Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Esther Nicholus Matiko (30 total)

MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-
Hospitali ya Mji wa Tarime hutoa huduma kwa wananchi wa Wilaya za Tarime, Rorya, Serengeti na nchi jirani ya Kenya na kwamba hospitali hii ina ukosefu mkubwa wa madawa na vifaa tiba:-
Je, Serikali ina mpango mkakati gani wa kuhakikisha hospitali hii inakuwa na madawa pamoja na vifaa tiba vya kutosha kutoka MSD?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali namba 55 la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa huduma na vifaa katika vituo vya kutolea huduma za afya ni mojawapo ya vipaumbele vya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015, Serikali ilipeleka kiasi cha shilingi bilioni 37.2 Bohari ya Dawa yaani MSD ili kuboresha uwezo wa Bohari ya Dawa kuhudumia vituo vya kutolea huduma za afya ambapo hospitali ya mji wa Tarime ilipata shilingi milioni 76.5.
Mheshimiwa Spika, aidha, katika bajeti ya mwaka 2015/2016, Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 51 kwa ajili ya dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kwa ajili ya hospitali ya Mji wa Tarime. Hadi sasa hospitali hii imeshapelekwa kiasi cha shilingi milioni 35.8.
Mheshimiwa Spika, pamoja na Serikali kutenga bajeti kwa ajili ya kununulia dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi. Serikali imejipanga kuimarisha ukusanyaji na udhibiti wa mapato yatokanayo na uchangiaji huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya ikiwemo hospitali ya Mji wa Tarime.
Mapato hayo yataelekezwa katika kuhakikisha dawa na vifaa vinapatikana muda wote vinapohitajika katika vituo vya kutolea huduma za afya. Mapato hayo ni kama ifuatavyo; uchangiaji wa papo kwa papo, mapato yatokanayo na Mfuko wa Taifa na Bima ya Afya na fedha zitokanazo na Mfuko wa Afya ya Jamii. Aidha, Serikali imeandaa Mpango wa Afya kwa wote na italeta Bungeni Rasimu ya Sheria ya Mpango huo ili kila mwananchi apate Bima ya Afya itakayosaidia kuondokana na changamoto ya kukosa dawa na huduma nyingine za matibabu.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-
Mnada wa Magena Wilayani Tarime ulifungwa na kusababisha adha kubwa kwa Halmashauri ya Mji wa Tarime kupoteza mapato ya ushuru wa mifugo inayouzwa nchi jirani ya Kenya, sambamba na ukosefu wa ajira kwa wakazi wa Tarime:-
Je, Mnada huu wa Magena utafunguliwa lini ili kutoa fursa za ajira na kuokoa mapato mengi yanayopotea kwa sasa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther N. Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mnada wa Magema ulikuwa kati ya minada 10 ya mipakani inayoendeshwa na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Mnada huo ulikamilika kujengwa mwaka 1995 na kufunguliwa mwaka 1996 na ulifanya kazi kwa takribani mwaka mmoja ambapo ng’ombe 104,000 waliuzwa na jumla ya Sh.260,000,000 zilikusanywa kama maduhuli ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza ikiwemo wizi wa mifugo na sababu za kiusalama, mnamo tarehe 14 Mei, 1997, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mara iliagiza mnada huo ufungwe. Ili kuwapatia wafugaji mnada mbadala wa mpakani, Wizara imejenga mnada eneo la Kirumi sehemu ambayo kuna kizuizi asili cha Mto Mara na ujenzi wa Mnada wa Kirumi unaendelea na umekamilika kwa asilimia sitini na unatarajiwa kufunguliwa katika mwaka wa fedha ujao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matunda ya mnada huu yameanza kuonekana ambapo Wizara kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa imekusanya jumla ya Sh.221,270,000 kutokana na mauzo ya ng’ombe 9,842, mbuzi na kondoo 4,886 kutoka Mikoa ya Rukwa, Simiyu, Shinyanga, Mara, Mwanza na Kagera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inatoa wito kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kusimamia ipasavyo ukusanyaji wa maduhuli katika minada ya awali ya Mtana, Kewenja, Nyamwaga na Chemakolele. Aidha, ili kupanua wigo wa ukusanyaji wa mapato, Wizara inatoa ushauri kwa Halmashauri za Wilaya ya Tarime kuongeza thamani ya mifugo kwa kujenga kiwanda cha kuchinja, kuchakata, kusindika na kufungasha nyama na bidhaa kadhaa ili kuziuza katika soko la kikanda na nchi za Afrika Mashariki na Kati.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-
Serikali ina mamlaka ya kutwaa ardhi na kubadilisha matumizi na kwa kufanya hivyo, Serikali inawajibika kusimamia na kuhakikisha wananchi wanaopisha matumizi mapya ya ardhi wanalipwa fidia stahiki ikiwa ni pamoja na kuwapa maeneo mbadala ili kuweza kuendeleza shughuli zao:-
Je, ni kwa nini Serikali imeshindwa kuwalipa fidia wananchi wa Kata za Nyamisangura na Nkende waliopo Halmashauri ya Mji wa Tarime ambao ardhi yao ilichukuliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) tangu mwaka 2007?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Matiko, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali huwa inatwaa ardhi kwa matumizi ya umma kwa kufuata Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999. Utaratibu huo hufuatwa kwa nchi nzima ikiwemo Nyamisangura na Nkende eneo ambalo linafahamika pia kwa jina la Nyandoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hilo lina Kiteule cha Askari wa Miguu kwa ajili ya ulinzi wa mpaka wa kati ya Musoma na Arusha. Mchakato wa kulitwaa eneo hili ulianza miaka ya nyuma na mnamo mwaka 2012 Wizara yangu ilitoa fedha kiasi kwa Halmashauri ya Mji wa Tarime ili kuwezesha kazi ya uthamini wa mali za wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya uthamini haikuweza kukamilika kwa sababu kiasi cha fedha kilichotolewa hakikutosha kumaliza kazi hiyo kutokana na ufinyu wa bajeti. Hivi sasa fedha za kukamilisha zoezi hilo zimepatikana na tayari zimeshatumwa kwa Halmasauri ya Mji wa Tarime.
Hatua inayofuata ni Halmashauri kukamilisha jedwali za uthamini na kuziwasilisha kwa Mthamini Mkuu wa Serikali kwa kupitishwa, kabla ya kuletwa Wizarani kwangu kwa ajili ya kuombewa fedha za malipo ya fidia kutoka Hazina.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-
Madiwani na Wenyeviti wa Mitaa/Vijiji wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu sana, hali wakiwa ndiyo viungo wa shughuli za maendeleo katika jamii:
(a) Je, ni lini Serikali itaaanza kuwalipa mshahara au posho Wenyeviti wa Mitaa au Vijiji?
(b) Je, kwa nini Madiwani wasiwe na ofisi zao kama ambavyo Wabunge hupewa ofisi zao?
(c) Je, ni lini Ofisi za Wenyeviti wa Mitaa au Vijiji zitajengwa ili kuepusha kuwa na ofisi majumbani kwako?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA): alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko Mbunge wa Tarime Mjini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua wazi kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Madiwani na Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa katika kusimamia shughuli za maendeleo nchini. Serikali imeweka utaratibu wa kuwalipa posho Viongozi hao kila mwezi ambapo kwa Madiwani posho hiyo imeongezeka kutoka 120,000 mwaka 2010/2011 hadi shilingi 350,000 mwaka 2015 kwa mwezi. Kwa upande wa Wenyeviti wa Vijii na Mitaa posho hizo zinalipwa na Halmashauri kupitia asilimia 20 ya mapato ya ndani inayojumuisha ruzuku ya fidia ya vyanzo vilivyofutwa. Tunafahamu ziko changamoto kwa baadhi ya Halmashauri kutolipa posho hizo kutokana na makusanyo madogo. Mkakati uliowekwa na Serikali ni kuongeza makusanyo ya mapato ya ndani kwa kubadili mifumo ya ukusanyaji pamoja na kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kujenga uwezo wa kulipa posho hizo.
