Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Angelina Adam Malembeka (30 total)

MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwa kuwa, adhabu mojawapo aliyoitaja ni kifungo cha maisha kwa wale ambao watapatikana hatia na huko gerezani tayari wameshakuwa na tabia kama hiyo, haoni kwamba kwa kuwaweka gerezani maisha wataendelea kufanya shughuli hiyo, kwa nini adhabu isiongezwe na waweze kuhasiwa ili wasirudie tena kitendo hicho?
Swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba vitendo vya ubakaji vinajirudia mara kwa mara; Je, anaweza kunipa taarifa kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita ni kesi ngapi zimepelekwa Mahakamani na ngapi zimetolewa hukumu. Ahsante.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge yeye anaona adhabu ya gereza haitoshi, hata kwenda jela maisha haitoshi ila anataka vile vile wahasiwe. Siwezi kuwa na jibu hapa kwa sababu hili ndilo Bunge linalotunga sheria za nchi, ningeomba tu Mheshimiwa Mbunge aje na hilo wazo liletwe mbele ya Bunge hapa, ni ninyi mtakaopitisha kwamba wanaume wahasiwe wanaokutwa na hilo tatizo au la, lakini siyo Serikali kuja na shauri hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, anataka kujua statistics, kujua ukubwa wa tatizo hili. Naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tatizo la kubaka na kulawiti nchi hii sasa hivi limefikia mahali pabaya kwa sababu, ukichukua takwimu za miaka mitatu au miaka minne iliyopita, tuna matukio kumi na tisa kila siku ya Mungu ya kubaka na kulawiti. Hayo matukio 19 ya kila siku ya Mungu ni yale ambayo yanaripotiwa, sasa siyo ajabu yakawa mara tatu ya hapo yale ambayo yanapita bila kuripotiwa na kupelekwa Mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hili ni tatizo kubwa, Waheshimiwa Wabunge lazima tushirikiane. Kati ya mwezi Januari mpaka mwezi Machi mwaka huu tu nimepata taarifa hapa kwamba tuna mashauri 2,031, miezi mitatu tu! Mpaka sasa naipongeza Mahakama kwamba pamoja na uchache wao wameweza kuzikamilisha kesi 111, watuhumiwa 96 wamefungwa. watuhumiwa 18 wameachiwa huru kwa kukosa ushahidi, lakini bado kesi 1,920 kwa miezi mitatu bado hazijakamilika. Hiyo ndiyo changamoto tuliyonayo ambayo naona Waheshimiwa Wabunge wote ni kazi yetu kuweza kuitatua.
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nilikuwa naomba kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwa kuwa Jeshi la Polisi pamoja na kazi nyingine kazi yake kubwa ni kulinda mali na raia, nilitaka kufahamu kuna ukweli gani kuhusiana na raia kupigwa na polisi huko Pemba? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Niabu Spika, sio kweli kwamba polisi wamekuwa wakipiga raia huko Pemba na ninaomba nichukue fursa hii mbele ya Bunge lako Tukufu kutoa mfano halisi ambao ulijitokeza siku za hivi karibuni kule Pemba kwa kitendo cha maigizo na usaniii kilichofanywa na watu kutoka chama cha upinzani cha kisiasa kwa makusudi kabisa ili kupotosha jamii na dunia kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati polisi imefanya kazi yake ya kuwakamata wahalifu ambao wanafanya vitendo vya uhalifu Pemba kuna mhalifu mmoja alijifanya kwamba amekufa na amepigwa na baada ya kuhojiwa na polisi alikimbia na kukamatwa, mtu ambaye amekufa anawezaje kukimbia.
Kwa hiyo, huo ni ushahidi wa usanii ambao unafanywa kwa kulipaka matope jeshi la polisi. Naomba dunia na Watanzania watambue kwamba polisi hata siku moja hawezi kufanya kazi kinyume na sheria, maadili yake na weledi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kauli hiyo sio kweli kinachofanyika ni kwamba kuna raia ambao wamefanya vurugu za makusudi na polisi inachukua jitihada za kuwakamata na kupeleleza na baadae kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimalizie tukwa kuendelea kutoa wito kwamba tuendelee kuhakikisha kwamba tunalinda amani ya nchi yetu lakini vilevile tusitumie kauli ama vitendo vilivyokuwa sio vya kweli kulipaka matope Jeshi la Polisi na kuipaka matope nchi yetu mbele ya Watanzania na mbele ya Jumuiya za Kimataifa.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwanza nilitaka kufahamu ni mikakati gani iliyowekwa na Serikali katika kuongeza vifaa tiba na wataalam katika Hospitali zote za Jeshi zikiwepo za Zanzibar?
Pili, ni lini Waziri atafanya ziara katika vituo hivyo ili kuona hali halisi ya utendaji kazi katika vituo hivyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, mikakati ya Serikali katika kuongeza vifaa tiba, dawa na watumishi kwenye Vituo vya Afya vya Kijeshi ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali kwenye bajeti zake kila mwaka imekuwa ikiongeza bajeti ya huduma za afya kwa ajili ya makamanda na wapiganaji wetu kwa sababu wanapewa umuhimu wa kipekee katika nchi yetu, lakini sambamba na kuongeza bajeti Serikali pia imeongeza mikakati ya kufundisha wataalam mahsusi kwa ajili ya majeshi na hivi karibuni tumepata wafadhili kutoka Ujerumani kupitia Serikali ya nchi hiyo ambao ni marafiki zetu ambapo wametujengea chuo kikubwa na cha kisasa cha kijeshi kwa ajili ya kutoa wataalam kwenye sekta za tiba na chuo hiki nikupe taarifa Kamati yako ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama inayoongozwa na Mheshimiwa Adadi mwezi Aprili, 2016 ilitembelea kwenye chuo hiki ambacho kimejengwa kwa msaada wa Serikali ya Ujerumani na wakajionea namna kilivyo kizuri na cha kisasa.
Mheshimiwa Spika, pia Kamati ilitupa ushauri kwamba kituo kile badala ya kuishia kutoa stashahada kiende mpaka ngazi ya degree na Jeshi likachukua ushauri ule na limekubali kukipandisha hadhi chuo hicho na mkakati wa kukiweka sawa inaendelea.
Sambamba na mkakati huo ili kutatua changamoto ya upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitenganishi kwenye jeshi kwa sababu ya umuhimu wao tayari mikakati ya kuajiri wataalam wapya wakimemo madaktari bingwa na madaktari wa kawaida pamoja na wataalam wengine imeendelea kutekelezwa. Mpaka kufikia mwezi Machi madaktari takribani 143 waliajiriwa mahsusi kwa ajili ya kutoa huduma majeshini.
Mheshimiwa Spika, lakini pia kupitia chuo hiki ambacho kimeaznishwa tunaamini katika miaka ya karibuni kutakuwa hakuna changamoto ya watumishi lakini pia kupitia kwenye kuongeza bajeti yetu tunaamini changamoto ya upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitenganishi nayo itakuwa imepatiwa ufumbuzi. Lakini suluhisho la kudumu ambalo Serikali inalifanya kwa sasa ni kutengeneza Bima ya Afya mahsusi kwa ajili ya makamanda na wapiganaji wetu na bima hii tayari imeshapata baraka za Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli na sasa hivi ndani ya Serikali mchakato wa kuirasimisha unaendelea ili ufike katika ngazi ya Baraza la Mawaziri na utekelezaji ufanyike.
Swali lake la pili, kwamba je Waziri itakuwa tayari kwenda kufanya ziara ninaomba nilichukue na nilifikishe kwa Waziri mwenye dhamana ili aweze kuzungumza na Mheshimiwa Mbunge na pengine kumpa majibu mahsusi kwamba ni lini ataenda kuvitembelea vituo hivi.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwanza, nilitaka nifahamu kwa wale waandishi na wachapishaji ambao wamechapisha vitabu vyenye maadili mabovu au wametoa taarifa za uongo kupitia vitabu hivyo wamepewa adhabu gani?
