Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Anastazia James Wambura (38 total)

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nipende kumkumbusha kwamba tunasema wasanii na wanamichezo wenye asili ya Kigoma, siyo wakazi wa Kigoma. Mrisho Mpoto mimi nazungumza naye, asili yake ni Kigoma ila amehamia Songea. Hata akina Diamond nao ni watu wa Kigoma lakini wanaishi Dar es Salaam. Nilitaka tuweke rekodi sawasawa maana huwezi kuwa msanii mzuri kama asili yako siyo Kigoma.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili madogo ya nyongeza. La kwanza, hii Sera ya mwaka 1999 ambayo inatamka dhahiri kwamba hizi Theater Centers zitajengwa Makao Makuu ya nchi, je, Mheshimiwa Waziri huoni kwamba sera hiyo imepitwa na wakati kwamba vijana wengi wako kwenye Majiji, Halmashauri na Manispaa zetu? Ni lini Serikali itaiangalia upya sera hiyo ambayo kusema kweli imepitwa na wakati kabisa hasa Sura ile ya Nne ambayo inasisitiza kwamba hizi Theater Centers zitajengwa katika Makao Makuu ya nchi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, niendelee kushukuru kwamba Mheshimiwa Waziri amekiri Kigoma imetoa mchango mkubwa na kwa kweli wasanii wale wengi wao wanatoka Kigoma, Kibondo na Uvinza. Napenda kujua ni kwa nini basi Wizara isitoe mwongozo technical kwa Wakuu wetu wa Mikoa na Ma-RAS wetu ili wajue kwamba sasa wakati umefika hizi Theater Centers zijengwe katika Halmashauri na Manispaa zetu zote katika nchi yetu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, WASANII NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Nsanzugwanko kwa jinsi anavyoshirikiana vizuri na wasanii. Vile vile tunathamini mchango mkubwa wa Waheshimiwa Wabunge wote katika kuitetea na kuwa mstari wa mbele kuboresha tasnia ya sanaa.
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ambalo linasema kwamba sera hii imepitwa na wakati, ni kweli tunakubali kabisa kwamba sera hii kwa namna moja au nyingine imepitwa na wakati. Kwa hiyo, kwa hivi sasa napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba Wizara yangu imeshaandaa Rasimu ya Utamaduni na imeshaiwasilisha katika ngazi za juu za maamuzi.
Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali inapongeza sana kazi za wasanii na hasa kwa jinsi wanavyojishughulisha na masuala ya kijamii. Tumekuwa tukiwaona wasanii kama Mrisho Mpoto na wenzake wakijishughulisha na kampeni za kuhamasisha usafi katika Majiji yetu. Kwa sababu hiyo basi tumeona pia kuna umuhimu wa kufanya maandalizi ya Sera ya Sanaa.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ambalo linataka Serikali itoe mwongozo kwa mikoa, tunakubaliana nalo kabisa kwamba tutatoa mwongozo huu. Pia napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba kupitia Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), Wizara inaendelea kutoa wataalam waliokamilika katika fani za sanaa na utamaduni ikiwemo utaalam wa uandaaji wa Majumba ya Sanaa. Hata hivyo, Wizara hii pia ipo katika mazungumzo na TaSUBa ili tuweze kuona ni namna gani tunaweza kutoa mafunzo nje ya kituo hiki.
Mheshimiwa Spika, napenda nichukue nafasi hii kuziomba Halmashauri zote ziajiri Maafisa Utamaduni. Ahsante.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Waziri kwa majibu yake mazuri na kwa mara ya kwanza Wizara hii imeonesha uhalisia wake kwa kutoa majibu kwa vitendo nawapongeza sana.
Pamoja na majibu haya mazuri ya vitendo, Halmashauri ya Jiji la Mwanza kama ambavyo imekuwa ikishiriki kwa asilimia kubwa katika kuboresha michezo, tayari imeshaandaa ramani ya uwanja mzima na imeshaanza kupita ngazi mbalimbali. Ninataka kupata tu maoni kutoka kwenye Serikali kwamba uwanja huu pamoja na kwamba utakuwa umetengenezwa eneo la kuchezea, lakini bado tutakuwa na changamoto kubwa katika eneo la mzunguko mzima kwa ajili ya kupata vyumba vya wachezaji kubadilishia nguo, lakini jukwaa kuu na maeneo ya kukaa ili uwanja ukamilike na kuwa uwanja wa kisasa. (Makofi)
Je, ni lini Serikali itakuwa tayari kusaidia Halmashauri ya Jiji la Mwanza kuhakikisha uwanja wa Nyamagana unakuwa ni wa kisasa na ambao unaweza kutumika na mechi za Kimataifa? (Makofi)
Swali dogo la pili tayari vifaa vimeshafika, ni lini ….
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Stanslaus naomba hilo swali la pili ufupishe kwa sababu la kwanza umelifanya refu.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini TFF waithibitishie Wizara watakuwa tayati kukamilisha uwanja huu maana tumesubiri sana na tunahitaji kuutumia haraka tunavyoweza? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi ambavyo amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba uwanja huu wa Nyamagana unakarabatiwa.
Katika kufuatilia tumebaini kwamba Mheshimiwa Stanslaus Mabula alipopata nafasi ya kuwa Meya tu mwaka 2012 Septemba alihakikisha kwamba anaondoa urasimu wa utoaji wa pesa mwezi Disemba, 2012 na mwaka 2013 mchakato wa kuanza kuagiza nyasi bandia ulikamilika, kwa hiyo nampongeza sana na ninaomba Waheshimiwa Wabunge tuige mfano wa Mheshimiwa Mabula. (Makofi)
Swali lake la kwanza ambalo ametaka kujua kwamba ni vipi sasa wanaweza wakakamilisha ule mzunguko mzima wa uwanja, nimhakikishie tu kwamba Wizara yangu ipo tayari kutoa ushirikiano (technical support) ili kusudi kuweza kuona kwamba ni jinsi gani sasa vile vyumba au eneo lote linaweze likazunguka, ikizingatia kwamba ni lazima kuwepo na facilities kama za vyumba za kubadilishia nguo na vyumba vya waandishi wa habari pamoja na vyumba vya matibabu ili kusudi uwanja huu uweze kukidhi viwango vya Kimataifa. Kwa hiyo, kupitia BMT Wizara yangu itatoa ushirikiano wa karibu sana na ninaomba Halmashauri pia iwe karibu na BMT.
Swali lake la pili sasa kwamba ni lini uwanja huu utakamilika, niseme tu kwamba Serikali inafanya kazi kama timu, kwa sababu nimeshatoa wito mkandarasi afanye kazi haraka, ninaomba Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Mwanza washirikane na Halmashauri, washirikiane na TFF ili kumsimamia mkandarasi huyu aweze kukamilisha haraka ujenzi wa uwanja huu.
MHE. HAFIDH ALI TAHIR: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu ya Naibu Waziri lakini nina swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila mwaka Shirikisho la Mpira la Ulimwengu (FIFA) huwa linatoa goal project kwa nchi kadhaa wanachama wa Shirikisho hilo. Tanzania tumekuwa tukipata goal project za viwanja mara nyingi;
Je, Mheshimiwa Waziri atakubaliana nami sasa wakati umefika kuishawishi TFF pale walipopata goal project basi safari hii uwanja kama huu wa Mwanza wa kuweka nyasi bandia uelekee Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba FIFA huwa ina goal project na inatoa support ya ujenzi wa viwanja kwa kuweka nyasi bandia kupitia TFF, napenda kumtaarifu Mheshimiwa Hafidh Ali kwamba uwanja wa Gombani uliopo Pemba tayari umeshapata msaada wa kuwekewa nyasi bandia kupitia ufadhili wa FIFA. (Makofi)
Hata hivyo hii haizuii kuna vigezo pia ambavyo vinatakiwa kufuatwa ili kusudi FIFA iweze kutoa ufadhili huu. Kigezo kimoja wapo ni kwamba uwanja ni lazima uwe wa Halmashauri, pia uwe ni uwanja ambao unaweze kuchezesha mechi za Kimataifa, vilevile wahusika wa uwanja huu wawe tayari kuchangia asilimia 16. Ahsante sana.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri kwa mpango huu wa hizi nyasi bandia zinazotolewa, je ni mpango wa kila Mkoa na kama ni kila Mkoa, je, ni lini Mkoa wa Simiyu mtatupa uwanja wa namna hii? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na uwanja wa Simiyu vigezo ni kama nilivyovitaja kama uwanja huu ni wa Halmashauri na unakidhi vigezo vya kuwa wa Kimataifa, goal project inaweze ikasaidia, lakini utaratibu ni kwamba TFF inaandika orodha ya viwanja vitano na kuandika details zake na vinapofika FIFA wao wanateua kulingana na ushindani wa kukidhi vigezo vya kutoa msaada. Ahsante.
MHE. COSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza nakubaliana na agizo la Serikali kwenye sentensi nne za jibu lake za mwisho, lakini sikubaliani kabisa na majibu aliyoyatoa na sababu za msingi ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kanuni za Mpira kabla ya adhabu yoyote kutolewa Chama cha Mpira (TFF) kinasubiri taarifa ya Refa na taarifa ya Kamishna au Msimamizi wa Mechi. Taarifa hizo mpaka wakati Rais wa TFF ana-twit, dakika ya 80 mechi inaendelea, alikuwa hana mezani, ni wakati gani Waziri ananiambia Rais huyu alitumia Kanuni? (Makofi)
Swali langu la pili; baada ya adhabu hii baadhi ya wanamichezo wamefungiwa maisha kwa tuhuma kwamba, palikuwa na makosa ya rushwa ambayo ni makosa ya jinai. Tunavyo vyombo ambavyo vinachunguza rushwa na ni kosa la jinai, ni uchunguzi gani ambao vyombo vya jinai vilitoa kwa sababu vilipewa agizo la kuchunguza suala hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Kanyasu kwa jinsi ambavyo anajitahidi kutetea timu yake ya Geita Gold Sports.
Mheshimiwa Mwenyekiti, alitaka kujua wakati ambao vikao hivi vilikaa, swali la kwanza hilo. Kama nilivyosema katika jibu la msingi vikao hivi vilikaa baada ya kupata malalamiko kutoka timu za Kundi „C‟ na ndipo vikao vikakaa, lakini Rais wa TFF alichukua tahadhari, sio kwamba, alitoa maamuzi, alikuwa anatoa tahadhari. Vikao vilivyofanya maamuzi ni vile ambavyo vilikaa baada ya kupata malalamiko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali lake la pili ni kwamba, ni ruksa kwa mtu binafsi au taasisi au timu kukata rufaa kwa kutumia taratibu ambazo zipo. Ahsante.

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Costantine John Kanyasu Mbunge wa Geita, naongezea katika majibu ya Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya kwanza, kama alivyosema Naibu Waziri, maelezo aliyoyatoa Mheshimiwa Mbunge na tuliwahi kuyatoa hapa Bungeni, tukasema wale ambao hawakuridhika na uamuzi uliofanywa na TFF, TFF uamuzi wao siyo wa mwisho, wafuate taratibu na watumie hayo ambayo wanaona ni upungufu katika uamuzi uliofanyika kukata rufaa. Sehemu ya kwanza hii, watumie nafasi hiyo wakate rufaa na Serikali tutasimamia haki yao ipatikane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili, ni kweli katika mchakato huu kuna tuhuma nyingi za rushwa na niliwahi kusema hapa Bungeni, tuhuma zile waliotuhumiwa sio wadogo wa chini peke yake ni pamoja na wa katika mhimili wenyewe unaosimamia soka. Hivi tunavyoongea chombo ambacho kinahusika na suala la rushwa, TAKUKURU wanakamilisha kazi yao ya uchunguzi, wakikamilisha na kama kutakuwa na watu watabainika kuhusika na rushwa hatua za Kisheria zitachukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni kuthibitisha kwamba, Serikali ya Awamu ya Tano imekusudia kufuta suala la rushwa kwenye michezo kwa sababu linatafuna na kuharibu michezo yetu.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza. Upo ushahidi wa matumizi yasiyo sahihi ya lugha ya Kiswahili miongoni mwa viongozi wa Serikali na miongoni mwetu Wabunge. Kwa sababu Bunge na viongozi wa Serikali ni miongoni mwa makundi ya jamii na taasisi zenye wajibu wa juu kabisa wa kulinda lugha hii na kwamba inaashiria tatizo hili haliko kwenye vyombo vya habari tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali inasema nini kuhusu upana wa tatizo hili hasa kwa wakati huu ambapo inatengeneza sera hiyo?