(b) Serikali inatambua umuhimu wa Madiwani kuwa na ofisi kutokana na majukumu makubwa waliyonayo. Ofisi ya Diwani inatakiwa kuwemo ndani ya ofisi ya Kata, ambayo ndani yake inajumuisha ukumbi wa mikutano ya Kamati ya Maendeleo ya Kata, Ofisi ya Mtendaji wa Kata na Ofisi za Maafisa Wataalam ngazi ya Kata. Ujenzi wa ofisi hizo unafanyika kupitia bajeti za Halmashauri kwa kuzingiatia vipaumbele vinavyopitishwa na Mabaraza ya Madiwani.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa ofisi za Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa unafanyika kupitia bajeti za kila Halmashauri. Hivyo kila Halmashauri inapaswa kuhakikisha inaweka kipaumbele na kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hizo kwa awamu.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-
Askari Magereza katika Mji wa Tarime wamekuwa wakilalamika kuwepo kwa mlundikano wa mahabusu ndani ya Gereza la Mji wa Tarime. Hii inatokana na mlundikano wa kesi ndani ya Mahakama ya Wilaya kwa kigezo cha upelelezi kutokamilika:-
(a) Je, kwa nini kesi zenye vigezo vya dhamana watuhumiwa wasipewe dhamana ili kupunguza mlundikano wa mahabusu na gharama kwa Serikali?
(b) Je, nini mkakati mahususi wa Serikali katika kuhakikisha Jeshi la Polisi linamaliza upelelezi kwa wakati ili kuweza kupunguza mlundikano?
(c) Je, ni hatua gani zinachukuliwa kwa Askari Polisi ambao wanawabambikia kesi wananchi na kupoteza nguvu kazi za Taifa kwa kuwafanya wananchi waishi Gerezani?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi nchini, chini ya Kifungu 64 cha Sheria na Mwenendo wa Makosa ya Jinai limepewa mamlaka ya kutoa dhamana kwa baadhi ya makosa kabla washtakiwa kufikishwa Mahakamani. Mara nyingi mahabusu wanaendelea kukaa magerezani licha ya makosa yao kuwa ya dhamana kwa kushindwa kukamilisha masharti chini ya Kifungu 148(5), (6) na (7) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20 na masharti mengine yanayotolewa na Mahakama.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutoa mafunzo ya upelelezi ya muda mfupi na muda mrefu nje na ndani ya nchi ili kuwajengea weledi wapelelezi na kufanya upelelezi kufanyika na kukamilika kwa wakati. Aidha, Wakuu wa Upelelezi wa Mikoa na Wilaya wanaendelea kuboresha mifumo ya usimamizi wa upelelezi na kukagua mafaili mara kwa mara ili kujionea mwenendo wa kesi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa siyo kweli kwamba Askari Polisi hukumbatia kesi za wananchi. Uhaba wa vitendea kazi vya uchunguzi ambavyo hupatikana Makao Makuu tu, vile ambavyo ni vya kisayansi kuchelewa kupatikana kwa majibu ya uchunguzi wa kisayansi kutoka vyombo vingine, ni baadhi ya sababu ambazo zinafanya baadhi ya upelelezi kuchukua muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, iwapo kuna malalamiko dhidi ya Polisi, uchunguzi hufanyika kwa mujibu wa Kanuni ya 103 ya Kanuni za Kudumu za Polisi na Askari akipatikana kwa makusudi akawa na hatia, hatua za kinidhamu na kisheria huchukuliwa dhidi yake.
MHE. ESTHER N. MATIKO Aliuliza:-
Kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa leseni za udereva katika Mkoa wa Polisi Tarime/Rorya kutokana na kutokuwepo kwa huduma hiyo. Hali hiyo inapelekea wananchi kupata adha kubwa ya kufuata huduma za leseni Musoma Mjini ambao ni Mkoa mwingine wa Polisi; kutokana na adha hiyo wananchi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali waliamua kujenga na kukamilisha jengo la usalama barabarani:-
(a) Je, ni lini Mkoa wa Polisi Tarime/Rorya utafungiwa mitambo ya kutoa leseni za udereva ili kuondoa usumbufu uliopo sasa wa kutumia gharama na muda kufuata huduma hiyo Musoma Mjini?
(b) Je, ni lini Ofisi za Mkoa wa Polisi Tarime/Rorya zitajengwa ili kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania na Jeshi la Polisi Usalama Barabarani imekuwa ikiboresha huduma za utoaji leseni za udereva na ukusanyaji wa ada za leseni ili kuhakikisha kuwa huduma hizi zinawafikia wananchi bila usumbufu. Serikali kupitia taasisi hizi imefunga mitambo ya kutoa leseni za udereva kila Makao Makuu ya Mkoa ambapo wananchi wote wanaohitaji huduma hizi hufika Mkoani na kuhudumiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kufunga mitambo hii kunahitajika maandalizi makubwa ya kifedha na uandaaji wa miundombinu ya mtandao, majengo na rasilimali watu. Kwa sasa, mitambo hiyo imefikishwa hadi kwenye Mikoa ya kikodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania. Serikali ingependa kufunga mitambo ya kutoa leseni za udereva katika ngazi za Wilaya ikiwemo Wilaya ya Tarime/Rorya. Hata hivyo, kwani gharama za kufunga mitambo hii katika Wilaya zote nchini ni kubwa mno. Serikali inao mkakati wa kufikisha huduma hizi Wilayani ikiwemo Wilaya ya Tarime/Rorya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kipolisi Tarime/ Rorya ni miongoni mwa Mikoa mipya ambayo bado haijajengewa ofisi mpya za kisasa ikiwemo Songwe, Katavi, Simiyu na Geita. Serikali inatambua uhaba huo wa ofisi katika mikoa hiyo na kuna mkakati wa ndani wa kujenga ofisi hizo kwa kutumia rasilimali zilizopo kama nguvu kazi ya wafungwa na kutengeneza matofali ya kujengea ofisi hizo muhimu kwa huduma ya Kipolisi na Idara zingine za Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
MHE. CATHERINE N. RUGE (K.n.y. MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-
Wilaya ya Tarime imepakana na Ziwa Victoria na Mto Mara ambao sehemu yake kubwa uko ndani ya Wilaya ya Tarime, licha ya kuwa karibu sana na vyanzo vya maji, wananchi wa Tarime Mjini kwa muda mrefu wamekuwa wanatumia maji ya Bwawa la Kenya Manyori lililojengwa na Mjerumani ambalo halijawahi kufanyiwa usafi tangu kuchimbwa kwake na kupelekea wananchi watumie maji yasiyo safi na salama kwa matumizi ya binadamu.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka maji ndani ya Mji wa Tarime kutoka Ziwa Victoria na Mto Mara kama ilivyowahi kuyapeleka Shinyanga?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta wataalam kusimamia na kuendeleza chanzo cha maji kilichopo japo hakikidhi mahitaji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeandaa mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda Mji wa Tarime. Usanifu na uandaaji wa makabrasha ya zabuni ya mradi huo ulikamilika mwaka 2012 na kwa sasa Serikali inafanya mapitio ya usanifu wa mradi huo (design review) na kazi hiyo inatarajiwa kukamilika mwezi Disemba, 2017. Baada ya mapitio ya usanifu wa mradi kukamilika na gharama za ujenzi kufahamika, Wizara itatafuta fedha kutoka kwenye vyanzo vya ndani na nje, kadri hali itakavyoruhusu ili mradi uweze kujengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) imeandaa mradi wa kuboresha chanzo cha sasa cha Mto Nyandurumo ili kiweze kuzalisha maji mengi zaidi. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya upanuzi wa choteo la maji (water intake) ili liweze kuingiza maji mengi zaidi.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-
Kufuatia utoaji wa elimu ya msingi bure, shule za msingi na sekondari ndani ya Halmashauri ya Mji wa Tarime zimekuwa na upungufu mkubwa wa madarasa na madawati hadi kufikia walimu kulazimika kufundishia chini ya mti na wanafunzi walio madarasani wanakaa kwenye sakafu kwa idadi kubwa kinyume na matakwa ya Sera ya Elimu.
Je, ni nini mpango wa Serikali wa kuhakikisha shule hizo ndani ya Halmashauri ya Mji wa Tarime zinaondokana na changamoto za miundombinu ya kufundishia na kujifunzia ili kutoa elimu bora?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya miundombinu ya elimu nchini ni matokeo ya mwitikio mkubwa wa wananchi katika utekelezaji wa Mpango wa Elimu Bila Malipo ambao umetoa fursa kwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule kupata fursa hiyo. Shule 30 za msingi katika Halmashauri ya Mji wa Tarime zinahitaji vyumba vya madarasa 625, vyumba vya madarasa vilivyopo ni 215 na upungufu ni vyumba vya madarasa 410. Aidha, madawati yanayohitajika ni 8,888; madawati yaliyopo ni 6,066 na upungufu ni madawati 2,823.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule nane za sekondari katika Halmashauri ya Mji wa Tarime zinahitaji kuwa na vyumba vya madarasa 133, madarasa yaliyopo ni 104 ma upungufu ni madarasa 29. Aidha, katika shule hizo kuna ziada ya madawati 421 kutokana na mwitikio mzuri wa wananchi na jitihada za Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo kupitia fedha za kuchochea Maendeleo ya Mfuko wa Jimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga shilingi 119,000,000.00 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 16, matundu 19 ya vyoo na kuongeza madawati 154 katika shule za msingi. Vilevile Serikali imetenga shilingi 172,500,000 kupitia ruzuku ya maendeleo na mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 22 na matundu ya vyoo 72.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-
