Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Oran Manase Njeza (15 total)

Halmashauri ya Mbeya ina vijiji vingi ambavyo havijapata umeme katika Mpango wa REA na pia utekelezaji wa REA II uko nyuma sana:-
(a) Je, ni vijiji vingapi vya Halmashauri ya Mbeya vimo kwenye REA II na mradi utakamilika lini?
(b) Je, Kwa nini mradi wa REA II haujalenga kupeleka umeme kwenye huduma za kijamii kama vile Shule, Zahanati, Nyumba za ibada na vyuo?
(c) Je, ni lini sasa vijiji vilivyobaki vitapewa umeme wa REA?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vya Halmashauri ya Mbeya vilivyomo kwenye REA Awamu ya Pili ni 27, vikiwemo vijiji vya Chang’ombe, Hatwelo, Haporoto, Idimi, Kasele, pamoja kijiji cha Wambishe.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi unaotekelezwa katika Awamu ya Pili , unafanywa na Mkandarasi SINOTEC ambao umefikia asilimia 54.33 na mradi huu unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2016/2017.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, katika miradi yote inayotekelezwa na Serikali kupitia Mfuko wa REA Vijijini, kipaumbele kimewekwa kwenye huduma za kijamii kama vile shule, zahanati, vituo vya afya, nyumba za ibada na mashine za kusukuma maji. Katika Mpango wa Awamu ya Pili ya umeme vijijini maeneo ya huduma za jamii ambayo yatafikishwa huduma ya umeme katika Halmashauri ya Mbeya Vijijini ni pamoja na shule za msingi 23, shule za sekondari tano, zahanati 10, kituo cha afya kimoja, pamoja na nyumba za ibada 42.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vingine vya Mbeya Vijijini ambavyo havikupata umeme kwenye Mpango wa REA kabambe Awamu ya Pili, vimewekwa kwenye Awamu ya Tatu unayotarajiwa kutekelezwa mara baada ya bajeti hii ya mwaka 2016 kupitishwa na Waheshimiwa Wabunge. Jumla ya vijiji 111 katika kata 30 za Mbeya Vijijini vimejumuishwa katika REA Awamu ya Tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya kupeleka umeme kwenye maeneo yanayojumuisha ujenzi wa shule za umeme pamoja na zahanati, inafanyika kwa ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 480; ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 530, ufungaji wa transfoma 137 za ukubwa mbalimbali pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 7,465. Gharama ya kazi hii inakadiriwa kufikia shilingi bilioni 51.52
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-
Katika Halmashauri ya Mbeya kuna mradi wa uchimbaji wa madini unaotarajiwa kuanza kwenye eneo la Mlima Songwe, lakini pia kuna mradi mwingine mkubwa wa joto ardhi kwenye Kata za Swaya, Ijombe na Bonde la Songwe.
(a)Je, kwa nini Serikali Kuu haihusishi Halmashauri ya Mbeya katika mradi hiyo ili elimu iweze kutolewa kwa wananchi?