Pili, kwa sababu matumizi, kwa mfano ya neno “hichi” badala ya “hiki,” “nyimbo hii” badala ya “wimbo huu,” uchanganyaji wa lugha ya Kiingereza kwa kiwango kilichokithiri kwenye sentensi za Kiswahili, vinakera. Tunaomba kujua ni lini sera hii inakuja kudhibiti hali hii inayoendelea? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Oscar Mukasa, Mbunge wa Biharamulo kwa jinsi ambavyo amejitahidi kuonesha ukinara katika kuikuza lugha ya Kiswahili. Naomba kujibu maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kumekuwepo na matumizi ambayo siyo sahihi ya lugha yetu ya Kiswahili na wengi tumekuwa tukishuhudia kwa mfano “hiki kikao” wengine husema “hichi kikao,” “hiki kitu”, “hichi kitu” na pengine kama alivyosema katika maelezo yake kwenye swali lake la msingi, ni kwamba hata watoto kwa sasa ukifuatilia utaona, “hiki kitu” kwa sababu tunatumia “hichi kitu,” sasa na wao wameanza kusema “hiko kitu.” Wameibadilisha, badala ya “hiki kitu,” sasa wanasema “hiko kitu.”
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile siyo katika Kiswahili tu, watu wamekuwa wakichanganya Kiingereza, lakini hata lugha zetu za asili vilevile wamekuwa wakichanganya Kiingereza. Kwa mfano, unaweza kumsikia mtu anasema “infact kwa kweli angambila nshomile.” Haya ni maneno ambayo yamekuwa yakichanganywa katika lugha za asili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wito wa Serikali ni kwamba tulinde Kiswahili na pia tulinde lugha zetu za asili kwa sababu zile lugha za asili ndipo tunapoweza kupata maneno ya kuongeza kwenye Kiswahili pale ambapo tutakuwa hatuna maneno mbadala ya Kiingereza. Kwa hiyo, tulinde lugha zetu zote, lugha ya Kiswahili na pia lugha ya asili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuongezea tu ni kwamba Serikali ipo tayari kupitia BAKITA kuja kutoa semina katika Bunge hili ili kusudi tuweze wote kwa pamoja kufuatilia na kutumia lugha ya Kiswahili kwa ufasaha. Nalisema hili kutokana na kwamba kuna visababishi ambavyo vinapelekea matumizi yasiyo sahihi au visababishi ambavyo vinaweza kumwezesha mtu atumie lugha ya Kiswahili kwa ufasaha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, katika nchi za Afrika Mashariki wanaotumia lugha ya Kiswahili kama lugha ya asili ni watu wapatao milioni mbili hadi milioni 15 kwa mujibu wa takwimu. Lakini wengi wao kuanzia milioni 50 hadi milioni 150, wengi wanatumia Kiswahili kama lugha ya pili. Kwa hiyo, wakati mwingine inatokea tafsiri ya lugha zile za asili kwa Kiswahili.
Vilevile kuna kisababishi kingine ambacho ni jinsi gani ile lugha ya asili inashabihiana na lugha ya Kiswahili. Kwa mfano, Kiswahili kina „r‟ na kina “l” lakini zipo lugha ambazo hazina „r‟ na hazina „l‟. Kwa mfano, kuna lugha moja ya asili isiyokuwa na „r‟, akitaka kusema „anataka kula‟ anasema „nataka kura‟ na mwingine akisema naomba kura anasema „naomba kula.‟ Kwa hiyo, hivi ni visababishi ambavyo vinapelekea matumizi sahihi au yasiyo sahihi kwa lugha ya Kiswahili.
Jambo lingine ni dhamira ya mtu ya kutaka kuwa kinara katika kutumia lugha ya Kiswahili. Kwa mfano, tunavyomwona Mheshimiwa Rwegasira, yeye ana dhamira ya kutakakuwa kinara. Kwa hiyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge na viongozi tuwe na hii dhamira.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni ile tabia ya kujisomea vitabu vya Kiswahili, magazeti, kamusi pamoja na kutumia miongozo mbalimbali. Hivi vyote hupelekea mtu kuweza kuongea Kiswahili kwa ufasaha.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili linahusiana na Sera ya Lugha…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa naomba ufupishe kidogo jibu linalofuata.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yetu inaendelea kukusanya maoni ya wadau kuhusiana na Sera ya Lugha ili kusudi kuweza kupata changamoto ambazo zinaikabili lugha yetu ya Kiswahili, lakini vile vile kujua ni jinsi gani tutazingatia masuala mbalimbali katika Sera ya Lugha na hivyo katika kipindi cha mwaka huu wa fedha 2016/2017 tunatarajia kwamba rasimu ya kwanza ya Sera ya Lugha itakuwa imekamilika na hivyo tuipeleke katika hatua za juu kwa ajili ya maamuzi.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na mimi kwa kuniona. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri wa Utamaduni, kuna baadhi ya nyimbo zinazoimbwa katika ma-stage show au zinazooneshwa katika runinga. Nyimbo hizi huwa zinatudhalilisha wanawake kuvaa yale mavazi yao ambayo yanaonesha, je, Serikali inazingatia suala hili au kisheria ni sawa kuimba nyimbo kama zile zinazotudhalilisha sisi wanawake?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kuhusiana na nyimbo ambazo zinadhalilisha wanawake ni swali jipya naomba alilete vizuri ili kusudi tuweze kulijibu vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunavyo vyombo ambavyo vinasimamia kwa kupitia sheria zetu. Tuna Bodi ya Filamu ambayo huwa inaangalia, inapitia maudhui yenyewe kama ni ya filamu au wimbo, lakini pia tuna Kamati ya Maudhui ambayo ipo chini ya TCRA. Kwa hiyo, kwa kutumia sheria zetu tunadhibiti hali kama hii. Vilevile wale ambao wanaona kwamba hali hairidhishi, tunaomba wawasilishe ni wimbo upi au ni filamu ipi ili kusudi hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ufasaha wa lugha yoyote ile ni ajira na Kiswahili ni kimojawapo. Tanzania ni kitovu cha lugha ya Kiswahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kufahamu Wizara ina mkakati gani wa kufunza na kutoa walimu wengi ambao wanaweza kupelekwa nchi mbalimbali, kwa mfano, Uganda, Rwanda sasa hivi wameanzisha Kiswahili kwenye shule zao na ninaamini Watanzania ndio wenye lugha fasaha ya Kiswahili. Je, kuna mkakati gani kufundisha walimu wa kutosha wa kuweza kuwapeleka nchi mbalimbali ambao wanazungumza Kiswahili na kutoa ajira kwa wananchi wetu? Ahsante.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kwamba kitovu cha Kiswahili ni hapa nchini kwetu Tanzania na kwa kulitambua hili, nchi za Afrika Mashariki wameamua Makao Makuu ya Kiswahili yawe hapa nchini na yamepelekwa Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo mafunzo ambayo yamekuwa yakitolewa na tumekuwa tukizalisha Walimu wa Kiswahili wengi kadri inavyowezekana; na siyo tu kuwazalisha, lakini kuwatafutia soko na wamekuwa wakipata masoko siyo tu katika Afrika na Afrika Mashariki, lakini hata nje ya nchi yetu na hasa China wamekuwa wakienda kwa wingi sana. Chuo Kikuu cha Zanzibar, kwa mfano SUZA, wamekuwa wakizalisha Walimu wengi sana wa Kiswahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia huu mchakato sasa wa utengenezaji wa Sera ya Lugha ambao utaipa nguvu kubwa Kiswahili kama lugha ya nchi yetu, tutaweka mikakati ya kutosha ndani mle na sheria baada ya sera kukamilika ambayo itatusaidia zaidi kukifanya Kiswahili kiendelee kuwa bidhaa na hivyo kuwapa soko kubwa walimu ambao tutakuwa tukiwazalisha nchini kwetu.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja
na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwanza nieleze masikitiko yangu
kwamba yaani kumbe mpaka leo Bodi haina tovuti, 2017, this is very bad, ni
jambo la kusikitisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niende kwenye swali langu la kwanza la
nyongeza, nimeona muainisho wa hizo gharama, wasanii wanapokwenda
kusajili, pamoja na hizo gharama lakini wanalazimika kwenda kupata huduma hii
Dar es Salaam tu haitolewi katika maeneo mengine. Wakishapata hii huduma ya
kutoka BASATA kusajili COSOTA na Bodi ya Filamu, kuna huduma nyingine
kwenda TRA ili wapate stika ambayo ni mapato na stika zinatolewa tu Makao
Makuu ya TRA Dar es Salaam. Je, Serikali iko tayari kuhakikisha kwamba angalau
Ofisi hizi za BASATA, COSOTA na Bodi ya Filamu zinakuwepo hata katika ngazi ya
mikoa ili kuwarahisishia wasanii na kuwapunguzia gharama? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuna hizi filamu za kutoka nje
maarufu sana kwa jina la mazagazaga kwa sababu unakuta wametandika chini
zimezagaazagaa, gharama yake maximum kwa CD moja ni Sh.1,200 lakini
hazitozwi gharama zozote za usajili wala hakuna mapato yoyote ambayo Serikali
inapata. Kwa kulinda kazi za ndani za wasanii wetu wa filamu wa ndani ambao
CD zao sasa zimeshuka thamani hadi Sh. 2,000 halafu wanashindana na za nje za
Sh.1,200 na Serikali inakosa mapato, je, inasemaji katika kudhibiti filamu hizi za
kutoka nje, imeshindwa kabisa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa
Naibu Spika, swali la kwanza anataka kujua kama kuna utaratibu wowote
ambao Serikali imefanya ili wasanii waweze kupata vibali kutoka mikoani.
Ninachoweza kusemea ni kuhusiana na Bodi ya Filamu, kama nilivyosema awali,
Bodi ya Filamu tayari inazo ofisi katika Wilaya na Mikoa na kule kuna Bodi za
Filamu za Mikoa na Wilaya ambapo RAS kwa upande wa Mkoa ndiye Mwenyekiti
na Afisa Utamaduni ndiye Katibu na kwa upande wa Wilaya DAS ni Mwenyekiti
na Afisa Utamaduni wa Wilaya ni Katibu na kuna wajumbe wengine katika Bodi
hizi. Kwa hiyo, vibali vinatoka pia katika wilaya na mikoa na siyo lazima wafuate
huduma hizi Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa TRA zipo ofisi za mikoa lakini
upande wa COSOTA sina uhakika sana. Hata hivyo, tunafanya mazungumzo na
vyombo vyote hivi ambavyo vinadhibiti wizi wa kazi za wasanii na wajumbe wake
wote ni wajumbe wa Kamati ya Urasimishaji na hivyo basi, tunafanya kila jitihada
ili tuweze kuona tunamkomboa msanii kuanzia ngazi za wilaya, mkoa na hata
makao makuu Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa BASATA, mpaka sasa tunataka
kufanya utaratibu wa usajili kwa njia ya mtandao pamoja na Bodi ya Filamu.
