Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Additional Questions to the Prime Minister from Hon. Amina Saleh Athuman Mollel (1 total)

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, vilevile naishukuru sana Serikali yangu inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi, nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa majibu mazuri yenye kutia moyo na faraja kwa watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina swali dogo la nyongeza na swali hili ni kwa mujibu wa Mwongozo wa Huduma kwa Watumishi wa Umma Wenye Ulemavu ambao katika kifungu cha 3 (12) chenye vipengele vya (a), (b), (c) na (d) vinatambua na vinasisitiza na kusema kwamba, nitanukuu kidogo; “kutambua kuwa ni haki ya watumishi wenye ulemavu kupatiwa mahitaji yao muhimu kama vile vifaa vya kuwaongezea uwezo, fedha kwa ajili ya matibabu na ukarabati wa afya zao (rehabilitation), nyenzo na vifaa hivi vitolewe na waajiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninataka kupata kauli yako Mheshimiwa Waziri Mkuu, baadhi ya waajiri hawatekelezi majukumu haya kwa watumishi wa umma wenye ulemavu. Kama baba mwenye dhamana, nini kauli yako kwa waajiri wasiotimiza wajibu wao kama Mwongozo wa Utumishi wa Umma unavyowataka kutekeleza mahitaji hayo kwa watumishi wa umma wenye ulemavu? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo ameeleza kwamba, uko mwongozo wa Serikali juu ya Watumishi wa Umma wanaofanya kazi kwenye taasisi zetu za Serikali, lakini pia sio Serikali tu, hata taasisi zisizokuwa za kiserikali, unawataka waajiri wote wanapowaajiri wenzetu ambao wana mahitaji maalum lazima watekelezewe mahitaji yao ili kuwawezesha kufanya kazi yao vizuri. Kwa maana hiyo, kwa upande wa Serikali Wizara zote ziko hapa, Mawaziri wako hapa, Makatibu Wakuu wanaisikia kauli hii na kwamba lazima sasa watekeleze mahitaji na matakwa ya Serikali ya kuwahudumia hawa watumishi wenye mahitaji maalum kulingana na sekta zao. Kama yeye yuko upande wa ukarani, basi wahakikishe ana vifaa vya kutosha kumwezesha kufanya kazi hiyo vizuri na hivyo kila sekta lazima apate huduma hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatoa wito kwa sekta binafsi kutoa nafasi zaidi za ajira kama ambavyo Serikali tunawaajiri wenye mahitaji maalum. Hakuna sababu ya kukwepa kuwaajiri ati kwa sababu unatakiwa kuwahudumia. Wote ni Watanzania na wote wana uwezo na tumethibitisha uwezo wao, pia hata Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, kuthibitisha kwamba sera hii ni yetu ndani ya Serikali ametoa ajira, ameteuwa watumishi ambao wana mahitaji maalum na hawa wote mahali pao pa kazi wanawezeshwa kwa vifaa vitakavyowawezesha kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nikuhakikishie tutaendelea kuajiri ndani ya Serikali na ninatoa wito kwa sekta binafsi ziajiri Watanzania wenzetu wenye mahitaji maalum wote ambao tunaajiri, wenye mamlaka ya kuajiri, na
Mwenyekiti wa Tume ya Ajira yuko hapa wa Chama cha Waajiri yuko hapa, asikie ili awaelekeze wenzake kwamba, ni wajibu wa kila muajiri kuwawezesha wenye mahitaji maalum kufanya kazi zao baada tu ya kuajiri, kama ambavyo Sera ya Serikali inahitaji kufanya hivyo. Ahsante.