Ardhi ikipimwa huwa na thamani na hivyo kuwafanya wamiliki kupata mikopo katika taasisi za kifedha na kuwekeza katika uchumi. Katika Jimbo la Tarime Mjini ni Kata mbili tu za Bomani na Sabasaba ndizo ambazo ardhi yake imepimwa kwa asilimia 75 kati ya kata nane zilizopo, hii inatokana na upungufu mkubwa wa wataalam wa kupima ardhi.
Je, ni lini Serikali itapeleka wataalam wa kutosha ndani ya Halmashauri ya Mji wa Tarime kuweza kupima ardhi kwa kata sita zilizosalia ili wananchi wa Tarime Mjini waweze kunufaika na ardhi yao?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini, swali lake Na. 359 kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kupanga na kupima ardhi nchini kwa manufaa ya wananchi wake. Halmashauri ya Mji wa Tarime ina wataalam wa ardhi wanne tu ambao ni Afisa Mipango Miji, Afisa Ardhi, Mchora ambaye ni Mrasimu Ramani na Mthamini Mali. Idadi hii ni ndogo ukilinganisha na kasi ya ukuaji wa Mji wa Tarime kwa sasa. Tatizo hili si kwa Mji wa Tarime pekee bali ni tatizo linalozikabili karibu Halmashauri zote nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ili kutekeleza azma ya kupanga na kupima kila kipande cha ardhi kwa nchi nzima, ikiwemo kusajili makampuni binafsi ya kupanga ardhi, yenye weledi wa kufanya kazi hiyo kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo. Hadi sasa tuna jumla ya makampuni 36 ya kupanga miji na makampuni 65 ya kupima ardhi yamesajiliwa ili kuongeza kasi ya upangaji na upimaji wa ardhi nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa inaandaa utaratibu wa kuwatumia wataalam wa sekta ya ardhi kutoka katika maeneo yenye watumishi wa kutosha kufanya kazi katika maeneo yenye uhaba mkubwa wa watumishi na hivyo kuharakisha kasi ya upangaji na kupima ardhi nchini. Halmashauri ya Mji wa Tarime ni mojawapo ya maeneo yanayotarajiwa kunufaika na utaratibu huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu pia inaendelea kuzihimiza Halmashauri zote nchini kutenga fedha za kutosha katika bajeti zao kwa ajili ya kuajiri wataalam wa sekta ya ardhi wanaokidhi mahitaji na hivyo kuongeza kasi ya kupanga na kupima ardhi katika maeneo yao.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-
Mnada wa Magena uliopo Halmashauri ya Mji wa Tarime una miundombinu yote licha ya kufungwa na Serikali bila sababu maalum na kusababisha adha kubwa kwa wananchi wa maeneo hayo pamoja na upotevu wa ushuru. Mwaka 2016 aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi alitembelea mnada huo na kuagiza mnada ufunguliwe.
Je, ni kwa nini mnada huu wa Magena haujafunguliwa mpaka sasa ili kutoa fursa za ajira na kuokoa mapato yanayopotea?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, na mimi naomba uniruhusu kwanza kukukaribisha kama vile walivyokukaribisha Waheshimiwa Wabunge wenzangu katika Bunge letu tukufu.
Mheshimiwa Spika, niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mnada wa Magena ulikuwa kati ya minada 10 ya mipakani uliokuwa chini ya Wizara ya Kilimo na Mifugo mwaka 1995. Mnada huo ulikamilika kujengwa mwaka 1995 na kufunguliwa mwaka 1996 ambapo ulifanya kazi kwa takriban mwaka mmoja, ambapo ng’ombe 104,000 waliuzwa na jumla ya shilingi milioni 260 zilikusanywa kama maduhuli ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza, ikiwemo wizi wa mifugo na sababu za kiusalama, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mara, tarehe 14 Mei, 1997 iliagiza mnada huo ufungwe na kuwapatia wafugaji mnada mbadala wa Mpakani. Kutokana na hali hiyo, uongozi wa Mkoa wa Mara uliiomba Wizara ya Maendeleo ya Mifugo ya wakati huu ifute mnada wa Magena na Kirumi Check Point iteuliwe kuwa mnada wa mpakani kwa kuwa tayari kuna kizuizi cha Mto Mara.
Mheshimiwa Spika, Wizara ilikubali ombi la uongozi wa Mkoa wa Mara na hivyo ikaanza kujenga mnada eneo la Kirumi sehemu ambayo kuna kizuizi cha asili cha Mto Mara na ujenzi huu umekamilika kwa asilimia 80 na unatarajiwa kufunguliwa mwaka huu wa 2017/2018. Kwa kuwa kazi ya Kituo cha Polisi inaendelea na kazi ya kuweka umeme katika eneo lile imekamilika.
Mheshimiwa Spika, mafanikio ya Mnada wa Kirumi yameanza kuonekana ambapo Wizara kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Mara, kuanzia mwezi Julai, 2016 hadi Februari, 2018 imekusanya jumla ya shilingi 221,270,000 kutokana na vibali na faini mbalimbali za ng’ombe 9,842, mbuzi na kondoo 4,886 kutoka Mikoa ya Rukwa, Kagera, Simiyu, Shinyanga, Mara na Mwanza waliokuwa wakisafirishwa kwenda Kenya bila ya vibali. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-
Halmashauri ya Mji wa Tarime imebahatika kuwa na Uwanja wa Ndege wa Magena ambao umekuwa ukitumiwa na watalii wanaokwenda Mbuga ya Serengeti, viongozi mbalimbali na hata Mgodi wa Acacia. Miundombinu ya uwanja pamoja na barabara zake ni mbovu sana.
(a) Je, ni lini Serikali itapanua uwanja huu na kurekebisha miundombinu yake ili ndege nyingi ziweze kutua kwa ajili ya watalii waendao Serengeti?
(b) Je, ni kwa nini Serikali haijajenga jengo la Uhamiaji katika uwanja huo ili kutoa urahisi wa watalii wanaotumia uwanja huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanja cha Ndege Magena kinachomilikiwa na Halmashauri ya Mji wa Tarime kina urefu wa mita 1,470 na upana wa mita 120. Kiwanja hicho kimekodishwa kwa mwekezaji ambaye ni Kampuni ya Coastal Aviation kwa mkataba wa kuilipa Halmashauri kiasi cha milioni 20 kila mwaka. Halmashauri imefanya ukarabati wa baadhi ya miundombinu ya kiwanja ikiwemo kujenga barabara yenye urefu wa kilometa 1.2 kutoka barabara ya Tarime – Sirari kwa kiwango cha changarawe ili kuboresha mazingira ya uwanja huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia halmashauri ya Mji wa Tarime ina mpango wa kujenga Ofisi za Uhamiaji ili kuweka utaratibu mzuri wa kuingia na kutoka kwa watalii wanaokwenda hifadhi ya taifa ya Serengeti.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM (K.n.y. MHE. ESTHER M. MATIKO) aliuliza:-
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limejitwalia maeneo ya wananchi wa Kenyambi na Bugosi kinyume kabisa na sheria baada ya kukaribishwa kwa hifadhi ya muda kufuatia kukatika kwa mawasiliano kati ya kambi yao iliyopo Kata ya Nyandoto na Tarime Mjini:-
a) Je, ni kwa nini Serikali imeshindwa kuwalipa fidia wananchi hao waliochukuliwa ardhi yao na JWTZ tangu mwaka 2007?
b) Je, ni kwa nini JWTZ wasirudi kwenye kambi yao iliyopo Kata ya Nyandoto yenye eneo kubwa kuliko kuchukua maeneo yaliyo katikati ya makazi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inatambua umuhimu wa kulipa fidia ya ardhi iliyotwaliwa. Uthamini kwa ajili ya fidia kwa wananchi umefanyika tangu mwaka 2013. Ufinyu wa bajeti ya Serikali ndiyo umechelewesha kufanyika kwa malipo ya fidia hiyo. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ilitenga shilingi bilioni 20.03 kwa ajili ya ulipaji wa fidia na masuala mengine yanayoendana na upimaji wa maeneo. Naamini fedha hizo zikipatikana, ulipaji wa fidia ya ardhi utafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Nyandoto lipo chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime. Mwaka 1992 Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania lilikabidhi eneo hilo kwa Halmashauri ya Wilaya ambayo imelipangia matumizi mengine.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-