Hivyo, niwahakikishie wasanii kwamba huduma hizi zitafikishwa kwao na
watakuwa hawapati usumbufu sana kufika Dar es Salaam kwa sababu
tunawatakia mafanikio.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa filamu za nje, nadhani wengi
tumekuwa mashahidi kwamba Serikali inafanya kila jitihada. Zoezi la urasimishaji
lilianza tangu mwaka 2009 ambapo kazi za wasanii zilianza kuwekewa ushuru wa
stempu tangu mwaka 2013 kwa Sheria ya Ushuru wa Stempu. Kwa zile kazi
ambazo zinatoka nje na hazifuati utaratibu zimekuwa zikikamatwa na wahusika
kuchukuliwa hatua. Napenda kuwatangazia kwamba zoezi hili ni endelevu,
tumekuwa tukifanya msako au opereshenitangu 2014 hadi 2016 na tunaendelea.
Hivyo, nawaomba wote ambao wanauza kazi za wasanii nje ya utaratibu
wafuate utaratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu
Spika, nakushukuru. Nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini pamoja na
majibu yake mazuri, naomba kuongezea kwenye sehemu ya pili ya swali la
Mheshimiwa Cosota Chumi. Ni kweli tatizo la kazi za sanaa kutoka nje katika nchi
yetu ni kubwa na baya na linaua kwa kiasi kikubwa kazi za sanaa za ndani. Ili
kushughulika na tatizo hili kuna sheria za vyombo zaidi ya vitano zinahusika. Kuna
Sheria za TRA, BASATA, Bodi ya Filamu, COSOTA, ukizijumlisha zote kwa pamoja
ndiyo at least unaweza kushughulika na tatizo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inapitia upya sheria hizi na kuangalia
upungufu uliopo, turekebishe na tuzi-harmonise kwa pamoja ili tuweze kulimaliza
tatizo hili. Kwa sheria zilizopo, namna ya kushughulika na tatizo hili bado ni ngumu
sana. Kwa hiyo, tunachoweza kuahidi hapa ni kwamba tunazipitia na tuko
mahali pazuri na tukilikamilisha zoezi hilo kazi hii itakuwa imekwenda vizuri na kwa
hiyo tutapambana na tatizo hili la piracy kwenye nchi yetu.
MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu hivi sasa imekuwa soko holela la kazi za wasanii ambazo zinaingizwa kiujanja ujanja
bila kufuata taratibu wala Serikali yetu kupata kodi kwa mujibu wa sheria, pia wasanii wengi wana malalamiko makubwa kwamba kazi zao zinazotumiwa na makampuni ya simu hawalipwi ipasavyo. Vilevile, wasanii wana
manung’uniko mengi kwamba kazi zao za sanaa wanapokwenda kuziuza wanadhulumiwa na wanapewa kwa bei chee. Je, ni lini sasa Serikali itaamua kuleta mabadiliko ya sheria hizi ambazo Naibu Waziri amezitaja, Sheria Na. 7 ya Mwaka 1999, Sheria Na. 4 ya Mwaka 1976 na Sheria Na. 23 ya Mwaka 1984. Sheria hizi zote zinaonekana zina miaka mingi haziendi sawa na mabadiliko ya kasi yanayokwenda katika sanaa yetu Tanzania. (Makofi) Swali la pili; je, Mheshimiwa Naibu Waziri, yuko tayari kuambatana nami kwenda kukaa na wasanii ili tuwasikilize matatizo yao na tuweze kushirikiana nao ili kuwapatia ufumbuzi na kuhakikisha kazi zao zinaleta tija kama ilivyokuwa kwa wasanii wa nchi nyingine?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kama alivyosema ni kweli
kwamba sheria zetu hizi zinazohusiana na usimamizi wa masuala ya sanaa na wasanii kwa ujumla zimepitwa na
wakati, kwa sasa tunachokifanya ni kuandaa sera kwanza kwa sababu tulikuwa hatuna Sera ya Sanaa, tulikuwa na Sheria ya Filamu lakini hatukuwa na Sera. Kwa hiyo, kwa sasa tunaandaa Sera ya Filamu na vilevile tunaandaa Sera ya Maendeleo ya Sanaa.
Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilisha sera hizi ambapo Sera ya Filamu tunatarajia kufikia mwishoni mwa mwezi wa Sita tuwe tumekamilisha kuandaa rasimu yake na baada ya kukamilisha sasa tutahuisha hizi sheria ili kusudi ziweze kuendana na wakati.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili; kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru na niseme kwamba tuna kila
sababu ya kumshukuru Mheshimiwa Rais na kumpongeza kwa kuanzisha Idara ya Sanaa katika Wizara yetu. Nia hasa ni kuhakikisha kwamba tunaongeza kasi ya maendeleo ya tasnia ya sanaa.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kuambatana naye kwenda katika Jimbo lake, nimekubaliana na hili. Hata hivyo
napenda kumjulisha kwamba Wizara yetu imeanzisha utaratibu kupitia utaratibu wa wadau tuzungumze. Kila
Jumanne tunaongea na wadau wa sekta zetu nne; Sekta ya Habari, Sekta ya Sanaa, Sekta ya Utamaduni pamoja na Sekta ya Michezo. Kwa hiyo, huwa tunaongea na wadau ili kupata changamoto na kupanga ni jinsi gani tuweze kutatua changamoto hizi.
Mheshimiwa Spika, hivyo nichukue nafasi hii kuwaalika wasanii wote pale ambapo tutakuwa tukizungumzia masuala yao siku ya Jumanne fulani kwa mwezi basi waweze kuhudhuria pale Dar es Salaam na hapa Dodoma. Maalum kwa Jimbo lake la Kinondoni, Wizara yangu iko tayari na binafsi niko tayari kuambatana naye ili tuweze kusikiliza matatizo ya wasanii. Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimshukuru Mheshimiwa Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri yenye matumaini. Ninashukuru Serikali inatambua kwamba uwanja ule unahitaji kukarabatiwa na kuwa uwanja wa kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwanja wa Lindi usifananishwe na viwanjwa vingine vilivyojengwa na Halmashauri. Uwanja wa Lindi ni miongoni mwa viwanja vitatu bora vilivyojengwa na wakoloni mana yake ni kwamba tumerithi kutoka mikononi mwa wakoloni ikiwemo kiwanja cha Mkwakwani - Tanga, kiwanja cha Dar es salaam na kiwanja cha Lindi Manispaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwanja ule umewahi kutumika kwa michezo ya Afrika Mashariki, kwa hiyo uwanja unahistoria ya kipekee kwamba timu za Afrika Mashariki zimechezwa katika uwanja wa Lindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wana-Lindi sasa tunahitaji kuona uwanja ule unabadilika na kuwa uwanja wa kisasa, tunaiomba Serikali ituambie itatusaidiaje kukarabati uwanja ule? Ninajua kwamba Halmashauri haina uwezo wa fedha wa kukarabati uwanja ule na kuwa uwanja wa kisasa, kwa hiyo ninaiomba Serikali ituambie ni namna gani itaweza ikatusaidia kukarabati uwanja na kuwa uwanja wa kisasa?
NAIBU WAZIRI, HABARI UTAMADUNI SANAA NA
MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Hamida kwa jinsi alivyokuwa mstari wa mbele kufuatilia suala la ukarabati wa uwanja huu wa mpira wa miguu wa Ilula (Lindi), kwa kweli hii imekuwa ni chachu kubwa sana katika maendeleo ya ukuaji wa soka katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niishauri Halmashauri ya Lindi kwamba iweke kipaumbele katika kutenga bajeti kwa ajili ya ukarabati wa uwanja huu. Pili, napenda kuchukua nafasi hii kumjulisha Mheshimiwa Hamida kwamba Serikali inalitambua hili na kutokana na hilo imekuwa ikitoa ushauri kwa TFF kuzisaidia Halmashauri kufanya ukarabati wa viwanja kwa kutumia wadau mbalimbali au wafadhili wa ndani na nje ya nchi, na kwa namna hiyo basi TFF imekuwa ikiweka katika orodha kila mwaka walau viwanja katika Halmashauri mbili hadi tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumtaarifu kwamba uwanja wa Ilula upo miongoni mwa orodha ambayo imewekwa na TFF kwa ajili ya ukarabati. Niseme tu kwamba TFF watakapotaka kufanya ukarabati itabidi waweke mkataba na Halmashauri ya Lindi na mkataba huo unasharti kwamba ni lazima kipaumbele cha matumizi kiwe katika mchezo wa mpira, ahsante sana.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa Chama cha Mapinduzi kirithi viwanja vilivyokuwa mali ya Watanzania kutoka kwa wakoloni wakati sasa nchi imekuwa ya mfumo wa vyama vingi; na kwa vile Chama cha Mapinduzi kimeshindwa kuitunza mali hii ya mayatima, ni lini Chama cha Mapinduzi kitarudisha viwanja hivi kwa Halmashauri au Serikali ili irudi mikononi kwa Watanzania wote badala ya kuendelea kudhulumu haki hii ya watanzania?[Neno kudhulumu siyo sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima napenda kuondoa neno kudhulumu na badala yake liwe kuirejesha haki hii kwa Watanzania wote.
NAIBU WAZIRI, HABARI UTAMADUNI SANAA NA
MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa hakuna hati yoyote inayoonekana kwamba Chama cha Mapinduzi kimechukua viwanja kutoka kwa mmiliki yoyote, hati zote zinaonyesha ni miliki ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo basi napenda kulithibitisha Bunge lako Tufu kwamba Chama cha Mapinduzi kinavifanyia ukarabati viwanja vyake kama zinavyofanya Halmashauri; kwa mfano uwanja wa Singida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Singida Mheshimiwa Martha Mlata anasimamia zoezi hili, upo uwanja wa Mbeya na wenyewe unafanyiwa ukarabati na Chama cha Mapinduzi kwa kushirikiana na wadau. Ahsante.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa sababu tunao uwanja wetu wa Taifa (Dar es Salaam) ambao ni wa kimataifa na ili kuutangaza uwanja huo, na ili kutangaza utalii na kuongeza ajira kwa nini Serikali sasa isije na mpango wa kuziomba Balozi zetu nje ili timu zao za Taifa huko ziliko zije kuutumia uwanja wetu wa mpira wa uwanja wa Taifa, na wakimaliza kucheza mpira au baada ya kucheza mpira wachezaji hao waende kwenye hifadhi zetu ili watangaze utalii wa nchi yetu kupitia uwanja wa Taifa?
NAIBU WAZIRI, HABARI UTAMADUNI SANAA NA
MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, wazo lake ni zuri, tumelichukua na tutakwenda kulifanyia kazi na tutarejesha majibu, ahsante sana.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali ya nyongeza ninayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, awali ya yote ninalipongeza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pongezi ziende kwa Spika wa Bunge kwa kuwa tayari wamekwishaanza kutoa huduma hii katika matangazo haya, wakalimani wamekwishaanza kutafsiri na kuwawezesha wenzetu viziwi kupata taarifa.
Kwa kuwa kilio cha haki ya kupata taarifa ni cha muda mrefu katika mjadala pia wa bajeti ya Wizara tulilizungumzia hili. Ningependa kupata commitment ya Serikali; je, ni lini sasa utekelezaji huu utaanza na kwa kuwa TBC ni televisheni ya umma, commitment ya Serikali kwamba Shirika hili litaajiri lini wakalimani wa lugha ya alama ili basi wenzetu viziwi waweze kupata taarifa?