(b)Je, wananchi wa Jimbo la Mbeya Vijijini watanufaika vipi na miradi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa kifungu Namba 95(1)(b) cha Sheria Sheria ya Madini Namba14 ya 2010, kabla ya kuanza utafutaji na uchimbaji wa madini, mmiliki wa leseni husika hutakiwa kupata kibali cha kumruhusu kuingia na kushughulika na utafutaji na uchimbaji wa madini kutoka kwenye Halmashauri za zilaya pamoja na mkoa. Kampuni za Cradle Resources Ltd/RECB Co. Ltd. ilipewa leseni tatu za uchimbaji wakati wa madini ya niobium. Leseni hizo ni ML 237, 238 na 239 zilitolewa mwaka 2006 zenye jumla ya ukubwa wa eneo la kilometa za mraba 22.06. Kwa sasa kampuni hiyo inakamilisha maandalizi kabla ya kuanza kwa ujenzi wa mgodi huo ifikapo mwaka 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa utafiti wa madini hayo ya niobium kampuni ya Cradle Resources Ltd/RECB Co. Ltd. inayomiliki leseni ilijitambulisha kwa uongozi wa mkoa wa Mbeya ikiwa ni pamoja na Gereza la Songwe ambapo mradi huo upo. Aidha, kampuni hiyo hivi sasa iko kwenye mazungumzo ya Gereza la Songwe pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani kuona namna ya kulihamisha Gereza hilo kabla ya kuanza uchimbaji kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa niobium utakuwa na faida kubwa kwa uchumi wa viwanda ikizingatiwa kwamba Serikali inajikita katika kufufua na kukuza viwanda nchini. Miongoni mwa matumizi ya madini haya ni kutumika kama alloy kwenye chuma kwa kuboresha uimara wake. Vilevile madini hayo hutumika katika kutengeneza mabomba mathalani mabomba ya kusafirisha gesi asilia. Matumizi mengine ya madini haya ni matengenezo ya sumaku pamoja na utengenezaji wa injini za ndege na rocket.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni ya Tanzania Geothermal Development Company Limited (TGDC) ni kampuni tanzu ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO) ambayo imepewa dhamana ya kusimammia miradi ya kufua umeme wa joto ardhi katika Ziwa Ngozi lililopo kati ya Mbeya Vijijini. Mradi huu pia utazalisha umeme wa megawati 20 kwa kuanzia na baadaye utaweza kuzalisha megawati 100. Shughuli za utafiti wa mradi huu zilianza mwaka 2015 na zinatarajiwa kukamilika mwaka 2018 kwa kuzalisha umeme wa megawati 20. Mwezi Agosti 2015, kampuni ya TGDC iliendesha mafunzo kwa viongozi wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya, watendaji wa Kata na vijiji wa Mbeya yaliyolenga kuwajengea uelewa wananchi hao. Aidha, mafunzo kama hayo yalitolewa kwa njia ya mihadara kwa wananchi wa Vijiji vya Ijombe, Mwakibete, Nanyara na Swaya vinavyozunguka maeneo yanayofanyiwa utafiti wa joto ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na joto ardhi kutumika kuzalisha umeme manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi wanaozunguka eneo la mradi ni pamoja na kutumia maji ya moto majumbani lakini pia katika vitalu vya kilimo. Kadhalika itatumika katika kufugia samaki, kukausha mazao, kujenga mabwawa ya kuogelea na kwa matumizi mengine ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla miradi ya uwekezaji hunufaisha wananchi wa eneo husika katika ukuaji wa shughuli za kiuchumi na ajira. Miradi hii miwili itakapotekelezwa wananchi wa Halmashauri ya Mbeya Vijijini, Rungwe, Mbeya pamoja na Watanzania wote watanufaika kwa kupata ajira, ushuru pamoja na tozo mbalimbali pamoja na huduma za jamii.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-
Mji Mdogo wa Mbalizi uliomo kwenye Halmashauri ya Mbeya ni kati ya miji inayokua kwa kasi sana lakini inakosa miundombinu muhimu na uhaba na maji pia.
(a) Je, ni lini Mji huo utapewa hadhi ya kuwa Halmashauri ya Mji?
(b) Je, ni lini Serikali itatatua tatizo kubwa la maji kwenye Mji huo?
(c)Je, ni lini Serikali itajenga vituo vya afya kwenye kata zilizo ndani ya Mji wa Mbalizi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, uanzishaji wa Halmashauri za Miji nchini unazingatia Sheria ya Serikali za Mitaa Sura 288 (Mamlaka za Miji) ambayo imeainisha taratibu na vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa. Hivyo, nashauri pendekezo hili lijadiliwe kwanza katika vikao vya Kamati za Maendelo ya Kata, Baraza la Madiwani na Kamati ya Ushauri ya Mkoa. Endapo vikao hivyo vitaridhia, Ofisi ya Rais - TAMISEMI haitasita kuyafanyia kazi mapendekezo hayo ya wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji Mdogo wa Mbalizi unapata maji kutoka chanzo cha Ilunga chenye uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 3,024 za maji kwa siku pamoja na visima kumi vya maji ambavyo vina uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 6,300 kwa siku. Mji wa Mbalizi umeingizwa katika Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Maji awamu ya pili ambapo Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kushirikiana na Halmashauri inakusudia kuunganisha Mji huo na Mamlaka ya Maji Mkoa wa Mbeya ili kupata maji yatakayotosheleza mahitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Mji wa Mbalizi wanapata huduma za afya kupitia Hospitali Teule ya Mbalizi pamoja na Hospitali ya Jeshi la Wananchi ambako Halmashauri imeendelea kutoa mchango wa dawa na watumishi. Hivyo, katika mwaka wa fedha 2016/2017, kipaumbele kimewekwa katika kukamilisha ujenzi wa zahanati nane ndani ya Halmashauri zilizoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi.
