalie jinsi gani tutafanya kuona nini kimetokea huko ilimradi tuliweke sawa ili kila mtu apate stahiki yake. Kama kuna maeneo mahususi katika Halmashauri husika, basi tutayatoa kwa lengo la kuweka mustakabali mzuri katika maeneo yetu hayo.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Wizara. Nikiri kweli kuwa wamefanya kazi nzuri ila katika haya majibu kuna Kijiji cha Mbuyuni bado hakijapata umeme pamoja na kuwa kimeorodheshwa kuwa kimo kwenye orodha ya vilivyopatiwa umeme.
Mheshimiwa Spika, tatizo lingine ni umeme uliokwenda Idunde umeruka Vijiji vya Rukwa na Kapalala; Je, ni lini Serikali itahakikisha hivi vijiji vilivyobaki vya Kapalala, Mbuyuni na Rukwa vitapatiwa umeme ikiwa ni pamoja na vijiji vya Kata ya Ikukwa ambayo ni karibu sana na Jimbo la Songwe navyo vitapatiwa umeme?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, nakiri kuwa Serikali imefanya kazi nzuri ya kupeleka umeme vijijini, lakini kwa mazingira ya vijijini wanahitaji vilevile huduma kutoka TANESCO; Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kuwa kutakuwa na huduma kwa wateja ambazo zitakuwa karibu huko vijijini ili waweze kupata huduma pamoja na hii huduma nzuri iliyofanyika kwa mpango wa REA? Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na namshukuru sana Mheshimiwa Njeza kwa maswali yake mawili ya nyongeza. Nampongeza pia kwa kazi nzuri kwenye Jimbo lake.
Mheshimiwa Spika, katika maswali yake la kwanza amejielekeza kwenye Kijiji cha Mbuyuni ambacho anasema kiko kwenye orodha ya vijiji vyenye umeme, lakini pia hakina umeme. Naomba hili nilichukue ili tuweze kufuatilia takwimu hii na nitampa majibu ya uhakika.
Mheshimiwa Spika, pia, katika swali lake hilo alielekeza vijiji ambavyo vimerukwa ikiwemo vijiji vya Kata ya Ikukwe. Naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi vijiji vyote vilivyosalia 7,873 nchi nzima vitapata miundombinu ya umeme kwa mizunguko. Mzunguko wa kwanza na mzunguko wa pili.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, vile 3,559 vya mzunguko wa kwanza kazi inaendelea mpaka Julai, 2019 kisha tunaanza mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili. Kwa hiyo naomba nimthibitishe Mbunge maeneo ambayo yaliyosalia yatapatiwa miundombinu ya umeme kupitia REA awamu ya tatu mzunguko wa pili.
Mheshimiwa Spika, ameuliza suala la namna gani wananchi wa maeneo ya vijijini watapata huduma ya TANESCO. Naomba nilithibitishie Bunge lako Tukufu kuwa, kazi ya kupeleka miundombinu ya umeme inahusu vijiji vyote na tunatambua baadhi ya vijiji viko mbali na ofisi zetu za TANESCO ambazo ziko kila Wilaya, tumeielekeza TANESCO kufungua ofisi ndogo ndogo kwenye miji mikubwa na miji ambayo iko karibu na maeneo ya vijijini.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nikuthibitishie hilo linafanyika na tumeshapokea orodha ya ofisi za TANESCO ndogondogo mpya ambazo zingine zitajengwa lakini pia tumeomba pale ambapo, maana yake ujenzi ni suala la muda mrefu, lakini pale ambapo kuna maeneo ya vijiji kwenye Kata kuna Ofisi za Watendaji wa Kata, basi kipindi ambacho wataanza kuunganisha wateja tumeomba TANESCO waende kutumia hizo ofisi kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi wetu na nia ni kurahisisha utoaji wa huduma hizi kwa wananchi wa vijijini. Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, nina imani wahanga wengi akiwemo ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa atakuwa amefurahishwa sana na majibu haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bandari yetu ya Dar es Salaam ina ushindani mkubwa sana kutoka Bandari za Angola, South Africa pamoja na Msumbiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Serikali itajenga Bandari ya Inyara ikiwa ni pamoja na reli ya kutoka Mbeya kwenda Ziwa Nyasa ili kukabiliana na ushindani huu wa kibiashara ambao ni karibu asilimia 70 ya biashara ya nje kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwa mizigo inayokwenda nchi za nje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mbalizi - Shigamba - Isongole na barabara ya Mbalizi - Makongorosi ambazo ni barabara za kimkakati na ilikuwa ni ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne na Rais wetu wa Awamu ya Tano?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niruhusu nimpe pongezi nyingi Mheshimiwa Mbunge Oran kwa kufuatilia mambo mbalimbali kwa sababu nafahamu anafuatilia masuala ya barabara, Uwanja wa Ndege wa Songwe, bandari kavu kama alivyouliza, lakini mambo muhimu kama ya kilimo na wachimbaji wake wadogo wadogo na mara nyingi tunapokea ushauri wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kujibu swali lake la kwanza kuhusu ujenzi wa bandari kavu hususan eneo la Inyara, niseme tu kwamba Serikali inafanya maandalizi muhimu kwa ajili ya ujenzi wa hii bandari kavu ikiwa ni pamoja na kutenga eneo la heka 108 kwa ajili ya ujenzi huo. Eneo hili tumelitazama kimkakati kwa kweli kwa maana ya kuangalia ile chain supply yaani kuwa na mnyororo wa muunganiko kwa maana kwamba eneo hili linapakana na barabara inayotoka Mbeya au Kyela kwenda Malawi pia iko kandokando ya reli ya TAZARA.
Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumejipanga kwa ajili ya kuboresha bandari hii na hatua ambayo tuko nayo ni kufanya tathmini ya maeneo ya wakazi wanaopitiwa na mradi huu ili tuweze kuwalipa fidia na harakati zingine zitakazofuata kwa ajili ya ujenzi wa bandari hii kavu ziwezi kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu barabara ya Mbalizi - Shigamba na barabara ya Mbalizi - Makongorosi ni barabara ambazo tumezizingatia pia katika bajeti yetu hii kwa maana ya kuziboresha. Mheshimiwa Mbunge anatambua kwamba tumetenga fedha nyingi kuboresha barabara hizi ili ziendelee kupitika wakati wote, wakati tunazitazama kwa ajili ya kuziboresha kwa kiwango cha lami.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba niiulize Serikali ni lini itapeleka maji kwenye Kata ya Mjele ambayo ni ahadi ya muda mrefu ya Serikali? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nitumie nafasi hii nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya na nimeshafika hadi Mjele. Namwomba sana Mhandisi wa Maji wa Jimbo la Mbeya Vijijini asilale ili kuhakikisha wananchi wale wanapata maji safi, salama na ya kuwatosheleza. Jambo la msingi sisi kama Wizara a-raise certificate tuko tayari kulipa kwa wakati ili wananchi waweze kupata maji.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na vilevile nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kutokana na ajali nyingi zinazotokea katika Wilaya ya Mbeya na hasa katika Milima ya Uyole na Mbalizi. Je, ni lini Serikali itafanya upanuzi wa barabara zinazoelekea kwenye nchi za jirani za Zambia na Malawi?
Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itajenga by pass ya Inyala – Simambwe na Inyala – Songwe? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza niseme kwamba study zilizofanyika zinaonyesha kuwa ajali nyingi zinazotokea asilimia 78 zinatokana na makosa ya kibinadamu (human behavior) na asilimia 12 iliyobaki ndiyo inasababishwa na mambo mengine ikiwepo miundombinu. Kwa ajali ambazo zinatokea katika Mkoa wa Mbeya niseme tu ajali iliyotokea juzi kwa mfano nimepata fursa ya kuwepo Mbeya juzi, eneo ajali ilipotokea ni eneo ambalo barabara ni nzuri na alama za barabarani zipo, inawezekana lilikuwa tatizo la kiufundi lakini tu kwa ujumla wake Serikali imechukua hatua ya kuendelea kuboresha barabara za Mbeya kwa sababu nature ya eneo la Mbeya ni milima na miteremko mirefu ili kuweza kupunguza ajali kwa maana kwamba ile barabara sasa anayoitaja Mheshimiwa Mbunge Inyala – Simambwe ni kati ya barabara ambazo tunaendelea kufanya usanifu ili tuweze kupunguza ule msongamano mkubwa wa magari.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa ujumla wake tu ninapende kutoa wito kwa watumiaji wa barabara kwamba maeneo haya ambayo yanakuwa na milima mikali na alama za barabarani zipo, watumiaji wa magari tuzingatie hizo kanuni za barabarani ili tupunguze ajali wakati Serikali inafanya juhudi za kuboresha barabara zake. Kwa hiyo, tatizo la Mbeya niseme kwa ujumla Serikali inalitambua na tunafanya haraka kuhakikisha kwamba tunaboresha miundombinu na kupunguza ajali katika eneo hili.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naomba niishukuru Serikali kwa majibu mazuri, na ni nia ya wananchi kuona kuwa eneo hilo linatengwa na kunakuwepo na viwanda ili wananchi wa Mbeya waweze kupata ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hiyo mikakati mizuri, ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Je, ni lini sasa Serikali itapeleka pesa kwa ajili ya kumalizia Kiwanda cha Kuchakata Nyama ambacho kimejengwa na Halmashauri ya Mbeya na ambacho vyombo vyote, vifaa vyote zaidi ya miaka miwili sasa viko mle ndani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa vile kuna wafugaji wengi katika Kata ya Mjele na tatizo lao kubwa ni mabwawa ya maji, je, ni lini Serikali sasa itapeleka miundombinu ya mabwawa ya maji kwa ajili ya mifugo na binadamu? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru kwamba amekubaliana na majibu ya Serikali kwenye swali la msingi na katika maswali yake mawili ya nyongeza, la kwanza, kuhusu mradi wa kiwanda cha kusindika nyama pale Mbalizi ambao uliwasilishwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini TAMISEMI kwa ajili ya kufikiriwa kupewa fedha ni miongoni mwa miradi ya kimkakati katika halmashauri hiyo ambayo imeombewa fedha kwenye dirisha maalum la miradi ambayo ni miradi ya kibiashara.