Pili, ninataka kujua kwa kuwa wananfunzi wanaotoka Visiwa vya Unguja huwa wanafanya mitihani ya Kitaifa sambamba na wenzao wa Tanzania Bara; je, Wizara inafanya utaratibu gani kuhakikisha kwanza mihtasari na vitabu kwa maana ya mitaala na vitabu inawafikia wanafunzi wa Zanzibar mapema ili na wao waweze kujisomea na kufanya vizuri katika mitihani ya Taifa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi vitabu vyote kabla ya kupitishwa vinatathminiwa na baada ya kutathminiwa, vinaangaliwa katika suala la maadili inayoendana katika misingi ya kwamba huyu mwanafunzi atafundishwa vipi. Lakini vilevile siyo maadili tu hata uchapishaji wake kitabu kilivyochapishwa kinaleta uhalisia wa yale yanayokusudiwa kufundishwa au laa! Kwa mfano, kama tuna lengo la kumfundisha mtoto kwamba haya ni mayai, basi tunategemea kwamba na kitabu hicho hata picha itaonyesha mayai ambayo ni meupe na itaonyesha kweli yale ni mayai, hayataonyeshwa mayai wakati hapo imechorwa embe. Kwa wanaokuwa hawajatekelza wajibu wao ipasavyo vitabu hivyo vinakuwa haviruhusiwi kupelekwa au kusambazwa au kuchapishwa kwa maana hiyo wanatakiwa kurekebisha hayo makosa. Hayo yalishafanyika hata katika vitabu ambavyo sisi wenyewe tulikuwa tukivishughulikia na tulivizuia visiweze kuendelea.
Pili; kwa upande wa Zanzibar kimsingi Zanzibar wao wanayo mamlaka yao ya elimu ambayo inashugulikia masuala yote hayo ya mitaala pamoja na vitabu. Lakini kwa kuwa sisi wote ni ndugu na tuna masuala ya ushirikiano wa kielimu huwa pia tunaweza kusaidiana katika masuala ya kitaalam lakini pia hata kuchukua best practice katika kutoka upande wowote wa nchi kwa faida ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, ningependa kuongezea kidogo majibu mazuri aliyoyatoa Naibu Waziri wa Elimu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nataka nitoe tu ufafanuzi kuhusiana na mitaala ya elimu ya sekondari kwa upande wa Zanzibar. Kama alivyoelezea Mheshimiwa Naibu Waziri kwa upande wa elimu ya msingi mitaala inatengenezwa na upande wa Zanzibar, lakini kwenye upande wa sekondari mitaala inatengenezwa na Taasisi ya Elimu Tanzania ambayo utaratibu ni shirikishi wakati wa mitaala inapotengenezwa tunawashirikisha upande wa Zanzibar na vilevile hata katika Bodi ya Taasisi ya Elimu Tanzania kunakuwa na uwakilishi wa Wajumbe wa kutoka Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na utaratibu wa usambazaji wa vitabu ili vifike Zanzibar kwa wakati, utaratibu ni kama unavyotumika Bara kwamba kwanza zoezi ni shirikishi la vinapokuwa tayari Wizarra ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar huwa inafanya hilo jukumu.
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri niliyopewa, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Serikali imejipanga vipi kwa ajili ya kutoa elimu ili fedha zitakazotolewa zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa taasisi nyingi za fedha zimeonekana zinatoa mikopo kwa wanawake na vijana, Serikali imejipanga vipi katika kuinua uchumi au kuwawezesha kiuchumi wazee? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE WALEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejipanga vizuri ili kuhakikisha kwamba elimu inatolewa kwa wajasiriamali wote hasa ukizingatia kwamba moja ya changamoto zilizopo kwa Mifuko ya mwanzo ilikuwa ni elimu ya ujasiriamali. Kwa hiyo, hilo tayari limeangaliwa na Serikali imejipanga vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu wazee, bado Serikali inaangalia changamoto mbalimbali na tayari Ofisi ya Waziri Mkuu inaangalia kwa mfano namna ya kurasimisha pensheni ya wazee, lakini suala hili linafanyiwa kazi na pale litakapokamilika basi taarifa rasmi itatolewa na ikibidi sheria rasmi itatungwa.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
La kwanza, kumekuwa na utaratibu wa Watanzania wanaofariki nje ya nchi, ndugu zao wanaokuwepo hapa nchini hupata taabu, adha na kucheleweshwa kuletewa maiti. Inafikia familia za kimaskini zinauza hata vitu vyake ili kuweza kuleta ile maiti nchini. Je, ofisi za Ubalozi zimejipanga vipi kuhakikisha Watanzania wenye hali duni maiti zao zinapopatikana kule ziletwe nchini haraka? (Makofi)
Swali la pili, kuna baadhi ya Balozi zina utaratibu wa kupanga siku maalum za kuwahudumia Watanzania, hususan tabia hiyo ilikuwepo katika Ubalozi wetu wa Afrika Kusini. Tabia ile ilileta matatizo na usumbufu kwa Watanzania ambao wanataka huduma katika ofisi za Ubalozi.
Je, sasa hivi wamejipanga vipi kuhakikisha Watanzania wanaotaka huduma kwenye Balozi zao nje ya nchi yetu wanapata huduma haraka? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba kwa nyakati tofauti kumeripotiwa baadhi ya Watanzania ambao wamefiwa na ndugu zao kupata taabu katika kusafirisha miili, lakini katika hali ya jumla Balozi zimekuwa zikisaidia sana pale wanapopata taarifa sahihi kwa wakati. Kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Mbunge kwamba mara nyingine ucheleweshaji unatokea kutokana na Balozi zetu kuweza kupata taarifa kwa wakati, lakini katika hali ya jumla, kati ya masuala ambayo Balozi wetu zinatakiwa zishughulikie ni kuhusu maslahi ya Watanzania wanaoishi huko ikiwa ni pamoja na pale wanapopata taabu, wanapopatwa na matatizo ikiwa ni pamoja na kifo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama kuna changamoto ambazo zimetokea, kila wakati Wizara imekuwa ikichukua changamoto hizo na kuzifanyia. Kwa hiyo, tunaamini huko mbele tunakoelekea, changomoto hizi zitaendelea kupungua na hasa sasa katika Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imejikita katika kuleta ufanisi na nidhamu katika utumishi wa umma. Kwa hiyo, tunaamini upungufu na changamoto ambazo zimekuwa zikitokea nyuma, zitapungua kama siyo kuondoka moja kwa moja.
Ni rai ya Mheshimiwa Mbunge kuhusu Balozi zetu kupanga siku maalum kwa ajili ya kuwatumikia na kutoa huduma kwa Watanzania, pendekezo la Mheshimiwa Mbunge ni zuri, Wizara italiangalia, lakini ifahamike kwamba hakujaripotiwa kwa kiwango kikubwa kuhusu Watanzania kushindwa kupata huduma za kibalozi, lakini kama nilivyosema tutalipeleka na kuliangalia na iwe ni moja kati ya njia za kususluhisha changamoto ambazo zinatokea.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, kwa kuwa utaratibu aliousema ulishawahi kufanyika katika wilaya mbalimbali hapa nchini na baadaye tukaambiwa utaratibu huo umesitishwa, je, ni lini zoezi hilo litaanza tena ili vijana waweze kujiunga na Jeshi?
Mheshimiwa Spika, pili, ni nini kauli ya Serikali juu ya ajira ya Jeshi kwa vijana wenye maadili mema na uwezo katika Mkoa wa Kaskazini Unguja na Tanzania kwa ujumla?Ahsante.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, utaratibu niliousema haujasitishwa, bado utaratibu huu unatumika, kila mwaka tunachukua vijana kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa kupitia katika wilaya na mikoa yao. Kwa hiyo, utaratibu huo bado unatumika. Mwaka huu tumefanya zoezi hilo mwezi Desemba na tunategemea tutakapopata fedha baada ya bajeti basi awamu inayofuata utaendelea.
