Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Faustine Engelbert Ndugulile (7 total)

MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE aliuliza:-

Hapa Tanzania kumekuwepo na migogoro mbalimbali ya ardhi kati ya wawekezaji na wananchi, wakulima na wafugaji, hifadhi na wananchi na baina ya wananchi wenyewe:-

(a) Je, Serikali ina mikakati gani ya kupanga matumizi bora na endelevu ya ardhi ili kuondokana na migogoro?

(b) Je, Serikali ina mikakati gani ya kuondokana na tatizo la maendeleo ya miji kutokuendana na kasi ya ukuaji wa miji?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha kuandaa Mpango wa Taifa wa Matumizi ya Ardhi wa mwaka 2013 mpaka 2033. Mpango huu ndiyo kiunzi wa matumizi ya ardhi yaani National Land Use Framework Plan unaotoa maelekezo ya namna ya kupanga maeneo yote nchini kuanzia katika ngazi ya Kanda, Mkoa, Wilaya na Vijiji. Mpango huu umeanza kutekelezwa kupita programu sita za kipaumbele ambazo ni makazi na miundombinu mikuu ya uchumi, kilimo na mifungo, ardhi ya hifadhi na utalii, maeneo ya nishati na madini, mipango ya matumizi ya ardhi kwa ngazi za chini, pamoja na programu ya kuboresha Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi. Kupitia programu hizi, ardhi kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii itategwa na hivyo kuondokana na migogoro baina ya watumiaji mbalimbali wa ardhi. Aidha, Serikali imeandaa programu ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi nchi nzima ili kuondokana na migogoro ya ardhi.

(b) Mheshimiwa Spika, katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na ongezeko kubwa la wakazi mijini ambako kumepelekea mamlaka za upangaji na uendelezaji miji kushindwa kutoa huduma za kijamii na kiuchumi kwa kiwango stahiki na hivyo kufanya miji yetu kukua kiholela. Katika kukabiliana na changamoto hizi, Wizara yangu imeendelea kuratibu uandaaji wa mipango kabambe ya Majiji na Miji mbalimbali nchini ambayo itatoa muongozo wa uendelezaji wa miji kwa kuzingatia mahitaji mbalimbali na hivyo kuondokana na tatizo la ukuaji wa miji isiyopangwa. Hadi sasa mipango kabambe ya Majiji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Miji ya Mtwara, Musoma, Iringa, Bariadi, Bagamoyo, Kibaha na Shinyanga iko katika hatua za mwisho za maandalizi na itakamilika kabla ya mwezi Agosti, 2016. Aidha, Mipango Kabambe ya Miji ya Tanga Singida, Tabora, Songea, Morogoro, Sumbawanga, Geita, Njombe na Mpanda ipo katika hatua mbalimbali za maandalizi.

Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa mamlaka za upangaji ambazo hazina mipango kabambe kutenga fedha katika bajeti zao ili kuharakisha uandaaji wa mipango kabambe na mipango ya kina itakayotoa mwongozo wa uendeleshaji katika miji yao na hivyo kuzuia tatizo la ukuaji wa miji isiyopagwa.
MHE. MARIAM N. KISANGI (K.n.y. MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE) aliuliza:-
Hivi karibuni Jimbo la Kigamboni limetangzwa kuwa Wilaya Mpya, hata hivyo wananchi wake bado wanapata huduma ya Mahakama kupitia Wilaya ya Temeke:-
(a) Je, Serikali itaanzisha lini Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni?
(b) Je, utekelezaji wa hatua hiyo utaanza lini?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Mahakama ya mwaka 1984, Sura ya 11, inaeleza kwamba baada ya kuanzishwa kwa Wilaya Mpya na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali uanzishwaji wa Mahakama ya Wilaya inabidi ufanyike. Hivyo, kutokana na Mheshimiwa Rais kuridhia kuanzishwa kwa Wilaya Mpya ya Kigamboni, Mahakama imeweka lengo la kujenga Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni kwa kadri fedha za miradi ya maendeleo zitakavyopatikana.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuanzishwa kwa Wilaya, Serikali inaendelea na mpango wa kuboresha majengo na miundombinu ya Mahakama zilizopo Kigamboni. Kwa sasa ujenzi wa jengo jipya la Mahakama kwenye eneo la Mahakama ya Mwanzo Kigamboni unaendelea na unatarajiwa kukamilika mapema Aprili, 2016. Jengo hilo jipya litakuwa na ukubwa wa kutosha na hivyo litakidhi uwepo wa Mahakama ya Mwanzo na ya Wilaya kwa kuanzia.