(a) Je, ni kwa nini Serikali imeshindwa kukamilisha mradi wa visima 23 ambavyo vingesaidia kama suluhisho la muda mfupi la tatizo la maji safi na salama katika Mji wa Tarime hususan kwenye maeneo ya Kata za pembezoni kama Nyandoto (Masurula), Nkende, Ketare, Kenyamanyori, Nyamisangura na Turwa?

(b) Mheshimiwa Rais alipofanya ziara Jimbo la Tarime Mjini Julai, 2018 aliwaeleza wananchi kuwa Serikali imetenga takriban shilingi bilioni 14 kwa ajili ya maji kutoka Ziwa Victoria ambayo itaondoa kabisa tatizo la maji katika Mji wa Tarime. Je, ni hatua gani imefikiwa kwenye ahadi hiyo hasa ikizingatiwa kuwa mradi huo upo kwenye mchakato kwa miaka mingi sasa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicolas Matiko, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) imeingia mkataba na Wakala wa Uchimbaji wa Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) kwa ajili ya uchimbaji wa visima 23 katika Mji wa Tarime kwa gharama ya shilingi milioni 536.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa DDCA wanaendelea na utafiti wa maji chini ya ardhi (hydrological survey) na matarajio ya kazi ya uchimbaji wa visima hivyo itakamilika mwezi Septemba, 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utekelezaji wa ahadi ya Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa wananchi wa Tarime, Serikali imeshapata fedha kutoka Serikali ya India kiasi cha dola za Marekani milioni 500 kwa ajili ya uboreshaji wa huduma ya maji kwa miji 28 ya Tanzania Bara pamoja na Zanzibar ambapo Mji wa Tarime ni miongoni mwa Miji itakayopata maji kupitia fedha hizo. Kwa sasa taratibu za kuwapata wataalam washauri watakaofanya usanifu wa kina na uandaaji wa makabrasha ya zabuni unaendelea. Matarajio ya ujenzi wa miradi hiyo itaanza katika mwaka wa fedha 2019/2020.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI (K.n.y. MHE. ESTHER N. MATIKO) aliuliza:-

