Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Janet Zebedayo Mbene (56 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kukushukuru kwa fursa hii ya kuchangia hotuba hii. Nampongeza Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Naibu Waziri wake, Watendaji Wakuu wa Wizara pamoja na Katibu Mkuu na Naibu Makatibu Wakuu na Watendaji wote kwa kazi nzuri na iliyotukuka inayofanywa na Wizara yao. Napongeza hotuba nzuri iliyosheheni mipango na utekelezwaji wake wenye uhalisia, inayotekelezeka na itakayoleta maendeleo ya uhakika katika sekta hii muhimu. Wizara iwatumie sana vijana wasomi katika sekta hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili Taifa letu liendelee kwa kasi ni lazima tuboreshe kilimo na viwanda kwa kuzingatia kuendesha kilimo cha kisasa kwa maana yake pana. Napendekeza kuundwa kwa vikosi kazi vya vijana wawazalishaji wa kilimo, ufugaji na uvuvi wa kisasa na hawa watengewe maeneo, waandikishwe kama vikundi rasmi na wajengwe uwezo wa kielimu, kimitaji, nyenzo, mbegu, mitamba na vifaranga vya samaki. Waunganishwe na masoko na wajengewe maghala.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuagiza mbegu nje ya nchi ilhali Tanzania ina ardhi kubwa na ya kutosha, vile vile tuna mashamba yaliyotengwa kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu ambayo yamekuwa na matumizi hafifu. Tunayo maeneo mengi yaliyotengwa na yanayofaa kufuga mitamba yatumiwe kikamilifu ili wananchi waweze kufuga mifugo bora kwa kipato, ajira, lishe hata biashara ya nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo yanayozalisha mazao ya aina mbalimbali kwa wingi hasa Nyanda za Juu Kusini, Kaskazini, Kusini na Magharibi yana changamoto kubwa ya maghala ya uhifadhi wa chakula kwa usalama, biashara na hata kuunganishwa na mfumo wa leseni za stakabadhi ghalani. Naomba kufahamu ni vigezo vipi vinavyotumika kugawa maghala haya? Ileje haijatengewa fedha za ujenzi wa maghala pamoja na kuwa ni wilaya mojawapo inayoongoza kwenye kuzalisha chakula. Naomba Serikali ipitie upya mgao huu na kuitendea haki mikoa yenye uzalishaji mkubwa na yenye fursa kubwa kwa maendeleo ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na lengo la kuboresha sekta hizi kuna haja sasa ya kutumia teknolojia ambayo imesambaa maeneo yote kuanzisha rural telecentres ambazo zitatumika kutoa taarifa za uzalishaji bora, masoko na taarifa za hali ya hewa kwa wazalishaji. Maafisa Ugani wapangwe upya kwenye vijiji na wapewe vigezo vya kazi zao na wapimwe kutokana na utendaji wao yaani tija itakayotokana na huduma kwa wazalishaji. Kila Afisa Ugani awe na mashamba ya mfano ya mkulima, mfugaji, mvuvi au yeye mwenyewe aoneshe mfano huo. Vijana wasomi watumiwe kwa kiasi kikubwa kwenye maeneo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna haja kubwa ya kuiboresha sekta ya ufugaji kwa kuboresha elimu ya ufugaji, kuboresha huduma za biashara ya mifugo kwa kuzingatia ubora wa mifugo inayokubaliwa Kimataifa ili tuweze kuuza nje mifugo na bidhaa za mifugo yetu na kuwaongezea wafugaji kipato. Vile vile kuna haja ya kuhamasisha matumizi zaidi ya bidhaa za ufugaji hapa nchini yaani nyama, maziwa, mayai na kadhalika. Hili likizingatiwa siyo tu litaboresha afya ya wananchi hasa watoto bali itakuza soko la ndani na kukuza kipato cha ufugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la masoko ya mifugo ni changamoto kubwa yanahitaji kufanywa ya kisasa zaidi kwa kuwa na huduma muhimu. Vile vile kutenga maeneo siyo tu ya kufunga bali ya kunenepesha mifugo kabla ya kupeleka sokoni. Serikali iainishe malengo yanayotegemewa kwenye maeneo kwa ufugaji, mapato tunayotegemea na mifugo mingapi inategemea kuhudumiwa katika mfumo huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na matatizo ya tabia nchi na umuhimu wa mazao ya uvuvi kwa lishe, ajira na mapato imefikia wakati sasa wa kuainisha kwa kasi na nguvu kubwa uvuvi wa mabwawa nchi nzima ili kutoa ajira nyingi hasa kwa vijana na lishe na biashara. Hii ni shughuli ambayo ni umuhimu na inatoa fursa kubwa sana kwa ajira na biashara. Tungependa kupata taarifa kamili ya mpango mkakati wa maendeleo ya uvuvi huu Tanzania mapema iwezekanavyo ikiainisha wapi Serikali inalenga kuwekeza mabwawa ya kuzalisha vifaranga, vyakula vya samaki na mabwawa yenyewe kila Wilaya yatakuwa mangapi, wapi na vijana wangapi wanalengwa na tunategemea kuongeza pato la Taifa kwa kiasi gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, uhusiano kati ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Viwanda. Ili Sera ya Viwanda ifane, kuna haja ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wakae pamoja na Wizara ya Viwanda ili kuhakikisha kuwa viwanda vya usindikaji vinajengwa sehemu zenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo, ufugaji na uvuvi. Hii itahakikisha mavuno yote ya kuchakatwa yako tayari wakati viwanda vinapojengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Ileje imepata bajeti ndogo sana ya kilimo chini ya TAMISEMI, hii ni fedha ndogo sana kwa uzalishaji mkubwa unaotakiwa Ileje. Vilevile Ileje pamoja na uzalishaji wa mazao mengi haijapangiwa maghala ambayo ni muhimu sana kwa uchumi wa soko. Naomba Wizara ipitie upya uamuzi wake wa kujenga maghala kwa kuzingatia uzalishaji uliopo. Serikali ipitie upya mgao wa fedha kimkoa kwenye kilimo. Mikoa inayozalisha kwa wingi iwezeshwe zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunazungumzia kuboresha kilimo cha kisasa na kwenda kwenye uchumi wa viwanda ni lazima tuwe na mpango wa haraka wa upimaji ardhi. Kwa kufanya hivyo itakuwa rahisi hata kwa wawekezaji wanaotaka kuja kuwekeza kwenye kilimo, ufugaji na uvuvi kufanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushirika bado hatujaupatia vizuri jinsi ya kutunufaisha. Tusimamie vizuri suala hili la ushirika na usimamizi wake na wazalishaji wenyewe wasimamie.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami naomba nichangie hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda kwa kuanza kwa pongezi kwake kwa maandalizi mazuri ya hotuba iliyosheheni mpangilio mzuri unaoonesha azma ya Serikali kutupeleka katika uchumi wa viwanda. Nimefurahishwa na suala zima la kuangalia umuhimu wa kuzingatia miundombinu muhimu, wezeshi kwa ajili ya kuanzisha viwanda au kuviendeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka na mimi niongezee hapo kuwa kwa sasa hivi kwa uzoefu tuliokuanao huko nyuma, kila Wizara inafanya kazi peke yake. Napenda kuona atakaporudi kuja kuwasilisha maadhimisho ya hotuba yake, atufahamishe juhudi ambazo anazifanya kushirikiana na Wizara nyingine ambazo moja kwa moja zinahusiana na masuala ya maendeleo ya viwanda kama nishati, maji, miundombinu, elimu, kazi ili kuhakikisha kuwa mipango yake itaweza kutekelezwa na masuala yote muhimu yatakuwa yamezingatiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tuna viwanda ambavyo tayari vinaendeshwa, vingine vipya, vingine vya zamani, lakini kwa bahati mbaya bado kuna matatizo ya kimsingi ya miundombinu muhimu, wezeshi kwa viwanda hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujua mipango iliyopo kwa viwanda vilivyopo kwanza kwa sasa hivi, ya kuhakikisha kuwa vinapata umeme wa kutosha, vinapata allocation ya gas kwa ajili ya kuzalisha umeme wa kuendesha shughuli zao, vinapata maji ya kutosha na zaidi ya yote miundombinu bora itakayowezesha mazao kwenda na kuondolewa kwenye viwanda hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna matatizo ya kimsingi ambayo lazima tuyatatue sasa kabla hata hatujafikiria kuanzisha viwanda vingine. Hii itakuwa ndiyo njia peke yake ya kuwavutia wawekezaji wa ndani na wa nje kuja kuwekeza katika viwanda nchi hii, baada ya kuona mifano mizuri ya viwanda ambavyo tayari viko nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda vilevile kutoa rai kwa Serikali kuwa hadi sasa tunavyozungumza, naamini kutokana na hilo kuwa kila Wizara inajiendesha yenyewe bila kuangalia mahusiano ya karibu yaliyo katika Wizara hizo, tunakuwa na migongano ya sera na sheria, hata taratibu za kiuendeshaji zinazosababisha kuwe na kukinzana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mdogo, ukizungumzia viwanda vinataka kuwekeza, lakini unakuta labda viwanda vinapotaka kuwekezwa sehemu fulani, mweka umeme yeye ile sehemu siyo kipaumbele kwake. Kwa hiyo, moja kwa moja kunakuwa kuna kukinzana. Kiwanda kinaweza kuanzishwa, soko linaweza kuanzishwa, lakini linachelewa kuanza kazi kwa sababu halijapata miundombinu muhimu ya umeme, maji na hata barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sasa kuona jinsi gani Serikali imejipanga, Wizara muhimu zikae pamoja kupanga mipango tangu mwanzo wanapotengeneza road map ya viwanda, hadi inapofika utekelezaji kuwa kila kitu kiko in place ili viwanda vikianza vianze kufanya kazi bila kusuasua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kuzungumzia suala zima la mambo ya vipimo na viwango. Tuna tatizo kubwa sana hata kwa viwanda vilivyopo katika uzalishaji uliopo wa viwango na vipimo sahihi vinavyoweza kuhakikisha kuwa bidhaa zetu zinapata ushindani unaostahiki. Tuna taasisi ziko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ambazo kazi yake ni kuhakiki viwango na vipimo. Kwa bahati mbaya, havina uwezo wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri sasa wakati tunajipanga kwenda kwenye uchumi wa viwanda, kuhakikisha taasisi muhimu kama hizi zinawezeshwa kwa maana ya taaluma, maabara, nyenzo zote zitakazowawezesha wao kuhakikisha kuwa viwango na vipimo viko sahihi ili bidhaa tunazouziwa ziwe zile ambazo zina ubora unaotakiwa au ubora ambao unaweza kushindana na bidhaa zinazotoka nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefurahi kuona katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri, ameelezea kuwa kutakuwa na mgawanyo wa viwanda nchi nzima kufuatana na rasilimali zilizopo. Hili ni wazo jema kwa sababu hii itaondoa ule mtindo wa zamani kuwa kila kitu kinalundikwa katika Miji Mikuu na sisi wa pembenzoni tunakuwa kila siku ni wa kuzalisha malighafi na tunashindwa mahali pa kuzipeleka. (Makofi)
Napenda kuona sasa kuona ramani kamili ya viwanda hivi hasa maeneo ya pembezoni au vijijini ambako kilimo kinaendeshwa kwa wingi na jinsi gani viwanda vya aina mbalimbali, vikianzia vile vidogo kabisa, vya kati na hata vikubwa vitakavyokuwa vimeainishwa. Hii itahakikisha Watanzania wengi wanashiriki katika uchumi wa viwanda, wanapata kipato, ajira na vile vile na maisha yao yanainuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia kwa ufupi suala zima la kukuza soko la ndani. Tumekuwa ni watu wa kuagiza bidhaa ambazo hatuzalishi na kuzalisha bidhaa ambazo hatuzitumii. Napenda kuona hili linabadilika kwa sababu bidhaa nyingi tunazoagiza kutoka nje kwa fedha nyingi, kwanza hazina ubora ambao tungeutegemea, lakini vilevile zinaua soko la ndani na vilevile zinaua ajira zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalima mazao mengi sana nchi hii ya kutosha kulisha nchi yetu hata na majirani. Huo ni mwanzo mzuri kwetu kwa ajili ya viwanda. Sasa napenda kupata kutoka kwa Waziri mkakati alionao wa kukuza soko la ndani kwa maana ya kuanza kuwekeza katika viwanda ambavyo vinazingatia mahitaji ya ndani kabla ya kuzungumzia masuala ya ku-export. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kujua, Mheshimiwa Waziri ana mkakati gani wa kupunguza uagizwaji wa bidhaa kutoka nje ambazo kwa kweli hatuzihitaji, ukizingatia kwa sisi wenyewe tunao uwezo wa kuzalisha? Tungependa kuona anaanza kupunguza kidogo kidogo uagizwaji wa bidhaa za nje ambazo haziitajiki na kuongeza uzalishaji wa bidhaa za ndani. Hii itawezekana akishirikiana na Wizara zinazozalisha mazao ya kilimo, ufugaji na uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la uwezeshaji wa wajasiriamali. Tanzania hii kuna mwenzangu mmoja ni Mheshimiwa Mbunge amesema kuwa kila mahali kuna frame. Mimi lile sioni kama ni jambo baya, ule ni ujasiriamali. Kinachotakiwa sasa ni je, wanawezeshwa vipi hawa wajasiriamali kwa maana ya mafunzo, nyenzo na mitaji? Napenda sana kuona Wizara hii ya Viwanda inaboresha kitengo kinachoshughulika na wajasiriamali ili tuone jinsi gani wamejipanga kuwasaidia wajasiriamali wale wadogo kabisa, wa kati, hata wakubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ndiyo ina taasisi muhimu zinazosaidia kujenga uwezo wa wajasiriamali kwa maana ya tafiti, masoko na uzalishaji, Iakini hatujaona moja kwa moja jinsi ambavyo wajasiriamali wetu wengi wananufaishwa na hizi taasisi. Tungependa sasa kuona ule mpango ambao upo chini ya Wizara wa industrial upgrading unatumika na kufanya kazi vizuri zaidi; kutoa mafunzo kuwatafutia masoko, kuwapa mbinu za uzalishaji na viwango na kuwaanzishia viwanda na kuwasimamia hadi wakomae. Kwa kuanzia na ngozi, nguo, usindikaji chakula, mafuta ya kula na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba sekta ndogo ndogo mbalimbali zichukuliwe na kupewa mafunzo, nyenzo bora za jinsi ya kuzalisha, jinsi ya kuanzisha viwanda na ku-maintain ubora na ku-maintain kufungasha vizuri katika njia ambayo inavutia walaji, lakini vilevile kuuza katika soko la ndani na hata la nje kwa maana ya masoko ya Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla. Wizara hii ni muhimu na ya kimkakati sana katika masuala ya kukuza uchumi na kuondoa umaskini. Hata hivyo, tungependa kuona moja kwa moja mchango wake unavyoonekana kufuatana na mipango yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sikatai sasa hivi ndiyo tumeanza hizi mbio za kwenda kwenye uchumi wa viwanda na kwa mwaka huu tunaweza tusione viwanda moja kwa moja; lakini japo ile mipango ioneshe mwelekeo wa Serikali katika kuhakikisha kweli hivi viwanda tutavifikia. Tuondoe hizi kejeli ambazo tunazisikia hapa kuwa ooh, mnasemasema tu! Oooh, mnapanga panga tu, uwezo wa nchi hii kuwa na uchumi wa viwanda upo, lakini tujipange vizuri, tuwe realistic, tusijiwekee malengo ambayo tutashindwa kuyafikia, lakini tuanze pole pole kwa mwelekeo mzuri utakaotuhakikishia kuwa mwisho wa siku tunaweza kufanya hili jambo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa sijawatendea haki akina mama na vijana kama sitazungumzia suala zima la mchango na ushiriki wa wanawake na vijana katika suala zima la viwanda. Wanawake na vijana ni wazalishaji wakubwa na wana jeshi kubwa nyuma yao. Hili ni lazima lichukuliwe maanani wakati wa mipango yote ya viwanda. Viwanda vidogo vidogo, biashara ndogo ndogo nyingi zinaendeshwa na makundi haya makubwa mawili, sasa tunapozungumzia viwanda vilevile lazima na wao tuwabebe, tuhakikishe kuwa akina mama na wao wanawezeshwa katika masuala ya usindikaji, vifungashio na mafunzo muhimu ya jinsi gani ya kuboresha huduma anazozitoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, akina mama wamekuwa ni wafumaji wa nguo; masweta, wengine tunatoka kwenye Mikoa yenye baridi sana, akina mama wangeweza kuwekewa viwanda vya kufuma masweta na soksi na nini, badala ya kuagiza sweta na uniform za watoto kutoka China, eeh wakawekewa mifumo hiyo wakafuma masweta wakawa wanauza katika nchi yetu hata nje ya nchi, hiyo ingekuwa ni ajira tosha na ingeinua kipato na maisha ya akina mama wengi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wengi sana wanamaliza vyuo vikuu na shule mbalimbali katika ngazi mbalimbali, wangetengewa hawa utaratibu kwa kupitia BRELA ambayo ndiyo inaandikisha makampuni wakawekewa namna ya kuandikisha makampuni yao, wakawekewa namna ya kufundishwa jinsi ya kuzalisha na kuanzisha biashara mbalimbali au uzalishaji mbalimbali wakapata ujuzi huo, wakaunganishwa na mitaji kutoka benki, wakaanzisha biashara zao wenyewe bila kungojea kuhangaika kuajiriwa na mtu yeyote. Hiyo ingekuwa ni njia moja ni rahisi sana ya kukuza viwanda nchini kwetu kuanzia vile vidogo vidogo na kadri wanavyoendelea kuwa wakubwa wakakua mpaka wakaja kuwa na viwanda vikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Roma haikujengwa siku moja ndugu zangu, lakini tukianza vizuri tunaweza tukafikia malengo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizugumzie sasa kidogo Mgodi wa Kiwira. Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira ni mgodi ambao uko Ileje, Jimbo ambalo mimi ndio Mbunge wake. Mgodi huu haujawahi kunufaisha Ileje. Kwanza ulikuwa hautambuliki kama uko Ileje wakati kijiografia na kwa njia nyingine zote uko Ileje. Haya, hayo tuyaache, hiyo ni historia!
Sasa hivi tunaambiwa mgodi ule upo tayari kufufuliwa na ule mgodi ulianzishwa ili makaa ya mawe yale yatumike kwa ajili ya umeme. Ileje ni Wilaya mojawapo ambayo haina umeme, viwanda, barabara, haina kitu chochote ambacho unaweza ukakizungumza kuwa ni cha maendeleo zaidi ya kilimo, lakini rasilimali zimejaa pale, zimetuzunguka. Napenda sasa Mheshimiwa Waziri utakapokuja hapa, uwaeleze wana Ileje mgodi ule utafufuliwa lini?
MHE. JANET Z. MBENE: Naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Naomba nichangie machache katika mpango huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka kuiomba Serikali kuwa, mipango inayotuletea kwa kweli ni mizuri sana na imepangwa kwa utaratibu mzuri sana wa kimkakati, lakini nafikiri katika mapendekezo mengi na maoni mengi yanayotolewa na Wabunge ni dhahiri kuwa, tuna tatizo la utekelezaji kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi hasa ile ya kimkakati imekuwa katika majadiliano kwa muda mrefu, tungetegemea sasa tuanze kuwa tumeweka mpango wa kuanza kuitekeleza. Tunajua kuwa mengine hatua ambayo imefikiwa ni nzuri, lakini kuna mambo machache tu ambayo yanatakiwa yakamilishwe ili miradi hii ianze kufanya kazi na ianze kutuletea faida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie miradi mikubwa ya kielelezo ambayo tumeipitisha hapa na imeonekana kuwa ingesaidia sana nchi yetu hasa katika wakati huu ambao tunalenga kuingia katika uchumi wa viwanda. Nataka nitaje mradi kwa mfano wa Mchuchuma na Liganga. Huu ni mradi ambao kwa kweli ungeanza kutekelezwa ilivyoandikwa au ilivyopangwa ni mradi ambao ungeiondoa nchi yetu katika uzalishaji wa chini na kutuingiza katika viwanda kwa haraka zaidi, maana ingetuletea malighafi muhimu sana kwa ajili ya viwanda vingine, lakini nasikitika kuwa mpaka sasa hivi bado haujakamilishwa na tunaambiwa kuwa pengine ni masuala machache tu yaliyobakia kujadiliwa. Je, kwa nini Serikali isiharakishe majadiliano hayo ili sasa huu mradi uanze kufanya kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunapozungumzia mradi huu wa Liganga na Mchuchuma, huu mradi utashughulikia makaa ya mawe, tunajua ni bidhaa ambayo ni kubwa, nzito na kwa vyovyote vile inahitaji miundombinu muhimu ya kusafirishia. Kulikuwa kuna mpango wa kujenga reli kwa ajili ya kupitisha makaa ya mawe kutoka katika maeneo ya mradi hadi bandarini, tungependa kujua fedha imeshawekwa kwa ajili ya kufanyia kazi hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo kwa kweli linawagusa wananchi moja kwa moja. Wenzangu wengine wamegusia ni suala la kilimo, ni suala la maji, ni suala la afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kukaa hapa tunazungumzia uchumi, tunazungumzia kilimo chenye tija bila kuzungumzia maji kwa maana ya umwagiliaji kwa maana ya maji salama yatakayotumiwa na wananchi, vilevile maji ya kusindika mazao ya kilimo na mazao ya mifugo. Kwa hiyo, tungependa sana kuona mkakati unawekwa kuhakikisha kuwa fedha ya kutosha inawekwa katika maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia kilimo, wananchi wengi wangependa kulima kisasa, mashamba makubwa kwa tija, lakini hawawezi kupata mikopo. Kwanza Benki ya Kilimo haina mtaji wa kutosha, pili mashamba yao hayajapimwa. Kwa hiyo, hata kama Benki ya Kilimo ingeweza kuwakopesha, hawatakopeshwa kwa sababu mashamba yao hayajapimwa, hivyo, tunajikuta bado tuna tatizo, tunazunguka palepale, tunazungumzia kilimo lakini hatuwezeshi kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa Serikali ije sasa ituambie kuhusiana na suala hili la kilimo ambalo ndilo linaloajiri wananchi wengi na ambalo linge-absorb vijana wetu wengi, wangelima kwa tija na kibiashara tusingekuwa tunalia kuwa vijana wengi hawana ajira. Vijana wengi wangefuga, vijana wengi wangekuwa wanauza na kusindika na tungekuwa hatuna shida na uchumi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji kama nilivyozungumzia, kuna mikakati iliwekwa hapa na Serikali, tukaipitisha Bungeni juu ya kuweka tozo maalum kwa ajili ya kuhakikisha kuwa Mfuko wa Maji unaundwa na unafanya kazi. Hatujui lile limefikia wapi, lakini tungependa Serikali iangalie uwezekano hata wa kuongeza ile tozo ili miradi ya maji yote itosheleze, bila maji ndugu zangu tutaongea mambo yote hapa lakini tunafanya kazi bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna suala vilevile la vituo vya afya na zahanati nchi nzima. Ndugu zangu tunapokuwa tuna matatizo ya maji ni rahisi sana wananchi kupata maradhi, wananchi wakipata maradhi tunazungumzia sasa kwenda hospitali ambako tena hakuna vifaa au huduma muhimu. Kwa hiyo, tunajikuta tunazunguka katika mzunguko wa umaskini na inefficiency ambayo kwa kweli hatuikubali kama Wabunge, maana sisi ndiyo tuko na wananchi kule tunasumbukanao sana juu ya masuala haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tuliomba, mwaka huu wakati wa bajeti tuliyoipitisha ya mwaka huu na mwaka wa kesho tuliomba tuongezewe fungu fulani kwa ajili ya kujenga zahanati na vituo vya afya ili vikamilike na vingi wananchi tayari walishajitolea, vipo. Tunaomba Serikali itusaidie kwa hilo, ile miradi muhimu ambayo ni kichocheo cha uchumi, cha uzalishaji kwa wananchi, ifanyiwe kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuisisitiza hii kwa sababu hiyo ndiyo miradi ambayo inawagusa wanawake wengi. Wanawake wengi ndio wazalishaji vijijini, wanawake wengi ndio wanaohangaika na maji, wanawake wengi ndio wanaohangaika na watoto wagonjwa na wao wenyewe wakiugua, lakini huduma zote ambazo zinawagusa akinamama ndio hizo ambazo tunazipigia kelele sasa. Tunaomba Serikali wakati mnaangalia mambo makubwa lakini na haya madogo msiyape kisogo kwa sababu yana umuhimu mkubwa sana kwa uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna masuala ya miradi ya mikakati ya kielelezo, kwa mfano, General Tyre. Hakuna asiyejua umuhimu wa General Tyre ilipokuwa ikifanya kazi na tunaambiwa kabisa kuwa ilikuwa tayari ianze kufanya kazi. Tunajiuliza kimekwama nini sasa kwa General Tyre kuanza kazi? Tungependa kujua General Tyre kwa nini haijaanzishwa mpaka sasa hivi wakati kila kitu kilikuwa kiko tayari kuendelea?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka vilevile kuzungumzia NDC - Shirika la Taifa la Maendeleo. Hili ni shirika ambalo limepewa majukumu maalum kusimamia au kuibua miradi ya maendeleo na limekuwa likifanya hivyo, lakini fedha linayopata ni kidogo mno kiasi kwamba unashindwa kuelewa watafanyaje kazi. Mradi huu tunaozungumza wa Liganga na Mchuchuma ni mradi ambao upo chini ya NDC, mradi wa magadi soda upo chini ya NDC na miradi mingine mingi ambayo tunategemea NDC waisimamie lakini bila kuwa na bajeti ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tungependa sasa hivi kusikia kutoka Serikalini mipango mikakati yao ya kuhakikisha kuwa hii miradi sasa inaanza kufanya kazi. Tumekuwa tukiizungumza na imekuwa katika vitabu vyetu kwa miaka mingi sana sasa, tungependa tujue Serikali imeshatenga fedha ya kutosha kwa ajili hiyo? Lakini kama wao wenyewe hawana fedha tulishakubaliana kuwa tuna mpango wa PPP jamani siyo kila kitu lazima Serikali yetu yenyewe ifanye na uwezo huo bado hatuna. Kwa nini tusiachie huu mpango wa PPP sasa ufanye kazi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa na nitafurahi sana kusikia Serikali ikisema kuwa kuanzia mwaka huu wa fedha tunaouendea tutakuwa na miradi kadhaa hata kama ni mitatu tu mikubwa ambayo inaendeshwa kwa mpango wa PPP ili kuipunguzia Serikali adha ya kuhakikisha inatafuta fedha yenyewe. Nchi nyingi zinazoendelea au zilizoendelea zilitumia mfumo huo kupunguza ule mzigo kwa Serikali kwa ajili ya bajeti yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nizungumzie masuala ya Economic Processing Zones na Special Economic Zones. Nchi nyingi kama China kwa mfano waliendelea haraka sana kiuchumi walipojiingiza katika mfumo huu wa maeneo maalum ya kiuchumi. Sisi tumeainisha maeneo mengi mengine tumeshalipa mpaka hata fidia, lakini hatufanyi chochote wakati huko ndio ambako tungehakikisha kuwa uwekezaji mkubwa unafanywa na sekta binafsi kwa ajili ya kuhakikisha kuwa tunaendeleza viwanda vyetu hasa vile vidogo na vya kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vichache ambavyo tayari vimeshaanzishwa kwa mfano pale Dar es Salaam tunaona kabisa jinsi ambavyo vinazalisha na vimezalisha ajira nyingi sana, imagine kila mkoa ambako kulikuwa kumeainishwa maeneo hayo ingekuwa yanafanya kazi sasa hivi tungekuwa tunalalamikia ajira wapi? Kwa hiyo, nataka kusikia EPZ na Special Economic Zones sasa hivi Serikali inakwenda kufanya nini kwa maana ya utekelezaji, kwa maana ya nadharia na mipango tunayo tunaijua muda mrefu. Tunaomba sasa ikafanyiwe kazi japo tuone mradi hata mmoja unaanza katika hii miradi mikubwa ambayo imewekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la bandari; tumekuwa na mipango mizuri tuliyoiweka kwa ajili ya kupanua bandari zetu, magati yale ili kuhakikisha kuwa meli zinakuja kuweka nanga na kutoa mizigo na kuchukua mizigo, lakini yamekuwa ni mazungumzo ya muda mrefu. Mpaka wenzetu sasa wamestuka wao sasa wameshaendeleza bandari zao na tupo kwenye ushindani mkali sana. Nataka kusema hivi, haya mambo ya kusema ooh! wawekezaji wanatupenda jamani tuachane na hizo ndoto, anakupenda kwa sababu kuna kitu atakuja kunufaika na wewe, hakupendi kwa sababu wewe ni Mtanzania au kwa sababu sijui una sura nzuri au kwa sababu una amani. Naomba ndugu zetu Serikalini mtambue kuwa biashara ni mashindano, Kenya wakimaliza bandari zao, Kenya wakimaliza reli zao hao mnaowaita marafiki zenu hamtawaona na tukishapoteza wateja siyo rahisi kuwarudisha jamani yaani hiyo ni economic sense ya kawaida kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali yangu sikivu, hebu sikieni hili for the last time, hebu fanyeni hivi vitu sasa hivi viwe reality. Tunashindwa hata jinsi ya kuvitetea kwa wananchi kwa sababu ni kila mwaka wanaviona, vyote vipo vimeainishwa katika Ilani yetu lakini utekelezaji lini sasa? Na kama hatuna fedha viko vyanzo sasa through sekta binafsi ambavyo vinaweza vikafanya. Rahisisheni masharti kwa sekta binafsi wa-engage wasikilizeni sekta binafsi wana mawazo mazuri, wale ni wafanyabiashara na wanajua jinsi ya kuendesha biashara kwa faida na faida hiyo itapatikana kwa wote; ninyi Serikali na wao sekta binafsi. Ningependa sana kusisitiza kuwa hayo ni mambo ambayo lazima sasa hivi tuyawekee mikakati ya kufanya, yapo kwenye vitabu, yapo kwenye Ilani lakini sasa tuanze utekelezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la wajasiriamali wadogo na wa kati, bila kuwawezesha hawa hata hao wakubwa ambao tunataka kufanya nao biashara itakuwa ni kazi bure, hawa wadogo ndio watakaosaidiana na wakubwa, watakuwa na mahusiano yanayoshabihiana. Wakubwa watakuwa ndio wanunuzi wa huduma za hawa wadogo na wadogo ndiyo watakuwa wanapata ujuzi kutoka kwa wakubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani tukawa tuna sekta ya chini kabisa na ya juu kabisa katikati hapa hakuna kitu, hakuna kitu kama hicho! Kwa hiyo, lazima wajasiriamali wadogo na wa kati wawe na mkakati maalum wa kuwasaidia kwa maana ujuzi, urasimishaji, lakini vilevile tuhakikishe kuwa kodi wanazotozwa jamani wanakuwa discouraged na kodi. Wanaanza tu hivi tayari wana mzigo wa kodi, haitawezekana kama tunataka kuwawezesha tuwape muda wafike mahali ambapo wataweza sasa kusimama ndiyo tuanze sasa kuwatoza kodi. Lazima tuwalee, mbona tunalea wakubwa, hawa wadogo kwa nini tunashindwa kuwalea na ni wazalendo na ndio watu wetu? Huko ndiyo vijana wetu watakapoponea katika masuala ya kiuchumi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna suala lingine la mabenki. Yamezungumzwa mambo mengi sana kuhusiana na mabenki kuwa yamekosa mitaji sasa yatakosa kukopesha, nataka kusema mabenki yetu yalikuwa yamelemaa, yalilemazwa na Serikali kwa ajili yalikuwa yanapata pesa za bure. Asilimia 20 ya Watanzania ndio ambao wanatumia mabenki, hawa wengine wote pesa zao ziko wapi? Mabenki yaanze kutoka sasa maofisini waende vijijini huko wakatafute wateja wakaweke kama ni agency, kama ni branches, chochote kile lakini wahakikishe kuwa wanazitafuta, fedha zipo, siyo za Serikali tu ndiyo fedha zao, wao watafute vyanzo vingine vya deposits.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Natoa pole zangu kwa wote wale waliofiwa na watoto na familia ya Mzee Sozigwa, familia ya Mzee Mwambungu na wengine wote ambao wamepata maafa hivi karibuni, Mungu alaze pema roho zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwashukuru sana na kuwapongeza Wizara ya Elimu kwa hotuba nzuri, napongeza Kamati zote mbili kwa maoni yao mazuri waliyoyatoa kwa Serikali, nitashukuru na nitafurahi kuona kuwa Serikali imeyazingatia maoni yote yale ambayo yanafaa katika kuboresha huduma zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi wamezungumza mambo mengi na nisingependa kuyarudia. Napenda kuzungumzia suala zima la kumuendeleza mtoto anapokuwa mdogo. Wengi tumezungumzia elimu kwa maana ya shule za msingi, shule za sekondari, vyuo na vyuo vya ufundi, lakini nataka turudi katika msingi wa kumlea mtoto ili aje kuwa mwanafunzi mzuri, aje kuwa mfanyakazi mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesahau kabisa suala la kumlea mtoto, kumjengea mtoto uwezo wake tangu akiwa mdogo kwa maana ya shule za awali. Imeonesha kabisa katika tafiti mbalimbali kuwa mtoto akianza kujengewa uwezo mzuri kiafya kwa maana ya lishe, lakini vilevile kiakili kwa maana ya kumpeleka kuanza kuchezacheza shuleni na wenzake, kuanza kujifunza ku-interact na wenzake, kuanza kucheza michezo ambayo inamjenga ubongo, kumfundisha utundu wa kutumia ubongo wake, anakuja kuwa mwanafunzi mzuri anapoanza shule ya msingi mpaka kwenda sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka kupendekeza kuwa Serikali iwe na mkakati wa kuhakikisha kuwa nchi nzima shule za awali zinatiliwa mkazo kama ambavyo tunatilia mkazo masuala mengine ya afya na maji, vilevile mtoto aanze kujengwa akiwa mdogo. Huwezi kumtoa mtoto aliyekuwa anakaa nyumbani siku zote ukampeleka miaka saba kuanza shule kwa mara ya kwanza, atakuwa hajapata ule msingi wa kumuwezesha. Haya mambo ya pre-school siyo mchezo, ni sehemu ambayo inaanza kumjenga mtoto jinsi ya kuelewa vitu lakini kutafakari mambo na vilevile kuzoea ku-interact na watoto wa aina nyingine. Kwa hiyo, ningependa sana hili nalo litiliwe mkazo kama ambavyo tunatilia mkazo masuala mengine ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la elimu ya watu wazima; wakati sisi tunakua kulikuwa kuna elimu ya watu wazima na ilikuwa inagusa watu wazima kwa maana ya wazee au watu wazima ambao hawakupitia shule, lakini hata wale vijana ambao kwa bahati mbaya kwa mazingira fulani walishindwa kuendelea na masomo halafu waka- regress. Unajua ubongo zoezi lake ni kuutumia, kuusomea, kufanyia vitu ambavyo unau-challenge ubongo ndiyo hata ile elimu uliyokuwa umeipata inaendelea kuwepo. Unaweza ukajikuta ulisoma halafu hata kusoma gazeti ukakushindwa kwa sababu umekaa umebweteka hutumii ubongo, kwa hiyo, wale pia walikuwa wanapewa elimu. Sasa hii elimu ya watu wazima sijaiona vizuri hapa, nimesoma imenionesha tu kuwa kuna fedha na mkakati wa kujenga uwezo au kuboresha uwezo wa taasisi yenyewe. Sijaona wapi inaonesha kule chini kwa wananchi elimu ya watu wazima itaendeshwa vipi, ningependa hilo lionekane kwa sababu ni muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafika mahali ambapo sasa mzazi hajui kusoma chochote, hajui hesabu, atamsimamia vipi mtoto wake kuhakikisha kuwa anafanya kazi zake za shule? Kwa hiyo, inakuwa vigumu kwa mzazi hata kusimamia mtoto masomo kwa sababu yeye mwenyewe hajui na hajiamini kuwa anaweza akamsimamia mtoto. Kwa hiyo, hilo la elimu ya watu wazima naomba lizingatiwe na lipewe kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vifaa vya wanafunzi wanaoishi na ulemavu. Watoto wengi bado hawawezi kusoma vizuri kwa sababu wanaishi na ulemavu lakini shule hazitoshelezi kwa mahitaji ya vifaa vyao, vitabu vyao na mambo yote yanayowezesha watoto wanaoishi na ulemavu kusoma vizuri kama watoto wengine wote. Hili naomba nalo lizingatiwe, hasa sisi tunaokaa kwenye Wilaya za pembezoni, kwa kweli hili suala hatulioni kabisa. Kwa hiyo, ni kitu ambacho lazima kiwepo. Kuwachanganya watoto wakati wote siyo vibaya lakini wakati mwingine inabidi wawe segregated ili wapate kujifunza vizuri wenyewe kwa pace yao. Maana mtoto anayeishi na ulemavu wakati mwingine kwa sababu ya ule ulemavu wake ukimuweka na watoto wengine inaweza ikawa inam-challenge zaidi, kwa hiyo inategemea ni level gani unamchanganya na watoto wengine, lakini vifaa havitoshelezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu VETA sijui ni kigezo gani kinatumika kuweka VETA kwenye Wilaya zetu, Wilaya yangu ya Ileje nilifanya juhudi zangu binafsi nikapata mfadhili akanijengea VETA ambayo Serikali iliahidi kuwa itaichukua, lakini wakanipa masharti kuwa lazima ile ardhi iwe imepimwa na mambo mengine yote. Sasa kutokana na changamoto za kupima ardhi tunazozijua, mpaka leo huu ni mwaka wa pili, hatujaweza kupima ile ardhi na kwa hali hiyo VETA imesimama pale haifanyi kazi. Nataka kuwaomba, kama vile ambavyo tuliweza kuijenga bila kuwa tumepima, basi muichukue ianze kufanya kazi wakati taratibu za kupima zinafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu vitabu; kama ambavyo tumekuwa tukiweka mkazo sana kwenye kujenga madarasa, tukajenga maabara, tukaanza kushughulikia miundombinu ya walimu na mafao yao; shule bila kuwa na vitabu vya kutosha nayo pia ni kazi bure. Imetubidi Wabunge tufanyekazi ya ziada kutafuta vitabu kwa ajili ya shule hasa vitabu vya sekondari, hii inakuwa ngumu. Vitabu ndiyo moja ya kitu ambacho ni ghali sana katika huduma za mwanafunzi. Sasa kuniambia kuwa mimi Mbunge au wazazi peke yao wakasimamie kutafuta vitabu, hasa kwa mfano vya sayansi, vya hesabu, vya lugha, inakuwa vigumu.

Kwa hiyo, naomba sana hili suala la vitabu nalo lizingatiwe, lipewe uzito ule ule tuliotoa kwa masuala ya madarasa, maabara na mambo mengine, kwa sababu bila vitabu pia kufundisha inakuwa vigumu, walimu wanapata shida sana kufundisha bila vitabu.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mabweni sijui hili nalo litashughulikiwa vipi. Wilaya yangu ya Ileje haina shule ya sekondari ya bweni ya watoto wa kike hata moja. Tunazungumzia miaka 42 tangu Wilaya ianzishwe. Tunajitahidi wenyewe sasa hivi kutafuta namna ya kuanzisha shule ya bweni ya wasichana lakini mnajua gharama za kujenga shule kwa kutegemea nguvu za wananchi labda na Mbunge wao. Tunaomba sana Wizara kama inaweza kutufikiria, watoto wa kike wengi wa Ileje wanapata mimba za utotoni na tatizo moja ni hilo kuwa wanakwenda mbali sana kusoma, wanakwenda Wilaya nyingine kwenda kusoma au wanasoma pale ndiyo wanapanga kwenye ma-gheto. Gheto za ya vijijini, imagine mjini ma-gheto yalivyo, vijijini ni mabaya namna gani. Hakuna umeme, hakuna maji, kwa hiyo wanajikuta wanasoma katika wakati mgumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika takwimu utakuta wasichana wa Ileje wanapata mimba za utotoni wengi, pengine hata Mkoa mzima wa Songwe sijui, lakini nazungumzia kule ambako nina uzoefu nako. Kwa hiyo, haya ni mambo ambayo tunahitaji sana Serikali myafanyie kazi, shule za wasichana za mabweni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi kuna suala zima la hayo Mabweni yenyewe. Mabweni yanajengwa lakini mengi hayajakamilika, mengine zile certificate contractors hawajalipwa, kwa hiyo, bado pamoja na kuwa kuna hostels chache zimejengwa lakini hazijaanza kutumika kikamilifu kwa sababu hazijkamilika na hiyo pengine ni ukosefu wa fedha au sielewi ni matatizo gani lakini kwa kweli haitusaidii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia suala zima la tafiti. Tumeona hapa fedha nyingi zinatolewa kwa ajili ya utafiti, tunajiuliza hizi tafiti huwa zinaishia wapi? Kwa sababu tukija kule kwenye Halmashauri zetu bado hatuoni mazao ya zile tafiti zikatusaidia katika kuboresha mazingira ya elimu na mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tungependa sana hizo tafiti, kwanza hata kule kule kwenye Wilaya zetu tupate hawa watu wanaokuja kufanya utafiti au watu wetu nao wachukuliwe kufanya hizo tafiti yaani wafadhiliwe kufanya hizo tafiti, vilevile matokeo ya utafiti yanapotokea basi yaletwe na kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumezungumzwa jambo la kufundisha watoto hapa masuala ya study za maisha. Nataka nitoe angalizo ndugu zangu, tuna miradi mingi ya Kimataifa inayoletwa kwenye nchi zetu ya kutufundishia watoto wetu masuala ya study za maisha. Naomba zichunguzwe kabla hazijaanza kupokelewa, watoto wetu wanafundishwa maadili ya ajabu, watoto wetu wanafundishwa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi ya kuchangia hoja hii muhimu ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Nashukuru kwa fursa ya kuchangia hotuba. Naipongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa uongozi wake na maamuzi ya haraka katika kushughulikia changamoto za sekta hii. Ninawapongeza Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako na Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya na Katibu Mkuu na watendaji wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza Maoni ya Kamati na Kambi ya Upinzani na ya Waheshimiwa Wabunge wote waliotoa maoni mazuri yanayoletea kuboresha sekta hii kwa ajili ya kujenga uwezo wa Taifa hili, kumudu weledi na rasilimali watu ya kutosha, ushindani wa soko na kuboresha kiwango cha elimu inayotolewa nchini. Naomba mchango wangu ufanyiwe kazi wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupata elimu bora ni msingi wa maendeleo ya mtu binafsi na kijamii na kiuchumi popote pale duniani. Kwa upande wa Tanzania, naipongeza Serikali ya CCM kwa jitihada zake za mwaka hadi mwaka za kuongeza fursa ya elimu sawa kwa wote na utoaji wa elimu bora ya msingi, sekondari na ngazi ya elimu ya juu, hili ni jambo la msingi ili kufikia malengo makuu ya maendeleo endelevu. Isitoshe, jamii iliyoelimika vizuri ni kiini cha kuleta maendeleo katika nyanja mbalimbali kwa uwiano wa usawa na pia kustawisha utawala bora. Ijapokuwa Tanzania imepata maendeleo makubwa katika kutoa elimu ya msingi, bado kuna upungufu mkubwa katika suala la ubora wa elimu wanayopata watoto. Kukaa shuleni hadi kumaliza darasa la saba pia ni tatizo sugu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunazungumzia elimu ya mtoto wa Kitanzania kama mkakati wa kujenga rasilimali watu yenye uwezo mkubwa wa kushindana katika soko la ajira na kufanya kazi kwa tija, tunaitaka Serikali izingatie yafuatayo na kuyafanyia kazi:-

Moja, malezi ya mtoto miaka ya awali hadi kufikia miaka mitano. Malezi na makuzi ya mtoto yanahusisha pande zote za mambo yanayoweza kumfanya mtoto akue vizuri tangu umri mdogo, ujana hadi utu uzima. Kwa hiyo, masuala ya afya ya mtoto tangu akiwa tumboni, anapozaliwa hadi anapobalehe, utu uzima na uzee, elimu ya mtoto huyu tangu anapozaliwa hadi uzeeni ni muhimu. Ndiyo maana ni vizuri Serikali ikafanya kazi kama kitu kimoja ili kujenga misingi ya kumletea elimu mtoto mwenye afya njema kiakili na kimwili. Maendeleo ya mtoto kupitia ngazi zote hizi ndiyo msingi wa maendeleo mengine yote yanayofuata katika maisha ya mtu huyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni kuhusu huduma za awali za mtoto kiafya, vituo vya kulelela watoto na shule za awali ni sehemu muhimu ya maendeleo ya mtoto kiakili. Pia inasaidia wazazi kupata nafasi ya kufanya shughuli nyingine za maendeleo ya familia. Vituo hivi vinawezesha watoto kuchanganyika na wenzao kwenye michezo mbalimbali na mafunzo mepesi yanayojenga uelewa, utambuzi na hata hisia zao juu ya masuala tofauti. Kipindi hiki ni muhimu kwa mtoto, kwani kinamtayarisha kwa shule rasmi na wanapokuwa tayari kwenda shule ukifika umri wa kwenda shule wanakuwa wachangamfu, wanakuwa rafiki zaidi na kujiamini zaidi. Wanakuwa na mahusiano mazuri na wenzao, ujuzi wa lugha na watakuwa na mawasiliano mazuri. Watoto walio tayari kwenda shule wana nafasi kubwa zaidi na kufanya vyema kwenye masomo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iliwahi kueleza Bungeni kuwa mahitaji halisi ya madarasa ya awali ni 16,014 ambayo ni sawa na idadi ya shule za msingi zilizopo nchini kwa sasa. Shule zenye madarasa ya awali ni 14,946 ambazo ni sawa na asilimia 93.33 ya mahitaji. Hivyo, shule za msingi 1,068 hazina madarasa ya awali. Tunapenda kufahamu sasa kama idadi hii imeongezeka?