Kwa hiyo, mchakato wake bado unaendelea, kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha miradi hiyo yote bado inafanyiwa upembuzi maalum ili utakapokamilika miradi ile ambayo itapatiwa fedha wahusika wa Halmashauri wataarifiwa. Hata hivyo ninaamini mradi huo ni mzuri na una faida na miradi kama hiyo Mbeya haipo mingi, kwa hiyo, ninaamini utapewa kipaumbele unaostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ni kuhusu bwawa kwenye eneo la wafugaji. Najua Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi alitembelea eneo hilo na akatoa ahadi. Mimi nataka nimwambie kwamba Serikali hii ni moja, nitafuatilia mimi mwenyewe kwa Wizara ya Mifugo ili kuhakikisha kwamba Halmashauri na wakazi wa eneo hilo wafugaji wanapata kile ambacho Mheshimiwa Naibu Waziri alikiahidi. Ahsante.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Swali langu, je, ni lini Serikali itaamisha gereza la Songwe ili kupisha mradi wa mgodi wa niobium ambao una thamani ya zaidi ya dola bilioni 6.8 ambayo ni sawa na shilingi bilioni 15. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lake linauliza ni lini, nadhani sitaweza kujibu kwa lini sasa hivi hapa kabla ya kuweza kulifanyia utafiti. Ningeomba anipatie muda nilifanyie utafiti jambo lake hili nijue hasa undani wa hili tatizo lake lilivyo ili niweze baadaye kukaa nizungumze naye pembeni kuweza kumfahamisha kama ni lini litahamishwa au kama kuna mipango mingine ambayo ipo ya kuweza kukabiliana na tatizo ambazo amelizungumza.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, kwanza nianze kabisa kuipongeza Serikali pamoja na changamoto zote hizi za miundombinu na idadi ndogo ya askari lakini bado wameimarisha ulinzi katika Wilaya ya Mbeya na hususani Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi.
Swali la kwanza, je, ni lini Serikali itapeleka shilingi milioni 120 ambazo zitaunga mkono shilingi milioni 200 walizotumia wananchi kukamilisha Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi?
