Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Maulid Said Abdallah Mtulia (11 total)

MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu hivi sasa imekuwa soko holela la kazi za wasanii ambazo zinaingizwa kiujanja ujanja
bila kufuata taratibu wala Serikali yetu kupata kodi kwa mujibu wa sheria, pia wasanii wengi wana malalamiko makubwa kwamba kazi zao zinazotumiwa na makampuni ya simu hawalipwi ipasavyo. Vilevile, wasanii wana
manung’uniko mengi kwamba kazi zao za sanaa wanapokwenda kuziuza wanadhulumiwa na wanapewa kwa bei chee. Je, ni lini sasa Serikali itaamua kuleta mabadiliko ya sheria hizi ambazo Naibu Waziri amezitaja, Sheria Na. 7 ya Mwaka 1999, Sheria Na. 4 ya Mwaka 1976 na Sheria Na. 23 ya Mwaka 1984. Sheria hizi zote zinaonekana zina miaka mingi haziendi sawa na mabadiliko ya kasi yanayokwenda katika sanaa yetu Tanzania. (Makofi) Swali la pili; je, Mheshimiwa Naibu Waziri, yuko tayari kuambatana nami kwenda kukaa na wasanii ili tuwasikilize matatizo yao na tuweze kushirikiana nao ili kuwapatia ufumbuzi na kuhakikisha kazi zao zinaleta tija kama ilivyokuwa kwa wasanii wa nchi nyingine?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kama alivyosema ni kweli
kwamba sheria zetu hizi zinazohusiana na usimamizi wa masuala ya sanaa na wasanii kwa ujumla zimepitwa na
wakati, kwa sasa tunachokifanya ni kuandaa sera kwanza kwa sababu tulikuwa hatuna Sera ya Sanaa, tulikuwa na Sheria ya Filamu lakini hatukuwa na Sera. Kwa hiyo, kwa sasa tunaandaa Sera ya Filamu na vilevile tunaandaa Sera ya Maendeleo ya Sanaa.
Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilisha sera hizi ambapo Sera ya Filamu tunatarajia kufikia mwishoni mwa mwezi wa Sita tuwe tumekamilisha kuandaa rasimu yake na baada ya kukamilisha sasa tutahuisha hizi sheria ili kusudi ziweze kuendana na wakati.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili; kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru na niseme kwamba tuna kila
sababu ya kumshukuru Mheshimiwa Rais na kumpongeza kwa kuanzisha Idara ya Sanaa katika Wizara yetu. Nia hasa ni kuhakikisha kwamba tunaongeza kasi ya maendeleo ya tasnia ya sanaa.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kuambatana naye kwenda katika Jimbo lake, nimekubaliana na hili. Hata hivyo
napenda kumjulisha kwamba Wizara yetu imeanzisha utaratibu kupitia utaratibu wa wadau tuzungumze. Kila
Jumanne tunaongea na wadau wa sekta zetu nne; Sekta ya Habari, Sekta ya Sanaa, Sekta ya Utamaduni pamoja na Sekta ya Michezo. Kwa hiyo, huwa tunaongea na wadau ili kupata changamoto na kupanga ni jinsi gani tuweze kutatua changamoto hizi.
Mheshimiwa Spika, hivyo nichukue nafasi hii kuwaalika wasanii wote pale ambapo tutakuwa tukizungumzia masuala yao siku ya Jumanne fulani kwa mwezi basi waweze kuhudhuria pale Dar es Salaam na hapa Dodoma. Maalum kwa Jimbo lake la Kinondoni, Wizara yangu iko tayari na binafsi niko tayari kuambatana naye ili tuweze kusikiliza matatizo ya wasanii. Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. MAULID S.A MTULIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, naungana naye katika umuhimu wa watu wetu kuchangia gharama, lakini anaonaje sasa Serikali dhana ya kuchangia gharama ikabaki katika kuchangia dawa pamoja na vipimo lakini wananchi wetu wakapata fursa ya kwenda kumwona Daktari bila kulipa pesa ya kumwona Daktari ili kuongeza idadi ya watu wanaokwenda kwenye vituo vya afya?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa kuna makundi yetu maalum ambayo kwa mujibu wa sheria yetu wanatakiwa wapate huduma za afya bure na kwa kuwa Wabunge wengi wamesimama hapa na mimi mmojawapo tunaonesha kwamba bado makundi haya hayapatiwi huduma ya afya bure. Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa yuko tayari sasa kufuatana na mimi kwenda katika hospitali zangu za Jimbo la Kinondoni kwenda kusisitiza na kuhakikisha wananchi hawa wanapata huduma bure?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Swali lake la kwanza kuhusu wananchi kupewa ruhusa ya kwenda kununua dawa na vifaa tiba katika hospitali lakini wakaonwa bure na Madaktari, sisi kama Serikali hatuna utaratibu huo kwa sababu tunafanya kazi kwa mujibu wa sera lakini pia mipango mbalimbali ya kimkakati ya kuhudumia wananchi.