Mheshimiwa Spika, kuhusu vijana anaowazungumzia Mheshimiwa Malembeka, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, ni kwamba tutakapotangaza tena kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa, nitawaomba vijana hao waombe kupata nafasi za kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa na ajira kwenda Jeshi la Wananchi zinapitia katika Jeshi la Kujenga Taifa. Si Jeshi la Wananchi peke yake, kwa sasa vyombo vyote vya ulinzi na usalama vimeamua kwa makusudi kwamba ajira zao zipitie JKT. Kwa hiyo Polisi, Magereza, Uhamiaji, Usalama wa Taifa, Jeshi lenyewe la Wananchi wa Tanzania wote wanachukua vijana waliopitia Jeshi la Kujenga Taifa, kwa hiyo nitawaomba wajiunge huko ili hatimaye waweze kupata ajira hizo.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Angelina mwenzangu, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Swali la kwanza, kwa kuwa Mheshimiwa naibu Waziri amekiri kuwa wananchi wanavamia na kuyamega maeneo ya Serikali kinyume na utaratibu; na kwa kuwa ametoa rai wananchi waondoke maeneo hayo kabla sheria haijachukua mkondo wake, sasa isije ikawa kwa wananchi kilio, kwa watendaji vigelegele.
Je, Serikali ina kauli gani juu ya watendaji ambao wanalipwa mshahara kwa kazi ya upimaji na katika maeneo yao hawajafanya lolote hadi sasa?
Swali la pili, kwa kuwa katika majibu ya msingi, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema gharama elekezi za huduma ya upimaji siyo kubwa kama inavyoonekana au inavyodhaniwa.
Je, kwa nini gharama hizo zisiwekwe wazi ili wananchi na taasisi nyingine wafahamu na kuzitambua na waweze kujipanga kwa ajili ya kulipia? Ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Swali la kwanza ameulizia habari ya adhabu kwa watendaji ambao wanafanya makosa na tunaadhibu pengine wananchi. Kama nilivyomjibu muulizaji wa swali namba 44 majukumu na uwajibishaji yako chini ya mamlaka husika hasa katika maeneo yetu kwenye Halmashauri za Wilaya. Kwa hiyo, haya yanapobainika basi tuyachukulie hatua papo hapo ili tusiweze kuwafanya wananchi waumie zaidi kwa makosa ya watendaji wetu.
Swali la pili, ametaka kuewekewa gharama za upimaji wazi. Naomba niseme tu tutazitoa na tutawagawia Waheshimiwa Wabunge wote, lakini kwa kifupi tu nikianza kuzungumzia habari ya miji kwenye Mamlaka za Miji na Manispaa katika gharama za upimaji kuanzia square meter moja mpaka square meter 400 gharama yake kwa maeneo ya residential ni shilingi 65 lakini maeneo ya commercial ni shilingi 350 kwa square meter, kwenye industrial ni shilingi 450 na kwenye maeneo ya social services ni shilingi 150. Kwa miji yetu ya kwaida kwenye township ni shilingi 200 kwa makazi, maeneo ya biashara ni shilingi 300, maeneo ya viwanda 350 na maeneo ya services ni shilingi 100. Vivyo hivyo kwenye trading center ni shilingi 100 kwa makazi, shilingi 200 kwa commercial, shilingi 200 tena kwa industrial na shilingi 100 kwa services. Kwa sababu mlolongo pia unategemeana na ukubwa wa kiwanja vina-range kuanzia shilingi 300,000 mpaka milioni 14 kutegemeana na ukubwa kuanzia hekari moja mpaka 10 ni shilingi milioni tatu, zinakwenda zinaongezeka kadri ya ukubwa, tutaziandaa na tutawasambazia Waheshimiwa Wabunge wote.
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa suala la kutelekezwa kwa watoto ni jambo ambalo wanawake/ Wabunge hatuwezi kulifumbia macho; ili kupata uhakika na ukweli kuhusu watoto wanaotelekezwa na Waheshimiwa Wabunge wanaume, kwa nini tusifungue Kituo cha Ustawi wa Jamii hapa ili kuweka mambo sawa? Ahsante. (Kicheko/ Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, inaonekana suala la utelekezaji wa watoto hapa Bungeni ni changamoto kubwa sana. Naomba nirudie majibu yangu ya msingi kwamba sheria ya mtoto imeweka utaratibu mzuri tu wa kushughulikia mashauri ambayo yanahusu utelekezwaji ama watoto kutopata matunzo vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusisitiza kwamba madawati yetu ya Halmashauri katika ngazi ya Halmashauri yatumike katika masuala haya.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, yenye data na yamenifurahisha. Pamoja na majibu hayo mazuri nina swali moja la nyongeza na ombi moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ahadi ya Mheshimiwa Rais juu ya kujenga viwanda ili kutoa ajira, kujenga uchumi na kutumia malighafi za eneo husika lilizungumzwa bila ubaguzi wowote na kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri katika majibu yake amesema jukumu la Serikali ni kuhamasisha na kuweka mazingira mazuri ya uwezeshaji na ujenzi ni jukumu la sekta binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi nimekuwa nikisikia Wizara hiyo ikisema hapa na kupiga debe kuhusu ngozi, pamba, matunda, sukari, ndizi, mihogo hadi pilipili sijasikia hata siku moja Wizara hiyo ikizungumza kuhusu mchakato wa karafuu. Ni lini sasa Mheshimiwa Waziri ataanza kuweka hamasa ya kasi ili Zanzibar tupate kiwanda cha kuchakata karafuu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu sasa, kwa kuwa suala la viwanda ni la nchi nzima bila kujali suala la Muungano na kuna vitu ambavyo vimefanyika Zanzibar bila kujali suala la Muungano nikitolea mfano wa barabara iliyojengwa round about ya Amani hadi Mtoni ambayo ilijengwa kwa fedha ya Muungano na kupewa jina la Mkapa Road, kwa nafasi hii kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Kaskazini Unguja naomba tujengewe kiwanda cha karafuu Zanzibar ili vijana wetu wapate ajira. Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge lile la kwanza ambalo litajibu na namba mbili, kuhamasisha uchumi wa viwanda nchi nzima ni jukumu la Wizara yangu na nitashirikiana na Mheshimiwa Mbunge twende Zanzibar niweze kuhamasisha kwa nguvu ileile ambapo nimeanzia sehemu nyingine. Katika utaratibu huo nitawahasisha wawekezaji ambao najua wapo kusudi tu- take advantage ya karafuu, mwani na michaichai kusudi tu- take advantage ya viungo hivi na manukato. (Makofi)
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na pia namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri katika majibu yake amekiri kuwa mitaala na vitabu vya elimu ya awali na msingi vinavyotumika upande wa Zanzibar ni tofauti na vya Bara.
Je, haoni kuwa kitendo hicho kinafifisha na kudhoofisha uwezo wa wanafunzi ambao wanaanza mitaala mipya badala ya kuendeleza ile waliyokuwa nayo na kusababisha wanafunzi kutoka Zanzibar kutofaulu vizuri mitihani yao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; kwa kuwa Naibu Waziri amekiri kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar huendesha mitihani ya elimu ya awali na msingi Zanzibar, na kwa kuwa Baraza la Mitihani Zanzibar lipo, Serikali haioni kuwa ni wakati muhimu sasa iruhusu mitihani ya kidato cha nne na cha sita ikatungwa na kusahihishwa na Baraza la Mitihani la Zanzibar na kupewa hadhi sawa ya Kitaifa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema awali, kwa kuwa vitabu katika eneo hili la mafunzo katika elimu ya awali na msingi vimekuwa vikitungwa upande wa Zanzibar, basi kwa kushirikiana imeonekana kwamba ni vyema wao wenyewe kuendelea kutunga hiyo mitihani. Hata hivyo tuelewe kwamba suala la Baraza la Mitihani ni suala ambalo lipo katika mambo ya Muungano katika jedwali la kwanza namba 16.
Kwa hiyo, kwa misingi hiyo pale inapotokea kwamba kuna haja ya kufanya marekebisho ina maana ni suala la Kikatiba ambalo inabidi kufuata taratibu za Kikatiba katika kupata marekebisho kama hayo. (Makofi)
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Ninampongeza na ninamshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jibu lake zuri ambalo limeleta uelewa na kuonesha nia ya kukufua ranchi zetu. Nilikuwa na maswali mawili ya ziada kama ifuatavyo:-