Swali la pili; je, ni lini Serikali itajenga Vituo vya Polisi katika miji inayochipukia ya Mjele, Ilembo pamoja na Igoma? Ahsante.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika umaliziaji pamoja na majengo mapya aliyoyasemea tutaweka kipaumbele katika mwaka huu wa fedha pamoja na bajeti zitakazofuatia kulingana na upatikanaji wa rasilimali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze tu Mheshimiwa Mbunge, amefanya jitihada kubwa sana katika jengo hili ambalo tunalisemea na aendelee na moyo huo huo na ndiyo maana wananchi wa Mbalizi pamoja na Mbeya Vijijini wanaendelea kumuamini na kuchangua.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, kwanza nianze kwa kumpongeza Waziri na Naibu Waziri kwa ziara walizozifanya kwenye Halmashauri ya Mbeya. Naibu Waziri alitembelea kata ambazo hazina umeme kabisa lakini zinalizunguka Jiji la Mbeya kama Kata za Swaya na Maendeleo. Je, ni lini hizi kata mbili nazo zitapewa umuhimu wa kupewa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tukushukuru sana kwa namna ambavyo umetambua mahitaji ya nishati na kuwapa fursa Waheshimiwa Wabunge kuuliza maswali mengi. Umenipa fursa ya kujibu maswali ya Mheshimiwa Njeza, Mheshimiwa Mwamoto pamoja na Mheshimiwa Frank.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Njeza na Mheshimiwa Mwamoto maswali yao yanalingana kwa sababu yamehusisha masuala ya umeme vijijini. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Njeza, tulifanya ziara Mbeya, pamoja na kwamba Jimbo lake ni Mbeya Vijijini, hapa amezisemea kata ambazo zipo ndani ya Jiji la Mbeya, na kama nilivyosema, Serikali imetambua ukuaji wa maeneo katika Miji, Manispaa na Majiji na ndiyo maana tumekuja na mradi huu unaoitwa Peri-Urban. Niliombe Bunge lako tukufu, tutakapowasilisha bajeti yetu ya mwaka 2018/2019 ituunge mkono katika miradi mbalimbali ukiwemo Mradi huu wa Peri- Urban kuupitisha kwa kishindo kisha tufanye kazi ya kupeleka umeme katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo, Mheshimiwa Mwamoto, ni kweli tulifanya ziara tena kwa mara ya kwanza Mawaziri wawili, Mheshimiwa Waziri mwenyewe na mimi Naibu Waziri tulikuwa kwenye kata hiyo aliyoitaja. Nataka niseme sisi lengo letu ni kupeleka nishati kwenye maeneo yenye uhitaji ikiwemo mojawapo ya maeneo ambayo kweli yanahitaji nishati ni eneo la viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwapongeze Mheshimiwa Mbunge na vijana hao kwa kutenga eneo la viwanda vidogo vidogo na kwa gharama za Serikali umeme utafika katika maeneo hayo na nitoe rai tu wao waendelee kujipanga kuunganisha lakini umeme utafika kama ambavyo tumeahidi katika ule mkutano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la mwisho la Mheshimiwa Frank, ni kweli Mji wa Tunduma ni mji ambao umekuwa na upo mpakani. Nataka niseme Mji wa Tunduma upo katika Mkoa mpya wa Songwe na wakati huo umeme katika Mkoa wa Songwe ulikuwa unatoka katika njia ya kusafirisha umeme ni ndefu kutoka Mbeya. Serikali ina mpango wa kujenga sub-station palepale Tunduma kwa ajili ya kuufanya Mkoa mzima wa Songwe upate nishati ya uhakika na wakati wote. Kwa hiyo, nimthibitishe Mjumbe kwa kuwa yeye Mheshimiwa Mbunge ni Mjumbe wa Kamati yetu ya Nishati na yeye pia atuunge mkono katika bajeti yetu ili mradi huu wa ujenzi wa sub-station pamoja na line ambayo inatoka Mbeya inayoenda Sumbawanga - Mpanda – Kigoma - Nyakanazi ya KV 400 ambayo yote kwa pamoja itachangia kwa upatikanaji wa umeme wa uhakika. Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana, ahsante sana.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niulize swali dogo tu, ni lini ujenzi wa Bandari Kavu utaanza ya Mbeya ambayo ni ya kimkakati kwa ajili ya kuhudumia mizigo ya nchi jirani za Zambia, Malawi na DRC? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Njeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba tunalo eneo ambalo tumelichukua kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania kwa ajili ya kuweka Bandari Kavu katika Mkoa wa Mbeya. Sasa hivi utaratibu unaoendelea ni kuhakikisha tunalipa fidia kwa wananchi kwa eneo lile ambalo kwa kweli nikiri kwamba ni la kimkakati kwa ajili ya kuhudumia mizigo ya Zambia, Malawi na hata DRC. Tukishamaliza mchakato wa kulipa fidia kwa wananchi, tutaweka mipaka na kutengeneza ramani kwa ajili ya kutengeneza bandari hiyo kavu ili iweze kutoa huduma hizo.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, nashukuru pia kwa majibu ya Serikali hasa kwa kutambua kuwa hizi ni barabara muhimu za kimkakati na kwa umuhimu huo huo ilikuwa ni ahadi ya kujengwa kwa kiwango cha lami, ambayo ilitolewa na Rais wa Awamu ya Nne Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete na pia ilikuwa ni ahadi ya Rais wetu wa sasa Mheshimiwa Dkt. John Magufuli kuwa hizi barabara zijengwe kwa lami. Kwa umuhimu huo huo katika Ziara ya Waziri pamoja na Naibu Waziri nao kwa wakati tofauti walitembelea hizi barabara na kuona umuhimu wake na sasa labda ningependa kama ilivyo kwenye swali langu la msingi, ni lini barabara ya Mbalizi – Shigamba – Isongole itajengwa kwa kiwango cha lami?