Serikali imekuwa ikitoa vifaa tiba na dawa vyenye thamani ya Tsh. 4,000,000/= kila baada ya miezi mitatu kwenye zahanati za Halmashauri za Mji wa Tarime kupitia Wakala wa dawa (MSD); kwa miaka miwili iliyopita Serikali imepunguza ugawaji wa dawa na vifaa tiba kutoka thamani ya Tsh. 4,000,000/= mpaka Tsh. 166,000/=; mfano zahanati ya Gamasara imepokea dawa na vifaa tiba vyenye thamani hiyo:-

Je, ni kwa nini Serikali iliamua kupunguza mgao wa dawa kutoka Tsh. 4,000,000/= mpaka Tsh. 166,000/= ilhali idadi ya watu inazidi kuongezeka katika Halmashauri ya Mji wa Tarime na Majimbo ya jirani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini, kama Ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupungua kwa bajeti ya dawa katika Halmashauri ya Mji wa Tarime kunatokana na tathmini ya uwezo wa kuagiza na kutumia dawa wa vituo vya kutolea dawa katika Mji wa Tarime. Mfano, Zahanati ya Gamasara, ilitengewa na kupatiwa kiasi cha shilingi milioni
17.25 katika mwaka wa fedha 2018/2019 na tarehe 30 Juni, 2019, zahanati hiyo ilikuwa imetumia kiasi cha shilingi milioni
4.25 pekee na hivyo kiasi cha shilingi milioni 13 ilichopewa kutumia katika mwaka husika kubakia Bohari ya Dawa (MSD). Hivyo tunazielekeza Halmashauri zote na vituo vya kutolea huduma za afya, kwamba wawe wanazingatia mipango yao ya bajeti katika manunuzi ya dawa na vifaa tiba ili kuweza kuhudumia wananchi ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ufaulu wa wanafunzi katika maomo ya Sayansi na hisabati yanaonekana kushuka kila mwaka, mathalani mwaka 2015 asilimia 85 ya wanafunzi walifeli somo la hisabati matokeo ya kidato cha nne. Aidha, katika masomo mengine ya Kemia, Fizikia na Biolojia ufaulu bado ni duni sana.

