Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Haroon Mulla Pirmohamed (6 total)

MHE. HAROON M. PIRMOHAMED aliuliza:-
Katika GN. Na. 28 ya mwaka 2008 inawataka wananchi wanaoishi katika vijiji 21 vilivyopo katika Jimbo la Mbarali, Wilaya ya Mbarali, Mkoani Mbeya wahame ili kupisha Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ingawa wananchi katika vijiji hivyo wameishi katika maeneo hayo tangu enzi za mababu zao:-
Je, ni lini Serikali itafuta GN. Na. 28 ya mwaka 2008 ili wananchi katika vijiji hivyo waweze kuishi bila kubughudhiwa pamoja na kuendelea na shughuli zao za kilimo na ufugaji?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Haroon Mulla Pirmohamed, Mbunge wa Mbarali, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tangazo la Serikali Na. 28 la mwaka 2008 lilihusu kuhifadhiwa Bonde la Usangu kama sehemu ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha hatua ambayo ulihusisha kutunza vyanzo vya maji kwa ajili ya shughuli za kilimo na kibinadamu, uzalishaji wa umeme na matumizi ya kiikolojia kwa maslahi mapana ya kitaifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wanaoishi katika vijiji 21 vilivyopo katika Jimbo la Mbarali, Wilaya ya Mbarali, Mkoani Mbeya wamewasilisha malalamiko yao Serikalini wakipinga uhalali wa mpaka mpya uliotokana na Tangazo la Serikali nililolitaja na hivyo kuendelea kuwepo ndani ya mpaka. Aidha, baadhi ya wananchi waliotii sheria na kuondoka katika maeneo husika wamelalamikia viwango vya fidia vilivyolipwa katika kipindi cha mwaka 2006 hadi 2008 baada ya taratibu zote za kiserikali ikiwemo kufanya tathmini kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikifanya kila jitihada kutatua mgogoro huo katika ngazi mbalimbali ikiwemo vikao vya ushauri baina ya wadau wakiwemo wananchi katika eneo husika, uongozi wa Wilaya ya Mbarali na Mkoa wa Mbeya, Wizara ya Maliasili na Utalii na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iliunda timu ya wataalam na kupitia upya mipaka iliyotangazwa ili kutoa ushauri wa kitaalam juu ya mipaka hiyo na kuwasilisha ripoti kwenye Kamati ya pamoja kati ya Mkoa wa Mbeya na Wizara ya Maliasili na Utalii na kuhakiki malipo ya fidia kwa wananchi waliohama kupisha eneo lililojumuishwa kwenye Hifadhi ya Taifa Ruaha.
Mheshimiwa Naibu Spika, uhakiki huo ulikusudia kuondoa malalamiko ya mapunjo yaliyojitokeza kutoka kwa baadhi ya wananchi, kupitia na kuhakiki maeneo yote ya mpaka ardhini ili kujua maeneo gani yataathiriwa na mpaka mpya na kuona ni kwa namna gani mpaka utaweza kurekebishwa bila kuathiri lengo kuu la kuhifadhi sehemu ya eneo hilo la Bonde la Usangu. Mapedekezo yatakayotokana na kazi hii yatatumika kufanya maamuzi sahihi juu ya mipaka ya eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kusisitiza kuwa eneo la Bonde la Usangu, lililotajwa kwenye GN. Na. 28 ya mwaka 2008 ni eneo linalolindwa kisheria na umuhimu wake bado uko pale pale. Hivyo, badiliko lolote la mipaka ndani yake litahitajika kufanyika kwa kuzingatia taratibu za kisheria kupitia Bunge lako Tukufu.
MHE. ORAN M. NJEZA (K. n. y MHE. HAROON M. PIRMOHAMED) aliuliza:-
Mji Mdogo wa Rujewa ni kitovu cha shughuli za biashara na Makao Makuu ya Wilaya ya Mbarali na kwa bahati mbaya barabara nyingi za mji huo hazipitiki kutokana na ubovu. Wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2015 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliahidi kujenga kilometa tano za barabara kwa kiwango cha lami.
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo kwa wananchi wa Mbarali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Haroon Mulla Pirmohamed, Mbunge wa Mbarali, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Halmashauri Wilaya ya Mbarali iliidhinishiwa na kupokea shilingi milioni 793.02 kwa ajili ya matengenezo ya barabara kilomita 20, kalavati kubwa 17 na matengenezo ya madaraja matano. Serikali itafanya kila liwezekanalo ili ahadi hiyo ya Mheshimiwa Rais iweze kutekelezwa ndani ya miaka mitano ya utekelezaji wa Ilani. Halmashauri imepanga kuweka kipaumbele na kutenga bajeti katika mwaka wa fedha 2018/2019 ili kuanza utekelezaji wa ahadi ya kujenga kilometa tano za barabara kwa kiwango cha lami kwa usimamizi wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini (TARURA).