MHE. ORAN M. NJEZA Aliuliza:-
Ili kuboresha elimu Serikali inashirikiana na Mashirika mbalimbali ikiwemo UNICEF ambao wanatoa misaada kwa sekta ya elimu:-
(a) Je, kwa mwaka 2014/2015 msaada wa UNICEF kwa Halmashauri ya Mbeya ulilenga mahitaji gani ya kuboresha elimu?
(b) Je, ni kiasi gani na asilimia ngapi ya msaada huo ulitumika katika miradi ya maendeleo ya elimu?
(c) Je, ni kiasi gani na asilimia ngapi ya msaada huo ulitumika katika matumizi ya kawaida?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/2015 Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) lilitoa msaada kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya uliolenga katika uendeshaji wa shughuli za elimu ya msingi, hususan kutoa mafunzo kwa walimu, wanafunzi, wazazi na walezi, kamati ya bodi za shule, wenyeviti wa vitongoji na vijiji, kuhusu malezi na haki za msingi za watoto kwa kupata elimu bora. Kwa kuzingatia makubaliano hayo yaliyopo kati ya UNICEF na Serikali fedha hizo ni kwa ajili ya kujengea uwezo (capacity building) na hazitumiki kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule.
(b) Mheshimiwa Spika, hadi Juni, 2015 Halmashauri ilipokea shilingi milioni 308.6 sawa na asilimia 64.8 ya shilingi milioni 475.9 zilizopangwa kutolewa na UNICEF kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
(c) Mheshimiwa Spika, fedha zote zilizopokelewa sawa na asilimia 100 zilitumika kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-
Uhitaji wa zao la pareto duniani ni mkubwa sana kiasi kwamba inahitajika kwa takribani tani 18,000 hadi 20,000 katika Soko la Dunia na Tanzania tuna uwezo wa kuzalisha hadi tani 8,000 tukiwa na mazingira rafiki.
(a) Je, ni kwa misingi gani pareto imepangiwa mnunuzi mmoja tu wa kigeni huku ikiwafungia milango wanunuzi wadogo wa Kitanzania?
(b) Je, Serikali inachukua hatua gani kusimamia bei
ya zao hilo ambayo imeporomoka kutoka shilingi 2,400 katika kipindi cha wanunuzi wengi hadi shilingi 1,500 chini ya mnunuzi mmoja?
(c) Je, Serikali ina mkakati gani wa muda mrefu na muda mfupi wa kuwawezesha wanunuzi wadogo wa Kitanzania kuingia kwenye ushindani na wanunuzi wageni?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, lenye sehemu (a),(b) na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Sheria na Kanuni za Pareto zinamtaka kila mnunuzi kuongeza thamani ya pareto kwa kuzidua sumu ya pareto kupata sumu ghafi. Pia mnunuzi anatakiwa kuwa na maabara ya kupima kiwango cha sumu kwenye maua na kuwalipa wakulima kulingana na kiwango hicho cha sumu. Kwa sasa mnunuzi aliyetekeleza masharti hayo ni Kampuni ya Pareto Tanzania. Serikali inasisitiza mnunuzi yeyote kutimiza vigezo vilivyopo katika sheria na kanuni ili kulinda ubora na soko.
Mheshimiwa Spika, bei ya zao la pareto hupangwa katika Mkutano Mkuu wa Wadau ambao ni wa Kisheria na hufanyika kabla ya mwezi Julai kila mwaka kabla ya kuanza msimu mpya. Mkutano huo, huhudhuriwa na wanunuzi na wawakilishi wa wakulima na viongozi wa Halmashauri zinazolima pareto nchini.