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kuinusuru Halmashauri ya Mji wa Tarime na janga hili la ufulu duni katika masomo ya sayasi?

(b) Je, nini mkakati wa Serikali katika kuiwezesha maabara za shule za sekondari zilizojengwa kwa nguvu kubwa ya wananchi ndani ya Jimbo la Tarime mjini kuweza kupata wataalam na vifaa vya maabara ili kuinuka ufaulu kwenye masomo ya Sayansi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko Mbunge wa Tarime Mjini lenye sehemu (a) na (b) kama ifutavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza mipango mbalimbali ya uboreshaji wa elimu ya sekondari nchini ili kuinua kiwango cha ufaulu na ubora wa elimu kwa ujumla. Serikali imeipatia Halmashuri ya Mji wa Tarime walimu 59 wa masomo ya sayansi ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji. Aidha, Serikali katika mwaka wa fedha 2019/20 imepanga kutumia shilingi bilioni 58.2 kupitia EP4R kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya elimu ya sekondari nchini ikiwemo Halmshauri ya mji wa Tarime. Vilevile kupitia mradi mpya wa uboreshaji wa Elimu ya Sekondari nchini, Serikali imepanga kutumia shilingi bilioni 48.9 kwa ajili ya kuboresha elimu ya sekondari nchini.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, katika shule zote tisa za sekondari zilizopo katika Halmashauri ya Mji wa Tarime wanafunzi wanafanya mitihani ya masomo ya sayansi kwa vitendo kwa kutumia maabara zilizopo. Hata hivyo, maabara hizo ni kweli zinakabiliwa na upungufu wa vifaa vya maabara na huduma nyingine kama maji na gesi. Katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali kupitia mpango wa EP4R imepanga kutumia bilioni 58.2 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya shule za sekondari ambapo jumla ya shule 70 zitapatiwa vifaa vya maabara zikiwemo shule za Halmashauri ya Mji wa Tarime.
MHE. ESTHER NI. MATIKO Aliuliza:-

Je, ni lini Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Tarime utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Mji Mdogo wa Tarime wanapata huduma ya maji safi na salama kupitia Mradi wa Maji wa Mserereko Nyandulumo; visima vitatu Rebu, Jeshi la wokovu na Viambwi, na bwawa la maji Tangota. Vyanzo hivi vyote vinazalisha wastani wa lita 1,200 kwa siku wakati jumla ya mahitaji ni lita 6,000 za maji kwa siku. Utekelezaji wa mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria utaweza kuhudumia maeneo yote ya mji wa Tarime kwa kuzalisha wastani wa lita 6,500 kwa siku ambazo ni zaidi ya mahitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika utekelezaji wa mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Tarime, Serikali imepata mkopo kutoka Serikali ya India kupitia Benki ya Exim jumla ya Dola za Marekani millioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji katika miji 28 ya Tanzania Bara na Zanzibar. Moja ya miji itakayonufaika na mkopo huo ni Mji wa Tarime ambao utatumia chanzo cha Ziwa Victoria. Kwa sasa mradi upo katika hatua za manunuzi ya wakandarasi wanaotarajiwa kuwepo eneo la mradi ifikapo mwezi Aprili, 2021 na ujenzi wa mradi unatarajiwa kuchukua miezi 24.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza: -

Je, ni lini Mnada wa Mifugo wa Magena uliopo Halmashauri ya Mji wa Tarime utafunguliwa kama ambavyo Serikali iliahidi Mwaka 2016?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba uniruhusu, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama katika podium hii, nimshukuru sana Mwenyezi Mungu na pili, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini kuhudumia katika Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya shukrani hizi, naomba sasa kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, nijibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mnada wa Mifugo wa Magena, ulikamilika kujengwa mwaka 1995 na kufunguliwa mwaka 1996, ambapo ng’ombe 104,000 waliuzwa na jumla ya Shilingi za Kitanzania 260,000,000/= zilikusanywa kama maduhuli ya Serikali. Hata hivyo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mara mwaka 1997 iliagiza mnada ufungwe kutokana na changamoto zilizojitokeza ikiwemo wizi wa mifugo na sababu za kiusalama. Uongozi wa Mkoa wa Mara uliwasilisha ombi rasmi Wizarani la kufuta mnada wa Magena na kupendekeza mnada huo uhamishiwe eneo la Kirumi Check Point.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ilijenga Mnada wa Kirumi wa Mpakani kwa gharama ya shilingi milioni 321.3 na ulifunguliwa rasmi tarehe 16 Oktoba, 2018. Aidha, tangu uanze kufanya kazi, jumla ya ng’ombe 34,855, mbuzi na kondoo 5,808 wameingia mnadani hapo na jumla ya shilingi milioni 428.9 zimekusanywa kama maduhuli ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia maoni kutoka mamlaka za Mkoa, Wizara itakuwa tayari kuurejesha Mnada wa Magena kwa kufuata taratibu za uanzishwaji upya wa minada na kwa mujibu wa Sheria ya Nyama Na. 10 ya mwaka 2006.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-