(i) Kwa kuwa katika maelezo yake amesema lengo kubwa ilikuwa ni kutoa mifugo bora kwa ajili ya nyama ndani ya nchi na kuuza nje ya nchi, na kwa kuwa Zanzibar inategemea kitoweo cha nyama kutoka Tanzania Bara, je,
Serikali ina mpango gani kupeleka nyama Zanzibar kwa utaratibu maalum?

(ii) Kwa kuwa Ranchi ya Ruvu likuwa inajengwa machinjio kubwa ya kisasa lakini mpaka sasa hvi imesimama na haijulikani itakamalika lini. Serikali ina kauli gani juu ya Ranchi hiyo ya Ruvu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, juu ya upelekaji wa kitoweo cha nyama ya ng’ombe Zanzibar hivi sasa wapo Watanzania wengi wanaofanya biashara ya kuchukua nyama ya ng’ombe na kupeleka Zanzibar na ziko kweli changamoto kadha wa kadha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kila mara changamoto tulizonazo huwa tunazifanyia kazi ya kuhakikisha tunazitatua na hatimaye kuweza kuwasaidia wenzetu kuweza kupata kitoweo cha nyama ng’ombe, mbuzi kwa uhakika na hilo tutaendelea kulifanya kadri litakavyokuwa likiibuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, juu ya machinjio ya Ruvu. Tupo kwenye mkakati mzuri wa kuhakikisha machinjio ya Ruvu inajengwa. Hivi sasa tumeshafanikisha kuona juu ya athari ya mazingira na hatua zingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati tulionao ni kutafuta pesa ya kuhakikisha kuwa mradi ule unakamilika na kuwaweza kuwasidia Watanzania kupata nyama ya uhakika, lakini vilevile kuweza ku-export nje ya nchi na hata kutengeneza vitu vingine kama vile mazao yanayotokana na ngozi za ng’ombe wetu.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, nimshukuru Mheshimiwa Waziri na kumpa pongezi kwa majibu yake ambayo yanaonyesha nia ya dhati ya Serikali kuwasaidia wafungwa wanawake. Maswali yangu mawili yanyongeza ni kama ifuatavyo:-

(a) Je, Serikali inawasaidiaje watoto ambao wapo gerezani na mama zao kielimu na kisaikolojia kwa kuzingatia haki za watoto husasan wanapotumikia kifungo hicho ambacho watoto wao hawahusiki nacho?

(b) Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa wanawake wafungwa ambao ni wajawazito wakatumikie kifungo hicho nje ili waweze kuwalea watoto wao katika familia huru badala ya kuwa gerezani?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Malembeka kwa jina maarufu Nyoka wa Kijani, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba wapo akina mama wafungwa ambao wanajifungua watoto wakiwa magerezani. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Nyoka wa Kijani, Nyara ya CCM kwamba utaratibu wa Jeshi la Magereza kupitia kanuni za Jeshi la Magereza watoto ambao wamekwishazaliwa magerezani wanpofikia umri wa kuanza awali wamekuwa wakisoma kwenye shule za awali zilizopo kwenye magereza zetu. Pia kwa kupitia watumishi wa magereza ambao wana utaalamu wa masuala ustawi wa jamii wamekuwa wakiwapa elimu pamoja na kuwafariji watoto hawa ili wajione wao siyo wafungwa ndani ya magereza isipokuwa wamezaliwa katika wakati ambao mama zao wapo magerezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kwamba kwa nini wafungwa ambao wanajifungua magerezani wasipate adhabu nyingine badala ya kuwafunga magerezani. Tunao utaratibu kupitia sheria yetu ambayo inaitwa Probation for Offenders pamoja na Community Services, wale ambao wana vifungo chini ya miaka mitatu tumekuwa tukiandaa utaratibu wa kuwaondoa magerezani ili wawe na vifungo mbadala. Hata hivyo, kuna utaratibu watoto wanaokuwa magerezani wanapofikia umri ambao wanaweza wakaishi uraiani bila kuwa na mama zao ndugu zao wamekuwa wakishirikishwa ili waweze kutoa malezi kwa watoto ambao mama zao wapo magerezani. Ahsante sana.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo yanaonesha kabisa Serikali ina nia nzuri ya kusaidia wananchi wake. Kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Kaskazini Unguja nilikuwa nina maswali mawili ya kuongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nilitaka kujua: Je, huduma ya uokoaji na kuzima moto kuna gharama zozote ambazo mhudumiwa anatakiwa alipe?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili: Je, kama gharama hizo zipo, ni utaratibu gani unatakiwa ufanywe ili aliyepatiwa huduma aweze kulipa bila kuwa na taharuki? Maana kipindi kile anakuwa amechanganyikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwa dhati kabisa nimpongeze sana Mheshimiwa Malembeka kwa kazi nzuri ambayo anayoifanya katika Mkoa wake wa Kaskazini. Kwa kweli anawatendea haki wapiga kura wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nikijibu maswali yake pamoja, kwanza huduma za kuzima moto ni za bure, hakuna gharama. Hata hivyo, kwa mujibu wa sheria ya Jeshi la Uokoaji na Zimamoto ya mwaka 2007 Sura ya 427, inaeleza kwamba Jeshi la Zima Moto na Uokoaji lina Mamlaka ya kuweza kutoa leseni kwa makampuni binafsi kutoa huduma hizo ikiwemo huduma ya kuzima moto pamoja na vifaa.