Mheshimiwa Spika, tunafuata Sera ya Afya ya mwaka 2007 pia Mpango wa Kimkakati wa Huduma za Afya Na.4 ambao unaanza 2015 - 2020. Pamoja na mikakati mbalimbali kama Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa na yote haizungumzii uelekeo huo.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, mwongozo ambao tunaufuata sisi kama Serikali ni kuwahudumia wananchi zaidi kwa kutazama mipango hiyo na uelekeo wetu kwenye mipango yote hii ni kuelekea kwenye universal health coverage ambapo kutakuwa kuna bima ya lazima ya kila Mtanzania. Tukianza kutekeleza mpango huo kama Bunge lako Tukufu litatupitishia sheria ambayo tunakusudia kuileta muda si mrefu basi kila Mtanzania atalazimika kuwa na kadi ya bima ya afya ya namna moja ama nyingine iwe ni CHF ama iwe ni Social Health Insurance kama NHIF.
Mheshimiwa Spika, kila Mtanzania akishakuwa na hiyo kadi yake maana yake sasa atakuwa anatibiwa kwa kutumia kadi ya bima ya afya. Huo ndiyo uelekeo na sio uelekeo anaouzungumzia Mheshimiwa Mtulia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu makundi maalum, hata hili suala la makundi maalum kuhudumiwa chini ya kiwango japokuwa tunalikubali, lakini dawa yake hasa ni huu mfumo wa kuwa na bima ya afya ya lazima kwa kila Mtanzanzia ambapo yale makundi maalum ambayo yanapewa msamaha kisera maana yake yatakuwa yanakatiwa bima kabla hayajaenda kutafuta huduma.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, wazee wote ambao wanastahili kupewa msamaha wa kupata huduma za afya basi wanakatiwa kadi za bima ya afya na Serikali kwa sababu wao wanapewa msamaha anapokwenda pale kutibiwa huwezi kubagua yupi ana kadi na yupi hana kadi, kila mtu ana kadi. Yupi kadi yake ni ya msamaha na yupi kadi yake ni ya kulipia, kila mtu atakuwa ana kadi na kila kadi itaheshimiwa na kituo chochote kile cha kutolea huduma za afya.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa msingi huo hata haya makundi maalum anayoyazungumzia yatapata huduma zilizo bora. Kwenye Ilani ya Uchaguzi kwa kuwa tunaelekezwa kufanya hivyo, namhakikishia miaka hii mitano haitakwisha kabla hatujaleta hapa Bungeni mapendekezo yetu ya Sheria ya Single National Health Insurance ambayo ni compulsory kwa kila Mtanzania.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kufuatana naye, anajua yeye ni rafiki yangu halina shida, tutafute muda twende Kinondoni tukatembelee, japokuwa mimi nimeshafika Kinondoni mara nyingi sana. Ahsante.
MHE. MAULID SAID A. MTULIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokanana taarifa zilizotolewa na TMA wameeleza kwamba baadhi ya mikoa yetu katika Tanzania itapata chini ya wastani wa kiwango cha mvua, kwa maana ya Pwani, Tanga, Zanzibar na Morogoro Kaskazini. Je, Serikali ina mpango gani kukabiliana na tatizo litakalotokana na upungufu huo wa mvua?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, tayari Serikali yetu kwa kushirikiana na wataalam mbalimbali duniani tunaanza kuandaa miradi ambayo itakuwa na efficiency kubwa kwa maana ya kutumia maji kidogo kwenye uzalishaji wa mimea. Teknolojia hiyo tunazidi kuichukua na kuiendeleza ili maji kidogo yanayopatikana yaweze kutumika vizuri na uzalishaji uwe mkubwa. Kwa hiyo, tumejiandaa, taarifa ya TMA tunayo na sisi tunaendelea kuifanyia kazi ili kuhakikisha kwamba production ya mazao hasa ya chakula itaendelea kuwa kama ambavyo matarajio yapo.