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa umuhimu huo huo ni lini barabara ya Itewe - Mlima Nyoka - Songwe ambayo ni by pass itajengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Njeza kwa kufuatilia maendeleo ya Jimbo lake hususan mambo ya miundombinu. Maana yake hii naiona ni style ya Mpwapwa hii ni Lubeleje style, maana kila ukikutana nae anazungumzia juu ya barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niseme tu kwamba barabara hii natambua kwamba ni ahadi ya Viongozi, lakini nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Mbeya Vijijini kwamba barabara hii ya Mbalizi – Shigamba – Isongole iko kwenye mpango mkakati wa Wizara kwa ajili ya kuiboresha. Kwa hiyo pindi tukipata bajeti tutafanya usanifu wa barabara hii na kuanza kuijenga katika kiwango cha lami. Vilevile kuhusu barabara hii ya Uyole – Mlima Nyoka hadi Songwe ambayo ni by pass Mheshimiwa Mbunge anatambua kwamba usanifu ulifanyika na kupitia Jiji la Mbeya na anafahamu kwamba eneo hili ni la uzalishaji mkubwa, kuna pareto inazalishwa kwa wingi lakini kuna viazi vinazalishwa kwa wingi, kuna mazao ya mbao, hii ni barabara muhimu pia kuna mahindi yanazalishwa kwa mwaka mzima katika eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba hivi leo mtaalam mwelekezi anakwenda kufanya mapitio ya barabara hii kwa sababu uko uelekeo sasa wa kupata fedha ya kuijenga barabara hii by pass muhimu ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami.

Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge nitaendelea kuku- update, kukupa taarifa zaidi tuone namna tunavyokwenda, lakini niseme tu kwa wananchi wa Mbeya Vijijini kwamba tumejipanga vizuri sasa kuanza kuijenga hii by pass kwa ajili ya huduma muhimu katika eneo hili.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo kwa Bagamoyo, Mji Mdogo wa Mbalizi ulianza mchakato wa kuomba iwe ni Halmashauri ya Mji kwa muda mrefu sana. Je, ni lini Serikali itaipa Mbalizi kuwa na hadhi ya Halmashauri ya Mji? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wanavyofahamu Wabunge wengi sana humu, kuna mapendekezo mbalimbali ya maeneo mbalimbali kuanzisha mamlaka mpya lakini najua kwamba Mbalizi ni miongoni mwa maeneo ambayo yalikuwa katika mchakato wa kupandishwa hadhi, lakini nimuombe Mheshimiwa Mbunge kwamba tuvute subira kwa sababu mpango wa Serikali wa sasa hivi wa maelekezo ni kutoanzisha mamlaka mpya lakini kwa vile jambo hili liko katika subira tuvute subira pale hali itakapokuwa sasa imekaa vizuri Mji wa Mbalizi ni miongoni mwa miji ambayo itapewa kipaumbele cha kwanza katika upandishaji wa hadhi. (Makofi)
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Kutokana na majibu hayo, inaonyesha kuwa mgodi huu utakuwa ni neema sana kwa nchi yetu kwa sababu ya uzalishaji wa hayo madini ya Ferro-Niobium ambayo ni muhimu sana kwa ujenzi wa madaraja, Reli ya Standard Gauge pamoja na mabomba ya mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa umuhimu huo, napenda kuuliza maswali madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, je, ni kwa kiasi gani hayo madini ya Ferro-Niobium pamoja na Niobium yenyewe yataongezewa madini ya chuma? Ni kwa kiasi gani haya madini ya chuma tutatumia madini yanayochimbwa hapahapa nchini kwetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, vilevile imeonyeshwa kuwa kuna fidia kwa ajili ya Gereza la Songwe. Je, mwekezaji au wawekezaji wana mkakati gani badala ya kutoa fidia tu lakini waboreshe miundombinu ya gereza hilo ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara, vituo vya afya na huduma zingine za elimu hasa kwa wananchi wa Kata ya Bonde la Songwe ambapo kiwanda hicho na mgodi huo upo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Oran Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Ferro- Niobium ni matokeo ya uchakataji wa madini hayo utakaofanyika. Pale Mbeya uchimbaji utakuwa ni wa Niobium peke yake lakini Niobium haiwezi kutumika peke yake ni mpaka pale utakapoichanganya na iron, ndiyo maana tunaita Ferro-Niobium kwa maana ya kutengeneza high strength low-alloy, kwa maana ya material ya kuunganisha vyuma. Ndiyo maana Mheshimiwa Mbunge anasema kwamba itatumika kwenye madaraja na kwenye pipes, ni kweli madini haya yakishakuwa Ferro-Niobium yanatumika katika kuunganisha vyuma vikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge analitambua hilo na sisi kama Serikali tunalitambua hili. Kwa umuhimu wa material haya ndiyo maana katika