Takwimu za Serikali zimeainisha idadi ya walimu wa shule za awali kiwilaya. Je, walimu hawa wanasomea kufundisha watoto hawa? Je, idadi yao inatosheleza mahitaji? Kama siyo, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha inatoa walimu wa kutosha kwa kila kijiji kuwa na shule ya awali? Naomba Serikali ije na mkakati wa shule za awali kila Wilaya kama ilivyo kwa zahanati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza kuwa Serikali itoe motisha kwa sekta binafsi kuhakikisha kuwa kila sehemu ya kazi au kiwanda au shamba kubwa la kibiashara linakuwa na kituo cha kulea watoto na vilevile kuwe na ramani za jinsi vituo hivi vitajengwa ili kuzingatia usalama wa watoto na upatikanaji wa huduma muhimu kwa mtoto, yaani kusoma, kucheza, kula chakula bora, kupumzika na kujisaidia. Hii itawafanya wazazi hata wa vijijini kuwa na imani kwenda kuwaacha watoto kwenye vituo hivi ili wao wakaendelee na shughuli nyingine za maendeleo, watoto wapate fursa ya kujifunza na kucheza na wenzao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu chakula na lishe bora shuleni; ipo haja ya Wizara za Elimu, TAMISEMI, Maji na Fedha kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha huduma zote zinazoainishwa kwenye hotuba hii vinafanikiwa, ikiwa ni pamoja na kuanzisha mpango wa kuwalisha watoto shuleni. Tunafahamu kuwa mpango huu uko katika hatua za awali na tayari baadhi ya shule zimeshaanza kupelekewa chakula kwa ajili ya kuwalisha watoto na kampeni za uhamasishaji kwa familia juu ya umuhimu wa lishe bora kwa watoto shuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa shule ambazo chakula kinatolewa, basi kiandaliwe vizuri na kiwe na lishe bora na kiandaliwe katika mazingira yanayoridhisha ili kuwaweka watoto katika hali ya afya njema. Tuna wajasiriamali wengi wanaotenngeneza majiko mazuri yanayofaa kutumika kwenye taasisi mbalimbali wapewe tender za kutengeneza majiko kwa ajili ya shule zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla watoto wanataka kuona mabadiliko na maboresho kwenye maeneo ya lishe ya mama na mtoto na watoto wote kwa ujumla kwa kuhakikisha kuwa uhakika wa chakula unakuwepo, kuendeleza tabia ya mazoea ya kula chakula chenye lishe bora na kuelimisha watoa huduma kuhusu tabia ya kula chakula chenye lishe bora na kuelimisha watoa huduma kuhusu tabia ya kula chakula chenye virutubisho vyote vinavyohitajika mwilini na njia bora za kuandaa chakula chenye lishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa mapendekezo yafuatayo ili kulinda haki za watoto na kufanikisha eneo la pili miongoni mwa maeneo kumi ya uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ushiriki wa Serikali na misaada mbalimbali, Wizara zinazohusika na masuala ya lishe kama vile Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu zitenge rasilimali na fedha za kutosha ili kuboresha lishe shuleni na katika familia. Pia Wizara hizi zihakikishe kuwa sheria husika zinatungwa na taratibu na viwango vinawekwa ili kuhakikisha upatikanaji wa vyakula vilivyosindikwa na vyenye lishe bora vinapatikana na kusambazwa kwa wingi nchini na kuwafikia walaji ili kuwakinga watoto na magonjwa kama yale ya utapiamlo na unyafuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Mheshimiwa Rais akutane pamoja na Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ili kujadili mikakati itakayofanikisha suala zima la kuratibu upatikanaji wa lishe bora katika jamii zetu. Serikali iwajibike kuanzisha programu mahususi za kusaidia familia moja moja kupata uhakika wa chakula na hivyo kufanikisha tabia ya kula chakula chenye lishe bora (kwa mfano kampeni ya nchi ya Rwanda ya kugawa ng’ombe mmoja kwa familia moja ambapo kila familia maskini hupewa ng’ombe mmoja wa maziwa kwa ajili ya lishe bora ya watoto).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuamsha na kuendeleza ufahamu kuhusu lishe bora kwa watoto; watoaji huduma, wazazi na jamii kwa ujumla, inapaswa kuelimishwa kuhusu uhakika wa chakula na masuala ya lishe kwa watoto kama vile njia bora za kutumia rasilimali chache zilizopo, uandaaji na ulaji wa chakula chenye virutubisho vya kutosha na utaratibu mzuri wa kulisha watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee lishe kama sehemu ya huduma ya afya. Zahanati na vituo vya afya viwe vinatoa taarifa na elimu kuhusu lishe bora kwa watoto na wajawazito na hata kwa wanawake wenye watoto wachanga pamoja na kutoa tiba ya kutosha na yenye kukidhi mahitaji ya watoto wachanga wanaosumbuliwa na magonjwa yanayotokana na lishe duni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu katika kuhakikisha upatikanaji wa chakula kwa wote; iko haja ya kuweka utaratibu au programu za kudhibiti bei za vyakula ili kupunguza uwezekano wa kupandishwa kwa bei hizo kiholela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kupanua wigo wa programu za chakula kwa watoto shuleni kwa kuongeza fedha na rasilimali nyingine husika ili kuongeza idadi ya shule zenye kutoa chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira ya usafi na usalama shuleni yako kwenye hali mbaya, ya chini kabisa, tofauti na miongozo iliyotolewa na Wizara ya Elimu na Ufundi, licha ya juhudi za Serikali za kuongeza vyumba vya madarasa pamoja na idadi ya shule za msingi, inaelekea mkazo mdogo sana umewekwa kwenye vyoo. Bado vyoo visafi na vyenye usalama kiafya ni muhimu kwa kujenga mazingira rafiki ya kufaa kwa kusoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za Serikali Tanzania za elimu ya msingi zinahitaji miundombinu bora na ya kukidhi mahitaji ili kuboresha mazingira na uwiano mzuri wa idadi ya wanafunzi na matundu ya vyoo yaliyopo shuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu huduma ya vyoo; shule zilazimike kuweka kipaumbele kukarabati miundombinu na kuboresha usafi wa vyoo na matundu ya vyoo yaliyopo shuleni ili kuepukana na maambukizi ya magonjwa. Pia kuweka mifumo mizuri ya kumudu takataka zinazozalishwa shuleni ili kuepukana na uchafuzi wa mazingira na kufurika kwa vyoo. Ukosefu wa huduma ya maji shuleni mara nyingi husababisha watoto kuwa watoro shuleni na maji machafu husababisha kuenea kwa magonjwa. Kwa hiyo, inapendekezwa kuhakikisha kwamba maji safi na yanayofaa kwa kunywa yanapatikana kwenye shule zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kiwango cha usafi wa mazingira na afya shuleni; shule zote lazima zikaguliwe na kuwajibika kwa lolote lile linalohusika na mazingira machafu na hatarishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina wajibu wa kusaidia shule aidha kwa kutenga fedha au kuzipatia rasilimali nyingine ili kutatua tatizo la mazingira machafu na hatarishi hasa kwa shule za Serikali zilizoko vijijini ambazo zinategemea mgao wa bajeti ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule nyingi pia zinakabiliwa na ukosefu wa maji safi na salama ya kunywa pamoja na viwanja vya michezo. Matundu ya vyoo na vyoo, upungufu uliopo ni kwenye kubuni michoro, kujenga na kutunza vyoo vilivyopo shuleni. Tunasisitiza kuwa vyoo vilivyopo havifai na ni vichafu kwa matumizi ya watoto. Isitoshe, kuna upungufu wa vyoo na matundu ya vyoo unaosababisha mistari mirefu ya watoto katika kutumia huduma hiyo na kuwachukulia muda wa kuwa darasani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingi wanazopata watoto ni kutokana na umbali wa vyanzo vya maji kutoka majumbani mwao. Umbali mrefu unaathiri jukumu la kusoma na mara nyingi wanachelewa au kutokwenda kabisa shuleni kutokana na uchovu. Zaidi ya hayo, suala la usalama wakiwa wanaenda kuchota maji kwa kuzingatia kuwa njia ya vichochoro wanavyopitia siyo salama kwa watoto hasa wasichana ambao huwa na hofu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uhaba wa maji; kaya na jamii nyingi zina upungufu wa huduma ya maji na zina mfumo mbovu wa usambazaji wa maji kama vile mabomba yaliyovunjika, hivyo hulazimisha kaya kununua maji kwa bei ghali kutoka kwa wachuuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ukosefu wa usawa wa jinsia; wasichana mara nyingi wanatumwa kwenda kuchota maji na wanalazimika kutembea masafa marefu kutafuta maji hayo, wakati wavulana wanaruhusiwa kwenda shule. Jukumu hili la kutafuta maji mara nyingi huwaweka wasichana kwenye hatari ya kunyanyaswa na kudhalilishwa kijinsia na hata kubakwa na watu wasiowajua wakati wakiwa njiani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza uwekezaji kwenye elimu ya awali kwenye maeneo yafuatayo; moja, makuzi ya awali ya maendeleo kiakili ya watoto. Nashauri wazazi/walezi na Wizara husika kubuni na kutekeleza shughuli mbalimbali zinazowawezesha watoto kukua kimaumbile na kiakili kwa kuanzisha shule za ziada za awali na kuwahusisha watoto kwenye shughuli za kuchangamsha akili, kutambua na kukuza vipaji na kukuza lugha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma ya mama na mtoto baada ya uzazi inahitaji kuboreshwa hasa kwa kupima, kinga na tiba kwa magonjwa sugu ya watoto na kupanua wigo wa huduma ili kuhakikisha kuwa watoto wote wanapata chanjo na kinga kwa magonjwa mbalimbali. Utengaji wa bajeti ya kuwekeza kwenye miradi na mipango ya malezi na makuzi kwa watoto pamoja na ile inayosimamiwa na Serikali na Taasisi zisizo za Kiserikali ili kuongeza msisitizo na mwonekano Kitaifa na kikanda wa suala hili la makuzi ya watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu ubora wa elimu; ufundishaji shuleni bado si wa kuridhisha nchini kote. Kuna changamoto katika mitaala iliyopo pamoja na mbinu za ufundishaji ambazo hazina mwelekeo mzuri utakaowajenga watoto kupata ujuzi wa kutosha wa kuchambua mambo na kuwa wabunifu na uthubutu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la upungufu wa walimu; mgawanyo wa walimu waliopo hauridhishi na husababisha shule nyingine kuwa na upungufu mkubwa zaidi. Isitoshe, pamoja na kwamba walimu wapo, mara nyingi wanakosa motisha na ari ya kufundisha na matokeo yake ni kutokufanya vizuri kwa watoto kwenye masomo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wenye ulemavu na wasichana hawapati elimu sawa na watoto wengine kutokana na mila na desturi ambazo zinawabagua. Vilevile makundi haya mawili hayathaminiwi na jamii zao ambazo huwapatia wavulana kipaumbele. Hali duni ya miundombinu shuleni/vifaa; shule zilizo nyingi hazipati mgao wa kutosha wa rasilimali na zimejengwa vibaya, hivyo kuyafanya mazingira ya kufundishia na kusoma kuzorotesha ufanisi katika kutoa elimu bora. Pamoja na hayo, shule nyingi hazina vyumba vya madarasa vya kutosha au vifaa vya kutosha kufundishia (karatasi, vitabu na kadhalika).

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu nyingine kubwa inayosababisha mahudhurio hafifu ya watoto shuleni ni umbali mrefu wanaohitajika kutembea kwenda shule. Zaidi ya hayo, njia nyingine wanazopitia ni hatarishi hasa kwa wasichana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla kuna umuhimu wa Serikali kufanya maboresho katika sekta ya elimu kwa kuwa na walimu bora wenye ujuzi na ari ya kufundisha ili kuleta ufanisi. Uwekezaji zaidi uongezwe katika kuboresha elimu iliyotolewa shuleni hasa kwenye shule za Serikali na zile zilizoko vijijini ambazo zimesahaulika kupita kiasi. Mafunzo zaidi kwa walimu yapewe kipaumbele na kuongeza vifaa shuleni kama vile vitabu, karatasi, kwa shule zote na siyo tu zile za watu binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni utoaji elimu bure kwa wote. Mazingira ya shule yaboreshwe ili kuvutia na kuwa toshelezi na rafiki kwa watoto wote ikiwa ni pamoja na wasichana na wale wenye ulemavu ili kukwepa ubaguzi na maendeleo hafifu shuleni.

Kuhusu ukaribu wa shule na huduma ya usafiri; wakati wa kuchagua sehemu za kujenga shule mpya, umbali watakaotembea watoto kwenda shule na ukaribu na shule vizingatiwe. Pamoja na hayo, njia za kwenda shule lazima zichaguliwe vizuri na kuchunguzwa ili kuwalinda watoto dhidi ya watu wenye nia mbaya na hatari kwa maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kuzuia mimba za utotoni, fursa ya kupata huduma za afya ya uzazi; juhudi zifanyike kutoa fursa zaidi kuwawezesha wasichana kupata huduma za afya ya uzazi katika maeneo yao wanapoishi na katika vituo vya afya/kliniki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu kuhusu mimba za utotoni shuleni, elimu ya afya ya uzazi isiishie tu katika ngazi ya shule za sekondari bali ipelekwe pia katika shule za msingi na katika Vituo vya Maendeleo ya Jamii ili kuwafikia wasichana ambao wako nje ya shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria na sera kuhusu suala la ngono kwa watoto hazitekelezwi ipasavyo wala kufuatiliwa kwa karibu ndani ya jamii nyingi. Juhudi zaidi zinahitajika kwa vyombo na watu wanaohusika na usimamizi wa sheria kuwajibika kufuatilia kwa makini na kupeleka Mahakamani kesi za kubaka, ngono za kulazimishwa na za kulipia kwa watoto na kuhakikisha wavunjaji wa sheria au wakosaji wanaadhibiwa vikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu wa usafiri wa wanafunzi, shule lazima ziwekeze katika mfumo na utaratibu mzuri wa usafiri kwa watoto badala ya kutegemea usafiri wa umma ambao huwaweka wasichana katika hatari ya kudhalilishwa kijinsia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu watoto waathirika wa mimba za utotoni na elimu; wasichana wanaoacha shule kwa sababu ya ujauzito waruhusiwe kurudi shuleni kumalizia masomo baada ya kujifungua. Shule lazima ziwahamasishe hawa wazazi ili watoto warudi shuleni na kuepuka kuwafukuza kwa kisingizio tu cha hali yao ya ujauzito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kukomesha ndoa za Utotoni. Tunaamini kuwa mimba za utotoni ni chanzo kikubwa cha ndoa za utotoni na tunasisitiza na kuhimiza kuelimisha jamii kuhusu hatari na madhara ya matokeo ya mimba za utotoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukatili dhidi ya watoto ni kitendo cha kuvunja haki za binadamu na tatizo la kijamii na kiafya lenye madhara makubwa. Ukatili unaondoa nguvu ya misingi mikubwa ya malezi ya watoto ambayo watoto wanahitaji ili kukua na afya na maisha yenye tija na pia ukatili unakiuka haki za msingi za watoto kupata ulinzi. Matatizo mengi yanayowakumba watoto humu Tanzania ikijumuisha kazi zinazowanyonya watoto, kuwasafirisha watoto kwenda kufanya kazi hatarishi za kuuza miili yao na ukatili wa kijinsia yanaathiri vijana zaidi ya watoto wadogo. Mara nyingi asasi zile zile na hata watu binafsi ambao wanategemewa kuwalinda watoto kama vile walimu, polisi, familia zenyewe zimetajwa kuwa zinahusika kuendeleza ukatili dhidi ya watoto na udhalilishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla watoto wanahitaji ulinzi dhidi ya ukatili na aina nyingine za unyanyasaji. Sheria kuhusu kazi ngumu kwa watoto na adhabu kali za wakosaji ambao wanakiuka na kuwafanyia watoto ukatili yashughulikiwe kikamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yafuatayo katika kulinda haki ya mtoto na kufanikisha utekelezaji wa eneo la tisa la uwekezaji:-

Moja, Sheria za Ajira ya Watoto na Sera. Serikali za Mitaa na wadau wengine wakuu lazima wawajibike katika kusimamia utekelezaji wa juhudi za kulinda haki za watoto. Serikali za Mitaa pia lazima kuongeza uelewa na kujiimarisha ili kumudu kwa ufanisi kusimamia kazi ya utetezi na ulinzi wa haki za watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yatima na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi; nashauri Serikali kuandaa mfumo wa ufuatiliaji wa ulinzi wa haki za watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi hasa wale wanaoishi mitaani. Hii itasaidia wanajamiii na viongozi wa Serikali za Mitaa kuchukua hatua za kupima maendeleo yaliyofikiwa katika kukomesha ukatili na udhalilishaji wa watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu makazi ya muda au makazi salama; watoto pia walipendekeza kuanzishwa makazi au vituo vya muda vya kutosha kulelea watoto wanaoishi mitaani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utekelezaji wa sheria; kutokana na ongezeko la ukatili kwa watoto, ajira za watoto na unyonyaji, watoto walipendekeza kusambaza sehemu zote nchini nakala ya Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu watoto wenye ulemavu; nchini Tanzania kama ilivyo katika nchi nyingine zinazoendelea na pamoja na kuwepo kwa sheria nzuri zinazolinda watoto, watoto wenye ulemavu, wanapata taabu sana wanapojaribu kuchukua fursa za kupata huduma mbalimbali kama vile huduma za afya, elimu na huduma nyinginezo wanazopata watoto wengine. Uelewa mdogo kuhusu ulemavu na fikra potofu za jamii kuhusu ulemavu na watu wenye ulemavu ni miongoni mwa vipingamizi ambavyo vinasababisha kupoteza fursa ya kuleta usawa miongoni mwa watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la ulemavu, kimsingi kuna haki ya msingi ya maisha na hali za watoto wenye ulemavu kuboreshwa hasa kwenye sera za shule na miundombinu na kujenga mazingira rafiki shuleni ambayo hayatakuwa tena na ubaguzi wala unyanyapaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu rafiki shuleni pamoja na majengo na madarasa ni muhimu yajengwe kwa kuzingatia kuweka sehemu maalum za kupita, alama maalum, vyoo maalum na aina nyinginezo za ujenzi unaokidhi mahitaji ya watoto wenye ulemavu wa aina mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria na sera zinazowalenga watoto wenye ulemavu lazima zisambazwe kwa watu wengi ili zifahamike na kufuatwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matengo ya Bajeti na rasilimali zaidi lazima zitengwe kwa ajili ya watoto wenye ulemavu ili kufanikisha utetezi na ulinzi wa haki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nashauri Serikali iongeze uelewa wa jamii kwani wale wenye ulemavu wa mtindio wa ubongo mara nyingi wanaeleweka vibaya na chanzo cha matatizo yao kubahatishwa tu (kwa mfano kudhaniwa kuwa wamerogwa) na hivyo jamii inahitaji elimu ya ufahamu ili kubainisha, kutofautisha na kuelewa aina mbalimbali za ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu kwa watoto wenye ulemavu shuleni; jamii husika na shule ziwajibike kuhakikisha kuwa watoto wote wenye ulemavu wanaandikishwa shuleni na kushiriki katika ngazi zote muhimu za elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na ninaomba maoni haya yaingizwe kwenye mipango ya Wizara ili kidogo kidogo yaanze kufanyiwa kazi na mpaka mwaka 2020 tutakuwa tumepiga hatua kubwa. Mungu awatie nguvu Waheshimiwa Mawaziri wote wawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia suala hili ambalo liko mbele yetu la mwongozo wa maandalizi ya mpango wa bajeti kwa mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa hizi, nataka kushukuru sana na kuipongeza Serikali kwa jinsi ambavyo wamekuwa wakiendesha shughuli za kimaendeleo kiasi kwamba Tanzania sasa hivi, imekuwa ikiendelea kwa kasi na kwa kweli hata takwimu tunazopata kutoka IMF na Mashirika mengine ya Kimataifa, Tanzania tunafanya vizuri sana kiuchumi, hata kwa Afrika Mashariki inasemekana sisi tunakuwa mara nyingi zaidi kuliko hata wanavyokua jirani zetu Kenya, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiongoza katika ukuaji wa uchumi kwa Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa juhudi za kufanya yote haya na vilevile kwa kusimamia mfumuko wa bei na kuweka katika hali ambayo ni nzuri na inayowezesha sasa biashara na uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nampongeza Mheshimiwa Rais Maguafuli kwa juhudi zake anazofanya katika kuhakikisha kuwa mapato yote yanayotakiwa kupatikana yanapatikana na juhudi hizo zinafanywa pamoja na Wizara ya Fedha. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Naibu wake, Katibu Mkuu na watendaji wake kwa jinsi ambavyo wamepanga mpango huu kwa njia ambayo kwa kweli inatoa matumaini na mwelekeo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi niiombe Serikali kuwa kwa jinsi ambavyo tumepanga mipango yetu na jinsi ambavyo tumeweka vipaumbele vyetu, basi tuhakikishe kuwa tunasimamia vipaumbele hivi na tunasimamia utekelezaji wa miradi ambayo tumejiwekea ya kipaumbele ili Taifa letu likue. Tumekuwa kwa muda mrefu tukiona miradi ya kielelezo ikiletwa Bungeni na kuoneshwa katika mipango, tunaomba sasa tuoneshwe inaanza kufanyiwa kazi. Miradi ya Mchuchuma na Liganga, miradi ya maeneo maalum ya uwekezaji, miradi ya kupanua bandari kwa sababu tunajua bila bandari kuwa imara na yenye kuwezesha usafirishaji wa mizigo na kupokea mizigo tutakuwa hatuwezi kuendelea na tutashindwa kupata mapato tunayoyategemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu imebarikiwa kuwa na madini, vito vya thamani sana, vito hivi namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa kuanza kuona jinsi gani ambavyo Tanzania na yenyewe sasa inufaike na vito ambavyo viko nchini kwetu kama Almasi, Tanzanite, Dhahabu na madini mengine ambayo ni muhimu sana katika kutuletea uchumi na kutuletea maendeleo ya haraka. Sasa haya yote yafanyike katika utaratibu ambao umewekwa katika mipango hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kupongeza vilevile Serikali kwa suala zima la bomba la mafuta la kutoka Uganda kuja Tanzania, huu nao ni uwekezaji muhimu kwetu lakini yote tunataka kusema tuhakikishe kuwa tunazingatia masuala yanayohitajika kifedha au kitaalam yafanyike kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna miradi ambayo ingekuwa imeshaanza sasa hivi tungekuwa tuko mbali. Tunasisitiza sana kilimo, kilimo ndiyo uti wa mgongo na kweli ni kilimo ndiyo kitakachotuwezesha kufikia maendeleo tunayoyahitaji kwa sababu kinaajiri watu wengi, kilimo kinasaidia vijijini, kinasaidia nchi nzima kwa chakula, lakini vilevile kwenye viwanda vyetu hatuwezi kwenda bila kilimo.

Kwa hiyo, tunataka kusisitiza suala la kilimo lipewe kipaumbele kama vile ambavyo miundombinu na miradi mingine inapewa kipaumbele, umwagiliaji kwa kutumia maji, tuhakikishe kuwa yale mambo yote muhimu ambayo yanawagusa wananchi moja kwa moja yanafanyiwa kazi na yanapewa kipaumbele. Kwa hiyo, kilimo, mbolea, maji, utaalam, mitaji ni vitu ambavyo lazima vishuke kwa wananchi wengi kwa ujumla vijijini ili tuweze kuhakikisha kuwa na wao wanafaidi hili suala zima la maendeleo ya haraka tunayoyapata hapa Tanzania. Maana maendeleo yako huku juu lakini bado hayajashuka chini kwa kuonesha jinsi ambavyo umaskini unapungua lakini watu wanaendelea kuwa na kipato, wanajiajiri na mwisho wa yote ufanisi unakuwa mkubwa kwa nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la utekelezaji wa sera ya viwanda. Tumekuwa tukizungumza sana kwa sasa hivi tunataka kujikita kwenye uchumi wa viwanda lakini tuna maeneo ambayo yalitengwa, ambayo kama yangetumika vizuri tungekuwa na maendeleo ya haraka zaidi ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia masuala ya maeneo maalum kwa ajili ya uchumi yaani SEZ au Export Processing Zones ambazo zilishatambuliwa na zimeshawekwa nchi nzima, tungehakikisha kuwa tunaanza japo na mbili kila mwaka au moja kila mwaka tuhakikishe kuwa sasa tunaeneza viwanda nchi nzima ili kuwe na uwiano wa maendeleo katika Taifa zima.

Kwa hiyo, ningependa sasa kusisitiza kuwa hilo suala la viwanda tuanze kwa kutumia yale maeneo ambayo tulikuwa tumeshayaweka na kwa kiasi kikubwa sana tutumie sekta binafsi.

Mheshimiwa wenyekiti, tumekuwa tuna tatizo la Deni la Taifa limekuwa likiongezeka sana kwa kipindi cha miaka miwili, mitatu. Linaongezeka kwasababu tunataka kufanya kila kitu sisi wenyewe. Hebu tuangalie uwezekano wa kushirikisha sekta binafsi. Wao wachukue ile miradi ambayo ni mikubwa inayohitaji hela nyingi, vilevile ambayo inataka ufanisi mkubwa kuiendesha basi tuingie ubia na sekta binafsi au tuwaachie wao waiendeleze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia mashirika ambayo hayafanyi kazi vizuri na yanakuwa mzigo kwa Taifa, hebu tuangalie sasa uwezekano wa kuziachia sekta binafsi wayaendeshe yale mashirika ambayo hayafanyi kazi vizuri ili Serikali isiwe na mzigo wa kuendelea kuyalisha na kuyahudumia wakati yenyewe hayarudishi kitu chochote kwa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nizungumzie suala zima la Tanzania sasa hivi tunajulikana kuwa tumepiga hatua kubwa sana na pengine tunaongoza kwenye financial inclusion (matumizi ya mitandao kwa ajili ya miamala ya fedha). Hebu tutumie fursa hiyo sasa kuhakikisha kuwa hiyo teknolojia hiyo inatumika katika kuwasaidia wakulima, wanawake, vijana vijijini kwetu ili na wao sasa waanze kunufaika. Kwa mfano, kupata mitaji, kupata taarifa pamoja na masuala mazima ya miundombinu muhimu ya umeme itakayowekwa katika maeneo yetu ya vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la sekta binafsi kwa kweli naliona kama ni suala ambalo lingetukomboa sana, sijui kwa nini bado Serikali yetu haijapenda sana kutumia PPP katika kuendesha shughuli zake. Jamani tuangalie mifano, tujifunze mifano ya wenzetu nchi nyingine. Ukienda Malaysia sasa hivi kila kitu kinafanywa kwa kutumia PPP, hebu tuanze japo kidogo eneo moja tuanze kusema hapa tuachie private
sector waendeshe na tutaona jinsi ambavyo inatupunguzia mzigo wa madeni, kwa sababu inabidi sasa mitaji itoke kwenye private sector.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kodi napongeza sana masuala ya ukusanyaji wa mapato, lakini bado kuna sehemu kubwa sana ya wananchi ambao wako kwenye sekta isiyo rasmi ambao bado hatuwatambui katika kutozwa kodi. Sasa hivi nimeona katika mpango kuna suala la urasimishaji wa wananchi katika masuala ya ujasiriamali na hivi. Ningependa vilevile kupongeza hilo likafanywe na Halmashauri zetu. TRA sidhani kama wataweza kwa sababu hawawatambui hawa watu, hawajui walipo lakini ikifanywa kwenye Halmashauri zetu wanawajua kabisa vijana gani wanazalisha nini, wako wapi, wafanyabiashara wadogo wako wapi, vikundi gani viko wapi, hiyo itarahisisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kutoa rai Serikali itumie Halmashauri zetu ili kwanza na wao pia wapate mapato lakini vilevile itarahisisha hili zoezi zima la kuwarasimisha watu hawa ambao tunataka kuwaingiza katika mfumo usiokuwa rasmi.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengine yalikuwa ni haya masuala ya bajeti yetu izingatie yale maeneo ambayo yanawagusa wanawake na vijana. Huko nyuma tuliwahi kuzungumzia masuala ya gender gudgeting, sasa sijui yaliishia wapi. Najua nitajibiwa kuwa unavyozungumzia hivi na wenyewe wamo, lakini hili suala bila kutambua moja kwa moja na kuiwekea mikakati na fedha itakuwa vigumu. Tuangalie maeneo ambayo yanawaathiri sana akina mama na vijana au na watoto. Masuala ya vifo vya akina mama wanapojifungua, masuala ya vifo vya watoto wa mwaka mmoja mpaka miaka mitano, yote ni masuala yanayogusa wanawake sasa kama Serikali ikijielekeza kuweka miundombinu inayofaa kwa hospitali, vituo vya afya kwa ajili ya hawa akina mama tutajikuta watoto wetu na akina mama wanapona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ukija kwenye suala la maji, najua Serikali imefanya makubwa sana juu ya maji na bado inaendelea kufanya. Maji ni suala ambalo ni la gender moja kwa moja. Wanaohangaika na maji ni akina mama na watoto wao. Watoto wa shule wanabebeshwa ndoo za maji asubuhi kabla hawajaenda shule hii ni kwasababu hatuna miundombinu mizuri ya maji na maeneo mengine yana maji mengi yanachohitaji ni miundombinu tu. Kwa hiyo, nafikiri Serikali iangalie zaidi suala la gender budgeting siyo kwa sababu ya wanawake per se, lakini kwa sababu ndio kitu sahihi kukifanya na kitaturahisishia maendeleo yetu katika vijiji vyetu.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija kwenye suala la elimu vilevile tuangalie hayo, watoto wa kike wengi pamoja na kuwa wanakwenda shule lakini hawamalizi kwa sababu ya miundombinu isiyofaa, ambayo haizingatii mazingira yao. Tunaiomba Serikali ijielekeze katika mabweni ya watoto wa kike, iangalie kuwa shuleni kuna maji ya kutosha, kuna vyoo vya kutosha kwa ajili ya watoto wa kike na huduma nyingine ambazo watoto wa kike wanazihitaji kwa sababu ya maumbile yao.

Kwa hiyo, hivi ni vitu ambavyo huwezi kuviepuka ukasema haya mambo ya wanawake, hapana! Bila kuyazingatia na kuyaweka kwenye bajeti utajikuta bado kila siku yale maeneo ambayo yanahusu wanawake na watoto yako nyuma.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba niishie hapo kwa rai ambazo nimezitoa kwa Serikali nikiamini watachukua maoni haya na kuyaingiza katika mipango yao ili kila kitu ambacho tumekizungumza hapa kikafanyiwe kazi kama ambavyo mpango ulivyoonesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana na naendelea kupongeza Serikali kwa juhudi zote ambazo inazifanya. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mungu kwa fursa ya kuchangia hotuba hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Viwanda pamoja na Naibu, Makatibu Wakuu na watendaji wa Wizara yake kwa hotuba inayoainisha mipango mizuri inayogusa maeneo yote muhimu yanayoleta maendeleo ya viwanda vidogo, vya kati na vikubwa. Hongera sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kupitia Wizara hii kwa mpango unaozingatia uanzishwaji wa viwanda kwa kuanza na mazingira bora ya kuwekeza kwenye viwanda ambayo ni rasilimali zilizopo nchini kama ardhi, mazao ya kilimo, ufugaji, uvuvi, misitu, mbegu za mafuta, pamba na kadhalika; miundombinu muhimu na wezeshi kama vile barabara, umeme, maji, mawasiliano na rasilimali watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa rai kwa Serikali kupitia Wizara ya Viwanda kuhakikisha kuwa wawekezaji wanaandaliwa sera na sheria zinazokinzana zirekebishwe ili kuepuka migogoro na wananchi na taasisi za Serikali zinazosimamia ukusanyaji mapato. Sheria, sera na taratibu za taasisi zetu zizingatie kuondoa urasimu na kuhakikisha kuwa maamuzi juu ya uwekezaji yanafanywa bila ucheleweshaji wowote na usumbufu kwa wawekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushirikiano kati ya Wizara ya Viwanda na Wizara nyingine wezeshi na uchocheo uchumi uanze tangu mipango inapoanza kuwekeza viwanda. Kwa hiyo ni mategemeo yetu kuwa Mheshimiwa Waziri atatuainishia mfumo uliopo wa mipango kati ya Wizara ya Viwanda na Uwekezaji, Nishati na Madini, Miundombinu, Maji, TAMISEMI, Kazi na Elimu ya Juu na Ufundi ili kila mmoja aonyeshe jinsi gani atachangia katika kukamilisha mipango ya kuendeleza viwanda hivyo na utekelezaji wa mipango hii. Hii itatatua changamoto nyingi zinazotokana na kuwa kila Wizara inajiendesha yenyewe bila kuwa na mawasiliano ya karibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuboresha mazingira ya viwanda vilivyopo kwa kuhakikisha kuwa wanapata huduma muhimu kujiendesha kama vile maji, umeme, miundombinu, masoko, maghala, mawasiliano na mitaji. Hii itakuza pato, kuongeza bidhaa na kuzalisha ajira za kutosha. Hii itasaidia kuwaaminisha wananchi na wageni wanaotaka kuwekeza kwenye viwanda na kuwavutia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru Serikali kupitia Wizara ya Viwanda kwa kuzingatia katika mpango huu wa kuendeleza viwanda kila kanda ya nchi kwa uwiano unaoendana na rasilimali zilizopo na comperative na competitive advantage. Hii itaondoa kuwa maeneo machache ya nchi yanaendelea zaidi wakati mengine yako nyuma ilhali wana fursa nyingi za kuwa na viwanda. Wilaya kama Wilaya yangu ya Ileje na nyingine nyingi zenye kuzalisha nafaka na mazao mengine kwa wingi zipewe kipaumbele tunapopanga kuwekeza viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kutoa rai kwa Serikali kuhakikisha sasa kuwa sambamba na uanzishwaji wa viwanda tuanzishe viwanda vyenye kuzingatia soko la ndani. Serikali ijipange kuzalisha bidhaa zinazofaa kutumiwa nchini ili kukuza soko la ndani na kwa hiyo kuongeza ajira na kuondoa umaskini. Kwa hili tunamuomba Waziri ahakikishe kuwa mipango inazingatia kukuza soko la ndani na soko la Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, tupatiwe mkakati wa kuanza kupunguza uagizaji wa bidhaa ambazo zinazalishwa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwango na vipimo. Bidhaa nyingi ambazo hazikidhi viwango zinaingia nchini na nyingine ni hatarishi, vilevile nguo na bidhaa za nguo zinazozalishwa na kuagizwa nchini au hata bidhaa za vifaa vya ujenzi hazizingatii vipimo sahihi; wanapunja kwa kupunguza sentimeta katika bidhaa. Hii inawadhulumu wananchi, kwa hiyo natoa rai kuwa TBS na WMA wajengewe uwezo wa kupatiwa wafanyakazi wengi zaidi ili waweze kukagua viwanda na bidhaa hizi ili viwango na vipimo vizingatiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu masoko na vituo vya mipakani, Tanzania ina mipaka mingi na majirani zetu ambayo kwa mtazamo chanya ni fursa muhimu ya kuboresha biashara ya mipakani na nchi jirani. Yapo masoko mengi ya mipakani na yapo maeneo kama Ileje ambayo hayajaendelezwa lakini yana uhitaji mkubwa wa kuendelezwa ili wananchi wa maeneo haya ambao wengi wao ni wanawake na vijana wapate kipato na kuinua familia zao na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ileje ina fursa ya kuwa na soko la kimataifa la mazao ya kilimo yaliyosindikwa ya ufugaji, uvuvi na misitu. Ileje inapakana na Malawi na Zambia lakini pia iko karibu na Mji wa mpakani wa Tunduma na hii kibiashara ni fursa kubwa. Ningependa Serikali itufahamishe jinsi ilivyojipanga kuboresha masoko yote ya mipakani kwa kuiwekea miundombinu muhimu na kujenga vituo vya forodha na soko la Kimataifa la Isongole.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu jinsia na maendeleo ya viwanda. Wanawake ni wazalishaji wakubwa wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, pia ni wafanyabiashara wazuri. Tungependa kuishauri Serikali izingatie umuhimu wa kundi hili muhimu kuzingatia maendeleo ya viwanda tangu ngazi ya mipango hadi utekelezaji. Wanawake wanahitaji viwanda vya usindikaji, kufuma masweta na nguo za baridi, nguo kama khanga, vitenge, vikoi na hivi pamoja na viwanda vya kusindika matunda, mboga na mazao ya mifugo, karanga na mafuta ya kula. Ningependa kujua jinsi gani wanawake watazingatiwa katika uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgodi wa Kiwira utafufuliwa lini? Naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa hii ya kuchangia hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango juu ya Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2018/2019 na Mwongozo wa mMaandalizi ya Mpango wa Bajeti kwa mwaka 2018/ 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mungu kwa kibali chake na rehema zake kwa kutuwezesha kukutana ndani ya Bunge lako tukiwa na afya na nguvu ya kufanya kazi. Ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa uteuzi wake alioufanya hivi karibuni kwenye Baraza lile la Mawaziri na niwapongeze wote walioteuliwa na kuzidi kushirikiana vizuri huku nikiwaasa kuwa Hapa ni Kazi Tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Rais Magufuli kipekee kwa kutimiza ahadi kwa Jimbo langu la Ileje, yeye mwenyewe kwa kutujengea barabara kuu ya kutoka Mpemba hadi Isongole kwa kiwango cha lami. Barabara ya kilometa 51.8 ambayo wananchi wa Ileje wameipigia kelele kwa miaka 42 sasa. Tunaishukuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kutimiza ahadi zake kwa Wilaya ya Ileje. Naishukuru Serikali kwa kutujengea Hospitali kubwa ya Wilaya Itumba ambayo itafanya upasuaji mkubwa. Tunaiomba Serikali itusaidie kumalizia hospitali hii ambayo imesimama kwa zaidi ya miaka miwili sasa. Hospitali hii inategemewa na itasaidia hata Wilaya ya jirani za Mkoa wa Songwe na Mbeya Vijijini ili imaliziwe na itazuia wananchi wa Ileje kukimbilia nchi jirani ya Malawi kupata huduma za afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kusaidia kuweka miundimbinu mizuri ya maji hasa maeneo ya Isongole, Itumba, Izuba Ilulu ambapo kumekuwa na ukame wakati wa kiangazi na kusababisha upungufu mkubwa wa maji wakati Mto Songwe uko hapo jirani kabisa. Hii imerudisha imani ya wananchi kwa Serikali kwa kiasi kikubwa sana na kuinua ari yao. Tunahamasisha Serikali kuhamasisha mipango yote ya maji kama ilivyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TRA walikuwa na mpango wa kujenga kituo kidogo cha forodha kwenye mpaka wa Tanzania na Malawi kwenye Mto Songwe. Eneo limeshapimwa na TRA wamejenga ofisi ndogo ya forodha lakini bado haitoshelezi. Mpaka wa Tanzania hauna ofisi ya Uhamiaji, Polisi, Kilimo, Jeshi la Wananchi na Idara nyingine muhimu za Kituo cha Forodha Mpakani. Tunaiomba Wizara itusaidie kituo hiki kijengwe kwa kwa sababu kinapunguza msongamano wa Tunduma, kwa njia ya Ileje inapendelewa na wenye magari makubwa kwa sababu hupitia Chitipa upande wa Malawi kutokea Isongole Ileje kuja Mpemba ni tambarare zaidi kuliko ile ya Kasumulo Kyela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia itawezesha kudhibiti mpaka huu ambao umekuwa na matukio ya wakimbizi wa Kisomalia na wengine kuutumia. Kwa hali hiyo huwezi jua athari gani nyingine zinaweza kutokea bila kuwa na kituo cha forodha sehemu muhimu hiyo ya mpaka. Aidha, hicho kituo kitasidia sana pindi mradi wa Bonde la Mto Songwe kati ya Malawi na Tanzania utakapoanza. Vyote hivi vitachangia kwa kiasi kikubwa kuchangamsha uchumi wa Ileje na Wilaya za jirani ambazo kwa muda mrefu zimedumaa kwa kukosa miundombinu ya kisasa na taasisi muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kumekuwa na mwelekeo Wizara ya Mambo ya Ndani wana mpango wa kujenga Chuo cha Uhamiaji cha Ulende katika Wilaya ya Ileje na eneo tayari limeainishwa, hii pia ingesaidia sana kujenga uwezo wa Maafisa Uhamiaji wa Tanzania lakini hata wale wa nchi za SADC na hii itasaidia kuinua uchumi wa Jeshi la Tanzania kwa ujumla. Hii ni miradi ya kitaifa naomba Serikali iangalie jinsi ya kutusaidia kwa kuingiza mipango yake ya kipindi hiki ili Ileje nayo ipate maendeleo ya haraka zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ileje ni kati ya Wilaya inayozalisha mazao ya kilimo kwa wingi sana hususani mahindi, ulezi alizeti, mpunga, kahawa, pareto, hiliki, tangawizi, ndizi, viazi mviringo, viazi vitamu, soya, maharagwe, karanga, matunda ya aina mbalimbali pamoja na mazao ya misitu ikiwa ni pamoja na mbao, nyuki na kadhalika. Zaidi ya hayo Ileje ina uwezo wa kuzalisha maziwa kwa wingi, mifugo midogo midogo, viungo na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na haya yote Ileje inakabiliwa na tatizo kubwa la upungufu wa maghala, masoko, Maafisa Ugani na kwa kiasi kikubwa mitaji kwa sababu maeneo yote ya Ileje hayajapimwa na tumehusisha upungufu wa wataalam wa kupima maeneo haya. Tunaomba Serikali iweke bajeti na nguvu ya ziada na ya upendeleo kwa maeneo ya pembezoni hasa Ileje na hasa kwa sababu tumejaliwa kuwa na hali ya hewa nzuri sana, udongo mzuri, mvua nyingi na za kutosha ni rahisi kwa kilimo na ufugaji huwainua na kupanua uzalishaji sana kwa mazao yote hayo na huwaondolea wananchi kwenye umaskini na ukosefu wa ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijikite katika mpango na nianze kwa kuwapongeza sana Serikali kwa kuwashirikisha wadau katika mchakato mzima wa kutayarisha mpango na mwongozo huu, ni jambo la kupongezwa kwa sababu limekuwa shirikishi zaidi. Lakini tunaiomba Serikali iyazingatie maoni haya na kuyazingatia katika Mpango ili uwe na tija zaidi. Maoni mengi ya wadau yanaonesha uzoefu wao kwenye soko na utekelezaji ambao umezidi ule ambao watumishi wa Serikali ambao wana ofisi tu au ni wa wananchi wanaotumiwa na masuala mbalimbali kwa hiyo, siyo ya kupuuzwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali imepokea na kuorodhesha maeneo waliyopata ushauri ninaomba Serikali itupatie masharti ya jinsi wanapanga utekelezaji na fedha itakayotumia, maoni yote yaliyo ukurasa wa tano wa Mpango huu wa 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti,ni kweli uchumi wetu umekua vizuri kwa muda mrefu lakini bado kwa kiasi kikubwa tuna utegemezi mkubwa kwa wafadhili wa fedha za nje ambazo haziji zote kwa wakati. Tupate sasa wakati wa kupunguza zaidi utegemezi huu na vilevile kutumia sekta binafsi zaidi kutengeneza miradi ili kupunguza utegemezi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mfumuko wa bei kuendelea kuwa mdogo tumeona kuwa umepanda kidogo kutokana na bei za chakula kupanda na bei zinapanda kwa sababu utaratibu wa soko la mazao nchini haujawa vizuri kitu kinchosababisha wakulima kukosa mapato stahiki na wateja pia wanaathirika na kuwapa faida kubwa walanguzi. Lakini kama haitoshi zao la mahindi limekuwa yatima nchini, liliachiwa na wakulima kuhangaika wenyewe wazalishe mazao mengine kama korosho, pamba na kadhalika kunachangiwa kwa kupatiwa pembejeo, madawa na kadhalika.

Je, ni kwa nini Serikali inaacha mazao haya yanayolisha nchi nzima na kuwawezesha wananchi kunufaika kwa biashara ya mazao yao? Serikali ije na mustakabali wa kuwasaidia wakulima wa mazao ya nafaka na jamii za kunde na ya mbegu za mafuta ili ziwe na tija na yachangie Pato la Taifa na kuwaodolea umaskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Deni la Taifa kuonesha liko himilivu, lakini tukiendelea hivi litatupeleka pabaya hususani kama hatutaongeza mauzo ya kuuzwa nje (exports) ili yabadilishe balance of trade yetu Tanzania. Nchi nyingi zenye deni kubwa vilevile ni nchi za viwanda zenye uchumi mkubwa, kwa hiyo malipo ya madeni hayo hayaathiri sana uendeshwaji wa uchumi. Lakini kwa Tanzania deni lilikua sana dhidi ya ukuaji wa uchumi kwa maana Pato la Taifa tutafikia hatari. Tujitahidi kuboresha na kuinua viwanda, kuanzisha viwanda vingi, huongeza masharti ya uwekezaji, kupunguza viwango vya kodi ili tupate ufanisi na mwisho wa madeni yote ya ndani na ya nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zinaonesha kuwa pato la ndani halitoshi hutokana na ukusanyaji mdogo wa mapato ya ndani, uzembe na hata rushwa. Vilevile sekta isiyo rasmi imesahauliwa katika suala nzima la makusanyo ya kodi. Sekta hii ni kubwa na ina wajasiriamali wa aina mbalimbali wadogo, wa kati na wanazalisha bidhaa na huduma za kutosha na kulipa kodi nyingi. Serikali ina mpango wa kurasimisha shughuli hizi, hili ni jambo la msingi na kwa hakika zimechelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali sasa hivi iweke utaratibu mzuri na ishirikishe. Aidha, Serikali ishirikishe taasisi zake zinasimamia vizuri sekta hii na kuwapatia huduma zao za kifedha na mafunzo ya kuwawezesha kuinua shughuli zao. Hii iendane na kuwapatia maeneo ya kufanyia shughuli zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza sana Serikali kwa kuanza kutengeneza miradi ya maendeleo kwa mwaka 2016/2017 pamoja na kugharamia ujenzi wa awamu ya kwanza wa reli ya kati kwa standard gauge kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro, pamoja na miradi mingine, miradi hii mikubwa itakayoleta mageuzi makubwa ya kiuchumi, Serikali ianze kutayarisha watumishi wa kuhudumia reli hii mapema kwa kuwapa mafunzo stahiki ili imalizike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya msingi inayopanuliwa iendane na ujenzi wa madarasa ya kutosha, vyuo vya kutosha, maji na vyumba vya walimu na maabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya viwanda ni muhimu sana na tuipongeze Serikali kwa kuwezesha viwanda hivi kuanza uzalishaji na kudumisha mahusiano mazuri nao. Tunaomba mvisaidie hivi viwanda kupata umeme wa gesi wa uhakika na kuhakikisha hawapati ushindani usio wa haki na bidhaa kwa mfano, mali zinazoingizwa na Good One wa China amekuwa yeye mwenyewe akiagiza na kuuza jumla na rejareja lakini huwahujumu wateja wake hao hao kwa yeye kuweka bei ndogo kwenye bidhaa zake na kufanya kushindwa kuuza. Huu ni mchezo mchafu, TFC walifuatilie hili kwa bidhaa zote zinazoingizwa na ambazo zina sababisha bidhaa za viwanda visishindwe kuuza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali itenge pesa za kujenga vituo vya afya Wilayani, aidha, zahanati nyingi zilizojengwa kwa nguvu za wananchi sasa zimaliziwe kwa awamu hadi na kuweka vifaa na watumishi wa kutosha zimalizike zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapongeza juhudi za kuboresha huduma ya maji nchini. Tunaishauri Serikali itoe kipaumbele kwenye uvunaji maji ya mvua katika maeneo yenye tatizo la umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania bado tunalalamikiwa kwa urasimu mkubwa katika kuhudumia wawekezaji na bado tunachukua muda mrefu, hutoa maamuzi na tunakuwa waoga kuamua. Hii inapunguza kasi ya kufanya biashara Tanzania.Jina la Tanzania sio zuri nje ya nchi, mwisho Serikali inatuhumiwa kuwa haizingatii mikataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali kwa kuboresha huduma za afya katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, lakini kuna haja ya kuhalalisha kuwa hospitali zote za Wilaya, Kata, Mitaa zinapata huduma muhimu za kutosha na vifaa na watumishi ambao wanahitajika sana kwenye maeneo yetu nchi nzima. Pesa ya kutosha hupewa kwa ajili ya huduma za afya nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti,kwa kuhitimisha nataka kuiomba Serikali itufanyie kuboresha maendeleo ya kilimo cha kisasa, miundombinu ya vijiji na mitaa. Wakati huo huo Serikali itoe kipaumbele katika kupima maeneo ya vijijini ili kurasimisha ardhi na kuwawezesha wazalishaji kukopa. Kilimo hakionekani kuwa kweli ni uti wa mgongo na kilete tija kubwa kwa ajili ya viwanda, ajira na mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serika ije Bungeni na mkakati wa kuanza kutekeleza miradi ya kielelezo na maeneo yale ya SEZ na EPZ ambayo yamekaa muda mrefu ilhali ni miradi muhimu kwa kuviwezesha kuanza viwanda kwa uhakika zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho tunaiomba Serikali itafakari kwa kina na kuzingatia maoni ya Wabunge kwenye Mpango wa 2018/2019.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuongea. Nianze kwanza kwa kuunga mkono hoja asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kumpongeza Waziri wa Fedha, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Makatibu Wakuu wote kwa bajeti nzuri ambayo inaelekea sana katika mfumo mzima wa kuboresha viwanda katika nchi yetu. Napenda vilevile kumpongeza Rais wetu wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, kwa hatua na ujasiri aliouchukua kusimamia rasilimali za nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha kuwa watu walewale ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakipigia kelele suala hili mara wamegeuka sasa wanaona kuwa ni vibaya lakini tuyaache hayo, wale wenye macho wameona, wenye masikio wanasikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitishiwa hapa kama ambavyo Viongozi wa Afrika huwa wanatishiwa wanapojitokeza kupigania rasilimali za nchi zao kuwa, watashitakiwa, hii ni mikataba mikubwa sana, haya ni Mataifa makubwa sana, hamuwezi kuwachezea hawa, wanaweza wakawafanya hivi, wakawafanya vile!

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake tumeona, huyo Rais wa Barrick Gold badala ya kutushtaki kaja mwenyewe, nginja-nginja na ndege yake mwenyewe kaja hapa anasema tuongee na hatujaambiwa, tumemsikia kwenye youtube anaongea! Tuongee tuangalie tunachotakiwa kuwalipa tuwalipe, sasa kiko wapi cha kushtakiana? Hatuwezi kuwa tunaishi kwa uwoga wakati rasilimali ni zetu wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais Magufuli endelea baba, sisi wananchi wako tuko nyuma yako, tunakuamini na tunajua unalolifanya ni kwa ajili yetu sio kwa ajili ya binafsi yako na familia yako. Endelea kutetea maslahi hayo kwa sababu huu ndio wakati muafaka, hukuwekwa pale kwa bahati mbaya, Mungu kakuweka hapo akijua makusudi gani anayo juu yako wewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wanaosema tunaendela kuibiwa, sijui kama wametambua kuwa katika yale mapendekezo ya Kamati ya Profesa Osoro kuna suala la kuzuia sasa madini yasisafirishwe nje moja kwa moja. Zinaenda kutengenezwa clearing houses na kila yanapoondolewa madini yatafanyiwa ukaguzi na asilimia moja itatozwa palepale kwa ajili ya ukaguzi huo kwa thamani ya madini yanayotoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachotaka kuiomba Serikali ni kuwa mfanye haraka hizo clearing houses ziwekwe na tayari hili zoezi lianze kusudi madini yasiendelee kutoka. Siamini hawa jamaa wana ujasiri wa kuendelea kutuibia harakaharaka baada ya kuona eti kuwa sisi tunawadhibiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nirudi sasa kwenye masuala mazima ya hotuba yetu. Miradi ya kimkakati ni miradi ambayo imekuwa ikizungumzwa kwa miaka mingi sana. Hebu sasa Serikali amueni jambo moja, malizeni zile taratibu zote zilizobakia ambazo ni chache sana za mikataba ya uwekezaji, za maeneo ya uwekezaji, taratibu za ulipaji wa fidia, ili sasa hii miradi ya kimkakati ianze kufanya kazi kwa sababu moja kubwa, miradi hii ikianza kufanya kazi suala zima la uchumi wa viwanda litakuwa dhahiri zaidi, maana hivi ndio viwanda mama vitakavyozalisha input za kuingia katika viwanda vyetu tunavyovitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme tayari tunao wa kutosha, miundombinu ya barabara imeshatengenezwa ya kutosha, reli imeshaanza, tunachongojea sasa ni hii miradi mingine ya kimkakati ambayo sasa itashirikiana katika kuhakikisha kuwa viwanda vyetu vinawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la maeneo maalum ya kiuchumi. Serikali ilituanishia maeneo maalum ya kiuchumi karibu nchi nzima, ilikuwa ni jambo jema sana, yenyewe pia yamesimama kwa muda mrefu. Hebu Serikali waje sasa na bajeti hata kama watakwenda kukopa, wamalize masuala ya fidia na miundombinu muhimu katika maeneo haya, halafu wayatangaze kwa sekta binafsi ya ndani na ya nje waje wawekeze ili wananchi kwanza wapate ajira lakini vilevile wapate mapato na nchi yetu iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna suala la PPP, najua kuwa PPP labda ni dhana ambayo haijatambulika vizuri au haieleweki vizuri kwetu. Hebu tutafute jinsi ya kuboresha uelewa wetu wa PPP tupate mafunzo Serikalini na sisi Wabunge vilevile tupate mafunzo ya kutosha, tujue jinsi gani ya kushauriana na hawa wawekezaji wanaokuja kuingia mikataba hiyo na sisi ili tupate mikataba ambayo itatunufaisha sisi wote. Kwa hiyo naomba PPP isitupwe pembeni tu kwa sababu hatuifahamu vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna suala zima la ukusanyaji wa mapato hasa kwenye Halmashauri. Tunashukuru sana Serikali kwa hatua ambazo wameziainisha ambazo wanaenda kupunguza tozo mbalimbali. Vilevile tunaomba sana kwa yale maeneo ambayo wamepunguzia Halmashauri uwezo wa kukusanya wenyewe, hebu watuhakikishie watakuwa wanaturudishia hizo fedha kwa muda mfupi kiasi gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wanavyofahamu hata sasa hivi Halmashauri zetu nyingi zinajiendesha kwa shida sana kwa sababu vyanzo vingi vilikuwa vimechukuliwa na Serikali Kuu. Wafanye hima watakapokusanya tu waturudishie, kama vile ambavyo kila mwezi wanatangaza wamekusanya kiasi gani basi mwezi huo huo watuambie na Halmashauri wanapeleka kiasi gani. Mambo yote sasa hivi ni kielektroniki, sioni kama kutakuwa kuna ugumu katika kurudisha hizo fedha kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni juu ya kupunguza kwa tozo, crop cess. Nafikiri katika Kamati ya Bajeti tulipendekeza kuwa kusema kuwa wanapunguza tozo peke yake na kuainisha kuwa mazao yawe ni chakula na mazao yawe ni biashara inaweza ikaleta mkanganyiko na vilevile ikatumika vibaya. Waweke tozo moja na kwa vyote ili ijulikane kuwa whether inatumika kwa chakula whether inatumika kwa biashara tozo ni hiyo moja. Wasitoe mwanya kwa watu kuanza kucheza na hiyo dhana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la ufuatiliaji wa mapato na tathmini zake. Tumekuwa mara nyingi tukikadiria mapato tutapata kiasi gani kwa vyanzo mbalimbali, lakini je tunafanya tathmini labda ya miaka miwili, mitatu kuona kuwa pamoja na kuwa tulikuwa tumeweka maoteo fulani tumekuwa tumefikia kiwango hiki tu, ili itusaidie tunapopanga tupange kwa uhakika zaidi kwa uhalisia zaidi tusipange kwa vitu ambavyo pengine hatutaweza kufikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia masuala ya elimu ya walipakodi na hasa kwenye masuala ya sekta isiyokuwa rasmi. Sekta isiyokuwa rasmi ni kubwa na itaendelea kukua na itaendelea kuwepo. Ni muhimu sasa kuhakikisha kuwa pamoja na hili suala la kuanza kuwaorodhesha au kuwa-register basi tuanze kutoa na elimu ya kulipa kodi, tuanze kuwaelekeza kodi zitakuwa za namna gani, watazilipa kwa mfumo upi, watazilipia sehemu zipi. Maana kodi zilizopo ni nyingi na zina sehemu nyingi mbalimbali za kwenda kulipia. Huu kwanza ni usumbufu lakini vilevile inaleta hali ya mkanganyiko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana watakapokuwa wakitoa elimu ya kulipa kodi wahakikishe kuwa wajasiriamali hasa wadogowadogo wanatambua kwanza wajibu wao wa kulipa kodi lakini kuwa watalipa kodi za aina gani wapi na kwa mtindo upi. Hii inatuhakikishia kuwa watu wengi watalipa kodi wakijua kuwa ni wajibu wao na siyo za usumbufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata kwa walipa kodi wa kawaida kwa wengine bado elimu hii haijaenea ndio maana bado kuna resistance, lakini nafikiri kwa kuongeza juhudi za TRA za kutoa elimu badala ya kujikita kwenye redio na kwenye TV peke yake itasaidia zaidi. Ningependa vilevile, kupendekeza hata mashuleni sasa suala la elimu ya kulipa kodi lianze kuwekwa ili watoto wakue wakiamini kuwa kulipa kodi ni sehemu ya kuchangia maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia sana kuzungumzia suala la Ileje. Ileje ni Wilaya au hata Mkoa nzima wa Songwe ni mkoa ambao unazalisha sana mazao mbalimbali ya biashara na ya chakula. Mungu ametujalia kuwa na hali ya hewa nzuri sana, lakini hatuna masoko ya uhakika kwa mfano kahawa. Kahawa yetu lazima ipelekwe ikaweke kwenye mnada wa Kilimanjaro. Hiyo inatuletea…….

