Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Marwa Ryoba Chacha (16 total)

MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:-

Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na uvamizi wa tembo kutoka Hifadhi ya Serengeti na kupelekea vifo na uharibu wa mashamba katika Wilaya ya Serengeti na maeneo jirani:-

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kunusuru maisha na mali za Watanzania waishio Serengeti?

(b) Je, Serikali ina mpango wa kutathimini upya fidia inayotolewa kwani haiendani na uhalisia wa uharibifu wa mali na upotevu wa maisha ya watu?
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa spika, kwa kuwa hii ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu katika jukumu hili nililopewa, napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu na kwa kweli namrudishia sifa na utukufu. Lakini pia napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa uteuzi huu na kwa kweli natoa ahadi kwamba sitomwangusha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa naomba nijibu swali la Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha, Mbunge wa Serengeti lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, kutokana na madhara yanayosababishwa na wanyamapori hususani Tembo, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ili kunusuru maisha na mali za wananchi waishio kando ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Hatua hizo ni pamoja na zifuatazo:-

i. Kuunda timu ya udhibiti wa wanayamapori hatari na waharibifu ambayo inajumuisha watumishi kutoka kikosi dhidi ya ujangili cha Bunda, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Pori la Akiba Ikorongo, Halmashauri ya Wilaya na Mwekezaji Grumeti Reserves. Lengo ni kuhakikisha kwamba tukio lolote la uvamizi wa tembo linashugulikiwa kwa haraka iwezekanavyo.

ii. Kuweka minara au madungu (observation towers) ambayo hutumiwa na Askari Wanyamapori katika kufuatilia mwenendo wa tembo ili wanapotaka kutoka nje ya maeneo ya hifadhi hatua za kuwadhibiti zichukuliwe mapema, kama ilivyofanyika katika Kijiji cha Rwamchanga mpakani na Pori la Akiba la Ikorongo.

iii. Kutumia teknolojia ya mizinga ya nyuki ambayo huwekwa pembenzoni mwa mashamba na kufanya tembo wanapoingia katika mashamba yenye mizinga kufukuzwa na nyuki.

iv. Kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii ili wananchi waepuke kulima kwenye shoroba za wanyamapori pamoja na umuhimu wa kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyeikiti, aidha, Serikali ina mpango unaoendelea wa kutumia ndege zisizokuwa na rubani (UAV) kwa ajili ya kufukuza tembo. Mafunzo kuhusu matumizi ya ndege hizo yanaendelea kutolewa kwa watumishi kwa kushirikiana na Taasisi ya World Animal Protection (WAP).