MHE. MARIAM N. KISANGI (k.n.y MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE) aliuliza:-
Hapo zamani kulikuwa na Shirika la Uvuvi la TAFICO lenye Makao Makuu yake Kigamboni ambalo lilikufa kutokana na uendeshaji mbovu:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua shirika hilo?
(b) Je, Serikali imejipanga vipi kusimamia deep fishing ili iweze kunufaika na mapato yatokanayo na uvuvi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) lilianzishwa mwaka 1974, lengo likiwa ni kuendesha shuguli za uvuvi kibiashara. Aidha, mwaka 1996 TAFICO iliwekwa chini ya iliyokuwa Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) kwa ajili ya utaratibu wa ubinafsishaji. Mwaka 2005 TAFICO iliondolewa kwenye orodha ya Mashirika yaliyotakiwa kubinafsishwa na kurejeshwa Wizarani kuendeleza ubinafsishaji wake. Hata hivyo, mwaka 2007 Baraza la Mawaziri lilisitisha uuzwaji wa TAFICO na kuelekeza kuwa mali zisizohamishika ikiwemo ardhi zibaki kwa ajili ya matumizi ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kwa kushirikiana na wadau wengine inaendela na mpango wa kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), ikiwa ni pamoja na kuwasilisha mapendekezo ya Baraza la Mawaziri kwa hatua husika.
(b) Mheshimwia Naibu Spika, ili kusimamia mapato yatokanayo na uvuvi katika ukanda wa uchumi wa bahari, Serikali zetu mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa pamoja zilianzisha Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu (Deep Sea Fishing Authority) kupitia Sheria ya Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu Na. 1 ya mwaka 1998 na marekebisho ya mwaka 2007. Taasisi hii ina jukumu la kusimamia uvuvi katika eneo la Uchumi la Bahari Kuu, ikiwemo utoaji wa leseni kwa meli za kigeni na za ndani zinazovua kwenye ukanda huo. Aidha, mamlaka inaendelea kufanya doria za anga na kuhuisha mfumo wa kufuatilia meli, kufuatilia vyombo vya uvuvi baharini (Vessel Monitoring System) ili taasisi iweze kudhibiti wanaovua bila kulipa leseni. Pia Serikali inaendelea na taratibu za kuwezesha ujenzi wa bandari ya uvuvi ambayo itawezesha meli za kigeni zinazovua bahari kuu kutia nanga hapa nchini na hivyo kuongeza ajira na kipato kwa Watanzania pamoja na Pato la Taifa kwa ujumla.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE aliuliza:-
Sekta ya Uvuvi hapa Tanzania inaajiri wananchi wengi lakini wavuvi hawanufaiki kutokana na changamoto mbalimbali:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupitia mlundikano wa leseni kwani kuna aina nyingi sana za leseni, kwa mfano, leseni ya chombo, leseni ya mvuvi, leseni ya aina ya samaki, leseni ya eneo la uvuvi na kadhalika?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha wavuvi nyenzo za uvuvi ili waondokane na uvuvi haramu?
(c) Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikiri kwamba ni kweli sekta ya uvuvi ina wananchi wengi wanaojihusisha na uvuvi moja kwa moja na wengine wanaojihusisha na shuguli mbalimbali za sekta hii ya uvuvi. Sekta ya Uvuvi husimamiwa na Sheria ya Uvuvi Na. 22 na Kanuni za Uvuvi za mwaka 2009. Kwa mujibu wa sheria hii, kuna leseni ya chombo, leseni ya uvuvi na leseni ya aina ya samaki.