jibu la msingi nimesema kwamba hii kampuni ikishaweka pale kiwanda, kwa maana ikishachimba Niobium itachanganywa na hiyo Ferro kwa maana ya iron kisha itauzwa nchi za nje. Kwa mfano, Amerika Kaskazini wanahitaji sana bidhaa hii kwa ajili ya utengenezaji au uunganishaji wa vyuma vikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni material ambayo yanahitajika sana duniani na sisi kama Serikali tunatambua. Tunasema kabisa kwamba tukishaweka kiwanda hiki pale, wakishachimba Niobium yetu haitatosha mahitaji kwa sababu itakuwa ni kiwanda peke yake Afrika ambacho kitakuwa kimejengwa pale Songwe na Niobium itakayohitajika, itahitajika hata ile ambayo ni nje ya Tanzania, ina maana Congo na Zambia wataleta Niobium yao hapa. Kwa hiyo, tutatumia Niobium karibu ya Afrika nzima katika kiwanda hiki ambacho kitajengwa Songwe. Kwa hiyo, tunatambua umuhimu wa kiwanda hiki na sisi kama Serikali tumeshikamana kihakikisha kwamba sasa tunakwenda kuhakikisha machimbo haya yanaanza na utengenezaji wa kiwanda kwa maana ya kuongeza thamani kinaanzishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili, tunatambua kweli machimbo au mgodi huu, yako chini ya Gereza la Songwe. Tunapenda kusema kwamba ile ziara ya Mheshimiwa Rais aliyokuwa amekwanda Mbeya imekuwa ni chachu kubwa sana kuhakikisha kwamba zile mamlaka husika kwa maana ya Wizara ya Mambo ya Ndani, Uwekezaji tunakweda kukaa pamoja kuangalia ni namna gani sasa mwekezaji huyu atalipa fidia na kuweza kuhamisha gereza lile kulipeleka pembeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua yuko tayari kulipa kiasi cha dola milioni saba kujenga gereza jipya ambalo litabeba wafungwa 500 na kujenga nyumba mpya kwa ajili ya wafanyakazi zaidi ya 120 na ataweka miundombinu ya umwagiliaji pamoja na barabara kuhakikisha kwamba anaboresha maisha na mazingira ya gereza lile ambalo litajengwa pale pembeni. Kwa hiyo, mamlaka husika zinafanya kazi kuhakikisha kwamba tunamsaidia mwekezaji huyu na masuala yote ya kodi tumeshayaweka sawa, tuna hakika kabisa tutakwenda kuanza mradi huu muhimu kwa Tanzania. Ahsante sana.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.

Na mimi napenda kujua pamoja na ujenzi wa hii reli ya Mtwara –Mbambabay, Serikali ina mkakati gani wa kujenga reli kati ya Inyala (Mbeya) na Kyela kwenye Ziwa Nyasa ambayo itakuwa ni kiungo kizuri kuunganisha reli ya TAZARA pamoja na Bandari yetu ya Mtwara?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, reli ya TAZARA ilijengwa kwenye miaka ya 1975. Sasa hivi Serikali ya Tanzania na Zambia tunafanya ukarabati mkubwa pamoja na kuongeza vichwa na mabehewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Ziwa Nyasa tumejenga matishari matatu ambayo tayari yanabeba mzigo. Hata hivyo, baada ya kukamilisha ukarabati huu na kuimarisha ili reli ile iweze kubeba mzigo uliotarajiwa wa tani milioni 5 kwa mwaka, basi tutaanza na stadi kwa ajili ya kuunganisha hicho kipande cha kutoka Mbeya kuelekea kule Kyela.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupewa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza nipende tu kuwashukuru Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, waliweza kufanya ziara katika Jimbo la Mbeya Vijijini na katika ziara hiyo waliahidi kuwa wangepeleka umeme katika Kata za Maendeleo, Itawa na Shizuvi, ikiwa ni pamoja na vijiji vinavyolizunguka Jiji la Mbeya. Sasa je, ni lini Serikali itapeleka umeme kwenye Kata za Maendeleo, Itawa na Shizuvi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oran Njeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tulitembelea Mkoa wa Mbeya, hususan Jiji la Mbeya na si chini ya mara mbili na kuwaahidi wananchi wa Kata za Maendeleo na Kata ambayo ameitaja ya Itawa, kwamba tutawapatia umeme na hususan katika mradi unaoendelea wa ujazilizi awamu ya pili, mzunguko wa kwanza, ambao hatua za manunuzi zimeshakamilika na kiasi cha shilingi bilioni 169 zimetengwa. Mkoa wa Mbeya ni miongoni mwa mikoa tisa ambayo itapata fursa ya ujazilizi awamu ya pili, mzunguko wa kwanza kama ambavyo imepata fursa ya ujazilizi awamu ya kwanza kutokana na mahitaji makubwa. Kwa hiyo nimpongeze Mheshimiwa Mbunge na nimuahidi kwamba maeneo haya yatapatiwa umeme katika mradi ambao utaanza Julai, 2019. Ahsante sana.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Kwanza nianze kuipongeza Serikali na kumshukuru Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa miradi ya maji katika Wilaya ya Mbeya.