(b) Mheshimiwa Spika, kulingana na Kifungu cha 71 cha Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009, Waziri mwenye dhamana ya Maliasili amepewa mamlaka kuandaa kanuni za malipo ya kifuta jasho au machozi kwa wahanga wa wanyamapori hatari. Aidha, Kanuni ya 3 ya Kanuni za malipo ya kifuta jasho au machozi za mwaka 2011, inaainisha kuwa malipo hayo yatafanyika endapo mwananchi atajeruhiwa au kuuawa, ama kuharibiwa mazao au mifugo na wananyamapori. Malipo hayo huzingatia uwezo wa fedha na upatikanaji wa taarifa za kweli kutoka kwa wahanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara itaendelea kurejea kanuni na viwango kadri hali ya maisha inavyobadilika.
MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:-
Wananchi wa Serengeti wamekuwa wakiathirika sana na wanyamapori hususan tembo ambao huharibu na kula mazao ya wananchi katika mashamba yao na kuikosesha Halmashauri mapato:-
(a) Je, Serikali itarejesha chanzo cha mapato yaani bed fee na sehemu ya gate fee kwa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti?
(b) Makampuni mengi ndani ya hifadhi yanagoma kulipa ushuru wa huduma (service levy) kwa Halmashauri. Je, Serikali inaisaidiaje Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kupata ushuru huu wa huduma?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha, Mbunge wa Serengeti, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Utalii Na. 29 ya mwaka 2008 ilifuta Sheria ya Hoteli Sura ya 105 ya mwaka 2006 iliyokuwa inaruhusu tozo za bed fee ambapo Tozo ya Maendeleo ya Utalii ilianzishwa. Tozo ya Kitanda Siku (Bed Night Levy) ambayo ni sehemu ya Tozo ya Maendeleo ya Utalii hukusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa niaba ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Tozo ya Maendeleo ya Utalii hugharimia shughuli za kuendeleza utalii nchini ikiwa ni pamoja na kutangaza vivutio vya utalii, kupanga hoteli kwenye daraja na kugharamia masuala ya kitaaluma yanayohusiana na utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Hifadhi za Taifa linayo mamlaka kisheria kusimamia kulinda na kuendeleza Hifadhi za Taifa. Aidha, makusanyo ya Gate Fee hufanywa na TANAPA ambapo kupitia vitengo vyake vya ujirani mwema vilivyoko kwenye kila hifadhi, huchangia moja kwa moja kwenye miradi ya maendeleo na huduma za kijamii pamoja na kutoa elimu ya mazingira kwa vijiji vinavyozunguka hifadhi hizo.
Kwa upande Wilaya ya Serengeti, kati ya mwaka wa fedha 2004/2005 mpaka 2014/2015, TANAPA iligharimia miradi 37 ya maendeleo na huduma za kijamii yenye thamani ya jumla ya shilingi 1,521,362,239.71.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu inayo taarifa kwamba kumekuwapo na mabishano ya kisheria baina ya Makampuni yanayotoa huduma kwa watalii na Halmashauri kuhusu uhalali wa makampuni hayo kulipa ushuru wa huduma, yaani Service Levy. Suala hili lipo Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, Civil Appeal No. 135 ya mwaka 2015 na kwa sababu hiyo, ni vema likasubiri maamuzi ya Mahakama. (Makofi)
MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:-
Wilaya ya Serengeti ni Wilaya yenye mbuga kubwa ya wanyama inayotambulika duniani na kupokea watalii wengi, lakini imekuwa kama kisiwa kwa kusahaulika kuunganishwa na barabara ya lami itokayo Makutano ya Musoma mpaka Mto wa Mbu:-
Je, ni lini barabara ya lami ya Musoma – Mugumu mpaka Mto wa Mbu itakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha, Mbunge wa Jimbo la Serengeti, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ta Makutano – Nata – Mugumu – Loliondo hadi Mto wa Mbu ina jumla ya kilometa 452. Kati ya hizo kilometa 192 zipo upande wa Mkoa wa Mara na kilometa 260 upande wa Mkoa wa Arusha.
Mheshimiwa Naibu Spika, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami, barabara ya kuanzia Makutano – Nata – Mugumu – Loliondo hadi Mto wa Mbu kilometa 452 umekamilika. Aidha, ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami unatekelezwa kwa awamu kutegemea na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya kwanza ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii, ulianza kutekelezwa kuanzia Makutano hadi Sanzate kilometa 50, mwezi Oktoba, 2013 na unaendelea. Aidha, ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya barabara iliyobaki ya Sanzate – Nata – Mugumu kilometa 75 na Loliondo hadi Mto wa Mbu kilometa 213 utatekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA (K.n.y MHE. MARWA R. CHACHA) aliuliza:-
Kumekuwepo na vifo vyenye utata wa kisiasa lakini inapotokea mpinzani kupoteza maisha havipewi kipaumbele katika upelelezi na hatua zinazochukuliwa:-
Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya hali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha, Mbunge wa Serengeti, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi Tanzania inathamini maisha ya raia wake wote bila kujali rangi, kabila, itikadi za kidini na itikadi za kichama. Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo ambapo katika utekelezaji wa majukumu yake hatua mbalimbali huchukuliwa ili kuhakikisha haki inatendeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imekuwa ikichukua hatua stahiki za kisheria kwa kila aina ya mauaji yanayotokea kwa raia na endepo mazingira ya mauaji yatakuwa yanalihusu Jeshi la Polisi basi Tume huru huundwa ili kuchunguza na kutoa ushauri kwa mamlaka husika na hatua stahiki huchukuliwa dhidi ya wahusika hao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutimiza wajibu wake wa kuwalinda wananchi wake pamoja na mali zao bila upendeleo wowote.
MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:-
Zao la tumbaku limekuwa likilimwa sana Wilaya ya Serengeti lakini kuna changamoto kubwa ya kukosa masoko.
Je, ni lini Serikali itasaidia upatikanaji wa kampuni zaidi ya moja kwenye ununuzi wa tumbaku ndani ya Wilaya ya Serengeti?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha, Mbunge wa Serengeti kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, majaribio ya kilimo cha tumbaku kibiashara Mkoani Mara yalianza mwaka 2008/2009 kwa lengo la kuwaelekeza wakulima kufuata mfumo wa Tanzania tofauti na hapo awali ambapo walilima tumbaku na kuuza kwa kufuata mfumo wa nchi jirani ya Kenya.
Kimsingi kilimo cha tumbaku mkoani Mara kulikuwa hakijaimarishwa na hivyo kutowanufaisha wakulima kama ilivyo katika maeneo mengine nchini. Aidha, kuendelea kulima tumbaku bila utaratibu maalum kulihatarisha kuenea kwa magonjwa ya tumbaku katika nchi hizi mbili.
Mheshimiwa Spika, msimu wa 2011/2012, Serikali kupitia Bodi ya Tumbaku ilirasimisha kilimo cha tumbaku mkoani Mara ikiwa ni pamoja na Wilaya ya Serengeti. Hatua ya kufunguliwa kilimo cha tumbaku mkoani humo ilitoa fursa kwa kampuni zilizopenda kununua tumbaku mkoani humo kufanya hivyo kwa kuzingatia kanuni na taratibu za zao hilo na pamoja na sheria nyingine za nchi. Hivi sasa Kampuni ya Alliance One ndio kampuni pekee inayonunua tumbaku mkoani Mara.
Mheshimiwa Spika, katika msimu wa 2013/2014 Serikali iliziandikia barua kampuni zote zinazonunua tumbaku nchini kuzijulisha uwepo wa fursa ya kuwekeza katika kununua tumbaku mkoani Mara. Hata hivyo, juhudi hizo hazijaleta matunda yaliyokusudiwa. Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wengine akiwepo Mheshimiwa Mbunge kuzishawishi kampuni hizo kuwekeza Wilayani Serengeti. Aidha, kwa kuwa Tanzania ina wanunuzi wachache, Serikali itaendelea kushawishi wanunuzi wengine hususan kutoka China kununua tumbaku ya Tanzania ikiwa ni pamoja na ya Wilaya ya Serengeti.
MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:-
Ujenzi wa Maabara za Shule za Sekondari Wilaya ya Serengeti umeshakamilika kwa kiwango kikubwa lakini maabara hizo zimebaki kuwa makazi ya popo:-
Je, ni lini Serikali italeta vifaa vya maabara kama ilivyoahidi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha, Mbunge wa Serengeti, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ina mahitaji ya vyumba vya maabara 63. Zilizokamilika ni 22 na zinatumika; maabara 29 zimekamilika lakini hazina vifaa na vyumba vya maabara 12 viko katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Mheshimiwa Spika, Serikali imetenga shilingi bilioni 16 kupitia mradi wa P4R kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya maabara zote zilizokamilika nchi nzima. Vifaa hivyo vinatarajiwa kupatikana kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MARWA R. CHACHA Aliuliza:-
Wilaya ya Serengeti ina Mbuga ya Wanyama ya Serengeti inayovutia watalii wengi duniani lakini inakabiliwa na uhaba wa maji.
Je, ni lini ujenzi wa chujio na usambazaji wa maji kutoka Bwawa la Manchira kwenda Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mugumu na vijiji vya jirani utakamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha, Mbunge wa Serengeti, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa chujio na usambazaji wa maji Mji Mdogo wa Mugumu utakamilika na kuanza kutoa huduma ifikapo mwezi Juni, 2017. Mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.49 kupitia Mkandarasi M/S Pet Cooperation wa Kahama kupitia Mamlaka ya Maji ya Mkoa wa Mara. Utekelezaji wa mradi umekamilika kwa asilimia 62.5 ambapo mkandarasi ameshalipwa shilingi milioni 933.8.
MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:-
Kumekuwa na mpango kabambe wa Mfuko wa Afya wa Bima (CHF) ambao ni “Papo kwa Papo na Tele kwa Tele”’ na Watanzania waliopo Serengeti wamekuwa wakichangia huduma hiyo lakini kila waendapo kwenye matibabu hupewa cheti badala ya dawa.
Je, ni lini Serikali itamaliza tatizo la ukosefu wa dawa kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma za afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mala Ryoba Chacha, Mbunge wa Serengeti kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa dawa unategemea upatikanaji wa fedha kupitia Mfuko wa Afya wa Pamoja ambapo Halmashauri hiyo imeshapokea fedha zote kiasi cha shilingi milioni 826.4 zilizotengwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri imepanga kutumia shilingi milioni 843 kwa ajili ya upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya vilivyopo. Kupitia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) Halmashauri zinakusanya mapato yatokanayo na uchangiaji kwa kuzingatia sheria ndogo za Halmashauri ambapo kipaumbele ni upatikanaji wa dawa. Natumia fursa hii kuzikumbusha Halmashauri kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuendelea kuhamasisha wananchi kuchangia mfuko.
MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:-
Wilaya ya Serengeti ni kitovu cha utalii na ni Wilaya inayopata watalii wengi lakini haina Hospitali ya Wilaya na hivyo kuleta usumbufu kwa wageni pamoja na wakazi wa Serengeti:- Je, ni lini Hospitali ya Wilaya itakamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha, Mbunge wa Serengeti, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Halmashauri
ya Wilaya ya Serengeti haina hospitali ya Wilaya, hivyo wananchi hutumia Hospitali Teule ya Nyerere yaani DDH ambayo inamilikiwa na Kanisa la Mennonite Tanzania. Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Serengeti ulianza mwaka 2009 katika Kijiji cha Kibeyo ambao unafanyika kwa awamu. Katika awamu ya kwanza, jumla ya shilingi bilioni 5.4 zilikadiriwa kutumika kwa ajili ya kuandaa michoro, kuanza ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje, pamoja na jengo la upasuaji (operating theater). Fedha hizo zinatarajiwa kupatikana kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo ruzuku kutoka Serikali Kuu, Mfuko wa Maendeleo wa Halmashauri, Benki ya Maendeleo ya Afrika, pamoja na mapato ya ndani ya Halmashauri (own source).
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa uandaaji wa michoro pamoja na jengo la upasuaji lenye vifaa vyote (operating theater) vimekamilika na kukabidhiwa kwa Halmashauri tayari kwa matumizi. Aidha, ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) upo katika hatua mbalimbali za ukamilishaji. Mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imeweka mpango wa kupeleka fedha ili jengo la wagonjwa wa nje (OPD) liweze kukamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni azma ya Serikali kukamilisha ujenzi wa hospitali mbalimbali za Wilaya hapa nchini ili kuwasaidia wananchi kupata huduma bora za afya.
MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:-
Katika bajeti ya 2016/2017 kipande cha barabara (Mugumu – Nata), ni barabara pekee inayounganisha Mkoa wa Mara na Arusha, kilitengewa fedha shilingi bilioni 12; tangazo la zabuni ya barabara lilitoka mara tatu na mwishoni mkandarasi wa kujenga barabara hiyo akapatikana, lakini Serikali ilikataa kusaini mkataba kwa maelezo kwamba Serikali haina fedha wakati fedha zilitengwa kwenye bajeti.
(b) Je, ni kwa nini Serikali haioni umuhimu wa barabara hii ambayo iko kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM?
(c) Je, Serikali inawaambia nini wananchi wa Mkoa wa Mara kuhusu ujenzi wa barabara hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hii ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu, naomba uniruhusu nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa rehema zake, na nimshukuru kipekee Mheshimiwa Rais kwa kuniteua ili niweze kutumika kama Naibu Waziri wa Ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha, Mbunge wa Serengeti, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara hii tayari imeshaiweka kwenye mpango wa ujenzi kwa kiwango cha lami barabara hii ya Mugumu – Nata yenye urefu wa kilimotea 41.725 na barabara ya kuunganisha Mji wa Mugumu zenye urefu wa kilometa 1.575 kwa kukamilisha usanifu wa kina na nyaraka za zabuni.
Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya uhakiki wa fidia ya mali za wananchi zitakazoathiriwa na ujenzi wa barabara ya Mugumu – Nata na tathmini hiyo imeshapelekwa kwa Mthamini Mkuu wa Serikali kwa mapitio na kuidhinishwa ili hatimaye malipo ya fidia kwa wananchi yafanyike.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilishaanza taratibu za ununuzi kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo, hivyo, baada ya malipo ya fidia kufanyika, taratibu za kumpata mkandarasi zitakamilishwa ili ujenzi kwa kiwango cha lami uanze. Aidha, kwa sasa Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) inaendelea kuifanyia matengenezo barabara ya Mugumu – Nata ili iweze kupitika majira yote ya mwaka.
MHE. SALOME W. MAKAMBA (K.n.y. MHE. MARWA R. CHACHA) aliuliza:-
Kiwanda cha Nguo cha MUTEX cha Musoma Mjini amepewa mwekezaji lakini mpaka sasa hakifanyi kazi vizuri:-