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi ya kuchangia hoja ya Wizara ya Elimu, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Profesa Ndalichako, Naibu Waziri Mheshimiwa Ole Nasha, Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu na watendaji wote kwa hotuba nzuri, na vilevile kwa kazi kubwa wanayoifanya kuhakikisha elimu inaendeshwa vizuri nchini kwetu katika kukuza rasilimali watu ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kupongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge la Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa taarifa nzuri iliyojaa uchambuzi na mapendekezo mazuri na ya kimkakati ambayo yakizingatiwa yote kwa ujumla wake yanaweza kuboresha kwa kiasi kikubwa sana sekta hii ya elimu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, napenda nijikite kwenye suala la VETA. VETA ni taasisi ya Serikali iliyoanzishwa kwa ajili ya kutoa elimu na mafunzo ya ufundi stadi, hizi zikiwa ni stadi za kazi kwa ajili ya kuandaa vijana na jamii kwa ujumla waweze kujiingiza katika shughuli zenye kuwapatia kipato cha kujikimu kimaisha na pia kuchangia katika pato la Taifa. Taasisi hii ya VETA inafanya kazi kubwa ya kuwapa vijana wetu stadi za kazi, lakini pia inatoa nguvu kazi kwa ajili ya viwanda. VETA pia ndio mojawapo ya mihimili ya kufanikisha mkakati wa Serikali kuanzisha viwanda. Bila nguvu kazi yenye stadi zinazohitajika na viwanda hatutaweza kufanikisha mkakati huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili, kulingana na sheria iliyoanzisha VETA ya mwaka 1994, VETA ni taasisi ambayo inaendeshwa kwa michango inayotolewa na waajiri kwa njia ya Skills Development Levy(SDL) ambapo waajiri wanakatwa asilimia 4.5 ya fungu la mishahara (wage bill) kila mwezi. Hata hivyo VETA inapata theluthi moja tu ya makato hayo, theluthi mbili zinabaki Serikalini. Sehemu kubwa ya waajiri wanatamani VETA ipate 100% ya makato yote yaani 4.5% inayokatwa ili soko la ajira lipate mafundi mahiri walioiva vizuri na mafunzo toka VETA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi inatakiwa iwajibike kwa waajiri ambao ndio wana gharamia uendeshaji wa taasisi hiyo. Hawa waajiri wako chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Watu Wenye Mahitaji Maalum. VETA ipo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Kimsingi VETA inatakiwa iwajibike kwa waajiri kwa njia mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kuhakikisha waajiri kuwa mafunzo yanayotolewa na VETA yanaendana na mahitaji ya waajiri na kuwa mitaala ya VETA inayotumika kufundishia inabadilishwa mara kwa mara kulingana na mahitaji ya waajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili kuhakikisha matumizi ya fedha za SDL (1/3 SDL) ambayo ni michango ya waajiri kuendeshea VETA inatumika kama ilivyokusudiwa. Pia waajiri wakipendezwa na matumizi ya michango yao wanaweza kutafuta njia nyingine za ziada za kuisaidia VETA ili ikidhi matarajio yao waajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo huu uliopo sasa ambao waajiri na VETA wapo kwenye Wizara mbili tofauti, VETA haitaweza kuwajibika kwa waajiri moja kwa moja. Hivyo uhusiano wa VETA na waajiri wanaoigharamia ni dhaifu. Hii inaweza kufanya waajiri kukosa imani na utendaji wa VETA maana hawana mamlaka juu ya utendaji wao. Waziri wa Elimu hana nguvu ya kisheria ya kuitisha kikao cha waajiri kuzungumzia masuala ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi zinazohitajika katika soko la ajira, kwa sababu hawa waajiri wako chini ya Wizara nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Waziri anayehusika na kazi hana nguvu ya kisheria ya kuiagiza mamlaka inayosimamia mafunzo ya ufundi stadi yaani VETA kurekebisha mitaala yao kutegemea mabadiliko katika soko la ajira maana VETA iko chini Wizara nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi kwa sasa inahusisha waajiri (wenye viwanda) kutoa mafunzo wakishirikiana na kupokezana na vyuo vya ufundi stadi (Dual Apprenticeship Training). Utaratibu huu unahitaji ushirikiano wa karibu sana kati ya waajiri (viwanda) na vyuo vya ufundi stadi. Hali ya namna hii inahitaji miongozo ya Wizara mama. Tunapokuwa na Wizara mbili tofauti ni vigumu sana kutengeneza miongozo hiyo kwa sababu tofauti za majukumu ya Wizara husika na hata usimamizi wake unakuwa mgumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri VETA iwekwe chini ya Wizara moja na waajiri yaani Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Watu Wenye Mahitaji Maalum. Hii italeta mahusiano mazuri kiutendaji na italeta ufanisi kiutendaji kwenye kipindi hiki muhimu cha kuandalia mafundi stadi kwa ajili ya ustawi wa viwanda vyetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande mwingine Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ina vitengo vingi sana. Wizara inashughulikia Elimu ya Juu, Elimu ya Vyuo vya Kati, Elimu ya Sekondari, Elimu ya Msingi, Elimu ya Awali, Elimu ya Watu Wazima, Elimu ya Ufundi, Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi, Taasisi ya Mitaala TIE, Baraza la Mitihani, TCU, NACTE, VETA, TEA, Maktaba ya Taifa, Bodi ya Mikopo na taasisi nyingine. Pia changamoto zilizopo katika Wizara hii ni nyingi sana na ni vigumu kuweza kupata muda wa kusimamia kikamilifu elimu na mafunzo ya ufundi stadi ambayo ina mtizamo tofauti na idara nyingine za elimu. Pia kuna hatari ya kuifananisha elimu ya ufundi stadi na elimu ya msingi au sekondari ambapo sehemu kubwa ya elimu ya ufundi stadi ni vitendo kuliko nadharia tofauti na elimu ya sekondari na msingi. Upana na utawala wa Waziri wa Elimu (span of control) ni pana sana jambo ambalo linaweza kuathiri ufanisi katika utendaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko nchi nyingi duniani ambazo sekta ya ufundi stadi ipo chini ya Wizara ya Kazi mfano, Korea Kusini, Indonesia, Singapore, Malaysia na kadhalika. Nashauri Serikali irejeshe VETA iwe chini ya Wizara ya Kazi kama ilivyokuwa zamani na hasa kipindi hiki tunapojenga uchumi wa viwanda ili VETA iweze kuwa na ushirikiano wa karibu na waajiri kwa nia ya kutoa stadi zinazohitajika kwenye soko la ajira yaani demand driven trainingAINING” katika kujenga uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Wizara imeonesha kwenye ukurasa 26 na 27 umezungumzia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA). Wilaya ya Ileje kupitia Mbunge tulipata ufadhili wa Balozi wa Japan na kujenga majengo ya VETA na kutokana na uwezo mdogo
wa Wilaya tuliwasiliana na Wizara yako na kuomba Serikali iichukue hii VETA na kuiendesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishauriwa tuongeze eneo, na kupima eneo la VETA ndipo Wizara kupitia VETA Makao Makuu wataichukua na kuiendesha. Yote haya yamefanyika na kwa barua ya Halmashauri ya Ileje ya tarehe 05 -11-2017 kuainisha kuwa tayari masharti yote yamekamilishwa na sasa tunaomba Serikali ichukue VETA Wilaya kuiendesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika kuona kuwa katika hotuba ya Waziri hakuna popote VETA ya Wilaya ya Ileje kuainishwa ili hali ni ahadi na maagizo ya Wizara yenyewe, VETA hii imesimama kwa miaka mitatu sasa hata mfadhili yaani Balozi wa Japan amesikitika sana na ameshindwa kuendelea kusaidia hadi VETA izinduliwe na ianze kazi. Kwa hiyo, ninaomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atueleze wana Ileje hii VETA yetu wataichukua lini? Kwa hiyo, nguvu za Mbunge na mfadhili ziende bure?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kutoa pendekezo kuwa Wizara ioneshe jinsi mitaala ya elimu ya ufundi stadi inaendana na mkakati wa Serikali ya uchumi na viwanda. Vilevile mitaala ya ufundi stadi iboreshwe na kuwekewa madaraja ya standard seven, form four, form six na wa diploma kwa maana ya kuzi-upgrade VETA nyingine into polytechnics ambazo zinatumia ujuzi juu na teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Wizara sana kwa kutupatia fedha za kukarabati shule za msingi kongwe tatu. Kati ya shule kongwe za msingi 14 za Wilaya ya Ileje, shule zilizosalia nazo ni kongwe, na miundombinu yake ya mwanzo na ni za ujenzi wa kutumia udongo. Kwa hiyo, ni hatarishi kwa wanafunzi maana zimeharibika sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ileje haina maktaba ya Wilaya tofauti na Wilaya nyingine, hili ni tatizo. Kuweka maktaba kungesaidia hata watu wengine kupenda kujisomea zaidi ya wanafunzi na watu wazima, lakini vilevile kwa wanafunzi na raia wanaohitaji kujiendeleza kimasomo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumejitokeza mtindo wa kugeuza vyuo vya kati kuwa vyuo vikuu, hii ni hatari. Vyuo vya kati viendelezwe kuwa vyuo bora kwa kutumia teknolojia sahihi na uhitaji wa viwanda na viweze kuzalisha watoa huduma katika viwanda vidogo na kwa viwanda vikubwa. Kwa mfano Singapore wameboresha vyuo vya kati, vinachangia ajira kwa asilimia 95 kwa kuimarisha mitaala ya kiteknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwangukia Mheshimiwa Waziri anisaidie nipate shule ya sekondari ya wasichana Ileje tena yenye mrengo wa sayansi, hisabati na teknolojia na lugha za kigeni. Tunajitahidi kujiandaa kama Wilaya kuanza shule hiyo, lakini Wilaya yetu ni maskini mno, ila wananchi wamejitolea maeneo mawili hata ya Ibada na Mlaly ya ekari 22 kila moja kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari za wasichana kidato cha kwanza hadi cha nne. Naomba sana Mheshimiwa Waziri anipe jibu la kututia moyo Ileje hususan kwa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ileje ina changamoto nyingi. Kubwa ni upungufu wa walimu 201 wa elimu ya msingi na wa shule ya sekondari hasa wa sayansi takibrani 50; na zaidi Idara ya Elimu Msingi haina gari tangu mwaka 2010. Shule za A-Level ni mbili tu Wilaya nzima. Tunahitaji kuongezewa shule nyingine mbili. Miundombinu ya shule zetu zote ni mibovu, haina vyoo, ofisi za walimu, nyumba za walimu, mabweni na madarasa. Tunaomba sana sisi wa Wilaya za pembezoni tuangaliwe kwa jicho la huruma, tumesahauliwa kwa muda mrefu. Tunaomba utusaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mungu kwa kutujalia uzima na afya ya kuweza kuhudhuria Bunge letu. Namshukuru Mungu kwa kutupa Rais mwadilifu mwenye mapenzi mema na wananchi wake na Makamu wa Rais na Waziri Mkuu na Baraza la Mawaziri wachapa kazi. Nampongeza Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo na Manaibu wake, Mheshimiwa Kakunda na Mheshimiwa Kandege. Binafsi natoa shukrani za pekee na za unyenyekevu kwa Rais na Baraza zima la Mawaziri kwa jinsi walivyotekeleza miradi ya maendeleo mikubwa Ileje ambayo ilisahauliwa miaka mingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TAMISEMI. Shukrani kwa Mungu. Pongezi kwa Serikali ya Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na Baraza lote la Mawaziri kwa mipango ya maendeleo mikubwa inayotekelezwa kwa ufanisi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Pongezi kwa ajili ya Ileje. Kwa heshima ya kipekee na kwa niaba ya Wanaileje napenda kuishukuru Serikali kwa mambo makubwa iliyofanya kuleta maendeleo Ileje. Napenda kupiga magoti kutoa shukrani za dhati kwa kuiwezesha Ileje kuinuka, kujulikana na kutambulika. Ileje sasa hivi inaonekana, barabara iliyopigiwa kelele kwa zaidi ya miaka 40 imepata mkandarasi yuko site na barabara itajengwa kwa kiwango cha lami kilometa 58, inategemewa kumalizika 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata fedha ya kujenga vituo vya afya viwili, Kituo cha Lubanda ambacho Mheshimiwa Waziri wa Afya mwezi uliopita alitembelea na Kituo cha Ibaba. Hii itatusaidia sana kupunguza athari zilizokuwa zinawapata wananchi kwa sababu ya jiografia na miundombinu na Ileje hizi ni kata ambazo hazifikiki kwa urahisi na ziko mbali sana na hospitali ya wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata fedha ya kujenga hospitali ya wilaya na inajengwa kwa kiwango cha asilimia 75, imesimama kwa miaka mitatu, lakini nashukuru kuwa nina taarifa kuwa, tumetengewa fedha ya kumaliza ujenzi wa hospitali hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ileje ilipokea fedha kwa ajili ya kukarabati shule kongwe na miradi mikubwa ya maji na masuala ya upimaji viwanja Ngulilo, Ilulu, Izuba. Kupitia Ofisi ya Mbunge nilitafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa VETA kutoka Balozi wa Japan. Chuo kimejengwa na nashukuru kuwa, Serikali imekubali kukichukua chuo hicho na kukimalizia na kukiendesha.

Tunaishukuru Serikali kwa jinsi ambavyo kwa mwaka mmoja uliopita hadi sasa tumetembelewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyeweka jiwe la msingi na Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Waziri kwa nyakati mbalimbali. Naamini huu ni ugeni mkubwa sana uliowahi kutokea katika historia ya Ileje. Hii, ilitutia moyo sana, lakini iliwawezesha Waheshimiwa viongozi hawa kujionea wenyewe changamoto na fursa za Ileje na kwa hivyo, kujua jinsi gani Ileje isaidiwe. Tunawaomba Mawaziri wengine wote watembelee maeneo yote ya pembezoni ili kujionea changamoto zao na kuzitatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi zote hizo nyingi na shukurani za unyenyekevu kwa miradi mikubwa ya maendeleo, yapo mambo machache ninayotaka kuiomba Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi. Tutashukuru kama fedha iliyotengwa kwa hospitali ya wilaya itatolewa mara moja ili huduma hii muhimu ya afya wilayani iimarike na tuache kupeleka wagonjwa Malawi maana Mbeya ni mbali sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ileje ni Wilaya ya mpakani mwa Tanzania na Malawi na kwa sehemu ndogo Mashariki Kusini na Zambia. Mpaka wenye umbali wa kilometa 108. Kwa hiyo, ni mpaka mrefu na wilaya yetu haina kituo cha mpakani madhubuti na mpaka wetu ni Mto Songwe. Kwa hiyo, tunaomba uhitaji mkubwa na wa haraka wa gari la doria kwa ajili ya kudhibiti mpaka wetu. Wahamiaji haramu wengi wanapitia Ileje kuingia Malawi kuelekea Afrika Kusini na imefikia hadi upande wa Malawi kuanzisha Kituo cha Wakimbizi kwa ajili hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu mwaka 2015, TRA walionesha haja ya kujenga kituo cha mpakani na tayari wameshapata eneo la kutosha Isongole, karibu kabisa na mpaka. Umuhimu wa mpaka huu ni mkubwa na hasa ikizingatiwa suala la usalama, lakini pia, kiuchumi na biashara za mipakani. Kwa kuwa, Barabara ya Mpemba – Isongole inajengwa itaunganisha Tanzania na nchi jirani ya Malawi na kituo hiki kitapunguza msongamano wa Kituo cha Tunduma na kuwezesha magari ya mizigo na abiria mengine kupitia upande wa Ileje hasa kwa yale yanayotokea Malawi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa zilizopo ni kuwa barabara ya Chilipa kutokea Ileje ni tambarare zaidi kulinganisha na ya Kasumulo kwa hiyo, madereva wa mizigo wangeweza kuitumia kwa urahisi zaidi. Vilevile Malawi na Tanzania tuna biashara kubwa na kituo cha forodha kitawezesha kukinga mapato mengi na kusimamia ubora wa bidhaa zinazopita hasa za mazao na mifugo kuzuia magonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunaipongeza Wizara kwa ubunifu wa kuhamisha Walimu wa masomo ya sanaa kutoka shule za sekondari kwenda kujaza nafasi shule za msingi, zoezi hili kama ilivyo kwenye wilaya nyingine chache, kwa Ileje limezua malalamiko kwa Walimu 83 walioguswa nalo na kuleta mgongano kwa kuwa, kuna imani kubwa kuwa zoezi limetumika kukomoa Walimu wanaoonekana kuwa wakorofi na kuhamisha wale ambao wana degree hadi masters na kuwaacha wenye stashahada kama agizo la Serikali lilivyokuwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi baada ya kuahidiwa malipo, hii inabadilika, kufuatia Walimu walioitwa mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama na kuhojiwa kwa vitisho. Zoezi la kawaida limegeuka kuwa vita kwa sababu, ya jinsi lilivyotekelezwa na Mkurugenzi wa Ileje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira umesimama kwa miaka zaidi ya nane na pamoja na STAMICO kuruhusu hakuna kinachoendelea kwa uhakika. Mwaka huu tulielezwa kuwa, uzalishaji wa majaribio umefanywa, lakini hatujajua kama unaendelea na kwa
utaratibu upi kwa sababu, mpaka sasa hatufahamu mwekezaji ni nani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile hatupewi taarifa juu ya taratibu za uhamishaji mgodi toka mwekezaji aliyeshindwa na STAMICO kama umekamilika ama vipi na suala la ubora wa makaa na matumizi kusudiwa. Wananchi wa Ileje wangependa kufahamu maana mgodi huu ni tegemeo lao kwa ajira na mapato kwa Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile daraja la mgodini Kiwira kutoka barabara ya Mto Mwalisi linahitajika kujengwa ili kuepuka usumbufu wa kupitia Wilaya ya Kyela kuja Ileje, umbali wa kilometa 36 wakati daraja linalohitajika ni kilometa saba tu kuufikia mgodi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingi za ndani ya Ileje zinazounganisha kata zinashindwa kujengwa kwa sababu ya ukomo wa bajeti. Changamoto ipo katika barabara zinazounganisha vijiji na vijiji, mfano, madaraja matatu kutoka Kijiji cha Bwenda kuja Makao Makuu Kata ya Lubanda mpaka uzungukie Kata nyingine ya Luswisi. Daraja toka Kata ya Ibaba kuunganisha Kata ya Ngalilo kupitia daraja la Shilinga lingesaidia kuwaunganisha wananchi na wilaya na mkoa wao lakini hawa wametengwa kwa kukosa daraja hili. Daraja la Kajeshi kuunganisha Sekondari ya Bupogo, daraja la Bupigu kwenda Chongo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umaliziaji wa zahanati pamoja na Mfuko wa Jimbo haujakamilika. Upungufu wa watumishi ni mkubwa sana Idara ya Afya na ukamilishaji wa vituo vya afya, zahanati na hospitali ya wilaya kutahitaji watumishi wengi zaidi. Vyoo mashuleni pamoja na Mfuko wa Jimbo bado kumalizika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Idara ya Elimu Sekondari na Msingi; kuna upungufu wa Walimu 50 na 482; Uchakavu wa miundombinu ya madarasa na nyumba za Walimu ambayo mengi yalijengwa kwa udongo muda mrefu; Ukosefu wa gari la Idara ya Elimu Msingi; na Upungufu wa matundu ya choo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kilimo kuna kuchelewa kwa pembejeo na Ukosefu wa masoko ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji. Upungufu watumishi idara ya maji na vitendea kazi kwa usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya maji. Kukosekana kwa chujio la maji kwa Mradi wa Maji Humba – Isongole kunafanya tuendelee kupata maji yenye matope na kwa hivyo, siyo salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutotolewa fedha yote ya miradi ya maendeleo na kwa wakati kunaathiri sana miradi ya maendeleo na kuchelewesha maendeleo ya wilaya ambayo tayari imekuwa nyuma kimaendeleo muda mrefu kwa sababu, miradi mingi inawekwa kwenye bajeti kila mwaka bila utekelezwaji. Serikali itoe kipaumbele kwa wilaya za pembezoni na hasa zenye mvua nyingi ili zipatiwe fedha ya kutosha kwa ukarabati wa barabara za vijijini katika wilaya hizi ili ziweze kutumika kwa mwaka mzima kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya wilaya hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu inasifika sana kwa utawala bora na tunaishukuru sana Serikali kwa kusimamia utawala bora na amani na utulivu mkubwa. Ziko nchi zinazotuzunguka ambazo hata kwenda kukutana na Waziri utoe rushwa? Pia mishahara inalipwa kwa kubahatisha, nchi zina rutuba lakini uzalishaji hakuna na wanaishia kutegemea nchi jirani. Amani haipo na mifumo yote imevurugwa. Sisi Tanzania tuna kila kitu, tunaomba sana watendaji wachache wanaotuvurugia utawala bora hasa Wakurugenzi na wale wasiozingatia maadili basi wachukuliwe hatua kali za kinidhamu ili iwe mfano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ileje tuna Mkurugenzi ambaye amevuruga sana Madiwani, Walimu, Watendaji chini yake na hata wananchi tumeshatoa malalamiko kwa Waziri Mkuu na kwa Waziri wa TAMISEMI. Tunaomba wamwelekeze aache au kwa kuwa, uwezo wake ni mdogo basi atafutiwe atakapoweza kufanya kazi vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii ya kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa hii. Vilevile nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Madini pamoja na Manaibu wake na Katibu Mkuu kwa hotuba nzuri sana iliyosheheni maelezo ambayo kwa kweli ni mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kwa kuanza na suala zima la kumshukuru Rais kwa maono yake kuhusiana na rasilimali za Taifa letu. Amechukua uthubutu wa hali ya juu na amepata vipingamizi vingi lakini mwisho wake tunaona kwa nini alikuwa anaelekea huko. Kwa kweli lengo kubwa ni kuhakikisha kuwarasilimali tulizonazo zinatufaidisha kwanza wenyewe Watanzania kabla ya watu wengine. Hatua zilizochukuliwa kwa kweli tunaziona kuwa zitatuboreshea mikataba na utendaji mzima wa sekta hii muhimu ya madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba vilevile nizungumzie suala zima la wachimbaji wadogowadogo. Wachimbaji wadogo kama ambavyo wachangiaji wengi wameeleza ni sehemu kubwa na ya muhimu sana katika sekta hii ya madini, lakini wanafanya kazi katika mazingira magumu sana na kwa kuwezeshwa na Serikali wanaweza wakajikwamua kiuchumi na wakachangia vikubwa zaidi katika Pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi ambayo wachimbaji wadogo wanafanyia kazi ni kama ya kubahatisha, ama wawe na leseni au wakiwa hawana lakini bado wanahamahama kwa kubahatisha kuwa labda hapa nitapata. Serikali iwaunganishe na wale wanaofanya geo- survey ili wanapopata leseni zile ziwe tayari zimeainisha madini yaliyoko ndani ni kiasi gani ili hata wao wenyewe wanapotia nguvu yao pale wawe na uhakika wa kupata mapato vilevile kuchimba kwa njia ambayo haiharibu mazingira yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala hilohilo la wachimbaji wadogo, wengi sana wanatumia nyenzo duni. Natambua sana hatua zilizochukuliwa na Serikali za kuwapa mitaji kwa njia ya ruzuku lakini kama ilivyo haitoshelezi. Wachimbaji wadogo wanaoomba leseni ni wengi na mahitaji yao ni makubwa. Kwa kupitia shirika zao zile mbalimbali, basi Serikali itafute njia ya kuhakikisha kuwa wanawaletea vifaa vinavyofaa, wanawapa mafunzo ya kutosha lakini maeneo wanayotengewa yawe ni maeneo yenye rutuba kwa maana ya madini ya kutosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku za nyuma kulikuwa kuna utaratibu wa Benki Kuu kununua dhahabu, ule utaratibu wenyewe haukuwa mbaya isipokuwa uligubikwa tu na tatizo kidogo mwishoni. Nafikiri ni wakati mzuri sasa wa kuangalia jinsi gani tunaweza tukarudisha mfumo ule. Wachimbaji wadogo wengi sana walikuwa wananufaika na ule mfumo kwa sababu walikuwa na soko la uhakika la dhahabu yao na ilikuwa inawezekana kupimwa wakajua thamani yake na inawasaidia hata wao wenyewe kwenda kupata mikopo kwa sababu tayari wana dhahabu mkononi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda hilo suala liangaliwe kwa sababu nchi nyingi na benki nyingi za dunia wananunua dhahabu mpaka sasa hivi. Sasa hivi tunaweza tukaingia ubia na wawekezaji ambao wao kazi yao itakuwa kuthamini hiyo dhahabu, kuihakiki na Benki Kuu inakusanya pesa inayotokana na hiyo dhahabu lakini vilevile kuihifadhi. Hii itakuwa ni njia mojawapo ya kuthaminisha dhahabu yetu na kutuweka katika hali ambayo kama Taifa kuwa na pato la kutosha hata kukopesheka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la makaa ya mawe. Tuna makaa ya mawe mengi sana nchini, tukianzia Ileje au Songwe, Ludewa, Ruvuma, Njombe, kote huku tuna machimbo mengi ya makaa ya mawe, inasikitisha kuwa mpaka sasa hivi uendelezwaji wake umekuwa wa kusuasua. Hiki ni chanzo muhimu vilevile kwa masuala ya viwanda na uzalishaji wa nishati ya umeme. Kwa hiyo, napenda sasa hivi tufikie mahali ambapo Serikali inajikita kwa nguvu zaidi katika kuwekeza kuchimba makaa ya mawe ambayo ni muhimu sana tunapoelekea uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua vilevile kuhusiana na STAMICO. STAMICO imepigiwa kelele sana, imelalamikiwa sana lakini STAMICO kama mnavyojua Mashirika ya Umma mengi ambayo yalikuwa yamepewa majukumu ya kuendesha shughuli mbalimbali, ni mojawapo ya mashirika ambayo yamekuwa hayapati fedha ya kutosha kuendesha shughuli zake. Tutawalaumu bure STAMICO hapa wakati kumbe hatuwawezeshi. STAMICO ina wataalam wazuri sana, ina miradi ilikuwa mizuri sana, kama walishindwa ni kwa sababu hawajawezeshwa vya kutosha. Sasa hivi Serikali ihakikishe kuwa STAMICO inapewa fedha ya kutosha, inasimamia vizuri migodi na miradi ambayo iko chini yake ili ilete tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nataka kuzungumzia Mkoa wangu wa Songwe, hususani Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira. Kumekuwa na sintofahamu ya muda mrefu sana kuhusiana na Kiwira, mara mwekezaji anakuja, mara wanasema hatoshi, mara inakuwa hivi mara vile. Sasa hivi tunaambiwa tangu Aprili mwaka uliopita STAMICO wameanza kufanya majaribio ya kuchimba makaa ya mawe na wameanza kuyauza. Napenda kujua sasa kama hiyo itakuwa ni mwendelezo na mikataba gani imeingiwa kati ya STAMICO na Wilaya yangu ya Ileje na Mkoa wetu wa Songwe kwa ujumla na nini tutegemee katika suala hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nitoe ombi kwa Wizara, tuna daraja dogo sana pale linalounganisha Mgodi wa Kiwira na Wilaya ya Ileje ambalo lingetoa fursa ya mkaa ule kusafirishwa lakini halifanyi kazi kwa sababu limekatika. Je, Serikali kwa kupitia Wizara hii wanaweza wakahakikisha kuwa wanatengeneza hilo daraja la kilometa 7 tu ambalo litawezesha sasa kupitika na makaa ya mawe yaweze kupita pale badala ya kuzungukia Kyela ambako ni mwendo mrefu zaidi na hasa tukiangalia kuwa mkaa huu unapelekwa Mbeya Cement ambako ni rahisi zaidi kupitia upande wetu wa Ileje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kujua ubora wa makaa haya. Mara tunaambiwa hayafai, mara tunaambiwa yanafaa, mara tunaambiwa yana ubora zaidi kuliko hata yale ya Afrika Kusini mara tunaambiwa sijui yakoje. Naomba tupate takwimu sahihi kujua kama kweli yana ubora gani na hatua zinazotegemewa kuchukuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie sasa suala zima la watoto wadogo wanaofanya kazi katika migodi nchi nzima. Kwa kweli hili ni janga na hizi ajira za watoto kwenye migodi zinaathiri sana watoto kiafya vilevile kielimu. Watoto hawa hawaendi shule kwa sababu wanatumika kwenye migodi na sehemu wanazofanyia kazi watoto hawa ni hatarishi sana. Mashimo tu ambayo hayana kinga aina yoyote wanadumbukizwa kule kwa sababu wao kwa udogo wao ni rahisi kupenya matokeo yake wanaathirika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya yote wanaathirika na zebaki wanayotumia kuchenjua ile dhahabu. Wengi sasa wamegundua kama wakienda kuchezacheza na ule udongo wakatia zebaki kidogo wanaweza wakaambulia vijiwe vya mawe ya dhahabu kwa hiyo wanafanya hivyo, lakini hii ina madhara makubwa sana kwao. Napenda Serikali kwa umoja wao kwa mfano, Wizara ya Madini, Wizara ya Elimu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, wote washirikiane kuona jinsi gani watahakikisha kuwa watoto wadogo hawafanyi kazi katika migodi ili waendelee na masomo kama kawaida na watakapokuwa wakubwa basi wataingia katika kazi hizi za migodini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusiana na wanawake. Wanawake wengi wamependa na wao kujiingiza katika shughuli za migodi lakini mazingira siyo rafiki kwao na vilevile na wao wanapata matatizo kama yale ya wachimbaji wadogo kwa vifaa duni na mitaji ni midogo. Kwa hiyo, wao pia kama kundi maalum la wazalishaji wangesaidiwa kwa sababu wana umoja wao tayari ambao unawawezesha na wao kuhusika katika biashara hii ya migodi. Tungependa kuona hilo likifanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini zaidi ya yote tunaomba sana data tupate kujua mawe ya aina gani, yana thamani gani, tunayo mengi kiasi gani na vito vya aina gani, vina thamani kiasi gani, tunayo kiasi gani. Hii kwanza moja kwa moja itatusaidia kama Taifa kujua utajiri wetu na kutuwezesha kuwa na ulinganisho mzuri duniani hata katika masuala ya mikopo na masuala mengine ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo napenda sana tuwe na takwimu za kutosheleza kuhusiana na rasilimali tulizonazo nchini. Kwa sasa hivi tunazungumzia madini lakini naamini ni kwa rasilimali zote ambazo Tanzania tunazo na ambazo kwa kweli Mungu ametupendelea na kutupatia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni yangu yalikuwa ni hayo, nilikuwa nataka tu kuhimiza suala zima la rasilimali hizi zianze kusaidia Watanzania kwanza na kama ni suala la sera kila mtu alielewe vizuri na ionekane pale ambapo kuna mapungufu basi turekebishe ili mwisho wa yote madini yetu yabakie nchini na yaweze kusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la kuyeyusha (smelting). Tumeambiwa kuwa tunajitahidi kwa kadri iwezekanavyo madini yasipelekwe nje yakiwa ghafi, lakini bado hatuna smelters za kutosha kuweza kuhakikisha kuwa hilo linafanyika. Tungependa Serikali ifanye makusudi kabisa kuwekeza katika suala hili kwa sababu hiyo ndiyo itakuwa njia pekee ya kuzuia madini kutoroshwa nje kwa njia ya magendo.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi ya kuchangia. Napongeza mapendekezo ya mpango kwa kweli ni mazuri isipokuwa naomba nijikite katika eneo moja au mawili hasa kwenye kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu umuhimu wa kilimo. Pamoja na kuwa tunasema kilimo ni uti wa mgongo ndiyo sekta itakayoleta ajira nyingi sana kwa vijana na itaondoa umaskini kwa kiasi kikubwa sana. Pamoja na kuwa na mikakati na miradi mingi ya kuendeleza kilimo katika nchi yetu mingi naiona bado iko katika mipango, utekelezaji bado haujaonekana kwa maana ya uboreshwaji wa kilimo ambacho kwa kiasi kikubwa takribani asilimia 65 mpaka 70 kinafanywa na wanawake vijijini ambayo ni nguvu kazi kubwa lakini wanafanya kazi kwa mazingira magumu sana. Changamoto zinafahamika na tungependa kuona kwenye mpango sasa jinsi gani hii mikakati na miradi mikubwa iliyoletwa akina ASDP II, SAGCOT na mikakati mingine yote katika sekta za uvuvi na ufugaji zinatiririka sasa kwenda kwa wale ambao ndiyo hasa wazalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko njia nyingi za kuendeleza kilimo kwa kukiboresha. Muda mrefu sana tumekuwa tukizungumzia mnyororo wa thamani, hiyo ilikuwa ni njia moja nzuri sana ya kuhakikisha kwanza kilimo chetu kinakuwa na tija lakini kinaleta ajira, kinaongeza thamani ya mazao yetu na kuwezesha soko la ndani kujihimili katika kujitosheleza kwa mahitaji yake na hata kuuza nje ya nchi. Hali ilivyo sasa hivi Serikali na wakulima wanagonganisha vichwa, kila tunakoenda wakulima wanalalamika sana na wana haki ya kulalamika kwa sababu wanatumia nguvu yao wenyewe nyingi, wanapoteza fedha nyingi lakini wanachokuja kupata baada ya kulima ni kitu ambacho kwa kweli hakiwatoshelezi wao hata Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema kuwa wakulima wengi ni wanawake lakini vilevile ajira nyingi zinaweza zikazalishwa kwa vijana kwa kutumia kilimo, ufugaji na uvuvi. Nini kifanyike, ni kuhakikisha kuwa zile changamoto zilizoainishwa ndiyo ambazo Serikali inaziwekea mkakati wa kuhakikisha kuwa wanazitatua. Upatikanaji wa mitaji kwa wakulima bado ni mdogo na unasuasua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hiyo Benki ya Wakulima iliyoanzishwa bado ina-deal na watu wa ngazi za juu, inataka vikundi vilivyosajiliwa na watu ambao wako kwenye mfumo rasmi, wakulima wetu wengi na vijana wetu wengi hawako kwenye mifumo hiyo. Kwa sababu hawako kwenye mifumo hiyo tulikuwa tunategemea benki ingeji-restructure iwakute hawa. Tanzania siyo peke yake inayofanya hivi, ziko nchi nyingi na zimefanikiwa kwa kuhakikisha kuwa mifumo yao ya kutoa mitaji kwa ajili ya kilimo inakwenda sambamba na aina ya wakulima tulionao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia suala la kuongeza thamani. Mnyororo wa thamani ndiyo utakaotuhakikishia kuwa kwanza tunaunganisha kilimo na sekta binafsi. Kwa sababu kwa upande mmoja sekta binafsi ndiyo inaingia katika mambo ya value addition na masoko na kwa kutumia weledi na nyenzo bora wanazotumia wao wanaweza kusaidia hata wakulima katika ngazi za chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu ambao wameendelea kwenye kilimo, kwa mfano Vietnam, South Korea, Thailand, wakulima wao wote bado ni wadogo lakini wametafuta hizo linkages na private sector, wakatumia outgrower schemes, irrigation schemes na ku-link na wanunuzi wakubwa wa nchi za nje kwa kutumia Serikali na wakafanikiwa sana. Sasa hivi wanatumia kilimo katika kuhakikisha kuwa wana export kwa wingi zaidi kutokana na hao wakulima wadogo wadogo. Naomba sana Mheshimiwa Dkt. Mpango angalieni jinsi gani mtaboresha mikopo na huduma za muhimu za ugani kwa wakulima wadogo ambao ni wengi na hapo ndiyo mtakapoona tija ya kilimo itakavyokuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la kuhakikisha kuwa nyenzo bora zinapatikana. Wakulima wengi ni wanawake, tuna TEMDO, CAMARTEC, TIRDO na SIDO, wanafanya nini kuhakikisha kuwa akina mama hawa wanatengenezewa nyezo zitakazofaa kutumia wao kufuatana na nguvu zao na uwezo wao na jinsi ambavyo wanajikita kwenye mashamba yao. Tuna taasisi, makampuni na mabenki tunachotakiwa sasa kama Serikali ni kuwaunganisha hawa sasa na wakulima, vijana kwa wanawake ili sasa tija ipate kuongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalalamikia masoko, lakini hata soko la ndani lenyewe hatujalitosheleza kwa bidhaa hasa zile muhimu zinazohitajika. Tunaagizaje tomato paste, tomato sauce na chill sauce, wakati nyanya zinaoza mashambani. Vijana wamekaa hawana kitu cha kufanya wakati teknolojia ya kufanya hivyo ni ya nyumbani kwa mtu, unajifungia store unatengeneza tomato paste, tomato sauce na concentrate za tomato ambazo unaweza kuuza mpaka nchi nyingine au unaweka wakati ambao siyo msimu unatumia, kwa nini bado hatujalifikiria hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna suala la umwagiliaji. Tanzania nafikiri ni nchi ya pili kama siyo ya tatu kwa wingi vya vyanzo vya maji lakini mpaka leo kilimo chetu kinategemea mvua. Napenda sana kuona zile scheme ambazo zimeshatengenezwa tayari lakini hazifanyi kazi zirekebishwe, zikarabatiwe ili wananchi walime kilimo cha umwagiliaji. Kila wilaya utakuta kuna scheme za umwagiliaji zimekufa au zina vitu vidogo tu vinavyohitaji matengenezo lakini havifanyiwi kazi tunafikiria mambo makubwa. Mambo makubwa ni mazuri lakini haya madogo ni mazuri zaidi kwetu sisi tunaotaka kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuuzungumzia SAGCOT pamoja na ASDP II. Hii yote ni miradi mizuri sana na inalenga kutukwamua lakini kwa kiasi kikubwa sana inategemea fedha ya nje. SAGCOT hundred percent I think ni hela ya nje. Sasa ikikosekana na wakati tunaona kabisa SAGCOT ndiyo ambayo inaelekeza sasa kilimo cha kisasa kwa kutumia mfumo wa sekta binafsi lakini tunawategemea watu wa nje. Napenda kuona Serikali na yenyewe inaingiza mkono wake kwa kuweka fedha ya kutosha kwenye SAGCOT ili sasa tuwe na uhakika kuwa huu mkakati utaendelea na kuwavuta watu wengi zaidi kuingia katika mfumo rasmi wa kuendesha kilimo na kukiendeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nirudi kwenye suala la vijana wetu, ajira nyingi sana za vijana zitatoka kupitia kilimo, ufugaji na uvuvi. Tujiulize kwa nini vijana hawapendi kuingia kwenye kilimo, ufugaji au uvuvi wa kisasa? Changamoto zao zinajulikana, vijana siyo watu wanaotaka kushinda shambani kutwa nzima na jembe. Ndiyo maana mpaka sasa hivi wengi wanaolima ni watu wazima na vijana wanawake lakini vijana wanaume wengi hawalimi kwa mtindo huu tunaoendelea nao sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kuona Serikali inakuja na mkakati wa ku-involve vijana kwenye kilimo specifically. Wale vijana wachache walioweza kulima wameona faida zake na huwaondoi huko. Kulikuwa na mradi wa MUVI ambao umekuwa ukisaidia vijana, wengi sasa hivi wamejikita kwenye kilimo na wanafurahia sana lakini bahati mbaya sasa na wenyewe wanakosa masoko kwa sababu hakuna ule mnyororo wa thamani ambao umeunganishwa katika hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kabla kengele haijalia Wizara haziongei, Wizara hazizungumzi, hakuna interconnection kama alivyosema Mheshimiwa Lucy asubuhi. Wizara ya Kilimo wana mikakati yao wanaendelea nayo huku na Wizara ya Viwanda wana mikakati yao wanaendelea huku wakati hawa ndiyo wanaotakiwa kuungana. Mpango utakapokuja sasa tuone kabisa ile link ya moja kwa moja kati ya kilimo na viwanda, uvuvi na viwanda, ufugaji na viwanda pamoja na ajira zao. Hii itaweza sasa kuona ile integration nzuri ya uchumi kuelekea uchumi wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la jinsi gani nguvu kazi watu inatayarishwa. Tuna miradi mikubwa mingi sana ambayo inaendelea sasa hivi, je, tunao wafanyakazi, vijana au watumishi wenye taaluma watakaokuja kufanya kazi kwenye miradi hii? Kwa hiyo, haya yote ni mambo ambayo ukiangalia lazima yawe linked…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naunga mkono lakini napenda sana kuona integration ya sekta zote muhimu au Wizara zote muhimu ku-converge kwenye uchumi wa viwanda. Hiyo ndiyo itakuwa njia peke yake ya kuhakikisha kuwa uchumi wetu na huu mpango unaenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia Mpango ulio mbele yetu. Namshukuru Mungu kwa neema na rehema zake kwangu na kwa nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, napenda kwa unyenyekevu mkubwa kuwashukuru wananchi wa Ileje kwa kunipa ridhaa ya kuwa Mbunge wao, nawaahidi kuwa sitawaangusha na nitawatumikia kwa nguvu zangu zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Naibu wake na Maofisa wote wa Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwongozo mzuri na Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano na wa mwaka mmoja. Mpango uliowasilishwa ni mzuri, lakini nianze kwa kumtaka Mheshimiwa Waziri atueleze wananchi wa Ileje kuwa wao atawawezesha vipi kuingia katika uchumi wa nchi? Mpango wa Maendeleo unaotarajiwa umeweka vipaumbele muhimu vilivyomo ukurasa wa 23 hadi 25.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na viwanda; wazo la viwanda ni jema hasa ukizingatia kuwa kwa muda mrefu bidhaa zetu nyingi zimekuwa zikiuzwa ghali na kwa hivyo kuwapatia fedha kidogo sana wazalishaji. Bidhaa nyingi zimekuwa zikipotea kabla na baada ya kuvuna na hii pia husababisha upotevu wa fedha za uzalishaji, hii pia imesababisha wazalishaji kupunguza nguvu ya uzalishaji kwa sababu ya kukosa soko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika kupanga maendeleo haya ya viwanda ni lazima mambo ya msingi yatakayowezesha ujenzi na uendeshwaji wa viwanda hivyo yapewe kipaumbele hususan miundombinu ya barabara zinazopitika kwa mwaka mzima, miundombinu ya umeme wa uhakika unaopatikana mwaka mzima, upatikanaji wa maji na upatikanaji wa malighafi za kutosha. Hali ilivyo sasa hata viwanda vilivyopo vina changamoto nyingi za miundombinu tajwa hapo awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuzungumzia viwanda bila kuainisha mpango wa kuboresha kilimo, ufugaji, uvuvi na uchimbaji wa madini ya aina mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo makubwa ya uzalishaji wa kilimo ndiyo kwa kiasi kikubwa ambayo yana miundombinu mibovu sana. Nitoe mfano wa Wilaya ya Ileje, ambao tangu tupate Uhuru na tangu Jimbo lile lianzishwe miaka 40 iliyopita halijawahi kupata barabara ya lami hata moja ilihali Wilaya nyingine zote zinazoizunguka Ileje wana barabara za lami. Sasa kwa hali hii Ileje itawezaje kuvutia wawekezaji wa kilimo cha biashara, uvuvi na ufugaji ambao utaleta ujenzi wa viwanda? Naiomba Serikali iwekeze katika miundombinu ya barabara Ileje ili na sisi Wanaileje tujenge viwanda kuanzia vidogo, vya kati na vikubwa. Suala la miundombinu Ileje ni nyeti na ni la muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuna umeme, barabara, masoko, kituo cha forodha, uhamiaji wakati kuna biashara kubwa sana ya mpakani na Malawi na ni njia ambayo ingekuza biashara kubwa sana na nchi jirani ya Malawi. Ileje ni Wilaya ambayo ingepata fursa sawa na Wilaya nyingine ingepiga hatua kubwa sana ya kimaendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo Ileje inahitaji ni kupimiwa ardhi ili wawekezaji waje kuwekeza. Ileje inahitaji kujengewa masoko na kituo cha mpakani kwa ajili ya kuendeleza vizuri biashara na nchi jirani za Malawi na Zambia. Ileje inahitaji taasisi za ufundi, majengo ya utawala na biashara ili Ileje isibakie kama kijiji kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazingatia kuboresha miundombinu yote na kuboresha kilimo, ufugaji na uvuvi, basi tuzingatie suala la kuwa wazalishaji wakubwa katika sekta hizi ni wanawake. Mpango huu uzingatie na ujielekeze katika masuala ya jinsia na makundi maalum. Tanzania ilishajiingiza katika mfumo wa gender budgeting, basi vipaumbele vyote vioneshe jinsi mipango hii inavyozingatia masuala ya kijinsia katika mikakati, katika bajeti zake ili wanawake, vijana, walemavu na wazee wawe sehemu ya Mpango huu wa Maendeleo. Nashauri Mpango huu uweke wazi mgawanyo huu ili makundi yote muhimu yashiriki kikamilifu katika maendeleo haya yanayotarajiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mpango unapaswa kuendeleza yale yote yaliyoanzishwa na Serikali kwenye kuleta usawa wa jinsia. MKUKUTA II, hasa ile cluster ya pili, Big Result Now ilizingatia usawa wa kijinsia. Je, hivi viko wapi sasa katika Mpango huu? Serikali ilikuwa imeshakuwa na mwongozo wa bajeti inayozingatia jinsia kwa Serikali za Mitaa, Serikali Kuu, Vitengo na hata BRN.
Mheshimiwa Mwenyekiti, chambuzi nyingi zilishafanywa kwenye sekta nne na kulikuwa na tamko la Serikali juu ya kila sekta kuainisha jinsi ambavyo imezingatia masuala ya kijinsia, takwimu zilitakiwa kunyumbulisha masuala ya kijinsia na labour force survey iliyofanywa ilionesha masuala ya kijinsia. Tathmini ya matumizi ya fedha za umma ilishafikiwa chini ya PER kama nyenzo ya kuhakikisha utekelezaji wa Mpango huu. Malengo ya milenia yalikwisha na sasa tuko kwenye SDGs ambavyo ni lazima ioneshe ni jinsi gani hayo yote yatashughulikiwa katika Mpango huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa takwimu kwenye maeneo yote muhimu kijinsia urekebishwe. Msingi wa usawa wa kijinsia ni muhimu kuhakikisha kundi kubwa la wanawake, vijana, walemavu, wazee na wanaoishi na VVU kuwa katika Mpango wa Maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fursa za kuingiza masuala ya jinsia kwenye Mpango; kwenye utangulizi Serikali ingefanya marejeo kwenye Mpango wa Maendeleo kuhusu masuala ya kijinsia na miongozo tuliyojiwekea katika kuingiza jinsia katika mipango ya maendeleo.
Lengo la tano, kuwe na utambuzi zaidi wa umuhimu wa usawa wa kijinsia. BRN imeainisha kipengele cha jinsia na ufuatiliaji na kutathmini mpango mzima, Mpango unyumbulishe viashiria vyote kutumia hali ya uchumi jinsia, walemavu na wazee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumziwa idadi, ni muhimu tukazingatia kutamka kuwa mfumo una taswira hasi kwa wanawake. Idadi ya Kaya zinazoongozwa na wanawake zinaongezeka, bado hatujasimama katika nafasi nzuri sana katika masuala ya jinsia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la viwanda; je, Serikali imezingatia vipi suala la ujuzi kwa maana ya:-
(i) Elimu - usawa na jinsia, ufundi, vyuo vikuu, ajira rasmi;
(ii) Kilimo - kina sura ya mwanamke ambaye hana umiliki wa ardhi wala nyenzo za kisasa za kilimo, ufugaji, mitaji na kadhalika. Viashiria vya umaskini vina sura ya wanawake vijijini. Je, hili limezingatiwa vipi kwenye Mpango huu?
(iii) Ajira - 1.4; wanawake wasiokuwa na ajira; je, Mpango unalishughulikia vipi? BRN - sura iko kimya kuhusu masuala ya jinsia katika BRN, asilimia tano tu ya wanawake wanamiliki ardhi wakati asilimia 44 wanafanya kazi za uzalishaji;
(iv) Mikopo - wanawake wengi sana hawana fursa, mfumo wa fedha ni mfumo dume;
(v) Huduma za jamii; na
(vi) Ukatili wa kijinsia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vifo vya mama na mtoto, utapiamlo, kukosa haki zao za msingi, kukosa kujiamini na mila na desturi, ugandamizi na sheria. Kuwe na lengo mahsusi la kuzingatia masuala ya kijinsia ili kuzingatia juhudi zilizofanywa na Serikali kujielekeza katika mikakati, viashiria na rasilimali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sura ya Tatu; mikakati yote haijanyumbulisha mtazamo wa kijinsia, kwa hiyo, lazima mikakati ioneshe jinsi wanawake, vijana, walemavu watakavyofikia malengo haya kwa kuwapa vipaumbele kwenye Mpango na kwenye bajeti tajwa. Kwenye kujenga uwezo, nini mkakati wa kuwajengea uwezo watendaji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, follow up issues katika Wilaya ya Ileje; kwanza ni ujenzi. Barabara kuu tano zinazounganisha Ileje na Kyela inayotokea Kusumulu - Kyela kupitia Kata ya Ikinga na Malangali hadi Ileje Mjini. Barabara inayounganisha Wilaya ya Rungwe na Ileje inayotokea Mji wa KK Rungwe na Ileje, barabara inayotokea Mji wa KK na kuingia Ileje kupitia Kata za Luswisi, Lubanda, Sange na Kafule. Barabara ya kuunganisha Wilaya ya Momba na Ileje, inaanzia Mpemba na kupitia Kata ya Mbebe, Chitete, hadi Itumba. Barabara inayounganisha Wilaya ya Mbeya Vijijini na Ileje kupitia Mbalizi, kupitia Vitongoji vya Mbeya Vijijini hadi Itale, Ibaba na Kafule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia skimu za umwagiliaji; zilizopo Ileje ni Jikombe iliyopo Chitete na Ikombe iliyopo Itumba yenye banio, lakini mifereji haijachimbwa. Jikombe ilichimbwa lakini mifereji haijasajiliwa, hivyo mfereji umekuwa ukijifulia fulia. Skimu ya Sasenge imebakiza mita 2000 kumalizia usafishaji wa mfereji mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miradi ya maji; Mradi wa Ilanga, Mlale- Chitete inasemekana mingine inasubiri makabidhiano ingawa Malangali na Luswisi inahitaji marekebisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme wa REA; vijiji vilivyopata umeme ni 35 ambavyo umeme umewashwa ni vinne tu. Ileje ina Vijiji saba. Vijiji ambavyo havipo katika orodha ya kuwekewa umeme ni 25. Je, lini Vijiji vilivyopo kwenye orodha vitakamilishiwa na ambavyo havimo kwenye orodha vitajumuishwa lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ardhi; Ileje imekuwa kwa muda mrefu ikikabiliwa na tatizo la watumishi katika sekta mbalimbali ikiwemo Maaafisa Tathmini (Valuers, Surveyors na Afisa Ardhi). Hii imeathiri kwa kiwango kikubwa upimaji ardhi na kutoa hati miliki kwa wananchi na wawekezaji wa viwanda, biashara na kilimo cha biashara. Hii inawanyima fursa nzuri za maendeleo wana Ileje na Taifa kwa ujumla. Lini Serikali itatupatia Wilaya ya Ileje Maafisa hawa muhimu ili kuharakisha upatikanaji wa hati hizi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kilimo, Ileje inalima kwa wingi nafaka zote unazoweza kuzifikiria, mazao ya mbegu za mafuta, matunda, mboga, pareto, kahawa, miti ya asali na pia ina fursa ya kulima cocoa, vanilla na mazao ya misitu. Kuna fursa ya ufugaji wa mifugo aina zote na nyuki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ileje inapakana na nchi jirani ya Malawi na Zambia, zaidi ya yote kwenye mpaka wa Tanzania na Malawi kuna kituo cha mpakani ambacho ni kichekesho! Askari wetu pamoja na Maafisa wa Uhamiaji wanakaa katika banda la ovyo, hakuna ofisi rasmi na isingekuwa mahusiano yetu mazuri na Malawi hawa wangeshindwa kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Uhamiaji iko katikati ya mji kwenye nyumba ya kupanga. Nafurahi kusikia kuwa, uhamiaji wana mpango wa kuja kujenga Chuo cha Uhamiaji Ileje na vilevile Kituo cha Forodha kinaenda kujengwa ili kihudumie mpaka na kuhakikisha biashara ya mpakani inafanywa kwa ufanisi zaidi kwa manufaa ya Taifa na wananchi wa Ileje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma za jamii kama afya, elimu, maji na mazingira pia zizingatiwe. Kuhusu suala la Watumishi wa Umma; kuna upungufu mkubwa wa watumishi katika Idara ya Ardhi, Elimu, Afya na Mazingira. Hii imeathiri sana utendaji na ufanisi na kuzorotesha zaidi maendeleo ya Ileje. Watumishi wengi hawapendi kufanya kazi Ileje na hawaripoti kabisa na hata wakiripoti huondoka na kuacha pengo.
Kuhusu huduma za fedha, ni chache sana, Benki iko ya NMB na Tawi moja tu. Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha huduma za kifedha katika wilaya nzima?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hitimisho; ni dhahiri kuwa, kwa hali hii Wilaya ya Ileje itachukua miaka mingi sana kufikia uchumi wa kati kama hatua kubwa na za haraka hazitachukuliwa katika:-
(i) Ujenzi wa miundombinu.
ii) Upatikanaji wa umeme.
(iii) Upatikanaji wa maji.
(iv) Ujenzi wa shule, vyuo na taasisi za kiufundi kama uhamiaji, mamlaka ya kodi, taasisi za kifedha, taasisi za kuhudumia wanawake, vijana, wazee, walemavu na wanaoishi na VVU.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kusikia kutoka kwa Waziri, ni nini mkakati wake wa kutuhakikishia Wanaileje kuwa na sisi tutafikia katika uchumi wa kati. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Namshukuru Mungu kwa kutuwezesha kufika hapa asubuhi ya leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nami naomba nichangie katika hotuba hizi mbili, kwanza kwa kuipongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa ushindi walioupata katika uchaguzi mkuu uliopita. Nampongeza sana Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, nampongeza sana Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Hassan Suluhu, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, nampongeza sana Rais Dkt. Ali Mohamed Shein wa Zanzibar kwa ushindi walioupata na kuaminiwa na wananchi kuwaongoza katika Awamu hii ya Tano. Napenda kuwapongeza vilevile Waheshimiwa Mawaziri kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais na viongozi hawa wakuu watatu niliowataja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nataka kuwatia moyo kuwa sasa hivi wanachokifanya kinaonekana, wananchi wanakikubali na hao wanaosema tunamsifia Rais Magufuli, Rais Magufuli ameanza kusifiwa mpaka na nchi za nje, nchi za Ulaya, watamsifia bure kama hafanyi kazi? Nataka hilo ndugu zangu tuliweke kwenye perspective. Nataka kuwapa moyo, tulikuwa tunapigiwa kelele humu ndani kila siku tunaambiwa muangalieni Kagame, muangalieni Kagame, Magufuli sasa anafanya style ile ile ya Kagame mnamsema, inaonekana hamna jema. Mheshimiwa Magufuli na Mawaziri wako songeni mbele, Tanzania inawaona, wananchi wanawakubali na wanawapongeza na wako tayari kufanya kazi pamoja na ninyi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kutoa pongezi hizo, nataka na mimi nichangie kuhusiana na masuala mazima ya utendaji wa Wizara hizi mbili hasa katika kuleta maendeleo ya wananchi katika maeneo ya Tawala za Mikoa na Mitaani.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natokea Ileje ambayo ni mojawapo ya Wilaya zilizoko pembezoni lakini zenye fursa kubwa sana za maendeleo kwa maana ya kilimo, ufugaji, uvuvi lakini inakabiliwa na tatizo kubwa la umaskini ambao unatokana na miundombinu mibovu. Ileje karibu inafikia miaka 40 sasa tangu ianzishwe kwa maana kuwa ilianzishwa tangu enzi za utawala wa kwanza wa nchi hii, lakini Ileje haijawahi kuona barabara ya lami hata moja. Matokeo yake mazao yote yanayozalishwa Ileje, uwezeshwaji wote unaofanyika Ileje, wananchi hawawezi kuinuka kwa sababu hawana kipato kinachotokana na biashara ya uhakika ya mazao yao au ya juhudi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Ileje imebarikiwa kuwa na rasilimali nzuri sana na hali ya hewa nzuri sana. Jiografia yake ni ngumu kidogo lakini vilevile ni baraka kwetu lakini bado tunakabiliwa na tatizo kubwa la miundombinu inayotuunganisha kwanza na Wilaya nyingine lakini vilevile kata kwa kata, vijiji kwa vijiji. Kutokana na muinuko na mabonde tunahitaji madaraja na vidaraja vingi sana Ileje na hivi vyote bado havijakamilika. Naomba sana Waheshimiwa Mawaziri mtakapokuja hapa mbele mtusaidie Ileje tunapataje barabara za lami zitakazotuwezesha na sisi kuendelea katika mfumo huu wa hapa kazi tu kwa kasi ambayo inategemewa. Ileje ina-potential ya kuzalisha kwa ajili ya viwanda vingi sana vya kuchakata mazao lakini hatuwezi kufanya hivyo kwa sababu hatuna miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna matatizo vilevile ya ukusanyaji wa mapato, hatuna vyanzo vya kutosha vya mapato kwa sababu hatufanyi biashara lakini vilevile tuna matatizo ya maghala na masoko ya uhakika kwa ajili ya kuuza mazao yetu. Ileje imepakana na nchi jirani za Malawi na Zambia. Kuna uwezekano wa biashara kubwa sana pale lakini hatuna masoko ya uhakika, hatuna vituo vya uhakika vya forodha vya uhakika kwa ajili ya kufanya biashara hizo. Nataka kuwaomba sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI utakapokuja hapa utuambie sisi utatujengea lini border post yenye uhakika ili na sisi tufaidi biashara kama Wilaya nyingine zinavyofaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitika sana pamoja na kusema kuwa Ileje inazalisha kwa wingi sana lakini nikiangalia katika bajeti iliyopangwa kwa kilimo tu peke yake kwa Ileje ni shilingi milioni 10. Mikoa mingine ambayo haina potential kubwa kama hiyo ya uzalishaji inapewa mamilioni ya pesa. Naomba sana mkija hapa muangalie mtakavyo re-allocate na sisi ambao tuna potential ya kuzalisha na kulisha nchi nzima tuweze kupatiwa fedha ya kutosha kuboresha miundombinu yetu ya kilimo, ufugaji na uvuvi ili tuweze kuchangia katika Pato la Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna tatizo kubwa sana la upungufu wa walimu, upungufu wa watendaji katika sekta ya afya na hata Mahakama. Tumekuwa tukipata vibali lakini bado hatujaweza kuajiri kwa sababu ya ufinyu wa bajeti. Tunaomba sasa mtusaidie, shule zimeongezeka, wanafunzi wameongezeka tutahitaji walimu zaidi na hata hawa wachache tuliokuwa nao tuna tatizo kubwa la utoro kwa sababu wengi hawapendi kufanya kazi Ileje kwa sababu ambazo tayari nimeshazitaja. Kwa hiyo, naomba sana sisi ambao tuko kwenye Wilaya za pembezoni msitusahau, mtuchukulie pamoja na wengine wote tuendelee kwa pamoja kwa sababu ni haki yetu na vilevile ni sawa kwetu sisi kupata fursa hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Bajeti hii ya Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuwa hapa kujadili suala hili muhimu sana, lakini vilevile napenda sana kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha - Dkt. Mpango na Naibu wake - Dkt. Kijaji, lakini vilevile Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara ya Fedha na wadau wote waliotufikisha katika kupata bajeti kama hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii kwa kweli ni nzuri sana, naipongeza sana kwa sababu kama walivyosema wenzangu imezingatia maoni mengi ambayo Wabunge na wananchi wamekuwa wakiyatoa kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii bajeti moja kwa moja inaenda kusaidia sana yale masuala mazima ya mazingira ya kufanya biashara au ya uwekezaji katika Taifa letu. Tozo nyingi zilizokuwa kero na ambazo zimesababisha wafanyabiashara kushindwa kufanya kazi vizuri kwa ufanisi zimepunguzwa na zingine zimeondolewa kabisa, tunapongeza sana kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuanza kuzungumzia suala moja ambalo limekuwa kama lina chukuliwa kwa upotoshwaji wa kiasi kikubwa sana nalo ni lile la kusema kuwa Awamu ya Tano Serikali imekuwa ikifanya miradi nje ya utaratibu, nje ya bajeti, nje ya mipango, hiyo si kweli na nafikiri wanaofanya hivi aidha wana nia ovu au hawaelewi! (Makofi)