Mheshimiwa Spika, Serikali inasisitiza wakulima kuzingatia kanuni za kilimo bora. Kwa mfano, pamoja na bei ya juu kuwa shilingi 2,200 msimu wa 2012/2013 na shilingi 2,700 msimu wa 2014/2015 ubora wa pareto ulikuwa chini ya asilimia moja. Baada ya baadhi ya wakulima kutekeleza kanuni za kilimo bora cha pareto katika msimu wa 2015/2016, ubora ulifikia asilimia 1.8 na bei ya juu kuwa shilingi 2,700.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, mkakati wa muda mrefu ni kuendelea kuhamasisha wazawa kujiunga pamoja na kukopa ili wawekeze katika viwanda vya kuongeza thamani ya zao la pareto kufikia kiwango cha crude extract na hatimaye kuingia kwenye ushidani na wanunuzi wa kigeni.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-
Ili kuboresha kilimo na ujasiriamali inahitajika elimu kwa wakulima pamoja na kuwa na vyanzo vya mitaji.
(a) Je, ni lini Serikali itaanzisha Mfuko wa Kuzunguka (Revolving Fund) kwa kila kijiji kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wakulima na wajasiriamali?
(b) Je, Benki ya wakulima ina mtaji kiasi gani na imetoa mikopo katika mikoa gani?
(c) Je, ni lini Benki ya Wakulima itaanza kutoa mikopo kwa wakulima wadogo wa Mbeya Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini, lenye sehemu (a), (b), na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya upatikanaji wa mikopo vijijini hali inayochangia kukosekana kwa mitaji katika kuendeleza shughuli za kilimo na ujasiriamali. Hata hivyo, kwa kuwa suala la kuanzisha Mfuko wa Kuzunguka (Revolving Fund) kwa kila kijiji kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wakulima na ujasiriamali linahitaji fedha nyingi na usimamizi wa karibu kuhakikisha fursa ya upatikanaji wa fedha hizo haitumiwi na watu wachache kwa manufaa yao, Serikali imefanya uchambuzi wa kina ili kuona namna bora ya kusimamia mifuko ya aina hiyo na ambayo itawanufaisha wakulima na wajasiriamali na kuandaa mapendekezo ya mfuko stahiki kwa ajili ya kuridhiwa na Serikali. Juhudi hizo zipo katika ngazi ya maamuzi Serikalini. Aidha, kwa sasa Serikali inawashauri na kuwahamasisha wakulima na wajasiriamali kuunda vikundi au kujiunga na vyama vya kuweka na kukopa yaani SACCOS ili waweze kukopesheka.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Juni, 2017 Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania imefikisha mtaji wa shilingi bilioni 65.6 ambayo umepanda kutoa shilingi bilioni 65.3 kama ulivyokuwa katika robo ya kwanza ya mwaka 2017. Kutokana na udhamini wa Serikali, benki imepata mkopo wa bei nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) kiasi cha shilingi bilioni 209.5 fedha ambazo zinatolewa kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza ya shilingi bilioni 104.6 imeshapatikana. Aidha, hadi kufikia Juni, 2017 TADB imetoa mikopo ya jumla ya shilingi bilioni 7.46 katika Mikoa ya Tanga, Morogoro na Iringa ambapo jumla ya wakulima 2,252 wamenufaika na mikopo hiyo moja kwa moja.
Mheshimiwa Spika, TADB inalenga kufungua Ofisi za Kanda nchi nzima ili kurahisisha na kupunguza gharama za upatikanaji wa mikopo. Benki itaanzisha Ofisi ya Kanda Mkoani Mbeya. Hata hivyo, kama ilivyofanyika maeneo mengine, kabla ya ufunguzi wa ofisi hiyo, wakulima wa Mbeya walio katika vikundi watanufaika na mikopo ya TADB kuanzia msimu ujao wa kilimo.
MHE. ORAN M. NJENZA aliuliza:-
Kuna mgogoro wa muda mrefu wa ardhi kati ya TANAPA na Wananchi wa Kata za Ilungu, Igoma, Uleuje na wananchi walikuwa tayari kuachia ardhi yao ili upanuzi wa Hifadhi ya TANAPA lakini Serikali imeshindwa kuwalipa wananchi hao fidia:-
(a) Je, ni lini Serikali itafanya tathmini mpya ya fidia kwa wananchi wa Ilungu, Igoma na Uleuje?