Je, ni kwa nini Hospitali ya Mji Tarime isipandishwe hadhi na kuwa Hospitali ya Kanda Maalum ya Tarime na Rorya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Mji Tarime ina Wodi nane na vitengo mbalimbali vya huduma ikiwemo maabara, jengo la mionzi, chumba cha upasuaji, huduma za mama na mtoto, chumba cha dawa, chumba cha magonjwa ya akili, macho, duka la dawa lakini pia miundombinu mingine. Hospitali hii inahudumia wastani wa wagonjwa 140 wa nje (OPD), lakini inahudumia wagonjwa 70 wanaolazwa kwa siku. Hospitali ina jumla ya vitanda 180.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kanda ya Ziwa tayari ina Hospitali ya Rufaa ambayo ni Hospitali ya Bugando iliyopo Mkoa wa Mwanza. Hivyo, Serikali haikusudii kuipandisha hadhi Hospitali ya Mji Tarime kuwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Maalum ya Tarime na Rorya. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza: -

Je, ni lini ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Musoma utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther N. Matiko, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha mchakato wa manunuzi kwa ajili ya kumpata mkandarasi atakaetekeleza mradi huu. Aidha, mkataba kati ya Serikali na mkandarasi Beijing Construction Group Co. Ltd umesainiwa Disemba, 2020 na utekelezaji wa mradi huu utakamilika kwa kipindi cha miezi 18, baada ya kuanza hatua za utekelezaji. Hivi sasa Serikali imemaliza awamu ya pili ya malipo ya fidia kwa wananchi watakaopisha mradi huu ili kuruhusu mkandarasi kuanza hatua ya utekelezaji wa ujenzi. Hata hivyo, Serikali imeshamkabidhi mkandarasi eneo la mradi.

Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Esther N. Matiko kwamba, Serikali ina nia ya dhati ya kukarabati na kupanua Kiwanja cha Ndege cha Musoma na utekelezaji wake utakamilika baada ya miezi 18 kama nilivyosema nilivyosema. Ahsante.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza: -

Je, ni lini mradi wa ujenzi wa soko la kisasa katika Halmashauri ya Mji wa Tarime wenye thamani ya shilingi bilioni 8.07 utakamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais -TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji wa Tarime ilikidhi vigezo vya kupatiwa Shilingi bilioni 8.07 kwa ajili ya ujenzi wa soko la kisasa kupitia utaratibu wa Miradi ya Kimkakati mwezi Februari, 2019. Kutokana na changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi ya kimakatati Serikali ilisitisha baadhi ya miradi ya kimkakati iliyoidhinishwa ukiwemo mradi wa ujenzi wa soko la kisasa katika Halmashauri ya Mji wa Tarime. Hata hivyo, Serikali imetoa kibali kwa Halmashauri ya Mji Tarime kuendelea na ujenzi wa Soko na katika mwaka wa fedha 2021/2022, shilingi bilioni tatu zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa soko katika Mji wa Tarime.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji Tarime inatarajia kutangaza kazi ya ujenzi wa soko la kisasa mwezi Julai, 2021 na ujenzi unatarajiwa kuanza mwezi Agosti, 2021 baada ya kumpata mkandarasi. Halmashauri imejipanga kukamilisha mradi huo ndani ya miezi 12 tangu tarehe ya kusaini mkataba.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-

Ukatili kwa watoto umekithiri nchini kama vile ubakaji, ulawiti, kuchomwa moto na mimba za utotoni.

(a) Je ni watoto wangapi wamefanyiwa ukatili huo kwa jinsia zao wa kike na wa kiume?

(b) Je kuna takwimu halisi ya hatua zilizo chukuliwa na Serikali dhidi ya matukio hayo nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko Mbunge Viti Maalum lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuanzia Januari hadi Septemba 2021 takwimu ya vitendo vya ukatili kwa watoto vilivyoripotiwa Vituo vya Polisi inaonyesha jumla ya watoto 6,168 wamefanyiwa ukatili na kati yao wanawake 5,287 na wanaume 881, waliobakwa ni 3,524, waliolawitiwa ni 637 kati yao wanaume 567 na wanawake 70, waliochomwa moto ni 130 kati yao wanaume 33 na wanawake 97, waliopata mimba ni 1,877.

Mheshimiwa Spika, kesi na watuhumiwa waliokamatwa na kufikishwa Mahakamani ni 3,800, kesi zilizo chini ya upelelezi ni 2,368 na kesi zilizohukumiwa ni 88 na nyingine ziko kwenye hatua mbalimbali Mahakamani. Nakushukuru.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itanunua Magari ya kisasa ya Zimamoto ili kunusuru maisha ya raia na mali zao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeandaa mpango mkakati wa kuimarisha huduma za zimamoto na uokoaji nchini kwa kuimarisha na kuongeza vifaa vya kisasa vya utendaji kazi katika Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Vifaa hivi vya kisasa vitaenda sambamba na upelekaji wa huduma ya zimamoto na uokoaji katika wilaya zote ambazo hazina huduma hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini imetenga bajeti ya maendeleo ya shilingi bilioni 2 katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya kununua magari mapya ya kisasa ya zima moto. Lengo la ununuzi wa magari haya ni kuongeza ufanisi kwenye shughuli za kuokoa maisha na mali za wananchi, pindi patokeapo ajali za moto na nyingine. Taratibu zote za ununuzi zikikamilika, magari ya kuzima moto yatapelekwa mikoa isiyokuwa na huduma ya zimamoto na uokoaji. Serikali itaendelea kutenga fedha kila mwaka ili kuliwezesha vitendea kazi stahiki Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza: -

Je, kwa takwimu ni wahitimu wangapi wa kada ya Ualimu wa masomo ya sayansi na hesabu hawajaajiriwa tangu mwaka 2015?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Esther Nicholaus Matiko, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tangu mwaka 2015 hadi 2022 jumla ya wahitimu 33,492 wa kada ya Ualimu wa Masomo ya Sayansi na Hisabati wamehitimu mafunzo katika Vyuo mbalimbali vya Ualimu na Vyuo Vikuu. Kati yao wahitimu 13,383 wameajiriwa katika shule mbalimbali nchini tangu mwaka 2015. Aidha, wahitimu 20,109 hawajaajiriwa katika shule za Serikali.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuajiri ili kukidhi mahitaji ya Walimu katika shule za umma. Nakushukuru sana.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza: -