Mheshimiwa Spika, pia napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa bajeti ya ziada ya shilingi bilioni 3.3 kwa ajili ya mradi wa maji uliotolewa kwa ajili ya Mji wa Mbalizi pamoja na Kata za Bonde la Songwe na Ilota. Pamoja na pongezi hizo, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, ni lini miradi ya maji itapelekwa kwenye Vijiji vya Ilembo, Santilia, Inyala pamoja na Ikukwa ambapo kunajengwa vituo vya kisasa vya afya na pia kuna Hospitali ya Wilaya?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni lini sasa Mradi wa Mbalizi utakamilika kuhakikisha wananchi wa Bonde la Songwe, Ilota na Mji Mdogo wa Mbalizi wanapata huduma ya maji ya uhakika? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayofanya katika Jimbo lake. Sisi kama viongozi wa Wizara, mimi pamoja na Waziri wangu tulishafika kule kuhakikisha Mradi wa Mbalizi wa kiasi cha shilingi bilioni 3 tunausimamia ili ukamilike kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge sasa hivi baadhi ya kazi zinafanywa na wataalam wetu wa ndani wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya. Ndani ya mwezi Machi, mradi ule utakamilika na wananchi wa Mbalizi watapata huduma ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu Mradi katika Vijiji vya Santilia pamoja na Ilembo na Ikukwa tulipata fedha zaidi ya shilingi bilioni 25 za Lipa kwa Matokeo na wafadhili wa DFID na Kijiji hiki cha Santilia kipo. Sasa tupo katika hatua ya manunuzi kuhakikisha tunaukarabati mradi ule na wananchi wake waweze kupata huduma hii muhimu ya maji.

Mheshimiwa Spika, nachotaka kumhakikishia kwa Vijiji vya Ilembo na Ikupwa katika awamu hii inayokuja ya fedha za Lipa kwa Matokeo tutaviweka katika kuhakikisha nao wanapata huduma hii muhimu sana ya maji. Ahsante sana.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, na inavyoonesha Benki ya Kilimo bado ina mahitaji ya mtaji mkubwa hasa ukizingatia kuwa kilimo kwa nchi yetu ndiyo tunakitegemea kwa kiasi kikubwa kwenye uchumi. Sasa ukiangalia katika jibu kwa Mkoa wa Mbeya ambayo imeoneshwa kuwa zimepelekwa shilingi milioni 700 lakini na hizi Wilaya alizozitaja Mheshimiwa Waziri siyo za Mkoa wa Mbeya ni za Mkoa wa Songwe. Kwa hiyo kwa jibu hilo inaelekea kabisa Mkoa wa Mbeya haujanufaika na mikopo ya Benki ya Kilimo.