(b) Kama Serikali imeshindwa kulipa fidia; je, ni lini itarudisha eneo hilo kwa wananchi wa Kata hizo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Oran Manase Njenza, Bunge wa Mbeya Vijijini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Taifa Kitulo ilianzishwa mwaka 2005 ili kuhifadhi vyanzo vya maji kwa ajili ya Bonde la Ziwa Nyasa, Bonde la Usangu na Mto Ruaha Mkuu ili kuhifadhi baioanuai ya aina za mimea adimu zikiwemo Chitanda. Hifadhi ya Taifa Kitulo imejumuisha maeneo yaliyokuwa yakimilikiwa na taasisi za Serikali. Maeneo hayo yanajumuisha Msitu wa Livingstone, Msitu wa Numbe na eneo lililokuwa shamba la mifugo (Diary Farming Company-DAFCO).
Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini iliyofanywa na Mkoa wa Mbeya kufuatia malalamiko ya wananchi wa Kijiji cha Kikondo, Kata ya Ilungu ilibaini kuwa kuna baadhi ya wananchi ambao taarifa ziinaonesha kuwa hawakulipwa fidia mwaka 1965 wakati shamba la DAFCO lilikuwa linaanzishwa. Serikali inakusudia kufanya uthamini kwa wananchi mwezi Februari mwaka 2018 ambao hawakulipwa fidia mwaka 1965. Aidha, Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Mbeya itahakikisha kuwa fidia inalipwa katika mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA (K.n.y MHE. ORAN NJEZA) aliuliza:-
Wananchi wa Jimbo la Mbeya Vijijini wanaipongeza Serikali kwa kuanzisha Wilaya ya Kipolisi Mbalizi.
• Je, ni lini Ofisi ya Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi itajengwa zikiwemo nyumba za kuishi askari?
• Je, Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi ina magari mangapi na Serikali ina mpango gani wa kuboresha miundombinu ya vituo vya polisi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua ukosefu wa Kituo cha Polisi chenye hadhi ya Wilaya na ukosefu wa nyumba za kuishi askari Wilaya ya Kipolisi Mbalizi. Ni lengo la Serikali kukamilisha ujenzi wa vituo vya polisi kwenye wilaya 65 zilizosalia na ujenzi wa nyumba za makazi. Ujenzi huu utatekelezwa kwa awamu kutegemeana na upatikanaji wa fedha zitakazotengwa katika bajeti kila mwaka na kutumia rasilimali zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi ina magari mawili, moja liko Mbalizi na lingine lipo kituo kidogo cha Inyara. Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya Vituo vya Polisi katika Halmashauri ya Mbeya na kwingineko kadri ya upatikanaji wa fedha utakavyoongezeka.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-
Barabara Kuu ya kwenda nchi jirani ya Zambia imepita katikati ya makazi ya watu na sehemu za biashara hasa katika Mji Mdogo wa Mbalizi na barabara hiyo inatumiwa na magari ya mizigo ambayo mara nyingi huwa ni chanzo cha ajali.
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara mpya ili kuhakikisha ajali zinapungua?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Tanzam highway inayoelekea nchi jirani ya Zambia ni barabara inayopita katika maeneo yenye makazi ya watu. Aidha, kutokana na tabia ya watu kupenda kufanya biashara ndogondogo kandokando ya barabara, kumekuwepo na msongamano mkubwa wa watu katika sehemu zinazopitiwa na barabara hii. Hali hii imejitokeza hasa katika maeneo ya Mbeya Mjini, Mbalizi, Uyole, Mlowo, Vwawa, Tunduma, Igawa, Chimala na Igurusi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ipo kwenye mpango wa kuikarabati barabara kuu ya Tanzam kuanzia Igawa hadi Tunduma ambapo katika mradi huo maeneo yenye matukio mengi ya ajali, ikiwemo eneo la mteremko wa Mbalizi, yataboreshwa ili kupunguza ajali. Mradi huu utajumuisha ujenzi wa barabara ya mchepuo kuanzia Uyole hadi Songwe na kazi hii ipo kwenye hatua ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-
Katika Mji Mdogo wa Mbalizi kuna ardhi ya ukubwa wa zaidi ya ekari 5,000 iliyotengwa kwa ajili ya Tanganyika Packers ambayo haijaendelezwa kwa zaidi ya miaka 30 iliyopita.