Mheshimia Naibu Spika, kwa hiyo, makampuni haya ndiyo ambayo yanaingia mikataba na Taasisi binafsi na ndiyo yanakubaliana malipo, lakini kwa maana ya huduma hizi za zimamoto ni bure.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na utaratibu ambao unatumika, unapiga namba 114 na kikosi chetu kinafika pale haraka iwezekanavyo kutoa huduma hizo bila malipo yoyote. (Makofi)
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake japo hayajaniridhisha kwa sababu swali langu la msingi nilihitaji kujua ni vijana wangapi kutoka Wilaya ya Kaskazini A na Wilaya ya Kaskazini B ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja ambao wamepata ajira katika jeshi kwa miaka mitatu, lakini amenipa jibu la jumla la Zanzibar yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilitaka kujua ni lini vijana wa Mkoa wa Kaskazini Unguja watapata ajira katika jeshi ili kuondoa malalamiko yaliyopo hivi sasa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili kwa kuwa manug’uniko ni mengi yanayotokana na vijana kujitolea kwa muda mrefu lakini hawapati ajira. Ni mkakati gani ambao Serikali umeupanga ili kuhakikisha vijana hawa wanapata ajira hiyo kwa kuzingatia pia jinsia maana hapa katika orodha yake inaonyesha wanaume 720 wanawake 280?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Malembeka kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la kwanza anasema sikumpa takwimu za ni vijana wangapi kutoka Wilaya ya Kaskazini A na B waliojiunga na JKT. Katika jibu langu la msingi nilitoa takwimu za jumla za vijana wanaochukuliwa kutoka Zanzibar na nikaeleza kwamba jukumu la kupanga idadi kwa Wilaya za Zanzibar linafanywa na SMZ. Kwa hivyo takwimu sina na Mheshimiwa akizihitaji itabidi azipate kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa sababu wao ndiyo wanapanga kwa mujibu wanavyoamua, sisi tunakabidhi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wao wanagawa wanavyopenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, katika hilo hilo la kwanza alikuwa anauliza lini vijana watapata ajira ili kuondoa malalamiko. Nataka ieleweke kwamba kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa lazima vijana waelewe kwamba siyo ajira, kujiunga na JKT ni kwenda kupata mafunzo ya kijeshi pamoja na study za kazi. Wachache watapata ajira katika vyombo vya Ulinzi na Usalama, walio wengi watabidi wajiajiri wenyewe au waajiriwe na sekta binafsi. Hili ni muhimu lieleweke, wasielewe kwamba kujiunga na JKT ndiyo ajira. Tunachukua vijana wengi na nilitoa takwimu hapa wakati wa bajeti yangu kwamba tunachukua takribani vijana 20,000 kwa mwaka. Vyombo vya ulinzi na usalama havina uwezo wa ku-observe kuchukua wote hao katika ajira, watapata wachache na walio wengi watakuwa wamepata study za kazi ili waweze kujiajiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ni mkakati gani wa kupatia ajira na kwa kuzingatia jinsia, hawa tuliowataja ni vijana wanaojiunga na JKT na siyo ajira. Kwa maana hiyo kule wanapofanya usaili kuna vigezo ambavyo vinafuatwa, mara nyingi wasichana hawajitokezi kwa wingi lakini wanaojitokeza wengine wanakosa sifa zinazotakiwa na ndiyo maana unaona kuna tofauti ya idadi hapa. Kwa hiyo, mkakati uliopo ni kuwasaidia vijana hawa, wale wanaokosa ajira katika vyombo vya ulinzi na usalama kuweza kuwapa study za kazi ili waweze kuajiriwa na sekta nyingine pamoja na kujiajiri wao wenyewe.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa
Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa kuwa Serikali ina mpango wa kununua meli nane kubwa za uvuvi, ambapo nne zitaenda Zanzibar na nne zitakuwa Tanzania Bara. Je, ni lini meli hizo zitanunuliwa ili zianze kutoa ajira na kutoa huduma kwa wananchi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa katika jibu lake la kwanza ameelezea hiyo ujenzi wa bandari ya uvuvi, ningependa kujua je, upande wa pili wa Muungano utashirikishwa vipi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa
Spika, ununuzi wa meli nane ambazo zimesemwa katika ahadi yetu ya Serikali ununuzi huu utaanza hivi karibuni kwa kuwa Serikali sasa iko katika mazungumzo na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo, maelezo na mazungumzo hayo yanaendelea, yakishafanyika Wizara ya Fedha sasa itaingia makubaliano na mfuko huu ili ununuzi uweze kuanza.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Mbunge alihitaji kufahamu kazi hii ya ujenzi wa bandari ambayo inaendelea kwa upande wa Bara na upande wa Zanzibar nini kinaendelea.

Mheshimiwa Spika, naomba nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba mazungumzo haya yanapoendelea kwa upande wa Bara pia upande wa Zanzibar wameanza mazungumzo na nchi ya Comoro na bandari ya Zanzibar pia itaanza kujengwa na ikijengwa maana yake ajira hizi sasa zitatolewa kwa pande zote.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza; kwa kuwa Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alitoa maagizo, taasisi na kampuni za Serikali kutumia Kampuni ya Ulinzi ya SUMA JKT. Je, hadi sasa ni makampuni mangapi au Taasisi ngapi za umma au Serikali zinazotumia Ulinzi wa SUMA JKT? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; je ni fedha kiasi gani hadi sasa Kampuni ya SUMA JKT inadai kwa wateja wake? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza la Mheshimiwa Angelina Malembeka kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze na kumshukuru sana Mheshimiwa Malembeka kwa namna ambavyo anafuatilia maelekezo ya viongozi wakuu, lakini pia kufuatilia maendeleo hususan ya SUMA JKT. Kwa kujibu maswali yake niseme tu baada ya maelekezo ya Amiri Jeshi Mkuu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kuyatoa juhudi zimefanyika mpaka sasa idadi ya malindo 443 tunayo, ikiwemo malindo 259 ya Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma na malindo 184 ya watu binafsi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, ni kweli kwamba baada ya maelekezo yale tumefanya ufuatiliaji kama Wizara kulikuwa na rekodi ya madeni ya shilingi bilioni kama kumi na mbili na milioni mia tano (12,500,000,000) hivi, lakini baada ya uhakiki, deni hilo lilikuwa kwenye bilioni kumi na mbili na milioni tisini na sita (12,096,000,000), lakini kwa juhudi zilizofanyika asilimia 70 ya madeni yale ya kama bilioni nane na milioni mia tano (8,500,000,000) hivi zimeshalipwa. Bado tunalo deni kama la bilioni tatu nukta tano (3,500,000,000). Kwa hiyo, niendelee kuwashukuru wateja wetu kwa kutupa kazi, lakini niwashukuru pia kwa kuendelea kufanya malipo.

Mheshimiwa Spika, pia niwaombe wateja wetu waendelee kufanya malipo ya madeni haya kwani yapo manufaa makubwa kwamba tunapokusanya fedha hizi tunaendelea kuongeza ajira mbalimbali kwa vijana wetu lakini pia kadri tunavyoongeza huduma hizi za ulinzi, usalama kwenye mitaa unaongezeka kwa sababu pale ambapo tuna walinzi wetu wa SUMA JKT, ni msaada mkubwa kwa maeneo pia ya jirani na malindo yao. Kwa hiyo tunaendelea kupata manufaa makubwa, lakini kubwa zaidi pia tunaongeza uchumi katika nchi yetu. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuongeza maswali mawili ya ziada. Swali langu la kwanza, nataka nijue kwa kuwa, suala la ubakaji na ulawiti na unyanyasaji kwa watoto haliko Tanzania pekee, lipo katika nchi mbalimbali. Nilitaka kujua Serikali inashirikiana na mashirika gani, ili kuhakikisha suala hili linakomeshwa?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa, kuna maafisa wa madawati katika maeneo kadhaa, ili kusaidia kupambana na masuala ya ulawiti, ubakaji na unyanyasaji kwa watoto, nilitaka kujua wanawawezeshaje maafisa wale, ili waepukane na rushwa, lakini pia waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, anataka kujua ni mashirika gani ya kimataifa au mashirika gani ambayo tunashirikiananayo katika kupambana na jambo hili. Kwa kweli, niseme tu kwamba, yapo mashirika mengi ambayo tunashirikiananayo. Yapo ya ndani na nje ya nchi ambayo tunashirikiananayo katika kupambana dhidi ya matukio haya ya uhalifu, hasa ya udalilishaji wa kijinsia. Kwa upande wan je huko tuna mashirika kwa mfano ya UNICEF, kuna shirika La WHO (World Health Organization), tuna UN Women, tuna USAID, tuna Save the Children, hapa tuna akina taasisi zile zinazoshughulikia masuala ya kisheria. Kwa hiyo, kwa ufupi tuna taasisi nyingi ambazo tunashirikiana nazo katika kuhakikisha kwamba, tunapambana dhidi ya haya matukio ya udhalilishaji.