Sasa swali langu; je, ni kwa kiasi gani Serikali imeweza kufanya tathmini ya mahitaji halisi ya mtaji wa Benki ya Kilimo? Na je, mtaji huo utapelekwa Benki ya Kilimo ukiondolea mbali hiyo mikopo ya ADB utapelekwa lini huo mtaji kwa Benki ya Kilimo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kiasi kikubwa ukiwapa wakulima mikopo risk kubwa iko kwenye bei kwa sababu bei za mazao hazieleweki, kuna risk sana kwenye bei. Sasa kwa kiasi gani Benki ya Kilimo kwa kutumia instruments za kibenki na vilevile kwa kusaidiana na taasisi zingine kama commodity exchange (TMX) zimeweza kutengeneza utaratibu wa kuondoa hiyo risk, wa ku-manage hiyo risk ambayo inatokana na changamoto za bei za mazao yetu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza lenye (a) na (b), tathmini ya mtaji na utapelekwa lini; tathmini ya mtaji ilishafanyika na kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi tunaangalia njia nyingine za ku-finance benki yetu ya kilimo ili iweze kuwa na uwezo wa kuwakopesha wateja wake ambao ni wakulima wadogo, wa kati pamoja na wakubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu Bunge lako tukufu likafahamu kwamba mabenki yote hayakopeshi kupitia mtaji, yanakopesha kupitia njia nyingine, co-financing agreement, ndiyo maana Serikali ilitafuta mkopo wa bei nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika na ikaipatia Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania. Kwa hiyo, hilo naomba Waheshimiwa Wabunge tulifahamu; hakuna benki yoyote inayokopesha kupitia mtaji wake, inakopesha kupitia amana na njia nyingine za utafutaji wa fedha ili iweze kuwahudumia wateja wake. Serikali ipo tayari kabisa kuiwezesha benki yetu kupitia mipango mingine ili ipate fedha za kutosha za kuwahudumia wakulima wetu ambao ndio lengo kubwa la uanzishwaji wa benki hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la risk ya masoko; TMX ambalo ni Soko la Bidhaa Tanzania, limeanza kazi vizuri mwaka huu na tayari tumeona baadhi ya mazao kwa mfano ufuta ambao umetafutiwa soko zuri na Soko letu la Bidhaa Tanzania wameweza kutafuta masoko na sasa tunaendelea kutafuta masoko mengine kupitia Soko la Bidhaa Tanzania kwa ajili ya mazao yaliyobaki ili kuwasaidia wakulima wetu kuondokana na vihatarishi vya ukosefu wa bei au bei isiyoeleweka kwenye masoko yetu.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Napenda tu kuuliza Serikali, tuna mradi mkubwa wa uchimbaji wa madini ya niobium katika milima ya Panda Hill Songwe; na kwa bahati nzuri ile miradi ita-attract direct investment ya karibu dola milioni 200 na wawekezaji wapo tayari; na katika ziara ya Mheshimiwa Rais alipofanya ziara kule Mbeya…

MWENYEKITI: Swali, swali!

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu: Je, ni lini Serikali itakamilisha mchakato wa kuwaruhusu hao wawekezaji waanze kuchimba haya madini ya niobium ili vile vile wajenge na kiwanda cha kuchakata hayo madini ambacho ni cha kwanza Afrika na cha nne duniani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kusema kwamba tunatambua kuhusiana na mradi huu wa Niobium ambao utafanyika katika milima ya Panda Hill na bahati nzuri nami nilipata bahati ya kukaa katika Wizara ya Madini, niliweza kuwaona wawekezaji hawa; na ni madini ambayo kwa kweli ni ya muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tulishaanza kuwashughulikia, pia tumekuwa na mashauriano na Wizara ya Madini pamoja na Wizara ya Viwanda kupitia EPZ. Tutakutana pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Madini pamoja na Wizara ya Viwanda ili kuweza kuona ni kwa namna gani tunakwamua mradi huu muhimu.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana ningependa kuuliza swali la nyongeza mji mdogo wa Mbalizi ulipewa mamlaka miaka 15 iliyopita na sasa hivi ina wakazi zaidi ya 100,000 na pia uwanja wa kimataifa wa Songwe uko katika eneo hilo. Sasa ni lini Mji mdogo wa Mbalizi utapewa hadhi ya kuwa Halmashauri ya Mji wa Mbalizi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi ni kwamba kwa sasa tunaendelea kuimarisha maeneo ya kiutawala yaliyoanzishwa. Wanapozungumzia kuanzisha halmashauri maana yake unaongezea miundombinu unahitaji huduma ya ukubwa zaidi na watendaji watakuwepo na majengo yataongezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuvumilia tuimarishe kwanza hii miji midog iliyopo halmashauri zetu na katika nchi hii kuna mikoa mingi pia bado haina majengo ya kutosha ya kuwa mikoa na watendaji wengine. Tuna upungufu wa miundombinu katika halmashauri zetu pia Waheshimiwa Wabunge wenyewe bado wanadai ofisi za Wabunge hazijajengwa. Kwa hiyo, nadhani ukiangalia mahitaji yaliyopo na kuongeza eneo la utawala nadhani tupeane muda kidogo tutekeleze haya yaliyopo tukamilishe tutazingatia baadaye maoni yake, ahsante.