MHE. MAULUD S. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii na mimi kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakubaliana kwamba maji ni uhai na kila mwananchi anahitaji maji; lakini tunakubaliana pia kwamba zamani tulikuwa na mabomba yetu ya Serikali ambayo wananchi walikuwa wanapata maji bure, lakini sasa hayapo.
Je, Serikali ian mpango gani kuyarejesha yale mabomba yetu ili wananchi wetu wapate maji bure kwa wale ambao hawana uwezo ukizingatia kwamba kuhitaji maji hakutegemei uwezo wa fedha za mtu? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba zamani kulikuwa na mabomba ambayo yalikuwa yanatoa maji bure na hivyo kusaidia wale watu wasiojiweza, lakini kwa sasa mamlaka zote zimepewa maelekezo na zina sheria kwamba kila mamlaka kwenye mkoa inashirikiana na uongozi wa mkoa kubaini wananchi wote ambao hawana uwezo kama wazee na wagonjwa, kwa hiyo wakiorodheshwa wanaendelea kupata kupata huduma ya maji bure.
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata fursa hii ya kuuliza swali la nyongeza.
Mimi katika maeneo yangu ya Jimbo langu la Kinondoni, hasa Magomeni Mtaa wa Kwa Suna, Hananasifu
Mtaa wa Mkunguni na mitaa mingine, nyumba za wananchi zilifanyiwa urasimishaji, lakini kwa masikitiko makubwa watu wakatumia fursa ile wengine kwenda kukopa. Nasikitika kwamba Serikali imeenda kuvunja nyumba zile bila kulipa fidia kwa wananchi wale.
Je, kwa nini Serikali inavunja nyumba zilizofanyiwa urasimishaji na kupata leseni za makazi bila kulipa fidia?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, anachokizungumza ni kweli, kuna maeneo yalifanyika hivyo, lakini suala la msingi hapa kupewa leseni ya makazi haina maana ya kwamba pale ambapo utaratibu wa mipango miji umeyapanga vinginevyo yale maeneo hautavunjiwa. Kwa sababu Dar es Salaam yenyewe sasa hivi iko katika mchakato na ninadhani imekamilisha mpango wa master plan ya mji ule.
Sasa pale ambapo inaonekana kabisa kwamba kuna suala zima la kutaka kuweka miundombinu inayofaa katika
eneo lile watu hawa wanaweza kuvunjiwa katika maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, lakini Wizara ilishatoa tangazo kwa wale ambao walikuwa na umiliki halali na wana hati
kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na wamevunjiwa kimakosa, tulisema walete orodha yao na watu wa mipango miji watakwenda kuhakiki waone kweli walivunjiwa kimakosa. Lakini kwa wale ambao waliendelea na ujenzi bila kuzingatia mipango miji imepanga nini katika ule mji hao hawatalipwa na itakuwa ni tatizo. Watu wa Hananasifu na Mkunguni kama alivyosema, kama hao wapo kulingana na maelezo niliyoyatoa, basi tupate wakiwa na hati zao kutoka Wizarani kwetu au kutoka kwenye ma nispaa inayohusika, tutawa-consider kulingana na malalamiko watakavyokuwa wameyaleta.
MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuuliza swali la nyongeza. Wakazi wa Jimbo la Kinondoni wanasumbuliwa na ukosefu wa maji hasa kutokana na mtandao wa maji, kwa maana ya mabomba mengi kuharibika au kutokuwa na huo mtandao. Je, Waziri ana mpango gani wa kutuletea mtandao wa maji katika Kata zetu za Tandale, Makumbusho, Kijitonyama, Kigogo, Hananasifu, Magomeni, Mzimuni ili kuhakikisha watu wote wanapata mtandao wa maji? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpe taarifa, wakati tunatekeleza miradi ya kupanua vyanzo vya maji vya Ruvu Juu na Ruvu Chini idadi ya wananchi Dar-es-Salaam ilikuwa milioni tano, leo hii idadi ya wananchi Jiji la Dar-es-Salaam ni milioni sita na laki nne, kwa hiyo, mahitaji ya maji yameongezeka, sio lita milioni 500 tena ni lita milioni zaidi ya 800. Kwa bahati nzuri tumeshachimba visima vya Kimbiji, Mpera, kwa hiyo, hatuna wasiwasi na maji yapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, wiki moja iliyopita, Mheshimiwa Mbunge mwenyewe ni shahidi, tumetangaza tenda kwa ajili ya usambazaji wa maji katika Jiji la Dar-es- Salaam baada ya kupata mkopo wa fedha Dola za Kimarekani milioni hamsini na saba. Kwa hiyo, maeneo yote aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge tunahakikisha kwamba, tunapeleka maji ili wananchi waweze kufaidi Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi, wananchi wote watapata huduma ya maji safi na salama.
MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii adhimu ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza, niipongeze Serikali kwa majibu mazuri ya kitakwimu na naamini kwa majibu haya na kuonesha kwamba tuna walemavu zaidi ya milioni mbili, itasaidia Serikali yetu kuja na mpango mkakati wa namna gani ya kuwasaidia. Nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa, hapo Dar es Salaam Mkuu wetu wa Mkoa alileta mpango kuleta vifaa vya kuwasaidia walemavu na walemavu wengi sana wakajitokeza, ikionesha kwamba kuna shida hiyo. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuhakikisha inawajengea uwezo walemavu, kwa maana wa viungo kuwaletea viungo ili wawe na uwezo wa kujitegemea wenyewe na wale wa kusikia wapate viungo vya kusikia ili waweze kujitegemea wenyewe na walemavu wengine? Pia, je, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea uwezo ili kupunguza athali ya ulemavu kwa kutumia viungo bandia?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa mbona umeuliza kwa nini mbili hapo, kuna swali lingine tena! Maswali ni mawili tu na umeshataja kwa nini mbili, kwa hiyo maana yake maswali yako mawili, maana nisije nikakosea kanuni hapa itakuwa balaa. Mheshimiwa Ikupa Stella Alex, majibu!
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maulid Said Mtulia, Mbunge wa Kinondoni kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeza Mheshimiwa Maulid Mtulia kwa jinsi ambavyo anafuatilia masuala ya watu wenye ulemavu. Pia naomba niweze kumjibu Mheshimiwa Mbunge, kwamba Serikali imekuwa na mipango mingi kwa upande wa uwezeshaji kwa watu wenye ulemavu, ikiwemo kuwapatia vifaa saidizi. Kwa sababu tunafahamu kwamba, mtu mwenye ulemavu, kulingana na aina yake ya ulemavu, asipowezeshwa kwa upande wa vifaa visaidizi, hawezi kujimudu. Kwa kuliangalia hilo, Serikali imekuwa ikitenga bajeti, lakini pia kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, tumekuwa tukigawa vifaa visaidizi kwa watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kwa kundi hili la watu wenye ulemavu, ili kuhakikisha kwamba wanaweza kufanya vizuri kama ambavyo nimeongea kwenye jibu langu la msingi, ni kwamba tumekuwa tukihakikisha kwamba tunawajengea uwezo kwa kuwawezesha katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kuhakikisha kwamba pia hata programmes ambazo tunakuwa tunaziandaa zinakuwa ni jumuishi kwa watu wenye ulemavu. Kwa hiyo, suala la vifaa kwa watu wenye ulemavu, tumekuwa tukilifanya kama Serikali. Tunaona hata katika shule zetu, tumekuwa tukitenga bajeti ambayo tunanunua vifaa visaidizi na kuvigawa kwenye shule zetu, lakini haviishii tu kwenye shule, tunavipeleka hata kwa watu ambao siyo wanafunzi.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,
WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ambayo ameyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri, nataka niongezee kidogo katika majibu hayo. Kwanza Serikali imeondoa kodi katika baadhi ya vifaa saidizi kwa kutambua kwamba kuna kikundi ndani ya nchi yetu ambacho wanavihitaji vile vifaa na vinaweza vikawasaidia kuwa na maisha bora, kodi hizo katika baadhi ya vifaa zimeondolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nilikuwa nataka niwape taarifa tu Waheshimiwa Wabunge, kuanzia mwezi huu wa Aprili, Hospitali ya Mifupa MOI, wataanza zoezi la kufanya upimaji pamoja na kutoa vifaa, viungo bandia kwa baadhi ya wale walemavu ambao wanavihitaji. Kwa hiyo, naomba kupitia Waheshimiwa Wabunge kutoa taarifa kwa watu hawa ambao wanahitaji viungo bandia, basi kufika katika Hospitali ya Taifa, MOI kwa ajili ya kuweza kupata vifaa hivyo. Hata hivyo, katika masuala ya vifaa vya usikivu tumekuwa tunaendelea na kampeni katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili vya kupandikiza vifaa vya usikivu, lakini vilevile kutoa vifaa saidizi kwa wale watoto ambao wanahitaji vifaa hivyo.
MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nitoe shukrani zangu za dhati kwa majibu mazuri ya Serikali. Vilevile niendelee kuhimiza Serikali kwamba mabadiliko ya Sera na Sheria ya Bodi ya Filamu yafanyike kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa wasanii wetu wamedhulumiwa kazi zao na wasambazaji walikuwa wanawaingiza mikataba kama wasimamizi badala ya wamiliki wa kazi; kwa kuwa sheria ipo kulinda haki za wasanii; na kwa kuwa nchi za wenzetu mfano Nigeria iliwahi kutoa tamko kuhakikisha kazi zote za wasani umiliki urudishwe kwa wasanii wenyewe, je, Serikali yetu ya Tanzania iko tayari sasa kutoa tamko kuhakikisha wale wote waliodhulumu kazi za wasanii umiliki unarudi kwa wasani wenyewe ili waweze kunufanika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa wasanii wetu wanaendelea kuzalisha kazi nzuri kabisa; na kwa kuwa walaji wengi katika jamii wanahitaji kuendelea kuziona kazi za wasanii na katikati yake kuna ombwe kubwa kwamba wasanii, waandaaji na walaji hawaonani, je, Serikali ipo tayari kuja na suluhisho kuhakikisha kazi za wasanii zinafika kwa walaji ili wasanii waepukane na kutembeza CD mkononi wao wenyewe?
NAIBU WAZIRI WA HABARI UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Said Mtulia, Mbunge wa Jimbo la Kinondoni kwa jinsi ambavyo amekuwa akipambania maslahi ya wananchi wa Kinondoni, ukizingatia kwamba wasanii wengi walioko katika jiji la Dar es Salaam wanaishi katika Wilaya yake ya Kinondoni. Kwa hiyo, nampongeza sana kwa kupambania maslahi ya wasanii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na swali lake la kwanza ambapo ametaka kujua kama Serikali tuna mpango gani wa kurejesha zile hakimiliki ambazo zimechukuliwa kutoka kwa wasanii. Kama ambavyo nimejibu kwenye jibu langu la msingi kwamba kwa Sheria ya Hakimiliki ya mwaka 1999 ambayo tunayo sasa hivi inatoa haki na uhuru kwa msanii mwenyewe kuamua ni namna gani ambavyo atataka kuuza haki yake. Kama akitaka kuuza kazi zake zote kwa maana kwamba anauza pamoja na ile master ya kazi yake au kuuza baadhi kazi zake. Kwa hiyo, ni suala la msanii mwenyewe kuamua anataka kuuza kazi zake kwa njia gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi kama Serikali kwa kutambua kwamba suala hilo limeleta mchanganyiko mkubwa sana na halina maslahi kwa wasanii, kitu ambacho tunafanya kwanza ni kutoa elimu kwa wasanii kuweza kutambua haki na thamani ya kazi zao, kwa sababu tumeona madhara makubwa sana ambayo yamekuwa yakiwapata wasanii pale ambapo wanauza mpaka umiliki wa zile kazi zao. Kwa hiyo, tunaelimisha wasanii kwanza waweze kutambua kwamba kazi zao zina thamani, ukiuza leo kazi yako pamoja na master ni kitu ambacho kitaendelea kutumika miaka mingi matokeo yake hayatakuwa mazuri kwa miaka ijayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaendelea kutoa wito kwa wasanii wote nchini Tanzania kwanza kutambua thamani ya kazi yao na kuona kwamba siyo jambo jema kuuza mpaka umiliki wa kazi zao. Hata hivyo, kwa sheria ambayo tunayo inatoa haki kwa msanii kuamua ni namna gani ambavyo atauza kazi yake. Kwa hiyo, sisi kama Serikali