Je, ile ahadi ya Rais kurudisha viwanda visivyofanya kazi ipo katika hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanda cha Musoma Textile Mills Limited kilianza uzalishaji mwaka 1980 kikiwa na uwezo uliowekezwa wa mita milioni 22 kwa mwaka. Bidhaa zilizokuwa zinazalishwa kwa kutumia pamba inayolimwa nchini ni kanga na kitenge. Kiwanda hiki kiliwekwa kwenye utaratibu wa kufilisiwa mwaka 1996.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na madeni makubwa ya benki, zoezi la ufilisi lilichukua muda mrefu na kukamilika mwezi Juni, 2006 ambapo kiwanda husika kilibinafsishwa kwa utaratibu wa ufilisi kwa Kampuni ya Lalani Group 2006.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampuni ya Lalani Group ilifanya ukarabati wa kiwanda na kuanza uzalishaji ambao haukudumu kwa muda mrefu. Mwezi Mei, 2008, Kampuni ya Lalani Group iliuza mali za MUTEX kwa Tanzania Commodities Trading Company ambayo ni Kampuni tanzu ya Kampuni ya Mohamed Enterprise Limited. Mauzo hayo yalifanyika kati ya makampuni hayo mawili katika utaratibu ambao haukuhusisha Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda kilifanyiwa ukarabati na uzalishaji wa kanga na kitenge ukaanza mwaka huohuo wa 2008. Uzalishaji umekuwa siyo wa kuridhisha kutokana na kuwepo kwa ushindani mkubwa katika soko la bidhaa kama hizo zinazozalishwa na zinazotoka nje ya nchi. Ilipofika mwaka 2016, kiwanda cha MUTEX kilisitisha uzalishaji kutokana na ushindani kuwa mkubwa na hivyo kutokufanya vizuri katika soko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua changamoto hiyo, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Kilimo, ziliandaa Mkutano wa Wadau wa Nguo na Mavazi tarehe 20 Aprili, 2018 ili kujadili changamoto zinazoikabili sekta hiyo ambayo ni muhimu sana kwa ajira na uchumi kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, muafaka ulifikiwa kuhusu suala la ushindani usio wa haki katika soko kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania iimarishe udhibiti wa bidhaa za nguo kutoka nje na kutoza kodi stahiki kwa mujibu wa sheria na viwango vilivyowekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza agizo la Rais, tumekubaliana na mmiliki wa kiwanda cha MUTEX na ameahidi kuwa katika kipindi cha miezi miwili uzalishaji utaanza. Aidha, kiwanda kimeandaa mpango wa kupanua shughuli zake kwa kuwekeza kwenye mitambo ya kuzalisha vitambaa vya aina ya Denim (Integrated Denim Manufacturing Facilities) vinavyotumika kutengeneza mavazi aina ya jeans katika kukabiliana na ushindani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu itaendelea kumfuatilia mwekezaji huyu na kuhakikisha kuwa anazalisha kama alivyoahidi.
MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:-
Ili kuinusuru amani ya nchi yetu baada ya Uchaguzi Mkuu ni kuwa na Tume Huru ya uchaguzi:-
Je, ni lini itaanzishwa Tume Huru ya Uchaguzi kwa mujibu wa sheria?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha, Mbunge wa Serengeti, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeanzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 74(1)-(15) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo imeainisha na kufafanua kuhusu muundo, majukumu pamoja na uhuru wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika utekelezaji wa majukumu yake ya msingi.
Mheshimiwa Spika, tangu kuanzishwa kwa Mfumo wa Vyama vingi vya Siasa nchini mwaka 1992, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeratibu na kuendesha kwa ufanisi chaguzi tano za Rais, Wabunge na Madiwani pamoja na chaguzi ndogo mbalimbali za Wabunge na Madiwani.
Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huu, Tanzania tayari inayo Tume Huru ya Uchaguzi.
MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:-
Kumekuwepo na tabia ya askari wa SENAPA kuwakamata wananchi ndani ya hifadhi na wakati mwingine wasipouawa huwapeleka mbali na Mahakama za Wilaya ya Serengeti.
(a) Je, ni lini vitendo vya mauaji ya watu wanaozunguka Hifadhi ya Serengeti vitakoma?
(b) Je, ni lini askari wa SENAPA wataacha kuwapeleka watuhumiwa waliokamatwa ndani ya hifadhi nje ya Mahakama za Wilaya?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha, Mbunge wa Serengeti, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Askari wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali iliyopo. Ni kweli kwamba baadhi ya wananchi wamekuwa wakikamatwa na kufanya shughuli au kuingia kwenye hifadhi bila ya kufuata taratibu zilizopo. Wengi wamekuwa wakijihusisha na ujangili ndani ya hifadhi. Kwa msingi huo, Askari wa Hifadhi huwakamata watuhumiwa wote na kuwafikisha katika Jeshi la Polisi na hatimaye Mahakamani kwa hatua zaidi. Jumla ya kesi 437 zimefunguliwa na zipo katika hatua mbalimbali za usikilizaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imepakana na Wilaya nane tofauti. Mtuhumiwa anapokamatwa ndani ya hifadhi, anapelekwa katika Kituo cha Polisi kilicho jirani kwa hatua zaidi. Baadhi ya watuhumiwa wamekuwa na tabia ya kufanya uhalifu kwa kufuata mienendo ya wanyamapori wahamao. Kwa mfano, kati ya mwezi Mei na Juni ya kila mwaka, wanyama wengi wanahamia maeneo ya Kusini na Magharibi mwa Hifadhi ambapo kiutawala yako Wilaya ya Bariadi na Bunda.
Hivyo baadhi ya watuhumiwa kutoka Wilaya ya Serengeti huenda katika Wilaya nyingine kufanya ujangili wa wanyamapori ambapo kwa kipindi hicho hawapatikani kirahisi katika aneo la Wilaya zao. Kutokana na hali hiyo, watuhumiwa wamekuwa wakikamatwa na kushitakiwa katika Mahakama za eneo au Wilaya waliyokamatwa wakifanya uhalifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vyema wananchi wakazingatia taratibu zote za Hifadhi na niwaase wananchi hao kuachana na ujangili ili kuepuka adhabu hizo na kuwataka washirikiane na Serikali kulinda hifadhi za Taifa.
MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:-