Mheshimiwa Spika, kuhusu vipi tunawawezesha hawa maafisa wa madawati; maafisa wa madawati tuna mambo mengi. La kwanza tuna mfumo maalum ambao upo kwa ajili ya uwezeshaji na ufuatiliaji wa matukio ya udhalilishaji, lakini pia tumekuwa tunawapa elimu ya kisheria, tunawapa elimu ya protections, tunawapa elimu ya kijamii. Elimu ambazo zinawasaidia wao kuweza kuchukua hatua pale tukio linapotokea, lakini zaidi tumeanzisha kwenye vituo pamoja na kwamba sio vyote, lakini vipo vituo ambavyo tumewawekea usafiri ambao huwa wanatumia kwa ajili ya kufuatilia hayo matukio mara tu yanapotokea. Nakushukuru.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Nimshukuru pia kaka yangu, Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa majibu mazuri yanayoridhisha na kutia moyo. Hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa kipato hicho ni kidogo, Serikali ina mpango gani wa kuongeza pato hili kwa pande zote mbili za Muungano na kuwasaidia wavuvi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kwa kuwa mgawanyo wa mapato ni wa kisheria, je, Wizara inawasaidiaje wavuvi kutoka Zanzibar wanaoleta samaki bara na wale wanaopeleka mifugo Zanzibar ili kuondoa kero na usumbufu unaowapata? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni jitihada gani za Serikali zinafanywa kuongeza pato hili kwa kuwa pato hili ni dogo. Kwanza naomba nimweleze Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote na Watanzania kwa ujumla, natoa shukrani nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita, Mama Samia Suluhu Hassan na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nane, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kuridhia mabadiliko ya sheria na kanuni ambazo zimekwenda sasa kufungua mwanya wa uwekezaji zaidi katika uvuvi wa bahari kuu. Hivi ninavyozungumza, tayari makampuni takribani 20 yameshakata leseni na kuingiza pato la zaidi ya shilingi bilioni moja kwa Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu; ni jitihada kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jitihada nyingine ambayo Serikali hizi mbili zimefanya ni kuhakikisha kwamba tunaweka kipengele ya uvutiaji kwa maana ya incentive. Tumeshatoa maelekezo kwa Mamlaka yetu ya Uvuvi wa Bahari Kuu kuitisha kikao ambacho kitatusaidia kuwaunganisha wadau wote kwa lengo la kwamba tuvitambue sasa vile vivutio ambapo tutawapa Waheshimiwa Mawaziri wawili; wa Jamhuri na yule wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, waweze kuvitangaza hadharani ili wawekezaji wajue iko fursa gani ya kuweza kuwekeza zaidi katika uvuvi wa bahari kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, baada ya hili la kuongeza kipato, ni nini tunafanya kuondoa vikwazo. Mambo makubwa mawili yanafanyika; hivi sasa timu zetu za wataalam kutoka Zanzibar na kutoka Bara zinakaa pamoja kujadili mambo makubwa mawili; la kwanza, ni leseni za wavuvi wa Zanzibar ziweze kufanya kazi hata huku Bara pia, lakini la pili ni kuondoa kikwazo kile cha mifugo inayotoka Bara kwenda Zanzibar na kulipiwa ushuru mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tupo katika hatua nzuri baada ya Wakurugenzi hawa kumaliza, watakaa Makatibu Wakuu na baadaye watakaa Waheshimiwa Mawaziri ili kufanya harmonization ya sheria hizi na hatimaye Watanzania wote wa Bara na Visiwani, waweze ku-enjoy rasilimali za Taifa letu. (Makofi)
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri yanayotia moyo. Lakini katika sentensi yake tu ya kwanza amesema ile ni Benki ya Maendeleo ya Kilimo na mimi nazungumzia wavuvi.

Sasa ninataka kujua, je, ni vigezo gani vinavyotumika ili hao wavuvi waweze kupata mikopo katika hiyo Benki ya Kilimo?

Swali la pili; ninataka kujua, kwa kuwa wavuvi wengi bado hawajapata elimu kuhusiana na mikopo hiyo; Je, Serikali ina mpango gani wa kuzungukia wavuvi hao ili wapate elimu waweze kunufaika na mikopo hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza kuhusu ni vigezo gani. Kwanza ni kuomba ama kama nilivyoeleza katika jibu la msingi, mtu mmoja ama kikundi, waombe kwa watoaji wa mkopo kwa maana ya benki. Tunashauri vikundi, hasa vya ushirika kwa kuwa ni rahisi zaidi kulingana na sera yetu kupata mkopo kisha benki watakapokuwa wameombwa wataeleza nini kimepungua na nini kinachohitajika ili mwombaji aweze kukamilisha utaratibu. Kwa hiyo namshauri Mheshimiwa Malembeka na wavuvi wote kutembelea katika mabenki mbalimbali na wanaweza kupata msaada wa kuelezwa ni nini hasa vile vigezo vinavyohitajika.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili la utoaji wa elimu ni endelevu na limekuwa likiendelea kufanywa wakati wote, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Malembeka ya kwamba tutaendelea kufanya kazi hii ya kutoa elimu kwa wavuvi wetu juu ya uvuvi endelevu katika Taifa letu na wenye manufaa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ameelezea jinsi gani walivyojipanga kutoa elimu ya kuondoa madhara ya uvuvi haramu; na mara nyingi uvuvi haramu hufanyika kwa vifaa duni na ambavyo siyo sahihi; na vifaa sahihi hupatikana kwa gharama kubwa; na wengi wanaofanya uvuvi haramu ni kwa sababu hawana vifaa vile: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kujua: Je, Serikali ina mpango gani ili kuinua kundi hili la wavuvi wadogo wadogo kiuchumi hasa katika Pwani yetu ya Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Angelina Malembeka kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze sana kwa kuwa amekuwa kila mara mstari wa mbele kwenye kuwasemea wavuvi hasa wavuvi wadogo wadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizi, ni kwamba mkakati wetu ni kuendelea kurekebisha sheria zetu na kuziboresha. Hili ni jambo la kwanza ili kusudi ziweze kuendana na wakati, maana wavuvi wamekuwa kila mara wanagundua zana mpya, zana ambazo labda wakati mwingine kwa upande wa sheria zetu tunakuwa nyuma ya teknolojia hizi ambazo wavuvi wamezigundua. Kwa hiyo, huu ni mkakati wetu wa kuhakikisha tunakwenda nao sambamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kurekebisha katika masuala ya kikodi. Tumekuwa tukifanya hivyo kila mara ili zana zetu ziweze kukidhi haja ya wavuvi kwa maana ya bei; na tatu ni mkakati wetu wa kuunda vikundi vya ushirika wa wavuvi na waweze kupata mikopo iliyo na riba nafuu kupitia Benki yetu ya Kilimo na hatimaye kuweza kuwasaidia kwenye kufanya shughuli zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge, tunayo dhana pana sasa ya uchumi wa blue ambayo tumedhamiria, Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kwamba tunahamasisha na kutangaza dhana hii ambapo katika ukanda wote mathalan wa bahari ya hindi tuweze kutumia ipasavyo rasilimali zote zinazopatikana ili kuweza kuwafanya wavuvi wetu wawe na kipato kinachotosheleza kwa ajili ya kaya kwa maana ya familia zao na kuweza kuwa na mchango mpana kwenye pato la Taifa letu.
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri yanayoeleweka na ambayo yamenijenga zaidi.

Mheshimiwa Spika, maswali yangu mawili ni kwamba; kwa kuwa fursa kwa watu binafsi ya kuanzisha ranchi, mashamba na bustani za wanyamapori imetolewa.

Je, hadi sasa ni watanzania wangapi wamepata fursa hiyo?