Swali langu la pili, kwa kuwa haki ya kupata habari ni haki ya Kikatiba, je, Serikali inatoa muda gani kwa wamiliki wa vyombo binafsi vya habari ili na wao basi waone umuhimu na kutekeleza haki hii ya Kikatiba ambayo ni ya Ibara ya 18(d)? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru sana kwa pongezi ambazo ametoa na tunazipokea, tunasema ahsante sana. (Makofi)
Katika swali lake la kwanza ambalo anahitaji kujua
sasa ni lini TBC itaajiri, nichukue nafasi hii kwa namna ya pekee kabisa kumpongeza Mheshimiwa Amina Mollel kwa jinsi ambavyo amekuwa amepambania haki za walemavu, na kwa kweli nakumbuka kabisa kwamba hata katika mjadala wa bajeti ya Wizara yetu alichangia suala hili na alitaka kujua ni lini hasa vyombo vya utangazaji vitakuwa vikitoa ukalimani wa lugha ya alama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi ni kwamba, katika kikao ambacho kilifanyika wadau wale walijipangia majukumu mbalimbali. Kwa upande wetu Wizara tuliipangia TBC iwe ni chombo cha mfano, ianze mara moja kutoa ukalimani wa lugha ya alama, na kwa kuanzia TBC tayari imeishatuma maombi ya kupata kibali cha kuajiri wakalimani wawili, hivyo wakati wowote kibali kitakapotoka basi TBC itaajiri ili iweze kuwa chombo cha mfano kwa vyombo vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kwamba ni muda gani tumeweka kwa vyombo vya habari. Kama mlivyosikia katika jibu la msingi ni kwamba, TCRA imepewa jukumu la kuchukua kanzi data kutoka TASLI ambayo ni orodha ya wale wakalimani ambao wana uwezo wa kutoa ukalimani katika vyombo vya habari, wakiishachukua taarifa hizi watakuwa wakipeleka kwa vyombo vya habari.
Sasa tatizo ambalo tunalo ni kwamba vyombo vya habari ni vingi, vyombo vya habari vya utangazaji televisheni, ni vingi takribani 32, lakini kwa mujibu wa TASLI wapo wakalimani 70 na kati ya hao wakalimani 15 tu ndiyo ambao wanaonekana kwamba wana ujuzi na uwezo wa kufanya ukalimani katika vyombo vya habari au utangazaji wa televisheni. Ndiyo maana sasa VETA na CHAVITA wamepewa jukumu la kutoa mafunzo kwa hawa wakalimani wengine waliobaki ili na wao waweze kufikia uwezo wa kutangaza katika vituo vya televisheni. Ahsante.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwamba katika hali halisi inavyoonesha kwamba Tanzania haijawahi kuwakilishwa nje ya michezo ya kuogelea, mpira wa miguu, riadha, ngumi katika ile michezo ambayo huwa inataka qualifications, lakini moja ya tatizo kubwa ni choice ya michezo yenyewe na pili ni ufadhili wa michezo yenyewe. Mimi siamini kwamba Serikali ndiyo isimamie kufadhili michezo kwa sababu ina-priority nyingi.
Je, Waziri haoni kwamba wakati umefika sasa kuja na mwongozo au sera ya namna ya corporate Tanzania kuchangia katika michezo? Kwa mfano Uingereza British lottery ndiyo inayodhamini Olympic system nzima ya Uingereza. (Makofi)
Swali la pili, ipo michezo ambayo kwa gharama zake
na kwa uenezi wake ni rahisi sana kuenea, mchezo chess investment kubwa wanayotaka ni chess board ambayo in-cost labda dola sita au dola saba, baada ya hapo ni kuwa-train tu watoto au vijana.
Je, Serikali inaweza kushaurika kwamba huu ni mmoja kati ya mchezo ambao unaweza kuwa kipaumbele katika Taifa, kwa sababu hauna gharama na kwa sababu unaweza ukaenea katika hali ya haraka katika nchi?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Ally Saleh Ally kwa jinsi alivyo mdau mkubwa katika maendeleo ya michezo na amekuwa akichangia sana sana masuala ya michezo katika Bunge hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lake la kwamba kuna michezo ambayo haijawahi kuwakilishwa Kimataifa, nitoe mfano tu kwamba kwa mchezo wa kuogelea nchi yetu imeshawahi kuwakilishwa, kuna vijana ambao walishawahi kwenda Canada na wakaiwakilisha nchi yetu, tuliwapa bendera na mmoja alishika namba nne, lakini pia hata riadha, walishawahi kuwakilisha nchi yetu kimataifa na mmojawapo ni Simbu na anamfahamu. Ndugu Simbu ameshawahi kutuwakilisha Kimataifa na Serikali huwa inatenga bajeti kwa ajili ya hawa, lakini hatua za awali huwa zinafanywa na Tanzania Olympic Committee ambapo inawaandaa wale wachezaji na fedha zinatoka Olympic Kimataifa na wanapofuzu sasa kushiriki mashindano yale Kimataifa ndipo Serikali inapowawezesha. Mwaka 2016/2017 Serikali ilitenga fedha na wanariadha wetu waliweza kuiwakilisha Tanzania katika michezo ya Olympic.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mwongozo wa ushiriki wa sekta binafsi tunakubaliana na hilo lakini tunakwenda hasa na sera kwa sababu, sera yetu inatutaka kusimamia michezo sio tu kwa kuegemea kutambulika Kimataifa, tunasimamia michezo kwa madhumini mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kuimarisha afya, afya ya Watanzania kwa ujumla, pia kudumisha amani, umoja, mshikamano na upendo, vilevile kuhakikisha kwamba tunatambulika kimataifa kama anavyosema na kumjenga Mtanzania kuwa jasiri, kukabiliana na matatizo mbalimbali. Kwa hiyo, yako masuala ya msingi ambayo yanatupelekea Serikali kusimamia michezo.
Kwa upande wa mchezo anaoupendekeza wa chess katika swali lake la pili, tunapenda sana kutoa wito kwa wananchi wote kwa wananchi wote kwamba pale ambapo kuna michezo wanayoiona ni mipya na inafaa kuingizwa katika sekta ya michezo na hasa katika shule za msingi na sekondari, ili wanafunzi wetu waweze kujifunza, tunahimiza kwamba wananchi kama hao, Walimu ambao wanaweza kufundisha michezo hiyo wajitokeze ili waweze kufundisha kwa sababu, Azimio la Michezo la Umoja wa Mataifa la mwaka 1978 linahimiza wananchi wafanye ile michezo wanayoiweza, michezo wanayoipenda, michezo ambayo wana amani nayo. Ahsante. (Makofi)
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii niulize swali la nyongeza.
Kwa niaba ya vijana wote wa Tanzania ambao wanaweza kuwa wanufaika wakubwa sana wa michezo naomba kuuliza swali la nyongeza lifuatalo:
Je, Serikali haioni umuhimu wa kwamba ni wakati muafaka wa kuwa na shule maalum kwa ajili ya kukuza vipaji katika michezo kama sports academy? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Ninampongeza kwa kuwatetea vijana kimichenzo, kama alisikiliza vizuri hotuba ya Mheshimiwa Waziri wakati akiwasilisha bajeti yake ya mwaka 2017/2018 ni kwamba tumedhamiria. Serikali sasa hivi imekwishatenga shule takribani 55 ambazo ziko katika Mikoa yote ya Tanzania, hizi ndizo ambazo tutazichukulia kama ndizo academy zetu. Vilevile michezo ya UMISETA, michezo ya UMITASHUMTA itasaidia sana kuibua vipaji, hata hivyo tunashirikiana sana na Wizara ya Elimu kuhakikisha kwamba michezo inafundishwa katika ngazi zote za elimu tangu awali, sekondari na vyuoni. Ahsante. (Makofi)
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa niweze kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni miongoni mwa
watu ambao ni washabiki na wapenzi wa ngoma za asili, pamoja na kwamba wewe ni mpenzi wa ngoma za asili, hata huku Dodoma kuna ngoma za asili zinaitwa Chigogo.
Je, Serikali imejipangaje kuwezesha wale wote ambao wanaanzisha ngoma za asili katika mashindano hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Swali lake liko nje ya michezo, lakini liko ndani ya Wizara yetu ni ngoma za asili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuhamasisha wananchi wote waendelee kuenzi ngoma za asili, hata vyombo vya habari tunavihamasisha ili viweze kupiga ngoma za asili katika vipindi vyake kwa zile asilimia 60 za local content ambazo zimepewa. Ahsante.

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu vizuri hilo swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kukupongeza wewe binafsi kwa ubunifu, ujasiri na uthubutu kuanzisha mashindano ya ngoma zetu za utamaduni katika Ukanda wa Kusini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lilivyoanza hili Waheshimiwa Wabunge ilikuwa kwa Wilaya mbili tu, Wilaya ya Rungwe na Kyela sasa imepanuliwa zaidi kuhusisha Mkoa mzima na Mikoa ya jirani. Ninatoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote katika maeneo yenu tusisubiri Serikali ianzishe hayo, hebu tufuate mfano alioutoa Naibu Spika, wote tuanzishe hayo mashindano. Sisi kama Serikali tutasaidia kuboresha hizo ngoma zetu za utamaduni. (Makofi)
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 inaitaja kazi ya uandishi wa habari kuwa ni jukumu la kisheria. Serikali inawachukulia hatua gani watu wanaowazuia waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa hivi karibuni kumekuwa na matukio kadhaa ya waandishi wa habari kuzuiwa kufanya kazi zao kama vile RC kuvamia kituo cha Clouds, baadhi ya waandishi kuvamiwa wakiwa kwenye mkutano wa CUF, baadhi ya Wakuu wa Wilaya kuwakamata waandishi wa habari na kuwaweka ndani na hata jana kule Arusha katika Shule ya Msingi ya Lucky Vincent waandishi wa habari kumi walikamatwa wakiwa wanatimiza majukumu yao. Ni lini Serikali itaacha tabia hii mbaya ya kuwakamata kamata waandishi wa habari wakiwa kwenye majukumu yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, WASANII NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana kwa maswali yake na kwa kutambua kwamba Sheria ya Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 inahimiza kwamba kazi ya waandishi wa habari ni jukumu la kisheria, nadhani sote tunakubaliana na hilo. Hata hivyo, anaposema kwamba kuna watu wanaozuiwa kufanya kazi zao, mimi naamini kwamba kama kweli waandishi wa habari wanafuata maadili na wanatafuta habari kwa ajili ya kujenga na siyo kuvuruga nchi, siamini kabisa kwamba kuna watu wanaoweza kuwazuia.
Sera yetu ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003 inahimiza kwamba taasisi zote za Serikali na wadau wote wa habari kutoa taarifa kwa wanahabari na inahimiza kabisa kwamba wale Maafisa Habari katika Mikoa na Halmashauri wawe tayari kutoa ushirikiano kwa wanahabari ili kusudi wanahabari waweze kutekeleza majukumu yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama kuna hili la watu wanaozuia, mimi naomba baadaye tuonane na Mheshimiwa Devotha Minja aweze kuniambia ni wapi kwa sababu ndiyo kwanza nasikia hilo. Sera yetu inahimiza kwamba ni wajibu kwa Maafisa wa Habari kuwapa ushirikiano wanahabari kwa sababu jukumu lao linatambulika kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili Mheshimiwa Waziri alilitolea ufafanuzi vizuri sana wakati anahitimisha hotuba yake hapa Bungeni. Kwa hiyo, naomba nisirudie tena maneno ambayo aliyasema Mheshimiwa Waziri hapa Bungeni.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Ahsante sana kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninalo swali moja la nyongeza.