(a) Je, ni lini Serikali itawarudishia wananchi wa Mji Mdogo wa Mbalizi eneo hilo kwa lengo la kuliendeleza kwa kubadili matumizi kutokana na kukua kwa kasi kubwa kwa Mji wa Mbalizi?
(b) Pamoja na kubadili matumizi ya ardhi hiyo, je, Serikali ina mpango gani kwa wananchi wanaotumia ardhi hiyo hasa ikizingatiwa kuwa wengi wao hawakupewa fidia yoyote?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, shamba namba 760 lenye hekta 102.4 na shamba namba 761 lenye hekta 1985.4 yaliyoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ambayo kwa pamoja yana ukubwa wa hekta 2,087.8 sawa na ekari 5,219.5 ni mali ya Serikali. Mwaka 1974 Serikali ilijenga Kiwanda cha Kusindika Nyama cha Tanganyika Packers kwenye shamba namba 760 na shamba namba 761 lilikuwa maalum kwa ajili ya kupumzisha mifugo na kuilisha vizuri kabla ya kuchinjwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya uzalishaji kiwandani kusimama kutokana na changamoto kadhaa za kiuendeshaji na kiuchumi, baadhi ya wananchi walivamia maeneo ya mashamba hayo na tarehe 4/3/2016, Halmashauri ya Wilaya iliomba kwa Msajili wa Hazina kubadilisha matumizi ya eneo hilo kuwa makazi na huduma nyingine. Ombi hilo lilikataliwa kwa kuwa nia ya Serikali kuliendeleza eneo hilo kama eneo la viwanda haijawahi kubadilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ndiyo maana ili kuona kuwa haki inatendeka Serikali ilifungua kesi Namba 1 ya mwaka 2015 Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya dhidi ya wavamizi ambayo ilihukumiwa tarehe 20/2/2018 kwa Serikali kupewa haki ya kuendeleza eneo lake. Taratibu za kisheria za kuwaondoa wavamizi ili eneo hilo litumike kama ilivyokusudiwa zitakamilishwa hivi karibuni. Serikali haijawahi na haina mpango wa kubadili matumizi ya eneo hilo, kwani kufanya hivyo kwa maeneo kama hayo ni kukwamisha juhudi za kujenga Tanzania ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo wananchi waliokuwa wanastahili fidia kwa mujibu wa sheria wote walilipwa.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-
Wananchi wa Jimbo la Mbeya Vijijini wanaipongeza Serikali kwa kuanzisha Wilaya ya Kipolisi Mbalizi.
• Je, ni lini Ofisi ya Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi pamoja na nyumba za askari zitajengwa?
• Je, Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi ina magari mangapi na Serikali ina mpango gani wa kuboresha miundombinu ya vituo vya polisi katika Halmashauri ya Wilaya Mbeya?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini kama ifuatavyo:-
i. Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi ni miongoni mwa Wilaya Mpya za Kipolisi zilizoanzishwa hivi karibuni. Jeshi la Polisi kwa kutambua ukosefu wa Ofisi ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya pamoja na nyumba za makazi ya askari linashirikiana na wananchi na wadau mbalimbali kujenga jengo la Ofisi ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya ambalo linajumuisha Kituo cha Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa jengo hili umefikia hatua ya umaliziaji na changamoto iliyobaki ni ujenzi wa nyumba za kuishi askari.
ii. Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi ina magari matatu ambapo gari moja ni chakavu linahitaji matengenezo ili liweze kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya vituo vya Polisi katika Halmashauri ya Mbeya pamoja na kwingineko nchini kwa awamu kwa kutegemea rasilimali zilizopo na upatikanaji wa fedha.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-

Wilaya ya Mbeya, Mkoa wa Mbeya na Wilaya za Ileje na Songwe Mkoa wa Songwe zinaunganishwa kwa barabara za vumbi kuanzia Mbalizi kuelekea Ilembo, Iwinji hadi Ileje na Mbalizi kuelekea Mshewe.