Swali la pili nilitaka kujua, kutokana na utaratibu huo hadi sasa hivi Serikali imepata faida kiasi gani? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa sasa jumla ya ma-butchery 71 ambayo yamekwisha sajiliwa na yanafanya kazi na kwa ujumla sasa siwezi kujua idadi lakini wamiliki ni pamoja na kuwa na leseni na kwa sasa hivi leseni zilizosajiliwa ni 71. Lakini pia faida zake tulizozipata ni pamoja na kupokea mapato jumla ya shilingi 229,500,000; lakini pia tumeweza kuongeza ajira kwa wananchi ikiwemo Madaktari wa Mifugo ambao wanapaswa kuajiriwa kwa kila mwenye butchery au shamba, bustani au ranchi ili kuwezesha hawa wanyama kupata huduma za kitabibu. Lakini pia tumeongeza ajira katika wahudumu wanao wahudumia hao wanyamapori ambao wapo katika ranchi hizo ama bustani. Ahsante. (Makofi)
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Halmashauri ya Manyoni ilitangaza nafasi au fursa ya kuwekeza kwenye Halmashauri yake hususan kwenye zao la korosho, lakini yale maeneo waliyoyapanga ndiyo njia kuu ya kupita tembo. Kwa hiyo, ukipanda, wakipita wanavunja, wakirudi tena wanakula yale majani. sasa nataka kujua Wizara hii lini itawasiliana na Halmashauri ya Manyoni ili wale ambao wamepata mashamba kwenye eneo lile ambalo ni njia ya tembo waweze kubadilishiwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwa na changamoto ya uvamizi wa wanyama wakali na waharibifu katika mashamba ya uwekezaji yaliyoko Manyoni. Tayari tumeshaanza kuimarisha doria kwa kuanzisha usimamizi wa doria kuzunguka mashamba hayo na tuna mpango sasa wa kuweka kituo ambacho kitakuwa ni kituo cha kudumu kwa ajili ya kudhibiti wanyama wakali na waharibifu.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza nampongeza kwa jibu lake zuri ambalo linaridhisha. Swali langu la kwanza; kwa kuwa deni hilo la wastaafu lilirithiwa kabla ya mpango maalum wa kufufua ATCL, nilitaka kujua sasa hivi Serikali ina mpango gani wa kuzuia kuzalisha madeni mengine mapya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kwa kuwa Serikali imejikita zaidi katika kutoa mafunzo mbalimbali katika vyuo vyake ikiwepo Chuo cha Usafirishaji, nilitaka kujua hadi sasa tuna marubani wangapi wazalendo ambao wako katika ndege zetu za ATCL? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nami niweze kujibu maswali mawili ya nyongeza, ya Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia masuala haya ya ATCL.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anataka kujua mpango wa kuzuia madeni mapya baada ya kuanza mpango ule wa ufufuaji wa kampuni hii yetu ya ndege nchini. Serikali imejipanga kuzuia ama kutozalisha madeni mengine. Hadi sasa tangu mwaka 2016 tumekuwa tukilipa wafanyakazi wote na hakuna deni jipya; lakini kwenye mwaka wa fedha huu 2022/2023 ambao tunaendelea nao tumetenga takribani kiasi cha shilingi bilioni 10 ili kulipa wafanyakazi wote waliokuwa wa ATCL kama deni la nyuma.

Mhehsimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili anataka kujua idadi ya marubani tulio nao hapa nchini hususan wanawake na wanaume. Tuna takribani ya marubani 106. Kati ya hao marubani 11 ni wanawake na marubani 95 ni wanaume; kwa maana ya kwamba hawa wanawake wanarusha ndege zote kwa sababu hapa nchini tuna ndege aina tatu ambapo tuna Dash 8Q400, Bombardier al maarufu Bombadier ama sasa hivi inaitwa DeHaveland lakini pia tuna Airbus 220-300 ambapo pia wanawake wanarusha na tuna Boeing 787-8 ambayo pia wanawake wanarusha hizi ndege. Na kati ya hao 106. 105 wote ni watanzania, ni mmoja tu ambaye sio Mtanzania.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri yenye ufasaha zaidi, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, katika majibu yake ameelezea uwezo wa gari pia uzima na usalama wa gari. Sasa hivi kuna magari mengi yanayobeba vinywaji baridi kusambaza madukani kumekuwa na utaratibu wa makusudi kuyapanua na kuyatanua magari yale kiasi kwamba hata dereva inabidi aweke nondo ili aweze kuipata ile site mirror vizuri. Je, Serikali ina kauli gani kuhusiana wamiliki wa magari hayo ambao wanapanua kwa makusudi magari hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili kwa kuwa pia ameelezea uzima na usalama wa magari, tuna magari mengi yanayobeba takataka lakini magari yale yenyewe ni sehemu ya takataka. Kama ni kweli yanakaguliwa kuangalia uzima wake na usalama, Serikali ina kauli gani kuhusiana na magari yanayobeba takataka ambayo yenyewe pia ni takataka? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Malembeka, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja kuhusu magari ya vinywaji baridi kupanuliwa kwa maana ya kuzidi uwezo wake wa kawaida, nadhani hili ni suala ambalo ni la viwango, tutashauriana na Wizara yenye dhamana ya Uchukuzi, na Wizara yenye dhamana ya Viwanda hili wanapokagua kwa maana ya TBS, magari yanavyoingia basi yazingatie uwezo na sura ya gari, sio ya upanuzi ambao unaathiri watumiaji wengine wa magari, kama alivyoeleza inatanuliwa mpaka site mirror zinaongezwa kiasi ambacho kinaleta usumbufu, ili watakapotoa viwango vile basi askari wetu wa usalama barabarani wanapotimiza wajibu wao wa kuona magari yanayostahili kuwa barabarani basi watasimamia kwa mujibu wa miongozo hiyo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu magari ya taka, ambayo amesema yenyewe ni takataka, nadhani nizielekeze mamlaka zinazoyaajiri magari haya kwa Mamlaka za Miji na Majini, wahakikishe kwamba wanateuwa wakandarasi wenye uwezo wa kutoa magari yanayofaa badala ya magari haya ya kubeba taka yenyewe yanakuwa sehemu ya uchafuzi wa miji yetu. Nashukuru.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri ya kutia moyo lakini pia nimpongeze Rais, Samia na Rais Mwinyi, kwa kutatua kero za Muungano hadi hadi kufikia 22 na kubakia kero nne. Swali langu ni kwamba kuna kauli gani ya Serikali juu ya kutatua hizo kero nne zilizo baki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Serikali imejipanga vipi kwa ajili ya utoaji elimu juu ya suala la Muungano kwa vizazi vijavyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwanza zinaendeleza ushirikiano ama zitaendeleza ushirikiano wa kuhakikisha kwamba changamoto zote zinazogusa kwenye Muungano zinatatuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukasema kwamba ili kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto hizi, ziko Kamati ambazo zimeundwa au iko Kamati ya majadiliano ya pamoja ambayo ndio inayosimamia utatuzi wa changamoto hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa kwamba pamoja na kwamba zipo changamoto zilizobakia lakini kwa kushirikiana na kamati hii tunakwenda kumaliza changamoto zote ili Muungano wetu huu saa uwe imara na uweze kudumu kwa muda mrefu. Kwa maana kwamba kuna Kamati za wataalam, Kamati za Makatibu Wakuu, Kamati za Mawaziri lakini kuna Kamati za Viongozi wakuu ambao hukaa kwa ajili ya kutatua changamoto hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa nimwambie Mheshimiwa kwamba baada ya kuwa tumetatua changamoto hizi, kinchofuata sasa ni kuwajulisha na kuwaeleza wananchi hatua tuliyofikia kama Serikali. Tumeanza na vyombo vya habari kuwaelimisha wananchi juu ya changamoto zilizokuwepo na zilizobakia. Kingine tumetoa tovuti maalumu www.vpo.go.tz wananchi wakienda hapo wanaweza kuona changamoto zilizotatuliwa na zile ambazo bado hazijatatuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya makongamano mbalimbali ambayo tumekuwa tukitoa elimu kuhusiana na masuala Muungano, nakushukuru.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza maswali mawili ya ziada.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Swali langu la kwanza kwa kuwa Madaktari Bingwa 2,098 wako katika sekta ya umma na Madaktari Bingwa 371 wako katika sekta binafsi; je, Serikali inawapatia marupurupu gani Madaktari Bingwa hao ili kulinda ajira zao wasiende sekta binafsi au nje ya nchi? (Makofi)

Swali langu la pili; Je, Serikali ina mpango gani wa kuweza kutambua taaluma bobezi ambazo huwa zinasomewa kwa muda mrefu, waweze kutambua bobezi hizo na kuweka mishahara mikubwa ili kuhamasisha watu waweze kusomea ubobezi huo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mawili mazuri.