Lipo tatizo kubwa na la muonekano na upatikanaji
wa TBC1 kwenye maeneo mengi ya Wilaya ya Mbinga lakini pia ukanda mzima wa Ziwa Nyasa hususani kule kwenye tarafa ya Mhagati, Tarafa ya Mkumbi lakini pia Tarafa ya Namswea. Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha upatikanaji wa TBC1 katika maeneo tajwa hapo juu ukizingatia hicho ndicho kituo pekee kutoa matangazo bila kulipia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kama tutakumbuka katika bajeti ya mwaka huu zilitengwa shilingi bilioni tatu zaidi kama fedha za maendeleo kwa TBC na hizi ni pamoja na kuboresha television ya TBC1 pamoja na usikivu wa redio. Kwa hiyo, mpaka sasa katika maeneo aliyoyataja ya Mhagati, Namsweha na maeneo mengine, TBC bado inafanya tathmini kuona mgawanyo huo wa fedha uelekee wapi kwa upande kwa radi na uelekee wapi kwa upande wa television. Naomba kuwasilisha na ahsante.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Wakati Tanzania inatoka katika mfumo wa analojia kuingia katika mfumo wa dijitali inaeleweka kwamba Startimes ndio waliopewa jukumu hilo na katika makubaliano ilikuwa kwamba unapolipia kile king’amuzi cha kwa maana ya kwamba hizi channel za hapa nchini ni bure lakini ni tofauti na ilivyo sasa ni kwamba wamekuwa wakiondoa hizi channel za hapa nchini hazionekani tena kama ilivyokuwa awali. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri na jitihada hizo, ninaomba kufahamu ni kwa nini Startimes imekiuka mkataba huo na badala yake hivi sasa hakuna tena kituo chochote cha television ambacho unaweza kukiona baada ya malipo tuliyokuwa tunapaswa kulipia kuisha?
NAIBU WAZIRI HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Amina Mollel, Mbunge wa Viti Maalum, kwa kuuliza swali ambalo limekuwa likiulizwa mara nyingi sana na wateja na watumiaji wa tv.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba wakati mwingine utakuta kwamba mteja anapokuwa amelipia kifurushi na kifurushi chake kikawa kimekwisha basi zile channel ambazo tunaziita kwamba ni free to air zinakuwa hazionekani. Sasa tatizo ni kwamba, kama nilivyotangulia kusema TBC1 peke yake ndiyo ambayo inaonekana katika hivi ving’amuzi vya DDT pamoja na DTH bure bila kulipia. Kwa hiyo, TBC1 hailipi chochote kwa hawa transmitters kabisa. Lakini Sheria ya Leseni walizopata hawa transmitters ina masharti kwamba hizi free to air zote wale wamiliki au makampuni ya televisheni wanatakiwa wawe wanalipa ada fulani kila mwezi, sheria inamruhusu yule transmitter kumkatia au kumuondoa pale ambapo atakuwa ameshindwa kulipa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tatizo linatokea kwamba hawa content providers wanapokuwa wameshindwa kulipa basi wanaondolewa na hawa transmitters. Kwa sasa hatua zimeshachukuliwa, TCRA imewaita na kuwataka wajieleze vizuri ni kwa nini hawalipi kwa sababu wao ndiyo wanaosababisha sasa hizi zisionekane na Sheria inawaruhusu wale transmitters waoneshe kama hawatalipa.
Kwa hiyo, kutokana na kutokulipa kwao ndiyo maana unakuta hizi free to air channel hazionekani lakini sio kwamba yule mteja ndiyo anayetakiwa alipe.
Mheshimiwa Spika, mteja ananunua kifurushi kwa ajili ya zile pay channels lakini sio kwa hizi free to air. Kwa hiyo kimsingi anatakiwa aendelee kuziona hata kama hakulipia/hakununua kifurushi. Kwa hiyo, pale itakapoonekana kwamba maelezo yao hayaridhishi watachukuliwa hatua kali. Hivyo nichukue nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuwataka wamiliki wote wa tv stations walipie mara moja ada zao za mwezi ili kusudi wananchi waweze kufaidi hizi free to air services. Ahsante.(Makofi)
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri katika swali ambalo nimeshawahi kuliuza leo ni mara ya tatu, naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa nilishawahi kuishauri Serikali kwamba moja ya sababu kubwa ambayo inasababisha timu yetu ya Taifa kutokufanya vizuri ni utitiri wa wachezaji wa kigeni kwenye nchi yetu na tulipoanza kwanza walikuwa wanaruhusiwa wachezaji watatu, baadae wakaongeza wakwa watano, leo ni saba. Sasa tunategemea Taifa Stars itafanya vizuri? Ningeshauri Serikali wapunguze idadi ya wachezaji wa kigeni abaki moja au wawili kwa sababu sisi tuna wachezaji wetu. (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa Bunge lilishawahi kutunga sheria ya kutenga fedha kutoka kwenye michezo ya kubahatisha kwenda kusaidia michezo ni kwa nini basi hizo fedha zimekuwa hazipelekwi ili kusaidia michezo maana sasa hivi ni sawasawa unakwenda benki kuchukua fedha wakati hujaweka pesa, usitegemee kama utapata. Naomba majibu.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ameonesha kwamba sababu mojawapo ya kushindwa kimichezo hasa mchezo wa soka ni utitiri wa wachezaji wa kigeni na kwamba pengine tupunguze idadi.
Mheshimiwa Spika, kwanza nimtaarifu tu Mheshimiwa Venance kwamba ni kweli wapo wachezaji wa nje takribani 40 katika timu zetu, lakini wachezaji wetu kwenda nje wako 14 tu. Kulingana na concern yake aliyoionesha ni kwamba sasa hivi tuko katika mchakato wa kupitia upya Sera ya Michezo ambapo maoni yanatolewa na wadau wengi na tunalichukulia hili kama ni maoni ya wadau akiwa mdau mmojawapo mzuri sana wa michezo. Kwa hiyo, katika kupitia sera hiyo ambayo iko katika hatua nzuri ambapo tunaiandaa sasa iende katika ngazi za juu zaidi, tutayachukua maoni yote kulingana na suala lake ambalo amelionesha ili tuweze kulifanyia kazi vilevile.
Mheshimiwa Spika, pili kuhusu kutenga fedha za michezo ya kubahatisha ni kweli kipindi cha nyuma hili suala lilikuwa halifanyiwi kazi japo linatakiwa kisheria, lakini kwa bahati nzuri napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba kuanzia mwezi wa saba fedha hizi zimetoka rasmi na zimekwenda BMT na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kuanzia sasa BMT itakuwa ikipata fedha za Bahati Nasibu ya Taifa. Lakini sio hivyo tu, tunalifanyia kazi ili kusudi michezo yote ya kubahatisha itoe kiasi cha fedha kwenda BMT ili kusaidia maendeleo ya michezo.
Mheshimiwa Spika, kabla sijamalizia nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Venance Mwamoto kwa jinsi alivyokuwa mdau wetu mzuri wa ukweli katika sekta ya michezo kwa jinsi alivyoshiriki, ameshirikiana na BMT kutatua mgogoro wa timu ya Lipuli ambayo sasa baada ya mgogoro huo kutatuliwa inaendelea vizuri na anifikishie salamu zangu kwa Serikali ya Mkoa vilevile. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia niwapongeze Waheshimiwa Wabunge ambao wameshiriki katika kuendesha ligi katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na yeye Mheshimiwa Venance Mwamoto nawapongeza sana, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Naibu Spika wetu, Mheshimiwa Flatei G. Massay, Mheshimiwa Ritta Kabati, Mheshimiwa Silvestry Koka na Waheshimiwa Wabunge wengine na niwaombe tuige mfano huu lakini kuna wengine ambao bado hawajajitokeza kutuambia lakini wanafanya zoezi hili. Nakushukuru sana.(Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza, Kwa kuwa, Serengeti Boys vijana wale walionesha umahiri mkubwa wa kiwango kile cha soka kinachotakiwa na wakatutangaza sana kule nje na sasa wamerudi. Je, Wizara ina mpango gani sasa kuwaendeleza vijana hawa ili kutokuwa na ile kazi ya zimamoto, wachezaji hawa wakaendelea kufanya vizuri wakati mwingine wa ligi za kimataifa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serengeti Boys imefanya vizuri na imetoa mfano mzuri katika timu za Taifa under seventeen, lakini nadhani sote tunakumbuka kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu hapa alipokuwa akifunga Bunge tarehe tano mwezi wa saba alitoa maagizo kwa TFF kwamba wawatunze vijana hawa wasiwaache wakapotea. Kwa hiyo, sisi kama Serikali/Wizara tulichokifanya ni kuwachukua vijana hawa na kuwaunganisha na majeshi. Kwa hiyo, mpaka sasa wanatunzwa katika kituo cha JKT na pale wanafanya mazoezi ya kila siku na baadae tunaweza kuwatumia katika timu za wakubwa za Taifa. Ahsante.
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kuuliza swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Waziri kumekuwa na tatizo la viwanja katika maeneo mengi, kwa mfano Mkoa wetu wa Manyara ni Mkoa unaoongoza Tanzania nzima kwa kuiletea nchi hii medali hasa kwenye michezo ya riadha. Lakini kumekuwa na tatizo la viwanja vya muda mrefu, wachezaji hawa wanaenda kufanya mafunzo Arusha.
Ni lini sasa Serikali itatujengea kituo cha mafunzo kwa ajili ya kuendeleza vipaji hivyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kusema katika majibu yangu ya swali la msingi ni kwamba tumezitaka Halmashauri zote nchini kutenga viwanja vya michezo ya aina mbalimbali hiyo ni hatua ya kwanza. Lakini hatua ya pili, Serikali tumeanzia na kujenga complex ya michezo kwa ajili ya michezo yote hapa Dodoma na nadhani tukiwa tunapita kuelekea Dar es Salaam tunaiona.
Mheshimiwa Spika, kimsingi niseme tu kwamba hata Sera yetu ya Michezo inaelekeza kwamba masuala ya viwanja vya michezo katika maeneo mbalimbali yanatakiwa ushiriki wa wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na makampuni na taasisi mbalimbali, hivyo niombe Halmashauri ishirikiane na wadau mbalimbali ili kuweza kuanzisha kituo cha michezo. Ahsante.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Serikali imekiri kuwa Redio ya Taifa haisikiki katika Wilaya ya Kyerwa na wananchi hao wanapofungua redio wanapata Redio ya Rwanda na Uganda kitu ambacho kimewafanya wananchi hawa kuonekana kama wametengwa kwa sababu hawawezi kupata taarifa ambazo ni muhimu zinazohusu Taifa lao.
Je Serikali haioni kuwa wananchi hawa wamekosa haki yao ya msingi ya kupata habari za Serikali hasa hasa kutoka kwa viongozi wao kama Mheshimiwa Rais anapokuwa anaongea na viongozi wengine? Hata mimi Mheshimiwa Mbunge ninapokuwa Bungeni nawawakilisha, hawa wananchi hawapati taarifa yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali haioni haja ya kuchukua hatua za dharura ili wananchi hawa waweze kupata taarifa ya Redio ya Taifa kwa sababu wanakosa hii haki ya msingi? Laini hata Televisheni ya Taifa haisikiki wala haionekani vizuri. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Innocent Bilakwate. Pia nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Innocent kwa maswali yake mawili mazuri.
Mheshimiwa Spika, kwanza, naomba unipe ridhaa ya kuelezea suala hili kwa kirefu kidogo kwa sababu tuna Wilaya karibu 84 ambazo hazina usikivu wa redio katika nchi hii na suala hili limesababisha Wabunge wengi mara kwa mara kuuliza maswali yanayohusiana na usikivu wa redio yao ya Taifa. Kwa hiyo, naomba nitoe ufafanuzi kidogo ili kusudi tuweze kusaidiana kwa pamoja na kuhakikisha kwamba tatizo hili linapata ufumbuzi.