hatuwezi kutoa kauli ya moja kwa moja kwa sababu sheria imewapa uhuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikija kwenye swali lake la pili ambalo amezungumzia kuhusu tatizo la usambazaji, ni kweli kwamba kwa miaka ya hivi karibuni tasnia yetu ya sanaa imekumbwa na changamoto nyingi ikiwepo suala la usambazaji. Kama ambavyo tunajua tatizo la usambazaji kwa miaka ya hivi karibuni lilisababishwa na kukosekana kwa kazi ambazo zina ubora na ubunifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, usambazaji ni biashara kama biashara zingine. Kwa hiyo, sisi kama Wizara tunaamini kwamba hakuna mfanyabiashara atawekeza mtaji wake kwenye biashara ambayo anaamini kwamba haiwezi kumpa faida hapo baadaye. Kwa hiyo, sisi kama Serikali tunaendelea kutoa wito kwa wasanii kwanza kutengeneza kazi ambazo zina ubora na zitaleta ushindani kwenye soko lakini zitavutia wasambazaji wengi kuja kuwekeza mitaji kwenye kazi zao hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwa sababu tunajua kwamba sasa hivi pia kuna mabadiliko ya sayansi na teknolojia na tumeshuhudia wasanii wengi sana wamehama kutoka kwenye mfumo wa kusambaza kazi zao kwa njia ya CD wanatumia njia ya mtandao. Kuna msanii anaitwa Wema Sepetu, kwenye filamu yake ya Heaven Sent. amefanya vizuri sana, amesambaza kazi yake kwa njia ya mtandao na mauzo yamekuwa mazuri. Kwa hiyo, nitoe wito kwa wasanii sasa waangalie namna gani ambavyo wataenda mbele zaidi kwa mabadiliko haya ya sayansi na teknolojia ili waanze kusambaza kazi zao kwa njia ya kimtandao.
MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali madogo mawili ya nongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini nina maswali yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, hivi sasa kuna mwamko mkubwa sana Nchini Tanzania kwa wazazi kutaka watoto wao washiriki kwenye michezo hasa ikichagizwa na mafanikio aliyoyapata kijana wetu Mbwana Samatta kucheza katika ligi ya Uingereza na mimi sasa hivi timu yangu ni Aston Villa, lakini kuna tatizo kubwa la vifaa vya michezo kwa wananchi wetu ili kuweza kushiriki vizuri michezo.

Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha vifaa vya michezo yote Tanzania vinapatikana kwa urahisi ili wazazi wachochee mchakato huu wa kuwa na wana michezo wengi Nchini Tanzania?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Wizara imesema suala la ujenzi wa viwanja ni la wadau na halmashauri na Halmashauri ya Kinondoni imeitikia wito huo kwa kuja na ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu pale Mwenge na vilevile kuna mchakato wa kujenga kituo cha malezi ya watoto ili tupate wachezaji bora kabisa. Serikali inatoa kauli gani kusaidia juhudi hizi ili wanaoonesha nia ya kuleta mabadiliko ya soka wapate kusaidiwa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Kinondoni kwa sababu amekuwa ni mdau mkubwa sana wa masuala ya michezo, lakini nadhani hiyo inatokana na kwamba Jimbo lake ni Jimbo ambalo lina wanamichezo wengi pamoja na wasanii wengi. Kwa hiyo naamini kwamba Mheshimiwa Mbunge anafanya kazi nzuri sana na wananchi wake wanajivunia hilo.