Pia Mamlaka ya Kusimamia Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) nao hutoa cheti cha usalama wa chombo. Aidha, Jeshi la Zima Moto na Uokoaji linataka kila chombo cha uvuvi kiwe na chombo cha kuzimia moto (fire extinguisher). Pia Mamlaka za Mtaa (Serikali za Mitaa) nazo zimetunga sheria ndogo ndogo kuhusiana na masuala ya uvuvi kama njia mojawapo ya kuongeza mapato katika maeneo yao. Hata hivyo, kwa sasa Serikali inapitia upya leseni na tozo zenye kero kwa wananchi ili kuona uwezekano wa kuzipunguza au kuzifuta ili kuwanufaisha wavuvi. (Makofi)
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikitoa elimu mara kwa mara kwa wavuvi juu ya athari zitokanazo na uvuvi haramu hususani kwa kutumia mabomu, sumu na zana zisizoruhusiwa kisheria. Aidha, Serikali imefuta Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye injini za kupachika (outboard engines), nyuzi za kushonea nyavu (twines), nyavu za uvuvi na vifungashio ili kupunguza gharama za zana na vyombo vya uvuvi.
Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya nyavu na zana za uvuvi ambapo hadi sasa viwanda viwili vya kutengeneza nyavu vya Imara Fishnet (Dar es Salaam) na Fanaka Fishnet (Mwanza) na viwanda vinne vya kutengeneza boti za kisasa vya Yutch Club, Sam and Anzai Company Limited, Seahorse Company Limited vya Dar es Salaam na Pasiansi Songoro Marine (Mwanza) vimekwishajengwa.
Vilevile Serikali imeanzisha utaratibu wa kuwawezesha wavuvi wadogo wadogo ambapo jumla ya shilingi milioni 400 zilitolewa kama ruzuku ya zana za uvuvi na Serikali ilichangia asilimia 40 na mvuvi alichangia asilimia 60 na kupitia utaratibu huu injini za boti 73,000 zilinunuliwa.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi kuanzisha viwanda vya kusindika samaki na mazao ya uvuvi ili kuyaongezea thamani mazao hayo. Jumla ya maghala 84 ya kuhifadhi mazao ya uvuvi na viwanda 48 vya kuchakata mazao ya uvuvi vimejengwa. Viwanda hivyo vipo katika maeneo yafuatayo: Ukanda wa Pwani kuna viwanda 36; Ziwa Victoria kuna viwanda 11 na Ziwa Tanganyika kuna kiwanda kimoja. Pia Serikali imeendelea kutoa elimu kuhusu njia bora za uchakataji na uhifadhi wa samaki na mazao yake kwa viwanda na maghala hayo ili kulinda soko la ndani na nje ya nchi.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE aliuliza:-
Pamoja na Jimbo la Kigamboni ni Wilaya ya Kipolisi, majengo ya Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Wilaya (OCD) na kituo chake ni chakavu sana:-
(a) Je, Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha Wilaya hii inakuwa na ofisi nzuri za polisi?
(b) Je, hatua hizi zitaanza kutekelezwa lini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Kigamboni ni moja kati ya Wilaya tano za Mkoa wa Dar es Salaam ambayo imeanzishwa mwaka 2006 chini ya mpango wa maboresho ya Jeshi la Polisi kwa lengo la kuboresha na kusogeza huduma za ulinzi na usalama karibu na wananchi. Kutokana na uhaba wa rasilimali fedha na majengo, huduma za kipolisi zilianza kutolewa katika jengo dogo la Kituo cha Polisi Kigamboni chenye hadhi ya Daraja la C.
(b) Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inakusudia kujenga vituo vyote vya polisi kwenye Wilaya ambazo hazina majengo yenye hadhi stahiki ikiwemo Wilaya ya Kigamboni. Ujenzi wa kituo hicho utafanyika eneo la Kibada mara fedha zitakapopatikana.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI (K.n.y. MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE) aliuza:-
Katika Kamati ya Bunge la Kumi Serikali iliahidi kufunga mtambo kwa lengo la kudhibiti takwimu za simu za nje na ndani ili kudhibiti mapato ya Serikali:-
(a) Je, utekelezaji wa suala hilo umefikia wapi?