MBUNGE FULANI: Hawaelewi.

MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tuna dira ya maendeleo ya 2025 ambayo imeanza kutumika tangu mwaka 2000, kwa bahati nzuri mimi mmoja wapo kati ya watu ambao tulikuwa tunahusika moja kwa moja katika kuitayarisha nikiwa Umoja wa Mataifa na wako wengine humu ndani, hata Dkt. Mpango mwenyewe alikuwa anahusika nafikiri akiwa aidha World Bank au akiwa Tume ya Mipango sikumbuki vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo dira imeainisha malengo makuu ya maendeleo yetu tunavyotaka kuyapeleka tangu wakati huo mwaka 2000, kati ya malengo matano makuu ambayo ndiyo hayo sasa yameletelezea kutengeneza mipango yetu ya maendeleo ya miaka mitano mitano hadi 2025, wa kwanza ilikuwa kuboresha hali ya maisha ya Watanzania kwa maana ya kuondoa umaskini; ya pili ilikuwa ni kuwepo kwa mazingira ya amani, usalama na umoja; ya tatu ilikuwa kujenga utawala bora; ya nne ni kuwepo jamii iliyoelimika vyema na inayojifunza na ya tano ilikuwa kujenga uchumi imara unaoweza kukabiliana na ushindani kutoka nchi nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka kuuliza katika mipango yote hii inayofanywa Awamu kwa Awamu ni upi ambao uko nje ya mikakati hii ya malengo haya? Hakuna na zaidi ya hapo pamoja ya kuweka malengo haya, tuliweka vilevile utekelezaji wake utakuwaje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulipanga kabisa tutaanza na nini, tutamaliza na nini, na systematically tumekuwa tukifanya hivyo, tumeweka kwanza mikakati ile ambayo itawezesha malengo haya kutekelezwa, tukaweka namna ya kufikia mikakati hiyo, tukaweka jinsi ya kutathmini tumefikia wapi na tunaendelea kurekebisha kadri tunavyokwenda. Sasa kwenda kuwaambia wananchi kuwa oooh, Stiegler’s Gorge sijui imetoka wapi, haijulikani hata ilikotokea, ooohh sijuii hii, hii Strategic Railway imetokea wapi siyo kweli, nendeni kwenye documents za Serikali hii miradi yote ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunachoweza kusema sasa nakushauri Serikali ni kuwa kwanza itekelezwe kwa wakati, kwa sababu tunachelewa, kama nchi tunachelewa, tumeambiwa tunatakiwa tushindane na nchi nyingine, hatuwezi kushindana bila kuwa na miundombinu ya kimkakati kama hii, hatuwezi kushindana kama hatuna sera zinazoweza kuongoza biashara zetu zifanyike vizuri, hatuwezi kushindana kama hatuwezi kuboresha mazao yetu na kuyauza katika masoko ya ndani na ya nje, sasa hivi vyote ni vitu ambavyo vinafanywa na Serikali kwa ajili tu ya kuhakikisha kuwa tunafika kule tunakokwenda kufuatana na dira yetu ya maendeleo ya 2000/2025. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nataka kusema tu wananchi wetu wa Tanzania wapuuze upotoshwaji huu unaofanywa, aidha, ni kwa makusudi au kwa kutokuelewa, lakini baada ya kusema hayo naomba sasa niingie katika suala zima la bajeti yenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naipongeza Serikali kwa kuangalia sasa yale mambo ambayo sisi tumekuwa tukiyalalamikia sana hasa yale ambayo yanahusu uendeshwaji wa biashara au uwekezaji nchini. Ni kweli Serikali imetambua kama kuna mambo mengi ambayo yamekuwa hayaendi vizuri na wakachukua hatua za kurekebisha. Kuna suala ambalo limezungumzwa hapa la tozo, tunafurahi sana kwa tozo nyingine zimeongezwa ili kulinda viwanda vya ndani, tozo nyingine zimeondolewa ili kuhakikisha kuwa ufanisi unapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa ninaomba Serikali iende mbali zaidi, unaweza ukatoa tozo au ukaongeza tozo ya mali inayoagizwa kutoka nje ili kiwanda cha ndani kichangamke au kifanye vizuri zaidi. Lakini bila kuangalia vile vikwazo na changamoto ambazo vinaathiri vile viwanda vya ndani kukua au kufanya kazi kwa ufanisi, tukajikuta sasa tumesababisha upungufu wa bidhaa kwa sababu bidhaa za ndani hazizalishwi. Je, Serikali imetazama hayo? Tunapozungumzia bidhaa kwa mfano za kilimo na uchakataji mazao, tumeangalia sasa uwezo wa viwanda vya ndani kuchakata mazao ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kutoa mfano mdogo tu kwa Mkoa wangu wa Songwe, tunazalisha sana mazao mengi ya kila aina na hivi karibuni tulituma ujumbe DRC Congo kutafuta soko. Wakatuhakikishia kuwa wao wanaweza kununua unga mwingi sana kutoka kwetu, unga wa mahindi na mchele. Tulivyorudi Mkoa wa Songwe tukajikuta kuwa hatuna viwanda vya kutosheleza ile order ambayo watu wa Congo wanaitaka, sasa hiyo ni changamoto. Kwa hiyo, unaposema labda unaondoa hivi kurahisisha viwanda vya ndani na bila kuangalia kama viwanda vya ndani vimewezeshwa ipasavyo tunaweza tukajikuta tumekwama.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika tukija hata kwenye hata hizi taulo za kike, tunaipongeza Serikali kuwa imegundua kuwa ile tozo lililokuwa limeondolewa ilikuja kunufaisha wafanyabiashara lakini taulo zile ziliendelea kuuzwa kwa bei ile ile ya zamani. Dawa kweli ni kuhakikisha kuwa tozo inarudi, lakini tozo inarudi, viwanda vya ndani vitaweza kuzalisha taulo zile za kutosha ili kufidia pale ambapo tunakosa na vilevile kwa bei ambayo itakuwa nafuu? Kwa sababu ilionekana pamoja na hayo bado bei ya zinazoagizwa kutoka nje ilikuwa ni bei ya juu.

Kwa hiyo, tulikuwa tunataka sana tuangalie zile malighafi zinazoingia katika kutengeneza zile taulo za kike zinaweza kuwa siyo pamba peke yake, kuna kile kitambaa cha kuhifadhia ambacho ndiyo kinasababishia ile taulo kuwa taulo jinsi inavyoitwa, tunacho sisi hapa Tanzania? Kama kinaagizwa, je, Serikali iko tayari kuondoa sasa tozo kwenye hiyo kwa ajili ya viwanda vinavyotengeneza hizo taulo za kike ili mwisho wa siku watoto wetu waweze kupata hizo taulo kama wanavyohitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakwenda mbio, hiyo ni kwa bidhaa nyingine zote ambazo zimewekewa tozo. Kwa mfano viberiti, dawa za meno, chuma kwa ajili ya misumari, sausage, peremende, chewing gum, chocolate, biscuits, maji. Kwa nini tumeongeza ushuru kwenye maji ya kunywa ilhali tunajua maji tuliyonayo Tanzania bado hatuna uhakika wa usalama wake kutokana na miundombinu ya maji bado haijatengemaa. Kwa hiyo, tulitaka Serikali itusaidie kuangalia hizi tozo ambazo nyingine zimeongezwa nyingine zimetolewa, je, zinatosheleza kKuhakikisha kuwa viwanda vyetu sasa vitaweza kuzalisha ili tupate bidhaa ndani ya nchi zinazotokana na viwanda vyetu kwa uhakika, kwa wakati na zenye ubora unaohitajika?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala zima la kilimo, hili litaendelea kujirudia kwa sababu ndiyo uti wa mgongo. Tunapozungumzia uti wa mgongo, kweli kilimo ni uti wa mgongo. Hebu Serikali iangalie sasa jinsi ambavyo itaruhusu kilimo cha kisasa, kilimo cha kibiashara, cha wakulima wakubwa, kwa kuweka urahisi kwao kuwekeza katika nchi yetu. Tuna ardhi nzuri sana, tuna mvua nyingi sana lakini wawekezaji wakubwa wa kilimo hawaji, kwa nini? Ni kwa sababu bado hatujaweka mifumo mizuri ya kuwapa uhakika wao kuwekeza na bila kusumbuliwa baada ya kuwa wamewekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mabonde mengi ambayo tunaweza tukalima mpunga, tunaweza tukalima ngano kwenye maeneo ambayo yanalima ngano, tuna maeneo mengi ya kilimo cha kila aina mboga mboga, lakini kwa nini hatuwekezi vya kutosha. Kwa sababu bado kuna changamoto...

NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa, ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania wa Mwaka 2018
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwa ufupi Muswada huu uliopo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu ni sehemu muhimu sana ya jamii yetu na kwa kweli wanapaswa kuthaminiwa kwa kiasi kikubwa sana. Ila nina tatizo kidogo baada ya kupitia huu Muswada kutofautisha sasa majukumu ambayo yanalengwa kufanywa na hii Bodi tunayotaka kuiunda na ile Teachers Service Commission. Naona kuna maeneo mengi ambayo yanafanana na mpaka najiuliza sasa nani atafanya nini na nani ataacha kufanya nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiria kuna haja ya kuangalia jinsi ambavyo aidha tuta-harmonize hiyo Teachers Service Commission tukaingiza hivi vitu ambavyo ni vipya kwenye Bodi vikaingia kule, au kama
alivyopendekeza Mheshimiwa Balozi Kamala basi tupitishe hii lakini tukiwa na mawazo ya kuja kutengeneza Professional Board ambayo itazingatia tu masuala yanayohusiana na kukuza taaluma ya ualimu kwa maana jinsi ambavyo wao wenyewe watakuwa na viwango vya juu vya weledi lakini vilevile vya kufundishia na watakuwa na njia ambazo watakuwa wanafanyiwa tathmini wa kuona jinsi gani ambavyo wanatenda kazi zao kwa njia ambayo inazingatia viwango ambavyo tunavitegemea kwa ajili ya elimu ya watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ina maana kuwa lazima sisi wenyewe tuwe na taasisi ambazo zinawafundisha vizuri walimu wenyewe ili na wao waje kufundisha vizuri watoto wetu. Hii naiona kuwa ni changamoto ambayo sasa hivi ndiyo inayotukabili. Suala la kuwa na viwango, taaluma ambayo inatambulika kwa walimu naona ni muhimu sana hasa kwa sasa hivi ambavyo tunajua kuna mabadiliko mengi yanayotokea duniani, kuanzia utandawazi na masuala ya mabadiliko ya teknolojia na mahitaji mengi ya Taifa letu au dunia kwa ujumla la maendeleo ambayo yanajitokeza. Hii lazima tuiangalie kwa uangalifu, wengi wamezungumza kuwa tuna taasisi nyingi zinasimamia walimu na kuna nyingi ambazo unaona kuna kazi zinaingiliana, kwa kweli tusipoangalia tutajikuta tunaongeza mzigo wa taasisi lakini tija itakuwa siyo ya kutosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa sana kuona Muswada huu unajikita kwenye jinsi gani tunawasaidia hawa walimu kufikia hivyo viwango. Naona tumezungumzia zaidi leseni, usajili, nidhamu na jinsi ya kuwawajibisha lakini sioni mahali ambapo tunazungumzia tunawaboresha vipi wao wenyewe ili wafikie hivyo viwango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua hata Professional Boards nyingine wana viwango vyao ili uweze kuhesabiwa kuwa wewe ni professional na ukawa registered kwenye hiyo board kuna hatua ambazo unachukua. Hapa sijui tutaangalia kitu gani, tutaangalia jinsi anavyofundisha darasani, elimu yake, nidhamu, jinsi ambavyo ni mbunifu katika kuweka mikakati ya kufundishia vizuri zaidi kwa watoto ambao labda wana matatizo maalum au tutaangalia kitu gani ili tuseme kuwa huyu sasa ndiyo anafaa kupewa leseni au usajili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumekuwa na mabadiliko mengi sana katika sekta yetu ya elimu. Ssijui katika kuleta Muswada huu mbele yetu tumeangalia sasa mambo yote haya, hizi reforms mbalimbali ambazo zimekuwa zikijitokeza na tumezi-incorporate katika Muswada huu ili sasa tuunde kitu ambacho kinazingatia yale mambo yote madogomadogo ambayo yamekuwa yakifanyika overtime katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi kwangu ni lazima utambuzi wa viwango uwe ni wa kisayansi zaidi, usiwe unaotokana na Bodi labda au watu walioko kwenye Bodi. Tuwe tuna vigezo vya kisayansi vinavyotokana na hii tasnia ya ualimu ambavyo mtu yeyote akiviona anaweza kusema huyu amekidhi au huyu hajakidhi. Isiwe ni kitu ambacho ni subjective kwa sababu naanza kuona hofu ya kuwa inaweza kuwa tu mtu fulani akaona hiki kwa mtazamo wake yeye kiko hivi akaona hakifai au kinafaa kumbe sivyo. Kwa hiyo, nataka ningeiona hiyo inajitokeza, kuwa vigezo vitakuwa ni hivi, mtu atakuwa anatakiwa awe amesomea hivi na hivi na atakuwa ana ufaulu huu na huu ndiyo sasa atatambulika kuwa sasa huyu ni professional na huyu ndiyo anapaswa kupata leseni na registration.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengi ambayo yamezungumzwa hapa. Kuna walimu wengine tumesikia hapa walimu wa kijitolea wamemaliza form six na form four wanajitolea na tunasikia kuna wahadhili ambao hawajasomea ualimu lakini wenyewe ni wataalam wa fani zao wanawekwa kuwa walimu, hivi vyote lazima vianishwe katika huu Muswada. Je, hawa watakuwa treated vipi, sasa watakuwa hawafundishi tena ama vipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna suala la shule za private sijalielewa vizuri, walimu wa shule za private na wao watafanyiwa registration na scrutiny ni hii au wao wanaachwa peke yao, wako nje au ndani ya huu mfumo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia masuala ya kuunganisha masuala ya hii professionalism tunayoitafuta hapa na masuala mengine yote ambayo yapo katika taasisi mbalimbali ambazo zimeundwa kwa ajili ya walimu. Hii itasaidia sasa kuja na kitu ambacho kinazungumza lugha moja. Wengine wametoa mifano hapa kwamba unaweza ukakuta kwenye TSC kuna jambo tofauti, ukaja kwenye Bodi yanakuwa tofauti kukawa kuna mgongano halafu maamuzi yakashindikana kupitishwa au yakapitishwa yakawa yanakiuka sheria ya upande mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuuliza kwanza tunavyozungumzia kuwawekea walimu huu utaratibu wa kuwa na Bodi yao ya professionalism, tunaweza kuoneshwa wapi ambako tunawaandaa sasa wakaelewa kuwa, sasa hivi huko tunakoelekea, ili upate leseni lazima uwe umekidhi viwango hivi na hivi na tunapowawekea viwango hivyo tuna matayarisho gani ya kuwafikisha hapo? Kwa sababu walimu lazima waendelezwe, wapate fursa za kujiendeleza na kuendelezwa, wapate misaada mbalimbali katika kazi zao wakiwa kazini au nje ya utaratibu wa kazi, lakini lazima wajengewe huo uwezo wa kufikia hiyo professionalism au hizo professional standards zinazotegemewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nataka kuuliza kama swali, hili suala la nidhamu ambalo naona kwa kiasi kikubwa sana ndilo lililotazamwa humu ndani, TSC na wenyewe wanalisimamia kipengele kwa kipengele. Sasa sijui sasa hivi suala la nidhamu na maadili ya walimu tutaliacha TSC au litahamia Bodi? Kama litahamia Bodi, TSC watakuwa wanafanya kazi gani? Kwa hiyo, nakuta kuna vitu vimeingiliana sana ambapo inanipa wasiwasi kama hii Bodi siyo duplication ya TSC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mapendekezo tu kwa kiasi fulani. Nafikiri tunapozungumzia kuwa na walimu bora ambao wana viwango vinavyohitajika na kuwa tunapata wanafunzi bora huku nyuma lazima kuwe kuna sehemu ya tatu inayozungumzia kuwawezesha hawa walimu kufikia hapo wanapotakiwa. Tuna haja sasa ya kuhakikisha kuwa teachers training inayotolewa kwa walimu inalingana na viwango tunavyotegemea kwenda kuviona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile lazima kuwe na vigezo maalum ambavyo vinatambuliwa globally, East Africa au Nationally kuwa hiki kweli ni kiwango ambacho huyu amekifikia na lazima apate leseni otherwise iwe hakukipata. Pia iwe rahisi walimu kufikia hivi viwango ambavyo tumeviainisha kwenye Bodi, isiwe tena ni kazi ngumu sana mwalimu kufikia huko. Kwa mfano, mwalimu anapotaka kwenda kujiendeleza, je, ni rahisi kiasi gani yeye kwenda kujiendeleza kwenye fani ambayo anaitegemea kwa sababu anajua ndiyo itakayomfikisha katika kiwango? Je, walimu wanaweza kupata scholarships? Je, walimu wanaweza kupata leave of absence waende wakasome? Je, walimu wanaweza wakapata usaidizi hata kama ni mikopo kwa ajili ya kujisomesha? Hivi vyote lazima viendane na utaratibu ambao tunataka kuunda, lazima kuwe kuna uwezeshwaji. Walimu wengi sasa hivi wanajihangaikia wenyewe. Kuna mtu kazungumzia kuku wa kienyeji, sijui kama ni sahihi, lakini ninachosema mimi ni kwamba wanaachiwa wahangaike wenyewe, lakini hata wakihangaika bado wakirudi hawapati stahiki zile ambazo zinahitajika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua huu Muswada hauzungumzii stahiki za walimu, lakini hivi vitu vinaendana. Mtu hawezi kuona sababu ya kuhangaika kwenda kujiendeleza na kufundisha vizuri zaidi na kutengeneza mikakati maalum ya kufundishia ambayo ni ubunifu wake mwenyewe kama hakuna mahali atakapopata recognition ambayo ni sahihi na ambayo anastahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka kusema kuwa huu Muswada unaweza kuwa ni mzuri lakini unahitaji maboresho mengi sana kadri ambavyo tumesikia uchangiaji kila upande umezungumzia. Huu Muswada sitaki kusema umewahishwa lakini naweza kusema labda haujaiva vizuri sana. Kwa hiyo, nataka kuomba, kama inawezekana tuuangalie vizuri zaidi kama utarudishwa kwenye Kamati, kama utarudishwa wapi ili ukaboreshwe. Kwa sababu naona una mwingiliano sana na Kamisheni nyingine za Walimu ambazo tayari tunazo, sasa hiyo inaweza kuwa ni tatizo tunavyoendelea mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii. Pia namshukuru Mungu kwa kutuamsha salama na kutufikisha hapa. Nami naomba nichangie mambo machache juu ya hii hotuba ya Mheshimiwa Profesa Maghembe. Nataka kuwapongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa hotuba nzuri iliyosheheni masuala mbalimbali ya maendeleo ya utalii na uhifadhi katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kusikitika juu ya bajeti ya Wizara hii. Wizara hii ni kati ya Wizara ambazo zinachangia pato kubwa sana kwa nchi yetu na ina fursa kubwa sana ya kuchangia pato letu la Taifa, lakini ni Wizara ambayo vilevile haitendewi haki inapokuja kwenye bajeti. Bajeti yake haiendani na uwezo wa Wizara hii kuiletea nchi yetu mapato. Wizara hii haitengewi bajeti ya kutosha kwa utangazaji, tumeona mifano mingi ya nchi jirani na nchi nyingine duniani kiasi ambacho wanatenga kwa ajili ya utangazaji peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuna vivutio vingi sana na tunapenda kujikumbusha kila mara, lakini vivutio hivyo tunavijua sisi tuliomo humu ndani, walioko nje ambao wanatakiwa kuja kuvifaidi hawavitambui. Kwa hiyo, ni muhimu kwa Serikali kuhakikisha kuwa matangazo yanapewa bajeti na profile ya kutosha ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha watalii wanavutiwa kuja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia utalii wa ndani. Bado utalii wa ndani haujapewa kipaumbele au haujazingatiwa. Sisi Watanzania vile vile tunaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa sana utalii wa ndani. Kama hiyo haitoshi, Maafisa Maliasili walioko katika wilaya hawazitendei haki fursa za utalii zilizoko katika wilaya zetu. Karibu wilaya zote zina nafasi na fursa za vivutio vya utalii, lakini inaonekana yanazingatiwa maeneo makubwa makubwa tu ya Kaskazini, hifadhi za wanyama lakini hatuangalii utalii wa aina nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija katika Mkoa wangu wa Songwe peke yake kuna vivutio vingi sana vya utalii. Kuna vijito au chemichemi za maji ya moto, hicho ni kivutio cha kutosha. Tuna kimondo Mbozi ni kivutio cha kutosha. Zamani tulikuwa tunasikia kinatajwatajwa sasa hivi hata kutajwa hakitajwi tena. Mikoa yetu sisi ni ya milima na mabonde ambayo ni mizuri sana kwa utalii wa kijiografia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watalii wengi wanapenda kupanda milima, trekking na camp sites. Watalii wengi wanapenda sana kuja kuangalia mazingira yetu jinsi tunavyoishi. Kwa hiyo, hivi vyote ni vivutio ambavyo vingepaswa kuendelezwa ili vilete kwanza ajira kwa wananchi walioko pale lakini vilevile vituletee mapato kwa ajili ya nchi yetu na kupanua wigo wa utalii ambao unapatikana kwenye nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika vilevile kuwa katika mradi au mpango wa BRN utalii haupo wakati tunajua kabisa kuwa ni chanzo kikubwa cha mapato. Napenda Serikali ituambie huo mpango wa BRN kwa nini umeacha utalii nje na kuacha kuushughulikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la miundombinu ya utalii, kuna matatizo makubwa ya miundombinu ya utalii kwa mfano barabara, hoteli katika maeneo mbalimbali ambayo watalii wanatakiwa kufikia hata katika Mlima Kilimanjaro. Tumesikia na wale waliopanda mlima ule wameona, vile vibanda vinavyotumika kufikia wageni havifai, sasa hivi vinatakiwa viboreshwe kwa kiasi kikubwa, kuna masuala ya vyoo na sehemu za kupumzika zote hazifai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mlima Kilimanjaro ni kivutio kikubwa dunia nzima na wageni wanaokuja pale ni wengi sana kwa nini isitengwe fedha kutokana na Mlima Kilimanjaro peke yake kwa ajili ya kuboresha ile miundombinu ya kutumika kwenda kupanda? Vilevile Watanzania wengi wahamasishwe na wawezeshwe kwenda kupanda Mlima Kilimanjaro, mlima uko kwenye nchi yao lakini wao wenyewe hawajaupanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia vilevile ufugaji wa nyuki na uhifadhi wa mazingira. Tanzania ni nchi ya pili Afrika kwa kuzalisha asali lakini hata kiwango ambacho asali hiyo inazalishwa bado ni kidogo sana. Tuna uwezo wa kuzalisha asali nyingi sana Tanzania, lakini Maafisa Maliasili wetu wala hili hawalizingatii. Wanakimbizana na kuuza magogo tu na kukata miti tu, jamani sasa hivi warudi kuzingatia mambo ya utalii katika maeneo yetu, lakini vilevile ufugaji wa nyuki na upandaji wa miti. Hii ndiyo njia pekee ambayo kwanza itatuletea uhifadhi lakini vilevile itatuwezesha kufuga nyuki wengi na kupata pato kubwa na kwa vijana wetu ufugaji wa nyuki ni ajira nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kurudi kwenye suala la Bodi ya Utalii. Pamoja na malalamiko kuwa haipati fedha ya kutosha lakini bado na yenyewe haitumii ubunifu wa kutosha. Kuna mambo mengine bodi inaweza kufanya bila kutegemea fedha nyingi. Nchi yetu mara nyingi inashiriki kwenye maonesho nchi za nje, ya kibiashara, mikutano mikubwa ya Kimataifa na maonesho ya mambo mbalimbali, hizi ni fursa zinazoweza kutumika vilevile katika kutangaza utalii wetu. Tuna fursa vilevile za sisi wenyewe kukusanya watu nje ya nchi, wafanyabiashara au watalii wenyewe, ma-agent wa utalii kuja katika maonesho hayo ili tuoneshe nini tunacho ili waweze kuvutiwa. Hili suala naona bado halijatiliwa mkazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mheshimiwa jana alisema kuwa ni wavivu, mimi naweza nikakubaliana naye, kwa sababu uvivu ni pamoja na kutokuwa mbunifu. Kama umepewa majukumu lazima uyatendee haki majukumu yako kwa kuhakikisha unajituma kwa kiasi kikubwa ili nchi yako ikafaidike. Hatuwezi kuendelea kuimba nyimbo za kuwa sisi tuna vivutio vingi wakati vivutio hivyo hatuviendelezi wala havituletei faida yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuongezea ningependa kutoa pendekezo kuhusiana na miundombinu ya hoteli. Tunasema kuwa sisi tuna upungufu mkubwa wa vitanda ndiyo maana watalii hawaji kwa wingi. Nataka kutoa pendekezo ambalo naomba lifikiriwe kuwa, mifano imeonekana kwa nchi nyingine kwa mfano Zambia, walitoa msamaha wa kodi na ushuru kwa wale wanaokuja kuwekeza kwenye hoteli za nyota tatu mpaka tano kwa kipindi cha miaka miwili wakati wanajenga na baada ya kumaliza ujenzi wakati wa kuanza ku-operate zile hoteli ndiyo wakaanza kulipishwa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengi sana walijitokeza kujenga hoteli katika sehemu mbalimbali za utalii na sasa hivi Zambia wanapata watalii wengi. Hebu na sisi tulitafakari hilo, tulifanyie mahesabu tuone, je, itatugharimu kiasi gani kwa muda wa miaka miwili, mitatu kuachia wawekezaji wajenge kwa misamaha maalum, baada ya hapo tuanze kuwatoza kodi inayostahili na tutahakikisha kuwa tunapata watalii wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwa hoteli zilizopo ziboreshwe, watenda kazi wafundishwe jinsi ya kuhudumia wageni ili tuweze kuwa na ubora unaohitajika kwa sababu tunalalamika sana kuwa wanakuja wageni kuja kufanya kazi katika hoteli zetu lakini ni kwa sababu wafanyakazi wetu labda hawajapata ujuzi wa kutosha jinsi ya kuhudumia watalii na kutoa huduma ambazo zinafaa kuvutia watalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja hii, lakini naomba yote ambayo tumeyatoa hapa yakazingatiwe. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri Mheshimiwa Maghembe, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Maofisa Watendaji wa Wizara hii kwa hotuba nzuri na mipango mizuri ya kuboresha shughuli za Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ina vivutio vingi vya utalii, lakini kwa uzoefu wa muda mrefu utalii huu umeonekana kuwa ni kwa ajili ya wageni tu wanaokuja Tanzania kufanya ziara za utalii nchini. Iko haja sasa kwa Wizara kuhamasisha utalii wa ndani ili na Watanzania nao wafaidi utalii na Taifa lipate kipato kutokana na hili. Serikali iweke mikakati mahsusi ya kuwavutia Watanzania wengi zaidi kushiriki katika utalii wa ndani. Makundi mbalimbali ya kijamii yawekewe vivutio na mikakati ya kutembelea maeneo ya utalii. Wizara kupitia Maofisa Maliasili waandae ratiba katika maeneo waliyomo ili watembelee vivutio vilivyo karibu na maeneo yao. Hii itajenga utumiaji wa utalii kidogo kidogo hadi hili lizoeleke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wapewe hamasa wakatembelee vivutio hivyo pamoja na kupanda Mlima Kilimanjaro na kufaidi mlima wetu ulioliletea sifa kubwa Taifa letu. Niwahimize Serikali kuwekeza kwenye matangazo ya ndani kwa kutangaza vivutio vilivyomo nchini ili wananchi watamani kuvitembelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuibua mazao mengine tofauti ya utalii ili kuvutia utalii zaidi, kushirikisha maeneo mengi zaidi na wadau wengi nchini kwenye shughuli za utalii na kujenga ajira na kuongeza mapato ya wananchi na Taifa kwa ujumla maeneo mengi ya Tanzania hasa ya milimani, kwenye maporomoko ya maji kuna fursa nzuri ya utalii wa jiografia kama mountain trekking, hiking, photographic tourism, cultural tourism na kadhalika. Utalii huu unaofanywa na jamii, vijiji na watalii wanapendelea kujifunza juu ya maisha yetu na utamaduni wetu. Ileje na Mkoa wa Songwe kwa ujumla wana fursa nyingi za cultural geographic tourism na Serikali iangalie jinsi ya kuboresha aina hii ya utamaduni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ileje ina misitu yenye aina ya nyani wa kipekee black and white collobus ambaye hapatikani sehemu nyingine yoyote. Mapori ya Kitulo yana aina ya maua ya orchids ambayo aina yake hazipatikani sehemu nyingine yoyote. Songwe, Mbeya na Nyanda za Juu Kusini kuna fursa nyingi sana za utalii kuanzia Udzungwa, Ruaha, vinajenga utalii wa Southern circuit, kwa hiyo Serikali sasa ihamishe nguvu kwenda kuendeleza utalii katika Southern circuit na ijumuishe aina zote za utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mikoa ya Songea na Mbeya wana utamaduni wa ngoma za kimila nzuri sana ambazo zingeweza kuwa sehemu ya utalii wa kiutamaduni. Hii ni fursa ya ajira kwa wananchi na mapato kwa Taifa. Nataka kuhamasisha Serikali kupitia Maofisa Maliasili wa Wilaya kuhakikisha kuwa wanaanza kuangalia utalii vilevile kwenye maeneo yao badala ya kujikita kwenye magogo na mazao ya misitu peke yake.
Watanzania wenzangu tubadilike na tuanze kushiriki utalii wa ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bajeti ya utangazaji wa utalii ni ndogo sana Tanzania ukiilinganisha na nchi jirani. Changamoto kubwa ya kukua kwa utalii nchini ni kukosa kufanya utalii vya kutosha. Vivutio vya utalii vitangazwe zaidi kwa watalii wa ndani na wa nje ili vivutio vifahamike na watalii waongezeke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii ni ndogo sana ukiitazama kuwa Tanzania inaongoza kwa vivutio vya utalii na kuliingizia Taifa pato kubwa. Inasikilitisha sana kuwa bajeti ya Wizara hii ni ndogo wakati Taifa linategemea sana sekta hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya utalii haipo kwenye mpango wa BRN pamoja na sekta hii kuchangia pato kubwa la Taifa. Hii ni hitilafu kubwa na inatakiwa irekebishwe haraka na Serikali itoe tamko juu ya mikakati yote hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna haja ya kuongeza uwekezaji katika vivutio vya utalii kwa mfano kuna huduma hafifu hasa vituo vya kufikia watalii kama hoteli, huduma ya kwanza kwenye vivutio kama Mlima Kilimanjaro. Huduma ya vyoo vizuri na sehemu za kupumzika. Gharama za kupanda Mlima Kilimanjaro ni kubwa na wananchi wa kawaida watashindwa kufaidi. Upatikanaji wa chupa za oxygen karibu na kileleni, kuwezesha Watanzania kuwekeza kwenye miradi ya utalii katika ngazi zote Wilayani. Serikali itoe tamko juu ya mkakati wa kuendeleza utalii katika ngazi ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ufinyu wa bajeti bado Bodi ya Utalii haifanyi kazi kwa kujituma, ubunifu wa maarifa yako mengi wangeweza kufanya kwa kutangaza utalii kwa kushirikisha wadau kwenye maonyesho ambayo watalipia wenyewe au kutumia fursa za maonyesho mengine na mikutano mikubwa ya Kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itoe kipaumbele kwenye kujenga miundombinu mizuri katika maeneo ya kitalii. Serikali imefanya nini katika mbinu kuhakikisha wanaweka kipaumbele kuonesha miundombinu ya biashara na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kupendekeza kuwa Serikali iondoe kwa miaka mitatu kodi na ushuru kwenye uwekezaji katika mahoteli ya kitalii, kuruhusu wawekezaji kujenga hoteli za kitalii za kiwango cha nyota tatu hadi tano. Katika kipindi chote cha ujenzi mwekezaji asitozwe chochote akimaliza na uendeshaji ukiaanza atozwe asilimia 15 mwaka wa kwanza na ikifika mwaka wa tatu wa uendeshaji alipe kodi zote, hii itaiwezesha Tanzania kupata vitanda vinavyotosheleza mahitaji na kupata watalii wengi. Pia hoteli zilizopo waboreshe miundombinu na huduma kwa kupatiwa mafunzo na wafanyakazi wenye uwezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ufugaji wa nyuki, Tanzania ina fursa sana na nzuri za kuzalisha asali kwa wingi duniani ambayo ikitumiwa ipasavyo itasaidia kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla. Tanzania ni nchi ya pili Barani Afrika na inazalisha tani 56,000. Hata hivyo, kiwango hicho ni kidogo kwa sababu Tanzania ina uwezo wa kuzalisha asali tani milioni 1,038 kwa mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa ninaloliona ni utashi hafifu wa jamii kujishughulisha na kazi za ufugaji nyuki na kupanda miti kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira. Serikali kupitia Maafisa Maliasili wahamasishe vya kutosha jamii juu ya faida ya ufugaji nyuki na upandaji miti ili ilete matokeo ya haraka kwa sababu asali ina faida kubwa ikiwemo ya kiafya na kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ihakikishe teknolojia ya kisasa inatumika kwenye ufugaji wa nyuki na kupanda miti. Idara ya Misitu iachane na shughuli za uchuuzi wa magogo na ukataji miti kiholela na badala yake wajikite kwenye upandaji miti ya kibiashara na kuhifadhi mazingira na hivyo hudumisha mazingira bora ya kuishi pamoja na ufugaji wa nyuki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Songwe na eneo lote la Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini, Rukwa kuna fursa kubwa sana kupanda miti na kufuga nyuki na hata kuendeleza utalii wa kitamaduni, kijiografia ki-photographic kuwepo kwa kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Songwe ni fursa kubwa ya kuboresha utalii na uhifadhi wa misitu na kukuza utalii katika Sourthen circuit.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaitaka Serikali kupitia Wizara hii kutumia Idara ya Misitu kutusambazia miche ya miti na mizinga ya nyuki ya kisasa. Pia kushirikisha sekta binafsi katika utalii kwa kupunguza tozo nyingi zinazowazidishia gharama na kupunguza idadi ya watalii.
Lakini pia kuunganisha watalii na wajasiriamali wadogo wadogo wanaotoa huduma na kutengeneza bidhaa za sanaa na kuwauzia watalii, kutoa mafunzo unganishi yatakayoweka programu za mafunzo, kuwatayarisha wananchi kwa pamoja kati ya sekta ya umma na binafsi ili ushiriki wa jamii ya wafanyabiashara na wafanyakazi wa maeneo hayo kwenye shughuli za utalii na uhifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na ninaunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri Mheshimiwa Maghembe, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Maofisa Watendaji wa Wizara hii kwa hotuba nzuri na mipango mizuri ya kuboresha shughuli za Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ina vivutio vingi vya utalii, lakini kwa uzoefu wa muda mrefu utalii huu umeonekana kuwa ni kwa ajili ya wageni tu wanaokuja Tanzania kufanya ziara za utalii nchini. Iko haja sasa kwa Wizara kuhamasisha utalii wa ndani ili na Watanzania nao wafaidi utalii na Taifa lipate kipato kutokana na hili. Serikali iweke mikakati mahsusi ya kuwavutia Watanzania wengi zaidi kushiriki katika utalii wa ndani. Makundi mbalimbali ya kijamii yawekewe vivutio na mikakati ya kutembelea maeneo ya utalii. Wizara kupitia Maofisa Maliasili waandae ratiba katika maeneo waliyomo ili watembelee vivutio vilivyo karibu na maeneo yao. Hii itajenga utumiaji wa utalii kidogo kidogo hadi hili lizoeleke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wapewe hamasa wakatembelee vivutio hivyo pamoja na kupanda Mlima Kilimanjaro na kufaidi mlima wetu ulioliletea sifa kubwa Taifa letu. Niwahimize Serikali kuwekeza kwenye matangazo ya ndani kwa kutangaza vivutio vilivyomo nchini ili wananchi watamani kuvitembelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuibua mazao mengine tofauti ya utalii ili kuvutia utalii zaidi, kushirikisha maeneo mengi zaidi na wadau wengi nchini kwenye shughuli za utalii na kujenga ajira na kuongeza mapato ya wananchi na Taifa kwa ujumla maeneo mengi ya Tanzania hasa ya milimani, kwenye maporomoko ya maji kuna fursa nzuri ya utalii wa jiografia kama mountain trekking, hiking, photographic tourism, cultural tourism na kadhalika. Utalii huu unaofanywa na jamii, vijiji na watalii wanapendelea kujifunza juu ya maisha yetu na utamaduni wetu. Ileje na Mkoa wa Songwe kwa ujumla wana fursa nyingi za cultural geographic tourism na Serikali iangalie jinsi ya kuboresha aina hii ya utamaduni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ileje ina misitu yenye aina ya nyani wa kipekee black and white collobus ambaye hapatikani sehemu nyingine yoyote. Mapori ya Kitulo yana aina ya maua ya orchids ambayo aina yake hazipatikani sehemu nyingine yoyote. Songwe, Mbeya na Nyanda za Juu Kusini kuna fursa nyingi sana za utalii kuanzia Udzungwa, Ruaha, vinajenga utalii wa Southern circuit, kwa hiyo Serikali sasa ihamishe nguvu kwenda kuendeleza utalii katika Southern circuit na ijumuishe aina zote za utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mikoa ya Songea na Mbeya wana utamaduni wa ngoma za kimila nzuri sana ambazo zingeweza kuwa sehemu ya utalii wa kiutamaduni. Hii ni fursa ya ajira kwa wananchi na mapato kwa Taifa. Nataka kuhamasisha Serikali kupitia Maofisa Maliasili wa Wilaya kuhakikisha kuwa wanaanza kuangalia utalii vilevile kwenye maeneo yao badala ya kujikita kwenye magogo na mazao ya misitu peke yake.
Watanzania wenzangu tubadilike na tuanze kushiriki utalii wa ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bajeti ya utangazaji wa utalii ni ndogo sana Tanzania ukiilinganisha na nchi jirani. Changamoto kubwa ya kukua kwa utalii nchini ni kukosa kufanya utalii vya kutosha. Vivutio vya utalii vitangazwe zaidi kwa watalii wa ndani na wa nje ili vivutio vifahamike na watalii waongezeke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii ni ndogo sana ukiitazama kuwa Tanzania inaongoza kwa vivutio vya utalii na kuliingizia Taifa pato kubwa. Inasikilitisha sana kuwa bajeti ya Wizara hii ni ndogo wakati Taifa linategemea sana sekta hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya utalii haipo kwenye mpango wa BRN pamoja na sekta hii kuchangia pato kubwa la Taifa. Hii ni hitilafu kubwa na inatakiwa irekebishwe haraka na Serikali itoe tamko juu ya mikakati yote hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna haja ya kuongeza uwekezaji katika vivutio vya utalii kwa mfano kuna huduma hafifu hasa vituo vya kufikia watalii kama hoteli, huduma ya kwanza kwenye vivutio kama Mlima Kilimanjaro. Huduma ya vyoo vizuri na sehemu za kupumzika. Gharama za kupanda Mlima Kilimanjaro ni kubwa na wananchi wa kawaida watashindwa kufaidi. Upatikanaji wa chupa za oxygen karibu na kileleni, kuwezesha Watanzania kuwekeza kwenye miradi ya utalii katika ngazi zote Wilayani. Serikali itoe tamko juu ya mkakati wa kuendeleza utalii katika ngazi ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ufinyu wa bajeti bado Bodi ya Utalii haifanyi kazi kwa kujituma, ubunifu wa maarifa yako mengi wangeweza kufanya kwa kutangaza utalii kwa kushirikisha wadau kwenye maonyesho ambayo watalipia wenyewe au kutumia fursa za maonyesho mengine na mikutano mikubwa ya Kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itoe kipaumbele kwenye kujenga miundombinu mizuri katika maeneo ya kitalii. Serikali imefanya nini katika mbinu kuhakikisha wanaweka kipaumbele kuonesha miundombinu ya biashara na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kupendekeza kuwa Serikali iondoe kwa miaka mitatu kodi na ushuru kwenye uwekezaji katika mahoteli ya kitalii, kuruhusu wawekezaji kujenga hoteli za kitalii za kiwango cha nyota tatu hadi tano. Katika kipindi chote cha ujenzi mwekezaji asitozwe chochote akimaliza na uendeshaji ukiaanza atozwe asilimia 15 mwaka wa kwanza na ikifika mwaka wa tatu wa uendeshaji alipe kodi zote, hii itaiwezesha Tanzania kupata vitanda vinavyotosheleza mahitaji na kupata watalii wengi. Pia hoteli zilizopo waboreshe miundombinu na huduma kwa kupatiwa mafunzo na wafanyakazi wenye uwezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ufugaji wa nyuki, Tanzania ina fursa sana na nzuri za kuzalisha asali kwa wingi duniani ambayo ikitumiwa ipasavyo itasaidia kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla. Tanzania ni nchi ya pili Barani Afrika na inazalisha tani 56,000. Hata hivyo, kiwango hicho ni kidogo kwa sababu Tanzania ina uwezo wa kuzalisha asali tani milioni 1,038 kwa mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa ninaloliona ni utashi hafifu wa jamii kujishughulisha na kazi za ufugaji nyuki na kupanda miti kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira. Serikali kupitia Maafisa Maliasili wahamasishe vya kutosha jamii juu ya faida ya ufugaji nyuki na upandaji miti ili ilete matokeo ya haraka kwa sababu asali ina faida kubwa ikiwemo ya kiafya na kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ihakikishe teknolojia ya kisasa inatumika kwenye ufugaji wa nyuki na kupanda miti. Idara ya Misitu iachane na shughuli za uchuuzi wa magogo na ukataji miti kiholela na badala yake wajikite kwenye upandaji miti ya kibiashara na kuhifadhi mazingira na hivyo hudumisha mazingira bora ya kuishi pamoja na ufugaji wa nyuki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Songwe na eneo lote la Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini, Rukwa kuna fursa kubwa sana kupanda miti na kufuga nyuki na hata kuendeleza utalii wa kitamaduni, kijiografia ki-photographic kuwepo kwa kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Songwe ni fursa kubwa ya kuboresha utalii na uhifadhi wa misitu na kukuza utalii katika Sourthen circuit.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaitaka Serikali kupitia Wizara hii kutumia Idara ya Misitu kutusambazia miche ya miti na mizinga ya nyuki ya kisasa. Pia kushirikisha sekta binafsi katika utalii kwa kupunguza tozo nyingi zinazowazidishia gharama na kupunguza idadi ya watalii.
Lakini pia kuunganisha watalii na wajasiriamali wadogo wadogo wanaotoa huduma na kutengeneza bidhaa za sanaa na kuwauzia watalii, kutoa mafunzo unganishi yatakayoweka programu za mafunzo, kuwatayarisha wananchi kwa pamoja kati ya sekta ya umma na binafsi ili ushiriki wa jamii ya wafanyabiashara na wafanyakazi wa maeneo hayo kwenye shughuli za utalii na uhifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na ninaunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JANETH Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa ya kuchangia katika Hotuba ya Wizara hii ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Nachukua fursa hii vile vile kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Balozi Dkt. Augustine Philip Mahiga, Naibu Waziri Dkt. Suzan Kolimba, Katibu Mkuu na watendaji wote kwa hotuba nzuri na taarifa nyingi za muhimu kwetu sisi juu ya utendaji wa Wizara hii muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua umuhimu wa vituo vya utoaji huduma mipakani hasa katika kurahisisha taratibu za uhamiaji, forodha, ukaguzi wa ubora wa bidhaa, usalama na ulinzi. Dhana hii na angalau vituo hivi kule vilikowekwa kwenye mipaka yetu kama Holili, Taveta, Horohoro, Tunduma na Sirari, Kyaka, Rusumo na kadhalika vimeleta matokeo mazuri sana katika maeneo yote tajwa hapo juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Ileje ina kituo muhimu sana kwenye Mto Songwe ambako tunapakana na Malawi kwenye Jimbo la Chitipa. Hata hivyo, inasikitisha kuwa ni miaka 42 tangu Wilaya ya Ileje ianzishwe lakini hakuna jengo, kituo wala miundombinu yoyote inayofaa kwa matumizi ya Serikali kuhakikisha kuwa biashara kubwa inayofanywa kati ya Watanzania na Wamalawi inasimamiwa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile soko lililoko Isongole, mita 100 tu kutoka mpakani, ni dogo kwa mahitaji ya biashara inayoendelea kati ya nchi hizi mbili.
Kwa bahati mbaya soko hilo limegeuzwa kuwa ghala la kuhifadhia mahindi na NFRA, hivyo hali hii imefanya lisitoshe kukidhi haja ya soko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Wizara chini ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki kujenga kituo cha pamoja mpakani na Malawi, pale Isongole ili huduma ziboreshwe maana tayari upande wa Malawi (Chitipa) wana miundo mizuri sana na wanatusubiri sisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukosefu wa miundombinu ya kituo hiki umesababisha wahamiaji haramu kutumia mpaka huu kuingia nchini na kutoka nchini kwenda nchi jirani. Silaha zimekuwa zikipitishwa katika mpaka huu huu na hivi sasa pombe haramu ya viroba ambayo imepigwa marufuku Malawi huingia kwa wingi nchini Tanzania kupitia mpaka huu, na vile vile kujikosesha fursa mbalimbali kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kukosekana kwa kituo hiki cha pamoja na huduma zote muhimu vile vile kunahatarisha usalama na ulinzi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naitaka Wizara itoe tamko ni lini Kituo hiki cha Pamoja cha Forodha kitajengwa pamoja na kuweka taasisi zote muhimu ili Ileje na Taifa zima liweze kufaidika. Kituo hiki kitafanya biashara iongezeke ndani ya Wilaya na hata fursa za uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawasilisha na naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Na mimi napongeza sana hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha, vilevile nataka niishukuru Serikali kwa mara ya kwanza kwa, tangu Wilaya yangu ya Ileje ianzishwe mwaka huu tumetengewa fedha kwa ajili ya barabara kwa kiwango cha lami kutoka Isongole kwenda Mpemba. Napenda kuishukuru sana Serikali kwa jambo hili na kwa kweli, wananchi wa Ileje wanaingojea hii barabara kwa hamu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nizungumzie suala zima la vipaumbele vyetu. Tumesema kuwa tunataka kuboresha kilimo na kimewekwa kabisa katika mpango mkakati wa kuendesha kilimo wa SAGCOT, lakini nasikitika kuwa inapokuja katika kupanga bajeti kilimo hakijapewa ile bajeti ambayo ingestahili kuhakikisha kuwa wananchi wengi ambao ndiyo wamegubikwa na umaskini wangeweza kunufaika kwa kuhakikisha kuwa fedha nyingi inakwenda katika kuhamasisha kilimo bora, ufugaji na uvuvi, ili wananchi wale ambao ndiyo maskini wangeweza kusaidiwa na mpango huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisemi kuwa miundombinu na sehemu nyingine ambazo fedha hizi zimepelekwa hakuhitajiki, vilevile lazima tuangalie sasa hivi nchi yetu bado ni maskini kwa sababu, wananchi wengi hawajaguswa na ukuaji wa uchumi ambao tumeupata, na njia moja kubwa ilikuwa ni kupeleka fedha nyingi katika sekta zile ambazo zinagusa wananchi moja kwa moja na mojawapo ndio hiyo kilimo, ufugaji na uvuvi.
Kwa hiyo, tungependa sana Serikali inapojielekeza katika Mpango wa Maendeleo huko tunakokwenda ihakikishe kuwa zile sekta ambazo ndiyo zinazogusa wananchi na zikawainua kiuchumi ndio zinapewa kipaumbele katika bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kurukia kidogo kwenye masuala ya utalii. Utalii ni sekta muhimu sana katika uchumi wetu na ni sekta ambayo ikisimamiwa vizuri italikomboa hili Taifa, lakini nasikitika kuwa bado kwenye masuala ya utalii hatujatoa vipaumbele vinavyostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona kuwa tumeweka kodi, tumeweka tozo mbalimbali ambazo moja kwa moja hizo zitaongeza gharama za utalii kwenye nchi yetu. Sasa hili wenzetu nchi jirani wameliona na wameziondoa, itabidi katika kuhakikisha kuwa tuna-harmonise hizi kodi za Afrika Mashariki tunaondoa hizo tozo ili kuhamasisha utalii mkubwa zaidi kuja Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la utangazaji wa utalii ni suala ambalo limepigiwa kelele sana humu ndani na Waheshimiwa Wabunge wengi na kwa kweli tunatia aibu kama Taifa. Bado hatujalipa umuhimu suala zima la kutangaza utalii wetu wa ndani pamoja na hata kwa wananchi wa nje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa sana kusisitiza kuwa Serikali itenge fedha ya kutosha katika kuhakikisha kuwa utalii wetu unatangazwa...
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa lakini vilevile na mimi naomba niungane na wenzangu kukutia moyo kwa kazi nzuri unayoifanya humu ndani. Umekuwa unasimamia vizuri Kanuni tulizojiwekea wenyewe Bungeni, umekuwa una misimamo mizuri ya kuhakikisha kuwa kazi za Bunge zinafanyika vizuri. Wale wanaokulalamikia ni kwa sababu wanataka kufanya kazi wanavyotaka wao wakati wakijua kabisa wana wajibu wa kutumikia wananchi. Sisi tuko nyuma yako, usitetereke wala usife moyo, kaza buti na kazi iendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo na mimi nimpongeze Waziri wa Fedha na Mipango pamoja na Naibu Waziri na Maafisa wake wote kwa hotuba nzuri iliyosheheni maelekezo mazuri sana lakini naomba nichangie machache. Kwanza kabisa, nataka kuzungumzia suala la Msajili wa Hazina. Naipongeza Serikali kwa kuitenganisha hii taasisi ikawa ya kujitegemea ili iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi mzuri zaidi. Nataka vilevile kuzungumzia kuwa Msajili wa Hazina sheria yake yeye na sheria za yale mashirika ambayo anayasimamia huenda kutakuwa na haja ya kuzipitia kuona kama kuna kusigana kwa aina yoyote.
Vilevile kazi ya Msajili wa Hazina ni kuhakikisha kuwa anasimamia vizuri uwekezaji wa Serikali katika mashirika mbalimbali. Katika kufanya hivyo anawajibika kuhakikisha kuwa haya mashirika yanaleta tija kwa Serikali na kwa nchi kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na zoezi la muda mrefu kuangalia jinsi gani mashirika haya yamekuwa yaki-perform ili kuona kama yameshindwa kufanya kazi ambazo zililengwa tangu mwanzo basi itafutwe njia nyingine ya kuyamiliki au kuyaondoa kabisa. Kwa hiyo, hatutegemei mpaka sasa kuendelea kubeba mashirika ambayo ni mzigo. Tunataka kuona vilevile kuna uratibu fulani unafanywa kwa mashirika ambayo yalianza miaka mingi iliyopita na kwa wakati ule pengine yalionekana yanahitajika lakini sasa hivi kufuatana na maendeleo ambayo yamejitokeza katika uchumi duniani na nchini kwetu labda hayana tena umuhimu huo au yanafanya shughuli ambazo zinafanana basi yaunganishwe au yawe harmonized kwa njia ambayo italeta tija kwa Taifa, badala ya kuwa na mashirika ya umma mengi yanatulia fedha tu katika gharama za uendeshaji lakini faida yake kubwa haionekani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumzia mashirika ambayo mengine yalikuwa ni ya research mbalimbali. Mengi yanafanana katika utendaji wao basi hebu tuyapitie tuangalie kama yanahitajika basi yaendelee kuwepo, la sivyo, tuyavunje na tuyaweke katika mfumo ambao utaleta tija na zile sheria ambazo zilikuwa zimeunda mashirika yale zinaweza zikapitiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka kuipongeza Serikali hasa kwa kupitia Msajili wa Hazina kwa kuongeza mapato hasa ile asilimia 15 ya ule mfumo wa kuratibu mapato yanayotokana na mawasiliano, lakini vilevile zile hisa zetu kwa TCC na TBL. Napenda kuwahamasisha kuwa wapanue wigo wa taasisi ambazo Serikali itawekeza tupate mapato zaidi. Mwenyekiti wa Kamati yangu alipokuwa akiwasilisha hapa amezungumzia kupanua wigo wa uwekezaji au hisa katika mashirika ya gesi, madini hata hayo hayo makampuni ya mawasiliano tungepaswa kuwa na hisa humo ndani. Mwelekeo uwe kuwa tunapoendelea sasa kila mwekezaji anayekuja hapa nchini Serikali au wananchi wa Tanzania wawe na hisa ndani ya kampuni hizo. Hii ndiyo njia pekee itakayowezesha kuwafanya Watanzania wengi zaidi kushiriki katika uchumi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala zima la Sheria ya Manunuzi. Hatujafika kwenye vifungu lakini naomba niseme kabisa na naomba na Wabunge wenzangu mniunge mkono tushike shilingi ya Waziri leo mpaka atakapotuambia lini Sheria ya Manunuzi italetwa hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tumeongeza fedha nyingi sana za mfuko wa maendeleo kwa hiyo fedha nyingi sana ya miradi itakwenda Majimboni, Wilayani na Mikoani, itasimamiwa vipi kama Sheria mbovu kama hii ya Manunuzi bado ipo? Sielewi kwa nini miaka kumi inapita sasa sheria hii inalalamikiwa kila Bunge lakini hakuna kinachofanyika. Sijui ni kwa sababu kuna watu wana maslahi nayo au ina ugumu gani wa kuileta Bungeni. Naomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu tushinikize sheria hiyo ije hata kama ni kwa udharura. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba vilevile nizungumzie suala la zile mashine za kielektroniki za kuratibu mapato pamoja na kodi. Hili jambo limetuletea mizozo mingi sana hapa Bungeni na hata kwa wananchi lakini najua tumefika mahali pazuri Serikali imekubali sasa kununua zile mashine na kuzigawa kwa wale ambao wanastahiki kuzipata. Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, naomba sasa hili jambo tusilifanyie siasa tena kwa sababu kwanza lina faida hata kwa wafanyabiashara wenyewe, lakini vilevile linatusaidia kupata mapato mengi zaidi kwa ajili ya uchumi wetu na kwa maendeleo ya nchi yetu. Naomba sasa Serikali ituambie ni lini mashine hizo zitapatikana zote kwa pamoja ili wafanyabiashara wanaohusika wazipate tuanze kupata hayo mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kutakuwa na ukusanyaji mkubwa wa mapato, wigo wa ukusanyaji kodi uongezwe kwa maana ya kwenda kwenye sekta isiyokuwa rasmi. Kwa kuwa tutaanza kuwa tunapata mapato mengi kwa kupitia mashine hizi basi vilevile uangaliwe uwezekano wa kupunguza viwango vya kodi ili watu wengi zaidi wavutiwe kulipa kodi. Maana kodi inaeleweka kuwa ni mchango wa maendeleo siyo adhabu na kama siyo adhabu basi iwekwe katika kiwango ambacho wananchi wengi zaidi watahamasika kulipa kodi wakijua kabisa wananachangia maendeleo ya nchi yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuzungumzia suala la Deni la Taifa na mimi nataka kujikita sana sana kwenye suala la Eurobonds. Nchi nyingi za kiafrika kwa kupitia Wizara zao za Fedha wameingia katika kununua madeni au kupata madeni kwa kupitia Eurobond. Wame-float Eurobond na wengi sasa hivi wako matatani. Ghana sasa hivi inatafuta kukwamuliwa na IMF kwa sababu wamefika mahali ambapo sasa uchumi umegoma hali kadhalika Mozambique, Namibia, Nigeria na Uganda. Sisi pia najua tumenunua Eurobond, je, tutegemee nini huko tunakokwenda maana nyingi karibu zinaanza kuiva na tayari chumi hizo ziko matatani. Najua kwa wakati ule mwaka 2008 kulikuwa kuna haja yakufanya hivyo kwa sababu ya uchumi ulikuwa umetetereka lakini na sisi tunavyojiingiza huko ni mkumbo au sisi tumejipanga vizuri zaidi kuwa hatutakuja kuathirika na hii Eurobond huko tunakokwenda? Ningependa kupata maelezo ya Mheshimiwa Waziri atuambie tunategemea kulipa nini, kwa vipindi vipi na itatuathiri au itatuletea faida kiasi gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ili kupunguza deni la Taifa kwa nini tusijiingize kwenye uwekezaji wa kutumia PPP? Mpaka sasa hivi tunazungumzia sheria, sheria imeshapatikana, tayari kuna wawekezaji wengi wanaotaka kuingia kuwekeza nchi kwetu katika mtindo huo lakini Serikali bado inaonekana kama ina mashaka ndiyo kwanza tunafikiria kukopa sisi wenyewe, hii itazidisha deni na tutashindwa kuhimili. Kwa nini sasa Serikali isiamue kujiingiza katika uwekezaji mkubwa kwa kupitia PPP? Nchi nyingi na wawekezaji wengi wana interest, wanatufuata hata sisi kuja kutuambia.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwa nini Serikali haifanyi biashara na taasisi zake yenyewe? Tunalalamikia TTCL lakini Serikali haiwapi biashara. Maofisi mangapi wana land line za kutosheleza ukilinganisha na simu za mkononi ambapo maafisa wao wote wanazo mikononi, mbili mbili au tatu tatu. Uchumi wetu utakuaje kama hatufanyi biashara na taasisi zetu wenyewe? Tunazungumzia mabenki, ni kiasi gani fedha ya Serikali iko kwenye mabenki ambayo sio ya Taifa ukilinganisha na yale ya kizalendo? Sisi wenyewe tunaanzisha taasisi halafu tunazikimbia, tunazikimbia zitafanya biashara na nani? Lazima tufanye biashara na taasisi zetu wenyewe. Nataka Serikali iweke mkakati na ije na agizo kabisa kuwa taasisi zake zote zitafanya kazi na Serikali, Serikali itakuwa mdau wa kwanza kwa taasisi za Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nami nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri iliyosheheni masuala mengi ya maendeleo ya Taifa letu. Pia nampongeza Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri wote walioko chini ya idara
zake zote nikiamini kuwa ushirikiano wao mzuri unaleta maendeleo mengi tunayoyaona sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka kuanza kwa kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kuendelea kuinua na kukuza uchumi wetu kwa asilimia saba kwa takribani miaka karibu 10 sasa. Nataka kuiomba Serikali yangu sasa iangalie jinsi ya kutafsiri ukuaji huu wa uchumi kwa wananchi wengi walioko chini. Naomba Serikali yetu sasa hivi mikakati yake yote ijielekeze zaidi kwa wananchi katika maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, tunazungumzia kilimo lakini bado hatujakipa umuhimu unaotakiwa. Watu wengi wanapata ajira zao, wanapata uchumi wao kifedha kupitia kilimo, ufugaji, uvuvi na shughuli zilizoko vijijini lakini mpaka sasa hivi dhana ya kilimo inaachiwa wananchi wenyewe kuhangaika peke yao. Sikatai Serikali imeingiza nguvu sana kwenye masuala ya pembejeo na vilevile mafunzo kidogo ya ugani lakini haujawa ni mkakati wa kitaifa ambao unaenea kila mahali na kuhakikisha kuwa kila mtu anayelima, anayefuga au anayevua anafikiwa. Tuna mifano ya mikakati ya kitaifa ambayo imefanywa na ikafanikiwa kama REA. Kwa nini tusifanye mambo hayohayo katika masuala ya uzalishaji ili sasa ule ukuaji wa uchumi ukaonekane katika ukuaji wa uchumi wa wananchi mmoja mmoja vijijni.
Mheshimiwa Spika, napenda sana kuhamasisha hili suala kwa sababu najua ukombozi wetu utatokana na wananchi wetu kuweza kuzalisha kwa tija, kuuza kwa tija na kuweza kumudu maisha yao. Nataka kuhamasisha uwezekano wa kuwa na mikakati ya kutoa mafunzo mahsusi
kwa vikundi vya wanawake, wanaume na vijana wanaofanya kazi za kilimo. Isiwe ni programu au mradi mmoja mmoja unaokwenda kule kwa ufadhili mmoja au mwingine lakini uwe ni mkakati wa Kitaifa. Mataifa yote yaliyofaidika na green revolution ulikuwa ni mkakati wa kitaifa. Naomba sana iangaliwe jinsi ambavyo kutakuwa na mkakati wa kuhakikisha kuwa uzalishaji unakuwa wa tija. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi wengine tunakotoka kilimo ndiyo kazi kubwa ya wananchi wengi na wengine tunatoka maeneo mazuri sana kwa kilimo lakini tumekwama miundombinu inayounganisha wakulima na masoko. Sasa hatuwezi kuzungumzia kilimo cha tija bila kuwa na miundombinu bora ya usafirishaji, maghala, maji na masuala kama hayo. Tunazungumzia vitu kimoja kimoja bila kuviunganisha, lile suala la mnyororo mzima wa uzalishaji naomba sana lizingatiwe. Mwaka juzi tulizungumzia sana masuala ya maghala pamoja na stakabadhi ya mazao ghalani. Sijausikia sana lakini napenda uendelee kwa sababu hata kule ambako umefanyika umekuwa wa tija sana na wakulima wengi wananufaika na inawasaidia kuondokana na yale masuala ya kulanguliwa.
Mheshimiwa Spika, nataka kuzungumzia suala zima la Maafisa Ugani. Hata kama hatuwezi kuwapata wale wataalam waliosomea degree lakini tufundishe watu vijijini, vijana wasomi ambao wamekaa bure wawe wanafanya hizi kazi za kuraghibisha masuala haya vijijini kwetu ili tuweze kuwa na watu ambao wanatoa taaluma japo kwa kiasi fulani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile nazungumzia masuala ya maendeleo. Kwa kweli nchi yetu ni kubwa sana na kweli sio rahisi kila mahali kukua kwa wakati mmoja. Hata hivyo, kwa miaka hamsini hii kuna maeneo ambayo yamekua sana na kuna maeneo ambayo bado yako nyuma sana. Naomba sana Waziri Mkuu na Serikali kwa ujumla, hebu waangalie na yale maeneo ya pembezoni ambayo yana tija na yana wananchi ambao ni wachapakazi lakini wanakosa zile huduma muhimu kama miundombinu na taaluma mbalimbali za kuwawezesha kukuza uchumi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi natokea Jimbo la Ileje, lina mvua nyingi sana, lina udongo mzuri sana, lina misitu lakini tuko nyuma kiuchumi kwa sababu ni Jimbo ambalo halina miundombinu hata kidogo yaani Ileje ni kama kijiji kikubwa. Umeme tunamshukuru Mungu sasa REA inakwenda lakini hakuna barabara ya lami hata moja, maji ni mengi sana lakini haina miundombinu ya kuyapeleka kwa wananchi. Tuna
maeneo mazuri ya kulima lakini wananchi watalima wayapeleke wapi mazao yao wakati hakuna barabara wala masoko? Kwa hiyo, haya ni mambo ambayo tunataka kuomba sasa Serikali hebu katika kuangalia maendeleo tujikite na kule pembezoni nako ili wananchi wa Tanzania
wa kule waone kuwa na wao tunapowapa hizi data za kukua kwa uchumi nao waone kweli wanakua.
Mheshimiwa Spika, nataka kuja kwenye suala lingine la maji. Kama hatuwezi kuzungumzia maji na kuhakikisha kuwa maji yanapatikana kwa kweli tunapoteza muda wetu. Tunazungumzia uchumi wa viwanda, tunazungumzia masuala ya usindikaji, tunazungumzia masuala ya kufuga kwa tija, tunazungumzia umwagiliaji, tutafanyaje bila kuwa na uhakika na maji?
Mheshimiwa Spika, kuna maeneo ambayo yana maji mengi, kuna maeneo ambayo hayana maji kabisa lakini utakuta treatment ni ile ile moja, haiwezekani! Sehemu ambayo ina maji mengi treatment yake au utaratibu wa kuhakikisha hayo maji yanapatikana unakuwa tofauti na kule
ambako hakuna maji kabisa. Kwa hiyo, ionekane kabisa hiyo tofauti lakini kama kila mahali watu wanazungumzia visima hata mahali ambapo kuna maji mengi, haiwezekani! Mimi kwangu sihitaji visima, nahitaji miundombinu ya kunipelekea maji kwa wananchi. Kwa hiyo, hayo nayo yatofautishwe wakati wa kuweka mikakati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka niende kwenye suala la VICOBA, SACCOS na Vyama vya Ushirika. Kwa kweli hili ndilo kimbilio la wananchi wengi kwa sababu mabenki hatuwezi kuyategemea, tumeshaona. Hata hivyo, SACCOS, VICOBA vinajiendesha vyenyewe havina mkakati wa Serikali wa kusema sasa tunatoa mafunzo ya aina hii. Wanaachiwa NGO’s, wanaachiwa taasisi zenyewe kujianzishia vitu vyao, kunakuwa hakuna mfumo ambao unalingana nchi nzima wa VICOBA, SACCOS ambavyo vinaweza vikategemewa hata kuwa ndio njia bora ya kupata mikopo.
Mheshimiwa Spika, najua Mheshimiwa Jenista ananisikia na amekuwa akilifanyia kazi sana ili tusaidie kuwe na mfumo mzuri wa VICOBA na SACCOS nchi nzima, hata kama ni kuwekea utaratibu wa sheria au kanuni ambazo zitatumika kila mahali ili mwisho wa yote hizi SACCOS na
VICOBA ndio zije zitengeneze benki za vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ajira kwa vijana. Ajira kwa vijana ingekuwa ni jambo rahisi sana kulifanya kama tungekuwa tuna njia ya kuhakikisha kuwa tunawaweka hawa vijana pamoja na kuwawezesha. Kwenda kuwaambia tu vijana, ‘mkalime, mkajiajiri’ bila kuwaonesha wakajiajiri vipi au waende wapi ndiyo watapata nini au kuwawekea mitaji au mafunzo, wataendelea kucheza pool, kunywa viroba, kuvuta bangi na kufanya uhalifu wa kila aina. Tuwe na system ya kuwawekea vikosi vya kazi. Mwaka wa kwanza, wa pili na wa tatu tuwawezeshe, mwisho wa yote hawa watakuja kuwa responsible. Kule ambako tunawawezesha mbona wanafanya kazi nzuri sana, sidhani kama vijana ni wakorofi kiasi hicho lakini hawana njia.
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti Ninamshukuru Mungu kwa rehema na neema yake. Napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri iliyosheheni taarifa zote muhimu zinazogusa kila sekta ya Serikali. Aidha, nawapongeza Mawaziri walio chini ya Waziri Mkuu Mheshimiwa Jenista Mhagama, Mbunge wa Peramiho na Mheshimiwa Anthony Mavunde, Mbunge wa Dodoma Mjini kwa kazi nzuri wanayoifanya chini ya uongozi wake mahiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ukuaji wa Uchumi; napenda kuzungumzia masuala kadhaa yahusuyo. Naipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kukuza uchumi wa asilimia 7.0 kwa zaidi ya miaka 10 sasa. Haya ni mafanikio makubwa sana kidunia na inaashiria kuweka mikakati na mipango mizuri ya kiuchumi na kimaendeleo ambayo imetekelezwa ukuaji huu. Pomoja na pongezi hizi, naomba niitakie Serikali kuhakikisha kuwa ukuaji huu wa uchumi unatafsiri kuwa maendeleo kwa mwananchi mmoja mmoja na kwa ujumla. Hii inawezekana kwa Serikali kuhakikisha kuwa inaweka miradi ya kimkakati katika sekta na sekta ndogo ambazo zinagusa moja kwa moja maisha na ufanisi wa wananchi
wetu wa hali ya chini hasa vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kupendekeza kuwa uwepo mpango kazi wa kuhakikisha vikosi vya vijana na wanawake kupitia SACCOs, ushirika na makundi mengine na kuwapatia mafunzo ya kuwajengea ujuzi katika kilimo, ufugaji, uvuvi wa kisasa. Sambamba na mafunzo Serikali iweke mkakati wa kuwapatia mitaji, vitendea kazi na pembejeo, lakini vilevile kuweka mkakati wa kujenga maghala, masoko na miundombinu ya barabara ya kuunganisha uzalishaji na masoko katika mnyororo wote wa thamani kwa kila zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo itakayoweza kufanya haya yote kisayansi na kuyasimamia. Hili haliwezi kuachiwa NGOs au watu binafsi kujianzishia vitu kiholela au wananchi wenyewe. Hili ni lazima lisimamiwe na Serikali yenyewe kama mkakati wa kushirikisha wananchi wote katika uchumi (inclusiveness). Mkakati tajwa hapo juu utajihakikishia ajira, kipato cha wananchi lakini na pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, afya ni muhimu sana kwenye ufanisi wa nchi. Sekta hii inajumuisha lishe na huduma za afya kwa muda mrefu wananchi wamehamasishwa sana kujenga vituo vya afya na zahanati kwa kujitolea. Nyingi zimekamilika kwa asilimia 80 au zaidi lakini zinahitaji
kumaliziwa. Naiomba Serikali ihakikishe kuwa zahanati na miundombinu hii inamaliziwa na kukamilishwa ili zianze kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la lishe bora bado halijazingatiwa na kuwekewa mkakati mahsusi ya kuhamasisha na kutoa mafunzo ya lishe bora. Kwa kutumia maofisa wa ustawi wa jamii. Vipindi vya redio na televisheni, vituo vya afya na ngoma na michezo ya kuigiza. Hii itasaidia
sana kupunguza utapiamlo na huduma kwa watoto wetu takriban asilimia 42. Vyakula vipo ni elimu tu ndiyo inayohitajika kuhakikisha matumizi mazuri ya vyakula mbalimbali ili kupunguza utapia mlo. Huu uwe mkakati mahsusi wa kuboresha lishe ya watoto na wanawake wajawazito.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Sekta ya Afya masuala ya vifo vya wanawake wakati wa kujifungua na vifo vya watoto wachanga na wale wa chini ya miaka mitano. Bajeti ya afya itenge fungu maalum la kuhakikisha vifaa tiba na huduma muhimu za wazazi zinakuwepo. Wahakikishe kuwa vifaa vya kupokelea watoto wanapozaliwa hospitali vinapatiakana ikiwa ni pamoja na maji, wodi, wauguzi na vyumba vya kupumzikia wanawake wanapojifunguapamoja na vyumba vya upasuaji. Haya yatapunguza kwa kiasi kikubwa sana vifo vya wazazi na watoto wakati wa
kujifungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu UKIMWI na watu wanaoishi na VVU changamoto kubwa ni mashine za kupima viral load na fedha ya dawa za kurefusha maisha lakini vile vile uhamasishaji kwa wananchi. Wazee bado hawajawekewa mkakati wa kitaifa kwa kuhakikisha matibabu, kupimwa afya, kuelimishwa juu ya maradhi yanayowasibu, lakini pia wazee waingizwe kwenye TASAF wote kupunguza hoja ya kuwapa kipaumbele.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa fursa ya kuchangia hoja ya Wizara hii muhimu na ya kipaumbele kwa mustakabali wa maendeleo, afya na ufanisi wa Taifa letu. Mengi yaliyochangiwa na Wabunge kuhusu utaratibu mzima na usimamizi wa Wabunge kuhusu utaratibu mzima na usimamizi wa miradi ya maji ni ya maana na ni lazima sasa hivi ufanywe uchunguzi wa kina kuhusu matumizi ya fedha nyingi sana za miradi ya maji ncjhi nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kuungana na Wabunge wenzangu waliopendekeza kuwa miradi ya maendeleo ya maji isimamiwe moja kwa moja na Wizara ya Maji yenyewe badala ya huu utaratibu wa sasa wa kuachiwa Halmashauri. Hii tunaiomba kwa sababu tumeona kule ambako Wizara imesimamia miradi imekuwa na ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuishauri Serikali kwa mara nyingine tena kuwa Tanzania ina mikoa mingi inayopata mvua nyingi sana na inaishia ardhini au baharini. Serikali ituoneshe mpango mkakati iliojiwekea wa kuvuna maji nchi nzima kutumia njia mbalimbali, kuchimba mabwawa makubwa ili yatumike kumwagilia mazao, kufuga samaki na kutumiwa majumbani na taasisi, kuwekwa matanki ya kukinga maji kwenye taasisi za kijamii na kaya za watu maeneo yote. Tunaitaka Serikali ije na mpango madhubuti ulioainisha maeneo ya kujenga mabwawa na kuweka matenki (mapipa).

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maji ishirikiane kwa karibu sana na Wizara ya Mazingira na Wizara ya Ardhi na ya Kilimo kwa ajili ya kuweka mipango ya pamoja ya uvunaji maji, ulinzi wa vyanzo vya maji na umwagiliaji na kilimo na ufugaji. Hili ni muhimu, tunaomba tamko na mkakati wa Wizara katika hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna miradi mingi mipya ya maji imeshapata kibali cha kuingiwa mikataba kutoka Wizara ya Maji, lakini haipelekewi fedha, je, utaratibu ukoje? Vilevile Halmashauri nyingi zimewasilisha hati za madai Wizarani, lakini fedha hazijatolewa na tunajua kuchelewa kulipa husababisha penalty ambazo zinatuletea gharama nyingine, je, kuna utaratibu gani katika ulipaji wa certificates?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna haja sana ya bajeti ya kuhamasisha na kutoa mafunzo ya umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji na kuweka adhabu kali kwa wote wanaovamia vyanzo vya maji kama ambavyo Maliasili wamesimamia maeneo yote ya hifadhi. Ninaomba Wizara ya Maji ijifunze kutoka nchi kama Israel, Afrika Kusini au Australia na hata nchi za Marekani Kusini juu ya jinsi ya kutunza maji yote yanayopatikana Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, usimamizi wa fedha inayotolewa kwenye miradi ya maendeleo ya maji si ndogo kwa kiwango chochote kile. Kitu kinachohitajika sasa ni jinsi ya kufanya ufuatiliaji na tathmini ya karibu ya matumizi ya fedha hii ili kila senti ilete thamani stahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo unda kamati ya kufuatilia matumizi ya fedha yote iliyoingizwa kweye maji kwa miaka mitano iliyopita. Naunga mkono hoja na naomba kuwasilisha.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mungu kwa wema wake kwa Taifa letu na kwa Bunge letu. Ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja iliyoko Mezani. Naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Waziri wa Wizara hii muhimu, Mheshimiwa Ummy Mwalimu; Naibu Waziri Mheshimiwa Dkt. Hamis Kigwangalla, Mbunge wa Nzega, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri na kubwa wanayoifanya kuhudumia wananchi kwa weledi mkuu na umahiri wa kiasi cha kuridhisha. Pongezi nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujikita kwenye wasilisho la Mheshimiwa Waziri kwenye eneo la maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto. Ni kweli, kuwa, kwa ujumla wake bajeti ya Wizara imeongezeka mara dufu, lakini Fungu 53 bado halijatendewa haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, idara hii ndiyo inayofanya kazi ya kuhamasisha wananchi tangu ngazi ya kaya, shina, kijiji, kata, tarafa, wilaya, mkoa hadi Taifa. Hii idara ikiwezeshwa kikamilifu itasaidia sana kuweka mazingira mazuri kiasi kwamba, hata huduma za afya uhitaji wake utapungua. Idara hii inapaswa kuwa na Maafisa Maendeleo ya Jamii, Maafisa Ustawi wa Jamii kila kata, ili wawe wahamasishaji na waraghibishi wa mafunzo yanayohusu usafi wa mazingira (sanitation), masuala ya lishe bora kwa ujumla, lakini pia kwa watoto wanawake na wazee, masuala ya chanjo mbalimbali, masuala ya ujasiriamali, biashara, masoko na kadhalika. Hata Mawaziri wa Sekta nyingine huwatumia hawa Maafisa Maendeleo kuhamasisha masuala mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali hii ni muhimu sana kuhakikisha kuwa Idara hii ina vitendea kazi vya muhimu kwa majukumu yake kwa maana ya magari, pikipiki, ofisi zinazokidhi, computer na watumishi wa kutosha na wenye weledi wa kutosha kwenye masuala haya. Hali iliyopo hairidhishi na maafisa hawa wengi wamekata tamaa. Idara hii ni muhimu sana kwa kuhakikisha kuwa mikakati ya kinga dhidi ya magonjwa, elimu kwa vijana juu ya mabadiliko ya maumbile na jinsi ya kupambana na mihemuko kwa njia sahihi na salama, idara iwezeshwe kutimiza haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, udumavu; napenda kuishauri Serikali kuendeleza mkakati ulioanzishwa na Mheshimiwa Jakaya Kikwete wa Scalling Up Nutrition (SUN) kitaifa. Serikali ilete Bungeni mkakati wa uwekezaji katika lishe ili kupambana na tatizo kubwa la udumavu nchini. Katika hili, pamoja na juhudi zinazofanywa za kuhamasisha lishe bora kwa mama mjamzito na mtoto, Serikali ifanye yafuatayo:-

Kwanza, katika mikopo inayotolewa kwa Serikali basi Serikali i-negotiate fungu la kuwekeza kwenye siku 1,000 za kwanza za mtoto. Kwa sababu, bado hatujaona kuwa hili ni kipaumbele katika Taifa. Kwa sababu kuwekeza katika siku za kwanza 1,000 za mtoto kutahakikisha vizazi salama kwa mama na mtoto, lakini pia, itapunguza vifo vya mama na mtoto na kuleta ukuaji wa uchumi kwa kiasi kikubwa.

Pili, Serikali iweke mazingira mazuri kwa sekta binafsi kuingia katika uwekezaji kwenye masuala/huduma/mazao ya lishe. Serikali haiwezi kulifanya hili peke yake.

Tatu, Serikali ianzishe Jamii ya Vijana wa Kujitolea (Volunteer Community Workers) ambao watafundishwa masuala ya uraghibishi wa afya vijijini na watakuwa wa msaada mkubwa kwa karibu sana na kuongeza tija kwenye shughuli za Wizara katika ngazi ya kaya, tawi, hata na wilaya. Hawa kwa kuwa, watatokana na maeneo hayo watakuwa na gharama ndogo.

Nne, Serikali katika kujenga maadili mema kwa jamii zetu iangalie uwezekano wa kuanzisha utaratibu wa wanawake watu wazima kutoa ushauri nasaha kwa vijana wanawake wakati wa balehe, ujauzito na wanapokuwa katika ndoa zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la wazee bado halijakaa vizuri kwa maana ya mkakati mahsusi wa kuwahudumia wazee kiafya, kiuchumi na kisaikolojia. Iko haja ya kuwa na njia inayotambulika ya kuwawezesha wazee kujisajili kwenye kata zao ili huduma kwao ziwe rahisi katika kila nyanja. Wazee mahitaji yao mengi ni ya kisaikolojia jinsi ya kuukabili uzee, lakini pia kiafya na mwisho lishe bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watoto Njiti; idadi ya watoto hawa inaongezeka katika watoto 10 wanaozaliwa mmoja ni njiti na wanapona kwa 40% tu. Hii ina maana vifo vya watoto wachanga vinachangia kwa 40% ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano. Kila siku watoto 100 wanakufa kwa sababu ya complications kama kushindwa kupumua na kuzaliwa kabla ya wakati. Kila mwaka watoto 213,000 wanazaliwa njiti, watoto zaidi ya 9,000 wanazaliwa kwa matatizo hayo. Vifo vya watoto njiti ni sababu ya pili kwa ukubwa wa vifo vya watoto wachanga Tanzania. Kumekuwa na ongezeko kubwa na hatua madhubuti zinahitajika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ihakikishe suala la watoto njiti linafahamika na jamii kwa ujumla kuwa sio mkosi, wala kosa lolote la mzazi, ukoo wala jamii na kuwa watoto njiti wanaweza kukua vizuri na kuwa raia wema na wenye akili timamu na afya njema, ilimradi wapate matunzo yanayofaa kwa kuwarudisha katika afya njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ihakikishe vituo vya afya na hospitali zinapata vifaa muhimu vya kuwatunzia watoto njiti kama oxygen concentrator ya kumsaidia mtoto kupata oxygen; neonatal jaundice and phototherapy ya kugundua jaundice(manjano) mapema; rescuscitation machine ya kumstua mtoto ili apumue mara tu akizaliwa maana mapafu yake yanaweza kuwa hayana nguvu ya kutosha; electric and manual suction machine ya kutoa uchafu kooni na puani kusafisha njia ya kupitisha hewa; digital thermometer ya kupima na kudhibiti joto la mwili wa motto; diaspect machine ya ku-check damu ya mtoto kama inatosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wazazi wafundishwe jinsi ya kutunza watoto njiti kwa kuhakikisha wanawabeba kama kangaroo na hawawaachi wazi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Spika, pongezi kwa kuweka mikakati mizuri na endelevu ya kuinua vipaji katika michezo kuanzia vijana wa miaka 13. Hii itatuhakikishia kupata wanamichezo mahiri wa kitaifa na kimataifa.

Mheshimiwa Spika, rai yangu; michezo hii iwe ya aina mbalimbali sio soka na netball peke yake bali izingatie riadha na michezo mingine. Timu hizi zizingatie jinsia ili kupata vijana wa kike na wa kiume katika michezo. Timu zizingatie watu wanaoishi na ulemavu na kuwawezesha. Suala la michezo ya wanawake halijapata kushughulikiwa ipasavyo na Serikali.

Mheshimiwa Spika, michezo mingi ni ile ya netball lakini wanawake wana uwezo wa kushiriki katika kila mchezo lakini hawawezeshwi. Kwa mfano, sasa hivi Timu ya Mpira ya Wanawake ya Chalinze ndio mabingwa wa Taifa lakini hawana uwezeshwaji na wamekwama kuendelea na mazoezi na hivyo kuhujumu fursa zilizopo mbele yao. Tunaiomba Serikali iwahudumie hawa wachezaji wa Timu hii ya Wanawake ya Chalinze badala ya kumuachia Mheshimiwa Salma Rashid Kikwete peke yake. Serikali iweke mkakati wa kujumuisha wanawake katika maendeleo ya michezo.

Mheshimiwa Spika, utamaduni; Serikali izingatie tamaduni zilizopo Tanzania na kuzifanyia kazi zile ambazo zinajenga heshima na maadili mema na kuzidumisha kwa kuzifundisha shuleni na kwenye sherehe mbalimbali, wakati huo huo wakiwaasa wananchi dhidi ya mila na tamaduni zinazodhalilisha watu kijinsia, kidini na kikabila.

Mheshimiwa Spika, ngoma zetu zidumishwe lakini wachezaji wavae nguo za heshima wakati wa kucheza, sio lazima watu wawe nusu uchi. Wizara ifanye kazi na Wizara ya Elimu na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Mheshimiwa Spika, kuunganisha juhudi za Wabunge na Serikali; Wabunge wengi wamekuwa wakitoa jezi na vifaa vingine vya kuwezesha michezo majimboni lakini wamekuwa wakifanya hivyo katika mazingira magumu maana majimbo yetu hayana viwanja vizuri vya michezo na hata baada ya kupata timu nzuri au wachezaji wazuri, hakuna mwendelezo maana hatuna Maafisa Michezo kwa hiyo usimamizi ni mgumu. Tunaomba Wizara itupatie utaratibu mzuri wa kuibua vipaji kwenye majimbo yetu.

Mheshimiwa Spika, majimbo yaliyopo kwenye maeneo ya milima yana uwezekano mkubwa ya kuzalisha wanariadha. Tunaomba maafisa michezo na vifaa vya kusaidia hilo.

Mheshimiwa Spika, kushirikisha Sekta Binafsi; michezo ni biashara kwa hiyo Serikali ifanye tathmini ya namna ya kushirikisha Sekta Binafsi, sio kufadhili timu ili kujitangaza bali kuwa na timu kikamilifu, kuajiri makocha, kufadhili viwanja vya michezo na kuziendesha ili Serikali ibaki kuweka mazingira mazuri kisheria na kisera. Serikali iwezeshe kutafuta wenye vipaji watakaochukuliwa na Sekta Binafsi kwenye timu za michezo mbalimbali, kwa mfano, Serikali itenge fedha ya kusomesha Maafisa Michezo vyuo vikuu, Makocha, Walimu wa Michezo, Waongoza Filamu, wataalam wa sanaa na utamaduni na filamu.

Mheshimiwa Spika, kwa kutumia maliasili zetu katika uwekezaji katika filamu, watengenezwe maeneo ya mbuga zetu, miji yetu, vijiji vyetu, milima yetu, maziwa yetu, mito na bahari na kutoa leseni/ vibali, hatimiliki kwa ajili ya kuja kutengenezea filamu. Hii itauza nchi yetu na kuviweka kwenye ramani ya medani za filamu nchini, vilevile inawezesha Watanzania kuajiriwa kwenye filamu na documentary hizi, wakati huo huo wakilipatia Taifa kipato kikubwa.

Mheshimiwa Spika, Wizara ishirikiane na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuona jinsi hili litakavyofanywa. Nchi yetu ilishawahi kutumika kutengeneza filamu lakini ilikuwa kabla ya uhuru lakini sasa mazingira ni mazuri zaidi, kwa hiyo Wizara itumie fursa hii kikamilifu.

Mheshimiwa Spika, magazeti na TV; Tanzania ina uhuru uliopitiliza wa habari kwa maoni yangu na kwa kweli kuwa na magazeti mengi sio tu kueleza lakini ni chanzo cha matatizo mengi yanayotokana na tasnia hii ya uandishi maana uandishi wa vyombo vyetu vingi hauridhishi hata kidogo. Kwanza ni lugha inayotumika, utafiti mdogo ungefanywa kwenye mambo mengi ya kiuchumi, kisayansi, kiteknolojia na kijamii. Wote wanaandika taarifa za kuambiwa, hakuna anayefanya utafiti na kutoa ripoti inayofundisha wananchi.

Mheshimiwa Spika, waandishi wetu wengi hawana ujuzi wa kutosha kwenye uandishi wa taaluma kiasi kwamba wawe wamebobea katika fani maalum. Suala la kuandika makala yasiyofanyiwa utafiti linaleta usumbufu, udhalilishaji na maumivu kwa wananchi wengi na hii haikubaliki. Tunaitaka Serikali ichukue hatua kali za kisheria kukomesha hili huko tunakokwenda.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa fursa ya kuchangia hoja hii muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu. Namshukuru Mungu kwa rehema na neema yake kwa Bunge letu na uongozi mzima. Pia nampongeza Mheshimiwa Waziri Kamwelwe na Manaibu wake wote na watendaji kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, Wilaya yangu ya Ileje imepata fedha za kujenga barabara kuu ya Mpemba - Isonpole kwa kiwango cha lami na tayari kazi imeanza. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa barabara hii ambayo ilikuwa ni ahadi yake na vile vile iko kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2015. Ahsante sana Mheshimiwa Rais, wana Ileje wana deni kubwa kwake, wameingoja barabara hii miaka 42.

Mheshimiwa Spika, ziko barabara za TARURA Wilayani Ileje ambazo kwa ugumu wake hazitaweza kujengwa na TARURA. Tulipeleka maombi ili zifikiriwe kujengwa na Wizara ya Ujenzi. Aidha, kuna barabara ambazo madaraja yalikatwa na mvua tangu 2016 na kwa hivyo wananchi wa Chitete na Mlale hawana mawasiliano kupitia Ilanga kitongoji kinachopakana na Wilaya ya Vwawa. Tunaomba sana watufikirie wana Ileje watupatie fedha za kujenga miundombinu ya Ileje, kwani ni migumu sana na hii imekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi kwa Wilaya ya Ileje.