Mheshimiwa Spoika, nikija sasa kwenye maswali yake mawili ya nyongeza; swali lake la kwanza amezungumza kwamba ipo changamoto ya vifaa vya michezo; na mimi nikiri kwamba ni kweli kumekuwepo na changamoto ya vifaa vya michezo, lakini kama Serikali hatujakaa kimya na tunayo Sera yetu ya Michezo ya Mwaka 1995 ambayo inazungumza kwamba suala zima la ujenzi wa viwanja pamoja na miundoimbinu yote ya michezo ni suala la Serikali lakini vilevile kwa kushirikiana na wadau.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa upande wetu sisi kama Serikali sasa hivi kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara tumekuwa tukihamasisha sana wafanyabiashara mbalimbali waendelee kuagiza vifaa vya michezo kutoka nje. Kama hiyo haitoshi kama Wizara vilevile kwa kupitia Sera yetu ya Awamu ya Tano ambayo ni Sera ya Viwanda tumekuwa pia tukihamasisha sana wawekezaji wa ndani pamoja na wawekezaji wa nje kuanzisha viwanda vya vifaa vya michezo kwa sababu tunatambua pamoja na kwamba vifaa vinakuwa ni adimu lakini pia changamoto kubwa imekuwa ni masuala ya kodi. Kwa hiyo hakuna namna nyingine ambayo tunaweza tukafanya kuondokana na tatizo hili, ni lazima sisi kama nchi tuhakikishe kwamba tuna viwanda ambavyo vinahusiana na uchakataji wa hivi vifaa vya michezo. Kwa hiyo, mikakati ipo na sisi kama Wizara tunaisimamia hiyo mikakati na tunamwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba, tatizo hili kwa kadri miaka inavyozidi kwenda tunaendelea kulifanyia utatuzi.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili amezungumza namna gani ambavyo Halmashauri ya Kinondoni imeonesha jitihad. Nikiri kwamba ni kweli Halmashauri ya Kiondoni imekuwa ni mfano katika kuweka miundombinu ya michezo na natambua kwamba pia Halmashauri hiyo sasa hivi inamiliki timu ya KCMC, kwa hiyo ni namna gani ambavyo wanaonesha kwamba wana jitihada kubwa ya kukuza sekta hii ya michezo. Kwa hiyo, niseme sisi kama Wizara kwa kupitia TFF tumekuwa tukiunga mkono jitihada kama hizi za wadau kwa kuwapatia vifaa mbalimbali pamoja na nyasi na vifaa vingine na hayo tayari yameshafanyika kwenye baadhi ya maeneo. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana pia na Halmashauri ya Kionondoni wapeleke maombi TFF ili waone ni namna gani ambavyo wataweza kusaidia hivyo vifaa ili huo uwanja uweze kukamilika na nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba, sisi kama Wizara tutakuwa pamoja naye kuhakikisha kwamba uwanja huo unakamilika, lakini vilevile support ya Serikali kupitia TFF iweze kuonekana. Ahsante sana.
MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nianze kutoa shukrani zangu za dhati kwa Serikali yetu kwa kutekeleza miradi mingi iliyokuja kutatua matatizo ya wananchi, hasa katika Jimbo letu la Kinondoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu ya Serikali nayakubali na ni ya muda mrefu. Wakati wa bajeti Mheshimiwa Matar aliiuliza Wizara ya Fedha kwa nini miradi kama hii ambayo wafadhili wako tayari kutoa pesa inacheleweshwa? Wizara ikasema, gharama hailingani na uhalisia. Je, majibu ya Serikali ambayo ime-quote gharama ile ile ya dola milioni 120 sasa wanaona gharama hizi zinaendana na wakati na zitaenda kutekelezeka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Serikali kama inakubaliana nasi, mradi huu ni muhimu kutekelezwa. Kama inaendelea kusema gharama hizi ni kubwa, wanafanya mazungumzo kuja kwenye gharama halisi au wanachagua kuweka wawekezaji wa ndani ili bonde hili lipate kujengwa na wananchi walipe fidia wapate kuishi maisha bora?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, gharama hizi ndizo gharama ambazo zimeandikwa kwenye andiko. Andiko lile ni zito na kubwa sana na bado mchakato unaendelea kwa sababu, keshokutwa mimi mwenyewe nitapokea uwasilishaji wa andiko hilo kutoka kwa wadau hawa waliolitayarisha.