MHE. HAROON M. PIRMOHAMED aliuliza:-
Barabara ya Rujewa – Madibira ni tegemeo na ni kiungo muhimu kati ya Rujewa – Madibira na Madibira – Mafinga na Serikali imekuwa ikitoa ahadi kwa muda mrefu kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami. Je, ni lini sasa barabara hiyo itaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Haroon Mulla Pirmohamed, Mbunge wa Mbarali, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Rujewa – Madibira – Mafinga yenye urefu wa kilometa 152.1 ni barabara ya mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS). Kazi ya usanifu wa kina na kuandaa nyaraka za zabuni kwa ajili ya kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami ilikamilika Agosti, 2012.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa sasa inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 kiasi cha shilingi bilioni 2.57 kilitengwa kwa ajili ya kuanza maandalizi ya ujenzi wa barabara hii. Aidha, kwa sasa Serikali itaendelea kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara hii ili ipitike kirahisi kwa wakati wote wakati inatafuta fedha za kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA (K.n.y. MHE. HAROON M. PIRMOHAMED) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itamaliza kujenga Skimu za Umwagiliaji za Ipatagwa, Kongoro/ Mswiswi, Motombaya na ujenzi wa Skimu mpya ya Mhwela mpaka Kilambo pamoja na ujenzi wa Banio la Igumbilo, Kata ya Chimala ambalo lilibomolewa na maji mwaka 2016?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Haroon Mulla Pirmohamed, Mbunge wa Mbarali, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika Bajeti ya Mwaka 2014/2015 ilitekeleza ujenzi wa Skimu za Umwagiliaji za Ipatagwa, Kongoro/ Mswiswi na Motombaya kwa kukarabati mabanio, kuboresha mifereji mikuu na miundombinu ya mashambani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2017/2018, Serikali kupitia Halmashauri ya Mbarali ilitumia kiasi cha shilingi milioni 20 kufanya ukarabati mdogo wa Banio la Igumbilo lililopo katika Kata ya Chimala ili kuwawezesha wakulima kuendelea kutumia banio hilo kwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji kwa muda. Ukarabati huu umesaidia na kufanikisha kilimo cha mpunga na mazao mengine kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutafuta fedha kupitia vyanzo mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa skimu mpya za umwagiliaji katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Skimu ya Mhwela mpaka Kilambo. Aidha, Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuweza kukamilisha na kuanza ujenzi wa skimu mpya za umwagiliaji.
MHE. ORAN M. NJEZA (K.n.y. MHE. HAROON M. PIRMOHAMED) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itafanyia ukarabati barabara za Mahongole – Kilambo kilometa 20, Igurusi – Utengule kilometa 22, Chimala – Kapunga kilometa 25 na Mlangali – Ukwavila kilometa 23?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Haroon Mulla Pirmohamed, Mbunge wa Mbarali, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali ina mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 685 zinazohudumiwa na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), kilometa 341 ni za kiwango cha changarawe na kilometa 344.5 ni za udongo.
Katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali ilipeleka jumla ya shilingi bilioni 1.065 sawa na asilimia 91 ya bajeti iliyopangwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara na madaraja katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali. Kazi zilizofanyika ni pamoja na ukarabati wa Madaraja ya Mporo III, Mporo IV na Manienga. Matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilometa 50 kwa kiwango cha changarawe, ukarabati wa sehemu korofi zenye jumla ya kilometa 30 na matengenezo ya kawaida kwenye barabara zenye urefu wa kilometa 67.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali imetengewa kiasi cha shilingi milioni 220 kwa ajili ya matengenezo maalum katika barabara ya Mlangali – Uturo- Ukwavila na Chimala-Kapunga kwa eneo korofi lenye jumla ya kilometa 11. Vilevile Halmashauri imetengewa shilingi milioni 12.18 kwa ajili ya matengenezo ya makalavati 21 katika barabara ya Igalako- Mwatenga - Kilambo.
MHE. DKT. TULIA ACKSON (K.n.y HAROON M. PIRMOHAMED) aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka maji maeneo katika maeneo ya Kata za Mahongele katika vijiji (6), Kata ya Mwatenga vijiji (4), Kata ya Kongoro/Mswiswi vijiji (2), Kata ya Utengule - Usangu vijiji (6), Kata ya Luhanga vijiji (4), Kata ya Itambo vijiji (4), Kata ya Chimala vijiji (7), Kata ya Ihahi vijiji (3), Kata ya Imalilo – Songwe vijiji (5), Kata ya Igaua vijiji (5), Kata ya Miyombweni vijiji (5), Kata ya Mapogoro vijiji (9) na Mji wa Rujewa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Haroon Mulla, Mbunge wa Jimbo Mbarali, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali kupitia Progamu ya Maji Vijiji tangu mwaka 2012 imefanya usanifu katika vijiji 16 na kujenga miradi ya maji katika vijiji Simike-Kata ya Utengule Usangu, Udindilwa - Kata ya Ruiwa, Igurusi - Kata ya Igurusi, Chimala - Kata ya Chimala, Mkunywa -Kata ya Madibira na Ubaruku - Kata Ubaruku. Pia Halmashauri kupitia kwa wadau wa maelendeleo (UNICEF) imechimba visima 25 katika vijiji mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kukamilisha miradi hiyo, Halmashuri inaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa Luduga Mawindi ambao hadi utapokamilika utagharima shilingi bilioni 9 na utahudumia vijiji sita vya Kata ya Mawindi na Ipwani. Mradi huu utatekelezwa kwa awamu tano na kwa sasa utelezaji unaendelea katika awamu ya kwanza ambayo imefikia asilimia 98 na awamu ya pili imefikia asilimia 75. Hadi sasa mradi huu umegharimu shilingi bilioni 2.9. Taratibu za kutangaza awamu ya 3 zinaendelea na awamu ya 4 na 5 zitatangazwa baada awamu ya 3 kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa lengo la kuboresha huduma ya maji katika Mji wa Rujewa mji huo pia umejumuishwa katika miji itakayonufaika kupitia fedha za mkopo kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 500 kutoka Serikali ya India ambazo zitatumika katika ujenzi na ukarabati wa miradi ya maji katika maeneo mbalimbali nchini.