(b) Je, ni kiasi gani Serikali imekusanya tangu utaratibu huo uanze na kabla yake mapato yalikuwaje?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania iliweza kusimika mtambo wa kuhakiki na kusimamia huduma za mawasiliano yaani TTMS hapa nchini mwishoni mwa mwaka 2013. Mtambo huu umeisaidia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuongeza ufanisi katika kusimamia sekta ya mawasiliano pamoja na kwenda sambamba na kasi ya mabadiliko yanayotokea katika sekta ya mawasiliano duniani kote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa mtambo wa TTMS umeiwezesha TCRA kuwa na uwezo wa kusimamia mawasiliano ya simu za kimataifa na zile za mwingiliano; kudhibiti mawasiliano ya simu za ulaghai za kimataifa; kusimamia ubora wa mitandao katika kutoa huduma bora kwa wananchi; kudhibiti namba tambulishi za vifaa vya mawasiliano nchini pamoja na usimamiaji wa miamala ya fedha inayopita katika mitandao ya simu hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio hayo, jitihada za kuboresha zaidi mfumo huu ili kuweza kubaini na kujiridhisha juu ya mapato yote yaani revenue assurance yatokanayo na huduma za mawasiliano kwa maana ya simu za sauti, data na SMS yanakidhi mahitaji ya Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na TCRA yanaendelea. Kwa vile vifungu vya mkataba wa TTMS vinamtaka mkandarasi kuweka mfumo wa kubaini na kujiridhisha juu ya mapato yote (Revenue Assurance System), Serikali kupitia TCRA imemwagiza mkandarasi aweke mfumo huo bila gharama za ziada kwa Serikali. Mkandarasi hatimaye amekubali kuweka mfumo wa Telecom Revenue Assurance ambapo unategemewa kukamilika mwishoni mwa mwezi Agosti, 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia Oktoba, 2013 hadi Februari, 2017 kiasi cha sh.63,015,450,230.40 zilipatikana na katika hizo Sh.56,987,368,631.08 zimewasilishwa Hazina na Sh.6,028,081,599.41 zimewasilishwa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa ajili ya kugharamia tafiti mbalimbali zenye manufaa kwa nchi yetu. Kabla ya mfumo huu, mapato haya hayakuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuwajengea uwezo wataalam wa TCRA ili waweze kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano hususan katika eneo hili la kuchakata taarifa mbalimbali za huduma za mawasiliano zinazopatikana kutoka kwa watoa huduma ili kuweza kubaini na kujiridhisha juu ya mapato yote.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE aliuliza:-
Wilaya ya Kigamboni ina uwekezaji mkubwa katika sekta ya nyumba na viwanda, mahitaji ya umeme kwa sasa ni zaidi MW 20; lakini ni MW 8 tu zinazopatikana, nao umekuwa ukikatika mara kwa mara kutokana na mahitaji makubwa pamoja na uchakavu wa miundombinu ya umeme.
(a) Je, Serikali ina mikakati gani ya kuhakikisha Kigamboni inapatikana umeme wa uhakika?
(b) Je, ni lini Serikali itajenga kituo cha kupoozea umeme (substation) katika Wilaya ya Kigamboni kutokana na mahitaji makubwa ya umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) inakamilisha utekelezaji wa mradi wa uboreshaji umeme katika Jiji la Dar es Salaam kupitia mradi wa TEDAP. Mradi huu unahusisha ujenzi wa vituo vya kupooza umeme vya Mbagala na Kurasini. Kazi ya vituo hivyo ni pamoja na kuimarisha upatikanaji wa umeme katika maeneo ya Kigamboni kwa kuwa Kigamboni sasa itakuwa ikipata umeme kutoka katika vituo hivi vya Mbagala na Kurasini badala ya Kipawa na Ilala kama ilipokuwa hapo nyuma. Ujenzi wa mradi huu ulianza mwaka 2012 na utakamilika mwishoni mwa mwezi Septemba, 2017.
(b) Mheshimiwa Spika, ili kulipatia ufubuzi wa kudumu tatizo la upatikanaji wa umeme eneo la Kigamboni, Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) linajenga njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 132 kutoka Kurasini kwenda Dege – Kigamboni na kujenga kituo cha kupooza umeme chenye uwezo wa kilovoti 132 chenye uwezo wa kufua umeme wa MVA 120 sawa na MW 100. Taratibu za ujenzi zimeanza mwezi Agosti, 2017 na kazi inatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2018. Gharama ya mradi huu inakadiriwa kufikia shilingi bilioni tano.