(a) Je, ni lini Serikali itaunganisha barabara hizo kwa lami?

(b) Je, ni lini Serikali italipa fidia wananchi waliopisha upanuzi wa barabara za Mbalizi, Mshewe, Mjele hadi Mkwajuni Songwe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara alizotaja Mheshimiwa Mbunge ni barabara za Mbalizi - Shigamba - Isongole zenye urefu wa kilometa 96.8 na barabara ya Mbalizi – Chang’ombe – Mkwajuni – Patamela – Makongolosi yenye urefu wa kilometa 117. Barabara hizo ni za Mkoa na zinahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mbeya na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Songwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Serikali kwa sasa ni kuunganisha Makao Makuu ya Mikoa na nchi jirani kwa barabara za kiwango cha lami, ambapo tayari Makao Makuu ya Mkoa wa Mbeya na Mkoa wa Songwe yameunganishwa kwa barabara ya lami ya Mbeya hadi Tunduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kwa kuzingatia umuhimu wa barabara hizo, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imefanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili kuijenga kwa kiwango cha lami kwa barabara ya Mbalizi – Chang’ombe – Mkwajuni – Patamela – Makongolosi kilometa 117, sehemu ya Mbalizi hadi Galula kilometa 56. Aidha, Serikali imekuwa ikizifanyia matengenezo mbalimbali ya barabara hizi za Mbalizi – Shigamba – Isongole kilometa 96.8 na barabara ya Mbalizi – Chang’ombe – Mkwajuni – Patamela – Makongolosi kilometa 117 kila mwaka ili ziweze kupitika na majira yote ya mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu wananchi watakaopisha ujenzi wa barabara ya Mbalizi – Mshewe – Mjele – Galula. Serikali itawalipa fidia kutokana na sheria na taratibu kabla ya kuanza ujenzi.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-

Je, ni lini uzalishaji wa madini ya Niobium utaanza katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu swali, niungane na Watanzania wote kuwatakia kheri Waislam wote katika Mfungo wa Ramadhani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Uchimbaji wa Madini ya Niobium unaomilikiwa na Kampuni ya Panda Hill Mines Limited, kampuni hii ina ubia na kampuni ya Cradle Resources Limited asilimia 50 na Tremont Investment asilimia
50. Kampuni hiyo inamiliki leseni tatu za Uchimbaji wa Kati wa Madini Na.237, 237 na 239 za mwaka 2006 zilizotolewa tarehe 16 Novemba, 2006 zikiwa na jumla ya kilomita za eneo la mraba 22.1. Mradi utausisha uchimbaji wa madini ya Niobium ambayo yataongezewa thamani kwa kuchanganywa na madini ya chuma na kuwa Ferro-Niobium, zao ambalo litauzwa kwa wanunuzi mbalimbali walioko Ulaya, Asia na Amerika ya Kaskazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji ameshafanya upembuzi yakinifu (feasibility study) uliokamilka mwaka 2016 na kujiridhisha uwepo wa mashapo ya kutosha utakaowezesha uhai wa mgodi huo ambao utadumu kwa takribani miaka 30. Hata hivyo, kufuatia mabadiliko ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2017, mwekezaji alilazimika kupitia upya na kurekebisha taarifa za upembuzi yakinifu ili kuzingatia viwango vipya vya mrabaha, kodi na hisa za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, mwekezaji amewasilisha andiko la mradi la kuomba ufafanuzi wa vipengele mbalimbali kwa sheria na kutoa mapendekezo yake juu ya utekelezaji wa mradi huo, pamoja na suala la fidia ya ardhi kwa Gereza la Mbeya ambalo linatakiwa kuhamishwa ili kupisha mradi huo. Baada ya kupokea andiko hilo, hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwemo majadiliano na mwekezaji ambapo Wizara inatarajia kutoa mapendekezo yatakayowezesha kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-

Halmashauri ya Mbeya ina upungufu mkubwa wa maji karibu kwenye Vijiji zaidi ya 153 na hasa katika Kata ya Mjele. Je, Serikali ina mpango gani wakupeleka maji kwenye Vijiji hivyo na hasa Vijiji vya Mjele, Chang‟ombe na Ipwizi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njenza, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua tatizo la maji lililopo katika Halmashauri ya Mbeya Vijijini, katika mwaka wa fedha wa 2019/2020, Serikali imepanga kutekeleza miradi tisa ya maji ambayo ni Idimi - Haporoto, Iwindi, Mshewe, Ipwizi, Mjele - Chang‟ombe, Galijembe, Nsenga - Wimba, Iyawaya na Isangala group . Kiasi cha shilingi bilioni 6.4 kimetengwa katika bajeti ya 2019/20 kwa ajili ya kazi hiyo. Hadi kufikia mwezi Disemba 2019, jumla ya miradi 2 ya Idimi - Haporoto na Iwindi imekamilika na kiasi cha fedha shilingi bilioni 1.5 kimetumika katika ujenzi wa miundombinu ya maji.