Mheshimiwa Spika, naambatanisha kwa barua husika maombi yetu kwa maandishi ili watufikirie.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia kwenye hotuba hii muhimu. Ninamshukuru Mungu kwa fursa ya kuwa katika Bunge hili Tukufu. Ninawapongeza Mheshimiwa Waziri Profesa Jumanne Maghembe na Naibu Waziri wake Engineer Ramo Makani na watendaji wa Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuchangia kwenye maeneo machache nikianza na hati za kumiliki misitu. Ninaomba kwa Wilaya na Mikoa yenye misitu mingi ya asili na ya kibiashara watu wakatiwe vitalu vya misitu kama watu wanavyopata hati za ardhi ili wawekeze kwenye upandaji miti na watumie hati hizo za vitalu vya miti kukopa kwa ajili ya kuendeleza misitu, ufugaji nyuki na viwanda vidogo vya mbao na samani za ujenzi na za taasisi na za majumbani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali kuzidisha juhudi na mikakati ya kulinda antiques za nchi hii hususani za kitamaduni zilizopo vijijini ambazo huondolewa kwa sababu ya umaskini na kutokuwa na uelewa. Wanachi wengi wamekuwa wakirubuniwa na wageni wanosaidiwa na wajanja wachache kuwashawishi kuuza antiques hizo za kihistoria za makabila na jamii mbalimbali. Kwa mfano kulinda antiques za fimbo, vigoda, mavazi ya machifu na viongozi mbalimbali wa kimila, samani, vyombo vilivyotumika kulima, kusaga nafaka, kuhifadhi chakula, kuwinda na uhunzi. Mavazi ya sherehe mbalimbali vyote vinapotea na kupoteza historia muhimu ya Taifa letu na jamii mbalimbali. Serikali ilitupie macho na kuweka mikakati ya kuzilinda na kuzihifadhi na kuziwekea kumbukumbu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukataji wa miti kwa matumizi ya mkaa umeongezeka sana hasa maeneo yenye ukame ambako misitu ni michache, na wakati huo huo matumizi ya gesi na umeme pamoja na majiko sanifu vimeongezeka. Ninaitaka Serikali kutoa takwimu za gharama ya kukata miti kwa kila gunia la mkaa na uharibifu wa mazingira. Tulinganishe uharibifu huu na gharama ya mbadala kama matumizi ya gesi, majiko sanifu na umeme tutaona jinsi gani matumizi mbadala ya nishati ni nafuu huko tunakoelekea. Gharama ya gesi ukishanunua mtungi ni rahisi kuliko mkaa. Kwa wastani mkaa unauzwa kwa familia ya kawaida ni gunia nne kwa mwezi 70,000 x 4 = 280,000/=; lakini gesi kwa mwezi ni mitungi miwili ya shilingi 90,000/= ukiongeza gharama ya mtungi 100,000 ni 190,000/=; ni dhahiri gesi ni nafuu. Kuhusu mkaa tutoe ulinganisho mkaa na gesi na tuwaelimishe wananchi gesi ni bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaitaka Serikali itafute njia ya kutoa elimu kwa mapana yake ili matumizi ya mkaa yaachwe kidogo kidogo. Serikali ianze kuwatoza wote wanaokata miti kwa mkaa wa kuuzwa ili walipie gharama ya kupanda miti hii, tusilionee haya hili, tutajuta baadae.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba kutoa ushauri kwa Serikali juu ya utalii wa fukwe. Utalii huu ni mojawapo ya eneo linalovutia sana watalii nchini na kwa hali hiyo kuna haja ya kuwekeza kwa kiwango kikubwa kwenye vivutio vya utalii wa fukwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna changamoto kubwa ya upungufu wa mahoteli ya kutosha kwa ajili ya watalii wanotaka kuja Tanzania. Nataka kupendekeza kuwa Serikali iboreshe mazingira ya uwekezaji kwenye ujenzi wa hoteli nyingi kwenye fukwe zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itoe msamaha wa ushuru wa vifaa vyote vya ujenzi wakati wa ujenzi wa hoteli hizi ili kwa miaka miwii au mitatu wawekezaji wajenge hoteli za viwango vya kimataifa na baada ya hapo tozo na kodi zote zihusike. Hii imefanyika Zambia na Mozambique na imewezesha utalii kukua sana. Wizara hii itumie wataalam kufanya benefit cost analysis ya wazo hili na nina hakika wataona kuwa kodi na ushuru tunaokosa sasa kutafidiwa kwenye mapato mengi ya utalii baadae. Wawekezaji wa ndani watahitaji kuwekeza. Serikali ipime maeneo kwenye ufukwe wa Bahari ya Hindi kuanzia Tanga hadi Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo dhana kuwa makaa ya mawe yanaweza kuwa mbadala wa mkaa wa miti, naomba Serikali ifahamishe wanachi juu ya hili. Makaa ya mawe yanahitaji majiko na tanuru maalum kabla ya kutumia kwa hiyo haitakuwa automatic.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yetu mengi hasa ya pembezoni kama Songwe na Ileje yana misitu, mabonde, mito mingi inayofaa kwa utalii wa utamaduni, wa kupiga picha na wa camp sites na kupanda milima. Lakini hatuna wataalam kabisa wa kuendeleza hayo. Tunaiomba Serikali itufikirie. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata fursa ya kuchangia Hotuba ya Wizara hii ya Viwanda na Biashara. Napongeza hotuba hii na naomba kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tuna dhamira ya kweli ya kujenga uchumi wa viwanda na biashara, ni lazima tuoneshe kwa vitendo. Kwa kuanzia na mkakati wa makusudi wa kutenga bajeti kubwa na ya kutosha kukidhi mahitaji ya kujenga mazingira yote wezeshi ya uwekezaji kwenye viwanda na biashara. Bajeti inayotengwa ni ndogo na inayotolewa ni ndogo zaidi, 30% kwenye matumizi ya kawaida na 6% maendeleo, ni ndogo mno kwa sekta muhimu kama hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji bado hii ni changamoto kubwa. Mwaka 2010 Serikali iliunda task force ya kutengeneza roadmap ya kuboresha mazingira ya uwekezaji baada ya kupata rank mbaya toka survey za kimataifa. Kwa hiyo Wizara nane kama Fedha, Viwanda, Kilimo, Uwekezaji, Nishati, Miundombinu, Ardhi na Maji wakapitisha roadmap iliyozingatia mambo yafuatayo:-

(i) Kurahisisha utoaji wa vibali vya ujenzi;

(ii) Ukaguzi wa maeneo ya biashara;

(iii) Ku-streamline malipo ya kodi mara mbilimbili kupitia taasisi mbalimbali;

(iv) Kuweka wathamini wa Serikali wa kikanda; na

(v) Kupitia sheria zinazoruhusu mlolongo wa roadblocks.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hii taskforce, Ofisi ya Waziri Mkuu iliratibu pamoja na wadau utayarishwaji wa mpango wa utekelezaji. Uliendelea na utekelezwaji wa maeneo yenye quick wins, kutengeneza mpango wa ufuatiliaji na tathmini na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, hiyo roadmap imefikia wapi katika kuboresha mazingira ya biashara? Sasa mwaka uliopita tukaja na blue print na yenyewe inatokana na ranking yetu kwenye doing business imeshuka, sasa vimefikia wapi? Win wins ziko wapi, mbona hali imezidi kuwa mbaya?

Mheshimiwa Naibu Spika, Kurasini Logistics Park, huko nyuma ililenga kutumia eneo ambalo lingekuwa kitovu cha biashara kati ya China, Tanzania na nchi zote za jirani yetu hadi Afrika ya Kati, chini ya ubia wa Tanzania (EPZA) na kampuni ya China. Tanzania ilikuwa kati ya nchi nne Afrika zilizoteuliwa kufaidika na uwekezaji huo na kuboresha biashara kati ya China na Tanzania. Sasa kwa nini tunabadilisha matumizi na kuingiza suala la kuunganisha magari?

Mheshimiwa Naibu Spika, majadiliano na maamuzi yanachukua muda mrefu sana, hii inakatisha tamaa wawekezaji na kuongeza gharama na kujenga mazingira ya rushwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu inayoenda kwenye viwanda vingi nchini na hata katika maeneo ambayo yamelengwa uwekezaji mkubwa mfano Mradi wa Liganga, Engaruka, viwanda vya Coca-Cola, TBL, Mbeya, Kilimanjaro na viwanda vingi vya Dar es Salaam, Chang’ombe na Keko.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa fursa ya kuiona siku hii ya leo, lakini vile vile naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Mwijage, Waziri wa Viwanda, kwa kweli ametutendea haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii hotuba kwa mtu ambaye anataka kuisoma na kuielewa, kwa kweli hakupaswa hata kuwa na maswali humu ndani. Nampongeza sana kwa kuwa hotuba hii imesheheni kila aina ya taarifa. Kuna takwimu, kuna maelezo, kuna mchanganuo; sasa sijui mtu unalalamika kuwa dhana ya viwanda huioni, unataka uione vipi?

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuipongeza sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, safari hii huu mkakati jamani utafanyika. Kwa vielelezo hivi vilivyomo humu ndani ni wazi kabisa viwanda vitakuja kufanyika. Mifano, tumeshaiona, viwanda vipya vimeshajitokeza vingi sana; someni haya majedwali jamani! Kama hamtaki kusoma hii literature yote kubwa, nendeni huku nyuma kwenye majedwali, yameainishwa kiwanda kipi, wapi, ukubwa gani, kwa faida ipi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niipongeze sana Serikali yangu, nimpongeze Mheshimiwa Waziri na watendaji wote walioko chini yake. Kwanza tunaambiwa kabisa katika maendeleo yoyote ya uchumi duniani, nchi lazima iwe na political commitment. Commitment tumeiona kwa kupitia Rais wetu na Marais wengine wote waliopita. Commitment ya kuwa na viwanda nchi hii imekuwepo na sasa hivi ndiyo imetiliwa mkazo zaidi kwa kuweka kabisa mkakati wa kuwa sasa hivi tunaelekea kwenye maendeleo ya viwanda peke yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa suala linalofuata ni taasisi. Tunaambiwa kabisa ili nchi iendelee au ionekanae kuwa inaendelea inapaswa kuwa na taasisi muhimu. Taasisi hizo zinahusiana na masuala ya hatimiliki. Sisi chini ya Wizara hii tuna Taasisi ya Property Rights, tuna Taasisi zinazosimamia ubora wa mazao au bidhaa, tuna taasisi zinazosimamia miundombinu ya viwanda vidogo na vikubwa, tuna taasisi zinazoshughulikia usuluhishi wa migogoro kwenye biashara, tuna taasisi ambazo zinakwenda kujenga ufanisi wa viwanda kuanzia vidogo kabisa hadi vile vikubwa; tuna sheria ambayo inasimamia, tuna mkakati wa kimaendeleo wa viwanda wa tangu 1996 mpaka sasa hivi ambao umerejewa na sasa hivi umeboreshwa. Sasa zaidi ya hapo tunawezaje kusema kuwa hatuna mwelekeo wa viwanda? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukitoka hapo tunakuja kwenye masuala mazima ya utekelezaji wa huo mkakati mzima wa viwanda nchini mwetu. Tunaona jinsi ambavyo kwa sasa hivi kwa mtazamo huu wa Serikali ya Awamu ya Tano kuwa sasa hivi viwanda hivi vinakwenda kuwajumuisha wananchi wengi zaidi. Kama zamani ilikuwa inaonekana viwanda viko sehemu chache tu za nchi, sasa hivi viwanda vinakwenda mpaka vijijini kwetu, vinakwenda mpaka kwenye Wilaya zetu, vinakwenda kwenye Halmashauri zetu, maeneo ya mikoa na wilaya ambayo yako tayari kwa ajili ya viwanda yameainishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri zetu wote wana ufahamu na uelewa kuwa wanahitaji kuwa na viwanda; tuna program zilizokuwepo chini ya Wizara hii zilizokuwa zikisema kila Wilaya iainishe zao moja ambalo wanaliona hilo ndiyo litakuwa linafaa kwa ajili ya kuendelezwa hadi kufukia level ya kiwanda; na hayo yamefanyika. Tuna Taasisi muhimu za kusimamia kama SIDO; kila mtu aliyesimama hapa amezungmzia SIDO, ni kwasababu ameuona umuhimu wake. Sana sana tutakachoweza kusema kwenye Serikali ni kuwa SIDO iwezeshwe zaidi kwa maana ya mitaji, kwa maana ya wafanyakazi, kwa maana ya program za kwenda kusambaza katika kila eneo kama ambavyo sera inasema.

Mheshimiwa Naibu Spika, tutazungumzia BRELA. BRELA zamani ilikuwa inasajili majina ya Makampuni kwa maana ya wakubwa. Sasa hivi hata akinamama zangu kule kijijini wanaweza kusajili majina ya Kampuni zao au shughuli zao wanazozifanya. Hii imerahisishwa kiasi kwamba hata hawana haja ya kutembea kwenda Dar es Salaam au kwenye Kanda yoyote, hata kwa kutumia mitandao tu ya simu, Mabenki ambayo yameunganishwa. Sasa jamani unalalamika kuwa eti sijui urasimu; urasimu umepunguzwa kwa kiasi kikubwa. Ni sisi sasa kama viongozi katika Halmashauri zetu kuhamasisha wananchi kuwaelewesha jinsi gani ya kutumia nyenzo hizi ambazo Serikali imeziweka.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuzungumzia suala la Stakabadhi ya Mazao Ghalani. Jamani, nani atakayeendelea kubisha sasa kuwa huo siyo mfumo ambao umewasaidia sana wakulima kupata bei bora kwa ajili ya mazao yao? Tuombe sasa mfumo huu wa stakabadhi uenezwe Tanzania nzima maana yake ulikuwa kwenye mazao machache, lakini vile vile haukuwa kila mahali. Wale wazalishaji wakubwa wa mazao ya kilimo na wengi wao wakiwa ni wanawake wangependa sana na wao sasa kujumuishwa katika mfumo huu na kwa hali hiyo haya maghala na huu usimamizi upelekwe mpaka kwenye Wilaya zetu ili sasa wananchi wetu waache kurubuniwa na madalali wa mazao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuzungumzia sera. Jana kuna mtu alikuwa anakashifu Sera ya Viwanda ya 1996 ambayo inaisha mwaka 2020. Mambo mawili makuu ambayo sera hii ilikuwa imelenga; kwanza ilikuwa ni kusambaza viwanda nchi nzima. Jamani, sera ikiwa inasema kitu kama hicho, ina ubaya gani? Inazungumzia inclusiveness ya viwanda nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Sera hii vile vile ilikuwa inazungumzia kueneza viwanda kwenye maeneo ya pembezoni. Mimi natoka kwenye eneo la pembezoni; Ileje ni Wilaya ya pembezoni na kwa muda mrefu sana tumekaa kwa kweli hatuna maendeleo makubwa sana zaidi ya kuwa ni wakulima wazuri, tunazalisha vitu vizuri. Sasa hivi naona Mkoa wa Songwe na wenyewe uko katika maeneo ya kuja kuwekezwa kwenye viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ktika Wilaya yangu, tayari SIDO wameshakuja kupata eneo na wako tayari kuja kuanzisha viwanda; Wilaya yangu sasa hivi inakwenda kubadilika, siyo ile Ileje ambayo mlikuwa mmezoea kuisikia. Wengine hata mlikuwa hamjui Ileje iko wapi? Sasa hivi mnaijua Ileje iko wapi. Ileje inaenda kupata barabara ya lami kubwa itakayofungua uchumi ule kwa kiasi kikubwa sana. Ileje kwa uzalishaji wake, sasa hivi inaenda kupata miundombinu ya Kituo cha Forodha mpakani na Malawi. Haya yote ni maendeleo. Tunaenda kupata Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda, yote haya ni maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachosema mimi, kilimo chetu sasa hivi kinaenda kufanya usindikaji wa hali ya juu. Nasema barabara ile itakapoanza tu, Ileje itakuwa kama mzinga wa nyuki, shughuli zitavyoanza pale. Sasa hivi tu tayari tuna watu wengi sana wako tayari kuja Ileje, wanavizia barabara ikifunguliwa tu! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, anisikilize. Afanye kazi kwa karibu sana na Waziri wa Maji ambaye namshukuru Mungu safari hii ametuwekea fedha ya kutosha kuboresha miundombinu ya maji Ileje. Mheshimiwa Mwijage, Ileje tunalima sana mazao mengi; nafaka, mazao ya biashara kama pareto, tunalima soya, alizeti, mihogo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba viwanda Ileje nimeshaongea na Mheshimiwa Waziri mara nyingi, maeneo yapo tunamkaribisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi, najua hii hoja naweza nikaizungumza kutwa nzima.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Mungu kwa wema na rehema zake nyingi katika maisha yetu. Nakushukuru kwa nafasi hii ya kuchangia hotuba hii ya sekta hii muhimu sana kwa ustawi na mustakabali mzuri wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Dkt. Charles Tizeba, Naibu Waziri Kilimo, Mheshimiwa William Olenasha, Katibu Mkuu na watendaji na wataalam wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya kusimamia sera, sheria na utendaji wa Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni sekta ambayo ikisimamiwa vizuri itainua uchumi wa Tanzania kwa kiwango kikubwa sana kama takwimu zinavyoonyesha. Naipongeza Serikali kwa kuja na mapendekezo mazuri ya kuboresha sekta zinazosimamiwa na Wizara hii. Hii inalenga moja kwa moja kuongeza mali ghafi muhimu za viwanda mbalimbali nchini kwetu hususan vijijini na wilayani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu kwa Serikali ni kukaa kwa pamoja kuweka mikakati inayojengana (complementary) ili kuhakikisha malengo ya uzalishali, tija na ubora vinafikiwa kwenye mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi. Nnazungumzia Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maji, Wizara ya Mazingira, Wizara ya Viwanda, Wizara ya Miundombinu na Wizara ya Nishati na Madini. Hii itawezesha kuhakikisha kuwa lengo letu kuu la kufikia uchumi wa kati na wa viwanda linafikiwa kwa ufanisi, gharama ndogo na matokeo makubwa kwa kuanzia na maeneo ya kimkakati yaliyoainishwa yote yawekewe huduma ya miundombinu muhimu ili yawe na tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba inaonesha kuwa sekta ya kilimo inachangia asilimia 29.1 ya pato la Taifa, ajira asilimia 65 na chakula kwa asilimia 100. Basi Serikali ione umuhimu wa kutoa kipaumbele kwenye sekta hii kwa kuwavutia vijana wengi zaidi kuingia katika sekta kwa njia zifuatazo:-

(i) Kuanzisha vikosi vya uzalishaji vya vijana kila kata nchini na kuainisha aina ya uzalishaji unaofaa kila eneo, ufugaji wa mifugo ya kawaida mikubwa kwa midogo, samaki kwa mabwawa, nyuki na kilimo cha aina mbalimbali;

(ii) Kuwapatia mafunzo ya taaluma ya kufanya shughuli hizi na mafunzo ya ujasiriamali;

(iii) Kuwezesha kujisajili kama kampuni au ushirika wa vijana na kuwaunganisha na vyombo vya kifedha kwa kupata mitaji; na

(iv) Vikundi viwe chini ya Halmashauri na Afisa Kilimo, Afisa Maendeleo ya Jamii, Afisa Misitu na Afisa Mifugo. Wote wawasimamie vijana hawa na kuhakikisha wanaendelea na miradi yao hadi kuvuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo maeneo na shughuli za masoko yatengwe na kuwekewa miundombinu mizuri ya kuuza mazao hayo na vijana wawezeshwe kuanzisha viwanda vidogo na biashara ndogo za mazao wanayozalisha. Hii itawafanya vijana wengi kubaki vijjijini kulima, kufuga, kusindika, kufanya biashara na kuacha kwenda kunyanyasika mijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungependa kuona jinsi Wizara hii inashirikiana moja kwa moja na Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwenye kilimo cha umwagiliaji. Hali kadhalika tuone miundombinu ya barabara na reli na umeme vinaendelezwa kwenye maeneo haya ya uimarishaji wa sekta hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Songwe, hususan Wilaya ya Ileje ambayo iko kwenye Programu ya Bonde la Mto Songwe ina eneo kubwa sana la takriban hekari 6,428 ambalo linafaa sana kwa kilimo cha mazao ya nafaka mbalimbali, ufugaji wa samaki, mifugo na mbogamboga na matunda. Licha ya maji ya Mto Songwe, Wilaya ya Ileje inapata mvua nyingi kila mwaka na ina rutuba ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaitaka Serikali iingize eneo la Bonde la Mto Songwe lililoko Ileje ili lipangiwe mkakati mzuri wa kuliendeleza kwenye mazao ya kilimo cha biashara, kwa mfano, kahawa, ufuta, alizeti, pareto, karanga, mpunga, matunda, mboga mboga pamoja na ufugaji wa samaki wa mabwawa, kuku, ng’ombe wa maziwa na wa nyama, nguruwe, mbuzi, kondoo na nyuki. Hii iendane na wazo la hapa juu la kuwawezesha vijana kwenye vikosi vya uzalishaji itainua ajira sana, mapato ya vijana wenyewe, Halmashauri na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ileje ni wilaya ya mpakani mwa Tanzania na Malawi na kwa kiasi Zambia lakini vilevile ni jirani sana na Wilaya ya Tunduma ambako biashara kubwa inafanywa na watu wa nchi za jirani hadi DRC Kongo. Halmashauri ya Ileje ilijenga soko kwa ajili ya mazao lakini NFRA wamekuwa wakitumia soko la Isangole kama maghala yao. Tunaitaka Wizara kujenga maghala makubwa sana kwa nafaka na mazao mengine ya biashara kama kahawa, pareto, viungo mbalimbali kama iliki, pilipili manga, mdalasini, tangawizi, cocoa na kadhalika. Tunaiomba Wizara itupatie maghala ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu pia kuwa SAGCOT inahusisha Mkoa wa Songwe. Pia tunaitaka Serikali itufahamishe hadi sasa Songwe na hususan Ileje inaguswa vipi na mradi huu na ni katika maeneo yapi na hawa wahusika kwa eneo letu ni akina nani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa ya kilimo chetu ni upatikanaji wa mvua za kutosha, mbegu bora na pembejeo. Tunaipongeza sana Serikali kwa kuja na pendekezo la kuboresha mfumo wa upatikanaji wa pembejeo. Huu ni mfumo wa kimageuzi na utahakikisha wakulima wengi kupata pembejeo na kulima vizuri zaidi. Tutashukuru kuwa sasa pembejeo zitapatikana kwa wakati na kwa bei nafuu na kuondoa malalamiko ya muda mrefu na vilevile kuhakikisha wakulima wanazalisha vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri atafute muda wa kutembelea Ileje yeye na maafisa/ wataalam wake waje kujionea wenyewe fursa nyingi zilizopo wilayani humo ili watuweke kipaumbele chini ya programu ya SAGCOT na mradi wa Bonde la Mto Songwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Songwe na Mkoa wa Mbeya na Iringa ni wakulima wakubwa wa arabica coffee, pareto, chai na viungo kwa kutaja machache. Japan wana soko kubwa la gourmet coffee na wanailipa bei nzuri. Wilaya hizi zina uwezo wa kuzalisha aina hii ya kahawa na kuiuza Japan. Tunaitaka Wizara ituunganishe na soko hilo lakini pia watupatie utaalam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba mnada wa kahawa ufanyike Songwe kwenye uzalishaji mkubwa wa kahawa na tunahitaji soko/viwanda vidogo vya kuongeza thamani ya pareto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata fursa ya kuchangia hoja hii muhimu katika Taifa letu. Naungana na wananchi wa Mkoa wa Arusha na Taifa zima kwa maafa ya vifo vya wanafunzi na Walimu wa shule ya Lucky Vincent. Mungu awafanyie wepesi wafiwa wote na Mungu awalaze marehemu wote mahali pema peponi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza Waziri wa Maji, Mheshimiwa Injinia Gerson Lwenge, Naibu Waziri Mheshimiwa Injinia Isaack Kamwelwe, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri sana wanayoifanya pamoja na ufinyu wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuanza kuchangia kwa kuonesha masikitiko kuwa Wizara muhimu kama hii ambayo inagusa moja kwa moja maisha na ustawi wa jamii nzima ya Watanzania imepewa bajeti ndogo. Nina imani kabisa kuwa Watanzania wakipatiwa maji safi na salama watakuwa na ustawi mkubwa wa kiafya, kiuchumi na kimazingira. Maji yataboresha afya za wananchi na kupunguza maradhi na vifo. Kwa kuzingatia umuhimu wa sekta hii tunahitaji kuona bajeti kubwa zaidi ikitengwa kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuliwahi kupendekeza kuwa Serikali izingatie changamoto za maji vijijini zaidi na wazingatie kwa njia mbili. Kwanza, yale maeneo yenye maji ya kutosha lakini wanahitaji miundombinu tu lakini pili ni yale maeneo yenye ukosefu kabisa ya maji kutokanana ukame au mvua isiyotosha. Mikakati ifanywe kutokana na changamoto zilizopo kuliko kutoa suluhisho aina moja kila sehemu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ileje na Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ni maeneo yenye maji mengi sana mwaka mzima kwa sababu ya mito, vijito na chemichemi nyingi kwa hivyo tusingetegemea kuwa wilaya na mikoa hii iendelee kuwa na tatizo la maji la miaka mingi namna hiyo. Je, ni lini sasa Wilaya ya Ileje na mikoa tajwa itapatiwa miundombinu tosha ya kueneza maji katika kata zote lakini zaidi kwa maeneo ya Tarafa ya Bulambya (Humba, Isongole, Chitete, Izubo, Mbebe, Mlale, Dubigu na Malangali).

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo haya wanategemea maji ya Mto Songwe ambayo ni machafu sana. Hata kule kwenye mabomba maji ni machafu sana. Tunaiomba Wizara itukamilishie hii miradi ili tuondokane na adha hii kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ileje ina skimu nyingi za umwagiliaji na zote hazifanyi kazi kikamilifu kwa sababu ya upungufu mdogo mdogo ambao kwa kweli haustahili kukwamisha mradi wa kipindi kirefu namna hiyo. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri atuwezeshe kumalizia skimu zote za umwagiliaji Ileje ili kilimo cha uwagiliaji kifanyike kwa tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ileje na Kyela ni sehemu ya mradi wa Bonde la Mto Songwe unaoendeshwa kati ya Serikali ya Tanzania na Malawi zinazopitiwa na Mto Songwe. Mradi huu upo Mkoa mpya wa Songwe na Ileje na Kyela Mbeya na kwa upande wa Malawi ni wilaya mbili zipo pembezoni mwa Mto Songwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo kuu la mradi huu wa Mto Songwe ni kutunza maji yanayosababisha mafuriko kipindi cha mvua na kuathiri wakazi wa nchi hizi mbili wanaoishi karibu na Ziwa Nyasa. Utekelezaji wa mradi huu ulilenga kujenga mabwawa matatu kandokando mwa Mto
Songwe mpakani mwa nchi hizo, karibu na Ziwa Nyasa. Mabwawa haya yangetumika kuzalisha umeme na pia kufanya kazi za umwagiliaji karibu hekari 3,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri ameainisha kuwa mradi huu uko kwenye awamu ya tatu. Je, hizo awamu mbili zilizopita zilihusu masuala gani? Vilevile Mto Songwe umekuwa ukihamahama kwa sababu ya mabadiliko ya tabia nchi huku ukiharibu rasilimali za wakazi wa bonde na kingo zake kutokana na mafuriko. Je, Serikali ina mkakati gani wa kudumu wa kudhibiti uharibifu huu?

Mheshimiwa Naibu Spika, wakazi wa Kata ya Bupigu Ileje walizuiliwa kutumia Bonde la Mto Songwe kwenye kata yao kwenye eneo ambalo lilikuwa lichimbwe bwawa kubwa mojawapo tangu wakati mradi ulipoanza hadi sasa. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza kushughulikia bwawa hilo sasa au kuwaruhusu wananchi waendelee na shughuli zao?

Mheshimiwa Naibu Spika, Mto Songwe una urefu wa kilomita 200 ndani ya Ziwa Nyasa, eneo la Bonde ni square kilometer 4,243, square kilometer 2,318 ziko Tanzania na square kilometer 1,025 ziko Malawi. Bonde lina wakazi 341,104 kati yao 210,005 ni wa Tanzania na 131,099 ni wa Malawi. Bonde la mto lina eneo la hekta 6,200 zinazofaa kwa shughuli za uzalishaji na hii ni sababu nyingine kubwa ya kuwa na mradi huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali inaweza kutupatia mkakati wa maendeleo ya bonde hili na ratiba nzima ya utekelezaji na fedha ya kuendeleza mradi huu? Je, Serikali itakaa lini na Halmashauri ya Ileje na Kyela kwa maana ya kutoa taarifa ya kina ya mipango ya utekelezaji wa mradi huu na nini utakuwa ushiriki wa Halmashauri hizi moja kwa moja lakini hata indirectly kwenye mradi huu? Je, kuna mpango gani wa kukutanisha Halmashauri za upande wa Tanzania na wa upande wa Malawi? Kutokana na mpango mkakati wa mradi huu nini kinategemewa kuwa matokeo makubwa ya mradi huu kwa nchi kwa ujumla lakini kwa Ileje na Kyela kiuhalisia?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuhitimisha, naunga mkono hoja ya kuangalia uwezekano wa kuiongezea bajeti Wizara hii na kuziweka fedha hizi kwenye Mfuko Maalum wa Maji Vijijini ili zisitumike vinginevyo. Tunapendekeza asilimia 70 ya fedha ya mfuko huu iende vijijini na asilimia 30 iende mijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.
Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Kamisheni ya Pamoja ya Bonde la Mto Songwe kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Malawi pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Amani na Usalama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nami napenda kuchangia hoja hii iliyopo mbele yetu. Kwanza naipongeza Serikali kwa kuleta hili Azimio hapa Bungeni kwa sababu hili suala la mradi wa Bonde la Mto Songwe ni la muda mrefu lakini sasa naona linafikia tamati na inasaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda kupongeza Serikali kuwa sasa hivi pia imeongeza wigo wa zile Wilaya ambazo zitaguswa na mradi huu au programu hii kutoka zile mbili za mwanzo iliyokuwa Ileje na Kyela, sasa mpaka Momba, Mbozi na Mbeya Vijijini, kwa hiyo hii vilevile italeta manufaa zaidi kwa wananchi wa sehemu hizo za Songwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda vilevile kuzungumzia kuwa kwa kweli hii programu imekuja wakati mzuri, kwa sababu kwa muda mrefu sana Mto Songwe umekuwa ukisumbua sana pale ambapo kunakuwa na mafuriko ambayo yanaletea kingo zake kuleta madhara mengi sana ya kimazingira pia kuharibu miundombinu ya eneo husika na kwa kudhibiti sasa hivi itatusaidia sana kuhakikisha kuwa Mto Songwe unadhibitiwa lakini vilevile unatumika vizuri zaidi kiuchumi kulinda mazingira, vilevile kuboresha maisha ya wananchi wa maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na maendeleo hayo inaonekana kuwa programu hii pia itasababisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya barabara, vituo vya afya, elimu na masuala ya utalii. Napenda kutoa rai kwa Serikali kuwa wakati wanapofikiria kufanya miradi hii basi wazingatie miradi au mipango ya miradi iliyoko pale kwenye eneo hilo ili tusiwe tuna miradi ambayo inakwenda sambamba wakati kuna haja ya kumalizia ile iliyopo ili tusilete ile duplication au kuzidisha ukiritimba kwenye shughuli za maendeleo za eneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda sana kutoa rai kwa Serikali juu ya kuhusisha wadau muhimu. Kwa sababu hata hapo nyuma ambapo mradi ulikuwa umefikiriwa kufanywa, kuna wananchi mpaka leo walikuwa wameambiwa kuwa maeneo yao wasiyatumie kwa sababu mradi utapita, kama mnavyojua ni miaka mingi tangu wazo liwekwe na wamekuwa kwenye hali ya sintofahamu wakisubiri nini kinaendelea. Kwa hiyo, safari hii tutakapomaliza kuridhia na itakapoanza kufanya hii programu basi wananchi wafahamishwe, Halmashauri husika zihusishwe moja kwa moja ili sasa wananchi watambue ni nini kitakuja kuendelea katika maeneo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuzungumzia masuala ya kujifunza kutoka kwenye matokeo ya miradi mingine ya haya mabonde, tumesikia hapa kuwa kulikuwa kuna mabonde kama tisa nchini ambayo yamekuwa na miradi lakini yamekuwa na ufanisi ambao wakati mwingine sio mzuri sana. Sasa hii ingekuwa ni fursa nzuri kwa mradi huu na wenyewe kuangalia jinsi gani watajifunza tusiingie tena katika matatizo yale ambayo yaliingiwa katika miradi ya huko nyuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Ruaha tunajua jinsi ambavyo shughuli za kibinadamu zimeathiri sana mto ule na mpaka sasa hivi unaathirika hata kina chake na kwa hiyo inaleta shida. Sasa na huu mradi nao ukaangaliwe katika mtazamo huo na zile Wizara zote ambazo zinahusika katika mradi huu basi ziwe na ushirikiano wa karibu ili kila mmoja asimame katika nafasi yake kuhakikisha kuwa mradi huu unakuwa wa manufaa kuliko kuwa wa hasara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala amelizungumzia Mheshimiwa Lissu pale ningependa kusema pamoja na kuwa amelizungumza kwa njia ambayo haikufurahisha basi likaangaliwe, ingawa mimi kwa uelewa wangu mdogo ingawa siyo Mwanasheria, huu ni mradi ambao unahusisha rasilimali zinazogusa nchi mbili. Kwa hiyo, naamini kutakuwa na makubaliano mazuri ya jinsi gani ya kusuluhisha usimamizi wake na sikuona kama kulikuwa kuna sababu ya kutoa maneno makali ambayo kwa kweli hayajengi.

Mwisho kabisa nataka kupongeza sana na kuomba Waheshimiwa Wabunge turidhie Azimio hili kwa sababu linakwenda kujenga na kuboresha miundombinu na rasilimali hii nzuri itatumika vizuri zaidi kuliko jinsi ilivyo sasa hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya SADC ya Usimamizi wa Mazingira kwa ajili ya Maendeleo Endelevu (The Southern African Development Community SADC – Protocol on Environmental Management for Sustainable Development)
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naridhia hizi itifaki zote ambazo tunataka kuzipitisha hapa, lakini nataka nijikite kwenye hiyo ya Montreal, Itifaki ya Montreal. Hii ni itifaki muhimu sana na ninaamini kama ingekuwa dunia haikupitisha hii saa hizi tungekuwa tunazungumzia hali mbaya sana kwa afya zetu kuhusiana na jinsi ambavyo tabaka ya ozone ambayo ingeshakuwa imeharibika kwa kiasi kikubwa sana. Itifaki hii sasa hivi inaendelea kulenga kuboresha kanda zetu au nchi mbalimbali jinsi ambavyo inajiwekea sasa mikakati zaidi ya kuhakikisha kuwa inaendelea kuzingatia utekelezwaji wa itifaki hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwetu sisi Tanzania ni muhimu sana kwa sababu tumeona kabisa jinsi ambavyo matatizo ya tabianchi yanatuathiri, na athari zinazotokana na mmomonyoko au ubomokaji wa ozone layer ni mbaya kuliko hata zile tunazozizungumzia za masuala ya carbon dioxide. Kwa hali hiyo nafikiri protocol hii ni muhimu sana kuizingatia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu ni moja tu kwa Serikali; itambuliwe kuwa huko nyuma utafiti uligundua kuwa hii ozone au hili tabaka linaathirika sana na kemikali zinazotumika katika kutengeneza viyoyozi, kutengeneza majokofu na kutengeneza haya makopo ya dawa za kupulizia. Na hivi karibuni tumeona kuwa majokofu na viyoyozi vingi chakavu vinaingia nchini, sijui ni nani anayekagua kuhakikisha kuwa havibebi zile kemikali ambazo huko nyuma ndiyo zilitambulika kuwa zinaathiri hili tabaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuwa kutokana na hii, hii gharama ya kuondoa, ya kusafisha hizi kemikali zilizoko katika matumizi ya wananchi ni kubwa sana. Huko nyuma kulikuwa kuna fungu lilikuwa linatolewa ambalo lilikuwa linapitishwa Umoja wa Taifa, nakumbuka kwa Tanzania Umoja wa Taifa walikuwa wanasimamia fungu hilo, kwa hiyo walikuwa wanafanya kazi na viwanda kuhakikisha kuwa wanaondoa hizi kemikali. Sasa sijui kwa sasa hivi kama lile fungu bado linaendelea kwa Tanzania.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. JANETH Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami kuchangia. Naomba kwanza kuwapongeza sana Wenyeviti waliowasilisha ripoti za Kamati zao. Kwa kweli, nasikitika kuwa, muda hautatosha sana kwa sisi kuchangia kikamilifu, lakini nitajitahidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja zinazotolewa na Waheshimiwa Wabunge kuhusiana na kuwa nchi yetu ina rasilimali nyingi sana, lakini bado tuko maskini, kwamba mazao yetu yanauzwa nchi za jirani. Labda kwa ufupi tu niseme kuwa na rasilimali za kutosha peke yake si sababu ya kuwa tajiri, ila tunachotakiwa kufanya ni jinsi gani tunakuwa na taasisi zitakazoweza kugeuza kwa tija rasilimali hizi na kuzifanya kuwa mali, mapato na bidhaa zitakazoendesha uchumi wa nchi, lakini suala la mazao yetu kuuzwa Kenya, Rwanda, Burundi au Uganda vile vile sio tatizo; sisi issue kwetu ni kuwa tunapata mapato kutokana na biashara hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sisi tuko kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa vyovyote vile itafika siku ambayo mazao, watu, bidhaa vitakuwa vinapita kama vile vinatoka hapa kwenda Morogoro. Kwa hiyo hilo lisiwe ni jambo la kuchukua muda mwingi kulizungumza,
tunachotaka kuona hapa ni kuwa mazao yetu au bidhaa zinazokwenda nchi nyingine yanasimamiwa vizuri, kwa maana ya bei nzuri na mapato yanayoingia katika Taifa letu, lakini vile vile na nchi yetu pia inaruhusiwa kuingiza mazao kutoka nchi nyingine za jirani kupitia kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna suala la magogo yanayotoka Congo na Zambia. Hakuna ubaya wowote magogo yale yakapitishwa Tanzania na sisi tukaya-export kama vile na sisi mali zetu zinavyokuwa exported na nchi jirani kwa sababu, mwisho wa yote ni biashara ya kimataifa. Kwa hiyo, nataka kuihamasisha Serikali, kama vile ambavyo sisi mazao yetu yanaenda kuuzwa nchi nyingine, basi na ya nchi nyingine yapitie kwetu, ili na sisi tuweze kuoata mapato yanayotokana na usafirishaji wa mazao hayo and afterall sisi ni hub kutokana na location yetu ya kijiografia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa vile vile kuzungumzia kwa kifupi sana suala la mashirika ya umma. Kwa kweli, mimi bado nina imani kubwa kuwa mashirika ya umma mengi ni mzigo kwa Taifa letu, kwa sababu, ni muda mrefu sana yanaendeshwa kwa hasara. Ingekuwa ni kampuni binafsi miaka mitatu, minne, mitano, inatosha kuonesha kuwa hili shirika halifai. Kwa hiyo, ninachotaka kusema aidha, tuweke menejimenti ambayo itayageuza haya mashirika yakaendeshwa kibiashara na kiushindani au tuyafunge kwa sababu, yanaendelea kutunyonya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tuhakikihe kuwa watu tunaowaweka pale, wanawekwa pale kwa ushindani wa uwezo wao na sio wa kuteuliwa. Hili, jambo nafikiri limeshazungumzwa sana humu ndani; ukimweka mtu kwa kumteuwa inakuwa vigumu hata kumdhibiti, lakini ukimwajiri mtu kwa vigezo unampima kwa vigezo vyake vya delivery, akishindwa ku-deliver unamwondoa. Kwa hiyo, kwa kweli, nafikiri kwenye masuala ya Mashirika ya Umma hata tungelipa hayo madeni sidhani kama tutakuwa tumetatua tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye suala la msingi ambalo nataka kulichangia leo, ni kuhusiana na kilimo. Bado kilimo ni fursa kubwa sana kwa Watanzania kujiondoa katika umaskini. Ningependa sana kuona Serikali sasa inakuja na mkakati badala ya kila siku kutuambia changamoto, tunazifahamu changamoto zote zilizoko kwenye sekta ya kilimo. Tunaomba sasa tupate mkakati wa Serikali, kwamba je, mnapanga kufanya nini, ili kilimo kiinuke? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kuwa tayari kuna mikakati kwenye mazao. Mazao muhimu ya kibiashara au ambayo tunapeleka nje yana bodi zake na vilevile Serikali imejitahidi sana kuondoa tozo zile ambazo zilikuwa sumbufu. Hata hivyo bado tunataka kuona jinsi gani sasa bodi hizi zinafanya kazi ya kuhakikisha kuwa, wakulima wanawezeshwa kulima kwa tija na wanapata mapato stahili na mwisho wa yote uchumi unakuwa na asilimia kubwa zaidi ya pato letu la Taifa linachangiwa na kilimo ambacho kina watu zaidi ya asilimia 70 ambao wanakitumikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa tamko lake la hivi juzi, kuwa sasa hivi wakulima waweze kuuza mazao yao wao wenyewe bila kupitia madalali. Hata hivyo, hata kwa hivyo vyama vya ushirika vya mikoa au vya wilaya lazima watendaji wawe wenye weledi, wenye kujua kuendesha shughuli hizo kibiashara na wawe wazalendo. Kwa hiyo turudi kule kule, tuajiri watu ambao wana uwezo wa kuendesha vyama hivi vya ushirika la sivyo tutarudi, tutakuwa tuna-recycle watu tunaita majina haya tunarudi huku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nataka kutoa pongezi sana kwa Mfuko wa Kahawa kwa jinsi ambavyo wamejitahidi kupunguza gharama za tozo. Hata hivyo bado tuna shida kubwa sana ya tozo nyingine ambazo zinatakiwa kuondolewa, ili ziwaguse wakulima moja kwa moja. Tozo nyingi zilizoondolewa kwa mtazamo wangu zinaenda kuwasaidia zaidi wasindikaji, lakini je, wasindikaji wa mazao mengine ni akina nani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasindikaji kwenye mazao mengine ni haohao wakulima, kwa hiyo unakuwa hujamsaidia sana, lakini kuna tozo ambazo zinaenda kugusa uzalishaji moja kwa moja. Ningependa Serikali iziangalie na hizo iziondoe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kukimbia haraka haraka kwa sababu ya muda. Kuna suala la korosho, zao la korosho limeonesha kabisa kuwa ni zao ambalo sasa hivi linafanya vizuri sana. Linafanya vizuri sana kwa sababu limewekewa mkazo na Serikali yenyewe, lakini vile vile na bodi yake. Nashangaa kusikia mtu hapa anasema eti zao la korosho halijasaidiwa chochote na Serikali, sijui huyu mwenzetu yeye yuko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la korosho limewekewa mikakati mizuri, linasimamiwa vizuri na sasa hivi linaenda vizuri. Pamoja na hayo kuna suala la kuhakikisha kuwa wazalishaji wapya wa korosho wanawezeshwa, wazalishaji wapya wa korosho wanapewa pembejeo… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami pia nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Naibu Waziri na Maafisa wote kwenye Wizara yake kwa hotuba nzuri. Naomba nianze kwanza kwa maombi maalum kwa Wilaya yangu ya Ileje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya yangu ya Ileje kwa ufadhili wa Balozi wa Japan tulijengewa Chuo cha Ufundi VETA tukaweza kupata majengo mawili na karakana na condition moja wapo ilikuwa Halmashauri imalizie jengo la utawala, vyoo na sehemu ya kulia chakula. Niliwaomba Wizara watusaidie wakatupa conditions kuwa tupanue eneo la hiki chuo, tusajili ile ardhi, kwa mfano tuwe na title deed, halafu ndiyo tutaikabidhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuliwaandikia barua mwezi tarehe 8 Novemba, 2017 kuwa tumekamilisha na tunaomba sasa waichukue ili waiendeshe na kumalizia miundombinu iliyobakia kama ambavyo wenyewe walikuwa wameahidi wangefanya. Sasa naangalia katika kitabu hiki cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 26 - 27 ambako ndiyo amezungumzia masuala ya VETA, sioni sehemu yoyote ambapo imetajwa Ileje na sielewi sasa hiki chuo kimeshasimama zaidi ya miaka mitatu hakifanyi kazi na ndicho chuo pekee cha ufundi Mkoa mzima wa Songwe. Pengine sasa wangetufikiria jinsi gani watatusaidia, japo kianze kufanyakazi. Kwa sababu hata mfadhili wa kwanza ameahidi kurudi tena kutusaidia lakini mradi kianze kwanza, hilo ni jambo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Ileje ni Wilaya ya pembezoni na ni Wilaya kongwe na kwa miaka mingi hatuna shule ya wasichana ya boarding wala ya day. Watoto wetu wa kike inabidi wakae ama kwenye mabweni machache ambayo hayatoshi au wapange kwenye nyumba za watu au wanakwenda Wilaya nyingine kabisa kwenda kusoma shule za sekondari. Tuna tatizo kubwa la mimba za utotoni kwa sababu ya matatizo yanayowapata wasichana katika hekaheka hizi za kutafuta elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile wazazi wanakuwa na gharama kubwa sana inapobidi wasafirishe watoto wao kwenda kuwapeleka kusoma Wilaya nyingine. Je, kwa nini Serikali haina utaratibu wa kuwa na shule ya wasichana ya sekondari kila Wilaya kama ambavyo ni utaratibu wa mambo mengine katika Wizara zingine? Tunaomba sana tusaidiwe tayari wenyewe tuna mikakati ya kuanza ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana, lakini tutahitaji Serikali na yenyewe kutia mkono wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maoni mengi yametolewa na Waheshimiwa Wabunge pande zote, ningependa hayo pia yazingatiwe. Kamati imetoa maoni mazuri sana, naomba yote kama ikiwekeza yazingatiwe kwa sababu ninaamini kabisa yakifanyiwa kazi hayo hii Wizara itafanya kazi nzuri zaidi na watoto wetu watafaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije sasa kwenye suala zima la VETA na Vyuo vya Ufundi Stadi au Vyuo vya Kati. Imetokea tabia au mtindo kuwa vyuo vya kati vikifanya vizuri vinapandishwa na kufanywa kuwa vyuo vikuu, nafikiri tunafanya makosa makubwa sana kwa kufanya hivyo. Vyuo vya Kati ni vyuo vinavyofundisha masuala ambayo ni ya moja kwa moja yanaweza kuingia katika ajira, kwenye viwanda na hali kadhalika, kwa sasa hivi tunazungumzia uchumi wa viwanda, huu ndiyo ulikuwa wakati sasa wa kuboresha vyuo vya kati, kuviongezea mitaala ambayo inalingana na mahitaji ya viwanda tunavyotaka kwenda kuvijenga na kuvifanya viwe vinatoa ufundi mzuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuhamasisha kama itawezekana, vyuo vya ufundi vyote vifundishe kwa mitaala yao kwa kiswahili, itawasaidia hawa mafundi wadogowadogo ambao wanatusaidia mitaani magari, redio, television, karakana mbalimbali hizi wale vijana wangefundishwa kwa Kiswahili kwa sababu wengi ni darasa la saba na form four tungejikuta tuna mafundi ambao wana weledi mzuri badala ya ule wa kubahatisha, vilevile tukajikuta kuwa tumeanzisha ajira nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado niko katika masuala ya vyuo vya ufundi, hasa VETA. VETA tumekuwa tukiichangia fungu la skills development levy ya asilimia 4.5; theluthi moja ndiyo imekuwa ikienda VETA moja kwa moja, theluthi mbili ya tatu imekuwa ikienda Serikali Kuu. Sasa hii inachangiwa na waajiri. Waajiri hawa hawajui ile theluthi mbili inakwenda kufanya kazi gani, kwa sababu lengo ilikuwa ni kupeleka VETA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu tayari waajiri wanakuwa na wasiwasi kwa nini hela haiendi yote VETA? Nashauri kwamba sasa hivi tunataka kwenda kwenye uchumi wa viwanda, VETA zetu lazima ziimarishwe, basi lile fungu lote la asilimia 4.5 liende VETA moja kwa moja kama ambavyo hiyo theluthi moja inakwenda. Hii kwanza itawafanya waajiri wenyewe wanaochangia kuwa na imani, lakini vilevile wanaweza hata kuweza kuchangia zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuhusu VETA na vyuo vya ufundi stadi viko chini ya Wizara ya Elimu lakini vinalenga waajiri ambao wako chini ya Wizara ya Kazi na Ajira.

Ninapenda kuihamasisha Serikali kama itawezekana na kama ambavyo inafanyika kwenye nchi nyingine nyingi, VETA na vyuo vya ufundi stadi viende chini ya Wizara ya Kazi na Ajira kwa sababu kwanza itakuwa ina uhusiano wa moja kwa moja na itajibu moja kwa moja hoja za waajiri juu ya mahitaji yao ya ajira. Jinsi ilivyo sasa hivi waajiri hawana namna ya kuongea na Wizara ya Elimu kuhusiana na masuala haya kwa sababu hakuna ule uhusiano wa moja kwa moja, lakini wakiwa kwenye kazi na ajira moja kwa moja kutakuwa kuna mahusiano ya waajiri ambao ndiyo wanawahitaji hao wafanyakazi wenye weledi na Wizara, lakini vilevile itapunguzia Wizara hii kazi nyingi. Hii Wizara inashughulikia mambo mengi mno, matokeo yake hata ufuatiliaji wa ufanisi unapungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara moja inashughulikia elimu ya msingi, sekondari, vyuo vikuu, ufundi stadi, maktaba, taasisi mbalimbali, sasa vitu vyote hivi viko chini ya Wizara moja halafu haohao wasimamie ubora, wasimamie utoaji huduma, wasimamie miradi, kwa kweli naona kama tumerudhika vitu vingi sana kwa Wizara moja. Serikali... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kuipongeza sana Serikali kuanzia na Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa hatua thabiti anazochukua za ujasiri na uthubutu wa hali ya juu katika kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi yetu sasa zinanufaisha Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, Naibu wake na Watendaji wote wa Wizara kwa hotuba nzuri sana mbili zote ambazo zimetolewa ambazo kwa kweli zimeonesha jinsi gani Serikali imekuwa sikivu, imezingatia masuala muhimu ambayo Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakiyatoa mara kwa mara, lakini imejielekeza sasa katika suala zima la uchumi wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, natoa pongezi sana kwa sababu nimeona jinsi ambavyo hii bajeti kwa kweli safari hii imefurahisha Umma mzima wa Watanzania. Kuna mambo machache tu ya kurekebisha ambayo yako chini ya uwezo wao na naamini kabisa watayafanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, nataka nianze kuzungumzia suala zima la amana pamoja na mikopo kwenye benki zetu. Bado kuna hatua kubwa sana inahitajika kufanyika katika kuelimisha wananchi wa Tanzania matumizi ya benki kwa maana ya kuweka akiba na mikopo. Bado benki zetu zinafanya kazi kwa kiwango cha chini sana kwa maana ya kuwafikia wananchi wengi ambao wanahitaji huduma hizo.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi kuna suala zima la huduma za kifedha kutumia mitandao. Hii ingekuwa ni fursa kubwa sana kwa benki sasa kujiunga katika huduma kama hizo kurahisisha kuwafikia wananchi kwa huduma za kifedha kwa maana ya amana pamoja na mikopo.

Mheshimiwa Spika, nikija kwenye suala hilo hilo la mikopo, kutokana na taarifa tulizopokea bado tuna tatizo kubwa la mikopo kwa sekta binafsi haliendi vizuri na hata kwa benki zenyewe. Hii imedhihirika kutokana na sababu kubwa za mikopo chechefu ambapo tumekuwa tukielezewa ambayo vilevile kwa upande mmoja inatokana kwanza, pengine na jinsi ambavyo benki yenyewe imekuwa ikitoa mikopo hiyo lakini kwa kiasi kikubwa inatokana na Serikali na Taasisi zake kushindwa kulipa Wakandarasi na watoa huduma wengi na hivyo kuwasababishia wao kushindwa kulipa mikopo yao benki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili naomba sana Serikali ilifanyie kazi kwa sababu uchumi unategemea sana mzunguko wa fedha. Sasa kama kuna fedha iko mahali imetumika lakini hairudi, inasababisha wafanyabiashara, wazalishaji wadogo na hata hao wanaoambiwa wamefunga maduka au wamehamia wapi na wapi, inatokana na kuwa labda wameshindwa kumudu sasa kuendesha biashara bila kurudishiwa madeni ambayo wanaidai Serikali. Napenda sana hilo lifanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile kuna suala zima la uwekezaji kwenye miradi ya umma au miradi ya kimkakati. Kwa muda mrefu sana humu ndani tumekuwa tukizungumzia miradi ya kimkakati ambayo kwa msingi wake, hii ndiyo ingezindua au ingefufua au ingechangamsha sana viwanda vyetu. Miradi ya chuma, makaa ya mawe, magadi (soda ash); hii ni miradi ambayo inajenga msingi wa viwanda. Sasa bila hii kuanzishwa na kuendelezwa tutashindwa hata kuendeleza viwanda ambavyo tunavitegemea.