Mheshimiwa Mwenyeikiti, ni kitu kizuri kwa kweli na ni kitu kikubwa sana. Kwa hiyo, ndani ya Serikali lazima tupewe muda wa kuchakata ili tuweze kutoka na kitu kizuri kwa sababu kusema ukweli gharama hizi pamoja na kwamba zinaonekana kubwa, lakini pia ni lazima tuone kwamba na huu Mto Msimbazi ni mrefu, lakini pia unaweza kugeuzwa badala ya kuwa tatizo ukawa na fursa kubwa kama nilivyosema kwamba kutakuwa kuna parking, kutakuwa kuna ma-conference na vitu vikubwa vingi sana ambavyo vitajengwa kando kando ya Mto Msimbazi, lakini pia kutunza ikolojia na kuleta ladha na uzuri wa maeneo ya Mto Msimbazi kuanzia mwanzo wake mpaka mwisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu gharama kwamba ni zile zile, ni kweli, bado mpaka sasa ni zile zile, lakini mchakato ndani ya Serikali unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake kwamba kwa kuwa, gharama ni zile zile sasa je, Serikali iko tayari? Ni kwamba Serikali kwa maana ya uzuri wa mradi iko tayari, lakini suala la fedha ni suala ambalo pia linahusika na Wizara ya Fedha. Nasi bado tunaendelea na mchakato katika eneo letu na baadaye taarifa hii tutaikabidhi na ikibidi hata kuja kufanya uwasilisho hapa Bungeni ili Wabunge muweze kuona na pengine wananchi nao waweze kujua namna ambavyo kwa kweli Mto Msimbazi na Dar es Salaam itakavyokuwa baada ya utekelezaji wa mradi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba wananchi wa Dar es Salaam, kama walivyoshiriki vizuri katika uandaaji wa mradi huu, basi tuendelee kushirikiana na wawe wavumilivu kwa sababu hili jambo siyo dogo, ni kitu kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.

(i) Hospitali yetu ya rufaa ya Mwananyamala ni miongoni mwa hospitali inayotoa huduma kwa wagonjwa wengi sana. Kiasi kwamba kwa siku moja inahudumiwa wangonjwa takribani 2000. Na idadi ya madaktari wetu si zaidi ya madaktari ambao wanajigawa katika shift tatu. Je, Serikali ina mpango gani kuongeza Watumishi Manesi, Wakunga na madaktari ili hospitali yetu iweze kutoa huduma bora zaidi?

(ii) Kwa kuwa hospitali yetu ya Mwananyamala imezungungwa na baadhi ya kata ambazo hazina hata zahanati, Mbunge wa Jimbo la Kinondoni ametoa pesa zaidi ya milioni 90 ili kujenga zahanati katika Kata ya Makumbusho. Je, Serikali ina waahidi nini wananchi wa Kata ya Makumbusho kuongeza ili ile zahanati ile iweze kukamika kwa haraka?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nimpongeze sana Mheshimiwa Maulid Mtulia, kwa jinsi anavyofuatilia upatikanaji wa huduma za Afya kwa wananchi wa Kinondoni, hakika Kinondoni imepata Mbunge wa Chama cha Mapinduzi ambaye anajua kufuatilia changamoto zinazowakumba wananchi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ni lini tutaongeza watumishi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwananyamala nakubaliana na Mbunge hata ukiangalia tu takwimu za wagonjwa ambao wanahudumiwa katika Hospitali zetu za Rufaa za Mikoa ishirini na nane, Mwananyamala inaona wagonjwa kwa mwaka takribani laki tatu. Ukilinganisha na Mount Meru inaona wagonjwa elfu ishirini na nne kwa mwaka, Manyara wagonjwa elfu ishirini na saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge haja ya kuongeza madaktari wauguzi na wataalamu wengine wa Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala. Nikuahidi tu Mheshimiwa Mbunge tunafanya mchanganuo wa hali halisi ya watumishi wa Afya katika Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali za Wilaya, Zahanati na Vituo vya Afya ili kabla ya kupata nyongeza ya watumishi tuweze kuwagawanya upya. Kwa sababu unaweza ukakuta kuna Mkoa wagonjwa wanaona ni wachache lakini wana watumishi wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hilo tayari tumelibainisha katika ngazi ya Wizara, lakini swali lake la pili kwamba kuna kata hazina Zahanati ikiwemo Kata ya Makumbusho, Mheshimiwa Mbunge tumeongea suala hili, na Ndugu yangu Mheshimiwa Jafo ambaye ni kaka yangu, ni pacha wangu katika utoaji wa huduma za Afya ngazi ya msingi yuko hapa, kwa hiyo tutalishughulikia, na tutahakikisha katika fedha ambazo tunazipata kwa ajili ya utoaji uboreshaji wa miundombinu ya huduma za afya za msingi basi tunakuletea Makumbusho ili kukuunga mkono kuweza kumaliza Zahanati ya Makumbusho.