Moja kwanza mpaka sasa kama ambavyo umeona hapa asilimia 75 ya Madaktari wako Serikalini na mpaka sasa Madaktari wengi na watumishi wengi wanapenda zaidi kufanyia kazi Serikalini, maana yake ni kwamba Serikalini kuna uhakika zaidi na incentive nyingi zaidi kuliko kwingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kama unavyojua kwamba Serikali inatoa incentive, mmemsikia Waziri wa Afya akisema kwamba tunatakiwa Madaktari wetu wamekuwa wakikimbia kwenye private sector wakati wa jioni wamekuwa wanafanya kazi, kwa hiyo sasa wameruhusiwa ndani ya hospitali zetu za umma wafanye private clinic humo humo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niweke vizuri pamoja na hayo yote ambayo Serikali inafanya bado tunafikiri tunahitaji wawe umma lakini pia wawe private sector, kwa hiyo pande zote mbili Madaktari wetu tungefurahi wakafanya kazi sehemu zote, wawe private sector wengine wawe public sector. Tungefurahi wafanye kote kwa sababu kote wanamhudumia Mtanzania yuleyule.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ni Je, Serikali inafanya nini kwa wale wanaosoma muda mrefu. Mheshimiwa Waziri wa Afya alipeleka hilo tatizo kwa Mheshimiwa Rais wetu. Mheshimiwa Rais wetu na ameshatoa maelekezo tukae na utumishi ili kujadili kuona Madaktari ambao wanasoma muda mrefu ni kwa namna gani utumishi wakaweka incentive au kuongeza mshahara kulingana na ule muda wanaosoma ili wengi wavutiwe kusoma masomo hayo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais wetu ameshatoa maelekeo ya kutatua tatizo hilo. (Makofi)
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali yanayotia moyo na kuonesha jinsi gani Serikali ina wajali wavuvi. Maswali yangu mawili ya ziada ni kama ifuatavyo: -

Swali la kwanza; je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu ya mikopo kwa wavuvi wadogo ili iende sambamba na mafunzo ya uvuvi wa kisasa?

Swali langui la pili; je, Serikali imejipangaje kuhakikisha masharti ya mikopo hiyo haiwakwazi na kuwabana wavuvi wadogo? Ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nami pia nimpongeze Mheshimiwa Mbunge Angelina Adam Malembeka kwa maswali mazuri na ya msingi.

Kwanza nimwondoe shaka kwa sababu haya ni maelekezo ambayo tumepewa na Marais wetu wawili, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Mwinyi kwamba kabla ya mikopo hiyo ni lazima sasa tuwapatie watu elimu ambayo itawasaidia kutumia kwa usahihi mikopo hiyo ambayo itatolewa, kwa hiyo jambo hilo tutalitekeleza kabla mikopo hiyo kuwafikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la masharti, jambo hilo ndio la msingi ambalo sasa hivi tumekuwa tukifanya kwamba tumepunguza masharti kwa kiwango kikubwa na asilimia kubwa ya hii mikopo haina riba, ni mikopo ambayo tunawawezesha tukianza na kuwapatia utaalam wa kisasa, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia fursa ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri yanayoridhisha.

Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza; je, Serikali imejipangaje kuhusu kulipa mafao ya wastaafu ambao hawajapata mafao hayo nikitolea mfano Wafanyakazi wa Shirika la Ndege Tanzania?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; je, ni hatua gani mnachukua kwa waajiri ambao hawalipi michango ya wanachama kwa wakati? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Malembeka kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na malipo au ucheleweshaji wa mafao tayari kwenye hatua hiyo tumeshavuka. Mpaka sasa mifuko yetu PSSSF pamoja na NSSF tayari tumekwishakuanza utaratibu wa ulipaji kupitia mfumo wa teknolojia ya TEHAMA ambapo wanachama wote wanapewa hata taarifa sasa kupitia simu za mkononi au simu ya kiganjani na yeyote yule ambaye amekuwa amecheleweshewa kupata mafao yake tumekuwa tukichukua hatua hasa katika kuhakikisha kwamba tunapata nyaraka zao sahihi na kwa wakati ili waweze kuweza kulipwa.

Kwa hiyo, wachache sana ambao wanapata changamoto hizo kwa sasa na ikitokea changamoto hizo zinatokea tumekuwa tukiwaomba aidha kupitia Mheshimiwa Waziri ambaye alizunguka Mikoa karibia nchi nzima kwa kupitia kikanda kwenye majiji alikutana na wastaafu na tumekuwa tukipokea na tuna desk maalum la kupokea changamoto hizo. Kwa hiyo, kama zipo nimuombe Mheshimiwa Mbunge anifikishie ikiwa ni pamoja na za ATCL kwa taarifa tulizonazo ofisini tayari wapo walikwishakulipwa zaidi ya wafanyakazi 500 na wale wachache ambao walikuwa wana changamoto ilikuwa ni kuhusiana na taarifa sahihi hazikuweza kuwasilishwa ofisini ili waweze kulipwa. Kama watakuwa wamepata nyaraka na taarifa sahihi tuko tayari kuweza kuwalipa mafao yao.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la waajiri kutokuwasilisha michango kwa wakati. Mifuko hii inazo sheria ambayo inaianzisha na katika sheria hizi zinaeleza ni kosa kwa mwajiri kutokuwasilisha michango kwa wakati katika mifuko hii kwa ajili ya wanachama na ikitokea hivyo hata mahakamani Bunge lako tukufu lilitunga sheria hii kwa kujua umuhimu wa watu hawa ni katika mfumo wa summary suit. Kwa hiyo, unapelekwa mahakamani, hakuna kujitetea na tunachua hatua.

Kwa hiyo, kama kuna maeneo ambayo watakuwa wamechelewesha michango kwa kweli nitoe rai kupitia Bunge lako tukufu kwamba tunawataka waajiri wote nchini kutekeleza hilo, kupeleka michango kwa wakati ya wanachama ili wasisumbuke, lakini pia sisi pia kutupunguzia mashauri yaliopo mahakamani, mpaka sasa tuna mashauri zaidi ya 26 na tumechukua hatua, ahsante.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri ambayo yametuwekea kumbukumbu kwamba, mara ya mwisho tulibadilisha fedha mwaka 1997 lakini jibu langu bado sijalipata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, ni mara ya kwanza kupata Rais Mwanamke Tanzania na Afrika Mashariki, ambaye ni mchapa kazi, jasiri na ameonyesha uwezo wa wanawake. Ambaye ameweza kutupa sifa Tanzania, Afrika na dunia nzima. Je, Serikali haioni kwamba, sasa ni wakati mwafaka wa kuweka sura ya Rais wa Kwanza Mwanamke katika Noti za Tanzania? (Makofi)

Swali langu la pili, kwa kuwa, Rais wa Kwanza wa Zanzibar amepewa nafasi katika sarafu ya Shilingi 500 na kutokana na kupanda kwa uchumi sasa hivi, Shilingi 500 haitumiki sana. Je, Serikali haioni kwamba sasa hivi ni fursa pekee ya kupandisha pia hadhi ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar, kumuongezea noti juu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Angelina kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala hili zipo taratibu mbalimbali ambazo hutumika katika uwekaji wa alama kwenye noti zetu au sarafu yetu. Hizi lazima zizingatie kufuata Taratibu, Sheria na Kanuni. Muda wa suala hili ukifika basi, maoni yake tumeyachukua na tunaenda kuyafanyia kazi. Muda ukifika zitawekwa, Inshallah. (Makofi)