Mheshimiwa Spika, kwanza ametaka kujua kwamba Serikali haioni kwamba wananchi wanakosa haki yao ya msingi ya kusikiliza redio yao ya Taifa. Nitoe tu maelezo kwa kifupi kwamba kuna matatizo ambayo yanasababisha au tuseme kuna factors ambazo zinasababisha kuathiri usikivu wa redio katika maeneo mbali mbali. Kwanza, ukirudi nyuma tulikuwa tunatumia mitambo ya medium wave ambayo ilikuwa inaenea katika nchi nzima lakini kutokana na uchakavu wa mitambo hii na gharama kubwa ya kuinunua au kuikarabati imebidi sasa tuweke mitambo ya FM katika kila mkoa. Kwa hiyo, kila mkoa una mtambo wa FM.
Mheshimiwa Spika, sasa masuala ambayo yanaathiri usikivu kwanza ni capacity ya ule mtambo wenyewe lakini pia uwepo wa milima katika maeneo husika kwa mfano kama eneo la Mheshimiwa Innocent kuna milima mirefu ambayo mitambo hii inashindwa kuufikia. Suala lingine ambalo linaathiri usikivu ni ule uharibifu wa baadhi ya vifaa kama power amplifier ambao unatokana na matatizo mbalimbali kama vile radi au kukatika kwa umeme. Katika eneo la Mheshimiwa Innocent, kule Bukoba upo mtambo ambao kuna kifaa kimeharibika – MOSFET imeharibika na imekufa kabisa, kwa hiyo, usikivu umeathirika katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, hatua za haraka ambazo tumeamua kufanya, kwanza nimeshatoa maagizo ili kusudi wataalam waende katika maeneo yake, katika Wilaya ya Kyerwa ili kuweza kuona jinsi gani ya kutatua tatizo hili kwa sababu kwanza uwezekano upo wa kuweka booster, lakini pia waone kama wanaweza wakanunua kifaa kile ambacho kimeharibika.
Vilevile kuna utaratibu ambao sasa hivi TBC inafanya kuubadilisha mfumo wa satellite uplink ambayo iko Mikocheni, tunaamini kabisa kwamba hii satellite uplink ikirekebishwa ikawa ya kisasa zaidi tutaboresha usikivu kwa asilimia takribani 15 hivi.
Kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge ambao maeneo yao hayana usikivu, kufikia mwisho wa mwaka huu tunaamini kabisa hii satellite uplink inaweza ikawa imerekebishwa, kwa hiyo, usikivu utakapokuwa umeboreka katika maeneo yao watupe taarifa. Vilevile, kutokana na uharibifu wa vifaa katika vile vituo vyenyewe, yale maeneo ambayo yana usikivu wakati wowote watakapoona usikivu umesita katika maeneo yale watupe taarifa mapema ili kusudi wataalam wetu waweze kufuatilia.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo tunafanya kwa sasa hivi ni huu utaratibu wa kuweka mitambo ya FM yaani kuongeza transmitter katika maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, nimetoa maagizo tayari kwamba wataalam wapite katika maeneo ya mipakani waone ni wapi panapostahili kuwekwa boosters lakini ni wapi pia ambao panastahili kuwekwa transmitters mpya. Ahsante. (Makofi)
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Spika, kwa maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri anasema takribani Wilaya 84 hazipati usikivu. Swali langu, ni kwa nini sasa ile kauli mbiu ya TBC ya Ukweli na Uhakika msiifute na muwe na kauli mpya?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, hatuwezi kufuta hiyo kauli mbiu kwa sababu tunatoa taarifa za ukweli na za uhakika, haihusiani kabisa na usikivu. Ahsante. (Makofi)
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Tarafa ya Amani tunaitegemea sana pale Muheza kwa mambo ya uchumi, kukosekana kusikilizwa kwa redio kwenye maeneo hayo pamoja na televisheni hususan kwenye Kata za Mbomole, Zirai, Misarai, Amani kwenyewe na Kwezitu kunawafanya wananchi hao kukosa uzoefu ili kuweza kujifunza sehemu nyingine. Swali langu la kwanza ni kama ifuatavyo:-
Kufuatana na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwamba katika mwaka huu wa fedha 2017/2018 zimetengwa bilioni tatu, nataka uwahakikishie wananchi wa Amani kwamba nao wako kwenye mpango huu ili waweze kupata uzoefu wa kuona televisheni yao na redio yao ya Taifa?
Swali langu la pili; utaratibu wa TBC wanapoweka minara kwenye vijiji kuwalipa fidia wananchi wa vijiji hivyo vya karibu ili kuimarisha ulinzi na pia kuhakikisha kwamba usalama wa minara hiyo inakuwepo. Kata yangu moja ya Potwe ina mnara wa TBC, lakini hawajapata fidia na ninaomba kama kwenye mpango huu wa sasa hivi, kwenye hii Tarafa ya Amani patakuwepo na mipango ya kuongeza usikivu, basi wananchi hao waweze kulipwa fidia.
Naomba uwahakikishie wananchi hao mambo hayo, nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza ametaka kujua hizo shilingi bilioni tatu kama wao nao wako kwenye mpango huu wa kuimarisha usikivu. Labda tu nitoe maelezo kama tulivyosema nadhani sote tulisikia hotuba ya Mheshimiwa Waziri akisoma katika bajeti yetu ni kwamba ziko Wilaya nyingi sana ambazo hazina usikivu. Ziko Wilaya takribani 84 usikivu wake ni hafifu sana. Tulipoanza kujaribu kuboresha usikivu katika Wilaya zetu tano tulianzia kwanza kwa mwaka huu wa fedha katika Wilaya ya Geita na tulipoweka mitambo ile ya FM katika Mkoa wa Geita tumegundua kwamba katika utafiti wetu ni kwamba masafa yale usikivu uko katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Geita na maeneo mengine.
Kwa mfano; usikivu umekwenda mpaka Geita Mjini, umekwenda Bukombe, umekwenda Chato, umekwenda Kahama, kwa hiyo, ni imani yangu kwamba tunapoboresha meneo ya Longido na maeneo ya Rombo pengine usikivu unaweza ukaboreka katika maeneo mengine. Kwa hiyo, siyo rahisi sasa hivi kuamua kwamba hizi shilingi bilioni tatu tunaweza kuzipeleka wapi, tunatarajia tuone kwamba effect inaweza au usikivu huu katika maeneo haya tutakayoboresha yanaweza yakaenda mpaka maeneo gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tuna mpango mwingine wa kufufua ile mitambo ya zamani, mitambo ya AM ambayo yenyewe inakwenda mbali zaidi. Mwanzoni tulikuwa na mitambo minne tu ambapo mmoja ulikuwa Dodoma, mwingine Mwanza, mwingine Dare es Salaam na mmoja ulikuwepo Nachingwea, ambapo yote hii ilikuwa inapelekea usikivu katika nchi nzima. Kwa hiyo, tumeshakubaliana na wadau wa maendeleo kwamba watatusaidia kufufua mitambo hii, ili kusudi tuweze kuboresha usikivu katika nchi nzima. Ahsante.
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa kama alivyosema muuliza swali wa kwanza TBC wameweza kupata shilingi bilioni tatu, naomba kumuuliza Mheshimiwa mjibu swali.
Ni lini Serikali itaweza kununua vifaa vidogo TVU au AVIWEST vifaa vile tukio linapotokea wanaweka pale pale tunakwenda kwenye breaking news, lakini TBC leo kwenye breaking news wanakodi vifaa, kifaa kimoja kinanunuliwa kama shilingi milioni 50 au shilingi milioni 60, hii ni aibu katika Serikali yetu.
Serikali waniambie ni lini wataweza kununua vifaa hivyo na kuvisambaza Tanzania kwa sababu masafa marefu hayasikiki. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana, kama nimempata vizuri Mheshimiwa Mbunge hii TVU ni kwa upande wa televisheni na ambapo tayari TBC imeshanunua vifaa hivi, ahsante.(Makofi)
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii nyeti. Wilaya ya Kakonko ni miongoni mwa Wilaya zenye matatizo ya usikivu wa TBC. Kule tunasikiliza Redio Burundi, ndugu yangu Mheshimiwa Mwamoto ni shahidi amekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kibondo kule. Maeneo ya Kibondo na Kokonko hakuna usikivu wa TBC. Katika swali la msingi imetajwa Wilaya ya Kakonko. Naomba kujua na nipewe time frame na Serikali ni lini, ni tarehe ngapi TBC itaanza kusikika Kakonko?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni kweli kwamba Kakonko ni moja ya zile Wilaya tano za mipakani ambazo zimetengewa fedha katika bajeti ya mwaka huu 2016/2017, ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwamba amekuwa akipambania usikivu katika Wilaya yake na ni kweli kwamba matangazo mengi wanayapata kutoka nchi jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utaratibu ambao tumeanza, tulianza na kufanya tathmini kwamba ni wapi minara iwekwe tayari tulishaomba masafa kutoka TCRA na tumepata, tayari mzabuni ameshapata zabuni ya kufanya kazi hii, lakini time frame tuliyopanga ni mwisho wa mwaka huu wa fedha usikivu utakuwa umeimarika katika Wilaya ya Kakonko na maeneo mengine ambayo ameyataja. Ahsante.(Makofi)
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Nkasi usikivu kwa ujumla hasa mwambao mwa Ziwa Tanganyika katika Tarafa ya Wampembe, Kata ya Kala, Wampembe, Kizumbi pamoja na Ninde hazina kabisa usikivu wa Redio Tanzania, bahati mbaya sana maeneo haya hayana mawasiliano ya barabara ya uhakika. Viongozi ni mara chache wanatembelea maeneo haya ukiacha DC, Mkuu wa Mkoa na viongozi wengine wa Chama. Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha usikivu katika eneo hili ili wananchi wa Ziwa Tanganyika mpakani kule wawe na usikivu wa kutosha kusikiliza matangazo mbalimbali ya nchi yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Kama nilivyotangulia kusema mwanzoni, tuna mpango wa kufanya suluhisho la kudumu ambalo tunaweza kukarabati ile mitambo michache ambayo inaweza ikafika eneo la nchi nzima. Kwa mfano, mtambo ule wa Mwanza unaweza ukaenda mpaka maeneo hayo na tayari tumeshaandika andiko kupeleka kwa mbia wetu wa maendeleo ambaye tayari amekubali kufanya ukarabati wa mitambo hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kabisa, kuliko kusubiri hizi fedha kidogo kidogo za kila mwaka ni bora tukaifufua ile mitambo ya AM ambayo haina matatizo kabisa na sifa zake ni kwamba inakwenda mbali sana na haipati pingamizi la milima.
Kwa hiyo, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge awe na subira ili kusudi tuweze kupata majibu kutoka kwa mbia wetu wa maendeleo na kuweza kufufua mitambo yetu ambapo maeneo hayo aliyoyataja yatapata usikivu pamoja na nchi nzima.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyoeleza Naibu Waziri, kazi za wasanii ni kuburudisha, kuelimisha, kuonya na kukosoa, wasanii wamekuwa wakifanya kazi hizi hata wakati wa kampeni tulishuhudia wasanii walivyofanya kazi yao vizuri na wakati mwingine waliimba nyimbo za kuponda upinzani na mlikuwa mkishangilia. Jambo la kushangaza hivi sasa wasanii wakiimba nyimbo za kukosoa Serikali wanashughulikiwa na mfano mzuri ni Ney wa Mitego pamoja na Roma Mkatoliki.