Mheshimiwa Spika, baada ya Serikali kukamilisha miradi yote iliyopo kwenye bajeti ya 2019/2020, jumla ya vijiji 21 vitapata huduma ya maji vikiwemo vijiji vya Mjele, Chang‟ombe na Ipwizi ambapo jumla ya wakazi wapatao 44,364 watanufaika.
MHE. ORAN M. NJEZA Aliuliza:-

Ili kuboresha kilimo na ujasiriamali inahitajika elimu kwa wakulima ikiwa ni pamoja na kuwa na vyanzo vya uhakika vya mtaji.

(a) Je, Benki ya Kilimo ina mtaji kiasi gani?

(b) Je, Benki ya Kilimo ina mkakati gani wa kuwafikia wakulima wadogo wa Wilaya ya Mbeya?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO Alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ilipatiwa mtaji wa shilingi bilioni 60 mwezi Novemba, 2014. Aidha, tangu ilipoanza rasmi shughuli zake mwaka 2015, Benki ya Maendeleo ya Kilimo imefanikiwa kujiendesha na kukuza mtaji wake hadi kufikia shilingi bilioni 67.5 zilizorekodiwa mwishoni mwa robo ya kwanza ya mwaka 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha kuwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo inakuwa na fedha za kutosha kwa ajili ya kutoa mikopo na hivyo kufikia malengo ya kuanzishwa kwake, Serikali imeipatia benki hii kiasi cha shilingi bilioni 103 kupitia mkopo wa gharama nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika. Aidha, kwa sasa benki inaendelea na mchakato wa kukamilisha masharti ya kupatiwa awamu ya pili ya mkopo wa shilingi bilioni 103 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania imefikisha huduma zake Mkoani Mbeya na kuongeza kasi ya utoaji wa mikopo kutoka shilingi milioni 799.9 mwezi Desemba, 2017 hadi shilingi bilioni 2.54 kwa taarifa ya mwisho wa mwezi Aprili, 2019. Mikopo hiyo imetolewa kwa miradi saba ya kilimo na kuwanufaisha wakulima 509 wa Wilaya za Mbozi, Momba na Mbarali.

Napenda pia kulifahamisha Bunge lako tukufu kwamba Benki ya Maendeleo ya Kilimo imefanikiwa kufungua ofisi ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Mkoani Mbeya. Malengo ya ufunguzi wa ofisi hiyo ni kuhakikisha kwamba benki inasogeza huduma zake karibu zaidi na wateja wake ambao ni wakulima wote wa Nyanda za Juu Kusini ikiwa ni pamoja na wakulima wadogo wa Wilaya ya Mbeya Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutumia nafasi hii kuwahimiza wadau wote wa kilimo nchini ikiwa ni pamoja na wakulima wa Wilaya ya Mbeya Vijijini, kuwasiliana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo ili waweze kupata maelekezo sahihi ya uandaaji wa miradi itakayokidhi vigezo vya kupatiwa mikopo na benki yao na pia kupatiwa maelezo ya fursa nyinginezo zinazopatikana katika benki yao.