Kulikuwa na mgogoro wa mipaka kati ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA) na vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo; wananchi wa vijiji hivyo walienda mahakamani na wakaishinda TANAPA kwa sababu mipaka iliyokuwa iwewekwa na TANAPA haikuwa shirikishi na haikufuata GN iliyoanzisha SENAPA:-

(a) Je, ni lini Serikali itapitia upya mipaka hiyo kwa kushirikisha vijiji husika na kuzingatia GN iliyoanzisha SENAPA?

(b) GN iliyoanzisha IKorongo Game Reserve inatofautiana na mipaka iliyowekwa; je, ni lini marekebisho yatafanyika ili iendane na GN?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha, Mbunge wa Serengeti, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, migogoro ya mipaka kati ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti na baadhi ya vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo haujatatuliwa kwa kuwa yapo madai ya Rufaa ya Ardhi Namba 256 ya mwaka 2018 katika Mahakama Kuu ya Jiji la Mwanza dhidi ya hukumu iliyotolewa na mahakama. Utatuzi wa mgogoro huo unasubiri matokeo ya rufaa iliyowasilishwa Mahakama Kuu dhidi ya hukumu iliyotolewa awali. Baada ya maamuzi ya mahakama kutolewa, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na vijiji husika itapitia upya mipaka kati ya hifadhi na vijiji kwa kuzingatia maamuzi ya mahakama.