• Swali la kwanza, je, ni wakati gani sasa kazi hizi za wasanii zinathaminika?
• Swali la pili, kwa bahati mbaya sana Rais ametoa maagizo ya wale ambao wamehujumu kazi za wasanii na kuacha kabisa kuwawajibisha Serikali yake ambayo imeshindwa kabisa kuthamini kazi nzuri iliyofanywa na Marehemu Mzee Francis Ngosha ambaye amekufa akiwa maskini wa kutupwa.
Je, Serikali inataka kukamata kazi za wasanii wakati ninyi wenyewe mmemuhujumu Mzee Francis Ngosha ambaye mpaka sasa hivi hana lolote, amekufa na hakuacha alama yoyote katika familia yake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli maswali yake yako nje kidogo na swali la msingi, lakini kwa sababu tu ya kumbukumbu tulizonazo, swali lake la kwanza linalouliza kwamba ni wakati gani kazi za wasanii zinathaminiwa? Kama alivyosema mwenyewe, kwamba kazi ya sanaa ni kuburudisha, kuelimisha, kuonya, kukosoa na kadhalika, niseme tu kwamba kazi za wasanii tunazithamini wakati wote hasa wakati zinapoelimisha, zinapoburudisha na kufanya kazi zile ambazo zinalijenga Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa kusema kwamba wasanii huwa wanashughulikiwa wakiikosoa Serikali, nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi hizi za sanaa zinasimamiwa na sheria. Tunayo Sheria ya BASATA Namba 23 ya mwaka 1984, tuna Sheria nyingine Namba 4 ya Bodi ya Filamu ya mwaka 1976 na tuna Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki Namba 7 ya mwaka 1999. Kwa hiyo, tunachohitaji ili tuweze kuzithamini kazi hizi ni kwamba wasanii wazingatie sheria, wafuate sheria na taratibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa wasanii ambao tunaona kwamba wameenda kinyume, hatua huwa zinachukuliwa na hatua zenyewe, kwa mfano kuna msanii mmoja anaitwa Nikki Mbishi ambaye alipewa tu onyo kutokana na kuweka picha ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne katika wimbo wake I am sorry JK. Hizo ni hatua tu ambazo huwa tunazichukua ili wasanii hawa wafuate sheria. Sheria ya BASATA inahitaji wasanii hawa wapitishe nyimbo zao BASATA ili ziweze kukaguliwa kabla hazijatolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wakiwa wamepitia kule ina maana kwamba watatoa kitu ambacho kinazingatia sheria na kinafuata maadili, sasa huu ni ukiukwaji wa maadili.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwingine ambaye ameshawahi kupewa onyo ni Diamond kupitia kwa Meneja wake, ambaye alitumia majina ya viongozi bila kufuata utaratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Ney wa Mitego, huyu aliimba wimbo wake wa Wapo ambapo ulifungiwa na BASATA kwa muda, lakini baadaye ulifunguliwa baada ya kuwa na makubaliano ya jinsi ya kuuboresha huo wimbo. Huyo mwingine Roma, hakuna hatua ambayo imechukuliwa na Serikali kwa mwaka huu kuhusu msanii huyo na ninadhani ninyi ni mashahidi kwamba alijieleza yeye mwenyewe kwa vyombo vya habari na Mheshimiwa Waziri pia alikuwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ambalo linamhusu Marehemu Francis Ngosha na Mheshimiwa Devotha anadai kwamba Serikali imemhujumu, hii siyo kweli, hakuna hujuma. Kimsingi yapo majina mezani mpaka sasa kama matatu hivi yanayohusiana na ubunifu wa nembo tunayoitumia, ambayo ni nembo ya Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mpaka sasa bado haijajulikana ni nani hasa ambaye ni mbunifu wa nembo hii. Kwa sababu kwa mfano, yupo Marehemu ambaye alishatangulia mbele za haki muda mrefu anayeitwa Abdallah Farhan wa Zanzibar, yeye vielelezo tayari vimeshakutwa katika kumbukumbu zake jinsi alivyokuwa akibuni nembo yetu ya Taifa, nembo ya Kenya pamoja na nembo ya OAU kipindi hicho alipokuwa akisoma Makerere University. Kwa hiyo, yapo majina ambayo yanadaiwa kwamba yalishiriki katika kutengeneza nembo hii. Ninaomba sana… (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana wataalam wafanye kazi ya kutambua ni nani hasa ambaye alishiriki kubuni. Kwa sababu Marehemu Francis yeye anajulikana kama ni mchoraji, lakini siyo mbunifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda niseme tu kwamba labda swali la Mheshimiwa Devotha Minja ni ishara ya wazi kwamba kuna uhitaji mkubwa sana wa kuwa na orodha ya wasanii na kazi ambazo wamezifanya na ni kitu ambacho sasa hivi Wizara tumeanza kukifanya ili kusudi tuwe na orodha ya wasanii wote katika nchi yetu na kazi ambazo wanazifanya ili mwisho wa siku utata kama huu usiweze kutokea tena. (Makofi)
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Moja kati ya changamoto kubwa za wasanii wa Tanzania ni kuibiwa kazi zao, lakini pia kutonufaika na kazi zao kwa sababu ya kazi hizo kutolindwa ipasavyo. Tunaona kuna upungufu mkubwa sana kwenye Sheria Namba 7 ya mwaka 1999, Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki.
Je, Serikali haioni kwamba huu sasa ni muda muafaka wa kuileta sheria hii kwenye Bunge lako Tukufu tuweze kuibadilisha na kuirekebisha ili iweze kusaidia wasanii wa Tanzania waweze kupata haki zao, kwa sababu wengi wanakufa masikini, wanaibiwa kazi zao mtaani lakini wanaowaibia tunawajua?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Hili suala tayari COSOTA imeshaliona, hii ni Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki. Kwa kuanzia imeanza kufanya utaratibu wa kubadilisha kifungu namba 46. Kwa hiyo, mchakato huu unaendelea, tuwe na subira ili marekebisho yaweze kufanyika ikiwa ni pamoja na kanuni zake. Ahsante.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali ya nyongeza ninayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, awali ya yote ninalipongeza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pongezi ziende kwa Spika wa Bunge kwa kuwa tayari wamekwishaanza kutoa huduma hii katika matangazo haya, wakalimani wamekwishaanza kutafsiri na kuwawezesha wenzetu viziwi kupata taarifa.
Kwa kuwa kilio cha haki ya kupata taarifa ni cha muda mrefu katika mjadala pia wa bajeti ya Wizara tulilizungumzia hili. Ningependa kupata commitment ya Serikali; je, ni lini sasa utekelezaji huu utaanza na kwa kuwa TBC ni televisheni ya umma, commitment ya Serikali kwamba Shirika hili litaajiri lini wakalimani wa lugha ya alama ili basi wenzetu viziwi waweze kupata taarifa?
Swali langu la pili, kwa kuwa haki ya kupata habari ni haki ya Kikatiba, je, Serikali inatoa muda gani kwa wamiliki wa vyombo binafsi vya habari ili na wao basi waone umuhimu na kutekeleza haki hii ya Kikatiba ambayo ni ya Ibara ya 18(d)? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru sana kwa pongezi ambazo ametoa na tunazipokea, tunasema ahsante sana. (Makofi)
Katika swali lake la kwanza ambalo anahitaji kujua sasa ni lini TBC itaajiri, nichukue nafasi hii kwa namna ya pekee kabisa kumpongeza Mheshimiwa Amina Mollel kwa jinsi ambavyo amekuwa amepambania haki za walemavu, na kwa kweli nakumbuka kabisa kwamba hata katika mjadala wa bajeti ya Wizara yetu alichangia suala hili na alitaka kujua ni lini hasa vyombo vya utangazaji vitakuwa vikitoa ukalimani wa lugha ya alama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi ni kwamba, katika kikao ambacho kilifanyika wadau wale walijipangia majukumu mbalimbali. Kwa upande wetu Wizara tuliipangia TBC iwe ni chombo cha mfano, ianze mara moja kutoa ukalimani wa lugha ya alama, na kwa kuanzia TBC tayari imeishatuma maombi ya kupata kibali cha kuajiri wakalimani wawili, hivyo wakati wowote kibali kitakapotoka basi TBC itaajiri ili iweze kuwa chombo cha mfano kwa vyombo vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kwamba ni muda gani tumeweka kwa vyombo vya habari. Kama mlivyosikia katika jibu la msingi ni kwamba, TCRA imepewa jukumu la kuchukua kanzi data kutoka TASLI ambayo ni orodha ya wale wakalimani ambao wana uwezo wa kutoa ukalimani katika vyombo vya habari, wakiishachukua taarifa hizi watakuwa wakipeleka kwa vyombo vya habari.
Sasa tatizo ambalo tunalo ni kwamba vyombo vya habari ni vingi, vyombo vya habari vya utangazaji televisheni, ni vingi takribani 32, lakini kwa mujibu wa TASLI wapo wakalimani 70 na kati ya hao wakalimani 15 tu ndiyo ambao wanaonekana kwamba wana ujuzi na uwezo wa kufanya ukalimani katika vyombo vya habari au utangazaji wa televisheni. Ndiyo maana sasa VETA na CHAVITA wamepewa jukumu la kutoa mafunzo kwa hawa wakalimani wengine waliobaki ili na wao waweze kufikia uwezo wa kutangaza katika vituo vya televisheni. Ahsante.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Tarafa ya Amani tunaitegemea sana pale Muheza kwa mambo ya uchumi, kukosekana kusikilizwa kwa redio kwenye maeneo hayo pamoja na televisheni hususan kwenye Kata za Mbomole, Zirai, Misarai, Amani kwenyewe na Kwezitu kunawafanya wananchi hao kukosa uzoefu ili kuweza kujifunza sehemu nyingine. Swali langu la kwanza ni kama ifuatavyo:-
Kufuatana na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwamba katika mwaka huu wa fedha 2017/2018 zimetengwa bilioni tatu, nataka uwahakikishie wananchi wa Amani kwamba nao wako kwenye mpango huu ili waweze kupata uzoefu wa kuona televisheni yao na redio yao ya Taifa?
Swali langu la pili; utaratibu wa TBC wanapoweka minara kwenye vijiji kuwalipa fidia wananchi wa vijiji hivyo vya karibu ili kuimarisha ulinzi na pia kuhakikisha kwamba usalama wa minara hiyo inakuwepo. Kata yangu moja ya Potwe ina mnara wa TBC, lakini hawajapata fidia na ninaomba kama kwenye mpango huu wa sasa hivi, kwenye hii Tarafa ya Amani patakuwepo na mipango ya kuongeza usikivu, basi wananchi hao waweze kulipwa fidia.
Naomba uwahakikishie wananchi hao mambo hayo, nakushukuru. (Makofi
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza ametaka kujua hizo shilingi bilioni tatu kama wao nao wako kwenye mpango huu wa kuimarisha usikivu. Labda tu nitoe maelezo kama tulivyosema nadhani sote tulisikia hotuba ya Mheshimiwa Waziri akisoma katika bajeti yetu ni kwamba ziko Wilaya nyingi sana ambazo hazina usikivu. Ziko Wilaya takribani 84 usikivu wake ni hafifu sana. Tulipoanza kujaribu kuboresha usikivu katika Wilaya zetu tano tulianzia kwanza kwa mwaka huu wa fedha katika Wilaya ya Geita na tulipoweka mitambo ile ya FM katika Mkoa wa Geita tumegundua kwamba katika utafiti wetu ni kwamba masafa yale usikivu uko katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Geita na maeneo mengine.