Je, ni kwa nini Serikali isianzishe madawati ya kijinsia katika ngazi za Kata na Vijiji kutokana na ongezeko la vitendo vya ukatili?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamaii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholus Matiko Mbunge wa viti maalumu kama ifuatvyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kudhibiti vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii ambapo imeratibu uanzishwaji wa madawati 420 ya Jinsia katika vituo vya Jeshi la Polisi, na 153 vya Jeshi la Magereza. Aidha, madawati ya ulinzi wa watoto yameanzishwa katika shule za msingi na sekondari. Vile vile, madawati ya jinsia yanaanzishwa kwenye vyuo vyote nchini pamoja na maeneo ya umma kama kwenye masoko. Kwa upande mwingine, kKamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto zimeanzishwa katika ngazi ya mtaa/vijiji hadi Taifa kwa asilimia 88. Madawati haya yanachangia kwa kiasi kikubwa katika kushughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia katika jamii. Ahsante
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza: -

Je, ni kwa nini Serikali imeshindwa kukamilisha ujenzi wa soko la kimkakati la Kimataifa la Remagwe?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na masoko ya Kimkakati kwa ajili ya kukuza biashara na mauzo nje ya nchi, kwa maendeleo na ustawi wa wananchi wake.

Mheshimiwa Spika, Serikali iliamua kuanzisha masoko ya kimkakati ya Kimataifa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa soko la Remagwe katika mpaka wa Sirari chini ya Mradi wa Uwekezaji wa Sekta ya Kilimo Wilayani, District Agricultural Sector Investment Project (DASIP) uliokuwa unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kukamilisha ujenzi wa soko hilo.

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza: -

Je, ni lini Wananchi wa Kitongoji cha Nyamichele watalipwa fidia kutokana na madhila waliyoyapata kutoka Mgodi wa Barrick?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mgodi wa Barrick North Mara kwa sasa hauhitaji eneo la Kitongoji cha Nyamichele kama wananchi walivyokuwa wametarajia hapo kabla.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Mgodi wa North Mara kutohitaji eneo hilo, kuna utaratibu ambao unaandaliwa na mgodi huo wa kutoa kifuta jasho kwa wananchi waliopata madhila kutoka kwa mgodi huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza: -

Je, lini Mlima Nkongore utarudishwa kwa Wananchi wa Kata ya Katare baada ya kuchukuliwa na Jeshi la Magereza?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge, Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya hifadhi na milima kama ilivyo kwa Mlima Nkongore, kisheria huwa yapo chini ya Halmashauri ya uendelezaji miji husika. Aidha, mwanzoni mwa mwaka 2016 baadhi ya wananchi walianzisha shughuli za kilimo cha mazao mbalimbali ikiwemo mazao haramu ya bangi katika eneo la kuzunguka Mlima Nkongore uliopo chini ya Halmashauri ya Mji wa Tarime.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia kilimo kilichokuwa kinafanyika katika maeneo ya Mlima Nkongore, pia kutokana na Sheria ya Mazingira Na. 20 ya mwaka 2004, kifungu cha 58(1) na (2) kinachozuia kufanya shughuli zozote zinazoweza kupelekea hifadhi ya mlima kuharibiwa kwa kuwa maeneo hayo yanatakiwa yahifadhiwe kisheria. Kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya cha tarehe 11 Novemba, 2017 kiliazimia kuwa eneo la Mlima Nkongore likabidhiwe kwa Jeshi la Magereza ili kuimarisha shughuli za ulinzi na usalama. Kupitia barua Kumb. Na. AB.284/311/01C/59 ya tarehe 17 Novemba, 2017 ni idhini rasmi ya kukabidhi eneo la mlima Nkongore kwa Jeshi la Magereza kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usalama pamoja na uhifadhi wa mazingira, ahsante.
MHE. GRACE V. TENDEGA K.n.y. MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza: -

Je, ni asilimia ngapi ya Watanzania wameandikishwa na kupatiwa Vitambulisho vya Taifa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: =

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia Tarehe 31 Julai, 2023, jumla ya Watanzania 11,242,736 wamepewa vitambulisho, sawa na asilimia 55 ya lengo la kuwapatia wananchi 20,294,910 wanaostahili kupewa. Mpango wa Serikali ni kuwagawia vitambulisho Watanzania waliobaki ifikapo Machi, 2024, ninakushukuru.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga Vituo vya Afya katika Kata za Mji wa Tarime kwa kuwa kuna Kituo kimoja tu cha Afya Nkende?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEORGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali ilitenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha kimkakati cha Ketare katika Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa kujenga jengo la kuhudumia wagonjwa wa nje (OPD), Maabara, Jengo la Wazazi, Jengo la upasuaji na Jengo la Kufulia na ujenzi umekamilika na kituo kimeanza kutoa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya Afya katika Kata za kimkakati kote nchini, zikiwemo Kata za Mji wa Tarime.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua changamoto za Viwanda vya Nguo nchini kwani ni viwanda vitatu tu kati ya 33 vinafanya kazi?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, sekta ndogo ya nguo na mavazi nchini ina jumla ya viwanda tisa vinavyofanya kazi hivi sasa. Serikali inaendelea kutatua changamoto zinazokabili viwanda vya nguo, ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini, kudhibiti bidhaa zisizo na ubora na bidhaa bandia kutoka nje ya nchi, kuongeza ushuru wa forodha kwa kanga na vitenge vinavyotoka nje ya nchi, kuhamasisha Taasisi za Umma na Watanzania kwa ujumla kununua bidhaa za nguo zinazotengenezwa na viwanda vya hapa nchini na kuweka miundombinu wezeshi.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.