(b) Mheshimiwa Spika, Pori la Akiba la Ikorongo lilianzishwa kisheria kwa GN 214 ya tarehe 10 Juni, 1994. Hapo awali pori hilo lilikuwa likisimamiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ambayo iliweka alama za mipaka ya pori hilo mwaka 2000 kwa kuzingatia GN husika. Aidha, kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi wa Kijiji cha Park Nyigoti yaliyoifikia Wizara yangu, kuwa sehemu ya eneo la kijiji hicho lipo ndani ya Pori la Ikorongo.

Mheshimiwa Spika, kufuatia kuwepo kwa malalamiko hayo, Wizara itashirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya uhakiki wa mipaka katika maeneo ya hifadhi yenye malalamiko ikiwemo kijiji cha Park Nyigoti ambacho kinapakana na Pori la Akiba Ikorongo.
MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:-

Mabwawa ya Mesaga, Nyamitita na Bugerera katika Wilaya ya Serengeti yalikuwa kwenye mchakato wa kujengwa kwa ajili ya umwagiliaji:-

Je, mchakato umefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha, Mbunge wa Jimbo la Serengeti, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa umwagiliaji Mesaga ulisanifiwa mwaka 2004 kwa ajili ya ujenzi wa bwawa na miundombinu ya shambani. Hata hivyo, fedha za ujenzi zilianza kupatikana mwaka 2014 na 2015 ambapo mradi ulipokea shilingi milioni 200 na shilingi milioni 198 mtawalia. Fedha hizo kwa pamoja zilitumika kuanza ujenzi wa utoro wa maji (spill way) kwa kuwa hazikutosha kuanza ujenzi wa tuta la bwawa na ujenzi wa mifereji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na changamoto ya fidia katika eneo hilo, Serikali imetoa maelekezo kwa uongozi wa wilaya kutatua mgogoro wa fidia kwa kupitia na kuhuisha gharama za mradi huo ili ziendane na wakati. Aidha, Serikali itashirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kuandaa andiko jipya la mradi kwa ajili ya kutafuta fedha za kukamilisha mradi huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa Nyamitita ulitekelezwa mwaka 2013 na unahusisha banio na mifereji ya umwagiliaji. Mradi huo unafanya kazi ingawa haujakamilika kutokana na ufinyu wa bajeti ambapo katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 217 ili kuendeleza ujenzi wa mradi huo na hivyo kuwanufaisha wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa umwagiliaji Bugerera unahusisha bwawa dogo la miundombinu inayoweza kumwagilia hekta 5 tu. Mwaka 2010, Serikali ilifanya upimaji na usanifu kwa ajili ya kuongeza ukubwa wa bwawa na kuongeza shamba la umwagiliaji hadi kufikia hekta 80. Aidha, Serikali itaendelea kutafuta fedha ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha mabwawa ya Mesaga, Nyamitita na Bugerera yanajengwa na kuwanufaisha wananchi wa Serengeti na Taifa kwa ujumla.
MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:-

Barabara inayojengwa kuunganisha Mkoa wa Mara na Arusha inasuasua sana, kwani tangu ilipoanza kujengwa 2013 mpaka leo hata kilomita 50 zimeshindwa kukamilika.

(a) Je, Serikali ina mkakati gani dhidi ya ukamilishaji wa barabara hii?

(b) Je, ni lini wananchi waliofanyiwa tathmini watalipwa fidia zao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha, Mbunge wa Serengeti, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara inayounganisha Mikoa ya Mara na Arusha yenye urefu wa kilomita 452 kutoka Makutano Juu (Musoma) – Natta – Mugumu – Loliondo hadi Mto wa Mbu ilifanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na kukamilika mwaka 2013. Aidha, baada ya kukamilika kwa usanifu ujenzi wa barabara hiyo umeanza kwa awamu ambapo kilomita 50 kutoka Makutano Juu hadi Sanzate na kilomita 49 kutoka Wasso hadi Sale Junction unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mkandarasi amechelewa kukamilisha kazi kwa wakati kutokana na changamoto mbalimbali. Hata hivyo, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia TANROADS imeshachukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha kuwa mkandarasi anamaliza kazi iliyobaki kwenye barabara ya Makutano – Sanzate inayotarajiwa kukamilika mwezi Septemba mwaka huu. Sehemu ya pili ya Sanzete – Natta yenye urefu wa kilomita 40 ipo katika hatua ya manunuzi kwa ajili ya kumpata mkandarasi. Aidha, kwa upande wa Mkoa wa Arusha, kilomita 49 kutoka Wasso hadi Sale ujenzi kwa kiwango cha lami unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wote waliofanyiwa uthamini wanaendelea kulipwa fidia zao kabla ya kazi ya ujenzi kuanza. Aidha, mpaka sasa waathirika nane (8) wamefidiwa kiasi cha shilingi 12.871 kwa Mradi wa Wasso – Sale kilomita 49. Katika Mradi wa Makutano – Sanzate kilometa 50 wananchi waliolipwa fidia ni watu 433 kwa jumla ya shilingi milioni 2.608. Ahsante sana.