Kwa mfano; usikivu umekwenda mpaka Geita Mjini, umekwenda Bukombe, umekwenda Chato, umekwenda Kahama, kwa hiyo, ni imani yangu kwamba tunapoboresha meneo ya Longido na maeneo ya Rombo pengine usikivu unaweza ukaboreka katika maeneo mengine. Kwa hiyo, siyo rahisi sasa hivi kuamua kwamba hizi shilingi bilioni tatu tunaweza kuzipeleka wapi, tunatarajia tuone kwamba effect inaweza au usikivu huu katika maeneo haya tutakayoboresha yanaweza yakaenda mpaka maeneo gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tuna mpango mwingine wa kufufua ile mitambo ya zamani, mitambo ya AM ambayo yenyewe inakwenda mbali zaidi. Mwanzoni tulikuwa na mitambo minne tu ambapo mmoja ulikuwa Dodoma, mwingine Mwanza, mwingine Dare es Salaam na mmoja ulikuwepo Nachingwea, ambapo yote hii ilikuwa inapelekea usikivu katika nchi nzima. Kwa hiyo, tumeshakubaliana na wadau wa maendeleo kwamba watatusaidia kufufua mitambo hii, ili kusudi tuweze kuboresha usikivu katika nchi nzima. Ahsante.
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa kama alivyosema muuliza swali wa kwanza TBC wameweza kupata shilingi bilioni tatu, naomba kumuuliza Mheshimiwa mjibu swali.
Ni lini Serikali itaweza kununua vifaa vidogo TVU au AVIWEST vifaa vile tukio linapotokea wanaweka pale pale tunakwenda kwenye breaking news, lakini TBC leo kwenye breaking news wanakodi vifaa, kifaa kimoja kinanunuliwa kama shilingi milioni 50 au shilingi milioni 60, hii ni aibu katika Serikali yetu.
Serikali waniambie ni lini wataweza kununua vifaa hivyo na kuvisambaza Tanzania kwa sababu masafa marefu hayasikiki. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana, kama nimempata vizuri Mheshimiwa Mbunge hii TVU ni kwa upande wa televisheni na ambapo tayari TBC imeshanunua vifaa hivi, ahsante.(Makofi)
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii nyeti. Wilaya ya Kakonko ni miongoni mwa Wilaya zenye matatizo ya usikivu wa TBC. Kule tunasikiliza Redio Burundi, ndugu yangu Mheshimiwa Mwamoto ni shahidi amekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kibondo kule. Maeneo ya Kibondo na Kokonko hakuna usikivu wa TBC. Katika swali la msingi imetajwa Wilaya ya Kakonko. Naomba kujua na nipewe time frame na Serikali ni lini, ni tarehe ngapi TBC itaanza kusikika Kakonko?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni kweli kwamba Kakonko ni moja ya zile Wilaya tano za mipakani ambazo zimetengewa fedha katika bajeti ya mwaka huu 2016/2017, ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwamba amekuwa akipambania usikivu katika Wilaya yake na ni kweli kwamba matangazo mengi wanayapata kutoka nchi jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utaratibu ambao tumeanza, tulianza na kufanya tathmini kwamba ni wapi minara iwekwe tayari tulishaomba masafa kutoka TCRA na tumepata, tayari mzabuni ameshapata zabuni ya kufanya kazi hii, lakini time frame tuliyopanga ni mwisho wa mwaka huu wa fedha usikivu utakuwa umeimarika katika Wilaya ya Kakonko na maeneo mengine ambayo ameyataja. Ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na matatizo ya usikivu pia TBC kuna matatizo ya weledi kwa watangazaji. Mfano, kuna watangazaji wa TBC walitangaza uongo kwamba Donald Trump alimpongeza President Magufuli, upambe uliopitiliza mpaka tajiri anashtuka. Sasa wale watu walisimamishwa lakini hivi karibuni nimeanza kuwaona kwenye tv. Walipewa adhabu gani ili wasirudie tena upambe? (Kicheko)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tulichukua hatua za kinidhamu kwa kosa ambalo ni la kiufundi tu ambalo mtu yeyote duniani hapa anaweza kulifanya. Yametokea matatizo kama hayo hayo Kenya yalifanyika na watangazaji wamerudi, tulichokifanya ni kuchukua tu hatua ya muda mfupi. Wazungu wanasema it’s a deterrent kwamba uwe muangalifu zaidi. Ni kitu kinafanyika kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii nikikuletea, tuchukulie tu mfano wa magazeti yote yanayochapishwa kila siku, ninakuhakikishia asilimia 60 utakuta kuna matatizo/makosa ndani, ni kitu cha ubinadamu. Ahsante. (Makofi)
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Nkasi usikivu kwa ujumla hasa mwambao mwa Ziwa Tanganyika katika Tarafa ya Wampembe, Kata ya Kala, Wampembe, Kizumbi pamoja na Ninde hazina kabisa usikivu wa Redio Tanzania, bahati mbaya sana maeneo haya hayana mawasiliano ya barabara ya uhakika. Viongozi ni mara chache wanatembelea maeneo haya ukiacha DC, Mkuu wa Mkoa na viongozi wengine wa Chama. Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha usikivu katika eneo hili ili wananchi wa Ziwa Tanganyika mpakani kule wawe na usikivu wa kutosha kusikiliza matangazo mbalimbali ya nchi yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Kama nilivyotangulia kusema mwanzoni, tuna mpango wa kufanya suluhisho la kudumu ambalo tunaweza kukarabati ile mitambo michache ambayo inaweza ikafika eneo la nchi nzima. Kwa mfano, mtambo ule wa Mwanza unaweza ukaenda mpaka maeneo hayo na tayari tumeshaandika andiko kupeleka kwa mbia wetu wa maendeleo ambaye tayari amekubali kufanya ukarabati wa mitambo hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kabisa, kuliko kusubiri hizi fedha kidogo kidogo za kila mwaka ni bora tukaifufua ile mitambo ya AM ambayo haina matatizo kabisa na sifa zake ni kwamba inakwenda mbali sana na haipati pingamizi la milima.
Kwa hiyo, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge awe na subira ili kusudi tuweze kupata majibu kutoka kwa mbia wetu wa maendeleo na kuweza kufufua mitambo yetu ambapo maeneo hayo aliyoyataja yatapata usikivu pamoja na nchi nzima.
MHE. COSATO DAVID CHUMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwanza nipende kumpongeza Mheshimiwa Mwakyembe nilimuona ameenda kumtembelea yule nahodha wa Serengeti Boys ambaye aliumia wakati wa mashindano ya Gabon. Hilo ni jambo jema maana linawatia moyo sana vijana wetu.
Mheshimiwa Spika, sasa nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, wakati Alphonce Simbu anakwenda kushiriki mashindano kule London Marathon, kati ya magumu aliyokutana nayo ni suala zima la yeye kusaidiwa katika kupata visa. Simbu aliondoka hapa Alhamisi kupitia Afrika Kusini na kwenda kushiriki mashindano siku ya Jumapili, kitu ambacho kilimuathiri sana katika performance yake. Kama angeweza kuondoka mapema maana yake angeweza hata kuwa mshindi kuliko kushika nafasi ya tano. (Makofi)
Swali, je, Serikali iko tayari kuwasaidia wanariadha ambao wame-qualify kwenda kushiriki mashindano makubwa ya Kimataifa katika kuhakikisha kwamba wanapata visa kwa wakati? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kama nilivyosema, mchezo wa riadha hasa katika kushiriki mashindano makubwa ya marathon kwa mfano, Tokyo Marathon inavutia watazamaji wa barabarani yaani wakati mbio zinakimbiwa kiasi cha watu milioni 1.7. London Marathon watu 800,000 wanakuwa wanashuhudia barabarani, Boston Marathon watu milioni moja.
Swali, je, Serikali ipo tayari kugharamia maandalizi ya wanariadha wetu ambao wanakuwa wame-qualify kwenda kushiriki mashindano haya makubwa ambayo kwa namna moja au nyingine watasaidia kutangaza Taifa letu katika utalii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nianze kwa kupokea pongezi za Mheshimiwa Waziri wangu Dkt. Harrison Mwakyembe kutoka kwa Mheshimiwa Chumi, nitamfikishia salamu hizi. Vilevile nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Chumi, kwa kujali kanuni na kujikita katika maswali ambayo yapo ndani ya swali la msingi, ambayo yanahusu riadha, namshukuru sana na ninampongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Vile vile nimpongeze sana kwa sababu yeye ni mwanariadha wa vitendo, kila siku asubuhi huwa tunakutana naye katika uwanja wa Jamhuri akikimbia. Nina imani kabisa kwamba sasa hivi anaweza akawa anakidhi vigezo vya mashindano ya kimataifa.
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Mheshimiwa Spika, kwanza nikubaliane naye kwamba kweli huyu Alphonce Simbu wakati anakwenda katika mashindano ya London alipata matatizo ya kupata visa. Hata hivyo baadaye alifanikiwa kutokana na Serikali kuingilia kati zoezi hili.
Mheshimwia Spika, sasa niseme tu kwamba, mashindano haya huwa yanasimamiwa na vyombo mbalimbali. Kuna yale mashindano ambayo yanasimamiwa na International Federations lakini yapo mashindano ambayo yanasimamiwa na Olympic Committees. Kwa mfano, yapo mashindano ambayo yanasimamiwa na Shirikisho la Riadha la Taifa, lakini pia mashindano ambayo yanasimamiwa na Tanzania Olympic Committee (TOC). Sasa haya ni yale ya Jumuiya ya Madola na yale ya Olympic. Ukiangalia mwanzoni Simbu hakupata matatizo wakati wanakwenda kwenye mashindano ya Olympic, ni kwa sababu hii TOC ilifanya maandalizi mapema.
Mheshimiwa Spika, sasa haya mashindano yake ya pili ni kwamba alichelewa na kwa maana hiyo, napenda kutoa wito kwa wanariadha wote ambao wanapata sifa au vigezo vya kushiriki mashindano yoyote ya kimataifa au kupata mialiko yoyote ya kushiriki mashindano ya kimataifa, wale mawakala au mameneja wao au mashirikisho au pengine vyama, tunavishauri viwasiliane na Serikali mapema ili kusudi Serikali iweze kufanya mipango na kuwasiliana na maafisa wetu wa Ubalozi na kuondoa usumbufu huu ambao ameusema; kwamba wakati mwingine unasababisha mtu kutokufanya vizuri. Kwa hiyo Serikali tukipata taarifa mapema, tunaweza tukasaidia kwa haraka sana ili kusudi mshindanaji na mchezaji ule aweze kupata visa mapema.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili linauliza kama Serikali ipo tayari kugharamia maandalizi. Maandalizi kimsingi yanafanywa na vyama, vilabu na mashirikisho. Kwa kuzingatia kwamba michezo hii ni mali ya jamii na wanamichezo wenyewe wanatokana na jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nirudie tu kusema kwamba maandalizi yanapofanyika mapema, na hasa ile mipango ya vyama au mashirikisho, inapotufikia Serikalini mapema inakuwa ni rahisi kwetu kujua wale wamekwama wapi, wanamikakati gani na hivyo tunaweza tukasaidia katika maandalizi.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano tu niseme kuna wanariadha ambao wanatarajia, wanavigezo vya kwenda kufanya mashindano ya Common Walk Games Australia mwezi wa nne ambapo wako sita. Tumeshaanza kufanya mazungumzo na Serikali ya Ethiopia ili kusudi waweze kuweka kambi ya miezi nane kule Ethiopia na kupata utaalam na kuweza kufanya vizuri katika mashindano hayo. Hata hivyo tuko katika utaratibu wa kutafuta vyanzo endelevu vya mapato ili kuweza kuwasaidia wanamichezo wote siku za baadaye. Ahsante. (Makofi)