Mheshimiwa Spika, tuna mradi wa Kilimanjaro machine tools, huu ulishindwa kuendelea kwa sababu huko nyuma ilibidi chuma kiagizwe kutoka nje, sasa tuna chuma nchini, kiendelezwe ili viwanda kama hivi sasa vianze kuchonga vipuri tunavyohitaji kwa ajili ya viwanda vyetu. Kwa hiyo, unaona moja kwa moja kuna muunganiko mzuri sana sasa hivi katika nchi yetu wa kiuchumi ambao utawezesha viwanda kukua kwa haraka sana. Tungependa sasa kuona jinsi ambavyo hii miradi ya kimkakati inaanza kufanya kazi. Tumeisikia kwa muda mrefu, tunataka sasa ianze kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, vilevile kuna suala zima ambalo nataka kuipongeza sana Serikali, wamejikita katika kuhakikisha kuwa kilimo, maji na miundombinu ya uwekezaji wa kwenye nishati unapewa kipaumbele. Hii vilevile ni misingi mizuri kwa ajili ya viwanda. Sasa kwenye kilimo nataka kuishauri Serikali, tusifanye kazi kwa mazoea. Kilimo kinahitaji mapinduzi makubwa sana ili kiwe kweli kilimo kitakacholeta tija. Tunatakiwa kuwekeza asilimia 10 ya mapato yetu kwenye kilimo peke yake. Hiyo ndiyo itatuwezesha sasa kukuza kilimo katika yale mazao ya msingi ambayo tunajua yatatusaidia katika viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna mifano ya nchi kama Vietnam. Vietnam mpaka mwaka 1990 walikuwa wanaagiza chakula nje. Sasa hivi katika nchi 10 au 20 zinazozalisha mazao ya kilimo kwa wingi, Vietnam na yenyewe imo ndani. Wameboresha kilimo chao na uzalishaji wao na ufugaji kwa ku-modernize, kwa kutumia teknolojia, kwa kutumia ubia na nchi zilizoendelea ili kuhakikisha kuwa wananchi wao wanazalisha kwa tija. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi kwa nini tusifanye hivyo? Sasa hivi tumeingia kwenye uhusiano wa Kidiplomasia na Israel. Israel wana teknolojia ya hali ya juu katika masuala haya ya maji, umwagiliaji na kilimo. Tunaweza tukaungana nao. Hii siyo ngumu sana, kwa sababu vijana wetu wakienda kule au wao wakija kwetu, moja kwa moja tunaweza tukajikuta tunakuza kilimo chetu.

Mheshimiwa Spika, tuna mazao tayari yanaonyesha tija kubwa sana. Kwa mfano, korosho, ufuta, mbaazi, nafaka za aina mbalimbali na dengu; sasa hivi tunahitaji kupeleka pia uzalishaji mkubwa kwenye kilimo cha mawese na alizeti. Yote haya ni mazao yanayotakiwa yapewe kipaumbele zaidi ya yale mazao ya kawaida ambayo tulikuwa tumezoea kuzalisha ya kahawa na mazao mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuki-diversify namna hii tutakuta kilimo chetu kinachangia pato kubwa zaidi kuliko ilivyo sasa hivi. Ni lazima sasa hivi tujipambanue na kilimo kama njia kubwa ya kuingia kwenye viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile biashara ni eneo ambalo tumekuwa tunakua vizuri, siyo Tanzania peke yake, lakini Afrika Mashariki, Afrika na hata dunia nzima. Tanzania tuko katika nafasi nzuri sana kwa sababu tuna maeneo makubwa ya mipakani. Cross border trade bado ni eneo zuri sana kwetu sisi Watanzania, lakini limegubikwa na mambo mengi ya urasimu ambayo yanafanya isiwe rahisi kwa biashara kuendeshwa kati ya mipaka yetu.

Mheshimiwa Spika, tuna matatizo ya watu wa customs, tuna matatizo ya uwezo mdogo wa kusimamia masuala haya, tuna matatizo ya rushwa, tuna matatizo ya bureaucracy, yaani licensing na zile taratibu nzima za kufanya biashara kati ya nchi na nchi bado hazijawa nzuri hata katika Kanda ambazo tayari tuko katika umoja. Kwa mfano, East Africa, tujaribu sasa kuondoa zile non-tariff barriers ambazop ndiyo zinazoturudisha nyuma, tuanze kufanya biashara sisi wenyewe kwa wenyewe. Tuachane na mambo ya kukimbizana na nchi za nje ambao wanatuletea vikwazo vingi sana. Tuna fursa kubwa sana sisi Waafrika kwa Waafrika kufanya biashara pamoja.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia hotuba hii muhimu. Niwapongeze sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Mambo ya Ndani, Naibu wake na Watendaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kazi kubwa na muhimu ya kulinda usalama wa raia na mali zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuanza kuchangia kwa kuzungumzia masuala ya Wilaya za pembezoni kama vile Ileje ambako tuna changamoto nyingi za kiusalama kwa sababu tuko mpakani na Malawi na Zambia, pia, kuna mwingiliano mkubwa wa wageni toka Somalia, DRC Congo, Zambia na Zimbabwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zetu ni kuwa Ileje yenye ukubwa wa kilometa za mraba 1,906 na yenye jiografia ngumu ya milima na mabonde na raia wake ambao wako mbalimbali sana na kwenye umbali mrefu kati ya kata na kata, kijiji na kijiji, ina kituo kimoja tu cha Polisi miaka takribani 44 ya Wilaya hii kongwe. Hiki ni kikwazo kikubwa kwa utoaji huduma, Kituo Kidogo cha Polisi cha Isoko wananchi wametumia nguvu zao kukijenga na kupaua. Tunaomba Serikali iwaunge mkono kukimalizia na kujenga nyumba za watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Ileje ina upungufu mkubwa wa Askari, Wilaya nzima tuna Askari 58, karibu ratio ya 1:5,000 askari kwa wananchi kwa projection ya mwaka jana, hivyo kuhatarisha ulinzi na usalama. Kituo chetu kimechakaa mno kwa sababu ni cha miaka mingi mno. Tathmini tuliyofanya tunahitaji milioni 38 kufanya ukarabati wa kituo pekee kilichopo Ileje. Tuna nyumba 10 za Askari ambazo zinahitaji ukarabati mkubwa na hazitoshi kwa mahitaji ya makazi ya Askari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Polisi cha Ileje kina upungufu mkubwa wa vitendea kazi, mafuta, spea tairi za magari na hata magari ya kufanyia kazi na hiki ni kikwazo kikubwa kwa utendaji wa Askari wetu ambao wanafanya kazi katika mazingira magumu mno. Maslahi na vyeo vya Askari wa Ileje bado ni duni sana na kwa kuzingatia ugumu wa maisha ya Ileje wanahitaji kuhamasishwa na kupewa stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vituo vyetu havipokei fedha ya kutosha kuendesha ofisi na hii inasababisha askari kuomba msaada wa Mbunge mara kwa mara ili waweze kufanya kazi. Tumeshawapatia mashine ya kudurusu ya kisasa, laptop, printer na scanner, vilevile nimechangia ma-box ya rim za karatasi, nimechangia matairi ya gari na kukarabati gari la Polisi, pia, nimechangia matengenezo mengine. Hii haipaswi kuwa kazi ya Mbunge, lakini kwa kuzingatia umuhimu wa usalama wa wananchi na mali zao imebidi iwe hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye masuala ya Jeshi la Zimamoto kuna haja ya kuhakikisha kuwa, kila jengo la biashara linajengwa liwe na ngazi ya dharura nje ya jengo kila ghorofa. Nyumba nyingi kwa sasa hazizingatii hili, tunataka Waziri atoe tamko kuhusu hitaji hili muhimu kwa usalama wa watu na mali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tunamwomba Mheshimiwa Waziri aje kutoa tamko la kuagiza kila jengo, hasa la kibiashara, kuwa na vitambuzi Moshi (smoke detectors) ili itoe taarifa ya awali kung’amua dalili za moto ndani ya nyumba, vilevile kuhakikisha vifaa vya kuzimia moto vinaonekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Traffic Police bado ni tatizo kubwa, kuna haja ya kuweka vifaa barabarani na kupunguza askari hawa ambao muda mwingi wanajali kuchukua rushwa badala ya kuelekeza watumiaji wa barabara kuzingatia usalama na kuwachukulia hatua madhubuti. Bado magari yasiyo na ubora wa kutumika yanaendeshwa, ilhali Askari Usalama wamejazana barabarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Wizara itafute Mwekezaji wa kuja kuwekeza kwenye vifaa vya ukaguzi wa magari kabla ya kuyapa leseni; vilevile waweke kamera barabarani na kutumia teknolojia ya kuwezesha kutambua magari yanayoendeshwa ili kutoa udhibiti na adhabu husika. Umefika wakati sasa ukaguzi ufanywe kidigitali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado Polisi wetu hawajaweza kushughulikia ipasavyo matukio ya ubakaji na udhalilishaji wa kijinsia ambayo yanaongezeka hata kuathiri watoto wachanga. Tunamwomba Waziri aoneshe kuguswa kwakwe na hili ili wananchi hasa wanawake wapate faraja kuwa mateso wanayopata mikononi mwa wanaume wao na watoto wao yatashughulikiwa kwa haki na usawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa nafasi ya kuchangia hotuba hii. Najiunga na Waheshimiwa Wabunge wote waliompongeza sana, Mheshimiwa Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, Mbunge Chato na watendaji wote wa Wizara yake kwa usikivu, ushirikiano, weledi, ufanisi anaoutumia kutekeleza majukumu yake kwa bidii sana. Kwa kweli tunamwombea heri na afya njema katika kutekeleza majukumu yake.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Ileje katika Mkoa wa Songwe imekua mfaidika mkubwa wa REA awamu zote. Ileje ni Wilaya ambayo imekuwa nyuma kwenye eneo la miundombinu ya aina zote, kwa hiyo kupata umeme kutasaidia sana katika kuchochea maendeleo kiuchumi katika Wilaya hii.

Mheshimiwa Spika, Awamu ya I na II aliacha vijiji vingi bila kuwekewa miundombinu ya umeme, ni mahali ambako laini kubwa imepita lakini watu hawajaunganishiwa umeme.

Mheshimiwa Spika, kati ya vijiji 71 vipo vijiji 24 ambavyo bado havina umeme. Ninaviorodhesha hapa kwa hatua za Mheshimiwa Waziri na watendaji wake.

Mheshimiwa Spika,

Na. Kata Na. ya Vijiji Kijiji
1. Bubigu 1 Mabula
2. Chitete 2 Chitete
3. Mbebe 3 Shinji
4. Ibaba 4 Shuba
5. Hale 5 Hega & Iwala
6. Humba 7 Yenzebwe na Nkanka
7. Ndola 8 Ibezya
8. Malangali 9 Chembe & Bulanga
9. Kalembo 11&12 Mbagala & Ibandi
10. Ikinga 13 & 14 Ibeta & Bwipa (shida kubwa)
11. Ngulilo 15, 16 & 17 Ngulilo, Shiringa & Ndapwa
12. Ngulugulu 18, 19 & 20 Chikumbulu, Kisyesye & Bujura
13. Lubanda 21 Mbembati
14. Luswisi 22 & 23 Makoga & Chibila

Mheshimiwa Spika, ninaomba sana Waziri atusaidie kwa hili.

Mheshimiwa Spika, ninaunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuchangia na mimi katika hotuba hizi mbili za Mawaziri hawa. Kwanza kabisa, namshukuru Mungu sana kwa ajili ya Tanzania, amani na utulivu uliopo. Namshukuru Mungu sana kwa Rais Dkt. Magufuli na Serikali yake nzima kwa ubunifu wanaoutumia katika kuhakikisha kuwa wanathubutu kuingia katika mikakati mikubwa ya kuiletea maendeleo Tanzania kwa haraka zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kumshukuru Rais Dkt. Magufuli kwanza kwa ahadi zake ambazo amekuwa akizitimiza kama sehemu ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. Kipekee nataka kusema kuwa namshukuru Rais Dkt. Magufuli na Serikali yake kwa sababu kubwa sana kwa ajili ya Ileje. Nataka itambulike kuwa Ileje ni Wilaya Kongwe na imekuwa nyuma kwa miaka mingi sana. Sasa kwa miaka miwili na nusu Ileje inakua kwa kiasi ambacho watu hawawezi hata kuamini. Wale wanaoijua wilaya ile wanakubaliana nami. Mimi naomba kwa heshima na taadhima nipige magoti hapa. Magoti yangu ni mabovu, lakini naomba kushukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alikuja akatuahidi barabara ya lami ambayo imepiganiwa karibu miaka 40 na sasa inajengwa kwa kiwango cha lami. Nina kila sababu ya kushukuru kwa sababu miaka 42 unangojea barabara ya lami ya kwanza katika Wilaya, kwa nini nisishukuru? Hivi ninavyozungumza tumepata fedha ya kwenda kumalizia Hospitali ya Wilaya kubwa ya kisasa. Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuja akaweka jiwe la msingi, alijionea mwenyewe jinsi ambavyo ile hospitali itakavyokuwa. Tulikuwa tunatibiwa Malawi, sasa watu watatibiwa Wilayani kwangu Ileje. Tumeenda kupata vituo vya afya viwili na magari yake ya wagonjwa. Hii ni Wilaya ambayo ilikuwa imesahauliwa, kwa nini nisiseme ahsante kwa Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi? Sasa hivi tunaenda kujengewa kituo cha forodha mpakani mwetu na Malawi na Zambia, hii vilevile ni juhudi ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya yetu ina mpaka mrefu sana karibu kilometa 108 na hizo hazina doria ya aina yoyote, hazina ulinzi wa aina yoyote. Wahamiaji haramu wengi wamekamatwa kule, wengine wamekufa kwenye mabonde yetu kule kwa sababu barabara zetu ni mbaya sana na wengine hawazijui wanapita usiku kutaka kuingia nchi za jirani wanakufa. Tunahitaji sasa gari ya doria, lakini ile barabara itakapojengwa Kituo cha Forodha nacho kikijengwa tuna uhakika Ileje itapanuka kiuchumi vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuishukuru Serikali kwa miradi mikubwa ya maji inayojengwa Ileje. Ileje tunakunywa maji ya matope. Tuna vyanzo vingi vya maji, tuna mvua nyingi, lakini miradi ya maji ilikuwa hakuna. Sasa hivi tuna miradi mingi ya maji, mmoja mkubwa sana unajengwa pale Isongole, utakaokidhi haja ya shida ya maji yote ya maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru vilevile kuwa sasa hivi TARURA wameweza kwa kiasi kikubwa kumudu barabara zetu za milimani ambazo zilikuwa hazipitiki kipindi chote cha mvua. Kipindi hiki japo kidogo watu wanaweza kuwasiliana. Hizi zote ni pongezi na shukrani kwa watu wa Ileje kwa ajili ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi, imeweza kututazama na sisi kwa jicho special. (Makofi)

Vilevile nataka kuishukuru Serikali kwa sababu tunaenda sasa hivi kujengewa barabara zinazounganisha vijiji kwa vijiji, kata kwa kata kwa kutumia TARURA. Ilikuwa unatoka kijiji kimoja inabidi upite kata nyingine kurudi kwenye kijiji cha Kata yako. Huo ulikuwa ni usumbufu mkubwa na kwa jiografia ya kwetu, hiyo ilikuwa ni adha kubwa lakini Serikali ya Chama cha Mapinduzi inaenda kutujengea. Ninachotaka kuomba sasa, tunaomba kwa haraka sana tupatiwe gari ya doria kutokana na kwamba sasa hivi uhalifu wa mpakani umeongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa vilevile tusaidiwe kuongezewa pesa TARURA; barabara zetu sisi na jiografia zetu ni ngumu mno; na kwa kuwa ni Wilaya ya pembezoni na ina changamoto nyingi, basi tuangaliwe kwa jicho la huruma zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru vilevile kwa REA. Ileje ilikuwa ni Wilaya iko gizani lakini REA sasa hivi imefunguka. Leo hii unasikia watu wa Ileje wanalalamika mbona leo umeme umekatika? Tulikuwa zamani hatuzungumzii mambo ya umeme, kwa sababu hatukuwa nao. Naishukuru sana Serikali kwa juhudi zao. Naomba hili zoezi la densification kwa ajili ya kuhakikisha miradi ya REA II inakamilika lifanyike haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna upungufu mkubwa wa watumishi; na yote hii inachangiwa vile vile na jiografia yetu. Wengi hawapendi kuwa kule, wengine wakija wanatoroka. Tuna upungufu wa watumishi kwenye sekta ya elimu na afya zaidi ya 580. Tunaomba sana zoezi la kuajiri litakapoanza basi na sisi watufikirie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuna tatizo kubwa Kiwira. Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira uko Ileje na nasikitika kwa miaka yote uliokuwa ukifanya kazi Ileje haijafaidika kwa sababu, kwanza ulikuwa unahesabiwa kwamba ni wa Kyela. Mradi ule sasa hivi unatambulika kuwa ni wa kwetu na tunaambiwa kuwa, STAMICO wameuchukua na wameshaanza majaribio ya kuchimba makaa ya mawe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka kujua sasa mustakabali wake ni upi maana hatujasikia Mkandarasi aliyepatikana ni nani na atauendesha vipi. Tunaambiwa bado kuna mambo ya kupata ile hati ya kukabidhiwa, haijakabidhiwa na yule aliyekuwa mwekezaji wa huko nyuma. Tunaomba hili lifanyike haraka ili wananchi wetu wapate ajira na ule mgodi utuletee faida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna daraja pale ambalo limeharibika la kilometa saba ambalo ndiyo linaunganisha Kiwira na Ileje. Sasa hivi inabidi unataka kwenda Kiwira uzungukie Kyela kutokea Kiwira mgodini, hiyo siyo hesabu nzuri kiuchumi. Tunaomba sana hili daraja la kilometa Saba tu lijengwe, ili sasa Ileje na mgodi wake wa Kiwira viunganishwe moja kwa moja kwa mawasiliano.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa fursa ya kuchangia hoja ya hotuba ya Wizara ya Madini. Namshukuru Mungu kwa kibali hiki. Nampongeza Mheshimiwa Waziri Angellah Jasmine Kairuki kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Madini na Naibu Mawaziri wake Mheshimiwa Biteko na Mheshimiwa Nyongo. Nawapongeza pia kwa hotuba nzuri iliyozingatia masuala yote muhimu pamoja na taarifa za ziada walizotupatia kwenye makabrasha maalum na maonesho yaliyoletwa kwenye viwanja vya Bunge ambayo yametuongezea uelewa wetu juu ya sekta hii muhimu sana kwa uchumi, lakini pia kutuwezesha kutambua changamoto zake na nini kinafanyika kukabiliana nazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa hatua madhubuti alizochukua kuhakikisha kunakuwa na usimamizi na udhibiti mzuri wa rasilimali za sekta hii kwa kuunda Kamati za kukagua makinikia yanayotokana na uchimbaji wa madini na vito na hatimaye kupitisha sheria za kimapinduzi zinazoliwezesha Taifa kuipitia upya mikataba yote ya madini na vito ambayo ilikuwa ina vipengele vyenye kutiliwa mashaka ili irekebishwe na Taifa lipate mapato stahiki kutokana na sekta hii ambayo kwa muda mrefu Taifa limekuwa likipoteza mapato mengi sana. Tunamwomba Rais zoezi hili lifanywe kwa rasilimali zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, niruhusu sasa nizungumzie suala la migodi ya makaa ya mawe ambayo yanapatikana maeneo ya Kiwira Wilaya ya Ileje, Ludewa, Ruvuma, Mbinga na Songea. Makaa ya Mawe ya Ngaka, Mbinga, Ruvuma yana ubora wa juu zaidi duniani. Mgodi huo una zaidi ya tani milioni 400 za makaa ya mawe na yanaweza kuchimbwa kwa miaka 100. Kwa hivyo, ni rasilimali ya uhakika na kutegemewa sana katika mkakati wa kuzalisha chuma kwa ajili ya viwanda nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa nini Serikali haitilii mkazo mradi huu ambao utafungua Taifa kiuchumi na kiviwanda? Hili ni eneo ambalo Serikali itakuwa na kila sababu ya kuingia ubia mkubwa na wawekezaji wa sekta binafsi na hata kuchukua mkopo ili kuendeleza migodi hii yenye kuleta faida kubwa na mapato makubwa kwa Taifa na kuongeza umeme kwa asilimia 40 kama takwimu za dunia zinavyoonesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, makaa ya mawe ni nishati kubwa kwa kutengeneza cement, kuzalisha karatasi na kwenye viwanda vya nguo na bidhaa nyingine nyingi za viwandani pamoja na uzalishaji wa umeme. Hii pia itaokoa fedha ya kigeni iliyokuwa ikitumika kuagiza makaa ya mawe toka Afrika Kusini.

Mheshimiwa Naibu Spika, STAMICO ndiyo iliyokabidhiwa Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira na taarifa zilizowasilishwa kwenye hotuba ya Waziri ukurasa wa 45 imeainisha kwamba STAMICO imeanza rasmi kuuza makaa ya mawe yanayozalishwa katika Mgodi wa Kabulo uliopo Ileje – Songwe kwa matumizi ya watumiaji wa viwanda wa ndani ikiwemo viwanda vya saruji na nguo. Uzalishaji wa majaribio ulioanza kwenye Kijiji cha Kapeta, Ileje tangu Aprili 30, 2017 na mpaka sasa imezalisha tani 6,197. Kiasi gani cha makaa haya yameshanunuliwa na Ileje kama Wilaya ina gawio la asilimia ngapi kutokana na mauzo hayo?

Mheshimiwa Naibu Spika, Ileje inahitaji daraja la kwenye Mto Mwalisi linalounganisha Ileje na Mgodi wa Kiwira ili ipunguze gharama za kusafirisha makaa kupitia Kyela na kuwezesha makaa hayo kuhifadhiwa Ileje na vilevile kupitishwa Ileje wakati wa kupeleka kwenye viwanda vya cement na hata vya nguo vitakapoanza. Tunaomba Wizara itenge bajeti ndogo kujenga daraja hili fupi la kilomita 7 kuokoa gharama.

Mheshimiwa Naibu Spika, muhimu zaidi napenda kuona Mgodi wa Kiwira na Kabulo ungeendelezwa sasa na kuajiri watu 7,000 wanaotegemewa huku ingeongeza mapato Ileje na Songwe kwa ujumla. Mheshimiwa Waziri atueleze mikataba gani ipo sasa kuendesha Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira na ile ya kati ya Halmashauri ya Ileje na STAMICO.

Mheshimiwa Naibu Spika, wachimbaji wadogo ni sehemu muhimu katika tasnia hii ya madini na wanachangia kwa kiasi kikubwa kwenye soko la ajira na kuliletea mapato Taifa na kuondoa umaskini. Wachimbaji wadogo wathaminiwe na kuwezeshwa. Maeneo wanayochimba wapewe leseni kwenye maeneo yaliyokwishapimwa rasmi na GST ili wasifanye uchimbaji wa kuhamahama unaoharibu mazingira na usiokuwa na tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, wazo la kutumia Tanzania kuwa kitovu cha vito na madini yetu ni zuri na linalohitaji kufanyiwa kazi kwa haraka. Kila eneo lenye uzalishaji wa vito lijengwe eneo la kucharanga vito na kuuza vito na mikufu, pete na vitu vya thamani. Vijana wetu wapewe mafunzo nje na ndani ya nchi kwenye usonara, design na wasaidiwe kupata vifaa na mitaji ya kujiendeleza kiajira na kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la migogoro ya maeneo ya wachimbaji wa tanzanite wadogo na wawekezaji wakubwa lifanyiwe kazi ili lisije umiza wawekezaji wadogo. Iko haja ya Wizara kuwa na kanzi data ya kila aina za madini na vito na kiasi kilichopo na thamani yake ili ituwezeshe kujua utajiri tulionao kama nchi na jinsi ya kuhakikisha kuwa inasaidia maendeleo ya kiuchumi ya Watanzania kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada kubwa za Serikali kusaidia wachimbaji wadogo, bado liko tatizo kubwa la watoto wanaofanya kazi kwenye migodi na ambao wanatumia zebaki kuchambua dhahabu na hii ni sumu ambayo wanaishika na inapochomwa pia inaingia kwenye mazingira. Watoto hawa vilevile huingia kwenye mashimo ya migodi iliyochimbwa kienyeji bila kinga zozote na hutumia kamba tu kuingia ndani ya mgodi na hii ni hatari sana kwa maisha yao. Licha ya kuwa wanakosa elimu, vilevile watoto wako kwenye kuvunja kokoto na kwenye vito Mererani. Wizara ishirikiane na Wizara ya Ajira, Mazingira, Elimu, Ustawi wa Jamii kuwaondoa watoto migodini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Wizara hizi mbili muhimu sana. Nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia siku njema, lakini vilevile nataka kuwapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara hizi mbili, Manaibu Waziri, Makatibu Wakuu na watendaji wote wa Wizara hizi muhimu sana kwa mustakabali na maendeleo ya nchi yetu. Hizi ni Wizara ambazo unaweza ukasema ni pacha; moja inasimamia Utumishi na Utawala Bora, nyingine inasimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika ngazi ya halmashauri na miji yetu. Kwa hali hiyo, kuna haja kubwa sana ya kuhakikisha kuwa kwanza zinawezeshwa kifedha, lakini vilevile kimfumo na pia kwa watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeanza hivyo kwa sababu tunapozungumzia utumishi na tunaposikia michango yote ya Wabunge ikilalamikia watumishi na upungufu wake nafikiri kuna haja sasa ya kuchukua hatua ya makusudi ya kimkakati ya kujaza hizi nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo kubwa la watumishi katika Wilaya zetu hasa kwenye sekta ya afya, kwenye sekta ya elimu, kwenye sekta ya maji yaani karibu kila sehemu ina matatizo ya upungufu wa watumishi. Mimi binafsi katika wyangu nia upungufu mkubwa sana wa Walimu katika shule za msingi na shule za sekondari, lakini hasa hasa katika shule za sekondari ni Walimu wa sayansi. Tuna tatizo kama alilolisema Mheshimiwa Maghembe kuwa sehemu nyingine ni kujaza nafasi tu za watu ambao wameondoka aidha kwa kustaafu, au kwa kufa, au kwa kuhama. Sasa hili ni jambo ambalo naamini halipaswi kuchukua mlolongo mrefu kama vile ambavyo tunavyongojea vibali vya ajira mpya labda nisahihishwe kuwa hivyo sivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nitakuwa mtovu wa shukurani kama sikutoa shukurani zangu kwa jinsi ambavyo wilaya yetu imepatiwa fedha ya kumalizia hospitali ya wilaya ambayo Awamu ya Nne tulipata fedha kwa ajili ya kuianza na sasa hivi tumepata bilioni moja na milioni mia tano kwa ajili ya kuimalizia. Naamini fedha hii itatosha kumalizia hospitali, itajenga nyumba za Wauguzi na vilevile kumalizia miundombinu yote iliyokuwa inahitajika, nawashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashukuru kwa kupata fedha ya vituo vya afya viwili vikubwa na tumeahidiwa kingine cha tatu, lakini niombe tupate na cha nne kwa sababu wilaya yangu mimi ina tatizo la miundombinu migumu; milima, mabonde na umbali kati ya kata moja kwenda nyingine. Hii kwa vyovyote vile inasababisha umbali kuwa mkubwa na bila kuwa na zahanati za kutosha hata vituo hivi vya afya vinaweza visisaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye zahanati; tulikuwa tumeweka kwenye bajeti yetu milioni 200 kwa ajili ya kukarabati maboma ya zahanati saba ambayo ilishapitishwa kuwa zitakuwepo, lakini ghafla tukaja kuambiwa tuziondoe katika bajeti yetu kwa sababu zinapelekwa Mbozi na Songwe. Hii imetuathiri sana kwa sababu haya maboma ya zahanati yameshafikia mahali pazuri kumaliziwa na hizi fedha tulikuwa tumeshazitarajia kwa sababu zilikuwa zimeshakubaliwa sasa kuja kuziondoa tu juu juu hivi zinatuathiri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema Wilaya yangu miundombinu ni migumu, usipokuwa na zahanati hata ya kuanzia tu kumtibu mwananchi kufikia vituo vya afya ni tatizo hasa wakati wa mvua. Naomba sana Wizara ya TAMISEMI mliangalie hilo na mturudishie ile shilingi milioni 200 ambayo mlikuwa mmeitoa wakati tayari tulikuwa tumeshakubaliana kuwa itakuwepo katika ceiling zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kushukuru kwa fedha iliyotolewa kwa Daraja la Mwalisi ambalo linaunganisha Wilaya yangu na Mgodi wa Kiwira. Hili daraja litatusaidia kwa sababu ilibidi kutoa makaa ya mawe na kuyapitishia Kyela na huko ilikuwa ni Wilaya nyingine of course na ilikuwa inaleta gharama kubwa na usumbufu kutokana na umbali wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuzungumzia suala la TASAF. TASAF imekuwa msaada mkubwa sana kwa nchi nzima na hata kwa Wilaya yangu. Nataka niombe vile vijiji 21 kati ya 71 ambavyo havijaingizwa katika mpango huu basi na vyenyewe viweze kuingizwa kwa sababu faida zake zimeonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kidogo nataka niongelee suala zima la TAKUKURU au masuala mazima ya ufisadi au rushwa. Tunashukuru kuwa imeanzisha Mahakama ya Ufisadi lakini kiwango cha watu wanaopelekwa pale cha bilioni moja ni kikubwa sana, mafisadi wengi sana wanaachwa hapa chini hawawezi kufikia Mahakama hiyo kwa sababu hawajatuhumiwa kwa kiwango hicho kikubwa. Kiwango hiki kingepunguzwa kidogo mafisadi au watuhumiwa wengi zaidi wangeweza kufikiwa na rushwa ikapungua lakini bado rushwa ipo na inalalamikiwa sana, tusijidanganye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo juhudi zinafanywa lakini bado rushwa nyingi ni tena inafanywa waziwazi katika taasisi zilezile ambazo zimekuwa zikilalamikiwa siku zote Polisi barabarani, Mahakama na sehemu zinazotoa huduma za afya na hata elimu. Naomba sana tusielegeze kamba rushwa bado ipo, wanagundua misemo mipya, ohoo, sijui kula samaki gizani, kuna maneno yanayotumika ambayo hayatufurahishi kwa sababu rushwa inaondoa haki za kimsingi za watu wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka kuzungumzia suala la watumishi. Watendaji wakubwa katika taasisi mbalimbali wanahitaji kupata mafunzo ya kutosha ya uongozi. Tulikuwa na vyuo vyetu vilikuwa vinatoa elimu hiyo lakini najua sasa hivi tuna Uongozi Institute, napenda sana kuona mpango mkakati wa jinsi gani ya kuwapeleka watendaji hawa kwenda kujifunza kwa sababu pamoja na kuwa ni viongozi wa taasisi mwenendo hauoneshi ile leadership ambayo inategemewa kwa viongozi wa ngazi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine ambalo linaanza kuzoeleka la Watendaji Wakuu wanaopata nafasi kuhamishwa kwenye taasisi aliyokuwa mwanzo kuanza kutengeneza himaya zao, wanaondoka na watu wao wote waliokuwa nao kwenye taasisi moja wanawahamishia kwenye taasisi nyingine na kuleta sasa tabaka za waliokuwepo na waliokuja, hii inaleta chuki na inavunja moyo wale waliokuwepo. Mimi nafikiri suala hapa ni kujenga taasisi imara siyo kujenga Watendaji Wakuu wa taasisi imara. Kwa hiyo, naomba hili pia liangaliwe la huu mtindo watu kuhama na ma-secretary wao na viti na meza za maofisini kama vile wanahama nchi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mungu kwa fursa hii ya kuwepo hapa kujadili hotuba hii ya Wizara muhimu sana katika kuchangia na kukuza maendeleo ya Taifa letu. Nakushukuru kwa fursa ya kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa George H. Mkuchika, Mbunge wa Newala na Waziri katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora; Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa, Katibu Mkuu na Watendaji wote na taasisi zote zilizo chini ya Wizara hii kwa kazi kubwa wanayofanya kuhakikisha kuwa utendaji wa Serikali ni mzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuipongeza Serikali kwa utekelezaji mzuri wa mpango wa kurasimisha rasilimali na biashara za wanyonge (MKURABITA). Mpango huu ni muhimu sana kwa kuhakikisha kuwa wananchi wote wenye uwezo wanajumuishwa kwenye uchumi wa nchi kwa kuwawezesha kutumia rasilimali za kukopa au kuwekeza kiuchumi. Kwa umuhimu wa mradi huu na faida na mafanikio yaliyopatikana hadi sasa, tunapenda kuona Serikali ikizidisha juhudi katika kuwekeza fedha nyingi zaidi kuthamini na kutoa hati nyingi zaidi nchi nzima hasa kule ambako fursa za kiuchumi ni kubwa na utayari wa wananchi kuchapa kazi ni kubwa pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta isiyo rasmi ni kubwa sana na ina mchango mkubwa katika kuondoa umasikini, kuongeza ajira na kuchangia pato la Taifa. Kwa hiyo, MKURABITA upanuliwe na uenee nchi nzima kwa haraka zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, TASAF, naipongeza Serikali sana kwa mpango huu wa ruzuku kwa kaya masikini. Mpango umeonesha matokeo mazuri sana. TASAF ipo sasa awamu ya tatu na inatekeleza mpango wa kunusuru kaya masikini kuanzia mwaka 2013. Kumekuwa na mafanikio makubwa kwa kaya zilizoandikishwa na kupata ruzuku. Maisha yao yameboreshwa na wanashiriki vizuri katika shughuli za kiuchumi kuweza kuongeza kipato zaidi katika sekta mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua mpango huu haukuwafikia masikini katika vijiji na mitaa yote na pia katika vijiji ambavyo vimefikiwa, kuna kaya nyingine masikini hazikuridhishwa kwa sababu mbalimbali. Kwa mfano Wilaya ya Ileje, kati ya vijiji 71 ni 50 tu zilizofikiwa. Vijiji 21 bado havijafikiwa. Sasa ni lini hizi kaya masikini zitaingizwa kwenye mpango? Ninapata maswali mengi kutoka Jimboni kwangu kwa wapiga kura wangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya uendelevu wa mpango huu: Je, kuna mikakati ipi ya ufadhili wa mpango huo? Kwa sababu sehemu kubwa ya fedha zinazotumika ni michango ya wadau wa maendeleo na Serikali inachangia kidogo, tunaona hata katika bajeti Serikali inatoa kidogo na sehemu kubwa ni fedha ya nje. Je, ikikosekana?

Mheshimiwa Naibu Spika, watumishi wa Umma wengi bado wanafanya kazi kwa mazoea. Wengi hawabebi haya maono ya Mheshimiwa Rais na wala hawaendani nayo. Hii inazorotesha watendaji, inapunguza tija na huzidisha gharama. Iko haja kuhakikisha kuwa Chuo cha Utumishi kinajikita zaidi katika mafunzo yaliyokuwa yakitolewa kwa watumishi wa kada ya kata ili kuwajengea uwezo wa jinsi ya kutekeleza majukumu yao Serikalini, kuwa na weledi wa masuala mbalimbali ya utumishi wa Umma. Hii itasaidia katika kuboresha ufanisi wa watumishi wa Umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, huko nyuma Chuo cha Mzumbe kilitumika kutoa mafunzo yaliyojenga uwezo wa Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma, lakini walipoamua kukigeuza kuwa chuo cha kawaida na kupoteza fursa ya kuwajengea uwezo viongozi wa Mashirika ya Umma. Kwa sababu hiyo, ninapendekeza ufanywe utaratibu wa kutumia Chuo cha Uongozi (institute) kutoa mafunzo ya Watendaji Waandamizi kabla ya kupangiwa taasisi za Umma kuziongoza. Hii itasaidia kuongeza ufanisi wao na kuboresha huduma za wateja wao na kuvutia uwekezaji, uzalishaji kwa jumla na kuongeza mapato ya Serikali na kukuza uchumi kwa jumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukuzaji wa taaluma, kukidhi ubora unaotakiwa, kuongoza taasisi zetu, uzingatiwe na hii iendane na suala zima la uteuzi wa watumishi wenye vigezo na watakaopewa viashria vya kutumika kuwapima. Vetting ya wateule wa taasisi inachukua muda mrefu na kusababisha kuzorota kwa kazi za Serikali na Mashirika yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, rushwa imepungua na kama inafanywa, kwa kiasi kikubwa watu wanajificha, lakini bado zile taasisi zilizoendeleza rushwa kama Polisi, Mahakama, Mamlaka ya Kodi, Hospitali na ambako rushwa bado inafanywa bila kificho. Ili kupunguza rushwa kubwa, tunaishauri Serikali ipunguze kutoka shilingi bilioni moja ili iwezeshe watu wengi zaidi wanaojihusisha na rushwa kupelekwa kwenye Mahakama ya Ufisadi na kupunguza vitendo vya rushwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, watendaji waliokuwa wanafaidika na mfumo uliokuwa unatoa mwanya wa rushwa wameamua kufanya kazi kwa kukomoa na kula rushwa kwa kisingizio cha Hapa Kazi Tu na hawa wamekuwa wakiharibu jina la Serikali na kuwapaka matope viongozi wetu. Iko haja ya kutupia jicho eneo hili kama TRA, Taasisi na Idara za huduma muhimu za Serikali zinazotoa vibali, leseni na kadhalika. Serikali ijitahidi kueneza mifumo ya TEHAMA ili kupunguza mawasiliano ya watu na watendaji hawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Mheshimiwa Waziri haijazungumzia lolote juu ya Watanzania walio ughaibuni kama sehemu yenye fursa ya utumishi wa Umma. Kwa bahati mbaya Watanzania wengi wamekuwa na mtazamo hasi dhidi ya Watanzania walioko ughaibuni, lakini mimi ninaamini kuwa tukiwa na utaratibu mzuri wa kuwatumia ni hazina kubwa kwa Taifa letu na wengi wanapenda kurudi kufanya kazi Tanzania wakipewa nafasi. Nchi nyingi hata za jirani wamewatumia sana raia wao walio ughaibuni na kunufaika na weledi na ujuzi wao. Wakati umefika kubadilisha mtazamo wetu juu ya wenzetu walioko kwenye Diaspora ili wachangie maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa fursa ya kuchangia bajeti hii. Nampongeza Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa maono yake makubwa ya kuwasogezea wananchi wa Tanzania huduma muhimu za jamii, hususan katika sekta hii ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto; Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile na Makatibu Wakuu wote kwa kazi kubwa na ya kutukuka wanayoifanya kwa uadilifu, upendo, bidii na weledi mkubwa. Tunapongeza huduma kubwa za kisasa na utaalam mkubwa katika hospitali zetu za rufaa. Nipongeze utolewaji wa miundombinu ya vifaatiba na madawa. Tunapongeza sana juhudi za kukuza uwezo wa watumishi wa sekta hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizo, naomba nitoe rai kwa Wizara hii kuzingatia umuhimu na haja ya kuajiri watumishi wengi katika zahanati na vituo vya afya, hasa katika kada ya Medical Officers ambao wanahitajika kwa wingi sana. Naomba kutoa rai pia kwa Wizara kuhakikisha kuwa zahanati zilizojengwa katika vijiji vyetu kwa nguvu za wananchi zinamalizika na zilizomaliziwa zipatiwe vifaa na watumishi ili zifanye kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Jimbo langu la Wilaya ya Ileje, Kituo cha Afya Mbebe bado hakijamaliziwa na kwa sasa kwa miundombinu ya Wilaya ya Ileje wananchi wanalazimika kupeleka wagonjwa Malawi ambako ni karibu zaidi kuliko kwenda Itumba kwenye Hospitali ya Wilaya. Zahanati ya Mapogoro hukohuko Mbebe haijamaliziwa na hivyo kuifanya Mbebe ikose huduma za afya kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi walijitoa kujenga Kituo cha Afya Itale, tunaomba Serikali itusaidie fedha za kumalizia kituo hiki cha afya. Tunashukuru Serikali kwa kutoa ambulance ndogo, tunaomba basi Kituo cha Afya cha Itale kikamilishwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaiomba Serikali itusaidie kuwezesha Vituo viwili vya Ibaba na Lubanda vilivyomaliziwa kwa fedha ya Serikali basi vizinduliwe ili vianze kazi. Mheshimiwa Ummy aliahidi ambulance Kata ya Lubanda, tunaomba sasa ipatikane.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Ikinga, Zahanati ya Kikota imemaliziwa ujenzi bado kufunguliwa. Tunaomba ifunguliwe ili wananchi wa Ikinga wapate huduma hii muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Isongole ni kubwa na ipo kwenye Mji Mdogo wa Wilaya ya Ileje. Kata hii ina watu wengi sana lakini inakosa kituo cha afya na kuifanya Zahanati ya Isongole kuzidiwa na wagonjwa na kushindwa kumudu mahitaji ya huduma za afya kwa wananchi. Sasa hivi barabara kuu inajengwa na imepita Isongole kwa hiyo kutakuwa na ongezeko kubwa zaidi la wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ileje ina miundombinu migumu sana na Mheshimiwa Waziri alishatembelea, anafahamu. Kata ya Ndola inahitaji kituo cha afya kupunguza adha kwa wananchi wa Ndola. Kata ina hosteli ya wasichana na changamoto zikitokea wanakosa huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Itumba ndiyo Makao Makuu ya Wilaya na ndipo ilipo hospitali ya wilaya. Tunaendelea kuishukuru Serikali kwa kutupatia fedha za kujenga hospitali ya wilaya shilingi bilioni 1.5 pamoja na zilizotolewa siku za nyuma. Hospitali itakuwa na majengo muhimu saba na itajitosheleza lakini kwa sasa tunahitaji X- ray mashine ya kisasa ya radiologist na friji ya kuhifadhia damu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Isoko ni hospitali ya mission lakini imekuwa ikitoa huduma kubwa sana kwa Wanaileje na kuunga mkono juhudi za Serikali. Tunaomba Wizara iwafanyie secondment Medical Officers kwenda Isoko kuziba pengo. Hospitali ya Isoko haina uwezo wa kuajiri Medical Officers kuziba pengo lakini kwa kuwa wanahudumia wananchi wa Ileje na Watanzania na kwa kuwa wanashirikiana na Serikali, tunaomba sana Serikali iridhie kutoa secondment kwa watumishi wawili au watatu kwenye ngazi ya Medical Officer ili kukidhi ufanisi wa huduma zinazotolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
The Written Laws (Miscellaneous Amendment) Bill, 2016
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Muswada huu. Niungane na waliokwishatangulia kutoa pongezi sana kwa Mwanasheria Mkuu pamoja na Mwenyekiti wa Kamati kwa ufafanuzi mzuri alioutoa kuhusiana na sheria zilizoletwa mbele yetu. Tumshukuru na Rais vilevile kwa kweli kwa kutimiza ahadi yake haraka sana kama ambavyo alikuwa ameahidi.
Mheshimiwa naibu Spika, napenda nijikite katika suala zima la hii Mahakama ya Mafisadi kwa jina la kawaida au wahujumu uchumi. Hapa nataka kuzungumzia uzoefu ambao tumeuona kuwa tunakuwa na vyombo kama hivi, lakini kwa sababu vinaendeshwa na wanadamu kunakuwa na upungufu wa kibinadamu na wao pia wanaangukia katika suala la uhujumu. Kunakuwa na ukiukwaji wa taratibu au maadili ya uendeshwaji wa shughuli hizi, sasa wao wanakuwa vile vile wakiukaji wa sheria. Unakuta mtu anasimamia suala la rushwa lakini na yeye mwenyewe anashawishika kuchukua rushwa au kuomba rushwa au yeye mwenyewe anapindisha sheria kwa ajili ya maslahi binafsi au ya kundi fulani.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka kupendekeza, kwa nini tusifikirie wakati tunaunda vyombo hivi au tunavyorekebisha masuala haya, tuwe vile vile na chombo kinachotetea maslahi ya wananchi wanapokuwa na malalamiko mbalimbali kuhusiana na jinsi ambavyo hizi sheria zinaendeshwa. Nazungumzia kitu ambacho Kiingereza kinaitwa ombudsman au a Public Advocate au a Citizen Advocate; ambapo Mwananchi kwa mfano, amepelekwa au taasisi imepelekwa kwenye Mahakama hiim ikakutwa kuwa imeonewa katika kupeleleza au kutoa hukumu; wao wenyewe vilevile wamevunjiwa haki zao fulani fulani, basi wawe na chombo cha kwenda kupeleka malalamiko yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukiona kuwa Polisi anavunja sheria, halafu anawekewa Polisi mwenziwe kumchunguza na kumpeleka Mahakamani. Kwa vyovyote vile unakuta pale kuna suala la conflict of interest, anakuwa hatendewi haki yule mwananchi aliyeathirika. Sasa kwa hili tuwe na chombo kinachosimamia hawa ambao wanaendesha hizi kesi ili na wao kama wakikiuka, au kama wananchi wana malalamiko fulani, basi wawe na mahali tofauti kabisa huru pa kupeleka shida zao ili sasa haki itendeke kwa uhakika zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, yangu yalikuwa ni hayo tu. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hotuba hii. Naomba nianze moja kwa moja kwa sababu ya muda, katika kuzungumzia masuala mawili muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni suala zima la uwezeshwaji au mazingira bora ya uwekezaji pamoja na kufanya biashara. Haya maeneo ni muhimu sana na ndiyo hasa yanabeba uzito mzima wa jinsi ambavyo maendeleo ya biashara au viwanda nchini kwetu yatakwenda. Kwa bahati mbaya sana, Wizara yenyewe inapata bajeti ndogo mno kiasi kwamba hata ile kazi ya kuandaa ule uwezeshwaji inakuwa siyo rahisi kiasi hicho. Tumejionea jinsi ambavyo bajeti iliyopangwa na bajeti iliyotolewa ni ndogo sana katika matumizi ya kawaida na hata ya maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, kuna suala zima la kuweka mazingira bora ya uwekezaji katika viwanda vyetu. Nataka kukumbusha Serikali kuwa mwaka 2010 task force iliundwa ya Wizara nane kwa ajili ya kutengeneza roadmap ya kuweka utaratibu ambao utarahisisha uwekezaji na vilevile kufanya biashara. Task force ile ilikuja na mapendekezo mazuri sana na chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kulikuwa kuna uratibu sasa wa jinsi gani ya kutekeleza yale mapendekezo yaliyotokana na ile roadmap ya kwanza ambayo ilikuwa inalenga ku-improve uncompetitiveness ya uendheshaji wa shughuli zetu nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sielewi ile ilifikia wapi kwa sababu mwaka jana tena tulikuja na blue print na vyote vinatokana na taarifa zinazotoka nje kuonyesha kuwa sisi ranking yetu inazidi kudorora. Sasa hii blue print haikuwa tofauti sana na ile roadmap ya kwanza lakini pamoja na hayo yote bado hatuoni jinsi gani ambavyo tuna mwelekeo unaotutoa hapa tulipo ambapo bado hatujakuwa na mwelekeo mzuri wa jinsi ya kuanzisha viwanda na kuviimarisha. Tunaona kabisa na ni ukweli usiopingika kuwa biashara zinadorora na nyingine zinafungwa, wawekezaji hawana amani kwa kifupi naweza kusema hivyo, wawekezaji waliopo na wale ambao wanataka kuja bado hawajakuwa na amani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu inasemekana ni ya amani na utulivu lakini kiuchumi na kibiashara hakuna huo utulivu wala amani. Nasema hivyo kwa sababu ya jinsi ambavyo shughuli zinaendeshwa; kwanza maamuzi yanachelewa sana kufanyika na hii tunazungumzia tangu vibali vinapoombwa mpaka proposal zinapoletwa na wawekezaji wanaotaka kuja kuwekeza mpaka inapofikia kuwa sasa wanaanza kufanya shughuli zao au wanaamua kuondoka. Huu muda ni mrefu mno kwa mtu ambaye anataka kuja kufanya biashara. Tunajua kabisa katika biashara muda mali, hawezi mwekezaji kuja kukaa miezi mitatu hotelini hapa anangojea decisions na wakati tumesema tuna TIC ambayo ni one stop center; hiyo one stop center kwa nini ichukue miezi mitatu kuamua jambo la mwekezaji anapokuja nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, kuna mambo madogo madogo mengi ambayo yanaleta tatizo; yamezungumzwa humu ndani masuala ya permit, ajira na hata mikopo kwa ajili ya wawekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie suala ambayo yamejitokeza katika ranking ya hivi karibuni ambayo ilipata kwa ajili ya Serikali yetu. tumefanya vibaya sana kwenye masuala ya cross border trade ambayo sisi tuna advantage kubwa sana; tuna fursa kubwa sana katika biashara ya mipakani kwa sababu tuna mipaka mingi sana Tanzania na wazalishaji wadogo wadogo wengi na hasa wakiwa akinamama ndiyo wenye nafasi kubwa sana ya kufanya hiyo, lakini tumefanya vibaya. Tuna fursa kubwa ya kufanya biashara sisi na nchi nyingi zinazotuzunguka pamoja na Afrika ya Kati, lakini tumekwama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna matatizo vilevile ya masuala ya kodi na hii inaletwa na biashara kuwa siyo nzuri sana kwa hiyo hata kodi kukusanya inakuwa vigumu. Tunajikuta tunazunguka katika vicious circle ya kutokuwa na mikakati mizuri kwa sababu tu ya jinsi ambavyo tunaendesha hizi shughuli zetu sisi wenyewe. Matatizo yote tuliyonayo ni…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri na Ofisi yake nzima kwa kutuletea Mpango mzuri ambao kwa kweli unatupa mwelekeo unaotosheleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile binafsi nataka nimpongeze Mheshimiwa Rais, hivi karibuni alitoka kuzindua barabara muhimu sana Mkoani kwetu na hususan Wilaya ya Ileje, barabara ya kwanza ya kiwango cha lami itakayokuja kutuunganisha mwisho wa yote na Wilaya ya Kyela. Hii ni barabara muhimu sana kwa uchumi wa Wana-Ileje na kweli naomba nimshukuru sana kwa hilo. Namwomba radhi kwa kumsumbua sana huko nyuma akiwa Waziri kuhusiana na barabara hiyo, lakini mwishowe amekuwa mwaminifu na barabara inajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, langu kubwa ni suala zima la ukuaji wa uchumi. Ukuaji wa uchumi umeendelea kuwa mzuri sana, kwa muda mrefu zaidi ya miaka kumi sasa nafikiri. Hili ni jambo jema sana, isipokuwa sasa tatizo ni kuwa ukuaji huu wa uchumi unachangiwa zaidi na maendeleo katika miundombinu. Ili ukuaji wa uchumi huu ulete tija ya maendeleo ya uchumi kwa wananchi mmoja mmoja na makundi ni lazima uunganishe uondoaji umasikini katika sekta zote muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kabisa kuwa ili Taifa hili liendelee kwa haraka zaidi lazima tufungamanishe ukuaji wa uchumi pamoja na ukuaji wa maendeleo ya wananchi kwa maana ya kuondoa umasikini. Najua kwa muda mrefu, nchi yetu imelenga kuondoa umasikini tangu Awamu ya Kwanza. Bahati mbaya sasa hivi umasikini bado upo na maeneo mengine umekithiri. Hii ni kwa sababu bado hatujaweza kuunganisha maendeleo ya huku juu na maendeleo ya huku chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tufanye nini? Kwanza, kuna suala zima la kuongeza tija ya uzalishaji kule ambako wananchi wapo. Hii itasaidia sana kuboresha maisha, ajira na mapato ambayo wataweza kuwekeza katika maendeleo yao lakini vilevile itaongeza Pato la Taifa kwa maana ya kuleta uchumi mkubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tumekua mpaka asilimia saba na nukta fulani tukilinganisha na lengo letu la kufikia asilimia 10. Tungeweza kukuza kilimo kwa asilimia 10 ambayo tunaitegemea tungejikuta sisi uchumi wetu umeongezeka zaidi ya lengo letu la asilimia 10. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kifanyike? Ni lazima sasa hivi Serikali ijikite katika kuongeza bajeti ya kilimo, ufugaji, uvuvi, biashara ndogondogo hasa za mipakani lakini vilevile kukuza soko la ndani la mazao ambayo tunazalisha sisi wenyewe. Tuna rasilimali nyingi ambazo zinaweza kutusaidia kuongeza mapato yetu lakini nyingi tunazisafirisha nje zikiwa ghafi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajikuta kuwa hata biashara yetu na nje yaani urari wa biashara umeshuka sana kwa sababu mazao tunapeleka nje yakiwa ghafi na mazao haya bei zake hatuzipangi sisi. Kwa hiyo, tunajikuta sisi ni watu wa kupokea bei badala ya sisi kutoa bei. Tungeweza kuweka viwanda vidogovidogo katika maeneo tunayozalisha, sisi wenyewe tungeongeza thamani na tukaweza kutumia kwanza hayo mazao tunayochakata kwenye soko letu la ndani na hivyo kuongeza ajira, kuongeza mapato na kuondoa umaskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda sana kuona jinsi ambavyo Serikali inakuja na mkakati mahsusi unaolenga kilimo cha kisasa, ufugaji wa kisasa, uvuvi wa kisasa. Hii itawezekana pale ambako wananchi hawa wanaozalisha wataunganishwa na taasisi za kifedha ili wapate mitaji itakayowawezesha wao kuwekeza katika maeneo haya kwa tija zaidi lakini vilevile, itawawezesha kupata mafunzo yatakayowawezesha kuwa wajasiriamali na wazalishaji wazuri na wanaozalisha kwa tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mifano duniani ipo ya nchi ambazo zilikuwa maskini au za chini kama sisi lakini wenzetu sasa hivi wako mbali. Vietnam ni nchi mojawapo ambayo unaweza ukasema wakati sisi tunapata uhuru na wao walikuwa katika ngazi ya kiuchumi sawa na sisi lakini sasa hivi wamepiga hatua sana. Siyo kwamba wao walikuwa na elimu kuliko sisi na wao viwango vyao vya elimu vilikuwa kama vya kwetu tu lakini walichofanya wao ni kuihusisha sekta binafsi kwenye ubia na wananchi katika uzalishaji wa kilimo, mifugo na viwanda vya kuchakata bidhaa zinazotokana na kilimo, mifugo na uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunaweza kufanya hivyo kwa kutumia ushirikiano wa Kusini kwa Kusini au nchi za kiafrika ndani kwa ndani. Haya ni mambo yanayowezekana, tujipange tuhakikishe kuwa tunaweka bajeti zinazotosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna vitengo katika Serikali vinavyohusiana na uwezeshaji wa vijana kwa kutoa mafunzo mbalimbali ambayo yatawawezesha vijana wetu wanawake kwa wanaume kuzalisha kwa tija lakini fedha inayowekwa pale ni ndogo. Kila siku Mheshimiwa Mavunde anajibu maswali hapa, anatutajia namba ya watu wachache sana wanaopata manufaa ya mafunzo haya. Hii Tanzania ni nchi kubwa, ina watu wengi na vijana ni wengi. Ukija na mifano ya vijana 7,000 waliofundishwa hiki au kampuni moja ya SUA iliyofanya hivi, hiyo haitoshi kabisa. Tuwekeze kwa kiasi kikubwa tutaona tija itakavyokuwa kubwa. Mwaka huu wakati wa bajeti nilisema tukiwekeza hata trilioni moja tu kwenye kilimo tutaona impact yake itakavyokuwa katika maendeleo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nachotaka kuhimiza hapa ni kwamba tunaendelea vizuri kiuchumi lakini tufike sasa mahali ambako tunakwenda pamoja katika masuala ya uzalishaji wenye tija. Tutumie sekta binafsi, ubia na teknolojia ili tuwawezeshe wananchi wengi zaidi na wao kuingizwa katika mfumo wa kifedha utakaowawezesha kupata mikopo na mitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile Benki Kuu itumie fursa ya kuwa wananchi wengi wa Kitanzania tayari wanatumia simu za mkononi na wanafanya miamala kwa kutumia simu na wao waje na bidhaa ambazo zinakidhi level hiyo ya wateja kuwatengenezea bidhaa ambazo wataweza kuzitumia kukopa, kuweka akiba lakini vilevile kwa kupunguza riba. Riba inawashinda wananchi wetu kukopa kwa sababu bado ni kubwa. Tunafahamu kuwa riba hata ikiwa asilimia 10 itawawezesha wananchi wengi zaidi kukopa vilevile wakakopeshwe katika njia ya makundi, maana mkulima mmoja mmoja inawezekana asiweze kukopeshwa na mabenki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka kabisa kuna wakati CRDB walianzisha mfumo wa kukopesha SACCOS halafu SACCOS wanakwenda kukopeshana wenyewe kwa wenyewe na CRDB wanakaa wanasimamia kuhakikisha kuwa ule mkopo unawezekana. Kwa kufanya hivyo, tutajikuta tunapunguza zile gharama za benki kujiingiza katika kumkopesha mtu mmoja mmoja lakini bado tukafikia uwezekano wa kukopesha wazalishaji wetu, wakulima, wafugaji, wavuvi, wakiwa katika makundi hayo au vyama hivyo vya ushirika na wakaweza kukopeshwa na wao wakaingizwa sasa katika mfumo mzima wa uchumi wa nchi na wakachangia pato kubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la biashara ya ndani. Kwa bahati mbaya Tanzania tunaagiza vitu vingi sana kutoka nje ambavyo tungeweza kuvizalisha wenyewe. Hili ni eneo ambalo lazima tulitilie mkazo na kwa vyovyote vile mimi sioni kama tuna haja ya kuona aibu kulinda viwanda vyetu au wazalishaji wetu, dunia nzima ndivyo wanavyofanya. Huwezi kwenda kumlisha mtoto wa jirani wakati wa kwako analia njaa jamani! Lazima tuhakikishe sisi wenyewe soko letu limejaa bidhaa tunazozalisha wenyewe na hii ndiyo itakayotuwezesha kuongeza mapato ya ndani. Tunategemea mapato kidogo sana kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa wachache sana wakati kuna fursa kubwa sana ya soko la ndani kwa wazalishaji wadogo wadogo ambao wangeweza kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante sana. Kengele ya pili.

MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Napongeza, hotuba ni nzuri ya kimkakati na naamini itaenda kujibu hoja nyingi ambazo zilikuwa zimeleta wasiwasi mkubwa sana katika sekta hii. Bado nasikitika tu kuwa Wizara hii bado inapewa bajeti ndogo ukilinganisha na mahitaji, na hasa ukichukulia kuwa ni sekta ambayo kwa kweli ingetutoa katika umaskini kabisa katika nchi yetu. Mimi ninaamini hivyo na nafikiri hata data zinaonesha kuwa kweli hii Wizara hata ingepata trioni moja tu ingefanya mambo makubwa sana kwa sababu ndio inayoajiri asilimia kubwa sana ya watanzania wakiwemo akina mama na vijana. Vilevile ndiyo inayolisha taifa zima na ingeleta fedha nyingi sana za kigeni ambazo zingetuwezesha sasa kufanya mambo mengine makubwa zaidi ya miundo mbinu na kadhalika, hayo ndio maoni.

Mheshimiwa Spika, lakini sasa hivi nataka kuzungaumzia sana suala zima la kilimo chetu, kwamba kimejikita sana kwenye mvua; na kama tunavyojua mvua huwezi kuitegemea kiasi hicho. Tumekuwa na scheme nyingi sana za umwagiliaji lakini kwa bahati mbaya scheme hizi zote zilikuwa zinasimamiwa kwa kiasi kubwa na fedha za nje, na hata hao wahisani wenyewe kuwa ndio waliokuwa wanaweka wakandarasi kuja kuendesha hizo scheme na nyingi hazikufanya vizuri.

Mheshimiwa Spika, ningependa kuomba sana Serikali ihakikishe kuwa inaweka fedha ya kutosha katika scheme za umwagiliaji; lakini vilevile waangalie ni kwa jinsi gani wanaweza kuwasaidia wanananchi wakulima wadogo wadogo katika kuanza utaratibu wa kuvuna maji ya mvua. Mvua huwa inanyesha nyingi sana kwa vipindi tofauti nchi kwetu lakini inaishia chini. Kama wananchi wangekuwa wanafundishwa jinsi kuvuna maji ya mvua kwa sehemu zao wenyewe walizopo ingesaidia hata kwa kiasi kikubwa sana kukidhi mahitaji ya maji katika maeneo yao na wengeweza kumwagilia, kufuga na kufanya shughuli zile zingewaletea kipato.

Mheshimiwa Spika, nataka nije kwenye suala zima la mazao ya kimkakati. Kuna mazao makubwa ya kimkakati ambayo yametajwa na katika mkoa wangu wa Songwe na hasa Wilaya ya Ileje; kuna mazao matatu ya kimkakati katika Tanzania lakini Wilaya yangu inayalima kwa wingi ikiwa ni pareto, kahawa, alizeti na bado kuna fursa ya kuzalisha mazao mengi kwa sababu ya hali hewa, udogo uliopo kule na watu wenyewe wanajituma sana katika kufanya kazi. Tatizo letu kubwa ni huduma za ugani. Huduma za ugani ni ndogo, tunahitaji wataalamu wengi sana wa kutuongoza katika kila kijiji.

Mheshimiwa Spika, vilevile suala lingine ni masoko; bado masuala ya masoko hayajakaa vizuri. tunajua Serikali imefanya makubwa sana na kwa kweli wametusaidia kwa kiasi kikubwa sana katika kuonyosha ule mfumo mzima wa soko lakini bado haujakamilika, bado kuna changamoto nyingi, kuna tozo nyingi na bado kuna tatizo la miundombinu ya kuyafikia masoko yale.

Mheshimiwa Spika, tungependa kuona sana Serikali ikihakikisha kuwa katika hata maeneo ambayo yana fursa nzuri za uzalishaji kama Ileje, Mbozi na Mkoa mzima wa songwe basi inaturahisishia miundo mbinu ambayo itawawezesha wananchi kufikisha mazao sokoni.

Mheshimiwa Spika, Vilevile Kuhusu Elimu Pamoja na Pembejeo Bora. Tuna matatizo makubwa ya pembejeo za kuwezesha mazao yetu kuwa na ubora na uzalishaji mwingi. Bado tuna fursa kubwa sana katika soko la dunia kwa kahawa na pareto. Pareto kwa Afrika tunaongoza sisi Tanzania, hiyo ingekuwa fursa kubwa sana kwetu kuhakisha kuwa tunawekeza nguvu zaidi katika zao hili kwa sababu tayari sisi tuna hiyo fursa kitaifa. Kwenye kahawa vilevile kuna masoko maalum ambayo tungeweza kuyalenga kwa mfano masoko ya organic, masoko ambayo yangeweza kuwa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Malizia Mheshimiwa dakika moja.

MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Spika, kwa hali hiyo ningependa sana kuona Wizara hii ikijikita kimikakati katika yale maeneo ambayo yana mazao ambayo tayari yana- advatage ya kuzalishwa kwa wingi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba hii muhimu katika maendeleo ya uchumi wa taifa letu. Ninaipongeza Wizara iliyoongozwa na Mheshimiwa Waziri Japhet Hasunga, Naibu Waziri Mheshimiwa Omary Mgumba, Naibu Waziri Mheshimiwa Innocent Bashungwa na Katibu Mkuu wa Wizara na watendaji wa Wizara kwa hotuba nzuri ya kimkakati ambayo itaenda kutatua changamoto nyingi zilizoko katika Wizara hii. Ni matumaini yangu kuwa, timu hii itaibadilisha kabisa tija ya sekta hii nchini.

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa mazao ya kimkakati, yaani kahawa, pareto, pamba, tumbaku, alizeti, parachichi, mbaazi, kunde, choroko, dengu, soya, kwenye mazao mchanganyiko Mkoa wa Songwe unazalisha kwa wingi kahawa tena ya arabika, pareto, cocoa, mpunga, parachichi, soya, mahindi, maharage, viungo na mboga. Fursa za kuendeleza mazao haya, hususan pareto, kahawa, cocoa, viungo na alizeti ni kubwa sana. Wakulima wamehamasishwa sana na wameitikia wito na wanazalisha kwa wingi hasa katika Wilaya ya Ileje.

Mheshimiwa Spika, iko haja ya Serikali kuwa na mkakati wa kuzingatia hatua zote za mnyororo mzima wa thamani katika kila zao muhimu na la mkakati, liwe la chakula au la biashara. Hii ni pamoja na uzalishaji, usafirishaji na uhifadhi. Soko linahitaji aina ya bidhaa, kiasi na ubora na kwa hivyo iko haja ya kuwekeza katika kukuza uzalishaji mkubwa. Uzalishaji mkubwa unahitaji teknolojia na matumizi bora ya pembejeo, mbegu bora, miche, mbolea, dawa, pamoja na kuimarisha shughuli za ugani, ili kulinda ubora na wingi wa uzalishaji mazao husika.

Mheshimiwa Spika, katika suala zima la ugani kuna changamoto kubwa ya upotevu mkubwa wa mazao wakati wa kuvuna na wakati wa kuhifadhi. Upotevu huu wa mavuno unatokana na changamoto ya uhifadhi, maghala, kwamba hayatoshelezi na kwa hivyo hata ile dhana ya kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani unashindikana, na kwa hivyo, kumfanya mkulima kukosa bei nzuri na huduma muhimu za kumlinda dhidi ya hasara na umasikini wa kipato.

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya yangu ya Ileje mazao yanayozalishwa ni pamoja na kahawa ya arabika, pareto, alizeti na kwa kiasi kidogo cocoa na korosho ambayo imeanza kulimwa. Eneo linalolimwa kahawa limeongezeka kutoka hekta 5,859 hadi hekta 6,229 ambapo jumla ya kata 10 zinajihusisha na kilimo cha kahawa. Uzalishaji kwa Ileje upo kati ya tani 550 hadi tani 800 kwa mwaka. Mwaka 2017/2018 tulipata tani 707.9, mwaka 2018/2019 tumeweza kupata tani 549.9. Kushuka huku kumesababishwa na hali ya hewa iliyoathiri kipindi cha kuchuma maua. Ileje na Mbozi ni wilaya mbili zinazozalisha kahawa ya arabika, kahawa hii inafanya vizuri kwa sababu, ya hali nzuri ya hewa, rutuba na mvua ya kutosha.

Mheshimiwa Spika, masoko ya kahawa bado ni changamoto japo bado mahitaji ya kahawa ni makubwa katika masoko ya nje kama Japan wanaonunua gourmet coffee kwa bei kubwa sana kwa sababu ni kahawa inayozalishwa bila kutumia kemikali (organic), Ulaya, Canada, India, China na kadhalika. Masoko haya yanatupa fursa ya kuona umuhimu wa zao hili, ili kuwekeza zaidi kuhakikisha tunaingiza fedha nyingi ya nje kujenga ajira za wananchi wengi zaidi.

Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali katika kurekebisha mfumo wa vyama vya ushirika; hii imesaidia sana, lakini bado elimu ya kutosha inahitajika kwa wananchi kuielewa hii dhana, hasa baada ya historia mbaya iliyojengeka huko nyuma.

Mheshimiwa Spika, tunaishauri Serikali iendelee kufanyia kazi suala la masoko. Kilimo hai kiendelezwe kwenye kahawa, hii itasaidia wakulima kupata bei nzuri. Serikali itueleze itaweka mkakati gani wa kuendeleza hili. Ugani kwenye kilimo cha kahawa unahitajika sana ili kuwawezesha wakulima kuongeza tija.

Mheshimiwa Spika, zao la pareto ni miongoni mwa mazao ya kipaumbele kwa Wilaya ya Ileje na ndani ya Mkoa wa Songwe. Zao linalimwa katika hekta nne vijiji 12 wakulima 3,500. Wakulima wanahitaji elimu zaidi, miche bora na utaalamu kuzingatia ubora wa zao wakipeleka sokoni, ili wapate bei nzuri. Serikali isaidie katika kuwasaidia wakulima kutengeneza makaushio bora na yanayozingatia utunzaji wa mazingira. Jumla ya tani 397 za mauwa ya pareto zilikusanywa mwaka hadi Aprili, 2019.

Mheshimiwa Spika, tunashauri Serikali ifanyie kazi changamoto zinazolikabili zao hili. Suala la masoko liendelee kufanyiwa kazi ili kupata masoko ya bei nzuri kwa wakulima. Kuboresha miundombinu ya hifadhi ya mazao (maghala).

Vyama vya ushirika kuwezeshwa kiuchumi/mitaji, ili kuwawezesha wanachama wao kuendesha shughuli za maandalizi ya zao hili.

Mheshimiwa Spika, parachichi ni zao linaloongezeka kwa umuhimu katika Wilaya yetu. Hili pamoja na pareto na hata kahawa bado vinaingiliwa sana na walanguzi, hasa kutoka Kenya. Je, Serikali inafanya nini kuzuia hili jambo ambalo linawanyonya wakulima na kuwanufaisha wakenya?

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba hii mbele yetu. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Biteko, Naibu Waziri, Mheshimiwa Haroon Nyongo (Mb), Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri na kubwa wanayofanya.

Mheshimiwa Spika, nchi yetu ina madini, vito na rasilimali nyingi za madini ya thamani na yasiyo na thamani lakini kwa umasikini uliopo hata maeneo yanayotoka madini au rasilimali hizi haziakisi utajiri huo. Hii inatokana zaidi na utekelezaji wa sheria na kanuni zetu katika kuwezesha mali hii kulisaidia taifa. Hatuna rafiki wa wazalishaji wa sekta hii kwa jinsi tunavyowanyanyasa kwa lugha, vitisho, kodi na tozo.

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Makaa ya Mawe Kiwira na Kabulo. Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira umesima kwa zaidi ya miaka tisa sasa. Mwaka 2018 uchimbaji ulianza kidogo katika mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kabulo; tangu wakati huo hatujapata taarifa yoyote mpya ya mendeleo ya migodi hii miwili. Hotuba ya Waziri wa Madini ukurasa wa 53 una-report kuwa STAMICO wamechimba tani 22,119 za makaa ya mawe na kuuza tani 7,664.8 tu.

Mheshimiwa Spika, lakini taarifa hii ni ileile tuliyopewa kwenye hotuba mwaka jana. Ina maana hatuna maendeleo yoyote yaliyofanyika tangu Aprili, 2018? Serikali itufahamishe ina mpango gani wa kufufua mgodi wa Kiwira na kuendeleza mgodi wa Kabulo. Tangu mgodi wa Kiwira usitishe chini ya Tanpower Resources Company Limited kumekuwa na sintofahamu ya nani muhusika mkuu wa mgodi huu baada ya kuondolewa kwa muwekezaji huyu aliyekabidhiwa mgodi tangu mwaka 2005; waliopewa silimia 70 ya hisa na Serikali kubaki na silimia 30.

Mheshimiwa Spika, tangu mgodi kurudishwa Serikalini mwaka 2009, NSSF walilipa madeni ya mgodi shilingi bilioni 28.72, Benki ya CRDB nayo ina deni, PPF, NSSF wanaudai mgodi Dola milioni saba. NSSF ilitaka kuchukua mgodi huo na kuuendesha na kulipa madeni yote. Hii ingewezekana kwa sababu mgodi una mali nyingi zaidi ya madeni.

Mheshimiwa Spika, mgodi wa Kiwira ulilenga kutumia Makaa ya Mawe kuzalisha umeme na kuuza TANESCO. Mgodi huu ulikuwa unatoa ajira 7000 kwa wananchi wa Ileje kwa uchache lakini kwa kiasi kikuba na Kyela na Rungwe. Mgodi ulikuwa unawezesha Halmashauri kupata mapato na vilevile kuchangamsha uchumi kupitia biashara na ajira zinazounganisha watoa huduma kwenye mgodi. Vilevile kwa familia za watumishi wa mgodi wanaonufaika na mgodi. Sasa hivi kusimama kwa mgodi huu kumezorotesha uchumi wa Ileje na wilaya za jirani kwa zaidi ya miaka tisa sasa na hivyo ni athari hasi sana kwa wilaya yenye rasilimali muhimu na kubwa kama mgodi huu wa makaa ya mawe.

Mheshimiwa Spika, aidha, huu mgodi huzalisha umeme; hii pia imeleta athari kwasababu maeneo haya yamekosa hii connection. Katika bajeti ya Wizara ya TAMISEMI ilitengwa bajeti ya kujenga daraja kwenye Mto Mwalisi linalounganisha mgodi wa Kiwira na Ileje. Je, hiyo fedha itatolewa lini ili kurahisisha usafirishaji wa makaa ya mawe?

Mheshimiwa Spika, Wana Ileje tunaomba sana Mgodi wa Kiwira na wenyewe uanze kazi; na vilevile na ule wa Kabulo uendelee kwa kasi zaidi kwa kutafuta masoko zaidi kwa mwe yanayochimbwa.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
The Written Laws (Miscellaneous Amendment) (No.2) Bill, 2016
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nami naipongeza sana Serikali kwa jinsi ambavyo wametuletea Miswada mbalimbali ambayo marekebisho yake kwa kweli yataboresha tija na utekelezaji wa masuala mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninajikita zaidi kwenye ule Muswada wa Sheria wa Ant-Trafficking in Persons. Nataka kuzungumzia kidogo juu ya hili suala. Nafikiri kuna haja sana ya Serikali kuweka mkakati wa kufahamisa wananchi juu ya tatizo hili la usafirishaji wa binadamu. Hili ni jambo ambalo linatendeka na watu wengi bado hawajaweza kulitambua vizuri kuwa linakaaje. Hili suala linaathiri sana wanawake na watoto, kwa sababu kwa kiasi kikubwa, wao ndio wanafanyiwa hivi vitendo, wengine ni kwa udanganyifu wanaambiwa wanaenda kutafutiwa kazi, wengine wanaambiwa wanaenda kusomeshwa, wengine wanaambiwa utaenda kufanya kazi nyumbani kwangu, wakifika huko wanaishia kwenda kuwekwa kwenye ukahaba na mambo mengine. Wanaumizwa, wanapigwa, wandhalilishwa kijinsia, wengine wanapoteza hata maisha, wengine wanapoteza viungo, wengine wametolewa mpaka vizazi. Hili ni jambo la kikatili, ambalo ni kubwa sana unaweza kufanyia mwanadamu yeyote hapa duniani. Watoto wetu wengi wameingia katika hilo kwa udanganyifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nchi zinazoendekeza au zinazoruhusu ukahaba, ndiyo nchi ambazo zinavutia sana hawa watu wanaofanya biashara hii. Ningependa sana Serikali pamoja na Sheria waliyoileta na mapendekezo ya kutoa adhabu wahakikishe kuwa na wananchi wa kawaida wanatambua jinsi gani hii biashara inafanywa ili wakiona dalili zozote waweze kutoa taarifa kwa vyombo vya dola. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nchini hii biashara vilevile ipo, wengine wanaambiwa wanaenda kuwa ma-housegirl, wengine wanaambiwa vitu vingine, lakini yote haya ni katika jumla ya usafirishaji. Wototo wetu wadogo wengi sana wa mitaani wanachukuliwa wanadanganywa wanapelekwa kwenye hizi biashara. Naomba sana hili jambo lisipuuziwe, ni jambo gumu na ni baya sana kwa jamii na linaathiri sasa saikolojia za watu wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujikita vilevile kwenye hii sheria inayohusiana na masuala ya elimu. Tunaipongeza Serikali sana kwa kuleta marekebisho yanayolenga kumlinda mtoto asome mpaka atakapomaliza masomo yake kabla ya kuolewa au kuoa. Pia ninaomba ijumuishe na watoto wa chini ya miaka 18 ambao wako nje ya mfumo wa elimu. Kuna wanaosoma tu hizi shule labda Vocational au tu evening classes au hata ambao wako tu nyumbani. Kwa sababu suala hapa ni mtoto, kwa mtu hajafIkia umri wa kuolewa au kuoa.
Ningeomba sana mlizingatie hilo, kwa sababu bado tuna watoto wetu wengi huko nje ambao hawako kwenye mfumo wa elimu, hawako kwenye mfumo wa shule, lakini bado ni wadogo. Sasa tukiiacha wazi hii, kwanza unaweza ukaleta hata wazazi wengine wakawatoa watoto shule ili wawaoze, lakini vilevile inaweza ikawasababishia wale watoto ambao hawako kwenye mfumo wa elimu kufanyiwa hili jambo la kuolewa au kuoa kabla hawajafikia umri wao. Kwa hiyo, ningependekeza Serikali iangalie kuwa suala ni kumlinda mtoto awe shule au awe nje ya mfumo wa shule.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuhusu suala la adhabu, kwa kweli kama ni kijana mdogo ambaye hajafikisha miaka 18 ambaye amempa mimba mwenzie, naamini Kamati ya Bunge imezungumzia sana kuwa hii watachukua hatua kufuatana na Sheria ya Mtoto. Lakini kusema kuwa eti mtu asifungwe miaka mingi kwa sababu nini? Jamani!
Mimi naomba tusitetee haya mambo, sisi ndiyo kina mama tunaodhalilika na haya mambo, tunayatambua, acha hii iwe ndiyo njia ya kumzuia mtu kufanya haya mambo, wanawake wakubwa wako wengi. Kwa hiyo, watu wanaweza wakaenda kwa hawa wakubwa waache watoto wetu wasome na atakayekiuka basi achukuliwe hatua kama ilivyotajwa na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuchangia Sheria ya Ushahidi ya Sura Na. 6 ambayo inamruhusu mtoto sasa kuwa ushahidi wake utumike kama hakuna ushahidi wa aina nyingine yoyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuunga mkono hili kwa sababu natambua kuna mazingira ambayo mtoto anaweza kuwa ameona kitu kweli na ikashindikana kutoa ushahidi kwa sababu tu eti hakuna ushahidi mwingine wa kum-backup.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kuomba sasa, Serikali ihakikishe kuwa huyu mtoto katika kutoa ushahidi wake hataathirika kisaikolojia, hatapata vitisho vya aina yoyote na atakuwa salama, kwa sababu watoto wengine wataogopa kutoa ushahidi wakiona kuwa kwa kutoa ushahidi anaanza labda kunyanyapaliwa hata kwenye familia au kwenye jamii kuonekana huyu mnoko, umeenda kusema ya nini? Wewe mtoto sijui kitu gani! Huna tabia nzuri!
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi vyote lazima viangaliwe, kwa sababu tunataka kuhakikisha kuwa haki inatendeka na kama mtoto aliyetoa ushahidi, aote ushahidi lakini naye apate kinga yake ya kumtosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yangu yalikuwa ni hayo, lakini napenda sana kuiomba Serikali isikilize kilio cha akina mama kuhusiana na masuala yote yanayohusiana na watoto wa kike. Hiyo ya kusema mtoto wa kike ndio amemtongoza mwanaume, sawa inaweza kutokea, lakini ni mara ngapi inatokea hiyo jamani? Tuangalie ile hali halisi jinsi ilivyo. Akina baba, mwende mkatafute akina mama wa umri wenu, mtuachie watoto wetu wasome.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Nami pia namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali asubuhi ya leo na kunipa pumzi yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Habari, Naibu Waziri na timu yake nzima. Napenda kuwapongeza sana Mwenyekiti wa Kamati husika pamoja na wajumbe wote wa Kamati ile. Napenda vilevile kuwashukuru wachangiaji wote wenye nia njema ambao wametoa michango mizuri sana ambayo inaenda kuboresha Muswada huu. Aidha, nataka kuishukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa jinsi ambavyo wamekuwa wasikivu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, imeelezwa hapa kuwa huu ni Muswada ambao umechukua muda mrefu sana kuletwa Bungeni, naamini huu ni wakati muafaka kwa Muswada huu kuja hapa. Naamini kuwa haya ni majira na nyakati sahihi kwa huu Muswada kufika hapa kwa sababu umepata nafasi ya kupitiwa na michango imetolewa mingi sana na tunaona jinsi ambavyo imeendelea kuboreshwa siku hadi siku, mwaka hadi mwaka hadi hivi leo tunaendelea kuujadili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niipongeze Serikali kwa sababu tayari kuanzia michango ilivyoanza kutolewa wamekuwa wakirekebisha yale maeneo ambayo yalikuwa yanaleta ukakasi katika Muswada wetu. Nataka kuamini sana kuwa Serikali yetu inaleta Muswada huu kwa nia njema kama ambavyo imekuwa ikifanya muda wote. Nataka kuamini sana kuwa Muswada huu umeletwa kwa nia njema ya kuhifadhi maslahi ya wanaotumikia tasnia hii ya habari hasa waandishi wenyewe lakini hata vyombo kuhakikisha kuwa vinawatendea haki watumishi wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana mambo mengi sana yaliibuliwa humu ndani ambayo yanasemekana kuwa ni historia na tulikuwa tunataka kuaminishwa kuwa tuendelee na historia ile kitu ambacho hakiwezekani kwa sababu dunia hii haijasimama pamoja. Tunaendelea na kila siku maendeleo mapya yanataka hatua tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia nchi nyingi ambazo zimekuwa na sheria kama hizi na hata kama zilikuja kubadilishwa lakini zilibadilishwa kufuatana na mazingira yanavyoibuka. Hizo nchi zinazoambiwa zimeendelea sana, nazungumzia nchi kama Norway ambao wao pia huko nyuma wamekuwa na Miswada kama hii, wameenda wakiibadili kufuatana na hali halisi ya uchumi na maendeleo ya teknolojia. Hata sisi kwa kuleta Muswada huu leo tunaangalia hali halisi ya mazingira waliyonayo waandishi wetu na katika tasnia nzima hii ya habari. Katika tasnia hii hakuna udhibiti wa aina yoyote, hakuna mpangilio wa aina yoyote, kila mtu anaendesha tasnia hii kwa jinsi anavyoona inamfaa yeye kwa maslahi yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kutokana na hali hiyo kuna wanaoumia na ndiyo maana Serikali imeona kuna umuhimu sasa kutokana na malalamiko ya hao hao wanaoumia kuona kuwa taaluma hii ichukuliwe kama taaluma nyingine yoyote. Kwa hali hiyo iwekewe utaratibu mzuri utakaohakikisha kuwa wanaohusika wanapata haki lakini vile vile Taifa halikoseshwi haki zake za msingi za kujieleza na vyombo husika havitumii nguvu yao ya kifedha kukandamiza wale ambao wanawatumikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikumbushe tu kuwa Marekani sasa hivi wao waliondoa mfumo wa kuwa na sheria ya kudhibiti habari, lakini badala yake wameweka sheria za kudhibiti ushindani ambazo vilevile zinahakikisha kuwa ushindani wa haki unafanyika katika kila taaluma na kila sekta. Hii ni kwa sababu inatambulika kuwa tasnia ya habari ina mchango mkubwa sana katika kushawishi sera za nchi, biashara na ushindani. Inaonekana kuwa kama watu matajiri, makampuni makubwa yakiachiwa wao kuendesha ushindani wanavyotaka wale wadogo watashindwa kumudu ushindani huo. Kwa hiyo, Serikali imeingiza sheria ambazo zinaleta ushindani bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi hatujafika mahali ambapo ushindani wa kibiashara au wa kiuchumi upo sawa kwa sababu bado nchi yetu inakua kiuchumi. Kwa hali hiyo, lazima hapa katikati kuwe na utaratibu wa kuhakikisha kuwa tasnia hii ya habari haitumiki vibaya. Tayari tumeshaona mifano, kuna watu wameingia humu ndani wote wanaimba chorus moja, hii moja kwa moja inaashiria kuwa kuna mahali wamepewa hiyo chorus waje waiimbe humu ndani. Hiyo tayari inaonekana jinsi ambavyo tasnia hii inaweza ikatumika kushawishi vibaya na inataka sasa kushawishi mpaka hata huu Muswada uende vile wanavyotaka wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaambiwa kabisa kuwa hii sheria imechelewa kuletwa kwa sababu kila mara kulikuwa kuna upinzani unaozuia isiletwe na ukichukuza upinzani huo ni kwa wale wenye vyombo vya habari sio waandishi, sio watumishi. Sasa hii inaonekana dhahiri tayari kuna utumiaji mbaya wa madaraka yao ya kiuchumi kutaka kukandamiza wengine kwa manufaa yao. Sasa Serikali imeona umuhimu huo kuwa sasa hivi lazima wale wanaotumikia tasnia hii wafanye kazi kwa utaratibu ambao unakubalika bila kuathiri uhuru wa vyombo vya habari, bila kuathiri watu wanaotaka kujieleza na kutoa maoni yao katika Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakubali kuwa maana nzima ya kuleta udhibiti katika tasnia hii kwanza ni kuhakikisha kuwa maslahi ya Taifa yanaliandwa lakini vilevile ni kuhakikisha kuwa tunapanua vigo wa ushindani, kuhakikisha kuwa kunawekwa viwango vya taaluma hii. Mengi yameshazungumzwa kuwa taaluma hii kwa kweli haikuwa inazingatiwa, waandishi walikuwa wanajiendea vyovyote vile, wameitwa majina mabaya sana kwa sababu tu ni kweli walikuwa hawatambuliki. Sasa kama tupo tayari kuweka viwango, kama tupo tayari kuhakikisha kuwa haki zao zinalindwa, kama tupo tayari kuhakikisha kuwa ushindani unakuwa sawa katika vyombo vya habari kuna ubaya gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kabisa maslahi ya Taifa sasa hivi lazima yazingatiwe kutokana na maendeleo ya teknolojia. Tunaona jinsi ambavyo vyombo vinatumika vibaya katika kueneza taarifa za uongo au za uchochezi au hata za kuharibia watu majina. Wote humu ndani kwa njia moja ama nyingine tumeguswa na haya mambo ya watu wanavyotuma taarifa ambazo sio za kweli, watu wanaunganisha mpaka picha anaonekana mtu kweli lakini sio yeye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa vitu kama hivi hatuwezi kuendelea kuviachia na kwa kufanya hivyo tutakuwa sisi wenyewe hatujitendei haki. Tunakubali kuwa kuna haja ya kuwa na uhuru wa kujieleza na hiyo imewekwa wazi na mapendekezo ambayo yanaletwa sasa hivi ya kufanya amendment kwenye huu Muswada yote yameangalia mambo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuzuia kutangaza vitu ambavyo sio vya kimaadili hivyo ni vitu vinazingatiwa hata na nchi zilizoendelea. Nataka niwakumbushe tu mfano ambao sio mzuri sana kwetu sisi wanawake lakini ni kitu kilichotokea. Marekani kuna msanii mmoja maarufu anaitwa Janet Jackson alikuwa ana-perfom, bahati mbaya nguo ikadondoka upande mmoja wa mwili wake ukaonekana watu wakairusha, ikaonekana kuwa ile ilikuwa ni makosa na waliofanya hivyo walitozwa faini kwa kufanya hivyo. Sasa bila kuwa na sheria utamtoza faini mtu wapi? Kwa hiyo, vitu vingine tukubali kuwa lazima viwepo. Tunachotaka kusisitiza hapa ni uhuru wa habari usiminywe na hii imezingatiwa jamani, angalieni amendment zilizoletwa zimeangalia hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia suala la sedition au uchochezi ambao unaweza ukaleta machafuko. Ndugu zangu, Serikali imekubali kuleta amendment kuhusiana na suala hili na tayari mmeshaanza kuona kuwa zile adhabu ambazo zilikuwa zimewekwa za kijumla ambazo zinajumlisha aliyechapisha au aliyeandika zimeondolewa, atalengwa mhusika peke yake. Hii ndiyo maana nzima ya Serikali sikivu imeona kwa kweli hakuna sababu ya kutomtendea haki mtu ambaye yeye hahusiki na kosa sasa inaenda kumwadhibu mwenye kosa peke yake. Vilevile lazima tukubali kuwa Serikali inabidi isimamie na iingilie pale inapoona kuwa kuna ukiukwaji wa haki au usalama wa nchi, sasa hiyo haiwezekani bila kuwa na Muswada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme tu maoni mengi yametolewa na ni mazuri sana na Serikali bahati nzuri inaenda kuyafanyia kazi. Sisi tutaendelea kutetea…
Ahsante sana na naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2018
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza nianze kwa kuunga mkono sana Muswada huu ulioko mbele yetu na naipongeza sana Serikali kwa kuleta mapendekezo haya ya mabadiliko ya Sheria hii ya PPP. Kwa kweli hii ni sheria ambayo tumekuwa tukiisubiri muda mrefu; tumelalamika sana humu ndani kuzungumzia kwa nini PPP? Hatimaye Serikali imesikia na imekuja na mapendekezo ya kuboresha Muswada huu ili sasa uanze kutumika vizuri na kwa njia ambayo inategemewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafurahi vilevile kuwa kwa maana hii sasa Serikali imefungua milango zaidi kwa sekta binafsi na imeweka maeneo mbalimbali ambayo sekta binafsi inaweza ikaingia ubia na Serikali katika ngazi ya Serikali Kuu, TAMISEMI na katika sekta nyingine kama za mafuta na kadhalika. Nafikiri hilo ni jambo muhimu sana la kupongezwa, kwanza itatujengea uwezo mkubwa na italeta ufanisi mkubwa katika kutekeleza miradi ya maendeleo ya nchi yetu na italeta ushiriki mkubwa zaidi wa wananchi kwa sababu tunaona sasa kuwa hata katika ngazi ya Halmashauri kutaweza kuwa na PPP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu imepiga hatua kubwa sana kimaendeleo kwa maana ya macroeconomic development, lakini bado tuna masuala makubwa sana ya umaskini na haya yote najua yatakuwa addressed kama tutakuwa na vibrant economy katika level ya Halmashauri zetu. Najua kuwa na PPP kutasaidia sana kuweka huru fedha ambazo zilikuwa zinaingizwa na Serikali katika miradi mikubwa mikubwa ambayo ni ya kibiashara zaidi na itawezesha Serikali sasa kuwekeza zaidi katika huduma za kijamii lakini ambazo pia zinaweza zikafanywa kwa kutumia ubia na sekta binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili kwangu naona ni faraja kubwa na ninafikiri ni jambo la kuipongeza Serikali sana bila kuangalia historia. Kwa sababu nachoona ni kuwa Serikali imekuwa ikijenga kidogo kidogo uelewa, ufahamu na uwezo wake ku-engage na private sector. Kwa hiyo, siyo suala la kusema walikuwa wapi, kwa nini hawakufanya hivi, suala ni kuangalia kwa sasa hivi tunakwenda wapi na mwelekeo ni mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri nianzie kwenye hili suala la solicited and unsolicited proposals. Kwa bahati nzuri safari hii Serikali imekuwa wazi zaidi juu ya unsolicited proposals kuwa itazikubali na imeweka na masharti. Siyo Serikali ya Tanzania peke yake inayofanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu kidogo nisome kitu hapa nilichokitoa katika semina tuliyoipata hivi karibuni inayozungumzia masuala ya unsolicited proposals. Unsolicited proposals zinakubalika lakini kwa masharti, dunia nzima; hata World Bank wanasema wao hawaruhusu unsolicited proposals unless zinapitishwa katika rigorous test. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ubaya wa unsolicited proposal inaweza kuwa ni wazo zuri lakini ni wazo limeletwa na mtu mmoja au nchi moja kutaka kuingia ubia na nchi nyingine, lakini wewe unayeletewa hiyo proposal hukuitaka, hukuiitisha lakini ni mtu anakuja kuuza wazo lake kwako. Una kazi ya ziada ya kulifanyia tathmini wazo hilo ili uone kama kweli liko feasible. Hiyo moja kwa moja ni kazi na ni gharama kwa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia pia wazo hilo linaweza kuwa limekuja kwa njia ambayo siyo ya wazi sana. Faida kubwa itakuwa ni ya yule aliyeleta proposal nchi mnaweza msifaidike, sasa hiyo ni lazima muifanyie kazi. Kwa hiyo, nimeshangaa kusikia mtu anasema hapa zile proposals mradi sisi hatutoi pesa yetu, basi tuziachie tu ziingie. Hakuna kitu kama hicho duniani, tutakaribisha vitu vya ajabu sana tusipoangalia ndugu zangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kutoa mifano. Afrika Kusini pia hawa-encourage sana unsolicited proposals na zikija zinapitishwa katika tathmini kama vile ni proposal ambayo imekuwa solicited ili kuifikisha katika level moja; na je, ingekuwa sisi ndio tumependekeza kufanya mradi huu, tungeupitisha jinsi ulivyo? Kwa hiyo, ndugu zangu, nataka tuwe makini sana na hizi unsolicited. Nashukuru kuwa Serikali imekubali kuwa itaziangalia na imeona kuwa kuna maeneo mengine inawezekana zikahitajika kwa sababu pengine hakuna mtu mwingine anayeweza kufanya kazi hiyo, lakini hiyo haituondolei ule umuhimu wa kuziangalia kwa makini zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kuwa kuna suala zima la SMEs. SMEs ni eneo lenye kuleta ajira nyingi sana kwa wananchi na kuongeza kipato kwa wananchi wengi sana na hasa zikifanywa kitaalam. Kama PPP itaruhusiwa katika maeneo haya, basi naamini Tanzania tutaona uchumi ukikua haraka sana kwa sababu wananchi wa kawaida katika biashara zao, makampuni au mashirika yao wanaweza sasa kuingia katika ubia na makampuni yanayotaka kufanya shughuli nao. Kwa mfano, kwenye kilimo, usindikaji, viwanda vidogo, teknolojia, masuala ya nishati na vitu mbalimbali ambavyo moja kwa moja vitafanya uchumi wetu ukue haraka zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotakiwa sasa ni uwezeshwaji wa kutosha. Lazima wananchi wa ngazi hizo wafahamishwe kwanza maana nzima ya kuingia katika ubia wa namna hii, lakini waelezwe vilevile jinsi gani wao wenyewe wanatakiwa ku-negotiate. Wafundishwe vilevile njia bora za kuendesha hii miradi. Kwa hiyo, nachoona hapa ni kitu ambacho ni kizuri sana kwa Tanzania na moja kwa moja najua kitaleta faida kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ethiopia sasa hivi wanaongoza katika uchumi Afrika. Ukienda Addis Ababa sasa hivi ni kama kuna vurugu fulani hivi; huku kunajengwa barabara, huku kunajengwa flyovers, huku kunajengwa EPZs, huku kunajengwa dams, all over the place na vyote ni PPP. Ethiopia walikuwa nyuma hivi karibuni tu lakini sasa hivi wamefika mbali, wametumia mfumo huu wa PPP na umewaendeleza sana. Kwa hiyo, hata sisi hili jambo siyo geni wala halitakuwa baya kwetu, tujifunze tu jinsi gani ya kusimamia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla kengele haijalia, nataka sasa niombe rasmi miradi hii yote ya PPP kuanzia wakati tunazungumzia kutengeneza maandiko, tuzingatie masuala ya jinsia. Kuna wanawake wengi ambao ni wazalishaji, wafanyabiashara na wana makampuni ya kila aina, naomba wawezeshwe na wawekewe sehemu katika kila hatua ya hii miradi ya PPP na wao washiriki, kwa sababu wanaweza na tayari kuna evidence kubwa sana kuwa wanawake wengi sana wanashiriki katika masuala haya. Wawekeeni kitengo maalum cha kuwaelekeza jinsi gani ya kufanya haya mambo, nakuhakikishia utaona jinsi ambavyo uchumi utakua kwa ushiriki mkubwa wa wanawake katika masuala haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna suala la account. Limezungumziwa suala la account lakini sikuelewa vizuri kama account iliyokuwa ikizungumzwa kuwa hela zitawekwa Benki Kuu ni zile tu za upande wa Serikali au ni pamoja na za wale wabia wa sekta binafsi? Kwa sekta binafsi naona inaweza ikawa shida. Kwa hiyo, hilo nafikiri liangaliwe vizuri zaidi, huwezi kuchukua hela za mtu binafsi ukamwingizia kwenye akaunti ya Benki Kuu bila yeye mwenyewe kuwa na ridhaa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliunga mkono tangu mwanzo kabisa, ahsante.
Sheria ya Fedha ya Mwaka 2019
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nami naunga mkono hoja hii lakini nina mambo machache ambayo napenda kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, napongeza sana hatua zote muhimu zilizochukuliwa za kupunguza tozo au kuongeza ushuru sehemu zile ambazo zinalenga kulinda viwanda vyetu vya ndani. Napenda tu kutoa angalizo katika suala zima la kulinda viwanda vya ndani; bado kuna vikwazo ambavyo inabidi navyo viondolewe katika viwanda hivi vya ndani ili kuhakikisha kuwa tozo ile iliyoongezwa kwenye bidhaa zinazoagizwa kutoka nje inatimiza lengo lake maana siyo automatic kuwa kwa sababu umepunguza tozo au umeongeza tozo ya bidhaa inayoagizwa basi kiwanda cha ndani kitakua. La hasha kinatakiwa kifanyiwe kazi na kama tunavyojua kuwa suala la kodi ni sehemu ndogo tu ya uwezeshwaji unaotegemewa kwenye viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi Serikali imeonesha wazi imeshaanza kuifanyia kazi blueprint lakini hii sehemu ambayo tunaiona sasa hivi ni ndogo sana ya blueprint nzima ambayo imechapishwa au imetengenezwa. Tunategemea kwa haraka sana blueprint yote itaanza kutekelezwa na Serikali. Hii ndiyo njia peke yake itakayowezesha sasa uchumi huu kuchangamka na kukua kama inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi bado roho yangu iko sana kwenye kilimo na naamini katika kilimo kwa kuwa Tanzania tuna ardhi nzuri sana inayofaa kwa kilimo lakini haitumiki vizuri. Najua sababu kubwa ni utaratibu mzima uliowekwa wa jinsi ya kuitumia hiyo ardhi kwa wawekezaji wanaohitaji kuwekeza kilimo cha kibiashara, kilimo kikubwa na cha kati. Siyo lazima nizungumzie watu wa nje tu, hata Watanzania walioko ndani bado kuwekeza katika kilimo inawashinda kutokana na vikwazo mbalimbali. Napenda sana navyo ningeviona katika Muswada huu ili tuone jinsi gani ambavyo kilimo kinaenda sasa kukuzwa kama vile ambavyo ndiyo lengo kubwa la Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo kinaajiri watu wengi sana na kinachangia kwa kiasi kikubwa sana kwenye mfumuko wa bei mdogo. Kilimo siyo sekta ambayo unaweza ukaipuuzia.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali sana kwa kuondoa import duty kwenye vifungashio vya mbegu lakini VAT bado haijaondolewa. Kwa hiyo, bado tunarudi palepale katika kuifanya mbegu ya Tanzania kuwa ghali kuliko mbegu inayotoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado tuko nyuma sana katika masuala ya biashara na hii inatokana na urasimu na mtazamo ulioko Serikalini, hasa kwa watendaji wetu au tuseme bureaucrats. Wengi wa watendaji wetu hawa hawajui biashara, hawajawahi kufanya biashara na hawana biashara na kwa hali hiyo wao mtazamo wao kwa private sector ni hasi. Napenda sana nione sasa hivi tunapata watendaji Serikalini ambao wametoka kwenye private sector au kwenye sekta binafsi, naamini watabadilisha ule mtazamo mzima wa jinsi gani biashara ifanywe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mdogo tu, tulipompata Mtendaji Mkuu wa National Housing, hata yule aliyekuwa TIC, walibadilisha kwa kiasi kikubwa sana jinsi ambavyo zile taasisi zao zimefanya kazi. Kwa hali hiyohiyo, ukimleta mtu ambaye ana uzoefu wa kufanya biashara atabadilisha kabisa jinsi ambavyo biashara zinafanyika. Kwa hiyo, tusione vibaya kuajiri Serikalini watu ambao wametoka kwenye sekta binafsi au kuweka kwenye boards watu ambao wametoka kwenye sekta binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie suala la maji. Bahati mbaya sana bado tunatoza kodi solar pumps au pampu zinazotumia nguvu ya jua na mitambo ya kuchimba visima au mabwawa. Sasa hii moja kwa moja inarudisha nyuma suala zima la upatikanaji wa maji kwa ajili ya matumizi ya wanadamu lakini kwa wanyama na kwa kumwagilia na kufugia samaki. Napenda sana kuona jinsi gani ambavyo kodi inapunguzwa au inaondolewa katika pampu hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati mbaya Tanzania peke yetu katika Afrika Mashariki ndiyo tunatoza kodi kwenye hizi pampu za sola; Kenya, Uganda, Rwanda hawafanyi hivi. Hii sasa inafanya sisi uwekezaji wetu katika suala zima la upatikanaji wa maji linakuwa dogo vilevile hata katika umwagiliaji na ufugaji wa samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuzungumzia suala la kuondoa ushuru katika majokofu au cold storage lakini hii imewekwa kwa ajili ya mbogamboga tu na tunafahamu kuwa cold storage inatumika hata kwa samaki, nyama na maziwa. Hii ingekuwa ni njia nzuri sana ya kuwawezesha hata akina mama vijijini wanaofuga ng’ombe wao kuwa na uwezo wa kuweka maziwa yao katika hali ambayo hayaharibiki na kuyafikisha sokoni. Kwa hiyo, mimi napenda kuona kuwa inapanuliwa badala ya kuwa kwenye horticulture peke yake basi iende mpaka kwenye mazao mengine ya ufugaji, hiyo ingesaidia vilevile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la taulo za kike. Nimekubali maelezo yaliyotolewa na Serikali kuhusiana na suala hili vilevile napenda sana kutoa angalizo kuwa zile bidhaa ambazo zinatoka nje zinazoingia katika viwanda hivi ni lazima nazo zitolewe ushuru au zipunguziwe kodi ili sasa hivi viwanda vya ndani viweze kuchukua hii fursa vizuri na kuifanyia kazi. Pia nataka kutoa angalizo au ushauri kwa Serikali, kwa kipindi cha mpito katika hii miaka miwili ambayo tunangojea viwanda vichangamkie fursa hii, Serikali ihakikishe kuwa inawezesha upatikanaji wa hizi taulo za kike kwa bei nafuu kwa maana ya kuweka bei elekezi vilevile labda kutumia MSD kama msambazaji mkuu wa taulo hizi za kike ili ziweze kuwafikia watu wote wanaolengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala zima la kuwatambua wafanyabiashara au wawekezaji wa kwenye sekta isiyokuwa rasmi. Hapa naona kama kuna kukinzana, kwa upande mmoja tumepunguza kodi ya mapato kwa wale wa sekta isiyokuwa rasmi kutoka Sh.150,000 kwenda Sh.100,000, tunaipongeza sana Serikali kwa hili lakini wakati huohuo tunazungumzia kuiwezesha sekta isiyokuwa rasmi peke yake, sekta rasmi hawajapunguziwa kodi kama hizo, matokeo yake ni kuwa watu wengi watapendelea kuendelea kukaa kwenye sekta isiyokuwa rasmi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunajikuta tunakuwa kama tunakinzana; huku tunataka kuirasimisha sekta isiyokuwa rasmi lakini huku tunaikandamiza sekta iliyokuwa rasmi. Kwa hiyo napenda sana kuona jinsi ambavyo tuna-balance hivi vitu ili sekta isiyokuwa rasmi iingie kwenye mfumo rasmi lakini wale ambao tayari wako katika sekta rasmi waendelee kunufaika na kukua na kuleta ufanisi mkubwa zaidi katika uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)